Search This Blog

CHOZI LA YATIMA - 1

 

    IMEANDIKWA NA : ATUGANILE MWAKALILE



    *********************************************************************************





    Simulizi : Chozi La Yatima

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Ilikuwa ni furaha kwa Sam na Latifa dhidi ya binti yao mpendwa na wa pekee Safina, binti waliyempenda kuliko kitu chochote kwenye maisha yao.

    Walifurahi sana pale binti yao alipoweza kushiriki mashindano mbalimbali ya watoto na kushinda.

    Walifurahi sana kwa mtoto wao huyo kumshinda mtoto wa kijapan kwenye mashindano ya uchoraji.



    Safina alikuwa ni binti mdogo, mzuri na mwenye kipaji. Kwakweli mtoto huyu alibarikiwa.

    Na kutokana na uwezo walionao wazazi wake, waliweza kuzunguka nchi mbali mbali ambako Safina aliweza kuonyesha kipaji chake.

    Waliweza kuzunguka nchi kama vile Japan, Ujerumani, Uingereza na hata Marekani.

    Mtoto Safina alipendwa na wengi kwa sauti nzuri aliyokuwa nayo.



    Safina hakuwa muimbaji na mchoraji tu bali pia alikuwa na uwezo mkubwa sana darasani hata walimu wake walikuwa wanashangazwa na uwezo wa binti mdogo kama Safina.

    LUCY: Unajua watoto wengi wa matajiri huwa hawana akili, ila namshangaa sana huyu Safina.

    REHEMA: Sio peke yako madam, wote tunamshangaa huyu mtoto.

    Walimu wengi walionyeshwa kushangazwa na kipaji alichonacho Safina.



    Sam na Latifa walijisikia fahari sana kuwa na mtoto kama Safina.

    LATIFA: Safina, ukiwa mkubwa unataka kuwa nani?

    SAFINA: Mum, nataka kuwa mwanasheria.

    LATIFA: Vizuri mwanangu, kwanini umechagua sheria?

    SAFINA: Nataka kutetea haki za binadamu.

    Latifa alijivunia kuwa na mtoto mwenye utambuzi wa maisha kama Safina.

    Latifa alikuwa na furaha sana, ingawa mtoto mwenyewe alikuwa mmoja ila aliona ndiye anayemfaa.

    Kutokana na nyumba kubwa waliyonayo ikabidi Latifa amuombe mdogo wake Suzan ili aweze kuishi nao na pia awepo mahali hapo pindi wanaposafiri.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    LATIFA: Kwakweli mdogo wangu najivunia sana kwa mtoto niliyenaye.

    SUZAN: Hata na mimi najivunia dada, mtoto wetu ana vipaji bhana. Sijui karithi kwa nani?

    LATIFA: Itakuwa kwangu.

    SUZAN: Hahaha, labda arithi na hicho kipaji chako cha ubishi dada.

    LATIFA: Ushaanza maneno yako, utanikera sasa hivi.

    SUZAN: Eeh natania dada, jamani hutaniwi!!

    LATIFA: Haya yaishe.



    Sam na Latifa wakaamua kwenda kuishi nchini Marekani kwa muda na mtoto wao Safina.

    Huko marekani wakakutana na mambo mengi na kujuana na watu wengi zaidi.

    Kipaji cha Safina kilimfanya ajulikane na watu wengi nchini humo, hadi Sam akapata wazo la kuomba uraia wa huko.

    SAM: Nadhani itakuwa vyema kama tukiwa raia wa moja kwa moja huku.

    LATIFA: Sikubaliani nawe, kwani nchi yetu ni nzuri pia.

    SAM: Latifa sikiliza nchini kwetu hawajui kukuza vipaji vya watoto lakini tukiishi huku mtoto wetu atakuwa famous(maarufu) tena atajulikana ulimwengu mzima.

    LATIFA: Jamani Sam, yatupasa tufurahie nchi yetu pia. Matunda ya mtoto wetu yatambae nchini kwetu.

    SAM: Aah tatizo lako ubishi kipaji yani wewe huwa unabisha hata yale mambo ya ukweli. Ila kiukweli mimi kama mimi naichukia nchi yangu.

    LATIFA: Usiseme hivyo bhana, kumbuka nchi unayoichukia ndiko ulipozaliwa na ndugu wote wapo huko.

    SAM: Sawa mama mzalendo, ila nchi yetu imelala sana tena iko nyuma kimaendeleo.

    LATIFA: Sasa tusipoiamsha sisi unategemea nani aiamshe!!

    SAM: Acha kunichekesha Latifa, tangu lini nchi ikaamshwa na watu wawili?

    LATIFA: Simaanishi mimi na wewe tu ila na wengine wenye mawazo kama yako.

    Sam hakuafikiana kabisa na mkewe, akaamua kwenda kuomba ushauri kwa rafiki yake wa huko ambaye alimshauri pia kuomba uraia wa nchi hiyo ili kuendeleza kipaji cha mtoto wao nchini humo.

    SAM: Unajua Latifa umezidi ubishi, nimejaribu kuzungumza na rafiki yangu Mike, naye kanishauri kuwa tuwe raia wa huku.

    LATIFA: Mike anakupotosha nakwambia, kwanza yeye ni mzungu, pili ni raia wa huku ungedhani angekushauri vipi?

    SAM: Uzungu sio tija Laty hata wao wamejaa Afrika, cant you see?

    LATIFA: Kumbe unajua kuwa hata na wao wamejaa Afrika sasa wewe unachokitaka huku ni nini.

    SAM: Sikuwezi mama, kweli ubishi kipaji chako.

    LATIFA: Sio ubishi Sam huo ndio ukweli.

    SAM: Haya mama mshindi ni wewe.

    Latifa alikuwa hafurahishwi kabisa na swala la kuwa raia wa Marekani, Safina ni mtoto kwahiyo ni kama bendera yafata upepo watakachosema wazazi wake kwake inakuwa ni sawa tu.



    Akiwa nchini Marekani, Safina aliweza kushiriki matamasha mbali mbali na kujuana na watoto wa huko.

    Ni hapo alipojuana na binti mwingine mdogo ambaye alikuwa ni raia wa Ujerumani. Wakafurahiana kama watoto na wakapendana. Kwakweli Safina na huyo rafiki yake, Blenda wakapatana sana.

    Ila ni mtoto mmoja ambaye alijikuta akitamani kumfanyia jambo baya Safina baada ya kushindwa kwenye shindano na Safina kuibuka mshindi, alikuwa ni mtoto wa kijapan ambaye alikuwa na chuki za wazi wazi dhidi ya Safina. Mtoto huyo aliitwa Chuck.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku moja Safina na mama yake wakiwa wanatoka supermakert, akatokea mtu na kurusha risasi ilikuwa bado kidogo tu impate Safina, kabla hawajakaa sawa tukio lingine likawapata tena hapohapo.





    Tukio lingine likawapata Safina na mama yake, ilikuwa gari ikiwafata na ilibakia kidogo tu wabamizwe na gari ile hadi pale walipotokea maaskari, na uzuri wa kule askari wako makini sana.



    Wakarudi nyumbani wakiwa na hofu kubwa.

    LATIFA: Unaona Sam, hii nchi haifai. Nchi gani unakaa na roho mkononi! Bora turudi nchini kwetu.

    SAM: Ila Latifa kukimbia tatizo si njia ya kusuluhisha, inapaswa tutafute muafaka kwanza.

    LATIFA: Sam, nampenda sana mwanangu kwakweli siko tayari kumpoteza huku Marekani, bora turudi kwetu kama kujijenga kule kwetu tumejijenga sana, tuna nyumba nzuri tatu, tuna viwanja vikubwa tu viwili na magari matatu yanatutosha kabisa Sam. Bora turudi bhana.

    SAM: Tena umenikumbusha, nataka nikirudi ninunue tena magari mawili halafu nataka kuongezea shamba lingine.

    LATIFA: Hapo ndio unaponifurahisha Sam, kwakweli mtoto wetu hatakiwi kupata shida hata pale tutakapofilisika.

    SAM: Hakuna kufilisika hapa kwa kazi na biashara tulizonazo ila maisha hayatabiriki na ndiomana tumeweka akiba.

    LATIFA: Na hilo ndio jambo la muhimu sana tulilofanya, kuweka akiba itasaidia maisha yetu na ya mtoto wetu hapo badae.

    SAM: Ndio mke wangu, akiba ni bora sana kuwa nayo.



    Sam akaamua kufatilia kwa matatizo yaliyowapata mkewe na mwanae na mwisho wa siku akagundua ni nani aliyefanya majaribio hayo ya kumdhuru Safina, ila rafiki wa Sam alimuomba Sam asiondoke kwani yeye atashughulikia mambo yote na yatakuwa sawa.

    Nia ya Mike ilikuwa ni kumshirikisha Safina kwenye tamasha kubwa nchini humo kwani angejipatia faida kubwa ukizingatia Safina ni miongoni mwa watoto waliotokea kupendwa gafla na watu mbalimbali.



    Mike alimsisitiza sana Sam kuweza kuwepo kwenye tamasha hilo, ingawa Safina alishajinyakulia tuzo mbali mbali kwa kipaji chake ila Mike aliwasisitiza kuwa hilo tamasha litakuwa ni zaidi ya matamasha yote waliyowahi kushiriki.



    Sam akapigiwa simu kuwa anahitajika kwao mara moja, kwahiyo Sam ikabidi afunge safari ya kurudi Afrika ila alishindwa kurudi na familia yake kwakuwa Latifa alitakiwa kukamilisha mambo mengine kwahiyo ikabidi awaache na wao wapange ratiba ya safari nyingine.

    Siku ya safari, Latifa na mwanae Safina wakamsindikiza Sam hadi uwanja wa ndege.

    LATIFA: Sam nasikitika unaondoka peke yako ila na mimi na Safina nadhani tutarudi baada ya wiki hii.

    SAM: Usijari mke wangu, mimi nipo kwaajili yenu, malizia tu hiyo kazi ndipo urudi sawa? Halafu tukiwa huko tutapanga tena safari ya kuja huku.

    LATIFA: Sawa mume wangu ila ingependeza kama tungerudi wote, hata hivyo nitakuwa huko wiki ijayo mume wangu. Ila ufanye hima kuupokea siku hiyo.

    SAM: Usijari, nisipowapokea nyie nimpokee nani tena!!

    Wote wakakumbatiana na kuagana.

    Sam akawaaga na kuondoka kwenda kupanda ndege.

    SAFINA: Mum, mbona dady kawahi hivyo?

    LATIFA: Kuna vitu kaenda kurekebisha ila usijari sisi tutaenda wiki ijayo na utamwona tena dady wako.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sam alipofika nchini alijikuta amepooza sana, ingawa nyumbani kwao alikuwepo Suzan ambaye walizoea kumuacha mahali hapo siku zote.

    SUZAN: Shemeji mbona umewaacha dada na Safina?

    SAM: Kuna mambo anamalizia ila karibia atarudi.

    SUZAN: Basi siku atakayorudi uniambie ili twende wote kuwapokea.

    SAM: Usijari nitakutaarifu.

    Sam alikosa raha kabisa, alionekana ni mtu mwenye mawazo muda wote.



    Siku ikafika, Safina na mama yake wakajitayarisha ili kurudi nchini.

    SAFINA: Mum, nitamiss vitu vyangu vya hapa.

    LATIFA: Usijari mambo yakikaa sawa tu tutarudi tena huku na ukizingatia kuna tamasha ambalo Mike ameliandb na amesema lazima ushiriki kwahiyo tutarudi tu.

    SAFINA: Mum, kwahiyo tutamkuta dady anatungoja?

    LATIFA: Ndio lazima atupokee ingawa sijawasiliana nae siku mbili hizi ila anaijua ratiba nzima ya kurudi kwetu kwahiyo atatupokea tu.

    Latifa akafunga kila kitu cha kule ambacho ni mali yao na kumkabidhi Mike kama alivyoachiwa maagizo na Sam hapo kabla.

    Mike ndiye aliyewasindikiza Latifa na mwanae, huku akimsisitiza Latifa kuwa wasikawie kurudi ili waweze kuliwahi shindano aliloliandaa ambalo Safina naye alipaswa kushiriki.



    Safina na mama yake walikuwa na furaha ya kwenda kukutana na ndugu zao wengine lakini kubwa zaidi ni kukutana na Sam maana ndani ya wiki tu walikuwa wameshamkumbuka sana.



    Walipotua nchini jambo la kwanza walilotarajia ni kumuona Sam aliyetakiwa kuwapokea, ila waliposhuka waliangaza huku na kule bila ya kumuona Sam.

    Cha kushangaza Latifa aliwaona ndugu watano wa Sam, wanawake wawili na wanaume watatu wote wakiwa wamevaa nguo nyeusi hao ndio walioenda kumpokea Latifa na mwanae.

    Kwakweli Latifa alishangb sana kuwa kwanini apokelewe na wale wakati matarajio yake ni kupokelewa na mumewe bwana Sam.



    Walipokuwa pale uwanjani Latifa na mwanae walishangazwa kwa kutomuona Sam maeneo yale na badala yake wakawaona ndugu watano wa bwana Sam wakiwa wamekuja kuwapokea tena wakiwa na nguo nyeusi.

    Latifa akapatwa na mshtuko bila ya kujua kilichoendelea, ikabidi amsogelee mmoja wa wifi zake ili amuulize.

    LATIFA: Aisha nini kinaendelea? Mbona siwaelewi? Na Sam je yuko wapi?

    AISHA: Hakuna kitu wifi, tumekuja kukupokea tu.

    LATIFA: Na mbona mmevaa nguo nyeusi?

    AISHA: Wifi hizi ni nguo tu kama nguo zingine.

    LATIFA: Ndio mvae wote?

    AISHA: Jamani wifi, mara nyingine nguo huvaliwa kama sare.

    LATIFA: Sare ya nini?

    AISHA: Wifi una maswali mengi sana, ila tambua kwamba kila sare huvaliwa kwa shughuli maalum.

    LATIFA: Kama shughuli zipi?

    AISHA: Kheee! Wifi utajua tu hukohuko mbele ya safari.

    Latifa alijaribu kuhoji ila hakupewa jibu la moja kwa moja, akapakizwa kwenye gari na safari ikaanza. Latifa hakuelewa kitu kwakweli na alishindwa kuhoji zaidi. Safina alikuwa kimya muda wote kwani hakuelewa kinachoendelea ila hata yeye alishangazwa kwa kutomuona baba yake.

    SAFINA: Mum, where is dady?

    LATIFA: I dont know.



    Siku mbili kabla ya kurudi Latifa na Safina, Sam alipatwa na kizunguzungu cha gafla akiwa ndani na kuanguka, hakuweza kupata msaada mpaka pale Suzan alipofika na kumkuta Sam akiwa chini hajitambui, ndipo hapo Suzan alipopiga kelele na watu kuja kusaidiana nae kumpakiza ndani ya gari na kumpeleka hospitali.

    Walipofika tu hospitali, Suzan alishangaa kuwaona wakaka watatu wa Sam wakiwa hapo hospital yani kama vile walikuwa wanangoja apelekwe mahali hapo. Na bila kuchelewesha, wakapata taarifa kuwa Sam ameaga dunia.

    Kwakweli Suzan nguvu ilimuisha kabisa, hakuamini macho yake kwani shemeji yake hakuugua kabisa.

    Na tangu siku hiyo msiba ukawekwa nyumbani kwa Sam na siku ya kurudi Latifa na mwanae ndio ilipangwa kuwa siku ya mazishi, ndiomana wale ndugu watano wa Sam walienda kumpokea Latifa na mwanae kule uwanja wa ndege.



    Lile gari walilopanda likawapeleka hadi nyumbani, Latifa alishangazwa kuona umati mkubwa wa watu wakiwa kwenye nyumba yao.

    LATIFA: Kwani kuna nini? Sam yuko wapi?

    AISHA: Wifi, Sam amekufa?

    LATIFA: Unasemaje? Sam amekufa? Sam gani? Sam wangu mimi?

    AISHA: Ndio wifi Sam amekufa.

    LATIFA: Aaah!! Hapana, nakataa tena nakataa kabisa. Sam wangu hawezi kufa.

    Latifa hakuamini hata kidogo kuwa aliyekufa ni Sam, jambo hilo lilimfanya asilie wala kutoa chozi la aina yoyote.

    Wengi walitegemea kumuona Latifa akijitupatupa lakini haikuwa hivyo kwani alionekana kawaida tu.

    MTU 1: Pengine ndio uzungu jamani!!

    MTU 2: Wee, uzungu gani huo? Hata wazungu wanalia, labda huyu mwanamke amemloga mumewe ndiomana halii.

    MTU 3: Jamani mambo ya ulaya hayo, utajuaje kama ana tabia za kizungu!

    MTU 2: Makubwa haya sijapata kuona, yani mtu anashindwa kulia kwenye msiba wa mume wake loh!!

    Latifa bado alionekana kawaida kabisa ingawa mdogo wake Suzan alikuwa akilia na kujitupatupa ila Latifa wala hakuwa na machozi yoyote.

    MTU 1: Ona mdogo mtu anavyolia kama yeye ndo alikuwa mkewe, au naye alikuwa naye!

    MTU 2: Aaah wapi!! Huyo analia sana sababu alizoea vya ubwelele kutoka kwa shemeji yake.

    Ni kawaida ya msiba kupatwa na watu wambea na wanafki kazi yao kuangalia matendo yanayotokea ili kuyajadili.



    Ukafika muda wa kwenda kuaga mwili wa marehemu, watu waliaga kwa huzuni sana kwani Sam alikuwa mtu wa watu hakujua kumbagua mtu yeyote yule.

    Ikafika zamu ya Latifa kwenda kuaga, akainuka na mwanae, hakutaka kushikwa kabisa kwani aliamini kuwa yeye si mfiwa. Kila mtu alimshangaa Latifa.

    Alipofika kwenye jeneza, alisogea na kuangalia hakuamini macho yake kumuona aliye kwenye jeneza ni Sam, akamshika sura huku akisema,

    "Sam kumbe aliyekufa kweli ni wewe? Kumbe ulikuwa unaniaga mara ya mwisho? Ukaondoka peke yako na kufa peke yako, kwanini Sam, kwanini Sam ufe? Safina anakuhitaji Sam, sitaweza peke yangu? Siwezi mimi, kwanini Sam? Amka jamani Sam wangu, Saaaaam......!!!"

    Kimya cha gafla kikatanda, Latifa alianguka juu ya jeneza. Wakamtoa akiwa mtu asiyejitambua tena. Wakamkimbiza hospitali, Safina hakuelewa chochote, alikuwa analia bila kuelewa jambo lolote na hakujua kuwa abaki na jeneza la baba yake au akimbilie hospitali alikopelekwa mama yake.

    Kabla hawajakaa sawa, taarifa mbaya inaletwa kuwa Latifa nae ameaga dunia.

    Safina alilia sana kwani hakujielewa kabisa.



    Ikabidi wafanye mazishi ya Sam na Latifa kesho yake, Suzan alilia hadi kuzimia hakuelewa kwanini imekuwa vile ilivyokuwa.

    Sam na Latifa wakaenda kuzikwa makaburi yaliyopakana.

    Safina alilia sana kuona wazazi wake wakifukiwa kaburini, alilia sana bila ya kuelewa cha kufanya.

    Alikuwa akibembelezwa na Suzan ambaye alionekana kuwa na uchungu zaidi.



    Waliporudi nyumbani kutoka makaburini, Safina akaanza kumuuliza Suzan.

    SAFINA: Mamdogo, kwanini mumy na dady wamefukiwa?

    SUZAN: (Huku akitokwa na machozi), wazazi wako wamekufa Safina.

    SAFINA: Kwani kufa ndio nini?

    SUZAN: Wameenda kwa Mungu na hawatarudi tena duniani.

    SAFINA: Sasa ndio wawafukie? Inamaana sitawaona tena?

    SUZAN: Ndio Safina, hawapo tena duniani.

    Basi Safina alilia sana tena kwa uchungu kwani ilikuwa mara yake ya kwanza kusikia habari za kifo.

    Hakuna aliyeelewa ni nini kitatokea baada ya hapo.



    Safina alilia sana tena kwa uchungu kwani ilikuwa mara yake ya kwanza kusikia kuhusu kifo, Suzan ndio alikuwa mtu pekee anayemfariji Safina.

    Matanga yakapita na wakaanua msiba, na baadhi ya ndugu wakarudi makwao.



    Siku moja Suzan akiwa mtaani akasikia watu wakizungumza bila ya kujua kuwa Suzan alikuwa ndugu wa marehemu.

    MTU 1: Nakwambia shoga yangu, wale wamemuua ndugu yao ili wapate mali.

    MTU 2: Hivi wamemuua kweli eeh!

    MTU 1: Ndio, Sam alikuwa tajiri sana. Sasa ndugu zake wameamua kumloga ili afe wapate mali zake.

    MTU 2: Mmh!! Kama ndio hivyo kweli binadamu ni wabaya jamani.

    Suzan aliposikia hayo aliendelea kuumia sana moyoni.

    "yani wamemuua shemeji sababu ya mali loh!! Itabidi niwe karibu kuhakikisha Safina anapata haki yake"



    Lisemwalo lipo, kaka wakubwa wa Sam ni kweli walifanya ushirikina na kumuangamiza mdogo wao.

    Walishirikiana na mtu mmoja mganga katika kufanya yote yale. Kaka zake hao ni Juta na Jese.

    JUTA: Unajua kaka pale msibani ilikuwa bado kidogo yule mwanamke aharibu.

    JESE: Hivi yule Latifa angeharibu eeh

    JUTA: Ndio angeharibu, bora yule mganga alimuwahi na kummaliza palepale kwenye jeneza la mumewe.

    Mdogo wao Peter nae akawepo kuchangia,

    PETER: Kiukweli sijapendezewa kabisa kwani mwanzo mlisema mtamuweka Sam zezeta tu ila badae mkaamua afe moja kwa moja, sasa kwanini mkammalizia na mke wake jamani?? Sijapenda kwakweli.

    JUTA: Acha ujinga Peter, yule mwanamke ana mashetani bora tumemuwahi lasivyo angetuumbua pale. Wee si ulimuona mtu mwenyewe alivyoingia msibani!!

    PETER: Ila sijapenda kwakweli, hata kama Sam tumeshea nae baba tu ila bado ni ndugu yetu.

    Sam na ndugu zake hao walikuwa baba mmoja ila mama tofauti, na yeye Sam ndio akawa wa mwisho kwenye uzao wa baba yao ambapo baba yake na Sam aliyeitwa Dunia alipomuoa mama yake na Sam aliyeitwa Safina hawakufanikiwa kupata mtoto kwa muda muafaka kwasababu ya tatizo la kizazi alilokuwa nalo Safina, ni hapo mzee huyo akatafutiwa mke mwingine na wazazi wake ili kukuza familia ila hakuweza kumuacha Safina kwani ndiye aliyekuwa mwanamke ampendaye kwa dhati.

    Akaishi na huyo mke mwingine aliyeitwa Anah kwaajili ya kupata nae watoto ila mapenzi yake yote yalikuwa kwa Safina.

    Na Kweli akafanikiwa kupata watoto watano na mwanamke huyo ambao ni Juta, Jese, Peter, Aisha na modesta.

    Kipindi ambacho Anah akiwa na ujauzito wa mtoto wake wa tano huyo Modesta ndio kipindi hiko ambacho Safina pia akapata muujiza wa kuwa na ujauzito, jambo lililomfurahisha sana Dunia, mapenzi yake yakazidi maradufu juu ya Safina.

    Dunia akapoteza hata uelekeo kwa huyo mke wake mdogo na watoto wake, hata Modesta alipozaliwa alishindwa kuyapata mapenzi ya baba vizuri kutokana na baba huyo kuweka ukaribu zaidi kwa mke wake mkubwa hadi pale alipomzaa mtoto aliyepewa jina la Sam, wakampenda sana, wakampa kila atakacho na kutokana na tabia ya upole na ukarimu alionao mtoto wao ilifanya watu wengi wampende kitendo hicho kiliwachukiza kaka zake ambao walikosa kupendwa kutokana na ukorofi wao.

    Sam alikuwa katika maadili mazuri, akaweza kusoma na kuwa na mali. Akaoa mke aliyempata kipindi yuko masomoni, ila kwa bahati mbaya mama mzazi wa Sam alifariki kutokana na ugonjwa wa kisukari na hata hivyo mzee Dunia nae hakuchukua muda mrefu akafariki.

    Latifa alipojifungua mtoto wa kike, Sam akaamua kumuita Safina kama ukumbusho wa marehemu mama yake.

    Sam hakuacha kuwapenda ndugu zake, aliwapa vitu vingi na kuwasaidia mambo mengi ila hakujua kama kikulacho kinguoni mwako kwani ndugu wengi wa Sam hawakufurahia utajiri alionao, hawakufurahia mali alizonazo, hawakupenda maisha ya furaha aliyoishi na mke wake ndiomana wakafanya kila njia kumteketeza na kumuangamiza na kweli wakafanikiwa kwani Sam akafa katika mazingira ya kutatanisha wakasingizia presha imemuua kumbe kuna mengi nyuma ya pazia ambayo si rahisi kuyajua kwa haraka.

    Walichotaka kikafanikiwa, na Sam kumuangamiza.



    Ikafikia siku ya kugawana mirathi, upande wa kike haukuhusishwa ingawa Suzan hakutaka kukaa mbali ili aweze kuitetea haki ya Safina.

    AISHA: Hivi wewe Suzan ukoje? Kikao hiki ni cha ndugu, wewe hakikuhusu hata kidogo.

    SUZAN: Hata mimi ni ndugu kwani dada yangu aliolewa kwenu.

    AISHA: Aliyeolewa ni dada yako na sio wewe, inakuwaje unang'ang'ania ukoo usio wako??

    SUZAN: Sijang'ang'ania kitu hapa ila na mimi nahusika.

    AISHA: Nishakwambia huhusiki, hebu toka na utupishe.

    SUZAN: Sitoki ng'oo hadi nijue kitakachoendelea hapa.

    Suzan akatulia pale pale kwenye kikao kisicho rasmi, Juta ndio akagawa hiyo mirathi. Wakamgawa na Safina kuwa itabidi akaishi nyumbani kwa Juta huko mkoani.

    SUZAN: Haiwezekani, mtagawanaje mali zote ninyi na kumuacha Safina wakati Safina hizi mali ni za wazazi wake?

    JUTA: Wewe kwanza hayakuhusu, vilevile Safina ni mtoto mdogo tena wa kike atapata mali kwa mumewe pindi akiwa mkubwa.

    SUZAN: Haiwezekani, hata mtoto wa kike ana haki yake. Ila nawaomba kitu kimoja tu mwacheni Safina nikaishi nae mimi kwani ameshanizoea.

    AISHA: Hahaha, acha kutuchekesha Suzy. Utaenda kuishi nae wapi? Ikiwa ulizoea vya kupewa na shemeji yako hapa!!

    JUTA: Kwanza wewe Suzy nenda zako, mambo ya ukoo huu hayakuhusu kwahiyo yaache kama yalivyo.

    Suzan akainuka na kutoka nje kwa hasira huku akijisemea.

    "ila kweli Safina ni mtoto wa ndugu yao kwahiyo watamtunza tu"



    Suzan akiwa njiani akakutana na rafiki yake, Maria.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MARIA: Suzan mbona unaonyesha kuwa na hasira na unaongea peke yako?

    SUZAN: Maria, wee acha tu mambo yanayoendelea ni makubwa.

    MARIA: Makubwa gani tena??

    SUZAN: Si ule ukoo wa shemeji, kwanza hata arobaini bado wameshagawana mali na kumsahau kabisa Safina.

    MARIA: Unajua Suzy, kitu pekee cha kumlinda Safina ni sheria kwani sasa ameshakuwa yatima.

    SUZAN: Rafiki yangu, mtu mwenyewe anayemtetea Safina ni mimi pekeyangu. Na mimi sijui kabisa hayo mambo ya sheria.

    Kwavile Suzan hakuwa na mahali maalum kwa kipindi hicho ikabidi amuombe Maria hifadhi kwa muda.



    Suzan na Maria walipokuwa wanaondoka, wakakutana na tukio la kushangaza sana njiani.



    Suzan na Maria walipokuwa wanaondoka, njiani wakakutana na tukio la kushangaza sana.

    Walimuona mtu kama Latifa mbele yao,

    MARIA: Suzy, sio dada Latifa yule?

    SUZAN: Mungu wangu!! Ni yeye kabisa, ila dada yangu ameshakufa Maria.

    MARIA: Ndio ameshakufa, ila yule mbona ni yeye kabisa.

    SUZAN: Hata sijui jamani, tufanyaje sasa.

    MARIA: Twende tukamuangalie vizuri kama ni yeye au sio yeye.

    Suzan akawa anasitasita, Maria akamshika mkono Suzan na kwenda mbele yao walipomuona Latifa, ile wamemkaribia na kutaka kumgusa akatoweka. Kitendo hicho kiliwashtua sana Suzan na Maria, wakajikuta wakitimua mbio na sehemu ya kwanza kupumzika ni nyumbani kwa Maria.

    Wote walikuwa hoi huku wakihema juu juu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    SUZAN: Maria, mbona sielewi kitu?

    MARIA: Hata mimi sielewi kitu Suzy.

    Wakatafakari bila ya kupata jibu la moja kwa moja. Wakajikuta wakiogopa kufanya kitu mmoja mmoja kwa kuhofia lile tukio kuwapata tena, wakajikuta hadi kuoga wakienda pamoja. Amakweli mtu akifa amekufa yani hata kama ulikuwa nae karibu vipi ila akikutokea lazima upate hofu moyoni.

    SUZAN: Unafikiria ni kwanini tumemuona dada Latifa njiani wakati amekufa?

    MARIA: Kwakweli nilikuwa nasikia kwenye story tu ila kitendo cha kumuona dada Latifa njiani wakati amekufa nimeamini kweli dunia ina mambo na kumbe zile story huwa ni kweli.

    SUZAN: Sasa inamaanisha nini?

    MARIA: Huwa wanasema ni mambo ya kishirikina, eti huwa mtu hajafa kweli na roho yake huwa bado inazunguka duniani ndiomana anaonekana pale tulipomuona.

    SUZAN: Na mbona akatoweka?

    MARIA: Kwasababu ile ni roho tu Suzy, haya ni mambo ya kishirikina hatutayaweza kwa uhalisia.

    SUZAN: Kwahiyo hakuna la kufanya?

    MARIA: Ndio hakuna la kufanya Suzy.

    SUZAN: Niliwasikia watu wakisema kuwa shemeji amerogwa, sikujua kama na dada yangu ni vilevile dah!!

    Suzan na Maria hawakujua cha kufanya.



    Kesho yake Suzan na Maria wakaamua kwenda nyumbani kwa Sam kumuangalia Safina, walipofika walimkuta Modesta na Aisha.

    SUZAN: Aisha, Safina yuko wapi?

    AISHA: Ameshaondoka tangu jana na kaka Juta, anaenda kuishi nae kule kwake mkoani.

    SUZAN: Yani hamkutaka hata nimuage kidogo?

    AISHA: Umuage wewe kama nani?

    SUZAN: Hata hivyo, nia yangu haikuwa mbaya bali nilitaka kumchukua Safina ili nikaishi nae.

    AISHA: Nilishakwambia kuwa wewe huwezi kukaa na Safina bhana. Kwanza ondokeni hapa.

    Suzan na Maria wakaamua kuondoka mahali pale.

    Walipoondoka mahali pale ikabidi Modesta nae amuulize Aisha.

    MODESTA: Kwahiyo ndio mmeamua kabisa kumpa kaka Juta huyo mtoto?

    AISHA: Kwani kuna tatizo gani? Juta ni baba yake mkubwa.

    MODESTA: Ila kumbuka kwamba kaka Juta ana roho mbaya sana, na huyo mkewe Sarah ndio kabisa yani. Mwanamke mkatili sana yule, kwakweli Safina atajuta kule jamani.

    AISHA: Kwahiyo ulitakaje?

    MODESTA: Kwanini usingemchukua wewe yule mtoto?

    AISHA: Kwenda zako huko, siko tayari kulea mitoto ya watu. Kama vipi mchukue wewe.

    MODESTA: Ningekuwa na mahali maalum pa kukaa ningemchukua kweli ila mimi sio mtu wa kugombea mali za marehemu kama wewe na kaka zako.

    AISHA: Unanichekesha Mode, kwahiyo umekuja hapa kufanya nini?

    MODESTA: Kutembea tu ila badae naondoka, sina muda wa kugombea mali za marehemu, naridhika na nilichonacho. Ila kumbuka kuwa siku zote mali ya dhuluma ina mwisho wake.

    AISHA: Nenda zako na wewe, na utakufa na umasikini wako.

    MODESTA: Bora kufa masikini kuliko kufa na mali ya dhuluma.

    Modesta alimwambia maneno ya ukweli Aisha ila kama ilivyokawaida watu hupenda kuukwepa ukweli, kwahiyo Aisha alifanya kupotezea tu.

    Kule Marekani nako, Mike alikuwa anashangaa kwa ukimya wa rafiki yake kwani hakupata simu toka kwake wala taarifa lolote, na lile tamasha ambalo Safina alitakiwa ashiriki lilipamba moto.

    Mike alijiuliza maswali mengi sana juu ya ukimya wa rafiki yake, alitamani amfate ila alishindwa pa kuanzia sababu ya kukosa mawasiliano, hakuwa na la kufanya zaidi ya kuendelea kungoja tu hadi pale watakaporudi. Hakujua kama Sam alishakufa kwani hakupata taarifa yoyote ile.



    Suzan akaamua kwenda kwa mama yake ili akashauriane nae kuhusu mambo aliyoyaona. Mama yake huyo alikuwa ni mama mdogo wa Latifa kwani Latifa na Suzani walikuwa ni mtoto wa mama mkubwa na mdogo yani mtu na dada yake.

    Suzan alimweleza mama huyo aliyeitwa Deborah kila kitu alichokishuhudia na Maria.

    SUZAN: Yani mama sikuamini macho yangu kama kweli niliyemuona ni dada Latifa, wanasema ni mambo ya kishirikina kwamaana hiyo dada yangu amerogwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    DEBORAH: Mwanangu ni kweli kabisa usemayo, mambo ya aina hiyo huenda sambamba na ushirikina. Ila kwanini mimi ni mtu wa kuonewa hivi?

    SUZAN: Kwanini mama?

    DEBORAH: Alikufa dada yangu kipenzi ambaye ni mama wa Latifa, alikuwa kifo cha kushangaza sana, wakaniambia ni ushirikina nami nikatulia kwakuwa kupambana siwezi. Akafa kaka yetu aliyebakia kama msaada kwangu naye ni ushirikina nikanyamaza. Na sasa ni mtoto kipenzi wa dada yangu, mtoto ambaye ni ukumbusho tosha kwangu, nae kafa kiushirikina na hapa pia nanyamaza sitafanya chochote kwakuwa sina la kufanya ila namuchia Mungu kwani najua siku moja uongo utajitenga kwenye ukweli.

    SUZAN: Kivipi mama?

    DEBORAH: Suzy mwanangu tambua kuwa ipo siku uongo utajitenga kwenye ukweli, hata Latifa alikataliwa na baba yake akiwa tumboni ila alipozaliwa mtoto kafanana nae hadi ukacha, hayo yote Mungu huyafanya katika kumueleleza mwanadamu.

    SUZAN: Sawa mama, ila mtoto wa Latifa nae kanyimwa mali zote. Watu wamenishauri kuwa sheria ndio itakayomlinda Safina.

    DEBORAH: Unajua sheria mwanangu?

    SUZAN: Sijui chochote kuhusu sheria mama.

    DEBORAH: Najua hujui, na pia najua utakuwa unajutia kwa kutopenda kusoma, ila hata mimi sijui sheria mwanangu cha msingi tumuombee tu Safina ili siku moja apate haki yake.

    SUZAN: Hiyo siku itakuwa lini jamani mama?

    DEBORAH: Siku hiyo ambayo uongo na ukweli utajitenga, tumuachie Mungu mwanangu yeye anaweza yote na ndio mtoa haki.

    SUZAN: Sawa mama.

    Suzan hakuwa na budi zaidi ya kukubali vile ambavyo mama yake amesema.



    Safina akiwa nyumbani kwa baba yake mkubwa, kwakweli hakuyaweza kabisa maisha ya pale ukizingatia mke wa mzee huyo alikuwa na roho mbaya na roho ya ukatili, na akajikuta akimchukia sana Safina, alimsema kila afanyacho na alikuwa akimtesa huku akimpa kazi nyingi ambazo Safina hakuwa na uwezo nazo.

    SARAH: (Akiongea kwa ukali), mbona hujaosha vyombo?

    SAFINA: I'm sorry mum.

    SARAH: Mara ngapi nimekukataza kuongea kizungu kwenye nyumba yangu? Unataka kunitusi ili nisielewe? Punguani mkubwa wewe, kuja hapa.

    Yule mama akamvuta Safina na kumpiga makwenzi, na kumfinya huku akimpiga mabao bila ya kujali kuwa yule ni mtoto mdogo tena yatima anayehitaji faraja.

    Safina akawa analia tu kwani kila siku ilikuwa ya mateso kwake.

    Siku zikaenda na mateso nayo yakazidi, na ikawa hakuna kwenda shule wala wapi.

    Siku moja yule mwanamke akampiga sana Safina kwa kosa la kuvunja kikombe wakati anaosha vyombo, alimpiga sana na kumfukuza kabisa.

    Safina alilia sana huku asielewe pa kwenda, ila aliondoka huku akiomba Mungu amsaidie. Alipofika stendi alikutana na gari la mizigo linaloenda mjini, akaomba msaada nao wakamfikisha hadi mjini. Alipokuwa mjini, alipita mzee mmoja mwenye gari na kumuuliza Safina kwasababu ilikuwa jioni.

    MZEE: Wewe si ndiye Safina mtoto wa marehemu Sam?

    SAFINA: Ndio ni mimi.

    MZEE: Unaenda wapi sasa?

    SAFINA: Nataka kwenda nyumbani.

    MZEE: Haya panda kwenye gari nikupeleke.

    Safina akapanda kwenye gari la yule mzee na yule mzee akamfikisha Safina hadi kwenye geti la nyumba yao halafu akamshusha na kwenda zake.

    Safina akagonga geti lao, hiyo ilikuwa kwenye mida ya saa moja jioni. Mlinzi akamfungulia, alipomuona kuwa ni Safina alifurahi sana ingawa alisikitishwa na hali aliyokuwa nayo Safina, basi Safina akaingia ndani na kutembea taratibu mpaka kwenye mlango wa nyumba yao, akufungua mlango na kuingia ndani.

    Alipoingia sebleni akamkuta shangazi yake na baba yake mkubwa wakiwa wameshika makaratasi ambayo hakuelewa yalikuwa ya nini.

    Safina alidhani watafuraì kumuona ila ilikuwa kinyume, kwani walipomuona tu wote wawili walishtuka na kumuuliza kwa pamoja.

    "unafanya nini hapa?"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Safina alishangaa swali hilo kwani watamuulizaje wakati pale ni kwao.

    AISHA: Wewe hujibu?

    SAFINA: Nimeamua kurudi nyumbani.

    AISHA: Umeamua kurudi nyumbani? Jibu gani hilo, mtoto wewe una kiburi sana.

    SAFINA: Sio kiburi, mama mkubwa amenifukuza kule.

    JUTA: Wee muwie radhi mke wangu hawezi fanya huo upuuzi, kwanza hebu tuondolee uchafu hapa.

    AISHA: Mmh kaka nawe!!

    JUTA: Nini sasa Aisha, umeanza kumtetea huyu mtoto.

    SAFINA: (Akidhania kuwa atapata ukombozi kutoka kwa shangazi yake huyo), nisaidie shangazi.

    AISHA: Kheee!! Unataka kuamia kwangu tena? Haya toka nje, husikii eeh!!

    Aisha akaanza kumburuta Safina hadi nje.

    Safina alilia na kusikitika sana kitendo cha yeye kufukuzwa kwenye nyumba yao.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog