Search This Blog

ROHO YAKE INADAI - 2

 

    Simulizi : Roho Yake Inadai

    Sehemu Ya Pili (2)





    .

    “Karibu,” alisema Mrs Garett akiufungua mlango kumkaribisha Padri Alfonso. Padri huyo alikuwa amevalia shati jeusi alilolichomekea vema, shingoni lilikuwa na doa jeupe. Mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea Biblia ya zamani.

    .

    .

    “Ahsante,” akasema kwa tabasamu, akazama ndani na kuketi kwenye kiti. Naye Mrs Garett akaketi akimwita Olivia ambaye alimwagiza alete chai kwa ajili ya mgeni.

    .

    .

    Padri akautazama uso wa Mrs Garett uliokuwa umeharibika kwa majeraha, akamuuliza mwanamke huyo, “Ni mume wako?”

    .

    .

    Mrs Garett akatikisa kichwa pasipo kutia neno. Macho yake yalikuwa mekundu, mdomo wake ulikuwa umevimba na upande wa juu wa shavu lake la kushoto kulikuwa kumevilia damu.

    .

    .

    “Pole sana.”

    .

    .

    “Nashukuru, usijali,” Mrs Garett akasema akijitahidi kutabasamu.

    .

    .

    “Yupo wapi sasa?”

    .

    .

    “Ameondoka. Alisema anasafiri hivyo atarejea kesho asubuhi.”

    .

    .

    Padri akatikisa kichwa. Baada ya muda mfupi mlango ukagongwa, akaingia mwanadada aliyekuwa amevalia sare ya mtawa wa kike rangi nyeusi na nyeupe. Mwanamke huyo mrefu mwembamba alikuwa amebebelea chupa mkononi mwake na sanamu ya msalaba yenye ukubwa wa wastani.

    .

    .

    “Anaitwa dada Magdalena. Tutakuwa naye kwa ajili ya sala,” alisema Padri. Mrs Garett akaagiza chai kwa ajili ya dada huyo.

    .

    .

    “Karibu sana, dada.”

    .

    .

    “Ahsante, nimekaribia.”

    .

    .

    “Nimefurahi sana kuja kunitembelea, natumai tatizo langu litakoma.”

    .

    .

    “Kwa uweza wa Mungu, litawezekana,” akasema Padri Alfonso. “Natumai tukitoka hapa, roho hiyo haitarudi tena kwenye makazi haya. Itakuwa mwanzo na mwisho!”

    .
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Basi baada ya maongezi hayo mafupi, mazingira yakaanza kuandaliwa kwa ajili ya sala. Olivia alikuja sebuleni, taa zikazimwa na mishumaa ikawasha na ile sanamu ya msalaba ikasimamishwa mezani.

    .

    .

    Dada Magdalena akachovya mkono kwenye maji yaliyokuwa ndani ya chupa na kukung’utia kwenye kila kona ya sebule akiteta maneno kadha wa kadha ya sala. Baada ya hapo akaungana na Padri Alfonso kuanza kusali, Mrs Garett pamoja na Olivia wakifuatisha yale yaliyokuwa yanatamkwa.

    .

    .

    Wakasali kwa takribani nusu saa. Wakiwa wanaendelea kufanya vivyo, Olivia akafungua macho yake na kuangaza. Akatupa macho yake huku na kule kana kwamba mtu anayehisi kitu.

    .

    .

    Mbali na sauti ya sala, kuna sauti nyingine alikuwa anaisikia kwa mbali sikioni mwake ikinong’oneza. Sauti ya mtoto wa kike. Sauti ikimwita jina lake.

    .

    .

    “Oliiviaaaa … Oliiviaaaa … njoo kwangu. Oliviaaaa … Oliviaaaa …. Njoo kwa …”

    .

    .

    Mara akamwona binti mdogo mlangoni! Binti huyo alikuwa ameshikilia mdoli mkono wake wa kuume. Alikuwa anamtazama Olivia kwa macho makali na kinywa chake amekiachama.

    .

    .

    Akaanza kupiga hatua kumsogelea Olivia. Hatua zake zilikuwa nzito kinyume kabisa na mwili wake. Kila alipokanyaga chini ilisikika tih! Tih! Tih!

    .

    .

    Olivia akajawa na woga mkubwa, akapiga kelele kali sana na kumshtua kila mtu!

    .



    .

    Kila mtu akaangaza. Hawakuona jambo. Wakamtazama Olivia na kumuuliza nini kimemsibu. Olivia akanyooshea mkono wake mlangoni.

    .

    .

    “Ni nini, Olivia?” mama akauliza kwa ukali kidogo.

    .

    .

    “Nimemwona mtu, mama. Nimemwona mtu mama!” akalia Olivia.

    .

    .

    “Umemwona wapi?” akauliza mama akiangaza macho yake. Olivia akaendelea kunyooshea mkono wake mlangoni. Macho yake yalikuwa yanatema machozi. Uso wake umejawa na mashaka tele.

    .

    .

    “Nimemwona pale mlangoni. Mtoto mdogo mwenye mdoli mkononi!”

    .

    .

    Mama akashika mdomo wake. Akamtazama Padri Alfonso na dada Magdalena.

    .

    .

    “Usijali, Mrs Garett,” akasema Padri. Akainama na kumshika mikono Olivia. Akamtazama kwa macho ya upole na tabasamu kwa mbali. “Mtoto mzuri Olivia, usiogope. Sawa? Sasa hivi tukienda kusali, usifumbue macho yako mpaka tutakapomaliza. Umesikia?”

    .

    .

    Olivia akatikisa kichwa kukubali aliachoambiwa. Bado macho yake yalikuwa yanatoa machozi na uso wake ukisema hofu. Padri akamfuta machozi kwa vidole vyake kisha akambusu kwenye paji lake la uso. Akamkumbusha tena, “usifungue macho yako.”

    .

    .

    Basi baada ya kumwambia hivyo, Padri akamtazama Dada Magdalena na kumpatia ishara ya kichwa. Dada huyo akachovya mkono wake kwenye maji na kukung’utia kule ambapo Olivia alisema amemwona mtu. Alipomaliza akajumuika na wenzake na kuanza kusali upya.

    .

    .

    Zikapita dakika nne za sala. Watu wote walikuwa wamefumba macho yao. Ni sauti tu ya padri ndiyo ilikuwa inasikika hapa. Na mbali na mishumaa ile iliyokuwa imewekwa pale mezani, hakukuwa na chanzo kingine cha mwanga humu ndani.

    .

    .

    Katika dakika hiyo nne ya sala, Olivia ambaye alikuwa ameyafumba macho yake kwanguvu akaanza kuhisi kitu. Alihisi kuna mtu anatembea akitokea kule koridoni kuja sebuleni. Akaogopa sana. Alinyamaza kimya na akijitahidi kutoyafungua macho yake kama alivyoelekezwa, lakini sikio lake la kushoto bado likaendelea kumfanya ahofie zaidi na zaidi.

    .

    .

    Vishindo vya mtu vilikuwa vinasikika vikifika sebuleni, na kisha vinafifia kwenda koridoni. Vinakuja tena na tena vinarudi kwenda koridoni. Zoezi hili lilijirdia mara tatu. Mara ya nne, vishindo vya miguu vilipokuja sebuleni havikurudi tena koridoni. Vikabakia palepale sebuleni!

    .

    .

    Hapa Olivia akahisi kubanwa na mkojo. Mwili wake ulisisimkwa sana. Alihisi baridi la ajabu linampitia na kila kinyweleo kilichopo kwenye mwili wake kimemsimama! Alitamani kukimbia. Alitamani kukaa. Alitamani kulia, alitamani kunyamaza. Alijikuta anatamani kila kitu!

    .

    .

    Ila kwa muda kidogo akahisi kimya. Hakusikia tena vishindo vya mtu na basi akapata angalau ahueni. Huenda mtu huyo atakuwa ameondoshwa na maombi. Akatamani kufungua macho yake atazame, ila akaogopa. Aliona ni kheri asifumbue macho hayo kama alivyoelekezwa kwani anaweza kuona mambo atayoshindwa kuyastahimili.

    .

    .

    Akaendelea na zoezi lake. Ila baada ya dakika moja, akaanza kusikia tena vishindo vile vya binadamu! Moyo wake ukaanza kupiga makasi. Ubaya ni kwamba vishindo hivyo vilikuwa vinamjongea! Na vilipomfikia karibu kabisa vikasimama. Kwa mbali sauti ya kike ikaita,

    .

    .

    “Oliviiaaa …”

    .

    .

    Sauti hii ilikuwa mithili ya upepo. Ilikuwa ni ya baridi sana. Ilipofika kwenye sikio la Olivia ilimfanya mtoto huyo ahisi baridi kali sikioni na shingoni. Alitamani kupiga kelele, lakini akajizuia. Ilihitaji moyo mkubwa sana kuvumilia haya.

    .

    .

    “Oliviaaaa … amka, amka! … Oliviaaaa … amka! Njoo uone mchezo mzuri kule msituni, kweli utafurahia! …” sauti ya baridi ilipulizia sikioni mwa Olivia.

    .

    .

    “Najua unataka kuuona … njoo, twende Oliviaa … twende upesi!”

    .

    .

    Olivia akajitahidi sana kujikaza. Hakufungua macho yake kumwona mtu huyo anayemwongelesha, wala hakumjibu. Alikuwa amefunga tu macho na kinywa chake japo anahofia sana.

    .

    .

    Basi baada ya mtu huyo kuona Olivia hasikii, akamsogelea karibu zaidi na kuanza kumshika! Kiganja chake cha baridi kilipapasa mkono wa Olivia, ukapandisha mpaka shingoni mwake. Ukapapasapapasa shingo ya Olivia, na kisha ukadumbukia mgongoni mwa mtoto huyo na kuendelea kumpapasapapasa!

    .

    .

    Hapa Olivia akashindwa kubana mkojo, akajikuta analowanisha mapaja yake kwa woga. Akatetemeka kwa hofu kupita kiasi, na kama zoezi hili lingeendelea kama kwa dakika mbili mbele, Olivia angepiga kelele na kufumbua macho, ila bahati likakoma na akabaki salama!

    .

    .

    Akahema kwanguvu. Akatazama kushoto na kulia, hakuhisi kitu. Akaendelea kuhema kwanguvu moyo wake nao ukipiga kwanguvu kwenda pole. Ikapita dakika moja kukiwa kimya.

    .

    .

    Ikapita dakika ya pili kukiwa kimya.

    .

    .

    Ikapita dakika ya tatu kukiwa kimya.

    .

    .

    Kwenye dakika ya nne Olivia akaanza kusikia kitu ambacho kilimshangaza. Si vishindo vya mtu wala kiganja kikimpapasa, bali sauti ya Padri Alfonso na Dada Magdalena. Watu hao walikuwa wanateta na kucheka. Wanagonga mikono yao na pia kulia!

    .

    .

    Olivia akaachama mdomo wake kwa kustaajabu. Hakuwa anaamini alichokuwa anasikia. Padri Alfonso na Dada Magdalena! Haiwezekani! Akatikisa kichwa chake. Hapana. Akatikisa kichwa chake. Hapana. Alikuwa haamini kitu alichokuwa anasikia. Alfonso na Magdalena walikuwa wanasali, ndivyo alivyokuwa anaamini na si vinginevyo.

    .

    .

    Lakini masikio yake yalikuwa yanamwambia tofauti. Padri Alfonso na Dada Magdalena walikuwa wakipanga kuwamaliza. Alfonso na Magdalena walikuwa wanapanga kuwatupia kule msituni! Na walipoelezana hayo wakawa wanacheka kwanguvu. Wanacheka kishetani!

    .

    .

    Olivia akafungua macho yake kwa mbali apate kutazama kama ni kweli alichokuwa anasikia. Alishindwa kuvumilia. Alitaka kushushudia namna ambavyo Padri na Dada walivyokuwa wanapanga madhalimu juu yao.

    .

    .

    Alichokiona kikamtisha, na kikamfanya afungue macho kwa nguvu kukodoa asiamini. Alimwona Padri Alfonso akiwa na uso mweusi, macho mekundu yenye mboni mithili ya mbuzi, meno makali yaliyochongoka, masikio marefu na ulimi mrefu mwembamba.

    .

    .

    Dada Magdalena alikuwa na uso mweupe pe wenye michirizi meusi. Macho yake yalikuwa mekundu na makubwa. Mdomo wake ulikuwa mweusi kana kwamba kunguru. Meno yake yalikuwa yamekaa hovyo na yenye rangi ya kuoza.

    .

    .

    Punde Olivia alipokodoa macho yake, Padri Alfonso na Dada Magdalena wakamtazama wakiwa wamekodoa. Nyuso zao zilikuwa zimesimama tuli kana kwamba zimegandishwa. Mara ghafla shingo zao zikaanza kupinda na kupeleka vichwa vyao kushoto, kulia, juu na chini! Kushoto, kulia, juu na chini!

    .

    .

    Olivia akamtazama mama yake kwa hofu. Mama alikuwa amefumba macho hajui kinachoendelea. Olivia akamwita na kumwita. Akamvuta mkono na kumtikisatikisa ila wapi! Mama hakufungua macho wala kumtazama.

    .

    .

    Basi padri Alfonso na Dada Magdalena wakaanza kumjongea. Olivia akamvuta mamaye kwanguvu sana kumwamsha aone, ila jitihada zake hazikuzaa matunda. Mama alikuwa kwenye usingizi mzito sana. Ni kana kwamba ametiliwa kiasi kingi cha madawa ya kulevya!

    .

    .

    Padri Alfonso na Dada Magdalena wakazidi kumsogelea Olivia wakitembea kama watu wasiokuwa na mifupa, wakijikunjakunja , wakijipindapinda, wakijikunjakunja na wakijipindapinda. Wakitazama kana kwamba watu wasiokuwa na kope.

    .

    .

    Mdomo wa Padri Alfonso ukaanza kuchuruza damu iliyofika kidevuni mwake na kudondokea chini. Macho ya Dada Magdalena nayo yakaanza kuvuja damu, ikipita mashavuni mwake na kudondokea chini.

    .

    .

    Walipomkaribia Olivia wakakunjua mikono yao yenye vidole vyembamba na kucha ndefu wakitaka kumyaka binti huyo. Olivia akapiga kelele kali sana akimkumbatia mama yake kwanguvu. Mara mama akafungua macho na kumtazama, “Una nini Olivia?”

    .

    .

    Olivia akamtazama mama yake akiwa anahema kwa hofu, akamnyooshea kidole upande wa Padri Alfonso na Dada Magdalena.

    .

    .

    “Kuna nini?” mama akauliza. Hakuwa anaona kitu. Hakukuwa na kitu. Padri Alfonso na Dada Magdalena nao wakaduwaa wakimtazama. Wote walikuwa kwenye hali yao ya kawaida.

    .

    .

    “Nini, Olivia?” Padri Alfonso akauliza akimjongea mtoto huyo. Olivia akapiga kelele kali na kukimbilia nyuma ya mgongo wa mama yake kujificha. Akalia sana.

    .

    .

    “Olivia,” Padri akaita. “Olivia, ulifungua macho?” akauliza kwa sauti ya chini akijaribu kumtazama binti huyo, ila Olivia hakutaka kabisa kumtazama Padri. Kadiri Padri alivyokua anasogea, ndivyo naye akawa anasonga mbali naye. Ila upande wa pili alipokuwa anaelekea akakutana na Dada Magdalena, naye akamuuliza, “Ulifungua macho?”

    .

    .

    Olivia akapiga tena kelele kali. Mama akamnyanyua na kumbeba.

    .

    .

    “Olivia, una nini?”



    .

    Olivia akamtazama mama yake na kumwambia kuwa Padri Alfonso na Dada Magdalena ni watu wa ajabu. Ameona kwa macho yake na akasikia kwa masikio yake wakipanga kuwaua na kwenda kuwatupia msituni.

    .

    .

    Mama akastaajabu. Akamwona Olivia amechanganyikiwa. Akajaribu kumtuliza na kumwambia alichokiona ni ndoto ama maruweruwe tu, si uhalisia.

    .

    .

    “Hapana!” Olivia akatikisa kichwa akilia. “Ni majini, mama! Ni majini!” Olivia akafoka. Padri Alfonso akatazamana na Dada Magdalena kwa macho ya mshangao. Walikuwa wanajiuliza ni nini kimemtokea binti yule kiasi cha kuropokwa namna hiyo.

    .

    .

    Lakini kila Padri Alfonso alipotaka kumjongea Olivia kumtuliza na kumsihi, Olivia akapiga kelele. Hakutaka mwanaume huyo amsogelee hata kidogo. Alimwogopa mno kama ukoma. Ikafikia kipindi mama ikambidi aende na Olivia chumbani.

    .

    .

    “Tulia hapa, sawa?” mama alimweka Olivia kitandani. “Hautaona wala kuhisi chochote. Sisi tutaendelea na kusali na tutakapomaliza, nitakuja kulala na wewe, sawa Olivia?”

    .

    .

    Olivia alikuwa anaogopa kuachwa mwenyewe, ila aliona ni kheri kuliko kwenda kule sebuleni kumwona Padri Alfonso na Dada Magdalena, basi akakubali japo kwa shingo upande.

    .

    .

    “Hatutachukua muda mrefu,” alisema mama, Mrs Garett, kabla hajambusu Olivia kwenye paji lake la uso na kwenda zake. Kwa nje akaufunga mlango. Olivia akabaki mwenyewe akiwa amejilaza na kuukumbatia mto alioufinya kwanguvu.

    .

    .

    Baada ya muda kidogo, akasikia sauti ya sala ikiwa inaendelea. Akiwa ametulia tuli, akawa anasikia kila kitu na kila jambo. Akafunga macho yake akitamani alale. Alitaka kutoka kwenye ulimwengu wake wa ufahamu kwa kuhofia pengine anaweza kuona mambo ambayo hataki kuyaona.

    .

    .

    Basi baada ya jitihada zake hizo, usingizi mwepesi ukamsomba na kumpatia amani ya muda. Na amani hii ikawa upande wake mpaka sala ilipokwisha.

    .

    .

    “Nashukuru sana,” Mrs Garett alimpatia Padri mkono wa shukrani. “Natumai hii haitakuwa mara yenu ya mwisho kuja hapa.”

    .

    .

    “Usijali,” akasema Padri Alfonso akitabasamu. “Tumetumwa kazi hii, nitajitahidi kukusaidia kwa kadiri niwezavyo, Mrs Garett.”

    .

    .

    Basi Mrs Garett akawasindikiza Padri Alfonso na Dada Magdalena mpaka nje ya nyumba yake na hatua kadhaa chache kisha akasimama akiwatazama wakitokomea.

    .

    .

    Alipojiridhisha akarudi zake ndani na kwenda kumwona Olivia moja kwa moja. Akamkuta amelala. Akaona si stara kumsumbua, akambusu tena kwenye paji lake la uso na kisha akaenda kuoga.

    .

    .

    Akiwa anaoga, akili yake ikawa inawaza yale yaliyokuwa yametukia kwenye sala. Maji ya kuoga yalikuwa ya moto na hivyo kumfanya apate starehe ya aina yake kwenye kuoga haswa kwenye mazingira ya baridi kama haya.

    .

    .

    Akili yake ikawanda na kuwanda kwa kuwaza. Kwa namna moja akajihisi atakuwa ametua mzigo wa mambo yale ya ajabuajabu yaliyokuwa yanamtokea. Alikuwa na imani sasa mambo yatakuwa shwari kabisa. Na uzuri yote yalifanyika pasipo mume wake kujua kitu.

    .

    .

    Ila akiwa hapa anaoga na kuwaza, mara bomba yake ya ‘maji ya mvua’ ikakata akiwa bado hajajiosha kuondoa sabuni mwili mzima. Usoni alikuwa ana sabuni hivyo aliogopa kufungua macho yake kutazama.

    .

    .

    Akapapasa bomba na kulitikisa. Akakunja uso akinung’una ni nini kimetokea. Sasa hakuwa na namna bali kuogea maji ya baridi yaliyokuwako kwenye ndoo kubwa zilizopo humo bafuni.

    .

    .

    Ila ndoo hizo zilikuwa mbali kidogo na yeye, konani mwa bafuni, kwahiyo ilimbidi afanye namna ya kuona ili azifikie. Basi kiuvivu, akafungua macho yake kwa mbali ajue tu uelekeo kisha afuate ndoo hizo. Ajabu alipofanya hivyo, akamwona mtoto mdogo kwenye kona! Akashtuka sana. Haraka alifuta sabuni kwenye macho yake kwa kutumia mkono na kisha akakodoa kuangaza.

    .

    .

    Hakuona mtu! Macho yakawa yanawasha kwa kuingiwa na sabuni. Haraka akafuata ndoo na kujisafisha alafu akatazama tena huku na kule. Hakukuwa na mtu.

    .

    .

    Akajimwagia maji akiwa na hofu. Ni kweli alimwona mtu ama mawazo yake? Hakuona mtu mpaka anmaliza kuoga. Sasa alikuwa anasikia baridi maana ameogea maji hayo. Haraka akaelekea chumbani kujikausha na kuvaa nguoze.

    .

    .

    Alipomaliza akaenda kumkuta Olivia chumbani mwake, akamkumbatia na kufunga macho alale. Kabla hajapata usingizi akawaza kuhusu kile kitu alichokiona bafuni. Hakuwa anataka kiwe kweli kabisa kwani aliamini sala waliyofanya iliondoa kila jambo.

    .

    .

    Akalazimisha akili yake kuwa kila jambo li shwari na hana haja ya kuhofia hata kidogo. Basi akalala na kukawa shwari mpaka asubuhi yake.

    .

    .

    Kukiwa ni majira ya saa tatu, yupo na Olivia sebuleni, wakapata mgeni mmoja, mwanaume mfupi mnene aliyekuwa amevalia sare za kampuni afanyayo kazi Mr. Garett. Mwanaume huyo alijitambulisha kwa jina la Jeff kama afisa msaidizi wa mawasiliano wa kampuni ya DOGOUT TIMBERS.

    .

    .

    Alisema ana haraka na hatokaa hapo muda mrefu. Ila uso wake ulikuwa umejawa na simanzi, hata tabasamu zake zilikuwa za kuongopa. Alipokunywa chai kidogo aliyolazimishwa na Mrs Garett akasafisha koo na kusema, “Nina habari mbaya, samahani sana kwa hilo.”

    .

    .

    “Mume wangu amefanyaje?” Mrs Garett akawahi kuuliza akiwa ametoa macho. Alianza kuhisi mwili wake unapata joto, moyo wake unaanza kupiga makasia.

    .

    .

    “Tafadhali, punguza munkari,” akasema Jeff akimshika Mrs Garett mkono. “Kila jambo litakuwa sawa, hapana shaka.”

    .

    .

    “Naomba uniambie mume wangu amekumbwa na nini?” akasisitizia Mrs

    Garett. Uso wake ulibadilika na kutisha kwa umakini.

    .

    .

    Jeff akashusha pumzi kwanza, kisha akasema, “Amepata ajali akiwa safarini …”

    .

    .

    Mrs Garett akaziba mdomo wake kwa mshangao.

    .

    .

    “Tunashukuru maana yu salama. Hivi tunavyoongea amelazwa hospitali kwa matibabu zaidi.”

    .

    .

    Machozi yakaanza kumtiririka Mrs Garett. Jeff akajitahidi kumpooza na kumfariji. “Atapona, usijali. Hatukutaka kukuletea habari hizi za kukuumiza ila hatukuwa na namna nyingine. Tangu alipofika hospitali, amekuwa akisema ukamwone kila anapopata nafasi finyu ya kuongea.”

    .

    .

    .

    ***

    .

    .

    Saa nne na nusu asubuhi …

    .

    .

    “Huyu ndiye mke wake!” alisema Jeff akimwonyeshea daktari. Uso wa Mrs Garett ulikuwa umefumwa na mashaka. Alikuwa anatetemeka sana. Daktari alimtazama kisha akanyanyuka toka kwenye kiti chake na kumwambia Mrs Garett, “twende, nifuate!”

    .

    .

    Mrs Garett akanyanyuka na kuongozana naye mpaka chumba alimwolazwa mumewe. Akamwona mume wake akiwa amefunikwa na P.O.P karibu mwili mzima. Ni uso tu ndiyo ulikuwa wazi. Basi akahisi moyo wake umezimama. Akakabwa na kilio cha uchungu. Haraka akamsogelea mume wake akiwa anatamani kumuuliza nini kimemsibu.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    “Ni ajabu akatoka hai kwenye ajali ile mbaya,” alisema Daktari akimsogelea Mrs Garett. Akamwekea mkono wake begani. “Kama alitoka kwenye gari ile iliyokuwa nyang’anyang’a, basi atatoka pia na hapa hospitali … usijali.”

    .

    .

    Tayari macho ya Mrs Garett yalikuwa yanatoa machozi kana kwamba mto. Alimwonea huruma sana mumewe. Hakukumbuka kuwa mwanaume huyo alitoka kumpiga na kumwaribu uso hapo nyuma, alichokuwa anajali ni uhai wake tu.

    .

    .

    “Ila,” Daktari akasema akimtazama Mrs Garett. “Mumeo amekuwa akikurupuka na kukuita kila muda. Amekuwa akitaka kukuona tangu anafika hapa. Ni mke wangu ni mke wangu kila anapofungua macho. Inaonekana anakupenda sana.”

    .

    .

    Mrs Garett akavuta makamasi asiseme jambo. Hawakujua ni namna gani ambavyo walimpatia maswali kumwambia habari hizo. Huo upendo wa mumewe umetoka wapi? Alihisi kuna kitu mumewe anataka kumwambia.

    .

    .

    Punde mumewe akafungua macho. Jicho lake la kushoto lilikuwa limevilia damu, la kulia ndilo lilikuwa zima ila nalo lilikuwa jekundu kwa chumvi ya machozi ya maumivu.

    .

    .

    “Mke wangu!” Mr Garett akaita. Akataka kunyanyua mkono wake amshike mkewe ila akashindwa. Daktari akamzuia na kumtaka atulie kwani mwili wake umejawa na majeraha ya kuvunjika.

    .

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mke wangu!” akaita tena Mr Garett. Macho yake yalianza kumimina machozi kwa wingi.

    .

    .

    “Nini shida?” mkewe akamsogelea kwa karibu akimtazama kwa huruma.

    .

    .

    “Kecie,” Mr Garett akajibu kwa sauti ya chini.

    .

    .

    “Kecie? Amefanya nini? - nini Kecie amefanya?” akauliza Mrs Garett.

    .

    .

    “Yupo hai,” akasema Mr Garett. “Kecie yupo hai … na anataka roho zetu!” aliposema hayo akanyamaza kimya, tuli.

    .

    .

    “Umemwona wapi Kecie?” Mrs Garett akauliza, ila mumewe akawa kimya. Mke akarudia tena swali, “Umemwonea wapi?”

    .

    .

    Hapa ndiyo akagundua kuwa mumewe alikuwa amefariki.



    Ila hakuamini, akamtazama Daktari na kumuuliza nini kimetokea? Mbona mumewe haongei? Daktari akamtoa nje na kubaki mwenyewe ndani ya chumba. Baada ya muda akatoka na kumweleza Mrs Garett kuwa mumewe alikuwa amefariki, hakuna namna bali afanye taratibu za mazishi.

    .

    .

    Siku ikawa mbaya sana kwa Mrs Garett. Akakabwa na uchungu mkubwa kifuani mwake. Hakutaka kuamini kama mumewe amefariki, mtu aliyemjua kwa miaka nenda rudi. Ama hakika kumbe kifo ni kitu chepesi tu!

    .

    .

    Unavyokisikia na ukubwa wake unaweza dhani kinachukua miaka kutokea, kumbe ni sekunde moja tu na habari yote hubadilika, ikiwamo na cheo cha jina lako.

    .

    .

    Basi Mrs Garett akiwa amekabwa na kilio na asijue cha kufanya, akaketi kwenye benchi ya hospitali akilia na kulia. Muda si mrefu akaja Jeff na kumpoza. Akamwambia kampuni itafanya jitihada zote kuhakikisha Mr Garett anapumzika salama, hivyo yeye watamchukua na kumrudisha nyumbani.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    .

    “Nini shida yako kijana?” Karani wa shule alimuuliza Brian aliyekuwa amesimama kandokando ya mlango wa ofisi ya mkuu wa shule, Dkt Hamill.

    .

    .

    Karani huyo alikuwa ni mwanamama aitwaye Georgina, mwanamke mnene mfupi mwenye miwani kubwa ya kumsaidia kuona.

    .

    .

    “Nahitaji kumwona mkuu wa shule,” akasema Brian. Georgina akamtazama na kumuuliza, “una shida naye gani?” Brian akabanwa na kigugumizi. iBahati, sauti ya Dkt Hamill ikaita tokea ndani kumtaka Georgina amruhusu mvulana huyo aingie kwani ana miadi naye.

    .

    .

    Brian akazama ndani na kusalimu kisha akasema amekuja kama ambavyo walikuwa wamepanga kuonana. Dkt Hamill alikuwa mezani akiparangana na baadhi ya mafaili, akamtaka Brian amngoje kwa dakika kadhaa kisha wataongea.

    .

    .

    Muda huo Brian akautumia kuzungusha macho yake ndani ya ofisi ya Dkt Hamill. Kulikuwa na picha kadhaa, ikiwemo zake na za familia. Alikuwa na watoto wawili na alivyokuwa kijana alikuwa mtanashati haswa. Mbali na picha hizo, kulikuwa kuna ofisi ndogo ya karani Georgina. Kwenye meza yake kulijawa na makaratasi mengi pamoja na mashine ya zamani ya ku - ‘type’.

    .

    .

    Brian akiwa anaendelea kukagua ofisi hii, macho yake yakaangukia dirishani na basi kutazama nje ya ofisi alipokuwa anawaona wanafunzi kadhaa wakiwa nje kwa ajili ya mapumziko.



    Huko nje akiwa anatazama, kwa mbali akamwona binti mdogo ambaye hakuwa amevalia sare. Binti huyo alikuwa ameshikilia mdoli mkono wake wa kuume na gauni lake lilikuwa limekomea juu ya magoti.

    .

    .

    Binti huyo mdogo alikuwa anatazama hapo dirishani. Ni kama vile alikuwa anamwona Brian na pia anamfanyia mazingatio. Brian akamtazama vema binti huyo. Akili yake ikamwambia ndiye mtu aliyemwona kwenye ndoto siku ile. Akili yake ikamwambia kuwa binti yule ni Kecie!

    .

    .

    Brian akafikicha macho yake kama mtu asiyesadiki. Alipotazama tena, bado akamwona binti yule! Alikuwa amesimama kama mstimu akimtazama, ila wanafunzi wengine walikuwa wanampita kana kwamba hamna kitu. Ina maana walikuwa hawamwoni!

    .

    .

    “Kecie!” Brian akasema kwa kunong’ona. Ajabu binti yule akatikisa kichwa chake kuitikia, na taratibu akaanza kujongea kufuata dirisha alimo Brian.

    .

    .

    Pale alipokuwa anakutana na wanafunzi wengine, Kecie akapita kana kwamba moshi ama kivuli. Macho yake yalikuwa yanatazama dirisha na macho ya Brian pekee. Hatua zake zilikuwa za taratibu ila zinazomfikisha kwa wepesi mno!

    .

    .

    Brian akatoa macho.

    .

    .

    “Kecie!” akanong’ona tena akiita. Moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi. Alisimama afuate dirisha kumtazama Kecie. Masikioni mwake alikuwa anasikia sauti ya kunong’ona, sauti ya kike, ikisema, “Niokoe, Brian … Niokoe, Brian.” Ila kabla hajafika dirishani, akashikwa mkono na kuvutwa.

    .

    .

    “Brian!” alipotazama akakutana uso kwa uso na Dkt Hamill. Dkt alikuwa anamtazama kwa mshangao, na pia Georgina alikuwa ameduwaa kumwangalia.

    .

    .

    “Nini shida?” Dkt Hamill akauliza. Brian akatazama kule dirishani, hakukuwa na mtu, hata wanafunzi walikuwa tayari wamesharudi kwenye madarasa yao.

    .

    .

    Dkt Hamill akamtazama Georgina na kumwambia, “Naomba utupishe.” Georgina alipofanya hivyo, Dkt Hamill akamkalisha Brian kwenye kiti kisha na yeye akaketi mahala pake.

    .

    .

    “Brian, niambie ulikuwa unaona nini dirishani?”

    .

    .

    Brian akatazama tena dirishani, kulikuwa kweupe hamna jambo. Akaurudisha uso wake kwa Dkt na kumwambia kwa sauti ya chini, “Kitu cha ajabu!”

    .

    .

    “Brian,” Dkt akaita. Akamtazama kwa macho ya udadisi na kumuuliza, “Kecie ni nani?”

    .

    .

    Brian akanyamaza. Bado alikuwa kwenye ombwe la mawazo. Hakuwa anajua cha kusema.

    .

    .

    “Brian, niambie kila kitu. Acha kunificha. Nitakusaidia.”

    .

    .

    Brian akavuta kwanza pumzi ndefu. Akatazama chini akifikiri jambo kisha akaamua kukata shauri kusema kila kitu kwa Dkt Hamill. Basi asifiche kitu akaeleza kinaga ubaga. Simulizi yake ikamwacha Dkt akiwa ameachama.

    .

    .

    “Brian, una kazi kubwa,” Dkt akasema na kisha akakuna kidevu chake. Akashusha pumzi ndefu na kupangilia vema maneno mdomoni.

    .

    .

    “Kecie hajafa. Yupo mahali na anataka ukamwokoe.”

    .

    .

    “Mahali gani?” Brian akauliza. Kabla Dkt Hamill hajajibu, akamwambia, “Brian, haitakuwa rahisi hata kidogo. Kecie sasa ni mali ya Helo!”

    .

    .

    “Kivipi?”

    .

    .

    “Michoro uliyoikuta kwa Faris kulikuwa na mwanaume kando yake, sio?”

    .

    .

    “Ndio,” Brian akajibu.

    .

    .

    “Maneno yale ambayo Faris ameyaandika kwenye kitanda ni yale aliyosema Helo pindi anakufa!”

    .

    .

    “Kwahiyo ina maanisha nini?”

    .

    .

    “Helo amerudi!” akasema Dkt Hamill. “Na ndiye huyo unayemwona akiwa anaongozana na Kecie.”

    .

    .

    “Sasa tutafanyaje?” akauliza Brian kwa kimuhe.

    .

    .

    “Bado sijajua, ila … kuna haja ya kwenda kuonana na Faris. Kuna mengi ya kujua toka kwake. Ni wazi yeye ndiye atakuwa daraja letu.”

    .

    .

    Kukawa kimya kidogo. Dkt akasonya na kutikisa kichwa.

    .

    .

    “Kwanini Helo hajaanza kuwamaliza watu wa mji huu?” akauliza akitazama dirishani. Hilo swali lilikuwa ni kubwa na lilimtafuna kichwa. Lazima kutakuwa kitu, aliamini.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    Kesho yake majira saa sita mchana …

    .

    .

    Watu kumi na wawili walikuwa makaburini wakiwa wamevalia nguo nyeusi. Walikuwa wameketi kwenye viti na mbele yao kukiwa na shimo refu lililofunikwa na jeneza.

    .

    .

    Padri Alfonso akiwa amevalia nguo zake za kazi ndiye alikuwa anaendesha misa. Na alikuwa ukingoni. Alipomaliza jeneza lilishushwa chini na watu wakaanza kuweka udongo wakianza familia ya marehemu.

    .

    .

    Wakatia pia maua na kisha watu wakaanza kuparanganyika kwenda majumbani mwao. Nyuma wakaachwa Mrs Garett, Olivia, Brian na mamaye.

    .

    .

    Wageni wakawa wanateta kuwapoonza wafiwa. Wakatembea mpaka kufikia kwenye gari la Mrs Garett, hapo mama huyo akaomba kuonana na kuongea na Brian faragha. Kabla Mama Brian hajapisha, akamtazama mwanaye kisha akainamisha kichwa kuafiki. Akatangulia zake.

    .

    .

    Brian akaingia kwenye gari la Mrs Garett akiketi viti vya mbele.

    .

    .

    “Brian,” Mrs Garett akaita kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa. “Kuna kitu nataka kukuuliza na tafadhali naomba uwe mkweli.”

    .

    .

    “Usijali, mama. Nitakuwa mkweli,” akasema Brian akianza kubuni kinachofuatia.

    .

    .

    “Ushawahi kumwona Kecie?” mama akauliza. Kisha akamtazama Brian machoni.

    .

    .

    “Kumwonaje, Mrs Garett?” Brian akauliza.

    .

    .

    “Kwa vyovyote tu,” Mrs Garett akasema. “Tangu amepotea, ushawahi kumwona popote pale … akifanya lolote lile? Tafadhali naomba kuwa mwaminifu.”

    .

    .

    Brian akanyamaza kidogo na kusema, “Nishawahi onana naye. Jana ilikuwa mara ya mwisho nikiwa shuleni.”

    .

    .

    Jambo hili likaonekana kumshtua kidogo Mrs Garett, akauliza, “Unapomwona anakuambia nini? … kuna kitu chochote anakwambia?”

    .

    .

    Brian akasita. “Kuna nini Mrs Garett?”

    .

    .

    “Nataka tu kujua … niambie, Brian.”

    .

    .

    Uso wa Mrs Garett ulionyesha mashaka ndani yake. Aidha kuna habari aliyokuwa anatarajia toka kwa Brian.

    .

    .

    “Huwa ananiambia nimwokoe,” akajibu Brian. “Kila ninapomwona ananisihi nimwokoe.”

    .

    .

    “Umwokoe?” Mrs Garett akastaajabu. Kwa akili yake alidhani Kecie atakuwa amemwambia Brian kuwa familia yake ndiyo imemuua. Hili swala la kuokolewa kwake lilikuwa jipya. Kecie anataka aokolewe na nini? Kutoka kwa nani?

    .

    .

    “Umwokoe?” akauliza.

    .

    .

    “Ndio,” Brian akajibu na kuongezea, “Pengine Kecie hajafa.”



    Mrs Garett akatoa macho ya mshangao. “Brian, sikuelewi. Nini unasema?”

    .

    .

    “Samahani, Mrs Garett. Ni simulizi ndefu kidogo na muda sina kwa sasa. Nakuahidi kuja kukuona baadae jioni. Kwa sasa kuna mahali natakiwa kwenda. Kuna mtu aningoja!”

    .

    .

    Basi Brian akaaga na kwenda zake. Mpaka anayoyoma Mrs Garett akawa anamtazama kwa namna ya kubanwa na maswali. Brian alimtibua kabisa akili yake na kumwacha kwenye hamu kubwa ya kutaka kujua.

    .

    .

    Hata bado hakumweleza kijana huyo ujumbe aliopewa na mumewe, Mr Garett, ya kwamba Kecie anawinda roho zao.

    .

    .

    Mrs Garett akajikuta anaona mate ni mazito kuyameza.

    .





    Aliwasha gari na kutimka eneo la makaburini bado kichwa chake kikishindwa kabisa kuacha mawazo juu ya Brian. Alikuwa anahofia sana. Alikosa kabisa amani. Ni kivipi Kecie amwambie Brian amwokoe? Ni kwamba Kecie yupo hai au?

    .

    .

    Mama huyu kwa muda akasahau kuhusu kifo cha mumewe. Hata kwa kiasi fulani akawa si mzingatiaji barabarani. Akiwa katika fikra zake hizo ni ghafula akamwona Kecie pembezoni mwa barabara! Haraka akaminya breki na kuangaza akiwa ametoa macho.

    .

    .

    Breki yake kali ilisababisha nusura agongwe na gari lililokuwa nyuma. Dereva wa gari hilo alifoka kumtuhumu kwa ujinga huo. Lakini Mrs Garett hakuwa anajali. Pengine hakuwa hata anasikia kelele hizo. Alitazama kule alipomwona Kecie lakini ajabu hakuona kitu tena! Hakuwa Kecie bali mtoto fulani ambaye alikuwa anatembea ameshikwa mkono na mama yake.

    .

    .

    Akashusha pumzi ndefu na kuendesha kujiondokea.

    .

    .

    **

    .

    .

    “Tushukie hapa,” alisema Dkt Hamill akizima gari. Alikuwa amevalia koti refu jeusi na kofia. Pembezoni mwake alikuwa ameketi Brian aliyekuwa anatazama huku na kule. Barabara ilikuwa pweke ikiwa imezingira na miti.

    .

    .

    Hakukuwa sehemu ya kufurahisha hapa. Ni sehemu iliyojawa na misitu na ipo pweke. Miti yake ni mirefu na imefunga anga kujaza giza.

    .

    .

    “Una uhakika?” akauliza Brian. Alihofia kushuka. Dkt Hamill alimtazama na kumtikisia kichwa alafu yeye akatangulia kushuka.

    .

    .

    “Papweke na pakimya sana!” alisema Dkt Hamill akiwa anafunga vifungo kadhaa vya koti lake. Alimtazama Brian aliyekuwa anaufunga mlango wa gari, akamwambia, “Hapa palikuwa pamejawa na watu.” akamgoja Brian asogee karibu kisha akaendelea kueleza, “Kila mtu aliona ufahari kuwa karibu na Helo. Lakini habari ilipokuja kubadilika, wakamtenga. Na baada ya nyumba yake kuchomwa, watu wakahamishwa kupelekwa maeneo mengine …

    .

    .

    Hapa pakabaki penyewe. Miti ikaota na kupazinga. Kukawa sehemu iliyosahaulika kabisa … sidhani kama kuna watu huja huku tena. Kufanya nini?”

    .

    .

    Brian akiwa anatoatoa macho kuangaza, akauliza, “Iko wapi hiyo nyumba yake?”

    .

    .

    Dkt Hamill akaonyeshea upande wao wa mashariki na kuanza kuufuata. Wakatembea kwa kama dakika tano, sasa wakaanza kuona mabaki ya nyumba fulani. Walipomalizia mwendo wao kwa dakika tatu, mbele yao sasa kukawa kumesimama nyumba kubwa ya ghorofa. Si nyumba, bali tuseme ghofu.

    .

    .

    Lilikuwa bado lina makovu ya kuchomwa na kuungua. Lilikuwa limefichwafichwa na majani baadhi ya sehemu zake. Rangi yake ya kijivu, rangi ya kuungua, ilikuwa imegeuka na kuwa kijani kwasababu ya kutambaliwa na majani na matawi ya miti.

    .

    .

    Lilikuwa ni ghofu kubwa. Na hivi halikuwa na watu na lipo misituni, lilikuwa laoghofya. Ni wazi ndani yake kutakuwa na wadudu ama wanyama ambao wangeweza kujeruhi mtu.

    .

    .

    “Hapa ndipo alipokuwa anakaa,” akasema Dkt Hamill akitazama ghofu hili kila upande.

    .

    .

    “Kumbe He --” kabla Brian hajamalizia, Dkt Hamill akamziba mdomo kwa kiganja chake. “Usitaje jina lake ukiwa hapa … sawa?”

    .

    .

    Brian akatikisa kichwa kukubali. Dkt Hamill akatoa kiganja chake na kuendelea kutazama jengo lile.

    .

    .

    “Kwanini?” Brian akauliza. “Kwanini tusitaje jina lake? Kuna shida yoyote?”

    .

    .

    Dkt Hamill akamtazama Brian na kumwambia, “Shida ipo tena kubwa … simulizi zina kweli ndani yake kwamba ukitaja jina lake ukiwa hapa kwenye makazi yake, basi ataitikia wito wako na kujitokeza… sidhani kama ungelipenda hilo lijitokeze.”

    .

    .

    Brian akanyamaza asitie neno. Basi wakalizunguka jengo hilo na kisha wakasimama mbele ya lango kuu la kuingilia.

    .

    .

    “Tunaweza kuingia ndani kutazama?” akauliza Brian. Dkt Hamill akanyamaza kwa muda kidogo kabla hajasema, “Sidhani kama hilo ni wazo jema.”

    .

    .

    “Ina maana tutaishia hapa baada ya kufunga safari yote hiyo?” Brian akatahamaki. Alikuwa ana hamu kubwa ya kuona na kutambua mapya. Basi Dkt Hamill kumtimizia haja yake, akamkumbalia, japo kishingo upande, wakaingia ndani.

    .

    .

    Hakukuwa na kitu zaidi ya mabakimabaki tu. Majani yalikuwa yameota karibia kila sehemu pia tando za buibui zikiwa zimetalaki ndani ya eneo. Kulikuwa ni giza na pakimya sana.

    .

    .

    “Nadhani inatosha, Brian,” akasema Dkt Hamill. “Twende sasa.” Lakini Brian hakuwa mwepesi kukubali. Ndiyo kwanza walikuwa wameishia sebuleni, kwanini wasitembelee kila eneo wakaona?

    .

    .

    “Dkt Hamill kwanini unahofia?” Brian akauliza. “Kuna chochote ambacho hujanambia?”

    .

    .

    “Hapana, ila sioni kama ni wazo zuri kuendelea kupekua nyumba hii,” akasema Dkt.

    .

    .

    “Kwahiyo tulikuja kuishia nje tu?”

    .

    .

    “Ndio. Si ulitaka kujua ilipo?”

    .

    .

    Brian akanyamaza. Akaendelea kutazama huku na kule akitaka kujua zaidi.

    .

    .

    “Brian, kama kuna namna ya kuepuka makubwa, basi tufanye hivyo. Hamna haja ya kuingia kwenye matatizo ya kujitakia, sawa? Mimi ni mzee sasa kuhangaikahangaika. Twende.”

    .



    Ila kabla Brian hajasema jambo, wakastaajabu mlango kufungwa! Wakatazamana kwa hofu. Dkt akarudia, “Twende! Twende, Brian!”

    .

    .

    Wakaufuata mlango na kujaribu kuuvuta, haukufunguka! Wakahangaika sana pasipo mafanikio mwishowe wakaona wakatumie madirisha. Wakafuata dirisha la kwanza kabisa toka walipo, wakavunja mabaki ya fremuze na kutoka.

    .

    .

    Ila wakati wanafanya vivyo, Dkt alijikata kidole chake cha mwisho. Kwakuwa hakukuwa na muda wa kungoja, walikuwa na haraka sana, Dkt Hamill hakujali. Muda si mrefu wakajikuta ndani ya gari na tayari ameshawasha watimke.

    .

    .

    Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, ndipo Brian akaona damu kwenye usukani. Dkt Hamill alikuwa anachuruza damu, na asioenakane kujali. Brian akatahamaki akimwambia,

    .

    .

    “Unavuja damu!”

    .

    .

    Dkt Hamill akatikisa kichwa chake asitie neno. Alionekana hayuko sawa. Sura yake alikuwa ameikunja kana kwamba anasikia maumivu na ana mawazo kwa wakati huohuo.

    .

    .

    Brian akaona si vema akiendelea kumwongelesha. Akanyamaza lakini kila saa akiwa anamtazama Dkt na kile kidole chake kilichojeruhiwa.

    .

    .

    **

    .

    .

    Upepo ulipuliza kidogo na kukoma. Damu bado ilikuwapo pale dirishani na hata kwa pembeni yake. Haikuwa imekauka. Kwa mtu mwenye macho makali angeliiona na kama angeigusa basi angeliondoka na doa.

    .

    .

    Baada ya upepo kukoma, kishindo cha miguu kilisikika kwa muda mfupi, na mara mtu mmoja ambaye hakuwa anaonekana kwa juu alijiri na kusogelea dirishani.

    .

    .

    Mtu huyu alikuwa amevalia suruali nyeusi ngumu na chini akivalia viatu vyenye visigino vya kutesa sakafu na ncha butu. Kishindo chake kilionyesha ni mtu mzito mwenye kilo zake.

    .

    .

    Alipofikia dirisha alisimama, akatia kidole chake kwenye matone ya damu yaliyokuwa yamedondoka kisha akapeleka kidole mdomoni kuyanyonya.

    .

    .

    Alipofanya hivyo, matone yote ya damu yakapotea! Na dirisha lililokuwa limevunjika, likajirudi upya na kuwa kama lilivyokuwapo hapo awali.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    .

    “Dkt Hamill!” Brian aliita kwa hofu. Dkt alikuwa amechoka, macho yake yanarembua, mwili umekosa nguvu! Hakuweza kumudu gari. Brian akashikilia usukani na kufanya jitihada kusimamisha chombo hicho.

    .

    .

    “Dkt Hamill!” Brian akaita. Akamtikisatikisa kichwa. “Dkt Hamill! Dkt Hamill!”

    .

    .

    Dkt Hamill alikuwa amechoka mno. Macho yake yalikuwa mazito na mdomo ulikuwa wazi akihema kwa uzito. Brian akahofia sana. Akamtazama kidole cha Dkt Hamill, bado kilikuwa kinachuruza damu. Haraka akafanya jitihada za kumfunga kidole hicho na kisha akamhamisha kiti, akawasha gari na kutimka upesi.

    .

    .

    Ni moja kwa moja akampeleka Dkt hospitalini. Akapokelewa na wahudumu na kuwekwa ndani kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

    .

    .

    “Una uhakika?” Dokta akauliza.

    .

    .

    “Ndio,” Brian akasema akitikisa kichwa. “Alijikata kidole tu, sikuona kingine zaidi ya hiko.”

    .

    .

    Dokta akashusha pumzi na kwenda zake akimtaka Brian aendelee kungoja. Baada ya kama lisaa limoja, Dokta akamfuata Brian na kumtaka akaonane na mgonjwa kwani ameomba hivyo.

    .

    .

    Brian aliyekuwa amepatwa na hofu, akanyanyuka na kwenda huko akisindikizwa na Daktari. Alipofika, daktari akaenda zake kuwapa faragha.

    .

    .

    “Brian,” Dkt Hamill akaita. Sauti yake ilikuwa kavu isiyosikika vema. Brian akasonga karibu na kumtazama kwa macho ya huruma.

    .

    .

    “Mimi sikuwa wa kuletwa hospitalini,” Dkt Hamill akasema kwa shida. Akageuza shingo yake kumtazama Brian. Akamtazama kwa sekunde kadhaa alafu ‘lips’ yake kavu ikasema, “Brian, sasa nitakuwa nimelaaniwa.”

    .

    .

    “Na nani?” Brian akauliza kwa pupa. Dkt Hamill akakohoa kwanza kisha akatafuta hewa yake na kusema, “Nitakuwa nimelaaniwa na Helo … Brian, maisha yangu hayatakuwa sawa tena.”





    Brian akashangazwa na maneno hayo. Akamuuliza Dkt Hamill kwanini anasema hivyo? Je kuvunja tu dirisha ndiyo imekuwa ya kupata laana?

    .

    .

    “Hapana, Brian!” akasema Dkt Hamill kisha akakohoa kidogo. Ilikuwa ni ngumu kuamini kama ameletwa hospitali leo. Ungeweza kudhani ni mgonjwa wa muda.

    .

    .

    “ … Ni damu. Ni damu yangu iliyobaki kule,” akasema Dkt kisha akatulia kama mtu anayeishiwa pumzi, sasa anaitafuta. “Nilijua toka nilipokuwa nimejakata pale. Hayakuwa mazingira ya kawaida. Lakini bado tulifanya busara kuondoka mapema. Huenda mambo yangekuwa mabaya zaidi.”

    .

    .

    “Nisamehe, Dkt Hamill,” Brian akalia. “Kama isingalikuwa mimi yote haya yasingejiri. Laiti ningekusikiliza …”

    .

    .

    “Ssshhh! …” Dkt Hamill akamnyamazisha Brian. “Huna haja ya kulia Brian. Hakuna kosa lolote ulilolifanya kwani kama mimi nisngetaka kwenda mule ndani basi nisingelikwenda.” akamshika Brian mkono na kumminya akimtazama kwa sura inayojitahidi kuumba tabasamu.

    .

    .

    “Brian, wewe ni kijana mwerevu lakini pia shupavu sana. Nimefurahi mno kukutana na wewe. Si vijana wengi wako kama wewe. Una kitu ndani yako. Najua unataka kuyajua mengi sana. Ila …” akakohoa. “Tazama yasije yakakugharimu.”

    .

    .

    Aliposema hayo akatulia kwa dakika moja, alikuwa anatazama chumba alicholaziwa kana kwamba ni kipya machoni. Aliporejesha macho yake kwa Brian, akasema, “Ni bora nikafa.”

    .

    .

    Kauli hiyo ikamshtua Brian, “Kwanini unasema hivyo, Dkt Hamill? Tafadhali usiseme hivyo!”

    .

    .

    Dkt akatabasamu. Akamtazama Brian aliyekuwa na sura ya hofu kisha akasema, “Brian, mimi ni mzee sasa. Si kama wewe. Wewe bado damu yako yazunguka, mwili wako una joto na hata akili yako inayoendelea kukua inafanya kazi upesi.

    .

    .

    Hutonihitaji tena mimi, Brian. Niliyokupa yanatosha. Nashukuru sana kwa kuwa na mimi japo kwa kipindi kifupi, umenipa faraja na ‘kampani’ ya rafiki.”

    .

    .

    Hapa ndipo Brian akajifunza ya kuwa Dkt Hamill hana familia. Yu mpweke sana na amekuwa akiishi hivyo kwa miaka mingi sasa. Mke na watoto wake wote walikufa lakini hakumwambia Brian nini kiliwaua.

    .

    .

    Kauli yake ya mwisho alimwagiza Brian aende nyumbani kwake, akamwelekeza wapi atapata ufunguo, azame ndani na kumletea nyaraka zake tatu kwenye kabati.

    .

    .

    Brian akitumia gari la Dkt Hamill, akaelekea huko, kulikuwa ni kingoni mwa mji wa Boston. Akaukuta ufunguo alipoelekezwa, akazama ndani na kunyookea kwenye kabati.

    .

    .

    Ilikuwa ni nyumba kubwa yenye vyumba takribani vitano ila vyote vikifungwa isipokuwa kimoja tu alimokuwa anaishi Dkt Hamill mwenyewe. Nyumba hiyo ilikuwa kubwa na kimya sana. Pia pweke. Brian alishangazwa namna gani Dkt Hamill alikuwa anaweza kuishi mwenyewe hapo.

    .

    .

    Asipeleleze sana, akarudi kwenye gari na kuanza safari ya kurudi hospitali. Alichukua takribani dakika kumi tu kutokana na mwendo wake wa kasi. Alipofika, ajabu hakumkuta Dkt Hamill. Dokta akamwambia tayari mzee huyo amekufa, amehifadhiwa mochwari.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Akashindwa kuzuia chozi. Akajihisi kuishiwa na nguvu. Aliketi kwenye benchi kama mtoto yatima akiwa na kujiona mpumbavu kwa namna alivyofanya mzee huyo akafariki. Alijiona muuaji. Alijiona mwenye makosa.

    .

    .

    Macho yake yakiwa yamejawa na machozi yaliyomfanya asione vema, Dokta akamjia na kumgusa bega. Akamkabidhi karatasi fulani na kumwambia, “Ni ujumbe wako alinambia nikupatie punde utakaporudi hapa.”

    .

    .

    Kabla Dokta hajaondoka akamshika Brian begani mara mbili kumpa pole.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    .

    Saa moja jioni …

    .

    .

    .

    Brian alikuwa amejifungia chumbani kwake, uso wake ukiwa mwekundu, macho yake bado yanachuruza machozi. Kitandani kulikuwa kuna zile nyaraka tatu ambazo Dkt Hamill alimwambia akazichukue, pamoja pia na ujumbe aliopewa na Dokta kule hospitalini.

    .

    .

    Alitazama nyaraka zile na ule ujumbe. Sijui alikuwa anawaza nini kichwani mwake. Kwa muda kidogo hakuwa anajua cha kufanya ilhali kila kitu kipo bayana ya kwamba yampasa atazame vilivyomo ndani.

    .

    .

    Baada ya kutulia kidogo ndipo akachukua ule ujumbe kwenye karatasi, akaanza kuusoma. Uso wake ulikuwa umepooza. Macho yake yalikuwa yanatia huruma.

    .

    .

    Taratibu akawa anapitisha macho kwenye ujumbe uliokuwa unasomeka kama ifuatavyo,

    .

    .

    “Inabidi niende, Brian. Sidhani kama nitakuwa nimekuacha mpweke. Nimeenda kwenye ulimwengu wa pili. Ulimwengu ambao siujui moja wala kumi yake. Nimekamilisha maisha yangu huku duniani. Lakini nakusisitizia Brian, mimi nimekwenda. Ni hivyo tu. Endapo ukiniona tena muda wowote mahali popote, basi jua si mimi.

    .

    .

    Kwenye hizo nyaraka tatu, tafuta muda usome kwa makini. Tafadhali usipuuze. Nakutakia kila la kheri ukatimize haja yako. Usiogope, Brian. Na usiache jitihada zako za kumwokoa Kecie. Huwezi jua utawaokoa na wakina nani pamoja naye.”

    .

    .

    Ujumbe ulikwisha ukimwacha Brian akidondosha machozi. Kichwa kilikuwa kinamgonga na alijikuta anaumia sana moyoni. Anaumia mno. Alisaga meno yake kwanguvu akiangushia kichwa chake kitandani.

    .

    .

    Hakukumbuka aliishia wapi kulia, usingizi ulimsomba kwa pupa sana kumpeleka kwenye ulimwengu wa kiza ila angalau wenye unafuu.

    .

    .

    “Brian! Brian! Tih-tih!-tih!” alikuwa anaitwa na mlango unagongwa. Ni kama takribani dakika ishirini tangu alipozolewa na usingizi. Alihisi huenda anaota, ila ilikuwa ni uhalisia. Alikuwa anaitwa.

    .

    .



    Mama yake alikuwa amesimama mlangoni akiwa ameshikilia kiuno chake kwa mkono wa kushoto, wa kulia akibondea mlango.

    .

    .

    Mara punde mlango unafunguliwa Brian akiwa anafikicha macho yake. Alimtazama mamaye na kumuitikia kilevi.

    .

    .

    “Uko sawa?” mama akauliza akifinyanga uso wake kwa hofu.

    .

    .

    “Ndio … niko sawa!” Brian akaongea kivivu. Macho yake bado yalikuwa mekundu ila kwakuwa alitoka kulala, mama yake hakujali sana. Alishani ni usingizi.

    .

    .

    “Mbona umelala pasipo kula?”

    .

    .

    “Mama sisikii njaa.”

    .

    .

    “Umekula wapi?”

    .

    .

    Brian kimya. Mama akamtazama na kutaka kumuuliza tena kama yupo sawa, ila akasita. Akadaka kiuno chake kwa mikono yote alafu akamwambia, “Una mgeni wako sebuleni. Anataka kukuona hivi sasa.”

    .

    .

    “Nani?”

    .

    .

    “Mrs Garett. Fanya uje haraka.”

    .

    .

    Mama aliposema hivyo akaenda zake kurudi sebuleni. Mama Kecie aliyekuwa ameongozana na Olivia walikuwa wameketi kwenye kochi la kwanza kabisa upande wa kulia wa mlango, akawaambia kuwa Brian yuaja muda si mrefu.

    .

    .

    “Kweli hamtahitaji kitu?” mama Brian akauliza wageni huku akiwapatia tabasamu.

    .

    .

    “Hapana,” Mrs Garett akasema akitikisa kichwa. “Tupo tu sawa, usijali.”

    .

    .

    “Hata chai? Ni baridi jamani.”

    .

    .

    “Sawa, tutashukuru.”

    .

    .

    Mama Brian akaenda jikoni na kurejea na vikombe viwili vya chai, akawapatia Mrs Garett na Olivia. Taratibu wakawa wanavuta kimiminika hicho cha moto kumngoja Brian.

    .

    .

    Punde Brian akafika sebuleni na kuwasalimu..

    .

    .

    “Pole kwa usumbufu.,” Mrs Garett alisema akimtazama Brian. Kwa kumtazama tu mama huyu hakuwa sawa. Sauti yake ilikuwa ajabu na uso wake ulikuwa ulioganda. Hakuwa na lepe la furaha. Ungelitabiri vema hakukuwa na kitu kilichomfurahisha siku nzima ya leo.

    .

    .

    “Usijali, Mrs Garett. Karibu.”

    .

    .

    “Brian, nina shida sana. Nahisi maisha yangu yapo hatarini.”

    .

    .

    Kauli hii ya upesi na iliyosikika vema ilimfanya Brian na mama yake wawe wasikivu zaidi.

    .

    .

    “Baada ya mume wangu kufa, ni mimi ndiye yuaja. Naombeni mnisaidie.” Mrs Garett akaanza kububujikwa na machozi. “Kecie anataka kuniua kama alivyomuua baba yake. Anawinda roho yangu!”

    .

    .

    Brian na mamaye wakatazama kwa puzo. “Kwanini Kecie akuue?” Briana akauliza. “Na kwanini alimuua baba yake?”

    .

    .

    Mrs Garett kwa kujikaza, akasema kila kitu. Hakutaka yale ya mficha maradhi. Alikuwa anataka msaada haswa. Alipomaliza kueleza, akajikuta anatoa machozi zaidi na kupaliwa na kilio. Alikuwa anamwomba msamaha mwanaye.

    .

    .

    Lakini kwanini alidhani Brian anaweza kumsaidia kwenye hilo?

    .

    .

    “Ni wewe tu na sisi ndiyo hutokewa na Kecie. Lakini akija kwako hukuomba msaada. Akija kwetu hudai roho zetu,” alisema Mrs Garett akitoa macho yake mekundu. “Kama Kecie hukuskiza wewe, naomba utuombee msamaha, Brian!”

    .

    .

    Mama Brian akamtazama mwanaye na kumuuliza, “Kecie, hukuomba umsaidie?”

    .

    .

    “Ndio,” Brian akajibu na kuongezea, “Huniomba nimwokoe!”

    .

    .

    “Umwokoe wapi? Kutoka kwa nani?”

    .

    .

    Brian akamtazama mama yake na kumwambia, “Toka kwa Helo.”

    .

    .

    “Ndiyo nani huyo?”

    .

    .

    Kabla Brian hajajibu, akaona kitu dirishani.



    .

    .

    Alikuwa ni mtoto akiwa amesimama na mwanaume mweusi asiyeonekana lakini wenziwe walipoangazia huko, hawakuona kitu! Kila kitu kilikuwa kimepotea katika kasi ya kufumba na kufumbua.

    .

    .

    “Kuna nini, Brian?” Mama yake akauliza.

    .

    .

    “Kulikuwa na mtoto akiwa amesimama pale na kando yake kuna mtu!” akasema Brian akinyooshea kidole kule dirishani. Ila hakukuwa tena na kitu! Na si kwamba watu hawakumwamini, la hasha. Ni kwamba tu hawakufanikiwa kushuhudia.

    .

    .

    “Brian! Kecie atakuwa ananifuata mimi!” akasema Mrs Garett akijawa na woga. Aliangazaangaza huku na huko. Hakuwa na amani. Hofu aliyokuwa nayo ilikuwa ni ile iliyo kuu.

    .

    .

    “Usijali, Mrs Garett!” Mama Brian akamfariji. “Leo utalala hapa wewe pamoja na Olivia. Nadhani msiba wa mumeo utakuwa umekuathiri.”

    .

    .

    Mama hao wakakumbatiana. Mama Brian akaendea chai ya Brian na ya kwake wakaendelea kukaa hapo wakiteta. Lakini kila saa Mrs Garett akawa anamsisitizia Brian ya kwamba endapo Kecie akijiri basi amwambie ya kwamba anaomba msamaha. Ambakizie roho yake.

    .

    .

    Usiku ukazidi kukua na mwishowe kabisa wakaenda kulala. Mrs Garett alienda kulala na Mama Brian huku Olivia na Brian kila mmoja akilala chumba chake.

    .

    .

    Usiku huo wakati watu wakipambania kupata usingizi, Brian yeye akawa ndiyo anautumia huo muda kusoma zile nyaraka za Dkt Hamill. Zilikuwa ni za kuogopesha lakini hakuwa anataka kuzieka chini mpaka kumaliza. Haikuwa kazi nyepesi.

    .

    .

    Basi na sehemu ya nyaraka hii yasomeka kama ifuatavyo …

    .

    .

    “… Kifo kina wivu sana. Kinatutenga na wale tuwapendao. Kimeniacha na kidonda kikubwa sana kwani kichwa changu kimekuwa hakikomi kuwaza na kukumbuka matabasamu ya mke na watoto wangu. Waliniacha kipindi nawahitaji sana. Pengine waweza kuwa unanionea huruma, lakini utakapomaliza kusoma haya, labda utaniona mimi ni mkatili sana. Mtu asiyestahili huruma hata lepe.

    .

    .

    Basi ningalikuwapo kijana nilikuwa mtanashati sana. Mwenye nguvu na kaliba ya kufanya kazi kwa bidii. Doa langu lilikuwa moja tu, nalo ni kupenda sana kujifunza na kujua. Sikuwa na jambo dogo, na niliamini kila lionekanalo kidole basi lina mwili mzima.

    .

    .

    Kutokana na hulka yangu hiyo, nikawa napenda sana kujitenga na kujisomea. Lakini pia kuchangamana na watu kuwauliza mambo kedekede ambayo nilikuwa nataka kuyafahamu.

    .

    .

    Baba yangu, Mr Lambert, alikuwa ni mtu mkorofi sana. Kwenye moja ya shamba lake la pamba alikuwa na watumwa weusi kumi na tano. Hakuwa anapenda kuniona nikichangamana na watumwa hao. Mara kadhaa alikuwa ananiadhibu kwa kunikuta nikiwa nakaa na kuongea nao, lakini sikuwa naskiza.

    .

    .

    Watumwa hao walikuwa na simulizi tamu sana, haswa mwanamke mmoja mzee aliyekuwa anaita Jasmine. Yeye alikuwa akiniona anafurahi na kunikumbatia tofauti kabisa na mama yangu. Alikuwa ananipenda sana, na alikuwa anajua nini napenda pia.

    .

    .

    Angeniweka kwenye mapaja yake na kuniambia simulizi mbalimbali, hata za kule Afrika. Lakini kwasababu ya umri wake, alikuwa ameona mengi. Alikuwa ni mkubwa kuliko hata baba yangu. Alinihadithia mambo mengi ya Boston ambayo hata baba yangu hakuwa anafahamu.

    .

    .

    Ni yeye ndiye aliyenieleza juu ya familia ya Helo. Kipindi kile akiwa msichana , japo bado mtumwa, alikuwa anatoroka kwenda kwenye maonyesho ya bwana huyo. Japo ilikuwa hairuhusiwi kwenda, na hata huko kwenye vibanda, watu weusi walikuwa hawatakiwi, hakukoma kwenda kufurahisha nafsi yake.

    .

    .

    Alikuwa ni jasiri. Mgongo wake ulijawa na makovu ya kupigwa, lakini hakuwa anaskiza. Alikuwa anaufuata moyo wake. Siku moja nilimuuliza, huoni kuwa mgongo wako unaisha kwa ukaidi? Basi akatabasamu na kunitazama na macho yake mekundu. Akanishika mashavu na kuniambia,

    .

    .

    “Kuna furaha gani kwa mtumwa aliye ndani ya minyororo? … hata nikikaa hapa, bado nitaonekana mkaidi kwa maana mtumwa hupewa jina hilo tangu na uzao wake. Maisha yake ni mafupi na yanapokoma hukusanywa kama kiroba na kutupiwa shimoni.

    .

    .

    Hamill, huoni kuna haja ya kuthubutu kutafuta tabasamu langu hata mara moja kwa miaka yote hiyo?”

    .

    .

    Hakika alinitia moyo sana na alinifanya nifuate nikipendacho pasipo kujali nini kitanitokea. Ilimradi nina furaha, basi yatosha.

    .

    .

    Lakini siku ile wakati Helo anachomwa moto baada ya kugundulikana kuwa ni mlozi, Jasmine alishuhudia kila kitu kwa macho yake. Alikuwa bado ni binti. Na kitu kile kilimuumiza sana. Hata alipokuja kunihadithia, japo ni miaka mingi ilipita, bado macho yake yalikuwa yanageuka kuwa mekundu. Na hakukoma kunihadithia hilo mara kwa mara.

    .

    .

    Hatimaye tabasamu lake lilikuwa limekoma. Hakuwa na la kumfurahisha tena isipokuwa mateso ya kitumwa tu. Lakini katika hilo nilikuja kugundua kuwa Jasmine alikuwa na ratiba ya kwenda msituni mwenyewe, tena pasipo kumuaga mtu.

    .

    .

    Mara kadhaa nilipokuwa namtafuta, hakuwa bandani wala shambani. Nilipomuuliza, hakuwa radhi kuniambia. Hivyo nikapanga kujua ni wapi huwa anaenda japo kwa siri. Niliwaza pengine atakuwa amepata kitu kingine cha kumfurahisha.

    .

    .

    Siku hiyo wakati namfuatilia nikaenda naye mbali kuzama msituni. Hakuwa anajua kama mimi namtazama kwa mbali. Alienenda ndani kabisa mpaka kwenye ghofu fulani kubwa. Humo akazama ndani na kukaa kwa dakika kadhaa.

    .

    .

    Sikujua alikuwa anafanya nini humo ndani. Nilitamani sana kujua. Ila kwa kuhofia kuonekana, ikabidi nikae mbali. Alipotoka nikakimbia upesi kurudi nyumbani.



    Siku iliyofuata hakwenda tena kule. Nikamfuata na kumuuliza, wapi huwa anakwenda? Mbona kuna muda namtafuta, simwoni! Hakunijibu, bali akaniuliza akinitazama kwa macho ya kuumba, ‘Hamill haujui ninapokwenda?’ Nikapandisha mabega yangu juu nikisema, sijui.

    .

    .

    Akatabasamu na kuendelea na kazi yake ya kufuma nguo. Nikadhani labda atakuwa aliniona nilivyokuwa namfuatilia, basi nikaona niwe mpole, nikamuuliza kule alikuwa ameenda kufanya nini?…”

    .

    .

    Hapa ndipo Brian alikuwa ameishia kusoma kabla hajasikia kelele kali zilizomshtua. Alidhani pengine ni masikio yake, ila alipotulia vema akasikia sauti zingine. Hapo akaamini kuwa ni uhalisia! Kelele zote hizo usiku za nini?

    .

    .

    Haraka akafungua mlango na kutoka nje. Akaenda chumbani kwa mama yake alipomkuta Mrs Garett akipiga makelele na mama yake akiwa anamtuliza. Akauliza nini kimejiri.

    .

    .

    “Mrs Garett amemwona Kecie bafuni!” Mamaye akamjibu. Uso wake ulikuwa umeelemewa na usingizi, mshangao na woga.

    .

    .

    “Yu kwapi Olivia?” Brian akauliza.

    .

    .

    “Chumbani huko!” mama yake akajibu. Kwa haraka Brian akapata wazo la kwenda kumwona binti huyo. Alifungua mlango pasipo hata kubisha hodi, akatupa macho yake kitandani.

    .

    .

    Olivia hakuwapo!

    .

    .

    Akatafuta kwenye kabati, chini ya kitanda na nyuma ya mlango. Olivia hakuwapo! Haraka akarudi kule kwenye chumba cha mama na kuwaambia kuwa Olivia hayupo! Wakamtafuta nyumba nzima, kweli hakuwapo.

    .

    .

    Wakiwa sebuleni, kwa mbali huko nje, Brian akamwona binti akiishilia na barabara! Akapayuka, “Yule kule!” haraka akafungua mlango na kumkimbilia binti huyo.

    .

    .

    “Olivia! … Olivia!” alimwita lakini Olivia hakuitikia. Aliendelea kutembea akitazama mbele. Brian akamfikia na kumnyanyua juu, akamwita, “Olivia! Olivia!” akiwa anampigapiga makofi shavuni kumwamsha.

    .

    .

    Macho ya Olivia yalikuwa yanatazama kule mbele alipokuwa anaenda. Kuna kitu alikuwa anaona. Akakinyooshea kidole. Lakini Brian alipotazama hakuona jambo.

    .

    .

    “Kuna nini Olivia?”

    .

    .

    Olivia hakuwa mtu anayejielewa. Bado macho yake yalikuwa yanaangazia kule mbele. Hakuonekana kama anasikia hata kile anachoambiwa.

    .

    .

    Baada ya muda fulani ndipo akamtazama Brian. Macho yake yalikuwa yanatisha. Na Brian asifahamu kinachoendelea, akajikuta anadondoka chini na kupoteza fahamu!





    Hewa inakuwa nzito sana. Hata harufu nayo pia inabadilika na kumfanya Brian apige chafya na kukurupuka. Hakuwa kwenye mazingira anayoyajua. Hapa chumba kilikuwa ni chembamba na kuta zake zilikuwa hafifu, kukuu.

    .

    .

    Mwanga ulikuwa hafifu sana. Mwanga ulioshindwa kupambana na giza.



    Brian akatazama kushoto na kulia. Hakumwona mtu. Alikuwa anatamani kunyanyuka, lakini mwili haukuwa na nguvu kabisa. Ni shingo tu ndiyo ilikuwa na uwezo wa kupeleka kichwa huku na kule.

    .

    .

    Punde mlango ukafunguliwa, Brian akatazama huko. Akamwona Kecie na gauni lake. Mkononi alikuwa na mdoli. Binti huyo akamsogelea karibu na kumtazama machoni.

    .

    .

    “Brian, naomba niokoe,” akasema kwa sauti ya upole.

    .

    .

    “Nikuokoe na nini, Kecie?” Brian akauliza.

    .

    .

    “Mimi ni mfungwa, Brian,” Kecie akasema. Mkono wake wa baridi ukamshika Brian. “Nipo kifungoni, nataka kutoka roho yangu iende kwa amani.”

    .

    .

    “Nani amekufunga, Kecie?” Brian akauliza. Kecie akatazama mlangoni na kupanyooshea kidole pasipo kusema kitu. Ajabu, Brian akapata nguvu ya kunyanyuka. Akatoka kitandani na kuuendea mlango, akaufungua na kutazama nje.

    .

    .

    Kulikuwa na korido ndefu sana. Sakafu yake haikuwa inaonekana kwani imetwaliwa na moshi. Kutani kulikuwa na fremu za picha na kwa mbali kulikuwa kunasikika sauti nzito ya mwanaume ikinena na hata kucheka.



    .

    Brian akapata shaka na walakini. Akatazama nyuma kumwangalia Kecie, Kecie akamnyooshea kidole huko huko mbele. Lakini Brian hakuwa anajua cha kufanya. Alinyanyua miguu yake kwenda mbele akiwa hafahamu anaenda kukutana na nani.

    .

    .

    Sakafu ilikuwa ya baridi kupita kiasi. Ilimfanya atetemeke na akunjekunje vidole vyake kila alipokuwa anakanyaga. Kwenye kuta, zile picha zilizokuwa zimetundikwa, zikawa zinanyamaza na kumtazama Brian alipokuwa anapita.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Picha hizo zilikuwa ni za sherehe. Zilikuwa ni za vifijo cha kipindi kile ambapo Helo alikuwa anatumbuiza. Bado picha hizo zilikuwa hai. Watu walikuwa wanafurahia na kushangilia mazingaombwe ya Helo, lakini Brian akitazama zilikuwa zinaganda na kuwa picha kamili!

    .

    .

    Brian akazitazama akisonga. Moyo wake ulikuwa unapiga kusema hofu iliyomtawala. Kadiri alivyokuwa anasonga kwenda mbele, ndivyo sauti ile aliyokuwa anaisikia kwa mbali ikawa inamjongea na hata kuleta maana.

    .

    .

    Kuna muda ilikuwa ni wimbo waimba. Na kuna muda kulikuwa na sauti ya mwanaume ikifoka ama kuteta. Mwanaume huyo ni nani? Na wimbo huo - ngoja! Atakuwa ni Helo. Brian alikuwa na kikao kichwani mwake. Na huyo anayemfokea ni nani?

    .

    .

    Hakukuwa na majibu zaidi ya yeye kusonga na kutazama kwa macho yake. Japo alikabwa na woga, hakika alitaka kujua. Alipofika kwenye mwisho wa korido, taratibu, akachomoza kichwa chake kuchungulia sebuleni.

    .

    .

    Kwa macho yake akamwona mwanaume fulani mzito aliyekuwa amevalia kofia ndefu kichwani yenye michirizi mekundu kwenye kingo zake. Mwanaume huyo alikuwa amevalia nguo za sherehe, zinazometa na kuvutia.

    .

    .

    Koti jeusi la kumbana, suruali iliyoshika mapaja na nyonga zake kisha kubwaga huko chini. Miguuni ana viatu vyenye visigino virefu na kuchongoka kwa mbele. Mikononi amevalia glovu nyeusi malighafi ya ngozi.

    .

    .

    Vitu vyote hivyo ambavyo vimetajawa vilikuwa vyametameta kana kwamba nyota angani!

    .

    .

    “Helo!” Brian akajikuta ananong’ona mwenyewe akistaajabu. Mbele ya macho yake alikuwapo mwanaume ambaye amekuwa akisikia tu simulizi zake. Mwanaume aliyewahi kutikisa Boston na Massachusetts nzima!

    .

    .

    Bado mwanaume huyo alikuwa amevalia nguo zake alizokuwa anatumbuiza nazo, hata picha zake huko ukutani zilikuwa zamwonyesha hivyo.

    .

    .

    Hakika alipendeza na basi ungetamani umwone akiwa anatumbuiza. Lakini endapo ungekumbuka kuwa mtu huyu ni mfu, ungepoteza hamu yote! Mtu aliyechomwa moto miaka iliyopita na hata nyumba yake kutiwa pia motoni, leo yu hai, mzima na anacheza!

    .

    .

    Pembeni yake kulikuwa na santuri ya kale iliyokuwa inamimina muziki wa bluzi. Hakika muziki huu ulikuwa unamkonga moyo wake, alikuwa akiimba pamoja nao na muda mwingine akijikuta anapiga kelele kali za nguvu!

    .

    .

    Lakini sura yake haikuwa inaonekana. Alikuwa amempa mgongo Brian. Kichwa chake anakitikisatikisa na mkono wake uliopo ndani ya glovu unatengeneza ala kwa vidole.

    .

    .

    Brian atamfanya nini mtu huyu? Akatazama nyuma, akakutana uso kwa uso na Kecie. Kecie hakusema jambo, bali akaendelea kumnyooshea kidole huko mbele, yaani sebuleni. Brian alipotazama tena kule sebuleni, Helo hakuwapo! Kiti pekee kilikuwa kinachecheza.

    .

    .

    Moyo wa Brian ukalipuka kwa woga sana. Akapepesa macho yake kule na kule, hakumwona Helo. Hakujua wapi ameenda, tena ‘hafla hivyo! Kurudisha uso kwa Kecie, hapo akamwona mwanaume mrefu akiwa amesimama! Mwanaume mzito aliyeshiba.

    .

    .

    Uso wake haukuwa unaonekana kwa kufichwa na kivuli cha kofia. Nguo zake zilikuwa zametameta, zang’aa, kana kwamba vito vya almasi vimeshikiziwa kwenye shuka.

    .

    .

    Alikuwa anatisha kwa urefu wake. Brian alitetemeka na akatamani kupiga kelele kwanguvu sana. Mwili ulimuisha nguvu. Mkojo ulimbana, maungio ya mwili yalipata ganzi!

    .

    .

    Kecie alijificha nyuma ya mwili wa mwanaume huyo, naye pia akiwa na uso wa hofu kuu.

    .

    .

    “Unafuata nini kwenye himaya ya walio wafu?” sauti nzito ikauliza.

    .

    .

    Brian hajajibu, akazabwa kofi kali sana. Akapaa juu na kwenda kujikita ukutani na kupoteza fahamu papo hapo! Hakujua tena kilichoendelea. Alipokuja kufungua macho, hajui hata majira, akajiona yu sebuleni kwao. Kichwa kilikuwa kinamuuma sana, haswa upande wake wa kulia.

    .

    .

    “Mama!” akaita.

    .

    .

    “Brian!” mama yake akamjongea upesi kumtazama. “Brian, mwanangu. Unaendeleaje?”

    .

    .

    “Kichwa kinaniuma sana …” Brian akatazama kushoto na kulia kwake, akamwona Mrs Garett na Olivia. Akaita, “… Olivia.” kabla hajaongeza neno, kichwa kikamgonga sana, akakunja uso wake kus’kizia.

    .

    .

    “Pumzika, Brian,” mama yake akamsihi. “ulipoteza fahamu ghafla.”

    .

    .

    “Mlikuta Olivia?” Brian akauliza.

    .

    .

    “Ndio. Olivia alikuwa ndani. Tulistaajabu kukuona wewe ukikimbia kwenda huko nje.”

    .

    .

    “Alikuwa ndani? Mbona sikumwona? Wote hatukumwona!”

    .

    .

    “Sisi tulimwona, alikuwa amelala kitandani. Tulikuambia lakini hukutuelewa. Tulistaajabu unakimbilia nje. Tulipokufuata tulikukuta ukiwa umezirai, umelala barabarani!”

    .

    .

    Brian akaduwazwa na hayo maelezo. Yule hakuwa Olivia? Mbona alimwona vivyo? Basi na ilikuwa ni njia ya Kecie kumpeleka kule kwenye ulimwengu mwingine. Ulimwengu ambao Helo aliuita wa wafu.

    .

    .

    Hakuwa anaota. Ulimwengu huo ni wa dhati. Maumivu ya kofi zito alilozabwa, bado alikuwa anayasikia sana yakiathiri sikio lake la kulia. Akawaza, atamwokoaje Kecie kule? Na je baada ya yeye kuondoka huko, Helo atamfanya nini Kecie?

    .

    .

    **

    .

    .

    Saa nane mchana.

    .

    .

    .

    Hakukuwa na shule siku hiyo, wanafunzi wote pamoja na wafanyakazi wa shule walikuwa wamehudhuria msiba wa Dkt Hamill. Shule ilikuwa pweke. Makaburi ya Boston yalikuwa yamefurika watu waliovalia sare za wanafunzi.

    .

    .

    Hakukuwa na ndugu, jamaa wala rafiki wa marehemu. Kwa heshima za wafanyakazi wenzake, shule ikiwa imesimamia kila jambo, Dkt Hamill akaagwa na kuzikwa.

    .

    .

    Watu walipotawanyika, Brian akaenda nyumbani kwa Dkt Hamill moja kwa moja. Alikuwa ndiye mtu mwenye ufunguo wa nyumba hiyo, pamoja pia na wa gari yake.

    .

    .

    Alipofika, akaitazama nyumba hiyo kana kwamba ni kitu anachokijua ila kilipotea kwa muda mrefu. Akaikagua sana kwa nje, kila kona, akajikuta anajawa na machozi machoni mwake. Aliingia ndani na kuendelea kupekua. Akatazama picha za Dkt Hamill na familia yake. Akapata maswali sana kichwani,.

    .

    .

    Familia hii ilipotelea wapi? Kwanini Dkt Hamill amekufa akiwa mpweke. Hana ndugu wala rafiki? Ni maisha gani hayo aliyokuwa anaishi? Alitamani sana kujua.

    .

    .

    Akiwa anaendelea kupekuapekua, akiwa kwenye ghorofa ya juu, kwa chini nje ya uzio, akamwona mwanaume mmoja akiwa amesimama … amesimama anamtazama!

    .

    .

    Mwanaume huyo alikuwa amevalia koti refu jeusi. Kichwa chake amekihifadhi ndani ya kofia na mikono yake ameidumbuliza kwenye mifuko ya koti.

    .

    .

    Brian akastaajabu kuwa mwanaume huyo amemwonaje akiwa juu huko? Na kwanini amesimama kana kwamba mnara akimtazama? Ni nani?

    .

    .

    Alipotazama vema akagundua mwanaume huyo ni Brewster! Mwanaume kikongwe ndani ya mji wa Boston. Mzee huyo anafanya nini hapo? Brian alishangazwa na namna ambavyo Brewster amekuwa wa kumfuatilia.

    .

    .

    Akashuka upesi toka ghorofani, akaendea geti na kutazama nje. Hakumkuta mtu! Brewster hakuwepo. Alikimbilia kaskazini mwa barabara na kusini lakini hakumwona mzee huyo. Haikujulikana wapi alielekea.

    .

    .

    Basi Brian akaona shughuli imetiwa doa, akafunga kila kitu na kwenda zake nyumbani, akiwa na maswali juu ya Brewster.

    .

    .

    Alipofika, kwakuwa alikuwa na njaa, akaendea jikoni na kupakua chakula. Alimkuta Olivia pekee sebuleni anatazama televisheni.

    .

    .

    “Wapo wapi hawa?” akamuuliza akitafuna.

    .

    .

    “Wametoka,” Olivia akamjibu kwa ufupi.

    .

    .

    Hapa ndipo Brian akakumbukua kuwa gari halikuwapo nje.

    .

    .

    “Wameenda wapi?”

    .

    .

    Olivia akapandisha mabega juu pasipo kutia neno, hakuwa anamtazama Brian. Basi Brian akaendelea kula, lakini ghafla kuna kitu kikamjia kichwani. Hakujua kwanini, ila alijikuta akikumbuka tukio la ajali ya Mr Garett!

    .

    .

    Aliyakumbuka yale maneno ya Mrs Garett kuwa bwana wake alimwambia kuwa Kecie anawinda roho yao kabla hajafariki, punde ndogo baada ya kupata ajali ya gari.

    .

    .

    Basi Brian akajikuta anakosa amani. Hata chakula hakukimaliza, akakiweka kando.

    .

    .

    “Wametoka muda mrefu?” Akauliza.

    .

    .

    “Tangu asubuhi,” Olivia akajibu, bado akiwa anatazama televisheni. Ila sauti yake ilikuwa tofauti kidogo. Hili kwa kiasi likampa mashaka Brian. Akaita, “Olivia!”

    .

    .

    Olivia akaitikia. Hakumtazama Brian. Uso wake ulikuwa umeng’ang’ania kutazama televisheni.

    .

    .

    “Olivia, nitazame.”

    .

    .

    Olivia akakaa kimya. Hakutikisika wala kupepesuka. Brian akarudia kumwambia akimtaka ageuke. Mara hii Olivia akajibu kwa swali, “Kwanini nigeuke?”

    .

    .

    Sasa mara hii sauti yake ndiyo ilikuwa tofauti kabisa. Sauti nzito ya kiume! Brian akajikuta akishtuka mno



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Moyo wake ukaenda mbio na mwili wake ukaanza kutetemeka kwa fujo! Kufumba na kufumbua, Olivia akageuza shingo yake kumtazama Brian! Lakini namna ambavyo alikuwa amegeuza kichwa hiko ilikuwa ni ya ajabu haswa! Mwili wake bado ulikuwa unatazama upande ilipo runinga, lakini uso wake ukiwa umegeuka nyuma kabisa!



    Kwa mtu ambaye ni mzima, hawezi kufanya hivi, labda tu awe amevunjika ajalini. Macho yake yalikuwa meusi ti! Mdomo wake ulikuwa mkavu kana kwamba muhogo uliotelekezwa juani.



    “Nini unataka kujua, Brian?” Olivia akauliza kwa sauti yake ya ajabu. Brian akabaki akiwa ametoa macho. Anahema kana kwamba mbwa aliyetoka kukimbizwa.



    “Nini unaogopa? Si umetaka nigeuke?”



    “Wewe ni nani?” Brian akauliza. Alikuwa amejiminyia kochini nusura atokee upande wa pili.



    “Mimi? - wataka kunijua mimi?” Olivia akauliza. Kwa haraka mwili wake ukageuka kufuata uso wake, akasimama na kumtazama Brian huku shingo yake ikiwa inakunjikakunjika hovyo kupeleka kichwa huku na kule.



    “Mimi ni mwenyeji wako, Brian! Hunijui?” Olivia akauliza. Brian akiwa anatweta kwa hofu kuu, akatikisa kichwa chake upesi. Paji lake la uso lilikuwa linatiririsha jasho.



    “Sikujui!” akasema. “Sikujui wewe ni nani!”



    Olivia akaangua kicheko na mara akakunja tena sura yake kwa hasira. Akamtazama Brian kiupande. “Mimi ni mwenyeji wako!” akamwambia kwa sauti yake ya mashine. Macho yake yaliyokoza uweusi yakiwa yametoka nje mithili ya balbu!



    “Ulikuja kwenye himaya yangu kun’tembelea … Je nataka kumtorosha mwanangu?”



    “Mimi hata simju-!” Brian hakumalizia kauli yake, akasombwa yeye pamoja na kiti. Ilikuwa ni nguvu ya ajabu. Alibamiziwa ukutani pasipo hata kuguswa, akaja kujikuta akiwa chini anagugumia na maumivu.



    “Kamwe!” Akasema Olivia akipeperusha kidole chake kushoto na kulia. “Kamwe … kamwe … usije kuthubutu!”



    Aliposema hayo akakunja ngumi ya mkono wake wa kuume, Brian akaanza kukabwa na mkono asiouona. Akadaka shingo yake akijitahidi kuhema. Mishipa ya shingo imemshupaa. Olivia akaendelea kuiminya ngumi yake. Brian akaendelea kuteseka maradufu, sasa hewa akiwa hapati! Jasho jingi lamchuruza. Macho yamemtoka nje! Alikuwa anaelekea kufa.



    Uso wake ulibadili rangi kuwa mwekundu, na kila mshipa uliokuwapo kichwani ukasimama dede! Kwa sekunde tatu tu za mbele, kijana huyu alikuwa anaiacha dunia.



    Kheri, huko nje sauti za watu zikajongea. Walikuwa ni watu wawili wanaongea na huku wakiwa mwendoni kufuata makazi ya wakina Brian. Hapa ghafla, Olivia akanyong’onyea na kudondoka chini akiwa hana fahamu! Hiyo ikawa ahueni ya Brian ya maisha yake yaliyokuwa yamebakia kwenye nyuzi nyembamba!



    Punde mlango ukafunguliwa, akaingia Mama yake Brian pamoja na Mrs Garett.



    “Mungu wangu!” Wakahamaki. Brian alikuwa ameegemea ukuta, yu hoi, na kwake pumzi ikiwa ni bidhaa yenye thamani kubwa akihangaika kuitafuta. Hata nguvu hakuwa nayo. Jasho limemvaa uso wake gubigubi. Anakohoa kwa pupa.



    Olivia alikuwa hayupo hata kwenye ulimwengu huu.



    “Brian, nini kimetokea?” Mama Brian akauliza akimkimbilia mwanaye upesi kumtazama. Mrs Garett naye akamsongea Olivia na kumpekua. “Amezirai!” akasema kwa mshangao. Baada ya muda kidogo, wakawa wamemweka Olivia juu ya kiti, na Brian naye amepumzishwa papo.



    Nyuso za wanawake hawa zilikuwa na taharuki na hofu juu. Walikuwa na kiu kikubwa cha kufahamu nini kilichojiri.



    Baada ya muda wa takribani dakika sita, Brian, akiwa ametulia na kurudi kwenye hali yake mbali na maumivu aliyokuwa anayahisi kwa mbali shingoni, akaelezea namna ambavyo mambo yalitokea. Habari hizo zikawashtua sana Mrs Garett na mama yake.



    “Namna gani nitamwokoa mwanangu lakini?” akalia Mrs Garett. A;lijikuta anatamani hata kumwona huyo ‘mwanaume’ ambaye amemshikilia mtoto wake huko eneo ambako palikuwa panaitwa ulimwengu wa walio wafu.



    Lakini Brian akamwonya. “Sidhani kama unataka kufika huko.” wakati Brian akisema haya, alikuwa ni mtulivu sana. Anajua anachokiongelea. Anajua kilichopo kule.



    “Si mahali salama hata kidogo. Panatisha, na kuna uwezekano hafifu wa kurudi hai.”



    Mrs Garett akakabwa na kilio cha gubi. Mama yake Brian akajitahidi kumpooza na kumtuliza. Punde kidogo Olivia akaamka. Hakuwa anajielewa. Aliambazaambaza macho yake huku na kule na kukutana macho kwa macho na Brian! Bado Brian alikuwa na hofu juu ya binti huyo.



    “Olivia!” Mrs Garett akamkumbatia mwanawe. Akambusu kwenye paji la uso na kumuuliza wapi alipokuwa. Nini anachokumbuka. Hamna kitu! Olivia hakuwa anakumbuka chochote kile zaidi ya mara ya mwisho kusinzia baada ya kutazama runinga kwa muda mrefu.





    **







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog