*********************************************************************************
Simulizi : Mtemi Nyantumu
Sehemu Ya Kwanza (1)
Wananchi waliendelea na shughuli mbalimbali za kilimo kama kawaida, kama ujuavyo kijijini.Jogoo akiwika tu, basi kila kaya waliweza kuamka na kujiandaa kuelekea mashambani, na huko walishinda kutwa nzima wakifanya shughuli mbalimbali za kilimo, wengine walimwagilia bustani zao, wengine walipalilia mahindi.Baadaye baada ya jua kuzama, waliweza kurudi katika majumba yao ……
Hayo ndiyo yalikua maisha halisi ya wananchi wa kijiji cha Mwantema, kijiji ambacho kilijitwalia umaarufu mkubwa miaka mingi iliyopita, kabla ya uhuru wa Tanganyika.Kijiji hiki ambacho kilitawaliwa na mtemi Nyantumu, mtemi ambaye alipokea utawala kutoka kwa baba yake kwa njia ya urithi, na haikuwahi kutokea uongozi wa kijiji cha Mwantema kutawaliwa na ukoo mwingine, tofauti na ukoo wa Nyantumu.
Japo wananchi wa kijiji cha Mwantema walionekana kuwa na furaha sana, huku kijiji chao kikiwa na chakula cha kutosha, tofauti na vijiji vingine. Lakini ndani ya mioyo yao walionekana kuchoshwa na utamaduni wa kikatili, utamaduni ambao ulipelekea watoto wengi wa kike kupoteza maisha. Haikupita mwezi bila kusikia mtoto wa mzee fulani kapoteza maisha akiwa anafanyiwa ukeketaji, leo familia ya mzee huyu iliomboreza kwa kumpoteza mtoto wao, lakini kesho kifo kama hicho kilisikika kwa mzee mwingine tena akiomboreza, huku watoto wote wakifa katika matukio yaliyofanana.
Wazazi wengi walikelwa na mila hii, lakini waliogopa kifo. Kwani mtemi aliteketeza ukoo mzima ,kama familia yoyote ikishindwa kuruhusu watoto wao wa kike kufanyiwa mila hii hatari.
Mtemi aliogopa laana kutoka kwa mzimu wao, mzimu ambao waliamini uliwalinda na kuwaepusha na njaa, pamoja na kuwalinda dhidi ya wanyama hatari wa pori la Nyankonko. Pori ambalo lilipatikana kilomita kadhaa kutoka katika makazi ya watu wa Mwantema. Ukame ulipoikumba ardhi ya Mwantema, mtemi Nyantumu aliamini kulikuwa na binti ambaye alizaliwa na kisha kufikisha umri wa kuvunja ungo huku akiwa haja keketwa. Mtemi aliamini mzimu wao Nkuru aliweza kukasirika, hivyo basi alituma askari wake kukagua kaya zote, na kama binti yoyote alipatikana katika kaya husika akiwa hajakeketwa, basi ukoo wote uliweza kuuawa, na hatimaye mvua iliweza kunyesha tena ……
Mtemi Nyantumu hakuwa na mchezo, hakuwa tayali kuona kijiji chake kikivamiwa na wanyama hatari wa porini, na pia wananchi wengi kufa kwa sababu ya njaa. Laana ambazo zilisababishwa na watu wachache ambao hawakutekeleza mila ya kijiji chao cha Mwantema, mtemi Nyantumu aliwaua bila huruma. Huku miili yao ikizikwa chini ya mti mkubwa wa ubuyu, mti ambao walifika kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kufanya tambiko, na kutoa kafara kwa mzimu wao Nkuru, mzimu ambao waliamini ulipatikana katika mti huo.
“Mke wangu, ujauzito wako una miezi tisa tayali …! naamini muda wowote nitaweza kupata mtoto mwingine wa kiume, lakini hata kama akiwa wa kike, siko tayali kumfanyia mila yetu hii, mila ambayo unaua mtoto wako kwa ujinga wako mwenyewe ……”,
“Kweli mume wangu, namuomba sana Mungu tupate dume la mbegu jingine,lakini ikatokea napata mtoto wa kike, ama zangu, ama za mtemi Nyantumu, hakeketwi mtu hapa……fyuuuuuh “,ulikuwa ni msonyo mkali wa kumalizia sentesi yake, msonyo ambao bila shaka ulimlenga mfalme Nyantumu, na wala sio mume wake, baba yake Nyoni.
“Babaa! Babaaa! Babaa! mbwa wangu kakamata sungura wawili shambani, leo ni kula nyama tu ……”,ghafla sauti nzito ya kiume, sauti ya kijana shupavu aliyeonekana kuwa na umri takribani wa miaka ishirini. Tangu azaliwe, wazazi wake hawakubarikiwa kupata mtoto mwingine kiasi kwamba waliweza kukata tamaa, lakini siku zote Mungu ndiye muweza wa yote, mama yake Nyoni alipata ujauzito mwingine baada ya Nyoni kuwa mtu mzima. Kitendo hichi kiliwafanya wawe na hamu ya kumsubili mtoto mwingine wa pili aweze kuzaliwa, huku wakiahidi kumuepusha na mila potofu na hatari ya kijiji cha Mwantema, kama akizaliwa akiwa na jinsia ya kike.
“Waaaoh ndo maana naiomba mizimu ya mababu nipate dume lingine, ona sasa! tangu asubuhi nimeshinda na mama yako hapa nyumbani, lakini kwa vile upo, shughuli za shamba hazijakwama hata kidogo, umetoka shambani na isitoshe umekuja na windo zuri, “,baba yake Nyoni alionekana kufurahia ujio wa mwanae kutoka shambani majira ya jioni, huku akiwa na sungura wawili mikononi mwake, na kuwafanya wazazi wake wote kutabasamu kwa furaha.
“Baba mimi nina jambo nataka niwambie, kila siku linaninyima usingizi, sina sababu ya kuendelea kukaa kimya, pengine mtakua na mipango mumeiandaa “,Nyoni aliongea huku akiketi kwenye jamvi ambalo baba yake na mama yake walikuwa wamekaa, huku wakitafuna karanga zilizokuwa zimemenywa na kisha kukaangwa.
“Jambo gani hilo mwanangu, mtoto wangu kipenzi Nyoni “,Mzee Mbutu aliongea huku akitayalisha masikio yake kusikiliza jambo ambalo mwanae Nyoni alitaka kumwambia. Aliamini jambo ambalo lilimnyima mwanae usingizi halikuwa la kawaida, na lilitakiwa lifanyiwe utatuzi haraka sana iwezekanavyo.
“Baba kama ujuavyo, nimeishi peke yangu kwa miaka mingi bila mdogo wangu, lakini mizimu ya mababu imembariki mama na muda wowote anaweza kujifungua mtoto mwingine… Je itakuwaje kama mtoto atakayezaliwa atakua wa kike?, kwa upande wangu sitakua tayali kushuhudia akikeketwa, anaweza kuvuja damu nyingi na kisha kupoteza maisha “, Nyoni aliamua kufunguka ya moyoni yaliyo mnyima amani, lakini jambo lililomtatiza ndilo jambo pekee ambalo aliwakuta baba yake na mama yake wakilizungumzia na kisha kuingilia mazungumzo yao bila kutambua mazungumzo yao yalihusu jambo gani. …
“Mwanangu Nyoni naamini wewe ni mtu mzima, umeishi kwa upweke muda mrefu. Upweke ulionao ni sawa na sisi wazazi wako, tulihitaji mtoto mwingine kwa miaka mingi sana, hivyo basi! hatutakuwa tayali kumuua mtoto wetu kwa mikono yetu wenyewe, kwahiyo ikitokea mtoto atakayezaliwa ni wa kike itabidi tusubili afikishe umri wa miaka kumi, kisha mtoroke naye…naamini utamlinda dhidi ya wanyama hatari ,njaa au kiu “,
“Sawa baba nimekubali, niko tayali kumlinda mdogo wangu kama akiwa wa kike “,
“Usjali mtoto wetu naimani unanguvu za kutosha kupambana na askari wa mfalme, kuhusu mzimu Nkuru, nitakupatia mkufu utauvaa shingoni wewe na mdogo wako, mzimu hautaweza kuwaona na kuwadhuru “,
Yalikuwa ni mazungumzo kati ya mzee Mbutu, mkewe aliyekuwa mjamzito wa miezi tisa pamoja na mtoto wao pekee wa kiume aliyeitwa Nyoni. Wote walikua na fikra sawa zenye upendo mzito kwa mtoto atakayezaliwa, hakuna yoyote kati yao ambaye alipenda kumuona mtoto atakayezaliwa, akiteseka dhidi ya mila potofu ya Mwantema, mila ambayo iliwanyanyasa watoto wa kike.
Mama yake Nyoni aliamini mkufu alioachiwa na mama yake kama urithi kabla ya kufa, ungeweza kumzuia mzimu Nkuru asiweze kuwadhuru watoto wake, watakapovuka mipaka ya kijiji cha Mwantema, kwani ilikua ni marufuku kuvuka mipaka kukimbia kijiji, na yoyote yule aliyekaidi aliweza kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Kwani mwili wake ,au mavazi yake hayakuweza kupatikana.
…………………………………
Asubuhi ;
Asubuhi siku iliyofuata, Nyoni alikurupuka kitandani baada ya kusikia kelele za kichanga katika banda la wazazi wake. …ilibidi atoke nje kwenda kushuhudia sauti ile nyororo, ya mtoto aliyeonekana kulia.
Aliogopa kuingia katika chumba cha wazazi wake, na ilikua sio jambo la heshima. Ilibidi asimame tu nje ,katika mlango wa banda la wazazi wake.
“Mungu wangu mwanangu, kazaliwa wa kike! Nitampoteza mwanangu jamanii “,..
“Usihuzunike mke wangu,mizimu ya mababu imetupatia mtoto hatuna budi kushukuru bila kujali jinsia ya mtoto ” yalikuwa ni mazungumzo yenye huzuni ndani yake. Japo mzee Mbutu na mkewe mwanzoni walikuwa tayali wamejadili namna ya kufanya mtoto atakapozaliwa wa kike, lakini walishindwa kuificha huzuni yao. Waliamini lazima watatengana na watoto wao, watakapotoroka katika kijiji cha Mwantema, wakikwepa kifo kutoka kwa Mtemi Nyantumu, watapo kataa binti yao asifanyiwe ukeketaji.
“Hamna namna wazazi wangu, imeshatokea! Msihuzunike, nitamlinda mdogo wangu, hakuna baya lolote litamkuta “,Nyoni aliongea kwa sauti kubwa kiasi, akiwa mlangoni baada ya kusikia maongezi ya wazazi wake. Muda mfupi baada ya mdogo wake wa kike kuzaliwa, majira ya saa kumi na mbili asubuhi …
Hali ya hewa nzuri iliwahamasisha wananchi wa kijiji cha Mwantema, kujiandaa mapema kwa ajili ya kuelekea katika shughuli zao mbalimbali hasa za kilimo. Lakini vichwa vyao vilijiuliza maswali mengi kichwani, kwani jua lilichomoza na kuwaka huku mvua ya manyunyu ikinyesha. Siku zote waliamini ishara ya mvua kunyesha huku jua likiwaka, basi kulikuwa na mtoto wa kike aliyeweza kuzaliwa katika kijiji chao cha Mwantema. …
Sio tu wanakijiji wa Mwantema waliokuwa na shauku ya kufahamu aliyejifungua mtoto wa kike, bali hata mtemi Nyantumu alitaka kujua sehemu ambako mtoto wa kike aliweza kuzaliwa, baada ya mvua ya manyunyu kuanza kunyesha huku jua likiwaka, kitendo kilichomfanya mtemi kutuma vijana wake kwenda kupepeleza sehemu ambako mtoto wa kike aliweza kuzaliwa asubuhi ile.
“Ninani kajifungua siku hii ya leo mtoto wa kike? ,wanawake watatu wote wana mimba, naomba nenda katembelee kaya zao, na atakaye kuwa amejifungua mtoto wa kike, nilitee taarifa tufanye maandalizi ya kutimiza mila atakapo fikisha umri wa miaka kumi na mbili, inatakiwa tuandike jina lake katika orodha tusiweze kusahau, na matatizo kutukumba “, mtemi Nyantumu aliongea, huku akikuna ndevu zake kuashiria kutatizwa na ishara aliyoiona. Aliamini mmojawapo kati ya wanawake watatu waliokuwa na ujauzito kijijini, aliweza kujifungua mtoto wa kike.
“Igweeeee mtemi Nyantumu, igweeeh nimekuelewa mtemi wangu mtukufu, utawala wako udumu milele ” ,ilikua ni sauti ya heshima kutoka kwa mmoja wa askari wa mtemi, akikubaliana na maagizo aliyopewa, maagizo ambayo alipaswa kuyatekeleza haraka sana iwezekanavyo. Bila kupoteza muda aliweza kuondoka, huku akiwa ameshika mkuki wake mkononi, mkuki ambao ilitumika kama siraha kwa askari wote wa kijiji cha Mwantema.
………………… …..……………
“Jua linawaka na mvua ya manyunyu inanyesha, hapa tayali kuna mtoto wa kike kazaliwa, kama sio mama Nyoni aliyejifungua ,basi atakua mama yake Kenza, kwani Mwamisa mimba yake bado changa sana “,
“Kumbe na wewe rafiki yangu unakitafakali kijimvua hiki, hata mimi njia nzima tangu natoka nyumbani, nilikua najiuliza maswali mengi sana kuhusu mnvua hii, unaonaje tukipita kwa mama Nyoni kumsalimia, kama kajifungua mtoto wa kike tutajua tu, kwani huzuni itaonekana katika uso wake, maana siku hizi watoto wanakufa sana wakiwa wanafanyiwa ukeketaji tofauti na sisi enzi zetu, sijui hata kwanini …!”,
“Eheeee! umenena rafiki yangu, kwavile ndo njia ya kuelekea shambani, inabidi tupite kumsalimia ,na kama kajifungua yeye, basi atakua na bahati mbaya,,, ” ,
Yalikuwa ni mazungumzo ya wanawake wawili ambao walikuwa wanaelekea shambani majira ya asubuhi, huku kichwani wakiwa wamejifunika majani ya mgomba, kuzuia matone ya mvua ya manyunyu, mvua ndogo sana ambayo ilikua ikinyesha huku jua likiwaka. Waliamua kupita katika nyumba ya mzee Mbutu kumjulia hali rafiki yao mama Nyoni, huku lengo kuu ni kutambua kama ndiye aliyesababisha ishara ile kutokea, ishara ya mvua ya manyunyu kunyesha huku jua likiwa linawaka.Hawakua wamekosea hata kidogo, na ishara ile haikuwahi kudanganya hata siku moja. Katika kijiji cha Mwantema siku hiyo majira ya asubuhi kuliweza kuzaliwa mtoto wa kike, na mama yake Nyoni ndiye aliyeweza kujifungua mtoto huyo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
………………………………
Baada ya mzee Mbutu na mkewe kusononeka, baada ya kupata mtoto wa kike. Hawakuwa na sababu ya kuendelea kuhuzunika, kwani wasinge jenga bali wangebomoa, hivyo basi waliamua kupiga moyo konde kulikabili tatizo ambalo liliweza kuwakabili.
Hawakuamini baada ya kutoka nje ya banda lao ili Nyoni aweze kumuona mdogo wake wa kike, kwani jua lilichomoza na mvua kunyesha. Ishara hiyo waliitambua sana, iliashiria ujio wa mtoto wa kike duniani, tena katika kijiji cha Mwantema. Walianza harakati ya kuficha siri hii, kwani muda wowote wangeweza kupokea mgeni kutoka katika ngome ya mtemi Nyantumu, au mgeni yoyote kutoka kijijini. …
“Mdogo wangu atakua mzuri na mrembo sana, nitamlinda kwenye shida na raha, usiku na mchana, masika na kiangazi, sitaruhusu kiumbe yoyote hatari amguse ……”,Nyoni aliongea huku tone zito sana, tone la machozi yaliyokuwa yamejikusanya katika jicho lake la kushoto ,likidondoka katika paji la uso wa mdogo wake, na kumnyanyua kisha kumbusu. Ilikuwa mara ya kwanza kuwa na furaha kupita kiasi, lakini furaha yake iliweza kuzungukwa na vikwazo vya kila aina, huku akiwa na kazi nzito ya kumlinda mdogo wake dhidi ya mila hatari, mila ya ukeketaji ambayo ilipitwa na wakati.
“Mke wangu, chukua manguo yako, tengeneza vizuri na yapachike tumboni, igiza kama vile bado ni mjamzito, machale yananicheza sana, na wewe Nyoni mpeleke mdogo wako ndani ……”,mzee Mbutu, baba yake Nyoni, aliongea huku akionekana kuwa na wasiwasi sana. Japo ilikuwa ni majira ya asubuhi, na isitoshe kimvua kilikua kinanyesha, lakini jasho lilimtoka mithili ya mkulima anayefanya shughuli zake nzito, shughuli za kilimo majira ya mchana, jua likiwa kali kupita kiasi. …
Mawazo yake yalikuwa sahihi, kwani baada ya mke wake kutii amli yake, na baada ya Nyoni kumpeleka mdogo wake Ndani. Wanawake wawili, rafiki zake mama Nyoni waliweza kufika nyumbani kwa mzee Mbutu.
“Igweeeeeh …mzee Mbutu, asubuhi iwe njema kwako na familia yako, tulizani mkeo kajifungua, tumepita kumjulia hali igweeeeh ” ,
“Igweeeh rafiki zangu, bado sijamleta mwana duniani, naiomba mizimu ya mababu izidi kunipa nguvu na afya njema igweeh “,yalikuwa ni majibizano kati ya mama Nyoni na rafiki zake, huku mama yake Nyoni akiwa amepakia nguo nyingi tumboni mwake, na tumbo kubwa mithili ya mimba kuonekana.
“Igweee rafiki wa mke wangu, rafiki yenu bado yu mjamzito ,nawatakia kazi njema za shamba igweeeh, muwe na siku njema “,baba yake Nyoni akiwa amesimama mlangoni na mke wake, aliwajibu wageni wake kwa busara na hekima bila woga, kitendo kilichowafanya rafiki zake mama Nyoni waamini majibu waliyopewa. Kwakuwa waliweza kutimiza malengo yao, na hawakua na nia ya kuwajulia hali familia ya mzee Mbutu, ilibidi waendelee na safari yao ya kuelekea shambani, kwani nyumba ya mzee Mbutu ilipakana na njia kuu ya kuelekea bonde la Salala. Bonde ambalo wanakijiji wa Mwantema waliweza kulima mashamba yao.
“Ing’aaaaaaa ……ng’aaaaaa ……ngaaaa nga…aa…a”,sauti ya mtoto mchanga iliweza kusikika na kutaka kuwaumbua wazazi wake Nyoni, lakini kama bahati tu, mwewe alipita juu ya nyumba katika safari zake, na sauti za mdogo wake Nyoni sauti yake kuchanganyikana na sauti za mwewe kwani zilifanana sana ……
“Duuuuh kumbe mwewe! Nilizani sauti ya kichanga? “,
“,Lakini sauti kama ya kichanga niliisikia mwanzoni kabla mwewe hajapita, lakini kama sio mwewe, sauti ya kichanga imetokea wapi, wakati mama yake Nyoni bado mjamzito na ana afya njema? ……”,rafiki zake mama Nyoni wakiwa wameiacha nyumba ya mzee Mbutu hatua kadhaa, waliendelea na mazungumzo yao huku wakiangalia juu, kumtazama mwewe aliyeruka kwa dharau na maringo, na kuachia kinyesi ambacho alimanusura kiwadondokee kichwani.
“Mizimu ya ukoo wa Nyantumu asanteni, kidogo niumbuke, “mama yake Nyoni aliongea huku akimnyonyesha mtoto wake ,kitendo kilichomfanya kichanga yule kunyamanza na kuacha kupiga kelele kelele ambazo pengine zingeleta matatizo..
“Kuanzia leo wewe ni Matumaini, umenusurika kutambulika kuwa umezaliwa na kunipatia matumaini kuwa utaendelea kuwepo na sisi, na hakuna lolote baya litaweza kukuta “,baba yake Nyoni, mzee Mbutu aliongea huku akimbatiza jina mtoto wake mchanga, mtoto wake wa kike aliyezaliwa.
Askari wa mtemi Nyantumu, askari ambaye alitumwa kwenda kupeleleza katika kaya za wanawake watatu, alikuwa amekalibia kufika katika nyumba ya mzee Mbutu. Moyoni mwake aliamini asilimia mia moja kuwa mama yake Nyoni ndiye aliyekuwa amejifungua mtoto wa kike, kwani alitoka katika kaya mbili mfululizo, kaya za wanawake waliokuwa na ujauzito lakini hakukuta hata mmoja ambaye aliweza kujifungua. Alipita kwa mama yake Kenza, tumbo lake lilikuwa bado kubwa kuashiria hakuweza kujifungua, baada ya kutoka kwa mama yake Kenza, askari yule wa mtemi Nyantumu alipita katika nyumba ya mwanamke aliyeitwa Mwamisa, huko nako alikuta Mwamisa bado yu mjamzito. Hatimaye hakuwa na shaka kabisa, nafsi yake ilimshauri arudi kwa mtemi na kumpatia taarifa, lakini aliweza kusita na kuamua kufika katika nyumba ya mzee Mbutu.
…………………………………
Mzee mbutu hofu ilimtanda, alikunja uso wake kwa mshituko wa ghafla, huku akiwa amepigwa na butwaa kwani alishindwa achukue maamuzi gani. Kurudi nyuma alishindwa, kwenda mbele alishindwa na kubaki amesimama tu mlangoni kama sanamu. Kitendo cha kumkuta kijana mwenye umli sawa na kijana wake Nyoni nje ya nyumba, kijana aliyekuwa ameshikilia mkuki huku akiwa kifua wazi. Bila shaka kijana yule alikuwa ni askari wa mtemi Nyantumu, kitendo ambacho kilimfanya mzee Mbutu apagawe na kukosa majibu ya kumpatia askari yule.Hayo yote yalitokea baada mzee Mbutu, baba yake Nyoni kufungua mlango wa nyumba yake, mlango ambao uligongwa kwa muda mrefu kuashiria ujio wa mgeni katika kaya ya wazazi wake Nyoni.
” Igweee mzee Mbutu, baba yake Nyoni. Mkeo yuko wapi?,nahitaji kujua kama amejifungua mtoto wa kike tuweze kumsajili na kumuandaa kumfanyia mila ” ,
“Mbona kimyaaa, usinishangae, niitie mkeo haraka sana, sina muda wa kupoteza igweeeeh!! “,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yalikuwa ni maswali mengi yaliyopenya katika masikio ya mzee Mbutu na kumvuruga akili yake. Aliamini mtemi Nyantumu alikuwa tayali ameshagundua kuhusu mkewe kujifungua na ndio maana askari wake aliweza kufika nyumbani kwake haraka sana bila kuchelewa, ili aweze kudhibitisha jambo hilo …
Kumbe kipindi askari yule anamuuliza mzee Mbutu maswali, Nyoni pamoja na mama yake waliweza kusikia kila kitu ambacho kiliweza kuendelea. Walitambua kuwa sauti kali ya hasira iliyosikika haikuwa ya raia wa kawaida, bali ilikuwa ya askari wa mtemi Nyantumu. Mama yake Nyoni japo alikuwa bado na afya mbovu baada ya kujifungua, lakini ilibidi apige moyo konde na kuwa jasiri. Bila kupoteza muda, alichukua nguo nyingi na kuzipachika katika tumbo lake. Umbo lake lilibadilika ghafla, tumbo lake lilionekana kubwa kama awali na kuonekana mjamzito.
“Mchukue mdogo wako, ingia katika chumba chetu, hakikisha mtoto hatoi chozi lolote lile …”,mama yake Nyoni aliongea na kumpatia maelekezo kijana wake Nyoni. Bila tatizo lolote, Nyoni aliweza kutii maagizo ya mama yake kipenzi, na kutokomea chumbani huku mdogo wake akiwa katika mikono yake.
……………………… ………
“Mke wangu yuko ndani bado ni mjamzito, subili nikamuitee…e…e …”,akiwa katika hali ya wasiwasi, mzee Mbutu aliongea na kumjibu askari wa mtemi Nyantumu. Jibu alilompatia lilimuongezea maswali mengi askari yule, kwani aliamini mama yake Nyoni ndiye aliyeweza kujifungua mtoto wa kike, lakini katika hali isiyo ya kawaida, mama yake Nyoni ilisemekana hakuweza kujifungua kutokana na maelezo ya mzee Mbutu.
Askari yule hakuweza kuamini, alijaribu kuyafikicha macho yake na kisha kumtazama tumboni mama yake Nyoni. Lakini bado macho yake hayakuweza kudanganya chochote kile, tumbo la mama yake Nyoni bado lilionekana kuwa kubwa.
“Hivi ni macho yangu au naota, au macho yangu mabovu!! Kama wanawake watatu nyote bado ni wajawazito, ni nani kajifungua mtoto wa kike katika kijiji chetu? “,
“Hata sisi hatufahamu askari mtukufu, mlinzi wa kijiji chetu, igweeeh mimi bado sijajifungua “,mama yake Nyoni aliongea na kumjibu askari yule wa mtemi Nyantumu, jibu ambalo lilimfanya askari yule kutoweka haraka sana huku akikimbia. Hakuamini kama alishindwa kukamilisha kazi aliyopatiwa na mtemi Nyantumu, na kumtambua mwanamke aliyejifungua mtoto wa kike ……
“Igweeeh karibu tena, “baba yake Nyoni, mzee Mbutu, aliongea na kumuaga askari aliyekuwa amefika umbali wa mita kadhaa kutoka nyumbani kwake. Baada ya kutoamini majibu aliyokuwa amepatiwa na kudhibitisha kwa macho yake mwenyewe kisha kutimua mbio, kwenda kumpelekea taarifa mtemi Nyantumu.
………………………………
Matumaini, mtoto wa kike mchanga wa mzee Mbutu, alinusurika kwa mala nyingine na kuzidi kuwafariji familia nzima, huku Nyoni akianza kupanga mipango namna ya kuzidi kumlinda mdogo wake mpaka hatua ya mwisho.Kwani aliamini kulikuwa na safari ndefu ilikuwa mbele yake, atakapojaribu kumtorosha mdogo wake asiweze kukeketwa.
………………………………
Mtemi Nyantumu aliketi chini ya mti wa maembe kwa muda mrefu sana, mti ambao ulikuwa nje ya kasri lake la kitemi, kasri ambalo lilizungushiwa uzio wa mianzi na kusukwa vizuri kwa kutumia kamba. Jua lilikua kali sana ,baada ya masaa mengi kupita, jua lilianza kuzama. Lakini muda wote huo mtemi Nyantumu alikuwa ameketi chini ya mti, katika jamvi zuri ambalo lilikuwa limepambwa na maua ya kuvutia. Shauku ya mtemi Nyantumu haikuwa ya kawaida, muda wote aliketi chini ya mti ule akimsubili kijakazi wake aliyemtuma kijijini. Alijiuliza maswali mengi kuhusu kuchelewa kurudi kwa askari wake, jambo ambalo halikuwa la kawaida.
Kwa mbali sana alimuona askari wake akija anakimbia ,huku akionekana kuwa na ujumbe mzito uliomfanya alete taarifa ile huku akikimbia. Askari waliokuwa katika ikulu ya mtemi walishika mapanga yao vizuri pamoja na mikuki na kujiandaa kwa vita, kwani wengine wafikili kukimbia kwa askari yule kulisababishwa na mnyama mkali aliyeingia kijijini na kuanza kumkimbiza. Lakini kadri alivyozidi kuisogelea ngome ya mtemi, ndivyo askari wa mtemi walivyoshusha siraha zao chini, baada ya kudhibitisha kutokuwepo na hatari yoyote ilee ……
‘”Igweeh kijakazi wangu, kuna nini? ” ,
“Mtemi wanawake wote watatu bado wanamimba ,sijui ishara hiyo iliyotokea inamaanisha nini!!, “
“Unasema ……?”,
“Ndio mtemi, hata mimi nimeshindwa kuamini, tukishindwa kumtambua mtoto huyu aliyezaliwa kijiji chetu kitakua hatarini ……”,
“Uko sahihi, nenda kapumzike, harafu kesho tutaenda kwa mzimu wetu Nkuru, naamini atatuonyesha mtoto huyu “,yalikuwa ni mazungumzo kati ya mtemi Nyantumu pamoja na kijakazi wake, baada ya kufika kutoka kijijini kutekeleza amli ya mfalme bila mafanikio ……
Ilikuwa ni asubuhi nyingine tena, asubuhi ambayo ilionekana kuwa mbaya sana. Mawingu mazito yalikuwa yametanda angani huku radi na ngurumo zikisikika kuashiria dalili ya mnvua. Japo hali ya hewa ilikuwa mbaya sana huku nyumba nyingi zikiwa bado zimefungwa, lakini mfalme na baadhi ya askari wake waliweza kutoka ikulu kwa ajili ya kuelekea kwenye mti wa tambiko, japo mvua ilionekana kuanza kunyesha muda wowote. Waliamini ni bora kunyeshewa na mvua kuliko kijiji chao kukumbwa na hatari kama hawataweza kwenda kwa mzimu wao Nkuru haraka sana na kumtambua mtoto wa kike aliyeweza kuzaliwa katika kijiji chao.
Safari iliweza kuanza kuelekea nje ya kijiji cha Mwantema, sehemu ambako kulikuwa na mti mkubwa wa Ubuyu. Mtemi Nyantumu alikuwa ameketi juu ya kiti cha kitemi, huku askari wake wanne wakinyenyua kiti chake kilichokuwa kimepachikwa kwenye machela ya kubebea wagonjwa..Siku zote mtemi Nyantumu hakutembea kwa miguu, popote pale alipotaka kwenda aliweza kunyenyuliwa huku akiwa ameketi kwenye kiti chake mpaka mahali husika.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hali ya leo mbaya sana, lakini hatuna budi kuwa na uzarendo wa kijiji chetu. Tusipofanya hivi, basi wanyama wakali wa pori la Nyankonko wanaweza kutuvamia na kuua watu wetu kama laana ya kutotimiza mila “,mtemi akiwa ameshikilia fimbo yake iliyong’aa sana, huku kichwani akiwa amevalia kofia yake kubwa ya duara, aliongea huku mkono wake wa kushoto ukishika na kuchezea cheni zake nyingi zilizojaa shingoni. Mapambo yote hayo ya mtemi Nyantumu, kuanzia fimbo, kofia pamoja na mikufu. Vyote viliweza kutengenezwa kwa madini ya dhahabu, na kumfanya mtemi Nyantumu kuonekana nadhifu na mwenye kupendeza.
“Igweeeh mtemi wetu Nyantumu, naamini tutapata jibu zuri kutoka kwa mzimu wetu Nkuru, daima laana haziwezi kutukumba sababu ya watu wachache kizembe namna hii……”,askari wa kuaminiwa sana na mtemi Nyantumu, askari ambaye alitumwa kijijini na kushindwa kumtambua mtoto aliyezaliwa. Aliongea kwa kujiamini na kumtia moyo mtemi Nyantumu, baada ya safari ndefu kuelekea katika mti wa mzimu Nkuru. Japo yalikuwa majira ya asubuhi mida ya saa mbili, wakiwa wameshaacha makazi ya Wanamutema, lakini jua lilikuwa bado halijachomoza kutokana na mawingu ya mvua angani …
…………………………………
“Mzimu Nkuru, mzimu wa kijiji chetu cha Mwantema. Juzi tuliona ishara ya mtoto kuzaliwa katika kijiji chetu, kwani jua liliwaka na mvua ya manyunyu kunyesha. Lakini tumeshindwa kumtambua mtoto huyo, tunaomba utuonyeshe mtoto huyo kabla balaa halijatukuta?? ……igweeeeh mzimu Nkuru”,yalikuwa ni maneno ya mtemi Nyantumu, maneno aliyoyaongea huku akimchinja mbuzi dume, mbuzi mkubwa aliyekuwa amenona sana. Damu ya mbuzi yule iliweza kumwagika na kunyunyiziwa katika mizizi ya mti ule mkubwa wa ubuyu, mizizi ambayo ilitokeza juu ya udongo. Haya yote yalitokea mala baada ya kufika katika mti wa tambiko, mti ambao ulipatikana nje ya kijiji cha Mwantema. Baada ya safari ndefu kwa takribani masaa matatu kwa miguu, huku dalili ya mvua ikionekana mawinguni.
“Igweeeeh mtemi wangu,ni kweli mtoto wa kike amezaliwa. Lakini nashindwa kumtambua mtoto huyu, inaonekana kuna nguvu inamsaidia asitambulike, nakuamulu kafanye kila njia mtoto aweze kutambulika. Bila hivyo, atafikisha umli sahihi akiwa bado hajafanyiwa mila, na mimi nitaweza kulaani kijiji chote, simba na chui wa Nyankoko watawavamia, na mimi sitawaletea mvua kama hamtatimiza mila ya kijiji chetu. Yoyote anayepinga mila, uwa ukoo wake na maiti zizikwe mahali hapa … “,sauti nzito ilisikika baada ya damu ya mbuzi aliyefanyiwa tambiko kunyunyiziwa kwenye mizizi ya mti wa ubuyu. Kumbe mti ule ndio maana uliweza kuaminika kuwepo kwa mzimu Nkuru ndani yake, kwani ulipasuka katikati na kuanza kuongea maneno ambayo yalimfanya mtemi kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana na agizo la mzimu Nkuru. Hawakutambua kuwa mama yake Nyoni alikuwa anamiliki mikufu miwili aliyorithishwa na marehemu mama yake, mikufu ambayo ilikuwa na uwezo wa kumfanya mtu yoyote kuto onekana mbele ya macho ya mzimu Nkuru atakapoivaa shingoni.
Kumbe Matumaini baada ya kuzaliwa, mama yake Nyoni mke wake mzee Mbutu. Alimvalisha mtoto wake kichanga aliyeitwa Matumaini moja kati ya mikufu ile kwa ajili ya kumlinda. Hofu juu ya hatari kumkuta mwanae ndiyo iliyomfanya kumvalisha mkufu ule mapema sana baada ya kuzaliwa.
…………………………………
Mzee Mbutu, Nyoni pamoja na mama yake. Waliketi sebuleni huku wakiendelea kupanga mipango namna ya kuendelea kumlinda Matumaini. Shughuli za shamba zilisita kwa muda kwani walikuwa tayali na chakula cha kutosha hasa mahindi na maharage, katika ghara lao la kuhifadhia chakula.
“Mtu yoyote akifika hapa, tutamwambia mimba imeharibika, kwani hawawezi kumuona mtoto tena hata kwa njia ya uchawi, mkufu aliouvaa unamfanya asionekane kwa kutumia uchawi “,mama yake Nyoni aliongea huku akiwatazama usoni mzee Mbutu pamoja na Nyoni. Kitendo cha Nyoni na Mzee Mbutu kutikisa vichwa, kilimfanya mama yake Nyoni kutabasamu kwani aliamini maelezo yake yaliweza kueleweka.
“Matumaini atakaa ndani mpaka miaka kumi na mbili, ikifika mtatoroka kuelekea kijiji cha pili kutoka hapa kijiji cha Ukarimu. Japo hakuna aliyetoroka na kurudi salama lakini nina imani nyie mtakua wa kwanza kurudi na kutuletea dawa ya kuzuia mila hii hatari na potofu ” ,Mzee Mbutu aliongea na kuzungumzia mahali ambapo Nyoni na mdogo wake Matumaini watatoroka na kuelekea, katika kijiji cha Ukarimu. Kijiji ambacho kilimiliki dawa ya kuzuia mila hatari kama ya Ukeketaji. Dawa hii ilimzuia mzimu Nkuru kuua watu ambao hawakuruhusu watoto wao kukeketwa, na ndio maana mzimu Nkuru uliuwa kila mtu aliyevuka mipaka ya kijiji cha Mwantema kwa lengo la kufika kijiji cha Ukarimu kuchukua dawa hii ya kupambana na mzimu Nkuru pamoja na mila yake hatari.
Mzimu Nkuru hakuwa peke yake kuzuia watu kufika kijiji cha Mwantema, bali kulikuwa na wanyama wakali wa pori la Nyankonko, simba pamoja na chui ambao waliuwa watu wote waliokatiza porini Nyankonko. Pori ambalo lilikuwa na njia kuu ya kuelekea kijiji cha Ukarimu.
“Sawa wazazi wangu, mimi ni shujaa, niko tayali kumlinda mdogo wangu kwa jambo lolote lile “,Nyoni aliongea huku akitabasamu na kuitazama sura ya mdogo wake Matumaini, sura ambayo ilionekana kutotambua chochote kile kilichokua kikiendelea, kutokana na umli mdogo wa siku tatu tu aliokuwa nao.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kijiji cha Mwantema kikaingiwa na hofu kuu, hofu ambayo ilitokana na tetesi za kuzaliwa mtoto wa kike kijijini bila kutambulika. Taarifa iliyotoka kwa mtemi Nyantumu mala baada ya kutoka katika mti wa mzimu wao Nkuru iliweza kuwakata maini, na wote kwa pamoja walibaki wameshika tama bila kutambua maamuzi ya kuchukua. Walitambua kuwa wanakijiji wengi wataweza kupoteza maisha kama mtoto yule akishindwa kutambulika mapema, kwani umri wa kumfanyia mila utafika na kupitiliza, jambo ambalo litapelekea mtemi Nkuru kulaani kijiji, laana ambazo zingeambatana na ukame pamoja na uvamizi wa wanyama wakali kutoka katika pori la Nyankonko.
“Igweeee Wanamutema, hali ya kijiji kwa sasa sio salama na kuna uwezekano wa kupata laana miaka kumi ijayo, nazani kila mmoja aliweza kuona ishara za kuzaliwa mtoto wa kike hapa kijijini siku chache zilizopita, lakini jambo la kushangaza, mtoto hajafahamika katika uwezo wa kawaida na hata kwa uchawi. Tunaomba wote kwa pamoja tushirikiane kumtambua mtoto huyu, bila hivyo familia zote zitadondosha chozi miaka ijayo “,mtemi Nyantumu alihutubia watu wake mala baada ya kuitisha kikao cha dharula, muda mfupi baada ya kutoka katika mti wa tambiko, mti wa mzimu wao Nkuru.
“Igweeeh mtemi tumekuelewa, nina imani tutatii amli yako, na kupeleleza kumtambua mtoto huyu, lakini nina hofu mama yake Nyoni ndiye aliyeweza kujifungua japo anatwambia mimba yake imeharibika ……”,mwanamke mmoja aliyeonekana kuumia sana baada ya kusikia taarifa hatarishi, taarifa ambayo iliashiria umwagikaji wa damu nchini Mwamutema. Aliongea kwa huzuni sana na kuelezea wasiwasi wake juu ya familia ya mzee Mbutu, familia ambayo ilipinga mila hatari ya ukeketaji.
“Ndio mtemi Nyantumu, nina imani hata mahali hapa kwenye mkutano wa kijiji hawajatokea ,ninaomba upelelezi wa hali ya juu sana ukafanyike katika nyumba yao “,mwanakijiji mwingine wa Mwantema aliweza kukazia maoni yaliyotolewa na raia aliyetangulia, na kuwaumbua familia ya mzee Mbutu kwani hakukuwa na mtu hata mmoja kutoka katika kaya yake aliyeshiriki mkutano wa dharula.
Sawa wananchi wangu najua mnaumia mnapokubali watoto wenu kufanyiwa mila, huku watu wachache wakishindwa kutekeleza maagizo na kutukaribishia matatizo kijijini, nawaomba bila kupoteza muda wote kwa pamoja tuelekee katika familia ya mzee Mbutu ……”,mtemi Nyantumu, mmoja wa watemi katili ambao walikuwepo nchini Tanganyika miaka mingi iliyopita,alizungumza na kutoa kauli ya mwisho iliyomfurahisha kila mmoja aliyehudhuria mkutano ule.Bila kupoteza muda kundi kubwa la watu lilianza safari ya kuelekea kwa mzee Mbutu,huku mtemi akiongoza msafara ule.…
…………………………………
Mzee Mbutu alishangazwa na mlio wa ngoma kubwa iliyopigwa na askari wa mtemi,askari aliyekatiza katika kila kona ya kijiji cha Mwantema.Askari yule aliwataka raia wote kuhudhuria mkutano wa dharula kwani mtemi Nyantumu alitaka kuhutubia wanakijiji.Kama kawaida yake,machale yalimcheza na kusita kutii amli hiyo,alichokifanya na kutumia muda huo kupanga mipango ya kuendelea kumlinda mtoto wake. Hakuwa na muda wa kupoteza kwani fikra zake ziliashiria uwepo wa hatari muda wowote, alichokifanya ni kumwelekeza Nyoni namna ya kufanya kuyaokoa maisha ya binti mdogo aliyeitwa Matumaini
“Nyoni, naomba mchukue mdogo wako muelekee shambani kujificha na mtarudi usiku ,nina wasiwasi kuna jambo baya linataka kutokea ……”,
“,Hata mimi mapigo yangu ya moyo yanapiga kwa kasi sana, bila shaka mkutano ambao mtemi kaitisha kuna jambo la hatari anataka kutangaza, nakuomba Nyoni tekeleza maagizo ya baba yako “,wazazi wake Nyoni waliongea huku wakitilia mkazo maneno yao, na bila kupoteza muda. Nyoni alimnyenyua Matumaini na kutokomea bondeni, sehemu ambako kulikuwa na mashamba ya Wanamutema.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
………………………………
“Igweeeeh mzee Mbutu mbona hujahudhuria kikao? “,
“Igweeeh mtemi wangu kipenzi, nilikua shambani mimi na mke wangu na ndio tunarudi kutoka shambani ” ,
“Sawa nimekuelewa, naomba tufanye ukaguzi katika nyumba yako, “,
“Sawa ,mnaweza fanya ukaguzi “
Mtemi Nyantumu akiongozana na kundi kubwa la Wanamutema, alizungumza na mzee Mbutu baada ya kuwasili katika nyumba yake na kufanya ukaguzi, kutambua kama taarifa ya mimba ya mke wake kuharibika ilikuwa ya kweli au ya uongo ……
“Mtemi hatujabahatika kuona chochote “
“Sawa askari wangu igweeeh “,
“Samahani kwa usumbufu mzee Mbutu, igweeeh ! Je Nyoni yuko wapi “,
“Bila samahani mtemi wangu igweeeh, Nyoni alibaki shambani anawinda na kuandaa kuni, bila shaka yuko njiani anakuja ” , mazungumzo ya mzee Mbutu yaliweza kuendelea mala baada ya ukaguzi katika kaya yake kukamilika, huku kukiwa hakuna chochote ambacho kiliweza kugundulika ……
Saa 5 baadae ……
Hatimae Kiza kiliweza kuingia, tayali ilikuwa yapata mida ya saa mbili usiku. Nyoni aliamini kulikuwa na usalama kijijini, hivyo aliamua kurejea kutoka mafichoni, katika mashamba ambayo yalitumika katika kilimo na Wanakijiji wa Mwamutema ……
Japo kijiji kilikua kimya na barabara ya kuelekea kijijini kutokuwa na watu, Nyoni alirudi nyumbani kifua mbele na kwa ujasiri mkubwa, bila hata kuogopa wanyama wakali, na hatime alifika nyumbani salama.
MIAKA 12 BAADAE;
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hatimae miaka mingi iliweza kupita, Matumaini aliweza kuwa mtu mzima, japo alikulia ndani kuficha siri isiweze kugundulika kijijini ……
Mama yake Nyoni alimsihi mtoto wake kutoivua cheni aliyoivaa shingoni, kila jambo ambalo aliweza kulifanya, alitakiwa kulinda mkufu ambao ulimlinda asiweze kutambulika na mzimu Nkuru. Lakini kwakua miaka mingi iliweza kupita, na umri wa Matumaini kupita bila kufanyiwa mila, hatimae Ukame uliweza kuikumba ardhi ya Mwamutema ……
Wanamutema wengi waliweza kufa kwa kukosa maji na chakula kwani mimea mingi iliweza kukauka, sio mimea tu bali hata mifugo mingi ilikufa kwa kukosa maji na chakula baada ya majani kunyauka. Hali hii ilipelekea mtemi Nyantumu kuanza kutafuta chanzo cha tatizo bila mafanikio kwani tayali miaka mingi iliweza kupita na alikua ameshasau ishara ya mtoto wa kike kuzaliwa, ishara ambayo ilitokea kijijini zaidi ya miaka kumi iliyopita.……
……………………………
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment