Search This Blog

MTEMI NYANTUMU - 4

 

    Simulizi : Mtemi Nyantumu

    Sehemu Ya Nne (4)





    Giza likiwa tayali limeshatanda ,ukimya ukiwa umetawala katika pori la Nyankonko tofauti na mida ya mchana ambapo sauti za ndege zilisikika kila kona ya msitu. Licha ya uwepo wa giza kali, kundi la kwanza la askari wa mfalme likiongozwa na mbwa liliendelea kusonga mbele bila kupumzika kufidia muda ambao waliupoteza baada ya kupita njia isiyo sahihi …



    Lakini katika hali isiyo kuwa ya kawaida, walijikuta wakifika eneo ambalo lilionekana kuwa na uwepo wa watu mahali pale. Kwani mahema mawili yalikuwa yametengenezwa, huku moto ukiwashwa kwa ajili ya kufukuza wanyama wakali …



    “Kuna watu mahali hapa, ngoja nisogee kuchunguza inawezekana ni maadui. Shikeni upinde wenu kwa makini kwa ajili ya kushambulia …”, kiongozi wa kundi la kwanza baada ya kuhakikisha mbwa wake wakiwa kimya ili wasiwashitue maadui, aliwapatia maelekezo askari wake kisha alijitupa chini kwenye majani na kuanza kujivuta kusogea eneo ambalo kuliwekwa kambi na watu wasiojulikana. Kambi ambayo bila shaka waliamini itakuwa ya Nyoni pamoja na dada yake. Kwani kulikuwa na mahema mawili yaliyotengenezwa pembeni ya njia ………



    ………………………………



    Mtemi Nyantumu na kundi lake waliketi pembeni ya mahema yao. Kwakuwa kulikuwa na giza pamoja na baridi kali, ilibidi wawashe moto kujipatia joto na kuwakimbiza wanyama wakali wasiweze kuwasogelea …



    Bila kutegemea walijikuta wakingiwa na hofu, kwani walianza kuzisikia sauti za mbwa wakija mahali walipokua. Ilibidi wawe makini kuzisikiliza sauti hizo, sauti ambazo ziliashiria ujio wa mbwa hao karibu zaidi kwani sauti zao za kubweka ziliongezeka kadri muda ulivyo zidi kwenda …



    Ilibidi wasimame na kujiandaa kukabiliana na maadui zao kwani waliamini mbwa hao hawakuwa peke yao .Lakini katika hali wasiyo itarajia,sauti za mbwa walizozisikia zilikata ghafla,na kuwafanya waamini kuwa maadui walikuwa wamefika karibu…



    “Kamateni siraha zenu,hakikisheni ukimya una tawala kwa ajili ya kumshambulia adui atakaye kanyaga mguu wake mahali hapa!,”



    “, Sawa mtemi,tumekuelewa”,



    Ilikua ni sauti ya askari wa kundi la pili ambalo liliongozwa na mtemi Nyantumu,kundi ambalo lilikuwa na malengo sawa na kundi la kwanza.Lengo la kumtafuta Nyoni pamoja na Matumaini katika pori la Nyankonko.Askari hawa wakiwa wameshikilia siraha zao vilivyo,mikuki pamoja na upinde huku wengine wakiwa na mapanga.Walitii amli ya mtemi wao na kujiandaa kwa ajili ya mapambano.Sio peke yao ambao walijiandaa kupambana na maadui bali hata mbwa wao walikaa kimyaa kutokana na mafunzo waliyopewa ili wasiweze kutambulika na maadui…



    Pori la Nyankonko;



    Mambo yanaiva katika pori la Nyankonko  ,kwani makundi mawili yalikuwa yakiviziana bila kutambua kuwa walikuwa ndugu wa baba mmoja na mama mmoja. Kwa kutumia ujuzi wao wa kivita, kila kundi lilimnyemelea mwenzake ili kumshambulia kisha kuibuka mshindi katika uwanja wa kivita …



    “Jamani, taratibu tuwakamate wakiwa hai! ” , alikuwa ni askari kiongozi wa kundi la kwanza, aliendelea kulihimiza kundi lake kuwa makini na kuhakikisha wanawatia nguvuni adui zao wakiwa hai. Aliamini kwa asilimia mia moja kuwa adui zake walikuwa ni Nyoni pamoja na dada yake, tofauti kabisa na fikra zake.



    “Igwee Ngungi, tumekuelewa …”,  askari wa kundi la kwanza ambao walikuwa wa kwanza kuingia msituni kumsaka Nyoni, waliongea kwa sauti ya chini sana ambayo haikusikika na mtu yoyote yule zaidi yao. Walimjibu kiongozi wao aliyeitwa Ngungi, neno ambalo lilimaanisha “shujaa ” kwa lugha ya Kimutema …

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ………………………………



    Kundi la pili nalo halikuwa nyuma  kujiweka sawa kumkabili adui yao, bila shaka waliamini Nyoni ndiye alikuwa akiwanyemelea ili kuwashambulia. Fikra zao hazikutofautiana na kundi la kwanza hata kidogo. Hivyo mtemi Nyantumu kwa dharau ya hali ya juu, alianza kujisogeza kabisa mbele ya askari wake kwani alimuona Nyoni kama mtoto mdogo kwake …



    “Hapa tuko karibu yao kabisa simnasikia wakinong’ona, kwahiyo ueni kabisa wapuuzi hawa!!  Maiti zikazikwe na ndugu zao kijijini ……”,



    “Igweee ngungi, “, kwa heshima kabisa kundi la pili waliitikia kauli ya mtemi wao Nyantumu, huku wakitumia jina la Ngungi wakimaanisha ni shujaa. Hawakuwa kinyume na neno walilolitamka, askari ambao waliongozwa na mtemi Nyantumu walikuwa sahihi kwa asilimia mia moja. Mtemi Nyantumu alikuwa jasili na shupavu, hakuwa muoga hata kidogo katika mambo muhimu ya kulinda utawala wake. Alikuwa tayali kumwaga damu ya watu wake, na kupambana na kiumbe yoyote yule aliyepingana na utawala wake pamoja na utawala wa mzimu Nkuru.



    “Igweee ngungi wa Wanamutema(igwee mashujaa wa Wanamutema)  shambulia!! “, mtemi Nyantumu alitoa amli kwa jeshi lake kuwashambulia adui zake, kwani waliamini bila kujitoa muhanga na kuwahi kushambulia. Basi adui yao angewashambulia haraka sana na kuwasababishia madhara, kwani giza lilikuwa kali sana na haikuwa rahisi kumuona adui yao kwa urahisi …



    Askari wake hawakuwa legelege katika swala la kutumia mikuki na upinde, walifyatua mishale mingi sana eneo ambalo walihisi maadui zao walikuwa wamejificha wakiwanyemelea. Bila kujitambua, ndugu walijikuta wakipigana vita wenyewe kwa wenyewe na kujisababishia  matatizo…



    “Laleni chini msishambulie, ni wenzetu!  igwee mtemi Nyantumu msitushambulie ni sisi kundi la kwanza la askari wako …”,



    “,Uwiiii, “



    “Yalaaa “,



    Kiongozi wa kundi la kwanza alitoa amli kwa askari wa kundi lake, aliwaambia walale chini kuepuka mishale ambayo iliweza kufyatuliwa. Hakuwa na sababu ya kuwaruhusu na wao kujibu mashambulizi kwani waliweza kuwagundua kuwa ni wenzao, kwani walisikia sauti ya mtemi Nyantumu kipindi akitoa amli kwa vijana wake. Lakini amli yake ilikuwa imeshachelewa, baadhi ya askari wa kundi lake waliteketezwa kwa mishale na kuuawa kama nzige.



    “Acha!  nimesema acha!  mnaua wenzenu! “, mtemi Nyantumu alifoka kwa hasira, hasa baada ya kusikia amli kutoka kwa kiongozi mkuu wa jeshi lake aliyempenda sana kupita maelezo. Sauti ya kamanda wake ilisisitiza askari wa mtemi Nyantumu wasitishe zoezi la kushambulia, lakini kauli yake ilisindikizwa na vilio vingi vya maumivu. Kitendo ambacho kilimfanya mtemi Nyantumu kujilaumu kwa maamuzi yake ya kukurupuka.



    Bila hiyana, askari ambao waliongozwa na mtemi Nyantumu walijutia jambo ambalo walilifanya, hasa baada ya kusikia sauti za machungu zikijibu mishale waliyo ifyatua upande wa pili wa kundi ambalo walifikiri ni maadui zao, kumbe sivyo. Walitupa siraha zao kisha kukimbia eneo ambalo kelele za majonzi na huzuni ziliweza kusikika zikitoa lawama. Sio askari pekee waliokimbia, bali hata mtemi Nyantumu alikimbia eneo la tukio huku mbwa wakibweka kwa fujo kwani waligundua walikuwa wakiwindana wao kwa wao.



    “Poleni sana, jamani!  Kila mmoja amsaidie mwenzake, halafu washeni moto tutazame majeraha yao tuone kama tunaweza kuwasaidia ……”, kiongozi wa kundi la kwanza, kiongozi mkuu wa jeshi la mtemi Nyantumu aligawa majukumu kwa vijana wake ili kuokoa maisha ya askari wake. Japo shambulio lilikuwa la sekunde tu, lakini askari zaidi ya mia moja walijeruhiwa.



    “Igweee mzimu Nkuru, na shujaa wako huyu apumzike kwa amani! “,mtemi Nyantumu alikutana uso kwa uso na maiti ya askari wake,baada ya kufika eneo la tukio. Askari ambaye alichomwa na mkuki tumboni. Mkuki ambao ulipenya na kutokezea mgongoni. Mtemi Nyantumu hakusita kudondosha chozi, kwani alijiona mwenye hatia mbele ya askari wake pamoja na mzimu Nkuru kwa maamuzi yake ya haraka  Ilibidi amuombee shujaa wake pumziko la amani kwani alikufa kishujaa katika uwanja wa kivita, kutetea utawala wa mtemi Nyantumu …



    “Na wapumzike kwa amani,!



    “Huyu mshenzi ndio kasababisha yote haya, tangu siku ya kwanza ni majanga tu. Tukimkamata, mkono wake halali yangu …”,



    “Mimi shingo yake halali yangu, “



    “Mimi nitamubaka dada yake mbele yake, “



    Askari wa mtemi Nyantumu walijawa na hasira baada ya kushuhudia majeruhi wa tukio lile, kilichowauma zaidi walipigana wao kwa wao sababu ya mtu mmoja ambaye ni kijana mdogo kabisa. Maiti zilikuwa nyingi zaidi ya unavyofikilia, kitendo ambacho kilionesha umahili mkubwa wa askari wa mtemi Nyantumu katika kutumia upinde na mikuki …



    “Jamani nafikilia sijui nitamfanya nini Nyoni kama nikimtia nguvuni, isitoshe kinacho niuma zaidi tumeuana sisi kwa sisi. Sijui ingekuaje kama na nyie mngejibu mashambulizi, naamini jeshi lote lingekwisha ……”,



    Mtemi Nyantumu alizungumza huku akiongoza askari wake wazima kutoa huduma kwa baadhi ya majeruhi huku wengi wakiwa tayali wamepoteza maisha. Kipindi hayo yote yaki endelea, moto mkubwa ulikuwa tayali umewashwa kwa sekunde chache tu na kuwapatia mwanga na kusaidia kufukuza wanyama wakali …



    “Lakini mtemi, nyoka aliyeuawa karibu na mahema yetu mnazani kauawa na nani kama sio Nyoni. Inatakiwa tuwe makini, kwani kama kajiamini kupita njia hii hatari na kufanikiwa kumuua Nyoka mkubwa kiasi kile. Basi kuna nguvu isiyo ya kawaida inamsaidia kupambana …” ,



    “Bila shaka ni mkufu aliouvaa yeye pamoja na dada yake, nina amini inamsaidia kujilinda …”, mtemi Nyantumu alimjibu askari wake aliyeonekana kuanza kumuogopa Nyoni, kwani ushujaa alio uonesha kupambana na nyoka mkubwa kiasi kile. Nyoka ambaye walifikili aliuawa na wenzao, kumbe sivyo ……http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    …………………………………



    “Tupumzike kaka!  mimi nimechoka, tutaendelea kesho “,



    “Kweli hata mimi nimechoka, tupumzike “



    “Msiwe na hofu, hapa ni mahali sahihi pa kupumzika. Halafu askari wa mtemi Nyantumu wako ndani ya msitu huu wanawafatilia, na hawajatambua kama tayali mmeshaniokota ” ,jiwe la ajabu la mzimu Nkuru liliongea, huku Nyoni na Matumaini wakiketi kwa mala nyingine chini ya mti mwingine kujipumzisha …



    Kwa msaada wa mwanga ambao ulitolewa na mzimu Ntema, kwani jiwe lake liling’aa sana. Walijiona walikuwa mahali salama, bila kutambua kuwa mzimu Nkuru alikuwa na uwezo wa kuendelea kuwafuatilia ili awadhuru licha ya kulindwa na mzimu Ntema.



    “Unasemaje?”., Nyoni hakuamini maneno ambayo yalizungumzwa na mzimu Ntema, ilibidi aulize vizuri ili kudhibitisha sauti iliyopenya katika masikio yake muda mfupi uliopita.



    “Ndio, wako ndani ya msitu huu, lakini wameshambuliana na kuuana bila kujitambua kwa sababu ya giza nene la msitu huu “,



    “‘Ndio wakome, siwapendi hata kidogo na roho zao mbaya “,Matumaini pamoja na jiwe la mzimu Ntema, walizungumza kuonesha hisia zao juu ya askari wa mtemi Nyantumu. Maneno yake mazito ya Matumaini, yalionesha ni kiasi gani alichukizwa na utawala wa kikatili wa mtemi Nyantumu …



    …………………………………



    Wanyama hatari wa pori la Nyankonko, wakiwa na njaa kali walianza kuhisi harufu nzuri ya damu katika mapua yao. Taratibu walianza kujongea eneo ambalo harufu hiyo ilitokea, bila kujali moto mkubwa ambao ulikuwa umewashwa. Lakini kwa upande wa mtemi Nyantumu waliendelea kuhudumia majeruhi wao, bila kujali hatari yoyote ile  ya kuvamiwa na wanyama wakali wa pori la Nyankonko. Waliamini kwa moto ambao waliuwasha, hakuna mnyama yoyote ambaye angeweza kuwasogelea ili kuwashambulia.



    Pori la Nyankonko;



    Simba wakubwa sana, waliendelea kusogea  sehemu ambayo harufu ya damu ilikuwa ikitokea. Uchu wa kula nyama ya binadamu, nyama ambayo ilipendwa sana kutokana na kuwa na chumvi nyingi ilisababisha mate mazito kujaa katika midomo yao huku udenda ukiwadondoka



    Walikuwa tayali kwa ajili ya kupambana na kiumbe yoyote yule ambaye angewazuia wasijipatie kitoweo …



    “Uuuuuuuuuuu!!



    muungurumo mkubwa ulisikika katika pori la Nyankonko, na kusababisha sauti za mwangwi kusikika kila kona ya msitu. Simba wale walitoa sauti hiyo, ili kuwaogopesha maadui ambao walionekana kuwasha moto ili kujilinda.



    …………………………………



    “Jamani ni simba! ” ,



    “Tena wengi sio mmoja!  ,kila mtu akamate siraha yake ili kuwashambulia ” ,



    “Haraka sana kamateni siraha zenu. Simba wanasogea haraka sana kutushambulia, msiogope chochote kile. Hasira za ndugu zetu kufa, tuzimalizie kwa simba hawa “, Mtemi Nyantumu alitoa maagizo kwa vijana wale, mara baada ya kugundua uwepo wa simba karibu yao ambao walikuwa wakiwasogelea. Moto ambao waliuwasha uliwasaidia kuwashuhudia vizuri maadui zao ambao walikuja kifua mbele, wakijiamini kwa kiasi kikubwa. Kwani waliwadharau binadamu kutokana na maumbo yao, maumbo ambayo yalionekana madogo zaidi mala tatu zaidi yao.



    “Shambulia!  ua kabisa Simba hao, siraha zetu ndio maisha yetu. Tukishindwa kuwaua na kuruhusu watusogelee, basi tutakua tumekwisha! “,Mtemi Nyantumu alitoa amli kwa jeshi lake, jeshi ambalo lilijawa na hasira baada ya kupoteza ndugu zao katika mazingira yasiyo tarajiwa. Bila kuchelewa, walikamatilia siraha zao kishujaa na kuanza kuwashambulia kikatili simba wale ambao haijulikani walitokea upande gani ……



    “Uuuuuuuu…u…u” ,muungurumo mzito uliojaa uchungu ndani yake, ulisikika kwa sekunde takribani mbili kisha kupotea huku sauti ya mwangwi ikijirudia rudia msituni. Simba zaidi ya ishirini walikuwa tayari wameuawa kikatili na askari wa mtemi Nyantumu. Askari ambao walikuwa na hasira, mara baada ya kupoteza uhai wa askari wenzao kwa kutumia mikono yao wenyewe. Jambo ambalo liliwauma na kuwakera kupita kiasi.



    “Mambo si ndio hayo, kwisha habari yao. Kazi nzuri vijana wangu “, Mtemi Nyantumu alitoa tabasamu zuri baada kugundua simba walikuwa tayali wameteketezwa na kuuawa kikatili bila huruma. Hakusita kuwasifia vijana wake kwa kazi nzuri ya kujifuta machungu na kupunguza hasira zao kwa kuwaua wanyama hatari ambao alimanusura wasababishe madhara mengine makubwa zaidi kwa askari wa mtemi Nyantumu.



    “Mshenzi kweli wewe, kufa na wasalimie kuzimu! Kufa!  Kufa! ” ,askari mwingine wa mtemi Nyantumu akiwa ameshikilia panga lake, aliendelea kumchoma tumboni simba mkubwa ambaye tayali alikuwa amesha poteza maisha. Hakujali kuwa simba yule alikuwa tayali ameshageuka mzoga, aliendelea kumchoma choma tumboni kwa hasira ili kuzimaliza hasira zake ambazo zilisababishwa na kitendo cha rafiki yake kuuawa tena kwa mikono yake mwenyewe. Muda wa masaa kadhaa yaliyopita,kwani walishambuliana wenyewe kwa wenyewe msituni bila kujitambua kutokana na giza hatari la pori la Nyankonko …

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ………………………………



    Ukarimu;



    Kama jinsi ambavyo serikali ya kijiji cha Ukarimu ilikuwa imekubaliana, jeshi kubwa la askari mia moja wakiwa na ujuzi wa kupambana kwa kutumia mbinu mbalimbali hasa ushirikina pamoja na matumizi ya mikuki. Walianza kukamatilia siraha zao, huku wakipakia vyakula mbalimbali hasa matunda pamoja na asali kwa ajili ya kujiandaa na safari mara kutakapo pambazuka. Safari yao haikuwa nyingine, zaidi ya safari ya kuelekea pori la Nyankonko kumtafuta mzimu Ntema. Mzimu aliyetupwa katika pori hilo miaka mingi iliyopita, kwa lengo la kuteketeza utawala wake na kupisha utawala wa mzimu Nkuru pamoja na mtemi Nyantumu. Ukoo wa Nyantumu ndio uliohusika na dhambi hiyo, ili kujipatia madaraka, sifa pamoja na utajiri katika ukoo wao.



    “Ninawatuma Nyankonko, japo sitakuwa pamoja na nyinyi. Lakini maisha mazuri ya wake zenu, watoto wenu pamoja na ndugu zenu, yako mikononi mwenu. Laana zinazo tukabili katika kijiji chetu na kupelekea kukosa maji pamoja na chakula ,tulizisababisha wenyewe kwa tamaa yetu na kumsaidia mtemi Nyantumu kuingia madarakani katika kijiji cha Mwantema na kusababisha vifo. Hivyo basi, hatuna sababu kumtoa madarakani ili kuepuka laana hizi. Hatua ya kwanza ya kumuondoa madarakani ni kumkomboa mzimu Ntema kutoka katika mazingira ya porini alikotupwa, ninaomba mjitume!! “,mtemi wa kijiji cha Ukarimu, mtemi ambaye alisifika kwa nguvu nyingi za kishirikina alizokuwa nazo. Nguvu ambazo aliwapatia hata askari wake kwa ajili ya kudumisha ulinzi katika kijiji chao, alihutubia jeshi lake ambalo lilikuwa bize kujiandaa kwa safari mara tu jua litakapo chomoza.



    “Ndio mtemi, tunakubali kupambana kufa na kupona kukomboa kijiji chetu, igweeh”, jeshi la kijiji cha Ukarimu, kwa heshima na nidhamu ya hali ya juu iliyo jaa uzarendo ndani yake. Waliitikia kwa sauti kubwa iliyopelekea wananchi wote wa kijiji cha Ukarimu kupiga makofi mengi, kuwapongeza askari wao kwa kiapo chao. Hawakuwa na shaka nao hata kidogo, kwani siku zote walipoenda vitani walirudi na ushindi na wala sio kitu kingine ……



    “Nina waamini vijana wangu, sina shaka na nyinyi hata kidogo! Nitakuwa nawapatia msaada pale utakapohitajika na pale nguvu zitakapowaishia. Nawatakia safari njema asubuhi ya kesho “, mtemi wa kijiji cha Ukarimu aliendelea kutoa maagizo kwa vijana wake, huku akionesha imani kubwa dhidi yao.Alikuwa sahihi kwa asilimia mia moja, jeshi lake halijawahi kushindwa hata siku moja katika mapambano ya aina yoyote. Haijalishi walipambana na kijiji kingine kupanua utawala wao, au kupambana na wanyama wakali. Waliibuka kidedea katika mapambano yao na kukipatia sifa kubwa kijiji chao …



    …………………………………



    Mwantema;



    Mzimu Nkuru alichanganyikiwa mara baada ya kugundua kuwa Nyoni na Matumaini walifanikiwa kumuokota mzimu Ntema. Alizidi kuwa katika wakati mgumu alipojaribu kuwazuia Nyoni na Matumaini wasiendelee na safari ya kuelekea kijiji cha Ukarimu kumalizia zoezi la mwisho, zoezi la kukata mti wake mwingine wa ubuyu. Mti ambao unapatikana katika kijiji cha Ukarimu, mti ambao ungesababisha utawala wa mzimu Nkuru pamoja na mtemi Nyantumu kufikia kikomo, kama ukikatwa chini ya uwepo wa Nyoni na Matumaini au mzimu Ntema. Kwani vijana hawa walikuwa tayali wamechaguliwa toka wakiwa tumboni, kwa ajili ya kuwaokoa Wanamutema kutoka katika utawala uliohimiza ukeketaji kwa watoto wa kike, na kupelekea vifo vingi katika kijiji chao.



    Hatimaye alianza kutabasamu, kwani aligundua jambo muhimu la kuwadhuru Nyoni pamoja na Matumaini. Aliamini wanyama hatari wa pori la Nyankonko walishindwa kumuua Nyoni pamoja na Matumaini kutokana na maumbo yao kuonekana kwa urahisi. Kwani walikuwa wakubwa kupita kiasi. Hivyo basi, wadudu wadogo zaidi wasio onekana kwa urahisi walitakiwa watumwe kwa ajili ya kumuua Nyoni na Matumaini …



    “Enyi! Enyi!  enyi nyoka na nge, utawala wangu uko mikononi mwenu. Nendeni msituni mkawaue Binadamu wote ambao wana hatarisha utawala wangu ……”, mzimu Nkuru alifahamu mipango ya jeshi la mtemi wa kijiji cha Ukarimu, hivyo basi kazi ya nge na nyoka wadogo anao watuma sio kupambana na Nyoni pamoja na dada yake peke yao. Bali hata jeshi la mtemi wa kijiji cha Ukarimu lilitajwa katika hatari ya kushambuliwa na wanyama wengine wadogo sana, wanyama ambao walipewa nguvu za kutosha za kishirikina na mzimu Nkuru  kutokana na maumbo yao madogo, ilikuwa rahisi sana kumshambulia binadamu yoyote yule na kumuua kirahisi .Ukizingatia uwepo wa vichaka na miti mingi katika pori la Nyankonko…



    Mwantema;



    Kundi kubwa la wanyama wadogo, wanyama ambao waliundwa na ng’e pamoja na nyoka wenye sumu kali aina ya Koboko. Walianza safari kutoka kijiji cha Mwantema kuelekea katika pori la Nyankonko mara baada ya kupokea maagizo kutoka kwa mzimu Nkuru aliyewatengeneza.



    Mzimu Nkuru aliamini wanyama hao watafanikiwa kumnasa au kumdhuru Nyoni pamoja na Matumaini. Japo ilikuwa vigumu kulikamilisha jambo hilo, chini ya ulinzi wa mzimu Ntema.



    “Ninaimani watafanikiwa, mzimu Ntema hana nguvu zozote kwa sasa kushinda nguvu zangu. “,



    Mzimu Nkuru alijitamba kwa sauti kubwa huku mti wake ukitikisika kwa fujo, na kupukutisha majani mengi sana. Aliyaongea hayo yote wakati akiwashuhudia wanyama wadogo alio watengeneza, wakitoweka mbele ya macho yake kuelekea katika pori la Nyankonko kumtafuta kijana hodari Nyoni …



    …………………………………



    Ukarimu;



    Jua lilichomoza, hali ya mawingu ilikua shwari na kuipendezesha anga la kijiji cha Ukijani. Ndege waliamka asubuhi na mapema kwa safari ndefu ya kwenda kutafuta maji mbali na kijiji, jambo lililopelekea anga lote la kijiji cha Ukijani kujaa makundi ya ndege ambao waliruka kwa fujo na kuimba nyimbo nzuri zilizomsikitisha yoyote yule aliyezisikiliza sauti zao. Kwani hakusita kukaa chini kuwashangaa, na kumshukuru muumba kwa uumbaji wake mzuri na wa ajabu …



    Hayo ndio yaliyo watokea askari takribani mia moja wa jeshi la kijiji cha Ukarimu. Kwani wakiwa safarini kuelekea katika pori la Nyankonko, makundi mengi ya ndege yalipita juu yao na kuwafanya wasitishe msafara wao ghafla ili kushuhudia ndege hawa wazuri waliovutia kwa kila kitu, rangi zao za kupendeza ambazo ziliendana kabisa na sauti zao. Hali hii ilipelekea nguvu kuongezeka ndani ya mioyo yao, kwani hawakuwa tayali kupoteza viumbe hawa waliopatikana katika kijiji chao kwa sababu ya njaa na ukame. Hivyo basi, msafara wao ulianza upya baada ya ndege kuwapita na kufika mbali sana, huku jeshi la kijiji cha Ukarimu wakiwa na nguvu mpya kumkabili kiumbe yoyote yule atakaye wazuia wasifanikishe kumuokoa mzimu Ntema kutoka katika mazingira mabaya ya pori la Nyankonko. Sehemu ambayo bila shaka yoyote ile kulifanya nguvu za Ntema kupungua kwani kafara haikutolewa kumuongezea nguvu kama ilivyokuwa zamani kipindi alipokuwa akiabudiwa na watu wa Mwantema …



    “Jua limeshachomoza, hatuna budi kusonga mbele na kuingia pori la Nyankonko machweo ikiwa bado haijafika …”,http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Sawa mkuu, “



    Kiongozi wa jeshi la kijiji cha Ukarimu alisikika akilihamasisha jeshi lake kuchapa mwendo, bila tatizo lolote vijana wake walitii amli yake na kuendelea na safari yao ya kulitafuta pori la Nyankonko …



    …………………………………



    Mwantema;



    Baba yake Nyoni alikosa raha, nafsi yake haikumpa matumaini ya mwanae kurudi akiwa mzima. Kisha afanikishe zoezi la kuwakomboa, kwani siku nyingi na wiki kedekede zilikuwa zimekatika akiwa hajapata taarifa yoyote kuhusiana na usalama wa watoto wake …



    Sio yeye tu, bali hata wananchi pamoja na wanakijiji wote wa Mwantema. Hawakuwa na uhakika kuhusu usalama wa mtemi wao Nyantumu pamoja na jeshi lake. Kwani siku zote wanyama wakali wa pori la Nyankonko, hawakuwa na msamaha kwa binadamu yoyote yule aliyeikanyaga ardhi yao …



    “Mimi siku tatu zinazokuja, zikipita!  Natoroka humu ndani na kwenda kuwafuata wanangu ……”,



    “Baba Nyoni tuwe wavumilivu, nina amini watoto wako salama na muda wowote watarudi kutukomboa “,



    “Hapana wifi!  mume wangu yuko sahihi, kukaa humu ndani ni sawasawa na kuwa mfu. Bora kutoroka tu na kufa kihalali ukipigania maisha ya watoto wetu! “,



    “Kweli mke wangu, uko sahihi. Lazima nitoroke mahali hapa …”,



    “,Basi sawa kama wazazi wa watoto mmekubaliana, sisi mashangazi na wajomba hatuna neno “,



    Mazungumzo yaliendelea katika gereza dogo ambalo lilijaa kero za kila aina, kwani wanawake na wanaume wote walifungwa ndani yake. Haijalishi walikuwa ni ndugu kiasi gani, lakini walifungwa sehemu moja bila kutoka nje. Jambo ambalo lilipelekea heshima kushuka baina yao, hasa katika suala la kujistili maliwatoni. Sio hilo tu, bali gereza hili lilijaa kinyesi kibichi cha ng’ombe kwa lengo moja tu la kuwakomoa wafungwa kwa makosa yao waliyo yafanya …



    Yakiwa majira ya asubuhi, siku nyingine tena ikiwa imeanza. Baba yake Nyoni anakosa furaha moyoni mwake, nafsini mwake alijiona kupungukiwa na watu muhimu katika maisha yake ambao ni watoto wake vipenzi Nyoni pamoja na Matumaini. Hivyo basi, aliahidi kutoroka na kuwafuata wanae mahali walipo na ikiwezekana kukamilisha ukombozi wa Wanamutema wote dhidi ya mila hatari iliyowakandamiza wanawake …



    …………………………………



    Matumaini akiwa amelikamatilia jiwe zuri lenye kung’aa, jiwe la mzimu Ntema. Alimuamsha kaka yake aliyekuwa akiponda usingizi bila kujali hatari yoyote.



    “Kaka! kaka! amka kaka! “,



    Matumaini aliendelea kumuita kaka yake bila mafanikio, tumbo lake lipanda juu na kushuka kuashiria hali isiyo ya kawaida ya upumuaji wake. Huku sauti nzito ikisikika mpaka mita kadhaa, sauti ambayo ilipelekea mwangwi kujibu sauti ya Nyoni …



    “Kaka!  acha kukoroma!  amka kwende,kumekucha! “,



    “Kumekucha?? “,



    “,Ndio, tunapoendelea kukaa mahali hapa. Jeshi la mtemi Nyantumu litatutia nguvuni …”,



    Nyoni alifumbua macho yake baada ya sauti ya dada yake kupenya katika masikio yake,kwani aliitwa mara kadhaa bila kuamka. Japo alifumbua macho yake, na kushuhudia mwanga wa jua uliopenya katikati ya miti mingi ya Nyankonko. Lakini hakuamini kama palikuwa pamekucha, alijiona kama alikuwa amelala kwa muda mfupi tu bila kutambua kuwa uchovu aliokuwa nao ndio uliopelekea jambo hilo …



    Maneno ya dada yake yalipenya hadi katikati ya ubongo wake, hatimaye mawasiliano ya hali ya hatari yalitumwa katika miguu yake. Kitendo kiichopelekea anyanyuke na kumshika dada yake mkono. Hawakuwa na muda wa kupoteza, zaidi ya kukimbia. Kwani kijana Nyoni aliyakumbuka maneno aliyoambiwa na mzimu Ntema, maneno ambayo yalihusu uwepo wa mtemi Nyantumu pamoja na jeshi lake katika pori la Nyankonko.



    Kwa kutumia akili yake ya kuzaliwa, bila hofu yoyote ile alitambua kuwa jeshi la mtemi Nyantumu lilikua karibu kuwakalibia mahali walipo. Kilichobakia ni kutimua mbio, bila kujali ulinzi alioahidiwa kupewa na mzimu Ntema.



    Kwani siku zote anayejisaidia ndio husaidiwa, jambo ambalo Nyoni alilitambua na kulizingatia kwa kiasi kikubwa …



    “Bado wako mbali, usiogope na wala usikimbie ukajikuta unaumizwa na miiba na pengine unaweza kukanyaga wanyama wakali …”,



    Mzimu Ntema alimsihi Nyoni asitishe kukimbia, kwani alizitambua fikra zake. Fikra ambazo ziliogopa kukamatwa na mtemi Nyantumu ,zaidi ya kukutana na simba wa mwituni tena wa pori la Nyankonko.



    “Hata mimi simuelewi, kakurupuka usingizini na kuanza kunikimbiza mbio ndefu …”,



    “Ni uoga tu, nilifikili hawa wapuuzi wametukalibia. Kwani tangu jana mpaka sasa, kama wangeamua kutokulala. Bila shaka sasa hivi tungezungumza lugha nyingine, kama si lugha ya Ukijani, kimuyeshi basi ni Kimutapa “,

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nyoni aliwajibu Matumaini pamoja na mzimu Ntema, huku akitaja lugha za mataifa makubwa ya kifalme. Falme ambazo zilijikuta zikipigana vita kutokana na ulafi wa madaraka, mali na visa vya mapenzi. Hadithi za kale ambazo kijana Nyoni alisimuliwa na baba yake, huku baba yake akidai kusimuliwa na babu yake …



    “Kaka! “



    “Nini na wewe unaita ita tu,! “,



    “Simba! “,



    “,Simba yuko wapi? au unaota mchana …”,



    “,Nyuma yako …”,



    “,Mamaaaa weeee!! “,



    Nyoni alipiga kelele kupita kiasi, sio kwamba alikuwa muoga lahasha. Simba alikuwa amemkalibia na kutaka kumlarua. Isitoshe, alifikili maneno aliyoambiwa na dada yake ambaye alikuwa ameshamuachia mkono wake na yeye kubaki nyuma alizani ni matani. Kumbe haikuwa masihara hata kidogo, Nyoni alipositisha zoezi la kukimbia. Alimuachia mkono dada yake huku yeye akibaki nyuma. Kumbe kitendo cha Matumaini kutembea kwa hatua kadhaa kisha kugeuka nyuma kumtazama kaka yake. Ndipo alipomshuhudia simba mkubwa aliyeonekana kuwa na njaa kali akimnyemelea kaka yake …



    “Linyoshee jiwe, lipige na mionzi ya jiwe la mzimu Ntema …”,



    Nyoni alianza kukimbia kuelekea mbele, uelekeo ambao dada yake alikuwepo. Jambo la kushangaza simba alimkimbiza, jambo ambalo lilikuwa la hatari kwa wote,Matumaini pamoja na Nyoni mwenyewe.



    Kwa imani kubwa dhidi ya mzimu Ntema, Matumaini alifuata ushauri wa kaka yake na kulinyoshea jiwe la mzimu Ntema simba lile dume. Simba ambalo lilikuwa na maumbile makubwa, kiasi kwamba yalilifanya kuonekana dume haswaa!



    “Asante mzimu Ntema! udumu milele! “,



    “,Na udumu milele “,



    Sifa kedekede zilisikika kutoka kwa Nyoni na Matumaini, kwani simba yule aliyeyuka ghafla kiasi kwamba hata nyoya lake moja halikuweza kuonekana tena. Mara baada ya kunyoshewa jiwe la mzimu Ntema, jiwe ambalo lilimteketeza simba yule kutokana na mionzi yake mikali …



    Nyankonko;



    Wanyama waliotumwa na mzimu Nkuru wanawasili katika pori la Nyankonko, kilichobakia ni kuingia katikati ya msitu kumtafuta kijana Nyoni pamoja na dada yake ili waweze kuuawa. Sio hao tu, bali walikuwa na jukumu la kuhakikisha kiumbe yoyote anayepinga utawala wa mtemi Nyantumu pamoja na mzimu Nkuru anashughulikiwa ipasavyo.



    Kwahiyo jeshi la mtemi Nyantumu lilikuwa salama kabisa kushambuliwa na wanyawa hawa wadogo ambao haikuwa rahisi kuwatazama kwa macho, kutokana na uwepo wa vichaka vikali ndani ya msitu wa nyankonko …



    Lakini kwa upande wa mzimu Ntema, hakuwa na nguvu za kutosha kupambana na mzimu Nkuru pamoja na viumbe vyake. Kwani nguvu zake zilikuwa zimepungua kwa kiasi kikubwa, kutokana na kutupwa ndani ya pori la Nyankonko kwa miaka mingi bila kafara yoyote kutolewa dhidi yake na kuzifanya nguvu zake kuwa imara …



    “Siwezi kupambana na maadui walioingia msituni, lakini kuna njia mojawapo ya kuwashinda na nyinyi kuwa salama …”,



    Jiwe la mzimu Nkuru lilitamka, na kusababisha Matumaini kushtuka ghafla. Kwani muda mrefu ulikuwa umepita, huku ukimya wao ukitawala zaidi ya kuchapa miguu yao kusonga mbele …



    “Maadui gani hao?  jeshi la mtemi? “,



    “,Hapana! kuna ng’e na nyoka wengi wametumwa kuwang’ata na kuwaua “,mzimu Nkuru alimjibu kijana Nyoni, swali la kizushi ambalo aliliuliza muda mfupi uliopita Na kujikuta lundo la maswali yakikisumbua kichwa chake, kwani majibu aliyompatia Nyoni hayakujitosheleza.



    “Unasemaje?kuna maadui wengine zaidi ya jeshi la mtemi Nyantumu, pamoja na wanyama wa msitu huu?  nani kawatuma kutushambulia? ” ,



    Nyoni alimshushia maswali mengi mzimu Nkuru, ili kuuweka huru moyo wake kwani maswali mengi yalimjaa mithili ya kidumu cha maji kijaacho  maji pomoni na maji mengi kumwagika kutafuta sehemu ya kujihifadhi kukwepa mubanano huo. Bila hiana yoyote, mzimu Ntema alitimiza wajibu wake na kujibu maswali yote ya Nyoni bila kubakiza hata chembe ya ukweli …



    “Mzimu Nkuru ndio kawatuma, ili awaangamize. Anaamini kwa asilimia nyingi siwezi kuwalinda kutokana na uhafifu wa nguvu zangu ……”,



    “Kwahiyo unatusaidiaje? “, Matumaini aliamua kuingilia mazungumzo, kwani hatari aliyosikia ikizungumzwa ilikuwa ni hatari kubwa kuliko zote ambazo walikutana nazo, wakiwa ndani ya msitu …



    “Mnatakiwa mnywe maji yaliyoosha au kusafisha jiwe langu. Wanyama hao hawataweza kuwadhuru kwa chochote…”,



    “Aaaaah, kumbe hivyo!  kazi rahisi sana, “, Nyoni aliongea kwa kutabasamu, alifurahishwa na mashariti machache aliyopewa kuhusiana na siri ya mafanikio yao na kuwashinda wanyama wa ajabu waliotumwa kuja kuwadhuru



    Haraka haraka alimpokonya dada yake kibuyu cha maji ya kunywa, na kisha kulidumbukiza jiwe la mzimu Ntema ndani ya kibuyu kile cha maji.Mkono wa kulia aliutumia kufunika mdomo wa kibuyu, huku mkono wa kushoto akiutumia kukamatilia vizuri kibuyu chake kisiweze kumtoroka katika mikono yake.



    Kisha kijana hodari Nyoni alianza kutikisa kibuyu, ili kuchanganya vizuri maji yaliyoko ndani ya kibuyu pamoja na jiwe la mzimu Ntema. Kwa sekunde chache tu, kila kitu kilikuwa kimekamilika. Aliamini dawa ilikuwa tayali kunywewa, na kuimalisha ulinzi wao …



    “dada kunywa! maji yatakayo baki nibakizie “,

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Msinywe maji yote, maji yatakayobaki inatakiwa tuwapatie askari wa kijiji cha Ukarimu, wako njiani wanakuja kunitafuta ndani ya pori hili. Na wenyewe wako hatarini kuliwa na wanyama hawa, hivyo tufanye haraka kusonga mbele tuyaokoe maisha yao …”,



    Mzimu Nkuru aliendelea kutoa maelekezo, maelekezo ambayo yaliweza kufumbua upya fikra za Nyoni kwani alifanya mambo kwa kujivuta sana tofauti na awali, kabla ya kumuokota mzimu Ntema..



    “Sawa mzimu Ntema, utawala wako udumu milele “,



    Nyoni alijibu maneno aliyoambiwa na mzimu Nkuru, kisha alipokea kibuyu cha maji kutoka kwa dada yake kukata kiu na kuyaokoa maisha yake kwenye hatari ya kuliwa na wanyama wenye sumu kali waliotumwa na mzimu Nkuru ……



    …………………………………





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog