Search This Blog

ROHO YAKE INADAI - 1

 

    IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



    *********************************************************************************





    Simulizi : Roho Yake Inadai

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Massachusetts, Boston, 1975.





    Mwanaume mmoja mrefu aliyevalia suti na koti refu jeusi alisogelea mstimu wa umeme na kusimama hapo. Mwanaume huyo alikuwa ni mzee wa makamo ya hamsini na, na mkononi mwake alikuwa amebebelea makaratasi kadhaa rangi nyeupe ielekeayo kuwa kahawia.





    Alikuwa ameupinda mdomo, na macho yake yalionyesha kuchoka. Hata mwendo wake uliunga mkono hilo. Alichomoa karatasi mojawapo kati ya zile alizozibeba, akaibandika hapo mstimuni na kabla hajatazama kama karatasi hiyo imekaa vema, akaendelea na safari yake.





    Bila shaka alikuwa na kazi kubwa mbele yake. Kazi ya kumaliza yale makaratasi aliyobebelea mkononi kwa kuyabandika kila mahali paonekanapo.





    Mzee huyu aitwa Brewster. Mji wote huu wa Boston wamtambua kama mfanyakazi wa daraja la chini kwenye ofisi ya serikali ya mtaa. Wakimtambua kama mmojawapo wa wakongwe kwenye kazi hiyo, haswa ya ubandikaji wa makaratasi na usambazaji mwingine wa taarifa.





    Sasa mzee huyu aelekea kuchoka, lakini bado haikuonekana ni nani anaweza kufanya kazi kama yeye. Kazi ambayo imejawa na kujitolea zaidi kuliko kipato.



    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi karatasi ile aliyoibandika ikiwa haijakaa vema, na pengine gundi ikiwa haijakolea, ikabanduka toka mstimuni na kudondoka chini. Upepo ukaipuliza na karatasi hiyo ikapepea na kupepea mpaka kwenye eneo la nyumba fulani ndogo iliyosanifiwa vema na mbao. Hapo mtoto mmoja akaiokota na kuitazama. Mtoto wa kiume mwenye makadirio ya miaka ya kumi na miwili ama mitatu.





    ATAFUTWA! Kichwa cha habari kilisomwa vivyo. NI MIEZI MIWILI SASA TANGU ASIONEKANE NYUMBANI KWAO. TOA TAARIFA OFISI YA SERIKALI YA MTAA PUNDE UTAKAPOKUWA NAYO.





    Tangazo hilo lilikuwa limeambatana na picha isiyo na rangi ya binti mdogo mwenye makadirio ya miaka kumi. Kwenye picha hiyo binti huyo alikuwa amebanwa nywele zake mafundo mawili na meno yake makubwa ya mbele hayakuwa yanaonekana akiwa ametabasamu. Alikuwa ana mapengo ila akionekana mwenye furaha.





    Binti huyo alikuwa anaitwa Kacie.





    “Brian!” sauti ya kike iliita. Basi mtoto yule aliyekuwa ameshikilia lile karatasi litangazalo kupotelewa kwa mtoto, akageuka kutazama mlangoni. Huko akamwona mamaye. Mwanamke mwembamba mwenye nywele nyeusi ti. Alikuwa amevalia gauni joshi la maua limfikialo magotini. Alikuwa amewekea mikono yake kiunoni.





    “Kwanini husikii, Brian?” mama akauliza.





    Brian akatazama tena lile karatasi alilolishikilia mkononi, kisha akakimbia kumfuata mamaye.





    “Mpaka sasa hivi hujala, unazurura tu. Sipendi hiyo tabia, Brian!” mama alifoka lakini Brian hakuonekana kujali sana. Aliendea sehemu ya kula akaketi, na punde mama yake aliyepitia jikoni akaja akiwa amebebelea chakula sahanini. Akamwamuru Brian afungue kinywa.





    “Chakula kiishe, Brian. Sawa?” mama akasema akitoa macho kutishia. Aliposema hayo akataka kwenda, ila akasita. Akatazama vema karatasi iliyokuwepo mezani, ile ambayo Brian alikuwa ameiokota huko nje. Hapo akaona picha na maelezo.





    Akainyakua na kuyasoma vema. Punde akasema, “Kacie.” kwa sauti ya chini na macho yake yakiwa yamebebelea fikira.





    “Nimemkumbuka sana,” akadakia Brian akitazama sahani yake ya chakula. Uso wake alikuwa ameufuma kwa huzuni.





    “Najua umemkumbuka sana, Brian,” mama akasema akifanya namna ya kuketi kando na Brian. “Usijali atapatikana. Sawa?”





    “Lini?” Brian akamuuliza mama yake. Bado alikuwa anatazama chakula chake.





    “Sijui lini, Brian, ila atapatikana tu,” mama akaeleza akimpatipati Brian begani.





    “Atakuwa ameenda wapi?” Brian akauliza. “Mbona hakuniaga? Nilimfanya chochote kibaya?”





    Mama akashusha pumzi. “Brian, hukumfanya chochote kibaya. Kacie atakuwa ametekwa na watu wabaya. Watu wadhalimu. Ndiyo maana huwa sipendi uwe unazurura zurura huko nje. Sio salama.”





    Brian akanyamaza kidogo. Bado alikuwa anatazama chakula chake lakini macho yake yakionyesha yu mbali kimawazo. Alipigapiga kijiko kwenye sahani, akiwa ametulia kabisa, akasema kwa sauti ya chini, “Labda Faris anajua Kacie alipo.”





    “Kwanini unasema hivyo?” mama akadadisi. Hapa alionekana kuwa makini sana. Alimtazama mwanaye kwa macho yaliyogubikwa na ndita.





    “Alikuwa wa mwisho kucheza na Kacie kule karibu na msituni,” akasema Brian kwa sautii yake ya chini kisha akamtazama mamaye. Mama akatikisa kichwa.





    “Brian, kula. Sawa?” Kisha akanyanyuka na kwenda zake.





    Kila mtu ndani ya mji anajua habari hizi za Faris kuwa mtoto wa mwisho kumwona Kacie kabla hajapotea lakini haikusaidia kitu kwenye upatikanaji wake. Tangu Faris amwone Kacie kwa mara ya mwisho amekuwa bubu. Amekuwa mlemavu wa akili. Amekuwa mtoto anayeongea maneno yasiyoeleweka.





    Amekuwa wa kufungiwa ndani. Hakuna anayeelewa anachoongea. Hakuna anayetaka kuwa naye karibu.





    Pengine Faris angeweza kutoa taarifa muhimu sana juu ya Kecie. Ila hilo halikuwezekana. Na basi kwa namna hiyo, taarifa hafifu za Kecie zilipatikana toka kwa polisi ambao waliona nyayo za Kecie zikizamia msituni.





    Na zaidi mdoli wake alioudondoshea chini kabla nyayo zake hazijapotea kabisa kwenye udongo. Mdoli huo tangu ulipopatikana, wazazi wake wameuhifadhi kama kumbukumbu ya mtoto wao huyo wa pekee.





    Umekuwa wakati mgumu sana kwao kuishi pasipo mtoto wao. Wamekuwa wapweke. Nyumba imepoa. Na hata juhudi zao za kupata mtoto mwingine ziligonga mwamba.







    ***





    Baada ya miaka kumi …







    Mambo kadhaa yalikuwa yamebadilika ndani ya mji wa Boston. Maendeleo huja pamoja na muda. Nyumba kadhaa zilikuwa zimejengwa, hata pia watu kadhaa wapya walikuwa wameongezeka ndani ya mji wa Boston. Idadi iliongezeka.





    Lakini mbali na mabadiliko hayo, bado Kecie hakuwa amepatikana. Hakuna mtu aliyekuwa anajua wapi Kecie alipo. Na kwasababu hii ya muda, kuna baadhi ya watu hata wameshamsahau Kecie isipokuwa wale watu wake wa karibu kama vile wazazi wake na wale marafiki.





    Ngo! Ngo! Ngo!





    Mwanaume mmoja mrefu mwenye nywele nyeusi alibisha hodi na kungojea majibu. Punde mlango ukafunguliwa na mwanamke mtu mzima, makadirio ya miaka kasoro na hamsini. Mwanamke huyo akatabasamu na kusema, “Brian … karibu!”





    Kijana yule akazama ndani. Na kumbe alikuwa ni Brian. Alikuwa amekua haswa, ila uso wake ule wa kitoto haukuwa umepotea. Brian ni mkimya. Macho yake ya pole na lipsi zake nyembamba.





    Alikaa kitini kama mtu anayehisi baridi, akatazama huku na kule.





    “Unaendeleaje Brian?” akauliza mwenyeji.





    “Naendelea vizuri, sijui wewe Mrs Garett.”





    “Sijambo. Mama yako aendeleaje?”





    “Hajambo. Amenituma nikufikiishie salamu zake.”





    “Ahsante sana, amekuwa mkarimu sana kwangu. Nawe pia … umepita muda mrefu lakini huachi kuja kun’tembelea.”





    “Usijali Mrs Garett. Kecie alikuwa ni rafiki yangu, na itabakia kuwa hivyo siku zote. Haijalishi nimebanwa kiasi gani, siku hii ni maalum sana. Kila inapowasili naienzi maana ndiyo siku ambayo nilimpoteza rafiki yangu Kecie.”





    Mrs Garett akanyamaza kidogo. Macho yake yalikuwa yanaelekea kuwa mekundu. Alisimama akamwambia Brian, “Ningoje, nakuja. Acha nikuandalie chakula.”





    Akaenda zake na Brian akawepo pale sebuleni peke yake. Akatazama huku na huko ndani ya sebule. Ni muda hakuwa amekuja hapa. Baada ya kama dakika moja, akasikia mlango unafunguliwa, kutazama akamwona binti mdogo makadirio ya miaka nane, tisa ama kumi. Binti huyo alikuwa amevalia gauni limfikalo juu kidogo ya magoti.





    Nywele zake zilikuwa nyeusi ndefu, ameziachia huru. Macho yake madogo yalikuwa na kiini cheusi. Mdomo wake ulikuwa mdogo kama ka-tone. Mashavu yake yalikuwa mapana na masikio yake mazuri yalikuwa yamesimama kuchomoza toka kwenye nywele zake.





    “Hey!” Brian akamsalimu lakini binti huyu hakujibu. Alimtazama Brian na kisha akaketi kitini pasipo kuongea jambo.





    “Hey, mimi ni Brian, wewe ni nani binti mzuri?” Brian alisema kwa tabasamu. Binti yule hakujibu, akaendelea kumtazama. Brian akanyamaza na muda si mrefu Mrs Garett akaja sebuleni.





    “Olivia, unafanya nini hapa?” kumbe yule binti aitwa Olivia. Alisimama upesi baada ya kuambiwa hivyo, na akashika njia kwenda zake. Akaelekea chumbani na kuufunga mlango.





    Mrs Garett akatabasamu akimtazama Brian, “Anaitwa Olivia. Nilimtoa kituo cha kulelea yatima aniondoe na upweke wa hapa nyumbani.”





    Kisha akaketi.





    “Unajua tangu nimpoteze Kecie nilikuwa mpweke sana, niliona kuna haja ya …”





    “Naelewa, Mrs Garett,” Brian akamkatisha mwanamke huyo. “Anaonekana ni mkimya sana.”





    Mrs Garett akatabasamu. “Ni mwenye aibu sana. Si mtu wa kuchangamana na wenzake. Nadhani kuna kitu kishawahi kumdhuru huko nyuma.” Mrs Garett akapandisha mabega juu. “Pengine atakuwa sawa akikaa hapa.”





    Wakateta kiasi, na baada ya kama robo saa, Mrs Garett akaleta chakula. Wakala ukimya ukiwa umetawala kwa kiasi kikubwa.





    “Vipi kuhusu Olivia?” Brian akauvunja ukimya. Aliuliza akiwa anatazama chakula.





    Mrs Garett akaguna. Akatafuna na kusema, “Atakuja kula ukiondoka. Nadhani nimekuambia ni mwenye aibu sana.”





    Brian hakuongea tena mpaka anamaliza chakula chake. Akamuaga Mrs Garett na kumwambia atakuwa anakuja hapo kadiri atakavyokuwa anaupata muda. Wakakumbatiana na Mrs Garett akamsindikiza Brian mpaka mlangoni.





    Brian akashika barabara kwenda zake. Alipotembea kwa hatua kumi, hakujua nini kilimshtua, akageuka na kutazama nyumba ya Mrs Garett. Kwenye mojawapo ya chumba, dirishani, akamwona yule binti Olivia akiwa anamtazama. Mkononi mwake alikuwa amebebelea mdoli.





    Mdoli wa Kecie.







    Brian akasimama na kutazama vema. Pengine alidhan hakuona vema, ila kweli alikuwa sahihi. Mdoli ule ulikuwa ni Kecie. Lakini Brian hakuwa anajiuliza sana kuhusu mdoli ule, bali Olivia. Alihisi pengine mtoto huyo hayuko sawa.





    Olivia baada ya kuona Brian anamtazama sana, akapotea pale dirishani. Alishusha pazia Brian akaenda zake.





    “Hey Brian!” gari ilisimama kandokando mwa Brian baada ya kijana huyo kutembea hatua kadhaa. Lilikuwa ni gari lisilo na paa, na ndani yake walikuwapo wasichana wawili. Mmoja alikuwa na nywele nyeusi na mwingine akiwa na nywele rangi nyeupe.





    Wasichana hawa walikuwa wamevalia matabasamu kwenye nyusoni. Macho yao yalionyesha uchangamfu lakini pia ujana wao.





    Tukirudi kwenye gari walilokuwa wanalitumia, ilikuwa wazi lilikuwa ni gari ghali sana. Ukitazama miaka hiyo na gari hilo waweza kuona ni mambo ambayo yanakinzana kwa namna fulani. Hili lilionyesha wasichana hawa ni watu wa aina gani.





    “Twaweza kukusogeza, Brian?” aliuliza msichana mwenye nywele nyeusi ambaye ndiye alikuwa dereva. Jina lake ni Wayde. Ni mtoto wa kwanza na wa pekee wa seneta wa Massachusetts, bwana Stuart McKenzie.





    Mwenzake aliyekuwa naye beneti aitwa Silvia. Ni rafiki mkubwa wa Wayde. Naye pia ni mzaliwa wa familia ya watu wenye hadhi, baba yake akiwa mfanyabiashara mkubwa wa silaha.





    Watatu hawa, Brian na Wayde na Silvia, husoma shule moja ya upili.





    Baada ya Wayde kumuuliza Brian, alimtazama Silvia na kucheka kisichana kisha wakarudisha tena nyuso zao kumtazama Brian ambaye alikuwa anaigiza kutabasamu.





    “Usijali, nitatembea tu. Si mbali ninapoelekea,” Brian akajibu akipandisha mabega yake.





    “Unaenda nyumbani kwenu?” Wayde akauliza.





    “Ndio, naenda nyumbani,” Brian akajibu. “Nimetoka kutembelea familia ya Garett na sina cha kufanya kwa sasa. Nadhani mama yanhu atahitaji kuniona.”





    “Mama yako atahitaji kuwa na mumewe kwa sasa!” Silvia akatania kisha wakacheka pamoja na Wayde. “Inabidi uwape nafasi na wao waonyesane mahaba. Vipi tukienda mahali kustarehesha akili? Najua utakuwa unamfikiria rafiki yako Kecie!” akasema Wayde akimtazama Brian kwa macho ya ushawishi. Brian hakuwa mtu wa kustarehe, bali wa kujifungia ndani kusoma ama kutazama mambo kadhaa.





    Hakuona kama ile ‘ofa’ ingempendeza, basi kwakuwa wasichana wale wasingemwaca kwa amani akaona awakubalie lakini kwa masharti.





    “Twende kwanza maktaba kuu, kuna vitu nataka kuvipitia huko.”





    “Umeanza sasa, Brian!” akalalama Wayde. “Huchoki kutazamana na vitabu wewe?”





    “Nimesikia kile kitabu cha Dokta Hamill kimekamilika,” akasema Brian. “Ningependa kukitazama, pengine naweza ku…”





    “Twende!” Wayde akamkatisha. Brian akazama ndani ya gari na kutimka mpaka maktaba kuu ya Massachusetts. Hakuwa na vigezo vya kuingia humo ndani, hakutembea na kitambulisho, ila kwakuwa alikuwa na Wayde alifahamu msimamizi hatompa pingamizi.





    Na kweli.





    “Unaweza kuingia ndani!” msimamizi akasema akimtazama kijana huyo kana kwamba mzazi anavyomtazama mwana mkaidi. Basi Brian akazama ndani na kunyookea moja kwa moja kwenye shelfu aijuayo, akapembua na kupembua, akatoa kitabu kimoja kilichosomeka, ‘NYUMA YA MITI - simulizi ya Massachusetts.’ kilichoandikwa na Dkt. Hamill Smith.





    Kilikuwa ni kitabu kipya kabisa, na bwana huyo aliyekiandika akiwa ni Mkuu wa shule wasomayo Brian na wenzake wale wawili, Wayde na Silvia.





    **





    “Muda wote huo?” akalalama Silvia akikunja sura. Walikuwa wamekaa kwenye gari kwa kama lisaa sasa wakimngojea Brian atoke maktaba. Hata makalio yalikuwa yanawauma sasa.





    Wayde akapiga honi mara nne akitazama mlangoni mwa maktaba. Sura yake ilikuwa imefura. Asingoje muda, Brian akatoka maktaba akiwa anakimbia. Akatumbukia ndani ya gari na wakaenda zao.





    “Huwezi amini nilichokiona, Wayde,” Brian akavunja ukimya. “Kile kitabu ni muhimu sana na kimenifanya nijue kuwa Dkt Hamill anajua mambo mengi sana kuhusu huu mji. Natazamia kuonana naye.”





    Hakuna aliyezungumza naye. Wote walikuwa wamekunja nyuso zao wasionekane hata kama wana dalili ya kuteta.





    “Samahani,” akasema Brian. “Nimewakwaza, ila sikudhamiria kuwa hivyo.”





    “Nimekusamehe, Brian,” akasema Wayde. “Ila siku nyingine sitakupitisha tena hapo. Ona hata tumeshachelewa!”





    Walikuwa wanaelekea kwenye tafrija ya mwenzao aliyekuwa anasheherekea kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Watu walikuwa wamefurika kwenye hiyo tafrija haswa vijana wa makamo ya miaka ishirini na. Walikuwa wanakunywa, na kucheza muziki uliokuwa unapigwa kwanguvu haswa.





    Brian hakuweza kustahimili mambo haya. Baada ya kuwapumbaza wakina Wayde, alitoka kwenda nje na kuketi huko. Alidhamiria kukaa huko mpaka tafrija hiyo itakapokwisha au yatakapopita masaa kadhaa ili akiomba ruhusa ya kuondoka isiwe tabu.





    Basi akiwa amekaa huko nje peke yake, na kwa mbali muziki ukiwa unaendelea kuchezwa, akili yake ikamezwa na mawazo. Na mawazo haya ni kuhusu kitabu kile cha Dkt Hamill. Alifikiria sana juu ya maudhui yake, na kwa namna kubwa akahisi kitabu kile kina kitu cha kumweleza juu ya kupotea kwa Kecie.





    Aliamini hivyo kabisa. Na akiwa mawazoni humo akapata haja ya kumwona Faris. Hapa akapata wazo. Kwakuwa wakina Wayde bado yupo ndani kwenye tafrija basi anaweza kutumia gari lake kwenda kumwona Faris mara moja nje kidogo ya mji wa Boston, huko walipohamia na familia yake.





    Hakungoja, akazama ndani kwenda kumwona Wayde na kumweleza haja yake. Kwakuwa Wayde hakuwa na ratiba ya kuondoka karibuni na pia vilevile alitaka kumfurahisha Brian, basi akampatia funguo kijana huyo aende huko atakapo.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Kuwa salama, Brian,” alimuaga hivyo na kumpatia busu shavuni. Basi Brian akashika barabara na kuendesha kwa mwendo wa wastani. Yalikuwa ni majira ya saa mbili usiku sasa.





    Baada ya kama dakika arobaini na tano akawa amefika mbele ya nyumba ya wakina Faris. Nyumba ilikuwa pweke iliyozingirwa na miti mingi. Kulikuwa ni giza japo taa zinawaka kutokana na mrundiko wa miti hii. Na zaidi kulikuwa kimya.





    Punde Brian alipozima gari, mlango wa nyumba hiyo ukafunguliwa akatoka mzee aliyevalia overoli na kofia. Mkononi alikuwa amebebelea bunduki ndefu ya kuwindia. Akaangaza kumwona mgeni.





    “Ni mimi Brian!” Brian akapaza sauti akinyoosha mikono yake juu.







    ***







    “Faris, una mgeni,” mama mmoja mzee mwenye uso wa kichovu alisema baada ya kuufungua mlango wa chumba, Brian akaingia ndani.





    “Usikae naye karibu sa …” mama alitahadhari, Brian akamkatisha.





    “Najua, usijali.”





    Mama akaenda zake.





    Chumba hiki kilikuwa hovyo sana. Nguo zilikuwa shaghalabaghala, huku na kule. Sakafuni kulikuwa na maji yaliyofanya matope.





    Kwenye kona ya kitanda alikuwa amekaa kijana wa kiume aliyekuwa ametulia sana. Amevalia shati lililochoka, na suruali iliyochanika mapajani. Nywele zake ni nyingi, macho yake ni mekundu. Mdomo wake mkavu na uso wake umepauka.





    Mikono yake yote miwili ilikuwa imefungiwa kwenye kingo ya kitanda kwa kamba nzito ya manila. Kamba hiyo ilifanya mikono yake kuwa mekundu na hata kutengeneza majeraha kadhaa.





    “Faris,” Brian akaita. “Ni mimi Brian, rafiki yako. Nimekuja kukuona.”





    Faris hakusema kitu. Alikuwa anatazama sakafu kwa macho poozi.





    “Faris!” Brian akamsogelea. “Ni mimi … ni mimi Brian, nitazame!”





    Faris hakujali. Ni kama vile hakuwa anasikia jambo lolote. Alikuwa kama alivyokuwa tokea mwanzoni.





    “Pole sana, Faris. Natamani sana kukusaidia urudi kwenye hali yako lakini siwezi kwa sasa. Nimekuwa mtumwa sana. Akili yangu haikomi kuwaza yale tuliyokuwa twafanya utotoni. Utoto wetu ulikuwa mzuri sana. Nashindwa kuacha Kecie na wewe mtokomee kabisa.”





    “Kecie!” Faris akafungua mdomo kwa mara ya kwanza. “Kecie … Kecie … Kecie!” alipaza sauti kana kwamba mtu aliyekumbuka kitu cha kuogofya.





    Akamtazama Brian. Akaendelea kurudia jina la Kecie akipaza sauti. Brian akajitahidi kumtuliza.





    “Nini wataka kusema, Faris? Sema nakusikia!”





    Faris alibwabwaja maneno mengi yasiyoeleweka. Alitota jasho jingi. Macho yalimtoka na mdomo wake akauchanua kadiri alivyoweza. Alijitahidi sana kuongea lakini hakuwa anaeleweka hata kidogo!





    Brian akiwa anajiuliza ni namna gani afanye, akaona kitu fulani kwenye kingo za kitanda cha Faris. Kulikuwa kuna mikwaruzo kadhaa, mikwaruzo ambayo alipoitazama kwa makini aligundua ni michoro.





    Michoro ya vitu vya ajabu.







    “Faris,” Brian akaita. “Ni nini hii?” akauliza akiwa anatazama michoro ile iliyochorwa na Faris kwenye kingo za kitanda. Tena kwa kukutumia kucha.





    Hakujua vitu avionavyo ni nini, michoro ilikuwa hafifu na isiyo ya wazi, ila kwa mbali alihisi kupata angalau wazo. Aliona kama vile kuna binti njiti, kuna mwanaume njiti mrefu na kuna mtu mwingine njiti kwa kando. Mkononi mwa binti yule njiti aliyekuwa amechorwa, alikuwa ameshikilia kitu.





    Juu kidogo ya mchoro huo, kulikuwa hakuonekani vema kwani damu zilizogandia zilikuwa zimetapakaatapakaa papo. Basi kwakuwa Brian alikuwa anataka kujua zaidi. Akakwangua damu hizo kwa kucha zake apate kuona kama kuna lolote.





    Akaona maandishi kadhaa hapo. Yalikuwa ni ya lugha ngeni ambayo hakuwa anajua ina maanisha nini. Ila akayanakili maneno yale na kuyahifadhi kichwani. Akaendelea kutazama na kutazama. Vingine hakuwa anavielewa kabisa, na ubaya hakuweza kumuuliza Faris amwelezee chochote kile.





    Kitu pekee ambacho Faris anajua kukitamka na kueleweka ni jina la Kecie tu. Na hajalishi imepita miaka mingapi, bado akisikia jina la Kecie hushtuka, hugomba, huogopa.





    “Faris,” Brian akaita. “Naenda rafiki yangu. Nitakuja kukutazama tena siku nyingine. Sawa?”





    Brian akasimama akimtazama Faris. Alikuwa ametulia tuli kama alivyomkuta mwanzoni. Na alipomtazama vema vidoleni mwake akaona ni namna gani Faris alikuwa amejiumiza na hata kujing’oa kucha kwenye vidole viwili vya kati. Yote kwasababu ya kuchuna kingo za kitanda kwa kuchora na kuandika.





    Akamwonea huruma sana. Akampa mgongo na kwenda zake kuwakuta wazazi wa Faris sebuleni.





    “Nashukuru, nataka kwenda sasa,” akasema akitabasamu kwa mbali. Baba Faris, bunduki yake ikiwa mapajani, akamtazama Brian kwa macho yake ya kizee kisha akamuuliza,





    “Kuna lolote umepata?”





    Sauti yake ilikuwa kavu kama ya mvuta sigara ama mnywa pombe kali.





    Brian akatikisa kichwa. “Hapana,” akajibu. “Ila nimefurahi kumwona.”





    Baba yake Faris akashusha pumzi ndefu puani. Akahamishia macho yake chini akibinua mdomo wake legevu. “Kuna muda natamani kummaliza apumzike … naona anateseka sana.”





    Akapinda tena mdomo wake na kunyanyua nyusi zake juu kadiri awezavyo.





    “Naumia sana kumwona katika hali ile. Japo sina kitu cha yeye kurithi, nilitamani sana awe na furaha kama watoto wengine.”





    “Pole sana, Mr York,” Brian akampooza. “Ila bado ana umri mdogo, na hatuwezi jua ya mbeleni. Ni mapema sana kukata tamaa.”





    “Mapema?” akauliza baba Faris. Macho yake yalionyesha udhaifu. Akatikisa kichwa chake kilichofunikwa na kofia. “Si mapema. Ona ninavyokongoroka, uzee unanitafuna. Mpaka arejee kwenye hiyo hali unayosema, bado nitakuwa hai?”





    Brian hakusema kitu, alitazama chini. Mkono wa baridi wa mama yake Faris aliyekuwa ameketi kwenye kiti cha karibu naye ukamgusa.





    “Nenda sasa. Muda wazidi kwenda na si vema kutembea nyakati za usiku ukiwa peke yako,” mama akamshauri akimtazama kwa macho ya msisitizo.





    “Nashukuru, niwatakie wakati mwema.” Brian akaaga akaendaze.





    Akatia chombo moto na kuanza safari yake ya kurudi kule kwenye tafrija kumkuta Wayde pamoja na Silvia. Alikuwa ndani ya muda. Hakutaka kuchelewa ili kuepusha kuwakwaza tena wale mabinti kwa kungoja muda mrefu, hata pia mama yake nyumbani.





    Akatembea kwa mwendo wa robo saa akivuka miti. Safari yake ikiwa imetawaliwa na ukimya wa hali ya juu. Na mbali na taa zimulikazo barabara kukiwa kiza totoro. Miti imefungamana chini na hata juu kusiwe na dalili ya kiumbe chochote.





    Nyuma kulikuwa giza na mbele kulikuwa giza. Upepo ukipuliza, miti ilikuwa inaruruma na kutengeneza sauti kana kwamba wanakwaya waimba. Upepo ukiwa umetulia, basi hakuna kinachosikika isipokuwa injini ya gari.





    Brian alikuwa anatazama aelekeapo kwa macho yaliyotuama. Alikuwa ana mawazo kichwani mwake, ungelitambua hilo kwa kuutazama tu usowe. Alikuwa amekunja ndita na kinywa amekiacha wazi. Kuna mambo yalikuwa yanamtatiza. Kuna mambo yalikuwa yanamnyima raha.





    Taswira ya Faris ilikuwa inamjia kichwani. Maneno yake yalikuwa yanajirudia masikioni mwake japo hayaelewi. Laiti angelikuwa anatembea eneo lenye watu, ni wazi angesababisha ajali. Mazingatio yake yalikuwa duni sana.





    Ila akiwa fikirani humo, akahisi kuona kitu. Kitu kilichomshtua. Ni kama vile alimwona binti mdogo aliyevalia gauni jeupe kandokando ya barabara akampita kwa kasi.





    Akageuza shingo yake kutazama nyuma kama atamwona binti huyo, hakumwona! Akawaza ni nini hicho? Ni kweli amemwona mtu ama ni mawazo yake. Na kama kweli kamwona mtu, ni nani na anafanya nini usiku msituni?





    Moyo wake ulipiga mafunda. Na kwa namna moja ama nyingine akaongeza mazingatio barabarani tofauti na hapo awali. Akaongeza pia na mwendokasi.







    ***







    “Nilidhani utatukalisha tena!” alisema Silvia akitabasamu. Alikuwa pamoja na Wayde wakiwa wamesimama na wasichana watatu pembezoni mwao, wote wakiwa wametoka kwenye tafrija iliyotoka kukoma muda si mrefu.





    Wakajipakia kwenye gari na kumtaka Brian awapeleke majumbani maana walikuwa wamelewa, wasingeweza kuendesha. Kweli walikuwa wananuka pombe na hata kuongea kwao na kujichekesha hovyo kulionyesha namna gani kilevi kilivyowakolea.





    Brian akawapeleka, na kama dereva wa taksi, akamshusha mmoja baada ya mwingine mpaka pale alipombakiza Wayde peke yake garini. Kwakuwa Wayde alikuwa anaishi karibu na Brian, haikuwa shida kwake kujisukuma kufika nyumbani hata katika hali yake ile ya ulevi.







    ***







    Saa nane na nusu mchana …







    Kengele ya mwisho wa vipindi iligonga, wanafunzi wakasimama na kila mmoja kuanza kufanya jitihada za kutoka ndani ya darasa isipokuwa kwa Brian pekee. Alikuwa ametulia kwenye kiti kama mtu ambaye hakusikia kengele. Watu wote walipotoka darasani ndipo akanyanyuka na kuweka begi lake mgongoni. Akiwa anatazama chini, akawa anatembea kwa mwendo wa taratibu kufuata geti lilipo.





    Alipochomoza tu nje, akapiga hatua tatu, mara akasikia sauti inamwita. Kutazama akamwona mwanaume fulani aliyevalia nadhifu. Alikuwa ameegemea gari jeusi la thamani.





    “Haraka, mvulana!” mwanaume huyo akamwamrisha. Brian alipofikia gari hilo, akaamriwa aingie ndani. Humo akakutana na Wayde akiwa pamoja na baba yake. Akapata hofu. Hata kusalimia alishindwa.





    “Kijana,” akaita baba yake Wayde. Mzee mnene mwenye mustachi mweupe kwa mvi. Macho yake yamezama ndani. Sauti yake nzito ya kukoroma.





    “Sitaki kukuona na binti yangu. Sawa?” akasema akimtazama Brian. Brian akatikisa kichwa. Na mzee yule asiseme kitu kingine tena, akampatia Brian ishara ya kichwa. Brian akatoka kwenye gari, gari likaondoka akibakia kulitazama likiyoyoma.





    Kwa hofu aliyokuwa nayo, akaona ni kheri arudi shule na akae huko mpaka atakapoona ametuliza nafsi. Alihofia pengine vijana wa seneta wangeweza kumfanya jambo endapo wangemwona mahali ambapo hamna watu.





    Akarejea na kukaa darasani peke yake, akawaza anawaza kumhusu Wayde. Ni nini jana kimetokea. Baba yake amejuaje kuhusu yeye.





    Akiwa kwenye lindi hilo la mawazo, akashtuliwa na sauti ya viatu. Alipotazama ni nani akamwona Dkt Hamill, mkuu wa shule, mwanaume mrefu mwenye makadirio ya miaka sitini na, yu mbele ya darasa. Akashangazwa. Haraka akamsalimu.





    “Mbona upo mwenyewe darasani? Kuna shida?” Dkt Hamill akauliza.





    “Hapana,” Brian akajibu. “Hamna shida.”





    “Kabisa?”





    “Ndio, hamna shida. Hamna shida kabisa.”





    “Sawa. Uwe na wakati mwema.”





    Lakini Brian kichwani mwake akaona hii ilikuwa ni fursa adhimu kwake. Dkt Hamill ni mtunzi wa kile kitabu kinachoelezea misitu ya Massachusetts. Kitabu anachokipenda na kumsisimua kwa habari zake. Kwanini asimuulize maswali kadhaa kukihusu? Habari za kinywa zaweza kuwa sisimuzi kuliko za maandishi!





    Basi akiwa anamtazama Dkt Hamill aenda zake kuufuata mlango, akapaza sauti, “Kitabu chako ni kizuri sana. Nakipenda haswa.”





    Dkt akasimama na kumtazama kwa tabasamu la mbali. Japo mwanaume huyu alikuwa ni mzee, alikuwa mkakamavu sana.





    “Kweli?” akauliza.





    “Ndio, kweli,” Brian akajibu. “Natumai nitakimaliza ndani ya juma hili nitakapopata muda … lakini,” akasita kidogo. “Lakini ni ya kweli yale yote uliyoyaandika mule?”





    “Ni kweli,” Dkt akamjibu. “Ni kweli kwa kila tone. Ila sitajibu swali lako lolote lile maana majibu yote yapo mulemule.”





    Dkt aliposema hayo akapiga hatua kuuendea mlango atoke. Brian akapaza tena sauti, “Nina swali moja tu. Na wala si toka kwenye kile kitabu. Tafadhali unaweza nisaidia?”





    “Lipi hilo?” Dkt akauliza. Brian akamtajia yale maneno aliyoyasoma toka kwenye kingo ya kitanda cha Faris. Dkt akamuuliza akimkazia macho, “Umeyaona wapi hayo maneno?”



    Brian akafikiria kidogo. Pengine hakuona tabu yoyote kuhusu hayo maneno lakini muitikio wa Dkt Hamill ukamfanya apate mashaka. Dkt aliyekuwa katika mpango wa kuondoka, akarejea na kusimama mbele ya Brian kungoja majibu.



    “Niliona tu mahali,” akajibu Brian. Hakutaka kusema uhalisia kwa kuhofia pengine anaweza kujikuta amemwingiza Faris na familia yake kwenye matatizo.



    Dkt akaketi juu ya meza, kisha akauliza kwa sauti ya upole, “Unaitwa nani kijana?”



    “Brian Woodgate.”



    “Brian,” Dkt akaita. Alikuwa anamtazama Brian kwa macho ya umakini. “Kuwa muwazi, sawa? Sina mpango wa kukudhuru bali kukusaidia … umeyaona wapi hayo maneno?”



    “Kwenye kitabu,” Brian akajibu.

    “Hakuna maneno hayo kwenye kitabu changu,” akasema Dkt Hamill.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Si kwenye kitabu chako,” Brian akajitetea. “Ni kitabu kingine kabisa nilichokutana nacho kule maktaba.”



    “Una uhakika?” Dkt akauliza akifinya ndita.



    “Ndio,” Brian akajibu akitazama chini. Dkt akatazama saa yake ya mkononi kisha akanyanyuka na kusema, “Muda wangu wa kuwapo hapa umekwisha. Nina kazi nyingi za kufanya nyumbani kwangu. Kama hutojali, kesho majira ya saa tano asubuhi, ufike ofisini, tutaongea mambo kadhaa.”



    Dkt akaondoka zake na kumwacha Brian akiwa mpweke darasani. Akiwa na mawazo kadhaa juu ya maneno yale ya Faris na namna ambavyo Dkt alivyoyapokea. Naye hakudumu muda, akaweka begi lake mgongoni na kwenda zake nyumbani.





    **



    Saa mbili usiku …



    Brian alikuwa na mama yake sebuleni mahali pa kupatia chakula. Mbali na sauti ndogo ya redio iliyokuwa inasikika kwa mbali, hakukuwa na sauti nyingine kubwa zaidi ya midomo inayotafuna.



    Walipomaliza kula, mama alitoa vyombo, na kabla Brian hajaondoka mama akamweleza kuwa kuna jambo anataka kuongea naye, basi akangoja kitini wakati mama anamalizia kazi kadhaa jikoni. Kichwani mwake akijaribu kubashiri ni kitu gani ambacho mama anataka kumweleza.



    Hapa akajikuta akili yake yote inakimbilia kwa Wayde. Pengine baba wa binti huyo atakuwa amekuja kumweleza mama yake kuhusu mahusiano yao. Kidogo akapata shaka, akapanga namna ya kulikabili hilo endapo mama yake atakapomhabarisha.



    Ni hivi, yeye hajui lolote kuhusiana na hilo jambo, anasingiziwa tu, akapanga vivyo.



    “Brian,” mama akaita akiketi. Alimtazama Brian katika namna ambayo ilimfanya ajue kuna mushkeli kwenye kauli ijayo.



    “Jana usiku ulikwenda wapi?” mama akauliza, na kabla Brian hajajibu akatahadharisha, “Usijaribu kuniongopea chochote, Brian. Ni kwa ajili yako.”



    Brian akapatishwa shaka na kauli ya mama yake. Hapa akawa njia panda kujua ni kipi haswa mama yake anakiongelea, kwenda kule kwa wakina Faris ama kwenye tafrija pamoja na wakina Wayde? Kutaka kujua hilo, akauliza, “Kwani kuna nini, mama?”



    “Brian, nimekuuliza,” mama akapandisha sauti. “Nahitaji majibu na si maswali.”



    “Nilienda kutembelea familia ya Garett!”



    “Alafu?”



    “Nikaenda kwenye tafrija ya kumbukumbu ya kuzaliwa ya mwanafunzi mwenzetu.”



    “Ukiwa na nani?”



    Hapa Brian akaanza kuhakikisha kuwa mawazo yake ya awali yalikuwa sahihi. Wanaenda kujadili lile swala la Wayde, mtoto wa seneta.



    “Nikiwa na marafiki zangu … watu ninaosoma nao darasa moja! Kuna ubaya kwenye hilo?”



    “Alafu ulipotoka hapo ukaenda wapi?”



    Hapa Brian akapata shaka, pengine alivyokuwa anawaza sivyo. Akajiuliza zaidi ni nini mama yake anajua kabla hajafungua mdomo wake aidha kuongopa ama kusema ukweli.



    “Tulipotoka hapo tukarudi nyumbani,” akajibu. “Hivyo ndivyo ilivyokuwa, hamna cha ziada.”



    Mama akanyamaza akimtazama kwa sekunde kadhaa kisha akamuuliza, “Haukwenda kwa wakina Faris?”



    Moyo wa Faris ukaruka pigo. Akahisi mstari wa baridi umempitia mwilini kwa wepesi. Mama amejuaje hilo?



    “Brian,” mama akaita. Akashusha pumzi ndefu na kutikisa kichwa chake taratibu. “Wewe ni mwanangu wa pekee, sina mtoto mwingine yeyote yule. Tangu baba yako alipofariki, wewe ndiye familia pekee niliyobaki nayo. Sitaki kukupoteza.”



    “Kivipi?” Brian akauliza.



    “Sitaki maswali, Brian!” mama akafoka. “Kuanzia leo hii sitaki kukusikia wala kukuona ukienda kwa Garett tena. Sitaki kusikia ukienda kwa wakina Faris pia. Tumeelewana?”

    Mama alikuwa amebadilika rangi. Uso wake ulikuwa unatisha. Macho yake yalikuwa mekundu yamekodoa.



    “Sawa, mama,” Brian akajibu kwa hofu. Mama akanyanyuka na kwenda zake chumbani akitembea upesi na kwa hasira. Alimwacha Brian akiwa na maswali, mama amejuaje kama alienda kwa wakina Faris?



    Aliwaza sana lakini hakupata jibu. Alijaribu kutengeneza kichwani namna ambavyo mama yake aling’amua safari hiyo, akashindwa. Akaona ni stara, siku ambapo mama yake atakuwa amepungukiwa na hasira, amuulize apate kujua.



    Basi akaendaze kulala.



    Baadae katikati ya usiku, kwenye majira ya saa nane ya saa yako, akasikia mlango wa chumba chake ukigongwa. Akafungua macho na kuweka shuka kando, akajiuliza kwa muda mfupi kabla hajapaza sauti,



    “Nani? - mama?” Hakukuwa na majibu. Hodi ikagongwa tena. Basi akanyanyuka na kwenda mlangoni kufungua. Hakuona mtu. Alitazama kushoto na kulia, patupu! Kabla hajatoka hapo mlangoni, akasikia tena hodi nyingine. Akashangaa!



    Alitega sikio lake kwa umakini, akagundua hodi hiyo ilikuwa inatokea kwenye mlango wa sebule. Akakunja ndita za mashaka, lakini akapata hamu ya kujua. Akanyanyua nyayo zake kuuendea mlango … alitembea taratibu, hakukuwa na vishindo vyovyote … sakafu yao ya mbao ilikuwa ya baridi … aliufungua mlango kwa upole na kutupa macho nje.



    Hakukuwa na mtu. Akaufungua mlango zaidi kutazama. Alitupa macho yake upande wa maghariki. Barabara ilikuwa pweke na upepo wa baridi ulikuwa unapuliza. Nyumba zote zilikuwa kimya. Hakukuwa na sauti ya kitu chochote isipokuwa ya matawi ya miti punde yakipulizwa na pepo.



    Alipotazama upande wa mashariki, moyo wake ukapiga fundo kubwa. Kwa mbali alimwona mtoto mdogo wa kike akiwa amesimama katikati ya barabara. Mtoto huyu alikuwa kwa umbali wa hatua thelathini toka kwenye nyumba yao. Alikuwa amevalia gauni jeupe linalokomea juu ya magoti, mkononi akiwa amebebelea mdoli.



    Moyo wa Brian ukaanza kwenda upesi.



    “Kecie! …” akajikuta anatamka. “Kecie, ni wewe?” alikuwa anauliza kwa sauti ya chini kana kwamba mtoto yule yupo kando yake. Bado kichwa chake hakikuwa sawa. Alikuwa anawaza ni nini anachokiona mbele yake. Ni jinamizi ama mzimu?



    “Kecie!” akaendelea kuteta, sasa akitoka nje ya mlango. “Ni wewe, Kecie? … ni wewe kweli?”



    Akapiga hatua mbili kuuacha mlango, macho yake yakimtazama yule mtoto amwonaye. Kwakuwa alikuwa mbali na kulikuwa kiza barabarani, hakupata kumwona uso wake vema. Ila yule mdoli, lile gauni, lilikuwa kweli ni la Kecie.



    Brian hakuwa na kumbukumbu kiasi hicho cha kuweza kukumbuka sawasawa kitu kilichopita miaka kumi, ila ndani ya chumba chake kuna matangazo yote ya kutafutwa kwa Kecie. Matangazo yaliyokuwa yanaelezea ni nini Kecie alivaa siku anapotea.



    Basi akaendelea kupiga hatua kumfuata yule mtoto, sasa hatua tano toka mlangoni. Ila mara, kwa mbali, akasikia sauti ya kike inamwita. … Briaaan! … Briaaan! … kana kwamba mtu yupo ndani ya chungu.



    Lakini kabla hajaitikia sauti hiyo, kwa macho yake, akashuhudia yule mtoto akigeuka na kuanza kwenda zake. Akapaza sauti kumwita. Mtoto hakusikia, akaendelea kwenda zake. Mara mtoto huyo akaanza kukimbia. Brian akiwa anashuhudia, japo kwa uhafifu wa uwezo wake wa macho, akamwona yule mtoto amesimama ghafla, na alipofinya macho yake kumtazama kwa umakini, akagundua kuna mtu pembezoni yake. Na mara mtu huyo akaanza kuondoka naye wakitokomea gizani!



    Alijitahidi kumtazama mtu huyo, hakubahatika kabisa kumwona. Alikuwa mweusi kufanana na giza. Akataka kuwafuata, ila aliponyanyua mguu, akahisi amedakwa mkono wake wa kuume, akavutwa kwanguvu!



    “Brian!” Kutazama alikuwa ni mama yake. Akatazama kule alipomwona mtoto, hakukuwa na kitu. Taa zilikuwa zinamulika barabara iliyokuwa nyeupe pe.



    “Brian, nini shida?” Mama akauliza. Bado Brian alikuwa haelewi kinachoendelea. Hakuwa anajua hata cha kusema. Basi mama akamrejesha ndani na kisha akaufunga mlango.



    “Brian!” mama akaita, na kuuliza, “Umeanza lini kuota ukiwa unatembea?”



    Kumbe yale yote ambayo Brian alikuwa anayafanya alikuwa usingizini. Lakini akiwa katika hali hiyo, akafungua mlango na kwenda mpaka nje ya nyumba.



    Akamweleza mama yake kilichojiri, nini aliona na kusikia.



    “Unafikiri mno kuhusu Kecie … Kalale, Brian. Tutaongea kesho.” mama yake akambusu kwenye paji la uso na kisha akaenda zake chumbani kulala. Brian naye akanyanyuka na kwenda kujitupia kitandani mwake bado akiwa na hofu. Aliwaza sana juu ya kile alichokiona. Kilimnyima raha na kumpatia maswali mengi ambayo hakuona dalili ya kupatia ufumbuzi.



    Ila akiwa hapo, anajibuabidua kutafuta usingizi, akatazama dirishani na kuona kitu. Kulikuwa kuna maandishi kwenye kioo cha dirisha. Alisonga kwa ukaribu na kutazama vema. Ni kweli alichokiona. Kulikuwa na maandishi yaloandikwa kwa herufi kwa kutumia kidole dhidi ya unyevu uliojishika kiooni.



    ‘NIOKOE, BRIAN’



    Maandishi yalisomeka vivyo.



    Brian akafikicha macho kwa kutoamini. Alipotazama tena hakuona kitu kiooni. Kioo kilikuwa kimefutwa seemu ile ya maneno na kubakia kisafi kabisa king’aacho. Akajiuliza ni macho yake, ni akili yake ama uhalisia? Alihisi kuchanganyikiwa!



    Alishindwa kabisa kujua mambo haya yanavyomtukia. Hakulala tena akabaki anawaza sana usiku mzima. Akawaza sana na kujikuta akianza kuunganisha matukio kadha wa kadha. Mosi, ule mchoro aliouona kwenye kingo ya kitanda cha Faris, na pili ile ndoto yake ya wima.



    Ina maana yule mtoto ambaye Faris alikuwa amemchora akiwa amesimama na mtu nyuma yake ndiyo wale ambao aliwaona kwenye ndoto? Yule mtoto aweza kuwa Kecie lakini yule mtu aliyekuwa amesimama naye ni nani? Ndiye aliyemteka Kecie? Na yeye ndiye aliyesema maneno yale ambayo bado hajayapatia ufumbuzi? Alichanganyikiwa kwa maswali. Alihisi kichwa kinamuuma.



    Jua lilipochomoza, mama yake alimgongea mlango kumuuliza hali yake. Aliamka toka kitandani kichwa kikiwa kizito. Akajikongoja mpaka sebuleni na kuketi kwenye kochi. Hakuonekana kama mtu mwenye dhamira ya kwenda shuleni siku hiyo. Macho yake yalikuwa mekundu na uso wake mzito.



    “Unajisikiaje, Brian?” mama yake akamuuliza. “Uko sawa?”



    “Siko sawa,” akajibu akitazama kando.



    “Nini shida?” Mama akauliza akimshika mkono.



    “Naota na kuona mambo ya ajabu,” Brian akajibu, kisha akakunja ndita zake kama mtu anayetaka kulia.



    “Ni sawa, Brian. Mara nyingiine hutokea mambo kama hayo. Usijali, utakuwa sawa,” Mama akampoza. Ila Brian akapata na mashaka. Mama yake alikuwa mtulivu sana kwenye mambo haya. Tangu jana usiku alipomkomboa toka kwenye ndoto mpaka leo hii anapomweleza mengine. Hali hii haikuwa ya kawaida.



    “Mama,” Brian akaita. “Kuna lolote unalolijua kuhusiana na hivi vitu? … tafadhali, kama kuna unalolijua niambie.”



    Mama akabinua mdomo wake na kupandisha mabega. “Sijui kitu, Brian. Naamini ni kwasababu ya wewe kumfikiria sana, Kecie. Nadhani inabidi upunguze sasa.”



    Ila Brian aliona kitu kwenye macho ya mamaye. Hakuwa anazungumza kwa mwili wake wote.



    “Mama, tafadhali naomba uniambie,” akasisitizia. “Najua kuna kitu unafahamu.”



    Mama akashusha pumzi ndefu. Akajitengenezea kwenye kiti na kumtazama Brian, kisha akatulia kwa kama sekunde sita pasipo kunena jambo.



    “Brian,” Mama akaita kwa sauti ya chini. “Nadhani unamfahamu Brewster”



    “Brewster!” Brian akalipuka. “Yule mzee anay…”



    “Ndiye huyo huyo!” mama akadakia. “Pengine ana mambo anayoyajua kuhusu wewe.”



    “Mambo gani hayo?”



    “Sijui. Ila anajua ….”



    Mama akashusha tena pumzi. Kwa muda kidogo kukawa kimya katikati yao.



    “Sikutaka kukuambia kabisa haya mambo lakini naona yanaweza yasikome. Jana wakati wa jioni, Brewster alikuja hapa kunigongea mlango. Nilishangazwa na ujio wake maana hajawahi kuwa mgeni wangu tangu nimjue miaka kenda iliyopita. Nilimkaribisha na akanieleza mambo ya ajabu…”



    Brian alikuwa makini akisikiliza, macho yake mekundu yalikuwa tenge na kwa muda mfupi, usingizi ulimtoweka kichwani japo kichwa chake bado kilimgonga kwa mbali.



    “… swali lake la kwanza kuniuliza ni wapi alipo mtoto wako? Nikamwambia sifahamu, ametoka muda mrefu. Akaniambia ulipo na mwishowe akanipa onyo pasipo kunielezea mambo mengi. Kama nataka uwe hai, basi nikusihi uache mambo unayoyafanya na uishi maisha yako.”



    “Kwanini alisema hivyo?” Brian akauliza.



    “Sijui!” Mama akajibu. “Hakunieleza mambo mambo mengi zaidi ya hayo, na hakukaa muda mrefu akaenda zake … sikufahamu alijuaje ulipo, na sijui ana nini kichwani kuhusu wewe.”



    “Alikueleza nitakuwa naota na kuona mambo ya ajabu?”



    “Alichoniambia ni kwamba, endapo usipofuata anachokisema basi maisha yako yatakuwa ya taabu sana. Utaishi kwa masumbuko, hofu na woga … Brian, sijui kama anachokisema ni kweli au lah! Ila nahisi kuna kitu hakipo sawa. Naomba uachane na mambo ya Kecie. Sawa?”



    Brian akatazama chini. Hakujibu, ikabidi mama yake arudie kuuliza.



    “Sawa, Brian?”



    “Sawa, mama … nitafanya hivyo.”



    “Nenda kapumzike sasa. Najua usiku haukulala.”



    Brian akanyanyuka na kwenda zake chumbani. Kulikuwa na mambo kadhaa yanampitia kichwani ila alipojitupia kitandani hakupata wasaa wa kuyafikiria, usingizi ulimnyaka na kumpoteza.





    ***





    Saa kumi jioni …





    “Oliviiia!” Sauti ya Mrs Garett ilitikisa nyumba. Alikuwa amekunja sura, ametoka chumbani anaelekea sebuleni akiwa ameweka mkono wake kiunoni.



    Akaendelea kuita na kuita, hakusikia wala kuona kitu. Alikasirika sana, akaketi kitini akiwaza Olivia atakuwa wapi. Alimkataza asiende kucheza pasipo kumwomba ruhusa. Alimkataza kwenda popote pale. Ina maana amekaidi agizo lake.



    Akiwa ametulia hapo kwa sekunde kadhaa, akasikia sauti ya kike ikiita, “Moooom! … moooom!” akashtuka.



    Sauti hiyo ilikuwa ni kana kwamba inatoka chini ya mto. Ilikuwa ni kana kwamba mtu anakabwa na sasa anajitahidi kuzungumza. Basi Mrs Garett akasimama na kuanza kuita tena kama mtu aliyekabwa na hofu.



    “Oliviaa! Oliviiiaa!”



    Sauti ile ya kike ikawa inamjibu, ikisikika kwa mbali. Haraka Mrs Garett akarudi tena chumbani akiita. Mara akamwona Olivia akiwa juu ya paa. Uso wake ulikuwa umetapakawa na woga. Macho yake yalikuwa yanatiririsha machozi.



    “Olivia!” Mrs Garett akatahamaki. Akafanya jitihada za kumshusha kisha akaenda naye sebuleni. Ila Olivia alikuwa mwoga sana, alikuwa anatazama nyuma kila mara kana kwamba kuna kitu kinamfuata.



    “Nini Oliva! Kuna shida gani?” Mrs Garett akamuuliza akimlazimisha amtazame usoni. “Niambie kuna nini? … Olivia, nambie!”



    Olivia alitazama koridoni. Macho yake yalikuwa mekundu mno, pua yake ilikuwa inachuruza kamasi jepesi. Akasema kwa sauti ya kilio, “Sitaki kucheza naye.”



    “Nani? Nani hutaki kucheza naye, Olivia?” Mrs Garett akauliza. Alikuwa anamtazama Olivia kwa macho na sura ya huruma.



    “Yule mtoto,” Olivia akaropoka. “Ananifuata chumbani, anataka kucheza na mimi. Analazimisha kwenda na mimi tukacheze.”



    “Mtoto gani? Niambie ni nani huyo?”



    Olivia akanyooshea kidole chake kwenye picha iliyopo ukutani. Mrs Garett kutazama, akaona ni picha ya Kecie. Akaachama mdomo wazi kwa kuduwaa.



    “Una uhakika ni yeye?” akamuuliza Olivia.



    “Ndio, ni yeye! Hunifuata kila siku usiku … mchana na jioni. Anataka twende tukacheze kule msituni!”



    Mrs Garett akashusha pumzi akikosa la kusema. Macho yake yakageuka kuwa mekundu. Alitazama chini akihangaika kutafuta neno la kuongea.



    Baada ya mfupi, akiwa ameongozana na Olivia, akatoka nyumbani akitembea kwa kasi. Alikuwa amevalia gauni jeusi na mtandio mweupe, Olivia, gauni rangi ya pinki lenye mauamaua shingoni.



    Moja kwa moja wakaelekea kanisani. Lilikuwa ni kanisa kubwa linalosimama upande wa kaskazini mwa mji wa Boston. Hapo Mrs Garett akaonana na padri Alfonso, mwanaume mrefu aliyevalia joho refu jeusi kasoro ya shingoni kuna doa jeupe. Alikuwa mtu wa makadirio ya miaka arobaini na tano.



    Mrs Garett akamweleza dhamira yake kuwa anataka kutubu na kuomba msamaha. Padri akampeleka kwenye chumba maalum, Mrs Garett akaketi kitako upande wa pili akitenganishwa na Padri kwa ukuta mwepesi wa mbao wenye matundutundu.



    Kabla hajaanza kusema kitu, akajikuta anaanza kumimina machozi.





    “Padri Alfonso,” Mrs Garett akaita. “Mimi ni mkosefu sana, naona hata sistahili kuwapo mbele ya madhabahu ya Mungu. Nimemwendea kombo. Nimemtendea ndivyo sivyo.”

    .

    .

    “Na hao ndiyo wakaribishwao hapa,” akasema Padri Alfonso kwa sauti yake nzito. “Usijali maana umejua uliikengeuka. Wewe ni bora kuliko wale wanaojihisi wako safi. Mkombozi wetu alikuja kwa ajili yetu waongofu na tulipotoka apate kutukomboa.”

    .

    .

    Mrs Garett akavuta kwanza makamasi, alafu akamtazama Olivia. Alikuwa amesimama mbali akiwa katika hali ya upweke na woga.

    .

    .

    “Padri Alfonso,” Mrs Garett akaita na kusema, “Nimekuja hapa kinyume kabisa na maagizo ya mume wangu. Hataki kabisa mimi kuja kanisani, hata akigundua anaweza kunikatakata vipande na kuwatupia nguruwe wanile. Lakini …”

    .

    .

    Akabanwa na kwikwi. Akajipangusa na leso yake kisha akaendelea kunena, “ … nimeshindwa kuvumilia hili. Limekuwa mzigo sana kifuani mwangu, siwezi tena kuhimili. Limenitesa miaka kumi sasa na naona inatosha.”

    .

    .

    “Ni nini hiko?” Padri akauliza.

    .

    .

    Mrs Garett akanyamaza kwa muda akijaribu kuremba dhambi yake, akashindwa kabisa kuifanya isionekane kali masikioni, akaamua tu kusema vivyo hivyo, “Nilimuua mwanangu.”

    .

    .

    Padri Alfonso akatulia kidogo kisha akamuuliza, “Una maanisha Kecie?”

    .

    .

    “Ndio. Nilimuua Kecie,” akajibu Mrs Garett akitazama chini na macho yake mekundu.

    .

    .

    “Kwanini ulimuua?” Akauliza Padri.

    .

    .

    “Ni simulizi pana kidogo,” akasema Mrs Garett. Akajipangusa machozi kisha akaendelea kuongea …

    .

    .

    Miaka kumi na mbili iliyopita …

    .

    .

    Ulikuwa ni mchana wa saa saba wakati mume wangu aliporejea nyumbani toka kazini. Anafanya kazi kwenye kiwanda hivyo nilistaajabu kwake kuwahi kurudi siku hiyo tofauti na ilivyo kawaida yake. Alikuwa amenuna sana kiasi cha kuogopa hata kuongea naye, ila baadae alipotulia akaniambia nini kinamtatiza.

    .

    .

    Hakuwa anamtaka Kecie pale nyumbani. Nilishangazwa sana na neno lake hilo. Sikuona mahusiano ya yeye kurudi kazini mapema na uwepo wa Kecie.

    .

    .

    Akiwa amefura kwa hasira, akanambia kuwa Kecie ni gundu kubwa ndani ya nyumba. Amekuwa ni mtoto wa mikosi na laana. Amekuwa ni mtoto anayemsababishia matatizo sana kazini kwake.

    .

    .

    Nilibaki naduwaa. Nilitaka kujua ni kwanini anasema hivyo lakini hakuniambia abadani. Kitu pekee alichoniambia ni kwamba amefukuzwa kazi. Aliponiambia hivyo akaenda zake ndani, na tangu hapo hatukuwa na mahusiano mazuri baina yangu na yeye.

    .

    .

    Basi siku zikapita. Mahusiano baina yake na Kecie yakawa mabaya sana sana. Hakuwa anataka kumwona kabisa. Na muda mwingine angempiga nusura kumuua. Alikuwa na chuki kubwa sana juu yake.

    .

    .

    Na kwakuwa hakuwa na kazi, tukawa tunaishi kwenye umasikini mkubwa sana. Nakumbuka siku nne zilipita tukiwa hatuna kitu mfukoni, tukiomba tu kwa majirani. Mume alikuwa anatafuta kazi, akizunguka huko viwandani na hata kuomba vibarua, akawa hapati ata cha ndani ya masaa.

    .

    .

    Siku moja, tukiwa chumbani, akiwa ametulia kabisa, akaniita, “Mke wangu, kuna kitu nataka kukwambia.” Nilikuwa nimechoka kwa njaa, tulikuwa tumepata chakula kidogo sana, hata majirani walikuwa wametuchoka.

    .

    .

    “Unataka sema nini?” nikamuuliza. Akaniambia, “Tumuue Kecie.” Nikashtuka sana. Nikamtazama na kumuuliza, “kwanini tumuue mtoto wetu wa pekee?”

    .

    .

    Aliposhusha pumzi ndefu, akasema ya kwamba tangu Kecie azaliwe amekuwa akiandamwa na mabalaa, tabu na mikosi. Amekuwa akipatwa na wakati mgumu sana hajapata kuona. Na kama Kecie akiendelea kuwapo hai, basi hali itakuwa mbaya zaidi na wote tutakufa kwa njaa, ikiwemo na huyo mtoto.

    .

    .

    Jambo hili likawa gumu sana kwangu. Kumuua mtoto niliyemzaa kwa uchungu si jambo jepesi hata kidogo. Nilikataa katakata, nikamfokea na kumtahadharisha asiwaze hilo kabisa maana halitakuja kuwahi kutokea. Haikuwa inaniingia akilini kuwa Kecie anaweza akawa sababu ya ufukara wetu.

    .

    .

    Basi siku zikasogea. Ikafikia kipindi mpaka tukaanza kuuza vitu vyetu vya ndani tupate chakula. Navyo vikakwisha. Hapa sasa Kecie naye akaanza kudhoofu sana. Mume wangu akanikumbusha lile jambo tena na tena.

    .

    .

    Siku moja, ikiwa ni majira ya usiku mwepesi, mume wangu akaja na babu mmoja ambaye alinitambulisha kuwa aitwa Tomas Fringe. Mwanaume huyo alikuwa mfupi na mwenye kubebelea briefcase rangi ya kahawia. Mume wangu alisema kuwa mwanaume huyo ni ‘mtaalamu’ na yupo pale kutusaidia.

    .

    .

    Akatuagiza tuzime taa nyumba nzima. Tukafanya vivyo. Tufunge madirisha na kila mlango, na Kecie awepo chumbani kwake. Tukafanya vivyo. Akatoa chupa fulani ya duaria yenye vitu vya kung’aa ndani yake. Na kwasababu giza lilikuwa limetawala ndani, mwanga wa chupa ile ndiyo ukawa umeng’aza.

    .

    .

    Ulikuwa ni mwanga wa kijani hafifu.

    .

    .

    Aliweka chupa hiyo mezani, akaisugua kwa viganja vyake akisema maneno ambayo sikuwa nayaelewa. Katika namna ya ajabu, chupa ile ikaanza kubadilika rangi kuwa nyekundu. Yule mzee, bwana Tomas Fringe, akamtazama mume wangu, kisha mimi. Akasema. “Kuna tatizo ndani ya nyumba yenu.”

    .

    .

    Hatukusema kitu, akaendelea kuongea baadhi ya maneno yake, taa ikazidi kukolea wekundu kuelekea damu ya mzee. Hapo akakoma na kutuuliza, “Tukiondoe kitu hiko?”

    .

    .

    “Ndio,” Mume wangu akawahi kujibu. Lakini Thomas akan’tazama na kuniuliza, “Upo tayari?” Nikamtazama mume wangu. Akan’tikisa kichwa kunishawishi nikubali, basi nami nikaridhia.

    .

    .

    Bwana yule akatutaka tuweke mikono yetu juu ya ile chupa na kufuatisha maneno kadhaa aliyokuwa anatamka. Tukiwa tunatamka maneno hayo, tukawa tunasikia mlango unagongwa kwanguvu! Mlango wa Kecie. Kama haitoshi akawa anatuita, analia kuomba msaada!

    .

    .

    Nilitaka kuacha, nilipatwa na shauku ya kwenda kumwona, lakini mzee yule akanikazia macho na kunipa ishara ya kuendelea kuteta aliyokuwa anasema. Tukaendelea.

    .

    .

    Kadiri tulivyokuwa tunasema, basi na makelele yale ya Kecie yakawa yanapungua, na ile taa inageuka rangi kuwa ya kijani. Tulipomaliza, taa ile ilikuwa kijani kilichokolea. Na katika namna ya kustaajabisha, nikaona kivuli cha mwanamke kikiwa ukutani kinatambaa kana kwamba mende!

    .

    .

    Kivuli hicho kikasimama sebuleni na kuangaza, kisha kikaambalia nje.

    .

    .

    “Vizuri!” akasema yule bwana Fringe akitutaka sasa tuache kushika chupa yake. “Sasa kazi imekwisha hatua ya kwanza, imebakia hatua ya mwisho.”

    .

    .

    Akaweka chupa yake ndani ya briefcase na kumuagiza mume wangu akamzike Kecie kule misituni. Akifanya vivyo atasema maneno kadhaa aliyomtajia na kila kitu kitakuwa kimekwisha. Ataona faida yake.

    .

    .

    Kwasababu za woga, Mume wangu akataka kwenda na mimi kule msituni. Bwana Fringe akamruhusu na alipoenda zake, sisi tukangoja usiku uwe mkubwa tukatimize kazi hiyo.

    .

    .

    Basi baada ya masaa kadhaa, tukabeba mwili wa Kecie na kwenda nao msituni, tukafukua shimo na kuutumbukiza humo. Mume wangu akawa anafukia wakati mimi nikiwa natazama huku na kule kuangazia usalama.

    .

    .

    Nikiwa naangaza, nikahisi kumwona mtu anatutazama! Alikuwa ni mwanaume mrefu mwenye mwili mpana. Tulikuwa katikati ya msitu. Nilihofia sana kumwona mtu huyo, niliona sasa habari yetu itajulikana Boston nzima, basi nikamshtua mume wangu na kumwambia kuna mtu kule. Upesi mtu yule akaanza kukimbia.

    .

    .

    Mume wangu akamkimbiza sana na hatimaye akampata. Alimrukia na kumdondosha chini. Akamtwanga na chepeo kichwani. Na kwasababu za kuondosha ushahidi tukamzika kisha tukarudi nyumbani upesi.

    .

    .

    Usiku huo sikulala kabisa. Nilitekwa na mawazo mabaya kabisa. Hata nilipopata lepe la usingizi, nikaota ndoto za ajabu ajabu. Nikawa macho mpaka jua linakucha.

    .

    .

    Lakini asubuhi hiyo, tukiwa bado hatujatoka kitandani, nikakumbuka jambo ambalo lilintia hofu. Nikamwamsha na kumwamba mume wangu ya kwamba usiku ule baada ya kumzika Kecie, hatukutamka yale maneno ambayo mtaalamu alituagiza.

    .

    .

    Mume wangu akashtuka sana. Ilikuwa ni kwasababu ya yule mtu aliyemkimbiza ndiyo maana akasahau. Tukapata sana maswali itakuaje, lakini mwishowe tukapuuzia, akinipa moyo kuwa kwasababu Kecie hayupo, basi mambo yatakuwa tu shwari.

    .

    .

    Kumbe tulikuwa tumekosea kabisa kabisa, Alfonso …

    .

    .

    .



    .

    Mrs Garett akaweka kituo na kufuata machozi kwanza. Akameza mate na kutazama pembeni akiendelea kusema.

    .

    .

    Basi kwakuwa tulikuwa tumekiuka kile tulichoambiwa na bwana Fringe, tukawa tunaishi kwa hofu kidogo labda pengine mambo yanaweza kukiuka, ila zikapita masiku pasipo jambo lolote kutukia. Tatizo lilikuwa tu kwamba, bado kwa upande wa mume wangu mambo yalikuwa yaleyale.

    .

    .

    Hakuwa anapata kazi popote pale, maisha yalikuwa magumu magumu magumu. Ikafikia kipindi mume wangu akaniambia, mke wangu kwakuwa tulikosea yale masharti, basi tumfuate tena bwana yule tumweleze, labda anaweza kutusaidia. Sikuwa na lingine zaidi ya kumkubalia, akafunga safari na kesho yake akaja naye nyumbani.

    .

    .

    Bwana yule akalalama sana kwa kufanyia uzembe jambo alilotuambia. Akasema kuwa yale yote tuliyoyafanya yalikuw bure, na basi kukata mzizi wa fitna, basi inabidi turudie tena lile swala upya. Lakini tutalirudiaje na wakati Kecie ameshakufa? Nikauliza.

    .

    .

    Yule bwana, Fringe kwa jina, akatuambia ataongozana na sisi kwenda huko msituni, tumfukue Kecie na turejelee zoezi. Niliogopa sana, mosi kwenda msituni, pili kwenda kuona maiti. Nilihisi mwili umekuwa wa baridi, natetemeka kila kiungo, lakini … lakini sikuwa na machaguzi. Ilibidi nifanye tulichokubaliana.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Tukatoka majira ya saa tisa usiku tukiwa watatu. Nakumbuka siku hiyo mvua ilikuwa inanyesha sana. Baridi lilikuwa kali pia kiasi kwamba barafu zilikuwa zimejaa njiani.

    .

    .

    Nikiwa nimejikunyata, tukaelekea huko msituni, siku hiyo hatukuwa tumebeba taa, wanaume wakachimba shimo na kumfukua Kecie. Mwili wake ulikuwa umejawa na udongo mweusi. Ulikuwa wa baridi mno kama barafu!

    .

    .

    Yule bwana, Fringe, akaniambia niushike mwili huo, nami nikafanya vivyo. Akafungua mkoba wake na kutoa ile chupa yake ya kioo cha duara. Akaipangusa akisema maneno kadha wa kadha, mara ikaanza kuwaka ikiwa ya kijani! Akatutaka tuiwekee viganja chupa yake ile na kusema maneno aliyokuwa anayatamka.

    .

    .

    Basi tukafanya vivyo, mwili wa Kecie ukazamishwa tena ndani ya shimo na mume wangu pamoja na bwana Fringe wakatenda kazi ya kuufukia. Walipomaliza, mume wangu akasema yale maneno ambayo bwana Fringe alimtaka ayatamke kisha kazi ikawa imeishia apo.

    .

    .

    Ila kabla hatujaondoka, Bwana Fringe alituuliza, “Kuna yeyote aliyewaona wakati mnamzika Kecie mara ya kwanza?” mimi na mume wangu tukatazamana, akawahi kujibu, “Hapana. Hamna aliyetuona.”

    .

    .

    Bwana Fringe akatabasamu, ila tabasamu lake lilinitisha zaidi. Mtu yule hakuwa wa kawaida. Kila nilipomtazama nilijikuta natetemeka kwa hofu. Na kila macho yangu yalipokutana na yake, nilihisi moyo wangu umesimama kwa muda. Sikuwa najua kwanini.

    .

    .

    Alitutazama na kutuambia, kwa ajili ya usalama wetu, tutangaze kuwa Kecie amepotelea msituni. Haitakuwa hoja sana kwani watoto kadhaa huwa wanapotelea huko misituni. Lakini nilipata swali, watu wataaminije hilo kwa wepesi?

    .

    .

    Bwana yule, Fringe, katika hali ya kustaajabisha akajua swali langu hilo kichwani, akanitazama na kunambia, “Usijali, Kecie atapotelea msituni na kila mtu ataamini hilo.”

    .

    .

    Sikujua amemaanisha nini, ila jua lilipokucha, nikastaajabu asubuhi ya mapema mlango ukigongwa. Nilipoenda kufungua nikakutana na Kecie mlangoni. Moyo wangu ulishtuka mno. Kwa muda nilijihisi nimepoteza nguvu. Sikuwa najua nini cha kufanya!

    .

    .

    Kecie akazama ndani na kwenda kuketi kitini. Nikiwa katika hali ya bumbuwazi, mara mume wangu naye akaja. Naye akashangazwa sana kumwona Kecie, ila Kecie hakuonyesha muitikio wowote ule. Alikaa pale kitini kana kwamba mdoli.

    .

    .

    Ni baada ya muda kidogo ndipo alinitazama na kuniomba nimletee mdoli wake aupendao. Nikampatia. Na asikae sana, akaenda zake nje. Sikuwa najua anaelekea wapi, nilitaka kumfuata lakini mume wangu akanikataza.

    .

    .

    “Mwache aende. Huwezi jua anaelekea wapi.”

    .

    .

    Ni siku hiyo ndiyo nikaja kuambiwa kuwa Kecie alipotelea kule msituni watu wakiwa wana ushahidi wa kuwa na Faris huko kama mtu wa mwisho.

    .

    .

    Tukiwa na mashaka, tukaenda kutazama lile shimo lake. Ajabu tukalikuta halijafukuliwa, lipo vilevile kama ambavyo tulikuwa tumeliacha. Tukastaajabu alitokaje humo. Lakini pia tukapata shaka sana kuhusu yule mtoto ambaye alikuwa naye kwa mara ya mwisho, yaani Faris.

    .

    .

    Tulijiuliza je atakuwa ameona chochote? Ajabu baadae tukaja sikia taarifa kuwa mtoto huyo amekuwa bubu tangu hapo. Hakuwa anaweza kuongea kabisa isipokuwa kubwatuka vitu ambavyo havieleweki, vitu ambavyo havina maana.

    .

    .

    Ila …

    .

    .

    Mrs Garett akanyamaza kidogo. Akashusha pumzi ndefu kwa pua yake ndefu alafu akajifuta mdomo wake na leso.

    .

    .

    Yule mtoto, Mrs Garett akaendelea kuteta, atakuwa ameona kitu. Ni wazi kuna kitu alikiona. Anataka kusema lakini hawezi. Amekuwa wa ajabu tangu hapo. Amekuwa wa kufungiwa hata leo hii.

    .

    .

    Tulitoa taarifa ya upoteaji wa Kecie. Matangazo yakawa yanabandikwa mara kwa mara lakini tukiwa tunajua kuwa ni bure, lengo lilikuwa ni kulaghai watu tu.

    .

    .

    Lakini mbali na hayo, tangu Kecie alipopotelea, hatukumwona tena. Japo nilisumbuliwa na ndoto za ajabu mara kwa mara hapo karibuni, sikumwona tena mwanangu huyo. Alikuwa ameenda zake.

    .

    .

    Mume wangu akaanza kupata kazi, tena akitafutwa. Ajabu ni kwamba kazi zote alizokuwa anapata zilikuwa ni za kufanya kazi kwenye viwanda vya mbao. Kila alipofanya kazi kwa muda mfupi, akawa anapandishwa nafasi na hata mshahara.

    .

    .

    Maisha yakawa mazuri haswa. Hata hapa katikati tukawa tumemsahau kabisa Kecie, japo kila tulipokuwa tunafanya jitihada za kupata mtoto zikawa zinagonga mwamba. Mpaka leo hii hatujabahatika kupata mtoto, wala dalili. Ndipo tukaona ni vema kutafuta mtoto yeyote wa kukaa naye nyumbani.

    .

    .

    Mrs Garett akamtazama Olivia.

    .

    .

    Ndipo tukampata yule binti yatima, aitwa Oliva.

    .

    .

    Padri Alfonso akasafisha koo lake na kuuliza, “Ina maana matendo uliyoyafanya ndiyo yanakusuta kuja kutubu?”

    .

    .

    Mrs Garett akatikisa kichwa na kusema, “Huenda matendo hayo ningelikuwa nimeyasahau. Ila nilichokujia hapa, ni kikubwa zaidi ya kutubu, kikubwa zaidi ya matendo hayo…”

    .

    .

    “Ni nini hicho?” Padri Alfonso akauliza.

    .

    .

    “Padri,” akaita Mrs Garett. “Nahitaji msamaha kwa Muumba wangu. Lakini pia nahitaji msaada …”

    .

    .

    “Sema nakuskiza,” Padri Alfonso akanguruma.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    .

    Saa mbili usiku …

    .

    .

    Watu kadhaa walikuwa barabarani. Nyumba ziizokuwa zimepakana na barabara zilikuwa zimewashwa taa kuangazia nuru.

    .

    .

    Wakiwa njiani kutoka kanisani, walikuta gari nje ya nyumba yao. Mrs Garett akasimama ghafla na kumtazama Olivia. “Usiongee kitu chochote, sawa?” akamwonya. Olivia akaitikia kwa kichwa kisha wakaendelea na safari yao iliyokomea mlangoni.

    .

    .

    Walimkuta Mr Garett akiwa ameketi sebuleni, anavuta sigara. Mwanaume huyo alitulia sana kana kwamba hakuna watu walioingia. Kiti alichokuwa amekalia kilikuwa chaenda mbele na kurudi nyuma. Uso wake ulikuwa hauonekani kwa wepesi kwa kujaliwa na moshi wa sigara.

    .

    .

    Mrs Garett akamsalimu, hakuitika. Mwanamke huyo akamtaka Olivia aende chumbani, Olivia akatii. Mrs Garett akaketi na kumtazama mumewe kwa sekunde kadhaa. Mr Garett akasimamisha kiti chake na kuzima sigara akiuliza, “Umetoka wapi?”

    .

    .

    Uso wake haukuwa na lepe la masikhara. Macho yake yalikuwa mekundu, na mdomo wake uliotoka kunyonya sigara ulikuwa mkavu na mweusi.

    .

    .

    “Nimetoka kanisani,” akasema Mrs Garett. Ghafla mumewe akanyanyua kisosi alimokuwa anakung’utia majivu ya sigara, akamrushia mkewe ghafula. Kama si Mrs Garett kukwepa, kisosi hicho kilikuwa kinapasua uso wake. Kilienda kwa kasi na kujibamiza ukutani. Kikapasuka kwenye vipandevipande milioni!

    .



    “Nilikwambiaje kuhusu kwenda kanisani?” akafoka Mr Garett akinyanyuka. “Nakuuliza wewe mwanamke, nilikuambiaje kuhusu kwenda kanisani!”

    .

    .

    Akamnyaka mkewe na kumtikisa kana kwamba dawa. Alimfokea na kumchapa makofi akimuuliza sababu ya yeye kwenda kanisani. Ilifikia kipindi Mrs Garett akajawa na damu usoni kwasababu ya kipigo, lakini bado hakusema kitu.

    .

    .

    Mumewe akaendelea kumpiga mpaka pale alipoanza kupoteza fahamu, akamwacha hapo sebuleni kitini na kwenda zake chumbani. Mrs Garett akawa anaona hafifu kwa mbali. Macho yake yalijawa na kitu kama vile ukungu na masikio yake yalikuwa ni kana kwamba yametoka kupuliziwa sauti kali, akawa anasikia kwa mbali sauti ya kitu kama kucha kikikwaruza bati.

    .

    .

    Akalia sana. Alisikia maumivu makali kichwani. Hakuweza hata kunyanyuka kwenda chumbani ikamlazimu alale papo hapo sebuleni akiwa amejikunyata kwa baridi.

    .

    .

    Baada ya dakikaa kadhaa kupita, Olivia akaja kumjulia hali.

    .

    .

    “Mama,” Olivia akaita. “Mama, upo sawa?”

    .

    .

    Aliona uso wa mama yake ukiwa umezibwa na damu. Alikuwa anaogopa sana. Alimtazama kwa huruma na woga pia ndaniye.

    .

    .

    “Mama, mama, mama,” akaendelea kuita akimsukumasukuma Mrs Garett. Alihofia huenda akawa amekufa basi machozi yakatawala macho yake.

    .

    .

    “Mama, amka,” akalia. “Mama, mama!”

    .

    .

    Mrs Garett akaitikia kwa mbali akiguna. Alimsikia Olivia kwa mbali sana. Alijaribu kufungua macho yake kumtazama mtoto huyo. Hakumwona vema. Alinyanyua mkono wake wa kuume na kuuweka shingoni mwa Olivia, akasema, “Usijali, Olivia. Niko sawa.”

    .

    .

    Sauti yake ilikuwa ni ya kunong’ona, ila angalau ilimfariji Olivia. Hakurudi tena chumbani, akaamua kulala na mama yake palepale sebuleni mpaka asubuhi.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    .

    Saa nne asubuhi …

    .

    .

    “Naweza kuingia ndani?” sauti iliulizia mlangoni. Ndani Dkt Hamill aliyekuwa anasoma kitabu akatazama mlango kwa jicho la nje ya vioo vya miwani kisha akairuhusu hodi hiyo kwa sauti yake ya kizee.

    .

    .

    Mlango ukafunguka na Brian akaingia ndani.

    .

    .

    “Brian!” Dkt Hamill akamkarimu kijana huyo. Akaweka kitabu chake pembeni na kumwelekezea kiti cha kuketi. Wakasalimiana.

    .

    .

    “Samahani, Dkt Hamill. Nisingeweza kuja jana maana sikuwapo shule, nilipata udhuru nyumbani.”

    .

    .

    “Ni sawa,” akasema Dkt Hamill kisha akavuta kitabu chake na kuendelea kusoma kana kwamba hamna mtu.

    .

    .

    “Dokta,” akaita Brian. “Nimekuja …”

    .

    .

    “Sawa,” akasema Dkt akiwa amegandisha macho yake kwenye kitabu.

    .

    .

    “Ulikuwa na ahadi na mimi,” Brian akasema. “Unakumbuka?”

    .

    .

    “Ndio, Brian,” akajibu Dkt Hamill. “Ila si leo, ilikuwa jana. Leo sina ratiba ya kuonana na mtu yeyote bali kusoma kitabu changu tu, Brian.”

    .

    .

    “Tafadhali, Dkt. Sitakaa sana kukuibia muda wako. Naomba tu unisaidie kuniambia maana ya maneno yale niliyokuambia nami ntaondoka zangu.”

    .

    .

    Dkt Hamill akamtazama Brian kwa macho ya nje ya kitabu, alafu akashusha pumzi ndefu na kuweka kitabu pembeni.

    .

    .

    “Brian, najua uliniongopea siku ile juu ya wapi uliyatoa hayo maneno,” akasema akiwa amekumbatisha mikono yake. “Pengine hutaki kunambia, natumai hata na haya ntakayokwambia utayafanya kuwa siri. Au si hivyo, Brian?”

    .

    .

    Brian akasita kidogo na kisha akasema, “Ndio, nitayafanya kuwa siri.”

    .

    .

    Basi Dkt Hamill akatabasamu na kisha akalaza mgongo wake kwenye kiti. Akamtazama Brian kwa sekunde kadhaa na kumwambia, “Kwasababu umetaka kuyafahamu, basi n’takujuza … Ila, ni kheri ukachunga sana mdomo wako. Najua kwenu vijana ni ajabu na ni ngumu sana kufanya hilo. Punde mjuapo jambo, basi mwataka mji mzima ufahamu. Lah!

    .

    .

    Si kila kitu ni cha kuwa bayana, Brian. Na naomba sana ushike hilo neno. Nimesemaje? …”

    .

    .

    “Si kila kitu cha kuwa bayana, Dokta.”

    .

    .

    “Sawasawa. Basi nami nitakueleza mambo hayo ya kale na ya kutisha. Na nitakueleza hayo kwa siku na siku, siwezi kuyamaliza yote kwa siku moja. Huenda si simulizi ndefu sana, ila ni kwasababu ya muda wangu. Sina muda wa kutosha. Hata haya nafanya kwakuwa wataka sana kufahamu.”

    .

    .

    Aliposema hayo, akanyamaza kwa sekunde kadhaa. Akasafisha koo lake na kisha akatazama chini.

    .

    .

    “Ni zamani sana ndani ya Boston. Bila shaka ni watu wachache sana walioshuhudia hayo wapo hai mpaka sasa. Hapa hakukuwa na watu wengi kiasi hiki cha leo. Kulikuwa na watu wachache hapa na pale na pia makazi.

    .

    .

    Basi miongoni mwa familia hizo zilizokuwapo hapa, kulikuwa kuna familia moja ya kilatini ya bwana maarufu aliyekuwa anaitwa Hernandez Lorenzo, ama wengi wakimwita Helo kwa ufupi.

    .

    .

    Bwana huyo alikuwa maarufu kwa michezo yake ya mazingaombwe katika eneo hili zima la Boston na hata Massachusetts nzima. Kila mtu alikuwa anampenda na kumtukuza. Banda lake lilikuwa linajaa kila mwisho wa wiki wa ajili ya kutumbuiza kiasi kwamba lilikuwa linatanuliwa kila mwisho wa mwezi kukidhi idadi ya watu.

    .

    .

    Mitaani na hata huko barabarani watu wakawa wanaita jina lake. Helo! - Mtu wa maajabu!! Helo - Mtu wa maajabu!! Mtu huyo akavutia watu wengi sana kuja Boston, kumjua na hata kumfurahia. Familia yake ikawa maarufu sana, na si tu hivyo, wakawa matajiri sana.

    .

    .

    Ila mambo yakaja kukengeuka punde baada ya jimbo hili kupata kiongozi mpya, Bwana Ralph Blacksmith. Mwanaume huyo aliyekuwa na kariba ya ukali na mpenda mabadiliko ya haraka, alitangaza ya kwamba hakuna mambo yoyote ya kiudanganyifu na kiutapeli yatakayofanyika ndani ya jimbo lake hili. Na swala hilo halikuishia hapo tu, bali likawekwa na kuidhinishwa mpaka kwenye mfumo wa sheria.

    .

    .

    Jambo si kwamba watu walikuwa wanapenda udanganyifu na kutapeliwa, lah! Ila vipi kuhusu mazingaombwe ya Bwana Helo? Wakajiuliza. Je yale nayo yalikuwa udanganyifu na utapeli?

    .

    .

    Kujibiwa hilo, katika hali ya kustaajabisha, siku moja maafisa wa serikali wakajaa wengi kwenye nyumba ya Bwana Helo. Wakaangusha banda lake pasipo huruma, na Helo akapewa onyo kali kuwa inambidi afanye kazi halali kujiingizia kipato na si utapeli na udanganyifu!

    .

    .

    Akasononeka sana. Haikujalisha aliomba namna gani, hakusikika na hakuna mtu aliyemjali. Lakini kama kuna kitu ambacho watu walikuwa hawakijui, Helo hakuwa tapeli wala mdanganyifu. Yote aliyokuwa anayafanya kwenye banda lake, hayakuwa udanganyifu hata kidogo, bali uchawi!

    .

    .

    Familia ya wakina Helo ilikuwa ya kichawi kutokea huko Amerika ya kusini. Hakuna aliyekuwa anajua hilo kipindi hicho. Ulozi ulikuwa umekatazwa kabisa ndani ya jimbo na kwa mtu yeyote aliyekuwa amebainika kujihusisha nao, adhabu yake ilikuwa ni kukamatwa na kuchomwa mbele ya kadamnasi ya watu!

    .

    .

    Basi kwasababu ya kukatazwa kwa mambo ya mazingaombwe, familia ya bwana Helo ikafilisika sana. Wakawa mafukara na kituko ndani ya jij. Kila walipopita wakanyooshewa kidole, wengine wakisanifu na wengine wakihuzunika.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Maisha yalibadilika ghafla! Kutoka kwenye shujaa mpaka tapeli wa Massachusetts. Kutoka kwenye umaarufu mpaka kujificha kwenye miti na ndani vyumbani.

    .

    .

    Hali hii ikadumu kwa mwaka mmoja tu. Fedheha, lawama, dharau zikachosha familia hii. Walitaraji mambo yangekuwa sawa, lakini pengine ilionekana ingechukua muda mrefu kuwa vivyo. Sasa Helo na familia yake wakaanza kuonyesha kucha na rangi zao halisi.

    .

    .

    Wakaapia kuwavuta kwenye fedheha na aibu wale wote waliokuwa wanawataka wao waishi kwenye shimo hilo. Basi mmoja mmoja akawa anakufa kila uchwao. Hali hii ikatisha sana Boston na hata Massachusetts nzima. Walipokuja kugundua ni Halo na familia yake wafanya vivyo, wakachoma nyumba yao. Wakawakamata na kuwachoma moto mbele ya hadhira.

    .

    .

    Huo ukawa mwisho wa Halo na familia yake. Nyumba yake, iliyokuwa imebakia kuwa ghofu, ikatengwa na hata mpaka sasa imebakia huko ndani ya misitu ikiwa pweke.

    .

    .

    Lakini kabla Helo hajafa, wakati moto wamuunguza kula mwili wake, alilia sana na kusema kuwa atarudi kulipiza kisasi. Alikuwa anaamini hakuwa na makosa, aliishi kwa upendo wote na wakazi wa Boston na Massachusetts nzima kabla ya wao kukengeuka.

    .

    .

    Neno lake la mwisho alilitamka kwa kilatini akisema wote mtakuwa wangu. Wote mtasujudia miguuni mwangu. Majivu yake yalienda kutupwa huko msituni na toka siku hiyo mpaka leo hii Helo akageuka kuwa historia ya kuwasimulia watu.

    .

    .

    Ni wachache sana waliojali yale maneno yake aliyoyasema wakati anakufa. Ila Helo alisema ukweli. Atarudi tena kwenye mji huu na atafanya kila mtu awe wake.”

    .

    .

    Brian alikuwa ameachama mdomo wake wazi akiskiza mpaka hapo mwisho. Alipoufumba akauliza, “Ina maana yale maneno maana yake ni ‘Helo, kuwa wangu!’ kwa kilatini?”

    .

    .

    “Ndio,” akajibu Dokta, “Hiyo ndiyo maana yake, ndiyo maana nikashangazwa sana na mahali ulipoyatolea hayo maneno. Ebu niambie uliyasikia wapi? Kuwa mkweli, pengine naweza kukusadia.”

    .

    .

    Dkt Hamill alimtazama Brian kwa macho ya kidadisi na hamu. Kabla Brian hajatia neno, akamuuliza, “Umeyasikia maneno hayo ndotoni au msituni?”

    .



    .

    .

    “Sijayasikia huko,” Brian akatikisa kichwa chake. “Ni kutoka kwa rafiSki yangu anaitwa Faris. Yeye amekuwa mgonjwa hivi sasa, hawezi kusema jambo lolote akaeleweka. Niliona akiwa ameandika maneno hayo kwenye kingo yake ya kitanda!”

    .

    .

    Dkt akanyamaza asitie neno. Aliminya tu lips zake na kuendelea kumtazama Brian.

    .

    .

    “Dokta,” Brian akaita. “Waweza kunambia maana yake ni nini? Kwanini ameandika maneno hayo?”

    .

    .

    Dokta akameza kwanza mate, kisha akamwambia Brian, “Muda wangu umekwisha. Sina muda tena wa kuongea na wewe. Tuonane kesho majira haya, sawa?”

    .

    .

    “Lakini Dokta,” Brian akataka kuongea. Dkt Hamill akamzuia na kumkumbusha makubaliano yao ya mwanzoni kuwa maongezi hayo ni marefu na vivyo hatoyamaliza yote kwa siku moja. Basi Brian, kishingo upande, akanyanyuka na kuuendea mlango. Dokta akamkumbusha, “Usisahau kuja kesho. Uwe ndani ya muda.”

    .

    .

    Akatikisa kichwa chake kuitikia na kisha akaenda zake. Siku hiyo alikuwa amegundua kitu kikubwa lakini kilichompa hofu zaidi. Alijikuta akitaka kufahamu zaidi kuhusu Halo, na je kuna mahusiano gani kati ya Halo na Faris? Na labda kupotea kwa Kecie msituni?

    .

    .

    Wakati anajiuliza hayo akaona ni vema kama asipomficha kitu Dkt Hamill. Inabidi amweke wazi, labda atakuwa anfahamu kila shaka alilo nalo kichwani. Basi akaapa kesho yake atakapopata fursa ya kuonana na Dkt Hamill atahakikisha analifanyia kazi shauri lake.

    .

    .

    Alipofika nyumbani, baada ya kula na kupumzika kidogo, akatoka pasipo kuaga. Akaenda nyumbani kwa Brewster, mwanaume mzee ambaye alimweleza mama yake juu ya safari yake ya kwenda nyumbani kwa wakina Faris, na pia kumtahadharisha asifanye tena hilo jambo.

    .

    .

    Alitumai atapata mawili matatu kwa mzee huyo. Alikuwa na maswali kadhaa ya kumuuliza.

    .

    .

    Basi kwa mwendo wa robo saa, akawa amefika nyumbani kwa mzee huyo. Ilikuwa ni nyumba ndogo iliyojitenga. Kulikuwa ni kimya sana. Nje ya nyumba kulikuwa kumejawa na majani makavu ya miti. Kibaraza hakikuwa kisafi, pia na vioo vilikuwa vimebadilisha rangi.

    .

    .

    Juu ya paa kulikuwa na kunguru wawili wakimtazama Brian kwa macho ya pembeni kabla hawajalia mara mbili na kupeperusbha mbawa zao.

    .

    .

    “... kuna yeyote ndani?” Brian aliita baada ya kugonga mara tano pasipo majibu. Aliacha kugonga akazunguka nyuma ya nyumba. Huko akakuta banda la nguruwe wawili wadogo. Akapumbazwa kuwatazama rangi zao na namna wanavyokula kwa kufakamia. Ila ghafla akasikia sauti kavu nyuma yake.

    .

    .

    “Hey! We mvulana.”

    .

    .

    Alipogeuka akamwona Brewster. Alikuwa amevalia shati refu na suruali pana. Uso wake ulikuwa mtulivu ila macho yake ya kizee ameyakodoa. Mashavu yake yaliyoanza kudondoka yalikuwa yamemezwa na vinyweleo vya ndevu vilivyosimama. Mdomo wake mwembamba ulikuwa unaonekana kwa hafifu kwasababu ya mustachi.

    .

    .

    “We ni nani na unafanya nini hapo kwa nguruwe wangu?” akauliza Brewster. Brian akamsogelea na kujitambulisha, akamwambia ya kwamba amekuja kumtembelea kwani kuna maneno mawili matatu anataka kuyaongea naye.

    .

    .

    “Ni wewe, Brian!” akastaajabu Brewster. Alikuwa ana tatizo la kuona mbali hivyo Brian alivyosogea karibu na kuongea ndipo akamtambua.

    .

    .

    “Ila sina miadi na wewe,” akasema Brewster. “Pia sina cha kuteta na wewe. Nadhani mama yako alikuambia kila unachostahili kujua, mvulana.”

    .

    .

    “Hapana,” akasema Brian. “Hakuniambia kila ninachokitaka zaidi ya kunipa vitisho. Nataka kujua kwanini? … ulinionaje?”

    .

    .

    Brewster akanyamaza kwa muda. Akamtazama Brian kwa sekunde kadhaa kisha akamsogelea karibu na kuinamisha kichwa chake amtazame machoni. Brewster alikuwa mrefu kuliko Brian, kwahivyo alipofanya vivyo wakawa sawa. Uso wake wa kizee haukuwa unavutia. Macho yake yaliyoanza kufifia kiini yalitazama macho ya Brian na kisha akasema, “Kuna ambacho haukuelewa? … si kila kitu kimejawa na maswali, Brian. Muda mwingine kuwa mwerevu ni kufanya unachoambiwa pasipo kutia mashaka. Ni faida kwako … lakini tu kama unahitaji roho yako.”

    .

    .

    “Kwanini unasema hivyo?” Brian akauliza. “Kwani kuna nini?”

    .

    .

    “Kuna kifo,” akajibu Brewster. “Huko nyuma ya maswali na kutaka kwako kutafutia majibu … kuna kifo. Ni juu yako kuchagua, aidha maisha ama kifo.”

    .

    .

    Brewster aliposema hayo, akaenda zake Brian akimtazama. Alipopiga hatua nane, akageuka na kumtazama Brian. Akamwambia, “Nenda nyumbani. Usifanye jambo lolote la kijinga.”

    .

    .

    Mzee huyo akaenda zake asigeuke tena. Brian akabakia akisimama, akitazama huku na kule, na hatimaye akaenda zake. Alipitia kwa rafiki yake fulani kisha ndiyo akaenda nyumbani. Ilikuwa ni majira ya jioni ya saa moja sasa. Akamkuta mamaye akiandaa chakula cha usiku.

    .

    .

    Akaketi sebuleni na kulaza kichwa chake kwenye kiti akitafakari siku yake nzima. Alitamani kumshirikisha mama yake lakini alihofia. Alishamkataza kuhangaika na mambo hayo, basi akawa anahangaika mwenyewe akipanga na kupangua vipande vya ‘pazo’.

    .

    .

    “Amekuambia chochote?” sauti ya mama yake ikamshtua.

    .

    .

    “Nani?” akauliza.

    .

    .

    “Kwani umetoka wapi? Si kwa Brewster?”

    .

    .

    “Umejuaje kama nimetoka huko?” Brian akauliza akiketi vema kitini kumtazama mama yake aliyekuwa amesimama hatua kadhaa toka kwake.

    .

    .

    “Amekuja hapa kunambia.”

    .

    .

    “Nani? Brewster?”

    .

    .

    “Ndio. Amekuja hapa akaniambia ulienda kumwona.”

    .

    .

    “Saa ngapi?”

    .

    .

    “Si muda mrefu tangu uondoke. Vipi amekuambia kitu?”

    .

    .

    Kabla Brian hajajibu, alikabwa na mawazo. Brewster amewezaje kufika hapo muda mfupi baada ya yeye kuondoka. Amefanya hilo kwa kasi gani? Mama yake alimshtua kwa kurejea kumuuliza, “Amekuambia nini?”

    .

    .

    “Hajaniambia kitu … hamna kitu alichoniambia,” alimalizia akitikisa kichwa. “Wewe amekuambia nini?” akauliza.

    .

    .

    Mama akaketi na kumtazama Brian, akasema, “Amenisisitizia uache kuyafuatilia hayo mambo.”

    .

    .

    Brian akasonya na kunyanyuka. “Kuna siku utaniambia mambo mengine zaidi ya hilo?” akaenda zake chumbani na kubamiza mlango.

    .

    .

    .

    **

    .

    .





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog