Search This Blog

ROHO YAKE INADAI - 4

 

    Simulizi : Roho Yake Inadai

    Sehemu Ya Nne (4)





    Asubuhi ya saa moja na nusu …

    .

    .

    “Naomba kahawa pekee,” alisema Mama Brian kwa sauti ya chini akimwambia mhudumu baada ya watoto kuagiza vifungua kinywa. Muda si mrefu mhudumu akarejea akiwa amebebelea hitaji la kila mmoja wao, akawapatia.

    .

    .

    Mhudumu huyu alikuwa ni mwanamke mrefu mwenye nywele nyekundu. Uso wa kiukarimu na mkakamavu. Hakuwa mnyimi wa tabasamu.

    .

    .

    “Samahani, dada,” Mama Brian akanena akimtazama mhudumu. “Keline yupo?”

    .

    .

    Mhudumu akakunja sura. “Keline?”

    .

    .

    “Ndio, Keline. Ni mhudumu wa hapa. Alituhudumia jana,” Mama akadadavua.

    .

    .

    “Anaitwa Keline?”

    .

    .

    “Ndio, Keline! Ni mnene mfupi.”

    .

    .

    Mhudumu akabetua mdomo. “Simfahamu.” akatikisa kichwa chake. “Hamna mtu anayeitwa Keline hapa.” Mama Brian akamtazama mwanaye pasipo kutia neno.

    .

    .

    “Vipi, kuna tatizo lolote?” Mhudumu akauliza.

    .

    .

    “Hapana, nashukuru,” Mama akajibu akiigiza tabasamu.

    .

    .

    “Una uhakika?”

    .

    .

    “Ndio. Hamna shida, ahsante.”

    .

    .

    Mhudumu akaenda zake.

    .

    .

    “Ulikuwa sahihi,” Mama akasema akimtazama Brian kisha akanyanyua kikombe chake cha kahawa na kujipasha mwili. Walipomaliza, wakiwa wamechukua kama robo saa tu hapo mgahawani, wakaendea gari lao na kufunga safari ya kwenda kuonana na Wisconsin.

    .

    .

    Mwanaume aliyewafanya wafunge safari iliyojawa na mashaka na mateso.





    Walipowasili, baada tu ya kuegesha usafiri wao, wakaendea mlango na kugonga hapo mara tatu. Punde mlango ukafunguliwa na mwanamke mwembamba mzee. Akawasalimu kwa tabasamu na kuwauliza shida yao.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Tunahitaji kuonana na Wisconsin,” Mama Brian akaeleza. Mlango ukafunguliwa kwa upana, wakakaribishwa kuingia ndani. Wakaketi sebuleni, na yule mwanamke mzee akaelekea ndani. Muda si mrefu, akaja Wisconsin na kuketi miongoni mwao.



    “Naona mmetunza muda.”



    “Ndio. Pengine utakuwa umeelewa kuwa tuna shida,” Mama Brian akasema akimtazama Wisconsin usoni.



    “Naam, niambieni basi shida yenu, nami nitawasaidia kwa kadiri ya uwezo wangu.”



    Mama akamtazama Brian na kumpa ishara ya kichwa, basi kijana huyo akaanza kueleza yale yote anayoyajua. Tangu Kecie alivyopotea, anavyojiri mpaka watu kupotea katika mji wa Boston. Wisconsin alipoyasikia hayo akashangazwa hata naye. Alikuwa anamfahamu vizuri Helo, simulizi zake alishawahi kuzisikia hapo kitambo.



    Basi akasema, “Ningojeni kwa dakika kadhaa.” yeye akaelekea kwenye chumba kimoja kilichokuwa katikati ya vyumba vinne. Akadumu huko kwa muda wa dakika kumi kisha akarejea sebuleni.



    “Nifuateni!”



    Akaongozana na wakina Brian mpaka kwenye kile chumba, wakazama humo. Kilikuwa ni chumba kipana kilichopakawa rangi nyekundu ukutani. Katikati yake kulikuwa na viti vitano vikiwa vimeizunguka meza moja ndogo.



    Hapo wakaketi na kukiacha kiti kimoja kikiwa wazi. Yule mwanamke mzee akaja akiwa amebebelea taa. Ulikuwa ni mshumaa ndani ya chupa kubwa kiasi mithili ya ile ya taa ya chemli. Akaiweka juu ya meza kisha akaendea mfuko fulani mweusi aliokuja nao na kuuweka karibu na Wisconsin alafu akazima taa.



    Sasa chumba kizima kikawa kinaangaziwa na mwanga wa mshumaa. Wisconsin akatia mkono wake kwenye ule mfuko alioletewa, humo akatoa mashine fulani mbili, akaziweka mezani. Akapekua tena mfuko wake na kutoa chombo fulani cha chuma, kilikuwa mithili ya sahani ila kikiwa na mguu wake.



    Baada ya hapo akachoma maani fulani aliyoyatia kwenye kile chombo. Harufu ya kunukia, moshi mweupe, ukatawala ndani ya chumba. Akachukua mashine moja na kui ‘set’ kwa mkono alafu akaiweka mezani. Ikawa inatoa sauti kubwa kiasi mithili ya mshale wa dakika.



    Sasa alipoona kila kitu kipo sawa, akamtazama Brian na kumwambia.



    “Kama Kecie huwa anakufuata kukuomba umsaidie, basi utakutana naye. Muulize kila unachotaka kukijua …” Lakini pia akamtahadharisha, “Kuwa makini sawa?”



    Basi baada ya hapo akamtaka Brian afunge macho yake kisha azingatie sauti ile inayotoka kwenye mashine. Wote wakashikana mikono na kuwa kimya. Sauti tu ya mshine … tap!-tap!-tap!-tap! … ikiwa inasikika chumba kizima.



    Basi Brian akiwa amefunga macho yake kwanguvu, baada ya dakika kadhaa, masikio yake yakaanza kupoteza uwezo wake wa kusikia ule mlio wa mashine. Punde kidogo akawa hausikii tena! Kulikuwa ni kimya kabisa masikioni mwake kiasi kwamba akaanza kustaajabu kama amekuwa kiziwi.



    Ila muda si mrefu sana, kwa mbaali akaanza sikia wimbo ambao hakuwa anaujua. Alichosikia ilikuwa ni sauti nyembamba ya mwanamke iliyokuwa inatetemesha na kuimba kwa maringo.



    Zaidi ya hapo, mwili wake ukaanza kuhisi baridi kali. Alijikuta anajikunyata na kung’ata meno Alihisi upepo unamtafuna kwa namna ulivyokuwa wa baridi haswa. Akastaajabu ni wapi alipo? Chumbani na baridi lote hilo? Akafungua macho yake kuangaza. Ajabu akajikuta kwenye ulimwengu wa tofauti!



    Alikuwa yu mwenyewe nje. Ni giza na kuna upepo mkali. Mbele yake kuna nyumba kubwa sana ambayo ipo kwenye mwanga hafifu. Nyumba hiyo ni ya zamani. Alipotazama vema aligundua nyumba hiyo ni ile ya bwana Helo!



    Basi akatazama kushoto na kulia kwake. Hakukuwa na msitu bali giza tu, hata kuona njia ilikuwa ni tabu. Lakini ndani ya nyumba ile iliyopo mbele yake, kulikuwa na mwanga hafifu waonekana madirishani. Mwanga mithili ya ule wa vibatari.



    Akiwa anaduwaa,



    “Brian!” Sauti ikamwita. Kutazama akamwona Kecie akiwa amesimama kandokando yake. Alikuwa ndani ya gaunile na mdoli wake mkononi. Brian akamjongea, “Kecie!”



    Kecie akamwonyeshea ile nyumba na kusema, “Nenda kule. Nenda kanikomboe!”



    Lakini kabla Brian hajaenda, akamuuliza, “Naendaje huko? N’tawezaje kumkabili mtu wa ajabu vile?”



    Kecie akamjongea na kumshika mkono. “Brian, kammalize. Kammalize niende zangu salama!”



    “Uende wapi?”



    “Brian, roho yangu ilishakwisha kufa. Nashindwa kupumzika kwa amani kwasababu ya Helo. Yeye hunirudisha tena duniani kumfanyia kazi yake. Nimekwisha kumaliza yangu.”



    “Kazi yako ilikuwa ipi?”



    “Kuwamaliza wale watesi wangu.”



    “Unamaanisha wazazi wako?”



    “Ndio, hao waliofanya nikaja huku … Brian, nilipatwa na hasira sana kuona nimesalitiwa na wazazi wangu. Nilishindwa kabisa kuwasamehe. Na pale Helo aliponiuliza ni nini ada yangu nikatende kazi yake, nikamwambia ni kuwamaliza watesi wangu.



    Akanikubalia. Akawa ananirejesha duniani nikaitende kazi hiyo. Sasa nimemaliza, ni zamu yangu kufanya kazi yake. Kuitesa Boston. Kuchukua watoto wote walipo ndani ya mji huo kisha Massachusetts nzima.”



    Kecie akaweka kwanza kituo, akatazama jengo la Helo kisha akaendelea kumsemesha Brian.



    “Inabidi Helo atoke kwenye ulimwengu huu, la sivyo Boston haitakuwa salama. Huu ni ulimwengu wa watu ambao roho zao bado hazijaenda, watu waliotendewa maovu, watu wenye visasi na vinyongo na wale walio hai uko duniani.



    Kadiri mtu awavyo hapa, anakuwa karibu na dunia. Anaweza kuitembelea na kuwaadhibu watesi wake. Inabidi Helo atoke hapa, akitoka hapa roho yangu na za wengine alizozifungia nazo zitaenda.”



    “Lakini kwanini ameweza kuwakamata na kuwatawala ingali wote miliuawa kama yeye?” Brian akadadisi. Kecie hakuwa na jibu. Zaidi alisisitizia tu ya kwamba Helo ana nguvu kupita kiasi. Ni kama vile amekuwa mtawala kwenye anga yao.



    “Inabidi afe tena kwenye huu ulimwengu. Unaweza kumuua Brian.”



    “Mimi? Nitawezaje Kecie? Sina nguvu kama yeye! Yeye si binadamu kama mimi? Nawezaje?”



    “Brian, mtu pekee anayeweza kumwangamiza Helo ni wa kutoka duniani. Hakuna yeyote aliyeko huku akamshinda yeye … tafadhali, jaribu. Najua unaweza. Najua utanikomboa rafiki yako …”



    Lakini Brian alikuwa na woga kifuani mwake. Alikuwa anaogopa kukumbana na marehemu uso kwa uso. Alistaajabu kwanini msalaba huu umemwangukia yeye.



    “Kwanini mimi?” akamuuliza Kecie.



    “Wewe ni rafiki yangu. Au sivyo hivyo Brian?” Kecie akauliza akimtazama machoni.



    “Lakini,”Brian akaeendelea kueleza shaka yake. “Ni lazima Helo afe au ni muhimu tu kwako kujiendea?”



    “Vyote ni muhimu,” akajibu Kecie. “Amezifungia nafsi zetu kwenye ghala lake kama watumwa, funguo anazo yeye mwenyewe muda wote zikiwa karibu … Brian, hata kama ukizipata funguo hizo nikawa huru, bado Helo atarejea kuisumbua Boston kwa kutumia watu wengine. Bado halitakuwa komo lake.”



    Basi Brian akawa hana lingine la kuuliza, akaanza kupiga hatua zake kuendea mlango wa jengo. Kabla hajaufungua, akachungulia ndani. Hakukuwa na mtu. Kiti kilikuwa peke yake, runinga inawaka.



    “Tumia mlango wa nyuma,” Kecie akashauri. Alikuwa tayari ameshafika kandokando ya Brian.



    Nyumba hii ilikuwa kubwa. Kuizunguka ilikuwa inachukua muda kidogo. Brian allipofika huko nyuma, akafungua mlango na kuzama ndani. Ajabu kulikuwa kiza. Ukutani, kulikuwa kuna taa inayoning’inia, akaikwapua na kutumia kuangazia hatua zake kwenye korido hili jeusi.



    Akatembea kwa hatua nne, akasikia kishindo kizito cha miguu ya mtu. Akasimama upesi akiwa amekodoa macho. Akaanza kutetemeka. Akatetemeka zaidi alipohisi kuna mtu nyuma yake, mpaka taa ikaanza kutikisika!



    Moyo ukamwenda mbio. Maungio yake ya miguu yakaanza kukosa nguvu.



    Baada ya sekunde kadhaa, kule chumbani, Wisconsin pamoja na wageni wake wakaanza kuona mwili wa Brian ukiwa unahangaika kitini. Brian, akiwa bado amefunga macho yake, alikuwa anapapatika haswa akiwa ameshikilia koo lake. Mdomo aliachama, ulimi ulimtoka nje!



    Mama Brian akamtazama Wisconsin kwa mshangao, akamuuliza, “Ana nini?”



    “Atakuwa anakabwa!” Wisconsin akamjibu.



    “Mwokoe basi!” Mama Brian akaropoka akiwa amelowana hofu.



    Basi upesi Wisconsin akafanya jitihada za kumwamsha Brian kwa kumfukizia moshi zaidi, akapiga chafya kali na kufungua macho yake aliyoyatumbua kwa upana wote. Alikuwa anahema kwanguvu. Jasho lilikuwa linamchuruza. Anahema kana kwamba mbwa aliyekimbizwa.



    “Brian, uko sawa?” Mama akawahi kumuuliza. Brian akakohoa kwanza mara tatu kisha akavuta pumzi ndefu na kutikisa kichwa chake pasipo kutia neno.



    “Nini umeona huko?” Wisconsin akamuuliza. Brian alipoka vema akaeleza kila jambo, yale aliiyoyauliza toka kwa Kecie na yale aliyoyashuhudia yeye mwenyewe. Wisconsin akatikisa kichwa chake na kusema, “Basi kazi ni kubwa.”



    “Kwanini?” Brian akawahi kuuliza.



    “Kwa maelezo aliyokupatia Kecie, ni lazima mzizi wa nguvu za Helo zitakuwa duniani na si kwenye ulimwengu wa wafu. Inabidi mizizi hiyo ikatwe kwanza kabla ya kwenda kumkabili. Na hiyo ndiyo sababu wafu wenziwe hawawezi kummudu, yeye yu kwenye ulimwengu wa aina mbili, ule wa wafu na walio hai.”



    “Kivipi?” Brian alihisi kuchanganywa na maelezo hayo. Wisconsin kabla hajaeleza zaidi, akawataka watoke ndani ya chumba hicho kwani walishamaliza zoezi lao kwa muda huo. Waende wakapate chochote kitu tumboni na kuliwaza akili zao alafu, kama kutakuwa kuna haja, watarejea na kuendelea.



    Wakaenda zao sebuleni na yule mzee aliyewakarimu akaleta chakula kidogo cha kupasha matumbo yao. Wakiwa wanaendelea kula, Wisconsin akawa anawapa historia za mji huo wa kihistoria na tamaduni. Mambo aliyokuwa anayaongea hayakuenda na umri wake. Alionekana mdogo ukilinganisha na simulizi zake za kale.



    “Umezaliwa mwaka gani?” Mama Brian akamuuliza. Alitabasamu kwanza alafu akasema, “Nashangaza na habari zangu, sio?” Mama Brian akatabasamu pasipo kutia neno.



    “Uso wangu unaendana na umri wangu. Mimi si wa zamani sana, lakini nayapata kuyajua mengi sababu ya kukutana na watu kila uchwao, watu wa umri mbalimbali, watoto, wazee kwa vijana. Nao wananieleza mengi … mengine yakufurahisha, yakutisha na hata kuhuzunisha.”



    “Ulianza kazi hii lini?” Mama akaongezea swali.



    “Muda mrefu,” Wisconsin akajibu. “Tangu ujana wangu.” kisha aliposema hivyo akamtazama Mama Brian. “Nilitamani sana kuwa daktari nisaidie shida za watu za kimwili. Lakini nikiwa nasoma, nilikuja kugundua ni lheri ya shida za kimwili, zaweza kuonekana na kuthibitishwa kiwepesi, lakini vipi kuhusu zile za kiroho, ambazo haziwezi kuthibitishwa maabara? … watu wakihisi miili yao haipo sawa, huenda hospitali, lakini vipi si kama miili bali ni hisia ndizo huwasumbua, ni wale waliokufa, majini ama waliolaaniwa?” Wisconsin akaweka kituo. Macho yake yalikuwa yametuama kama mtu anayefakiri jambo. Mama Brian akamuuliza, “Ni hilo ndilo likakufanya uende kwneye taaluma hii?”



    “Ndio,” Wisconsin akajibu. “Haswa baada ya rafiki yangu mkubwa, Thompson, kukumbwa na tatizo hilo. Nilishuhudia namna alivyokuwa anateseka. Kila siku akiniambia anakabwa usingizini, anamwona mpenzi wake aliyefariki njiani kila asubuhi ajapo shule. Niliumia maana sikuweza kumsaidia. Sikutaka mtu mwingine ayapitie yale ambayo Thompson aliyapitia.”



    “Yuko wapi hivi sasa huyo Thompson?”



    “Amefariki.”



    “Aliuawa na huyo mpenzi wake?”



    “Hapana, aliamua kujiua mwenyewe. Alishindwa kuvumilia. Alinyonga kitanzi na kujitundika apate kujinusuru toka kwenye maisha ya tabu aliyokuwa anaishi.” Wisconsin alinywea sana akiyasema hayo. Japo kitu hicho kilitokea muda mwingi ulopita, bado lilimbakizia kovu kubwa moyoni mwake. Bado akilieleza ni kama vile limetukia jana tu.



    Akashusha pumzi ndefu na kukuna kichwa chake. Akanywa mafundo mawili ya kahawa alafu akamtazama Brian aliyekuwa ametuama muda wote huo, akamuuliza, “Ulikuwa rafiki mkubwa sana wa Kecie, sio?”



    Brian akatikisa kichwa na kusema, “sasa ndo’ nalijua hilo.”



    “Kwanini? Ulikuwa hujui toka kitambo?”



    “Sikuwa najua kwa namna hiyo. Kecie alikuwa ni rafiki yangu, rafiki mpenzi, ila nahisi kulikuwa na mwingine ambaye ndiye alikuwa rafiki yake mkubwa.”



    “Nani huyo?”



    “Faris. Anaitwa Faris. Hata wakati Kecie anapotea msituni, aliyemwona ni Faris.”



    “Faris?”



    “Ndio.”



    “Ni nani huyo? Yupo wapi kwa sasa?”



    “Alikuwa ni jirani yake pia rafiki yake. Tangu Kecie alipopotea, Faris amekuwa bubu, haongei chochote akaeleweka. Anaishi maisha ya ajabu sana. Ni kama vile mnyama maana hufungiwa chumbani akiwa ndani ya kamba.”



    “Mbona hukuniambia hilo hapo awali?” Wisconsin akastaajabu, akauliza, “anaishi wapi huyo Faris?”



    “Nje kidogo ya mji wa Boston, yeye na familia yake.”



    “Inabidi tukaonane nae. Ni muhimu!”



    “Kwanini?” Mama Brian akauliza upesi kisha akaongezea, “Sidhani kama wazazi wake hupenda kuwaona watu wakiwa wanawatembelea.”



    “Itabidi tufanye kila namna tuonane naye,” Wisconsin akasisitiza. “Faris atakuwa na jambo litakalotusaidia kumshida Helo. Yeye alikuwa mtu wa mwisho kumwona Kecie. Kuwa kwake bubu kunamaanisha kuna kiu hatakiwi kusema. Kuna jambo lililofanya akafumbwa mdomo. Inabidi tulijua jambo hilo.”



    “Tutalijuaje na yeye ni bubu?” Mama akaongezea swali lingine. Wisconsin akamtoa shaka. “Tutajua tu.” akasema pasipo kutoa maelezo yoyote ya ziada.



    “Tutafunga safari kumwendea punde jua litakaposimama katikati ya anga,” akasema na kisha akaenda zake chumbani akiwaacha wageni wake mezani.





    **



    Saa nane ya mchana …





    Wisconsin aliweka mkoba wake mweusi kwenye buti la gari kisha akajiweka ndani ya chombo hicho tayari kwa ajili ya safari. Dereva, Mama Brian, alikuwa tayari ameshakaa kwenye kiti chake. Kwenye viti vya nyuma walikaa watoto, Brian na Olivia.



    Chombo kikatiwa moto, wakahepa zao kushika barabara. Hawakutumia tena njia waliyokuja nayo bali ya ziada ambayo Wisconsin aliwaelekeza. Wakadumu kwenye gari kwa takribani masaa mawili kuelekea matatu kasoro tu dakika chache, wakawa wamefika mbele ya nyumba ya wakina Faris. Nyumba iliyojitenga na kuzingirwa na miti mirefu.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kulikuwa kimya. Giza lilikuwa limeshaanza kuingia, ila bado taa hazikuwa zimewashwa. Ni kama vile hakukuwa na mtu hapa. Mazingira yake hayakuwa yakuvutia.



    “Ndiyo hapa,” akasema Brian. Wakasongea mlango na kuugonga mara tatu, hakukuwa na majibu. Brian alitazama ndani hakuona kitu, taa zilikuwa hazijawashwa hivyo ilikuwa ngumu kuona.



    “Nadhani hawapo,” akasema Brian. Punde wakaona gari aina ya ‘pickup’ likiwa linasonga kuja eneo walilopo. Lilikuwa ni pickup ya zamani, iliyochoka. Taa yake moja tu ndiyo ilikuwa inawaka. Likaegeshwa, toka ndani akashuka bwana York na mkewe, wazazi wa Faris.



    Bwana York alikuwa amebebelea gobore akiwa amelishikilia katika namna ya kujilinda. “Ni wakina nani nyie?” akapaza sauti yake kavu. Hakuwa anaona vema. Alikuwa amekodoa haswa na kufanya uso wake utishe.



    “Ni sisi, majirani zako!” Mama Brian akajitambulisha.



    “Majirani? Majirani zetu ni miti tu! Ninyi ni wakina nani?” Bwana York akafoka. Mkewe ndiyo akamwambia kuwa ni familia ya wakina Brian, hivyo aweke silaha yake chini.



    “Mmekuja kufuata nini hapa?” Bwana York akauliza. Bado silaha yake alikuwa akiielekezea kule kwa wageni.



    “Tuna maongezi kidogo, tafadhali tunaomba mtuskize.”



    Mke wa bwana York akamtaka mumewe atulize munkari wawakaribishe wageni kwani wametoka mbali, si bure kuna jambo lililowafungisha safari.



    “Wanataka nini lakini?” bwana York akawaka. “Tulihama kwenye ule ulimwengu kuja kutafuta amani huku msituni, kwanini bado wanatufuata?”



    Mama Brian akamsogelea bwana York na kumweleza, “Tumekuja na mtaalamu. Anaweza kumsaidia Faris endapo wakimpa nafasi.”



    Bwana York akamtazama Mama Brian. Angalau sasa macho yake ya kizee yaliweza kumwona. Akamwambia akiwa amekunja uso wake, “Faris hayupo hapa.”



    “Yupo wapi?” Mama Brian akauliza.



    “Ameshakufa,” bwana York akamjibu kisha akatembea zake kwenda ndani. Mama Brian akamtazama mama yake Faris kwa mshangao, akamuuliza, “Ni kweli?”



    Mwanamke huyo akamtikisia kichwa. “Ndio. Ni kweli.” mara macho yake yakaanza kuwa mekundu, uso wake ukionyesha kulia.



    **

    .

    Akaongozana na wageni wake mpaka ndani alipowaketisha na kuwapatia vikombe vya kahawa kisha akawaeleza kilichomsibu Faris.

    .

    .

    “Hali yake ilikuwa mbaya zaidi. Alikuwa anadhoofika siku baada ya siku. Alikuwa anapiga kelele sana usiku na hakuwa anataka kumwona mtu yeyote,” Mrs York akaweka kituo na kufuta kwanza machozi yaliyokuwa yanammiminika. Pua yake ilikuwa nyekundu na mdomo wake mkavu.

    .

    .

    “Kila siku baba yake alikuwa ananisihi anataka kumuua lakini mimi nikiwa namkataza. Japo alikuwa vile bado sikutaka aondoke. Bado nilikuwa na matumaini huenda akaja kupita jaribu lake hilo, ila kila siku matumaini yalikuwa yanafifia. Hakuonyesha dalili yoyote. Kila siku ilikuwa ni mbaya zaidi ya iliyopita.

    .

    .

    Alikuwa anachanganyikiwa maradufu. Ndipo baba yake akalazimisha kuwa ampumzishe …” Hapa Mrs York akakabwa na kilio kwa muda. Ilimchukua kama sekunde tano kuendelea kuongea tena, “Alimpiga risasi mbili zilizomlaza mfu kisha tukaenda kumzika. Sasa akiwa amelala kwa amani.”

    .

    .

    Mrs York akiwa amebanwa na kwikwi, akaendelea kupambana na mito ya machozi. Roho yake ilikuwa inamuuma. Angalau alikuwa ameyasahau haya.

    .

    .

    “Tunaweza kuona mlipomzikia?” Brian akauliza. Pasi na hiyana, Mrs York akaongozana nao mpaka nyuma ya nyumba, huko wakalikuta kaburi la Faris. Wakaomboleza hapo,

    .

    .

    “Aliishi maisha ya tabu sana,” Mrs York akasema. “Maisha yake yalijawa na majeraha, kilio, hofu, masumbuko na mateso. Ni kheri hata akiwa amekufa kuliko maisha yale.”

    .

    .Mama Brian akamtazama Wisconsin na kumuuliza, “Sasa tutafanyaje na tuliyemfuata hayupo?”

    .

    .

    “Labda kuna mengine yanaweza kutusaidia,” akasema Brian

    akiwatazama mama yake na Wisconsin, kisha akamtazama Mrs York na kumuuliza, “Kwenye chumba cha Brian kuna chochote mlichobadili?”

    .

    .

    Mrs York akatikisa kichwa chake. “Tangu alipokufa, chumba chake tulikifunga na kufuli.”

    .

    .

    Basi wakaenda huko chumbani, Brian akimwambia Wisconsin kuwa Faris alikuwa akichora michoro kadha wa kadha kwenye mbao ya kitanda. Pengine picha hizo akizitazama, ataweza kugundua jambo.

    .

    .

    Wisconsin akachukua kioo cha kukuzia toka kwenye mkebe wake, kisha wakaelekea kwenye chumba hicho na kuanza kupembua kwa macho kingo zote za kitanda. Na hata kule ukutani ambapo Faris alikuwa amechorachora ama kuandika vitu ambavyo havijulikana maana zake.

    .

    .

    Wisconsin alinakili kwenye kijitabu chake kila jambo aliloliona, baada ya dakika kumi, akawa amemaliza zoezi lake hilo wakarejea sebuleni. Wisconsin akatoka tena kuuendea mkoba wake, akatoa kitabu fulani kikubwa na kuja nacho ndani.

    .

    .

    Akatumia karibu nusu saa kutazama kile kilichopo kwenye kijitabu chake na kufananishia na yale yaliyopo kwenye kitabu chake kikubwa alichotoa garini. Alipomaliza, sasa akawa amepata maana kamili.

    .

    .

    “Faris alikuwa anajua mambo mengi, ni ajabu hatukuyajua kabla ya kufa kwake. Alitamani kuyasema, lakini haikuwa inawezekana. Hata alipotumia alama, bado mlishindwa kuyajua.”

    .

    .

    Wisconsin akafungua ukurasa wa kwanza kabisa wa kijitabu chake kidogo, akaonyeshea ule mchoro wa msichana na mwanaume pembeni yake. Msichana na mwanaume njiti. Msichana akiwa ameshikilia mdoli wake mkononi.

    .

    .

    “Huu ndiyo ulikuwa mchoro wake wa kwanza kabisa. Mchoro wa kitu cha mwisho alichokiona pindi akiwa timamu. Huyu ni Kecie na hawa wanaume wawili, mmoja ni Helo, mwingine ni yule mwanaume aliyeuawa na familia ya Mrs Garett kwa ajili ya kuficha siri. Kwahiyo Faris alikuwa anamfahamu Helo. Alimwona kwa macho yake.

    .

    .

    Na huu ujumbe ambao umewekwa hapa kwenye huu mchoro ni ushahidi tosha kuwa Helo alimtaka Faris aungane nae kama ilivyokuwa kwa Kecie. Ujumbe huu umeandikwa kwa lugha ya kilatini ukimaanisha ‘kuwa wangu.’ kwahiyo Helo alijaribu kumshawishi Faris aende naye.”

    .

    .

    “Mbona sasa akabakia? Tena akiwa hawezi kuongea?” Brian akauliza kwa pupa.

    .

    .

    “Kwasababu aliweka agano na Kecie,” akajibu Wisconsin akionyeshea michoro kadhaa aliyoinakili toka kwa Faris. “Kwenye michoro hii ukiitazama vema utaona maneno ya kilatini yakimpa Faris kikomo. Helo aliweka agano na Kecie kuwa Faris atakuwa hai, ila akiwa salama zaidi kwake, ndiyo maana Faris alikuwa bubu.”

    .

    .

    “Na hiyo michoro mengine?” Mama Brian akauliza.

    .

    .

    “Kecie alikuwa anamtembelea Faris mara kwa mara. Unaweza kuona hapa … hapa … na hapa, na hata lile la watoto kupotea, Faris alikwishalifahamu, unaweza kuona mchoro huu, watoto wakiwa wamesimama na mwanaume yule mrefu.”

    .

    .

    “Aliyajuaje?” Mrs York akauliza. Wisconsin akamtazama Brian na kumuuliza, “Haujawahi kupata ishara yoyote toka kwa Kecie?”

    .

    .

    Brian akafikiri kidogo, mara akasema, “Nadhani nilikuwa napata ishara! Mara ya kwanza kabisa kabla watu hawajaanza kupotea, tuliona maneno fulani ya damu ukutani tukiambiwa tutazame mji wetu. Nakumbuka pia wakati Olivia anaondoka kuelekea msituni, nilisikia mtu anagonga mlango! Nilipoenda kutazama sikuona mtu bali nilihamaki Olivia akiishia!”

    .

    .

    “Hivyo tu?” Wisconsin akauliza. Brian akaendelea kusema, “nakumbuka tena jana, wakati mama akiwa amevamiwa na kukabwa, kabla ya kusikia chupa ikipasuka, nilisikia mtu akigonga dirishani mwangu mara tatu! Simjui mtu huyu ni nani, ila kila baada ya hapo napata kushuhudia jambo.”

    .

    .

    “Ni Kecie!” akasema Wisconsin. “Alikuwa anawatumia ninyi wote kuwapa ishara ya kile kilichokuwa kinatokea.”

    .

    .

    “Sasa kwanini Kecie hakumwambia Faris amwokoe? Badala yake Brian?” Mama Brian akauliza.

    .

    .

    “Kwasababu Faris asingeweza kumwokoa tena Kecie kwasababu ya agano waliloweka. Faris alibakiziwa uhai, kumbuka, kwasababu ya Kecie. Asingeweza tena kwenda kumwokoa, la sivyo agano lingetenguliwa!”

    .

    .

    “Sasa tunafanyaje?” akauliza Brian. “Tutamalizaje Helo?”

    .

    .

    “Unakumbuka nilikuambia kuwa nguvu za Helo hutokana na mihimili iliyokuwapo duniani?” Wisconsin akauliza, kabla hajajibiwa akaendelea, “Hata hilo Faris alikuwa analitambua.”

    .

    .

    “Ni mihimili gani hiyo?” Brian akawahi kuuliza kwa pupa. Wisconsin akaonyeshea kidole chake kwenye moja ya mchoro wa Faris. “Unaona huu mchoro, huyu mwanaume aliyesimama katikati ni Helo, unaweza kumtambua kwa namna ambavyo Faris amekuwa akimchora. Na hawa wawili kushoto na kulia kwake, ndiyo mihimili yake.”

    .

    .

    Brian na wenzake wakatazama hao watu wawili wakijaribu kuwang’amua. Mmoja wao Brian akamtambua upesi. “Huyu atakuwa ni padri Alfonso!” Kwenye mchoro mtu huyo alikuwa ana alama ya msalaba kichwani.

    .

    .

    “Na vipi kuhusu huyu?” Wisconsin akauliza akionyeshea ule mchoro wa mwanaume mwingine.

    .

    .

    “Huyu sijajua atakuwa ni nani,” akasema Brian. “Ila huyu Padri Alfonso hawezi kutusaidia kumpata huyo mwingine?”

    .

    .

    “Si rahisi kihivyo,” akasema Wisconsin. “Kumaliza hii mihimili haitakuwa kazi rahisi hata kidogo lakini kuwatambua ni nusu ya kumaliza kazi hiyo.”

    .

    .

    Basi walipomaliza zoezi lao hilo, wageni wakaaga wanaenda zao. Kwakuwa Mr York alikuwa chumbani amejifungia, Mrs York akawasindikiza wageni wao mpaka kwenye gari. Wakajipaki na kwenda zao. Yalikuwa ni majira ya saa tatu usiku sasa.

    .

    .

    Wakiwa kwenye gari wakawa wanakata misitu kwenda Boston. Walitembea kwa muda wa nusu saa. Kulikuwa kimya msituni lakini pia kiza.

    .

    .

    “Itabidi unipatie hifadhi kwa muda wote huo wa kazi,” Wisconsin alimwambia Mama Brian. Wote walikuwa wamekaa mbele, watoto wapo nyuma.

    .

    .

    “Ondoa shaka,” Mama Brian akamwambia. “Utakaa mpaka utakaponiambia tatizo limekwisha.”

    .

    .

    Mama Brian alipomaliza kusema hayo, mara gari likatikisika kana kwamba limekanyaga kitu. Mara kidogo taa zikaanza kufifia pamoja pia na mwendo. Mara likazima na kusimama!

    .

    .

    Ilikuwa ni katikati ya msitu. Mbele ni miti na nyuma ni miti!

    .

    .

    “Hapana! Hapana!” Mama Brian akalalama akipiga usukani. Hakuwa anaamini macho yake. Gari lazima msituni tena usiku kama ule, hatari iliyoje.

    .

    .

    “Sasa tunafanyaje?” akauliza.

    .



    Wisconsin na Brian walishuka toka kwenye gari na kuanza kulipekua gari wajue limepata shida gani. Matairi yalikuwa sawa, injini nayo ilikuwa sawa na hata kila kitu kilichokuwa kinaonekana kwa macho kwa wepesi vilikuwa sawa.

    .

    .

    Basi Wisconsin akalala na kutazama huko chini. Akisaidiwa na kurunzi akapekua huku na huko, hakuwa anaona jambo lolote. Akiwa anaendelea kuangaza, mara akaona miguu ya mtu ikiwa imesimama kwa upande wa pili! Hii haikuwa ya Brian. Ilikuwa ni miguu meupe pe. Miguu mipana na iliyokomaa.

    .

    .

    Wisconsin akastaajabu. Haraka akatoa uso wake chini atazame huko alipoona hiyo miguu, ajabu hakuona kitu. Brian akamuuliza, “Vipi?”

    .

    .

    Wisconsin akiwa ametoa macho akamuuliza, “Haukuona mtu yeyote hapo?” Brian akatikisa kichwa kukataa. Hakumwona mtu. Basi Wisconsin akadhani pengine ni macho yake. Akalala tena chini na kuendelea kutazama kama ataona hitilafu ya gari.

    .

    .

    Akiwa anaendelea kutazama, akaona tena miguu ya mtu! Mara hii haikuwa imesimama, bali inakimbia. Haraka akanyanyuka na kuangaza. Hamna mtu.

    .

    .

    “Haujaona mtu akikimbia?” akamuuliza Brian. “Hapana, sijaona!” Brian akajibu akirusha macho huku na kule. “Vipi, kuna nini?” Brian akauliza.

    Wisconsin kabla ya kujibu, akatazama kwanza pande zake zote, karibu na mbali. Hakuona chochote. Akamtazama Brian na kumwambia, “Nimeona mtu.” Brian akashtuka,

    .

    .

    “Yuko wapi?”

    .

    .

    “Nimemwona wakati nikiwa chini. Ajabu nikiamka, simwoni!”

    .

    .

    “Una uhakika?”

    .

    .

    “Ndio … Brian, turudi ndani ya gari.”

    .

    .

    Basi upesi wakarejea kwenye viti vyao.

    .

    .

    “Hamna shida,” akasema Wisconsin. “Gari lipo sawa.”

    .

    .

    “Sasa nini tatizo, mbona limezima?” akauliza Mama Brian kwa hamaki.

    .

    .

    “Nadhani tatizo litakuwa ni mambo mengine,” akasema Wisconsin. “Ila kwa upande wa gari, hamna tatizo.”

    .

    .

    Basi wakakaa hapo kwa muda wakiwaza namna ya kufanya. Hawawezi kulala ndani ya gari msituni. Muda ukazidi kwenda wasipate la kufanya. Wakakubaliana endapo wakiliona gari linakuja walisimamishe na kuomba msaada.

    .

    .

    Nusu saa ikapita, bado kimya. Kila mtu alikuwa ameegesha kichwa chake kwenye kiti kwa uchovu. Waliposikia sauti wakaangaza barabarani, hakuna kitu. Ni upepo tu ukicheza na matawi ya miti.

    .

    .

    Lisaa likapita, bado kimya. Sasa wakaanza kusinzia. Macho yalikuwa mazito. Walikuwa wamechoka mno na hakukuwa na soga za kuwafanya wakodoe.

    .

    .

    Wakiwa wamelala, baada ya muda fulani, Brian akajikuta akiwa amefumbua macho. Akatupa macho yake kutazama huku na huko ndani ya gari. Amah! Akastaajabu Olivia aliyekuwa amekaa naye pembeni hakuwapo! Nao mlango wa nyuma wa upande aliokuwa amekaa Olivia ulikuwa wazi.

    .

    .

    Akarusha macho yake kutazama. Hamaki akamwona Olivia akiwa anaishia msituni! Haraka akamshtua mama yake na Wisconsin waamke. Ajabu hawakuamka! Aliwasukumasukuma, aliwaita kwanguvu lakini waapi! Hawakuamka wala kushtuka. Ni kama vile walikula madawa ya kulevya! Kila Brian alipotazama msituni, Olivia aliendelea kuishia.

    .

    .

    Basi akatoka ndani ya gari na kukimbia upesi kwenda kumwokoa Olivia. Alimuita kwanguvu akiwa anamkimbilia. Olivia hakuwa anasikia, alikuwa anaendelea kutembea tena akiwa amefumba macho. Alikuwa umbali wa kama hatua thelathini na tano toka Brian alipo.

    .

    .

    Brian akakazana kukimbia. Alipomkaribia akamnyaka na kumkumbatia.

    .

    .

    “Olivia, uko sawa?”

    .

    .

    Ila aligundua Olivia ni wa baridi sana. Ni kama vile ni maiti na si binadamu. Akamtazama usoni, binti alikuwa amefumba macho. Akajaribu kumwamsha, haikuwezekana. Akaweka sikio lake kifuani mwa mtoto huyo, hakuwa anasikia mapigo yoyote yale! Akastaajabu.

    .

    .

    Aliporudisha macho yake usoni mwa Olivia, akastaabu mtoto huyo amefumbua macho! Macho yake yalikuwa meusi ti, na uso wake mweupe ulianza kuchipuka michirizi meusi.

    .

    .

    Brian akashtuka, Olivia akatabasamu. Nayo meno yake yalikuwa kana kwamba mkaa kwa uweusi, na yote yakiwa chonge. Kabla Olivia hajasema jambo, mdomo wake ukaanza kuchuruza udenda mweusi, na mara akanyanyua mkono wake wa kuume akitaka kumnyaka Brian.

    .

    .

    “Olivia, amka!” Brian akapayuka akiwa anasonga kurudi nyuma. Olivia akaongeza kasi ya miguu yake kumfuata.

    .

    .

    “Amka! Olivia, amka!” Brian akaendelea kuita lakini Olivia hakuwa anajali hata kidogo. Bado alikuwa anamsogelea Brian huku akiwa amenyoosha mkono wake wa kuume akitaka kumnyaka. Mwishowe Brian akajigota kwenye mti, Olivia sasa akamkaribia!

    .

    .

    “Hapana, Olivia! Hapana! Hapanaa!” mara Brian akapiga kelele kali sana, kule ndani ya gari Wisconsin akaisikia na kukurupuka. Kutazama nyuma, mlango ulikuwa wazi, na Brian hayupo! Olivia pekee ndiye kalala kwenye kiti.

    .

    .

    Upesi akamwamsha Mama Brian.

    .

    .

    “Brian ameondoka!”

    .

    .

    Basi haraka wakatoka na kwenda kumtafuta. Mama Brian akabebelea kurunzi, Wisconsin akibebebelea gongo kubwa. Wakawa wanaangaza huku na kule, wakijongea kwa woga na tahadhari.

    .

    .

    Mara wakasikia tena sauti ya Brian kwa mbali. Wakakimbilia huko upesi, wakamkuta Brian akiwa amelala chini pamoja na Olivia! Wakastaajabu. Mbona walikuwa wamemwacha Olivia kwenye gari!

    .

    .

    Mama akamnyakua Brian na kumweka kwapani, wakabaki wanamtazama Olivia.

    .

    .

    “Wewe ni nani?” Wisconsin akauliza akiwa ameshikilia gongo lake vema kwa tahadhari. Olivia hakujibu, bado alikuwa yu katika hali ya kutokuwa na fahamu. Wisconsin, akiwa amejikaza kisabuni, akamgusa Olivia kwa gongo lake. Mara akaanza kuonyesha ishara ya kuamka.

    .

    .

    Ila kabla hajatengemaa, Brian akawa amerejewa na fahamu zake kamili. Alipotazama na kumwona Olivia, akashtuka sana. Akasema akinyooshea kidole, “Huyo si Olivia! Si Olivia!” Wisconsin na Mama wakasonga nyuma kwa tahadhari.

    .

    .

    Olivia akanyanyua uso wake na kuwatazama. Alikuwa na uso wa Olivia tumjuae. Macho yake yalikuwa ya binadamu, pia uso wake mwekundu wenye kutia huruma.

    .

    .

    Akaita kwa sauti ya upole,

    .

    .

    “Brian.”

    .

    .

    Watu wote walikuwa wamekaa mbali wakimtazama kwa mashaka. Wisconsin alikwisha andaa rungu kwa kazi ya ziada.

    .

    .

    “Mbona nipo hapa?” Akauliza. “Tunafanya nini hapa?” uso wake ulikuwa umejawa na ndita za hofu na kukanganyikiwa. Macho yake punde yalianza kulowana maji.

    .

    .

    Brian akasema, “wewe si Olivia!” huku akitikisa kichwa. Alipomalizia kauli yake hiyo, wakasikia sauti ya honi barabarani! Honi ilipigwa mara tatu! Wakatazamana. Walidhani ni gari la msaada. Haraka wakaanza kukimbia kwenda kule barabarani. Olivia naye hakubakia nyuma, akaongozana nao akikimbia kadiri ya uwezo wake.

    .

    .

    Walipofika, hawakuona gari jingine isipokuwa la kwao. Ajabu lilikuwa limewaka taa na fyagio zake za kioo zikienda kushoto na kulia. Wakashangaa, “limewaka!”

    .

    .

    “Nani kaliwasha?” Mama Brian akauliza. Haraka wakaliendea na kutazama ndani kupitia madirisha, wakamwona Olivia! Alikuwa ameketi kwenye kiti cha dereva akitazama mbele kana kwamba anaendesha.

    .

    .

    "Olivia!” Mama akaita. Akajaribu kufungua mlango, haufunguki! Akapigapiga kioo kumshtua, hamna majibu. Olivia alikuwa anatazama mbele, akitabasamu, akipeleka usukani kushoto na kulia.

    .

    .

    “Mama,” Brian akaita. Alikuwa ameshaanza kupata hofu. Wisconsin alimshika Mama Brian mkono akamwambia, “Huyo si Olivia!” mara Olivia aliyekuwepo kwenye gari akageuza uso wake na kuwatazama. Ajabu uso wake ulibadilika ghafla na kuwa mweupe pe kama kitambaa. Michirizi meusi ikachipuka usoni. Macho yamekuwa meusi ti na fidhi zake zikajazwa na meno mithili miba.

    .

    .

    Mioyo yao ikawalipuka. Hakuwa Olivia! Mara gari likaanza kwenda. Olivia aliyekuwapo ndani akiangua kicheko haswa. Walilikimbiza lakini ikafikia pahala wakachoka, wakabaki wamesimama wakitazama gari layeya. Wanahema kama mbwa.

    .

    .

    Mara gari nalo likasimama, kama umbali wa hatua hamsini za mtu mzima toka walipo. Wakatazamana. Ila kabla hawajalijongea, wakamtafuta kwanza Olivia. Hakuwapo miongoni mwao.

    .

    .

    Walipotazama vema, kumbe walimwacha nyuma wakiwa wanalikimbilia gari. Taratibu alikuwa anakuja kwa kukimbia akiwa amechoka haswa, anaburuza miguu.

    .

    .

    Lakini kabla hajawafikia, nyuma yake, kwa mbali, walimwona kuna mtu anamjia. Mtu mrefu mweusi. Hawakujua mtu huyo ni nani, ila alikuwa anakuja kwa kasi mno! Mioyo ikawalipuka.

    .

    .

    Brian akapayuka, “Olivia, kimbia!” lakini Olivia hakuwa anaweza kukimbia tena zaidi ya pale. Miguu yake haikuwa na uwezo huo tena.

    .

    .

    Na mtu yule nyuma yake alikuwa anakaribia kwa mafungu na mafungu. Basi Brian akajikuta anaanza kukimbia upesi kumwendea Olivia. Alikuwa akikimbia huku akiita. Alipomfikia akamnyaka mtoto huyo na kuanguka naye chini. Yule mtu aliyekuwa anamkimbiza, akapita vuuup kama kivuli! Haikuonekana tena ameelekea wapi. Alipotea kana kwamba mwanga wa umeme ukizima.

    .

    .

    Wisconsin na Mama Brian wakasonga karibu. Wakamnyanyua Brian na Olivia toka barabarani. Mama akamtazama Olivia kwa kumkagua, “Upo sawa?”

    .

    .

    Olivia akatikisa kichwa. “Ndio, niko sawa.” uso wake ulikuwa na woga sana. Alimkumbatia Mama Brian kwanguvu akilia.

    .

    .

    “Nyamaza, Olivia. Yatakuwa sawa, usijali,” mama akamtuliza. Akambusu kwenye paji lake la uso na kumyanyua kumweka kwenye nyonga yake. Wakajongea gari na kukwea, wakaliwasha na kutimka zao. Gari halikuwa na shida tena kama hapo awali.

    .

    .

    “Inabidi tumalize kazi ndani ya siku tatu tu,” akasema Wisconsin. “Endapo siku hizo zikizidi, tutakuwa katika hatari ya kupoteza maisha.”

    .

    .

    “Kwanini?” Mama Brian akauliza.

    .

    .

    “Punde tutakapoanza kushughulika na mihimili, kazi itakuwa kubwa sana. Kama vita hiyo ikizidi zaidi ya siku tatu basi ni wazi tutakuwa tumeshindwa. Ni siku tatu tu zimebaki tangu mwezi kupevuka kuwa kamili. Inabidi tutumie siku hizo, vinginevyo itatuwia vigumu.”

    .

    .

    Basi baada ya maneno hayo hakukuwa na soga zinginezo. Kulikuwa kimya tu. Bado watu walikuwa na mashaka, wakawa wanatazama huku na kule madirishani wakiomba wafike salama.

    .

    .

    **

    .

    .

    Saa tatu asubuhi …

    .

    .

    Kilikuwa ni kipindi cha pili, somo la Jografia. Ingawa Brian alikuwa darasani, akili yake ilikuwa mbali sana. Alikuwa anamtazama mwalimu, ungeweza kudhani yupo makini, lakini akili yake ilikuwa kwenye masumbuko.

    .

    .

    Alikuwa anawaza mambo yaliyotukia jana, lakini zaidi alikuwa anawaza kumhusu yule mhimili wa pili baada ya Padri Alfonso. Atakuwa ni nani? Akaweka tama akiendelea kuwaza.

    .

    .

    Muda si mrefu, akamwona kuna mtu anaingia darasani . Hakumwona mtu huyo ni nani, ila alikuwa ni mwanaume aliyekuwa amevalia koti refu jeusi na kofia. Alimnyookea mwalimu na kuongea naye kidogo wakinong’ona. Brian akawatazama kwa umakini.

    .

    .

    Walizungumza kwa kama dakika moja wakipeana ishara ya kutikisiana vichwa kwa kuelewana. Punde kidogo katika maongezi yao, wakiwa wananong’ona, wakataja jina la Brian! Brian akaduwaa. Hakusikia maneno yote yale waliyokuwa wanayazungumza isipokuwa lile jina lake tu.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Akajiuliza ni nini mwalimu wake na yule mgeni asiyemjua walikuwa wanaongelea mpaka kumtaja? Mara maongezi yao yakakoma, walinyamaza kwa kama sekunde mbili, alafu wakageuza nyuso zao kumtazama Brian. Kisha wakatabasamu.

    .

    .

    Brian akapigwa na kofi la hofu. Yule mwanaume mgeni alikuwa ameziba uso wake kwa rangi nyeupe na nyekundu hivyo hakuwa anatambulika. Mwalimu naye alikuwa amegeuka uso wake ukiwa unatisha kusivyo kawaida.

    .

    .

    Katika namna ya ajabu, wakiwa wanatembea kana kwamba wanapelekwa na umeme, wakaanza kusonga kumfuata Brian! Walikuwa wamekodoa macho na mikono yao wameinyoosha kumkamata kijana huyo.

    .

    .

    Brian akapatwa na woga sana. Akajibania ukutani kwanguvu akijikunyata. Akafumba macho na kukunja uso wake kwa hofu. Punde akahisi mkono wa baridi ukiwa umemkamata, akapiga kelele kali.

    .

    .

    “Brian!” mwalimu akaita. Brian alipofungua macho, akamwona mwalimu wake akiwa amesimama kando. Ndiye yeye alikuwa amemshika. Hakukuwa na mtu mwingine pamoja naye! Darasa zima lilikuwa limetulia, wanafunzi wote wanamtazama.

    .

    .

    “Brian, una shida gani?” mwalimu akauliza akimtazama kwa ukaribu. “Uko sawa?”

    .

    .Brian akakwapua mkoba wake na kwenda nje ya darasa. Akaketi nje kwenye benchi akiendelea kuwaza kile alichokiona. Alihisi anachanganyikiwa. Aliona atoke mazingira hayo ya shule aende kuliwaza akili yake huko nje.

    .

    .

    Akatembeatembea akiwa amedumbukiza mikono yake mfukoni. Akatazama magari na makazi ya watu. Akatazama wapita njia na anga, angalau akili yake ikapumzika. Hapo ndiyo akapata wazo la nini cha kufanya.

    .

    .

    Upesi akaanza kutembea akielekea upande wa mashariki na ilipo shule yao. Baada ya kutembea kwa kama dakika nane tu, akawa amefika mbele ya ofisi kubwa ya mtaa waishio. Hapo akatoa karatasi kadhaa kwenye mkoba wake na kuzishika mkononi. Zilikuwa ni karatasi zenye nembo na jina la shule yake.

    .

    .

    Akazama ndani ya ofisi, akajitambulisha kwa majina na kusema haja yake kwa dada wa mapokezi ya kuwa amekuja kufanya ‘projekti’ fupi kama mojawapo ya kazi walizopewa huko shuleni.

    .

    .

    “Sitachukua muda wako, dakika tatu zinanitosha kabisa. Nahitaji kufahamu tu watu ambao wamefanya kazi kwa muda mrefu sana hapa ofisini, kujua idadi yao ili tuone ni namna gani vizazi tofauti vinavyofanya kazi kwa pamoja,” akajieleza Brian akijitahidi kutopepesa macho yake. Basi yule mdada wa mapokezi akamtazama kidogo kisha akatikisa kichwa, “Nyie wanafunzi huwa wasumbufu sana …” akasema huku akiwa anafungua droo yake. “Mkija hapa hamjui kama watu wana kazi zao, nyie mnataka tu mfanyiwe ya kwenu mwende!”

    .

    .

    Akafunga droo na kumpatia Brian karatasi kadhaa, Brian akaanza kuzipitia kwa wepesi. Alichukua muda mfupi sana, dakika moja tu, akayarejesha.

    .

    .

    “Umemaliza?” akauliza dada wa mapokezi akistaajabu. Brian akatabasamu, “Ndio, ahsante.” akanyanyuka na kutoka ndani ya ofisi. Akatembea upesi kuelekea getini, ila kabla hajatoka, akakutana na Brewster. Mzee huyo alikuwa ametoka kubandika matangazo ya watu wengine waliopotea kwa usiku wa jana. Alimtazama Brian kisha akamuita kwa sauti yake kavu. Brian akahofia.

    .

    .

    “Hujambo?” Brewster akasalimu akisogea karibu.

    .

    .

    “Sijambo.”

    .

    .

    “Mama yako anaendeleaje?”

    .

    .

    “Vizuri.”

    .

    .

    Brewster akanyamaza kwa muda kidogo akiwa anamtazama Brian. Akamsogelea karibu zaidi.

    .

    .

    “Brian, usije tena ukaingia nyumbani kwangu pasipo ruhusa, sawa?”

    .

    .

    Brian akameza mate pasipo kusema jambo.

    .

    .

    “Tumeelewana?” Brewster akauliza tena akimkodolea macho Brian.

    .

    .

    “Mimi sikuingia kwako,” Brian akajitetea. “Sijui ni nini unazungumzia.”

    .

    .

    Brewster akatabasamu na kuuliza, “Brian, unadhani kuna kitu unaweza kufanya ukanificha?” kabla Brian hajajibu, Brewster akaongezea, “Natambua kila jambo, Brian. Mimi si mzee wa kawaida kama unavyowaza.”

    .

    .

    “Najua!” Brian akasema akitikisa kichwa. “Najua wewe si mzee wa kawaida.” Brewster akatabasamu kusikia maneno hayo kisha akasema, “Ni vema umelitambua hilo. Kuwa makini basi.”

    .

    .

    “Nishakuwa makini,” akajibu Brian kisha akaondoka zake. Hakujua amepatia wapi nguvu ya kumjibu Brewster namna ile. Moyo wake ulikuwa unapiga lakini akijikaza kisabuni.

    .

    .

    .**

    .

    .

    “Nimeshajua ule mhimili mwingine wa Helo!” akasema Brian, Wisconsin na Mama yake wakimtazama. Walikuwa wameketi sebuleni katika majira haya ya jioni ya saa kumi na moja.

    .

    .

    “Brian!” Mama akamkatiza mwanaye. “Usiniambie ni Brewster!”

    .

    .

    “Ndio! Ni yeye!” Brian akasisitiza.

    .

    .

    “Sikia, Brian. Najua unamchukia Brewster, ila si kiasi hiko! Tafadhali.”

    .

    .

    “Mama, si kwamba namchukia, hapana! Nimethibitisha kabisa. Brewster ndiye yule mhimili wa pili. Tazama … Helo, Hernandez Lorenzo, alikuwa ni mtu mwenye asili ya latini. Jina lake linaeleza vema juu ya hilo, hata pia kwa Padri Alfonso, jina lake ni ushahidi. Lina asili ya kilatini.”

    .

    .

    “Sasa vipi kuhusu Brewster?” Mama akauliza. “Nalo lina asili ya Latini?”

    .

    .

    “Hapana. Leo nilienda kufuatilia kule kazini kwa Brewster, ofisi ya mtaa, nikagundua kuwa jina lake la mwisho ni lenye asili ya Latini, nalo ni Lorenzo! Kwa ufupi Brewster huitwa Brelo. Mpaka hapo kutakuwa kuna shaka juu yake?”

    .

    .

    Wisconsin aliyekuwa anakuna kidevu chake akaguna. “Ni bayana atakuwa anahusika. Ila watu hawa wawili watakuwa wana mahusiano gani na Hernandez?” akauliza.



    “Ni lazima watakuwa wana mahusiano fulani, mlishawahi kuwaona wakiwa pamoja?” Wisconsin akauliza.



    “Hapana!” Mama Brian akajibu kisha akamtazama Brian, naye Brian akaunga mkono hoja ya kuwa hawajawahi kuwaona watu hao pamoja. Wisconsin akabidua mdomo wake kwa kutafakari. “Pengine huwa wanakutana tusifahamu,”



    “Labda,” Mama Brian akaunga mkono hoja. Wisconsin akawakumbusha tena ya kwamba wana siku tatu tu za kufanya maamuzi na kumaliza kazi kwahiyo basi wataanza kutumia usiku wa siku hiyo kuanza kukaribia lengo lao.



    “Leo itabidi twende kanisani,” akasema Wisconsin kisha akamtazama Brian. Akarudia kusema, “Leo itabidi twende kanisani.”



    “Kufanya nini?” Brian akauliza.



    “Kufanya upekuzi,” Wisconsin akajibu. “Itabidi tuwatembelee watu hao kwa njia ya nyama na ya kiroho pia. Inabidi tujue mazingira yao kwanza kabla ya kukabiliana nao … kiuhalisia bado hatujajua upande upi ni wadhaifu zaidi.”



    “Kwahiyo leo tutaenda kwa mtindo gani?” Akauliza Brian. Wisconsin akamjibu, “Kwa nyama … kwa miili yetu ya kawaida.” Brian akaridhia lakini ikiwa wazi kuwa ametwaliwa na hofu. Wisconsin akasimama na kwenda zake akimtaka, itakapofika majira ya saa tano usiku, wawe tayari kwa ajili ya safari.



    Basi kama wasemavyo kuwa muda husonga zaidi ukiwa unangoja, nao ukawadia kwa upesi, Wisconsin akamtaarifu Brian, ambaye alikuwa yu tayari, waende zao. Walikuwa wamebebelea kurunzi na silaha baridi, mathalani chepeo dogo la kufytua na panga ambavyo walivitia kwenye begi. Lakini pia kwa kuficha nyuso zao, wakabebelea pia barakoa kisha wakaelekea eneo husika.



    Wakiwa wamebebelea kila aina ya tahadhari, wakarusha macho yao wakiwa wamejibana kwenye ukuta wa kanisa. Kulikuwa kimya, mazingira yalikuwa tulivu kabisa. Ndani ya kanisa taa zilikuwa zinawaka pia vilevile kwenye makazi yanayopakana na kanisa, yaani ya watumishi, nayo yalikuwa kwenye mwanga. Mbali na hapo maeneo mengine yalikuwa kizani.



    Ndani ya kanisa kulikuwa kuna watu wawili wakiwa wanafanya usafi, wote walikuwa ni wanawake waliovalia nguo nyeusi. Mbali na hapo hapakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa anaonekana machoni.



    “Sasa tunaendea wapi?” akauliza Brian. Wisconsin akapekua kwanza eneo kwa macho yake mepesi alafu akasema, “Tutaenda mule kutazama!” kidole chake alikionyeshea kwenye stoo ya kanisa.



    Wakangoja punde, wafanya usafi wale wakamaliza kazi yao na kufunga milango ya kanisa kisha kujiendea zao. Sasa wakasonga langoni, wakakuta kumefungwa.



    “Sasa?” Brian akauliza. Mara Wisconsin akatoa ‘plies’ yenye meno ya ncha kali, akamega kitasa wakazama ndani. Kulikuwa giza, taa zilizimwa. Na kwa usalama wao, hawakuziwasha, wakanyookea moja kwa moja kule stoo. Wakawasha kurunzi zao na kuangaza.



    Wakiwa humo wanaendelea na upekuzi, kwenye moja ya nyumba ya watumishi wa kanisa, mwanaume mmoja akaona mwanga kwenye dirisha la juu la chumba cha stoo. Mwanaume huyu alikuwa mpana mwenye mustachi na nywele za kahawia. Alikuwa ni kasisi.



    Alipata shaka kuona mwanga ule, akatazama majira yake na kuona si sawa. Aliporudisha tena macho kule stoo, akaona mwanga huo ukiwa wafifia na mara kukua, akagundua ni kurunzi. Hapa akapata shaka zaidi. Basi kutibu nafsi yake, akatoka ndani akatazame huko kunani.



    Akabebelea gongo mkono wake wa kuume na kutembea upesi kuendea kanisa. Alipofika, akaona sababu ya yeye kuwa na shaka zaidi, kwani aliukuta mlango ukiwa umevunjwa. Akawasha taa na kuangaza. Hamna kitu.



    Akaanza kujongea kuelekea stoo akitembea kwa staha. Alipofika napo akawasha taa, hamna kitu. Alitazama vema akaona vitu vikiwa vimeparanganyika kuashiria kuwa viliguswa. Akapata na maswali, yu wapi mvamizi huyo?



    Mara akasikia sauti ya kishindo cha mtu nyuma yake, akatazama upesi. Huko napo hakuona kitu, lakini pale madhabahuni akaona joho la madhabahu likiwa linacheza, basi akahisi hapo pana mtu. Akasonga.



    Alipofika akafungua upesi, akamwona Brian, lakini kabla hajafanya jambo, akastaajabu amekitwa kichwani, akadondoka kupoteza fahamu. Lakini kinyume na matarajio, akatiririka ngazini na kujikita kichwa. Hamaki akafa!



    Wisconsin na Brian wakapata mshangao haswa, nini wafanye? Basi kwa kufikiria upesi, wakambeba kasisi yule na kumtoa nje waende kumtupia huko. Kwakuwa kulikuwa na giza, hawakuonekana, wakafika korongoni na kuumwagia huo mwili.



    Ila kabla hawajaenda, Wisconsin akaona jambo. “Ngoja!” akamwambia Brian akimshika bega. Akamulika kule korongoni kisha akasema, “Twende kule!”



    “Kufanya nini huko?” Brian akauliza. Wisconsin hakujibu, badala yake akaongoza safari kwenda huko. Brian akaongozana naye na ajabu baada ya muda kidogo wakajikuta ndani ya korongo kubwa ambalo hawakuwazia kuwapo. Korongo hilo lilikuwa linaelekea msituni zaidi na zaidi.



    Wakalifuata na kutazama wakitumia kurunzi yao. Walipotembea kwa takribani dakika sita, wakaona mwili wa mwanamke mmoja ukiwa umetupiwa huko. Wakautazama, hawakuwa wanautambua. Wisconsin akaupiga picha mwili huo kwa kutumia kamera yake ya kizee, kisha wakaendelea kutazama kwa kusonga mbele.



    Lakini Brian hakuwa ameridhia kabisa juu ya hili. Hakuwa anataka waende mbele zaidi maana alikuwa amejawa na hofu kubwa. Kia hatua waliyokuwa wanapiga kusonga mbele ilimfanya aogope zaidi na zaidi.



    “Wisconsin!” Brian akaita na kusema, “Turudi nyumbani.”



    “Brian, umeanza woga saa hii?” Wisconsin akastaajabu. “Kama waogopa bonde hili, tutapanda hayo ya mbele?” Basi Brian akapiga moyo konde, wakaendelea kusonga. Lakini sasa kila walipokuwa wanazidi kwenda mbele wakawa wanaona maiti zaidi na zaidi! Wisconsin alizipiga picha, mwishowe akachoka.



    Walistaajabu wingi wa maiti zile, haswa juu ya nani ambaye amewaua wote hao? Na kwasababu gani? Wakaendelea kusonga zaidi na zaidi wakizama msituni, ila punde Brian akamshika Wisconsin mkono na kumwambia, “Ebu mulika kule!” ulikuwa ni upande wao wa kushoto umbali wa hatua kama kumi na tano za mtu mzima.



    Wisconsin akamulika. Hakukuwa na kitu.



    “Vipi, Brian?”



    “Niliona mtu kule … mtu amesimama!”



    “Una uhakika?” Wisconsin akauliza akirejesha kurunzi yake eneo aliloambiwa na Brian.



    “Ndio, nina uhakika! Nimeona mtu kule.”



    “Pengine macho yako, tumalizie kisha tuondoke zetu upesi!” Wisconsin akashauri. Ila kabla hawajasonga tena, Brian akamwona mtu upande wao wa kulia. Alikuwa ni mwanaume mrefu mweusi. Hakuwa anaonekana vema. Brian akamshtua Wisconsin na kumwambia amemwona mtu kule.



    Wisconsin alipomulikia kurunzi, ajabu kurunzi ikazima! Akaipigapiga kiganjani, haikuwaka! Na sasa hapo ndipo yeye aliposhuhudia kuwa kweli kule alipoambiwa atazame, kuna mtu! Akahangaika sana na kurunzi, hatimaye ikawaka.



    Akamulikia huko, ajabu hawakumwona mtu!



    “Tuondoke!” Wisconsin akasema akitangulia. Wakaanza kukimbia upesi kutoka eneo hilo. Ila kabla hawajafika mbali, kurunzi ikazima kabisa! Wakawa hawaoni pa kukanyaga. Ubaya hata mbalamwezi nayo haikuwapo kuwaangazia.



    Wakawa wanaenda kipofu wakikanyaga miili ya watu. Wakidondoka na kuanguka. Wakipepesuka na kukazana. Wakiwa wamejawa na hofu kuu vifuani mwao.



    Punde nyuma yao wakaanza kuhisi kuna mtu yuaja. Walisikia kishindo kikali kikitembea kwa kasi. Na ndani ya muda mfupi, Brian aliyekuwa nyuma, akadakwa bega lake na kuvutwa kwanguvu. Akapiga kelele kali akidondoka chini!



    “Brian!” Wisconsin akaita. Hakuwa anaona kinachoendelea ila akisikia sauti ya mtu akiburuzwa na kugugumia kwa kufungwa mdomo. Akarudi kiupofu akikodoa macho yake akitamani kumwokoa Brian.



    “Brian!” Wisconsin akaita kwa hofu. “Upo wapi?” sauti ya Brian akigugumia ikaendelea kufifia ikipotelea. Ghafla mwanga mkali mweupe ukamulika na kumfanya Wisconsin afiche macho yake kwa maumivu. Mara akasikia amri, “Mikono juu! Tulia vivyo hivyo!”



    Akiwa amefichama macho yake dhidi ya mwanga mkali, akayatupa nyuma yake kumtafuta Brian. Bahati akamwona kijana huyo akiwa chini, naye amejikinga na mwanga mkali uliokuwa unawamulika.



    .

    Wakasikia mtu yule anayewamulika akiwajongea. Walikuwa wamesimama tuli, mtu huyo aliposonga karibu zaidi yao ndipo wakagundua alikuwa ni polisi, akiongozana na Dada mmoja mnene ndani ya sare yake.

    .

    .

    Polisi akawaamrisha waondoe barakoa zao upesi na wanyooshe mikono yao juu, lakini swala hili likawa gumu. Wisconsin hakuwa radhi kutii agizo hilo, hata Brian naye alisita kulitenda. Walizihitaji barakoa zile kwenye nyuso zao. Polisi akarejea amri yake kwa nguvu, “Ondoa barakoa hizo!” akiwa amewaonyeshea mdomo wa bunduki.

    .

    .

    Polisi huyu alikuwa mnene kwa umbo, mfupi. Amevalia kofia, uso wake umekatwa na mustachi mwembamba.

    .

    .

    Mara Wisconsin akaigiza kubanwa na kikohozi. Akakohoa kwanguvu akiwa amedaka kifua chake kwa maumivu. Polisi akazubaa. Haraka Wisconsin akainyaka bunduki ya polisi kwa mkono wake wa kuume, mrefu wenye nguvu, akaivuta na kumkandika nayo Polisi kwenye paji lake la uso, Polisi akadondoka chini kama kifusi!

    .

    .

    Wisconsin akafoka, “Kimbia, Brian!” kisha wakaanza kukimbia upesi ndani ya msitu. Wisconsin aliitupa bunduki ya polisi wakiwa huko njiani, wakatokomea.

    .

    .

    “Upo sawa?” Dada akamuuliza Polisi aliyekuwa anaugulia kwa maumivu huku akimsaidia kunyanyuka.

    .

    .

    “Niko sawa, wapi wameelekea?” Akauliza Polisi akiangazaangaza. Paji lake la uso lilikuwa jekundu. Dada akamwonyeshea upande, na mara mwanaume huyo akaanza kukimbia kwenda huko. Mwili wake ulikuwa mzito sana, alipokimbia kwa hatua kadhaa akajihisi kuchoka!

    .

    .

    Alisimama akahema kama mbwa. Alimradi alipata silaha yake, basi akaona hamna haja ya kukimbizana na wahalifu. Kwa msaada zaidi akawataarifu wenziwe kwa kutumia ngowe ya mawasiliano kisha akarejea kumkuta Dada.

    .

    .

    “Twende!” akamwambia akiongoza njia.

    .

    .

    “Umewaacha wauaji waende?” Dada akastaajabu.

    .

    .

    “Sitaweza kuwapata humo msituni,” akasema Polisi alafu akageuka na kumtazama Dada. Bado alikuwa anahema kana kwamba mbweha. Akamwambia, “Usijali, tutawapata tu. Nimeshawatarifu wenzangu. Bils shaka ndani ya muda mfupi watakuwa wameuzingira msitu huu kwa ajili ya doria.”

    .

    .

    Kabla Dada hajatia neno, Polisi akamuuliza, “Ulikuwa una taarifa yoyote juu ya miili ya watu hawa iliyotupwa huku?”

    .

    .

    Dada akatikisa kichwa chake na kusema, “Hapana. Sikuwa najua chochote. Kama isingekuwa nimeona damu kule kanisani nikafuatilia, basi hata sasa nisingekuwa najua kama eneo hili lina maiti za watu.”

    .

    .

    “Una uhakika?” Polisi akauliza akimkazia macho Dada. “Ndio, nina uhakika!” Dada akajitetea, naye akiwa ametoa macho.

    .

    .

    “Unajua ni miili mingi,” Polisi akasema. “Inakuaje ukashindwa kutambua?”

    .

    .

    Dada akajibu, “Sina taratibu ya kuja huku korongoni. Hamna mtu yuaja huku.” Polisi akaguna na kusema, “Mna kesi ya kujibu ninyi nyote. Lazima mtoe maelezo yenye kuleta maana.”

    .

    .

    Baada ya kusema hayo, Polisi yule akasonga zake mbele kutoka humo korongoni, nyuma yake Dada akimfuata. Akapiga hatua tatu, mara kurunzi lake lenye mwanga wa fujo likazima!

    .

    .

    “Pumbavu!” akalaani. Sasa kulikuwa giza kabisa hata kuonana ni ngumu! Alipigapiga kurunzi lakini haikuwaka abadani, akastaajabu ni nini shida. Betri zilikuwa nzima, nayo kurunzi ilikuwa mpya tu.

    .

    .

    Akiwa anahangaika na kurunzi hiyo, mara Dada akapiga kelele ghafla akisema, “Kuna mtu!” Polisi akarusha macho yake kutazama kule alipoonyeshea Dada, hakuona kitu! Akauliza, “Ni nini shida yako?”

    .

    .

    “Nilimwona mtu kule!” Dada akajibu.

    .

    .

    “Na giza lote hili?” Polisi akauliza akikejeli, kisha akasema, “Ebu twende. Fanya upesi!” wakaendelea kutembea wakienda kwa makisio. Wakatembea kwa hatua tano tu, mtu yule ambaye Dada alimwona, mrefu mweusi, akajiri tena kandokando yake! Dada akapiga kelele kali.

    .

    .

    Polisi alipogeuza shingo yake kutazama, akastaajabu amedakwa koo na kuchanwa. Akavuja damu lukuki akikoroma kuelekea kifoni. Mikono yake iliyomziba koo ikajawa na damu pomoni. Akiwa anatetemeka, akadondoka chini na kufa.

    .

    .

    Dada akapiga kelele za woga. Naye punde akazabwa kibao kikali, akapaa na kudondokea mbali kama gunia la mkaa. Kabla hajajigeuza, miguu ya muuaji ikawa imemfikia kwa ajili ya kumaliza kazi.

    .

    .

    **

    .

    .

    “Mpo sawa?” Mama Brian akauliza. Wisconsin na Brian wakazama kwanza ndani na kujitupia kochini ndipo kumjibu. Punde huko nje gari la polisi likakatiza na king’ora chake.

    .

    .

    Wisconsin na Brian walikuwa wamechoka mno. Wanahema kwanguvu. Walipata wasaa mchache wa kuvuta pumzi zao kisha ndiyo wakaendelea na maongezi.

    .

    .

    “Tumefanikiwa … kwa kiasi chake,” Wisconsin akaeleza. Mara hodi ikagongwa mlangoni. Punde kidogo Mama Brian akaenda kufungua mlango.

    .

    .

    “Habari yako?” alikuwa ni Polisi. Kwa idadi walikuwa wawili, mmoja yu karibu na mlango, mwingine yu kwa nyuma kidogo.

    .

    .

    “Safi,” Mama Brian akajibu na kuuliza, “Kuna shida yoyote, afisa?”

    .

    .

    “Haujasikia au kuwaona watu wowote wakikatiza muda huu?” Polisi akauliza huku mikono yake akiishikisha mkanda wake mpana wenye kifuko cha kuhifadhia bunduki ndogo.

    .

    .

    “Watu? …” Mama Brian akatahamaki. “ Hapana! Sijawaona.



    “Mbona upo macho mpaka muda huu?” Polisi akauliza. Mama Brian akatazama eneo lote la jirani, ni nyumba yake tu ndiyo ilikuwa mwangani. Akatabasamu kidogo na kusema, “Nilikuwa natazama maigizo kwenye runinga mpaka sasa.” Polisi akatupa macho yake ndani kuangaza. Hakukuwa na mtu isipokuwa viti vitupu tu.



    Akauliza. “Unaishi na nani?”



    “Wanangu wawili, wa kike na kiume,” Mama Brian akajibu.

    .

    .



    Polisi akauliza, “Hao pekee?” Mama Brian akajibu, “Ndio, hao pekee.”

    .

    .

    “Una uhakika?” Polisi akauliza akimkazia macho.

    .

    .

    “Ndio, hao pekee!” Mama Brian akastaajabu akisema, “Najua watu nikaao nao.”

    .

    .

    “Tunaweza pekua ndani?” Polisi akamuuliza, asingoje ruhusa akazama ndani akifuatiwa na mwenziwe, wakaanza kupekua ndani. Sebuleni wakaona viatu vya kiume pea mbili vikiwa vimejawa na matope.

    .

    .

    “Vya nani hivi?” Polisi akauliza.

    .

    .

    “Vya mwanangu!” Mama Brian akajibu. Moyo wake ulikuwa umeanza kukita upesi. Alijawa na woga. Polisi alivichukua viatu hivyo na kuvinusa, akaviona vina joto kumaanisha vimetoka kuvaliwa muda si mrefu. Hakusema jambo, wakaendelea kupekua mule ndani sehemu moja baada ya nyingine wakianza na jikoni.

    .

    .

    Walipoelekea vyumbani, Mama Brian akapata shaka zaidi. Alifichama kinywa chake kwa mkono akiwa ametoa macho. Alijua ameshakwisha. Nini atafanya Brian na Wisconsin wakitiwa nguvuni?

    .

    .

    Chumba cha kwanza, Polisi wakamkuta Olivia akiwa kitandani amelala. Wakatazama uvunguni na kufungua makabati kuangaza, hawakuona kitu. Basi wakatoka na kuendea chumba cha pili. Huko wakamkuta Brian akiwa amejifunika shuka, amelala. Tena akikoroma na kuacha mdomo wake wazi kana kwamba mtu aliyelowea usingizini.

    .

    .

    Polisi wakatazamana alafu mmoja wao, yule kimbelembele, akafunua shuka la Brian kumkagua miguu. Brian alikuwa amevalia suruali ileile aliyotoka nayo msituni, ilikuwa imejawa na matope. Polisi wakapata shaka juu yake. Lakini kabla hajamwamsha, polisi mmoja, yule akaae nyuma, akasema, “Tazama!”

    .

    .

    Mwenzake akageuka upesi kutazama. Ilikuwa ni dirishani. Wakasonga na kutazama vema, huko wakaona watoto wawili wa kike wakiwa wanatembea kana kwamba watu waliovunjikwa na viungo. Wamefumba macho wakitembea kwa upofu.

    .

    .

    “Wapo na nani?”

    .

    .

    “Wenyewe!”

    .

    .

    “Wanaenda wapi?”

    .

    .

    “Sijui!”

    .

    .

    Walitazama nyuma na mbele yao, hakukuwa na mtu akiongozana na watoto hao. Basi wakaona vema, mmoja atoke kwenda kutazama na mwingine abaki mule chumbani. Basi yule Polisi aliyembele ya mwenziwe, akatoka.

    .

    .

    Alipofika huko nje, akawaita watoto hao wawili waliokuwa wanatembea, lakini hawakumsikia. Walikuwa ni wa kike, mapacha, wamevalia nguo za kulalia.

    .

    .

    Polisi akawajongea na kuwatazama vema. Akajitahidi kuwaamsha asifanikiwe. Mwenzake alikuwa dirishani akimtazama kana kwamba runinga.

    .

    .

    “Mnaenda wapi? … Hey! Hey!” akawapigapiga mashavu. Akawatikisatikisa kichwa lakini bado.

    .

    .

    Muda kidogo, yule polisi aliyekuwa amekaa dirishani akimtazama mwenzake, akamwona mtu fulani akiwa anakuja kumjongea mwenziwe na wale watoto. Alimtazama mtu huyo lakini hakuweza kumtambua. Mtu huyo alikuwa akiambatana na mtoto mwingine kwa pembeni yake.

    .

    .

    Akajaribu kumshtua mwenzake, “Tazama nyuma yako! Hey! Tazama!”

    .



    Mwenzake huyo alipotazama, kabla hajajitetea na bunduki yake, akanyakwa koo na kunyanyulia juu haswa kisha akaminywa kwanguvu mpaka koo lake kuanza kuchuruza damu. Bunduki ambayo huenda ingemsaidia kutetea uhai wake, ikadondokea chini.

    .

    .

    “Hapana! Hapana!” mwenzake akatahamaki pale dirishani. Upesi akatoka kwenda kumsaidia mwenzake abaki na pumzi. Alipofungua mlango, akamnyooshea mtu yule bunduki na kumfyatulia tatu. Ajabu hazikusaidia. Zaidi yule mtu wa ajabu akamtupia mwenzake chini na kumfuata yeye kwa kasi!

    .

    .

    Naye akamyaka shingo na kumnyanyua juu, akamminya koo na kumpasua, kisha akalichanja na kumfanya avuje damu kama sharubati toka kwenye kopo. Polisi huyo akapoteza uhai. Dubwana hilo likamtupa na kisha likapotea zake!

    .

    .

    Baadhi ya watu wakafungua milango na madirisha kutazama. Milio ya risasi iliwaamsha na kuwapa mashaka. Wakaona maiti mbili za polisi na wale watoto wakiwa wanatembea. Kwakuwa hali ilikuwa shwari, wakatoka kwenda kutazama.

    .

    .

    Waliwaokoa wale watoto na pia wakatoa taarifa polisi wakidhani polisi wameuawa na majambazi baada ya kurushiana risasi.

    .

    .

    Muda mfupi, polisi wengine wakaja na kuanza kuipemua miili na kukusanya taarifa toka kwa washuhudiaji. Hawakuelewa jambo. Hakuna aliyesema amewaona hao watu waliokuwa wanapambana na polisi, lakini pia vilevile hakuna aliyetoa maelezo ya kueleweka juu ya watoto wale mapacha waliokuwa wanatembea wenyewe usiku huo.

    .

    .

    Wakiwa kwenye mahangaiko ya kutafuta taarifa sahihi, Mama Brian akatoka akiwa amejikunyata, amejifunika blanketi, akawaambia polisi, “Mimi najua nani waliyekuwa wanapambana naye.” kwa maelezo zaidi, polisi mmoja akaongozana na Mama Brian kwenda ndani kumhoji.

    .

    .

    “ … Mtu huyo ndiye ambaye hupoteza watoto kila siku. Polisi hao walipotaka kuwaokoa watoto hao, ndipo akajiri na kuwamaliza,” Mama Brian akaeleza. Polisi akamuuliza, “Unamjua yupoje na wapi anaishi?”

    .

    .

    Mama Brian akanyamaza kwanza kisha akauliza, “Hata nikisema mtasadiki?”

    .

    .

    “Usijali,” Polisi akamtoa hofu. “Unaweza tu kueleza.” basi Mama Brian akamweleza kinagaubaga ya kuwa mtu huyo ni Helo, Hernandez Lorenzo, wa miaka mingi iliyopita. Nyumba yake ipo msituni na anafanya kila anachofanya kwa ajili ya kulipiza kisasi kwa mji wa Boston.

    .

    .

    Polisi akanakili maelezo yake yote, ila yakamletea shaka kwenye kuamini. Simulizi ile ilikuwa ni ya kufikirika zaidi kuliko uhalisia. Ni kwa namna gani mtu mfu akarejea na kufanya mauaji?

    .

    .

    “Nashukuru sana.” Polisi akampatia mkono na kunyanyuka, “Naweza kwenda sasa. Au kuna cha ziada wataka kuniambia?”

    .

    .

    Mama Brian akamjibu, “Ndio, kipo!”

    .

    .

    “Niambie.” Polisi akasema akimpatia masikio yake kwa utulivu. Mama Brian akasema, “nendeni mkatazame kwenye korongo la kanisa …”

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    .

    Gari la polisi lilisimama, wakashuka wanaume wawili waliovalia sare. Mmoja wao alikuwa ni yule Polisi aliyemhoji Mama Brian. Mkononi alikuwa amebebelea ngowe ya mawasiliano na bunduki ndogo. Mwenzake anayemfuatia alikuwa mikono mitupu ila viganja vyake vikiwa karibu na mkanda wake uliobebelea silaha.

    .

    .

    Ndani ya muda mfupi, wakaonana na Padri Alfonso na Dada Magdalena, wakawafanyia mahojiano mafupi kabla ya kuwataka waongozane kwenda korongoni. Padri Alfonso akapata shaka, akauliza, “Afisa, kuna lolote lile?”

    .

    .

    “Tunataka kupatazama!” Polisi akasema kwa amri basi Padri Alfonso na Dada Magdalena wakaongozana nao kwenda huko kwenye korongo. Walipofika, polisi hao wakangaza na kuangaza, hawakuona kitu.

    .

    .

    “Mnaweza kutuambia mnatafuta nini ili tuwasaidie?” akauliza Padri Alfonso. Polisi akamwambia, “Usijali.” kisha wakajikokota zao kwenda kwenye usafiri wao na kutimka.

    .

    .

    “Hamna kitu!” akasema Polisi dereva na kuongezea, “Nilijua tu mama yule atakuwa na matatizo.” wakayoyoma wakati Padri Alfonso na Dada Magdalena wakiwatazama. Walipoishilia, Padri Alfonso akauliza, “Watakuwa wameambiwa na nani kuhusu korongo lile?”

    .

    .

    Dada Magdalena akajibu, “Si wengine bali wale waliokuja kulitembelea.” Basi Padri Alfonso akashusha pumzi ndefu na kusema, “Nadhani umefikia mwisho wao!” na mara katikati yao akasonga mtumishi mwingine. Naye alikuwa ni Dada kama yule Magdalena, akasimama kandokando yao na kuuliza, “Nami nafanyaje?”

    .

    .

    Padri Alfonso akamtazama na kuweka mkono wake begani. Kumbe alikuwa Dada yule aliyekumbwa na kadhia na yule polisi wa mwanzoni wakiwa korongoni kuwafuata wakina Brian.

    .

    .

    “Dada Marietta, wewe bado u mpya kabisa,” akasema Padri Alfonso. “Utafanya kazi pamoja na Dada Magdalena akuonyeshe namna ya kuenenda. Ila bila shaka usiku wa leo umekuwa mrefu sana, tuuache uende.”

    .

    .

    Dada hao wakainamisha vichwa vyao, Padri akaenda zake.

    .

    .

    **

    .

    .

    Saa nane ya mchana …

    .

    .

    Akiwa juu ya baiskeli yake, Brian alirusha macho yake huku na kule kuangazia kama kuna tangazo jipya la watoto waliopotea. Hakukuwapo, yote yalikuwa ya zamani. Mpaka anafika nyumbani hakuona tangazo lolote tofauti na yale aliyoyaona hapo kabla.

    .

    .

    Akazama ndani na kuteta machache na Wisconsin juu ya mpango wao. Bwana huyo akamwambia kuwa siku hiyo wataenda kumtembelea Brewster majira ya usiku. Brian akauliza, “Haitakuwa hatari kutokana na yale yaliyotokea jana yake?”

    .

    .

    Wisconsin akakuna kidevu chake na kumwambia Brian, “Hatuna muda, ni lazima tufanye hivyo. Kama tusipoyatembelea maeneo haya tukiwa na mwili wa nyama, basi itakuwia vigumu utakapoenda huko kiroho. Lazima ujue ni maeneo yapi utakayokatiza na kuyafanyia kazi.”

    .

    .

    Basi japo kishingo upande, Brian akaridhia. Akala na kupumzika kidogo. Baadae kwenye majira ya jioni akajikwea kwenye baiskeli yake na kwenda kule kwenye makazi ya marehemu Dkt Hamill. Alipoingia, akaegesha baiskeli yake pembeni kidogo ya geti kisha akaanza kusonga kuendea jengo hilo.

    .

    .

    Akiwa bado hajalifikia, akastaajabu kusikia sauti ya geti likifungwa. Akapata shaka. Haraka akakimbilia getini na kujaribu kulifungua. Halikufunguka. Akajaribu kwanguvu zote lakini bure, hakuweza kufungua. Akajiuliza nani kamfungia humo?

    .

    .

    Akapigapiga geti kwanguvu akiita watu wamsaidie lakini hakuna mtu aliyemsikia wala kujali. Mpaka mikono ikawa inamuuma asifanikiwe kitu. Mara akasikia sauti nyuma yake ikimwambia, “Acha kujichosha, Brian.”

    .

    .

    Haraka akatazama nani huyo amwongeleshaye, hamaki akamwona Brewster! Alikuwa amesimama mbele ya mlango wa jengo akiwa ameshikilia bakora ya kutembelea. Yu ndani ya suti nyeusi na kofia yake.

    .

    .

    “ … tupo wawili tu humu, acha kusumbuka.” akamalizia na kisha akatabasamu. Brian akamuuliza, “Ni nini unataka kwangu?”

    .

    .

    “Unajua nitakacho,” Brewster akamjibu kisha taratibu akaanza kusonga kumjongea. “Nilijitahidi sana kukuepusha na kifo, lakini …” akabinua mdomo wake. “ … hukutaka kusikia, Brian. Umekuwa mkaidi sana. Sasa mimi nifanye nini?”

    .

    .

    Brian akamnyooshea mkono na kumwamuru, “Usinisogelee!” Brewster akaangua kicheko kisha akauliza, “Nikikusogelea, utanifanya nini, Brian?” Kabla Brian hajajibu, Brewster akiwa anatembea taratibu, akasema, “Leo ni mwisho wako. Hamna mtu wa kukusaidia, ni mimi na wewe tu … mimi na wewe, Brian.”

    .

    .

    Brian akapiga kelele kuomba msaada. Brewster akacheka sana mpaka kushika mbavu zake. Akakohoa mara kadhaa na kusema, “Brian, acha kupoteza nguvu zako bure. Ni-me-ku-a-mbi-a …” wakati Brewster anaongea akawa anabadilika toka kwenye ubinadamu kwenda kwenye ushetani. “… u-po-na-mi-mi-tu! Ni we-we-na-mi-mi-tu!”

    .

    .

    Uso wake ukageuka na kuwa wa mnyama. Mikono yake ikavimba na kuchomoza makucha vidoleni. Ulimi ukamtoka nje na meno yakapandana kwana kwamba tengo la miba! Miguuni akavalia kwato za ng’ombe.

    .

    .

    Brian akaogopa sana. Akakimbia kuufuata ukuta na alipoenda mbali akajitahidi kuurukia ukuta atorokee kwa nje, lakini ukuta ulikuwa mrefu sana. Hata aliponyoosha mikono yake, hakufua dafu. Akajaribu na tena na tena. Mara mkono wake wa kuume ukafanikiwa kushika kingo ya ukuta. Akijitahidi kuunyoosha mkono wa pili, ule wa kushoto, udake ajivute, akashikwa na kuvutwa chini! Akadondoka na kulalama kwa maumivu.

    .

    .

    Brewster akamdaka shingo na kumminya kwanguvu. Brian akaanza kutapatapa.

    .

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nakumaliza, Brian!” akasema Brewster ambaye hakuwa binadamu tena bali mnyama. Brian akaendelea kutafuta pumzi yake na kupigania uhai wake pasipo mafanikio. Ni bahati wakati anatafuta la kufanya, akamkita Brewster kwenye sehemu zake za siri na kumsababishia maumivu makali!

    .

    .

    Akamwacha Brian na kukimbizia mikono yake yote sehemu zake za siri, ndipo Brian akachoropoka na kukimbia haswa. Alikuwa anahema kana kwamba mbwa. Na baada ya muda mfupi akawa haonekani wapi amekimbilia.

    .

    .

    Basi Brewster akiwa anagugumia sana kwa maumivu, akasimama, bado uso wake ukionyesha anahisi maumivu, akatazama huku na kule kumtafuta Brian. Macho yake yalikuwa mekundu yaliyojawa na hasira.



    “Nitakuua, Brian!” akasema akiwa anakunja ngumi yake kwanguvu. Meno anayasaga.

    .

    .

    Akanguruma kana kwamba simba kisha akaanza kumsaka Brian ndani ya eneo hilo akitumia pua yake kama nyenzo kuu. Akanusanusa na kusonga. Akanusa na kusonga. Akatazama kushoto na kulia. Akasonga.

    .

    .

    Mwishowe akafika nyuma ya nyumba ambapo aliamini Brian atakuwa huko. Akaangaza macho, kheri akaona mlango ukiwa wazi. Akaamini alikuwa sahihi. Akasonga na kuzama ndani, bado akitumia pua yake kama dira.

    .

    .

    Alipoendelea kunusa zaidi, akajikuta mbele ya kabati kubwa. Hapo akaguna kwa kebehi na kusema, “Unaweza kukimbia, Brian, ila si kujificha.”

    .

    .

    Mara akaanza kufungua milango ya makabati kwa pupa na kutupia humo macho yake kutazama. Mlango wa kwanza, hakubahatika kuona kitu, wa pili nao wa tatu, hakukuwa na kitu zaidi ya nguo tu! Sasa mlango uliobakia, ule wa nne, akajua Brian yupo humo.

    .

    .

    Basi akavuta pumzi kwanza, alafu puh! Akaufungua. Loh! Namo hakukuwa na kitu. Hajakaa vema, kabati likaanza kuinama. Akadhani pengine ni macho yake, kumbe lah! Kabati lilikuwa linadondoka.

    .

    .

    Likamparamia na kumwangusha chini kama mbuyu. Brian akatoka kwa nyuma yake na kukimbia upesi kwenda ndani. Muda mfupi, hauonekana tena wapi alipoelekea.

    .

    .

    Brewster aliyeachwa akiwa amevamiwa na kabati, akalalama sana kwa maumivu. Kana kwamba kabati lile ni bua, akalinyanyua na kulitupia kando kwa nguvu! Kabati likaparanganyika na kuwa vipisi vya mbao.

    .

    .

    Uso wake ulikuwa unatoa damu na alikuwa pia amekasirika maradufu. Akapiga kelele kali na kunyanyuka kisha kwa pupa akaanza kumsaka Brian! Akanusa na kufuata harufu mpaka kufika chumba kimoja ambacho kilikuwa kimefungwa. Akabamiza mlango kwanguvu, ukavunjika kutengeneza tobo!

    .

    .

    Akaubamiza tena na tena, mlango ukawa inyang’anyang’a, akazama ndani na kuangaza. Hakukuwa na mtu, chumba kilikuwa kitupu kabisa. Hakuamini macho yake, mbona amesikia harufu humo? Alipotazama vema, akagundua ya kuwa Brian alikuwa ametupia nguo yake humo.

    .

    .

    Akaifuata na kuinyanyua kuipeleka puani. Akainusa. Ama kweli, alikuwa amedanganywa! Akasaga meno yake kwa hasira kisha akatoka humo chumbani.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    “Tafadhali, kubali! Tafadhali! Tafadhali!” Brian alilalama akiwa anaibonda simu ya mezani kiganjani mwake. Alikuwa anataka kuwasiliana na polisi ama familia yake lakini simu hiyo ilimsumbua. Kila alipotia namba, ikakata. Kila alipotia namba …

    .

    .

    “Shabash!” akalaani. Akiwa yu kifua wazi, mjawa na hofu, akawaza nini cha kufanya. Hakuwa anajua sasa. Endapo Brewster angelitokea hapo basi angemmaliza mara moja.

    .

    .

    Akatazama kushoto na kulia. Makabati hayakuwa sehemu salama ya yeye kujificha. Na hata kitanda kilichokuwamo humo ndani hakikuwa na uvungu.

    .

    .

    Akiwa anawaza vivyo, mara akaona simu ile ya mezani ikiwa inawaka taa. Taa ndogo nyekundu ambayo ilikuwa imepachikwa kwenye kitako chake. Basi haraka Brian akapata moyo. Upesi akaikwapua simu hiyo na kuibandika sikioni, akapiga polisi.

    .

    .

    Simu ikaita mara mbili, mara ikapokelewa na sauti ya kike.

    .

    .

    “Unaongea na idara ya Polisi, Boston. Una dharura yoyote?”

    .

    .

    Kabla Brian hajafungua mdomo, mlango ukabamizwa kwanguvu na kupasuka! Kutazama akamwona Brewster, macho kwa macho. Akiwa amejawa woga, akapayuka simuni kuwa anahitaji msaada kuna mtu anataka kumuua.

    .

    .

    “Upo wapi? Tupe anwani yako tafadhali!” sauti ile ya kike ikanguruma. Brian kufungua mdomo wake, Brewster akawa tayari ameshamfikia. Akamnyonga shingo yake kwanguvu!

    .

    .

    Bado Brian alikuwa ameshikilia simu mkononi. Brewster alikuwa anamtazama kwa hasira na hamu ya kumfundisha adabu. Kutetea uhai wake, Brian akambamiza Brewster usoni kwa kutumia simu ile ya mkononi.

    .

    .

    Simu ikavunjika na kumwacha Brewster bado yupo ‘gado’. Kwa upesi, Brian akanyanyua tena kitako cha simu na kumkandika nacho Brewster usoni, karibu kabisa na jicho lake la kushoto, hapo Brewster akahisi maumivu. Jicho lake lilijeruhiwa pia.

    .

    .

    Brian akamng’ata mkono kwanguvu, kwa hasira Brewster akamtupia ukutani yeye akiugumia maumivu. Brian akakajibamiza na kulala akihisi maumivu makali kichwani. Alipomtazama Brewster akamwona akiwa anajirepea kukaa sawa. Akafikiria upesi na kuona ni hekima kuruka kupitia dirishani kuliko kukaa humo angoje kuuawa.

    .

    .

    Akajivuta upesi, akipumbaza maumivu aliyokuwa nayo, akasongea dirisha na kujitupia huko nje pasipo kujali kuna urefu wa aina gani. Akafikia bustanini na kujeruhi mguu wake wa kushoto kwa kujichanja na ua kubwa komavu. Mguu ukawa unavuja damu. Tumbo nalo na kifua vyamuuma mno. Alikuwa ameruka toka ghorofa ya pili!

    .

    .

    Akatema damu na kutazama kule juu alipotoka, dirishani akamwona yule dubwana akiwa anamtazama. Basi akajikokota kusimama, kisha akanza kujongea kwenda getini. Mwendo wake wa chechema sababu ya majeraha.

    .

    .

    Brewster akabinua mdomowe. Na hamaki, kufumba na kufumbua, naye akajitupa kurukia kule chini! Akafikia kwato zake na kusimama imara kabisa. Taratibu akaanza kumfuata Brian akiwa anajua ashakuwa njiwa wake. Hana haja ya kumfukuza.

    .

    .

    “Huu ni mwisho wako, Brian. Haijalishi ni namna gani unauchelewesha.”

    .

    .

    Brian akakunja shingo kumtazama. Uso wake nao ulikuwa unavuja damu toka upande wa kulia wa paji lake la uso. Macho yake yalikuwa mekundu … mekundu yakionyesha maumivu mazito anayopitia.

    .

    .

    “Simama, Brian. Naapa hutosikia maumivu hata kidogo. Nitakumaliza pasipo maumivu yoyote yale,” akasema Brewster huku akisugua kwato zake ardhini. Brian hakujali, akaendelea kusonga kwa mwendo wake wa kinyonga. Punde, Brewster akakimbia na kusimama mbele yake. Alikimbia kwa kasi sana, si ya binadamu. Kiganja chake kipana kikadaka shingo ya Brian na kumnyanyua juu! Akamuuliza, “Utajitetea na nini hivi sasa?”

    .

    .

    Brian akiwa ametulia kana kwamba mtu anayengoja kifo kimtwae, akachuruza damu mdomoni. Tone lake likamdondokea Brewster jichoni na kumfanya kiumbe huyo afumbe macho. Akapepesapepesa na kuyafungua tena.

    .

    .

    Ajabu alipotazama, akaona mkono wa Brian ukiwa unaishilia kooni mwake. Hakutambua nini kilichotokea, ila ghafla akahisi maumivu makali mno na damu zamtiririka! Kumbe Brian aliuwa ana kipande ha chupa mkononi mwake. Kipande alichokiokota wakati ananyanyuka toka pale chini alipoangukia.

    .

    .

    Alimkita nacho Brewster mara tatu shingoni pasipo kukoma, Brewster akayakodoa macho haswa! Brian asiwe hata na lepe la huruma, akaendelea kumtoboatoa shingoni kana kwamba anataka kutengeneza nyavu. Damu zikamruka kwa hasira!

    .

    .

    Upesi Brewster akamwachia na kisha akadaka shingo yake iliyokuwa inavuja damu pomoni. Akalia kwa uchungu wa maumivu. Akamtazama Brian kwa hasira, akajaribu kumdaka ila mkono wake ukalegea kwa kukosa nguvu. Akadondoka chini akiendea pumzi yake ya mwisho.

    .

    .

    Brian akabaki akimtazama kandokando yake. Pale Brewster alipokata pumzi, akamtupia kipande kile cha kioo alichomuulia nacho, yeye akaenda zake taratibu akifuata geti. Taratibu kwa mwendo wa kinyonga. Kabla hajafikia geti, akatazama nyuma. Haki alikuwa amemuua dubwana.

    .

    .

    Simulizi ya daudi na Goliathi.

    .

    .

    “Mungu wangu, Brian!” Mama akatahamaki baada ya kumwona mwanae. Ndiyo kwanza Brian alikuwa amewasili eneo la nyumbani. Alikuwa anakokota baiskeli yake ambayo punde aliiangushia kando na msingi wa nyumba.

    .

    .

    Mama yake akamsogelea upesi kumtazama.

    .

    .

    “Nini kimekutokea?” Mama akauliza akiwa anamkagua kwa macho. Punde mlango ukafunguliwa, Wisconsin akatoka ndani. Naye akarusha macho yake kumtazama Brian kisha haraka akasonga eneo la tukio.

    .

    .

    “Alikuwa ni Brewster,” Brian akasema na kusita. “… Nimemuua!”

    .

    .

    Mama akaziba mdomo wake kwa kiganja chake cha kulia. Akauliza, “Umemuulia wapi? Watu wamekuona?” Brian akatikisa kichwa na kujibu, “Hamna aliyeniona. Tulikuwa peke yetu.”



    Mama akamtazama mguuni, akamwona akiwa amelowanisha suruali na kiatu chake kwa damu.

    .

    .

    “Twende ndani, hapa si salama,” akashauri Wisconsin. Mama akaona ni stara, hata hivyo Brian alikuwa anahitaji huduma ya kwanza. Upesi wakazama ndani na Mama akamshughulikia Brian kwa dakika kadhaa kabla ya kukaa na kuendelea na maongezi yao.

    .

    .

    “ … alibadilika na kuwa mnyama,” Brian akasema kwa sauti yake ya pole. “Alitaka kuniua. Aliahidi kufanya hivyo. Kila alipodaka shingo yangu nilimwona akiwa na dhamira hiyo. Kunimaliza.”

    .

    .

    Akaweka kituo kirefu akitazama mkono wake wa kuume ambao ulifungwa ‘bandage’. Kwa muda kidogo akamezwa na kumbukumbu juu ya namna mkono huo ndio ulivyomkita Brewster kwa chupa mpaka kumuua. Akasema, “sikumbuki ni roho ya namna gani ilinivaa. Nahisi nami nilikuwa mnyama kama yeye. Sikujiuliza mara mbili, hata sasa nashangaa.

    .

    .

    Kitu pekee nilichokuwa nataka kukiona ni yeye akidondoka na kuwa mfu. Nikamtifua shingo yake …” Brian akaeleza akiwa mbali kifikra. Ni kama vile alikuwa anshuhudia anachokisema. “… nilimtifua kana kwamba plau inavyotafuna ardhi hata akalegea na kudondoka chini … akawa mfu.”

    .

    .

    Wisconsin akamwekea mkono begani na kumminya kidogo, akasema, “Wewe ni shujaa, Brian.” macho yake yalikuwa yanamaanisha anachokisema. “Kecie hakukosea kukuchagua wewe. Aliona kipi kipo ndani yako.”

    .

    .

    Mama Brian akamkumbatia mwanae kwa mara nyingine kisha akambusu mara mbili kwenye paji la uso. “Najivunia kuwa nawe, Brian.” akamtazama mwanaye kwa macho yanayolenga machozi. Wisconsin naye akamfariji na kisha kumwambia, “Inabidi niende huko kwenye hiyo nyumba.”

    .

    .

    “Kufanya nini?” Mama Brian akatahamaki. Akajigeuza vema amtazame Wisconsin.

    .

    .

    “Inabidi niende, kuna kitu nataka kutazama,” akasema Wisconsin kisha akasimama asiseme kitu gani champeleka huko. Akafungua mlango na kujiendea zake akimwacha Mama Brian kwenye bumbuwazi. Mwanamke huyo aliona kwenda huko ni kujitakia maswaibu kama yale ya Brian. Aliogopa.

    .

    .

    Basi sasa tangu Wisconsin alipoyoyoma, akawa anahesabu masaa na dakika. Akawa anatazama saa yake mara kwa mara na hata njia kuangaza kama bwana huyo anarejea. Mpaka kufikia majira ya saa mbili usiku, hakuonekana. Mama Brian akapata shaka sana, hata Brian alitia doa imani yake.

    .

    .

    “Atakuwa salama kweli?” Mama akamuuliza Brian. Alishika tama macho yake yakiwa yamejawa na ndita za woga. Brian akamjibu, “Anajua kujitazama. Haina haja ya kuhofia sana.”

    .

    .

    Punde kidogo mlango ukagongwa, Mama akadamka upesi kwenda kutazama. Hakuwa Wisconsin, bali jirani tu.

    .

    .

    “Habari?”

    .

    .

    “Salama.”

    .

    .

    “Samahani kwa usumbufu, vipi runinga yako yafanya kazi vema?” akauliza jirani. Mwanamama mwenye nywele nyeupe na mashavu mekundu. Kwenye nyonga yake alikuwa amembebelea mtoto mdogo wa kike makadirio ya miaka miwili.

    .

    .

    “Sijajua, acha nitazame,” akasema Mama Brian alafu akaendea runinga yake na kuiwasha. Ilikuwa ajabu runinga hii haikuwa imewashwa mpaka sasa, pengine ni kwasababu hakukuwa na mtu mwenye mpango nayo. Kila mmoja alikuwa anamuwazia Wisconsin. Labda Olivia angelikuwa sebuleni, angeliwasha.

    .

    .

    “Naona kuna matatizo,” akasema Mama Brian. Runinga haikuwa inaonyesha kitu isipokuwa chenga nyeupe tu. Hakujali sana, akaweka rimoti juu ya runinga na kumrudia mgeni wake.

    .

    .

    “Naona kuna matatizo, haionyeshi kitu!”

    .

    .

    “Ni ajabu,” mgeni akasema akitikisa kichwa chake kisha akabinua lips zake nyembamba.

    .

    .

    “Vipi, kuna lolote?” Mama Brian akadadisi.

    .

    .

    “Yah!” Jirani akaitikia kwa uhakika. “Walikuwa wanamwonyesha mtoto mmoja aliyepotelea msituni na kupatikana!”

    .

    .

    “Kweli?” Mama Briana akakodoa macho.

    .

    .

    “Ndio!” akajibu yule jirani. “Ni ajabu. Ni yeye pekee ndiye aliyefanikiwa kurudi baada ya kupotea. Simulizi yake hakika ilikuwa inasisimua! Ila sikufahamu nini kimetokea maana runinga ilizima picha nikadhani ni kwangu tu.”

    .

    .

    “Haukusikia chochote kile?” Mama Brian akauliza. Habari hii ilimvutia. Kwa muda akasahau kuhusu swala la Wisconsin. Hata Brian aliyekuwa ndani naye akasimamisha masikio kuskiza.

    .

    .

    “Sikusikia jambo la maana,” akajibu jirani. “Kabla ya mtoto huyo kuongea, basi runinga ikakata mawasiliano mpaka sasa.”



    “Umemtambua mtoto huyo?” Mama Brian akauliza. Jirani akatikisa kichwa. “Hapana. Si wajua Boston ni kubwa!”

    .

    .

    Basi akaendaze, huku nyuma Mama Brian na mwanae wakabakiwa na maswali. Walitamani kumwona mtoto huyo, au kusikia taarifa zake kwani kwa namna moja ama nyingine walikuwa wanazihitaji.

    .

    .

    Brian akasema, “Nadhani kesho naweza kuzipata taarifa hizo vizuri.”

    .

    .

    “Wapi?” Mama akauliza.

    .

    .

    “Shuleni,” Brian akajibu na kuongezea, “Shule ni kubwa, sidhani kama atakosekana mtu mwenye habari hizo kwa undani.” Wazo hilo likajenga hoja kichwani kwa Mama. “Itakuwa vizuri ikiwa hivyo!” akanyanyuka na kwenda jikoni kufanya utaratibu wa chakula. Baada ya muda, chakula kikawa tayari.

    .

    .

    “Brian, unahitaji chakula kwa sasa?”

    .

    .

    “Hapana. Namngoja kwanza bwana Wisconsin.”

    .

    .

    Mama akenda chumbani kumwita Olivia, punde akarejea naye, Olivia alikuwa amelewa usingizi, akampatia chakula, kisha akaketi kitini.

    .

    .

    “Hauli?” Brian akamuuliza. Akatikisa kichwa chake na kusema, “Hapana, Sijisikii. Acha tumngoje Wisconsin kwanza.”

    .

    .

    Kukawa kimya kidogo. Ni Olivia ndiye aliyevunja ukimya kwa kuomba atazamae runinga.



    “Haionyeshi, mpenzi!” Mama akamjibu, ila akanyanyuka na kuendea rimoti ili athibitishe maneno yake kwa Olivia. Akawasha runinga. “Ona! Haionye--”

    .

    .

    Hajamalizia, akashangaa picha zaonekania kideoni! “Brian, tazama!” Mama akapayuka. “Inaonyesha hivi sasa!”

    .

    .

    Brian akauliza, “Ni chaneli gani ilirusha ile habari?” Mama naye hakuwa anajua. Wakapata kibarua cha kukagua chaneli zote kwa wepesi. Hawakuona kitu. Chaneli zote zilikuwa zaonyesha mambo mengine. Ila kuna moja bado ilikuwa giza.

    .

    .

    “Ebu ngoja!” Brian akamtaka Mama yake asubiri kwanza hapo penye giza. “Hamna kitu!” Mama akasema.

    .

    .

    “Hapo huwa ni chaneli gani?” Brian akauliza. Mama akapandisha mabega. “Sijui! Nitajuaje na haionyeshi?” Olivia akasema, “Ven 24! … inaitwa Ven 24.”

    .

    .

    “Umejuaje?” Mama akauliza.

    .

    .

    “Kwasababu ndiyo chaneli inayofuata baada ya kutoka Kids Date,” Olivia akajibu akiwa anatafuna.

    .

    .

    “Najua zilipo studio zao,” Brian akasema, “Kesho nitaenda huko kuwauliza. Nadhani tutapata jambo.”

    .

    .

    “Ila Brian,” Mama akatilia shaka. “Ni saa tatu sasa yaelekea na nusu, vipi kuhusu Wisconsin?” Kabla Brian hajajibu, Mama akaamka na kuuendea mlango, akafungua na kuchungulia nje. Hakukuwa na mtu, barabara ilikuwa nyeupe. Akafa matumaini.

    .

    .

    “Inabidi tufanye jambo, Brian,” Mama akashauri.

    .

    .

    “Niende kumfuatilia?” Brian akauliza. Mama akabanwa na

    kigugumizi.

    .

    .

    “Sidhani kama ni wazo jema. Pengine tuwataarifu polisi.”

    .

    .

    “Unadhani kweli hilo ni wazo jema?” Brian akauliza na kuongezea, “Kumbuka ni mauaji!”





    Mama akakosa la kusema. Hakujua nini afanye. Bahati ndani ya muda mfupi wakasikia mlango unagongwa na mara Wisconsin akaingia ndani. Wakalipuka kwa furaha wakimkaribisha kwa hamu tele ya kutaka kujua nini hicho kimemkalisha muda mrefu hivyo mpaka wakapata hofu kubwa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kabla Wisconsin hajasema jambo, akaomba aletewa chai ya moto ajipashe mwili. Akanywa mafundo matatu ya chai hiyo na akiwa ametuama kwa fikra kisha akasema akimtazama Brian, “Brewster ameenda. Ulifanya jema sana kumuua akiwa katika mwili wake wa ulimwengu mfu. Endapo angekufa akiwa kwenye mwili wake wa kawaida basi mtihani ungekuwa mkubwa kwenye ulimwengu wa kiroho. Bado angalikuwa hai.”



    “Lakini kwanini ukakawia hivyo?” Brian akauliza. Wisconsin akamjibu, “Kwasababu kulikuwa kuna mambo mengi ya kutazama.” kisha akamuuliza, “Unamjua vema bwana mwenye nyumba ile?”



    “Dkt Hamill?”



    “Ndio. Unamjua vizuri mtu huyo?” Wisconsin akauliza.



    “Siwezi kusema namjua sana, sikupata muda mrefu wa kukaa naye,” Brian akajibu. Wisconsin akamuuliza, “Kwa muda huo ukamfahamu ni mtu wa aina gani?”



    “Ni mtu mkarimu … pia mpweke,” Brian akajibu. Wisconsin akanyamaza kwa sekunde tatu, bado akimtazama Brian, kisha akamuuliza, “Una uhakika?”



    Brian akatikisa kichwa. “Ndio, nina uhakika. Alinifanyia sana ukarimu. Siwezi kumsahau.”



    “Sawa,” Wisconsin akasema na asiseme tena lingine. Brian akauliza, “Vipi kuna lolote?” Wisconsin akamtazama na kutikisa kichwa. “Hamna kitu. Tutaongea zaidi kesho, nahitaji kupumzika hivi sasa.”



    “Ngoja basi ule,” Mama Brian akashauri. “Hapana,” Wisconsin akajibu. “Sijiskii njaa, nitakula kesho.” alafu akaenda zake.



    Akiwa anaenda, Brian akagundua Wisconsin alikuwa na alama ya damu kwenye nguo yake. Akataka kuuliza lakini akaona ni stara kunyamaza. Wisconsin hakuwa kwenye hali ya kuongea, pengine kesho atafunguka zaidi.



    “Vipi kuhusu yule mtoto wa kwenye runinga?” Mama akauliza. “Unadhani kuna haja ya kumwambia?”



    “Ndio,” Brian akajibu na kuongeza, “lakini si kwa sasa. Unamwona hayupo kwenye mandhari hayo. Kesho nikitoka shule, nitateta naye vizuri.”



    Basi Mama na Olivia nao wakaaga wanaenda kulala, Brian akabakia mwenyewe sebuleni akitazama runinga. Hakuwa mtazamaji mzuri wa runinga ila aliguswa tu kutazama kwa muda huo akidhani pengine anaweza kuona jambo kuhusu yule binti aliyekuwa anahojiwa.



    Akaweka chaneli hiyo na kutazama, kulikuwa bado ni kiza. Si sauti wala picha yoyote ambayo ilikuwa inaonekana ama kusikika. Akatazama kwa sekunde kadhaa kisha akasimama na kuisogelea runinga. Akaendelea kutazama kwa makini. Baada ya muda kidogo, akahisi amesikia sauti ya kitu.



    Akatazama kushoto na kulia kwake, hakukuwa na kitu. Alipotulia ndipo akajua ya kuwa sauti hiyo inatokea kwenye runinga. Ilikuwa ni sauti ya watu wakiruruma kwa chinichini. Brian akatazama runinga kwa macho ya ndita. Bado hakukuwa na picha, na sauti hii ilikuwa inaendelea kusikika. Ni ya nini?



    Brian akaongeza sauti asikie lakini ajabu sauti hiyo haikuwa inaongezeka, ilibakia vilevile japo iliongezwa! Brian akalazimika kuegesha sikio lake kwenye spika za runinga. Akatulia tuli akisikiza kwa umakini…



    “ … ruruma rurururuma … zizizissiiizii … vitiviikiviiizz … shishshishizz … trrriikk … chiiichiiib …” sauti ilinguruma pasipo kueleweka. Ilikuwa ni sauti nzito ya kiume. Brian alijitahidi sana kuisikiza aone kama atapata kitu lakini hakuambulia jambo. Akiwa anataka kuachana na sauti hiyo, mara akasikia sauti ya kike! Akatulia tena na kuskiza kwa umakini …



    “tiiipttiiiiifff … reeegghaaatt … katkatgushik … chat,chat,chat … sssshhhhhh…” sauti ya kike ilinong’ona na kuendelea kunong’ona. Brian akajitahidi kuiskiza ili aone kama ataitambua sauti hiyo lakini hakufanikiwa. Ilikuwa ni ngeni kabisa.



    Baada ya muda kidogo sauti hiyo ikakoma na kukawa kimya. Brian akatazama runinga kama kuna picha. Hakuona kitu. Akarudisha tena sikio lake kwenye spika ya runinga na kuskiza. Hakusikia kitu. Akakaa kwa kama dakika tatu kungoja kama kuna sauti ama picha itaonekana, hakuona wala kusikia kitu. Basi akaona ni kheri akazima runinga akalale.



    Akaminya kitufe chekundu cha rimoti na kisha akaweka rimoti juu ya runinga, akageuka na kwenda zake azime taa kisha aende kulala. Alipofikia ‘switch’ kabla hajazima, akasikia sauti tena. Akageuka na kutazama runinga kwa hofu. Hakuona jambo ila sauti iliendelea kusikika.



    Akiwa hapohapo ameduwaa, sauti ile ya runinga ikaendelea kuongezeka zaidi na zaidi mpaka kufikia kikomo chake cha mwisho na kuwa kelele kali! Haraka Brian akawahi rimoti na kujitahidi kupunguza mpaka kuwa sauti ndogo kabisa, kisha akatahamaki. Mbona nilizima runinga hii?



    Akaiwasha tena na kuizima wa uhakiki. Akaiwasha tena kwa mara ya pili na kuizima kwa uhakiki zaidi alafu akaweka rimoti juu ya runinga na kuiendea ‘switch’ azime taa ya sebuleni.



    Akazima taa, kukiwa kimya na salama. Kabla hajaelekea chumbani akaitazama tena runinga. Ilikuwa kimya na nyeusi. Hakukuwa na kiashiria chochote cha shaka. Basi akaelekea chumbani mwake akapumzike.



    Akiwa amepiga hatua tano koridoni ambapo kiza kilikuwa kimetawala kwa taa kuzimwa, mara akaona mwanga hafifu ukimulika ukuta. Akasimama na kutazama akijiuliza mwanga huo unatoka wapi.



    Alipotazama vema akagundua kuwa unatokea sebuleni. Haukuwa mwanga wa taa, bali runinga! Moyo wake ukakita fundo. Nani amewasha runinga na hakumwacha mtu sebuleni? Akajiuliza aende kutazama ama aachane nayo aende zake chumbani ajifungie na komeo?



    Akapiga hatua mbili kusogelea mlango wake, akaona mwanga ule wa runinga ukiwa unachezacheza kuonyesha kwamba kuna kitu kinachorushwa kwenye kideo, kioo cha runinga kinaonyesha matangazo ya picha! Hapa akasita na kujiuliza, moyo wake ukiwa unaelekea kuchanganyia mwendo.



    Aende kutazama ama aelekee chumbani mwake afunge mlango na kujifunika shuka gubigubi?



    Akadaka komeo la mlango wa chumba chake. Akaminya komeo mlango ukafunguka. Kabla hajaingia, akasikia sauti ya runinga! Akatuliza vema masikio yake kuhakikisha. Ni kweli, ni sauti ya runinga. Kwahiyo sasa haikuwa picha pekee, bali pia na sauti yake!



    Sauti hii Brian alipoisikiliza vema akagundua ni ya mahojiano kati ya mtangazaji na binti mdogo wa kike. Ilikuwa ya mahojiano yale ambayo waliyakosa sababu ya mtandao wa chaneli kuzimika. Basi akaona ni stara kukakata shauri akasikize, au angalau achungulie kinachoendelea.



    Akarudishia mlango wake wa chumbani kisha taratibu akaanza kusonga kwenda sebuleni. Kwa mwendo wake wa majeraha, taratibu taratibu.



    Alipofika kwenye kingo ya korido, akarefusha shingo yake kuchungulia. Kwenye runinga akamwona mtangazaji na binti mdogo wa kike akihojiwa. Uso wa mtangazaji aliuona, ila sura ya yule binti hakuiona kwani alikuwa ameipatia mgongo kamera. Kilichokuwa kinaonekana ni nguo na nywele zake alizobana mafungu mawili.



    Mbali na runinga, Brian akatazama kukagua sebule nzima kama kuna mtu aliyewasha na kutazama runinga. Hakuona mtu. Sebule ilikuwa tupu na pweke, basi akahamaishia macho yake runingani kuendelea kutazama. Wakati huo moyo wake bado haujatulia. Hata kichwa chake kinamgonga kuashiria mambo hayako vile yanavyotakiwa kuwa.



    “ … Ni nani alikuwa anakuitia msituni?” Mtangazaji akauliza. “ … ulimwona kwa sura?”



    Binti yule runingani akatikisa kichwa na kusema, “Nilimwona.”



    “Yupoje?” Mtangazaji akauliza. “Unaweza kumwelezea kwa umbo na sura yake?”



    Kabla binti huyo hajajibu, Brian akashtushwa na hodi mlangoni! Moyo wake ukapiga bampa na kuanza kwenda kasi maradufu. Alihisi hofu sana. Miguu yake ilianza kutetemeka mpaka kugongana.



    Hodi ikapigwa tena, na mara hii anayegonga akasema, “Heey!”



    Ilikuwa ni sauti ya kike. Brian akajaribu kuwaza ni ya nani, upesi akili yake ikamkumbuka yule jirani. Ni yeye ndiye alikuja akagonga mlango muda ule alafu akasema heey!



    Ina maana amekuja tena? Brian akawaza. Muda huu?



    “Tafadhali,” sauti ikasema mlangoni. “…Naweza kuja kuangalia hicho kipindi?”



    Brian akatoa macho kwa kuduwaa lakini pia kwa woga. Akasonga hatua kadhaa kulifuata dirisha kisha akatupa macho yake nje kutazama mlangoni. Hapo akamwona jirani yao akiwa pia na mtoto wake ambaye ananesanesa kumbembeleza.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog