Search This Blog

UNA NINI LAKINI MELISSA - 2

 

    Simulizi : Una Nini Lakini Melissa

    Sehemu Ya Pili (2)











    Akamwambia kuna mengi anataka kuteta naye ila yote hayo yapasa yawe ya siri baina wao. Hategemei kumwona mtu yeyote anapata kuyafahamu, na basi kwa kufanya hivyo atakuwa amejiweka shidani.



    Maneno hayo yakamfanya Darren awe mtulivu na msikivu sana maana yalimaanisha ni jambo kubwa lenye uzito. Baba yake, Mr Gerald, akanywa kwanza fundo la glasi ya whisky kisha akamtazama mwanaye machoni.



    "Sikia, Darren," akasema kabla hajasafisha koo lake na kujipangusa kwa mgongo wa kiganja. "Kuna mambo ya ajabu ajabu hapa katikati. Najua hauyafahamu na nilipata kumsisitizia sana mama yako akwambie lakini hakuwa tayari. Mpaka kifo kinamkuta hajatekeleza ahadi yake hiyo..."



    Akaweka kituo akitazama sakafuni kifikira. "Ulikuwa ni wakati mgumu sana, kwangu na kwake. Tangu yu kwenye usichana mpaka tulipokupata wewe. Nakumbuka, pindi alipokuwa msichana mdogo, alikuwa anapitia mambo ya ajabu sana. Ndoto za ajabu. Na mara kwa mara akinambia anaona watu wa ajabu wakimjia.



    Kuna muda tulikuwa tunashindwa kulala. Angesema kuna mtu nyuma ya mlango. Mtu dirishani. Mtu koridoni. Mtu kila sehemu! Hatukuwa na amani, na, Mungu nisamehe, nilishawahi kufikiria kuachana naye maana hayakuwa yanavumilika."



    Akanywa tena fundo la whisky. Kuyaongea hayo aliyokuwa anaongea, ilimpasa apashe kichwa na kujitoa ufahamu.



    "... lakini kila nilipokuwa nataka kumwacha, ningalijiuliza, vipi ingekuwa mimi? Ningejisikiaje mtu angeniacha kwasababu ya matatizo yangu? Bila shaka ningehisi nimetupwa na kukomolewa, basi nikapiga moyo konde. Maisha ya taabu, taabu sana.



    Tukahama pale tulipokuwa tunakaa kwa kudhani aidha hapafai, lakini bado matatizo yakawa yaleyale. Shida haikuwa nyumba. Shida ilikuwa damu. Damu ya mama yako. Na hata angeenda wapi, basi angelibadilisha jambo."



    Aliposema hayo akanyamaza kana kwamba anapangilia sentensi kichwani. Na kabla hajateta lingine, akanywa tena whisky, tena saa hii mara mbili tofauti na hapo awali kisha akanguruma kama simba kwa kuwakwa na koo.
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    "Unakumbuka kwenye msiba wa bibi yako?" Akauliza.



    "Ndio, nakumbuka," Darren akajibu.



    "Uliona bibi yako alizikwaje?" Baba akauliza, naye Darren alipofikiria kidogo akasema, "Hatukumuaga kama wengine. Na hakukuwa na kiongozi wa dini kuendesha misa!"



    "Unadhani kwanini?"



    "Sijajua kwanini ... lakini ... mimi sikuwahi kuona ubaya wowote wa bibi alipokuwa hai!"



    "Ni sawa. Na hamna shida yoyote katika hilo. Lakini utakuwa umejifunza kuwa mama yako hakuwa na mahusiano mazuri na bibi yako, japo alikuwa mama yake. Ni aghalabu angeenda kumtembelea na kumjulia hali. Sio?"



    "Ndio."



    "Darren, Bibi yako hakuwa mtu wa kawaida. Na alimweka kifungoni mama yako kwa takribani miaka tisa! Sijui nisemeje, sikuwa mtu wa kuamini hayo mambo hapo kabla, ila baada ya kukutana na mama yako ndipo nikaelewa juu ya uwepo wake.



    Ni kama kheri, tukiwa tumehamia kwenye makazi mapya, baada ya kukaa hapo kwa miezi mitatu, tukapata jirani ambaye alitokea South Carolina. Jirani huyu baada ya kukaa siku tatu tu kando na sisi, akafahamu yale tuliyokuwa tunapitia.



    Nakumbuka siku moja nikiwa natoka kazini, aliniita na kunambia angependa kuongea na mimi mambo kadhaa. Nilisita kidogo ila sikuona haja ya kumkatalia. Nikasonga akanipatia kiti nikae sebuleni mwake. Hapo akaniuliza akiwa amenikodolea macho yake ya kizee, 'una shida kubwa, sio?'



    Mimi nikamkatalia, lakini aliweza kuona ndani yangu. Kwa upole akasema anataka kunisaidia na kama nikiwa tayari kukiri kuwa nina hiyo shida basi atakuwa radhi. Mimi nikakataa. Sikuwa namfahamu hata kidogo na nilihofia asije akaniongezea matatizo mengine zaidi ya yale niliyokuwa nayo.



    Basi nikaondoka nikiwaza sana. Kesho yake nilipopita hapo kwake, nikamkuta kibarazani. Nikamsalimu na kwenda. Siku hiyo usiku nikapata tabu sana. Mama yako alinikaba mno na kwa macho yangu nikashuhudia nyayo za damu koridoni! Nikakoma ubishi.



    Kesho nilipotoka kazini nikamwendea yule mama na kumwambia nina shida. Naomba anisaidie kwa namna yoyote ile. Na atakapoweza, basi nitajikunja kwa kadiri ya uwezo wangu nimpatie chochote cha thamani.



    Kwa wakati huo nilikuwa nimekonda sana. Sitamaniki. Hata nguo zangu nazoendea kazini zikiwa zimefubaa, chafu na kukuu. Sikuwa na raha na maisha haya.



    Yule mama akaniambia yu tayari kunisaidia, cha muhimu nimlete mke wangu kwake nikiwa na petali nne za maua zamaridi, mafuta ya ngamia na matumbawe toka baharini.



    Japo masharti yalikuwa magumu, nikaridhia. Ugumu wake haukuwa sawa na ule nlokuwa napitia kila siku. Nikatafuta vitu hivyo na ndani ya siku mbili nikavipata vyote. Nikambeba mke wangu na kumpeleka huko.



    Basi mama yule akafanya mambo yake. Sikuelewa anachofanya, alikuwa anaongea kwa lugha ya ajabu. Alitengeneza maji na kuchanganya na petali zile za zamaridi kisha akampaka Sarah mafuta yale ya ngamia kwenye paji la uso.



    Na kama nakumbuka vema, alichukua unga nisiojua wa nini, akautia kwenye maji yenye zile petali alafu kama haitoshi, akamchanja Sarah kwenye mkono wake wa kushoto, akakinga damu na kuweka humo.



    Mwishowe akatengeneza uji mzito ambao akawa anachovyea na kuandikia kwenye kitabu akiwa ananena kwa lugha ya ajabu. Alipomaliza kuandika, akakizungusha kile kitabu kichwani mwa Sarah na kumgusishia kwenye paji la uso kisha akamwambia naye aseme maneno alokuwa anayatamka.



    Sarah alipofanya hivyo, akazirai. Mama yule akan'tazama na kunambia, kitabu kile kiende kuhifadhiwa mbali msituni kwani ndiyo roho pekee salama ya Sarah. Kadiri kitabu kitakapokuwa salama, naye atakuwa vivyo. Lakini kitakapoharibika, naye ataenda vivyo hivyo.



    Na kwa kadiri ambavyo kitabu hicho kitakuwa hai, hamna mtu yeyote mbaya anaweza kumdhuru, akisisitizia zaidi juu ya majini. Watamwogopa kama ukoma na watamkimbia popote pale atakapokanyaga."



    Basi hapa Darren akajikuta akimkumbuka Melissa. Mbona alikuwa akimkimbia mama yake? Lakini hakuwaza sana, akaendelea kumpatia masikio babaye aliyekuwa na mengi ya kumwambia.



    "Na tokea hapo mama yako hakusumbuliwa tena. Na punde bibi yako alipofariki, ni yeye ndiye akashauri kuwa nyumba ile iuzwe. Na hata vile vilivyomo ndani visichukuliwe hata kimoja kwa kuhofia vyaweza kubeba na kusafirisha matatizo!"



    Darren akakumbuka kuhusu ile picha ya bibi yake na namna ambavyo mama yake alivyokuwa ameghafirika kuitafuta. Akajikuta akitikisa kichwa kwa masikitiko. Sasa ndiyo alijiona mjinga.



    "Mama yako," baba akaendelea kuteta kwa huzuni, "alikufa kwasababu ya moto uliochoma msitu wa kule California. Kitabu chake kitakuwa kimeungua na basi hivyo maisha yake. Hamna kitu ambacho kingeweza kumwokoa.



    Lakini nahofia sana, Darren. Nahofia zaidi kuhusu maisha yako. Sidhani kama yatakuwa sawa na kuondoka kwa mama yako. Hata yangu pia. Naamini uwepo wake ulitufanya tukawa salama zaidi."



    Akashusha pumzi ndefu kisha akahitimisha kwa kusema, "Na kwa usalama wetu Darren, inabidi tuachane kabisa na ile nyumba. Ile ya bibi yako. Usiende tena huko, wala kuhusiana nayo kwa njia yoyote ile. Sawa?"



    Darren akatikisa kichwa. "Sawa." Macho yake yalikuwa mekundu yaliyochoka.



    Basi tangu hapo, miaka ikaenda na kwenda. Baba yake Darren akasumbuliwa sana na ugonjwa wa saratani ya koo kwasababu ya uvutaji mkubwa wa sigara hivyo akajifia na kumwacha Darren peke yake.



    Baada ya mwaka mmoja, Darren akamwoa mwanamke mrembo aitwaye Josephine, na kuwa na familia. Akaishi mbali kabisa na nyumbani, huko New York. Ndani ya mwaka mmoja wakajaaliwa mtoto wa kiume waliyemwita William.



    Lakini ...



    Darren atabaki vipi salama na ingali damu yake ndi' ile ile ya mama yake? Kama ametoka kwenye tumbo la aliyetoka kwenye tumbo la asiye binadamu, kivipi anasalimika kwa upesi?



    ***





    "Nadhani leo nitakawia kutoka kazini," alisema Darren akiwa anakunywa chai. Pembeni yake alikuwapo mkewe akiwa amembebelea mtoto. Darren alikuwa ameshajiandaa kikazi, amevalia suti na tai yake nadhifu.



    "Kwanini?" Josephine akauliza akimtazama kwa shaka. Hakuwa kuzoea mambo hayo ya mumewe kukawia hivyo alitarajia kutakuwa na sababu kubwa.



    "Nina kazi kubwa sana," akasema Darren. "Na nisipozimaliza leo basi itaniwia ugumu sana hapo baadae."



    Mkewe akaelewa lakini asisite kumwonyesha mumewe kuwa atamkumbuka. Na basi atakapopata namna, ajitahidi kuwahi.



    "Usijali," Darren akamtoa shaka kisha akambusu kwenye paji la uso kabla hajasimama. "Nitajitahidi mpenzi wangu. Ila ukiona nimekawia zaidi basi usikasirike ... unajua namba yangu, utan'pigia nikikawia kufanya hivyo."



    Basi akaenda zake baada pia ya kumwaga mwanaye ambaye sasa alikuwa na mwaka mmoja tangu azaliwe. Akajiweka kwenye gari na kisha akaanza safari ya kwenda kazini.



    Akaendesha salama mpaka alipokuja kukuta foleni baada ya kama dakika arobaini na tano akiwa barabarani. Akiwa hapo, kwa kuepuka kuboreka kwa kungoja, akawasha redio na kuskiza habari za asubuhi.



    Zikapita habari kadhaa, hakuzijali sana japo alizipa sikio. Kidogo akiwa anaskiza ndipo ikaja habari ya ghalfa juu ya ajali kubwa ilotokea huko kaskazini mwa Marekani, hapa akajikuta akiguswa na kujawa na umakini. Akategea sikio na akili yake yote kwa sauti aliyokuwa anaisikia redioni.



    Basi akapata kupashwa kuwa moto mkubwa umetafuna msitu wa Orleans. Bahati hakuna taarifa ya mtu yeyote mpaka muda huo ambaye ameripotiwa kufa au kudhurika.



    Habari hii japo ilipita na kuendelea na zingine, bado ikabakia kwenye kichwa cha Darren. Alipata kukumbuka juu ya moto ule uliokula msitu miaka ile ulivyommaliza mama yake katika namna ya ajabu. Alijikuta akimkumbuka mama yake, baba yake, bibi yake na hata Melissa!



    Mawazo yake yote yalihama, na kwa muda akawa hana raha. Hata akajisahau kuwa yu barabarani na basi inabidi aweke msisitizo mkubwa asisababishe ajali kama si kuwakwaza wengine.



    Alikuja kushtuliwa na honi kali nyuma yake maana foleni ilikuwa inaenda sasa. Naye akatia gari yake moto na kusonga mpaka kazini. Bado alikuwa ndani ya muda. Akajiweka kitini na kuanza kupangilia mambo yake atakayoanza kuyafanya moja baada ya jingine. Lakini kabla hajaanza, mawazo yale ya moto yakamteka tena!



    Akabaki hapo kwenye kiti akiwaza sana. Alikuja kustaajabu amekula lisaa lizima na dakika zake tena akishtuka baada ya mhudumu akija kumuuliza kama angependelea chai au kahawa kwa siku hiyo.



    "Mungu wangu!" Akalalama akitazama saa ya ukutani. "Nimechele .... Jack, niletee kahawa tu! ... sawa? Haraka basi!"



    Akaanza fanya kazi zake moja baada ya nyingine. Alipomaliza za makaratasi, basi akaenda 'lab' huko nako akahangaika kwa masaa kabla hajaenda kupata chakula cha mchana. Ni ndani ya jengo hilo hilo. Akiwa hapo anakula, naye mfanyakazi mwenzake aitwaye Roby akaja na kujiunga naye.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa ni mwanaume 'blonde', mwembamba na mwenye kuvalia nguo zilizomzidi. Macho yake yalikuwa yamefunikwa na miwani yenye fremu nyembamba ya chuma. Mdomoni amebana toothpick.



    "Hey, Darren!"



    "Hey!"



    Akaweka sahani yake yenye chakula mezani kisha akavuta kiti na kuketi.



    "Unaendeleaje leo?"



    "Nimebanwa sana na kazi. Ni siku ngumu."



    "Ooh! Pole, nami ilikuwa hivyo jana yake. Nadhani ni muda wa kufikiriwa kuongezewa mshahara sasa."



    Darren akaendelea kula pasipo kusema kitu.



    "Darren, hauniungi mkono kwenye hilo?"



    "Hata nikikuunga, itasaidia nini Roby?" Akasema Darren akitafuna. "Hamna cha kufanya. Kama kingekuwepo basi kingeshafanyika kwa muda mrefu tu."



    "Kwahiyo umeridhika na hali?"

    "Roby, sina muda wa kuongea sana ndugu yangu. Natazamia nimalize chakula kisha nikamalize viporo vyangu."



    "Sawa. Ila Darren nina wazo ..."



    Darren akamtazama pasipo kunena kitu.



    "Si jipya sana. Ni kuhusu lile wazo lako ulilowahi kunambia hapo kabla."



    "Wazo gani?"



    "La kufungua sehemu yetu kule uliponambia."



    "Haiwezekani kwa sasa. Kwa muda ule kulikuwa kuna sponsorship. Haukuniunga mkono kwa woga wako. Sasa unadhani saa hii tutafanya nini? Una pesa hiyo?"



    Kabla Roby hajajibu, Darren akanyanyuka na kugonga meza, "baadae, Roby!" Kisha akaenda zake. Akarudi 'lab' na kuendelea na kazi zake. Mpaka jioni akawa amemaliza huko. Sasa akawa amebakia na kazi ya kuandika ripoti tu.



    Akiwa amejichokea, ila hana namna, akaandika ripoti hizo mpaka majira ya saa nne usiku. Watu waliondoka kazini na sehemu kubwa ya jengo ikawa ipo gizani kutokana na kutokuwa na watu.



    Na zaidi kukawa kimya. Hata Darren akawa anasikia sauti ya keyboard ya tarakilishi kana kwamba honi ya gari. Kila alipokuwa anabofya ikawa inatoa mlio wa nguvu. Na ni kwasababu kulikuwa na ukimya tu eneoni.



    Akiwa anaandika, mara akasikia jambo. Ilikuwa ni kama sauti ya watu wakiteta kwa umbali mdogo, basi akaacha kuchapa kazi yake na kusimamisha masikio. Punde sauti hiyo ikakoma. Basi naye akaachana nayo na kuendelea kuchapa kazi yake.



    Akachapa kidogo, sauti ile ikajirudia tena. Alisikia watu wanateta japo hajui wanazungumzia nini. Na zaidi mmoja wao akaangua kicheko! Kicheko hicho kikavuma kana kwamba mtu huyo alikuwapo karibu kabisa. Na kwa namna kubwa kikamuogofya Darren!



    Akatoka kwenye kiti chake na kuujongea mlango, akaufungua na kutazama nje. Hakuona kitu. Akapaza sauti, "helloooooow!" Napo hakusikia kitu isipokuwa mwangwi wa sauti yake kumrudia.



    Akanyamaza akisimama hapo askize. Kidogo akasikia tena sauti za watu, zilikuwa zinatokea kulia kwake. Akapaza tena sauti, "Helloooow! Kuna mtu huko?"



    Kimya. Mara akasikia kicheko na kilipokoma kukawa kimya kama shimoni. Akastaajabu. Akaanza kupiga hatua kwenda kule aliposikia sauti ile. Alipojongea mpaka mwisho, akaangaza kama ataona kitu. Hola!



    Kidogo akasikia, 'tap!' Alipogeuza shingo yake kutazama nyuma, akaona taa ya ofisi yake imezimwa! Moyo ukamlipuka. Kabla hajafanya jambo, akasikia sauti kubwa ya kitu kama alarm! Mwili ukamtetemeka kwanguvu!



    Alipoweka akili yake sawa ndipo akabaini huo ulikuwa ni mlio wa simu yake. Simu ilikuwa inaita. Basi haraka akaendea ofisi yake na kukamata simu, mkewe alikuwa anampigia. Alipopokea, akajongea 'switch' ya kuwashia taa na kuibofya. Hakukuwa na umeme!



    "Bado upo kazini?" Mkewe aliuliza.



    "Ndio, nipo kazini, ila ..." akajaribu tena kwa kubofyabofya switch. Bado matokeo yalikuwa yaleyale. " ... ningoje maana nakuja muda si mrefu!"



    Akakata simu na kukusanya kilicho cha kwake. Umeme haukuwapo hivyo asingeweza kuendelea na kazi tena. Akafunga ofisi na kutoka ndani lakini akilaumu kwani alikuwa amebakiza kazi kidogo sana amalize kabisa.



    Akatembea kama hatua nane, mara umeme ukarudi! Akasimama na kujiuliza arudi ofisini ama aendelee na safari yake ya kwenda nyumbani? Basi baada ya kujiuliza huko kwa muda mfupi, akaona kheri akamalizie kazi kabisa kesho awe huru.



    Akarejea na kuketi kitini kisha akawasha tarakilishi. Akaanza kuchapa na kuchapa. Ila hakudumu sana, akasikia tena sauti ya watu ikiteta na kucheka! Na mara hii, umeme ukamkatikia ndani ya ofisi!



    Kidogo, akasikia sasa watu wakiteta ndani ya ofisi. Tena si mbali kabisa na yeye. Kwa kando ya kushoto.



    ***

    Akaogopa sana hata kushikwa na kitete cha hofu kuu. Aliwahi simu yake na kumulika awaone watu hao lakini hakufanikiwa kuona jambo. Alikuwa mwenyewe tu!



    Akatwetwa jasho akihema. Moyo nao ukaenda pupa. Akiwa amewasha taa ya simu, akakusanya kila kilicho cha kwake asibake tena hapo. Akauendea mlango na kuufungua, hamaki haukufunguka! Aliuvuta na kuuvuta lakini kazi bure. Mlango ulikuwa mgumu kwenda mbele wala nyuma!



    Akastaajabishwa na hili maana hakuwa ameutia loki mlango huo. Akaangaza kushoto na kulia kama ataona ufunguo lakini napo ikawa kazi bure, hakuona kitu. Basi akazidi kupatwa na hofu. Akazidi kuhemkwa akihisi kabisa hayuko mazingira salama.



    Akihisi kitu fulani kibaya kitamtokea muda wowote ule. Basi jasho likazidi kummiminika. Akalowana makwapani, mgongoni na kifuani. Paji lake la uso likajawa na maji yatiririkayo ingali macho akiwa ameyakodoa haswa.



    _Hakukuwa na mtu wa kumsaidia?_ Akawaza kichwani. Alitazama dirishani asione jambo bali kiza tu. Akapata wazo la kuita. Kweli akaita kwanguvu mara tatu akiomba msaada kwa yeyote aliyekuwapo karibu.



    Lakini kuita kwake huko akaja kukuona ni bure. Hakusikia muitikio wala kitu chochote kile. Akajikuta anapoteza matumaini ya kusaidiwa. Akaumwa na kichwa akiwaza afanye nini. _je avunje mlango?_



    Ila mlango huo haukuwa mwepesi hata kidogo. Kama ni kuuvunja basi yampasa atumie nguvu kubwa sana maana hakuwa na dhana hata moja mkononi. Na akisha kuuvunja je? Nini atakuja kusema kesho yake kwa mkuu wake wa kazi akamwelewa?

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Darren!" Akasikia sauti ya kike ikimwita kwa kunong'ona. Haraka akageuka na kuangaza akitumia simu yake. Uso wake ulifumwa kwa hofu sana na mkono wake ulioshikilia simu ulikuwa unatetemeka!



    "Nani wewe? Unataka nini kwangu?" Darren akafoka. Mara akasikia sauti ya kiume ikimjibu kwa nje, "mimi mlinzi! Wewe nani humo?"



    Darren akabaini kuna mtu amekuja kumsaidia. Akachungulia dirishani na kumwona mwanaume aliyevalia zare akiwa amesimama hapo. Akamsihi, "nisaidie kufungua mlango tafadhali!"



    Yule mlinzi akabinya komeo na mara mlango ukafunguka! Haukuwa umefungwa kabisa.



    "Mbona mlango u' wazi?" Akauliza mlinzi. Naye Darren hakuwa na majibu, na kwasababu ya kuona vitimbi, hakutaka kustaajabu, akajitoa nje na kufunga mlango huo.



    "Nashukuru sana," akamwambia mlinzi kisha akatupa miguu yake kujiondokea. Mlinzi akamtazama akiishilia kisha akatikisa kichwa na kusema, "ukisoma sana tabu pia." Alafu akajiendea zake.



    Darren akanyookea sehemu ya kuegeshea magari, akajipakia kwenye lile lililo kwake kisha akatimka. Hakuwa sawa kiakili. Na alijitahidi sana kuhakikisha hawazi yale mambo yaliyomtukia ofisini ili asije pata ajali barabarani kwasababu ya msongo.



    Alipofika akamkumbatia mkewe kwanguvu na kumbusu kwenye paji lake la uso. Mtoto alikuwa tayari ameshalala.



    "Darren," Josephine akaita. Uso wake ulikuwa hauna furaha. Ulijawa na makunyanzi na macho yake yakiwa mekundu. "Nilikukumbuka sana. Saa tano hii yaelekea saa sita. Hujawahi kuja nyumbani muda huu."



    "Najua, mke wangu," Darren akampoza. Akamkumbatia na kumwambia, "haitatokea tena. Nakuahidi."



    Basi Josephine hakuteta tena kuhusu hayo, akamwandalia mume wake chakula na kumkaribisha ale. Naye japo alikuwa tayari ameshakula, kwasababu ya kumpa motisha mumewe, akala pamoja naye.



    Wakala kwa ukimya kwa kama sekunde kumi na mbili kabla Josephine hajauvunja ukimya kwa kumuuliza mumewe, "Ulisikia zile habari za moto?"



    Darren akashtuka. Hata mkewe akatahamaki kwanini mumewe alishtuka vile. Bwana akasema, "sitaki hizo habari!' Akiwa amekunja uso. "Sitaki kuzisikia hata robo. Sawa?"



    Hata Josephine hakujibu. Alikuwa amebanwa na tahamaki. Darren akasimama na kwenda zake ndani akiwa ameacha chakula pale mezani.



    _Ana nini huyu?_, Josephine akabaki akiduwaa. Akajiuliza akiwa anatazama kile chakula kilichobakia. Mwishowe akakipeleka jikoni na kisha akazima kila kitu aende kumkuta mumewe chumbani.



    Alipofika huko, akamkuta Darren akiwa bafuni anakoga. Basi akamgojea kitandani amuulize kulikoni. Alipotoka akamwomba msamaha kama alimkwaza, halikuwa lengo lake.



    Lakini pia akataka kujua nini kilikuwa kinamsumbua mumewe. Kwanini aligeuka na kuwa mbogo upesi hivyo? Tangu ameolewa naye hakuwahi kumwona akiwa vile. Shida kitu gani haswa?



    "Josephine, sitaki kusikia habari zile ulizonambia. Huwezi jua zimenisababishia matatizo kiasi gani. Tafadhali nisizisikie tena. Nakuomba." Huo ukawa usemi wa mwisho kwa Darren kabla hajajilalia. Na siku hiyo hakumkumbatia mkewe kama ilivyo ada.



    Alijilaza kando ya kitanda akiwa anatazama ukutani. Mkewe naye akalala, tena haikuchukua muda sana akapitiwa na usingizi akimwacha Darren macho.



    Baada ya muda kidogo, Darren akaamua kujigeuza na kumkumbatia mkewe. Hapo baada ya muda kidogo akabebwa na usingizi mzito. Alikuwa amechoka sana. Ni hofu tu ndiyo ilimkawiza.



    Yalipotimia majira ya saa tisa ya usiku, muda wa shetani, majira ya malaika mkengemfu, Darren akagutuka toka usingizi asijue nini kimemwamsha! Alitazama kushoto na kulia kwake. Kote kulikuwa salama. Akarejesha kichwa chake kitandani aendelee kulala.



    Lakini kabla hajaupata huo usingizi, ghafla ya ajabu akasikia mtoto akilipuka kwa kilio! Akashtuka sana. Mtoto huwa analala chumba cha pili yake hivyo ni ngumu kujua kinachomsumbua. Inamlazimu mtu aende kumtazama.



    Basi akajaribu kumwamsha Josephine, ila akawa mzito. Aliishia kugugumia na kuguna. Naye Darren akawaza mwanamke huyo atakuwa amechoka kwa kulelea mtoto siku nzima, hivyo acha amsaidie kwa kwenda kutazama.



    Akatoka kitandani na kufungua mlango, alafu akaelekea kule kwenye chumba cha mtoto kwa upesi. Alipoingia humo akamkuta mtoto akilia sana. Mdomo ameutanua na macho yake yanamwaga machozi.



    Akamnyanyua na kumbembeleza. Baada ya muda kidogo mtoto akanyamaza lakini asilale. Akambembeleza tena zaidi na zaidi, bado hakuwa anataka kulala. Mpaka kwenye majira ya saa kumi inayoelekea saa kumi na moja, ndipo mtoto akaanza kufumba macho yake kwa usingizi.



    Basi akamlaza na yeye kurudi chumbani akajilalie kwa muda mdogo uliobakia. Alichoka sana. Alipojiweka tu kitandani akajikuta akipitiwa na usingizi mkali wa kumlaza fofofo.



    Kuja kuamka, ilikuwa ni saa nne ya asubuhi!



    "Josephine! Josephine! Mbona hukunamsha lakini?" Akang'aka akiwa amewehuka. Alikuwa nyuma ya muda sana. Saa nne! Kazi gani hiyo ya kwenda muda huo?



    "Nilikuamsha Darren!" Akasema Josephine. "Mara ya kwanza ukanambia nikuache ulale maana umechoka. Mara ya pili ukanambia nisikusumbue!"

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Mimi?" Darren akatoa macho akijinyooshea kidole.



    "Ndio, wewe Darren!" Josephine akamjibu akimbembeleza mtoto. "Sasa ningefanyaje? Nikaona nikuache!"



    Darren akajaribu kufikiria hicho anachomwambia mkewe. Hakuwa anakumbuka hata tone. _Yeye kusema hayo?_



    Kama haitoshi, Josephine akamwambia kuwa, "uliamka mara ya tatu wewe mwenyewe. Ukaenda bafuni na kisha ukatoka kutazama dirishani. Nilipokuuliza hauendi kazini leo? Ukanijibu wataka kupumzika. Darren haukumbuki au wataka tu kun'tania?"



    Darren akatikisa kichwa. Akajikuna kichwa akijaribu kuwaza lakini hakuwa anakumbuka lolote lile. Akachukua simu yake na kumpigia dada Fiona, secretary, kumuuliza juu ya kazini.



    "Sikia Fiona, sijiskii vema. Naomba uniandikie note umpelekee boss."



    "Nimwambieje?" Fiona akauliza. "Muda huu kweli ni wa kutoa taarifa, Darren?"



    "Tafadhali Fiona, fanya namna yoyote kunisaidia. Nitashukuru ukifanya hivyo."



    Kukawa kimya kidogo.



    "Sawa," Fiona akajibu na kuongezea, "na vipi kuhusu ofisi yako?"



    "Imefanyaje?" Darren akauliza.



    "Darren hujui ulichofanya?" Fiona akauliza kwa mshangao.



    "Sijakupata, Fiona. Ni nini unaongelea?"



    "Ofisi yako iko wazi, kila kitu kimevunjwa na kuchanwa. Nayo pia nimwambieje boss?"



    Darren akaachama kwa mshangao.



    Si kwamba hakuwa amesikia alichoambiwa na Fiona, lah, ila hakuwa anaamini. Akauliza, “Unasemaje, Fiona?”



    Fiona akarudia tena kumwambia alichomwambia hapo awali. Basi Darren akakosa ustahimilivu, akasimama na kujiandaa upesi aende huko tofauti kabisa na alivyokuwa ameshapanga. Ndani ya muda mfupi akawa kwenye gari lake, upesi akatimka.



    Akiwa barabarani, akitingwa sana na mawazo, almanusura kumgonga mpita njia. Ni shukrani gari lake liliweza kusimama kwa wepesi kabla ya kumsomba mhanga. Akasimamisha gari na kushusha pumzi ndefu apunguze mihemko na kujiweka sawa kisha akaendesha tena mpaka ofisini.



    Huko mtu wa kwanza kuonana naye akawa ni Fiona. Akiwa ametweta, akamwambia, “Tafadhali, Fiona. Nambie kilichojiri.” naye Fiona akamweleza kinaganaga kuwa ofisi yake imekutwa wazi na ikiwa shaghalabaghala!



    “Lakini imewezekanaje?” Darren akastaajabu. “Jana nimeondoka baada ya kuifunga!”



    Fiona akapandisha mabega. “Darren, nitayajuaje yote hayo?”



    Darren akauliza, “Bossi yupo ndani?” Fiona akamjibu kwa kutikisa kichwa. Darren akanyookea huko. Akagonga mara moja na kufungua mlango. Boss alikuwa amejilaza kwenye kiti chake kirefu akiwa amekumbata viganja vyake. Amevalia suti nyeusi na tai nyekundu.



    Darren akajieleza kwanini hakuwapo kazini siku hiyo, kuwa anaumwa, na hayo ya ofisi kukutwa wazi na vitu vikiwa hovyo, yeye hana habari nayo. Basi Bossi akamsikiza mpaka alipomaliza kisha asiseme jambo, hata salamu akiwa hajaitikia, akafungua droo ya meza yake na kutoa barua bahashani, akampatia Darren.



    Darren akaitazama barua hiyo na kumuuliza, “Ya nini?”



    “Utakapoisoma, utajua ya nini?” Mkuu akamwambia na kisha akamwonyeshea mkono mlangoni.



    “Tafadhali, mkuu,” Darren akaomba. “Uniskize na kila ninachokuambia toka kwenye kinywa changu ni cha kweli tupu.”



    “Darren!” Boss akaita kwa sauti kuu. “Naomba uende!”



    “Tafadhali, naomba uniskize,” Darren akaendelea kuomba. Basi Boss akamwambia, “kaniletee hiyo kazi unayonambia uliifanya hiyo jana usiku!”



    Upesi Darren akatoka na kwenda ofisi kwake. Huko kweli akakuta vitu vikiwa hovyo sana hata akatahamaki asipate majibu. Akajaribu kutazama tarakilishi yake, nayo ilikuwa imepasuliwa kioo, mashine ilikuwa chini! Akaishiwa na nguvu.



    Akajikuta akikaa chini akiwa ameshika kichwa chake. Hakuwa anajua cha kufanya. Hakuwa anajua nini cha kusema. Kwa kama dakika tano akiwa amekaa hapo akapata wazo la kwenda kuonana na mlinzi. Alipoenda kwenye kibanda chake, hakumkuta. Mlinzi huwa anakuja nyakati za jioni na si muda ule.



    Basi Darren akajikuta hana cha kujitetea. Akiwa ameinamisha kichwa chake chini akajongea kujiondokea. Kabla hajafika langoni, akaitwa, alipogeuka akamwona Roby.



    “Ngoja, Dareen!” Roby alimpungia akikimbia. Alipomfikia akamwomba wakaketi kule mgahawani kwani anataka kuteta naye kidogo. Basi wakaongozana kwenda huko, na walipoagiza chakula, Roby akasema, “Nimesikia habari zako, Darren. Ni nini kimetokea?”



    Darren akamweleza yale anayojua. Roby alipoyasikia akashangazwa, lakini hakusita kumpatia moyo. “Yote ni maisha, Darren. Nadhani sasa ni muda wa kuangalia mlango mwingine.”



    Akamshika bega na kumwambia, “Ni muda wa kufanyia kazi lile shauri lako hivi sasa.”



    “Nitawezaje, Roby?” Darren akasema kwa sauti ya chini. Macho yake yalikuwa yameingia ndani. Mdomo wake umemkauka. “Sina pesa hivi sasa. Nitawezaje kuyafanya hayo?”



    Roby akatikisa kichwa. Akafikiri kidogo kisha akamwambia, “Ebu ngoja. Nadhani kuna kitu tunaweza kufanya. Niachie hii siku na kesho yake, nitakutafuta. Sawa?”



    Basi Darren alipomaliza kula akajiendea zake. Alikuwa ametingwa sana na mawazo. Hata alipofika nyumbani kwake, mkewe akatambua kuwa mumewe hakuwa sawa. Alipomuuliza nini shida, Darren akampatia barua toka kwa bosi wake. “Nimefukuzwa kazi.”



    Josephine akasoma barua hiyo na mpaka alipomaliza, machozi yakawa yamemjaa machoni mwake. Alikuwa amevunjika moyo, lakini akamtia moyo mumewe. “Usijali. Ni changamoto za maisha tu. Litapita.” kisha akambusu na kujilaza kifuani mwake.



    Siku hiyo ikaenda Darren akiwa na mkewe na mtoto wake. Hata siku inayofuata wakaamka na kudumu siku nzima nyumbani. Darren akacheza na mwanaye na pia mkewe. Ilikuwa ni siku nzuri. Hakuwahi kukaa na familia yake katika namna ile tangu pale alipoipata. Kwa muda akasahau matatizo yake.



    Siku iliyofuata, kama vile Roby alivyomuahidi, akamtafuta kwa njia ya simu. Walipoongea wakapanga kuonana majira ya jioni Roby akitoka kazini. Basi majira hayo yalipofika, Darren akaenda nyumbani kwa Roby kukutana naye.



    Wakateta kujuliana hali kabla Roby hajaanza kumwambia Darren lengo la wito wake hapo.



    “Lile wazo lako laweza kutimia Darren. Tunachokihitaji hivi sasa ni dhamira ya kweli, na si pesa!”



    “Umepata pesa?” Darren akawahi kuuliza akitoa macho.



    “Tuliza munkari, Darren,” Roby akasihi. “Sijapata pes yoyote, ila pesa ipo. Tunachotakiwa kufanya ni kuandika muswada wa mipango yetu, muswada mzuri wa kueleweka, alafu kuna mahali tutapeleka na kupata pesa.”



    Darren akanywesha uso. “Roby, unadhani ni kitu chepesi namna hiyo?”



    “Skiza, Darren. Najua ninachokuambia. Na ninakuambia kwa uhakika wote. Kuna kampuni mimi nimeshaongea nayo, nao wako radhi kusaidia kwa kila namna. Niamini mimi. Najua wewe ni mzuri kwenye maandishi, andika hiyo kazi nami nitakuonyesha namna mambo yanavyokwenda,” alisema Roby kwa kujiamini kisha akanyanyua glasi yake ya kinywaji na kuigongesha na ya Darren.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tutafanikiwa, Darren. Amini hivyo.”



    Basi Darren akarudi nyumbani akiwa na mwanga wa matumaini. Akamkumbatia mkewe na kumjuza habari hizo, naye mkewe akafurahishwa sana. Akamwombea afanikiwe zaidi na zaidi.



    Ulipofika usiku wa saa mbili, akaanza kuandika ule muswada ambao Roby alimtaarifu. Akaandika kwa ustadi akitumia masaa. Alipomaliza akausoma tena upya na upya. Akarekebisha aliyoyaona yanastahili, kisha akajilaza ikiwa ni saa tisa kasoro usiku.



    Kesho yake akaonana na Roby na kumpatia ile kazi. Naye Roby akaipitia na kupendezwa nayo sana. Akatabasamu na kumwambia Darren, “Tumeshapata pesa hapa!”



    Akamwahidi wataonana mwisho wa juma tena akiwa na majibu ya maana. Na kweli ilipofika mwisho wa juma, Roby akamwambia Darren wakutane kumpatia majibu ya ule muswada, ila si nyumbani tena bali kwenye jengo refu la HIGH TOWERING CONSULTANCY.



    Darren akiwa na hamu kubwa, akajongea huko. Akakutana na Darren na mwanamke mrembo aitwaye Isabel. Mwanamke huyo alikuwa amevalia suti ya kijivu ilivyomkaa vema. Uso wake ulikuwa umepambwa na miwani nzuri ya macho. Nywele zake nyeupe na laini.



    Kwa makadirio alikuwa na miaka thelathini na tano, sita ama saba. Hakuwa mnyimi wa tabasamu. Tabasamu lake zuri. Na alikuwa mtu mchangamfu, nadhifu mwenye macho ya kuvutia.



    Roby akamtambulisha Darren kwa Isabel na kisha Isabel akajitambulisha kwa Darren kama ‘Executive Director’. Waliposalimiana na kutambulishana Isabel akakiri kuvutiwa na ule muswada na basi wao kama kampuni watawekeza takribani dola za kimarekani milioni kumi!



    Swala hilo likamgusa sana Darren. Haukuwa uwekezaji mdogo huo kabisa. Aliona sasa ndoto yake inaenda kukamilika. Akashukuru na kisha akauliza ni kivipi uwekezaji huo utakuwa unarejeshwa.



    Isabel akatabasamu kwanza kabla hajajibu, “ni mpaka pale mtakapoanza kutengeneza faida. Kampuni itakuwa inachukua gawio la asilimia ishirini tu la faida yenu nzima!”



    Darren akaridhia. Akamkumbatia Roby akimwona kama malaika mwokozi kwake. Wakafungua akaunti ya pamoja na pesa ikaingizwa baada ya siku mbili tu. Na pasipo kukawia wakapata eneo na kuanza kulifanyia kazi kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya huduma za tiba ya wanyama.



    Kwa kama mwezi mmoja tu, kila kitu kikawa tayari na huduma zikaanza kutolewa. Isabel naye akatembelea hilo eneo na kuomba kupewa mrejesho wa maendeleo ya huduma kila mwisho wa mwezi, lakini zaidi alikuwa amekuja na mbwa wake kwa ajili ya kumpatia chanjo.



    Darren akamshughulikia kikamilifu na Isabel kabla hajaenda, akampatia Darren kadi yake ya biashara.



    “Utan’tafuta utakapokuwa na tatizo.”



    Kisha akamtazama Darren machoni na kumwambia, “Sawa?”



    Darren akajibu, “Sawa.” akitabasamu.



    Aliporudi nyumbani alikuwa amechoka sana, lakini kabla hajajilaza akapata kuongea na mkewe juu ya maendeleo yake ya kazi. Mkewe naye akafurahishwa sana na hatua za mumewe, basi zaidi akamtia moyo.



    Akamsihi tu kuwa anampenda na kila anapokuwa anakutana na gumu lolote basi akumbuke kuwa familia yake inampenda sana. Usiku ukawa mzuri na hata walipoimalizia kwa kula na kuoga.



    Kesho yake kama ilivyo ada, Darren akaamka na kwenda kazini. Akafanya sana kazi pamoja na mwenziwe, kisha jioni ilipoingia Roby akamhasa waende mahali kupata chochote kitu kabla hawajaachana. Naye Darren akapendezwa na hilo wazo.



    Wakaenda kwenye moja ya mgahawa wa KFC, hapo wakaagiza chakula na kinywaji. Wakala wakifurahia utamu wake na huku wakipiga soga za hapa na pale.



    "Darren," Roby akaita na kusema, "Nadhani sasa ni wakati wa mimi kuoa!"



    Darren akashangazwa. "Kweli?" Akamtazama Roby akikodoa.



    "Ndio. Nina mpango huo. Vipi wasemaje?"



    "Sina neno. Ni wazo zuri ila sijawahi kumwona mpenzi wako. Huwa unamficha kwa wivu nini?" Darren akasema na kisha wakaangua kicheko.



    "Hapana ndugu. Nadhani tunapishana muda ndo' maana hujapata kumjua. Mwisho huu wa wiki tutakutana wote, nitamvesha pete ya uchumba!"



    "Wow! Ni wazo zuri sana. Nami nakuunga mkono, Roby. Bila shaka itakuwa siku nzuri sana baina yetu."



    “Ni kweli. Nampenda sana mchumba wangu. Japo bado mambo hayajakaa vema, naona ni muda stahili wa kumwonyesha mapenzi yangu kwake.”



    “Nakupongeza sana kwa hilo. Vipi itakuwa ni surprise ama?”



    “Ndio, itakuwa ni surprise. Naomba unipe wazo juu ya hilo, Darren. Sitaki aone kama niliyekuwa nikiyapanga yote haya.”



    Basi Darren akampatia mawazo yake naye akayapenda sana. Wakakubaliana cha kufanya na muda wa kuyafanya kisha wakaagana na kila mmoja akaenda na njia yake.



    Darren alipofika nyumbani akampasha habari hizo mkewe. Naye akafurahishwa nazo sana. Akakumbuka kipindi Darren anamvesha pete. Ilikuwa ni siku ya ajabu asiyoweza kuisahau maishani mwake.



    “Ile siku ilikuwa ya kusisimua sana, Darren. Nami siwezi kusahau tabasamu lako na namna ulivyonipigia magoti. Haki ulifanya moyo wangu ukimbie kwa haraka. Nilijihisi fahari sana.”



    Darren akafurahishwa na hayo maneno. Akanyanyuka na kumbeba mkewe kisha akamuuliza, “Na vipi kuhusu siku ile nilipokuwa nawe kanisani?”



    Josephine akacheka kidogo akiziba mdomo wake kisha akatazama dari. “Loh! Ile ilikuwa ni siku ya maajabu kwangu, Darren! Nakumbuka kila jambo tangu asubuhi mpaka usiku wake. Nawezaje kusahau?”



    Basi Darren akampeleka mkewe chumbani na kumlaza kitandani. “Tazama. Wewe ndiye furaha yangu ya kweli. Upendo wako umejaza ndani ya moyo wangu na mimi nafurahia uwepo wako kila siku.”



    Ni kweli Darren alimpenda sana mkewe. Alishamsahau kabisa Melissa na vimbwanga vyake. Hakuwa anamkumbuka tena mdhalimu huyo. Mwanzoni hakuwa anaamini kama atakuja kumsahau Melissa. Alikuwa ameganda sana kwenye kichwa chake. Alimpa sana moyo wake. Ila kwa sasa dunia ilikuwa imegeuka.



    Tena imegeuka na kubadili mhimili kabisa.



    Lakini kwa Melissa …



    Vipi kwa Melissa?



    Darren hakuwa anajua. Na natamani asingekuwa analijua kamwe. Melissa alikuwa karibu yake kuliko alivyokuwa anadhani. Melissa alikuwa karibu yake pengine kuliko muda wowote ule.



    Melissa alikuwa anafanya kazi yake. Tena taratibu na kwa ustadi wa hali ya juu. Mkono wake ulikuwa unagusa njia. Masikio yake yanaskiza upepo ukitikisa vipande vya majani. Sauti yake inaimbia fukweni mwa bahari.



    Machho yake yakitawanyika kila pande. Na ndimi zake zikiwa zinasukutua mdomo kwa kila kona yake.



    Melissa alikuwa ni shetani ambaye Darren asingewahi kumwazia kuwa. Ile tamu kwenye chungu. Lile tone la sumu ya mamba kwenye maji yaliyojaza jaba la miamba.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku zikapita, tena zikikimbia haswa. Na ile siku ya Roby kumvesha pete mchumba wake ikawadia. Siku hiyo Darren na Roby wakawasili mapema sana. Wakatengeneza mazingira ya kufanya mambo yao, ilikuwa ni pembeni ya fukwe ya bahari, na muda wa mchumba wa Roby kuwasili ulipowadia, Darren akajificha.



    Walikuwa wameadhimia punde pale mpenzi wa Roby atakapotokea, basi Darren atajivika barakoa usoni na kuigiza amemkaba Roby na kumchoma kisu. Lakini kwa wakati huo huo atampatia Roby kijumba cha pete, hivyo wakati mchumba wa Roby atakapokuwa anamlilia mpenzi wake anayekufa, Roby atatoa kijumba cha pete na kumwomba akubali kuwa mke wake!



    Ulikuwa ni mchezo wa hatari.



    Basi Roby akamkumbatia mpenzi wake na kumuuliza kama amefurahia kuwapo hapo mwisho huo wa juma. Naye mpenzi wake akasema amefurahia.



    Naye mpenzi wake huyo alikuwa ni Melissa.



    Uzuri wake ulikuwa upo palepale. Macho yake mazuri ya kumlaghai nyoka atoke shimoni. Uso wake mtamu na sauti ya kukimbiza mapigo ya moyo.



    “Kwanini umeamua kunileta ufukweni, Roby?” Melissa akateta kwa sauti yake tamu.



    “Haujapapenda?” Roby akauliza wakiwa wanasonga mbele.



    “Nimepapenda,” Melissa akamjibu. “Ila sikuwa nadhani kama utanileta huku. Kama ningelikuwa najua na kujipanga basi ningebeba na nguo za kuogelea. Au wewe umebebelea?”



    “Hapana. Nipo kama nilivyo mpenzi.”



    Basi wakazidi kusonga mbele zaidi na zaidi Roby akimvuta Melissa eneo la tukio. Ndani ya moyo wake alikuwa ana hamu kubwa ya kumshangaza Melissa. Alitamani kumwambia kuhusu mpango wake ila akajitahidi kujibana. Alitamani kupayuka kwa kupaliwa na furaha lakini akajibana sana.



    Wakazidi kusonga.



    Walipopiga hatua kama tatu tu ndipo Darren akawa amehakiki kile alichokuwa anakiona. Alimwona Melissa! Mwanamke aliyekuwa amemsahau. Alimwona Melissa, mwanamke mwenye kubebelea kitanzi mkononi mwake!



    Akabaki akiduwaa, ameachama mdomo na kung’aza macho yake. Na pasipo kutarajia, Melissa akarusha macho kumtazama pale alipokuwapo. Macho kwa macho wakakutana.



    “Melissa!” Darren akatamka akitikisa kichwa chake. “Niache Melissa!” akanong’oneza. “Niache Melissa!” kisha akajikusanya na kukimbia sana. Aliliendea gari lake na kuzama ndani akitupia barakoa yake pembeni.



    Hakuamini alichotoka kuona. Ni kweli amemwona Melissa! Moyo wake ulimwenda mbio mno. Akahema sana akitokwa na jasho. Akataka kuwasha gari aende lakini mikono ikamtetemeka sana. Akaona ni kheri angoje kwani anaweza pata ajali akilazimisha kwenda.



    Kule fukweni Roby akangoja sana. Akatazama kushoto na kulia akiwa anaishiwa na uvumilivu. Darren yuko wapi?



    “Mpenzi,” Melissa akaita na kuuliza, “Kuna tatizo?”



    “Hapana. Hamna ta--” Roby akateta akitupa macho. “Hamna tatizo!”



    Basi baada ya kukaa sana hapo pasipo kuona kitu, akaamua kuondoka zake na mpenzi wake. Moyoni akabeba kinyongo kikubwa juu ya Darren. Akabeba pia na maswali, kwanini Darren amemfanyia hivyo? Kama kungalikuwa na tatizo si angemwambia mapema?



    Moyo wake ukawa mzito. Akaghafirika sana.



    Walipoenendea mahali ambapo Roby alipakia gari, Melissa akazama ndani lakini Roby akang’aza tena macho kama atamwona Darren. Bahati upande wake wa kulia, kwa mbali, akaona gari la Darren! Basi akalijongea upesi akimwambia Melissa amngojee kwa dakika chache.



    Alipolifikia gari hilo, kwa ndani akamwona Darren, basi akaanza kufoka kabla hajafika, “Mambo gani hayo Darren unanifanyia? Ikama ungalikuwa hautaki si ungelinambia?”



    Akachngulia dirishani kumtazama Darren. Akamwona akiwa amefumba macho kama mtu aliyemezwa na usingizi. Lakini matundu ya pua yake yakiwa yanachuruza damu kwa wingi!



    Akatahamaki! “Darren!” akaita akifungua mlango upesi. Akamtikisa Darren kwanguvu akimwita lakini Darren hakuitikia kabisa. Zaidi damu zikarukia mpaka kwenye mikono ya Roby. Basi upesi Roby akamhamishia Darren kwenye kiti cha abiria na kisha akawasha gari kumwahisha Darren hospitalini upesi awezavyo!



    Akiwa njiani, Darren akanong’ona kwa mbali, “Ni jini … Roby, Roby, ni jini … atakuua … ata--”



    “Nini unasema Darren?” Roby akapaza sauti kuuliza, akitamani kumtazama Darren, akitamani kutazama barabara. Lakini Darren hakuweza kuongea tena. Macho yakajawa na ukungu na mwishowe akapotelea kabisa gizani.



    “Roby …”



    ***







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog