Search This Blog

UNA NINI LAKINI MELISSA - 1

 

    IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



    *********************************************************************************





    Simulizi : Una Nini Lakini Melissa

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Darren alipotazama saa yake ya mkononi akatambua wazi kuwa amekawia. Akasonya akijivuta toka kwenye kitanda. Ilikuwa ni saa tatu asubuhi na alitakiwa kufunga safari mnamo saa kumi na mbili asubuhi. Tafakari. Haraka akaelekea bafuni kukoga na asipake mafuta wala kuchana nywele, akavaa na kujiondokea kwenda kituoni akapande basi.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alipofika huko, akalazimika kusubiri kwa lisaa limoja kabla hajapata basi analotakiwa kulipanda. Alipolikwea, akaenda nyuma kabisa ya basi na kuketi akilaza kichwa chake dirishani, basi ule usingizi alioukatiza, ukamsomba tena na kumfanya alale fofofo mpaka kuchuruza mate.



    Akalala kwa lisaa limoja kabla hajashtuliwa na simu yake mfukoni. Simu ilikuwa inatetemeka na kutoa sauti kwa pamoja. Akaichomoa na kuitazama akiwa amefichama macho yake kama mtu aliyemulikwa na mwanga mkali usoni. Akaona ni Melissa kiooni! Melissa mpenzi wake.



    Kabla hajapokea, akasafisha koo lake na kufanya zoezi la kuzungumza asigundulikane ametoka kulala, kisha,



    “Melissa …”



    “Umelala, Darren?” Ilikuwa ni kauli ya kwanza toka kwa mwanamke huyo. Japo Darren alijitahidi kuficha, bado haikusaidia. Ikambidi tu atabasamu.



    “Sijalala, Melissa.”



    “Mbona sauti yako kama ya mtu aliyetoka kulala?”



    “Masikio yako tu. Mimi niko kwenye basi sasa, hausikii?”



    “Unaenda wapi, Darren?”



    “Kwa bibi!”



    “Mbona hukunambia?”



    Darren akapiga kofi paji lake la uso. “Nilisahau, Melissa. Nisamehe.”



    “Unarudi lini?”



    “Nadhani keshokutwa. Sitakaa sana huko.”



    “Keshokutwa ndo’ hutokaa?”



    “Melissa, ni baada ya siku moja tu ambayo ni kesho. Kuna umbali gani hapo?”



    Kukawa kimya kidogo. Sauti ya Melissa ikaguna alafu ikasema, “Sawa. Safari njema, Darren!”



    “Ahsante, mpenzi.” Darren akakata simu na kuegesha kichwa chake dirishani ila mara hii hakulala tena bali akitazama yanayoendelea huko nje ya basi. Angalau usingizi ulikuwa umekwisha japo bado macho ni mazito. Alipiga mihayo mara kadhaa hapa na pale.



    Basi kichwani mwake, kwa kukosa cha kufanya, akaanza kuwaza mambo kadhaa, haswa ya huko anapoelekea. Huko kijijini, countryside, kutembelea nyumba ya marehemu bibi yake.



    Kichwani mwake akapata kuona picha ya bibi yake kipindi yu hai. Namna alivyokuwa mcheshi na mchangamfu lakini pia mkarimu. Akajikuta akitikisa kichwa kwa masikitiko. Hakika atamkumbuka sana. Na pengo lake ni wazi litaonekana. Alikuwa anawapa sababu ya wao kutembelea kijijini lakini hivi baada ya kifo chake, hakutakuwa na safari hiyo tena, aliwaza Darren. Hata wazazi wake wameshakaa na kuamua kuwa nyumba hiyo ya marehemu iuzwe.



    Hakupenda hilo lakini hakuwa na namna. Hakujua ni nini wazazi wake waliwaza kichwani mpaka kufikia maamuzi hayo, ila kwa uono wake yalikuwa ni maamuzi ya kipumbavu. Ya kipumbavu sana!



    Akajikuta akisonya mwenyewe na kutikisa kichwa. Akasonya tena na kutikisa kichwa kabla hajaamua kuachana na mawazo hayo na kupekua simu yake kubwa. Akapekua ghala lake la picha na video kisha akazama mtandaoni



    Kwa umbo, Darren alikuwa ni kijana mrefu mwenye mwili uliojengeka vema. Nywele zake nyeusi, uso wake mrefu, macho yake yamechongoka kana kwamba ya nyoka, lips zake nyembamba na kidevu chake chembamba kimefunikwa na ndevu.



    Ni mtaalamu wa mifugo, Veterinarian ama vet kwa ufupi. Lakini mbali na kazi yake hiyo hobby yake kubwa ni kuogelea. Ila mara kadhaa apatapo muda hupenda pia kusoma vitabu na kuangalia tamthilia.



    Kwakuwa alikuwa tayari ana kazi yake na umri wake, 25, ulikuwa unamruhusu kutoka nyumbani, basi alifanya hivyo. Alipanga katika jiji la California, ambapo palikuwa karibu na eneo lake la kazi, lakini pia karibu na mpenzi wake Melissa.



    Melissa, mwanamke mwembamba chotara wa kilatini na kizungu, alikuwa ni mfanyakazi katika supermarket moja ndani ya jiji la California. Alikuwa ni mwanamke mzuri haswa. Macho yake yangekufanya uzame mtaroni ukimtazama. Tabasamu lake lingekufanya usahau kumdai ulichomkopa.



    Nywele zake ni laini kama hariri ya sufi. Cheko lake ni kama ndege wa asubuhi huko msituni. Mwendo wake ni wa madaha akiona huruma kukanyaga ardhi. Na zaidi umbo lake, aliloliteka toka kwa mama yake mlatini, lingekufanya ukawa mdhaifu wa maungio ya mwili. Si kwamba alikuwa na umbo kubwa, hapana! Ila mwanamke ambaye kila kiungo chake kimekaa pahala pake, na si kuparamiana.



    Kila kitu kilikuwa ‘balanced’. Mungu alitenda. Na huenda wewe ungemwona mwanamke wa kawaida, tena sana, ila kwa Darren, huyu alikuwa ndiye alfa na omega. Hakuwahi kumwona mwanamke kama huyu.



    Kila anapomtia machoni lazima ahisi vinyweleo vyake vimesimama, moyo wake unaruka pigo, na mate yanamkauka mdomoni! Anamwona kila siku lakini bado hajamzoea. Na kama ukimuuliza nini lengo lake maishani, basi atakwambia la kwanza ni kumwoa Melissa. La pili ni kumwoa Melissa na la tatu ni kumwoa Melissa!



    Lakini kuna kitu hajafahamu kuhusu Melissa. Na kuna kitu pia hajafahamu kujihusu yeye pia. Hawezi kumwoa Melissa. Na Melissa hawezi kuolewa na yeye. Huenda jambo hili likawa ni gumu sana kwa Darren, ila ndiyo uhalisia wenyewe.



    Pengine mtu angekuja na kumwambia hilo angemwona ni adui, na angempa ushahidi wa mahusiano yao yaliyodumu kwa miaka miwili. Lakini bado isingetosha kupinga ukweli. Watu hawa hawawezi kuwa pamoja! Si ardhini, majini ama hewani.



    Ninayekuambia haya naitwa Byron. Si mtu wa maana sana ila ni muhimu ukalishika jina langu kwa manufaa ya huko mbeleni. Na vipi kuhusu mwonekano wangu? … Mimi ni mwanaume mwenye miaka sabini na nane. Kichwani nimejawa na mvi. Mkononi mwangu nabebelea fimbo ya kunisaidia kutembea maana miguu yangu imechoka na mwili wangu umevikwa joho rangi ya kahawia.



    Hayo yanakutosha. Mengine utayajua kadiri na muda.



    Baada ya kuchoma masaa matatu njiani, Darren alishuka toka kwenye basi na kuanza kujongea upande wake wa kaskazini. Alipotembea kwa takribani dakika kumi, akawa amefika mbele ya nyumba zee ya marehemu bibi yake. Hapo alikuwa ana kazi moja tu ya kufanya, nayo ni kusafisha nyumba hiyo ipasavyo.



    Nyumba hii ilikuwa na vyumba viwili tu, ila uwanja wake wa nje ndiyo mpana. Hivyo basi Darren akaona ni stara akaanza kusafisha nje kwanza, alafu huko ndani, hamna shida, atapafanyia kazi ambayo alifahamu fika haitamchukua zaidi ya lisaa.



    Akateka fyekeo na jembe. Akavuja jasho kwa muda wa masaa matatu kabla hajawa hoi na kwenda ndani kuoga, kula na kupumzika. Kesho yake akamalizia huko nje, na keshokutwa yake, akawa anahusika na ndani tu. Akapasafisha kwa kufyagia na kudeki.



    Akiwa anasafisha chumba cha bibi yake, ndipo akakutana na picha kadhaa za zamani. Katika picha hizo, akamwona bibi na babu yake wakiwa vijana, pamoja pia na mama yake angali mdogo. Akafurahi sana. Akaketi kitandani akiendelea kuangalia picha hizo.



    Lakini katika moja ya picha hizo, kuna ambayo ilimshangaza Darren. Kulikuwa na watu wanne pichani wote wakiwa ni mabinti. Binti mmoja alimtambua kuwa ni bibi yake, wa pili hakumtambua kabisa, wa tatu pia, ila wa nne alimtambua baada ya kumtazama vema, lakini hakuamini.



    Binti huyo wa nne alikuwa ni Melissa!



    “Hapana,” akajisemea mwenyewe akitikisa kichwa. Akaigeuza picha na kuitazama kwa nyuma, ilikuwa imeandikwa mwaka kwa peni, mwaka 1956! Darren akatahamaki.



    Akafikicha macho yake na kuangaza tena. Hakuna kilichobadilika. Melissa alikuwa pichwani! Picha moja na bibi yake wakiwa ujanani.



    Darren Akadhani amewehuka.



    Mama akatoa macho kwa mshangao. “Hapana!” akakanusha akitikisa kichwa. “Hapana, mpenzi. Ni hatari!”



    “Huoni ni hatari akiendelea kutokujua?” Baba akauliza. Mama akatazama chini akiwa na sura ilonywea. Alikuwa anahofia.



    Alikuwa anatakiwa kuhofia.



    ENDELEA

    Hakusema jambo mpaka pale Baba alipomshika bega na kumwambia kwa upole, “nikamwambie? Niruhusu nifanye hivyo!”

    Mama akatikisa kichwa. “Hapana, Gerald. Si muda sahihi hivi sasa. Ni mapema sana. Tungoje kidogo tafadhali.”

    Baba akamtazama asiseme jambo bali kushusha pumzi ndefu puani na kisha akajiendea zake ajiandae kuoga. Muda si mrefu, Darren akaaga anakwenda. Mama akamwomba sana ile picha ya Bibi lakini Darren akagoma kumpatia. Kwa kumpoza akamwambia kuwa atamrudishia kesho kutwa yake.

    “Nakuahidi mama,” Darren akaapa kabla hajaenda zake. Alinyookea nyumbani kwake kisha akampigia simu Melissa akimwomba aje nyumbani kwake kwani kuna dharura.

    Kama baada ya lisaa, Melissa akawa amefika hapo. Alikuwa amevalia topu nyeupe na jeans nyeusi. Alipendeza. Tuseme hata akivalia gunia mwanamke huyu hupendeza kutokana na umbo na uzuri wake.

    Akamkumbatia Darren na kisha akamjulia hali kwa tabasamu pana. Lakini akafanikiwa kuona jambo usoni mwa Darren. Mwanaume huyo hakuwa sawa.

    “Kuna tatizo Darren?” akauliza kwa sauti yake ya chini.

    Darren ndipo akatoa picha ile, picha ya Bibi yake na wale wenza, na kumwonyeshea Melissa. “Melissa huyu ni wewe?”

    Kwa mwanzoni Melissa akapigwa na butwaa. Mtu alikuwa akifanana naye vilivyo. Ilikuwa ni ajabu. Akachukua kama dakika mbili akitazama picha ile kisha akamuuliza Darren, “umetoa wapi picha hii?”

    “Kwa Bibi yangu,” Darren akajibu. “Yule niliyekuambia kumhusu.”

    “Yule marehemu?” Melissa akauliza upesi. Brian akatikisa kichwa. “ Ndiye huyo huyo!”

    “Na yeye ni yupi kati ya hawa?”

    “Huyu hapa!” Darren akaonyeshea kwa kidole. “Hapa ni mnamo miaka ya alfu moja mia tisa na hamsini!”

    Melissa akaendelea kuitazama ile picha kana kwamba mtu anayekumbuka jambo. Darren akamuuliza, “Vipi Melissa? Umemtambua huyo mtu?”

    Melissa akatikisa kichwa akiendelea kutazama ile picha alafu nwishowe akairejesha mikononi mwa Darren na kusema, “Anafanana na mimi sana!”

    “Ndio! Hata mimi nilishangazwa sana ndiyo maana nikaibeba nije nikwonyeshe!”

    Melissa akawa amenyamaza kimya. Macho yake yalionyesha yu mbali kifikra. Darren akamtazama na kumwita mara mbili kabla mwanamke huyo hajashtuka na swali, “Unaweza ukanipeleka huko kwa Bibi yako?”

    “Amefariki!” Darren akamjibu akimtolea macho. “Au wataka kuona kaburi?”

    “Twende hivyo hivyo!” Melissa akasihi. “Sidhani kama kutakuwa na shida, Darren!”

    Darren akafikiri kidogo kisha akamwambia wataenda huko mwisho wa wiki kwani atabanwa na kazi hapa siku za usoni.

    “Darren,” Melissa akaita akijitengenezea kumtazama mwanaume huyo. “Naomba, nipo chini ya miguu yako, tafuta siku ya karibuni. Mpaka mwisho mwingine wa wiki ni mbali sana!”

    Darren akashangazwa na hitaji hilo la ghafla. “Melissa, ni haraka mno! Vipi kuhusu rat—”

    “Tafadhali, Darren!” Melissa akanong’ona kwa huruma. Macho yake yalipoa na uso wake ukiwa kama ule wa mtoto aombapo kitu. Darren akashindwa kukataa. “Sawa, basi tufanye keshokutwa.”

    “Kwanini sio kesho?” Melissa akauliza kwa upole. Darren akamtazama kwanza mwanamke huyo, alafu punde uso wake ukawa mgumu, “Melissa kwani kuna nini huko kitakachopotea tukikawia?”

    “Darren, ungalikuwa wewe umefanana na mtu pichani hivi usingelipata hamu ya kujua?”

    “Sawa,” Darren akalegea. “Tutaenda huko hiyo kesho.”

    Basi baada ya hapo wakafanya mpango wa chakula, wakawasha pia na runinga watazame baadhi ya filamu. Wakachoma hapo masaa mpaka kiza kilipoingia. Wakala na kuendelea kutazama runinga wakiwa wanapeana mabusu na maneno matamu.

    Usiku ulipokuwa mkubwa zaidi wakaenda kitandani, na kabla ya kulala ‘wakanyooshana migongo’. Wakachoka sana na basi usingizi ukawakwapua kwa upesi sana wasidumu hata lisaa.

    Wakiwa wamelala, ni saa tisa ya usiku, ghafla Melissa anaamka na kuketi kitako kitandani. Kuna jambo linamtatiza kichwani. Anamtazama Darren, yu hoi hajielewi. Basi anatoka kitandani na kwenda kuifuata ile picha ya Bibi pale mezani.

    Akaiteka kwa mikono yake membamba kisha akairejea kuitazama kwa macho yake makavu pamoja na kiza. Baada ya sekunde mbili, akasema kwa kunong’ona, “Tabitha … Cassandra … Bessie.!”

    Akisema majina hayo akawa anamtazama mmoja baada ya mwingine. Punde akasikia Darren akijigeuza kitandani, upesi akatazama. Mwanaume huyo hakuwa ameamka. Bado alikuwa kwenye lindi kubwa la usingizi. Melissa akaachana naye na kuendelea kutazama ile picha, mwishowe akaiweka kifuani mwake akiwa na uso wa mawazo.

    “Tabitha, nangoja jua lichomoze,” akasema hivyo na basi akarejea kitandani mwake na kulala.

    Masaa yakazidi kusonga mpaka kufikia majira ya saa kumi na moja. Hapo Darren akashtuka toka usingizini na kuangaza. Alidhani pengine amekawia. Akafungua dirisha na kutazama nje, bado kiza. Basi kabla hajajirudisha kitandani akaenda chooni kwa haja ndogo.

    Alipotoka huko, kama bahati tu, akajikuta macho yake yakiangukia mezani pale alipoacha picha yake. Akasonga karibu na kuitazama tena picha ile akitumia msaada wa taa ndogo ya mezani.

    Akajikuta anatabasamu kumwona mtu mithili ya Melissa. Ila alipoitazama picha hiyo zaidi akagundua yule Melissa wa pichani alikuwa ana kovu dogo chini ya goti lake la kushoto. Aliweza kuona hivyo maana gauni lilikuwa limeishia magotini.

    Basi kwa hamu ya kutaka kujua akamsogelea Melissa kitandani kisha akamtazama mguu wake wa kushoto. Hapo akaona kovu lile lile la kwenye picha! Ni kovu dogo ambalo hakupata hata kulijua kwa muda wote huo ambao amekuwa na Melissa kwenye mahusiano.

    “Inawezekanaje?” akajiuliza. Akairejesha picha ile mezani kisha akazima taa na kurejea kitandani. Akalala nyuma ya mgongo wa Melissa aliyekuwa amelala kiubavu na kidogo akapitiwa na usingizi.

    Ila hapo Melissa akafungua macho. Macho yake yalikuwa makavu tofauti na mtu atokaye usingizini. Melissa hakuwa amelala. Melissa alisikia na kuona kila kitu ambacho Darren ametoka kukifanya.

    Hakufanya kitu na badala yake akalala. Asubuhi ya saa moja kamili wakaamka na kujiandaa kwa ajili ya safari. Kufikia saa tatu tayari wapo kwenye basi wakienda kijijini, countryside.

    Walipopoteza masaa matatu barabarani wakafika kituoni. Wakatembea kwa ufupi kabla ya kufika kwenye nyumba kubwa ya Bibi. Hapo Melissa akasimama kuitazama nyumba hiyo kwa umakini. Naye Darren aliyekuwa ametangulia mbele ikamlazimu amrejelee, akatabasamu akimwambia, “Ndiyo hapa! … ni pazuri, sio?”

    “Ndio, ni pazuri!” Melissa akajibu pasipo kumaanisha kwa uso wake, wakazama ndani. Humo akang’aza sana macho, ndani ya nyumba nzima na pia huko nje kana kwamba mtu anayetaka kununua akitaka kubaini madhaifu.

    Walipokuwa nje, akamwomba Darren amwonyeshe kaburi la Bibi yake. Naye Darren pasipo ajizi, akampeleka magharibi ya mbali ya nyumba hiyo na kumwonyeshea, “Ndiyo hapa!”

    Melissa akasoma kibao cha kaburi. Kilisomeka kwa jina la Cecilia Goodwin. Akauliza, “hili ndilo jina la bibi yako?”

    “Ndio,” Darren akamjibu.

    “Ahsante. Tunaweza tukarudi ndani.”

    Wakarudi huko na Darren akampatia Melissa picha za Bibi yake. Kwa taratibu akazitazama moja baada ya nyingine.

    “Sikumwona mtu huyo tena,” alisema Darren. “Yupo kwenye picha moja tu.”

    Melissa asiseme kitu akaendelea kukagua picha zile. Alipomaliza akamkabidhi Darren na kisha akalaza kichwa chake kochini. Darren akazirejesha picha hizo na kisha kujumuika na Melissa hapo sebuleni.

    Usiku ulipowadia, Melissa akamnong’oneza Darren kwenye sikio lake la kulia, “Nakuhitaji mpenzi.”

    Darren akamtazama mwanamke huyo kwa kukodoa, “Melissa, tumefanya jana tu!”

    Melissa akang’ata lips zake na kulegeza macho. “Kwani kuna ubaya, mpenzi?” akauliza akiweka kiganja chake kifuani mwa Darren.

    “Hamna ubaya ila si kawaida yako.”

    Melissa akatabasamu. Akafungua kifungo kimoja cha shati la Darren. “Sasa nitafanya nini na ingali u karibu yangu, tena tukiwa wapweke wenye nafasi?” akateta kwa sauti ya puani.

    Darren asijibu, mwanamke huyo akaanza kubusu kifua chake na hatimaye akatimiza adhma yake. Darren akawa hoi kana kwamba amelima ekari za mbaazi. Hata alipojilaza hapo kochini akawa kama mfu!

    Basi Melissa akajivalia nguoze na kisha akaelekea stoo. Huko akateka chepe na kutoka ndani ya nyumba kisha akaelekea moja kwa moja kule mashariki ya mbali kukuta kaburi la Cecilia Goodwin, bibi yake Darren.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hapo kabla hajafanya chochote akaita kwa kunong’oneza, “Tabitha!”

    Kisha akaanza kuchimba kaburi.



    Akafukua kwanguvu ya ajabu. Alipumzika takribani mara mbili kwenye zoezi lake hilo kabla hajalimalizia kabisa. Akakuta jeneza kubwa ambalo alilitengua na chepe lake kisha akaliweka wazi.



    Humo ndani yake akaukuta mwili wa Cecilia. Ulikuwa unaelekea kuharibika sasa, mikono yake imejifumbata kifuani. Akaukunjua na kisha akauketisha kitako na kusemezana nao!



    Namna gani mtu aongea na wafu?



    Melissa aliupiga mwili ule kofi dogo kisha akaita, “Tabitha! Tabitha! Tabitha!” mara tatu, na mara mwili ukafungua macho. Macho yaliyokuwa na rangi nyekundu kana kwamba uji wa volkani!



    “Tabitha …” Melissa akasema kwa kunong’ona. “Kwanini lakini?” kisha akauliza.



    “Kwanini lakini?” Akarudia tena. Saa hii macho yake yakiwa yanalenga machozi. “Nilidhani wewe utakuwa wa tofauti, Cecilia. Nilikuwa nimekosea kukuamini hivyo?”



    Mwili ule ambao umefungua macho haukunena kitu. Uliendelea kumtazama Melissa ambaye alikuwa akiutazama na kuuliza kwa tija. Mwishowe Melissa alipomaliza kusema aliyokuwa anahitaji, akaurudisha mwili huo ndani ya jeneza lake, lakini kabla hajaufungia, mwili huo ukamshika mkono kwanguvu!



    Ukafungua kinywa kutaka kusema jambo lakini mdomoni ukaishia kutoka upepo tu. Hakuna lililosikika. Melissa akiwa analia, akautazama. Napo asiseme tena kitu, akaenda zake. Na pasipo kurudishia kifusi alichokichotea nje, akaenda zake kumkuta Darren ndani ya nyumba.



    Akanyookea bafuni na kukoga kisha akarejea sebuleni ambapo bado Darren alikuwa amejilaza. Akaketi pembeni yake alafu akalaza kichwa chake kochini akiwaza sana. Alishindwa kujizuia kutoa machozi. Kila alipoyafuta yakamiminika zaidi na zaidi. Mwisho wa siku akayaacha yamiminike kama mto.



    Yakamwagikia Darren na kumwamsha. Darren akamtazama kwa kuduwaa. “Melissa, haujalala?”



    Melissa hakujibu. Aliendelea kumwaga machozi. Basi Darren kwa kuguswa na moyo wa huruma, akamfariji mpenzi wake akitaka kujua ni nini kinamliza. Lakini Melissa hakuwa tayari kunena. Na kadiri Darren alipokuwa anamuuliza, akawa anapandwa na hasira.



    Hatimaye alimkaba Darren na kumnyanyua juu kama sufi! Darren akapapatika akirusharusha miguu. Melissa akambamizia ukutani na kusema akiwa amefuma uso wake kwa hasira, “Nitakuua, Darren!” akarudia tena, “Nitakuua, Darren!”



    Darren akatoa macho akikosa hewa. Akiwa anaelekea kujikatia roho, Melissa akambamizia kichwa ukutani, mwanaume huyo akazirai! Akamwacha aangukie chini na kisha yeye akarejea pale kitini. Akakaa hapo akiendelea kuwaza.



    Akiendelea kumwaga machozi.



    **



    Ngo! Ngo! Ngo! Ngo! Darren alisikia sauti hiyo kwa mbali. Kichwa kilikuwa kinamuuma na bado hakuwa amefumbua macho. Macho yalikuwa mazito sana lakini akajitahidi kupandisha kope.





    Alipotazama akajiona yupo sebuleni, na zaidi akiwa ameegemea ukuta. Kiuno chamuuma na pia kichwa. Kiuno ni kwasababu ya kukaa muda mrefu.



    Akastaajabu akiangazaangaza. Hodi ikabishwa tena. Basi akasimama na kusonga mlangoni, hapo akakutana na mzee mmoja aliyevalia kofia ya ‘cowboy’ na overall ya jeans, mkononi amebebelea reki.



    Mzee huyo mwenye sauti kavu, akasema, “Wewe kijana, ni wewe ndiye umefukua kaburi kule?”



    Darren akatahamaki mzee huyo akimweleza kuwa kaburi lipo wazi. Pasipo kupoteza muda, wakaongozana mpaka huko na Darren akakuta kweli kaburi li wazi mpaka jenezani!



    Akazama ndani ya shimo na kutazama jeneza. Lilikuwa limetenguliwa. Akahofia pengine itakuwa kuna vitu vimeibwa humo ndani. Basi akalifungua jeneza na kutazama mwili. Ulikuwa sawia ila macho yakiwa wazi. Akatahamaki.





    Ni nini kinatokea hapa?



    “Kijana ni nini kinaendelea?” akauliza yule mzee aliyekuja kumshtua Darren. Naue Darren hakuwa na jibu kwani hakuwa anajua lolote lile. Basi kwa kushirikiana na yule mzee wakafukia tena lile kaburi na alivyoenda kule ndani akampasha habari hizo Melissa. Melissa akaigiza kushtushwa.



    “Inawezekanaje?”



    “Sijui. Ni ajabu! Nadhani mahali hapa hapatakuwa salama tukienda. Napata mashaka sasa,” alisema Darren akiketi kitini. Akafikiria kwa muda kidogo kabla Melissa hajamkalia mapajani na kumtazama kimahaba.





    “Unaonaje tukaendelea kukaa hapa kwa muda mpenzi?”



    “Melissa, wewe ni mzima kweli? Vipi kazini?”



    Melissa akaguna. “Kwani kazini kwenu hamna kuumwa?”



    “Sijatoa taarifa hiyo!”



    “Kwani hamna wanaoumwa ghafla, Darren?” Melissa akanong’oneza. Darren akasisimkwa na mwili. “Lakini Melissa …”



    “Lakini kitu gani mpenzi?” Melissa akauliza akikata kiuno chake kwa mbali.



    “Ni hatari!” Darren akashukiwa.



    “Hatari lakini salama,” Melissa akamwambia kwa sauti laini kisha akambusu mdomoni. “Nataka kukaa na wewe zaidi Darren. Hamna mahali nitakapokuwa huru na wewe kama hapa. Hutaki hilo, mpenzi?”



    “Unajua nataka lakini mazingira mpenzi yana--”



    Melissa akakamata mdomo wa Darren na kuunyonya. Alishajua amefanikiwa kumteka mwanaume huyo, hatakiwi kuongea zaidi. Akamchezea mpaka alipoona yeye kuwa inatosha sasa.



    Lakini baadae, ikiwa ni kwenye majira ya saa saba usiku, Darren anashtuka kitandani na kujikuta yu peke yake. Anatazama kushoto na kulia pasipo kumwona mtu aletoka kulala naye. Anastaajabu! Anapatwa na hofu.



    Akatoka kitandani na kuangaza sebuleni, hamna mtu. Akaangaza chumba cha kwanza, napo hakuambulia jambo. Ila akiwa humo anasikia sauti ya kitu kikigongwa kwa taratibu … Tih! Tih! Tih!



    Anafuatisha masikio yake ajue wapi sauti hiyo inatokea, mwishowe anajikuta ndani ya chumba cha tatu. Ila anapofika humo, sauti hiyo hukata. Anatazama kila kona ya chumba hiko pasipo kuona lolote la kutia shaka.



    Hatambui nini kinaendelea.



    Anajaribu kuita kwa taratibu, “Melissa!” na mara umeme unazima anakuwa kizani. Inachukua kama sekunde mbili tu, umeme unarudi! Darren anapotazama mlangoni, anauona mlango ukiwa wazi, unacheza kwenda mbele na nyuma!



    Moyo wake ukapiga kwa hofu. Akapiga moyo konde na kuufuata, kisha akachungulia huko nje. Hakuona jambo nyuma yake, lakini mbele yake, alipotazama vema, akaona kutakuwa na mtu huko. Kule sebuleni kulikuwa na mwanga aliouhisi ni wa runinga. Lakini kama hiyo haitoshi, aliona pia na kivuli cha mtu!



    Akaita, “Melissa!” na kuuliza, “ni wewe?”



    Ajabu kile kivuli kikaanza kucheza kikizungusha kichwa chake kushoto na kulia, kulia na kushoto kana kwamba mwehu!



    “Melissa!” Darren akaita tena. Saa hii sauti yake ilikuwa inatikisika. Alikuwa amejawa na mashaka zaidi. Mashaka juu ya Melissa. Mashaka juu ya roho yake!



    Basi hakuwa na namna. Alijivika uanaume akasonga mbele japo kwa hatua za kusita. Alipojivuta mpaka sebuleni na kuchungulia, hakuona kitu! Alipotazama kile kivuli ndipo akajua kinatokea kwenye mwanga wa nje, mwanga upenyao dirishani!



    Akatazama huko dirishani, akamwona mtu ambaye kabla hajamtambua, upesi akatoka mwangani na kujificha!



    “Ni nani wewe?” Darren akauliza akijitahidi kukaza sauti. “Ni nani wewe, jitokeze kabla sijakufyatulia risasi!” akatishia lakini isisaidie kitu. Hakuna mtu aliyejitokeza wala kunena na yeye.



    Basi akaenda stoo upesi na kuchukua fyekeo. Akiwa amelishika vema mkononi, akafungua mlango na kwenda nje. Akaita, “Melissa!” kimya. “Melissa!” kimya.



    Akaizunguka nyumba nzima lakini hakuona kitu. Akiwa amerudi pale pale dirishani, akaona kivuli tena, mara hii kikiwa kinatokea ndani na si nje kama ilivyokuwa hapo awali! Kivuli hicho kikiwa ni matokeo ya kuhakisiwa kwa mwanga wa runinga.



    Basi haraka Darren akatazama ndani, lakini napo akiwa bado hajamwona mtu huyo vema, akapotelea koridoni!



    Basi upesi akakimbilia ndani. Akatazama kushoto na kulia, hakumwona mtu. Akatazama koridoni, napo hakumwona mtu. Akahisi mtu huyo atakuwa ameenda vyumbani, basi akaanza kusonga kwenda huko. Chumba cha kwanza akafungua na kutupa macho. Hamna mtu!



    Chumba cha pili aliposhika mlango tu, runinga ikazimwa sebuleni! Alirusha macho yake akaona ni kiza huko. Moyo wake ukaruka pigo. Akahisi sasa anapoteza nguvu mwilini.



    Hajakaa vema, akahisi uzito machoni, mara kidogo akapotezaa fahamu akidondoka kama furushi!



    Alipokuja kupata fahamu, kwa mbali, akajiona yu ndani ya shimo. Na kwa juu kuna mtu mwenye chepeo akimwagia mchanga humo shimoni! Akimwaga kifusi kwa kifusi!



    **

    Akapiga kelele kali akisimama na kujipangusa michanga, akitema michanga. Alipotazama kule juu amwone ni nani anamwagia michanga hiyo amfukie kaburini, hakumwona!

    Hakukuwa na mtu tena. Akapagawa. Akachanganyikiwa akijitahidi kujinasua shimoni. Alipotoka, akiwa ametota haswa, akaangaza macho yake kushoto na kulia akihema kwanguvu.

    Na punde asikae hapo sana, akakimbia kwenda kule kwenye jengo, kabla hajafika akasikia sauti ya kike inamwita, "Darreeeen!" Alipogeuka kutazama akamwona Melissa kwa mbali. Melissa akiwa amevalia gauni jeupe lionyeshalo kwa ndani.

    Na gauni hilo likiwa limechafuliwa kwa mabaki ya damu.

    "Melissaa!" Darren akaita. Aliachama mdomo wake kwa kuduwaa na macho akiyakodoa. "Melissaa!" Akaita tena, mara hii akaanza kukimbia kurudi kule alipotokea, kule alipokuwa anamwona Melissa.

    Alipomfikia akamkumbatia kwanguvu na kumuuliza, "Ulikuwa wapi Melissa? ... ulikuwa wapi mpenzi wangu?"

    Lakini Melissa hakuwa anaongea kitu. Alimtazama Darren usoni kana kwamba mdoli. Naye Darren akapata shaka, "Melissa, upo sawa?"

    Kabla Melissa hajajibu, Darren akasema, "Twende ndani!" Akimvuta Melissa mkono. Ila ajabu mkono wa Melissa ukanyofoka! Akajikuta ameubebelea na huku Melissa akiwa amesimama kama mstimu.

    "Nini hiki?" Darren kutahamaki. Mara Melissa akakunja sura na kumtazama Darren kwa hasira. Akapanua mdomo wake kwa upana zaidi kisha akapiga kelele kali mno. Akamsogelea Darren kwa ukaribu na kumzaba kibao kikali, Darren akarukia mbali!

    Alipokuja kufumbua macho yake akajikuta yu kitandani. Alikurupuka na kuangaza kando yake, alikuwa mwenyewe! Akaita, "Melissa?" Kimya. Akanyanyuka toka kitandani na kutazama koridoni. Hakukuwa na mtu. Akaita tena na tena, mara akasikia sauti ya mtu akigugumia kwa kilio huko sebuleni.

    Akasonga huko na kuangaza. Kitini akamwona Melissa wake akiwa amejikunyata. Melissa analia.

    "Melissa!" Akaita kwa sauti ya chini akisonga. "Melissa, kwanini unalia?"

    Akaketi karibu ya mwanamke huyo. Akauweka mkono wake begani mwake na kumuuliza, "Melissa, kwanini unalia, mpenzi? ... hautaki kuwapo hapa? Wataka tuondoke?"

    Melissa hakusema kitu. Akaendelea kulia. Naye Darren akaacha kumuuliza maswali na badala yake akawa anambembeleza tu anyamaze. Aliponyamaza akamkumbatia Darren kwanguvu na kumwambia, "nisamehe mpenzi?"

    Darren hakumuuliza kisa nini. Aliona Melissa hayuko sawa na hakutaka yawe magumu zaidi. Atamuuliza baadae yote yakipoa na kuwa sawa. Akambusu mpenzi wake kwenye paji la uso na kisha akamkumbatia tena.



    ***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    "Kweli!" Mama yake Darren, Sarah, alisema kwa mshangao. Alikuwa amekurupuka toka usingizini muda mfupi hapo nyuma, kando yake akiwa ameketi mume. Wote walikuwa na nyuso za kuhemkwa.

    "Kwahiyo?" Baba akauliza. "Tunafanyaje sasa?"

    "Twende!" Mama akaropoka. "Twende, Gerald!"

    "Wapi?" Baba akatahamaki. "Unajua saa hizi ni muda gani, Sarah? Ni saa nane ya usiku!"

    Mama akatazama kushoto na kulia kwake kisha akameza mate. Alifungua dirisha akatazama nje. Alikuwa amechanganyikiwa.

    "Gerald!" Akaita. "Kama tusipofanya namna Darren anaweza akafa." Alipoteta hayo macho yake yakawa mekundu ghafla na kumwaga chozi.

    "Usijali, Sarah. Hamna kitakachotokea mpenzi. Ni ndoto tu. Atakuwa salama," alisema Gerald.

    Mama akainamisha kichwa akiendelea kulia. "Sijawahi ota ndoto kama hii kwa muda mrefu, Gerald. Nadhani kuna haja ya kwenda Reish jua litakapochomoza."

    "Kufanya nini huko?" Gerald akang'aka. Sarah akamtazama akikunja ndita. "Una wazimu, Gerald? Unadhani ni sawa, sio? Huoni hali yangu ya mwanzoni itakuwa inaninyemelea?"

    Gerald akashusha pumzi ndefu kisha akajirejesha kitandani. Sarah akamtazama pasipo kutia neno kisha akaendelea kuwaza zake na kidogo Gerald, mumewe, akamsihi alale na jua litakapokucha atafanya vile ambavyo anataka.

    Basi akajilaza kitandani. Lakini hakufumba macho bali akiwandawanda huku na kule. Hata mumewe akapotelea usingizini na huku yeye bado anatazama kushoto na kulia. Hakuwa na usingizi. Alimwazia mwanaye vibaya. Alimwazia hayuko salama.

    Akajigeuza huku na huko na hatimaye jua likachomoza. Akaamka na kuanza kujiandaa. Mumewe akamkuta akiwa tayari.

    "Ulilala kweli, Sarah?"

    Sarah akatikisa kichwa kuafiki lakini mumewe akatambua wazi kuwa mwanamke huyo hakulala. Macho yake yalikuwa mekundu yaliyochoka

    Akajiandaa ndani ya muda mfupi na wakafunga safari na mkewe kwenda mahali huko, mbali kabisa katika jangwa la misitu.

    Mahali huko palikuwa panaitwa Reish.

    Walipozama ndani ya msitu huo wakanyookea mti mkubwa, Sarah akazamia humo ndani akimwacha Gerald hapo nje.



    **



    "Nadhani utakuwa sawa, si ndio?" Darren alinena punde alipomshusha Melissa nje ya makazi yake tokea kwenye taksi.

    "Yah! Nitakuwa sawa," Melissa akajibu. Uso wake ulikuwa mpole. Alitabasamu kwa kuigiza alafu akaanza safari yake ya kwenda ndani. Darren akabaki hapo akimtazama mwanamke huyo akiishilia. Ila kidogo simu yake ikamtoa mawazoni na kumfanya aitazame. Alikuwa ni mama yake. Akaipokea na kuiweka sikioni.

    Kabla hajaongea hata neno, Melissa aliyekuwa amekaribia na mlango wake akasimama. Alihisi jambo. Akageuza uso wake kumtazama Darren lakini Darren hakutuama tena pale, dereva taksi akatia moto chombo na kuyeya!

    Melissa akalitazama gari hilo mpaka lilipopotea kabisa alafu akazama ndani moja kwa moja mpaka chumbani kwake. Akajitupia kitandani akiwaza mambo kadhaa, na mara kwa mara akawa anasema mwenyewe, "Tabitha! Tabitha!"

    Baadae akatoa picha ya bibi yake Darren kwenye mfuko wake na kuiweka mezani.

    Akaitazama picha hiyo kwa muda alafu akafunga madirisha ya chumba chake na kuwasha mishumaa. Baada ya hapo, toka uvunguni mwa kitanda chake akatoa majani makavu yaliyotunzwa ndani ya kisosi, akayatia moto na kuyafukizia ndani akinuwia. Alipomaliza akaichora picha ile ya bibi yake Darren akinena maneno ya kilatini. Punde mtu mmoja mmoja ndani ya picha akaanza kupotea na hatimaye akabakia bibi peke yake wengine wote wakiwa hawaonekani!

    Watu hao waliopotelea pichani, katika namna ya ajabu, wakajiri kandokando ya mlango! Ila nyuso zao hazikuwa tena za mabinti wachanga kama vile ilivyoonekana, bali za wazee waliokongoroka. Na hapo, kufumba na kufumbua, naye Melissa akawa mzee kama wao! Wakakumbatiana kwanguvu kabla Melissa hajawaambia kwa uchungu, "Tabitha alitusaliti! ... Tabitha aligeukia binadamu!"

    Ndipo akawaeleza ya kwamba nyumba yao ya kale, nyumba ya majini, ipo hai tofauti kabisa na vile Tabitha alivyokuwa anawaambia ya kuwa imepotea. Imemezwa!

    Habari hizo zikawashangaza wale wazee. Wakataka kuiona nyumba hiyo lakini haikuwa inawezekana katika miili yao kwani Tabitha aliipoteza kabisa. Basi wakamsihi Melissa airudishe nyumba ile kwenye mikono yao haraka iwezekanavyo. Lakini pia awamalize binadamu hao mara moja. Binadamu wanaoishi hapo, na wale watakaokuja kukaa hapo.

    Kwa kufanya hivyo atawarudisha wenzake tena duniani. Na watatawala tena kama ilivyokuwa kabla ya Tabitha kuwatia kifungoni na Melissa kutorokea mbali!

    **

    "Darren, picha iko wapi?" Kabla hata ya salamu mama akauliza. Alikuwa ametoa macho haswa kiasi cha kumwogopesha Darren.

    "Picha gani?" Darren akauliza. Mama akamkaba koo na kupaza, "Picha ya bibi yako! Ile picha ya bibi yako iko wapi?"

    Basi Darren akatazama kwenye mkoba wake. Hakuiona. Akahisi kuchanganyikiwa. "Ilikuwa humu ... ilikuwa humu!"

    "Iko wapi sasa?" Mama akafoka kiasi cha kumshangaza Darren. "Mama kuna nini kwani?"

    "Nataka picha!" Mama akasema kwa sauti ya chini ya msisitizo. "Nataka picha, Darren. Picha!"

    "Haipo humu. Nadhaniii..."

    "Unadhani nini? Nani kaichukua?" Mama akauliza akitoa macho. Darren akajibu, "Melissa. Nadhani kaichukua Melissa!" Basi upesi Mama akamdaka mkono na kumwambia, "twende huko upesi!"



    ***



    Darren hakuwahi kumwona mama yake kwenye hali hiyo na tangu alipowahi kumwambia juu ya Melissa, uzuri na uchangamfu wake, mama hakuwahi kuguswa kiasi cha kutaka kumwona Melissa. Lakini mbona hili la picha? Akapigwa na butwaa.



    Mama yake alimkokota mpaka nje mbele ya gari la baba yake, akamweka ndani na kuwasha chombo kabla hajakanyagia mafuta pasipo kujali! Gari likapepea kama kishada kutafuta makazi ya Melissa!



    Ndani ya muda mfupi wakaja jikuta wapo kwenye foleni ndefu. Mama akakasirika akipiga usukani kwanguvu. Darren akaendelea kutahamaki.



    “Mama, una nini?”



    “Darren, kwanini ulimpa Melissa ile picha?” Mama akafoka. Macho yake yalikuwa mekundu kana kwamba kitambaa.



    “Sikumpatia,” Darren akajitetea, “Nilitahamaki haipo kwenye begi langu na si vinginevyo!” Lakini Mama bado akamwona ni mjinga. “Darren, nilikuambia nini kuhusu ile picha mara ya kwanza nilipokuona nayo?”



    “Najua, nakumbuka. Sijafanya kwa kudhamiria. Tafadhali!”



    Mama akalaza kichwa chake kwenye kiti akitema hewa ndefu.



    “Mama,” Darren akaita. “Kwani picha ile ina nini? Naomba uniambie kwanini umekuchanganya namna hii?”



    Mama hakumjibu, alikuwa anatazama magari meengi yaliyokuwa yamesimama mbele yake akitamani ayatafune au ayakanyage kwa juu aende zake. Akiwa anatazama, akajikuta chozi linamtoka kwenye jicho la kulia. Akalipangusa na kuvuta kamasi jepesi puani.



    “Mama!” Darren akaita kwa sauti kuu. “Kwanini hutaki kunambia? Kwanini unaninyamazia? Hunisikii?”



    Mama akamtazama kana kwamba mbogo aliyejeruhiwa na kisha hakusema kitu. Macho yake yangekufanya usikie njaa hata kama umetoka kula. Yangekufanya utafute mlango wa kutokea kama ni mgeni. Na kama basi ni mtoto angelia pasi na kifani. Hata Darren aliogopa. Hajawahi kumwona mama yake akiwa anatisha vile tangu amepata ufahamu kama mtu mzima!



    Magari yakaruhusiwa kwenda, na mama akatia chombo moto. Akaendesha upesi kumchukua dakika nane tu kufika mbele ya makazi anayokaa Melissa. Hapo wakapanda ngazi upesi na punde wakawa wapo mlangoni wakigonga.



    “Melissa!” mama aliita lakini kulikuwa kimya. Na akiwa hapo akahisi harufu ya yale majani ambayo Melissa aliyachoma kwenye kibakuli. Akachanganyikiwa. “Melissaaa!” akaita akibamiza mlango makofi, lakini bado kulikuwa kimya. Kimya baridi. Basi Mama akamwamuru Darren avunje mlango huo wapate kuingia ndani.



    “Mama, upo sawa kweli?” Darren akatoa macho. Mama akarudia kumwambia, “Vunja mlango Darren!” kisha na kuongezea, “Au nivunje mimi?”



    Lakini Darren bado alisita kufanya hivyo. “Mama, tutaitwa wezi. Tutavunjaje mlango wa mtu ambaye hayupo!”



    “Vunja, Darreeen!” Mama akafoka akitoa macho kana kwamba simba. Basi Darren akaupiga mlango huo kumbo la nguvu, nao ukavunjika wakazama ndani! Mama akatazama kushoto na kulia, kulia na kushoto. Melissa hakuwapo! Wala nayo picha haikuwa mahali panapoonekana.



    Walichoambulia kuona ilikuwa ni kile kibakuli cheupe cha udongo ambacho Melissa alichomea majani na marker pen nyekundu. Lakini Mama akawa amejua kilichotokea. Aliidaka marker pen ile na kuitazama vema kana kwamba anatafuta jambo kwenye ramani, kisha akasema kwa sauti ya chini, “Darren, tumekawia.”



    “Tumekawia na nini?” Darren akawahi kuuliza.



    Mama akamwambia kana kwamba bibi anayesimulia simulizi wajukuuze, “Wanaamshwa tena, Darren!” akasema akitazama dari. “Watakapoamka tena, wote hao, hatutakuwa na uwezo wa kuwazuia tena.”



    Alafu ghafla akamtazama Darren na kumkwida shati lake. “Darren, si kwamba watachukua tu nyumba yetu, bali wataiteka dunia nzima. Darren inabidi tuwazuie. Tuwazuie haraka iwezekanavyo!”



    Na alipomaliza kusema hayo akadondoka chini na kuzirai!



    “Mama! Mamaa!” Darren akasumbuka naye. Akampepea na kumpepea lakini haikusaidia, mama hakuwa na fahamu hata lepe! Basi akambeba na kurupukurupu mpaka chini kwenye gari. Akampakia ndani na kisha akarejea tena kule juu kwa Melissa. Akaurudishia mlango baada ya kutazama kuwa kila kitu kii chema alafu akamrejea mama yake na kumwendesha kumpeleka nyumbani.



    Akiwa njiani, akajaribu tena kumpigia Melissa. Hakuwa anapatikana! Akang’ata meno yake kwanguvu akinguruma. “Upo wapi Melissa? Upo wapii?”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alimfikisha mama yake nyumbani. Akamlaza kitandani akijaribu kumpepea na kuhakikisha kuna hewa ya kutosha ndani. Baada ya muda kidogo, Mama akaamka kichwa kikiwa kinauma. Akamtazama Darren wake kwa macho ya upole na pasipo kusema kitu akatabasamu kwa mbali.



    “Mama,” Darren akaita akiweka kiganja chake kwenye paji la uso la mama yake, kisha akawa anamtengenezea nywele. “Unajisikiaje hivi sasa?”



    “Vizuri,” mama akasema kwa kunong’ona.



    “Mama, unaweza ku--” kabla hajamalizia nayo simu yake ikaita. Alikuwa ni Melissa.



    “Ni Melissa huyo?” Mama akauliza. Darren akamtazama na kumlaghai, “Hapana.” kisha akatoka kwenda kando aongee kwa uhuru.



    “Melissa,” akaita kwa kunong’ona kisha akauliza, “Upo wapi?”



    “Nipo kwako,” Melissa akamjibu.



    “Unafanya nini huko na mimi sipo?”



    “Nimekuja kukutazama wewe, Darren. Unaweza kuja hivi sasa?”



    Darren kabla hajajibu, akageuka atazame ndani. Hamaki akakutana uso kwa uso na mama yake! Akashtuka kiasi cha moyo wake kutaka kutoka nje.



    “Darren,” Mama akasema kwa sauti ya chini, lakini kwa namna alivyokuwa anamtazama Darren ni kana kwamba simba awindaye kwa kunyata. Akasema, “Tunaenda wote huko, Darren.”



    “Wapi?” Darren akauliza kana kwamba hajui kinachoendelea. Mama akamjibu, “Huko aliko Melissa!”



    “Sijaongea na Melissa mama,” Darren akadanganya na kuapa lakini mama akabaki akimtazama asiseme jambo la nyongeza.



    “Kweli, sijaongea naye mama. Naomba tafadhali upumzike. Nakuja muda si mrefu.”



    Kimya.



    “Mama, mbona unanitazama hivyo?”



    Kimya.



    “Mama, una shida gani? Mbona upo hivyo?”



    Kimya. Mama aliendelea kumtazama Darren kwa macho ya kwenye kona. Mwishowe Darren akaanza kuhisi moyo wake unapiga kwa kasi. Alianza kuogopa. Basi akaona ni kheri akaongozana na mamaye huko kwake.



    Wakashuka na kujipaki kwenye gari alafu moja kwa moja wakaelekea huko. Walitumia kama dakika ishirini na nane barabarani. Walipofika na kufungua mlango, hawakumkuta yeyote. Chumba kilikuwa kitupu!



    Darren akampigia simu Melissa, na kidogo simu ikapokelewa.



    “Upo wapi, Melissa?”



    “Darren …” Melissa akaita na kusema, “Nilikuita wewe, na si familia nzima.”



    Darren akatazama nje ya dirisha lake kama atamwona Melissa. “Upo wapi?” akauliza akiangazaangaza.



    “Utakapokuwa mwenyewe, nitakuambia,” Melissa akamjibu, na kabla hajatia neno, mama yake akampokonya simu na kuongea na Melissa.



    “Binti wa shetani, popote utakapokuwa, nitakutafuta na kukumaliza. Kwa nguvu na akili yangu yote, kwa udi na uvumba, nitakutia mikononi na kukuangamiza.



    Hauna nafasi tena kwenye dunia hii. Na kama walivyoenda wenzako na wewe utaenda vivyo hivyo. Sitabakiza hata unywele wako kwenye uso wa dunia. Mifupa yako nitaivunjavunja kutengenezea unga wa sigara na meno yako nitayatengenezea mkufu nikauvae shingoni mwangu.”



    Alipomaliza, akakata simu na kumpatia Darren. Alafu ghafla akadondoka na kuzirai tena. Kabla Darren hajahangaika naye, akaita kwa sauti ya chini, “Mama.” kisha na kusema, “Wewe ni nani? … Melissa …” akatazama simu yake na kuuliza tena, “wewe ni nani?”





    Alishinwa kupata majibu. Alijikuta kwenye maswali ya mkanganyiko juu ya mama yake na Melissa. Wana nini kati yao? Wana nini ambacho hakijui? Wana nini ambacho wanamficha?



    Akaketi kitandani akiwaza na kuwazua. Hata alipompigia Melissa hakupokea bali tu akituma ujumbe kuwa wataongea punde atakapokuwa peke yake. Mwishowe akaamua kuzima simu akidhamiria kutomtafuta tena Melissa.



    Akambeba mama yake na kumweka kitandani. Alafu akafungua madirisha apate hewa wakati akiangalia kuandaa mengine. Alipomaliza kila kitu, akajilaza kitandani akiwaza sana. Mwishowe usingizi ukambeba.



    Kidogo akiwa usingizini, akasikia hodi mlangoni. Akafumbua macho yake kwa uvivu akitazama mlango. Kidogo akajikusanya kitandani na kusogea karibu akiuliza ni nani anayegonga. Hakujibiwa. Alipoufungua akamwona mwanaume fulani mwenye mwili mpana akiwa amevalia koti la sufi na shati jepesi kwa ndani. Mwanaume huyo shingoni alikuwa amechora ‘tattoo’. Na uso wake mpana ulikuwa na kovu kwenye fuvu la shavu la kushoto. Macho yake yalikuwa madogo yaliyozama ndani, ila aliyakodoa.



    Akauliza kwa sauti kavu, “Wewe ni Darren?” Darren akatikisa kichwa. “Naweza kukusaidia?”



    Bwana yule hakujibu, badala yake akatazama ndani na kisha akarudisha macho yake kwenye uso wa Darren. Mara akamsukumia kando na kuzama ndani pasi na ruhusa.



    “Hey!” Darren akapaza, “Unataka nini?” lakini bwana yule hakumjali, akiwa anasonga kwa hatua nzito, akawa anamuelekea Sarah, mama yake Darren.



    Basi Darren upesi akaamka na kumkimbilia. Akamrukia mgongoni na kumkaba lakini hakuwa na nguvu ya kushindana na mtu huyo. Kwa kutumia mkono mmoja akanyofolewa mgongoni na kutupiwa ukutani. Alijibamiza sana kichwani kiasi cha kupoteza uwezo wa kujimudu kusimama tena, basi kwa mbali akawa anatazama kinachoendelea akiwa hana msaada wowote.



    Bwana yule akamfuata mama yake na kwa kutumia mikono yake mipana akamkaba koo na kumminya kwanguvu. Akamminya sana. Darren akanyoosha mkono wake wa kuume akitaka kumsaidia mama yake. Akaita kwa kunong’ona. Lakini hayo yote hayakuwa na msaada. Hakuwa anajiweza.



    Mbele ya macho yake bwana yule akammaliza mama yake na kisha akaondoka zake. Darren akatiririsha chozi akinong’ona, “Mama … mama … mama.”



    Mara akasikia sauti ya kunong’ona, “Nipo hapa mwanangu.”



    Alipotazama kushoto kwake ndipo akagundua kuwa mama yake alikuwa ameketi hapo. Alikuwa ameshaamka toka kwenye usingizi wa kukosa fahamu na kumbe yeye alikuwako usingizi akiona hayo yote!



    Akamkumbatia mama yake kwanguvu akisema, “Mama, upo hai!” mama yake akamdaka kichwa na kumpapasa. “Nipo hai mwanangu. Nani alikuambia nimekufa?” akasema kwa tabasamu.



    Darren akamtazama mama yake, na kabla hajasema jambo, wakasikia hodi mlangoni. Darren akashtuka sana. Akamtazama mama yake kwa kukodoa na kumwambia, “Jifiche!”



    “Kwanini?” Mama akashangaa. Darren hakumpa maelezo zaidi badala yake akamsisitizia ajifiche wakati yeye akiwa anatafuta silaha. Alipopata kipande cha nondo akauendea mlango. Na kabla hajaufungua, akamsisitizia tena mama yake ajifiche. Mama hakuwa anajua kinachoendelea, akabaki akiduwaa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nani?” Darren akauliza mlangoni. Kimya. Akauliza tena, “Nani?” mara hii sauti yake ikiwa na amri ndani. Mara akajibiwa na sauti ya kike, “Ni mimi!” basi akadhani ni Melissa. Akafungua mlango, uso kwa uso akakutana na jirani yake; mdada mrefu mwembamba aliyening’iniza headphone shingoni, kichwa chake amekifunika na kofia ya soksi nzito.



    “Hey, Darren!”



    “Hey, Rosetta. Mambo?” Darren akasalimu akificha mkono wake wenye nondo nyuma.



    “Safi. Samahani kwa usumbufu, Darren. Nina ujumbe wako.” Rosetta aliposema hayo akachomeka mkono wake mfukoni na kutoa kikaratasi cheupe alichomkabidhi Darren na kumwambia, “Ni kutoka kwa Melissa!”



    “Yuko wapi?” Darren akawahi kuuliza.



    “Ameshaondoka,” Rosetta akajibu na kuongezea, “Nilimkuta chini. Aliponiona akanipatia na kisha yeye akaondoka zake mara moja.”



    “Sawa, ahsante,” Darren akafunga mlango na kufungua ujumbe ule aliokabidhiwa. Ulikuwa ni wa ishara na hakuelewa jambo. Ni alama mbalimbali ambazo alihisi anaumwa na kichwa kuzichambua.



    Akampatia ujumbe huo mama yake na kumuuliza kama kuna chochote anaweza kuambulia. “Umetoka kwa Melissa.”



    Mama akatazama lakini naye hakupata kitu, ila alihisi kuna jambo. Na jambo hilo si zuri! Akamwambia Darren, “Mtafute Melissa!” naye Darren akatumia simu yake kupiga, hakuwa anapatikana. Ndipo akamshauri mama yake, “Acha niende kwake mwenyewe. Pengine ntaonana naye kuliko tunavyoongozana kila muda.”



    Kwa kishingo upande, mama akaridhia. Basi Darren akashuka chini akimwacha mama yake ndani. Akakwea usafiri na kwenda moja kwa moja kwenye makazi ya Melissa.



    Aliposhuka toka kwenye gari akaangaza mazingira alafu taratibu akiwa amedumbukiza mkono wake wa kuume mfukoni, akajongea. Kichwani akiwa anamuwazia Melissa. Akaapa kuwa akimkuta mwanamke huyo basi ni lazima amwambie kinachoendelea. Hatomwacha mpaka amweleze hayo. Amechoka kuzungushwa sasa.



    Kama baada ya dakika tano akawa mlangoni mwa chumba cha Melissa. Akaukuta wazi. Akausogeza na kuzama ndani. Kila kitu kilikuwa sawa ila chumba kilikuwa kitupu. Hamna mtu!



    Akaita akikagua lakini napo hakukuwa na jambo. Akaduwaa. Akampigia simu Melissa lakini napo haikuwa inapatikana, sasa akachoka kabisa, akajitupia kitandani.



    Akangoja hapo kwa masaa lakini Melissa asionekane. Akajigeuza huku na kule, kule na huku. Akapiga simu na kutuma ujumbe, bado hamna kitu! Mpaka inafika saa nne usiku alikuwa kapa.



    Basi akaona ni stara alale hapo, ili Melissa akirudi amkutie hapo. Lakini kabla hajafanya hivyo, akaona amtaarifu mama yake juu ya uamuzi huo. Akampigia simu. Nayo ikaita pasipo kupokelewa. Akapiga mara sita, majibu yakawa yaleyale. Akapata shaka.



    Akaamua kurudi kwake kumkuta mamaye. Ndani ya dakika kadhaa akawa amefika mlangoni. Akabisha mlango usifunguliwe. Napo akausukuma pasipo mafanikio. Mlango ulikuwa umefungwa kwa komeo ndani.



    Ikambidi afanye jitihada za makusudi kuzama ndani. Akauvunja mlango kwa teke zito kisha akajivuta kwenda kutazama kitandani. Kulikuwa kimya kana kwamba hamna kiumbe chochote humo. Ukimya huo ukamtisha zaidi Darren.



    Akajongea, na alipofika kitandani, akamwona mama yake katika hali ya kushangaza. Hakuwa mama tena, bali mwili tu! Tena mwili uliokauka kaukau na kubabukababuka kama ngozi ya kenge!



    Darren akahisi kupoteza nguvu. Aakamshika mamaye ambaye haikuwa inaeleweka nini kimemtokea kisha akalia kwanguvu sana. Akalia kwanguvu sana!



    Hakuwa anaamini kama mama yake amefariki. Ilikuwa ni kama miujiza mbele ya macho yake. Na ni kweli ni muujiza. Imekuaje? Amekufaje kwa namna hiyo ingawa alimwacha akiwa salama salmini?



    Hata wakati gari la wagonjwa na polisi wanawasili, bado Darren alikuwa anadhani yu ndotoni. Kwa mujibu wa taarifa ya kiuchunguzi wa mwili, ikabainika kuwa Mama yake Darren, Sara, alikuwa amechomwa moto mpaka kufa. Lakini hakuna aliyekuwa anajua huo moto ulitokea wapi? Na nani aliyemchoma? Ilikuwa ni kitendawili mtu kuungua ndani ya nyumba peke yake huku kila kitu kikibaki salama!



    Majirani hawakuwa na habari yoyote juu ya tukio hilo.

    Na hata Polisi walishindwa kutoa majibu ya kueleweka.



    Darren na baba yake, bwana Gerald, wakafanya taratibu za mazishi wakiridhia kuwa siku inayofuata Sarah azikwe kwa maana hafai kukaa zaidi. Basi kama hivyo walivyokubaliana, kesho yake wakawa wapo makaburini.



    Mbele yao akasimama kiongozi wa dini pamoja pia na jeneza lililomhifadhi Sarah lakini Darren akiwa yupo mbali sana kimawazo. Kitu pekee alichoambulia toka kwenye kinywa cha kiongozi wa dini aliyekuwa amesimama mbele yao ilikuwa ni swala la moto tu.



    “... hamna anayejua moto ulianzia upande upi wa msitu,” kiongozi wa dini alinena kwa msisitizo. “Watu walikuja kufahamu ukiwa tayari umetafuna karibia nusu na robo yake. Ukiwa unawaka kwa fujo mno, na madhara yake yakiwa makubwa! …”



    Kutoka kwenye maongezi hayo, Darren akajifunza kuwa kumbe siku ile ambayo mama yake alifariki, ilitokea ajali kubwa ya moto huko California.



    Kidogo akashangazwa na jambo hilo, lakini hakuhangaika nalo sana. Alikuwa ana vitu vingi vya kujadili kichwani mwake. Wakamzika mama na kisha wakarudi nyumbani. Huko ndo’ baba yake akamwambia, “Kuna kitu nataka tuzungumze.”





    ***





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog