Search This Blog

JENEZA LA AJABU - 4

 

    Simulizi : Jeneza La Ajabu

    Sehemu Ya Nne (4)





    “Hebu mkamateni, mkamfunge kwenye mti wa mateso “,Malikia alitoa amli Njoshi akamatwe kwani hisia za mapenzi zilitoweka ghafla, baada ya Njoshi kuwadanganya, bila kutambua kuwa majini hawadanganyiki, walikuwa na uwezo wa kutambua chochote kile bila kuambiwa na mtu yoyote.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haraka sana askari wa msituni wakiwa na hasira sana na Njoshi, kwani aliwaua ndugu zao. Walimchukua Njoshi na kisha kumfunga katika mti mrefu, mti wa ubuyu uliopatikana katikati ya ngome ya malikia. Mti huu uliitwa mti wa mateso, kwani wadudu wakali kama siafu na nge wenye sumu kali, walipatikana katika mti huo na kumuadhibu kila aliyefungwa mahali hapo.



    “Aiwee…eh mizi…mu ya mababu nakuf…aaa!! ” ,Njoshi alipiga kelele huku maumivu makali akiyasikia, kwani baada ya kufungwa katika mti huo. Siafu pamoja na nge wengi walimtapakaa mwilini na kumshambulia, huku viumbe wote wa msituni wakicheka kwani waliamini tayali kisasi chao kilikuwa kimefanikiwa.



    Tofauti kabisa na malikia, hakuwa na furaha kabisa kwani alitokea kumpenda Njoshi ,hivyo ilimbidi afanye hivyo kwani Njoshi alionekana mbishi na mwenye dharau, baada ya kumdanganya.



    “Utakaposema ukweli, sababu iliyokuleta msituni, ndipo utatoka mahali hapo ” ,malikia aliongea huku akijiamini, maneno ambayo Njoshi hakuweza kuyasikia kwani tayali alikuwa amepoteza fahamu.



    Ikulu kwa mfalme;



            Watu walishindwa kupata usingizi katika ngome ya mfalme, tofauti kabisa na siku zingine. Waliendelea kulia huku wakiwa wameketi, wamekizunguka kitanda ambacho kulikuwa na maiti ya mfalme iliyokuwa imefunikwa kwa shuka zuri jeupe, huku sehemu ya kichwa chake ikiachwa wazi.



    Wake kwa waume, ndugu pamoja na vijakazi wa mfalme, hawakusitisha sara zao kwa mizimu ili siku inayofuata Njoshi aweze kurudi na jeneza kutoka msituni. Bila kutambua kuwa Njoshi alikuwa tayali ameshakamatwa, na alikuwa anapatiwa mateso makali.



    “Eeeh mizimu ya mababu, mrudisheni Njoshi wangu salama “,binti mfalme Grace, mpenzi wake Njoshi, yeye aliendelea kulia huku akijuta kumruhusu kipenzi chake kwenda msituni..kifo cha baba yake japo kilimuumiza lakini baba yake hakuwa muhimu sana katika maisha yake kama alivyo Njoshi. Aliamka kutoka katika kiti chake alichokuwa amekalia sebuleni, kiti kizuri kilichotengenezwa kwa miti na kisha kuelekea chumbani kwake na kuwaacha ndugu zake wakiwa wanaendelea kuhuzunika huku wakiutazama mwili wa mfalme,ambaye tayali alikwishakufa.



    Mwamutapa;



           Mama yake Njoshi anaota ndoto ya ajabu,anaota kuwa Njoshi akiwa msituni alienda kuoga katika mto uliopita katikati ya msitu.Akiwa anaogelea,Mamba aliweza kumwona Njoshi na kisha kumkimbiza.Kutokana na Njoshi kuchoka sana na safari  ndefu msituni,alichoka kuogelea haraka kumshinda mamba yule na kujikuta akitafunwa na yule mamba.



    “Aiweeeh ……mizimu ya mababu mwanangu yuko hatarini,muepusheni na balaa”,mama yake Njoshi alikurupuka kutoka usingizini,na kisha kumuombea mwanae kwa mizimu iweze kumlinda kwani aliweza kuota ndoto ya kutisha,ndoto ambayo alimaanisha Njoshi alikuwa katika hatari kubwa.Kwani kitendo cha Njoshi kutafunwa na mamba katika ndoto,kilimaanisha hatari kubwa iliweza kumkabili Njoshi usiku huo,usiku wa kuamkia siku ya jumatano.Bila shaka mama yake Njoshi alikuwa sahihi kabisa,kwani usiku huo mwanae alikuwa amefungwa katika mti wa mateso msituni,huku akiliwa na siafu pamoja na nge wenye sumu kali.Mateso haya yalikuwa makali sana na kupelekea Njoshi kupoteza fahamu.



    Mwamutapa;



     Ngesha baada ya kufika nyumbani kwao na kumkuta mama yake akiwa anamsubilia huku hofu kubwa ikimtawala kwani alikuwa na hofu kuhusu usalama wa mwanae. Mama yake hakuamini pale tu Ngesha aliporudi nyumbani akiwa mzima wa afya, na alipojaribu kumuulza alikuwa wapi?, Ngesha alimsimulia mama yake kila kitu bila kuficha chochote kile. Kiasi kwamba kifo cha mfalme hakikuwa siri tena, kwani tayali Ngesha na mama yake walikuwa tayali wameshafahamu.



    Kutokana na usiku kuwa tayali umeingia ,Ngesha na mama yake walipata chakula na kuelekea vitandani kujipumzisha, huku mama yake Ngesha akikosa usingizi kabisa mpaka kunakucha siku ya jumatano, kwani alikuwa na mawazo mengi kuhusu kifo cha mfalme, jambo ambalo aliweza kuambiwa na mwanae Ngesha.



    Mwamuyeshi;



    Mji ukiwa umechangamka sana huku shughuli mbalimbali hasa biashara zikiendelea,kwani ndio ilikua shughuli kuu katika nchi hii tofauti na nchi jirani ya Mwamutapa,kwani Mwamutapa walitegemea sana kilimo. Mganga maarufu katika nchi hii akiwa amepanda farasi wake, alijaribu kupenya katikati ya soko ambalo lilikuwa na watu wengi sana mida ya asubuhi. Soko hili lilikuwa limepakana na ikulu ya mfalme Muyeshi, kiasi kwamba njia pekee ya mkato kuelekea ikulu kwa mfalme iliweza kufurika watu na kuziba njia hiyo. Bila kukata tamaa, mganga yule alizidi kupenya katika kundi lile la watu na hatimae aliweza kufanikiwa, kwani alionekana kuwa na haraka sana.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ikulu kwa mfalme Muyeshi;



    Pilika pilika za hapa na pale zikiwa zinaendelea katika jengo kubwa la mfalme Muyeshi, huku vijakazi wa mfalme wakisafisha mazingira ya ikulu, katika asubuhi nzuri ya siku ya jumatano.



    Mfalme Muyeshi akiwa ameketi nje ya jengo lake, huku akiota jua zuri la asubuhi. Alishashangaa kumuona mganga wake aliyemtegemea akifika ikulu, huku akionekana kuwa na jambo muhimu sana ambalo liliweza kumleta ikulu, bila kuitwa na mfalme.



    “Aiweeh mfalme wangu Muyeshi, nimekuja haraka sana kwako, kuna tatizo “,mganga yule alimsalimu mfalme Muyeshi, huku akishuka juu ya farasi wake na kisha kumfahamisha mfalme kuwa kulikuwa na tatizo ambalo liliweza kumleta.



    “Aiweeeh mganga wangu kipenzi, tatizo gani limekuleta kwangu asubuhi yote hii “,mfalme aliweza kumjibu mganga wake na kumpatia swali mganga yule.



    “Rafiki yako Mutapa, mfalme wa Mwamutapa alifariki jana, lakini kifo chake sio siri tena, watu wake wameanza kufahamu “,mganga aliongea maneno ambayo yaliweza kumshitua mfalme, kwani mfalme aliweza kuitambua hatari ambayo ingemkuta rafiki yake baada ya kifo chake kufahamika, kwani hata jeneza la ajabu lipatikane lisingeweza kusaidia chochote kile. Bali mfalme Mutapa angekufa bila kufufuka tena, na huo ndio ungekuwa mwisho wa utawala wake.



    “Ondoka haraka sana, nenda kazuie hili jambo lisiweze kutokea, nenda katoe taarifa ikulu kwa mfalme Mutapa, ili wote wanao ifahamu siri hii waweze kuuawa haraka sana “,mfalme aliongea na kisha kutoa askari kumi wenye farasi ili waweze kumsindikiza mganga yule na kumpatia ulinzi wakati wote, na bila kupoteza muda, kundi la watu kumi na moja walianza safari kuelekea nchi jirani ya Mwamutapa haraka sana.



    Msitu wa majini;



    Mapenzi bwana, ni kitu cha ajabu sana. Huwezi amini, malikia wa majini alishindwa kupata usingizi usiku uliyopita, alizunguka huku na kule katika ngome yake huku akimtazama Njoshi aliyekuwa amepoteza fahamu huku akiwa amefungwa kwenye mti wa mateso. Alitamani amuone Njoshi akifumbua macho, lakini Njoshi alizidi kuyafumba macho yake mithili ya mtu aliyefariki dunia. Lakini fikra za malikia zilikwenda mbali sana, kiasi kwamba alitamani kumtoa Njoshi katika mti ule, lakini moyo wake ulisita, lakini aliapa kumtoa katika mti ule asubuhi siku iliyofuata siku ya jtano.



    “Lazima nimtoe hapa alipo, siko tayali kuumia wakati mwenye maamuzi ni mimi “,malikia aliongea huku akimalizia kuwatoa nge na siafu kwa kutumia kijiti katika mwili wa Njoshi, na kisha kuelekea chumbani kwake kupumzika.



    Jua likichomoza vema na kuufanya msitu wa majini kuonekana vizuri sana, huku rangi ya kijani ya miti ikipendeza na kuvutia machoni kwa ndege pamoja na viumbe wote wa msituni. Malikia alikuwa wa kwanza kusikia sauti nzuri za ndege zikifurahia maua katika ngome yake, na jambo la kwanza aliweza kuamka na kwenda kumtazama Njoshi.



    “Mhhh kaenda wapi tena?, au ametoroka “,ilikuwa ni sauti ya mshangao kutoka kwa malikia, msichana pekee katika msitu wa majini. Kwani majini wote wa kike waliweza kutoweka baada ya mfalme kushindwa kutimiza laana yake.kwani alimkamata malikia akifanya mapenzi na jini mwingine wa msituni tofauti na yeye, kutokana na hasira mfalme aliapa kumuua malikia huyo lakini hasira zilipopungua alishindwa kufanya hivyo kwani alimpenda sana japokuwa alimsariti, Kutokana na miiko ya majini hao wa msituni,kwani kiongozi wao anapotamka jambo lazima alitimize. Wanawake wote msituni pamoja na mfalme waliweza kutoweka ,na kumuacha malikia akiwa mwanamke pekee wa kijini msituni.



    Hali hii ilipelekea malikia kumchagua jini yoyote wa kiume wa kulala naye, pale tu alipokuwa na hisia za kufanya mapenzi. Kwani tayali mume wake ambaye alikuwa ni mfalme wa msituni, alikuwa hayupo tena.



    Kwa upande wa majini wa kiume, baada ya kutoweka kwa wake zao, walijikuta wakijaribu kumbaka malikia baada ya kushindwa kuzuia hisia zao na kuambulia kuuawa na malikia, kwani alikuwa na nguvu sana kuwashinda. Hivyo basi, kuchaguliwa na malikia kulala naye lilikuwa ni kama jambo la bahati kwa majini wa kiume, na wengi waliomba mizimu waweze kuipata bahati hiyo bila mafanikio.



    “Wote poteeni muelekee msituni, adui katoroka “,malikia alitoa amli baada ya majini wote wa msituni kukusanyika. Huku yeye akiwa ametoka ndani kwake kukagua mali zake, kwani baada ya kukuta Njoshi hayupo katika mti wa mateso. Aliamua kuelekea ndani kukagua mali zake na kukuta fimbo ya kifalme ikiwa imeibiwa, lakini mkanda pamoja na panga vilikuwepo kwani vilifichwa sehemu ambayo haikuwa rahisi kuviona. Malikia aliamini Njoshi hatafika mbali ,kwani alikuwa na majeraha makubwa  na pia hakuwa na siraha yoyote ya kumlinda.



    Msitu wa majini;



    Njoshi anapata fahamu usiku wa manane, huku ngome ya malikia ikiwa kimya sana kwani majini wote walikuwa wamelala. Akiwa na maumivu makali, huku damu ikichuruzika kutoka mwilini mwake, kutoka katika majeraha ambayo aliweza kung’atwa na nge pamoja na siafu. Aliyazungusha macho yake kuangaza kila sehemu katika ngome ya malikia, lakini hakuweza kumwona jini yoyote aliyekuwa akimtazama.



    Haraka haraka bila kupoteza muda kwani aliona huo ndio ulikuwa wakati sahihi wa yeye kutoroka, alijaribu kufungua kamba ngumu ya katani iliyotumika kufunga mikono yake katika mti wa mateso, na hatimae aliweza kufanikiwa.



    Baada ya kujifungua kamba kutoka katika mti ule, alichukua begi lake ambalo alikuwa bado amelivaa, kwani hawakumnyanganya baada ya kulikagua na wala hawakukuta kitu chochote. Lakini alipotaka kujifuta damu mwilini mwake, aliamua kukagua begi lake ili aone kama chochote niite kupata kitambaa chochote aweze kufuta damu na kusafisha majeraha yake.



    “Eeeeh mizimu ya mababu nini hiki?, “,Njoshi aliongea baada ya kukuta kipande kidogo cha jiwe ndani ya begi, lakini kipande hiki kiling’aa kama dhahabu. Kipande hiki kilifichwa ndani ya begi, sehemu ambayo ilikuwa ni ngumu kuliona kama ukikagua begi kwa papala, kama alivyofanya jini aliyekagua begi mwanzoni kwani siku zote haraka haraka haina baraka. Njoshi alitaka kulitupa jiwe hili, lakini roho yake ilisita kwani aliyakumbuka maneno ya mama yake kuwa asiweze kuliacha begi lile. Hivyo aliamini lazima jiwe lile litakuwa na msaada kwake, na bila kupoteza muda kuendelea kulishangaa jiwe lile ,aliliweka mfukoni ili atokomee kutoka katika ngome hatari ya malikia.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Heeeeeh ……mbona kama mazingaombwe,! “Njoshi alishangaa baada ya kuliweka jiwe lile mfukoni, na kuona majeraha yote yakipona huku sumu ya nge ikimtoka mwilini.



    “Ahaaaah, tayali nilishafahamu hili jiwe ni muhimu kwangu “,Njoshi alitamka maneno yale kwani tayali alitambua jiwe lile ndio lililomponya, hivyo basi alilifunga vizuri katika mfuko wa kaptura yake lisiweze kudondoka na kupotea.



     Baada ya jambo hilo kutokea, Njoshi alielekea ndani kwa malikia huku majini wote wakishindwa kugundua chochote, jambo ambalo lilikuwa la ajabu sana. Aliendelea kupenya ndani kwa malikia, na kukagua kila kona lakini hakuweza kuliona panga wala kitambaa chake. Njoshi aliendelea kupekua huku na kule lakini hakufanikiwa, hivyo basi aliamua kuahirisha kila kitu ili atoke ndani ya msitu kuyaokoa maisha yake kabla hapajakucha, kwani tayali alikuwa hajaona fimbo ya kifalme wala panga pamoja na kitambaa.



    Njoshi akiwa anatoka katika lango la malikia, alishangaa kuona kabati moja iliyokuwa karibu na mlango wa nyumba ya malikia ikijifungua huku miale kama ya jua ikitoka mfukoni mwake. Akiwa anashangaa miale ile, aliamua kulitoa jiwe lile mfukoni kwake, na baada ya kulishika mkononi, miale mikali ilitoka katika jiwe lile na kusababisha kufuli kubwa la ajabu katika kabati ile kujifungua.



    “Aiseeeh asante sana mama, jiwe hili linamsaada mkubwa kwangu, sikujua kama linanguvu kiasi hiki “,Njoshi aliongea maneno ya furaha huku akiitazama fimbo ya kifalme, fimbo iliyokuwa inang’aa sanaa kwani ilitegenezwa kwa dhahabu, madini ambayo yalionekana kutumika pia kutengenezea jiwe la ajabu ambalo lilionekana kuwa msaada mkubwa kwa Njoshi. Haraka sana ikiwa tayali giza limeanza kutoweka, huku sauti za ndege walioamka mapema zikianza kusikika, Njoshi aliichukua fimbo ile na kisha kuchukua kalamu ya ajabu iliyokuwa pembeni ya fimbo ile ndani ya kabati.



    “MFALME NJOSHI “,yalikuwa ni maneno ambayo Njoshi aliweza kuyaandika katika fimbo ya kifalme, kwa kutumia kalamu ya ajabu na kisha kucheka kwa sauti kubwa sana, kicheko cha furaha kwani tayali angeweza kuwa mfalme kama akifanikiwa kutoka nje ya msitu na fimbo ile ya kifalme. Japo Njoshi alicheka kwa sauti kubwa, majini ambao walionekana kulala sana siku hiyo, hawakuweza kusikia chochote kile bila kufahamu kuwa jiwe lile ndio liliweza kufanya maajabu yale yote.



    “Hapa ngoja nikatengeneze JENEZA LA AJABU, harafu nirudi nyumbani “,Njoshi alizungumza kwa ujasiri huku akitabasamu, na kisha kutimua mbio kuelekea katikati ya msitu kutengeneza jeneza la ajabu, jeneza ambalo mfalme Mutapa atafufuka baada ya wiki moja kama akizikwa ndani yake.



    Bila kutegemea Njoshi aliweza kupita katika geti la malikia, geti ambalo lilinyunyiziwa maji ya ajabu na kumgandisha binadamu yoyote ambaye angeyakanyaga maji hayo.Lakini kwa wakati huu, alipita bila tatizo lolote jambo ambalo lilimfanya Njoshi alibusu jiwe lile, jiwe ambalo alilishika kwa nguvu katika mkono wake wa kulia kwani ndio siraha pekee aliyonayo kwa muda huu.



    “Hapa tayali nimefanikiwa ,mimi ni mshindi “,Njoshi aliongea maneno haya huku akitokomea vichakani, lakini baada ya Njoshi kutoa mguu wake katika ngome ya malikia. Malikia alishtuka na kufuatiwa na majini wote, huku kila mmoja akiwa hajitambui. Hali hii ilimfanya Malikia kutoka nje, na kushangazwa kutomkuta Njoshi katika mti wa mateso, aliporudi ndani alishangaa kukuta kabati likiwa wazi huku fimbo ikiwa imeibiwa. Akiwa na mshangao na kushangaa namna Njoshi aliweza kufungua kabati, na ngome yote wasiweze kusikia hakupata jibu sahii. Harakaharaka aliwaita majini wote na kutoa amli Njoshi aweze kutafutwa haraka sana.



    Ikulu kwa mfalme Mutapa;



    Hofu juu ya mfalme kutofufuka tena inaikumba familia ya mfalme Mutapa, kwani mganga kutoka Muyeshi alifika na kueleza kila kitu ambacho alikigundua kutokana na uwezo aliokuwa nao.



    “Haraka sana mama yake Njoshi auawe mala moja, baada ya hapo Ngesha na mama yake muwaue pia “,mtoto mkubwa wa mfalme, mtoto aliyeonekana kuwa katili sana, alitoa amli kwa askari wake na bila kupoteza muda askari waliondoka kutekeleza amli. Hayo yote kipindi yanatokea, Grace alikuwa chumbani kwake akimuwaza mpenzi wake Njoshi, bila kufahamu kuwa tayali askari waliweza kutumwa na kaka yake wakamuue mama mkwe wake. Jambo ambalo angelipinga, kama angeshuhudia kipindi amli hiyo ikitolewa.



    Mwamutapa;



    Siku zote misemo ya wahenga huwa inamaanisha kitu fulani,kama vile msemo maarufu unaosema ‘siku ya kufa nyani miti yote hutereza ‘



    Msemo huu ulidhihirishwa kwa mama yake Njoshi, kwani siku hiyo aliahirisha kwenda shamba aweze kumsubili mwanae ,kwani ilikua ni siku ambayo Njoshi alitakiwa arudi kutoka msituni.Lakini pia siku hiyo mama yake Njoshi alisahau kutazama kioo cha ajabu ,kioo ambacho kilikua katika chumba maalumu katika nyumba kubwa waliyonayo.Siku zote kioo hicho alikitazama kila asubuhi anapoamka,na kufahamu jambo ambalo lingetokea siku hiyo.Hivyo basi  kama asingesahau kutazama kioo hicho cha ajabu,inawezekana angeepuka kifo.



    ********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Asubuhi na mapema siku ya jtano ,mama Ngesha aliamka na kuandaa chai ili waweze kuelekea shambani yeye na mwanae.Siku hii aliamka mapema tofauti na siku zingine,kwani alikosa usingizi mzima akiyatafakali maneno ambayo aliambiwa na mwanae usiku uliopita kuhusu kifo cha mfalme.Kifo ambacho kilikuwa siri,huku mfalme akiugua kwa takribani mwezi mzima,wananchi wakiwa hawafahamu.



    “Amka unywe chai twende shamba”,mama Ngesha alimwamusha mwanae aliyeonekana kulala sana siku hiyo ,tofauti na siku zote.



    “Mama naumwa sana,leo tusiende shamba,baki nyumbani,ukiniacha utakuta nimekufa”,Ngesha aliongea maneno yaliyomfanya mama yake asitishe kwenda shambani siku hiyo amuuguze mwanae,kwani alionekana kuchemka sana ,pale mama yake alimpomshika katika shingo lake na kulihisi joto kali la mwane likiwa limepanda sana,na kusababisha Ngesha atokwe na jasho mwilini.



    “Sawa tutabaki wote,vua shati lako joto lipungue mwilini, ukihitaji chochote niite, mimi niko nje napukuchua mahindi “,mama yake Ngesha alimtoa hofu mwanae, na kisha kutoka ndani ya chumba cha mwanae. Bila kutambua kuwa kifo kilikua mbele yao.



    Mwamutapa;



    Ikiwa mida kama ya saa nne hivi asubuhi,siku ya jumatano.Mama yake Njoshi alikuwa ameketi nje ya nyumba yake,akifurahia hali ya hewa nzuri ya siku hiyo.Siku zote mganga hajigangi,kwani japokuwa alikuwa na ujuzi wa kutabiri,pamoja na uganga wa kienyeji,taaluma aliyoirithi kutoka kwa mumewe kipenzi bwana Nyangoma,lakini alisahau kutazama kioo cha ajabu,kioo ambacho kilikuwa mithili ya video na kuonyesha matukio yote ambayo yangetokea katika siku hiyo.Tabasamu liliondoka ghafla,kwani alikuwa na furaha sana akitegemea Njoshi kurudi siku hiyo lakini alishangaa kuona kundi kubwa la askari wa mfalme Mutapa wakiwa na mapanga,hali ambayo ilimtia hofu mama yake Njoshi.



    “Huwezi kutangaza siri za mfalme,na lazima ufe ,……aiweeeh askari waaminifu wa mfalme, tekelezeni amli mliyopewa “,mmoja wa askari alimueleza mama yake Njoshi kosa lake, huku askari wengine wakimshikilia kwa nguvu mama yake Njoshi aliyekuwa akitaka kukimbia.



    Miale ya jua ilipenya katika macho ya mama yake Njoshi, na kuzidii kuongeza kasi ya machozi kutiririka katika paji lake la uso. Alitazama anga zuri sana, anga ambalo lilikuwa na mawingu yaliyoonekana kujongea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Alitamani aendelea kutazama uzuri wa dunia, lakini macho yake yalimshinda nguvu, yalitamani yaweze kufumba na kukwepa machungu na maumivu yale. Damu zikiwa zinachuruzika kwa wingi kutoka katika tumbo la mama yake Njoshi, akiwa amelala chali kwani alidondoka baada ya kuchomwa kisu kikubwa aina ya jambia tumboni mwake na kisha kutokeza mgongoni. Kwa mbali sana macho yakiwa yanaiaga dunia, alihisi kichwa kikiwa kizito sana huku dunia ikizunguka kwa kasi, na huo ndio ukawa mwisho wa mama yake Njoshi.



    “Chimba shimo na kisha fukieni mzoga huu “,askari mmoja katili aliyeonekana kuwazidi cheo wenzake, askari ambaye alikuwa hana uchungu wa mama kama vile yeye alizaliwa na ng’ombe. Alitoa amli maiti ya mama yake Njoshi kuzikwa pale pale nyumbani kwake, huku akiifananisha maiti ya mama yake Njoshi kama mzoga.



    Ikulu kwa mfalme;



    Grace alitoka chumbani huku akitabasamu kwa mbali,kwani aliamini muda sio mrefu kipenzi chake Njoshi atarudi kutoka msituni.Lakini alipigwa na butwaa baada ya kutoka nje na kukuta wageni kutoka Mwamuyeshi akiwemo mganga na mtabiri mkubwa wa nchi ya Mwamuyeshi,mganga ambaye alitoa siri ya kutafutwa jeneza la ajabu ili mfalme atakapokufa, azikwe katika jeneza hilo na kufufuka tena.



    “Aiweeeh mtukufu malikia, wageni hawa wmeleta ujumbe kuwa mama yake Njoshi anaijua siri kuhusu kifo cha mfalme,na tayali amewambia baadhi ya wananchi. Hivyo basi, kaka yako ametuma askari waende kumuua “, mapingo ya moyo ya Grace binti mfalme yalianza kwenda kasi, mala baada ya kusikia taarifa mbaya kutoka kwa kijakazi wa mfalme,kijakazi aliyekutana naye kipindi anatoka chumbani kuelekea nje na kuamua kuuliza kuhusu ujio ule wa wageni kutoka Mwamuyeshi bila taarifa.



    Grace kipenzi chake Njoshi ,hakuwa tayali kushuhudia kifo cha mama mkwe wake kikitokea,alianza kutimua mbio na kisha kupanda farasi mmoja wa wageni aliyeonekana kushangaa mazingira mapya ya mfalme Mutapa bila kufungwa kamba.Farasi huyu alimilikiwa na wageni  wale kutoka Mwamuyeshi.Lakini bila hata kuwapatia salamu,Grace aliruka juu ya farasi yule,kitendo kilichofanyika kwa sekunde tu na kisha kutokomea kwani geti lilikuwa wazi kutokana na usafi uliokuwa ukiendelea.



    Mwamutapa;



    Ngesha na mama yake wanauawa kikatili kwa kuchomwa na visu tumboni,baada ya kumkuta mama yake akiwa nje ya nyumba yake akipukuchua mahindi.Alipojaribu kuulizwa kuhusu Ngesha ,alidanganya na kusema kuwa Ngesha hakuwepo nyumbani ,alierekea shambani.Kelele za uchungu na maumivu zilisikika ,baada ya panga kubwa kupenya katika tumbo la mama yake Ngesha na kutokea upande wa pili wa mwili wake.Kelele hizo zilimfanya Ngesha atoke chumbani huku akikimbia bila kujali ugonjwa aliokuwa nao,alitoka nje huku akitimua mbio ili aweze kumuokoa mama yake kutoka hatarini,baada ya kusikia nje  kilio cha mama yake.



    “Mkamateni,ueni na huyo”,amli ilitolewa na askari wawili walimkamata Ngesha,huku mmoja akishindilia kisu chake tumboni mwa Ngesha.Huku Ngesha akilia kwa uchungu,baada ya kutoka nje na kushuhudia maiti ya mama yake.



    “Mama…aaaa…aa…aa!!,”Ilikua ni sauti ya Ngesha iliyopungua kadri muda ulivyokwenda,na kisha kudondoka chini na kupoteza maisha.Kitendo hichi kiliwafurahisha askari wale wa mfalme,kwani waliweza kufanikisha kazi waliyotumwa kuifanya na mtoto wa kiume wa mfalme.



    “Tuzifukie maiti haraka sana,kisha tupotee mahali hapa kabla hatujagundulika”,kiongozi wa askari wale alitoa amli,huku maiti za Ngesha na mama yake zikitupwa ndani ya shimo ambalo tayali lilikuwa limechimbwa mbele ya nyumba yao,na kisha kufukiwa.Vifo vyote vilivyotokea,wananchi wengine hawakutambua chochote kwani nyumba za Mwamutapa hazikuwa zimekalibiana.Nyumba moja ilikuwa mahali hapa,na nyingine ilikua kule,jambo ambalo ilikua ni ngumu kujua kitu kilichoendelea kwa jirani.



    Msitu wa majini;http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Njoshi akiwa tayali amekimbia mpaka katikati ya msitu,sehemu ambayo aliambiwa atengeneze jeneza la ajabu.Aliketi kupumzika,huku akiwa ananjaa kali sana kwani ilikua ni siku ya pili hajatia chochote kile kinywani mwake tangu aingie msituni.



    “Nitakula nikifika nyumbani, ngoja nitengeneze jeneza la huyu mbwa anayepingana na mapenzi ya mungu”,Njoshi alijitia moyo kuhusu njaa kali iliyokuwa ikimsumbua, lakini alipotaka kutengeneza jeneza, aliweza kugundua kuwa hakuwa na panga lolote lile.



    “Ngojaa kwanza, jiwe hili ni la ajabu sana linaweza kunisaidia “,Njoshi aliongea na kisha kuchukua jiwe lake ambalo tayali alikuwa amelihifadhi mfukoni.



    “Jiwe kata mti “,



    “Jiwe kata mbao “,



    “Jiwe pima urefu wa mfalme ……”



    “Jiwe tengeneza jeneza la ajabu ……”,



    Njoshi bila kutegemea, aliweza kutoa amli kila baada ya sekunde chache, kwa jiwe lile, jiwe ambalo liling’aa kama dhahabu na liliweza kufanya kila jambo alilolitaka. Hatimae jeneza la ajabu, tena jeneza ambalo lilipakwa rangi kwa msaada wa jiwe la ajabu, likawa limekamilika.



    ••••••••••••••••••••••••••

    Malikia anaamua kuongoza watu wake yeye mwenyewe, kwenda kumtafuta Njoshi kwani fimbo iliyoibiwa ilikuwa ni muhimu sana kuliko kitu chochote kile. Bora uwadanganye, na wala sio kuiba fimbo ya kifalme, fimbo ambayo ilikuwa inauhusiano mkubwa na majini,ndio maana walihifadhi fimbo hizo na kuzimiliki wao.Fimbo ya kwanza iliibiwa,na ndio ambayo wafalme wa Mwamutapa walirithishana vizazi na vizazi.Hivyo basi,majini hawakuwa tayali kuipoteza fimbo nyingine,fimbo ambayo ilikuwa imebakia moja tu katika msitu wao wa majini.



    Mwamutapa;



    Grace aliiacha ngome ya kifalme, na kukatiza katika mitaa ya Mwamutapa, spidi ya farasi wake haikuwa ya kawaida hata kidogo. Kwani vumbi lilitimka na kuwaachia karaha baadhi ya raia aliokutana nao. Jambo hilo liliwashangaza watu wengi, kwani siku zote Grace hakutumia farasi, bali alitembea kwa miguu huku akitoa misaada mbalimbali hasa kwa wazee aliokutana nao njiani. Pia haikuwa kawaida binti mfalme kutembea mtaani bila hata askari yoyote wa kumlinda, jambo ambalo lilimtatiza mzee mmoja ambaye alimanusura agongwe na farasi ambaye Grace aliweza kumpanda.



    “Hapa kuna kitu, lazima nitambue mtoto wa mfalme anaelekea wapi, na kwanini anaonekana hana raha “,mzee huyo aliyekuwa mdadisi wa mambo, mzee ambaye hakutaka jambo lolote liweze kumpita. Alinyanyuka kutoka katika mtaro baada ya kujitupa kuyaokoa maisha yake, akimkwepa farasi aliyekuja uelekeo wake kwa kasi sana huku farasi akionekana kuwa na nguvu nyingi kumshinda mtu aliyemwongoza, hivyo jambo lolote lingeweza kutokea. Na baada ya kunyanyuka aliamua kufuatilia mwisho wa farasi yule, baada ya kugundua kuwa binti mfalme ndiye aliyekuwa amempanda.



    “Aiweeeh mizimu ya mababu, na upumzike kwa amani kipenzi changu, mama Njoshi, mama wa kipenzi changu,, naahidi kulipiza kisasi”,Grace alitamka maneno ya huzuni na hasira huku machozi yakimtoka,baada ya kufika nyumbani kwa kina Njoshi na kukuta mazingira yakiwa yamevurugika.Alijaribu kuingia ndani,kwani mlango wa geti ulikuwa wazi,alikutana na sehemu ikiwa imechimbwa na kufukiwa kiholela.Baada ya kumwita mama Njoshi kwa muda mrefu na kuzunguka kila sehemu ya nyumba bila kumwona mtu yeyote ,aliamua kuchukua jembe lililokuwa pale nje na kisha kufukua sehemu ile iliyoonekana kufukiwa muda mfupi uliopita.



    Machozi yalimtoka baada ya kukuta maiti ya mama yake Njoshi ikiwa imefukiwa mahali pale, huku akiwa ameuawa kikatili. Lakini kipindi haya yote yakiendelea, mzee yule aliyekuwa akimfuatilia Grace, aliweza kushuhudia yale yote yaliyotokea kwani alikuwa akichungulia kupitia uwazi mdogo alioutoboa katika uzio wa nyasi wa nyumba hiyo.



    “Mmmh mama yake Njoshi kauawa, mmh kisasi tena, mfalme ndio kamuua, ngoja nikawapatie Wanamutapa wote taarifa hii “,mzee yule alisitisha zoezi lile la kuendelea kuchungulia, na kisha kutimka mbio kutoa taarifa kwa wanakijiji wote kuhusu kifo hicho cha utata. Chezea mzee huyu wewe!, mzee huyu alikuwa mmbea sana, kuwashinda hata wanawake wote unaowafahamu wewe ndugu msomaji.



    Msitu wa majini



    Mida kama ya saa sita mchana, Njoshi akiwa amebeba jeneza zito, jeneza la ajabu, alitembea taratibu kutoka nje ya msitu.. Huku akiwa ameshika fimbo ya kifalme katika mkono wake wa kulia, fimbo ambayo iliwawezesha majini kuishi msituni katika ardhi ya Mwamutapa, na kuumiliki msitu huo. Fimbo hiyo ambayo ilikuwa imebakia moja tu katika himaya yao, baada ya fimbo ya kwanza kuibiwa miaka mingi sana iliyopita, enzi na enzi, vizazi na vizazi na kumilikiwa na ukoo wa mfalme Mutapa kwa kurithishana. Wafalme waliamini ukimiliki fimbo hiyo ufalme wako utadumu kwa muda mrefu, na pia hutasumbuliwa na majini wa msituni, majini ambao waliuvamia msitu kutoka baharini baada ya kufanya makosa na kufukuzwa huko. Na kuamua kuanzisha makazi hayo katika msitu huo.



    Majini hawa baada ya kufukuzwa baharini, waliiba fimbo mbili za ajabu fimbo ambazo ziliwalinda wasiweze kuuawa na majini wenzao wa baharini baada ya kuwakosea ,kwani walitakiwa wauawe mala baada ya kufukuzwa kutoka baharini.



    Wakiwa wanazagaa huku na kule, waliweza kufika katika msitu mzuri, msitu wenye maua ya kupendeza huku matunda mengi yakipatikana katika msitu huo, waliamua kuanzisha makazi mahali hapo. Mahali hapa si pengine, bali ni katika msitu huu unaopatikana katika nchi ya Mwamutapa.



    Majini hawa baada ya kuingia msituni, walibalikiwa kuwa na mali nyingi, kiasi kwamba waliweza kuvamiwa na binadamu waweze kuwaibia mali zao. Binadamu wa kwanza aliwaibia fimbo yao, na kuiandika jina lake la ukoo, jina Mutapa na huo ndio ukawa mwanzo wa ufalme wake, ufalme wenye nguvu na katili kwa raia wake vizazi na vizazi. Fimbo hii ilimsaidia mfalme asiweze kudhurika na majini wa msituni, majini waweze kukaa msituni siku zote na wasiikalibie ngome yake kumdhuru. Pia fimbo hii ilimsaidia azidi kuwa tajili mfalme Mutapa huku akirithisha ufalme watoto mpaka wajukuu zake huku wakitumia jina lile lile Mutapa.

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hivyo basi, majini wa msituni walishindwa kulipiza kisasi kwani wasingeweza kuisogelea ngome ya mfalme, kwani tayali fimbo iliweza kuwazuia. Waliamua kuachana naye kwani walikuwa na fimbo nyingine, fimbo ambayo majini wote waliandika majina yao na kuwazuia majini wa baharini kuingia msituni kuwaua.



    Lakini kijana Njoshi kaingia msituni kwa mala nyingine na kuiba fimbo iliyobakia, na kufuta majina ya majini wote wa msituni katika fimbo ya kifalme, na kuandika jina lake. Bila kutambua kuwa, baada ya kufuta majina ya majini wale na kuandika jina lake, tayali majini wa baharini wangeuvamia msitu na kuwaua majini wale kwani walitakiwa kuwaua baada ya kufanya makosa na kufukuzwa baharini.



    “Hayuko mbali, yuko anatoka nje ya msitu, kamateni, ikiwezekana ueni, kabla hatujavamiwa na kuuawa na wenzetu wa baharini, kwani tayali wako njiani kutoka katika bahari ya hindi wanakuja “,malikia aliongea huku akionekana kuogopa sana,, kitendo kilichowafanya kuongeza mwendo, kwani majini wote walikuwa wakipaa kama ndege kwa wakati huo na kukata upepo kumkimbiza Njoshi, kutokana na mabawa makubwa yaliyotokea kimaajabu katika miili yao.







    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog