Search This Blog

ROHO YAKE INADAI - 3

 

    Simulizi : Roho Yake Inadai

    Sehemu Ya Tatu (3)





    Saa tatu usiku …





    Walikuwa sebuleni wanakula chakula cha usiku. Walikuwa wamekawia kula leo maana chakula kiliandaliwa kwa kuchelewa. Kulikuwa ni kimya mbali na sauti ya vijiko vikigonga sahani na midomo ikitafuna.



    Brian alikuwa anamtaza Olivia mara kwa mara. Macho yake hayakukaa muda pasipo kuangukia kwa mtoto huyo. Bado alikuwa na hofu naye. Alidhani pengine aweza badilika kuwa kama alivyokuwa muda ule, lakini haikuwa hivyo mpaka wanaelekea kumaliza kula.



    “Brian,” mama akaita. Yeye alikuwa ashamaliza kula. “Vipi msiba? Kila kitu kilienda sawa?”



    Brian akatikisa kichwa pasipo kutia neno. Akaendelea kula.



    “Tulitoka leo, kwenda nje kabisa ya mji. Ni kwasababu ya haya mambo yanayotokea, ila bahati haikuwa kwetu, hatukufanikisha!” mama alizungumza. Maongezi haya yakamvutia Brian, akamtazama mamaye na kumpa miamko yote impasayo mtu aliye makini.



    “ … Tulienda kumtafuta mtaalamu wa mambo ya majini, ila hakuwapo. Inaonyesha ni mtu wa ratiba nyingi. Tungempata pengine angesaidia.”



    Mama alipomaliza kusema hayo, Brian akaendelea kula. Hakuona kipya. Alikuwa anatafuna lakini asihisi ladha ya chakula. Mawazo yake hayakuwapo hapo kabisa. Mama akamtazama na kisha akasafisha koo lake, Brian akampatia macho.



    “ … kwahiyo tukaona itakuwa kheri endapo tungetafuta namna nyingine, hivyo tukaenda kanisani kumwona padri aje kutusaidia kwa maombi.”



    “Padri Alfonso?” Olivia akauliza kwa macho yalojawa woga. Mrs Garett akamtazama na kumtikisia kichwa kuafiki. Olivia akakunja uso wake na kulalama. “Simtaki padri Alfonso!” akarudia tena, “Simtaki padri Alfonso!” alafu akaangua kilio.



    “Usijali, Olivia,” akasema Mrs Garett. “Kila kitu kitakuwa sawa!” akambeba binti huyo na kumweka mapajani mwake akimbembeleza. Brian hakutia neno, akaishia kutazama tu. Na alipomaliza kula, akaenda zake chumbani.



    Alipojilaza, akatazama zile nyaraka tatu alizoachiwa na Dkt Hamill. Akainyaka ile ambayo alishaanza kuisoma. Akatafuta eneo alipoishia na kuendelea kuipitia taratibu …



    “ … Jasmine kabla hajanieleza kule alienda kufuata nini, akatikisa kwanza kichwa chake,” Dkt Hamill aliendelea kuhadithia kwenye nyaraka. “ … alifuma mafundo matatu alafu akaniambia kama unataka kujua basi kesho tuongozane kwenda huko. Nilihofia. Japo nilikuwa nataka kujua nini kipo kule, bado nilikuwa na hofu kifuani mwangu. Basi hapo akawa amenikata hamu, na pasipo kuaga nikajiendea.



    Kesho yake nikamfuatilia, hakwenda kule msituni. Wala keshokutwa, wala mtondogoo. Ila siku iliyofuata, majira ya jioni, akapotea nyumbani. Nilimtafuta kila kona pasipo mafanikio basi nikajua ya kuwa atakuwa ameenda kule msituni.



    Nikaelekea huko. Na basi kama ilivyokuwa siku ile, alipotoka nikakimbia zangu kurudi nyumbani bado nikiwa sijui ni nini mtumwa huyo anafanya mule ndani. Siku hiyo, kwenye majira ya saa mbili usiku, Jasmine akaniita. Ilikuwa ni rahisi kwa maana nilikuwa nimejiketia nje.



    Akaniambia, “Hamill, twende kule bandani kuna jambo nataka kukwambia!” Nikaongozana naye kwenda huko. Akaniketisha barazani na kuniuliza, “Unapenda mazingaombwe? Unafurahi kuyaona?”



    “Ndio, napenda!” nikamjibu.



    “Basi kesho twende kule msituni! Twende ukaone mazingaombwe ya kufurahisha!”



    “Lakini mimi naogopa kwenda msituni!” nikamwambia nikimtazama kwa hofu. Akacheka. Akanidaka mkono na kunitazama machoni. “Hamna haja ya kuogopa, upo na mimi! Usijali, nyumbani hawatajua. Kwani mimi niendapo kuna yeyote ajuaye?”



    Nikalala siku hiyo nikiwa na mawazo lakini pia hamu. Nilikuwa napenda sana kwenda kuyashuhudia mazingaombwe. Nilijiuliza kumbe Jasmine huenda kwenye lile ghofu kutazama mazingaombwe! Ni nani anayafanya mule?



    Wasaa ulipowadia, nakumbuka ilikuwa ni kwenye majira ya jioni ya mapema, Jasmine akauteka mkono wangu na kutokomea nami msituni. Hakuna mtu aliyetuona. Hata watumwa wengine hawakuwa wanajua. Tukatembea upesi sana.



    Njiani Jasmine akinieleza namna nitakavyofurahia mazingaombwe ninayoenda kuyaona!



    .

    Basi kwasababu ya mwendo wetu huo, tukawasili eneoni mapema. Ilikuwa ni kama baada ya dakika sita tu! Tayari jengo ghofu lilikuwa mbele yetu. Lakini kabla hatujaingia humo, ajabu nikasikia sauti kali ya risasi! Nilishtuka mno!

    .

    .

    Sikuwahi nimewahi kusikia sauti kali kama hiyo. Huwa nasikia risasi ila si kwa ukaribu kiasi kile. Nilipotazama kando, nikamwona Jasmine akiwa hatamaniki kwa damu! Uso wake wote ulikuwa umefumuliwa na risasi! Haki sikuwahi kuona picha ya kinyama kama ile.

    .

    .

    Tundu kubwa lililopasua kichwa cha Jamsmine na kutapanya uso wake lilikuwa linachuruza damu kedekede. Nikatazama, kwa hofu, wapi ilipotokea risasi ile. Macho yalikua yamenitoka na moyo wanienda kwa pupa sana.

    .

    .

    “Hey Hamill!” nikasikia sauti kavu ikiniita. Kutazama upande wangu wa kulia, nyuma, hatua kama arobaini na mbili, nikamwona baba yangu. Mkononi alikuwa amebebelea gobore kubwa alilokuwa amelitua. Kumbe ndi’ yeye aliyemuua Jasmine.

    .

    .

    “Upo sawa?” akaniuliza akijongea. Nilikosa cha kumjibu. Nilipandwa na hasira mno. Nilimtazama kwa ghafira nikitamani kummaliza. Lakini yeye hakuwa anajali. Aliposonga karibu nami, akani ‘patipati’ kichwani na kumtazama Jasmine aliyekuwa maiti. Akamtemea mate.

    .

    .

    “Kufa wewe malaya!”

    .

    .

    Kwa hasira nikajikuta namshika baba yangu pindo lake la suruali na kumuuliza, “Kwanini umemuua Jasmine?” mara machozi yakaanza kunivuja. Nilishindwa kuuweka mdomo wangu sawa, ulipinda kana kwamba upinde wa mshale.

    .

    .

    “Unasemaje?” baba yangu akafoka. “Alikuwa anakupeleka wapi huyu malaya?” akaniuliza. Asingoje hata jibu, akasema, “Nilimkanya mara kadhaa akae mbali na familia yangu, hakusikia! Kwa maana mgongo wake hausikii tena mijeledi, ngoja na tuone kama kichwa chake kinaweza kuwa sugu mbele ya risasi!” aliposema hivyo akaguna akibinua mdomo.

    .

    .

    Akanyanyua mwili wa Jasmine na kuupeleka ndani ya ghofu. Akautupia humo na kukung’uta mikono yake kwa kumaliza kazi. “Twende!” akaniamuru.

    .

    .

    “Siendi popote!” nikamwambia. Na nisimngoje aniambie kitu, nikakimbia nisijue wapi naelekea. Nikakimbia tu kwenda mbali na baba yangu. Nilimchukia sana. Nilimwona ni mtu asiyefaa kabisa.

    .

    .

    Nikakimbia kadiri ya uwezo wa miguu yangu. Nilipochoka, nikalala chini na kulia sana. Pale nilipokuwa nimelaza kichwa changu pakalowana kwa machozi.



    Nilikaa huko mpaka giza lilipoanza kumeza uso wa nchi. Niliogopa sana kuwa msituni nyakati za usiku ila niliona ni kheri kuliko kwenda nyumbani. Basi nikajikunyata kwa baridi na kulazimisha usingizi unitwae.

    .

    .

    Ila kila mara nikawa nashtuka. Wanyama wakikatiza ama matunda yakidondoka ama miti ikisogezwa na upepo, nilikuwa nafungua macho na kuangaza. Nilikuwa naogopa. Sikuweza kudhani usiku ule ungekuwaje.

    .

    .
    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikiwa sijapata usingizi, nahangaika kufumba na kufumbua macho, nikasikia jina langu likiitwa kwenye miti! Nikanyanyua uso wangu haraka na kuangaza. Ilikuwa ni sauti ya kike. Punde kidogo nikaona mwanga wa taa kwa mbali. Haraka nikanyanyuka na kwenda kufichama nyuma ya mti kuchungulia.

    .

    .

    Nikaendelea kuitwa. Mara ya tatu nikatambua kuwa sauti hiyo ni ya mama yangu, nikaguswa moyoni. Nikaitikia na kukimbia kwenda kumkuta mama. Alikuwa mwenyewe katikati ya msitu. Mkono wake wa kushoto ulikuwa umebebelea taa, na ule wa kulia ukiwa umebebelea gongo kubwa kumlinda.

    .

    .

    Aliponiona akafurahi sana. Akanikumbatia kwanguvu akitupia taa kando. Akanibusu na kunikumbatia tena kwanguvu.

    .

    .

    “Twende nyumbani!” Akasema akinishika mkono. Alikuwa ni jasiri wa namna gani. Alikuja mwenyewe msituni kunitafuta, akimwacha baba peke yake nyumbani akivuta tumbaku. Asingeweza kulala ndani mimi nikiwa nje. Kuna muda nilikuwa najiuliza, ilikuaje mama yangu akaolewa na mwanaume katili kama baba yangu? Ila niliamini watu wadhalimu huitaji zaidi malaika kama mama yangu kuliko wawahitajivyo wadhalimu wenzao.

    .

    .

    Tukafika nyumbani salama, naye baba asiseme jambo, mdomo wake ulikuwa umetingwa na shughuli kubwa ya kunyonya tumbaku na kutemea moshi nje.

    .

    .

    Siku hiyo nikalala kwa maruweruwe sana. Jua liliponyanyuka, nikashukuru. Nikaomboleza kifo cha Jasmine na hata ile safari yetu ya kwenda kwenye mazingaombwe. Ningeenda na nani na yeye ashakufa? Niliogopa kwenda mwenyewe ingawa eneo nalifahamu.

    .

    .

    Basi nikaachana na mpango huo. Na sasa nikadhani ya kuwa Jasmine atakuwa ameenda milele. Nisingemwona wala kumsikia tena. Hakuna mtu anayemkumbuka mtumwa. Hakuna anayejali wala kutunza tarehe yake ya kifo, labda wenzake.

    .

    .

    Ila nilikuwa mwongofu. Nilikosea kuwaza hivyo. Roho ya Jasmine haikwenda, ilirejea kudai haki yake ya uhai. Ilirejea ikiwa si ya yule Jasmine nimjuaye, mwenye upendo, mpole na mkarimu. Ilirejea ikiwa ya muuaji asiye na chembe ya huruma. Aliyejawa na kisasi kikubwa!”

    .

    .

    Brian akaishia hapa kusoma. Macho yalikuwa yamechoka sasa na hakuweza kuendelea tena. Akaweka nyaraka ile kando na kuchukua muda kidogo kuyawaza yale aliyoyasoma, Hakuchukua muda, usingizi ukamkwapua asiamke mpaka asubuhi.

    .

    .

    Hakukuwa na shule hivyo hakuwa na sababu ya kuwahi. Akajibandua kitandani majira ya saa tatu asubuhi, akaoga na kuosha uso alafu akajivuta sebuleni. Huko akamkuta mama yake, Mrs Garett na Olivia. Walikwishaamka na tayari wamejipatia kifungua kinywa.

    .

    .

    “Brian, leo ndiyo siku ambayo Padri atakuja hapa. Naomba uwapo mapema nyumbani,” mama akakumbushia. Brian asionyeshe muitikio wowote, akaenda jikoni na kutwaa chakula cha asubuhi. Baada ya hapo, hakukaa sana nyumbani. Hakuona shughuli ya kufanya papo. Alipata wazo la kwenda kwa Brewster, kwakuwa ni asubuhi, aliamini atamkuta mzee huyo.

    .

    .

    Aliamini ana mambo kadhaa ya kuteta naye ingawa mlengwa wake hakuwa mtu wa kuunga mkono. Mkimya. Na kwa namna moja ama nyingine, anatisha.

    .

    .

    Kuna kitu alihisi hakipo sawa na mzee yule. Brian aliamini. Na pia alihisi kuna mambo ambayo mzee yule anayajua ila mdomowe kautia gundi.

    .

    .

    Akaendea stoo na kuchukua baiskeli yake, akakwea na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Brewster. Kama ilivyo ada nyumba hii ilikuwa imetulia haswa. Ni kama vile hakukuwa na mtu aishiye hapa. Kunguru walikuwa wametandia kwenye paa, wakitazama huku na kule, huku na kule.

    .

    .

    Brian akasonga karibu. Akaugonga mlango na kuita. Hakukuwa na majibu. Akachungulia ndani, hakumwona mtu. Sebuleni kulikuwa na kiti kimoja cha kucheza. Mbali na kiti hicho hakukuwa na samani nyingine. Sebule ilikuwa pweke, hodi ikibishwa inasikika na mwangwi.

    .

    .

    Brian akashusha pumzi na kujiuliza kwa sekunde kadhaa. Akakata shauri la kwenda nyuma ya nyumba hiyo. Huenda Mr. Brewster akaja kumkutia huko kama ilivyokuwa siku ile.

    .

    .

    Napo huko akakaa kwa muda mrefu akimtazama nguruwe wa Brewster. Mzee huyo hakutokea. Akawaza kuondoka, ila kabla hajafanya hilo, akapata wazo. Vipi akizama ndani ya nyumba ya mzee huyo na kutazama? Kupekua kidogo?

    .

    .

    Huenda nikagundua mambo ambayo hataki kuniambia, akawaza. Akili yake ikatumikisha viungo vyake vya mwili kutenda wazo hilo la kidhalimu. Akauendea mlango wa nyuma na kufanya namna kwa kuufungua kwa ndani baada ya kusukuma dirisha.

    .

    .

    Taratibu akaurudishia mlango huo na akarusha macho yake kukagua nyumba hiyo. Ilikuwa imejawa na tando za buibui kwenye kona zake. Kuta zilikuwa na ukungu. Harufu iliyokuwamo ndani haikuwa ya kuridhisha.

    .

    .

    Brian aliwaza ni namna gani mzee huyo anaishi humo. Alifika sebuleni, akakagua. Uso wake ulikuwa umeumba ndita kwa kutopenda anachonusa. Alipomaliza kutazama sebuleni, akaendea korido kwenda kukuta vyumba viwili vya nyumba hii.

    .

    .

    Ila kadiri alivyokuwa anapiga hatua kwenda huko, nayo harufu ikawa inazidi maradufu. Hakujua ni nini inanuka. Ilikuwa ni harufu kali ya kitu kilichooza.

    .

    .

    Alijaribu kuusukuma mlango wa kwanza, ukafunguka. Akachungulia humo ndani. Kulikuwa na kitanda chakavu chenye godoro lililotobokatoboka. Akaangaza huku na huko. Hakuona kitu zaidi ya tando za buibui, nguo zikiwa zimezagaa huku na kule.

    .

    .

    Akaachana nacho na kwenda kwenye chumba cha pili. Akajaribu kukifungua, mlango ukakubali. Harufu ile aliyokuwa anaisikia, sasa ikazidi mara tatu yake! Ilikuwa ni kali mno kiasi cha kuwa ngumu kuvumilika.

    .

    .

    Brian akabana pua yake kwanguvu. Akaangaza huku na kule chumbani. Hakukuwa na kitu! Chumba kilikuwa kitupu. Kimejawa na nzi na kina kiza kiasi kutokana na kutofunguliwa kwa pazia.

    .

    .

    Ila kabla Brian hajakiacha chumba hiki, akaona mlango mdogo kwa sakafuni. Kulikuwa na andaki kwenye chumba hiki. Na Brian akawaza kuwa huko ndipo kwenye kitu kitoacho harufu.

    .

    .

    Akabaki njia panda, aende kutazama, ama ajiondokee upesi kabla hajakutwa?



    Akawaza kwa muda mchache, akaamua kwenda kutazama. Ila kabla hajatimiza adhma yake hiyo, akachungulia dirishani kukagua kama Brewster hayupo karibu. Alipojiona yu mwenyewe eneoni, akafungua mlango wa handaki na kutupia macho yake humo ndani.

    .

    .

    Kulikuwa kuna giza hivyo basi hakuonekani. Brian hakuweza kuona chochote kile pasipo kujali namna gani alikodoa. Kutakuwa kuna namna, aliwaza. Akatazama huku na kule akitafuta taa ya kutazamia humo ndani. Juu ukutani akaona taa inaning’inia. Akaisongea na kuikwapua. Akaiwasha na kufungulia mlango wa handaki.

    .

    .Akanyooshea mkono wake ndani ya handaki. Kutazama akaona vitu kadha wa kadha vikiwa ndani ya mifuko ambayo imetandiwa na nzi. Handaki ilikuwa kubwa, asingeweza kuliona lote kwa juu.

    .

    .

    Basi akashuka chini na kuendelea kuangaza. Kulikuwa na vitu vingi ambavyo vimefungashwa na kukalia hovyo. Vyote vilikuwa vinatoa harufu kali. Ndani humu kulikuwa na harufu na hewa nzito sana.

    .

    .

    Brian akainama na kubinyabinya miongoni mwa mizigo iliyokuwamo humo. Akiwa anaangaza, mara akaona kichwa kikubwa cha mnyama. Akakisongea kukitazama vema. Kilikuwa ni kichwa cha mnyama paa. Kilikuwa kinaelekea kuoza sasa.

    .

    .

    Ina maana kwenye mizigo yote ile kulikuwa na nyama za wanyama? Akajiuliza Brian. Ila bado roho yake haikuwa imeridhika. Alitaka kutazama kwenye mifuko ile mingine kulikuwa na nini pia.

    .

    .

    Akatoboa mfuko mmoja. Kabla hajatazama vema, akasikia sauti ya kengele. Akashtuka. Kengele hii ilikuwa ni ya baiskeli! Nani amebofya baiskeli yake? Ina maana Brewster amefika? Akapatwa na maswali mengi lakini zaidi hofu sana!

    .

    .

    Moyo wake ulianza kwenda mbio sana. Kichwa kiliwaka moto, je atoke upesi humo kwenye handaki ama abaki? Kwakweli hakuwa anajua cha kufanya. Alihisi kuchangayikiwa.

    .

    .

    Haraka akapanda ngazi kuendea juu. Alipofika kwenye kamlango ka handaki, akasikia mlango unafunguliwa, na punde vishindo vya miguu! Akawaza upesi. Akitoka, humo chumbani hakuna mahali pa kujificha, itabidi aende chumba kingine. Ni wazi ataonekana.

    .

    .

    Kwa upesi akawaza na kuamua kubakia humohumo ndani kwenye handaki. Akasimamisha masikio yake asikie kinachoendelea.

    .

    .

    Brewster alisafisha koo lake na kuketi kitini. Mkono wake wa kuume ulikuwa umebebelea mfuko mweusi wenye kitu ndani. Alikuwa amechoka, lakini pia macho yake yalionyeshea mawazo fulani. Si makubwa. Hakuwa anahofia.

    .

    .

    Kwenye koti lake akatoa kiko na kukiwasha. Akawa anavuta akiwa anachambua mawazo yake kichwani. Taratibu akawa anaenda mbele na kurudi nyuma, anaenda mbele na kurudi nyuma akibembea. Mdomo wake unanyonya kiko na kutemea moshi nje. Macho yake yanatazama dirisha, mlango, paa, korido, kila sehemu.

    .

    .

    Baiskeli aliyoikuta nje. Nyayo za viatu. Mlango kuukuta wazi. Vyote vilikuwa vinatafuna kichwa chake kwa nafasi yake. Lakini ilikuwa ni ajabu kwani hakuonyesha hofu ambayo pengine mwanadamu mwengine angeonyeshea.

    .

    .

    Alikuwa mtulivu.

    .

    .

    Alipovuta kiko chake kwa dakika kumi pasipo kusikia jambo, akapaza sauti yake kusema, “Ni kheri ukaja sebuleni! Utakaa huko mpaka muda gani? Nimechagua amani badala ya shari na wewe.”

    .

    .

    Sauti yake ilisikika kila eneo ndani ya nyumba yake. Alipolijua hilo, akaendelea kuvuta kiko chake akimpa muda mvamizi ajitokeze yeye mwenyewe. Akavuta tena kwa takribani dakika tano, bado kukawa kimya. Basi akazima kiko chake na kusimama.

    .

    .

    “Kwakuwa umekuwa punda wa kulazimishwa kunywa maji ya mtoni, acha nikupe ukitakacho!” akasema kwa sauti kubwa. Akashika njia kuendea kile chumba chake cha kwanza. Mwendo wake ulikuwa wa kikakamavu mbali na umri wake. Bado alikuwa ana nguvu za kujisogeza, na hata kupambania maisha yake.

    .

    .

    Alienenda kwa tahadhari na alipozama ndani ya chumba hicho, nyuma ya mlango akatoa gobore lake na kulitazama kama lina risasi humo ndani. Alipoliona li vema, akalikoki tayari kwa shambulizi.

    .

    .

    “Toka na ujisalimishe kwa usalama wako!” Brewster akafoka. Akatoka kwenye chumba alichomo na kuendea kile chumba pekee kilichobakia. Bado alikuwa anatembea kwa tahadhari sana. Alipofika humo, akagundua ya kuwa, taa ile atumiayo kuzamia kwenye handaki haikuwapo!

    .

    .

    Akatazama mlango wa handaki. Akapata sasa shaka kuwa mvamizi atakuwa humo ndani. Taratibu akauendea mlango huo, akafungua na kuonyeshea kinywa cha gobore humo.

    .

    .

    Akajaribu kuangaza kwa macho yake ya kizee. Hakuwa anaona kitu! Ndani kulikuwa ni giza. Na pia kuingia humo pia ilikuwa ni hatari.

    .

    .

    Brewster akawaza cha kufanya. Hakuwa mtu mwoga ila ilimlazimu achukue tahadhari hapa. Akafyatua risasi moja ndani ya handaki. Mwanga wa risasi ukalipuka na kuangaza humo. Kwa kiasi kidogo, Brewster akawa ameona sasa.

    .

    .

    Akajiveka ujasiri na kuzama humo. Akashusha mguu kwa taratibu, akiwa anaangaza huku na huko ingawa haoni. Alipofika katikati ya ngazi, akafyatua tena risasi apate kuona lakini pia kumtisha mvamizi aliyekuwamo humo ndani.

    .

    .

    Ila hakujua kuwa risasi hizo zilionyesha pia mahali yeye alipo.

    .

    .

    Aliposonga hatua tatu, ghafla akastaajabu amedakwa mguu, akadondoka chini na kubiringita kwenye ngazi mpaka chini. Akapoteza fahamu kwa muda.

    .

    .

    Haraka Brian akatoka ndani ya handaki, ndani ya nyumba, akajikwea kwenye baiskeli na kutokomea upesi akiwa na pupa sana! Hata hakuamini kama ametoka salama.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    .



    “Nadhani leo itakuwa vema tukipika mboga za majani!” Alipendekeza Mrs Garett baada ya kuulizwa na Mama yake Brian. Tangu amekuja kwenye nyumba hii, ni nyama tu ndiyo imekuwa ikitembelea jiko.

    .

    .

    “Basi kama ni hivyo, sina haja ya kuanza kuandaa mapema,” akasema mama Brian kisha akaketi kochini. Hapo sebuleni walikuwa wote, hao wanawake pamoja pia na Olivia.

    .

    .

    Baada ya Mrs Garett kutazama runinga kidogo, Mama Brian akamuuliza, “Ni nini mipango yako baada ya mumeo kufariki?”

    .

    .

    Mrs Garett akaguna na kushusha pumzi ndefu. “Sijajua. Unajua sijapata muda wa kutulia tangu mume wangu afariki. Akili yangu inashindwa kuwaza mambo ya kujiendeleza, bali hofu hofu hofu tu!” aliposema hayo, akamtazama Olivia, alafu akapeleka sura yake kando na kusema kwa sauti ya chini.

    .

    .

    “Likipita hili nitatuliza kichwa changu niangalie chakufanya sasa. Natumai kila kitu kitakuwa sawa.”

    .

    .

    Mama Brian akamwekea mkono wake begani. “Kila kitu kitakuwa sawa, usijali.” Mrs Garett akatikisa kichwa chake kuitikia. “Hata wewe umewezaje kwenye hali hii?” akauliza. Mama Brian akatabasamu na kusema, “Nishazoea. Ni muda sasa nikiwa mwenyewe. Japokuwa mume wangu aliniacha na kiasi kidogo cha pesa, niliweza kukikuza.

    .

    .

    Nilihangaika sana mwanzoni, kwa upweke na kwa kutokuwa na uzoefu. Ila kadiri na muda nikazoea. Niko sawa sasa,” akamalizia kwa kutabasamu. Mrs Garett naye akatabasamu.

    .

    .

    “Nitashukuru sana mambo yatakapotulia.”

    “Usijali. Kila kitu kitakuwa sawa. Ngoja padri Alfonso akija leo tuone nini kitatokea. Naamini atatusaidia.”

    .

    .

    Mara mlango ukafunguliwa na Brian. Alikuwa anatiririsha jasho na anahema kwa pupa. Kila mtu akamshangaa kwa namna alivyokuwa. Hakusalimu, akaenda ndani upesi, ila mara akarudi na kusema, “Akija mtu yeyote kuniulizia, sipo!”

    .

    .

    “Kuna nini Brian?” mama akauliza. Swali hilo lilimkutia Brian akiwa koridoni anazama ndani ya chumba chake. Alikuwa yu harakani mno. Mama hakuhangaika naye, wakaendelea na mambo yao.

    .

    .

    Muda nao ukaenda mpaka kufikia jua kuzama na ilhali hakuna yeyote aliyekuja kumuulizia Brian. Ikiwa inaelekea majira ya saa mbili na nusu usiku, Padri Alfonso na dada Magdalena wakafika hapo nyumbani. Walikuwa wamekawia kwasababu ya kutingwa na shughuli fulani fulani za huduma huko kanisani.

    .

    .

    Padri Alfonso alikuwa amevalia joho jeupe. Dada Magdalena amevalia gauni jeusi na kiremba cheupe, shingoni amebebelea rozari.

    .

    .

    “Karibuni sana!” Mama Brian akasema kwa tabasamu pana akiwapa mkono wageni wake. “Nimefurahi sana mpo hapa. Najua mmeacha kazi zenu lukuki kuja kutuhudumia.” Hakika wanawake hawa wakafurahi sana. Ila si kwa Olivia. Yeye alikuwa ameketi kwa mbali, macho yake yakibeba hofu. Alikuwa anawatazama Padri Alfonso na dada Magdalena kana kwamba vinyago vitishavyo. Hakuwa na amani.

    .

    .

    “Mngependelea chai?” akauliza Mama Brian.

    .

    .

    “Hapana.” Padri Alfonso akatikisa kichwa. “Tunashukuru. Muda umeenda, nadhani tungeendelea tu na huduma yetu.”

    .

    .

    “Olivia!” Mama Brian akaita. “Kamwite Brian aje sebuleni.”

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Olivia akasimama na kwenda. Punde kidogo akarudi na Brian ambaye alisalimu na kisha kuketi. Aliketi karibu na Olivia, kochi moja.

    .

    .

    Basi kidogo maongezi yakachukua nafasi mama akimtambulisha Brian na kutoa historia kidogo ya familia yake. Wakati huo Brian akatambua ya kuwa Olivia hakuwa sawa. Alikuwa anahofia. Macho yake yalikuwa yanamtazama padri Alfonso.

    .

    .

    Brian akajaribu kutazama kile akitazamacho Olivia. Ilikuwa ni kwenye pindo la mfuko wa joho la padri. Hapo alipotazama vema, akaona kitu kama damu kwa ndani ya mfuko. Akapata shaka.

    .

    .

    Akiwa kwenye hilo ombwe, mara mlango ukagongwa. Na sauti kavu ya kizee ikasema, “Hodi!”





    .

    Brian akatoa macho kwa mshangao. Aliogopa. Alihisi hiyo hodi haitomtendea jema.

    .

    .

    “Brian, kafungue mlango,” mama akamwamuru. Brian akasita. Alimtazama mama yake kwa sekunde chache kisha akanyanyuka. Hata mama alihisi Brian hayupo sawa. Aliufungua mlango na uso kwa uso akakutana na Brewster!

    .

    .

    Mzee huyo alikuwa amekodoa macho haswa. Kwenye paji lake la uso upande wa kulia alikuwa amevilia damu. Brian akamsalimu. Alikuwa anaogopa kwa namna ambavyo Brewster alivyokuwa anamtazama.

    .

    .

    “Mama yako yupo?”

    .

    .

    “Ndio, yupo. Karibu.”

    .

    .

    Brewster aliingia ndani, akasalimu kila mtu. Kwakuwa kulikuwa na watu wengi humo, akaomba kuonana na mama Brian faragha. Basi Mama Brian akaomba radhi na kisha akaelekea nje pamoja na Brewster.

    .

    .

    Huko wakakaa kwa muda wa kama dakika tano. Waliteta wakiwa hawasikiki na hata mmoja wa walioko ndani. Walipomaliza, Brewster hakurudi tena ndani hata kuaga, akaenda zake, Mama Brian akarudi ndani peke yake.

    .

    .

    “Samahani kwa usumbufu.”

    .

    .

    “Usijali,” akasem Padri Alfonso kisha akauliza Mama Brian akiwa anaketi kitini. “Unamjua yule mzee?”

    .

    .

    “Aaahmm … ndio! Kiasi chake.”

    .

    .

    Padri Alfonso akatikisa kichwa na kunyamaza asitie neno. Mama Brian akauliza, “Vipi kuna shida yoyote?”

    .

    .

    “Ndio, ipo.”

    .

    .

    “Ipi hiyo?”

    .

    .

    “Watu wanasema si mtu mzuri. Hana marafiki wala mtu wa karibu. Ni mtu anayependa upweke. Mara kadhaa nimekuwa nikiletewa mashataka yake kanisani.”

    .

    .

    “Umejuana naye lini?” Dada Magdalena akamuuliza mama Brian.

    .

    .

    “Si muda mrefu sana.”

    .

    .

    “Na tangu ulipojuana naye umemwona ni mtu wa namna gani? … Anakuletea habari gani?” Dada Magdalena akaendelea kuuliza. Kidogo Mama Brian akasita. Akamtazama Padri Alfonso na Dada Magdalena kisha na kusema, “Habari za kawaida tu. Hamna cha zaidi.”

    .

    .

    “Hamna shida. Tulikuwa tuna hofu kutokana na historia yake. Nadhani sasa tunaweza kuendelea na huduma yetu,” akasema Padri Alfonso. Basi wote wakanyanyuka na kisha taa zikazimwa na kuwashwa mishumaa kwa maelekezo ya Padri.

    .

    .

    Dada Magdalena akafukiza, na kumwagia maji maeneo mbalimbali ya nyumba. Maji ya baraka. Kisha wakafunga macho na sala ikaanza baada ya kuimba na kusema kwa pamoja vifungu kadhaa.

    .

    .

    Wakasali kwa dakika sita mfululizo pasi na kukoma. Kwenye dakika ya saba, Brian akavutwa mkono wake wa kuume. Upesi akafungua macho na kutazama. Akamwona Olivia akiwa amejawa na hofu usoni. Macho yake yanatiririsha machozi.

    .

    .

    “Nini, Olivia?” Brian akauliza kwa kunong’ona akitumia haswa uso wake kufikisha ujumbe. Olivia akaonyeshea koridoni. Brian kutazama hakuona kitu. “Kuna nini?” akauliza tena kwa mtindo uleule.

    .

    .

    Olivia akatikisa kichwa. Kwa sura na mkono wake, akaonyeshea kulikuwa na kitu. Brian akamhimiza afunge macho, asitazame popote pale. Olivia akatazama tena kule koridoni kwa mashaka, kisha akafunga macho yake, Brian akafuatia.

    .

    .

    Sala ikawa inaendelea. Baada tena ya dakika mbili, Olivia akamvuta Brian mkono. Brian akafungua macho yake kumtazama. Lakini kabla hajasema kitu, akaona mtu anaishia koridoni upesi. Olivia akanyooshea kule koridoni na kumwambia Brian kwa ishara ya kinywa, “Kuna mtu kule!” sasa hivi Brian hakuwa na haja ya kubisha kwani kwa macho yake alishuhudia.

    .

    .

    Alikuwa nani yule?

    .

    .

    “Kuna mtu kule!” Olivia alisema akiwa anachuruza machozi. Sauti yake ilikuwa inasikika kwa chini maana alikuwa ananong’ona. Basi Brian akatoka pale eneo la sala na kwenda koridoni kutazama. Alirusha macho yake, hakuona kitu! Ila mlango wa chumba chake ulikuwa wazi. Ulikuwa unachezacheza kuashiria umeguswa.

    .

    .

    Akawaza. Mtu yule amekimbilia chumbani mwake? Basi akaanza kuchukua hatua kwenda huko kutazama. Olivia alikuwa anamtazama kwa hofu, ni kama vile alikuwa anataka kumzuia asifanye hilo.

    .

    .

    Brian akasonga. Kulikuwa ni giza, ila kwakuwa nyumba za jirani na huko nje taa zilikuwa zinawaka, basi akaweza kuona akanyagapo. Taratibu akasonga na kusonga. Alipofikia mlangoni, akatazama ndani ya chumba chake. Hakuwa anaona jambo.

    .

    .

    Akasonga kuzama ndani. Alikuwa ana hofu. Alikuwa anatembea kwa tahadhari macho yake akiyatupa kule na kule. Alipodumbukia kabisa ndani ya chumba, akasikia sauti ya kishindo cha mguu. Akapatwa na woga. Kutazama mlangoni alikuwa ni Olivia.

    .

    .

    “Olivia, rudi sebuleni!” Brian akamwambia kwa kunong’ona. Olivia akatikisa kichwa na kusema, “yupo kule!”

    .

    .

    “Wapi?” Brian akauliza.

    .

    .

    “Jikoni!” Olivia akajibu akionyeshea kidole. Basi Brian, upesi, akatoka na kwenda jikoni akiongozana na Olivia. Walipofika huko hawakukuta kitu.

    .

    .

    “Hamna kitu, Olivia.”

    .

    .

    “Nilimwona! Alinichungulia na kisha akakimbilia huko!”

    .

    .

    Brian akashusha pumzi ndefu. “Olivia, huyo mtu hataki tuwepo kwenye sala. Anatusumbua tusishiriki huduma. Turudi kwenye maombi na sasa tusitazame wala kuhangaika naye.”

    .

    .

    Olivia akajibu kwa kumeza mate. Brian akautwaa mkono wake na kumrudisha sebuleni lakini binti huyo akitazamatazama huko nyuma, pembeni na kule aelekeapo.

    .

    .

    Wakajiunga na sala. Wakafunga macho yao kwanguvu wakitulia. Kheri wale waliowaacha hawakutambua kama waliondoka. Au labda walitambua wakanyamaza.

    .

    .

    Sala, kama walivyoiacha, ikaendelea. Sasa hivi wakadumu kwa dakika moja tu, na mara Brian akaanza kuhisi upepo kana kwamba wapo nje ya jengo. Akakunja uso wake kwa maulizo, ila hakufungua macho yake. Punde, sauti ya sala ikakoma!

    .

    .

    Brian akiwa amefumba macho yake, yu gizani, akajitahidi kuskiza asisikie kitu. Muda kidogo akasikia sauti ya Olivia ikimwita! Akafungua macho kutazama, akamwona Olivia akiwa kando yake. Ila hawakuwa ndani bali nje! Kiza. Kimya.

    .

    .

    “Olivia tuko wapi hapa?” Brian akauliza akitazama kila pande yake. Wote walikuwa wamejawa na hofu. Olivia alikuwa anachuruza machozi lukuki hata kunena hawezi.

    .

    .

    Kutazama vema, wakagundua eneo walilopo ni la kanisa. Hapo palikuwa ni uwanjani. Hatua kama ishirini na nne mbele upande wao wa kaskazini kulikuwa na jengo kubwa la kanisa la Boston!

    .

    .

    Wamefikaje hapa?

    .

    .

    “Brian!” Olivia akaita. Akanyooshea kidole chake upande wa mashariki, huko, kwa mbali, Brian akamwona mtu akiwa amevalia nguo nyeupe. Mrefu, amesimama wima. Na kando ya mtu huyo, akamwona mwingine kama kivuli, ila kichwa chenye kiremba cheupe!

    .

    .

    Punde watu hao wakaanza kuwasogelea! Mwendo wao ulikuwa ni kana kwamba watu wasio na maungio ama wamevunjika mifupa lakini wakitaka tu kutembea! Waliogofya. Na japo walikuwa mbali, macho yalikuwa yanang’aa kama taa ama paka awapo gizani.

    .

    .

    “Kimbia!” Brian akaropoka. Upesi wakaanza kukimbia na Olivia kuelekea kule kanisani. Hawakuwa wanaona majengo mengine yoyote zaidi ya kanisa. Mbali na jengo hilo kulikuwa na misitu tu ikiwa imewazingira!

    .

    .

    Wakakimbia kwa kasi na kukomea kwenye lango la kanisa. Wakajaribu kulifungua, haikuwezekana. Lilikuwa limetiwa ‘lock’, basi haraka wakaachana nalo na kuuendea mlango mwingine mdogo. Wakaujaribu, huo ukafunguka.

    .

    .

    Wakazama ndani upesi na kuurejeshea. Wakiwa wanahema kwa pupa, macho yamewatoka, wakapata tulizo ya kuwa huenda sasa wakawa salama. Ila punde wakapata hisia tofauti! Ni kama baada ya sekunde sita tangu kuingia humo. Walihisi hawakuwa wenyewe, kuna watu wengine zaidi ya wao ndani ya jengo.

    .

    .

    Kutazama kwenye ukumbi wa kanisa, vitini, kulikuwa na watu wameketi. Na walipotazama madhabauni, kulikuwa na padri, Padri Alfonso, akiongoza misa.

    .

    .

    Nyuso za watu wote hawa hazikuwa za watu wa kawaida. Zilikuwa ni nyuso nyeupe zilizojawa na michirizi meusi kana kwamba vijito vya mito. Midomo meusi. Macho ya njano na nyekundu yaliyokuwa yanawatazama watu walioharibu misa yao, Brian na Olivia!

    .

    .

    Kwa muda kidogo Brian akakosa la kufanya. Olivia akalia kwa hofu. Waliona huo ndiyo mwisho wa maisha yao. Waumini wote wakasimama na wakiongozwa na Padri Alfonso na Dada Magdalena wakawasogelea Brian na Olivia ambao hawakuwa na mahali pengine pa kukimbilia. Walijaribu kufungua mlango pasipo mafanikio.

    .

    .

    Waliwapowasogelea kabisa, wakasimama wote na kusema kwa pamoja, “Unaona nini Brian?” kisha wakanyoosha mikono yao kuwadaka.

    .

    .

    Brian na Olivia wakapiga kelele kali. Wakawashtua watu wote waliokuwepo kwenye sala. Wote wakakoma kusali na kuwatazama kwa mshangao.

    .

    .

    “Brian! Olivia! Mmekumbwa na nini?” mama Brian akauliza. Brian kabla hajajibu kitu, akarusha macho yake kwa Padri Alfonso na Dada Magdalena. Dada Magdalena akatabasamu.



    Brian akalipuka kwa hofu. Akamnyooshea kidole Dada Magdalena na kusema, “Ni mashetani!”



    “Unasemaje Brian?” Mama akauliza akiduwaa.



    “Ni mashetani!” Brian akalia. Aliwanyooshea kidole Padri Alfonso na Dada Magdalena. “Hawa ni mashetani! Mashetani! Tokeni nyumbani kwetu. Mashetani!”



    Ikawa vurugu asitake kusikia wala kuambiwa kitu akaelewa. Aling’ang’ana Padri Alfonso na Dada Magdalena ni mashetani, watoke nyumbani kwao! Waende zao.



    Basi sababu ya vurugu hii, Padri Alfonso na Dada Magdalena wakaaga waende zao. Mama Brian akawaomba radhi kwa yote yaliyotokea.



    “Usijali,” Padri Alfonso akasema akiufuata mlango. Nyuma yake Dada Magdalena akimfuatia. Wakaenda zao na amani ikarejea kwa muda kwenye nyumba ya wakina Brian. Ila walezi wakiwa hawajui liendealo. Kwa namna moja wamechanganyikiwa, wamejawa na maswali pia hofu.



    “Brian, Olivia, mnaweza mkatuambia nini shida?” mama aliuliza. Sebule ilikuwa imetulia tuli. Taa zimewashwa na hata madirisha yamefunguliwa.



    “Ni mashetani!” Brian akasema akitazama chini kama mtu anayateswa na fikira. “Nimewaona kwa macho yangu. Tumewaona! Padri Alfonso na Dada Magdalena ni mashetani! Si watu wa dini!”



    “Mmewaona wapi?” Mrs Garett akauliza.



    “Kule kanisani!”



    “Lini?”



    “Leo! Leo wakati tunasali!”



    Mrs Garett na Mama Brian wakatazamana. “Brian, ulienda kanisani muda gani na wakati ulikuwapo hapa?” waliwaona Brian na Olivia ni watu waliochanganyikiwa. Maelezo yao yalikuwa hayawaingii akilini. Yalikuwa ni ya kufikirika. Vitu visivyowezekana!



    “Sijui huu mji unaelekea wapi? …” akasema Brian kwa sauti ya pole. Macho yake yalikuwa pole. Anatazama meza akiwandawanda mawazoni. “ … Naogopa sana. Sijui ni wangapi ni binadamu kama sisi, nyumba ngapi zimetwaliwa na kukaliwa na mashetani … Inatisha…”



    Brian aliposema hayo, akanyanyuka akitaka kwenda zake chumbani.



    “Ngoja, Brian,” mamaye akamshika mkono. “Ulimwona Brewster?” Brian kusikia hivyo, akaketi chini. “Ndio, nimemwona.”



    “Alikuja kwa ajili yako.”



    “Kukuambia kuwa nimevunja nyumba yake?”



    “Umevunja nyumba yake?” Mama akashangaa. “Hapana, si hilo!”

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Amekuambia nini?” Brian akauliza akimtazama mamaye kwa mshangao.



    “Amenipa onyo tu kama ilivyo kawaida yake … Brian, ulienda kwenye nyumba ya marehemu?”



    “Marehemu?”



    “Mkuu wenu wa shule aliyefariki majuzi!”



    “Dkt Hamill! … Brewster amekuambia nini?”



    “Jibu, ulienda huko?”



    Brian akanyamaza kidogo.



    “Ndiyo nilienda. Jana.”



    “Ulienda kufanya nini huko na mwenyewe hayupo? Amekwishafariki!”



    “Mama, Dkt Hamill alikufa mbele ya uwepo wangu. Nyakati zake za mwisho alikuwa na mimi. Kuna ubaya ga--?”



    “Brian! … tafadhali unaweza ukakaa mbali na matatizo kwa muda?”



    Brian akakuna kichwa chake akikitikisa. “Mama, nimechoshwa na hili! … ina maana umemweka Brewster awe ananifuatilia si ndio?”



    “Mimi na wewe tunajua hilo haliwezekani. Umemsikia Padri Alfonso alivyokuwa anamwongelea Brewster. Sipendi kumwona, lakini haimaanishi nisimsikilize anachoniambia! Na ni kweli aniambiayo.”



    “Kwanini ananifuatilia? Kwanini mimi?”



    “Na hilo ndilo linalonipa hofu. Brian, kaa mbali na mambo ya ajabuajabu. Tafadhali.”



    Brian akakaa kimya. Alikua anawaza kichwani mwake. Mbona Brewster anamfuatilia? Lakini zaidi, mbona hakumwambia mama yake kuwa amevunja nyumba yake kuingia ndani? Ina maana hajajua kuwa ni yeye?



    Hapana. Kama anajua vitu ambavyo hudhani yu mwenyewe, ataacha kujua jambo kama hilo la kwenda kwake? Ilikuwa haiingii akilini.



    Brian akanyanyuka na kwenda chumbani. Akatulia kitandani mwake akiwaza juu ya yale mambo aliyotoka kuyaona. Yalikuwa ni mambo mengi ya kumuumiza kichwa. Mengi ya kumuogopesha. Aliwaza nini yatakuwa mwisho wa yote hayo?



    Alinyanyuka akaendea dirisha la chumba chake na kutazama nje. Alitazama nyumba za jirani zilizopo karibu mpaka zile zilizokuwapo mbali. Akawaza sana. Je katika nyumba hizo, kuna watu kama wakina ‘Padri Alfonso?’. Alipata hisia za kumwogopa kila mtu sasa, lakini zaidi Brewster. Kwanini mwanaume huyo anamfuatilia kiasi hiko? Na kule kwenye handaki lake ….



    Aliendelea kutazama nje kana kwamba mtu atazamaye runinga kisha akasombwa na mawazo. Alikaa hapo kwa takribani dakika tano, akashusha pumzi ndefu, na kugeukia kitanda chake. Akapiga hatua tatu kukifuata, ila kabla hajakifikia, akasikia dirisha linagongwa!



    Haraka akageuza shingo yake kutazama. Hakuona kitu! Akasonga kulifuata dirisha na kutazama nje. Hakuona kitu. Akatikisa kichwa na kurudi kitandani. Akanyaka ile nyaraka ya Dkt Hamill ambayo bado hajaimaliza, akaiweka machoni apate kuendelea kuisoma.



    Kabla hajaanza akasikia sauti ya dirisha likifunguka. Haraka akatupa macho yake kutazama. Akaona dirisha likiwa wazi, kioo kimefunguliwa. Akatazama kwa kama sekunde tano, hakuona jambo. Ila kidogo, akaanza kusikia sauti ya watoto.



    Akaweka nyaraka yake pembeni na kunyanyuka taratibu kufuata dirisha atazame. Alipofika, akachomoza kichwa chake nje ya dirisha. Akatazama barabarani upande wa kushoto. Hakukuwa na kitu. Upande wa kulia. Hakukuwa na kitu!



    Kabla hajarudisha kichwa chake ndani, mara kioo cha dirisha kikashuka chini na kukaba shingo yake. Akapapatika upesi kujinasua toka kwenye dirisha. Alipojinasua, akabaki anahema kwanguvu na kushika shingo yake kwa maumivu makali.



    Hata mate aliona hayapiti kooni. Alipata woga, kila saa akitazama dirishani.



    **





    Baada ya kuzima bomba la maji mvua, Mrs Garett alitoka bafuni alimokuwa anaoga. Alifunga vema taulo lake kifuani na moja kwa moja akaendea sinki kwa ajili ya kusugua meno akamilishe zoezi lake la usafi.



    Alitia dawa kwenye mswaki na kuanza kujisafisha. Hakuwa na hili wala lile. Macho yake yalikuwa yanatazama kioo muda wote akijikagua uso. Kumbe bado alikuwa kijana, alijiona. Kumbe bado anaweza kupata mwanaume mwingine na kuwa na familia, aliwaza kichwani.



    Aliposafisha meno yake na kutema povu la dawa, akainua uso wake kutazama kioo. Ajabu akamwona Kecie nyuma yake! Akapiga kelele za woga macho yakiwa yamemtoka. Haraka akatazama nyuma, hakumwona mtu! Aliporudisha uso wake kwenye kioo, akakutana uso kwa uso na Kecie! Akapiga kelele kali za kumshtua kila mtu ndani ya nyumba.



    Ndani ya dakika tatu, Mama Brian na Brian wakafika bafuni. Ila walikuwa wamechelewa. Mrs Garett alikuwa tayari amekwishakufa. Kichwa chake kilikuwa kimepondwapondwa kwenye sinki, sinki lote limekuwa jekundu kwa kujawa na damu!



    “Mungu wangu!” Mama Brian akatahamaki akiwa ameziba mdomo wake. Muda si mrefu macho yake yakawa mekundu na kutiririsha machozi. Alimkumbatia mwanae na kuendelea kulia.



    Brian akambembeleza mamaye akiwa anatazama mwili mfu wa Mrs Garett. Ila akiwa anatazama vema, akaona maandishi yakiwa yameandikwa kwa damu karibu na dirisha la bafuni! Alipoyafinya macho yake kutazama vema, akauona maandishi hayo yakisomeka, “Tazame vema mji wenu!”





    **





    Baada ya siku mbili tangu Mrs Garett azikwe … saa saba mchana.





    Brewster akiwa amebebelea karatasi kadhaa mikononi mwake na mashine ya chuma ya kubania makaratasi hayo, alionekana akiwa anatembea kwa pole barabarani.



    Alijongea kufuata mstimu mmoja pembezoni ya barabara, akabandika picha tatu tofauti za watoto waliopotea. Mmmoja alikuwa wa kike, wawili wa kiume. Alipofanya hivyo, akaendelea na mwendo wake wa taratibu kufuata mstimu mwingine kutimiza majukumu yake.



    “Umeona matangazo ya wale watoto waliopotea?” aliuliza Mama Brian akiwa amesimama dirishani anamtazama Brewster akiishilia. Brian akanyanyuka upesi na kwenda dirishani kuangaza. Hakuona vema, akatoka kwenda nje kuufuata mstimu uliobandikiwa tangazo aone vema.



    Akasoma matangazo yote hayo matatu na kugundua kuwa miongoni mwa wale waliopotea, mmoja wao anamfahamu fika. Alikuwa ni Silvia! Silvia rafiki yake mkubwa na Wayde. Wayde mtoto wa seneta wa Massachusetts!



    Akaachama kwa mshangao. Nini kinaendelea?



    .

    Akarudi ndani na kumwambia mama yake kuwa mmoja wa wale waliopotea anamjua kwani wanasoma naye darasa moja. Na basi kutaka taarifa zaidi, akajipaki kwenye baiskeli yake, hakuweza kungoja, akaenda moja kwa moja kwa wakina Silvia.

    .

    .

    Huko akamkuta Wayde akiwa ameketi kibarazani. Akamsalimu na kumuuliza nini kimejiri. Wayde alikuwa anachuruza machozi. Pua yake imekuwa nyekundu kwa kuifikicha.

    .

    .

    “Silvia amepotea, Brian!” Wayde akalia. Akamkumbatia Brian na kuendelea kulia. Brian akapata kibarua cha kumbembeleza binti huyo kwa muda kidogo kabla hajatulia na kuendelea na maongezi yao.

    .

    .

    “Ni jana tu, Brian!” akasema Wayde akiwa amebanwa na kwikwi. “Ni jana tu amepotea katika mazingira ya kutatanisha! Yaani siamini, Brian! Siamini kabisa! Nimejawa na hofu sana.”

    .

    .

    “Ilikuwaje akapotea? Unaweza ukaniambia mazingira ya kupotea kwake?” Brian akauliza akimtazama Wayde usoni.

    .

    .

    “Brian, usiku wa kuamkia juzi, wakati tukiwa tunaenda klabu, Silvia aliniuliza kuhusu ndoto za ajabu! Sikumwelewa, na sikutilia sana maanani. Najuta kwanini nilifanya hivyo. Aliniambia Wayde, nimeota naitwa usiku wa manane. Kuna mwanaume ananiita. Kuna mtoto ananiita. Watu hao wamesimama mlangoni, wamesimama dirishani!”

    .

    .

    “Ni wakina nani? Aliwatambua?”

    .

    .

    “Hapana. Aliniambia ni kama vivuli tu. Ajabu ni kwamba walikuwa wanamuitia kwenda kutazama mazingaombwe!”

    .

    .

    “Ikawaje akanusurika siku hiyo?” Brian akadadisi.

    .

    .

    “Wakati anatoka chumbani kwake, katika hali ya kutojielewa, akakutana na mama yake koridoni! Mama yake alimkurupusha na kumuuliza nini alikuwa anafanya, lakini hakuwa anajua kitu! Hakujua hata alifikaje pale koridoni. Kitu pekee alichoweza kumbuka ni kuitiwa kwenda kutazama mazingaombwe na wale watu!”

    .

    .

    “Kwahiyo ndiyo haohao watakaokuwa wamemchukua?”

    .

    .

    “Ni nani mwengine, Brian? … asubuhi ya leo, wazazi wake walikuta chumba chake kikiwa wazi, pia mlango wa sebuleni. Na skafu yake imeokotwa huko msituni.” machozi yakabubuja macho ya Wayde. “Silvia ametokomea huko!”

    .

    .

    “Polisi wanasemaje?” Brian akauliza.

    .

    .

    “Wamesaka msitu wote tangu asubuhi. Hakuna walichopata zaidi ya skafu yake.”

    .

    .

    Brian akashusha pumzi na kushika tama akitazama barabara. “Brian, kuna lolote unajua?” Wayde aliuliza. Brian akatikisa kichwa akibinua mdomo. Akasema, “ni ajabu. Watu watatu wapotea ndani ya siku moja! Si jambo la kawaida hata kidogo.”

    .

    .

    “Ni lazima kutakuwa na kitu,” Wayde akaunga mkono hoja. “Ngoja tuone ripoti ya polisi itasemaje. Ila …” Wayde akabinua mdomowe. “Sidhani kama kutakuwa na cha maana.”

    .

    .

    “Kusipokuwa na cha maana utafanya nini?” Brian akamtazama Wayde. “Kuna kitu unaweza kufanya kwa ajili ya rafiki yako?”

    .

    .

    “Chochote kile,” akasema Wayde akitikisa kichwa. “Kwanini unaniuliza hivyo Brian?”

    .

    .

    “Nimetaka tu kujua,” Brian akajibu kisha akasimama na kumuaga Wayde. “Ningependa kukaa na wewe lakini unajua ku--”

    .

    .

    “Unamwogopa baba yangu, sio?”

    .

    .

    Brian hakutia neno.

    .

    .

    “Usijali, Brian. Naelewa. Unaweza kwenda, lakini utakapopata kitu kuhusu Silvia, usisite kunijuza.”

    .

    .

    “Ni mwanafunzi mwenzagu. Najali pia,” akasema Brian kabla hajajiweka kwenye baiskeli yake na kwenda zake.

    .

    .

    .

    **

    .

    .

    Saa mbili usiku …

    .

    .

    Baada ya ukimya mdogo wakiwa wanatazama runinga, Brian akamtazama mama yake na kumwita. Akamwambia kwa sauti ya chini, “Mama, Kecie ameanza kuua watu!”

    .

    .

    “Kwanini unasema hivyo, Brian?”

    .

    .

    “Nimekaa nikafikiri sana. Sasa ndiyo nimepata maana ya ujumbe ule ambao tuliukuta bafuni baada ya Mrs Garett kuuawa … unaukumbuka ujumbe ule?”

    .

    .

    “Ndio.”

    .

    .

    “Naona vitakuwa na mahusiano na huku kupotea kwa watu. Kwanini alituambia tutazame mji wetu?”

    .

    .

    Mama akabaki kimya.

    .

    .

    “Lakini kwanini muuaji huyo alituambia hivyo? Kwanini ametupa ujumbe huo baada ya Mrs Garett kuuawa?”

    .

    .

    Hakuna aliyekuwa anajua. Walijawa na hofu. Hawakufahamu kama kupotea huko kwa watu kutakoma ama kutaendelea tena kesho yake. Lilikuwa ni swala la muda tu.

    .

    .

    Basi baada ya muda kidogo, Brian akanyanyuka na kwenda zake chumbani. Alikuwa anataka kulala. Siku mbili za nyuma amekuwa akishughulika sana, haswa kutokana na msiba wa Mrs Garett, hivyo hakupata muda wa kupumzika vema.

    .

    .

    Lakini basi kuvutia usingizi, akanyaka nyaraka ya Dkt Hamill aendelee kuisogeza karatasi kadhaa. Hakuwa ameipitia nyaraka hiyo tangu majuzi. Hakuwa na huo muda.

    .

    .

    Alifungua alipoishia akaendelea kupekua kwa macho tangu pale ambapo mtumwa Jasmine alikuwa ameuawa na baba yake mzazi kisha kutupiwa ndani ya jengo ghofu la Helo.

    .

    .

    “ … nakumbuka siku hiyo, ilikuwa ni usiku nikiwa chumbani mwangu, nikasikia sauti kali ya mama yangu. Haraka nikanyanyuka na kwenda chumbani kwake. Nilidhani ni baba ndiye anampiga mama, lakini nilipofika nikakuta habari tofauti. Mama alikuwa analia kwa woga wa kumwona mfu!

    .

    .

    ‘Kuna nini?’ nikamuuliza. Alikuwa amesimama kwenye kona ya chumba chake na bado sikuwa nimeona wapi baba alipo. Mama alikuwa anamimina machozi na ndita amezikunja haswa.

    .

    .

    Akaninyooshea kidole nyuma yangu, yaani nyuma ya mlango. Nilipotazama nikauona mwili wa baba ukiwa umelala unachuruza damu nyingi mno. Nikaogopa haswa. Nikamuuliza mama nini kimemuua baba, akanijibu, ‘Jasmine!’

    .

    .

    Nikastaajabu. Jasmine atakuwaje amemuua baba ingali amekufa?

    .

    .

    ‘Nimemwona kwa macho yangu!’ akasema mama akiwa ametoa macho ya woga. ‘Nimemwona Jasmine na amesema amerudi kulipa kisasi!’

    .

    .

    Habari hizi zikaniogopesha kweli. Kesho na keshokutwa yake tukafanya utaratibu na baba akazikwa. Ila mambo bado yakaendelea kutokuwa shwari. Baada ya baba kufa, sasa watumwa wakaanza kupotea mmoja mmoja tukiambiwa ameelekea msituni! Ni kama mchezo, mwishowe wote wakapotea asibaki hata mmoja. Kwenye eneo zima, nyumba yote, tukabaki wawili tu mimi na mama yangu.

    .

    .

    Hapo ndipo nilipogundua ya kuwa msitu ule umelaaniwa. Na aliyeulaani msitu ule ni yule ambaye anaishi humo. Helo. Kama vile alivyouawa kwa hatia, na kutupiwa huko, basi wote wale wanaouawa kwa hatia na kutupiwa humo msituni, huamka tena na kwenda kuwaangamiza wale waliosababisha vifo vyao.”

    .

    .

    Brian alipofikia hapo, akafunga nyaraka na kujiuliza maswali juu ya hiko alichokisoma. Ina maana kile kilichotokea kwa Jasmine ndicho ambacho kinatokea kwa Kecie saa hii? Kama ilivyokuwa kwa Jasmine, Kecie aliuawa na kwenda kuzikiwa huko msituni. Kama pia ilivyokuwa kwa Jasmine, naye Kecie akawamaliza wazazi wake waliomuua.

    .

    .

    Alafu kama ilivyokuwa kwa Jasmine, baada ya kumuua mtu aliyemuua, watumwa wenzake wakaanza kupotelea msituni, navyo kwa Kecie baada ya kuua wazazi wake, watu wameanza kupotelea msituni!! Ajabu. Ina maana Kecie alikuwa anajua kitakachofuatia baada ya yeye kummaliza mama yake? Ndio. Na ndiyo maana akaacha ujumbe wa kutazama mji?

    .

    .

    Briana akapatwa na maswali haswa. Ina maana Kecie alikuwa anawatahadharisha? Kwanini afanye hivyo? Ina maana si yeye anayewapoteza hao watu msituni, bali Helo!

    .

    .

    Helo anamtumikisha Kecie kufanya mambo yake ya kupoteza watu. Kecie hataki, na ndiyo maana anataka Brian amwokoe? Brian akajikuta anaketi akichakata mawazo haya. Sasa alipata picha kamili juu ya kinachoendelea. Ila bado hakuwa anajua cha kufanya. Atafanyaje kumwokoa Kecie?

    .

    .

    Mara akasikia hodi mlangoni! Akashtuka haswa akikodoa macho.

    .

    .

    “Nani?” Akauliza. Hakukuwa na majibu, akasita kwenda kufungua. Hodi ikapigwa tena. Akaamua kunyanyuka na kuusogelea mlango. “Nani?” akauliza tena. Hakukuwa na majibu. Brian akaamua kufungua mlango na kutazama nje.

    .

    .

    Hamaki, kule sebuleni akauona mlango ukiwa wazi! Na kama haitoshi, akamwona Olivia akiwa anaishia, anaenda zake!

    .

    .

    “Olivia!” Brian akapaza sauti. Haraka akatoka chumbani na kukimbilia nje.



    Alimuwahi Olivia na kumsimamisha. Binti hakuwa anajitambua. Brian alijaribu kumwamsha toka usingizini pasipo mafanikio. Bado Olivia alikuwa anataka kwenda, anataka kusonga mbele! Macho yake yalikuwa yamepandisha kiini cheusi juu kupotea!

    .

    .

    “Olivia, amka! Oliviaa!” Brian aliita akimtikisa Olivia kwanguvu. Akaita pasipo kuchoka, hatimaye Olivia akarejewa na fahamu! Alikuwa anahema kana kwamba ametoka kukimbizwa. Alitazama kando na kando akaitaajabu kwanini yupo hapo.

    .

    .

    “Olivia, upo sawa?” Brian akauliza. Olivia akatikisa kichwa. Uso wake ulikuwa umejawa na woga. “Nipo wapi hapa Brian?” akauliza.

    .

    .

    “Upo nje! Ulikuwa umetoka, unaondoka!” Brian akamjibu akimtazama mtoto huyo kwa matumaini. Lakini ghafla, Olivia akatazama nyuma ya Brian na kuduwaza macho. Akaachama mdomo na kumuuliza Brian, “Ni nani yule?”

    .

    .

    Brian akageuza shingo kutazama. Ajabu akamwona mwanaume mrefu mweusi aliyekuwa anaongozana na mtoto akija kwa kasi kuwafuata. Moyo wake ukaruka pigo. Haraka akamnyakua Olivia na kuanza kukimbia naye haraka!

    .

    .

    Alitupa miguu kadiri alivyokuwa anaweza. Kila alipotazama nyuma akaona mwanaume yule akimjongea kwa kasi ya ajabu. Alikuwa anakimbia kana kwamba upepo!

    .

    .

    “Wanatufikiaa!” Olivia akapiga kelele. “Brian, wanatufikiaa!” Olivia akalia. Lakini nini afanye Brian? Alikuwa anakazana kadiri ya uwezo wake wa mwisho. Alikimbia haswa. Alikuwa amebakiza hatua chache tu kufikia mlango wa nyumbani, ila ajabu napo, mlango huo ukaanza kujifunga wenyewe taratibu!

    .

    .

    Kwa mahesabu ya wazi, Brian asingeweza kuufikia mlango huo kabla haujajifunga.

    .

    .

    “Tafadhali, usifunge!” Brian akalia. Hakuwa anaweza kuongeza tena kasi kwani hapo alikuwa tayari kwenye kikomo. Alichokifanya, alipoukaribia kidogo mlango, wazi akiona unaelekea kufunga, akaruka hewani kuuparamia.

    .

    .

    Akadondokea chini kama mzigo, Olivia akiangukia upande mwingine. Lakini kabla hajaugulia maumivu, akaukita mlango kwa mguu wake wa kuume, mlango ukafunga! Haraka akanyanyuka na kuutia komeo kisha akasimama hapo akiskiza nini kitaendelea.

    .

    .

    Punde akasikia kishindo cha mtu mlangoni. Mlango ukagongwa mara mbili na sauti ikanong’ona, “Heeeeeyy! … wataka kucheza?” Brian hakusema kitu. Alikuwa amesimama hapo kuugandamizia mlango akiwa amejawa na woga.

    .

    .

    “Najua unataka kucheza, sivyo hivyo Brian?” sauti iliendelea kunong’ona. “Najua unapenda kucheza … njoo basi, twende tukacheze … eti?”

    .

    .

    Brian hakusema kitu, akaendelea kuwa kimya. Naye Olivia alikuwa ametulia akimtazama Brian.

    .

    .

    Wakasikia kishindo kile cha miguu kikisonga kwenda mbali na mlango na kisha kurudi karibu. Kwenda mbali na kisha kurudi karibu. Mara kikakoma. Alafu sauti ile ikauliza, “Brian, hutaki kumwona Silvia?”

    .

    .

    Brian akakodoa kwa mshangao.

    .

    .

    “Yupo wapi?” akaropoka kuuliza.

    .

    .

    “Yupo kule, twende ukamwone!” sauti ikamjibu. “Twende upesi!”

    .

    .

    “Anafanya nini huko?”

    .

    .

    “Anatazama mazingaombwe! Hutaki na wewe kuona?”

    .

    .

    “Sitaki!” Brian akafoka. “Sitaki kukuona maishani mwangu. Sitaki uje kwetu. Kaa mbali na sisi!” Brian alisema machozi yakiwa yanamtoka. Mara kukawa kimya kwa sekunde tano, hakuwa anasikia kitu. Alitega masikio yake vema akiwa anatazama madirishani.

    .

    .

    Mara akasikia sauti ya kike, “Brian, niokoe! Niokoea tafadhali!”

    .

    .

    Brian akagutuka. “Silvia!” akajikuta anaropoka. “Silviaa!”

    .

    .

    “Ndio, Brian!” sauti ya kike ikamjibu. “Naomba uniokoe Brian!” sauti ikalia. “Naomba uniokoe, tafadhali!” ikaendelea kulia na kulia. Brian akatamani kufungua mlango. Alitazama kitasa akitaka kukiminya, Olivia akapaza sauti, “Hapana, Brian!”

    .

    .

    Brian akamtazama Olivia.

    .

    .

    “Usifungue, Brian. Usifungue! Sio Silvia huyo.”

    .

    .

    Mara mlango ukaanza kupondwa kwanguvu! Nguvu ya kuponda ilikuwa kubwa sana. Ukuta ulikuwa unatikisika. Bawaba zilikuwa zinalegea. Olivia akaenda kumsaidia Brian kuminya mlango lakini haikusaidia chochote kwani mlango uliendelea kupondwa kwanguvu sana. Ukaanza kutia ufa kana kwamba gogo lililooza likikitwa na ncha ya shoka kali.

    .

    .

    Mara,

    .

    .

    “Briaaaan!” sauti ya kike ikaita. Brian alipotazama koridoni akamwona mama yake akiwa amesimama, anawatazama kwa mshangao mkuu. Ni ghafla pia mlango ukaacha kupondwa na kukawa kimya kabisa kana kwamba hakuna kilichotokea!

    .

    .

    “Brian, kuna nini?” mama akauliza akijongea. Brian alikosa cha kusema akabaki kimya. Mama alisonga karibu akatazama mlango. Ulichora ufa haswa. Bawaba zilikuwa zimetema nati zake. Ukuta ulikuwa umechimba mistari!

    .

    .

    **

    .

    .

    Mama alifikicha macho yake kisha akamtazama Brian aliyekuwa ameketi kwenye kiti pamoja na Olivia. Akashusha pumzi ndefu na kukuna kichwa chake kilichojawa na nywele.

    .

    .

    “Hili ni tatizo kubwa mno, kila siku linazidi kukua. Kama tusipochukua hatua za mapema, linaweza kutugharimu.”

    .

    .

    Kukawa kimya Mama aliponyamaza. Vinywa vilikuwa vizito. Akili zilipoa. Ni kama vile walikuwa wamenyeshewa mvua.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    “Nadhani inabidi turudi kule kwa mtaalamu demonolojia,” Mama akaendelea kuteta. “Bila shaka yule ndiye mtu pekee aliyebakia wa kutusaidia.”

    .

    .

    “Tutaenda lini?” akauliza Brian.

    .

    .

    “Jua litakapochomoza,” mama akajibu na kuongezea, “Jiandaeni kabisa maana umebaki muda mchache kwenda huko … nadhani tutalala hukohuko.”

    .

    .

    Mama aliposema hayo akaenda zake. Kweli jua lilipochomoza wakajikwea kwenye gari wakiwa wamebebelea mahitaji kadhaa tayari kwa ajili ya safari. Brian aliona ni stara kubeba zile nyaraka tatu za Dkt Hamill, alizitia garini akilenga kuendelea kuzisoma safarini.

    .

    .

    Wakafunga nyumba, safari ikaanza.

    .

    .

    Wakatembea kwa muda wa masaa mawili. Wakaacha mji wote nyuma na kuzama katikati ya misitu. Mwendo ulikuwa wa upesi maana safari ilikuwa ndefu. Basi Brian, ambaye alikuwa ameketi nyuma peke yake, akawa ameegamishia kichwa chake kwenye kiti akitazama miti irudiyo nyuma.

    .

    .

    Alikuwa ametulia haswa. Alikuwa anawaza mambo yake kichwani. Lakini ukimya wake huo haukudumu kwa muda mrefu. Akiwa hana hili wala lile, mara akaanza kusikia sauti nyembamba ikimnong’oneza masikioni … “Brian, unataka kucheza?” akashtuka kidogo na kutumbua macho. Akatazama kila pande akiwa amekunja ndita.

    .

    .

    Sauti ile masikioni ikacheka ikiishilia … “Wataka kuniona?” ikanong’ona. “Wataka kuniona Brian?” mara Brian alipotazama kushoto kwake akamwona mtu aliyevalia nguo nyeupe akikatiza ghafla kana kwamba radi! Akatoa macho kushangaa!

    .

    .

    Akakunja uso wake kuangaza. Alitupa macho kwenye kioo cha nyuma cha gari lakini hakumwona mtu. Alishusha vioo vyote vya nyuma, akatazama pasipo mafanikio.

    .

    .

    Basi punde, upepo mkali ukapuliza. Sijui ulikuwa umetokea wapi. Ulizama ndani ya gari kwakuwa vioo vvya nyuma vilikuwa wazi. Ajabu ukasomba zile nyaraka za Dkt Hamill na kuzimwagia nje!

    ukazipeperusha huku na huko kutawanyika.

    .

    .

    “Mama, simamisha gari! Simamisha garii!” Brian akawaka akimpigapiga mama yake begani. Mama akasimamisha gari upesi, na kumtazama Brian kwa taharuki. “Vipi?” Brian alitoka kwenye gari upesi kukimbilia nyaraka zake. Zilikuwa zinapeperushwa upesi na upepo kuzama msituni!

    .

    .

    Aliikimbiza mojawapo lakini upepo ulizidi kuitokomeza. Mwishowe alisimama akadaka magoti yake akihema kwanguvu. Hakuamini macho yake, nyaraka zilikuwa zimepotea mbele ya macho yake!

    .

    .

    Basi akiwa hapo, sura imemvurugika kwa kuchoka na mawazo, akaona mojawapo ya nyaraka yake ikiwa pembezoni mwa mti mkubwa umbali wa kama hatua kumi toka alipo kwa upande wa mkono wake wa kushoto.

    .

    .

    Akasimama na kutazama vema. Ni kweli alichokuwa anakiona. Nyaraka ilikuwa imetuama hapo. Basi akakata shauri kuifuata. Alipopiga hatua tatu, akastaajabu kuona mkono ukitokea nyuma ya mti, ukaivuta ile nyaraka upesi!

    .

    .

    Akakimbia kutazama, hakukuta kitu! Akabaki akiduwaa. Mara akasikia sauti ya makaratasi nyuma yake yakifunguliwa na upepo! Akageuka kutazama. Uso kwa uso akakutana na kiumbe ambacho hakuwahi kukiona wala kuja kukikumbuka. Asijue kinachoendelea, akadondoka chini na kupoteza fahamu!

    .

    .

    .

    .

    “Briaaaaan!” mama aliita akiangaza huku na kule. Kandokando yake alikuwa pia Olivia naye akirusha macho kumtafuta Brian ndani ya msitu huu mkubwa.

    .

    .

    “Briaaan!” mama aliendelea kuita. Macho yake yalishaanza kuwa mekundu akitaka kulia. Alipotembea kwa muda kidogo, akaona alama za miburuzo kwenye majani! Akajikuta analalama akiziba mdomo, “Mungu wangu, Brian!”

    .

    .

    Alitazama kufuatilia alama hiyo ya miburuzo, kwa mbali akamwona mtu fulani akiishilia akiwa anavuta mwili wa Brian!



    “Ni Brian!” mama akaropoka kwa kuduwaa. Haraka akaanza kukimbia kumfuata Brian. Nyuma yake Olivia alikuwa anamfuata kwa kasi. Ajabu alipokimbia kwa muda fulani, akampoteza yule mtu anayemburuta Brian! Hakuwa anaonekana tena.



    Akaangaza kushoto na kulia, kulia na kushoto, hakuona kitu! “Briaaan!” akaita. “Briaaaan!” machozi yakamshuka haswa akiwa anapoteza matumaini ya kumpata mwanae. Ila ghafla akiwa anaangaza, mara akauona mwili wa Brian kwa mbali ukiwa umelala.



    Akausogelea upesi. Akiwa amebakiza hatua chache, akasimama na kuangaza. Alihisi hayupo mwenyewe. Alihisi kuna mtu anamtazama mahali. Akageuka na kumwita Olivia. Akamdaka mkono binti huyo na kisha akasonga naye mbele taratibu na kwa tahadhari.



    “Brian!” mama akaita akimtazama Brian ambaye bado hakuwa na fahamu. Alipomkaribia, akamtikisatikisa akimwita. Punde Brian akaamka. Akatazama kando na kando, akauliza, “Nipo wapi?”



    “Amka twende!” mama akamwambia akimnyanyua. Wakaanza kutembea kurudi kwenye gari lao. Wakatembea kwa kama dakika kumi na tano kwakuwa walitembea pole.



    Walipofika barabarani, kuangaza, gari halikuwepo! “Mungu wangu! Mungu wangu!” mama akalalama. Akakimbia kwenda huku na huko, gari halikuonekana. Hakufahamu ni kwamba limepotea ama limeibwa!



    “Sasa tutafanyaje pasipo gari?” mama akauliza akishika kichwa chake kwa mawazo. Hakukuwa na mwenye majibu. Kila mtu alikuwa ameduwaa wasijue cha kufanya.



    Baada ya muda wakakata shauri kutembea kwa miguu. Endapo litatokea gari lolote, wataomba msaada. Basi wakatembea kwa muda wa karibia lisaa limoja pasipo kuona gari lolote. Walichoka ila hawakuwa na budi kuendelea na matembezi. Wasingependa usiku kuwakuta humo katikati ya miti.



    Wakatembea kwa robo saa zaidi ndipo wakasikia honi ya gari nyuma yao. Wakashtuka na kuangaza kwa furaha. Waliamini msaada sasa umewadia. Kweli kutazama lilikuwa ni gari, wakalipungia mkono kuliomba msaada. Gari likasimama na upesi wakaliendea.



    Vioo viliposhushwa, wakawaona Padri Alfonso na Dada Magdalena! Mioyo yao ikawashtuka.



    “Habari zenu?” Padri Alfonso akasalimu kwa tabasamu.



    “Njema,” akajibu Mama Brian.



    “Vipi, mbona msituni muda huu?”



    “Aaaahm ni simulizi ndefu kidogo … vipi? Nyie mwaenda wapi?”



    “Tunaenda kwenye huduma ya pamoja ya Massachusetts! Bila shaka mnahitaji msaada.”



    Kabla Mama Brian hajaitikia, akamtazama Brian na Olivia. Wote wakamtikisia kichwa kutoafiki. Mama akarejesha uso wake kwa Padri kisha akatabasamu. “Nashukuru. Nyie mnaweza kutangulia tu.”



    “Kweli?” Dada Magdalena akauliza.



    “Yah! Tangulieni tu hamna shida.”



    Padri Alfonso akamtazama Mama Brian kwa sekunde kadhaa kisha akaatia moto chombo na kuondoka. Mama Brian na wanawe wakabaki kutazama gari hilo likiishilia. Japo walihitaji msaada, waliamua tu liende.



    Wakaendelea kutembea kwa miguu. Ikapita dakika kumi, wakaona gari jingine. Wakalipungia mkono kulisimamisha.



    “Samahani tunaomba mtusogeze!”



    Lilikuwa ni gari lenye nafasi kubwa kwa nyuma, wakajipaki na safari ikaendelea. Wakatembea kwa muda wa kama dakika kumi na mbili wakipulizwa na upepo huko nyuma.



    Ila ghafla, Brian akamshtua mama yake. “Mama, tazama!” alikuwa amenyooshea kidole chake mbele. Kutazama, Mama akaona gari lao likiwa limejiegesha kando.



    Akiwa haamini, akakodoa lakini bado kitu kikiwa ni kilekile. Ni kweli lilikuwa gari linalowahusu. Basi wakawaomba wale waliowasaidia wasimamishe ili washuke.



    “Hapa?” akauliza dereva akiwa anashangazwa kidogo na ombi hilo. Gari lilisimama, wakashuka. Wakalifuata gari lao na kulikagua vema. Ndilo lenyewe! Hakukuwa na mtu ndani. Ni tupu.



    Mama akafungua mlango wakazama ndani, akaliwasha wakaendelea na safari. Ila nani aliyelileta gari hilo hapo? Na aliwezaje wakati funguo hakuwa nayo? Hayo yalikuwa ni maswali ambayo hayakuwa na majibu.



    Wakatembea kwa muda wa lisaa limoja kamili. Walibakiza sehemu ndogo tu kumaliza msitu huu. Wakiwa wanatafuna sehemu hiyo ya mwisho, wakakutana na gari lile lililokuwa limewabebelea Padri Alfonso na Dada Magdalena!



    Gari hilo lilikuwa limesimama kando, limeharibika. Padri Alfonso na Dada Magdalena walikuwa nje wakihangaika nalo. Lakini walipoliona gari la wakina Brian, wakaacha shughuli yao na kulipungia mkono kulisimamisha.



    “Habari?” Mama Brian akasalimu akitazama gari lile lililogoma kwenda.



    “Habari si nzuri, tumeharibikiwa na gari letu,” akasema Padri Alfonso. “Vipi mnaweza kutusogeza tuendako?” Padri akauliza. Mama Brian akawatazama wanawe, wote wakampatia nyuso ngumu kama ishara. “Sidhani kama mtaenea humu. Kuna baadhi ya mizigo.”



    Padri akatazama kulikagua gari kisha akauliza, “Hawezi kuingia hata mmoja wetu basi?”



    Mama Brian akabanwa. Akawatazama wanae kabla hajajibu kitu. Alikosa namna ya kumkatalia padri basi akasema, “kwa mmoja … aahm … tunaweza kwenda naye!”



    Padri akatabasamu. Akamtazama Dada Magdalena na kumwambia aingie ndani ya gari, yeye atangoja lingine lijalo. Basi Dada Magdalena akazama ndani na safari ikang’oa nanga. Wakatembea kwenda kumalizia msitu ule waende zao kwa mtaalamu.



    Safari ikaenda na kuenda. Ndani ya gari kulikuwa ni kimya. Hakukuwa na soga yoyote ile. Wakakata lisaa limoja. Wakakata lisaa la pili. Bado wapo ndani ya msitu usio na kikomo.



    Lakini mama Brian alitwaliwa na shaka. Makadirio yake ya muda yalikuwa kinyume kabisa na alichokuwa anakiona. Kwa ufahamu wake safari iliyobakia haikuwa ya kuchukua masaa mawili kuimaliza. Alistaajabu! Kila alipokanyaga mafuta, ni miti tu ndiyo ilikuwa mbele na nyuma yake. Miti pasipo kikomo!

    http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akasimamisha gari.



    “Nahisi nimepotea!” akasema.



    “Kwani unaelekea wapi?” akauliza Dada Magdalena akitabasamu kwa ukarimu.



    “Naenda mbele. Nashangaa msitu haukomi!”



    Dada Magdalena akatabasamu. “Pengine ni macho yako tu. Mbona tunasogea?”



    “Najua barabara hii! Hii si mara yangu ya kwanza kupita. Haikuwahi kuwa ndefu kiasi hiki!”



    “Vipi tukatumia sjia fupi basi?” akauliza Dada Magdalena.



    “Njia ipi?”



    “Kuna njia ya vumbi naijua. Mngependa tupite?”



    “Hapana!” Brian akawahi kujibu. “Tutatumia njia hiihii!”



    “Mafuta yanaelekea kuisha,” mama akasema. “Endapo tukiendelea kuzunguka humu, basi muda si mrefu gari litazimika lisiamke tena!”



    Kukawa kimya kidogo. Ni kama vile watu walikuwa wanategeana kuongea. Brian akauvunja ukimya. “Dada Magdalena,” Brian akaita akimtazama Dada huyo usoni. “Tumekukosea nini?” akamuuliza.



    Dada Magdalena akakunja uso kwa mshangao.



    “Usin’tazame hivyo. Unajua ninachokiongea. Tunajua kuwa wewe si mwenzetu. Wewe ni jini. Jini miongoni mwetu binadamu! … mnaweza mkatupa kipindi cha amani kidogo tafadhali?”



    Dada Magdalena akamtazama Mama Brian. “Anasema nini huyu?” akauliza.



    “Anasema wewe ni jini!” Olivia akadakia. Uso wake ulikuwa umefumwa kwa hasira zaidi kuliko woga. “Wewe na Padri Alfonso ni majini. Tumewakosea nini? Tuacheni!” Olivia akamalizia kwa sauti ya chini iliyokaribu na kulia.



    Dada Magdalena akaziba mdomo wake kwa mshangao. Akafanya ishara ya msalaba na kukutanisha viganja vyake kana kwamba anataka kusali. Macho yake yalikuwa yanaelekea kuwa mekundu kwa kutaka kulia.



    “Sijui nini mnaongelea. Kwanini mnanisemea hivyo? Kuna lolote baya nimewatendea?”



    “Dada Magdalena,” Mama Brian akashika hatamu ya kunena. Aligeuza shingo yake vema kumtazama anayemwongelesha. “Tafadhali. Sipendi kwenda mbali kwa maneno ambayo aidha nami naweza kuja kuyajutia hapo mbeleni … naomba ushuke twendelee na safari yetu.”



    “Lakini mtaniachaje msituni?” akauliza Dada Magdalea kwa uso wa huruma.



    “Nimekuomba,” Mama Brian akamsisitizia. “Nimekuomba ushuke toka kwenye gari yangu!”



    Dada Magdalena akamtazama Mama Brian kwa sekunde kadhaa pasipo kusema jambo. Mara akaanza kubadilika. Mwili wake ukawa mweupe ukichomozwa na michirizi meusi kana kwamba mizizi ya miti. Macho yake yakabadilika na kuwa ya paka. Mdomo wake ukawa mweusi, kucha kama chui, meno kama simba!



    Ghafla akamnyaka Brian aliyekuwa amekaa naye nyuma, akamnyonga kwanguvu akipanua kinywa chake kipana! Brian akahangaika kujitetea. Upesi Mama akamkita Dada Magdalena kichwani kwa kutumia ‘fire extinguisher’, Dada Magdalena akapata maruweruwe.



    Hajakaa vema, Brian akamkita teke zito. Mama alishafungua mlango. Dada Magdalena akajikuta chini, gari likatimka kwa kasi!



    Wakati Dada Magdalena anajikusanya chini, mara miguu ya mwanaume ikamjongea na kukoma mbele yake. Alikuwa ni Padri Alfonso. Alitazama mbele gari la wakina Brian likitokomea.



    .

    Basi baada ya safari hii kudumu kwa muda fulani, Mama Brian akaweka gari kando mahali wapate kula na hata kutia mafuta garini. Walichukua kama dakika kumi na tano hapo. Wakajipakia tena kwenye gari na kuendelea na safari yao.

    .

    .

    Wakadumu tena barabarani kwa muda wa kama lisaa, ndipo wakafika eneo walilokuwa wanaliendea, mji wa Northampton. Hapo wakatembea kwa dakika chache tu kabla hawajafika mbele ya nyumba fulani iliyo pweke. Mama Brian akazima gari na kusema. “Tumefika!”

    .

    .

    “Ndiyo hapa?” Brian akauliza akiwa anaangaza macho yake. Punde wakamwona mwanaume aliyevalia suti nyeusi na kofia yake. Mdomoni alikuwa ameshikilia kiko chake kwa meno akijaribu kufunga mlango wake. Kuna mahali alikuwa anataka kwenda, hata mkononi mwake alikuwa amebebelea mkebe.

    .

    .

    Mama Brian akashuka upesi na kuita, “Wisconsin!” mwanaume

    yule akaacha shughuli yake na kumtazama. Ilikuwa ajabu kuwa hakumwona ilhali gari hilo lilikuwa limejiegesha karibu na makazi yake. Ila baada ya Mama Brian kujongea ndipo tukajifunza kuwa jicho lake moja la upande wa kushoto lilikuwa bovu. Yeye hutumia jicho moja tu, ambalo ameliveka miwani ya kioo kimoja.

    .

    .

    “Hello mama!” Wisconsin akasalimu akivua kofia yake, kisha akaendelea na zoezi lake la kufunga mlango. “Samahani!” Mama Brian akasema akijitahidi kusonga karibu. Akadaka ngazi kupanda kwa upesi.

    .

    .

    “Sisi ni wageni wako. Naomba utuskize!”

    .

    .

    Wisconsin alipomaliza kufunga mlango wake. Akatazama jua na kisha akamtazama Mama Brian. “Samahani. Sina ratiba ya kufanya lolote leo hii, muda huu!”

    .

    .

    “Hunikumbuki?” Mama Brian akauliza akiwa ametoa macho. Wisconsin, mwanaume mtanashati mwenye makamo ya umri wa miaka arubaini, akamtazama na kisha akabinua mdomo. “Hapana.”

    .

    .

    “Oooh! Ndio. Tulipokuja mara ya kwanza hatukukuta … samahani, nina shida sana.”

    .

    .

    Wisconsin akatabasamu. Akaweka mkebe wake kwenye kwapa alafu akasema kistaarabu. “Mama, mimi hufanya kazi kwa ratiba. Nina ratiba nyingine hivi sasa. Samahani sitaweza kukuhudumia.”

    .

    .

    “Tumetoka mbali sana kuja kukuona.”

    .

    .

    “Italia?”

    .

    .

    “Boston!”

    .

    .

    “Si mbali. Kama hutojali, naweza kwenda?”

    .

    .

    “Tafadhali. Na --”

    .

    .

    “Nazidi kukawia. Naomba niende.”

    .

    .

    “Niambie basi muda wako. Lini unafanya kazi?”

    .

    .

    “Keshokutwa kuanzia jua linapokuwa katikati mpaka kuzama.” Wisconsin aliposema hayo, akaenda zake. Mama Brian akabaki amesimama, anamtazama mwanaume huyo akiishilia.

    .

    .

    “Amesemaje?” Brian akamuuliza. Yeye na Olivia walitoka ndani ya gari baada ya kumwona Wisconsin akiishilia. Mama alidaka kiuno chake akatikisa kichwa.

    .

    .

    “Itabidi tulale huku hivi leo.”

    .

    .

    Wakarejea kwenye gari na kutafuta ‘motel’ safi walipopata vyumba vizuri vya kulalia lakini pia huduma zinginezo zikiwa si haba. Huduma kama vile chakula na vinywaji. Moteli hii ilikuwa wazi masaa ishirini na nne kutokana na kwamba watu husafiri muda wote.

    .

    .

    Basi baada ya kuona vyumba vyao, wakaendea mgahawa na kutulia hapo watete mawili matatu. Mezani kulikuwa na vinywaji laini, hususani sharubati.

    .

    .

    Lakini wakiwa hapo wanateta juu ya mji ule wa Northampton, macho yao yakadakwa na taarifa runingani. Ilikuwa ni taarifa ya habari kutokea Boston.

    .

    .

    “ … watoto nane wanaripotiwa kupotea leo katika mji wa Boston ukiwa mwendelezo wa matukio ya watoto kupotea kwa wingi kwa siku za karibuni. Sasa ndani ya siku tatu, takribani watoto kumi na tano wamekwishapotea huku karibia wote wakiripotiwa kuyoyomea ama kuonekana mara ya mwisho msituni!

    .

    .

    Kamanda wa polisi wa mji wa Boston anathibitisha taarifa hiyo na kueleza kuwa wanaendelea kulifanyia kazi kiupelelezi zaidi. Hofu inazidi kuwatanda wazazi na vilio vinatawala majumbani.

    .

    .

    John Bleach, KK tv!”

    .

    .

    Mama Brian akatikisa kichwa, akasema kwa kuchoka, “wameendelea kupotea na leo.”

    .

    .

    “Inabidi tufanye jambo haraka,” Brian akanguruma. Uso wake ulionyesha kuguswa na habari. Kwa muda kila mtu hakugusa bilauri yake ya sharubati. “La sivyo, watoto wote watatokomea. Mji mzima!”

    .

    .

    Mama Brian akarusha macho yake nje ya vioo vya dirisha. Alikuwa anatafakuri. Japo macho yake yalikuwa yanatazama magari yakatizayo, akili yake ilikuwa inahaha ikimnyima amani.

    .

    .

    Akasema, “Tunamhitaji sana Wisconsin.” sauti yake ilikuwa nzito kwasababu ya kubana koo lake kwa viganja vyake vyembamba ili ajipatie joto. Mhudumu akamtazama.

    .

    .

    Alikuwa ni mwanamke mnene ndani ya sare. Mashavu yake makubwa yalikuwa mekundu yenye vidotidoti vingi rangi ya zambarau. Kidevu chake kilikuwa kimemezwa na shingo. Mdomo mdogo kana kwamba ndege.

    .

    .

    “Umekuja kwa ajili ya Wisconsin?” mhudumu huyo akauliza. Mama Brian na wanawe wakamtazama.

    .

    .

    “Mmekuja kwa ajili ya Wisconsin?” Mhudumu akarejea kuuliza. Mkononi alikuwa amebebelea kikombe cha udongo akikifuta kukikausha na maji.

    .

    .

    “Ndio. Tumekuja kwa ajili yake,” Mama Brian akasema kwa kujiamini. Mhudumu yule akawatazama alafu akaendelea na kazi zake. Aliondoka pale ‘kaunta’ akaelekea ndani, jikoni. Akawaachia wageni maswali.

    .

    .

    “Atakuwa na nini?” mama akauliza kiretorikali.

    .

    .

    “Pengine anachakutuambia,” Brian akabashiri akiwa anatazama kule kaunta kama atamwona yule mhudumu. Kwa muda hakutokea. Alipotokea alikuwa ameshabadili sare zake, sasa amevalia nguo kama raia wa kawaida. Gauni jeusi pana.

    .

    .

    “Tunaweza kuongea na wewe?” Mama Brian akamwomba. Mhudumu huyo akasimama akiwa anawatazama kwa mashaka. Akatikisa kichwa chake, mashavu yakacheza, kisha akaendelea zake na safari kuufuata mlango wa kutokea.

    .

    .

    Mama Brian akanyanyuka kumfuata. Wakina Brian wakabaki wakimtazama mama yao akizungumza na yule mhudumu. Punde akarejea naye mezani.

    .

    .

    “Hawa ni wanangu, huyu anaitwa Brian na huyu Olivia,” Mama akatambulisha kwa tabasamu. Mhudumu akaketi na kusema, “Mimi naitwa Keline.” alikuwa anaonyesha woga usoni mwake.

    .

    .

    “Keline, kuna kitu chochote unataka kutuambia?” Mama akauliza akimtazama Keline kwa uso wa kudadisi. “… kumhusu Wisconsin. Chochote kile unachoweza kutuambia?”

    .

    .

    Keline akatazama kwanza nje. Akarudisha macho yake madogo mezani na kisha akatazama chini. “Si mtu mwema,” akasema kwa sauti yake ndogo.

    .

    .

    “Kwanini unasema hivyo?” Brian akauliza. “Kuna tabu yoyote?”

    .

    .

    “Ndio … Wisconsin aliua wazazi wangu. Amenisababishia jeraha kubwa. Sitaweza kumsamehe kamwe!” macho yake yakaanza kujawa na machozi. Akavuta makamasi mepesi na kuendelea kunena, “Anasema kuwa anawasaidia watu dhidi ya nguvu za giza. Lakini yeye mwenyewe ni nguvu hizo, tena zaidi kwa maana amejiveka koti la kondoo.

    .http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    .

    Analaghai watu, na kila anayedai kumsaidia, hufa baada ya majuma matatu!”

    .

    .

    Keline aliposema hayo akanyanyua uso wake na kumtazama Mama Brian. “Baba yangu alikufa majuma matatu baada ya kuonana naye. Naye mama ‘angu alipokwenda kumwomba msaada, naye akafa baada ya majuma matatu. Nisingependa mkapitia kwenye adha hiyo.”

    .

    .

    Sasa Keline alikuwa anatiririsha machozi zaidi. Alitoa leso yake na kujipangusa. Akasimama na kuaga. Mama Brian na wanawe wakabaki wakimtazama mwanamke huyo akiishilia, anajifuta machozi na amebanwa na kwikwi za kilio.

    .

    .

    Alipopotelea, Mama Brian akauliza, “Sasa tunafanyaje?” alionyesha kuchanganyikiwa.

    .

    .

    “Tunaenda kumwona Wisconsin kesho kama tulivyokubaliana naye,” akasema Brian.

    .

    .

    “Lakini umesikia habari zake?” Mama akauliza. Brian akatazama kwanza nyuma yake na kule mlangoni kisha akamwambia mama yake kuwa ana mashaka na Keline.

    .

    .

    “Kwanini?” mama akauliza.

    .

    .

    Brian akamtonya kuwa wakati Keline anaongea alifanikiwa kumtazama mkono wake wa kulia, akamwona akiwa na pete ambayo alimwona nayo Padri Alfonso wakati alipokuja kufanya sala nyumbani kwao. Hilo likamshangaza mama yake.

    .

    .

    “Una uhakika?”

    .

    .

    “Ndio, nina uhakika. Nimeona kwa macho yangu mwenyewe!”

    .

    .

    Swala hilo likazua hofu miongoni mwao. Na pengine kwa kiasi fulani halikumkonga sana Mama kwenye kuliamini. Pete zi nyingi. Vipi kama ya Kelie haikuwa na mahusiano na Padri Alfonso? Aliwaza akiwa kitandani kwenye chumba cha peke yake.

    .

    .Ila kule dirishani, kivuli cha mtu kikakatiza. Mtu mwenye mwili mpana.

    .



    Mama Brian hakuwa na hili wala lile. Alikuwa anaendelea kuwaza mambo yake hayo kichwani. Lakini mtu yule aliyekuwa anakatiza dirishani, akasimama na akageuza uso wake kutazama dirishani.

    .

    .

    Akajongea karibu na karibu. Sasa akawa karibu kabisa na dirisha kiasi kwamba mtu aliyekuwepo ndani akahisi kufifia kwa mwanga! Mama Brian akageuza shingo yake kutazama. Hakuna kitu! Akapata shaka kidogo ila mwishowe akapuuzia na kulaza kichwa chake kitandani.

    .

    .

    Basi taratibu usingizi ukaanza kumnyemelea. Macho yakawa yanafumba pasipo ruhusa. Akaona si stara kulala pasipo kuoga. Akanyanyuka afanye jitihada za kuoga upesi kisha arejee kitandani. Punde akawa bafuni akikoga akiimba na kuburudika na maji ya moto yaliyompa faraja dhidi ya hali ya baridi.

    .

    .

    Akiwa anaoga huko, akahisi kuna mtu ndani. Akajawa na shaka. Alitulia askize vema, akahisi kishindo cha mtu kikikatiza chumbani. Na mara akahisi mtu huyo akinong’ona huko. Basi haraka akatoka bafuni na kwenda kutazama. Hakuona mtu.

    .

    .

    Alitazama huku na huko pasipo mafanikio. Mwishowe akarejea bafuni aendelee kuoga. Akamaliza salama na kutoka akijifuta maji. Akiwa anaendea kitanda chake, akagundua kuwa kuna nyayo za miguu kwenye sakafu.

    .

    .

    Nyayo hizo zilikuwa zimetwaliwa na mabaki ya maji. Na alipozifuatilia, akagundua zimetokea kwa nje! Haraka akatazama mlango kama umefungwa. Akaukuta ukiwa salama, umetiwa ‘lock’. Sasa mbona nyayo za mtu ndani?

    .

    .

    Akarejea kuketi kitandani akiwa amejawa na hofu. Akawa amepata mawazo maradufu. Akiwa bado yupo hapo, kama baada tu ya dakika tatu, taa zikaanza kufinyafinya. Mara umeme nao ukakatika! Akaduwaa.

    .

    .

    Sauti yake ya kuhema ikawa inasikika vema sasa. Kulikuwa ni kimya, kimya ya tuli. Hata mende angepita ukutani, basi ungemsikia.

    .

    .

    Mama Brian akatulia tuli kana kwamba maji mtungini. Alitumai umeme utarejea muda si mrefu. Na kama usiporejea basi atakuwa kwenye hali mbaya maana alikuwa anahofia juu ya yule mtu aliyeacha chapa za nyayo chumbani.

    .

    .

    Kila alipomuwaza mtu huyo akahisi baridi kali. Moyo wamwenda mbio. Kichwa nacho chamgonga ‘alarm’ titi! titi! titi!

    .

    .

    Ikapita kama dakika moja. Bado kulikuwa kimya. Ila mara Mama Brian akaanza kuhisi kuna mtu chumbani, hayuko mwenyewe! Alihisi kabisa uwepo wa mtu mule ndani. Vinyweleo vilimsimama na baridi likamzidi mwilini.

    .

    .

    Kama haitoshi, punde akaanza kusikia mtu akikanyaga sakafu taratibu. Alipiga hatua zake kila baada ya sekunde mbili kisha kukoma. Sekunde mbili kisha kukoma. Mama Brian akapata wazo la kuliendea dirisha afungue mwanga uingie ndani.

    .

    .

    Haraka akasonga. Kwakuwa dirisha alikuwa anajua lilipo, hakuhitaji mwanga kulitambua. Akanyoosha mkono wake na kupapasa. Akapapasa na kupapasa. Akapapasa chini … akapapasa juu … hakuhisi dirisha!

    .

    .

    Akaona atumie mikono miwili kupapasia, hakuwa anaaamini anachohisi kwani ilikuwa kinyume na matarajio yake, lakini napo akapapasa pasipo kushika kitu isipokuwa ukuta pekee!

    .

    .

    Sasa akawa anahema kwanguvu sana. Pumzi ya hofu. Alipata mashaka juu ya uhai wake akajikuta anatamani kupiga kelele kali sana za kuomba msaada.

    .

    .

    Akajikunyata. Kichwa chake kiligoma kabisa kuwaza cha kufanya. Yaani hakuwa anajua kabisa afanye nini kwa muda huo. Ulikuwa ni wakati mgumu sana kwake.

    .

    .

    Basi akiwa ametulia, amejikunyata akitazamia nini kitatokea, akaanza kuhisi mtu anapanda kitandani. Godoro lilibonyea na kitanda kikatoa mlio. Hapa ndiyo Mama Brian akaona ni muda stahiki wa kupiga kelele. Hakuwa amepanga hata hivyo, alijikuta akipanua kinywa apige yowe kali.

    .

    .

    Kwanguvu zote akafanya hivyo, ila ajabu sauti haikutoka hata punje! Kilichosikika ni ile sauti ya pumzi tu mtu apumuapo. Mama Brian akajaribu tena na tena kupiga kelele. Kazi bure. Sauti haikuwa inatoka. Ilikuwa imekaua kabisa kooni!

    .

    .

    Hapa akakutana uso kwa uso na kifo kwenye kona. Hakuwa na pakukimbilia wala cha kujitetea nacho. Punde kidogo akavamiwa na mtu asiyemjua, akaanza kumkaba akimminyia kwenye godoro!

    .

    .

    Akapapatika kudai roho yake. Akagahangaika haswa akipambana kwa nguvu zake zote, hakufua dafu! Akiwa anatetea uhai wake, akajikuta akipiga teke chupa iliyokuwa imesimama kwenye droo ya kitanda. Ilikuwa ni chupa ya kioo yenye sharubati ndani yake kwa nusu ujazo. Ikadondoka na kusababisha kelele kali!

    .

    .

    Kwakuwa mazingira yalikuwa tulivu, sauti hiyo ya chupa ilisikika moteli nzima.

    .

    .

    “Ni muda wako wa kufa!” mnyongaji akasema kwa kunong’ona. Mikono yake ya baridi ilikuwa imeminya shingo ya Mama Brian kwanguvu kiasi cha kumfanya mwanamke huyo atoe macho na ulimi nje. “Huwezi kushindana … sawa? … huwezi kushindana …” akaendelea kunong’ona akiwa na uhakika na kazi yake.

    .

    .

    Ila ghafla, mlango ukagongwa. Muda tu kidogo ukavunjwa kwanguvu, Brian akaingia na kuangaza mule kizani ambapo sasa mwanga angalau ulipenya kutokana na mlango kuwa wazi.

    .

    .

    “Mama!” Brian akaita akiwa na uso uliopaliwa na woga. Akamsikia mama yake akikohoa kitandani, akamsongea upesi na kumtazama amjulie hali. Umeme ukarejea. Mama alikuwa amedaka shingo yake akikohoa na kuhangaika kupata hewa.

    .

    .

    “Nini kimetokea?” Brian akauliza. Kabla hajajibiwa akaongezea lingine, “Uko sawa?”

    .

    .

    Maswali yote hayo mama hakuweza kumjibu kutokana na hali aliyomo. Alikuwa ametoka kukabwa ikibaki sekunde kadhaa tu akate pumzi. Shingo yake haikuwa sawa, haswa koo. Na pia hata kichwa kilikuwa kinamgonga sana kutoka na kubanwa kwa mishipa ya fahamu kwanguvu, kwa muda mrefu.

    .

    .

    Basi mama akachukua kama dakika sita kukaa angalau sawa. Kabla hajanena kitu, akakagua chumba kwa macho yake yalikuwa yamegeuka kuwa mekundu, akatazama kila kona, kila eneo. Punde wakafika walinzi wa motel, mmoja alikuwa amebebelea bunduki aina ya gobore mwenzake akiwa amebebelea fimbo iliyosanifiwa vema kiulinzi.

    .

    .

    “Kuna shida yoyote?” mmoja akauliza wakiwa wanatazama kwa macho juujuu. Brian akafoka, “nyie mnaona vitu vipo sawa? Walinzi wa aina gani ninyi mteja anakumbwa na kadhia kwa muda wote huo pasipo msaada?” sauti ya Brian ilikuwa kubwa na ilisikika moteli nzima.

    .

    .

    Walinzi wakaomba radhi. Hawakukaa sana hapo wakaenda zao. Mama Brian akatoka kwenye chumba chake na kwenda kulala pamoja na watoto chumba kimoja.

    .

    .

    “Nina uhakika kabisa atakuwa ni yule mhudumu,” alisema Brian. “Padri Alfonso bado anatufuatilia hata sasa.”

    .

    .

    Mama alikuwa ameketi ametulia. Hakuwa na nguvu ya kuzozana wala kuteta. Hata hamu hakuwa nayo. Alikuwa amezubaa kana kwamba kuku mgonjwa. Kwake ilikuwa ni miujiza muda huo kuwa hai.

    .

    .

    **

    .

    .





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog