Simulizi : Mama Usinifundishe Uchawi
Sehemu Ya Nne (4)
Binti Mngane alipohakikisha mwanae amemaliza kufagia banda la kuku alikwenda ndani kukaa kwenye mkeka ukumbini. Sharifu alipomwaga taka akajongea hadi chumbani na alipofika kitandani akajitupa kifudifudi masaa mawili mbele. Sharifu akakamatwa na usingizi mzito, akiwa amesinzia akaingia Mzee Damanda chumbani kwake kimiujiza na kuanza kuzungumza naye kupitia ndoto.
“Kibaraka wangu,” Mzee Damanda akaita.
“Naam” aliitika Sharifu ndotoni.
“Nimekuja, kuna jambo limenileta.”
“Jambo gani?.”
“Umepita mwezi sijawaona kilingeni kulikoni?.”
“Kulikuwa kuna mambo kidogo tunaweka sawa.”
“Unakumbuka katiba yetu?.”
“Nakumbuka.”
“Zipi?.”
“Usimjaribu mwanachama mwenzio. Usitangaze siri za chama na kuhudhuria kilingeni kila siku.”
“Safi...mbona nyinyi mnakiuka katiba?.”
“Tunapitiwa kiongozi wetu...lakini kuanzia leo nakuahidi hatutokosa kilingeni.”
“Sawa...naondoka ila mkae mkijua nisipowaona siku zijazo nitajua cha kufanya.”
“Nimekuelewa kiongozi, kuanzia leo tutakuwa kilingeni pamoja wala hatutokuangusha tena.”
Mzee Damanda alipoondoka, Sharifu akakurupuka ndotoni. Akanyanyuka kitandani akaelekea moja kwa moja alipo mama yake. Akamkuta mama yake ukumbini ameketi kwenye mkeka na hawamu hii akiwa anamenya ndizi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mama,” Sharifu akaita.
“Eeehe niambie...naona umeshaamka,” Binti Mngane aliongea huku macho yake yakitazama chini akichukua ndizi nyingine.
“Nimeamka...lakini nimeamka na habari mbaya” aliongea Sharifu kisha akasimama mbele ya mama yake sawa sawia.
“Kutoka, wapi?” aliuliza Binti Mngane kwa kutahamaki.
“Kwa, Mzee Damanda.”
“Anashida gani tena?.”
“Kaja kutupa onyo kwa sababu hatuhudhurii kwenye kilinge.”
“Mh! ni kweli...sasa wewe ulimwambiaje?.”
“Sikumwambia chochote, zaidi ya kukiri kosa na kuomba msamaha.”
“Nakuasa mwanangu tujirekebishe bila hivyo mwaka huu tutaumbuka.”
Sharifu baada ya kuzungumza na mama yake akamuaga mama yake kuwa anakwenda nyumbani kwa kina Kondo kupiga stori kidogo. Mama yake akamruhusu aende lakini wakati anaanza safari njiani akakutana na bibi kikongwe asiyeweza kutembea kutokana na kuvimba miguu.
“Mjukuu wangu” aliita Kikongwe yule mara baada ya kumuona na kupishana naye Sharifu.
“Naam” aliitika Sharifu kwa busara.
“Naomba msaada.”
“Msaada upi?.”
“Wa kunipeleka nyumbani.”
“Sitoweza bibi kuna mahali nawahi.”
“Naomba unipeleke nitakupa zawadi tukifika nyumbani kwangu,” Kikongwe yule alimrubuni Sharifu kwa zawadi.
“Zawadi ipi?.”
“Wewe nipeleke zawadi hiyo utaiona tukifika,” Sharifu akakubali kumpeleka Kikongwe yule kwake kwa kumbeba mgongoni kwa sababu ya kutoweza kutembea vizuri.
Wakiwa wapo njiani Sharifu akahisi maumivu makali mgongoni. Akapeleka nyuma mkono wake wa kuume kulipo na maumivu ili apate kuthibitisha kama kweli ana jeraha au laa. Ghafla yule bibi akabadilika kuwa Chui mwenye miguu minne na kumrarua Sharifu mkono alioupeleka nyuma kupapasa. Sharifu akamtupa pembeni kikongwe yule kwa hasira. Baada ya kutupwa kikongwe yule akawa anacheka kwa sauti ya juu huku sauti yake ikisikika kufika masafa ya mbali.
“Msaada ninaotaka kukupa unaona haufai?. Unaamua kunidhuru?,” Sharifu aliongea kwa ghadhabu.
“Lengo langu si msaada kutoka kwako lengo langu ni kukuua,” Kikongwe yule alisema kwa ujasiri uliotukuka. Sharifu akacheka kisha akasema naye kwa ujasiri bila hofu.
“Unajiamini sana...ngoja nami uone nipoje.”
Sharifu muda huo huo naye akabadilika kuwa Simba mwenye pembe ndefu na meno makali mithili ya sindano. Alipojibadilisha vile tu moja kwa moja akamvamia kikongwe yule aliyejibadili Chui na kupeana mikong'oto ya haja. Mikong'oto ikatembezwa yapata masaa mawili kisha kila mmoja akawa pumzi kisoda. Sharifu hakukubali kushindwa japo alichoka lakini akamkabili vyema kikongwe yule na hatimaye kikongwe yule akashindwa akatafuta upenyo akakimbia. Sharifu akacheka sana na akaongea kwa dharau.
“Ulijua nipo kijingajinga, nina nguvu balaa. Nenda kajipange na nguvu zako za mtoto mchanga.”
Sharifu akahairisha hadi safari yenyewe kutokana na kuchafuka mara baada ya kurudi kwenye hali ya ubinadamu akarudi nyumbani. Akafika nyumbani akakuta kumetulia na hadi mama yake hakuwepo. Hakuwa na shaka sana, hivyo akaingia chumbani huku moyoni akijiuliza baadhi ya maswali.
“Kikongwe yule katokea kijiji gani?...na lengo la kuniua ni nini?.”
“Mama anaweza kumjua kweli?...looh! simjui hata jina kikongwe yule.”
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nitamweleza mama kwa maumbile, kama atamjua anitajie jina lake nimjue.”
Sharifu akiwa yupo kitandani bado akiwa anajisemesha mara usingizi ukamjia na akawa anakoroma bila kujijua. Masaa kadhaa mbele alikuja kushtuka mara baada ya kusikia mlango wake wa chumbani ukigongwa. Akakurupuka kutoka kitandani na kwenda kumfungulia anayegonga.
“Mama ulikuwa wapi?,” Sharifu aliuliza mara baada ya kuona kuwa aliyekuwa anagonga ni mama yake.
“Nilikuwa mtaa wa pili nikiazima pipa la kupikia pombe...si unajua kesho pombe kwangu?,” Binti Mngane akajibu na kuuliza.
“Umelipata pipa lenyewe?.”
“Nimelipata...ila ni chafu kanisaidie kuliosha.”
“Kuna kazi kwa sasa unataka kufanya?.”
“Nataka nifue nguo mara moja maana zimekuwa chafu sana.”
“Sawa...mimi ngoja nikasafishe pipa hilo,” Sharifu baada ya kupeana majukumu na mama yake, kila mmoja akaingia katika kazi yake.
Baada ya saa moja wote wakawa wamemaliza kazi wakaenda kuketi ukumbini kwa pamoja wapige soga. Sharifu akaanzisha mazungumzo mara baada ya ukimya wa mama yake wa muda mrefu.
“Mama, hivi hapa kijijini kwetu kuna bibi vikongwe wangapi?.”
“Wawili,” Binti Mngane alijibu huku akitabasamu.
“Nani na nani?.”
“Bi Kazimoto na Bi Tuni...kuna nini kwani?.”
“Leo njiani, nimekutana na bibi kikongwe akanidhuru.”
“Yupoje, kikongwe huyo?.”
“Miguu yake, imevimba na mfupi.”
“Oooh!, huyo atakuwa Bi Kazimoto.”
“Unamjua?.”
“Eeenh!.”
“Anaishi wapi?.”
“Ni jirani yetu, anaishi nyumba tatu za mbele zinazofuata...alitaka kukudhuru kisa nini?.”
“Sijajua...sio kunidhuru tu, alitaka aniue kabisa.”
“Toba!!!, majirani wananitafuta nini?...ujaumia sana?.”
“Sijaumia sana ameniweka kajeraha kidogo tu...lakini nina hasira naye.”
“Unatakaje?.”
“Kama unapajua kwake, baadaye unipeleke nikamalize hasira zangu.”
“Usijali, baadaye tukitoka kilingeni nitakupeleka,” Binti Mngane alipiga soga na mwanae hadi nyakati za kupika chakula zikafika.
Akanyanyuka kwenye mkeka pale ukumbini na kuelekea jikoni kupika chakula cha usiku. Sharifu hakutaka kuendelea tena kukaa pale ukumbini. Akaamua kuchukua mkeka na kwenda kujilaza nje kwaajili ya kupunga upepo wa jioni.
**********
Nyumbani kwa Bi Kazimoto furaha haikuwepo. Alikuwa anawaza na kuwazua kwa jinsi alivyokosa ushindi.
“Mtoto yule anatumia uchawi wa aina gani?...atakuwa anatumia uchawi wa kale nini?.”
“Yaani kitoto kile kinishinde mimi............?. Sikubali nitajipanga tena.”
Bi Kazimoto kwa siku ile ilikuwa ya huzuni kwake na mbaya zaidi kila akifikiria tukio lile. Akahisi homa, yaani hakutamani hata chakula cha aina yoyote kipite kinywani mwake. Yaani siku ile chakula hakikuwa kitamu upande wake hivyo akalala bila kula kitu chochote siku hiyo.
**********
Binti Mngane alipoivisha chakula na kula yeye na mwanae wakaingia kila mmoja kwenye chumba chake kwa ajili ya kwenda kujipumzisha mwili. Binti Mngane akiwa usingizini akazama moja kwa moja kwenye ndoto, ndoto ikampeleka ajione yupo na mumewe wanazungumza.
“Mwanamke mbaya sana, yaani umeniua kwa kunitoa kafara kwasababu ya kunufaisha uchawi wako,” Baba Sharifu alinung'unika kwa kumnung'unikia mkewe kwa kumwaisha kaburini.
“Si kusudi langu, ni kusudi la mizimu kunilazimisha kutoa kafara kinguvu,” Binti Mngane alijitetea ili asionekane mbaya na mumewe.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mbona hujamweleza mtoto uchafu uliofanya...halafu unajitetea leo. Lazima nikuue,” Baba Sharifu aliongea na kutaka kupeleka mikono yake kwenye shingo ya mkewe amkabe.
“Tobaaa!!!, roho yangu,” Binti Mngane alishtuka kwa kukurupuka ndotoni huku akihema kwa kasi kama mwizi aliyekimbizwa na raia.
Sharifu kwa makelele ya mama yake akashtuka usingizini. Akaamka na kwenda chumbani kwa mama yake akaone kilichomkuta mama yake.
“Mama kuna nini?” aliuliza Sharifu mara baada ya kufika chumbani kwa mama yake.
“Hamna kitu mwanangu” alificha kusema Binti Mngane.
“Siwezi kuamini, makelele yote yale unaniambia hakuna kitu...nahisi kuna kitu unanificha.”
“Mh! basi uchelewi kukuza mambo nitakuambia.”
“Hayo ndiyo maneno.”
“Nimeota ndoto mbaya sana.”
“Ndoto gani hiyo?.”
“Nimeota baba yako anataka kunikaba shingoni,” Sharifu alicheka sana baada ya kuelezwa ndoto aliyoota mama yake kisha akasema huku akitabasamu.
“Kumbe nawe mama muoga?.”
“We!!!!!! lazima mtu uwe muoga, yaani uote unakabwa na marehemu unafikiri mchezo.”
“Si mchezo, lakini nawe usiwe unapuuzia ndoto za wenzako.”
“Nimekuelewa...hata hivyo muda umekwenda sana nenda kalale upunguze usingizi ili baadae uwahi kuamka,” Binti Mngane baada ya kumwambia mwanae akaendelea kulala.
Sharifu alipomuaga mama yake akarudi chumbani kwake kuendelea na usingizi. Saa nane kamili ya usiku ikagonga wote kwa pamoja wakaamka wakajibadili mwonekano. Sharifu akavaa kaniki nyekundu kiunoni na akajifunga usongo mwekundu kwenye paji la uso. Binti Mngane yeye akavaa kaniki nyeusi kiunoni na akajifunga kiremba cheusi kichwani. Wote kwa pamoja wakayayuka chumbani wakaja kukutania nyuma ya nyumba yao kisha safari ya kuelekea kilingeni ikanzia hapo. Walipofika kilingeni wakakuta wanachama wenzao na Mzee Damanda wamefika muda na wanaendelea na mkutano.
“Mh, kuonekana kilingeni hadi mfuatwe nyinyi mmekuwa nani?. Hata huyo raisi mwenyewe hawi hivyo............. Nawashangaa nyie kajamba nani mnavyojisikia kuja kilingeni,” Mwanachama mmoja mwanamke anayetambulika kwa majina ya Fatuma Nyanduru alisikika akiongea kwa kuwakejeli Binti Mngane na mwanae.
Binti Mngane akamtuliza mwanae kwa ishara ili kuepusha shari mbele ya mkuu wao. Hivyo basi wakanyamaza kimya bila kujibu chochote. Wakasikiliza kikao kile mwanzo mwisho kwa umakini mkubwa kisha kikao kilipoisha Sharifu na mama yake wakataka kuondoka. Mzee Damanda akawazuia mara baada ya kuona wachawi wote washaondoka kilingeni.
“Mmenifurahisha sana kuja kilingeni leo, pia mmenifurahisha kwa kuonyesha utii mbele yangu pindi Fatuma Nyanduru alivyowatupia maneno makali.............. Kweli nawapa hongera sana kwa hili” alitoa pongezi Mzee Damanda kwa vibaraka wake.
“Kiongozi siku zote sisi ni wapole sana kwa wanachama wenzetu. Yote hayo ni kwaajili ya kutovunja katiba iliyowekwa,” Binti Mngane akasema.
“Vizuri sana...endeleeni kuwa hivyo mkiendelea hivyo mtanipa heshima mimi na chama kwa ujumla” alizidi kuongea Mzee Damanda.
“Tunakuahidi sasa na siku zijazo mimi na mwanangu hatutokuangusha.”
“Nitafurahi sana na nitajivunia kuwa nanyi siku zote.”
“Shukrani...sasa kiongozi ngoja tukuache kuna mahali tunawahi,” Binti Mngane aliaga huku akiangalia hali ya hewa juu ya anga ilivyotulia.
“Mnaweza kwenda ila nawaombeni chonde chonde msiache kuhudhuria kilingeni.”
“Tutaudhuria usihofu juu ya hilo...acha sisi leo tuondoke,” Binti Mngane alipomaliza kuongea maongezi na Mzee Damanda, wakayayuka na mwanae wakatokea kwenye uwanja wa nyumbani wa Bi Kazimoto. Walipofika wakakuta mazingira ya nyumbani kwa Bi Kazimoto yamepoa sana.
“Huyu kikongwe yupo kweli?,” Binti Mngane akauliza.
“Kwa ukimya huu sidhani, nahisi katoka,” Sharifu alijibu huku akipiga jicho kila pahala kama pengine ataweza kumuona Bi Kazimoto.
“Ana nguvu kiasi hiki hadi anajua ujio wetu.”
“Sidhani.”
“Kama kweli ana nguvu kiasi hiki, kikongwe huyu kiboko.”
“Hana lolote subiri nimtafute, nikimpata atajuta.”
“Lakini kuwa makini,” Sharifu pale alipokuwa akayayuka kwaajili ya kwenda kumtafuta adui yake. Hatimaye alikuja kumuona kikongwe yule msalani akitetemeka kwa hofu.
”Ajuza huku unafanya nini?,” Sharifu aliuliza kwa kebehi.
“Nilifahamu ujio wenu nikajificha.”
“Sasa kilichokufanyisha ujifiche ni nini...wakati wewe ni galacha wa nguvu za giza.”
“Nimegundua kuwa wewe ndiye galacha, nguvu zako sikupati hata kidogo.”
“Naona unapiga tantalila nyingi, ebu twende ukapigie huku,” Sharifu alimaliza mazungumzo na Bi Kazimoto kisha upesi akamkumbatia na kuyayuka naye hadi alipo mama yake. Binti Mngane alipoona Bi Kazimoto analetwa na mwanae akaangua kicheko cha ajabu kilichokuwa kikijirudia kama mwangwi.
“Wewe kikongwe, kula kwako kote chumvi unashindwa hadi na mtoto wa juzi...kweli unanistajabisha.”
“Nakustajabisha kweli, lakini ukweli mwanao ana nguvu za ajabu ambazo sijawahi kukutana nazo tokea nizaliwe,” Bi Kazimoto aliongea huku rohoni akiwa na roho ya uwoga.
“Umeligundua hilo...kwanini sasa umetafuta vita?.”
“Sikujua, lakini kwasasa nimeshajua sitoendeleza tena vita nae,”
“Sharifu mwanangu kikongwe huyu simwelewi...tumpe hukumu gani?,” Binti Mngane alimgeukia mwanae na kumuuliza swali mara baada ya kuona Bi Kazimoto mbabaishaji.
“Tumsamehe tu mama” alijibu Sharifu bila kufikiri.
“Tumsamehe!!!, haiwezekani yaani mtu alitaka kukuua bila sababu halafu leo hii tumsamehe kirahisi.... Jambo hili siafiki,” Binti Mngane alimwambia mwanae kwa sauti ya kukalipia hadi Sharifu akashikwa na uoga.
“Mimi siwezi kutoa hukumu kwa kikongwe huyu, kwasababu roho ya huruma ishanijia...kama kuna uwezekano tumwachie tu,” Sharifu alizidi kumpigia kampeni Bi Kazimoto asiweze kupatiwa hukumu na mama yake.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nishakuambia kuwa mimi siafiki jambo hili...na kwa kuwa hutaki kutoa hukumu kwa kikongwe huyu mimi nitatoa,” Binti Mngane alizidi kung'ang'ania Bi Kazimoto apate hukumu. Akazidi kuongea kwa sauti ya ukali kidogo.
“Nitampa hukumu moja tu, kuanzia leo atakuwa Mbuzi,” Kikongwe yule aliposikia kuwa atakuwa Mbuzi akaomba msamaha kwa kupiga magoti aweze kusamehewa.
“Nisameheni jamani, mkinigeuza kuwa Mbuzi unadhani kwa maisha haya si mtaniweka kwenye wakati mgumu” alizidi kuomba asamehewe Bi Kazimoto.
Sharifu akamuonea huruma sana Bi Kazimoto. Akafikiria sana jinsi ya kumsaidia na akaumiza kichwa kuwazua ni jinsi gani atamtoa Bi Kazimoto kwenye hukumu, lakini ikashindikana kumsaidia kutokana na mama yake kutilia mkazo. Binti Mngane kwa nyakati zile roho ya huruma hakuwa nayo akasimama kwenye dhamira yake kuu. Akanyoosha kidole cha husda kwa Bi Kazimoto na papo hapo Bi Kazimoto akageuka Mbuzi mweusi anayelia na kutapatapa kwa huzuni.
“Kwisha, habari yako,” Binti Mngane aliongea na kuachia kicheko cha pongezi chenye kubeza.
“Sijapenda,” Sharifu aliongea kwa unyonge huku akimtazama Bi Kazimoto kwa jicho la huruma.
“Kwanini?.”
“Alikiri kosa.”
“Shenzi kabisa, ebo!!! kwanini unakuwa kama Kinyonga?,” Binti Mngane aliuliza huku akionyesha kuchukizwa.
“Najuta,” Sharifu alijibu huku akisikitika.
“Ebu...usiniletee ujinga na usinipotezee muda kazi ishaisha tuondoke,” Binti Mngane alifoka hadi macho yakawa mekundu kwa hasira.
Sharifu hakutaka kumtibua mama yake akatii amri wakainama kisha wakayayuka na kila mmoja akatokea chumba chake. Alipofika chumbani Sharifu hakuwa na furaha alizidi kufikiria hukumu ile aliyopewa Bi Kazimoto siku hiyo akakosa kabisa lepe la usingizi akawa anajilaumu tu.
“Kwanini, sikumsikiliza Bi Kazimoto?,” Sharifu roho ilimsuta na kujiona mkosaji.
“Ona sasa nimekusababishia hukumu ya kinyama.”
“Nisamehe sana, Bi Kazimoto.”
Sharifu akiwa kitandani anajisemesha mara usingizi ukamrubuni hatimaye akalala usingizi wa pono. Kutaharuki asubuhi kumekucha akasogea dirishani kuhakikisha asubuhi hile kama kweli imewasili, mwanga mkali uliopenya dirishani na kuwika kwa Jimbi kukamthibitishia Sharifu kuwa kumekucha.
“Nilijua nimewahi kuamka!!!...kumbe mama ameshaamka,” Sharifu aliongea huku akimshangaa mama yake mara baada ya kutoka chumbani.
Akazubaa kwa muda kwa kuganda kama sanamu la Michelini kwenye mlango wake wa chumbani, akimwangalia mama yake akifagia ndani huku akiimba nyimbo ya kichawi inayovuta nyota kwa binadamu ambaye hana kinga.
“Habari,” Sharifu baada ya kumsogelea mama yake jirani akatoa salamu.
“Salama,” Binti Mngane aliitika salamu ya mwanae.
“Naona kumekucha.”
“Kumekucha...hali ya hewa ya ubaridi ya leo ni nzuri na siku nzuri.”
“Inapendeza.”
“Kabisa...uwanja umefagiliwa?.”
“Bado!.”
Sharifu akachukua ufagio wa chelewa akatoka nje kufagia uwanja. Dakika kadhaa zikapita akawa amemaliza kufagia akarudi ndani, awamu hii akamkuta mama yake amekalia Kigoda anamenya Mihogo ya chai.
“Nakuona mama yangu, unatayarisha maakuli” aliongea Sharifu kwa utani huku akienda kukaa sakafuni kando ya mama yake.
“Eeeh, ujui kama uhai ni kula.”
“Mambo hayo ni ya kisayansi, nitajulia wapi wakati hata kielimu ngazi za juu sijafika.”
“Najua ni jinsi gani unaumia, tungefanikiwa kukusomesha nahisi sasa ningefurahia matunda...ila usijali sana maana kufeli mtihani si kufeli maisha,” Binti Mngane alimfariji mwanae.
“Sitojali na wala sitojilaumu, nitapambana mpaka tone la mwisho.”
“Kabisaa...wengine wengi hawajasoma lakini wana maisha bora kutokana na kujiongeza,” Binti Mngane alimweleza mwanae kisha akaelekea jikoni kubandika Mihogo mara baada ya kumaliza kumenya.
Sharifu akanyanyuka sakafuni mara baada ya mama yake kuelekea jikoni, akatoka nje na kuelekea kwenye banda la kuku kufagia. Alipofika eneo la bandani akaruka kimo na kupiga ukunga mara baada ya kudhurika mguuni.
“Mamaaaaa.”
“Nini, kimetokea?,” Binti Mngane aliuliza mara baada ya kufika sehemu ya tukio na kumkuta mwanae amekaa chini akiugulia mguu.
“Nyoka.”
“Amekufanyaje mwanangu.”
“Amening'ata mguuni.”
“Kakung'ata!!!!,” Binti Mngane alishangaa kisha akanyanyua mguu wa mwanae na kusotea. Muda kadhaa tu Sharifu akarudi katika hali yake na akatoa shukrani kwa mama yake.
“Asante.”
“Usijali, ni wajibu wangu kukutunza.”
“Lakini mama kwanini ukunifunga kamba?.”
“Kamba ingekukinga tu na isingekuponyesha, ndiyo maana nimetumia nguvu zangu kukuponyesha.”
“Umewezaje?.”
“Nimeweza kwa kuwa hujarogwa. Mara nyingi wachawi kumponyesha mtu aliyerogwa ni ngumu kutokana na nguvu za giza zilizotangulia lakini kwa mtu aliyepata matatizo kwa uwezo wa Mungu tunaweza kumtibu kwa kuwa hazijatumika nguvu zetu za giza.”
“Nimekuelewa...inamaana Nyoka huyu hajatumwa kwa nguvu za giza?.”
“Hajatumwa ingekuwa katumwa kwa nguvu za giza nisingeweza kukuponyesha na ingepelekea sumu kukudhuru,” Binti Mngane alimweleza mwanae huku akimnyanyua kisha akarudi jikoni.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sharifu aliponyanyuliwa akaingia bandani kufagia, ndani ya dakika tano Sharifu akamaliza kufagia banda la kuku hatimaye akarudi ndani. Aliporudi ndani akamkuta Binti Mngane kashaandaa chakula ukumbini.
“Upo shapu!!!?,” Sharifu alimuuliza mama yake kwa mshangao mara baada ya kuketi kwenye mkeka kilipo chakula.
“Kwanini?.”
“Ushaivisha chakula, mara hii!!!.”
“Kupika mbona aichukui muda mwingi dakika kadhaa tu unaivisha chakula.”
“Kwako...lakini wengine ni wazito wakiwa jikoni, unalijua hilo?.”
“Sio wote, ni baadhi.”
“Kweli?.”
“Eeenh.”
“Najivunia kuwa na mama, shapu na mwenye hekima,” Sharifu alimpatia sifa mama yake.
“Ushaanza kunipaka mafuta, kwa mgongo wa chupa.”
“Kwanini nikufanyie hivyo?.”
“Haya...chai ya leo unaionaje?.”
“Haina sukari.”
“Ni kweli...leo sukari imeisha na nimeona uvivu kwenda dukani.”
“Haina shida, kwa kuwa tushazoea shida zetu.”
Wakati Sharifu na mama yake wakiendelea na maongezi na vicheko huku wakiendelea kula, wakakatishwa maongezi na mtu aliyekuwa anabisha hodi katika mlango wao wa ukumbini.
“Nenda kamwangalie, anayegonga mlango,” Binti Mngane alimtuma mwanae.
“Sauti hiyo kama naijua,” Sharifu aliropoka kwa kukisia.
“Sauti hiyo ya nani?.”
“Sio ya jirani yetu.”
“Jirani yetu nani?.”
“Mama Nguya.”
“Ebu...kaangalie usikisie,” Binti Mgane alimwamrisha mwanae awahi kwenda kufungua mlango.
Sharifu alikwenda kufungua mlango hakuamini japo moyo wake ukaamini na kujawa na furaha. Alipokutana ana kwa ana na shangazi yake mara baada ya kufungua mlango.
“Hausindile?,” Sharifu alimsalimu shangazi yake kwa lafudhi ya kirugulu.
“Hanoga...Mai nimemkuta?,” Shangazi yake Sharifu alijibu na kuuliza kwa lafudhi ya kirugulu naye.
“Umemkuta...ataenda wapi kwani?. Yupo mng'anda ametulia tu,” Sharifu alijibu hatimaye akamkaribisha Shangazi yake.
Sharifu akaongozana na shangazi yake ndani, wakamkuta Binti Mngane akiendelea kula huku kavuta mdomo mbele kama mtu aliyechukuliwa mume. Alimchukia sana wifi yake kutokana na ugomvi wao wa awali wa kurushiana vijembe vya majivuno.
“Wifi mbona mvivu kutembea?,” Shangazi yake Sharifu aliuliza kwa upendo.
“Unadhani, nimelishwa miguu ya kuku kama wewe,” Binti Mngane alijibu kwa kubeza.
“Wifi sijaja kwenu kwa shari nimekuja kumuona mtoto wa kaka yangu,” Shangazi yake Sharifu aliongea kwa upole.
“Umesikia mwanangu, anaumwa au amefariki?.”
“Nilijua umebadilika wifi.”
“Nimekuwa kinyonga siku hizi?.”
“Sharifu mwanangu mbona simwelewi mama yako?.” Sharifu hajasema, akadakia kusema Binti Mngane kwa kumtupia wifi yake maneno ya shombo.
“Unielewi kwani nimelewa?...na kwanza una uwezo wa kuwa na mtoto wewe?.”
“Maneno gani unaongea mbele ya mtoto?” aliuliza Shangazi yake Sharifu.
“Kama tasa tusiseme?.”
“Kweli, hadi hapo nishagundua wifi yangu kwamba bado unanichukia..........sawa bwana lakini Mungu yupo, ipo siku atasikia kilio changu,” Shangazi yake Sharifu aliongea kwa simanzi huku machozi yakitiririka.
Shangazi yake Sharifu akaendelea kutoa machozi na kichwa akiwa kainamisha chini. Sharifu akaona huruma kwa shangazi yake. Akamsogelea karibu akamwinua shangazi yake kisha akambembeleza anyamaze. Haikuwa kazi rahisi kumnyamazisha, ilikuwa ni kazi pevu kweli kweli.
“Nyamaza shangazi, utaendelea kulia hadi saa ngapi...uoni kama unachokoza homa,” Sharifu aliongea huku akizidi kumbembeleza shangazi yake na kumfuta machozi kwa kutumia mkono.
“Siwezi kujizuia kuacha kulia...labda hivi mama yako ndiyo anapenda.”
“Kulia umelia vya kutosha, ebu...sasa nyamaza niweze kuwapatanisha,” Binti Mngane alicharuka mara baada ya kusikia mwanae anataka kumpatanisha na adui yake akavunja ukimya na ndimi yake ikapayuka.
“Sharifu unasemaje?” aliuliza Binti Mngane.
“Nataka, niwapatanishe” alijibu Sharifu.
“Mimi siwezi kupatanishwa na tasa.”
“Mamaaa una nini?.”
“Kwani, unanionaje?.”
“Matendo yako leo siyaelewi!.”
“Kivipi?.”
“Sasa unachomfanyia shangazi ni sawa?.”
“Wewe unaonaje?.”
“Si sawa.”
“We mtoto nawe usinichanganye haya ni maamuzi yangu mimi sihitaji mtu yeyote aniingilie..................... Kwanza naona anavyoendelea kukaa anazidi kunipa kero hebu aondoke tu,” Binti Mngane alimchukia sana wifi yake hatuwezi jua kwa kosa gani kubwa mno labda ni haki yake kumchukia.
“Shangazi haondoki hapa. Akiondoka tu bila yeye mwenyewe kuamua nami naondoka,” Sharifu akatetea.
“Ondoka! Si umeamua?. Ila yakikushinda utarudi,” Binti Mngane alisema kwa jazba.
Binti Mngane baada ya kuona wanamchelewesha kufanya shughuli zake, akaenda mlangoni akafungua mlango kisha akawatoa kwa kuwatimua. Sharifu hakutaka kubisha na kuendelea kuleta mzozo, akamshika mkono shangazi yake kwa hasira na kuondoka naye.
“Kwa nini usingebaki?. Ungeniacha mimi niende?,” Shangazi yake Sharifu wakiwa njiani alimuuliza mtoto wa kaka yake.
“Nishaamua kuondoka nawe...acha tu twende wote shangazi,” Sharifu alijibu kisha akamfariji shangazi yake kwa kumshika mkono huku wakiwa wanaendelea na safari.
Shangazi yake Sharifu hakupinga sana chaguo la mtoto wa kaka yake. Akakubali kwenda naye nyumbani lakini wakiwa bado wapo njiani Binti Mngane akatuma Njiwa kimiujiza ili aende kumdhuru wifi yake. Huyo Njiwa akatii agizo na kwenda moja kwa moja na kutua kwenye kichwa cha shangazi yake Sharifu kisha akamdonoa na kuondoka. Ghafla shangazi yake Sharifu mara baada ya kudonolewa akajihisi kizunguzungu kisha akadondoka chini.
“Umepatwa na nini?,” Sharifu aliuliza huku akijitahidi kumwinua shangazi yake.
“Kichwa kinaniuma sana,” Shangazi yake Sharifu alijibu mara baada ya kuinuliwa na mtoto wa kaka yake.
“Kinaumaje?.”
“Kina gongagonga kama nyundo.” Sharifu akagundua kitu na akajua zaidi kuwa mama yake anahusika asilimia mia kwa ugonjwa uliompata shangazi yake kutokana na mzozo uliotendeka hivi punde tu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jitahidi kutembea, tukifika nikakutengenezee dawa,” Sharifu alisihi kisha akamkokota shangazi yake polepole.
“Siwezi kutembea, naona viungo vya mwili vyote vimekaza,” Shangazi yake Sharifu aliongea kisha akapata kizunguzungu tena. Kizunguzungu kikamfanya alegee mwili na kumfanya Sharifu akose nguvu ya kummudu shangazi yake na kusababisha kudondoka tena chini kwa pamoja.
“Tutafanyaje?,” Sharifu aliuliza huku akilaza kichwa cha shangazi yake kwenye miguu yake mara baada ya kudondoka.
“Tupumzike kidogo, nikipata ahueni tutaondoka.”
“Hapana.”
“Kwanini?.”
“Ukipumzika njiani unaweza kuzidiwa...ngoja tu nikubebe ukapumzike nyumbani.”
Shangazi yake Sharifu akakubaliana na ushauri wa mtoto wa kaka yake . Akakubali kubebwa ili mradi awahi kujipumzisha nyumbani, walipofika Sharifu akatandika mkeka nje shangazi yake apunge upepo huku yeye akimtengenezea dawa. Dakika chache akachemsha dawa na ikawa tayari kwa kunywa.
“Dawa, tayari amka unywe,” Sharifu alimwamsha shangazi yake mara baada ya kuonekana kulala nyakati zile.
“Shangazi amka basi,” Sharifu aliendelea kumwamsha shangazi yake kwa muda mrefu bila matokeo yoyote ya kujibiwa.
Ndipo akaja kugundua kuwa shangazi yake hayupo naye tena duniani, kwa maana ameaga dunia. Sharifu akaumia sana na hadi akashindwa kujizuia kuachia kilio. Akatoa kilio huku akipiga yowe kuwaita majirani, punde baadhi ya majirani wakasikia wito wakafika sehemu ya tukio wakamkuta Sharifu nje akiwa ameshikilia mwili wa shangazi yake.
“Nini kimewakuta?,” Jirani mmoja mwanamke aliyetambulika kwa jina la Mama Chausiku aliuliza na kuonyesha dalili ya kutotambua kilichotokea.
“Mama Chausiku, jirani yetu amefariki,” Jirani mwengine wa kiume aliyeelewa kilichomkuta shangazi yake Sharifu alijibu swali la Mama Chausiku.
“Eti?,” Mama Chausiku alimuuliza Sharifu apate uhakika na kuonyesha kutoamini.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Eeenh, amefariki shangazi yangu,” Sharifu alijibu huku akiwa bado analia.
Mama Chausiku akamuonea huruma sana. Pale alipokuwa Sharifu akachutama, akasogeza kichwa cha Sharifu kwenye kifua chake kwa kumfariji kisha akaomba baadhi ya vijana wabebe mwili wa jirani yao waupeleke ndani. Vijana wakauinua mwili wa shangazi yake Sharifu na kuingiza ndani kisha wakatoka nje wakasaidiane na Mama Chausiku kumnyamazisha Sharifu. Wakamnyamazisha na hatimaye Sharifu akanyamaza kisha akapanga siku na majira ya mazishi. Kwa kuwa shangazi yake Sharifu alifariki jioni Sharifu akapanga mazishi yafanyike kesho yake jioni ya saa kumi na moja kasoro. Kesho yake jioni muda uliopangwa watu wakajiandaa kwenda kuzika wakazika na watu wakatawanyika kurudi majumbani.
**********
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment