Simulizi : The Return Of The Ambrosy
Sehemu Ya Nne (4)
"Namba yangu umeitoa wapi? Na kwanini ananifuata fuata sana?.." Kwa hasira kali Walemi alimuuliza Dito. Ajabu Dito aliangua kicheko kwanza na kisha akasema "Sio namba tu wala picha,mpaka jina nakufahamu. Wewe si Walemi?.."
"Mungu wangu" Alishtuka Walemi wakati huo huo Dito alikata simu huku akimuacha Walemi akiwa na sintofahamu juu ya Dito alipoitoa namba yake. Machele yakamcheza, akaanza kuhisi kuwa huwenda Ambrosy akawa anamchezea mchezo. Lakini suala hilo hakutaka kuliamini sana na ndipo siku moja walipokutana Walemi akijaribu kuligusia suala hilo.
"Ambrosy"
"Naam! Walemi"
"Hivi wakati unanisajilia namba, kuna mtu ulimpa?.."
"Mtu? No sijampa mtu yoyote namba yako, kwani vipi?.."
"Kuna mtu ananisumbua sana, niambie jamani kama kuna mtu umempa"
"Hapana Walemi siwezi kufanya hivyo, labda ili uamini kama kweli sijampa mimi hebu mpigie hapa hapa" Alisisitiza Ambrosy. Hima Walemi aliingiza mkono katika pochi yake akatoa simu kisha mara moja akaanza kuitafuta namba ya Dito. Alipoipata akapiga ambapo simu iliita bila kupokelewa, lakini aliporudia mara ya pili Dito alipokea, akasema "Naona mzigo upo tayari, haya niambie nikukute wapi?."
"Ammh hapana Dito, ila nakuandalia siku za usoni utaupata tu wala usiwe na tabu. Lakini Dito!.."
"Sema nakusikiliza"
"Nataka kujua namba yangu umeitoa wapi"
"Ahahaha hahaha" Dito aliangua kicheko kisha akajibu "Walemi, ukitaka kujua hilo basi leta mkwanja kwanza mengine yatafuata ama kama pesa huna basi jiongeze kama mwanamke" Hapo Walemi alikata simu, machozi yalimtoka kwani akifanyacho Dito hakuweza kupendezwa nacho.
"Huyu mtu unaagenda naye ipi?.." Aliuliza Ambrosy kwa shauku ya kutaka kujua. Walemi alichia tabasamu hafifu kisha akasema "Ammh unajua mambo ya uswahili, yani ukimuwekea mtu dhamana kwa jambo fulani basi utakuta anakusumbua kama kukopesha uhai" Alidanganya Walemi.
"Ulimuwekea nani dhamana?.." Aliongezea kuhoji Ambrosy. Walemi akajibu "Kuna rafiki yangu mmoja hivi, ila usijali wala usiwe na hofu nitamuhimiza ili amlipe ili huyu mtu akome kunisumbua"
"OK lakini usije kufanya tena mchezo huo, unajua hapa mjini usimuamini kila mtu la sivyo utajikuta unachezea kifungo kwa mslahi ya mtu mwingine" Alisema Ambrosy. Baada ya mazungumzo mawili matatu wawili hao waliachana huku Walemi akimuasa Ambrosy siku moja afike mahali anapoishi. Ambrosy alikubaliana naye, hivyo aliahidi Kufika bila kukosa.
Hakika Dito aliumiza ubongo wa Walemi,kutokana na mambo anayo mfanyia. "Milioni sita nipatie ili picha hizi niweze kuzifuta" Aliyakumbuka maneno hayo ya mwisho aliyowahi kuzungumza naye,na hapo Walemi akajikuta akishusha pumzi ndefu huku akijiona kama mkosaji katika hii dunia. Alijitafakari "Hivi kwanini inakuwa hivi? Kila hatua nipigayo inakikwazo, ni lini na mimi nitavuna furaha kama watu wengine? Je, nikimueleza Ambrosy tatizo hili si atanibwaga na kuniona muuaji, na kama nitalifumbia macho mwishowe sinitajikuta naishia jela? Ooh Mungu wangu nisaidie mimi.. "Yote hayo Walemi alikuwa akiyatafakari ndani ya ubongo wake ikiwa usiku wa pata saa nane ambapo alishindwa kabisa kusinzia. Moyo ulimuuma sana, akajiona sasa hana thamani tena ya kuendelea kuishi duniani na hapo ndipo alipoamua kuamka akakata kamba ya kuwekea nguo kwa niaba ya kujiua sababu aliona heri kufa kuliko kuwa daraja hapa duniani.
Ulikuwa ni uamuzi mgumu kiukweli lakini ilimbidi afanye hivyo ili kuepusha dhahama kuu inayotarajiwa kumtokea siku za usoni. Hatimaye harakati zote za kuitundika kamba zilikamilika, machozi yakimtoka katika mboni zake alisimama juu kwenye stuli akakivaa kitanzi na punde akaisukuma stuli kwa kutumia miguu yake. Walemi alisafa, alirusha miguu huku na kule wakati huo huo Siwema aliamka kutoka usingizini ambapo alistushwa na kitendo hicho alichokuwa akikifanya Walemi. Muda mchache baada Siwema kuamka, kamba ile ilikatika kabla hata roho haijaacha mwili. Walemi akawa ameanguka chini huku mikono yake akiipapasa shingo.
"Kwanini umeamua kufanya hivi Walemi? Je, unataka kunipa kesi ili nikafungwe? Kitu gani kimekupelekea mpaka kutaka kujiua?.." Aliuliza Siwema huku akiangua kilio, muda huo ilikuwa yapata usiku wa tisa sasa. Na wakati Siwema anasema hayo mara ghafla simu ya Walemi ikaita. Siwema alipokea ikasikika sauti ya Ambrosy ikisema" Mmh my love, samahani kwa kukusumbua ila yote ni shauri ya upendo wangu kwako. Huwezi amini Walemi wangu nimemaliza kukuota sasa hivi. Je, nikwambie nimeota ndoto gani?.. " Maneno yote hayo Ambrosy alikuwa akiyaongea huku simu akiwanayo Siwema akiwa ameiweka sikioni.
" Shemeji?.. "Alisema Siwema kwa sauti ya kilio. Ambrosy alistuka, kisha akasema" Naam kuna nini?.. Mbona hivyo?.. "Alitaharuki Ambrosy, hivyo Siwema akapata kumuelezea kila kitu.
Palipo pambazuka Ambrosy alifika nyumbani anapoishi Walemi, hapo akapata habari kamili ingawa bado Walami aliweza kuonyesha ugumu wa kueleza sababu hasa iliyompelekea kutaka kujiua. Ili baki siri yake moyoni. Na baada ya siku kadhaa mbele hatimaye Ambrosy anaamua kuwapangishia nyumba Siwema na Walemi sehemu nyingine tofauti na hapo paawali. Ambrosy kamwe hakufurahishwa na mazingira aishio kipenzi chake, ikawa ndio sababu kubwa iliyomfanya kuwahamishia kwenye nyumba nzuri iliyopo Mkocheni A. Na kutokana na utajiri aliokuwa nao aliweza kuwafungulia duka kubwa la nguo Kinondoni. Rasmi sasa Siwema akaachana na kazi ya umama ntilie ilihali Walemi naye alirudishwa shule kujiendeleza kwani Ambrosy umri wa binti huyo bado unaruhusu lakini pia aliona Elimu ndio zawadi pekee inayomfaa mpenzi wake huyo.
Baada ya miaka miwili kupita, jioni moja Siwema aliweza kumwambia Walemi maneno mazuri ikiwa kama kumbushia ili asijisahau. Siwema alisema
"Umepata mwanaume sasa, ila unatakiwa utulie sawa Walemi?..ona kutoka kwenye maisha ya umama ntilie mpaka kuuza duka la nguo huku ndani full kiyoyozi, si bahati hiyo?.." Walemi aliposikia maneno hayo alicheka kidogo kisha akajibu "Ni kweli uyasemayo lakini dada siku zote pesa haiwezi kununua upendo,Mwanaume anaweza kumjali mwanamke. Akamsomesha akamnunulia Gari,akampa kile chochote anacho kitaka lakini abadani mwanamke huyo asimpende na ajabu akatokea mwanaume kapuku, hohe hahe asiye na mbele wala nyuma, huyo akatokewa kupendwa sana kuliko yule mwenye pesa zake "
" Mmh unamaana gani Walemi. Chonde chonde usije ukamkwaza huyu kijana. Maana naona sasa kama tayari umeanza kuota mapembe, hebu kumbuka kwanza ulipotoka Walemi. Ujue leo hii tupo hapa sababu ya huyu kijana kwahiyo endapo kama utajivuruga itakula kwako na kwangu pia. Tulia mdogo wangu" Alihamaki Siwema akitilia shaka maneno aliyoyasema Walemi. Kwa mara nyingine tena Walemi aliangua kicheko kisha akasema "Dada Siwema ni vile hujui tu nini moyo wangu unataka. Sio Gari na wala sio vijipesa hivi anavyonipatia Ambrosy. Ukweli nina siri nzito ndani ya moyo wangu ila ipo siku utajua nina maana gani kukwambia maneno hayo "
Maneno hayo ya Walemi yalimfanya Siwema kuwa na hofu juu yake, lakini yote kwa yote hakutaka kuendelea kujaji kuhusu suala hilo.
Maisha yalisonga,raha mstarehe baina ya Walemi na Siwema pamoja na familia yake. Walemi alikazana katika masomo yake huku kijana Ambrosy akijitahidi sana kutumia pesa nyingi kuhakikisha binti huyo hayumbi kwa vyovyote vile, secondary alimaliza kidato cha kwanza mpaka cha sita. Mpaka hapo ni Elimu iliyomtosheleza kabisa.
"Hakika ni jambo la furaha sana, lakini vile vile napenda nikushukuru sana mpenzi wangu Ambrosy kwa kuniamini ambapo umetumia ghalama zako kuhakikisha Walemi mimi napata Elimu iliyo bora..kwa sababu awali nilikuwa nimeshakata tamaa lakini ukanitia moyo kwa kuniambia kuwa elimu haina mwisho ila kwa hapa nilipofikia acha nipumzike kwanza "Alikuwa ni Walemi aliyekuwa akiyasema maneno hayo kwa sauti nyororo akimwambia Ambrosy muda huo wakiwa kwenye moja ya kumbi ya starehe.
" Ahahah ah. Hahahahaha "Alicheka Ambrosy baada kuyasikia maneno kisha akasema. " Laiti kama ningelikuwa na uwezo, basi jina lako ningeliandika angani ili kila mtu alionapo ajue kuwa Ambrosy anakupenda. Umekuwa mtu mzima sasa na umekuwa mzuri sana maradufu Walemi wangu. Aamh! Mbali na hilo, mimi nasema kwamba elimu yako bado sijalizika nayo. Pumzika huku ukijua kwamba darasa bado linakuhitaji. Ambrosy sioni tabu kuteketeza pesa juu yako " Alisema hivyo kijana Ambrosy. Walemi alionekana kufurahi sana machoni mwake,ambapo aliweza kushusha pumzi ndefu na kisha kusema.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hata kwangu umekuwa bora Ambrosy, istoshe na huo uzuri wako ndio kabisaaaaa unazidi kunichanganya. Kutoka moyoni mwangu natamka ni wewe tu Ambrosy uliyeshika uhai wangu ukiachana na Muumba, lakini pia nipo tayari kurudi darasana nakupenda sana Ambrosy, lakini?.."
"Aaah lakini nini mama, hivi unajua kuna kitu nimeandaa kwa ajili yako?.." Alidakia Ambrosy kabla Walemi hajamaliza kusema alichokuwa akikiongea.
"Kitu? Kitu gani hicho?.." Aliuliza Walemi kwa taharuki.
"Bado mapema sana ila ipo siku utajua tu" Alijibu Ambrosy. Walemi akawa mpole kungojea siku hiyo kwa hamu kubwa.
Baada ya kadhaa kupita,Ambrosy alimpigia simu Walemi, ilikuwa ni jioni yapata saa kumi na mbili. Ambrosy alipiga simu kumuhitaji Walemi nyumbani kwake. Walemi alifika mara moja kwa muda muafaka pasipo shaka, alimkuta Ambrosy sebuleni akiwa ameketi kwenye sofa huku juu ya meza zikionekana bia rukuki na vinywaji vingine mbali mbali.
"Baby mbona hivi? Leo kuna jambo gani hapa?.." Aliuliza Walemi kwani hakuwahi kumuona Ambrosy akifanya kitendo hicho. Ambrosy aliangua kicheko, alipokatisha cheko hilo akasema "Unakumbuka nilikwambia nini siku ile?.." Ambrosy alihoji.
"Ulimiambia nini?.." Alijiuliza Walemi wakati huo akiinua uso wake juu akijaribu kuvutia kumbukumbu, hatimaye alikumbuka na hivyo alishusha chini uso wake kisha akajibu "Uliniambia kwamba kuna kitu umeandaa kwa ajiri yangu na ukanitaka nisiwe na haraka"
"Ahahaha hah" Alicheka Ambrosy kwa mara nyingine tena halafu akaongeza kusema "Naam! Basi siku yeyewe yenyewe ndio hii" Ambrosy alipokwisha kusema hivyo, punde si punde waliinuka watu kutoka nyuma ya masofa wengine wakitoka vyumbani na wote kwa pamoja wakiimba nyimbo ya kumtakia heri ya kuzaliwa Walemi. "Happy birthday to youuuuu. Happy birthday to youuuuu. Happy birthday dear Walemi, happy birthday to youuuuu" Shangwe na furaha ilizuka mahali hapo, watu hao wa karibu wa Ambrosy walisheherekea siku ya kuzaliwa Walemi. Hakika Walemi hakuamini machoni mwake, aliona jambo la ajabu sana kwani hajawahi kufanyiwa kitendo hicho zaidi ya kuishi kutazama kwenye mikanda ya sinema. Cake ililiwa, walevi walikunywa pombe achilia mbali vyakula mbali mbali navyo vilichukuwa nafasi yake, watu walikula na kusaza. Baada ya shangwe hizo kufikia tamati, hatimaye Ambrosy anapata kumtambulisha Walemi mbele ya rafiki na jamaa zake Hao. Kwa sauti ya furaha na tabasamu Ambrosy alisema.
"Jamani awali ya yote napenda kuwashukuru rafiki zangu na jamaa zangu pia kwa kuhudhuru sherehe hii, hakika nimefurahi sana." Aliposema hivyo alikaa kidogo kisha akaendelea kusema "Basi mbali na hilo, siku kama ya leo ambayo ndio siku aliyozaliwa Walemi, ndio siku ambayo pia nilipanga niweze kumtambulisha kwenu kama shemeji yenu. Mtanisamehe sana kwa kuchelewa kufanya hivyo ila najua niliwambia kuwa nina mchumba, na ndio huyu sasa leo mnamuona mbele yenu. Anaitwa Walemi. Walemi hawa ni marafiki zangu ingawa humu humu kuna jamaa zangu, naomba uwasome sura ili usije ukatongozwa na mmoja wao" Alisema hivyo Ambrosy huku akitupia na utani kidogo kitendo ambacho kilipelekea kuzua vicheko vya hapa na pale. Na mara baada kuhitimisha vicheko hivyo Ambrosy aliendelea kusema" Basi ndio hivyo huyu ndio mpenzi wangu wa kufa na kuzikana, kiukweli ni bora uchukue roho yangu kuliko kunipokonya Walemi. Nampenda sana. Kwahiyo nafikiri kesi mpaka hapa imeisha au sio jamani?.. "
" Ni kweli lakini bwana ndugu yangu Ambrosy, unajua bwana wewe ni mtu mwenye heshima zako bwana. Hivyo basi bwana ni vizuri ukifunga naye ndoa kabisa kuliko kuendelea kuishi naye kiujanja ujanja, hivyo ni dhambi na utaonekana na wewe muhuni bwana. Asio bwana "Alikuwa kijana aliyeitwa Malima. Kijana mwenye mbwembwe nyingi za kuvunja mbavu pindi anapoongea, kwani mbali na kupenda kutumia neno (bwana) vile vile Malima alikuwa akiongea akitupa mikono huku na kule mfano wa kocha anayewapa maelekezo wachezaji wake. Kwa mara nyingine tena vicheko vilisikika,hasa hasa Walemi. Alicheka sana.
"Aamh kuhusu hilo wala usijali swahiba wangu, nalifanyia mpango madhubuti kabisa. Ila kuna mambo nayaweka sawa nikiwa tayari tutaarifana tu" Alisema Ambrosy.
Hatimaye shughuli nzima mahala hapo ikawa imemalizika, ilikuwa ni siku tofauti kabisa kwa Walemi,kwani mbali na kufanyiwa sherehe hiyo vile vile alipewa gari ya kutembelea aina ya Halya. Jambo hilo lilizidi kumchanganya sana Walemi, kwa tahatuki kubwa akauliza.
"Khaa Ambrosy unataka kusema hii gari ya kwangu?.."
"Ndio gari ni yako, hebu ingia ndani basi" Alijibu Ambrosy. Haraka Walemi aliingia ndani gari hiyo na kuaza kutazama huku na kule akiangalia maadhali ya ndani katika gari hiyo. Furaha isiyokifani ilizidi kumjaa Walemi,hima alimlaki Ambrosy na kumbusu mashavuni, na hata walipotoka ndani ya gari bado Walemi alimkumbatia Ambrosy kwa tabasamu bashasha huku akithubutu kurukaruka na kumshangilia. Mwishowe alitulia kisha akasema "Hakika Mungu akuweke umri mrefu Ambrosy, wewe ni mwanaume sahihi kabisa kwangu"
"Usijali masuala haya ni ya kawaida sana, na fanya hivi sababu unaishi ndani ya moyo wangu" Alijibu Ambrosy. Hakuishia hapo, zaidi alimpeleka mahali alipomfungulia duka kubwa la nguo. Jambo ambalo liliendelea kumpagawisha Walemi, alilia kwa machozi hasa akikumbuka maisha aliyokuwa akiishi kipindi cha nyuma. Alikumbuka kuwa aliwahi kunusurika kufa kwa kutolewa sehemu za siri achilia mbali kifo cha Emakulata, kuuzwa kimwili lakini pia alikumbuka na mauaji aliyoyafanya kwa dalali aliyefanya naye Mapenzi kwa dhumuni la kutafutiwa kazi lakini mwisho wa mchezo dalali huyo alimgeukia ambapo Walemi aliamua kuchukua uamuzi wa kumchoma kisu. Na baada kuyakumbuka matukio hayo tofauti tofauti, pumzi alishusha kisha akasema "Nakushukuru sana mume wangu" Ambrosy akiwa na uso wenye tabasamu akajibu "Happy birthday my wife" Maneno hayo yalimfanya Walemi kulijibu tabasamu hilo la Ambrosy halafu akamkumbatia.
Sasa Walemi anapata kufundishwa kuendesha gari, ilikuwa ni kituko barabarani lakini ndani ya siku tano binti huyo alifahamu kuendesha gari,hivyo kwenye mizunguko yake alikuwa akitembea na gari. Siku ya kwanza kurudi nayo nyumbani Siwema hakuamini machoni mwake baada Walemi kumwambia kuwa Ambrosy amenunulia gari. Kwa furaha Siwema alimwambia "Walemi Walemi. Chonde chonde, narudia tena kukuasa kuhusu huyu mbaba,kiukweli ni mtu wa muhimu kwako" Maneno hayo Siwema alikuwa akimwambia Walemi ilikuwa asubuhi mapema, muda huo Walemi alikuwa akijipodoa kwa niaba ya kutoka akielekea shopping. "Walemi unanielewa lakini?.." Aliuliza Siwema kwa msisitizo. Walemi akajibu "Ndio nimekuelewa dada yangu hilo ndoa shaka" Alipokwisha kujibu hivyo aliaga akaondoka zake. Akiwa ndani ya Gari yake,foleni kubwa barabarani. Gari zikitembea pole pole na kusimama,kwa mbali Walemi alimuona mtu ambaye alihisi kumfahamu.. Lakini kwa kuwa muda huo gari zilikuwa zimesimama aliamini mtu huyo akijongea karibu yake ataweza kumuona vizur ili ajue kama ni yeye ama amemfananisha. Hatimaye mtu huyo alimkaribia gari la Walemi, kwa macho yake mawili Walemi anapata kumuona Daniel wake kwa mara nyingine tena tangu wapotezane miaka kadhaa nyuma kipindi alipokuwa omba omba barabarani. Daniel alikuwa akivuka barabara akizipiga hatua za haraka haraka huku akitazama kulia na kushoto wakati huo mkononi akiwa amebeba mazagazaga mbali mbali akiuza kwenye magari yaliyokuwa yamesimama kungojea taa ya kijani iwaruhusu kuondoka. Daniel anapata kulifikia gari ya Walemi, hapo Walemi alishusha kioo huku Daniel akiamini ni mteja ambaye anahitaji bidhaa yake,hivyo alikuwa shap kuzipamba. Lakini mwisho wa yote Walemi akasema "Wewe? si Daniel ?.." Daniel alishtuka baada kusikia ametajwa jina lake. Kwa macho ya taharuki akamtazama Walemi kisha akahoji "Ndio ni mimi kwani vipi, Uliwahi kuniona wapi? "
"Zamani sana ila huwezi kunikumbuka kwa haraka lakini mimi ni mpenzi wako Daniel. Naitwa Walemi" Alijibu Walemi huku akitokwa na machozi ya furaha. Daniel kwa mshtuko akajikuta akidondosha mazagazaga yake kisha akarudi kuuliza "Ni wewe Walemi wa Dodoma?.." Walemi akajibu "Ndio mimi mwanamke wa ndoto zako Dani, nakupenda sana"
Daniel alishtuka sana asiamini masikio yake wala macho yake,muda huo huo taa ya kijani iliwaka kuruhusu magari yaendelee na safari. Hapo Walemi alimtaka Daniel aingie ndani ya gari ili wazungumze mengi zaidi wakiwa sehemu tulivu, lakini kwa kuwa Daniel alikuwa yupo katika harakati za kuuza bidhaa alizokuwa nazo ilimpelekea kukataa jambo hilo.
"Hapana Walemi, nipo katika biashara labda tupeane mawasiliano tutawasiliana baadaye" Alisema Daniel.
"Daniel? Hivi unanipenda kweli?.." Akiwa na hasira Walemi aliuliza hivyo ilihali huku nyuma baadhi ya magari yakimpigia honi huku mengine yakimzunguka na kisha kuendelea na safari.
"Acha ujinga wewe bwege na ki-gari chako cha mkopo" Ilikuwa ni sauti ya kondakta wa daladala. Kondakta huyo aliongea maneno hayo kwa jazba kubwa akikerwa na kitendo cha Walemi kuendelea kusimama wakati taa tayari imeruhusu.
"Dani hebu panda kwenye gari tuondoke tafadhali nakuomba" Alisisitiza Walemi, ukweli binti huyo hakutaka kumpoteza tena Daniel kwa mara nyingine tena na ndio maana alijitahidi kumlazimisha Daniel akubali ombi lake jambo ambalo kijana huyo mwishowe aliweza kukubaliana nalo. Safari ya kuelekea shopping iliahilishwa, Walemi akaenda moja kwa moja anapoishi Daniel.
"Hapa ndio nyumbani Walemi, naishi na rafiki yangu ila yeye bado yupo katika mizunguko yake" Alisikika akisema hivyo Daniel mara baada kufika nyumbani. Ni uswahilini mitaa ya Tandale kwa mtogole ndipo Daniel alipoweka makazi yake akiwa sambamba na rafiki yake kipenzi. Walemi aliitazama chumba hicho cha Daniel,alitupia macho yake kila kona na mwishowe aliishia kushusha pumzi kisha akasema "Yeah! Sio haba Daniel, maisha ya kigheto ghetto haya"
"Ndio hivyo Walemi, enhee kabla yoyote unatumia kinywaji gani?.." Aliuliza Daniel.
"Wala usijali, mimi nipo vizuri kabisa Daniel" Alijibu Walemi huku bado macho yake yakiendelea kukitazama chumba cha Daniel.
"Aah Walemi! Hata maji basi.." Alisema Daniel, ila bado Walemi alikataa katu katu, na hivyo nafasi hiyo wakaitumia kuongea mambo mbali mbali hasa Walemi akigusia suala la Daniel kulowea ndani ya jiji la Dar es salaam pasipo mawasiliano yoyote.
"Kwanza leo ndio nimeamini kwamba milima haikutani lakini binadam hukutana. Pili naomba nisamehe sana sana, ukweli nilifanya kosa kubwa mno. Lakini Walemi ulitegemea ningefanya nini mimi? Pesa Sina na tayari kijiji kuzima kilitambua kuwa Dani kaenda Dar kutafuta maisha akirudi amuoe Walemi. Lakini nimehaso vya kutosha ila sijafanikiwa, shilingi kwa upande wangu ikawa taabu kupatikana.. Kwahiyo nikaona sio vema kurudi mikono mitupu mpenzi wangu "Alisema maneno hayo Daniel kwa sauti ya upole iliyojaa huzuni ndani yake.
" Hatakama Dani, mapenzi sio pesa. Ungerudi nyumbani kuliko kulowea mjini. Kwanini lakini, eeh kwanini Daniel?.."Aliongea kwa jazba Walemi huku akiangua kilio hasa baada kukumbuka tabu na karaha alizokumbana nazo pindi aliporoka nyumbani kwao kwa kukacha pendekezo la wazazi wake baada kumtafutia mwanaume mwingine ilihali tayari alishatia nadhiri kuwa ataolewa na Daniel.
NI changamoto ngumu sana alizopitia Walemi kabla haja chukuwa uamuzi wa kutoroka, maneno rukuki ya kukatishwa tamaa aliambiwa,sio ndugu tu bali hata marafiki zake nao walimpasha kwa maneno mbali mbali yaliyoweza kumsononeshe.
"Walemi, mwanamke ni kama tunda mbivu, likikaa muda mrefu bila kuliwa litaharibika"
"Unamaana? Kusema hivyo Angel"
"Nina maana kwamba umri wako sasa sio wa kukaa nyumbani kusubiri pesa ya sabuni kwa mama na baba yako, wachumba wapo kwanini usiolewa?.."
"Nitaolewa tu lakini hapa kijiji mwanaume pekee atakaye nioa ni mmoja tu. Si mwingine bali ni Daniel..."
"Dani? Hahaha hahaha! Hebu acha utani bwana, mbona unandoto za abunuwasi?. Daniel kukuoa wewe ni sawa na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano. Fikiria miezi mingapi sasa imepita? Je, alishawahi hata kukupigia simu kukujulia hali? Ama ulishawahi hata kuongelea suala la uchumba wenu? Pevuka Walemi, Dar es salaam kuna wanawake wazuri sana, wenye ngozi nadhifu na wanaojua kuvaa lakini pia wanye pesa zao. Kwahiyo usishangae siku Daniel huyo unayemtegemea akija kumtambulisha mkewe kwa wazazi wake. Hapo utakuwa na lipi la kusema na magaga yako, ngozi imekupauka kama ganda la muhogo wakati huo huo wanaume uliowakataa nao sasa watakuona takataka. Sijui utakuwa mgeni wa nani hapa kijijini.. ". Maneno hayo Walemi akiyakumbuka,maneno aliyowahi kuongea na rafiki yake wa karibu sana aliyeitwa Angel. Machozi yakiendelea kumtoka alimgeukia Daniel na kisha akaumuuliza. "Au haukuwa na mpango na mimi?.. "
" Hapana sio hivyo Walemi ila nadhani kila kitu nimeshajieleza, na vile vile tayari nimekuomba msamaha. Nisamehe Walemi, pia ikiwezekana tuwe kama zamani, nipo chini ya miguu yako tafadhali" Alijibu hivyo Daniel na punde akapiga magoti chini kuendelea kuomba msamaha,Walemi alimuinua akamuhakikishia kuwa kamsamehe,jambo ambalo liliwafanya wawili hao kukumbatiana huku mabusu moto moto yakichukua nafasi. Siku hiyo hakuna kilichofanyika japo Walemi aliondoka gheto jioni sana.
" Walemi?.. "
"Abee Daniel.."
"Hivi kweli umenisamehe?.."
"Ndio Daniel, kwani vipi huamini?.."
"Laah! Sio kwamba siamini ila nataka nihakikishe"
"Ndio nimekusamehe, tena kuwa huru kabisa ndani ya moyo wako. Halafu istoshe nimekukumbuka kiutu uzima, hivyo jiandae siku yoyote nitakupa taarifa ili nije unigalagaze. Tukumbushie enzi! Ama hupendi?.."
"Ahahaha hahaha" Daniel aliangua kicheko, alifurahishwa na maneno ya Walemi wakati huo akimtazama maumbile yake jinsi Walemi alivyojazia vile vile akionekana kuwa na ngozi nyororo isiyo na mfano kisha akajibu "Nataka sana, kwanini nisitake? Wakati wewe ndio nyongo mkalia ini!!?"
"Basi jiandae. Nakupenda sana Dani wangu" Aliongezea kusema Walemi safari hiyo akifungua pochi yake, alitoa kiasi cha pesa shillingi laki tatu akampatia Daniel halafu akaongeza kusema "Nusu ya kwako mwenyewe na hiyo nyingine utajua namna ya kumpoza bosi wako"
"Walemi! Pesa yote hii ya kwangu?" Aliuliza Daniel kwa taharuki ya hali ya juu. Walemi alicheka kidogo kisha akajibu "Yeah,mbona ndogo sana? Usijali bwana Daniel vitu vidogo hivyo"
"Loh! Asante sana Walemi" Alishukuru Daniel huku akizitazama mara mbili pesa alizopewa na Walemi ilihali muda huo Walemi alifungua mlango wa gari yake akaingia ndani kisha akaliwasha akaondoka zake huku kando watu wa uswahilini wakiishia kulitazama gari hilo la ghalama lililofika uswazi, kwani ni nadra sana gari la kifahari la namna hiyo kutinga maeneo ya uswahilini.
********http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku wa siku hiyo Walemi alilala kwa furaha kabisa, kila alipojaribu kufumba macho yake alihisi kumuona Daniel . Alijipindua kitandani huku na kule mfano wa chatu amezapo windo lake, hiyo yote ikiwa ni furaha bashasha iliyotawala moyoni mwake.
" Walemi?.. "
"Abee Lameki.."
"Hivi kweli umenisamehe?.."
"Ndio Dani, kwani vipi huamini?.."
"Laah! Sio kwamba siamini ila nataka nihakikishe"
"Ndio nimekusamehe, tena kuwa huru kabisa ndani ya moyo wako.Halafu istoshe nimekukumbuka kiutu uzima, hivyo jiandae siku yoyote nitakupa taarifa ili nije unigalagaze. Tukumbushie enzi! Ama hupendi?.."
"Ahahaha hahaha! Nataka sana, kwanini nisitake? Wakati wewe ndio nyongo mkalia ini" Walemi aliyakumbuka maneno hayo aliyokuwa aliyaongea na Daniel. Hakika ni maneno ambayo yalimfanya muda wote kinywa chake kutasamu.
Siku zilisonga, ukaribu wa Walemi na Daniel ukashika kasi. Na wala Walemi hakumwambia ukweli kama tayari anamahusiano na mtu mwingine,hata pindi Daniel alipomuuliza suala hilo aliishia kudanganywa tu ili aendelee kuwa naye mwanaume wa ndoto yake. Daniel naye alikubalina na uongo huo Walemi pasipo kujua kuwa anadanganywa. Siku kadhaa mbele, Walemi alimpigia simu Daniel. Ilikuwa jioni sana yapata saa kumi na mbili,muda huo Daniel alikuwa katika mihangaiko yake ya kila siku.
"Hellooo Daniiii!.." Alisikika akisema Walemi kwa sauti ya kudeka.
"Mmh habari yako mpenzi" Alidakia Daniel kwa sauti ya juu wakati kabisa huku kwa mbali zikisikika sauti za magari na honi. Walemi akaongeza kusema.
"Nzuri tu mpenzi wangu, bado hujatoka kazini?.."
"Aah! Ndio ndio" Dani alijibu.
"Jamani pole Dani wangu. Lakini usijali leo ndio siku yenyewe,nitakuja kulala huko huko sawa mpenzi ili nikuondoe uchovu wako sawa!?.. "
"Ahahahhahaha Walemi bwana! Sawa mapenzi, basi nikitoka nitakupigia simu. Nikishaweka mazingira safi gheto" Alisema Daniel akianza kwa kaungua kicheko.
"Sawa mpenzi wangu" Kwisha kukubaliana hayo alikata simu kisha punde akampigia rafiki yake anayealala naye ghetto.
"Ahahah. Sawa bro usiwaze kuhusu hilo. Unajua inabidi umkande vizuri ili asizidi kukusahau bwana" Alitania rafiki yake Daniel, ni baada Dani kumpasha kuhusu ujio wa Walemi.
Muda muafaka ulipotimia, wawili hao walikutana. Siku hiyo wakaifanya siku ya furaha kwao kwa kula na kunywa kisha wakaenda kupumzika. Lakini wakati wapo kitandani, kabla hawajafanya kitendo chochote ghafla simu ya Walemi ikaita. Namba iliyompigia ilihifadhiwa jina (My love Ambrosy)
"Huyu ni nani?.." Aling'aka Daniel mara baada kuona jina hilo. Walemi alitabasamu kisha akasema "Usiwe na pupa mpenzi wangu, huyu alikuwa mpenzi wangu wa zamani sana. Nashangaa leo kanitafuta wakati nimeshamuonya."
"Walemi. Hivi unanichukuliaje mimi? Naomba useme ukweli Ambrosy ndio nani?.." Alizidi kusisitiza Daniel kitendo ambacho kiliweza kuzua tafarahi ilihali simu ikiita mara mbili mbili, na mwisho wa mzozo Walemi akasema "Huyu alikuwa mpenzi wangu zamaani sana,ili uamini kuwa simtaki pia ananikera ngoja nikite" Walemi alipokwisha kusema hivyo akakata simu kisha akaizima na mara moja akamkumatia Daniel tayari kwa tendo..
Walemi na Daniel walifurahia tendo siku hiyo,hakika ilikuwa siku ya furaha sana kwao kwani walikumbushia mambo waliyokuwa wakiyafanya miaka kadhaa nyuma kipindi wapo Dodoma.
Kesho yake asubuhi Walemi alimuaga Daniel kisha akaondoka zake huku nyuma akimuachia kiasi kadhaa cha pesa ya matumizi, Daniel alishukuru sana.
Alipofika nyumbani alimkuta Siwema yupo sebuleni, siku hiyo hakwenda kazini. "Habari yako dada yangu" Walemi alimsalimu Siwema. Siwema alistuka akamtazama kisha akamuuliza mahali alipotoka na ni sababu ipi iliyomfanya asilale nyumbani "Nililala kwa rafiki yangu, shaka ondoa" Alijibu Walemi wakati huo akiambaa na njia ya kuelekea chumbani.
"Walemi acha kuwa muongo mdogo wangu? Kama ulilala kwa rafiki yako iweje uzime simu?.." Aliongezea kusema Siwema kwa sauti ya ukali kabisa. Lakini sauti hiyo katu haikuweza kumfanya Walemi kuwa chini, zaidi naye alisema "Kama hutaki kuamini ninacho kwambia basi, sababu siwezi kukulazimisha ukukubali"
"Khe! Walemi? Leo hii unanijibu mimi hivyo?.." Siwema kwa sauti ya upole iliyojaa taharuki alisema hivyo. Hapo Walemi hakuongeza neno Lolote, alifunga mlango wa chumba chake kisha akajilaza kitandani huku sebuleni akimuacha Siwema akiwa na sintofahamu.
Tabia ya Walemi sasa ilianza kubadirika, kila mwisho wa wiki alikuwa akikutana na Daniel ambapo walitumia pesa kwa fujo huku wakionyeshana mapenzi mubashara. Hali hiyo ilimpelekea Walemi kujisahau, alizama katika penzi la Daniel akaliweka kando penzi la Ambrosy. Wala hakukumbuka hata mara moja kumtafuta Ambrosy, bali alimtafuta pindi anapokuwa na shida kama ya pesa.
Ni kitendo ambacho kilimtia hofu Ambrosy, na siku moja alimuita ili aweze kuzungumza naye ajue ni kitu gani hasa kinacho msibu Walemi mpaka kumpelekee kuwa kimya mara kwa mara.
"Walemi my Dear! Nimekuita ili nijue ni nini hasa kinacho kusibu, sababu umekuwa tofauti kabisa na zamani. Simu hunipigii mpaka nikupgie mimi, hata nikikupigia tuanongea muda mchache sana unadai uko bize aidha mara nyingine unaamua kunikatia bila sababu.. Hivyo leo nataka tatizo hili tulimalize ili tuwe kama zamani, nakupenda sana Walemi kwahiyo sipendi ukose raha katika maisha yako"Yalikuwa maneno ya Ambrosy aliyokuwa akiyaongea mbele ya Walemi wakati huo wako kwenye moja ya kumbi ya starehe huku maongezi hayo yakisindikizwa na vinywaji baridi. Walemi aliposikia maneno hayo alishusha pumzi kidogo kisha akajibu" Ni kweli Ambrosy, lakini hapa katikati kuna mambo mabaya niliyoyasikia nyumbani huko kijijini, kiukweli ni mambo ambayo yalinifanya niwaze sana ila kwa sasa nipo free, kwahiyo muda wowote nitakapo kuwa na nafasi ukinihitaji nitafika "Alidanganya Walemi ingawa ni maneno ambayo yilimfanya Ambrosy kuachia tabasamu,na punde akaongeza kusema" Kwanini hukuniambia? Ama hujui kama tatizo lako ndio tatizo langu?.. "
" Hapana ila sio mbaya, uje Ambrosy nakupenda sana kwahiyo sitaki nikupe mzigo mkubwa wakati unamikakati mingi ya kufanya "Alijibu Walemi. Wawili hao walifikia muafaka, Ambrosy aliamini Walemi bado anamuwaza akilini mwake ilihali Walemi yeye akimfikiria sana Daniel kuliko anavyojidhania Ambrosy. Hayo yote ikiwa ni matakwa ya moyo, kwani licha ya Ambrosy kuwa na pesa ila Walemi hakusita kumpenda mwanaume anayeishi moyoni mwake ambaye ni Daniel. Mjasiri haachi asiri, ndivyo ilivyokuwa kwa Walemi. Alizarau upendo wa Ambrosy mwanaume aliyemjali na kumthamini, upendo wa dhati akaelekezea kwa Daniel mwanaume ambaye alianza naye mahusiano muda mrefu kabla hawajapotezana.
Hali hiyo ilikuwa endelevu, lakini baada wiki kadhaa kupita tangu Ambrosy akae kitako na Walemi, hatimaye siku moja Siwema naye anapata kumkalisha Walemi kitako.
Siwema alisema "Walemi, kwanini unazidi kubadirika siku baada ya siku? Sio vizuri mdogo wangu, hebu kumbuka maisha ya nyuma kwanza nafikiri utapata somo kuwa unachokifanya sio kitu kizuri"
"Dada umekuwa muongeaji sana siku hizi, sijui kwanini?.." Alijibu Walemi kwa sauti ya nyodo, jibu ambalo lilimshangaza Siwema wakati huo huo Ambrosy aliingia ndani. Kwa mwendo wa madaha huku mkononi akiwa na bakora ya ghalama aliyokuwa akitembea nayo aliketi kwenye sofa kisha akasema" Habari zenu?.. "
" Salama tu Ambrosy karibu "Alijibu Siwema kwa sauti ya upole iliyojaa taharuki ndani yake. Muda huo Walemi uso wake ulionyesha haibu, ambayo ilimpelekea kuinamisha uso wake na hata asimtazame Ambrosy.
" Walemi! Ni kipi ulichokosa kwangu?.. Ujue Walemi wa sasa sio yule aliyekuwa mama ntilie miaka kadhaa nyuma wala sio Walemi yule ambaye alikuwa akizurumiwa pesa na wateja wake. Na sio Walemi yule aliyekuoa akivaa nguo moja elimu ya darasa la saba. Yani Walemi umebadilika sana, kwanini lakini? Nimejitahidi kukupa kila kinacho stahili lakini bado tu hujalizika nikufanyie nini we mwanamke wa kigogo?.."Kwa uchungu na hisia kali Ambrosy aliongea hivyo. Kisha akatulia wakati huo huo akimtazama Walemi ambaye naye alikuwa bado amejiinamia akiona haya. Ambrosy alikohoa kidogo,safari hiyo alimgeukia Siwema kisha akamwambia
" Siwema, ukweli nilimpenda sana mdogo wako. Bila shaka hata wewe unajua lakini kumbe mimi nilipenda sehemu nisiyopendwa. Na kwakua mimi sio chaguo lake acha nikae kando ili nimuache na mwanaume anayempenda. Moyo wangu jiwe, kila kitu niwaachia lakini ninacho kitaka kutoka kwa Walemi ni kitu kimoja.. Sitaki anipigie simu wala kunifuata" Siwema alishtuka ukiachilia mbali Walemi ambaye naye alishtuka baada kusikia uamuzi huo wa Ambrosy. Hapo Siwema alipiga magoti kumuombea msamaha Walemi, lakini Ambrosy muda huo alikuwa amefura hasira hivyo alinyanyuka akaondoka zake wakati huo akiacha bahasha kubwa ya kaki kwenye sofa. Siwema alilalama akimlaumu Walemi, ajabu Walemi alionyesha kutoshtushwa wala kujali lawama za Siwema. Zaidi alinyanyuka akaelekea chumbani kwake ambapo huko alijitupa kitandani kisha akachukua simu yake akatafuta namba ya mpenzi wake ampendaye, si mwingine ni Daniel. Wakati wawili hao wakiongea kwa njia ya simu, huku nyuma sebuleni Siwema aliifungua bahasha ile aliyoiacha Ambrosy, hatimaye aliifungua ili ajue ndani kuna nini.
"Mungu wangu!.." Alishtuka Siwema, asiamini kile alicho kiona. Ni picha za Walemi akiwa na Daniel katika moja ya kumbi ya starehe. Wapenzi hao walipigwa picha pasipo wao kujua huku wakiwa wamekumbatiana. Siwema alishangaa sana ila hakuwa na lakufanya zaidi alinyoosha mikono juu akimuacha Mungu kwani alifahamu fika Walemi tayari kabadilika.
NI habari mpya na zakushangaza pia pindi Walemi alipowaeleza marafiki zake kuwa ameachana na Ambrosy,hakika walimcheka sana na kumuona mjinga maradufu.
"Walemi unawezaje kupiga teke fuko la hela? Hivi unataka kusema kuwa umeshindwa kukaa na wote wawili?" Alisikika akisema hivyo moja ya rafiki yake wakati huo wakiwa kwenye kumbi ya starehe. "Unamaana gani?.." Aliuliza Walemi huku akionyesha kushangazwa na maneno ya rafiki yake.
"Wewe ni mkubwa Walemi, nashangaa umekosaje akili ya kula na kipofu. Ulicho kisahau ni kitu kimoja tu. Ulishindwa kupima mzani ulizidisha sana kilo upande mmoja.." Alijibu rafiki yake wa pili. Lakini bado Walemi alikuwa hajaelewa, hivyo alirudia kuuliza "Kwahiyo nifanye nini.." Hapo kimya kilitawla kidogo, ila punde si punde mmoja wao alisema, kwa sauti ya kilevi kabisa. "Wewe unachotakiwa kwa sasa rudisha makucha ndani, hima mrudie Ambrosy muombe msamaha najua atakisamehe, wanaume kwetu ni dhaifu sana hata awe gaidi kiasi gani. Akisha kusamehe sasa ndipo hapo utatakiwa kuishi naye kwa lengo moja sababu moyo wako unanafasi ya mtu mmoja tu ambaye ni Daniel..."
"Lengo? Lengo lipi hilo?.." Alirudi kuhoji kwa mara nyingine tena Walemi. Rafiki yake huyo alikunywa bunda moja ya bia kisha akaongeza kusema "Muue Ambrosy ili ubaki na kipenzi cha moyo wako. Najua kampuni zake zote zitakuwa chini yako, kwahiyo pesa zote na mali zake nyingiinezo zitakuwa chini yako. Hapo utafurahia maisha ya Daniel wakati huo tayari Ambrosy katangulia mbele ya haki. Acha ujinga we mgogo mrudie Ambrosy ukamilishe kazi "
Akili za kuambiwa changanya na zako,Walemi alikujikuta akishindwa kuufanyia kazi msimo huo. Pasipo kufikiria alifanya kama alivyoshauriwa, hivyo alimtafuta Ambrosy kwa njia ya simu na kisha kumuomba radhi huku akitokwa na machozi.
Siku hiyo ilikuwa jioni sana, yapata saa kumi na moja Ambrosy akiwa njiani akielekea Airport ili asafiri kwenda Africa kusini, ghafla simu yake ya mkononi iliita. Haraka sana aliingiza mkono mfukoni akachomoa, alishtuka kuona namba ya Walemi "Mmh!.." Aliguna kidogo kisha akabonyeza kitufe cha kijani akaweka simu sikioni.
"Hello Ambrosy" Ilisikika sauti ya Walemi ikisema hivyo, ni sauti ambayo aliitoka kwa kilio kitendo ambacho kilimfanya Ambrosy kushtuka. "Mmh habari yako?.." Alijibu Ambrosy kwa sauti ya chini kabisa. Hapo Walemi alikaa kimya kidogo halafu akaongeza kusema "Najua ni jinsi gani nilivyokukosea Ambrosy, hakika najutia makosa yangu. Nahisi sasa dunia kuiona chungu na kuilaumu nafsi yangu.. Ambrosy wewe ndiye mwanaume uliyenijali kwa hali na mali hivyo kukukosea kwangu naona ni dhambi kubwa ambayo inanitesa kila siku. Nimeamua kukupigia ili nikuombe msamaha, kwani najua msamaha wako utaweza kuniweka pema huko ninakoelekea. Nakupenda sana Ambrosy nisamehe sana "Walemi alipokwisha kusema hayo alikata simu. Ambrosy alishtushwa na maneno hayo, alijua dhahili shahili Walemi anataka kujiua. Hivyo alimtaka dereva wake asimamishe gari haraka sana na wageuze kurudi nyumbani. Na wakiwa njiani kwa mara nyingine tena siku ya Ambrosy iliita, safari hiyo aliyempigia ni Siwema. Ambrosy alipokea, Siwema akasema "Ambrosy tafadhali njoo nyumbani nakuomba sana"
"Sawa nakuja" Alijibu Ambrosy wakati huo huo akampasa dereva wake aongeze kasi kidogo.
Muda wa lisaali moja Ambrosy alifika nyumbani hapo alipokuwa akiishi Siwema na Walemi, ndipo alipowapangishia mara baada kuanza uhusiano na Walemi binti ambaye hapo awali alikuwa mama ntilie.
"Haya niambie kuna tatizo gani? Na Walemi yuko wapi?.." Aliuliza Ambrosy kwa sauti ya juu huku akihema haraka haraka.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Yupo ndani, sijui ametoka wapi nimeshtukia tu ananipita hapa sebuleni bila hata kunisalimia moja kwa moja akaingia chumbani kwake akajifungia mlango" Alijibu Siwema. Ambrosy alishusha pumzi ndefu kisha akazipiga hatua kuusogelea mlango wa chumba cha Walemi ambapo alipo ukaribia aligonga wakati huo akimtaka Walemi afungue mlango. Ujio wa Ambrosy ulimfanya Walemi kujiweka katika hali ya huzuni na majonzi, akiwa kitandani alinyanyuka akafungua mlango kisha akarudi kujitupa kitandani ilihali muda huo Ambrosy alimfuata.
"Walemi kwanini unakuwa hivyo? Wewe utabaki kuwa mwanamke wa moyo wangu ila niliamua kuchukuwa ule uamuzi ili uone msimamo wangu..." Aliongea Ambrosy. Ni maneno ambayo yalimfanya Walemi kujinyanyua kitandani, akamtazama Ambrosy na punde si punde machozi yakamtoka. Machozi ambayo Ambrosy aliyafuta kisha maongezi mengineyo yakachukuwa nafasi ikiwa tayari muunganiko wa pande zote mbili ukiwa umerudiana.
Naam! Jambo usilo lijua ni sawa na usiku wa giza. Na zimwi likujualo halikuli ukakwishwa, Ambrosy anajikuta akimpa nafasi Walemi kwa mara nyingine tena katika maisha yake, hakika kijana huyo alionyesha kuwa na mapenzi ya dhati kwa Walemi hali ya kuwa Walemi asimpende hata lepe. Furaha isiyo kifani ilitawala moyoni mwa Walemi, haraka sana alikutana na marafiki zake tena. Aliwaeleza kuwa amefanikisha kumrudusha Ambrosy, habari ambayo iliwafanya wote kwa pamoja kufurahia jambo hilo, hivyo walikunywa na kula siku hiyo.
"Walemi wewe ni mwanamke wa shoka" Alisifu mmoja ya rafiki yake. Mwingine naye aliongeza kusema "Ulicho kifanya ni kitu kizuri sana, kwahiyo umebakisha kitu kimoja tu.. Kumuondoa duniani ili mirathi yote iwe chini yako uweze kufurahi maisha ya kipenzi cha roho yako"
"Mmh ni kweli lakini yataka moyo" Alijibu Walemi. Jibu hilo liliwashangaza sana rafiki zake, wote kwa pamoja waliangua vicheko kisha mmoja akasema "Walemi, hivi ushamba wa Dodoma bado tu haujatkutoka? Kaa utambue mwanaume ni kiumbe wa ajabu sana sababu amepewa tamaa. Huko mtaani anaweza kukutana na mwanamke mzuri kuliko hata wewe akampenda halafu wewe ukaachwa. Shosti akili kichwani mwako utakuja kujuta hapo baadaye "
" Mmmh "Aliguna Walemi mara baada kuyasikia maneno hayo. Punde mwingine alisema." Kabisa, acha ujinga chukuwa maamuzi magumu. Hivi unafikiri hawa wanawake wanaomiliki gari za bei ghali hapa mjini ni kwa nguvu zao? La hasha wengine walipata bahati kama yako na hawakuweza kuichezea,sasa wewe unapata bahati hiyo unaichezea shauri yako utarudi kijijini kulima " Walemi alizidi kujazwa maneno rukuki, lakini mwishowe wa yote aliomba akafikirie kwanza ndipo atatoa jibu kamili.
NI jambo ambalo lilimkosesha usingizi, alilala akilifikiria suala hilo la kumuua Ambrosy ili apate kumiliki mali alizo nazo. Walemi hakuishia hapo tu alikumbuka pia maisha ya kijijini, akarudi pia kukumbuka tabu alizopata kwa mara ya kwanza alipofika jiji Dar es salaam, akachekecha mawazo yake akifikiria pindi Ambrosy atakapo mbwaga na kumpokonya kile alicho mpa. Hapo pumzi alishusha baada kujenga picha kichwani mwake kisha akajisemea "Huu ni wakati wa kufanya maamuzi yaliyo sahihi. Lakini itawezekana vipi kurithi mali zake ilihali mimi bado mchumba na sio mkewe?.." Swali hilo lilimtatiza sana, ndipo kwa mara ya tatu akakutana na marafiki zake na kisha kuwaeleza jambo hilo. Mmoja alisema" Unachotakiwa ni wewe kufunga naye ndoa na sio kitu kingine "
" Wazo nzuri sana "Wengine waliunga mkono. Hatimaye habari hiyo inapata kumfikia Ambrosy, hakika alifurahi sana na hapo ndipo alipoamini kuwa Walemi kabadirika kajifunza kutokana na makosa yake. Hima wawili hao walitangaza ndoa, ndugu jamaa na marafiki walihudhulia sherehe hiyo ambayo iliendeshwa kifahari sababu ya pesa alizokuwa nazo Ambrosy. Watu walikula na kunywa mpaka kusaza huku Siwema akimpa hongera Walemi kwa kufanikiwa kufunga ndoa na Ambrosy ilihali Walemi yeye lake akiwa nalo rohoni.
******BAADA YA MWEZI MMOJA *****
Ndoa iliendelea kudumu kwa furaha na mapenzi moto moto, kila mmoja alieleza malengo yake juu ya maisha ya kuishi ya mke na mume. Ambrosy alienda mbali kumtaka mkewe kuwa siku moja wafunge safari kwende Dodoma kuwasalimu ndugu na jamaa zao lakini pia ikiwa kama nafasi ya kujitambulisha mbele ya wazazi wake. Walemi alicheka kidogo kisha akasema "Wazo lako wala sio baya mume wangu, lakini pia mbali na hilo mimi nina jambo nataka nikueleze"
"Jambo gani? Wala usiwe na hofu niambie tu" Alijibu Ambrosy, muda huo ilikuwa asubuhi sana alikuwa akijiandaa kwa safari ya kuelekea Canada katika biashara zake. Walemi baada kupewa nafasi ya kuzungumza alishusha pumzi kwanza kisha akasema "Tangu mimi na wewe tuanze kuwa wapenzi hatujawahi hata siku moja kufanya mapenzi, muda wote upo bize kwanini lakini?.."
"Ahahah ah hahaha" Alicheka Ambrosy, akamtazama Walemi na kisha kujibu "Nilikuheshimu sana, sikuwa tayari kufanya mapenzi kabla hujawa mke wangu halali. Pia mbali na hilo mwezi sasa umekatika tangu tufunge ndoa, ila kama unavyoona mwezi huu wote nipo bize kufuatilia vibali vya biashara yangu. Kwahiyo kuwa mvumilivu, nikirejea kutoka Canada itakuwa siku ambayo mimi na wewe tu na sio kazi tena.. Nakupenda sana mke wangu "Alimaliza kwa kicheko Ambrosy kisha akaagana na mkewe akaondoka zake.
Safari sio kifo, ndivyo ilivyokuwa kwa Ambrosy ila urejeo wake ndio ukawa kifo sababu usiku huo huo aliporudi ndio siku ambayo Walemi alikamilisha azma yake. Alithubutu kumuua Ambrosy kwa kumuweka sumu kwenye chakula. Taharuki kubwa ilizuka moyoni mwake, hofu ilimjaa baada kufanya kitendo hicho, lakini yote kwa yote ilishatokea na mirathi yote akarithi yeye kama mke halali wa marehemu Ambrosy. Na kibaya zaidi Ambrosy hakuwa na wigo mkubwa wa ndugu, vile vile hata hao wachache nao walikuwa na uwezo wa kifedha. Na wengi wao waliishi nje ya nchi. Wapo waliokuwa wakiishi Marekani, India, Dubai na Uingereza. Labda laiti wazazi wake wangelikuwa hai, lakini wote walishatangulia mbele ya haki. Hivyo basi mali zote zikawa chini ya Walemi.
Msiba ulipo malizika, Daniel na Walemi wakapata nafasi ya kuishi kama mke na mume ndani ya jengo la kifahari alilokuwa akiishi Tajiri Ambrosy. Suala hilo liliweza kuzua taharuki kwa baadhi ya rafiki na jamaa wa karibu wa marehemu Ambrosy, baadhi waliamini Walemi kamuua makusudi lakini pia wengine walibaki kujua ni mipango ya Mungu lakini yote kwa yote Walemi hakujali zaidi ya kummilikisha mali zote Daniel
"Walemi! Wataka kuniambia mali zote hizi ziwe chini yangu?.." Aliuliza Daniel asiamini kile anachokiona.
"Ndio Dani kwani tatizo liko wapi? Siku zote waswahili husema cheka na watu uvae viatu Daniel". Alisema Walemi. Maneno ambayo yalimchanganya Daniel ambapo alihoji "Unamaana gani?.."
"Maana yangu ni kwamba,mama ambaye nilikuwa naishi naye siku zooote alikuwa ni raia wa Africa kusini ila alikuwa hapa nchini kwa ajili ya biashara zake. Kwahiyo mwishowe ameamua kurudi nchini kwao ameniachia vitu vyote hivi kwa sababu nilikuwa naishi nae vizur sana "Alidanganya Walemi. Daniel alikubaliana na maneno hayo. Hapo sasa maisha yakawa raha mstarehe kati yao.
Maisha yalisonga. Miaka miwili sasa ikakatika tangu kifo cha Ambrosy,penzi la Walemi na Daniel lilizidi kunoga ipasavyo. Daniel akawa mtanashati kijana nadhifu mwenye haiba ya kuvutia. Alithubutu kuwapandishia vioo waliokuwa watembeza biashara wenzake barabani,wala hakuweza kukumbuka asili yake maisha ya uswahili. Lakini wakati hayo yakiendelea kwa Daniel, kwingeneko mambo yalikuwa tofauti kwa Walemi. Hofu dhufo lihali ilimjaa baada siku moja kwenda kuudhuru kaburi la Ambrosy na kukuta upande mmoja umefukuliwa huku kwenye msalaba yakionekana maandishi yaliyoandikwa The return of the Ambrosy! Maandishi hayo yaliandikwa kwa damu..
Lilikuwa jambo la kushangaza sana,Walemi alishangazwa na kitendo kile cha kufukuliwa kaburi la Ambrosy. Lakini baadaye jambo hilo alilichukulia kawaida, hivyo ikabaki siri yake juu ya tukio hilo.
*********
Naam! Yote hiyo ilikuwa kumbukumbu iliyokuwa ikizunguka kichwani kwa Walemi. Awali baada kukuta kaburi limefukuliwa upande mmoja alichukulia kawaida lakini baada kumtokea ndipo alipoamini kuwa Ambrosy karejea. Pumzi alishusha Walemi baada kuyakumbuka matukio hayo tofauti tofauti aliyokumbana nayo mpaka pale alipofikia hatua ya kumuua Ambrosy. Kutoroka kijijini akikimbia ndoa ya kulazimishwa. Kunusurukia kutolewa sehemu ya siri baada kukutana na mtu ambaye alidai kumsaidia. Pia mbali na hilo, vile vile tukio la kumuua dalali aliyemlaghai kingono akidai kuwa atamtafutia kazi. Kwa mara nyingine tena Walemi alishusha pumzi ndefu huku hofu dhufo lihali ikizidi kumjaa. Muda huo huo Daniel alitoka ndani pale sebuleni alipokuwa ameketi akipata kifungua kinywa, aliamua kumfuata nje mkewe na alipomkaribia akasema "Unajua Walemi suala hili linaniumiza sana kichwa. Mwanzo sikutaka kuamini lakini kwa sasa ndio naanza kuamini. Wewe ni mshenzi na pia ni muongo sana. .." Maneno hayo Daniel aliyesema huku akionekana kukasirika. Walemi alipoyasikia alimgeukia akahoji ." Dani unamaana gani?.. "
" Maana yangu ni kuwa wewe ndiye uliyemuua huyu Ambrosy. Na ndio maana kuna kipindi enzi ya uhai wake aliwahi kunionya juu yako "Daniel alijibu.
"Kaa kimya Daniel. Pumbavu mkubwa wewe. Huwezi kuropoka maneno hayo mbele yangu Dani. Wewe ni kapuku huna mbele wala nyuma, niliamua kufanya hivi ili tutimize ndoto zetu za Kuja kuwa mke na mume. Je, ni ngejali pesa leo hii Dani ungekuwa na mimi? Hata siku moja isingetokea wewe kutembelea gari ya ghalama aidha kuishi katika jumba hili. Nimefanya hivi sababu ya upendo wangu kwako, leo hii unaongea pumba? Mjinga sana wewe " Walemi aliongea maneno hayo kwa sauti ya juu kabisa. Maneno ambayo yalimchoma Daniel akawaza na kuwazua akaona kweli Walemi amempenda na hivyo hapaswi kumuumiza kwa lolote kwa chochote kwani pasipo binti huyo asingeheshimka mtaani. Daniel baada kuona jambo hilo alilofanya Walemi ni sahihi, hatimaye alijishusha akamuomba msamaha vile vile akaahidi kulikabili kwa vyovyote vile ilimladi kumtokomeza marehemu Ambrosy.
" Katika maisha yangu sijawahi kuona mtu aliyekufa akarejea tena Duniani, jambo hili ni jipya kwangu. Dan unadhani Ambrosy karudi na nia gani?.. " Alisema Walemi. Daniel alikaa kimya akitafakari. Baada ya kimya kifupi alisema "Ukistaajabu ya Musa utayaona ya filauni. Walemi, kwanza nashukuru kwa msamaha wako maana siku zote ulimi hauna mfupi, kwa hiyo niliteleza tu kidogo ikapelekea kuongea maneno yale. Lakini mbali na hilo nikwambie kitu..." Kabla Daniel hajaendelea kusema alichotaka kumwambia mkewe ghafla simu yake ya mkononi iliita. Daniel alipokea, ikasikika sauti ikisema" Hello bosi, maduka yako matatu yanateketea kwa moto hivi sasa. Na chanzo cha moto hakijurikani"
"Unasema?.." Alishtuka Daniel vile vile Walemi naye akishangazwa na mshtuko wa mumewe. Hata alipokata simu alimuuliza kipi kimetokea? Daniel akajibu "Nimepigiwa simu hapa, naambiwa maduka yetu matatu yanateketea kwa moto muda huu"
"Eenh Mungu wangu" Alisikitika Walemi, aliona tayari muda wa kuishi kwa tabu umewadia, pole pole akajikuta akijutia uamuzi aliochukua kwani alijua tayari maisha ya umasikini hayapo mbali yake. Kupitia hilo ikabidi awatafute wale marafiki zake moja baada ya mwangine ili awaeleze kinacho endelea tangu ipite miaka kadhaa kifo cha Ambrosy,nia kubwa aombe ushauri kipi afanye kama hapo awali walivyomshauri mpaka kufikia hatua ya kumua Ambrosy. Mtu wa kwanza kumpigia alikuwa Penina, huyu ni moja ya watu waliomshawishi sana amuue Ambrosy "Hello Penina habari yako" Alisema Walemi kwa sauti ya upole iliyojaa huzuni ndani yake. Penina akajibu "Ni nzuri poleni maana nasikia mumeo alilazwa hospital baada kuanguka usiku"
"Ni kweli Penina ila mbali na hilo, kuna kitu nataka unishauri ama kama utaweza basi nisaidie" Aliongezea kusema Walemi, Penina bila kujua shida aliyonayo Walemi alijibu haraka haraka "Nitafute wiki ijayo, kwa sasa nipo ndani ya gari naelekea Airport nina safari ya kwenda Kenya" Penina alipokwisha kusema hivyo alikata simu. "Mmmh" Walemi aliguna kisha akajiuliza "Mbona hakutaka hata kunisikiliza? Au tayari anajua ujio wa Ambrosy?.." Alishusha pumzi ndefu Walemi wakati huo huo alimpigia mwingine ambaye aliitwa Dolin, ajabu Dolin alipopokea simu alisema "Afadhali uliponipigia Shoga yangu, kuna jipya! Usipostaajabu ya Musa utayaona ya filauni. Labda nikuulize kwanza swali, hivi unauhakika kabisa Ambrosy alikufa? Au huyu niliyekutana naye ni ni pacha wake?.."
"Kwanini unaniuliza hivyo Dolin?.."http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nataka kujibiwa, masuala kama haya sitaki kuhusishwa mimi simo na kuanzia sasa usinitafute" Dolin naye alipokwisha kusema hivyo alikata simu.
Hapo sasa Walemi anajikuta yupo katika wakati mgumu, wale marafiki waliomshauri leo hawaoni tena, anashindwa afanye nini. Hakika alilia sana. Muda huo huo alionekana Daniel akiwa amependeza tayari kwa safari ya kuelekea huko ulikozuka moto.
Kipindi hayo mambo yanapamba moto nyumbani kwa Walemi, upande wa p Dolin, moja ya marafiki zake Walemi akiwa bafuni alioga kisha akatoka. Lakini ghafla alisikia sauti ya mtu akicheka, Dolin alishtuka haraka sana akarudi nyuma kufungua mlango wa bafu ili atazame kuna nani bafuni. Hakuona mtu, na hivyo alizipiga hatua kuelekea chumbani kwake ambapo huko nako alikuta mambo ni tofauti kabisa. Alikuta kitanda kimetandikwa, vile vile alikuta chumba chake chote kikinukia marashi aliyokuwa akiyatumia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Mmh! Mbona sielewi? Haya mambo niyaajabu sana" Alijisemea Dolin wakati huo moyoni akiwa na hofu mwili wote ukimtetemeka, na hata asiamini kile anachokisikia wala kukiona. Hofu ikiwa bado imeshika kasi moyoni mwake, aliendelea kujifuta maji na taulo lake , punde si punde humo chumbani kwake alihisi kuna mtu anatembea. Ghafla alipotazama sakafu aliona nyao za damu zikisogea mahali alipokuwa amesimama! Dolin aliogopa, hima alirudi nyuma muda huo huo akasema "Ushindwe kwa jina la yesu" AJABU baada Dolin kukemea. Sauti nyingine ambayo ilifanana na sauti yake Ilisikika ikisema "Return of the Ambrosy". Hapo Dolin alishtuka wakati huo huo alitokea mwanamke aliyefanana naye kila kitu mwanamke huyo alikuwa amevaa nguo ambazo Dolin alikuwa amepanga kuzivaa jioni hiyo!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment