Simulizi : Nilivyokutana Na Mzimu Facebook
Sehemu Ya Tatu (3)
“Naitwa Abdul,” nilijitambulisha huku nikimpa mkono mmiliki wa fremu hiyo, alikuwa ni mwanaume na alionekana kuwa mzee wa makamo.
“Ooh! Nafurahi kukufahamu kijana,” aliniambia huku akinitazama, nilipouangalia uso wake ulionyesha wazi kwamba hakuamini kama ningeweza kuipangisha fremu yake, yaani hakuwa na imani na mimi hata kidogo.
“Nashukuru mzee,” nilimwambia huku nikiachia tabasamu pana.
“Naitwa Mzee Akilimali,” alijitambulisha.
“Sawa mzee,” nilimwambia kisha nikamuona akivuta pumzi ndefu na kuziachia kwa pupa. Akatulia kwa muda wa sekunde kadhaa huku akionyesha kutafakari jambo fulani.
“Kwahiyo kijana unataka kupangisha fremu yangu?” aliniuliza baada ya kupita sekunde kadhaa, ni kama vile alikurupuka na kusahau kwamba hapo awali dalali Macho alikwisha kumueleza kila kitu kuhusu mimi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndiyo mzee nahitaji tena haraka iwezekanavyo,” nilimwambia kwa ujasiri mkubwa maneno yaliyozidi kumfanya mzee Akilimali azidi kunishangaa, macho yalikuwa yamemtoka, hakuamini hata kidogo.
“Kijana upo serious kweli kwamba unataka kupangisha fremu?” aliniuliza.
“Ndiyo mbona kama huniamini mzee?”
“Hapana sio kwamba sikuamini ila nyie vijana wa siku hizi mnasumbua sana, leo unaweza kusema unataka fremu halafu kesho mara umeghairi ndiyo maana nakuuliza mara mbilimbili ili tusije tukasumbuana baadaye maana mimi mambo ya uswahili siyawezi kabisa.”
“Hahaha! Mzee niamini bhana nataka kupangisha kweli hiyo fremu ila pia kama unaiuza niambie tuongee niinunue kabisa iwe yangu.”
“Kuuza hapana, Macho kwani hukumwambia kila kitu?” aliniambia kisha akamuuliza swali dalali Macho ambaye kwa muda wote huo wa mazungumzo alikuwa kimya.
“Nilimwambia kila kitu lakini shida yake kubwa ilikuwa ni kukutana na wewe ana kwa ana na ndiyo maana nikaamua kumleta,” alijibu Macho.
“Sawa. Sasa kijana fremu yangu napangisha kwa laki tano kwa mwezi, upo tayari?”
“Ndiyo mzee nipo tayari.”
“Ok basi kama upo tayari itabidi nikuandalie mkataba.”
“Leo leo au?”
“Leo? Mbona una haraka sana?”
“Kwa sababu na shida mzee.”
“Wewe njoo kesho mkataba wako utakuwa tayari.”
“Nitashukuru sana mzee.”
“Sawa.”
Moyo wangu ulitawaliwa na furaha sana siku hiyo hasa baada ya kugundua kwamba hatimaye nilifanikiwa kupata fremu na muda huo kitu kilichokuwa kimebakia ni kupewa mkataba na kulipia kodi.
Siku hiyo ilipita, siku iliyofuata mapema sana nilienda nyumbani kwa mzee huyo ambapo nilikuta tayari ameshaniandalia mkataba wangu. Niliusoma kwa umakini na nilipomaliza nilitakiwa kuweka saini ili kuthibitisha.
Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, niliweka saini na kitu kilichokuwa kimebakia kilikuwa ni kulipia kodi ya miezi sita kama mkataba ulivyokuwa ukijieleza.
“Kwahiyo hiyo milioni tatu unalipa Cash ama benki?” aliniuliza mzee Akilimali.
“Nafikiri benki itakuwa sehemu salama zaidi mzee,” nilimjibu.
“Kweli kijana basi ngoja nikupe namba ya akaunti ili ukalipie,” aliniambia kisha akaniandika namba ya akaunti ambayo nilitakiwa kulipia hizo milioni tatu kama kodi ya miezi sita.
“Ahsante mzee nitafanya hivyo,” nilimwambia.
“Sawa kijana,” aliniambia.
Siku hiyo sikutaka kupoteza muda hata kidogo, nilipoondoka nyumbani kwa mzee huyo moja kwa moja nilienda mpaka benki ambapo nilitoa kiasi cha shilingi milioni tatu na kukilipia kwenye akaunti ya mzee Akilimali. Baada ya kumaliza kufanya muamala huo nilimjulisha na kuniambia kwamba kweli aliiona na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kumiliki fremu hiyo ambayo nilipanga kufanya biashara ya mgahawa.
***
Ukumbuke mpaka kufikia katika kipindi hicho nilikuwa nikifanya vitu kwa siri sana. Mjomba wangu hakufahamu kitu chochote kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia. Ilikuwa ni siri yangu pamoja na washikaji zangu ambao ndiyo walikuwa wakifahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yangu.
“Deal done washikaji,” nilisema huku nikiwatazama washikaji zangu ambao muda huo walionekana kutoamini kile nilichokuwa nikiwaambia.
“Hongera sana mzee baba,” aliniambia Deo.
“Ahsante.”
“Mzee baba hongera, kilichobaki ni kufanya vitu kwa vitendo sasa,” aliniambia Nickson.
“Yeah, hilo ndilo lililobaki.”
Nilikuwa nimedhamiria kufanya biashara katika maisha yangu. Katika kipindi cha muda mrefu nilikuwa nikiishi na wazo la kufanya biashara ya mgahawa bila kuamini kama kuna siku wazo hilo lingetimia na kuwa kweli.
Kuna muda sikutaka kuamini kwamba nilikuwa nimefanikiwa kutimiza wazo hilo lakini huo ndiyo ukweli ambao nilitakiwa kukubaliana nao tena kwa asilimia zote mia moja.
***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kupita siku kadhaa nilianza ukarabati katika fremu hiyo. Nilitaka kuibadilisha na kuifanya kuwa kama vile nilivyokuwa nikiiwaza kichwani. Nilipomuelezea fundi dhamira yangu alinielewa na hivyo kuikarabati na kuweka vile nilivyomwambia.
Niliweza kufanya kila kitu ndani ya muda kwa sababu nilikuwa na pesa za kutosha. Baada ya kupita wiki moja hatimaye nilifanikiwa kusimamisha biashara ya mgahawa ambapo niliajiri wafanyakazi watatu.
Ulikuwa ni mgahawa mzuri ambao niliufungua maeneo hayo ya Buza Kanisani. Ulimvutia kila mteja ambaye aliingia na kuhudumiwa.
Naweza kusema kwamba mgahawa wangu ndiyo ulionekana kuwa mgahawa tishio kwa migahawa mingine ambayo niliikuta.
“Huyu jamaa amejipanga aisee, yaani mgahawa una kila kitu,” jamaa mmoja aliniambia, hakujua kama mimi ndiye nilikuwa mmiliki wa mgahawa huo.
“Ahsante nimejitahidi lakini,” nilimjibu kwa makusudi huku nikitabasamu.
“Inamana wewe ndiye mwenye huu mgahawa?” aliniuliza.
“Ndiyo, vipi sifananii eeh?”
“Acha masihara yako hivi ukijiangalia unaweza kumiliki mgahawa kama huu? Wewe labda uwe mlinzi.”
“Hahaha.”
“Kweli tena.”
Huyo hakuwa mtu wa kwanza kutoniamini kwamba nilikuwa mmiliki wa mgahawa huo. Kila mtu aliyeniona na kuambiwa kwamba mimi ndiye nilikuwa mmiliki halali hakuamini hata kidogo.
***
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea sikuacha kumwambia Farhia kwa sababu yeye ndiye ambaye alinipa pesa na kunitaka nizifanyie biashara. Sikutaka kwenda kinyume na makubaliano hayo na hivyo nilifanya kama alivyoniambia. Baada ya kufanikiwa kufungua mgahawa huo, nilipiga picha na kumtumia WhatsApp.
“Hongera sana mpenzi wangu, umefanya kitu kikubwa sana,” alinitumia ujumbe huo baada ya kuziona picha nilizomtumia.
“Ahsante ila shukrani zote hizi unastahili wewe kwa sababu kama sio wewe nadhani hili lisingeweza kutimia kabisa,” niliandika na kumtumia.
“Abdul ni mara ngapi nakwambia kwamba nafanya haya yote kama wajibu wangu kwako?”
“Naelewa mpenzi lakini penye ulazima wa kukushukuru acha nikushukuru, umekuwa msaada mkubwa sana kwangu. Kwa nini hutaki kukubali hilo?”
“Unataka kujua kwa nini sitaki?”
“Ndiyo.”
“Kwa sababu wewe ni mume wangu.”
Nilipousoma ujumbe huo alionitumia nilisita kuandika na kumjibu, nikabaki nikirudia kuusoma mara mbilimbili kama mhariri ambaye alikuwa makini kukagua makosa ya kiuandishi katikia kazi ya fasihi.
Nilihisi kama mwili wangu umepigwa na ganzi na ni hapa ambapo nilianza kuhisi harufu ya manukano ambayo hapo awali sikuihisi harufu hiyo kabisa. Nilishindwa kuelewa harufu hiyo ilitokea wapi muda huo kwani nilikuwa nimejifungia chumbani na hakukuwa kuna mtu mwingine zaidi yangu.
Wakati pua zangu zikiwa makini kunusa harufu hiyo ya manukano na kuanza kutafakari yalitokea wapi muda huo mara simu yangu ikawa inaita, haraka sana nilipokea baada ya kuliona jina la Farhia.
“Kwa nini hujibu meseji zangu? Na unafanya nini?” aliniuliza maswali mawili kwa mpigo, nikashindwa kujua nilitakiwa kuanza kumjibu swali lipi.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitendo cha kuchelewa kujibu meseji kwa Farhia kilionekana kuwa ni kosa kubwa tena la jinai. Alionyesha ni kwa jinsi gani hakupendezewa nacho na ndiyo sababu akaamua kunipigia simu na kuanza kunilaumu.
Wakati ambao nilikuwa nikitafakari ni swali lipi ambalo nilitakiwa kuanza kumjibu. Nilibaki kimya kwa muda wa sekunde kadhaa, muda huo nilionekana kama mtu ambaye alikuwa akitafakari jambo fulani kwa kina na nilipomaliza ndipo hapo ambapo nikajikuta nikimuita kwa sauti ya chini.
“Niambie ulikuwa unafanya nini muda wote huo?” aliniuliza tena, safari hii sauti yake ilisikika kama mtu ambaye alikumbwa na hasira.
“Mbona sijafanya kitu?”
“Una uhakika?”
“Ndiyo.”
“Kwanini umekaa kimya hivyo?”
“Sijafanya kitu lakini?”
“Nitaamini vipi?”
“Niamini mpenzi wangu.”
“Unanisaliti?”
“Sijakusaliti Farhia na siwezi kukusaliti, hebu jaribu kuniamini hata kidogo basi.”
“Niambie kwanza ulikuwa unachati na nani?”
“Sijachati na mtu.”
“Kweli?”
“Ndiyo huo ndiyo ukweli wangu.”
Nilipomwambia hivyo akanyamaza kwa muda, upande wa pili nikamsikia akivuta pumzi na kuziachia. Mpaka kufikia hapo niligundua kwamba alikuwa ni msichana mwenye wivu mkubwa sana kiasi kwamba alianza kunihisi vibaya. Alichokuwa akikiamini nilikuwa nikimsaliti na hakupendezewa na hilo hata kidogo.
Alikasirika na ni hapa ambapo nilipata kazi ya kuanza kumbembeleza mpaka pale ambapo alitulia na kuniamini kwa mara nyingine.
Kama ni mapenzi basi yalinichanganya kiasi cha kunipa uchizi. Kila nilipokuwa nikiisikia sauti ya Farhia masikioni mwangu, kiukweli ilinisisimua na kuufanya moyo wangu utawaliwe na furaha.
“Natamani sana siku moja nikuone,” nilimwambia kwa sauti ya chini.
“Kwanini unatamani unione?” aliniuliza.
“Kwa sababu nakupenda sana na sitamani kuona tukiendelea kuishi mbali mbali.”
“Usijali ipo siku utaniona mpenzi.”
“Lini?”
“Utaniona tu kwani wasiwasi wako ni nini?”
“Sina wasiwasi ila shida yangu nikuone tu.”
“Hivyo tu.”
“Ndiyo.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Halafu ukishaniona utafanyaje?”
“Nitafurahi.”
“Kwahiyo shida yako ni kufurahi?”
“Ndiyo.”
“Sawa.”
“Kwahiyo?”
“Kuhusu nini?”
“Kukuona.”
“Nimekwambia sawa, utaniona.”
Baada ya kumaliza kuwasiliana naye, kichwa changu kikapata kazi ya kuanza kuufikiria uzuri wake. Sikutaka kuufikiria tu pasipo kuziangalia picha zake, nilichokifanya nilizifungua kwenye simu yangu na kuanza kuziangalia. Hiyo ndiyo ilikuwa starehe yangu kubwa.
Wakati nikiendelea kuziangalia picha ile harufu ya manukato mazuri ikazidi kutawala chumbani kwangu. Nilishtuka sana kwa sababu haikuwa hali ya kawaida ambayo niliizoea lakini cha ajabu pua zangu zikatokea kupendezewa na harufu hiyo.
Nilipigwa na butwaa, nikatoka kitandani na kuyaangaza macho yangu huku na kule, hakukuwa na mtu yeyote zaidi yangu. Wakati nikiendelea kushangaa kioja hiko ndipo hapo kwa nyuma nikaanza kuisikia sauti ya msichana ambaye alikuwa akiniita, nilipogeuka nikamkuta Farhia akiwa amekaa kitandani, alikuwa akitabasamu.
Kwanza nilishtuka sana mara baada ya kumuona kwa wakati huo. Ni kweli nilimwambia kwamba nilitamani kumuona lakini ilikuwa si katika mazingira yale. Kichwani mwangu likajitengeneza swali, ilikuwaje mpaka akapajua ninapoishi tena mpaka kufikia hatua ya kuingia ndani ya chumba changu? Hapo ndipo nilipozidi kuchanganyikiwa ndugu msomaji wa mkasa huu.
“Vipi mbona umeshtuka?” aliniuliza kana kwamba ilikuwa ni hali ya kawaida ambayo nilikuwa nimeizoea na hivyo kitendo cha kushtuka siku hiyo nilionekana kama nipo tofauti.
“Umepajuaje hapa?” nilimuuliza huku nikiendelea kushangaa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Jamani kwani kuna ubaya mimi kupafahamu mahali anapoishi mpenzi wangu?”
“Hakuna ubaya ila…” nilimwambia lakini kabla sijamalizia sentensi yangu nikamuona akitoa tabasamu pana kisha akatoka pale kitandani na kuja kunikumbatia, hakunipa muda wa kujielezea hata kidogo.
“Nakupenda sana Abdul,” aliniambia wakati alipokuwa amenikumbatia.
Kiukweli nilishindwa kumjibu kitu na badala yake nikabaki nikijiuliza maswali lukuki yaliyokosa mtu wa kunijibu kwa wakati huo. Nilijiuliza aliingiaje ndani ya chumba changu kwa sababu nilifunga mlango. Inamaana kumbe hata ile harufu ya manukato niliyokuwa nikiyasikia alikuwa ni yeye?
Kiukweli nilichanganyikiwa, nilikuwa nimekumbatiana naye lakini bado niliendelea kujiuliza maswali yaliyokosa majibu.
Ni hapa ambapo mwili wangu ulikuwa ukitetemeka mno, kijasho chembamba kilikuwa kikinitoka. Moyo wangu ulikuwa umejaa hofu katika kipindi hicho. Ni kama vile Farhia alitambua hali niliyokuwa nayo katika kipindi hicho, alichokifanya akajitoa katika kumbato na kuanza kunipapasa mwili wangu, ni ndani ya dakika kadhaa nikajikuta nikifanya naye mapenzi.
***
Nilishtuka na kujikuta nipo kitandani, kumbe matukio yote yale yaliyokuwa yametokea yalikuwa ni kwenye ndoto na wala sio kweli kama nilivyokuwa nikiamini. Nikaamka na kuanza kujiangalia, nilikuwa kwenye hali mbaya sana na cha ajabu nilijikuta nimejichafua.
Ni hapa ambapo nikaanza kumkumbuka Farhia. Mawazo juu yake yalikuwa yakinitesa mno. Katika kipindi hicho hali ilikuwa tofauti, mawazo juu yake yalikuwa zaidi ya usiku niliyomuota.
Nilipoamka nilijiandaa harakaharaka na kisha kuelekea chuo. Katika kipindi chote hicho nilikuwa nikimfikiria Farhia tu.
Ukumbuke mpaka kufikia hapo tayari nilikuwa nimefungua mgahawa wangu na ulikuwa ukiniingizia pesa kila siku.
Kuanzia hapo maisha yangu yalianza kubadilika kwa asilimia kubwa, sikuwa Abdul yule ambaye nilianza chuo nikiwa sina kitu. Kutokana na mafanikio niliyoyapata ndani ya muda mfupi yalimshangaza mjomba wangu mpaka kufikia hatua ya kuniuliza kulikuwa kuna siri gani iliyokuwa ikiendelea nyuma ya pazia na hakuifahamu.
Ilibidi nimwambie kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yangu mpaka kufikia hatua ya kufungua mgahawa kwa siri na ndiyo uliokuwa unaniingizia kiasi kikubwa cha pesa.
Nilipomwambia hivyo alionekana kushtuka, hakuamini hata kidogo, akatulia kwa muda huku akionekana kutafakari jambo fulani.
“Pesa umepata wapi?” aliniuliza swali ambalo nililitegemea kuwa ndiyo lingekuwa swali la kwanza kuniuliza.
“Halafu nilisahau kukwambia kitu mjomba,” nilimwambia.
“Kitu gani?”
“Kuna kipindi nilishiriki shindano la bahati na sibu, sikukwambia ila ndipo niliposhinda na kupata pesa za kufungua biashara hiyo.”
Huo ndiyo uongo niliyoutumia kumdanganya mjomba wangu, japokuwa alikuwa na wasiwasi lakini mwisho wa siku ilibidi akubaliane na kila kitu kwani mafanikio yangu yalionekana.
***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kupita miezi kadhaa Farhia aliniambia alitamani sana kuniona nikiishi maisha ya kujitegemea kwa sababu alitaka kunipa utajiri. Hilo halikuwa tatizo hata kidogo, nilichokifanya nilimshirikisha mjomba wangu kuhusu mpango huo ambapo aliniruhusu na hivyo kutafuta nyumba ambapo nilipanga maeneo ya Kurasini.
Naweza kusema kila kitu kilichokuwa kikiendelea katika maisha yangu Farhia ndiyo alikuwa sababu. Alidhamiria kunipa utajiri. Kuna wakati ulifika nikawa najiuliza hivi kulikuwa kuna umuhimu gani wa kwenda chuo kusoma? Niende nikafanye nini na wakati nilikuwa na pesa?
Hapo ndipo nilipoanza kusikia sauti mbili moyoni mwangu, sauti ambazo zilikuwa zikipambana, kila moja ilitaka niisikilize. Kulikuwa kuna sauti moja iliyosikika kwa ukubwa kabisa, hii ilikuwa ikiniambia kwamba sikutakiwa kuendelea na chuo kwa kuwa nilikuwa na pesa, na hata kama ningeendelea basi nilikuwa nikipoteza muda wangu.
Mbali na sauti hiyo pia kulikuwa na sauti nyingine ambayo ilisikika kwa upole mno tena kwa chini kabisa. Hii ilikuwa tofauti na ile nyingine, ilikuwa ikinikumbusha kwa kuniambia kwamba sikutakiwa kuacha chuo, hata kama ningepata mabilioni ya pesa kiasi gani bado sikustahili kuacha kwa sababu kuna watu mitaani wanatamani kusoma lakini wamekosa nafasi hiyo, mimi niliyeipata sikutakiwa kuichezea hata kidogo.
Hicho ndicho kilikuwa kipindi ambacho pesa zilinichanganya kiasi ambacho sikuona umuhimu wa kuendelea na chuo tena. Kama kila kitu nilichokuwa nikikihitaji nilikipata katika maisha yangu sasa kulikuwa kuna ulazima gani wa kuendelea na masomo? Na wakati hata kama ningesoma mwisho wa siku ningetafuta kazi kwa ajili ya kupewa pesa.
Hilo ndilo lilikuwa swali kubwa ambalo nilijiuliza na jibu lake lilikuwa ni moja tu kwamba sikutakiwa kuendelea na chuo kwa sababu nilikuwa nikipoteza muda wangu.
Hayo ndiyo yalikuwa maamuzi niliyoyachukua lakini nilipowashirikisha washikaji zangu walilipokea kwa mtazamo tofauti. Kwanza walishtuka sana, kile nilichowaeleza siku hiyo kilionekana kuwashangaza mno.
“Unasemaje?” aliniuliza Nickson huku akinitazama, hakuamini kama ningeweza kuchukua maamuzi magumu kama hayo.
“Nataka kuacha chuo,” nilimjibu kwa kujiamini.
“Acha ujinga wewe, mimi sikushauri uache ni bora ukafanya biashara zako huku ukiendelea na chuo kama wengine wanavyofanya,” aliniambia Deo huku akinishauri.
Japokuwa nilidhamiria kweli kuacha chuo na kufanya biashara lakini maneno ya Deo yalikuwa na mantiki kubwa sana. Ni hapa ambapo nilijiona kukurupuka na kuchukua maamuzi pasipo kutenga muda wa kufikiria mara mbilimbili.
Baada ya kugundua kuwa sikuchukua maamuzi yaliyokuwa sahihi sikuona haja ya kuacha chuo, isipokuwa niliendelea huku nikifanya biashara zangu kama kawaida.
Ukumbuke nilikuwa bado sijaonana na Farhia ana kwa ana. Niliishia kuchati naye facebook na hata kuwasiliana kwenye simu.
Naweza kusema hayo ndiyo yalikuwa mapenzi yetu na huwezi kuamini mpaka kufikia hapo sikushtuka hata kidogo, kila kitu alichokua akinifanyia katika maisha yangu nilijionea sawa, wakati mwingine nilimuona kuwa msichana wa kipekee mwenye mapenzi mazito na mimi.
***
Baada ya kupita mwaka mmoja maisha yangu yalibadilika. Nilikuwa miongoni kati ya wanachuo waliyokuwa na maisha mazuri. Kila mtu alishangazwa na mabadiliko yangu, ni katika kipindi hicho ambapo nilinunua gari ndogo aina ya Toyota IST.
“Kuna nini?” aliniuliza Farida huku akinitazama kwa macho yaliyoashiria kuwa na maswali mengi yaliyokosa majibu.
“Kuna nini kivipi yaani?” nilimuuliza huku nikiachia tabasamu pana.
“Unafanya kazi gani?”
“Jamani sasa hilo ni swali gani la kuniuliza Farida.”
“No, hebu niambie maana sikuelewi unajua.”
“Hunielewi kivipi? Nimebadilika nimekuwaje?”
“Diploma one tayari una gari?”
“Sasa wewe unashangaa mimi kuwa na gari mbona huniulizi kuhusu mgahawa wangu.”
“Unamiliki na mgahawa?”
“Ndiyo mbona muda mrefu hivyo.”
“Heee! Makubwa.”
Farida hakutaka kuamini, kile nilichomwambia kilimshangaza na kumfanya asijue ni nini kingine ambacho alitakiwa kuniambia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huyo hakuwa msichana wa kwanza chuoni hapo kunishangaa, kila msichana alishangazwa na mabadiliko yangu na ni katika kipindi hicho ambapo nilianza kusumbuliwa. Kila msichana alionekana kunitamani na kuhitaji kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mimi.
Niliyakumbuka maneno ya Farhia ambayo aliniambia ni kwa jinsi gani alivyokuwa akinipenda na kwamba sikutakiwa kumsaliti hata kidogo. Maneno hayo yalijirudia vyema kichwani mwangu lakini kuna muda nilionekana kuyasahau, hapa ni baada ya kuzidi kuzoeana na Farida mpaka kufikia hatua nikaanzisha uhusiano naye wa kimapenzi.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wangu wa kumsaliti Farhia. Japokuwa nilimpenda na alinifanyia mambo makubwa katika maisha yangu lakini yote nilijisahaulisha.
Kitendo cha kumsaliti Farhia na kuanza kutembea na wasichana wengine, kilisababisha nikapata mkasa mpya mwingine ambao ulinifanya niogopeke na wanachuo wote.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment