Search This Blog

MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN (2) - 1

 








IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



*********************************************************************************



Simulizi : Mkufu Wa Malkia Wa Gosheni (2)

Sehemu Ya Kwanza (1)







ILIPOISHIA



“Nimewapa muda ili mnipe sababu za kuwaachia uhai wenu.”



Hawakujua anayenena ni nani. Wakauliza ila hawakujibiwa. Walitawaliwa na hofu kubwa. Ukapita kama dakika tatu, na mara popo wakavamia eneo hilo. Wakatanda kiti na mara akatokea mtu hapo!



Popo wale wote walipotelea ndani ya mwili wa huyo mtu. Yaani yeye ndiye aliyekuwa popo hao wote.



ENDELEA



Mtu huyu alikuwa ni yule kaka yake Venin! Uso wake ulikuwa unatisha na mwili wake ukiwa mwembamba na mweupe pe! Macho yake yalikuwa mekundu na nywele zake zikiwa ndefu na nyeupe kama sufi.



Akatabasamu na kumtazama Rhoda, akamtazama na Tretho na kisha Bonas. Wote walikuwa na hofu kwenye viini vya macho yao. Basi akafurahi zaidi na kuwataka watu hao wampatie sababu za yeye kuwaacha hai.



Akawaambia damu zao ni muhimu mno kwake. Alikuwa anawatazama tokea muda kwani alikuwa anatarajia ujio wao tangu pale ambapo mdogo wake alimwambia kuwahusu.



“Yule mjinga alinitaarifu juu ya ujio wako. Na hata akadiriki kuwaombea niwabakize hai. Lakini sasa akasahau namna gani ninavyotaka kutoka katika ardhi hii ya kijinga. Nataka kuwa huru. Nataka kuurejea utawala wangu!”



Akaangua kicheko. Lakini kabla hajaendelea, Rhoda akamtaka awabakize hai kwani ana sababu ya kumpa. Mlozi yule akauliza kwa hamu sababu gani hiyo. Rhoda akamwambia atamsaidia kuuteka upya utawala wake.



Mlozi akastaajabu na akataka kujua kivipi Rhoda atafanya vivyo. Rhoda akamwambia mlozi huyo kwamba anahitaji muda zaidi wa kutengua hicho kitendawili. Mlozi asiamini kauli ya Rhoda akaagiza watu hao watiwe ndani mpaka pale mwezi utakapozuka kwa ajili ya kufanya ibada yake.



Kwa makadirio aliyoyafanya, ilikuwa bado siku tatu ama mbili na mwezi utaonekana angani. Siku hiyo ndiyo itakuwa mahususi kwake kuchinja binadamu hao na kufanya hitimisho ya kafara yake ambayo ilishatanguliwa na wale wengine.



Basi pasipo kujulikana nini kimetokea, popo wakazuka na kuwatwaa wakina Rhoda kwa mtindo wa kimbunga. Wakawafungasha na kwenda kuwamwagia ndani ya chumba kimoja dhoofu, na kikuukuu, lango likafungwa!



Chumba hicho kilikuwa kimejawa na kila aina ya wadudu, kuanzia wanaotambaa mpaka wanaoruka. Harufu yake haikuwa ya kuvutia kabisa, ukitazama dirisha lilikuwa lipo mbali na ni dogo.



Rhoda akamuuliza Tretho kama kuna la kufanya wajiokoe toka mule. Tretho akasema wasubiria aone kama kuna namna. Akatazama huku na kule, japokuwa kulikuwa ni giza, akaona panya mmoja ukutani.



Basi akamdaka na kumnyonga kwa mikono yake upesi na kumnyofoa kichwa. Panya akamwagika damu. Tretho akapakaa damu hiyo mikononi mwake na kwenye paji lake la uso, kidogo. Alafu akamtupia panya kando!



“N’taomba muwe kimya kidogo,” akasema akiketi kitako. Akaweka mikono yake mbele mithili ya ombamba, akasema maneno kadhaa yasiyotambulika ni ya lugha gani. Baada ya kama dakika tatu, akafumbua macho yake na kumwambia Rhoda ajiandae na afanye kazi yake.



Rhoda akawa ameshajua nini kinafuata. Ilikuwa ni kazi ya kukariri maneno atakayoyatema na kisha amwambia atakaporejea fahamuni.



Haikupita muda Tretho akaanza kuyatema maneno hayo. Hakuchukua muda mrefu akarejea fahamuni na kumuuliza Rhoda nini alichoambulia. Rhoda akamwambia.



Mzee huyo akatikisa kichwa na kusema:



“Haiwezekani.”



“Kwasababu gani?” Rhoda akawahi kuuliza akitoa macho.



Tretho akasema jengo lile ambalo wamo ndani, siyo hata jengo halisi bali ni ulozi wa kufikirika tu. Ni jengo kwa mujibu wa macho yao na wala halipo kiuhalisia! Ni ngumu sana kutoka maana mfumo wake ni wa kilozi wa ngazi za juu.



“Kwahiyo tutafia humu?” Rhoda akakabwa na hofu. Tretho hakuwa na jibu la kumpatia zaidi tu ya kumtazama kwa macho ya njia panda.



Kukawa kimya kwa muda.



Lakini katika usiku huo huo, usiishe, kuna mambo mengine bado yalikuwa yanakuja. Unakumbuka wakina Rhoda walikumbwa na kadhia ya kimbunga cha popo wakiwa eneo gani?



Eneo la wale wabibi!



Basi na humo Tanashe kila mtu na himaya yake. Kila mtu na kaya yake, na hakuna mwingine wa nje anayetakiwa kuingia katika hema ya mwenzake katika namna yoyote ile!



Wakitambua kwamba wanadamu hao walikuwa wametia miguu kwenye ardhi yao, wale bibi watatu wakawa wamapanga kufanya jambo. Na jambo hili halikuwa lingine bali kwenda kutwaa kile kilicho chao!



Walikuwa wamevalia magauni meusi na kofia ndefu zilizochongoka. Kila mtu alikuwa ana jicho moja moja na kipande cha mti mkononi. Mti mwembamba wenye kafundo ka rungu kule mbele.



Kabla hawajatoka kwenye jengo lao, wakahakikisha kila kitu kipo sawa na salama. Kufumba na kufumbua, wakapotea mazingirani! Hawakuonekana hewani, wala ardhini. Ila baada ya punde, kule upande wa yule mlozi wa jengo la kufikirika, Tretho akahisi jambo.



Wenzake walikuwa wamelala akawaamsha na kuwaambia: “Kuna watu wanakuja!”



Wakatazama huku na kule wasione jambo. Tretho naye hakuwa na viambata vyake vyovyote vya kazi, vyote vilipotelea huko.



Basi baada ya muda wakajikuta wanapoteza fahamu na wakadondoka chini kama vifurushi. Tayari walishabebwa!





***





“Naomba uniwie radhi, mimi.”



“Nshakwambia sitaki kusikia wala kuambiwa chochote!”



“Kaka, usilipe baya kwa baya. Mabaya mawili hayatengenezi zuri moja!”



“Kwani yeye hakulijua hilo hapo kabla?”



Yalikuwa maongezi moto kati ya Sultana na Karim. Sultana alikuwa ameketi sebuleni wakati Karim akiwa amesimama mwili wake ukifunikwa na kanzu ya rangi ya zabibu. Sultana alikuwa amejivika gauni refu lenye rangi ya maji ya bahari. Zaidi alikuwa amejivika hofu na mashaka kwani laka yake hakutaka kuelewa na alikuwa amedhamiria haswa kulipiza kisasi kwa Sultan.



Sultana akauliza, hii vita itatupeleka wapi na je haoni kama itamaliza himaya yao nzima? Karim akacheka kwanza alafu akadaka kiuno chake kwa mikono miwili. Akasema kwani Sultan hakuyajua hayo?



Vipi kama majeshi yake yangefanikiwa kummaliza? Leo angekuwepo hapo?



Basi zogo hilo lisipate suluhisho, Karim akaenda zake ndani na kumwacha dada yake akilalama. Hakutaka kujali na wala hakutaka kusikia tena juu ya mada hiyo. Akasema kama kweli Sultan anaomba msamaha basi alete mwenyewe miguu yake pale na si kumtuma mkewe.



“Kwani wewe ndiye mkosaji?” alimuuliza dadaye. “Kama anataka amani aje apa na ameze majivuno yake kukiri makosa. Amenidhalilisha sana, na anataka kunimaliza pia.”



Sultana akabakiwa na mawazo sana. Ni nini afanye na hakuwa radhi kurudi nyumbani akiwa na jibu hasi? Aliona mkono wake ndiyo ulianzisha vita hiyo na hivyo hana budi kuimaliza!



Akala na kufikiri sana. Akatoka nje kwenda kurandaranda na baadae hata akarudi ndani pasipo kupata majibu. Nafsi yake ikamwambia ajaribu tena kuongea kwa mara nyingine pindi watakapokuwa mezani kupata chakua cha mchana na kakaye.



Labda anaweza kutengua mawazo yake.



Akafanya hivyo. Lakini Karim hakutia neno hata moja pasipo kujali namna gani dada yake ameongea. Alikuwa kimya akishurutisha mdomo wake kula.



Sultana akaghafirika. Akasusa na kula. Akanyanyuka na kwenda zake jikoni aondoke hata pale kwenye uwepo wa kaka yake ‘mkaidi’. Moyo wake ukapuliza kwa haraka na kuuma.



Akafikiri na sasa shetani akatia nanga kwenye akili yake. Akawaza kumuua Karim, nduguye! Hilo likawa suluhisho lake la mwisho kumaliza mjadala. Hakukuwa na njia nyingine sasa kukwepesha vita hii.



Akatazama pembeni na kukwapua kisu kimoja kirefu. Akakificha nyuma ya mgongowe na kwenda hatua za pole. Moyo wake ulikuwa unakita na kukimbia sana kwa hofu lakini haukufanikiwa kusimamisha miguu yake.



Akamsogelea Karim aliyekuwa amempa mgongo, akamkita kisu cha ubavu! Karim akapiga kelele moja kali kabla hajamshika dada yake mkono na kumtazama kwa macho mekundu yanatoa chozi, na mdomo uliochama.



Akamuuliza dadaye kwa sauti ya kutiatia maji:



“Mkono wako ndugu yangu ndiyo unaonimaliza?”



Sultana akajikuta anabubujika machozi mengi akimshuhudia kakaye akipokwa uhai. Akajuta sana na labda akadhani ni macho yake, kaka ataamka. Haikuwa hivyo. Kaka akasema kauli yake ya mwisho:



“Na hamtabaki salama!” kisha akaenda.



Sultana akamburuza kaka yake mpaka chumbani. Akafuta damu zote zilizokuwa pale na akarejesha mazingira kama yalivyo. Hakuona tena salama kukaa hapo, na basi akamwita mwanajeshi aliyekuja naye na kumtaka waondoke upesi.



Wakapanda farasi na kupotea wakimwacha Karim huko chumbani amefungiwa na kisu chake bado kipo ubavuni.



Njia nzima Sultana akawa anabubujika machozi! Moyo wake ulikuwa mzito ukibeba manung’uniko na lawama. Sura ya kaka yake haikuacha akili yake salama.





***





“Mama, mfalme ni wa baridi!” Ilikuwa kauli ya Tattiana punde tu mama yake alipomuuliza juu ya huko alipotokea.



Yalikuwa ni majira ya mchana na ndiyo muda ambao Tattiana alikuwa amerejea toka kwa mfalme baada ya kuruhusiwa. Sasa alikuwa ameketi na mama yake sebuleni mama akiwa na hamu kubwa ya kujua yaliyojiri.



Mama akamuuliza mfalme ni wa baridi kivipi? Tattiana akaeleza vema. Alishindwa hata kumkumbatia wala kukaa naye karibu. Kwani alikuwa ana baridi kana kwamba barafu la kule kaskazini ya Kinabey!



Mama akastaajabu. Linawezekaaje hilo? Ila kama haitoshi, Tattiana akasema ya kwamba mfalme alimwambia hiyo iwe siri yake na asimwambie mtu mwingine yeyote!





“Unayosema ni kweli?” mama akauliza. Tattiana akamthibitishia hilo kwa kumwonyeshea vidole vyake vilivyosinyaa. Hata alipomgusa mamaye bado alikuwa ana kaubaridi kwa mbali.



Mama akamuuliza kwahiyo haukufanya naye mapenzi. Tattiana akatikisa kichwa na kumwambia mamaye kwamba wamefanya ila kwa wakati huo mfalme hakuwa katika hali hiyo ya ubaridi.



“Alikuwa kama mimi na wewe, ila ajabu baadae akabadilika!”



Wakawa wamemezwa na maswali wasijue majibu. Lakini mama akamwambia Tattiana itampasa avumilie kwani hata iweje ni lazima ampate mfalme. Asahau hayo yote na yatakuja kupatiwa ufumbuzi huko mbeleni.



“Tuangalie hili la hapa mbele kwanza. Hayo tutaja tatua tukiwa ndani ya nyumba.”



Mama hakukaa sana, akaaga anaenda mashariki kupeleka mzigo kwa mfanyabiashara mmoja wa huko. Akamtaka Tattiana apumzike na wataongea kadiri na muda utakavyokuwa unaenda. Wala asiwe na hofu.



Alipotoka, Fanty akaungana na dadaye. Akampeleleza juu ya huko kasrini mwa mfalme lakini Tattiana hakusema hata jambo. ila kabla binti huyo hajanyanyuka na kwenda, Fanty akamwambia habari za Roboth!



Jana yake mwanaume huyo alikuja nyumbani muda mfupi tu baada ya yeye kutoka kwenda kwa mfalme. Tattiana akamezwa na hiyo mada na akataka kujua zaidi.



“Mama amesema hataki kumwona Roboth tena hapa!” Fanty akamalizia habari kwa amri. Mara Tattiana akanyanyuka akibebelea gauni lake na mkono, mbio akatimka kuelekea nje!



Kichwani Roboth alikuwa ametawala. Aliona ana haja ya kuonana na mwanaume huyo na kumweleza yale yaliyojiri kwani hajawahi kumkosea kwa namna yoyote ile, hivyo hakuwa na sababu ya kumhukumu.



Japokuwa Fanty alimuita na kumkata kufanya hilo, Tattiana hakujali wala kusimama. Akaendeleza mbio ambayo ilikomea mbele ya jengo la wakina Roboth. Jengo kuukuu na lisilovutia.



Akaita Roboth mara mbili na mara akatoka mama mmoja mnene mwenye mashavu makubwa na kamdomo kadogo. Alikuwamama Roboth. Akamwambia Roboth ametoka kwenda ng’ambo ya mto.



Pasipo kungoja, Tattiana akafyatua tena miguu yake kwenda huko alipoambiwa. Hakungoja maelezo yoyote yale kwani alishajua mahali ambapo atamkuta Roboth huko. Ni mahali kulekule ambapo walikuwa wanapenda kupeana miadi ya kukutania.



Akasimama na kuvuta pumzi, kisha akaendelea na mbio. Akasimama tena na kuendelea na mbio, mpaka anafika alikuwa hoi bin taaban! Akamkuta Roboth akiwa ameketi juu ya jiwe kubwa lililokuwa limesimama kwenye maji ya mto.



Alikuwa na macho mekundu na sura nyong’onyevu. Mdomo wake ulikuwa umekauka. Alikuwa amekumbatia miguu yake akitazama maji yanavyotiririka.



Tattiana akaita, na mara Roboth akamfuata na kumkumbatia. Akashtaki yale aliyoambiwa na Fanty, kisha akauliza:



“Ni kweli hayo?”



Kwa namna ambavyo alikuwa anamtazama Tattiana, akamfanya binti huyo adondoshe chozi. Na kabla hajajibu chochote, akamkumbatia tena Roboth na kumweka kitako. Akamwambia yale aliyoasikia ni kweli, na ameshalala na mfalme.



Moyo wa Roboth ukajikunja kwa uchungu. Akahisi kana kwamba mtoto aliyetengwa na wazazi wake. Ama yule aliyeadhibiwa vikali asijue kosa lake ni nini. Tattiana akamwambia ni kwasababu ya familia yake, anafanya hivyo.



Roboth aliyejawa na uchungu hakuelewa sababu hiyo, akajikuta analia! Akanyanyuka na kwenda mbali. Akamwambia Tattiana hataki kumwona tena na moyo wake kamwe hautamsamehe.



Tattiana akabaki akilia. Alipojiona ni mwepesi sasa na angalau machozi yake yamepunguza uchungu alonao, akanyanyuka na kurudi nyumbani njia nzima akimfikiria Roboth.



Alijiona yupo njia panda na hajui cha kufanya. Aende kwa mfalme wa ‘baridi’ ama abaki na Roboth, kipenzi cha roho? Je Familia itamwelewa?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Alipofika nyumbani akamkuta mama yake na Fanty wakiwa wamekaa sebuleni. Kwa namna mama yake alivyomtazama, akafahamu tayari Fanty atakuwa amemfikishia taarifa juu ya huko atokako.



Mama akamuita na kumuuliza wapi alipotoka. Pasipo woga akasema ametoka kwa Roboth, alafu akakimbilia chumbani na kujifungia!





***





Ngo! Ngo! Ngo!



Hodi ilibishwa mara moja. Punde mlango ukafunguliwa na Bozi aliyetazama kushoto na kulia kisha akamruhusu mgeni wake aingie ndani.



Alikuwa ni mwanaume aliyevalia sare za jeshi. Akaketi mezani na kumwambia Bozi taarifa za Benadi. Ya kwamba mwanaume huyo alikuwa ameuawa huko karibia na kwake baada ya kuonekana kusaliti kile walichokubaliana.



Bozi akatahamaki kwa taarifa hizo. Hakutegemea kama Benadi angejitosa nje ya chombo chao. Sasa mpango wake wa kufanya tukio la mapinduzi lilikuwa hatihati kutekelezeka kwa njia ya amani.



“Tulimgundua akifanya mawasiliano ya siri na Malkia. Alimwandikia barua kumuonya juu ya mpango wetu.”



Mwanajeshi akatoa barua waliyoikamata toka kwa Benadi na kumkabidhi Bozi ambaye aliifungua haraka na kuipitia kwa macho yake ya kizee.



‘_Malkia wangu mtukufu, maisha yamebadilika … sasa wale uliowakomboa toka kwenye mikono ya wanyang’anyi na waonevu, wamekugeuka. Wanataka damu yako. Wanataka kula nyama yako na kunywa damu yako. Wale uliowahangaikia, leo wanahangaika kukutoa kitini na kukufanya mkimbizi_



_Malkia wangu, sijahusika na sitahusika na mpango huo. Ila tayari watu uliowapa imani yako wamekugeuka. Vita hii ni kubwa kuliko ile uliyopambana hapo awali kwa kuwafahamu maadui. Leo hii adui ni yule ambaye unakula naye meza moja_’



Barua ikaendelea kueleza na pia kutaja wale wote ambao anawajua wakihusika na mpango huo. Mpaka Bozi anamaliza kuisoma, alikuwa amepandwa na hasira za kutosha. Alijawa na jazba. Na akaona Benadi alikuwa anastahili kunyongwa kabisa kwa waya wa chuma.



“Mwili wake upo wapi?” akauliza. Mwanajeshi akamwambia wameuhifadhi ndani na walikuwa wanasubiria amri yake ili waufukie. Basi kutaka kuamini Bozi akaongozana na mwanajeshi huyo kwenda kuuona mwili.



Akakuta mfuko mkubwa uliohifadhi mwili wa Benadi. Akaufungua mfuko huo na kuangaza. Mwili ulikuwa wa baridi tayari. Tumboni ulikuwa na majeraha matatu ya kisu!



Benadi alishindiliwa visu vitatu kabla uhai wake haujachoropoka! Alikuwa ameenda na mapenzi yake, uaminifu na msimamo wake. Bozi akatabasamu na kisha akaufunga mwili huo baada ya kutupia humo barua ya Benadi iliyoishia njiani.



Akatoa amri mwili huo ukafukiwe, na kisha aitiwe wajumbe wake kwa ajili ya majadiliano. Akaenda zake.



Punde wajumbe wakawa wamefika nyumbani, Dummy na wale wenzake watano: watatu walikuwa ni wanajeshi, wawili wafanya biashara. Bozi akawaambia mpango wa kutumia njia ya amani hauwezi ukafanikiwa.



Benadi ameshakwenda, Fluffy na Seth wamewashikilia. Pasipo shaka hili jambo litatengeneza mashaka. Upesi inabidi wachukue hatua kabla mambo hayajawageukia. Wakakubaliana.



Usiku huo wakavamia makazi ya Malkia, wamtie nguvuni yeye na watu wake. Jeshi lipo tayari na linangoja amri muda wowote. Bozi akateta na wale wanajeshi na akawataka wanajeshi wanne atakaongozana nao kwenda kwa Malkia.



Ndani ya muda wa dakika kumi tu, kila kitu kikawa tayari. Bozi alipewa kikosi kizima cha wanajeshi kuongozana nacho. Akachukua hatua kwenda kwenye kasri ya Malkia akiwa anajiamini, analindwa.



Akazama kasrini, wanajeshi wake wakipambana na walinzi na kuwamaliza. Akafika mpaka ndani mwa Malkia lakini hakukuta mtu. Wakasaka kasri nzima pasipo kumwona yeyote. Si Malkia wala Zura!



Bozi akashusha bendera ya Sawaridi na kupandisha ya kwake. Bendera nyekundu yenye upanga wa njano. Akatangaza mapinduzi, Malkia amekimbia himaya na kuacha mikononi mwake! Akatangaza ni muda wa himaya kurudi mikononi mwa wenyeji, mikononi mwa wanaume!



Wanajeshi wakatapakaa huku na huko kumtafuta Malkia, lakini hakuna hata aliyempata wala kuona kiashiria. Hawakujua wapi alipo, wapi amejifichia! Watu ndani ya himaya wakashikwa na taharuki juu ya nini kinachoendelea.



“Mkuu, hata Fluffy na Seth hawapo ndani!” alisema mwanajeshi mmoja mkakamavu. Bozi akashupaza shingo yake, akauliza imewezekanaje kwa watu waliofungiwa na mlango mgumu? Mwanajeshi akajibu wamekuta shimo kubwa chumbani.



Mateka hao watakuwa wametorokea kwa kupitia shimo hilo ambalo lilienda umbali wa nusu kilomita toka kwenye chumba hicho!



“Sasa wapo wapi?!” akafoka Bozi.



“Nao hatujawaona, mkuu!” akajibu mwanajeshi. Bozi akawafukuza wakawatafute na wawalete haraka iwezekenavyo. Wakatazame huko njiani mpaka mpakani. Wahakikishe hakuna sehemu ya himaya itakayoachwa pasipo kutazamwa!



Basi wanajeshi wakaenda nje haraka kutimiza agizo. Wakachukua kama lisaa, lakini bado hawakufanikiwa. Wakarudi kasrini kumtaarifu Bozi. Ajabu wakamkuta amefariki!



Kichwa chake kilikuwa kimewekwa kifuani mwake wakati kiwiliwili kikiachwa solemba. Kiwiliwili hicho kilikuwa kimetuama kwenye dimbwi zito la damu!



Wanajeshi wakahamaki na kushikwa na hofu. Haraka wakatoka na kwenda kwa Dummy wakampashe habari. Lahaula! Hawakumkuta Dummy, bali mwili wa Dummy! Dummy alikuwa amekufa!



Alikuwa ananing’inia na kamba shingoni. Kamba iliyojishikiza kwenye kingo ya dirisha. Wanajeshi wakatokwa na macho.





Kila kitu kilich0kuwa kinatokea mbele ya macho yao hawakuwa wanaamini. Ni kama vile mchezo wa kuigiza! Hawakuelewa nini kinaendelea na nani anasababisha. Zikapita dakika kadhaa na mara wanajeshi hao wakaseikia kelele huko nje.



Kutoka kutazama, wakamwona Malkia akiwa beneti na Fluffy, Seth na Zura. Watu hawa walikuwa wamesimama juu ya jukwaa, na watu wakiwa wamekusanyika kuwatazama.



Mara wakakamatwa na wenzao na kuwekwa chini ya ulinzi. Wakaona na wenzao wengine nao wakiwa chini ya walinzi. Wakafahamu sasa mapinduzi yao yamekwama. Kule mbele wakaona na wale wanaume wafanyabiashara waliokuwa wanahusika na mapinduzi.



Walikuwa wamepiga magoti wakiinamisha vichwa vyao chini. Nyuma ya migongo yao walikuwa wamesimama wanajeshi waliokuwa wamebebelea silaha. Mapinduzi yalikuwa yamekomea mbele ya midomo ya bunduki!



Malkia akapaza sauti yake, na watu wote wakanyamaza. Akaeleza kila njama iliyokuwa imepangwa juu yake, kila hatua na kila mwenendo. Namna alivyokuwa amejifanya mjinga kwa kutokujua chochote, na namna ambavyo aliacha watesi wake wajigambe na kujivuna.



“Hakuna mtu anayejua nguvu na uwezo wangu, hata mimi pia. Kadiri ninavyopitia matatizo na changamoto, ndivyo ninavyovumbua na kujua uwezo wangu zaidi na zaidi! Lisilokuua linakutia nguvu.”



Lakini zaidi Malkia akaeleza namna gani alivyoumizwa na njama hizo, kwani ni kiashiria cha kutokuwa na imani naye. Zimemfadhaisha na kumfanya ajihisi mtupu kwani kwake alikuwa ameachukulia kama sehemu za familia. Kutaka kummaliza kumemfanya ajihisi yatima.



Wakati akieleza hayo machozi yakambubujika. Akashindwa kuongea, Zura akambembeleza na kumfuta machozi. Kisha akaendelea na kusema. Akashukuru kwa yote na sasa umefikia wakati wa yeye kuondoka.



Pale hapakuwa nyumbani, na hata jitihada zake za kupageuza kuwa hivyo, hazikufanikiwa! Sasa anataka aende awaache kama alivyowakuta, na ulimwengu wao wa kibabe, kumwagana damu!



“Inatosha. Nitatafuta nyumba yangu pale ilipo. Nitarejea kwetu.”



Baada ya kusema hayo akashuka zake na kuongoza njia mpaka kwenye farasi wake. Akamkwea, nyuma akiongozana na Zura, Fluffy pamoja pia na Seth.



Ingawa watu walimwomba Malkia asiondoke, kwa machozi na manung’uniko, vilio na simanzi, Malkia hakukata shauri na kubaki. Alifunga masikio na macho, akaenda zake.



Japokuwa ilikuwa ni nyakati za usiku, safari yake haikukoma. Wakatembea kwa umbali wa nusu saa kabla hawajaamua kusimama na kupumzika. Baridi lilikuwa kali. Upepo ulikuwa unapuliza sana.



Wakatandika shuka chini na kumruhusu Malkia ajilaze kwanza. Alafu wakatandika na mashuka yao baada ya kuwasha moto wa kuwapasha joto. Moto ulikuwa mkubwa mno kiasi cha kuonekana hata kwa umbali mrefu.



Hapo ndiyo Fluffy akamweleza Malkia juu ya karatasi yake, ile ambayo mama yake alimkabidhi. Karatasi iliyokuwa inaeleza juu ya siri za huko Misri. Malkia akawahi kumuuliza karatasi hiyo ipo wapi kwani amekuwa akivutiwa sana na habari za himaya ya huko.



Fluffy akamwambia ilikwapuliwa, hanayo tena.



“Haukumbuki hata kidogo?” Makia akamuuliza. Fluffy akatikisa kichwa, na kabla hajasema jambo Seth akadakia. Yeye anaikumbuka karatasi hiyo kwa kichwa. Fluffy na Malkia wakamtazama kwa macho ya mshangao.



“Kweli?” Fluffy akauliza. Kuthibitisha ambacho alichosema ni kweli, akatoa taarifa chache za huko. Alah! Alikuwa anakumbuka kana kwamba anasoma mahali.



“Twaweza kwenda huko?” Malkia akauliza. Lakini kabla hajajibiwa na yeyote, mwenyewe akajikosoa. Huko palikuwa mbali sana. wanahitaji rasilimali ambazo hawana kwa muda huo.



Fluffy akapendekeza jambo, wakiwa nyumbani kwao kwa ajili ya mapumziko, watafute jambo la kufanya na kuanza kujipanga kwa ajili ya safari hiyo ambayo inaweza kubadili kabisa maisha yao.



Lakini Zura akawakatisha, na akamkumbusha Malkia jambo. Ya kwamba anaweza kufanikisha hilo kwa kutumia mkufu wake. La hasha! Malkia akasema. Hawezi kwenda mahali ambapo hapafahamu.



“Mkufu haukumbuki sehemu mpya, lah! Unakumbuka mahali ambapo ulishawahi kuwapo.”



Wote wakakubaliana kutafuta njia. Ilibidi safari hiyo ya kuelekea Misri ifanikiwe wakiamini kila kitu kina mara ya kwanza.



Huko Misri wanaenda kutafuta kofia ya dhahabu ya Farao, kofia ambayo ilikuwa na madaraka ndani yake. Nguvu ndani yake. Mamlaka ndani yake! Kofia ambayo imefichwa kwa miaka mingi sasa.



Na aliyeificha akifariki akiwa amemwambia siri hiyo mtu mmoja tu. Mtu ambaye ameshakuwa mzee na sasa hana haja nayo. Mzee huyo anayeishi kando kando ya bahari ya Mediterania.



Lakini kwenda mbele na nyuma, kupata kofia hiyo haikuwa kitu chepesi wala cha mzaha. Kulikuwa kuna majaribu kadha wa kadha ndani ya Piramidi ya Giza! Majaribu ya nguvu za giza.



Majaribu ya vinyamkera na vitu visivyoeleweka. Kubwa zaidi ikiwa ni kupambana na jeshi la wafu waliokufa na kufukiwa kwa miaka alfu mbili sasa!



Juu ya yote haya, bado Malkia na wenzake walikuwa na imani. Isipokuwa Zura. Moyo wake haukumtuma na aliona safari hiyo ni kujipeleka kwenye domo la simba mwenye njaa!



Lakini hakukatisha watu tamaa. Akakaa na jambo lake kifuani akiamini pengine hali inaweza ikabadilika muda wa mbeleni, ama siku za usoni.



Asubuhi wakaendelea na safari yao.





***





“Nimeshakamilisha kila kitu,” akasema bibi mmoja kuwaeleza wenzake. Yalikuwa ni majira ya asubuhi iliyo tulivu na yenye giza. Walikuwa wamesimama ndani ya sebule yao wakijiandaa kwa ajili ya tambiko.



Tambiko na zindiko zito la kunuwia madaraka na mamlaka juu ya mwili wa Rhoda. Mwili waliokuwa wameuteua kwa ajili ya zoezi lao la kutoka ndani ya himaya ya Tanashe.



Uchaguzi wao ulizingatia jinsia lakini pia na mamlaka aliyokuwa nayo mhusika ndani ya himaya ya Gosheni.



Kama kawaida kulikuwa ni giza ndani. Mishumaa ilikuwa imewashwa na kitabu chao kikubwa cha kilozi kilikuwa kimefunguliwa na kutengwa mahali palipokuwa panahitajika kusomwa.



Kurasa mia tano hamsini na mbili!



Mwili wa Rhoda ulikuwa umelazwa juu ya kiti, ukiwa hauna fahamu. Miili ya Bonasi na Tretho ilikuwa pembeni kwa ajili ya kutoa damu ya kafara. Nayo si kwamba haikuwa na fahamu, bali haikuwa na uhai.



Basi bibi yule mmoja, ilikuwa ngumu kuwatofautisha kutokana na ufanano wa mavazi na sura, akasoma kilichokuwa kitabuni kwa sauti kubwa. Alipomaliza aya moja tu, radi zikaanza kutia na kunguruma huko nje!



Pepo kali ikapuliza lakini haikuzima mishumaa!



Bibi akasoma ukurasa mmoja mzima, akafungua ukurasa mwingine wa pili. Mara mwili wa Rhoda ukasimama na kukakamaa kana kwamba sanamu. Bibi akaendelea kusoma.



Akiwa amebakiza aya tatu amalize ukurasa, mwenzake mmoja akausogelea mwili wa Rhoda na kusimama mbele yake. Aya moja iliposomwa na kuisha, mara bibi huyo akazama ndani ya mwili wa Rhoda!



Ikafuatia aya ya pili, na hapo bibi mwingine, wa pili, akasimama mbele ya Rhoda. Aya hiyo ilipomalizika, naye akazama ndani ya mwili wa Rhoda. Sasa akabakia bibi mmoja tu.



Akabeba kitabu akiendelea kusoma aya iliyobakia. Alipoimaliza, naye akapotelea ndani ya mwili wa Rhoda. Kitabu kikadondokea chini! Rhoda akafungua macho. Macho yake yalikuwa na rangi nyekundu wakati kiini chake kikiwa cha kijani!



Hapo Rhoda akawa ni wakati uliopita. Mwili ulikuwa wa Rhoda lakini nafsi na roho zilikuwa za wale bibi!



Zikapita dakika kumi. Mara ikatokea rundo moja kubwa la popo lisijulikane limetokea wapi! Popo hawa wakazingira nyumba ya wale bibi na kuifunika kabisa kana kwamba ni giza, hamna kitu! Popo hao wakajikusanya na mara akatokea binadamu.



Binadamu huyo hakuwa mwingine bali kaka yake Venin! Macho yake mekundu yalikuwa yamebebelea ghadhabu. Nywele zake nyeupe kama sufi zilikuwa zinapepea pamoja na nguo yake.



Akatazama na kusaka huku na huko. Akaona kitabu chini na miili ya Tretho na Bonas. Mwanaume huyo akapiga kelele kali. Akalia.



Alishajua nini kilichofanyika na tayari alikuwa katika kundi la mkosaji. Akalalama, akageuka kundi kubwa la popo na kupotea eneo hilo kufumba na kufumbua!



Akaenda kuranda randa huku na huko kutafuta wale wabibi na kumtafuta Rhoda lakini hakuona kitu ndani ya himaya.



Mwili wa Rhoda ulikuwa tayari umeshatoka ndani ya himaya! Mlozi huyu akawa hana cha kufanya zaidi ya kuutazama ukitokomea. Roho ikimuua na kumsuguza.





***





"Tattiana!" Sauti ya mama ikaita baada ya kugonga mlango mara tatu. Kimya.



Mama akaendelea kugonga na kuita. Bado kimya. Mtoto hakutoka ndani tokea jana yake mpaka muda huo sasa ukielekea kuwa mchana.



Hakula chakula cha usiku na wala chai hajatia tumboni.



Mama akaita mara tano kabla hajaamua kuacha na kwenda sebuleni kumuita Fanty ambaye naye alimwambia amejaribu sana pasipo mafanikio. Tattiana hakuufungua mlango.



"Atakuwa ana shida gani?" Mama akauliza akiwa na uso wa mkanganyiko. Wakafika mlangoni na Fanty akaambiwa auvunje mlango wakapate kumjulia hali.



Fanty pasipo hiyana akauvunja mlango. Ndani wakamkuta Tattiana akiwa amelala kitandani. Hata hakushtuka! Wakamsogelea na kumwamsha, Tattiana hakuamka!



Tattiana hakutikisika!



Tattiana alikuwa amekunywa sumu.





****



“Mama tunafanyaje?” akataharuki Fanty. Mama akiwa amechanganyikiwa akakosa cha kujibu kwa muda kabla ya kuja kukumbuka kumpeleka Tattiana kwa daktari. Haraka wakafanya mpango wa kumsafirisha mpaka kwa daktari ambaye hakai mbali sana na eneo hilo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Daktari akampokea haraka na kumtazama kwa kumfungua kinywa na kunusa harufu. Na kwa kumtazama ncha za vidole vyake. Akagundua ni sumu ya aina gani, basi upesi akakusanya madawa yake na kuanza kuyaponda, kumpakaa na kumnywesha Tattiana ambaye kwa mbali alikuwa anahema.



“Msijali,” daktari akasema akitabasamu. “Atakuwa sawa tu.”



“Kwa muda gani?” akauliza Mama. Sura yake ilitepeta hofu.



“Itachukua muda kidogo, kwani sumu aliyokula ni kali – mti wa kolkol. Laiti msingemuwahisha yangeweza kutokea makubwa – kufa ama kupooza.”



“Kwahiyo kama muda gani anaweza kuwa mzima kabisa?” mama bado akasisitizia kuuliza. Aliona lile jambo linaweza likaathiri mahusiano ya Tattiana na mfalme. Alikuwa anataka mwanae apone, tena kwa haraka.



Lakini hilo likaonekana ni gumu kutokea. Mwili si puto kuupelekesha, mama akatakiwa kujazwa na stara.



“Kuna nini?” Melkizedek akauliza hata kabla hajatua chini toka kwenye mgongo wa farasi. Alimjongea mkewe upesi na kumuuliza nini kimetokea na mtoto yupo wapi. Huko alipotoka ameambiwa amewahishwa kwa muuguzi.



“Yupo salama sasa,” mama akasema. Akamweleza kila kitu mumewe, na jambo hilo likamstaajabisha Melkizedek. Akatafuta faagha nzuri wakakaa na mkewe na kuteta kwa undani.



“Sasa tunafanyaje?” akamuuliza mkewe. Na kabla hajajibiwa, akauliza tena: “Huoni kama huyo kijana anaweza akaja haribu sherehe?”



Mama akabinua mdomo akitikisa kichwa. Akaafiki:



“Ni kweli. Mume wangu, tufanye mpango wa kummaliza kabla hajatia futa kwenye moto.”



Lakini kwa upande wa Melkizedek hakuona haja ya papara hiyo. akatia tahadhari:



“Ila huoni tunaweza tukafanya mambo yakawa mabaya na makubwa zaidi.”



“Kivipi?”



“Kama Tattiana amethubutu kujaribu kujiua kwasababu hiyo, je pale atakaposikia Roboth amefariki nguo itavaliwa?”



“Pasipo shaka!” akasema mama. “Tattiana hatakuwa na mtu wa kumzuzua tena, na haki atatulia sasa. Kadiri Roboth anavyozidi kuwa hai, sherehe hii ipo hatiani!”



Baba akawaza na kuwazua. Bado kifuani mwake akaona kuna haja ya kutumia diplomasia, basi akapanga kuonana na Roboth ili atete naye, pengine anaweza kuelewa na kusikia.



Kutoa roho ya mtu ni haja isiyo na komo.



Kabla ya kuondoka, Melkizedek akataka kumwona mwanae. Akazama ndani alipomkuta daktari kando ya bintiye, akamtazama na kumwona amelala. Akamuuliza daktari juu ya maendeleo yake kabla hajaondoka.



“Yupo salama, ila itamchukua kama juma moja kamili kurejea hali yake ya awali.”



Pembeni alikuwapo Fanty, na baada ya kumuaga mama yake, akaenda moja kwa moja kwa Roboth kumfikishia habari juu ya hali ya dada yake. Anaumwa yu hoi, amekunywa sumu.



“Yupo wapi kwa sasa?” Roboth akauliza kwa pupa. Alishtushwa na habari hizo. Akataka hata kuchoropoka na kwenda huko, lakini Fanty akamuhasa hilo halitakuwa jema na linaweza likamwingiza matatizoni.



“Mama na baba watakuwa wanajua sababu ni wewe. Nimekuja hapa kwasababu ya kukupasha tu habari maana niliona wastahili kujua hilo,” akasema Fanty, na baada ya hapo akayeya zake akimwacha Roboth amejawa na mawazo si kidogo.



Hakuona kama nyumbani panakalika, wala hakuwa na hamu ya chakula akaacha hata kile alichokuwa anakitafuna. Mapenzi yalimkaba nyongo.





---





“Na sasa?” Phares akauliza. Alikuwa amesimama pamoja na mwanajeshi wake, yule aliyempatia kazi ya kumtazama Tattiana kwa kila nyendo.



“Na sasa yule binti amepelekwa hospitali. Hali yake haikuwa nzuri, anaonekana kupoteza fahamu.”



“Na sababu itakuwa ni nini?” Phares akaguswa. Macho yake yalikuwa na kiu ya taarifa zaidi.



“Sijajua tatizo ni nini. Lakini moja kwa moja itakuwa inahusika na yule kijana.”



“Roboth, sio?” Phares akauliza.



“Ndiye mwenyewe,” Mwanajeshi akajibu. Basi Roboth akatikisa kichwa chake na kisha akanyamaza kwa muda akikuna kidevu chake. Akawaza jambo fulani kichwani, na hiki kitu kilikuwa ni ile siri yake. Je Tattiana atakuwa kamwmabia Roboth juu ya hali yake?



Akamwagiza jicho lake la tatu, yule mwanajeshi, aende akaendelee kufuatilia kwa ukaribu, na sasa pia amtazame Roboth kwa umakini.



“Kuna haja ya kumkamata, mfalme wangu?” mwanajeshi akauliza.



“Hakuna haja hiyo,” Phares akajibu. Akasisitizia tu jambo la kuwa karibu na wahusika mpaka pale atakapoona kama kuna haja hiyo.



Basi mwanajeshi akaondoka zake upesi kwenda kutimiza majukumu.





***





“Mpenzi, unaumwa?”



“Najisikia hovyo. Mwili unaniuma.”



“Amka basi upate chochote kitu, hujala tangu asubuhi.”



Sultan alikuwa ameketi juu ya kitanda chake kikubwa kilichotandikwa shuka jeupe. Mito ilikuwa imejazana kupendezesha kitanda hichi cha thamani, ambacho nguzoze zilikuwa ni dhahabu na vishikio vyake vikiwa vya fedha.



Japokuwa kitanda hichi kilikuwa nadhifu, kinavutia na kuhamasisha usingizi, kwa Sultana huyu mkubwa kilikuwa kichungu mithili ya shubiri. Usingizi ulikuwa hauji na kilikuwa kana kwamba kina miba.



Usiku anatazama paa, kuta na dirisha za nyumba. Anageukia huku na huko wakati akimsikiza mumewe anayekoroma kwa kulowea kwenye usingizi. Analia na kumwaga machozi. Makamasi yanamchuruza.



Kila anapofumba macho, anamwona kaka yake! Wakati alipokuwa amepotelea upeponi, ni yeye ndiye alikuwa anajiri kwa kaka yake na kumwomba amrejeshe ulimwenguni, leo hii yeye ndiye mhanga! Yeye ndiye anasakwa kwa mkono wake uliomwaga damu.



Amekonda na hana taswira ya Usultana.



“Sijiskii kula, habibi,” akajibu na mdomo wake mkavu.



“Usipokula utaishije?” Sultan akamuuliza akimshika bega. “Ni muda sasa hauli, nini shida?”



Sultan alikuwa amechanganyikiwa maana kwa mujibu wa daktari wake, hakuona shida yoyote kwa mkewe. Alimpima kila aina ya vipimo avijuavyo lakini akaambulia patupu! Ana nini?



“Lazima ule. Ona unavyokuwa mdhoofu. Hapana lazima ule!”



Sultan akamnyanyua mkewe na kumsaidia kumshika mkono mpaka mahali pa kupatia chakula. Akamuagiza kijakazi alete vyakula aina zote mezani ili mkewe apate kujichagulia.



Ikafanywa kama ilivyoagizwa lakini bado tumbo la Sultana likashindwa kutia kitu tumboni. Kila harufu ya chakula aliyoisikia, ilikuwa ni kama kinyesi kwenye pua yake, akashindwa kutia kinywani!



Sultan akafadhaishwa sana. Hali hii ilimkera ndaniye na hakuwa na budi kuitafutia ufumbuzi. Siku hiyo akaita jopo lake la wazee na kuwaomba ushauri. Nini afanye? Akili yake ilikuwa imegoma kabisa kuzalisha jambo. Alikuwa mkavu.



Mzee mmoja akamsahauri amwite daktari, Sultana akamwambia alishafanya hivyo na hakuna matunda. Mzee mwingine akamshauri ampeleke kwa mtaalamu kwani atakuwa anasumbuliwa na mzimu wa mtu aliyemuua!



Bado hapo pakawa pagumu kwa Sultan, mganga yupi huyo? Ndio, kuna waganga wengi na maarufu huko nje na mbali ya himaya yake, lakini mpaka awafikie Sultana atakuwa hai?



Yule mganga pekee ambaye ndiye wanamtegemea ndiye huyo ameuawa. Hakukuwa na msaada karibu.



Akiwa mafikirioni, Sultan akamkumbuka bibi yake mke wake mdogo. Kuna siku moja mke wake mdogo alimwambia bibi yake ni mjuzi wa madawa kadhaa. Pengine anaweza akamsaidia, akawaza.



Akamshirikisha mawazo yake hayo mkewe. Akamshawishi wachukue hiyo njia.



“Hapana,” akasema Sultana. “Niache tu hapa nyumbani.”



“Nikuache alafu iweje, mke wangu? Baniani anaweza akawa mbaya, kiatu chake kikakusaidia.”



Wakazoza kwa muda kidogo kabla Sultan hajaamua kama alivyoamua. Lazima waende kule kwa mke mdogo kupata msaada.



Akawaambia wapambe na vijakazi wake wajiandae kwa ajili ya safari.





***





“Mfalme!” sauti iliita kwanguvu. Phares alikuwa ndani kuna kajikazi akikifanya, akinyoa ndevu, akashtushwa na sauti hiyo ya nguvu. Akatulia na kusikiliza tena upya, sauti ikajirudia. Basi akaacha kazi zake na kwenda mlangoni.



Alikuwa amevalia nguo za kawaida, suruali na shati juu ya kulalia. Akatazama nje kwa mashaka. Akamwona mwanajeshi amesimama kwa ukakamavu.



“Mfalme, madam Rhoda amewasili!”



“Unasema?” Phares akatoa macho.



Mwanajeshi akarejea kauli yake. Basi haraka mfalme akajivesha na kwenda kukutana na Rhoda. Bado kichwani hakuwa amejawa na imani juu ya kauli hiyo. Lakini kweli akaenda kuamini kwa kumwona mwanamke huyo akiwa anavutia kama vile amemwona kwa mara ya kwanza!



Rhoda akamkumbatia mfalme upesi, na kumwambia:



“Nimefanikisha.”



Akamwonyesha mfalme mkufu!





Phares akajazwa na tahamaki. Lakini akatazama kando na kando, hakuona watu wengine! Akamuuliza Rhoda wenzako wako wapi? Basi Rhoda akiwa na sauti ya uchungu akasema wote wameshakufa! Hawakuweza kupambana na madubwana ya huko Tanashe.



Mfalme akaguswa sana na habari hiyo. Aliumia. Alimkaribisha Rhoda ndani na akataka kujua nini kilitokea huko kwenye himaya ya walozi. Rhoda akatunga uongo akimsimulia Mfalme madubwana na vibwengo vya huko Tanashe, mfalme akashangazwa na kuogofya.



“Hakika wewe ni jasiri!” akasema. “Inataka moyo kutoka na pumzi yako katika himaya hiyo.”



Rhoda akapokea pongezi zake kwa tabasamu. Mfalme akamwambia sasa wameshapata mkufu huo aliokuwa anautaka, nini kitafuata? Rhoda akaomba akapumzike kwanza, watakuja kuongea baadae kwani amechoka hoi.



Mfalme akamwambia hamna shaka, amefurahi kumwona tena na sasa akiwa amerudi kamili. Akamsindikiza kumtoa Rhoda. Akaagiza apewe farasi na walinzi kadhaa wa kumsindikiza aendako. Amri ikatekelezwa na Rhoda akaendaze.



Basi mfalme akarejea ndani na kuketi kitini. Akawaza sana juu ya ule ujio wa Rhoda. Si kwamba aliwaza Rhoda amefanikiwaje kutoka huko Tanashe, la hasha! Bali atafanyaje endapo mwanamke huyo akijua habari za Tattiana?



Akakosa raha kwa muda kwani alimuhofia Rhoda. Hakuwa mwanamke wa kubeza hata kidogo na kila siku amekuwa akilithibitisha hilo kwa matendo yake. Akaapa kufanya mahusiano kati yake na Tattiana kuwa siri mpaka pale atakapoona sasa kuna ulazima wa kuweka wazi.



Wakati huo akiwa anafanya utaratibu wa kusoma namna mambo yatakavyoenda na Rhoda.



---



“Ameenda ndani!”



“Na mahesabu amepitia?”



“Hajayapitia!”



Walikuwa wanateta wafanyakazi wa Rhoda. Mama mmoja mtu mzima pamoja na kabinti fulani kadogo. Walitahamaki maana haikuwa kawaida kwa Rhoda kurejea na kisha kwenda ndani kujipumzisha kabla hajapitia mahesabu ya biashara yake.



Hata kama amechoka kiasi gani.



“Lakini huwezi jua, pengine atarejea,” alisema yule mtu mzima. Yule binti akabinua mdomo wake pasipo kusema jambo. mioyo yao ilikuwa imejazwa na hofu kwasababu walikuwa wanajua walichofanya.



Wafanyakazi hawa walisomba chakula cha biashara majumbani mwao huku wakijitahidi kubalansi mahesabu daftarini yasilete utata. Ila bado wakaogopa macho ya Rhoda. Na hata wakaapa endapo wakitoka salama na hili basi wataachana na huo mchezo mara moja.



Lakini hawakufahamu, hawakutakiwa kuwa na hofu kabisa kwani mwanamke yule aliyekuwa amejiweka huko ndani hakuwa Rhoda! Walikuwa ni wale wabibi wakiwa na lengo na kuteka himaya na si kuhangaika na mgahawa.



Humo ndani chumbani, Rhoda akavua nguo na kulala kitandani. Akapiga makofi mara tatu, na mara wale wabibi wakachoropoka toka mwilini mwake na kuketi kando. Wakaanza kujadili yale waliyoyaona kule kasrini!



“Kuna haja ya kummaliza Mfalme?” mmoja akauliza. Walikuwa wanafanana usiweze kuwatofautisha. Mwingine akakataa kwa kusema hawana sababu ya kumuua mfalme mpaka pale watakapohakikisha kila kitu kipo sawia.



Wakiwa wanaongea huko, mmoja wa wafanyakazi wa mgahawani akapanda juu akija chumbani mwa bosi wake, Rhoda. Ila akasita baada ya kusikia sauti kadhaa zikitoka chumbani humo. Akastaajabu ni Rhoda anateta na nani?



Basi akasimama kwa muda kusikiza. Bahati isiwe kwake hakupata kusikia ya maana, ila moja! Nalo ni kufungwa kwa mgahawa. Haraka akashuka chini kwenda kutaarifu wenzake kwamba mgahawa unafungwa.



“Hatutaweza kufanya kazi zetu kama watu hawa watakuwa wanatuzonga hapa kila siku,” walikubaliana wale wabibi. Kwahiyo basi waufunge ili wapate kutambaza madawa na mambo yao.



“Unasema nini?” akauliza mfanyakazi mmoja baada ya kusikia umbea toka kwa mwenziwe.



"Nimesikia akiongea na wenzake huko chumbani!"



"Wenzake gani na tumemwona akipandisha mwenyewe?"



Kukawa na zogo kidogo lililokuja kukoma punde baada ya kusikia sauti ya vishindo vya miguu. Alikuwa ni Rhoda! Wote wakanyamaza na kutazama.



Wakaambiwa mgahawa umefungwa. Wakaondoka wakitazama chini ila wakibeba ujumbe kwamba Rhoda alikuwa anaongea na watu chumbani.



"Kwanini umewaacha wakaondoka?" Rhoda akaongea. Ndani yake ni wale wabibi ndiyo walikuwa wakizozana. Sio wote waliafiki jambo lile la wafanyakazi kuondoka wakipendekeza wangewamaliza na kuwanyonya damu.



Lakini je kama wangelifanya hivyo si ingezua tafrani mapema kabla ya shughuli? Hapo angalau wakawa wameridhia.



Chonde chonde na tamaa za mwili!





***





“Inatosha,” akasema Malkia akimtazama mama Fluffy aliyekuwa anataka kumwongezea chakula.



“Mbona kidogo?” mama akauliza.



“Huyo ndiyo zake, huwa hali kabisa!” akadakia Fluffy akiungwa mkono na Zura. Wanawake hawa walikuwa wameketi pamoja na Seth ndani ya sebule, nyumbani kwa wakina Fluffy. Sebule hii haikuwa kubwa japo ilivutia. Chakula kingi kilikuwa kimewekwa kwenye sinia kubwa lakini kila mtu akiwa na sahani yake.



Mama akasema namna alivyofadhaishwa na yale yaliyotokea huko Sawaridi. Alishangazwa sana na fadhila ya punda waliyoionyesha binadamu wale. Akaapa: watarudi kama walivyokuwa hapo awali, utawala ule ni wa kambale asijulikane baba na mtoto ni nani.



Haki Mungu alisahau kumpatia binadamu tembe ya kuridhika!



Kwenye maongezi yao hayo, Fluffy akagusia kuhusu swala la kwenda Misri. Akamwambia mama yake ya kwamba ameshea siri hiyo pamoja na wenzake na ataongozana nao kwenda huko. Basi huo mjadala ukateka anga na mama akafunguka zaidi kuhusu huko. Habari anazozisikia na kweli yake pia.



Alisema ni safari hatari mno, ila atawaunga mkono kwakuwa ni lazima jiwe hilo lije kupinduliwa. Haliwezi likakaa hivyo milele na milele.



“Naamini mkiunganisha nguvu mtalifanikisha jambo. Mnatakiwa kuwa makini na waangalifu mno. Msiruhusu hata mmoja wenu akapotea, ama akachukuliwa!”



“Na nani?” Malkia akauliza. Mama Fluffy akawaeleza huko njiani kuna majaribu na vishawishi mbalimbali. kuna maadui wa kila aina na wenye kila ushawishi. endapo mmoja wao akipotea, basi itakuwa rahisi kwao kuanguka kwa haraka.



“Atatoa majina yenu, na punde yatakapojulikana, safari itakuwa imeshia hapo!”



Wakaaswa wasiitane kwa majina yao halisi huko njiani. Na wasije wakamwambia mtu yeyote yule jina lao halisi.



“Majina yenu yana siri kubwa na yanahusiana na maisha yenu. Yakiwa kinywani mwa adui ni hatari, atakuita na utamfuata pasipo kujua. Atakunong’oneza usingizini na kuamrisha viungo vya mwili wako na vikatii!”



Nani ambaye hakuogopeshwa na hizi habari? Zura akasafisha koo lake na kuuliza: kwani hatuwezi tukaachana na hii safari ya maruwani? Mama Fluffy akamweleza: kila kitu kikubwa na kizuri kina changamoto zake. Haitakiwi ajiulize akifeli itakuaje, bali akifaulu itakuaje.



“Endapo mkipata kitu hicho, basi mtatengeneza himaya kubwa kama ya Misri. Kila himaya itakuwa chini yenu, na hakuna hata mmoja atayenyanyua mkono wake kuwadhuru akafanikiwa.”



Malkia akaiona Goshen kichwani mwake. Hicho ndicho pekee alikuwa anawaza. Hata wenzake walipolala kupumzisha miili yao na safari ndefu, yeye kwa siri akajikata mkono kutoa damu, kisha akapotea kwenda kutembelea Goshen.





***





Asubuhi ya mapema:





Hodi ilibishwa kwa mbali, na kabla haijaruhusiwa, mlango ukafunguliwa taratibu, Roboth akaingia. Akatazama kushoto na kulia mbele na nyuma yake kabla hajaurudishia mlango taratibu na kisha akapiga hatua kumfuata Tattiana aliyekuwa amelala.



Akamuita kwa kunong’oneza. Tattiana akaamka na kumtazama, ila hakuona anamuona vema. Si kwasababu ya usingizi bali kwasababu ya sumu iliyokuwepo mwilini. Akauliza: nani wewe unayeniita mapema hii kabla jua halijakucha? Roboth akajitambulisha.



Tattiana akampapasa Roboth, na kisha akatabasamu baada ya kujidhirisha ni yeye kweli. Akamuuliza amefikaje pale? Roboth akamwambia ametoroka nyumbani kwao na amedandia ukuta wa hospitali. Amekuja hapo kumwona yeye.



“Wazazi wangu wakikukuta hapa watakuua!” akasema Tattiana.



“Sijali kama wataniua, alimradi nimekutia machoni. Nisamehe sana kwa niliyoyafanya. Sikujua kama yangeweza kukufanya ujaribu kujitoa uhai,” alisema Roboth.



Walishikana mikono wakiongea kwa kutazamana machoni, japokuwa Tattiana hakuwa anaona kitu bali kivuli. Ila haikupita muda mrefu daktari akaja kumjulia hali Tattiana. Roboth haraka akajificha nyuma ya kabati, akihema taratibu kuzuia asibainike.



“Wazazi wako wamefika. Wanataka kukuona pia,” daktari alisema akitabasamu. Tattiana naye akatabasamu ila moyoni akijazwa na hofu. Vipi kama Roboth akionekana?



Wakati daktari akitoka ndani kwenda nje kuwakaribisha wazazi, akagundua kuna alama za nyayo za viatu. Akasita na kumuuliza Tattiana: kuna yeyote aliyekuja kumwona kabla yake?



Upesi Tattiana akatikisa kichwa na kusema: Hapana, nilikuwapo mwenyewe usiku mzima na hata asubuhi hii.



“Una uhakika?” Daktari akauliza. Tattiana akatisa kichwa akisema uhakika anao. Akarudia ya kwamba alikuwa mwenyewe muda wote ule tangu alipoachwa. Daktari akaondoka zake kwenda kuwaita wazazi ambao hawakuchukua muda mrefu kabla hawajafika ndani.



Wakamjulia hali binti yao wakifurahishwa na namna ambavyo mwili wake unarejea haraka katika hali yake. Wakampongeza daktari kwa juhudi na kazi yake inayoonekana.



Mama akamwambia Tattiana: asije akarudia tena kufanya hivyo kwani ataua wazazi wake kwa presha. Walikuwa wanawaza sana kumhusu na walikosa raha kabisa ndani ya nyumba. Tattiana akaomba msamaha. Lakini wakati huo akili yake ilikuwa inamuwaza tu Roboth, na si kingine.



Alikuwa na hofu, na ilizidi pale alipomwona daktari akienda kabatini kutazama madawa. Akahisi mwili wake unatetemeka. Japokuwa hakuwa anaona vema, alijitahidi kuangaza ajue kitakachoendelea huko.



Baba akamuuliza kama kuna tatizo lolote, akakana lakini uso wake ukimsaliti.



“Mwanangu,” mama akaita. “Nakuomba sana mama, kaa mbali na yule mwanaume. Nakupenda sana na sitaki kuona ndoto yako inayoyoma. Kumbuka hii ni nafasi kubwa sana kwetu na kama tukija kuipoteza tutajutia. Msimu wa ndoa karibu unakaribia, na huenda mfalme akakuchukua. Naomba ujitunze na uwe makini sana. skauti wa mfalme wanaweza wakawa wanaranda.”



Tattiana hakusema kitu, akatazama chini. Aliogopa kunena lolote kwa kuhofia kumuumiza Roboth ambaye alikuwa na uhakika anayasikia yote hayo. Basi akaishia kutikisa kichwa.



Baba yake akamwambia mfalme aweza kuja kumjulia hali. Asije akathubutu kumwambia kilimchofanya akanywa sumu, kwani atakuwa ameharibu kila kitu. Amwambie alikula chakula njiani alichopewa na mwanamsafiri asiyemfahamu.



“Sawa?” baba akauliza.



Tattiana akatikisa tena kichwa pasipo kutia neno.



“Weka maanani, familia yetu ipo mikononi mwako,” baba akasema kabla hawajatoka kwenda nje. Roboth akatoka naye nyuma ya kabati akamuaga Tattiana. Alimwambia atakuja siku nyingine kumjulia hali. Akachoropoka kwa kupitia dirishani.



Pasipo kujua mlinzi wa mfalme alikuwa anamtazama, Roboth akaangaza huku na huko kutazama usalama wake alafu akakatiza kueleka nyumbani. Ni punde ndogo tu alipishana na familia ya Melkizedeck wakijikokota toka hospitalini.



Akatembea kwa kasi. Lakini mbele yake akakutana na mwanajeshi yule wa mfalme. Akaogopa sana. alitaka kukimbia, lakini mwanajeshi akamtahadharisha:



“Usithubutu.”



Basi akasimama na kutazama kwa woga. Moyo wake ulikuwa unakimbia kwa kasi, akihofia kwenda kuswekwa korokoroni.



Mwanajeshi akamuuliza ametokea wapi? Akadanganya. Mwanajeshi akamtahadharisha tena:



“Usithubutu.”



Kwa hofu, Roboth akaeleza ukweli kuwa alitoka kumwona Tattiana. Mwanajeshi akamuuliza kwa utaratibu kama anataka uhai wake ama lah! Roboth akasema bado anataka kuishi, basi mwanajeshi akamwambia aachane na Tattiana.



“Wewe ni nani ukashea na mfalme mwili mmoja? … Una umri mdogo kufa, ardhi bado haikutamani. Fuata ushauri wa mdomo wangu kabla hujafuata ushauri wa upanga wangu.” Mwanajeshi akajiendea. Roboth akakanyaga mguu kwenda nyumbani.



Saa hii hakuwa anakimbia, bali anatembea, tena akiwa ameweka mikono yake nyuma. Kichwa chake kilichoelemewa na mawazo kilikuwa kinatazama chini.





***





“Baba, kila kitu kipo sawa,” alisema kijana mwenye makamo ya miaka thelathini na tatu, nne ama tano. Kwa jina anaitwa Oragon. Alikuwa amevalia joho rangi nyeusi mikononi akilikunja. Nywele zake zilikuwa vurugu na ndevu zake zilizojaza uso zilikuwa zimetapakaa vijani vidogo vidogo rangi ya zambarau.



Maneno haya alikuwa anamwambia mzee yule wa baraza – kuwadi aliyefanikisha kumkutanisha Tttiana na mfalme. Mzee huyu alikuwa ameketi kwenye kiti akijipatia kahawa nyeusi ndani ya kikombe kidogo cheupe. Kwa pembeni, kulikuwa kuna birika kubwa la chuma.



“Sawa, nakuja,” akasema mzee huyu alafu akanywa mafundo mawili ya kiuoga akikimbiza lips zake toka kwenye moto wa kinywaji. Oragon akaenda zake akifuata korido nyembamba na kupotelea.



Nyumba hii haikuwa kubwa sana wala ndogo lakini ilikuwa chakavu. Hapa sebuleni ungeona viti kadhaa vya mbao imara. Kioo cha wastani juu ya ukuta na vibandiko kadhaa vya urembo, ila vikiwa vimechoka.



Ungeweza kubashiri kwa upesi nyumba hii haikuwa na jinsia ya kike ndani.



Mzee akanyanyuka akiwa amebebelea kikombe chake, akafuata korido iliyomchukua Oragon na muda si mrefu akajikuta kwenye chumba kikubwa kilichokuwa kimeshamiri matunda mekundu yenye vishiko vidogo vya majani rnagi ya zambarau.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Matunda hayo yalikuwa yamejaa pomoni na yakitengwa kimakundi makundi kutokana na hatua ambayo yamo. Ukitazama makundi makundi hayo vema, utaona kila kundi lina mwonekano sawa wa matunda, toka kwenye yale yaliyokoza mpaka yale yaliyoanza kubadilika rangi kuwa kahawia.



Mbali na matunda walikuwepo wanaume wawili vijana, mmoja ndiye yule Oragon na mwingine alikuwa ameketi kitako, akiwa naye amevalia joho jeusi na nywele zake kichwani zilikuwa nyingi mno na nyeusi ti, jinale Ottoman.



“Safi sana, mmefanya kazi vema,” alipongeza mzee akiangaza macho yake na huku akitabasamu. Akamuuliza Oragon kama tayari wameshapakia mzigo na kuuhifadhi ndani ya magunia na makapu. Oragon akamwambia tayari kila kitu.



Mzee akafurahi na kupongeza. Sasa akamwambia Ottoman akaandae farasi watatu kwa ajili ya safari. Oragon akamuuliza: huoni itakuwa hatari kusafirisha mzigo huo wakati jua lawaka? Kwanini wasingoje watu wakiwa vitandani usiku wa manane?



“La hasha!” mzee akapaza sauti. “Mchana ndiyo muda mzuri kwani hamna mtu anayetilia shaka, watadhani ni wakulima. Lakini nyakati za usiku wanajeshi wanaranda huku na huko, ni rahisi kutiliwa shaka na kukaguliwa! Utasema unapeleka wapi mzigo wakati huo?”



Ottoman akarejea na kuwaambia farasi wapo tayari kwa ajili ya safari. Mzee akamuuliza kama ameweka tayari majani ya mzeituni kwa ajili ya kukata harufu ya matunda hayo huko nje? Oragon akasema ni jambo la dakika tu, atafanya hivyo wakiwa wanashindilia matunda mengine kwa juu kuficha magendo yao.



Basi kila kilipokuwa vema machoni mwao, Oragon pamoja na Ottoman wakajipaki kwenye farasi wao wawili waliofungiwa mkokoteni.



“Kuwe makini,” mzee akawaambia, na safari ikaanza.



Ingawa walipokuwa wanaelekea hapakuwa panazidi maili tatu, nyumbani kwa Melkizedeck, ila ilikuwa ni kama vile maili mia kutoka na kile walichokuwa wamekibeba. Hii ilikuwa ni safari yao kwanza wakibeba matunda hayo ambayo ni marufuku kabisa kuuzwa ndani ya himaya wala nje ya himaya – kwa jina Cedar.



Matunda haya yalikatazwa kuuzwa kwakua ni maarufu sana kwa sumu yake kali ambayo wadhalimu huwa wanayatumia kutengenezea silaha mbalimbali zenye madhara makubwa.



Lakini pia yanatumika kwenye ulozi, wachawi wakiyatumia kwenye mauaji ama utengeneza maagano. Ndiyo maana matunda yakapewa jina la ‘matunda ya shetani’ watu hawa wakiamini yana mahusiano na lile lililomfukuza Adam na Hawa bustanini. Wengine wakiyaita ‘matunda ya nyoka’.



Kukamatwa ukiwa unayapanda, ingemgharimu mkulima mikono na macho yake. Na ukiwa unayauza, inagharimu maisha ya mfanyabiashara akinyongwa mbele ya umati wa watu.



Lakini mbali na hayo, matunda haya yalikuwa na gharama kubwa mno endapo mfanyabiashara angelipata mteja! Faida yake ilikuwa ni kabambe na inaweza kukuamsha tajiri ilhali ulilala maskini.



Wateja wake ni walozi, wakabaji wa jangwani na wakwapuzi wa ndani za himaya. Wachache sana wakiwa watu wakubwa ambao wangetaka kuyanunua kwa ulinzi binafsi.



Si ajabu mtu kukupatia kipande cha dhahabu kubadilishana na matunda haya. Ila biashara yake ilikuwa ni ya siri mno! Watu wangeliweza kuuziana mbele yako na wewe usijue kinachoendelea.



Oragon na Ottoman wakakata maili moja wakitembea na farasi wao. Waliendelea na safari wakitazama usalama kwa hali na mali. Macho yao yalikuwa huko nje yakipekua na kupekua. Na kama vile mbwa wanaonusa, wakawa wanazikwepa zile barabara zenye wanajeshi!



Wakafika mbele ya nyumba ya Melkizedek. Hapo wakakutana na walinzi waliowasimamisha na kuwataka wajitambulishe. Oragon akawambia wao ni wageni wenye miadi, haraka waruhusiwe kuingia ndani.



Walinzi hao wakawa wagumu kutii, Oragon akawafokea akitaka kuingia ndani kwa lazima. Melkizedeck alisikia makelele akatoka nje na kuwataka wakina Oragon waruhusiwe. Wakazama ndani wakielekeza farasi wao nyuma ya nyumba.



Wakapakua mzigo na kuingiza ndani upesi!



Lakini kule getini, kwa mbali kabisa, yule mlinzi wa mfalme aliona sakata lile la wakina Oragon wakiwa wanazoza na walinzi. Hakujua nini kile ambacho wakina Oragon wamebeba na kwanini wanapeleka kwa Melkizedeck.



Basi akangoja kwa nje. Na baada ya dakika kama kumi na kitu, Oragon pamoja na mwenzake wakatoka na farasi wao wakiwa watupu. Mwanajeshi huyu akaanza kuwajongea.



Punde akawafikia na kuwasimamisha. Akawauliza wametokea wapi na walikuwa wamebebelea nini.







Kigugumizi kikamkaba Oragon. Kwa muda kidogo hakuwa na cha kujibu ispokuwa kupigwa na butwaa. Mwanajeshi akautumia mwanya huo kurusha macho yake mule ndani ya toroli kupekua huku na huko.



“Kuna vitu tulivipeleka kwa bwana Melkizedek,” akasema Oragon lakini hakuwa anajiamini hata kidogo. Macho yake yalimsaliti. Hata mikono yake aliyokuwa ameilaza juu ya mapaja ilikuwa inatetemeka kwa hofu.



Mwanajeshi yule wa mfalme katika upekuzi wake, akaona kijani kidogo rangi ya zambarau, akakiokota na kukitazama, asichukue muda mrefu akawaruhusu Oragon na Ottoman waondoke zao. Akasimama na kuwatazama wakiishia, alafu akatoa lile jani na kuendelea kulitazama.



Akalinusa na kulipekuapekua. Lilikuwa geni machoni mwake, lakini siyo geni! Akili yake ilisema amewahi kuliona mahali lakini macho yake yakikataa na kusema akionacho ni kipya kinyemi.



Akaliweka lile jani mfukoni mwake, na kisha akajipaki juu ya mgongo wa farasi wake akajiondokea.



“Tatizo wewe muoga sana!” Ottoman alimsonta Oragon. “Ulivyokuwa unatetemeka maana yake nini? Ulikuwa unahofia kitu gani wakati unajua mzigo tumeshautua?”



“Otto, usijifanye zuzu, usijifanye zuzu nakwambia! Unadhani tungekamatwa pale ingekuaje? Upo tayari kwenda kunyongwa?”



Ottoman akaangua kicheko kikali.



“Sasa ukamatwe kwa ushahidi gani, Oragon? Kwa farasi na toroli?” Akauliza na tena akaangua kicheko wakati Oragon akimtazama kwa macho makavu.



“Unajua haya siyo matani,” Oragon akanena. “Unadhani yule ni mtoto mdogo kuvumbua nyendo? Ulimwona namna alivyokuwa anatazama lile jani?”



“Jani lipi?” Ottoman akauliza. Alionyesha kushtushwa. Macho akayakaza na mdomo akaachama.



“Jani lipi? – kwani hukumwona?”



“Sikumwona!” Ottoman akapaza. “Sikumwona akiwa ameshika chochote.”



Basi Oragon akamwambia mwenzake ya kwamba mwanajeshi yule aliona baki la jani la Cedar kwenye kitoroli cha farasi, na janii hilo amebaki nalo. Ottoman akawa mgumu kuamini. Na hata upesi akatazama kwenye kitoroli. La haula akaona kijani kingine. Haraka akakikwapua na kukikagua. Kilikuwa ni cha Cedar!



Akamuuliza Oragon nini watafanya? Jani la tunda lile lilikuwa tofauti na majani ya mimea mingine yoyote, kuanzia rangi mpaka na umbo. Mwanajeshi yule akijua walibebelea matunda hayo haitakuwa nongwa kwa Melkizedek?



“Shida sio hiyo tu. mwanajeshi yule atakuwa ametutilia shaka, nap engine kutuacha kwetu huru ni kwasababu anataka kufanya upelelezi, ajue wapi tulipotoa matunda hayo, na tunayafanyia kazi gani. Hiyo si tu kwamba tupo hatarini, bali Melkizedek vilevile.”



Kwa muda wakakosa cha kusema. Furaha ya kuufikisha mzigo salama ilibadilika na kuwa huzuni ghafla. Mpaka wanafika karibia na maeneo ya nyumbani ndipo wakafungua vinywa kujiuliza kama kuna haja ya kumwambia baba yao kuhusu habari za huko watokako.



“Puuzia! Huoni tutakuwa tumejichongea?” akasema Ottoman. “Mwache baba aendelee kuwa gizani na kwenye amani.”



“La hasha!” Oragon akapinga. “Unadhani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumesuluhisha tatizo ama kulitengeneza jipya? Baba ana wadhfa mkubwa serikalini, tumuweke wazi atajua namna ya kuenenda.”



Mpaka wanafika hawakuwa wamekubaliana. Yalikuwa ni majira ya jioni. Walimkuta baba yao akiwa ameketi nje ya nyumba akiwasikiliza watu wawili; mwanamke na mwanaume walioonekana kujawa na mgogoro. Wakasalimu na kwenda zao ndani bado wakiendeleza mjadala.



Baba yao alimaliza kuongea na wageni, akaingia ndani. Akauliza:



“Kunani? Mbona mzozo ndani ya nyumba yangu?”



Oragon na Ottoman wakatazamana pasipo kusema kitu.



“Si nawauliza nyie? – nini shida nasuluhisha ya wengine na huku kwangu kwafukuta?” mzee akauliza akiketi kwenye kiti chake kilichopakana na meza yenye birika la kahawa.



Oragon akajitoa kimasomaso kumweleza baba yake. Akamwambia wamefika salama huko walipoelekea, lakini kuna mwanajeshi kawaona. Baba akapigwa bumbuwazi. Macho yalimtoka na kuwa mekundu ghafla. Mkono wake wa kizee ukakamaa akamwaga kahawa yake kikombeni.



Akauliza tena kana kwamba hakusikia na mara hii alikuwa amesimama. Oragon akaogopa kurudia kunena. Lakini baba hakungoja Oragon aseme tena kauli yake, akarusha birika la kahawa! Oragon na mwenzake wakalikwepa, likagonga ukutani.



Baba akawashutumu kwa uzembe. Akawakumbushia ni kwa namna gani aliwaambia wawe makini kwani swala hilo ni la maisha na kifo.



“Tulikuwa makini, ba …” Ottoman alijaribu kufungua kinywa, baba akafoka kumkatiza:



“Nyamaza! … mnajua ni namna gani mlivyo mzigo hapa. Mnajua kabisa nafanya haya kwasababu tu ya kuwakomboa nyie na familia zenu alafu bado mnaleta uzembe! Mnataka nikaishie kitanzini na huu uzee wangu?”



Baba akakunja ngumi na kuketi chini. Akasaga meno akitafakari kwa kina. Zikapita dakika kama tano, akili yake ikawa imetulia, akawauliza wanaye kama wanamjua huyo mwanajeshi kwa sura na wapi walikutana naye?



Kwa maelezo waliyotoa, mzee akagundua mwanajeshi huyo atakuwa ametumwa na mfamle kumfuatilia Tattiana na familia yake. Akatulia na kupembua pumba na mchele. Akaagiza tena kahawa, haraka akaletewa mezani. Akanywa mafundo mawili na kusema:



“Sasa mnanisikia, hakuna namna nyingine hapa ya kujiokoa zaidi ya kuhakikisha jambo letu linakuwa siri. Kadiri jambo hili litavyokuwa siri na ndivyo na sisi tutakavyokuwa hai na kufanikiwa … Hatuwezi kumhonga mwanajeshi huyo maana bado haitaondoa siri hiyo kichwani mwake. Kwahiyo ni njia gani iliyobakia?”



Akawatazama wanaye machoni, Ottoman akajibu:



“Kumuua.”



Baba akatabasamu na kutikisa kichwa. Akasema:



“Inabidi auawe. Tena haraka iwezekanavyo!”



Oragon akaanza kutetemeka tena.





***





Usiku ulikuwa umekua sasa, watu wakawasha maginga ya moto kupata nuru. Majumbani na hata kwenye vilabu vya kunywea pombe, na huko njiani, watu walikuwa wanapewa mwanga na moto uliokuwa unametameta kwenye vichwa vya miti.



Lakini kinyume kabisa na hivyo, makazi ya Rhoda yalikuwa gizani. Hakukuwa na kona hata moja ya nyumba iliyokuwa nuruni, kote kulikuwa giza kana kwamba shimo ndani ya msitu mkubwa!



Mazingira yalikuwa tulivu mno, usingeweza kusikia kitu chochote kama ungelikuwa maeneo hayo ya karibu na pengine ungejihisi umekuwa kiziwi.



Kwa kadiri muda ulivyosonga mbele, hakukuwa na dalili ya kubadilika kwa mazingira hayo na basi hali hiyo ikawavutia wakwapuzi, wale ambao tamaa za kumiliki vitu na mali za haraka zilikuwa zimewajaa.



Kwa mbali walevi wawili wakipita, wakasimama na kutazama makazi hayo ya Rhoda. Wanaume hawa walikuwa wamebebelea chupa za vileo mikononi, wakiyumba na kuropoka kilevi. Mavazi yao yalikuwa madabwada na yanayonuka mikojo.



Mmoja akampiga mwenzake begani akamwambia: huoni kama kule kuna fursa? Vipi kama tukipata chochote kitu tukaenda kuongeza kinywaji kingine klabuni? Lakini mwenzake akajawa na tahadhari, akamuuliza vipi kama kuna watu?



“Watu gani wa kuishi gizani?” akasema yule mlevi anayemmshawishi mwenziwe. Kwa kuwa midomo ya walevi haijawahi tosheka na kileo, miguu yao ikasogelea eneo la tukio. Wakatazama kule na huku, hawakuona mtu wala dalili!



Basi yule mlevi aliyemwonyesha mwenzake fursa, akasema:



“Kaa hapa na mimi nitaingia ndani. Utakapoona kuna hatari yoyote utanitaarifu nitoke upesi!”



Akazama ndani mwenzake akiwa anayumbishwa na upepo kutazama huku na huko kuhakikisha na kudumisha usalama. Akili yake ilikuwa inawaza ni kwa namna gani atakavyokuwa anafaidi vileo vingi vya kumwaga muda si mrefu.



Hawakujiuliza wenyeji wapo wapi, na wala hawakutaka kujisumbua.



Ikapita dakika mbili … tatu … nne, mlevi aliyekuwepo ndani akaropoka:



“Alah! Kuna vitu vingi vya thamani!”



Sijui alikuwa anaonaje ndani ya kiza. Mwenzake akamhasa avikombe vyote waende zao haraka. Baada ya maongezi hayo kukawa kimya kidogo mbali na sauti ya sahani iliyoanguka.



Baada ya muda kidogo, sauti kali ya mlevi ikatoka ndani! Akalalama anauawa! Mara akalalama ananyonywa damu! Mlevi aliyetenga kama mlinzi asifanye jambo, mara akaona mkono wa mwenzake chini ya mlango. Kufumba na kufumbua, mkono huo ukavutiwa ndani!



Basi akawehuka kwa hofu. Akakimbia kadiri ya uwezo wake akipiga yowe! Kuna wauaji! Kuna wanyonya damu kwa Rhoda!





Mlevi huyo akayoyomea gizani asijulikane wapi ameelekea. Lakini sauti yake bado ikisikika akitangaza yale ya kwa Rhoda, kwamba kuna muuaji, kuna mnyonya damu! Sauti hiyo ikasikika huko mashariki, magharibi na kaskazini, na kusini.



Haukupita muda mrefu, kama robo saa hivi, maaskari watatu waliobebelea silaha, mikuki mirefu na majambia viunoni mwao, wakajiri na kusimama mlangoni mwa makazi ya Rhoda. Askari hao walikuwa wamejitengeneza na kujiandaa kivita.



Lakini tofauti na hapo nyuma, makazi ya Rhoda saa hii yalikuwa yapo kwenye mwanga! Maginga ya moto yalikuwa yamepachikwa yakiwaka kila eneo. Ilkuwa ni rahisi kumwona hata sisimizi akikatiza.



Askari mmoja akamuuliza mwenzake:



“Hivi kweli mmemuamini yule mlevi mkosa kazi?”



“Tutafanyaje sasa na tumepewa agizo?” mwenzake akamrushia swali.



“Kwani hatuwezi tukaenda kufuata mambo yetu mengine? – Kwani tunakuja kufuatiliwa kama tulifika?”



Mwenzao mwingine aliyekuwa kimya akaugonga mlango mara tatu na kupaza sauti ya mamlaka kuwa askari walikuwa wamesimama hapo. Baada ya muda mfupi, mlango ukafunguliwa na Rhoda akatokea akiwa amevalia gauni jepesi rangi ya maziwa.



Nywele zake ndefu zilikuwa zinatekenya mabega, uso wake ulionyesha uchovu, macho yake yakiwa na rangi nyekundu.



“Habari, mam?” askari wakasalimu.



“Vipi kuna nini?” Rhoda akauliza. “Mbona na mikuki na majambia muda huu?”



“Tumekuja kufanya upekuzi na majadiliano kidogo. Twaweza kuingia ndani?”



Mlango ukafunguliwa na maaskari wakazama ndani. Mazingira yalikuwa tulivu na ndani ya mipango. Kila kitu kilikuwa mahala pake usione kama kuna haja ya kuamini uhalifu ulitendeka. Lakini nyumba hii ilikuwa tupu na pweke. Hakukuwepo na mtu mwingine isipokuwa Rhoda mwenyewe.



“Mam, kuna mtu ama watu wowote waliokuja hapa kwako muda si mrefu?” askari akauliza.



“Hapana, siijapata kumwona mtu yeyote tangu giza lilipoingia,” Rhoda akajitetea kwa kujiamini. Macho yake hayakupepesa na aliwatazama maaskari kwenye viini vyao vya macho.



“Nyumba yako ilikuwa giza kwa muda gani?” askari mwingine akauliza.



“Sikumbuki ni kwa muda gani kwani nilikuwa nimelala. Si muda mrefu nimeamka. Nisingeweza kuwasha taa nikiwa usingizini,” Rhoda akatema cheche.



“Hauna mtu wa kufanya vivyo? Bila shaka hapa haupo mwenyewe, au wote mlikuwa mmelala?” askari akauliza.



Mara Rhoda akashika kifua chake kama mtu aliyekitwa na mshtuko wa moyo. Aliachama mdomo wake akikunja sura. Alikakamaza mwili wake kana kwamba amepigwa na shoti ya umeme.



“Vipi mam, upo sawa?” askari wakauliza kwa mshangao. Rhoda hakujibu kwa wakati, bali akawa anasikilizia jambo mwilini mwake kana kwamba anahisi kitu kikitembea. Alihema mafundo matatu makubwa, alafu akawatazama maaskari.



“Nipo sawa, samahanini kwa usumbufu.”



“Hamna haja ya kwenda hospitali?”



“Hamna! Nipo sawa, msijali … kwa sasa naishi mwenyewe hapa. Sina mfanyakazi wala biashara yoyote.”



Maaskari wakatazamana. Mmoja akawahi kuuliza:



“Unaishi peke yako ndani ya makazi yote haya? – Huofii?”



Rhoda akatikisa kichwa pasipo kutia neno.



“Na vipi kuhusu biashara yako, mbona kuisitisha?”



“Ni sababu tu za kiuchumi na mambo yangu binafsi.”



“Sawa, tutafanya ukaguzi mfupi ndani ya nyumba yako. Unaweza ukawa shahidi wa hilo.”



Rhoda akasita kwanza. Kuna jambo alikuwa analichambua kichwani mwake. Muda mfupi, akasema:



“Sawa, hamna shida.”



Maaskari wakakagua sebule, jikoni na eneo la mgahawa. Hawakupata chochote cha kumtilia Rhoda mashaka, basi wakaaga wapate kwenda zao. Rhoda akawatakia kheri na akasimama mlangoni akiwatazama maaskari hao wakiyoyoma.



“Si niliwaambia!” Askari mmoja akashupaa. “Mnakaa kumsikiliza mlevi! Ujinga mtupu, nini sasa mmepata!”



“Mengi tumeyapata,” akajibu mwenzake na kuongezea: “Ulikuwa unajua kama Rhoda amefunga biashara yake?”



“Ningelijua hilo hata huko mtaani!”



“Na je swala la yeye kuishi peke yake?”



“Hata hilo pia!”



“Lakini kwanini kafunga biashara yake? Sijui kama mfalme ana habari nalo hilo. Imekuwa ghafla sana!”



“Pengine inaweza ikawa sababu ya ile safari? Nasikia watu wote alioenda nao walikufa na ni yeye peke yake aliyerudi salama. Ajabu! Huwezi jua, labda anasumbuliwa na msongo wa mawazo.”



“Lakini kuishi peke yake ndiyo kutapunguza ama kukuza tatizo?”



Maaskari hawa hawakuchoka kuteta huku wakiendelea kwenda na kwenda. Walikuwa na maswali mengi sana juu ya Rhoda na hali yake, mengine wakipingana na mengine wakiungana mkono.



Rhoda aliyekuwa anawatazama maaskari wakipotelea gizani, akarudi zake ndani na kuufunga mlango. Akaenda chumbani moja kwa moja akaufunga mlango tena kwa ufunguo alafu akavua nguo zake upesi na kujilaza kitandani. Wale wabibi watatu wakatoka mwilini mwake kana kwamba pesa itokavyo ndani ya mfuko wa suruali.



Mwili wa Rhoda ukabakia kitandani usionekane kuwa hata na lepe la uhai ama fahamu.



“Ndiyo nini ulikuwa unataka kufanya? Ulikuwa unataka kuwatafuna na maaskari wale pia?” bibi mmoja aliwaka akimsontea kidole mwenzake aliyekuwa amesimama katikati.



“Kwanini unakuwa hivyo lakini? Unashindwa kujizuia?” akasema bibi mwingine upande wa kushoto, naye akimsontea mwenzake wa katikati. “Ni uroho wa kiasi gani huo? Ni uchu kiasi gani mpaka unashindwa kujizuia!”



“Nijizuie mpaka lini?” akawaka bibi wa katikati. “Nijizuie mpaka lini? Kama nyie mwaweza kujizuia. mimi siwezi! Ni siku ya ngapi sasa? Mlitaka tuwaache wale wafanyakazi, tukawaacha! Kwenda kuwinda huko nje, hamtaki! Mwataka nini?”



“Lakini haya hayakuwa makubaliano yetu. Vipi kama leo huko watu wote wakajua sisi ni walozi toka Tanashe? Mpango wetu utatimia?”



“Mpango upi?” akashupaa msemwaji.



“Mpango wa kugeuza hapa kuwa kasri ya mfalme. Kummaliza mfalme na kuitwaa milki yake yote hii! Huujui mpango huo?”



“Mpaka utimie mimi n’takuwa nakula na kunywa nini? – zile nyama kavu za ng’ombe na ilhali napishana na harufu ya damu na nyama ya binadamu kila nikatizapo?”



Mzozo ukawa mkubwa, lakini ukaja kukoma punde baada ya kukubaliana kesho kwenda kumwona mfalme Phares. Lengo kubwa ni kujua mfalme huyo ana mpango gani na kama wanaweza wakautimiza mpango wao haraka iwezekanavyo.



Usiku ukazidi kwenda na kukua zaidi. Lakini kama haikutosha, ndani ya usiku huo, bibi yule msemwaji akatengeneza hirizi yake ya unga na kuwapulizia wenzake wakalala kama mizoga. Akatoka zake ndani na kwenda huko nje kwenda kutafuta nyama na damu!





***





Upepo mkali ukapuliza ghafla na kunyanyua blanketi alilokuwa amejifunika Fluffy. Walikuwa wamelala juu ya mwinuko kidogo mkavu wenye uhaba wa mimea. Eneo hilo lilikuwa lina miinuko kadha wa kadha, na ilikuwa ni mojawapo ya njia wanayotakiwa kukatiza wakiwa ndo kwanza wapo kwenye safari yao changa ya kuelekea Misri.



Fluffy akapigwa na baridi kali, akaamka na kuona blanketi limechepuka. Kabla hajanyanyuka, akatazama kwanza kushoto na kulia kwa usalama kisha akauamsha mwili wake kufuata blanketi.



Mbali kidogo na walipojilaza, walikuwa wamekaa farasi wanne, na pembeni kuna mizigo. Fluffy akiwa anarejea mahali walipokuwa wamelala, akagundua kuna mtu mmoja hakuwapo. Haraka akapiga hatua kwenda kutazama. Alikuwa ni Malkia!



Pasipo kumwamsha mtu, akatazama huku na huko, hakuona alama yoyote ya Malkia. Basi akapatwa na maswali!



Mara punde, Malkia akajiri nyuma yake. Alikuwa na uso wenye hofu na akihema kana kwamba ametoka mashindanoni. Fluffy akakurupuka kwa hofu na kumuuliza ni wapi alipokuwa?



Malkia akavuta kwanza pumzi. Akaketi kitako na kumwambia Fluffy:



“Kule Goshen kuna shetani! … kule Goshen kuna shetani ananyonya damu na kuua watu!”



“Shetani gani?” Fluffy akapaliwa na swali. Mara Zura na Seth nao wakaamka na kubutwaa kumwona Malkia akiwa haehae.





“Kuna nini?” Zura akauliza. Walitambaliwa na hofu kwenye nyuso zao na pengine walidhani kuna jambo limetokea pale kwenye mazingira yao. Wakatazama huku na huko kwa woga.



Malkia akamdaka Zura na kumwambia ametoka Goshen na huko ameona mwanamke mzee akiua watu na kuwanyonya damu. Mwanamke huyo ni mlozi na ni mkazi wa huko Tanashe.



“Amefikaje huko?” Akauliza Zura.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



“Sijui amefikaje, sijui kumetokea kitu gani ndani ya Goshen. Hakupo salama kabisa!” akasema Malkia akiwa na uso wenye tambazi la woga haswa. Alitazama huku na huku, kule na kule.



“Sasa tunafanyaje?” akauliza Malkia. “Tunafanyaje na hao wabibi wameshaingia ndani ya Goshen?” Malkia akapapatika. Zura akamshika na kumtuliza, akamwambia:



“Huna haja ya kuhofia maana hofu yako haitasaidia jambo. Tuliza kwanza kichwa.”



“Zura, natulizaje kichwa na watu wangu wanauawa? Nitakaaje na amani? Na unajuaje kama wapo walozi wengi ndani ya himaya?”



“Najua mawazo yote hayo mwanangu. Lakini tukibebwa na pande la hofu, mioyo ikitwaliwa na kihoro, akili itafanya kazi? shusha kwanza pumzi yako, tuliza moyo wako na basi akili yako itafanya kazi ya kufanya maamuzi yaliyo bora.”



Malkia akanyamaza na huku macho yake yakiwa mekundu. Ni ghafla usiku wao ukageuka kuwa mchana kwa watu kuketi na kuanza kuteta badala ya kulala. Seth alikusanya vijikuni akawasha moto kwa ajili ya kuwapa joto.



Wakauzingira moto huo wakiwa wamejikumbatia.



“Kutakuwa kuna namna ambayo mlozi huyo ameitumia kuingilia ndani ya Goshen,” akasema Zura. “Na namna hizo huwa ni mbili tu, mosi, kwa kutumia mwili wa binadamu kama kinga dhidi ya dawa zilizowekwa mipakani, na pili, hii huwa aghalabu sana, ni kwa kujiboresha kilozi ili kupambana na madawa yaliyowekwa mpakani. Hatujajua mlozi huyo ameingilia na njia gani, ila naamini itakuwa kwa njia ya kwanza.”



“Kwanini unaamini hivyo?” akauliza Fluffy.



“Kwasababu kama mlozi huyo angeingia toka Tanashe kwa nguvu za kujiimarisha kilozi, basi angekuwa tayari ameshaibeba himaya nzima na kuiweka kiganjani. Kusingekuwa na binadamu wa kumuzia hata kidogo. Angekuwa na nguvu kubwa ya kutetemesha himaya!”



“Sasa atakuwa ametumia mwili gani wakati mimi nilimwona akiwa kwenye mwili wake halisi?” akauliza Malkia.



“Kutumia mwili wa binadamu ni kwa madhumuni ya kuvukia tu mpaka na si kingine. Punde mlozi anapotoka ndani ya Tanashe anaweza akaishi miongoni mwetu kama binadamu wa kawaida na msitambue. Anaweza akajivika mwili alioutumia au lah! Si lazima.”



“Atakuwa ametumia mwili wa nani sasa? na huyo mtu alifikaje huko Tanashe wakati katazo lajulikana. Alama zimebandikwa kwenye kila kona ya mpaka kwamba usivuke kwenda ng’ambo ya pili?” Malkia akanena.



“Hilo ni swali la kujiuliza,” akasema Zura. “Lakini halitakuwa na umuhimu wowote kwa sasa, bali kufikiria namna ya kumkabili ama kuwakabili walozi hao walioingia Goshen.”



“Basi nina wazo!” Seth akapaza sauti. Watu wote wakamuazima macho na masikio.



“Malkia ana uwezo wa kwenda Goshen kwa kupitia mkufu wake, yeye ana fursa ya kuwahabarisha watu wa huko juu ya uvamizi wa watu hao ndani ya himaya?”



“Atafanyaje hayo na wakati himayani wanaamini yeye ni mfu?” Zura akauliza.



“Hilo wala halina shida, atakachokifanya yeye ni kumnong’oneza mfalme akiwa usingizini, mara tatu! Kuna walozi himayani! Kuna walozi himayani! Kuna walozi himayani! Baada ya hapo atataja makazi ya walozi hao. Basi punde mfalme atakapoamka, atajua ni ndoto, na mwenye hekima atachukua hatua. Asipofanya hivyo, atamtembelea tena usiku ujao!”



“Na vipi kama Malkia akipambana na mlozi huyo?” Fluffy akauliza.



“Hilo si wazo jema!” Seth akapinga upesi. “Endapo Malkia akiuawa akiwa kwenye kivuli chake cha mkufu, hataweza tena kuuongoza mkufu wake. Hatakuwa na mamlaka hayo tena!”



Basi maongezi hayo yakawa yamekomea hapo kabla ya mengine kushika hatamu, wakaanza kujadili kuhusu safari yao ya kwenda himaya ya Misri.



Usiku ulikuwa uanendelea kuyoyoma na hawakuona kama kuna haja ya kulala tena, kwani muda si mrefu walitakiwa kujikusanya na kuchanja njia.



“Sikumbuki vema,” alisema Seth. “Ni muda mrefu kidogo sijakatiza wala kutumia hii njia lakini nashauri tukatumia njia ya upande wa mashariki.”



“Una uhakika itakuwa salama?” akauliza Zura.



“Hakuna usalama watu wakiwa nyikani,” akajibu Seth na kuongezea: “Hakuna njia yoyote iliyo salama. Tukisema tutafute iliyo salama, basi tutageuza migongo yetu kurudi nyumbani. Ila kuna ambazo zaweza kuwa na unafuu!”



“Ndiyo hiyo ya Mashariki?” akauliza Fluffy.



“Ndio, kwa mujibu wa mawazo yangu, unajua mimi siyo Dummy. Ila ninachojua ni kwamba katika njia hizi, kuna mojawapo ina watu wa Azeth!”



“Ndiyo wakina nani hao?” Malkia akauliza.



“Ni watu jamii ndogo ya majayanti! Wakubwa kupanda juu kwa idadi ya mikono kumi na miwili ya mtu mzima, na upana magogo matano ya mzeituni.”



Habari hizo zikawastaajabisha watu. hakuna aliyewahi kusikia habari za watu hao hapo kabla.



“Walikuwa wengi mno na tishio kwa himaya kadha wa kadha, lakini baadae baa kubwa la njaa lilipotokea, wakaanza kulana wenyewe kwa wenyewe. Tunaweza kusema kwa kiasi kikubwa walijipunguza wao kwa wao. na kwa sisi binadamu, hivyo vilikuwa ni vita vya panzi … mpaka sasa, ni koo moja tu ya jamii hiyo ndiyo iliyobakia. Lakini hilo halimaanishi kuwa siyo hatarishi, la hasha! Ni viumbe wasiopenda kuingiliwa, hawana urafiki na binadamu. Na zaidi ya yote wanakula nyama ya binadamu …”



“Hakuna namna ambayo tunaweza tukatumia kujikinga?” akauliza Fluffy.



“Sidhani,” akajibu Seth akitikisa kichwa. “Lugha yao ni ngumu sana, nilijiaribu kujifunza lakini bado nikatoka mtupu, lakini naweza kujaribu kuwasiliana nao endapo tukikutana nao.”



Majadiliano hayo yakawavusha giza mpaka alfajiri. Wakafungua vinywa, na kuanza na safari, wakiielekea kule ambapo Seth alikuwa amewashauri, upande wa Mashariki.



Lakini hakuna hata mmoja wao aliyekuwa anajua kuwa upande huo ndiyo ule wanaotakiwa kuukwepa. Ulikuwa ndiyo upande wenye viumbe walivyotoka kuvizungumzia – Azeth!





***





“Hatujamwona!” Oragon alimwambia babaye aliyekuwa ameketi kwenye kiti chake akinywa kahawa taratibu kuondoa baridi la asubuhi.



Oragon alikuwa amesimama upande wa kulia wa mwenzake: Ottoman aliyekuwa amejikalia kimya. Mikononi mwao wote walikuwa wamebebelea majambia ya vita, na wakiwa wamevalia nguo za mapambano.



Baba akanywa fundo moja la kahawa yake, alafu akaijazilishia na nyingine toka kwneye birika.



“Kwahiyo kama hamjamwona, mmepanga nini?” baba akauliza. Oragon akamtazama mwenzake Ottoman, kisha kimya.



“Nimeuliza, kwahiyo kama hamjamwona mmepanga nini? Au hamjui kwamba huyo mtu amekuwa ni hatarishi sana kwetu? Mnayachukuliaje haya mambo? … mnaendaje kumsaka mtu usiku mzima na kurudi pasipo majibu ya maana! Mlienda kutafuta ama kulala?”



“Tumetafuta, baba! Tumetafuta katika mazingira yale yale lakini hatukufanikiwa kabisa. Pengine alikuwa ametoka,” akasema Ottoman. Mwenzake, Oragon, akajazilishia:



“Tutaendelea tena kumtafuta, mpaka tumpate!”



Baba akanyanyuka na kwenda zake chumbani. Akarudi akiwa amevalia joho lake safi na fimbo yake mkononi.



“Naenda huko hekaluni, n’tayajulia yote huko! Pumbavu nyie!” akatoka ndani na kujiweka kwenye mgongo wa farasi kuanza safari ya kwenda kwa mfalme.



Kichwani mwake alijawa na mawazo. Kama mawazo hayo yangekuwa na uzito wa kilo, farasi yule asingeweza kumbeba hata kidogo.



Baada ya muda mchache akawa amefika makaoni. Akapita getini akipewa heshima zote, moja kwa moja akaenda kuonana na mfalme. Akamkuta kiongozi huyo akiwa ameketi na yule mwanajeshi ambaye watoto wake wametoka kumtafuta usiku mzima na kumkosa.



Moyo wake ukapiga fundo kubwa.





“Alah!” mfalme akahamaki. “Karibu sana mzee, mbona ujio wa ghafla hivi?”



“Niwie radhi mfalme wangu, hakika n’takuwa nimekukwaza!” akasema mzee akiinamisha uso wake. Mfalme akamkarimu na hata akamtaka mwanjeshi wake awape faragha wapate kuteta.



“Niambie ni lipi hilo shida?” mfalme akauliza. Walikuwa tayari wameshaketi mezani wakiwa tayari wamehudumiwa kila aina ya chakula.



“mfalme wangu, hamna shida ya kushtusha bali nimekuja kwa ajili ya kesi yangu ya kale. Umefikia wapi kumpata yule mwanamwali? Naona kimya,” mzee akasema akimtazama mfalme kwa shauku. Basi mfalme akacheka na chakulache mdomoni. Akasema:



“Mzee! Wajua mfalme hawezi kuingiza mguu mahali pasipo salama. Nafanya tafiti kwanza kama anastahili kuletwa ndani ya kasri!”



“Hakika!” mzee akaunga mkono. “Na hilo ndilo ambalo limenikimbiza kuja hapa upesi. Je, mfalme wangu, nani umemuweka huko kumfuatilia mwanamwali huyu?”



Mfalme akasema ni yule mwanajeshi aliyemkuta naye, na pia akasema yale ambayo kibaraka wake huyo ameyagundua kwa Tattiana. Mzee akatahamaki, akasema:



“Mfalme, kwanini unamwachia kijana huyo badala ya kummaliza? Anawezaje kutaka kula meza moja na mfalme na ilhali mikono yak ni michafu?”



Mfalme akatikisa kichwa na kutabasamu kwa mbali. Hakuona haja ya kufanya hivyo kwani alikuwa anaamini upendo hauilazimshwi. Si kwakuwa yeye ni mfalme na basi kila amtakaye atamtaka pia.



“Ninamfuatilia kujua kama ananipenda na yuko radhi kuwa nami, na si vinginevyo. Kama moyo wake haupo upande wangu, basi akatafute furaha uko kwingine. Si kwasababu mimi ni mfalme basi nina vibali vya mioyo ya watu.”



Jambo hili halikuwa jema sana kwa mzee wa baraza. Kwake ilikuwa ni lazima Tattiana afunge ndoa na mfalme kwasababu ya biashara yake. Kwake hilo halikuwa chaguo bali lazima. Hivyo akaapa kufanya jambo juu ya hilo lakini asisahau lililomleta, akaulizia na ratiba ya mwanajeshi yule kule kwa Tattiana. Mfalme akamweleza maelezo ambayo kwake aliyaona yana tija. Basi akaaga na kwenda zake.



Akasindikizwa na mawazo kichwani. Akafika nyumbani na kuteta na wanaye. Akawaambia juu ya mwanajeshi yule na ratiba zake na kisha akawatonya juu ya Tattiana na mahusiano na mwanaume mwingine.



“Inabidi mwanaume huyo ashghulikiwe upesi. Endapo akimfanya mfalme akamwacha Tattiana, basi tutakuwa kwenye hali mbaya sana.”



Basi akawapa wanaye kazi mbili, mosi kummaliza yule kibaraka wa mfalme, na pili wamshughulikie Roboth, yaani wamuue. Yote hayo yafanyike kwa siri pasipo kutengeneza venge la mashaka.



“Inafaa wakauawa kwa sumu ya siku mbili,” mzee akapendekeza.



“Tutaitolea wapi sumu hiyo?” akauliza Ottoman. Mzee akawapa kazi ya kwenda kumtafuta mbapa huko maporini na ni yeye ndiye atafanya utaalamu wa kutengeneza sumu hiyo kwa ustadi.



“Baba…” akaita Oragon, “Unamaanisha Mbapa nyoka?” akastaajabu.



“Ndiye mwenyewe,” mzee akaajibu. “Unadhani utaipata sumu kwa nyani?”



Hakutaka mjadala kwenye hilo, akawataka waende upesi kutekeleza agizo. Wakiwahi watamkuta jikoni akiandaa vihitajika.





***





“Tupumzike kwa ajili ya kupata chakula sasa,” akasema Malkia akishuka toka kwenye mgongo wa farasi. Wakasimamisha farasi zao na kuketi chini ya mti mkubwa wenye kivuli cha kutosha. Wakatoa vyakula kwenye vihifadhio vyao na kuanza kutafuna. Vilikuwa ni vyakula vikavu walivyovishushia na vinywaji.



“Hivi vyakula havitaweza kumaliza hata robo ya safari yetu,” alisema Seth. “Kuna haja ya kutafuta vyakula kama tunahitaji kuishi.”



“Tutavipatia wapi vyakula hivyo?” akauliza Zura. Malkia na Fluffy walikuwa watazamaji wakiendelea kutafuna.



“Humuhumu ndani ya msitu,” akasema Seth. “Kuna matunda na wanyama. Tukamate kadiri tuwezavyo kwani hatupo mbali na jangwa. Tusipokuwa na akiba ya kutosha, hatutaweza kutoka hai kwenye jangwa hilo.”



Kila mtu akakubaliana na wazo la Seth, wale kisha watazame ndani ya msitu nini watapata vya kutia mifukoni.



Seth alipomaliza kula, akanyanyuka na kusonga kando kwa ajili ya haja ndogo. Akarejea upesi na kufunga kila kitu kwenye mifuko na kuweka juu ya farasi. Lakini uso wake ulikuwa na mashaka, na mikono yake ilikuwa inatetemeka.



Malkia akamtazama na kumuuliza:



“Seth, kuna shida?”



Seth hakusema kitu. Akahema kwanza na kutazama chini. Alikuwa amepaliwa woga, ukimwona ukamjua.



“Tuondokeni upesi!” akaropoka akipanda juu ya farasi.



“Seth, kuna nini?” Fluffy akaropoka. Wakawa sasa wanatazama huku na huko kana kwamba wana miadi na vibwengo.



“Tumepita njia ya Azeth!” Seth akasema. Uso wake ulikuwa na mafinyazi ya woga. “Pandeni farasi tuondoke upesi kabla hatujakutwa hapa!”



“Si ulisema lakini …” Fluffy akataka tia neno, Seth akamkatiza, “Hatuna tena muda huo. Nilikosea! Panda farasi twende!”



Wakapanda farasi na safari ikaendelea kwa kasi mno! Seth akawaambia alipoenda kule kukojoa, kwa bahati akaona nyayo ya Azeth.



“Ni kubwa kutengeneza bwawa la kuogelea. Na nyayo hizo si za muda mrefu!”



Kama dakika tano kupita wakiwa wameshaondoka, jitu kubwa likafika kwenye mti waliokuwa wameketi wakila. Alikuwa amevalia ngozi ngumu yenye manyoya manyoya akiziba sehemu zake za siri. Masikio yake yalikuwa marefu, pua ndefu na macho makubwa yaliyozama ndani. Ndevu zake zilikuwa nyingi zikitiririka mpaka kitovuni mwake. Mkono wake wa kushoto alikuwa ameshikilia gongo kubwa.



Alikuwa ni mkubwa haswa. Tembea yake ilikuwa inatikisa ardhi na hata matunda yale yaliyokuwa yamekwiva mtini yakadondoka yenyewe.



Jitu hilo lililokuwa pweke, likatazama pale chini ya mti na kuokota mabaki ya chakula yaliyoachwa hapo. Akanusanusa mabaki hayo, akatupa macho yake huku na huko. Akatazama nyayo, akagundua kulikuwapo na binadamu na farasi wakiwa wamekatiza hapo.



Akatazama njia kwa urefu wake wote lakini hakuona kitu. Basi akapaza sauti yake kubwa akisema:



“Hababth hababth! Tefu na shik! Tefu na shik! Worota nabigh!”



Sauti yake ilikuwa kubwa mno zaidi ya ile ya kipaza sauti. Ilisafiri kwenda kila pande ya maeneo hayo ya karibu na wenzake wote wakaisikia. Habari habari! Kuna wavamizi! Kuna wavamizi! Funga malango!



Akarudia mara mbili kusema na kisha akaanza kukimbia. Sauti yake haikubagua, ikawafikia hata Malkia na wenzake.



“Wamegundua uwepo wetu!” Seth akaropoka. “Ongeza kasi!”



Wakakimbia haraka sana waking’ang’ania barabara. Lakini baada ya punde, mbele yao wakaona magogo makubwa yakirushiwa barabarani. Magogo hayo yalikuwa makubwa kiasi kwamba hawakuona hata mbele walipokuwa wanaelekea.



“Tunafanyaje sasa?” Zura akayuya kwa tepe za hofu. Kule mbele wakatokea majitu matatu waliotupia yale magogo njiani, wakaanza kusogea kuwafuata Malkia na wenzake.



“Geuza, tukimbie!” Malkia akaagiza. Basi upesi wakageuka na kuanza kurudi nyuma walipotokea. Napo hawakukimbia kwa muda mrefu, wakaona majitu mengine mawili yakijongea. Sasa hawakuwa na pa kukimbilia, isipokuwa pembeni, ndani ya misitu!



Haraka wakazama humo na farasi zao. Lakini farasi hawakuweza kukimbia sababu ya idadi kubwa ya miti, na hata matope, basi Malkia na wenzake, hawakuwa na budi, wakalazimika kushuka wakimbie kwa miguu.



Kabla hawajakimbia, Malkia akambusu farasi wake na kumnong’oneza. Farasi akakimbia upesi kuelekea kushoto kwake wakati mwenzake akiwa haelewi cha kufanya. Malkia akiwa nyuma, wakakimbia kadiri ya uwezo wa miguu yao, wakizama msituni, kujiokoa na majitu yaliyokuwa yanakuja kwa kasi ya kishindo kikuu!



Majitu hayo yakamkamata farasi aliyekuwa amebakia akisimama, wakamtafuna kama karanga! Kasi yao wakipasua na kusukuma miti ilikuwa kubwa, na punde wakawa wamewafikia walengwa wao kiasi cha kunyoosha mikono kuwadaka. Lakini ghafla wakasimama na kuwatazama Malkia na wenzake wakiendelea kukimbia kwa juhudi zote.



Hatua tatu mbele, mara Malkia na wenzake wakajikuta wameingia mtegoni. Ardhi ilifunguka wakazama ndani ya shimo kubwa lenye giza, huo ukawa mwisho wa mbio zao za sakafuni.



Baada ya muda mfupi, Malkia na wenzake wakawa wamefungiwa kwenye magogo makubwa, wamewekwa begani mwa majitu wakipelekwa wasikokufahamu.



Kwa mwendo wa kama dakika kumi, wakafika kwenye kijiji cha wana Azeth, kwenye kijiji hicho hakukuwa na nyumba hata moja bali mashimo makubwa. Majitu hayo yalikuwa yakiishi ndani ya mashimo hayo kama panya buku.



Magogo yakatupwa chini mbele ya jitu moja lililokuwa limevalia bangili na mikufu ya mafuvu ya vichwa vya watu. Kisha wale waliowaleta wakina Malkia wakainamisha vichwa vyao na kusema:



“Khari eta bumva … khari atta kevha.”



Lile jitu lililovalia mkufu wa mafuvu likabinua mdomo wake na kisha likasimama. Likanyoosha mikono yake juu ya kupaza sauti kuwaambia majitu yaliyokuwa yamesimama na kumtazama kwa ukakamavu.



“Veta zhi voyaaaaaa!”



Majitu yale yakaanza kushangilia yakicheza mithili ya watoto. Malkia akamuuliza Seth:



“Nini wanaongea?”



Seth akamwambia kwa sauti ya chini, na sura yake ikiwa imelowa huzuni:



“Wanatupeleka motoni!”



Kabla Malkia hata hajafikiria cha kufanya, magogo yakanyanyuliwa na yale majitu yakaanza kuimba yakielekea upande wao wa kaskazini. Wakafika kwenye tanuri kubwa, wakawasha moto.



Zura akamtazama Malkia, macho yake yalikuwa mekundu, akamuuliza:



“Malkia, ndiyo tunakufa?”



Malkia akamtazama pasipo kusema jambo. Akajikuta chozi linamtoka.





Hakushindwa kujinasua toka kwenye huo mtego lakini hakutaka kutoka peke yake. Hawezi kuokoa nafsi yake akawaacha wenzake wateketee. Akajikuta anajuta sana kwanini usiku kuamkia siku hiyo hakuwa amelala kwani angelipata kuyaona haya yote kwa kupitia njozi, na basi wakajiokoa.



“Teraneth abissa yaka yaka twee! Kashek vatta, munir vuninga!” akasema lile jitu lenye mkufu wa mafuvu ya binadamu. Mdomo wake ulikuwa mpana, sura ya kutisha, sauti kubwa ya kutetemesha anga. Akiwa hapa kwenye mwanga, akaonekana vema, kumbe jicho lake la kushoto lilikuwa limepooza, halikuwa linaona na rangi yake ilikuwa nyeupe kahawia.



Akaendelea kuongea na kuongea. Na majitu yote yalikuwa kimya yakimtazama na kumsikiza, lakini pia yakijawa na uchu kutamani nyama ya Malkia na wenzake. Hata sijui wangeweza kuwaganaje baada ya nyama hiyo kuchomwa.



Lakini katikati ya maneno hayo, mawingu yakaanza kujikusanya angani. Jua likamezwa, mwanga ukawa hafifu. Haikupita punde ndefu, matone ya mvua yakaanza kushuka taratibu taratibu, mara yakachanganyia kwa kasi. Moto wa tanuru ukazima!



Yule jitu lenye mkufu wa mafuvu ya binadamu likaagiza Malkia na wenzake wafunguliwe na wakatupiwe ndani ya jela kwa ajili ya kuchomwa siku au muda mwingine. Wakaenda kutupiwa ndani ya shimo na geti kubwa, zito la miti likaziba njia.



Ndani ya shimo kulikuwa kuna mwanga hafifu, na joto pia. Na maji ya mvua yalikuwa yanaingia sema pasipo kuwafikia. Shimo lilikuwa limechimbwa na kukukunjwa kona mbili. Maji yaliyoingia yalipitiliza kuzamia chini.



“Malkia, ile ilikuwa jitihada yako?” akauliza Zura. Malkia akatikisa kichwa.



“Hapana, sikufanya chochote kile. Pengine muda wetu wa kufa bado haujawadia.”



“Inabidi sasa tufanye jambo. Hatuwezi tukakaa kungojea mpaka tuje kuchomwa,” akashauri Fluffy. Seth akasafisha koo lake na kusema:



“Wanaamini Mungu wao hayupo tayari kuipokea sadaka yao na ndiyo maana mvua ikanyesha. Kwahiyo kwa sasa wapo kwenye maombi kumwomba Mungu wao akubali sadaka yao. Endpao Mungu wao akiikubali, basi watarudia zoezi lao muda kama huu kesho yake.”



Zilipopita kama dakika kumi, wakasikia sauti ya kufunguliwa lango, na mara kishindo kikubwa kilichowatikisa.



“Wanakuja!” Zura akapayuka. Wakasogelea ukutani kwa woga. Likatokea jitu moja lililowatazama kwa mahesabu, na kisha likamyaka Malkia.



“Shabi naba atruu!” akanguruma jitu hilo. Seth na wenzake wakajaribu kumkomboa Malkia pasipo mafanikio. Jitu lile liliwasukuma kwa kuwapiga kumbo kwa mkono wake tu, wote wakaachwa hoi hawajiwezi. Likaondoka na Malkia!



“Wanampeleka wapi?” akauliza Zura. Alikuwa ana hofu. Macho yake yalikuwa mekundu akihema kwa pupa.



“Sijui wanampeleka wapi,” akasema Seth. “Wamesema yeye ndiye ameteuliwa.”



“Ameteuliwa na nani?” Zura akauliza tena.



“Sijui!” akajibu Seth akipandisha mabega.



Malkia akapelekwa mpaka mbele ya yule jitu kiongozi, lilikuwa limeketi kwenye kigoda kikubwa chini ya mti mkubwa mithili ya mbuyu, nyuma yake lilikuwa limesimama jitu kubwa mkononi limebebelea rungu. Akaamrishwa apige magoti. Mvua bado ilikuwa inanyesha lakini chini ya mti huo haikuwa inapenya.



Yule Jitu likamwongelesha Malkia kwa lugha isiyoeleweka, Malkia akashindwa kujua dhamira yake nini. Kwa ishara akamwambia hamwelewi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Kule shimoni, bado Seth na Zura walikuwa wanaendelea kuulizana maswali ambayo hayakuwa na majibu. Zura alikuwa anataka kujua Malkia atakuwa anafanywa nini huko alipopelekwa. Alikuwa anataka kujua kama kuna namna ya kumkomboa Malkia na wao wenyewe, maswali ambayo Seth hakuwa na majibu yake.



Ndani ya muda mfupi, wakasikia lango linafunguliwa na mara kishindo kikubwa. Wakamwona yule jitu ambalo lilikuja mara ya kwanza kumchukua Malkia. Likawatazama kwa mahesabu, na mara likaegesha macho yake kwa Seth na kusema;



“Bharu zuk pazam?” wewe ndiye unayejua lugha? Seth akatikisa kichwa chake akasema:



“Yu!” ndio.



Yule jitu likamnyakua Seth na kwenda naye. Likaenda kumtupia mbele ya kiongozi wao. Basi akaanza kuulizwa maswali na yeye akiyakalimani kumwelezea Malkia, na majibu ya Malkia akiyapeleka kwa jitu.



Jitu lile kiongozi lilikuwa linataka kujua wao ni wakina nani na wametokea wapi. Kwanini sadaka yao imekataliwa na mungu wao, haijawahi kutokea. Malkia akajieleza kinaga ubaga. Jitu lile likataka kujua kuhusu huko wanapoeanda, yani Misri. Malkia akamdanganya kwa kumwambia kuna kitu wanaenda kuchukua.



“Nabir sik batchu!” akasema yule jitu kiongozi. Yaani na yeye anataka kwenda huko. Malkia akakataa kwa jitihada zote, lakini lile jitu halikutaka kuelewa abadani. Akasema kama hawataki kwenda naye, basi atawatoa sadaka hata kwa lazima.



“Marheb na kebu. Tulisha mujhu na beedi!” akawapatia muda wa kufikiria na kutoa majibu mpaka pale kesho asubuhi. Jitu lile lililowaleta likawakusanya na kuwarejesha kwenye shimo na kuwafungia humo.





***





“Umemaliza kufanya kazi yako?” Sauti ya mama ikauliza. Roboth alikuwa chumbani na mama alikuwa amesimama mlangoni akiegesha sikio lake mlangoni.



“Nimemaliza kila kitu mama, tayari!” Roboth akajibu tokea ndani.



“Una uhakika? Unajua sitaki kugombana na mtu, Robo!”



“Nimemaliza kweli mama!” Roboth akapaza sauti. Mara huko nje ikasikika sauti ya farasi, mama akashtuka, na upesi akatoka kwenda kutazama. Akakuta farasi watatu wakiwa wamewabebelea wanaume watatu, wawili miongoni mwao walikuwa ni wanajeshi waliobebelea mikuki, na mmoja aliyekuwa ametangulia mbele, ni bwana Melkizedek.



Pasipo kusalimu, Melkizedek akashuka toka kwenye mgongo wa farasi na kumuuliza mama yupo wapi mwanaye, Roboth?



“Kuna nini bwana?” mama akauliza. “Karibuni ndani, si vema wageni kukomea nje.”



“Hauna sebule ya kunikaribisha mimi kuingia ndani. Mwambie huyo mwanao namhitaji hapa nje sasa hivi!”



“Amefanya nini lakini?”



“Muite hapa, na utajua.”



Mama akamuita Roboth. Melkizedek akamwambia akae mbali na mwanaye kama anataka usalama wa maisha yake na ya familia yake kwa ujumla. Akae mbali na mwanae, na akikaidi hayo yatamtokea puani. Alipomaliza kusema, akamgeukia na mama akamwambia amkanye mwanae, asilete damu yake ya kimaskini kwenye familia yao.



“Kwaheri,” Melkizedek akaaga na kwendaze. Mama akabaki ameduwaa. Akatazama Melkizedek mpaka anapotelea. Akamgeukia mwanae na kumuomba ajiweke mbali na watoto wa watu kwani yeye hataki matatizo na mtu.



“Unajua baba yako amefariki. Sisi ni familia isiyo na uwezo wala jina lolote ndani ya Goshen. Tafadhali jiepushe na watu wenye meno. Tafadhali Roboth!”



Roboth hakusema kitu. Akainamisha uso wake na kuingia ndani, chumbani. Akajilaza na kulia kwa kumwaga machozi. Akajikuta anauchukia sana umasikini kuliko shetani. Moyo wake ukamuuma sana kwanini hali yake ni dhalili.



Hakubanduka hapo kitandani mpaka jua lazama, usiku unaingia.



Kwenye majira ya saa sita ya usiku kwa mishale ya saa ya sasa, Roboth akakurupuka kitandani akiwa anakohoa. Hali ya hewa ilikuwa nzito, na kadiri alivyokuwa anahema, ndivyo alivyokuwa anakohoa. Akasikia vishindo vya watu dirishani. Haraka akafungua pazia kutazama. Kwa mbali akaona watu wakiyoyoma.



Hakuweza kuzingatia kwa maana alikuwa anakohoa sana. Mama yake akaamka upesi na kuja kugonga mlango. Akamkuta mwanaye anakohoa na huku akivuja jasho jingi. Akamuuliza nini shida, Roboth akashindwa kuongea kwani alikuwa anakohoa kupita kiasi. Alipokuja kutulia, akamwambia mamaye ameona watu wakiwa wanayoyoma.



Zikapita dakika kadhaa, Roboth akatulia na kumweleza vema mama yake. Hakupata usingizi tena, akajilaza akawa anatazama huku na huko.



"Unaendeleaje sasa?" Mama akamuuliza Roboth. Yalikuwa majira ya saa moja asubuhi kijana huyo akitaka kwenda kuhudumia mifugo yao bandani.

"Nadhani naendelea vizuri sasa," akajibu Roboth. "Huna haja ya kuhofia tena mama."

"Lakini ni wakina nani hao waliokuja huo muda? Na nini wanataka hapa?" Mama akauliza.

"Sijui!" Roboth akapandisha mabega yake juu. Mama akamtazama na kumwambia akimkazia macho.

"Robo mwanangu, kuwa makini na tafadhali jiwekw mbali na Tattiana kabisa. Haya yote ni kwasababu ya huyo msichana. Najua tu hiyo ndiyo sababu maana sisi hatuna kitu kuchukiwa na yeyote yule. Sina hata deni!"

Roboth akatikisa kichwa akitazama chini. Hakusema kitu akajiondokea zake mama yake akimtazama akienenda.

"Ndiye kitu pekee nilichobaki nacho. Tafadhali, Mungu nilindie mboni yangu," akasema mama machozi yakianza kujikusanya machoni. Mwanaye alipozama bandani, naye akazama ndani.



***



"Itamchukua muda gani kufika?" Akauliza Sultan. Alikuwa ameketi kitandani miguu yake ipo chini. Ameshika tama akitazama ukuta kwa macho ya mawazo.

Nyuma yake kitandani alikuwa amelala Sultana mdogo akiwa amejifunika shuka mpaka kiunoni. Alikuwa anamtazama mumewe kwa macho ya mazingatio.

"Nadhani leo ndiyo ataingia," akasema mwanamke. Unajua safari toka kule mpaka hapa yachukua muda sana, ukizingatia pia na umri wake. Tumpe muda."

"Lakini muda haupo upande wetu!" Sultan akasema kwa mkazo. "Tukiendelea kungoja mke wangu atafia kitandani. Haitakuwa na maana tena kwake kuja."

"Hatakufa, usijali," Sultana mdogo akamfariji akimpapasa mgongo kwa kiganja chake kilaini.

"Hatakufa?" Sultan akatahamaki. Akamtazama mkewe na macho duwazo.

"Umemuona namna alivyo? Kila siku anakonda na kudhoofika. Analia usiku mzima na analalama siku nzima. Uso wake umekuwa mweusi na hakuna tena nguo inayomkaa mwilini! Amekuwa mtu wa kufunikwa na shuka, wa kulishwa na kunyweshwa kwa nguvu!"

Macho ya Sultan yakawa mekundu. Akayafunika kwa kiganja chake akiinamisha uso wake chini.

"Sikuwahi kujua kama kuna kitu kitakuja kunishinda ingali mimi ni Sultan. Nilidhani ukiwa kiongozi mkubwa, basi utafanya vile unataka, vile unapenda, tena kwa wakati wowote! Hautakuwa na shida yoyote kwani utatimiza mambo kwa kutoa amri tu. Kumbe nilikuwa nakosea. Sikuwa sahihi hata kidogo, na ona sasa ninavyohenyeka. Usultan wangu umeshindwa kufua dafu na sasa namwona mke wangu akifa mbele ya macho yangu nikiwa sina la kufanya."

Sultana mdogo akanyanyuka na kumkumbatia mumewe kwa nyuma. Akamtaka asihuzunike sana kwani yeye yupo na anaamini haya yote yatakwisha kwa kheri.

"Hakuna lisilo na mwisho, laaziz. Litachukua muda lakini litakoma tu. Naamini bibi atamsaidia kabisa akarejea kwenye hali yake."

Japokuwa kinywa cha Sultana huyu kilitoa maneno matamu kama tende, moyoni mwake kulikuwa kuna mgogoro mkubwa. Hakuwa na raha kabisa. Sultan alikuwa kivuli tu mbele ya macho yake.

Tangu amefika mwanaume huyo hajamgusa kwa lolote, hili lawezejanaje na ingali aliweka dawa zake kama alivyoelekezwa na bibi yake? Kwenye pindo la nguo, na hata barabarani?!

Kila alipomtazama Sultan, hakuona kama mwanaume huyo anamtazama kwa mahaba. Kila alipojaribu kumchombeza, kumlaghai ama kumchokomoa kimahaba, hakufanikiwa abadani!

Alishakaa kila mkao, akamgusa kila eneo, lakini mwili wa mwanaume huyo haukufanya kazi. Ni kama vile alikuwa anabonyeza kitufe ambacho waya wake umekata ama ushaota kutu.

Ina maana dawa za bibi zimegoma kufanya kazi? Alikuwa anangoja kwa hamu bibi yake afike na kumuuliza swali hilo. Mwanaume ameshakuja kwenye himaya yake, tena adui yake akiwa hoi, kwanini ashindwe kumpata?

"Unasikia huko nje?" Sultan akamshtua kwa kumtikisa. Akakurupuka na kuuliza.

"Kuna nini?"

"Nadhani kuna ugeni," Sultan akajibu. "Ina maana hujasikia?"

"Hapana! Sijasikia," Sultana akasema akipandisha mabega.

Basi wakanyanyuka na kujiandaa, punde kijakazi akaja na kuwaambia kuna ugeni wa bibi huko sebuleni. Wakiwa wamejiandaa, wakatoka kwenda kukutana na bibi. Wakamkaribisha kwa bashasha na kumpatia pole ya safari.

Bibi alikuwa amevalia gauni lake refu maridadi likiwa na urembo urembo wa maua ya kudarizi.

"Niwape pole nyie mnaouguza. Vipi, hali ni shwari?"

"Hapana!" Akasema Sultan akitikisa kichwa. "Hali si nzuri kabisa!"

Haraka Bibi akaenda kuonana na mgonjwa. Alikuwa amelala kitandani akiwa anapepewa na kijakazi wa kike ambaye alitoka punde baada ya watu kuingia.

Mgonjwa huyo alikuwa amejifunika shuka mpaka mabegani. Nywele zake zilikuwa hovyo, sura yake ilikuwa imekondeana, na macho yake yalikuwa yameingia ndani yakizungukwa na rangi nyeusi.

Alikuwa mdhaifu, hata kugeuza macho ilikuwa shida. Hakuwa na nguvu hiyo! Bibi akamtazama na kumpekua, alipomaliza akaenda kuleta vitu vyake na kisha akaomba apewe faragha afanye kazi yake. Basi Sultan na Sultana mdogo wakatoka ndani. Lakini hawakwenda mbali, wakawa wamesimama kwa umbali mdogo toka mlangoni hivyo wakawa wana uwezo wa kusikia yanayoyukia ndani, japo si kila kitu.

"Unadhani atapona?" Sultan akauliza. Alikuwa amejawa na hofu. Mikono yake ilikuwa inatetemeka kwa mbali.

"Atapona usijali," akasema Sultana japo kinafki.

Wakasimama hapo kwa muda wa kama dakika kumi, mara wakasikia sauti kali ya Sultana ikitoka ndani ya chumba. Alikuwa analia kama mtoto lakini hakudumu muda mrefu, akanyamaza na Bibi akatoka chumbani akiwa anatota jasho. Wakaelekea pamoja sebuleni.

"Pole kwa majaribu haya," Bibi akamwambia Sultan. "Tuna kazi kubwa sana ya kufanya kumrejesha mkeo katika hali yake ya kawaida."

"Ni nini shida?" Akauliza Sultan.

"Unaijua shida, Sultan," akajibu Bibi. "Na kwenye hiyo shida, nawe mkono wako unahusika. Inabidi nawe pia uhusike kwenye kuitafutia ufumbuzi."

"Niko tayari kwa lolote ilimradi mke wangu apone!"

"Safi. Tatizo kubwa tulilo nalo ni kupambana na roho ya ndugu yake ambayo inamuwinda na kumkosesha raha na amani. Anashindwa kulala, kula wala kupumzika."

"Tutapambana vipi na kitu kisichoonekana?" Akauliza Sultan kwa pupa.

"Inawezekana, lakini kazi inakuwa kubwa kwasababu ya roho hii iliyoteketezwa haikuwa na hatia. Na pia, ilikuwa ya mlozi mwenye nguvu!"

Kukawa kimya kidogo. Bibi akaongezea kwa kusema:

"Ngoja tuone kwanza. Kuna dawa nimempatia, tuvute subira kwa siku tatu!"

"Ni dawa gani?" Akauliza Sultan.

"Dawa ya kufukiza kwa ajili ya kukimbiza na kutuliza roho za waliokufa."

Punde Bibi alipomaliza kusema hayo, kukatokea sauti kali tokea chumbani. Sauti hiyo haikuwa ya Sultana tena bali ya mwanaume!

"Ni nani huyo?" Sultana mdogo akalipuka kwa hofu. Bibi akawatuliza na kuwaambia hizo ni roho ndizo zahangaika. Lakini sauti hiyo ya ajabu haikukoma, ikaendelea na kadiri inavyoendelea ikawa inakua na kukua.

Kama haitoshi, mlango ukaanza kubamizwa kwa nguvu sana! Sultan na mkewe mdogo wakawa wanahofia sana. Hata walinzi walikuja na kuuliza kama kuna namna wanaweza kufanya.

"Hapana, tunashukuru!" Bibi akawataka waende nje, na akaagiza mapazia ya madirisha yote yashushwe. Muda kidogo ulivyoenda, mlango wa chumba alichofungiwa Sultana mkubwa ukaanza kuvunjwa!

Hapo Bibi akamwambia Sultan na mke wake mdogo watoke nje upesi wamwache peke yake ndani. Haraka wakafanya hivyo, Bibi akafunga milango yote kwa funguo.

Na punde, Sultana mkubwa akatoka chumbani akiwa ameshamaliza kuvunja mlango wote! Alikuwa anatembea kwa nguvu kamili na macho yake yalikuwa na rangi ya bluu!

Akamtazama Bibi, na kumnyooshea mkono akinguruma kama simba.



Bibi akasema maneno fulani kwa lugha ngeni. Akayarudia maneno hayo mara tatu huku akihakikisha macho yake hayabanduki usoni mwa Sultana mkubwa. Alikuwa anamtazama ndani ya macho yake ya bluu pasipo na hofu.

Maneno hayo yalipokuwa yanatamkwa, Sultana mkubwa akawa anaghafirika. Anatoa sauti kali ya kilio, lakini hakukoma kumsogelea Bibi. Alikuwa na dhamira ya kutimiza hilo!

Basi Bibi akabadili maneno na kuanza kutamka mengine. Nayo akatamka mara tatu kama yale ya mwanzoni. Mara Sultana akaanza kupepesuka kana kwamba anasukumwa na upepo mkali. Akarudi nyuma hatua tatu, lakini kwanguvu, akapambana na kuendelea na zoezi lake la kusonga mbele!

Sasa alikuwa amebakiza hatua chache kumfikia Bibi! Akanguruma kama simba akiwa amekunja vidole vyake kama waya wa chuma. Mishipa ilikuwa imemsimama kama mabomba ya maji na jasho likimchuruza.

Ungeweza kubashiri ni namna gani angefanya endapo angemtia Bibi mikononi. Alionekama ana njaa ya uhai wa mtu, ama damu ya mtu! Hakuonekana kama mwenye masikhara hata kidogo.

Kwa mara nyingine, Bibi akasema maneno yake ya ajabu:

"Mere na kebu, khakav shindavata meril!" Akarudia tena:

"Mere na kebu, khakav shindavata meril! ... Mere na kebu, khakav shindavata meril!"

Sultana akaanguka chini! Puh! Akatulia tuli kwa muda wa kama sekunde kumi na tano. Ni kama vile hakuwa hai. Hakuonekana kama ana dalili za kuhema. Bibi akamtazama kwa umakini na kwa tahadhari. Alikuwa ameegemea ukuta, macho yake akiwa kayafinya na makunyanzi yake ya uzee.

Baada ya sekunde kumi na tano, Sultan akaanza kuonyesha ishara ya kuhema taratibu. Bibi akaita:

"Samiraa! ... Samiraa!"

Kulikuwa kimya. Sultana alikuwa anaendelea kuhema taratibu akiwa ameegemeshea uso wake chini. Bibi akapiga hatua mbili kumsogelea. Ila bado akiwa kwenye tahadhari, hakutaka kuwa karibu kabisa na mwanamke huyo.

Akaita:

"Samiraa! ..."

Kimya. Akasogea hatua nyingine karibu.

"Samiraa!"

Kimya.

Mara Sultana akaanza kuhema kwanguvu, kwanguvu na kwanguvu! Kabla Bibi hajafanya kitu, Sultana akanyanyuka na kusimama upesi mno kwa haraka ya kufumba na kufumbua, akamsukuma Bibi kwa mbali akitumia mikono yake yenye nguvu!

Bibi akarushwa kana kwamba amepigwa na shoti ya umeme. Akabamiza ukutani na kudondoka chini akilalama kwa maumivu. Si kichwa wala kiuno kilichokuwa muhali.

Basi Sultana ambaye sasa alikuwa amezidi kunenepeana misuli, akapaza sauti yake kwa hali ya juu! Hakuwa binadamu sasa bali mnyama. Rangi yake ya mwili ilikuwa nyeusi, macho yake makubwa rangi ya bluu na mdomo mpana mwekundu.

Alipomaliza kunguruma, akamfuata Bibi aliyekuwa hoi chini, akamkaba kwanguvu huku akilaani kwa maneno ya lugha isiyoeleweka. Bibi akahangaika sana kujikomboa na uhai wake. Lakini nguvu zake hazikuwa kutosha abadani kupambana na jitu lile.

Akaminywa sana koo. Mikono yake ya kizee ikajitahidi kupapasa na kupambana. Macho yake yaanza kutokomea utosini, na mapigo yake ya moyo yakaanza kupungua. Alikuwa anaelekea kufa!

Mikono yake ikaanza kulainika. Ikapapasa mikono ya muuaji wake taritbu ikielekea kuanguka chini.

Lakini kabla zoezi halijafanikiwa, mara pazia la dirisha linafunguliwa na mwanga wazama ndani. Alikuwa ni Sultan anachungulia, na hiyo ndiyo ikawa salama ya Bibi!

Haraka Sultana akamwachia Bibi na kukimbilia kule dirishani. Akapambana na dirisha kwa fujo kana kwamba anapambana na mtu. Sultan akarudishia pazia upesi. Lakini Sultana akalivutia pazia chini, na akaendelea kupambana na dirisha. Afadhali dirisha lilikuwa ni la chuma.

Kadiri Sultana huyo alivyokuwa anapambana hapo, akapoteza nguvu na mwishowe akadondoka chini na kuzirai.

Sultan na mkewe mdogo wakaingia ndani upesi. Wakamkuta Bibi akiwa hajitambui, yupo hoi.



***



"Nadhani ndiyo siku yenyewe. Leo itakuwa hatma yetu," akasema Seth. Wakiwa ndani ya shimo walikuwa wanasikia milio ya ngoma huko nje kwa mbali.

Malkia alikuwa amekaa chini akiwa amejikunyata, Zura alikuwa amejilaza, pamoja pia na Fluffy.

"Sasa tutafanya kitu gani?" Akauliza Fluffy. "Tutaondoka na hao watu kwenda nao Misri?"

"Haiwezekani!" Akadakia Malkia. "Hilo haliwezekani hata kidogo!"

"Lakini kwanini?" Akauliza Seth. "Huoni kama hilo ni bora kuliko kufa hapa?"

"Tutaenda nao mpaka wapi, Seth?" Akauliza Malkia akisimama. "Huoni kama kwenda nao ina maanisha tutakuwa chini yao safari yote? Na hata hicho tunachoenda kufuata huko, kitakuwa ni chao?"

"Malkia, inabidi tufanye kitu. Hatuwezi tukafa hapa!" Akasisitizia Fluffy.

"Muda si mrefu tutakuja kuchukuliwa hapa, hicho mnachowaza mkiseme haraka!" Akasema Seth. Kwa muda kukawa kimya kidogo.

Huko nje, jitu moja kubwa likapewa ishara ya kichwa na mkuu wao. Majitu yote haya yalikuwa yameshakusanyika mbele ya tanuri kubwa lililokuwa linawaka moto wa kijani. Wote walikuwa wamesimama isipokuwa mkuu, yeye alikuwa amekalia kigoda kikubwa mkono wake akiuegemezea juu ya goti.

Basi jitu lile lililopewa ishara likajiondokea kuelekea shimoni walipotiwa mateka Malkia na wenzake. Punde, likatoka na mateka likiwa limewakusanyia kwenye mkono wake mmoja. Likawabwaga mbele ya mkuu!

"Tevtev kashiromata lasopa?" Mkuu akanena akiwa ametoa macho. Alikuwa anamtazama Malkia akiwa anangojea kwa hamu kauli itakayotoka kinywani mwa mwanamke huyo.

"Anauliza umefikia maamuzi gani?" Seth akakalimani kilichonenwa.

Malkia kabla hajajibu, akamtazama Seth na macho ya sisitizo, kisha akamwambia kwa sauti ya pole:

"Nimekuamini." Alafu akamgeukia Mkuu yule wa Azeth, akamwambia kwamba wameridhia kwenda nao kwenye safari ya Misri. Mkuu wa Azeth akatabasamu na kutikisa kichwa chake. Akampomgeza Malkia kwa maamuzi yake, kisha akateua watu wawili wa kuongozana nao kuelekea Misri.

Lakini kabla, akawataka Malkia na wenzake wawapatie faragha, wakasogea kando. Mkuu huyo akawa anateta na watu wake akiwapa maelezo.

"Unadhani atakuwa anawaambia nini?" Fluffy akauliza. Macho yao yalikuwa yakiwatazama majitu hayo yakinong'ona.

"Sijui atakuwa anawaambia nini, ila si kizuri kwetu," akasema Malkia.

Haikupita muda mrefu, wakaitwa. Wakakabidhiwa majitu yale mawili kwa ajili ya kuendelea na safari.

"Seth, una uhakika na kile ulichokisema?" Malkia akauliza.

"Ndio, kwa asilimia zote. Usijali," Seth akasema kwa kujiamini akitikisa kichwa. Safari ikaanza.

Hakukuwa na maongezi sana huko njiani. Kabla hawajakiacha mbali kijiji cha Azeth, farasi wa Malkia akajiri tokea misituni. Malkia akamkumbatia na kumpanda mnyamawe anayempenda.

Lakini walivyotembea kwa umbali mfupi tu, farasi huyo akaanza kulegea na kukosa nguvu. Ghafla akadondoka chini na kupoteza fahamu. Malkia pamoja na wenziwe wakastaajabu nini kilitokea.

Jitu moja, kati ya wale majitu mawili ya Azeth, likampekua farasi huyo kwa kumnusa na kumkagua mwili, kisha likasema:

"Venerdi kashaka!"

"Anamaanisha nini?" Malkia akawahi kuumuliza Seth.

"Amepewa sumu!" Seth akajibu upesi.

"Waulize kama kuna namna ya kunsaidia, tafadhali!"

Seth akafanya hivyo. Malkia akaona majitu yale yakitikisa kichwa.

"Tafadhali, waombe wamsaidie. Tafadhali!" Malkia akasisitiza.

Seth akawaambia. Wale majitu wakamjibu kuwa farasi huyo atakuwa amekula majani ya sumu, au amepewa sumu.

"Na wakina nani?" Malkia akawahi kuuliza.





Wale majitu ya Azeth wakatazamana na kuteta kidogo, alafu mmoja akamtazama Seth na kumpatia majibu.



"Wanaasema hapa karibuni kuna binadamu huwa wanakuja kuwinda, huwaua wanyama kwa kutumia sumu na hata huwa wanawadhuru wao kwa kutumia sumu hiyo. Wanadhani hao ndio watakuwa wanahusika."



"Na dawa je?" Akauliza Malkia. Seth akamjibu na dawa pia inapatikana kwa hao watu, lakini ni hatari sana kwenda huko kwani si watu marafiki.



"Malkia, ni bora tukaendelea na safari," Seth akashauri. Malkia akakaa kimya kwanza, wote wakimtazama, mara akanyanyuka na kusema:



"Siwezi nikaondoka, na siwezi kuendelea na safari hii mpaka pale nitakapomtibia farasi wangu."



"Lakini Malkia, ni hatari!" Akasisitizia Fluffy. Malkia akamtazama na kumwambia:



"Huyu farasi si tu mnyama kwangu, bali familia. Tangu nikiwa mtoto amekuwa nami mpaka sasa. Siwezi nikamwacha sasa, afe nami namtazama."



"Sasa utafanyaje? Wataka kwenda hivi?" Akauliza Seth.



"Nitaenda. Hata kama ikinibidi niende mwenyewe," Malkia akajibu kwa kujiamini.



Seth na wenzake wakabaki wakitazamana. Hawakujua cha kufanya. Hawawezi kumwacha Malkia aende peke yake, ila si kutafuta visa huku? Kwenda tena kufanya vita na watu wengine na huku wametokea pona chupu?



"Ni wapi walipo watu hao?" Akauliza Malkia kwa kupaza sauti. Seth akamtazama akitamani kumzuia.



"Fanya upesi, maana muda haupo upande wangu!" Malkia akasihi akimtazama kwa macho yasiyo na utani. Upepo ukavuma kuinamisha miti na kukimbiza ndege.





***





Giza lilikuwa linaingia sasa, taa za makazi ya zamani ya Rhoda bado hazikuwa zimewashwa na chumbani kulikuwa kuna mzozo ukisikika. Mzozo huu haukuwa wa mwingine, bali wa wale bibi walozi toka Tanashe.



Walikuwa wamesimama wima, mwili wa Rhoda ukiwa kitandani, ila hawakuwa watatu, bali wawili, nyuso zao zikiswahibu mambo hayakuwa shwari hata.



Wakinyoosheana vidole vyao virefu, na wakitoleana macho ambayo kila mmoja wao alikuwa analo moja moja! Wakapayuka na kupaza sauti.



"Mpaka lini?" Mmoja akauliza.



"Sasa unadhani tutafanyaje na ndivyo imekuwa vivyo?" Mwingine akajibu kwa kuuliza.



"Tutafanyaje!" Mwenzake akatahamaki. "Tukiendelea hivi, tutafikia wapi? Tumekuja huku kunywa damu za watu ama kushika dola?"



"Natambua hilo. Na si kosa la yeyote yule kati yetu!"



"Vipi kama akikamatwa huko? Vipi ikagundulikana? Itakuwa bahati yetu kama tukarejeshwa Tanashe tukiwa hai. Si tu kwamba tutapoteza uhai, bali lengo lililotuleta huku!"



"Sasa wapaza koromo na mtu angali hayupo? Yasaidiani?"



"Napaza kwakuwa wewe ndiye ulikuwa naye mara ya mwisho kabla hajatokomea tena. Ulishindwa mzuia? Ama amekupa nawe ahadi ya kukuletea pande la nyama ya binadamu?"



"Hakuniaga! Na sikuwa naye tukisongamana kama vifungo. Sijui na wala sihusiki na tukio lake la kwenda huko!"



Kukawa kimya kidogo wakivuta kwanza pumzi na kupunguza msongamano wa pumzi za jazba vifuani mwao. Wakaketi kila mtu akigeukia upande wake. Mwili wa Rhoda ulikuwa katikati yao.



"Tulipanga kwenda kuonana na mfalme, hayajatimia kisa yeye, siku imeisha. Tuliweka mwili wa binadamu yule mlevi ukauke kwa ajili ya kutengenezea dawa, kaumaliza kwa kuutafuna." Akasema kikongwe mmoja akishika tama.



"Hatuwezi kumbadili, tumesema na sasa imeshageuka kuwa matumbuizo masikioni mwake. Amekuwa samaki mkavu, sufuriani hatoshi," akasema mwingine. Wote wakiwa wameshika tama.



"Hakuna namna, inabidi tufanye maamuzi magumu," akasema mwingine.



"Yapi hayo?"



"Kummaliza!"



"Unasema?"



"Ndio, kama ulivyonisikia."



"Huoni kama tutakuwa tumeenda mbali sana?"



"Itabidi twende huko mbali kama njia ya karibu hamna. Unafikiri ni nini tutafanya? Hatuwezi tukamfungia, atatoka. Hatuwezi kumrudisha Tanashe."



Mara wakasikia sauti ya mlango ukisukumwa huko sebuleni. Haraka wakatazama kioo chao cha kilozi na kugundua ni mwenzao.



"Anarejea!"



Mlango ukarejeshewa na mlozi huyu aliyeingia, akapaza sauti akiulizia wenzake kama wapo. Akawasha taa zao za maginga ya moto na kisha akapandisha ngazi kuelekea juu kuwakuta wenziwe.



Akafungua mlango asione kitu. Kitanda kilikuwa kitupu, hawakuwepo wale vikongwe wala mwili wa Rhoda! Akapaza sauti kuita wenzake akijiuliza wapi walipo.



Napo mule chumbani akawasha ginga la moto lililokuwa linaning'inia ukutani. Akaangaza kushoto na kulia, hakuona kitu. Akaguna na kuketi kitandani. Nguo yake ilikuwa ina mabaki ya damu kwa shingoni na kifuani.



Akanyanyuka na kwenda kabatini, akafungua na kuangaza. Ila ghafla akahisi kuna watu nyuma yake, basi akageuka upesi. La haula! Akaona panga likiwa hewani, hajahema, likamkita kichwani na kudondoka chini!



Haikupita muda mrefu, vikongwe wawili wakatoka ndani ya jengo wakiwa wamebebelea kifurushi cheusi. Wakiwa wamejawa na tahadhari wakaelekea nyuma ya nyumba na kuchimba shimo kisha wakazamisha kifurushi kile ndani yake.



"Kazi imekwisha," mmoja akasema akikung'uta mikono yake. Basi wakatoka huko nje na kurudi zao ndani.



"Tutamkumbuka sana."



"Hakika! Hatujawahi kuwa pungufu namna hii, ila sasa tunaweza tukatimiza mipango yetu."



Wakapandisha juu kuelekea chumbani. Ila muda si mrefu, mlango ukagongwa mara tatu. Wakatazamana na kuulizana kabla hawajateka kioo chao na kutazama. Wakamwona askari akiwa amesimama na mwanaume mmoja ambaye hawakumtambua.



"Unahisi nini?" Akauliza mmojawao. Punde wakashuka chini wakiwa tayari wamevalia mwili wa Rhoda.



"Vipi muda huu?" Wakauliza.



"Tafadhali, tumekuja kufanya ukaguzi," akajibu Askari. Na kumbe yule mwanaume aliyekuwa kando yake alikuwa ni yule mlevi ambaye mwenziwe alikufa baada ya kuingia ndani ya jengo la walozi hawa.



"Ukaguzi?" Akatahamaki Rhoda. "Kuna nini?"



"Madam, hamna maelezo ya ziada kwenye hilo. Tunaomba tuongozane wote kwenda ndani," Askari akasema kwa mkazo. Basi wakazama ndani kupekua kama Rhoda yu mwenyewe. Walipomaliza pasipo matunda, wakamtaka waelekee uani.



Rhoda akasita. Akamtazama yule mlevi kwa jicho hasidi, ila mwishowe wakaamua kuelekea huko.



"Fukua!" Akaamuru askari akimkabidhi Rhoda chepeo. Mpaka hapo wale vikongwe wakatambua kuwa watakuwa wameonekana walipokuwa wamemzika mwenzao.



Wafanye nini? Wakaanza kujadiliana ndani ya kifua cha Rhoda.





Haikupita muda mrefu, mara Rhoda akageuka na kumzaba Askari kwanguvu kwa chepeo, Askari akadondoka chini na kuzirai! Kisha akamtazama yule mlevi ambaye tayari alikwishakaa mbali kwa woga.



Akamwambia akimnyooshea kidole:



"Kifo kinakuita. Na hicho ndicho utapata kama malipo ya kufuatilia ya Ngoswe!"



Ajabu ni kwamba mara hii sauti ya Rhoda ilikuwa ni yale vikongwe kabisa na si ile ya kuigiza. Basi yule mlevi akaogopa na moyoni akahisi ni jini lipo mbele yake. Akasisimika ngozi na kusimamisha vinyweleo.



Rhoda akapandisha chepe lake juu kwanguvu, kufumba na kufumbua, akautupa mkonowe alambe kichwa cha mlevi yule 'mchonganishi', vuuuup! chepe likapita kando! Mlevi alilikwepa na kudondoka chini! Haraka akanyanyuka na kukimbia kama mwehu.



"Hawezi kutoroka!" Rhoda akafoka na sauti yake ya kizee. "Hawezi kuwa hai!"



Akaanza kumkimbiza mlevi yule kwanguvu zote akitaka kummaliza kuzika ushahidi. Haki mwendo wake ulikuwa mkali na punde ndogo tu akawa amemfikia mlengwa wake, lakini kabla hajamdaka, mlevi akapiga kelele kali za woga. Kuna watu walikuwa wanapita kwa mbali, wakasimama na kutazama, Rhoda akajificha upesi na kumwacha mlevi atokomee!



"Ni jinii! Ni jiniiii!" Mlevi alikuwa anapayuka visigino vya miguu yake vikigusa kisogo. Lakini nani atamzingatia mlevi? Wakamtazama wakimkebehi:



"Ama kweli pombe si supu!" Kisha wakajiende zao. Huku Rhoda akiachwa na manung'uniko na majuto!



"Nini sasa tumefanya?"



"Usijali sana, yu mlevi. Umeona, kinywa chake hakitaaminika."



"Nani kasema? Mbona kimetuletea askari?"



"Sasa tungefanyaje? Kumkimbiza mwehu aliyekwapua nguo kipindi tunaoga? Lisingetufanya tukaonekana wazima!"



"Hapana! Hapana! Ni lazima tumpate na kumuua. Tena mwili wake tuukaushe na kuutokoa dawa. Yeye ndiye mtu pekee hatari kwetu aliyebakia. Si salama moyo wake kuendelea kudunda," wakajadili wakiufuata mwili wa Askari waliounyanyua na kuuingiza ndani.



Wakauficha na kukubaliana kuutokomeza kwa namna ya kilozi. Lakini pia usiku ule usikome mpaka pale watakapomtia mikononi yule mlevi, na kumtenda vile wanataka.



Kujua siri za ndani, ni kazi ya mwandani na si hayawani. Akiijua hayawani, siri haipo sirini bali kinywani. Yeye ni nani? Lazima afukiwe chini! Chini! Chini! Wakaimba vikongwe. Na kisha wakacheka kuujaza usiku.





***





"Hapa ndipo penyewe?" Akauliza Malkia akikodoa.



"Ndio, kama kweli watakuwa wametuelekeza vema," akajibu Seth. Walikuwa wamejibana nyuma ya mti mkubwa wakitazama vibanda fulani vilivyokuwa vimerundikana. Vibanda hivi vilikuwa vina mwanga hafifu, na watu kadhaa walionekana huku na kule wakiwa ni wafupi kimaumbo.



Walikuwa wamevalia ngozi za wanyama kuziba sehemu zao za siri. Usoni walikuwa wamejichora michoro ya ajabu kwa kutumia wino mweupe. Kichwani walikuwa wamevalia mataji ya majani makavu.



"Sasa?" Akanong'oneza Seth akimtazama Malkia.



"Tumkamate yeyote yule," Malkia akajibu. "Si walisema yeyote anajua kuhusu dawa?"



Wakapanga cha kufanya. Muda si mrefu wakafanikiwa kumvuta mmoja kwa kuigiza sauti ya mnyama na kuchezesha majani. Wakamziba mdomo na kumlaza chini, Seth akamuuliza kuhusu dawa.



"Totos tatip!" Akajibu kiumbe kile akitoa macho makali.



"Anamaanisha nini?" Malkia akamuuliza Seth.



"Anasema hatuelewi!" Seth akajibu na kisha akabadili lugha kumuuliza yule kiumbe kwa lugha anayoijua. Bado wakaambulia patupu. Mateka hakuwa tayari kusema kitu.



"Mwambie hatuna muda, na akiendeleza ukaidi tutamuua!" Malkia akasisitiza, Seth akafikisha ujumbe. Lakini kwa kebehi, kiumbe kile kikajibu:



"Haogopi na yuko tayari kufa!"



Malkia akaweka upanga wake shingoni kwa mateka huyo na kuubinyia hapo. Akatishia mtu huyo aseme, lakini bado hakufua dafu.



"Nadhani ni bora tukaenda naye. Hapa si salama, ataenda kusema huko huko mbele ya safari!" Seth akapendekeza. Malkia akaona ni sawa, wakamfunga yule mateka na kumlazimisha atembee.



Lakini mateka akaendeleza ukaidi. Na mara hii, akafanya ujanja wa kutaarifu wenzake kwa kutumia sauti ya mluzi. Kabla Seth hajawahi kumfumba mdomo, tayari ujumbe wa kutosha ulikuwa umeshawafikia wenzake.



Hawakuchukua muda mrefu, wakazingirwa na wanaume watano wakiwa wamebebelea silaha walizoziweka mdomoni. Zilikuwa ni mabomba madogo yaliyobebelea sindano zenye sumu!



"Seth, usiniambie tunatekwa tena!" Malkia akafadhaika. "Hapana, inabidi tufanye namna."



Lakini kabla hawajaifanya hiyo namna, wakastaajabu wamechomwa mwilini na sindano za sumu. Hawakuchukua hata sekunde tatu, wakadondoka chini wakiwa wamepoteza fahamu!

.

.

"Pengine itatuchukua muda kuliko tunavyodhani..."



"Na unavyodhani, hakuna namna nyingine ya kufika huko upesi?"



"Una maanisha njia za mkato?"



"Ndio!"



"Labda zipo. Ila hakuna ninayoijua, mimi sijawahi kufunga safari kwenda Misri!"



"Hata mimi pia, nilidhani labda unaweza ukawa umesikia."



"Hapana. Ila naamini Seth atakuwa anafahamu."



"Seth? Naogopa sasa kila atakaloniambia."



"Kwanini?"



"Hukuona alipotupeleka?"



"Huwezi jua. Ni mara yake ya kwanza tu, bado namuamini."



Malkia alisikia sauti hizo zikilumbana kwa mbali masikioni mwake. Akafungua macho na kuangaza. Kulikuwa kuna mwanga, lakini hakuwa anaona vema, aliona maruweruwe na mwanga mkali wa jua ulikimbizia uso wake pembeni.



Alikuwa juu ya kitu kinachotembea akiwa amelazwa. Kando yake pia kulikuwa kuna mtu amelazwa kama yeye.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ilimchukua kama dakika moja mpaka alipoanza kuona angalau, japo si vema. Ni kama vile ukungu ulikuwa umejaa machoni mwake. Aliwaona watu kwa mbali, akawatambua kama Fluffy, Zura na wale majitu mawili wakiwa wanatembea.



Akakohoa.



"Zura, Malkia ameamka!" Fluffy akaropoka kwa furaha. Haraka wakamsogelea Malkia na kumuuliza hali yake. Hapo Mallkia akatambua yeye na Seth wamewekwa juu ya kibebeo kidogo cha mbao juu ya farasi.





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog