Search This Blog

NILIWAROGA WALIMU MPAKA BASI - 5






Simulizi : Niliwaroga Walimu Mpaka Basi
Sehemu Ya Tano (5)






… Nilikasirika sana, nilimwona ni mwalimu aliyekuja kwa sababu maalum na si ajabu alinilenga mimi kwani wakati anasema atakayekosa atamchapa viboko alikuwa akiniangalia. Niliamini ili anyooke, alihitaji adhabu kali itakayomshikisha adabu moja kwa moja na kuacha tabia hiyo. Kabla hata hajaanza kuuliza hayo maswali yake nilijibadili palepale nilipokuwa nimekaa. Kwa mtu mwingine aliniona nipo kama nilivyo, lakini mwenyewe sikuwa hivyo. Nilimnyooshea mkono nikafanya kama nampiga makofi ya mashavuni, kukasikika mlio wa pa! Pa! Pa! Wakati mlio huo unasikika yule mwalimu alikuwa akinesea kulia na kushoto kama inavyokuwa kwa mtu anayepigwa vibao. Wanafunzi wote walikuwa wakilishuhudia tukio hilo huku wakishikwa na mshangao. Mwanafunzi mmoja aliyekuwa kwenye dawati la jirani yangu alinigeukia na kuniuliza kama naona mwalimu anavyofanya, nikamjibu ndiyo. Yeye aliniona mimi nipo kawaida kumbe mwenzake nilikuwa namshughilikia yule mwalimu. Nilipoacha, mwalimu akasimama kwa muda, akajishika mashavu yote huku akijisugua, alikuwa akisikia maumivu makali sana. Mara, alituangalia wanafunzi wote kwa zamu kisha akasema: http://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Endeeleni na kujisomea, mwalimu atakuja baadaye.” Alitoka kurudi ofisini huku mkononi amebeba vitabu vyake alivyokuja navyo. Darasa lilibaki kimya kwa muda, baadaye minong’ono ya hapa na pale ilitawala, kila mwanafunzi alionekana akiongea na mwenzake. Yule mwanafunzi jirani yangu akanigeukia na kuniuliza: “Hivi hawa walimu wanakumbwa na kitu gani wakiingia humu darasani?” “Mh! Sijui wenyewe bwana. Mimi sijui lolote. Kwanza akili yangu haiko sawasawa,” nilimjibu hivyo, lakini akaendelea kuuliza: “Au humu darasani siku hizi kuna majini?” “Huenda. Unajua shule nyingi zina majini siku hizi.” “Yatakuwa yanatoka wapi?” “Baharini.” “Aaa. Sasa mbona madarasa mengine hayana?” “Majini yanaanza na darasa moja baadaye yanahamia darasa lingine.” Hayo yalipita, wanafunzi walikuwa wamekaa kwa majonzi, hofu na wasiwasi, lakini mimi sikuwa na hali hiyo kwa sababu nilikuwa ndiye niliyesababisha matukio yote. Mara, mwalimu mkuu aliingia. Alionekana anataka kusema jambo, alisimama kwa muda mbele karibu na ubao lakini hakutoa sauti. Alituangalia wanafunzi wote kisha akatoka. Nilijua wanakwenda kufanya kikao lakini moyoni niliamua safari hii nisiende halafu nijue nini matokeo yake. Mara tukasikia kengele ikigongwa, wanafunzi tukatoka kwenda mstarini. Mwalimu mkuu peke yake ndiye aliyekuja mstarini. Alisimama kwa muda kama mtu aliyekuwa akisubiri wanafunzi watulize kelele ndipo aongee alichotaka kuongea. Baada ya kama sekunde fulani hivi walimu wengine walitokea wakaja kusimama jirani na mwalimu mkuu huku wakionesha sura za simanzi. Ilikuwa hali mbaya sana kila mwanafunzi alikuwa ametulia mstarini. Mwalimu mkuu akaanza kwa kusema: “Nadhani kila mmoja anajua tunapopiga kengele nje ya utaratibu wa siku zote, yaani saa nne, mchana na muda wa kuondoka basi kuna sababu maalum, si ndiyo jamani?” Wanafunzi wote tuliitikia ndiyo. Akaendelea: “Kuna tatizo kubwa limeingia hapa shuleni kwetu. Baadhi ya walimu limewatokea majumbani, lakini wengine limewatokea hapahapa shuleni. Si vizuri niliweke wazi hilo tatizo, ila sisi kama walimu tumekaa, tumejadiliana na kuamua kuwapa likizo ya muda.” Cha kushangaza, baadhi ya wanafunzi walipiga mayowe ya furaha, mwalimu mkuu akashangaa. Mwalimu mmoja akamwambia kuwa wengine wanafurahi kwa sababu hawalijui hilo tatizo, wangelijua wasingeshangilia. Hata hivyo mwalimu mkuu hakuwa tayari kuliweka wazi. Alisema tuondoke mpaka siku tutakayoitwa tena kurejea shuleni hapo. Palepale wanafunzi tulitawanyika, wengine walirudi madarasani kuchukua madaftari yao, wengine waliyokuwa nayo waliondokea hapo kwenda majumbani. Lakini njiani wanafunzi walionekana wakitembea makundimakundi huku wakijadiliana. Wengine walikuwa wakitaka kujua kuna nini kilitokea shuleni.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/ Wanafunzi wa darasani kwangu ndiyo waliokuwa wakijua na kuwaambia nini kimetokea. Nilipofika nyumbani, nilimkuta mama anachambua mboga ya kisamvu, aliponiona akashtuka na kuniuliza: “Kuna nini tena leo?” Niliachia tabasamu na yeye akacheka. Alishajua hakuna kitu kizito sana ndiyo maana nilitabasamu. Nilikaa jirani yake na kuchukua majani ya ile mboga na kuanza kumsaidia kuchambua. “Mama walimu wameturudisha majumbani. Wamesema wametupa likizo fupi hadi hapo watakapotuambia turudi shuleni.” “Kisa?” mama aliniuliza akiacha kchambua majani aliyoyashika mkononi. Nilimweleza kisa chote mwanzo hadi mwisho yaani hadi vile nilivyowafanyia wale walimu. Mama akawa ananisikiliza huku amenitumbulia macho. Nilipomaliza alicheka sana akanipa mkono ili kuugonga, nikafanya hivyo. “Unajua kwanini wamewapa likizo?” aliniuliza mama. “Sijui mama.” “Wanataka kuleta mganga shuleni.” “Ili?” “Ili wamjue ni mwanafunzi gani mwenye uchawi.” “Mama wakinishika mimi je?” “Hapo ndipo pa kupashughulikia sasa.” “Tufanyeje?” “We si unajua kila kitu? Kazi ni kwako tu.” Yale majani ya mboga niliyoyashika kwa ajili ya kuchambua niliyarudisha kwenye ungo na kuwaza maneno ya mama na jinsi ya kuyafanyia kazi.





 “Mh! Mbona kama kazi kubwa, nitaweza kweli? Ina maana mama yuko tayari mimi mwanaye niadhirike? Maana nikishikwa uchawi mimi watu wote watajua nimefundishwa na mama,” nilisema moyoni. Niliamua jambo moja kutoka moyoni, kushughulika na walimu ili kama kweli kuna zoezi la kuwaleta waganga shuleni life haraka sana. “Nitakusaidia mwanangu, naona kama unawaza sana,” alisema mama, maneno hayo yaliamsha furaha ndani ya nafsi yangu. “Sikia mwanangu, usiku wa leo mimi na wewe tutatoka, tutakwenda kushughulika na walimu hao, tutajua cha kufanya, hakuna litakalofanyika kuhusu wewe. Hakuna mganga wala mganguzi atakayekuja shuleni, tulia.” Baada ya hapo niliendelea na mambo mengine ya nyumbani, nilikwenda kuteka maji bombani, nikaenda kununua vitu fulani sokoni kisha nikasubiri usiku uingie ili tukatimize lile la kutoka na mama kwenda kufanya mambo yetu. Usiku wa siku hiyo, mama alikuja chumbani kwangu akiwa amevaa vazi aina ya kaniki. Alivaa kwa mtindo wa kukatiza kiunoni na nyingine kwenye mabega. Hakuniamsha kwa kuwa alinikuta sijalala. Tulipokutananisha macho aliinua mikono juu kama anayeniambia njoo hapa. Nilinyanyuka kitandani polepole kisha nikashusha miguu chini na kusimama, nikatembea kumfuata pale alipo. Nilipomfikia, mama alinishika kichwa, kufumba na kufumbua tukatua chini ya mti mmoja mkubwa. Wakati natoka kitandani sikuwa nimevaa nguo zaidi ya nguo ya ndani tu. Mama alivua upande mmoja wa kaniki na kunivisha huku akisema: http://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Usionekane na binadamu mwenye macho ya kawaida kama walimu wako.” Tulitembea kwa miguu kutoka pale chini ya mti hadi kwenye kichaka chenye majani makavu. Hiki kichaka kilikuwa kimezungukwa na pori, mpaka leo hii sijajua lile ni eneo gani na wala sikuwahi kumuuliza mama, naye hajawahi kuniambia. “Hiki ni kichaka chenye dawa ya kutuliza ubongo, unaijua dawa hiyo?” “Siijui mama, kazi yake nini?” “Kazi yake ni kuushika ubongo wa binadamu kuwa kama mpira, binadamu hawezi kuwaza kitu unachokikusudia. Walimu wote tutawapa, hakuna atakayewaza kumfuata mganga, maana watasahau hata kuongelea habari za huyo mganga” alisema mama. Ulikuwa usiku mnene, lakini tuliweza kwenda kwenye mti mmoja mkavu, una majani mapana yaliyokauka, matawi madogo madogo. Ukiuangalia kwa makini unaweza kuufananisha na mkungu lakini wenyewe mdogo. Mama alisema mizizi ya mti ule ndiyo dawa ya kuuzubaisha ubongo wa binadamu. Alisema mti ule una tabia ya kutoota pamojapamoja jambo ambalo wahenga waliamini kizazi chake kinasahau tofuti na miti mingine ambayo huota kwa kufuatana. Kuitoa ile mizizi hatukuwa tunachimba bali mama alisimama, akaangalia juu, akasema maneno mawili matatu, mizizi yenyewe ikaanza kutoka kuja juu ya udongo na kujipanga kama kuni ndogo. Baada ya hapo tuliichukua na kurejea nyumbani. Hatukuweza kulala. Kwenye saa nane usiku, tulianza kazi ya kuisaga ile mizizi hadi kuwa unga baada ya hapo tukachanganya na unga wa kawaida, kisha akasema: “Huu unga, kila mwalimu anatakiwa ale kwenye uji, chai au ugali, lakini hata kwenye mboga, ndipo dawa yetu itafanya kazi vizuri.” “Kwa hiyo kumbe anaweza kula kwenye chakula chochote kile?” nilimuuliza. “Ee, ilimradi ale.” “Lini sasa?” “Lini sasa maana yake nini? Wewe umesema mmerudishwa shule hadi mtakapotangaziwa unadhani na wao suala la kumleta mganga shuleni watakaa nalo wiki nzima? Uende usiku huu kabla hakujakucha.” “Ha! Mama si nitawakuta wamelala?” “Sasa ukiwakuta wamelala si ndiyo vizuri watakuwa wamekurahisishia kazi.” “Sasa si watakuwa hawajapika mama?” “Wewe usiwe mjinga, chukua unga ndani humu. Changanya na maji, halafu tia hiyo dawa, nenda kwa walimu wako, kila mmoja umlishe akiwa usingizini.” Ndipo nilipoanza kupata picha kwamba, kumbe naweza kuwalisha ile dawa walimu wakiwa kitandani. Sikumuuliza mama swali lingine, ila nilisimama, nikaenda jikoni ambako nilichota unga kwenye bakuli, nikapitia maji na kurudi kuchanganya na ile dawa. Baada ya kukoroga vizuri, nikawa nimeshika bakuli lenye uji mzito sana. Nilimuaga mama kwamba aniombee kwa Mungu nifike salama na nifanikiwe kuwalisha dawa walimu wote wa shuleni. Nilishika bakuli mkono wa kulia, nikatoka hadi nje na kusimama katikati ya uwanja wa nyumba yetu. Niliinua mguu mmoja na kuupiga chini, kufumba na kufumbua nilitua kwenye genge la wachawi ambako ndiko tunakokutania mara kwa mara. Mzee mmoja alishangaa kuniona peke yangu tena nikiwa na bakuli mkononi, akauliza: “Lengo lako lilikuwa kufika wapi?” Nilicheka sana, kwani ni kweli sikuwa na lengo la kutua pale ila nilifanya makosa wakati natoka nyumbani sikupiga dira mapema. Mchawi anapotaka kwenda mahali kwa njia ya uchawi ni lazima awe na dira kama atakosa dira atajikuta anafika kwenye genge au kambi ya kukutania wachawi wa eneo lake. Basi, sikumjibu, nikashika njia ya dira ya kufika kwa Mwalimu Cecilia. Kufumba na kufumbua nikatua nje ya nyumba yake. Nilitembea hadi kwenye mlango mkubwa. Nilisimama na kujinyoosha sana kisha nikapiga mwayo, ghafla nikatokea sebuleni. Nikasimama kwenye mlango wa kuingilia chumbani, nikafanya kama pale nje, kufumba na kufumbua nikawa chumbani kwa mwalimu huyo.



… Nilimkuta amelala usingizi ule wa fofofo, hajitambui kwa lolote lile, tena alikiwa akikoroma kwa sauti ya juu. Nilipanda kitandani, nikasimama kwa muda halafu nikashuka. nilifikiri kwa muda mfupi, nikapata wazo kwamba kabla ya kumlisha dawa mwalimu huyo nimpe adhabu kidogo. Nilimwita kwa ishara ya mkono naye akaamka na kutoka kitandani polepole, akasimama akiniangalia. Katika hali hiyo ingwa alikuwa ameamka na kusimama huku akiningalia lakini mwenyewe hakuwa kijua kuwa amemka na yupo na mimi chumbani mle. Niliangaza kila kona ndani ya chumba chake nikaona boksi la vitabu, nikaliendea. Nilipolinyanyua lilikuwa zito sana, nikamwamuru alibebe, akalibeba kisha nikamwamuru atembee mpaka mlangoni, akatembea akiwa bado amebeba boksi lile. Nilimfungulia mlango, akatoka na boksi lake kichwani hadi sebuleni huku akiwa amekunja uso kuashiria kuwa ameelemewa na uzito. Kule sebuleni nilimtangulia, nikasimama pembeni, nilichofanya nikawa namnyooshea kidole ambapo yeye akawa anafutisha, kidole changu kilipoelekea, akaenda mpaka ukutani na kumrudisha hadi chumbani. Nilimfanyia hivyo kama mara ishirini hadi nilimwona amechoka, jasho jembamba lilimchuruzika kwa sababu ya uzito wa lile boksi na vitabu vyake ndani pamoja na kule kutembeatembea kwa nenda rudi, nenda rudi. Tulirudi chumbani akatua boksi, nikampandisha kitandani, haikupita muda mrefu akarudi katika hali yake ya usingizi kama nilivyomkuta pale nilipokuwa nikiingia. Baada ya muda mfupi akiwa anakoroma kwa usingizi ndipo nilipomnywesha ile dawa. Hapa kabla ya kuendelea kusimulia niweke wazi jambo ambalo pengine wengi mlikuwa hamlifahamu. http://deusdeditmahunda.blogspot.com/Ni kwamba, mchawi anapokulisha dawa yake wewe ukiwa usingizini, utakuwa unaota ndoto na ndoto hiyo utakuwa unaota uko kwenye shughuli yoyote ile yenye watu wengi mnakula nyama. Hivyo kama itatokea unota unakula nyama kwenye shughuli ujue kuwa kuna uwezekano ulikuwa ukinyeshwa dawa au kulishwa nyama na mchawi. Mara nyingi sana unapotokewa na hali hiyo, yaani kulishwa dawa au hata nyama, ukiamka asubuhi utajikuta tumbo limejaa au kuhisi kitu kama kuvimbiwa. Wengine wanaweza kushinda mchana kutwa wakiwa hawajisikii vizuri. Basi, baada ya kumlisha zile dawa nilitoka nje kwa staili ileile kama nilivyoingia na kuondoka zangu. Sikurudi nyumbani, nilisimama nje nikatafuta mwelekeo wa kwenda kwa mwalimu mwingine kumnywesha dawa hiyo. Usiku huo nilizunguka sana kwa kwenda kwa kila mwalimu hadi ilipofika saa kumi alfajiri nilikuwa nimewamaliza wote na kurudi nyumbani. Nilimkuta mama amekaa nje akinisubiri. Lakini alikaa katika hali ya kichawi, yaani kama angetokea mtu wa kawaida asingejua kama pana mtu pale nje. Alinipokea kwa furaha hadi ndani huku akinipongeza kwamba nimezidi kuwa jasiri na kunihakikishia kuwa sasa kazi nilikuwa naiweza vilivyo. “Si umewamaliza wote?” aliniuliza mama kwa shauku. “Nimbakishe nani mama? Walimu wote hawana kazi. Halafu nikawa nawapa adhabu, mwalimu mmoja nilimbebesha boksi la vitabu, mwingine nilimtoa hadi nje na jembe akalima kwanza mpaka nilipohakikisha kuwa amechoka ndipo nikamlisha dawa na kwenda kwingine. Mwalimu mwingine nilimpigisha deki nyumba nzima, alipomaliza akiwa hoi kwa kuchoka ndiyo nikamlisha dawa yangu. Mama alicheka sana, alicheka hadi akataka kuanguka. Kwake ilikuwa furaha sana kuona naweza kufanya mambo makubwa kama hayo tena nikiwa peke yangu. “Wewe binti yangu ni kiboko. Umeweza kweli!? Umekua sasa, wewe ni zaidi ya mama yangu mzazi, nakupenda sana mwanagu,” mama aliniambia huku akinishikashika sehemu mbalimbali za mwili wangu. Kesho yake asubuhi, mwalimu mmoja alipita kila nyumba na kusema wanafunzi wote tunatakiwa turejee shuleni kesho kutwa yake ili tuendelee na masomo yetu. Tulipofika shuleni keshokutwa yake, kama kawaida masomo yalianza. Sikusikia cha uchawi wala nini, dawa niliyowalisha walimu iliwafanya washindwe kutekeleza jambo walilokuwa wamepanga. Ila sasa kwa kuendelea kuwakomesha nikaanza kuwachezea walimu palepale shuleni bila ya wao kujua kinachoendelea. Mfano wa hilo, siku moja walimu walituagiza kwenda na majembe kwa ajili ya kulima shamba la shule. Mimi nilipofika na jembe langu wakati wa kulima ulipofika, nilimshikisha mwalimu mmoja bila mwenyewe kujua, akaenda kulima lakini akionekana anayelima ni mimi.







“Huyu mwalimu alilima mimi nikiwa nimesimama na walimu wengine wakadhani ni yule mwalimu anayelima. Ilifika mahali niliwachukua walimu wengine na kuwashikisha majembe ya wanafunzi wengine ili na wao waanze kulima. Walimu wote wakawa wanalima na wanafunzi waliokosa walimu wa kuwapokea majembe. Walilima bila wao kujijua kama wanalima na wanafunzi walijua wanalima wenyewe bila walimu, lakini usahihi ni kwamba walimu walikuwa sambamba nao ila kwa macho ya kawaida haikuwa rahisi kwa mtu ambaye si mchawi kuona. Ilifika mahali mwalimu mkuu akasema wanafunzi turudi shuleni. Nilimnyang’anya jembe langu yule mwalimu kisha nikawasukumia upepo wanafunzi wengine ambao nao walikwenda kunyang’anya majembe yao kwa walimu. Hayo yote yalifanyika kimazingara. Baada ya walimu kuachia majembe yetu, nikawaachia ufahamu ambapo walijikuta wamechafuka sana miguuni kwa sababu udongo wa shamba la shule ni ule mwekundu. Walimu wote walishtuka na kukimbiakimbia huku na kule wakisema wamepatikana na wachawi. “Ni nini jamani? Hata mimi?” mwalimu mkuu naye alisema akiruka kutoka sehemu aliyosimama kwenda nyingine. Bahati nzuri ni kwamba, wanafunzi waliokuwa wakilima na sisi tusiolima wote tulichafuka miguu, kwa hiyo hawakuwa na wa kumsingizia kwamba anahusika. Mwalimu mkuu aliamuru wanafunzi na walimu wote tukimbie kurudi shuleni ambako mambo yote yangejulikana. Tukiwa njiani, baadhi ya walimu walilalamika kuchoka, mmoja akasema ameumia kidole lakini hakumbuki ni wapi alijiumiza. Tulipofika shuleni mwalimu mkuu akasema wanafunzi wote tusimame katika mstari mmoja ili aongee, walimu wake wakaenda kusimama jirani na yeye. “Jamani wanafunzi, wote kilichotokea kule mmekiona, walimu wenu si mnawaona, wamechafuka miguuni mpaka kwenye magoti, tena afadhali sisi walimu wa kiume, wa kike wao wamechafuka zaidi sababu wanavaa sketi na magauni.” Nilitamani kumuuliza mwalimu mkuu kwa hiyo hoja yake ni nini kwa maneno yake yale, lakini nilijizuia tu kwa sababu ya heshima. “Sasa kinachoonekana hapa walimu walikuwa wakilimishwa na wachawi,” alisema mwalimu mkuu. Wanafunzi wote tulibaki kimya, naamini kila mmoja wetu alikuwa akiwaza linalomjia kwenye ubongo wake. Sikuwa na wasiwasi kwa sababu nilishawatengeneza wote, hakuna aliyekuwa na ubavu wa kusema waletwe waganga ili kumkamata mchawi shuleni. Wakati mwalimu mkuu akiendelea kuzungumza, nilijigeuza, nikatoka mstarini huku taswira yangu ikiendelea kuonekana mstarini. Niliwafuata walimu, nikawapulizia upepo wa kutoka kinywani mwangu kisha nikawachukua wanafunzi nane waliokuwa mstarini wakaja kusimama pale wakawa walimu, wale walimu nikaenda nao kwenye darasa moja ambapo niliwabebesha madawati. Kila mwalimu mmoja alibeba dawati moja lenye kuchukua wanafunzi wawili. Baada ya kubeba madawati, niliwatoa hadi mstarini kisha nikawazungusha sehemu mbalimbali za shule. Madawati ni mazito sana, lakini walilazimika kubeba kwa sababu ya nguvu za kichawi. Nilimwona mwalimu mkuu akizogoana na wale wanafunzi waliosimama jirani yake. Alikuwa akiwaambia waongee wanachotaka lakini wakawa wanagoma, sasa akawa anawaambia kama wao wenyewe hawataki kuongea nani ataongea badala yao? Kumbe hakujua kama wale ni wanafunzi ambao nao akili zao zilivurugika kwa sababu ya uchawi. Wale walimu niliowabebesha madawati walianza kutokwa na jasho sasa, waliloa nguo, mashati ya walimu wa kiume yalikuwa chapachapa na vumbi juu, nikawaamuru warudishe madawati kwenye darasa husika. Walipomaliza, tulitoka nao nje, tukarudi mstarini ambapo kufumba na kufumbua kila mhusika alitwaa nafasi yake. Yaani wale wanafunzi walirudi mstarini pamoja na mimi na wale walimu waliokuwa na kibarua cha kubeba madawati nao walirudi sehemu yao. Mwalimu mkuu alishtuka na kusema: “Haa! Walimu wangu, nini kimewapata muda huu?” Wanafunzi nao walijishika vinywa, hata mimi pia. Tulikuwa tukishangaa wale walimu, walikuwa wamechoka sana. Nilimwona mwalimu mmoja wa kiume akiingiza mkono mfukoni mwake, akatoa kitambaa na kujifuta jasho ambalo lilikuwa likimchuruzika kama yuko kwenye mvua. Hakuna mwalimu hata mmoja aliyesema neno kwa wakati huo kwa kuwa walikuwa wakihema kwa kasi, si unajua kubeba kitu kizito kwa muda mrefu. Mwalimu mmoja akanyoosha mkono juu, mwalimu mkuu akamruhusu azungumze. “Mwalimu, hii hali itatufikisha pabaya sana. Kuna mtu anacheza huu mchezo, najua kule tumelimishwa, hapa hata sijui tumefanywa nini, lakini kama tulibeba kitu kizito kichwani.” “Ina maana walimu nyie wenyewe hamjui mlichobeba, eti walimu?” “Hatujui.” “Mimi nahisi gunia la mahindi,” alisema mmoja, wanafunzi tukacheka sana. Mwalimu mkuu alikuja mbogo kwa sisi kucheka, akauliza kisa cha kucheka, hakuna aliyekuwa na jibu. Lakini kusema ule ukweli wale walimu walichafuka sana. Ilibidi mwalimu mkuu awaruhusu warudi majumbani kubadili nguo kwani walionekana kama vichaa, chukulia walichochafuka shambani halafu na ile shughuli ya kubeba madawati. Baada ya walimu kuondoka, mwalimu mkuu aliongea kama kwa kubembeleza. Alisema kama kuna mchawi kati yetu sisi wanafunzi aache kwani kwa kuendelea nao, walimu watashindwa kufundisha vizuri na matokeo yake wanafunzi hatutafanya vizuri katika masomo yetu. “Na kama huyo mchawi hapatikani katika nyinyi wanafunzi basi mkirudi nyumbani leo mkawaambie wazazi wenu kilichotokea, ni mengi yametokea lakini sitaki kuyasema,” mwalimu mkuu alilalamika sana. Kabla hajaendelea, mimi nilinyoosha mkono juu ili nipewe nafasi ya kusema mawili matatu. http://deusdeditmahunda.blogspot.com/





… “Wewe unataka kusema kuhusu nini?” “Niongee kidogo mwalimu.” “Kuhusu la uchawi au una lako jingine?” “Hilihili la uchawi.” Nilimwona mwalimi mkuu amenitumbulia macho kama asiyeamini alichokisikia kutoka kwangu. Sababu kubwa ya kutoamini nadhani ni kitendo cha mimi kutaka kuongelea hilo wakati kuna wanafunzi wakubwa zaidi yangu walikuwa kimya. “Enhe, ongea unachotaka kuongea wewe.” Nilimuuliza mwalimu hivi: “Niliwahi kusikia serikali yetu haiamini mambo ya kichawi, uongo kweli?” Mwalimu mkuu akajibu ni kweli kabisa. Nikaendelea kumuuliza: “Je, sasa hayo maagizo unayotupa tukapeleke nyumbani si kuifanya serikali iamini ushirikina maana shule hizi si za serikali?” Mwalimu mkuu akanifokea, akasema nikomee hapohapo, yeye kama mwalimu mkuu hawezi kuiona shule inaangamia kwa sababu ya kuogopa serikali haiamini uchawi. “…ni kweli serikali haiamini uchawi lakini mimi naamini, na mimi ndiye mwalimu mkuu wa shule hii. Hapa shuleni uchawi umezidi sana au wewe unawa…” Sikusubiri amalize kwani nilijua anataka kusema nini, nikamtumbulia macho huku moyoni nikisema maneno yangu ya kichawi, akashikwa na ububu wa muda. Hata kutuamuru tuondoka mstarini alitumia ishara ya mikono, wanafunzi tukatawanyika. Siku hiyo nilipofika nyumbani nilimwambia mama kilichotokea, nikamwambia ushauri wangu ni kuachana na walimu kwani wote wameonesha hawajiwezi. “Kama ni kuwachezea, tumewachezea sana, tumewaumiza sana, tuwaache tu sasa, mimi wamenichosha sana,” nilimwambia mama, akasema sawa lakini akasema anachofurahi ni kwamba, nimewaroga walimu wangu hadi nimechoka mwenyewe, tukacheka na kuendelea na mambo mengine.



MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog