Simulizi : Mkufu Wa Malkia Wa Gosheni (2)
Sehemu Ya Tatu (3)
La kwanza akauliza, natoka nyumbani na machungwa, lakini natembea na maji, alafu narudi nyumbani na machungwa pia. Lakini nikikasirika vyote navipoteza njiani. Mimi ni nani na kivipi hivyo vyawezekana?
Kiumbe kikafikiri kwa kina kwa muda wa dakika kadhaa kisha akasema jibu ni Jua. Anatoka nyumbani na machungwa kumaanisha anachomoza na rangi hiyo, anatembea na maji kumaanisha akiwa angani kunakuwa rangi ya bluu, na anarudi nyumbani na machungwa pia kumaanisha anazama tena na rangi hiyo.
Na akikasirika, vyote: maji na machungwa hupotea kwa njia ya ukame.
Akapata!
Seth akamuuliza swali la pili, ni nini kina majiji lakini hakina nyumba, kina misitu lakini hakina miti na kina maji lakini hakina samaki?
Kiumbe kikafikiri na kujibu: ramani!
Akapata. Kikafurahi mno. Sasa kilikuwa kimebakiza swali moja tu, na endapo akilipata basi itakuwa zamu yake kuuliza maswali upya. Akajawa na hamu ya kusikia swali hilo.
Seth akashusha pumzi ndefu kisha akarusha turufu yake ya mwisho.
Mfalme hana mtoto wa kiume, mtoto wa kike wala Malkia. Kwasababu hii ni lazima aamue nani atarithi kiti chake akifa. Kufanya hilo akaamua atawapatia watoto wote ndani ya himaya mbegu moja moja. Mtoto yeyote atakayekuwa na mti mkubwa mzuri kuliko wote atafanikiwa kuupata ufalme.
Mwishoni wa shindano hilo, watoto wote wakaja kwenye kasri ya mfalme wakiwa na miti mizuri mno vyunguni. Baada ya mfalme kutazama kila chungu vya watoto wote hao akaamua kumpatia ufalme mtoto mdogo aliyekuja na chungu kitupu.
Kwanini alimchagua mtoto huyu mwenye chungu kitupu juu ya wote wenye miti mizuri?
Kiumbe yule akakuna kichwa. Akajibu ni kwasababu binti huyo alikuwa ndiye pekee mwaminifu kati ya wote hao kwani mfalme alitoa mbegu isiyozaa.
Akapata!
Sasa zoezi likajirudia tena sasa wakiwa wamepewa nafasi moja moja tu za kuulizana maswali. Kiumbe kikaanza kuuliza, Seth akafanikiwa kujibu, kisha naye akatupa lake. Hatimaye kile Kiumbe kikafurukuta pasipo mafanikio.
Ni vitu gani viwili kamwe huwezi kuvila kwenye mlo wa asubuhi? Lilikuwa swali dogo lakini likamtotesha kiumbe wa ajabu. Akafikiri sana na mwishowe akamwomba Seth ampatie majibu baada ya kukosa kabisa.
Seth akamjibu vitu viwili ambavyo kamwe huwezi kuvila kwenye mlo wa asubuhi (breakfast) ni mlo wa mchana (lunch) na mlo wa usiku (dinner).
Kiumbe yule akanyong'onyea sana kushindwa. Lakini hakuleta ukaidi akakubali kwa moyo wake wote.
Akawambia Seth amekua akiwaua watu wote anaokutana nao ndani ya jangwa hilo kwa kushindwa kumjibu mafumbo yake, ila yeye ameweza na akafanikiwa kumpatia swali alilolishindwa, basi anastahili zawadi yake.
Akamwelekeza Seth namna ya kufanya kutimiza adhma yake kisha akaaga na kwenda zake.
"Umefanikiwa Seth?!" Fluffy akalipuka kwa furaha. "Umefanikiwa!"
Seth akawapa furaha zaidi kwa kuwaeleza kuwa kiumbe yule amewapatia namna ya kufika Misri kama zawadi. Hawatakuwa na haja ya kutembea wala kupoteza masiku tena!
Kila mtu akajawa na furaha kifuani mwake. Fluffy akambusu Seth mabusu kedekede wakicheka.
"Ni namna gani hiyo?" Malkia akauliza. Seth akawaambia watatembea kwa takribani kilomita moja kuelekea mashariki mwa jangwa, huko watakutana na mapango matatu, wataingia pango la katikati na kusema kwa kilugha cha yule kiumbe kwamba wamemshinda kwa mafumbo.
Akisema hivyo watasikia sauti ikiuliza fumbo hilo lililomshinda kiumbe, watakapolitaja, litatokea kwenye kuta ya pango na mara wataona njia humo, wataifuatisha na kujiri waendako!
Usiku huo ukawa mwanana kwao. Fluffy akalala kifuani mwa Seth kwa furaha. Lakini hilo jambo halikumpendeza Malkia.
Asubuhi yake jua liliposimama, wakafuata maagizo kama walivyopewa na Seth. Kuzama pangoni wakajikuta kando kando mwa bahari wakiwa wamelala wasielewe wamefikaje hapo.
Ni mawimbi ya bahari ndiyo yaliwaamsha baada ya kuchapa miili yao.
Wakaamka na kuangaza. Lakini kabla hawajafanya kitu wakastaajabu wamezungukwa na maaskari waliobebelea majambia marefu. Askari hawa walikuwa wamevalia sketi ngumu, vifua vyao vikiwa wazi!
Wakawaamuru waweke mikono kichwani na wajieleze wao ni wakina nani na hapo wanafanya nini kabla hawajakatwakatwa na vipande vyao kulishwa papa baharini.
***
Kabla hawajasema jambo, mara wakasikia sauti ikisema:
"Waacheni!" Wote wakageuka na kutazama. Wakamwona mzee mmoja aliyevalia joho lililochoka rangi ya grey. Alikuwa na nywele ndefu zinazogota mabegani pamoja na ndevu nyingi zilizojawa mvi.
Miguuni alikuwa peku, na kwenye mkono wake wa kuume alikuwa ameshikilia fimbo ndefu akitembea nayo.
"Waacheni nawafahamu hao!" Mzee huyo akasema akiwakaribia wahusika wake - wanajeshi farasini na wakina Malkia.
"Una uhakika?" Mwanajeshi mmoja akauliza.
"Unadhani mie mwehu?" Akajibu mzee yule. "Kuna faida gani kusema nawajua watu nisiowafahamu?"
Basi mwanajeshi aliyeuliza, ambaye alionekana ndiye mkubwa kwa cheo, akamtazama babu huyo alafu akawatazama na wakina Malkia. Ni kama vile alikuwa na shaka ndaniye lakini akapuuza, akawaamuru wenzake waondoke.
Wakayoyoma.
"Wewe ni nani?" Malkia akamuuliza yule babu. "Kwanini umetusaidia?"
Yule babu akawatazama pasipo majibu, kisha akawaamuru wamfuate. Wakasita. Wakamtazama yule babu akienda zake kisha wakatazamana wao kwa wao. Wakaamua kumfuata.
Wakatembea kwa umbali mrefu kidogo kabla hawajaingia kwenye nyumba fulani kubwa kuukuu, wakawafungia farasi wao nje na wao wakakaketi sebuleni.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sebule hii ilikuwa hafifu kwa samani. Sakafuni kulikuwa kuna mkeka tu rangi ya zambarau. Waliketi hapo na yule babu akaenda zake chumbani, ndani ya muda mfupi akarejea na kuungana nao mkekani.
Alikuwa sasa ananukia marashi ya tofauti na hapo awali. Bila shaka alikuwa ameenda kuyapaka huko chumbani. Marashi haya yalikuwa ni makali, lakini yanayovumilika.
"Natambulika kwa jina la Waheed," akajitambulisha kwa jina moja. Seth akashtushwa na jina hilo kwani maanaye haikuwa nzuri.
"Waheed si jina langu halisi," akaendelea kufafanua babu huyu. "Lakini ndilo jina ninalotambuka nalo kwa watu wengi waishio hapa. Kwahiyo si mbaya nanyi mkaniita hivyo."
"Kwanini Waheed? Kwanini jina hilo?" Seth akawahi kuuliza. Babu yule akatabasamu kisha akapandisha mabega yake. "Ndivyo walivyoamua kuniita. Wananichukulia mimi ni Waheed. Matendo yangu kwao wanayaona yatoka kwa Waheed. Nami sina muda wa kuwasahihisha, nimewaacha wabaki na mawazo yao hayo."
"Na kwanini umeamua kutusaidia?" Malkia akalirudia swali lake.
"Kwasababu mlikuwa mnahitaji msaada," akajibu Waheed, kisha akatabasamu. "Unadhani nisingewasaidia pale mngekuwa wapi saa hii?"
"Ulijuaje tunahitaji msaada?" Akauliza tena Malkia.
"Watu waliozingirwa na wanajeshi wanahitaji kitu gani zaidi ya msaada?" Waheed naye akauliza.
Kukawa kimya kidogo. Waheed akasema:
"Kabla ya kuniuliza maswali yenu ilibidi mnishukuru kwanza. Sasa hivi mngekuwa ndani, mnangojea maswali mengi sana maana nyie ni wavamizi."
"Nani kakuambia sisi wavamizi?" Seth akawahi kuuliza.
"Mnaonekana nyie ni wavamizi. Hamuonekani kama watu toka Misri. Ama tuseme macho yangu yanawaona nyie sio wa Misri."
Akabinua mdomo wake na kuendelea kueleza:
"Pengine si mimi tu, hata wale wanajeshi waliwatilia hofu kuwakuta mmelala ufukweni. Watakuwa wamedhani mmefika hapo baada ya chombo chenu kwenda mrama ama kupata hitilafu baharini."
"Na wewe unadhanije?" Malkia akauliza. Waheed akacheka kisha akamtazama Malkia kwa macho yake madogo aliyoyafumbua kwa upana.
"Hamjapata hitilafu yoyote baharini. Wala hamjatumia njia ya baharini kufika hapa. Niliona kwa macho yangu mlipotokea pale kimiujiza," alieleza akatabasamu.
"Najua mnaweza mkawa na maswali mengi juu yangu ila mimi nipo hapa kwasababu ya kuwasaidia kufikia lengo lenu."
"Lengo gani?" Malkia akauliza.
"Mwanamke, acha kuuliza maswali mengi. Jua najua kila kitu kuwahusu. Wewe unaitwa Sandarus, huyu ni Seth, Zura, Fluffy na huyo mwingine anaitwa Alk. Bado unadhani kuna kitu sikijui?"
"Wewe ni nani haswa Waheed?" Fluffy akauliza. Wote vichwani walikuwa na swali hilo. Walikuwa wamekubaliana kuwa Waheed hakuwa mtu wa kawaida.
Waheed asiongee jambo, akapasha viganja vyake alafu alafu akawaonyeshea Malkia na wenzake taswira viganjani. Wakajiona walipotokea hadi namna walivyofika hapo.
Waheed alipomaliza kuwaonyesha hayo, akawaambia atawasaidia kuipata hiyo kofia ya Pharaoh waliyokuja kuitafuta. Hapo ndiyo Malkia na wenzake wakachoka.
Hadi hili alijua?
Hawakupata muda wa kuuliza zaidi, Waheed akawataka wapumzike watateta zaidi baadae. Akawapatia chakula na mahali pa kupumzika.
- JE, WAHEED NI MTU WA KUMWAMINI?
- YUKWAPI MTU YULE PEKEE AISHIYE KARIBU NA BAHARI YA MEDITERANIA AMBAYE WAKINA MALKIA WALIAMBIWA WAMTAFUTE?
***
Hii ilikuwa ni siku ya tatu sasa. Siku hii haikuwa ya kawaida kwa Venet, bali siku maalum. Tena maalum sana!
Anga lilikuwa limependezeshwa na picha kamili ya mwezi. Mwezi mweupe ulio kamili ambao unaweza ukadhani unaelekea kugongana na dunia kwa namna unavyoonekana vema na kwa ukaribu.
Siku hii iliyokuwa inangojwa mno na Venet hatimaye iliwadia. Siku ya kafara! Siku ambayo mwezi unaonekana vema.
Venet akiwa ameshaandaa kila kitu katika uwanja wake wa sadaka, kama vile kisu kikali, kaniki nyeupe na nyekundu na kitabu chake cha ulozi juu ya meza, akawasogelea vikongwe pamoja pia na mwili wa Rhoda. Akatabasamu kwa furaha.
"Leo siku imewadia," akawaambia vikongwe. Kufumba na kufumbua akageuka kuwa kundi kubwa la popo lililotawala na kumeza eneo zima!
Wakaruka juu sana na kutengeneza maumbo yasiyoeleweka huko angani. Lakini ajabu Venet akajiri nyuma ya vikongwe aliowaacha chini kisha akaelekea kufuata kitabu chake. Akakifungua na kukitazama kisha akakifunga. Alikuwa tayari ameshakariri cha kusema.
Akanyoosha mikono yake juu alafu akapaza sauti kutamka maneno hayo aliyoyakariri. Akayarudia mara sita. Kila alipoyarudia maneno hayo wale popo waliokuwepo angani wakawa wanadondoka wakiwa wafu. Mpaka anatimiza idadi ya sita, popo wote wakawa wamekwisha angani!
Sasa Venet akaanza kuomba mwili mpya. Akatamka maneno anayoyajua yeye bado akiwa amenyoosha mikono yake juu.
Basi kufumba na kufumbua, wale vikongwe pamoja pia na mwili wa Rhoda ukageuka kuwa kundi kubwa la popo! Wakapanda juu kabisa.
Venet akaanza kuwaita kwa kutumia maneno yake ya kilozi, popo hao wakashuka kwa kasi na kupotelea mwili wake wote! Venet akajihisi mwenye nguvu zaidi.
Akajihisi mpya kama vile ametoka kuzaliwa muda si mrefu.
Akacheka sana. Akafurahi sana. Hakuna siku aliyofurahi maishani mwake kama hii!
Hakupoteza muda, kama mtu asiyeamini, akaanza safari yake ya kwenda himaya ya Goshen. Alijigeuza kuwa kundi kubwa la popo na alipofika mpakani akageuka kuwa Rhoda!
Kama ungelipata bahati ya kumwona usingeliweza kutambua kasoro hata moja kwenye mwili wa mwanamke huyo. Alitembea kwa madaha mpaka yalipo makazi yake, akafurahi sana.
Bado yote haya yalikuwa ni kama ndoto. Hakuamini sasa ametoka kwenye kifungo chake cha maisha. Sasa amekuwa huru!
Akacheka haswa.
Lakini furaha yake hii haikudumu, akasikia sauti huko nje ya nyumba ikimuamuru atoke ndani upesi!
Walikuwa ni wanajeshi wa Phares wapo nje. Walishajua Rhoda amerejea himayani na sasa walikuwa hapo kutekeleza agizo la kumkamata mwanamke huyo mara moja kama vile walivyoagizwa.
Venet akajiuliza kipi cha kufanya. Akaona ni kheri akaficha makucha yake kwa sasa. Atulie aone mchezo unaendaje hapa. Hakuona haja ya kujifanya mjuaji kwenye ngoma ya kigeni.
Basi taratibu akatoka ndani na kwenda kukutana na rundo kubwa la wanajeshi likiwa limemebelea kila aina ya silaha kana kwamba wamekuja kumkamata mhaini mwenye nguvu isiyo mithilika.
Venet akastaajabu jeshi hili! Asiongee kitu akasukumwa na teke mpaka chini. Akafungwa mikono akidhihakiwa kwa kuitwa mlozi mkubuhu, muuaji na shetani asiyestahili hata tone la huruma!
Japokuwa sifa hizi zilikuwa ni za kweli, Venet akaona amedharauliwa mno. Akajiona ameshushwa na sasa anafanana na taka shimoni. Si mwenye thamani. Lakini bado akavumilia.
Akiwa chini, Alphan akaweka mguu mgongoni mwake akimwambia:
"Ulidhani sitakukamata? Pole sana. Hatimaye mwisho wako umefika. Utatundikwa mbele ya kadamnasi kila mtu aone namna unavyopapatika ukitokwa na roho."
Alafu akamtemea kohozi ptuuh! Venet akatetemeka kwa hasira. Akajihisi moyo wake unasagwa na mche wa kinu. Akang'atameno kwa uchungu akimtazama Alphan kwa jicho la kizandiki, Alphan akatabasamu na kumkebehi.
Akifanya hayo wanajeshi wake wakawa wanashangilia kana kwamba bondia wa nyumbani anamshushia makonde bondia mgeni.
Mwishowe Venet, aliye katika mwili wa Rhoda, akafungashwa safari kuelekea lupango. Huko njiani akavutwa kama ng'ombe. Alikuwa peku akichomwa na miba na kutobolewa na mawe.
Watu njiani wakauliza kulikoni, wakaambiwa ni mlozi huyo. Basi nao wakaokota mawe na kumrushia, kama hayakuwepo wakamwagia mavumbi ama kumtemea mate!
Venet aliwezaje kuyavumilia yote haya?
Muda wote huo akawa anatazama chini akifunikwa na nywele. Alikuwa anautazama udongo anaoukanyaga. Mdomoni kuna kitu alikuwa anateta lakini hakikusikika.
Akafika lupango na kutiwa ndani akisukumiwa humo. Alikuwa peke yake katika chumba hiki, bila shaka walihofia kumchanganya na watu wengine kwasababu za usalama.
"Utakaa humo mpaka utakapokuja kuonja kitanzi!" Akasema Alphan akimuaga.
Basi huko nje kukawa sherehe kwenye kilabu cha pombe. Hatimaye mlozi amekamatwa! Watu wakanywa na kufurahi.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Habari zikasambaa ndani ya himaya nzima kwamba Rhoda ni mchawi na amekamatwa akitokea Tanashe. Habari hizi zikawashtua watu na kuwasisimua.
Mwaname yule mrembo, amekamatwa ulozi? Anhaa... basi ndo maana jengo lake likawa ghofu hivi ghafula? Ndiyo maana biashara yake ikatokomea kusikojulikana?
Watu sasa wakapata majibu. Kila mtu akawa anangoja kesho yake mwanamke huyo atundikwe kunyongwa kwenye uwanja wa hadhara. Wote waende kushuhudia!
**
"Mfalme, tumeshamtia nguvuni!" Akasema Alphan muda mfupi baada ya kuonana na mfalme, usoni akiwa na tabasamu pana.
Mfalme akatahamaki kidogo. Alikuwa yupo juu ya mgongo wa farasi akiwa ametoka safarini. Alimtazama vema Alphan aliyekuwa na pumbazo la furaha usoni, akamuuliza:
"Yupo wapi sasa?"
"Kule chimboni, unataka kumuona?"
"Ndio ila si kwa sasa. Naomba nipumzike kidogo, nadhani unaona nilipotokea."
Alphan akainamisha kichwa chake chini, mfalme akazama ndani alipopata kujimwagia maji na kisha kuketi mezani na mchumba wake, bibie Tattiana.
"Pole kwa safari," mwanamke akamkarimu.
"Ahsante, umeendeleaje hapa na upweke?" Mfalme akauliza kwa uso mtam.
"Upweke?" Tattiana akadakia kwa toni laini. "Sidhani. Nawezaje kuwa mpweke wakati kuna watu wengi hapa?"
Mfalme akatabasamu.
"Kwahiyo ulikuwa na nani akikusaidia kusogeza muda?"
"Watu wengi tu ... Nilikuwa nikiongea na wale wamama."
"Wamama? Unamaanisha wale vijakazi?"
"Sijiskii vizuri kuwaita hivyo. Ni watu wazima kama mama yangu!"
Mfalme akaangua kicheko kisha akamshukuru Tattiana kwa kumfanya afurahi kwani alikuwa ametingwa sana kichwani na hakutegemea kama atapata kuonja hata tabasamu mpaka siku hiyo inakoma.
Habari hiyo ikamvutia Tattiana, akataka kujua nini kilimsibu mfalme. Mbona alitoka na furaha kasrini?
Mfalme akanywa kwanza mvinyo alafu akashusha pumzi ndefu. Akawaamuru vijakazi wake wote wawapatie faragha kabla hajafungua jumba lake la maneno. Wakamtii.
"Kulikuwa na kikao huko himaya ya Mamu. Wafalme wote wa ukanda huu walikuwa wamekutana huko, nami nilipokea ujumbe wa kuhitajika.
Sikutaka kuupuuzia huo wito, nikautii. Lakini niliyokutana nayo huko, yamenitia simanzi na kunitetemesha mwili!"
Tattiana akashindwa kungoja,
"Nini hiko?' Akawahi kuuliza.
Mfalme akaminya mdomo wake akitazama meza. Alafu kwa utulivu akiwa mbali fikirani, akasema:
"Mfalme wa himaya ya Maam anakaribia kufa. Hivi tuongeavyo, yupo hoi taabani kitandani, ni pumzi tu ndiyo wanamhesabia. Hawezi kupona abadani. Anatia huruma sana, haswa nikiwatazama wajane na watoto atakaowaacha bado wakiwa wanamhitaji.
Lakini inaniumiza zaidi na kunikosesha amani kwani kifo chake kina mahusiano na mikono yangu!"
Hapa Tattiana akaogopa. Akatoa macho akikunjama ndita, akamuuliza mfalme kivipi ahusike na kifo cha mfalme wa himaya nyingine? Lini alienda huko akamshikia upanga ama kumtumia maadui wammalize?
Mfalme akamwambia hakuna lolote kati ya hayo aliyoyaainisha amepata kulifanya. Mfalme wa Maam anaweza akawa na maadui ndani ama nje ya himaya yake, hilo halikujalisha. Hakuna mtu anayependwa na wote.
Ila shida inakuja kwamba mfalme huyo amejazwa sumu na tunda la Cedar! Hapa ndipo panamtia hatiani kwani tunda hilo linapatikana ndani ya Goshen pekee!
Ni kivipi tunda hilo likafika huko na hata kutumika kumdhuru mtu huyo mwenye nafasi ya juu ndani ya himaya?
Kwahiyo Goshen inatuhumiwa kwa haya mawili. Mosi, kurudia biashara ya kuuza matunda hayo haramu yaliyopigwa marufuku. Na pili, baya zaidi, kutuhumiwa kufanya jaribio la kumuua mfalme huyo wa Maam kwasabababu zisizojulikana.
"Amah!" Tattiana akaufunika mdomo wake kwa bumbuwazi.
"Kwahiyo hivi tunavyoongea," mfalme akaendelea kumwaga maneno. "Nimepewa takribani siku tano tu kutoa maelezo na ushahidi. Litakaposhindikana hilo, basi hatua stahiki na kubwa zitachukuliwa."
"Zipi hizo?" Tattiana akataka kujua.
"Mosi, Goshen kutengwa na himaya zote na huku wananchi wake wakifanywa kuwa haramu katika kila ardhi watakayokanyaga. Pili, himaya zote kuungana na kuiteketeza Goshen kwenye uso wa dunia. Ama tatu, mfalme wa Goshen kunyongwa mpaka kufa kwenye karamu ya mwaka!
Adhabu itateuliwa kutokana na maelezo yatakayotolewa."
Tattiana akahisi moyo wake umekuwa mzito ghafla. Hata akastaajabu ni kwa namna gani mfalme aliweza kukenua kwa kicheko muda mfupi hapo nyuma.
"Sasa tutaepukaje kikombe hiki?" Akauliza akijawa na woga.
"Kwa njia moja tu," akajibu mfalme. "Nayo ni kumpata mtu aliyepanda, kuchuma na kusafirisha Cedar kwenda huko."
"Hakuna mbadala mwingine!" Akamalizia.
Haki Tattiana akavuja jasho. Hili lilimtetemesha kwa woga haswa. Mfalme alinyanyuka akaenda zake akimwambia aenda kupumzika kwani baadae ana kazi kubwa ya kufanya.
Basi Tattiana akaachwa mpweke mezani. Hakudumu hapo muda mrefu wakaja wale vijakazi ambao walikuwa wameshamzoea mwanamke huyo kwa wepesi. Wakastaajabu kumkuta tofauti.
Lile tabasamu walilomuona nalo hapo awali halikuwapo tena.
"Nini shida ewe kipenzi cha mfame?" Wakamdadisi. Tattiana asiseme ukweli, akalaghai tumbo lamsumbua. Lakini vijakazi hao walikuwa watu wazima, wakautambua huo uongo.
"Pole, kipenzi cha mfalme. Twaweza saidia?" Akauliza mmoja wao.
"Hapana, msijali," Tattiana akawatoa hofu.
"Au pengine tayari ushambebea mfalme mtoto?" Kijakazi mwengine akatania. Wakacheka.
"Atafurahi sana, mfalme. Bila shaka furaha yake itauneemesha hata na sisi."
"Hapana, sina ujauzito," Tattiana akasema kwa tabasamu la bati. "Ni tumbo la kawaida tu."
Wale vijakazi wakamshauri abebe mimba ya mfame haraka iwezekanavyo. Asikawie kwani hiyo ndiyo njia madhubuti ya kumtia mfalme mkononi.
"Mfalme hawezi akamwacha mwanamke aliyemtia mimba. Hata kama akikuacha, basi utahudumiwa kifalme maisha yako yote."
Tattiana akashukuru kwa ushauri ila akaanza kukereka na uwepo wa vijakazi karibu naye. Si kwamba hakuwa anawapenda, la hasha! Walikuwa ni wanawake wacheshi wenye upendo lakini kichwani mwake hakuwa sawa.
Akaona kheri aondoke akakutane na mfalme chumbani.
"Unamwonaje?' Kijakazi mmoja akauliza. Aitwa Lucy.
"Yu safi sana, nampenda," mwingine akadakia, anaitwa Bella, alafu wakacheka na kugongesha viganja vyao.
"Ila naamini sasa penye miti panakosa wajenzi," Lucy akasema akishika kiuno.
"Kwanini?" Wenzake wakawahi kumuuliza.
"Laiti ningekuwa ndimi mimi nimechaguliwa na mfalme," akaweka kituo akatikisa kichwa.
"Nisingepata hata muda wa kukaa na nyinyi vijakazi maana kila saa ningekuwa nampatia vitu vitamu mfalme. Akigeuka nipo hapa, akikohoa naitika. Akicheua mimi nabeua. Akipika mimi napakua."
Wenzake wakaangua kicheko. "Na ndiyo maana hujawahi chaguliwa!" Akasema Bella.
"Unadhani kwanini? Kwani mimi ni mbaya?" Lucy akauliza akijitazama.
"Wala si mbaya, sema una mdomo. Uliumbwa mdomo kabla ya vingine vyote mwilini!"
Lucy akasonya kisha akaenda zake.
"Wivu tu wawasumbua!"
**
"Mfalme anaingiaaa!" Sauti kubwa ya mwanajeshi ilipiga yowe kutaarifu maafisa wa gerezani na wafungwa wote juu ya ujio huo mkubwa.
Yowe hilo likafuatiwa na mlio wa pembe mara moja kwa sauti kuu.
Mfalme, akiwa ameongozana na walinzi, pamoja pia na viongozi kadhaa wa juu, akiwemo Alphan, wakazama ndani ya gereza na kukatiza koridoni mwa vyumba walimojazwa wafungwa.
Wakiwa wanapita, baadhi ya wafungwa wakawa wanapaza sauti kumuomba mfalme awasamehe wapate kutoka kwani wamekaa muda mrefu mno.
Zilikuwa ni kelele sasa, mfalme asijue zipi za kusikiliza ama kuacha. Nao maafisa magereza wakawa wanajitahidi kuwanyamazisha wafungwa hao wasimsumbue mkuu.
Lakini kabla mfalme hajakatiza bewa hili la wafungwa wanaume, akamwona kikongwe mmoja ndani ya chumba cha lupango. Akajikuta anamwonea huruma.
Akamsogelea na kumtazama.
Kikongwe huyu alikuwa yu hoi, amevalia nguo za kusitiri sehemu zake za siri tu. Nywele zake zilikuwa zimenyonyoka, mwembamba mno na mwenye macho madogo yaliyozama ndani.
Alitamani naye amuite mfalme amuokoe lakini hakuwa na uwezo huo. Hiyo nguvu hana. Ila ajabu mfalme akasikia kunong'ona kwake.
"Unaitwa nani?" Mfalme akamuuliza.
"Nebukadeza," akajibu yule kikongwe kwa shida. Sauti yake ilikuwa chini mno.
"Umefanya kosa gani kuwekwa humu?" Mfalme akauliza. Kabla kikongwe yule hajajibu, akadakia afisa magereza.
"Alikuwa muuzaji wa matunda haramu!"
"Cedar?" Mfalme akauliza.
"Ndio, mfalme!" Afisa magereza akawahi kujibu.
Nebukadeza akatazama chini. Matumaini yake ya kutoka ndani ya chumba cha gereza yakafifia kama siyo kufa kabisa.
"Ni kweli?" Mfalme akamuuliza. Kwa sauti yake ya chini inayokwaruza, Nebukadeza akasema:
"Ndio, ni kweli mfalme. Naomba unisamehe. Niruhusu nikafie nyumbani kwangu, watoto wangu wanizike," Akalia. "Nakuomba, mfalme!"
Mfalme akamtazama afisa magereza na kumuagiza amwachie huru Nebukadeza mara moja. Afisa akashangaa.
"Mfalme, alikuwa muuz--"
"Nimeshasikia," mfalme akamkatiza. "Muweke safi, usiku huu nitakuwa na maongezi naye kwenye meza moja.'
Afisa akapokea amri hiyo na kufanya kama alivyoagizwa. Mfalme akaendelea na safari yake ndani ya gereza mpaka alipofika bewa ya wanawake kukutana na Rhoda.
Huko akamkuta mwanamke huyo akiwa ameketi amegeukia ukutani.
"Amekuwa akiketi hivyo tokea tulipomleta. Na muda mwingine amekuwa akiongea maneno yasiyoeleweka," akaeleza Afisa magereza. Mfalme akamwamuru amfungulie mlango akaongee naye yeye mwenyewe.
"Ni hatari, mfalme!" Afisa akapaza sauti. "Anaweza kukudhuru, si wa kumsogelea karibu!"
Mfalme asiseme jambo akamtazama Afisa yule kwa uso wa kukunja ndita. Haraka Afisa akafungua mlango asiseme kitu tena.
Mfalme akamjongea Rhoda na kuketi naye karibu.
"Rhoda, kipi kimekukumba?" Akauliza kwa sauti ya chini. Rhoda hakujibu. Mfalme akarudia tena swali.
"Naomba uniambie, nakusikiliza."
Wakati huo wanajeshi wakiwa wamekaa tenge kwa lolote litakalotokea. Walikuwa wameshikilia silaha zao vema wapate kuhudumu endapo mfalme atahitaji msaada muda wowote ule.
Bado Rhoda akawa kimya. Mfalme naye akanyamaza. Baada ya ukimya wa sekunde kadhaa, Rhoda akageuza shingo yake kama roboti, akamtazama mfalme na kutabasamu.
"Kumbe wewe ndiwe mfalme?" Akauliza kwa sauti ya kiume! Mfalme akaogopa. Rhoda akaendelea kukunja shingo yake mpaka nyuma ya mgongo, akamtazama Alphan kwa jicho jeusi!
Ilikuwa ni maajabu namna alivyokuwa anatengua shingo yake ikienda popote anapotaka. Hakuna binadamu wa kawaida angeweza kufanya hivyo kabisa.
Alimtazama Alphan pasipo kusema kitu. Upesi mfalme akatoka zake ndani ya chumba hicho, kikafungwa mara moja!
"Nitakuja kukusalimu siku moja," Rhoda akasema. Mfalme akamwambia hatopata siku hiyo kwani kesho atanyongwa mbele ya hadhira.
Rhoda akacheka sana. Akacheka sana, kisha akanyanyuka na kusogelea mlango.
"Ngoja tuone nani ataning'inia kwenye hicho kitanzi kwanza," akasema kwa kujiamini. Mfalme akaenda zake asimjibishe. Sasa akiwa ameamini kwa asilimia zote, Rhoda ni mlozi.
Hakuongea na yoyote yule mpaka anafika kasrini. Kichwani alikuwa anawaza ni kivipi Rhoda amefikia hali ile? Nini kimemsibu?
Akajikuta anamwonea huruma sana mwanamke huyo. Hakuwa na budi sasa bali kuidhinisha zoezi la unyongaji.
"Mfalme .. mfalme ... mfalme!" Tattiana aliita, mfalme akakurupuka toka kwenye dimbwi la mawazo.
"Chakula tayari," Tattiana akamwambia kwa sauti nyororo. "Na mgeni wako pia ameshafika."
"Mgeni?" Mfalme akatahamaki. "Mgeni gani huyo?"
Tattiana alipomweleza akakumbuka ni yule kikongwe, Nebukadeza. Akatikisa kichwa chake na kunyanyuka aende huko.
**"Upo sawa?" Tattiana akamuuliza.
"Ndio!" Mfalme akajibu akijinyoosha. "Nipo sawa tu."
Tattiana hakumuuliza tena lakini alijua mfalme hayupo sawa. Mawazo yalikuwa yanamsumbua. Alitamani kumsaidia lakini hakuwa na namna.
Akaongozana naye mpaka mezani kisha wakaketi wote pamoja na yule mgeni Nebukadeza ambaye alifika kuitikia wito wa Mfalme.
Nebukadeza, kwa heshima zote, alimsalimu mfalme na kumshukuru sana kwa kumsaidia. Hana cha kumlipa, nk Mungu pekee ndiye atamrudishia fadhila.
"Sina mali yoyote, zote zilitaifishwa, bali familia yangu tu. Nisamehe, mfalme, kwani sina cha thamani cha kukulipa. Naomba upokee mzigo huu kama shukrani yangu kwako."
Nebukadeza akanyanyua kifurushi cha rangi ya maziwa na kukiweka mezani kumsogezea mfalme.
"Natumai itakupendeza, mfalme wangu," akasema kwa sauti yake kavu. "Ni cha kitambo sana lakini kina thamani kukitunza."
Mfame akashukuru pasipo kutazama kilichomo ndani. Akamuita kijakazi na kumuagiza apeleke chumbani kwake, akiweke mezani.
"Beba kwa uangalifu," Nebukadeza akamsisitiza kijakazi kisha akamtazama akiondoka na kifurushi hicho kuelekea alipoelekezwa.
"Nebukadeza," mfalme akaita. "Nina shida kubwa sana na natumai utanisaidia," akasema kwa msisitizo.
"Ewe mfalme," Nebukadeza akaita. "Ulinipa mkono nilipokuwa mpweke. Dhoofu lihali, ukanikomboa dhidi ya kifo cha aibu na ukanipatia nafasi tena kwa macho yangu ya kizee kuona familia yangu. Nitaanzia kwenye kona gani ulimwenguni kutokukusaidia? Hata kama itanigharimu maisha yangu, ni tayari!"
Mfalme akamshukuru na kumsihi aendelee kula wakiongea.
"Nimefurahi sana kusikia hivyo. Sina mengi sana toka kwako ila kutambua kuhusu biashara uliyokuwa unafanya."
"Biashara ile haramu?" Akauliza Nebukadeza.
"Ndio," mfalme akamjibu. "Nataka kujua kila chembe ya biashara hiyo. Kila nukta kila tembe. Usinifiche jambo kwani mimi ni mhitaji."
Nebukadeza akaapia kutoficha chochote. Akamwambia mfalme namna biashara hiyo ilivyokuwa na pesa na jinsi inavyoenenda kwa siri kubwa mno kuanzia kwa wafanyabiashara, wanunuzi na hata wasafirishaji.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hapa kunakuwa na ubunifu mkubwa sana. Kila mtu hutafuta namba ambayo ataweza kutoa mtunda hayo nje ya mipaka. Kwa upande wangu, nilikuwa nikitumia mbegu kubwa ya mapapai. Napasua mapapai hayo na kuyajaza matunda kwa ndani kisha nikiyaunga tena.
Lakini baadae nikaja ona njia hiyo ni hatarishi kwani ukaguza ulizidi mpaka kufikia pahala pa tunda moja moja kukaguliwa tofauti na hapo awali yalipokuwa yanakaguliwa yale ya juu tu. Hapa ikanibidi nibalishe namna.
Sasa nikaanza kufuma matoroli ya farasi yaliyokuwa na nafasi uvunguni ambamo humo nikajaza matunda haya pasipo shida yoyote, nikiyafunika na vipande vya mbao thabiti vilivyobanwa na misumari mirefu."
Mfalme akashangazwa na janja hiyo.
"Ikawaje ukakamtwa?" Akauliza.
"Ilikuwa ni siku moja nikiwa mpakani nakaguliwa. Siku hiyo nilipakia mzigo wangu kama ilivyo ada. Lakini sijui nini kilitokea, labda uvungu wa kitoroli haukuwa umefungwa vema, tunda moja likadondoka. Huo ukawa mwisho wangu."
Mfalme akamtaka amweleze ni wapi wanapotoa hayo matunda. Wanawauzia wakina nani huko nje ya mipaka ya Goshen, yaani wafanyabiashara. Na kama yupo tayari kumsaidia kuwang'amua watu hao, nje na ndani, kwa kutumia ufahamu na uzoefu wake wa muda mrefu.
Nebukadeza pasi hiyana akaeleza kinagaubaga. Pia akamuahidi mfalme kumsaidia katika kila hali atakapouhitaji msaada wake.
Wakakomea maongezi yao hapo sasa wakaendelea kula tu. Walipomaliza Nebukadeza akaaga na kwenda zake. Mfalme akarejea chumbani pamoja na Tattiana.
Wakaongea kidogo tu, mfalme akapitiwa na usingizi. Alikuwa amechoka. Tattiana akamwacha mwanaume huyo apumzike wakati yeye akiendelea kufikiria yale yaliyokuwa yanaongelewa pale mezani.
Hakujua kwanini lakini maongezi yale yalimpatia shaka. Namna Nebukadeza alivyoeleza kwa undani kulianza kumpa hofu juu ya mienendo ya familia yake na kile kitu cha siri.
Vipi kama mzee wa baraza akawa anatumia wadhifa wa baba yake kutimiza haja yake kama fadhila kwa mzee huyo kwa 'kumuuza' kwa mfalme?
Mawazo haya yalimfanya Tattiana aone kuna haja ya kwenda nyumbani.
- JE, ATAFANIKIWA KWENDA? AKIENDA HUKO ATAELEZA NINI?
- NEBUKADEZA ATAFANIKISHA KUKAMATWA KWA MZEE WA BARAZA NA MELKIZEDEK?
**
Giza la usiku lilikuwa limeshatawala.
Kwenye nyumba ya Alphan familia ilikuwa imeketi mezani kupata chakula cha usiku. Alphan akiwa pamoja na watoto wake wawili wa kike walionekana kujazwa na furaha.
Vicheko na matabasamu vilitawala meza. Kila mtu angetamani familia hii. Usiku huu ulikuwa bora kwao kwani baba alileta habari njema. Habari ya kujivunia.
Habari ya kumkamata mlozi.
Kama vile babu ama bibi wafanyavyo kwa wajukuu zao, Alphan aliwahadithia watoto zake kila hatua aliyopitia mpaka kufanikisha zoezi hilo. Habari hizi zilikuwa za kusisimua na kuvutia. Na kwa namna Alphan alivyozieleza, zilikuwa ni kana kwamba tamthilia ya majigambo jukwaani.
Watoto wake wakajivunia kuwa na baba mwerevu, shujaa na mzalendo.
"Inabidi mfalme akuzingatie," akasema mmoja.
"Hakika atafanya hivyo," Alphan akajivuna. "Ni kazi kubwa hii!"
Wakacheka.
"Lakini nimefanya kwa moyo wa kuipenda ardhi yangu," Alphan akasisitizia.
Wakala na kumaliza. Wakaagana wakapate kupumzika. Alphan akiwa wa kwanza kwenda chumbani mwake, akakoga kwanza kisha akatazama baadhi ya nyaraka kadhaa kabla hajaulaza mwili wake kitandani.
Hakuchukua muda, akamezwa na usingizi.
Usiku ukaendelea kuyoyoma.
Katikati yake, kwa majira ya sasa mishale ya saa nane ama tisa, popo akatua dirishani mwa Alphan. Kama ilivyo kawaida ya kiumbe huyu, alikuwa amebinuka, miguu juu kichwa chini.
Akamtazama Alphan aliyekuwa hajielewi usingizini kwa sekunde kadhaa kisha akapaa kutokomea!
Lakini mara huko nje, mlangoni mwa chumba cha Alphan ukasikika mzigo mkubwa ukidondoka chini. Tih!
Nini hicho? Hakuna kitu kingine kinachokaa mlangoni mwa Alphan zaidi ya mlinzi wake. Punde mlango ukafunguka, na kundi kubwa la popo likaingia! Chumba kikawa giza.
Asubuhi palipokucha, Alphan hakuwa kitandani! Walinzi wakamtafuta nyumba nzima pasipo mafanikio. Waliambulia maiti ya mwenzao tu.
Watoto wa Alphan wakasaga meno wakiia kwa hofu. Ni jana tu walikuwa wanacheka na kufurahi.
Baadae kidogo, taarifa zikaja. Alphan ameonekana. Lakini hakuwa hai, mwili wake umeshapoa kuwa baridi wa mauti!
Amekutwa uwanjani akiwa ananing'inia kitanzini. Hana alama wala ishara ya jeraha lolote.
**
Taarifa hizi zikasambaa himaya nzima. Watu wakashangaa na kujiuliza ni nani aliyemnyonga Alphan? Na kwa muda gani alitenda hayo?
Lakini kuna mlevi mmoja yeye alishuhudia. Jana usiku akiwa safarini kurudi nyumbani kwake, kama kawaida kipindi cha usiku mzito, akiwa chakari, akastaajabu kuona kundi kubwa la popo!
Kwa uoga akajilaza chini na kuendelea kuangaza. Akaona kundi hilo la popo likizonga jukwaa la kunyongea ambalo liliandaliwa kwa ajili ya mlozi, na mara popo hao walivyoondoka, basi akaona mwili hapo ukiwa unapapatika kufa!
Kwa woga akakimbia mno akidhani naye aweza dakwa akanyongwa pasipo na makosa.
Habari hizo za mlevi, wakaziamini baadhi tu. Wengi wakipuuza kinywa cha mlevi hakiwezi kutoa taarifa za maana. Tangu lini popo akambeba mtu akamnyonge?
Taarifa hizi zilipomfikia mfalme, akaenda upesi eneo la tukio kushuhudia. Hakuamini macho yake. Alphan alikuwa wa kwanza kuonja kitanzi! Akakumbuka maneno ya Rhoda kule gerezani.
"Mfalme," akaita mwanajeshi, "tumnyonge yule mlozi haraka iwezekanavyo, la sivyo atasababisha maafa zaidi!" Akashauri.
Na hili ndilo lililokuwapo kwenye akili ya mfalme. Rhoda aangamizwe upesi kabla hajaendelea kuangamiza wengine.
Basi mfalme akaruhusu Rhoda akatolewe gerezani na kuja kunyongwa asubuhi yote hiyo. Na taarifa itolewe himaya nzima juu ya zoezi hilo.
Haraka taarifa zikasambaa, watu wakajongea eneo la tukio kuja kushuhudia. Wakati huo mauaji ya Alphan yakiwa ndiyo mada kuu midomoni mwa watu.
Kila mmoja alikuwa ana hamu ya kumwona Rhoda. Mwanamke huyo amekuwaje na amekumbwa na nini? Mwanamke ambaye alishafikia hatua ya juu kabisa ya mafanikio. Akionana na mfalme anapotaka. Akifanya biashara yake iliyochanua!
Ilikuwa kitendawili.
Baada ya muda mfupi farasi watano wakaonekana wakijongea eneo la tukio. Farasi wawili walikuwa wanavuta kitoroli kilichofunikwa kama kijibanda. Na wengine watatu waliobebelea walinzi wakisindikiza farasi hao wawili.
Wakafika na kijibanda kile kikafunguliwa akatolewa Rhoda. Gauni lake lilikuwa chafu lisilotamanika. Nywele zake zilikuwa hovyo. Mikono yake ilifungwa pamoja pia na miguu, lakini katika namna ya kumruhusu atembee.
Akapandishwa jukwaani na kukabidhiwa kwa mnyongaji, mwanaume mpana aliyevalia kinyago cha ngozi usimfahamu ni nani. Kabla hajanyongwa akapewa fursa ya kuongea maneno yake ya mwisho.
Akatazama watu waliokusanyika hapo, kisha akamtazama na mfalme aliyekuwa ameketi kwenye jukwaa lake, pembeni akiwa ameketi Tattiana. Akatabasamu.
"Kwahiyo wote mmekuja hapa kunitazama nikifa?" Akauliza. Sauti yake ikawashtua watu waliokusanyika kwani ilikuwa ya kiume wakati mwili ni wa kike.
Akacheka.
"Hamuwezi kuniua. Hamtaweza hata kidogo. Nilishakufa hapo awali, mtaniuaje kwa mara ya pili?" Akauliza. "Maiti inaweza kufa kwa mara ya pili?"
Kukaibuka zogo miongoni mwa watu.
"Hii ni himaya yangu. Ni kitendo cha muda tu kuiweka kwenye mikono yangu. Mimi ndiyo kiongozi wenu mpya, mkubali ama mkatae!"
Mnyongaji akamvika mfuko kichwani, muda wake wa kuongea ulikuwa umeisha, akasogezwa kitanzini na kuveshwa kamba.
"Anyongwe! Anyongwe! Anyongwe!" Sauti za watu zikapaza kwanguvu. Rhoda alipomezwa na kitanzi, myongaji akaufuata mti wa mbao wa pembeni kidogo aufyetue ili sakafu iteguke Rhoda aning'inizwe.
Akafyetua mti huo, na mara mwili wa Rhoda ukashuka chini kwa kasi na kuning'inia. Lakini ajabu, Rhoda hakuwa anapepesuka wala kupapatika kama mtu afanyavyo wakati akinyongwa.
Alikuwa ametulia tuli, hali iliyowashangaza watu. Amekufa ama lah? Baada ya muda mdogo kupita, mnyongaji akautoa mfuko uliomziba Rhoda uso. Ajabu akamkuta mwanamke huyo anatazama!
Watu wakapigwa na butwaa. Alikuwaje hai na huku bado kitanzi kikiwa kimekaba koo lake!
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Rhoda akaanza kucheka kwanguvu! Kwanguvu na kwanguvu! Watu wakajawa hofu vifuani.
Katika hali ya kushangaza anga likaanza kuwa jeusi. Mawingu yalianza kujikusanya na kulificha jua! Mfalme akaagiza upesi mwanamke huyo arejeshwe gerezani, na watu wote watawanyike.
Haraka Rhoda akakusanywa na kutiwa kwenye kibanda, akarejeshwa gerezani. Laiti wangelichelewa na giza likatawala, Rhoda angeligeuka kuwa kundi kubwa la popo!
Popo hawezi kumudu mazingira ya jua, mchana kweupe, na ndiyo maana Venet akabakia katika mwili wa Rhoda hata katika majaribu hayo.
"Sasa mfame, nini tunafanya? Je tumchome moto?" Akauliza mzee mmoja wa baraza.
Mfalme akakuna kidevu chake akiwaza. Hakuwa na majibu kwa wakati huo, akaomba apatiwe muda wake pekee yake apate kuchambua mambo kwa weledi. Basi kila mtu akamwacha kasrini akibakia mwenyewe na Tattiana.
Mfalme akajaribu kula chakula cha mchana lakini akashindwa. Hakikupita kooni kabisa. Tumbo lake halikuwa na hamu na kila saa taswira ya Rhoda ilikuwa inamjia kichwani, na yale maneno ya kuteka himaya mikononi mwake.
Je Rhoda ndiyo ile ndoto aliyoiota siku ile ya popo walioteketeza himaya nzima ya Goshen? Akawaza. Kusema ukweli alikuwa na mawazo mengi sana, ukijumlisha na yale ya himaya ya Maam.
Alikosa raha kabisa.
"Lakini mfalme wangu, mimi nina swali katika haya," akasema Tattiana. Alikuwa amejilaza kandokando ya mfalme aliyekuwa anatazama dari akiwa mbali kifikra.
"Je inawezekana kumrejesha Rhoda kule Tanashe asirejee tena hapa?"
Mfalme akamtazama Tattiana.
"Ametokea huko akaja hapa. Itawezekanaje kumrudisha huko asirudi?"
Tattiana akaguna.
"Kama ni hivyo, aweza kwenda na kutoka Tanashe, mbona walozi wote hawaji isipokuwa yeye?"
Mfame akawa kimya kidogo. Tattiana akaendelea kuteta:
"Kwa nijuavyo, mlozi anapoingizwa Tanashe, basi anakuwa hana uwezo wa kutoka tena humo. Inakuaje Rhoda anaweza kufanya hilo na ingali ulozi upo mwilini?"
Mfalme akaendelea kuwa kimya akinyavua hayo maswali. Hakika yalikuwa na mantiki ndani yake.
"Inawezekana Rhoda si mchawi!" Tattiana akatema bomu.
"Inawezekanaje na umemuona akiwa vile?" Mfalme akafungua kinywa kuuliza.
"Inawezekana mwili wa Rhoda ukawa ndiyo umetumiwa na wachawi na si kwamba yeye ni mchawi."
"Kivipi?"
"Hukuona hata sauti iliyokuwa inamtoka?" Tattiana akauliza. "Alikuwa anaongea kwa sauti ya kiume, kuna mwanaume ndani yake! Na huyo mwanaume ndiye mlozi."
Mfalme akawa kimya.
"Huyo mlozi anautumia tu mwili wa Rhoda," Tattiana akaendelea kutema cheche. "Na ndiyo maana anaweza kuingia na kutoka Tanashe kinyume na walozi wengine!"
Hilo jambo likagonga kichwa cha mfalme. Kweli lilileta maana. Akamshukuru Tattiana kwa wazo hilo yakinifu.
"Sijui kwanini sikuwaza hivyo," akalaumu. Haraka akawaita wazee wa baraza na kuwashirikisha hilo wazo. Akawauliza ni nini cha kufanya, nao wakamjibu inabidi wamtafute mtaalamu atakayewasaidia kumtoa mlozi huyo ndani ya mwili wa Rhoda.
Lakini,
"Tutampatia wapi huyo mtaalamu?" Mfalme akauliza.
Mzee mmoja akapendekeza wafunge safari kumwendea Venim!
"Huyo naye si mlozi?" Akauliza mzee mwingine.
"Baniani mbaya kiatu chake dawa!" Akasema mtoa wazo.
Kwa pamoja wakaonekana kuliunga mkono hili shauri. Waende kwa Venim. Japo yupo mbali, ndiye mtu wa pekee aliye karibu kwao kwa jambo la utaalam.
Basi pasipo kupoteza muda, ikabidi wateuliwe watu wa kwenda huko kusimamia hilo jambo. Wakateuliwa wazee wawili na kupewa kikosi cha wanajeshi kuwalinda safarini.
Mmoja wa wazee walioteuliwa alikuwa ni baba yao Oragon na Ottoman. Ebu tutumie jina iwe rahisi kumrejelea, mzee Harid.
Wakapewa muda mchache wa kujiandaa kabla ya kuanza safari hiyo mara moja.
"Wanangu," Harid akaita akiwatazama watoto wake wa kiume. "Nimetumwa na mfalme kwenda mbali sana na nisingeweza kukataa. Kwa muda wote huo nitakaokuwa huko, hakikisheni kila jambo laenda sawa hapa, mmeshakua. Mnatambua kila njia. Sawa?"
Lakini mzee kabla hajaondoka akawapa angalizo muhimu.
"Kuweni waangalifu mno, na mkalitende lile nililowaambia kwa ustadi mkubwa. Endapo pumzi ile ikiendelea kudumu, hakuna tena biashara!"
Alipomaliza kusema hayo akaenda zake kutimiza agizo la mfalme. Walikusanyika mbele ya kasri wakapatiwa kila hitaji, pamoja na walinzi, farasi wakaanza kuvuta matairi.
"Sasa na sisi tunaoachwa tunafanyeje?" akauliza Tattiana wakiwatazama wazee na kikosi chao cha wanajeshi wakiyoyoma.
Mfalme akashusha pumzi ndefu, alafu akamwita mmoja wa majemedari na kumuagiza ahakikishe wanamtazama vema Rhoda kule gerezani.
Kila muda awepo ndani ya chumba chake, akiwa anachungwa na macho na silaha. Agizo likaenda kutekelezwa.
Wakaongezwa wanajeshi wawili kutimia watano mbele ya lango la chumba cha gereza cha Rhoda. Wanajeshi hawa wote wakiwa wamebebelea mikuki ama mapanga. Au vyote.
Rhoda akawatazama kisha akatabasamu. Akawaambia:
"Acha niwahadithie simulizi moja ya kunguru." Aliposema hayo akasimama na kuanza kusogea kwenye lango la chuma.
"Hakuna ndege yoyote aliyekuwa anamchukia kunguru. Alikuwa anavutia kwa rangi yake, sauti ya kinanda na mwonekano wake wa kifalme. Kila alipokatiza ndege wote wakatua na kumtazama. Haki walimpenda! Japo baadhi walimuonea wivu.
Lakini unajua nini kilitokea kunguru akawa mweusi mpaka mdomo na miguu? Akapoteza rangi zake za thamani, sauti yake tamu na madaraka mbele ya wengine? Unajua?"
Mwanajeshi mmoja akatikisa kichwa kwa ishara. Mara akadondoka chini na kufa papo hapo. Rhoda akacheka kweli.
"Mnaona?" Akauliza. "Hakuna anayeweza kunilinda. Ninaweza kuwamaliza wote hapa pasipo kuweka kidole changu kwenye miili yenu."
Akakamata chuma za lango kwanguvu. Wanajeshi wakahofu.
"Muda wangu utakapofika, wote mtasujudia miguuni mwangu. Mtaniita mfalme mkiimba nyimbo za kunisifu. Kwa atakayekaidi, atageuka kuwa vumbi la majivu!"
Akanyamaza kidogo akiwatazama wanajeshi ambao walionyesha uso wa hofu.
"Pale jua litakapozama, gereza hili litakuwa mali yangu. Kila nafsi iliyokuwemo humu itakuwa yangu. Wekeni hili kichwani." Akarudia tena. "Pale jua likizama ... pale jua liki ZAMA... tunzeni hilo kichwani."
Akacheka tena kwanguvu akirejea pale alipokuwa ameketi awali. Akakaa kimya asiseme tena jambo lolote.
**
"Waheed!" Malkia akaita akigonga mlango wa chumba. "Waheed! Waheed!" Kimya.
Akaenda kukutana na wenzake waliokuwa wameketi sebuleni, akawaambia hamna matokeo.
"Jamani!" Akashangaa Zura. "Tokea asubuhi atakuwa amelala tu mpaka saa hii?"
"Labda anaumwa!" Akasema Fluffy. "Vipi kama tukafungua mlango kumtazama?"
"Kama yuko uchi je?" Malkia akauliza, na kuongezea: "Sidhani kama itakuwa ustaarabu."
Kukawa kimya kidogo. Walikuwa kwenye bumbuwazi. Iweje mwenyeji wao huyo asiitikie hodi zilizobishwa kwa muda wote huo tangu asubuhi?
Yupo ndani kweli? Na kama yupo, atakuwa mzima? Wakatafakari cha kufanya. Walikuwa wanataka kwenda safari lakini haikuwa kheri kwenda pasipo kuaga japokuwa walishamtanabaisha mwenyeji wao juu ya hilo.
"Ebu kajaribu tena," akashauri Seth. "Mara hii piga hodi kwanguvu zako zote!"
Malkia akaenda tena, akafanya kama alivyoagizwa. Bado hakufanikiwa. Sasa wakajawa na shaka kubwa. Hamna nyingine zaidi ya kuvunja mlango.
Alk, jitu la Azeth, likabeba jukumu hilo. Kwa mkono wake wa kuume likausukuma mlango ukajidondokea.
Kutazama kitandani, Waheed hakuwamo!
"Unaona? Hata hayupo!" Akasema Fluffy.
"Sasa tunafanyaje?" Zura akauliza. "Tutaenda hivyo hivyo?"
Seth akaguna. "Litawezekanaje hilo na huku hatumjui hata huyo mwanaume tunayeenda kumtafuta huko? Kitu pekee tunachofahamu anaishi karibu na bahari ya Mediterania, hakuna zaidi!"
Kweli. Walikuwa wanamtegemea Waheed peke yake kufanikisha hilo zoezi. Sasa ikawabidi tu waketi kumngoja.
Wakakaa mpaka majira ya jioni. Jua limelegea kwa kuishiwa nguvu. Bado Waheed hakuja. Wakakata tamaa ya safari yao. Isingewezekana tena kwenda huko kwa siku hiyo.
Lakini kabla jua halijapotea kabisa, wakamwona mtu kwa mbali akiwa juu ya farasi mweupe. Kwa mbali tu wkaamtambua mtu huyu alikuwa ni Waheed! Nywele na ndevu zake za kumwaga.
Wakasimama kumngoja, isipokuwa majeruhi Seth.
"Lakini sikumwona akitoka nyumbani leo!" Seth alistaajabu. "Tokea asubuhi ya mapema sana nilikuwapo macho. Nikasikia mtu chumbani kwake."
Ilikuwa ni ajabu. Aliondoka muda gani? Mbona hakuaga? Mbona aliondoka na alikuwa anajua taarifa za wageni wake kufunga safari kwenda kumtafuta mzee yule wa kando ya bahari?
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Waheed alikuwa anayatambua maswali haya yatakuwa yanawatatiza vichwani mwao. Alipomfungia farasi wake, akawataka waende ndani kuteta kidogo. Akawaomba radhi kwani alipata dharura. Na hakuwa na namna zaidi ya kwenda kuikabili.
Hakuwaeleza dharura hiyo ni nini, lakini alisisitizia ilikuwa ni muhimu isiyoepukika.
"Mniwie radhi sana. Nimewaangusha."
Malkia akamuuliza sasa ni lini wataenda huko walipokubaliana kwani muda waenda. Hawaweza kukaa hapo milele.
Waheed akatabasamu kwanza,
"Siku yoyote ile, hata kesho ni sawa!" Akajibu kwa kujiamini kisha akanyanyuka na kuwaaga, aelekea chumbani kupumzika kwani amechoka.
Akiwa anaelekea huko, Malkia akagundua pindo la nguo ya Waheed lilikuwa na damu. Na hata kandokando ya kiganja chake cha mkono wa kulia, kulikuwa na masalia ya damu!
Akapata wasiwasi. Ni wapi alipotoka Waheed? Akajiuliza nafsini, lakini hakuwashirikisha wenzake, akalimezea.
Aliamini kuna jambo lipo mgongoni mwa Waheed.
**
Hatimaye Jua likazama. Giza likashika amri ya uso wa dunia.
Kulikuwa ni kimya na giza. Giza na kimya kwenye ardhi ya Goshen. Kimya isipokuwa gerezani ambako kulikuwa kuna zogo na maneno ya hapa na pale, kama ujuavyo mahali ambapo watu wamekusanyika kwa pamoja.
Lakini tofauti na kwengine, kwenye chumba cha Rhoda, alipokuwa mwenyewe, kulikuwa kimya. Kimya haswa Rhoda akiwa ameketi anatazama ukuta.
Lakini kimya hiki hakikudumu kwa muda mrefu, Rhoda akasimama na kunyoosha viungo vyake kisha akawatazama walinzi.
"Muda wangu umefika!" Akasema kwa tabasamu.
Ila muda wake huu ulikuwa ni upi? Mbona mwezi ulikuwa umefichama angani na si mzima kama yeye atakavyo kila atakapo kufanya jambo, haswa kubwa!
Walinzi wakiwa wanashangaa, mara Rhoda akageuka kuwa kundi kubwa la popo likatawala gerezani na kufanya kuwa kiza totoro!
Baada ya hapo milio ya watu wakipiga yowe za kifo zikatawala. Pale popo wote walipojikusanya na kuwa mwili wa Venet, hakuna hata mtu mmoja, mwanaume kwa mwanamke aliyekuwa hai ndani ya gereza.
Wote walikuwa maiti wamelala chini!
"Naomba uende kwenu, hapa si salama kwako usiku huu!" Mfalme Phares alimwambia Tattiana. Alimsihi binti huyu tangu jioni lakini akawa mkaidi.
"Sitaenda popote, mfalme, nitakuwa mtu wa aina gani kumkimbia mwenzangu wakati wa shida?" Tattiana akajibu.
Wasiendelee kuongea, hodi ikabishwa akaingia jemedari. Alikuwa mwenye sura ya hofu. Alikuwa anahema kwanguvu na kutota jasho.
Akamwambia mfalme,
"Watu wote wameuawa gerezani, na haijulikani wapi Rhoda ameenda!"
Mfalme akashtuka kusikia habari hizo. Haraka akasogelea dirisha na kuangaza nje. Kulikuwa kimya.
Akatazama kila upande lakini hakuona kitu. Wanajeshi walitapakaa kasrini wakiwa wamebebelea silaha wamejiandaa kwa vita!
Hali ya tahadhari ikatangazwa himaya nzima, watu wakihusiwa kukaa ndani mpaka pale taarifa itakapotolewa.
Muda ukasonga. Bado hakukuwa na kitu.
Kulikuwa kimya mno kiasi cha kudhani aidha umekuwa kiziwi.
***
Baada ya muda kusonga zaidi, ndipo wanajeshi baadhi wakaleta taarifa kasrini ya kwamba Rhoda ameonekana tena kule gerezani! Alikuwa amesimama pamoja na maiti akipaza sauti kuteta lugha isiyojulikana.
Basi haraka mfalme akaagiza majemedari wamkamate mwanamke huyo na wahakikishe wanamtia nguvuni asizae shaka.
Lakini angalizo wasimuue kwani anamhitaji akiwa hai.
Wanajeshi, kwa woga wakabeba agizo hilo na kwenda eneo la tukio. Walifika na kuwakuta wenzao huko ambao hawakuwa wanajua cha kufanya zaidi ya kumtazama Rhoda akiendelea na mambo yake yasiyoeleweka.
Apiga kelele akitazama anga. Aomba na kunung'unika katikati ya maiti.
Wakafikishiwa agizo la mfalme kuwa wamkamate na si kumtazama. Kwani kuna yeyote anayejua anachokifanya?
Haraka, wakaona ni busara kutumia mshale wenye kileo na dawa. Huku Rhoda akiendelea na ibada, akaja shtuka ncha ya mshale imepenya mguuni mwake. Akalalama kwa maumivu!
Akauchomoa mshale huo na kutazama ulipotokea kwa hasira kali kiasi kwamba aliyerusha akaona kifo chaja! Mara akageuka kuwa kundi la popo wengi, lakini hakufika mbali, popo hao wakadondoka na kurejea katika mwili wa Rhoda!
Alikuwa amechoka, macho yanaona kizunguzungu, kichwa chamzunguka. Alijikongoja kumfuata adui yake aliyemrushia mshale lakini safari haikukamilika, akapoteza fahamu!
Wanajeshi wakafurahi kwa ushindi. Haraka wakamkusanya na kwenda kumtia kwenye gereza lake la pekee la shimo. Humo wakamfunika na wavu mkubwa na mzito wa chuma. Wakamiminia dawa wavu huo, na kisha wakaenda kumpasha habari mfalme.
Himaya nzima ikajawa na furaha. Sasa walikuwa salama! Lakini salama hii haikuwa salmini. Bado Venet alikuwa hai, si mfu. Na wala ule wavu mzito wa chuma hauwezi kumzuia abadani, lakini sema tu ni mpaka pale mwezi utakapochomoza na kuonekana mzima angani.
Venet alishindwa kutengeneza jeshi kwa kutumia miili ya wafungwa aliowaua kwasababu hakukuwa na mwezi mzima angani!
Alishindwa kuiweka Goshen mkononi kwasababu hakukuwa na mwezi mzima angani!
Laiti mwezi huo ungelikuwa umelitawala anga, lilikuwa ni jambo la kufumba na kufumbua macho tu, Goshen yote ingeshanyauka! Hakuna ambaye angemzuia Venet na jeshi lake.
Abadani!
**
"Sasa tunaweza tukalala," mfalme alimwambia Tattiana akitabasamu.
"Pole sana, mfalme," Tattiana akamsabahi. "Haikuwa kazi nyepesi kabisa. Haki kazi hii ni kubwa na ngumu tofauti na kila aliyepo huko nje anavyoiangazia."
Mfalme akamshukuru Tattiana kwa msaada wake na kumtia nguvu. Asingeliweza mwenyewe kabisa. Akamzawadia Tattiana kumbatio la nguvu alafu akaenda zake kuoga na kurejea kulala.
Hakuchukua muda mrefu, usingizi ukampitia. Lakini Tattiana akibakia macho kwa muda mrefu. Alikuwa anawaza mambo kadhaa, kuhusu Rhoda na kuhusu nyumbani kwao.
Akapanga kesho aende nyumbani kusalimia. Kuna mambo fulani inabidi akayafikishe huko.
Sasa alipofikia hitimisho lake hilo akajaribu kulala. Akajaribu kweli lakini akashindwa. Alikuwa anasikia baridi mno. Akanyanyuka na kwenda kufunga madirisha kisha akaenda kulala tena.
Mwishowe akaona kuna haja ya kubadili kitanda. Hakuweza kulala na mfalme. Mfalme alikuwa wa baridi, na hata sasa kitanda chake kizima.
Akatoka ndani aekelekee kwenye kile chumba chake alichokabidhiwa hapo awali. Akiwa njiani kuelekea huko akahisi kuna mtu ama watu mahali wakiteta. Akashtuka.
Alitulia na kusikiliza kidogo, akasikia kwa mbali watu wakinong'ona. Sauti yatokea upande wake wa kushoto, ambao kuna njia ya kutoka nje ukasimama kwenye kibaraza ghorofani.
Taratibu akasogea huko lakini moyo wamdunda haswa. Akashika kitasa cha mlango na kuufungua. Akamkuta Lucy, kijakazi wa kasri, akiwa amesimama mwenyewe!
"Lucy!" Akaita. "Wafanya nini huku muda huu?"
Lucy akatabasamu. "Nimepumzika tu, kipenzi cha mfalme. Sina usingizi."
Tattiana akatazama kushoto na kulia.
"Ulikuwa unaongea na nani?" Akauliza. Lucy naye akatazama kushoto na kulia kisha akapandisha mabega.
"Nilikuwa mwenyewe, hamna mtu! Hamna ninayeongea naye!"
Tattiana akamsogelea na kushika vyuma. Wote wakawa wanatazama himaya ya Goshen kwa chini.
Kulikuwa kimya kidogo upepo ukipuliza.
"Mbona upo hapa?" Lucy akamuuliza. "Umemuacha mumeo na nani?"
Tattiana akatabasamu. Naye akasema hana usingizi ndo maana alikuwa anatembea tembea. Lucy akamuuliza huwa anafanya hivyo kila siku?
"Hapana, vipi na wewe huwa unakaa hapa kila siku?"
"Hapana!"
Tattiana akaaga akaenda zake. Asingeweza kuendelea kukaa pale kwani alikuwa anasikia baridi. Akiondoka, Lucy akamtazama mwanamke huyo mpaka anaishia.
Jicho lake halikuwa la shwari. Alifunga mlango na kuendelea kukaa huko nje, na muda si mrefu sauti za kunong'ona zikarejea tena.
**
Ngo! Ngo! Ngo! Mlango wa Waheed ulilia. Mwanaume huyo akanyanyuka kitandani na kufungua dirisha kuangaza. Ilikuwa ni asubuhi iliyoanza kuonja mwanga wa jua.
Akapaza sauti yake:
"Nakuja!"
Baada ya muda mfupi akatoka ndani ya chumba chake na kwenda kukutana na Malkia na wenziwe waliokuwa wameketi sebuleni.
"Nyie huwa hamlali?" Akasema kipiga mihayo.
"Ulituambia tudamke mapema kwa ajili ya safari," Zura akakumbusha.
"Ooh! Mmejiandaa tayari, sio?"
Halikuwa swali hili hivyo hakuna aliyemjibu, basi akawaambia wanyanyuke na mara moja waendee farasi wao waondoke.
"Hujiandai?" Fluffy akamuuliza akistaajabu. Waheed akajitazama,
"Kwani kuna shida?"
Hata hakunawa uso, wakaenda na safari yao iliyodumu njiani kwa masaa. Jua likiwa limechachamaa, yani mchana sasa, ndipo wakawasili mbele ya nyumba ya mzee huyo wanayemhitaji.
Ilikuwa ni nyumba ndogo dhaifu. Mlango wake ulikuwa mbovu na madirisha madogo yaliyofunikwa pia. Usingeweza kudhani hapo anaishi mzee anayetunza siri ya kofia ya Pharaoh wa kale.
Kofia yenye mamlaka ndani yake, aghalabu na aghali mno.
Kulikuwa kimya eneo hilo. Wakabisha hodi na mara mlango ukafunguliwa na mzee mmoja aliyevalia joho la rangi ya kijivu. Akawakarimu.
"Samahani, tumemkuta mzee Desmo?" Akauliza Waheed. Mzee yule akawasihi waingie ndani, wakaketi chini na kuwaambia mzee huyo amefariki hivi jana na tayari wameshamzika.
"Asubuhi ya mapema tulimkuta akiwa amelala kitandani anavuja damu. Koo lake lilikuwa limechanwa linamimina damu nyingi hata kuongea hakuweza mpaka anakufa. Haijajulikana nani kamuua mpaka sasa, na sijui sababu gani ya kumuua mtu kama yule asiyekuwa na mali wala familia."
Habari hizo zikawadhoofisha wakina Malkia. Sasa kama mwanaume huyo waliyeambiwa wamtafute ameuawa, watafanikiwaje?
"Vipi hakumsikia mtu nyakati hizo za usiku?" Malkia akauliza. Mzee yule akatikisa kichwa,
"Mimi ni jirani yake lakini sikusikia hata kidogo. Hata mlango wake haukuwa umevunjwa ulifungwa vile vile kwa ndani. Hatujui muuaji huyu alifanyaje hili tukio, lakini ni wazi hakuwa mtu wa kawaida!"
Baada ya maelezo hayo, wakatoka ndani na kuwaendea farasi wao.
"Sasa tunafanyaje?" Akauliza Seth aliyekuwa mgongoni mwa Alk.
"Hata sijui," akajibu Malkia. Wakawafikia farasi wao na kuwakwea. Safari ya kurudi kwa Waheed ikaanza.
"Je mimo nikiwaambia namna mtasadiki?" Akauliza Waheed. Wote wakamtazama.
"Mimi ninajua njia kama ajuavyo Desmo. Najua wapi kofia hiyo ilipo ndani ya piramidi. Njia gani tupitie kuingia na njia gani tutatumia kutokea."
"Una uhakika?" Akauliza Seth.
"Asilimia zote!" Akajibu Waheed kwa kujiamini.
"Sasa mbona haukutueleza hayo mapema kwamba unayajua?" Fluffy akauliza.
Waheed akatabasamu.
"Niliona niwaache mpaka mhakiki kwa mtu mliyekua mnamwamini ninyi."
"Kwahiyi utatupeleka huko?" Akauliza Seth.
"Usijali, kama mtahutaji nitawapeleka, kwanini nisifanye hivyo?"
Kwa wakati huo wakiongea, Malkia alikuwa anatazana mikono ya Waheed. Mwanaume huyu alikuwa haogi wala hanawi. Bado mabaki yale ya damu aliyomwona nayo jana yalikuwapo.
Akamkagua na kucha zake, akaona zilivyo nyeusi lakini pia zikiwa na mabaki ya damu. Akapata maswali kichwani.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni Waheed ndiye aliyemuua Desmo. Akawaza.
Desmo aliuawa usiku.
Siku ile asubuhi ambayo walipanga kwenda kumtembelea mwanaume huyo, Waheed alitoweka na kurejea asubuhi ya mapema akiwa na mabaki ya damu.
Alitokea wapi?
Akakumbua mbali zaidi, ilikuwa ni usiku wa jama yake kabla Waheed kutoweka, ndiyo walikuwa wamepanga kwenda kwa Desmo. Je Waheed alimmaliza Desmo ili apate fursa ya kwenda nao ndani ya Piramidi?
"Waheed," Malkia akaita. "Kwanini unatusaidia? Ni nini unataka kwetu kama fadhila?"
Waheed akashangazwa na swali hilo la ghafla.
"Nawasaidia kwasababu mnahitaji msaada. Au nimekosea?" Akageuza mambo.
Malkia akamkazia macho na kumuuliza:
"Hauna mpango wowote kwenye hili? Una uhakika?"
Waheed akanyamaza kwanza akitazamana na Malkia. Mara maongezi yao yakakatwa na sauti ya Zura aliyekuwa anashangaa kwa mbali kuona kimbunga cha vumbi.
Hawakuongea tena mpaka wanawasili nyumbani. Baadae wakapata chakula na kutulia. Waheed akaanza kuwapatia maelezo juu ya kile watakachoenda kufanya kesho yake.
"Kwanza inabidi tufahamu mpaka sasa hakuna yeyote aliyewahi kufanikiwa kutoka ndani ya piramidi hilo akiwa hai. Kila anayeingia anaishia humo humo na kujiunga kwenye jeshi la wafu."
Kihistoria,
"Piramidi hilo lililaaniwa na linalindwa na roho ya Pharao mdhalimu kuwahi kutokea katika historia ya Misri. Pharao huyo akiwa na jeshi lake walikuwa ni tishio mno ndani na nje ya Misri kwa ubabe, ukatili na unyang'anyi!
Lakini habari yao ikaja kukomeshwa na mungu wa vita na bahari. Wakatupiwa ndani ya piramidi yeye na jeshi lake wasitoke humo kamwe. Wakaishi mpaka kufa.
Lakini kimwili tu, kiroho wapo hai. Mfalme huyo bado anaendelea kutawala humo ndani ya piramidi na jeshi lake likimlinda.
Kofia yake ya madaraka ipo kichwani mwa fuvu lake la kichwa, na japo kalala bado anailinda kama vile ajuaye kuwa kila mtu anaitaka kofia hiyo. Na punde atakapoipata, basi atakuwa ana madaraka makubwa sana, hata lile jeshi la wafu litamtumikia!"
Habari hizo zikawasisimua Malkia na wenzake. Ila Zura akawa na swali.
"Kwanini umeshindwa kuchukua kofia hiyo na nguvu zako zote?" Aliuliza. Waheed akatabasamu.
"Si rahisi kama udhanivyo," Akamjibu. "Ndani ya piramidi lile hakuna mlozi anayeweza kufanya ulozi wake. Kila mtu ni wa kawaida punde tu aingiapo ndani."
"Kwahiyo hata pharao mwenyewe aliyepo madarakani hajataka kwenda kuichukua kofia hiyo?" Akauliza Seth.
"Ndio," akajibu Waheed. "Hakuna anayethubutu kwenda huko, achia mbali wakisema pharaoh yule alikuwa amelaaniwa."
Akameza mate kwanza.
"Kwahiyo ile kofia ambayo anayo Pharao wa sasa si ile ya zamani japo naye amerithi. Ile imetengenezwa na masonara wa kawaida tu wakati ile ya Pharaoh aliyetupiwa ndani ya Piramid yake ikiwa imetengenezwa na miungu!" Waheed aliendelea kudadavua.
"Kwahiyo kama tukiipata kofia hiyo, utawala wa Misri utatupokonya?" Akauliza Malkia.
"Hapana, sidhani kama watafanya hivyo," akajibu Waheed. "Sema wanaweza kuwaomba ama kuingia makubaliano kwa kuwapatia kitu chenye thamani zaidi kwa mabadilishano."
"Kama kipi chenye thamani kuliko kofia hiyo?" Malkia akaendelea kuuliza. Waheed akapandisha mabega.
"Sijajua. Ila hawatakosa cha kuwavutia ili muwakabidhi kofia hiyo."
"Na kama tukikataa kuwapa?" Malkia akauliza tena.
Waheed akanyamaza kidogo akifikiria. Hakuwa na majibu kamili. Akakatisha maongezi kwa kuwasihi wapumzike kwani wametoka safari ndefu. Hivyo akamwacha Malkia na kiu ya taarifa zaidi.
Akaenda zake ndani ya chumba kujilaza. Akawaza mambo kadhaa aliyoyafanya kwa siku hiyo, lakini akawaza na lile alilolifanya usiku wa kuamkia siku hiyo.
Ulikuwa ni usiku wa aina yake kwake, usiku wa kipekee. Ndani ya usiku huo alitoka kwenye makazi yake na kisha kwenda kwa Desmo akitumia nguvu za kilozi kumtambua!
Akakumbuka namna alivyomuona mzee huyo akitoka kuvua samaki, mkononi amebebelea kikapu. Mzee huyo akazama ndani na kisha akamfuata humo na kumkaba, kumuua!
Akabeba kumbukumbu yake yote kuhusu Piramidi alafu akayeya.
Basi akajikuta anatabasamu. Alijivunia alichokitenda. Lilikuwa jambo muhimu. Sasa anamiliki kumbukumbu hiyo muhimu ambayo itamsaidia kupata kofia ya Pharao.
Kwa kuwatumia wakina Malkia, ambao aliamini wana dhamira na uwezo huo, kivipi ataikosa kofia? Hakuona namna kabisa.
Basi akatabasamu tena.
**
Usiku ni huu.
Baada ya usiku wa jana ambao ulikuwa na tafrani ndani yake, watu wakitaarifiwa wakae ndani tu, sasa usiku huu uliofuatia ulikuwa ni 'dhahabu'. Ulikuwa ni muda mwanana wa kwenda kutekeleza yale aliyoyaagiza baba.
Kila kitu kilishawekwa katika mifuko na safari ilishafungwa mpaka maeneo ya tukio. Eneo hili halikuwa mbali sana na vilabu vya pombe. Tuseme kama nusu kilomita hivi.
Mazingira yalikuwa tulivu. Haswa yalihamasisha tendo. Kwa kunong'oneza, wakiwa ubavuni mwa nyumba, Oragon akamuuliza Ottoman,
"Si ndiyo hapa?"
Ottoman akajibu kwa kutikisa kichwa. Akaongezea:
"Na kile ndo chumba chake!" Akaonyeshea dirisha.
Basi wakasonga taratibu mpaka hapo dirishani. Kulikuwa kumefungwa. Taratibu wakakazana kupafungua wapate kupenyeza dawa.
Lakini kwa mbali,
"Nani wale?" Akauliza mwanaume mmoja akimwonyeshea mwenzake kwa kidole kule walipo wakina Ottoman. Wanaume hawa wawili, walikuwa ni walevi wametokea kilabuni, sasa wanaelekea majumbani.
Ni usiku mkubwa.
"Watakuwa wezi!" Akajibu huyu mlevi wa pili. Basi wakiwa wanayumba kama jahazi baharini wakaanza kusonga kusogelea eneo la tukio, walipokaribia wakapaza sauti kuita wezi! Ottoman na Oragon wakakurupuka kwa woga.
Haraka wakakimbia kwa kasi hata walevi wale walipowakimbiza hawakufua dafu. Wakawadandia farasi zao na kutokomea haraka kuokoa roho zao.
Walevi wakarudi eneo la tukio. Wakawakuta Nebukadeza na mwanae wa kiume wakiwa nje, mikononi wamebebelea silaha.
Wakawapasha habari.
Wakaelekea kule dirishani, huko wakakuta kamfuko kadogo chini. Wakaokota na kukatazama. Nebukadeza akagundua ni sumu.
"Hawakuwa wezi, walikuwa wauaji!"
"Wanataka kutuulia nini?" Akashangaa mwanawe. Nebukadeza akawatazama walevi wale wawili na kuwauliza:
"Mliwaona watu hao?"
"Kwa mbali!" Mlevi mmoja akajibu.
"Mie nilimwona!" Mwingine akadakia akinyoosha kidole kana kwamba mwanafunzi yu darasani. "Ni watoto wa mzee Harid!"
Mwenzake akamtazama.
"Una uhakika?" Akamuuliza.
"Kwanini nisiwe nao? Unadhani nimelewa!" Akafoka mwenzake.
"Unamjua mzee yule ni mmojawapo wa wazee wa baraza?" Nebukadeza akawaambia. "Endapo mtakuwa mmesema uongo basi itawagharimu."
Mlevi aliyesema hayo akaapia akichinja shingo yake kwa kidole, nimemwona kwa macho yangu meupe hivi ... hivi!"
***
Kesho yake Nebukadeza akanyanyuka kwenda kutoa taarifa juu ya jaribio lake la kuuawa. Akamfikishia shauri hilo kamanda wa ukanda wao, na kama haitoshi kwa kuhofia ushawishi wa mzee Haridi unaweza ukaingilia kesi hiyo, akaomba akaonane na mfalme.
Kwakuwa alishawahi kufika hapo, hata walinzi hawakuwa na tabu naye, wakamhusia angoje mfalme ahabarishwe. Punde akaruhusiwa. Akaonana na mfalme aliyekuwa ameketi kwenye bustani yake pamoja na Tattiana.
Akamweleza mfalme yale yaliyotokea usiku wa jana. Habari hiyo ikamshtua mfalme.
"Una uhakika lakini?" Akauliza.
"Ni kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi," Nebukadeza akajibu.
"Lakini kwanini wajaribu kukuua?" Mfalme akauliza akitafakari. Lakini kwa muda huo Tattiana akaanza kupata picha kamili kichwani.
Baba yake Oragon na Ottoman, mzee Harid, anafanya biashara ya kuuza Cedar! Akahisi moyo umemlipuka kama bomu kwani alifahamu wazi mzee huyo atakuwa anashirikiana na baba yake, bwana Melkizedek.
Sasa watoto wa mzee huyo wanataka kumuua Nebukadeza kwakuwa alikuwa anatoa siri za biashara hiyo.
"Hiyo sumu ipo wapi?"akauliza mfalme. Nebukadeza akamwambia amemkabidhi kamanda. Haraka mfalme akaagiza sumu hiyo iletwe pale kasrini na mtaalamu pia afike hapo mara moja.
Hazikupita dakika kumi vyote alivyoagiza vikawa vimefika.
Mtaalamu akatazama na kuichambua sumu ile, kisha akampa mrejesho mfalme.
"Ndiyo ile, mfalme. Iliyomuua yule mtumishi wako!"
Mfalme akakasirika sana. Tattiana naye akajawa na jazba. Kama ndiyo ilimuua yule mtumishi wa mfalme, basi ndiyo iliyommaliza na Roboth pia!
Ina maana kifo cha Roboth kilifanywa na wakina Oragon na Ottoman! Akapasuka moyo. Kwanini wafanye hivyo? Roboth aliwakosea nini kumuua?
Akili yake nyepesi ikamwambia huo ulikuwa ni mkakati wa Mzee Harid kuhakikisha anaolewa na mfalme ili apate kudumisha uhusiano baina yake na familia yake kwa mirija ya fadhila!
Yani mdhalimu yule anadiriki kukatisha maisha ya mtu kwa lengo la fadhila!
Akajikuta anajawa na chuki. Kidonda chake kilichoanza kupoa kikaanza kuchipuka upya.
Mfalme akaagiza watumishi wake wakawamate na kuwaleta Oragon na Ottoman mbele yake haraka iwezekanavyo. Wana kesi mbili za mauaji wanatakiwa kuzitolea majibu.
***
"Tazama huko!" Akaropoka mwanajeshi mmoja yeye akienda upande wa kulia wa nyumba. Walikuwa watano kwa idadi na wote wakaizingira nyumba ya mzee Harid na kuipekua.
"Hawapo!" Akatoa ripoti mwanajeshi mmoja kumwambia mkuu wao. "Tumetazama kila sehemu, watakuwa wametoroka!"
Lakini punde,
"Mkuu, tazama hichi!" Alipayuka mwanajeshi mmoja akimsogelea mkuu wake. Mkononi alikuwa amebebelea majani.
Mkuu wao akayatazama na kisha akayanusa.
"Cedar! ... ni Cedar!"
Akaagiza msako wa kutafuta matunda hayo kila sehemu, basi msako ukarudiwa kwa mara ya pili. Kila kitu kikafunuliwa, kila sehemu pakawekwa wazi kupekuliwa.
Jikoni, wakapata baadhi ya matunda hayo ambayo waliyakusanya wapate kuyabeba kama kielelezo.
"Toa taarifa mipaka yote ifungwe, hamna mtu yoyote kutoka nje ya himaya," akaagiza mkuu wa kikosi. Basi taarifa ikatolewa kwa mlio wa pembe ambayo ilivuma ndani ya himaya nzima na hata maeneo ya karibu.
Mipaka ikafungwa.
**
"Mama!" Tattiana alipaza sauti punde alipoingia ndani ya eneo lao la nyumbani. Alikuwa anakimbia farasi kamwacha getini kwa walinzi.
"Mama!" Akaendelea kuita mpaka alipoingia ndani. Hakumkuta mtu sebuleni, na hata nyumba haikuonekana na dalili ya mtu yoyote!
Akagonga milango na kupita kila chumba. Hamna mtu. Sasa walikuwa wameenda wapi?
Akaketi sebuleni tumbo likimsokota. Jasho likimtoka.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hata hamu ya kukaa hakuwa nayo akawa ananyanyuka na kuangaza kila mara kutazama kama wazazi wake watarejea.
Haikuwa hivyo mpaka muda mrefu ulipopita, baba na mama wakaja. Sasa Tattiana akapata wasaa wa kutoa donge lake linalomsumbua kooni.
Akawaeleza ameshajua biashara wanayofanya na mzee Harid, na hivi anavyoongea tayari mfalme amewaagiza watumishi wake wakawakamate watoto wa mzee huyo baada ya kufanya jaribio la kumuua Nebukadeza!
Melkizedek akaumwa kichwa kusikia hayo. Mkewe akaumwa tumbo. Sasa ndani hakukuwa kunakalika. Wakahisi hata nao wanakuja kukamatwa.
"Sasa tunafanyaje, Melkizedek?" Mama akauliza. "Wale watoto wakikamatwa watatutaja, itakuwa ndiyo mwisho wetu gerezani!"
Hata Melkizedek alikuwa anasikia? Wala! Kichwani alikuwa anasikia sauti ya chaki mpya ikwaruayo ubao ... kriiiiiiiiii! Na kadiri mkewe alivyokuwa anapiga kelele, akahisi kuumia masikio zaidi.
"Kelele!" Akafoka akibamiza meza. Akasimama akitazama kwa hasira. Alikuwa amechanganyikiwa. Akawaita watumishi wake na kuwaagiza wafanye usafi kila eneo huko ghala, wahakikishe hakuna linalobaki!
Basi haraka agizo likatekelezeka. Melkizedek akahakikisha hakuna lililobakia, sakafu nyeupe. Akafukia na yale mabaki yote ya majani ya cedar.
Kisha sasa akaketi sebuleni. Kichwa kilikuwa chekundu. Macho yake yamefura.
"Nililikataa hili. Nilijua madhara yake. Ona sasa tumehatarisha yote!" Akalalama akishika kichwa. Majuto ni mjukuu.
Sasa kiza kilikuwa kinazidi kinaingia, Tattiana akaaga aende zake kasrini kwa mfalme akiahidi atarejea kuwapasha habari zaidi endapo akikumbana na jipya.
Akajipakia juu ya farasi na kwendaze.
Melkizedek akaendelea kuketi pale mezani kwa muda mrefu hata mke wake aende na kurudi akimkuta hapo. Alikuwa amesononeka na amejawa na woga.
Kwanza ameigharimu himaya yake ya Goshen, pili amegharimu na biashara yake aliyohangaika kuijenga maisha yake yote.
"Nisamehe mume wangu," akasema mkewe. "Nimekuwa mshauri mbaya kwako."
Melkizedek hakusema kitu, akanyanyuka na kwenda zake chumbani akimwacha mkewe hapo mezani akimtazama anaishilia.
**
Alipokaribia lango la kasri ya mfalme, akasimamisha farasi wake na kutazama. Akaona kikundi cha wanajeshi kinaingia ndani ya jengo.
Akajiuliza je wamewakamata wale vijana. Alijikuta moyo wake unakita kana kwamba yeye ndo' mzazi wa watoto hao.
Akazama ndani, kwa uoga akarusha macho. Hakumwona Oragon wala Ottoman! Angalau akahema.
"Mpenzi wangu, wapi ulienda?" Phares akauliza.
"Nilitoka kwenda nyumbani, nilikuaga," Tattiana akajitetea.
"Ooh! Nilisahau," mfalme akaweka kiganja chake kwenye paji la uso. "Nahisi mambo mengi yananichanganya.
"Vipi umewakamata?" Tattiana akauliza.
"Hapana!" Mfalme akajibu akionyesha kufadhaika. "Lakini hawana pa kwenda. Nitawakamata tu kwani mipaka imefungwa, wataenda wapi."
Tattiana akawa kimya.
"Upo sawa?" Mfalme akauliza.
"Ndio ... nipo sawa, mfalme!" Tattiana akaropoka.
"Vipi nyumbani?" Mfalme akauliza.
"Wanaendelea vizuri," Tattiana akajibu kwa uso unaomsaliti. Hakukaa sana na mfalme akaenda zake ndani akimwacha mfalme nje.
Akaketi sebuleni akishika tama. Hakuwa na raha. Unaitolea wapi na huku roho za wazazi wako zipo rehani? Akiwa hapo Lucy akaja.
"Ewe kipenzi cha mfalme, nini kinakusibu?" Akamuuliza.
Tattiana akamtazama na kumwomba ampatie faragha kwani hayupo sawa.
"Nahitaji kuwa mwenyewe kwa sasa," akasema akimtazama Lucy kwa uso wa kumaanisha.
"Sawa, malkia wangu mtarajiwa. Ila huwezi jua, pengine ningekusaidia ulipo kwama. Ujakazi wangu si ukilema."
Tattiana hakusema kitu. Akaendelea na mawazo yake kana kwamba hamna mtu. Lucy akaguna na kumshauri aende kule alipomkuta jana usiku.
"Nikiwa nimekwazika ama nina mawazo huwa narnda kule na kusimama mwenyewe. Natazama watu walivyo wengi, upepo wanipiga na jua likizama. Nikitoka hapo nakuwa na kichwa chepesi."
Lucy alipomaliza kushauri, akaenda zake akihofia kuendelea kumkera Tattiana.
Tattiana akaendelea kuwaza. Na baadae akaona atende kama vile Lucy alivyomshauri, pengine inaweza kumsaidia. Akanyanyuka na kwenda uani mwa ghorofa, akasimama na kutazama.
**
"Mkuu, una wageni toka Goshen!" Alisema jabali.
"Toka Goshen?" Akashangaa Venim. Hakutegemea kabisa kulisikia jina hilo tangu alipoachana na wakina Rhoda ambao walimsaliti.
Akiwa anakula na kunywa damu ya kondoo, akasita kwanza. Akanyanyuka upesi na kujifuta damu kwa mgongo wa kiganja. Alikuwa amevalia joho jeusi lililofubaa. Kwa mbali alikuwa amefanana na kakaye lakini ukimsogelea karibu, alikuwa ni wa tofauti.
Kwa akili yake mara moja aliposikia Goshen alimkumbuka Rhoda. Mwanamke aliyeweka naye miadi akamtekeleza. Mwanamke aliyetokea kumpenda, akamjaza mikononi mwake lakini akaponyoka.
Basi haraka, isijulikane ametembeaje, akawasili sebuleni na kuwakuta hapo wazee wawili wa baraza. Akatahamaki na kufadhaika pia.
"Mnahitaji nini hapa? Kuuawa?" Akauliza akichezea kucha zake ndefu. Alikuwa anatisha. Kama ni mwoga ungezirai kwa uwepo wake.
"Tumekuja kukuomba msaada. Tusaidie!" Akasema mzee Harid. Venim akacheka sana akiketi. Akakunja nne na kuwatazama wazee hao.
"Goshen! Goshen! Mmeniona mpumbavu sana, wa kuja na kunisaliti? Leo mnataka mwataka nini kwangu?"
Wazee wakaeleza wanaomba msaada wa kukombolewa himaya yao dhidi ya mlozi anayetaka kuibeba. Hata wakasema hawajui huko walipoondoka, maana wametoka muda mrefu, huenda ameshaiteka tayari.
Venim akastaajabu. Ni mlozi gani huyo? Wale wazee wakamweleza hata hawamjui jinale lakini amekalia mwili wa mwana Goshen, hivyo anaweza kutoka na kuingia ndani ya Tanashe.
Ni hatari, amefanya himaya nzima ishikwe na taharuki.
Haraka Venim kusikia maelezo hayo, akahisi jambo, haraka akaendea kioo chake na kutazama. Akamwona kaka yake akiwa ndani ya shimo pamoja na mwili wa Rhoda. Akawaonyeshea wale wazee.
"Ndiye huyu?"
"Naam, huyo ndiye. Amezama ndani ya mwanamke huyo aliyemlaza kando"
Venim akamwonea huruma sana Rhoda. Kumbe ndiye amekuwa nguo ya kaka yake, Venet! Lakini zaidi akajionea huruma mwenyewe kwani kama kaka yake ametoka, basi atakuja kummaliza.
Ana kisasi naye cha damu.
Akashusha pumzi ndefu. Akawaomba wazee wampatie muda kwanza wa kuwa mwenyewe apate kufikiria.
Akawaza sana nini afanye, je arekebishe makosa yake ya awali kwa kumsaidia Venet ama amsaidie Rhoda, mwanamke anayempenda, na kwa wakati huo akijiweka salama dhidi ya kaka yake anayetaka kumuua?
Kichwa kikamuua kwa mawazo. Na anapokuwa na mawazo hunywa damu kwa wingi. Akanywa karibia ndoo nzima asiridhike!
Akiwa anawaza hivyo, mzee wa pili wa Goshen akamfuata huko uani na kumshtua akihitaji jibu. Venim kwa hasira akamkaba mzee huyo na kumining'iniza kama unyoya!
"Sikuwaambia mnipatie muda?" Akafoka. Akaminya koo la mzee huyo nusura amuue, kisha akamtupia nje!
Kwa usiku huo mzima akakesha akiwaza, kesho yake asubuhi akaonana na wazee wa Goshen apate kuwaambia alichoamua.
Mkononi alikuwa amebebelea kikombe kikubwa cha chuma kilichojaa damu. Macho yake yalikuwa mekundu na mwili wake ukifunikwa na joho rangi ya zambarau iliyokoza.
"Nimeamua kuwasaidia," akasema akiweka kituo. Wazee wakafurahi.
"Lakini kwa sharti moja," Venim akaongezea. "Kwa sharti moja tu."
"Lipi hilo?" Akauliza mzee Harid.
"Nitakapomtoa huyo mlozi nje ya mwili wa huyo mwanamke, basi huyo mwanamke atakuwa wangu. Nitaondoka naye."
Hapa wazee wakatazamana. Wakakabwa na kigugumizi. Lakini laiti wangejua hata Venim naye alikuwa anataka kumrejesha Venet ndani ya Tanashe kwa hali na mali kwasababu ya usalama wake, basi wangeweza kumtikisa kiberiti.
Lakini hawakuwa wanafahamu. Na kiu yao ya kuikomboa Goshen ilikuwa kubwa kuliko kumpata Rhoda, basi wakakubali.
"Mnaweza mkaenda!" Venim akawaambia.
"Sio twende wote?" Mzee Harid akatahamaki. "Huoni tunahitaji kwenda huko upesi?"
"Hamna haja hiyo," Venim akawatoa hofu. "Venet alizaliwa kipindi mwezi unapevuka, ni mlozi anayebadilika kuwa popo na nguvu zake zote huchepuka pindi mwezi unapokuwa kamili. Pale mezi unapoonekana mzima angani, hakuna mlozi yeyote anayeweza kupambana naye, si ardhini wala baharini."
Akakaa kimya kidogo kisha akaendelea kunena:
"Itachukua siku nne mpaka mwezi upevuke kuwa kamili. Kwa siku zote hizo hatafanya jambo, lakini mwezi utakapowaka, atawafufua watu wake wote aliowaua na kuwageuza popo. Wote watakuwa jeshi lake na atakuwa ana uwezo wa kuimeza himaya yoyote ile mbele yake."
"Sasa wewe utakuja muda gani?" Akauliza mzee Harid.
"Pale nitakapoona ni muda huo," Akajibu Venim. "Sitabisha hodi, wala hamtajua saa, mtanikuta ndani ya himaya yenu. Mkampe taarifa hizo mfalme wenu.
Nitamsaidia, lakini namtaka Rhoda."
Baada ya jibu hilo sasa hakukuwa na la kungoja. Japo walikuwa wamechoka, walianza safari ya kurudi nyumbani kurudisha jibu ya kazi waliyotumwa.
Hawakupata hata muda wa kupumzika, ukizingatia nao uzee nao ulikuwa umeshashika mwili.
Lakini laiti mzee Harid angelitambua kuwa huko anapoelekea pameshachafuka. Angeomba hifadhi himaya zingine. Wanawe walikuwa wamegeuka digidigi wakihaha huku na kule kukwepa mkono wa dola.
Mambo hayakuwa mambo kabisa. Palikuwa hapakaliki, hapalaliki, hapaliki wala hapanyweki! Hapakuwa sehemu ya kwenda kabisa.
Kwa akili yake ya kibinadamu hakujua yaliyo mbele yake, na ndani ya upeo wake alikuwa anadhani sasa baada ya ngurumo na tafrani za hapa na pale, sasa hali ilikuwa inaelekea kuwa shwari.
Huku wameshapata msaada toka kwa Venim, kule nyumbani ameshaacha maagizo ya kuuawa kwa Nebukadeza. Alijiona shujaa. Na muda mwingine alikuwa anatabasamu mwenyewe kama mwehu akipigia pia mahesabu kwamba mfalme hatowaacha patupu kwa kazi waliyofanya.
Alishapanga kwenda kutia chumvi zoezi hilo ionekane kwamba wamepitia magumu mno mpaka kufanikisha. Na kuhakikisha hilo linatimia, akampanga na mzee mwenzake.
"Utaniacha mimi niongee na mfalme, sawa?"
Lakini mwenzake huyu hakutaka kushiriki kwenye udhalimu wake, akasema ataenenda katika njia ya haki. Haoni haja ya kudanganya.
"Unataka fadhila hata katika hili la kukomboa ardhi yetu mama?"
"Mshenzi!" Mzee Harid akamlaani. "Hiyo ardhi yako mama inakupa mchanga ule? Mbona akili yako imelala kiasi hiki?"
"Hata iweje, sitashiriki kwenye huo upuuzi wako!" Mwenzake akagoma. "Ukisema uongo mimi nitaweka bayana kila ndimi yako."
Basi Harid akapandikiza chuki. Akamtazama mwenzake kwa jicho la ukali. Walipokaribia korongoni akachomoa kisu chake kirefu, na kabla hajamkita mwenziwe, akapiga makelele ya kumwita msaliti wa taifa kisha akamshindilia kisu tumboni mara mbili!
Upesi wanajeshi wakaja kutazama ndani ya kitoroli cha farasi. Majeruhi alikuwa amelowa damu anagugumia kwa maumivu, hawezi hata kuongea. Hawezi kujitetea.
Mzee Harid, akiwa amekunja sura, akaendelea kumwita msaliti mpaka mzee huyo anaondokewa na roho yake akimnyooshea kidole Harid.
"Ni msaliti huyu!" Akaropoka Harid. "Anataka kwenda kumlaghai mfalme ampatie robo ya ufalme wake!" Akashutumu. "Watu hawa si wa kukaa hai bali kuuawa!"
Wanajeshi wakaubeba mwili wa marehemu na kuutupia makorongoni uliwe na ndege. Sasa Harid akawa peke yake ndani ya kitoroli cha farasi.
Kama vile alivyotaka kuwa mwenyewe kwenye mpango huo. Basi akatabasamu. Basi akatabasamu.
Mambo yalikuwa bambam!
Akipanga namna ya kumuingilia mfalme na kupata 'mafao' ya kazi yake.
"Huwezi kumtembeza mzee maili kwa maili bure!" Alijisemea kama mwehu.
**
"Tupite njia hii!" Waheed alielekeza. Walikuwa wameshalifikia piramidi wanalotakiwa kuingia na sasa wakiangazia njia ya kuzama humo ndani.
Kulikuwa na takribani njia nne, lakini kati ya hizo, njia tatu zilikuwa za kukuongoza kifoni moja kwa moja. Na moja tu ikiwa ndo njia angalau yenye 'usalama'. Uchaguzi ulikuwa unaanzia hapa.
Wakalizunguka piramidi na kudaka njia waliyoelekezwa. Mikononi walikuwa wamebebelea maginga ya moto lakini bado hayajawashwa. Kila mmoja alikuwa nalo kwenye mkono wake wa kuume, hata Seth aliyekuwa mgongoni mwa Alk - jitu la Azeth.
"Linaonekana ni dogo kwa kulizunguka lakini kwa ndani ni kubwa mno," Waheed akatoa maelezo. "Kulimaliza ni safari ya siku tatu na humo ndani tutakutana na mitihani kadha wa kadha lakini angalizo, hakuna kuitana majina ndani ya piramidi. Na endapo mwenzako akifa, hata utakapomuona tena kwa mara nyingine kumbuka huyo si mwenzako tena, bali adui.
Akifanikiwa kukulaghai, basi ni wewe ndiye utakayekufa na kwenda kuungana na jeshi la wafu alfu mbili wanaolinda kofia ya Pharao."
Wakazama ndani.
Lakini kumbe kuna wanajeshi ambao waliwaona wakina Malkia wakidumbukia humo. Wanajeshi hawa walikuwa watano kwa idadi. Ni wale wale ambao walikuwa wanataka kuwakamata wakina Malkia ufukweni kabla ya kuja kuokolewa na Waheed.
"Mkuu, tuwafuate?" Akauliza mwanajeshi mmoja. Mkuu akamtazama na kumtusi,
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Lini uliona wanaongia mule wakatoka hai? Kama umechoka pumzi nawe waweza kwenda kama mawaheed wale!" Mkuu alifoka kisha kukawa kimya kwa mbali wakiendelea kutazama wakina Malkia wakiyoyoma ndani ya piramidi na maginga yao ya moto waliyoyawasha.
Mkuu akajikuta anatabasamu.
"Kumbe ndiyo maana Waheed aliwakomboa watu wale?" Akauliza kwa kebehi. "Si mbaya Misri ikampoteza mjinga mmoja himayani!"
Wakacheka kuumiza mbavu zao.
***
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment