Search This Blog

NILIVYOKUTANA NA MZIMU FACEBOOK -1

 




IMEANDIKWA NA : JUMA HIZA



*********************************************************************************



Simulizi : Nilivyokutana Na Mzimu Facebook

Sehemu Ya Kwanza (1)





Ninapouangalia mtandao huu wa kijamii wa facebook huwa ninajihisi kusisimka mwili. Wakati mwingine nikisikia au kuona kuwa kuna marafiki ambao wamekutana facebook na urafiki wao kudumu mpaka kufikia hatua ya kufanya mambo ya kimaendeleo, kiukweli siamini hata kidogo, nahisi kama ni utani na kwamba hakuna ukweli katika hilo.

Hii inatokana na mkasa ambao umewahi kunikuta katika maisha yangu. Kimsingi nimewahi kukumbwa na mikasa mingi maishani ambayo kwa namna moja ama nyingine ninaweza kuisahau lakini mkasa huu wa kukutana na mzimu facebook kiukweli ni mkasa ambao nimeshindwa kabisa kuufuta kichwani mwangu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Ninajitahidi kusahau kila kitu na kutokukumbuka yaliyotokea lakini ninapopata nafasi ya kukaa peke yangu na kutafakari baadhi ya mambo mawili matatu hususani ya maisha yangu nashangaa kuona nikijiwa na kumbukumbu za matukio yote yaliyotokea ambayo yananifanya nisisimkwe mwili kila ninapouona mtandao huu wa kijamii wa facebook.

Kwa jina ninaitwa Abdul Mohamed, nimezaliwa miaka ishirini na tano iliyopita katika kijiji cha Makanya kilichopo wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro. Mimi ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia yenye watoto watatu ya mzee Mohamed na mkewe Bi. Nanzighe.

Nakumbuka baada ya kumaliza darasa la saba ambapo nilifaulu vizuri na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, mjomba wangu aliyejulikana kwa jina la Machepele aliamua kunichukua kutoka kijijini huko na kunileta jijini Daresalaam ambapo alikuwa akiishi mtaa wa Toangoma uliyokuwepo wilaya ya Temeke.

Lengo kubwa la mjomba wangu kunichukua na kuanza kuishi naye lilikuwa ni kwa ajili ya kunisomesha kwani aliamini kama ningeendelea kusoma sekondari kijijini humo kamwe nisingeweza kufanikiwa na kuzitimiza ndoto zangu kielimu. Hii aliamini baada ya kuona kaka zangu walionitangulia, Isa na Hamis ambao wao waliamua kuacha shule na kuanza kuchimba mawe, Changoko kwa lengo la kujipatia pesa kwani hali ya kimaisha nyumbani haikuwa nzuri, tuliishi maisha yaliyojaa dhiki kubwa.

Hatimaye nilianza kuishi maisha mapya jijini Daresalaam huku kila kitu kikionekana kuwa kigeni machoni mwangu kwani hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika katika jiji hilo ambalo kiukweli niliishia kuliona kwenye filamu za kibongo na wakati mwingine kusimuliwa stori mbalimbali zilizohusu jiji hilo na vioja vyake.

Kama nilivyoahidiwa na mjomba kunisomesha ndivyo ambavyo alifanya kwa vitendo, hakutaka kwenda kinyume na ahadi yake.

Alinipeleka shule ambapo nilisoma shule ya sekondari ya Pius kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne, matokeo yalipotoka sikufanikiwa kuchaguliwa kuendelea na kidato cha tano na sita hivyo niliamua kujiunga na chuo cha Tanzania Institute Of Accountany (TIA) ambapo nilisomea uhasibu kwa ngazi ya cheti na baadae kujiunga na diploma.

Katika kipindi ambapo nilijiunga na chuo hiko na kufanikiwa kuanza kusoma, nilionekana kuwa kijana mpole sana na msikivu mno. Nadhani hii ni kutokana na hulka yangu niliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Naweza kusema kwamba sikuwa kijana mwenye makuu hata kidogo na tabia hii ndiyo iliyosababisha mpaka nikatokea kupendwa na baadhi wa wanachuo wenzangu. Walivutiwa na upole niliokuwa nao kiasi kwamba kilifikia kipindi wakaamua kuniita jina la utani la Mr. Mpole.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu ya chuo kuwahi kuishi kwa mara ya kwanza. Hakika nilijisikia furaha sana moyoni mwangu, kila kitu kilionekana kuwa faraja maishani na ni hapa ambapo nilizidisha juhudi katika masomo yangu huku miaka kadhaa ijayo nikiwa najiona kuwa mhasibu mkubwa katika benki kuu ya Tanzania (B.O.T).

***

“Mambo Abdul,” ilikuwa ni sauti nyororo ya msichana mmoja mrembo aliyejulikana kwa jina la Farida. Huyu nilikuwa nikisoma naye.

“Poa tu Farida sijui wewe,” nilimjibu huku nikimtazama usoni kwa macho yaliyogubikwa na aibu tele.

“Safi,” aliniambia kisha hakutaka mazungumzo yaishia hapo tu, alichoamua kukifanya ni kuanza kupiga stori na mimi. Tulizungumza mambo mengi sana mpaka kufikia muda ambao aliniuliza kwamba nilikuwa natumia jina gani facebook ili akanitafute.

“Facebook?” nilimuuliza huku nikionyesha kushtuka. Kwa jinsi nilivyokuwa nikionekana muda huo nilionyesha dhahiri kwamba sikufahamu kitu chochote kuhusu mtandao huo kwanza ilikuwa ni taarifa ngeni kwangu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Ndiyo ina maana huna akaunti?” aliniuliza Farida huku akinitazama usoni.

“Hapana sina akaunti. Kwani hiyo facebook ipoje?” nilimjibu huku nikitaka ufafanuzi juu ya mtandao huo wa facebook ambao ulionekana kuwa mtandao mpya masikioni mwangu. Sikuwahi kuusikia mahali popote pale hapo kabla.

Baada ya kupita sekunde kadhaa ndipo hapo ambapo Farida alianza kunielezea jinsi mtandao wa facebook ulivyokuwa. Aliniambia kwamba facebook ulikuwa ni mtandao wa kijamii ambao unawaruhusu watumiaji wake kuchapisha na kutumiana taarifa kwa njia ya maandishi, picha au video lakini pia unaweza kutafuta marafiki wanaotumia kokote kule duniani kwa ajili ya kubadilishana nao mawazo juu ya maswala mbalimbali pamoja na mambo mengine mengi ambayo ningeweza kuyafanya endapo kama ningefungua akaunti na kuwa miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo.

Mpaka kufikia hapo nilihisi kuchanganyikiwa, Farida aliendelea kunisifia mambo mengi juu ya mtandao wa facebook kiasi kwamba nilijikuta nikitamani na mimi kuwa miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo.

***

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya jumamosi, majira ya usiku kama saa tatu hivi. Nilikuwa chumbani kwangu, akili yangu ilichanganyikiwa baada ya Farida kuniambia mambo mengi kuhusu mtandao wa facebook. Nilichokifanya muda huo nilichukua simu yangu ya kupangusa kisha nikawasha data, kwa kuwa nilikuwa mzuri kwenye upande wa kuielewa lugha ya kingereza hivyo nikaingia facebook na kuanza kufuata maelekezo mwenyewe jinsi ya kusajili akaunti.

Baada ya dakika kadhaa kupita nikawa tayari nimeshafungua akaunti yangu facebook na kitu cha kwanza ambacho kiliniletea muda huo ilikuwa ni kuwaAdd marafiki.

Nakumbuka mtu wa kwanza kabisa kumuomba urafiki alikuwa ni Wema Sepetu kisha kufuatiwa na msichana mmoja mrembo ambaye alikuwa akijiita Princess Naah. Baada ya hapo kazi ilikuwa ni kuendelea kuwaomba urafiki wasichana warembo ambao nilikutana nao humo facebook.

Hapa niseme tu ukweli kwamba akaunti yangu ya facebook iliongoza kuwa na marafiki wengi wa kike kwa sababu nilihitaji kuwa na urafiki nao. Kila picha ya msichana mrembo ambaye nilikutana naye facebook na kumuangalia kama hakuwa rafiki yangu basi hapo hapo nilimuomba urafiki. Hiyo ndiyo ilikuwa kazi yangu kubwa baada ya kujiunga na facebook.

Baada ya kupita wiki moja nilitumiwa ujumbe facebook na msichana mmoja ambaye alikuwa akiitwa Farhia. Huyu alikuwa ni msichana mrembo mno, picha zake alizokuwa amezipost katika akaunti yake, zilitokea kunichanganya kiasi kwamba nilipouona ujumbe wake aliyonitumia ulizidi kunivuruga akili yangu. Nilirudia kuusoma ujumbe huo mara mbilimbili huku nisiamini kama msichana huyo ndiye ambaye alidiriki kunitumia ujumbe mtu kama mimi. Hata hivyo sikutakiwa kuzubaa hata kidogo, niliamua kumjibu na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa chatting zetu.





Farhia: Mambo Abdul.

Mimi: Poa tu Farhia sijui wewe, u mzima?

Farhia: Yap…wa afya kabisa hofu kwako tu mkaka.

Mimi: Niko poa sana Farhia.

Farhia: Uko wapi?

Mimi: Nipo Dar, wewe je?

Farhia: Mimi nipo Zanzibar my.

Mimi: Oh! Karibu sana Dar.

Farhia: Ahsante my na wewe karibu pia kwetu.

Mimi: Ahsante sana, usijali siku moja nitakaribia huko naamini utakuwa mwenyeji wangu.

Farhia: Okay! Nilikuwa nakusalimia tu my, asante kwa muda wako na nikutakie siku njema.

Mimi: Na kwako pia Farhia.

Farhia: Ahsante.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mpaka kufikia hapo sikuamini hata kidogo, nilihisi kama nipo ndotoni. Nilipomaliza kuchati naye nilirudia tena kuingia kwenye akaunti yake na kuanza kuziangalia picha zake.

Kiukweli bado sikuamini kama msichana huyo mrembo mwenye asili ya kihindi kwamba ndiye nilikuwa nikichati naye muda huo. Kuna mambo ambayo nilitakiwa kuyaamini katika maisha yangu lakini sio jambo hilo la kuchati na msichana mrembo kama alivyokuwa Farhia katika kipindi hicho.

Sijui nianzie wapi kumsifia msichana huyu ili unielewe kwamba alikuwa ni mrembo kiasi gani, kwa kumwangalia alikuwa na sura yenye mvuto mno, mpole aliyejawa na usikivu wa hali ya juu. Nilitamani muda wote kumwangalia na ni hapa ambapo niliamua kuzipakuwa baadhi ya picha zake na kuzihifadhi kwenye simu yangu kama kumbukumbuku.

Labda nikwambie kitu kimoja kuwa huo haukuwa ndiyo mwisho wangu wa kuchati na Farhia facebook isipokuwa ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuendelea kuchati naye huku tukizidi kuzoeana taratibu taratibu.

Baada ya kupita siku kadhaa tangu nilipofahamiana na Farhia facebook na kuanza kuchati naye, nilijikuta nikianza kumpenda na kuhitaji kuwa naye kimapenzi.

Nilishindwa kumwambia ukweli wa hisia zangu hizo kwa sababu ya kuhofia uzuri wake, niliamini fika kuwa ni lazima alikuwa na mwanaume ambaye ndiye aliyemuhudumia kwa kila kitu hivyo hata kama ningemweleza ukweli kwamba nilimpenda asingeweza kunikubali na badala yake tungegeuka kuwa maadui.

Siku ziliendelea kukatika, maisha ya chuo nayo yaliendelea kusonga mbele kama kawaida. Kuna kipindi kilifika nilishindwa kabisa kujizuia kuona nikiendelea kuchati na Farhia pasipo kumwambia ukweli wa moyo wangu. Ni hapa ambapo nilijikaza kisabuni na kuamua kumwambia ukweli kwamba nilikuwa nikimpenda na kumuhitaji zaidi ya kitu kingine chochote katika maisha yangu.

Farhia: Abdul.

Mimi: Naam.

Farhia. Kwanini mimi na asiwe mwingine?

Mimi: Kwa sababu unastahili. Farhia mapenzi ni hisia za ajabu mno, hazitarajiwi, huja ghafla! kiukweli sijawahi kukuona wala kuisikia sauti yako lakini nimejikuta nakupenda. Sijui utanifikiriaje ila nimeamua kukwambia ukweli ili ujue ni kwa jinsi gani ninavyokupenda.

Farhia: Mmh!

Mimi: Mbona umeguna?

Farhia: Umenishangaza ujue.

Mimi: Nimekushangaza na nini tena my?

Farhia: Kwahiyo umependa picha zangu na sio umempenda Farhia….right?

Mimi: Hapana, nimekupenda wewe.

Farhia: Nyie wanaume ni waongo sana.

Mimi: Naomba uniamini Farhia, mimi nipo tofauti na hao wanaume wengine unaowazungumzia, ninajiheshimu na nina mapenzi ya dhati.

Farhia: Kweli au unanidanganya?

Mimi: Kweli naomba uniamini wala sioni sababu ya kukudanganya.

Farhia: Mmh!

Mimi: Pleasee… naomba unielewe.

Farhia: Naomba nipe muda nifikirie kwanza.

Mimi: Mpaka lini jamaniii?

Farhia: Nitakwambia wewe usijali ila niache nifikirie kwanza.

Mimi: Sawa ila nategemea jibu zuri litakalo upoza moyo wangu, nakupenda sana Farhia.

Farhia: Usijali Abdul.

Hakukuwa kuna jibu ambalo nilikuwa nasubiria kwa hamu zote kama jibu la Farhia. Kila siku nilikuwa nikiingia Facebook na kuangalia kama msichana huyo alinitumia ujumbe wowote lakini sikukutana ujumbe huo. Hilo likanifanya nihisi kama msichana huyo alikasirika na kwamba hakutaka tena mazoea na mimi kwa sababu tu nilimtongoza.

Haikuwa siku ya kwanza, ya pili wala ya tatu. Farhia aliendelea kukaa kimya bila kunitumia ujumbe wowote. Ni hapa ambapo uvumilivu ulinishinda, nikaamua kumtumia ujumbe, nikaamuliza kama nilimkosea na hakupenda maneno ambayo nilimwambia lakini kitu cha ajabu ni kwamba aliendelea kukaa kimya. Hakunijibu chochote kitu ambacho kiliniweka kwenye wakati mgumu wenye mawazo, ukizingatia kwamba mpaka kufikia kipindi hicho sikuwa nina namba yake ya simu hata pale nilipoamua kuingia kwenye akaunti yake kuangalia kama aliweka namba za simu lakini sikukuta kitu.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Hilo lilinifanya nizidi kunyong’onyea na kuamini kwamba nilimpoteza msichana huyo. Wakati mwingine nilikuwa nikijilaumu kwa maamuzi ambayo niliamua kuyachukua ya ghafla! hata kama nilitokea kumpenda vipi sikutakiwa kukurupuka kumweleza haraka kiasi hicho.

Baada ya kupita wiki moja huku nikionekana kuanza kumsahau Farhia ambaye aliamua kunikalia kimya na hakutaka kabisa kunijibu kitu chochote.

Nakumbuka siku hiyo majira ya usiku nilipokuwa kitandani nikitafuta usingizi, sikuwa na lepe hata moja la usingizi. Nilichoamua kukifanya muda huo nilichukua simu yangu na kuingia facebook kuperuzi.

Hamad!

Nikakutana na ujumbe ambao alinitumia Farhia. Kwanza sikutaka kuamini, nilihisi kama maruweruwe. Haraka sana nikaufungua ujumbe huo na kudhani kwamba kama ningechelewa basi ungefutika. Alikuwa ameniandikia ujumbe wa kuniita kama ilivyokuwa kawaida yake, nilipomwangalia muda huo alionekana kuwa Online, sikutaka kupoteza muda, haraka sana nikamjibu ujumbe huo na ni kama vile alikuwa akinisubiria kwani nilipomjibu hapohapo nikamuona akiandika na kunijibu. Basi tukaanza kuchati usiku huo.

Mimi: Niambie my.

Farhia: Safi za masiku tele?

Mimi: Nzuri tu, si wewe hutaki kunijibu meseji zangu?

Farhia: Hapana sio kama nilikuwa sitaki kukujibu.

Mimi: Ila?

Farhia: Kuna matatizo yalinitokea.

Mimi: Matatizo gani?

Farhia: Usijali lakini nipo salama.

Mimi: Kweli?

Farhia: Yeah…siwezi kukudanganya.

Mimi: Sawa...yaani nimekaa kusubiria jibu langu mpaka nikakata tamaa.

Farhia: Hapana Abdul usiseme hivyo ila kuna kitu kinanisumbua moyoni mwangu.

Mimi: Kitu gani tena?

Farhia: Niambie ukweli kwanza.

Mimi: Ukweli gani nikwambie?

Farhia: Unanipenda kweli?

Mimi: Ndiyo ninakupenda sana Farhia.

Farhia: Na upo tayari kukubali kufanya kile ambacho nitakwambia?

Mimi: Yeah…nitakubali kukifanya ili ujue ni kwa jinsi gani ninavyokupenda na kukuhitaji.

Farhia: Okay! Nimekukubalia ombi lako lakini kuna kitu kimoja nitataka ukizingatie.

Mimi: Kitu gani hicho…niambie.

Farhia: Abdul.

Mimi: Naam.

Farhia: Kama umeamua kunipenda tafadhali ninaomba unipende mimi tu, sitaki unichanganye na wanawake wengine, ukifanya hivyo utakuwa umenikosea sana na sitaweza kukusamehe.

Mimi: Farhia mpenzi, kuhusu hilo ondoa shaka kabisa, nakuahidi kukulinda na kukuheshimu. Nimefurahi kwa kunikubalia ombi langu, nakupenda sana.

Farhia: Nakupenda pia, tafadhali naomba usiniumize Abdul.

Mimi: Siwezi kukuumiza Farhia, naomba uniamini.

Farhia: Nakuamini.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Nilipomaliza kuchati na Farhia, sikutaka kuamini. Nilihisi kuchanganyikiwa. Muda huo nilikuwa nimelala kitandani lakini kutokana na furaha ambayo nilikuwa nayo nilijikuta nikiinuka na kuanza kuzunguka mule chumbani kama mwendawazimu.

Kitendo cha Farhia kunikubalia na kuwa wapenzi kilimaanisha kwamba huo ndiyo ungekuwa mwanzo wa kwenda kuwatambia marafiki zangu, Deo Massawe na Nickson Govinji ambao siku zote chuoni hapo walikuwa wakinitambia kwa kutembea na mademu wazuri.

Nilikuwa mwenye furaha mno, wakati mwingine nilitamani papambazuke mapema ili kesho yake niende chuo kuwatambia washikaji.





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog