Search This Blog

MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN - 2

 






Simulizi : Mkufu Wa Malkia Wa Gosheni

Sehemu Ya Pili (2)







Bado jua halikuwa limezama.



Rhoda, baada ya kumaliza kazi zake za kukokotoa mahesabu ya chakula, alikuwa amesimama kwenye dirisha la chumba kidogo kilichopo kwenye sakafu ya juu pa mahala pake pa kazi. akiwepo kwenye kaghorofa hako, alipata kutazama madhari kiasi ya tawala ya Goshen, lakini akili yake haikuwepo pale, macho yake yalisema.



Alikuwa anamuwaza Phares, ndio. Akili yake tokea jana inasumbuka kuchambua maneno aliyopewa na Phares kumhusu malkia Vedas. kwa namna kubwa sana anahofia aidha Phares anajua lengo na dhamira yake iliyopo kichwani juu ya malkia, ila kivipi? Na yeye je, Phares, yupo upande gani?



“Anaweza akanisaidia?” alijiuliza. “Hilo ni wazo la kijinga kabisa,” akajipinga.



“Inawezekana akawa ananichunguza. Inawezekana akawa ananivutia kwenye mdomo wa mamba.” Kichwa chake kilikosa majibu na nafsi yake ilijawa na kiu kubwa, lakini pia na uoga ndani yake. Kuna muda alijikuta anatetemeka kabisa.



Baada ya kufikiria kwa kina, aliamua jambo. Alikwapua koti lake alilokuwa amelitundika kando, akalivaa na kushuka chini. Aliaga wafanyakazi wake akaondoka. Alikwea farasi akaelekea upande ilipo kasri ya malkia. Muda mfupi tu akawa karibu na eneo hilo. Hakuingia ndani, lah! Aliangaza macho yake akamwita mlinzi mmojawapo.



Aliongea naye kwa sauti ya chini kisha akampatia kiasi fulani cha fedha, mlinzi akaondoka, ila Rhoda akabakia. Mara hii alisogea mbali kidogo na kasri, akajifichaficha.



Dakika tano mbele yake, ndani ya kasri, anatoka mlinzi mwingine mrefu mwenye mwili mpana. Kichwani amevaa kofia ngumu na uso wake umejawa na ndevu nyingi. Anatazama huku na kule, anamuona Rhoda. Taratibu anasogea.



“Nina kazi nataka kukupa,” Rhoda alisema baada tu ya kujuliana hali. Mwanaume yule mlinzi alikuwa anamtazama kwa umakini akimskiza.



“Najua hautoniangusha na nakuahidi kukupa pesa nzuri sana.” Rhoda kabla ya kuendelea, alitazama kwanza usalama. “Kuna taarifa nataka toka kwa malkia na yule bwana ‘ake. Nataka kujua vyote wanavyovifanya, kujadili na kupanga. Najua wewe huwa unaongozana nao mara kadhaa, unaweza kuifanya?”



“Ndio,” alisema mwanaume yule jabali kwa sauti yake nzito. Hakuonekana kama mtu wa kufikiria mara mbili. Rhoda alitoa kiasi fulani cha pesa akamkabidhi.



“Kadiri utakavyokuwa unaniletea habari, nitapandisha pesa.” Mwanaume yule alitabasamu pasipo kusema jambo, akaondoka kurudi kasrini. Rhoda alimsindikiza na macho yake mpaka anatokomea, kisha akakwea farasi wake na kuondoka.

Wakati anaondoka, akiwa mbali, Phares aliyekuwa kwenye ghorofa ya juu alimwona mwanamke huyo aliyekuwa anapepea juu ya farasi. Bahati nzuri hakujua ni wapi ametokea, ila alijikuta anapata shaka na haja ya kujua.

.

.



Alitazama mpaka Rhoda anaishia ndipo akafunga pazia la dirisha.

.

.

.

.

.

.

.

*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

.



Phares alielekea sebuleni alipoketi na kukunja miguu yake kutengeza nne. Baada ya muda mfupi kijakazi akafika kumuuliza hitaji lake, akaagiza kahawa nyeusi.

.

.

Mwanaume huyu alikuwa amevaa koti la bluu lenye fito za rangi ya dhahabu mikononi. Suruali yake pia, iliyomkaa vema, ilikuwa ni ya rangi ya bluu na chini kwenye enka ilijazwa pia michirizi ya rangi ya dhahabu. Chini kabisa kulikuwa kuna kiatu cheusi cha ngozi kilichofungwa barabara! Alinawiri na ni wazi alikuwa na mtoko.

.

.

Baada ya kahawa kuletwa, alikunywa mafundo mawili tu akashindwa kuendelea. Alimkabidhi kijakazi kikombe cha kahawa akishukuru.

.

. “Tokea nimekunywa kahawa ya yule mwanamke, bado haijatoka kabisa gegoni,” alijisema akirejelea kahawa ya mgahawa wa Rhoda. .

.

Alinyanyuka upesi akajinyoosha mwili.

“Labda nahitaji kwenda tena kuionja.” Alitazama jua kwa kupitia dirishani akaliona karibia kuzama.

.

.

“Bahati mbaya muda haupo upande wangu,” alilaani kisha akasonya. Alielekea bandani kumtwaa farasi wake kisha akiongozana na walinzi watatu, akatoka ndani ya eneo la kasri kuelekea mpakani.

.

.

Alimwacha malkia Vedas akiwa amelala hoi bin taaban baada ya kupeana raha za kitandani. Hakumuaga, ingawa alijua wazi hilo jambo litakuja kuzua ugomvi hapo mbeleni, hakujali. Kuna mambo aliona hayana haja kumshirikisha ya malkia. Kuna mambo aliamini anaweza kuyakabili yeye mwenyewe pasipo kusumbuka na mwanamke huyo.



Baada ya mwendo wa robo saa, sasa giza likiwa limeingia, Phares alifika kwenye kambi ya wanajeshi iliyowekwa mpakani kwa ajili ya kujilinda dhidi ya uvamizi wa jeshi la Jayit.

.

.

Alipokelewa na kupelekwa moja kwa moja kwenye hema la viongozi wakuu. Huko aliketi akamiminiwa mvinyo kwenye bilauri. Taratibu akawa anakunywa huku wakibadilishana maneno. .

.

“Taarifa yenu ilinishtua. Ni nini haswa kinachoendelea?” aliuliza Phares.

.

.

“Ni mambo ya kutisha,” akajibu mkuu wa jeshi. “Tulishindwa kuvumilia ndio maana tukaamua kumshirikisha malkia. Mbona hujaja naye?”

.

.

“Amechoka, anahitaji kupumzika,” alijibu Phares. “Nipo hapa kwa ajili ya kumuwakilisha. Mnaweza kunambia yaliyotokea?”

.

.

“Nadhani ingekuwa bora ukajionea mwenyewe,” alisema mkuu wa jeshi kisha akasimama akimtaka Phares aongoze safari kwenda nje.

.

.

Wakiongozana na walinzi watano, mkuu wa jeshi, makamu wake na Phares waliongozana mpaka mbele kidogo ya mpaka wao, wakasimama hapo. Japokuwa ilikuwa ni usiku, mwanga hafifu uliokuwepo ulitosha kuonyesha nyayo lukuki za watu juu ya ardhi. .

.

“Hatujajua watu hawa ni wakina nani na walikuja hapa muda gani. Muda wote tumekuwa lindo, hatukuona watu wa aina yeyote!” Mkuu wa jeshi aliweka kituo akamtazama Phares. Uso wa mkuu huyo ulikuwa una hofu. .

.

“Jana wakati wa usiku, kuna baadhi ya wanajeshi walidai wamewaona vivuli vya watu vikikatiza. Mbaya zaidi ni kwamba mpaka sasa kuna wanajeshi takribani nane ambao haijulikani wapi walipo. Mara yao ya mwisho walikuwa lindo kandokando na mpaka. Tumetafuta kote pasipo kufanikiwa. Kitu pekee tulichokiona ni kile …”



Mkuu wa jeshi alinyooshea kidole upande wake wa kulia. Mwanga wa viginga vya moto ulipomulika huko, yakaonekana masalia ya damu. Phares alisogea eneo hilo akatazama vema. .

.

“Hatujajua ni damu ya nani,” alisema mkuu wa jeshi. “Ila tunadhani inaweza kuwa ya wanajeshi wetu, na wameuawa na hawa wenye hizi nyayo.” .

.

Baada ya maelezo hayo, walirejea ndani ya mpaka mpaka hemani. Waliketi wakajaziwa mvinyo kwenye bilauri.

.

. “Inabidi hatua zichukuliwe haraka. Leo usiku wa manane tunaweza kuvamiwa,” alisema Phares kwa kujiamini, makamu mkuu wa jeshi akapaliwa. Alikohoa mara tatu kabla hali haijawa shwari.

.

.

Phares alikunywa fundo moja la mvinyo. Kichwa chake kilikuwa kazini kusaka mawazo na namna ya kufanya, ila kabla hajatia tena neno, kelele kali ya yowe ilisikika nje, wakashtuka. Mara sauti ikaita mlangoni mwa hema.

.

. “Mkuu, kuna kitu unapaswa kuona!” Haraka mkuu wa jeshi, makamu wake na Phares wakatoka ndani. Nje walimkuta mwanajeshi mmoja akihangaika huku akishikiliwa na wenzake wawili. Mwanajeshi huyo aliyekuwa ameshikiliwa alisema kwa papara:

.

.

“Sijachanganyikiwa! Ni kweli nimeona, mkuu!”

.

.

“Umeona nini?” Phares aliwahi kuuliza.

.

.

“Nimemuona Malkia!” akajibu mwanajeshi yule.

.

. “Nimemuona Malkia Sandarus! Kwa macho yangu nimemwona akitembea!”

.

. “Amerukwa na akili!” mkuu wa jeshi alisema kwa mapuuzo, ila Phares hakuchukulia jambo hili masikhara. Aliamrisha mwanajeshi huyo aachiwe huru kisha akamuuliza:

.

.

“Umemuona wapi?”

.

.

“Kule!” mwanajeshi akanyooshea kidole upande wake wa mashariki.

.

.

“Unaweza ukanipeleka?”

.

.

“Ndio!”

.

.

.

.

.

.

~ Ina mana Mwili wa Malkia uendeshwao na ramli za bibi wa Tanashe umeshawasili Goshen?? ~ .

.

Nini Karim amemficha Sultan?? Sultan atagundua?? .

.

~ Goshen imejiandaa kuwapokea "wageni wao wa usiku" toka kwa Jayit wakiwa chini ya jenerali mpya bwana Rayden??

.

. ~ Nini hatma ya Zura aliye ulimwengu wa chini?? .

.

~ Rhoda na Phares, nani atamzidi mwenziwe kete??





Haraka Phares akiongozana mbele kabisa na mwanaume yule mshahidi, walielekea kule kuliponasibiwa kuonekana kwa Malkia. Hii ilikuwa ajabu na kila mtu alitaka ashuhudie muujiza huu, hivyo wengi wakaenda.

.

.

Walifika huko wakahaha. Walizivunja shingo zao kwa kutafuta, walizungusha macho yao kwa kusaka, patupu! Hakukuwepo yeyote.

.

.

“Una uhakika ni hapa?” Phares alimuuliza mshahidi.

.

.

Wengine walikuwa tayari wameanza kupuuza, na hata kujutia juhudi zao kwenda eneo lile.

.

.

“Ndiyo ni hapa!” Alisisitiza mshahidi. “Nilikuja kukojoa nikamwona.”

.

.

Mkuu wa jeshi alisonya. Aliamuru mshahidi atiwe pingu na kufungiwa ndani kabla hajaleta madhara mengine, amri ikatimizwa. Watu waliondoka toka eneo hilo la tukio akiachwa Phares pekee.

.

.

Mwanaume huyo aliendelea kutazama huku na kule, bado hakuamini kama mwanaume yule ni mwehu kwa kuona tukio alilolisema. Alijongea huku na kule akiangaza. Mara akaona nyayo za mtu kwenye mchanga mzito wa tope. Alizitazama vema nyayo hizo akagundua ni za mguu wa kike.

.

.

Alipata maswali juu ya nyayo hizo, ila muda wa kutafuta majibu hakuwa nao, akaondoka kurejea kule hemani kwa ajili ya kuandaa mipango kabambe ya kujilinda. Hili swala aliliweka kama kiporo.

.

.

Hemani mipangoni, kwanza, akaagiza watu wote wanaoishi karibu na mpaka wakae ndani kwa muda wote huo wa usiku, asionekane yeyote akiwa anazurura. Vilabu vyote vya pombe vifungwe mapema, na atakayekaidi ataadhibiwa vikali. Agizo likatekelezwa ndani ya muda mfupi tu.



Baada ya hapo mitaro mirefu ilichimbwa kwa awamu mbili, ya kwanza karibia na mpaka, ikikaribiana kabisa na mashimo ya awali, ya pili ikiwa hatua kadhaa mbele. Jeshi lilijigawa makundi tatu katika idadi ifuatayo:

.

.

la kwanza lililokaribu na mpaka lilikuwa na wanajeshi wengi, la pili lililotenganisha na la kwanza kwa mfereji mrefu, lilikuwa na wachache ukilinganisha na la kwanza, la tatu pia vile vile likifuata mtindo huo wa kupunguza idadi.

.

.

Mbali na hapo, wanajeshi watatu walikuwa mbele ya mpaka. Hawa walikuwa mahususi kwa ajili ya kutambua hatari upesi na kutoa taarifa. Njia hii ilionekana yenye ufanisi zaidi ukilinganisha na mtu mmoja kukaa mtini kutazama, japokuwa ilikuwa ndiyo yenye hatari zaidi.

.

.

Kwenye mifereji mirefu iliyochimbwa, ilisakafiwa na majani makavu. Majani haya yakaloweshwa na mafuta ya taa. Yaliwekwa juu katika mfumo wa kwamba, kama wewe ni mgeni basi hauwezi ukatambua hilo.

.

.

Mipango yote hiyo ilifanyika ndani ya dakika kumi tu! Phares aliasisi na kusimamia kila jambo. Wanajeshi wakaelimishwa namna ya kujipanga na kupambana. Baada ya hapo kukawa kimya kila mtu akiketi mahala pake alipotakiwa kuwepo kwa mujibu wa mpango, kisha kukawa kimya cha kifo.

.

.

Ndani ya nyumba ndogo ambayo haipo mbali sana na mpaka, takribani kama nusu maili, mwanaume aliyekuwa amevalia shati chakavu lenye kifungo kimoja, suruali kuukuu inayoishia kwenye enka ya miguu, alikuwapo sebuleni akinywa pombe iliyotunzwa ndani ya chupa ya hovyo.



Nywele zake zilikuwa vurugu. Aliketi kwenye kiti kana kwamba mgonjwa mahututi asubiriaye kumuona tabibu kwa hali zote. Ila kwa namna alivyokuwa anapeleka chupa mdomoni na kugida, ndipo ingekuacha mdomo wazi kwa kujiuliza anatolea wapi nguvu hiyo?

.

.

Mwanaume huyo, asiyeeleweka ni aliyekula chumvi nyingi au lah, alinyanyuka toka kochini baada ya kuhakikisha amemaliza kinywaji chote kilichomo ndani ya chupa. Alipindua mdomo wa chupa akaungalizia chini, hakukuwa na kitu. Alilaani. Alijivuta kuelekea jikoni, akiwa njiani macho yake yakamtaarifu kuna mtu amekatiza dirishani.

.

.

Nani! Alishtuka na moyo wake. Taarifa ilitolewa muda si mrefu kwamba haitakiwi yeyote kuwapo nje ya nyumba kwa usiku mzima, sasa huyo aliyekatiza ni nani? Ni adui? Au ni mwananchi ambaye hana habari?

.

.

Haraka mwanaume huyo, mlevi, alikimbilia upande wa pili wa nyumba yake, dirishani akatupa macho njiani. Mara akamuona yule aliyekuwa anakatiza. Alikuwa ni mwanamke ndani ya nguo kuukuu. Hakumtambua mwanamke huyo ni nani, lakini alitamani kumfahamu. Akili yake ya kilevi ilimtuma apaze sauti kuita, akafanya hivyo.

.

.

Sauti ya mwanamke iliyotoka jikoni, inaweza kuwa ya mkewe, ikamkaripia mlevi huyo dhidi ya kupiga kelele. Asikome mwanaume huyo akaendelea kuita. Mara mwanamke akageuka. Hakuwa mbali sana na nyumba lakini mwanga wa muda huo ulikuwa hafifu kuonekana vema.

.

.

“Hairuhusiwi kuzurura nje we mwanamke! Nenda kwako upesi!”

.

.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mwanamke huyo alisimama, kama mwanasesere, akamtazama mlevi huyo pasipo kusema jambo. Mlevi alitwaa ginga la moto lililokuwa linaning’inia ukutani mwake, akaonyeshea kule alipo mwanamke yule. Hapo ndo akamwona.



Malkia Sandarus!

.

.

Haraka mlevi alikimbilia jikoni kumwambia mke wake alichokiona. Ni kama vile pombe iliyeyuka kichwani. Macho yalikuwa yamemtoka, uso ukibebelea kitendawili. Mke wake alimpuuza, hakumwamini. Mlevi aliendelea kumsumbua mkewe mpaka pale alipokubali kwenda naye kutazama. Mke alirusha macho nje ya dirisha, hakumuona mtu. Alisonya akalaani akiondoka kwenda jikoni.

.

.

Mlevi alibaki akitazama pale dirishani kama vile mtu asiyeamini. Alifikicha macho yake, akatikisa kichwa. Alitazama na kutazama, hakuona mtu. Mwishowe aliamua kurudi kwenye kiti chake.

.

.

“Naomba chupa nyingineee!” alipiga kelele.

.

.

“Hiyo uliyokunywa inakupa mawenge, unataka nyingine!” mkewe akafoka. “Embu nenda kalale huko!”

.

.

“Nimemuona kweli! Naapa!”

.

.

“Kalalee!” Mke alifoka tena.

.

.

Katika kambi ya jeshi huko mpakani, kilikuwa ni kimya kirefu sasa baada ya kila kitu kusukwa na kupangwa vema. Mpaka muda huo walikuwa tayari wamedumu kwenye ulimwengu wa ububu kwa takribani robo saa na huku hakuna lolote lililotukia. Ukimya huo ukahamisha mawazo ya Phares.

.

.

Aliwaza kumhusu Vedas huko kasrini. Nafsi yake ilimsuta kwanini hakumuaga mwanamke huyo. Lakini kilichomshangaza na kumpa maswali zaidi, ni kwanini mwanamke huyo hajaja kumuulizia mpaka muda huo?

.

.

Ameshindwa hata kutuma watu kuja kumtazama kama yupo hapo kambini? Au amechoka ukaidi wake ameamua amwache? Hakupata jibu.

.

.

Alichojua ni kwamba amekosea, na aliona sehemu pekee ya kurekebisha makosa yake ni kushinda vita. Atarudi nyumbani akiwa na tabasamu pana, atapanua mikono yake amkumbatie malkia.



Alidumu fikirani kwa ziada ya dakika kumi, mambo yakaanza kuwika. Sauti kali ya filimbi iliita kuwashtua. Filimbi hiyo ilikuwa ni kiashiria cha ujio wa adui. Haraka kila mtu alipasha mwili wake moto tayari kwa ajili ya pambano.

.

.

“Wanakujaa!” Sauti ilisikika kwanguvu. “Hawaonekanii!” Taarifa nyingine ikaja upesi. Vishindo vya watu lukuki wanaokuja vilisumbua masikio ya kila mmoja, lakini hakuna aliyefanikiwa kuona wageni hao. “Shikilia mpangooo!” alipaza Phares. Mstari wa kwanza wa wanajeshi ukakaa tenge kwa ajili ya kuwakabili maadui.

.



Jeshi la Jayit, lililokuwa linaonekana kwa uhafifu, lilikuja kwa kasi mno, vishindo vyao vilieleza. Wakiwa hawana hili wala lile, lukuki waliparamia na kuzama ndani ya mfereji mrefu wa kwanza. Haraka moto ulitupiwa humo, kufumba na kufumbua likatokea tanuru kubwa! Viumbe wote waliozamia humo waliteketezwa kama makaratasi wakipiga yowe kali.

.

.



Kwa wanajeshi kadhaa, wa Jayit, waliofanikiwa kuvuka mfereji huo wa kwanza nao hawakufika mbali wakadhibitiwa kwa urahisi. Moto uliokuwa unawaka kwa pupa nyuma yao ulitoa mwanga mkali ambao uliwaonyesha vizuri wanajeshi hao mbele ya macho ya wanajeshi wa Goshen, waliotumia wingi na silaha zao kuwamaliza.

.

.

Baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, kundi lote la kwanza la wanajeshi wa Goshen likalala chini ghafla. Wanajeshi wote wa Jayit waliovuka mfereji wa kwanza, pasipo matarajio, wakaanza kupokea mvua ya mishale ya moto. Hata wale ambao walikuwa bado hawajavuka, nao waliteketezwa kwa mishale hiyo iliyoshushwa kwa fujo.

Wakati mapambano yakiendelea, kundi la pili liliungana na la kwanza kuwaongezea nguvu, mfereji wa pili ukawashwa moto. Sasa mapambano yakawa yanatukia katikati ya mifereji miwili yenye kuwaka moto, na huku kundi moja tu la jeshi la Goshen, lile la tatu, likiwa ndio limebaki pasipo kuguswa. Kundi hilo kazi yao ilikuwa ni kuwadungua wanajeshi wa Jayit kwa ncha za mishale.

.

.

Kutokana na kuwekwa katikati ya moto, wanajeshi wa Jayit walishindwa kurudi walipotokea, wala kuingia ndani ya Goshen. Kushambuliwa kwa kushtukizwa kuliwapukutisha wapambanaji wao wengi, na hali ya kuwekwa hadharani na mwanga wa moto, kulirahisisha kazi kwa wana Goshen, ikawa kama wanapambana na wanadamu wenzao.

.

.

Vita ilidumu kwa muda wa dakika arobaini na tano tu, ushindi mnono ukaenda kwa Goshen. Ni wapambanji wanne tu wa Jayit ndio waliobaki hai wakikimbia kuokoa nafsi zao, ikiwemo kamanda wao mkuu mpya, bwana Raiden. Salama ya wanaume hao ilikuwa ni kutoingia kwenye uwanja wa vita, wao walibakia kando wakitazama.

.

.

“Waacheni wakaupeleke ujumbe,” alisema Phares akiwakataza wanajeshi kuwafukuzia maadui hao. Walifurahia ushindi, Phares akiteka nyoyo za wapambanaji kwa michoro na mipango yake thabiti iliyozaa matunda. Walimnanyua kama mtoto wakamrusha juu juu kama kitenesi.

.

.

Hakukaa tena hapo, Phares akaaga anataka kurudi kasrini baada ya kazi yake kuisha. Akisindikizwa na wanaume watatu wenye silaha, akaondoka zake akitumia farasi wenye nguvu waliokuwa wanakimbia kama upepo.

Hakudumu sana njiani akawasili kasrini. Alikuwa na tabasamu pana usoni, na pia mwenye nguvu na hamu ya kueleza yale aliyotoka kukumbana nayo alikotoka, haswa ushindi. Haraka alishuka toka kwenye mgongo wa farasi akakimbilia ndani. Lakini kuna kitu hakikuwa sawa, na pengine furaha yake aliyokuwa nayo ilimfanya asichambue mazingira vema.

.

.

Mbele ya uzio mkubwa wa kasri walikuwapo walinzi kama kawaida, wakisimama kwa ukakamavu huku wakishikilia silaha zao, hata ndani ya uzio vilevile hali ilikuwa vivyo hivyo, wanaume waliobebelea silaha wakisimama kwa ukakamavu. Lakini baada ya kupita ngazi ya kwanza kwenda chumba cha juu cha malkia, hakuonekana tena mlinzi yeyote. Hii haikuwa kawaida.

.

.

Phares alinyoosha miguu yake mpaka mlangoni mwa chumba cha malkia alipoubetua kitasa na kuzama ndani. Alikaribishwa na vitu vilivyokuwa shaghalabaghala, mathalani meza ilivyovunjika na bilauri kadhaa za maua zikiwa chini. Hapo ndipo moyo wake ukalipuka kwa hofu, bup!

.

.

Haraka alikimbia akarusha macho yake kitandani, huko akauona mwili wa malkia Vedas ukiwa umelala, na vitu zaidi vilivyovunjika na kuwa hovyo. Aliuendea mwili wa malkia akiita, lakini hakukuwa na jibu. Alisogea karibu zaidi, sasa kwa hofu, akagundua jambo chungu alilogoma kuamini kwa hapo awali. Malkia alikuwa amekufa!

.

.

Majeraha kadhaa yalikuwa usoni mwa marehemu; pua na mdomo wake vilikuwa vinachuruza damu, nywele zake zilikuwa hovyo na gauni lake alilolivaa lilikuwa limechanwa kifuani. Lakini zaidi ya yote, hakuwa na mkufu!

Phares aliushika mwili wa Vedas, akagundua bado ni wa moto. Hii ilimaanisha ameuawa muda si mrefu. Haraka alitoka ndani ya chumba akawaita walinzi na kuwapasha habari. Alikuja kugundua walinzi wa karibu wa malkia walikuwa wamejeruhiwa vibaya, na hata wengine kufa, na kufungiwa ndani ya stoo.

.

.

Haraka alitoa agizo la mipaka yote kufungwa, doria na msako kufanyika mpaka muuaji apatikane.

.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

.

Wamkamate mtu yeyote yule watakayemuhisi, yeyote yule atakayekuwa anafanana na Malkia Sandarus!

.

.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

.

Ni furaha iliyoje kwa vikongwe wa Tanashe! Macho yao sasa yalikuwa yanaona kitu walichokuwa wanakitafuta kwa muda mrefu, na si kingine hiko bali ni mkufu.

.

.

Kwa kupitia kioo chao cha kilozi, waliona vyote vilivyojiri. Furaha yao ilikuwa kubwa zaidi kwasababu sasa walikuwa wamelipiza kisasi kwa mwanamke aliyewafanyia mchezo mchafu wa kuwasaliti, bibie Vedas, basi vinywa vyao vyenye upungufu mkubwa wa meno vikawa wazi muda wote kwa tabasamu na macheko. Kazi pekee sasa iliyokuwa imebakia mikononi mwao, ikawa ni kuuingiza mwili wa Malkia ndani ya himaya ya wachawi, Tanashe.

.

.

Kazi hii haikuwa nyepesi kama mtu anavyoweza kudhani. Tamu ni kwamba vikongwe hawa wa Tanashe walitambua hilo jambo na hawakutaka kumwaga supu ingali wamebakiza fundo moja.

.

.

Ramli zao zilisogeza miguu na mikono ya Malkia upesi. Hawakutaka kuharibu umakini wao kwa fanikio la fataki. Malkia akiwa amebakiza kama nusu kilomita kuingia ndani ya Tanashe, ghafla anakutana na wanajeshi watatu, wanamuamuru asimame papo hapo.

Wanajeshi hawa walikuwa juu ya migongo ya farasi wakiwa wameshikilia viginga vya moto. Kwenye mapaja yao walikuwa wamebebelea mifuko ya jambia ndefu. Macho yao yaliyokuwa na shaka yalimtazama mwanamke waliyemsimamisha, ambaye alikuwa ameinamisha chini uso wake.

.

.

“Wewe nani na unaelekea wapi?” aliuliza mwanajeshi mmoja kwa sauti ya ukali. Kimya, hakukuwa na majibu.

.

.



Wanajeshi wakachomoa jambia zao. “Wewe!” alifoka mwanajeshi mwingine akipiga bega la mwili wa Malkia kwa bapa la jambia.

.

.

“Hujasikia ulichoulizwa? – wewe nani, unatoka wapi na unaelekea wapi?” Hakukuwa na majibu.

.

.

Wanajeshi walitazamana kwa nyuso za mashaka. Mmoja alijivika ujasiri akashuka chini, akatumia ncha ya jambia lake kunyanyua uso wa mwanamke waliyemsimamisha. Uso uliposimama, wakamuona Malkia Sandarus. Ajabu! Ndio, hawakuwa wanafananisha.

.

.

Kabla wanajeshi wale hawajatoka kwenye taharuki, mwanaume aliyekuwa karibu alinyanyuliwa mithili ya mtoto. Alirushwa kwanguvu kuwakumba wenzake aliowadondosha chini kama matofali. Kabla wanaume hao hawajajikusanya, tayari mwili wa Malkia ulikuwa umetwaa jambia la mmojawao, na katika kasi ya ajabu, ukawamaliza wanajeshi wale kana kwamba wadudu.

.

.

Farasi mmoja alichukuliwa, mwili wa Malkia ukajiweka juuye na kisha kuondoka kwa kasi kumalizia safari ya Tanashe. Farasi aliachwa mpakani, Malkia akazama ndani ya himaya.

.

.

Alitembea kwa muda mdogo tu kabla ya kukomea mbele ya mlango wa nyumba ya vikongwe. Alipokelewa kwa shangwe kubwa, na baada tu ya mkufu kutwaliwa na vikongwe wale, alipoteza nguvu na kuanguka chini kama mzigo, vikongwe wakambebelea na kumuingiza ndani.



“Hana kazi tena, tumuue!” alisema kikongwe mmoja. Ilikuwa ni vigumu kuwatofautisha maana kila mmoja alikuwa na jicho moja, wakivalia mashuka meusi.

.

.

“Hapana!” akawaka mwingine. “Usiwe mpumbavu asiye na akili. Unajua kabisa mkufu huu huendana na damu ya huyu kiumbe. Tukimmaliza ni vipi tutapata utawala wa mkufu?” Kweli.

.

.

Damu ya Malkia ilikuwa inahitajika, ama basi kiungo chake kwa ajili ya kukamilisha ibada. Ila vikongwe hawa hawakuona haja ya kuharakisha hivyo. Walitoka kufanya kazi kubwa kwa muda wote huo na wakaona haja ya wao kupumzika kisha kumalizia zoezi lao kesho yake usiku. Waliona linapendeza hili, wakakubaliana.

.

.

Muda ukiwa unaendelea kuyoyoma, huko mbali ya jengo kubwa la kuogofya la vikongwe hawa, anakatiza fisi mkubwa. Fisi huyu alikuwa anaperuzi na kuzurura huku na kule. Lakini ghafla, akiwa kazini, anakutana na nyayo juu ya ardhi. Ananusa nyayo hizo, anasikia ladha ya binadamu. Anafuatilia nyayo hizo taratibu, zinamuelekeza mpaka kwenye jengo la walozi vikongwe.

.

.

Fisi huyo alisimama, umbali wa kama hatua thelathini, akarusha macho yake kutazama jengo la vikongwe. Alitazama hapo kwa muda pasipo kuona kitu, ila kabla hajaondoka, anapata fursa ya kuuona mwili wa Malkia kwa kupitia dirishani. Si kwamba alikuwa amesogea karibu, la hasha! Aliliona hilo wakati vikongwe wakiupeleka mwili huo chumbani.

.

.

Fisi alijikuta akibweka kidogo kwa bumbuwazi, kisha haraka akaondoka toka eneo hilo kwa mbio kali.

.





Usiku ulikua na kukua, mwishowe kukakucha kukipokelewa na habari za kifo cha Malkia Vedas. Habari hii ilikuwa nzito, shughuli zote ndani ya tawala ya Goshen zilisimama kupisha msiba huo. Kila mtu alishangazwa katika namna yake, ingawa si wote walioumizwa. Malkia Vedas hakuwepo ndani ya mioyo ya watu kabisa.

.

.

Watumishi walitumwa huku na huko kusambaza taarifa za msiba wa Malkia Vedas kwenye tawala zingine za ng’ambo. Mpaka kufikia mchana, habari hizo zilikuwa zimesambaa vya kutosha, ila muitikio wake ulikuwa finyu. Hakuna tawala iliyokuwa na uhakika kama itahudhuria msiba huo.

.

.

Mahema yalitengwa na maeneo pa kupokelea wageni. Maiti ya Vedas ilifungwa katika sanda ya gharama na kutunzwa kwenye chumba mahususi cha maiti. Watu kadhaa, haswa wa ndani ya himaya walijongea maeneo ya uwanja mkuu palipokuwa panaendeshwa ratiba za msiba. Hata wao hawakuwa wengi.

.

.

Miongoni mwa hao watu alikuwapo mwanamke aliyevalia gauni refu jeusi, kofia yenye miwani ya wavu, glovu nyeusi na viatu virefu vyeusi. Japokuwa alikuwa masitikoni, alikuwa amependeza. Midomo yake ilikuwa na rangi nyekundu na macho yake yakitingwa na rangi nyepesi nyeusi. Mwanamke huyu alikuwa Rhoda.

.

.

Aliketi mahala pa juu, sehemu za watu muhimu. Alipoketi alijipepelea na kipepeo chake chenye matundu kadhaa akirusha macho yake huku na kule kama mtu anayehesabu watu. Nani alikuwa anamtafuta? Haikujulikana. Kama vile alikata tamaa, akaacha kuangaza na kupoza machoye. Ila mara akasikia sauti ya mtu inamuita. Aligeuza macho akamuona mwanakijiji.



“Unaitwa kule!” Alisema mwanakijiji huyo akinyooshea kidole upande wake wa kaskazini. Rhoda alipotazama, akakutana na Phares. Alimpa ishara ya kumuita.

.

.

Phares alikuwa amevaa suti ya kaki ya ngozi iliyokuwa imedariziwa na nyuzi za dhahabu. Nywele zake zilikuwa zimechanwa vema ziking’aa, ndevu zake pia. Alivutia kutazamwa.

.

.

Rhoda alisimama, akiwa ameshikilia gauni lake, akaondoka kumfuata mwanaume huyo. Aliketi kandokando yake pasipo kuongea kitu. Baada ya kama dakika moja ndipo wakaanza kuteta, Rhoda akiwa wa kwanza kutoa sauti yake inayolaghai masikio ya nyoka wa pangoni.

.

.

“Nimesikia ameuawa, nani kafanya hivyo?”

.

.

Phares alivuta pumzi ndefu.

.

.

Hakujibu kwa papara bali alingoja. Macho yake yalikuwa madogo na mekundu. Mahali alipokuwa ameketi palikuwa papweke, konani mwa uwanja, ila aliweza kuona kila linalotukia.

.

.

“Sijajua nani aliyefanya hilo tukio, na sijajua nini lengo lake juu ya hili.”

.

.

“Hujapata kiashiria chochote?” Rhoda aliuliza.

“Nilichokipata ndicho kinanipa mashaka,” akasema Phares kwa ufupi.

.

.

Aliendelea kutazama watu lakini fika akili yake ikiwa inadadavua. Rhoda hakuuliza tena, alikuwa anangoja jibu la swali lake.

.

.

“Aliyemuua Vedas ni Malkia Sandarus,” alisema Phares. Rhoda akashindwa kujizuia na kutabasamu.

.

.

“Phares, nini unaongea? – Malkia Sandarus aliyekufa kitambo?”

.

.

“Ndio maana nikakuambia nilichokipata kinanipa mashaka.”

.

.

“Ila inawezekanaje? Umejuaje hayo?”

.

.

“Ni kwa mujibu wa maneno ya mlinzi,” alijibu Phares, kisha akaongezea:

.

.

“Mlinzi wa malkia alipambana naye kabla hajashindwa, akajeruhiwa na kutupiwa stoo.”



“Ndio amesema ni Malkia?”

.

.

“Ndio. Adui alikuwa na mwili wa Malkia Sandarus!”

.

.

“Vi – vipi? Kuna kitu chochote amechukua?”

.

.

Rhoda alilipuka na swali. Uso wake ulibebelea shaka. Kuna namna alikuwa ameguswa. Phares alimtazama akaona shaka lake hilo usoni.

.

.

“Vipi, kuna tatizo?”

.

.

“Hapana, nilitaka tu kujua,” alipoza Rhoda. Alijitahidi kuigiza kila jambo li shwari.

.

.

“Sijaona chochote ambacho amechukua mtu huyo,” alisema Phares. Moyo wa Rhoda ukawa wa baridi kabla haujalipuliwa na muendelezo.

.

.

“Isipokuwa tu mkufu.”

.

.

“Mkufu!”

.

.



“Ndio, mkufu,” alijibu Phares. Pasi na shaka hakuona kama kuna jambo kubwa hapo. “Nimeshangazwa kwanini ameubeba mkufu huo? – kuna lolote unalolijua kuhusu huo mkufu?”

.

.

“Hapana,” alijibu Rhoda uso wake ukimsaliti. Phares alimtazama mwanamke huyo, alikuwa amepoteza amani. Uso wake ulibebwa na mafuriko ya mawazo.

.

.

“Rhoda,” aliita. “Kuna shida yoyote?”

.

.

“Hapana, Phares.”

.

.

“Hapana, Rhoda. Kuna jambo unanificha. Naomba unieleze kuhusu huo mkufu, na kama unajua kama kuna lolote linalohusiana na marehemu Malkia Sandarus na mkufu huo.”

.

.

Mdomo wa Rhoda ulikuwa mzito. Alikuwa anataka kusema lakini moyo wake ukimkataza. Ila akinyamaza, mkufu huo utageuka ndoto, wapi ataupata na anauhitaji?

.

.

Kwa namna kubwa aliona Phares ndiye pekee anayeweza kuutafuta huo mkufu na kuusogeza tena karibu, kwahiyo hakuwa na budi kupambana na moyo wake kueleza.

.

.

“Phares,” Rhoda aliita. “Mkufu ule ni mali kubwa sana. Ni nguvu, na ni madaraka.”

.

.



“Kivipi?”



Kabla Rhoda hajaendelea, sauti kubwa ya pembe la ng’ombe iliita. Phares alinyanyuka akamuaga Rhoda.

.

.

“Bila shaka nahitajika. Nitakutafuta tuongee zaidi.”

.

.

Rhoda alimshika mkono Phares. Kuna kitu alitaka kusema ila akaamua kughairi na kuishia kusema:

.

.

“Sawa, tutaongea.” Phares akaondoka. Alipoishilia, Rhoda akanyanyuka kwenda mpaka kwenye kasri kumtafuta mlinzi wa marehemu, yule aliyempatia kazi ya upelelezi.

.

.

Alimuulizia mlengwa wake, akaelekezwa na kumpata baada ya kuhonga kiasi fulani cha dinari. Mwanaume huyo alikuwa amefunga mikono yake kwa kitambaa, uso na kichwa chake pia vikiwa na majeraha.

.

.

Walisogea na Rhoda mpaka kando ya kificho.

.

.

“Nini kilitukia?”

.

.

“Ni Malkia Sandarus!” alistaajabu mlinzi. Aliongea akiugulia maumivu.

.

.

“Ni ajabu sana, sikuweza kufua dafu hata kidogo. Kila nilipojitutumua niliishia kugaragazwa kwa maumivu. Yule si Malkia kabisa!” alitikisa kichwa mlinzi.

.

.

“Si Malkia. Kuna roho ndani yake. Macho yake yalikuwa yanaogopesha. Nguvu zake hazikuwa na mithili.”

.

.

“Kuna lolote alilosema?” Rhoda aliuliza. Mlinzi akatikisa kichwa.

.

.

“Hapana, hakusema kitu. Wakati akitenda hayo yote alikuwa kimya asiyefungua kinywa.”

.

.

“Ulimuona wakati anakwapua mkufu wa malkia?”

.

.

“Hapana. Alihakikisha kwanza amemalizana na sisi kabla hajaingia chumbani. Alitu muda mchache sana kutimiza haja yake.”

.

.

“Unadhani atakuwa ameupeleka wapi ule mkufu? Una wazo lolote wapi alipotokea?” Mlinzi akatikisa kichwa na kubinua mdomo wake.



“Ila kuna taarifa zinaweza zikasaidi kujua. Kuna wanajeshi watatu wameuawa karibu na mpaka wa Tanashe. Jambo hilo linanifanya niamini mtu huyo atakuwa ameelekea huko baada ya hayo mauaji.”

.

.

“Tanashe! – himaya ya wachawi?”

.

.

“Ndio!”

.

.

“Kuna mtu yeyote anayeweza kudiriki kwenda huko?”

.

.

“Kama tu kuna sababu kubwa ya kufanya hivyo.” Haraka kichwani mwa Rhoda ikaja taswira ya Phares. Huo unaweza ukawa mlango wa kutokea, alijisemea. Ila ni wazi atahitaji nguvu kubwa ya ushawishi. Kutobakiza hata tone moja la shaka kwenye kichwa cha mwanaume huyo.

.

.

Aliaga akaondoka. Alibakiwa na kazi moja kubwa sasa, namna ya kufua na kuondoa shaka kwenye moyo wa Phares; namna ya kumpa sababu nzito mwanaume huyo.

.

.

.

.

.

.

.

*** .

.

.

.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

.

.

Giza kali lililoambatana na milio ya wadudu lilikuwa linazonga macho. Si kwamba giza hili liliingia muda huu, hapana. Lilikuwa ndilo lililopo kila siku kwenye himaya hii ya Jayit, Devonship. Laiti kama wewe binadamu ungekuwamo humo basi ungelazimika kutumia kurunzi, la sivyo usingefika popote.

.

.

Basi kulikuwa kimya, wakati huko ulimwengu mwingine kukiwa ni majira ya mchana sasa. Kwenye kasri ya Jayit kulikuwa kimya zaidi. Maginga machache ya moto yaliyokuwa yanawaka, bado hayakutosha kupambana na giza hivyo basi kulikuwa na kagiza chenye ladha nyekundu kwa mbali.

.

.

Ndani ya kasri hiyo kulikuwa kana kwamba shimo. Ungeweza kusikia sauti za watu wakihema, ila usingewaona. Na pia ungeweza kuwasikia watu wakitembea, lakini pia usiwaone. Yani shughuli zinakuwa zinaendelea kama kawaida, ila katika hali ambayo macho ya mwanadamu yasingeweza kufua dafu.

Sauti ya kimiminika ilivuma, kisha ikafuata sauti ya kuamuru:

.

.

“Basi inatosha.” Sauti ya kimiminika ikakoma, ikafuatiwa na sauti ya koromeo likipokea kilichomiminwa: gulp! – gulp! – gulp! Aaaagh…

.

.

“Nimeshaamua,” sauti ya Jayit ilisema kimamlaka, ikaongezea: “Sidhani kama nahitaji tena ushauri. Tufunge mjadala kwenye hili.”

.

.



“Lakini mkuu, nadhani ingekuwa ni nafasi ya wewe kutusikiliza sasa baada ya mpango wako wa kwanza kufeli,” ilisema sauti moja kavu ya kizee.

.

.

“Laiti kama ungekuwa umetupa fursa ya kusikia tuliyosema hapo awali, haya yasingetukia.”

.

.

“Kwahiyo unanikosoa, Badili?”

.

.

“Hapana, mkuu, ila nadai nafasi ya kusikilizwa. Wote tunajenga nyumba moja, hatuna haja ya kugombea fito.”

.

.

Kulikuwa kimya usijue kama watu wapo ama wameondoka. Baada ya muda kidogo, kama dakika moja na ushenzi, kukasikika sauti ya kusafisha koo, kisha:

.

.

“Sawa, nawasikiliza. Mlikuwa mnasemaje?”

.

.

“Mkuu, adhabu ya kuwaua wanajeshi walioponea vitani, pamoja na kumining’iniza jemedari Raiden, ilikuwa kubwa sana. Tumepungukiwa sana kijeshi, tumebakiwa nao haba, bila shaka tulikuwa tunawahitaji. Ila kwakuwa ya nyuma si hoja, tutazame ya mbele.” Sauti hiyo ilikomea hapo, na mara ikapokelewa na nyingine. Hii ya sasa ilikuwa laini, ila pia ya mtu aliyekula chumvi, na mtulivu.

.

.

“Tuna haja kubwa ya kutulia kwa sasa, kama kweli tuna nia ya kuweka himaya zote hizi chini yetu.”

.

.

“Kutulia?” Sauti iliuliza.

.

.

“Ndiyo, kutulia,” sauti ya awali ikavuma.

.

.

“Endapo tukivamia kwa papara tutaendelea kuwa wahanga wa kushindwa. Habari zitavuma kote, na kila himaya sasa watakuwa wanajipanga ama kujua namna ya kutukabili.”



“Kwahiyo mnashaurije? Tunatulia namna gani?”

.

.

Sauti nyingine, ile kavu iliyokuwa inaongea hapo awali, ikaendeleza soga.

.

.

“Tumekaa tukajadili, tukashauriana na kukubaliana. Njia nzuri ya kuujua udhaifu na mipango ya kila himaya, ni kwa kupandikiza watu wetu. Mkuu, tunahitaji kupandikiza watu tunaowaamini kwenye kila himaya kubwa. Watu hawa majukumu yao yatakuwa ni kupenya kututafutia nyaraka na taarifa muhimu. Kutujuza nini kinaendelea, nini kinapangwa na kutekelezwa.”

.

.

Akadakia mwingine.

.

.

“Kwa kufanya hivyo, tutajua nini cha kufanya, namna gani ya kuingia na kushambulia. Kuna baadhi ya himaya hazihitaji nguvu, bali tu ulimi na masikio.”

.

.

“Hamuoni kwa kufanya hivyo tutangoja milele kukamilisha kazi yetu?”

.

.

“Ni bora kungoja kwa uhakika kuliko kuwahi kwa mashaka,” ilisema sauti kavu kwa namna ya kujiamini.

.

.

Hili swala lilikuwa gumu kupenya kwenye kichwa cha Jayit. Alikuwa anaamini nguvu zake za kilozi kuliko utumizi wa akili na mwili kwenye utendaji. Kwa namna alivyofanya matambiko ya kuita nguvu za babu na bibi yake, alitegemea asingekutana na nguvu zozote za kumpinga. Alitegemea awe mfalme wa himaya zote wakati wa usiku, jambo ambalo amelifanikisha kwenye himaya tatu tu. Alikuwa na njaa zaidi.

.

.

Ni kweli wapambanaji wake walikuwa hawaonekani wakati wa usiku. walikuwa ni wenye nguvu na wepesi zaidi. Ila kwa Goshen walikutana na kisiki. Hata kama Jayit angefanikiwa kushinda himaya zote, akashindwa kwa Goshen bado angeliona yu mtupu. Na bado mwenye deni kubwa la kutimiza.



Kishingo upande, alikubaliana na mawazo ya washauri wake, ila akawapa majukumu ya kutafuta watu hao ambao wao wanaona wanafaa kwa ajili ya kazi ya upandikizwaji. Watu hao wafundwe na kisha kutumwa haraka iwezekanavyo, wakianzia Goshen.

.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

.

Siku na muda uliwadia. Ulikuwa sasa ni usiku wa ile kesho waliyokuwa wanaisema jana yake. Vioo kikubwa viliwekwa sebuleni kwenye kila kona. Marashi ya maiti na moshi wa kijani ulitawala. Mwili wa Malkia Sandarus uliwekwa juu ya meza nyembamba ndefu ukiwa umelala kana kwamba maiti ndani ya jeneza. Juu yake uliwekwa mkufu.



Vikongwe walikuwa wamevalia magauni marefu meusi, yalikuwa yamewabana. Nywele zao zilikuwa zimesimama kwa kuwa hovyo. Vifuani mwao walikuwa wamebebelea mikufu yenye vidani vya vichwa vya mijusi. Mikononi pia walikuwa wamevalia bangili za chuma zilizokuwa na alama zisizoeleweka. Wote walikuwa peku.



Mwili wa Malkia ulikuwa umevikwa joho jekundu lililomfunika mpaka miguu. Alikuwa ameogeshwa na hata nywele zake kuchanwa. Japokuwa alionekana asiye na uhai, bado uzuri wake wa asili ulikuwa unang’aa. Ni kama vile mwanamke mrembo aliyekuwa amelala juu ya mchanga wa bahari akiwa anapunga upepo kipindi cha joto.



Vikongwe wale watatu, kila mmoja wao akiwa na jicho moja, waliuzunguka mwili wa Malkia wakiimba nyimbo ya lugha ngeni. Walienenda mizunguko mitatu kabla hawajasimama na kuutazama mwili uliokuwa mbele yao, mwili wa Malkia Sandarus uliokuwa umepooza kwa kulala. Walitazamana, wakapeana ishara. Mmojawao akarudi nyuma na kurejea na kitabu kimoja kikubwa, kikuukuu.



Kitabu hiki kilikuwa kina jalada gumu mno. Mbele yake, jaladani, kilikuwa kumechora nyota kubwa yenye pembe sita. Nyota hii ilikuwa imeundwa na pembetatu mbili zilizokuwa zimeingiliana, moja ikitazama chini na nyingine juu. Mbali na nyota hiyo kulikuwa na maneno na ishara kadha wa kadha ambazo kuzing’amua kulihitaji ujuzi.



Kitabu hicho kilifunguliwa mpaka kwenye kurasa inayokaribia na mwisho. Hapo kulikuwa kuna mchoro wa mtu akiwa amelazwa kama vile ulivyofanywa mwili wa Malkia. Juu ya mchoro kulikuwa kuna kichwa cha habari, na chini yake kulikuwa kuna maelezo lukuki, ambayo yalianza kusomwa na kikongwe aliyekuwa amebebelea kitabu hicho.



Akiwa anasoma maneno hayo, taratibu hali ya hewa ikawa inabadilika. Radi na ngurumo ziliita, pepo kali nayo ikavuma. Ndani ya nyumba kukaanza kuwa giza ingali kulitundikwa maginga ya moto kadha wa kadha. Mpaka maneno yanamalizwa kusomwa, tayari kulikuwa giza totoro, radi zilikuwa zinafululiza na upepo ukichachamaa.

Kitabu kiliwekwa chini kisha ukatwaliwa mkasi mdogo. Ulikuwa una kutu na mpini wake ukiwa na rangi nyekundu. Kikongwe aliyekuwa amebebelea mkasi huo aliunyakua mkono wa mwili wa Malkia, akaweka mkasi wake kwenye kidole cha mwisho apate kukikata.



Kabla hajafanya hivyo, mara mlango wa sebule yao ukagongwa mara tatu, na sauti ikaita:

“Faki hapa mlangoni.” Haijulikani ni kwa muda gani, ila huko nje ya nyumba ya vikongwe walikuwa tayari wameshajaa fisi si chini ya mia mbili! Walikuwa wakubwa mno kimaumbo. Na nyuso zao zilionyesha hamu, kama sio utayari wa kushambulia.

.

.

.





Kusikia jina la Faki, tena katikati ya shughuli nzito kama ile, haikuwa habari nzuri kabisa. Vikongwe walitinduka akili. Walitazamana katika macho ya kujiuliza nini cha kufanya, na bahati mbaya zaidi muda haukuwepo upande wao.



Haraka mmoja aliunyanyua mwili wa Malkia na kukimbia nao chumbani. Kitabu na mkasi vilitupiwa kando, ila kwakuwa muda haukutosha kuondosha kila kitu kitakachozua maswali, basi yakaachwa mengineyo. Kikongwe mmoja akaufuata mlango na kuufungua. Macho yake yalikutana ana kwa ana na bwana Faki aliyekuwa anatabasamu, tabasamu la kinafki.



Mwanaume huyo alikuwa amevalia suti nyeusi za mtindo poa wa kale. Nywele zake zilikuwa zimelala kana kwamba zimemiminiwa mafuta malaini. Uso wake, ufananao na wa fisi kwa namna zote, ulikuwa umezingirwa na ndevu zilizotindwa vema. Macho yake madogo yenye kona nyembamba yalikuwa yamezingirwa na rangi nyeusi. Kwa kuhitimisha, chini aling’ara kwa viatu vyeusi viangavu.



“Unahitaji nini kwenye upande wetu?” Aliuliza kikongwe. Uso wake ulijawa na fura. Ndani ya macho yake ungeweza kuona moto wa jazba.



“Nadhani tungeanza na salamu kwanza,” akasema Faki akiendeleza upana wa tabasamu. Hakuonekana kujali, wala kuhofia, lakini pia hakuonekana mwenye hasira. Ila kwakuwa moyo wa mtu ni chaka, basi ni vema tukaishia hapo.



“Kwani umekuja kufuata salamu huku?” aliuliza kikongwe. “Hapana,” akajibu Faki. “Ila nijuavyo mimi huwa tunasalimia wageni na kisha tuwakaribisha ndani.”

“Basi ni huko si hapa,” Kikongwe akaweka kituo. Faki alitabasamu tena alafu akawatazama wanyama wake kana kwamba anawahesabu. Alipogeuka alishusha pumzi akipandisha mabega. “Sawa, basi tusipoteze muda sana, acha niende moja kwa moja kwenye lengo. Tumekuja kuchukua cha kwetu.”



“Cha kwenu?” Kikongwe aliangua cheko la lazima. “Mlikiweka lini?” aliuliza.



Hapo Faki akaifinyanga sura yake kwa kughafirika. Alimsogelea zaidi kikongwe akamchoma kwa ncha ya kidole.



“Skiza we ajuza, kitu chochote kinachogusa ardhi yangu, chochote kile! Hata awe inzi ama sisimizi, basi ni changu! Changu peke yangu! – naomba kilichomo changu humo ndani. Tena upesi!” Kikongwe alitabasamu, meno yake meusi kama makaa ya mawe yakasalimu.



Aliufungua mlango wazi, akimtazama Faki. “Nenda kachukue hicho cha kwako,” Kikongwe alisema. Faki alirudisha tabasamu, hakusema jambo, akachukua hatua kuzama ndani.



Kitendo cha kumalizia mguu wake wa pili, mara ghafla akaona jumba lote limekuwa giza. Hakikuonekana kitu chochote hata kwa kukodoa. Kufumba na kufumbua mara sakafu nayo ikaanza kutitia! Faki alielea akienenda kwenye shimo asilolijua komo lake. Alihofia! Alipiga kelele kali. Alizamisha mkono wake ndani ya mfuko kisha akautoa haraka na kupakaza kiganja chake usoni.



Mara akajiona yu sebuleni, salama salmini! Alikuwa yu chini ameketi kitako, na wale vikongwe wakiwa wamesimama hatua chache mbele yake. Kumbe ilikuwa kiini macho! Hakukuwa na kitu kama kile, bali tu ulozi ulioundwa na kufundwa na vikongwe.

Faki akapiga kelele kutoa ishara kwa fisi wake waliokuwa nje. Ilikuwa ni nduru kali. Haraka kama upepo, fisi wakaanza kushambulia kwa kuvamia nyumba ya vikongwe. Ilikuwa ni patashika! Katika namna ya ajabu, vikongwe waligawanyika na kuwa watu kumi na tatu kwa idadi. Watu hawa wote walikuwa wana taswira ya vikongwe, usijue nani ni nani. Ila walikuwa na nguvu mno.



Walipambana na fisi kwa kuwatawanya na mikono yao. Fisi nao walitumia kucha na meno yao kupambana. Fisi huyu akirushwa kando, ama kuvunjwa shingo, basi anakuja mwingine au wengine upesi! Vikongwe waliraruriwa na kung’atwa, ila, wasiwe nyuma, nao waliwapokonya uhai fisi kadha wa kadha. Vita haikuwa lelemama!



Sebule iliharibika ikawa nyang’anyang’a. Vioo vilivyokuwa vimewekwa kwenye kona vilivunjika. Meza zilivunjwa, vyugu vikatawanyika. Sebule ilikuwa kana kwamba imetupiwa guruneti.



Fisi walipambana kwenda chumbani kuutwaa mwili wa Malkia, lakini hawakuwafanikiwa abadani. Kila walipotaka kudaka korido, mikono ya vikongwe ilifunguka na kuwatwaa, iliwavunja na kuwatengua. Hata kama walipambana kwa kutumia kucha na meno yao, hawakufua dafu.



Mpaka lahitimu lisaa limoja, fisi wote walikuwa wameshalazwa chini, hawajiwezi. Walikuwa wanakoroma kwa kuchoka ama maumivu. Fisi pekee aliyekuwa amebakia akiwa amesimama kwa miguu yake, alikuwa ni Faki! Bado alikuwa kwenye mwili wa binadamu. Muda wote huo alikuwa anatazama pasipo kufanya jambo.

Vikongwe walirudi kwenye miili yao mitatu. Walikuwa wanavuja damu kwa majeraha, ila bado walionekana wenye nguvu za kupambana zaidi. Faki alifungua vifungo vya koti lake akiwatazama vikongwe hao.



“Nisingependa tufikie huku,” alisema. “Ila kwakuwa mnataka, basi haina tabu.”



“Lenye alfa lina omega, Faki. Hutotoka hai.”



Wakasema vikongwe. Isipite muda wakanena maneno yao yasiyoeleweka, mara hali ya hewa ikaanza kubadilika. Hewa nzito ya kijani ilijaza chumba. Hewa hiyo ilikuwa inazunguka kana kwamba kimbunga ikielekea juu.



Ilipopotea, vikongwe hawakuonekana wapi wameelekea. Alionekana mtu mmoja jabali asiyeeleweka jinsia.



Alikuwa amejaza mikono kama vinu. Nywele zake zilikuwa ndefu zilizokatikakatika. Uso wake ulikuwa umekunjamana usijue pua wala mdomo vipo wapi. Kitu pekee kilichokuwa kinaonekana kwa uzuri, ni jicho moja kubwa. Jicho hili lilikuwa limekaa kwenye paji la uso.



Jitu hili likapiga kelele kali, upepo mkubwa ukazuka. Faki alimtazama kwa namna ya maulizo. Alikuwa tayari ameshafungua viifungo vya koti na shati lake. Basi akaweka mikono yake chini. Na mara akaanza kukengeuka kuwa mnyama. Mnyama huyu alikuwa mpana. Alijawa misuli. Meno yake yalirefuka na kucha zikamtoka. Manyoya nayo yalifumuka yakafunika mwili mzima.



Alikuwa fisi kamili sasa! Alinguruma kana kwamba simba. Alianza kusonga kwenda kushoto na kulia akionyesha meno yake makubwa, makali. Kufumba na kufumbua, jitu lile kama jabali likamvamia mbwa huyo. Walitupiana chini wakagaragazana.



Jitu jabali lilimnyakua mbwa likamrushia ukutani, ukuta ukacharaza nyufa kede kwa kishindo kikubwa. Fisi alinyanyuka haraka sana kana kwamba hajaumia. Alirusha miguu yake kumfuata jitu jabali. Jitu likamkamata mnyama huyo, ila kabla halijamfanya kitu, liling’atwa kwanguvu shingoni. Likapiga kelele kali za maumivu!



Kwanguvu alimnyofoa fisi, akamrushia tena ukutani.



Shingoni alikuwa na jeraha kubwa linalovuja damu. Alifunika jeraha hilo na mkono wake wa kushoto. Ule ukuta aliorushiwa fisi kwa mara ya pili, ulidhoofika mno, ukashindwa kustahimili na mara ukadondoka kumfunika fisi, Faki.

Jitu jabali halikutaka kungoja.



Akiwa amefunika jeraha lake shingoni, alikimbia kuelekea alipo fisi. Alidaka mkia wake akamvuta kana kwamba paka! Alimzungusha kana kwamba panga la feni alafu akamrushia tena ukutani. Fisi alipiga kelele kali. Alibomoa ukuta na kujeruhi mkono wake wa kuume.



Jitu likapiga kelele kali kutangaza ushindi. Alikuwa sasa anaelekea kummaliza adui yake, ila kabla hajafika, fisi watatu wakamrukia mgongoni kumparua na kumng’ata. Jitu jabali likatumia mkono wake kuwafagia fisi hao. Liliwatupia chini kama mkulima amwagavyo jasho kwa kidole. Kisha likawasinya kuwavunjavunja!



Fisi wakawa chapati. Jitu jabali liliporusha macho yake kutazama kule alipommwagia Faki, halikumwona! Alikuwa amepotea. Lilipepesa macho yake huku na huko pasipo mafanikio. Lilipiga hatua likiangaza. Lilitumikisha masikio yake kuskiza, lakini bado hakupata kitu.



Lilisogelea eneo lenye kifusi ambapo ndipo Faki alitupiwa, akatazama hapo hatua za mnyama lipate kujua mwelekeo. Likiwa hapo, mara likasikia mngurumo nyuma yake. Liligeuza kichwa kutazama, uso kwa uso likakutana na fisi hewani akiwa ameachama mikono. Kabla jitu halijafanya kitu, likavamiwa na kuangushwa chini.



Fisi aliwahi kuung’ata mkono wa kuume wa jitu. Aliung’ang’ania mno akijaribu kuunyofoa. Jitu lilituma mkono wake wa kushoto kumtoa fisi, fisi akaukwepa mkono huo na kuuparua kwa kucha zake dhalimu. Jitu likapiga kelele. Ila halikukoma. Sasa lilituma mikono yake yote miwili inayochuruza damu, haraka, likamkamata fisi shingoni.

Lilimminya kwanguvu zake zote mpaka aliposikia fisi akilalamika, na hatimaye mlio – kakak! Fisi akawa ametulia tuli, ulimi nje. Jitu likamtupia fisi kando na kisha likanyanyuka.



Vita sasa ilikuwa imekoma, vikongwe wakiwa wamebakia kama washindi. Miili yao ilinyofoka toka kwenye mwili ule mkubwa wa jitu jabali. Walikuwa wana majeraha makubwa na tena wakiwa wamechoka mno. Walitazama mazingira yao wakalaani. Walielekea chumbani kuutazama mwili wa Malkia pamoja na mkufu.



Lahaula! Mwili haukuwepo wala mkufu. Walitazama huku na huko, hakukuwa na kitu! Walitoka ndani ya chumba, wakaenda huko nje kuangaza. Napo hawakuona lolote. Mwili ulikuwa umeondoka na mkufu wake!

“Hapana!” aliwika kikongwe. “Hapana! Hapana! Hapanaa!” alilia kwa uchungu. Alipiga kelele kali zilizoita Tanashe nzima.



Labda wangeweza kusahau kuhusu mkufu, ila majeraha yaliyokuwa yametapakaa kwenye miili yao yangewakumbusha, tena kwa maumivu makali! Maumivu pasipo mbivu.

.

.

.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

.

.

“Mheshimiwa, una mgeni,” ilikuwa sauti ya mlinzi ikimnong’oneza Phares aliyekuwa chumbani akiketi kwenye kiti kirefu. Phares akatikisa kichwa chake, mlinzi akaondoka.



Mkononi mwake, Phares, alikuwa amebebelea mkufu wa dhahabu wenye kidani kikubwa chenye muundo wa saa. Kidani hiki, ndani yake, kilikuwa kina mshale mmoja uliokuwa unazunguka, na macho ya Phares yalikuwa yanafuatisha mshale huo.



Akili yake haikuwepo pale. Kwa namna moja, mshale ule uliokuwa unazunguka ulikuwa unamfanya asahau ulimwengu wa karibu na kuuwaza ule wa mbali. Kama si mlinzi kuja kumshtua, basi angeendelea kukodolea kidani kile kilichomteka mawazo.



Alinyanyuka akatengenezea shati lake jeupe lenye urembourembo kolani. Alikuwa amependeza kwa suruali yake nyeusi na viatu vyake vya ngozi rangi ya kaki. Alienda sebuleni, na pengine pasipo kuwaza nani anayemuita. Huko akamkuta Rhoda, mwanamke aliyempokea kwa tabasamu karimu, pana. “Habari, Phares!” alisalimu Rhoda akisimama.



“Njema, karibu.”



“Nimeshakaribia. Haukuwa unautegemea ujio wangu.”



“Kabisa, sikudhani kama ningepata pata mgeni kama wewe muda huu.”



Walipeana mikono wakiisindikiza na tabasamu, kisha wakaketi.



“Nimeshangazwa sana na msiba huu,” alisema Rhoda.



“Kila mtu ameshangazwa,” akadakia Phares. “Ila tumeona ni muda wa kwenda mbele sasa.”

“Sawa, ila ndio kwa muda mfupi kiasi hiki?”



“Ndio. Msiba haukuwa na watu kabisa, si wa nje wala wa ndani. Yanini udumu kwa masiku?”

Hakukuwa na maneno, kukawa kimya kwa muda. Rhoda alikuwa anaigiza kana kwamba ameguswa.



“Rhoda,” Phares aliita. “Ni nini umekuja kunambia?” akauliza.



Rhoda akashusha pumzi ndefu na kutazama chini. Hii ndiyo ilikuwa nafasi adhimu aliyokuwa anaitaka. Akili yake ilianza kuwazua upesi namna gani awasilishe mawazo yake. Basi akajikuta anatabasamu kabla hajasema.



“Hamna kitu kikubwa saana nilichonacho Phares, ila tu jambo dogo ninalotaka kukusitizia na kukuomba vilevile.”



“Lipi hilo? – Ni kuhusu mkufu?”



Moyo wa Rhoda ukatatuka kwa hofu. Macho ya Phares yalikuwa yanamtazama kwa umakini, akajitahidi kubakiza utulivu wake. Ni jicho moja tu la kushoto ndilo lilipepesuka.



“Ndio, ni kuhusu mkufu.”



“Bila shaka umekuja kuniomba nikautafute.”

Rhoda akakaukiwa kauli. Ni kana kwamba Phares alikuwa anajua haja yake hivyo basi akawa anamsanifu.



“Ni kwanini unautaka sana huo mkufu, Rhoda?” “Phares, laiti ungalikuwa unajua uwezo na nguvu ya mkufu huo, usingalikuwa hapa. Ungelikuwa huko nyikani kuutafuta.”



“Rhoda, sina haja na madaraka.”



“Si tu madaraka, Phares. Mkufu ni zaidi ya hilo! Kwani nini haja ya moyo wako?” Phares alikuwa kimya kidogo kama mtu anayetafakari. Rhoda alimtazama kwa uchu wa kungojea jibu.



Phares aliangaza huku na huko, na mara macho yake yakawa mekundu. “Nina haja moja kubwa, Rhoda. Haja ambayo inanipa maswali kedekede na kunikosesha amani kabisa ...”



“Ipi hiyo?” Rhoda alishindwa kuvumilia.



“Haja ya kujua asili yangu,” Phares akajibu na kuongezea: “Haja ya kujua wapi nilipotokea, wapi nyumbani kwetu, wakina nani wazazi wangu, wakina nani ndugu zangu. Haja hii imekuwa ikinitesa kwa karne sasa.”



“Phares, imewezekanaje ukafikia umri huu usijue kwenu ni wapi? Ulishawahi kuwa mtumwa?”



“Sijui.”



“Hujui? Ulishawahi kupata tatizo lolote la kumbukumbu?”



“Sikumbuki.”



“Ulikutanaje na Vedas?”



“Rhoda, sifahamu. Hakuna jambo nafahamu, hakuna jambo nakumbuka. Kila ninapovuta kumbukumbu zangu, mtu wangu wa kwanza kumuona ni marehemu Vedas. Si kingine!”



Hapo Rhoda akapata mashaka. Akili yake iligoma kabisa kuzaa majibu. Ila waswahili husema kufa kufaana, Rhoda akaona kuna fursa ndani ya tatizo hilo.



“Phares, unahitaji kuutafuta mkufu. Utakusaidia.” Phares akatabasamu kiupande. Aliona sasa hamu ya Rhoda inamvusha mipaka.



Alisimama akatengenezea koti lake akisema:

“Nadhani tutaongea siku nyingine, Rhoda.”

Rhoda akasimama haraka. Alimshika mkono Phares akimtazama usoni.



“Phares, kama unataka kujua, tafuta mkufu! Muda si mrefu wazee hawa wa baraza watajiuliza kuhusu wewe. Watakuuliza umetokea wapi na familia yako ina hadhi gani. Wanaweza hata wakakufukuzia mbali. Utaenda wapi na huna familia? Upo tayari ukaanze moja na ulikaribia mia? … Fikiri!”



Phares hakujibu kitu, ila maneno hayo hayakutokea upande mwingine wa sikio. Aliukwapua mkono wake toka kwa Rhoda, akaenenda zake. “Nahitaji muda,” alisema pasipo kujigeuza.



“Ila kumbuka muda ni mnafki!” Rhoda akamsisitizia. .

.

.

.







Phares alipotelea ndani akimuacha Rhoda anamtazama. Mwanamke huyo alipoteza kama dakika tatu kufikiria, akiwa amesimama.



Alitoka zake ndani kwenda kumtafuta kibaraka wake, kuna mambo alitaka ayaweke sawa. Baada ya punde alimpata, wakasogea kando pasipo na watu.



“Nimeshaongea naye,” alisema Rhoda. “Ila bado sijapata kujua msimamo wake haswa kwenye hili jambo.”



“Kwahiyo tunafanyaje?” akauliza kibaraka. Mwanaume mlinzi mwenye mwili wa mapambano.



“Inabidi tuendelee kumtia hamasa,” alisisitiza Rhoda. “Kama tukimuacha, anaweza akapoteza hili jambo akilini mwake.”



“Sawa.”



“Jitahidi. Nadhani hujasahau kama kuna pongezi kubwa ndani ya hili.” Kibaraka alitikisa kichwa chake kuridhia. Rhoda aliaga akiahidi wataonana kesho, ila kuna jambo mwanaume akalikumbuka.



Alimuita Rhoda akamwambia kwa sura yenye ukakamavu. “Keshokutwa kuna wito wa baraza.”

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Rhoda akapigwa na bumbuwazi. “Kweli?”



“Ndio.”



“Umepata wapi hizo taarifa? Mbona Phares hajaniambia.”



“Nakaa, nakula na kulala humu kasrini. Natambua kila korido.”



Rhoda aliinamisha chini kichwa chake akitafakari. Hili jambo lilikuwa ni nyeti na muhimu.



Inampasa ahakikishe kwamba Phares anabakia madarakani, la sivyo, haja zake zote zitakuwa zimekoma. Na kama kuna sehemu ya kuhakikisha hilo, basi ni barazani.



Ila hana nafasi yoyote kwenye baraza. Ni kwa namna gani mawazo na mapendekezo yake yakatasikilizwa na kutiliwa maanani? Anapata mashaka.



“Namjua mzee mmoja tu wa baraza, anaishi nyumba ya tatu mashariki ya kasri hili. Unawafahamu hao wengine?”

“Ndio, nawafahamu. Hawana muda mrefu barazani.”



“Kivipi naweza kuwajua?”



“Kwa kumtumia huyo unayemjua. Ana ushawishi mkubwa barazani kwa uzoefu wake.”



Macho ya Rhoda yalisadifu akili yake inayotatua mawazo. Aling’ata lips kisha akaliza vidole vyake.



“Tuonane kesho.” Aliondoka upesi akishikilia gauni lake lisimkinge kutembea. Alikwea mgongo wa farasi wake mweupe aliyekuja naye, akapotea eneo hilo la utawala.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

.

“Tokea amenikabidhi sijaona chochote. Ndege hasogei na hakuna linalotukia. Nashindwa kuelewa.” yalikuwa maneno ya Sultan aliyekuwa amejilaza kwenye kitanda kikubwa, pembeni yake akiwa na mwanamke mwembamba mrembo, mke wake wa tatu.



Yalikuwa ni majira ya jioni, hali ya baridi ikipuliza kwa mujibu wa vipindi vya msimu. Sultan pamoja na mkewe walikuwa wamejifunika shuka zito la manyoya lililokuwa linajitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana kuwapa joto.



Mandhari yalikuwa yanavutia, vitu vikiundwa na madini ya silva ama vumbi la dhahabu. Chumba kilikuwa kinameta. Nadhani si vema kujadili gharama ya samani hizo kwakuwa zaweza kutupa mishtuko ya moyo.



Mwanamke huyu, mke wa tatu wa Sultan, alikuwa mrembo haswa. Japokuwa hakuwa ametia kiungo chochote usoni mwake, bado alikuwa anavutia. Macho yake kama ya mtu aliyetoka usingizini. Mdomo wake, mdogo mwekundu, ni kana kwamba anabusu muda wote. Nywele zake ndefu nyeusi ya bendera zilikuwa zinamsumbua kiuno.



Macho yasikulaghai, mwanamke ni ndani. Hata kama awe ameumbwa siku Mungu hana msongo wa mawazo, kama ndani ni shetani, uzuri wake unakuwa vumbi peponi.



Mwanamke huyu anamtazama Sultan, kisha anapeleka vidole vyake vilaini kumchezea chezea mwanaume huyo ndevu.



“Pole sana mpenzi wangu,” anasema kwa sauti ya puani. “Sasa umepanga kufanya nini?” aliuliza kiudadisi. Sultan alisafisha koo lake na kutulia kwanza kwa sekunde sita kabla ya kufungua lips zake kavu kusema:



“Nitamfunda adabu, naona ananichezea. Kesho nitatuma jeshi langu likamtie nguvuni. Nitachoma dhana zake zote na kumtia ndani ajifunze.”



Mke akatabasamu kwa mbali. “Sasa kama ukimkamata na kumfunga, utapataje hicho kitu unachokitafuta?” Aliuliza kwa sauti ya upole iliyobembeleza masikio ya Sultan, ila swali hilo lilikuwa gumu, Sultan hakuwa na jibu.



“Sijui nafanyaje. Naelekea kukata tamaa sasa.”



Mwanya huu ulikuwa adhimu kwa mke huyu wa tatu. Alishusha mikono yake mpaka kwenye kifua cha Sultan, akawa anachezea nywele za mwanaume huyo akimtazama kana kwamba chakula kitamu kinachomtesa kwa harufu.



“Mpenzi, huna haja ya kukata tamaa,” alinong’oneza na kuendelea: “Ulifanya makosa kutonishirikisha. Laiti kama ningelikuwa nalijua, ungelishapata kito chako hicho cha thamani.”



Sultan hakuwa amemueleza mke huyu kama anachotafuta ni mkufu, bali kito fulani cha thamani. Baada ya hiyo kauli alimtazama mwanamke huyu kwa macho ya kuguswa, akauliza:



“Ungelifanyaje?” Mwanamke akatabasamu.



“Ningelitimiza wajibu wangu kama mkeo, kwa kukushauri namna ya kupata mwarobaini wa tatizo.”



Sultan alikaa kimya, asitie neno. Kwa muda kidogo kulikuwa kimya, ila mke akiendelea kukanda kifua cha mumewe katika namna lainishi.



“Najua hupendi nikimuongelea mke wako wa kwanza, ila jua ya kwamba Karim ana kiburi cha udugu nawe. Anajua hata asipofanya yanayokupendeza, damu ya mkeo itamlinda. Kama mke wako angelitumia ushawishi wake kwa nduguye, haya yangekuwa historia.”



Bado kulikuwa kimya kwa Sultan.



“Hakuna mtu yeyote mwenye uwezo kumzidi Karim maili za mbali sana pande zote za dunia toka kwenye kasri yako. Haingii akilini kuniambia ameshindwa.”



Hapo Sultan akaguna kuashiria kukubali. “Inahitaji theluthi tu ya uwezo wa Karim kupata hicho kito,” aliendelea kusema Mke huyu wa tatu.



“Auhitaji jeshi, wala vita. Naomba unipe nafasi hiyo nami nijaribu kukusaidia. Pengine naweza leta matokeo chanya.” Sultan alinyamaza kwa dakika kama moja. Alikuwa anatafakari. Alitazama dari kana kwamba anaona ramani. Alishusha pumzi ndefu, akamtazama mkewe kwa macho yaliyojawa uchovu.



“Nisingependa kukubebesha shida zangu ...”



“Hapana!” mke akadakia upesi. “Ni faraja kwangu kumhudumia na kumsaidia mtu ninayempenda.”



Ni kama vile mawazo yalimtinda zaidi Sultan. Aliwaza, ila mwishowe akaamua.



“Sawa, unaweza ukanisaidia.” Mke alimbusu shavuni na kumshukuru. Baada ya lisaa limoja, Sultan alijiandaa na kuondoka akirejea kasrini. Alipoyoyoma, mke huyu naye alijiandaa upesi, akiwa ameongozana na walinzi wake wanne, alikwea farasi wake na kuanza safari ya kuelekea kaskazini ya mbali na makazi yake.



Alikuwa amevalia gauni refu zito, jeupe kwa rangi. Kola yake ilikuwa na mawe madogo madogo mengi yenye rangi ya dhahabu. Juu ya gauni hilo alivalia koti kubwa lenye manyoya mengi ya mnyama. Nywele zake ndefu alikuwa amezibana. Uso wake usiwe na kikolombwezo chochote, ila alipendeza. Miguu yake mirefu ilikuwa imefunikwa na viatu imara vya ngozi.



Safari yake ilidumu kwa masaa manne, alifika ikiwa ni usiku. Mbele ya nyumba ndogo yenye chumba kimoja na sebule, ila ikiwa imefumwa kwa ustadi. Mlango wake ulikuwa mkubwa, madirisha madogo. Bomba kubwa refu la kutoa moshi lilikuwa linatazama angani.



Mke huyo wa tatu wa Sultan aliwaamuru walinzi wake wangojee hapo nje wakati yeye akienenda ndani. Walinzi wakatii. Aliugonga mlango mara tatu akiita bibi. Punde mlango ukafunguliwa na mzee wa makamo ya umri wa miaka hamsini na ushee.



Nywele zake zilikuwa nyeusi, mvi za kutafuta. Alikuwa amejitanda shuka kubwa lililofunika mwili wake wote kuanzia shingoni mpaka miguuni. Uso wake ulifanana na wa mgeni wake. Japo alikuwa mzee, hakuwa haba kwenye kujitunza.



Alijikuta anatabasamu punde tu alipomwona mgeni. Alimkumbatia na kumkaribisha ndani kwa furaha.



“Umenikumbuka mjukuu wangu, mbona muda huu?”



“Nina shida, bibi,” alisema mke wa tatu wa Sultan. “Nimeshindwa kuvumilia mpaka usiku ukome.”



“Shida gani hiyo? Ni kuhusu Sultan?”



“Ndio.”



“Umefanya nini tena? Sina nguvu ya kukimbizana barabarani kwenda kuwasuluhisha, mjukuu wangu.”

“Sio hivyo, bibi. Kuna kitu nataka unisaidie. Ni muhimu sana. Lina uzito sawa na lile ulilowahi fanya miaka miwili nyuma.”



Kabla ya miaka hiyo miwili nyuma, mke huyu wa Sultan hakuwa kitu mbele ya jamii. Hakuna aliyekuwa anamjua wala kumheshimu zaidi tu ya kutamaniwa na wanaume mbalimbali, aliowaona wa hovyo.



Siku moja Sultan akiwa anakatiza maeneo ya karibu na bibi huyo aliyekuwa anaishi na mke huyu wa tatu wa Sultan, ndipo maisha yalipobadilika. Bibi huyu akiwa anafahamu fika mjukuu wake ni mrembo, na Sultan angevutiwa naye, basi anaamua kutumia ulozi.



Anasema maneno kadhaa akiwa ameshikilia pindo la gauni lake chakavu, basi Sultan anakatiza kando kando ya kisima alipokuwapo mjukuu wake akifua nguo. Na kutokana na joto la kipindi hicho, binti huyo alikuwa amevalia nguo nyepesi iliyoonyesha umbo lake zuri.



Sultan alisimamisha msafara wake akaagiza aitiwe mwanamke huyo aliyemuuliza maswali kadhaa kisha akaondoka. Baada ya siku moja, vibaraka wa Sultan walitumwa kwenda kumtwaa mwanamke huyo na hayo mengine yote yakawa historia. “Mjukuu wangu, unanitisha,” alisema bibi. Mjukuuye akamshika mkono.



“Si kikubwa, bibi. Kuna kitu Sultan anakitaka. Kinamnyima furaha na amani kabisa. Endapo nikimsaidia kupata kitu hicho, ni wazi nitakuwa nimeteka nafasi kubwa ya moyo wake. Mtoto wangu anaweza akarithi kiti cha utawala.”



Bibi aliukunja uso wake.



“Kitu gani hicho?”



“Ni kito fulani cha thamani. Je bibi una namna yoyote ambayo inaweza ikasaidia kukipata na huku kipo mbali na himaya yetu?”



“Inawezekana, ila kuna baadhi ya mambo inabidi kwanza yawekwe sawa.”



“Yapi hayo?”



“Punguza hamu, mjukuu wangu. Bila shaka leo unalala huku. Pumzika, tutayajenga.”

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

.

.

.

Baada ya kufuatilia kwa takribani siku nzima pasipo mafanikio, ikiwa ni usiku sasa, vikongwe watatu wa Tanashe wanafika kwenye mpaka wa mashariki wa himaya yao. Walidumu hapo kwa muda mchache kabla hawajagundua nyayo za binadamu.



Nyayo hizo zilikuwa ni za mguu wa kike. Walizitazama wasichukue muda mrefu kuugundua ukweli mchungu, nyayo zile zilikuwa za mtu wanayemtafuta, si mwingine bali Malkia. Hakuna mwenye nyayo kama zile Tanashe nzima.



“Ameshaondoka, imewezakanaje?” aliuliza kikongwe mmoja. Nyuso zao zilijawa na huzuni.



“Sijui ni nini kilitokea. Siju ni nini kimempa uhai?” Kulikuwa kimya kwa muda kidogo kabla mmoja hajauliza:



“Itakuwa tulifanya makosa kumlaza na mkufuwe. Hakuna kingine kilichompa uhai zaidi ya mkufu ule. Ule ni mkufu wake na hatukufanikiwa kuchukua kibali hicho kwasababu ya Faki.”



Kukawa kimya tena kidogo. Upepo ulikuwa unapuliza, giza lilikuwa limetanda.



“Kwanini hatukumuona upesi kwenye rada zetu na ilhali alikuwa ndani ya Tanashe? Au atakuwa alitoka nje ya himaya hii tukiwa kwenye mapambano?”



“Yote yanawezekana. Kama bado alikuwa ndani ya Tanashe wakati tunamsaka, basi itatuwia vigumu sana kumrudisha mikononi mwetu. Maana itakuwa inamaanisha hatuna uwezo wa kumuona tena. Sijui uwezo huo ameutoa wapi?”

Akadakia mwingine:

“Na Sijui atakuwa ameelekea wapi? Kufanya nini?”



Walitamani sana kufahamu lakini haikuwezekana. Hawakujua kwa wakati huo Malkia alikuwa juu ya farasi aliyemkwapua hatua chache baada ya kutoka Tanashe akielekea himaya ya masonara.



Mwanamke huyo kifuani alikuwa amebebelea mkufu. Ngozi yake ilikuwa laini inayong’ara. Uso wake ulikuwa na uhai. Nywele zake zilikuwa ndefu, nyeusi. Alikuwa ni yule Malkia! Malkia wa Goshen tuliyekuwa tunamfahamu, mzuri atakayekufanya uache shughuli zako kumtazama.



Alikuwa amedumu kwenye safari hii kwa masaa kadhaa, na sasa alikuwa anaingia msituni kabla hajaumaliza na kudaka jangwa. Alipomaliza msitu huo mpana wenye miti na mandhari ya kuogofya, alimuacha farasi hapo atumie miguu yake kusema na jangwa.



Hakugeuza shingo nyuma kutazama alipotoka. Hakuwa na dalili hata ndogo za kuogopa. Baridi kali lililokuwa linampiga lilimfanya ajikunyate, lakini si kusitisha safari yake. Alizamisha miguu yake ndani ya mchanga na kuichomoa. Hakuchoka.



Safari yake inakuja kukoma katikati ya usiku. Alisimama kana kwamba aliona jambo. Alichota mchanga akaujaza kiganjani mwake kisha akaumwagia mbele yake kama hatua moja, mara shimo kubwa likatokea hapo. Lilikuwa ni lile lililommeza Zura.



Malkia alirusha macho yake ndani ya shimo hilo, hakuona kitu. Kulikuwa ni totoro haswa. Alisimama hapo kama anayechambua kiza anachokiona. Mara akajirusha kuzama humo ndani!



Kishindo kiliashiria amefika chini. Alikuwa haonekani kabisa. Hakukuwa na mwanga wowote ule. Punde baada ya kishindo hicho, sauti ya farasi inasikika. Sauti hii haikomi baada ya mara moja, inaendelea zaidi na zaidi. Inakuwa kelele sasa.



Malkia anasogea taratibu, vishindo vyake vya miguu vinasema. Haichukui muda mrefu, kidani chake cha mkufu kinawaka, sasa anaona anapopakanyaga, anaona pia anapoelekea. Ila mbele bado ni kiza. Haoni komo la shimo.



Anatembea kama hatua nane akiangaza, mara anasikia vishindo vya watu vikikatiza upesi, anasimama! Anaminya kidani cha mkufu wake na mara kunakuwa giza totoro. Alitembea hatua mbili, akaachia kidani hicho, mara mwanga ukachipuka haraka. Uso kwa uso Malkia akaona kundi la watu wa ajabu mbele yake!



Tabasamu linamtoka usoni.

.

.

Watu hawa walikuwa ni wakazi wa humo shimoni. Nyuso na miili yao ilikuwa kama fuku. Haijulikani ni lini waliwahi toka nje wakaona mwanga wa jua. Japokuwa tulipata kuwajua watu hawa pale walipomtia Zura nguvuni, ila hii jamii ilikuwapo, haswa wakielezewa vizuri vitabuni.



Ni miaka kadha wa kadha iliyopita. Kwa mujibu wa imani ya hawa watu wa shimoni, binadamu aliumbwa kwa mchanga, hivyo basi ndani ya mchanga ndipo mahali anapotakiwa kuishi. Ndipo kwenye uhai wao. Harufu ya mchanga na udongo ndiyo sahihi kwao, na si marashi ya ‘hovyo’.



Kwa karne lukuki jamii hii imekuwa chini, ikidharauliwa, ikipuuzwa na kutotiliwa maanani. Imekuwa inayodharauliwa na hata wengine wakidhani viumbe hawa ni simulizi tu, hawajahi kuwepo! Sasa hii ilikuwa ni fursa yao ya kurudi na kuudhirishia ulimwengu kwamba wapo, na ni wenye nguvu kuliko ilivyowahi kuwa.



Watadhihirisha hili wakiupata mkufu. Mkufu ambao wamekuwa wakifuatilia kwa muda mrefu kwa macho yao ya tatu. Walijua Zura waliyemteka, atamleta Malkia. Na kweli sasa Malkia amekuja, yu mbele yao.



“Tunaomba mkufu!” alisema mwanamke mwenyeji akimnyooshea Malkia kiganja cha mkono wake. Mwanamke huyo alikuwa anatisha kiasi cha kutosha kabisa kumtishia mtoto anayegoma kunywa uji.



Meno ya mwanamke huyo hayakueleweka rangi. Macho yake yalikuwa mekundu uso ukiwa umefunikwa funikwa na mapande ya mchanga. Wenzake nao pia walikuwa vivyo hivyo kimavazi na kimuonekano.

Mwanamke huyu pasi na shaka ndiye alikuwa kiongozi. Ungeweza kumtambua kwa wepesi kwa nywele zake, aina ya rasta, ndefu zilizokuwa zinagusa kiunoni. “Mkufu upi unaozungumzia wewe?” aliuliza Malkia. Uso wake ulikuwa umejaa kebehi ila mikono yake ikiwa imejiandaa kwa ajili ya vita.



Kwa wakati huo bado farasi alikuwa anaendelea kulia, zaidi na zaidi.



Katika namna ya kipekee kabisa, Malkia anatetema maneno kadhaa yasiyoeleweka, maneno haya yalikuwa kwenye lugha isiyofahamika. Mara ghafla, anawaka kama jua! Wenyeji wanaficha macho yao kwa ukali wa mwanga, pale mwanga unapozima, taswira ya Malkia inaonekana akiwa amevalia nguo za mapambano mkononi akiwa amebebelea panga refu linalong’aa.



Nywele zake zilikuwa zimepigwa pasi vema. Nguo yake ya ngozi ilikuwa imembana katika namna vema ya kumlinda. Sketi yake ilikuwa imecharangwa, na kiunoni ikikobelewa na mkanda wa chuma. Miguuni alikuwa amevalia buti nyembamba za ngozi zenye ncha ya chuma. Kichwani alikuwa amevaa shada la malkia: rangi ya dhahabu lenye ncha ya msalaba mdogo.



Alikuwa mithili ya Malkia wa shaba! Malkia wa falme kubwa ya uajemi!



Vita ilianza, mtu mmoja akipambana na lukuki. Malkia alikuwa mwepesi mno kucheza na ncha ya panga lake. Hakuna shambulizi liliilomgusa hata kidogo. Kila mkono uliomgusa ulikatiwa chini, kila adui aliyesogea karibu aliishia kulazwa chini hajiwezi.

Mkuu wa wenyeji wa shimoni, yule mama, alikuwa amesimama kando akitazama namna wapambanaji wake wanavyopukutishwa. Ilikuwa ni kama miujiza. Watu wake walikuwa wenye kasi mno, ila bado hawakuweza kumkabili Malkia aliyekuwa akiruka, kupotea, na kurusha panga lake kana kwamba mkufunzi mkubwa.



Kwa namna alivyokuwa akishuhudia, mwanamke huyu kiongozi, akaona hitaji la kutafuta namna ya kufanya. Baada ya dakika kama tano, Malkia anawamaliza maadui aliokuwa anapambana nao, ambao wote wanageuka kuwa michanga wakitengeneza kifusi. Anarusha macho yake huku na huko kumsaka mwanamke yule kiongozi, hamuoni!



Alitazama huku na kule. Alisogea akaangaza, bado hakuona jambo. Haikujulikana ni wapi mwanamke yule alipoelekea. Baada ya Malkia kutofanikiwa kumuona adui yake, aliamua kuendelea na safari. Alifuata sauti ya farasi, lakini bado mkononi mwake akiwa amebebelea panga lake refu katika njia ya tahadhari.



Alipiga takribani hatua tano. Mara nyuma ukutani, macho yanafunguka na kumtazama Malkia. Usingeweza kubashiri kama pale kuna mtu. Kumbe ndio alikuwa amejificha mwanamke yule kiongozi!



Rangi ya mwili wake ilikuwa ndiyo ile ile na ya ukuta, mchanga! Endapo akifunga macho basi usingeweza kabisa kabisa kusema kama kuna mtu papo. Alimtazama Malkia kwa macho makali. Malkia akisogeasogea mbali, basi akawa anayafumba macho hayo na punde basi tunayaona macho hayo karibu tena na Malkia.



Mtu huyu alikuwa anasogea ukutani!



Malkia alisonga na kusonga na safari yake. Alikaribia kabisa sauti ya farasi. Alipochukua kona yake ya kushoto, shukrani ziende kwa mwanga wa mkufu, akaona banda la ukubwa wa wastani. Ndani yake lilikuwa limemtunza farasi mkubwa mweupe anayevutia.



Mara tabasamu linachipuka kwenye uso wa Malkia. Alikuwa ni farasi wake, Rob! Farasi aliyekua naye tokea utotoni. Mnyama anayemchukulia kama familia yake. Kwake kumwona farasi huyo ilikuwa ni miujiza, hakutegemea kabisa! Alijikuta akijawa na furaha mno. Machozi yalimlenga. Farasi naye alipiga kelele za furaha.



Pasipo kupoteza muda, Malkia alianza jitihada za kuuvunja mlango amweke huru farasiwe. Alitumia kitako cha panga kutwangia komeo. Alipiga mara ya kwanza na pili, komeo likatenguka. Ila kabla hajamalizia, mara ghafla anapigwa na rungu nyuma ya kichwa, anadondoka chini kama mzigo.



Macho yake yanapoteza uwezo, anaona maruweruwe! Mwili nao unakosa nguvu anashindwa kujinyanyua chini. Anabakia akigugumia kwa maumivu akijibaraguza.



Sauti kali ya cheko ilivuma toka kwa mwanamke yule mchanga. Sasa alikuwa anaonekana vema baada ya kujibandua toka ukutani. Alimtazama Malkia aliyekuwa hajiwezi, akang’aka:

“Amka sasa!” Aliangua tena kicheko. Malkia alijitahidi kunyoosha mkono kufuata panga lake lililokuwa kando, mara adui yake akalipiga teke panga hilo kwenda mbali.



Mwanamke huyu aliyeumbwa kwa mchanga, sasa alikuwa amejiona yeye ni mshindi. Ilikuwa imebakia kitu kidogo sasa kumaliza kazi. Alinyanyua mkono wake wa kuume, uliobebelea rungu zito, tayari kwa ajili ya kummalizia Malkia aliyekuwa hajiwezi pale chini.

Kabla mkono huo haujatekeleza kazi, ghafla anasikia sauti ya mlango wa banda. Anatazama huko. Kabla hata hajapumua, uso kwa uso alikumbwa na farasi aliyemsukuma na kumrushia mbali kama pande la gogo!



Farasi wa Malkia alivunja mlango uliokuwa umebakizwa na komeo goigoi. Mwili wake mzito na wenye nguvu ulitosha kabisa kufanya tukio hilo, hakuwa radhi kumuona Malkia akiuawa mbele ya macho yake. Alipiga kelele kali akisugua kwato za miguu yake kwenye udongo.



Mwanamke yule aliyeumbwa na michanga akanyanyuka kwa hasira. Macho yake makali yalimtazama farasi aliyemjeruhi. Alikwapua rungu lake lisilofahamika wapi alipolitoa, akamuenendea farasi kwa pupa. Loh! Hakufika. Mara akaanza kupuputika kuwa mchanga!



Ncha ya panga la Malkia lilikuwa limetoboa mgongo wake na kutokea kwa mbele, tumboni. Malkia alikuwa ameshafika nyuma yake na kumshindilia chuma hicho mwilini. Kasi yake ilikuwa ya kushangaza sana, hata adui yake hakupata kubashiri.



Alipapasa kichwa cha farasi wake, akasema:

“Anayetaka kukudhuru, inabidi apitie kwangu kwanza.” Alimkumbatia farasi wake kwanguvu. Alimkwea na kuanza kusaka ndani ya eneo hilo kumsaka Zura. Eneo lilikuwa kubwa mno kuliko alivyotarajia. Alizunguka sana pasipo mafanikio. Alipaza sauti yake kuita, lakini bado hakufua dafu, akakata tamaa.

Akiwa anarudi alipotokea, yani kwenye mdomo wa shimo, akapata wazo. Aliona ni vema kunena na mkufu wake. Aliuvua akaufichama kwenye kiganja akiacha kauwazi kadogo alimotia mdomo na kunong’oneza:



“Zura, Zura, Zura upo wapi?” Aliposema hayo alitulia kwa dakika moja kabla hajarudia tena kunong’oneza:



“Zura, Zura, Zura upo wapi?” Sauti yake japokuwa ilikuwa ya kunong’oneza, ilifika kwenye kila kona ikibembeleza kuta. Aliweka mkono wake huo uliofichama mkufu sikioni, akasikia sauti kwa mbali ikigugumia. Ilikuwa ni ya Zura! Alisema na moyo wake. Alizidisha sauti yake kwa kusema:



“Zura! Zura! Zura, upo wapi? Zura! Zura! Zura, upo wapi?”



Sauti yake ilifika vizuri kwenye masikio ya Zura aliyekuwa amelala kizani. Zura alikuwa amechoka mno kiasi cha kushindwa kuongea.



“Zura! …” Malkia aliita, kabla hajaendelea, sauti ikamjibu kwa kukoroma:



“Malkiaa … aa … Malk …” Malkia alichanganyikiwa.



“Upo wapi?” aliuliza kwa pupa. Bado sauti ya Zura ilikuwa ni ya kukoroma, hakuweza kuisikia vema. Aliendelea kuuliza na kuuliza, akaambulia la maana moja:



“Nipo kwenye shimo, shimoni.” Baada ya hapo Malkia hakusikia lingine la maana zaidi tu ya pumzi ya Zura iliyokuwa inafoka kwanguvu.



Alitafuta na kutafuta hilo shimo ndani ya shimo kwa dakika kadha wa kadha. Alikuja kugundua mahali fulani penye uchohoro finyu, hilo ni baada ya farasi kusimama hapo akigoma kuondoka.



Alishuka toka kwenye farasi wake akapenya uchochoroni. Alikutana na ngazi zilizomzamisha shimoni, huko akamkuta Zura akiwa amelala chini.



“Zura!” Malkia alijikuta akiita kwa furaha. Alimgeuza Zura akamtazama usoni. Kwa msaada wa mwanga wa mkufu wake akauona uso uliochoka, macho yaliyopanda juu na mdomo mkavu mno.



Akamnyanyua Zura huyo kama karatasi akamweka begani. Alitembea naye kurudi huko alipotokea, alipofika kwenye uchochoro akapata kazi maradufu. Ilimbidi amsimamishe Zura ndipo apite naye. Akafanya vivyo na kufanikisha. Alimkweza Zura kwenye farasi kisha naye akafuata, farasi akatimka.



Ndani ya muda mfupi, walifika kwende domo la shimo. Mwanga wake ulikuwa hafifu mno na kama isingelikuwa kumbukumbu basi huwezi jua kama hapo ndipo unapotulia pindi unapozama shimoni humo.



Farasi alisimama akiwa hajui pa kuelekea. Malkia aliufichama mkufu wake mikononi , kiganjani, akasema maneno kadhaa ya ajabu, mara kufumba na kufumbua yeye, farasi pamoja na Zura wakapotea! Walitokea kwenye fukwe ya bahari wakiwa wamejilaza.



Wimbi la bahari liliwamwagia maji, farasi na Malkia wakashtuka. Malkia alimtoa Zura toka eneo la bahari kisha akaanza kuangaza angaza mahali alipo. Palikuwa ni pageni kwake. Hakuwa anapafahamu kabisa. Palikuwa pametulia na kusionekane kama kuna dalili yoyote ya makazi ya watu.



Alimpakia Zura kwenye mgongo wa farasi kisha akaanza safari ya kutafuta msaada wa makazi. Muda ulikuwa ni alasiri sasa.

.

.

.

.

.

.

.

. ***

.

.

.

.

*** .

. .

.

. “Bibi, mimi naenda,” ilisema sauti ya kike ndani ya kijumba kidogo maridadi. Sauti hii ilikuwa ni ya mke wa tatu wa Sultan Mansoor aliyekuja kuonana na bibiye kwa ajili ya msaada ghafi.



“Mbona mapema hivyo mjukuu wangu? Haungoji jua lichomoze kuondoa hili baridi?” alisema bibi akiwa amevalia shuka zito lililomfunika gubigubi. Macho yake yalikuwa mekundu yakionyesha ametoka usingizini. Miguu yake ilikuwa ndani ya viatu vyepesi vyenye malighafi ya sweta.



Mke wa Sultan alikuwa amevalia gauni zito jembamba linalombana. Mikono yake ilikuwa imefunikwa na soksi nyeusi za mikononi.



Shingoni alikuwa amejiviringishia kitambaa kizito cha kaki, kichwani akivalia kofia kubwa nyeusi. Shukrani ziende kwa bibi yake anayemtunzia nguo.



“Singoji tena, bibi,” alisema Mke huyu wa Sultan. “Nimengoja vya kutosha. Inabidi niondoke sasa.”



“Aaahaa! Kwakuwa umepata ulichokuwa unakitaka enh?”



“Hapana, bibi! Unataka nikae hapa mpaka lini? Nilimuahidi Sultan kuwa ntampatia suluhisho la tatizo lake haraka. Unataka nipoteze imani yake kama ilivyopotea kwa mke wake wa kwanza?” Bibi akawa kimya. Alimsogelea mjukuu wake akamshika mikono na kumtazama machoni.



“Kuwa makini sana,” alisema. “Hakikisha unafuata kila nilichokuagiza usisahau hata tone.”



“Ndio, bibi. Usijali.”



“Embu niambie nilikuambia nini?”



“Jamani, bibi. Yani nianze kuyasema yooote yale tuliyaongea. Nakumbuka bana.” Bibi alimbusu mjukuu wake kwenye paji la uso kumuaga. Mke huyo wa Sultan akatoka na kuungana na walinzi wake, safari ikaanza kurudi kwenye makazi ya sultana huyu mdogo, mbichi.



Mpaka kwenye majira ya mchana uliokomaa wakawa wamewasili. Kitendo tu cha mwanamke huyu kuingia ndani na kujimwagia maji, Sultan Mansoor anaingiza miguu yake.

Ujio wa Sultan huyo ulimpatia tabasamu pana mke. Alioga vema na kujinyunyuzia marashi. Alivalia nguo sisimuzi tayari kwa ajili ya kumalizia kazi. Kazi ambayo tayari bibi yake alishaimaliza kwa utalaamu wake wa mikono.



Lakini maskini sultana huyu hakujua. Dawa aliyopewa na bibiye aliidondosha njiani akiwa anarejea. Miruko ya farasi aliyempanda ilitoa dawa hiyo toka kwenye mfuko mdogo wa ngozi uliokuwa ubavuni mwa farasi. .

.

.



.

Walitembea kwa muda mrefu wakisaka. Bado Zura alikuwa hoi asiyejiweza juu ya farasi aliyekua anatembea kwa madaha ya uchovu, basi ikawalazimu wapumzike maana majira hayakuwa haba kwani jua lilikuwa kali la utosi na hawakutia lolote mdomoni.



Waidhoofu. Zura alifungua macho kwa mbali lakini alishindwa kunena lolote. Mdomo wa Malkia ulikuwa mkavu akitamani apate hata tone moja la maji. Viungo vyake vilikuwa dhaifu achia mbali kuuma kwasababu ya kipigo.



"Zura ..." Malkia aliita kwa sauti kavu. Zura hakuitikia. Alimtazama Malkia kwa macho dhaifu.



"Unapajua hapa?" Malkia aliuliza. Zura hakuwa hata na nguvu ya kutikisa kichwa wala kutazama mazingira anayoulizwa. Alimtazama Malkia kisha akafumba macho.



"Kaeni hapa, nakuja," Malkia alijitesa kwa kunena. "Naenda kutafuta msaada la sivyo tutafia hapa." Alinyanyuka akitembea kigoigoi.



Lakini je, alishindwaje kutumikisha mkufu wake kujua makazi ya hilo eneo kama vile alivyofanya akampata Zura? Si kwamba hakujaribu, la hasha! Alishindwa.



Sauti toka tumboni iligoma. Maneno toka kichwani yalipotea. Labda ni kwasababu ya uchovu mzito, na njaa. Ila kiuhalisia bado ni sababu mchekechea.



Shida halisi ni kwamba huwezi tafuta kitu usichokijua. Sawa sawa na kwamba huwezi kukumbuka kitu ambacho hujawahi kukiona, kukisikia ama kukihisi.



Malkia alikuwa mgeni asijue hata kama kuna watu, ni kivipi sasa atawatafuta? Asijue hata kama kuna makazi ya watu, ni kivipi sasa atayatafuta? Jibu lilikuwa moja na pekee, kwa kubashiri tu.







Alitembea kwa muda wa kama nusu saa. Miguu yake ilitapanya michanga mingi tajiri rangi ya kaki. Ilikuwa inazama na kuchomoka. Zoezi hilo gumu halikudumu kwa muda mrefu, akachoka zaidi, akadondoka na kupoteza fahamu.



Upepo ulikuwa unapuliza sana. Vumbi lilikuwa linatimka, na uhaba wa miti ulifanya vumbi hilo kusafiri kwa umbali mrefu likitamba. Hali ya hewa haikuwa inaeleweka kama ni ya baridi ama joto, hivyo basi tuseme tu ya katikati.



Ni punde baada ya Malkia kudondoka, wanaume wawili waliovalia nguo nyeusi kuukuu; makoti na suruali za kubana, wanajiri. Nywele zao zilikuwa hovyo. Nyuso zao zilikuwa zimejazwa masizi. Hivyo basi wakawa wanafanana kama mapacha. Tofauti mmojawao alikuwa anavuta tumbaku.



"Na mimi zamu yangu sasa!" Alisema mwingine akimpoka mwenzake tumbaku mdomoni. Walivutana kugombea tumbaku hiyo, ila ghafla wakakoma. Mmoja aliona mwili wa Malkia kwa mbali.



Aliyeona mwili huo alitabasamu akimtazama mwenzake.



"Ona!" Alinyooshea kidole. Wakajikuta wanafurahi. Walikimbia haraka kuufuata mwili wa Malkia. Walipoufikia, waliukagua kagua wakimgeuza Malkia kana kwamba samaki kikaangoni.



"Mimi nachukua viatu!" Mmoja alisema.



"Mie nachukua mkufu!" Mwingine akadakia. Basi yule wa kwanza akaona kapunjwa. Alichelewa kuuona mkufu ambao mwenzake alikuwa tayari ameshauwahi.



"Hamna, huo mkufu tutagawana!"



"Kwani viatu vyako tumesema tugawane?"



"Unafananisha viatu na Mkufu? Mkufu huo waonekana ni aghali sana!"







"Kila mtu na bahati yake! We umechagua viatu mie nikachagua mkufu!"



"Hapana! Tumbaku uvute wewe, na mkufu pia?" Walianza kuvutana. Aliyechagua mkufu aliuzamisha mfukoni apate mwanya mzuri wa kupambana. Hawakujali tena tumbaku, ikatupiwa huko. Waligaragazana mpaka pale walipopata fahamu na akili.



"Tuondoke kwanza eneo hili. Si salama!" Wakaondoka zao wakiwa wamebebelea mkufu na viatu vya Malkia. Walimuachia Malkia nguoze na panga lake kando. Wakatokomea.



Lilipita lisaa limoja kavu. Wanawake wawili juu ya farasi mweusi, wakiwa wamebebelea chupa kubwa za maji, walitokea wakishika barabara ipitayo kando kidogo na mwili wa Malkia usiojitambua kwa lolote. Wanawake hao walikuwa wamebebelea vifurushi vikubwa viwili vilivyofumbatwa kwa nguo nyeusi.



Walikuwa ni wafanya biashara. Walitoka mbali kupeleka bidhaa zao. Walibebelea pia silaha, jambia, kwa ajili ya usalama wao wawapo njiani. Walijifunika na mashuka meusi na viremba. Nguo zao zilikuwa za watu wa tabaka la kati.



"Atakuwa amepoteza fahamu," alisema mwanamke mmoja.



"Na ameibiwa pia," akadakia mwanamke mwengine. Walishuka toka kwenye farasi wao wakamsogelea Malkia.



Walimkagua kwa macho yao yaliyokolezwa wanja. Hawakuwa wameshitushwa maana ilikuwa ni kawaida kuwapata watu wakiwa wamejifia ama kujidondokea ndani ya eneo hilo, nusu jangwa. Walimtazama Malkia kwa muda wakagundua alitokea upande gani kwa mujibu wa nyayo za viatu vyake ambavyo havikuwapo.







"Amekosa maji na chakula, kachoka sana. Tumsaidie?" Aliuliza mmoja. Rangi yake ilikuwa nyeupe yenye nyeusi ya mbali.



"Wakina Jelly wameshamkwapua," alisema mwingine. Huyu yeye alikuwa mweupe pe! Na kidogo mtu mzima.



"Umejuaje?"



"Hii tumbaku hapa! Na hata hizi nyayo ni za kwao," alisema mwanamke huyo akionyeshea vitu alivyovitaja.



"Washenzi sana hawa, ila mwisho wao unakaribia wao na kundi lao. Hakuna refu lisilo na ncha." Aliendelea kusema mwanamke huyo mweupe.

.

.

.

.

.

.

---

.

.

.

.

.

.



Malkia anaamka na kujikuta ndani ya chumba kikubwa asichokijua. Anaangaza kila pande; kando yake anamuona pia Zura. Haraka alijipapasa kifuani, hakukuta kitu. Alikurupuka kitandani akauendea mlango. Alitulia hapo akisikiliza sauti zilizokuwa zinateta huko nje.



Hakukuwa na silaha aina yoyote humo ndani. Maongezi aliyokuwa anayasikia yalikuwa ni kuhusu biashara, hakuna lolote kuhusu mkufu wala kumhusu yeye. Hivyo bado akawa njia panda.



Watakuwa wamenikwapulia mkufu wangu? Alisema kifuani. Ila kwanini wamenileta mpaka hapa kama ni watu wenye nia mbaya? Tena mie pamoja na Zura! Lakini ... lakini mkufu wangu umeenda wapi?



Akiwa hapo anajipa maswali, mlango ulifunguliwa. Alikuwa ni mwenyeji wake, mwanamke yule mweupe wa kufifia.



Alimtazama Malkia kwa tabasamu, akasema:



"Umeamka!" Kabla Malkia hajasema kitu, mwanamke huyo alipaza sauti kumpasha mwenzake habari njema.



"Ulikuwa hujiwezi kabisa, tumekuokota jangwani. Pole na karibuni sana."







"Ahsante," Malkia alijibu. "Naitwa Fuffy, twende ukamsalimu mama yangu." Malkia aliongozana na mwanamke huyo, Fuffy mpaka huko nje ambapo alikutana na mwanamke yule mtu mzima. Alimsalimu na kisha akaketi kitako.



"Ulikuwa unatokea wapi?"



"Sikumbuki. Tulikuwa tunasafiri na mara nikajikuta hapa baada ya kufumbua macho yangu yaliyopigwa na usingizi," alilaghai Malkia, kisha akauliza;

"Hapa ni wapi?"



"Hapa ni tawala ya Kando. Unaonekana wa tofauti kabisa. Yeyote atakayekuona atajua wewe ni mgeni." Kweli.



Mwanamke huyo pamoja na mwanaye walionekana ni kama watu wenye asili ya India, kwa macho, ngozi na nywele zao. Malkia, pamoja na Zura, asili zao zilikuwa tenge. Ni kama watu wa mchanganyiko wa ngozi nyeupe na nyekundu.



"Tawala yako inaitwaje?" "Goshen - Inaitwa Goshen." Mwanamke huyo akabinua mdomo, "siifahamu. Sijawahi hata kuisikia."

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Je, mmenionea mkufu wangu?" Malkia aliuliza. Macho yake yalikuwa makubwa zaidi akimtazama mwanamke aliyemuuliza swali.

"Sijaona mkufu wako. Sikukukuta nao, wala viatu."



Malkia alinywea. Uso wake ulikuwa mweusi. Alihisi mpweke upesi. Mwili wake ulipoteza nguvu.



"Ni wa thamani sana?" Aliuliza mwanamke.

"Ndio, ni wa thamani mno. Ni zawadi nilipewa, isingependeza ukapotea kwa namna yoyote ile. Inabidi kila saa uwepo shingoni mwangu."



"Pole sana. Kuna wahalifu wawili wamekukwapulia. Wanajulikana kwa jina maarufu la Jellys. Ni wezi maarufu jangwani. Wana kundi lao hatari sana."



"Naweza nikajua wapi walipo?"







"Binti yangu, huwezi kupambana nao. Kwa usalama wako ni bora ukaachana nao. Funika kombe mwanakharamu apite."



"Tafadhali, naomba unisaidie. Hayo mengine nitajua namna ya kufanya."



Mwanamke huyo alimtazama Malkia kwa macho ya mkazo. Alistaajabu namna gani anavyojiamini. Alivuta pumzi ndefu kisha akasema:



"Usijali, nitakuambia. Kula na kunywa kwanza." Malkia hakuwa tayari kufanya vivyo, ila kwa msukumo wa mwenyeji wake, aliridhia. Mpaka kufikia jioni, yeye pamoja na Zura walikuwa wanaojiweza na wenye nguvu. Walionekana ni binadamu sasa.



"Jua linaelekea kuzama," alisema mwanamke yule, ama tumjue kwa jina la mama Fluffy. "Si salama kutembea huko nje. Hautapata hata nafasi ya kufika huko unapopataka."



"Hapana," Malkia akatikisa kichwa. "Uliniahidi utafanya hivyo!" Fluffy alimtazama akamshika mkono.



"Sandarus," aliita. "Hakuna asiyetaka kukusaidia. Sisi ni wenyeji huku, tunafahamu. Wakati huu si mzuri. Labda unafananisha huko utokako na hapa, hapa ni tofauti. Jua likiwa hafifu ni hatari. Wakwapuzi wanazunguka, na hata wauaji."



"Vipi kama wakiuuza ama kuupeleka mbali mkufu wangu?"



"Usipate shaka na hilo," alisema Mama Fluffy. "Huwa wanaenda kuuza vitu vyao vya wizi siku ya nne ya wiki. Huko kaskazini ya mbali huwa na mnada siku hiyo." Kidogo moyo wa Malkia ulituama.



Usiku huo alijifunza kuhusu familia hiyo mwenyeji namna wanavyofanya biashara. Ni wataalamu wanaohusika na kutengeneza urembo kama vile bangili na cheni wakitumia ghafi kama vile shanga, madini ya kopa na hata dhahabu.







Malkia alipata wasaa wa kutazama bidhaa zao. Hakika zilikuwa zinavutia. Zilikuwa zimesukwa kwa ubunifu na namna ya kuvutia sana. Hapo basi Malkia akapata wazo. Wazo aliloliona ni jema kwenye ulinzi wa mkufu wake.



"Naomba unifanyie kitu Fluffy," alisema. Mama Fluffy alikuwa ameshajiondokea kwenda kupumzika. Malkia alikuwa yupo na Fluffy na Zura pekee.



"Naomba unitengenezee mkufu kama ule wa kwangu."



"Siujui."



"Usijali, nitakuchorea. Naomba unitengezee miwili. Naihitaji sana. Nitajitahidi kukulipa." "Wala hakuna haja ya kunilipa, Sandarus. Nitakufanyia maana umekuwa rafiki yangu."



"Sina namna ya kukushukuru."



"Usijali. Ila nina ombi moja tu kwako."



"Lipi hilo?"



"Nitaomba niondoke na wewe. Naomba usiniache hapa kwenye hii tawala." Jambo hilo lilimshtua Malkia.



Alimtazama Zura wakiwa kwenye bumbuwazi. Itawezekanaje hilo? Ila hakutaka kumwangusha binti huyo mapema, akamwambia:



"Fanya kwanza hiyo kazi, mengine yatafuata."

Fluffy alitikisa kichwa kukubali.



"Sawa."

.

.

.

.

.

.

***

***

.

.

.

.

.

.

.

.



Mazingira yalishawekwa tayari kwa ajili ya kikao. Uwanja wa mkutano ulikuwa umerembwa, vinywaji vikitambazwa juu ya meza ndeefu iliyosindikizwa na viti vyenye migongo mirefu.



Vitambaa vyenye rangi ya bendera ya Goshen, viliziba kuta. Kulipendeza. Wahudumu lukuki, wanawake warembo ndani ya sare, walikuwa wamesimama wakishikilia bilauri za mivinyo tayari kwa ajili ya kutoa huduma.







Punde wanaume takribani watano, wazee wa baraza, wakiwa wamevalia majoho ya kaki yenye fito nyekundu shingoni wanatokea na kuenendea viti kuketi. Punde napo, Phares anatokea. Alikuwa amevalia shati jeusi lililokaba shingo pasipo na vifungo. Suruali yake ya ngozi ilimkaa vema, pembezoni ikiwa na mtindo wa maua yaliyodariziwa.



Aliketi na kikao kikafunguliwa kwa kusimama wote na kupeana mikono. "Pasipo kupoteza muda. Wote tunafahamu nini kimetuleta hapa," alisema mzee mmoja wa baraza. Kichwa chake kilikuwa kitupu kisicho na nywele. Alikuwa amejitambulisha kama msimamizi wa tafrija hiyo, yani msema chochote.



"Kama ilivyo desturi yetu. Kila mmoja atajitambulisha ni mzee toka nyumba ipi ya baraza; yaani yupo hapa kuwakilisha upande upi wa tawala. Kisha baada ya hapo, tutakunywa kwa na kuteta kwa nusu saa. Alafu ndipo kazi yetu ya uteuzi na maamuzi itafunguliwa rasmi."



Ratiba hiyo ilifuatwa. Kila mzee alijitambulisha, ikiwemo pia na Phares aliyejinasibu kwa kusema maneno machache tu kuwa yeye alikuwa msaidizi wa marehemu Malkia Vedas. Maswali hayakuulizwa hapo, ratiba ya kunywa ikawadia.



Wahudumu walifanya kazi yao kwa ufasaha. Kila kikombe kilichokauka kilijazwa kwa haraka. Makoo yaligeuka mitaro ya jiji na hivyo basi muda mfupi mbeleni vibofu vikaanza kuajiriwa kuwapeleka watu vyooni.



Kwenye korido ya kuelekea chooni alikuwapo mwanaume mlinzi, yule kibaraka wa Rhoda. Alikuwa amesimama kwa ukakamavu. Macho yake yalikuwa kazini. Mkono wake wa kuume ulikuwa umeshikilia mkuki mrefu mkali. Kiunoni alining'iniza kisu kirefu kilichofunikwa na mfuko mgumu wa ngozi.





Alikuwa hapo akingojea. Mipango yake ilikuwa ni kuchochea uteuzi wa Phares kama kiongozi mpya wa Goshen, kwa njia yoyote ile. Kazi hiyo alipewa na bosi wake, mwanamama Rhoda, punde baada ya njia ya kidiplomasia kufeli.



Subira yake ilivuta kheri. Alimuona mzee mmoja wa baraza akielekea chooni. Alitazama huku na kule kama kuna yeyote anayemuona, alipoona safi, akanyoosha miguu naye kuelekea chooni. Alifungua mlango akazama ndani, kisha akaufunga. .

.

.

.

.

.

***

***"Nani huyo anashindwa kubisha hodi?"



Aliropoka mzee wa baraza akishikilia dhakari yake inayokojoa. Alikunja shingo kutazama, uso kwa uso akakutana na pande la mwanaume aliyesimama kana kwamba mlinzi wa mfalme.



"Kumbe wewe!" Alifoka. "Pumbavu, huna adabu enh? Umechoka kazi!" Kibaraka wa Rhoda hakujibu kitu.



Alidaka koo la mzee huyo kama kuku akamnyanyua juu na kumbamizia ukutani kwanguvu. Kiganja chake kipana kilimeza shingo yote ya mzee aliyeishia kupata taabu kupumua. Alihangaika akitia huruma.



"Sikiliza na uelewe," alisema pande la jibaba. "Sina muda wa kupoteza hapa na wewe. Nimekufuata humu kukuambia juu ya jambo moja tu: mpigie kura Phares. Hakikisha anapita!" Mzee hakuweza kusema jambo kwasababu ya kukabwa.



Uso wake ulikuwa mwekundu mdomo akiutapanya. Mikono yake miwili ilishindwa kuondoa mmoja uliomkaba pasipo kujali namna gani alivyokuwa akihangaika.



"Endapo asipopita, kwa namna yoyote ile, basi jua hautabaki salama." Mwanaume huyo kijakazi wa Rhoda alipomaliza kusema hayo, alimuachia huru mzee. Alibandua kiganja chake kooni akamshudia mzee akidondoka chini akitafuta hewa.



Hakuketi kumsubiri, aligeuka akaondoka. Alipofika mlangoni, aliitwa na sauti iliyokuwa inatoka kwa taabu.



"Kijana!" Akasimama. "Unadhani utatumia mabavu yako kubatilisha kura yangu?" Mzee aliuliza. Bado alikuwa chini ashindwe kujinyanyua.



"Kamwe! Kama wataka kuniua, basi karibu. Nimeshakula chumvi za kutosha. Ila ukae ukijua kwamba, mawazo yangu ni yale yale na nitayasimamia milele kwa faida ya himaya ya Goshen, na si mtu mmoja!"





Mwanaume yule kibaraka wa Rhoda alifungua mlango. Kabla hajatoka ndani, alimtazama mzee huyo wa baraza na kisha akasema kwa sauti ya utulivu:



"Sawa kuhusu wewe, lakini vipi kuhusu mke wako, Rabina, na watoto wako wawili; Asilam na Poogi? Nao unataka wafe?" Kauli hiyo ilimgutua mzee. Hakutegemea kama familia yake ilikuwa bayana kiasi hicho. Alinyanyuka.



"Usije ukathubutu kugusa familia yangu!" Alifoka.



"Kama unataka kunijaribu, nenda kinyume na nilichokuambia. Utawakuta wote mizoga! Kuanzia mkeo aliye nyumbani, mpaka watoto wako wanaoishi upande wa Duke," alisema kibaraka wa Rhoda kabla hajatoka ndani na kuurudishia mlango.



Mzee allipatwa na uoga sasa. Alijihisi yu uchi. Kitendo cha kuambiwa mpaka makazi ya wanaye kilizidi kumzuzua na kumkatia pande hofu. Alisimama akaenda zake. Akiwa anakatiza kuingia ndani ya uwanja wa baraza, alitazamana na mwanaume yule kibaraka wa Rhoda. Mwanaume huyo akamuonyeshea ishara ya uangalizi kwa kunyooshea vidole vyake viwili machoni.



Mzee huyo alijirudisha kwenye kiti chake kikao kikaendelea kama ada. Muda wa kunywa ulikuwa umeshapita sasa na hivyo basi ukawa umewadia ule wa kufanya uteuzi.



Kati ya wazee watano wa baraza, ni wawili tu ndio walikuwa wazima. Wengine wote walikuwa hoi kwa kilevi. Kwa mujibu wa utaratibu, wazee hao wakawa wameshajitoa kwenye maamuzi ya siku. Hivyo basi uteuzi ukawa unaelekea kufanywa na wazee wawili tu.





"Basi na utaratibu uheshimiwe," alisema mzee wa baraza aliyeketi kando na yule aliyetoka kubanwa chooni. Wao pekee ndio walikuwa hai muda huo, pamoja na Phares ambaye aligusa glasi moja tu ya mvinyo kisha akaacha.



"Kama ilivyo ada huu ni wasaa sasa wa kuteua kiongozi mkubwa wa Goshen; mfalme. Mfalme atakayekuwa juu ya nyumba zote ndani ya mipaka yetu, kuanzia kaskazini mpaka kusini, magharibi mpaka mashariki.



Mfalme atakayetuwakilisha nje ya mipaka na kutuongoza ndani ya mipaka. Ambaye neno lake litakuwa sheria, mkono wake utakuwa ngao." Baada ya kusemwa maneno hayo, alitajwa Phares peke yake kama mtu anayewania ama kupendekezwa kwa ajili ya nafasi hiyo. Hakukuwa na mwengine, hivyo basi wajumbe wakawa na fursa ya kupembua na kumchambua mlengwa, Phares.



Aliulizwa kuhusu historia yake, akashindwa kuitaja. Hakuwa anakumbuka kitu kuhusu historia yake. Si lolote, si chochote. Hakuona haja ya kuongopa, akasema ukweli.



"Tangu nipate fahamu zangu, sijawahi kujua kingine zaidi ya Goshen. Nimejikuta najua himaya hii nikiwa katika umri mkubwa.



Nilijikuta namjua Vedas kabla ya mtu mwingine yeyote. Hakuna aliyewahi nambia asili yangu, chimbuko langu. Kila niliyemuuliza kuhusu wazazi wangu, hakuwa anajua.



Nilipomuuliza Vedas, alisema yeye ndiye mama na baba yangu. Sikuwahi kumuelewa mpaka anakufa." Maneno hayo yalizaa tafakuri kwenye vichwa vya wajumbe. Walikosa cha kuuliza maana hakuwepo wa kumuuliza. Ilibidi kikao kiendelee.





Waliuliza kuhusu uzoefu wa mtahiniwa kwenye mambo ya uongozi, naye Phares akapata kuwaonyesha juu ya uwezowe kipindi chote cha utawala wa Vedas. Namna alivyofanikiwa kupambana na kuwashinda maadui.



Baada ya hapo kukawa hamna tena maswali, kura ikapigwa. Kila mdomo wa mjumbe ulikiri kuridhishwa na Phares, kwahiyo mtahiniwa huyo akawa amefaulu.



"Kwanzia sasa wewe ni mfalme mteuliwa. Utakuwa mfalme kamili pale utakapoapishwa mbele ya hadhara! Siku tano baada ya kikao cha uteuzi." Akadakia mzee mwingine, yule aliyekabwa chooni.



Sauti yake ilikuwa mfifia. Uso wake ulikuwa na ajizi na ayasemayo. "Kwa mujibu wa kanuni na taratibu, hakuna yeyote mwenye uwezo wa kutengua maamuzi ya baraza. Na hivyo basi maamuzi yake yaheshimiwe."



Baada ya hapo, kikao kikafungwa kwa kupeana mikono. Muda mfupi mbeleni tarumbeta kubwa likapulizwa kuihabarisha Goshen yote kwamba kiongozi mpya amepatikana.



Tarumbeta hili lililia mara tatu likigeuziwa kila pande. Basi kila kona ya Goshen wakajua nini kilikuwa kinaendelea. Walikuwa na hamu kubwa ya kumjua kiongozi wao mpya.



Sauti hiyo ya tarumbeta ilipofika masikioni mwa Rhoda, ilizaa tabasamu pana. Alijikuta akiangua kicheko yeye mwenyewe. Alisugua viganja uso wake uking'aa kwa furaha.



"Hatimaye," alijisemea. "Hatua moja baada ya nyingine. Sasa Goshen inakaribia kujaa kiganjani mwangu." Alichoropoa chupa ya mvinyo toka kabatini akagida. Alicheka tena.







"Ni punde ... si muda mrefu. Himaya zote zitakuwa chini yangu. Chini yangu mimi Rhoda," alisema kwa msisitizo kana kwamba kuna mtu alimkatalia.



Alikunywa na kunywa, akiwa anamalizia chupa ya mvinyo wake huo, kibaraka wake akiwa ameongozana na wanawake wawili wanafika nyumbani kwake. Wanawake hawa walikuwa juu ya farasi mmoja, wakati pande lile la mtu, kibaraka, akiwa juu ya farasiwe.



Wanawake hawa wawili ni miongoni mwa wale walikuwamo kwenye mkutano wa baraza la wazee wakihudumia. "Karibu sana!" Rhoda alipaza sauti. Aliwakarimu wageni wake kwa bashasha. Aliwahudumia kwa kuwamiminia mvinyo kwenye glasi ya kila mmoja.



"Ilikuwa ni kazi nyepesi, haikutuwia vigumu," alisema kibaraka kisha akaisindikizia na fundo kubwa la mvinyo.



"Ndani ya muda mfupi tulikuwa tumeshamaliza kila kitu.



"Bila shaka mlifanya kama nilivyowaagiza," alidakia Rhoda.



"Ndio, mam," akajibu mwanamke mmoja miongoni mwa wale wawili. "Punde baada ya mzee wa kwanza wa baraza kutoka, tulipata mwanya wa kuwatilia madawa kwenye vinywaji wale wawili uliotuagiza.



Tulipata shaka juu ya yule aliyeenda chooni, ila Nade alimalizana naye huko huko. Hivyo hakukuwa na shida kabisa." Rhoda akatabasamu.



"Hongereni sana kwa kazi nzuri. Ila si kwamba tumemaliza, hapana. Ni hatua moja tu katika safari ambayo ndio kwanza inaanza. Tuwe makini sana, nitawahitaji zaidi."





Aliposema hayo akabandika matabasamu kwenye nyuso za wageni wake kwa kusema;

"Ntawapa mara mbili ya ujira tuliokubaliana, maana mmenifurahisha."

.

.

.

.

.

.

***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

.

.

.

.

.

.

Usiku ulikuwa umekua zaidi. Tungelinganisha na majira ya huku, basi tungesema ilikuwa ni saa saba ya usiku, tena yenye madakika zake, si changa.



Wakati wengine wakiwa wamejifunika na wapo juu ya vitanda kuitafuta asubuhi, vibaraka wawili wa Karim, mganga maarufu, walikuwa ndani ya msitu mkubwa wakijikunyata.



Hali ya hewa ilikuwa ya baridi msituni humo. Pia msitu ulikuwa umelowana kwa mvua zilizokuwa zinanyesha mara kwa mara. Hakukufaa kwa malazi ya binadamu. Sauti za vyura zilikuwa zinaita. Na hata wadudu walikuwa wakirandaranda huku na kule.



Vibaraka hawa wawili wa Karim walikuwa wamejifunika na blanketi moja zito. Ila chini walikuwa wamelalia kitambaa chepesi juu ya udongo mbichi, hivyo basi mwili wao bado ulikuwa unakosa joto jema kupambana na hali ya hewa ya muda huo eneo hilo.



Ila kutokana na uchovu mzito wa kutembea juu ya migongo ya farasi kwa siku kadha wa kadha, walikuwa hoi na mazingira hayakutosha kuwanyima usingizi. Walilala kando ya farasi zao.



Kuna muda fulani, vyura waliacha kulia, na wadudu waliacha kukatiza, kukawa kimya. Ila muda huo hakuwa unadumu sana, ni takribani kama dakika moja tu kisha mambo yanaendelea kama kawaida.



Hali hii ilitokea kwa mara tatu. Ilipotokea kwa mara ya nne, mambo hayakuwa kama awali. Kuna kitu cha kushangaza kilijiri. Kitu hichi hakikujulikana kama ni binaadam ama kiumbe kingine. Kilikuwa kinang'aa kwa kuwakawaka kimulimuli.





Umbo halisi la kitu hiki bado lilikuwa ni tenge. Kiliwasogelea vibaraka wa Karim katika hali ya kuwakawaka na kuumiza macho. Kilipokaribia, joto liliongezeka na punde vibaraka wakaanza kuvuja jasho kwa wingi kama vile wamemwagiwa maji.



Mmoja alikurupuka. Alitazama kando na kando, hakuona kitu. Sauti za vyura na wadudu zilikuwa zinaita kama kawaida. Alipotazama takribani kwa dakika moja pasipo kuona lolote, aliamua kujilaza.



Alilala kwa dakika mbili tu, hali ikaanza kubadilika tena kwa joto kuongezeka. Alikurupuka akaangaza. Mwili wake ulikuwa unavuja jasho mno, ila ajabu akiamka alikuwa anakuta hali ya hewa baridi kupita kiasi. Fika akajua mambo hayako sawa. "Saud, amka!" Alimkurupua mwenzake kwa kumsukumiza sukumiza mgongo.



"Nini bana..." Saudi akalalamika kimang'amung'amu.



"Amka tuondoke!"



"Twende wapi usiku wote huu? Tulale bana mie niko hoi mtepe," alisema Saud. Yote haya alikuwa ananena akiwa amefumba macho. Sauti yake ilikuwa ya kunguruma na mwili wake ukiwa teketeke dhoofu.



"Saud, tuko kwenye himaya ya watu," alisisitizia mwamshaji. Hakuonyesha lepe la masikhara hata kidogo. "Amka tusonge, hapa si salama!"



"Mie siendo popote bana ... we nenda! Niache!"



Alifoka Saud. Bado alikuwa yu usingizini. Macho yake hayakuwa yamefunguka. Hata mdomo wake ulikuwa umebanwa kivivu, alikuwa anaongea aking'ata meno.





Haraka mwamshaji aliamka akasimama. Alitazama kila pande. Japokuwa hakuona kitu, lakini moyo wake ulikuwa unapiga kwa kasi. Alikuwa anahisi kabisa kuna kitu. Kuna wakati vinyweleo vilikuwa vinamsimama! "Saud, mie naenda!" Alisema akimsukumiza mwenzake kwa mguu. Saud aliitikia kwa miguno pasipo kujihangaisha.



Mwamshaji alimfuata farasi wake akamfungua kamba apate kuondoka. Ila kabla hajayoyoma, aliona ni vema tena kumshitua Saud, mwenzake. "Saud, unakumbuka Karim alituambia nini tukiwa njiani? Tupo kwenye himaya ya wengine, tuwe makini. Ni vema tukaepusha shari kadiri tuwezavyo. Si kila mara kinga zetu zitafanya kazi." Mwamshaji alikuwa anaongea na sikio la kufa, hakueleweka. Mara hii Saud hakuonyesha muitikio, hata kwa kuguna. Alikaa kimya kana kwamba maiti.



Mwishowe, mwamshaji alijiondokea akiongozana na farasi wake. Punde hakuwa anaonekana. Saud alibakia peke yake sasa akikoroma kwa uroho wake wa usingizi. Alijikobeka blanketi mpaka shingoni. Alijikunyata vema kujipa joto.



Baada ya dakika kama tano hivi, milio ya chura ilikoma ghafla. Hata wadudu nao walinywea. Kulikuwa kimya mno kiasi kwamba unaweza kudhani umekuwa kiziwi. Kimya hiki kilidumu kwa muda. Kiumbe kile kiwakacho hakikuonekana, hatukujua kilikuwepo wapi.



Saud alikuwa ameachama mdomo akimwaga udenda. Hakuwa na habari yoyote. Akiwa anaendelea kulala, mara mdudu mmoja mweusi mwenye ukubwa wa mende, anajongea kuufuata mdomowe. Mdudu huyo anazama ndani ya mdomo wa Saud. Kisha kunaendelea kuwa kimya.





Hakuna lolote linalotukia kwa takribani sekunde tano. Baada ya hapo, Saud anakohoa mara moja. Mara tena ... mara tena na tena! Anakohoa mno mwishowe anaamka kwa kushindwa kulala.



Alishikilia kifua chake akiendelea kukohoa zaidi na zaidi. Alianza sasa kukohoa damu. Kikohozi hakikukoma abadani. Alikohoa mpaka akaanza kukosa hewa. Alisimama akikohoa. Matokeo yake, alipoteza fahamu. Alidondoka chini akilala ameachama.



Zilipita dakika tatu. Ghafla, Saud anaamka! Aliamka kana kwamba mzimu unafufuka kaburini. Macho yake yalikuwa ya kijani. Lips zake zilikuwa nyeusi kana kwamba kunguru. Aliachama mdomowe, mara wakatoka wadudu lukuki! Wadudu hawa walikuwa wote wa aina moja. Vilevile kama yule aliyemuingia mwanaume huyo hapo awali.



Saud alisimama akaangaza. Mara akaanza kuelekea kule alipoelekea mwenzake.

.

.

.

Alitembea kwa kasi akitupa macho yake ya kijani. Alinusanusa huku na kule akipiga hatua. Kadiri muda ulivyokuwa unaenda ndivyo akawa anabadilika rangi na kuwa mweusi zaidi. Alitisha sasa kuliko hapo awali.



Misuli ya mwili ilimsimama ikichora rangi nyeusi. Nywele zake za kujiviringita, nazo zilianza kukakamaa kana kwamba miba. Lips pia zilikakamaa mithili ya ukuta usiopakwa plasta. .

.

.

Mabadiliko haya yalishangaza kwa namna yalivyokuwa yanatukia kwa haraka. Yalianza kutengeneza picha ya mdudu sasa kutoka katika mwili wa binadamu. Yangeweza kabisa kukufanya usimfahamu Saud kama ndiye huyo maana hawakuwa wanafanana kabisa na awali.

.

.

.

Saud aliendelea kutembea akisaka. Alitembea kwa muda wa kama robo saa kabla hajamtia machoni mlengwa wake. Alikuwa amelala, pembezoni mwake pia farasi akiwa usingizini.

.

.

.

Hapo Saud akajidondosha chini. Ilikuwa ni ghafla. Alianza kutambaa kana kwamba mdudu! Mikono na miguu yake yote ilikuwa inamsukuma kwenda mbele. Macho yake yalikuwa yanamtazama mlengwa wake kama vile chui anavyotazama kitoweo akiwindacho.

.

.

.

Alijongea zaidi na zaidi. Akiwa anakaribia, mara yule anayewindwa, Fadhil kwa jina, akaanza kusumbuka. Ni kama vile alikuwa anaota ndoto ya jinamizi. Hakudumu muda mrefu usingizini, akashtuka!

.

.

.

Alipotazama kando, alimuona Saud wa ajabu. Alishtuka mno. Alijivuta upesi kujikomboa. Saud naye alisogea kwa haraka katika mtindo wake ule ule wa kujivuta kama mnyama. Haraka Fadhil alivuta mkebe fulani wa ngozi uliokuwa kando yake, alizamisha mkono humo akatoa unga fulani mweupe.





Unga huo aliufichama ndani ya mkono wake wa kulia katika mtindo wa ngumi. Haraka, alipulizia ngumi hiyo upepo kana kwamba anazima kiberiti kinachowaka, alafu akaumwagia usoni mwa Saud.

.

.

.

Saud akaukunja uso wake akiugulia maumivu. Alipiga chafya mara lukuki akitoa wadudu puani. Kila alipopiga chafya, wadudu kama watatu ama wanne walirushwa nje ya mwili. Hilo jambo likamfanya Fadhil apigwe na butwaa kwa sekunde kadhaa kabla hajafanya maamuzi.

.

.

.

Aliutumia mwanya huo kumpanda farasi wake na kumuamrisha akimbie. Alienda kwa umbali wa kama kilomita tatu kabla hajampunguza mwendo farasi kwa kujihisi yupo salama.

.

.

.

Msitu ulikuwa umepungua ukubwa. Sasa kulikuwa kuna miti michache na vichaka vichaka vya hapa na pale. Hapakuwa panatisha sana kama kule alipotoka, ingawa usiku ni usiku tu, bado una yake ya kukutia homa ya hofu.

.

.

.

Fadhil alishuka na kujilaza chini. Akili yake ilibanwa na tafakari juu ya Saud na mabadiliko yake, hakujua nini kimemtokea. Lakini pia hakusita kukumbuka maneno ya Karim, mkuu wao, akiwasisitizia namna ya kujilinda dhidi ya wadhalimu watakaokutana nao huko njiani.

.

.

.

"Sijui kama atapona," alisema Fadhil. "Nimemwagia unga mwingi sana wa tawarikh. Bila shaka atapiga chafya mpaka kifo."

.

.

.

Unga huo ni miongoni tu mwa madawa waliyopewa na Karim yapate kuwasaidia wakiwa njiani. Mkebe ule aliokuwa ameubeba na kuulaza kando, ulikuwa umehifadhi madawa mbalimbali yote kwa ajili ya ulinzi.





Alijihisi yupo salama kabisa akikaa karibu na mkebe huo. Alichokuwa anakifanya ni kuuweka karibu na mkono wake wa kuume, mkono wa mapambano tayari kwa lolote litakalojiri.

.

.

.

Akiwa hapo anaendelea kuwaza, akalala. Usingizi nao ulikuwa mzito sana kwasababu ya mrundikano wa uchovu na ufinyu wa muda wa kupumzika. Ilimchukua muda mchache sana kuzama.

.

.

.

Baada ya muda mfupi, ikiwa ni kama dakika nane tu baada ya Fadhil kuzama usingizini, sauti ya vishindo vya miguu inasikika taratibu. Sauti hiyo inaongezeka ukubwa kadiri muda unavyosonga.

.

.

.

Punde miguu meusi ya mwanaume inafika na kusimama kando ya kichwa cha Fadhil. Miguu hii ndiyo iliyokuwa inatoa vishindo. Ilikuwa imesimamisha mishipa meusi kana kwamba bomba. Na mara kadhaaa ilikuwa inapitisha wadudu kama vile chemba ya kinyesi.

.

.

.

Dakika mbili mbele, sauti kali ya makelele inasikika. Sauti hii ilikuwa ni ya Fadhil. Ndege waliruka kwa uoga na hata wadudu wakanyamazama kwa punde.

.

.

.

.

.

. ***

.

.

.

.

.

.

Bado jua halikuwa limechomoza, ila ilikuwa tayari asubuhi. Malkia akitambua hilo, aliamka na kuanza kujiandaa kwa ajili ya safari yake ya kwenda kwenye himaya ya genge la wanyang'anyi.

.

.

.

Alipakia panga lake refu, akaweka pia viatu vyake tayari. Alioga na kujivesha nguoze kisha akamuamsha Fluffy.

.

.

.

"Mapema yote hii Sandarus?" Fluffy alijibaraguzia usingizini.

"Amka maana ni safari ndefu,"alisema Malkia.

"Si ndefu sana bana," akajitetea Fluffy. Bado hakuwa amefungua macho.







Malkia asiseme kitu tena, alisimama kandokando mwa kitanda cha mwanamke huyo mwenyeji wake. Alisimama hapo akimtazama kana kwamba anamshuhudia akifanya jambo. Fluffy alipofungua macho, akamuona Malkia akiwa amesimama kimstimu. Basi akawa hana budi zaidi ya kuamka.

.

.

.

Alijiandaa upesi, akaenda kumtwaa farasi wake zizini pamoja na Malkia. Kabla hawajaondoka, Fluffy alimuaga mamaye akawatakia kheri.

.

.

.

Walipojiweka kwenye migongo ya farasi, mara Zura akatokea.

"Mnaenda wapi mkiniacha?" Aliuliza. Alisimama mbele ya farasi akizuia njia.

"Zura pumzika, mama. Bado haujawa sawa," alisema Malkia.

"Nani kasema siko sawa, Malkia. Siwezi nikakuacha uende peke yako," alisema Zura. Kwa msisitizo alimsogelea farasi wa Malkia akamkwea.

"Nimeshajiandaa tayari. Tunaweza tu kwenda," Zura alihitimisha. Malkia hakuwa na neno zaidi, ilimbidi aende na mwanamke huyo mkongwe.

.

.

.

Walitembea kwa muda wa kama masaa manne pasipo kukoma. Ghafla Fluffy, aliyekuwa mbele akiongoza safari, alinyoosha mkono wake wa kuume juu. Malkia akamsimamisha farasi wake.

.

.

.

Mahali hapo palikuwa pakavu. Kulikuwa kuna mti mmoja tu uliosimama ukitia huruma. Mti huu haukuwa na tone hata moja la majani. Ulikuwa umekauka kaukau.

.

.

.

"Umeona mti huo?" Aliuliza Fluffy akinyooshea kidole mti. "Huo ndio mpaka wa himaya ya genge la wanyang'anyi. Tukiuvuka tunakuwa ndani yake."

.

.

.

Fluffy akanyooshea tena kidole chake kaskazini ya mbali. "Umeona kule?"

Aliponyooshea kulikuwa kuna jengo moja refu. Halikuonekana vema kwasababu ya umbali.





"Pale ndio kuna makao ya genge hilo. Wanapaita kwa makuhani. Ndipo anakaa kiongozi wao, wanayemuita kuhani mkuu."

"Na wapi wanapotunza mali wanazoziiba?" Aliuliza Malkia.

"Itakuwa ni hapo hapo tu," akajibu Fluffy. "Humo ndimo mahali salama kuliko pengine ndani ya himaya hii."

.

.

.

Kukawa kimya kidogo.

.

.

.

"Haja yetu ni kufika pale salama," alisema Fluffy. "Najua haitakuwa rahisi kukatiza mpaka tufike huko. Tutakutana nao hapo katikati, na waweza kuwa wakorofi kupitiliza. Yatupasa tuwe makini, lakini pia watulivu. Nitawaomba muwe kimya nifanye nao mazungumzo."

.

.

.

Baada ya kusema hayo, waliruhusu farasi wao kuzama ndani. Walitembea kwa takribani dakika kumi tu, wakaanza kuona wanaume kadhaa wakiwa wanawatazama.

.

.

.

Wanaume hao walikuwa wanafanana kwa namna walivyo hovyo. Nguo zao hazikuwa maridadi, hata nywele zao pia. Kwa macho tu ungepata kuwashuku kuwa ni vibaka, wakwapuzi. .

.

.

Waliwatazama wageni waliongia himayani kwa macho mhalifu. Ni kana kwamba fisi anavyomtazama swala mdhoofu. Taratibu walianza kujikusanya, wengine wakibebelea silaha. Wakajongea karibu.

.

.

.

"Leo nyama imejileta yenyewe jikoni," alisema mwanaume mmoja kiongozi wa genge. Walikuwa kama mia moja kwa idadi ya hapo. Baadhi walikuwa wamebebelea mapanga, wengine rungu na fimbo. Wengine mikono ikiwa mitupu.

.

.

.

Malkia alipeleka mkono wake kwenye panga, Fluffy akawahi kumtuliza. Alimtazama na kumtikisia kichwa kumpa ishara, kisha akawatazama wenyeji wao.

.

.

.

"Hatujaja kwa vita bali amani," Fluffy alipaza sauti. "Shida yetu ni kuonana na kuhani mkuu!"





Mwanaume yule kiongozi akacheka.

"Kuhani mkuu?" Aliuliza kwa kebehi. Alimsogelea Fluffy akampapasa paja akisema:

"Mie ndiye kuhani mkuu."

.

.

.

Wenzake wote wakaangua kicheko. Meno yao yalikuwa yana rangi ya ajabu ajabu usielewe hata ukitaka kuelezea. Wengine walikuwa na mapengo makubwa kama mapango, lakini hawakuonekana kama wanajali.

.

.

.

Fluffy aliutoa mkono wa mwanaume huyo pajani mwake, akisema:

"Najua wewe si kuhani mkuu. Tafadhali naomba nionane naye. Pengine mwaweza juta nikimuelezea haya mnayoyafanya."

.

.

.

Wanaume wakaangua kicheko tena. Mara hii wengine walishikilia mbavu zao kwa maumivu.

.

.

.

"Mwanamke, unadhani unaweza kututisha?" Aliuliza kiongozi. Aliurudisha mkono wake kwenye paja la Fluffy.

.

.

.

"Labda tu nikuambie kwa ufupi. Leo hatujaambiwa kama tutakuwa na ugeni wowote hapa. Hivyo wewe na hawa wenzako tunaweza tukawafanya chochote tunachotaka na tusiulizwe na yeyote!"

.

.

.

Baada ya mwanaume huyo kiongozi kusema hayo, alitembea kidogo kusogea mgongoni mwa Fluffy, akamchapa kofi mwanamke huyo kalioni.

"Leo utanihudumia mrembo," alisema kisha akawageukia wenzake.

"Chagueni mnaowataka!"

.

.

.

Wanaume wakapiga makelele kushangilia utadhani mashabiki walioshuhudia goli dakika za mwishoni.

.

.

.

Ikabidi sasa wanawake wajihami, hakukuwa na namna ya amani tena. Malkia alichomoa panga lake akalikamata vema mkononi. Fluffy pia alichomoa panga toka kwenye mfuko uliopo pajani akalishikilia tayari kwa ajili ya vita.





Kabla ya vita hiyo haijaanza, mara mlio mkubwa wa mluzi uliita na kuwashtua, wote wakatazama mlio huo unapotokea. Walimuona mwanaume mmoja mrefu akiwa amevalia koti refu la ngozi. Mwanaume huyo alikuwa anaongozana na wanaume wanne waliokuwa wamejaza misuli mwilini.

.

.

.

Mwanaume huyo ndiye kuhani mkuu. Kichwa chake hakikuwa na nywele hata punje. Uso wake ulikuwa una makovu ya kukatwakatwa, ulitisha. Wanaume aliokuwa anaongozana nao walikuwa vifua wazi. Mikononi mwao walibebelea mapanga marefu makali.

.

.

.

Mara wanaume wote wale waliokuwa wanawakarahisha wakina Malkia wakapiga magoti wakisema:

"Karibu kuhani."

"Kuna nini hapa?" Akauliza kuhani mkuu. Sauti yake ilikuwa kavu na nzito. Macho yake yanayotisha yalikuwa yanawatazama Malkia na wenziwe.

.

.

.

"Tumekuja kuonana nawe," alisema Fluffy.

"Nyie ni wakina nani?" Akauliza Kuhani mkuu. "Na mnataka nini kwangu? Ujio wenu sina miadi nao."

"Tafadhali tunaomba tukaongelee hilo mahala tulivu. Bila shaka hiyo ndiyo njia sahihi ya kumpokea mgeni," Malkia alipaza sauti yake.

.

.

.

Kuhani mkuu alitabasamu. Hakuona haja ya kuhofia ugeni huo, tena wa wanawake ndani ya tawala yake. Aliwakaribisha wageniwe makaoni.

.

.

.

Wakiwa wanaelekea makaoni huko, Malkia na wenzake waliendelea kuona wanaume zaidi na zaidi, wakiwemo hata wale wanaume wawili walioukwapua mkufu.

.

.

.

Mpaka wanafika makaoni, ni takribani wanaume mia tano walionekana. Ni wengi si haba.

"Karibuni sana," alisema Kuhani mkuu. .

.

.

Sebule ya makao yake ilikuwa imegengenezwa kwa vifaa skrepa vyenye kutu na kuchakaa. Hakukuwa kunavutia hata kidogo. Ilimlazimu mtu akae kwa mashaka hapo.







Pangaboi lilikuwa linazunguka taratibu likitoa mlio wa kuchoka. Hata viti navyo vilikuwa vinaita kwa milio mtu akijigeuza. Tabu hiyo iliwafanya wageni watulie pasipo kusonga ili mazingira yawe tulivu wapate kuongea.

.

.

.

"Naitwa Sandarus, ni mwanamke mfanyabiashara toka ng'ambo. Hawa uwaonao hapa ni washirika wenzangu."

"Karibuni," akasema Kuhani mkuu na kisha akauliza: "Niwasaidie nini?"

"Nimekuja hapa kufuata mkufu wangu," Malkia akaenda moja kwa moja kwenye hoja pasipo kuzunguka. .

.

.

Sauti yake ilikuwa ya kujiamini, na macho yake yalikuwa yanamtazama Kuhani mkuu pasipo kupepesa.

.

.

.

Kuhani mkuu alitabasamu.

.

.

.

"Mkufu wako? Upi huo?"

"Kuna vijana wako waliubeba mkufu wangu nikiwa sijitambui. Unafanania na huu..." Malkia alichomoa mfano wa mkufu wake akaonyeshea. Mkufu huu alitengenezewa na Fluffy. Kuhani mkui aliutazama mkufu huo kabla hajaukwapua na kuutia mfukoni mwake.

.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

.

.

"Labda kuna kitu hujakijua, Sandarus. Na ninadhani ni kwasababu ya ugeni wako eneo hili. Si mbaya nikakujuza."

Kuhani mkuu alijitengenezea vizuri, akamtazama Malkia kwa uso wa kuogofya.

"Kitu kikija hapa, ni chetu. Hakuna mtu yeyote anayediriki kuja kudai chochote hapa. Hakuna na haijawahi tokea!" .

.

.

Akatabasamu.

.

.

.



ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog