Search This Blog

MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN - 1

 




IMEANDIKWA NA : STEVE MOLLEL



*********************************************************************************



Simulizi : Mkufu Wa Malkia Wa Gosheni

Sehemu Ya Kwanza (1)



Jua lilinyanyuka na kuangaza ardhi ya Goshen: mojawapo ya tawala kubwa iliyopata kutokea mashariki ya mbali katika karne ya kumi baada ya kuzaliwa kwa kristo.



Ndege wake wakubwa wenye rangi za kuvutia waliamka wakaruka huku na kule wakitandaza sauti zao nyembamba. Sauti hizo marigoli zikawasili masikioni mwa malkia Sandarus na kumwamsha. Alikuwa amevalia nguo nyepesi za kulalia zilizokuwa zinaangaza kuonyesha mwili wake mchanga wa miaka ishirini na tano.



Kichwa chake chenye hekima kilikuwa kimefunikwa na nywele nyingi rangi ya kahawia. Miguu yake mirefu ila yenye nyama ilisimika ardhini na kusimamisha mwili wake mrefu mwembamba. Alah! Alikuwa mzuri haswa. Macho yake yalikuwa makubwa yaliyolegea. Mdomo wake ulikuwa mdogo ila hakika ukichanua kwa tabasamu ungekufanya uache shughuli yako na kumtazama.



Nyonga zake zilijiachanua na kukikimbia kiuno. Vidole vyake vilikuwa vyembamba virefu vyenye kucha bawabu. Tumbo lake flati na mapaja mekundu. Amini nakuambia siwezi kumaliza kuongelea uzuri wake kwani nikifanya hivyo tutajaza kitabu hiki.



Alipiga mihayo akanyoosha viungo vyake. Aliendea dirisha akafungua na kuangaza kutazama nje ya jengo lake kubwa la kifalme. Huko akaona makazi ya wananchi na wananachi wake wakiamka, wakikatiza na hata wakishughulika.



Alitabasamu akarejea kitandani kabla tu ya punde kijakazi wake kuingia akiwa kavalia gauni refu la kaki na kiremba kizito. Aliinama kumsalimu malkia kisha akamtazama na tabasamu.



“Malkia wangu, nimewasili. Nini wataka?”



“Hakuna ninachohitaji Zura.” Alisema Malkia Sandarus kwa sauti yake nyembamba ila yenye amri ndani yake.



Zura, kijakazi wa malkia, alikuwa ni mwanamama mzee wa miaka arobaini na tano. Si tu kwamba alikuwa ni kijakazi, bali pia alikuwa kama mama kwa Malkia huyo aliyempoteza mama yake punde tu alipozaliwa. Na kwa mujibu wa taratibu za kipindi hiko, Sandarus alipata mwanaume akiwa mdogo kabisa wa umri wa miaka mitano.



Alichukuliwa na mfalme wa Goshen, kwa jina Loop, kwa mujibu wa kumlelea ili aje kumuoa. Na kwa wakati wote huo, Sandarus akamjua Zura kama mama. Ni pale tu alipokuwa ndipo akapata kuujua kweli hizi chungu: hana mama, hampendi mwanaume aliyeozwa naye, baba yake hayupo tena hai, hana kaka wala dada, lakini pia pale alipo si nyumbani, nyumbani kwao ni kusini ya mbali kwenye utawala wa Maam.



Baba yake alikuwa mtu mkubwa kwenye hiyo tawala na kama mojawapo ya njia ya kuunganisha tawala hizi mbili: Goshen na Maam, babaye akamtoa akaolewe huko.



Tokea akiwa mtoto, Zura alimlea kama mwanaye. Lakini zaidi ya hapo alifanikiwa kumuandalia mazingira mazuri malkia huyo kuwa karibu sana na wananchi wake. Akiwa mtoto, alienda kuchota maji na hata kucheza na wanachi wa kawaida.



Hakuwa na majivuno wala malezi ya kunanga, matokeo yake watu wengi ndani ya tawala hiyo wakampenda na kufurahishwa naye.



“Ungependelea chakula gani mama?” Zura alimuuliza malkia akiwa ameinamisha uso wake chini. Malkia Sandarus alitabasamu akamjongea karibu na kumshika mabega.



“Unajua nini napendelea, mama.”

“Naitwa Zura, malkia.”

“Najua.”

“Ukiniita mama, nitashitakiwa. Nimeonywa sana juu ya hilo. Sina hadhi ya kuwa mama wa malkia.”

“Tafadhali. Siwezi kuacha kukuita mama. Na kama kuna yeyote atakayekufanya kitu basi atashughulika na mimi.”



Zura hakusema tena kitu. Amekuwa akisema hilo jambo la kuitwa mama kila siku na inaonekana anaongea na sikio la kufa. Aliufunga mdomo wake akafuata chakula akipendacho malkia wake: Aliporejea na kuhakikisha malkia wake anakula, aligeuza aondoke ila akaitwa pale tu alipofika mlangoni.



“Mfalme anaendeleaje?” Aliuliza Malkia Sandarus akila.

“Unamaanisha mumeo?” Zura aliuliza.

“Namaanisha mfalme.” Malkia Sandarus akajibu. Zura aliguna kwanza kisha akachukua hatua chache zilizomfikisha kitandani alipoketi na malkia wake.

“Malkia, inabidi ifikie mahali ukubali ya kwamba mfalme ni mumeo. Hakuna kitakachobadili hilo kamwe.”

“Sitaki kuongelea hayo mambo, mama.”



Hilo ndilo lilikuwa jibu la Malkia Sandarus kila alipoongea na Zura kumhusu mumewe – Mfalme Loop. Hakumpenda mwanaume huyo.



Matendo yake ya kumbaka kila siku kwanguvu lakini pia kumpiga mara kwa mara kulimfanya Malkia Sandarus amchukie mwanaume huyo zaidi. Ni kwakuwa tu aliwapenda watu wa Goshen ndiyo mana alikuwepo pale, ni kwakuwa tu watu wa Goshen walimpenda ndio mana alikuwa pale la sivyo angekuwa tayari ameshatoroka, kama kila siku anavyosema.



Baada ya kumaliza kula na kujiandaa kwa mavazi maridadi Malkia Sandarus aliongozana na Zura wakaenda kwenye kingo ya mto wa Boa wakiongozana na walinzi watano waliojibebelea kwenye farasi.



Huko walinzi walikaa kando kidogo kuwapisha wanawake hao kuteta na kutembea. Walisogea mbali zaidi na walinzi, Zura akamshika mkono Sandarus na kuhakikisha kwanza kama wapo mwenyewe. Ni kweli walikuwa wenyewe. Sasa akamnong’oneza:

“Kuna kitu nataka nikuambie.”



Malkia Sandarus aliogopa. Hakuwahi kumuona Zura katika hali hiyo na bila shaka sasa alitegemea kuna kitu makini anataka kuambiwa. Zura alitazama tena kushoto na kulia akarudia:

“Kuna kitu nataka nikuambie.”



“Sema.” Malkia Sandarus alisema kwa pupa. Sauti yake ililowa hofu. Alikuwa anaishiwa staha ya kungoja sasa. Zura alishusha pumzi ndefu, akasema:

“Kuna kitu niliambiwa nikupatie.”



“Kitu gani?”



“Mkufu. Baba yako kabla hajafariki alinihasa nikupatie mkufu huo. Lakini kwa siri sana, na haitakiwi yoyote aone wala kuuvaa kabisa.”



Malkia alikunja sura. Kuna kitu alihisi akipo sawa. Alijua baba yake amefariki tena kabla hata hajapata uwezo wa kumkumbuka kwa undani. Kwanini leo hii anapewa hiko kitu?



Na kwanini mkufu na si kingineko? Maswali hayo yalikuja upesi mno kichwani kwake. Aliyauliza Zura akamjibu kwa utulivu:

“Nimeshindwa kabisa kuendelea kutunza jambo hilo kifuani mwangu. Ila ujue kwamba wakati baba yako anafariki aliniita faragha akanipatia mkufu huo kwasababu aliniamini. Aliniambia hata mfalme asijue hilo. Aliniambia na kunielekeza mengi juu ya huo mkufu, lakini pia …” Hakumalizia. “Lakini nini?” Malkia aliwahi kuuliza.



Zura alitazama chini asiseme kitu. Alitazama tu maji ya mto yakitiririka. Kifuani mwake kuna jambo alikuwa anataka sema ila alikuwa anaogopa. Haikuwa na mantiki sasa kulificha jambo hilo ilhali ameshagusia jambo la mkufu, moyo wake ulimwambia.



Wakati akiyafikiria hayo Malkia alikuwa anamtazama kwa matamanio ya kutaka kusikia.



“Unatakiwa uvae mkufu huo baada tu ya mfalme kufa.” Alisema Zura.

“Kwanini?” Malkia Sandarus akauliza.

“Sijajua kwanini ila ndivyo baba yako alivyoniambia.”



Haikuleta maana kwanini mkufu huo una masharti hivyo. Hakuna aliyejua, hata Zura mwenyewe aliyekabidhiwa alikuwa ana ufahamu finyu juu ya hilo.



Waliondoka huko mtoni wakaelekea mpaka nyumbani kwa Zura, huko mkufu ukachopolewa toka kwenye kiboksi kidogo cheusi cha mbao, akakabidhiwa Malkia Sandarus. Mkufu huo ulipoketi kwenye kiganja cha mwanamke huyo, uling’aa kisha ukazima ghafla.



“Ndio huo!” Zura alisema.



Ghafla mlango ulifunguliwa akaingia mwanaume mnene mwenye ndevu na nywele nyingi. Alikuwa ni mume wa Zura. Mkufu ulifichwa haraka asipate kuuona. Alipomuona Malkia alipiga magoti akasalimu.



“Naweza nikaenda?” Malkia aliuliza akimtazama Zura.



“Ndio waweza kwenda, malkia wangu.”



Kabla hajaenda, akasema:

“Nitahitaji kukuona muda si mrefu.”



Aliondoka akaenda kuketi mwenyewe chumbani kwake. Alitazama mkufu ule aliopatiwa akiupekuapekua na maswali mengi yasiyo na majibu yakigonga kichwani. Mwishowe aliutia ndani ya kiboksi na kukiweka chini ya uvungu mwa kitanda.



Baada ya siku mbili, mfalme Loop alifariki dunia. Msiba wake ulivuma na wakuu wa tawala kadha wa kadha wakahudhuria. Alifariki akiwa na miaka mia moja kamili.



Msiba wake ulidumu kwa juma moja kisha baraza la wazee wa tawala la Goshen likaketi kwa ajili ya kuzungumza na kupanga juu ya nani ataendeleza utawala tangu mfalme akiwa hai hakufanikiwa kupata hata mtoto mmoja toka kwa wake zake wote wanne.



Kwenye majadiliano ya baraza hilo akateuliwa Mzee Fursa kusimamia tawala ya Goshen kwa muda wa takribani mwezi mmoja wakati mchakato wa kumpata mrithi ukifanyika kwa kukusanya maoni toka kwa wajumbe na pia wananchi.



Ndani ya muda huo wa mwezi, siku moja ikiwa ni katikati ya usiku mnene, Malkia Sandarus aliamka toka usingizini baada ya kusikia sauti ya kitu kikigonga mbao.



Alifungua macho yake akastaajabu kukuta chumba chake kikubwa chenye kila aina ya samani za ghali na za kupendeza kikiwa na mwanga mwekundu hafifu. Alifuatilia mwanga huo akagundua unatoka chini ya uvungu wake wa kitanda.





Alitaka kuita mlinzi aliyekuwa amesimama nje ya mlango, ila akasita. Alijibandua toka kitandani akachungulia chini ya kitanda, akaona mwanga huo watoka ndani ya kisanduku kile cheusi alichokabidhiwa na Zura.



Ilikuwa ni mkufu? Alijiuliza na nafsiye.



Alivuta kisanduku hicho akakifunua na kutazama. Kweli ilikuwa ni mkufu! Ulikuwa unawaka kama vile ulivyowaka kwa mara ya kwanza ulipotiwa mkononi mwake. Alibakia akiutazama mkufu huo na kujiuliza maswali kadhaa: kwanini unawaka? Kwanini alikabidhiwa tena kwa masharti?



Akiwa anaupekuapekua kwa kuugeuzageuza, pasipo kujua mwanga wa mkufu huo ukapenya chini ya mlango na kutua kwenye kiatu kikubwa cha mlinzi aliyekuwa amesimama huko nje.



Mlinzi alipata wasi akagonga mlango kuulizia usalama. Ila ajabu, mwanga wa mkufu ulijifinya na kupotea ghafla.



Malkia Sandarus aliurudisha mkufu huo ndani ya kisanduku kisha akajilaza. Usingizi haukumjia haraka kwasababu ya mawazo yaliyokuwa yamemtinda. Alitamani pakuche ili apate fursa ya kuulizana hilo jambo na Zura maana ndiye mtu pekee anayeweza kujadili naye juu ya mkufu huo.



Palikucha na alipoamka tu, alikutana na uso kwa uso na Zura. Alikuwa tayari ameshafika kwa ajili ya kufanya usafi na kusikiliza haja za malkia wake. Malkia alimueleza yale yote aliyopata kuyaona usiku, Zura akamkumbusha:

“Malkia wangu, uliambiwa uvae mkufu huo punde tu mfalme atakapokufa.”



“Na je nikiulizwa ni wapi nilipoutoa, nitasemaje?”



“Utalaghai mfalme alikuletea kama zawadi toka tawala za mbali.”



Malkia Sandarus alivaa mkufu huo, punde ukawaka na kuzima kama vile ulivyofanya kipindi cha kwanza kabisa. Hapo zikapita siku kadhaa na kukaribia kabisa siku ya kuwasilishwa maoni na mapendekezo ya wajumbe na wananchi juu ya nani atachukua utawala wa Goshen. .

.

.

.

.*** .

.

.

.

Katikati ya usiku mnene wa kuamkia siku ya mapendekezo na maoni, Malkia Sandarus alihisi joto kali kwenye kifua chake. Aliamka upesi kutazama akakuta kidani cha mkufu wake chawaka na kumetameta.



Alidhani ni kama siku zile, ila baada ya muda kidogo akagundua haikuwa kama siku zile kwani siku ile mkufu huo hakumuunguza na wala haukuwa wa moto kama siku hiyo. Haraka alivua akauweka mkononi. Ilimchukua muda mfupi tu akagundua kwamba kuna kitu.



Ndio.



Ukiachana na mwanga uliokuwa unamulika, kulikuwa kuna kitu ndani ya mwanga huo. Alitazama ukutani akaona picha ya mtu ndani ya huo mwanga. Alikuwa ni mwanaume mnene, mrefu mweusi.



Alitazama vema akagundua mwanaume huyo alikuwa ni mzee Fursa. Alikuwa anaongea na wazee watatu wa baraza na kandokando mwao walikuwepo wanajeshi watatu.



“Hatuwezi tukakubaliana na hili.” Sauti ya Fursa ilisikika toka mkufuni. Malkia Sandarus alisogeza masikio yake kwenye mkufu huku macho yake yakiangaza ukutani. “Mwanamke atatuongozaje?



Siwezi kabisa nikaheshimu maoni haya. Na hii ni kwa ajili ya Goshen. Endapo tukiruhusu akashika madaraka, basi lazima tutayumba na hakika Jayit muuaji atatuvamia na kuifanya hii tawala kuwa simulizi.”





Jayit ni mtawala wa Devonship. Tawala hiyo ipo upande wa magharibi ya mbali na tangu iundwe haijawahi kupatana na tawala ya Goshen hata kidogo. Chanzo cha chuki na uhasama wao ni vita iliyotokea huko miaka ya nyuma kwasababu ya kugombania ardhi ya makaburi.



Mtawala huyo wa Devonship alitaka ardhi hiyo kwa madai babu yake alizikwa hapo. Anahitaji ardhi hiyo hata kama kwa muda huo hakuwa tena mkazi wa Goshen. Hakuna aliyejua mpaka sasa kwanini anataka makaburi hayo, ila ndani ya roho yake alikuwa na kazi nayo kubwa na muhimu mno.



Kazi hiyo kwa miaka nenda rudi haijapata kutimia kwasababu tu ya kuhofia utawala wa Goshen chini ya familia ya Loop.



Ila kwa sasa familia hiyo imeenda baada ya mazishi, na haijaacha hata mtu wa kuendeleza utawala huo uliokuwa na mahusiano makubwa na tawala za karibu. Sasa Jayit anaona hiyo ni fursa marigoli kupata anachokitimiza. Hiyo ndio fursa adhimu ya kutimiza haja zake:



Kupata ardhi ya makaburi!



Malkia Sandarus alishika mdomo wake kwa mshangao akitazama ukutani. Hakuamini alichokuwa anakiona. Hakuamini kama mzee Fursa anaweza akapanga tukio kama lile la kupuuza mapendekezo na maoni ya wananchi. Na si tu kwamba ameishia hapo ila sasa alikuwa ameagiza wanajeshi wale watatu waje kummaliza!



Kwa muda kidogo Malkia hakuamini kile alichokuwa anakiona. Kwa namna moja ama nyingine alihisi analaghaiwa na ule mkufu ambao umepanga kumkosanisha na watu wake. Ila baada ya muda mfupi alijikuta ananza kusadiki.



Alisikia sauti ya mwanajeshi ikilalamika kwa maumivu mlangoni kisha akasikia kishindo cha mtu akidondoka. Ghafla mwanga wa mkufu ulizima na kukawa giza. Na sasa mlango wake ukawa unapigwa kwanguvu ukilengwa kuvunjwa! Moyo wake ulitatuka. Ni haraka akajikuta anapata joto kali mwilini la kutosha kabisa kumvujisha jasho.



Afanye nini? Akili yake ilijiuliza na kuanza kuchambua upesi. Kama angeendelea kukaa mule ndani ya dakika moja basi angekuwa mikononi mwa wale wanaokuja kuuchukua uhai wake kama vile walivyoagizwa na Fursa.



Alisimama upesi akaendea dirisha la chumba chake. Alitazama chini akapaona mbali, je angojee wanaokuja? Hapana! Alijitupia huko nje akafikia kwa kudondoka kama mzigo.



Akaumia mno, ila hakutaka kukaa hapo akanyanyuka na kuanza kukimbia. Wanaume wale waliokuwa wamemfuata walimtazama kwa kupitia dirishani na kumnyooshea kidole kabla hawajatoka hapo upesi kwenda kumfuata.



Ajabu Malkia alikuwa anakimbia kama chizi. Alikuwa anajificha kama mwivi akijibanza na kutokozea kule. Hakutaka kukutana na mlinzi yeyote hivyo alikuwa makini mno kutazama na kuhakikisha kabla hajachomoza na kupiga kwata.



Aliendea banda la farasi huko akapiga mluzi na haraka farasi wake rangi nyeupe akajiri toka gizani. Alimkwea wakaondoka upesi toka eneo lile.



Ilikuwa ni usiku mkali na kulikuwa tulivu mno. Watu waliopo nje walikuwa kwenye vibaa vidogo wakinywa mivinyo na kucheza, nao pia walikuwa wachache mno.



Makelele ya farasi wa Malkia akikimbia huko nje ndiyo yalisikika kwanguvu. Mwezi ulikuwa unafifia na kufunikwa na mawingu mara kwa mara. Hali ya hewa ilikuwa baridi, mbwa waliokuwa wamelala nje walikuwa wamejikunja kujipa angalau joto.



Farasi wa Malkia alisimama mbele ya nyumba ya Zura, Malkia akashuka na kugonga mlango hapo mara tatu huku akimuita Zura kwa jina. Zura aliyegundua kwamba hiyo ni sauti ya malkia wake aliamka haraka akaufungua mlango.



Alistaajabu kumuona Malkia yupo hapo kwa muda ule wa usiku mzito tena akiwa peke yake. Kabla hajauliza nini kilitukia, Malkia alimtaka apande farasi waondoke upesi.





“Tunaenda wapi malkia wangu?”



“Nakuamuru panda farasi!” Alifoka Malkia Sandarus. Zura hakubisha tena akakwea farasi huyo na haraka wakaondoka eneo hilo.



Ilichukua muda mfupi sana farasi watano waliowabebelea wanaume wenye miili mikubwa ndani ya sare za walinzi wakafika mbele ya nyumba ya Zura. Wanaume wawili walishuka upesi toka kwenye farasi wao wakauvunja mlango.



Waliwasaka Malkia Sandarus na Zura nyumba nzima lakini hawakuona kitu. Walimkwida mume wa Zura na kumtoa ndani ya nyumba wakamrushia nje kana kwamba mbwa.



“Wapo wapi?” Aliuliza mlinzi mmoja mrefu zaidi ya wote.



“Sijui walipo. Naapia kwa Mungu!” Alijibu mume wa Zura akiwa anatetemeka. Uso wake ulitia huruma mno. Mlinzi alisonya kwa kupuuzia kisha akamwambia kwa kufoka:

“Utasema tu!”



Alimnyanyua juu kisha akamtupa tena chini. Mume wa Zura alipiga kelele kali za maumivu. Kiuno chake kiliteguka na mkono wake wa kulia ulivunjika. Alisikia maumivu makali lakini wanaume wale hawakujali juu ya hilo.



“Wapo wapi?” Swali lilirudiwa. Jibu lilikuwa ni lile lile toka kwa mume wa Zura. Walimtesa mpaka pale walipohakikisha mwanaume huyo hayupo hai tena.



Walimuingiza ndani kwake wakatimka. Walitafuta ndani ya mji mzima, hawakumpata Malkia. Walirudi kwa bwana Fursa wakamfikishia hizo taarifa.



“Kamtafuteni mpaka nje ya mji!” Fursa alibweka. “Ni lazima apatikane kwa gharama yoyote ile. Ni lazima apatikane kabla hakujakucha!”



Wanaume wale waliondoka upesi kwenda kumtafuta Malkia Sandarus kwa mara ya pili. Mara hii waliongozana na mbwa watatu. Walizunguka mji mzima lakini hawakumpata.



Walitoka sasa nje ya mji wakirandaranda maporini lakini napo huko hawakufanikiwa mpaka wanafika mpakani mwa tawala yao. Walikuwa wamechoka pasi mafanikio.



“Atakuwa ameelekea nje ya Goshen.” Mmoja alisema.



“Basi hakuna haja ya kuendelea kumfuatilia. Huko lazima atauwawa.”



Waliridhia juu ya hilo kabla hawajarejea kwa Fursa na kumueleza. Japokuwa hawakumpata Malkia ila taarifa hiyo ya kutokuwepo ndani ya himaya ya Goshen ilimpatia ahueni.



“Huko nje ya Goshen hawezi akadumu.” Alisema Fursa akitabasamu. “Ni wazi wachawi wa Tanashe watamfanya kitoweo.”



Usiku huo wote aliumaliza kwa kunywa mvinyo pamoja na wazee wenzake watatu wa baraza. Walikuwa wanfurahia hatimaye kuiweka Goshen mikononi mwao.



“Hakutakuwa tena na mwingine wa kuchukua utawala huu zaidi yangu.” Alijigamba Fursa. “Mtu pekee aliyekuwa ana kura zaidi yangu haonekani. Wananchi watajua amekimbia himaya yake!”



Walicheka wakaendelea kunywa na kunywa.



Wakati usiku huo ukiwa ni murua kwao, kwa Malkia Sandarus na Zura ilikuwa ni kinyume: walikuwa porini wakipigwa baridi kali, lakini pia walikuwa nje ya himaya ya Goshen. Ilibidi wafanye hivyo kwa usalama wao kwani ndani ya himaya yao hakukuwa salama tena.



“Sasa tutafanyaje malkia wangu?” Zura aliuliza baada ya Malkia kumueleza kila kitu.



“Sijajua bado.” Akajibu Malkia Sandarus. Alikuwa anatembea kigoigoi akimvuta farasi wake.



“Basi tupumzike, malkia wangu. Kadiri tunavyokwenda huko tunasogelea hatari. Tunazidi kuiacha Goshen!” Alishauri Zura. Malkia aliona wazo hilo ni jema akamfungia farasi wake mtini wakaketi chini.



Walijikunyata kwa baridi. Walikumbatiana wapashane moto. Kutokana na usiku kuwa mwingi na pia uchovu, hawakudumu macho wakalala.



Baada ya lisaa limoja, bado ikiwa ni usiku katikati ya msitu huo uliokuwa kwenye himaya ndogo ya Tanashe, vishindo vya watu wakitembea na sauti zao zikiteta ndani ya lugha isiyoeleweka vilisikika kwa mbali.



Vishindo na sauti hizo zilikoma baada ya muda mfupi na watu hao waliokuwa wanaongea na kutembea wakaonekana: wabibi watatu wakiwa wamevalia mashuka meusi. Bibi mmoja alikuwa hana macho kabisa, mwingine alikuwa ana jicho moja na wa mwisho alikuwa na macho yote mawili.



Yule mwenye macho mawili alikuwa wa kwanza kuwaona Malkia Sandarus na Zura mtini. Yeye ndiye aliwasimamisha wenzake akawaonyeshea kwa kidole.



Waliteta ndani ya lugha yao isiyoeleweka kisha wakaanza kuwafuata binadamu hao wakiwa na nyuso zenye hamu ya kujua. Kabla hawajafika, Malkia alishituka toka usingizini. Haraka pia akamuamsha na Zura.



“Nyie binadamu mnafanya nini Tanashe?” Aliuliza mwanamke mwenye macho yote mawili. Yule ambaye hakuwa na macho kabisa alinyofoa jicho moja la mwenzake huyo kisha akalipachika usoni kwake apate kuona. Sasa kila mmoja akawa na jicho moja.



“Tumepotea!” Alisema Malkia. Bibi wale wakacheka kwanguvu.



“Hakuna anayepotea ndani ya Tanashe.” Alisema mmojawao. “Kama ukija huku basi inakuwa imepangwa!”



“Basi inakuwa imepangwa!” Akaitikia bibi mwingine kwa furaha.



“Basi inakuwa imepangwa!” Akamalizia bibi mwingine kwa furaha.



“Tafadhali, msitudhuru.” Alisema Zura. “Naomba mtupe hifadhi. Nasi tutakuja kuwarejeshea mara mbili ya fadhila zenu.”



Bibi wale walitazamana kisha wakaangua vicheko. Nyuso zao zenye jicho moja moja zilikuwa zinatisha kwa makunyanzi. Midomo yao ilikuwa na meno machache yakiwa yamekaa mbali mbali.



“Hakuna atakayewadhuru.” Alisema bibi mmoja. “Mtakuwa salama pasipo shaka lolote.”



“Pasipo shaka lolote!” Akaitikia bibi mwingine kwa furaha.



“Pasipo shaka lolote!” Akamalizia bibi mwingine kwa furaha.



Malkia alitazama na Zura pasipo kusema kitu. Mioyo yao ilikuwa na shaka, ndio. Ilikuwa ni ngumu kuwaamini bibi wale wageni machoni mwao kama kweli wanachosema ndicho wanamaanisha.



Lakini sasa watafanya nini? Ilionekana wazi hawakuwa na machaguzi mengi, hivyo japokuwa walikuwa na hofu wakaamua kuridhia kwenda na bibi wale.



Walitembea kwa mwendo wa dakika kama tatu wakafika kwenye nyumba moja kubwa mno. Nyumba hiyo ilikuwa kimya isisikike chochote, pia ilikuwa giza.



Ilizingirwa na miti mirefu kila pande, kwa giza la usiku ule kama usingeliambiwa kama pale kuna nyuma basi usingelitambua.



Mlango ulifunguliwa na wale wabibi wakatangulia kuingia ndani. Waliwasha maginga machache ya moto na kukawa kuna nuru japo si yenye nguvu. Malkia Sandarus na Zura waliketi kwenye viti walivyoelekezwa kisha wakaletewa mabakuli mawili ya supu.



Harufu yake ilikuwa kama mizoga. Hakika kama ungelipata kunusa ungekaribia ama ungelitapika kabisa. Malkia na Zura walishindwa kupeleka mabakuli hayo kinywani wakayatua mezani.



Hapo ndio Malkia akaona wabibi wale watatu wakiteta huku wakimtazama. Alipata shaka. Aliimshirikisha jambo hilo Zura, Zura akamtaka awe na subira lakini pia wawe makini.



Bibi wale waliokuwa wamekaa mbali kidogo walisogea karibu wakamtamzama Malkia.



“Wewe ni Malkia wa Goshen?” Aliuliza mmojawao. Kabla Malkia hajajibu, akamtazama kwanza Zura.



“Ndio. Mimi ni Malkia.”



“Na huo ni mkufu wako shingoni?” Swali hilo lilimshitua Malkia Sandarus. Moyo wake ulipasuka na kuzizima. Alijiuliza mara tatu kwanini ameulizwa swali lile. Je bibi hao watakuwa tayari wamegundua nguvu yake? Mdomo ulikuwa mzito kufunguka.



“Ndio ni wa kwake.” Akajibu Zura. Bibi wale walitazamana na kuteta kwa lugha isiyoeleweka, kisha tena wakarudisha nyuso zao kwa Malkia.



“Tunaweza kuuona?”



Zura na Malkia wakatazamana. “Nadhani umekwisha uona.” Zura alijibu.



“Namaanisha tunaweza tukaushika?” Alipendekeza bibi mmoja, wenzake wakatikisa kichwa kuonyesha wanaunga mkono hoja. Zura wakatazamana tena na Malkia.



Macho yao yalikuwa yana hofu na maswali ya mashaka ndaniye. Ila mwishowe Malkia aliuvua mkufu wake akawapatia. Kila bibi alinyoosha mkono wake ili autwae mkufu huo. Mwenye mkono mrefu aliupata akiwa wa kwanza, ila punde mkufu huo ulipofika kiganjani mwa bibi huyo ukawaka na kuwa wa moto.



Uliunguza mkono wa bibi aliyeupokea, bibi akaudondosha chini! Haraka bibi wote walisogea mbali na mkufu huo uliokuwa unawaka na kutoa nuru kubwa ndani ya nyumba.



Wakati wakifanya hivyo walikuwa wanateta na lugha yao isiyoeleweka. Malkia alichutama akautwaa na kuuvaa mkufuwe.



“Umetoa wapi hiki kitu?” Aliuliza bibi mmoja akimtazama Malkia.



“Nimeutoa kwa baba yangu.” Malkia alijibu.



“Baba yako anakaa wapi?”



“Alikuwa anakaa Maam. Amefariki kwa sasa!”



Wale bibi wakatazamana na kuteta kwa muda wa kama dakika tano kisha wakarudisha tena nyuso zao kwa Malkia.



“Unaweza ukatupeleka kwenye kaburi lake?”



“Mkafanye nini?”



“Kuna mambo machache tunataka kuongea naye.”



“Mtaongeaje na mtu ameshakufa.”



“Tunaweza kuongea na wafu. Tafadhali tupeleke.”



Malkia Sandarus alitazamana na Zura kisha akarudisha uso wake kwa bibi wale waliokuwa wanamtazama kwa uso wa ukame na hamu ya majibu.



“Nikiwapeleka mtanipa nini kama mrejesho?”



“Tumekupa hifadhi!”



“Hapana, hifadhi pekee haitoshi. Bila shaka kuna jambo kubwa mnataka kuling’amua.”



Bibi wale walitazamana wakateta kwa lugha yao ya kipekee kwa dakika moja kisha wakamrudia tena Malkia.



“Tutakueleza matumizi yote ya mkufu huo.”



“Malkia wangu, ni hatari kufuata hayo wanayoyataka.” Alinong’oneza Zura. “Huwezi jua wana lengo gani.”



“Usijali, nitalitilia hilo maanani.” Malkia alinong’oneza kumwambia Zura. Alikubaliana na bibi wale kuwapeleka huko makaburini, wale bibi wakafurahi mno.



Waliwataka Zura na Malkia Sandarus wawafuate kuelekea uani kwani kuna njia ya haraka kufika huko Maam ndani ya muda mfupi. Zura na Malkia wakatii.



Walielekea huko wakakuta chungu kikubwa cheusi kilichokuwa kinafuka moshi wa kijani. Wabibi wale walikizingira chungu hiko na kusema maneno kadhaa kabla hawajatia majani fulani humo chunguni na kuwaamuru Malkia na Zura waingie.



Ili kuwapa imani na kuwaondoa hofu, bibi wawili walitangulia kuingia humo chunguni. Walizama wasionekane wapi walipoelekea. Zura na Malkia walifuatia nao wakazamia, wakafuatiwa na bibi mmoja aliyebakia.



Yani kufumba na kufumbua tu wakajikuta ndani ya himaya ya Maam! Kwa Malkia na Zura likawa la kushangaza sana hilo. “Ueleko upi yapo hayo makaburi?” Aliuliza bibi mmoja upesi.



Malkia akawawelekeza na punde wakaanza kuelekea huko. Walipofika bibi wale walizingira lile kaburi la baba yake Malkia na punde likafunguka!



Alitoka humo mtu mithili ya zombie. Akiwa kama mtu anayejua alichoitiwa alielekea moja kwa moja kwa wale bibi, akaongeleshwa na lugha isiyoeleweka. Alitikisa kichwa mara mbili kuitikia. Alipotikisa kichwa mara ya tatu alimgeukia Malkia Sandarus na Zura.



Macho yake yalikuwa yanang’aa kwa wekundu. Uso wake japokuwa haukuwa na nyama lakini ulionekana kughafirika. Alipiga hatua ndefu kuwafuata Malkia na Zura na mkono wake wa kuume ulikuwa unanyooshea kifuani palipokuwa na mkufu!



Hapo Malkia akaamka toka usingizini. Kumbe ilikuwa ni ndoto! Akiwa anahema kwa pupa na macho yake yakiwa yamemtoka, alitazama kushoto kwake. Huko akawaona wale bibi wakiwa wamesimama.



Walikuwa vilevile kama alivyowaona ndotoni. Alimuamasha Zura upesi, bibi mwenye macho mawili akawauliza:

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

“Nyie binadamu mnafanya nini Tanashe?”



Malkia akatahamaki zaidi kwani lilikuwa ni swali lilelile aliloulizwa akiwa ndotoni.



Na sasa hapo ndipo akajua ya kwamba yale aliyoyaona ndotoni yalikuwa ni yale yatakayotukia mbele yake.



Sasa afanyaje?

.

Nyie binadamu mnafanya nini Tanashe?” Malkia akatahamaki zaidi kwani lilikuwa ni swali lilelile aliloulizwa akiwa ndotoni. Na sasa hapo ndipo akajua ya kwamba yale aliyoyaona ndotoni yalikuwa ni yale yatakayotukia mbele yake.



Sasa afanyaje?



Hakuwa na muda wa kumueleza Zura juu ya yale aliyopata kuyashuhudia ndotoni. Waliongozana na bibi wale kama ilivyokuwa kwa mujibu wa ndoto mpaka pale walipofika kwenye nyumba kubwa nyeusi ambamo waliingia na mjadala kuhusu mkufu ukazuka baada ya muda mfupi, bibi wale wakiwa wanataka kuuona na kuugusa.



Hii ndiyo nafasi! Akaamini Malkia Sandarus. Kama kweli alikuwa anataka kuokoka dhidi ya wale vigagula basi ilimbidi atumie mwanya huu vema. Aliuvua mkufu wake akiwa anajua fika ya kwamba utawaunguza wale viumbe.



Alipomkabidhi bibi mmojawao, ulimuunguza akaudondodha chini. Malkia akauwahi mkufu wake na kuwanyooshea kana kwamba silaha.



“Kaa mbali!” Alifoka. Bibi wale walisogea mbali na walihofia. Walikumbatiana kwa woga na ni wazi nyuso zao za kizee zilizojikunja zilionyesha hofu. Malkia alimtazama Zura akamtaka anyanyuke kitini waondoke upesi. Zura akatii.



Walisogelea mlango, bado Malkia akinyooshea mkufu wake kwa wale bibi, wakaondoka kumfuata farasi waliyemkwea na kumuamrisha aondoke haraka! Farasi alikimbia upesi na ndani ya muda mfupi alikuwa amemezwa na giza asionekane hata mahali alipoelekea.



“Umeruhusuje akaondoka?” Alilalama bibi mmoja kana kwamba hakuwepo wakati tukio linatokea.



“Ila hawezi akafika mbali,” Mwingine naye akasema.



“Ndio, hawezi akafika mbali. Ila tumeshakosa ule mkufu. Vipi kama wakiupata wachawi wengine?” Aliuliza mmoja kwa jazba. Ilikuwa ni ngumu kweli kuwatofautisha tangu kila mmoja alikuwa na jicho moja tu.



“Endapo wakiupata wachawi wengine basi itakuwa mbaya sana kwetu.” Aliendelea kuongea.



“Sasa tutafanyaje?” Akauliza mwingine.



“Inabidi tuwafuatilie mpaka pale tutakapoupata mkufu huo. Hatuwezi tukaipoteza hii nafasi!” Alilonga mmoja kwa shari. Haraka bibi hao watatu waliungana wakatengeneza mtu mmoja mkubwa mno mwenye macho matatu.



Mikono yake ilikuwa imejaza kimraba na miguu yake ilikuwa mipana kama shina la gogo. Kabla hajaondoka kwenda kuwafuatilia Malkia na Zura, alinguruma kama simba. Kunguru wote waliokuwa wanazunguka hilo eneo wakakimbia wakitawanyikia kila pande.



Mtu huyo mkubwa, ama tunaweza kumuita jitu, alikimbia upesi akitupa miguu yake chini na kusababisha kishindo kikubwa, kishindo ambacho hata kama ungelikua maili moja mbali basi ungelipata kukisikia.



Kichwa chake kilichokuwa juu kilimuwezesha kutazama kila pande na basi akawa anabashiri wapi anaowatafuta wameelekea. Kila alipopita miti ilitikisika na viumbe wakakimbia kuokoa maisha yao.



Baada ya kukimbia kwa muda wa dakika nne tu, sauti yake ya kishindo ikawafikia Malkia na Zura ambao bado walikuwa juu ya mgongo wa farasi.



“Malkia, wanakuja!” Zura alisema kwa hofu. Malkia hakutia neno, zaidi alimwamrisha farasi wake aongeze mwendo.



Haikujalisha ni kwa namna gani farasi alivyokimbia, jitu lilizidi kuwakaribia zaidi na zaidi. Hata kwa mtoto angeliweza kubashiri ndani ya muda finyu Malkia na Zura watakamatwa.



“Malkia, anazidi kutukaribia!”



Malkia aligeuza uso wake kutazama. Hapo farasi akajikwaa. Alidondoka akawamwagia Malkia na Zura mbali! Malkia alibiringita mara tatu wakati Zura akibiringita mara tano kabla hajatulia tuli.



Malkia alinyanyua uso wake akamtazama Zura, hakuonekana kama ana fahamu. Alimtazama na farasi wake akamuona anagugumia kwa maumivu.



Kwa muda kidogo hakujali kama anakimbizwa bali kutazama usalama wa wenziwe. Alipokuja kutazama anayewakimbiza, alishangaa kumuona tayari amemfikia mguuni! Alijaribu kunyanyuka, akakandikwa kofi zito akazirai.





Jitu lilimbeba Zura na Malkia likaondoka nao. .

.

.

.

.

*** HAKUNA ZAIDI … ZAIDI YA MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

Jitu lilifika nyumbani kwake akawatua mateka wake. Punde akaparanganyika na kuwa wale bibi watatu.



“Tunawaua?” Mmoja aliuliza.



“Hapana!” Mwingine akajibu. “Tunamuhitaji zaidi akiwa hai.”



“Kwanini?”



“Huyu ni Malkia!” Alifoka. “Tukimtumia huyu Goshen itakuwa chini yetu.”



“Tukimtumiaje?”



“Tukimtumiaje! – Kwani hujui? Mbona akili yako imelala sana wewe?”



Kukawa kimya kidogo.



“Tukikamata kichwa cha Malkia, tutapata yale yote tunayoyataka toka Goshen!” Alisema mmojawao. Walifurahi wakionyesha vinywa vyao vyenye uhaba wa meno.



Ulikuwa ni wasaa mzuri sasa kurudi kwenye ardhi ya Goshen baada ya kufukuzwa huko kwa muda mrefu tangu pale walipogundulikana ni wachawi.



Ilikuwa ni desturi. Tanashe ni tawala ya wachawi ambao wamerundikwa hapo toka kwenye tawala mbalimbali baada ya kuvumbuliwa toka kwenye jamii zao ya kwamba ni wachawi.



Kwa mtu yeyote pale anapogundulikana kuwa na sifa zozote za kilozi, basi adhabu yake huwa ni kumtupia kwenye ardhi hiyo ya Tanashe – ardhi iliyolaaniwa.



Ardhi isiyo na maji wala chakula. Na kama mtu ni kweli alikuwa mlozi, akishaingizwa Tanashe huo unakuwa mwisho wake kwani hawezi toka tena humo kurudi tawala aliyotokea.



Mipaka yake imetiwa dawa madhubuti ambayo hakuna mchawi yeyote anayeweza kuvuka na kwenda kwenye tawala yoyote za karibu. Huko ndani ya Tanashe atajua anakula ama kunywa nini. Atajua anaishije muda uzidi kusonga.



Wachawi wengi walipoteza familia zao. Hawakuweza tena kuona aidha watoto, wake ama waume zao baada ya kupelekwa Tanashe.



Si tu kwamba kwasababu hawakuweza kutoka humo, bali pia binadamu wa kawaida wasio wachawi hawakusogelea tawala hiyo. Watu kadhaa ambao walijaribu kuingia humo waliishia kuwa vitoweo na isijulikane hata walipoelekea.



Sifa kubwa ya tawala hiyo ya Tanashe ilikuwa ni kutokuwa na alama yoyote ya binadamu pale jua linapochomoza. Kama ungelikuwa karibu na mpaka ukatazama ndani ya tawala hiyo muda wa mchana, usingeona chochote bali mithili ya jangwa.



Lakini ifikapo usiku, mji unakua na unaweza ukawaona watu wanakatiza katiza. Na kama basi upo karibu, si ajabu kuona mtu anakutazama huku akikulaghai kwa kukuita.



“Usisogelee karibu na Tanashe!” Lilikuwa ni mojawapo ya onyo maarufu walilokuwa wanapewa watoto na aidha wazazi wao ama watu wazima.



Hakuna mtoto aliyepotea kwa kuingia humo alafu akapatikana. Inasemekana wakiingia humo nao wanawakuwa walozi.



Kuelekea upande wa kaskazini wa tawala ya Tanashe ndipo kulipokuwa kunapatikana tawala ya Devonship chini ya katili Jayit. Tofauti ndogo zilizokuwepo kati ya tawala hizi ni swala la uongozi na pia mawio na machweo ya jua.



Tanashe haikuwa na kiongozi, bali tu kila eneo lina mchawi anayelitawala. Lakini pia vilevile jua lilikuwa linachomoza na kuzama kwenye tawala hiyo. Kinyume na Devonship, mtawala alikuwa mmoja tu tawala nzima: Jayit, na ndani ya tawala hiyo jua halikuwahi kamwe kuonekana!



Mkufu wa Malkia uliviringishwa ndani ya kikaratasi cheusi na mmoja wa wale bibi. Alipomaliza kuufungasha vema mkufu huo, aliwatazama wenzake wakaanza kujadili ni namna gani ya kuufanya mkufu huo.



Ila wakiwa wanajadili wakagundua kuna umuhimu wa kujua ni wapi mkufu huo ulipotokea kwa minajili kwamba ndipo itakuwa rahisi kwao kuuongoza lakini hata kuuamrisha kutokana na matakwa yao.



“Tunaweza kutawala Tanashe na mkufu huu!”



“Sio tu Tanashe. Tunaweza tukarejea Goshen kwenye familia zetu na kutawala huko!”



Walienda uwani mwa nyumba yao kubwa, huko waliteka kioo cha saizi ya kati na fuvu mbili za vichwa vya binadamu. Waliviweka pamoja juu ya meza.



Meza hiyo pia ilikuwa imeshikiliwa na mifupa ya miguu ya binadamu. Walifungua kile kikaratasi kilichofichama mkufu kwa malengo kwamba wautoe mkufu huo na kuutazamisha kwenye kioo ili wapate kuona kwa kupitia kioo chao, wapi haswa chimbuko la mkufu huo.



Mmojawao akiwa ameushikilia huo mkufu kwa kile kikaratasi ili asipate kuungua, aliutupia huo mkufu juu ya kioo, na kisha kwa pamoja wakasema maneno yasiyoeleweka.



Punde macho ya fuvu zile mbili za binadamu yakaanza kufuka moshi wa kijani. Moshi huo ulitanda karibia eneo lote. Bibi wale walitabasamu wakijua sasa pale moshi utakapokoma wataweza kuona yale wanayoyataka ndani ya kioo chao cha ajabu.



Moshi ukakoma.



Walitazama kwenye kioo upesi wakiwa na nyuso za hamu. Ajabu hawakuona chochote!



“Unaona kitu?” Mmoja aliuliza.



“Hapana, sioni. Najiona mwenyewe na nyie.”



Punde kioo kikaanza kupiga ufa kana kwamba ukuta. Kklaakk! Kakkaakakakk! Kakaaakkak! Kufumba kufumbua kikapasuka kwanguvu. Vipande vyake viliruka juu na vikawaingia machoni mwa wale bibi wakaishia kulalama kwa maumivu wakishikilia nyuso zao.



Haikupita punde, wakasikia sauti za fisi mbele ya nyumba yao. Kila mmoja alinyofoa jicho lake akalipangusa dhidi ya vioo na kuyarudisha tena usoni.



“Nani huyo?” Mmoja aliuliza.

“Si mwingine bali ni Faki!” Mwingine akajibu.

“Atakuwa anataka nini?”



Swali hilo lilikosa majibu. Waliuchukua mkufu kwa kutumia kile kitambaa mmojawao akauficha sehemu za siri na kisha wakaenenda huko nje waliposikia sauti ya fisi akibweka.



Walikuta fisi wakubwa karibia mia moja na hakukuwa na alama yoyote ya binadamu.



“Unahitaji nini Faki?” Bibi mmoja aliuliza. Wote walikuwa wamekunja mikono yao wakiiweka kifuani.



Fisi walikaa kitako, kutoka nyuma yao akasogea fisi mkubwa kuliko wote. Alipojongea mbele aligeuka na kuwa binadamu mrefu mwenye misuli ya kutosha.



Alikuwa mweusi mwenye ndevu nyingi. Uso wake ulifanana na fisi kabisa. Hakuwa amevalia kitu chochote, hivyo alikuwa uchi mnyama. Alisogea karibu na bibi wale watatu akapandisha nyusi moja juu.



“Nahitaji mlichokichukua kwangu,” Alisema Faki kwa kujiamini.



“Kipi tumechukua kwako?” Bibi mmoja aliuliza. Faki akatabasamu kwa kejeli.



“Hamjaingia kwenye himaya yangu leo hii?” Aliuliza. Bibi wakatazamana na kisha mmoja akajibu:

“Tumeingia lakini tulikuwa tunafuata kitu chetu.”



Faki akatabasamu.



“Hamuwezi mkafuata kitu chenu kwangu. Kitu kikiwa kwenye himaya yangu, ni changu. Naomba mnipatie sasa hivi!”



“Faki, hatuwezi tukakupa kisicho chako,” alisema bibi mmoja.



“Ila mliweza kuingia kwenye eneo langu, si ndio?” Akauliza Faki. Kukawa na kaukimya kafupi.



“Sina muda wa kupoteza hapa na nyie vikongwe. Naombeni kilicho changu niende.”



“Unakijua hata hicho unachodai ni chako?” Aliuliza bibi.



“Najua ndio,” akajibu Faki. “Ni binadamu – wawili!”



“Tutakupa mmoja.”

“Nataka wote!”

“Tutakupa mmoja tukagawane.”

“Nimesema nataka wote!”

“Basi hautopata kitu!” Alisema bibi mmoja kwa kujiamini akimtazama Faki machoni.



Faki alirudi nyuma kuungana na fisi wenzake. Ndani ya muda mfupi aligeuka mwili akawa fisi mkubwa kama alivyokuwa hapo awali. Pasipo kupoteza muda, bibi nao wakajikusanya na kuwa mtu mkubwa mno mwenye macho matatu.



Alinguruma kama simba akielekeza mdomo wake angani. Faki alibweka naye kwanguvu kisha akaamrisha fisi mia moja aliokuja nao wamshambulie yule mtu mkubwa – jitu!



Kufumba na kufumbua ikawa vita!





Fisi wakamrukia yule jitu wakamrarua na kumng’ata. Lakini naye jitu asiwe nyuma alikuwa anawakamata na mkono wake mkubwa akawavunja vunja ama kuwatupia mbali.



Makelele ya fisi na ya jitu yalitapakaa. Malkia Sandarus na Zura waligutuka toka kwenye usingizi mzito wa kutokuwa fahamuni. Walikuwa wamefungiwa kwenye kichumba kidogo cheusi chenye dirisha dogo juu.



Kwa mujibu wa dirisha hilo, anga lilikuwa linaanza kung’aa kuelekea asubuhi ya mapema zaidi.



“Zura, mkufu upo wapi?” Aliuliza Malkia. Alikuwa anaogopa, kama ungelimuona tu uso wake basi ungeling’amua hilo.



“Sijui Malkia wangu,” Zura alijibu. Malkia alipapasapapasa shingo yake lakini hakuona kitu, mkufu haukuwepo! Aliendea mlango wa chumba hicho akajaribu kuufungua, akashindwa.



Zura alimtengea Malkia wake mkono kama ngazi, Malkia akaupanda na kuchungulia nje kwa kupitia ka mwanya ka dirisha. Huko nje akaona pambano kubwa kati ya fisi na lile jitu kubwa. Aliperuzi huku na kule kutafuta lakini hakuona mkufu wake.



Ndani ya muda mfupi wakasikia mlango unafunguliwa. Haraka walifuata mlango huo, wakamkuta farasi wa Malkia! Ilikuwa ni ajabu. Kwa kutumia mdomo wake, farasi huyo alipindua kitasa akijua fika ndaniye mulikuwa na dereva wake, malkia wake: Sandarus.



Ilikuwa ni bahati kwa farasi huyo kuachwa peke yake pale Zura na Malkia walipotwaliwa. Yule jitu, ama wale bibi, hawakuona umuhimu wa kumchukua farasi huyo. Walimuacha wakitumai hatodumu muda mrefu kabla hajaliwa na viumbe vingine ndani ya Tanashe.



Hawakufahamu kwanini farasi huyo alikuwa ni wa Malkia. Hawakujua kwamba kiumbe huyo ana uwezo wa kumtafuta Malkia wake popote pale ndani ya maili tano. Mnyama pekee ndani ya Goshen anayemjua bwana wake na hayupo radhi kumtumikia mtu mwingine yeyote zaidi ya huyo.



“Roob!” Aliita Malkia akimkumbatia farasi wake. Alimkwea yeye pamoja na Zura akamuamuru kuzunguka ndani ya nyumba ile kubwa wakitafuta mkufu wake.



Walizunguka kote lakini hawakuuona. Walizunguka uani wakawa wanachungulia mpambano ambao bado ulikuwa unaendelea – kati ya fisi na jitu. Lengo lao lilikuwa ni kutafuta mkufu wa Malkia. Jitu alikuwa amejeruhiwa vibaya mno akivuja damu, na hata fisi nao hawakuwa wengi – kama arobaini tu ndio bado walikuwa hai.



Kitendo cha Malkia kuchungulia, mkufu ulianza kuhangaika ndani ya sehemu za siri za jitu.



Ulijinyongorota ukaenda huku na kule kwa nguvu ukitaka kuchoropoka. Ulimsumbua jitu huyo kiasi kwamba akapoteza kabisa atensheni kwenye mpambano. Fisi walimshambulia vibaya mno. Walimdondosha chini na kuendelea kumng’ata. Mkufu ulitoka ndani ya vazi lake ukaenda upesi kwenye mkono wa Malkia. Haraka Malkia akamruhusu farasi wake akimbie!



Sauti ya farasi akikimbia ikakamata masikio ya fisi. Faki – fisi mkubwa kiongozi – akaamuru fisi wote kumkimbiza farasi yule aliyebebelea binadamu. Fisi wote walio hai wakaanza kumfukuza farasi huyo kwa kasi. .



.

.

.*** HAKUNA ZAIDI … ZAIDI YA MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! *** .

.

.

.

.

Farasi wa Malkia alikimbia upesi. Mbio zake hazikuweza kumithilika na zile za fisi wanaomkimbiza. Japokuwa fisi walikuwa wanakimbia taratibu ukilinganisha na farasi wa Malkia, hawakuonekana kuchoka ama dalili za kukata tamaa!



Kama ingelikuwa muda ulikuwa upande wao basi wangelihakikisha wanawapata binadamu wale juu ya mgongo wa farasi, ila jua la asubuhi lililokuwa linachomoza likawakatisha hamu, tena wakiwa wamekaribia kumkamata farasi huyo aliyetupa miguu yake kuvuka mpaka na kuingia ardhi ya Goshen.



Fisi hao waligeuka na kuanza kukimbia kurejea kwenye makazi yao. Kadiri walivyokuwa wanakimbia, na jua lilivyokuwa linachomoza, walikuwa wanageuka kuwa binadamu.

.

.





Mwishowe walipotea isijulikane wapi wameelekea. Malkia na Zura waliwatazama wakiyoyoma huku mioyo yao ikidunda kwa mjazo wa hofu na mashaka.



Ilibaki kidogo tu wangekuwa habari nyingine, waliamini hivyo. Walimeza mate wakiwa wanahema kabla hawajageuza kwenda kwenye makazi ya Zura.



Jambo hilo lilifanyika kwa siri mno, Malkia hakuhitajika kuonekana. Zura alihakikisha hilo linatimia mpaka wanafika nyumbani kwake alipokuta mzoga wa mumewe ukiwa umelazwa chumbani.



Zura aliumizwa sana na hilo tukio, akalia sana. Kwa kusaidiana na Malkia walifukua kaburi na kumzika mwanaume huyo ndani ya nyumba ili wasipate kuonekana, kisha wakajipumzisha.



Walikuwa wamechoka mno. Karibia usiku wote hawakuwa wamelala, lakini pia walitumikisha viungo vyao haswa kurandaranda huku na kule hivyo walivyojilaza tu kitandani usingizi haukuwaonea huruma, ukawakomba.



Walikoroma kwa usingizi baada tu ya muda mfupi.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

Jua lilisimama, na kama ingelikuwa ni nyakati za sasa za kutumia saa basi bila shaka kwa muda huo ilikuwa ni saa nne ya asubuhi.



Siku ilikuwa nzito haswa. Uwanja mkubwa wa tawala ya Goshen ulikuwa umefurika mno, na kabla haujaingia ndani basi ungekutana na rundo kubwa la rafasi waliowaleta wageni toka tawala mbalimbali waje kushuhudia kusimikwa kwa kiongozi mpya wa ardhi hiyo, Bwana Fursa.



Nyimbo zilizosindikizwa na vifaa vitamu kama vinubi na firimbi, ziliita kwenye kila kona ya uwanja. Watalaamu wa kucheza walijimwaya uwanjani wakisogeza muda taratibu, huku wasiwe peke yao wakasindikizwa na vinywaji na vyakula vya kumwaga.



Katikati ya uwanja bendera ya kila tawala ilisimikwa ikawa inapeperuka kwa madaha. Kulikuwa kuna tawala tano uwanjani kwa kujibu wa idadi ya bendera; bendera nyekundu yenye jua jeupe katikati ikiwakilisha tawala ya Maam; bendera nyeusi yenye matone meupe kumi na saba ikiwakilisha tawala ya Kusi; bendera nyeupe yenye mikuki miwili meusi iliyokinzana ikiwakilisha Goshen; bendera ya bluu yenye mchoro mkubwa wa samaki ikiwakilisha Theon; na bendera ya mwisho ikiwa na rangi nyeusi, nyekundu na nyeupe bila ya mchoro wala picha yoyote ikiwakilisha tawala ya Bhotu.



Karibia waanchi wote wa Goshen walikuwepo hapo. Wachache ambao hawakuwepo walikuwa aidha vilabuni wanakunywa pombe zao ama wapo mashambani wanawajibika.



Lakini kila mtu alikuwa na ratiba ya kuja eneo hilo, kilichowatofautisha ni ratiba tu. Miongoni mwao wengi walikuwa wanangojea jua likikaribia kufika katikati ya anga ndipo waanze safari kujisogeza.



Kwa mujibu wa desturi ya Goshen, mfalme husimikwa pale jua linapokuwa katikati ya anga. Hiyo ni ishara ya kuonyesha utawala wake utakuwa wa haki usio na pendeleo na pande yoyote. Unapofika muda huo tu, watu hufurahia wakimtazama mfalme akivekwa taji la kifalme.



Matarumbeta hupigwa, vigelegele vinapigwa na jeshi linasalimu amri mbele yake.



Watu wote uwanjani wakiwa wanangoja muda huo adhimu, Fursa akiwa katikati ya wapambe wake watatu, aliitwa kando na mwanamke mnene ila mwenye umbo lisilojificha. Alikuwa ni malkia, mke mkubwa wa mfalme aliyefariki. Aliinama akamng’ata Fursa sikio kabla mwanaume huyo hajanyanyuka upesi na kusogea mbali kidogo na umati.



“Naona unanisahau, Fursa.” Alisema malkia huyo akiwa amekaza sura.



“Sijakusahau Veda.” Akajitetea Fursa.



“Kumbuka bila mimi usingelikuwa hapa.”



“Najua, Veda. Tutaongelea tu haya mambo, usijali.”



“Lini na leo ndio unaapishwa kuwa mfalme?”



“We jua tutaongea kwani kuna haraka gani? Endapo tukifanya haraka tutawapa watu mashaka!”



“Sawa. Ila kaa ukijua kwamba, ukimwaga mboga mie n’tamwaga ugali. Ukianza mie n’tamaliza!”



Baada ya Veda kutoa tisho hilo, alitimka. Fursa aliminya mdomo wake kisha naye akarejea kule alipokuwa awali. Nyuma yake alikuwa anaongozana na mababa watatu waliobebelea mikuki ya chuma.



Ila huyu baba ana siri gani na Veda, mke mkubwa wa mfalme?



Turudi nyuma.



Kabla mfalme hajafa, Veda alikuwa ana mahusiano ya siri na Fursa. Nyuma ya mgongo wa Mfalme watu hawa walikuwa wanafanya mapenzi na huku wakipeana ahadi motomoto za kuja kutawala Goshen siku za usoni.



Ilifikia kipindi Veda, mke mkubwa wa mfalme, akashika ujauzito lakini kuepusha shari alikunywa madawa na kutoa mimba hiyo, lakini bado penzi lao halikukoma, Veda akiwa amechochewa kuingia kwenye mahusiano hayo kutokana na uwezo mbovu wa Mfalme kumpa huduma kitandani.



Mwishowe, Veda alimtilia sumu mumewe kwenye kikombe cha kahawa. Tokea hapo, Mfalme akawa dhoofu lihali. Hakuweza kutembea wala kuongea vema. Macho yake yaliingia ndani akawa haoni.



Mdomo wake ulikuwa mkavu muda wote na mapigo yake ya moyo yakawa ya kusuasua ama kupiga kwa mfululizo. Alikuwa hivyo mpaka kufa kwake. Japokuwa kuna muda alishuhudia mke wake, Veda, akiwa anazini na Fursa, alishindwa kufanya chochote wala kumwambia yoyote. Hata machozi hakuwa nayo!



Sasa Veda alikuwa anamkumbushia Fursa miadi waliyowekeana: ya kwamba kiti cha umalkia ni chake pekee. Hakuna atakayekikaimu, na tena wakishakuwa mume na mke, Fursa hatokuwa na mwanamke mwingine yoyote isipokuwa yeye.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Fursa alikuwa ameshasahau miadi hiyo. Madaraka matamu bwana! Akili yake yote ilikuwa ni kutazama namna gani atakuwa anajisikia akiwa kwenye kiti cha kifalme kinachoogopwa na kuheshimiwa na wote baada tu ya miungu yao.



Muda ulisonga kwenye ardhi ya Goshen na sasa ulibakia muda mchache sana kwa jua kuwasili katikati ya anga. Shamrashamra zikawa kubwa zaidi na watu, wale waliokuwa mbali na hilo eneo, wakanyoosha miguu yao kuja eneoni maana kitovu cha shughuli kilikuwa kimekaribia kuwadia.



Fursa alinyanyuka akajongea katikati ya uwanja. Hapo aliketi akakutana na wazee watatu wa baraza ambao mmojawao alikuwa amebebelea mto mwekundu wenye taji la dhahabu na vito vya thamani.



Taji hilo ndilo lilikuwa lakaribia kupachikwa kwenye kichwa cha Fursa ambaye macho yake ya tamaa yaligoma kubanduka kwenye taji hilo lililokuwa linametameta na kuita.



Alijikuta anameza mate kana kwamba anangojea chakula kitamu kilichokuwa kinamtesa na harufu yake nzuri.



Ikiwa imebakia sasa sekunde, na Fursa akiwa amesimama tayari kwa ajili ya kupachikwa kofia na watu wote wamesimama kushuhudia hilo, ghafla mawingu yasijulikane yametoka wapi yalijikusanya kwa kasi na kubana anga. Jua halikuonekana tena na kukawa giza.



Hali hiyo ilitengeneza hofu.

.

.

.

.

.

. *** HAKUNA ZAIDI … ZAIDI YA MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.



Farasi wa Malkia Sandarus alisimama ghafla akapandisha miguu yake ya mbele juu. Mgongoni mwake alikuwa amembelea Malkia lakini pia Zura. Wanawake hao walikuwa njiani kwenda uwanjani kutengua ama kupinga kusimikwa kwa Fursa kama mfalme.



Ila kabla hawajafika huko, walistaajabu hali ya hewa inabadilika ghafla mbele ya macho yao kiasi kwamba hata farasi pia alihofia!



Walitahayuri, na bado wakiwa hapo wakasikia sauti kubwa ya kishindo inakuja. Haraka Zura alikamata bega la Malkia akapayuka:



“Malkia, ni Jayit anakuja!”



Malkia alikuwa mgumu kuelewa, ila baada ya muda mfupi alielewa kile alichokuwa anakinena Zura: Jayit anakuja! Hakuna mahali Jayit anakanyaga pakawa na mwanga wa jua. Kila mtu anajua kwenye utawala wa Devonship hakuna kitu kinaitwa jua wala mwanga wake.



Ina maana sasa Jayit anakuja!



Ilikuwa ni taharuki. Malkia hakutaka kuacha tawala yake akimbie. Alitaka kuhakikisha anamuona Jayit lakini pia kumzuia asidhuru watu wake. Akiwa humo tahamuni, akakumbuka jambo, ila kwa muda alikuwa amekawia kufanya lolote.



Wakati akiwa amelala kuna muda alihisi kifua chake kikiwa cha moto. Ilikuwa ni mkufu wake ukiwa unampasha habari juu ya yale ambayo yangetokea muda si mrefu mbele. Ulionyesha ujio wa Jayit, lakini pia ukionyesha yale ambayo angeyafanya mwanaume huyo kwenye tawala ya Goshen.



Masikini Malkia hakuweza kusikia wala kuona yote hayo. Usingizi mzito mno aliokuwa nao ulimnyima hiyo fursa. Alikuwa amechoka mno na mwili wake ulikuwa unahitaji sana kupumzika.



“Malkia, tuondoke!” Alisisitiza Zura. “Huu sio muda wa kubakia tena hapa. Kama kweli unaipenda Goshen, ni bora tukaondoka sasa. La sivyo utauwawa na hautopata tena fursa ya kuwa nao wala kuwasaidia.”



Huo ulikuwa ukweli mchungu kwa Malkia. Machozi yalimtiririka. Alimgeuza farasi wake akamkimbiza kuelekea upande karibu zaidi wa mpaka wa Goshen.



Waliridhia kuelekea utawala wa Maam, huko wakafanye kuyachimbua mengi juu ya mkufu ule alionao Malkia. Waliamini kwasababu mkufu huo umetoka huko basi ni lazima kutakuwa kuna mabaki ya historia juu yake. Historia ambayo inaweza ikawapa muelekeo wa kipi cha kufanya na namna gani ya kufanya.



Kutokana na giza lililokuwepo, baada ya muda hatukuwaona walipoelekea. Hata rangi nyeupe ya farasi ilikuwa imemezwa.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

Farasi wengi weusi walisimama mbele ya uwanja mkubwa wa Goshen. Watu wegine walikuwa wamekimbia kwa kuogopa, ila wengi wao walibakia eneo hilo wakiamini ya kwamba ndipo ni salama kuliko pengine.



Wanajeshi walikuwa wamejaa, hivyo walitumai endapo litakapotokea lolote basi wanajeshi hao watalinda pumzi zao.



Wanaume waliokuwa wamebebelewa kwenye farasi hao weusi walikuwa ni watu wenye miili mikubwa. Walikuwa na nywele nyingi na mikononi mwao walikuwa wamebebelea mapanga marefu yaliyokuwa yanametameta kwa ukali.



Toka katikati ya farasi hao ambao walikuwa wamajipanga kwa nidhamu kubwa, alitokea mwanaume mrefu mwembamba. Nywele zake zilikuwa ndefu mno zilizogota kwenye mabega. Macho yake yalikuwa mekundu kama amevuta marijuana. Mdomo wake ulikuwa mweusi kama wa kunguru. Alitisha kumtazama. Alitisha akikutazama.



Alikuwa ni Jayit!



Mkononi mwake alikuwa na panga jembamba zaidi ya walinzi wake, ila lilikuwa refu na kishikizi chake kilikuwa na fuvu dogo la kichwa cha binadamu.



Uwanja mzima ulikuwa kimya. Japokuwa wengine hawakuwa wanamuona Jayit, walikuwa wanahisi uwepo wake. Kitendo cha jua kuzizima ilikuwa ni alama tosha.



Jayit alitembea kumfuata Fursa. Alipofika hata salamu hakutoa, akasema:



“Nahitaji makaburi.”



Sauti yake ilikuwa ya chini lakini nzito mno. Fursa kabla hajajibu alitazama kwanza uwanja mzima, akaona jinsi watu wanavyomtazama. Hakutaka kuwaangusha, tena akiwa ni kiongozi ambaye muda si mrefu kuna uwezekano wa kuwa mfalme.



Alikataa kumpa Jayit uwanja wa makaburi, lakini pia akamtaka mwanaume huyo aondoke kwenye ardhi ya Goshen upesi!



Jayit alitabasamu tabasamu la upande mmoja kisha akaguna. Alimtazama Fursa kwa macho yake makali. Fursa alitetemeka mwili mzima. Jayit alitabasamu tena kisha akaliza vidole vyake … pat!



Mara giza likaongezeka maradufu. Sasa hakukuwa na uwezekano wa kuonana na yeyote yule!



Jua lilikuja kurejea baada ya dakika tano ama zaidi. Si Jayit wala watumishi wake walioonekana mahala popote pale! Fursa, akiwa ameongozana na walinzi wake kadhaa, alielekea upesi kwenye eneo la makaburi. Huko alikuta makaburi mawili yamefukuliwa na mifupa haipo. Makaburi hayo yalikuwa ya babu na bibi wa Jayit.



Sasa Jayit alikuwa amepata kile alichokuwa anakitaka kwa muda mrefu. Hakuna aliyekuwa anajua ataenda kufanyia nini hayo mabaki, na ilimuogofya kila mtu.



Hakuna aliyedhani mtu kama Jayit anaweza akawa na dhamira safi. Hakuna! Na hakuna pia aliyekuwa na uthubutu wa kwenda kwenye tawala yake kumuuliza ilhali sasa alikuwa tayari ameshatimka.



Ilikuwa tumbo joto.



Zoezi la kumsimika mfalme lilisitishwa maana jua lilikuwa tayari limeshatoka katikati ya anga, na watu pia hawakuwa kwenye munkari wa hilo zoezi tena bali uwoga. Fursa alighafirishwa mno na hilo. Uso wake ulikuwa mwekundu na kwake kesho ilikuwa mbali mno.





Kusogezwa kwa zoezi hilo mbele kilikuwa kikombe kigumu sana kukitia mdomoni.



Hakutaka kuongea na mtu yeyote bali kwenda kujifungia ndani ya chumba chake alimojitupia kitandani na kuanza kutafakuri. Aliwaza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa tukio.



Kwa namna moja ama nyingine alijiona mjinga kwa kutaka kuitawala Goshen nafasi ambayo itamuweka roho yake rehani kutokana na maadui kadha wa kadha, ila baada ya pia kuchambua faida atakazopata akiwa katika hicho kiti, basi akajiona sahihi kuwinda kiti hicho cha kifalme kwa juhudi zote.



“Hakuna atakayenizuia.” Alisema mwenyewe akisaga meno. Macho yake yalikuwa mekundu na mdomo wake aliubinua, ila baada ya muda mfupi akanywea, ni baada ya mawazo juu ya Jayit kumjia kichwani.



Aliwaza na kuwazua namna gani ataweza kumdhibiti mwanaume huyo mdhalimu. Lakini pia aliwaza mwanaume huyo amepanga nini kwa Goshen siku za usoni? Mpaka anachoka, hakuwa amepata jibu lolote.



Aliamua kupuuzia akaugeuza mwili wake upande wa pili wa kitanda. Usingizi ulimjia, ila kabla hajalala akasikia hodi, na kabla hajaitikia, mtu akaingia. Alikurupuka akatazama kwa hasira, ila ghafla uso ukatengeneza tabasamu.



Alimuona mwanamke mrefu mwembamba mwenye shepu ya kuvutia na macho ya kuibia. Alikuwa anatembea kwa madaha, nywele zake ndefu zikiwa zinamghasi. Kifua chake kilikuwa kimejaa. Mdomo wake mwekundu ulikuwa na umbo la kopa.



Anajulikana kwa jina la Rhoda, ama Roy – mwanamke mrembo ndani ya tawala ya Goshen.



Aliendea kitandani akaketi. Na kabla ya kumpa salamu Fursa alimpa kwanza mabusu matatu motomoto kisha akamtazama mwanaume huyo kwa macho ya kulaghai.



“Hata mimi hutaki kuniona?” Aliuliza. Fursa akatabasamu na kumshika kidevu mrembo huyo.



“Nawezaje kukataa kuonana na mwanamke kama wewe, malkia wangu ajaye.”



Rhoda akatabasamu. Kisha akambusu tena mwanaume huyo pasi na kikomo.





***





Ni baada ya masaa matano ya kuwa njiani ndipo Malkia na Zura wakafika ndani ya himaya ya Maam wakiingia upande wa kusini wa tawala hiyo.



Farasi alipunguza mwendo akawa anatembea mpaka wanafika mbele ya nyumba ya babu na bibi wake Malkia Sandarus. Walibisha hodi mara mbili akatoka mwanamke kikongwe ambaye hakuwatambua wageni mpaka pale walipojitambulisha.



“Mjukuu wangu Sandarus!” Bibi alitahamaki. Alimshika mjukuu wake usoni akiwa anatabasamu. Ulikuwa umepita muda mrefu sana hakumuona mjukuu wake kipenzi: miaka kadha wa kadha, alitegemea hata kufa pasipo kumuona. Alimkumbatia mjukuu wake kwanguvu kisha akamwambia:



“Nyumba yangu ni ndogo sana kuruhusu wageni wako.”



Malkia Sandarus akatabasamu.



“Bibi sijaja na watu, nimekuja na mtu mmoja tu.”



Bibi alishangaa lakini pia akapata hofu, iweje malkia atoke umbali wote huo kuja pale akiwa na mtu mmoja? Malkia alimtaka kwanza bibi yake awaruhusu kuingia ndani kisha atamueleza yote.



Wakaingia ndani na kumweleza kila kitu kikongwe huyo mpaka kufikia hapo. Walimwambia wanahitaji kujua mahali mkufu huo umetoka na nini hasa nguvu yake. Bibi akauomba huo mkufu autizame, Malkia akampatia.



Bibi aliupapasa mkufu huo akiutazama na macho yake mabovu. Baada ya dakika kama moja alikunja sura yake akauliza:



“Baba yako alikupa lini huu mkufu?”



“Wakati anakaribia kufariki.”



Bibi akaendelea kuupapasa mkufu huo kwa dakika tena kadhaa. Ni kama vile kuna kitu alikuwa anakisikia na alikuwa anajaribu kuwa mtulivu ilia pate kukisikia vema.



“Bibi, unaujua?”



Bibi hakujibu upesi. Alitulia kwanza alafu akashusha pumzi.



“Huu mkufu baba yako aliutoa mbali sana. Alikuwa ananambia kila siku una nguvu mno, lakini hakupata kunambia vingine zaidi. Hakunambia hata kama alilenga kukupatia huu mkufu. Alikuwa msiri sana.”



“Kwahiyo bibi hujui kabisa wapi mkufu umetoka?”



“Sijui mjukuu wangu.”



Kukawa kimya kwa muda kidogo.



“Ila …” Bibi alidokeza. Malkia na Zura wakamtazama upesi kwa hamu ya kusikia. “Kuna mahali naweza nikawaelekeza. Mahali ambapo ni maarufu kwa kazi za sonara. Huko najua hautoweza kukosa majibu kuhusu huo mkufu. Hata kama watakuwa hawajautengeneza wao, basi watakuwa wanajua wapi ilipo asili yake.”



“Wapi huko?”



“Mnasikika kama watu waliochoka. Acha kwanza niwaandalie chakula, n’tawaambia zaidi.”



Japokuwa macho yake hayakuwa mazima, bibi aliwaandalia wageni wake chakula kitamu. Ilikuwa ni mboga za majani alizoziunga vema kwa ustadi, akazichanganya na nyama ya bata mkubwa aliyemchinja mwenyewe.



Wahenga na washenga wanasema ng’ombe hazeeki maini, hilo likathibitishwa na bibi huyu. Uzee wake haukufanya mkono na ulimi wake kufeli. Aliwapa sababu wageni wake kwanini alikuwa mmojawapo wa wanawake kamili ndani ya tawala ya Maam.



“Ahsante bibi, chakula kitamu,” alisema Malkia akijilamba.



“Ndicho chakula ulichokuwa unakipenda tangu utotoni mwako,” bibi akasema. Alitoa vyombo vyake pasipo kutaka msaada kisha akaketi na kuwaendelezea maneno:



“Taji zote za kifalme hutengenezwa huko, pete pia na mabangili ya kumeremeta na kupendeza. Ni umbali mrefu sana toka hapa, itamgharimu mtu juma zima mpaka kufika huko.



Panaitwa Osheni, ama panajulikana kama tawala ya masonara. Utapita milima mikubwa ya Wawetu na msitu mkubwa wa mianzi kabla hamjafika hapo. Ila mkiwa njiani, kumbukeni mkikutana na yeyote yule msithubutu kumuongelesha. Hata kumsalimia!”



Malkia na Zura walitaka kuondoka upesi ila bibi akawazuia kwani muda ulikuwa umeenda sana. Aliwataka walale pale kisha asubuhi wadamkie safari yao, wakakubali. Walibakia hapo wakapiga soga na bibi huyo mpaka giza lilipoingia. Bibi aliwapikia tena chakula cha usiku wakajipumzikia.



Hakukuwa tena kikubwa kilichojiri mpaka pale baadae mbeleni ambapo Malkia alipata taarifa juu ya yale yaliyojiri huko Goshen, ya kwamba mfalme bado hajapatikana kwasababu ya majira kubadilishwa.



Hiyo ilikuwa taarifa njema kwa Malkia. Ilimpa sababu mojawapo ya kutabasamu ndani ya siku hiyo ngumu.

.

.

.

.

.

.

*** .

.

.

.

.

Mkononi mwa Veda kulikuwa kuna bilauri ya mvinyo. Bilauri hiyo ilikuwa ni ya pili baada ya kumaliza ya kwanza aliyoigida upesi. Pembeni ya kitanda chake kulikuwa kuna meza kubwa na juu ya meza hiyo kulikuwa kuna bilauri kubwa lililobebelea kinywaji cha mvinyo.



Veda alikuwa amechoka kumsubiria Fursa ambaye alipeana naye ahadi ya kukutana majira ya usiku. Yalikuwa sasa yamepita masaa manne toka pale muda wa ahadi ulipokuwa na Fursa hakuonekana wala hakukuwa na dalili yake.



Veda alikuwa amevalia nguo nyepesi iliyoacha viungo vyake moto nje. Macho yake yalikuwa yanarembua na alikuwa anapiga mihayo mara kwa mara. Kama isingelikuwa kinywaji alichokuwa anakinywa, basi angelikuwa amelala.



Ni mvinyo pekee ndio ulikuwa unampa kampani. Hata hamu yake ya kimwili aliyokuwa nayo ikimngojea Fursa kwa bashasha zote, ilianza kupotea. Mwili wake uliokuwa moto kwa hamu za mapenzi ulianza kuwa baridi na kupooza. Na marashi yake aliyokuwa amejipulizia yalikuwa yanaelekea kuisha.



Alimaliza mvinyo wake ndani ya bilauri hiyo ya pili, akachota mvinyo mwingine. Wakati sasa anakunywa huu, ndipo Fursa akatokea. Aliketi kitandani mwa mwanamke huyo, akamtazama kwa sura ya kichovu. Veda alimlaumu Fursa kwanini amechelewa, Fursa akatumia sababu za uongo kumlaghai.



Masikini mwanamke huyo hakuwa anajua ya kwamba Fursa alikuwa ametoka kujimwaya mwaya na mrembo mwingine kwa jina Rhoda, mwanamke ambaye alimkamua mwanaume huyo manii zote akimuacha amechoka hajiwezi.



“Kwahiyo haunipi leo?” Aliuliza Rhoda kwa malalamiko.



“Nimeshakuambia nimechoka. Ntakupaje sasa?” Akajibu Fursa pasipo kumtazama mwanamke huyo.



Veda alijitahidi kuchokonoa hisia za Fursa kwa kumbusubusu mwanaume huyo shingoni, kumpapasa maeneo ya aanjoli, lakini ikawa bure. Mwishowe Fursa alisimamama akamtazama mwanamke huyo. Akawambia hampendi na hana malengo yoyote na yeye. Akamwambia matumizi yake yamekwisha na hamtaki tena!



Kwa Veda hiyo ikawa kama ndoto. Machozi yalimshuka upesi akauliza kana kwamba hakusikia.



“Fursa hunitaki?”



Haikuwa ndoto bali uhalisia, Fursa alikuwa hamtaki tena. Veda alitishia kusema yale maovu aliyofanya na mwanaume huyo lakini Fursa hakuogopa, akamjibu kiulaini:



“Hautopata muda huo.”



Veda hakuelewa nini Fursa anamaanisha. Hakujua kwamba mwanaume huyo alikuwa tayari ameshasuka mipango yake thabiti.



Alipotoka tu ndani ya chumba, aliingia mwanaume mmoja mwenye mwili mkubwa akiwa ameshikilia kiroba cha kahawia. Alichomoa kisu chake kiunoni, akamchoma Veda mara mbili tumboni kisha akamwingiza mwanamke huyo ndani ya kiroba akiwa anavuja damu.



Na kama alivyopewa maelekezo, kuhakikisha maiti hiyo haionekani popote pale ndani ya Goshen, mwanaume huyo alienda kumtupia Veda Tanashe kwa malengo kwamba akawe kitoweo cha wachawi.



Mwanaume huyo alikung’uta mikono yake kwa kumaliza kazi kisha akaondoka.



Baada tu ya muda mfupi, bibi watatu wakafika kwenye mwili huo. Walimkuta Veda akiwa anapumua kwa mbali mno. Walimtwaa upesi na kumpeleka kwenye nyumba yao. Huko walimrepea mwanamke huyo kwa kumtia dawa zao za kichawi, kufumba na kufumbua Veda akawa hai na mwenye nguvu.



Alitaka kuondoka kurejea Goshen akammalize Fursa, ila bibi wale wakamkatalia abadani. Walimpatia kazi aifanye kama malipo ya kumsaidia kuukoa uhai wake. Na kazi hiyo haikuwa nyingine bali kutafuta mkufu wa Malkia kwa hali na mali maana yeye alikuwa na uwezo wa kutoka Tanashe.



“Lakini Sandarus ameshakufa!” Alisema Veda. “Hapana, hajafa.” Akajibiwa na bibi mmoja. “Yu hai huko Maam, na jua likichomoza anaelekea kwenye tawala ya masonara.”



“Usijali.” Akasema bibi mwingine. “Tutakupa njia rahisi ya kumpata.”



“Ila…” Akadakia bibi mwingine. “Kaa ukijua ukitutoroka, tutajua na hautodumu zaidi ya masaa manne kabla hujafa!”



Tisho hilo lilifunga mjadala kabla bibi hawajampatia Veda jicho moja kubwa walilomtaka atumie kama dira ya kumpatia Malkia. Walimueleza namna ya kutumia dira hiyo kwa ufanisi.



Pale kiini chake cheusi kitakapogeuka na kuelekea kwenye upande wowote basi huko ndipo alipo wanayemtafuta. Veda akaelewa, ila kabla hajaenda akapatiwa na usafiri.



Usafiri huu ulikuwa ni wa ajabu na uliomshangaza Veda. Walikuwa kunguru wengi mno. Alistaajabu ni kwa namna gani atatumia kunguru hao kwenye usafiri. Bibi walimtoa hofu na kumwelekeza maneno kadhaa tu, Veda akawa mtaalamu. Ni kupiga tu mluzi kunguru wote wanamzunguka wakiwa wanapaa, na akiwa katikati humo basi atanyanyuka toka ardhini na atapata kuwaelekeza ndege hao wapi aelekee. Watatii!



Lengo ni moja tu, kuupata mkufu wa Malkia. Na hata kama itamlazimu kumuua Malkia basi afanye hivyo. Hata kama itamlazimu kuusukuma mlima, basi afanye vivyo.



Hakuna chochote kinachopasa kumzuia. Mkufu ni lazima uje kwenye mikono ya bibi wale kwa gharama yoyote ile, aidha ya mali ama damu!



Basi kunguru wakamzunguka Veda na kumnyanyua, wakamtoa eneo lile.

.

.

.

.

.

***

.

. .

.

.

.

Ulikuwa ni muda wa asubuhi ya kuelekea mchana Malkia na Zura wakiwa mgongoni mwa farasi kukata mbuga kuitafuta Osheni – tawala ya masonara.



Walikuwa wamebebelea chakula na maji waliyopewa na bibi yake Malkia vipate kuwasaidia njiani. Chakula kilikuwa ni mikate migumu na nyama kavu, viliwekwa kwenye kimfuko cha ngozi, wakati maji yakiwa yamefungashwa kwenye kibuyu kilichozibwa na mdomo mweusi.



Tangu walipoanza safari hiyo, hawakupumzika hata mara moja. Safari ilikuwa ndefu hivyo hawakutaka kuirefusha zaidi kwa kupumzika pasipo na mahitaji.



Lakini jua lilipokuja kutuama katikati ya anga, iliwalazimu kupumzika. Walikula kidogo na kunywa kukanda makoo yao makavu, kisha safari ikaendelea. Walitembea kwa muda wa kama lisaa ama zaidi, wakafikia milima ya Wawetu. Huko wakaona mito yenye maji safi, ambapo walichota maji na kuongezea yale yaliyokuwa kwenye kibuyu chao.



Wakatembea ndani ya milima hiyo ya Wawetu kwa takribani masaa sita. Hata jioni iliwakuta wakiwa katika safu hiyo ya milima yenye baridi kali hivyo wakalazimika kupumzika wakiwa wamejikunyata na kukumbatiana ili wapeane joto.



Lakini wakiwa hapo, hawakujua, kulikuwa kuna mtu anawatazama. Mtu huyo kwa siri sana aliwakata jicho. Nyayo zake zilizokanyaga chini hazikutoa sauti yoyote na macho yake makubwa kama bundi yalikuwa yanang’aa.



Hatukumjua ni nani huyu na anataka nini.



Kwa usiku wote hakufanya kitu. Malkia na Zura walidamka mapema ya asubuhi wakaendelea na safari yao. Walitembea kwa takribani masaa matatu wakaingia ndani ya jangwa kavu.



Humo wakakumbana na joto kali ukiambatana na mvuke wa joto uendao juu. Farasi alipunguza mwendo akawa anatembea.



Punde waliwaona watu watatu wanakuja tokea mbali. Mwanzoni waliwaona kama watu wadogo lakini kadiri walivyokuwa wanajongea wakawa wanapata maumbo yao kamili.



Walikuwa ni wanaume watatu waliojifunika vichwa na nyuso kwa vitambaa wakiwa wamevalia kanzu za kahawia, zikitofautiana kwa kukoza tu.



Walitupa salama zao kwa Malkia na Zura, wakiwa na sura zenye ukarimu na matabasamu ya bashasha. Walikuwa ni wazuri kwa uso wakiwa wametinda vema ndevu zao. Rangi yao ilikuwa nyeupe lakini nywele zao zilikuwa nyeusi ti.



Zura na Malkia walipuuzia salamu hizo wakaendelea na safari. Walikumbuka kile ambacho bibi aliwaambia ya kwamba wasiongee na yeyote njiani.



Waliwatazama tu wanaume hao pasipo kuwaongelesha. Na mara wanaume wale walipopishana na farasi wa Malkia, wakapotea kama upepo!



Malkia na Zura walishtushwa sana na hilo. Iliwafanya wajione hawapo wenyewe eneo lile. Kwa namna moja ama nyingine walijiuliza ingekuwaje kama wangeliitikia salamu ile.



Walichoka kutembea wakapumzika. Miguu ilikuwa inawauma na miili yao iliyokong’otwa na jua ilikuwa imevuja jasho na kuchoka. Waliketi chini ya mtende wakapata kula na kunywa kidogo.



Kutokana na kuchoka, walipitiwa na usingizi mwepesi. Ila baada ya muda mfupi walisikia sauti ya watu ikiwajongea. Waliamka upesi wakatazama. Walimuona mama mmoja mweusi akiwa ameambatana na watoto wawili waliovalia kimasikini.



Walikuwa wamechoka mno wakitembea kwa kuburuza miguu yao. Midomo ilikuwa mikavu na yenye kiu. Macho yalikuwa meupe kama watu wakosefu wa damu. Walikuwa wanatia huruma na imani vilevile.



Walisimama mbele ya Malkia na Zura wakaomba maji maana wana kiu, na chakula maana wana njaa. Malkia na Zura walitazamana kwanza kabla ya kuchukua maamuzi yoyote. Walihofia inaweza ikawa mtego.



Japokuwa kweli watu wale walikuwa wanatia huruma, je ni kweli ni binadamu ama majini? Hata kuwauliza wametokea wapi hawakuweza, waliogopa, hivyo walibakia wakiwatazama watu hao mpaka pale walipoondoka.



Japokuwa watu wale walibembeleza wajibiwe kama watapewa chakula na maji au lah, Malkia na Zura walinyamaza kimya. Ilihitaji moyo mkubwa kufanya hilo kwani waombaji walikuwa wanalia na nyuso zao kweli zilionyesha mahitaji.



Ajabu watu hao walipoondoka, baada ya kouona hawasikiliwi, walipotea kufumba na kufumbua! Haikuonekana wala kujulikana wapi wameelekea. Hapo ndio Malkia na Zura wakafahamu kwamba watu wale hawakuwa binadamu wa kawaida.



“Tuondoke!” Alisema Malkia. Walinyanyuka wakatembea wakimvuta farasi.



Walitembea mpaka pale jua lilipozama na kuwa usiku, wakapumzika.



Maajabu ya jangwa ni kwamba, mchana huwa ni joto kali mno wakati usiku kukiwa ni baridi kali. Malkia na Zura walijikuta wanajikunyata wakitetemeka kwa baridi hiyo katili.



Katikati ya usiku huo uliorandana na pepo kali zilizotimua vumbi, Malkia alishituka usingizini baada ya kusikia joto kifuani. Ulikuwa ni mkufu wake unawaka. Aliutazama ndani ya kidani akaona tukio lililokamata akili yake.



Kulikuwa kuna rundo kubwa la kunguru wakipaa angani. Hakuona mtu yeyote kati ya kunguru hao, na hakujua hao kunguru wametokea wapi na wanataka nini.



Ilikuwa ni fumbo gumu kwake.



Kunguru hao walikuwa wakubwa wenye mbawa pana. Walikuwa wanaruka kwa kuzunguka kitu ambacho Malkia hakuwa anakiona. Kasi yao ilikuwa kubwa sana na ingemtaka mtu kuwa makini ili apate kugundua kuwa hao ni kunguru, la sivyo ungeweza sema ni ukuta mweusi!



Ghafla kidani cha mkufu kilizima na kumwachia Malkia kwenye dimbwi la mawazo. Aliwaza na kuwazua ni nini kile. Mwishowe aliishia kwa kuweka tahadhari ya kwamba anatakiwa kuwa makini atakapoona ndege hao kwani mara zote mkufu humwonyesha ya mbele.



Asubuhi na mapema waliamka, Malkia akamwambia Zura yale aliyoyaona. Waliweka nadharia ya kuwa makini kisha wakaendelea na safari yao, ila kwa sasa wakiongeza kasi ili kunguru hao wasiwakute wakiwa jangwani pasipo na msaada.



Farasi alikimbia na kukimbia. Walitazama nyuma mara kwa mara kama wanafuatwa lakini hawakuona chochote. Wakiwa wanakaribia kumaliza jangwa wakamuona mwanamke mmoja amelala chini kama mtu asiyejitambua.



Alikuwa amevalia gauni refu jeusi akiwa peku. Nywele zake ndefu zilikuwa zinadeki ardhi wakati mdomo wake ukiwa umeachama kama mtu aliyepitiwa na usingizi wa pono.



“Ebu ngoja!” Aliamuru Malkia.



Macho yake yaliyoganda kwa mwanamke yule yaligundua jambo ambalo hakutaka kuliamini. Yule mwanamke alikuwa ni mke mwenzake. Tena mke mkubwa. Yaani alikuwa Veda!



Amefikaje pale? Aliwaza. Kwa namna moja ama akadhani Fursa atakuwa amemtimua mwanamke huyo. Fursa ana roho mbaya sana, aliamini. Lakini pia kwa namna nyingine akadhani aidha alikuwa amefananisha.



Hata kama amefukuzwa na Fursa, amefikaje pale?



Labda kwa muda wote ambao hawajaonana, mwanamke huyo alikuwa yu njiani ama amefika huko. Kichwa chake kilimpa mawazo hayo. Kabla hajamshika bega na kumvuta, Zura alimtahadharisha aachane naye lakini Malkia akasita.



Hakuweza kumuacha mtu wa himaya yake, tena mtu aliyeshea naye nyumba moja. Alimgeuza Veda akimuita jina. Mara Veda akafungua macho yake na kumtazama Malkia.



Kufumba na kufumbua nguo ya Veda ikageuka kuwa kunguru lukuki. Kunguru hao walimzingira Malkia na Veda wakawanyanyua juu. Baada ya muda mfupi, Malkia alidondoshwa chini, kunguru wakakimbia!



Malkia alijitazama kifuani, hakuona kitu. Mkufu ulikuwa umeenda. Alikwea farasi akawakimbiza kunguru hao lakini hakufanikiwa. Walimuacha asijue la kufanya.



Alibubujikwa na machozi ya kujaza beseni. Zura alimbembeleza akimtaka aache kulia.



“Sasa tutafanyaje?” Aliuliza Malkia.



“Tuendelee na safari yetu,” akajibu Zura.



Hekima na busara yake ilifikia maamuzi hayo. Aliona hakuna tija nyingine zaidi ya kuendelea kutembea kukamilisha safari yao. Washamla ng’ombe mzima, basi mkia wasiusaze.



“Tunaenda kufanya nini kama hatuna mkufu?” Aliuliza Malkia.



“Mkufu wako tutaupata tu. Lakini hatuwezi tukafunga tena safari hii.” Alijibu Zura.



Sauti yake ya kiutuuzima ilimfanya Malkia apate angalau faraja. Alimkumbatia Malkia na kumbembeleza kama mwanae.



Laiti kama kuna watu wangelitaka kummaliza Malkia Sandarus basi ingelikuwa kazi rahisi sana kama wangelianza na Zura. Kwani bila ya mwanamke huyu, Malkia ni mtupu mno; mpweke na asiye na tumaini.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

Uso wa Veda ulijaa furaha baada ya kuupata mkufu. Si tu kwamba alikuwa amekamilisha kazi aliyotumwa, la hasha! Alikuwa amelipiza kisasi kwa Malkia Sandarus kwa kumchukulia bwana wake, marehemu mfalme wa Goshen.



Siku zote Veda hakuwa anawapenda wake wenzake hata kidogo. Aliona wote wamekuja kumnyakua mume wake toka kwenye mikono yake.



Aliwaona kama wezi ambao wamekuja kupokonya tonge ambalo alilipika kwa mkono wake mwenyewe. Aliishi kwa kuwachukia na hata kuwafanyia fitna kwa mumewe ili awachukie.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Leo amepora mkufu wa mmojawao, lilikuwa jambo la fahari kwake. Lakini zaidi ya hapo lilimpa maswali kadhaa.



Ule mkufu una nini? Kwanini bibi wale wanautaka kiasi kile? Kwanini upo kifuani kwa Malkia Sandarus? Kazi yake nini?



Maswali hayo yalimpa hamu ya kutaka kufahamu zaidi na zaidi. Alihairisha safari yake ya kwenda Tanashe akawa anajadili na kichwa chake juu ya mkufu ule. Alipata hamu akauvaa. Macho yake yalibadilika yakawa ya bluu. Alijihisi mwepesi na mwenye nguvu zaidi.



Alijikuta anatabasamu akasema na nafsi yake:



“Huu mkufu kwanzia leo ni wangu!”



Hakujali wale wabibi wanaomngoja Tanashe. Alijua fika hawawezi kumfanya lolote kwakuwa wakimuua hawatopata mkufu ule kwasababu wao wenyewe hawawezi toka Tanashe.



Na hata kama wakimuua, hajali pia, hana tena cha kupoteza maishani. Mtu pekee aliyekuwa anampenda amemsaliti; mume wake amekufa; hana familia. Ya nini aogope kufa?



Alibebwa na kunguru wake akaenda mpaka kwenye himaya ya Goshen. Kwa siri aliingia ndani ya ikulu ya tawala hiyo akimtafuta Fursa, mwanaume aliyejeruhi moyo wake. Kisha akitoka hapo awatafute na wapambe wote wa mwanaume huyo.



Wote hao alikuwa amepanga kuwazawadia kifo.



Ilichukua dakika tatu tu, wote hao waliokuwa kwenye orodha ya Veda wakawa wananing’inia shingo zao zikikabwa na vitanzi! Kuanzia Fursa mpaka na wapambe wake. Bila kusahau mwanajeshi yule aliyemchoma kisu mwanamama huyo.



Zilipita siku mbili za msiba Fursa akiwa mfalme aliyedumu kwa muda mfupi zaidi madarakani, siku mbili tu! Baada ya msiba kukoma, Veda alijitangaza kuwa malkia wa tawala hiyo.



Kila mtu akamwogopa kwa maajabu yake ya kubebwa na ndege na macho yake ya bluu lakini pia kwa namna alivyoua wanaume watano ndani ya muda mfupi vile. Watu wote wa Goshen pamoja na jeshi wakainamisha vichwa vyao chini kumpokea kiongozi wao huyo mpya, malkia Vedas Alturo!

.

.

.

.

.

*** HAKUNA ZAIDI … ZAIDI YA MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

Kama ulidhani bibi wale watatu wa Tanashe walikuwa wametulia wakati hayo ya Veda yakitokea, basi umekosea.



Kwa muda wote huo bibi hawakuwa na furaha kwa namna walivyosalitiwa, ama kupokwa tonge mdomoni. Walijaribu kumuua Veda kama vile walivyomuahidi endapo akikiuka, lakini hawakufanikiwa.



Mkufu ulimlinda mwanamke huyo dhidi yao. Kama angelikuwa hajauvaa basi kazi ingelikuwa rahisi, ila haikuwa hivyo.



Wakajuta kwanini hawakuwaza tokea hapo mwanzoni ya kwamba mwanamke huyo anaweza kuuvaa huo mkufu. Walijiona wajinga na wasio wataalamu wa mambo ya kiulozi. Walibakia kulaumiana na kutupiana shutuma ambazo hazikuwasaidia kwa muda huo.



Wakati huo upande wao wa kaskazini ya mbali, kwenye tawala ya Devonship chini ya Jayit, kulikuwa kuna tafrija nzito muda huo. Jayit alikuwa amechinja ng’ombe thelathini na tisa kwa ajili ya damu, huku akiwafukia wengine tisa wakiwa hai.



Vitambaa vyeusi na vyekundu vilikuwa vimetandazwa kwenye ikulu yake yenye rangi nyeusi. Wanaume tisa wenye mvi nyeupe walikuwa wameketi kwenye viti vyeusi wakimtazama mfalme wao aliyekuwa anatazama mafuvu ya vichwa mawili aliyoyaweka mezani.



Jayit alikuwa amevalia gauni jekundu mkononi akishikilia panga lake refu jembamba. Alisugua mafuvu yale mawili kwa panga lake mpaka pale alipopata unga mweupe. Aliuchota unga huo akauweka kwenye karatasi nyeusi aliyoikunjama.



Mafuvu hayo mawili yalikuwa ni ya babu na bibi yake waliokufa miaka kadhaa huko nyuma. Bibi na babu yake hao walikuwa ndio wachawi pekee waliobakia Goshen wakati wengine wote wakitupiwa Tanashe.



Uchawi wao ulikuwa ni mkubwa kiasi kwamba hakuna aliyethubutu kuwagusa, wala kuwahisi kama ni walozi. Nusu ya idadi ya watu wa Goshen walikuwa wameuliwa na watu hao na hakuna aliyegundua.



Kwa miaka nenda rudi, bibi na babu yake Jayit walitawala tawala zote pasipo wafalme wa tawala hizo kujua. Wakati wafalme wakitawala tawala zao mchana, bibi na babu wa Jayit walikuwa wanazitawala usiku.



Hakuna aliyeweza kuwazuia, hata kifo chenyewe kilishindwa. Ni pale tu walipofuja ulozi wao na kujidhuru wenyewe ndipo walipokufa, la sivyo wangeishi milele! Uchawi wao haukuwa wa kujifunza, bali wa damuni.



Sasa Jayit alikuwa anataka nguvu hiyo; nguvu ya kizazi chao; nguvu ya babu na bibi yake. Ingawa alikuwa ana nguvu zake binafsi lakini bado kwake haikuwa inatosha kabisa. Alitaka nyongeza. Alitaka zaidi!



Alitaka kutawala tawala zote wakati wa usiku!





Sasa Jayit alikuwa anataka nguvu hiyo; nguvu ya kizazi chao; nguvu ya babu na bibi yake. Ingawa alikuwa ana nguvu zake binafsi lakini bado kwake haikuwa inatosha kabisa. Alitaka nyongeza. Alitaka zaidi!



Alitaka kutawala tawala zote nyakati za usiku!



Alibwia unga wa wa mafuvu ya babu na bibi yake akiwa ameuchanganya na madawa kadhaa. Aliumung’unya unga huo na kuumeza kana kwamba anakunywa dawa ya klorokwini, alikuwa amekunja sura akiusikilizia unga ukizama mwilini. Alipotulia baada ya sekunde tatu tu akaanza kubadilika mwili kuwa mtu wa ajabu zaidi!



Rangi yake ya mwili wake iligeuka na kuwa nyekundu. Mkia ulichomoza ukiwa na kishungi cha simba. Kwenye paji lake la uso, pembe mithili ya za ng’ombe zikachomoza. Alitisha! Lakini zaidi ya hapo, alikuwa na nguvu mno kiasi kwamba alipokuwa anakanyaga sakafu ilipasuka ama kutitia.



Wazee tisa walipiga magoti wakamsujudia. Si tu hao, hata raia wake wasioleweka ni watu wa aina gani nao wakapiga magoti ya kusujudu kumkaribisha kiongozi wao mpya.



“Sasa ni muda wetu!” Alifoka Jayit, umati wa watu wake ukimsikiliza vizuri. “Ni muda wa Devonship kutawala tawala zote! Ni muda wa Devonship kutawala nyatakati zote za usiku!” alisisitiza maneno hayo kwa kuyarudia mara tatu.



Alinyoosha mikono yake membamba juu radi nyekundu zikapiga kwa fujo. Wafuasi wake walifurahia na kupiga nderemo. Wote waliimba:

“Wasaa umewadia! … wasaa wa kutwaa vilivyo vyetu!”



Jayit alimlisha pia farasi wake madawa, mnyama huyo akawa wa ajabu. Macho yake yaligeuka kuwa mekundu na misuli yake ikakamaa kana kwamba alikuwa ananyanyua vyuma. Nywele zake za shingoni zilikuwa ndefu zaidi na meno yake yakachongoka mithili ya mnyama chui!



Hapo Jayit akajikuta anatabasamu kwa furaha. Moyoni alishajua hakuna atayeweza kumzuia, hakuna atakayediriki kunyanyua kiungo chake chochote kuziba njia yake kwahiyo basi kwanini ajinyime furaha? Kama kuna siku njema kwake, basi ile ilikuwa ni mojawapo.



“Mkuu, tunangojea tu amri yako,” alisema mwanaume mmoja mrefu mweusi mwenye kipara. Alikuwa ni mmojawapo wa wanajeshi wa Jayit, tena kiongozi mkuu kwa vyeo.



Uso wake ulikuwa mpana wenye makovu mbalimbali ya kuchanwachanwa kiasi kwamba alikuwa kama kapeti iliyochoka. Kwa jina alizoeleka kuitwa Tititat japokuwa jina lake kamili ni Titus Titanium.



“Ngoja kwanza Tititat,” alisema Jayit akiwa anakunywa damu ndani ya bilauri la kioo. “Wala halihitaji papara hili jambo. Huyu kuku ni wa kwetu, hatuna haja ya manati!”

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

Tangu pale kifo cha Fursa kilipotokea, Rhoda hakuwa na furaha tena. Mara nyingi alijikuta akiwa amekunja uso wake, amejikunyata na kukaa mbali na watu. Macho yake yalijaa machozi na hata urembo wake ukaanza kutiwa doa kwa kutojijali.



Yote hayo si tu kwamba yalisababishwa na kutokuwa na uwezo wa kujihudumia vema, bali pia mawazo juu ya kesho yake. Japokuwa alikuwa amejishikiza kwa kufungua mgahawa mpya wa chakula kutokana na pesa alizozichuma toka kwa Fursa, bado aliona maisha ni magumu mno.



Hakukuwa na mtu yeyote anayejuana naye serikalini, hili lilikuwa ni tatizo kwake na kwa biashara, na pia hakuwa mzoefu wa kuchakarika kutafuta pesa bali kupewa.



Maisha yaligeuka chini juu, juu chini. Alitokea kuwa na kinyongo kikali dhidi ya malkia Veda kwani alijua fika huyo ndiye aliyemuua Fursa. Alijikuta anamchukia mwanamke huyo mno, lakini bahati mbaya hakuwa na chochote cha kufanya zaidi tu ya kuungulia kifuani.



Akiwa anapika chakula cha wateja wa mchana kwenye mgahawa wake mpya unaosuasua, wateja watatu, wanaume, waliingia na kuketi.



Walikuwa wanaongea kwa sauti kubwa na isingekuwia vigumu kujua ya kwamba walitoka kunywa kwanza kabla ya kupitia pale. Walikuwa wanacheka hovyo, macho yao yalikuwa mekundu wakinukia pombe kana kwamba pafyumu ya Kurusumu.



Pasipo kuficha, walikuwa wanaonyesha chuki zao za wazi kwa malkia Veda wakimuita ni malaya aliyemuua mume wake na amedhamiria kuwaua na wao pia.



“Hivi kweli tumeshindwa kabisa kumtoa huyo mwanamke madarakani?” Aliuliza mlevi mmoja. “Yani siamini kabisa kama inakaribia juma moja sasa.”



“Nani wa kumtoa?” Akauliza mwingine. “Ni mshirikina mno, we hujaona Fursa na wenzake walivyonyongwa kama kuku?”



“Sasa kama mshirikina, kwanini hakupelekwa Tanashe kwa wachawi?” Aliuliza mlevi mwingine.



“Ukute mme wake pia alikuwa anajua!”



“Una maanisha marehemu mfalme wetu?”



“Ndio. Mbona hakupelekwa huko? Ni kwasababu alikuwa mke wa mfalme.”



“Unamaanisha kwamba mfalme naye alikuwa mchawi?”



“Ndio! Na watakuwa waligombana, mke akamuua mume wake. Sasa alivyoona Fursa amechukua madaraka, akaamua amuue!”



Mlevi mmoja akatikisa kichwa chake kwa masikitiko.



“Aibu iliyoje hii kuongozwa na mchawi? Yaani nikiwa huko nje nitaona hata aibu kusema nimetokea Goshen. Si wataniona mchawi!”



“Lakini Malkia wetu ameenda wapi?”



Aliuliza mlevi mmoja. Swali hilo likazua mtafaruku mkubwa. Hakuna aliyekuwa anajua wapi alipo Malkia Sandarus, waliamini atakuwa amekufa kwani kama angekuwa hai basi wangepata kusikia habari yake.



Walevi hao walipiga kelele haswa lakini Rhoda hakuzisikia hata kidogo. Alikuwa amezama kwenye mawazo asipate muda wa kusikiliza chochote huko nje.



Hata hakujua kama kuna wageni mpaka pale aliposhituliwa na walevi hao wakimtuhumu kutowajali.



“Samahani sana wateja wangu,” alinyenyekea Rhoda. Walevi walimpuuza wakaagiza chakula. Baada ya muda mfupi chakula kililetwa mezani walevi wakawa wanakula. Walimaliza na Rhoda akadai pesa yake.



“Mbona bei ghali hivyo?” Alilalama mlevi mmoja.



“Jamani si mnajua kodi zimepanda,” Rhoda alieleza. “Wakulima nao wamepandisha bei ya mazao yao, kila kitu sasa kimekuwa ghali!”



“Ah! Ah! Hatuwezi kulipa hiyo pesa!” akasema mlevi mmoja akinyanyuka. Wote walisimama na wakakataa kulipa pesa.



Rhoda alipambana apate pesa yake lakini hakuweza. Bei ilikuwa juu na walevi hawakutaka kuelewa sababu ya hilo. Japokuwa pia walipotoka kunywa pombe bei ilikuwa imepanda vilevile, hawakuwa wamejali hilo isipokuwa tu kwenye chakula.



Walimpiga kikumbo Rhoda, wakadhihaki na kushombo:

“Katafute bwana huko! Hii kazi si yako.”



“Au kama unataka twende tukalale wote nikupe pesa!”



Walicheka wakaondoka zao.



Rhoda alijikusanya akawahi chakula chake kinachoungua jikoni kabla ya kuja kuketi kuwaza na kuwazua akitoa chozi.



Mwishowe aliamini kweli ile haikuwa kazi yake, upishi na kuuza mgahawa, na inambidi afanye juhudi za kutafuta kazi nyingine anayoiweza zaidi.



Mawazo yake yalimtuma amtafute mwanaume mwingine anayejiweza kwa mali na hali. Akimpata mwanaume huyo aombe ndoa, ama basi amchune vya kutosha asimbakize hata harufu ya damu ili apate pesa za kutosha kufanya mambo mengine na si kuuzia chakula masikini wenzake waliojaa maudhi, makwazo na majaribu.

.

.

.

.

.

*** .

.

.

.

.

Ndani ya siku tatu bado wanaendelea na safari. Kuamkia siku ya nne ndipo Malkia Sandarus na Zura walitia miguu ndani ya tawala ya Osheni – tawala ya masonara.



Hakuwa na mwenyeji yeyote huko hivyo basi ikawalazimu kutafuta msamaria mwema atakayewakarimu baada ya kutokuwa na pesa za kukodi chumba. Walimpata mwanaume mmoja, sonara mdogo, aliyewapa chumba kimoja wapate kujikusanyia humo. Wakapumzika kwa masaa kadhaa kisha wakaoga na kula chakula kidogo walichopewa.



“Mbona mmetoka mbali hivyo kuja hapa?” Aliuliza msonara yule mkarimu. Alikuwa ni mwanaume mnene mwenye nywele ‘rafu’. Nguoze zilikuwa zimechoka na si nadhifu.



“Tumekuja kutafuta taarifa juu ya mkufu,” alijibu Malkia. Alimueleza kila kitu msonara yule mdogo juu ya mkufu wake. Akajaribu pia na kuuchora chini ili apate kumtengenezea taswira kuhusu nini anaongelea.



“Siujui kusema ukweli. Na sifahamu ni wapi waweza kupata taarifa yake,” alijibu msonara mdogo kwa masikitiko.



“Hamna yeyote ambaye unadhani anaweza akatusaidia?” Aliuliza Zura.



Msonara alifikiria kwa muda mfupi, akasema:

“Labda naweza nikawaelekeza kwa wasonara fulani wa kati. Pengine wanaweza wakawa na taarifa.”



Msonara huyo mdogo aliwaelekeza Malkia na Zura wapi watawapata wasonara hao wa kati ambao walikuwa watatu kwa idadi. Pasipo kupoteza muda, Zura na Malkia wakawaendea wasonara hao kuelezea haja zao.



Lakini hata huko napo hawakupata kitu. Hakuna aliyekuwa anafahamu kuhusu huo mkufu, wala hakuna aliyeamini kama Sandarus ni malkia. Labda kutokana na mwonekano wake usioonyesha kama kweli ni malkia.



Walirudi kwa msonara mdogo na kumpasha habari. Msonara huyo alisikitika sana. Alijua sasa kazi itakuwa kubwa na huku upenyo wa kufanikiwa ukiwa mdogo sana.



“Hao niliowaambia ni masonara maarufu wa kati. Sasa hapo hakuna tena cha kufanya zaidi ya kwenda kwa msonara wa juu. Itakuwa ajabu sana kama na yeye hatokuwa na taarifa ya kitu kikubwa kama hicho kwenye fani hii ya usonara.”



Matabasamu yakajaa kwenye nyuso za Malkia na Zura.



“Ila si rahisi kabisa kumpata msonara huyu. Anafanya biashara za juu na uongozi wa tawala mbalimbali. Ratiba yake ni ngumu na kazi zenye faida kubwa zimepangana kwake.”



Matabasamu yakajifinya.



“Na ukizingatia, hamna atakayeamini wewe ni malkia,” alimalizia msonara.



“Tutaenda tu kujaribu,” alisema Malkia. Msonara mdogo pasipo na hiyana akawaelekeza wapi watampata mtu huyo.



“Ni maarufu sana, hamwezi mkapotea.”



Japokuwa ilikuwa inaelekea jioni, Malkia na Zura hawakutaka kukoma kuendelea kusaka. Walielekea kule walipoelekezwa, kwa msonara mkubwa, huko walikuta nyumba kubwa mno yenye fensi kubwa ya mawe. Mlangoni kulikuwa kuna walinzi wawili, warefu wenye sura kavu za kazi, waliobebelea mapanga marefu yanayometameta.



Walieleza haja yao kwa walinzi hao ili waruhusiwe kuingia ndani. Walinzi waliangua kicheko na kuwataka wapotee eneo hilo haraka iwezekanavyo.



“Embu tutoleeni uchafu hapa!” Aliamuru mlinzi mmoja kwa sura ya ukali. “Hapa wanakuja watu wakubwa tu, watu wenye heshima zao!”



Malkia na Zura walijitetea lakini hawakusikilizwa wala hawakuaminiwa, mwishowe walinyakuliwa wakaenda wakamwagiwa mbali.



“Ole wenu tuwaone tena!” Mlinzi alitoa kitisho kabla hawajarejea lindoni mwao upesi.



Malkia na Zura walirudi kwa msonara mdogo wakiwa na huzuni. Mioyo ilikuwa imewavunjika wasiwe na matumaini. Msonara aliwakaribisha akiwataka wavute subira kwani waweza wakafanikiwa.



“Msijali, hiko chumba kipo tu wazi tangu mwanangu afariki dunia mwaka jana,” alisema msonara mdogo. “Nipo mpweke sana, mke wangu pia alifariki, nafurahia nyie kuwepo hapa maana mnanipa faraja.”



Wanawake hao walipika chakula cha usiku huo, wakala na kulala. Walidumu hapo kwa siku nne pasipo kufanikiwa. Hawakupata nafasi ya kumuona msonara mkubwa, kila siku walipojaribu waliishia kukimbizwa na walinzi.



Waliwaza kukata tamaa, lakini je kufanya hivyo si nikumaanisha muda wote huo waliotumia kuhangaika ni bure? Walipowaza hapo basi wakajipa moyo wa kuendelea kuvuta subira. Walikuwa nyumbani kwa msonara wakifanya kazi za hapa na pale.



Kwenye siku ya tano, majira ya jioni, msonara alikuja nyumbani akawapasha habari.



“Kesho kuna ujio mzito kwa msonara mkubwa, Mfalme toka Uarabuni anakuja. Hiyo inaweza ikawa nafasi yenu ya kuingia ndani na kukutana na msonara huyo!”



Taarifa hiyo ilikuwa njema, lakini ilikuwa imebeba hatari ndani yake, hatari ambayo inaweza pia kuukwapua uhai wa mtu. Malkia na Zura walitokea kulitambua hilo na hivyo basi wakadhamiria kujiandaa.



Kuna mambo kadhaa waliyaomba toka kwa msonara, bahati nzuri msonara akaahidi kuwasaidia.



Kesho ilipowasili, kwenye majira ya alasiri, msafara mkubwa wa farasi wa Mfalme toka Uarabuni ulijongea ndani ya himaya ya Osheni. Kwa idadi ya harakaharaka kulikuwa kuna farasi themanini na ushenzi. Farasi wanne wanaovuta kitoroli kilichojifunga vema, ndio walimbebelea mtawala. Farasi wengine wakiwa ni wa walinzi na wanawake walioongozana na Mfalme huyo.



Ni katikati ya farasi hao waliowabebelea wanawake, ndipo Malkia na Zura wakajichomeka. Walikuwa wamejivika kufunika sura zao wakiacha macho tu, nguo ambayo ilivaliwa na wanawake wote msafarani hivyo hawakugundulikana kwa upesi.



Lakini pia tendo hilo lilifanyika kwa wepesi mno kiasi kwamba halikukamata ‘atensheni’ ya watazamaji wala walinzi.



Malkia na Zura waliingia ndani ya jengo la msonara wanayemlenga. Na wakati msonara huyo akimkaribisha mgeni wake, wao walishuka toka farasini wakazunguka nyuma ya nyumba kwa siri na tahadhari.



Walitaka kujitunza humo kwa muda mrefu unaowezekana huku wakiwinda nafasi ya kuonana na msonara mkubwa.



Walijua fika wageni wale, toka uarabuni, watalala pale kutokana na muda waliongia jengoni, lakini pia waliamini ndani ya muda huo watapata tu fursa ambayo msonara atakuwa mpweke, na hiyo ndiyo itakuwa nafasi yao.



Lakini je watadumu humo jengoni mpaka kumuona msonara wakiwa hawajakamatwa? Hapo ndio palikuwa shida.



Kutokana na nyumba hiyo kuwa kubwa mno, walifanikiwa kujificha mara kwa mara pale walipohisi usalama wao upo mashakani.



Waligundua ndani ya nyumba ile, ama jumba, ulinzi haukuwa mkubwa sana kama vile ilivyokuwa kule nje. Basi kwa kutumia mwanya huo, waliweza kujificha mpaka pale katikati ya usiku.



Mfalme toka uarabuni alikuwa amelala, hata wapambe wake pia. Msonara naye alikuwa amelala ndani ya chumba chake kilichojaa samani akiwa na wanawake wale aliokuja nao Mfalme.



Akiwa humo anatafuta usingizi, mlango wa chumba chake ulifunguliwa akaingia Malkia Sandarus, na punde Zura naye akazama. Msonara alishituka akiwatazama wanawake hao.



Alihofia usalama wake. Hata wanawake aliokuwa amelala nao, walikurupuka wakiwa na nyuso zenye mashaka. “Tafadhali naomba usipige kelele,” alisema Malkia Sandarus. “Nimekuja hapa tokea Goshen, nimekuja kuonana na wewe unisaidie.”



“Nikusaidie nini?”



“Ni kuhusu mkufu fulani!”



“Mkufu upi? Unadhani mimi najua mikufu yote duniani?”



“Haujui yote, ila utakuwa unaujua huu!”



Msonara, pasipo kujali, alipaza sauti yake kuwaita walinzi. Malkia alitaka kukimbia lakini Zura akamzuia. Walinzi walifika wakawatwaa wanawake hao. .



Walipelekwa kwenye chumba kidogo chenye giza wakatupiwa humo na kufungiwa. Malkia alipaza sauti kumuita msonara akimuomba amsikilize lakini hakuna alichopata zaidi tu ya mwangwi.



Alijikuta anakata tamaa, akaketi chini na kuanza kububujikwa machozi. Zura alimbembeleza asilie lakini Malkia alishindwa kuacha. Alifanya hivyo mpaka pale aliposikia sauti ya vishindo vya miguu inakuja. Alinyanyuka upesi akashika nondo za mlango apate kuangaza.





Alimuona mtu ambaye si msonara kama vile alivyotarajia. Hakuwa mtu anayemjua hata, bali mwanaume mmoja aliyevalia kanzu rangi ya maziwa akiwa na nywele nyeusi mno na tena ndefu mpaka mgongoni. Alikuwa ni mwarabu, hata kwa kumtazama tu ungelijua. Uso wake ulikuwa mrefu ukijaaliwa vinyweleo lukuki.



Alijikuta anawaza maneno yale aliyoambiwa na Malkia. Kwa namna moja ama nyingine yalimnyima raha kwa kujijirudufu masikioni mwake. Aliketi akashika tama. Alisimama akashika kiuno. Mwishowe akaamua kuufuata mlango na kwenda kule kwenye chumba walichokuwa wamefungiwa Malkia na Zura.





Alikuwa wanawake hao wamelala. Aliwaamsha na kumtaka Malkia amwambie juu ya ule mkufu aliokuwa anataka kumtaarifu hapo awali. Uzuri Malkia pasipo kusita, akamweleza juu ya mkufu huo – nguvu yake na hata umbo. Mpaka anamaliza habari hiyo, msonara alikuwa ametwangwa bumbuwazi. Mdomo wake ulikuwa umeachama na macho yake nusura yaache uso kwa kunyofoka.





“Upo wapi huo mkufu?” Lilikuwa ni swali la kwanza toka kwa msonara. Macho yake yalionyesha uchu ambao uligoma kungoja.

“Kabla hatujakwambia ulipo, kwanza unaweza ukatupa taarifa ya mkufu huo?” Aliuliza Zura upesi.





Msonara aliagiza mlango ufunguliwe, akaongozana na wanawake hao mpaka kwenye sebule yake kubwa. Huko toka kwenye kabati lake la kuhifadhia vitabu, alitwaa kitabu fulani kikubwa mno chenye jalada chakavu la kijivu.





Alikiweka mezani na kukifungua haraka mpaka kwenye kurasa namba mia nane ambapo hapo akaonyesha picha ya mkufu. Mkufu huo ukiwa unafanana vilevile na wa Malkia.





“Mkufu huu ulipotea zamani sana, umetafutwa kwa muda mrefu mno pasipo mafanikio. Kwenye kila himaya palipitishwa msako mkali lakini hakuna kilichofanikiwa.”

Msonara akafungua kurasa ifuatayo.





Alisogelea mlangoni akamtazama Malkia. Uso wake ulikuwa mpole ukionyesha kuguswa. Macho yake yalitaka kujua na mdomo wake haukukawia muda mrefu kabla haujafunguka kuuliza kilichotokea.





Kwa wakati huo wote msonara yule mkubwa alikuwa ndani ya chumba chake akiendelea kula raha na wanawake wale alioletewa kama zawadi toka uarabuni. Kila mwanamke aliyemzingira aligusa upande fulani wa mwili wa msonara huyo aliyeishia kusikilizia ‘unyoda’ kwa kurembua macho kana kwamba anapitishiwa upamba masikioni.





Raha hiyo ilidumu kwa masaa kadhaa, ni kana kwamba kuamshwa kwa msonara huyo na Malkia kulikuwa ni kama vile aliamshwa atende yale, ila kwakuwa kila kitu kina mwisho wake basi akafikia kikomo ambapo wanawake walichoka wakalala. Yeye msonara aliutafuta usingizi lakini hakuupata hata lepe!

“Huu mkufu haijulikani haswa ni wapi ulipotengenezwa. Inaaminika asili yake ni kwenye utawala wa wasioonekana – upo chini ya bahari. Ni mojawapo ya mkufu wenye nguvu, lakini unakuwa na nguvu mno pale tu unapokuwa na mtu ambaye ametengenezewa mkufu huo.”





Malkia akapata shaka.





“Unajuaje kama mtu fulani ametengenezewa huo mkufu?”





“Sina huo utaalamu,” akajibu msonara. “Hiyo sio kazi yangu, kazi yangu mimi ni kuutafuta huo mkufu kwa hali na mali maana utaniongeza utajiri mara tatu ya hapa nilipo.”





“Kwani upo wapi huo mkufu?” Aliuliza msonara baada ya kueleza kifupi. Malkia na Zura walitazamana na kisha Zura akanena:

“Tafadhali tuambie zaidi. Tutakusaidia kuupata huo mkufu.”





“Mtanisaidia? Kwani upo wapi?”



“Tuambie kwanza.”



“Mnataka kujua nini?”



“Tunataka kujua nguvu ya mkufu huo kwa mwenyenao.” Msonara alibinua mdomo wake, akafungua tena kitabu kama mtu asiyetaka.





“Mkufu huo unaweza ukaongozwa na watu mbalimbali, lakini wenye sifa moja tu – damu inayorandana na ile iliyokuwepo ndani ya kidani chake. Mtu mwenye damu hiyo utamtambua pale tu akapouvaa huo mkufu na asipate tatizo lolote wakati kinyume na hapo mtu ataungua kama vile ilivyo kwa wadhalimu.”





Akavuta pumzi.





“Kwa kupitia mkufu huo, mtu atakuwa na nguvu mno zaidi ya binadamu wa kawaida. Ataweza kupotea lakini pia kunuwia na jambo likatokea.”





“Lakini pia kati ya wote hao wenye damu hiyo, kuna mmoja ndiye anayestahili mkufu huo. Mmoja tu. mmoja ambaye anaweza akaona maono ndani ya mkufu huo. Mmoja ambaye mkufu unamteua pale anapokuwa karibu yake.”

Japokuwa taarifa hiyo haikuwatosheleza sana kiu zao, angalau ziliwapa mwanga wakapata kuyajua ambayo hawakuwahi kuyajua. Kwa namna moja ama ya ziada iliwafanya waone hatari walizozipita zimewapa manufaa.





“Haya huo mkufu upo wapi?” Aliuliza msonara.



“Haupo hapa!” Malkia akajibu. “Umeibwa.”



“Na nani?” Msonara aliwahi kuuliza.



“Hatujajua ni nani. Aliutwaa shingoni mwangu na kupotea.”



“Shingoni mwako?”



Malkia alichukua fursa hiyo kujitambulisha yeye ni nani na wapi alipoutoa mkufu huo. Pia akamweleza na safari yake tokea Goshen mpaka pale.





Ilimuwia vigumu msonara kuamini ya kwamba yule ni malkia. Hata kama ingelikuwa ni wewe usingeliamini. Lakini kwasababu kulikuwa kuna kitu cha thamani kubwa anakitaka, basi alilazimisha nafsi yake kuamini. Na badala ya kughafirika, akawapa makazi wanawake hao akihakikisha wanapata huduma zote wanazostahili binadamu.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.



Uwanja mdogo ndani ya hekalu ya malkia Vedas Alturo ulikuwa umekaliwa na wanaume watano wazee wa baraza wakiwa wanamngojea malkia wao atoke chumbani alimokuwa anajipara.





Walikuwa wanateta kwa sauti ya chini ama tuseme wananong’onezana. Nguo zao za mashuka walizovaa ziliwafanya waonekana wazee zaidi na huku vichwa vyao visivyo na nywele vikiwafanya tena waonekane kama watoto! Ilikuwa mvurugano.





Ila baada ya punde kukawa kimya, malkia alikuwa anaingia. Wote walisimama wakiwa na nyuso za utulivu. Baada ya malkia kuketi kwenye kiti chake ndipo nao wakaketi na malkia akafungua kikao.

Ajenda kubwa ilikuwa ni ulinzi wa himaya yao, Goshen. Malkia alitoa agizo la kuimarishwa kwa jeshi kwa kuwatafuta wanajeshi wa ziada nje ya himaya yao kwa madai ya kwamba usalama wake na wa himaya yao kwa sasa upo shakani. Hakuwa pale kujadili bali kutoa amri.





Aliamuru wazee hao wafanye hiyo kazi kwa juma zima lililombele yao. Alikuwa anahitaji wanajeshi alfu moja zaidi ya waliopo.





Baada ya maelezo hayo, kikao kikavunjwa ukiwa sasa umebakia utekelezaji tu.





Wazee hao wa baraza walitokomea, akatokea mwanaume mrefu mwenye mwili uliojaza, kwa jina aitwa Nedal. Alikuwa amevalia kama mwanaume aendaye vitani. Nywele zake ndefu zilizolala zilimfanya apendeze kumtazama. Uso wake mwembamba mrefu ulikuwa umependezeshwa na ‘vindevu’ vya mbali vilivyogoma kusikia makali ya wembe. Macho yake yalikuwa kama ya paka lakini yamelegea kwa kiasi.





Huyo alikuwa ni mtumishi wa siri wa malkia Vedas Alturo. Tangu pale alipoketi kwenye kiti cha madaraka alimteua mwanaume huyo kuwa mtumishi na kada wake ambaye hatakuwa anajulikana kwa yeyote yule. Kazi yake ni kusambaa huku na huko. Kuangaza huku na kule kumletea taarifa malkia wake, Vedas Alturo.





Kazi yake ni kuwa macho ya mwanamke huyo hata pale anapokuwa ndani ya hekalu yake basi apate kujua kila mtaa, na kila kilichomo.

Ni kwa kupitia mwanaume huyu, malkia Vedas alipata tarifa ya kwamba utawala wake ni mojawapo ya utawala unaochukiwa na majirani, yupo hatarini na endapo akikumbwa na vita hatakuwa na pa kukimbilia.



Si kwamba ni kwa bahati mbaya Nedal alikuwa amechaguliwa kufanya hiyo kazi, bali ni kutokana na ujasiri na ushujaa wake. Haogopi kufa wala kujeruhiwa kwa kile anachokisimamia. Unaweza mwita mwanaume wa shoka ama jembe linalosukumwa na nguvu ya sembe.





Vedas alipomuona mwanaume huyo alitazama kwanza kila upande wake kama kuna usalama kisha akapandisha kichwa chake juu kumruhusu Nedal aongee. Alijua kabisa Nedal haji pale pasipo kuwa na taarifa nyeti na hivyo lilikuwa ni jukumu lake kumtegea sikio.





“Malkia wangu,” Nedal alianza kwa kusema hivyo. “Malkia Sandarus bado yupo hai. Inasemekana yupo kwenye himaya ya masonara – huko Osheni, na ameonana na msonara mkubwa!”





Malkia Vedas akapaliwa na hizo taarifa. Alikohoa mara nne kabla hajatulia na kuuliza:

“Anafanya nini huko?”



“Bado sijajua, malkia. Mawakala wangu bado wanatafuta”



“Nedal!” Malkia alijikuta anaropoka.



“Naam!”



“Nataka huyo mwanamke afe haraka iwezekanavyo!”



“Sawa malkia wangu.”



“Muda wa kumfuatilia umeshatosha sasa.”



“Sawa malkia wangu!”



Nedal aliondoka akimwacha malkia Vedas akiwa ametwaliwa na mawazo juu ya Sandarus. Hakuwa na raha kabisa kwa siku hiyo nzima mpaka pale usiku akienda kitandani. Na kutokana na mawazo hayo si bure akaweweseka ndotoni kumuota Sandarus.





Alimuona mwanamke huyo akiwa na upanga mrefu na mnene mkononi mwake. Uso wake ulikuwa mwekundu ukiwa moto. Alikuwa anataka kumpokonya mkufu lakini hakufanikiwa, ila badala yake mkufu ukatwaliwa na mtu mwingine ambaye Vedas hakumjua ni nani.

Alikurupuka toka usingizini akahema kama mbwa. Alipapasa kifuani mwake akakuta mkufu. Alishusha pumzi ndefu kisha akalaza kichwa chake kitandani.





Ndoto hiyo ilizidi kumuongezea mawazo na kumnyima raha kabisa kwani sasa alikuwa ana mambo mawili makubwa ya kung’amua.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

Ikiwa ni asubuhi isiyo ya mapema, Rhoda, akiwa amependeza kwa kuvalia gauni fupi rangi ya bluu bahari, alikuwa amesimama pembeni ya nyumba kubwa makazi ya baraza la wazee.





Alikuwa hapo akitega kama kuna mwanaume yeyote mzito serikalini atakayetokea kuvutiwa naye, kwahiyo basi alikuwa amejijaladia haswa akiwa anarembua macho yake makubwa laini kama mlenda.





Si kwamba alikuwa havutii wanaume wengine hohehahe, la hasha! Wanaume hao hawakutaka kujisumbua kwa mwanamke huyo kwa maana walijua fika hawatomuweza kumgharamia. Tunaweza sema ‘matawi ya juu’ hivyo basi walikuwa wamewaachia ‘wakubwa’ wafaidi.





Rhoda alisimama hapo kwa muda wa kama nusu saa wanaume wawili wa baraza wakatoka ndani. Walimtazama pasipo kuonyesha haja, wakaondoka zao. Rhoda alisonya akaendelea kuvuta subira.





Akiwa anaendelea kukaa hapo, alisikia sauti za wanaume zikiteta ndani. Alitamani kusikia kile kinachozungumzwa kwahiyo akajisogeza karibu zaidi atege sikio, bahati nzuri walinzi hawakumuona, hata kama walimuona basi walimpuuzia kwa kutoona kama ana sababu yoyote ya kuwafanya wahofie.





Rhoda alisogea mpaka dirishani ‘akanyuti’. Kwa muda mchache tu aliokaa hapo akapata kusikia jambo moja hatari. Jambo ambalo lilimfanya aachame mdomo kwa bumbuwazi kama sio kustaajabu.

Ilikuwa ni sauti kama tatu hivi za wazee wa baraza. Walikuwa wanaongea kwa sauti ya chini lakini iliyonguruma vya kutosha kumfanya Rhoda asikie. Walikuwa wanapanga kufanya mapinduzi kwa kumuua malkia Vedas Alturo, lakini kwanza wakidhamiria kumkwapua mkufu mwanamke huyo wakiamini ndio umpao kibri.





“Wakati alivyokuwa hana mkufu hakuwa na madhara.” Ilisikika sauti ya mzee mmoja. Waliteta na kuteta mwishowe wakaagana. Hapo ndio Rhoda akabanduka na kuondoka upesi.





Alienda nyumbani kwake akajilaza kitandani akiwaza kile alichopata kusikia. Anawaza kama anaweza akawa na nafasi katika mpango huo. Anafikiri kama anaweza kuokoa maisha yake mabovu kwa kujihusisha na mpango huo.





Anawaza na kuwaza. Anatafakari asikome.

Kama akiamua autumia mwanya huo, basi je awe kwenye upande gani. Wa wale wazee kwa kuwataarifu ya kwamba atawafichia siri, au awe upande wa malkia Vedas kwa kumtaarifu yanayofanyika nyuma ya mgongo wake, yaani afunike kombe mwanakharamu apite?

Anafikiria.





Akajikuta anatabasamu asifahamu sababu.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

. .

.

Siku bado haikuwa imeisha japokuwa ilikuwa ni jioni.





Malkia Sandarus na Zura walikuwa wamejilaza chumbani mwa yule msonara mdogo waliyemrejea majira ya mchana na kumpasha yale yote yaliyopata kutokea kule kwa msonara mkubwa.





Walikuwa wamejipumzisha ingawa kwa wakati huo msonara mkubwa alikuwa anatambua wapi walipo. Alikuwa ameahaidiana na wanawake hao wasiende popote kabla hawajakaa na kuongea vizuri baada ya ugeni, toka uarabuni, kuondoka.



Wakiwa humo chumbani wakipanga na kuyateta yale waliyobashiri yatakuwa yanatokea huko Goshen, msonara mdogo aligonga mlango na kuwataarifu ya kwamba wana mgeni.





Walipoenda nje walikutana na sura ya kiarabu. Yule aliyewafuata ndani ‘ya selo’ walipokuwa wamefungiwa.





Mwarabu huyo aliwasalimu kwa ufupi kisha akasema:

“Sultan anahitaji kuonana na nyie faragha.”





Malkia na Zura hawakuwa na muda wa kuteta zaidi ya kuongozana na mjumbe huyo.

Walitembea umbali mdogo wakakutana na farasi aliyebebelea toroli dogo tu la kawaida usidhani kama humo ndani kuna mtu mkubwa.





Malkia na Zura waliingia ndani wakakutana na Mfalme, ama sultan, toka Uarabuni. Alikuwa amependeza kwa nguo zake zenye darizi ya dhahabu. Ingawa alikuwa na umri mkubwa, bado alionekana mbichi kwa kuvutia.





Hujulikana maarufu kama sheikh Mansoor. Mwanaume mrefu mwenye mwili mpana na macho makali lakini yenye uchangamfu ndaniye.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Baada tu ya kusalimu. Mansoor aliuliza:

“Nimeambiwa mna mkufu wa tawala ya wasioonekana.”





Zura na Malkia wakatazamana. Moyo wa Malkia ulilipuka. Alijihisi hayuko sawa, na kwa namna moja ama nyingine kichwani aliwaza ya kwamba ameenda Osheni kutafuta matatizo zaidii na si suluhisho.

.

.

.

.

.“Tafadhali, usiogope,” alisisitiza Sultan, ama Mfalme Mansoor. Alikuwa amejawa na tabasamu. Uso wake ulikuwa mweupe na ungeliona furaha ndani yake.





“Sina huo mkufu, kiongozi,” alisema Malkia Sandarus. Uso wake ulikuwa unamaanisha alichokisema japokuwa ilimuwia vigumu Sultan kuamini.





“Nitakupatia utajiri mkubwa mno,” alisema Sultan. “Sio kwamba ni ahadi. Punde tu utakaponipa mkufu huo nitakupatia utajiri wako papo hapo.”



“Naelewa Sultan,” Malkia alidakia. “Ila nasikitika kukwambia sina hicho unachokitaka.”





Uso wa Sultan ukanywea. Alimtazama mjumbe wake aliyempasha hizo habari za mkufu, mjumbe naye akatia rupia kubembeleza. Bahati mbaya kwao bado jibu likawa ni lilelile, sina mkufu!



“Mkufu umekwapuliwa na mtu nisiyemjua wakati nikiwa njiani kuja huku,” alisema Malkia Sandarus. Alielezea hali ilivyokuwa na mwishowe yeye na Zura wakatoka ndani ya kitoroli cha farasi kurudi kwa msonara mdogo.





Sultan hakuamini kile Malkia alichosema. Aliamini hiyo itakuwa ni janja tu ya mwanamke huyo kuuficha mkufu huo. Alimtazama mjumbe wake na macho meusi, akamwagiza:



“Wafuatilie popote watakapokuwepo. Hakikisha unaupata mkufu na kuuleta kwangu.”





Mjumbe alitikisa kichwa kukubali kisha akatoka ndani ya toroli tayari kwa ajili ya kutimiza agizo.





Alitembea haraka mpaka pale alipowatia machoni Malkia na Zura ndipo akapunguza mwendo. Kila wanawake hao walipogeuka nyuma, alijificha asionekane. Alifanya hivyo mara kwa mara mpaka Malkia na Zura wanazama ndani ya nyumba ya msonara mdogo.

Alisimama hapo kwa sekunde kadhaa. Alitafakari cha kufanya akaona kuendea nyumba jirani na itunzayo wahusika wake ndilo jambo muhimu. Afike hapo na kuomba makazi ya muda mfupi, hata kama yatamgharimu mali. Alijua ya kwamba watu wanaoishi mtaa ule ni watu hohehahe, masonara wadogo wanaobangaiza, hivyo basi hawawezi wakakaba tamaa zao ipasavyo.





Kwahiyo aliujongelea mlango wa jirani akagonga na kuongea na mwenyeji. Alimweleza haja yake na akakubaliwa baada ya kutumia ushawishi wa pesa. Mjumbe huo wa Sultan alitaka chumba kilicho karibu na dirisha kwasababu ya malengo yake.





Mwenyeji wake pasi na kinyongo akampatia. Hakujua bwana huyo ana nini kichwani, hakutaka hata kuwaza tangu yeye ataingiza pesa za kutosha, basi.





Lakini kwenye ulimwengu huu haupo mwenyewe. Wakati mtumishi huyo wa Sultan akiwa kwenye harakati zake hizo, naye alikuwa anachorwa pasipo kutambua.





Mwanaume mrefu mwembamba alikuwa anamtazama tokea wakiwa ndani ya kitoroli cha farasi. Alimfuatilia wakati anawafuatilia Malkia na Zura, mpaka pale alipojihifadhi eneo jirani ndipo akang’amuka na kuondoka.





Alitembea upesi na kwa uangalifu kutazama na kuhakiki kama yu mwenyewe. Alitembea na kutembea akakomea kwenye geti la jengo la msonara mkubwa.





Alinong’onezana na walinzi kisha akaingia ndani. Moja kwa moja alionana na Msonara mkubwa ambaye alikuwa anamsubiria kwa hamu kubwa. Alikuwa ameketi sebuleni akikuna ndevu zake.





Kitendo cha kutomuona Sultan ndani ya jengo lake akiwa ameondoka pasipo kumuaga kilimpa shaka na kumfanya atake kujua, ndipo akamtuma wakala wake upesi akatazame, huenda labda akawa amepokonywa tonge mdomoni na wasonara wengine.

Bahati nzuri akagundua hakuwa amepokonywa tonge, ila bahati mbaya zaidi alikuwa yu njiani kupokonywa sahani kabisa!





“Unasema ukweli?” Aliuliza Msonara mkubwa akitumbua macho.



“Ni kweli kabisa,” akajibu wakala wake.



“Nimemuona mtumishi wa Sultan anawafuatilia wale wanawake na amechukua makazi mahala pa karibu.”





Msonara mkubwa akashika kichwa chake akiachama. Ilikuwa wazi sasa Sultan Mansoor atakuwa ameshajua habari za mkufu. Hii haikuwa habari nzuri kwake hata kidogo. Alighafirika na aliomba aachwe mwenyewe apate kutafakari.





Alikaa hapo sebuleni mpaka pale Sultan aliporudi. Walihudumiwa chakula na vinywaji wakiwa wanateta mambo kadhaa ya biashara. Msonara mkubwa hakutaka kuvamia lile swala lake kwa pupa kwa kuhofia kumshitua Sultan, hivyo alifanya jambo hilo kwa ustadi; aliliweka kando kwanza kisha kadiri muda ulivyosonga akafungua kucha zake.





“Nimeshangazwa ulitoka pasipo kuniaga. Kuna jambo ulienda kulifuatilia?” Aliuliza Msonara akinywa chai yenye kila vikorombwezo. Macho yake yalikuwa yalikuwa yanamtazama Sultan na fika yalimuona mwanaume huyo akiwa ameguswa na hilo swali.





“Nilienda tu kutembea,” alijibu Sultan kiwepesi.



“Tu?”



“Ndio, kwani kuna shida yoyote?”



“Hapana. Ni kama tu nilivyosema, nilishangazwa.”



Kukawa kinywa kwa dakika mbili wakinywa na kula. Kila mtu alikuwa anawaza yake kichwani. Ni kama vile walikuwa wanategeana nani aanze kuongea. Walikuwa wanatazamana kwa kuibiaibia.



“Kuna lolote umeliona au umeligundua huko nje?” Msonara mkubwa alikuwa wa kwanza kufungua mdomo wake.

“Ndio,” Sultan akajibu. Msonara mkubwa akakabwa na kiu ya kutaka kusikia. “Nimeona tawala yenu inazidi kutanuka,” alimalizia Sultan. Taarifa hiyo ikamkwaza Msonara, si hiyo aliyokuwa anaitaka. Aliishia kuguna akabadili mada.





“Naweza nikafahamu ni lini unaondoka kiongozi?”



Sultan akamtazama na jicho lenye ng’eng’e.

“Muda si mrefu, usijali,” alijibu kwa sauti nzito. Hawakutia tena neno, lakini vichwa vyao vyote vilikuwa vinachambua, kukeketa na kung’amua.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

Wakati wa mchana Rhoda anaendea nyumba moja ya wastani, ndaniye anaishi mmoja wa wazee wa baraza la uongozi wa tawala ya Goshen. Ni mmojawapo wa watu wale waliokuwa wananasibu tungo zao juu ya kumpindua malkia Vedas.



Rhoda alipiga hodi akasimama mlangoni hapo. Alikuwa amevalia kinadhifu akificha utupu wake na gauni refu la kijivu lenye ngozi mabegani. Nywele zake alikuwa amezikusanya vema na kuzibana hivyo kuupa uso wake nafasi nzuri ya kuonekana. Alivutia kutazama na harufu yake ya uwaridi ilikuwa inamvutisha mtu kuwa naye kando.



“Naweza nikakusaidia?” Aliuliza Mzee wa baraza. Uso wake haukuwa rafiki. Alikumbuka kabisa uso wa mgeni wake ni wa mwanamke aliyewahi kuwa na mahusiano ya kisiri na Fursa. Na kwa namna moja ama nyingine akadhani mwanamke huyo atakuwa amekuja kumpapatikia maana hana pa kujishikiza kwa sasa.





“Samahani kwa usumbufu,” alichombeza Rhoda. “Nina maongezi na wewe.”



“Sema, nakusikia,” akasema mzee huyo akiwa ameushikilia mlango wake. Kiwiliwili kilikuwa ndani nje akichomoza kichwa tu.

“Najua mlichopanga kufanya,” alisema Rhoda. “Nataka na mimi nishirikishwe.”



Mzee wa baraza akatoka ndani vizuri. Aliufunga mlango akimtazama Rhoda kwa macho ya mkazo.



“Unasemaje we mwanamke?”



Rhoda alieleza kila kitu ya kwamba alisikia kile wazee hao wamepanga kufanya, hivyo basi anaomba naye apewe nafasi la sivyo ataenda kumpasha habari malkia.



Mzee wa baraza alicheka kinafki, akauliza:

“Unadhani nani atakuamini malaya wewe?”

“Hata kama asiponiamini, kuna kitu ataweka kichwani juu yenu,” alijibu Rhoda. “Na maana yake ni kwamba hamtofanikiwa maana jicho lake litakuwa nanyi muda wote.”



Uzuri mwanamke huyo alikuwa amekaa mahali ambapo mzee huyo hakuweza kumdhuru. Palikuwa ni karibu na njia pana ipitishayo watu mara kwa mara. Isingekuwa hivyo pengine mzee yule angechukua hatua mkononi kwa namna alivyokuwa anamtazama Rhoda.

Rhoda alishika njia kuondoka, lakini mzee huyo akamwita.



“Unataka nini?” Aliuliza.



“Nataka mali kuficha siri yenu,” akajibu Rhoda.



Mzee wa baraza alimtazama Rhoda kwa macho ya kishetani. Ingawa alimkubalia mwanamke huyo yale anataka, ni dhahiri shayiri uso wake ulionyesha atapanga ya kidhalimu.



“Hili ni kati yangu mimi na wewe tu, usije ukathubutu kufanya lolote la kijinga,” alionya Rhoda. “Utakapofanya chochote jua n’takuwa nimetangulia hatua mbele yako.”



Alikomea hapo akaondoka zake. Mzee wa baraza aliingia ndani akiwa amefura. Alijiandaa kwa kujiveka mavazi kisha akatoka kwenda kukutana na wenzake apate kuwapasha habari, hii ilikuwa kinyume na makubaliano aliyoyaweka na Rhoda.

Lakini mzee huyo wa baraza pasipo kujua, Rhoda alikuwa anamfuatilia. Kwa mbali kabisa Rhoda alimtazama mzee huyo akitembea kwenda nyumba moja baada ya nyingine.

Rhoda alijikuta anasonya akatikisa kichwa chake.



“Punda!” Alilaani. “Huwezi kumlazimisha kunywa maji mtoni.”



Sasa alikuwa amebakiza chaguo moja tu; kwenda kwa malkia Vedas. Chaguo hili hakuwa analipenda, ila sasa ndilo pekee lilikuwa limebakia mkononi mwake. Hakuwa na namna.

.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

.

Jua lilizama na hivyo usiku ukawasili. Huu ndio ulikuwa wasaa wa Jayit kuamka.



Japokuwa kwenye himaya yake ya Devonship jua halijawahi kuonekana, kitendo cha himaya zingine kuwa giza humpa faraja na kuona sasa ulimwengu wote upo mikononi mwake; hujihisi hana mipaka; hujihisi mwenye nguvu zaidi.



Alimuita jemedari wake wa vita, Tititat. Mwanaume huyo mzito wa kushiba akafika mbele yake ndani ya muda mfupi. Alikuwa tayari amejiandaa kwa vita akiwa amebebelea panga lake lenye kiu ya damu. Macho yake makubwa yalikuwa yamechomoza akiwa anahema kwanguvu.



Jayit aliwagiza aite jeshi lote mbele ya hekalu kwani ana neno la kuwapa. Tititat akafanya kama alivyoagizwa. Jeshi lote lilijaa mbele ya hekalu la kiongozi wao wakisubiria agizo.

“Leo ndio siku!” Sauti ya Jayit ilinguruma kama radi. Kila kitu kilikuwa kimya kikimsikiliza.



“Leo ndio siku ya kuonyesha utawala wetu maana hakuna wakutuzuia pale jua linapozama!”



“Woi! Woi! Woi!” Jeshi likaitikia kwanguvu.



“Leo tunaenda kuonyesha nguvu zetu!”



“Woi! Woi! Woi!”



“Ni leoo!”



“Woi! Woi! Woi!”



“Na leo ni zamu ya Maam! Kachukueni vyote vilivyomo huko. Katekeni vyote vya thamani na mvilete nyumbani! Msiache chochote cha dhahabu wala shaba!”

“Woi! Woi! Woi!”



Jeshi likapotea kuelekea kule lilipoagizwa, Tititat akiliongoza. Ndani ya muda mfupi tu halikuonekana. Ni vumbi tu ndilo lilibakia!

Jayit alirudi ndani ya hekalu lake akaketi kitini. Kwa kutumia ramli yake ya kichawi aliona jeshi lake likiyoyoma, likitenda na hata likirejea.



Huko Maam kuliachwa patupu vitu vyote vya thamani vikikombwa. Sio tu hivyo, bali hata watu waliuawa damu ipatikane. Damu kwa ajili ya wanajeshi hao wa Devonship kama kiburudisho kazini.



Ilikuwa ni ajabu mno, wanajeshi wa Devoship hawakuonekana pale walipokatiza ama kufanya matendo yao. Ni vishindo tu ndivyo vilikuwa vinasikika! Ungeshangaa tu kuona mtu anadondoka chini akipapatika, ama vitu vikibebwa na kupotea!



Jayit alishindwa kuzuia tabasamu lake la mamba usoni kwa kuona mafanikio hayo. Wakati sasa jeshi lake larejea, alichezesha ramli yake na kutazama himaya ya Goshen.



Alitazama himaya hiyo kila mahali akakomea mahali aishipo mtawala. Alitazama eneo hilo kwa makini, akamwona malkia Vedas akiwa kitandani anafanya mapenzi.



Alijaribu kumtazama mwanaume huyo aliyekuwa anafanya tendo hilo na malkia, akashindwa kabisa kumng’amua, hakuwa anamjua. Alibakiwa na maswali kede kichwani, lakini mwishowe aliamua kuyapuuzia na kumtafuta malkia mwingine amjuaye, Malkia Sandarus.



Ni kwa muda Jayit hakuwa amepekuwa wala kuifuatilia tawala hiyo. Hakuwa hata anajua kama kwa sasa ipo chini ya mwanamke Vedas Alturo.



Alimtafuta Malkia Sandarus nyumba nzima hakumwona. Staajabu alikuja kumpata akiwa ndani ya himaya ya masonara, tena ndani ya nyumba ndogo ya msonara akiwa amelala chini pembeni ya mwanamke ambaye hakumfahamu.

Hakubanduka hapo upesi, akatazama kwa makini na mazingira ya eneo hilo. Ndani ya muda mfupi akagundua kuna wanaume wawili walio karibu na hilo eneo. Wanaume hao walikuwa hawajalala, bali wapo macho kwenye hali ya ulinzi. Mmoja alikuwa akichungulia kupitia dirishani, wakati mwingine akiwa ameketi mbali kidogo lakini akitazama nyumba aliyomo Malkia Sandarus.



Jayit alipata hamu ya kujua zaidi. Kwa namna moja ama nyingine hisia zake zilimtuma ya kwamba pale kutakuwa kuna kitu cha thamani kinachowindwa, na basi tamaa ikamkaba. Jeshi lake lilipowasili, alimwita Tititat kando na kumtaka aende Osheni – tawala ya masonara haraka iwezekanavyo. Aende huko akapeleleze. Aende huko akawinde hicho kinachowindwa.



Pasipo kukawia, Tititat akamkwea farasi wake na kuanza safari ya kwenda Osheni.

.

.

.

***

.

.

.

Usiku ulienda upesi kukakucha ndani ya himaya ya Osheni. Watu waliamka wakashika kazi za kurepea na kuandaa vito vya dhahabu ama vito vingine vya thamani kama vile almasi na kadhalika. Kila mtu aliwajibika, na kama ungelikuwa hapo ukaona basi ungelisema ala! Huu ndio mji wa wachapakazi.





Malkia Sandarus na Zura nao wasiwe nyuma, walikuwa wanafanya usafi ndani ya makazi waliyokuwa wanaishi. Ilifikia pahala wakagawana kazi hizo ili wafanye ufanisi kwahiyo basi Zura alibakia nyumbani wakati Malkia Sandarus akienda kuchota maji.





Alienda safari nne na chungu chake kichwani, akayamiminia maji hayo kwenye bilauri fulani kubwa. Lakini baada ya hapo, hakuonekana tena akileta maji. Ilichukua muda mrefu, na sasa Zura anapata shaka.

Alitoka ndani akaangazaangaza kila kona pasipo kumuona Malkia. Aliamua kufunga safari kwenda huko kisimani yapatikanapo maji. Akiwa njiani, anaona watu kadhaa wakiwa wamejizonga na wanateta kitu.



Alipata shaka na miguu yake ilichanganyia upesi kwenda eneo la tukio.



Alifika akasogeza watu kando apate kuona. La haula! Akaona kitu cha kushangaza; akaona kitu kilichompokonya nguvu.



Alikuwa ni malkia! Akiwa chini amekobekwa kisu kifuani. Hakuwa na dalili yoyote ya uhai. Na tayari mwili wake ulikuwa wa baridi.



Zura alimtikisa malkia wake pasipo mafanikio. Alimpiga makofi aamke lakini napo alijichosha tu kwani Malkia Sandarus alikuwa amekufa!

Mwanaume aliyemuua alikuwa hatua kadhaa mbali na eneo hilo. Alikuwa ni mwanaume yule aliyetumwa na malkia Vedas Alturo; alikuwa ni mwanaume yule aitwaye Nedal!



Lakini wakati akifanya mauaji hayo, wanaume wawili: wakala wa Msonara mkubwa na mtumishi wa Sultan Mansoor, walishuhudia tukio zima. Hawakuwa na la kufanya zaidi ya kutazama, kwani wao hawakuwa na lingine linalowahusu zaidi ya mkufu! .



Macho pima yalimtoka Zura. Kama vile wewe usemavyo haiwezekani, ndivyo naye alivyokuwa anasema rohoni; Malkia atakufaje? Alibishana na uhalisia. Alijihisi hana nguvu na anahitaji mtu wa ziada aje kumzindua toka kwenye ndoto hiyo ya kutisha. Alimwaga machozi na kusaga meno. Alijaza watu kwa kilio lakini hawakuwa na msaada kwake zaidi ya kumtazama na kuteta.



Hakunyanyuka kwenda popote mpaka pale Msonara mdogo alipokuja baada ya kukosa wageni wake nyumbani. Alimtwaa yeye pamoja na mwili wa Malkia kwenda nyumbani.



Msonara mdogo aliufungasha mwili wa marehemu vema, kwanzia juu mpaka chini. Hilo lilifanyika baada ya pale kujihakikishia ya kwamba mwanamke huyo, Malkia ambaye hakupewa heshima yake anayostahili, amekufa kweli. Hakuwa anapumua na mapigo ya moyo yalishakwenda. Taratibu hata mwili wake ulikuwa unadaka baridi kuendelea kuthibitisha ya kwamba hakuna dalili zozote za uhai sasa zilizobakia.



Ni simanzi iliyoje? Kumbe safari ya kuja Osheni ilikuwa ni ya kutafuta kifo!

Basi kutokana na imani haba juu ya kifo hiki cha Malkia Sandarus, ikamchukua Zura siku mbili ajiaminishe ya kwamba ni kweli kile kilichotukia. Hakuwa analala kabisa, pale alipopata lepe la usingizi aliishia kukurupuka kwa kumuona Malkia ndotoni.



Alikuwa anautazama mwili wa Malkia mara kwa mara na hata muda mwingine akidhani ama ameuona eti umesogea! Hapana, yalikuwa mawenge.



Kwenye siku ya tatu ndipo likachimbwa shimo refu na Msonara mdogo peke yake, maana hakupata msaada toka kwa wenzake, kwani nani anamjua Zura ama Malkia Sandarus kwenye tawala ile ya masonara? Mwili wa Malkia ulidumbukizwa shimoni, ukafukiwa. Msonara msogo akamwomba Zura warudi nyumbani.



Zura ambaye hakulala hata usiku huo, alidamka asubuhi na mapema kwenda kwa Msonara mkubwa kumpasha habari pasipo kujua ya kwamba mwaume huyo tayari ni mjuzi. Zura aliaga anataka kuondoka kurudi nyumbani maana haoni tena mantiki ya kujiweka ndani ya himaya hiyo. basi pasipo kinyongo, Msonara mkubwa akampatia kheri zake kumtakia safari njema.



Zura alijipaki juu ya farasi wa Malkia, akiwa amefungasha chakula na maji, akaanza safari yake. Alijihisi mpweke sana, lakini kinyume na uhalisia huo, katu hakuwa mwenyewe, ingawa hata kama angelitazama umbali wa maili moja kila upande hakika asingelimuona yeyote mwenye muda naye.

.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.



Kwanini twasema hakuwa mwenyewe basi? Pasi na shaka unawakumbuka wajumbe wawili: mmoja wa Sultan na mwingine wa Msonara mkubwa. Wajumbe hawa pale walipopata kuona kifo cha Malkia Sandarus walipeleka taarifa hiyo kwa wakuu wao.



Wote, Sultan na Msonara, wakakabwa na donge la simanzi, lakini mbali na hapo wote, sare, wakajawa na hamu ya kutaka kumfahamu zaidi huyo aliyemuua Malkia, kwanini kafanya hivyo? Walihisi kwa njia mojawapo atakuwa ana mahusiano na mkufu, si bure!



Wakati huo Nedal, mwanaume muuaji, alikuwa yu njiani kurudi Goshen kwa kasi kubwa kwa minajili ya kufikisha taarifa njema ya kifo cha Malkia Sandarus kwa Vedas. Lakini pasipo kujua, mjumbe wa Sultan na wa Msonara mkubwa walikuwa wanamfwatilia.



Yani mtu pekee aliyepata fursa ya kuwaona wenzake pasipo yeye kujulikana alikuwa ni mjumbe wa Msonara mkubwa tu. Alijiweka nyuma sana na alihakikisha macho yake yanawatungua walengwa wake yasiwaacha wapweke.



Kwahiyo basi, wakati Zura anajikongoja kuja huko nyuma, tayari wanaume watatu walikuwa wapo mbele yake, yaani Nedal, mtumishi wa Sultan na wa Msonara mkubwa. Si madogo haya!



Lakini kabla haijaenda siku moja nzima, mwanaume shupavu Nedal akagundua anafwata, tena na wanaume wawili. Ilikuwa wakati jua laelekea kupoteza nguvu zake lizidiwe na kiza, wanaume hao wakaingia ndani ya jangwa kubwa lisilozibwa na chochote kile.



Ni humo ndipo kila mmoja akamgundua mwenzake maana hakukuwepo na cha kujifichia. Kwa mara ya kwanza Nedal alihisi watu hao walikuwa wasafiri wengine kama yeye, ila muda ulivyozidi kusonga akajenga shaka.



Kila mmoja alibebelea tahadhari, na ilikuwa kana kwamba wanategeana nani aufungue uwanja wa mapambano basi uwanja uwake moto. Kwa upande wa Nedal, alijihisi yupo mwenyewe, yani wale wanaume wawili wapo pamoja wametumwa kumwangamiza, sababu yake kichwani ikiwa ni mauaji ya Malkia Sandarus. Basi hiyo hali ikamjengea hofu zaidi.



Alimwamuru farasi wake akimbie upesi zaidi, farasi akatii. Kama vile kipenga kimepulizwa, mtumishi wa Sultan na yule wa Msonara mkubwa nao wakawatimua farasi wao basi pakawa mithili ya shindano. Farasi na jangwa wapi na wapi? Ndani ya muda mfupi farasi wote wakachoka taaban! Nguvu za miguu zilimezwa na mchanga kina wa jangwani, hata kutembea walishindwa wakaketi. Huo ukawa fursa sasa wa binadamu hao kuonyeshana umwamba.



Kila mtu alishikilia jambia lake kwa ajili ya vita. Pasipo hata kuulizana chochote, jambia zikaanza kutemeshwa cheche kwa misuguano!



Ziliteka hewa zikirushwa huku na huko. Sasa hapo ikawa ni ustadi wako kwenye kukwepa ndio ungekukomboa, lakini pia maarifa yako kwenye kuitupa kumlenga adui wako.



Mungu wangu! Nedal alikuwa mwepesi zaidi ya wote. Alikwepa jambia za wenzake kama wafanyavyo wasichana wa mchezo wa rede. Ndani ya sekunde kumi aliwasoma maadui zake, akafurahi kukuta ya kwamba hata nao pia walikuwa wanawindana.



Mkono wake wa kulia ulikuwa una nguvu lakini pia mwepesi kwenye kufanya maamuzi. Alikuwa anaondoa ncha ya jambia za wenzake kwa kutumia jambia lake. Na pale aliposhindwa, basi akazikwepa stadi. Lakini yeye pale aliporusha shambulizi lake liliwaacha hoi maadui wake kwa kuwavujisha damu.



Basi punde, mtumishi wa Sultan na yule wa Msonara mkubwa wakaangushwa chini wakiugulia maumivu ya kifo. Nedal alihakikisha vifo vyao kisha akawakatakata vipande vya nyama alivyovitia ndani ya mkoba wake wa chakula. Alitwaa farasi wote, wa wale wafu, akaendelea na safari yake kwa kutembea.



Huko mbeleni alipumzika baada ya kuchoka, akawasha moto na kula chakula chake alichokisindikizia na nyama ya wenzake aliyoikausha na kuioka kwa moto.

.

.

.

.

.

.

. ***

.

.

.

.

.

.

Rhoda hakulala kwake kwa kuhofia usalama dhidi ya wazee wa baraza ambao alishajua nyendo zao.



Asubuhi anajiandaa na kujitanda vema uso wake asipate kujulikana. Anatazama usalama wake kwanza kwa kutazama nje kupitia dirishani, baada ya kuona papo shwari basi anatoka akitembea haraka haraka.



Hakuna anayeweza kumgundua, hata kumdhania. Hivyo basi anafanikiwa kwenda umbali wa maili moja na kadhaa kwa mguu mpaka karibu kabisa na hekalu ya malkia Vedas Alturo. Njiani alikuwa anaigiza kuulizia bidhaa, ama kukunjakunja kona za hapa na pale ili iwe ngumu kumbashiri adhma yake.



Alifika hekaluni hapo sasa akawa ana kazi moja ya namna ya kuingia kwenye hekalu hiyo akapate kusema jambo na malkia. Kazi hiyo haikuwa rahisi hata kidogo. Si rahisi kama unavyodhani kuonana na kiongozi wa juu kabisa, tena wewe ukiwa mtu tu wa kawaida usiye na nafasi yoyote kwenye uso wa dunia zaidi ya kuitwa baba au mama.



Lakini sasa kwa maajabu, Rhoda anafanya kazi hiyo iwe tofauti, anaifanya iwe nyepesi kabisa.

Aliongea na mlinzi mmojawapo langoni juu ya lengo yake, lakini mlinzi kwa kutomwamini hakumruhusu kabisa. Rhoda aliapa kwa Mungu wake juu ya adhma hiyo lakini bado hakufua dafu kabisa, basi akaamua kutumia utu wake kupata nafasi hiyo ambayo hakutaka kuipoteza. Alimwahidi mlinzi utupu wake endapo kama atamruhusu. Alitumia macho yake ya udanganyifu na nguvu ya uzuri wake, akashinda.



Hakuwepo mwanaume wa kuacha hiyo fursa hapo. Mlinzi huyo alikuwa na sura mbaya mno isiyomvutia yeyote. Alikuwa ananuka jasho na hata mdomo pia. Kwa namna yote tu alikuwa ana ‘ugwadu’ mkali ambao hakutegemea kama kuna mwanamke yeyote angekubali kuusawiri, tena wa kariba ya Rhoda: mwanamke ambaye waweza kuona utamu wake kwa kumtazama tu.



Bahati iliyoje hii? Alisema na nafsi yake. Alijikuta anatabasamu kuonyesha meno yake ambayo kwakweli siwezi sema yalikuwa rangi gani, maana sielewi.



Kichwani aliwaza na kuamini Rhoda hawezi akawa na hatari yeyote kwa malkia, hivyo basi hiyo ahadi yake ni lazima tu itatimia.



Rhoda hakuwa mjinga kumteua mwanaume huyo. Na sasa lengo lake lilikuwa linaeleka kutimia. Aliingia ndani ya uzio mkubwa wa hekalu akiongozana na mwanaume huyo aliyerahisha kila kitu. Aliketi ndani ya chumba kikubwa chenye samani ghali za kuvutia kwa ajili ya kumngojea malkia.



Rohoni alitamani pale pangekuwa kwake. Ilikuwa imekaribia sana kuwa hivyo kabla ya Fursa kuuawa na huyo anayekutana naye ndani ya muda mfupi.



Alijikuta anapandwa na hasira na chuki, lakini akaona hazina maana sasa kwani anaweza kutimiza malengo yake hayo kwa njia nyingine. Moja jumlisha tatu ni nne, lakini pia hata mbili jumlisha mbili ni nne. Aliutuliza moyo wake na kungojea. Baada ya dakika tano, akasikia vishindo vya mtu vinakuja, na punde akamuona malkia.



Alikuwa amevaa gauni jeusi lililobana mwili wake. Nywele zake zilibanwa na kibanio kizuri cha dhahabu. Uso wake ulikuwa umeparwa vema akiwa ananukia kama gadeni ya maua. Kiatu chake kilikuwa cha ngozi halisi ya simba. Mkononi alikuwa amebebelea fimbo nyeusi nyembamba yenye michongo ya mauamaua.



Kwa namna alivyokuwa anaonekana, Rhoda alijiona takataka kwa muda japokuwa kiuhalisia, malkia Vedas Alturo hagusi hata robo ya uzuri wa Rhoda.



Kitamu ni chumvi, mama.



Malkia Vedas alitabasamu kumwona Rhoda. Si kwamba anamfahamu, hapana bali kumkarimu. Laiti kama angelijua ndiye aliyekuwa anampokonya Fursa, si bure naye angemmaliza. Rhoda naye alitabasamu, si kwamba alifurahi, bali aliona anakaribia kumaliza safari yake. Alitamani awe anguko la malkia Vedas Alturo, na basi kile alichokuwa anafanya kilikuwa sahihi.



Alinyenyekea akieleza yote yale aliyopata kuyasikia toka kwenye vinywa vya wale wazee wa baraza. Alijipendekeza ya kwamba anampenda malkia na asingependa jambo kama hilo la mapinduzi lipate kutokea, lakini pia hakusita mwishoni kudadavua ukata unaokumba maisha yake. Machozi yalisaidia kufanya simulizi yake hiyo kuwa ya kugusa.



Malkia alimsikiliza mwanamke huyo mpaka pale alipomaliza, kisha akasema kwa ufupi:

“Nimekusikia. Waweza kwenda.”

Rhoda aliishiwa na nguvu. Aliona jambo lake halijapewa uzito ule aliotegemea. Uso wake ulikunjamana na alijaribu kusisitizia zaidi pasipo mafanikio. Malkia aliondoka zake kurudi alipotokea, na punde wanaume wawili wakaja kumtoa Rhoda ndani. Walimwacha nje ya uzio alikopokelewa na mlinzi yule aliyeweka naye ahadi.



“Sasa?”



Rhoda alisonya akimtazama mwanaume huyo kwa macho ya kukata. Aliondoka zake pasipo kutia neno. Alikuwa ameghafirika mno na aliona sasa amepoteza dira.



Hakutegemea kama malkia angekuwa vile baada ya kumpa habari nyeti kama zile. Alijiona mtupu na mpumbavu kwa kuhatarisha maisha yake. Alikuwa amelikoroga na sasa aliona analinywa.

Alifika kule alipotokea, bado akiwa amejijaladia vema asionekane. Aliingia ndani ya kuvua nguo hizo, ila mara akasikia sauti kali ya mlango ukivunjwa! Alitazama akaona wanaume wawili, majibaba ya watu, waliovalia vinyago wakiwa wamebebelea jambia zimetazo. Wanaume hao pasipo kusema kitu, walitazamana kana kwamba wanaulizana kama mhusika wao ndiye yule, mmoja akapandisha kichwa juu kuthibitisha taarifa.



Rhoda alipiga ukunga kwa kuona sasa roho yake ipo mkononi. Alikimbia kufuata mlango wa nyuma lakini akaishia kwenye mikono minene ya wanaume wale waliokuja pale kutwaa roho yake kama vile walivyoagizwa na wazee dhalimu wa baraza. Wanaume hao walikuwa wanamtazama Rhoda tokea alipotoka ndani ya hekalu ya malkia, masikini Rhoda akijidanganya ya kwamba yu mwenyewe.



Alinyanyuliwa juu kwa mkono mmoja, mwanaume aliyemdaka akamuuliza:

“Unadhani unaishi mwenyewe kwenye ulimwengu huu?” Alitupwa mbali akajibamiza kwanguvu nusura apoteze fahamu ila akaishia kupata maumivu makali ya kichwa.



“Tunakubaka kwanza ndio tukumalize, malaya mkubwa wewe!” Alifoka mwanaume aliyemtupa Rhoda mithili ya kiroba cha chumvi.



Rhoda hakuwa anaona vizuri: kichwa kilikuwa kinampasua na macho yake yalikuwa yanaona ukungu. Alikuwa tayari kwa lolote lilikuwa linataka kumtokea. Hakuwa na nguvu ya kupambana wala kupiga kelele. Alikuwa amejilaza akiachama mdomo, macho yake yakiwa kama mtu mwenye usingizi mzito.

Ajabu, kabla hajaguswa, alisikia makele makali ya maumivu yaliyofuatiwa na vishindo vikubwa vya watu wazima, kisha swali likaulizwa:

“Ndiye huyu?”



“Bila shaka atakuwa ndiye yeye!” swali likajibiwa. Mara Rhoda akajihisi kubebwa na punde akawa hajielewi kabisa. Hakujua wapi alipokuwa anapelekwa na ni wakina nani wamemtwaa.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

Harufu kali ya damu iliteka pua ya Zura aliyekuwa juu ya mgongo wa farasi.

Kulikuwa na baridi kali kwa muda huo na alikuwa amejikunyata akibana kinywa chake kwa kung’ata meno. Uso wake ulikuwa mweusi wakati pua yake ikiwa nyekundu kama macho yake.



Alisimama akaangaza pande zake zote pale alipofika mahali ambapo harufu ilizidi. Kwa msaada wa fisi waliokuwa wanakula mabaki ya nyama za miili ya watumishi wa Sultan na wa Msonara mkubwa, Zura akaona ni wapi harufu ile ilikuwa inatokea. Alijikuta anakunja sura yake, lakini bado asidhani kama ile nyama ilikuwa ni ya binadamu.



Kabla hajasonga mbele, akaona vichwa viwili vya binadamu vikiwa vinanyofolewa nyama. Alitaka kutapika lakini hakuwa na kitu tumboni. Alijikuta anasisimkwa kwa hofu iliyompelekea amtimue farasi wake haraka. Ila tokea hapo akawa na woga zaidi. Alikuwa anatazamatazama kando na nyuma yake kila mara. Muda wote alihisi anaweza akauwawa kama wale watu aliowaona wakiliwa, na tena hivi yupo mwenyewe basi ikawa tabu si kidogo.



Lakini inawezekana ukawa umesahau jambo, embu acha basi nikukumbushe; unamkumbuka Tiktak – mfuasi mweledi wa Jayit? Unakumbuka naye alitumwa kuja Osheni baada ya Jayit kutazama ramli yake iliyomwonyesha Malkia akiwa Osheni – tawala ya masonara? Basi sasa alikuwa karibu ya eneo hilo akija Osheni.

Juu ya farasi wake akimbiaye kama upepo, alikuwa ametuama. Farasi wake huyo hakuwa amepumzika tokea safari ilipoanza, na wala hakuonekana kama ana dalili zozote za kuchoka.



Sasa ndani ya maili moja tokea alipokuwepo Zura, alikuwepo Nedal akiwa amejipumzisha. Lakini pia Tiktak akija kwa kasi.



Ni ngumu kubashiri Tiktak ataanza kukutana na nani na atamfanya nini, hii ilitegemea na muelekeo wake. Lakini je akikutana na Nedal, binadamu huyo ataweza kuzuia mkono huo wa kushoto wa Jayit? Na je akikutana na Zura, mwanamke huyo atabakiziwa roho yake? Itakuwa ngumu kukupatia majibu. .

.



Upepo ulipuliza kando, Tititat akabadili mwelekeo. Hii ilikuwa kheri tena ya haja kwani kwa sasa shari ya kukumbana na aidha Nedal au Zura ilikuwa finyu ya mraba. Na ikawa hivyo Tititat asimwone yeyote isipokuwa miili ya wale wafu – wajumbe waliouwawa na Nedal.

Aliona eneo hilo akiwa umbali wa hatua kama hamsini. Sauti ya fisi ilibeba hisia zake na kumfanya atazame eneo hilo. Roho yake ilimtuma ajongee papo na mwili wake ukatii, basi akasogea.



Alituama eneoni hapo kwa muda akiperuzi na macho yake. Hakuona cha maana basi akaendelea na safari yake. Lakini kichwa chake hakikutaka kubanduka kwenye tukio hilo. Aliendelea kuwaza miili ile kiasi kwamba alijiona mwehu. Watakuwa tu ni masikini waliofia njiani! Alijipa ahueni. Lakini makazi ya watu yana umbali kiasi gani cha kuwafanya wafie jangwani? Basi watakuwa wameuawa! Akahitimisha na wazo hilo jepesi japokuwa bado lilinanga kichwa chake.



Dhamira yake kuja kule ilikuwa ni kumtafuta tu yule aliyeagizwa amtafute – Malkia Sandarus, maana ana kitu cha thamani ambacho mfalme wake, Jayit, amekibashiri. Kitu ambacho kinawindwa. Kitu ambacho hakijulikani ni kipi. Ajabu hili! Uwezo hulevya.



Ni kwa wakati huo, Zura, mwanamke pekee aliyekuwa ndani ya jangwa, alikuwa amejilaza juu ya mchanga wa jangwa akiwa amejifunika shuka dhoofu. Baridi lilikuwa kali na likamtenda akajikunyata. Farasi wake aliketi kando ila bado yeye macho yake yakiwa wazi, akiyatupa huku na kule.



Kwa muda huo kulikuwa tulivu na si ajabu hata wewe ukadhani ndio muda mwema wa kujipumzisha.



Si kwamba Zura alikuwa amesahau yale aliyoyaona ya miili ya wafu, la hasha! Macho yake yaligoma kufumba kwa kuhofia usalama wake. Mkono wake wa kuume ulikuwa umeshikilia kisu chake kidogo alichokiweka kiunoni ya kwamba kwa lolote litakalojiri basi atajitutumua kujiokoa.



Alitenda vivyo kwa masaa kama manne, macho yaangaza. Lakini Mungu hakuwa mjinga kuweka usingizi uambatane na kufunga macho, kwani nayo yahitaji kupumzika. Basi taratibu Zura akawa anashindwa kuyaokoa macho yake na usingizi, akalala! ‘kajoto’ alikojitengenezea kwa kujikumbatia mwenyewe na kujitandaza shuka kakampa ahueni, hakujua hata ni muda gani mkono wake uliacha kisu.



Aliufaidi huo usingizi kwa lisaa limoja tu kabla hajashtushwa kwa kukosa hewa! Kabla ya tukio hilo, farasi alilia lakini Zura hakusikia. Shingo yake ilikabwa vilivyo kiasi cha kutoa macho akipapatika kutaka kujikomboa. Uso wake uliunda huruma na mbashara aliona uso wa mtoa roho.



“Shhh! Nyamazaa!” Sauti ya kiume ilinong’oneza masikio ya Zura. Alikuwa ni Nedal akimtenda mwanamke huyo. Usiniulize alifika hapo muda gani maana sitakuwa na jibu.



Mikono minene ya mwanaume huyo ilikuwa imeficha shingo ya Zura barabara, uso wa mwanamke huyo ukachomoza mishipa ya damu kana kwamba mito juu ya ramani. Kwa namna alivyokuwa amebanwa, alisahau hata kama ana kisu. Mikono yake yote ilikuwa inang’ang’ana kuivuta mikono ya Nedal, kazi ambayo haikuonyesha dalili yoyote ya kuleta matunda.



Ikiwa imebakia sekunde sasa Zura afariki, twaweza sema hivyo, mara alijikuta akipata ahueni ya ghafla baada ya mikono mizito ya Nedal kubanduka shingoni mwake! Hakuamini kama amepona. Farasi alimtwanga Nedal teke zito la kichwani, Nedal akazirai.



Kabla ya kufanya lolote, Zura akahangaika kwanza kuvuta pumzi kwa nguvu zake zote. Alikohoa na kukohoa. Alishikilia shingo yake iliyokuwa inamdai maumivu makali. Kwa muda wa kama dakika tatu alikuwa anavuta pumzi tu.



Alichomoa kisu chake akamtazama Nedal aliyekuwa amezirai. Alijitahidi kumng’amua mtu huyo lakini hakuwepo kumbukumbuni mwake hivyo akashindwa kuelewa ni sababu gani ilivyomfanya mwanaume huyo atake kumuua. Alitaka kummaliza kwa kumkobeka kisu cha kifua, akashindwa. Roho yake ya huruma ilikuwa kubwa kuliko ya ukatili.



Alinyanyuka akampongeza farasi wake kwa kumbata kabla hajamkwea na kuondoka toka hapo kwa kasi kubwa.



Hakusimama mpaka pale farasi alipochoka, akashuka toka mgongoni mwa mnyama huyo akawa anatembea. Hakutaka kulala kabisa japokuwa mwili ulikuwa unahitaji hiyo huduma. Alihofia, tena maradufu! Aliuona usingizi kama kifo.



Alitembea kwa muda wa lisaa akipambana na pepo kali ya jangwa. Ila ghafla akiwemo metembezini, akajikuta akizama kwenye tego. Alikanyaga eneo fulani ambalo lilimomonyoka upesi na kummeza kana kwamba mdomo wa mamba. Si yeye wala farasi wake aliyebakia kwenye uso wa dunia!



Palikuwa kimya ghafla usiwaze kama kulikuwa kuna viumbe hai hapo sekunde tano nyuma.

.

.

.

.

***



.

.

.

.***

.

.

.

.

.

Masaa mawili tangu pale jua lilipochomoza, Rhoda anaamka toka kwenye usingizi mzito.

Ni ndani ya chumba kikubwa mno chenye samani za gharama ndefu mathalani kitanda kikubwa na kipana, madirisha makubwa, kabati kubwa, vigoda na viti vya kujipumzishia.



Rhoda alitazama huku na kule. Hakuwa anajua pale alipo wala hakujua amefikaje, lakini punde akili yake pevu ilimwambia yu ndani ya hekalu ya mfalme, ndiyo! Hakuna chumba chochote chaweza kuwa vile ndani ya himaya yote ya Goshen. Japokuwa Rhoda hajawahi kutembelea vyumba vyote ndani ya himaya ya Goshen, aliamini hivyo.



Pasipo juhudi tabasamu likachipuka usoni mwake. Hatimaye amefanikiwa! Aliwaza. Kwahiyo malkia Vedas amesadiki yale aliyomwambia? Ndio!



Alifuata dirisha mojawapo akaangaza kutazama nje. Uso wake ulijawa tabasamu. Alijiona yuko juu ya dunia. Alitazama karibia himaya yote ya Goshen asiamini. Niko ndotoni au? Hapana bwana! Alipepesa macho yake ahakikishe kama anaota. Alitabasamu mpaka jino la mwisho.



Mara mlango ulifunguliwa, akaingia mwanaume mmoja jabali akiwa amevalia nguo za watunza usalama. Alikuwa ni mojawapo wa wanaume wale waliomkomboa Rhoda toka kwenye mikono ya wauaji. Alimtazama Rhoda na macho makavu akisema:

“Nifuate!”



Kisha akaondoka. Rhoda alimfuata mwanaume huyo mpaka mahali penye kibaraza kinachotazama kaskazini mwa himaya ya Goshen. Hapo alimkuta Vedas akiwa na mwanaume mmoja mgeni machoni: alikuwa ni mrefu, mwili wa kiume, nywele nyeupe, macho yenye kiini cha kijani na kidevu pacha akiwa amevalia nguo iliyomkaa vema.



Alikuwa ndiye mwanaume yule Jayit aliyemwona kwenye rada zake akifanya mapenzi na Vedas.



Rhoda alitoa heshima yake kwa malkia kabla hajaamriwa aketi chini. “Nimehakiki yale uliyoyasema ni kweli,” alisema malkia Vedas.



“Na kutokana na uzalendo wako basi nimeamua kukutunuku kwa hilo.”



Rhoda aligundua ya kwamba malkia alituma wanajeshi wake wamfuatilie baada ya kutoka pale hekaluni akiamini ya kwamba kama ni kweli yale aliyoyasema basi ni lazima wazee wale dhalimu wa baraza wangechukua hatua na kujiingiza mkenge.



Lakini zaidi ya hapo, Rhoda akajuzwa kuwa wazee hao tayari wameshauawa. Mbaya si wale tu wadhalimu, bali wote. Miili yao ilikuwa nje inaning’inia kwenye vitanzi. Hapo Rhoda akaguswa, lakini pia akashangazwa na roho ya Vedas. “Nimeona nikupe nafasi kubwa sana kwenye usalama,” alisema Vedas. wakati akiongea hayo alikuwa anatazama himaya yake.



“Lakini kabla ya kukupa nafasi hiyo, nataka nihakikishwe zaidi juu ya uwezo wako. Kwahiyo kwa mwezi huu wote utakuwa chini ya uangalizi wangu. Utakuwa ukiishi kwako kama kawaida lakini huduma zako zote zikitokea hapa. Utakuwa unafanya kazi zako kama kawaida lakini lengo lako likiwa ni moja tu – kuwa jicho langu la ndani.



Kuna watu wengi kwenye himaya hii. Si wote wenye nia nzuri na mimi, na si wote wenye nia nzuri na Goshen. Na bahati mbaya sipo kila mahali kuhakikisha hilo.



Nahitaji kuona kila mahali. Nahitaji kumsikia kila mtu. Kutimiza hilo basi nakuhitaji wewe. Kwa kazi yako unayoifanya, upo karibu sana na midomo ya watu. Nataka uniletee kila wanachokiteta.”



Baada ya maelezo hayo, Rhoda aliondoka zake kurudi nyumbani. Alipewa dinari nyingi sana za kumfaya afanye chochote anachotaka maishani. Aliagizwa aboreshe kazi yake ya mama n’tilie na kila baada ya siku mbili awe analeta mrejesho wa yale anayoyasikia na kuyaona. “Una uhakika hili litafanya kazi?” Aliuliza Vedas akimtazama mwanaume aliyekuwa kando yake.



Mwanaume huyo alitabasamu. Hakuwa na papara. Macho yake yalikuwa yanatazama uwanda wa Goshen. Ukimwita Phares, utakuwa hujakosea. Phares, mwanaume wa chupa; Phares, mwanaume aliyeghaniwa na malkia Vedas; Phares, mwanaume asiye na makazi bali kwenye ulozi wa Vedas; mwanaume ambaye Vedas anamwamini kuliko yeyote.



“Pasi na shaka, itafanya kazi,” alijibu Phares. “Na kama isipofanya kazi basi ndiyo itakuwa fursa yako ya kutimiza haja yako ya kummaliza.” Malkia Vedas alitabasamu kwa mbali, ila tabasamu lake hilo halikudumu likajifinya na kuunda uso wa kazi.



Siri ilikuwa sirini.

Malkia Vedas anapata kufahamu mahusiano ya Rhoda na marehemu Fursa. Jambo hili analing’amua baada ya kutonywa na mojawapo wa wanajeshi wake ambaye alikuwa anajua juu ya mahusiano hayo yaliyokuwa ya siri. Malkia anataka kummaliza Vedas akiwa usingizini, lakini Phares anamsihi amwache hai kwani ana matumizi ya faida kabla ya kumalizwa.

.

.

.

. ***

.

.

.

Ilikuwa ni zaidi ya juma moja lakini si zaidi ya mwezi tangu Sultan alipowasili kwenye himaya yake, tawala kubwa Arabuni, akiwa amebebelea vipuri kadha wa kadha vya dhahabu alivyotoka navyo Osheni.



Alikuwa hana furaha na mtingwa wa mawazo. Lakini pia mkimya aliyependa kujitenga mara kwa mara. Mke mkubwa wa Sultan anasumbuliwa sana na hili jambo. Anatamani kujua kinachomsibu mumewe japokuwa zoezi hilo limekuwa gumu kila mara anapojaribu.



Ndani ya siku hiyo, Sultan anashindwa kuendelea kubeba jambo hilo kifuani. Alimwita mkewe mkubwa akamtaka aketi pembezoni. Alimweleza juu ya mkufu wa himaya ya wasioonekana, ambao habarize alizikuta Osheni, na jitihada zake alizofanya kuuweka mkufu huyo kimyani.



Anatatizwa na ukimya wa mjumbe wake, na hajui ni nini shida haswa. Kwa namna kubwa anahisi ameshaupoteza. “Huenda mjumbe wangu akawa ameshauwawa,” alisema Sultan. Uso wake ulikuwa mwekundu, macho yake yakilegea kwa uchovu.



Mke wake alimsogelea karibu zaidi akamwekea mkono begani. “Mbona hukunambia hili jambo mapema mpenzi?” “Na sikutaka hata kulisema. Hili ni jambo la siri, na nyie wanawake hamna vifua.” “Ila si mimi, Sultan.” Alijigamba mke mkubwa. “Ni siri zako ngapi naziweka kwenye uvungu wa kifua changu?” “Najua ni nyingi ila hii ni kubwa zaidi. Hili jambo ni watu wachache sana wanalijua, na kama lingekuwa linajulikana na wengi lingeshazua vita.” Mke akaguna. Alishusha pumzi ndefu na kuivuta. Alikunja sura yake akijaribu kuchekecha jambo alilolikumbuka.

“Mpenzi!” aliita.



Sultan akaitika kwa kumtazama mke wake huyo; mwanamke mtu mzima ila mwenye uzuri kwa kukusisimua moyo; mwanamke aliyekuwa amejiremba itakiwavyo kila kitu kikiwa kwenye kiti chake.



“Lakini unaonaje ukajaribu kwa Al Karim!”

alisema mke.



“Al Karim?” Aliuliza Sultan akitafakari. “Ndio, kwa Al Karim. Hakuna asiyejua habari zake zinazovuma kutokea kaskazini. Mjuvi na mtaalamu wa ramli. Kwanini usiende kumweleza shida yako? Bila shaka atajihisi fahari kumhudumia Sultan.”



Sultan alinyamaza akiwazua. Baada ya dakika mbili alirudisha macho yake kwa mkewe akauliza: “Tunaweza tukamwamini kweli?”



“Bila shaka,” akajibu mke mkubwa. “Ni binamu yangu, mtoto halisi wa mjomba wangu, kaka wa kwanza wa baba yangu. Endapo nikimtaka afunge mdomo, basi atatenda.” Sultan alishawishika kuchukua hiyo njia. Siku iliyofuata, asubuhi na mapema, akadamka pamoja na mkewe mkubwa wakaongozana na msafara wake kuelekea kaskazini mwa himaya yake kubwa.



Alitumia siku moja njiani kabla ya kufika kwenye nyumba kuukuu ya bwana Al Karim. Alipewa mapokezi makubwa sana japokuwa alikuja kwa kush’tukiza. Walichinjwa wanyama kadhaa na mivinyo ikamwagikia vinywani.



Jioni ya siku hiyo, akiwa na Al Karim pekee, Sultan alieleza haja yake ya moyo iliyomleta pale. Haja hiyo ikamshtua Al Karim kwa kina. Macho yalimtoka pima na mdomo wake ukaachama.



“Sultan, ni kweli usemayo?” “Pasi na shaka, Sultan hawezi kuongopa.”



“Ni wangapi wajua kuhusu hili?”



“Wachache mno.”



“Lakini Sultan, wajua ni namna gani mkufu huu waweza leta balaa?”



“Najua, lakini ni vema tukafikiria mema yake kwanza kabla ya mabaya.”



“Sultan wangu,” Al Karim aliita kwa sauti ya upole. “Endapo kama wenye nao wataamka, basi watatuteketeza wote.” Alionya.

“Kivipi?” Sultan akauliza.



“Huu mkufu ni wa himaya ya wasioonekana. Hakuna himaya yoyote inayoweza kuwazuia hawa. Endapo kama wakija kudai chao, himaya yetu itageuka kuwa majivu!”



“Na vipi kwa himaya hizo watakaoumiliki? Huoni watatugeuza sisi majivu kabla ya hao wasioonekana?” Mzozo huu uliishia kwa Sultan kushinda akitumia madaraka yake kama silaha.



Al Karim alipiga ramli akitumia kioo chake cha ajabu, akauona mwili wa mjumbe wa Sultan ukiwa umebakia mifupa sasa. Alijaribu kuutafuta mkufu lakini hakuuona. Sultan akamwagiza amtafute Zura.



Zoezi hilo lilichukua kama dakika tatu, kioo kikawa giza. Al Karim alitikisa kichwa chake, akasema:

“Sultan, hatuwezi kumpata!” “Unamaanisha nini?” “Huyo Zura hayupo duniani!” Sultan akakunja uso.

.

.





“Una maanisha nini?” Sultan alitamba.

“Hayupo kwenye uso wa dunia,” Al Karim akajibu. “Yani simwoni kwenye rada zangu.”

Sultan akashusha pumzi ndefu. Alikuna ndevu zake kidevuni akibinua mdomo.



“Inawezekana akawa amejificha ama amefichwa,” alidadavua Al Karim.



“Kama angelikuwa amefariki basi ningelijua.”

“Sasa tunafanyaje?” akauliza Sultan.



“Nitamtuma wakala wangu mwaminifu amtafute,” akajibu Al Karim kisha akaenda kwenye chumba chake chenye mlango mweupe. Humo akatoka na kitu cha pembetatu kilichofunikwa na kitambaa chekundu.



“Nini hicho?” Sultan aliwahi kusibu.

“Ni wakala wangu mwaminifu,” Al Karim akajibu na kisha akafunua kitambaa kile chekundu.



Lilikuwa ni banda dogo la chuma lenye umbo la pembe tatu likiwa limemtunza bundi mweupe mwenye macho mekundu. Ndege huyo alikuwa anatisha kumtazama, si tu kwasababu alikuwa ni bundi, hapana! Kichwa chake kilikuwa kimebebelea pembe ndogo juu ya macho yake makubwa kama mayai ya mbuni. Ukubwa wake ulitosha kujaza banda. Na alipopanua bawa, rangi nyekundu ilionekana ubavuni.



Al Karim alisema maneno kadhaa ya Kiyunani kisha akafungua banda la bundi huyo aliyetoka na kutuama juu ya bega la kushoto la Al Karim.



“Ndiye huyo?” Sultan aliuliza. Al Karim akatikisa kichwa.



“Ndiye yeye – wakala wangu mwaminifu. Macho yake ni yangu. Mabawa yake ni miguu yangu.”



Al Karim alimtuliza bundi wake mkononi kisha akamtaka Sultan aseme nani anataka amuone. Sultan akadadavua mazingira na umbo la Zura, Al Karim naye akatia neno lake papo na kumwachia huru bundi aliyerukia angani.



“Kazi imekwisha, Sultan,” alisema Al Karim. “Ntakupa mrejesho pale litakapopatikana jambo.”



Siku iliyofwata, asubuhi na mapema, Sultan akaondoka kurudi kwenye makazi yake. Hakuwa na matumaini makubwa juu ya kupatikana kwa mkufu.



Mkewe mkubwa alimsihi atulizane kila jambo litakuwa sawa, kwani Al Karim hajawahi kushindwa jambo. Hakuna rekodi ya jambo lolote lililowahi kuzidi uwezowe. Hapo angalau Sultan akawa ametua hofu kwa kiasi chake.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

Siku mbili zinapita hakuna ambacho Tititat anakipata katika himaya ya masonara. Amezunguka sana kumtafuta Malkia lakini hakufanikiwa. Baada ya kufanya upelelezi wake mdogo anajikuta makaburini, juu ya kaburi la Malkia Sandarus. Alizikiwa hapo. Simulizi yake iliishia hapo.



Ulikuwa ni muda wa usiku mwepesi wa saa moja. Hakukuwa na mtu makaburini isipokuwa Tititat aliyeonekana anawaza jambo la kufanya muda si mrefu mbeleni. Baada ya kutimiza dakika kumi na tano katika eneo hilo pasipo kuona mtu, Tititat alianza kuchimba kaburi la Malkia akitumia mikono yake.



Kwa kasi kubwa alitenda zoezi hilo pasipo kuchoka. Halikuwa la ajabu hilo kwasababu muda huo ndio ulikuwa muda wao, wana Jayit, kuwa na nguvu; muda wa usiku! Kama amefungiwa mota alichimba kaburi, akaufikia mwili dakika tano tu.



Aliupekua mwili huo pote, hakuona kitu: hakukuwa na cha thamani! Sasa kile kitu cha thamani, kisichojulikana, alichotumwa na mfalme wake atakipatia wapi? Alijiona anashindwa.



Akiwa ndani ya shimo la kaburi, anasikia sauti za watu wawili wakiwa wanateta. Walikuwa ni vijakazi wa Msonara mkubwa. Walikuwa wametoka matembezini na sasa wanarejea kwenye makao yao haraka kabla ya mkuu wao hajafika.

.

.

Huko walipotoka walikuwa wamekunywa na kujilewea kwahiyo midomo yao haikuwa na stara, wala vichwa vyao havikuwa vinachambua vema mazingira waliyomo.

.

.

Walikuwa wanahororoja kuhusu mkufu. Habari hizo walizisikia kwa mkuu wao ambaye anahangaika mno kuutia mkononi. Mmojawao alimuuliza mwenzake kama mwenzao aliyemfwatilia Zura amekwisharejea.

.

.

Hapo mjibuji mwenye mdomo ‘pochi’ akaanza kufumbua mambo ambayo yalimvuta Tititat.



“Bado hajarejea, nahisi atakuwa tayari amekufa!”



“Umejuaje?”



“Muda wote huo hakuna taarifa yoyote ile. Unadhani kuna nini tena hapo? … ila kweli nakwambia, mkuu wetu kuna muda hana akili hata punje!”



“Enh!”



“Ohoo! Nakwambia ukweli. Hivi yeye kabisa kwa akili yake akawaamini wanawake wale mafukara watakuwa na kitu cha thamani kama kile? Eiiiish! Upuuzi!”



“Tatizo lako unapenda sana kudharau watu wewe! Mi naamini atakuwa amejiridhisha kwanza kabla ya kuamua vile.”



“Waii! Nakwambia tena, kuna muda mkuu wetu hana akili; zote huenda makalioni!”



“Akiupata je huo mkufu, n’kufanyaje?”



“Ntakununulia bilauri kumi na tano za pombe!”



“Kwa mshahara gani unaolipwa? Mie nitataka bilauri mbili tu.”



“Na asipoupata wewe utanipa ngapi?”



“Kumi na tano!”



Walikuwa tayari wamesogea mbali. Tititat alichungulia akaona sasa ni salama kwake kutoka ndani ya shimo. Alirudishia udongo alioutoa ndani ya kaburi hilo haraka kisha akaondoka kuwafwatilia wajumbe wale waropokaji.



Alitembea kwa uangalifu mno kiasi kwamba wajumbe walevi wasingewaza kama kuna mtu nyuma yao. Hata kama wangeliwaza hivyo na kutazama, bila shaka wasingelimuona yeyote kwa jinsi Tititat alivyokuwa amefanana na kiza.

.

.

Walifika getini kwa nyumba ya Msonara wakaingia ndani. Tititat alitazama eneo hilo kwa umakini na akaanza kupanga namna ya kuingia humo apate kuonana na Msonara mkubwa. Aliamini kwa kupitia msonara huyo, atapata majibu kadhaa ya maswali yatakayomsaidia kupata kitu cha thamani, ambacho tayari alishakijua ni mkufu.

.

.

Ilichukua dakika kumi tu, Tititat akawa tayari yupo ndani ya jengo la Msonara mkubwa lenye ulinzi wa haja. Hatukujua kaingiaje ila tunaona miili ya walinzi ikiwa chini imelala haijitambui au inavuja damu pomoni. Hakuna kelele yoyote iliyosikika mpaka Msonara mkubwa anafikiwa ndani ya chumba chake alimokuwemo na mwanamke mmoja mrembo mrefu mwembamba.

.

.

Kabla Msonara hajashangaa, alikuwa tayari amekabwa ngeta nzito wakati mwanamke wake akiwa amezirai kwa kumwona tu Tititat.

.

.

“Mkufu upo wapi?” aliuliza Tititat.

.

.

Kwa sekunde tu Msonara mkubwa alikuwa anavuja jasho, macho yamemtoka pima akipata uchungu wa roho kunyofoka.

.

.

Tititat alifungua mikono yake kumwacha mwanaume huyo avute hewa. Kwa papara Msonara akahema akikohoa. Tititat alirudia tena swali lake akimtazama Msonara usoni:

“Mkufu upo wapi?”

.

.

“Sijui,” alijibu Msonara mkubwa. “sijui ulipo!”

.

.

Tititat akadaka tena shingo ya mwanaume huyo na kuiminya kwanguvu. Macho ya Msonara yalipanda juu kwenda ubongoni. Tititat alimwacha tena avute hewa, kisha akarudia swali lake.



“Mi mwenyewe nautafuta, sijui ulipo!”

.

.



“Unautafutia wapi?”

.



“Kuna wanawake wawili ndio walikuwa na taarifa na huo mkufu. Mmoja amekwishafariki, mmoja amekwenda zake. Sijui ameenda wapi!”

.

.

Tititat alidaka tena shingo ya Msonara. Kabla hajaiminya, Msonara aliropoka:

“Ngoja weee, nasema baba!”

.

.

Tititat akamwacha.

.

.

“Kweli sijui! Sijui wapi alipoelekea, ila walinambia wametokea Goshen, nadhani huko ndipo atakuwa anaelekea. Nimemtuma mjumbe wangu amfwatilie.”

.

.

Tititat alinyanyuka akatoka ndani ya chumba hicho. Alimwendea farasi wake aliiyekuwa amemfungia porini, akamkwea na kisha kuanza safari akirudia njia aliyokuja nayo.

.

.

Kituo chake cha kwanza kilikuwa kwenye ile mizoga aliyoiona jangwani. Alimsimamisha farasi wake hapo akatazama. Ni mifupa tu ndiyo ilikuwa imebakia. Alijiuliza mizoga ile ilikuwa ya nani, akakumbuka maneno ya wale wajumbe walevi, mmoja anaweza akawa mjumbe wa Msonara. Na je huyo wa pili? Anaweza akawa ndiye huyo mwanamke? Nani kawaua?

.

.

Aliondoka na maswali yake hayo kichwani akibashiri kuyapatia majibu mbele kwa mbele. Aliamini kama mwanamke huyo, Zura, atakuwa hai basi atamwona kabla hata hajafika Goshen, hata kama alifunga safari hiyo kwa muda. Hilo kwake lilikuwa inawezekana maana yeye hakuwa na mapumziko njiani: farasi wake alikuwa hachoki wala yeye vilevile.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

Dhumuni la Rhoda halikuwa limepotea. Wakati huu wa usiku akiwa ndani ya mgahawa wake mkubwa na unaovutia, alikuwa anawaza na kuwazua juu ya malkia Vedas. Ndio, bado alitaka kummaliza. Hiyo ndiyo ilikuwa haja ya moyo wake. Lakini sasa alikuwa na wazo jipya, kuutwaa ule mkufu uliotuama kwenye kifua cha mwanamke huyo.



Aliwasikia vema wale wazee wa baraza wakinadi mkufu ule kwamba ndio unaompa kiburi mwanamke huyo kwani hapo kabla, kipindi akiwa mke wa mfalme, hakuwa hivyo.

Sasa kuutwaa mkufu huo maana yake ni nini? Kumfanya malkia awe mdhaifu: kumfanya asiwe na sifa ya kuongoza: kumfanya malkia ajione mtupu.

.

.

Yeye, Rhoda, hakuwa na haja ya kutawala Goshen, kama ingelitokea hilo basi ingelikuwa bonasi kwake. Hakumpenda Vedas toka rohoni, alishindwa kabisa kulizuia hilo kuonekana.

.

.

Kumwona mwanamke huyo anatawala, kwake lilikuwa ni jambo la kushoto mno.

Mawazo yalimtinda sana, ila kwakuwa sasa hivi alikuwa na wafanyakazi lukuki ambao walikuwa wakimfanyia kazi, basi hilo halikuathiri biashara yake kwa vyovyote vile.

.

.

Kazi yake ya usimamizi haikuhitaji kuwa macho muda wote, bali tu uwepo wake eneo la kazi.

.

.

Akiwa humo mawazoni, alirudishwa fahamuni na sauti kali ya kicheko. Akiwa amekunja sura alimtazama mteja aliyekuwa anacheka hivyo. Alitamani kumfukuza lakini alishindwa.

.

.

Alimtazama mteja huyo kana kwamba mama amtizamavyo mwana mkaidi. Aliishia kusonya na kuendelea kupepesa macho yake kwa wateja wengine.

.

.

Kwenye kona kabisa ya mashariki mwa mgahawa, aliwaona wanaume watatu wasio na nywele kichwani. Walikuwa wamevalia nguo zilizowakaa vema, mikononi zikiwa zimejaladiwa na ngozi. .

.

Viatu vyao vilikuwa vikubwa lakini imara. Migongoni mwao walikuwa wamebebelea majambia marefu. Na kwenye kingo za viuno vya walikuwa wana visu virefu vilivyofunikwa na vifuko vya ngozi.

Pasipo na shaka robo, wanaume hao walikuwa ni wanajeshi wa himaya fulani, ama basi ni mesenari wa mtu fulani ama taasisi fulani kubwa. Rhoda alivutiwa sana kuwatazama, na akili yake ilimjuza akaamini kuna jambo anaweza kupata toka kwenye vinywa vya wanaume hao.

.

.

Alisogea karibu akaweka masikio yake bayana kusikia. Kwa muda wanaume wale waliteta maongezi yasiyokuwa na maana nzito kwa Rhoda. Mwishowe Rhoda akaamua kujitoa kimasomaso kwa kujongea kwenye meza ya wanaume hao. .

.

Alijitambulisha yeye ni nani eneo hilo na akaomba ruhusa ya kuketi.

.

.

“Samahni kwa usumbufu, nimeona ni sura ngeni mgahawani mwangu. Nikaona sio shida endapo tukafahamiana.”

.

.

Uzuri na ustaarabu wa kuigiza wa Rhoda uliwateka wanaume wale. Pasipo hata kusita wakajinasibu ya kwamba wao ni wapita njia tu wakitokea huko magharibi ya mbali kabisa. Wamepita hapo kula baada ya kuambiwa ndio mahali bora kabisa.

.

.

“Ahsanteni sana,” Rhoda alisema. “Nimefurahia sana uwepo wenu hapa kwani bila shaka utapanua biashara yangu kwa kwenda kusambaza habari njema kunihusu.”

.

.

Waliendelea kula na kunywa wakiteta ya hapa na pale. Baada ya muda mfupi Rhoda akaanza kupata yale anayoyataka.

.

. “Ni himaya kama tatu zimeshapitiwa na jeshi hilo la usiku. Zimeachwa hazina hazina yoyote na watu wameuawa wengi mno!” alisema mwanaume mmoja.

.

.

Alikuwa anatoa taarifa ya huko walikotoka: namna gani himaya kadhaa zilivyoachwa hazijiwezi baada ya kuvamiwa na jeshi kubwa la usiku: jeshi lililosemwa kama lenye nguvu na halizuiliki.



“Watu wa huko wanasema wavamizi hao walikuwa wanatisha. Walikuwa wenye kasi kiasi cha kumaliza kazi yao ndani ya himaya nzima kwa muda usiozidi dakika kumi tu!” alisema mwanaume mwingine akitafuna kipande cha nyama.

.

.

“Inaaminika jeshi hilo litaendelea kupita kwenye himaya kadha wa kadha. Mpaka sasa wameshapita kwenye himaya tatu, na haingii akilini kama wataishia hapo.”

.

.

Taarifa hiyo ilimsisimua Rhoda, na aliona ni sahihi kabisa endapo angemtaarifu malkia Vedas. Ndio, hakuwa anampenda mwanamke huyo ila aliona anastahili kupata taarifa hiyo kwa usalama wa raia wengine na hata wake ndani ya himaya.

.

.

Hakungoja muda mrefu baada ya wageni wake kuondoka, alijikusanya akaenda kwenye hekalu la malkia, pasipo na mushkeli akaruhusiwa kuingia ndani. Aliketi mahali pa mapokezi wakati kijumbe akiwa ameenda kutoa taarifa juu ya ugeni wake.

.

.

Baada ya dakika mbili akatokea Phares. Alikuwa amevalia taulo tu kifua chake chenye manyoya kikiwa wazi. Alikuwa ametoka kuoga: mwili wake ulikuwa umetambaliwa na maji. Hakuwa amevaa nguo ya ndani, maungo yake yakawa yamejichora tauloni.

.

.

Alimkarimu Rhoda kwa tabasamu. Alimwambia Malkia ametoka kidogo kwahiyo anaweza akamweleza tu shida yake. Rhoda hakupenda kumwambia hilo jambo Phares, ila kwakuwa hakuwa na namna, ilimlazimu atende hivyo.

.

.

Bahati njema, akiwa kati ya maelezo malkia Vedas akawasili. Alighafirika kumwona Phares yupo vile, kimwonekano, na kisha yu karibu na Rhoda. Kwa namna fulani aliona Rhoda anaweza kumkwapua mwanaume huyo kama alivyofanya kwa Fursa. Wivu ulimjaa. Na macho yake dhahiri yalionyesha hivyo.



Phares aliondoka zake upesi akamwacha malkia Vedas na Rhoda. Alinadi anakwenda kuvaa nguo na kujiweka sawa. Alipopotelea ndani, malkia Vedas akamuuliza Rhoda:

.

.

“Umeona nini?”

.

.

“Wapi, malkia wangu?” Rhoda akajibu na swali.

.

.

“Umeona nini kwa yule mwanaume?”

.

.

“Sijaona kitu, malkia.”

.

.

Vedas akamtazama Rhoda machoni. alitamani kumwambia kuhusu habari za Fursa ila akafanikiwa kuzuia mdomo wake.

.

.

“Umekuja kuleta habari gani?”

.

.

Rhoda akamweleza kila kitu juu yay ale aliyoyasikia kule mgahawani. Vedas alishtushwa na hizo taarifa. Aliapa atazifanyia kazi, na akampongeza Rhoda kwa kazi aliyofanya.

Ila kuna kitu bado kilikuwa machoni mwake.

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

. “Nimeonaa!” Ilikuwa ni sauti kali ya bibi mlozi ikibweka. Sauti hiyo ilitoka nje ya nyumba yao kubwa kuukuu iliyo ndani ya himaya ya wachawi, Tanashe.

.

. “Umeona nini?” wenzake wawili waliuliza kwa pamoja. Mmoja alikuwa hana macho; mmoja alikuwa nalo moja wakati yule aliyepaza sauti akiwa na macho mawili.

.

.

“Nimemuona Malkia Sandarus!” alipaza tena sauti. Bibi yule ambaye alikuwa hana jicho haraka akaunyoosha mkono wake na kunyofoa jicho moja toka kwa yule mwenye mawili, akalipachika kwake.

.

.

“Umemuona wapi?” wenzake wakauliza tena kwa uso uliolowa hamu.

.

.

Walikuwa ndani ya sebule yao inayonuka mizoga. Moshi ulikuwa umetanda ukitokea kwenye pipa lao, uwani, lililokuwa linapika chakula chao cha usiku.

.

.“Nimemuona kwenye rada zangu za macho mawili na kioo msumbusi. Yupo Osheni!”

“Hilo tunalijua, ndio yupo Osheni.” Wenzake wakadakia.

.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

.

“Hapana! Siyo kama vile nyie mjuavyo. Yupo Osheni, lakini tayari amekufa! Amefukiwa ndani ya ardhi!”

.

.

Bibi mmoja akajikuta ametabasamu.

.

.

“Kwahiyo unataka kusema …”

.

.

“Ndio!” yule msemaji mkuu akadakia.

. . “Tunaweza tukamtumia sasa. tunaweza tukamfanya akawa kikaragosi chetu!”

.

.

.

Basi wasipoteze muda roho ya Malkia ilitafutwa na kuvutwa mpaka mezani mwa ajuza hao. Ilikuwa ni furaha kubwa kuitwaa roho hiyo ambayo ilikuwa ina matumizi adhimu kabisa.



Bibi hao watatu walinuwia maneno ya lugha ngeni kisha wakaiacha roho hiyo irudi huko ilipotokea. Baada ya muda mchache, kioo chao chenye nguvu ya ajabu kikaonyesha mwili wa Malkia Sandarus ukifunua macho.



Wakatabasamu na kupongezana.



Macho ya malkia yalikuwa mekundu yanayong’aa hivyo uso wake ukawa unatisha. Kwa kasi kubwa alifanya jitihada za kufukua udongo uliomfunika, ndani ya dakika moja akawa tayari ametoka shimoni yupo juu ya uso wa dunia.



Alikuwa hatamaniki kwa uchafu. Uso na mwili wake ulijawa udongo, ukichanganya na muda ulikuwa ni usiku na macho yake yalikuwa mekundu yanayong’aa basi unaweza ukajikuta unakimbia pasipo kutambua miguu imetolea wapi uwezo huo.



“Mkufu upo wapi?”



Sauti ya kunong’oneza iliuliza masikioni mwa mwili wa Malkia.



Alitazama upande ilipo Goshen, akanyooshea kidole. “Fwata mkufu huo haraka!” Sauti ikaamuru, na punde mwili wa Malkia ukaanza kuchukua hatua za haraka kuelekea Goshen kuutwaa mkufu.



Kiza kilikuwa ni kinene lakini hakikuwa kikwazo kabisa. Mwili wa Malkia ulitembea pasipo hofu yoyote. Kile ambacho mwili huo ulipata kuona, basi ndicho ambacho bibi wale waliopo Tanashe wakawa wanaona.



Zaidi ya hapo wao ndiyo wakawa watu wa mwisho kuamua nini mwili huo ufanye. Walifanya hayo kwa kunena tu.



Baada ya mwendo wa dakika kama ishirini, mwili wa Malkia uliingia ndani ya jangwa kavu katili lililojawa na michanga. Ndani ya jangwa hilo akapokelewa na mbwa mwitu watatu wakubwa. Walikuwa na njaa mno, matumbo yao yalikuwa migongoni, na pengine walijua sasa matumbo yao yatajazwa angalau na vipande vya nyama.



Mbwa hao walisogea kwa wepesi wakazingira mwili wa Malkia. Walikuwa wananguruma wakichuruza mate. Macho yao yalijawa uchu haswa wakitegeana nani aanzishe shambulizi.



Mwili wa Malkia pasipo na papara ulisimama katikati ya mbwa mwitu hao. Ulikuwa unawatazama hao wanyama pasipo hata tone la hofu, na pengine akiwa anasubiria ashambuliwe ili naye apate kuonyesha uwezo wake.



Mbwa mwitu mmoja, mwenye baka kubwa jeusi mgongoni, alirukia mwili wa Malkia akang’ata mkono. Wenzake nao papo hapo wakarukia mwili huo kwa mkupuo kila mmoja akang’ata kipande chake cha mwili. Ajabu ni kwamba mwili wa Malkia haukufurukuta wala kulalamika kwa maumivu, uliendelea kutulia kana kwamba hakuna jambo lililotukia.



Ila hali hiyo haikudumu kwa muda mrefu, punde uso wa mwili wa Malkia ukabadilika na kujikunja. Mwili ulitumikisha mikono yake kumtwaa mbwa mmoja baada ya mmoja, ukavunja shingo zao na kuwatupilia mbali kisha safari ikaendelea.



Hakuna jeraha lolote lililoonekana kwenye mwili wa Malkia; si mchubuko wala damu. Hili lilikuwa la kutisha, sijui liliwezekanaje ila ndiyo ulikuwa uhalisia.

Macho ya kutisha ya mwili huo yalituama barabarani yasipepese wala kuvutiwa na kingine chochote njiani. .

.

.

.

.***



.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

Ndani ya asubuhi kavu yenye upepo, malkia Vedas alikuwa yu mbele ya kioo kikubwa kilichomtaswira vema. Alikuwa anajikagua baada ya mpambaji wake, bi Sanur, kumaliza kazi ya kumpara.



Alikuwa amevalia gauni refu jeusi lililobana kiuno na mikono; kichwani alivalia kofia ya dhahabu; miguu yake ilifunikwa na viatu nyeusi vigumu vyenye umbo la mtumbwi; kifua chake kilibebelea mkufu ung’aao aliofanikiwa kuufananisha na hereni zake ndefu nyembamba.



Aliridhika na mwonekano wake, akapandisha kichwa chake juu kumruhusu bi Sanur ajiendee. Mwanamke huyo alipotoka, malkia akamtazama Phares aliyekuwa amejilaza kitandani akifunikwa na shuka kubwa zito lililodariziwa na nyuzi za dhahabu.



“Nimependeza?”



Phares akabinua mdomo wake.



“Ungeniuliza hapo kabla,” alijibu kisha akaongezea akiwa anaketi; “Una tatizo gani? – hauko sawa.”



“Sina tatizo, Phares,” malkia alitoa jibu jepesi. Phares alitupia mbali shuka akamfuata malkia. Mwanaume huyo alikuwa amevalia nguo ya ndani tu akiacha wazi mwili wake wa vinyweleo.



“Nimekwambia hauna haja ya kuhofia kiasi hicho, malkia wangu,” alisema Phares kwa sauti tulivu. “Kila kitu kitakuwa sawa kabisa, niamini.”



“Una uhakika gani, Phares?” Uso wa malkia Vedas ulikuwa umepoa, ni macho yake tu ndiyo yalionyesha uso huo una uhai.



“Nina uhakika, malkia wangu. Naamini jeshi letu na wewe pia utatulinda.” Malkia hakusema kitu, aliminya lips zake akapandisha kichwa chake juu kwa upole. “Ahsante kwa kuniamini, Phares. Nakuhitaji sana pembeni yangu. Unanifanya nijione mwenye nguvu sana.”



“Usijali, malkia wangu.”

“Tunaweza tukaenda wote?”

“Hapana, hii kazi inabidi ufanye wewe mwenyewe. Huu ndiyo muda wa kuonyesha wewe ni jemedari na ni mtu ambaye wanaweza wakamtegemea.” Malkia Vedas alivuta pumzi ndefu na kuitua. Alikumbatiana na Phares kabla hajatoka ndani ya chumba kwenda kwenye uwanja mkubwa wa Makarez kukutana na jeshi lake lililojipanga vema kumngoja.



Mapema baada ya malkia kupewa taarifa na Rachel juu ya uvamizi wa usiku unaofanywa na jeshi la Jayit likipora vitu vya thamani na hata kuua watu tena kwa njia za ajabu, aliona kuna haja ya kujiandaa kukabiliana na hali hiyo mapema iwezekanavyo. Alihofia kupoteza tawala yake. Hakutaka kitu hicho kije kutokea kamwe.



Lakini juu ya yote hayo alikuwa amejazwa hofu na aliona kabisa vita hiyo haikuwa ndogo. Tangu alipokuwa binti mdogo alikuwa anasikia habari za kuogofya za tawala ya Devoship chini ya mdhalimu Jayit. Namna gani tawala hiyo hula watu, jua halichomozi na hukaliwa na vibwengo vya kila aina. Kama haitoshi namna gani Jayit alivyovamia Goshen muda si mrefu uliopita akufukua makaburi ya babu na bibi yake pasipo kuzuiliwa na yeyote.



Phares alimjaza matumaini moyoni na mipango kichwani mwake. Aliondoa hofu usoni mwake akijivesha ujasiri kukutana na wanaume wake wa mapambano. Aliketi juu kabisa kwenye kiti kirefu chenye urembo wa kuvutia, pembeni wakiketi kamanda mkuu wa jeshi na kaimu wake. Baada ya kamanda mkuu kuongea na jeshi lake machache kuhusu ujio na uwepo wa malkia eneo hilo, malkia akasimama na kuanza kupayuka.

“Kama tusipopambana kwa moyo na nguvu zetu zote, tutapotea kwenye uso huu wa dunia,” alisema akijawa na tambo. Uso wake ulikuwa mkakamavu na hakuonyesha hata tembe ya woga.



“Goshen ilikuwepo, ipo na itaendelea kuwepo daima. Hakuna mtu yeyote anayethubutu kugusa tawala hii kwa gharama zozote zile, waliojaribu wanafahamu haswa. Na yeyote atakayejaribu pia atafunzwa.” Hakusema maneno mengi sana zaidi ya kueleza hali ambayo tawala yao imo kwa muda huo.



Aliketi kisha akawa anateta na viongozi wakuu wa jeshi juu ya mipango ya namna gani wanaweza wakawa salama dhidi ya adui yao ambaye haijajulikana ni muda gani atashambulia.



“Ni muda wa usiku tu?” Aliuliza kamanda mkuu wa jeshi.



“Ndio,” akajibu malkia. “Huo ndo’ muda ambao matukio yameripotiwa kufanyika.”



“Mfumo wa mawasiliano inabidi uwe imara sana na tuweke tabaka la kwanza mipakani.”



Alisema makamu kamanda.



“Ndio,” akadakia malkia. “itabidi kuwe na matabaka manne ya wanajeshi: tabaka la kwanza litaketi mpakani, tabaka la pili litakuwa ni kiunganishi kwa maana ya mawasiliano na la tatu litakuwa ndiyo tabaka la mwisho likiwa limejazwa na silaha nzito na idadi kubwa ya wapambanaji. Hawa wataungana na tabaka la pili upesi, watamshambulia adui kwa kumshtusha wakimzingira na kumuweka katikati.



Kwa muda wote huo inabidi kuwe kuna mwanga wa kutosha mipakani na hali ya utulivu ili kusikia msogezo ama mguso wowote. Lakini pia maeneo kadhaa yachimbwe mashimo na kupachikwa mitego mikubwa.



Kwa namna yoyote ile, wavamizi hawatakiwi kuvuka zaidi ya maili tano toka mpakani.” Malkia alidadavua kisha akasimama na kwenda zake akiwaachia wakuu wa jeshi utendaji.

Muda ulienda kwa kasi sana. Ulipowasili muda wa jioni tayari kila kitu kilikuwa kimeshafanyika kama kilivyoagizwa. Wanaume lukuki walikuwa mipakani wakiwa wamebebelea maginga ya moto. Mashimo yalikuwa yameshachimbwa na kufunikwa kwa nyasi. Miti minene iliyobebelea ncha kali ilikuwa imetandikwa chini kwenye baadhi ya maeneo ikisubiria kufyatuka. Juu ya mti mrefu kulikuwa kuna kiota kiliichomhifadhi mwanajeshi mmoja aliyekuwa ana jukumu la kutazama usalama kwa umbali.



Ulinzi huo ulikuwa mkubwa kwenye upande ule ambao unatazamana na uelekeo wa tawala ya Devonship. Huko ambapo kila mtu alitegemea ndipo watatokea wavamizi.



Mpaka inafika majira ya usiku mkali hakuna chochote kilichokuwa kimeonekana. Hata wengine wakadhani inawezekana usiku ukawa umepita na shwari yake. Ila kadiri muda ulivyozidi kuzama usikuni, mambo yakaanza kubadilika!



Giza lilikuwa kali kupita kiasi, nyota na mwezi vilipotea angani. Moshi mweusi ulitanda taratibu isijulikane unatokea wapi. Hewa ilianza kuwa nzito na joto likaongezeka.



“Unawaona?” Alipayuka mwanajeshi mmoja kumuuliza mwanaume aliyekuwa yuko juu kiotani.



“Sioni chochote mkuu!”



“Tazama vizuri!”



Mwanaume yule aliyekuwepo kwenye kiota alitumbua macho yake asione jambo. Alitumia hata hadubini lakini napo hakuambulia kitu.

“Hamna kitu mkuu! – sioni kitu!” Mashaka yaliwajaa wakihisi kabisa adui atakuwa yupo karibu. Lakini kwasababu hakukuwa na uhakika wa hilo jambo, basi taarifa kwenda tabaka la pili haikutolewa.



Hali hiyo ya kuogofya ilidumu kwa dakika tano, mara vishindo vya watu vikaanza kusikika kwa fujo! Mwanaume yule wa kiotani alijaribu kutumia mashine yake ya kuona lakini hakuona kitu. Sasa hapo wanajeshi wakagoma kusubiria adui aonekane, walitoa taarifa kwa wenzao wa tabaka la pili kisha wakajiandaa kwa ajili ya vita.



Walisubiria kwa lisaa limoja, hawakuona yeyote! Gahafla vishindo vilizima na kisha kukawa kimya. Moshi mweusi ulipotea na nyota na mwezi vikarudi angani pasipo kutokea lolote!



Lilikuwa ni jambo la kustaajabisha: sasa vile vishindo vilikuwa vya nani?

.

.

.

.

.

.

***

.

.

.

.

.

.

“Sultan, una mgeni.” Alisema mtumishi mwenye kiremba kikubwa kichwani baada ya kuruhusiwa kuingia ndani ya chumba kikubwa cha Sultan.



Sultan alijinyanyua toka kitandani, akavalia gauni jeupe refu akatoka ndani ya chumba kwenda kukutana na mgeni wake aliyeitiwa. Uso wake ulikuwa umejawa na uchovu na ajabu sana siku hiyo hakuwa amemuuliza mtumishi wake juu ya mgeni. Hali hiyo ilimfanya mke wake mkubwa, aliyemwacha kitandani, ajiulize maswali kadhaa akijaribu kukumbuka kama mumewe alikuwa na miadi yoyote ile siku hiyo.



Naye alinyanyuka toka kitandani akajivesha gauni refu rangi ya pinki kisha akasogelea mlango. Aliufungua kidogo akatulia hapo ambapo palimwezesha kabisa kusikia kilichokuwa kinaendelea kwenye mazungumzo kati ya Sultan na mgeniwe.



“Muda wote huo!” Sultan alifoka. “Ndio, Sultan. Si kwamba ameketi, la hasha! Anafanya jitihada lakini bado hazijazaa matunda.”



“Zitazaa matunda lini?” Sultan alipayuka.



Wananchi wote wanamjua Sultan huyu ni kiongozi mstahimilivu na mwenye kujawa na busara. Laiti kama wangelimwona hapa, basi wangefuta mawazo yao yote hayo. Sultan hakuwa na stara kabisa linapokuja swala la mkufu. Kwa muda alikuwa anakuwa mnyama asiyefugika.



Mgeni, mtumishi wa Al Karim – mganga maarufu, aliamua kuwa kimya kwa kukosa jibu la swali la Sultan. Aliona kabisa namna Sultan alivyokuwa ameghafirika na kwa namna moja ama nyingine akajikuta anafahamu kuwa hamna jibu lolote litakalomridhisha Sultan isipokuwa kupatikana kwa mkufu tu.



“Namuhitaji huyo ndege!” alisema Sultan.



“Ndege yupi?”



“Ndege wa Al Karim. Huyo bundi mweupe.”



Mtumishi wa Al Karim akaduwaa.



“Haiwezekani, mkuu.”



“Kwanini isiwezekane?”



“Si kila mtu anaweza kumwongoza ndege yule isipokuwa Al Karim mwenyewe!”



“Wewe kibaraka!” Sultan alifoka. “Kamwambie mkuu wako Sultan anamtaka huyo ndege, tena haraka sana!” Mtumishi wa Al Karim, mwanaume mwembamba ndani ya kanzu pana, alisimama akatoa heshima zake kwa Sultan na kisha akaondoka kuufikisha ujumbe aliopewa kwa Al Karim. Farasi wake rangi ya kahawia alikimbia upesi mno.



Wakati huo mtumishi huyo akiwa njiani kurudi kwa bwana wake, bundi wa Al Karim alikuwa kwenye anga la tawala ya Osheni. Macho yake makubwa yalikuwa yanangazaangaza jangwani huku mabawa yake yakikata upepo.



Alitembea eneo hilo kwa muda kidogo, akamwona mtu kwa mbali akiwa juu ya farasi. Alishuka chini apate kumtazama mtu huyo vema.



Alikuwa ni Tititat! Alikuwa juu ya farasi wake aliyekuwa anatembea taratibu.



Ndege huyo alimfwatilia Tititat kwa ukaribu. Tititat alikuwa anafwatilia nyayo fulani alizoziona mchangani. Nyayo hizo zilitokomea kwenye eneo fulani lililomwacha Tititat na maswali kadhaa kichwani. Alishuka toka mgongoni mwa farasi akapekua aneo hilo na macho.



Alitembea hatua tano kwenda mbele, ila ghafla akarudi nyuma na kujirushia mbali. Mchanga uligawanyika na kutengeneza shimo kubwa ambalo kama si Tititat aliwahi kuruka, angekuwa amemezwa.

Yote hayo ndege yule alikuwa anayaona. Na maana yake ni kwamba Al Karim alikuwa anayaona.



Tititat alinyanyuka akalitazama lile shimo na macho ya mshangao. Moja kwa moja akapata kuamini kuwa lile shimo ndilo litakuwa limemmeza mtu aliyekuwa anafwatilia nyayo zake. Vipi kama mtu huyo atakuwa ndiye anayemhitaji? Alijiuliza. Alitazama ndani ya shimo lakini hakuona chochote isipokuwa kiza kikali. Alitaka kuondoka lakini akasita. Aliona kuna haja ya kuzama humo ndani.



Alimnong’oneza kitu farasi wake kisha akajirushia ndani ya shimo. Alitumia dakika tatu njiani kabla hajafika kwenye ukomo wa shimo. Alijikusanya akanyanyuka. Alitazama kila upande lakini hakuona kitu bali giza tu.



Alipapasapapasa na mikono yake akagundua kuna njia. Alianza kufwata njia hiyo akatembea kwa muda wa dakika tano kabla hajasikia sauti kali ya mwanamke iliyomshtua. Sauti hiyo ilikuwa ni ya makelele isilete maana yoyote. Haikukoma mara moja bali iliendelea zaidi na zaidi.



Tititat alifwatilia sauti hiyo akagundua mahali alipokuwepo palikuwa ni kama ukumbi baada ya kujikuta kila upande aliojaribu kwenda kulikuwa kuna njia. Masikio yake yalimwongoza mpaka akafika eneo fulani alilolikuta lina mwanga hafifu lakini hakukuwa na kitu.



Alitazama eneo hilo kwa mshangao, ila ghafla akajikuta amezibwa mdomo. Pap! Pap! Shingo yake ikakatwa na kisu kidogo kikali, akadondoka chini kama mzigo!







Ni ghafla alitokea mwanamke mnene mfupi akiwa amevalia gauni refu rangi ya krimu. Nywele zake zisizo na matunzo zilikuwa ndefu mno. Alikuwa ana macho makubwa yaliyozingwa na rangi nyeusi. Mikono yake ilikuwa mirefu na yenye kucha za kuchomoza. Kwenye mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea kisu kifupi ila chenye makali ya kutisha.



Kwa mujibu wa uso wake alikuwa ana hasira. Macho yalikuwa yamemtoka na mdomo ameubinua kana kwamba ametoka kuonja chakula kilichosheheni chumvi. Aliutazama mwili mfu wa Tititat kama vile anangoja jambo. Ni utadhani hakuamini kama ‘mvamizi’ yule amekufa. Aliinama akapitisha kidole chake kwenye damu ya kijani ya Tititat na kisha akailamba.



Ptuuh! Alitema rundo la mate pembeni. Sura yake ilijikunja mara tano zaidi. Alipiga mluzi mkali na ghafla wakatokea watu lukuki waliofanana na huyo mwanamke kwa nyuso za kutisha, macho makubwa yaliyosheheni ukuta mweusi. Watu hao wote walikuwa wamevalia magauni rangi ya krimu. Utofauti wao ni alama tu zilizokuwa zimepachikwa kwenye magauni hayo.



Wengineo walikuwa na alama ya pembetatu yenye nyota nyeusi katikati. Wengine walikuwa na alama ya nyota kubwa pekee wakati wengine wakiwa na alama ya vipande vya miti vilivyotengeneza umbo la X huku umbo hilo likifichama nyota kana kwamba inahitaji kivuli. Miongoni mwa wenye alama hiyo alikuwa ni yule mwanamke aliyefanya mauaji.



Watu hao waliongea kwa mfumo wa kunong’onezana tena kwa lugha isiyojulikana ni ya ulimwengu wa wapi. Macho yao yalikuwa yanatazama mwili wa Tititat wakiufanyia upembuzi.

Ingawa lugha yao haikuwa inaeleweka, matendo yalikuwa yanatosha kujieleza. Walikuwa wanakinzana juu ya mwili ule mfu. Ila baada ya kuonja damu, kila mtu alijikuta anaitema na kughafirika mara kede. Walikasirikiana hata wenyewe kwa wenyewe. Kila mmoja akapotea kwenda upande wake kwa kasi aliyokuja nayo. Ghafla!



Ni kwamba ile haikuwa damu wanayoitaka, hilo lilikuwa wazi. Sasa ni ipi wanaitaka? Na ni kwa ajili ya nini? Na Zura je aliyezama humo shimoni yu wapi?



La haula! Sauti ya Zura ilisikika ikiita kwa kilio. Mwanamke huyo hakuonekana yupo wapi. Sauti yake iliyojaa uchovu na uchungu ilikuwa inatokea gizani, giza totoro! Iliomba msaada kwa nguvu zote. Baada ya muda ikanyamaza na kukawa kimya. Aidha alikuwa amechoka ama hakuwa na matumaini tena.

.

.

.

.

.

.

. *** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

.

.

Shimo lile lilimpatia maswali mengi bwana Karim aliyekuwa anatazama kwa kupitia rada. Bundi wake aliyekuwa anawandawanda juu ya shimo hilo kwa muda mrefu hakupata kuona kitu zaidi ya giza totoro. Alingoja kama Tititat atatoka mule shimoni lakini napo hakukuwa na majibu. Sasa kuna nini mule ndani? Ama kuna njia? La hasha! Kama kungalikuwa na njia basi Tititat angelizama na farasiwe.



Karim aliendelea kutumbua macho hapo kwa imani ya mshumaa iliyokuwa inateketea kadiri na muda. Kwa namna yake aliamini pale, shimoni, kutakuwa na jambo mujarabu analotakiwa kulifahamu hivyo hakumwondoa bundi wake hapo wakati yeye akiendelea kutatua mawazo.



Giza lilimkuta bado akiendelea kuwazua. Na likakua na kukua mpaka pale wakala wake alipofika kumfikishia ujumbe toka kwa Sultan Mansoor. Wakala wake huyo alikuwa amechoka kwa safari yake ndefu. Uso wake ulikuwa umepooza na macho yake yalikuwa yamelegea kudai usingizi.



Karim alimpokea mtumishi wake huyo akamwagizia kahawa nzito. Wakati mtumishi huyo anakunywa, basi akapata kumpasha mkuu wake ya Sultan.



“Amesema anamhitaji bundi apate kumwendesha yeye atakavyo!”



Karim alishtushwa na hiyo kauli. Alikunja sura yake akiuliza:



“Umemwambia ya kwamba hataweza kumwongoza?”



“Oooh mkuu wangu,” Wakala akanasibu.



“Nimepata kumwambia lakini hakutaka kusikia abadani. Sultan anautaka mkufu kwa uchu mkubwa mno.” Sultan alisonya akikuna kidevu chake.



Alitafakari kwa muda kidogo kisha akapaza sauti yake kuita watumishi wake wawili ambao walikuja upesi. Mmoja alikuwa mwembamba na mrefu kumpita mwenzake. Mwingine alikuwa mfupi na mnene kumshinda mwenzake. Wote walikuwa wamefunga vichwa vyao na viremba vikubwa nadhifu.



“Nimewaita hapa kuna mahala nataka niwaagize,” alisema Karim. Masikio na macho ya watumishi wake yote yalikuwa kwake.



Karim aliwaelekeza watumishi wake, wale wawili aliowaita, jografia ya eneo lile alilopata kuliona kwa kupitia macho ya bundi. Aliwataka waende huko wakapeleleze ni nini kilichomo mule ndani na haraka warejeshe taarifa kwake. Aliwataka wajiandae kwa usiku huo kwa ajili ya kufanya zoezi hilo siku inayofuata.

Baada ya maelezo hayo bwana Karim aliwataka watumishi wake waende kupumzika. Alibakia sebuleni yeye mwenyewe akiendelea kuwaza na sasa akimtafakari Sultan Mansoor. Hakujua afanye nini kumkabili kiongozi huyo. Ni wazi ilikuwa ngumu sana kwake kumtoa ndege wake, lakini sasa Sultan ataelewa?



Aliamua kwenda kujipumzisha akitegemea kufunga safari ya kwenda kwenye kasri ya Sultan Mansoor jua litakapochomoza. Ingawa bado hakuwa na jibu kamili kama atamtoa ndege wake au la!

.

.

.

.

. *** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

.

*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.



Jua lilichomoza taratibu likamkuta Rhoda kazini kwake. Alikuwa anarandaranda huku na kule kuhakikisha kila kitu kipo mahala pake. Alipoona kila jambo li’ barabara, akaketi sasa na kuanza kukokotoa mahesabu ya mahitaji yake ya siku.



Mgahawa wake ulikuwa mkubwa na wenye mvuto. Kila mtu ndani ya Goshen aliona fahari kuja kula hapo. Hata wageni nao pia walijituliza hapo kujaza matumbo na kupumzisha miili yao. Ingawa mgahawa huo ulidumu kwa muda mfupi, habari yake ilikuwa imesambaa kwenye himaya nzima ya Goshen. Hakuna mahala pa chakula paliposogelea eneo hilo.



Heshima aliyokuwa anaitaka Rhoda sasa ilikuwa imeanza kujengeka mbele za watu. Mafanikio yake hayakuwa ya kubeza hata kidogo. Alikuwa anajituma akiamka kabla ya jua, na akilala baada ya jua. Akili yake ilikuwa imetuama kwenye biashara yake. Kila kitu alikitunza na kukirejelea daftarini.



Akiwa anapitisha macho yake kwenye daftari lake kwa macho makini, mkono wa kuume ulimgusa begani. Aligeuka akiwa amefura. Hakutaka mtu yeyote amsumbue pindi anapofanya kazi yake ya ukokotozi, wafanyakazi wake wote hulitambua hili. Kabla hajafungua mdomo wake kurusha maneno makali, akakutana na uso wa Phares ukiwa unatabasamu. Uso wake ulinywea upesi na tabasamu likazaliwa.

“Karibu!”



Alifunga daftari lake upesi akisimama.



“Ahsante, habari yako?” Phares alisalimu.



“Njema tu. Vipi wewe? – mbona mapema hivi, kuna tatizo?”



“Hapana, hamna tatizo,” alijibu Phares.



Rhoda aliagiza kiti upesi, kikaletwa, ila kabla ya Phares kuketi aliuliza:



“Hapa hatutoonekana na wateja wako?”



Rhoda akamtaka mwanaume huyo waelekee upande wa pili wa mgahawa kulipokuwa kimya na tulivu. Waliketi huko na kuanza kuteta wakiwa wanakimbiza baridi na uchovu kwa kahawa iliyoletwa na kijakazi.



“Pole sana kwa ujio wangu wa kush’tukiza.”



“Wala usijali. Ila nikiri tu kwamba nina hamu sana ya kujua kilichokuleta hapa asubuhi yote hii kabla jua halijakomaa.” Phares alitabasamu akikiweka kikombe juu ya kisosi cheupe.



Uso wake uliolimwa na kutunzwa vema ulikuwa unapendeza, ukijumlisha na mavazi yake meusi ya ngozi aliyokuwa amevaa, alikuwa anakidhi vigezo kuitwa mwanaume maridadi.



“Nimekuja kukuona tu, Rhoda. Kuna ubaya?” aliuliza Phares.



“Malkia yupo?”



“Ndiyo yupo. Usijali, huamka saa tano asubuhi.”



“Kwahiyo hajui kama upo hapa?”



“Ndio.”



“Akijua huoni utan’sababishia matatizo?”



Phares alitabasamu tena. Aliona hofu ya Rhoda usoni.



“Nimesema usijali, Rhoda. Au hupendi mie nikikutembelea?”



“Napenda,” Rhoda alijibu kiunyonge.



“Karibu sana. Ila siamini kama umekuja kwa ajili tu ya kuniona. Ni bora ukaniweka wazi.”



Phares alikunywa kwanza kahawa kana kwamba yupo mwenyewe. Alishindwa kujizuia kujilamba kwa utamu wa kinywaji hicho. Aliweka kikombe chini pale alipomaliza, kisha akamtazama Rhoda aliyekuwa ana hamu kubwa ya kufahamu.



“Naweza nikapata kikombe kingine cha kahawa?” Rhoda aliagiza kahawa nyingine. Wakati wanasubiria, Phares alimtazama Rhoda machoni akamwambia:



“Kuna mambo kadhaa nataka kuyafahamu toka kwako. Naomba unipe ushirikiano kwa kunambia ukweli tupu.” Moyo wa Rhoda ukaguta, alihisi kuna jambo halipo sawa.



Kijakazi alifika na kahawa akaiweka mezani kisha akaondoka. Phares alidaka kikombe cha kahawa akakiweka kando ya karibu.



“Ningependa kufahamu familia yako, Rhoda. Baba na mama yako walikuwa wakina nani kwenye himaya hii ya Goshen?” Rhoda alishusha pumzi yake.



Alirejelea kumbukumbuni akamweleza Phares kwamba japokuwa baba yake alikuwa ni afisa mdogo tu wa serikali na mama yake akiwa mama wa nyumbani, walikuwa pia wanajihusisha na kilimo. Pesa zao kidogo walizozipata ziliwafanya wamsomeshe japokuwa kidogo.



Baadaye baba yake alikuja kufukuzwa serikalini akituhumiwa kuiba pesa. Maisha yakawa magumu mno. Baba yake hakudumu sana kabla hajafariki na kumwacha na mamaye ambaye naye hakuchukua muda, akafariki.



“Ikawaje baada ya hapo?” Aliuliza Phares. Macho yake yalikuwa kwa Rhoda wakati mdomo ukiwa kikombeni.



“Nilikuwa nabangaiza tu nikitafuta mahali pa kukaa na chakula pia.” Rhoda hakutaka kuongelea sana jambo hilo. Alishatoa historia ya baba na mama yake, aliona inatosha sasa. Phares naye aliligundua hilo, akaamua kwenda moja kwa moja kitovuni.



“Rhoda, kuna jambo lolote unalifikiria kuhusu malkia?”

Rhoda alishtushwa na hilo swali. Alijiuliza maswali kadhaa kichwani akiyaficha kwa kuuliza:



“Una maanisha nini?”



“Namaanisha kuna jambo lolote umeshawahi kufikiri kuhusu malkia?”



“Ndio nafikiria mengi tu kuhusu malkia. Kwanini nisimfikirie?” Phares akatabasamu tabasamu la bezo.



“Unajua nini namaanisha, Rhoda. Ila sawa kwasababu hautaki kusema siwezi nikakulazimisha. Lakini nilikuwa naona kuna haja ya wewe kunijuza hilo jambo. Huwezi jua …” Rhoda alikuwa kama amepigwa butwaa. Phares alimaliza kunywa kahawa yake akasimama akitabasamu.



“Ahsante sana kwa kahawa. Nimefurahi sana kukuona na nadhani haitakuwa mara yangu ya mwisho kuonana nawe.” Alitoka ndani akaondoka akimwacha Rhoda ametambaliwa na bumbuwazi usoni.



Rhoda alipohakikisha mwanaume huyo katokomea, alirejea kwenye kiti chake akitafakari na kutafakari. Ni nini kile Phares ameongea? Kitu gani anahisi juu yake? Alikosa amani. Alianza kughani mawazo mabaya juu ya mwanaume yule, anaweza akawa mlozi?



Hakugusa kabisa daftari lake la ukokotozi. Na hakuonekana kama ana dalili ya kufanya hivyo karibuni.

.

.

.

.

.

. *** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

. *** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

. “Ulikuwa wapi?” Aliuliza malkia Vedas. Macho yake makali yalikuwa yanamtazama Phares aliyekua hana mchecheto. “Nilikuwa nimetoka kunyoosha miguu,” alisema Phares. Alijitupia kitandani akajichanua.



Malkia alimtazama mwanaume huyo kwa uso wenye mashaka. Alimjongelea kitandani akaketi.

Alikuwa amevalia gauni la kulalia na mkufu wake ukiwa unaning’inia shingoni.



“Unajua nimekutafuta sana Phares. Umeanza lini tabia ya kuondoka humu pasipo kuniaga?”



“Niliona nitakusumbua, ulikuwa umelala.”



“Ungeniamsha tu, ukanambia. Umeonana na nani huko?”



Phares akasita kujibu. Alitazama dirishani akasema:



“Nimeonana na watu wengi tu.”



“Kama nani? – Nimeuliza kama nani, Phares? Rhoda?”



“Rhoda? Hapana!” Kabla mzozo huo haujakua zaidi, hodi ilibishwa mlangoni. Phares aliuendea mlango akafungua na kumkuta mwanajeshi hapo.



“Kuna taarifa nataka kumfikishia malkia,”

alisema mwanajeshi huyo.



“Unaweza ukaifikisha kwangu,” alisema Phares na kuuliza: “taarifa gani?”



“Ni kuhusu kule mpakani.”



“Kuna nini?”



“Kuna mambo ya ajabu kila usiku. Vishindo vya watu vinavuma …”



“Na kisha hamuoni watu,” Phares akadakia.



“Hilo mlishalisema, kuna lingine jipya?”



“Ndio, lipo. Leo tumegundua nyayo za watu mita kadhaa toka ulipo mpaka wetu. Ni nyayo za watu wengi mno waliokatiza jana maana juzi hazikuwapo.”



“Mliwaona hao watu wakikatiza?”



“Hapana. Tulikuwa macho usiku mzima, hatukuona yeyote.” Phares akashusha pumzi nyepesi. Alimshukuru mwanajeshi kwa taarifa na kisha akamtaka aende.



Alimrudia malkia Vedas kitandani akamwambia taarifa kinyume.



“Kuna nini?” Vedas aliwahi kuuliza kwa pupa. Phares alitabasamu kana kwamba hamna tatizo. Alimshika malkia kiuno akamtazama machoni.



“Ameleta ripoti ya ulinzi wao mpakani, hakuna cha ziada.”



“Kweli?”



“Hakika, hauniamini?”



“Nakuamini,” akasema malkia kwa sauti ya chini.

.

.

.

.

.

*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.

.

.

Wakati giza linaanza kuingia kwenye uso wa dunia, kwa upande wa himaya ya Devonship, ndo’ lilikuwa linakoza zaidi.



Ndani ya kasri kubwa ya kutisha ya mtawala Jayit, kwenye chemba moja ndogo upande wa kushoto, kulikuwa kuna kikao cha dharura kilichomjumuisha Jayit na wazee wawili.



Wazee hao walikuwa wamevalia majoho meusi na vitambaa vyekundu kichwani. Jayit alikuwa kifua wazi akivalia kataulo kadogo chekundu pamoja na viatu vya wazi vyenye vichwa vya kenge.



Nje ya kasri hiyo kulikuwa kuna kundi la wanaume wapatao hamsini kwa mahesabu ya harakaharaka wakiwa wanazungukazunguka huku na kule kuhakikisha usalama wa eneo hilo. Mikononi walikuwa wamebebelea dhana kadha wa kadha mathalani: mikuki, jambia na mishale.



Jayit alikohoa kusafisha koo. Alikuna kifua chake kilichokuwa kinamimina jasho kutokana na hali joto iliyokuwa imeshamiri chembani kisha akasema:



“Ni muda sasa sijapata kumuona kwenye rada zangu. Hayupo hata kwenye uso wa dunia. Nachelea kusema atakuwa hana uhai.”



Kukawa kimya kidogo. Ni moshi tu uliokuwa unatoka kibuyuni ndio ukakamata anga.



“Ni mpambanaji wangu mahiri sana. Nawaza ni mtu wa uwezo gani aliyepata kumuua … lakini yapasa maisha yaende mbele, ndio maana nikawaita hapa ili mnipe mawazo ni nani anayestahili kukaimu nafasi ya Tititat.”



Zoezi hilo lilianza kwa kupendekeza kwanza majina, kisha uchambuzi wa nguvu na mapungufu ya kila mmoja. Mwishowe jina la Raiden, mwanaume mrefu hodari mwenye uso mithili ya faru, akapitishwa.



“Baadae itabidi aapishwe na kutawazwa,” alisema Jayit.



“Hatuna muda wa kupoteza, kazi ya kuivamia Goshen yatungoja.” Wazee wale wawili wakatazamana.



“Kuna shida?” aliuliza Jayit.



“Ndiyo ipo,” akajibu mzee mmoja. “Huoni kama itakuwa mapema sana kuivamia Goshen kwa sasa?”



“Mapema?”



“Ndio, mkuu. Mimi nadhani tungeendelea na himaya zingine dhaifu na ndogo kwa ajili ya kumkomaza Raiden ambaye bado ni mchanga kwenye uongozi kwasababu hajapata muda wa kufuliwa zaidi. Baada ya hapo ndipo turejee Goshen.”



“Naunga mkono hoja,” akasema mzee wa pili.



“Goshen wamejiandaa kwa ujio wetu, itamuwia vigumu Raiden kupambana ilhali ni mpya kitini. Tumpe muda zaidi.”



“Muda?” Jayit aling’aka. “Sisi ndiyo wafalme wa usiku, hakuna yeyote anayeweza kutuzuia punde jua linapozama, ya nini tuhofie?” Macho yalimtoka.



Uso wake ulikakamaa. “Hata kama tukimpa uongozi mtoto mdogo, anaweza kufanya hiyo kazi pasipo na shaka lolote. Unapofika usiku, hakuna kiumbe chochote cha kutuzuia. Dunia hii yote inakuwa mali yetu.”



Akahitimisha: “Usiku wa kesho wa Goshen, ndio utakuwa muda wetu wa kuvamia, kubeba tunavyovitaka na kutoa sadaka inayotupendeza. Kaendeleeni na kazi zenu!”



Siku na jua lake liliangaza. Karim aliamka mapema sana siku hii akajiandaa kwa kutafuta nguo zake nadhifu na kumfungulia farasi wake mpendwa, mkubwa na mwekundu.



Lakini pia akawataka vijakazi wake wawili wapate nao kujiandaa kwa ajili ya safari. Safari hii ilikuwa ni ndefu, ya kwenda kwa Sultan, hivyo basi akapakia maji na hata chakula vya kutoshea njiani.



Walitembea kwa masaa kede huko njiani wakipumzika na kulowanisha tena makoo yao makavu, na kujaza matumbo yao kisha safari ikadumu. Hawakukoma mpaka pale walipotia timu kwenye hekalu la Sultani Mansoor. Hapo walipekuliwa na walinzi kisha wakaruhusiwa kuzama.



Sultan hakuwepo mazingira ya nyumbani kwa muda huo, alikuwa ametoka kwenda ziwani – mahali ambapo hupenda sana kwenda kupumzisha akili yake pindi anapokuwa amechoka. Akiwa huko hupenda kuvua viatu vyake kuacha miguu yake mipana ibarizi na kuchezea maji baridi ya ziwa.



Vijakazi ndani ya hekalu la Sultan walimhudumia Karim pamoja na vijakazi wake. Mganga huyo maarufu akadumu kwa lisaa limoja mbele kabla ya Sultan na mke wake mkubwa kuwasili makaoni mwao, sehemu maridadi inayomeremeta kwa usafi na samani ghali. Karim na vijakaziwe walisimama kumlaki kiongozi huyo. Baada ya kusalimiana na kuketi, hakuna lililokawia zaidi ya maongezi kiini.



Japokuwa mke wa Sultan alikuwa amejitenga, macho na masikio yake yalikuwa pamoja na maongezi hayo. “Ndege yupo wapi?” Aliuliza Sultan akijaribu kuangaza. Karim alishusha pumzi akanyoosha mkono wake.

“Sijaja naye, Sultan. Nimekuja kwanza kuteta nawe.” Uso wa Sultan ulibadilika kwenda kwenye shari. Hakungoja Karim aendelee kusema, akamkatiza.



“Sitaki maneno tena Karim, nimeshayasikia vya kutosha. Nilidhani kijakazi wako amekufikishia vema ujumbe wangu, ila naona kumbe hukuupata.”



“Niliupata, Sultan.”



“Sasa kipi hakijaeleweka?”



“Nimeelewa kila jambo, Sultan. Lakini nasikitika kusema hilo jambo halitawezekana. Huyo ndege …” Sultan alipiga makofi mara mbili, mara wakajiri wanaume watatu waliobebelea majambia marefu yanayometa.



Walikuwa wamevalia kanzu rangi ya krimu na kofia nyekundu, balaghasia. Nyuso zao zilikuwa kazi. Walimtazama Sultan, Sultan akawaelekezea kwa Karim na vijakaziwe.



“Sultan! Mbona …” Karim alinyanyuliwa mkebe mkebe. Alimuomba Sultan aachiwe kwani amesilimu. Walinzi wakamuacha akaketi chini. Alimtazama kijakazi wake mmoja na kumpatia ishara, kijakazi akasimama na kwenda nje. Wakati akimngojea arejee, alitazamana na mke mkubwa wa Sultan, ndugu yake. Hawakusema jambo.



Kijakazi alirejea akiwa amebebelea mkoba wa ngozi, akampatia Karim. Karim alitazama ndani ya mkoba huo kabla hajaanza kutoa kitu kimoja baada ya kimoja. Mayai matatu makubwa yenye rangi nyeupe ya kufifia, manyoya kadhaa, vibuyu viwili virefu rangi nyeusi pamoja na kioo saizi ya kati.



Alipotoa hayo aliingiza tena mkono wake ndani ya mkoba ila mara hii hakutoka na kitu. “Ni hivi hapa Sultan,” alisema Karim akikabidhi mkoba, juuye ukiwa umebebelea vitu vile alivyovitoa. Sultan alivipokea na kuomba kusaidiwa namna ya kumwamuru na kumuongoza ndege tumishi, Karim akafanya hilo zoezi.

Lakini kuna kitu bado alikuwa nacho mkononi, amekificha katika namna ya kutoonekana. Aliuweka mkono wake huo nyuma nyuma, akarudi kuketi wakati Sultan akiendelea kufaidi maono yake kupitia macho ya bundi. Alipomtazama mke mkubwa wa Sultan alimuona anamtazama. Na macho yake ni dhahiri shayiri yalikuwa naye kwa muda mrefu. Akapata shaka.



Kwa muda wote alitulia. Sultan alipomaliza kutazama kioo, akiwa amefurahi, akampongeza sana Karim kwa kazi yake na kumtaka akae zaidi hekaluni kwani amemtendea mema.



“Nashukuru sana, Sultan,” alisema Karim. “Nimefurahishwa pia lakini nasikitika kusema sitaweza kukaa hapa zaidi ya kesho, kule nyumbani kuna kazi lukuki za kufanya.”



“Kwani huna vijakazi wa kutosha?” aliuliza Sultan. “Sema kama hawakidhi nikuongezee."

“Hapana, wanatosha,” akadakia Karim. “Kuna baadhi ya kazi hakuna mtu anaweza fanya isipokuwa mimi binafsi.”



Walipiga domo hapo kwa muda wa lisaa, Sultan akaaga anaenda kupumzika yeye pamoja na mkewe. Karim na vijakaziwe waliachwa hapo sebuleni, lakini vijakazi wakijaa tayari kuwahudumia.



Baadaye majira ya jioni, Karim alikuwa ameketi peke yake kwenye uwanja wa hekalu. Alikuwa anawaza juu ya mambo kadhaa. Baada ya muda aliupeleka mkono wake ndani ya mfuko wa kanzu aliyoivaa, akatoa kidude fulani mithili ya kijiti kidogo cheusi kifupi chenye michoro kadhaa maridadi.



Alikitazama kidude hicho akatabasamu. “Nilikuona,” sauti ya kike iliita pembeni yake, akashtuka na kuficha kitu hicho. Alitazama sauti ilipotokea, akamkuta mke mkubwa wa Sultan. Akashusha pumzi.



“Kumbe wewe!” Mke wa Sultan alitabasamu. Alikuwa yu mwenyewe. Aliketi pembeni ya Karim.



“Ni kitu gani kile ulificha?” Aliuliza. Karim alitazama kando na kando, akajibu:

“Sijaficha kitu.” Mke wa Sultan akatabasamu.



“Sawa, nitaenda kujadiliana na Sultan kama wewe hautaki.” Karim akatahamaki.



“Tafadhali usifanye hivyo, ni kitu cha siri sana.”



“Kitu gani hicho?” Karim akameza mate kwanza. “Najua wewe ni damu yangu, huwezi ukanisaliti.” Mke wa Sultan akatikisa kichwa.

.

.

.

.

.

.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

.

*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***

.

.

.

.

.







ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog