Search This Blog

MKE WANGU NUSU JINI, NUSU MTU - 1

 




IMEANDIKWA NA : ALLY MBETU



*********************************************************************************



Simulizi : Mke Wangu Nusu Jini, Nusu Mtu 
Sehemu Ya Kwanza (1)


 Niliwahi kujiuliza kama iko siku na mimi nitapata nafasi ya kusimulia popote pale mkasa uliowahi kunikumba miaka ya nyuma. Ni kuhusu mke wangu niliyefunga naye ndoa ya serikali. Nilibaini kwamba alikuwa mtu lakini pia alikuwa jini kwa sababu mbalimbali, anasema Abigaeli, mkazi wa Kibaha, Mkoa wa Pwani.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Anaendelea: Siku ya kwanza kukutana na mke wangu ilikuwa kwenye kikao cha kupokea mahari ya mtoto wa kaka yangu aliyekuwa anataka kuolewa na Msambaa mmoja kutoka Lushoto, Tanga. Ilikuwa mwaka 2002.



Kuna kitu kilitokea kwenye kikao hicho na kama ningekuwa makini, nisingeingia kwenye matatizo makubwa yaliyowahi kunipata katika maisha yangu.



MSICHANA MREMBO ANAOMBA NAMBA

Kitu hicho ni kwamba, baada ya kikao, msichana mrembo ambaye alikuja kuwa mke wangu alinifuata na kuniomba namba zangu za simu, nikamtajia, akaziingiza kwenye simu yake.

Alipoondoka, baadhi ya ndugu tuliokuwa pale tuliulizana yule msichana ni nani. Hakuna aliyekuwa na jibu. Bahati nzuri ndugu mmoja wa upande wa wanaume waliyoleta mahari alikuwa hajaondoka, tukamuuliza kama walikuja na msichana yule, akakataa kutomtambua tena huku akisisitiza kwamba, walikuja kumi tu na yeye ndiye alibaki kumalizia mambo mengine.



Kaka aliniuliza aliponifuata kuniomba namba ya simu alisema anatokea upande gani katika tukio lile, nikamwambia kwa waleta mahari.

Nilianza kuingiwa na wasiwasi mkubwa, niliwaza mengi. Kaka alinilaumu akiniambia kwamba siku nyingine nisikubali mawasiliano na watu ambao hawajulikani sawasawa. Lakini nilijitetea kwa kusema mtu kusema kaja na watu wengine ambao kweli walikuwepo sidhani kama unaweza kumtilia shaka.



WIKI MOJA MBELE

Wiki moja baada ya tukio hilo la kuombwa namba, nilipigiwa simu na mtu aliyedai kuwa yeye ndiye yule msichana, akasema anaitwa Munil.



Alisema amenipigia simu ili kunijulisha kwamba, yule mchumba aliyekuja kutoa mahari kwa kaka amefariki dunia kwa ajali mbaya ya gari iliyotokea nusu saa iliyopita.

Nilishtuka sana kusikia taarifa hizo kwani zilikuwa za ghafla sana kwangu. Lakini jambo jingine sasa, niliamini yule msichana ni ndugu na wale walioleta mahari ila pengine yule mtu wa mwisho hakumjua tu.



Nilimshukuru kwa taarifa kisha akakata simu. Nikampigia kaka kumuuliza kama analijua hilo, naye alishtuka, akasema hajasikia, akaomba nimpe dakika tano tu ahakikishe kwa ndugu wengine halafu atanirudia. Lakini kaka hakuniuliza nilikozitoa habari zile.



Baada ya dakika tano kweli kaka alinipigia, akasema hakuna ndugu hata mmoja aliyesema kama ni tukio la kweli. Akasema amepiga simu ya mhusika mwenyewe anayedaiwa kupata ajali, haipo hewani.



MSICHANA AMTATIZA KAKA

Niliendelea na shughuli zangu, nusu saa mbele kaka akanipigia tena na kuniuliza zile habari aliniambia nani, maana hata huyo binti wa kaka aliyekuwa anataka kuolewa, alipopigiwa simu alisema hajui na inaweza kuwa habari za uongo ingawa na yeye alipompigia simu huyo mchumba wake hakumpata.



Nilipata wakati mgumu sana kumwambia kaka kwamba aliyenijulisha ni yule msichana kwani alishanionya kutofanya mawasiliano na watu nisiowajua. Lakini ningemtaja nani sasa.

Ilibidi nimwambie ukweli, kaka akashtuka. Akasema:



Hivi huyo msichana ni wa kivipi kwanza? Yaani taarifa apate yeye, wengine wasijue? Au kamgonga yeye?

Mimi sijui kaka, lakini yeye ndiye kanipigia simu, nilimjibu.

Mara, kaka akasema anapokea simu nyingine inaingia kwake atanipigia.

Zilipita dakika kumi nzima, kaka akapiga na kuniambia habari za mchumba wa binti yetu kufa katika ajali ya gari ni za kweli na maiti ipo katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha.



MAUZAUZA KWA MBALI

Nilishtuka sana, nikamuuliza kama anakwenda hospitalini, akasema anakwenda ukweni kwake ambako kutakuwa na kikao kifupi na mimi nikaondoka kwenda huko kwenye kikao. Nikiwa pale, nilitarajia sana kumwona yule msichana lakini kila nilipoangaza macho sikumwona, nikaamua kumpigia simu, akapokea ndani ya sekunde mbili tu baada ya kuita, akasema:

Nakuona hapo.



Niligeuka kulia, kushoto, mbele, nyuma lakini sikumwona. Nikamuuliza uko kwa wapi kwani, akasema yupo kwa ndani kisha akakata simu. Sasa nikajiuliza, kama yupo kwa ndani ananionaje? Nikampigia tena, akapokea haraka sana kama mwanzo, nikamuuliza:

Kama kweli umeniona nimevaaje? Mimi nahisi hujaniona ila unabashiri tu.

Si wewe umesimama, umevaa shati jeusi na suruali nyeupe.

Nikakata simu kwani ni kweli nilikuwa nimevaa nguo hizo. Safari hii nilipokata akanipigia yeye, nikapokea huku nikisema moyoni huyu mwanamke ni jini nini? Mbona kama simwelewielewi?

"Haloo," aliita.

"Haloo," nilisema.



"Mbona una wasiwasi na mimi. Mimi si jini bwana, ni binadamu mzuri tu," kisha akakata simu.

Kwangu ulikuwa mtihani mkubwa. Kwa nini aseme yeye si jini wakati mimi nilikuwa nawaza hivyo?

"Hapana, wala sina wasiwasi na wewe. Ila nashangaa unasema unaniona mimi sikuoni halafu unasema unaniona ukiwa kwa ndani. Sasa unanionaje?



"Nilikuwa nakuona kwenye dirisha lakini sasa nakuona sawasawa maana nimetoka nje.

Niliangalia mlangoni nikamwona kweli akiwa anawaka kwa uzuri wake, mweupe pee! Kama Mwarabu. Alionekana kuwa tofauti na wengine pale.







Wakati yote hayo yanatendeka, watu walikuwa wakilia sana. Hata mimi niliweza kuongea na simu kwa sababu nilisimama mbali kidogo na watu walikuwa wakiendelea kumiminika eneo hilo la msiba, hasa wanawake.

"Nimekuona sasa Munil. Da! Umependeza sana leo," nilimwambia.

"Kweli ee?"



"Kweli kabisa. Da! Yaani, una mvuto we mtoto wa kisasa," sasa nilikuwa katika hali ya kimahaba maana hata sauti yangu iliashiria hivyo. Na yeye alionekana kupenda kuendelea kuzungumza na mimi huku sauti yake tamu ikirindima masikioni mwangu.



Kikao kilikuwa kikiendelea, mimi nikaenda kusimama mbali zaidi huku nikiendelea kuongea na Munil ambaye sasa naye alizidisha maneno ya mahaba kwangu. Lakini ghafla nilijikuta namuuliza swali nje ya mazungumzo yetu:

"Hivi Munil, huyo kijana aliyefariki dunia kwa ajali wewe ni nani yake?"

"Mtoto wa shangazi," Munil alinijibu kwa haraka sana kuonesha kwamba hakuwa na wasiwasi na alichokisema, nikaamini lakini kichwani yakaja mawazo mawili tofauti, kama kweli ni mtoto wa shangazi yake mbona amevaa vizuri sana yeye halafu ni kwa nini siku ya kutoa mahari, ndugu mmoja alisema hamjui?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Umenielewa Abigaeli?"



Nilishtuka sana kujua kwamba Munil analijua hadi jina langu kwani katika mazungumzo yetu sijawahi kumwambia ila la kwake alinitajia mwenyewe.

"Kumbe unalijua jina langu?"

"Si nililisikia siku ile ya kutoa mahari."



"Ooo! Sawa," nilisema kwa kujibalaguza tu lakini kila nilipofikiria moyoni sikukumbuka kama siku ile kuna mahali jina langu lilitajwa kwa namna yoyote ile.

Oke, basi baadaye," alisema Munil na kukata simu.

Wakati naongea nilikuwa naangalia upande wa barabara watu wanapotokea, kwa hiyo msiba niliupa mgongo.



Nilipogeuka kuangalia kama nitamwona Munil, sikumwona nikajua alirudi ndani.

Nilitembea kurudi msibani lakini mawazo yangu yote yalikuwa kwa Munil.

"Mtoto mzuri sana tena sana. Ameumbika kwelikweli. Sijui ana jamaa yake? Anafaa kupigwa ndoa," nilisema moyoni mwenyewe huku nikiwa nakaa.

Ile namalizia kukaa tu, meseji ikaingia kwenye simu yangu, moyoni nikasema siyo Munil huyo?

"Abigaeli nakupenda sana, naamini kuwa na wewe ni furaha ya maisha yangu."

Wakati nasoma meseji hiyo mwili ulikuwa ukinisisimka na kuhamishia mawazo yangu kutoka pale hadi kitandani. Nikamjibu haraka sana:

"Mimi ndiyo naamini nitakuwa na furaha zaidi yako kwani nimetokea kukupenda sana Munil. Tutafute muda tuongee basi, sawa mpenzi?"



"Sawa sweetheart wangu, utaniambia basi," alinijibu kwa maneno ya mahaba nikazidi kuchanganyikiwa. Nilitamani kuaga palepale ili niondoke nikakae mahali halafu nimwite Munil aje tuzungumze kwa kupanga mambo yetu, hasa kuhusu mustakabali wake na wangu, namaanisha ndoa!



NALISHANGAA HILI NALO



Nikiwa nimetulia nikaamua kuisevu namba ya Munil kwani sikuwa nimeisevu, cha ajabu nilipokwenda kwenye eneo la kusevu nikaambia tayari jina hilo lipo mwenye simu yangu, nikafuatilia na kubaini jina la Munil One!

"Mh!" niliguna kwanza. Nilikataa kichwani kwamba sijawahi kusevu namba ya Munil kwenye simu yangu, nilikuwa nimeishika namba yake kichwani. Nikawaza.

"Munil One Munil One? hapana, sijasevu namba kama hii kwenye simu yangu," niliendelea kuwaza na kujiridhisha kwamba hakuna kitu kama hicho.



"Kuna kitu kinaendelea kwa Munil," nilisema mwenyewe moyoni.

Kama ndiye aliyenitoa kwenye mawazo, akaniambia tuondoke kwa muda tutarudi baadaye. Nilitamani kumwambia atangulie nitamfuata baadaye maana nilitaka kukutana na Munil kwanza ili tumalize mambo yetu.



Hata hivyo, nilishindwa kutumia ujanja wowote, tukaondoka na kaka huku njiani akisema sisi ni wakwe pale kwa hiyo si lazima tujishirikishe sana lakini baadaye tungerudi tena.

Mbele kwa mbele nilikwenda kuachana na kaka, mimi nikakatiza mitaa na kutokea kwenye Baa ya Kontena



ambako nilikaa kwenye kona na kumtumia meseji Munil ili kama anaweza aje pale. Meseji niliiandika hivi:

"Mpenzi, kama unaweza njoo hapa kwenye Baa ya Kontena."

Nilishtuka sana meseji ilipomfikia kwangu ikaandika Munil Only!! Badala ya Munil One!



"Ha! Nooo! Kuna kitu, inawezekanaje kwanza?" nilijiuliza. Kama kuna mtu aliyeniona sura muda huo aligundua kuna jambo la kushtua limenipata.



"Nakuja mpenzi wangu," Munil alinijibu bila kuniuliza hiyo baa iko wapi! Lakini hilo halikunishangaza sana kwani kwa mji mdogo kama wa Kibaha sidhani kama ni ishu kubwa.

Ilikuwa ndani ya dakika tano tu, Munil aliingia kwenye baa hiyo akiwa amebadili nguo. Alivaa gauni nyeupe, refu hadi kufunika miguu wakati awali alivaa gauni jekundu pia refu!







Alikuja moja kwa moja nilipokaa mimi kwenye meza ya peke yangu, akanibusu kwanza kisha akavuta kiti na kukaa huku akiniangalia kwa uso uliojaa tabasamu laini. Kwa mara ya kwanza mimi na Munil tulikaa pamoja hapo kwenye baa.

Nilianza kuhisi ni mwanamke wa tofauti sana kwani walio wengi hawapendi kukaa baa, hasa kwa mwonekano wake wa kiimani. Hakuwahi kuniambia wa imani gani lakini jina lake, Munil lilitosheleza kunijulisha yeye ni nani.Kwa hiyo kuja kwake baa niliamini kulitokana na upendo wake kwangu ambao ulitimilika. Nilifurahi sana maana hata wakati anakaa hakutoa kauli ya kuashiria kwamba hapendi kukaa baa.



SWALI LA KWANZA KWA MUNIL



"Munil sikumbuki kama nimewahi kuisevu namba yako, lakini ghafla kwenye simu yangu imeonekana kuseviwa kwa jina la Munil One halafu sasa Munil Only, ni nini kimetokea mama?"

Wakati namuuliza hivyo Munil nilimkazia macho nikiamini ataogopa kama anajua mchezo lakini wala!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Aliniangalia kawaida na nilipomaliza akaachia tabasamu lakini huku akisema:

"Jamani, mimi ndiyo nikuulize wewe mwenye simu lakini wewe ndiyo unaniuliza mimi. Mimi mwenyewe mfano simu yangu, namba unaweza kuisevu kabisa lakini ukinipigia badala ya kutokea jina zinaonekana namba tu. Kuhusu kusevu inawezekana ulinisevu ila umepitiwa na kumbukumbu, mbona hilo ni suala la kawaida sana baba."



Munil alivyoniita baba, nilifurahi sana. Nilijiona mimi ndiyo mimi hakuna mwingine duniani. Munil alikuwa msichana mzuri sijapata kuona tangu nimezaliwa. Hata alipoingia pale baa alitazamwa na kila mtu.



Kuhusu alilolisema la simu, nilikumbuka tatizo lake hata kaka analo kwenye simu yake, anasevu jina lakini zinatokea namba kwa hiyo kaka kila akipigiwa simu huwa na kazi ya kumuuliza mpigaji, nani mwenzangu? Nikaamini kuwa huenda ni matatizo ya simu yangu.



Niliyafanya mambo hayo yawe yameisha, akaagiza soda kama nilivyofanya mimi. Lakini pia akataka na sambusa mbili kwa kumwambia mhudumu.Wakati tunakunywa huku yeye akisubiri sambusa zake, mimi nilihisi muda umekwenda na anaweza kumaliza soda yake bila kinywaji kuletwa kwa hiyo nikamuhimiza mhudumu aharakishe.



"Usijali baba, nitakwenda mimi mwenyewe," alisema Munil, mimi nikainama kuangalia meseji kwenye simu yangu, kuinua kichwa nikaona sambusa kwenye kisahani cha chai, nikashtuka."Nani kaleta?" niliuliza. Kisa cha kuuliza ni kwa sababu kuinamisha kwangu kichwa chini kusoma meseji na kuinua ilikuwa ndani ya sekunde kama kumi tu, halafu nilipoona hiyo sahani sikumwona mhudumu akiondoka kwenye meza yetu na wala sikumwona Munil akirudi kuja kukaa.



Kwa wakati ule haikuwa rahisi kusema yote, lakini baada ya kuyapitia yaliyotokea ndiyo maana nayasema haya kwani niligundua baadaye sana kwamba nilikuwa nimepatikana kwa mke wangu ambaye alikuwa nusu ni mtu, nusu ni jini kamili.



Nilipata wakati mgumu sana kuwaza kuhusu sambusa, Munil aliniambia amezifuata yeye lakini kusema ule ukweli hakuzileta yeye na wala hazikuletwa na mhudumu wa baa ile. Nilinyamaza tu lakini akili ikiendelea kuchangamka kuwaza.

"Baba," aliniita Munil baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu.

"Niambie mama."

"Utakwenda kuzika?"

"Kwani mwili unakwenda kuzikwa wapi?"

"Lushoto."

"Itabidi niende sijui? We unasemaje?"

"Twende wote."

"We utaenda?"

"Mimi tena, yaani ndugu halafu nikose?!"

"Basi na mimi nitaongozana na wewe."

"Sawasawa."



Siku hiyo baada ya kuachana na Munil nilikwenda nyumbani. Niliwaambia majirani kwamba nitasafiri kwenda Lushoto, Tanga kwa mazishi. Lakini kwa sababu ya uchovu niliamua kutokwenda msibani kulala mpaka kesho yake ambapo ningesafiri, hata kaka nilimwambia hivyo.

Ilikuwa usiku wa saa nne nikiwa kitandani, nilimkumbuka Munil kwamba hatujawasiliana kwa muda mrefu, tangu tulipoachana kule baa, nikachukuwa simu ili nimtwangie lakini kabla simu haijaita, mlango mkubwa uligongwa, nikakata simu na kuuliza.



"Nani?"

"Munil."

Nilishtuka, nikaguna kwanza na kujiuliza mwenyewe:

"Amepajuaje hapa au hanitafuti mimi."

"Nakuja," nilisema kwa sauti nikitoka kitandani.



Nilifungua mlango, nikakutana na macho ya Munil. Safari hii alikuwa mzuri zaidi ya wakati wowote ule. Alizidi kuwa mweupe pee! Aliwaka mtoto kama Mwarabu vile. Akaachia tabasamu.



"Karibu Munil."

"Asante," alisema akiingia ndani.

"Umepajuaje hapa Munil?"

"Nimeulizia."

"Umeniuliziaje? Maana sijawahi kukwambia naitwa nani."

"Si unaitwa Abigael jamani au?"

"Ndiyo lakini lini nilikwambia hilo jina langu Munil?"

"Na wewe bwana, hebu tuyaache hayo."



Niliamua kuyaacha kweli kama alivyotaka Munil, nikamkaribisha chumbani huku nikimuuliza:

"Msibani umeaga unakwenda wapi?"





"Nimesema nakwenda kwangu."

"Kwani we hukai pale?"

"Hapana."

"Unakaa wapi?"

"Si hapo nyuma tu."

"Hapo nyuma tu? Kwenye nyumba ya nani?"

"Nyumba ya mzee Ngurumo."

"Mzee Ngurumo! Kwani pale pana wapangaji?"

"Si ndiyo mimi sasa."

"Mh! Nilijikuta nikiguna tena maana nyumba aliyoitaja kweli ipo. Mzee Ngurumo namjua vizuri sana lakini pale nyumbani kwake hapana mpangaji, ni familia tu na tena ana watoto wa kiume pekee!

"Mbona kama umeshangaa sana, vipi?"

"Sijashangaa sana ila nimeshangaa."

"Umeshangaa nini?"

"Si huyo mzee Ngurumo."

"Kwamba?"

"Kwamba ana wapangaji pale kwake. Nilikuwa sijui."

Munil aliniambia atalala kwangu usiku huo hadi alfajiri ya saa kumi na moja atarudi msibani. Hata asingesema hivyo yeye, mimi mwenyewe nilitaka kumwambia asiondoke ili tuandike historia ya kwanza katika uhusiano wetu.

Tuliongea mengi sana na Munil hadi kufikia kuwekana wazi kwamba nini anataka, nini hataki. Kitu kimoja kilinishangaza sana, Munil alisema katika mambo anayoyapenda maishani mwake ni mafuta mazuri, yaani pafyumu au manukato.

"Ni kwa nini?" nilimuuliza kwa kusisitiza mshangao.

"Basi tu, yaani nimejikuta nikipenda sana. Unajua baba, mama, wadogo zangu na hata ndugu wengine wote wanapenda sana mafuta mazuri.

Wakati Munil ananiambia hayo, alikuwa akinukia mafuta mazuri sana.

Sasa ulifika muda wa mimi na Munil kulala. Nilimwambia apande kitandani, akasema anapenda kulala mwanzo wa kitanda lakini kwa sababu amenipenda sana anakubaliana na mimi. Alitangulia kupanda kisha nikafuata mimi.

Ilikuwa mara yangu ya kwanza kulala na Munil na kukutana naye kimapenzi. Alinioamba tuzime taa, nilikataa lakini akasisitiza kwamba huwa anajisikia vizuri zaidi akiwa na mwanaume kwenye chumba chenye giza nene.

Ili kuzima taa ilibidi mimi nitoke kitandani kuifuata swichi, nikaweka mguu mmoja chini, kabla sijaweka wa pili, Munil akasema:

"Ngoja niende mimi."

Niliona ugumu yeye kwenda kwenye swichi maana kama ni kutoka ingebidi aniruke kwanza. Kilichotokea, nilimwona Munil akiamka kitandani lakini sikumbuki nini atap! Giza!

"Hee!" Nilishtuka, nikapapasa ubavuni kwangu ili kuona kama Munil yupo au, nikamwona amejaa tele!

"Umezimaje taa Munil?"

"Si nilikwenda."

"Siyo kweli Munil. Hujatoka kitandani."

"Ha! Sasa kama nisingetoka kitandani ningezimaje?" Munil aliniuliza akinishangaa.

Niliamua kukubaliana naye lakini kutoka moyoni nilikataa kwamba, Munil aliizima taa bila kutoka kitandani! Sasa nikawa najiuliza alifanyajefanyaje? Ina maana alipeleka mkono mpaka kwenye swichi? Haiwezekani. Nilikataa kimoyomoyo.

Basi, mimi na Munil tuliingia kwenye tukio la kihistoria ambapo kwa mara ya kwanza tulifanya mapenzi tena bila kondom na cha kushangaza sana ni kwamba, Munil nilipomwambia habari ya kondom alisema haina haja kwa sababu kama mimi nina Ukimwi siwezi kumwambukiza yeye na kwamba yeye ni mzima wa afya!

Nilishangaa sana kwa tamko lake hilo, nilianza kuhisi sipo na mwanamke wa kawaida lakini hilo pia nikalivumilia kwa namna nyingine tena.Tulipomaliza, bado kukiwa na giza, Munil alitaka kwenda chooni, akaniambia anaomba kwenda chooni, nikamwambia unapajua? Maana choo chenyewe kilikuwa ndani kabla hujatoka uani.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Aliniambia anapajua, nikashangaa. Nikamuuliza uliwahi kuingia kwenye nyumba hii, akasema ndiyo. Nikamwambia basi nenda nione. Niliamini amesema tu lakini hakijui choo kilipo.Alipotoka kitandani alivaa taulo langu lakini nilishikwa na mshtuko kusikia akitembea kwa kunyata tena kama mwanaume aliyevaa viatu vya mchuchumio, maana vilikuwa vikilia koo, koo, koo.

Alipofungua mlango nikatoka haraka sana kwenda kuwasha taa ili nione alikuja na viatu gani. Nilijua kama sitaona viatu basi nitajua alivaa viatu vya mchuchumio na ndivyo vilivyotia mlio wa koo.

Ile nawasha taa tu, nikasikia sauti ikiniuliza:

"Hivi mbona kama una wasiwasi na mimi, kuna nini kwani?"

Alikuwa Munil amelala kitandani akiniangalia kwa macho makali na yenye hasira.

"Ha! Kwani si ulisema unakwenda nje kujisaidia?" nilimuuliza nikitetemeka.

"Mimi sijatoka kitandani baby. Sasa kama ni kwenda chooni si ningekwambia unisindikize, mi napajua chooni kwenu? alisema Munil.

Nilizima taa ili nirudi kulala lakini wakati nazima kabla ya tendo hilo niliangalia chini na kubaini kwamba hakukuwa na viatu vyovyote. Nilitupia macho kiaina miguuni kwa Munil pale kitandani lakini sikuona kitu kwani miguu yote ilikuwa ndani ya shuka.

Nilirudi kulala, ile namalizia tu kujifunika shuka, mlango ukasukumwa, akaingia mtu. Nilijua ni mwizi sasa, nikauliza:

"Wewe ni nani unayeingia?"

"Jamani baby, kwani si nilikwambia nakwenda chooni, mbona unachanganyikiwa lakini?"





Kabla sijamjibu nilipeleka mkono pembeni yangu kuona kama Munil alikuwepo, lakini hapakuwa na mtu!

?Munil,? niliita huku nikitoka kitandani na kusimama katikati ya chumba nikiwa nahema kwa kasi, woga ulinishika, miguu ilitetemeka kama mtu aliyekutana na kiumbe wa ajabu kwenye njia iliyosonga akiwa peke yake.

?Abee,? aliitika Munil aliyeingia.

?Kwa nini unanifanyia mambo haya??

?Yapi dear?? Munil aliniuliza huku akifunga mlango na kuzima taa.

?Inakuwaje nikuone kitandani halafu pia wakati huohuo nikuone unaingia, halafu kitandani haupo??



nilisema kwa sauti ya juu. Nadhani hata nje walisikia kama kulikuwa na watu.

?Baby hilo ndilo tatizo lako. Yaani wewe umenifanya mimi ni jini siyo? Niwe kitandani halafu niwe nimetoka nje, inawezekanaje?? alihoji Munil akiwa amewasha taa sasa. Alisimama mlangoni akiniangalia kwa macho yaliyojaa mshangao.

?Baby, kwani una nini?? aliniuliza.



Nilimsimulia hali ilivyokuwa, akasema itakuwa nina mawazo mengi juu yake ndiyo maana namuwewesekea mpaka namwona mara mbilimbili.

Basi, nilijipa moyo, nikamshika mkono Munil na kumpandisha kitandani kisha na mimi nikapanda. Niliamua mara hii tulale na mwanga hivyo sikuzima taa.Sikuchukuwa muda mrefu sana nilipitiwa na



usingizi na kuota ndoto. Niliota niko kwenye jumba moja kubwa sana la kifahari. Ukuta wote ulipambwa kwa dhahabu, juu badala ya kuezekwa mabati, kulipigwa madini ya shaba. Ilikuwa sehemu ya peke yake.



Eti humo nilikwenda kuulizwa ukweni kama nitamuoa binti yao au la! Binti mwenyewe alikuwa amenipeleka kwa wazazi wake nikaulizwe vile alisimama katikati ya sebule kubwa akiniangalia kwa macho mazuri huku akiachia tabasamu laini. Alikuwa binti mzuri kwa namna yoyote ile, sura hadi



umbo lakini alionekana si mtu mweusi, kama Mwarabu au Mzungu aliyechanganya damu.

Wazazi wake waliniangalia kwa macho ya kunikubali huku baba mtu akiniambia kama nitakubali kumuoa binti yao atanipa sehemu ya mali yake ili kuendeshea maisha na binti yao lakini kama



sitakuwa tayari kwa ndoa, yule baba aliniambia angenichinja kwa sime akitumia mkono wake.

Wakati anasema kama siko tayari kumuoa binti yake atanichinja kwa sime, alitoa mfano, akaenda kwenye kona ya sebule, alitumbukiza mkono mahali na kutoa sime, akanifuata na kuniwekea shingoni, wakati anaanza kuchinja nikashtuka kutoka usingizini huku nahema sana na jasho jembamba likinishuka mwilini.



?Vipi baby?? aliniuliza Munil baada ya kuamka kwangu huku nikihema kwa kasi.

?Da! Nimeota ndoto mbaya sana,? nilisema.

?Ipi??Nilimsimulia ndoto hiyo Munil lakini kila nilipokuwa namuweka wazi yeye alikuwa akicheka tu mwishowe akasema:

?Baby.?

?Naam.?

?Kwani hujui kwamba ndoto huja baada ya shughuli nyingi mpenzi wangu??

?Ndoto huja baada ya shughuli nyingi wakati umeona mtu anataka kunichinja na sime?? nilimuuliza kwa kumshangaa sana.?Ni kweli, lakini ni ndoto tu. Kwani umewahi kuota ikawa kweli?? aliniuliza.

?Sijawahi.?

?Sasa kwa nini hii unaogopa sana??

?Nahisi kama kweli, si unaona jasho! Tena ngoja niamke niswali,? nilisema lakini kabla sijaamka Munil alinizuia akisema haina haja ya kuswali kwa vile ile ni ndoto tu.

* * *



Alfajiri, Munil aliniamsha akiwa ametoka kuoga, akasema anakwenda msibani. Nilitoka kitandani, akaniuliza kwa nini naamka, nikamwambia nataka kumpa pesa, akacheka sana.

?Sasa sisi wanawake tunataka usawa kila siku, si inatakiwa mimi nikupe pesa wewe badala ya wewe



kunipa mimi?? Wakati Munil akisema hivyo alitumbukiza mkono kwenye mkoba wake na kutoa noti mpya za shilingi elfu kumi, akanitupita kitandani kisha akasema baadaye.

Sikumbuki kama nilimwona Munil akiondoka japokuwa alifungua mlango. Ninachokumbuka ni



kwamba, akili yangu ilihamia kwenye zile pesa, kwamba ni shilingi ngapi.Niliinua shingo kuangalia nje kupitia dirisha ili nimwangalie Munil anavyotoka lakini sikumwona nikashangaa kwani asingeweza kutoka eneo hilo la nyumbani bila kuonekana kwa kupitia dirisha. Halafu, ghafla nilisikia kama sauti

ikiniambia??hivi kwa kumbukumbu zako, Munil alivaa viatu gani??

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Nikajiuliza hivi kweli, Munil alivaa viatu gani? Sikupata jibu, nikachungulia chini sikuona. Ghafla kwa nje nikasikia ko ko ko! Munil anaondoka sasa. Nilichungulia tena dirishani, mlio wa viatu chini ulisikika lakini nikawa simwoni mtu na uelekeo ukitokea nyumbani ni mmoja tu, njia inakwenda imenyooka.

Nywele zilinisisimka, nikaa kitandani na kusema:



?Ee Mungu, kama huyu mwanamke ni jini nijulishe, kama si jini pia nijulishe.?

Nilipomaliza kusema, nikaulizwa na sauti akilini.?Hivi, hata Munil alipokuja pale baa kukusaliamia ulimwona amevaa viatu gani??Moyoni nilijijibu kwamba, sijamwona Munil akiwa amevaa viatu tangu nimemfahamu.


ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog