Search This Blog

MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN (2) - 4

 










Simulizi : Mkufu Wa Malkia Wa Gosheni (2)

Sehemu Ya Nne (4)







Ghafla sauti ya kitu kizito kikiburuzika ikawashtua, haraka wakaangaza nyuma yao na kushuhudia mlango wa piramidi ukijifunga. Sasa kukawa kiza kamili. Lakini kwa msaada wa maginga yao ya moto wakaona angalau njia.



Waheed akiwa ametangulia mbele, wakatembea kwa tahadhari. Wakitazama huku na huko. Na mioyoni mwao wakijua wazi hawapo eneo salama. Si ajabu lolote kutokea muda wowote.



Baada ya kutembea kwa takribani dakika tatu, wakaukuta mchoro ukutani upande wao wa kushoto. Mchoro ulikuwa ni wa tai aliyembania nyoka chini kwa miguu yake mizito na kucha zake kali.



Na tai huyu alikuwa akimdonoa nyoka huyo.



Waliposonga hatua chache mbele, wakakuta vyumba vitatu vidogo, na njia ilikuwa imekomea hapo. Kwenye kila chumba kulikuwa kuna meza ndogo na bakuli ya dhahabu juu yake.



Wakasonga na kutazama vilivyomo ndani. Kwenye bakuli la chumba cha kwanza, mulikuwa na mchele. Kwenye bakuli la chumba ya pili, mulikuwa na tende, na kwenye bakuli la chumba cha tatu, matufaha.



Kabla hawajafanya jambo, maandishi ya kiarabu yakatokea ukutani yakimaanisha: "na kila mmoja achague bakuli lake."



Basi kwasababu walikuwa wengi kuliko mabakuli yaliyokuwapo, ikabidi wajigawe wawili wawili. Zura na Fluffy wakalifuata bakuli la kwanza, lenye mchele, Alk akiwa amembelea Seth mgongoni wakalifuata la pili, lenye tende, na Malkia akiwa na Waheed wakaliendea lile bakuli la tatu, lenye tufaha.



Kila mmoja akachukua kilichomo kwenye bakuli lake na kukipeleka mdomoni kukitafuna. Punde walipomeza, wakajikuta wametokea mahali pengine wasipopafahamu!



Wale waliobwia mchele wakajikuta ndani ya maji. Waliotafuna tende wakajikuta wapo jangwani. Na waliokula tufaha wakajikuta wapo ndani ya msitu mkubwa!



Lengo likiwa moja tu, kuutafuta na kuupata ufunguo wa mlango wapate kuendelea na safari.



Baada ya kuangaza huku na huko, Waheed akamwambia Malkia:



"Nifuate!"



Wakiwa wametingwa na majani lukuki, miti mirefu yenye matawi mengi, wakapiga hatua wakielekea upande wao wa kaskazini.



Lakini kwa upande wa wakina Fluffy mambo hayakuwa mambo! Zura alikuwa amechoka. Hakuwa anaweza kuogelea. Alikuwa anazama akinywa na kupaliwa na maji kwa pupa!



Fluffy alikuwa na kazi mbili, mosi apambane kuokoa nafsi yake na pili ya Zura. Lakini naye hakuweza kudumu hivyo kwa muda mrefu, akachoka. Sasa si yeye wala Zura aliyekuwa anajua wapi wanapelekwa na kasi kali ya maji!



Wakabiduliwa kana kwamba samaki mfu.



**



Fundo kubwa la upepo lilipuliza na kusogeza dirisha. Tattiana akashtuka toka kwenye usingizi mwepesi, akadamka na kuangaza. Hakukuwa na kitu!



Akatazama pembeni yake akamwona mfalme akiwa amekwisha lala. Akanyanyuka na kuendea dirisha apate kulifunga.



Alipofanya hivyo akarejea kitandani lakini hakulala, akaketi na kushika tama. Akajiuliza kwanini aliamka, alitambua hatopata usingizi tena humo chumbani.



Alianza kusikia baridi kana kwamba yupo juu ya kilele cha mlima. Akaamua kutoka humo aende chumbani kwake akipanga kesho asubuhi kurejea mapema chumbani mwa mfalme kama alivyofanya jana yake na mfalme asijue kitu.



Lakini kama ilivyokuwa jana yake, akiwa anaelekea huko akitembea taratibu, akasikia sauti za watu wakinong'ona! Akashtuka.

Akatazama kule kwenye mlango wa ua ya ghorofa kisha taratibu akaanza kujongea kwenda kule. Alitaka kujua leo Lucy alikuwa anaongea na nani usiku mzito kama huo.



Akapiga hatua kama tano, akabakiza mbili tu kutimiza lengo. Lakini ghafla! Mlango ukafunguliwa kabla hajaugusa. Na mara Tattiana akakutana uso kwa uso na Bella, kijakazi mwingine wa kasri mbali na Lucy, akitokea huko nje!



Bella akashtuka na kushika kifua chake kwa mshangao. Akashusha pumzi ndefu na kuuliza;



"Kipenzi cha mfalme, hujalala hata sasa?"



Tattiana alirusha macho yake nyuma ya Bella. Akaangaza lakini hakuona mtu huko. Alijawa na shaka, akamuuliza Bella.



"Ulikuwa unaongea na nani, Bella?"



Bella kabla hajajibu akageuza uso wake kutazama nyuma alipotokea kisha akapandisha mabega.



"Hapana, sikuwa naongea na mtu!"



"Una uhakika?" Tattiana akamkazia macho.



"Ndio, nina uhakika!"



Tattiana akasonga kwenda kutazama kule nje. Akaangaza asione mtu yeyote. Akamrudia Bella na kumuuliza:



"Lucy yupo wapi?"



"Amelala," Bella akamjibu.



"Mbona wewe hujalala mpaka saa hii?" Tattiana akauliza.



"Sina usingizi," Bella akajibu. "Nikaona nitembee tembee tu!"



Kwa muda kidogo Tattiana akanyamaza akimtazama Bella machoni. Bella akatazama chini.



"Nisamehe, kipenzi cha mfalme. Sitarudia tena kutembea nyakati za usiku kama nimekuogopesha."



Tattiana hakusema kitu.



"Kweli sikuwa naongea na mtu!" Bella akaendelea kusisitizia. "Nilikuwa mwenyewe napunga upepo!"



Sura yake ilikuwa inatia huruma. Kwa ishara ya kichwa Tattiana akamruhusu aende zake kisha yeye akasonga kwenda kutazama huko nje.



Akafunga mlango na kukaa huko kwa muda. Upepo ulikuwa mkali. Na kulikuwa kimya haswa. Hakuona wala kuhisi kitu zaidi ya baridi, akatoka na kwenda zake chumbani kwake akalale.



Lakini Bella, akiwa amejibanza ngazini, akamtazama mwanamke huyo akiyoyoma. Akahesabu dakika kadhaa kisha akarejea kule alipokuwa mwanzo, nyuma ya mlango wa uani.



Akaufunga kabisa mlango huo kwa komeo huko kwa nje kuepusha usumbufu.



Ndani ya muda mfupi, sauti ya kunong'ona ikaanza tena. Ikadumu kwa kama robo saa, kisha Bella akatoka na kuelekea zake kwenye chumba walalacho vijakazi. Chumba hicho alikuwa anaishi yeye na wenzake watatu, akiwamo Lucy.



Chumba kilikuwa kipana mno na kila mmoja alilala kwenye kitanda chake.



Vitanda vyote vilikuwa na umbo la duara vikivutia machoni kwa mtindo wake.



Vijakazi wote walikuwa wamelala, isipokuwa huyu Bella aliyeingia hivi punde.



"Lucy!" Bella akaita kwa kunong'oneza. "Lucy, amka!"



Lucy alikuwa ameshabebwa na usingizi. Ilikuwa ngumu kumwamsha, lakini kwa usumbufu wa Bella akaamka akiwa amejawa na mang'amung'amu.



"Ni nini lakini?" Akauliza kilevi.



"Yule kipenzi cha mfalme ameniona!"



Hapo usingizi wote ukamkatika Lucy. Akamtazama mwenzake kwa macho ya kukodoa.



"Unasemaje?"



"Ameniona kule!" Bella akapayuka kwa sauti ya chini.



"We!" Lucy akabweka. Haraka Bella akawahi kumfunga mdomo.



"Ongea taratibu! Watu watasikia..."



Lucy akameza mate.



"Alivyokuona akafanyaje?" Akauliza akiwa mjawa wa hamu. Bella akamwambia ilitokea kama ilivyokuwa kwake, kabla hajaufungua mlango akamuwahi na kujifanya amegutuka.



"Una uhakika hajakusikia?" Lucy akauliza.



"Sidhani," Bella akajibu. "Lakini sasa lazima atakuwa na hofu nasi. Huoni inabidi tufanye jambo kabla mambo hayajaharibika?"



Lucy akajivuta na kuketi kitako.



"Unadhani jambo gani linastahili tufanye?"



"Tuhamishe madhabahu!" Akashauri Bella. "Pale atakuwa ameshapakariri, huenda akawa anapita mara kwa mara. Hata tukikutana naye tena pale, ni nini tutasema?"



Lucy akaridhia jambo hilo, wabadilishe madhabahu. Basi akamsihi mwenzake kesho yake aende kutafuta kila linalohitajika wakamilishe adhma yao hiyo.



Wakalala.



**



Hata sasa na ni usiku mzito, Ottoman na Oragon walikuwa nje kama mayatima ama mafukara. Upepo wa baridi ulikuwa unawapuliza kwa kasi na hawakuwa na nguo za kujikinga wala kujisitiri zaidi ya walizonazo mwilini.



Walikuwa wamejilaza chini ya mti mkubwa wa mkuyu wakiwa wamejikunyata kana kwamba watoto wachanga, vifurushi vyao wakivitumia kama mto.



Hata usingizi huu ulikuwa ni wa mashaka, kama ule wa sungura, kwa kulaza jicho moja huku jingine likiwa kazini. Utapataje amani na unatafutwa na wanajeshi huku na huko himaya nzima? Tena kwa kesi kubwa ya cedar!



Kulikuwa kimya lakini haukudumu. Ndani ya muda mfupi tu, Oragon akakurupuka, akamwamsha Ottoman kwa fujo.



"Wanakuja, amka!"



Ottoman akasimama upesi kumkuta kaka yake. Wakatazama mbali upande wa mashariki, huko wakaona kikosi cha wanajeshi walio juu ya farasi wakifanya msako. Mikononi wameshikilia maginga ya moto.



Basi upesi wakaanza kukimbia kuokoa nafsi zao. Wakazama zaidi msituni, ndani ndani. Wakatembea kwa kama lisaa, na basi wakaja jikuta wamekaribia mpakani. Hapo mpakani walikuwa wamesimama wanajeshi wanne wakiwa wanarandaranda, mikononi wamebebelea mikuki.



Hakukuwa na njia ya kupita zaidi ya hapo. Hapo kwenye geti lichungwalo na wanajeshi. La sivyo warudi ndani ya Goshen ambapo palikuwa ni hatari zaidi.



"Sasa tunafanyaje?" Akauliza Ottoman.

Hakukuwa na mwenye jibu. Lakini walipoendelea kukaa hapo wakasikilizia, mara kwa mbali, ndani ya msitu wakaona mwanga wa maginga ya moto!



Wale wanajeshi walikuwa wanakuja!



Hapa sasa wakachanganyikiwa. Sasa ilibidi wachague moja kati ya haya, waende kukutana na wanajeshi wa mpakani ama wale wa msituni.



Oragon akafanya maamuzi. Akajitokeza akinyoosha mikono juu akielekea langoni mwa mpaka. Hata Ottoman akabaki anashangaa.



"Wewe ni nani na unaenda wapi?" Akafoka mwanajeshi akimwonyeshea mkuki. Akaamriwa asimame pale pale alipo, akithubutu kupiga hatua ya ziada, ataukosa uhai wake!



"Naitwa Oragon, nipo na kaka yangu Ottoman. Tunataka kuvuka mpaka," Oragon akajieleza kwa kujiamini. Wanajeshi wale wakatahamaki. Majina hayo hayakuwa mapya masikioni mwao.



"Oragon, hujui mipaka imefungwa mpaka pale taarifa itakapotolewa?" Akauliza mwanajeshi. Punde akamwona na Ottoman akijongea karibu kwa uoga.



"Najua," Oragon akajibu. "Lakini ninaomba msaada!"



Mwanajeshi akamtazama kisha akamuuliza:

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Hata kibali cha kuvuka mpaka unacho?"



"Hapana, sina!" Oragon akajibu. "Lakini nina kingine cha ziada."



Akatoa fedha nyingi kwenye kifurushi chake na kumwonyeshea mwanajeshi. Mwanajeshi akasogea karibu. Akazichukua fedha hizo, na kisha akaamuru geti lifunguliwe vijana hao wapite baada ya kuwapooza wenzake kwa fedha kichele.



Oragon na Ottoman wakatoka Goshen! Wakapotelea huko kwenye himaya ya kigeni. Himaya wasioijua hata kwa chembe!



Tangu wazaliwe hawakuwahi kuuvuka mpaka wa Goshen mpaka wamefikia umri huo. Leo ikawa mara yao ya kwanza.



Alitakalo mwana ndilo hulipata. Waswahili hawakunyima maneno.



Wakatembea kwa lisaa limoja wakikata pori. Wakaona nyumba kadhaa, na kwakuwa walikuwa wamechoka, sasa wanahitaji mapumziko, wakazijongelea nyumba hizo waombe msaada wa kulaza mbavu zao.



Wakabisha hodi lakini hawakufunguliwa. Ulikuwa ni usiku sana. Ni ngumu kuamini mtu akugongeaye nyakati hizo. Hivyo juhudi zao zikashindwa kuzaa matunda.



Sasa wafanye nini? Wakaamua kujongea tena mbele pengine wanaweza wakapata msaada. Lakini wakatembea kwa umbali mrefu, wakachoka. Wakaamua kujilaza kandokando kidogo mwa barabara pakikucha wajue wa pa kuenenda.



Wakang'ang'ania vifurushi vyao wakijipa matumaini watakuwa salama.



Lisaa limoja likapita, hata usingizi wakazama. Ila asubuhi pasikuche, wakakurupushwa na wanaume watatu waliobebelea maginga ya moto.



Wakahofu sana wakijiminya kwa karibu. Wanaume wale, ambao hawakuwa na taswira ya kuvutia, wakawauliza wao ni wakina nani na kwanini wapo pale muda huo?



Basi wakajieleza. Wale wanaume wakawaambia.



"Tufuateni, tutawasaidia."



Wakaongozana nao wakielekea kusini, kwa mwendo wa dakika chache, wakafika kwenye nyumba moja ndogo mithili ya ghofu.



"Hapa ndiyo kwetu!" Mwanaume mmoja akatamba. Wakawakaribisha kwa ukarimu.



Nyumba hii ilikuwa ni kuukuu haswa. Haikuwa na samani za maana, imejawa na tando za buibui na uchafu.



Lakini ilikuwa kheri, kuliko kulala nje, akawaza Oragon akiipekua nyumba hii kwa macho.



Wakashtuliwa,



"Mbona mwalala haraka na hatujawakarimu vema?" Alisema mwanaume mmoja mfupi kuliko wote. Uso wake ulikuwa umejawa na ndevu lukuki macho tu yakionekana.



Basi wakapewa bilauri za pombe wanywe. Wakanywa na kisha wakalala kama wafu. Walipoamka asubuhi, wakajikuta hawana kitu! Vifurushi walivyokuwa wamevibebelea vilikuwa vimeenda. Na hata nguo walivuliwa wakibakizwa uchi wa mnyama!



Wakachanganyikiwa. Wakatazama ndani huku na kule, hakuna mtu. Walipotazama nje, wakaona wanajeshi kama kumi kwa idadi ya haraka. Mbele ya wanajeshi hao alikuwa amesimama mzee mnene mwenye ndevu nyeupe, kiremba kichwani na joho la rangi ya maziwa.



Mzee huyo alikuwa anaikagua nyumba waliyomo kwa macho akishika kidevu chake. Alifanya zoezi hilo kwa muda mfupi, kisha akawatazama wanajeshi na kuwaagiza:



"Ichomeni tu!"



Ginga la moto likawashwa.





Kabla halijashikishwa kuni za nyumba mara Oragon na mwezake wakapiga kelele wapo ndani. Nyumba isichomwe!



Mzee yule akatahamaki na kuuliza ni nani aliye ndani ya nyumba yake pasipo kibali? Akaamuru watoke nje mara moja.



Lakini tupo uchi, wakasema wakina Oragon. Mzee yule akajua wanatania, akatishia kuchoma nyumba hiyo awageuze mishikaki kama hawatotii amri yake.



Basi Oragon na kaka yake wakatoka nje wakiwa wamehifadhi sehemu zao za siri kwa mikono.



Ha! Watu wakastaajabu. Mmetoka wapi wakaulizwa, nao pasipo hiyana wakasema wametokea Goshen, wakajikuta hapo baada ya kulaghaiwa na wanaume kadhaa waliowapatia kilevi.



Vipi wamewabaka pia? Wakaulizwa. Wakajitazama upesi na kutikisa vichwa vyao.



"Hapana, tupo salama!"



Mzee yule akacheka akikuna ndevu zake.



"Mshukuru kwa hilo!" Akawatazama kwa huruma. Akaagiza wale wanajeshi wawasitiri wanaume hao kwa mashuka yao migongoni. Kisha akawaambia hapo ni kwake, hao wanaume waliwadanganya. Hapo hapana mtu mkazi kwa muda sasa.



Lakini akawatoa hofu,



"Nitawasaidia. Wala msijali."



Angalau wakapata ahueni kwani hawakuwa na pa kwenda. Ukizingatia hawana hata senti pamoja nao.



"Tunashukuru sana. Hatuna fadhila za kukulipa."



Mzee akawaambia wasijali. Akajitambulisha kwao kwa jina la Raam, mmoja wa makuhani katika himaya hiyo.



"Sisi ni binadamu. Shurti kusaidiana," akasema Raam kisha akawatazama wanajeshi alioongozana nao na kuwaagiza wachome nyumba hiyo kama alivyowaambia hapo awali.



**



Jua lilipommulika machoni alikurupuka akaketi kitako. Akatazama kushoto na kulia, hakuona mtu. Alikuwa ameketi pembezoni mwa mto mpana ambao ulishapooza maji yake ukielekea kufifia.



Nguo zake zote zilikuwa zimelowana. Tumbo limejaa maji na amechoka mwili.



Alikuwa ni Fluffy!



Anahema kwanguvu. Anakohoa maji na kuyatapika kabla hajasimama upesi baada ya kumkumbuka Zura.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Anajawa hofu zaidi baada ya kukumbuka mwanamke huyo hajui kuogelea. Anaanza kumtafuta akiangaza huku na huko.



Akataka kuita jina ila haraka akajifumba mdomo. Alikumbuka hairuhusiwi kuitana majina ndani ya piramidi!



Lakini, akajiuliza, mimi ni ndani ya piramidi? Akatazama juu akaliona anga. Pembeni msitu mkubwa ulikuwa imemzonga na kwa mbele kidogo tu kulikuwa na mto mpana.



Piramidi gani hii?



Mara akasikia sauti ya njiwa, haraka akatazama. Akang'amuka mawazoni na kuendelea kumtafuta Zura. Akatembea sana kurudi chanzo cha mto kilipo lakini hakumwona Zura.



Amekufa?



Alitembea sana mwishowe akachoka. Akaketi chini kandokando ya mto. Akiwa amekata tamaa, anatazama chini, akastaajabu kusikia bega lake limeguswa!



Haraka akatazama, hakuona mtu. Akasimama na kukodoa macho lakini hakuambulia jambo. Baadae kidogo kwa mbele, akamwona mama yake!



Moyo ukapiga kwata. Akayafikicha macho na kuangaza tena. Bado mama yupo! Akaita na kuuliza:



"Mama umefikaje huku?"



Mama yake akatabasamu. Alafu akamwita,



"Njoo mwanangu. Umeteseka mno. Njoo angalau nikukumbatie."



Fluffy akapatwa na kigugumizi. Akamtazama mwanamke huyo vema. Kweli alikuwa mama yake. Hakuwa na kasoro hata robo. Alikuwa amevalia nguo anayoipenda na nywele zake amezichana vema.



Tabasamu lake likakumbusha Fluffy mbali sana. Na kwakweli alikuwa amemiss kuwa ndani ya mikono ya mama yake.



Akaanza kusogea.



Lakini anasita. Akiwa amebakiza hatua tatu, anasimama na kumtazama mama yake vema. Pengine ataona kasoro.



"Haujammiss mama?" Mama akauliza. Bado mikono yake ilikuwa imejitawanya kumkaribisha Fluffy kwa kumbato. "Mama amekumiss mno. Na anatamani urudi nyumbani. Maisha bila wewe yanakuwa tofauti sana."



Fluffy akagoma kusogea. Akaanza kupiga hatua kurudi nyuma. Ni kama alirejea kwenye fahamu zake na kuhisi kile hakikuwa kitu kinachowezekana.



Mama yake amefikaje hapo? Alipoanza kujiuliza hivyo, moyo wake ukapiga maradufu. Akajawa na hofu.



Mama akashusha mikono yake, kisha akasema:



"Najua alipo mwenzako."



"Nani?" Fluffy akawahi kuuliza.



"Unayemtafuta," mama akajibu. "Najua alipo."



"Yupo wapi?"



Mama akageuka na kumwonyeshea kidole upande wa pili wa mto. Fluffy aliporusha macho yake kuangaza, akaona mwili wa Zura ukiwa umejilaza kama mfu.



Akahofu.



"Amekufa?" Akauliza. Kabla hajapata jibu akatumbukia mtoni na kuanza kupambana na maji kwa hali na mali!



Maji yalikuwa mengi tofauti na kule alipokuwa mwanzoni. Alijikakamua haswa kupambana na maji hayo yashukayo chini, lakini ghafla katika zoezi hilo, akadakwa mguu. Akaanza kuvutiwa chini ya mto, kinani!



Akiwa amebana pumzi, akapambana sana kuunasua mguu wake. Kila alipokuwa anafanikiwa kuunasua huu ukadakwa mwingine! Akiendelea kuvutwa chini kabisa ya mto ambako kulikuwa kiza. Maji yake yalikuwa ya baridi tofauti na yale ya juu, tena yakiwa yametulia hayatembei.



Pumzi ikaanza kukata kifuani mwa Fluffy, akaanza kuyanywa maji kwa pupa. Akafikishwa kabisa chini ya mto, gizani, akakata tamaa ya maisha.



Lakini bahati, akahisi amekalia jiwe. Upesi akapata tumaini. Haraka akili yake ikafanya kazi, akang'oa jiwe hilo kisha kwanguvu akalisiginia kwenye mkono uliomshikilia miguu.



Ukamuachia!



Kwa haraka akaogelea kurudi juu. Alipofika akapiga mafundo matatu makubwa ya hewa kisha akaanza kufanya jitihada za kwenda ng'ambo akamkute Zura.



Kwa chini, kile kiumbe kilichomvuta, nacho kikapanda kwa haraka kikinyoosha mkono amdake tena mguu! Hatimaye akafanikiwa kuunyaka, ila sasa Fluffy alikuwa ameshafika fukweni. Maji yalikuwa machache. Akageuka na jiwe kubwa amponde huyo kiumbe, akashangaa kumkuta ni mamaye.



Anamtazama kwa sura ya huzuni. Fluffy akasitisha zoezi.



Lakini mbona alitaka kuniua chini ya maji? Akajawa na shaka. Mbona bado hajaachia mguu wangu? Anataka kunivutia tena ndani ya maji?



Punde ya ghafla, mama akamvuta kwanguvu ndani ya maji, hapo Fluffy akapoteza simile. Akambamiza na jiwe mara tatu kichwani.



Puh! - puh! - puh!



Kiumbe kikamwacha mguu na kuzama chini. Mara Fluffy akajikuta amebebelea ufunguo mkononi badala ya jiwe. Kutazama kando, akamwona Zura akikohoa na kujivuta taratibu.



Kufumba na kufumbua wakajikuta kwenye kile chumba walimochotea mchele bakulini. Walikuwa wameshinda zoezi lao!



Wakatazama wenzao kwenye vyumba vingine. Hakuna aliyekuwepo.



Vyote vilikuwa vitupu!



**



"Jana usiku ulikuwepo wapi?" Phares alimuuliza Tattiana. Yalikuwa ni majira ya saa tano asubuhi na mfalme alilikumbuka hili baada ya kulisahau kuliuliza tangu asubuhi na mapema.



"Mimi?" Tattiana akaigiza kushangaa. "Mbona nilikuwepo!"



"Hapana," mfalme akatikisa kichwa. "Kuna muda niliamka sikukuta!"



"Ohooo!" Tattiana akaigiza kutabasamu. Akamsogelea mfalme na kumshika kidevu. "Nilitoka kidogo kwenda kule kwenye chumba changu."



"Kufanyaje?"



"Aaahm ... kuna vitu nilikuwa nimeenda kutazama."



"Vitu gani hivyo? ... zile nguo nini?" Mfalme akauliza kisha akatabasamu kwa mbali. Pasipo kujua akampatia Tattiana upenyo.



"Yah! Nilikuwa natazama zile nguo!" Tattiana akaongopa. Hakuwa anajua hata nguo gani zinaongelewa hapo.



"Umezipenda?" Mfalme akauliza, kabla Tattiana hajajibu akaongezea: "Kuna nguo nyingi sana za Vedas kwenye lile kabati. Ukipata muda zitazame zaidi. Kama utakayoipenda, chukua kisha vaa nikuone utaonekanaje. Sawa?"



"Sawa, mfalme."



Phares akaondoka zake akimuahidi atarejea muda si mrefu. Lakini akimwacha Tattiana na hamu ya maswali. Kumbe kile chumba kilikuwa ni cha malkia Vedas? Hakuwa anajua siku zote hizo.



Kwa muda kidogo akamkumbuka malkia huyo namna alivyokuwa anaogopeka himaya nzima. Namna simulizi zake za kuogofya zilivyosambaa ndani ya himaya.



Akajikuta anapata hamu ya kujua zaidi. Akaenda kwenye kile chumba na kuanza kupekua makabati. Kulikuwa na nguo nyingi mno. Nyingi zikimvutia na nyingi zikimkera.



Lakini katika msako wake huo kabatini, konani, akakutana na chupa.



Chupa hii ilikuwa pana nyeusi. Ndani yake kulikuwa na mwanga hafifu wa kijani. Akaiteka kwa mikono yake na kuiangaza vema.



Kwa mbali akagundua chupa hii ilikuwa inatoa mlio wa mapigo ya moyo!



**



Akashangazwa sana na hilo. Asiamini akaiweka chupa hiyo sikioni aisikie vema. Tih! - tih! - tih! Chupa ilikuwa inalia. Akatamani kuifungua, lakini akasita!



Ni nini hiki? Vipi nikikifungua itaniathiri? Akajiuliza kifuani. Akakitazama tena kitu hicho, na mara akasikia mlango unagongwa! Haraka akaificha chupa hiyo mgongoni.



"Samahani ewe kipenzi cha mfalme," alisema kijakazi. "Nahitaji kufanya usafi!"



"Saa hii?" Tattiana akatahamaki.



"Ndio. Huwa nakifanyia usafi majira haya baada ya kwengine.'



Tattiana akafikiria kidogo kisha akasema:



"Hapana! Acha tu, kwa sasa nina matumizi nacho!"



Kijakazi akaenda zake. Tattiana akaketi kitandani na kufungua ile chupa. Moshi mkubwa rangi ya kijani ukatoka humo. Haraka Tattiana akaifunga.



Lakini moshi huo uliotoka ukasambaa humo chumbani na kuenea. Akashangaa mbona umeongezeka kiasi hicho? Katika namna ya kushangaza akaona moshi ukijikusanya na mara ukajiumba kiumbe mkubwa wa kiume mwenye ndevu zilizojivingirita kutengeneza namba moja.



Kichwani hakuwa na nywele. Mikononi alikuwa ana bangili na sikio lake moja alikuwa ametoga hereni ya duara.



Tattiana akaogopa sana. Akajikunyata kwa hofu akisogelea konani mwa kitanda. Mwili wake ukatetemeka na akatamani kupiga yowe.



"Nefil njhami khatu habab?" Akauliza yule kiumbe. Tattiana akamtikisia kichwa akimwambia hamwelewi. Lakini kile kiumbe kikarudia tena swali lake mara mbili. Kimya. Mara akapotea.



Akamwacha Tattiana kwenye maswali kedekede. Akaitazama ile chupa kwa mshangao na kwa kutaka kujua zaidi, akaifungua tena!



Moshi ukazagaa na yule kiumbe akatokea kwa mara nyingine. Akamuuliza swali lile lile:



"Nefil njhami khatu habab?"



Tattiana hakuwa anaelewa. Akamuuliza yule kiumbe yeye ni nani na ametokea wapi? Hakujibu. Akabaki kurudia swali lake mpaka akapotea.



Tattiana akarejesha chupa kabatini kuificha alafu akaenda nje akiendelea kuiwaza. Hata baadae akataka kumuuliza mfalme lakini akaogopa.



Akajiuliza vipi kama chupa hiyo itakuwa ya kwake, inamhusu? Vipi kama kiumbe kile akawa anakimiliki yeye? Hakutaka kuwa msumbufu ama kumfanya mtu aanze kumtilia macho kila anachofanya. Akaona kheri anyamaze.



Atafuatilia zaidi.



**



Usiku ...



Matarumbeta matatu yakalia kwa kuigana sauti. Mfalme alikuwa amesimama nje ya kasri yake akiambatana na viongozi kadhaa. Walikuwa wamesimama hapo wakiwapokea wazee waliowatuma kwenda kwa Venim.



Baada ya mfupi, wakagundua ni mzee Harid pekee ndiye alirejea. Wakamkarimu na kumkaribisha ndani asifahamu kabisa kama mambo yameharibika. Akaeleza yaliyotokea huko.



Venim yupo tayari kuwasaidia, ila kwa malipo. Anamhitaji huyo mwanamke aliyevaliwa na mlozi, ambaye ni Rhoda. Na kama haitoshi anahitaji kiasi fulani cha dhahabu ambacho atampelekea.



Hiyo ya dhahabu akiwa ameliongezea yeye mwenyewe apate 'cha juu'.



"Anamtaka Rhoda?" Mfalme akauliza kana kwamba hakusikia. Hili swala lilimuwia vigumu kidogo kuliridhia.



"Ndio, anamhitaji mwanamke huyo," Venim akasisitizia. "Bila shaka hatuwezi kuiteketeza Goshen nzima kwasababu ya mwanamke na vipande kadhaa vya dhahabu. Si ndio?"



"Kabisa," mfalme akaitikia. "Hatuna budi kufanya kila lililo mikononi mwetu kuikomboa Goshen."



Mzee Harid akamtazama Tattiana na kutabasamu. Tattiana akamkazia macho akimtazama kwa uso mgumu. Moyoni mwake alikuwa anaungua na hasira dhidi ya mzee huyo.



Alipomuona akamkumbuka Roboth na namna alivyokufa kinyama. Akatamani kumrukia mzee huyo na kumraruararua.



"Unaendelaje binti yangu?" Harid akauliza. Tattiana akamtazama pasipo kumjibu. Kinywani mwake alikuwa akisaga meno.



Akataka kunyanyuka, lakini mfalme akamzuia kwa kumdaka mkono kisha akatazamana na wanajeshi wake waliokuwa eneoni na kuwapa ishara kwa kichwa. Mara wanajeshi wakamsonga mzee Harid na kumweka chini ya ulinzi.



"Mfalme, nini hiki?" Harid akatahamaki.



"Hiko ndicho unachostahili!" Mfalme akamjibu. "Hicho ndicho wanachostahili wauaji na wafanyabiashara haramu!"



Harid akazidi kutahamaki. Akakabwa na kigugumizi.



"Muuaji? Mimi? Biashara gani? Mbona hakuna ninachoelewa hapa? ... kujitolea kwangu kumekuwa kosa!

"

"Nyamaza!" Mfalme akamkaripia. "Unavyozidi kuongea upuuzi wako ndivyo na ukubwa wa adhabu yako itakavyokuwa! Kila kitu kipo bayana. Hakuna cha kuficha tena Harid! Damu ulizozimwaga zitakuwinda."



Mfalme akaongea kwa hisia sana. Akapiga meza na kutangaza:



"Kuanzia leo cheo chako cha uzee wa himaya umevuliwa. Utakuwa mfungwa mpaka kifo chako!"



Harid akalia kwa sauti kuu.



"Nisamehe mfalme! Nimekosa sana. Nami ni mzee mno niache nifie nyumbani kwangu mikononi mwa watoto wangu!"



"Watoto gani?" Mfalme akauliza. "Hao unaowaagiza wakaue watu? Hawapo, wanatafutwa himaya nzima. Na watakapopatikana watafungwa wakamalizie ujana wao wote gerezani!" Mfalme alifoka.



Mzee Harid akamwaga machozi. Akamwomba mfalme ampatie angalau nafasi ya kwenda kutembelea nyumba yake kabla hajapelekwa huko wanapotaka kumpeleka.



Mfalme akakataa. Harid akamwomba zaidi. Tattiana akamsihi mfalme amkubalie mzee huyo ombi lake la mwisho. Mfalme akakubali.



Harid akachukuliwa chini ya ulinzi mkali, akapelekwa mpaka nyumbani kwake. Huko akapekua nyumba yake nzima, mpaka kule mafichoni ajuapo yeye na wanaye tu, hakuona senti hata moja!



Fedha zote alizozihangaikia hazikuwapo! Hakubakiziwa hata tone.



Akaishiwa nguvu.



"Oragon ..." akaita kwa uchungu. "Ottoman!" Akayarudia majina hayo ya wanawe mpaka wanajeshi walipokuja kumzoa na kumtupia ndani ya toroli la farasi.



Akamimina machozi njia nzima. Hata haikujulikana alikuwa anatakia nini hizo pesa na wakati anaenda gerezani.



Akawekwa kwenye chumba chake cha pekee, komeo zikakaba mlango.



"Hayo ndiyo maisha yako mapya!"



**



"Kwanini lakini uliamua kufanya hivyo?" Tattiana alilalamika akishikilia nondo za lupango. Macho yake mekundu yalikuwa yanamtazama mzee Harid aliyekuwa ameketi chini kimya.



Yalikuwa ni majira ya asubuhi.



"Roboth alikutendea nini baya ukammaliza kinyama vile?" Tattiana aliongea kwa sauti ya kilio. "Alikutendea nini?" Akafoka. "Alikutendea nini?" Akarudia tena.



Harid akamtazama kwa jicho la hasira.



"Nyamaza!" Akapaza sauti yake. "Ewe mwanamke mpumbavu usiye na macho wala akili."



Akanyanyuka na kusogea.



"Unadhani ungekuwa meza moja na mfalme, ukalala naye kitanda kimoja, ukaishi naye nyumba moja pasipo mimi? Nani ameroga hiko kichwa chako ewe ng'ombe uliyepelekwa mtoni usijue kunywa?" Harid akalalama. "Kwanini umekuwa wa kushupaza na kutoona wema?"



"Wema gani? - kumuua Roboth?" Tattiana akalia.



Harid akamtazama kwa msisitizo na kumwambia kwa sauti ya chini:



"Nilikupokonya moja ili ubaki na moja la maana, sema ahsante angalau. Lililobakia mkononi mwako ni la thamani mno. Hauoni namna mfalme akupendavyo? U mpofu wa aina gani wewe?"



Tattiana akataka kunena, Harid akamkatiza.



"Najua moyo wa mfalme upo mikononi mwako. Nenda kamshawishi kwa sauti yako tamu karibu na sikio aniachie huru."



"Sahau kuhusu hilo!" Tattiana akamwambia akitikisa kichwa. "Halitawezekana angani wala ardhini."



Harid akatabasamu.



"Nadhani umesahau baba yako anahusika kwenye hili. Sasa chaguo ni lako. Ukamwambie mfalme anitoe ama niropoke kila kitu kwenye masikio yake."



Tattiana akakaukiwa maneno mdomoni.



**



Akajilaza kitandani akiwaza na kuwazua.



Alikuwa ana mafundo moyoni na mawazo mengi kichwani. Alihisi kuchanganyikiwa. Hakupata hata usingizi.



Akaketi kitako na kushika tama. Akawaza siku yake nzima kuanzia kwa yule kiumbe aliyemwambia maneno ya ajabu asiyoyaelewa mpaka kwa Harid aliyempa vitisho. Akaona ni mzigo mkubwa. Kichwa chake hakiwezi peke yake.



Akamgusa mfalme na kumtikisa.



"Mfalme, naomba niongee nawe," akanena moyoni. Kinywa kilikuwa kizito kutamka.





**



Mfalme hakuamka kwani alikuwa kwenye usingizi mzito. Tattiana alimwamsha kwa uoga akimparasa. Hata maneno aliyokuwa anayatamka hayakutoka kinywani, yakaishia mdomoni.



Alikuwa anaogopa. Mfalme atamwelewa? Au atakuwa amemrahishia uchunguzi wake na basi atatuma wanajeshi wake wakamnyake baba yake?



Akasimama na kwenda dirishani. Akaendelea kuwaza. Akiwa hapo akasikia sauti ya kitu kama sufuria kikianguka. Akashtuka lakini hakudiriki kutoka nje ya chumba.



Hakujisikia kwenda mahali popote leo hata kule chumbani kwake. Basi akasimama hapo dirishani kwa muda mrefu mpaka aliposikia sauti ya mfalme ikimuita.



Hakujua ilikuaje akaamka.



"Mbona upo dirishani saa hii?" Mfalme akamuuliza. Akamjibu hana usingizi. Mfalme akanyanyuka na kumfuata.



"Una tatizo gani, Tattiana. Nieleze?"



"Hata nikikueleza utaelewa?" Tattiana akajiuliza moyoni. Akamtazama mfalme na mara akashindwa kujizuia kulia. Mfalme akambembeleza sana. Akamsihi amweleze kinachomsibu. Yupo radhi kumsaidia.



Basi Tattiana akafungua kinywa chake. Akamweleza mfalme kwamba baba yake naye anahusika na biashara ya Cedar.



Mfalme akatahamaki.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Unasemaje?" Akauliza kwa hasira. Lakini uso wa huzuni wa Tattiana ukayeyusha hasira yake ngumu.



"Alifanya hivyo kwa kulipa fadhila kwa mzee Harid baada ya mzee huyo kukukutanisha na mimi. Hakuwa na namna, kwani hakuna familia isiyotaka kutoa malkia."



Akapiga magoti na kulia miguuni mwa mfalme.



"Naomba umsamehe baba yangu. Naomba utusamehe kwani tumekuingiza kwenye matatizo makubwa!"



Mfalme akakosa cha kusema. Akajaribu kuukaza moyo wake lakini akashindwa. Akamnyanyua Tattiana na kumsihi anyamaze. Amemwelewa na atalifanyia kazi.



Kesho yake asubuhi Melkizedek akaitwa kasrini na kuketi meza moja na mfalme pamoja na Tattiana. Alikuwa anaogopa mno. Hakuweza hata kumtazama mfalme usoni akatazama chini.



Mfalme akamtaka amweleze kila kitu asifiche jambo. Melkizedek akaweka bayana tangu siku ya kwanza kukutana na mzee Harid na namna alivyomwambia kumhusu binti yake.



"Nipatie msichana huyu, hakika anaweza kuyadaka macho ya mfalme akamuoa."



Lakini hakumweleza kama angehitaji fadhila hapo baadae. Bahati mfalme alipompenda mwanae, sasa ndipo alipoanza kutaka kutumia hiyo fursa.



"Sasa ni wakati wa malipo. Inabidi ufanye hivyo ili nami nikatie juhudi asiishie kwenye uchumba bali aolewe kabisa," akahadithia Melkizedek. "Na malipo yake hayakuwa fedha, ningempatia, yalikuwa kumsaidia kupitisha cedar mpakani."



Alipoeleza hayo, mfalme akakasirika sana. Kumbe Harid alitumia nafasi yake ya kutokuwa na mke kama mtaji? Hakujua mzee huyo alikuwa dhalimu kiasi hicho.



Kwasababu hii ilikuwa siku moja kabla hajaitwa na baraza la wafalme, akaona ni bora akafanya jambo. Akawaagiza watumishi wake wajiandae kwa ajili ya safari ya kwenda Maam hivi punde.



Wakamtoe mzee Harid gerezani, wamtie kambani na kumpakia kwenye toroli.



"Naweza nikaenda nawe?" Tattiana akauliza.



"Hapana," mfalme akamjibu kisha akamshika mikono. "Bakia na Goshen. Hili inabidi nikalifanye mwenyewe."



Baada ya chini ya lisaa, mfalme akaanza safari yake kwenda Maam akiwa ameongozana na kikosi chake kikubwa cha wanajeshi, viongozi kadhaa pamoja na mfungwa, mzee Harid.



Wakatumia masaa kadhaa kufika huko. Hayakuwa mengi, kama mawili ama matatu, kwani Maam haikuwa mbali sana.



Wakakutana na baraza la wazee la himaya hiyo, kwani mfalme alikuwa hoi kitandani. Wakibashiri hata leo ikipita hajafariki, basi itakuwa miujiza ya miungu yao.



Mfalme akawaomba msamaha kwa yote yaliyotokea. Akawaambia wamefanikiwa kumpata yule aliyehusika na biashara hiyo. Na wamemleta wamfanye watakavyo.



Harid akapokelewa na kuhamishiwa kwenye gereza la Maam tayari kwa ajili ya kunyongwa kesho yake mbele ya watu.



"Ina maana amehusika mtu mmoja tu na hii biashara?" Mfalme akaulizwa.



"Hapana," akajibu akitikisa kichwa. "Alikuwa akifanya pia na wanawe, bado wanatafutwa. Inaaminika watakuwa wamekimbilia himaya zingine."



Mfalme akajua sasa mambo yatakuwa yamekwisha. Lakini kinyume na hayo, baraza la Maam likamwambia alichofanya bado hakikuwa kinatosha! Uzembe wa himaya yake unapelekea mfalme wao kufa, kumtoa mtu mmoja kutawezaje kufidia hilo?



"Tayari uhusiano kati ya Maam na Goshen umepasuka," akaeleza mzee mmoja wa baraza. "Inabidi zifanyike jitihada za ziada kuurejesha upya. Sasa kesho kutwa tutamkabidhi mtoto wa kwanza wa mfalme madaraka ya baba yake. Mtoto huyo atahitaji kupata mke. Mke mzuri atakayekuwa malkia wa Maam. Ni kheri kumtafutia mke huyo huko Goshen kwa dhumuni la kuboresha uhusiano wetu tena."



Mfalme hakuwa na namna ya kulikataa hilo. Aliona ni kheri, akaahidi kulifanya. Akaaga na kabla hajaondoka akaenda kuonana na Harid gerezani.



"Najua umemhifadhi, Melkizedek kwasababu ya Tattiana," Harid akamwambia mfalme. "Nimeshiriki naye kwenye hili kwanini yeye amepewa huruma?"



"Kwasababu ulimlazimisha alifanye kama malipo," mfalme akamweleza.



Harid akatabasamu kisha akamwambia mfalme.



"Mimi ni mzee. Kifo changu hakitajalisha sana. Mbali na hivyo umri wangu mwingi umeishia kuitumikia Goshen kwa kuwa mshauri wa mambo kadha wa kadha. Najua ambacho watakuwa wamekueleza. Nina uzoefu mkubwa na hayo mambo."



Akaweka kituo wakitazamana na mfalme. Kisha akauliza:



"Je, hawajakueleza kwenda kumtafuta mke kwa ajili ya mfalme wao ajae?"



"Hayo mambo hayakuhusu!" Mfalme akamkaripia. Mzee huyo akatabasamu kisha akasema:



"Kuwa mwaminifu, Phares. Hakuna msichana mzuri ndani ya himaya nzima kushinda Tattiana. Bado haujamuoa. Mtoe kwa ajili ya Goshen."



Mfalme akampuuzia. Akageuza mgongo wake aende. Harid akapaza sauti.



"Kama wewe hautawaambia kuhusu hilo. Mimi nitawaeleza!"



Mfalme akageuka na kumtazama Harid kwa jicho batili.



**



Koh!- Koh!-Koh!



Sauti ya kikohozi iliwashtua Fluffy na Zura. Walikuwa wamejikunyata ndani ya chumba chao chenye bakuli la mchele. Wakanyanyuka upesi na kuangaza kwenye chumba kingine, hamaki wakamwona Malkia na Waheed wakiwa wamejilaza wamechoka mno na wana majeraha kadhaa.



Wakawakimbilia na kuwauliza kulikoni. Malkia akawaambia wamepitia jaribu kubwa mno. Huko porini walipokuwa walikutana na watu wote wawapendao ambao walikufa huko miaka ya nyuma, na hawakuweza kuyashinda hayo kupata ufunguo pasipo kuwaua tu.



Wakiwa hapo mara wakasikia sauti ya kiume ikilia. Wakatazama chumba cha tatu, wakamwona Seth na Alk! Seth alikuwa anamimina machozi. Macho yake yalikuwa mekundu, mwili wake umejawa na mchanga. Wakamuuliza kulikoni?



Akawaleza amemuona baba yake baada ya miaka na miaka sasa kupita. Lakini si hilo linalomliza. Bali kumwona baba yake akifa mbele ya macho yake, mikononi mwa Alk.



"Hakuwa baba yako huyo!" Malkia akamtoa hofu.



"Ndio," akajibu Seth. "Hakuwa baba yangu, alikuwa ni jini na mara tulipommaliza akatupatia funguo. Lakini amenikumbusha baba yangu!" Seth akalalama. "Ni kitambo sana sijamwona."



Fluffy akamkumbatia Seth kumpa pole. Akamfuta machozi na kumtaka waendelee na safari. Washukuru wametoka wazima kwenye kila pambano. Kamwe haikuwa rahisi.



Basi wakaunganisha funguo zao na mara mlango mkubwa ukatokea ukutani. Wakaufungua na kuendelea kutembea.



Baada ya muda kidogo, wakakutana na watu watatu. Wanawake waliopendeza haswa. Wamebana nywele zao, wananukia na wamejipara wakavutia.



Wanawake hao walikuwa wakiongea kuhadithiana jambo fulani lililoonyesha kuwavutia. Lakini hawakuonyesha kama waliwaona wakina Malkia, wakapishana nao kama kivuli, wakaendelea na safari yao wakihadithiana mpaka wanapotelea.



Dakika mbili mbele, wakawaona tena wanawake hao. Sasa walikuwa wawili na si watatu kama mwanzoni. Walikuwa wamevalia majoho ya dhahabu, nywele zao ndefu wameziachia, wejipara usoni wakavutia, wananukia mithili ya bustani. Weupe waking'aa kama mwezi.



Walikuwa wana furaha wakihadithiana jambo. Na kama wale watatu waliopita, nao wakawapita wakina Malkia kama kivuli. Wakayoyoma wakiendelea kuhadithiana kwa furaha.



Mbele tena kidogo, wakamwona mwanamke mwingine akija. Sasa hivi alikuwa yu mmoja tu. Alikuwa amevalia joho la kupendeza akitembea taratibu anatazama chini. Alionyesha yu mpweke na hana furaha.



Alipowakaribia wakina Malkia akanyanyua uso wake na kuwatazama. Wakashtuka. Kinyume na wale wanawake wengine waliopita, huyu hakuwa mzuri hata kidogo. Mdomo wake ulikuwa umechanwa mpaka sikioni. Wanja aliokuwa ameupaka kuzunguka macho yake ulikuwa umevuja kwa machozi.



Akawauliza:



"Mimi ni mzuri?"



**





Malkia na wenzake wakatazamana. Hakuna aliyejibu. Mwanamke huyo akarudia tena swali lake akisisitizia.



"Mimi ni mzuri?"



"Ndio, ni mzuri!" Malkia akajibu kwa haraka. Basi yule mwanamke akamjongea karibu na kumtazama. Akachomoa kisu kwenye pindo la nguo na kutaka kumchana Malkia mdomo afanane naye.



"Kama mimi ni mzuri, acha nawe uwe mzuri!"



Malkia akamdaka mkono huo wenye kisu na kumzuia. Lakini mwanamke huyo alikuwa ana nguvu kupitiliza. Malkia hakuweza kufua dafu hata kidogo. Kisu kikamkaribia usoni kumchanja. Haraka wenzake wakamsaidia kumkomboa.



Wakamshika mwanamke huyo wa ajabu. Lakini nao hawakuweza kabisa. Kufumba na kufumbua wakarushiwa mbali kana kwamba ni midoli. Akiwemo pia na Alk - jitu la Azeth!



Mwanamke huyu hakuwa mtu wa kawaida bali jini. Jini la Urembo. Jini lenye nguvu. Jini linalotisha. Aligeukia jini ndani ya piramidi baada ya kutupiwa humo pamoja na Pharao.



Zamani alikuwa ni mwanamke mrembo mno ambaye alitamaniwa na kila mtu ndani ya himaya ya Misri. Alivutia kila alipopita si kwa mavazi tu bali harufu, ucheshi wake na upendo.



Lakini kiasili hakuwa mzaliwa wa Misri bali toka himaya ya Kijapani iitwayo YASHITA. Alikuwa ni binti wa mfalme aitwaye Haiku. Na akiwa bado mdogo baba yake akamtoa kwa Pharao kama njia ya kuimarisha mahusiano yao.



Hivyo akakulia Misri na kuwa gumzo kwa urembo wake. Akawa pia kipenzi kikubwa cha Pharao mbali na wake zake wengine, kitu ambacho kikasababisha chuki na hata hamu ya kumteketeza mwanamke huyo usoni mwa dunia.



Basi akafanyiwa visa kadhaa na wake wenza. Wakampandikizia chuki ya ubaguzi kwa wa Misri, wakamtenga na kumnyooshea kidole kila alipokuwa anakatiza.



Lakini hivyo vyote havikumfanya Pharao amchukie kipenzi chake hicho mpaka siku ya mwisho. Na hiki ndicho kikamgharimu mwanamke huyu. Akiwa kama kipenzi cha Pharao akatupiwa ndani ya piramidi pamoja na mumewe kwa kushindwa kumshauri abadili aina ya uongozi wake.



Sasa ndani ya piramidi amekuwa jini. Si binadamu tena!



Malkia na wenzake wakahangaika kupambana naye, ila wakaishia kubamizwa. Kupigwa na kutupiwa maili moja mpaka wakawa hoi. Kiu cha jini huyu kilikuwa ni kupasua mdomo wa Malkia ufananie na wa kwake.



Wakachukua kama dakika nane kupambana naye mpaka pale Seth alipopaza sauti kuita:



"Yeko!"



Jini akamtazama na kumsogelea. Alikuwa anamtazama kana kwamba anamfananisha Seth na mtu anayemfahamu.



"Yeko!" Seth akaita tena. "Wewe si mzuri, wala si mbaya. Wewe ni wa kawaida."



Haraka jini akamnyanyua Seth kwa mkono wake mmoja akimbana shingo. Akamtazama na macho yanayotisha alafy akamuuliza:



"Mimi ni mzuri?"



Seth akiwa amebanwa koo, na huku wenzake wapo hoi wasiweze hata kuja kumwokoa, akajitahidi kusema:



"Wewe si mzuri, si mbaya! ... wewe ni mwanamke wa kawaida."



Mara akaanza jini akaanza kudondosha machozi. Akanywea uso. Akamshusha Seth akimtazama kana kwamba mama amtazamavyo mtoto wake aliyeumia. Alafu asiseme jambo, akaondoka zake.



Seth akadaka koo lake na kukohoa mara kadhaa. Wenzake wakaja kumjulia hali hapo na kumuuliza aliyajuaje ya jini yule?



"Nilikumbuka nshawahi kusikia habari zake nilipokuwa mtoto. Kwenye moja ya kitabu toka Misri waliwahi kuandika habari za MALKIA TOKA NG'AMBO YA MBALI, ndani yake wakielezea malkia huyo alivyotoka YASHITA na kuja kuiteka Misri kwa urembo wake."



"Sasa mbona ukimwambia mzuri anakataa?" Malkia akauliza.



"Ukimwambia mzuri anaona unamkejeli kwasababu yeye si mzuri tena kama hapo nyuma. Na ukimwambia mbaya anajisikia wivu kwakuwa wewe utakuwa mzuri kushinda yeye. Hivyo kwa namna yoyote anataka kuharibu uso wako. Lakini ukimwambia wa kawaida kama wengine, basi anaridhika na kwenda zake."



Wakaendelea na safari yao. Wakatembea mpaka wakachoka miguu, wakaona wapumzike kidogo kisha wakaendelea tena na safari.



Mbele wakakutana na kikomo kukiwa na milango miwili. Kila mlango ulikuwa na rangi yake. Wa kwanza mweusi na wa pili mwekundu. Hapo Waheed akawaambia waupite ule mweusi.



Wakaufungua na kuzama humo. Kulikuwa ni giza tupu. Hawakudumu muda mrefu maginga yao ya moto yakazima yenyewe na kufanya sasa kuwa giza totoro!



Kwa uoga wakiwa wanapapasa, wakaendelea kutembea wasione hata wanapoelekea. Baada ya muda wa kama dakika nne, wakaona uwazi mdogo kwa mbali mbele. Ilikuwa ni sehemu ya kutokea. Mlango ulikuwa u wazi.



Walipotoka wakagundua mmojawao hakuwapo! Zura hakuwa pamona nao! Wakaangaza wasimwone. Wakataka kurudi ndani lakini Waheed akawaonya.



"Mtakaporudi huko, hamtatoka na mwingine mmoja!"



Kwa Malkia onyo hilo likawa upunguani. Hakutaka kuelewa hata kidogo, alitaka kwenda ndani kumtafuta Zura. Asingeweza kumwacha mwanamke huyo peke yake hata kidogo.



"Hakuwahi kuniacha hata siku moja. Kila nilipoenda alikuwa na mimi. Kila nilipomhitaji mama, alikuwa na mimi. Nitakufa nikimlinda," alisema Malkia macho yake yakiwa mekundu.



"Utakosa kofia ya Pharao!" Waheed akamkumbusha.



"Kofia ni nini mbele ya mama yako?" Malkia akamuuliza. "Waweza kumtoa sadaka mama yako kwasababu ya madaraka?"



Kabla hajangoja majibu akauendea mlango na kuzama ndani. Mlango ukajifunga. Wote wakabaki wameduwaa wanautazama mlango wasiamini kama Malkia amezama humo.



Wakangoja na kungoja. Kimya. Wakakaa hapo na hata kulala wakingoja. Bado kimya.



Muda ukazidi kuyoyoma.



Hatimaye Waheed akawaambia waondoke zao kuendelea na safari. Wakagoma. Wakamwambia watangoja hapo mpaka Malkia arejee.



"Ulikuwa unalifahamu hili?" Seth akamuuliza Waheed. "Ulikuwa unafahamu tukipita pale mmoja wetu atapotea?"



Waheed akakaa kimya.



"Ulikuwa unafahamu?" Fluffy akapayuka naye kuuliza. Wote wakamtazama Waheed kwa macho batili.



"Ndio, nilikuwa nafahamu," Waheed akajibu. "Nilikuwa nafahamu lazima wa mwisho atapotea, nafsi yake itaenda ndani ya mlango ule wa kiza."



"Kwanini ukatupitisha kama ulijua?" Seth akawaka kumuuliza.



"Kwasababu hiyo ndiyo ilikuwa njia pekee salama," Waheed akajibu. "Kama tungepita kwenye mlango mwekundu, wote tungekufa. Asingetoka yoyote. Lakini ndani ya mlango wa kiza mnauza nafsi moja kuokoa wengine."



"Mnauza?" Fluffy akastaajabu.



"Ndio, mnauza," Waheed akajibu. "Nauli ya kukatiza hapo inalipwa kwa nafsi moja. Lazima mmoja wenu afe kwa niaba ya wengine!"



"Kwahiyo hawatarudi?" Fluffy akauliza kwa woga.



Waheed akabinua mdomo wake.



"Utarudishiwaje pesa uliyotumia kununua bidhaa na wakati bidhaa hiyo umeshaitumia?" Waheed akauliza.



Kukawa kimya.



Muda ukapita wakiwa kimya.



"Twendeni, hatuna cha kufanya," Waheed akawaeleza. Kwa unyonge wakanyanyuka na kuendelea na safari wakiwa na mioyo mizito. Wakiwa na sura ya huzuni na mawazo kedekede kichwani. Walijihisi wapweke.



Lakini kwa upande wa Waheed yeye ilikuwa kinyume. Kifuani mwake alikuwa ametunza furaha. Moyoni mwake alikuwa na amani.



Alijikuta anatabasamu mara kwa mara kama mwehu.

Lakini Zura na Malkia wapo wapi? Nafsi zao zilizotumika kama nauli zimeendea wapi? Kujiunga na jeshi la wafu? Ama ndiyo zimeenda kule pasipo na njia tena ya kurudi?



Hakuna mtu anayejua. Kila mtu, hata wewe unajiuliza maswali haya. Lakini pengine ni wazi una matumaini. Bado unadhani watakuwa huko sehemu fulani. Wapo salama na hawajadhurika.



Si wewe peke yako unayewaza hayo. Kwa kuwafanya wapate amani ya moyo, ndivyo hata wakina Seth walivyokuwa wanawaza. Malkia na Zura wapo sehemu. Wapo salama. Wapo hai.



Japokuwa kila kitu kilikuwa kinapingana na mawazo hayo ila bado tu waliamini. Kama wasingeliamini hivyo hata hii safari wasingeendelea nayo.



**



Juu ya madhabahu pakawekwa mishumaa kumi na mbili, idadi ya mwezi katika ulimwengu wa kilozi, kisha kijakazi, mwanaume jabali, akapaza sauti yake kusema:



"Habti habti habti! Segoth kil vi njham!"



Wenzake wote waliokuwa chini ya madhabahu hiyo wakapaza sauti zao kuitikitia habti! Habti! Habti! Mara tatu.



Wote walikuwa wamevalia majoho meupe na kufanya eneo hilo kuonekana mithili ya anga lililojawa na ndege yange yange.



Baada ya kusema hayo, wakanyamaza kimya kana kwamba hamna mtu hapo. Punde akaonekana Venim akipanda hapo madhabahuni, mkononi alikuwa amebebelea kitabu kipana kikuukuu chenye kava gumu.



Yeye pekee ndiyo alikuwa amevalia joho jekundu. Na pia tena yeye pekee ndiye alikuwa ameachia nywele zake wazi. Wengine wote walikuwa wamejivesha viremba. Rangi nyeupe.



Madhabahu ilikuwa imezungushiwa mabakuli yaliyojaa damu. Kwenye kila kona kiliwekwa kiota chenye mayai matatu matatu ya ndege bundi. Na katikati kabisa ya madhabahu hiyo, kulikuwa na taswira ya mwezi angani.



Venim akaweka kitabu chake mezani, alafu akawatazama vijakazi wake waliokuwa wamejikusanya hapo na kuongea maneno kadhaa akiwataarifu nini wanafanya hapo na kwanini wanafanya hivyo.



Akiwa anateta kwa kujigamba akasema kwa kujiamini ni wakati wa kumrejesha Venet mahali anapostahili kwakuwa ana kisasi nao cha damu. Vijakazi wote wakafurahia wakinyoosha mikono yao juu na kupiga nduru.



Lakini kwanini wanafurahia kiasi hiki? Je hawakutaka mtu na kaka yake warejeshe familia yao?



Simulizi ilianzia mbali kidogo. Wakati Venet akiwa mlozi mbabe mwenye sauti na maamuzi ya kutetemesha anga, kila mtu alimtii na kumuogopa. Hata wale walozi wadogo wadogo walijikuta wakijisalimisha mikononi mwake na kuungana naye kama vijakazi.



Lakini baada ya Venet kudondoka, wote wakahamia kwa mdogo wake, Venim, kwakuwa yeye ndiye pekee aliyebaki mwenye nguvu na mamlaka. Kitendo hiki kikamghafirisha sana Venet. Si tu kwamba akaona mdogo wake amemsaliti, bali pia na wajakazi wake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



Akaapia kwa damu. Siku atakaporejea himayani, kwa mkono wake, atateketeza wote hao. Kila mwili utabakia kama jivu juu ya uso wa dunia. Watang'ata meno na kulia kwa uchungu.



Sasa nani anataka haya yamtokee? Kwa hali na mali inatakiwa Venet abakie Tanashe. Azeekee na kufia huko huko kwa usalama wao!



Venim akafungua kitabu na kuanza kupaza sauti kwa hali ya juu, wajakazi wake nao wakamfuatisha wakitengeneza ala ya muziki. Aliposoma kurasa tatu, mara anga lililokuwa jeupe likawa jeusi ti! Radi zikaanza kunguruma. Mabakuli ya damu yakaanza kutikisika.



Akaendelea kusoma na kusoma. Wajakazi wakaitikia kisomo. Damu zikaanza kukauka mabakulini. Na yale mayai ya bundi yakapiga nyufa!



Ardhi ikatetemeka. Upepo mkali ukakatiza na kuzima mishumaa yote. Na mara kipande cha mwezi kilichokuwepo angani, nacho kikayoyoma isijulikane kimeenda wapi!



Anga likawa jeusi kana kwamba ni usiku ama mvua nzito yataka kunyesha.



**



Akiwa ndani ya shimo, akastaajabu kuona anga likibadilika rangi. Moshi mzito mweusi ilikuwa unatanda angani, ukafanya bluu kuwa nyeusi tena nyeusi totoro.



Nani alikuwa anageuza mchana huu kuwa usiku? Akajiuliza akisogelea nondo na kuzidaka kwa mikono yake mipana. Akataka kujibadili kuwa kundi kubwa la popo, akastaajabu anashindwa.



Akajaribu kadiri ya uwezo wake akastaajabu anafeli. Akatoa macho kwa mshangao. Nini kinatokea? Anga lilikuwa jeusi, kwanini anashindwa kugeuka?



Akiwa kwenye bumbuwazi, akaona bundi wakikatiza angani. Wakilia milio ya ajabu. Wakitanua mbawa zao kana kwamba tai. Wakirandaranda huku na kule!



Hapa alichokiwaza kichwani akajikuta anakikataa. Hapana! Akasema akitikisa kichwa. Haiwezekani. Hapana! Akatikisa nondo kwanguvu.



Akatumia nguvu zake zote kutikisa nondo hizo atoke lakini hakuweza kabisa. Mwishowe akachoka. Akaketi akiwa amejawa na maji machoni.



Alijihisi mdhaifu. Mtupu. Mchovu.



"Zama zimekwisha Venet," akasikia sauti ikimwambia. Akatazama kuangaza lakini hakumwona mtu huyo.



"Zama zako zimeisha, yakupasa urudi ulipotokea."



Punde akamwona Venim! Alikuwa amesimama kandokando na mfalme Phares.



Akasimama akisaga meno. Akamtazama Venet kwa macho ya hasira. Akaukunja uso wake akiminya nondo kwanguvu.



"Ni wewe!" Akafoka. "Ni wewe Venim!"



Akafoka kwa sauti kali. Hakutaka kukubali kuwa mdogo wake amemshinda kwa mara nyingine tena. Hakutaka kuukubali udhaifu huu lakini ndiyo ulikuwa uhalisia!



Akiwa ndani ya mwili wa Rhoda akajimenya na kutoka nje. Akamlilia sana kaka yake amsaidie, asimtupe kama alivyofanya hapo awali lakini vyote hivyo vikawa nyimbo kwenye masikio ya Venim. Macho yake yalikuwa yanatazama mwili wa Rhoda ulioketi pembeni.



Alishajua fika kile anachokiongea Venet hakikuwa kitu akimaanishacho hata kidogo. Hakuwa pale kumsaidia bali kumwangamiza.



Punde Venet akamwona Venim akipokea kikopo kidogo cha chuma chenye mkanda wa chuma. Kikopo hiki kilikuwa kinafuka moshi mzito mweupe. Venim akachuchumaa kisha akaanza kufukizia moshi huo ndani ya shimo alilomo Venet.



Ndani ya muda mfupi moshi ukajaa humo, Venet akasikika akikohoa na akihangaika kuhema. Akitapatapa huku na kule.



"Pole, kaka. Namhitaji huyo mwanamke. Na wewe pia nahitaji urudi Tanashe," Venim akasema akitazama shimoni japo hakuwa anamwona Venet kwasababu ya kuzongwa na moshi mzito.

"Nakulaani, ewe mbwa!" Sauti ya Venet ikasikika moshini. "Nakulaani kwa kushirikiana na binadamu kwasababu ya mwanamke. Nakulaani kwa kufunga anga langu kwa kujaza bundi. Nakulaani kwa kuufunga mwezi angani. Nakulaani kwa usaliti wako.



Binadamu watakuwa anguko lako. Huyo mwanamke atakuwa anguko lako."



Baada ya hayo Venet hakuongea tena. Alikohoa mara mbili kukawa kimya.



Moshi ulivyotoweka, Venet akaonekana akiwa amejilaza chini asionyeshe dalili ya kuwa mzima. Venim akaamuru shimo lifunguliwe na watu hao wawili watolewe. Agizo likatekelezwa.



Venet akaenda kutupiwa ndani ya Tanashe. Rhoda akahifadhiwa vema kwa ajili ya Venim kwenda naye.



"Na mifuko yako ya dhahabu i tayari," mfalme alimwambia Venim.



"Mifuko gani?" Venim akastaajabu.

"Ile uliyosema tukuandalie kama malipo," mfalme akaeleza. Venim akakana kusema kitu hicho. Mfalme akajua kumbe Harid alidanganya.



"Naweza nikaondoka sasa. Nimeshamaliza kazi yangu," akasema Venim akimpatia mfalme mkono wa kheri.



**



Alipokuja kushtuka alijikuta kitandani. Hakukumbuka amelala usingizi huo kwa muda gani na hakukumbuka aliulala akiwa wapi.



Akatazama kando na kando. Chumba kilikuwa kikubwa na ukutani kulikuwa kuna mifupa ya binadamu, mpaka mafuvu.



Akaunyoosha mwili na kupiga mihayo. Akanyanyuka na kuendea dirisha, akatazama nje. Mazingira haya yalikuwa mageni. Hapana! Si mageni! Akalumbana kifuani mwake.



Akakunja uso wake kuangaza vema. Punde, mlango ukagongwa na Venim akaingia.



Rhoda akatoa macho.



Alah!



Alikuwa kwa Venim!



Kwa bashasha la furaha, Venim akamweleza mwanamke huyo kuwa amemrudisha kwenye uhai wake uliobebwa na walozi. Na sasa amekuwa wake. Amekuwa wake kamili!



Rhoda hakuelewa kitu hapa. Au tuseme hakutaka kuelewa kitu hapa. Akauliza:



"Mfalme alikupa ukaenda nami?"



"Ndio, kwa roho nyeupe," Venim akajibu akitabasamu.



Rhoda akatazama dirishani njia ya kuelekea Goshen. Akakamata nondo za dirisha na kusaga meno. Akatazama njia hiyo kwa sekunde kadhaa, alafu akasema kifuani mwake.



"Goshen, hata ukinitupia katikati ya mamba nikaliwe, bado nitarejea nikiwa nawaongoza mamba hao."





Sasa akakubaliana na kichwa chake kwamba kazi aliyonayo ni kutafuta namna ya kurejea tena Goshen. Arejee kwa nguvu zote. Arejee kama Malkia.



Huko ndipo alipozaliwa na ndipo atakapofia. Si pengine pale.



"Twende tukale malkia wangu," Venim akamwambia akimtoa hapo dirishani. Wakaongozana mpaka chini mezani. Rhoda alikuwa na njaa na hakuona haja ya kubisha. Tumbo lake lilikuwa tupu kwa kutokula muda mrefu.



Meza ikachafuliwa kwa masinia ya vyakula na mabilauri kedekede. Lakini Rhoda akashindwa kula. Hakukuwa na chakula cha kumridisha wala kuendana naye pale mezani.



Masinia yalikuwa yamejaa viungo vizima vizima kama vile macho, masikio ya wanyama mbalimbali na hata binadamu! Viungo hivi vilikuwa vimechemshwa tu na kutiwa siniani.



Kutazama bilauri, zote zilikuwa zimejawa na damu. Hazikuwa za mvinyo kama vile Rhoda alivyokuwa amewaza. Basi tumbo likaanza kumchefua. Akataka kutapika lakini hakuwa na kitu tumboni.



Haraka akatoka katika meza ile iliyokuwa inamkifu, akaenda zake kando akapate hewa safi. Pale mezani palikuwa pananuka, na kama angeendelea kuketi hapo basi angejikuta anapoteza fahamu kwa ubongo kukosa hewa ya oksijeni.



"Nini shida Malkia wangu?" Venim akamuuliza. "Je hujapenda chakula tulichoandaa kwa ajili yako?"



"Chakula gani kile?" Rhoda akafoka. "Unadhani mimi ni kama nyie kunilisha vyakula vya ajabu?"



"Samahani sana, Malkia wangu," Venim akamwambia akimshika mkono. "Ni makosa yangu. Hatufahamu nini binadamu hupendelea hivyo tukaandaa chakula chetu bora kabisa. Niambie unataka nini, nami nitakuletea mezani kufumba na kufumbua."



"Inawezekana?" Rhoda akauliza



"Hakuna kisichowezekana kwa Malkia wangu," Venim akamjibu. "Kama nilimtoa sadaka kaka yangu kwa ajili yake, nitashindwaje kumuwekea chakula mezani?"



Rhoda akatabasamu. Kauli hii ilimkonga moyo. Lakini pia ikaonyesha mwanzo mzuri kwenye harakati zake.



'Hakuna kisichowezekana kwa Malkia wangu.'



Akajikuta anatabasamu tena alafu kwa madaha akasema chakula anachokitaka na namna anavyopenda meza iwe. Ndani ya muda mfupi, meza ikajawa na nyama za kuokwa, mbogamboga mbalimbali na matunda ya kila aina.



Mabilauri yakajaa mvinyo mwekundu na meza ikapambwa kwa maua ya uwaridi. Pakavutia haswa. Sasa Rhoda akajongea kitini na kula atakavyo. Venim akawa anamtazana Rhoda akitafuna na kunywa. Moyoni akajihisi faraja.



Alikuwa anapenda kila kitu kuhusu Rhoda. Alifurahi sana kumwona mwanamke huyo karibu yake na akajiapia hatomruhusu tena aende mbali na upeo wa macho yake.



Ilikuwa ni kama bahati mwanamke huyo kurejea tena mikononi mwake. Ulikuwa ni kama muujiza. Akajiwekea agano la kumlinda kadiri ya uwezo wake na kuhakikisha mwanamke huyo anapata furaha mbele ya macho yake.



"Venim," Rhoda akaita akiwa ameshikilia kipande cha nyama mkononi.



"Itapendeza ukiniita mumeo," Venim akamrekebisha kwa tabasamu na kumuuliza: "Unasemaje Malkia wangu?"



"Nina ombi moja mume wangu," Rhoda akasema kwa sauti ya chini. Venim, moyo wake ukiwa umepozwa na sauti hiyo, akauliza kwa staha:



"Lipi hilo?"



"Nataka unifunze ulozi," Rhoda akajibu kwa uhakika. Venim akastaajabu. Ila si kwa ubaya, alipenda wazo hili. Hakutegemea kama Rhoda angelipenda kujua ulozi. Sasa akaona dhamira yake ya kuwa Malkia kamili wa himaya yake inaenda kutimia.



"Kweli unataka kujua, malkia wangu?"



"Ndio. Sidhani kama ni vibaya?"



"Hata kidogo. Nitajivunia kukuelekeza hayo. Ukiyajua, utajua Malkia wa himaya yangu vema. Tutatengeneza himaya imara na yenye nguvu kuwahi kutokea."



Rhoda akatabasamu. Akaupumzisha mdomo wake kuongea akaendelea kutafuna, lakini kichwani mwake akiendelea kuyapanga mambo. Hakutaka kupoteza muda kabisa. Kila sekunde kwake ilikuwa inahesabika.



Ilikuwa na thamani mpangoni mwake.



**



"Vipi, mmepaonaje hapa kwangu?" Aliuliza kuhani Raam akikuna ndevu zake nyeupe. Mbele yake alikuwa wamesimama Oragon na Ottoman wakiwa wamevalia nguo nadhifu. Sasa wamekuwa vijakazi wa mwanaume huyo maarufu himayani kama kuhani.



"Tunakushukuru sana," akasema Oragon. "Hatukuwa na pa kwenda ukatupatia hifadhi. Hata hapa si tu tunaishi bali tunapata kila hitaji letu."



Raaam akatabasamu.



"Msijali. Kuleni na mnywe. Ishi kama mpo nyumbani. Binadamu tuneumbwa kutegemeana na kusaidiana."



"Ahsante sana," Ottoman akasema akikumbatisha viganja vyake. "Hatuna cha kukulipa kabisa. Umekuwa mkarimu sana kwetu."



Raam akaenda zake. Oragon na Ottoman wakaendelea na kazi zao za hapa na pale lakini kumbe Raam alikuwa amesimama kwa mbali akiwatizama.



Akikuna ndevu zake, akawatazama wanaume hao kwa muda wa dakika kadhaa kisha akatabasamu tena na kwenda zake akiyoyoma sasa.



Vijana wale wa Harid wakamaliza kazi zao na kuketi mezani kujipatia chakula cha mchana. Ndani ya muda mfupi, wakaja wanaume wengine wawili, ambao nao walikuwa vijakazi wa Raam, wakaungana nao mezani kula.



"Ni raha iliyoje mnaipata hapa?" Akauliza Ottoman. "Mnakula kama si vijakazi. Mnavaa kama si vijakazi. Mna uhuru kama wanawe!"



Vijana wale wawili wasiseme jambo wakamtazama Ottoman kisha wakaendelea kula. Kukawa kimya kidogo kabla Oragon hajauvunja kwa kuuliza:



"Raam hana familia?"



"Hana," akajibu kijakazi mmoja. "Anaishi mwenyewe na vijakazi wake."



"Na uzee wake wote, hana hata mtoto wa kurithi mali zake na kumlinda?" Oragon akaendelea kuuliza.



"Hana," akajibu kijakazi mwingine. "Umwonavyo ndivyo alivyo."



"Kwanini?" Ottoman akadakika kuuliza.



Wale vijakazi wawili wakatazamana alafu mmoja wao akasema:



"Msijali. Kadiri mnavyoendelea kukaa hapa mtafahamu kila jambo. Kwahiyo tunzeni macho na masikio yenu."



Oragon na Ottoman wakatazamana. Hawakuuliza tena wakajaza midomo yao na vyakula.



**



"Nakuomba mara moja," ilikuwa sauti ya Raam ikimwambia Oragon. Majira yalikuwa ni usiku. Oragon alikuwa akifutafuta buibui konani mwa nyumba.



Akaacha kazi yake na kuitikia wito. Akaongozana na Raam mpaka chumbani kwake, Raam akaketi kitandani wakati Oragon akiwa amesimama.



Raam akamtazama Oragon kisha akamwambia

"Njoo uketi hapa," akionyeshea mkono kandokando yake.



"Hapana," Oragon akajibu. "Hapa panatosha tu mkuu."



Raam akaminya mdomo wake na kuuliza:



"Kuna kitu nilishawahi kukuomba tangu umekanyaga hapa?"



"Hapana," Oragon akajibu akitikisa kichwa.



"Basi hiki ndiyo cha kwanza," Raam akasema. "Njoo ukae hapa!"



Oragon akatii agizo. Akaenda kuketi kando na Raam. Raam akatabasamu. Akaweka mkono wake begani mwa Oragon alafu akamwambia mwanaume huyo:



"Tangu siku ya kwanza nilipowaona, nilivutiwa nanyi. Mlionekana vijana watanashati, wenye nguvu zao. Nisingeweza kukataa kuwasaidia."



Akiwa anaongea hayo akawa anasogezasogeza pua yake shingoni mwa Oragon. Oragon akakereka mno lakini akazuiza hasira zake.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Niliwaona mkiwa watupu hamna nguo. Hicho kikawa kitu changu kizuri kabisa kukiona kwa siku hiyo nzima. Miili yenu iliyojawa misuli na umbo la ukakamavu. Hakika mlinivutia."



Akatulia kimya. Oragon akasali moyoni mwake isiwe kama ambavyo ameshaanza kuwaza. Mwili ukamtetemeka. Akatamani hata ayayuke na kupotea.



"Natamani niwaone kama nilivyowaona siku zile," Raam alimnong'oneza Oragon sikioni, kisha akamng'ata kidogo. "Unaweza ukanionyesha tena uufanye usiku wangu kuwa wa kipekee?"



Oragon akashindwa kuvumilia. Akanyanyuka haraka na kumtazama Raam kwa macho ya mshangao. Akamuuliza:



"Ni nini unataka kwangu?"



Raam akacheka.



"Ni mjinga tu ndiye atakuwa hajanielewa ni nini nataka," akajibu akitazama sehemu za siri za Oragon.



"Siwezi!" Oragon akafoka. "Sahau kabisa hilo. Siwezi nikafanya huo ushenzi!"



Raam akaguna kwa kebehi kisha akanyanyuka.



"Pengine wewe ni mgeni inabidi nikupe elimu kidogo. Ndani ya himaya hii mimi ni kuhani. Kila mtu ananiheshimu na kunisikiliza. Unadhan kama ukikataa nitakuacha hai uende huko kutema maneno?"



Akapiga hatua kumsogelea Oragon.



"Utachagua moja. Unihudumie ama nikuue kisha nikuzike asijue mtu yoyote yule!"



Raam akavua nguo zake na kubaki mtupu. Akamsogelea Oragon kwa ukaribu na kuweka mkono wake sehemu za siri za mwanaume huyo. Akazipapasa akitabasamu.



Oragon akakosa uvumilivu. Akamsukuma Raam kwanguvu, mzee huyo akadondoka na kujikita kichwa kwa mbao ya kitanda. Akakata moto.



Oragon akatoa macho kwa mshangao.



**



"Ottoman, amka! Amka twende!" Oragon alipaza sauti akiunyaka mkono wa kaka yake na kumvuta toka kitandani.



"Nini? Mbona hivyo?" Ottoman akastaajabu.



"Nahisi nimemuua Kuhani!" Oragon akajibu kwa sura ya mkanganyiko. "Twende kabla hatujakamatwa!"



Lakini getini kulikuwa kuna walinzi. Wanaume watatu waliobebelea silaha. Wangefanyaje?



Na wakiendelea kukaa hapo, sebuleni wakiwa hawajui la kufanya, wale vijakazi wengine wawili watakawakuta. Watawaacha?



**

Hakukuwa na namna. Iliwabidi waruke ukuta kwa kusaidiana wakatokea huko upande wa pili na kuanza kukimbia. Hawakujua wanapoelekea ila alimradi waondoke na kuacha mbali nyumba ya kuhani huyo.



Walipokimbia sana, wakasimama wapumzike. Mapafu yalikuwa yamekaukiwa. Wakashika magoti yao wakihema kama mbwa.



Walikuwa wanavuja jasho haswa. Macho yamewalegea kana kwamba wamepigwa na moshi. Ottoman hata akaketi chini baada ya kuhisi viungo vinamuuma haswa.



Hapa ndiyo akamuuliza mwenzake, nini kilimsibu kujaribu kumuua kuhani? Oragon akamwambia mwanaume huyo alimtaka kimapenzi.



Ottoman akatoa macho.



"Una maanisha nini?"



"Alitaka nimlale!" Oragon akajibu kwa midadi.



Ottoman akashika mdomo wake kwa mshangao. Ilikuwa ngumu kuamini mzee yule, mwenye nafasi yake kubwa ndani ya himaya, alikuwa na michezo hiyo.



Kumbe ndiyo maana hana mke wala mtoto! Wakang'amua. Lakini sasa tunafanyaje na wapi tunaenda? Swali lilikuwa hapa. Na wapi pia watapata chakula?



Wakakaa hapo kama kinda za ndege zilizompoteza mama yao. Na kwakuwa walitoka mbio kwa kuhani, hawakuwa wamebeba chochote kile mikononi mwao. Hata 'vituguo' vya kujihifadhi ama kujifunikia.



Wakalala wakiwa wamejikunyata, miili yao ikipambana na baridi kali. Wakisimamisha masikio yote kusikia ujio wa shari toka pande yoyote ya dunia.



**



"Mbona nakuita muda wote huo, hukunisikia?" Raam alifoka. Alikuwa yupo uchi chini sakafuni akiwa ameshikilia kichwa chake kinachomimina damu. Sakafu ilikuwa imetapakaa damu. Na mwili wake ulikuwa umeshika damu upande wake wa kushoto alioulalia.



Mbele yake alikuwa amesimama bwana Marimari mmoja wa vijakazi wake wa ndani.



"Sikukusikia, mkuu," akasema Marimari. Alikuwa amepigwa na butwaa kumwona mkuu wake katika hali ile aliyomkuta.



"Wako wapi wale vijana wapya?" Akauliza Raam. Kabla hajasubiria majibu akaagiza: "wakamateni na muwamalize mara moja!"



"Hawapo!" Marimari akampasha. "Sijawaona kwa muda sasa hapa ndani hata nikajua umewatuma huko nje."



Raam akashika kichwa chake kwa maumivu. Habari hizo zikamuumiza kichwa zaidi. Akajitahidi kunyanyuka akisaidiwa na Marimari, akajiveka joho jepesi na kutoka ndani kwenda kuonana na walinzi wake langoni.



Akamtaka abakie mlinzi mmoja tu, hao wengine wote, pamoja na wale ambao hawapo zamu, wajumuike wakawatafute wakina Oragon popote pale walipo.



"Mtakapowakamata, muwamalize asijue mtu yeyote yule. Sawa?"



"Sawa, mkuu!" Wakaitikia kwa ukakamavu.



"Ni wageni himayani hivyo hawatawasumbua kabisa. Mkiulizia mtawapata kwa urahisi, na hata wakichangamana na wenyeji mtaweza kuwachambua. Vilevile mkiwaua hakuna atakayewaulizia wala kusumbuka nao," Raam aliwapasha zaidi. Baada ya maelezo hayo, wanajeshi wakaenda zao kwenda kuwasaka vijana hao.



**



Kwa mbali wanaume wawili walionyeshea kidole upande wao wa kulia wakinong'onezana. Mmoja alikuwa mwanaume mfupi na mwingine mrefu. Kwakuwa ilikuwa giza, ilikuwa ngumu kuwatambua.



Baada ya kunong'onezana huko wakasogea kwa haraka na kusimama mbele ya wanaume waliokuwa wamejilaza chini.



Walikuwa ni wakina Oragon!



"Nyie!" Wakawaamsha wakiwasukuma na miguu. "Amka! Amka! Amka!"



Wakina Oragon wakamka kwa hofu kubwa wakidhani wameshatiwa nguvuni. Walipotazama vema wakagundua ni wale wanaume waliowakwapulia kila kitu chao. Wakataka kuzua ugomvi, lakini mara wanaume wale wakachomoa jambia zao na kuwatishia kuwanyofoa uhai.



"Tulieni hivyo hivyo kabla hatujawatoboatoboa!"



Wakanywea akama ukili majini. Wanaume hao wakawasachi mifukoni lakini hawakupata kitu. Badala yake wakina Oragon ndiyo wakawaomba wawafadhili kwani hawana mbele wala nyuma.



"Naomba mtupatie fedha kidogo," akasema Oragon. "Hatuna hata cha kutia mdomoni."



Wale wanaume wakatazamana, alafu yule mfupi akarudishia jambia lake kiunoni na kuwaambia kama wanataka kula basi waungane nao la sivyo waozee hapo.



"Mnafanya shughuli gani?" Ottoman akauliza.



Wanaume hao wakacheka alafu mrefu akasema:



"Yani mpaka sasa hamjajua tu tunafanya shughuli gani?"



Kisha wakacheka tena.



**



"Mwambie ntalizingatia, anipatie muda tafadhali," alisema Phares akimwambia mwanaume mgeni aliyekuwa ameketi naye. Mwanaume huyu alikuwa ana ndevu za wastani, nywele nyeusi ti ndefu mpaka begani, na kwenye kifua chake upande wa kushoto alikuwa ametundika alama ya ndege, ishara ya himaya ya Maam.



Mwanaume huyo, mjumbe wa Maam, akanyanyuka na kumpatia mkono mfalme.



"Nitamfikishia habari hizo, lakini nisiwe muongo, hamna muda wa kungoja tena. Keshokutwa anaapishwa kuwa mfalme na hawezi akaapishwa pasipo kuwa na mke."



Mjumbe huyo akashusha pumzi ndefu na kutengenezea nguo yake.



"Kwahiyo kiuhalisia muda ulionao ni kesho tu mpaka majira ya jioni," akasema mjumbe kisha akaondoka zake mfalme akimsindikiza kutoka naye nje. Mjumbe huyo alipoyoyoma mfalme akarudi zake ndani akiwa na mawazo.



Sasa ni rasmi kijana wa mfalme alikuwa anamtaka Tattiana akawe malkia wake. Harid alishampasha habari kijana huyo kuwa Tattiana ndiye mrembo himaya nzima.



Na ubaya zaidi, hata mjumbe huyu aliyetumwa kuja hapo himayani, alikutana na Tattiana akasadiki hayo maelezo. Akasema Alah! Kweli huyu afaa.



Sasa afanyaje?



Mfalme akahisi kichwa kinamuuma. Hakuwa radhi kumpoteza Tattiana hata kidogo.



**



Ni usiku sasa. Tattiana hakuwa katika chumba kimoja na mfalme kama inavyotakiwa, bali katika kile chumba alimokuwa anaishi malkia Vedas.



Humo alikuwa tayari ameshafungua kabati na kuchukua chupa ile ya maajabu. Anaitazama na kujiuliza maswali kichwani.



Anaisikiliza chupa hiyo na kusikia ikidunda mapigo ya moyo. Anasikiliza tena na kuhakiki kweli, yalikuwa ni mapigo ya moyo.



Leo anapata wazo na kuanza kung'amua kitendawili hiki. Alijiuliza:



"Nimelala na mfalme kwa muda wote huo, amekuwa baridi mpaka nashindwa kulala. Lakini pia sijawahi kusikia mapigo yake ya moyo, hata nilipolaza kichwa changu kifuani mwake.



Ina maana hana moyo?" Akajiuliza akitazama chupa ile.



"Au moyo wake ndiyo huu chupani?"



Habari hiyo ikaleta mantiki.



"Lakini nani kauweka moyo huo humo? Inawezekanaje mfalme akaishi na huku moyo wake upo chupani?" Maswali hayo yalimpasua kichwa. Na kama haitoshi basi, yule kiumbe anayetoka nje ya chupa pale ifunguliwapo, ni nani?



Akakumbuka yale maneno yake: "Nefil njhami khatu habab?" Anamaanisha nini?



Ikiwa ni usiku sasa mkali, akiwa ndani ya mawazo haya, mara anasikia harufu ya ajabu. Akanusanusa kuhakiki. Hakuijua harufu hiyo ni ya nini. Na kadiri na muda ilikuwa inaongezeka!



Akashindwa kuipuuzia. Akaificha chupa kabatini na kuanza kuifuatilia harufu hiyo. Akafungua milango na kutembea akikatiza korido kadhaa akiacha pua ifanye kazi yake.



Mwishowe akajikuta amefika kwenye kingo ya kasri. Kwenye kakona kidogo alikuwa amesimama Bella akiwa ameshikilia miti kadhaa mikononi mwake. Miti hii ilikuwa inafuka moshi mweupe.



"Bella," Tattiana akaita. "Unafanya nini hapo muda huu?"



Bella hakujibu. Akawa anamtazama Tattiana kana kwamba alikuwa anamtarajia. Tattiana akasogea karibu zaidi. Kuangaza akaona askari kadhaa wakiwa wapo chini.



Hakuelewa kilichokuwa kianendelea pale.



"Bella, unafanya nini hapa? Na hao maaskari mbona wapo chini?"



Tattiana akawatazama vema wale maaskari. Akagundua walikuwa wamekufa. Macho na midomo yao ilikuwa wazi!



Akamezwa na hofu. Lakini kufumba na kufumbua, kabla hajatenda hata jambo, akasukumizwa kwanguvu na mtu tokea nyuma. Akajigonga na kizuizi cha kibaraza, akabinuka na kudondokea chini!



Bella na Lucy, aliyetokea nyuma, wakamtazama. Lucy akabinua mdomo wake na kusema:



"Amekwisha."



Bella akamalizia.



"Tufanye upesi!"



Baada ya muda mchache, ikagundulikana Tattiana amedondoka chini. Hata mfalme akaamshwa na kujuzwa hilo. Ilikuwa bado ni usiku wa manane. Tattiana hakuwa anajielewa, na kama kuna hatua basi za kuelekea kifoni, yeye alikuwa amebakiza moja tu.



Hakuwa anaelewa chochote kile. Hakuwa hata na punje ya fahamu. Alipoteza damu nyingi. Mifupa yake mingi ilikuwa imevunjikavunjika. Hata kama angelipona, basi kamwe asingeliweza kurejea kwenye hali yake ya kawaida.



Angeweza kupooza mwili ama kuwa mlemavu wa kudumu.



Mfalme akachanganyikiwa sana. Ni nini kilitokea? Tattiana alifika huko kufanya nini? Ilikuwaje akaangukia chini? Vijakazi wote pamoja na walinzi wakaitwa na kuulizwa kilichotokea.



Nani alimwona Tattiana na mpaka anadondoka walikuwa wapi?



Kukawa kimya. Hakuna aliyesema jambo. Kila mtu aliogopa kwani kama ingebainika anahusika, angechukuliwa hatua kali maana mfalme anampenda sana Tattiana.



Lakini baadae, baada ya kubanwa sana wakitishiwa kufungwa maisha yao yote, Bella kwa uoga akasema huwa anamwona Tattiana majira ya usiku akizungukazunguka.



"Sijui huwa anafanya nini," akaeleza. "Ila si mara moja wala mbili."



Kidogo naye mmoja wa wanajeshi walinzi wa kasri akasema pahali pale alipotelezeaTattiana na kudondoka palikuwa pana mafuta. Hicho ndicho kimemwangusha.



Maneno haya yakawa mengi sana lakini ukweli ukabakia kwamba mtu pekee atakayetoa taarifa sahihi ni Tattiana na si mwingine. Mdomo wake ndio pekee utakaoeleza ukweli wa mambo.



Lakini sio leo wala kesho. Mwili wake ulikuwa umekusanyiwa kitandani daktari akihangaika kuokoa uhai wake.



"Itachukua muda mrefu sana kurejea. Amedondoka vibaya na kuathiri uti wake wa mgongo," daktari alieleza.



Mfalme akamsihi arejeshe uhai wa mwanamke huyo kwa namna yoyote ile. Hatamwelewa kabisa mwanamke huyo akifariki. Yupo tayari kwa gharama yoyote na chochote atakachohitaji atampatia.



"Umenielewa?" Mfalme akamkaba daktari.



"Ndio, nimekuelewa," daktari akasema kwa hofu.



Baadae taarifa zikasambaa himaya nzima. Melkizedek na mkewe wakashtushwa mno na habari hizo hata wakafunga safari upesi kwenda kumwona mtoto wao.



Mama alipomwona akalia sana. Akamuuliza mwanaye aliyekuwa hamsikii, nini ilikuwa shida? Kwanini amejiingiza matatizoni hivyo?



Kwa uchungu aliokuwa nao, hakutaka kurudi na mumewe nyumbani. Alitaka kubaki na mwanaye hapo kasrini anapotibiwa. Kwa mfalme hakuwa na shaka, akaona kheri.



Mama huyo akaketi kandokando ya mwanae akimtazama, machozi yanambubujika.



"Nitahakikisha kila kitu kinakuwa sawa," mfalme alimtoa hofu Melkizedek. "Nitampatia kila huduma na ulinzi wa kutosha. Usijali."



"Nashukuru sana," Melkizedek akampatia mkono mfalme. "Natumai mkononi mwako yupo salama."



Mfalme akamsindikiza mpaka nje, bwana huyo akaenda zake.



**



"Sasa tunafanyaje?" Aliuliza Bella akimtazama Lucy aliyekuwa amejilaza kitandani. Walikuwa ndani ya chumba peke yao. Wakati Lucy akiwa amejilaza miguu ipo chini, Bella alikuwa ameketi kitako.



Wote walionekana kutingwa na mawazo. Hawakuwa na raha. Hawakuwa na amani.



"Mimi nilidhani atakufa!" Akalalama Lucy. "Mwanamke ana roho ngumu yule. Kudondoka kote huko!"



"Tunafanyaje sasa?" Bella akarudia swali lake ambalo halikupatiwa jibu. Alikuwa ana hofu mpaka anatetemeka. "Akiamka si atatutaja?" Akaendelea kulonga. "Na akitutaja si ndo mwisho wetu huo!"



"Usijali," Lucy akampoza. "Hawezi amka yule. Hata akiamka atakuwa bubu, si kwa namna alivyodondoka."



"Mmh," Bella akaguna. "Unadhani itakuwa hivyo? Mfalme ameweka madaktari wote nguli ndani ya himaya wamtimbu mtu mmoja. Unajua hilo?"



"Najua!" Lucy akajibu akinyanyuka. "Lakini kifo kamwe hakizuiliki hata uwe na madaktari wangapi. Kikija kinakuja tu. Cha muhimu ni kumtazama kwa jicho makini. Tukimwona anapata ahueni, ama anaelekea kupona, basi tunammaliza!"



"Utaweza kwa namna anavyolindwa vile?" Bella alikuwa na shaka.



"Inawezekana!" Lucy akajibu akibinua mdomo. "Hakuna lisilowezekana, kumbuka tupo chini ya paa moja."



Kisha akauliza:



"Zile maiti umezihifadhi vizuri?"



"Za wale maaskari?" Bella akauliza.



"Ndio, kwani kuna zingine?" Lucy akabweka.



"Nimezihifadhi pazuri hamna shaka," Bella akachonga.



"Sasa inabidi tumalizie lile zoezi letu," Lucy akahusia. "Ila itabidi tutulie kidogo kwani kwa sasa ulinzi utakuwa mkubwa sana."



**



Baada ya kutembea kwa muda mrefu, Waheed akawaasa wapumzike angalau kidogo wavute pumzi. Wakaketi na kunywa maji kulainisha makoo yao.



Kulikuwa na ka giza hafifu kama vile jioni. Walitulia hapo kana kwamba wapo msibani. Hakuna mtu aliyekuwa anamwongelesha mwenzake wala kuongea. Hawakuwa na furaha. Haikuhitaji kusoma vitabu kulijua hilo.



"Tutadumu humu mpaka siku gani?" Fluffy akauvunja ukimya. Aliuliza akiwa amejikunyata kana kwamba anasikia baridi kali.



"Siku tatu," Waheed akajibu. "Vipi kuna tatizo?" Kisha akauliza.



Fluffy akamtazama kama mhaba wa matumaini, alafu akasema:



"Nataka kutoka nje."



Wenzake wote wakamtazama.



"Nataka kwenda nyumbani na kuachana na haya yote," akaongezea. Na punde macho yake yakawa mekundu kama bendera. Mara yakavujisha maji.



"Usilie, Fluffy," Seth akamuasa akimshika bega. "Yote yanakaribia kwisha. Tumeshamaliza."



"Sidhani," Fluffy akajibu akivuta makamasi. "Nimechoshwa na haya. Nini maana ya safari hii kama tunatoka tofauti na tuliongia? Hata tutakapopata hicho tunachokihitaji, nini itakuwa furaha yake?"



Maneno haya yakamgusa kila mmoja isipokuwa Waheed. Alikuwa anamtazama mwanamke huyo kwa mapuuzo akitamani hata kumziba mdomo.



"Tumehangaika mno kufika hapa, alafu tunakuja kupotezea hapa! Yale yote ya mwanzoni yanakuwa bure? Tuliyafanya yanini?" Fluffy aliendelea kumwaga maneno.



Alikuwa na uchungu kifuani mwake na kadiri alivyokuwa anaongea ndivyo akawa anazidi kuupata zaidi. Machozi yalizidi kummiminika na ikafikia pahala akawa hawezi hata kuongea.



Kifua kilimbana. Kwikwi zilimzidi na kuubana ulimi. Seth akahangaika kumbembeleza pasipo mafanikio. Ikafikia kipindi sasa Waheed akashindwa kuvumilia.



Akatamani kuropoka, ila akaona hamna haja hiyo. Akajitahidi sana kudumu na hasira yake. Alisimama akawaambia waondoke kwani muda wa kupumzika sasa umekoma. Alifanya hivyo kukatisha yaliyokuwa yanaendelea.



Basi wakanyanyuka na kuendelea na safari yao. Wakatembea kwa umbali wa nusu kilomita kabla hawajakutana na njia panda. Hapo wakasimama kidogo kutafakari.



Lakini ndani ya Waheed kulikuwa na roho ya kidhalimu. Roho ya kinyama.



Katika hali ya mshangao akachomoa kisu chake kiunoni alafu haraka, kufumba na kufumbua, akamkita Alk kifuani, akamkita pia na Fluffy!



Wakadondoka chini wakiugulia maumivu makali. Waheed, pasipo huruma, akamkita pia na Seth aliyekuwa hawezi kujitetea kwa kujaa na majeraha miguuni.



Wote wakalala chini wakiwa wanavuja damu lukuki, kisu cha Waheed kikichuruza kwa kushiba damu.



Waheed akatabasamu. Sasa alikuwa amekamilisha kazi. Akasimama kuwatazama watu hao wakikata roho. Na walipotimiza zoezi hilo, akaendelea na safari yake roho ikiwa nyeupe.



Hakuwahitaji tena watu hao. Hawakuwa na faida tena kwake. Alikopita huko ndipo alipokuwa anawahitaji kama sadaka. Sasa aendako ni kushuka tu. Anaweza maliza mwenyewe.



Akatembea akiwa ana furaha. Anajihisi mwepesi akifahamu fika, safari yake inakaribia kukoma na hivyo basi ataanza kula matunda ambayo alikuwa anayatamani kwa muda mrefu.



Matunda ambayo alikuwa anayapigia mahesabu tangu alipokuwa kijana.



Nani hataki madaraka bana? Waheed alijiona kichwani mwake akiwa mtu mkubwa mno. Mtu anayesikilizwa na kuheshimiwa. Lakini zaidi mtu anayeogopeka!



Alijiona akiwa ana ubavu, amezungukwa na dhahabu na vitu vya thamani. Akiwa tishio mpaka himaya zingine.



Mate yakamtoka.



Hatimaye ndoto yake hii ilikuwa inaelekea kutimia. Ndoto aliyoivutia subra kwa miaka nemda rudi. Sasa atakapoitia kofia hiyo mikononi kila mtu atajua kumbe hakuwa Waheed.



Kumbe hakuwa punguani bali mtu anayejielewa. Mtu wa maana na mwenye malengo yake!



Alilenga haswa kuuthibitishia ulimwengu juu ya hilo ...



**



"Umekunywa chai nlokuandalia?" Aliuliza bibi akimtazama kwa macho ya huruma.



"Hapana, sijanywa," akajibu kwa sauti ya chini. "Sijiskii kula chochote kile."



Bibi akashusha pumzi alafu akaketi na kumtazama mwanamke huyu, mke mkubwa wa Sultan.



Afya yake bado haikuwa imerejea kama hapo awali japo kidogo ilikuwa kheri. Alikuwa amevaa joho pana na uso wake wake haukuwa umeparwa hata kidogo. Ulikuwa umepooza na kunywea.



"Sasa kama usipokula mjukuu wangu, huoni tutarejea kule kule tulipotokea? Sultan hatapendezwa na hili hata kidogo," bibi alisema akimwekea mkono begani. Japo huyu mwanamke hakuwa mjukuu wake, alijitahidi kumwonyesha upendo.



Alitaka arejee katika hali yake. Lakini si kurejea kule kasrini. Lah! Kule kasrini alikuwa anataka mjukuu wake aendelee kukaimu.



"Sultan!" Akasema mke huyu mkubwa kwa uchungu. "Hanijali tena. Hana muda na mimi. Hanipendi tena. Hajui nimefanya yote haya kwasababu yake. Amesahau nimekuwa hivi kwasababu ya pumzi yake!"



"Usiseme hivyo mjukuu wangu," bibi akambembeleza. "Sultan bado anakupenda. Na hata iweje bado wewe utabakia kuwa mkewe daima."



Sultana mkubwa akajikuta akibubujikwa na machozi. Alihisi upanga unachana moyo wake alipokumbuka mahaba ya Sultan. Namna mwanaume huyo alivyokuwa anamkarimu na kumwonyesha kila aina ya upendo.



Leo yupo hai, ila kamsahau kana kwamba kafariki!



"Tangu alipoondoka hapa hajawahi kurudi hata siku moja kunijulia hali. Hata kutuma vijakazi wake kuja kuniulizia, hakuna! Ni upendo gani huo unaousema?" Sultana akalia. Hata bibi akambembeleza pasipo mafanikio.



Lakini pia ndani ya kifua cha bibi huyu moyo ukamchoma na kumsuta. Alijionea haya kwa kila chozi alilodondosha mwanamke huyo kwani mkono wake uliokuwa unambembeleza nao ulikuwa unahusika kumliza.



Alikuwa anajua kila kinachoendelea hapo. Alikuwa anafahamu fika kwanini Sultan hakuwa anakuja kumsalimu mke wake wa kwanza kwa maana alimpatia mjukuu wake dawa.



Dawa ya kumpumbaza Sultan. Dawa ya kutia kwenye pindo la nguo la mwanaume huyo na ya kumwagilia njiani apitapo.



Sultan akamsahau kabisa mkewe wa kwanza. Si tu yeye bali wanawake wote kwake wamekuwa vinywesi.



Baada ya kushindwa kumbembeleza Sultana, bibi akaenda zake chumbani kuupooza moyo wake. Kadiri alivyokuwa anamwona Sultana akilia kwa uchungu, naye akajikuta anaumia. Alijilaza kitandani na kuwaza.



Akawaza.



Akawaza.



Hakuwa na cha kufanya. Akapiga moyo konde Sultana atazoea hali kadiri muda uendavyo, japo alikiri ilikuwa ni ngumu.



Akadumu humo chumbani mpaka akasikia Sultana amenyamaza. Akajishauri kwenda kumuona, lah! Akaona hamna haja, ngoja atulie avutevute muda kwanza. Pengine akienda huko upesi anaweza akamtifua tena kidonda.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

**



"Ameenda!" Alisema kijakazi akitoa macho. Alikuwa ni mwanamke aliyejisitiri mwili wake kwa nguo ndefu na kiremba kichwani.



"Ameenda wapi?" Bibi akauliza upesi. Macho yamemtoka pima. Alikuja hapa upesi baada ya kutomwona Sultana huko chumbani. Gauni lake alikuwa amelishikilia mkononi limpe uhuru kunyanyua miguu.



"Sijui ameenda wapi!" Kijakazi akajibu akipandisha mabega."Hakuongea na mtu!"



Bibi akawafuata walinzi langoni, nao akawauliza. Kweli wakakiri kumwona Sultana akiondoka na farasi lakini hawakujua wapi anaenda. Hakuwashirikisha.



Bibi akachanganyikiwa. Hakutamani kusimama wala kukaa. Alihisi Sultana atakuwa ameenda kasrini. Hakuna mahali kwengine zaidi ya huko.



Akang'ata lips.



Hatakiwi kwenda huko. Akasemea kifuani. Huko atatibua mambo!!



**



"Ana miadi na wewe?" Lilikuwa swali la pili. Mlinzi alikuwa anamtazama kana kwamba uji uliokatika, lango akiliweka nyuma ya mgongo wake.



"We mshenzi," Bibi akafoka akimnyooshea kidole. "Acha kunichosha! Sina muda wa kulumbana na wewe hapa. Unajua mimi ni nani kwa Sultan?"



Kabla mlinzi hajajibu kitu, akasukumiwa kando, Bibi akaingia zake ndani upesi. Akiwa ameshikilia gauni lake, akarusha hatua kubwa na kuzama ndani.



Akaangaza. Kulikuwa kimya!!



Punde kijakazi akaja na kumkarimu.



"Sultan na Sultana wake wapo wapi?" Bibi akauliza pasipo kuchelewa. Kijakazi akamwelekeza wapo wamepumzika uani.



Bibi akauliza tena.



"Sultana mkubwa alifika hapa?"



Kijakazi akakataa, hakumwona. Labda vijakazi wengine kwani hapo wapo wengi. Basi Bibi akaamua kwenda zake huko uani kukutana na Sultan na mkewe.



Alipofika akakuta viti vitupu!



Moyo wake ukaanza kumwenda mbio!! Alihisi kuna jambo haliko sawa. Na jambo hili halikuwa dogo kabisa.



Akiwa ametoa macho ya hofu, akaongoza miguu yake upesi kwenda mpaka chumbani kwa Sultan. Akabisha hodi mara tatu. Hakukuwa na majibu.



Akafungua mlango na kuzama ndani. Kweli akathibitisha ile hofu aliyokuwa nayo haikuwa bure. Kwa macho yake alishuhudia maiti mbili kitandani. Moja ya Sultan na nyingine ya Sultana mdogo, yaani mjukuu wake!



Mashuka yalikuwa yamelowana damu. Walikuwa watupu, wameachama na macho yapo wazi.



Bibi akajawa na machozi lukuki lakini akashindwa kupiga kelele za yowe kwani alijikuta kifua kimembana ghafula!



Hakutaka kuamini alichokiona. Wala hakutaka kusadiki kama ni ndoto. Kwake vyote hivyo vilikuwa ni vibaya asivyotaka hata kujaribu kutokea!



Alimtazama mjukuu wake kisha Sultan. Bado miili yao ilikuwa ya moto. Je, muuaji yupo wapi? Haraka akatazama bafuni na kila eneo ndani ya chumba. Hakuona mtu.



Alijawa na hasira mno mpaka akawa anatetemeka. Hakujua angemfanya nini Sultana pindi angemjaza mkononi.



Pasipo kukawia, akatoa taarifa kwa walinzi juu ya mauaji hayo, wote wakaungana kumsaka Sultana mkubwa alipo. Waliamini bado yupo ndani kwa maana hakuonekana akipita tena langoni. Na ilikuwa wazi yeye ndiye alitekeleza mauaji hayo.



Atakapokamatwa, adhabu yake ni kunyongwa mpaka afe!! Kisha abakizwe hapo mpaka kunguru na tai wambakize mifupa.



Wakamsaka huku na kule. Baada ya muda kidogo, mmoja wa walinzi akapaza sauti:



"Yupo huku!"



Haraka wakenda huko. Ilikuwa ni stoo. Wakamkuta Sultana mkubwa akiwa ananing'inia kitanzini!!



Ameacha ujumbe karatasini ukiwa umeandikwa na damu. Karatasi imeshikizwa na ncha ya kisu ukutani.



**



Wakautoa mwili huo na kuuweka chini. Bibi akachukua kile kikaratasi kilichoachiwa ujumbe na kukipeleka machoni akisome.



'Kama ilivyokuwa na mwanzo, hii ndiyo mwisho. Maisha haya hayana maana tena kwangu. Na siwezi kuwaacha watu wakifurahia kwa mgongo wa maumivu yangu.'



Bibi akajawa na machozi machoni. Duku likamkaba kooni akatamani kupiga yowe. Akasaga meno yake kwanguvu akiumia sana kifuani.



Habari ilikuwa imekwisha!



Hakukuwa na Sultan tena wala Sultana zake. Wote wakawa habari ya upepo!!



**



"Amkeni!" Sauti ilifoka. Oragon na Ottoman wakakurupuka na kukaa sawa. Mbele yao walikuwa wamesimama wale wanaume wawili waliowakarimu na kuwapatia makazi.



Wanaume hao hawakuwa wamevalia vema. Wapo hovyo na wala wasiokane kujali. Mmoja wao, yule mfupi alikuwa anachokonoa meno yake na jiti kubwa. Meno yake yalikuwa na rangi ya kahawia.



Mwenzake huyu mrefu alikuwa amesimama akishikilia kiuno chake akiwatazama wakina Oragon kwa macho malegevu.



"Mnalalaje mpaka saa hii?" Akauliza huyu mrefu. "Mmeridhika na hali zenu, sio?"



Oragon na Ottoman wakatazamana wasijibu kitu zaidi ya kutazama chini. Si kwamba walikuwa wamechelewa sana. Wala. Bado jua halikuwa limesimama. Kulikuwa kuna ka-giza ka-asubuhi. Ndege wakiwa wanaimba madirishani.



"Amkeni. Leo kuna kazi kabambe ya kufanya," alisema mfupi baada ya kuchomoa jiti lake mdomoni. "Hapa hamna kula bure, lazima mfanye kazi."



Ni kweli hata maandiko yasema pasi na kazi pasi na kula. Lakini kazi hii wanayotaka kuwapatia vijana hawa majira haya ya asubuhi ya mapema hivi, ilikuwa ni ipi?



Oragon akaamka na kaka yake. Wakasimama na kuwafuata wanaume wale wenyeji wao mpaka kwenye kachumba fulani kadogo kachafu kamejawa na vitu lukuki. Humo yule jamaa mrefu akatoa kifurushi kidogo na kuwakabidhi.



"Mnaona hiyo?" Akauliza akikaza macho yake malegevu. "Mnatakiwa kupeleka kwa Rabis."



Kabla wakina Oragon hawajauliza Rabis ni nani, yule jamaa mfupi akadakia na kuwadadavulia:



"Rabis ni mkuu wa wahuni wote ndani ya himaya. Lazima kila mmoja atoe kodi kwake kila baada ya majuma kadhaa. Sasa hakikisheni hiyo imefika mikononi mwake. Mtajitambulisha kama wana wa mwewe!"



"Wana wa mwewe?" Ottoman akashangaa.



"Ndio," yule jamaa mrefu akajibu upesi. "Ukimwambia hivyo atawaelewa. Nyie fikisheni mikononi mwake."



"Anapatikana wapi?" Oragon akauliza. Mtu yule mfupi akampatia ramani.



"Hakikisheni mnaufikisha mzigo huu mikononi mwake ... mikononi mwake ... alafu mseme amewatuma wana wa mwewe. Tumeelewana?"



**



Baada ya kutembea kwa umbali wa muda kidogo, Oragon aliamua kumshirikisha mwenzake maswali kadhaa yaliyokuwa yanamtatiza kichwani. Mkono wake wa kuume alikuwa amebebekea kifurushi walichoagizwa. Jasho linaamchuruza.



"Kwanini wametutuma mzigo nyeti kama huu kwa mtu wao mkubwa kiasi hicho? Hawakuweza kuupeleka wenyewe?"



"Pengine walitaka tu na sisi tushughulike," Ottoman akajibu. Alikuwana anatafuma muwa.



"Sidhani, sidhani kabisa!" Oragon akakataa akitikisa kichwa. "Kupeleka kodi. Tena kwa huyo mkubwa wao, alafu watutume?"



Akamtazama kaka yake vema.



"Hatujui huko tuendako, twaenda na ramani. Hata sura ya Rabis hautuifahamu. Huoni ni hatari?"



Ottoman hakujibu kitu. Kwake hakuona tabu, akaamua kuwa bize na kutafuna mua wake.



"Na hiyo kodi ni nini haswa?" Oragon akaendelea kuuliza. "Vipi kama ni zile fedha zetu walizotukwapua?"



Hapo kidogo Ottoman akaguswa. Akamtazama kaka yake kwa macho ya tahadhari.



"Oragon!" Akaita. "Oragon, sitaki kuingia kwenye shida nyingine saa hii! Tafadhali mimi nishachoka kuishi kama digidigi!"



Akameza fundo la muwa kisha akaendelea.



"Hata kama tukikwapua hiyo kodi tutaenda kuishia wapi?"



"Nani kasema tunaikwapua?" Oragon akajishuku.



"Sasa kuniuliza maana yake nini?" Ottoman akamtambia. "Tafadhali, tuufikishe huyo mzigo unapotakiwa. Naomba tuishi kwa amani."



Kukawa kimya kwa dakika kadhaa wakitembea. Lakini wasidumu muda mrefu, mara wakasikia vishindo vya miguu nyuma yao. Walipotazama wakawaona wababa wawili wakija kwa kasi.



Kutazama vema, walikuwa ni vijakazi wa Mzee Raam!!



Lahaula!



Haraka wakaanza kukimbia. Wakipishana na watu huku na huko. Lakini hawakufika mbali wakakutana na mwingine mbele yao. Akawadaka!!



"Leo ndiyo mwisho wenu!" Akasema mbaba huyo kisha akacheka. Wakawabeba wakina Oragon na kutokomea nao mbali na watu ili wakawamalize huko!



Huko ambapo hamna mtu atajua. Wala atayejali.



Wakazama msituni. Mmoja wao alikuwa tayari ameshachukua kile kifurushi walichokabidhiwa vijana hao wakipeleke kwa Rabis. Walipozama msituni kinani wakawatenga vijana hao wakiwa tayari wamewafunga mikono na miguu.



Mmoja wao, yule mpana, jabali, akachomoa jambia lake tayari kuwanyofoa roho.



"Sala zenu za mwisho?" Akauliza wakati awaulizao amewafunga kitambaa mdomoni. Ooh! Akakumbuka, akawaondolea kitambaa mdomoni na kurudia swali lake.



"Tunakuomba usituue!" Akalia Ottoman. "Tumefanya kosa gani mpaka tukastahili haya?"



"Hamjui?" Muuaji akauliza. "Mmeona hayo?" Akaonyeshea kidole mazingira yaliyowazunguka. Kulikuwa kuna mifupa na baadhi ya miili ya watu iliyooza. "Wote hao wamekufa kwasababu sawa na ya kwenu. Kosa la kujua siri ya kuhani!"



Baada ya kusema hayo, hao wanajeshi, vijakazi wa Raam, wakacheka kama mazuzu. Wakina Oragon wakapaza makelele ya kuomba msaada. Wakazidi kuwafanya wanaume hawa waangue kicheko.



"Unadhan kuna anayekusikia?" Akauliza muuaji kwa sura ya mzaha. "Hakuna anayesikia kelele zako. Na hata wale watakaosikia wanaogopa kuja!"



Akanyua jambia lake juu, lakini kabla halijatua mara muuaji akadunguliwa na mshale wa shingo. Akadondoka akitapatapa. Hawajakaa vema, na wale wawili nao wakala mishale ya vifua na kufa papo hapo!!



Mara wakatokea wale majamaa waliowatuma wakina Oragon. Mikononi mwao walikuwa wamebebelea pinde za mishale. Wakawajulia hali wakina Oragon na kuwafungua kamba zao.



Wakawaeleza kumbe walikuwa wakiwafuatilia kwa nyuma tangu walipotoka kwenye makazi yao. Lakini kuna jambo walilisikia kutoka kwa wale wajakazi wa Kuhani.



Siri.



Ni siri gani hiyo? Wakawauliza wakina Oragon. Ni siri gani inayowatia hatiani mpaka kutaka kuuawa? Na hata wengine wakiwa tayari wameshanyofolewa roho zao kwasababu hiyo?



"Kuhani ni shoga," Ottoman akawahi kunena. Wale majamaa wakaachama midomo yao wazi kwa kuduwaa.



"Anataka vijakazi wake wamhudumie, mimi nilishindwa," alieleza Oragon. "Sasa akasema hiyo ni siri, hayuko radhi himaya yote ikajua. Ndo maana anawinda roho zetu!"



Wale majamaa wakatahamaki. Alah!! Lilikuwa jambo kubwa hili? Wakatazamana na macho ya kustaajabu alafu yule mfupi akauliza:



"Ni kweli?"



"Ndio, ni kweli!" Oragon akamsisitiza.



Mara wale wajamaa wakaangua kicheko. Sasa kwanini hamkuwapatia hiyo huduma? Wakauliza. Lakini wasijali sana, wakawataka wakina Oragon waendelee na safari yao ya kwenda kwa Rabis.



"Fanyeni upesi muda unaenda!"



Wakaelekea zao.



Wale majamaa wakabaki hapo wakijiuliza cha kufanya. Lile jambo la Kuhani lilikuwa kubwa na lingeweza kuwaingizia fedha kubwa wakawa matajiri.



Akili zao za kipumbavu ziliwaza!



Twaweza uaga ufukara hapa. Wakawa wanasemezana huku wakiishilia.



**



Siku hii ikiyoyoma, wakafika mbele ya makazi ya Rabis. Nyumba kubwa chakavu. Mbao zake zilikuwa zimetoboka na zimefubaa. Mabati yake yamerendemka na kuota kutu.



Hapo nje kulikuwa na zizi kubwa la nguruwe. Zizi hili lilikuwa chafu, limejawa na nguruwe lukuki waliokuwa wamepoteza rangi za muonekano wao. Lakini walikuwa wamenona haswa.



Sijui walikuwa wanakula nini!!



Mbali na nyumba hiyo, hakukuwa na nyumba nyingine kwa pembeni wala hatua kadhaa kwa umbali. Nyumba ilikuwa imejitenga kana kwamba ipo jangwani.



Pweke.



Kunguru kadhaa walikuwa wamesimama juu ya paa. Wanatazama huku na kule.



Kabla Oragon na Ottoman hawajapiga hatua kujongea ndani ya nyumba, wakaisikia sauti kali ya mtu akilia! Kunguru wote waliokuwa juu ya paa wakarusha mbawa zao kuruka!



Oragon na Ottoman wakatazamana.





Walikuwa na hofu mioyoni mwao. Akili yao ilitengeneza picha kubwa Rabis kama bonge la mtu anayeogopeka na hata kuua ama kutesa wanaomkosea. Penngine mawazo yao yalikuwa sahihi.



Ila ni mpaka pale walipoenda kuthibitisha kwa macho yao.



Wakabisha hodi mara mbili mlangoni na punde wakasikia kishindo kizito kikijongea mlango. Huyu ndiye Rabis! Wakatetemeka mioyo.



Mara mlango ukafunguliwa na jibaba kubwa lililoshikilia panga mkononi. Nguo zake zilikuwa chafu zimelowana damu. Alikuwa ana ndevu na nywele lukuki kichwani.



Macho makubwa ya kutisha. Pua ndefu iliyochongoka ila mdomo usionekane kisa kufunikwa na ndevu.



Aliwatazama wakina Oragon pasipo kuteta jambo. Alafu akaufungua mlango wazi waingie. Wakazama humo ndani na kukuta watu kadhaa, kwa haraka kama vile kumi na wawili, wakiwa wamesimama na kila mtu akiwa na mzigo wake, aidha ndani ya kifurushi, ama mkoba.



Lakini humu ndani palikuwa pakubwa sana. Kwa mbali kidogo na watu waliosimama kulikuwa na kama kimadhabahu kidogo. Kuna kiti hapo na mtu mmoja mfupi, miguu hata haigusi chini, alikuwa ameketi.



Alikuwa ana nywele ndefu nyeusi. Vidole vyake vimejawa pete za dhahabu na shingo yake pia. Mikufu inayong'aa!



Chini yake kulikuwa kuna vifurushi kadhaa vikiwa vimewekwa hapo.



Kushoto kwake kulikuwa kuna damu zimetapakaa. Mwili mmoja umelala hapo kimfu. Si bure alikuwa ndiye yule aliyepiga kelele muda si mrefu, kunguru wakawehuka.



Mbali na hapo humo ndani hakukuwa na kitu kingine cha maana zaidi ya samani zilizochoka, mkangafu, japokuwa palionekana ni eneo zuri likifanyiwa matengenezo.



Lile jibaba liliwaelekeza wakina Oragon mahala pa kusimama, kule walipo wenzao, kisha likaenda kusimama kando na yule mtu ambaye ameketi kwenye kiti. Ambaye bila shaka ndiye Rabis!



Akamuagiza,



"Pelekea nguruwe!" Akionyeshea maiti iliyokuwepo hapo chini. Yule jibaba likaunyanyua ule mwili, bado ukiwa unaendelea kuvuja damu, akaenda nao nje.



Si bure wale nguruwe walikuwa wanono kiasi kile. Wanalishwa nyama za binadamu!! Oragon na mwenzake wakatetemeka. Hawakujua ni kwanini mtu yule aliuawa. Pengine nao watauawa kama yule kisha wakalishwe nguruwe!!



Tena lililowapa uoga zaidi, hawakuwa wanamjua Rabis hata punje. Hawakuwa wanajua mwanaume huyo anataka nini, nini miiko yake wala laana!



Basi wakiwa wanameza mate, wakanyamaza watazame namna mambo yanavyoenda.



Wakasonga kwenye ule mstari. Mtu wa kwanza wakamwona akiwa amefikisha mbele kifurushi chake. Rabis akatazama kilichomo ndani na mara akamtikisia kichwa.



Mtu huyo akaenda zake!



Akaja wa pili na wa tatu. Wote hawakuwa na shida. Lakini mmoja aliyefuata alikuwa ameshikilia kifurushi kilichosinyaa. Uso wake ulikuwa na woga. Mikono yake ilikuwa inatetemeka.



Alimkabidhi kifurushi Rabis, Rabis akakitazama kisha akamtazama yule jabali lake la pembeni, mara jabali akamnyaka huyo jamaa na kumsukumia chini. Akamkatakata!!



Kisha kama kawaida akamnyanyua na kwenda kupeleka maiti kwenye banda la nguruwe wamtafune!



Ulipopita muda mfupi, wakina Oragon nao wakafika mbele ya Rabis. Walikuwa wanatetemeka sana. Walimkabidhi Rabis kifurushi chao kisha wakajitambulisha, wao ni wana wa mwewe!



Basi Rabis akawatazama kana kwamba anawapekua. Akatazama na ndani ya kifurushi kisha akabinua mdomo wake.



"Wana wa mwewe!" Akasema kwa kebehi. "Mnajifanya wajanja sio?"



Oragon na Ottoman wakatazamana. Kisha wakatikisa kichwa.



"Yani ushuru wote ninaowadai, muda wote huo, huu ndiyo mmeniletea?" Rabis akauliza akitoa macho.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Hapana, sisi hata hatujui. Wametukabidhi tulete tu hapa hakuna lolote tunalolifahamu."



Rabis hakuamini. Akamuagiza yule jabali awakamate na kuwashughulikia vijana hao haraka iwezekanavyo!!



Basi wakina Oragon wakadakwa kwa mkono mmoja tu, wakatupiwa chini. Jabali akapandisha panga lake nene juu! Mara



"Msituue! Tuna kingine cha kuwapa!" Akaropoka Oragon.



Rabis akamzuia jabali kutenda kazi yake, kisha akauliza:



"Ni nini hicho?"



**





ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog