Simulizi : Nilivyokutana Na Mzimu Facebook
Sehemu Ya Pili (2)
Siku iliyofuata nilienda chuo kama kawaida, huko hakukuwa kuna kazi nyingine zaidi ya kuwatambia washikaji zangu juu ya Farhia ambaye nilimpata kutoka facebook.
Kutokana na uzuri niliyowaambia kwamba msichana huyo alikuwa nao, kwanza wao wenyewe hawakutaka kuamini hilo hata kidogo, walihisi kwamba nilikuwa nikiwapiga fiksi muda huo na kwamba msichana huyo hakuwa mzuri na labda pengine alikuwa na uzuri wa kawaida tu ila kutokana na kuongeza kwangu chumvi nyingi ndivyo kulimfanya msichana huyo azidi kuonekana kuwa mzuri kupita kawaida.
“Hebu tuonyeshe kwanza picha zake tumuone maana usije ukatupiga fiksi hapa mzee baba,” alisema Deo huku akitaka nimuonyeshe picha muda huo.
“Yap! Halafu hivi anaweza kweli kumzidi hata Maria kwa uzuri?” alisema Nickson huku akiuliza swali hilo.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Huyu Maria aliyekuwa akimzungumzia muda huo, alikuwa ni msichana mrembo ambaye aliwahi kutwaa taji la Miss katika chuo hiko.
“Kwani huyo Maria ni nani? Farhia kamzidi kila kitu,” nilisema kisha nikachukua simu na kuanza kuwaonyeshea picha za Farhia.
“Mzee baba ndiyo huyu Farhia mwenyewe?” aliniuliza Deo huku akionekana kutoamini kile alichokuwa akikishuhudia kwa muda huo.
“Yeah mzee baba huyo ndiyo Farhia mwenyewe, sema unamuonaje kwanza mtoto vipi anafaa kwa matumizi?” nilimwambia kisha nikamuuliza swali hilo la kimakusudi kabisa, nilichokuwa nikikitaka muda huo ni kuwatambia tu, wala sikuwa na nia nyingine kabisa.
“Duh! Huyu demu ni mzuri kinoma, hebu kwanza nipe namba yake,” aliniambia Nickson huku akiendelea kuzitazama picha za Farhia kwenye simu yangu. Alionekana kuchanganyikiwa vibaya mno.
“Ili ufanyaje?” nilimuuliza huku nikimtazama kwa macho yaliyoashiria kumnyima namba waziwazi bila kificho.
“Si ili nimsalimie shemeji yangu jamani au hutaki?” alinijibu kisha akaniuliza huku akitabasamu.
“Yeah siwezi kukupa namba zake,” nilimwambia.
“Kwanini?” aliniuliza.
“Muda bado, ukifika nitakupa ila kwa sasa acha nitambe naye kwa sababu ndiyo ameshakuwa shemeji yenu hivyo,” niliwaambia huku nikiendelea kutamba kama nilivyokuwa nimedhamiria.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kila kitu katika maisha yangu, niliendelea kuwatambia washikaji zangu huku penzi langu na msichana Farhia likizidi kupamba moto.
Mpaka kufikia katika kipindi hicho hatukuwa bado tumeonana ana kwa ana lakini kupitia mtandao wa facebook aliweza kunipa namba zake za simu kisha tukuwa tunazungumza na hata wakati mwingine kuchati WhatsApp na kutumiana picha mbalimbali.
Hilo lilinifanya nizidi kumuamini sana Farhia na kumpenda kuliko msichana mwingine yeyote yule hapo chuoni. Kila nilipokuwa nikiziangalia picha zake na kuuona uzuri aliyokuwa nao, sikufichi nilijihisi kusisimka mwili, maana alikuwa ana shawishi kabisa.
***
“Dah kweli mwanangu umepata zali,” aliniambia Deo huku akionekana kunionea wivu. Mpaka kufikia muda huo hakutaka kuamini kama Farhia nilikutana naye facebook na kwamba mtandao huo ndiyo uliyonipatia msichana mrembo kiasi hicho.
“Kwanini mzee baba?” nilimuuliza.
“Unajifanya hujui sio,” alinijibu.
“Sema sasa ueleweke mbaba,” nilimwambia.
“Huyu Farhia amenichanganya kinoma, unajua bado siamini kama umempata facebook,” aliniambia.
“Huamini nini sasa, ndiyo unatakiwa uamini hilo kwamba facebook imenipa demu mkali,” nilimwambia huku nikicheka.
“Hivi kwani hana ndugu zake?” aliniuliza Nickson.
“Sijui kama anao,” nilimjibu.
“Acha zako hizo, tukunjulie moyo washikaji zako na sisi tupate hifadhi kwa wahindi,” aliniambia Nickson kwa utani kisha wote tukacheka.
Kiukweli naweza kusema kwamba katika kipindi hicho moyo wangu ulikuwa unaishi kwa msichana Farhia, aliuteka moyo wangu kiasi kwamba nilihisi kuchanganyikiwa kila nilipokuwa nikiliona jina lake ama kuziona picha zake kwenye simu yangu.
Hali hiyo haikuwepo kwa upande wangu tu bali hata kwa washikaji zangu, na wao pia walionekana kuchanganyikiwa na msichana huyo mpaka kufikia hatua ya kutamani kuwa mimi lakini hilo lilikuwa ni jambo lisilowezekana hata kidogo.
Siku zilizidi kukatika, maisha ya chuo nayo yaliendelea kama kawaida. Nilikuwa nikisoma kwa bidii hali iliyosababisha hata katika upande wa matokeo yangu kuwa mazuri.
Baada ya kupita mwezi mmoja tangu nilipofanikiwa kuanzia rasmi uhusiano wa kimapenzi na Farhia, nilitamani sana kumuona ana kwa ana na hapa ilikuwa ni baada ya kukumbwa na wivu mkubwa ambao ulikuwa unanipeleka puta. Yaani kwa jinsi nilivyokuwa nikiziangalia picha zake ukijumlisha na uzuri aliyokuwa nao, nilihisi fika kwamba huko Zanzibar alipokuwa akiishi kwa wakati huo ni lazima wanaume walikuwa wakimsumbua sana na hii ingesababisha anisaliti usaliti ambao ungeuumiza mno moyo wangu.
Sikutaka kuumia kwa sababu ya mapenzi mazito niliyokuwa nayo dhidi yake hivyo nilitaka kuonana naye ili kusudi wivu niliyokuwa nao unipungue japo kidogo.
“Mh!” aliguna Farhia, wakati huo nilikuwa nikizungumza naye kwenye simu.
“Nini?” nilimuuliza.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yaani mimi nije huko,” alinijibu.
“Ndiyo kwani kuna tatizo gani mpenzi wangu? Si unakuja mara moja halafu unaondoka zako, au hujanimisi, hutaki kuniona? Niambie ili nijue,” nilimuuliza huku nikionekana kujawa na wivu kiasi cha kunielemea kabisa.
“Nitakuja na utaniona mpenzi wangu wala usijali,” alinijibu kwa sauti nyororo ya chini iliyozidi kunichanganya mno akili yangu.
“Mpaka lini jamaniii?”
“Subiri nitakwambia mpenzi.”
“Au mimi nije huko?”
“Uje wapi? Huku Zanzibar?”
“Ndiyo kwani kuna tatizo gani mpenzi?”
“Hapana usije huku mimi nitakufuata huko.”
“Lini sasa?”
“Mpenzi wangu mbona una haraka hivyo, mimi tayari nimeshakuwa wako, usiwe na wasiwasi utaniona tu.”
“Hivi kwa uzuri uliyokuwa nao kuna mwanaume ambaye anaweza kuwa mpole au kukubali aendelee kukaa mbali na wewe ili hali anakupenda?”
“Najua mpenzi na ninaelewa kila kitu.”
“Sasa kwanini hutaki nije nikuone, natamani nikushike walau na mimi nijihisi nina mpenzi. Hivi tutaendelea kuishi mbali mpaka lini?”
“Muda utazungumza, usijali utaniona.”
“Lini?”
“Hata leo.”
“Acha utani wako, unajua nipo serious.”
“Hata mimi pia nipo serious.”
“Haya bhana, umeshinda.”
“Nakupenda sana Abdul.”
“Nakupenda zaidi yako,” nilimwambia.
Naweza kusema kwamba hicho kilikuwa ni kipindi cha furaha. Katika mapenzi hakuna kitu kizuri kama kumpenda mtu ambaye anakupenda, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwangu. Nilimpenda msichana ambaye alinipenda tena zaidi ya upendo nimpendao. Hakika nilijisikia furaha isiyokuwa na kifani moyoni mwangu.
***
Siku hiyo ambayo nilimwambia Farhia kwamba nilitamani sana kumuona na kuwa karibu naye. Usiku wa siku hiyo niliota ndoto iliyonionyesha kwamba nilikuwa naye ufukweni mwa bahari. Tulikuwa wawili tu ufukweni humo na tulikuwa tukizungumza kuhusu mipango yetu ya kufunga ndoa kwa siku za mbeleni.
Asubuhi ya siku iliyofuata nilishtuka kutoka kwenye ndoto hiyo ambayo ilinisisimua kwa kiasi fulani, wakati mwingine nilikuwa nikitabasamu baada kukumbuka baadhi ya matukio ya kwenye ndoto hiyo.
Baada ya kupita dakika kadhaa huku nikionekana kuitafakari ndoto hiyo niliyoiota mara simu yangu ikaanza kuita, nilipoangalia kwenye kioo niliona jina la Farhia, nikapokea huku nikitabasamu.
“Mambo mpenzi vipi umeamkaje?” aliniambia kisha akaniuliza kwa kunijulia hali yangu.
“Nimeamka salama sijui wewe?” nilimjibu kisha nikamuuliza.
“Nipo salama mpenzi ila umefurahi kuniona?” alinijibu kisha akaniuliza swali lenye utata.
“Kukuona kivipi?” nilimuuliza huku nikishangaa.
“Ndiyo kwenye ndoto si tulikuwa wote ufukweni?” alinijibu kisha akaniuliza swali ambalo kiukweli lilinishangaza mno. Nikajiuliza kimoyomoyo kwamba alijuaje kwamba nilimuota katika mazingira hayo lakini nikakosa mtu ya kunijibu kwa wakati huo.
Nilihisi kupigwa na ganzi mwili mzima, nilibaki kimya kwa muda wa sekunde kadhaa huku nikiwa bado nimeiweka simu sikioni.
Muda huo nilijaribu kutafakari swali alilokuwa ameniuliza Farhia kuhusu ndoto niliyomuota usiku wa kuamkia siku hiyo, na kitu cha ajabu ni kwamba aliifahamu ndoto yenyewe. Hilo lilinifanya nishtuke.
“Umejuaje kwamba nimekuota hivyo?” nilimuuliza huku nikionyesha kushangaa.
“Kwa sababu nami nimeota ndoto ya aina hiyo.”
“Unasema kweli?”
“Ndiyo mpenzi wangu, naomba uniamini.”
“Duh!”
“Nini?”
“Unajua hii sio hali ya kawaida kabisa.”
“Kwanini?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuota ndoto zinazofanana.”
“Ni kweli ila nadhani inatokana na mapenzi ya dhati tuliyokuwa nayo.”
Baada ya Farhia kuniambia maneno hayo nijikuta nikitabasamu na kuamini kile ambacho aliniambia. Wakati mwingine niliamini katika mapenzi unapokuwa na hisia kali na mwenza wako ni lazima umuote na hivyo ndivyo ilivyotutokea, tulikuwa tunapendana sana kiasi kwamba kilifikia kipindi hata kuna muda ndoto zetu zilifanana.
Nilimuamini sana Farhia na hilo ndiyo kosa kubwa ambalo nililifanya katika maisha yangu. Kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea kutokea, sikukitilia mashaka hata kidogo, moyo wangu bado uliendelea kumuamini msichana huyo na kumpenda kuliko msichana mwingine yeyote.
***
Baada ya kupita kipindi fulani, siku moja nilipokuwa nikichati na Farhia facebook, alianza kuniambia kwamba alizaliwa katika familia ya kitajiri. Baba yake muarabu aliyenitambulisha kwa jina la Shirhan Haroon, alikuwa ni mfanyabiashara ambaye alikuwa akimiliki pesa ndefu na hii ndiyo sababu iliyomfanya aonekane kuwa na maisha mazuri tena ya kitajiri. Aliendelea kuniambia kuwa hakupenda kuniona nikiishi maisha ya shida hivyo alipanga kuyabadilisha maisha yangu katika kipindi hicho. Nilipousoma ujumbe wake huo, nilishtuka.
Mimi: Unataka kuyabadilisha maisha yangu?
Farhia: Ndiyo.
Mimi: Kivipi?
Farhia: Usishtuke Abdul, nataka nikupe utajiri.
Baada ya kuusoma ujumbe huo, nilishtuka, sikuamini hata kidogo.
Mimi: Hebu acha utani wako, yaani unipe utajiri?
Farhia: Ndiyo mpenzi.
Mimi: Mh! Sawa haina noma.
Farhia: Huniamini?
Mimi: Nakuamini.
Farhia: Sawa, nikuulize kitu?
Mimi: Yeah! Niulize.
Farhia: Una akaunti benki?
Mimi: Hapana sina.
Farhia: Kwanini?
Mimi: Kwa sababu sina pesa nyingi za kuhifadhi huko, kwenye simu zinatosha.
Farhia: Okay basi itabidi ufungue akaunti benki.
Mimi: Halafu?
Farhia: Niwe nakutumia pesa.
Mimi: Sawa nitafanya hivyo.
Siku hiyo nilichati na Farhia muda mrefu, nilipomaliza kuchati naye, nilizima data na kufanya mambo yangu mengine. Nilifanya hivyo lakini akili yangu haikuwa sawa hata kidogo, muda wote nilikuwa nikimfikiria Farhia. Aliniambia kuwa hakutaka kuona nikiishi maisha ya shida hivyo alitaka kunipa utajiri.
Hebu jifikirie umekutana na mtu mtandaoni, facebook tena hujawahi kumuona lakini ikatokea ukamtongoza na hatimaye mkawa wapenzi. Uhusiano wenu wa kimapenzi umedumu kwa miezi kadhaa halafu ghafla! mwenzako adai kwamba anataka kuyabadilisha maisha yako, yaani anataka kukupa utajiri.
Hivi kama ingekutokea wewe katika maisha yako unafikiri ungefanyaje? Au ungejisikiaje?
Bila shaka najua ungejisikia furaha, yaani ungejiona kupata bahati kubwa sana katika maisha yako ambayo hukutegemea kama kuna siku ungeipata.
Hivyo ndivyo ambavyo nilijisikia siku hiyo, sikuamini kama katika maisha yangu, nilikuwa kwenye uhusiano na msichana huyo ambaye alitokea katika familia ya kitajiri, yaani kuhusu suala la pesa kwake halikuwa tatizo hata kidogo.
Kama alivyoniambia Farhia kwamba nilitakiwa kufungua akaunti benki ndivyo ambavyo nilifanya siku iliyofuata. Nilienda kwenye benki ya National Microfinance Bank (NMB), nikafungua akaunti na kisha kufanikiwa kwa asilimia mia moja.
Kwa kuwa hakuwa mpenzi sana wa kuongea kwenye simu, jioni ya siku hiyo niliingia facebook na kuanza kuchati naye.
Mimi: Asalaam Aleykum.
Farhia: Waaleykum Msaalam.
Mimi: Vipi unaendeleaje?
Farhia: Naendelea salama, sijui wewe za chuo?
Mimi: Namshukuru Mungu masomo yanaenda vizuri.
Farhia: Ulifanya kama nilivyokwambia?
Mimi: Kufanya nini?
Farhia: Kuhusu kufungua akaunti benki.
Mimi: Ndiyo, nimefungua tayari.
Farhia: Benki gani?
Mimi: NMB.
Farhia: Vizuri sana, nipe namba ya akaunti.
Mimi: 40501904052
Farhia: Sawa, nitakutumia pesa.
Mpaka kufikia muda huo nilichanganyikiwa, sikuamini kama msichana huyo alikuwa amedhamiria kweli kufanya kile alichokuwa akiniambia muda huo. Ni hapa ambapo nilijiambia kwamba ili niweze kumuamini ni mpaka pale ambapo angenitumia pesa.
Siku hiyo ilipita, hatimaye siku iliyofuata ikawadia, kama utani siku hiyo Farhia alinitumia milioni mbili.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sijui niseme nini ili ujue kwamba siku hiyo nilikuwa kwenye furaha kiasi gani. Naweza kujifananisha na mtu ambaye alicheza bahati nasibu kisha akashinda, bila shaka ni furaha isiyokuwa na kifani ambayo mtu huyo ilimkumba basi na mimi siku hiyo furaha hiyo hiyo ilinikumba moyoni mwangu.
Farhia: Nimekutumia milioni mbili mpenzi, umeiona?
Mimi: Ndiyo nimeiona, ahsante sana.
Farhia: Usijali, hiyo utaitumia kwa mahitaji yako madogo madogo.
Mimi: Lakini ni nyingi sana.
Farhia: Usijali mpenzi, zitumie kwa mahitaji yako muhimu, utakazozibakiza utawanunulia ndugu zako zawadi.
Mimi: Sawa ila sijui nikushukuru vipi?
Farhia: Hupaswi kunishukuru, nafanya hivi kama wajibu wangu kwako.
Mimi: Nakupenda sana.
Farhia: Nakupenda pia.
Kuna wakati sikuamini hata kidogo kama kweli niliweza kutumiwa kiasi hicho kikubwa cha pesa tena kwenye akaunti yangu, nilichokifanya nilienda ATM kuzitoa na ndipo hapo ambapo niliamini na kuhakikisha kwamba ni kweli.
***
Kwa kuwa nilipenda kila kitu ambacho kilikuwa kikitokea katika maisha yangu niwajuze marafiki zangu, sikutaka kuwaficha kuhusu hilo la Farhia kunitumia pesa. Nilipowaambia, walionekana kutoniamini hivyo nilichokifanya nikaongea kwa vitendo, nikawaonyesha kiasi cha pesa ambacho alinitumia.
“Mwanangu huyu demu usimuache,” aliniambia Deo.
“Kwanini?” nilimuuliza.
“Yaani mpaka anakutumia pesa basi huyo amekupenda kweli,” alinijibu.
“Inaonekana kwao huyu demu ni wa kishua sana?” aliniuliza Nickson.
“Sio inaonekana, ni wa kishua, baba yake anamiliki visima vya mafuta uarabuni.”
“Duh! Sio poa mzee baba.”
“Yaani we acha, siamini.”
“Sema acha kukaa kifala, mwambie akupe mtaji ufanye biashara, mademu wa hivi hawatabiriki ukizubaa kesho utakuta kadata na mwingine,” aliniambia Deo maneno ambayo yalikuwa na mantiki kubwa sana.
“Kweli mwanangu hapo umeongea jambo la msingi.”
“Wewe endelea kukaa kifala, wenzako tunatamani bahati kama hizo tunakosa,” aliniambia.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wangu wa kuzitumia pesa za Farhia, kila nilipokuwa nina shida iliyohitaji pesa aliweza kunisaidia huku akionekana kutojali kitu.
Alidhamiria kuyabadilisha maisha yangu na kweli baada ya kupita mwezi mmoja, alinipigia simu na kuniambia kwamba alipanga kunipa mtaji wa kufanya biashara hivyo alichokihitaji muda huo nimwambie ni biashara gani ambayo nilitaka kuifanya na ingegharimu kiasi gani cha pesa.
“Nafikiri kufanya biashara nyingi sana,” nilimwambia.
“Zipi hizo?” aliniuliza.
“Nafikiria kufungua mgahawa, duka kubwa la nguo na hata kujenga nyumba kwa ajili ya kupangisha.”
“Ni biashara ipi ambayo ungependa uanze nayo?”
“Nafikiri biashara ya mgahawa kwa sababu nimeanza kutamani kuifanya muda mrefu.”
“Unafikiri utaweza kweli kuifanya?”
“Ndiyo halafu sio lazima nifanye mimi, nitaajiri watu ambao watakuwa wananisaidia, mimi kazi yangu itakuwa ni kusimamia tu.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Okay na umeshapanga ukajua ni mtaji kiasi gani unahitaji?”
“Kwa haraka haraka nikipata milioni kumi naweza kumaliza kila kitu.”
“Basi nitakutumia milioni hamsini ili kama kuna shida yoyote itatokea uweze kuimaliza,” aliniambia maneno ambayo yalinifanya nikumbwe na bumbuwazi, nilishindwa kuongea mpaka pale ambapo simu upande wa pili ilikatwa.
Nilipotajiwa kiasi cha shilingi milioni hamsini nilichanganyikiwa vibaya mno, wakati mwingine sikuamini hata kidogo, nilihisi kama nilisikia vibaya, nilichokifanya muda huo nilimuuliza kwa mara nyingine ili asaili kauli hiyo iliyonipa utata kwa kiasi fulani.
“Hallo, hallo,” nilisema kwa pupa bila upande wa pili kujibiwa kitu na ndipo hapo ambapo nikaangalia na kukuta simu tayari ilikuwa imekatwa. Nikazidi kuchanganyikiwa.
Sikujua kama nilitakiwa kufurahia ama la, isipokuwa nilichokifanya, nilimpigia simu rafiki yangu Deo na kuanza kumueleze kile kilichokuwa kimetokea siku hiyo, bado sikuonyesha kuamini hilo hata kidogo, nilihisi kama nilikuwa katika ndoto na hivyo muda wowote ningeweza kuamka.
“Amesema anakupa milioni hamsini?” aliniuliza Deo huku sauti yake ikiashiria wazi kwamba alishtuka.
“Ndiyo yaani mzee baba nimechanganyikiwa hapa sielewi, naona kama mapichapicha,” nilimjibu.
“Tatizo unapenda kukaa kifala sana, sasa unachanganyikiwa nini hapo, changamkia fursa, hiyo ni bahati usiichezee mzee baba.”
“Dah.”
“Kwahiyo umepanga kuifanyia nini hiyo milioni hamsini?”
“Biashara.”
“Hiyo ya mgahawa uliyomwambia, si ndiyo?”
“Ndiyo.”
“Safi ni wazo zuri sana, kesho ukija chuo tutaongea mengi.”
“Haina noma kaka.”
“Poa poa.”
Siku hiyo sikuweza kupata hata lepe moja la usingizi, ingawa nilikuwa nimejilaza kitandani lakini akili yangu haikuwa chumbani humo kabisa. Nilikuwa nikifikiria hizo milioni hamsini nilizoambiwa kwamba ningetumiwa kwa ajili ya kufanya biashara.
Ndugu yangu, hata kama ungekuwa ni wewe usingeweza kupata usingizi siku hiyo. Hebu jifikirie katika maisha yako tangu uzaliwe hujawahi kushika hata milioni moja halafu leo katika mazingira kama hayo mtu anakwambia kwamba anataka akupe milioni hamsini kwa ajili ya kufanya biashara, sikufichi ni lazima ungechanganyikiwa, yaani usingeamini hata kidogo.
Hivyo ndivyo ambavyo nilikuwa siku hiyo, naweza kusema nilichanganyikiwa, muda wote nilikuwa nikiyakumbuka maneno ya Farhia. Wakati mwingine ni kama vile nilikuwa nikiisikia sauti yake ambayo ilinisisimua kupita kawaida.
Ni hapa ambapo nilianza kuziangalia picha zake ambazo nilizihifadhi kwenye simu yangu kama kumbukumbu. Nilipokuwa nikiziangalia nilijikuta nikikumbwa na furaha isiyokuwa na kifani. Naweza kusema moyo wangu ulikuwa umezama kwenye dimbwi la mapenzi yake.
Huo ndiyo ulikuwa muda wa kuufikiria utajiri ambao nilikuwa nikienda kuupata katika maisha yangu. Kulikuwa kuna wana chuo wengi sana niliyokuwa nikisoma nao, wengine walikuwa wakifanya biashara na wengine walikuwa ni waajiriwa.
Nilifahamu fika kuwa na mimi nilikuwa nikienda kuwa miongoni mwao tena ningewazidi kwa kila kitu. Nilipokuwa nikifikiria hayo, nilijikuta nikitokwa na tabasamu pana.
Siku hiyo sikuweza kulala usingizi kama niliyozoea kulala siku zote. Asubuhi ya siku iliyofuata ilipowadia niliamka na kujiandaa kama ilivyokuwa kawaida yangu, nilipomaliza nilienda chuo.
Muda wote nilionekana kutawaliwa na furaha isiyokuwa na kifani. Nilipofika chuo kama kawaida niliendelea na ratiba ya siku hiyo na mara baada ya kumaliza vipindi nilikaa na marafiki zangu na kuanza kujadiliana nao kuhusu suala hilo la kufanya biashara ambalo lilikuwa linanisumbua mno kichwa changu.
“Kwanza kabla ya yote inabidi ukubali kufanya biashara unayoipenda,” aliniambia Deo kisha akanipa muda ya kutafakari kauli hiyo.
“Hilo nakubali,” nilimwambia.
“Unajua utakapoamua kufanya biashara unayoipenda ni lazima utafanikiwa na utaifanya kwa umakini,” aliniambia.
“Hilo ni kweli kabisa.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Inabidi ujitoe, usikubali kubweteka hata kidogo.”
“Na kingine cha kuongezea hapo inabidi umuheshimu sana Farhia kwa sababu ni mwanamke ambaye anaonyesha ni kwa jinsi gani anakupenda, kwa mwanamke ambaye hakupendi hawezi kukufanyia mambo yote hayo,” aliniambia Nickson.
“Naelewa kaka.”
“Usije ukafanya uzembe ukampoteza maana utakuwa umefanya ujinga mkubwa sana,” aliniambia Deo.
“Siwezi kufanya hivyo,” nilimwambia.
“Kuwa makini mzee baba.”
“Sawa.”
Tulizungumza mambo mengi sana siku hiyo, Nickson alionekana kutoamini kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yangu, kitendo cha kumpata Farhia facebook kiasi kwamba ulifikia wakati akawa ananipa pesa, hilo lilizidi kumchanganya.
Baada ya kupita siku tatu Farhia alinitumia kiasi cha shilingi milioni hamsini benki. Alinipigia simu na kuniambia kwamba kiasi hicho cha pesa alichonitumia nilitakiwa kukitumia kwa ajili ya kufanya biashara na sio kwa ajili ya matumizi mengine.
“Sawa mpenzi wangu nimekuelewa, ahsante sana,” nilimwambia huku nikimshukuru.
“Naomba kuwa makini Abdul,” aliniambia.
“Usijali, nitakuwa makini na ninakuahidi kwamba sitokwenda kinyume na mipango yangu,” nilimwambia huku nikimuondoa wasiwasi uliyoonekana kumuingia kwa wakati huo.
“Sawa nitafurahi sana kama utafanya hivyo,” aliniambia.
Ingawa Farhia alinitumia milioni hamsini na kunitaka nizifanyie biashara kiukweli mpaka kufikia muda huo sikuonyesha kuamini hilo hata kidogo. Kuna vitu ambavyo nilitakiwa kuviamini lakini sio hilo la kutumiwa pesa kwa ajili ya kufanya biashara.
Kama ni bahati basi nilipata bahati kubwa sana katika maisha yangu. Naweza kuifananisha bahati hiyo na mtu ambaye alikuwa amelala masikini na kisha kuamka akiwa tajiri. Hivyo ndivyo ambavyo ilinitokea, katika kipindi ambacho nilikuwa sina wazo la kupata utajiri ndipo hapo ambapo utajiri ulinifuata, hakika sikutaka kuamini hilo.
Kwa kuwa nilikuwa nimedhamiria kufanya biashara kutoka moyoni mwangu sikutaka kupoteza muda, siku hiyo baada ya kutumiwa pesa na Farhia, siku iliyofuata nilimtafuta dalali ambapo nilimwambia dhamira yangu ilikuwa ni kupata fremu kwa ajili ya kufanya biashara ya mgahawa.
“Fremu zipo ni pesa yako tu,” aliniambia dalali aliyekuwa akiitwa kwa jina la Macho.
“Kuhusu pesa ondoa shaka bro,” nilimwambia huku nikimuondoa wasiwasi, yaani kwa jinsi nilivyokuwa nikizungumza muda huo, nilitamani dalali aniulize nilikuwa nina kiasi gani benki maana nilihisi kuwehuka.
“Sawa kuna fremu moja ipo maeneo ya Buza Kanisani, itakufaa,” aliniambia.
“Ipoje?”
“Kubwa halafu nayo ilikuwa ni mgahawa sema jamaa aliyeipangisha alishindwa kulipa kodi.”
“Naweza kuiona?”
“Leo?”
“Ndiyo kama itawezekana.”
“Haina noma, twende,” aliniambia.
Tuliondoka mpaka kufika Buza Kanisani ambapo dalali Macho alinionyesha fremu hiyo. Nilipoiona niliipenda sana na hapo hapo nilimwambia kwamba naitaka na hivyo anikutanishe na mmiliki aliyekuwa akiipangisha.
“Hebu subiri kwanza mbona wa moto sana,” aliniambia huku akinituliza muda huo.
“Nisubiri nini tena wakati nimekwambia naitaka,” nilimwambia.
“Hata kama ila hatuendi hivyo, unatakiwa kuwa mpole kila kinafuata taratibu.”
“Sawa nakusikiliza.”
“Huyu mwenye fremu anaishi Tabata.”
“Tabata ipi?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kimanga.”
“Kwahiyo?”
“Kama una muda niambie nikupeleke ukakutane naye ila tukifika huko sio uanze kuleta porojo, kama unaitaka kweli sema nikupeleke.”
“Bro mpaka nimekutafuta uje nina shida, naitaka hii fremu, nipeleke kwa mmiliki,” nilimwambia huku nikionyesha msisitizo wa kauli hiyo.
“Sawa ila itabidi unipooze kidogo, siunajua jiji hili joto halafu koo limenikauka,” aliniambia kwa sauti ya kulalamika kisha nikampa noti ya shilingi elfu kumi.
“Hapo sawa, umecheza kama pele mwanangu,” aliniambia huku akiachia tabasamu pana.
Hakukuwa kuna muda wa kupoteza tena, kwa kuwa nilihitaji kuonana na mmiliki wa fremu hiyo ana kwa ana hivyo dalali alinipeleka mpaka nyumbani kwake alipokuwa akiishi maeneo ya Tabata Kimanga.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulipofika nyumbani kwake na dalali kuanza kunitambulisha kwa mmiliki huyo kwamba mimi ndiye niliyetaka kuipangisha fremu yake nilimuona akinishangaa, kwa jinsi alivyokuwa akinishangaa ni wazi kwamba hakuamini kwa umri niliyoonekana kuwa nao kama ningeweza kuwa na pesa za kupangisha fremu hiyo iliyokuwa na gharama.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment