IMEANDIKWA NA : IRENE MWAMFUPE NDAUKA
*********************************************************************************
Simulizi : Niliwaroga Walimu Mpaka Basi
*********************************************************************************
Simulizi : Niliwaroga Walimu Mpaka Basi
Sehemu Ya Kwanza (1)
Siku hiyo mvua ilinyesha sana halafu shuleni kulikuwa na mitihani na mama alinitaka nirudi nyumbani kufanya kazi fulani, kwa hiyo nikaamua kumfuata mwalimu mkuu ambaye alikuwa ofisini kwake kwa lengo la kumbadilisha akili aseme wanafunzi wote turudi nyumbani hadi kesho yake.
“Nilisimama nje ya mlango wake, nikainama kwa sekunde chache, nilipoinua uso, nilibadilika ghafla na kuwa mwanafunzi wa kiume wa pale shuleni anayeitwa Juma Amosi.
“Nilishika mlango na kuufungua, nikazama ndani. Mwalimu mkuu alikuwa akitafuta mafaili kwenye kabati kubwa la ofisini kwake. Alishtuka kuona mlango umefunguliwa bila kugongwa.
“Ilikuwa ukitaka kuingia kwenye ofisi ya mwalimu mkuu ni lazima ugonge mlango na ukaribishwe kwa sauti, kinyume cha hapo usimame mlangoni mpaka atakapotoka au kukukaribisha kama una uhakika alikusikia.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wewe Juma ni kwa nini umeingia bila kupiga hodi?” mwalimu aliniuliza. Nilisimama katikati ya ofisi kama mwanajeshi, nikamkazia macho badala ya kumjibu, niliulekeza mkono wangu usawa wake, ukamfikia kwa kurefuka, nikamshika kichwani.
“Palepale akaanza kutabasamu huku akisema nikapige kengele ili wanafunzi wakusanyike mstarini kwa ajili ya kuwaambia jambo la dharura.
“Nilipotoka kwenda kugonga kengele, nilisimama mlangoni tena, nikabadilika na kuwa mjusi, nikakimbia chini kwenda mpaka kwenye mti wa kengele, nikabadilika tena na kuwa Yusta yuleyule. Nikagonga kengele.
Kwa kengele ya muda ule kila mtu alijua kulikuwa kuna dharura, kwa hiyo wanafunzi wakatoka kwenda mstarini ili kusikiliza.
Nilikwenda mstarini kwa kuzunguka nyuma ya shule ambako haikuwa rahisi mtu kuniona kama mimi ndiye niliyegonga kengele, nikafika mstarini na kusimama.
Baadhi ya walimu walitoka ofisini kwao na kuja usawa wa mstari huku wakionekana kushangaa.
“Nani amegonga kengele?” aliuliza mwalimu mmoja aliyejulikana kwa jina la Cecilia Kizigo.
“Hatujui,” wanafunzi mbalimbali walijibu huku wengine wakiendelea kushangaa.
Mara, mwalimu mkuu alitoka akiwa ameshika kitabu mkononi. Alitembea mpaka usawa wa walimu wa kawaida, naye akauliza kengele ni ya nini?
Walimu wengine wakamjibu hawajui. Sasa ikawa nani kapiga kengele, nani kapiga kengele. Kumbe mwanafunzi mmoja aliniona nikipiga mimi kama Yusta, akanitaja. Kwanza kabla hajanitaja alinyoosha mkono, mwalimu wa zamu akamuita jina:
“Hamisa unasemaje?”
“Mwalimu mi nilimwona Yusta akipiga kengele.”
“Yusta toka mbele,” yule mwalimu aliniamuru, nikapita mbele nikiwa na wasiwasi, lakini si sana.
“Nani alikwambia ugonge kengele?” yule mwalimu wa zamu aliniuliza kwa ukali.
“Juma.”
“Juma gani?”
“Juma Amosi.”
Niliposema Juma Amosi tu, mwalimu mkuu akatingisha kichwa kama anayekubaliana na mimi.
“Kweli atakuwa Juma Amosi. Alikuja hata kwangu akasema kengele igongwe anataka kuzungumza jambo.”
Walimu walionekana kumshangaa sana mwalimu mkuu kwa kauli yake hiyo, pengine kwa sababu haijawahi kutokea siku mwanafunzi akataka kengele igongwe ili aongee, mara nyingi wafanyao hivyo ni viongozi wa shule.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Juma Amos,” mwalimu wa zamu alimuita mbele, akatoka.
“Naam mwalimu.”
“Ulitaka kuongea kitu gani wewe mpaka ukaenda kwa mwalimu mkuu na kuomba kengele igongwe?”
Juma Amos alionesha kushangaa, akaniangalia mimi kwa macho ya kunisuta, lakini na mimi nilijikausha.
“Mwalimu mimi namshangaa sana Yusta, sijamtuma.”
“We!” mwalimu mkuu alikuja juu, akaendelea:
“Wewe hukuja ofisini kwangu ukasema unataka ugonge kengele ili uongee jambo?”
“Mwalimu sijaja.”
“Weee,” mwalimu mkuu aliwaka tena. Cha ajabu, Mwalimu Cecilia akamtetea Juma Amosi kwamba, yeye mpaka kengele inagongwa alikuwa darasa la akina Juma Amosi, hajamwona akitoka zaidi ya muda ule kengele ilipogongwa.
“Mimi kwa macho yangu amekuja ofisini kwangu, akasema kuna kitu anataka kuzungumza na wanafunzi wote, nikamwambia akagonge kengele, sasa mwalimu unapomtetea unafanya makosa. Na yeye anapokataa namshangaa sana,” alisema mwalimu mkuu.
Mimi nikamkazia macho Mwalimu Cecilia kama ninayemwambia aseme lingine, mwalimu mkuu ameshapigilia msumari. Lakini baadhi ya wanafunzi wa darasa moja na Amos niliwaona katika sura za kushangaa tukio la mwenzao kuambiwa alitoka darasani.
“Yusta,” aliita mwalimu mkuu.
“Bee.”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Si Amos ndiyo amekwambia ukagonge kengele?”
“Ndiyo mwalimu.”
“Mwalimu Yusta ni mwongo sana,” alisema Amos.
“Mwalimu mimi si mwongo, ni mkweli.”
Mabishano kati yangu na Amos yalidumu kwa dakika moja nzima huku walimu wote wakiwa wametukodolea macho.
Nilipoona hakutapatikana mshindi, niliamua kuchukua uamuzi mwingine. Nilimkazia macho mwalimu mkuu, kisha nikasonya ndani ya moyo, palepale mwalimu akaanza kuchekacheka na kusema:
“Sasa sikilizeni. Mimi naamua, wanafunzi wote mrudi nyumbani mpaka kesho. Maana hapa mambo yameshaanza kuwa mabaya.”
Wanafunzi walifurahi sana, lakini walimu walionekana kutomwelewa mwalimu mkuu kwa uamuzi wake huo tena wa ghafla:
“Mwalimu, yaani suala la nani kamtuma Yusta akagonge kengele ndiyo litutoe nje ya shule muda huu hata saa tano bado huku leo tuna mitihani? Mimi sikubaliani hata siku moja,” alisema Mwalimu Cecilia.
“Hiyo hali ya hewa unayosema imeshakuwa mbaya ni ipi?” alihoji mwalimu mwingine ambaye tulizoea kumwiita Mikogo kwa jinsi alivyokuwa akitembea kwa kunesanesa na urefu wake.
“Mimi nikiamua jambo nimeamua, sidhani kama hapa kuna suala la mjadala, nimeamuanimeamua,” alisema mwalimu mkuu huku akigeuza na kurudi ofisini kwake.
Kufumba na kufumbua, wanafunzi tulishaanza kushika njia ya kurudi majumbani kwa mwelekeo mmoja. Kabla hatujamaliza kuondoka eneo la shule, kengele iligongwa tena, wanafunzi tukasimama kuangalia shuleni.
Tulimwona Mwalimu Cecilia akituita kwa ishara ya mkono, wengine walirejea lakini wengine, nikiwemo mimi tuliangalia mbele na kutokomea.
Nilimkuta mama akinisubiri. Aliponiona alikunja sura, akaniuliza:
“Kwa nini umechelewa?”
“Nilikuwa naweka mambo sawa mama. Kulitaka kutokea kikwazo.”
“Nani alitaka kuweka kikwazo. Niambie sasa hivi nimjue. Mimi sipendagi mambo ya kijingajinga wakati nina uwezo,” alisema mama akionesha hatanii.
“Mwalimu Cecilia na Mikogo.”
Mama aliingia ndani ghafla, nikamfuata. Alichukua ungo akaja nao sebuleni, akaubwaga kwenye kiti kisha akainua mikono juu kama mchungaji anayeomba dua.
“Agggggggh! Mwalimu Cecilia. Mmmmh! Agggggh! Mwalimu Cecilia.”
Palepale Mwalimu Cecilia alitokezea kwenye ungo akiwa amekaa ofisini kwake.
“Wewe mwalimu na huyo kikaragosi mwenzako, Mwalimu Mikogo, ole wenu kumwingilia mwanangu kwenye maisha yake. Nasema ole wenu,” mama alisema akimnyooshea kidole Mwalimu Cecilia pale kwenye ungo.
“Umenielewa?”http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mwalimu Cecilia alimwitikia kwa kubetua kichwa, kisha akapotea. Mama alichukua ungo na kuurudisha chumbani kwake, akatoka akisema:
“Inabidi ubadili nguo twende sasa.”
“Tunakwenda wapi mama?” mimi niliuliza.
“Kabadili nguo wewe.”
Nilitii. Nilikwenda chumbani kwangu uani, nikavua sare za shule na kuvaa gauni na khanga kwa kuizungushia.
Nilipotoka, mama alitoka nje, nikamfuata, akafunga mlango kwa funguo, nikahisi tunakwenda mbali na nyumbani. Alipiga magoti mbele yangu akaniambia nipande mgongoni mwake, nikafanya hivyo.
Baada tu ya kupanda, kufumba na kufumbua tulijikuta tupo mjini Handeni. Mama aliniambia tulikwenda kumsaidia mwenzake kuroga watu wenye watoto hospitalini. Yaani wanawake wenye watoto wamelazwa au wamewapeleka kliniki.
Ilivyo ni kwamba, kwa huku Handeni, wakati wa msimu wa kilimo cha mahindi, wakulima ndiyo huitumia nafasi hiyo kuroga au kufanya vitendo vya kishirikina ili kupata mazao mengi.
Unaweza kukuta mkulima anamiliki shamba la miguu ya mtu mzima mia moja tu kwa mapana na marefu yake, lakini mazao atakayoyatoa hapo utashangaa. Hatofautiani na mtu mwenye shamba la maeka kwa maeka. Hii mara nyingi hutokana na mambo au niseme vitendo vya kishirikina.
Tulifika hospitalini na kumkuta huyo mwanamke anayesaidiwa na mama. Alisimama pembeni ya geti lakini hakuna mwanadamu wa kawaida aliyekuwa na uwezo wa kumwona kwa macho ya kawaida.
Alipotuona, alituita kwa kufanya ‘tsii’. Hivi ndivyo wachawi wengi wanavyoitana. Kama umewahi kupita mahali ukasikia ‘tsii’ jua kuna wachawi hapo wameitana.
Mimi na mama tulitembea kumfuata pale, akatoa vitambaa vyeusi viwili, vyote akavipokea mama. Kimoja akajifunga kwenye paji la uso kuzungukia kisogoni, kingine akanipa mimi na kuniambia nijifunge kama yeye.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilifanya hivyo. Baada ya hapo tukaanza msafara wa kwenda ndani ya hospitali. Tulipofika mlango mkubwa, yule mwanamke akageuka, akawa anatembea kinyumenyume kwenda. Mama naye akafanya hivyo na mimi nikaiga bila hata kuelekezwa na wao.
Ili kujua kama wenzangu bado wananyoosha au wamekata kulia au kushoto, niliinama zaidi na kuwaangalia kwa kupitia katikati ya miguu, sikuwaona, nikashtuka na kusimama, nikageuka ili niwaangalie vizuri.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment