Search This Blog

MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN (2) - 5

 










Simulizi : Mkufu Wa Malkia Wa Gosheni (2)

Sehemu Ya Tano (5)





Sasa alikuwa anafahamu safari yake inaelekea ukingoni. Moyoni alijawa na furaha sana na hakutaka kungoja tena kuijaza zawadi mikono mwake.



Waheed akatabasamu. Mbele yake kulikuwa kuna lango kubwa. Lango kubwa la chuma. Na humo ndani ndimo kuna kofia ya pharao!



Akasogelea lango hilo na kuweka kiganja chake hapo. Mara lango likang'aa na kujiandika maneno kadhaa:



'Ndani mfalme amepumzika. Ni nini unataka?'



Waheed akatabasamu mwenyewe. Alikuwa ana hamu pomoni kushuhudia kwa macho yake kitu ambacho amekuwa amehadithiwa maisha yake yote.



Basi kwa kutumia kidole chake akaandika:



'Nataka kofia ya pharao'



Akangoja majibu. Kimya.



Akaweka tena kiganja chake juu ya lango. Mara maneno yale yaliyotokea awali yakajiandika tena.



'Ndani mfalme amepumzika. Ni nini unataka?'



Waheed akaandika:



"Nataka kofia ya Pharao'



Ikawa kimya tena. Hakupata majibu. Akaweka kiganja kwa mara nyingine. Mara hii akaandika anaomba kofia ya Pharao. Bado majibu yakawa yaleyale. Kimya. Akaweka tena kiganja na sasa akaandika tafadhali naomba kofia ya Pharao.



Majibu hayakubadilika. Kimya.



Akashika kiuno chake akiwaza. Fikra ikamjia kichwani. Akaweka kiganja tena kwenye lango, mara hii akaandika:'



'Nataka kumwamsha Pharao!'



Mara lango likaandika kuuliza:



'Unacho cha kumfanya aamke?'



Waheed akafikiri kwanza. Tamaa ikamzidi hamu akaandika kujibu:



'Ndio.'



Mara lango likafunguka. Waheed akazama ndani na lango likajifunga. Humo ndani kulikuwa na kama kauwanja. Kwa mbele, juu kidogo, kulikuwa na kiti kimoja kikubwa kilichotengenezwa kwa dhahabu.



Kwenye kiti hicho alikuwa kulikuwa kumekaliwa na mifupa ya binadamu. Haikuonyesa chembe ya uhai. Mifupa hiyo ilikuwa ni ya Pharao aliyekufa miaka lukuki huko nyuma!!



Juu ya fuvu ya mifupa hiyo kulikuwa na kofia ya dhahabu! Kofia inayometameta. Kofia ambayo kwa kuitazama ungetambua ni ya thamani kiasi gani!



Japo ilikuwa ya muda mrefu hapo nyuma, kofia hii bado ilikuwa mpya. Inavutia machoni na kushawishi kuinyakua!!



Waheed mate yakamtoka. Sasa kazi kwake ilibakia moja tu. Kwenda kuinyakua kofia ile na kutokomea zake akaitawale dunia.



Lakini kabla hajapiga hatua kuifuata kofia hiyo, akawaza. Li kwapi jeshi la wafu?? Lile alilokuwa anaambiwa habari zake za kutisha kwamba ukizama humo basi utapambana nalo??



Akatazama kando na kando, hakuona kitu! Kakiwanja haka kalikuwa cheupe, mabaki tu ya vitu vya kale hapa na pale. Mbali na mifupa ya Pharao hakukuwa na mifupa mingine ya ziada.



Basi Waheed akaanza kujongea kuelekea kitini. Moyoni alikuwa ana hofu, akawa anatazama nyuma na pembeni yake mara kwa mara.



Akafika kitini hapo. Akameza mate kwanza. Akashika kofia ile na taratibu akainyofoa kichwani kisha akatulia kusikilizia kama kuna lolote litatokea. Kimya. Hakuna kitu!!



Akatabasamu na kushusha pumzi ndefu.



Akakumbatia kofia ile na kuanza kupiga hatua za haraka kwenda langoni. Akaweka kiganja chake hapo, na mara Lango likaulizia ahadi aliyoiweka hapo awali kwa njia ya maandishi.



"Umeshamwasha mfalme?"



Kabla Waheed hajajibu, mara lango likaandika tena:



"Ahsante kwa kutimiza ahadi."



Hapa Waheed akashtuka. Ahadi gani hiyo? Mbona hakumwamsha mfalme??



Kutazama nyuma, hamaki akaona mifupa ile iliyokuwa imeketi pale kitini, imenyanyuka!!



Pharao alikuwa ameamka!



Mara Lango likafunguka, Waheed akataka kukimbia, lakini asiende popote akakutana na JESHI LA WAFU mlangoni!!



Watu hawa wote walikuwa ni mifupa tu. Mikononi mwao walikuwa wamebebelea mapanga yaliyoota kutu. Wengine wakiwa na mikufu shingoni ama pete za dhahabu vidoleni.



Waheed alipotazama vema, akashtuka, kwa kando alimuona Seth, mara akamwona na Alk - jitu la Azeth, mwishowe Fluffy!!



Watu hawa wote walikuwa wafu. Miili yao bado ilikuwa na mabaki ya damu na matundu ya visu walivyokitwa na Waheed.



Nao walikuwa tayari miongoni mwa jeshi la wafu. Macho yao yalikuwa mekundu na makali. Sura zao za kutisha. Sura za kazi!!







Waheed akameza mate kwa uoga. Aliona sasa maisha yake yamefika ukingoni. Kazi yote aliyoifanya haikuwa na matunda yoyote yale.



Akatamani kudondosha chozi. Moyo wake ukapiga sana wakati kichwa chake kikiwaza nini afanye.



Akasikia kishindo nyuma yake. Kugeuka na kuangaza akaona mifupa ya Pharao tayari imemfikia! Pharao akanyoosha mkono wake akitaka kofia yake. Waheed akaitazama kofia kwa matamanio.



Hakutaka kuiachia!!



"Tafadhali," akapaza sauti. "Naomba unikabidhi kofia hii!" Akasema akikunja shingo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Pharao akamtazama kisha akamuuliza:



"Kwasababu gani nikupatie kofia hiyo?"



"Kwasababu nimeihangaikia vya kutosha!" Waheed akajitetea. Pharao akacheka.



"Umeihangaikia?" Akauliza kwa kebehi. "Kwa kuua wenzako na kuwatoa sadaka?" Pharao akawanyooshea kidole wakina Seth.



Kisha akatikisa kichwa.



"Hapana! Huwezi ukapata kofia hiyo. Roho yako haistahili. Roho yako bado haipo tayari! Utaenda kuendeleza yaleyale yaliyonifanya nikalaaniwa na kutupiwa humu!"



"Hapana!" Waheed akajitetea. "Sitafanya hivyo. Naahidi kuwa mwema."



"Mwema?" Pharao akastaajabu. "Mwema na hali ushamwaga damu za wenzako ndani ya Piramidi hili. Zipo za kulilia?"



Pharao akamsogelea Waheed karibu.



"Kofia hiyo kamwe haitabakia tena hapa Misri. Itaondoka kwenda mbali na haitarudi hapa kamwe. Katika ardhi hii ililaaniwa ... katika ardhi hii haitabakia."



Mara lile jeshi la wafu likajigawa pasu kwa pasu, na mara akaonekana Malkia akiwa anaongozana na Zura!! Malkia alikuwa amebebelea panga mkononi mwake, wakati Zura akiwa ameshikilia ginga la moto.



Waheed akashangaa sana. Imewezakanaje??



Malkia na Zura wakasonga mpaka pale walipokuwa wamesimama. Pasipo kuongea jambo, wakamtazama Waheed na kisha Pharao.



"Unamwona mwanamke huyu?" Pharao akamuuliza Waheed. "Alifika hapa akiwa wa kwanza baada ya kumezwa na mlango wa kiza. Na alikuja kwasababu ya kumwokoa mwenzake aliyemezwa hapo awali. Wewe ungekuwa na roho hiyo?"



Waheed hakuwa na jibu. Pharao akaendelea kunena.



"Alifika hapa tayari mwenzake akiwa amezingirwa na jeshi langu kuuawa. Akaomba nimbakizie uhai. Nikamuuliza kwanini nimbakizie uhai huo? Unajua akasema nini?"



Waheed akatikisa kichwa.



"Akasema yupo radhi kutoa mali yake ya thamani sana, alimradi nibakize uhai wa mwenzake. Alikuwa radhi kufanya hivyo. Tena pasipo kinyongo chochote. Kabla sijakubali, akavua mkufu wake na kunikabidhi.



Nikautazama mkufu huo. Alaah! Nikagundua ni wenye thamani na nguvu kubwa mno. Ni kwamba tu mkufu huo uliingia ndani ya Piramidi hii ndiyo maana ukashindwa kuonyesha uwezo wake ila huko nje ni amali kubwa sana.



Lakini alikuwa radhi kuitoa, pasipo kinyongo chochote, akitaka nibadilishane nayo kwa uhai wa mwenzake."



Pharao akauliza tena:



"Wewe ungeweza ilhali ulikuwa tayari kumuua yoyote yule upate kofia yangu? Unanishawishije hutaenda kufanya hivyo hivyo huko nje?"



Pharao akampokonya Waheed kofia yake kisha akamsogelea Malkia na kumkabidhi kofia hiyo mikononi mwake.



"Unastahili kuwa na hili."



Lakini Malkia akapokea kofia hiyo kwa machozi. Akamwambia Pharao.



"Nisingalipajua hapa kama asingelikuwa yule!" Akamnyooshea kidole Fluffy. "Hii ramani ilikuwa yake. Tulianzia kwake, japo safarini tukawa wote. Na nisingefika hapa bila wale." Akawatazama wakina Seth na Alk.



Kisha akauliza:



"Ni nini kofia hii pasipo kuwa nao pamoja?" Akamrudishia kofia Pharao kisha akamwomba:



"Warudishie uhai wao. Nipo radhi kuondoka nao wakiwa hai pasipo kofia hiyo."



Pharao akanyamaza kwanza. Akaiveka kofia yake kichwani kisha akawasogelea wakina Seth. Akawatazama na kuwagusa vifuani mwao. Mara wakawa wazima!!



Wakakumbatiana na wakina Malkia kwanguvu wasiamini macho yao.



"Nakushukuru sana," Malkia akatetema kwa furaha. "Sasa tunaweza kwenda."



"Si kwa haraka hivyo!" Akasema Pharao, kisha akavua kofia yake na kumkabidhi Malkia mkononi.



"Bado unastahili kuwa nayo!"



Malkia akadondosha machozi ya furaha.



"Kuanzia sasa utakuwa jemedari mkuu wa jeshi la wafu. Watasikia sauti yako popote pale utakapokuwepo, na watafuata amri yako kwa maisha yao yote yasiyo na kikomo!"



Baada ya hapo, jeshi likaanguka chini kusujudu mbele ya Malkia. Kisha likatengeneza njia ya Malkia na wenzake kukatiza.



"Sasa mnaweza kwenda," Pharao awakaonyeshea mkono njiani. Malkia na wenzake wakashika njia kujiendea. Waheed alipotaka kuongozana nao, Pharao akamdaka bega na kumwambia:



"Wewe utabaki na mimi hapa!"



Waheed akaogopa. Akahofia sana.



"Kwanini? Nami naomba niende."



"Si mapema hivyo!" Pharao akasema akitisa kichwa chake kisha jeshi la wafu likasonga karibu kumtwaa Waheed.



**



"Hatimaye tumetoka!" Seth alisema kauli ya kwanza baada ya kutoka katika lango la Piramidi. Haikuwa jambo la kawaida hata kidogo. Hakuna mtu aliyewahi kuingia humo akatoka akiwa hai.



Wao walikuwa watu wa kwanza kuvunja mwiko huo. Walijawa na matabasamu na sura zilizoshiba furaha. Hakika hili lilikuwa jambo kubwa. Si kutoka tu hai, bali kutoka na kile walichokuwa wameenda kukifuata.



Kofia ya pharao!!



Malkia alikuwa ameishikilia kofia hiyo mkononi akiitazama na kuipapasa kila muda. Katika hali isiyo kawaida kofia hiyo ilikuwa imeshajitengeneza kutoshea kichwa cha Malkia.



Hiyo ilionyesha kofia hiyo ni ya kwake, mali yake, si ya mtu mwingine yeyote yule!



"Sasa ni muda wa kurudi kwenye himaya yetu," akasema Malkia kwa ujasiri.



"Sasa ni muda wa kurudi tunapotakiwa kuwa!" Lakini vipi kuhusu Alk? Akauliza Seth. Je, yeye atarejea kule kwa wenzake, Azeth, ama wataongozana naye njia moja?



"Tamil khati zha guin?" Seth akamuuliza Alk akimwekea mkono begani. Jitu hilo likatikisa kichwa chake. Macho yake yalikuwa mekundu. Aling'ata meno yake kisha akasema;



"Zeth jhin. Sikaf jaitu anil." Akimaanisha nimepata familia yenye upendo wa dhati. Nami nina furaha nayo.



Malkia na wenzake wakafurahi mno kusikia hayo. Walikuwa zaidi ya watu wanaojuana. Walikuwa ni familia yenye upendo wa dhati.



Lakini furaha yao hiyo haikudumu kwa muda mrefu, mara wakazingirwa na jeshi la Misri!!



Wanajeshi walikuwa juu ya migongo ya farasi mikononi mwao wakibebelea silaha mathalani mikuki na mishale.



"Hapo hapo mlipo simameni!" Amri ikatolewa na mkuu wa kikosi. Alikuwa ndiye yule mwanajeshi aliyewaongoza wenzake kutaka kumkamata Malkia siku kwanza kuingia Misri kabla ya kuokolewa na Waheed.



"Ninyi ni wezi. Na mlikuja hapa Misri kuja kutuibia??" Alifoka mwanajeshi huyo kisha akatoa amri:



"Kabidhini hiyo kofia mara moja kabla sijaamuru mgeuzwe marehemu ndani ya sekunde!" Aliongea akiwa na uso usio na lepe la masikhara hata punje!!



Malkia akatikisa kichwa akibinua mdomo.



"Haiwezekani," akawaambia wenzake. "Kuhangaika wenyewe ndani ya piramidi alafu waje kulichukua mlangoni?



Basi Malkia akaivaa kofia ile, kisha akanuwia maneno kadhaa kifuani mwake. Kabla hajaufungua mdomo, mara chini ya ardhi ikaanza kutikisika. Kufumba na kufumbua wakaanza kunyanyuka viumbe!!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Walikuwa ni JESHI LA WAFU!!



Walikuwa mamilioni!!





Wanajeshi wa Misri wakajawa na uoga. Hata farasi zao wakaanza kukimbia. Walikuwa ni wachache mno ukilinganisha na jeshi la wafu. Na hata kama jeshi la wafu wangelikuwa wachache bado wasingelifua dafu, utapambanaje na watu wasio kufa??

Wale wanajeshi wakaidi wakajitutumua kupigana. Wote wakageuzwa marehemu. Yule kiongozi wa kikosi akaokoa nafsi yake kwa kukimbiza miguu ya farasi wake mpaka kwa mfalme.

Huko akatoa taarifa kuwa kofia ya Pharao imekombolewa toka kwenye piramidi!! Na wameshindwa kupambana na mwivi.

Basi mfalme akashangazwa sana na hizo habari. Nani kaikomboa kofia hiyo?? Amewezaje?? Na zaidi ya hapo mfalme akahofia sana kama kofia hiyo isipokuwa mkononi mwake.

Alihofia pengine mtu huyo aliyepata hiyo kofia ataitumia kuiweka himaya ya Misri chini ya miguu yake. Kitu ambacho hakuwa radhi kitokee!!

"Taarifu majemedari wote. Hii ni tangazo la tahadhari. Jeshi zima liende huko, wakapambane na kuhakikisha wanaipata kofia hiyo!"

Ndani ya dakika chache jeshi la himaya nzima ya Misri likajikusanya, na wakiwa wanaongozana na majemedari wao hodari, wakaelekea eneo la vita.

Wakawakuta wenzao hoi mno. Wamebaki wachache kumalizwa!! Wakatumia kila zana na akili zao kupambana. Wakatumia nguvu mno kuhakikisha wanaipata kofia, hawakuwa abadani!

JESHI LA WAFU lilikuwa la kipekee. Hawakuwa wanapigana katika njia ya binadamu hata kidogo. Walikuwa na uwezo wa kuzama ardhini kama fuku kisha wakaibukia kwa adui!!

Hata wakikatwa na mapanga, walikuwa wanakusanya tena mifupa yao na kusimama upya. Wanajeshi wa himaya ya Misri wakatepeta. Wote wakauawa isichukue hata lisaa limoja!

Habari zikasambaa himaya nzima. Huko kuna mwanamke anamaliza jeshi!! Wengine wakajifungia ndani ya makazi yao, wengine, waliojawa ma ujasiri, wakaends huko kutazama kinachotokea.

Haikuwa habari ya kuaminika upesi!!

Baada ya Malkia kumalizana na jeshi la Misri, akiwa anaongozana na jeshi lake la wafu wakaelekea mpaka ikulu ya mfalme. Wakasimama nje, Malkia akapaza sauti:

"Ewe mfalme wa Misri uliyetuma majeshi yake kunimaliza, nimefika langoni mwako nami nikiwa sina ubaya nawe. Tafadhali jitokeze!"

Walinzi wa hapo kasrini walikuwa wamejawa na hofu kisado. Japo walikuwa mbele kutimiza kazi yao, miili ilikuwa inavuja na mioyo kuwaenda mbio.

"Nenda kaonane naye!" Mke wa mfalme alimshauri mumewe. Walikuwa wamejifungia ndani. Mlango umefunikwa na kila zana ya ulinzi ma wanajeshi ishirini wakiwa wamesimama langoni hapo.

Mfalme alikuwa anaogopa. Mwili wake ulimtetemeka na akili yake haikuwa inafanya kazi kwa muda huo hata chembe.

Baada ya mkewe kumsisitizia atoke na kwenda kumalizana na Malkia kidiplomasia. Akapiga moyo konde na kwenda huko nje.

Hakukuwa na haja ya kuendelea kujificha zaidi. Kwani kiuhalisia kama Malkia angeamua kuzama humo ndani, asingeshindwa kama aliweza kuteketeza jeshi la watu maelfu!

"Unataka nini ndani ya himaya yangu?" Mfalme akauliza. Alikuwa amesimama juu ya kilinge akimtazama Malkia kwa chini.

"Hakuna ninachotaka toka kwako kwani sijapungukiwa," Malkia akaongea kwa ujasiri. "Nipo hapa si kukuondoa madarakani, wala kuhangaika na chochote na himaya yako. Nipo hapa kuongea na wewe."

Malango yakafunguliwa, Malkia akazama ndani akiongozana na wakina Seth. Hata hakuketi. Akamwambia Mfalme wanahitaji manowari moja kubwa ya kusafiria kurudi huko walipotokea.

"Ninyi ni wakina nani na mmetokea wapi?" Mfalme akauliza.

"Mimi ni Malkia Sandarus, hawa washirika wangu, tumetokea Goshen!" Malkia akamjibu. "Nisingependa kumaliza siku yangu nikiwa hapa, bila shaka hata wewe ungependa hivyo. Nahitaji kuondoka. Harala iwezekanavyo kwani nina safari ndefu majini."

Mfalme akanyamaza kwanza akifikiri. Punde akasema yuko radhi kuwapatia manowari wanayoihitaji. Tena hata kama ni nne, moja ikawabeba na nyingine tatu ikabeba mali atakazowapatia.

Lakini wamwachie ile kofia tu!!

"Haitawezekana," Malkia akasema akimtazama mfalme machoni. "Hii nimekabidhiwa mimi na si mwingine yoyote yule."

Kisha akatoa msimamo wake,

"Ni aidha utupatie manowari tuondoke zetu ama tuendelee kubaki hapa ... na kukuteketeza!"

Mfalme akameza mate. Alighadhabika lakini hakuwa na cha kufanya. Jeshi lake lote limeshakwisha na malangoni wamejipanga wafu wakingoja amri.

Akawapatia malkia manowari moja ya kifalme. Na kama haitoshi akaongozana mpaka bandarini, akitaka kushuhudia mwanamke huyo akiondoka zake na namna gani atapakiza jeshi lake ndani ya manowari moja!

Ajabu machoni mwake walipofika huko, akastaajabu kuona jeshi la wafu linapotelea ardhini na Malkia pamoja na wenzake pekee wakikwea chomboni na kwenda zao.

Watu wa Misri wakawa wamesimama wanaduwaa. Hawakuamini macho yao.

Mwanamke!!

Amechukua kofia ya Pharao ndani ya piramidi! Kwa mfalme ilikuwa ni aibu na fedheha kubwa. Alivuliwa nguo mbele ya wananchi wake!!

Macho yake yalijawa na machozi akiwatazama wakina Malkia wanayoyoma. Aling'ata meno yake kwa hasira.



**



"Ni hapa!" Akasem Oragon akimtazama yule jabali wa Rabis. Walikuwa ndani ya msitu mkubwa ambamo humo walimwambia Rabis kunapatikana kitu cha pekee chenye thamani zaidi ya uhai wao.

Humo kuna kitu ambacho kingemfanya Rabis abadilishe mawazo yake ya kuwamaliza kwa kosa ambalo kiuhalisia hawakulifanya wao bali wale majamaa zao waliowatuma.

"Una uhakika?" Aliuliza jabali la Rabis. Mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea chepeo kubwa na mkono wake wa kuume akiwa ameshikilia jembe.

"Ndio tuna uhakika!" Akadakia Ottoman. "Humo kuna kifurushi cha dhahabu majamaa wale walikifukia!"

Kwa akili yao walikuwa wanataka kumtega jabali huyu wapate kujikomboa. Pindi tu atakapoanza kuchimba ardhi basi watatazama jiwe, ama watatumia moja ya dhana zake kummaliza. Ama kote ikishindikana, basi wakimbie kuokoa uhai wao.

Lakini kinyume na mawazo hayo, yule jabali akaenenda tofauti!! Aliwatazama na kisha kila mmoja akampatia dhana yake na kuwaamuru wachimbe haraka iwezekanavyo.

Basi wakina Oragon wakaanza kuchimba. Vichwani mwao wakiwaza namna gani watajikomboa na jabali lile. Kila walipomtazama wakakutana naye macho kwa macho!! Hakuwa anabandua macho yake wala kuyapeleka pembeni.

Baada ya muda kidogo yule Jabali akaanza kuwapa vitisho kwa sauti yake nzito.

"Tupo katikati ya msitu mkubwa, hata nikiwaua hakuna atakayewasikia. Nikishawamaliza nitawatupia mbwa mwitu mizoga yenu, hamtabaki hata chembe!"

Wakina Oragon wakazidi kujawa na hofu. Walikuwa wanasali kila aina ya sala vifuani mwao wapate kukomboka hapo, japo hakuwa wanajua ni kwa namna gani.

Kweli vile mungu wao akazisikia hizo sala. Wakiwa wanaendelea kuchimba ardhi kwa kitu ambacho hakipo, mara wakasikia sauti za watu! Jabali akashtuka na kuangaza.

Ndani ya muda mfupi watu hao wakatokea. Walikuwa ni wanajeshi wa himaya. Na humo ndani msituni walikuwa wakifanya msako wa watumishi wa kuhani Raam baada ya kuhani huyo kutoa taarifa kupotea kwao na wananchi kusema mara yao ya mwisho kuwatia machoni walikuwa wakielekea msituni wakiwa wamembebelea kijana mmoja begani.

Hii ikawa kama bahati ya mtende haswa kwa wakina Oragon. Kwenye macho yao, hawakuwaona wanajeshi kama binadamu bali malaika wa ukombozi.

Kitendo tu cha kuwaona wakajikuta wamepata ahueni vifuani mwao.

"Ninyi ni wakina nani na mwafanya nini humu msituni?" Kiongozi wa kikosi akauliza.

Basi yule jabali haraka akawahi kwa kusema wao ni wamanchi tu wa kawaida na wapo humo msituni wakichimba andaki la kuhifadhi vitu vyao vya thamani visije kwapuliwa na wezi waliotapakaa.

"Mwongoo!" Ottoman akamkatiza. Aliwatazama wanajeshi kwa sura ya imani akawaambia: "Ametuteka na akatuamuru tuchimbe kaburi atuzike!"

Kabla wale wanajeshi hawajafanya lolote, mwanajeshi mmoja akamsogelea yule mkuu wao wa kikosi na kumnong'oneza:

"Unamkumbuka Yabin? Yule mhalifu anayetafutwa himaya nzima kwa mwaka sasa? ... si ndo huyo hapo!"

Yule jabali akahisi huu mchezo. Tayari ameshashtukiwa. Mkuu wa kikosi alimtazama kisha akamuuliza ataje jina lake. Wakati huo wanajeshi wengine wakisonga karibu kujiandaa kwa lolote litakalotokea.

Jabali likaguna. Mara likajifyatua na kudaka dhana toka kwa Oragon na Ottoman, mkono wa kulia akashika jembe na wa kushoto chepeo tayari kwa ajili ya kupambana.

Wanajeshi nao wakashika silaha zao, mikuki na majambia. Vita ikaanza!!

Kwa kunguru punde panzi wapambanapo, kwake si tanga bali sherehe. Taratibu wakina Oragon wakatoroka na kukimbia kadiri ya uwezo wao kuukata msitu.

Hawakupumzika abadani, mapafu yakanyauka na midomo ikawakauka mate. Pindi walipofika mitaani wakajikuta hawawezi tena kukimbia!

Miili ilikuwa imechoka na kila kiungo sasa kipo hohehahe.

Wakaomba hifadhi. Wakakaa hapo kwa muda kidogo baada ya kukarimiwa kwa kupewa maji na chakula kidogo.

Lakini kabla hawajatoka humo wakagundua huko nje wanajeshi walikuwa wanarandaranda huku na kule, wengine wakiwa juu ya farasi na wengine kwa miguu.

Na haikuwa sayansi ngumu hii kuitambua, kuwa wao ndio walikuwa wakitafutwa!



***Wakajawa na hofu sana na pengine sasa vichwa vyao vikakubaliana kuwa kamwe hawataishi kwa amani ndani ya himaya ile ya kigeni.



Toka wameingiza mguu wao humo maisha yao yamekuwa ya kuhaha. Kuhangaika na kurandaranda. Swala hili liliwaumiza sana.



Na wakafikiria kama kuna haja ya kukimbilia himaya nyingine pengine huko watapata ahueni. Lakini vipi napo pakawa hapana unafuu? Watakimbilia kwenye himaya za watu mpaka lini? Swala hili likawaumiza vichwa haswa.



Baadae walipoona hali ni shwari, wakaaga na kwenda zao. Kwa tahadhari kubwa wakatembea mpaka kurejea kule kwa majamaa zao. Walipofika hawakuwakuta, nyumba ilikuwa tupu.



Wakatulia na kungoja. Wakarafuta kama kulikuwa na chochote cha kutia mdomoni maana matumbo yalikuwa matupu, napo wakakosa. Vyombo vilikuwa vichafu na vikavu!!



Tangu asubuhi walipoamshwa na kuwajibishwa kwenda kwa Rabis hawakuwa wametia kitu mdomoni mpaka muda huo, achilia mbali vitumaji na vituchakula walivyovipata toka kwa msamaria mwema aliyewasitiri.



Njaa ilikuwa inawaum na kadiri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo hali ikazidi kuwa mbaya zaidi.



"Tunafanyaje sasa?" Ottoman akauliza. Alikuwa amekunja sura kulalama na njaa ikwanguayo tumbo.



"Sijui," Oragon akamjibu kaka yake akipandisha mabega. "Tungoje, labda wanaweza wakaja na chakula."



Wakangoja lakini wakijua jambo hilo ni la uwezekano mdogo tu. Wale majamaa kurejea na chakula, haikuwa kitu cha kuipa kipaumbele, ila hawakuwa na namna zaidi ya kungoja.



Wakakaa humo mpaka wakaanza na kusinzia. Majira ya jioni kabisa, jua likiwa limeshafifia wakasikia sauti ya tangazo huko nje. Wakakurupuka toka katika usingizi wao wa njaa na kuangaza dirishani.



Wakawaona wanajeshi wawili wakiwa juu ya farasi wakitangaza juu ya sherehe ya unyongaji inayoenda kufanyika hapo karibuni baada ya kufanikiwa kumkamata mhalifu mkubwa himayani.



Hivyo wananchi wote walikuwa wanakaribishwa kuhudhuria sherehe hiyo itakayoanza dakika chache mbele kwenye uwanja wa halaiki!



Wakina Oragon wakataman sana kwenda kushuhudia lakini wakaogopa. Waliona ni kama kujipeleka kwenye mdomo wa mamba. Huko wakionekana wanaweza wakakamatwa na wao kunyongwa pia!



Basi wakaendelea kutulia humo ndani lakini katika hali ya kushangaza, baada tu ya dakika chache mtaa wote ukakauka!! Hakuonekana mtu hata mmoja akikatiza, wala sauti ikisemaza.



Oragon na kaka yake wakatazama nje kupitia dirishani. Huku na huko. Hapa na pale. Kimya!!



Hakukuwa hata na ishara ya binadamu. Laiti kama mtu angekuja hapo muda huo basi angesema mji huo ni maghofu tu ya watu wa kale.



"Otto," Oragon akaita. "Twende tukatafute chakula sasa!'



"Wapi?" Ottoman akashangaa. Uso wake ulieleza hofu.



"Huko majumbani!" Oragon akamjibu. "Watu wote wameondoka, wameenda kutazama unyongaji. Twende tukapekue vyakula sasa!"



Ottoman akasita. Ila atakula nini endapo akigoma?? Akajiuliza. Hakuwa ma budi kukubaliana na kakaye.



Kwa tahadhari wakatoka ndani, wakachungulia njia. Kulikuwa salama. Wakajongea ado ado na kuzama ndani ya nyumba moja iliyokaribu baada ya kuhakiki usalama wake.



Humo kulikuwa giza wakawa wanatumia milango yao ya ufahamu kusonga.



Wakapekua huku na huko. Kweli wakapata chakula. Wakala na kushiba, na hapo ndipo wakapata wazo jingine. Wasile tu chakula bali watazame na kubeba vitu vingine vya thamani!



Lengo lao likiwa ni kutengeneza tena fedha zao zilizoibiwa kisha watazame ustaarabu mwingine.



Wakaanza kukomba kila walichokiona kinang'aa na kukitia kifurushini. Walipomaliza ndani ya nyumba hiyo wakaenda nyingine na nyingine mchezo ukiwa ni huo huo, somba na uweke ... somba na uweke.



Nyuso zao zikajawa na matabasamu.



Walipozama kwenye nyumba ya nne, nyumba waliyoapa kuwa itakuwa ya mwisho kisha waende zao, wakasikia sauti ya mtu humo. Haki wakashtuka na kutepeta hofu!!



Sada wakajua mwisho wao umewadia. Endapo mwenye nyumba yu ndani, basi ni hilo ni komo.



"Nyie ni wakina nani?" Sauti iliulizia gizani. Jua lilikuwa limeshaanza kupotea sasa hivyo hizi nyumba zilimezwa na kiza.



"Nyie ni wezi enh?" Sauti ikauliza tena. Oragon na kaka yake wakatazamana. Macho yao yalikuwa yanang'aa kana kwamba paka gizani. Walijawa na woga. Hawakuwa na cha kujibu.



Mara wakasikia vishindo vya mtu, na punde akatokea yule aliyekuwa anawauliza. Kumbe alikuwa ni miongoni mwa wale majamaa zao!!



Yule mtu mfupi.



Akacheka sana kisha akawapongeza wakina Oragon.



"Sasa mmekwiva haswa! Tunaweza tukafanya kazi pamoja."



"Ulikuwa unafanya nini humu?" Oragon akamuuliza. Jamaa akatabasamu kisha akatoa jiti lake mfukoni na kuanza kusugulia nalo meno.



"Unamuuliza mwizi anafanya nini ndani ya nyumba? ... nilikuwa natekeleza kazi yangu kama nyie mfanyavyo!"



"Sisi sio wezi!" Akasema Ottoman.



"Ni wakina nani basi kama sio wezi? Mnafanya nini hapa marafiki zangu?" Jamaa kafupi akauliza.



"Sisi sio marafiki zako!" Oragon akafoka. Kisha akamtazama Ottoman na pasipo kuongea wakatoka ndani ya nyumba hiyo.



Nyuma yao yule jamaa mfupi akawafuata.



"Leo hamnitaki? Na kuwasaidia kote huko?" Mgongoni mwake naye alikuwa ana kafurushi ila si kikubwa kama kile cha wakina Oragon. Pengine yeye alikuwa ameanza kazi muda mfupi hapo nyuma na ile nyumba ndiyo ilikuwa nyumba yake ya kwanza.



Wakina Oragon wasimjali wakanyoosha miguu yao kujiendea.



"Naweza nikawasaidia zaidi. Mtaenda wapi ndani ya himaya hii kama hamtanisikiliza?" Akaendelea kuongea. Mara ghafla Ottoman akageuka na kumkunja nguo.



"Achana na sisi! Mlitarajia tutakufa mlivyotutoa sadaka kwa Rabis? Mmekosea sana. Haujui ni mangapi tumepitia na hili si la mwisho!"



Aliposema hayo akamsukumiza jamaa huyo, akadondoka chini wakaendelea na safari yao.



"Hamuwezi kuishi ndani ya himaya hii pasipo sisi!" Akaropoka jamaa huyo akiwatazama wakina Oragon wanaishia. "Mtakamatwa na kuuawa muda si mrefu!"



Wakina Oragon hawakumjali. Wakaendelea kukazana wakiwa sasa wamepata kiburi na mali walizonazo.



Lakini wasifike mbali, wakasikia sauti za farasi!! Mioyo ikakita. Walikuwa ni wanajeshi!!!



Kabla hajawafanya lolote, mara yule jamaa mfupi akapaza sauti kuwaita.



"Njooni huku!"



Akielekea upande wake wa kushoto kwa kasi. Hawakuwa na budi zaidi ya kumfuata jamaa huyo upesi!



**



"Nimeipata!" Lucy alipaza sauti yake kwa furaha. Alimkumbatia Bella kwanguvu zake zote kisha akambusu shavuni mara tatu!



"Nini kimekupata??" Bella akashangaa. Lucy akarudishia mlango wa chumba chao baada ya kutazama usalama alafu akamketisha Bella kitako juu ya kitanda.



"Kazi yetu sasa imekwisha!" Akasema kwa furaha. "Nimepata moyo wa mfalme!"



"Lucy, nini wasema?" Bella akatahamaki.



"Nilikuwa nakwambia mfalme si mtu wa kawaida, ukawa huamini. Leo nimeupata moyo wake chupani kabatini!"



"Hakika?" Bella akauliza akikodoa macho.



"Ndio, hakika! Nimepata moyo wake kule kabatini umo ndani ya chupa!"



"Sasa?" Bella akauliza. "Mbona umeuacha huko?"



"Usijali," Lucy akamtoa hofu. "Nimeuhifadhi mahali salama kabisa. Leo majira ya usiku wa kutosha tumwite mkuu na tumwambie kila kitu kipo tayari sasa!"



Bella akamnyaka Lucy na kumkumbatia.



"Hatimaye tutarudi kwenye miili yetu," akasema kwa tabasamu pana. "Hatimaye tunarudi nyumbani!"



"Hapana!" Lucy akatikisa kichwa. "Sio tu tunarudi nyumbani bali na hapa tunapafanya kuwa nyumbani!"



Wakacheka haswa.



Sasa walikuwa wamefikia kwenye komo tamu. Kukusanya tu taarifa za Goshen na kuzifikisha kwa Jayit hakukuwa kunatosha. Leo imekuwa bahati iliyoje kupata kitu cha zaidi mbali na matarajio yao!!



Kitu cha thamani, aghalabu, amali! Hakika walitegemea kingemfurahisha mkuu wao.



Baadae baada ya kutengenezea madhabahu yao vema, wakamwalika mgeni wao kukaimu. Wakamweleza kinaganaga kuwa vita imeshakwisha. Hawana tena haja ya kumwaga damu.



GOSHEN IPO MIKONONI MWAO!!



Basi Jayit akiwa mjawa wa tabasamu, akawaambia wajiandae kesho karamu yaja!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Furaha iliyoje hii? Basi wakina Bella na Lucy wakajazwa na furaha kubwa kwani hatimaye kazi waliyokuwa wanaifanya kwa muda mrefu imezaa matunda!



Sasa miili yao ya kilozi ambayo ilikuwa imepokonywa na kisha kukabidhiwa ya binadamu, itarejea. Watapata tena wasaa wa kujumuika na watawala wenzao wa kiza.



Lucy hakulala usiku huo akawa tu anatafakari ni kwa namna gani atakavyozawadiwa kwa kutenda kazi kwa ufasaha. Kila saa akajikuta anacheka ama kutabasamu mwenyewe.



Baada hata akaona anajidanganya kitandani, akatoka na kwenda nje kwene kishikio cha nje cha ghorofa hii ya kasri, akaangaza huku na huko huku na huko.



Yote hii sasa ilikuwa mali yao! Yote hiyo haitakuwa Goshen bali Devoship. Aliwaza.



**



"Mmehakikisha kila kitu kipo sawa?" Aliuliza mfalme kwa sura ya uchovu. Macho yake yalikuwa yamelegea. Uso umepauka. Ni kama vile hakulala usiku mzima.



Alitembea kigoigoi akionekama mkosefu wa nguvu.



"Kila kitu kipo sawa," akajibu Lucy akitabasamu. Mkononi alikuwa ameshikilia karai dogo lenye dawa ndani yake, kimiminika cha kijani iliyopauka.



Aliposema hivyo, akafungua mlango na kuzama ndani kwenda kumkuta Tattiana. Leo ilikuwa zamu yake kumhudumia. Chumbani alikuwapo pia mama na daktari wakiwa wanamtazama mgonjwa huyo ambaye bado hajapata fahamu.



"Umeyachanganya vizuri?" Daktari alimuuliza Lucy.



"Ndio," Lucy akatikisa kichwa."kila kitu kipo sawa."



Daktari akainusa kwanzs ile dawa. Akaridhia. Ilikuwa sawa. Akachukua kitambaa chake cha sufi na kukidumbukiza katika bakuli kisha akaikamua na kuiweka juu ya paji la uso la Tattiana.



Baadae akahamishia kitambaa hicho shingoni.



Wakati akifanya hayo, mama pamoja na Lucy wakawa wanamtazama kwa umakini.



"Itamchukua muda gani kurejea?" Akauliza Lucy akiigiza kuwa na sura ya huruma. Daktari akamtazama na kumwambia:



"Ni jambo la muda." Kisha akamtazama mama na kuendelea kusema:



"Atapoa tu. Asingelikuwepo hapa kama angelitakiwa kufa."



Lucy akatabasamu. Ila moyoni mwake akajisemea ... atakufa tu.. akabaki hapo akimtazama Tattiana kwa dakika kadhaa kabla hajanyanyuka na kwendaze.



"Usikae mbali," daktari akamhasa.



**



Lucy akatazama kushoto na kisha kulia kwake. Akatembea kwa hatua kadhaa kabla hajafika sebuleni. Hapo alipotazama akamwona mfalme akiwa amejilalia amejishikia tama.



Akasita kwanza na kumtazama mfalme kwa dakika kadhaa. Alionekana ana mawazo, hana furaha. Hakukuwa na sababu nyingine zaidi ya Tattiana.



Lucy akatabasamu.



"Karibuni utapumzika toka kwenye mawazo hayo," akasema kwa kujishaua. Mara mfalme akakurupuka na kumtazama.



"Unasema na mimi?" Akauliza pasi na uhakika. Lucy akiwa amehofia, akakana na kisha haraka akaendelea na safari yake.



Mfalme akarejea kulala.



Lucy akaendea chumbani kukutana na Bella.



"Kuna haja ya kummaliza??" Alimuuliza mwenzake huku akijilaza. Bella akamtazama kwa mashaka.



"Nani?" akauliza kana kwamba hajui mada.



"Tattiana!" Lucy akajibu akitazama dari.



"Hamna haja hiyo. Ni kupoteza nguvu tu bure. Kabla hajanyanyuka na kutoka kitandani, mfalme wetu atakuwa ameishakuja ns kuinyakua himaya. Ya nini kujichosha??"



"Sijui kwanini," Lucy akanena. "Ila najisikia kumuua kabisa. Sipati amani rohoni mwangu kumwona yupo hai!"



"Kwasababu gani?"



"Nimeshakwambia sijui kwanini!" Lucy akasema kwa msisitizo. "Simpendi haswa. Sitaki hata kumwona. Leo nimepewa zamu ya kuandaa na kupeleka dawa. Natamani nitie sumu!"



Bella akatikisa kichwa.



"Huna haja hiyo! Zaidi utajiweka tu hatarini ukauawa kabla hata hujaona matunda ya kazi yako." Akamsihi: "tulia. Bado kitambo kidogo tu."



Lucy akanyamaza asinene tena. Ila moyoni mwake bado aliendelea kuteta.



**



Usiku mzito ...



Kelele kali ya sauti ya kike ilisikika kwanguvu!! Kisha kukawa kimya tuli.



Sauti hiyo ilimgutua mfalme toka usingizini akatazama kando na kando kwa macho yake yaliyolewa usingizi.



Alipoona ni kimya na hakuna dalili ya kusikia chochote, akasonya alafu akalaza kichwa chake kitandani. Akadhani ni mawazo tu ndiyo yanamtesa.



Tangu Tattiana apate majeraha kwa kuanguka ghorofani, hakuwahi kupata amani moyoni. Usiku amekuwa wa kuweweseka. Amekuwa akimuota Tattiana akimshtumu kwa kutomsaidia, ama akimlilia amuokoe!



Basi akalijumuisha hilo pamoja na kelele hiyo. Na kumbe alikuwa amekosea. Kelele hiyo haikuwa ndoto bali uhalisia.



Hakuwa anaota!!



Kelele hiyo ilikuwa ni ya mmoja wa kijakazi wake aliondani ya himaya akiwa anatolewa roho.



Kiufupi kasri ilikuwa imeshatekwa na mfalme hakuwa anajua!! Wanajeshi wote ndani ya kasri walikuwa wameshauawa. Wapo chini wanavuja damu. Na mtu aliyekuwa anawaua hakuwa anaonekana!!



Muda si mrefu kasri zima likawa gizani. Hakukuwa na ginga hata moja lililowaka sehemu yoyote ile!!



Ngo! Ngo! Ngo! Mlango wa mfalme ukagongwa. Hakusikia kwa mara ya kwanza. Hodi ikarudiwa na mara mfalme akaamsha kichwa chake toka kitandani.



Kiulevi wa usingizi, akauliza:



"Nani?" Akistaajabu nini kimezima ginga la moto lining'inialo kwenye kaeneo kake spesheli ukutani.



Hakujibiwa. Akarudia kuuliza tena. Mara hii akajibiwa kwa ufupi:



"Mfalme wa usiku!"



Akatahamaki. Aidha aota, akawaza. La hasha! Ni mzima. Mwanajeshi gani huyo anamchezea zengwe? Hajui kama mfalme anahitaji kupumzika?



Akaghafirika.



Kabla hajajitoa kitandani, akastaajabu kumwona mtu kasimama pembezoni. Alikuwa ni mweusi ti! Akashtuka mno.



Asifanye kitu, mtu huyo akatoa mikono yake nyuma na ule wa kushoto ulikuwa umebebelea chupa yenye moyo wa mfalme!



Hata mfalme mwenyewe hakuwa anajua kama moyo wake upo chupani!! Siku zote hizo alikuwa akiishi akidhani yeye ni binadamu lakini kiuhalisia si binadamu hata chembe!



Mwili alionao si wa kwake bali wa marehemu, na ndiyo maana ni wa baridi kila uchwao. Hakuwa anajua kama hana familia.



Hakuwa anajua kama yeye aliumbwa tu Vedas kama mwanaume wa kumtimizia mahitaji yake ya mapenzi. Na kuhakikisha hilo, moyo wake akautia ndani ya chupa autende atakavyo.



Na ndivyo ilivyokuwa mpaka Vedas akafariki!!



"Helow mfalme," mtu yule mweusi kana kwamba kivuli akanena. "Sasa ni muda wako wa kurejea kwenye uhalisia wako ... Kule ulipotokea!"



Mfalme akapapatika



"Wewe ni nani??"



"Mfalme mpya!"



"Mfalme toka wapi??"



"Toka Devonship!"



"Shabash! Wewe ni Jayit!"



"Ndio. Na wewe ni nani?"



"Mimi ni mfalme ... mfalme wa Goshen! Mimi ni Phares!"



"Phares nani??"



Mfalme hakuwa na jibu. Akamfokea Jayit akimfukuza apotee katika himaya yake kabla hajamteketeza.



Jayit akacheka sana alafu akamuuliza:



"Unifukuze? Unifukuze kwa jeshi gani??" Kisha akaweka kituo. "Jeshi lako lote limekuwa mfu. Hakuna mwanajeshi anayesimama hivi sasa hata mmoja!"



Mfalme akabaki anaduwaa.



"Hakuna kitu hata kimoja nisichokifahamu kuhusu wewe, ama Goshen hii kwa ujumla. Ilinilazimu kuwa mpole kwa kitambo kirefu kabla ya kuamka upya! ... sasa nimeamka kuja kuchukua kilicho changu!"



Asipoteze muda zaidi, akatazama kile chombo kilichobebelea moyo wa mfalme. Hakikuwa na mfuniko. Ndani yake kulikuwa kuna moyo tu unaodunda. Akaunyaka na kuujaza mkononi.



Kisha akaubana kwanguvu!!



Mfalme akaanza kuhangaika na kutapatapa. Jayit akaendelea kuuminya moyo huo mpaka vidole vyake vikakutana, na mara mfalme akafa papo hapo!!



Jayit akautupia kando huo moyo kisha akamsogelea mfalme. Akampulizia pumzi puani akisema:



"Amka sasa na uwe wangu."



Mara Phares akafungua macho!! Yalikuwa ya kijani yenye kiini cheusi cha nyoka. Akasimama na kusujudu miguuni mwa Jayit.



Jayit akamshika kichwa kumbariki. Sasa akamfanya awe jemedari wa majeshi yake yote. Bendera ikapandishwa juu ya kasri kuashiria utawala mpya!



Utawala wa Jayit.



"Naam kila kitu sasa kinapendeza," akasema Jayit akikalia kiti cha mfalme. Akaveshwa n kofia ya mamlaka na kukabidhiwa fimbo ya utawala.



Kifuani mwake kila kitu kikawa shwari. Hatimaye Goshen imekuwa yake. Imejaa mikononi mwake kama ambavyo alikuwa akitaka siku zote hizo.



Kabla ya usiku huo kuisha, akaendea kule kulipokuwa makazi yake ya zamani, walipokuwa wanaishi babu na bibi yake kisha akatembelea himaya nzima kufanya ziara.



Alipomaliza hapo akarejea kasrini. Wale watu waliokuwa wamelala majumbani mwao wasidhani kama kuna lolote lile limetokea himayani.



Huko Lucy akamkaribisha kwa bashasha la furaha akiwa anaongozana na Bella. Wakamsindikiza Jayit mpaka chumbani kwake kisha kiongozi huyo akawataka waandae eneo kwani watakuwa na kikao muda si mrefu hapo kasrini.



Wakafanya hivyo. Baada ya muda mfupi Jayit akawa ametinga eneoni akiwa ameandaliwa kiti chake, wazee wa baraza nao wa tawala ya Devonship wameshajaa vitini.



Nyuso zilikuwa za kutisha. Kama ungalikuwa mwanadamu muoga basi usingeliwatazama watu hawa mara mbili. Wengine mpaka mapembe walikuwa nayo.



Macho ya ajabu. Masikio marefu. Midomo na meno ya kutisha. Sauti za kunguruma na mauombo yasiyo ya kawaida!



Wote walikaa kimya wakimtazama mfalme kwa macho ya utulivu. Wanajeshi ndiyo ambao walikuwa wamesimama wakishikilia silaha zao vema mikononi.



"Hatimaye tumelifanikisha!" Jayit akafungua kikao chake kwa kauli hiyo. Watu wote wakashangilia. Hai! Hai! Hai!



Jayit pasipo kuwa mchoyo wa fadhila, akapeleka sifa kwa wanawake Lucy na Bella kwa kutenda kazi zao vema na wasingelifanikisha hilo kama isingelikuwa juhudi zao.



"Leo nitawakabidhi zawadi zao. Lakini pia watapata miili yao waliyoiacha kitambo."



Baada ya hapo, Lucy na Bella wakasonga mbele ya Jayit. Wakawekewa mikono vichwani na Jayit akiteta maneno kadhaa. Mara wanawake hao wakadondoka chini na kupoteza fahamu!



Dakika chache mbele wakarejesha fahamu zao wakiwa kwenye miili mingine wakati ile waliyokuwa nayo awali ikiwa bado imebaki chini.



Walizama kwenye miili ya wanawake wa ajabu. Miili yao halisi!!



Lucy alikuwa mrefu mno, mwembamba, kichwa chenye umbo la pembe tatu na nywele nguvu zilizokakamaa kama msumari! Bella yeye alikuwa ana umbo la wastani, hakuwa mrefu wala mfupi, mnene wala mwembamba.



Macho yake yalikuwa madogo kama ya paka. Masikio yake marefu kama ya punda. Mdomo wake ulikuwa na lips pana. Na meno yake yalikuwa madogomadogo yaliyochongoka.



Walifurahi kurejea kwenye miili yao. Walitazamana kwa furaha kisha wakamtazama Jayit, kiongozi wao aliyeketi kitini.



"Nawatunuku nishani ya uongozi ndani ya himaya hii mpya. Mtakuwa viranja na kila mmoja atasikia sauti zenu na kuzifuata!"



Kama haitoshi Jayit akawapa zawadi nyingine. Vipande vikubwa vya ardhi ndani ya himaya ya Goshen.



Lakini Lucy, kinyume na mwenzake, Bella, hakuwa amefurahishwa sana na hayo. Kuna kitu alikuwa anakitaka na alikingoja mpaka kikao kinakata bado hakukipata.



Aliketi akiwaza wakati wenzake wakiwa wanafurahia tafrija kwa kula na kunywa. Hakuwa na habari kilichokuwa kinaendelea kikaoni hapo zaidi tu ya kinachoendelea kichwani mwake.



Baada ya wanawake hao kupewa nishani zao, Jayit akawagawa wazee wa baraza na kila mmoja kumpa madaraka yake. Kikao kikavunjwa.



"Lucy, kuna shida?" Bella aliuliza akimtazama mwenzake. "Tumepewa vyote hivyo bado hujafurahi?"



Lucy hakujibu. Uso wake ulikuwa umejawa na kiburi. Bella akahofia kumwongelesha tena.



Wakiwa wamekaa hapo kana kwamba watoto yatima wakati wenzao wakifurahia siku, mara mfalme akawaita wasonge karibu. Akawauliza kumhusu Tattiana. Binadamu pekee aliyebakizwa hai na huru ndani ya kasri, mamaye akiwa tayari ameshatupiwa jelani.



"Yule alikuwa ni mchumba wa mfalme!" Bella akajibu.



"Alikuwa anafuatilia nyendo zetu. Tukamuwahi kwa kumwangushia chini toka ghorofani!" Lucy akaongezea taarifa.



"Oooh!" Jayit akasema akikuna kidevu. Kuna jambo alikuwa analiwaza kichwani. Aliwaweka hapo wakina Lucy pasipo kuwaongelesha kwa muda wa kama dakika tatu kisha akavunja ukimya kwa kusema:



"Nimempenda!"



Kauli hiyo ikapasua moyo wa Lucy. Alimtazama Jayit kwa macho makali akiwa haamini alichokisikia.



Wakatazamana pia na Bella.



"Mfalme," wakaita kwa pamoja. "Unasema??"



"Nimempenda," Jayit akarudia kunena akisimama.



"Lakini itawezekanaje kumpenda binadamu??" Lucy akauliza. Jayit akamtazama kwa sekunde kadhaa kisha akamwambia:



"Nitamfanya awe kama sisi!"



Kabla Lucy na Bella hawajatia neno, bado wamebakia kwenye bumbuwazi, Jayit akaondoka zake akienda kule chumbani ambapo Tattiana alikuwa amelazwa.



"Haiwezekani!" Lucy akapiga kelele. Macho yake yalikuwa yamejaa machozi kedekede. Amekunja uso wake kwa kutokuamini alichokisikia wala kukiona.



Alidhani angeupata moyo wa Jayit baada ya kufanya kazi ile kubwa. Alidhani sasa atakuwa malkia wa himaya hiyo, lakini mambo yameenda kombo!



Tena yanaenda kombo kwa binadamu.



Mfalme amempenda binadamu!! Ilikuwa ngumu kuamini. Pengine anaota, akafikicha macho yake kwanguvu.



"Nilikuambia!" Lucy akakamata nguo ya Bella. "Nilikuambia nimuue yule mzandiki lakini hukutaka kunisikia! Ona sasa! Ona sasa!"



Akanyanyuka na kukimbilia chumbani akivuja machozi. Bella akamtazama rafiki yake akiishilia asijue la kufanya.



**



Mkono mwembamba wa Jayit uligusa paji la uso la Tattiana akiwa anamtazama mwanamke huyo kwa macho ya pole.



Alivutiwa naye. Alichezea nywele zake kama sufi akitabasamu mwenyewe. Hakika Tattiana alikuwa mrembo hata kama alikuwa majerahani.



Jayit akawaza namna atakavyokuwa naye hapo kando kama malkia. Haki akapata picha ambayo ilimfanya atabasamu kwa upana zaidi.



Tangu alishatimiza lengo lake la kwanza, la kuipata Goshen, sasa kulikuwa na haja ya kumalizia hili la pili. Kuwa na malkia! Awe kamili.



Alipomtazama Tattiana kwa muda kidogo akamchanja na ukucha wake mrefu, kisha akakinga damu ya Tattiana ndani ya chupa ile iliyokuwa imetunza moyo wa Phares. Akaifunga vema chupa hiyo na kuitazama.



Akateta maneno kadhaa ya kunuwia. Na hilo likawa agano kati yake na Tattiana kama vile Vedas alivyoweka agano na Phares.



Alipoona kila kitu ni vema, akampulizia Tattiana pumzi yake puani na kumwamuru asimame. Kufumba na kufumbua, Tattiana akarejea fahamuni!!



Macho yake yalikuwa ya kijani lakini uzuri wake ukibakia palepale. Alimtazama Jayit pasipo kusema jambo, Jayiy akamwambia:



"Wewe ni wangu. Utafuata kile nitakachokuambia. Utacheza kila nitakachoimba."



Tattiana akapokea maagizo hayo na wakakumbatiana na Jayit.



"Wewe ni malkia wangu wa usiku!" Jayit akambatiza.



**



"Mama!" Mtoto akaita akifungua dirisha. Kwa makamo ya upesi alikuwa mwenye miaka kumi na mbili. "Tuliwahi sana kulala??" Akauliza akimtazama mama yake aliyekuwa ameketi kandokando.



Muda ulikuwa umeenda sana lakini jua halikuwa limechomoza!! Hata usingizi ulikuwa umekoma sasa watu wakakaketi vitandani.



"Nashindwa kuelewa," mama akajibu akipandisha mabega. "Nilidhani pengine ni mimi peke yangu ndiyo nimebadilika!"



Hawakukaa muda, mara mlango wao ukagongwa. Kabla hawajaufungua ukavunjwa na wanaume wawili, vijakazi wa Jayit, wakazama ndani na kumbeba mama na mwana wake!



"Twende! Twende upesi!!"



Kumbe na huko nje watu lukuki walikuwa wameshageuzwa kuwa watumwa!! Wamewekwa kwenye misafara iliyokuwa imesimamiwa na wanajeshi wa ajabu wa Jayit.



Wanaswagwa kuelekea jela!!



Kilio.



Simanzi.



Taharuki.

Wananchi wote walikamatwa na kutupiwa gerezani wakabaniwa humo na makomeo makubwa ya chuma. Na kwa wale ambao hawakupata nafasi humo, basi zikachimbwa jela za mahandaki, wakatupiwa humo.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Jayit akaona sasa kila kitu ni kheri. Kila kitu kinapendeza machoni mwake. Akamuita jemedari wake wa jeshi, bwana Phares, akamwambia:



"Hakikisha hakuna binadamu yeyote aliye nje ya gereza!"



Mbali na agizo hilo akasisitiza kuwa binadamu wote hao walio ndani ya gereza wawe wanakula nyakati za jioni tu! Mlo mmoja kwa siku.



Na mali zote walizozikusanyia huko majumbani mwao ziletwe kasrini haraka iwezekanavyo!



Nani atampinga mfalme?? Msako ukarejewa kwa mara ya pili nyumba baada ya nyumba, kila chenye thamani kikasombwa na kila mnyama akauawa.



Hakukutakiwa kubakia na chochote kile kilicho hai nje ya gereza. Phares alipohakikisha hilo, akawasili kwa mfalme kumrejeshea matokeo.



Jayit akatazama ghala, hakika lilikuwa linapendeza. Limesheheni dhahabu kedekede. Silva na fedha. Akafurahi sana. Akacheka kuumiza mbavu zake.



Lakini kama haitoshi, kuna jambo alilikumbuka. Akamuuliza jemedari wake:



"Na vipi kuhusu Cedar?" Kisha akatabasamu. Alifurahishwa sana na kumbukizi hii. Ilikuwaje akawa amesahau muda wote huo??



Jemedari akamwambia matunda hayo yapo kedekede himayani. Ampatie muda mchache akapate kuyatafuta na kuyaleta.



Jayit akamshika bega akitabasamu.



"Safi sana. Na utakapofanikisha hilo, upesi matunda hayo yaanze kuuzwa. Ulimwengu mzima wakajue wapi yanatokea, wapi watakapoyapata!"



Lakini si kwamba Jayit alikuwa amelenga kutengeneza faida. La hasha! Fedha na dhahabu kwake si mali. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kutumia matunda hayo kama silaha!



Alipanga kuyawekea himo vimelea vya kilozi na basi kila atakayelishika, si kula tu, basi ataishia kuwa mwovu, mdhalimu!!



Na kwa kupitia hivyo basi atatawala himaya lukuki! Mwishowe atatawala ulimwengu mzima!!



Wazo liliyoje hili?? Alimkubatia mkewe na kwenda naye chumbani.



"Hakika leo nimefurahi sana," alimweleza Tattiana ambaye alimkatia jina jipya, akimwita Kanius.



"Kanius, mke wangu, sitaki furaha hii ikome hata kidogo. Nataka nifurahi siku zote nikiwa hapa. Nawe utanitendea nini?"



Kanius akatabasamu. Akanyanyua mkono wake wa kuume na kumshika mumewe shavuni.



Akasema:



"Nitakuzalia mtoto wa kiume!"



Jayit akalipuka kwa furaha. Alikunwa sana na hili. Aliweka mkono wake wa kushoto tumboni mwa Kanius akapapasa na kutomasa.



"Utakaponipatia mtoto, nitafurahi sana. Nitakupa nusu ya ufalme wangu wote!"



"Usijali, mpenzi," Kanius akapokea ahadi hiyo kwa tabasamu zito. "Ni lazima nikupatie mtoto!" Akaapa.



"Tena wa kiume wa kurithi kiti chako."



Basi mfalme wake akambusu kwenye paji lake la uso kisha akalaza kichwa chake kifuani. Kanius akachezea nywele za mumewe.



Baada ya muda kidogo wakashiriki tendo lao la kwanza la ndoa, wakiwa watu wenye nguvu na upendo wa ajabu.



**



Chozi likamshuka Lucy. Akajikuta anang'ata meno yake kwa hasira.



Alichokuwa anakisikia kilikuwa ni sahihi kabisa, ila aligoma kuamini. Masikio yake yaliyokuwa yamekaa karibu na mlango wa chumba cha mfalme, yalimletea taarifa mbaya mno kupata kuisikia maisha yake yote.



Sauti za miguno ya mahaba kati ya Tattiana (Kainus) na Jayit!!



Alihisi moyo wake unasagwa kusikia hivyo. Aliumia mno. Alishindwa kuvumilia akaenda zake chumbani alipojitupia kitandani na kulia sana.



Lakini bado kifua chake hakikuwa chepesi hata kidogo. Alinyanyuka akaendea kioo na kujitazama. Nini kasoro yake??



Hakuiona!!



Ni nini Jayit alikosa kwake?? Nini anataka akashindwa kumpatia??



Akiwa hapo, rafiki yake Bella akaingia akiwa amebebelea maua mkononi. Usoni mwake alikuwa amejawa na tabasamu pana na alipoketi akamuita Lucy na kumweleza:



"Hatimaye nimepata ardhi ninayotaka mfalme anipatie. Kule bondeni mikindani, kuna maua mazuri ya kuyala. Pia ardhi yenye rutuba ya kupatia funza kila asubuhi kama kifungua kinywa."



Ila mwenzake hakuwa anamsikiliza, akaligundua hilo. Zaidi akagundua alikuwa analia. Akaweka maua yake pembeni na kumfuata.



"Lucy, nini shida? ... bado unamlilia mfalme??"



Macho ya Lucy yalikuwa yamejawa na maji mpaka kuona vema hakuwa anaweza. Kifua chake kimembana kwa kwikwi na pua imeziba kwa mafua.



"Niambie," Bella akasema kwa sauti ya chini. "Pengine naweza kusaidia."



Lucy akanyamaza kimya. Bella akavuta subira akimwacha avute hewa kwanza kupooza kifua.



"Bella," Lucy akaita kwa sauti ya chini. "Mfalme na Tattiana wamepanga kupata mtoto!!"



Bella akakodoa macho. Akajitahidi kubana hisia zake za kushangaa asimtishe zaidi Lucy.



"Hakuna kitu kama hicho Lu--"



"Nimewaacha wanafanya mapenzi saa hii!" Lucy akamkatisha Bella akimtazama kwa macho yake mabichi.



"Vipi kama Tattiana akashika mimba??"



Bella akakosa cha kusema. Mdomo ukawa mzito.



"Kama akipata mimba, sitakuwa na changu tena. Mfalme hatowez kuwa na mimi milele!" Akalia. "Lakini inawezekanaje? ... inawezekanaje yeye akaja na kumteka upesi hivyo?"



Bella akambembeleza rafiki yake pasipo mafanikio. Lucy akaapa:



"Lazima nimmalize Tattiana!" Alisema akikunja ngumi kwanguvu. "Lazima nimmalize kwa mikono yangu mwenyewe. Kwa namna yoyote ile!"



"Lakini ..." Bella akamkatiza. "Huoni ni hatari? Vipi kama mfalme akijua adhma yako hiyo? ... si atakumalizia mbali!!"



"Ni bora ikawa hivyo!" Lucy akaropoka. "Ni kheri nikafa kuliko kuishi kuona haya niyaonayo sasa. Kamwe siwezi kukubali!"



Bella akakosa cha kuongea. Aliketi kitandani akayanyaka maua yake na kuyakumbatia



**



Venim alinyoosha mkono wake kupapasa kitanda. Akafungua jicho lake na kuangaza.



Alikuwa mwenyewe kitandani. Akakunja uso. Akanyanyua shingo yake na kurusha macho ndani ya chumba kikubwa walichomo, hakuona kitu.



Akasonya.



"Huyu mwanamke kaenda wapi mapema yote hii??"



Akangoja kidogo hapo kitandani, pengine Rhoda ataonekana. Muda ukaenda kukiwa kimya. Venim akanyanyuka na kujiveka joho lake lililojaa mkononi baada tu ya kubanduka kitandani.



Lakini kabla hajatoka chumbani, akasikia miguno na sauti kubwa ya kike. Akajongea dirishani na kuangaza nje. Kwa mbali akamwona Rhoda akiwa anajaribu ulozi aliomfundisha hivi karibuni.



Mwanamke huyo alikuwa akitumia ulozi wa mishumaa mitatu mekundu kwa ajili ya kumudu hali ya hewa. Akifanikiwa kuumba moto, na kutengeneza pepo.



Ila bado akiwa si mjuzi haswa.



Venim akashuka kwenda kukutana naye. Akamkumbatia mkewe kwa nyuma na kumuuliza:



"Ulitoka muda gani kitandani?"



Rhoda akaguna.



"Muda si mrefu!"



"Unanidanganya. Muda si mrefu alafu ukavifanya hivi vyote kwa muda gani?"



"Kwani ni vingi kuchukua muda mrefu?"



"Ndio. Kwako ni vingi."



Rhoda akajichomoa toka kumbatoni, akamtazama Venim machoni.



"Unadhani mimi ni mgumu kujifunza na kushika?"

Venim akabinua mdomo.



"Naona wewe ni mwanafunzi bora."



Rhoda akatabasamu na kuendelea na zoezi lake. Venim akamtazama mwanamke huyo kwa macho ya mapenzi. Akamsogelea tena na kumuuliza:



"Mpenzi, lini utanikabidhi mwili wako? ... nachoka kungoja."



Rhoda akarembua macho na kushika kiuno.



"Umesahau ahadi yetu?" Akauliza kisha akajipatia jibu: "Sitashiriki na wewe kwenye lolote lile mpaka pale utakapokuwa umenifunda kila kitu!"



"Kila kitu??" Venim akatoa macho.



"Ndio," Rhoda akajibu kwa maringo. "Kila kitu ... nami nitakupa kila kitu.





Hicho ndicho alikuwa anahitaji Rhoda kwa Venim na si kingine. Kujua kila kitu anachokijua mwanaume huyo. Hilo ndilo lilikuwa lengo lake hapo na kingine kile.



Na alikuwa anaomba ayajue hayo kabla hajamkabidhi mwili wake Venim. Hakuwa anataka kabisa. Na kichwani mwake alishapanga kuwa akishafahamu hayo yote anayoyataka, basi Venim asahau kabisa kuhusu kumpata.



Utalalaje na mwanaume asiyekusisimua wala kukuvutia kwa lolote lile?? Alijisemea kifuani. Venim hakuwa na sababu hata punje ya kumfanya ahamasike kufanya tendo.



Kila mwanaume huyo alipomuwekea mkono mwilini alihisi kutetemeka. Alikuwa ni wa baridi kama chura. Na kila anapomtazama anaogopa. Hajaizoea sura yake kabisa japo wanaishi chini ya paa moja.



Atawezaje kumpa mwili mwanaume wa hivi??



Lakini zaidi ya hapo, alikuwa anajikinga asije kujikuta anabeba mimba ya Venim pasipo kutaka. Kwa mbingu ama kwa ardhi, hakuwa anataka jambo hili litokee kamwe!!



Kubeba mimba ya Venim kutakuwa ni agano ambalo litamuwia vigumu kulivunja. Hakutaka kabisa kuwa na familia na mwanaume huyu wa ajabu, na aliapa kujitahidi kuzuia hilo.



"Basi kuanzia sasa, tutabadili ratiba," alisema Venim. "Nitakuwa nakufundisha jua linapochomoza, linapokaa katikati na linapozama kila siku!"



Rhoda akafurahi.



"Upo tayari?" Venim akamuuliza akitabasamu.



"Ndio, nipo tayari muda wowote."



"Lakini," Venim akampa tahadhari. "Mafunzo mengine tutayafanya nyakati za usiku wa manane peke yetu ndani ya misitu. Na mengine yakihusisha kuua viumbe hai kama binadamu. Utakuwa na moyo wa kustahimili hayo??"



Rhoda hakufikiria mara mbili akasema:



"Nipo tayari!" Kwa uso wa ujasiri. Venim akatabasamu.



"Sawa," akamshika Rhoda mkono. "Lakini pia kuanzia sasa itabidi uanze kubadili vyakula unavyokula. Hauwezi kuwa mlozi kamili kama waendelea kula vyakula vya binadamu!"



"Vyakula gani hivyo?" Rhoda akauliza kwa macho ya kidadisi.



Venim akamwambia ataanza kwanza kwa kunywa damu ya watu. Kisha baada ya hapo, ataanza kula nyama zao pia. Rhoda akaridhia.



"Nitajitahidi."



Hakika hapo Venim akashangazwa na ujasiri huo wa Rhoda. Hakusita kabisa kukubali yote hayo. Hakuonyesha hata chembe ya woga machoni mwake!!



Lakini Venim akashindwa kujua dhamira halisi ya Rhoda. Mapenzi yalimpofusha macho na kuzubaisha akili. Kila kitu kuhusu Rhoda alikiona chema na kisicho na shida.



Aliamini Rhoda ameamua kubadilika ili aendane na mumewe. Jambo ambalo lilimfanya awe na furaha sana moyoni.



Akamfundisha Rhoda ulozi siku hiyo nzima kabla jioni hawajapumzika na kutia chakula tumboni.



Katika meza ya chakula, Rhoda akakabidhiwa bilauri kubwa lililojaa damu.



"Leo utaanza na hilo," Venim akamsihi.



Rhoda akala chakula na kumaliza, kisha taratibu akaanza kunywa damu aliyojaziwa bilaurini. Kabla hajanywa, harufu ikamkereketa. Akataka kutapika!



Haraka akaliweka bilauri chini akikunja uso. Venim akatabasamu. Akamtia moyo ni mara yake ya kwanza hivyo ni kawaida. Atazoea tu hivi karibuni.



"Taratibu taratibu, usijali."



Rhoda akanyanyua tena bilauri la damu na kulipeleka mdomoni. Akajitahidi kupambana na harufu. Akaria mara moja.



Ila sasa akashindwa kuzuia kutapika. Haraka akanyanyuka na kukimbilia kando akatapika chakula chote akichokula.



Venim akahofia. Akamtaka aache hilo zoezi kwa siku hiyo, atalifanya hivi mbeleni. Rhoda akatulia kwanza kuvuta hewa. Alipotosheka akarudi kitini na kushika tena bilauri.



Alitaka ajaribu tena!!



Lakini Venim akamzuia. Hapa akagiza vijakazi wake waondoshe bilauri hilo mbali.



"Pengine tujaribu njia nyingine," akapendekeza.



"Njia gani hiyo?" Rhoda akauliza upesi.



Venim akafikiria kidogo kisha akamtahadharisha njia hiyo ni fupi, ila hatari zaidi. Na endapo akiifuata njia hiyo basi atatoka katika mfumo wake wa binadamu moja kwa moja na kuwa kama yeye.



Hata mtu atakapomuona popote pale basi atajua kuwa yeye ni mlozi - mtu mwenye nguvu za kilozi ndani yake!!



"Ni njia ipi hiyo??" Rhoda akauliza kwa shauku.



"Njia ya ubatizo!" Venim akamjibu. "Utakapobatizwa utapewa jina lako la kilozi na mwili wako wa kipekee. Upo tayari?"



"Ndio, nipo tayari," Rhoda akatikisa kichwa.



"Sawa. Basi keshokutwa pindi mwezi utakaposimama kamili angani, tutaenda huko kaskazini ya mbali kwa ajili ya shughuli hiyo."



Rhoda akatabasamu. Mapigo yake ya moyo yalienda mbio kwa furaha.



**



"Nefil njhami khatu habab? ... Nefil njhami khatu habab?" Sauti hii ilikuwa inaongea huku ikififia.



"Nefil njhami khatu habab?" Ilivuma. Ikashuka mawimbi ... "Nefil njhami khatu habab?" Ikaishilia kwa mbaali ... "Nefil njhami khatu habab?"



Sauti hii ilifanya hivi mara tatu lakini hakuna mtu aliyekuwa anasikia wala kuijali. Iliishia kusema hivyo na mwishowe ikapotea kabisa!



Ulikuwa ni usiku mzito. Huko gerezani wengine walikuwa wanateta, wengine walikuwa wamelala, wengine walikuwa wanalia.



Kila mmoja alikuwa amejazwa na hofu kifuani mwake. Ungeliona hilo usoni. Hakuna aliyekuwa anajua kuhusu kesho yake. Mambo yaligeuka, tena upesi! Hakuna aliyepewa hata muda wa kufikiria.



Ni kama vile kufumba na kufumbua macho, A ikawa Z!!



Kwenye chumba kimoja cha gereza, mama Tattiana alikuwa amekaa akiegemea nondo. Uso wake ulikuwa mkavu, macho yaliyolegea kwa kuchoka kulia. Mashavu yalikuwa na michoro kadhaa ya machozi.



Amekuwa akimlilia mwanae aliyemwacha kasrini. Hajui hatma yake ni nini huko kama yu hai au mzima. Wakati wengine wakipata usingizi, hata wakajilaza, yeye hakuwa nao hata lepe!



Wakati wengine wakiwa wanateta, yeye alikuwa anagugumia na moyo wake. Ni bora angekuwa naye mule gerezani akamwona na kumshika.



Alijua hata angeomba akamwone mwanae asingeruhusiwa hata kidogo. Hakuwa na namna. Japo walikuwa ndani ya himaya moja, alijihisi ametupiwa himaya ya mbali mno.



Nini mama pasipo mtoto??



Kong! Kong! Kong!!



Nondo zikagongwa na kumshtua kila mmoja ndani ya chumba. Wote wakatazama langoni. Walikuwa ni vijakazi wawili wa Jayit, sura mbaya za kuogofya. Mikononi wamebebelea jambia ndefu zinazong'aa. Walisimama hapo na kuwakagua kwa macho yao yanayotisha!!



Kisha wakatazamana na kuteta katika lugha ambayo hakuna mwingine aliyewaelewa. Na mara wakafungua lango na kuwabeba wanawake wawili.



Wanawake hao wakalia kwa hofu kuu. Wakalia wakiwaomba wenzao wawasaidie lakini nani atathubutu??



Kila mmoja alikuwa anatetea uhai wake. Waliishia kuwatazama wanawake hao waliobebwa kwa macho ya hofu mioyo ikiwaenda mbio.



Hawakujua wenzao walipelekwa wapi na walienda kufanywa nini. Lakini majambia yale mikononi mwa wale vijakazi yaliwatisha. Pengine wameenda kutolewa sadaka!!



Hata wale waliokuwa na usingizi ukakoma, wote wakabaki macho wakilia na kuomboleza. Wakanena na kuelezana.



Lakini tofauti na mawazo yao, baada ya dakika kadhaa, wanawake wale waliobebwa wakarejeshwa tena chumbani. Walikuwa hoi wanalia!!



Wakatupiwa ndani na lango likafungwa!



"Ni nini kimewakumba huko?" Wenzao wakawauliza. Wakaeleza kuwa wamebakwa kwa zamu. Na haikujalisha ni kwa namna gani walilia kwa maumivu makali waliyoyasikia, hakuna aliyejali.



Wakiwa wanaongea hapo, mara wakashtushwa tena na sauti ya lango likigongwa!!



Kong! Kong! Kong!



Wakatazama.



Huko wakawaona vijakazi wengine wawili wa Jayit. Kabla vijakazi hao hawajafungua lango, wakamtazana mama Tattiana kisha wakaongea katika lugha yao ya pekee.



Mama Tattiana akapata hofu nzito. Sasa akajua zamu yake imewadia!!



**





Lango likafunguliwa akachomolewa na kubebwa asijue aendako. Alipiga yowe la kilio lakini hakuna aliyemsikiza wa kumjali.



Waliomjali hawakuwa na uwezo wa kumwokoa kwani walikuwa ndani ya jela wakibanwa na malango ya vyuma.



Mama akatolewa mpaka nje, huko akastaajabu kuona bado akipelekwa tu asipopafahamu. Baada ya punde akatambua ni njia ya kwenda kwenye kasri ya mfalme.



Hapo akapatwa na maswali. Ni nini anapelekewa huko?? Je aenda kuuawa ama nini??



Akili yake yote ikawaza pengine anaenda kuuawa aliwe nyama na mfalne yani Jayit. Akafika kasrini na kabla hajazama ndani akapata fursa ya kumwona Phares.



Hapo akakurupuka na kuanza kuita akidhani Phares anaweza kumsaidia. Hakujua Phares hakuwa mkwewe tena. Hakufahamu kuwa Phares amebadilishwa na sada si binadamu!



Akatupwa kitini na kuamriwa aketi hapo pasipo kuhangaika kama kweli anapenda uhai wake. Naye kwa uoga angelifanya nini zaidi ya kutii??



Akitazama huko na huko wanajeshi walikuwa wamejaa. Watu wa ajabu. Watu wa kutisha. Moyoni akaapa kama angelitoka huru mule kasrini basi ataenda kutoa sadaka kwa mungu wake. Sadaka ya mnyama mnono kabisa katika fungu zima.



Ila sadaka hiyo ataitolea wapi na ilhali Jayit kakusanya kila kitu?? Na huo atautoa wapi wakati yu chini ya ulinzi gerezani??



Hakuwaza hayo. Macho yake yalikomea kwenye pumzi yake tu.



Muda si mrefu, akasikia sauti za viatu zikigonga sakafu. Haraka akatazama sauti hiyo inapotokea. Mara akamwona Jayit akiwa anaongozana na Kainus pembeni yake.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Mama akastaajabu. Mwanae alikuwa hai!! Tena mzima wa afya!! Hakuamini macho yake.



Lakini ngoja ...



Mbona macho yake yana umbijani?? Mbona rangi ya ngozi si nyevu tena?? Hakujali! Mwanae alikuwa hai, hilo ndilo la maana haswa.



"Tattiana mwanangu!" Akapayuka akisimama. Alimtazama mwanae machoni na kila jambo kwake akaona kheri.



Ila Kainus hakuwa anamjua mtu huyu! Alistaajabu kumwona hapo na akamtazama Jayit akimuuliza:



"Ni nani huyu??"



"Mimi ni mama yako!!" Mama akapaza sauti. "Tattiana mimi ni mamayo!"



"Mimi si Tattiana!" Kainus akafoka. "Naitwa Kainus ... sawa?"



Mama akaduwaa. Kainus?? Akamtazama Jayit na kumuuliza:



"Nini umemfanyia binti yangu??"



Akafoka kwa hasira. "Umemtendea nini??" Akanyanyuka akamuadhibu Jayit ila akadakwa na kuketishwa kitini kwa nguvu.



"Tulia hapo ama uuawe!" Mlinzi alifoka. Macho yake yalikuwa yanamaanisha anachokisema. Hakuwa na tembe za masikhara hata punje!!



Jayit akamtazama Kainus na kumpa ishara. Kainus akaendea njia ya kushoto na kumpatia faragha Jayit na mama yake Tattiana.



"Nimeambiwa wewe ni mkwe wangu," Jayit akasema akiketi kwenye kiti chake cha kifalme kilichokuwa kimekaa kwa mbali kidogo na mbele ya kile alichokalia mama yake Tattiana.



Akatabasamu.



"Nimefurahi kuonana na wewe."



Ila mama alikuwa anamtazama kwa jicho la hasidi. Hasira zilijionyesha kwenye paji lake la uso.



"Ni nini umemfanyia mwanangu ewe dhalimu??" Akafoka.



"Nimemsaidia," Jayit akasema akipandisha mabega. "Hauna shukrani nimemrudisha kwenye uhai na fahamu zake?"



"Fahamu gani??" Mama akadaka kamba. "Mbona hamtambui mama yake?"



"Ni kwasababu yupo ulimwengu mwingine. Mbali na huu. Huko ambapo hasikii shida wala mateso kama aliyokuwa anayapata awali."



"Nini unataka kwangu?"



"Safi sana!" Jayit akatikisa kichwa. "Hapo ndipo nilikuwa nataka ufike. Nimekuleta hapa kwa lengo moja tu, ukae na mwanao kumwondolea upweke. Wewe ni mtu ambaye naweza nikakuamini kwenye hilo ..



Bado hajazoeana na watu na hana marafiki. Hata waliopo hawataweza kumhudumia kama nitakavyo ufanye wewe."



"Nitakaaje na mtu asiyenitambua??" Mama akauliza.



"Usijali," Jayit akamwondoa shaka. "Hilo niachie mimi, najua cha kufanya. Alimradi tu umtunze vema kwenye hali yake."



"Hali gani hiyo??"



"Mwanao ana ujauzito," Jayit akasema kwa furaha. Lakini kwa mama hii kauli ilikuwa ni kama kisu kikali kilichochoma kifua chake.



Kwa muda kidogo alikosa cha kunena. Alidhani hakusikia, ama pengine alisikia lakini hakikuwa kinamhusu.



"Unasema??" Akauliza apate uhakika.



"Mwanao ana mimba. Kwahiyo anahitaji uangalizi wako."



Swala hili lilikuwa la kustaajabisha. Hata kwa mama halikumuingia akilini. Ni siku mbili tu tangu Jayit aje hapo na kuweka makazi, siku hizo zatosha mtu kuwa na mimba??



"Ana mimba ya nani?" Mama akauliza akitoa jicho. Akawaza pengine itakuwa ya Phares.



"Ana mimba yangu," Jayit akajibu akionyeshea kucha kifuani mwake. "Amebeba mtoto wangu tumboni. Nataka apate kila aina ya matunzo kabla hajajifungua hivi karibuni!"



Hivi ni nini huyu anaongea?? Akajisemea mama kifuani. Hakuwa anamweleza Jayit hata kidogo. Aliwaza pengine atakuwa amerukwa na akili!



Lakini kuna kitu alikuwa amesahau. Jayit hakuwa binadamu wa kawaida kama yeye, wala hakuwa anafanania na kiumbe chochote kile aina ya mamalia, hivyo hilo lingeweza kuwezekana!



Akamjuza mama. Mimba yake itadumu mwezi mmoja tu ndani ya tumbo la Kainus. Kisha atamzalia mtoto wa kiume atakayekaimu nafasi yake.



Kwa muda wote huo wa mwezi, Kainus anatakiwa kula chakula anachokitaka na kwa muda wowote ule anaoutaka.



Kwa ufupi, asiwe na shida yoyote ile. Hata pale atakapohitaji kulishwa basi ifanyike hivyo pasipo maulizo.



Lakini Jayit akatahadhari. Kwa muda wote ambao Mama atakuwa anakaa na mkewe hapo kasrini, atamrejesha mwanamke huyo kwenye hali yake ya ubinadamu. Na usiku au muda wowote akiwa anahitaji kuwa naye basi atarejea kuwa Kainus!



Asifikirie kutoroka hata kidogo kwani hawataweza kufanikiwa hata robo. Haitamchukua pumzi tatu atakuwa keshampata na adhabu yake ikiwa ni kuuawa, kisha kugeuzwa kuwa jini la ardhini!



Maisha yake yawe kama fuku ama fumbatu wa mchangani!



Mama akaogopa mno. Na kwa kumdhihirishia kuwa ana uwezo, Jayit akamteka mama huyo mkono na kuongozana naye mpaka chumbani alalapo na Kainus.



Akaufungua mlango na kumtaka mama aingie ndani. Alipofanya hivyo na kutazama kitandani akastaajabu kumwona Tattiana! Alikuwa mzima wa afya.



Alikuwa ni yule Tattiana anayemjua yeye. Wakafuatana na kukumbatiana kwanguvu na mwanaye. Jayit akaondoka zake akiwaacha peke yao.



Mama akapapasa tumbo la mwanae. Lilikuwa gumu kuonyesha ndaniye muna kitu. Akatahamaki. Kumbe aliyoeleza Jayit yalikuwa yana kweli ndani yake!!



Tattiana akalia sana. Akamwomba mama yake amkomboe lakini hakuwa na uwezo huo. Watakimbilia wapi na wakati Jayit amefumba himaya nzima kwa walinzi wake??



Na wataenda wapi ilhali ana kiumbe cha mlozi huyo tumboni??



**



"Bella!" Lucy aliita baada ya kufungua mlango kwanguvu. Alikuwa ametoka kukimbia kwa kasi kufika hapo.



Akatazama huku na kule, hakumwona mtu chumbani. Akalaani. Akatoka na kwenda huko nje kutafuta. Baada ya muda mfupi akamwona Bella akiwa amesimama kwenye bustani ya maua.



Akatabasamu.



Akaendea huko akikimbia.



"Bella! Bella!" Akaita akihangaika kuvuta pumzi. Bella akatahamaki na kumtazama.



"Ni nini??"



Lucy akacheka kwa taabu kwa kukosa pumzi.



"Tattiana amerudishwa kwenye umbo la binadamu!!"



"Umejuaje??" Bella akamtazama rafiki yake kwa mashaka. Alihisi pengine amechanganyikiwa.



"Nimejuaje?" Akashangaa Lucy. "Nimesikia kwa masikio yangu haya!"



Akacheka tena.



"Sasa ni wakati wa kummaliza. Siwezi nikachezea nafasi hii tena nikaja chelewa."



"Lu--"



"Ah! Ah! Usianze kuniambia mambo yako. Niambie kitu kimoja tu, utanisadia ama lah??"



Kabla Bella hajasema kitu, Lucy akamwambia:



"Tayari nina mpango."



"Upi huo?" Bella akawahi kuuliza.



Lucy asiwe na haraka akamtaka waketi na kumweleza mpango wake huo alioufuma kwa ustadi. Basi wakaketi kama Lucy alivyokuwa anataka.



Wakiwa wana maua mikononi mwao wakawa wanaongea taratibu. Walikuwa peke yao hivyo hawakuwa na haja ya kuogopa. Upepo ulikuwa unapuliza vema, kwa ujumla hali ya hewa ilikuwa shwari.



"Unajua mama yake Tattiana ameletwa kasrini," Lucy akafungua mjadala wake. Bella alikuwa anamsikiliza kwa umakini. "Ameletwa hapo ili amtunze mwanae ambaye ni mjamzito. Lakini kufanikisha hilo, kwakuwa Tattiana hamtambui mama yake akiwa Kainus, basi mwanamke huyo amerejeshwa kwenye hali yake ya binadamu."



Lucy akaweka komo hapo avute pumzi. Akalinyongorota ua alilolishika mkononi alafu akamtazama Bella akisema;



"Pengine mfalme anaweza kudhani nina chuki na Tattiana, hivyo kikitokea kifo chakw cha ghafla akanishuku. Sasa mimi nataka kumtumia mama yake Tattiana kukamlisha hili."



Bella akaguna. Hakungoja hata mwenzake amalizie habari. Akauliza:



"Unadhani mama anaweza kumuua mwanaye??"



Lucy akatikisa kichwa.



"Tatizo lako wewe mdomo wako umeshinda kasi miguu. Tulia nikueleze."



Bella akabinua mdomo wake asiseme jambo. Akaendelea kutega sikio kwa umakini japo alikuwa akitazama maua yaliyopo mkononi mwake.



"Ndio nataka kumuua Tattiana. Lakini nitafanya hivyo nikiacha mikono yangu ibakie safi. Hakuna mtu atakayejua kama nimemuua mimi. Na nitafanya hivyo kwa kumtumia mama yake mwenyewe, baada ya kumpumbaza na chami ya Quidus."



Bella akamtazama Lucy kwa macho ya uhaba wa imani. Na Lucy akilitambua hilo, akamwonyeshea kiganja chake kama ishara ya kutomtaka aongee.



"Ngoja nimalize ... najua utakuwa unajiuliza ni wapi nitatoa chami hiyo ya Quidus. Ila jua nitaipata! Nitatumia kila tone ya akili yangu kuhakikisha nanyofoa karatasi hizo kwenye kitabu kikuu."



Mara Bella akasimama. Alikuwa na uso wa kuparamiwa. Alishikilia gauni lake akamwambia Lucy:



"Sipo tayari!"



Lucy naye akasimama.



"Ni nini shida yako ewe mwanamke??"



"Lucy," Bella akaita. "Hizo nyayo zako za hatari siwezi kuzifuata. Nilikuwa radhi kufanya jitihada zozote alimradi nikusaidie ila si katika kimo hicho!"



Akashika kiuno chake akauliza:



"Unajua ni nini kinampata yoyote yule anayekaribia kitabu kikuu cha ANGA JEUSI LA KALE??"



"Najua kila kitu. Mimi si mjinga!" Lucy akajitetea.



"La!" Bella akatikisa kichwa. "Wewe ni mjinga. Na nishaona njia zako zinanielekeza kombo. Mimi si mjinga kama wewe. Mapenzi yamekupofusha, huoni, yamekuzibua masikio, husikii!"



Alah! Aliposema hayo akaokota maua yake na kwenda zake. Lucy akabaki akimtazama mwenzake huyo akiyoyoma. Hakusema kitu ila moyoni mwake alikuwa anaungua.



Alisaga meno. Macho yalijaa machozi. Uso wake ukawa mwekundu. Ni nani atakayemuelewa??



Akaketi chini akiwaza. Sasa mpango wake haukuwa siri kwani Bella alikuwa amehofia kushiriki. Je kama akiutekeleza, Bella atabaki akifunga kinywa chake?



Ulikuwa ni mpango hatari haswa.



**



Ni nini kitabu hiki kikuu?? Ni kitu gani hiki ambacho kimetetemesha moyo wa Bella na kumtibua kichwa??



Hichi kitabu ni kama bibilia kwa waumini wa kikristo. Ama kurani kwa wale waislamu. Kilikuwa ni kitabu kikuu. Kikuu haswa ndani ya falme ya Devonship!!



Kilikuwa ni kitabu kinachokaliwa na Jayit pekee. Kitabu kikuu cha ulozi ambacho kilipewa jina la ANGA JEUSI LA KALE kwasababu ulozi wake uliotunzwa humo ndani ndiyo ambao unafanya anga lao lawa jeusi miaka nenda rudi!



Kila siku kuna kunakuwa giza. Ambamo ndani ya giza hilo ndipo kuna nguvu ya Jayit na falme yake.



Kitabu hiki ni SIRI. Ni kharamu kwa mtu mwingine kukitia mkononi isipokuwa Jayit peke yake!



Ndani ya hicho kitabu, kuna ulozi wa kila aina. Wa kila namna aitumiayo mfalme huyo. Ni MOYO wake. Yoyote yule atakayekiuka na kukitia mkononi, basi atakutana na adhma itakayomtenda vibaya asisahau maisha yake yote!



Tangu uwapo wake, hakuna hata aliyewaza kukishika ndani ya falme hii.



Isipokuwa sasa huyu mwanamke ... Lucy! Yote kisa mapenzi. Anataka kuchezea moto.



**



Mpaka anaanza kusinzia, hakumwona Lucy yupo wapi. Bella huyu akajiuliza. Akawaza na kuogopa labda ndiyo Lucy ameendea kile kitabu.



Akajikuta moyo wake unamdunda sana. Alistaajabu kwanini Lucy amekuwa mkaidi kiasi hiko.



Alijigeuza kitandani huku na kule akiwaza. Mpaka anapata usingizi hakuwa amepata jibu wala kumwelewa Lucy. Aliona aihifadhi mikono yake badala ya kuitia ndani ya boksi hatari la bahati nasibu.



Akalowea usingizini.



Ikapita muda kidogo, mlango ukafunguliwa taratibu akazama Lucy. Haikujulikana ametokea wapi lakini hakuwa amekosea kufika hapo muda huo. Alikuwa ana mpango kabambe.



Akaketi kitandani na kumtazama Bella. Alikuwa anahema kwanguvu kuonyesha amezama usingizini. Lucy akatoa kifuko kidogo cha ngozi kwenye pindo lake la nguo, kisha akakifungua kwa kuvuta kamba.



Akazamisha vidole vyake ndani ya kifuko akatoka na unga kiasi. Akamtazama tena Bella kwa sekunde kadhaa. Kisha akasema:



"Kwaheri, rafiki."



Akaurushia unga huo usoni mwa Bella mara moja tu. Na mara Bella alipovuta hewa, akaamka na kuanza kukohoa kwanguvu mno akikaba koo lake.



KOH!! - KOH!! - KOH!!



Lucy akamtazama pasipo kujishughulisha. Bella akamtazama Lucy kwa macho ya hasidi ila hakuweza kufanya chochote kile.



Alikuwa anakohoa sana na mwishowe akakakamaa kuwa gogo! Akiwa amenyooshea mkono wake kwa Lucy.



Alikufa akiwa anajua nani aliyemuua.



**



Aliposhusha mzigo wake akatazama kombo na kombo. Hali ilikuwa shwari. Haraka akaanza kufukua ardhi kwa nguvu zake zote.



Huku nyuma ya kasri hakukuwa mahali panapotembelewa mara kwa mara, isipokuwa kwa sababu maalum au kama kuna haja kubwa.



Palikuwa ni mahali mahususi palipotengwa kama sehemu ya kupumzikia mfalme na mkewe, malkia.



Lucy alishaganya utafiti mdogo akaona hiyo ni mahali patakapokuwa salama kwake kuzika mwili wa Bella kisha akaseme mwanamke huyo hakuonekana pindi atakapoulizwa.



Akachimba shimo la wastani. Hakuchukua muda mrefu sana. Akautumbukiza humo mwili wa Bella kisha akaufunika kwa mchanga.



Akakung'uta mikono na kushusha pumzi ndefu. Kazi ilikuwa nzito. Alijipongeza kwa kuimaliza. Akatazama tena kushoto na kulia, hali bado ilikuwa shwari.



Akachomoka hapo kurudi chumbani kwake. Aliwaza leo atakuwa mpweke sana kwa kuwa peke yake ndani ya chumba kikubwa. Ila ni bora akawa hivyo ... ni lazima atekeleze mpango wake.



Bella alishageuka kuwa adui.



Akiwa ameacha kaburi hilo nyuma kwa hatua kadhaa, hata ajasonga sana mbali, mara akasikia sauti ya kiume ikimwamuru asimame!!



Akahisi mwili umepigwa na ganzi! Alisikia mtetemo mkubwa tokea kichwani mpaka miguuni. Moyo ulikita na kuanza kukimbia kwa kasi sana.



"Ni nini umefukia pale??" Sauti ikauliza. Lucy akakosa cha kujibu. Alikosa hata cha kudanganya.



Mara huyo mwanaume aliyemsimamisha akamtaka ageuke na warejee pale alipofukia jambo akaone. Lucy akageuka akiwa na uso wa hofu. Na kumbe mwanaume huyo alikuwa mlinzi wa kasri.



Akamwomba kwa utashi wake wote amwachie huru. Atampatia zawadi kubwa ambayo hataisahau maishani yake yote.



"Hapana!" Akajibu mlinzi. "Twende huko nikaone ulichokifukia."



Sasa Lucy akawaza, afanye nini kumtoka mwanaume huyo? Hakuwa radhi kushindwa mapema yote hiyo.



Aliamini anaweza kummudu mwanaume huyo mlinzi.



Lakini kabla hajafanta jambo, mara akaongezeka mlinzi mwingine hapo wakawa wawili!! Hakujua mlinzi huyu ametokea wapi. Alifika hapo haraka akiwa anataka kujua kinachoendelea na mwenzake akamjuza.



Wote sasa wakamsihi Lucy afukue alichokifukua. Wakamsimamia mpaka mwanamke huyo alipofanya kama alivyoagizwa. Walipoupekua mwili ule wakagundua ni wa Bella.



"Umemuua mwenzako!!" Mlinzi mmoja akafoka. Kisha akatazamana na mwenzake na kuambiana:



"Tumpeleke kwa mfalme!"



Lucy akahisi ameishiwa nguvu.





Akawaomba sana wale walinzi wamstahi na yupo tayari kuwapatia hata nusu ya mali yake aliyopewa na mfalme. Bado wakashupaza shingo zao. Wakambeba mwanamke huyo kumpeleka kwa mfalme.



Lakini ajabu, walipofika karibia na kasri, mlinzi mmoja akachomoa jambia lake na kumshindilia mwenzake ubavuni! Mwenziwe akapepesuka na kudondoka.



Kisha mlinzi huyo akamtazama Lucy na kumwambia, "ahadi yako imenisisimua. Tutazame namna utanipatia fadhila hiyo kibindoni nifiche siri yako."



Lucy akafurahi. Hakika yule mlinzi kwake alikuwa mwema japo si kwamba alilenga kumtunuku kama adhanivyo. Akatabasamu na kumwambia yule mlinzi kwamba wakutane kesho yake korongoni napo huko watateta yaliyo mema maana sasa ana haraka.



Basi mlinzi akafurahi na ahadi hiyo, akamwachilia Lucy aende zake. Lucy akaenda na kujifungia chumbani asiamini kama amefanikiwa kupita kwenye tundu lile la sindano!



Alijaribu kulikumbuka lile tukio mara kwa mara, basi akaishia kutabasamu mwenyewe. Haki yalikuwa majira yake ya bahati. Na akaamini kama tukio lile lilifanikiwa, basi hata na hili laenda kufanikiwa.



Hili ka kumpata mfalme.



Lakini ngoja ... akawaza. Bado alikuwa na shughuli moja ya kufanya mbele yake. Shughuli muhimu sana katika njia ya kumtia mfalme mkononi. Nayo ikiwa kumuua Tattiana.



Na akaendelea kuwaza. Vipi kama akafanikisha hilo na mwishowe bado mfalme akawa hayupo radhi kuwa naye? Basi hapa akasononeka na moyo wake. Akaumia sana rohoni hata machozi yakamtoka.



Akawaza namna ilivyokuwa kule Devonship. Namna gani baba yake, aliyekuwa mzee wa baraza, alivyojaribu kumpendekeza kwa mfalme awe malkia lakini juhudi zikagonga mwamba!



Akajigeuza kitandani akatazama dari akiendelea kuwaza, na hatimaye akapata la kumfariji. Endapo mfalme akiwa hatakuwa radhi kuwa naye, basi atamroga!



Hatashindwa kufanya hivyo, maana atakuwa ana kitabu cha ulozi cha mfalme mkononi! Hapa akafuta machozi yamitiririkayo mashavuni kisha akatabasamu.



Pene nia pana njia.



**



"Mama," Tattiana alita akiwa amejilaza kitandani. Akamshika mamaye mkono na kumtazama machoni. Alikuwa amechoka, na hata mama yake aliyekuwa ameketi kando kando yake alionyesha uchovu usoni. Macho yake yalikuwa yamelegea na uso wake umepauka.



Tumbo la Tattiana lilizidi kukua. Ungeweza dhani ana mimba ya miezi saba sasa. Hata kiumbe kilichopo tumboni kilianza kuchezacheza huku na huko!!



Alijawa na hofu moyoni mwake. Na hasira pia.



Akasema, "ni nini raha ya mama abebaye mimba ya mtoto asiyempenda? ... nini raha ya kubeba na kuumia kwa maumivu ya kujifungua kwa kiumbe usichotaka hata kukiona?"



Mama yake akamminya mkono akitiririsha chozi. Hakuwa na cha kuongea. Alitazama chini moyoni mwake akiungulia kwa maumivu.



Tattiana akasema, "nateseka na hili, na yahali maumivu haya sitayafurahia mwishoni. Sijui ni soni gani itanijaa usoni nitakapoambiwa mama wa kiumbe cha ajabu huko mtaani, ama kuitwa malkia wa yule mwovu!"



Maneno haya yakazidi kumuumiza mama. Hata akamtaka mwanae asiongee zaidi. Akiwa ameng'ata meno, akamtazama mwanaye kwenye kiino cha macho na kumwambia kwa uchungu,



"Mambo yamebadilika. Huko nje si kama zamani tena kuona watu wakienda mashambani asubuhi, wakarudi na vikapu vya matunda jioni. Sio Goshen ile tena. Sasa huko njiani wanazurura walozi usiweze kutofautisha Goshen na Tanashe.



Jua limegoma kuwaka, anga limekuwa jeusi milele. Hata mwezi nao hauonekani wala nyota. Tumekuwa himaya ya mashetani! Walozi na wadhalimu wapo huru na huku binadamu wakiwa nyuma ya vyuma vya gereza, wakifanywa mateka wa sadaka na kubakwa. Ni kivipi tutajinasua?"



Mama akaangua kilio. Tattiana akamshika bega na kumbembeleza anyamaze. Hakukuwa na haja ya kulia, akifanya hivyo naye atashindwa kujizuia yahali anajua hali aliyomo.



"Inabidi tutoroke humu ndani, mama!" Tattiana akasema. "Siwezi nikakaa humu ndani kujifungua hiki kikaragosi cha walozi. Tufanye namna kujinasua!"



Mama akaguna na kushika tama. Akauliza, "tutawezaje hayo na ingali mlinzi ameketi mlangoni? Kasri limejaa walinzi na hata huko nje wametapakaa kila kona ya nchi?"



Tattiana hakuwa anajua ni namna gani watavuka vikwazo hivyo, ila alidhamiria kutoka hapo kwa namna yoyote ile.



"Njia itapatikana mama. Hatuwezi tukakosa namna. Kadiri tutakavyokaa humu, nitajifungua kisha nitarejeshwa kuwa Kainus. Nami utakuwa ndiyo mwisho wangu kuwa binadamu!"



Lakini mama akawa na hofu. Na hofu hii haikuwa juu ya maisha yake bali ya mwanawe. Jambo hili halikuwa la mzaha kabisa.



"Mama," Tattiana akaita kisha kusema, "ni kheri tukafia njiani kuliko kukaa hapa pasipo kufanya jambo." Kisha akampa moyo, "tutafanikiwa, mama."



Baada ya ukimya kidogo, Tattiana akamtaka mama yake aanze maandalizi ya kutoroka. Na kwakuwa yeye ndiye mzima wa afya, basi atalisimamia hilo ipasavyo. Ana wajibu wa kufahamu idadi ya walinzi kila kona, hata na njia ambazo zina unafuu.



Afanye zoezi hilo ndani ya siku mbili, akusanye taarifa zote muhimu, kisha watoroke kunusuru nafsi zao. Wakimbilie huko kwenye falme zingine watakapokuta binadamu wenzao.



**http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



"Sasa umekuwa tayari. Umekamilika haswa!" Alisema Vemim akitabasamu. Macho yake ya kilozo yalikuwa yanamtazama Rhoda ambaye alikuwa amebadilika kabisa! Uso wake ulikuw mweupe isivyo kawaida.



Kiini cha macho yake kilikuwa kimemeguka na kuwa kama cha mbuzi. Nywele zake zilikuwa nyeupe pe, na zimekuwa ndefu kuliko kawaida, sasa zinagota magotini. Kucha zake nazo zimerefuka na kuwa majembe.



Mdomo wake umekauka, na kinywani meno yamekuwa marefu yakachongoka kama ncha za mshale! Nacho kidevu chake kimekuwa kirefu zaidi.



Walikuwa wamesimama mbele ya madhabahu wakiwa wameshikana mikono. Venim akiwa amevalia joho lake la matukio maalum na pia vilevile Rhoda akiwa amejiveka joho jeupe lililopitiwa na mstari mpana mwekundu katikati.



Madhabahuni hapo palikuwa pamejazwa na mifupa ya binadamu, haswa mafuvu. Kila kona kulikuwa kumewashwa ginga la moto na kushikizwa. Sakafuni kulikuwa kuna ng'ombe mkubwa dume akiwa amechinjwa kwa ajili ya sadaka.



"Na kuanzia sasa, hautoitwa Rhoda tena bali Venis!" Venim akamtawaza Rhoda. Naye akafurahi na kulirejea jina lake jipya kwa tabasamu. "Venis!'



"Naam!" Venim akaitikia. "Na punde tutakapomzika huyu fahali, basi tutakuwa tumekamilisha zoezi letu mwanzo na hata mwisho!"



Venis hakutaka kungoja, maji ameshayavulia nguo zote kwanini wasiyakoge? Basi akamtaka Venim amalizie zoezi hilo upesi. Siku hiyo haikuwa ya kulala kabisa!



Wakiwa wameongozana na vijakazi wao, wakambeba fahali yule na kwenda mashariki ya mbali. Huko kwenye milima ya Kaanjin. Wakachimba shimo kubwa na kumzika humo huyo fahali kisha Venim akateta kwa lugha yake na mara kaburi likaanza kufuka moshi!



Akacheka na kutangaza sadaka imepokelewa. Akamkumbatia Venis kwanguvu na kumnong'oneza, "hatimaye nimetimiza haja yako, sasa nawewe utatimiza yangu?"



Venis akatabasamu pasipo kutia neno. Jibu alikuwa nalo moyoni mwake.



Na basi usiku ulipofika, kinyume kabisa na vile ambavyo Venim alikuwa amezoea kabla ya ujio wa Rhoda kwa kuutumia muda huo kuamka, alikuwako kitandani pamoja na mkewe, Venis.



Kulikuwa kimya miongoni mwao, Venis akiwa amegeuzia uso wake kando na wa mumewe, Venim.



Basi Venim akakohoa kidogo alafu akamgusa mkewe bega. Alipoona kimya, akajikongoja na kumnong'oneza Venis sikioni, "nakuhitaji."



Basi Venis akageuka taratibu na kumtazama muewe. Alafu akatabasamu. Alafu akapitisha mkono wake kifuani mwa Venim kana kwamba anatoboa boksi na mara akanyofoa moyo wa mwanaumre huyo na kuuminya mkononi mwake!



Moyo bado ulikuwa unadunda. Moyo bado ulikuwa wa moto!



Venim akiwa amekabwa na kifo, hakupata kunena neno. Akabaki ameachama. Anatoa macho. Anakufa!! Venis akambusu paji lake la uso na kumwambia kwa sauti ya chini, "ahsante kwa kila kitu."



Kisha akautia moyo wa Venim mdomoni na kuutafuna.





Venim akawa historia. Akalala kitandani akiwa ameachiwa tundu kubwa kifuani mwake. Macho yake yamekodoa kwa kutokuamini. Mpaka anakata roho alikuwa anamtazama Venis. Mpenzi wake wa moyo aliyegeuka kuwa muuaji wake!



Basi Venis akatabasamu na kucheka kwa nguvu. Kifuani mwake alikuwa mweupe kwa kujawa na amani. Sasa kazi imebakia moja tu, nayo ni kupambana na Goshen, kisha kuitawala!



Usiku ukawa mrefu sana kwake maana alibanwa na kufikiria namna ya kuikamata himaya ile. Hakutaka kuwaza namna atakavyokuwa na furaha pindi atakapokaa katika kiti kile cha kifalme kwa kuwa haitakuwa na kifani!



Palipokucha, akaitisha jeshi lote uwanjani na kisha akawatangazia mabadiliko. Kuanzia sasa, ni yeye ndiye atakuwa kiongozi mkuu wa falme hiyo, kwa hivyo wamsikize na kumtii.



Jambo hilo likazua zogo kidogo miongoni mwa askari. Ni kivipi linatokea hivyo kwa wepesi? Yu kwapi Venim - jemedari wao?



"Amekufa!" Venis akasema kwa kujiamini. Akatazama jeshi lake lote la mamia ya melfu, alafu akaongezea. "Nimemuua kwa mkono wangu mwenyewe na kisha moyo wake nikautafuna! ... na hivyo ndivyo ndivyo n'tafanya kwa wale wote watakaokaidi!"



Lakini nani atasadiki hayo? Wote walikuwa wanaamini Venim ni bwana wa vita. Simba wa mapambano. Ni kwa namna gani amalizwe kiurahisi hivyo? Tena na mwanamke!!



Basi Venis akacheka sana. Nyuso za watumishi wake zilikuwa zimejawa na mashaka kwa hivyo alitaka kuwaonyesha umwamba wake hadharani. Namna gani alivyokuwa si mtu wa kutiliwa shaka hata doa!



Akasema, "tazama kule!" Akinyooshea mkono wake magharibi ya mbali. Askari wote wakageuza nyuso zao kuangaza. Kwa mbali jua lililokuwa linachipuka lilikuwa linawaziba kutokuona vema, lakini waliona mwili wa binadamu huko.



Na mwili huo ulikuwa unaning'inia kitanzini. Basi Venis akasema, "na yule ndiye shababi wenu mliyekuwa mnamsujudia! Yupo pale nimeshamuua! Je bado hamsadiki na uwezo wangu?"



Bado hawakuamini kama ni Venim yule, mtu mmoja akatumwa akatazame. Upesi akakimbia kwenda huko. Baada ya muda mfupi, akarejea akiwa na uso wa huzuni na mshangao. Akasema, "ndiyo, malkia. Ni bwana wetu yule!"



Askari wakajazwa na hofu. Miongoni mwao kuna ambao hawakutaka kuwa chini ya Venis, basi wakadondosha ngao zao na mmoja akapaza sauti kwa niaba yao.



"Sisi hatuwezi kumtumikia bwana mwingine zaidi ya Venim!" Wakataka kuondoka zao, walikuwa kama kumi kwa idadi. Venis akapaza sauti yake kuu kuwaita. Na mara kwa haraka, akatokea akiwa karibu na wale askari. Akamkaba yule kiongozi wao na kumnyanyua juu kama karatasi!



Basi wale askari wengine tisa, wakataka kumwokoa mwenzao. Wakamtupia Venis mikuki! Ikamtoboa na kutokea upande wa pili, lakini ajabu Venis hakutetereka. Akaendelea kumkaba yule kiongozi wao na punde akakauka kuwa kama gofu!



Venis akamtupia chini kisha wakageukia wale wengine tisa. Walikuwa wamesimama kwa hofu kuu. Wanatetemeka miguu yao yagongana. Mmoja wao akajikaza nafsi na kujitoa mhanga. Haraka akakimbia kumfuata Venis, ila kufumba na kufumbua akajikuta amenyofolewa koo kwa kucha kali, amelala chini akivuja damu lukuki!



Wale wengine nane wakaogopa sana. Hata wakapiga magoti na kusujudu wakisema, "tusamehe ewe malkia. Nasi hatukujua haya. Tumeshasadiki kuwa bwana wetu yupo ndani yako!"



Na basi jeshi zima likapiga magoti na kusujudu mbele ya Venis kuwa kiongozi wao mpya. Wakaapa kumtumikia kwa nguvu na akili zao.



Venis akatabasamu. Akacheka tena na kusema, "inukeni kwani ninyi mmeshakuwa wangu hata sasa!"



Jeshi likainuka na basi Venis akawaambia kuwa kuna kazi ya kufanya mbele yao. Kazi kuu na watakapoikamilisha hiyo atawapatia zawadi ambayo hawatakaa waisahau maishani mwao!



Akaapa kuwafanya bora zaidi. Maisha yao yatakuwa na kheri kuliko ilivyo sasa maana watakula watakacho na kunywa wanachopenda. Maisha yao yatakuwa paradiso tofauti na walivyokuwa watumwa chini ya Venim.



Basi askari wakajawa na shauku kuskiza. Venis akawahabarisha juu ya kazi hiyo, akasema, "Tutakuwa safarini tangu leo kuelekea falme ya binadamu, huko tutakamata kila kilicho chao na kukifanya chetu. Tutakusanya dhahabu na fedha zao zikawe za kwetu. Na pia tutakunywa damu zao asubuhi, mchana na jioni!"



Habari hizo zikawafurahisha askari. Ni muda sasa hawakufanya matukio kama hayo tokea walipokuwa chini ya Venet. Kwao ikawa sherehe, maana walipata uhakika wa kunywa damu za watu kwa wingi wautakao. Kubaka wapendavyo na hata kukejeli binadamu kwa uwezo wao hafifu.



Basi Venis akawataka wakafungashe haraka kila kinachohitajika, na safari ianze. Askari wakatokomea kwenda kwenye makazi yao. Baada ya lisaa limoja wote wakawa tayari wamekusanyika mbele ya kasri ya malkia Venis kumngoja.



Venis akawatazama askari hao na hakika moyoni akapata faraja. Walikuwa wengi vya kutosha. Na walikuwa wana ari. Aliona machoni mwake hakuna askari binadamu atakayeweza kuzuia vikosi vyake. Kwa hivyo himaya inaenda kuwa mikononi mwake!



Akapandisha mkono wake wa kuume juu ukiwa umebebelea jambia. Nao askari wote wakafanya hivyo wakipiga nduru. Wakaimba Malkia! Malkia! Malkia!



Venis akashuka chini na kumkwea farasi wake. Alikuwa wa rangi nyeupe, mwenye uso wa ajabu. Kwenye paji lake la uso alikuwa amechomoza pembe moja ndefu iliyochongoka.



Basi na safari ikaanza. Safari ya kuelekea Goshen.



**



Mama Tattiana aliingia chumbani alimo mwanae, akasema, "Mwanangu, mambo si mepesi hata kidogo!"



Akaketi kitandani alipokuwa amelala mwanaye. Alafu akamtazama akiwa na uso uliopungukiwa subra. Akasema, "nimetazama kila njia na kila kona na kila chochoro, hakuna palipo salama. Hakuna pa kupita mwanangu!"



Macho ya mama yalikuwa mekundu. Alikuwa amepungukiwa na imani ndani yake. Tattiana akamshika mamaye bega na kumwambia, "usijali, mama. Kama hukuona njia leo huko ulipoenda si mwisho wa tumaini letu."



Mama akakunja sura, akasema, "sasa tutapita wapi? Angani? Sisi sio ndege!"



Tattiana akashusha pumzi na akasema, "Hapana. Hivyo ulivyoona haiwezi kuwa hivyo hivyo muda wote. Kuna wakati walinzi hao watakuwa wanapumzika toka kwenye majukumu yao. Inabidi ujue ratiba zao."



Mama akastaajabu. Aliona kazi inakuwa kubwa kuliko alivyowaza lakini mwanae akamtia moyo. Lazima wafanye hivyo, la sivyo watafia hapo.



"Mama," Tattiana akaita. "Kesho lazima uwe mwisho wetu kuwa hapa maana nahisi kabisa keshokutwa naweza nikajifungua. Huku chini pametanuka na hata viungo vyangu sasa havipo kama hapo awali."



Mama akamshika mkono, na kumtazama machoni. Akasema, "nitajitahidi mwanangu ... basi kula kwanza na upumzike, baadae nitaenda tena kutazama."



Mama akamlisha na kuhakikisha mwanaye ameshiba na yupo katika hali nzuri. Yakapita masaa kadhaa, Tattiana akabebwa na usingizi. Alipokuja kufumbua macho, hakumkuta mama yake. Alikuwa tayari keshajiendea.





**



"Simama hapo hapo!" Sauti kali ilitokea nyuma yake. Haraka akasimama akitetemeka miguu. Moyo wake ukaanza kwenda mbio akichanganyikiwa hana la kufanya.



Basi akasikia vishindo vya miguu vinajongea karibu yake, na alipovisikia karibu zaidi vikakoma, na mara sauti nzito ikauliza, "ni nini unafanya hapa mara ya pili sasa nakuona? Je watazama njia ya kutoroka?"



"Ha - hapana!" Mama akanena akikunja uso wake kwa hofu kuu. Aka akasikia ubaridi wa upanga begani mwake alafu akaulizwa:



"Bali?"





Akabanwa na kigugumizi. Hakujua cha kujibu. Alihisi mdomo umekuwa mzito na mwili umeishiwa nguvu. Akageuka na kumtazana mlinzi aliyekuwa amemshikia upanga, akasema kwa huruma, "Nisamehe!"



Yule mlinzi akavuta hewa kwa mshangao. Alah!! Akaanza omba msamaha maana yule aliyemsumbua ni mkwe wake na mfalme.



"Nisamehe!" Akapiga magoti akikutanisha viganja. "Niwie radhi, sitarudia tena!"



Mama akabaki anaduwaa. Bado hakujua ni nini mlinzi huyo alikuwa anafanya.



"Tafadhali, usimwambie mfalme tafadhali. Ataninyonga kwa mkono wake wa kushoto!"



Hapo mama sasa akaelewa. Akamtaka mlinzi huyo anyanyuke upesi kwani hatomfanya lolote. Aliponyanyuka, mama akajikaza. Akaona anaweza kutumia fursa hiyo kujikomboa na kutimiza haja yake.



Akamuuliza yule mlinzi, "Njia hii huwa mnailinda masaa yote?"



Mlinzi yule akatikisa kichwa. Kisha akamwambia mama Tattiana kuwa wana ratiba ya kulinda eneo lao kwa mujibu wa nyakati. Akamweleza nyakati hizo. Basi mama Tattiana akafurahishwa. Akaendelea kuongozana na mlinzi huyo mpaka pale alipopata haja ya moyo wake.



Kisha kuua ushahidi wa hilo zoezi, akamwambia yule mlinzi kwamba mfalme amemtuma akatekeleze zoezi hilo. Yule mlinzi akaamini.



Mama akaenda zake na kwenda kukutana na mwanae akamweleza yaliyotokea.



"Umefanya kazi kubwa," Tattiana akampongeza. "Sasa tunaweza kutoroka!"



Ila mama akasita. Akamwambia mwanaye kuwa bado hawapo tayari. Kuna vitu baadhi anatakiwa kuvifanya kabla hawajaamua kudumbukiza miguu yao yote dimbwini.



"Tumetambua kuhusu hilo la nje, ila hapa ndani bado ni shida. Naomba nilifanyie kazi kwa muda huu."



Basi Tattiana akaridhia mama akatende kazi yake.



**



"Oragon!" Ottoman aliita akimtikisa kaka yake usingizini. "Amka! Muda umeenda sasa!"



Oragon akaamka na kujinyoosha mwili. Akatazama dirishani, mwanga ulikuwa unapiga. Akapiga mihayo na kujibandua toka kitandani.



Akauliza, "Kwani nini?"



Ottoman akamuuliza, "kwani hujui? ... amka twende sasa! Muda haungoji!"



Oragon akafikicha macho yake yaliyolewa usingizi. Akamtazama vema Ottoman, alikuwa amebebelea kifurushi mgongoni.



Akauliza, "Cha kwangu kipo wapi?"



Ottoman akastaajabu, "mimi nitajuaje ulipokiweka?"



Usingizi ukamkata Oragon. Akatazama huku na huko. Alikuwa amesahau alipoweka kifurushi chake. Na alihofia kwa namna wanavyokaa mule ndani na wadokozi na wezi, pengine hakitakuwapo.



Akasaka chumba kizima, hakuona! Jasho likamtiririka. Baadaye ndipo akagundua alikuwa amekiweka uvunguni mwa kitanda. Haraka akatazama. Napo hakikuwepo! Kilikuwa kimebebwa.



Akaketi akishika kichwa. Roho ilimuuma sana kukipoteza kifurushi chake. Alilalama na akitaka kwenda kuwatafuta wale majamaa wawili wanaoishi nao, ila Ottoman akamsihi asifanye hivyo. Watapoteza muda ilhali wana safari.



Kishingo upande, Oragon akaridhia. Sasa walikuwa na kifurushi kimoja tu cha thamani. Wakaanza safari yao kwa tahadhari.



Njia nzima wakawa wanaangaza usalama wao. Kama wangelikamatwa na askari basi ungekuwa mwisho wao papo hapo. Wakafanikiwa kutembea kwa muda nusu saa. Wakafika mahali ambapo askari walikuwa wamejikusanya kwa uwingi wakiwa wanateta. Wakabadili njia.



Wakatembea tena kwa mwendo wa dakika arobaini na tano, mbele yao wakawaona askari wanne wakiwa juu ya farasi. Walikuwa wameshikilia mikuki na migongoni wakiwa wamebebelea pinde za mishale.



Wakajibanza nyuma ya migongo ya watu, wakafanikiwa kupita salama. Sasa wakawa wamebakiza kama hatua kama mia mbili kuukuta mpaka wa falme ya Goshen. Huko nyumbani walipoamua kurudi baada ya kushindwa maisha himaya zingine.



Ila wakiridhia na kutenda hilo baada tu ya kudhani kuwa Goshen mambo yatakuwa yamebadilika maana walishaona ishara kadhaa. Moja, matunda ya Cedar yamekuwa yakiuzwa falmw zingine tofauti na awali. Pili, walisikia utawala wa Goshen umebadilika japo hawakujua umebadilikaje.



Hadithi za kutisha walizozisikia kuhusu Goshen hazikuwaingia akilini maana waliamini hakuna mtu yeyote aliyekuwa anaijua Goshen mbali na wao ambao ni wenyeji.



Basi wakiwa wanasonga, wamekaribia na mpaka, wakaanza kuona mwanga ukipungua. Anga lilianza kutwaliwa na wingu jeusi zito kana kwamba mvua yataka kushuka!



Wakadhani wafanye upesi kabla mvua hiyo haijawashukia. Wakakimbia na kuzama ndani ya himaya ya falme ya Goshen. Sasa wakajikuta wapo kizani.



Kiza lisilo na kikomo na hapo hawana hata tone la ginga la moto kuwapa mwanga.





**



"Mfalme! Mfalme!" Sauti ya kijakazi wa Jayit ilipaza. Alikuwa ana uso uliowehuka na macho yaliyobebelea hofu.



Kichwani alikuwa amefunikwa na ngao ya chuma. Mkononi amebebelea jambia refu lenye kutu. Mwili wake ulikuwa umemomonyoka akitembea kama mtu aumwaye mifupa.



Alisimama mlangoni mwa chumba alalacho mfalme, akiwa mhafifu wa subira. Alitamani hata apasue mlango na kuzama ndani.



Basi muda si mrefu mlango ukafunguliwa, Jayit akatoka. Alikuwa amevalia joho lake refu jeusi lililotengenezwa na ngozi za binadamu.Macho yake yanatisha na kuwaka mithili ya paka! Uso wake unaogofya. Na hata ananuka umauti!



Akamuuliza yule kijakazi kuna nini? Basi yule kijakazi akiwa anaogopa mno, akasema, "Ee mfalme, tumevamiwa!"



Jayit akatoa macho. Akatisha zaidi! Akamnyaka yule kijakazi wake na kumuuliza, "ni nani huyo anathubutu kumvamia Jayit?? Jabali la mwamba mgumu. Mfalme wa anga jeusi?"



Kijakazi yule akiwa anatetemeka, akasema, "sijui Ee mfalme. Ila naye si binadamu. Ni mlozi! Na amesema anataka kuonana nawe kule kondeni!"



Jayit akang'ata meno na kunguruma kama simba! Akafoka, "yu kwapi jemedari?" Kijakazi akamjibu yu tayari kondeni akiwa na askari. Basi Jayit akaagiza kijakazi huyo atoe taarifa ya kuvamiwa falme nzima. Wote wakutane huko kondeni!



Basi ndani ya muda mfupi, tarumbeta kubwa likalia likipulizwa juu kabisa ya jengo la kasri. Falme nzima ikapata kusikia! Na kujua kuwa ipo hatarini.



Wapo vitani.



**



"Wewe ni nani? Na unathubutuje kutia mguu kwenye makazi yangu?" Sauti nzito iliuliza ilhali mtu aulizaye akiwa haonekani.



Venis aliyekuwa amesimama mbele ya jeshi lake mamia ya maelfu, akakunja shingo kuangaza. Mbele yake, hatua hamsini, alikuwa amesimama Phares akiwa na askari wapatao mia tatu kwa idadi. Askari hao hawakuwa wanamtisha hata kidogo japo alipigwa na mshangao kukuta Goshen imekaliwa na walozi!



Hakuwa anajua mabadiliko hayo yamefanyika lini na nani akiyaongoza. Ila kama kuna kitu alikuwa anaamini, basi na kuitia Goshen mikononi mwake.



"Wewe ni nani?" Venis akapaza sauti. Kisha akakodoa macho yake, "Kama u kweli wajiamini, jitokeze na upambane kilingeni!"



Lakini kama kuna kitu hakukijua, ni kwamba aliyekuwa anaongea ni Jayit. Jabali la kilozi. Lakini pia Jayit hakuwa peke yake wakiwa hawaonekani. Walikuwa na kundi lake kubwa lingine la kijeshi mbali na lile lililokuwapo pale!



Na wakati huo Venis akiwa anatafuta nani anaongea na yupo pande gani, basi jeshi la Jayit lilikuwa tayari limeshamzunguka.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

"Wataka kuniona, sio?" Akasikia swali. Kabla hajajibu, kugeuka kushoto akastaajabu kumwona Jayit amesimama akimtazama. Mikono yake ameitandaza kana kwamba anangoja kumbato.



"Umeniona sasa," mwanaume huyo akasema kwa kiburi cha majivuno. "Sasa unaweza ukaniambia unataka nini kwangu?"



Kabla Venis hajajibu, akastaajabu kuwaona askari wa Jayit wakiwa wamemzunguka. Kwa haraka walikuwa kama wanaume alfu tano! Hakuona wametokea wapi. Alijikuta tu tayari yu mtegoni.



Akajikaza na kusema akimtazama Jayit, "nimerudi nyumbani. Na kamwe hautanizuia kuichukua Goshen!"



Jayit akapaliwa na kicheko. Akacheka sana tena sana. Akiwa kichekoni, akapiga makofi mawili, na mara jeshi lake likavamia askari wa Venis.



Mapambano makubwa yakazuka! Ila askari wale wa Venis wangewezaje kupambana na watu wasioonekana?? Ndani ya nusu saa, wakajikuta wote wakiwa wameshauawa! Hakuna hata mmoja aliyebaki anahema.



Napo ndipo Jayit akakoma kucheka. Akakaza uso na kumsogelea Venis. Akamuuliza, "ulikuwa unasema??"



Basi Venis akatazama nyuma yake, hakukuwa kumebakiwa na mtu hata mmoja, lakini hakujita, akajikaza na kumsogelea Jayit, akamwambia anataka kuichukua na kuiweka Goshen mikononi mwake.



Jayit akatabasamu. Akamwambia mwanamke huyo kuwa hana huo uwezo, na kamwe hawezi kumtikisa kwani yeye bado yu mchanga.



"Mimi ni Jayit! Jabali la kwenye miamba. Siwezi kutikiswa na yeyote yule juu ya uso wa dunia. Hata wewe naweza kukumaliza kwa kutumia mkono wangu mmoja tu!"



Venis akang'ata meno kwa hasira! Na mara akaanza kupambana na Jayit, hakuna askari aliyethubutu kuwasogelea maana walipigana katika ulimwengu wao wa tofauti kabisa!



Walipigana kwa ustadi wa ulozi, walipigania hewani pasipo kugusa ardhi. Na wakiwa kwenye pambano hilo, upepo mkali ukazuka, wale askari wote wakalazwa chini, wasione kinachoendelea. Katikati ya Jayit na Venis kulikuwa na kitu kama mduara wenye mwale mkali uliokuwa unawaumiza macho kila walipojaribu kuangaza.



Ila mara, wakamwona Jayit akiwa ametupwa nje ya mwale huo unaong'aa. Akadondoka chini kama mzigo wa kuni, kisha akalalama kwa maumivu na kukohoa mara mbili.



Akatazama mwale wa mwanga angani, mara ukanyauka na Venis akaonekana akiwa amesimama anaelea. Mkononi mwake alikuwa amebebelea moto uunguzao ila yeye usimguse!



Kabla Jayit hajafanya jambo, mara Venis akatupa mikono yake kwenda kwa jeshi la Jayit! Askari mamia wakashikwa na moto kana kwamba wamemiminiwa petroli.



Wakawaka haswa. Wakapiga kelele kali za maumivu wakikimbia huku na huko!



Venis akacheka akielekezea kichwa chake angani. Mikono yake inayowaka moto alikuwa ameitanua kana kwamba ndege anayetaka kupaa.



Alikuwa ana haja ya kucheka. Alimjulia adui yake. Alifanikiwa kujua siri ya kumsumbua Jayit, jabali la mwamba, ya kwamba alikuwa ni mdhaifu awapo mwangani. Jayit ni mtu wa giza, mtu wa kiza. Hawezi kuwa na nguvu zake akiwa mwangani!



Na basi kulitambua hilo, Venis akajizingira na mwanga mkali. Kisha akamshambulia Jayit kwa upanga wake wa kilozi.



Askari wa Jayit wakamezwa na hofu. Waliona sasa wanakwisha. Venis akawatazama tena kisha akawamwagia moto pasipo huruma. Wakaungua mamia kwa mamia. Wakakimbia huku na huko wakilia!



Venis aliporudisha uso wake kumtazama Jayit, akastaajabu hayupo! Akatazama kila pande, Jayit hakuonekana. Basi kwa hofu akaanza kurusha moto kila upande, kushoto na kulia, juu na chini!!



Akaangaza akikunja shingo huku na kule akitoa macho yake yanayotisha!



Sasa akawa amepatikana. Hatimaye akarudi kwenye kiwanja cha kujidai cha Jayit maana mwanaume huyo mlozi alikuwa amefichama akiwa anamtazama, akimvizia kumpa shambulio kali litakalomwacha hoi hajiwezi.



Basi kufumba na kufumbua, mara akahisi mtu nyuma ya mgongo wake. Kabla hajashtuka, akadidimiziwa kisu mgongoni kikatokea tumboni!



Akaachama mdomo na kutoa macho ya kifo. Jayit akamfunika kinywa na kiganja chake kipana kisha akampulizia upepo masikioni kisha akachomoa kisu chake na kumwacha Venis adondoke chini.



Ila bado hakuwa amekufa.



**



"Mke wa mfalme ametoroka!" Askari mmoja alifoka. Lucy akafungua mlango na kuchungulia kwa jicho moja. Koridoni akawaona askari watatu waliobebelea mikuki, walikuwa wanapashana habari za kutoroka kwa Tattiana na mama yake.



"Lazima tuwatafute," askari mmoja akasema akiwa na uso wa woga. "Mfalme hatotuelewa. Atatuua. Hima twende!"



Mara wote watatu wakatokomea wakikimbia upesi. Basi Lucy akafungua mlango zaidi na kutoka. Mkononi mwake alikuwa amebebelea kitabu kile KIKUU. Alikuwa ametoka kukiiba!



Haraka akashika njia kukimbilia chumba chake. Alipokamata kona ya kwanza akakutana na askari. Akasimama haraka, wakatazamana. Askari akatazama mkononi, akaona kitabu kile KIKUU mkononi mwa Lucy.



Kabla hajafanya kitu, Lucy akamuwahi kwa kumpiga ma kitabu kichwani. Askari akadondoka chini kwa kuzirai! Lucy akaendelea kukimbia na mwisho wa siku akaingia chumbani na kujifungia.



Haikuwa ngumu sana kwani askari hawakuwapo wengi kasrini. Waliosaliani kama kumi tu kwa idadi.



Basi haraka, Lucy akafungua kitabu kile KIKUU na kuanza kupekua. Kilikuwa ni kikubwa mno. Hakuna kitabu kikubwa cha kilozi kama hiki. Kutafuta kitu unachokitaka, ilihitaji utulivu mkubwa na muda haswa.



Ila Lucy alikuwa tayari alimradi lengo tu litimie! Lengo la kupata chami ya kumfanya Mfalme ampende. Asisikie wala kuona yeyote zaidi yake tu!





**



"Kazana!" Mama alisema akitazama mbele. Tattiana alikuwa amechoka kukimbia. Miguu inamuuma. Anahisi mwili wake umekuwa mzito kupitiliza!



Walikuwa ndani ya msitu wakikimbia kutafuta himaya nyingine wanusuru nafsi zao. Walikuwa wanafahamu fika kama wakishindwa kutoroka siku hii basi hawatakuja kufanikiwa milele. Hii ndiyo ilikuwa siku pekee. Vita iliyozuka, iliwapa mwanya wa kujivinjari na kutimiza mpango wao kwa wepesi.



Tattiana akasimama akihema kama mbwa. Akashika kiuno chake akipambana kupata hewa.



"Nimechoka!" Akanena kwa tabu. "Nimechoka, mama!"



Mama naye akadaka kiuno chake, alikuwa amechoka mno. Ila hakuwa na budi kuendelea kukimbia. Akamsisitizia mwanae aamke waendelee kukimbia kwani la sivyo, watakutwa hapo na kukamatwa.



Tattiana akashindwa kabisa kuendelea. Aliomba aheme kwanza. Wakangoja kwa sekunde kama ishirini hivi, na mara wakasikia sauti ya kishindo cha watu wakija! Wakashtuka. Walikuwa ni askari wa Jayit. Wale wanaume watatu.



Basi Tattiana na mama yake wakaanza kujikongoja kukimbia. Mwendo wao ulikuwa hafifu maana walichoka sana. Na hawakuwa wanaona vema mule msituni kutokana na kiza.



Kwa hivyo ndani ya muda mfupi tu, wale askari watatu wakawaona.



"Wale kule!"



Wakakimbia kwa kasi na kuwanyaka.



"Mlidhani mnaweza kutoroka kirahisi hivyo?" Askari mmoja akawauliza kwa kebehi. Wakaangua kicheko. Tattiana na mama yake wakalia wakiwaomba wawaachilie, ila askari hawakujali. Wakawaswaga waende mbele!



Wakasonga hatua kumi tu, mara askari mmoja akapigwa na jiwe kubwa la kichwa. Akadondoka chini maiti! Wenzake wakatahamaki na kuangaza.



Huku na huko, huku na huko, mara wakatokea Oragon na Ottoman! Mikononi mwao walikuwa wamebebelea magongo makubwa. Wakawafokea wale askari wa Jayit wawaachilie wanawake hao mateka haraka iwezekanavyo!



Wale askari wakacheka. Mikononi mwao walikuwa wamebebelea jambia ndefu zinazong'aa. Alafu wakina Oragon wamebebelea magongo na kuwatishia. Lilichekesha hili!



"Mtatufanya nini tusipotii amri yenu?" Akauliza askari mmoja.



"Tutawamaliza!" Akajibu Oragon akijikaza.



Basi wale askari wakawavamia wakina Oragon na kuanza kupambana nao. Vijana hao hawakuwa na ujuzi wowote wa sanaa ya mapambano. Pili, hawakuwa na silaha ya kivita, kwa hivyo, Walikuwa wanapigana kwa nasibu. Kwa wazi wasingeweza kufua dafu kwa wale majabali!



Basi baada ya muda mfupi, Oragon akawa amesimikwa jambia ya tumbo. Akapiga kelele kali ya maumivu. Ottoman akawehuka kwa hasira lakini hakuwa na cha kufanya.



Aliambulia kumtwanga askari mmoja gongo la kichwa na kumdondosha chini, ila naye akawahiwa kusimikwa jambia ya kifua. Akadondoka chini akimimina damu pomoni.



Askari pekee aliyebakia, ambaye ndiye alimsimika jambia, akamsogelea na kumtazama kwa kebehi. Akatabasamu.



Ila mara ghafla, akakitwa na jiwe kubwa kichwani. Lile lililomkita mwenzake wa awali. Akadondoka chini na kufa papo!



Alikuwa ni mama Tattiana ndiye aliyemsulubu. Haraka akiongozana na mwanae, wakamfuata Ottoman kumjulia hali.



"Ottoman!" Mama Tattiana akaita. Ottoman akatabasamu. Kaka yake Oragon alikuwa tayari ameshakata kauli.



Ottoman akamtazama Tattiana kwa macho yake yanayofifia. Kisha akasema kwa kinywa chake kinachotema damu.



"Nisamehe, Tattiana."



Tattiana akavuja machozi. Akamshika Ottoman mkono. Ottoman akafariki.



Tattiana akiwa hapo anamtazama Ottoman, mara akabanwa na uchungu wa kujifungua. Akalia kwa maumivu makubwa. Mama yake akajaribu kumtuliza na kumsaidia.



Ndani ya muda mfupi akajifungua kiumbe cha ajabu. Binadamu si, mnyama si.



Akiwa mjawa wa hasira za kisasi, Tattiana akanyaka jambia ya wale askari, kisha akamchoma kifuani yule mwana aliyemzaa, mara mbili pasipo kujiuliza!!



**



Kule uwanja wa vita ...





Puuh!! Venis alidondoka chini kama mzigo, Jayit akanyoosha mikono yake juu, askari wake wakapiga kelele kuu ya ushindi.



Sasa Venis hakuweza kuamka tena. Alikuwa ameshindwa! Alikuwa amechakazwa vya kutosha. Hakuwa na ulozi wowote mwili mwake kumnusuru na kadhia hii.



Upepo ambao Jayit aliupuliza kwenye tundu lake la masikio ulimmaliza na kumgeuza kuwa mtu wa kawaida mbele ya jabali huyo.



Jayit akacheka sana. Akapiga kifua chake konde kwanguvu na kumtazama Venis aliye hoi hajiwezi. Akasema,



"Mimi ni jabali! Jabali wa kiza kikuu. Hakuna anayeweza kupambana nami akatoka na uhai! Kaskazini ya dunia. Kusini ya dunia. Si magharibi wala mashariki! ... hakuna!"



Mara akashtuhwa na sauti ya kike. "yupo wa kupambana nawe!"



Akageuka haraka na kuangaza. Upande wake wa magharibi akamwona Malkia Sandarus akiwa anakuja, anatembea kwa madaha. Pembeni yake walikuwapo Fluffy, Zura, Alk na Seth!



Kichwani Malkia alikuwa amevalia kofia ya Pharao, na kifuani mwake ana mkufu wake amali.



Jayit akatazama vema. Watu hao hawakuwa na jeshi. Na wala mikononi mwao hawakuwa na silaha! Zaidi Malkia alikuwa ameshikilia kamba kumvuta farasi wake.



Basi akacheka. Akauliza, "na wewe ni nani??"



Malkia hakujibu mpaka alipomsogelea karibu. Akamwambia, "Mimi ni Malkia Sandarus. Jinamizi ndotoni mwako. Mtawala wa haki wa Goshen. Nimerudi nyumbani."



"Malkia Sandarus?" Jayit akavuta kumbukumbu. Alah! Akamkumbuka. Akacheka zaidi na kumuuliza, "haujionei huruma kukaa mbele yangu? Jabali wa miamba?"



Malkia akatabasamu. Kisha akatikisa kichwa chake na kusema, "yakupasa wewe ndiye ujionee huruma. Umewachezea wanangu vya kutosha. Sasa mama yao yupo hapa. Kwa usalama wa uhai wako, kimbilia Tanashe kabla sijaruhusu mikono yangu ikutawanye!"



Jayit akaguna kwa dharau. Akatazama kando ya Malkia na kusema,



"Naona umejipanga haswa!"



Askari wake wakaangua kicheko.



Malkia akamwambia, "Basi na kwakuwa umekuwa mkaidi, acha nikufunze!"



Akatanua mikono yake, mara ardhi ikaanza kutikisika. Kufumba na kufumbua, watu wakaanza kutokea chini ya ardhi!



Mamia! ... mamia! ... mamia! ... maelfu! Maelfu!! Maelfu!!



Jayit akaachama kwa kushangaa. Akasema: "jeshi la wafu!!" Hakika akapaliwa na hofu.



Haraka akatekenya ulozi wake na kupotea eneoni mara moja, akaacha jeshi lake likiwa limezingirwa na maelfu ya askari waliokufa miaka nenda rudi huko nyuma!



Jeshi nalo likatwaliwa na woga. Hawakuwahi kuona mifupa ikiwa imesimama. Inaongea. Inatembea. Inabebelea silaha!!



Basi jemedari wao, bwana Phares, akajitutumua, na kuwaamuru washambulie. Loh!! Wakakutana na kitu wasichokitarajia. Kitu ambacho hawakuwahi kukutana nacho kwenye uwanja wowote wa vita!



Utapambanaje na watu wasiokufa?? Hata pale walipopotea kimazingara, askari wa jeshi la wafu nao wakazama ardhini na kutambua nyendo zao. Wakawamaliza!!



Ndani ya muda mfupi maiti zikazagaa na kufunika ardhi. Malkia akatanua mikono yake, na kufumba macho. Mara hao maiti wakaanza kunyanyuka na kujiunga jeshi la wafu!



Wote.





**





Akiwa na uso wenye hofu, alifungua makabati na kila droo. Hakuona kitabu!!



Akashika nywele zake akiwa amewehukwa. Alichanganyikiwa haswa. Kitabu kiko wapi?? Alikihitaji kupambana na jeshi la wafu!



Alikihitaji kupata chami ya kumudu jeshi lile la kutisha! Jeshi la watu wasiokufa!!



Akainamisha mgongo wake atazame uvunguni, hakukiona, alipoamka akakutana uso kwa uso na Malkia!



Pia uso kwa uso na ncha ya jambia iliyomtoboa kifua.



Akapiga kelele za kuugulia. Kama haitoshi, Malkia akachomoa jambia yake upesi kisha akamfyeka kichwa. Mwili wa Jayit ukadondoka chini, kichwa kikimbilia uvunguni!

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Basi jua likarejea angani, kukawa kweupe. Mabaki yote ya Jayit yakaungua kwa kushindwa kustahimili mwanga wa jua, hakuna hata chembe ya Devonship iliyobaki! Wote waliungua na kugeuka majivu!



Watu wote wa Goshen wakafunguliwa toka vifungoni. Nao wakambeba Malkia juu wakamzungusha himaya nzima kwa furaha kubwa! Hata wakina Tattiana wakasikia kelele hizo, nao wakajikokota kushuhudia.



Malkia alikuwa amerudi!



Goshen ilikuwa imerudi, hatimaye.



MWISHO

0 comments:

Post a Comment

Blog