Simulizi : Mkufu Wa Malkia Wa Gosheni (2)
Sehemu Ya Pili (2)
Macho yake bado hayakuwa yanaona vema. Na kando yake, Seth bado hakuwa ameamka
"Tumefikaje hapa?" Akauliza Malkia kwa mbali. Akajaribu kuamka lakini akashindwa, hakuwa na nguvu.
"Tulikuja kuwaokoa," akajibu Fluffy. "Ila pasipo msaada wa hawa Azeth tusingeweza abadani!"
Zura akamkatiza.
"Nadhani ni sahihi ukapumzika, Malkia," akasema akiwa amemuwekea kiganja kwenye paji lake la uso. "Mlidungwa sumu kali na wale watu. Miili yeni imechoshwa sana kwani mlikuwa mkitota sana. Pumzika sasa, tutaongea hapo baadae."
Malkia akataka kunyanyuka. Zura akamrudisha chini.
"Tafadhali. Kama unataka kuishi, fanya ninachokuambia, Malkia. Bado tunakuhitaji."
Malkia akataka kusema jambo, ila kichwa na macho vikamzidi uzito, akapitiwa pasipo ruhusa!
"Unadhani atakuwa sawa?" Akauliza Fluffy.
"Natumai atakuwa sawa. Yeye ni Malkia, hakuna hii safari pasipo yeye."
Yalikuwa ni majira ya mchana wa jua la kando kidogo huko angani. Hali ya hewa haikuwa haba, upepo ulikuwa unapuliza kuashiria ujio wa nyakati za vuli ndani ya himaya ya Goshen. Anga nalo halikuwa kavu bali lililojawa na mawingu kadha wa kadha mashariki kwa magharibi.
Ingawa jua halikuwa mbali sana na utosi, lilikuwa dhaifu. Na mara nyingi likiwa linamezwa na kutemwa na mawingu yale yaliyokuwa yamejazana angani. Mchezo huo ungeweza kukugharimu muda wako kwa kuzubaa kuangaza, ukivutiwa na yale maumbo mbalimbali ya mawingu yalivyokuwa yanapokezana kulidaka jua na kisha kumtupia mwenzake mithili ya mchezo wa mpira wa pete.
Kwa wakati huo, Melkizedek pamoja na mkewe walikuwa wapo hospitalini na nyuso za furaha. Siku hiyo kwao ilikuwa pendwa kwani binti yao aliyekaa hospitalini kwa muda, hatimaye alikuwa anaruhusiwa kurejea nyumbani.
Melkizedek kuhakikisha hakuwa mikono mitupu, akabebelea maua ya uwaridi, mafuta ya mizeituni na marashi ya violeti. Mama naye asiwe nyuma, akabebelea mkufu wa thamani, bangili na kibanio cha nywele chenye vijenzi vya almasi.
"Sasa mnaweza kwenda naye nyumbani," akasema daktari kwa bashasha la tabasamu. "Yupo kheri kabisa. Tumehakikisha hakuna hata tone la sumu lililobakia mwilini!"
"Ahsante sana daktari," Melkizedek akamkabidhi mkono, na kuuliza: "Sasa naweza nikamwona mwanangu kipenzi?"
"Bila shaka!" Daktari akawaelekeza mahali watakampokuta, basi wakaenenda. Wakamveka na kumnyunyuzia mafuta mwana wao na kumbeba kuelekea naye nyumbani kwa rashasha za furaha.
"Hakika umependeza. Kweli wewe wastahili kuwa mke wa mfalme!" Akasema mama akimtazama mwanae, Tattiana. Binti akatabasamu asiseme jambo.
Kichwani kwake hakuwa sawa, bali aliyetingwa na mawazo. Japokuwa kitoroli kile cha farasi cha thamani walichopanda kilikuwa kikiwapeleka kando na kando kwa mwendo, akili yake ilikuwa imetulizana tuli kumfikiria Roboth.
Kwa muda sasa hakuwa amekuja kumwona hospitali. Si kawaida yake. Atakuwa amekumbwa na nini?
Kabla ya kujiuliza kuhusu usalama wa mpenzi wake huyo, Tattiana alikuwa amejawa na wivu kifuani. Akajiuliza, atakuwa amempata mwanamke mwingine wa kumsahaulisha laaziz wake kitandani? Lakini mbona huwa anasema kuwa yeye ndiye mwanamke pekee mwenye nafasi moyoni mwake?
"Nakuapia, Tattiana. Wewe ndiye mwanamke wa maisha yangu. Kama moyo wangu ungalikuwa na sebule na vyumba vitatu, vyote ningekukabidhi wewe mie nikajilaza kibarazani." Sauti ya Roboth ikatembelea masikio yake.
Ikajirudia tena na tena, basi akajikuta anatabasamu mwenyewe macho yake yakiwa mbali milimani. Hakutoka kwenye fikra hizo mpaka alipowasili nyumbani. Akala na kunywa na kisha akajiweka chumbani kwake. Hakutaka kukaa na watu, hata kaka yake Fanty.
"Mpatie muda wa kupumzika, bado hayuko sawa," Mama akahauri. Fanty kishingo upande, akiwa anamtazama dada yake aliyekuwa amejilaza kitandani, akafunga mlango na kwendaze.
Tattiana akaamka na kwenda dirishani, akatazama mandhari ya huko nje na angani. Moyoni akawa anasema na muda. Alikuwa anangoja jua likaribie kulala, afanye jambo.
Alipohakikisha majira yamefika, na hakukuwa na wazazi nyumbani, akatoka chumbani akimuaga na kumpa maagizo kaka yake.
"Chunga mdomo wako, nitarejea hivi punde. Mlango wangu nimeutia ufunguo, watakapotaka kuniona, uwaambie nahitaji kupumzika. Sawa?"
Akakwea na kuruka ukuta aende kwa 'kina Roboth akajua hatma yake. Akatembea na kukimbia kama mwizi. Kabla ya jua kulitelekeza anga akawa amefika, akamkuta Roboth bandani akihudumia mifugo.
"Robo!" Akaita.
Roboth akashtuka kumwona Tattiana. Haraka akatazama nyumbani kwao kisha akamvutia binti huyo bandani.
"Umefikaje hapa? Mama yangu amekuona?"
"Hapana, sijaonana naye. Haukuja kuniona hospitali ... vipi, umeshapata mwanamke mwingine?" Akauliza Tattiana akiwa anamtazama Roboth machoni.
Roboth akatikisa kichwa.
"Hapana, sijapata mwingine. Na sitaweza kupata." Alipomaliza kauli yake hiyo akakohoa. Akataka kuendelea kunena, ila akakohoa tena na tena! Kuanzia hapo hakupata ahueni, akawa anakohoa na kukohoa.
"Roboth, vipi upo sawa?" Tattiana akajawa na mashaka. Hata Roboth akashindwa kujibu kwa kukohoa. Akakohoa mno kiasi cha kukosa pumzi. Mwishowe akadondoka na kuzirai!
Tattiana akatoa macho ya mshangao. Hakujua kipi afanye, akatoka nje ya banda na kuangaza. Kisha akarudi tena akiwa amechanganyikiwa. Akajitahidi, kwa nguvu zote, akambeba Roboth na kumpeleka ndani.
Akamlaza kitandani na kumpepea akitumia nguo yake.
"Roboth! Roboth!" Akaita akimpigapiga Roboth mashavu. "Amka! Amka, Roboth!"
Macho yake yakaanza kuwa mekundu. Punde yakajaa na kuanza kutiririsha machozi!
Akamtazama Roboth aliyekuwa ametulia tuli, akagundua mwanaume huyo alikuwa ametokwa na vipele vidogo vyekundu nyuma ya mikono yake.
Akavutiwa kutazama zaidi. Ni nini kinamsumbua Roboth? Akamtazama shingoni, mgongoni na hata miguuni, kote huko akaona dalili ya vipele hivyo vyekundu kwa mbali.
Akafungua kinywa cha Roboth, ndani ya lips zake akaona uweusi usio wa kawaida. Hapo Tattiana akajua ya kwamba Roboth anaumwa. Hakujua ni ugonjwa gani, ila alikubaliana na moyo yake kuwa si mdogo kabisa.
Akiwa kwenye buwazo hilo, mama yake Roboth akaingia ndani na kustaajabu kumwona.
"Umefuata nini hapa?" Mama akauliza akimtazama kwa macho ya uhasidi. Lakini kabla hajajibiwa, akauliza maswali mfululizo kuhusu hali ya mwanae. Akapiga magoti na kuanza kumuita akimtaka aamke.
"Umemfanya nini mwanangu?"
"Sijafanya kitu, mama. Amedondoka baada ya kukohoa mno," Tattiana akajitetea. "Atakuwa anaumwa sana. Tumpeleke hospitali. Hali yake si nzuri kabisa!"
Mama akajawa na kilio asiseme kitu. Giza lilikuwa linaingia na Tattiana alitakiwa arudi nyumbani. Akavua mkufu wake aliovekwa na mamaye, na kumkabidhi mama yake Roboth.
"Mkufu huu ni wa thamani kubwa. Naomba uuze upate pesa ya kumuwahisha hospitali, na matumizi mengine madogomadogo!"
Aliposema hayo akanyanyua gauni lake na kutoka ndani upesi! Akaanza kukimbia kurudi nyumbani akiomba akute hali shwari huko aendako.
Aliuondoa tu mwili wake nyumbani kwa 'kina Roboth, ila akili na moyo wake aliviacha huko. Aliendelea kuvuja machozi akijiuliza juu ya hali ya mpenzi wake, na hata akijuta kwanini alimshutumu na kumdhania ubaya.
Moyo wake ukawa mzito. Kichwa chake kikawa kinagonga kama saa ya ukutani. Joto la mwili wake likapanda. Usipite muda mrefu, akadondoka chini!
Kwa mbali kichwani kwake akawa anasikia watu wakicheka na kuteta. Hakuwa anawajua watu hawa ni wakina nani. Hakuwa na nguvu ya kunyanyuka kabisa. Na kabla hajapotea kabisa kwenye ulimwengu wa kupoteza fahamu, kwa mbali akasikia sauti ya daktari:
"Hatakiwi kufanya kazi yoyote ngumu, bali apumzike kwa muda mrefu. Mwili wake bado unahitaji muda kurejea katika hali yake ya kawaida."
Na mara akazima asisikie chochote tena.
"Dada!" Sauti iliita. "Tatty! Tatty!" Fanty alimtikisa Tattiana huku akimtazama kana kwamba anahisi amefariki.
Alikuwa amefanikiwa kumfikisha binti huyo nyumbani kitandani muda si mrefu. Na ni kama bahati tu, muda mchache nyuma baada ya kuona dada yake hajarejea ndani na wakati muda ukiwa umeenda, akaona kuna haja ya kwenda kumtafuta huko kwa 'kina Roboth kabla wazazi hawajarejea na kumweka kikaangoni.
Njiani akamwona akiwa amezingirwa na watu waliokuwa wamepigwa butwaa kumwona binti huyo akiwa amejilaza chini. Akiwa ametaharuki kwa hofu, akasogea na kuangaza. Shukrani ziende kwa macho yake ambayo yalifanikiwa kukumbuka gauni alilotoka nalo dadaye.
Akamweka mgongoni na safari ya kwenda nyumbani ikafanyika kwa haraka, Fanty asipumzike kabisa barabarani. Akikimbia na kutembea upesi.
'Vipi kama nikaonekana na mama au baba? Vipi kama Tatty atakuwa amefariki? Itakuaje wakifahamu ameenda kumwona tena Roboth?Na wakija kugundua nilimruhusu kutoka?'
Maswali hayo yakamkosesha Fanty raha kabisa. Alipofanikiwa kufika nyumbani, akahisi kana kwamba amefika mbinguni. Hakuamini kukuta nyumba tupu! Akamlaza Fanty kitandani na sasa akihangaika kumwasha kabla wazazi hawajafika.
"Kwanini lakini Tatty unafanya hivi?" Akalalama. Alikuwa na hasira na huruma kwa pamoja. Akapata wazo la kwenda kuteka maji na kuyatumia kumwamshia dada yake, hakufanikiwa. Punde akasikia sauti ya farasi huko nje. Haraka akatoka ndani ya chumba na kwenda kuwalaki wazazi wake.
"Mgonjwa anaendeleaje?" Lilikuwa swali la kwanza baada ya salamu.
"Anaae - yupo vizuri! Vizuri tu." Fanty akafumuka kujibu akilazimisha tabasamu. "Amepumzika sasa chumbani kwake muda si mrefu sana."
"Sawa sawa!" Melkizedek akatikisa kichwa. "Anatakiwa apumzike sana kurejesha afya yake.
Wakaingia ndani na kujipatia mlo wa jioni pamoja kama familia, Tattiana akiwa ndiye pekee aliyekosekana kutimiza orodha.
"Nadhani inabidi umwite aje kula, hawezi akalala na tumbo tupu," mama akapendekeza. Fanty akatikisa kichwa akisema:
"Hapana! Ashakula muda mfupi kabla hajapumzika. Hataweza kula tena kwa sasa!"
"Una uhakika amekula vema?" Melkizedek akauliza.
"Ndio," Fanty akajibu. "Amekula chakula cha kutosha - sahani mbili!"
Wakamaliza kula, lakini kabla ya kwenda kulala, mama akaona ni vema endapo wamgemwona mtoto kwanza. Akalipendekeza hilo kwa mumewe baada ya kumdaka mkono wakiwa koridoni kupita kwenda kujipumzisha chumbani.
"Amepumzika, huoni tutamsumbua?" Melkizedek akauliza akiwa anarembua macho kwa mzigo wa usingizi.
"Hapana!" Mama akatikisa kichwa. "Tutaendaje kulala kwa amani na hata hatujamtia machoni?"
Wakafungua mlango taratibu na kuingia ndani ya chumba cha binti yao. Wakasogea karibu na kumwangalia kwa matumaini. Tattiana alikuwa amelala na gauni lake akionekana kama mtu aliyelevyeshwa na usingizi mzito.
Mama alimtazama kwa mazingatio, lakini baba baada ya kumwona tu binti, hata macho yake yakaanza kufumba fumba kwa usingizi. Hakuwa na cha kuhofia.
"Twende sasa," akamwambia mkewe.
"Tangulia, nakuja," mama akashauri. Naye Melkizedek hakubisha, akageuza na kwenda zake akitembea kwa kishindo.
Alipofunga mlango, Mama akaweka mgongo wa kiganja chake cha mkono kwenye paji la uso la Tattiana. Akamtazama na gauni lake vema, akaondoa shaka, kweli lilikuwa lina udongo na vumbi.
Kama hatoshi, Tattiana hakuna na mkufu aliompatia walipoenda kumchukua hospitalini.
Akatazama ndani ya chumba pengine alikuwa ameuvua na kuuhifadhi, napo hakuuona. Akapata shaka. Akaketi na kufikiri. Akatoka ndani ya chumba na kwenda moja kwa moja jikoni, akatazama chungu kikubwa cha chakula na mboga.
Akagundua kiasi cha chakula kilichopo hakihakisi idadi ya walaji. 'Sahani mbili' za Tattiana na chakula walichokula wao kisingebakiza lumbesa la chakula chunguni.
Akatazama na matunda. Hayakuguswa zaidi ya yale waliyokula wao mezani. Mama akapata uhakika kuwa Tattiana hajala, lakini hakutaka kusumbua, akaenda zake chumbani, akaoga na kujilaza kitandani.
"Melky," akamuita mumewe, kisha akasema: "Kuna kitu nahisi hakipo sawa."
Kimya.
"Melky," Akaita tena. Akanyanyuka na kumtazama mumewe, alikuwa amejilalia na mdomo akiwa ameachama. Hakuwa kwenye ulimwengu huu kabisa bali sayari ya njozi asifahamu hata lepe ya lile linaloendelea ulimwenguni mwa binadamu.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama akaishia kusonya na kugeukia upande wa pili kulala.
***
Usiku ukazidi kuwa mzito.
Ndani ya kasri ya mfalme wa Goshen kulikuwa kimya na patulivu. Walinzi walikuwa wamesimama kiukakamavu malangoni wakiwa wamebebelea mikuki mirefu yenye vishungi vyekundu.
Macho yao yalikuwa yanawaka kama taa, yakikodoa kama bundi. Walikuwa wameingia lindoni muda si mrefu sana kuwapokea wenzao waliokesha hapo mchana kutwa.
Kama haitoshi, wengine walikuwa wakirandaranda huko nje, kwa miguu na kwa farasi, lakini vyote katika hali ya ukimya, wakihakikisha usalama upo wa kutosha, hakuna kitu kitakachomnyima mfalme usingizi.
Ndani ya chumba cha kuvutia cha mfalme, mfalme alikuwa mpweke kitandani. Alikuwa amelala akiwa ameukumbatia mto wake mkubwa uliodariziwa kwa nyuzi za dhahabu. Kitanda kilikuwa kikubwa kuwa peke yake, vilevile na chumba pia.
Kwa mbali ungeweza kusikia sauti yake akikoroma. Alikuwa amepotelea usingizini kabisa. Kazi za wakti wa mchana zilimchosha mwili na akili.
Lakini leo hii, ilikuwa ni siku yake ya yeye kupata ujumbe. Akiwa amelowea usingizini, kwa mbali akasikia sauti ya kike ikimnong'oneza. Kwa mara ya kwanza hakusikia vema, ila sauti ile ikarudia sentensi moja mara tatu.
"Mfalme, kuna walozi ndani ya himaya yako ... mfalme, kuna walozi ndani ya himaya yako ... mfalme, kuna walozi ndani ya himaya yako."
Sauti hiyo ikakoma kama sekunde nne kisha ikasema tena:
"Wanakumywa damu na kuwaua watu ... wanakunywa damu na kuwaua watu ... wanakunywa damu na kuwaua watu."
Mfalme akasikia vema sana. Lakini sauti ile ikaacha kunong'oneza, ikafoka:
"Amka! Nenda Kawatafute!"
Mfalme akakurupuka toka usingizini. Akiwa ametoa macho akakodoa kutazama kushoto na kulia akihema. Kwa mbali akasikia vishindo vya miguu vikipotelea!
Basi akanyanyuka, akafungua mlango wake na kutupa macho. Hakuona kitu! Akatoka ndani ya chumba na kwenda kutazama. Huku na kule, hakubahatika kuona chochote alichoshuku. Akarudi chumbani na kuketi kitandani.
Akafikiria sana ila mwishowe akaamua kuachana na mawazo hayo na kulala. Alipoamka akaonana na waziri wake wa ulinzi, bwana Alphan, akampasha habari juu ya ndoto yake.
"La haula!" Alphan akashangaa. Akamshauri mfalme wake kulifanyia kazi hilo jambo na atakuja kumpatia habari karibuni.
"Ulitilie maanani," mfalme akasisitizia. Alphan akanyanyuka aende zake, lakini kabla hajakwenda mfalme akakumbuka na kumuuliza jambo, ni kuhusu yule mwanajeshi wake aliyempatia kazi ya kumfuatilia Tattiana.
"Sijamwona!" Alphan akatahamaki. Hii haikuwa kawaida yake, mfalme akang'aka. Ni nini kimemkumba? Akataka kujua, basi akamuagiza Aplhan akafuatilie hilo jambo kwanza kabla ya mengine.
Alphan akaendaze na kumwacha mfalme. Baada ya muda mfupi akarejea akiwa haehae. Alimkuta mfalme akiwa anakunywa divai kwenye meza yake tukufu.
"Ewe mfalme, kijakazi wako ameishiwa na nguvu. Ametokwa na madonda mwilini na sidhani kama ataliona jua la kesho!"
Mfalme akatahamaki. Haraka akaelekea kumsabahi kijakaziwe. Akamkuta akiwa amejikunyata, dhoofu lihali hajiwezi.
"Ni nini kimekukumba?" Akauliza akijawa na shauku kubwa kujua lakini kijakazi wake hakuwa na hali kujibu. Alikuwa anatetemeka, akipambana na baridi kali alilolisikia peke yake.
Alipojitahidi kufungua kinywa, akashindwa. Mdomo wake ulikuwa umepasuka konani. Na ajabu hakudumu muda mrefu, akafariki!
Mfalme hakuamini macho wala masikio yake. Akachanganyikiwa kwa mawazo. Akauliza watu wa karibu ni nini kilimkumba mtumishi wake huyo, wakamwambia hawajui. Ni alikuja tu akiwa anakohoa damu!
Wakataka kumzika upesi, lakini mfalme akazuia zoezi hilo na kusihi mwili huo upelekwe hospitali na ukaguliwe.
"Nataka kujua nini kimemuua!" Mfalme akasema. Mwili ukapelekwa hospitali na daktari akaomba muda apate kuuchunguza mwili huo na kung'amua nini chanzo.
Mfalme akarejea himayani mwake, akiwa anawaza sana kuhusu lile jambo la mtumishi wake, majira ya jioni kuelekea usiku, akapokea mgeni - Rhoda. Akamkarimu mezani wapate tia chochote kinywani.
"Ni muda umepita sasa hujaja kuniona. Kuna shida yoyote?" Mfalme akauliza. Rhoda akatabasamu na kutikisa kichwa.
"Hapana, mfalme wangu. Ni kazi tu zimenibana."
Mfalme akaguna na kisha akauliza ni kazi gani hiyo kwani amesikia na kuhakikisha kwamba biashara yake imefungwa kwa muda sasa.
Rhoda akatabasamu.
"Ni kweli, mfalme. Tumeifunga ... yani, nimeifunga."
Mfalme akashikwa na butwaa kwani alitegemea Rhoda angeeleza pia na sababu za yeye kufanya hivyo, ila akawa kimya mpaka pale mfalme alipomuuliza nini kimemsibu.
Rhoda hakuwa na majibu ya kueleweka. Mfalmw hakuelewa na kwa kutumia akili zake za kiutu uzima akajua kuna shida iliyofichwa nyuma ya pazia ila hakuhangaika nayo, akanyamaza.
"Kwahiyo nini mpango wako kwa sasa?" Mfalme akauliza akinywa divai. Rhoda akajiumauma, hakuna ambacho mfalme aliambulia. Akawaza sana yule Rhoda wa zamani si huyu wa sasa. Rhoda alikuwa ana hamu ya biashara na mkono wake haukulaza damu kwenye fursa.
Mfalme akajawa na hamu kujua ni nini hicho ambacho kimemleta Rhoda hapo hekaluni.
"Sina mengi sana, mfalme. Kubwa lililonileta hapa ni kutaka kufahamu, huoni sasa ni muda muafaka kwako kuwa kwenye mahusiano? Goshen inahitaji Malkia."
Mfalme akatabasamu. Akamwambia Rhoda kuwa swala hilo halihitaji haraka, analifanyia kazi taratibu.
Rhoda akatabasamu akimtazama kwa macho ya kimahaba. Alitaka kusema jambo, lakini akakatizwa na sauti kali ya Aplhan. Alikuwa anakuja akirusha miguu yake kwa mbali.
"Kuna jambo, mfalme! Kuna jambo!"
Aliposogea karibu akapaza sauti kusema ni kweli kuna walozi ndani ya himaya. Rhoda akamtazama Alphan kwa macho ya kizandiki.
"Una uhakika?" Mfalme akauliza.
"Ndio, mfalme. Nimepata uhakika haswa."
Wakati huo Mfalme ameteta na Alphan, Rhoda akautumia huo mwanya kumtilia mfalme unga mweusi ndani ya kikombe chake cha divai.
Mfalme alipokuja kumtazama, alimtaka awapishe kwani wana maongezi binafsi. Rhoda akanyanyuka na kutoa heshima zake kisha akaondoka akiwa ana mawazo.
Akawaza ni mlozi gani aliyekuwa anamuongelea Alphan. Akawaza kama atakuwa ni yeye na nini mfalme atafanya. Roho yake haikuwa na amani kabisa.
"Unadhani kuna mlozi yupi? Hamna mwingine zaidi yetu!" Alisema kikongwe mmoja punde tu walipofika nyumbani kila mtu akajimega toka kwenye mwili wa Rhoda.
Wakaketi kitandani wakiwa wamejawa mawazo. Tumaini lao likawa lipo kwa Mfalme tu kunywa kile kinywaji walichotia dawa yao.
"Endapo akinywa, tutatoka ndani ya mwili wa Rhoda na kuzama kwenye wake."
Huko kasrini Alphan akamwambia mfalme juu ya yale yote aliyoyasikia huko mitaani na namna habari za walozi zilivyotapakaa. Mfalme akapigwa na bumbuwazi.
"Kwahiyo Alphan, wataka kuniambia ile nyumba ya Rhoda ndiyo imekuwa jumba la walozi?" Mfalme akatahamaki.
"Ndio, mfalme!" Aplhan akasisitiza kwa kutikisa kichwa akiketi chini. Mfalme akanyamaza kimya. Akang'ata kidole chake akiwaza.
Akateka kinywaji chake cha divai akakimiminia kinywani kisha akamtaka Alphan amuitie wanajeshi watano atakaowapa maagizo ya kwenda kutekeleza.
Wanajeshi hao walipokuja, Mfalme akawapa zoezi la kumtazama Rhoda kila aendapo. Kazi yao ni kuamka asubuhi na kwenda kuketi mahali wakimtazama anachofanya asubuhi mpaka jioni.
"Nahitaji mrejesho kila jioni."
***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Tattiana yupo wapi?" Mama alipaza sauti baada ya kutoka chumbani kwa Tattiana pasipo kuona mtu.
"Sijui!" Akajibu Fanty akipandisha mabega. Mama akamsogelea na kumkunja shati akirudia swali lake. Fanty naye akarejelea kumwambia hajui.
Mama akiwa ameng'ata meno akamwambia Fanty kuwa anajua kinachoendelea, wala asijaribu kumficha. Anafahamu jana Tattiana hakuwa nyumbani, alitoka, na pia hakuwa amekula usiku kama alivyomdanganya.
Fanty akajawa na hofu. Alitamani kusema wapi alipo Tattiana ila hakuwa anajua abadani zaidi ya kuotea pengine atakuwapo kwa Roboth. Tattiana alitoroka, hakuthubutu hata kumwambia.
Mama asitake kuelewa, akafungasha akidhamiria kwenda huko kwa kina Roboth. Jambo lilishamfika kooni, sasa hakuna budi kulivaa.
Akapanda farasi na upesi akafika nyumbani kwa wakina Roboth, kabla hajafanya chochote akapokelewa na sauti ya kilio ya Tattiana. Upesi akashuka na kuzama ndani, akamkuta Tattiana akiwa amekaa pembeni ya mwili mfu wa Roboth.
Roboth alikuwa amefariki, hatamaniki kumtazama. Hata mama akapigwa na ganzi ya bumbuwazi na simanzi.
Tattiana akamuona mama yake, kwa hasira akiwa analia kwa sauti kuu, akapaza sauti kumtusi mama yake na kumuita muuaji asiye na lepe la huruma.
"Amekukosea nini kijana wa watu? Aliwakosea nini!" Akafoka
Mama akapigwa na tahamaki. Hakujua kitu ambacho Tattiana anasema. Hakuwa anamuelewa na hakuwa anajua kitu kinachoendelea pale.
Tattiana akiwa anajiamini kwamba anachokifanya ni sahihi, akamfokea mno mama yake, kama haitoshi akamfukuza hataki kumuona kabisa.
"Mimi si mwanao tena, sitaki kukusikia wala kukuona kabisa!" Akamalizia na kumwambia mama yake akamfikishie hizo habari na baba yake huko nyumbani.
Mama akiwa ameishiwa na nguvu, na anasikia baridi kana kwamba amemwagiwa maji ya mtoni, akarejea zake nyumbani. Hamu yote ilikuwa imemuisha!
Roho ilikuwa inampwita na kichwa chake hakikuacha kumtamka Roboth wa ajabu aliyemuona. Ni nini kile?
Mawazo yake yote hayo yakamkuta na mumewe aliyerejea na kumuuliza nini kimemjiri na mwana wao wa kike yupo wapi. Mama alipomueleza, baba hakuchukua muda, upesi akapanda farasi na kwenda kwa wakina Roboth.
Hakukuta mtu! Loh! Akashangaa akitafuta huku na huko. Akauliza jirani, akaambiwa wametoka kwenda kuzika. Basi haraka akaenda huko na kukuta watu wanne tu! Mama yake Roboth, Tattiana na wanaume wawili waliokuwa wamejifunika manailoni meusi.
Kabla hajafanya kitu akaona wanaume wale wakijifungua nailoni zile nyeusi mikononi mwao na kuanza kumdai fedha mama yake Roboth. Mama akasema hana kitu.
"Mama acha kututania? Tumezika huo mzoga wako alafu unatuambia huna kitu? - unajua ni kwenye hatari gani tumejiweka kufanya kazi hiyo?"
Vijana hao hawakumuelewa huyo mama wakataka hata kuchukua hatua mikononi. Kama si Melkizedek kuingilia hapo upesi basi jambo lingezuka.
"Nitalipa mimi!" Akasema Melkizedek, baba yake Tattiana. Wote wakageuza shingo zao kumtazama.
"Sitaki!" Mama akafoka. Akakataa katakata, hataki mwanaume huyo amlipie chochote kile. Lakini angewapa nini wanaume wale waliotoa jasho lao?
Melkizedek akatoa pesa yake, wanaume hao wakaenda zao wakilaani na wakinenea vibaya ule mwili waliouzika. Wakiusema kuwa unanuka na wala haueleweki.
"Unahitaji nini hapa?" Mama yake Roboth akauliza. Alikuwa anafanana macho na Tattiana. Yalikuwa mekundu yaliyovimba. Na sura zao zikiwa zimelowana huzuni tepe kwa kuondokewa na mpendwa wao.
Melkizedek akamwambia hajafuata lolote lile isipokuwa kumchukua mwanaye, lakini Tattiana akagoma kwenda akimweleza hamtambui kama baba yake.
"Mnataka nami mkaniue kama Roboth?"
"Nani amemuua Roboth?" Melkizedek akashangaa.
"Hujui?" Tattiana akang'aka. Akatoa maneno makali kisha akamtaka mama yake Roboth waende zao. Hakumtaka kumsikiza baba yake kabisa, na akamuonya kumfuata tena.
"Sasa tunafanyaje?" Melkizedek akamuuliza mkewe punde alipoketi kitini baada ya kurejea nyumbani.
Wote walikuwa wamechoshwa na vile walivyoviona, vichwani wakiteswa na maswali kadhaa - haswa nini kimemkumba Roboth? Kwanini Tattiana anaamini wao ndiyo wamemuua?
"Ama ulifanya jambo pasipo kunambia?" Melkizedek akamuuliza mkewe.
"La hasha! Sijui lolote," mama akajibu akikunja sura, kisha akauliza:
"Na ya mfalme je akiyajua haya?"
Wakakosa maneno ya kusema. Walikuwa zaidi ya dimbwini, dimbwi la mawazo.
***
Ndani ya Usiku mzito.
Baada ya siku nzima pevu, ya kupanga na kuhusia wapambanaji wake juu ya walozi wanaotafutwa ndani ya himaya ya Goshen, Alphan sasa akaupata usingizi aliokuwa anautafuta kwa kitambo.
Muda ulikuwa unaenda sasa, na analiona angetakiwa ameshawatia nguvuni walengwa wake lakini haikuwa vivyo. Mambo hayakuwa mepesi!
Lakini si haba, alikuwa amepiga hatua kusogelea malengo yake. Tayari kwa fununu alishajua nyumba ya Rhoda haikuwa tena nyumba ya binadamu wa kawaida.
Habari zimesambaa himayani kuhusu yanayotendeka hapo. Taa haziwashwi ingali kuna watu. Na hata Rhoda kutoonekana tena kama ilivyokuwa hapo awali. Achilia mbali, maneno ya walevi na wale vijakazi wa ndani.
Alphan kuhakikisha hakosi jambo, ameshapandikiza watu wake hapo kutazama na kufuatilia kila nyendo.
Lakini basi, wale walozi walikuwa tayari wameshaling'amua hilo. Walishajua kila ambacho Alphan anakifanya, na hata alichopanga kufanya.
Sasa wamepanga kumuangamiza, kisha wammalize na mfalme! Watajivika mwili wake kama walivyofanya kwa Rhoda, na sasa wakatawale Goshen milele!
Usiku ulivyozidi kutambaa, Alphan akajikuta hayupo peke yake ndani ya chumba.
Akashtuka na kuangaza akiuliza kama kuna yeyote ndani ya chumba asimtambue. Hakukuwa na majibu. Akiwa anahema, akawasha taa yake na kuitupa huku na kule, hakukuwa na jambo!
Basi akadhani ni wenge, akazima taa apate kulala. Loh! Taa kuzima akawaona watu wawili waliosimama kwenye kingo ya kitanda. Mwili ukamtetemeka, akataka kupiga kelele kali la hofu.
Lakini hakuweza abadani!
Kwani kabla hajafanya kitu, alihisi mwili umeishiwa nguvu, sauti haitoki!
Watu wale aliowaona, kwa raha zao, wakaanza kumjongea kumfuata. Wakamkamata koo na kumminyia kitandani. Wakamkaba mpaka pale walipohakikisha amelegea kuukosa uhai.
Kisha wakapotea kama upepo vuuuupp!
Mkono wa Alphan uliokuwa ukipambana kidhaifu ukadondokea kwenye mbao ya kitanda na kutoa sauti, haraka mwanajeshi mmoja huko nje akapaza sauti kuuliza kama kila kitu ni shwari humo ndani.
Alipoona kimya, haraka akaingia ndani na kuangaza. Akamwona mkuu wake akiwa hajielewi, ni mfu kasoro robo tu! Na wala hakukuwa na ishara yoyote kama kuna mtu aliingia ndani.
***
Asubuhi...
Mfalme Phares akiwa anapata kifungua kinywa, haraka anaingia kamanda wa vita na kusimama kando kando yake, akatoa heshima zake na kumwambia mfalme ya kwamba kuna msiba, wa yule kijakazi wake aliyekuwa yu hoi kwa kuumwa!
Mfalme akasikitika sana kwa kupoteza dhana yake muhimu.
Kabla hajasema neno lolote, yule kamanda akaongezea taarifa ya kwamba kila mtu anaogopa kuushika wala kuuzika mwili wa mtumishi huyo.
Mfalme upesi akaacha chakula chake na kukimbilia huko kwenye mazishi. Akakuta watu wachache waliokuwa wamejifunika pua zao na watu kadhaa kwa mbali wakiwa wanateta - hawa walikuwa wanataka kuuzika mwili huo.
Wote wakamsalimu mfalme na kumkaribisha eneoni .
"Mfalme, japo tumetangaza dau kubwa kuuzika mwili huu, hakuna anayethubutu," alisema mwanaume aliyekuwa anasimamia shughuli.
Akampeleka mfalme kuutazama mwili wa marehemu kisha akaagiza watu wauzike upesi kama mfalme alivyoagiza. Wanaume watatu waliovalia mifuko wakatekeleza agizo hilo.
Mfalme akakaa na kutazama mpaka shughuli hiyo ilipoisha, kichwani akiwa ana maswali lukuki ambayo hakuyapatia majibu.
Punde akakumbuka kuna kazi alimpatia daktari kuhusu marehemu, hivyo haraka akaagiza daktari huyo aje upesi kumdadavulia asichokifahamu. Ndani ya muda mfupi mlengwa akaja.
"Samahani, mkuu. Hivi ndiyo nilikuwa najiandaa kuja kukuona," akasema daktari kwa unyenyekevu. Mfalme asijali akamtaka ampe maelezo ni nini kilimuua mtumishi wake hadidi?
Basi daktari akatoa makaratasi yake na kuanza kuyapitia kabla hajasafisha koo lake na kusema:
"Mfalme wangu, sumu iliyotumika kumuulia mtumishi wako ni kali sijapata kuona tangu nianze kazi hii. Inafelisha viungo vya mwili kwa taratibu lakini kwa uhakika. Mwili hukakamaa na kwa wakati mmoja kumenyeka kana kwamba nyama iliyochemshwa kwa juma zima!"
Maneno ya tabibu huyu yakazidi kumpa maswali mfalme, ni nani amempatia mtumishi wake sumu hiyo? Na kwanini?
Alirudi kwenye ngome yake kisha akaitisha kikao cha dharura na matabibu wote wa kienyeji ndani ya himaya, akawauliza nani ana ujuzi wa kutengeneza sumu hiyo; ajabu hakuna aliyekuwa anaijua!
Hata nao walikuwa kwenye bumbuwazi.
"Pengine ungeuliza na wazee wa baraza!" Akashauri mtabibu mmoja.
"Kwanini nifanye hivyo?" Mfalme akauliza.
"Kwasababu wao hujua mengi, wana maarifa makubwa yaliyojenga misingi kwenye himaya hii!" Mtabibu akajibu.
***
Mchana wa jua la utosi...
Baada ya kijakazi wa Sultan kuingia ndani ya chumba, akainamisha kichwa chake na kumwambia Sultan wake:
"Ameamka!"
Haraka Sultan akiongozana na Sultana mdogo wakatoka ndani na kwenda chumba kingine walipomkuta Bibi akiwa amelala anatazama paa. Wakamjulia hali.
Bibi alikuwa amechoka, hata kuongea kwake ilikuwa tabu. Alimuuliza Sultan juu ya maendeleo ya mkewe mkubwa, wakamwambia bado naye yu usingizini.
"Inawezekana akawa amepona?" Sultan akauliza.
Bibi akatikisa kichwa chake;
"Hapana, bali ametulia. Nilifanya makosa sana, hata nisingekuwa hai mpaka sasa. Tatizo lake ni kubwa mno, siwezi kulimudu."
Sultan akafa moyo.
"Kwahiyo umeshindwa? Kabisa? Haitawezekana kumrejesha kwenye hali yake?"
Bibi akashusha kwanza pumzi ndefu. Akawaambia anahitaji muda na pia watu wa kuonana nao.
"Sitaweza peke yangu, inabidi nifunge safari kwenda ng'ambo ya Mashariki."
"Itachukua muda gani?" Sultan akauliza.
"Siku moja tu," Bibi akajibu, kisha akatulia akifikiria. Punde akamwambia Sultan.
"Lakini ni kwa sharti moja."
Sultan akamuuliza ni lipi hilo? Bibi akamtazama machoni na kumshika mkono wake wa kuume.
"Utimize agizo langu la mwisho nitakalokuomba."
Basi Sultan akaapa atatimiza lolote lile atakalotaka Bibi huyo endapo tu akimrejesha mkewe mkubwa kwenye hali yake ya awali.
Na basi akawaagiza vijakazi wake wajiandae kwa safari ya kumsindikiza Bibi kwenda ng'ambo ya Mashariki. Baada ya muda mfupi, maandalizi yakawa tayari. Bibi akapata chakula na kisha kuanza safari.
Akadumu juu ya mgongo wa farasi kwa takribani masaa mawili kabla hajawasili mbele ya ngome kubwa ya mishumaa. Akawazuia vijakazi aliokuja nao wakati yeye akizama ndani ya ngome hiyo.
Baada ya kama nusu saa, akatoka akiwa mpweke. Akakwea farasi na kutazama ngome hiyo kana kwamba kuna kitu anangoja kitokee.
"Hatwendi?" Akauliza kijakazi.
"Hapana!" Akajibu Bibi. "Tutangoja hapa mpaka itakapofika zamu yangu kuingia ndani."
Hakuna kijakazi aliyeelewa, ila wakanyamaza kwa maana haikuwa kazi yao. Wakaendelea kungoja.
Ikapita lisaa bado wakingoja tu.
Likapita na lisaa lingine la pili. Kijakazi akauliza mbona wameketi hapo kwa muda na hakuna kitu wala hawaoni mtu wanayemngoja?
Bibi hakujibu kitu, kama dakika mbili mbele, akashuka toka kwenye farasi akazama tena ndani ya ngome. Mara hii akatoka na mwanamke mwembamba mrefu, akakwea naye farasi wakaanza safari ya kurudi nyumbani.
Ajabu ni kwamba hata pale vijakazi walipotazama nyuma kuangalia ngome ile ya mishumaa, hawakuiona tena! Ilikuwa imefutika.
Waliwasili nyumbani, wakaandaa mazingira ya kazi, na punde zoezi likaanza. Mungu si Athumani, kila jambo likaenda kama lilivyopangwa. Wakafanikiwa kutoa roho ya mfu ndani ya sultana mkubwa.
"Samira!" Bibi akaita. Sultana mkubwa akafungua macho yake na kuitika. Sultan akafurahi sana! Hatimaye alikuwa ameshinda vita.
Akamuuliza Bibi ni nini angependa amfanyie kama zawadi ya kumtendea wema usio na kipimo kwake. Bibi akamvuta kando na kumwambia ana ombi moja tu, nalo ni la mjukuu wake kuwa mke mkubwa.
Hapo Sultan akahisi mwili wake umekuwa wa baridi. Alidhani pengine Bibi huyo angeomba theluthi moja ya utawala wake, na angekuwa radhi kabisa kumpatia. Ila hili swala kwake lilikuwa gumu.
Lakini atafanyaje na ingali alijifunga na kinywa chake kwa kiapo cha kutimiza chochote? Akainamisha kichwa chake chini.
"Atakuwa anakaa hapa?" Akauliza.
"Ndio," Bibi akajibu. "Na mjukuu wangu atahamia kasrini."
Sultan akasita kutoa maamuzi, Bibi akamsihi afanye upesi kwani anataka kumruhusu mgeni wake toka kwenye ngome ya mshumaa aendeze.
Baada ya dakika tano, Sultan akarejea na Bibi ndani ya chumba. Wakateta kidogo na mara akaomba faragha na mkewe mkubwa. Akatumia fursa hiyo kumueleza kwamba atamwacha hapo kwasababu za kiusalama na maendeleo yake kiafya.
Ila Bi mkubwa akawa mwerevu kutambua kuna jambo halipo sawa, akamuuliza:
"Unampeleka kasrini?"
Sultan akahisi ulimi mzito.
Japo alijiumauma, Bi mkubwa alimuelewa na hakutia neno. Macho yake yalikuwa mekundu lakini mdomo wake hakuthubutu kuufungua. Moyoni aliumia. Aliugeuzia uso wake ukutani akijikunyata kana kwamba anasikia baridi kali.
Mumewe akamsihi asinyong'onyee, amefanya hayo kama fadhila kwa kusaidiwa kwake, lakini mke hakusema jambo! Sauti pekee iliyotoka kwake ilikuwa ya kupandisha mafua tu.
Alijikunyata kwa kujihisi mpweke, mkosefu na asiye na msaada kwa mara ya kwanza tangu aolewe na Sultan. Alijiona ameshindwa na anashuhudia ngome yake ikianguka mbele ya macho yake.
Sultan akiongozana na mkewe mdogo wakafunga safari kuelekea kasrini. Walisindikizwa na Bibi ambaye aliishia njiani na kuwatakia kheri katika maisha yao. Akawasihi wasimsahau wakamkumbukia wakiwa shidani pekee.
Lakini pia akamkumbatia mjukuu wake na kumng'ata sikio.
"Fanya kama vile nilivyokuelekeza. Usifanye makosa!"
Sultana mdogo akaitikia kwa kutikisa kichwa kisha hao wakaenda zao Bibi akiwatazama mpaka walipoishilia, kisha akamgeuza farasiwe na kurudi nyimbani kumkuta Bi. Mkubwa.
Vita yao walikuwa wameishinda! Mioyo yao ilikuwa mepesi iliyojawa na furaha.
***
Saa mbili usiku...
Moto waliokuwa wameuwasha, sasa ulikuwa umekoza, basi juu yake wakaweka nyama walizozipata kwa kutega wanyama wadogo wadogo kama vile sungura ambao waliwatega majira ya jioni.
Kandokando ya moto huo walikuwa wameuzunguka Malkia, Fluffy, Seth, Zura na wale majitu mawili toka Azeth.
Moto ulikuwa ni mkubwa kiasi cha kuwapatia joto la kutosha dhidi ya baridi ya pepo iliyokuwa inapuliza. Kulikuwa kimya, makelele yalitoka kwa wadudu tu na moto uliokuwa umeshamiri.
Mkono wa Seth ulikuwa unageuza geuza nyama kuhakikisha haziungui. Walikuwa wanasikia njaa hata wakitamani wale nyama mbichi. Kwa siku nzima hawakutia lolote mdomoni zaidi ya kutembea tu!
Hata huu ukimya wao ulisababishwa na utupu wa matumbo yao.
Lakini zaidi ya hapo, Malkia hakuwa nao kimawazo. Kichwani alikuwa anafikiria mambo kadhaa, na si mengine bali kuhusu Goshen. Pengine mawazo yake haya yalimwokoa dhidi ya hisia za njaa.
Zura akamtazama na kumshtua kwa kumsukuma kidogo.
"Nini unawaza hivyo?" Akamuuliza akimtazama kama mama amtazamavyo mtoto wake mtundu aliyejifunza.
Malkia akatabasamu na kumwambia si mambo makubwa hata. Bado Zura akampekenyu akitaka amueleze ni nini hiko haswa. Malkia akashusha pumzi ndefu alafu akamwambia Zura kuwa anawaza kuhusu wale walozi kule Goshen!
Zura asiseme kitu, akaunyakua mkono wa kushoto wa Malkia kisha akautazama. Akatikisa kichwa chake. Mkono ulikuwa umejawa na makovu ya kuchanjwa chanjwa.
Akamuuliza;
"Ni mara ngapi utakuwa ukifanya hivi?"
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Malkia akitabasamu akiukwapua mkono wake na kuufichama.
"Mkono wako umekuwa ramani sasa kwa kuuchanja chanja upate kwenda Goshen. Utakuwa ukifanya hivyo mpaka lini?" Zura akamuuliza akimkazia macho.
Malkia akamjibu hawezi kutokufanya hivyo. Hawezi kupambana na haja yake ya kwenda Goshen. Ni lazima aende huko. Kama haitoshi, akabadili mada kwa kumwambia mambo kadhaa aliyoyagundua huko karibuni. Mambo haya yakamwacha Zura kinywa wazi.
"Unasema kweli?"
"Ndio, nyumba ya Rachel kwa sasa ndiyo imegeuka pango la walozi. Wanatumia mwili wa Rachel kufanya mambo yao pasipo kugundulikana. Na hivi ninavyokuambia, wamepanga kummaliza mfalme!"
"Sasa utafanyaje? Kummaliza mfalme maana yake kuweka himaya mikononi mwa walozi!?" Zura akatahamaki.
"Ndio!" Malkia akamjibu na kuongezea: "Natazamia namna ya kufanya. Usiku uliopita nimeshindwa kufanya jambo kwakuwa mfalme hakulala nimjie njozini. Alikesha usiku mzima kusoma na kuandika makaratasi!"
"Na usiku huu je?" Zura akauliza. Macho yake yalikuwa yanamaanisha alichokuwa anakiteta. Malkia akamwambia bado hakujua kama inawezekana akafanya vivyo. Basi Zura akamsihi sana afanye hivyo kwa ajili ya kuikoa Goshen.
"Inabidi uende, lakini uniahidi itakuwa mara yako ya mwisho kwenda huko!"
Kabla Malkia hajasema kitu, Seth akawashtua kuwaambia chakula ki tayari na kwasababu walikuwa na njaa, basi hawakuweza kungoja wakadaka upesi nyama na kuzikimbizia mdomoni.
Wakatafuna kwa dakika kadhaa kabla Zura hajamkumbushia Malkia juu ya walichokiongea. Malkia akamuahidi kulifanyia kazi punde tu watakapomaliza kula.
Na pasipo kupoteza muda, akafanya kama alivyoahidi. Akapotea eneoni akaenda kujiri ndani ya ngome ya mfalme. Kwa hatua za tahadhari akatembea kuelekea chumbani mwa mfalme huyo.
Kuzama ndani hakukuta mtu! Akajiuliza ni wapi atakapokuwa amekwenda. Akawaza pengine anakoga, lakini hakusikia maji. Au pengine yupo nje akiendelea na kazize?
Kuhakikisha akatoka na kwenda kutazama kule mfalme aketipo akiwa anafanya shughuli zake. Ajabu napo hakukuta mtu! Akapata hofu.
Sasa hakuwa na namna ya ziada zaidi ya kukagua jengo zima!
Kwa hofu, na tahadhari yakinifu akaanza kupekua jengo mahali kwa mahali. Miguu yake ilikuwa inabembeleza sakafu usisikie chochote hata akipita nyuma yako.
Akakaribia kumaliza jengo lote hili pasipo kumwona mfalme! Hapa sasa moyo wake ukaanza kwenda mbio kwani aliwaza mawazo mabaya, pengine wale walozi wamekwisha mkwapua!
Akiwa amesimama anawaza la kufanya, mara anajikuta ameshikwa mkono! Na mara amezibwa mdomo na kuamriwa anyamaze kimya. Anapata hofu nzito.
Akiwa ameminywa hivyo na mikono ya kiume, sauti ikamuuliza yeye ni nani, ametoka wapi na pale anafanya nini?
Kwakweli Malkia alibanwa na hofu. Alijua sasa mwisho wake umefika. Aliwaza mengi kichwani kwa wakati mmoja. Alifikiria namna ya kujichoropoa lakini hakuwa na mabavu ya kujichoropoa dhidi ya nguvu zilizomshikilia.
Mwanaume yule aliyemkaba akamvutia ndani ya chumba cha mfalme kisha akafunga mlango. Malkia akamtazama usoni na kugundua kumbe alikuwa ni Phares!
"Nimekuwa nikitegemea ujio wako hapa hivi karibuni!" Akasema mfalme akitabasamu, kisha akaketi na kumtazama Malkia kwa macho ya maulizo.
Akamwambia bila shaka yeye ni Sandarus, Malkia akastaajabu amejulikanaje? Lakini Mfalme akamwambia yote ni kwakuwa amekuwa akisikia habari zake kila uchwao. Hakuna mtu atakayekuja Goshen asimtambue.
"Lakini niliambiwa umekufa ... niliambiwa haupo himayani hapa ... na wengine wakanambia upo mbali huko kusikojulikana. Yote haya yanawezekanaje kwa wakati mmoja na wewe kuwa hapa?"
Malkia akamwambia Phares hataweza kuelewa kwani ni kisa kirefu mno. Kwa sasa amekuwa akiitazama na kuilinda Goshen kwani ndipo nyumbani kwake hata akienda pande ipi ya dunia.
Phares akataka kufahamu ni wapi alipo na anawezaje kufika ndani ya kasri ingali kuna walinzi kedekede huku na huko. Anawezaje kuingia ndani ilhali malango yamefungwa?
"Mfalme, siwezi kuzuiwa na kuta wala kufuli yoyote kutembelea sehemu yoyote ya Goshen," Malkia akajibu kwa kujiamini. Phares akashusha pumzi ndefu na kumtazama mwanamke huyo vema. Kichwani alikuwa na maswali mengi lakini alianza kufadhaika kwa kukosa majibu mujarabu toka kwa Malkia.
Akachakata na kuchuja maswali yake, akaamua kuuliza swali kuu lililobeba dhamira.
"Nini kimekuleta hapa kwangu?"
"Kukutahadharisha!"
"Juu ya nini?"
Kabla Malkia hajasema kitu, maginga ya moto yakaanza kufinyafinya kana kwamba yamepitia shurba ya pepo kali. Wakatahamaki!
Wakasikia ardhi ikitetemeka na vitu vikianguka. Wakajiuliza ni nini hiko, mara ghafla maginga ya moto yakazima kukawa kiza totoro!
Mfalme akapapasa papasa, akamuita Sandarus lakini hakupata majibu yoyote. Muda si mrefu akasikia mlango wake ukigongwa kwanguvu!
Mara mlango ukavunjwa wakaingia wanaume wawili wakiwa wamebebelea maginga ya moto. Wakapaza sauti kumuita mfalme. Walikuwa ni wanajeshi.
"Nipo hapa!" Phares akajitokeza. Lakini akaangaza huku na huko kumtafuta Malkia, hakumwona. Alitwaa ginga moja la moto na kuangaza kila mahali ndani ya chumba, hakumwona Malkia!
Akabakiwa na maswali kedekede kichwani.
Wakati huo upande wa pili wa shilingi!...
"Amepotea!" Akafoka bibi mlozi akipiga kofi la lawama. Alikuwa na mwenzake wakiwa wanatazama chupa mithili ya chemli mezani.
Ndani ya chupa hiyo kulikuwa kuna mwanga na taswira ya kile kilichokuwa kinaendelea ndani ya ngome ya mfalme! Walikuwa wanamwona mfalme akiwa na walinzi wake wakiangaza na kuangaza huku na kule.
Chumba kilikuwa kimejawa na giza. Na ni chupa ile ya chemli peke yake na macho ya walozi hawa ndiyo yalikuwa yaking'aza.
"Tulikuwa tumeshampata! Hii ilikuwa ni tende jangwani!" Akalalama mmoja wao akitikisa kichwa. Mwenzake akamshtumu:
"Ni wewe ndiye ulipuliza kwanguvu!"
Naye akamrudishia kwa kumuuliza:
"Na wewe ulivyotikisa kama kibuyu?"
Wakarushiana lawama kama watoto kila mmoja akimlaumu mwenzake kwa kupoteza nafasi ile adhimu ya kumtia mikononi Malkia. Sasa amekwishapotea na hata hawajui wapi alipoenda, wala alipotokea.
Walipotuliza shurba zao, wakaulizana juu ya nini cha kufanya. Kwa muda wakafikiria na kupendekeza kumalizana na mfalme kwa usiku huo. Yaani wahakikishe kila jambo wanamaliza.
"Huwezi jua Sandarus alikuwa amekuja kufanya nini? Anaweza kumuepusha kwa kumtahadharisha, kitumbua kikaingia mchanga!" Akasisitizia mmoja.
Kwa pamoja wakakubaliana kuwa usiku huo ulikuwa wa dhahabu kwao hivyo basi waufanye uwe kheri. Wakaandaa kila wanachotakiwa kuwa nacho. Wakaketi sasa kungojea tu muda muafaka uwasili wakati huo Wakitazama chupa yao.
Mfalme akalala. Wakamhesabia muda. Waliporidhika sasa atakuwa amelowea usingizini, wakajivika majoho mekundu yenye kofia za kujishkiza, alafu wakashikana mikono na kuteta maneno ya kigeni, mara wakapotea!
---
Ndani ya chumba kulikuwa ni kiza. Mfalme alikuwa mwenyewe juu ya kitanda kikubwa akiwa amejichanua kama ua bustanini.
Juu ya mwili wake alikuwa amejifunika shuka kubwa zito la manyoya manyoya. Si kwamba kulikuwa kuna baridi kali, la hasha! Hali ya hewa ilikuwa ya kawaida, na kwa watu wengine ambao wamezoea baridi, huu ulikuwa wasaa wao wa kuyasahau mashuka na kujitutumua ndani ya nguo nyepesi nyepesi.
Kulikuwa kuna ukimya wa kutosha kwa mtu kulala na kunogewa usingizini. Kwa mbali kama ungelisikiliza kwa umakini basi ungegundua mfalme alikuwa anakoroma.
Punde! Bibi walozi wanatokea konani. Wameifungua mikono yao wakiiangaza huku na kule kana kwamba wanapungia umati mikono. Walipoona shwari, wakatoa kitabu chao ndani ya joho alafu wakakiweka mezani na meza wakaisogezea karibu na kitanda alipokuwa amelala mfalme.
Upesi, mmoja akafungua ukurasa nambari mia tatu ishirina na nane, wakavuta pumzi na kuanza kusoma wote kwa pamoja, wakienda sawa kituo kwa kituo!
Wakamaliza ukurasa wa kwanza, wakahamia wa pili na kisha wa tatu mpaka wakamaliza hiyo sura! Ajabu hakukuwa na mabadiliko yoyote. Mwili wa mfalme ulikuwa umelala kama hapo awali!
Wakatazamana na kuulizana kama kuna kitu hakijaenda sawa. Kuhakikisha, wakarudia tena zoezi lao! Sasa wakilifanya kwa utaratibu na umakini mkubwa.
Lakini bado matokeo yakawa yaleyale! - hakuna kilichobadilika. Hapa sasa wakakubaliana kuna jambo halipo sawa!
"Tunafanyaje?" Mmoja akauliza.
"Turudie tena! Mara hii utaweka kiganja chako kwenye paji lake la uso."
Wakakubaliana. Wakarudia tena zoezi lao ambalo bado halikuleta matunda yoyote yale zaidi ya fadhaiko. Wakakata tamaa na kuondoka zao wakiwa wamejawa na maswali chungu nzima!
Imewezekanaje?http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mahali pekee ambapo zoezi hilo haliwezi kufanya kazi ni endapo tu mhanga anayefanyiwa akiwa mlozi ama si binadamu. Ina maana mfalme ni mlozi? Ina maana mfalme si binadamu?
Wakabaki kama mbweha aliyepokwa mnofu na mwewe!
Hawakujua cha kufanya. Walikuwa wameganda kwa mawazo kwa muda usiojulikana. Mambo yalikuwa mazito wasijue namna ya kuyamaliza. Wakajadili na kuamua kufanya utafiti kumhusu mfalme.
Inabidi wajue ametokea wapi, familia yake, na yeye ni nani haswa? Njia pekee ya kuyafahamu hayo yote ilikuwa kumtumia Rhoda kwa macho ya mapenzi.
Atamlainisha mfalme na mwisho wa siku wakapata wanachokitaka.
"Tutafanyaje sasa tukigundua naye ni mlozi?" Akauliza kikongwe mmoja. Mwenzake akamung'unya kwanza lips zake akifikiria. Akajibu:
"Hakutakuwa na namna, itabidi tuenende katika hiyo njia!"
"Unasema?!" Mwenzake akatahamaki. "Kwahiyo tutarudi tena Tanashe?"
"Ndio! Unajua fika dawa ipo kule. Ni lazima turudi kule kama kweli tukigundua mfalme ni mlozi kama sisi!"
Hapana, roho ya huyu mmoja ikasita kabisa. Alihofia mno kurudi Tanashe. Alijiona ni kama wanarejea kwenye mdomo wa simba waliyemkwepa. Lakini mwenziwe akamtoa hofu:
"Tuna mwili wa binadamu, nini kitashindikana? Tutatoka na kuingia kama tufanyavyo chumbani!"
Japo kishingo upande akaridhia. Pasipo kupoteza muda, wakaadhimia patakapokucha waende kuonana na mfalme wakiwa wamejivika mwili wa Rhoda, na wafanye kila walijualo kuupata ushindi!
***
Kama ulidhani usiku ulikuwa umekoma, basi umekosea. Bado kulikuwa na kiza kinene na kukiwa kimya. Kwa majira ya sasa, tungesema ni mishale ya saa tisa kasoro ya usiku.
Wote walikuwa wamejilaza wakiuzingira moto ambao umefifia ukilinganisha na hapo awali, lakini Zura alikuwa bado yu macho. Aligeuzia mwili wake juu akitazama anga na huku mawazo yake yakiwa yanamsumbukia Malkia.
Muda unazidi kwenda sasa, wala harudi. Nini kimemkumba huko aliko? Japo hakuwa anajua, alihisi kuna kitu hakipo sawa na nafsi yake. Alihisi Malkia si mzima.
Ni kheri akiwa fikirani, akahisi kitu kizito kimedondoka kando yake. Na mara sauti ya mtu akikohoa kwa pupa!
Basi haraka akageuka na kutazama, kifuani akijazwa na hofu. La haula! Akamwona Malkia akiwa amejilaza, amechoka! Anakohoa pasipo kupumzika.
Akamfuata upesi na kuuliza nini kimetokea. Lakini Malkia hakuweza kumjibu mpaka pale alipokoma kukohoa na kisha akavuta pumzi ya kutosha.
Akamweleza Zura namna gani mambo yalivyotokea kule Goshen alipotaka kumhabarisha Mfalme juu ya walozi. Punde akajikuta yupo kizani, pumzi imekuwa nzito, anaishiwa na nguvu!
Wazi akatambua lilikuwa shambulizi toka kwa wale vikongwe kwani hawakutaka amhabarishe mfalme juu ya njama zao. Kwa haraka, kwakuwa alipoteza dhana yake ya kujichanja, akajing'ata apate damu kumruhusu arudi pale.
Zura akashangazwa sana na hiyo habari. Akamwonea huruma Malkia lakini pia akajawa na hofu kuhusu Goshen.
"Ina maana walikuwa wanatarajia ujio wako?" Akauliza Zura.
"Pasi shaka, hata na mfalme pia alikuwa akinitarajia!" Malkia akajibu.
"Kwahiyo wote wanajua sasa kama upo hai! Na kama upo hapa!"
"Hapana! Hawafahamu nilipo, ila wamefahamu kuwa nipo."
Zura akatulia kwa sekunde kadhaa akimtazama Malkia. Akautazama mkono wake aliojing'ata, akakabwa na donge la huruma. Akatikisa kichwa chake na kumwambia Malkia.
"Inabidi uache sasa. Kwa hakika!"
Malkia akamtazama asiseme kitu. Zura akaendelea kumhasa kuwa yu hatarini kwa sasa. Adui zake wameshajua kuhusu uwepo wake na hivyo basi watajipanga kumdhibiti, ama kummaliza kabisa!
"Maadui? - maadui wangapi?" Malkia akauliza. Alikuwa akiamini maadui zake ni walozi tu. Ila Zura akamfungua macho kwa kumweleza hata mfalme ni adui yake.
"Uongozi ni mtamu. Uongozi hulevya. Kiti cha mfalme hupambwa na nadiri za dhahabu. Ni kiti aghali na chenye mamlaka. Ni kiti juu ya viti na nyumba zote. Sasa nani atataka kukiacha kwa wepesi?"
Zura akamshika mkono Malkia.
"Hata mfalme anahofia kiti chake. Wewe ni tishio kwake, tambua hilo. Habari zako anazo. Hafurahishwi na ushawishi wako ndani ya himaya ... atakumaliza hata kama aonyesha tabasamu kwa sasa. Mkono unaobebelea kisu waweza kufichwa nyuma ya mgongo!"
Baada ya Zura kusema hivyo, akamwacha Malkia ayameze maneno yake. Yeye akageukia upande wa kushoto apate kulala, lakini Malkia akamuuliza:
"Huyo ameenda wapi?"
Zura kutazama akagundua jitu moja halikuwapo. Akastaajabu kwani hakukumbuka ni muda gani mtu alitoka hapo ingali alikuwa macho! Akanyanyuka na kuketi kitako, akaangaza.
Hapa akawaza pengine mawazo aliyokuwa nayo yalimfanya asisikie kitu. Akamtazama Malkia na kumwambia hajui jitu hilo limeenda wapi!
Basi haraka wakamwamsha Seth na Fluffy, wakawaambia habari hizo. Wakaulizana na kuona kuna haja ya kufanya msako kumtafuta. Wakawasha maginga ya moto na kuanza msako!
Jitu lile lingine lililokuwa lipo usingizini, hakuwa anajua hata kinachoendelea. Alikuwa usingizini akikoroma kama mlevi.
Wakina Malkia wakatazama huku na huko, wakatembea kule na kule, hawakumwona mwenzao! Wakatembea kwa muda wa kama dakika ishirini, hawakufanikiwa!
Seth akatoa angalizo huenda wakapotelea huko kadiri wanavyozidi kwenda, hivyo warudi na wataendelea kesho jua likichomoza.
"Hapana!" Malkia akakataa. "Kama yupo matatizoni huoni kesho tutakuwa tumeshachelewa? Tumtafute hivi sasa. Sitaweza nikapata usingizi nikalala."
Basi wakaendelea na kutafuta. Baadae kidogo, wakasikia kishindo! Wakaangaza, hawakuona mtu. Lakini kabla hajawapiga hatua zozote kusonga mbele, wakasikia sauti ya mtu akitafuna.
Kwa ujasiri wakasonga kufuata sauti hiyo, njiani wakaona vipande vipande vya mwili wa mnyama, kama vile miguu na kichwa. Kusonga mbele, wakamkuta mtu wanayemtafuta.
Alikuwa ameketi akiwa anamla mnyama, mithili ya swala, akiwa mbichi atiririkaye damu!
Wakamwambia wamekuwa wakimtafuta, kwanini aliondoka pasipo kuaga. Akajitetea kuwa alienda kutafuta chakula kwani hakuridhika na tumbo lilikuwa linalalama njaa!
Basi wasipoteze muda wakamtaka afungashe warejee. Jitu lile likasomba nyama zake na wakafunga safari wakitembea upesi. Kufika mahali walipokuwapo, wakastaajabu kutomkuta yule waliyemuacha amelala!
"Mungu wangu!" Malkia akashika kichwa.
Walichoka lakini wasingeweza kulala. Ilibidi naye huyo wamtafute wapi alipoelekea. Walihofia usalama wake, wapi alipo na nini atakuwa anafanya.
Je naye atakuwa ameenda kutafuta chakula kama mwenzake, yaani hakushiba? Seth akakataa.
"Alikuwa ameshiba. Nilimpatia kipande cha nyama akasema hataweza hata kutafuna!"
Sasa basi kaenda wapi usiku wote huo? Wakaanza kusaka huku na kule. Wakiangaza chini alama za miguu. Wakaenda mbali sana. Hata wakaanza kutumia jina la jitu huyo kumsakia, wakimuita huku na kule. Wakisahau ya kwamba walikatazwa kuitana majina wakiwa safarini!
Na basi, punde kifupi wakaanza kusikia sauti za watu kwa mbali masikioni mwao. Sauti hizo zilikuwa ni mwangwi wa zile sauti walizokuwa wanaita.
Wakatazama huku na huko kutazama sauti hizo zinatoka wapi, hawakuona mtu yeyote. Hapo Malkia akakumbuka onyo lile walilopewa na mama yake Fluffy, upesi akawakataza wenziwe kuita majina. Lakini tayari alishachelewa!
Bado sauti zile zilizokuwa zinahakisi za kwao, zikaendelea kururuma na kuwaogopesha. Lakini zaidi ya hapo, ilikuwa kheri kwani hawakudhurika na lolote lile.
Shida ikawa kwa yule aliyekuwa anaitwa. Akiwa yupo mbali kabisa na ulimwengu wa wenzake, na pengine akiwa hajui kwanini na kivipi yupo huko, akawa anaendeshwa kama toroli bovu!
Macho yake yalikuwa yamepanda juu mithili ya mtu aliyelewa madawa. Miguu yake ilikuwa inatembea kwa kuburuza. Mdomo wake ulikuwa wazi, mikono yake ikiwa imelegea kana kwamba amepooza.
Masikioni mwake alikuwa anasikia sauti ya kike ikimwita jina. Na hakuwa na nafasi ya kukataa sauti hiyo. Mwili ulikuwa umekubali, akili haikuwapo!
Kwa takribani dakika kumi na, akawa anatembea na mwishowe akakaribia shimo la tewa! Shimo lenye mdomo mkubwa kama kinywa cha mamba. Shimo jeusi linalomeza watu. Shimo lisilo na kikomo!
Na kadiri alivyokuwa akisogelea shimo hilo, basi na ile sauti inayomuita ikazidi kulowana utamu. Kwa sauti ya kinubi ikawa inaita.
Jitu hili, ambalo lilifanywa kama mtoto sasa, likawa limebakiza hatua nne tu kudumbukia shimoni. Halikusikia chochote na masikio yake, bali sauti ya kumwita ... sauti ya kumvutia shimoni..
Lakini ghafla,
"Heeey!" Sauti ya kiume ikaita nyuma yake ".. heeey! ... simama! Simamaa!"
Wala hakusikia. Sasa akawa amebakiza hatua moja tu azame shimoni! Huku nyuma yake kukavuma vishindo vya miguu vikija upesi, na mara mtu akamrukia na kummwagia pembeni.
Alikuwa ni Seth! Lakini kumwokoa jitu hilo kukamtia yeye hatiani. Akaserereka na kuzamisha mwili wake ndani ya shimo, akibakiza mikono tu iking'ang'ania kingo ya shimo!
Kama si haraka wenzake kumuwahi, basi alikuwa anazama. Walifanikiwa kumdaka mikono na kumvuta kwanguvu. Lakini hawakufua dafu! Seth alikuwa anavutwa shimoni pia!
Mikono meupe iliyotokea kwenye kuta za shimo, ilikamata miguu yake na kumvutia ndani kwanguvu. Seth akajitahidi kuchoropoa miguu yake kwa nguvu lakini kazi ikawa kinyume na alivyofikiria. Hakuweza kuishinda nguvu mikono ile!
Basi ikawa vuta n'kuvute! Kila pande iking'ang'ania mwili wa Seth.
Ni bahati wakati zoezi hilo likiendelea, lile jitu lililookolewa na Seth likarejea fahamuni! Lilkahema mafundo makubwa makubwa kana kwamba limetoka kunusurika kuzama na maji.
Lilipotazama kando ndipo likawaona wenziwe waking'ang'ana, basi upesi likawaongezea nguvu kumvuta Seth, wakafanikiwa!.
Wote wakajilaza pembeni wakihema kwa shughuli pevu! Walifanikiwa kumkomboa Seth lakini alikuwa amejeruhiwa miguuni kwa kucha za mikono ya shimoni, hivyo hakuweza kusimama wala kutembea.
Wenziwe wakambeba na kurejea kule walipokuwapo mwanzoni. Wakakuta moto ushazima, wakauwasha na kuketi kumganga Seth. Yale majitu mawili yakitafuna majani waliyochuma kwenye miti kadhaa na kisha kumuwekea kwenye majeraha.
"Ulifikaje kule?" Malkia akamuuliza yule jitu waliyemkomboa. Jinale aliitwa Ghaut. Kwa msaada wa ukalimani toka kwa Seth, wakawa wanawasiliana.
"Anasema wakati amelala alisikia kishindo cha mtu akiwa anakimbia kumzunguka. Akakurupuka na kutazama, akajikuta yu mwenyewe! Na kwa mbali alipoangaza, akamwona mtu akiishia akikimbia," Seth alikalimani maneno ya jitu.
"Ulifanikiwa kumtambua mtu huyo na alipoelekea?" Malkia akauliza.
Jitu likatikisa kichwa, likajibu huku Seth akikalimani.
"Japo nilimkimbiza nikidhani anaweza kuwa ni wa miongoni mwetu, sikufanikiwa kumwona. Kila nilipokimbia, akafichwa na miti. Akamezwa na miti. Zaidi nikajikuta nikipotelea ndani ya msitu nisijue wapi nilitokea!"
Simulizi hiyo ikatetemesha mioyo yao. Mule msituni hawakuwa wenyewe. Na sasa kwa matendo walikuwa wamejifunza kuwa hawatakiwi kuachana hata mara moja!
"Kesho tutaumaliza msitu huu endapo tutatembea kwa zaidi ya masaa nane pasipo kupumzika. Na baada ya hapo, tutaingia kwenye jangwa la Medek-taum kabla ya kwenda kukutana na bahari," alisema Seth akitoa ramani ya mwenendo wao.
"Na je kuna cha kukitarajia huko?" Zura akauliza upesi. Wote wakamtazama Seth kwa jicho la shauku.
Seth akapandisha mabega na kusema:
"Pengine yapo ya kuyatarajia. Kwakuwa jina la jangwa hilo humaanisha kifo-mezani. Sidhani kama jina hili liliwekwa kwa bahati mbaya."
Moto ukaendelea kuwaka na kuwaka. Hakukuwa na mtu mwenye dalili ya kulala tena.
***
"Kila kitu kipo sawa?" Akauliza kikongwe. Mwenzake akatikisa kichwa pasipo kutia neno, lakini uso wake haukuwa wenye furaha.
Juu ya kitanda kulikuwa kuna furushi kubwa jeusi. Wao wenyewe walikuwa wamevalia mashela meusi mikononi wakifunikwa na glovu za nyavu.
"Hatuna namna. Lazima tufanye hivi," akaendeleea kusema kikongwe wa kwanza kufungua mdomo.
"Lazima turudi Tanashe. Twende kule tukachote dawa za kuja kumaliza kazi. Umeona mwenyewe mambo yalivyogoma.
Mwenzake akamtazama akiwa kimya kwa muda kidogo, alafu akamwambia:
"Hili si chaguo jema."
Baada ya hapo hakusema tena kitu. Wakazama ndani ya mwili wa Rhoda na safari ya kwenda Tanashe ikaanza.
Yalikuwa ni majira ya saa kumi ya usiku! Huko nje hakukuonekana na mtu yeyote akirandaranda bali hali ya ukimya mkubwa. Kwa mtu wa kawaida, angeliogopa. Angelitembea kwa kutazama nyuma kila saa.
Walozi hawa, pasipo tembe ya hofu, wakakata safari wakijongea kwenda mpakani mwa Goshen na Tanashe. Japo miili yao bado ilikuwa ndani ya Goshen, akili zao zilishafika Tanashe wakiwaza yatakayojiri huko.
Lakini wakiwa wamekaribia mpakani, wakagundua hawakuwa wenyewe safarini! Kuna watu walikuwa wanawasindikiza. Na watu hawa si wengine bali wanajeshi waliowekwa na yule Afisaa usalama, bwana Alphan baada ya shuku za hapa na pale!
Wanajeshi hawa walikuwa kazini wakitimiza maagizo ya kufuatilia kila jambo alifanyalo Rhoda.
"Tukimbilie Tanashe!" Kikongwe mmoja akasema ndani ya Rhoda. Lakini mwenzake akapinga hiyo hoja. Endapo wakiwaacha wanajeshi hawa hai, basi habari zao zitasambaa na hata watakaporudi Goshen mbivu na mbichi zitakuwa bayana.
"Kwahiyo inabidi tuwaue. Hatakiwi kubaki hai hata mmoja wao!"
Basi kufumba na kufumbua, vikongwe wakatoka ndani ya mwili wa Rhoda kimiujiza! Haraka wakatapakaa na kuwakamata wanaume watano waliokuwa wamebebelea silaha. Wakawaviringita na kuwanyofoa uhai mara moja, kisha wakaendelea na safari yao kuzama Tanashe.
Baadae jua lilipochomoza, watu wakazingira miili ile ya wanajeshi wakiwa wamestaajabu. Habari zikasambaa ndani ya himaya nzima, muda si mrefu wakafika wanajeshi wengine kuja kuchukua miili ya wenzao.
Kitendawili kikawa ni nani aliyewaua wanajeshi hao? Na kafanya hivyo kwa dhamira gani? Wakapembua mazingira ya tukio, wakagundua hakukuwa na mabaki yoyote kumwonyesha muuaji - si alama za miguu, wala chochote alichoacha.
Muda kidogo, Alphan, mkuu wa jeshi, akawasili eneoni kuja kuhakiki taarifa alizopata.
Alikuwa mchovu na uso wake ukiwa mweusi kwa mbali. Kiafya hakuwa sawa. Alikuwa anakohoa mara kwa mara. Macho yake yalijifinya na shingo yake ilikuwa na alama za mikwaruzo na mgandamizo.
Akatazama miili ya wanajeshi wake kisha akasonya na kutikisa kichwa. Akaamuru itolewe pale ikahifadhiwe kisha, akiwa ameongozana na wanajeshi wanne, akaelekea mpaka nyumbani kwa Rhoda.
Baada ya kugonga kwa muda pasipo majibu, wakachukua hatua ya kuvunja mlango. Wakasaka nyumba nzima, wasifanikiwe kumwona Rhoda popote pale.
Hapo Alphan akatengeneza makisio kichwani. Moja kwa moja akaenda kuonana na mfalme, wakapata chai pamoja mezani.
Akamweleza mfalme juu ya makisio yake.
"Rhoda ameenda Tanashe," akafungua mjadala kwa kauli hiyo. Mfalme akamkabidhi macho na masikio yake apate kusikia.
"Tanashe?"
"Ndio. Ameenda huko ... inaweza kua ajabu lakini ndio ukweli. Askari wangu niliowaweka kumtazama kila nyendo zake, wamekutwa mpakani mwa Tanashe wakiwa wamekufa. Wamefikaje huko? Wakiwa wanamfuatilia Rhoda, pasi na shaka. Na hivi tunavyoongea, Rhoda nyumbani kwake hayupo!"
Maneno hayo yakajenga jumba la ukweli ndani ya kichwa cha mfalme. Aliacha hata kunywa chai akawa anaskiza na kutafakari.
"Unadhani atakuwa ameenda kufanya nini huko?" Mfalme akauliza.
"Sijajua," Alphan akabinua mdomo. "Ila chochote atakachokuwa ameenda kukifanya huko, hakitakuwa na nia njema kwetu."
Basi mfalme akaagiza punde tu Rhoda atakapoonekana, atiwe nguvuni na aletwe kwake haraka iwezekanavyo. Alphan akapokea maagizo hayo kwa heshima zote.
"Mbali na hayo, nini shida Alphan? Haupo sawa, kuna jambo lolote?" Mfalme akauliza baada ya kumtazama na kumkagua Alphan vema. Sasa alianza kula na kunywa.
"Hamna shida, mkuu," Alphan akaficha. Macho yake yalikwepa kumtazama mfalme.
"Hapana, kuna shida," mfalme akasisitiza. "Unaonekana dhaifu. Kipi kinakutatiza?"
Alphan akalazimika kueleza kuwa alikabwa usiku wa kuamkia jana yake. Hakumwona mtu aliyefanyia hivyo na kama isingelikuwa askari wake kuwahi kuingia ndani basi angelikufa!
"Mikono yake ilikuwa migumu na mizito kama chuma. Haikujalisha ni kwa namna gani nilipambana, nilikuwa mdhaifu mno niliyeelemewa hata na mikono na miguu yangu!" Akaeleza Alphan.
"Na tangu hapo, sijapata kurejea kwenye hali yangu. Napata shida kuongea, kumeza na hata kugeuza shingo. Najihisi mchovu, na usiku kwangu umekuwa wa kipekee!"
Mfalme akamuuliza kama aliacha mlango wazi na pengine mtu aliyefanya tukio hilo aliacha alama yoyote. Alphan akakanusha yote hayo. Kitu ambacho kilitengeneza kitendawili miongoni.
"Lakini nina mashaka ya dhati na Rhoda," akamalizia Alphan. Mfalme akapaliwa.
***
Jua lilikuwa linaelekea kufutika kwenye uso wa dunia, lilikuwa jekundu zaidi na dhaifu. Njia za kila pande zilikuwa zimetawaliwa na wakulima na wafugaji wakirejea kwenye makazi yao.
Lakini miongoni mwa watu hao, alikuwapo Fanty. Alikuwa anakazana kutembea akihema kama mbwa. Alionekana ametembea kwa muda mrefu na hata anapoenda bado ni parefu. Alirusha mikono na miguu yake kana kwamba yupo kwenye gwaride.
Baada ya kitambo kidogo, alikuwa amewasili mbele ya nyumba ya wakina Roboth. Akapaza sauti kubisha hodi. Punde akatoka mama na kumjulia hali.
"Samahani, naweza nikaonana na dada yangu?" Fanty akaomba. Mama akamwambia Tattiana ametoka kwenda kuteka maji, hivyo amngojee kwa muda kidogo.
Bahati kabla hawajakatisha maongezi hayo, Tattiana akaonekana akiwa anakuja, ndoo ya maji aliiweka kichwani. Basi haraka, Fanty akamuwahi dada yake na kumtua ndoo, kisha wakapata muda wa kuteta wakiwa wenyewe.
"Maisha gani haya umechagua, Tatty? Ona ulivyovaa? Unafanya kazi kama punda?"
Tattiana akaghafirika. Akamtaka kaka yake aondoke kama hicho ndicho kimemleta. Fanty akaomba msamaha na kumweleza dhamira ya ujio wake pale.
"Nimekuja kukuomba urudi nyumbani. Tunakukumbuka sana."
Tattiana akatikisa kichwa akimtazama Fanty ndani ya macho.
"Siwezi, Fanty! Siwezi kwenda kukaa chini ya paa moja na wauaji. Siwezi kabisa..."
"Hapana!" Fanty akamkatisha. "Waliomuua Roboth si baba wala mama. Hawahusiki!"
"Nini unaongea, Fanty?" Tattiana akamkaripia. "Ni wakina nani walikuwa wanamchukia Roboth mbali na mama na baba?"
"Siwezi jua. Ila nakuhakikishia kabisa, si wao waliohusika. Nami nilikuwa kama wewe, nikiamini kwa dhati mikono yao ndiyo imemmaliza Roboth mpaka usiku wa jana niliposikia wakigombana chumbani."
"Wakigombana?"
"Ndio. Jana kulikuwa kuna ugomvi mkubwa sana. Baba alikuwa anamshutumu mama kwamba ni yeye ndiye atakuwa anahusika na mauaji ya Roboth. Yeye alikuwa anataka wamalize haya mambo kidiplomasia kinyume na mama."
"Kwahiyo mama ndiyo kamuua Roboth?"
"Sidhani," Fanty akajibu. "Baba alipoondoka, mama alilia sana. Mpaka muda ninaokuja hapa, mama hajapata kula tangu jana. Amekuwa akilaani na akilaumu. Kama angelikuwa amelitenda hilo, asingelikuwa kwenye hiyo hali."
Kukawa kimya. Tattiana akazama kwa kina kwenye dimbwi la mafikirio.
***
Baadae kwenye majira ya usiku wa saa tatu, endapo tungetumia majira ya sasa, Tattiana akashuka mbele ya geti la hekalu ya mfalme.
Alikuwa amevalia gauni jeusi alilopewa na mama yake Roboth. Halikuwa limemkaa vema, ila angalau lilimsitiri na kupunguza maswali toka kwa walinzi.
"Mwambie mfalme, Tattiana amekuja kumwona," akasema kwa kujiamini kisha akasimama kungoja. Baada ya muda mfupi, akaruhusiwa kuingia ndani akisindikizwa na mwanajeshi mmoja.
Akaelekezwa pa kukaa.
Akiwa amekaa hapo, akatoa kisu nyuma ya mgongo wake. Akakiweka kwenye mkono wake wa kuume na kisha akaufichama chini ya meza.
Punde mfalme akaja na kumjulia hali akitabasamu.
"Hello, mrembo. Umenikumbuka?"
Tattiana hakujibu, bali akamtazama mfalme na macho makali, mekundu. Mfalme akagita na upesi akamuuliza ni nini kinamsibu kuwa katika hali ile?
Tattiana hakujibu. Hakuwa amekuja hapo kuongea bali kutenda. Alikuja hapo kutimiza mauaji na si kingine! - kumuua mfalme wa Goshen.
Hakujali wala kujisumbua kabisa juu ya nini kitatukia baada ya kufanya hilo. Alichojali yeye ni kutimiza adhma tu. Hata kama akinyongwa, basi nafsi yake itakuwa nyepesi. Atakuwa ametua mzigo. Atakuwa amelipiza kisasi kwa ajili ya Roboth!
"Tafadhali, Tattiana. Usifanye hivyo ... tafadhali!" Sauti ya mama yake Roboth ilimlilia masikioni. Ni muda kidogo tu hapo nyuma, mama huyo alimkabidhi gauni lake binti huyo pasipo kudhani kama anaenda kutekeleza mauaji.
Alimkabidhi akidhani anaenda kusalimu, ama kuonana na marafiki. Lakini mawazo yake hayo yakakengeuka punde alipomuona Tattiana akisoma kisu jikoni.
Kwa uoga, akiwa amekumbatia mlango, akamuuliza:
"Unapeleka wapi kisu hicho?"
Mikono yake ilikuwa inatetemeka. Alihisi miguu yake haina mifupa kwa kukosa nguvu.
Tattiana hakusema maneno mengi zaidi ya haya:
"Naenda kuilaza salama nafsi ya mpenzi wangu."
Mama Roboth akalia kwa kumzuia na kumwomba. Lakini wingu jeusi la chuki lilikuwa limeshamvaa Tattiana. Alihisi jabali lipo shingoni mwake, limemziba koo, linamsugua. Atalitua endapo tu atatimiza haja yake.
Hivyo akaendaze.
"Tattiana ... Tatiana!" mfalme aliita akiketi. "Kuna shida gani mama? Niambie nini kinakutatiza?"
Sasa Tattiana alikuwa anavuja machozi, anasaga meno. Ile fursa aliyokuwa anaingojea ilikuwa imewasili, mfalme yupo karibu naye tayari kwa ajili ya kummaliza.
Moyo wake ukaanza kwenda mbio - gidim! - gidim! - gidim! - gidim!
Hakuona tena ukarimu kwenye uso wa mfalme wala utu wake. Haraka akanyanyuka, upesi akautupa mkono wake wa kuume uliobebelea kisu kwenda kifuani kwa mfalme!
Tap! Mfalme akaunyaka mkono huo, lakini tayari ncha ya kisu ilikuwa imezama kidogo kutia kovu mbavuni. Mfalme akalalama kwa maumivu. Upesi wanajeshi wakawasili na kumkamata Tattiana.
"Nitakuua tu! ... nitakuua kwa mkono wangu mwenyewe! ... nitakuua muuaji mkubwa wewe!" Tattiana akawa anaropoka huku akitolewa kupelekwa anapostahili. Alikuwa anaongea kwa pupa, kwa hasira. Hakutathmini ayanenayo.
Anadhani atapata wapi tena nafasi ya kummaliza mfalme? Pengine angeanza kulilia uhai wake.
Upesi mfalme akagangwa jeraha lake. Akatiliwa dawa na kupachikwa 'kaplasta' hapo jerahani. Lakini ajabu ni kwamba, mfalme hakutokwa na damu.
Kile kisu alichokitumia Tattiana, bado kilikuwa cheupe peh, hata hakikunuka damu nchani. Mfalme akiwa amejilaza kitandani kifua wazi, akakitazama kisu hicho akiwa anamfikiria Tattiana. Kuanzia namna alivyomtia machoni, akamwona akiwa na macho machovu, mekundu, yaliyovimba. Nguo iliyomzidi na mdomo usiotaka kuongea.
Akatambua mambo matatu: mosi, Tattiana alikuwa amelia mno hapa karibuni kiasi cha kuvimba macho. Pili, ana hasira, gubu linalomtafuna kifuani kiasi cha kutaka kuua. Tatu, hayupo kwenye mazingira mazuri, ama pengine amejitenga na mazingira yake. Kuvaa nguo kama ile akiwa anakuja kumtembelea 'mfalme' kama mchumba, haikuwa kitu cha kawaida.
Kwa muda wa kama dakika ishirini, macho yake yalikuwa kwenye kisu lakini fikra zake zikiwa mbali.
Akashusha pumzi ndefu kisha akaweka kisu pembeni. Punde akaingia mwanajeshi wake, akapiga magoti kusujudu akiomba mfalme ambakizie uhai wake na hatorudia tena kufanya uzembe.
"Hatukumkagua kwa kutokuwa na mashaka naye. Hatukutegemea kama anaweza fanya jambo kama hilo kutokana na mahusiano baina yenu," akalia.
"Mahusiano gani?" Mfalme akamuuliza. Lakini kabla mwanajeshi huyo hajajibu, mfalme akamtaka asimame na kusahau yaliyopita.
"Nenda kamwambie fanisi wa jela na mateso, asimguse binti huyo. Nitaja kuongea naye!" Akatoa agizo. Mwanajeshi yule akalipokea na kwenda zake. Upesi!
***http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nimefanya kosa gani? ... huoni ungekuwa umedhulumu nafsi yangu kwa kunitoa uhai pasipo kujua kisa?" Akasema mfalme baada ya kunywa mafundo mawili ya mwinyo. Macho yake yalikuwa yanamtazama Tattiana kwa uangalifu mno, na yakimsoma kwa ustadi.
Sasa Tattiana alikuwa ameshaveshwa nguo maridadi. Akiwa anaonekana kupata maji mwilini, aling'aa na nywele zake zikiwa na mabaki ya matone ya maji.
Lakini bado hakutaka kuongea jambo. Bado moyo wake ulikuwa mgumu. Alimtazama mfalme kwa macho ya kizandiki na wala hakuwa na hamu ya kutia mdomoni kile ambacho kimewekwa mezani.
Mfalme, asiwe na papara wala kumezwa na hasira, akaongea naye japo alinena mwenyewe kwa muda mrefu kwani Tattiana hakutaka kumsemesha. Mfalme alitaka haswa kujua nini kinamsimbu binti huyo, hakutaka kuhukumu kipofu. Aliamini kuna jambo lipo nyuma ya mkono wake.
Baada ya kuvuta subira kwa muda, Tattiana akaanza kumwaga machozi. Kupaliwa na mafua ya kilio na kuwa mdhaifu. Akaanza kumshtumu mfalme kwa kumuua kipenzi chake.
"Kwanini umekuwa na roho mbaya kiasi hiki?" Akalia. "Mbona nilikubali kuwa nawe?"
Mfalme akastaajabu. Akakanusha kwa nguvu zote kuwa ahusiki hata kidogo na mauaji hayo. Hana mkono wake kwenye hilo, hata ukucha.
Na kwa kuweka bayana zaidi, akamwambia Tattiana kuwa alimweka mtu wake awe anamtazama na kumfuatilia, lakini mwishowe akafariki kwa sumu. Na mpaka sasa hakujua sumu hiyo alipewa na nani na kwanini?
Kwa hisia kali, akamwelezea Tattiana ni namna gani mtumishi wake huyo alivyoteseka kabla ya kifo chake, na hata maiti yake kutengwa kiasi cha kutumia nguvu za mamlaka yake kulazimisha azikwe.
Habari hizo zikamkumbusha Tattiana juu ya Roboth. Aliona maelezo yote ya mtumishi huyo ndiyo yale yaliyotukia kwa Roboth. Akatahamaki.
Lakini inawezekanaje?
Baada ya kumwambia hizo habari mfalme, basi kesho yake mfalme akadamka na kwenda kwa wakina Roboth. Akaamuru mwili wa Roboth ufukuliwe na kufanyiwa uchunguzi.
Hakwenda mbali, uchunguzi ukafanyika na akapata matokeo. Roboth alikuwa amelishwa sumu ile ile iliyommaliza mtumishi wake!
Akashusha pumzi ndefu.
Alikuwa amechanganyikiwa akiwaza. Ina maana muuaji wa yule mtumishi wake ndiye muuaji wa Roboth? Ana haja gani ya kufanya hivyo?
Akawateua wanajeshi wake wanne wakafuatilie hilo jambo. Wapeleleze kumjua muuaji na wamlete mbele yake haraka iwezekanavyo.
"Ndani ya majuma matatu natarajia mtakuwa na majibu ya kueleweka."
Akawapa pia na jukumu la kumfuatilia nyendo za Tattiana kwani kwa sasa hakuna mtu wa kufanya hivyo.
"Mtanieleza kila kitu kinachoendelea. Kwa sasa hayupo sawa. Anaweza akafanya tukio lolote baya kujidhuru, hivyo jicho la karibu linahitajika."
Baada ya kupewa maelezo hayo, basi wanaume hao wakaenda kutekeleza maagizo waliyopewa. Na kwa wakati huo, Tattiana akafunga safari toka nyumbani kwa wakina Roboth mpaka nyumbani kwao.
Alikuwa bado amevalia gauni lake jeusi. Hakuwa na furaha usoni na ndani. Farasi wake alikuwa anatembea taratibu, mwendo wa ndani ya muda.
Macho yake yalikuwa mekundu na yenye maji kwa mbali. Pua yake ilikuwa nyekundu, ila uso wake ukiwa mweusi zaidi.
Familia yake ikamkarimu. Wakamwambia walimkumbuka sana kwa muda wote huo ambao hakuwapo. Wanampenda na wamefurahi sana kurudi kwake.
"Mama yako alikuwa halali. Chakula kilikuwa hakipiti kooni wala kutulia tumboni. Tulikuwa tukiishi kwa hofu sana," alisema Melkizedek.
Wakala kama familia kufurahia umoja wao. Wakiwa wanakula, Tattiana akawaeleza kuwa alienda kumtembelea mfalme kuhusu Roboth. Wazazi wake wakashtuka.
Wakahofia pengine mtoto ameshaharibu mambo huko. Macho na masikio yao yote yakatekwa na kinywa cha Tattiana. Lakini wakaja kufahamu habari ilikuwa tofauti, na hata mfalme hakuhusika na mauaji hayo ya Roboth. Mbali na hapo, hata mtumishi wake aliuawa kwa namna ya kufanana na Roboth.
"Hili swala sasa limekuwa ni kitendawili kikubwa!" akastaajabu Melkizedek. "Ni nani sasa awe amehusika na mauaji hayo ya kutisha? Na haja yake ni nini?"
Hakukuwa na mtu mwenye majibu. Na kadiri swala hili lilivyokuwa linaulizwa, ndivyo lilivyofanya jambo hili lionekane kubwa kupita kiasi.
Wakamaliza kula, na kabla ya kutawanyika, wakasikia hodi toka mlangoni. Walikuwa ni Oragon na Ottoman wakiwa wamefika hapo na farasi wawili wanaovuta mkokoteni.
Melkizedek akanyanyuka na kwenda nje akiiacha familia yake mezani.
"Ni wakina nani hao?" Tattiana akauliza akijaribu kuangaza dirishani.
"Huwajui? - ni watoto wa yule mzee!" Fanty akamjibu dadaye. Tattiana asiulize tena, akawa ameshajua 'yule mzee' ni nani anayeongelewa hapo, mzee wa baraza.
"Kuna masanduku huwa wanayaleta hapa nyumbani kila baada ya siku tatu," Fanty akaendelea kuongezea taarifa. "Majira yao ni ya usiku kama hivi ... sijui ni nini wanaleta la --"
"Fanty!" Mama akaita kumkatiza. "Ng'ata ulimi wako!" Akamuagiza akimtazama kwa macho dhalili.
Tattiana akakabwa na dukuduku, lakini akaliminyia kifuani. Akatambua kuna jambo limefinywa na hatakiwi kulijua. Akapanga kuutega muda na Fanty apate kumweleza anayoyafahamu.
Akatazama tena nje, akaona baba yake akiendelea kuongea na Oragon na Ottoman. Walikuwa wamesimama kwa umbali kiasi kwamba huwezi kuwasikia wanaongelea nini.
Ila akatambua baba yake alikuwa anasisitizia jambo kwa vijana wale. Huwa akifanya hivyo pindi akiwa na hasira au amekwazwa na jambo. Akatamani kulijua jambo gani hilo, basi akajikuta anatazama sana dirishani.
"Tattiana," Mama akamuita. Akamwagiza amletee maji ya kunywa. Tattiana akanyanyuka na kwenda jikoni.
"Hivi ndivyo unawaambia watu huko nje? Kama unavyomwambia Tattiana?" Mama akamuuliza Fanty.
"Hapana -ma-"
"Na ufunge bakuli lako vivyo hivyo!" Mama akatoa macho. "Sawa?"
Fanty akamtazama mamaye kana kwamba mtoto aliyedokoa nyama na kuificha shavuni. Macho yake yakatazama chini, kabla hajajibu, Tattiana akawa amefika na maji yake mkononi.
Akaweka mezani. Na kabla hajaketi, akatazama nje. Hakumuona baba yake wala wale watu aliokuwa anaongea nao.
Punde, alipoketi akamwona baba yake akiingia ndani. Alikuwa amekunja ndita. Hakuongea na mtu, akiwa anarusha miguu yake kwanguvu, akanyookea chumbani.
Hakuna mtu aliyesema kitu. Ni kama vile walikuwa wanategeana nani aanze. Walitazama kwa wizi. Punde mama akaamka.
"Tattiana, ukapumzike sasa. Tutaongea zaidi kesho," Mama akaaga kwa namna hiyo.
Kisha akamtazama Fanty.
Kisha akaenda zake.
Isichukue muda, Fanty akanyanyuka akitaka kwenda. Tattiana akamwita na kumtaka akae watete kidogo.
"Mbona haraka hivyo? Una usingizi?" Akauliza Tattiana akiwa anatabasamu kwa mbali. Macho yake mekundu yalikuwa yamejawa na bashishi la ufahamu. Fanty akiwa anajua nini dada yake anataka, akamtazama kwa kumsusa na kuigiza kwamba amechoka.
"Naomba nikalale tafadhali," alisema akaenda zake. Tattiana hakuamini macho yake, akamshuhudia kaka yake akipotelea.
Akashangaa familia ile imekumbwa na nini? Akatazama nje, hakukuwa na mtu mbali na walinzi kule getini. Akaangaza angaza kama ataona jambo, hakufanikiwa.
Akanyanyuka zake na kwenda chumbani.
Lakini kuna jambo hapa. Alikiri. Ila akaona ule haukuwa muda wake sahihi wa kujihangaisha na chochote. Ametoka kwenye mengi na makubwa. Anahitaji kupumzika sasa. Aliburuza miguu yake kwendaze.
Usiku ukazidi kukua.
***
"Mzigo umefika?" Baba akauliza punde tu alipowatia wanae machoni.
"Ndio," akajibu Ottoman. "Umefika."
Wakawafungia farasi wao na kisha kuketi na baba yao sebuleni. Wakamwambia kuna ujumbe toka kwa Melkizedek.
"Amesema huu mzigo tuliompelekea utakuwa ndio wa mwisho kwake. Hatapeleka tena mwingine!" Alisema Ottoman. Mzee akakunja sura.
Akauliza
"Kwasababu gani?"
Ottoman akamtazama Oragon, Oragon akashika zamu kumwambia baba yake.
"Amesema kwa sasa ulinzi utakuwa mkali sana, ni hatari!'
"Lini uliwahi kuwa salama?" Akastaajabu mzee. "Siku zote ulinzi umekuwa hivi, amekuwa mgeni tangu lini?" Akabamiza meza.
"Amesema ni baada ya kifo cha mmoja wa wanajeshi wake! Yule mwanajeshi uliyetuagiza tumuue."
Mzee akasita kutia neno. Akakunja ngumi na kutazama kando. Alikuwa anawazua kichwani. Macho yake yalikuwa yamefura kwa hasira.
"Hapana," akatikisa kichwa. "Hapana hapana! Pengine ana sababu nyingine ila si hii!" Mzee akakataa.
"Mfalme amejua mtumishi wake ameuawa kwa sumu. Hivyo familia ya Melkizedek wanaweza pia wakawa wamewekwa kwenye jicho la karibu kiuchunguzi, kwani pia amesikia na kuhakikisha kifo cha Roboth - yule mwanaume aliyekuwa na mahusiano na binti yake," Oragon akamdadavulia baba yake.
Mzee asiseme kitu, akashusha pumzi ndefu. Akawataka wanawe wakapumzike. Wote wakaondoka na kumwacha mwenyewe.
Usiku kwake ukawa mgumu.
Akafikiria sana, mwishowe akaenda zake kujilaza kitandani. Huko akaendelea kuwaza na kuwazua mpaka pale usingizi ulimpokwapua.
Hata hivyo usingizini akawa anakurupuka na majinamizi.
**
Baada ya kusema maneno matatu, mlango ukafunguka.
Giza lilikuwa limenoga haswa, na jengo zima lilikuwa jeusi ti!
Vikongwe wakazama ndani na kuangaza angaza kukagua mali yao. Bado walikuwa ndani ya mwili wa Rhoda. Mkononi walikuwa wamebebelea kifurushi kidogo cha kitambaa cheusi.
"Hatimaye tupo nyumbani!" Wakasema Rhoda akitabasamu.
Hawakudumu ndani ya mwili huo, wakauvua na kuuacha kitini ili wapate wasaa wa kutengeneza na kufanya kilichowaleta Tanashe.
Ndani ya kifurushi walikuwa wamejaza dawa walizozipitia na kuzichuma maeneo mbalimbali ndani ya Tanashe. Kwasababu ya kazi hiyo, hawakupata wasaa wa kutia mguu nyumbani kwao tangu wazame ndani ya himaya hiyo masaa mengi tu yaliyopita.
"Ila nimechoka haswa," akasema kikongwe mmoja. Acha tuwatofautishe kwa idadi ya macho yao. Huyu aliyesema hii kauli alikuwa na jicho moja, mwenzake akiwa na mawili kamili, ambapo moja alikuwa amelitohoa toka kwa yule mwenzao waliyemuua.
"Umeanza uvivu wako!" Akasema huyu mwenye macho mawili. Wakati huo alikuwa amebebelea chungu kikubwa akikipeleka uani.
"Siku nzima tumekuwa tukiinamisha migongo huko. Hujachoka?" Akauliza kikongwe wa jicho moja. Mwenzake hakumjibu kwa haraka, alikuwa anakagua kile chungu alichokileta akiwa amezamisha kichwa ndani.
Alipokitoa akamuuliza mwenziwe:
"Umechoshwa na nini?" Pasipo kumtazama. Alikuwa anaendelea na shughuli zake za maandalizi.
Mwenziwe akalalama kuchoka, mwili mzima unamuuma, hawezi kumpa mkono wa msaada kwa muda huo. Basi yule kikongwe mwenye macho mawili akabakia akipambana na zoezi hilo. Sasa hawakuongea kwa muda kidogo.
Alipokamilisha nusu ya kila kitu, mafiga, vyombo na kuviweka hapo vitu vyote vitakavyotumika, akamtazama mwenzake. Akamkuta amekwisha lala!
Akaishia kusonya na kisha akatafuta mwanya naye ajipumzishe. Akilini hakuwa na msongo kwani alishajua amemaliza kupanga kila kitu.
Dakika kama tano zikapita wote wakiwa wamelala.
Lakini punde, kule kwenye dirisha la upande wa kushoto, popo akatua.
Popo huyo, akiwa amebinuka kichwa chini miguu juu, akawasha macho yake makubwa kumulika mazingira ya sebuleni.
Akakaa hapo kwa dakika moja, na mara akawasha mbawa zake kutimka!
**
Popo akatua kwenye bega la kulia la kaka yake Venin, mwanaume mweupe mwenye macho makubwa mekundu, nywele ndefu nyeupe mithili ya sufi.
Mwanaume huyo jabali alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa amevalia joho lake zito jeusi. Kwenye kola kulikuwa na ufito wa rangi nyekundu iliyokolea.
Alionekana bora kuliko hapo awali.
Uso wake wa kutisha ulikuwa umetulia tuli, macho yake yakionyesha hayupo karibu kimawazo.
Popo yule aliyemtulia begani, akamnong'oneza jambo sikioni, na mara mwanaume huyu akatabasamu kuonyesha meno yake mabaya rangi ya njano kisha akasimama na kunyoosha mikono yake yote miwili angani.
"Wakati umefika!" Akapaza sauti. "Wakati umefika! Wakati umefika!" Kisha akanyamaza akitazama dari.
Na kwa sauti ya chini akasema:
"Muda wa kulipa kisasi ..." huku akitikisa kichwa. "muda wa kumwaga damu ... muda wa Venet!" Na kumbe hili ndilo lilikuwa jina lake.
Venet.
Kaka wa mlozi Venim. Mwanaume aliyebeba kisasi cha kumuua mdogo wake kwa kumtuhumu kumsaliti, na hata kumgeuka pindi alipotakiwa amtumie watu wa kumtoa Tanashe.
Mwanaume aliyepigwa zongo dakika za mwisho na vikongwe kwa kufanikiwa kuondoka na mwili wa Rhoda.
Sasa ilikuwa zamu yake.
Kufumba na kufumbua akageuka kundi kubwa la popo kiasi kwamba mwanga uliokuwa eneo hilo wote ukamezwa na kuwa giza!
Mara popo hao wakatoka nje kwa fujo! Hao wakayoyoma. Hao wakayoyoma!
Wakielekea kule lilipo jengo la vikongwe.
***
Usingizi ulikuwa mzito na mtamu mno kunyanyua kope. Unaweza kusema hivyo kwani kwa sasa walikuwa wanakoroma kwa mbali.
Ni kweli walikuwa wamechoka mno kwa kazi waliyoifanya siku nzima. Walilala kwa amani zote wakiwa wamejawa na matumaini.
Matumaini ya kwenda kuiteka Goshen na kuiweka kwenye viganja vyao. Matumaini ya kuwa walozi wa kwanza kutawala himaya ya binadamu. Wafanye wanavyotaka. Wafanye inavyowapendeza.
Lakini hawakujua matumaini haya yalikuwa hatiani sasa. Yalikuwa mashakani, tena mashaka makubwa!
Hawakujua hata muda huo walikuwa tayari wameshatiwa nguvuni. Hawakuwa kwenye nyumba yao kama pengine walivyokuwa wanadhani vichwani mwao.
Hawakujua kwa muda huo, Venet alikuwa yu mbele yao akiwatazama!
Venet akiwa ameketi kwenye kiti chake, akaliza vidole vyake vya mkono wa kushoto. Mara wakatokea popo huko wasipojulikana. Venet akawaelekeza popo hao kwa kidole kwenda kwa wale vikongwe ambao walikuwa wamefungwa mikono na miguu kwa minyororo.
Popo wakawavamia wale vikongwe na kuwakurupusha toka usingizini. Wakastaajabu sana kujikuta pale. Wakaogofya sana kumwona Venet mbele yao.
Sasa wakajua wamekwisha!
Venet akatabasamu.
"Karibuni, warembo!" Akasema kwa dhihaka. "Mpo mahala sahihi!"
Kisha akanyanyuka na kuanza kusonga hatua za taratibu kuwafuata wale vikongwe waliokuwa wameshikiliwa na minyororo kutani.
"Nisingependa kuongelea ya nyuma, hayo yashapita na yamekwenda. Ila naona mliona haitapendeza endapo msiponipatia nami nafasi, sio?" Akauliza Venet akimpigapiga vikofi kikongwe mwenye macho mawili.
Alikuwa anatabasamu, alikuwa ana furaha kifuani mwake.
Akacheka sana. Akawadhihaki sana wale vikongwe. Akawatambia sana. Na mwishowe akawahabarisha wawe tayari kwa ajili ya kafara lake kwani mwezi ulio mzima utaonekana angani ndani ya siku tatu zijazo.
"Punde mwezi huo utakavyotawala anga, hakuna kati yenu atakayesalimika. Kiu yangu itakatwa!"
Akaendea kioo chake cha kilozi na kumtafuta mdogo wake Venim. Akampatia ujumbe mfupi, anakuja yu njiani.
Ajiandae kwa kifo chake.
"Labda unipatie sababu ya muhimu ya kukubakizia uhai wako. La sivyo ..."
Akapotea kiooni.
**
Asubuhi ...
Baada ya kupata kifungua kinywa, Tattiana akiwa mwenyewe mezani, akatazama nje kwa kupitia dirishani. Hakukuwa na mtu.
Nyumba nzima alikuwa yeye mwenyewe. Alichelewa kuamka. Hakujua baba na mama yake wameenda wapi wala Fanty.
Akajiuliza kuwahusu hao. Akanywa chai taratibu akiwaza. Alipomaliza akawa ameboreka kwa kutokuwa na shughuli ya kufanya.
Hapo ndipo wazo likamjia. Kama yupo mwenyewe nyumbani kwanini asijue kile ambacho wengine hawataki akijue?
Alipambana sana na hili wazo. Ni kama vile mwili wake ulikuwa hautaki wakati akili inataka. Akajaribu kujizuia, ila mwishowe akashindwa. Akanyanyuka na kupitia mlango wa nyuma aende stoo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alikuwa anataka kwenda kuchungulia vile vitu ambavyo vililetwa na Oragon na Ottoman. Vilikuwa ni vitu gani hivyo ambavyo hataki kuelezwa?
Akafungua stoo na kuzama ndani. Kulikuwa ni giza, kuona vema ilimbidi akazane kukodoa macho.
***
Akakapekua huku na huku. Akashika hiki na kile na kukifunua lakini hakuona kitu zaidi ya majani ya farasi. Akakasirika.
Akasema pengine mzigo huo unaweza ukawa kwenye stoo ya pili. Basi akiwa amejawa matamanio ya kutaka kujua, akatoka ndani ya ile stoo ya kwanza na kwenda ya pili.
Alikuwa mwangalifu mno.
Akafungua mlango na kuzama humo, napo akaanza kupekua kama alivyo fanya kwenye stoo ya kwanza.
Hakumaliza zoezi, akasikia geti huko likifunguliwa! Akashtuka. Pengine wazazi wake walikuwa wamerejea.
Basi haraka, akaenda kwenye mlango wa stoo na kuchungulia akiwa anaomba ujio huo uwe ni wa Fanty. Moyo wake ulikuwa unaenda mbio kuliko kawaida. Alianza kujuta kwanini alienda kule stoo.
Kwa macho yake akamwona baba na mama yake wakiwa juu ya farasi wanajongea kuja zilipo stoo. Huko ndipo banda la farasi lilipo. Akapata woga pengine wanaweza kuingia stoo ama kutuma vijakazi wachote nyasi kwa ajili ya farasi.
Hapo ndipo itajulikana kuwa yupo humo.
Atasema alikuwa anafuata nini mule? Akachanganyikiwa. Alifahamu wazi wazazi wake watajua lengo lake lilikuwa ni kutafuta kile Oragon na Ottoman walicholeta.
Hawakuwa wajinga kutolitambua hilo.
Moyo wake ukazidi kwenda mbio kadiri wazazi wake walivyojongea. Akajificha kwenye manyasi akiomba asikamatwe na huku akijilaumu kwa kujitakia shida.
Wazazi wake wakawafungia farasi wao, kisha Melkizedek akamtala kijakazi awalishe farasi hao mara moja. Kijakazi akatii agizo hilo na akazama stoo kuchukua manyasi.
Mbaya akaingia stoo aliyokuwamo Tattiana! Mwanamke huyo akajikunyata apotelee nyasini. Kijakazi akanyofoa nyasi kwa wingi kuzijaza mikononi, kabla hajaondoka, akaona viatu vya mtu.
Akashtuka.
Akazimwaga nyasi pembeni na kutazama viatu hivyo. Akagundua kuna mtu hapo. Mara Tattiana akajitokeza akiwa anavuta hewa kana kwamba ametoka chini ya maji.
"Binti wafanya nini nyasini huku stoo?" Kijakazi akauliza kwa kustaajabu. Tattiana akamsihi apunguze sauti yake.
Kisha kabla hajajibu, akanyanyuka na kwenda kuchungulia wazazi wake kama wameenda ndani. Hakuwaona. Akamtazama kijakazi na kumwambia asimwambie yoyote yule juu ya tukio lake la kukutwa nyasini.
"Sawa?" Akamtolea macho kijakazi, kisha upesi akazama ndani.
Akaenda kuketi sebuleni akiwa mwenyewe akizuga kuwa na kikombe cha kunywa maji. Ndani ya muda mfupi mama akatokea chumbani mwa Tattiana na kumwona binti huyo sebuleni.
Mama akajongea kumfuata akiwa analinyanyua gauni lake refu rangi ya samawati. Alikuwa anatembea kwa maringo kama msichana wa juzi. Akaketi na kusalimiana na mwanaye.
"Ulikuwa wapi?" Mama akauliza.
Tattiana akatabasamu kiuongo.
"Nilikuwa nipo ndani, tumepishana kidogo tu," Tattiana akajibu. Mama akamtazama kwa jicho la mashaka.
Uso wake ulitosha kuonyesha hakumwamini Tattiana. Lakini hakubangaiza kumlazimisha aseme kweli, akatabasamu.
"Ni vema. Tuliondoka asubuhi ukiwa bado umelala. Tuliona usumbufu kukuamsha."
"Mlienda wapi?"
"Kuonana na baadhi ya wafanyabiashara ... makubaliano kadhaa kadhaa, si unajua."
"Mlienda na Fanty?"
"Ndio. Unajua tunamuandaa kuwa mrithi wa biashara zetu. Anatakiwa kuanza kuvaa hivyo viatu sasa."
"Na vipi kuhusu mimi? Hamna mpango huo?"
Mama akatabasamu.
"Wewe unaenda kuwa mke wa mfalme, si mfanyabiashara."
Tattiana hakusema kitu. Alikabwa na fikira kadhaa kichwani. Ulimi wake ulikuwa mzito kunena. Hakuwa na tabasamu usoni.
"Unahitaji kujifunza siasa," mama akamwambia. "Upate kujua namna gani siasa za kila himaya zilivyo ili umsaidie mfalme kutawala."
Bado Tattiana akawa kimya. Mama yake akanyanyuka, akamtazama na kisha kwenda zake chumbani pasipo kumuaga.
"Hatakiwi aendelee kukaa hapa," mama akasema akiufunga mlango wa chumbani. Melkizedek alikuwa ameketi kitandani.
"Kadiri atakavyokaa hapa, na matatizo yatakuja," mama aliendelea kuongea, ila Melkizedek akiung'ata ulimi wake.
"Ameenda leo kupekua kule stoo, ni wazi alikuwa anatafuta ule mzigo. Kama usingekuwa umesafirishwa asubuhi ya mapema, angeuona!"
"Umejuaje alienda huko?" Melkizedek akauliza.
"Nywele zake zimejaa nyasi za farasi!" Mama akajibu akiketi kitandani.
"Hatujui ni lini pia kaka yake atamweleza. Najua Fanty hataweza kukaa na kitu hiki kifuani kwa muda mrefu."
Melkizedek akashusha pumzi ndefu. Akakuna ndevu zake akiwaza.
"Sasa tunafanyaje?" Akauliza.
"Inabidi Tattiana aende kwenye hekalu la mfalme akaishi huko," mama akapendekeza. "Hiyo ndiyo njia pekee itamweka Tattiana mbali na hapa lakini kwa wakati huo karibu zaidi na mfalme."
"Unadhani inawezekana?" Melkizedek akamtazama mkewe.
"Ndio inawezekana!" Mama akajibu kwa kujiamini. "Tumtumie yule mzee, atalifanyia wepesi."
Melkizedek akashika kichwa chake kama dafu. Hakupenda hili wazo.
***
Katikati ya usiku wa manane...
Baada ya kuota ndoto mbaya ya kutisha, Phares akashtuka akiwa anahema kwanguvu! Alikuwa kifua wazi, shuka akiwa amelitupia kando.
Akatazama kushoto na kulia kwake. Chumba kizima hakikuwa na mtu isipokuwa yeye. Punde mlango ukafunguliwa akaingia mwanajeshi akiwa ameelekezea mkuki mbele.
Akamuuliza mfalme kama kuna shida. Mfalme akamweleza ilikuwa ni ndoto tu, hakuna cha ziada.
"Mfalme wangu, una uhakika?"
"Ndio, hakika. Nashukuru."
Mwanajeshi yule kwa mashaka, akaushika mlango aufunge kwenda zake lakini mfalme akamwita na kumshirikisha juu ya ndoto yake.
"Unajua maana yake ni nini?" Mfalme akamuuliza kijakazi wake huyo ambaye naye alikuwa amepigwa na butwaa la hofu.
"Hapana, mfalme, sitambui maana yake," akajibu kijakazi. "Ila itakuwa na maana nzito sana, ni kheri ukawashrikisha wazee wa baraza wanaweza wakakupa neno," akashauri.
Mfalme akapendezwa na wazo hilo, akamshukuru kijakazi wake na kumtaka aendelee na kazi zake kama ada. Akabaki mwenyewe chumbani.
Akaendelea kutafakari juu ya ndoto ile kiasi kwamba mpaka kunakaribia kukucha ndipo akapata usingizi. Alipoamka akawapa ujumbe watumishi wake kwenda kuwaita wazee wa baraza waje hekaluni mara moja.
Baada ya nusu saa, wazee wakawa wamewasili, watano kwa idadi, wakiwa na hamu ya kujua kilichomo ndani ya wito huo wa ghafla.
"Nimewaita hapa maana nimeota ndoto kuu ya kutisha. Nami najua ninyi ni wazee, mmeona mengi, hamuwezi mkakosa neno," Phares akafungua kikao kwa haja yake.
Alikuwa ameketi mbele kabisa wakati wazee wa baraza wakiwa wameizingira meza kumtazama. Juu ya meza kulikuwa kuna matunda ya kila aina, pamoja pia na divai. Nyuma ya wazee hao walikuwa wamesimama vijakazi wakingojea kuagizwa ama kuhudumia.
Phares akiwa na hisia kali, akaanza kupambanua ndoto yake. Ameota ndani ya usiku wa giza totoro, akiwa amelala usingizi mzito, akasikia kelele kali toka nje ya hekalu lake.
Akakurupuka kwa hofu, na moja kwa moja akawaza pengine kuna vita imejiri.
Basi kabla hajafanya jambo, mlango wake ukafunguliwa na mwanajeshi wake akazama ndani. Akiwa ana sura yenye hofu, akamwambia wamevamiwa! Na afanye haraka amtoroshe kabla hajatiwa nguvuni.
Hakuwa na muda wa kujiuliza. Mwanajeshi wake akamnyaka mkono na kumkimbizia nje. Huko akaona anga likiwa jeusi ti! Na sasa sauti za yowe na makelele zikivuma huku na huko kwa karibu masikioni mwake.
Ajabu ni kwamba kila alipomuuliza mwanajeshi wake wamevamiwa na nani, hakusema, akazidi tu kusihi waondoke eneo hilo haraka iwezekanavyo.
Wakampanda farasi na kwenda mbio mno. Wakiwa wameliacha jengo kwa mbali, akakunja shingo kutazama nyuma. Ajabu, akaona jengo likimezwa na rundo kubwa la ndege, ambao moja kwa moja aliwafahamu ni popo.
Akiwa kwenye bumbuwazi hilo, mara akashangazwa, hata mbele yake, kufumba na kufumbua, rundo kubwa la popo likaibuka na kuwameza!
"Ikawaje?" Akauliza mzee mmoja kwa shauku. Phares akameza kwanza mate kabla ya kuendelea kusimulia.
Hakujua kilichotukia ni nini baada ya hapo, ila alistaajabu akija kuupata ufahamu akiwa mwenyewe. Amebaki na nguo za ndani tu! Alikuwa mchafu mno, hatamaniki.
Akaangaza huku na huko, hakuona kitu wala yeyote. Goshen ilikuwa imegeuka nusu jangwa. Alipotembea, akaishia kuona mifupa ya watu ikiwa imezagaa.
Akahofu.
Hata jengo lake la kifalme kilikuwa limegeuka kuwa ghofu. Mito ilikuwa inatiririsha damu na mabwawa yakiwa yananuka kifo.
Miti ilikuwa imekauka. Nyasi zimekuwa za njano. Huku na kule kulikuwa kumepatapakaa mabaki ya miili ya watu, haikuwezekana kukanyaga ardhi kwa hatua tatu!
Akashangazwa. Ni kwa muda gani mambo hayo yametukia? Mbona yanaonekana yamechukua karne ilhali alifumba na kufumbua tu macho?
Akiwa bumbuwazini, mara akaona tena kundi la popo angani. Akakimbia kwa nguvu zake zote lakini hakufanikiwa, akamezwa tena na popo hao lukuki!
Akatokomea kizani.
Aliporudi kwenye mwanga, ndipo akawa amekurupuka kuamka.
"Sasa ndoto hii maana yake nini?" Akauliza.
Wazee wakatazamana kwa nyuso za bumbuwazi.
"Bila shaka janga kubwa laja!" Akasema mzee mmoja. "Nashauri tuchukue hatua za haraka."
"Hatua zipi hizo?" Akauliza mzee mwingine. Alikuwa ni Baba yake na Oragon na Ottoman. "Hatua zitakuja baada ya kujua tatizo. Tulijue kwanza ndipo tutafute namna ya kulikabili."
"Lakini popo si ishara nzuri kabisa," akasema mzee mwingine. Yeye alikuwa ni mzee zaidi kuliko wote. "Popo humaanisha giza maana huishi nyakati za usiku. Popo humaanisha kisanga maana ni ndege na wakati huo huo mnyama anayebeba mimba!
Nakumbuka, kipindi cha mfalme Gayun, aliota popo ndani kwake. Hakudumu hata siku mbili, akaumwa ugonjwa wa ajabu, akafa akiwa amekakamaa. Baadae tukaja kugundua kumbe kilikuwa ni kisasi cha Jayit kwani mfalme Gayun alikuwa amedhamiria kuivamia Devonship."
Mada ikawa moto zaidi. Lakini ubaya hamna yeyote miongoni mwao aliyefanikiwa kutoa maelezo ya kueleweka. Basi mfalme akatoa kazi kwa wazee hao kusaka majibu ya ndoto yake hiyo ndani ya siku mbili.
Kwa atakayefanikiwa, basi atapewa zawadi nono. Lakini pia kwa atakayefikisha taarifa za uongo, ataadhibiwa vikali! Kikao kikafungwa kila mtu akiwa ana hamu na zawadi hiyo ya mfalme. Lakini pia wakiwa na hofu na mkono mzito wa adhabu.
Isipokuwa baba yake Oragon tu.
Yeye aliamini zawadi hiyo likuwa ni ya kwake. Aliapia ndani ya moyo wake lazima aipate kwa njia yoyote ile.
Ya kheri ama ya shari!
***
Joto lilikuwa kali mno!
Hakukuwa na dalili zozote za upepo wala mawingu angani. Anga lilikuwa la bluu na katikati yake likiwa limesimama jua linalomimina miale kwa fujo.
Hakukuwa na mti wa kujikingia kivuli wala ukuta wa kuuegemea. Hakukuwa hata na tone la maji ardhini, wala mmea wowote uliochipukia.
Palikuwa panatisha.
Palikuwa ni jangwa la kifo mezani! Ndani ya jangwa hili, mtu alikuwa anakamuliwa haswa maji yote mwilini na jua kali kisha anaachwa chini amekauka kama mbao!
Ndani ya jangwa hili, hauwezi kutembea zaidi ya nusu saa. Mwili unakuwa upo hoi mno kupambana na mchanga wa jangwa wenye kina kirefu.
Ndani ya jangwa hili, haikuwa inawezekana kuona mbele zaidi ya hatua thelathini. Utaona maruweruwe kwa mvuke wa jua.
Ndani ya jangwa hili, ndipo walikuwamo Malkia na wenziwe!
"Haya maji hayawezi yakatutosha kabisa kabisa," alisema Seth aliyekuwa mgongoni mwa farasi akiwa anatazama vijidumu vidogo walivyokuwa wamebebelea.
Wenzake wote walikuwa wanatembea kwa miguu isipokuwa yeye kwasababu ya majeraha.
Majasho yalikuwa yanawatiririka, na vinywa vyao vilikuwa vikavu kama pamba. Macho yao yalionyesha wapo hoi. Mwendo wao haukuwa na nguvu ndaniye.
Kulikuwa kimya akosekane hata wa kumwongelesha Seth. Kila mtu alikuwa anapambana na hali yake.
Wakatembea kwa dakika kadhaa, lakini ghafla Fluffy akadondoka chini kama mzigo! Wakatahamaki. Wakamjulia hali lakini mwanamke huyo alikuwa hawezi hata kuongea.
Wakamnywesha maji kulainisha koo lake kavu. Lakini bado hakuwa na nguvu ya kusema kitu. Macho yake yalikuwa yanaeleaelea kama mtu aliyebwia mihadarati.
Basi Ghaut, jitu la Azeth, likamnyanyua mwanamke huyo na kumpakiza kwenye mgongo wa farasi wa Malkia, wakaendelea na safari.
"Tumechoka. Inapasa tupumzike," alisema Zura kwa sauti kavu.
"Lakini tutapumzikia wapi wakati kote ni juani?" Akauliza Malkia. Wakaangaza huku na huko, huku na huko.
"Kule!" Seth akaponyooshea kidole upande wake wa mashariki. "Kutakuwa kuna mapango katika ile miamba. Twendeni!"
Hakuna aliyebishia wazo lake. Wakaongozana kwenda huko. Kweli wakakuta mapango, hatimaye wakapumzisha miili yao dhidi ya jua lenye hasira.
Wakanywa maji kidogo kidogo kulowanisha tu vinywa.
Basi kwasababu za uchovu, wakapitiwa na usingizi.
Lakini je, makazi haya waliyoyapata. Hayakuwa na wenyewe? Ni kweli waliyakuta matupu yaliyokaa hapo kwa bahati tu?
***
Hakuna mtu aliyewaza hayo. Kila mmoja alikuwa hoi. Walitazamia kupumzika tu wapate kupooza miili yao iliyomchemshwa na jua.
Lakini japokuwa walikuwa kivulini, bado wakaendelea kutota kana kwamba wamemwagiwa ndoo za maji, ama wapo mvuani.
Kama kuna mahali utakapokiri pasipo kulazimishwa kuwa maji ni uhai, basi ni hapa. Utahitaji maji muda wote. Kila saa ulimi wako utakwangua mdomo kama taulo.
Ndani ya pango hili , miale ya jua haikuwa inafika, ila joto lake lilikuwa kali mno kana kwamba tanuri la kuchomea mkaa. Lakini utafanyaje? Bado palikuwa ni kheri.
Basi wakauvuta usingizi.
Lakini kwenye pango hilo walilokuwa wamelala, ndani kabisa kule kizani, ni siri kulikuwa kuna mifupa ya wanyama na hata binadamu. Mifupa hii ilikuwa mingi ikirundikwa kutengeneza kichuguu!
Na hata pangoni hapo ukitazama vema ardhi yake ngumu, utagundua kulikuwa kuna nyayo za miguu ya kiumbe!
Miguu hii haikuwa ya kawaida. Ilikuwa ni myembamba yenye vidole virefu. Ikiachana kwa umbali mkubwa hatua kwa hatua.
Zaidi ya hapo, kiumbe huyu alikuwapo ndani. Ndani ya pango. Kwenye kina cha pango. Macho yake yalikuwa yanang'aa kama yale ya paka akiwa gizani.
Macho haya yalikuwa makubwa, na yakifanana haswa kimuonekano na bundi.
Kiumbe huyu alikuwa ni nani? Si tu kwamba hakuna anayemjua, bali hakuna hata aliyekuwa anafahamu kama yupo hapo!
Kiumbe huyu alikuwa anawaona vema wageni wake japo wao walikuwa hawamwoni wala kumhisi. Alikuwa anawatazama wageni kimawindo akiwapigia mahesabu kwa namna atakavyopata mifupa yao kuongezea idadi ya ile aliyokuwa nayo.
Basi kutimiza adhma yake hiyo, kuwatafuna na kuwapembua mifupa wageni ambao hakutoa jasho kuwatafuta, akaanza kuwajongea.
Kitu pekee ambacho kingekufanya ukajua anajongea, ni kusogea kwa macho yake yaliyokuwa yanang'aa. Na sauti za mifupa aliyokuwa akiikanyaga ikivunjikavunjika taratibu.
Kiumbe huyu alikuwa mjawa wa akili pia. Pale alipohisi mmoja wa mgeni wake atashtuka kwa sauti ya kusogea kwake, basi akasimama na kuvuta muda. Kisha akaendeleza safari baada ya kuona mazingira ni mazuri.
Sasa akawakaribia wageni wake akiwa amebakiza hatua chache tu kuwatia kinywani. Hapo akaanza kuonekana angalau kwa mbali. Rangi yake ilikuwa nyeupe.
Akapiga hatua tena, lakini ghafla akasita. Bado alikuwa kizani. Aliutokeza mguu wake kwenye mwanga, ila kwa haraka mno akaurudisha gizani.
Aliungua!
Akangurumia kooni kwa maumivu. Mara Seth akakurupuka na kuangaza. Hakuona kitu. Kiumbe kile hakikuwapo tena pale kilipokuwa. Haikujulikana kimeyoyomea wapi!
Seth asikubali kwamba hamna kitu, akaendelea kurusha macho yake, ila mwishowe akachoka na kuamua kulaza kichwa chini. Lakini hakulala tena usingizi. Kuna shaka alilipata.
Baadae jua lilipopungua makali, wakaamua kusonga na safari yao. Bado walikuwa wana mwendo mrefu wa kwenda. Walishapumzika na kupata nguvu mpya.
Wakatembea mpaka usiku ukawafikia. Angalau wakawa wamevuta mguu kwa kiasi chake. Kwa siku hiyo ikawa imetosha sasa, wapumzike kwa ajili ya kesho yake.
Wakatandika juu ya mchanga na kulaza miili yao baada ya kula akiba ndogo ya chakula.
Kulikuwa kuna baridi sasa. Upepo ulikuwa unapuliza kwa fujo na hata mara nyingine ukisomba mchanga. Usingedhani kama eneo hili ndilo lilikuwa lina joto la pasi wakati wa mchana.
Wakati watu wote wakiwa wamelala, kupo kimya, wamepotelea usingizini, yeye Malkia alikuwa anakodoa macho. Hakuwa na usingizi. Kichwa chake kilikuwa kimebanwa na mawazo kadha wa kadha.
Alikuwa anawaza wapi watapata maji. Wapi watapata chakula. Ni wazi walivyokuwa navyo visingeweza kumaliza hata siku tatu. Sasa itakuaje? Watafia jangwani?
Akageukia kila upande, akiwaza asiwazue. Hakupata majibu pasipo kujali alijikakamuaje. Mwishowe, akajilazimu kuamini njia itapatikana japo hakujua ni kwa namna gani.
Angalau sasa usingizi ukaanza kumnyemelea. Akalala.
Hakujua ulipita muda gani akiwa usingizini, ila mara akasikia sauti ya mtu kwa mbali ikiwa inaita. Mwanzo akadhani ni ndoto. Lakini sauti hiyo ikaendelea kuita tena na tena! Akashtuka na kuangaza.
Ajabu, upande wake wa magharibi akamwona mtu akiwa anazama mchangani. Moyo wake ukapiga fundo kubwa - bumm! Na kuanza kukimbia harakaharaka - bum! bum! - bum! bum! - bum! bum!
Wenzake wote walikuwa wamelala. Hamna aliyekuwa na habari. Lakini miongoni mwao, hakuwapo mmoja. Naye ni Ghaut - jitu la Azeth!
Malkia akaamsha wenzake upesi na kuwahabarisha. Kwa haraka wakanyanyuka, isipokuwa Seth mwenye majeraha, wakakimbia kwenda kumsaidia Ghaut aliyekuwa anamezwa na shimo la mchanga.
Lakini ajabu ni kwamba Ghaut huyo hakuwa akipiga makelele wala kufanya jitihada zozote za kujikomboa. Hakuwa katika fikra wala fahamu zake kamili. Masikioni mwake alikiwa anasikia sauti tu iliyompumbaza.
Wenzake wakabahatika kumdaka mkono mmoja. Mwili wake wote ulikuwa umemezwa tayari. Wakajaribu kumvuta kwa nguvu zao zote. Wakashindwa.
Ghaut akaenda mbele ya macho yao!
Wakajaribu kufukua lakini wapi. Hakukuwa hata na dalili ya shimo. Wakaketi wakiwa wamebaki na majonzi na maswali vichwani.
"Nilisikia sauti nikiwa usingizini," Malkia aliteta. "Ilikuwa inaita Ghaut Ghaut, lakini nikadhani ni ndoto. Kumbe ndiyo ilikuwa inamchukua!"
Wakastaajabu sana. Hawakutarajia kama lile jinamizi la majina lingeendelea kumuwinda Ghaut mpaka kule jangwani. Walidhani waliliacha msituni. Hawakutarajia pia kama shimo lile limezalo watu lingejiri mpaka mchangani.
Usiku ukawa mbaya kwao. Wakapoteza hamu yote ya kulala. Wakaketi ama kujilaza wakijikunyata. Ilikuwa ni kama ndoto ndani ya dakika chache tu kumpoteza mwenzao asionekane hata mwili!
Kukawa kimya. Sauti ya upepo pekee ndiyo ikivuma na kupuliza huku na huko.
Usiku ukazidi kusonga.
Zikiwa zimepita kama dakika thelathini tangu Ghaut amezwe na mchanga, Seth akawashtua tena wenzake baada ya kuona kitu cha ajabu kwa mbali.
Kilikuwa ni kile kiumbe kilichokuwamo ndani ya pango! Sasa jua lilikuwa kimetokomea, anaweza kuringa na kutamba. Sasa ulikuwa ni muda wake. Alikuwa amekuja kudai mifupa ya wageni wake.
***
Kiumbe huyu alikuwa mwembamba mwenye rangi nyeupe ya kufifia. Kichwa chake kisichokuwa na nywele kilikuwa cha duara inayokaribia pembe tatu, macho yake makubwa rangi ya kijani, kifua chake kimechomoza mbavu, mikono mirefu na mipana.
Alikuwa anatembea kilevi lakini akionyesha mwenye nguvu. Miguu yake ilikuwa inatawanya michanga ya jangwa kana kwamba maji. Mdomo wake mdogo wenye meno ya paka ulikuwa wazi akiwatazama walengwa wake anaotaka kuwatia kinywani.
Na mate yalikuwa yanamchuruza.
Kiumbe gani hiki? Wakajiuliza wakina Malkia wakitumbua macho. Hawakuwa wanaamini wanachokiona. Hawakujua kiumbe hicho kinataka nini lakini kwa haraka wakaamini hakijaja pale kwa kheri.
"Wewe ni nani?" Seth akapaza sauti. "Unataka nini?"
Kiumbe kile wala hakikuongea, kikazidi kusonga kuwajongea kana kwamba hakijasikia. Seth akabadilisha lugha takribani nne akimuuliza kiumbe kile maswali hayohayo, hatimaye akafanikiwa!
Aliongea lugha anayoielewa. Lugha hii ilikuwa ni ki-injin, lugha inayozungumzwa na idadi ndogo sana ya watu waishio mabarafuni. Ilikuwa na maneno machache, na endapo ukiiskiliza vema utatambua inarudiarudia sana maneno lakini kumaanisha maana tofauti.
"Kukluf kazif tekop, meshan kabac tubuknova," akateta kiumbe yule akiwa anazidi kusogea.
"Anasema nini?" Zura akawahi kuuliza kwa hofu. Macho yake yalijawa woga, mikono yake ilikuwa inatetemeka.
Seth, kwa haraka, akawakalimania kwamba kiumbe yule anaitwa Kazif na amekuja hapo kuchukua kilicho chake.
"Kipi hicho?" Malkia akawahi kuuliza. Alimgeuzia uso Seth lakini macho yakiwa kwa yule mgeni wao anayezidi kujongea.
Seth akamuuliza tena yule kiumbe kwa lugha anayoielewa, hapo amekuja kufuata nini hicho kilicho chake? Kiumbe kile pasipo hiyana, akasema mifupa. Anahitaji kwenda kujaza pango lake zaidi.
Malkia akataka kunyanyua panga, Seth akawahi kumtazama na kumzuia kwa ishara ya kumwonyesha kiganja.
"Acha tuongee naye kwanza."
Kisha akamwomba kiumbe yule aketi chini wapate kuteta. Wao hawana maana ya kuzua shari. Kwa kusikia ombi hilo, kiumbe kile kikaketi kikiwatazama. Zura na Fluffy wakazidi kupata hofu. Kiumbe hicho hakikuwa kinavutia kukitazama hata kidogo.
Kadiri kilivyosogea basi kingekufanya tumbo likusokote kwa woga. Miguu ife ganzi. Na haswa kikikutazama, ungeweza kupata haja zote kwa mpigo!
Tangu kiumbe hichi kiliposogea hapo, hali ya hewa ikageuka na kuwa baridi zaidi. Ungemtazama vizuri ungebaini alikuwa anafuka moshi. Moshi wa barafu.
Si bure hakuwa anapatana jua maana angeweza kuyeyuka.
Basi Seth akamwomba awabakizie uhai wao, na watakaporejea toka safari yao ya mbali watampatia zawadi kama fadhila. Kiumbe hicho kikakataa na kusema:
"Habaq quatta kilim meshan, juata himas!" Akimaanisha kama wamemkatalia ombi lake basi wacheze naye mchezo. Seth akamuuliza mchezo gani huo, Kazif akamwambia unaitwa 'Yuaj si Kobil' - maji ama damu.
Akauelezea mchezo huo. Atawauliza mafumbo matatu na endapo wakiyakokotoa atawapatia maji, na endapo wakishindwa basi wao watampatia damu.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kuweka nao makubaliano.
"Hapana," Malkia akakataa. "Hatuwezi kucheza naye mchezo huo wa hatari kiasi hicho. Tupambane naye!"
"Lakini vipi kama tukapoteza zaidi kwa kupambana naye kuliko njia hii ya kidiplomasia?" Akauliza Seth. "Vipi kama tukashinda, tukabaki salama na maji akatupatia? Si rahisi kupambana na kiumbe hiki!"
Lakini bado Malkia akawa na woga. Seth akamsihi wachague mchezo huo, na kwa pamoja watashirikiana kufumbua mafumbo hayo. Vichwa vitano si sawa na kimoja.
Basi wakamruhusu kiumbe yule aanze kuuliza mafumbo yake. Hapa chini kama yalivyotafsiriwa:
La kwanza, kikapu kina matufaha matano na nina watoto watano. Nitayagawanyaje haya matufaha matano kwa watoto wangu na kwa wakati huo tufaha moja likabaki kapuni?
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Tumekwisha!" Akasema Fluffy akitoa macho. "Mbona anauliza maswali ambayo hayawezakani!"
Seth akasafisha koo lake kisha akafikiri kidogo. Akajibu atawapatia matufaha manne kwa wale watoto wa nne, alafu mtoto wa tano atampatia tufaha likiwa limebaki ndani ya kikapu.
Wakastaajabu mojawapo ya chupa yao imejawa na maji. Walikuwa wamepata!
La pili, anayekitengeneza, hakihitaji. Anayekinunua hakitumii. Anayekitumia hawezi kukiona wala kukihisi. Ni nini hicho?
Seth akatabasamu, haraka akajibu ni sanda. Basi chupa lao la pili likajawa na maji. Wakafurahi. Kile kiumbe kikang'ata meno yake kwa hasira. Sasa akadhamiria kuuliza fumbo gumu la mwisho ili angalau asiwe amepoteza muda wake bure.
La tatu, nyakati za mchana huzitumia dirishani, nyakati za chakula naenda mezani, nyakati za usiku najificha hamnioni. Mimi ni nani?
Seth akatabasamu tena, upesi akajibu ni nzi. Bobo lao moja lilio tupu likajaa maji! Alikuwa amepata! Sasa kiumbe huyu akawa ameshindwa kutimiza adhma yake. Lakini kwa ukaidi, akasema anaongezea swali moja la mwisho.
Seth na wenzake wakatahamaki. Malkia akasema yule kiumbe hakuwa anataka kuwaacha hai, inabidi wapambane. Lakini Seth akawatoa hofu, hawakuwa na haja hiyo. Wamwache huyo kiumbe atupe turufu yake ya mwisho.
La nne, kuna wadada wawili: mmoja anamzaa huyo wa pili, alafu naye huyo wa pili anamzaa huyo wa kwanza. Hawa wadada wawili ni wakina nani?
Seth akamtazama Malkia kisha Fluffy na baadae Zura. Akawauliza kama wana majibu, wote wakasema hawana. Wakajawa pia na hofu baada ya kuona Seth anawauliza wao. Walikuwa wanamtegemea yeye kwenye hili.
Lakini mara Seth akatabasamu, akamtazama kiumbe yule na kumjibu dada hao ni usiku na mchana.
Kiumbe kile kikakasirika mno. Alikuwa ameshindwa! Akasaga meno yake na kupiga ngumi kiganja chake. Akamwambia Seth kwamba ameshinda kwa leo lakini anajua itawachukua siku kadhaa kumaliza jangwa hilo kwahiyo kila siku usiku atakuwa anawatembelea na kuwauliza mafumbo kadhaa.
Hawatayapata siku zote hizo, aliamini na kuwaaminisha. Akaenda zake akiwa ameghafirika.
"Uliyajuaje mafumbo yote yale?" Fluffy akamuuliza Seth akiwa na kimuhe. Seth akamwambia baba yake alikuwa akimuuliza sana akiwa mtoto, vile vile vitabu vingi alivyovisoma. Wakampongeza sana kwani alisaidia kupata maji ambayo hawakujua wangeyapatia wapi.
Lakini kwa wakati huo, yule kiumbe, akiwa amepania kwa dhati, akaenda kukesha usiku mzima kupitia mafumbo yake aliyoyaandika kwenye kuta za pango. Hata kula hakutaka!
Kasrini, Goshen.
Ni asubuhi iliyokuwa inakaribia mchana lakini si muda mrefu watu walitoka kupata kifungua kinywa. Kwa mbali farasi watatu walionekana wanajongea kwenye lango la kuingilia. Farasi hawa wa rangi ya 'brauni' walikuwa wanakimbia kwa kasi.
Walipokaribia karibu na kusimama ikaonekana kumbe migongoni mwao walikuwa wamewapakia Tattiana na Mama yake wakiongozana na mzee wa baraza. Wakajitambulisha kwa ufupi pale langoni, wakaruhusiwa kuingia ndani kuonana na mfalme.
Baada ya dakika kadhaa za kungoja, mfalme akaja kuungana nao mezani na sasa mzee wa baraza akashika hatamu kueleza kilichowaleta hapo.
Kwa heshima yake, akasema wazazi wa Tattiana wameridhia kumleta binti yao aje akae hapo kama mchumba wake mpaka pale atakaporidhia kumuoa.
Wameamua hivyo kwa kuona itakuwa njia nzuri kwa binti huyo kuanzisha mahusiano na mume wake wa baadae na pia itamsaidia kiakili na hata kimwili kwasababu kadhaa kama vile upweke anaokumbana nao hapa karibuni.
Na kama haitoshi itaanza kumjenga na kumwandaa kubeba majukumu yake kama mke wa kiongozi mkubwa ndani ya himaya. Kama Malkia.
Mfalme akalipokea swala hilo kwa mikono yote miwili lakini akastaajabu kwanini imekuwa ghafla hivyo. Limekuwa ni jambo la kushtukiza mno. Alitakiwa aarifiwe kama mhusika.
"Ni kweli," akaafiki mzee wa baraza. "Tumefanya makosa makubwa sana. Lakini fadhila zi juu yetu maana wewe umekuwa mfalme msikivu na unayejali. Nakuomba sana msamaha, mfalme. Na nakuomba ulipokee shauri letu hili kwa mikono yote miwili."
Phares akafikiri kwa muda kidogo. Kisha akauliza:
"Lakini na binti huyu ameridhia? Nami ningependa kumsikia akitia neno kwenye hili."
Basi Tattiana akapewa fursa ya kuongea. Akiwa ameinamisha kichwa chake chini, akasema ameridhia hilo na yupo tayari. Mfalme akajikuta ametabasamu.
"Basi hamna shida. Niko tayari," akasema kwa akimkabidhi mkono mzee wa baraza na hata baadae mama yake Tattiana kisha akawasindikiza kwenda zao wakati wakimuacha binti ndani.
"Muende kwa kheri zote," mfalme akawabariki.
Waliingia farasi watatu ila sasa wakatoka wawili tu. Mfalme akawatazama wageni wake hao wakiishilia akitabasamu, alafu akaenda zake ndani kukutana na mchumba wake.
"Jisikie upo nyumbani," akamkarimu Tattiana lakini akamwambia hatokaa naye kwa muda huo kwani kuna kazi moja ndogo anatakiwa kwenda kuitekeleza nje ya kasri.
Kabla hajaondoka, akapiga makofi matatu wakaja vijakazi wake na haraka vijakazi hao wakagawanywa na kuteuliwa watatu kwa ajili ya kumtazama na kumhudumia Tattiana.
"Nitarejea muda si mrefu, kipenzi," mfalme akaaga na kwenda zake. Tattiana naye akaenda ndani alipoelekezwa kama chumba chake maalumu baada ya chumba hicho kufanyiwa matengenezo na kupambwa inavyotakiwa.
Chumba hichi kilikuwa kikubwa mno, kitanda kipana cha duara, kimejawa na maua yanayovutia na samani zake zilikuwa za gharama kubwa.
Tattiana akajiweka kitandani akilala chali. Asidumu hapo muda mrefu, mawazo yakamkaba koo. Kichwa chake kilirejelea na kuchambua siku nzima ilivyokuwa mpaka yeye kuishia hapo. Alikuwa anaona kila kitu kichwani kwake kana kwamba tamthilia kwenye televisheni.
Wakati mambo hayo anayoyawaza yakitukia hakuwa na muda wa kuyachambua vema, sasa alikuwa mwenyewe kitandani, huu ulikuwa ni muda muafaka kwake kufanya zoezi hilo.
Akakumbuka namna mzee yule wa baraza alipofika nyumbani kwao asubuhi ya mapema, akazungumza na baba na mama yake kisha akaitwa na kupewa maagizo pasipo kuombwa neno.
Ni bayana walikuwa wanamjadili yeye. Lakini mbona wamemuondoa nyumbani haraka kiasi hicho? Ni nini kipo nyuma yake? Akili yake nyepesi ikamwambia sababu ni kile kitu ambacho huwa kinaletwa pale nyumbani.
Hatakiwi kukijua.
Wazazi wake na mzee yule wa baraza walikuwa wamefanya njama aondoke pale ili siri yao ibaki salama.
Lakini kwanini wanashirikiana kwenye hili? Aliamini kabisa mzee yule hakuwa anafanya haya bure. Lazima kuna fadhila anapata hapa, ipi hiyo?
Ule mzigo! Akalipuka kifuani mwake. Fadhila hii ni ule mzigo wanaoleta watoto wa yule mzee kila usiku pale nyumbani.
Mawazo haya yakamwogopesha sana Tattiana. Aliamini kabisa mzigo ule si wa mema, usingefichwa.
Na je mfalme anajua kuhusu hayo?
Akagaragara kitanda kizima akiwaza na kuwazua.
***
"Umezipatia wapi?" Zura akamuuliza Fluffy huku akimpokea mzigo wa kuni kadhaa. Fluffy alikuwa ametoka safari kidogo akiongozana na Alk, jitu pekee la Azeth lililobakia. Watu hao walisafiri kwenda kuangaza kama watapata kuni za kuanzishia moto wa kuwasitiri na baridi la usiku unaokaribia kuingia.
Fluffy akatabasamu akiketi.
"Tumetoa mbali sana," akajibu kwa kujigamba. "Tumezitoa mbali kweli."
Zura akaguna. "Wewe ungeweza kwenda mbali ndani ya jangwa hili?"
"Kwanini nisiweze?" Fluffy akauliza.
"Si ungeanguka kama jana!" Seth akatania wakacheka. Fluffy akaeleza wamezitoa kuni hizo upande wao wa kusini walipokuta miti kadhaa ya tende. Kwa msaada wa Alk wakavunjavunja miti hiyo iliyokauka na kuileta papo.
"Mmefanya jambo la maana sana," Malkia akawapongeza. "Tunaweza sasa tukapasha hata vyakula vyetu vilivyopoa na kuchukiza."
Mara akakumbuka jambo, akamuuliza Seth:
"Vipi yule kiumbe wako hawezi akatoa chakula? Yeye ni maji tu?"
Wakacheka.
"Lakini mimi namhofia sana," akasema Zura. "Anapokuwa karibu yangu nahisi kukosa pumzi. Naomba leo asije akatokea kwani naweza nikazirai."
Malkia akaongezea hapo. Tatizo ni kwamba yeye hamuamini kabisa yule kiumbe. Na anaona hata Seth akifanikiwa kujibu mafumbo yake yote bado atatafuta namna ya kuwamaliza tu.
"Sasa tutafanya nini?" Seth akauliza. Akasema hawana budi kumwamini kiumbe huyo kwani ndilo chaguzi pekee walilo nalo.
"Tofauti kabisa na binadamu, viumbe hawa huwa waaminifu. Cha msingi ni kutumia zoezi lake hili kujikwamua zaidi maana kiuhalisia hatuwezi kupambana naye. Mtu anayeweza kujaza vyombo maji usijue yametokea wapi, ni nini utamfanya?"
Kukawa kimya kidogo. Wakawasha moto kujipa joto na hata kupasha vyakula vyao wapate kutia kitu tumboni.
Muda ukapita, na kidogo yule kiumbe akajiri. Leo alikuwa amewahi kuliko jana. Aliketi asimwongeleshe yoyote yule isipokuwa Seth aliyemtaka waanze zoezi lao mara moja!
Lakini kabla ya kuanza, Seth akwamwambia ana ombi kwake juu ya zoezi lao. Kiumbe yule, pasipo hiyana, akamkaribisha apate kumsikia.
Seth akamwambia anataka waboreshe zoezi lao, leo na yeye apewe fursa ya kumuuliza mafumbo kadhaa kiumbe huyo. Na endapo akifanikiwa kumuuliza akashindwa, basi azawadiwe zawadi kubwa. Si maji.
"Kanji keti na?" Zawadi gani hiyo? Kiumbe akauliza. Seth asifikiri sana akamwambia anataka awasaidie kukamilisha safari yao ndefu ya kwenda Misri.
Kiumbe kile kikatulia kwanza kwa muda mchache kisha kikamwambia Seth kuwa atafanikisha ombi lake hilo kwa makubaliano makubwa pia kwa upande wake.
Endapo Seth akikosa swali lake lolote, basi atawamaliza wote kwa kuwanyonya damu na kukusanya mifupa yao.
Seth akabaki na njia panda. Akawatazama kwanza wenzake kabla ya kujibu.
"Vipi? Amekuambia nini?" Malkia akamuuliza. Ulimi wa Seth ukawa mzito. Akashusha pumzi ndefu kisha akatazama chini. Wenzake wote walikuwa wanamtazama kwa hamu kubwa.
Akawauliza:
"Mnaniamini?"
"Kwani kuna nini Seth?" Malkia akauliza kwa tembe za hofu. Seth akarudia swali lake:
"Mnaniamini?"
"Ndio, tunakuamini," Malkia akajibu.
"Hata kwa kuweka maisha yenu rehani?" Seth akauliza tena. Hapa Malkia akasita kujibu. Akawatazama wenzake kwanza alafu akamtaka Seth aeleze anamaanisha nini. Lakini kwa kuhofia kuwatisha, Seth hakusema kitu.
Akawasihi wamwamini na wamwombee. Mtihani huu ni mkubwa na pia matokeo yake. Baada ya hapo akamtazama kiumbe yule na kumwambia yupo tayari sasa kwa zoezi lao.
Kiumbe hicho kikawa cha kwanza kuuliza mafumbo yake. La kwanza akauliza, kwanini kondoo weusi hula kidogo kuliko kondoo weupe?
Seth akamjibu ni kwasababu kondoo weusi ni wachache kuliko kondoo weupe ulimwenguni.
Kiumbe kikatupa tena sarafu yake ya pili kwa Seth akimuuliza, kina mbavu na uti wa mgongo, kinammeza binadamu mzima na kumtema akiwa hai. Ni nini hiko?
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Seth baada ya kufikiri kidogo akajibu ni nyumba. Akapata. Kiumbe kikakunja sura. Sasa alikuwa amebakiwa na nafasi moja ya mwisho ya kuuliza kabla Seth hajashika hatamu kumuuliza yeye.
Kikafikiri kidogo, alafu kikauliza, upi ni muda bora wa kula chakula cha mchana?
Swali hili lilikuwa fupi na dogo lakini likamuumiza kichwa Seth. Akawaza kwa muda kidogo kabla hajapata jawabu mujarabu, baada ya chakula cha asubuhi! Muda bora wa kula chakula cha mchana ni baada ya chakula cha asubuhi.
Akapata!
Kiumbe kile kikanyong'onya. Alikuwa ameshindwa. Sasa ikawa zamu ya Seth kumtupia yeye mafumbo ayang'amue.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment