Search This Blog

UFALME WA NUGUTU - 1

 







    IMEANDIKWA NA : NEA MAKALA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Ufalme Wa Nugutu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    "Wanakuja hao..! Hakikisha hamna anayetoroka akiwa hai!",

     "Sawa mkuu, shambuliaa......"

    zilikuwa kauli za Viongozi wa jeshi la ufalme wa nchi ya Nugutu, ambao waliamuru maadui zao wote kuangamizwa na asibaki hata mmoja, ivyo agizo lao lilitimizwa na mashujaa wao na kuleta ushindi kwa nchi yao.

    "Uishi miaka mingi Nugutu, Kimbilio la wanyonge Nugutu, Nchi yenye Baraka na neema Nugutu"

    Mashujaa wa Nugutu waliendelea kuimba huku wakirejea nyumbani kwa furaha sana. Wakiwa karibu kabisa na lango la kuingilia kwenye ufalme wao, tayari wake zao na watu wengine walishajipanga kwa ngoma, makofi na nderemo kushangilia ushindi ulioletwa na makamanda wao.



    Nugutu ni nchi inayoongozwa kwa kuzingatia mashauri ya wazee wenye hekima na hata wale wenye ukaribu zaidi na miungu, Hivyo katika maamuzi yeyote yanayohusu wananchi au nchi kwa ujumla, lazima wazee wakae waombe miungu yao ili iwaoneshe njia sahihi ya kuamua. Ushindi wao ulichagizwa na maamuzi yenye busara pamoja na maombi kwa miungu ya Nugutu.



    "Ndugu zangu wananchi, afya ya mfalme wetu si nzuri ivyo kuanzia kesho tutaanza maombi kwa miungu yetu ndani ya siku 9, hili kujua ni mtoto yupi sahihi kushika nafasi ya mfalme Gaiya"



    Yalikuwa maneno ya msemaji wa mfalme akitoa taarifa kwa umma wa Nugutu, sherehe ziliendelea huku kila mmoja akifikilia lake juu ya mrithi wa ufalme wa Nugutu ukizingatia mfalme Gaiya alikuwa na wake 6 na watoto 32 ivyo ilikuwa kazi ngumu kutabiri nani hasa atashika milki ya baba yake.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku zikasogea hatimaye siku ya 9 ikabisha hodi, wazee wakakusanyika barazani tayari kuongea na mfalme Gaiya juu ya mrithi wake. Wazee na wakuu wa kila idara wakawa tayari kusikiliza ni nani aliyeteuliwa na miungu ya Nugutu kushika nafasi ya Mfalme Gaiya,

     "Uishi miaka mingi mfalme"

    "Uishi..!!"

    Mzee mmoja alisema na wenzake wakaitikia na kuinamisha vichwa vyao chini kutoa heshima kwa mfalme, ambaye alijikongoja na kufika hapo barazani kusikiliza nani aliyeteuliwa kuwa mtawala wa Nugutu.

     "Mheshimiwa mfalme! Utukuke sana! Kama ilivyo ada kwa wazee na wananchi kufanya maombi na matambiko kwa miungu ya Nugutu, kila linapokuja swala linalohitaji maamuzi magumu. Mfalme mtukufu tunasikitika kukwambia kuwa kati ya vijana wako 20 wa kiume hamna hata mmoja aliyeidhinishwa na miungu yetu kushika nafasi yako, na kwa vyovyote itakavyokuwa ufalme hauwezi kwenda nje ya kizazi chako kitukufu," alisema Mzee Bongwa ambaye ndiye msemaji mkuu wa wazee.



    Mfalme akashtushwa sana na taarifa hiyo, minong'ono ya chinichini ikaanza tapakaa ndani ya baraza lile, mfalme akavunja mkutano na kuahidi kulitolea ufumbuzi swala hilo ndani ya saa 72.



    **************



    Mfalme akaamua kweenda kwenye hazina za siri na muhimu sana ambazo mfalme pekee ndio ustahili kuingia humo, mbali na ugonjwa wake mfalme akajikongongoja huku akisindikizwa na jeshi lake na alipokaribia hazina hiyo ya kifalme, akaamuru jeshi limsubiri kisha yeye pekee akaendelea na safari na kuingia ndani ya pango ambapo hazina ya kifalme imeifadhiwa humo. Alipoingia upepo mkali ukavuma, ardhi ikatetemeka radi ikapiga, mfalme akachoma ubani na kupiga magoti hali ile iliendelea kwa muda wa saa 3 mfululizo kisha mfalme akaanguka na kupoteza fahamu.



    Siku mbili zikapita bila kuwa na taarifa yeyote juu ya mfalme, wanajeshi walioambatana na mfalme wakaanza kuingiwa na hofu uenda kitu kibaya kimemkuta mfalme wao, hata hivyo wakashauriana waendelee kusubiri. Siku ya tatu asubuhi na mapema wakaona mfalme Gaiya akitokeza huku akiwa amebeba kifurushi kilichofungwa fungwa vizuri kwa kitambaa cheupe, wakainamana chini na kutoa heshima zao kwa mfalme.

    "Kuna kazi moja ya kufanya kabla hatujarudi Nugutu, ni lazima twende Kigomile huko ndiko iliko nuru na hatima ya ufalme wa Nugutu" alisema mfalme.

    "Na iwe kama ulivyosema mfalme," wanajeshi wakaitikia na kuinamisha vichwa vyao na kuanza safari ya kuelekea Kigomile.



    *****************



    Katika jumba la kifalme sintofahamu ikaendelea kutawala vichwani mwa wazee wa baraza, malkia na hata watoto wa mfalme kwani ni takribani siku 5 zimepita toka mfalme aondoke katika milki yake. Hawakupata taarifa yeyote kuhusu yeye wala jeshi aliloondoka nalo, ikabidi malkia aitishe kikao cha dharua kwa wazee wa baraza na wakuu wa kila idara.



    "Hatuwezi kuendelea kukaa bila kuwa na kiongozi, siku 5 zimepita na hatuna taarifa yeyote juu ya mfalme, mimi nashauri tumteue mtoto wa kwanza wa mfalme ashike nafasi yake hadi atakaporejea mfalme Gaiya," alisema malkia ambaye ni mke wa kwanza wa mfalme.

    Baraza la wazee likabaki kuitafakari ile kauli ambayo malkia aliitamka, mgawanyiko ukatokea baadhi ya wazee wakaungana na kauli ya malkia na wengine wakapinga na kutaka waendelee kusubiri, majibishano yakawa makali zaidi huku kila upande ukitetea hoja zake.

    "Kuna vitu vya kupuuzia lakini si miiko na maagizo ya miungu ya Nugutu, haina haja kuingiza maswala binafsi katika hatima ya ufalme huu wa nchi hii, tunaweza kujiweka hatarini kwa kutokufikiri kwetu, lazima tusubiri hadi mfalme atakapo rejea ndivyo mambo mengine yataendelea," Alisema mzee Bongwa.



    Maneno ya mzee huyo yakawanyamazisha wazee ambao walishaanza kutoka nje ya miiko ya Nugutu, lakini uchu wa madaraka ukamfanya Malkia atake kupindisha baadhi ya sheria na kwa gharama yeyote ile mtoto wake aapishwe kuwa mfalme wa Nugutu.

    "Sawa tutasubili kwa siku 2 zaidi hadi siku ya 7 kama hakutokuwa na taarifa yeyote basi mtoto wangu lazima aapishwe na kuwa mtawala wa Nugutu" alisema malkia.

    Tofauti iliyopo kati ya nchi ya kifalme ya Nugutu na falme nyingine ni mke wa mfalme kuwa na nguvu ya kuamua mambo pale mumewe anapokuwa nje ya ufalme.



    ***************



    Mfalme na jeshi lake wakafika katika nchi ya kigomile, ikawalazimu kupia njia ya msituni ili kutokea sehemu ambayo mfalme aliikusudia. Kadri walivyozidi kuyakaribia makazi ya watu ndivyo kelele za vilio zenye kuomba msaada zilivyozidi kusikika masikioni mwao. Wakaongeza mwendo hili kujua kilichojili, wakafika na kukuta watu wengi wakiwa wameuawa na mali zao kuchukuliwa na nyingine kuteketezwa. Mfalme na jeshi lake lenye vijana wapatao 100 wakasogea kijijini hapo kwa tahadhari kubwa, akaamuru jeshi litawanyike na kutoa msaada kwa majeruhi waliosalia. Mbali na kuwa mtawala wa nchi ya Nugutu, mfalme Gaiya alisifika kwa roho ya huruma, karibu kila falme ilitambua hilo. Wakati wanajeshi wake wakiendelea kutoa msaada ghafla wakajikuta wakiweka katikati ya jeshi kubwa la nchi ya Kigomile ambalo kwa kukadilia wanaweza fika wanajeshi 300.



    "hatukutegema kama ninyi mnaweza kuleta maafa katika nchi yetu ya kigomile, kwa kuwa hamkutaka kuongea nasi na mkafika kuteketeza watu wangu wa kigomile na mali zao hivyo pasi kusita nasi lazima tuwaangamize" ilikuwa kauli ya kikakamavu iliyotolewa na mfalme wa kigomile dhidi ya mfalme wa Nugutu na wanajeshi wake.







    "Shambuliaaaa....!!"

    "Yeah......"

    Jeshi la Kigomile likaanza kusogea kwa kasi ya ajabu kuelekea alipo mfalme wa Nugutu, wanajeshi kwa haraka sana wakamzunguka mfalme wao hili kumuepusha na hatari ambayo tayari ilikuwa mlangoni. Jeshi likazidi kusogea, bila kutarajia mfalme Gaiya akaamuru wanajeshi wake wakae chini na kumuacha yeye akisimama. Mfalme akanyanyua juu kitu mithiri ya fimbo iliyotengenezwa kwa madini ya shaba. Papo hapo radi likapiga na nchi ikatetema, jeshi la kigomile likapunguza kasi na kuanza kurudi nyuma anga likawa jeusi, kiza kikatanda kwa muda na mvua ikaanza kunyesha. Hali hiyo ikawafanya wanajeshi wa Kigomile kusimama na kushangaa maajabu yale, Mfalme akashusha fimbo yake na hali ikawa shwari. Jeshi lote la Kigomile likainama chini na kutoa heshima zao kwa Mfalme Gaiya, kisha mfalme akapaza sauti na kusema,

    "sisi hatuna ubaya na watu wa kigomile na kamwe hatuwezi wafanyia ubaya, tumekanyaga ardhi kwa sababu hatima ya nchi ya Nugutu ipo humu".

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kusema hayo, mfalme wa Kigomile akaomba radhi na kuwakaribisha kwa maongezi, Mfalme Gaiya akaridhia hivyo yeye pamoja na jeshi lake wakapewa sehemu ya kuishi katika jumba la kifalme hadi pale watakapo kamilisha shida yao.

    Usiku mfalme akaamka na kuanza kufanya maombi kwa miungu ya Nugutu, kama kawaida akanyanyua fimbo yako na  Mvua kali ikaanza kunyesha usiku huo, mwili ukatetemeka mithiri ya mtu aliyepigwa shoti ya umeme kichwa kikamuuma macho yakawa mazito, hatimaye akaona taswira ya mwanamke aliye na kijana mmoja wa kiume ambao uhusiano wao ulionesha dhairi kuwa ni wa mama na mwana. Akaona pia msichana mrembo sana akiwa na ujauzito ambapo alipotazama vizuri aligundua kuwa yule ni mke wa yule kijana, wakati akiendela kutazama yale ghafla wale watu wakaonekana kung'aa zaidi na nyota zikawa zinazunguka. Hapo hapo mfalme akaanguka na usingizi ukamchukua.



    Asubuhi na mapema Mfalme akaamka akakusanya jeshi lake, na kwenda kuitafuta sehemu ile ambayo aliiona usiku wa jana, wakazunguka sana hadi jua lilipokuwa la utosi akaamuru wakae kivulini na kupumzika, Afya ya mfalme ikadhidi kudhoofika kutokana na mizunguko anayoifanya. Akiwa chini ya mti akawa kama anakumbuka kitu kisha akaanza kutabasamu na kusema,

    "Nuru ya Nugutu hii mahala hapa".

    Wanajeshi wakawa wanashangaa na hawakuelewa nini mfalme wao anachomaanisha, ikabidi waongeze umakini kumsikiliza kile anachotaka kusema.

    "Nuru ya Nugutu hii mahala hapa!".

    Akasema tena na kuanza kukohoa kwa nguvu mno wanajeshi wote wakashikwa na tahayaruki wasijue watamsaidia vipi mfalme wao, walivyoangaza huku na huko wakabahatika kuona nyumba iliyo pembezoni kidogo na mto. Hivyo wakambeba mfalme hadi mahali hapo, wakamkuta mwanamke mmoja wa makamo na akashtuka sana kuona jeshi likiwa nyumbani kwake, mfalme akaletwa humo ndani na yule mama akajikuta akitoa machozi pindi macho yake yalipotua kwa mfalme Gaiya.

    "Gaiya! Gaiya....!" yule mwanamke akaita huku machozi yakimtoka.

     Mfalme katika hali ile ya ugonjwa akashindwa kuvumilia machozi naye yakambubujika, yule mwanamke akaendelea kusema,

    "Imekuaje mfalme mtukufu kuja kuanguka nyumbani kwangu?".

    Mfalme hakujibu kitu zaidi ya kukohoa mfululizo, ikabidi yule mama anyanyuke kwa haraka na kuchukua majani flani ambayo akayaponda na kuyachuja kisha akachanganya na maji na kuwaomba walinzi wa mfalme wamnyweshe. Nao wakafanya kama yule mwanamke alivyowaagiza baada ya dakika 3 mfalme akawa sawa kabisa.

    "Ooh! Nunilai sikutegemea kukuta ungali hai, ila kwa nguvu za miungu ya mababu zetu waliolala ardhini leo nimekukuta bukheri wa afya, nimefurahi sana," alisema mfalme.



    Mfalme hakuona sababu ya kuficha chochote walinzi wake, akawaambia kuwa huyo mwanamke ndiye yule aliyemuona usiku uliopita pindi alipokuwa akifanya maombi na kizuri zaidi kabla hajamuoa mke wake wa kwanza alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamama huyo. kutokana na tofauti za kifalme na kitamaduni mwanamke yule alikataliwa na kufukuzwa katika nchi ya Nugutu maisha yake yakawa kigomile, pindi alivyofukuzwa tayari alishakuwa na ujauzito na akajifungua mtoto wa kiume aliyempa jina la Makala, Makala naye alifanikiwa kuoa na mke wake kwa wakati huo alikuwa mjamzito. Hivyo miungu ya Nugutu inamtaka Makala kushika nafasi ya yake.

    Kisha mfalme akakaa faragha mpenzi wa moyo wake, wakaongea mengi huku shauku kuu likiwa juu ya kuona damu yake ambayo hakuiitia machoni toka ilipoingia katika dunia hii. Kwa kua Makala alikuwa muindaji hivyo ikawabidi wasubiri hadi jua lilipozama. Kweli muda ulipowadia mfalme akamuona kijana huyo mwenye afya na nguvu tele akiwa amebeba swala wawili mabegani mwake. Mfalme hakuwa na shaka juu ya kijana yule kwa kuwa alifanana nae kwa kiasi kikubwa.



    *******************



    "Kwa mamlaka niliyopewa na miungu ya Nugutu, namsimika Msongo ambaye ni mtoto wa kwanza wa mfalme Gaiya kuwa mrithi halali wa ufalme wa baba yake"

    Wananchi na baraza zima la wazee wakapiga makofi kuashiria kumpokea kiongozi huyo mpya japo si wote ambao walikubaliana na uteuzi huo wengi waliamini ulikuwa ni kinyume na matakwa ya miungu ya Nugutu.

    Msongo baada ya kurithi kiti cha ufalme, akafukuza wazee wote ambao walikuwa kinyume nae na kuweka wazee wengine katika kila idara,

    "Kuanzia leo maamuzi ya nchi hii yatatolewa na mimi, hakuna tena ibada wala kafara za kishenzi kwa miungu yenu," alisema msongo mbele ya baraza aliloliteua.

    Baraza likainama chini na kusujudu ikiwa ni ishara ya kutoa heshima kwa mfalme msongo. Ndani ya siku chache kila kitu kikabadilika ndani ya Nugutu, wananchi wakalazimishwa kulipa kodi kwa mfalme na aliyeshindwa kufanya hivyo basi hukumu ya kifo ikawa juu yake, taratibu umaarufu wa Nugutu ukaanza kuporomoka wananchi wake wakaanza kukimbia kwenda nchi za jirani.



    Miungu ya Nugutu ikachukizwa sana na vitendo anavyovifanya mfalme Msongo, Viongozi wa Ibada wakaligundua hilo na kumuagiza mzee Bongwa kwenda kutoa taarifa kwa mfalme,

    "Mfalme mtukufu miungu ya Nugutu imekasirika sana juu ya vitendo unavyovifanya, hivyo itakubidi ukaiangukie na kuiomba msamaha la sivyo Nugutu itakuwa si mahali salama pa kuishi mtu," alisema Mzee Bongwa.

    Mfalme akachukizwa mno na taarifa hiyo akaitwa wanajeshi wake na kuamuru mzee huyo afungwe gerezani.







    Baada ya kukaa Kigomile kwa siku kadhaa hatimaye Safari ya mfalme Gaiya kurudi Nugutu ikaanza, akaambata na mtoto wake makala, akimwacha mkewe wa enzi pamoja na mke wa makala nyuma na akihaidi kuja kuwachukua baada ya kufika Nugutu. Mfalme alishajua kilichotokea Nugutu hivyo kuambatana na wale wanawake ingekuwa tatizo zaidi katika kutetea ufalme wa Nugutu usianguke. Njiani nyimbo za kuisifu Nugutu zikatawala wanajeshi wakaonesha mapenzi mazito kwa mfalme wao, lakini waliacha kuimba baada ya kukutana na kundi la wananchi kutoka Nugutu wakikimbia toka nchini mwao. Mfalme Gaiya alisimamisha jeshi lake na wananchi wake wakaeleza kila kilichotokea Nugutu, mfalme alilia sana na kuamuru wapige kambi mahali hapo.

    Taarifa juu ya ujio wa mfalme Gaiya ukafika kwa mfalme Msongo kupitia mashushu ambao wanazunguka huku na kule kutafuta habari nyeti hasa zenye tija kwa Taifa. Kiukweli hakuwa tayari kuachia madaraka, akaamuru jeshi kwa siri liende kummaliza baba yake kabla hajaingia Nugutu.



    Kwa kutumia fimbo yake Mfalme Gaiya akalazimika kujitenga pembeni na kufanya maombi walau apate fununu juu ya kitakachotokea baada ya muda mfupi. kama kawaida mwili ukatetema, kichwa kikamuuma na macho yakawa mazito mno, akaona jeshi la Nugutu likija kwa kasi sana pale walipo, la kuhuzunisha zaidi akaona jinsi wanajeshi wake na wananchi wote wanauwa na hatimaye akabaki yeye pekee na mtoto wake Makala, hata hivyo jeshi likafanikiwa kumuangamiza mfalme Gaiya na Makala. Mfalme baada ya kuona tukio lijalo na ni wazi hawezi kubadili hatima ya lolote aliloliona akahuzunika sana. Bila kuchelewa akamwita Makala na kumkabidhi ile fimbo,

    "Mwanangu toka hapa nahisi mambo yapo shwari hivyo rudi kwa haraka ukamwangalie mama yako na mkeo kisha uje nao Nugutu," alisema Mfalme Gaiya.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mfalme alishaona litakalotokea hivyo akawa anatafuta njia walau ya kumuokoa mwanae ambaye aliamini kabisa kwa kupitia yeye Nugutu itakuwa sehemu nzuri. Akawatazama wananchi kisha akawaamuru waondoke kwa haraka, Makala naye bila kupoteza muda akafanya kama baba yake alivyoamuru, baada ya muda mchache akawa tayari ameshavuka mto, wakati akipandisha mlima akasita na kuangalia alipomuacha baba yake. Hakuamini alichokiona, mpambano mkali kati ya wanajeshi wa baba yake na wale wa Msongo ukawa unalindima, hata ivyo haikichukua muda tayari wanajeshi watiifu wakawa wamemalizwa. Makala akashuhudia kwa mbali baba yake akikatwa kichwa akajikuta anaishiwa nguvu na kukaa chini. Papo hapo ardhi ikatetema, anga likawa jeusi, radi ikapiga na mvua kubwa ikanyesha, upepo mkali ukaanza kuvuma na kuvunja matawi ambayo yakawa yanawaangukia wanajeshi na kuwajeruhi, hali ikazidi kuwa mbaya kwa lile jeshi lililotumwa kumuangamiza mfalme Gaiya.

    Mzee mmoja aliyeambatana na wale wanajeshi waasi akakata kidole chake na kunyunyiza damu yake ardhini, uso wake ukabadilika kukatokea na upepo mkali toka kaskazini na mwingine kusini ukakutana kati na kumgawanya yule mzee vipande viwili kisha upepo ukatulia na hali ikawa shwari.



    Makala alipata kuyashuhudia hayo yote yaliyotokea, mwili wa mfalme ukabebwa na kupakiwa kwenye punda, kisha mzee mwingine akafukiza ubani na akawa kama anahisia kali juu ya kitu fulani, akaangaza pande zote nne za dunia kisha akasema,

    "Kuna wanadamu wameshuhudia kila kilichotokea hapa, ivyo wao kuendelea kuishi itakuwa tatizo kwetu na hata kwa mfalme Msongo, sharti wote waangamizwe".

    Sauti ile ikapaa hadi kufikia masikioni mwa Makala akashtuka na kuwamuuru wananchi wakimbie, yule mzee akatoa kicheko cha ajabu hapo hapo wakatokea ndege wakubwa kuliko kawaida na kuanza kuelekea alipo makala na Kundi Lake. Hawakufika mbali wananchi wakawa wakishambuliwa na ndege wale hadi mauti yalipowashika, sasa akabaki makala pekee akajikuta anakimbia bila mpango, huku ndege wakimfukuza kwa nyuma. Akafika mahali akajikwaa na kuanguka, mbaya zaidi akawa amemuangukia nyoka aina ya kobra ambaye akamuuma Makala mguuni na kumuachia sumu. Hali ikabadirika, mapigo ya moyo yakapunguza kasi, macho yakapunguza uwezo wa kuona na ndege waliokuwa wakimfukuza wakatua alipoanguka Makala.



    ************************



    Huzuni ikatanda katika anga la Nugutu hasa baada ya mfalme Msongo kutangaza kifo cha baba yake, wananchi wakalia na kuomboleza, ikapelekea hadi wengine kujitoa uhai wao. Tumaini la ukombozi juu ya uonevu na ukatili wa mfalme Msongo likafifia mioyoni mwao kila mmoja akajua kuwa maisha yake yapo mikononi mwa mfalme msongo. Ile Nugutu iliyosifika kuwa na ukarimu na upendo wa hali ya juu sasa imegeuka na kuwa Nugutu iliyo jaa chuki, udhalimu na kila aina ya uovu.

    "Mtukufu mfalme nyota yako inaonesha kufifia hivyo bila shaka ufalme wako upo mashakani," Alisema mmoja kati ya waganga wanaoishi katika jumba la kifalme.

    Mfalme Msongo huwa anapenda kujua vikwazo vyake na kuviondoa kabla ya kuleta madhara ila safari hii alihisi kuwa ni tatizo kubwa, akaita waganga na wachawi wote akawaamuru wapige bao ili waone ni kitu gani kinasababisha nyota yake ififie.



    Kafara nzito ikafanyika, waganga wakafanya kila wawezalo kuhakikisha nyota ya mfalme Msongo inarudi katika ubora wake na hakika wakafanikiwa hilo, hivyo mashaka na hofu juu ya utawala wake vikaondoka.

    Mfalme Msongo akawa mkatili zaidi kwa raia wake, chochote alichoitaji toka kwa watu wake basi alikipata, mfalme akawa anadiriki kunyang'anya hadi wake za wananchi wake huku akiamini kuwa kizuri chochote ni lazima kiwe mali ya mfalme.



    ******************



    Ndege walipoona hamna dalili yeyote ya uhai kwa Makala ambaye alishambuliwa na nyoka, wakaondoka na kupotea kabisaa. Masaa mengi yakapita, Giza likaaingia na baridi likawa kali mno, umande ukaanguka na kumfanya Makala aamke pale alipokuwa. Mwili ukawa mzito sana, maumivu yakawa makali lakini hakuwa na namna zaidi ya kujikongoja kutafuta mahali ambapo angeweza kupata msaada, akatembea kwa muda ambao hakuufahamu hatimaye akaona kuna moto umechochewa na kuna watu wameuzunguka. Akajikongoja kwa hatua kadhaa lakini hali yake ikazidi kuwa mbaya akajikuta akianguka, kishindo cha kuanguka kwake kikawashtua wale watu wakiokuwa wakiota moto na kufanya wamsogelee.

    "Aah! Huyu ni Makala mkaza mwana wetu" alisema mzee mmoja.

    Wote waliokuja kumtazama wakahakikisha kuwa ni kweli wanamfahamu, wakambeba kwa haraka na kuanza kumfanyia huduma ya haraka haraka

    "Amepatwa na nini?" kijana mmoja akauliza

    "Mhm inaonesha ameumwa na nyoka mwenye sumu kali, embu niletee kisu change," alijibu Mzee.

    Baada ya sekunde kadhaa kisu kikaletwa mzee akamchanja Makala sehemu aliyoumwa na nyoka kisha akaponda majani flani na kumfunga ile sehemu aliyoumwa. Akachemsha mizizi ya mti uliopo shambani kwake na kumnyweshwa maji yake kisha akamlaza kwenye kitanda cha kamba.



    Baada ya siku kadhaa Makala akarudi katika hali yake ya kawaida akawasimulia wakwe zake kila kilichotokea, wote walimuhurumia sana lakini hawakuacha kumtia nguvu sababu ukombozi wa Nugutu u damuni mwake.

    Makala akarudi nyumbani kwake na kukuta tayari mkewe ameshajifungua mtoto wa kiume ambaye walimpa jina la Mdidi. Makala akaridhia jina hilo na akafanya ibada maalumu ya kumkabidhi mtoto wake chini ya uangalizi wa miungu ya Nugutu. Wakati ibada inaendelea mvua nyepesi iliyoashiria Baraka ikanyesha, Makala akaacha mvua iyo impate mwanae kisha wakarudi ndani.



    "Mama..! Kuna siri nzito juu ya Mdidi, kwa kuwa sijui hatima ya maisha yangu ya baadae, basi ni vyema nikawashirikisha ili sote tujue. Mdidi ndiye nuru na ukombozi wa Nugutu, katika maisha yake adui wake wa kwanza na wa mwisho ni mwanamke hivyo maagizo niliyopewa Mdidi asipewe nafasi ya Kupenda kabla hajafikisha robo karne. kwa hiyo tunamiaka 24 ya kumuongoza na kumlinda asiingie katika Ulimwengu wa huba," alisema Makala.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Kauli iyo ilikuwa kama kisu moyoni mwa mama yake Makala na mkewe, kwani wote waliduwazwa na sharti lile,

    "Eenh tutaweza kweli mwanangu, mboni mtihani huo," alisema mama yake Makala ambaye pia ni bibi yake Mdidi.

    "Ukweli sio rahisi kuwekea ukuta hisia za mtu," mke wa Makala naye akachangia ambaye ndiye mwenye mtoto huyo.

    "Jamani haina ya kufikilia kushindwa vita tusivyopigana, hivyo wote kwa pamoja lazima tuungane na tuhakikishe tunamlinda, kitu kingine Mdidi lazima akue katika Nchi ya Nugutu hili aone maisha halisi ya kule. Hivyo basi kesho sote tutaamia huko, usiulize tutafikia wapi na tutaishi vipi ila mwanetu ni lazima aone manyanyaso na mateso yanayosababishwa na utawala wa Mdogo wangu Msongo,”alisema Makala.



     BAADA YA MIAKA 18



    Maisha ya Nugutu yalibadilika sana, utu haukuepo tena, maamuzi ya mfalme yalikuwa yakikatiri mno. Watu wakawa watumwa ndani ya nchi yao, umaskini ukakithiri mno kila kona watu walikufa kwa njaa.

    “hivi mama tutaendelea kuwa wanyonge mpaka lini, angalia uonevu huu mimi siwezi kuvumilia".

    "Mdidi mwanangu kwa sasa hatuna la kufanya ila ipo siku mungu atatufungilia njia na kuepukana na haya mateso"

    Mama yake mdidi akamjibu mwanae lakini kabla hawajaendelea kuongea mbiu likalia kuashiria wito kwa wanakijiji wote kukusanyika kwa chifu kujua kilichojili.

    "Ndugu zangu wanakijiji tunasikitika kutangaza kifo cha binti Mloka, hivyo wanakijiji wote tutakuwa hapa kwa muda wa siku 3, tukiomboleza na kama ilivyo utaratibu rambi rambi zote lazma zifikie kwangu kwa ajili ya kuiwasilisha kwa mfalme Msongo," alisema Chifu wa eneo hilo.

    "Samahani mkuu, rambirambi itaendaje kwa mfalme wakati mfiwa yu hapa?" Mdidi akauliza.

    "Wewe kijana! Nani aliyekupa mamlaka ya kuhoji?" Chifu akauliza.

    "Sio haki mkuu kama mfiwa yu hapa, basi rambirambi hustahili kumfikia yeye na si mfalme..!"

    Minong’ono ikaanza na mkuu wa kijiji akaamuru askari wa mkamate kijana yule aliyekuwa anapinga agizo la mfalme.

    "Tafadhali chifu mtukufu naomba msamehe kijana wangu, maana hajui alisemalo" mama Mdidi akatoka ili kumtetea mwanae asikamatwe.

    "We mwanamke mfunze mwanao, leo namsamehe ila siku nyingine akirudia lazima akutane na adhabu itakayomfaa" Chifu aliongea kwa sauti kali.

    Mama mdidi akamchukua mwanae na kurudi naye nyumbani kwa haraka.

    "Mdidi mwanangu kwa nini wanitenda hivi, kiburi cha baba yako naona umekirithi wewe, tafadhali mwanangu sitaki kikukute kama kilichomkuta baba yako" mama aliongea huku machozi yakimtoka.

    Mdidi akamkumbatia mama yake kisha akasema

    "Unaweza niambia kilichomsibu baba yangu?".

    "Ndio lakini si sasa," alisema mama.

    "Mama siku moja muindaji alienda kuwinda lakini akapotea njia na kujikuta yupo kati ya msitu wenye miiba na wanyama wakali, Mungu mkubwa wakaotokea waindaji wengine watatu wakipita njia hiyo, yule muindaji wa awali akaomba msaada toka kwao, lakini walikataa kata kata kumsaidia. Je mama unahisi nini kitamkuta yule muindaji aliyekosa msaada?".

    "Mhm! mwanangu lazima atadhurika kwa kuchomwa na miba pia maisha yake yatakuwa matatani kwa kushambuliwa na wanyama wakali".

    "Umejibu vyema mama, hivyo ndivyo ninavyojisikia mimi unavyokataa kuniambia kuhusu baba angu mzee Makala"

    Mama Akainamisha kichwa chini na kufikiri kwa muda mrefu, kisha akamtazama mwanaye, akakohoa kidogo na kusema,

    "Baba yako alikuwa ni shupavu na mwenye ujasiri wa kupinga mabaya yanayofanywa na mfalme Msongo, nadhani unakumbuka vizuri ulikuwa na wadogo zako wawili, ambao wote hatupo nao duniani. Vifo vyao vilikuwa vya kutatanisha sana, desturi unayoiona leo ya msiba kuwa kwa chifu ilianza kitambo sana. Pindi msiba wa mdogo wako ulivyotokea basi mimi na baba yako wote tukaamia kwa chifu na kipindi chote cha matanga tulilazimika kuulisha umati wote kwa chakula kizuri. Chakula cha chifu kilikuwa ni nyama tuu, baba yako akalazimika kwenda mwituni kuwinda lakini kwa siku hiyo hakufanikiwa hivyo chifu na wazee wengine wakakosa nyama ya kula, chifu alikasirika sana na kuondoka siku hiyo hiyo"



    Hadi kufika hapo machozi yalizidi kumtoka mama Mdidi, mwanaye akamkumbatia kwa nguvu mama yake na kumtuliza, mama akashusha pumzi kisha akaendelea na simulizi.

    "Tulivyoamka siku iliyofata, mdogo wako aliyebakia nae akawa ameaga dunia, tuliumia sana tukapeleka taarifa kwa chifu, lakini chifu alicheka na kutuambia kuwa ile ni adhabu ya kutowapa nyama siku ya mwisho ya msiba. Baba yako roho ilimuuma mno uvumilivu ukamshinda akaenda kupiga mbiu ya dhalura na wanakijiji wote wakakusanyika.



    "Yatosha sasa, mpaka lini tutaendelea kuwa watumwa katika ardhi ya kwetu wenyewe, nilifikiri ni kipindi cha kupeana faraja hasa baada ya kuondokewa na mwanangu mpendwa lakini imekuwa ndivyo sivyo, nimelazimika kuingia mwituni kutafuta kitoweo kwa ajili ya chifu na wazee. siku moja tuu bahati haikuwa upande wangu leo nimeadhibiwa kwa kuondokewa na mwanangu mwingine, hii si haki, tuamke na tutee haki zetu”. baba yako alisema hayo kwa uchungu mkubwa lakini hamna hata mmoja aliyemuunga mkono, kila mmoja akaenda upande wake. Tulimzika mdogo wako tukiwa wawili, baada yapo tukakataa mila zote za Nugutu, tukawa tunafuata njia na miiko ile ya babu yako........"

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mama kufika hapo akasita kidogo kutaja jina la babu yake Mdidi, akafikiri tena kisha akanywa maji kulegeza koo lake na akaendelea na simulizi,

    "Baba yako akawa mstari wa mbele kupinga zile mila kandamizi lakini kilichokuja mkuta mwanangu ni mauti, baba yako aliuawa kinyama na kiabu sana. Mfalme Msongo aliamuru baba yako akamatwe na kuuwawa kwa kukatwa kiungo kimoja kimoja mbele ya wananchi wote, hivyo mwanangu sitaki na wewe yakukute hayo".

    Mama akamaliza kumuelezea kijana wake, Mdidi akamuhurumia sana mama yake, hakuyashuhudia hayo sababu alikuwa mdogo mno. Wazazi wake walijitahidi kumficha ili asijekudhurika.

    "Mama nakuahidi sitofanya tofauti na mapenzi yako, lakini sitoweza kuvumilia haya yote, nitapambana kwa ajili ya baba yangu, wadogo zangu na watu wote wa Nugutu," alisema Mdidi.

    "Mwanangu bado kitambo kidogo tuu kila kitu kitakuwa sawa".



    ***************************



    Siku zikapita hatimaye msimu wa kukusanya vijana na kuwaingiza katika jeshi la Nugutu ukafika, Mdidi akawa mmoja kati ya vijana waliotakiwa kwenda mafunzoni kwa ajili ya kulitumikia taifa lao.

    "Mwanangu jambo moja nakusihi jitunze sana na kamwe usiruhusu mwanamke yeyote auteke moyo wako".

     Hayo yalikuwa maneno ya mwisho toka kwa mama kabla ya mdidi kuelekea kwenye mafunzo ya kijeshi.

    “Sawa mama, nitayazingatia yote uliyoniambia, nakuahidi nitakuwa mwanajeshi mwema na mwenye kufata haki,” alisema Mdidi na Kuondoka.



    Miezi 6 ikapita, vijana wakawa tayari kabisa kwa ajili ya kula kiapo cha utiifu kwa mfalme na milki yote ya Nugutu, nyota ya mdidi ikawa inang'aa sana, akawa wa kwanza kwa kila jambo swala lililowafanya wenzie wamuonee kijicho. Mdidi akawa na nguvu za ajabu zilizomchanganya hata yeye mwenyewe, hakuwa anajitambua kuwa yeye ni mtu wa aina gani hasa, ikafika kipindi mdidi akawa anauwezo wa kutembea hewani pasipo kuanguka, mabadiliko yale yalimtisha sana lakini ikabaki kuwa siri ya moyo wake.



    Jeshi jipya likapewa jaribio la kuvamia kijiji kimoja kilichopo nchi ya jirani na kuteketeza kila watakachokikuta, wote wakatii amri na kuelekea walipoamriwa. Walipofika bila kuuliza wakaanza kuteketeza kila kitu, Mdidi alichukizwa na hiko kitendo cha kuua watu wasio na hatia, akasimama katikati na kuwazuia wenzie wasifanye ukatili huo. Kwa wenzie hiyo ilikuwa ni kama nafasi waliyoitafuta kwa muda mrefu, kabla hajafanya kitu tayari mishale isiyo na idadi ikatua mwilini mwake, akarudi nyuma kwa kuyumba yumba na akaanguka na kutumbukia mtoni.







    Mkondo wa maji ukamchukua na kumtupa kando ya mto, kwa bahati nzuri siku hiyo ilikuwa siku ya wasichana wa kijiji hiko kwenda mtoni na kufanya shughuli zao, baadhi ya wasichana wakamuona na kumpa taarifa mtoto wa chifu wa sehemu hiyo. Wakamsogelea baada ya kumchunguza wakagundua bado anapumua japo kwa mbali, kwa kuwa ilikuwa ni kosa la jinai kwa mwanaume yeyote wa sehemu hiyo kuonana na wasichana wanapokuwa mtoni. kwa kutambua hilo ikabidi binti chifu afanye kila liwezekanalo kuokoa maisha ya Mdidi japo hakuwa anamfahamu, akaamuru walinzi wake ambao nao ni wakike wampeleke kwenye nyumba yao iliyopo juu ya mlima nao wakafanya hivyo. Binti Chifu akatengeneza dawa kwa kutumia majani, magome na mizizi na kumnywesha, pia akachemsha majani mengine na kumkanda mwili wote, kwa muda wa siku 3 kazi ilikuwa hiyo tuu.



    Siku ya 4 mdidi akarejewa na fahamu na kujikuta katika mazingira mageni kabisa, akataka kuinuka lakini mwili ukakataa. Baada ya muda mfupi akaingia msichana ambaye alipomuona Mdidi ameamka akatoka nje kwa haraka na kupiga ukunga,

    "Dada! Mgonjwa ameamka...!"

    Haukupita muda mrefu yule msichana akawa ameingia na yule aliyemuita dada yake, wakasogea hadi alipolala Mdidi,

    "Nini kimenikuta na hapa nipo wapi?" Mdidi akauliza

    "Tulikuokota mtoni, ukiwa na hali mbaya sana, hivyo tukakusaidia na kukuleta hapa".

    "Nyie ni akina nani?”

    "Mimi ni mtoto wa chifu Mzovu, na huyu ni kijakazi wangu, tumekukuta na majeraha mengi sana, tuambie nini kilichokusibu?".



    Mdidi akavuta kumbukumbu juu ya kilichomkuta, kichwa kikaanza kumuuma sana, akaugulia maumivu kwa kukishika kichwa chake. Walivyoona Mdidi yupo katika hali ile wakaamua wamuache apumzike kisha wakaondoka na kuahidi kurudi jioni.

    Baada ya muda kichwa kikaacha kumuuma na Mdidi akapitiwa na usingizi, wakati yupo ndotoni akawa anasikia sauti ikimwambia,

    "Jitahidi safari bado kidogo...!"



    Hakuelewa sauti ile inamaana gani akaja kushtushwa na binti chifu ambaye alimletea chakula, akakipokea na kuanza kula maana alihisi njaa sana. Baada ya chakula binti chifu akamtaka Mdidi anyanyuke walau afanye mazoezi ya kutembea na kuweka mwili katika hali ya kawaida, kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kusimama peke yake ikabidi binti chifu amsaidie kusimama. Viganja vya mwanadada yule vikatua juu ya mwili, na hapo akaanza kupata hali ya tofauti ambayo hakuwai kusikia toka azaliwe. Mdidi akashtuka mno nakumsukuma binti chifu pembeni.

    "Umekutwa na nini wewe?" Binti chifu akauliza.

    "Nashukuru kwa msaada wako, ila tafadhali usinikaribie," alisema Mdidi.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kumbukumbu ya maneno aliyoambiwa na mama yake ya kutoruhusu kukaribiwa na mwanamke ikamjia kichwani mwake. Kauli ile ikamfanya binti chifu acheke mno,

    "Kama ningekuwa na nia ovu usingekuwa hai muda huu, nimeanza kuugusa mwili wako na kuutibu ukiwa hujitambui leo ndo unajifanya kukataa nisikuguse," alisema Binti chifu.

    "Siwezi kukaa tena hapa lazima niondoke jioni hii," alisema Mdidi.

    Akachukua fimbo na kujikongoja kutafuta njia ya kuondokea, lakini kabla hajafika mbali akahisi kuishiwa nguvu na kifua kumbana, mwili ukakataa kwenda mbele wala kurudi nyuma akaanza kuyumba kama mlevi. binti chifu alivyoona hivyo ikabidi akimbie na kumshika asianguke, mapigo ya moyo yakaenda kwa kasi mno, binti chifu akaita walinzi wake wakasaidiana kumbeba na kumuingiza kwenye ile nyumba akachemsha maji kisha akaanza kumkanda. Kadri alivyokuwa karibu na kijana yule ndivyo hisia kali za upendo zilivyozidi kukomaa juu yake, wakati huo mdidi akiwa hana wazo lolote juu ya mambo hayo.

    Mdidi akafumbua macho na kukuta yule binti akimkanda alipomtazama machoni akaona kitu ambacho mara nyingi hata kwa mama yake anakiona, ule upendo ambao mama yake alikuwa akimuonesha ndio huo ambao huyo binti anamuonesha, ukweli akachanganyikiwa mno,

    "Kwanini mama amenizuia nisiwe karibu na wasichana, amesema kuwa adui yangu wa mwisho ni mwanamke, mboni sioni ubaya wowote machoni pake au kuna kitu kingine ambacho mimi sikifahamu?" mdidi alijiuliza lakini asipate jibu.



    ***********************



    Siku zikazidi kwenda hatimaye afya ya Mdidi ikarudi katika hali yake ya kawaida, akatamani kurudi alipo mama yake, akaamua amuage binti chifu kuwa anaondoka

    "Unaondoka bila hata kuuliza jina langu? Mbona umekuwa mgumu kuelewa, yote niliyoyafanya kwako leo unataka kuondoka na kuniacha hivi hivi" binti chifu akashusha maswali mfulilizo kwa mdidi ambaye alikuwa hajui ajibu nini au afanye nini kwa mwanadada yule.

    "Samahani binti chifu!"

    "Sio binti chifu jina langu ni Nkalo".

    "Mimi sijui nikwambie nini au nikulipe nini uridhike, nahisi sina cha kukupa kitakachofanana na wema wako"

    "Mdidi tafadhali nioe, nyumbani nimeandaliwa mwanaume wa kunioa lakini moyo wangu haupo kwake".

    Kauli hiyo ilikuwa kama shoti ya umeme kwa mdidi kwani mlishtusha na ikamduwaza sana asijue nini la kumjibu,

    "Sema kitu mdidi, naitaji uwe mume wangu tafadhali"

    Mapigo ya moyo yakawa yanaenda kasi sana hakuwai kufikilia kitu hicho katika maisha yake na kila alipokumbuka kauli ya mama yake akajikuta haelewi nini afanye, ni kweli Nkalo amemsaidia hadi kuwa katika hali aliyokuwa nayo lakini swala la kumuoa kwake lilikuwa gumu zaidi ya msaada aliopewa.

    "Nkalo kuna vitu ambavyo nahitaji kuvipatia majibu, kabla sijaamua swala lolote kuhusiana na wewe, tafadhali nipe muda"

    "Hapana mdidi niahidi kwanza kwa vyovyote itakavyokuwa utanioa", Nkalo akazidi kusisitiza.

    "Samahani Nkalo siwezi kukuahidi chochote" mdidi akajibu na kuanza kuondoka.

    "Mdidi! Mdidi..............." Nkalo akaita.



    Mdidi hakutaka kugeuka, roho ilimuuma ila akawa hana namna ya kufanya, Nkalo akazidi kumuita tena na tena, lakini hakuitika wala kugeuka nyuma, akaendelea na safari huku chozi likimtoka kwa mara ya kwanza ameshindwa kulipa fadhila. Mdidi alizunguka lakini asione njia itakayomuwezesha kufika kwao kadiri alivyo zidi kusonga mbele ndivyo msitu ulivyozidi kuwa mnene, akafika mahali ikamlazimu akae na kutafakari mara mbili, wakati akiendelea kutafakari hayo, kundi la watu waliobeba silaha za jadi wakamzingira,

    "Wewe ni nani na unataka nini katika milki yetu?".

    "Jamani nimepotea njia mimi ni mtu wa Nugutu nahitaji kurudi kwetu," alijibu Mdidi huku akiwa na wasiwasi.

    Walivyosikia ni mtu wa Nugutu wakatengeneza mistari miwili na kufanya kitu kama njia akatokea mzee moja mwenye umri kati ya miaka 80 na 90, akamtazama vizuri mdidi kisha akapiga magoti na kusujudu na wale wengine wakafanya kama alivyofanya yule mzee.

    "Uishi milele eenh mfalme mtukufu...!".

    "Uishi milele eenh mfalme mtukufu"

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakarudia maneno yale mara 7 kisha ngoma zikapigwa na nyimbo za shangwe zikaimbwa, Mdidi akabebwa juu juu na kufikishwa kwenye kijiji kimoja ambacho kilikuwa na watu wachache, wakamkalisha kwenye kiti chenye enzi, yule mzee akamkabidhi fimbo kisha wanakijiji wote wakainama na kumsujudia.

    "Uishi miaka mingi eenh mfalme, uishi miaka mingi eenh mfalme"

    Wakarudia maneno hayo mara 14 kisha ngoma zikapigwa na nyimbo zikaimbwa, wakati hayo yote yanaendela Mdidi alihisi kama vile anaota, hakuelewa nini maana ya yale yote.

    "Tumeiona nyota ya mfalme Gaiya machoni pako, wewe ndiye mrithi wa ufalme wa Nugutu...."





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog