Simulizi : Ufalme Wa Nugutu
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mama kuna jambo nataka kukwambia ambalo toka nikanyage ardhi hii sijamwambia yeyote”.
Mama akamtazama Mdidi kisha akamwambia
“Sema tu mwanangu usiwe na hofu”,
“Kiukweli mimi sina muda wa kuendelea kuishi hapa, shida yangu kubwa ni kufika katika milima ya Madora”.
“Mdidi hamna mtu anayeweza kufika mlima Madora na akarudi akiwa hai”
Mama alipotamka ile kauli Mdidi akakumbuka kauli ile ya wawindaji wenzio kuwa,
“Hamna anayeweza kwenda njia ya kaskazini na akarudi akiwa hai”
Hapo akili yake ikafunguka na akahisi uwenda upande wa kaskazini ndipo ilipo milima ya Madora, lakini kwa nini haionekani kama kweli milima hiyo ipo upande huo wa kaskazini, Wakati akifikiri hayo mama akaendelea kumwambia.
“Milima ya Madora inahifadhi hazina ya ufalme mkubwa humu duniani nao ni ufalme wa Nugutu, wengi wamejaribu kwenda huko lakini hamna aliyerudi akiwa hai”
“Mama nataka niende huko nikajue kwa nini watu walioenda huko hawajarudi?”
“Mhmhm! Mdidi kwa nini utake kuhatarisha maisha yako? Hata ivyo milima hiyo japo ipo karibu sana na hapa lakini kwa macho ya kawaida huwezi kuiona”.
“Mama! Tafadhali nisaidie nifike huko naahidi kuja kukwambia kila kitu nitakaporudi”
“Kwa kuwa umesisitiza, nitakusaidia ila itabidi ulale na ikifika saa nane kamili (8:00) usiku uamke nikuoneshe jambo”.
Mdidi akakubali na baada ya kula akaoneshwa chumba na kuingia kulala, ukweli usingizi haukuja kila alipojaribu kulala, akawaza vitu vingi mno mara akasikia mlango unagongwa akaamka na kufungua akakuta ni mama yake na Batuli, akimuashiria watoke nje ya nyumba. Mdidi akafanya hivyo, Mama akamwambia
“Fumba macho uso wako uelekee upande wa kaskazini”
Ajabu alichokiona pindi alipoelekeza uso wake upande ule wa kaskazini. Akaona taswira nzuri ya Mlima ukiwa unang’aa sana katika kila pande. Mdidi akafumbua macho na kutazama upande ule ule lakini hakuona kitu, alipofumba macho yake ndipo alipoweza kuuona tena mlima ule.
“Haya sasa mwanangu turudi ndani,” alisema mama Batuli.
Wakaingia ndani na mama akaendelea kumpa habari zaidi kuhusu mlima ule.
“Hayo ndiyo maajabu ya mlima ule uwezi kuuona kwa kutazama kawaida, vile vinavyong’aa inasemekana ni madini yenye utajiri mkubwa na wengi walitamani kuupata utajiri huo lakini wakaishia kufa, unatakiwa uanze safari yako kesho wakati wa jua la utosi inasemekana muda huo walinzi wa mlima ule wanakuwa wamelala”
Mdidi aliyashika yote aliyoambiwa na mama yake Batuli, akarudi chumbani na usingizi ukamchukua.
Asubuhi na mapema, akaamka baada ya kupata kifungua kinywa akarejea kwa Ngoo, hakuona busara kumficha juu ya safari yake ikabidi amuelezee kinaga ubaga japo Ngoo hakuonesha kufurahia safari ile kwa kuwa alijua ni wazi asingeweza kurudi akiwa hai, lakini akawa hana namna ya kufanya ikabidi akubaliane na maamuzi ya Mdidi.
************
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Safari ya kuelekea katika Milima ya Madora ikaanza, alitembea mno hatimaye akafika kwenye ile njia panda na akaanza kuifata njia ya kaskazini kama alivyoelezwa na mama yake Batuli. Njia hiyo ilikuwa kimya hakusikia sauti ya kiumbe chochote zaidi ya miti iliyokuwa ikitikiswa kwa upepo.
Akaendelea na safari hatimaye akafika sehemu ambayo kila akitaka kwenda mbele anazuiwa ikabidi atoe ramani yake na kuiangalia, akaisoma akagundua sehemu alipo kuna lango kuu litakalomuwezesha yeye kuingia sasa katika mlima mtukufu wa Madora, akafumba macho na kuona njia akaifata hadi akaingia ndani zaidi, wakati yupo ndani akasikia sauti kali za kuogofya pia akahisi kama kuna watu wanamkaribia akataka kufumbua macho lakini akakumbuka kauli ya mama yake Batuli,
“Uwezi kuona njia kwa kutazama kawaida, lazima ufumbe macho na usonge mbele”
Hakufungua macho akaendelea kuifata njia ile hadi akatokea sehemu moja ambayo kukawa na pango kubwa alipofika hapo hakuweza kuona tena mbele, ikabidi afungue macho yake, akashawishika kutazama nyuma alipotokea, alivyogeuza tuu shingo yake akashtushwa na kile alichoshuudia, akahisi miguu inakosa nguvu akatamani kukimbia japo hakuelewa akimbilie upande gani.
Mafuvu ya watu yalikuwa yametapakaa kila kona, akaamini yale maneno aliyokuwa akiambiwa kuwa hamna aliyefika kwenye mlima Madora na kurudi akiwa hai. Akajipa moyo na kuwa tayari kupambana na lolote litakalo tokea, akaendelea kupiga hatua kulifata lile pango kabla hajafika ikatokea midudu ya ajabu ikawa inakuja kwa kasi kumuelekea ikabidi achomoe jambia lake tayari kwa kupambana nayo, alivyolinyoosha lile jambia mwanga mkali ukatoka na ndani ya dakika ile midudu ikapotea, Mdidi akabaki kulishangaa jambia lake.
Akaendelea na kuingia ndani zaidi hapo akatoa ramani na kuitazma akagundua kuwa aliitajika kukaa kwenye kigoda kilichopo mbele kidogo na aliposimama, kwa tahadhari kubwa akasogea, alipojiridhisha akakaa katika kile kigoda, ghafla majani yakaota na mizizi kumzonga kisha ikamfunika kabisa na kumzamisha ardhini.
Wakati hayo yanaendelea kwa Mdidi, Jeshi la Nugutu likafika na kuzunguka eneo hilo, baada ya kuchunguza kwa muda, askari akasogea mbele ya wenzie na kusema,
“Hamna dalili ya kuwepo kwa mtu yeyote au kitu chochote hapa”.
Mzee mmoja aliyeambatana nao akasogea na kuiangalia sehemu hiyo kwa umakini kisha akageuka na kuwatazama maaskari,
“Anayestahili tayari amefika eneo hili ondokeni hapa mpo hatarini”
Hamna aliyemuelewa nini mzee Yule anamaanisha, wengi wakajawa na maswali lukuki yaliyokosa majibu.
“Maisha yenu yapo hatarini kimbieni”
Mzee Yule akapaza sauti iliyowashtua wanajeshi wale lakini kabla hawajaenda popote ile midudu ya ajabu ikatokea na kuanza kuwashambulia, hakuna aliyeweza kujitetea kila mmoja akajikuta akikimbia bila mpangilio. Ndani ya muda mfupi jeshi lote likateketea na kubaki mifupa.
*****************
Wiki ikapita bila ya Mdidi kurejea kijijini kila mmoja akaamini kuwa uenda amefariki, huzuni na simanzi vikamkuta Batuli na mama yake bila kumsahau Ngoo nae, wote wakaamua kufanya ibada ya kumuombea apumzike kwa amani kama ilivyo tamaduni ya jamii nyingi za kiafrika, wakachukua shuka alilojifunika kabla ya kuondoka na kuamua kwenda kulizika, ilikuwa yapata saa 6 mchana ghafla hali ikabadilika upepo mkali ukavuma, wingu zito likatanda na jua likafifia, kiza kinene kikatokea, kijiji kizima kikajawa na tahayaruki hasa baada ya kutazama upande wa kaskazini ambapo milima ya Madora ipo.
Mlima ukaonekana uking’aa zaidi jambo ambalo si lakawaida kuwahi kutokea, kila mtu akaacha shughuli aliyekuwa akiifanya moto mkubwa ukazuka, ajabu moto ule haukuweza teketeza chochote, kila kitu kilionekana kuwa kama kilivyokuwa awali katika mlima. Ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi likautikisa mlima ule hatimaye mvua kubwa ikanyesha na kusafisha anga lote. Baada ya kitambo kidogo mvua ikakata na milima ya Madora ikawa inaonekana vizuri tena bila hata ya kutumia macho ya ndani, wazee wenye kujua siri ya mlima huo wakakusanyika na kuwaondoa hofu wanakijiji ambao wengi walishikwa na tahayaruki.
“Hazina iliyohifadhia kwa miaka mingi imeenda kwa mtu sahihi na mtu huyo amevunja lile tabaka la kutouona mlima na kuweka tabaka jipya ambalo linatuwezesha wote kuuona mlima wa Madora na milima mingine iliyo jirani, sasa tutaweza kuitumia njia ya kaskazini bila ya kuwa na hofu yeyote”
Wanakijiji wakafurahishwa na taarifa hiyo ingawa hakuna aliyejua ni nani hasa aliyekuwa mrithi wa hazina ile iliyoifaziwa kwa miaka mingi.
**************
Mdidi akarejea kijijini huku akiwa na muonekano tofauti na alivyokuwa awali, safari hii alionekana mwenye kujiamini zaidi hata kwa hatua moja aliyoipiga, Mama Batuli alifurahi mno kumuona Mdidi akiwa salama.
“Siamini kama umerejea ukiwa hai!”
Lakini kabla hajasema lolote wazee wakijiji kile wakawa wamefika na walipomuona Mdidi wakainamisha vichwa vyao kutoa heshima zao.
“Uishi miaka mingi eenh! Mfalme wa Nugutu”
Kauli iyo ikamchanganya Mdidi na hata mama Batuli,
“Yawezekanaje haya! Wewe kuwa mfalme?” mama Batuli akauliza.
“Tumefatilia nyota yake na ikatuelekeza hapa na huyu ndio sababu ya yote yaliyotokea ile siku katika milima ya Madora na yeye ndiye mrithi halali wa Ufalme wa Nugutu”
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ndani ya dakika chache wanakijiji wakawa wamekusanyika na wote kwa pamoja wakainamisha vichwa vyao wakisema;
“Uishi miaka mingi eenh mfalme”
“Hapana mimi sistahili kunyenyekewa hivyo inukeni!” alisema Mdidi na wote wakatii.
“Tuambie lolote eenh mfalme nasi tutalitimiza”
Mdidi akajawa na hofu, hakufikiria kuwa anaweza kuonekana watofauti hata watu kumpa heshima kubwa vile baada ya kutoka katika mlima uliokuwa na hazina ya Nugutu.
“Ndugu zangu wakati umefika sasa wa mimi kurejea kule nilipotokea”
“Andamana nasi eenh Mfalme, usituache upweke hapa, tupo radhi kukutumikia na kutimiza yale yote utakayotuamuru,” akasema mzee mmoja kwa niaba ya wanakijiji wote.
“Bado ninajukumu kubwa la kuokoa watu ambao wanateseka kwa muda mrefu sasa, nahidi kurejea pindi ntakapomaliza kazi yangu”.
Wanakijiji wote wakainama na kusema kwa sauti moja iliyojaa unyenyekevu na utii,
“Uishi miaka mingi ee mfalme”.
Safari ya kwenda kigomile ikaanza huku akiwa ameambatana na Batuli pamoja na mama yake,
“Natamani sana kumuona binti yangu Nkalo, na sijui itakuaje macho yabgu yatakapotua kwa chifu Mzovu” mama akajikuta akiongea mfululizo pasipo kuwa na majibu sahihi.
“Batuli mwanangu hivi karibuni utakutana na dada yako pamoja na baba yako” mama alionekana akiwa na shahuku kubwa sana ya kumuona binti yake pamoja na mumewe chifu Mzovu japo wengi waliamini mama huyo amekwishafariki.
******************
Wakafika kigomile na wakakuta hali yenye utata, wanajeshi wa mfalme Msongo walitapakaa kila kona na ukaguzi ukawa mkali kwa kila anayetoka na kuingia kigomile. Ikabidi wasimame ili kutafuta namna ya kuingia Kigomile. Mdidi akaamua kuwatanguliza Batuli na mama yake alafu yeye atatumia njia nyingine kuingia kigomile.
Batuli na mama yake wakafika sehemu ya ukaguzi, wale walinzi walipomuona Batuli wote wakazani kuwa ni Nkalo wakampisha sababu walijua ni mtoto wa chifu Mzovu,
“Umemtoa wapi huyu mama na ni muda gani ulitoka Kigomile?” askari mmoja akaauliza,
“Wee! Acha kupoteza muda msindikize hakikisha anaingia hadi nyumbani ndio urudi hapa”
“Sawa mkuu”.
Batuli na mama yake wakasindikizwa hadi mlangoni kwa chifu Mzovu, mlango ukagongwa na kijakazi wa ndani akafungua, alipomuona Batuli akashtuka sana, hadi wale maaskari waliowasindikiza wakahisi hali ya utofauti.
“Vipi binti kuna tatizo?” askari akauliza.
“ha-pa-naa’ akajibu kwa kusitasita.
“Haya sisi twaenda”
“Karibuni”
Kijakazi aliwakaribisha Batuli na mama yake ndani, na wakati huo chifu mzovu akawa anakuja sehemu hiyo, moyo wake ulilipuka mno, hasa alipomuona mkewe na kipenzi chake cha enzi Tuwapime,
“Tuwapime! Ni wewe kweeli!?”
“Ni mimi Mzovu”
Mzovu akamkimbilia na kumkumbatia Kipenzi chake, wakati anamkumbatia macho yake yakatua moja kwa moja kwa Batuli, wala hakupata shida kumtambua sababu alifanana kila kitu na dada yake Nkalo.
“Batuli mwanangu!”
“Baba!”
Wote wakakumbatiana kwa pamoja machozi ya furaha yakatiririka mashavuni mwao,
“Yuko wapi Nkalo wangu?” mama akauliza, baba akawa anasita kujibu.
“Mboni unambii alipo binti yangu!”
Chifu akavuta pumzi ndefu kisha akamwambia.
“Nkalo kwa sasa yupo Nugutu, na hivi karibuni ndoa yake na mtoto wa mfalme wa Nugutu itafungwa!”.
“Sasa kwanini umemwacha aende peke yake?”
“Nkalo mapenzi yake yapo kwa mtu mwingine na kwenda kule ni sababu amelazimishwa na kama atakataa maisha ya watu wote wakigomile yatakuwa hatarini ndio maana ukaona ulinzi mkali kuzunguka eneo lote hili” mama akakumbuka swali ambalo walinzi walimuuliza Batuli, moyo wake ukajawa na huzuni kuu.
“Niambie mliwezaje kufika hapa baada ya miaka mingi kupita”,
“Mdidi…”
Kabla hajamalizia sentesi yake nje kukasikika kishindo kikubwa na wote wakatoka nje kushuhudia ni nini kimetokea. Kila mmoja alistaajabu kumuona Mdidi akipambana na kuwateketeza maaskari waliokuwa wakiilinda Kigomile, kadri alivyozidi kuwaua ndivyo mwili wake na jambia vilivyozidi kung’aa.
“Mhmh! Huyu si binadamu wa kawaida” Chifu Mzovu akasema,
“Yeye ndiye aliyetusaidia hadi sisi kufika hapa”
Chifu akashangaa mno kusikia vile. Jeshi likazidi kuongeeka kupambana na Mdidi, Mdidi akachoma jambia ardhini apo apo kimbunga kikali kikazunga kikawazungusha wanajeshi wote, kisha akachomoa jambia na kulishika wanajeshi wote wakamuinamia.
“Tuamuru lolote nasi tutalifanya” wanajeshi wote kwa sauti moja wakasema, hasira za Mdidi zikatulia na kule kung’aa kukaisha,
“Tuishi kwa amani na kwa kupendana, si vizuri kuangamiza watu wasio na hatia”
“Sisi ni wanajeshi watiifu toka Nugutu, tunafata agizo la Mfalme Msongo”
“Kuanzia sasa mtasikiliza maagizo yangu” wote kwa pamoja wakasema.
“Uishi miaka mingi”.
Mdidi akafanikiwa kurejesha amani iliyopotea katika milki ile ya Kigomile. Chifu Mzovu akamshukuru sana Mdidi,
“Nimeamini kuwa kweli wewe ni mrithi wa ufalme wa Nugutu”.
Mdidi akamuinamia chifu kisha akamuuliza
“Yuko wapi mama yangu?”
“Nasikitika kukwambia kuwa mama yako ametekwa na Yule msichana mliokuwa mkiishi naye ni mtu mbaya sana”
“Wamempeleka wapi mama yangu?”
“Yupo Nugutu”.
Mdidi alipopata taarifa ile hakutaka kusubiri akageuka na kuanza safari ya Nugutu lakini kabla hajafika mbali Chifu akamuita na kumwambia,
“Si mama yako pekee aliyekuwa huko hata Nkalo pia, Na ndani ya siku hizi chache Nkalo atalazimika aolewe na mtoto wa Mfalme Msongo”.
“Sawa acha niende”
“Tafadhali andamana nasi!” ilikua kauli ya wale wanajeshi
“Hii ni vita yangu nyie tulieni tu,” Mdidi aliwatazama na kuwaambia.
“Tafadhali turuhusu tuambatane nawe kuna familia zetu kule zinazoteseka na ukatili wa Mfalme Msongo”
Safari ya kwenda Nugutu ikaanza, Mdidi akiwa na wanajeshi ambao wakajifanya kama wamemteka nyara, wakafika katika lango kuu la kuingilia Nugutu na taarifa zikamfikia mfalme Msongo ambaye alifurahi sana kuona adui yake yu mikononi mwake.
Mdidi alifikishwa mbele ya baraza la viongozi wa Nugutu,
“Muonekano wake ni kama mfalme Gaiya” akasema mzee moja.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wengine wakamuunga mkono, Mdidi kwa asilimia kubwa amerandana sana na Mfalme Gaiya kipindi alivyokuwa kijana na hata uzee wake.
“Kesho kabla ya ndoa ya kijana wangu, nitamchinja huyu aliyenisumbua kwa muda mrefu na baada ya ndoa nitamkabidhi mwanangu ufalme wa nchi tukufu ya Nugutu, mpelekeni kizuizini”.
Maaskari wakampeleka kizuini ambapo Mdidi shida yake kubwa ni kuonana na mama yake, kabla hajafikishwa kizuizini njiani akakutana na Balanoga, wakatazamana kwa muda kisha Mdidi akafungua kinywa chake na kusema,
“Nilikukabidhi mama yangu umtunze, yuko wapi?”
Balanoga akaangua kicheko na kumpiga kofi mdidi,
“Sikuwahi kufikiria kuwa utakamtika kirahisi hivi, na kesho kabla hujafa nitahakikisha unashuhudia kifo cha mama yako na mwanamke umpendaye kuolewa na mwanaume mwingine”
Hasira na uchungu mzito vikamshika Mdidi akanza kubadirika ila akajitahidi kujizuia sababu kama angeziruhusu hasira zijae basi angeharibu mpango mzima.
“Kabla ya kifo cha mama yangu na ndoa ya Nkalo, tafadhali nikutanishe nao japo kwa dakika chache” Balanoga aliamini kuwa Mdidi hana tena nguvu zile alizokuwa nazo awali,
“Sawa ombi lako limekubaliwa”, akawaamuru maaskari wamfate huku wakiwa wameshika Mdidi.
Mdidi machozi yakamtoka alivyomuona mama yake akiwa katika hali mbaya vile, mama akainuka na kumpiga kofi mwanae
“Nani alokwambia uje huku ungeniacha nife”
“Siwezi kuishi bila ya wewe mama, kama kufa tutakufa wote” wakakumbatiana huku mama machozi yakimtoka mno, mdidi akamnong’oneza mama yake jambo Fulani.
“Haya inatosha twende ukamuone huyo kinyago wako”
Balanoga akasema, na wakatoka kuelekea kwenye nyumba iliyo pembezoni kidogo mwa eneo la mfalme Msongo, mlango ukafunguliwa na akaonana na Nkalo uso kwa uso, Nkalo hakuamini alipomuona Mdidi, machozi yakamtoka akashindwa kuongea jambo.
“Tafadhali naomba uondoke hapa” Nkalo akasema,
“Eenh! Umeona hata mwanamke uliyedai unampenda leo hataki kukuona, Mpelekeni kizuizini sasa hasubiri hukumu yake kesho,” Balanoga akasema na Maaskari wakatii.
******************
Hayawi hayawi sasa yamekuwa siku iliyosubiliwa na wengi ikawadia, kila mmoja akawa eneo lake kusubilia kile kitakachokwenda kutokea.
“ndugu wananchi wa Nugutu leo tutaenda kushuhudia matukio manne muhimu, tukio la kwanza ni kifo cha mwanamke aliyezaa mtoto ambaye kwa namna moja au nyingine alitishia furaha ya mfalme wetu Msongo, tukio la pili ni harusi ya Lukoha bin Msongo na Nkalo bin mzovu, tukio la tatu ni kuuwawa kwa Mdidi na tukio la mwisho ni Lukoha kutawazwa kuwa mfalme mpya wa Nugutu”
Watu wote wakapiga makofi na kushangilia ingawa wapo ambao walihuzunishwa na vitendo hivyo, baada ya muda mfupi Mfalme akafika eneo hilo na watu wote wakasimama na kuinamisha viichwa vyao.
“Uishi miaka ee mfalme”
Mfalme nae akainamisha kichwa kisha akakaa na watu wote wakaa, akaamuru Mdidi aletwe bila kupoteza muda maaskari wakamleta uwanjani, mfalme akacheka sana
“Leo ni siku yako ya kufa kifo cha aibu lakini si haraka hivi lazima ushuhudie watu unaowapenda wakiingia tabuni mmoja baada ya mwingine, Mleteeni mama yake”.
Mfalme akaamuru na maaskari wakaenda lakini walipofika kule wakakuta chumba cheupe wakarudi na kusema,
“Mtukufu mfalme tumetafuta kila mahari lakini hatukumuona mama yake” Mdidi akatabasamu na kumuangalia mfalme msongo kwa dharau.
“Hawezi kutoka Nugutu bila idhini yangu nendeni mkamtafute” maaskari wakaondoka.
“Nendeni mkamlete Nkalo”
Maaskari wakaenda na waliporudi majibu yalikuwa kama yale aliyopata kwa mama yake Mdidi,
“Huu ni uzembe usiovumilika haiwezekani watu wakapotea hivi hivi huku ninyi mkikaa tuuu nendeni mkamtafute na huyo hakikisheni anakuja akiwa hai,” Mfalme alitoa agizo uwanja mzima ukajawa na minong’ono ya hapa na pale, kila mmoja akazungumza analoliwaza.
“Mtukufu mfalme tumepekuwa kila mahali lakini hatujawaona”.
Mfalme akachukia mno akaamuru maaskari wale wote wafe baadhi ya maaskari wakagoma kuwaua wenzao hapo hapo mapambano yakazuka baadhi wakakaidi amri ya mfalme na baadhi wakatii amri ya mfalme.
Mdidi alivyoona madhara ya pambano lile yatakuwa makubwa na hakupenda damu imwagike ikabidi aingilie kati, askari mmoja akamrushia jambia na akalichoma katikati ya uwanja, hapo hapo kimbuga kikazuka, naye akaanza kubadirioka na kung’aa kama almasi. Baada ya dakika kama kumi akachomoa lile jambia na kulishika mkononi maaskari wote wakamuangukia na kusema.
“Tuamuru lolote nasi tutalifanya!”
Mfalme msongo akajawa na mshangao usio na kifani,
“Ile ndiyo nguvu iliyopo kwenye hazina ya Nugutu na huyu sasa ndiye mtawala halali” akasema mzee mmoja aliye karibu na mfalme, mfalme akachukia na kutoa jambia na kumua pale pale.
“Mshambulieni”
Msongo akatoa agizo lakini kila mtu aliogopa kumsogelea Mdidi, Msongo alipoona vile akafungulia jeshi la Giza, hapo midudu ya ajabu ajabu ikazuka na kuiamuru imshambulie Mdidi, Mdidi akanyoosha jambia na mwanga mkali ukatoka ambao ndani ya sekunde chache midudu ile ikapotea.
Baraza zima la utawala wa Nugutu wote wakapiga magoti na kusujudu, Mdidi akamshika mfalme Msongo na kumrusha katikati ya uwanja akanyanyua upanga wake ili kumuangamiza kabla hajafanya lolote akasikia,CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana mwanangu usimuue, damu iyo ni sawa na damu ya baba ako”
Mdidi akashusha upanga wake baada ya kusikia sauti ya mama yake, Mfalme Msongo alilia sana, watu wote wakamtukuza na kumsifu Mdidi kwa kuleta ukombozi,
“Kuliko aibu hii ni bora nife” akasema Msongo na kujichoma visu visivyo na idadi.
Maisha ya Nugutu yakabadilika na kuwa ya furaha na upendo mwingi mno, Mdidi akamuoa Nkalo na kuifanya kigomile na Nugutu kuwa moja, Chifu Mzovu alifurahi sana kuungana na mkewe, pia Nkalo alifurahi kumuona mama yake ambaye kwa muda mrefu alijua amekufa, wale washauri wote wa mfalme Msongo wakaukumiwa kifo na Balanoga aliamua kujiua.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment