Search This Blog

NILIJIUNGA NA DINI YA SHETANI - 3

 







    Simulizi : Nilijiunga Na Dini Ya Shetani

    Sehemu Ya Tatu (3)



    ILIPOISHIA:

    Kimoyomoyo nilijisemea kuwa lazima nifahamu mambo mengi kuhusu elimu ya utambuzi na kuutafuta ukweli kama hicho kinachoitwa dini ya shetani kinahusiana na shetani kweli au ni propaganda za kuwachanganya watu akili.

    SASA ENDELEA...



    Baada ya muda niliianza safari. Kwa jinsi nilivyokuwa nimemzoea mama, nilijikuta machozi yakinitoka wakati akinipungia mkono wa kwa heri. Nilijisikia vibaya sana kwenda kuishi mbali naye kutokana na jinsi nilivyokuwa nampenda lakini kwa sababu ilikuwa ni lazima niondoke, sikuwa na la kufanya.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Basi liliianza safari kutoka jijini Mbeya alfajiri na mapema, tukasafiri kwa saa nyingi barabarani tukiyapita maeneo kama Makambako, Ipogolo, Ilula, Mikumi, Morogoro, Chalinze na hatimaye tukaanza kuingia jijini Dar es Salaam.



    “Mbezi! Mbezi wakushuka,” nilimsikia kondakta wa gari akisema, nikajua tayari tumeanza kuwasili jijini Dar es Salaam. Baadhi ya abiria wakasimama na kuanza kujiandaa kuteremka. Nilipotazama pembeni, niliona watu wengi na magari yakipishana kwa kasi, nikawa nashangaa kwani kila kitu kilikuwa kigeni kwangu.

    Sikuzoea pilikapilika za mjini, nikawa nashangaa kila kitu. Tuliendelea na safari, gari likawa linaenda taratibu kutokana na msongamano mkubwa wa magari. Nakumbuka miongoni mwa vitu nilivyokuwa navisikia sana kuhusu Jiji la Dar es Salaam, ni foleni kubwa barabarani ambayo sasa nilikuwa nikiishuhudia kwa macho yangu.

    Kulikuwa na magari mengi barabarani kiasi cha kufanya tuchukue zaidi ya dakika arobaini kutoka Mbezi mpaka kwenye taa za kuongozea magari za Ubungo. Tulipofika hapo, gari lilisimama kwa muda, kwa kuwa niliwasikia watu wakisema kuwa hapo ndiyo Ubungo, nilichukua begi langu na kutaka kuteremka lakini kondakta akaniambia nisubiri mpaka tuingie stendi.



    Hatimaye basi nililokuwa nimepanda likaingia kwenye stendi ya Ubungo na kusimama. Abiria wote wakaanza kuteremka, na mimi nikachukua begi langu na kuteremka. Kwa bahati nzuri kumbe baba mkubwa alikuwa tayari amewasili pale stendi akiwa na mkewe na mwanaye mmoja wa kike, nilipoanza kushuka tu, nikamsikia akiniita jina langu.



    Nilifurahi sana kwani tayari nilishaanza kuchanganyikiwa, nikiwa sijui nielekee wapi. Walinipokea kwa furaha, tukakumbatiana na kusalimiana. Wakanipokea mzigo na kuniongoza mpaka nje ya stendi ambapo tulipanda teksi na safari ya kuelekea Kimara Kona alikokuwa anaishi baba mkubwa ikaanza.



    “Tulizungumza mambo mengi kwenye gari, wakawa wananiuliza hali za wazazi na ndugu zangu wengine niliowaacha Tukuyu. Niliwajibu kuwa wote wapo salama na wanawasalimia sana. Baada ya muda, tulikuwa tayari tumefika Kimara, dereva akasimamisha taksi kisha tukateremka. Wenyeji wangu wakaniongoza mpaka nyumbani.



    “Karibu sana, hapa ndiyo tunapoishi,” alisema baba mkubwa wakati akifungua geti, tukaingia ndani huku nikiwa na furaha tele ndani ya moyo wangu. Nilifurahi sana kufika Dar es Salaam. Kesho yake, baba mkubwa alienda kunitembeza mjini, akanipeleka Posta, tukaenda mpaka Feri na kuvuka ng’ambo ya pili, Kigamboni kwa kutumia kivuko.



    Tulirudi na tukaelekea Kariakoo.

    Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu, kuanzia wingi wa watu, magari, maghorofa marefu na kila aina ya mambo ya kuvutia.



    “Kumbe ndiyo maana wanasemaga mjini kuzuri, cheki maghorofa?” nilijisemea kimoyomoyo tukiwa tunakaribia Kariakoo. Tulipofika baba mkubwa alininunulia zawadi ndogondogo kisha tukaondoka. Akanipeleka mpaka Manzese, tukapanda mpaka kwenye daraja maarufu ambalo nilikuwa nalisikia sana nikiwa nyumbani Tukuyu.



    “Na mimi nataka kupiga picha juu ya daraja,” nilimwambia baba mkubwa ambaye bila hiyana alimuita mpigapicha, tukapiga kadhaa. Nilipanga kwenda kuwaringishia wenzangu nikirudi Tukuyu kwani hakuna aliyewahi kufika Dar es Salaam zaidi yangu. Baadaye tulirudi mpaka nyumbani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tukiwa tumekaribia, nililiona jengo moja lililokuwa na maandishi ukutani yaliyosomeka FAJI. Kumbukumbu zangu zikarudi kwenye kile kitabu changu, nikakumbuka kuwa kilielekeza kuwa Kimara Kona kuna sehemu panaitwa Familia ya Jitambue au kwa kifupi FAJI ambapo elimu ya utambuzi inatolewa.



    Nikashusha pumzi ndefu huku kimoyomoyo nikichekelea kwani kile nilichokuwa nakitaka sasa kilikuwa kimekaribia kutimia. Nilipaangalia vizuri kwa lengo la kukariri uelekeo ili nisipotee hata nikirudi peke yangu. Kwa kuwa haikuwa mbali sana na nyumbani kwa baba mkubwa, niliishika ramani vizuri.



    Siku kadhaa baadaye, jioni niliaga nyumbani kuwa naenda kunyoosha miguu. Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeanza kufahamu sehemu mbalimbali, niliruhusiwa, nikaelekea moja kwa moja pale kwenye jengo la FAJI, nikaenda mapokezi na kupokelewa na mwanamke mmoja wa makamo, akawa ananiuliza anisaidie nini.

    “Nataka kuonana na mwalimu wa Utambuzi aitwaye Munga,” nilisema huku nikiwa sina uhakika na nilichokuwa nakiulizia. Sikumfahamu Munga ila kupitia kile kitabu nilichokuwa nimenunua, nilisoma kuwa mwalimu wa masomo ya utambuzi katika kituo hicho alikuwa akitambulika kwa jina hilo.



    Mwanamke yule wa makamo aliyekuwa amekaa juu ya meza kubwa pale mapokezi, alinitazama kwa muda halafu ukimya ukatanda kwa sekunde kadhaa. Nilipomtazama machoni, niligundua kuwa alikuwa akitokwa na machozi. Sikuelewa sababu za kumfanya atokwe na machozi wakati nilimuuliza kistaarabu.

    “Ma’mdogo mbona unalia? Kwani kuna nini?” nilimuuliza huku nikianza kuingiwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu. Alinitazama tena, badala ya kunijibu akaniuliza natokea wapi?



    “Natokea Tukuyu, nimekuja kuishi kwa baba mkubwa, anakaa hapo mtaa wa pili,” nilimjibu, akaniambia kuwa Munga alishafariki dunia miezi kadhaa iliyopita. Nilishusha pumzi ndefu nikiwa siamini kile nilichokisikia.



    “Amefariki?” niliuliza tena huku machozi yakianza kunilengalenga, nilisogea pembeni mpaka kwenye benchi, nikakaa huku mwili ukiwa umeniishia nguvu kabisa. Niliona kama safari yangu ya kutaka kufahamu mambo mengi kuhusu elimu ya utambuzi ilikuwa imefikia mwisho.



    Nikiwa katika hali ile, mwanaume mmoja wa makamo aliyekuwa na mvi kichwa kizima, begani akiwa amebeba begi dogo, aliwasili. Akavua viatu nje na kuingia mpaka pale ndani, akanisabahi kwa uchangamfu kama tuliyekuwa tunajuana naye kwa siku nyingi, akaenda kumsabahi na yule mama wa makamo kisha akarudi na kukaa karibu yangu.



    “Bila shaka wewe ni mgeni hapa,” aliniuliza, nikatingisha kichwa kama ishara ya kumkubalia. Akaniuliza kuwa uso wangu ulionesha kuwa nina majonzi, ni jambo gani lilikuwa linanisumbua? Kabla sijamjibu, yule mama wa mapokezi alidakia na kumweleza kuwa nilienda pale kumuulizia Munga, nilipopewa taarifa juu ya kifo chake ndiyo nikawa kwenye hali ile.



    “Usijali, kama Munga hayupo wapo wengine wanaoweza kukusaidia ulichokuwa unakitaka, pengine kwa kiwango cha juu kuliko hata huyo Munga. Pia inawezekana unasikitika kwa sababu huelewi tafsiri ya kifo,” alisema yule mzee ambaye baadaye nilikuja kumtambua kuwa anaitwa Mhagama.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Angalau moyo wangu ulitulia, nikainua kichwa changu na kuanza kumtazama, akanipigapiga mgongoni kama ishara ya kunifariji, kisha akaanza kuniuliza juu ya historia yangu na asili yangu. Nilimjibu kuwa nimetokea Tukuyu, nikamweleza kuhusu familia yetu, kwamba baba yangu ni mchungaji na kumweleza jambo lililonipeleka pale.



    “Unataka kujua kuhusu nini hasa?”

    “Nataka kujitambua, nataka kujua kuhusu mimi na dunia ninayoishi. Nataka kujua uhusiano kati ya maumbile na ulimwengu,” nilimjibu, akanitazama kwa makini usoni kama anayejiuliza ‘utaweza kweli?’.



    “Basi hakuna shaka, hapa ndiyo umefika, naamini kila unachohitaji kukijua utakipata, cha msingi ni uvumilivu wako na juhudi kwenye masomo,” aliniambia, nikamuomba anifafanulie kuwa kuna masomo ya aina gani yaliyokuwa yanafundishwa pale.



    “Kuna madarasa mengi ya utambuzi, wanaoanza kuna darasa lao, wale wanaofahamu kidogo kuna darasa lao lingine na wale waliofuzu kuna darasa lao pia. Kuna madarasa ya meditation kulingana na ngazi kama ilivyo kwenye masomo ya utambuzi, naamini utafurahia,” alisema Mhagama huku akinitazama kwa furaha.



    Baada ya maelezo yale, aliniambia kuwa nilikuwa nimefika siku muafaka kwani kulikuwa na mafunzo siku hiyo, akaniambia baada ya muda wanafunzi wengine wataanza kuwasili eneo lile.



    Kweli baada ya muda, niliona watu mbalimbali wakiwasili eneo lile, vijana kwa wazee, wanaume kwa wanawake, wakawa wananisabahi kwa uchangamfu. Kitu nilichojifunza mapema ni kwamba wanafamilia wa Jitambue walikuwa na upendo mkubwa sana ndani ya mioyo yao. Kila aliyekuwa akinipita alikuwa akinisabahi kwa uchangamfu licha ya umri wangu mdogo, nikajihisi kama nipo nyumbani.



    “Hata wewe ukianza kusoma masomo ya utambuzi, utajikuta taratibu ukianza kuwapenda binadamu wenzako na kuondoa roho za chuki, visasi, wivu na kuwawazia wengine mabaya. Hapa tunafundishana namna ya kuishi kama ambavyo Mungu alikusudia binadamu tuishi,” alisema Mhagama, nikashangaa kumsikia akimtaja Mungu.



    “Mbona watu wanasema wanaojifunza utambuzi wanajifunza kumwabudu shetani?” nilimuuliza kwa shauku, akanitazama usoni na kuniambia kwa mafumbo: “Huwezi kuujua mti mpaka wewe mwenyewe utakapoamua kuwa mti.”



    Nilitafakari maana ya fumbo lile lakini sikupata majibu, akaendelea kuniambia kuwa kuna falsafa na propaganda nyingi sana zinazoenezwa juu ya watu wanaoutafuta ukweli, akaniambia niwe makini na nielekeze nguvu zangu zote kwenye kuusaka ukweli badala ya kusikiliza maneno ya watu.



    Baada ya kuniambia hivyo, tayari watu wengi walikuwa wameshaingia ndani ya jengo hilo, akanishika mkono na kuniambia nimfuate. Nilifanya kama alivyonielekeza, tukaongozana mpaka kwenye chumba maalum kilichokuwa upande wa kulia wa jengo lile.



    Tukaingia na kukaa kwenye jamvi kama wenzetu tuliowakuta, majadiliano yakawa yanaendelea. Kuna hoja ilitolewa juu ya vyakula ambavyo binadamu anapaswa kula ili awe na afya njema ya akili na roho, watu mbalimbali wakawa wanachangia.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Binadamu tuliumbwa kula mbogamboga, nafaka na matunda ndiyo maana hata mpangilio wetu wa meno (dental formula) ni tofauti na wanyama wanaokula nyama,” alisema mjumbe mmoja, mwingine akaunga mkono hoja ile.



    “Ni makosa sana kuendekeza kula vyakula kama nyama nyekundu, vyakula vya kwenye makopo na vinywaji vyenye kemikali, maisha ya binadamu siku hizi yamekuwa mafupi, yaliyotawaliwa na magonjwa mengi kwa sababu tunaishi kinyume na Mungu alivyokusudia alipotuleta duniani.”



    Nilivutiwa sana na mada ile, nikawa nasikiliza kwa makini. Baada ya kumaliza majadiliano, lilifuata zoezi la kufanya meditation kwa pamoja.



    Hakuna kitu nilichokuwa nakisubiri kwa hamu kama muda huo wa kufanya meditation ya pamoja. Lengo langu lilikuwa ni kujifunza kama ninavyofanya meditation mwenyewe huwa napatia au nakosea, nikawa nasubiri kwa hamu kuwaona watu walionizidi umri na uzoefu wakifanya.



    Tulielekezwa kukaa kwenye jamvi kwa mfumo wa duara, katikati pakawekwa mshumaa mkubwa uliokuwa unawaka. Tukaelekezwa kuwa siku hiyo tutafanya meditation ya mshumaa, kila mmoja akakaa vizuri tayari kwa kuanza.

    Niliposikia kuna meditation ya mshumaa, shauku ndani ya moyo wangu iliongezeka maradufu, nikawa nasubiri nione inavyofanywa.



    Baada ya dakika chache, tulielekezwa wote kuutazama ule mshumaa uliokuwa unawaka katikati yetu, tukaambiwa tusipepese macho na kuelekeza akili zote kuutazama mshumaa ule. Aliyekuwa anatoa maelekezo alisisitiza kuwa tutazame ile sehemu ya juu iliyokuwa inawaka, akasema tukishautazama kwa dakika kadhaa, atatoa ishara maalum ambapo wote tutatakiwa kufumba macho.



    Tulianza kuutazama mshumaa ule huku kila mmoja akipumua kwa uhuru, ukimya wa ajabu ukatanda mle ndani. Nilikuwa makini kuhakikisha sikosei hata kidogo, nikawa nautazama ule mshumaa huku nikiwa na hamu kubwa ya kuona kitakachotokea.



    Baada ya kuuangalia kwa dakika kadhaa, nilianza kuona hali ambayo nilishindwa kuitafsiri. Watu wote waliokuwa mle ndani sikuwaona tena, nikawa nahisi kama nilikuwa peke yangu chumba kizima, jambo ambalo halikuwa kweli. Baada ya muda, yule aliyekuwa anatoa maelekezo alitoa ishara kama alivyokuwa ameeleza awali, watu wote tukafumba macho.



    Kingine kilichonishangaza ni kwamba hata baada ya kufumba macho, niliendelea kuuona ule mshumaa ukiwaka kupitia kile ambacho baadaye nilielezwa kuwa ni jicho la tatu.



    Nilitulia katika hali ile kwa muda mrefu, nikaanza kujihisi kama nahama kifikra kutoka pale nilipokuwa nimekaa na kwenda sehemu ambayo siijui.

    Sikuona kitu chochote zaidi ya giza nene huku ule mshumaa ukizidi kufifia kabla ya kupotea kabisa kwenye fikra zangu. Nikawa naendelea kuvuta pumzi ndefu na kuzitoa kupitia mdomoni mwangu.



    Nikiwa kwenye hali hiyo, mara nilianza kuona picha ya nyumbani kwetu Tukuyu, nikawa naiona nyumba yetu jinsi ilivyo kutoka pande zote. Niliiona kutokea juu, kutoka kushoto, kulia, mbele na nyuma kisha nikajihisi kama nimeingia ndani.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikawa nawaona baba na mama wakiwa sebuleni wanatazama runinga.

    Nikawaona pia ndugu zangu wengine wakiendelea na kazi zao za kawaida pale nyumbani, kimoyomoyo nikawa natabasamu kwani licha ya ukweli kwamba nilikuwa mbali sana na nyumbani, kiakili nilikuwa nimefika.



    “Na huo ndiyo mwisho wa meditation ya mshumaa kwa leo,” nilisikia sauti ikisema, nikashtuka sana kiasi cha kuwashtua watu waliokuwa pembeni yangu. Kilichofanya nishtuke ni kwamba tayari nilishakuwa kwenye ulimwengu mwingine kiasi cha kusahau kabisa kwamba nilikuwa nafanya meditation.



    Nilijiona kama nipo nyumbani Tukuyu kumbe katika hali halisi nilikuwa pale kwenye kile kituo, Kimara Kona jijini Dar es Salaam. Nilijifikicha macho huku nikijihisi aibu kwa jinsi nilivyokuwa nimeshtuka, nikawa nawatazama kwa macho ya wizi wale watu niliokuwa nimekaa nao ambao wote walikuwa wakinitazama.



    “Haya sasa umefika muda wa kila mmoja kutueleza katika hii safari yetu ya meditation ameona nini. Tunaanza na ndugu yetu mgeni, naona umeshtuka kuliko kawaida, hebu tuambie umeona nini,” alisema yule kiongozi huku akinioneshea ishara mimi. Nilijiumauma kidogo kisha nikaanza kueleza nilichokiona.



    Karibu wote walicheka sana walipogundua kilichonifanya nishtuke kiasi kile, zoezi la kila mmoja kueleza alichokiona likaendelea mpaka wote walipoisha. Nilichokibaini ni kwamba, japokuwa wote tulikuwa tumekaa sehemu moja, wakati wa meditation kila mmoja alisafiri kivyake na kwenda sehemu tofautitofauti.

    Baada ya kumaliza zoezi lile, tuliekezwa kuwa muda wa kuendelea na masomo ya kawaida ya utambuzi ulikuwa umewadia, yule kiongozi akatuelekeza kuwa kila mmoja aelekee kwenye darasa lake. Watu wote wakainuka na kuelekea kwenye madarasa yaliyokuwa mlemle ndani ya jengo.



    Nilibabaika kidogo kwani sikujua mimi napaswa kuingia darasa gani, nikaelekezwa kuwa nilitakiwa kwenda kwenye darasa la wanafunzi wanaoanza masomo kama mimi, nikaenda kuungana na wenzangu kadhaa kisha mwalimu akaanza kufundisha.



    Kabla ya kuendelea na kipindi, tulitambulishana tena kisha wakawa wanakumbushana walichojifunza kipindi kilichopita.

    “Somo la leo linahusu uchawi, tutajifunza maana ya uchawi, jinsi unavyoweza kukupata na jinsi ya kujikinga,” alisema mwalimu huku akiandika ubaoni kwa kutumia ‘marker pen’.



    Nilikaa vizuri kwenye kiti changu na kuanza kusikiliza kwa umakini huku nikiandika dondoo muhimu kwenye kijitabu changu kidogo.

    “Uchawi ni kitu gani? Hili ni swali gumu sana kuliko unavyofikiri. Tumezoea sana kusema kuna uchawi au hakuna lakini mtu anapotuuliza huo uchawi ni kitu gani ndipo tunapogundua kuwa tumekuwa tukizungumzia kitu ambacho hatukijui.



    “Je, uchawi ni kuwa na vifaa ambavyo mtu anaweza kuvitumia kutengeneza nguvu yenye kuweza kusafiri na kwenda kumdhuru amtakaye? Je, uchawi ni uwezo wa mtu kuweka sumu kwenye maji au chakula na watu wakafa polepole au ghafla?



    “Je, uchawi ni mbinu ambazo mtu anaweza kuzifanya na kusababisha mwingine afukuzwe kazi bila sababu ya msingi? Je, ni uwezo wa mtu kumghilibu mke au mume wa mwenzake hadi akatoka kwenye ndoa yake halali?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Uchawi unatajwa sana kwenye matukio mengi kama kuugua, kufukuzwa kazi, kufa, kuachwa na mpenzi, mke au mume, ajali na mambo mengine kama hayo lakini je, tunaujua huo uchawi?” alisema mwalimu na kuanza kutuuliza mmojammoja tueleze jinsi tunavyoufahamu uchawi.



    Kila mmoja alieleza alivyokuwa anaufahamu uchawi lakini nilichobaini, wengi hawakuwa wakijua ni kitu gani zaidi ya kuonesha hofu juu ya jambo hilo. Hata

    mimi nilikuwa miongoni mwa wasiojua chochote, kilichonisaidia ni kwamba

    nilishawahi kusoma kwenye kile kitabu changu kilichoandikwa na marehemu

    Munga.



    Baada ya majadiliano, kila mmoja akiwa ameshaeleza japo kwa kifupi alivyokuwa anaujua uchawi, mwalimu alitutaka sote tutulie ili atueleze jambo ambalo hatukuwa tukilijua, akaanza: “Neno uchawi limekuwa likitumika

    na kuhusishwa na mambo mengi yanayotokea katika maisha ya kila siku

    ya mwanadamu kwa karne nyingi sana.



    Inaaminika kuwa uchawi ulikuwepo duniani hata kabla ya kuzaliwa kwa Kristo.

    “Katika vitabu vitakatifu, uchawi umezungumziwa mara nyingi na umekuwa ukihusishwa na matukio mengi. Maneno kama pepo wachafu, mizimu na matambiko kila yanapotumika, huwakilisha uchawi.



    “Licha ya kuwa dhana hii ni kongwe na imekuwepo kwa miaka mingi, bado

    kumekuwa na ugumu mkubwa katika kuelezea huo unaoitwa ‘uchawi’ ni

    kitu gani hasa. Sote hapa tumekuwa tukilisikia sana neno hili ‘Uchawi’ na

    bila shaka tumeshashuhudia matukio ambayo tuliambiwa na tukaamini kuwa

    yamesababishwa na uchawi.



    “Uchawi umekuwa ukihusishwa katika matukio kama vifo, mtu kuugua ugonjwa wa ajabu, kupata ajali katika mazingira ya kutatanisha, kufukuzwa kazi, kuugua kichaa, ndoa kuvunjika, kuachwa na mpenzi, kutopea kwenye tabia hatarishi kama ulevi au matumizi ya madawa ya kulevya, kufeli mitihani, kufilisika, biashara kudorora na kufa.



    “Katika maeneo ambayo mpaka leo imani hii bado inapewa nguvu, uchawi

    umekuwa ukitajwa karibu katika kila tukio linalotokea. Ni nadra sana kusikia jambo fulani limetokea au limempata mtu bila ya uchawi kutajwa. Katika maeneo kama Bagamoyo, Tanga, Sumbawanga, visiwani Zanzibar na sehemu nyinginezo, imani hii bado imekuwa ikipewa nguvu kubwa sana

    katika jamii.



    “Pamoja na kuwa uchawi umekuwa ukitajwa katika mambo mengi kwa maelfu

    ya miaka, bado ni wachache sana kati yetu wanaoweza kueleza kwa ufasaha maana ya uchawi.



    “Wengi wetu tumeendelea kuamini, kuogopa na kuzungumzia juu ya kitu ambacho hatukifahamu kabisa. Wataalamu wengi wamekuwa wakijaribu

    kwa miaka mingi kufanya utafiti juu ya maana, asili na namna uchawi

    unavyofanya kazi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Licha ya jitihada hizo za kuutafuta ukweli juu ya uchawi kuanza karne nyingi zilizopita, mpaka leo bado hakuna majibu ya kuridhisha juu ya uchawi. Tumezoea sana kusema kuna uchawi au hakuna uchawi, lakini tunapoambiwa tuelezee huo uchawi ni kitu gani, wengi huwa tunashindwa kutoa majibu.



    “Hapa niliwapa nafasi ya kila mmoja kueleza namna anavyoufahamu uchawi lakini wenyewe mmeshuhudia mlivyokuwa mnajikanyaga. Hii ni kwa sababu uchawi hupimwa kwa matokeo na siyo sifa nyingine.



    “Tunasema huu ni uchawi kwa sababu tumeona jambo fulani likitokea au kufanyika kwa njia ambayo hatuwezi kuielezea, au katika namna ambayo

    hatukuitegemea, njia ambayo hatuwezi kuielezea au kwa njia ambayo inaashiria

    ubaya au uhasidi. Nje ya matokeo, hakuna uchawi.



    “Huwezi kukuta uchawi ukiwa umetundikwa au ukiwa umewekwa mahali, bali unaweza kuuona ukifanya kazi. Kama utakuta hirizi, tunguri au mapembe yenye manyoya mahali, huwezi kusema huo ni uchawi, bali ni vifaa ambavyo hutumika kwa shughuli mbalimbali. Vinaweza kuwa vinatumika kwa uchawi au kwa shughuli nyingine lakini siyo kwamba vyenyewe vinaweza kuwa uchawi.



    “Kwa kuwa uchawi umekuwa ukitajwa karibu katika kila jambo tangu karne nyingi zilizopita, ni dhahiri kuwa kweli upo na unafanya kazi. Lakini kwa nini ufanye kazi kwenye maeneo yote hayo?



    Kwenye kufa, kuugua, kufilisika, kupoteza hamu ya tendo la ndoa, kuishiwa nguvu za kiume, kushindwa kufanikiwa maishani na kila mahali? Ni kwa sababu ni matokeo na siyo kitu halisi tunachoweza kukishika au kukiona na kusema huu ndiyo uchawi.



    “Uchawi ni matumizi mabaya ya nguvu zisizoonekana, zinazozalishwa na

    binadamu kutaka kumuonea, kumtishia na kumdhuru binadamu mwingine. Nguvu hizi huzalishwa kwa mawazo, vitendo na kauli.



    “Baada ya kuzalishwa, nguvu hizi hurushwa kwenda kwa mtu au kitu kilichokusudiwa na zinapomuingia mhusika, husababisha madhara makubwa

    yanayoonekana na yasiyoonekana.



    “Ni ukweli usiopingika kuwa kuna idadi kubwa ya binadamu wenye uwezo

    wa kuzalisha nguvu zenye uwezo wa kuwadhuru wengine. Inawezekana

    anayezalisha nguvu hii mbaya yenye kudhuru (uchawi) akawa anajua

    anachokifanya, lakini pia kuna wakati mtu anakuwa hajui kuwa anazalisha nguvu mbaya inayodhuru.



    “Kwa asili, kila binadamu ana uwezo wa kuzalisha nguvu kutoka ndani yake, na

    anaweza kuishi kwa sababu yuko ndani ya nguvu. Mawazo yetu yanazalisha nguvu, kauli zetu zinazalisha nguvu na matendo yetu yanazalisha nguvu.

    “Kuna watu ambao wana nguvu za moja kwa moja ambazo wamezaliwa nazo,

    wakati wengine wana nguvu za kunuiza ambazo huwa wanajifunza.



    “Nguvu yoyote inayozalishwa na binadamu inaweza kuwa katika sura ya

    uharibifu au uadilifu. Inategemea ni nguvu gani na lengo la kuizalisha ni ipi. Nguvu tunazozizalisha zina matokeo ambayo tunaweza kuyathibitisha.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nguvu zisizoonekana ambazo ndizo zenye nguvu kubwa kuliko zinazoonekana hujibainisha kwa matokeo yake. Kwa leo tuishie hapa, kuna yeyote mwenye swali?” aliuliza mwalimu, sote tukabaki tukitazamana mle darasani. Nilianza kuhisi kama kichwa kinaniuma kwa aliyoyasema,

    nikashusha pumzi ndefu na kuanza kutafakari.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog