Search This Blog

NILIVYOTESEKA KWENYE MIANZI YA KICHAWI - 1











    IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS

    *********************************************************************************



    Simulizi : Nilivyoteseka Kwenye Mianzi Ya Kichawi

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    KIJIJI cha Nangose kipo jirani na mji wa Masasi njiani kuelekea kijijini kuna mimea mingi sana iitwayo mianzi ambayo watu huikata kwa matumizi mbalimbali kama vile kujengea nyumba, kutengenezea ungo au vyombo maalum wenyeji huviita ichinumba ambavyo hutumika kunywea pombe ya kienyeji ya mtama, wengine hutengeneza fimbo maalum ya kutembelea, au mipini ya majembe na kadhalika.

    Mimi naitwa Issa Namakoto, nakusimulia simulizi hii nikikurudisha nyuma miaka kadhaa iliyopita tukiwa Dar es Salaam tulipata taarifa kuwa Nangose kuna bustani ya ajabu ya mianzi iliyopandwa kimstari na mtu asiyejulikana.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku moja mimi na rafiki zangu 25 tuliamua kwenda kujionea bustani hiyo, tulifunga safari yetu tukitokea Dar es Salaam, tulikuwa vijana watupu wa kike na kiume.

    Tuligeuza ziara hiyo kama pikiniki fulani. Wakati tunasafiri tulipofika Nangurukulu, njia panda ya kwenda Kilwa, tulipumzika kwa ajili ya kula chakula cha mchana.

    Tulijaribu kuhoji wenyeji tuliokuwa nao kwenye basi na tuliambiwa kuwa ndani ya bustani hiyo kuna maua mazuri yaliyokuwa yamezunguka mianzi hiyo ya ajabu na kulikuwa na mtunzaji ambaye alikuwa ni mtu mwenye umri mkubwa aliyekuwa akisimulia mambo ya bustani hiyo.

    Aliyekuwa anatusimulia pale Nangurukulu alitufanya tutamani kufika mapema katika bustani hiyo ili tushuhudie maajabu tuliyoambiwa yapo. Msimuliaji huyo alisema kuwa watu wanaokwenda kujionea maajabu hayo lazima watimize masharti fulani ambayo mtunza bustani huwaambia.

    Baada ya kula safari ilianza kwa furaha kubwa, ndani ya basi ‘kosta’ kulikuwa na mazungumzo yanayohusu bustani hiyo ya ajabu na mwenzetu mmoja alisema aliambiwa kuwa ndani yake kuna matunda pori matamu sana ambayo hayana msimu.

    Basi letu dogo lilipita Lindi mjini saa nane mchana na dakika chache baadaye tukafika Mnazi Mmoja, njia panda ya Lindi na Masasi na Mtwara.

    Hapo pana pilikapilika na kuna mizani ya kupimia magari mazito.

    Baada ya kufika hapo, dereva alituambia tushuke kwa ajili ya kununua chochote tulichohitaji na kujisaidia, alitupa dakika kumi na tano.

    Kwa kuwa mimi ni mpenzi sana wa korosho, nilinunua za shilingi mia tano na soda.

    Muda tuliopewa na dereva ulipoisha tuliingia kwenye gari na kuanza safari na kwenda moja kwa moja hadi Mtama, (Jimbo la Mbunge Nape Nnauye) tukafika saa nane na nusu na njiani kabisa tukakutana na umati ukicheza ngoma, ulikuwa ukikatiza barabara kuu ikabidi dereva asimame, kuwapisha.

    “Nadhani hawa wanasherehekea mambo ya jando na unyago kwa sababu kipindi chenyewe kilikuwa cha mavuno,” nilijisemea.

    Tulipotoka pale Mtama usingizi ulinishika, nikalala usingizi mzito na nilishtukia nikiambiwa kuwa tumefika Ndanda. Hapa ni maarufu kwa mikoa ya kusini kutokana na kuwa na hospitali kubwa ya misheni na shule ya sekondari.

    Nilifikicha macho na kuona mji. Siyo mji mkubwa, una barabara ya lami moja tu na kando ya barabara kuu tunayopita kuna soko. Tulikuta wenyeji wakiuza mbaazi kwa mafungu na abiria waliokuwa wakisafiri kwa mabasi makubwa walikuwa wanajinunulia mbaazi hizo.

    Wakati tunatoka Dar tulielezwa kwamba tukifika Ndanda kuna mtu mmoja anaitwa Ngalipambone ataungana nasi na ndiye atakayetuongoza hadi Nangose. Kutokana na urefu wa jina lake watu wanakatiza na kumuita bwana Ngali.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haikuwa ngumu kumpata kwa sababu alikuwa anawasiliana na dereva wa basi letu mara kwa mara kwa njia ya simu.

    “Habari zenu jamani!” Alisalimia bwana Ngali.

    “Nzuri, shikamoo!” tuliitikia na kuamkia kwa pamoja kama vile kulikuwa na mtu aliyekuwa akituamuru.

    “Marahaba. Mimi naitwa Ngali. Nimeambiwa niwapeleke kwenye bustani ya mianzi ya Nangose.”

    “Ni kweli bwana,” alisema dereva.

    “Kutoka hapa siyo mbali sana na tutafika leoleo,” akasema bwana Ngali na kuketi kwenye kiti cha mbele kwa dereva msaidizi, ambaye aliinuka na kwenda kusimama mlangoni kama kondakta wa daladala afanyavyo.

    Bwana Ngali ndiye alikuwa kinara au dira ya kwenda kwenye bustani hiyo ya ajabu ambayo watu wamekuwa wakiisifia.

    Baada ya kufika mjini Masasi hatukukaa, basi lilielekezwa kuifuata barabara ya Nachingwea. Ni mwendo mfupi tu kutoka hapo kwenye njia panda ya kwenda Tunduru ambapo kuna gereza la wilaya tukamsikia bwana Ngali akimuamuru dereva afuate njia ya Nachingwea;

    “Pinda kushoto,” tukaiacha barabara kuu na kuifuata ya vumbi. Dakika kama tano bwana Ngali akasema;

    “Saa tumefika Nangose, pinda kulia kama tunaelekea Nchoti.”

    Lakini baadaye tukaingia barabara yenye vumbi jekundu ilikuwa kama tunaelekea Kijiji cha Nchoti lakini tukapinda tena kulia.

    Tulianza kuona bustani ya ajabu na tulipofika eneo fulani bwana Ngali alisimama katikati ya basi akasema:

    “Jamani mimi hapa ndiyo mwisho wa safari yangu. Bustani ya mianzi ni hii kuanzia hapa, huko mbele kuna mtu mtamkuta ambaye ndiye atakuwa mwenyeji wenu.”

    Nilijiuliza huku ni porini sasa huyu bwana Ngali atarudi kwa njia gani mjini? Hata hivyo, wakati nawaza hayo nilishtukia pikipiki ikitoa mlio, kumbe alimpigia mtu wa bodaboda akawa anatufuata kwa nyuma.

    Alishuka kwenye basi letu, akapanda pikipiki na kutoweka. Dereva wetu aliendelea na safari hadi katikati ya bustani ya mianzi. Ilikuwa nzuri sana ambayo sijapata kuona maishani mwangu.

    Mianzi ilikuwa imepandwa kwa mstari na pia kulikuwa na maua ya kila aina. Ajabu ni kwamba sehemu zote tulizopita zilikuwa kavu, majani yalikauka lakini katika bustani hiyo ni tofauti sana. Mianzi yote, maua na miti ni ya kijani kibichi.

    Alitokea mzee mmoja ambaye alionekana kuwa ni chotara, alikuwa na ndevu nyingi nyeupe na alikuwa na mvi karibu kichwa chote, mashavu yalikuwa yamemshuka kwa uzee.

    “Karibuni wajukuu zangu,” alisema mzee huyo tukamuamkia.

    Nilimsogelea kwa kuwa mimi ndiye nilikuwa mkuu wa msafara. Alinishika mkono mwilini nikaona kama nimepigwa shoti ya umeme! Nikapiga yowe!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilimuangalia usoni baada ya kuniachia akawa anatabasamu, nikajua kuwa alikuwa na mapengo na meno yake yalikuwa meusi kama vile anakula ugoro.

    “Nisikilizeni. Mimi naitwa Mzee Mavaka. Huyu kiongozi wenu nimemuonesha kuwa katika bustani hii hakuna mchezo. Kila unachokiona kiheshimu. Ukitaka kuchuma chochote ni lazima uniambie mimi ili niweze kutoa baraka za kufanya hivyo.

    Hii ni bustani iliyohifadhiwa na himaya ingine ili kutoa funzo kuwa mazingira yanapaswa kutunzwa hivi. Kwa hiyo usichume kitu bila ruhusa yangu, nawajua nyinyi vijana wa Dar mlivyo wabishi, ubishi wenu uishie kulekule kabla ya kuingia katika bustani hii tukufu ya Nangose, sawa?”

    Tukaitikia kwa pamoja “Sawaaa.” Ilikuwa kama vile tuliambiana.

    “Mianzi hii mnayoiona ni ya aina yake, imepandwa kwa mstari na kwa umaridadi kama mnavyoona na kila kitu kilichomo ndani ya bustani hii ni fahari ya dunia hii. Ogopeni, heshimuni. Ona jinsi nyasi zilivyofyekwa na vipepeo wanavyofurahia mandhari hii.

    aribuni zingatieni sheria hiyo ya kutochuma chochote bila ruhusa yangu,” alionya.

    Alitupeleka kwenye mgahawa wa bustani tukala chakula bure. Ajabu ni kwamba tulikuta ‘bufee’ yenye kila aina ya chakula na kila mtu alikuwa anajipakulia mwenyewe chakula akipendacho.

    Pia kulikuwa na vinywaji baridi vya kila aina. Tulimuuliza yule mzee Mavaka nani analipia bili ya chakula, akasema hiyo analipa mwenye bustani. Tulimuuliza ni nani? Hakujibu akawa anatabasamu tu!

    Vijana wa Dar kama unavyowajua ni wabishi, wakaanza kuchuma ‘maembe ya kusini’ wenyewe huziita embe mali, wakawa wanakula, ulikuwa ni msimu wa maembe. Wengine hasa wasichana wakawa wanachuma maua yenye harufu nzuri na kuyatunga kwenye nyuzi zao kisha kuzivaa shingoni bila kupata idhini ya yule mzee.

    Tuliendelea kutembelea bustani ile na kugundua kuwa kulikuwa na sehemu ambayo ilikuwa na maji yametuama ni kama bwawa kubwa na kulikuwa na mtu ameketi kando yake, tulikwenda kuangalia anafanya nini, kumbe alikuwa anavua samaki ajabu ni kwamba alikuwa hatuangalii, alikuwa anavua samaki mmojammoja kwa kutumia ndoana na kuwaweka kwenye kapu kubwa.

    “Mzee shikamoo.” Nilimuamkia.

    “Siwezi kukujibu salamu yako,” alijibu kijeuri yule mzee.

    “Sasa mzee mbona unajibu hivyo, tumekukosea nini? Sisi ni wageni hapa.”

    “Makosa mliyoyafanya mnajifanya hamyajui mpaka mimi niwaambie?”

    “Tuambie mzee, sisi ni kama wajukuu zako.”

    “Kwanza ondokeni hapa kwenye bwawa la samaki, watoto wajinga sana nyie, wajukuu zangu gani msiosikiliza mnachoambiwa na wakubwa wenu? Nasema ondokeni!” alizidi kufoka, alituangalia, macho yake yalikuwa mekundu kama mtu aliyevuta bangi!

    Tuliondoka eneo hilo, mbele yake tuliona kuna mianzi mizuri sana na watu wanaikata ile iliyokomaa tu na kuipakia kwenye gari.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Jamani habari za hapa,” niliwasalimia watu wale.

    “Nzuri. Mnataka mianzi? Kuna masharti ya kuikata,” alijibu mmoja wa wale vijana waliokuwa wakikata na wengine walikuwa wakiipakia kwenye gari aina ya Canter.

    “Masharti gani? Hayo ni mambo ya kizamani bwana,” mwenzetu mmoja akasema.

    “Siyo mambo ya kizamani, kuna masharti msipoyatekeleza mtapata madhara mazito. Tunaambiwa ni hatari na unaweza kupoteza wenzako wote uliofuatana nao.”

    “Watapoteaje? Acheni hayo, uongo mtupu,” akadakia kijana mwingine miongoni mwetu.

    “Wewe unayetueleza habari hizo umewahi kushuhudia mtu akiadhibiwa kwa kula matunda au kukata mianzi katika bustani hii tangu uzaliwe?” akadakia dada mwingine.

    “Mimi sijashuhudia lakini kuna simulizi nzito sana nimesimuliwa na wazee kuhusu bustani hii ya mianzi ya Nangose.”

    “Kwanza tueleze kwa nini inaitwa bustani ya mianzi ya Nangose wakati kuna matunda mengi kama vile miembe na maua ya kila aina?”

    “Hilo mimi siwezi kujibu, kwa kuwa mimi siye mwenye bustani,” alijibu kijana huyo.

    Yupo kijana miongoni mwetu alichuchumaa na kuchukua mundu na kwenda kukata mianzi michanga ili aone kama inatoa pombe ya ulanzi kwani yeye ni mtu wa Iringa.

    Mara nilimuona mzee Mavaka aliyetupokea akitoka kwenye ule mgahawa akiwa ametoa macho na mwili kumtetemeka.

    “Nani kakata mianzi michanga na kuchuma maembe na maua bila idhini yangu? Nyinyi vijana wa Dar habari zenu nimezisikia ndiyo maana nikawaonya kabla, nimeona kwenye chombo ndani mkichuma embe na maua na sasa mmekata mianzi, sasa mtaona cha mtema kuni,” alifoka mzee Mavaka.

    Huku akitetemeka, sekunde chache tukashuhudia tetemeko la ardhi! Bustani yote ikawa inatetemeka! Mianzi ikawa inatupiga, yowe zilikuwa nyingi na hatukuwa na uwezo wa kukimbilia kwenye basi.

    Nilishuhudia ardhi ikizama huku baadhi ya wenzangu wakiwa wamezimia kutokana na kupigwa na mianzi. Kipande cha ile bustani kiliendelea kuzama huku tukiwa juu yake, nikawa naona giza linaanza kuingia kadiri tulivyokuwa tunazama nuru ya jua ikawa inapotea machoni mwangu badala yake nikawa nasikia sauti za kutisha.

    Mshangao uliniingia baada ya kuona kutitia huko kwa bustani kuliendelea kwa saa nzima nikawa sioni chochote isipokuwa giza lilikuwa totoro. Moyo wangu ulinienda mbio nikijua kuwa sasa utakuwa mwisho wa maisha yetu.

    Nilianza kutetemeka wakati ardhi ikizidi kuzama, ilikuwa kama tupo kwenye lifti na tunashushwa chini kutoka ghorofani, swali likawa tunazamishwa na nani na je, tutapona au mwisho wa yote ni kufunikwa na ardhi? Moyoni niliwalaumu wenzangu kwa kutofuata masharti ya bustani ile ya Mianzi ya Nangose.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ajabu ni kwamba pamoja na ardhi kuendelea kuzama, sikusikia sauti yoyote kuonesha kuna mashine inaendesha kipande kile cha ardhi kukipeleka chini zaidi ya ardhi.

    Kwa kuwa saa yangu ilikuwa inatoa mwanga kwenye giza nene, niliiangalia nikagundua kuwa sasa ni saa mbili tukizama ardhini, sekunde kama kumi hivi nilianza kuona mwanga unajitokeza ukitokea chini ya ardhi.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog