Search This Blog

UCHAWI WA MAMA MKWE - 4

 







    SIMULIZI : UCHAWI WA MAMA MKWE

    Sehemu ya Nne (4)




    Asubuhi nyumba ya jirani ilikuwa imejaa watu ambao walikuwa wakipiga kelele.

    "Mchawi, mchawi kanasa ndani." Umati ulikuwa mkubwa sana na kelele zikawa nyingi, mume wangu aliamka.
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Baada ya mume wangu kuamka, alifikicha macho kutoa matongotongo machoni kisha akasimama na kujinyoosha mwili.

    "Mhhhh Mama Ajigale, mwili unauma sana," alisema.

    "Pole sana, kwani ulifanya kazi gani?"

    "Hakuna, vipi mbona kuna kelele huko nje?"

    "Nasikia kuna mchawi kanasa katika nyumba ya huyo shoga yangu."

    "Shoga yako yupi?"

    "Yule aliyekuja hapa nyumbani na kusema atatupeleka kwa baba yake akatufanyie zindiko."

    "Acha utani, kwake ameshikwa mchawi?"

    "Siyo ameshikwa. Amenasa!"

    "Unatania?"

    "Husikii kelele huko nje? Njoo hapa dirishani uone."

    "Kwani hapo dirishani huyo mchawi aliyenasa anaonekana?"

    "Hapana uje uone watu walivyojazana nje ya madirisha."

    Mume wangu alifika dirishani.

    "Kwa kuwa yule mama mwenye nyumba ni rafiki yako nenda kamuone," aliniambia, bila ajizi nilijitanda kitenge changu na kwenda kujionea japokuwa picha nzima nilikuwa naijua kutokana na kusikia waliyokuwa wakiyafanya wachawi usiku hapa nyumbani kwangu.

    Nilifika pale na yule shoga yangu aliponiona aliniita pembeni akaanza kunisumulia:

    "Unajua mama Ajigale, kama nilivyokuambia jana kuwa nyumbani kwako kuna wachawi wanakuja kila siku usiku huku wengine wakitumia ungo."

    "Nakumbuka uliniambia hivyo tena mbele ya mume wangu, huyo aliyenaswa ni nani?" Nilianza kumpeleleza.

    "Shoga namjua basi? Labda wewe ukimuona unaweza kumfahamu."

    Jirani yangu huyo alinipenyeza licha ya kuwepo watu wengi, walimpisha kwa kuwa walikuwa wanajua kuwa yeye ndiye mama mwenye nyumba, huku nami nikijitahidi kumfuata.

    Tulifika ndani ya nyumba na kumkuta mchawi akiwa bado ameganda katikati ya sebule huku watu wakiwa wamejazana kwenye madirisha ili waweze kumuona, alikuwa amevaa kaniki kiunoni.

    "Ua, mchawi huyo, ua, mmwagie mafuta ya taa, achomwe moto," yalikuwa ni maneno ya watu waliokuwa wamefurika nje ya nyumba hiyo.

    Niliingiwa na hofu kubwa hasa niliposikia watu wengine wakisema mchawi yule achomwe moto.

    Lakini hata mume wa rafiki yangu niliona ana wasiwasi baada ya kusikia maneno hayo kwani alianza kuhangaika kupigia simu watu ambao mimi sikuwajua.

    "Jamani njooni haraka wasije kumdhuru huyu mchawi," alisikika akisema.

    Nilimuaga shoga yangu nikachomoka kasi kuelekea nyumbani kwangu, njiani nikakutana na mume wangu ambaye alikuwa amevaa bukta, fulana na makubazi miguuni.

    "Ehee, huyo aliyenaswa unamfahamu?" simjui, yupo tu pale sebuleni anang'aang'aa macho."

    "Sasa wenye nyumba wanasemaje?"

    "Baba mwenye nyumba nimemuona akihangaika kupiga simu kwa watu ambao siwajui, anawaambia waje kumnasua mchawi."

    "Amepiga simu polisi?"

    "Sijui."


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Lakini akishafika huyo mtu akamnasua, huyo mchawi atapita wapi? Ni wazi atauawa palepale nje ya nyumba yake ni vema akaita kwanza polisi."

    "Hilo naona hajakumbuka, amepaniki, ni vema ukawahi kumpa ushauri huo."

    "Hapana turudi sote tukatoe ushauri kwa pamoja."

    Nilikubaliana na mume wangu hivyo nikageuza njia na kuanza kuelekea tena kwa jirani yetu.

    Tulipofika watu ndiyo walizidi, bahati nzuri tulikuta kuna waandishi wa habari wa Gazeti la Uwazi ambao baada ya kutuona walitukabili.

    "Mama samahani, mimi ni Chande Abdallah na huyu ni bosi wangu Makongoro Oging' waandishi wa gazeti la Uwazi, tumeambiwa wewe ulikuwa ndani, unamfahamu huyo mchawi aliyenaswa?"

    "Kaka mimi huyo aliyenaswa kweli nimemuona lakini simfahamu kwa jina wala sijawahi kumuona hapa mtaani."

    "Lakini watu wanasema wewe na mama mwenye nyumba ni marafiki, je, umeonana naye na mmeshauriana nini?"


    Tumeshauriana kwamba waitwe polisi."

    "Polisi wataweza kumnasua mchawi aliyenaswa?" alizidi kunidadisi Chande na nikagundua kuwa sikumalizia kile nilichokuwa nataka kumfahamisha.

    "Ahhh. Kweli, ni kwamba nimeshauri waitwe polisi kwa usalama wa huyu mchawi kwani kama itatokea akanasuliwa kisha kutolewa nje ya nyumba, ni wazi watu wenye hasira kali watamgombania na kumtoa uhai," nilijibu na Chande akawa anaandika kwenye kijitabu chake.

    Niliwaacha waandishi hao na kwenda kwa mama mwenye nyumba ambaye alikuwa na mumewe nami na mume wangu.

    Mume wangu alipewa jukumu la kuita polisi naye akapiga namba 112 na polisi wakaitikia.

    "Polisi naini, naini hapa, tukusaidie nini?" Simu ilisikika kwa sababu aliweka spika ili tusikie wote tuliokuwa tumemzunguka.

    "Hapa Mtaa wa Pwiriri, kuna mchawi amenaswa."

    "Sawa, sasa mnataka msaada gani kwa sababu sisi polisi hatuwezi kumnasua!"

    "Hapana msaada wetu ni kwamba tunataka mje kulinda usalama wake na wa mali pia kwa kuwa watu wanatishia kumlipua kwa mafuta ya taa. Sasa wakifanya hivyo akiwa ndani ni wazi kwamba vitu vingi pamoja na nyumba vitatekelea, tafadhalini njooni," alizidi kuomba mume wangu.

    "Nimekuelewa, tunakuja," alisema polisi huyo na kukata simu.

    Nje ya nyumba fujo zilizidi na wakati tunatafakari nini cha kufanya, aliingia mtu mmoja ambaye alikuwa ni mzee wa makamo.

    "Baba karibu sana. Umekuja na teksi?" alihoji mwenye nyumba.

    "Ndiyo," alijibu mzee huyo.

    "Sawa. Shilingi ngapi anataka?"

    "Nimeshamlipa," alijibu mzee.

    "Jirani zangu huyu ni baba yangu mzazi na ndiye aliyenitengenezea nyumba hii ili wachawi wasiingie," akatutambulisha.

    "Shikamoo baba," tulijishitukia mimi na mume wangu tukimuamkia kwa pamoja kama vile kuna mtu alituamuru kufanya hivyo.

    "Mzee hawa ni jirani zangu, baba na mama Ajigale, tunaishi nao vizuri. Ilikuwa tuwalete kwako Jumapili ijayo ili kuwazindikia nyumba yao," alisema baba mwenye nyumba.

    "Bado hamjachelewa, walete tu. Tumalize kwanza hili lililonileta," akasema.

    "Hapana baba tusubiri kwanza polisi. Si unaona jinsi fujo zilivyotanda hapo nje?"

    Kabla hajajibu lolote tulisikia ving'ora vikilia nikajua kwamba hao ni polisi wanakuja. Hata hivyo, nilishanga kusikia ving'ora vya magari mawili nikajiuliza kwa nini wamekuja na magari mawili kana kwamba kuna fujo tayari zimefumuka.

    Nilichungulia dirishani nikaona kumbe walikuwa wameongozana na gari la Kikosi cha Zima Moto.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Watu waliokuwa wamejazana mlangoni akiwemo mama mkwe wangu walipisha na kuweka njia bila hata kuamrishwa baada ya kumuona mkaguzi wa polisi yaani Inspekta Kijo akija ndani pamoja na maofisa wengine wa polisi.

    Aliingia akiwa na askari sita wote wakiwa na silaha za kivita, Semi Machine Gun (SMG).

    "Nani mhusika mkuu hapa," alisema Inspekta Kijo.

    "Ni mimi hapa, hawa ni jirani zangu na huyu ni mke wangu," alijibu baba mwenye nyumba.

    "Huyu ndiye mchawi aliyenasa hapa?"

    "Ndiyo."

    "Ina maana hawezi kujisogeza kabisa?" aliuliza swali yule inspekta wa polisi, swali ambalo halikuwa na jibu kwa sababu alimuona na kama angeweza kujisogeza tusingesema alinasa.

    "Sasa mtamnasuaje?" aliuliza tena.

    "Yupo mtu wa kumnasua, huyu baba yangu, tulikuwa tunawangoja nyinyi mje kwa usalama wa huyu mchawi. Tulifikiri kama tungemnasua bila nyinyi kuwepo, watu wenye hasira wangeweza kumuua."


    Mzee wa baba mwenye nyumba alichukuwa dawa nyeusi na kuichanganya kwenye maji kisha kummwagia yule mchawi aliyenasa ndani miguuni mara tatu, akamsukuma na akapepesuka, ikawa tayari amemnasua.

    Ua mchawi huyoooo, chinja, piga maweee," zilikuwa ni kelele za wananchi waliokuwa wamejazana nje ya nyumba.


    Polisi wanne wenye silaha ilibidi watoke nje na kuwatawanya watu wenye hasira. Hata hivyo, bado watu walikuwa wabishi kuondoka ndipo askari mmoja akalipua bomu la machozi.

    Moshi ulifumuka na kujaa nje lakini mwingine uliingia ndani na kutufanya nasi kububujikwa na machozi kutokana na muwasho wa moshi huo ulipoingia machoni.

    Wakati watu wanakimbia huku na huko kutona na woga wa kishindo cha mlio wa bunduki na moshi wenye pilipili, polisi walitumia mwanya huo kumtoa ndani mchawi na kumuingiza katika gari lao, Difenda'.

    Walimchukuwa na mzee wa baba mwenye nyumba ile na mmiliki wa nyumba na mkewe. Mimi nilishauriwa na mume wangu nimsindikize jirani yangu kwa kuwa ni shoga yangu.

    Tulifika polisi na kukuta makamanda na askari wengine wa vyeo vya chini wakitusubiri kwa kuwa habari ile ilisambaa kwa kasi kubwa mji mzima. Wote tuliingizwa katika chumba kimoja pale polisi na tukaketi kwenye viti. Yule mchawi aliambiwa asimame, akaanza kuhojiwa.

    "Wewe mchawi unaitwa nani?" alihoji afisa mmoja wa polisi huku akiandika kwenye jalada.

    "Naitwa Pimbi Msafiri,"

    "Unaishi wapi?"

    " Nangose."

    "Dini yako?"

    "Mpagani."

    "Hebu eleza ulifikafikaje katika nyumba uliyokutwa na ilikuwaje ukakutwa ndani katika nyumba ya watu?"

    "Mimi nilialikwa na wachawi wenzangu pale Kijiji cha Nangose na wakaniambia kuwa tuna safari ya mbali. Tuliambiwa tutasafiri kwa ungo. Wakasema mwenyeji wetu huko ni bibi wa Ajigale.

    "Mimi sikumjua huyo bibi na hakika nilikuwa kama bendera fuata upepo"

    Yule askari polisi alitugeukia sisi.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Jamani ile nyumba ndiyo anayoishi bibi wa Ajigale?" akauliza askari.

    "Hapana. Hiyo nyumba ni ya huyu mama jirani yangu," alisema shoga yangu huku akinyoosha mkono kuelekeza kwangu. "Na huyu ndiye mama Ajigale."

    "Sasa wewe mchawi mbona unataka kunichanganya? Nakuuliza uliingiaje pale uliponasa, unasema mambo ya nyumba nyingine, ohoo, usinichezee," alifoka.

    "Hapana afande, nakuja hukohuko. Nimeanza mwanzo ili unielewe."

    "Endelea."

    "Lengo la safari ilikuwa kwenda kufanya uchawi katika nyumba ya akina Ajigale. Sasa tuliondoka kwa ungo kutoka Nangose na baada ya kufika kwa bibi wa Ajigale, alitoa mashitaka kuwa mama wa nyumba niliyoingia alitangaza kuwa huwa anatuona kila tunapofika pale usiku."

    "Kwani huwa mnafika mara kwa mara?"

    "Ndiyo, huwa tunafika mara nyingi."

    "Mkifika huwa mnafanya nini?"

    "Hakuna cha maana tunachokifanya. Huwa tunamchukuwa mwenye nyumba na kwenda naye makaburini."

    "Makaburini kufanya nini?"

    "Si ndiyo uchawi wenyewe? Tunakwenda kumchezea maana kwa kufanya hivyo mama yake yaani bibi wa Ajigale hufurahi."

    "Anafurahia kitendo hicho cha kumchukuwa mwanaye?"

    "Ndiyo na anasema anataka amfundishe uchawi ili akifa arithi mkoba wake wa kichawi."

    "Akitataa je?"

    "Hawezi kukataa, atapumbazwa kwanza kwa dawa za kichawi kabla ya kuambiwa uamuzi wa mama yake, angezidi kukataa, hakungekuwa na namna nyingine zaidi ya kumfanya kitoweo."

    "Mlikuwa hamumuogopi mkewe wakati mnamchukua?"

    "Mkewe tulikuwa tunamtia dawa ya usingizi, kwa hiyo tukimchukuwa mumewe alikuwa haoni na hata mumewe alikuwa hajui kinachoendelea."

    Aliposema hayo niliishiwa nguvu kwa kuona hatari ambayo mume wangu anataka kufanyiwa na mama yake, kwamba angekataa uchawi, angeliwa nyama yake? Hilo lilinitisha zaidi.

    Lakini mchawi yule hakujua kuwa mimi nilikuwa sipumbaziki na dawa zao, nilikuwa naona kila kitu kama nilivyosimulia hapo mwanzo.

    "Sasa ikawaje mkaenda nyumba ya jirani?"


    "Ilikuwa tunakwenda kuwanyamazisha kwa sababu Bibi wa Ajigale (mama mkwe wangu), alisema kesho yake wangekwenda kwa mzee wao ili awape dawa ya zindiko la nyumba ya Baba Ajigale kitu ambacho bibi hakupenda. Nilitumwa nikawamalize."

    Maneno hayo yalimtia hasira mume wa shoga yangu na nilikuwa namuona dhahiri alikuwa akitetemeka pale alipokuwa ameketi. Naamini ingekuwa pale siyo kituo cha polisi, angemrukia na makubwa yangetokea.

    Jibu lile lilimfanya polisi aliyekuwa akichukuwa maelezo ageuze shingo na kutuangalia kama vile ni mtu aliyekuwa anasema kimoyomoyo mngemalizwa nyie'. Akaendelea kumhoji:

    "Ukawamalize kwa kutumia silaha gani?"

    "Tulikuwa na mabomu ya kichawi, alikuwa ameyachukuwa Bibi wa Ajigale."

    "Mlilipua hilo bomu?"

    "Hapana, huwa ni la kutegea mlango wa chumbani na mimi ndiye ilikuwa nikifika mlango wao wa chumbani, bibi anikabidhi kisha nimalize kazi. Lakini kabla hata sijakaribia mlango wa chumba, nikiwa sebuleni nikanasa. Nilijikuta siwezi kusogeza mguu wala kurudi nilipotoka. Hayo ndiyo maelezo yangu."

    Yule afande aliyekuwa akimhoji alimpa kusaini kila karatasi aliyoandika maelezo yake naye alifanya hivyo huku akitetemeka.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Polisi aligeuka na kutuangalia kwa mara nyingine. Alisimama na kujinyoosha kisha alimuita askari mmoja ambaye hakuwa na cheo chochote, wenyewe huwaita praiveti akamuamuru amchukue yule mchawi Pimbi Msafiri akamfungie mahabusu.

    "Sasa mzee njoo nawe nipate maelezo yako. Jamani huyo bibi anayetajwa mnamjua?" aliuliza yule Inspekta wa polisi.

    "Ni mama mkwe wake huyu mama," yule baba mwenye nyumba jirani yangu akajibu huku akinyoosha kidole kuelekeza kwangu.

    "Duh, mama mpo salama hapo kwenu kweli?"

    Niliona aibu sikujibu swali hilo kwa sababu ukweli ni kwamba mimi pia nazozana mara kwa mara na mama mkwe wangu kutokana na tabia yake ya kishirikina na hasa alipogundua kuwa kuna mpango wa kwenda kwa mzee wa jirani yangu akatupe dawa ya zindiko ili tuizindike nyumba yetu baada ya wao kugundua kuwa wachawi walikuwa na kawaida ya kuja usiku kutuwangia.

    Baba mwenye nyumba baada ya kuhojiwa jina lake na kabila pamoja na dini yake, mahojiano na polisi yalikuwa hivi:"Mzee uliamua uwapeleke jirani zako kwa baba yako akafanye zindiko kwenye nyumba yao, kwa nini ulivutika kufanya hivyo?"

    "Nilivutika kwa sababu niliona jirani zangu wanateswa na wachawi kila siku usiku."

    "Wewe ulikuwa ukiwaona hao wachawi?""Ndiyo. Nilikuwa nawaona na mara nyingi tulikuwa tunaamshana na mke wangu na kushuhudia vituko vyao bila wao kutuona. Tulipoona wamezidisha vituko tukawa tunaacha taa zetu bila kuzima ili waingiwe na woga, lakini wakawa hawajali."

    "Ukafanyaje?"

    "Nilimtuma mke wangu huyu akawaambie na alipowaambia mama mkwe wake huyu mama alikuwepo ndipo usiku wa leo walipoamua kutuangamiza kama mchawi Pimbi alivyokueleza. Hawakujua kuwa nyumba yetu imezindikwa na siyo rahisi mchawi kuingia na kuleta madhara. Hayo ndiyo maelezo yangu."

    Mzee huyo alisainishwa na polisi maelezo hayo. Yule askari alisema tusubiri kidogo kwani anakwenda kwa mkuu wa kituo kumpa taarifa na kupata maelekezo yatakayofuata. Hakuchelewa alirudi akasema:

    "Tumekubaliana kwamba bibi naye akakamatwe, ahojiwe. Hivyo, mzee kaingie kwenye gari difenda' la polisi ukatuoneshe nyumba tukamtie mbaroni."


    Mzee huyo alisainishwa na polisi maelezo hayo. Yule askari alisema tusubiri kidogo kwani anakwenda kwa mkuu wa kituo kumpa taarifa na kupata maelekezo yatakayofuata. Hakuchelewa alirudi, akasema:“

    TUMEKUBALIANA kwamba bibi naye akakamatwe, ahojiwe. Hivyo, mzee kaingie kwenye gari ‘difenda’ la polisi ukatuoneshe nyumba tukamtie mbaroni.”

    Mzee mwenye nyumba aliingia kwenye gari lakini mimi pia kwa kuwa majirani walisema ndiye ninayeishi naye niliambiwa niwemo kwenye msafara.

    “Lakini mume wangu ambaye ndiye mama yake yupo nyumbani, nendeni tu mtamkuta,” nilijitetea kukwepa kwenda kumkamata mama mkwe wangu.

    “Hapana mama, mambo ya wanaume huyajui, tunaweza kufika pale tukakuta huyo mumeo hayupo,” alisema askari polisi.

    “Mama twende tu, tutarudi wote.”

    “Basi kama ni hivyo tuondoke na mkeo,” nikashauri.

    “Sawa, twendeni kwani gari hili lina nafasi kubwa.”

    Mwendo wa gari haukuwa mrefu kwa sababu dereva aliwasha king’ora, hivyo magari barabarani yakawa yanatupisha.

    Tulifika nyumbani tukamkuta mume wangu akiwa ameketi nje ya nyumba na mama mkwe alikuwa ndani.

    Mume wangu macho yalimtoka kutokana na kusikia king’ora cha gari la polisi likiwa na askari wawili likisimama mbele ya nyumba yetu.

    “Mzee habari za hapa?” askari kiongozi wa msafara alimsalimia mume wangu.

    “Nzuri jamani, kuna nini?”

    “Tumekuja kumchukuwa mama yako.”




    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mama?”

    “Ndiyo anahusika na…?”

    “Anahusika na nini wakati tukio linatokea alikuwa hapa nyumbani?”

    “Hapana. Ametajwa na yule mchawi aliyenasa ambaye tunamshikilia kituoni.”

    “Mchawi?”

    “Kwani mzee huna habari kwamba hapo kwa jirani yako kuna mchawi leo usiku amenaswa?”

    “Najua na mke wangu nimemuagiza amsindikize shoga yake.”

    “Yupo kwenye gari na shoga yake. Alijaribu kukataa tusije naye lakini nimemlazimisha na tunaye kwenye gari pamoja na majirani zako.”

    “Ahaa, mke wangu shuka basi tujadili kabla mama hajachukuliwa,” akasema.

    “Mzee huo siyo utaratibu, lakini muite na mzungumze,” alielekeza yule askari.

    Nilishuka na kumfuata mume wangu. Tuliingia ndani na kumkuta mama mkwe akiwa ametoa macho kama vile amekabwa.

    “Ehee huko polisi mambo yalikuwa vipi?” aliniuliza mume wangu kwa kunong’ona ili askari aliyekuwa nje ya nyumba yetu asiweze kutusikia.

    “Yule mchawi kamtaja. Kasema walikuwa na mama mkwe lakini yeye ndiye aliyeingia ndani na mama akabaki nje,” nami nilimnong’oneza.

    “Hakuna njia, inabidi tumsindikize.”

    Tulitoka nje tukiwa na mama, kama ilivyo ada, watu wakajaa tele nje ya nyumba yetu wakitaka kujua kwa nini polisi wamefika tena kwa king’ora.Watu walizungumza mengi, wengine wakisema mama mkwe ndiye aliyesababisha yule mchawi anase, wengine wakawa wanasema naye aliingia ndani lakini kwa kuwa ni ‘mzima’ kishirikina, alichomoka na kumuacha yule mchawi kijana akiwa ameng’ang’ana sakafuni.

    Lakini wapo waliopatia na kusema kwamba mama mkwe wangu alimsindikiza yule mchawi kuwamaliza wale majirani huku wengine wakimtoa kabisa na kuona kuwa yeye alikwenda kuwaonesha nyumba tu ili mchawi amalize kazi kwa wale jirani.

    Mazungumzo hayo watu walikuwa wakiyasema kwa sauti na sisi wote tulikuwa tukiyasikia waziwazi na kumuongezea hofu mama mkwe wangu ambaye alikuwa hajui hasa atakachofanywa polisi.

    Nilimuangalia nikamuona anatetemeka kama vile alikuwa anaumwa malaria kali kwani hata kanga ilikuwa inamshinda kuifunga ikawa inaanguka, uzuri ni kwamba ndani alikuwa na gauni refu.

    Ilibidi kila wakati nimfuate na kumfunga vizuri kanga yake iliyokuwa ikianguka wakati tunakwenda kupanda gari la polisi.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kabla sijapanda gari nilimuuliza mume wangu kama mtoto wetu Ajigale alikuwa ndani au la kwa sababu alitakiwa aende shule, akasema alimkodishia teksi na tayari ameshafika shuleni kwa sababu aliwasiliana na mwalimu wake wa darasa akamjuza.

    Mama mkwe aliingizwa kwenye gari nami nikamfuata lakini mume wangu alikuwa akitufuata kwa nyuma akiwa kwenye gari lake.Kama tulivyokuja nyumbani, safari ya kurejea polisi ilikuwa fupi tulifika na kukuta watu kibao wakiwa wanangoja ili wajue kitakachoendelea.





    Je, nini kitafuata? Fuatilia mkasa huu wa kusisimua Kesho..... 




    ITAENDELEA     

0 comments:

Post a Comment

Blog