Search This Blog

UCHAWI WA MAMA MKWE - 3







    SIMULIZI : UCHAWI WA MAMA MKWE

    Sehemu ya Tatu (3)


    Moyo ulinipiga, nikawa najiuliza ni nini mume wangu anataka kuzungumza na shoga yangu lakini sikupata jibu. Nilijiuliza sana kwa sababu hakuwahi kuniambia kama anawahitaji hawa majirani zetu hata siku moja, nilibaki nikiwa nimepigwa butwaa.

    Mama mkwe naye alikuwa mtu wa wasiwasi baada ya kuona shoga yangu anarudi kwenye kisebule cha nje. Akawa anadhani kuwa inawezekana anataka kumueleza habari za wachawi kutuchezea usiku.


    Haraka sana alichukuwa kigoda na kukiweka kwenye kona ya kisebule cha nje, akaketi. Mimi na jirani yangu tulikaa kwenye viti vya plastiki ambavyo huwa vinakaa pale sebuleni kila siku.

    Mume wangu alikwenda kuegesha gari kwenye banda lake na mtoto wetu Ajigale alitoka garini mbio na akaingia ndani, nilimuelekeza kuwa chakula kipo kwenye hotpoti' juu ya meza ya chakula na mchana wa siku hiyo nilikuwa nimeandalia pilau.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kumuambia hivyo alitoka mbio kuingia ndani maana tulikuwa tumemkuna' kwani pilau ndicho chakula anachokipenda sana.

    Baada ya sekunde kadhaa mume wangu alifika pale kwenye kisebule. Kulikuwa na kitu ambacho hakikuwa na mtu, hivyo aliketi.

    "Ndiyo jirani, kaka hajambo?"

    "Hajambo, vipi leo nakuona kama vile umewahi sana."

    "Ahhh leo nimeamka naumwa mwili wote kama vile nilikuwa nafanyishwa mazoezi."

    "Umepima, isije ikawa malaria?"

    "Nilipima. Mimi nilikuwa na wasiwasi sana. Unajua siku hizi ukijisikia homa yale mawazo ya malaria huna, unafikiria homa ya dengue."

    Tulicheka wote watatu isipokuwa mama mkwe aliyekuwa ameketi kwenye kigoda akiwa bize kusuka mkeka wake.

    "Unajua huu ugonjwa wa dengue ni gumzo sasa nchi nzima. Tumuombe Mungu atuepushie mbali. Sasa ulipopimwa wamegundua nini?" jirani aliendelea kudadisi.

    "Hawajaona ugonjwa wowote wakasema labda ni uchovu wa kazi."

    "Hapana shemeji yangu. Mimi nilikuja hapa kumjulisha mkeo jambo zito kidogo."

    "Jambo zito, umenishitua, kuhusu nini tena shemeji?"

    "Nilimwambia kuwa nyinyi katika nyumba yenu mnaishi kitoto kwa sababu huwa kuna wachawi wanakuja usiku na kuondoka na mtu mara kwa mara hapa kwenu."

    "Unayoyasema shemeji ni kweli au unaota au unanitania?

    "Shemeji tangu lini nawatanieni? Nasema hayo siriasi kwa sababu nawapenda."

    "Wewe umejuaje au umeonaje?"

    "Sikufichi shemeji mimi nyumbani kwetu baba yangu ni fundi sana wa mambo mengi ya kishirikina, yeye harogi lakini ana uwezo wa kukuzindika na kukufanya uweze kuona wachawi."

    "Kweli shemeji?"

    "Kwa nini niseme uongo, kweli na ndiyo maana mimi huwa naona kuna kitu kinachofanyika hapa kwako. Tushukuru kwamba hukuweka ukuta na badala yake umezungushia seng'enge, hivyo kuwa rahisi kwangu kuona kinachofanyika hapa."

    "Dahh kama ni hivyo tumo hatarini. Mumeo anayajua haya?"

    "Yeye pia kazindikwa anaona wachawi, wakija hapa huwa aliye macho anamuamsha mwenzake, anajua kila kitu."

    "Sasa mbona hajaniambia mambo ya hatari kama hayo?"

    "Aliniambia kazi hiyo niifanye mimi kwa kumuambia mkeo maana yeye na wewe wote muda wenu wa kurudi kazini huwa mbaya."

    Wakati shoga yangu akimuelezea mume wangu mambo hayo ya kilozi, mama alikuwa akinikodolea macho huku akiweka vidole vyake mdomoni, niligundua kuwa ananikataza kusema chochote kuhusiana na jambo hilo.

    Anaelewa mimi pia najua kuwa wachawi huwa wanakuja nyumbani mwetu na yeye ndiye mwenyeji wao.

    Anajua pia kuwa usiku uliopita ambao mume wangu analalamika kuwa anaugua mwili, yeye mama mkwe aliongoza wachawi wenzake kumchukua na kumpeleka wanakojua wao nami niliona.

    Hata hivyo, ukweli ni kwamba sijui walikwenda kumfanyia nini lakini kitu kimoja ambacho ni wazi kabisa ni kwamba kwa siku zote ambazo wanakuja wachawi, mume wangu hajimudu kunipa haki yangu ya kindoa.

    "Sasa jirani kwanza nakushukuru kwa kutupa habari hiyo mbaya. Lakini haitoshi kutuambia tu, tueleze sasa tufanye nini kuondokana na hali hiyo?"

    "Kwani jamani sikuwaambia? Kwamba baba yangu ni mtaalam wa kuzuia ushenzi huo mnaofanyiwa."

    "Ina maana unaweza kutupeleka kwa baba yako ili akatuzindike na sisi pamoja na nyumba yetu?"
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Maelezo ya yule jirani yetu yalimchanganya mume wangu lakini mimi sikuwa na presha kwa sababu nilikuwa najua zaidi ya maelezo yaliyotolewa. Tofauti ni kwamba mimi nilikuwa najua kuwa aliyekuwa akichukuliwa na kupelekwa kusikojulikana ni mume wangu.

    Nilifarijika kwa sababu mama mkwe sasa ameshuhudia kuwa aliyesimulia au kutoa siri ya tukio hilo la usiku siyo mimi, hivyo mimi kumuona yule jirani yangu kuwa ni mwokozi wa roho yangu.

    Tulikubalinana na yule jirani kuwa kesho atatupeleka kwa baba yake ambaye ni mtaalamu wa mambo ya ulozi.

    ***

    Usiku wa siku hiyo ulikuwa wa balaa kubwa kama ilivyo ada wachawi walifika nyumbani kwetu saa nane au saa tisa za usiku wakiwa katika kikundi na kumchukua baba watoto wangu. Ni mama mkwe alikuwa akisimamia zoezi hilo. Mimi kama ilivyokuwa mwanzo nilijifanya nimelala fofofo.

    Lakini baada ya majadiliano kati ya kundi lile la wachawi na mama mkwe iliamriwa kuwa asichukuliwe mume wangu na badala yake nichukuliwe mimi.

    Niliogopa sana na kuamini kuwa sasa muda wangu wa kuishi hapa duniani umekwisha.

    Niliamini hivyo kwa sababu nilikuwa sijui chochote kilichokuwa kimeamriwa nje ya nyumba baada ya kuondoka na mume wangu kwani baada ya dakika chache niliuona msafara ukirejea chumbani huku ukiwa umembeba mume wangu.

    Nilijua kuwa kilichokuwa kimefanyika ni kubadilishana mimi na mume wangu lakini sikujua kabisa sababu ya wachawi wale kufanya hivyo na hicho ndicho kilichokuwa kikinitisha zaidi.

    "Kwani huyu unataka tumchukue unataka akafanye nini?"

    "Nataka naye tukamfundishe uchawi."

    "Tukamfundishe uchawi, kwani huyu mkweo ni ndugu yenu?"

    "Ni makubaliano kati yake na mumewe."

    "Alikuambia?"

    Mama mkwe alikaa kimya kwa muda bila shaka alikuwa akitafakari nini cha kujibu. Baada ya sekunde kadhaa alibadili jibu akawaeleza kuwa ni yeye aliyeamua hilo.

    "Unajua kuna koo hazitaki kushiriki mambo ya ulozi."

    "Najua."

    "Kama unajua kwa nini unampangia mwanao jambo zito kama hili?" alikuwa akiulizwa na mtu mmoja ambaye alikuwa anaonekana kama ndiye kiongozi wao na nilijua hilo kutokana na mtu yule kuvaa shanga nyingi shingoni na kuonekana dhahiri kwamba alikuwa na amri za mara kwa mara kwa wale wachawi ambao walitekeleza kila alichowaambia.

    Sijawaeleza kwamba wachawi hawa ambao walikuwa hawapungui kumi kila mmoja alikuwa amevaa nguo nyeusi na nyuso zao zilikuwa zimepakwa majivu na ilikuwa siyo rahisi kumtambua mtu kwa sura.

    Sikuwa na la kufanya pale kwa sababu nilijisemea kimoyomoyo hapa nikijifanya nakataa safari yao, basi wanaweza kunimaliza kwa kuniua moja kwa moja.'

    Nilipakwa yale majivu kisha nikajikuta nikiinuliwa juu kwa juu kama maiti huku nikiwa nimefunikwa na nguo nyeusi.

    Baada ya kutoka nje ya nyumba yetu niliiangalia ile nyumba ya jirani yangu nikagundua kuwa taa za ndani zilikuwa zinawaka, nikatambua kuwa walikuwa macho na waliona kila kilichoendelea pale. Lakini nadhani hawakuwa na uwezo au labda nao waliogopa kuingilia kati mambo haya ya kichawi.

    Nililazwa nje ya nyumba yetu na mchawi mmoja akawa ananitambuka huku akisema maneno ambayo nilikuwa siyaelewi. Mchawi yule alifanya hivyo zaidi ya mara kumi.

    Baadaye nilinyanyuliwa na kuwekwa kwenye chombo chao ambacho ni ungo mkubwa. Niliketishwa kisha kukawepo na mtu aliyekuwa amekaa nyuma yangu na kunishikilia nisianguke.

    Nami kwa kuwa nilijua hatari ya kujionesha kuwa niliona kila kitu, nilijilegeza ili yule mtu aliyekuwa amepewa kazi ya kunishikilia aamini kuwa nilikuwa sijielewi.
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Nilipakatwa na wakati natafakari nini cha kufanya mama mkwe aliwaeleza wachawi wenzake kwamba kuna mama jirani amegundua njama zao.

    "Yupo mama jirani hapa amegundua mchezo huu tunaoufanya," alisema mama mkwe.

    "Ulijuaje kuwa amegundua?" kuna mchawi mwingine aliuliza, sikuweza kumuona kwa sura kwa sababu nilikuwa nimefumba macho kudanganya kwamba sijifahamu kutokana na dawa walizokuwa wamenipaka usoni.



    Naamini dawa zile walizopaka kwenye sura yangu zilikuwa zikiaminiwa na wachawi wale kuwa zingenifanya nikose fahamu kwa sababu walifanya hivyo kwa mume wangu chumbani na tulimuacha akiwa hajitambui.

    "Alikuja mchana na kuwaambia hawa (yaani mimi) na mwanangu (mume wangu)," alisema mama mkwe.

    Baada ya kutamka maneno hayo, wachawi wale walipigwa na butwaa nami nikashushwa katika ungo ambao waliuandaa ili niruke nao.

    Baadaye mchawi mwingine ambaye alionekana kana kwamba ndiye mwenye madaraka zaidi pale au kiongozi aliamuru turudi kwanza ndani.



    "Hapa nje kufanya mashauri hayo siyo mahali pake, naomba turudi ndani ili tukayaongee haya," alisema kiongozi wa wachawi.

    "Sawa, kwa hiyo tumrudishe mama Ajigale ndani siyo?" aliuliza mama mkwe.

    "Ndiyo maana yake. Hujanielewa? Vijana fanyeni kazi yenu," alisisitiza yule kiongozi.

    Nilijikuta nikinyanyuliwa juu kwa juu hadi chumbani kwetu.



    Nilikuta mume wangu akiwa bado hajitambui na pembeni yake kulikuwa na mwanamke mwingine mchawi ambaye alikuwa akimlinda ili kuhakikisha kuwa hazinduki kabla mimi sijarejeshwa kutoka huko walikotaka kunipeleka.

    Baada ya kuingizwa ndani nililazwa kando ya mume wangu na kundi kubwa la wachawi walikuwa wamekizunguka kitanda.

    "Sasa tusimulie, huyo mama jirani alikuwa akiwaambia nini hawa wanao?" alisema huyo mchawi kiongozi ambaye jina lake zikuweza kulifahamu.



    "Aliwasimulia kuwa kuna wachawi huwa wanafika hapa na kumchukua mtu, lakini aliwaahidi kuwa atawapeleka kwa baba yake ili akawape zindiko kwa hiyo naamini kesho atafanya hiyo kazi," mama mkwe alisema.

    "Kama hivyo ndivyo naomba kitu kimoja, mtu mmoja aende sasa hivi kwenye nyumba ya mama huyo jirani akaone kama ana ubavu wa kutuzuia kufanya kazi yetu hususan kumchezea."



    Aliamrishwa mtu mmoja kati ya wale wachawi waliokuwa wamezunguka kitanda kufuatana na mama mkwe wangu hadi kwa yule mama jirani yetu.



    Walitoka na kwenda moja kwa moja kwa mama jirani. Sikuthubutu kufumbua macho ili kuona alikuwa amefuatana na nani lakini nilisikia wakitoka huku wakiwa wanashauriwa kutoacha usinga ambao hufanya kutengua zindiko lililowekwa katika nyumba wanayopania kufanya uchawi wao.



    Watu hao wawili walifika katika nyumba ya jirani yetu na walikuta bado taa zikiwa zinawaka nje na ndani.

    "Anza wewe mwenye usinga kwenda kuingia ndani," ulikuwa ni ushauri wa mama mkwe.

    Yule kijana aliyepewa kazi hiyo alimuangalia mama mkwe na kumtupia swali.

    "Nikiingia ndani, nifanye nini?"

    "Wewe ingia tu, si tunaangalia kama nyumba hii ni nyepesi au nzito?"

    "Hilo ni jambo gumu. Kama nyumba ni nzito itakuwaje?"

    "Kama ni nzito tutarudi kwa kiongozi wetu pale nyumbani kwa mwanangu halafu atajua cha kufanya."

    ***


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mle ndani wale wachawi waliobaki na kiongozi wao kazi yao ilikuwa kuchezacheza huku wakiimba kwa sauti ya chini sana.

    Mmoja ambaye naamini ndiye alikuwa kiongozi wao alikuwa akitia uvumba kwenye chetezo ambayo walikuja nayo na moshi ukatanda chumba kizima.


    Muda mfupi baadaye nilisikia sauti kali kama ya radi, nilipigwa na butwaa na kujiuliza kama nje kuna mvua au ni nini, sikuwa na jibu.

    Baada ya dakika kadhaa kupita na wachawi wakiendelea kucheza ngoma za kichawi kwa kutumia manyanya, aliingia mama mkwe huku akitweta kama mtu aliyekuwa akikimbizwa.


    Mama mkwe alianza kueleza yale niliyoyaeleza juu kwamba walifika katika nyumba ya jirani yetu na walikuta bado taa zikiwa zinawaka nje na ndani ya nyumba.

    Akasema walibishana na kujiuliza nini watafanya mle ndani, "Nikiingia ndani, nifanye nini?"

    "Wewe ingia tu, si tunaangalia kama nyumba hii ni nyepesi au nzito?"

    "Hilo ni jambo gumu. Kama nyumba ni nzito itakuwaje?"

    "Kama ni nzito tutarudi kwa kiongozi wetu pale nyumbani kwa mwanangu halafu atajua la kufanya," nimemuambia na ndiyo maana nimerudi.



    "Sasa nyumba ni nzito ya huyo jirani ina maana ina zindiko?" alihoji kiongozi wa wachawi.

    "Ndiyo maana yake kwa sababu yule kijana ameingia ndani, lakini ameshindwa kutoka, kwa maana nyingine ameganda, hawezi kunyanyua mguu."

    Wachawi wote mle chumbani waliachana na mimi na mume wangu na kumzunguka mama mkwe ambaye alisimulia mengi na hasa jinsi alivyotumia usinga ili kumuokoa kijana aliyekuwa amefuatana naye lakini ikashindikana.



    "Kilichobaki sasa ni sisi kwenda kwenye nyumba hiyo jirani ili kuangalia jinsi ya kumuokoa mwenzetu."

    "Lakini nani ana zana za kumnasua mchawi akinasa?" aliuliza mama mkwe.

    Mtu mmoja alisema yeye anao unga mweusi ambao ni mchanganyiko wa mkaa wa mifupa ya sokwe mtu na mafuta ya simba dume na ya nyani ambayo huwekwa kwenye tunguri.

    Watu wengine wawili na mama mkwe pia yule mwenye dawa walikwenda nyumba jirani kwenda kumuokoa mwenzao aliyenaswa ndani ya nyumba lakini baada ya dakika thelathini walirudi wakiwa hawana mlengwa.



    "Imeshindikana, ile nyumba ni hatari," alisema yule mwenye tunguri huku mama mkwe akitetemeka.

    "Mama mbona unatetemeka sana?" alihoji kiongozi wa wachawi.

    "Natetemeka kwa sababu yule mwenzetu kama itashindikana kumnasua na akakaa pale mpaka kesho asubuhi, nitaumbuka, kwa kuwa yule mama mwenye nyumba ile anajua wachawi huwa wanafika hapa, basi gogo litaniangukia."



    Iliamriwa kuwa kiongozi wao aende kwake akachukue dawa ambayo waliamini kuwa ni bora kuliko ile ya usinga ili waweze kwenda kumnasua mwenzao.



    Kitendo kile kilinifurahisha kwa sababu badala ya kunichukua mimi ili wanipeleke huko walikotaka kunipeleka sasa kazi iligeuka, ikawa ni kazi ya kumnasua mwenzao.

    Walitoka chumbani kwetu na kusimama sebuleni lakini kila lililokuwa likizungumzwa nilikuwa nalisikia.

    Chumbani kwangu kulikuwa na saa ya ukutani niliiangalia nikaona inasomeka kuwa ni saa tisa na nusu usiku na nilijaribu kumtingisha mume wangu, ikawa ni kazi bure kwani alikuwa amelala fofofo kutokana na dawa alizopakwa na wachawi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Jamani kaeni tu kwenye hizo sofa tumsubiri kiongozi," nilitambua sauti hiyo kuwa ni ya mama mkwe, alikuwa akiwakaribisha wachawi wenzake kama vile wapo pale kihalali kwa mambo halali.

    Kimyaa kilitawala kwa dakika kadhaa na nikawa natamani nishuke nikawachungulie lakini moyo uliniambia nisifanye hivyo kwa usalama wangu.



    Jogoo alisikika akiwika na jimbi langu (jogoo wangu) naye alidakia na kuwika, hali hiyo ilinifanya niinue kichwa na kuangalia tena saa, ikawa inasomeka kuwa imetimia saa kumi na dakika tano.

    "Hii hali inatisha sana, unasikia majogoo wanawika, hiyo inaashiria kuwa kunakucha na watu wataanza kutoka mitaani hasa wale wanaokwenda kuchukua bidhaa sokoni," alisikika mama mkwe akizungumza.

    "Sasa tufanye nini? Inatakiwa akili ya ziada kuamua cha kufanya," hiyo ilikuwa sauti ya mwanaume ambaye sikumjua kwa jina.



    "Au hapa tulipo kuna mtu ambaye ana dawa ya kumfanya mtu asionekane?" alikuwa ni mama mkwe akiwatupia swali wenzake.



    "Hilo ungelikumbuka wakati mkuu anakwenda nyumbani kwake kwa sababu kama hiyo dawa ipo, tungeitumia kama tutashindwa kumng'atua kwa leo pale aliponasa mwenzetu," alidakia mwanamke mwingine ambaye pia sikumfahamu kwa jina wala kumtambua kwa sauti yake. 


    Wakati wakiwaza hayo yule kiongozi mkuu wa wachawi akawa ameingia na tunguri zake nne zenye shanga.


    Walijitahidi kufanya shughuli zao za kishirikina kwa kujifanya kurusha kombora' lao la kichawi huku wakisema kwamba likitua kwenye nyumba ile ya jirani, litasambaratisha dawa zilizomfanya mwenzao anase.

    Nilisikia wakibishana wengine wakidai yule mkuu wao kakosea kuchanganya unga wa dawa walizotumia kutengeneza kombora hilo.

    Kwa kuwa kikao chao walikuwa wakifanyia kwenye sebule yetu, nilisikia wakisema dawa walizotia kwenye pembe ya nyati hazikutimia.

    Sikujua ni dawa gani walizotia kwenye ile pembe lakini nilisikia mtu akiambiwa apulize kuelekea kwenye ile nyumba ya jirani.

    "Nimepuliza limekwenda lakini sasa itabidi watu waende kumalizia kule kule kwenye nyumba," alisema yule mtu aliyekuwa akionekana kama kiongozi wao.

    Baadaye alitumwa mama mkwe na kijana mwingine kwenda kwenye ile nyumba ya jirani ili kumalizia dawa nyingine za kumnasua.

    Wachawi wengine wote walikaa kwenye kochi pale sebuleni kana kwamba walikuwa ni wageni wetu rasmi ambao walisubiri chakula au hotuba ya kukaribishwa na mwenye nyumba.

    Walikuwa wakinong'ona maneno ambayo mimi nilikuwa siyasikii lakini nahisi walikuwa wakijadili ugumu au kazi waliyonayo ya kumnasua mwenzao ambaye alinasa kwenye nyumba ya jirani.

    Nilijitahidi kumtingisha mume wangu ili kuona kama ataamka lakini ilishindikana kwani alikuwa akiendelea kukoroma kutokana na dawa walizomnusisha.Wakati naendelea kumtingisha mume wangu huku nikiwaza

    nini cha kufanya ili kumzindua nilisikia kishindo cha mlango wa barazani kufunguliwa.

    Nilijikusanya pale kitandani na nikaenda kuchungulia nikashuhudia mama mkwe akiwa na yule kijana wakiwa wamesimama mbele ya wachawi wenzao.

    "Imeshindikana," alisema mama mkwe.

    "Inamaana ile dawa haikufanya kazi?" alihoji yule kiongozi wao.

    "Ndiyo maana yake. Tumejitahidi kupuliza ile pembe nyingine kwa kupitia dirishani, ameshindwa kunasuka. Alikuwa akisema miguu imeganda kama vile imepakwa supagluu."

    Wakati wanazungumza hayo muda nao ulikuwa siyo rafiki yao kwani majogoo yalianza kuwika kuashiria kuwa kunakucha.

    "Sasa jamani tumeshaumbuka, tufanye nini?" alihoji mama mkwe.

    "Hakuna cha kufanya, tungoje jua lichomoze tuone mwenye nyumba atafanya nini," alisema kiongozi wa wachawi.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaongeza: "Cha kufanya kila mmoja arudi nyumbani lakini ni muhimu kuwahi eneo la tukio ili kuhakikisha tunamlinda mwenzetu."

    "Tutamlindaje wakati amenasa na tumejaribu kumnasua tumeshindwa?" alihoji mwingine.

    "Kumnasua kweli tumeshindwa lakini tunapaswa kuhakikisha kuwa tupo pale kwa sababu siku hizi kuna mtindo mbaya sana wa kuua watu," akasema yule kiongozi.

    "Umesema kweli, wote tuwe pale," akadakia mama mmoja ambaye sikumfahamu.

    "Unajua tukiwa wote pale tutazuia watu wasimpige au kumchoma moto. Ni hatari sana kama tutamuacha peke yake," alisisitiza yule mchawi kiongozi.

    "Lakini mimi sitaweza kwenda pale, nitakuwa nimeumbuka sana," ilikuwa ni sauti ya mama mkwe.

    "Sawa, wewe usiende lakini hutaeleweka vibaya?" alihoji kiongozi wao.

    "Hapana. Nikiamka tu nitajifanya nina malaria."

    Wote walikubaliana kwamba asubuhi wawe eneo la tukio na watu wakijazana basi nao wawe kama mashuhuda lengo kuu ni kuzuia mauaji kwa mwenzao.

    "Nenda chumbani kampake dawa ya kumzindua yule baba mwenye nyumba," aliamuru kiongozi wa wachawi.

    Haraka sana nilifumba macho huku nikiyafunua kidogo, kwa kuwa kulikuwa na giza hakuweza kuona kuwa naona.

    Nilimuona yule mchawi akifungua kibuyu kidogo na kumpaka mume wangu dawa sehemu ya pua.







    ITAENDELEA   

0 comments:

Post a Comment

Blog