Simulizi : Siku 100 Za Mateso Ya Kuzimu
Sehemu Ya Tatu (3)
Moshi mzito ulikuwa ukizunguka kama kimbunga mbele yao. Ajabu ni kwamba, moshi huo ulikuwa hausambai! Ilikuwa ni Moshi mrefu uliolingana na kimo cha miti ndani ya msitu ule. Ulikuwa umejikusanya pamoja na kuleta taswira ya kitu kama wingu jembamba lakini refu kwenda juu.
Katikati ya Moshi huo kulitoka ngurumo za kuogofya. Ngurumo nene. Sauti ile ambayo haikujulikana mara moja ni ya kiumbe gani, ilikuwa ikiunguruma kwa sauti ambayo haikuwa na chembe ya amani.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ungepata bahati ya kuona na kusikia kitu kile, ungekuwa sahihi kabisa kama fikra zako zingejenga dhana kuwa ndani ya moshi ule kulikuwa na kiumbe kisicho cha kawaida.
Hata hivyo, fikra zako zingesutwa na macho yako.Kamwe macho yako yasingeona kitu chochote katikati ya moshi ule wa aina yake!!.
Dalili mbaya zikaonekana.
“ Tukimbie…” mzee William alipaza sauti. Lilikuwa ni kosa. Kwani punde tuu baada ya kuzungumza maneno yale, moshi ule wa ajabu ulijongea kwa kasi ya kimbunga kwa mzee yule!
Mzee akabaki ameganda. Miguu yake haikuweza kutii agizo la ubongo wake, akashindwa kabisa kupiga hatua na kutimua mbio. Miguu yote ilikufa ganzi!
Moshi ule wa ajabu ukawa unaelea mbele ya uso wake. Sauti nzito za ghadhabu kutoka katikati ya moshi ule zilizidi kusikika, ilikuwa ni mara mbili ya ile ya awali. Ilikuwa ni kama vile ule ushauri wa kukimbia aliotolewa na mzee William ulichukiza.
Macho ya Amosi na Ngumije hayakupepesa. Wote wawili walikodolea tukio lililokuwa kikiendelea. Kadhalika, akili zao ni kama zilisimama kufanya kazi. Walikuwa wamebung’aa wakitizama tukio litakalomtokea mwenzao bila kuifikiria hatima ya maisha yao.
Hatimaye moshi mchache ulisambaa kwenye miguu ya mzee Wiliiam!.Haja ndogo ilimtoka mzee yule. Mapigo ya moyo yakamdunda kwa kasi. Hakujua ni kitu gani kingetokea kwenye maisha yake wasaa ule. Hakutaka kabisa kujidanganya kwamba yale yalikuwa ni mazingaombwe ambayo yangepita tu kama upepo.
Ghafla, alijikuta akipigwa mtama. Mzee Wlliam alibweka kama mbwa aliyejeruhiwa na fisi mwenye njaa, aliyempiga mtama huo hakumwona, ingawa alihisi kabisa kupigiwa na kitu kigumu. Akiwa nchini akigaagaa, moshi ule wa ajabu uliendelea kutambaa miguuni mwake
Kule walipokuwa wamesimama Amosi na Ngumije, wakapatwa na taharuki. Nyuso zao zenye hofu zilipatwa na taharuki baada ya kuona mwenzao akipaa kimo cha ndama na kujibamiza ardhini kama Lobota la nguo za mtumba.
Wakaendelea kushuhudia mzee yule akinyanyuliwa juu kama vile mwewe anavyobeba kifaranga angani, wakaendelea kuona Moshi ule ukiendelea kujisukasuka kwenye miguu ya mzee William, nafsi zao zilikiri kuwa moshi ule wa kichawi ndio ulikuwa ukitekeleza tukio lile.
Wakashuhudia kitu kingine cha kutisha. Mzee William Alikuwa akipiga yowe la uchungu na hofu kubwa. Ghafla alianza kubamizwa kwenye miti.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Puuu!!...puuu..puuu!!” ebwana wee!. Tukio lile lilitisha.
Mzee nyule alikuwa akibamizwa kwenye miti vibaya sana. Alituimika kama fimbo kuadhibu miti ile!
Alipiga yowe mara mbili tatu, kisha akanymaza tuli.
Dakika moja badaye mwili wa mzee Wiilliam alichiwa na kutupwa chini. Mwili ule ulikuwa hautamaniki, ulikuwa umepondwapondwa na kuharibika vibaya sana.
Tayari mzee William alikuwa maiti! Amosi na mwenzie walipagawa vibaya sana. Walizinduka kifikra na kuona walitakiwa kuokoa roho zao kwa namna yoyote ile.
Walitimua mbio za farasi, walikuwa wakikimbia huku wakipiga yowe. Kifo cha mzee William kiliwatisha vibaya sana.
Amosi alikuwa mbele hatua kama tatu, Ngumije alikuwa nyuma yake, hawakujua wapi ndani ya msitu huo itakuwa salama. Pamoja na kutojua hilo lakini waliona ni kheri wafe wakiwa wanakikimbia, kuliko kukaa na kukingoja kifo kije kitwae roho zao.
Walikimbia bila kuchoka ndani ya msitu. Walipuyanga hovyo bila kujua ni wapi wanakwenda. Kiasi cha kilometa tano ama sita walichoka kukimbia.
“Tupumzike,” Ngumije alisema huku akitweta. Amosi alikuwa akilia kama mtoto. Tukio walilokuwa wameliona kwa wenzao lilikuwa la kutisha.
“Ufukweni ni wapi?” Amosi alihoji. Tumaini pekee walilobaki nalo ni kufika ufukweni. Waliamini kuendelea kuwa ndani ya msitu huo ni kuendelea kurandaranda kwenye himaya ya majini na mizimu.
“Tumepotea..”
“Mungu wangu sasa tufanyeje?”
“Sijui..”
“Nafikiri tumezidi kuingia katikati ya msitu,” Amosi akasema huku akitupa macho huku na kule.
“Tuendelee kukimbia hadi tufike ufukweni…hiyo ndio sehemu salama kwetu.”
Hapakuwa na mjadala mrefu. Baada ya Amosi kusema, mbio zikaendelea. Amosi mbele Ngumije nyuma. Walipokuwa wamekimbia kama mita 20 ghafla sauti kali ikasikika nyuma ya Amosi!.
Alipogeuka hakuamini alichokiona. Moshi ule wa ajabu ulikuwa umemnyanyua Ngumije kichwa chini miguu juu.Ngumije alikuwa akipiga kelele vibaya sana, alitambua ilikuwa ni zamu yake kufa.
Amosi alichoka. Dalili za kubaki peke yake ndani ya msitu zilionekana.
Ngumije akiwa kaning’inizwa angani, naye akaanza kubamizwa katika miti, alikuwa
akipigwa kwa nguvu. Damu iliruka kila mahali.
Amosi macho yalimtoka. Maswahibu yaliyokuwa yakimpata mwenziye alitarajia naye kukutwa nayo.
Hakutaka kuendelea kushangaa. Ingawa alitambua naye atakufa, lakini hakupenda kabisa kufa kibudu. Alitimua mbio.
Akiwa katika mbio ndefu, mbio zisizojulikana wapi anakwenda, nyuma yake aliisikia vema sauti ya mwenziye akipiga yowe. Kelele za uchungu zitokanazo na kubamizwa kwenye miti na kiumbe cha ajabu zilipenya kwenye ngoma ya masikio ya Amosi.
Kadiri alivyokuwa akiendelea kwenda mbele, ndivyo mfifio wa sauti ya mwenziye aliyekuwa akiuawa uliendelea kuishilizia.
Naam. Hatimaye ndani ya msitu kukawa kimya!. Amosi litambua kwamba, hakuna kilichokuwa kinasikika tena zaidi ya pumzi zake mwenyewe.
Mihemo ya kuvuta na kutoa pumzi ndicho pekee kilichokuwa kikisikika. Alikimbia na kukimbia. Hakujua wapi patakuwa hatma ya mbio zile sanjari na mkuki wa kifo uliokuwa nyuma yake.
Waswahili husema, hakuna marefu yasiyo na mwisho. Baada ya mbio ndefu, bila kutegemea Amosi alijikuta anatokea sehemu ambayo hakuitarajia!
Ilikuwa ni sehemu yenye uwazi mkubwa, katika uwazi ule, kulikuwa na kijiji, palikuwa na nyumba nyingi zilizojengwa karibu karibu.
Shughuli za kijamii katika kijiji hicho zilikuwa zikiendelea, kama ungepata bahati ya kuona shughuli zilizokuwa zikifanyika, ungeona, watu wakilima bustani, wasichana walikuwa wakitwaga nafaka, vijana walikuwa wakichunga mifugo, lakini pia kulikuwa na uwanja wa mpira wa miguu ambapo watoto walikuwa wakicheza mpira.
Amosi alisimama, alikuwa mita kama ishirini kutoka eneo lile la wazi ambalo lilitenganishwa na msitu ule aliokuwa ametoka.
Akawa anatembea huku miguu yake ikiwa na kigugumizi kama alitakiwa kujitoma ndani kabisa ya kijiji kile ama arudi ndani ya msitu akabiliane na moshi wa ajabu!
Akiwa anahema kama jibwa koko lililonusurika kutafunwa na fisi mwenye njaa, mara mpira uliokuwa ukichezwa na watoto ukapigwa na kufikia miguuni mwake.
Mtoto mmoja katika wale wengi waliokuwa wakicheza katika uwanja ule wenye nyasi za kijani kibichi, akaukimbilia mpira.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mtoto aliyekimbilia mpira alipomfikia Amosi ambaye mpira ule ulikuwa mbele ya miguu yake, macho yao yalipo kutana, alijikuta akipigwa na butwaa. Kitu alichokiona kwa yule mtoto kilimfanya awe na mashaka na akili yake.
Akawabaki ameganda, huku ubongo na milango yake ya fahamu ukisimama kwa sekunde kadhaa kufanya kazi yake sawasawa kutokana na uzito wa kile alichokiona kwa mtoto yule.
“Hivi naota ama!” alinong’ona peke yake wakiwa wanaangaliana na mtoto yule.
“Naomba mpira wangu,” mtoto alizungumza kwa sauti ya upole.
Sauti ya mtoto yule ilikuwa ni kitu kingine kilichoendelea kumvuruga vibaya sana. Kitu alichokiona kwa mtoto yule ilifamfanya ajihisi huenda alikumbwa na wazimu.
Alikuwa amejiona yeye!. Mtoto yule alikuwa ni yeye mwenyewe!.
“Siwezi kujisahau mwenyewe,” akajimbia akilini, tukio la kukutana na mtoto ambaye aliona nafanana kila kitu na yeye alipokuwa angali mtoto lilimfanya kusahau kabisa juu ya moshi ule wa ajabu ulioua wenzake wote ndani yam msitu.
“Wewe ni mimi!” hatimaye akasema
“Unasemaje?” mtoto akauliza.
“Jina lako unaitwa nani?” Amosi hakujali swali la mtoto yule, naye akamtupia swali.
“Naitwa Amosi Mikidadi” yule mtoto akajibu bila kubabaika.
“Unasemaje!!!!”
“Naitwa Amosi….” Amosi alipagawa, mazingaombwe yaliyokuwa yakimtokea maishani mwake yalimwelemea.
“Mama yako anaitwa Greta Shangwera?” Amosi akamuuliza mtoto yule kwa sauti ya hamaki.
“Ndio”
“Kaka yako anaitwa Kiba na unawadogo zako wawili mapacha Sarah na Sophia.”
“Ndio,” Mtoto yule alijibu, naye alionekana kumshangaa mtu yule mgeni kaijuaje familia yake.
Amosi alichoka, hakujua ameangukia kwenye duani gani, na nini maana ya mambo yote yale.
“Je, unaweza kunipa mpira wangu?” Hatimaye mtoto yule alisema. Pamoja na kwamba naye alionekana kushangaa mtu yule mgeni kaijua vipi familia yake, lakini dakika hiyohiyo ilitosha kumpuuza!.
Watoto wenzake pia walikuwa wakipaza sauti kumtaka mwenzao awahishe mpira. Walionekana kufurahi maisha hasa yatokanayo na burudani ya mchezo huo.
“Nahitaji kuonana na wazazi wako.” Amosi akaongea kwa sauti yenye kushurutisha zaidi kuliko kuomba.
Lakini kabla ya kujibiwa mara ngurumo za ajabu zikasikika nyuma yao. Sauti zile zilitokea msituni. Ilikuiwa ni ngurumo za moshi ule wa ajabu.
Ngurumo zile zilizua kizaaazaa katika kijiji hikcho, kila mtu alikimbia, baadhi ya wazazi wakakimbilia katika uwanja ule wa mpira kwa ajili ya kunusuru maisha ya watoto wao.
Ilikuwa ni hekaheka, kufumba na kufumbua mara mwanamke mmoja ambaye hakujulikana alikotokea aliwasiri pale alipokuwa yule mtoto mwenye kuitwa Amosi na kumnyakua kama kifaranga.
Amosi naye akachanganyikiwa, alichanganyikiwa kwa mambo maawili, mosi ni ile ngurumo ya moshi ule hatari, pili mtu aliyemnyakaua mtoto, mtu yule aliyefanya tukio hilo alikuwa ni mama yake mzazi, Bi Greta shangwera. Na mtoto aliyebebwa na mwanamke yule alikuwa ni yeye mwenyewe!!!
TAHARUKI KUBWA iliendelea kutokea kwenye ule mji, kelele za woga na tahadhari kwenye kijiji kile zilisikika. Ngurumo za kutisha, zikitoea ndani ya msitu, zilizidi kurindima.
Mambo yote hayo, hayakufanya ile tahayari ya Amosi kuondoka, bado aliendelea kuduwalia mauzauza yale.
Vipi ajione mara mbili, yanii ajione yeye angali mdogo, akiwa mikononi mwa mama yake, mama ambaye alifariki siku kadhaa zilizopita,kabla ya kutokea kwa ajali ya ndege na mwili kutoweka.’
“Kimbia wewe utakufa,” mtu mmoja alimbwatukia. Akili ya kijana yule ikazinduka. Ufahamu wake ukatoka katika ututusa. Wakati huo huo wale watu aliokuwa akiwakodolea macho walipotelea katika kijumba kidogo cha makuti.
Walisalia watu awachache ambao nao walijitoma katika nyumba ama vyumba zao na kukomea milango, hali ilivyoonesha ni kama balaa lile lilikwisha zoeleka.
Amosi alikuwa akitimua mbio huku akiangalia ni sehemu gani angeweza kujibanza, mbele yake akona nyumba. Watu kadhaa walkuwa wakijitoma, upesi naye akakimbia na kuingia ndani. Mlango ukakomewa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Giza ndani ya kijumba likatamalaki. Ukimya ukachukua hatamu. Hakuna kilichosikika zaidi ya zile sauti za ngurumo zilizotokea msituni.
Kadiri sekunde zilizvyozidi kuyoyoma ndivyo, sauti za ngurumo zilivyokisigolea kijiji. Amosi akazidi kujikunyata, picha ya jamaa zake wakifa kifo cha kinyama ndani ya msitu ikawa inajitengeneza kichwani mwake.
Ngurumo zikakivaa kijiji. Ikawa ni mithili ya helkopta inayoshuka kwa kasi katika uwanja. Amosi akaendelea kujikunyata.
Dakika chache badaye, mara sauti zile zikatulia. Ilikuwa ni Ghafla. Yanii ni kama vile umeme uliokuwa ukiendesha kadhia ile ulikatika!.
Dakika tano badaye, mchakato wa nyayo za mtu zikasikika.
“Imeondoka,” mtu mmoja alisema.
“Una uhakika?” mtu mwingine akahoji, Amosi akabaki kimya, mambo yale yalikuwa ni mapya kwake.
“Dunia gani hii!!” akajiuliza kimoyomoyo.
Mtu mmoja alifungua mlango, mwanga ukakivaa chumba, watu sita waliokuwa ndani ya chumba kile, wakajitoa mafichoni.
“Wewe ni nani?” sauti moja ikamuuliza, baada tu na yeye kutoka nje ya kijumba kile. Akageuka, akakutana na sura ya mwanaume wa makamo.
“Naitwa Amosi”
“We Mgeni hapa?”
“Ndio”
“Umetokea wapi?”
“ Mimi ni moja ya wahanga wa ajali ya ndege ya Panasonic Airline, tumeanguka siku tatu zilizopita huko ufukweni, watu wengi wamekufa hata wale waliokuwa wamebahatika kunusurika wamekutana na shambulio baya sana ndani ya msitu” Amosi alisema.
Mzee yule akaonekana kukanganywa na hadithi ile aliyopewa. Akamkazia macho kisha akamwambia:
“Njoo huku”
Akamwonoza hadi kwenye nyumba moja ya bati, ilikuwa ni nyumba nzuri kuliko zote zilizokuwa katika kijiji kile.
Aliingia ndani ya nyumba ile. muda mfupi badaye akatoka akiwa ameongozana na wazee wawili, na vijana watatu.Vijana wale walikamata silaha za jadi.
Macho ya Amosi yaliposaili nyuso za wanaume wale vijana, akajikuta katika taharuki nyingine kubwa.
Miongoni mwao, alikuwepo baba yake.. Mikidadi.. Ajabu katika nyakati zile alionekana kuwa ni kijana wa miaka 29 ama 33.
Macho yakamtoka pima. Akabaki akimwangalia kijana yule ambaye kimsingi alikuwa ni baba yake mzazi, alimwangalia kwa mshangao mkubwa.
“Mtu mwenyewe ni huyu” mwenyeji wake,aliambia ile timu aliyotokanayo nje.
“Hujambo?” mzee mmoja akamwongelsha huku akimwangalia kwa jicho kali.
“Sijambo” akajibu huku akimwangalia baba yake ambaye wasaa ule alionekana kijana.
“Unasema unaitwa nani na umetokea wapi”
“Naitwa Amosi mikidadi,..” alisema kisha akaendelea.
“Nilikuwa natokea Marekani, naekea Tanzania katika mazishi ya mama yangu bi Greta Shangwera”
Kauli ile ikaibua mshangao mwingine kwa wale watu, lakini zaidi alikuwa ni Mikidadi.
“Unasema nini wewe!” watu wote wakauliza kwa pamoja.
Amosi akarudia tena kujieleza katika namna ileile.
Vicheko vikaibuka, lakini hali ilikuwa tofauti kwa Mikidadi, ambaye aliona kijina yule wa rika lake kama anamfanyia uchuro.
“Huyu si mzima” mzee mmoja akasema.
“Kabisa, vijana wa siku hizi wanaharibikiwa sana na bange” mwingine akashadadia.
“Huyu mtu katumwa huyu, haiweziekani anifanyie uchuro wa kiwango hiki” Mikidadi akahamaki.
“Hebu tulieni kwanza, tulieni kwanza tuendelee kumuuliza” nmzee mmoja akawatuliza.
“Umesema ulikuwa unaelekea wapi vile?”
“Tanzania” Amosi akajibu, macho na uso wake vilionyesha alikuwa akitambua kitu anachokizungumza.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tanzania ndio wapi?”
“Hamuijui Tanzania?” naye akawauliza kwa
mshangao,
“hatupajui’walijibu.
Tanzania ni nchi ipo bara la Afrika, ukanda wa Mashariki”
“Si mnaona sasa, ndio maana ninawaeleza huyu kijana ni mwehu.
“Tangu lini Afrika Mashariki kukawa na nchi iitwayo Tanzania, nijuavyo mimi huko kuna nchi iitwayo Tanganyika”
“Hapana jamani Tanganyika ilikuwa zamani ikiwa bado haijaungana na taifa la Zanzibar lakini baada ya mapinduzi ya Zanzibar nchi hizo ziliungana na kuunda nchi ya Tanzania.” Amosi alilalama.
“Duh! Kwa hiyo mwenzetu huu ni mwaka gani?” mzee mmoja akahoji kwa dhihaka.
“Huu ni mwaka 2017”
“Jamani tutawanyike hapa hakuna mtu timamu bali mwendawazimu tupo mwaka 1960 yeye anasema ni 2017 karne ambayo hatudhani kama tutafika huko”
Mzee aliyeonekana kama kiongozi alisema, wakaondoka wakimwacha peke yake. Amosi alichoka.
Alishindwa kutambua eneo alilokuwa amengukia ni dunia gani. Alijiona yupo kuzimu. Hakujua ni namna gani ataweza kurudi katika dunia yake. Kule alikokuwa, kulitisha!. Jamii aliyokuwa huko ilikuwa ikiishi katika mwaka 1960!.
Amosi aliendelea kuzungumza na kujiuliza maswali peke yake. Watu waliokuwa wakipita karibu yake walimsikitikia kwa kuona mwendawazimu aliyeathiriwa na na matumizi ya madawa ya kulevya.
Jua la jioni nalo lilikuwa likiishilizia, katika kijiji hicho, wanakijiji walionekana kutojali balaa na maafa yaliyosababishwa na moshi ule wa ajabu. Kimwonekano ni kama walikuwa wameizoea kadhia ile maishani mwao.
Taratibu nuru ikazidi kumezwa na giza, watu nao wakawa wanapotea taratibu na kujichimbia katika makazi yao. Amosi alitambua muda si mrefu usiku utaingia, na akaiona changamoto ya kupata mahali pakujihifadhi kwa siku hiyo.
Ndio. Nani angekubali kumfadhili malazi mwendawazimu? Alilitambua jambo hilo. Akaona kuna kila sababu ya kufanya kitu.
Ni jambo gani afanye ili amshawishi mtu na aweze kumfadhili mwendawazimu sehemu ya kuishi kwa usiku huo? lilikuwa ni jambo gumu lililohitaji utulivu wa fikra ili apate wazo kabla ya kuingia katika utekelezaji wake.
Aliangaza katika vijumba vilivyokuwa vimepangana hovyo akavutiwa na nyumba moja kubwa iliyokuwa imezungushiwa uzio wa makuti huku kando kukiwa na zizi dogo la mbuzi. Akaikabili nyumba hiyo.
Alibisha hodi mara mbili, akasikia akiitikiwa na sauti mchanganyiko za watu waliokuwa nyuma ya nyumba hiyo.
Muda mfupi badaye mlango ulifunguliwa. Hakuamini aliyekutana naye!. Alikuwa ni mama yake. Bi Greta.
Walibaki wakiangaliana. Msichana yule alimwangalia Amosi katika namna ya kukalahishwa na matendo ya mtu huyo anayedai kwamba yeye ni mama yake.
Amosi alitambua ni lazma atumie njia yoyote awashawishi watu hao kumpa hifadhi, alijua kuendelea kuwanga’nga’nia kama wazazi wake hakuwezi kumsadia chochote.
“Sikutegema kama nyumba hii ningewakutana nanyi…”
“Sema shida yako?” Greta alimkatisha kwa ukali, huku akimkata jicho baya. Kabla Amosi hajaendelea Mikidadi akatokea. Naye akashangaa kumkuta kijana yule.
“ Wewe shida yako nini?”
“Naombeni jambo moja tu…” Amosi alisema harakaharaka, dalili ya amani kutoweka ilionekana kwa watu wale.
“Shida gani?”
“Nisaidieni sehemu ya kulala.”
“Kwanini hapa na siyo nyumba nyingine ?” Mikidadi alisema kwa ghadhabu.
“Dhamira haikuwa kwenye familia hii. Imetokea tu.”
“Unadhani kwa nini natakiwa nikukaribishe katika mji wangu?” Mikidadi aliendelea kumuuliza maswali ya papo kwa hapo, alionesha kuchukizwa na uking’anga’nizi wa mtu yule aliyeibuka katika kijiji kama mzimu.
CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nisaidie kwasababu mimi ni mgeni hapa, niko katika matatizo makubwa sana, sijui niko wapi na ninako elekea sipajui” Amosi alizungumza.
Mikidadi na Greta walimtizama kijana yule wa rika lao usoni, waliona uso uliohitaji msaada, uso wenye mashaka na wasiwasi, lakini pia waliona uso wa kijana wa kisasa. Walitatizika kwa jambo moja tu. Madai ya mtu yule. ukimya wa mfupi ukapita. Mikidadi akashusha pumzi nyingi halafu akamuuliza swali jingine tofauti.
“Kwanini unasema sisi ni wazazi wako ilihali tunalingana kiumri?”
“ Sijui. Na nisieme tu sitambui ni kitu gani kinatokea maishani mwangu, kwani si hilo tu, ulitako lipo jingine linaloumiza ziadi kichwa changu.”
“Lipi ?”
“Ni kuhusu Amosi. Huyo mtoto wenu. huyo ni mimi mwenyewe, naamanisha mimi na yeye ni mtu mmoja”
“Nini!!” Mikidadi na Greta wakauliza kwa mshangao.
“Ndio”
“Kibaaa!...kibaaa!..weee kibaaa!” Mikidadi alipaza sauti kuita.
Wakati akiwa anaita jina hilo , Amosi aliendelea kustajabu, alimtambua mtu huyo aliyekuwa akiitwa ni kaka yake.
Kiba alitokea. Naam kwa mara nyingine Amosi alipigwa na bumbuwazi baada ya kumwona mtu yule. Aikuwa ni kijana mdogo, lakini alimtambua. Alikuwa ni kaka yake halisi. Kiba.
“ Utamwonyesha sehemu ya kulala. Kule zizini.” Mikidadi alisema akionyesha kutotaka tena kusikiliza upuuzi wa mtu yule. Akili yake iliendelea kuamini mtu huyo ni mwendawazimu.
Baada ya kukabidhiwa kwa Kiba, hakuna tena aliyepoteza muda wake kuzungumza na Amosi, walirejea ndani kumalizia sehemu ya siku hiyo.
Amosi aliongozana na Kiba hadi kwenye zizi dogo la mbuzi ambalo ndani yake kulikuwa na kitanda cha kamba kilichotengenezwa kiustadi sehemu ya juu, kikiwa kimetandikwa kwa ngozi ya ng’ombe.
“Utalala humu” Kiba alimwambia.
“Ahsante Kiba, hivi kweli hata wewe hunijui?”
“Nikujulie wapi? Kwani wewe ni nani, mbona sijawahi kukuona hata siku moja.”
“Basi…Basi… Basi…inatosha mtoto mzuri, nakushukuru kwa ukalimu. Sawa?” Amosi alisema ili kuua ‘soo’ hakupenda wazazi wa mtoto yule watambue kama aliendelea kueleza mambo yale kwa mtoto yule.
Wakati huo tayari giza nene lilikuwa limekwisha tanda, kichwa cha Amosi kilizidi kugubikwa na mawazo lukuki, katika kuwazawaza huko akabaini jambo moja ambalo lilimstua tena vibaya sana.
Alitambua siku hiyo ilikuwa ni siku ya nne tangu amepata ajali, na alikuwa hajala chochote. Ajabu. Hakuwa na njaa wala mwili wake haukuonyesha kudhofu.
Nafsi yake Ilikiri kulikuwa kuna miujiza isiyo ya kawaida ilikuwa ikipita kwenye maisha yake, alilia kimyakimya. Hofu na mashaka ilimtawala. Alisalimu amri, na kukubali kwamba kulikuwa na uchawi wa ajabu mno uliokuwa ukimpitia mishani mwake.
Hakujua usingizi ulimpitia muda gani, alilala huku ndoto za ajabu zikipita kichwani mwake, alizinduka mapema Alfajiri. Akiwa bado hajapata uimara wa akili, kwa ambali akasikia sauti ya mtoto mdogo ikimsulia kitu.
Alitambua sauti hiyo ilikuwa ya Amosi, yanii yeye mwenyewe!. Na kitu alichokuwa anasimulia mtoto huyo ni ndoto alizoota usiku, ajabu ni kwamba ndoto zile zilikuwa zikisimuliwa ndizo alizoota yeye mwenyewe!!
Mauzauza yale yaliendelea kuikoroga akili ya Amosi vibaya sana, hakujaua mantiki ya yeye kukutana na mazingaombweo yale ni nini.
Akiwa bado amejikunyata ndani ya zizi lile, sauti ya mtoto yule aitwaye Amosi, iliendelea kusikika ikisimulia kutokea nje ya zizi alimokuwa amelala Amosi. Alikuwa akimsimulia juu ya ndoto alizoota usiku wa kuamkia siku hiyo, ndoto ambazo Amosi pia aliziota yeye usiku.
Bi Greta na mumewe hawakuonekana kama ni watu wenye kujali masimulizi ya mtoto yule, walipuuza. Hata yeye mwenyewe alijipuuza.
Kamwe hawakutambua kama tukio hilo lilikuwa likiikoroga akili ya Amosi aliyekuwa bado amejilaza kivivu katika kitanda cha kamba ndani ya zizi lile.
Kama ilivyokawaida, siku mpya iwadiapo, pilika na hekaheka za huku na kule ziliendelea. Amosi alijiondoa kitandani na kutoka nje ya banda lile.
“Habari za asubuhi” Amosi alitoa salamu baada ya kutoka nje ya banda.
“Salama, hujambo” Mikidadi na Greta waliitikia kwa pamoja.
“Sijambo.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bila shaka tumetimiza makujumu yetu kama binadamu….” Mikidadi alisema. Kisha akaendelea.
“Ni jukumu lako kuangalia maisha sehemu nyingine sasa” alizungumza uso wake ukionesha kutohitaji ukaribu na mtu yule tena.
Amosi alitikisa kichwa kinyonge kukubaliana na maneno yale.
“Basi kila la kheri kijana” akasema tena bila kumwangalia usoni.
“Mimi ni mtu wa aina gani mimi…” Amosi aliwanza akiwa anazipiga hatua kutoka nje.
“Eti anajiuliza yeye ni mtu wa aina gani…hahaha!” mtoto yule mdogo aitwaye Amosi, alisema kwa ucheshi huku akicheka. Alikuwa ameyasikia mawazo ya Amosi!!.
Amosi alishituka. Alisita kutembea akageuka na kumwangalia mtoto yule. Alipigwa na butwaa kuona mtoto yule ameweza kutambua anachowaza. Lakini hata hivyo akiwa katika taharuki ile, yeye pia alingiliwa na sauti za ajabu kichwani mwake.
Ilikuwa ni kama vile amevaa visikilizio vya sauti masikioni(hear phone) Alikuwa akisikia mawazo ya mtoto yule masikioni mwake.
“Anawezaje kusikia ninachowaza?” Amosi aliwaza, uso wake ulionesha kuwa na taharuki isiyo na mfano.
“Hahaah!!. eti anasema anawezaje kusikia anachowaza,” Amosi mtoto akaropoka tena kwa sauti, akazisema waziwazi fikra za mtu mzima yule.
Mikidadi akabakia akiwashangaa wale watu wawili, alimtizama mtoto wake Amosi ambaye alikuwa akiropoka na kucheka hovyo kwa vitu ambavyo hakupata kuelewa maana yake nini, lakini ajabu katika mambo hayo aliyokuwa akiripoka mtoto yule alistajabu kuona mtu yule akiwa ni mwenye mshangao mkubwa kutokana na maneno yale ambayo yeye aliyachukulia kama ya kitoto tu.
“Vipi mbona kama umedata, kulikoni” Mikidadi alimstua Amosi ambaye kwa wakati huo alikuwa kwenye taharuki kubwa.
Amosi alishusha pumzi ndefu, hakujibu kitu zaidi ya kuondoka. Alitoka nje ya nyumba hiyo na kulandalanda mtaani huku kichwa chake kikizingirwa na mawazo lukuki. Kuna wakati alihisi huenda anakaribia kuapata wazimu kama
Sauti zilizokuwa zikisikika masikioni mwake kama kavishwa ‘hearphone’ ziliendelea kusikika masikioni mwake.
Yalikuwa ni mawazo ya mtoto yule aitwaye Amosi. Yeye mwenyewe! Fikra na mawazo ya kitoto yaliendelea kugonga masikoni mwake, nafsi yake ikaendelea kukiri kwamba mtoto yule aitwaye Amosi alikuwa ni yeye mwenyewe!.
Ilikuwa ni mazangaombwe ya ajabu mno kuwahi kutokea maishani mwake.
“Wewe mtoto,” Amosi alimwita mtoto yule mawazoni.
“Unasemaje?” sauti ya mtoto mawazoni ilimjibu, ingawa alikuwa umbali mkubwa kutoka nyumba ya mikidadi ambayo alimwacha mtoto yule, lakini sauti yake ilisikika barabara masikioni mwake. Ilikuwa ni mfano wa mazungumzo baina ya mtu mmoja na mwingine huku masikioni mwao wakiwa wamevaa ‘hearphone’
“Tunawezaje kuzungumza kwa mtindo huu?” Amosi akamhoji
“Sijui”
“Sasa nataka nikambie kitu”
“Kipi?”
“Wewe ni mimi!”
“Nini?”
“Nasema wewe ndio mimi” Amosi akasema kwa ukali kidogo.
Ghafla akamsikia mtoto yule akilia, lakini safari hii sauti ilikuwa tofuati na ile itokayo mawazoni, hii ilikuwa ni sauti itokayo kinywani.
Sauti hizi mbili zilikuwa na tofauti, ile ya mawazoni ilikuwa ni sauti iliyotulia, ni kama ilichujwa katika amplifaya tofuati na hii ya pili ambayo hutokea kinywani. Yenyewe ilikuwa ni sauti ambayo ilikuwa na kelele nyingi za pembeni, haikuwa na ubora mzuri .
Wakati mtoto Amosi analia sauti ya kufokewa na mama yake ilisikika masikioni mwa Amosi alieykuwa umbali wa mita kadhaa kutoka kwenye mji ule. Na alisikia waziwazi mama yake akimtuhumu kwa kujivika wendawazimu wa kuongea peke yake.
Amosi akatambua wakati anafanya mazungumzo na mtoto yule, pamoja na kwamba alikuwa akimjibu kwa mawazoni lakini inawezekana alikuwa akifumbua mdomo wake na kuongea hali iliyofanya kuonekana mwendawazimu kwa watu waliokuwa karibu yake.
“Anaongea peke yake kama mwendawazimu!! ” Bi greta Shangwra alifoka, sauti ile inaposikika ndani ya masikio ya mtoto Amosi, ndivyo hivyohivyo husafiri hadi kwenye masikio ya Amosi mkubwa!!
Ndio hali hiyo ilikuwa ni lazma itokee. Maaana watu wale wawili, ni mtu mmoja!!
Sauti ya mtoto Amosi iliendelea kupenya kwenye masikio yake ikitokea kule nyumbani alikokuwa akiadhibiwa na mama yake.
Mauzauza yale yaliendelea kumshangaza, hakujua ni kwa jinsi gani, mwisho wa mambo yale utakavyokuwa.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sauti za mawazoni zikazidi kugonga kichwa chake ndani kwa ndani. Ukulele wa sauti mchanganyiko, ukamwondolea utulivu wa nafsi, kwakutumia vidole vyake vya shahada akajiziba masikio akidhani atazua sauti zile.
Lakini wapi, bado ukulele ukazidi kumtesa, kadiri mkanganyiko ule wa mingiliano wa sauti mbalimbali ulivyokuwa ukimsumbua ndani ya kichwa chake, ukamfanya apuyange hovyo.
Akawa mithili ya mtu aliyepandwa na mapepo. Akawa, anapiga yowe lenye kuashairia kukarahishwa na mwingiliano wa sauti tofuati zilizokuwa zikitokea umbali mfupi kutokea kule nyumbani kwa mtoto yule ambaye alikuwa ni yeye mwenyewe!.
Sauti zile ambazo zilikuwa zikigonga kwa nguvu ngoma ya masikio yake, yalikuwa ni mazungumzo baina ya Amosi aliyekuwa akifokewa na mwanamke ambaye alikuwa si mama wa kitoto kile tu, ambacho pia kilikuwa ni yeye mwenyewe, lakini hata msichana yule alikuwa ni mama yake mzazi!.
Mama alikuwa akimfokea mtoto kwa kujifanya majinuni, kwakuzungumza peke yake. Kamwe, mwanamke yule hakutambua kwamba mtoto yule, hakuwa akijitia wendawazimu, bali, alikuwa akiwasiliana na mwili wake mwingine uliokuwa umbali mfupi kutokea katika mji ule, mwili huo ukiwa katika mwonekano wa kiutu uzima!
Ndio hakujua!.
Wakati maswahibu yale yakitokea kwa mtoto yule, Amosi naye aliendelea kuwa katika hangaiko la miingiliano ya sauti kali zilizokuwa zikigonga kwa nguvu masikioni mwake.
Huku mtoto analia kwa sauti, kule mama anafoka kwa nguvu, basi ikawa ni mwendo wa lapsha kubwa kichwani mwake.
Ghfla! Sauti zile zilikata! Ukimya wa kawaida ukarudi kichwani mwake! Ilikuwa ni kama vile mawasilino ya simu yanayofanyika baina ya mtu mmoja na mwingine na mara simu ya upande mmoja ikakatika ghafla.
Amosi alibaki ameduwaa, mdomo ukiwa wazi, macho yamemtoka pima, picha ya mtu aliyerukwa na akili ikaonekana kwa kila aliyemtizama Amosi pale mtaani.
Alitafuta sehemu ya kivuli akajipumzisha, pumzi zikiwa zinamtoka kwa nguvu, aliketi kitako huku akitafakari maisha yake mapya katika sehemu ile ya ajabu.
Wiki moja ilikuwa imekatika tangu apate ajali mbaya ya ndege na kudondokea kwenye kisiwa kile cha ajabu. Ni yeye peke yake aliyekuwa amebakia akiwa hai, wenzake wakiwa wamepoteza maisha kwa kuawa na kiumbe cha ajabu, kinachoishi ndani ya msitu unaopatikana kwenye kisiwa kile.
Nafsi yake ilikiri, uhai wake hadi wakati huo ulitokana na yeye kubahatika kuishi kwenye kijiji kile ambacho watu wake bado wako kwenye maiaka ya takribani miaka 40 iliyopita, kubwa kuliko vyote anajiona yeye akiwa angali mdogo pamoja na familia yake ikiwa inaishi hapo.
Akiwa pale kivulini, alilia kama mtoto, alijiona yupo kuzimu, na hakujua ni kwa namna gani anaweza kutoka kwenye lile balaa maishani mwake.
Akiwa katika hali ile, akakumbuka kitu!! Na alipokumbuka kitu hicho moyo wake, ukamlipuka, ndani ya muda mfupi faraja fulani ikagubika moyoni mwake.
Ilikuwa ni kumbukumbu dhidi ya simu yake ndogo ya mkononi. Wakati kumbukumbu ya simu yake inapita akilini mwake, kumbukumbu ya siku ya kwanza anazinduka akiwa kapoteza fahamu ndani ya msitu ikamjia. Matukio yote ya siku ile ya mwanzo alipojikuta yupo kwenye ardhi ya msitu huo yakapita kwa kasi kichwani mwake. Akakumbuka neno ‘network error’ lilikuwa likitokea kwenye simu ile ambayo sasa alikuwa ameikumbuka tena, maneno yale yaliyokuwa yakimaanisha kuwa, kulikuwa na tatizo la mtandao.
Akaendelea kukumbuka alivyokuwa akipuyanga huku na kule kuitafuta netiweki bila mafanikio yoyote.
Harakaharaka akaitoa simu ile ambayo alikuwa ameitelekeza kwenye mfuko wa suruali kwa siku zaidi ya tano.
Macho yake yalipotua kwenye kioo cha simu ile hakuamini kile alichokiona tena! Maandishi yaliyosomeka ‘network error’ hayakuwepo! Badala yake, yalitokea maneno mengine.
Maneno yaliyotokea yalikuwa ni ya ajab! Na yalisomeka hivi: ‘Find the bastard’ yakiwa na maana mtafute mwanaharamu.
Alibung’aa kwenye simu ile ambayo ilikuwa imebakiza asilimia chache sana kabla ya kuzima chaji. Neno lile lilimfanya jasho limchuruzike maungoni mwake.
Kumbukumbu dhidi ya Marehemu mama yakeambaye alikuwa akimsafirisha kwenye ndege ya ‘Panasonic Airline’ akiwa maiti kabla ya kupata ajali ile na kutokewa na mwanamke yule katika ufukwe akiwa hai na kumpa kipande cha ubao kilichoandikwa ‘find the bastard’ kumbukumbu ile ikamrudia.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa dakika nzima aliendelea kuikodolea macho simu ile kana kwamba ndio kwanza anaiona kwa mara ya kwanza, ama simu ile ndio yenye majibu ya kitendawili kilichokuwa kikitokea maishani mwake.
Naam, nafsi yake ilikiri kwamba kivyovyote vile huyo ‘Bastard’ ndiye atakayekuwa akifahamu kitu fulani ambacho kinaweza kumpa maana ya mambo yote.
Kwa dakika nzima aliendelea kuikodolea macho simu ile kana kwamba ndio kwanza anaiona kwa mara ya kwanza, ama simu ile ndio yenye majibu ya kitendawili kilichokuwa kikitokea maishani mwake.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment