Simulizi : Wakala Wa Shetani
Sehemu Ya Pili (2)
Eeh.
Unaitikie eeh, nilikuambia nini baada kukutana na Ngwana Bupilipili? Mama Sabina alimkazia macho mumewe ambaye alionesha hayupo makini.
Ooh! Nimekumbuka, ina maana mtoto huyo atakuwa wa Ngwana Bupilipili?
Huo ndio wasiwasi wangu mkubwa, japokuwa sina uhakika.
Sasa kama ni mtoto wa Ngwana Bupilipili kwa nini amfiche, una uhakika anaweza kuwa wake?
Sina uhakika, lakini sasa hivi nakwenda kujifanya naomba moto ili nijue mtoto aliyelia anatoka nyumba ile.
Lala mke wangu, achana nao.
Hapana mume wangu, kutakuwa na kitu, kama ni kweli kwa nini wamfiche? alihoji mama Sabina.
Mama Sabina alinyanyuka kitandani alipokuwa amekaa kwa ajili ya kulala. Alitoka na kumwacha mumewe akimsubiri mkewe alipokwenda kufanya uchunguzi wake.
Alikwenda hadi kwa jirani yake Ngwana Bupilipili, alipofika aliwasikia wakizungumza mtu na mkewe ndani.
Mmh, mtoto huyu alitaka kutuumbua, alimsikia Mathayo akizungumza.
Alikuwa amekojoa ndo maana kalia, sijui sauti yake imefika mbali?
Mmh, sidhani, lakini watu wote wamo ndani hawawezi kujua nani mwenye mtoto asubuhi.
Mmh, afadhali.
Mama Sabina hakutaka kuwashtua, alirudi hadi ndani mwake na kumweleza mumewe aliyosikia kwa jirani zao.
Sasa mke wangu kwa nini wanafanya siri, kwani mtoto wao ana nini?
Labda albino?
Mmh! Inawezekana maana mvua ya leo si ya kawaida, haijawahi kutokea kijijini.
Kwa hiyo?
Hiyo kazi niachie nitaifikisha kwenye kamati ya kijiji, kama ni kweli tutaweka ujirani pembeni, hawezi kutuletea balaa kama hili, hebu ona hasara iliyoingia. Tumepoteza mifugo kibao.
Na kweli mume wangu, lazima tuwashtaki hasa aliyeniuma ni yule ngombe mjamzito aliyekuwa na mapacha.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Tulale mke wangu, tutayajua yote asubuhi.
Walizima taa na kujilaza.
Kabla ya kuanza kulala mama Sabina alikuwa na wazo, alimshtua mumewe aliyekuwa amegeuka kumpa mgongo ili aanze kuutafuta usingizi.
Mume wangu kabla ya kulala nilikuwa na wazo.
Lipi tena mke wangu?
Kuhusu jirani yetu.
Mmh, ulikuwa na wazo gani?
Nilikuwa nataka kesho alfajiri niwahi nijifanye naenda kuomba moto, kisha niwaeleze kuwa nimemsikia mtoto kisha niliwasikia wanasema.
Wazo lako ni zuri, lakini kama mtoto ni albino siamini kama watakubali zaidi ya kukataa.
Sasa unanishauri nini?
Wee waache tu ili tuwashitukize.
Lakini mume wangu kama mkikuta mtoto si albino tutajipa picha gani kwa jirani yetu kama sio uhasama wa kisasi.
Usemalo ni kweli, basi fanya ulivyofikiria tutajua tufanye nini?
Haya, tulale.
Kila mmoja aligeukia kwake na kuvuta shuka.
****
Siku ya pili Mathayo na mkewe walidamka alfajiri na kukusanya vitu muhimu vya kutumia huku wakiendelea kuomba Mungu awaonee huruma kwa ajili ya kukiponya kiumbe kile.
Baada ya kuandaa kila kitu walitoka taratibu na kushika njia ya shambani japo ilikuwa ikitisha sana kutokana na hali ya hewa ya ukungu iliyotanda alfajiri ile.
Waliondoka na kurudi shambani kwao, walikuta maji yamepungua sehemu nyingine na kuwafanya wavuke bila kuingia ndani ya maji ambayo yalikuwa ya baridi kali.
Walifanikiwa kufika hadi sehemu ya pangoni ambayo maji yote yalikuwa yametoka. Ngwana Bupilipili alimuandalia mtoto sehemu nzuri na kumlaza kisha na yeye kujilaza pembeni yake huku akimwacha mumewe aende shambani kufanya usafi na matengenezo ya sehemu zilizoharibika.
Mathayo alikwenda hadi shambani na kuanza kazi ya kurekebisha baadhi ya sehemu zilizozolewa na mvua ambayo iliharibu mazao mengi katika mashamba.
Kitu cha ajabu pamoja na mvua kunyesha sana, shamba lao tu ndilo ambalo mazao yao yalipona. Hata mifugo yake nayo ilipona tofauti na majirani zake ambao mashamba yao mengi yaliharibiwa na mvua.
****
Mama Sabina aliyepanga kuamka alfajiri kwenda kuwaona Mathayo na mkewe, baada ya kuamka alikuwa amechelewa. Alipishana dakika dano tu, wakati yeye anaamka wao wanaondoka tena kimyakimya. Alipofika kwenye nyumba ya jirani yake alijua bado amelala.
Alikwenda hadi kwenye mlango wa jirani yake na kusikiliza akidhani atawasikia wakizungumza au hata sauti ya mtoto. Kwa ukimya ule aliamini bado wamelala, aliamua kuwagongea.
Hodi.. Ngwana Bupilipili hodi hapa..., kila alipogonga hakukuwa na jibu, aligonga huku akiliita jina la Ngana Bupilipili, hakukuwa na jibu. Alipoangalia aliona mlango umefungwa kwa nje kuonesha hakukuwa na mtu ndani.
Alirudi haraka kwa mumewe aliyekuwa bado amelala huku amejikunja gubigubi kwa baridi la alfajiri.
Mume wangu hawapo.
Kina nini hao? baba Sabina aliuliza.
Si Mathayo na mkewe.
Si nilikuambia.
Kuhusu nini?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Huenda mtoto wao ni albino."
"Mmh, kweli hilo nalo neno," mama Sabina alimuunga mkono mumewe.
"Dawa ni kuitisha kikao na kuwaeleza watu."
"Itakuwa vizuri."
"Ila nimepata wazo kabla ya kukurupuka lazima tufanye uchunguzi wa kina."
Walikubaliana kwanza kufanya uchunguzi kabla ya kuitisha kikao. Baba Sabina aliamua shauri lile kulipeleka kwenye kikao cha kijiji.
Asubuhi ileile baba Monika aliwazungukia wajumbe wa almashauri ya kijiji na kuwaomba wakutane baadaye. Kikao kiliitishwa na kamati ya kijiji ilielezwa. Baada ya wajumbe kukusanyika, baba Sabina aliwaeleza alichowaitia.
"Ndugu wajumbe, nimewaiteni kuhusiana na kitu kimoja ambacho kimetokea si cha kawaida," alisema huku akitembeza macho kwa wajumbe wote waliokuwepo pale ambao walionekana wakimsikiliza kwa makini.
"Kipi hicho?"
"Si mnafahamu mke wa Mathayo alikuwa mjamzito?"
"Ndiyo, na mimba yake ilikuwa imebakiza muda mchache," alijibu mjumbe mmoja.
"Basi kuna taarifa zilizo rasmi kuwa mke wa Mathayo ameshajifugua, ila hajulikani mtoto wa jinsia gani. Sababu iliyonifanya niwaiteni ni tabia yao waliyoianza ya kutoka alfajiri na kurudi giza limeingia.
"Wasiwasi wangu kwa nini afanye vile hata kama hataki watu wajue mkewe amejifungua pia kuiona sura ya mtoto wao? Wasiwasi wangu huenda mtoto yule ni albino."
Albinoo!!" Walishtuka wajumbe wote.
"Ndiyo, kutokana na kauli aliyosikia mke wangu lazima tuwe na wasiwasi huo."
"Aah, albino, una uhakika na usemalo?" aliuliza mjumbe mmoja.
"Huo ni wasiwasi wangu, japo sina uhakika, nilikuwa nataka tuwatume vijana waende kule shamba ili wafuatilie wajue yule mtoto kama ni wa kawaida waachane naye, kama ni albino hapo ndiyo atatujua sisi tufanye nini."
"Inawezekana huenda hata mvua iliyonyesha ni laana ya kumkumbatia albino, kama ni kweli lazima apewe adhabu kali ambayo itakuwa fundisho kwa wanakijiji wote," alisema mwenyekiti.
"Kama ni kweli adhabu inayowafaa tuwafungie ndani ya nyumba yao kisha tuwatie moto na kufa kwa kuteketea kwa moto," mwingine alitoa wazo.
"Yaani kama ni kweli wafe kifo kibaya sana, hamuwezi kuamini mimi mifugo yote imekufa kwa mvua, kumbe kuna washenzi wanakumbatia laana," mjumbe mwingine alisema kwa uchungu.
"Nafikiri tusipoteze muda, majira ya saa tatu asubuhi vijana waelekee shambani kwa Mathayo ili kufanya uchunguzi. Walichaguliwa vijana sita na kupewa silaha tayari kwa kupambana na kitu chochote, wakaelekea shambani kwa Mathayo.
***
Mathayo, akiwa anaendelea kurekebisha shamba lake, aliponyanyua macho aliwaona vijana wakija kwa kasi wakielekea shambani kwake. Wasiwasi wake huenda kuna siri ya mtoto wao imevuja. Watu walikuwa mita mia saba kufika shambani.
Aliacha kila kitu na kukimbilia pangoni kumweleza mkewe kuwa mambo yameharibika, alipofika alimkuta mkewe akikoroma akionekana yupo kwenye usingizi mzito.
"Mke wangu...Mke wangu."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kila alivyomwita kwa sauti ya chini hakusikia ilibidi amtikise kwa nguvu ili aamke.
"Mume wangu niache nilale nimechoka sana," Ngw'ana Bupilipili alisema bila kufumbua macho.
"Hapana mke wangu, amka, kuna watu wanakuja kumfuata mtoto wetu."
"Atiiii?" alishtuka na kuamka akiwa ametumbua macho.
"Kuna watu wanakuja upande wetu, inaonekana wanakuja kwetu tena si watu wa heri."
Kauli ile ilimfanya mke wa Mathayo ataharuki.
Alikusanya vitu muhimu na kutokomea kwenye msitu huku mumewe akibakia eneo lile kuangalia nini kinaendelea. Ng'wana Bupilipili alimfunga mwanaye madhubuti kifuani na kuanza kupanda milima kuondoka eneo lile kwa ajili ya kumnusuru mwanaye.
Wakati mkewe akiondoka eneo lile, Mathayo alitoka nje ya pango lile kuondoa ushahidi huku akimuomba Mungu mkewe azidi kukimbia na kumuokoa mtoto wao. Alijikuta akipata ujasiri wa ajabu na kuwa tayari kufa kuliko kumpoteza mtoto wake.
Kilichompa ujasiri kilikuwa kitu kimoja, matukio ya athari za mvua. Katika mvua ile sehemu nyingi zilizoharibika pamoja na mifugo kufa zilikuwa za majirani zao, lakini kwao palikuwa salama kama mvua ilipita ilinyesha kidogo. Hata uharibifu katika mashamba, shamba lao ndilo pekee lililosalimika.
Mawazo yake yalibadilika na kuamini mtoto wao si mkosi kama alivyofikiria.
Aliamini kama mtoto wao angekuwa mkosi basi balaa kubwa lingewakumba wao kuliko wanakijiji wenzao. Ilikuwa ajabu kubwa asilimia kubwa ya wananchi wa kijiji kile walipata matatizo ya kubomokewa nyumba na kuezuliwa paa. Kwao kulikuwa salama katika nyumba na mifugo hakuna uliokufa hata mmoja.
Kwa majirani zao ilikuwa kilio cha kusaga meno, mvua iliwatia hasara kubwa na hakuna hata mmoja aliyepona katika mvua ile ambayo iliacha simulizi kijijini pale.
Ajabu nyingine, mvua ile haikuua mtu hata mmoja zaidi ya kufanya uharibifu na hasara kubwa. Mathayo akiwa bado yupo nje ya pango kuangalia hali ya usalama huku akiomba kimoyomoyo mkewe asionekane, vijana wa kijiji walifika na kumuuliza.
"Mkeo yupo wapi?"
"Mke wangu wa nini? Na imeanza lini kuuliziana wake zetu?" Mathayo alikuwa mkali na hakutaka kutoa ushirikiano.
"Bado hujatujibu, mkeo yupo wapi?" Mmoja ya vijana wale alimuuliza kwa sauti kali.
"Sijui," Mathayo alijibu kwa mkato.
"Unajitia kiburi sio?" walimuuliza kwa sauti ya kitisho.
"Najitia kiburi ili iweje?" Mathayo bado hakutikiswa na kauli za vijana wale.
"Jamani kwa nini tunamchelewesha," mmoja alisema huku akitaka kumsukuma Mathayo.
"Jamani tuwe wapole, hili jambo hatujawa na uhakika nalo," mmoja alitaka watumie busara kuliko nguvu.
"Basi atujibu mke wake yupo wapi?"
"Kabla sijawajibu hii imeanza lini na leo iwe mara ya pili?" Mathayo bado alisimamia msimamo wake.
"Sikiliza Mathayo, mkeo alikuwa mjamzito na taarifa zilizotufikia ni kuwa ameshajifungua lakini mtoto wenu inasemekana mnamficha. Wasiwasi wa wanakijiji huenda ni albino na ndiye aliyesababisha balaa kubwa kijijini kwetu, hivyo tulikuwa tunataka tumuone ili tupate uhakika kwa kile kinachosemwa," mmoja aliyeonekana mwenye busara alisema kwa upole.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Basi kwa taarifa yenu mke wangu bado hajajifungua na sijui nani aliyewadanganya kuwa mke wangu kajifungua."
"Bwana Mathayo, huu tunaoonesha hapa ni ustaarabu, lakini tunajua yote, hata jana usiku jinsi mlivyokuwa mkiongea baada ya mtoto wenu kulia na kushauriana jinsi ya sauti ilivyofika mbali.
"Sasa ndugu yangu hatukuja kupigana bali kuelewana, kwanza wewe ni kiongozi wa usalama kijijini, kwa nini tugombane kwa jambo la kuelewana? Tuoneshe huyo mtoto ili tumuone kama ni albino au la," kijana aliyeonekana ana busara alisema huku akiendelea kumbembeleza Mathayo.
"Nimewaambia mke wangu hajajifungua labda mlisikia nyumba ya jirani si kwangu," Mathayo bado alikuwa mbishi.
"Sawa nyumba ya jirani mke wako yupo wapi?"
"Suala la mke wangu haliwahusu, mke wangu ananihusu mimi na si mwingine."
"Sikiliza Mathayo, wewe si mgeni wa kijiji hiki, pia hata wewe ni kamanda wa baraza la usalama la kijiji. Unajua kabisa mtu anaposhukiwa na kitu lazima apekuliwe, lakini wewe tunakufanyia ustaarabu basi tuoneshe ushirikiano," hawakuchoka kumbembeleza.
"Si kwangu, napenda maisha yangu niishi nipendavyo mwenyewe na si kuingiliwa na mtu."
"Jamani tunamchelewesha," mmoja uzalendo ulimshinda.
Alijitokeza na kusukuma kifuani kwa nguvu na kumfanya Mathayo kudondoka chini na kufikia jiwe. Bila huruma walimpita na kuingia pangoni na kufanikiwa kuzikuta nguo za kike na vipande vya kanga kuonesha ni za mtoto mchanga.
Baada ya uchunguzi na kuridhika kuna kila dalili za kuwepo kwa mtoto mchanga, walimgeukia Mathayo na kumuuliza:
"Hizi nguo za nani?"
"Za mke wangu," alijibu kwa mkato.
"Na hivi vipande vya nguo vya nani?" alionesha vipande vya nepi.
"Sivijui," Mathayo alijibu kwa mkato.
"Sisi hatutaki shari na mtu, hebu tuione mimba ya mkeo kisha tuendelee na mambo mengine, sisi tumetumwa kuna watu wanasubiri majibu, tukirudi tutawajibu nini?"
"Nimeshawaeleza kuwa mambo ya mke wangu ni ya ndani, hayamhusu mtu yoyote kuyajua, kama mtoto akizaliwa mtamuona tu wala hamtamtafuta kama jambazi."
"Jamani hatukuja kufanya mjadala wa albino au kumtafuta, tusipoteze muda. Tumwekeni chini ya ulinzi ili aseme mkewe yupo wapi," mmoja aliyekuwa hana subira aliingilia kati baada ya kuona Mathayo hataki kuonesha ushirikiano.
Walipotaka kumweka chini ya ulinzi, Mathayo hakukubali kushikwa kirahisi. Hapo ndipo ugomvi mzito ulipoanza. Ikawa piga nikupige, Mathayo katika ugomvi ule alijikuta akimkumbuka mtoto wake wa kwanza albino aliyeuawa na wanakijiji na kujikuta akipandisha mori ya ugomvi.
Wanakijiji walimshambulia Mathayo kwa marungu na mapanga, naye alikuwa na ubavu wa kupigana hivyo alikabiliana nao vilivyo. Baada ya kuzidi kujeruhiwa na kumwaga damu nyingi, alikumbuka silaha yake shambani.
Alitimua mbio kuelekea shambani, vijana wale nao hawakumuacha walimkimbiza. Alipofika shambani alichukua silaha yake. Kwa vile alijua uhai wake upo mikononi mwake, alijibu mashambulizi. Damu ikawa inamwagika ovyo, kila mmoja alitetea uhai wake kwani vita ilikuwa kubwa. Kila mmoja alipigania roho yake.
Japokuwa Mathayo alikuwa peke yake lakini aliweza kupigana kwa nguvu zake zote kutetea uhai wake. Pamoja na kipigo alichokipata kuwa kizito kwa kupasuliwa sehemu kubwa ya mwili wake, bado aliendelea kutetea uhai wake kwa nguvu zake zote mpaka tone la mwisho la damu yake.
Hakukubali kufa kikondoo, alipigana kwa uzoefu, alikuwa ni mmoja wa wapiganaji waliokuwa wakitegemewa na kijiji wakati wa kupambana na wezi wa ng'ombe. Aliweza kuwamaliza vijana wote kwa panga lake. Pamoja na kuwamaliza wote, hali yake ilikuwa mbaya sana kutokana na kupata majeraha mengi na kupoteza damu nyingi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alijaribu kutembea kumfuata mkewe, lakini alishindwa kutokana na kusikia kizunguzungu kikali kilichosababishwa na kutokwa na damu nyingi kwenye majeraha mazito ya visu, mapanga na marungu aliyopigwa na wanakijiji wenzake.
Mathayo alitembea kama mlevi, mwili wote ukiwa umemjaa damu kama alikuwa akiogelea kwenye dimbwi la damu.
Aliyaona mauti mbele yake yakimuomba kumpa msaada wa kumfikisha ahera. Lakini hakuwa tayari kuiacha dunia na mwanaye kipenzi ambaye mapenzi ya dhati yalikuja muda mfupi kabla ya kifo chake.
Alijifikiria mkewe atabaki katika hali gani, mwanaye naye maisha yake yatakuwa katika hali gani kama yeye akifa. Aliamini bora yeye angekufa kwa kipigo kile lakini alihisi hata akifa bado maisha ya mwanaye yapo hatarini. Ilikuwa lazima mkewe angetafutwa na kuuawa kama walivyomfanya yeye pamoja na mtoto wao kipenzi ambaye mpaka muda ule alikuwa hajapewa jina.
Moyo ulimuuma sana, alijitahidi kunyanyuka alipokuwa ameanguka na kuanza kutembea kwa magoti kwani miguu haikuwa na nguvu ya kusimama.
Hakukubali, alijitahidi kutembea kwa shida kwa kujilazimisha kufuata njia aliyokimbilia mkewe. Kila hatua macho yalipunguza nguvu ya kuona kwa mbali, ilikuwa kama kibatari kilichoishiwa mafuta kilichokuwa kinataka kuzimika.
Dunia aliiona ikizunguka, kila hatua mbili alianguka chini. Kiza kinene kilizidi kutanda mbele yake, alipoanguka hakuweza kunyanyuka tena.
Mkewe Ngw'ana Bupilipili alikuwa amefanikiwa kukimbia na kwenda kujificha juu kilima kimoja. Sehemu aliyojificha aliamini mtu akitokea kwa mbali lazima angemuona.
Akiwa amepumzika baada ya kutembea umbali mrefu na kumfanya pumzi zimjae kifuani na kukaa chini huku akitweta, kwa mbali alimwona mtu kama mumewe akija huku akipepesuka na kila hatua mbili alianguka chini.
Baada ya muda alimuona akidondoka chini na hakuweza kunyanyuka tena. Alisubiri labda atanyanyuka lakini ilionesha hawezi tena.
Kitendo kile kilimpa nguvu na kujikuta akimpitia mwanaye huku akijisemea; ;liwalo na liwe.' Alimfunga mwanaye kwapani na kuteremka kumfuata mumewe ili kutaka kujua amepatwa na masaibu gani.
Alikwenda kwa mwendo wa kukimbia bila kuangalia hata chini, kuna wakati alianguka na kugaagaa na mwanaye, hilo hakuliona zaidi ya kumkimbilia mumewe ili ajue anakumbwa na nini.
Alipomkaribia mumewe, alishtuka sana baada ya kumwona akiwa kama kaoga mvua ya damu, kila kona mwili ulikuwa ukitoka damu, nguo ilikuwa haionekani rangi zaidi ya damu kila sehemu.
Wakati huo, mumewe alikuwa amelala chini huku akitetemeka, machozi yakimtoka kama maji, alimsogelea mumewe na kumwita jina lake.
"Mathayo," hakukuwa na jibu.
"Mume wangu," alimwita kwa sauti huku akimuinamia.
"Na...na..ni? M..m..ke..ke wa..ngu?" Mathayo aliuliza akiwa hawezi kuona kutokana na damu kujaa machoni.
"Ndiyo mimi mume wangu, kulikoni kuwa katika hali hii?" mkewe aliuliza huku akilia kwa uchungu.
"M..m..mke wa..wa..ng..."
"Ni mimi mume wangu."
"Na..na..kufa...mke..wangu."
"Hapana usife mume wangu, nani kafanya hivi?"
"Wa..wa..na..na..ki...ki..jiji."
"Kwa ajili gani?"
"Ya mtoto wetu."
"Mungu wangu! Ndiyo wakufanye hivi?"
"Mm..mm..ke wa..wa..ngu."
"Abee mume wangu."
"Mm..tu..nze mtoto we..wetu...yupo..wa..wapi m..m..to..to?"
"Si atakuumiza mume wangu?" Ng'wana Bupilipili alimuonea huruma mumewe.
"Ha..ha..pana," Ng'wana Bupilipili alimpa mtoto mumewe aliyekuwa amejilaza kwenye mikono ya mke wake huku sehemu aliyoangukia ikitota kwa damu iliyokuwa imeanza kuganda. Baada ya kumpa mtoto alimkumbatia na kutabasamu huku machozi ya uchungu yakimtoka kwa kutengana na familia yake aliyoipenda sana katika maisha yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa amemkumbatia mwanaye ambaye alikuwa ametapakaa damu ya baba yake mwili wote, Mathayo aliacha kutabasamu na kuanza kulia huku akimuomba msamaha mkewe kwa fikra zote mbaya na alichotaka kumfanyia mtoto wao.
"Mm..ke ..wangu ..nisamehe..sa..sana, nilikuwa ..na..na mawazo mabaya ..kwa mtoto...lakini ..naomba unisemehe...m..m..ke wangu..ka..ka..b..b..bla ya kuf..f..f..fa," Mathayo alizungumza kwa shida.
"Huwezi kufa mume wangu Mungu atakusaidia," Ng'wana Bupilipili alilia kwa uchungu huku akiangalia majeraha makubwa yaliyokuwa katika mwili wa mume wake.
Aliamini kupoteza damu kule na majeraha ya visu, mapanga na marungu katika uso wa mumewe kungemsababishia mauti. Pia mdomo haukuwa na meno kutokana na kipigo cha wanakijiji. Alijiuliza ataishi vipi na mtoto yule na wapi atakwenda kuishi kama mumewe atakufa na nini hatima ya yeye na mwanaye?
"M..mm..mke ..wa..wangu," Mathayo aliita kwa shida.
"A..a..be..be..beee," Ngwana Bupilipili aliitikia huku akilia.
"Usilie..mke ...wa..ngu nakufa ..mimi ..la..lakini ...mtoto wetu..sa..salama..mm..mmtu..nze..na..na..na..ku..ku.f.f.f."
Matayo alimshika mkewe mkono kwa nguvu kisha alimuachia taratibu akiwa tayari amekata roho. Ng'wana Bupilipili aliangua kilio cha moyoni kwa kuogopa kupiga kelele ambazo zitawafanya wanakijiji wajue yupo wapi.
Kwa ujasiri mkubwa alimfunga vizuri mtoto wake kisha aliivuta maiti ya mumewe pembeni. Aliokota kipande cha mti na kuanza kuchimba kaburi la mume wake. Kutokana na ardhi kuwa laini, alichimba kwa urahisi kaburi fupi.
Baada ya kuchimba aliuvuta mwili wa mume wake uliokuwa umecharangwa kwa mapanga kama ng'ombe buchani. Kabla ya kuufukia alilia na kuapa kulipa kisasi kwa kifo cha mumewe na mtoto wao wa kwanza aliyeuawa na wanakijiji.
"Mume wangu nakuahidi nami nitakufa kama wewe, kifo chako lazima nilipe kisasi. Kwa hili Mungu atanisamehe. Umekufa katika kipindi kigumu sana maishani mwangu, umeondoka nikiwa bado nakuhitaji sana. Mwenetu Kusekwa alikuwa akihitaji malezi na busara zako. Mume wangu damu yako haitamwagika bure."
Baada ya kulia kwa uchungu alimzika peke yake na mwanaye aliyekuwa mgongoni asiyejua lolote lililokuwa likiendelea wakati ule. Baada ya kumzika, alisali sala ya mwisho na kuelekea juu ya kilima.
Ngw'ana Bupilipili baada ya kufika juu ya kilima alimuweka mtoto wake chini na kuangua kilio cha sauti ya juu kumlilia mume wake huku akiendelea kujiapiza kulipa kisasi kwa njia yoyote ile.
Alimuangalia mtoto wake aliyekuwa amelala huku akinyonya vidole vyake bila kujua nini kilichokuwa kinaendelea. Ndani ya muda mfupi aligeuka yatima baada ya baba yake kuuawa kikatili akimsaidia mwanaye aliyekuwa akiwindwa kutolewa uhai wake.
Alijiuliza pori lile atakwenda wapi na maisha yake yatakuwaje? Muda huo wingu zito lilianza kutanda na kufanya eneo lote liwe na giza kuonesha mvua kubwa ingeteremka muda si mrefu.
Aliamini kama mvua itanyesha lazima mwanaye atakufa kwa vile hakukuwa na sehemu ya kujificha.
Kwa uchungu mkubwa alipiga magoti na kunyoosha mikono juu kuomba msamaha wa Mungu.
Eeh Mungu baba! Wewe ndiye uliyetuumba wanadamu na kutupa haki sawa japo tumezidiana madaraja. Lakini haki ya kuishi ni ya kila kiumbe. Eeh, Mungu kosa langu nini kuendelea kuniadhibu kiasi hiki? Kama kweli kosa langu ni kuzaa mtoto albino basi Mungu nihukumu kwa hilo, nipo tayari kufa kifo cha aina yoyote kama kweli kosa langu ni kuzaa mtoto albino.
Lakini naamini viumbe vyote vilivyopo duniani na mbiguni ni vyako wewe na hakuna binadamu aliye juu ya mwenzake bali wewe Mungu wetu peke yako. Eeh, Mungu nimepoteza mwanangu wa kwanza kwa imani za ushirikina bado tena muda mfupi nimepoteza mume wangu.
Eeh, Mungu! Hebu nihurumie sijui hatima ya maisha yangu, hata uhai wa mwangu upo mashakani, Kwa nini Mungu umeendelea kuwaachia watu waovu waendelee kutenda unyama?
Mungu umetukataza tusiuane kwa vile kuua ni dhambi, kwa nini umewapa nguvu watu wadhalimu wanaotoa roho za watu bila huruma? Baada ya kifo cha mume wangu sasa unataka kuniua mimi na mwanangu kwa mvua nzito. Narudia kama ni kosa au mkosi kujifungua mtoto albino nipo radhi kufa kifo chochote.
Mimi ni kiumbe dhaifu nisiye na mamlaka yoyote juu yako, nakabidhi mwili wangu kwako na wa mwanangu ili utuhukumu kwa kosa letu. Lakini siku zote huamini Mungu wewe ni mpole mwenye huruma, hakika utasikia kilio changu na kunipa ulinzi wa milele...Asante Mungu kwa kusikiliza shida zangu, Asante Mungu wewe ni mfariji wa milele asante... asante Bwana wa Majeshi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ngwana Bupilipili alifumbua macho taratibu na kukutana na maajabu mbele yake. Wingu lote lilisambaa na hali ya kawaida ilijirudia. Nilipiga tena magoti kumshukuru Mungu kwa kujibu maombi yake kwa muda mfupi. Kisha alimchukua mwanaye aliyekuwa amepitiwa na usingizi alipokuwa amemlaza.
Alimweka mgongoni, wakati akimfunga mtoto kwa mbali aliona kundi kubwa la wanakijiji waliokuwa na marungu, mapanga, mikuki, mishale na upinde wakielekea upande alipokuwa.
Alijua wamekuja kwa shari kuwatafuta, pia aliamini hawakuwa na habari kama Mathayo amekufa.
***
Baada ya kutokea mauaji ya kutisha, taarifa zilizowafikia kijijini ziliwaeleza vijana wote waliotumwa kumkamata Mathayo na mkewe wameuawa. Mbiu ya mgambo ilipigwa, wanakijiji wote walikusanyika na kupewa taarifa za kusikitisha za vifo vya vijana wao saba wa kijiji kile ambao waliuliwa na Mathayo na mkewe kisha kukimbia.
Kilikuwa kilio kizito kijijini pale, liliteuliwa kundi kubwa la wanakijiji na kuingia msituni kumsaka Mathayo na mkewe. Walijiandaa kwa silaha kali huku wakitanguliza vijana mashujaa ambao walitumika katika vita ya kijiji kwa kijiji.
Mke wa Mathayo aliwaona kwa mbali wakija, alijua hali ile lazima ingetokea. Alimfunga vizuri mtoto wake akiamini hata kama angeruka kutoka upande mmoja kwenda mwingine asingemuangusha.
Baada ya kujua mwanaye amekaa vizuri kifuani, naye alikaza nguo zake vizuri na kujifunga furushi la vitu vyake mgongoni. Alianza kuondoka eneo lile na kukimbia zaidi mbele kwa mwendo wa kasi huku akikimbia kwa kuruka mawe na mabonde.
Aliweza kukimbia bila kupumzika kwa mwendo wa saa mbili. Baada kufika katikati ya mbuga akiwa amechoka, alimteremsha mtoto wake na kumlaza pembeni na yeye kujilaza pembeni akiwa hoi. Kutokana na uchovu alipitiwa na usingizi mzito pembeni ya mti mkubwa.
Sauti za watu waliokuwa wakibishana pembeni yake, juu ya kuendelea na kumtafuta, zilimshtua Ngwana Bupilipili. Kwa haraka alipeleka macho kwa mwanaye aliyekuwa bado anauchapa usingizi asijue kuwa watoa roho walikuwa karibu yake wakipanga jinsi ya kuuchukua uhai wake.
Watu wale walikuwa wamempa mgongo wakijadiliana, ilionesha kabisa nyuma ya mti aliojilaza mbele yake ilikuwa ndiyo mwisho wao wa kuendelea kumtafuta.
Jamani tutakwenda mpaka wapi kuwatafuta watu bila kujua wamekimbilia wapi? sauti ya mwanakijiji mmoja ilisema ambayo haikuwa ngeni kwake.
Ni kweli maana tunatafuta kama vipofu, huenda tumewapita huko nyuma, mwingine alichangia.
Sasa mnashauri tufanye nini?
Turudini muda huu ni mbaya mvua inaweza kushuka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment