IMEANDIKWA NA : ALLY MBETU 'DR AMBE'
*********************************************************************************
Simulizi : Wakala Wa Shetani
Sehemu Ya Kwanza (1)
UTANGULIZI:
KILA binadamu yupo duniani kwa ajili ya kuishi. Hakuna aliyeumbwa kupata mali kwa ajili ya kumpoteza mwenzake bali imeumbwa riziki ya mtu ipitie kwa mtu. Wengi wamesahau kila kiumbe kitaonja mauti siku yake ikifika lakini si kwa utashi au tamaa za watu bali kwa mapenzi ya Mungu. Wengi huamini wataishi milele na kuwageuza wenzao kama chambo au ngazi ya kufikia utajiri au mafanikio kwa vile uhai wao unanukia harufu ya fedha. Ili kujua kwa nini uhai wa watu wengine una harufu ya fedha ungana tena na yuleyule mwandishi wako mahiri katika riwaya nyingine ya kusisimua
TUWE PAMOJA
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kilikuwa kiumbe cha ajabu ambacho japokuwa kilifanana na umbile la kibinadamu lakini kilikuwa na matendo ya kinyama. Wengi walifikiri ni mzimu lakini haukuwa mzimu, alikuwa binadamu tena albino ambaye alionekana kuishi maisha marefu kama mnyama wa porini huku akiwa hana kiungo kimoja cha mwili, mkono wa kulia.
Umbile lake lilikuwa lenye afya njema, akiwa na nywele nyingi nyeupe na ndefu kama rasta. Ndevu nyingi, kucha ndefu na mavazi yaliyochakaa yaliyoonesha kutojua maji kwa kipindi kirefu zaidi ya mvua iliyomnyeshea.
Chakula chake kilikuwa nyama mbichi na matunda ya msituni. Macho yake yaliyokuwa mekundu na muda mwingi aliangalia chini. Alionekana kuwachukia binadamu kuliko kitu chochote.
Siku ya kwanza kukutana naye, aliua watu zaidi ya watatu, ikabidi itumike nguvu kwa kumpiga risasi ya kupoteza fahamu ndipo walipoweza kumkamata.
Daktari aliyepelekwa kwa ajili ya kumchunguza alinyongwa kwa kamba alizokuwa amefungwa nazo. Japo alikuwa kiumbe wa kawaida lakini mazingira yalimfanya aonekane kama mnyama. Baada ya kumkata nywele na kucha, bado alionekana mtu mwenye hasira, asiyependa kutazama watu usoni.
Mkono mmoja uliokuwa umekatwa ulibaki na kovu la muda mrefu, lingekuwa bichi labda wangesema ni mmoja wa majeruhi wa kukatwa kiungo cha mkono katika janga lililolikumba taifa la kuuawa kwa kukatwa viungo walemavu wa ngozi, albino.
Lakini alionekana mtu aliyeishi maisha ya porini kwa kipindi kirefu japo haikufahamika ni muda gani alioishi porini.
Kingine kilichowashangaza watu ni hali ya kuwa kama mnyama asiyependa wanadamu zaidi ya wanyama. Tofauti yake nyingine, alikuwa na roho mbaya kuliko ya simba.
Hakupenda chakula kilichopikwa, alipenda vyakula vibichi kama nyama mbichi na matunda, hivyo ndivyo vilikuwa vyakula vyake vikuu.
Wataalamu wa kujua matatizo ya binadamu walikutana na kumchunguza kwa muda. Vipimo vyote vilionesha yupo katika hali ya kawaida. Umri wake ulionesha kuwa na miaka kati ya 35 na 40. Mmoja wa wataalamu aligundua kuwa mtu yule aliishi maisha ya porini kwa muda mrefu hali iliyosababisha awe na hulka kama mnyama.
Walikubaliana kumtengenezea mazingira ya kumrudisha katika hali ya ubinadamu. Pamoja na kuwa haongei lakini alionesha dalili za kusikia kwani alikuwa makini kusikiliza kila kilichokuwa kikizungumzwa.
Mtaalamu wa saikolojia ya binadamu aliwaeleza kuwa baada ya muda atarudi katika hali ya kawaida na kuamini mtu yule alikuwa na siri nzito ya kumfanya aishi maisha kama mnyama kwa muda mrefu porini na kuwa kiumbe mwenye hasira, asiyependa kutazama watu machoni.
Walimtengenezea mazingira ya upendo huku muda wote akiachwa peke yake akiwa amewekewa muziki wa taratibu wa vyombo vitupu. Mtaalamu aliwaambia kupitia muziki wa vyombo vitupu, taratibu ataanza kujengeka kifikra na kujiona ni binadamu. Pia walikuwa wakimwekea picha za sinema zenye kuonesha maisha ya upendo ya watu tofauti wakiwemo albino na watu wa kawaida.
***
Mtu yule aligunduliwa katika msitu mnene pembezoni mwa Mji wa Mangu na wataalamu wa masuala ya utengenezaji wa mvua ambao waliletwa nchini kukabiliana na ukame baada ya taifa kukumbwa na janga kubwa la ukame uliosababisha mabwawa ya maji katika vyanzo vya umeme kukauka, hali iliyosababisha mgao mkubwa wa umeme.
Marafiki wahisani wa nchi zilizoendelea, walijitolea kuleta wataalamu wake kwa ajili ya kutengeneza mvua kwa bei nafuu. Nchi ya Thailand, moja ya marafiki walikubali kusaidia wataalamu pamoja na mitambo ili kumaliza tatizo la ukame lililoikumba nchi yetu iliyokuwa katika hatari ya kuingia gizani baada ya mabwawa yote kuwa
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
kwenye hali mbaya kwa kina cha maji kuendelea kupungua kila kukicha.
Kikosi cha wataalamu kilizunguka sehemu yenye milima yenye miti mingi ambayo wangeweza kuitumia kutengeneza mvua. Msitu wa Nyashana uliokuwa pembezoni mwa Mji wa Mangu ulionekana kufaa kuzalishia mvua.
Baada ya kuuchagua msitu ule, kazi ilianza mara moja kwa kuanza kupima. Wakiwa wanapima kwa kutumia kiona mbali, waliweza kumuona mtu ambaye baada ya kumvuta karibu kwa mitambo ya kiona mbali, walihisi ni mzimu, wakashawishika kusogea karibu zaidi ili wamuone vizuri.
Walipomkaribia yule mtu ambaye wao walijua ni mzimu, alikimbia na kupotelea mapangoni. Walisitisha kazi ya kupima na kuanza kumtafuta yule mtu kutaka kujua mwisho wake na kwa nini yupo sehemu ile. Siku ya kwanza, mpaka giza linaingia hawakufanikiwa kumuona.
Wataalamu hawakukubali kumkosa, wakapanga kurudi siku ya pili alfajiri na kujificha. Walifanikiwa kumuona majira ya saa moja asubuhi akitoka kwenye pango lake, akawa anajinyoosha mwili.
Alipopiga miayo, meno yake yalionekana yamebadilika rangi na kuwa kama ya simba. Weupe wa meno yake ulipotea kabisa. Mzungu mmoja alijitokeza mbele yake, yule mtu alipomuona alishtuka na kutimua mbio kwa kukwea miti na mawe kwa mkono mmoja kama sokwe.
Kila mmoja alipigwa na butwaa na kujiuliza kwa nini mtu yule yuko vile, suala ya mzimu walilifuta japo alikuwa na nywele nyingi ndefu, kucha ndefu na nguo chakavu.
Wapo waliodhani ni msukule, baada ya kukimbia waliingia sehemu aliyotoka, ndani ya pango lililokuwa na giza nene. Kwa msaada wa tochi yenye mwanga mkali, walifika hadi ndani ya pango. Ndani ya pango hilo walikuta mifupa mingi ya wanyama, matunda yaliyoliwa nusu na nguo chakavu zilizokuwa kama godoro.
Hawakuishia hapo, walizunguka kila kona lakini hawakukuta kitu kingine zaidi ya vile vitu walivyoviona. Kutokana na kuonekana mtu yule ni vigumu kumkamata, walitengeneza mtego na kuondoka.
Siku ya pili walipofika walimkuta amenasa lakini akionekana kutaka kujinasua kwa kujitupa ovyo, walipomkaribia ili wamkamate aliwazidi nguvu kwa kutumia mkono mmoja aliweza kufanya uharibifu mkubwa kwa kuharibu vifaa ambavyo walivichukua kwa ajili ya kumrekodi mtu yule na kuua watu watatu.
Ilibidi wakimbie na kesho yake walikuja na bunduki yenye kutumia risasi ya kupunguza nguvu mwilini, apigwapo mtu huanguka lakini hafi. Ilibidi waende kwa taadhari kubwa wakiwa na baadhi ya wanajeshi wenye siraha kali kwa ajili ya kujihami.
Walifanikiwa kupiga risasi ya mgongo wakati akitaka kuwatoroka baada ya kuwashtukia. Alipopigwa alianguka chini na kupoteza fahamu, kufanikiwa kumchukua na kuondoka naye. Mtu yule baada ya kumuweka katika chumba ambacho wataalamu waliamini huenda atarudiwa na
akili ili waweza kumuuliza vitu kama atakuwa na kumbukumbu navyo na sababu ya kuishi kule porini kama mnyama.
Baada ya kumuua daktari ilibidi wawe makini naye huku wakijitahidi kufanya uchunguzi zaidi kujua sababu ya kuishi maisha yake. Mwanzo muda wote alikuwa amechukia lakini kila siku zilivyokuwa zikienda ndivyo alivyokuwa akibadilika. Katika chumba walichomuweka
walimwekea tivii ambayo walimwekea picha za katuni na za maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi waliokuwa wakiishi maisha ya upendo na watu tofauti.
Kuna siku wakati akiangalia katuni za Tom na Jerry aliangua kicheko mpaka machozi yakamtoka. Waliokuwa wakimfuatilia waliweza kugundua maendeleo makubwa kutokana na chombo kilichowekwa kurekodi matukio yake yote. Waliweza kumfungulia hata kukaa na watu bila kuonesha tabia za awali za kinyama na kuwachukia watu hata macho yake hakuangalia chini tena.
Taratibu aliweza kuwasiliana na watu kwa lugha ya Kiswahili cha kuungaunga chenye lafudhi ya Kisukuma. Baada ya kumrudisha kwenye afya yake, wana saikolojia walikaa naye kutaka kujua sababu ya yeye kuishi katika maisha yake. Baada ya kutulia kwa muda machozi yalianza kumtoka taratibu na kuweka michirizi juu ya mashavu yake kuonesha amekumbuka jambo lililouumiza moyo wake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya muda mtaalamu aliyekuwa akimfuatilia toka mwanzo alimpa maji kwenye glasi na kumuomba ayanywe yote. Alikunywa maji yote na kutulia kwa muda kisha taratibu alianza kusimulia kisa kizima cha yeye kuishi porini kama mnyama kwa miaka yote hiyo bila kuonwa na mtu yeyote.
MIAKA 50 ILIYOPITA
Katika kijiji kimoja pembezoni mwa mji wa Mwanza karibu kabisa na ziwa Nyanza ambalo sasa hivi linaitwa Victoria. Majira ya saa mbili usiku Minza alikuwa akijigeuza katika kitanda cha kamba kilichotandikwa ngozi ya ng'ombe juu yale huku ameuma meno.
"Ngoshi wane;Mathayo."( Mume wangu ;Mathayo)
Alimwita mumewe kwa sauti ya chini huku akifinya shuka kwa vidole vya mkono wa kushoto na mkono mwingine kujipigapiga kwenye paja kutokana na maumivu ya uchungu wa kujifungua.
Mathayo aliyekuwa ametoka nje kuvuta gozo lake aliisikia sauti ya mkewe kwa mbali. Aliliweka gozo lake pembeni ya mlango na kuingia ndani ambako kibatari nacho kilikuwa kisisinzia kutokana na kuishiwa na mafuta.
"Mwana Bupilipili ginehe hange?" (vipi tena?)
"Nalebona makanza gashika." (Muda umefika)
"Dogweta ginehe lolo?" (Tutafanya nini sasa?)
"Nene ango nalebyalela henaha do." (Mimi najifungulia hapahapa.)
"Yayah nke wana doganhwitane o mama Sabina." (Hapana mke wangu tukamwite mama Sabina.)
"Nale shaka hamo nagobyala mbelengw'elo bakomolaga" (Na wasiwasi wa kuzaa albino watamuua.)
"Ndoho odobyala mbelengw'elo hange." (Hapana hatuwezi kuzaa tena albino.)
"Nalemaga nilekage nabyale ngw'enekele olo odohayaga no bebe jaga"( Nasema sitaki niache nizae mwenyewe kama hutaki na wewe ondoka.) Ngw'ana Bupilipili alikuwa mkali baada ya kuona mumewe hamuelewi.
Mathayo hakuwa na jinsi alikubaliana na mkewe kumzalisha mwenyewe. Sababu kubwa ya mkewe kukataa kumwita jirani yao mama Sabina ili aje amzalishe ilitokana na desturi ya pale kijijini unapojifungua mtoto albino hutengwa kwa kufukuzwa kijiji alichopo au mtoto wako kuuawa kwa kupewa sumu.
Mwaka miaka miwili iliyopita ngw'ana Bupilipili alijifungua mtoto wa kike ambaye alikuwa albino uongozi wa kijiji uliwaeleza wachague kitu kimoja kufukuzwa kijijini au mtoto auawe. Ngw'ana Bupilipili alikubali kufukuzwa lakini mumewe alikubali mtoto auawe.
likuwa vita kubwa kati ya mume na mke baada ya mtoto wao kuuawa, ilibidi familia ya mke na mume kuingilia kati ikiwa pamoja na tambiko ili tatizo lile usitokee tena kwenye familia. Wao waliona ni mkosi mkubwa mtu kuzaaa mtoto albino.
Hali ile iliendelea kila siku kwa familia zote zilizozaa mtoto albino pale kijijini watoto wao kuuawa kwa kuonekana mikosi au kufukuzwa kijijini kama wakigoma mtoto wao kuuawa.
Wakiondoka na kwenda porini walitumwa vijana waliokwenda kumpora yule mtoto na kumuua. Wanawake wote kijijini walikuwa katika hali ya wasiwasi kwa kila mwanamke aliyebeba ujauzito alikuwa katika wakati mgumu mpaka atakapojifungua na kukuta mtoto wa kawaida.
Ngw'ana Bupilipili toka abebe ujauzito amekuwa hana raha kwa kumuomba Mungu usiku na mchana asizae tena mtoto albino hata kupanga siku ya kujifungua iwe siri kati yake na mumewe tu. Kila siku alimuomba Mungu asizae mtoto albino aliogopa kumpoteza tena japokuwa moyoni alijiapiza hata kuwa tayari mwanaye auawe na kuwa tayari kutengwa na kijiji na ayakaye muua lazima kwanza amuue yeye.
Ilibidi adanganye kwa kurudisha siku za ujauzito wake nyuma, kila alipoulizwa kuhusu ujauzito wake una miezi mingapi. Alirudisha miezi miwili nyuma ili atakapo jifungua ajue afanye kitu gani kama atajifungua mtoto albino.
Ndipo siku ya kujifungua ilipowadia hakutaka aitwe mtu yeyote kushuhudia anazaliwa mtoto gani kwa kuhofia siri yake kutoka nje kama atajifungua mtoto albino. Mumewe baada ya kukatazwa na mkewe asimwite mtu yeyoye aliamua kumsaidia mkewe kujifungua.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa vile alikuwa na uzoefu aliweza kumsaidia mkewe kujifungua mtoto salama. Baada ya huduma zote mtoto alilazwa pembeni huku wakijitahidi kuzuia sauti ya mtoto kabla ya kujua mtoto aliyezaliwa ni wa aina gani ni albino au wa kawaida.
Mathayo baada ya kumhudumia mtoto wake na mkewe ambaye aliweza kukaa mwenyewe, kazi akawa kumtazama mtoto aliyezaliwa wa aina gani. Uchunguzi ulionesha mtoto yule ni albino. Walijikuta wote wakikosa raha hasa ngwana Bupilipili ambaye aliamini ana mtihani mkubwa wa kumpoteza tena mtoto mwingine ambaye amekaa naye tumboni kwa kipindi kirefu halafu watu wamchukue na kwenda kumuua kiurahisi.
Unaona sasa mume wangu, ungemwita mama Sabina lazima siri hii ingetoka nje.
Sasa tutafanyaje na hali hii imetokea?
Dawa ni kumficha mtoto wetu ili wasijue nimejifungua.
Tutamfichaje? Pia mtu aliyejifungua anajulikana kwa tumbo kupungua na mtoto wetu tutamlea vipi usionekane kwa watu? Mathayo aliona mtihani mgumu.
Mume wangu nitaendelea kuweka nguo tumboni siku zote ili lionekane kubwa.
Tumbo sawa litaonekana kubwa, mtoto tutamweka wapi? Tukimficha ndani lazima atalia na kutoa sauti majirani watataka kujua ni mtoto wa aina gani. Na wakimuona hawatakubali kumuacha lazima watamuua, pia kutupiga faini ya ngombe watano huoni kama zizini kwetu ngombe watapungua?
Hilo nililijua toka mwanzo na nilijipanga kwa ajili ya hili, ngwana Bupilipili alimtoa hofu mumewe aliyeonekana kuchanganyikiwa zaidi.
Tutafanyaje mke wangu, huwezi kuamini hapa akili haifanyi kazi kabisa, siwezi kupoteza mtoto wa pili hivi hivi. Mke wangu sikubali nitaua mtu safari hii siwezi kukubali mtoto wangu auawe, Mathayo alisema kwa uchungu kumuunga mkono mkewe.
Nimepanga kitu kimoja kama nitajifungua albino.
Kipi hicho? Mathayo aliuliza kwa shauku ya kujua mke wake amepanga nini.
Usiku huu tutakwenda hadi kwenye mlima wa karibu na shamba letu, kuna pango nimeliandaa kwa ajili ya kumficha mtoto wetu.
Mke wangu unataka kuniambia usiku huu tutamwacha mtoto peke yake kisha turudi nyumbani?
Hapana, kila siku tutatoka alfajiri hadi kwenye pango hilo, kisha wewe utaingia shambani nami nitakuwa karibu na mtoto mpaka atakapokua kidogo, tutatoroka usiku kwa usiku na kwenda kijiji kingine.
Lakini mke wangu ni kijiji gani tutakachoweza kuishi na mtoto huyu bila matatizo?
Mume wangu hebu tufanya hili kwanza mengine yatafuata baadaye.
Usiku uleule walimchukua mtoto wao na kutoka naye kiza kwa kiza. Japokuwa usiku ulikuwa mkubwa wenye kutisha, Ngwana Bupilipili alionesha ujasiri wa ajabu kwa kumuongoza mumewe hadi shambani kwao ambapo pembeni yake kulikuwa na kilima kidogo ambacho ndipo alipoandaa pango la kumtunzia mtoto wao.
Walitumia majani makavu kuyawasha moto ili kutengeneza tochi ya dharula kumulika sehemu ile. Mumewe alishangaa kukuta sehemu ile imetengenezwa vizuri sana.
Mke wangu umetengeneza lini huku?
Toka nilipopata wazo la kujifungua tena mtoto albino basi nilijawa na mawazo ya kunusuru maisha ya mwanangu na kupata wazo la kupatengeneza huku.
Walimlaza vizuri mtoto wao kisha Ngwana Bupilipili alijilaza pembeni ya mwanaye, naye Mathayo alilala pembeni kidogo ya mkewe, kwa vile muda ulikuwa bado usingizi uliwapitia.
Waliamshwa na sauti ya mtoto aliyekuwa akilia, Ngwana Bupilipili alishtuka usingizini na kukuta kumeanza kupambazuka, alimnyonyesha mtoto wake aliyeonekana ana njaa. Wakati huo mume wake alikuwa amekwisha amka na kutoka nje kuangalia hali ya usalama.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mke wangu wacha nirudi nyumbani nikawaandalieni chochote kitu.
Hakuna tatizo usisahau dawa zangu tumbo nalisikia kwa mbali.
Hakuna tatizo mke wangu.
Mathayo kabla ya kuondoka alimtazama mkewe na kisha mtoto wake ambaye hakuwa na habari yeyote zaidi ya kuchezesha mikono na miguu baada ya kushiba na kufurahi kuja dunia salama, bila kujua hatari iliyo mbele yake ya kuonekana mkosi kwa jamii.
Bila kutegemea machozi yalimtoka kumwonea huruma mkewe ambaye aliamua kuishi maisha ya siyo yake kuhofia uhai wa mtoto wao.
Pia alimuonea huruma mtoto wao ambaye bado alikuwa hajapewa jina kutokana na misukosuko ya moyo wa kutaka kuokoa kwanza maisha yake baada ya wanakijiji kuona watoto maalbino ni mkosi kama wakiachwa kijiji kitapata balaa kubwa.
Japokuwa awali naye alikuwa ni mmoja wa watu walioamini albino ni mkosi, lakini mambo yalibadilika baada ya kutokewa yeye. Mwanzo naye alishiriki kuwaua watoto wa wenzake. Siku zote msiba wa mwenzio hauumi lakini msiba ikiwa kwako utajua uchungu wake. Mathayo baada ya mkewe kujifungua mtoto wa kwanza albino alikubali auawe lakini mkewe alisimama kidete asiuawe na kuwa tayari wafukuzwe kijijini.
Wakati wanahama kijiji walipovamiwa na vijana wa kijiji wenye jukumu kusaka na kutoa uchafu wa watoto wanaoonekana wanaleta mikosi kijijini. Mtoto albino alipouawa nyumba ilifanyiwa tambiko na kutengwa kwa muda wa wiki mbili.
Kilio cha mkewe baada ya kubeba ujauzito wa pili cha kuhofia uhai wa mtoto wake kilimfanya Mathayo naye abadili uamuzi na kuwa tayari kukisaliti kijiji pindi mkewe atakapo kifungua mtoto albino. Aliapa moyoni hatakubali kumtoa mtoto wake auawe tena.
Michirizi ya machozi iliendelea kumtoka huku miguu ikiwa mizito kunyanyuka. Mkewe alimwona na kunyanyuka alipokuwa amejilaza na mtoto na kumfuata mumewe. Alimkumbatia na kumbembeleza huku akimpigapiga mgongoni taratibu.
Mume wangu hii ni mitihani aliyotupa Mungu tunatakiwa kupambana nayo, tunatakiwa tumtegemee yeye kwa kila kitu na kumtumai kwenye majaribu mazito kama haya. Hakika tutashinda japo kukua mwenetu itakuwa sawa kabisa na ngamia kupita kwenye tundu la shindano. Lakini tukimuamini yeye lolote kwake linawezekana, Ngwana Bupilipili alimpa moyo mumewe.
Ni kweli la..la..kini... Mathayo hakumalizia kutokana na donge la uchungu kumkaba kooni huku machozi yakimdondokea mkewe.
Hakuna cha lakini, tumuachie Mungu ndiye aliyetupa kiumbe huyu, mbona kuna viumbe wasio na faida duniani wanaishi kwa furaha itakuwa mwanadamu. Mungu atamlinda mwanangu, nina imani atakuwa tu na siku moja kutoa ushuhuda hata kama wazazi wake tumetangulia mbele ya haki, Ngwana Bupilipili alizidi kumpa moyo mumewe.
Nashukuru mke wangu kunipa moyo.
Ni wajibu wangu, basi wahi ukaandae chochote kitu, njaa naisikia imeanza kunichonyota.
Mathayo aliondoka kwenye maficho na kurudi nyumbani kumuandalia mkewe chakula kutokana na njaa kali iliyokuwa imemshika hasa baada ya kujifungua hakuwa ameweka kitu tumboni. Alipofika nyumbani alimchemshia uji na viazi ambavyo vilikuwa vimebaki jana yake. Haraka
haraka alianza kurudi shambani. Hakufika mbali mvua kubwa ilianza kunyesha.
Hakukubali kusimama, alitembea nayo huku akilowa kila kona ya mwili. Alipofika pangoni alimkuta mkewe akiwa amemkumbatia mtoto wake ambapo maji yalikuwa yameanza kuingia ndani ya pango.
Wasingeweza kutoka nje kutokana na mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha kuwa kubwa. Mathayo alipofika aliingia mle pangoni alipokuwa mke wake na kiza kilianza kutanda huku baridi ikizidi kuwa kali.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mvua nayo ilikuwa kama imetumwa kwani ilizidi kuongeza kasi ya kunyesha ikiambatana na upepo mkali. Maji yakazidi kuingia kwenye pango, kila dakika yalizidi kujaa na kuelekea mafutini huku Ngwana Bupilipili akimkumbatia mwanaye na kuendelea kumuomba Mungu asitishe mvua ile kwani haikuonesha dalili za kukatika mapema.
Maji nayo yalizidi kupanda juu kuelekea kiunoni, mvua nayo ndiyo kama imechochewa kuni kwa jinsi ilivyokuwa ikinyesha kwa kasi huku upepo ukizidi kuvuma.
Walifikiria watoke nje ili wakimbilie kwenye makazi ambako kulikuwa mbali, waliamini wasingefika kwani wangeweza kuuawa hata na radi ambayo ilikuwa ikipiga kwa nguvu na upepo mkali.
Nje kulikuwa hapatamaniki kutokana na mvua na upepo mkali uliokuwa ukivuma hadi kuifanya baadhi ya miti kungoka. Ilikuwa mvua ambayo haikuwahi kunyesha muda mrefu pale kijijini.
Pangoni maji nayo yalizidi kujaa na yalivuka kiunoni kuelekea kifuani. Ilibidi mtoto wamweke mabegani, hawakuacha kumuomba Mungu kila dakika ili kuwanusuru na janga lile zito ambalo lilikuwa lina kila dalili za kuchukua uhai wao.
Mvua nje iliendelea kunyesha na maji nayo kila dakika yalizidi kujaa mle pangoni. Yalivuka kifuani na kuanza kuelekea shingoni. Mathayo na mkewe waliamini kabisa hakukuwa na dalili zozote za kutoka salama. Ila Mathayo alikumbuka huenda mvua ile ni laana ya kumficha mtoto wao albino ambaye alionekana kama mkosi.
Wazo lake alifikiria kumtupa yule mtoto ili waangalie itakuwaje. Aliona ampe mkewe wazo aone atalipokeaje.
Mke wangu nilikuwa na wazo.
Wakati huo walikuwa wamekumbatiana huku mtoto wao wamembeba kichwani japokuwa walianza kuchoka kutokana na kuiweka mikono juu kwa muda mrefu.
Wazo gani mume wangu? Siamini kama tutatoka salama, muda si mrefu maji yatatufunika. Ona sasa hivi yanakimbilia kidevuni...Eeeh, Mungu, sikiliza kilio chetu waja wako, Ngwana Bupilipili hakuacha kumuomba Mungu muda wote.
Mke wangu nina wazo moja, japo huenda usiliafiki lakini nahisi ndilo litakaloyaokoa maisha yetu.
Wazo lipi mume wangu? alisema huku akiyapuliza maji yaliyotaka kuingia mdomoni.
Mimi nafikiria kabisa mvua hii si bure, huenda tumevunja mila na desturi.
Kuvunja kivipi?
Ni wazi huyu mtoto ni mkosi na hii mvua ni hasira ya mizimu.
Sasa hizo hasira zao sisi zinatuhusu nini?
Huenda wameamua kututia adabu kwa kiburi tulichokionesha kwao.
Sasa wewe ulikuwa na wazo gani? Naona muda si mrefu maji yatatufunika hata mikono imeishiwa nguvu kwa sababu ya kumshikilia mtoto kwa muda mrefu.
Kwa nini tusimtupe huyu mtoto?
Mume wangu unasemaje? kauli ile ilimshtua Ngwana Bupilipili.
Tumtupe huyu mtoto ili kuyaokoa maisha yetu.
Tukishamtupa tupata nini?
Nina imani mvua itakoma na sisi kuokoka.
Mume wangu, maisha yako ni bora kuliko ya mtoto wetu?
Hapana mke wangu, siku zote vitu vya jadi si vya kuvipuuza, matokeo yake leo tunakufa tunajiona.
Mume wangu, kwa taarifa yako mtoto wangu siwezi kumtupa kama tutakufa basi tutakufa wote na kama kupona ni pamoja na mtoto wetu.
Mke wangu, unafanya mzaha, tutakufa huku tunajiona.
Hata siku moja siwezi kuua mwanangu, mimi ndiye ninayeujua uchungu wake. Kama tutakufa sawa lakini tukipona naomba uachane na mimi, nitajua jinsi gani ya kuishi na mwanangu, Ngwana Bupilipili alimjia juu mumewe.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mke wangu kwa nini hutaki kuwa mwelewa, mtoto nini? Tutatafuta mwingine lakini hatuwezi kuwa na bomu ambalo linatulipukia tumelikumbatia.
Kwani tatizo nini? We toka, niache peke yangu nife na mwanangu. Kama kufa nitaanza mimi kisha mwanangu atafuatia.
Mmh! Sawa nitafanyaje nawe umekuwa mbishi.
Siamini kumbe nawe ni walewale, basi wafuate ili waje wamchukue mtoto wangu wakamuue kama mlivyomuua mwanangu wa kwanza, Ngwana Bupilipili alisema kwa uchungu huku machozi yakimtoka.
Maji ya pangoni yalikuwa ya baridi na kiza kinene kilitanda mmle ndani kutokana na mvua ambayo ilianza kupunguza kasi yake. Lakini wingu lilikuwa bado zito likiambatana na baridi kali.
Waliendelea kuwemo mule pangoni, mtoto wao alikuwa bado yupo juu huku mikono yao ikizidi kuchoka. Nje mvua ilikuwa imekoma, hata maji kuingia pangoni yaliacha lakini bado maji yalikuwa chini ya kidevu.
Kutoka ndani ya pango ilikuwa vigumu kwa vile hapakuwa na sehemu ya kushika, pia giza la mle pangoni liliwafanya wasione njia ya kutokea nje.
Waliendelea kukumbatiana huku baridi la maji kilizidi kuwapiga, Ngwana Bupilipili alianza kutetemeka kwa meno kugongana.
Mume wangu nasikia baridi kali sana, pia nahisi mtoto atatuponyoka muda si mrefu, mikono imeishiwa nguvu kabisa.
Hataanguka mke wangu, nitamshikilia mpaka pumzi zangu za mwisho, Mathayo alimpa moyo mkewe.
Mume wangu bado siamini kama mtoto albino ni mkosi, kuna viumbe wangapi duniani ambao kwa akili ya kibinadamu tunawaona hawana thamani? Lakini kutokana na umuhimu wake wote Mungu amewathamini na kuwapa kipaumbele. Sasa itakuwaje kwa kiumbe huyu aliyepungukiwa na madini mwilini? Mwanangu na bundi nani mwenye thamani?
Mtoto.
Sasa mbona bundi hasakwi na kuuawa ila wanakimbilia kuua viumbe wasiyo na hatia. Hizo ni imani zisizo na ukweli zaidi ni kukubaliana na ujinga wa mtu mmoja na kuufanya ndiyo sheria.
Kwa kweli hata mimi bado sijaelewa hili suala la kuuawa albino ni nani aliyetoa wazo hilo.
Mume wangu unachekesha, yaani unachukua uamuzi wa kumuua mtoto wako kwa vile watu wamesema. Lakini hujui lolote kwa kile unachokifanya? Ngwana Bupilipili alimshangaa mumewe.
Mke wangu kwa hilo nakiri kosa, lakini nami naamini albino si mkosi.
Hivi mume wangu kama ningekukubalia tumtupe mtoto na baada ya siku ukayajua haya tunayozungumza, ungefanya nini?
Kweli ingeniuma, lakini ningekuwa nimefanya kosa la majuto.
Mungu naye alishusha baraka zake, maji pangoni yalipungua kwa kasi, baada ya dakika ishirini maji yote yaliisha mle pangoni na kuweza kutoka salama na mtoto wao hadi juu ya pango.
Kila mmoja alikuwa akitetemeka kwa baridi kali, wingu bado lilikuwa limefunga na kufanya hali ionekane kama saa moja usiku na kumbe ni saa tano asubuhi. Walijiuliza watawezaje kurudi nyumbani kubadili nguo, kama kawaida mkewe pamoja na kuwa katika hali ngumu ya baridi, uchovu na njaa kali, aliamua kurudi kijijini na kumuachia mumewe mtoto ili akaandae chakula na kurudi na nguo za kubadili.
Aliendelea kumshukuru Mungu kwa kumlinda mtoto wao ambaye hakuguswa na maji. Kwa muujiza ule aliamini kabisa mtoto wao si mkosi kama walivyofikiria. Kwa mvua ile lazima kuna kitu kingetokea hata radi ambayo ingempiga na kumuulia mbali, lakini alibakia salama bila kupata madhara yoyote.
***
Alirudi hadi kijijini huku njia nzima ikiwa na vidimbwi vya maji. Kuna sehemu ilibidi avue nguo na kuziweka kichwani kutokana na mito kujaa maji na kufikia kifuani. Alitembea kwa shida bila kukutana na mtu. Alifika nyumbani na kuandaa chakula kingi ambacho wangekula kwa siku mbili. Baada ya kuandaa chakula, wakati wa kutoka alikutana uso kwa uso na jirani yake, mama Sabina.
Jirani salama?
Salama.
Mvua imekuponesha?
Mmh! Namshukuru Mungu nimepita salama.
Mmh! Kuna usalama kweli? Alimuuliza huku akimuangalia tumboni.
Kwani vipi?
Mbona kama tumbo la mtu aliyejifungua?
Mama Monika, mbona maneno ya uchuro! Nijifungue kisha nikae kimya? Ngwana Bupilipili alipindisha ukweli.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aah! Basi macho yangu, kwani tumbo lako lilikuwa kubwa na sasa limepungua kidogo.
Bado mwezi mmoja.
Haya safari ya wapi tena na mvua hii?
Shamba.
Shamba wakati mvua ilikuwa ikitishia usalama?
Kuna sehemu ziliharibika mume wangu anazitengeneza hivyo nilikuwa nampelekea chakula.
Haya dada.
Waliachana huku mama Monika akiwa haamini kabisa kauli ya Ngwana Bupilipili juu ya kuwa na ujamzito. Wasiwasi wake huenda amejifungua njiti na mtoto akawa si riziki. Kwa hiyo aliona aibu kusema. Lakini kwa ujirani wao aliamini kama kumetokea tatizo lolote wasingemficha.
***
Kutokana na mawazo mengi, mama Sabina alimpita mumewe aliyekuwa akitoka ndani.
Mama Sabina mbona hivyo?
Aah, kawaida tu mume wangu.
Halafu nimemuona mke wa Mathayo akielekea shamba, kuna nini wakati leo hali si nzuri, hata njia ya kuelekea shambani imejaa maji? baba Sabina alimhoji mkewe.
Unajua kuna kitu kinanichanganya.
Kitu gani tena mke wangu?
Unajua tokea jana asubuhi nilipokwenda kumjulia hali Ngwana Bupilipili sikumkuta na baada ya muda nilimuona mume wake akiingia ndani majira ya alfajiri na baada ya muda alitoka na kikapu kilichoonekana kuna chakula.
Siamini kama alifika mbali, baada ya kushika njia ya shamba tu mvua ilianza kunyesha. Lakini ajabu sasa hivi mke wake amerudi pia ameondoka na chakula na tumbo lake limepungua. Isijekuwa amejifungua mtoto ambaye hajatimia na kuamua kumzika ya bila kutushirikisha.
Sasa kwa nini wafanye hivyo? baba Sabina aliuliza huku akiwasha gozo lake.
Ndilo swali linaloniumiza akili.
Ulipomuuliza alisemaje?
Anasema yupo sawa, lakini kuna kitu ananificha...Halafu mimi nilifikiri kwa vile mvua imekatika kuna haja ya wao kurudi nyumbani. Nasikia mashamba mengi yamejaa maji sasa wao wanakwenda kufanya nini?
Mmh! Swali zito.
Lakini kuna kitu tutajua tu.
Mke wangu lisikuumize akili hilo, achana nalo.
Mama Sabina alielekea jikoni kuandaa kifungua kinywa na kumwacha mumewe akilipuliza gozo
***
Baada ya mkewe kutoka, Mathayo alibakia na mtoto huku akiamini kabisa mvua ile ni mkosi wa kumficha mtoto albino ambaye alionekana ni mkosi. Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa kwa wanakijiji kama wakijua ukweli.
Lazima hasira yao ingekuwa kubwa mara dufu hata kuwafanyia kitendo kibaya ikiwemo kuwaua kwa kuwafungia katika nyumba yao kwa muda mrefu ili wafe kwa njaa au kuwachoma moto wakiwa ndani.
Alijawa na mawazo mengi juu ya kuendelea kuwa na yule mtoto, bado aliamini ule ni mikosi na huenda ungewasababishia matatizo makubwa. Wazo alilokuwa nalo lilikuwa ni kukiulia mbali kile kitoto na kumweleza mkewe kuwa kilidondokea kwenye maji.
Lakini aliamini mkewe hawezi kumwamini hasa baada ya kutaka kumuua. Alijua chochote kibaya hata kama cha bahati mbaya kitaonekana cha makusudi.
Hali ya kusimama kwa muda mrefu huku akimbeba mtoto bila sehemu ya kukaa ilimtesa sana. Kutokana na kujaa maji na matope kila sehemu, hakukuwa na sehemu ya kumweka mtoto ili apumzike. Aliona mateso yale yalikuwa ni ya kujitakia, aliamini hakukuwa na haja ya kuteseka kama wangemuulia mbali yule mtoto.
Baridi lilikuwa kali mpaka likaanza kumwingia tumboni na kuzidi kumweka kwenye wakati mgumu. Kuna wakati alichoka sana na kuamua kutafuta sehemu yenye mwinuko kidogo na kukaa ndani ya maji.
Kila mateso yalivyozidi kumpata alizidi kumchukia yule mtoto na kufikia kuwaza kwenda kwa siri kwa wana kijiji kuwaeleza habari za mkewe kujifungua mtoto Albino ili achukuliwe na kuuawa.
Aliamini ile ndiyo njia itakayowafanya waishi maisha ya amani. Pamoja na kuyawaza yote, bado aliamini mkewe lazima atamfikiria vibaya. Alijuta kutoa wazo la kumuua yule mtoto, aliamini kama angekaa kimya mkewe asingejua mpango wake, hivyo, ingemrahisishia kutimiza dhamira yake bila mkewe kujua.
Kilichomchanganya zaidi akiwa katikati ya dimbwi la mawazo, mtoto alianza kulia tena kwa sauti ya juu. Wasiwasi wake mkubwa kama atatokea mpita njia lazima angemsikia na kusogea. Alijitahidi kumbembeleza lakini mtoto aliendelea kulia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alijiuliza mkewe kachelewa wapi au njia imefunga kutokana na maji kuwa mengi, alipata wazo la kumfuata mkewe akiwa na mtoto wao na mengine yangejulikana hukohuko.
***
Wakati mama Sabina akimtafakari Ngwana Bupilipili na mumewe, juu ya mabadiliko alioyaona juu yake.
Pia, mumewe na mawazo mabaya kwa mtoto wao. Ngwana Bupilipili alikuwa njiani kurudi shamba alipomuacha mumewe na mtoto. Ilibidi apite njia ileile ya kuingia ndani ya mito na vidimbwi vya maji ambavyo vilikuwa havikwepeki.
Alishangaa kukutana na mumewe njiani, ile ilimshtua na kumuuliza.
Vipi mbona huku unakwenda wapi?
Nilikuwa nanyoosha miguu kidogo kukaa sehemu moja nilichoka, Mathayo alidanganya.
Mume wangu unakuja huku watu wakimuona utanibebea mbeleko gani? Ngwana Bupilipili alimlalamikia mumewe.
Mke wangu nisingefika mbali.
Mmh! Sawa, vipi ameanza kulia muda mrefu?
Si mrefu sana lakini nilichanganyikiwa nashukuru umerudi haraka, sijui ungechelewa ningemfanyaje?
Inawezeka amekojoa, Ngwana Bupilipili alisema huku akimchukua mwanaye, mwili wote ukiwa umetoka maji na kuhisi baridi kali.
Alimpakata mwanaye na kuanza kumnyonyesha, hapakuwa na sehemu ya kukaa kutokana na kila kona kujaa maji. Yalikuwa nki mateso mazito sana katika maisha yao.
Walikubaliana kurudi nyumbani kiza kikiingia ili kumpeleka mtoto kwenye joto kwa kuogopa mtoto kupatwa na ugonjwa wa Nimonia.
Waliendelea kuvumilia kukaa kule shamba pamoja na baridi kali pia wingu zito likitanda tena kuonesha mvua ingeteremka tena wakati wowote.
Ngwana Bupilipili alimuomba Mungu kwa kila lugha aliyoifahamu ili mvua isishuke kwa kuamini lazima mtoto wao watampoteza kwa baridi au kufa maji. Alijua kama mvua itanyesha muda ule lazima hata maisha yao yatakuwa mashakani kwa kushindwa kuona sehemu watakayojificha kutokana na kiza kilichoanza kutanda tena.
Baridi lilizidi kuwa kali huku wakimkumbatia mtoto wao kwa kumweka kati ili apate joto la wazazi wake, kutokana na ubaridi kuwa mkali na sehemu ya kukaa haikuwepo, ilikuwa ni adhabu kubwa sana kwao kusimama kwa muda mrefu bila kukaa huku wakipokezana kumbeba mtoto.
***
Usiku uliingia wakiuona huku wakiwa hoi kama wapo kwenye adhabu. Mathayo bado aliamini ule ni mkosi kutokana na kukiuka masharti ya kumficha yule mtoto Albino. Lakini aliogopa kumweleza mkewe kwa kuamini hatakubaliana na chochote atakachomweleza.
Kiza kilipoingia waliongozana na mtoto wao huku wakitetemeka kurudi kijijini kwa kuingia kwenye vidimbwi vya maji kuna kipindi walipita kwenye maji yaliyowafikia vifuani.
Ilikuwa adhabu kubwa kama ingekuwa amri ya Mathayo angemtupa mtoto ili afie mbali na yeye kurudi kijijini bila hata mshipa wa fahamu kumgonga kama amepoteza damu yake. Aliamini tabu yote ile isingewafika kama wangekubali kumtoa mtoto wao na kuuawa.
Wasiwasi wake kama kijiji kitajua kuwa mkewe amejifungua mtoto albino, basi wangetengwa pia kutozwa faini ya ngombe na kuchukuliwa sehemu ya shamba. Alimuona mkewe kama anataka kumitia kwenye umaskini kwa kunyanganywa mali zake kwa ajili ya mtoto ambaye hata wakimficha lazima angeonekana tu, kwani lazima amgelia na sauti ingesikika kwa watu.
Walirudi nyumbani kwa taadhari kubwa huku mkono wa Ngwana Bupilipili ukiwa hauchezi mbali na mdomo wa mtoto wake ili akitaka kulia amzibe mdomo asitoe sauti.
Walifanikiwa kuingia ndani kwao bila mtu yeyote kuwaona. Baada ya kuingia ndani waliwasha moto ambao waliuota na miili yao kupata joto kisha waliandaa chakula cha usiku.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Muda ulikuwa umekwenda sana, ilikuwa inakimbilia saa tatu usiku. Lakini ilionekana ni kama saa sita za usiku kutokana na kiza na wingu zito la mvua.
Baada ya kula walichemsha maji ya moto na kwenda kuoga kutokana na kushinda na kupita kwenye maji machafu.
Kwa vile mtoto alikuwa amelala baada ya kunyonya na kushiba. Walikwenda kuoga kwa pamoja, wakiwa wanaoga mtoto alianza kulia na kutoa sauti ambayo kutokana na utulivu wa usiku ilifika mbali.
Ngwana Bupilipili aliposikia sauti ya mtoto aliacha kuoga hata bila kukumbuka nguo alitoka mbio kuwahi kumnyamazisha. Kwa vile ilikuwa kiza hakuna ambaye alimuona ametoka bila nguo.
Alipofika alimbeba mtoto wake na kuanza kumnyonyesha huku akimbembeleza, ilionekana alikuwa amejikojolea na kutokana na hali ya baridi ilimfanya alie.
Baada ya kunyonya na kumbadili nguo alinyamaza na kupitiwa tena na usingizi.
Baada ya kumlaza alirudi bafuni na kumalizia kuoga, wakati huo mumewe alikuwa ameishamaliza kuoga na kukaa na mtoto.
****
Mama Sabina usiku ule alikuwa akiangalia mifugo kabla ya kulala, alisikia sauti ya mtoto akilia, lakini hakuwa na uhakika inatoka wapi.
Sauti ilimjulisha ni mtoto mchanga na eneo lile hakukuwepo na mtoto mchanga. Baada ya kuhakikisha mifugo ipo tayari alirudi ndani ambako mumewe alikuwa amekwishatangulia kitandani.
Mume wangu nimesikia sauti ya mtoto mchanga akilia, alisema huku akirudisha mlango kabla ya kupanda kitandani.
Mtoto mchanga? mumewe alishtuka huku akigeuka.
Eeh.
Sasa tatizo nini?
Unajua hapa kitongojini kwetu aliyekuwa na ujauzito wa kujifungua ni mke wa Mathayo Ngwana Bupilpili.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment