Search This Blog

SIKU 100 ZA MATESO YA KUZIMU - 1

 







    IMEANDIKWA NA : ALLY KATALAMBULA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Siku 100 Za Mateso Ya Kuzimu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    KISIWA cha Guam kilichopo katika bahari ya Pasific ndio kisiwa kikubwa kuliko kisiwa kingine chochote katika bahari hiyo, kisiwa hicho kiko umbali wa kilometa zaidi ya 800 kutoka nchini Marekani ambapo huchukua masaa zaidi ya 18 kusafiri kwa ndege kutoka mji wa New York hadi kufika katika kisiwa hicho.

    Kama ungepata bahati ya kuona mandhali ya Msitu mkubwa unaopatikana kwenye kisiwa cha Guam ungeona miti mirefu yenye matawi mapana, sanjari na nyasi fupi zenye ukijani kibichi wenye kuvutia.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jioni moja katika msitu wa Guam zilisikika sauti za mbwa zilizokwenda sambamba na sauti za milunzi ya ndege waliokuwa wakishangilia na kuimba nyimbo zisizo na maana yoyote kwenye masikio ya binadamu.

    Hali ye hewa ilikuwa shwari, jua la jioni lilikuwa linazama taratibu huku likiacha mwanga wenye rangi ya njano na mionzi yenye joto hafifu. Kadiri muda ulivyokuwa unayoyoma ndivyo mwangwi wa sauti za mbwa na ndege zilivyokuwa zikiyeyuka taratibu, mambo yale yakawa yanatendeka taratibu, yanii mwanga wa jua ukawa unazidi kufifia, giza likawa linachukua hatamu na sauti za mibweko ya mbwa ikawa inaishilizia.

    Hatimaye giza lilingia, na muda mfupi badaye, kila kitu kikawa kimya!

    Wakati mabadiliko hayo ya kidunia yakiendelea kutendeka katikati ya msitu ule, kulikuwa na mwanaume mmoja aliyekuwa taabani, alikuwa amelala chini, damu nyingi zilikuwa zimetapakaa mwilini mwake.

    Alikuwa na majeraha makubwa mwilini.

    Mtu huyo ambaye umri wake ungeweza kuukisia kati ya miaka thelathini ama thelathini na tano, alikuwa amevaa suti nyeusi ambayo ilionekana kuwa ghari kabla ya kutapakaa damu na vumbi.

    Hali ilivyoonyesha ni kama alipoteza fahamu kwa muda mrefu sana kutokana na maswahibu yaliyomkuta, alikuwa akihema kwa tabu.

    Wakati huo giza lilikwisha ingia na kumeza nuru yote ya nchi. Wingu jeusi la mvua lilionekana kwa mbali, kukawa na ngurumo ndogo za radi zilizokwenda sambamba na mvumo wa upepo, kiasi cha lisaa limoja tangu nuru imezwe na giza zito, matone ya mvua yakanza kushuka kidogo kidogo kwenye msitu ule wa Guem. .

    Matone ya mvua yalipomdondokea mtu yule, fahamu zikamtwaa! akafumbua macho, akakunja sura alipogundua anamaumivu makali sana mwilini mwake.

    “Aaagh!” alitoa mguno. Maumivu makali yalimwathibu alipojaribu kusimama.

    Alijikaza, akajikaza na kujikaza, hatimaye akanyanyuka na kukaa kitako huku mgongo wake akiwa ameuegemeza kwenye mti, akawa anahema kwa nguvu kama katoka kwenye mbio ndefu, alitumia dakika moja kufikiri ni jambo gani limemfanya awe pale.

    Alionyesha taharuki kubwa baada ya kukumbuka kila kitu kilichotokea hadi kupelekea kuwa katika hali ile.

    Alitizama juu kama mtu aliyetegemea kuona kitu fulani, lakini baada ya kuona hakuna alichotegemea akajawa na woga.

    Alijinyanyua kwa tabu na kusimama wima, akapiga hatua moja, akaona anaweza kutembea. Akawa anachechemea huku akitizama huku na kule kama mwenye kutafuta kitu fulani, bado hakuweza kuona kile alichotarajia.

    Giza lilikuwa nene ndani ya msitu huo, mvua ndogo ikawa inanyesha na kukatika huku upepo ukivuma kwa kasi.

    Yule mtu alipuyanga katika ule msitu kwa muda wa kama nusu saa, kwa mbali akawa anasikia sauti ya kitu kama mawimbi. Naam!...Yalikuwa ni mawimbi ya bahari yaliyokuwa yakijisukuma kwa nguvu katika pwani na kurudi baharini.

    Akaongeza mwendo kuelekea uelekeo ambao sauti ya mawimbi ya bahari yalisikika, alipita kwenye madimbwi na matope, akakatiza vichakani na hatimaye alitokea kwenye fukwe.

    Giza lilikuwa limezagaa eneo lote la fukwe wa bahari, yule mtu alibaki akimangamanga macho huku na kuleCHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Any one here?” alisema kwa lugha ya Kingereza akimaanisha kama kuna mtu yoyote pale. hakuna kilichosikika zaidi ya mawimbi ya habari yaliyokuwa yakijisukuma kwa nguvu ukingoni mwa bahari.

    Mvua ilipungua kidogo, na haikuchukua muda mrefu zaidi ikakatika.

    Mtu yule aliketi chini kwenye mchanga akionekana kukata tamaa, bado maumivu ya majeraha mwilini mwake yalizidi kumsurubu, akiwa chini alingiiza mkono mfukoni mwake kisha akatoa simu ndogo ya mkononi.

    Simu ile ilikuwa imezimwa, akaiwasha... Nuru ya mwanga ikaonekana, uso wake ukaonekana kuwa na faraja, lakini faraja yake ilidumu kwa dakika chache baada ya ile simu kuwaka.

    Kwenye kioo cha simu ilionesha kutokuwepo na mtandao, lilitokea neno lilisomeka ‘network error’ alizima simu na kuiwasha tena, bado simu ile iliendelea kuwa na tatizo la mtandao. Network ilikuwa haipo.

    Alisimama akawa anatangatanga mwelekeo mmoja hadi mwingine, mkono alioshika simu ukiwa juu, akijaribu kuona kama atabahatisha mtandao lakini bado neno ‘network error’ liliendelea kutokea kwenye kioo cha simu yake.

    Alikata tamaa, kwa msaada wa mwanga wa simu yake saa yake ya mkononi ikamwonesha ilikuwa ni saaa tatu usiku.

    “Kwa nini niwe hapa? Na kwanini niwe peke yangu? Kitu gani kilitokea” mtu Yule alinong’ona, maswali aliyokuwa akijiuliza hapakuwa na wa kumpa majibu.

    Alibaki njia panda!!



    Giza zito lililokuwa limezagaa kwenye kisiwa cha Guem lilizidi kumchanganya mtu yule, akawa anapuyanga ukingoni mwa ufukwe akiwa hajui ni wapi anakwenda!

    Kijiupepo kilichotokea baharini kilifanya maungo ya mwanaume yule kutetemeka, baridi ikawa ni kitu kingine kilichochochea maumivu ya jeraha baya lilikokuwa ubavuni mwake.

    Sauti moja akilini ikamweleza:

    “Endelea kusonga mbele, huko ndiko kuna msaada,” aliitii sauti ile kwa moyo mmoja, akazidi kuzipiga hatua kwenda asikokujua.

    Kadiri muda ulivyokuwa ukiyoyoma ndivyo giza zito lilivyokuwa likitanda katika anga na kufanya usiku huo kuwa na weusi wa kutisha, kelele ya mawimbi ya maji yaliyokuwa yakijibamiza kwenye ufukwe na kurudi baharini, ndicho kitu kipee kilichosikika. Eneo lote lilikuwa kimya.!!

    Akiwa ametembea umbali wa kama nusu kilometa, ghafla!!! kishindo kikubwa kikasikika umbali wa kilomita kama mbili ama tatu.

    “Boooooom!”



    ilikuwa ni sauti ya kitu kama bomu. Ndani ya muda huohuo mwale mkali wa moto ukaonekana angani na kutawanyika katika anga, giza nene lililokuwa limetanda likang’aa.

    Mtu yule alibaki ameduwaa kwa kile alichokiona, akili yake ikahamanika kwa tukio lile. Akakimbia kwa kuchechemea kuelekea kule moto ule ilipokuwa ukiwaka.

    Alipokuwa akikaribia kwenye tukio lile, sauti za watu waliokuwa wakilia na kuomba msaada zilisikika. Akazidi kusogea. Sauti zile zikazidi kulindima masikioni mwake, hatimaye akafika eneo lile na kujionea tukio lililokuwa likiendelea.

    Ndege kubwa ya abiria ya Panasonic Airline ilikuwa ikiungua vibaya mno, ndani kulikuwa na watu alishuhudia tukio baya sana, abiria waliokuwa wakiungulia ndani ya ndege hiyo hapakuwa na hata mtu mmoja aliyejishugulisha kutoa msaada kwa watu wale. kila mtu alikuwa bize kukoa roho yake.

    Kulikuwa na pilikapilika eneo lile, huyu alienda kule huyu alirudi huku, zilisikika sauti za akina mama zikiwaita watoto wao.

    Wengine walikuwa wakiomba msaada wa kimatibabu kutokana na kuvunjika na kupata majeraha milini mwao, hakuna aliyemjali mwenzake wakati ule. Kila mtu aliangalia uhai wake.

    Yote hayo yalishuhudiwa na yule mtu akiwa hatua chache kutoka eneo lile lenye patashika.

    Kwa mara nyingine tena akatupa macho kwenye kioo cha simu yake, bado mtandao ulikuwa haupo.

    “Please help me....help to move out from fire,” sauti ya mtu mmoja alisikika ikiomba msaada kuondolewa karibu na moto.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Harakaharaka mtu yule mwenye simu isiyo na mtandao, alitoa msaada na kumsogeza mbali na moto uliokuwa unawaka kwa kasi eneo lile.

    “Na mimi nisaidie,” mtu mwingine alimwambia..

    Jamaa mwenye simu isiyokuwa na mtandao ikabidi afanye kazi ya kuwasogeza watu wote waliokuwa karibu na moto uliokuwa unawaka kwa kasi.

    Zoezi lile halikuchukua zaidi ya dakika kumi na tano, watu kadhaa walikuwa mbali na moto. Kwikwi za kilio pekee ndizo zilizosikika.

    “Tusikilizane..” hatimaye mtu yule alisema mbele ya majeruhi wale.

    “We had a very bad plane accident, most of our fellow passangers lost their lives, we have to thank God for saving us although we don’t know where we are….. there is no telephone network in this place, so we have to be patient till tomorrow to see what we can do.”(Tumepata ajali mbaya ya ndege, abiria wenzetu wengi wamekufa, sisi tumshukuru Mungu kwa kutunusuru ingawa mahali tulipo hatujui ni wapi na hakuna mawasiliano, Lazima tuvumilie hadi kesho asubuhi ili tuone nini tutafanya) mtu yule aliwaambia kwa sauti.



    “Jina lako nani kijana?” mzee mmoja alimuuliza.

    “Naitwa Amosi....Amosi Mikidadi ”

    “Naitwa William John, una roho nzuri sana Amosi,” alisema yule mzee...akapiga kimya kifupi halafu akaendelea kumuuliza.

    “Ulikuwa unasafiri na ndege hii kwenda wapi kabla ya ajali kutokea.”

    “Nilikuwa nasafirisha maiti ya mama yangu aliyefariki jijini New York kwa maradhi ya kansa...nilikuwa naelekea Tanzania kufanya mazishi...”

    “ Kwahiyo maiti ya mama yako imeungulia ndani ya ndege!!”

    “Ndiyo...”

    “Pole kwa hilo Amosi.” Mzee William akasema.



    Amosi akatikisa kichwa, alipotizama kwenye kioo cha simu yake, neno network Errors liliendelea kuwepo.



    Kadiri muda ulivyokuwa ukiyoyoma, ndivyo ndege ile ilivyokuwa ikiishilizia kuungua, masaa manne badaye hakuna kilichosalia, yalibaki majivu na mabati ya ndege.



    Ilikuwa yapata saa kumi kasoro alfajiri, kikundi cha watu wale ambao walikuwa ni manusura Panasonic Airline walikuwa wamejikunyata huku kila mmoja akimwomba mungu wake kukupambazuke salama ili waweze kupata msaada.

    Watu zaidi ya 15 kunusurika kwenye ajali ile ilikuwa ni rekodi ya aina yake katika dunia, kila mtu aalishangaa kuwa hai katika ajali mbaya ya ndege.

    Waliendelea kujikunyata wakiteketemeka kutokana na baridi na ukali wa maumivu ya majeraha katika miili yao.

    Wakiwa kwenye utulivu ule, mara ilisikika sauti ya ikitokea ndani ya msitu!!.

    “Msaada...nakufaaa....nisaidieni,” sauti ilisikika.

    “Ni nani huyo?” mtu mmoja aliuliza.

    “Atakuwa mwenzetu,” mtu mwingine alijibu.

    “Kakumbwa na nini?”

    “Sijui”

    “...Sasa?”

    “Tukamsaidie”

    “Na giza lote hili!” mwingine alidakia kwa woga. Kelele za mwanamke zikazidi kuvuruga nafsi zao.

    Kelele zile zilimvuruga zaidi Amosi, Aliduwaa. Hakuamini kile kilichokuwa kikisikika masikioni mwake.

    Sauti ile ilikuwa ni ya mama yake. ambaye alimsafirisha ndani ya ndege akiwa maiti iliyohifadhiwa ndani ya jeneza!!!!!.



    “Si alikuwa maiti na ameungulia ndani ya ndege!” akaong’ona peke yake akiwa na wasiwasi.



    “Sasa vipi tena sauti ya mtu aliyekuwa amekufa itokee ndani ya msitu!!” akaendelea kuwaza.

    “Ni sauti ya mama yangu,” hatimaye Amosi akawaambia kwa sauti ya juu.

    “Unasema!!” mzee William akahamaki.



    Amosi akaendelea kuduwaa, mshangao mkubwa ukajitengeneza usoni mwake, jambo lile lilikuwa la ajabu sana, pengine sauti ile angekuwa amesikia yeye peke yake, angeweza kujifariji kwamba ni mawenge ndio yanayomsumbua, lakini sauti ya mama yake ilisikika kwa kila mtu aliyekuwa naye mahali pale.

    “Lakini ulisema mzazi wako ulimsafirisha katika ndege akiwa ni maiti! Sasa kwanini tena useme anayepiga makelele huko porini ni mama yako?” mzee William akauliza tena baada ya kuona Amosi yupo kimya.

    “Hicho ndicho kinaniumiza kichwa pia,” hatimaye Amosi akajibu kwa huzuni.

    “Sasa?”

    “Nakwenda kumfuata.”

    “Kumfuta nani?”

    “Mama yangu.”CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Umfuate vipi mtu ambaye ni mfu...Utawezaje Kwenda na giza hili?.” Mzee William akasema kwa ukali.

    “Siwezi kukaa hivi hivi nikisikia sauti ya mama yangu mzazi ikitaka msaada huko gizani... naondoka kwenda kutoa msaada,” Amosi naye akamjia juu.

    Sauti ya mwanamke ikitokea kwenye msitu ule, ikawa inaendelea kusikika.



    Bila kuchelewa Amosi akasimama na kuanza kutembea haraka haraka kuelekea mahali ilikokuwa inasikika sauti ile.

    Wenzake wakabaki wakimshangaa, hakuna hata mmoja aliyekuwa tayari kuongozana na Amosi kwenda ndani ya msitu uliokuwa mbele yoa.

    Wote wakabaki wamejikunyata pale ufukweni huku hofu zikiwa zimetawala vifuani mwao.



    ****

    MASAA 9 KABLA YA AJALI YA NDEGE



    Amosi Mikidadi, mwanaume mrefu mwembamba mwenye misuli iliyokakamaa maungoni mwake, alikuwa amevaa suti nyeusi ya bei mbaya, alikuwa amesimama mbele ya mlango wa chumba cha mizigo wa ndege ya Panasonic Airline, alikuwa ameshikilia kijitoroli kidogo kilichokuwa na muundo kama kitanda cha machela ya wagonjwa.

    Juu ya hicho kitoroli kidogo kilikuwa kimebeba jeneza zuri la rangi ya damu ya mzee.

    Ndani ya jeneza lile kulikuwa na maiti, mwili wa mama yake mzazi aliyefariki dunia kwa maradhi ya kansa, mwili huo ulikuwa ukifanyiwa taratibu ya kuhifadhiwa kwenye chumba cha mizigo kabla ya safirishwa hadi nchini Tanzania ambapo huko pia mwili huo ungesafirishwa hadi mkoani Geita kwa ajili ya kufanyiwa mazishi.

    “Alifariki lini?” mfanyakazi wa shirikika la ndege la Panasoci Airline alimuuliza Amosi

    “Siku tatu zimepita.”

    “Mwili wa marehemu hauvuji damu?” akauliza tena huku akiweka arama ya tiki kwenye kalatasi.

    “ndio,”

    “Maiti imehifadhiwa ndani ya nailoni?”

    “Ndio.”

    “Jina la marehemu?”

    “Greta Shang’wela,” mhudumu akendelea alama ya tiki kwenye kalatasi.

    “Ni nani yako?”

    “Mama yangu”

    “Haya. Ingiza maiti ndani.”

    Amosi aliingiza mwili wa mama yake ndani ya chumba kile cha mzigo, kisha akatoka nje na kurudi sehemu ya wasafiri wanaondoka kusubiri muda wa kuingia kwenye ndege tayari kwa safari ndefu ya kuelekea Afrika Kusini ambapo huko angeunganisha ndege nyingine ya kuelekea Tanzania.



    Moyo wake ulikuwa kwenye majonzi, jitihada za kuokoa uhai wa mama yake ziligonga mwamba, donge zito lilimkaba kooni, mama yake aliyekuwa ndio kila kitu katika maisha hakuwepo tena duniani.

    Alijikaza kiume, lakini hakuweza kuzuia machozi yasimbubujike, alitizama saa yake ya mkononi na kuona zilikuwa zimesalia dakika ishirini kabla ya ndege yao kuondoka.

    Akaona huo ndio wakati muafaka wa kufanya kitu ambacho alijizuia kukifanya kwa siku tatu, akachukua simu na kuanza kutafuta majina ya watu fulani.

    Naam!. Hatimaye akampigia namba moja, simu iliita kwa muda mrefu lakini haikupokelewa. Akapiga tena.

    Safari iliita tena kwa muda mrefu, ikiwa inakaribia kukatika, ikapokelewa, sauti ya nzito ya mtu wa upade wa pili ikionekana kama ilikuwa usingizini ikasikika.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Sema, bwa’mdogo.”

    “Safi, mbona umekawia kupokea simu ulikuwa umelala?”

    “si unajua huku ni usiku, sijui ninyi huko ni saa ngapi.” sauti ya mzungumzaji upande wa pili ikisika ikiongea kivivu, Amosi akameza funda la mate, swali lile halikuwa na umuhimu wowote kuliko habari alizotaka amueleze mtu yule.

    “Nisikilize Kiba...”

    “Eeh.”

    “Mama hatunaye tena duniani.”

    “Unasema!!” jamaa akahamaki

    “Amefariki tangu juzi, nipo safarini muda huu, nakuja na mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi.

    “Jitahidi habari hizi usimweleze mtu yeyote hapo nyumbani, nimeona nikwambie wewe nikifahamu ni kaka na mwanaume jasiri unayeweza kustahimili jambo hili, naomba hata baba pia usimweleze, tunawea kujikuta tukiwapoteza watu wawili kwa wakati mmoja,” Amosi alimweleza mtu yule aitwaye Kiba.

    Kwikwi ndogo za kilio zilisikika upande wa pili...Amosi alipiga kimya kidogo kisha akasema tena:

    “Natarajia kuwasili Dar kesho mchana, nikifika tutawasilina kwa ajili ya kuwapasha habari ndugu, jamaa na marafiki.....Tii.tii.tii!”

    Sauti ya salio kuisha ikasikika, na mara sekunde iliyofuatia simu yake ikakatika lakini akiwa tayari amekiwsh atoa taarifa katika familia juu ya kifo cha mama yao.

    Aliendelea kuketi kwenye benchi lile hadi tangazo liliposikika kutokea kwenye spika zilizokuwa ndani ya uwanja ule kuwataka abiria wa ndege ya Panasonic Airline kuingia ndani ya ndege.

    Abiria wakasimama na kuelekea ndani ya uwanja, Amosi naye alikuwa ni miongoni mwao.

    Muda mfupi badaye, ndege ilikuwa ikakata mawingu ikiwa zaidi ya kilemeta 8000 kutoka jiji la New York.

    Wakiwa angani umbali zaidi ya futi 4000 mara sauti ya mhudumu ikasikika kupitia kwenye spika zilizokuwa ndani ya ndege hiyo.

    “Ndugu abiria,”sauti ilianza kusema.

    “Ndege yetu imezima injini ya upande mmoja, marubani wetu wanaangalia uwezekano wa kutafuta uwanja wa dharula kwa ajili ya kutua, tunaomba muwe watulivu.”

    Taarifa hiyo ikazua taflani, watu ndani ya ndege wakaanza kupiga kelele za hofu, sauti zile ni kama vile ziliongeza nuksi, ndani ya muda huohuo ndege ile ikaanza kutoa mkoromo mbaya, na mara ikaanza kushuka kwa kasi kuelekea ardhini tayari kwa kujibamiza.



    Vilio vya watu vikalindima, sauti ya mkoromo wa injini ya ndege ikawa kubwa, mchanganyiko ule wa sauti ukafanya makelele mengi ndani ya ndege ile.

    Amosi alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa kwenye hofu kubwa ya kifo, zikiwa zimebakia futi taklibani elfu mbili kabla ya chombo kile kujibamiza ardhini, bawa moja la ndege hiyo likanyofoka!

    Tendo lile likaifanya ndege hiyo kuanguka kwa kujigeuzageuza juu chini, hakika kama ungepata bahati ya kuona tukio lile, ungeona namna ilivyokuwa ikijivingirisha katika anga huku ikishuka kwa kasi kubwa moshi mwingi ukifuka.

    Kila sekunde iliyokuwa ikisogea ndivyo, namna matukio ya kutisha kwenye ajali ile yalivyokuwa yakiendelea kutokea, kwa muda wa sekunde zisizozidi kumi, tayari kulikotea tukio jingine baya.

    Baada ya bawa moja kuchomoka, ile ndege iligawanyika vipande viwili, kipande kimoja kilitenganisha abiria waliokuwa wameketi viti vya upande wa kushoto, wakati kipande kingine kilibaki na abiria wa upande wa kulia!

    Kadhalika, kama macho yako yangekuwa na bahati ya kuona balaa hilo, yasingeacha kushuhudia watu walivyokuwa wakimwagwa kama mchele nje ya ndege hiyo.

    Waliobakia kwenye vipande vile vya ndege, ni wale waliokuwa wameketi vitini huku wakiwa wamefunga mikanda.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Amosi Mikidadi alikuwa miongoni mwa abiria ambao hawakufunga mikanda, akili yake ikiwa haijapata uimara, naye alijikuta akitupwa angani na kuanza kuanguka kuelekea ardhini.

    “Paaaa!..”kishindo kikubwa kilisika, Ndege ya Panasonic Airline ilijibamiza.

    Watu wengi walipoteza maisha, wachache walionusurika ni wale waliomwagwa wakiwa angani na kuangukia kwenye maji, wenye uwezo wa kugolewa walipiga mbizi hadi pwani.

    Amosi alitupwa msutuni na kijibamiza kwenye miti damu nyingi zikamtoka, giza kubwa likazikumba mboni zake.

    ****

    Taarifa ya kupotea kwa Ndege ya panasonic Airline, zikasambaa kama moto wa kifuu dunia nzima, habari kutoka mamlaka ya hali ya hewa ya nchi ya marekani(America Metoarogical Agency) zikatoa taarifa kwamba ndege hiyo iliyokuwa na abiria takribani mia mbili hamsini haijulikani ilipo!

    Taarifa hiyo ikamstua kila mtu, lilikuwa ni tukio lililogusa hisia za watu wengi duniani, kupitia kamera mbalimbali za setilite waliweza kuiona picha chache za ndege hiyo ikiwa angani muda mfupi bada ya kupaa, lakini hapakuwa na picha hata moja iliyoonyesha namna ukomo wa safari yake.

    Jambo hilo lilimchanganya kila mtu. Baadhi ya watu wakaanza kuhusisha Uchawi!!!



    ******



    Nchini Tanzania huko mkoani Geita, katika familia ya mzee Mikidadi, Kiba alikuwa katika mkanganyiko mkubwa juu ya taarifa ya msiba aliopata.

    Alikuwa ni mtoto mkubwa wa familia ya mzee Mikidadi kati ya watoto wanne wa mzee huyo mstafu wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ)

    Yeye akiwa mwajiriwa wa kampuni Geita Gold Miningi, hakuweza kusafiri na mama yake ambaye alikuwa mgonjwa wa muda mrefu wa Maradhi ya Kansa.

    Kutokana na kunyimwa ruhusa katika kampuni aliyokuwa akihudumu, jukumu la kwenda kumuuguza mama yao ilibidi alisimamie na mdogo wake Amosi.

    Tofauti na Kiba, Amosi mtoto ni pili wa mzee mzee yule mstaafu, alikuwa ni miongoni mwa wavulana wachache wenye umri chini ya miaka 30 waliokuwa na mafanikio Makubwa ya Kimaisha katika mkoa wa Geita.

    Hii ilitokana na biashara ya ununuzi wa madini ambayo aliyanunua kwa wachimbaji wadogo kutoka kwenye machimbo ya dhahabu ya Nyamalembo.

    Alisafiri na mama yake wakitokea hospitali ya Muhimbili ambako alipata rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi.

    Katika familia, mama yao alikuwa ndio kipenzi cha kila mtoto, hapakuwa na mtu aliyekuwa na furaha tangu mwanamke yule akumbwe na maradhi yaliyomlaza kitandani kwa kipindi kirefu.

    Wakiwa ni watu wenye mategemeo tangu asafirishwe kwa ajili ya matibabu nchini Marekani hawakujua kabisa kama mtu yule alikuwa ameaga dunia.

    Mtuu pekee aliyekuwa nchini ambaye alikuwa amekwishapata kujua kuhusu kifo cha mzazi wao ni Kiba pake yake.

    Alikesha usiku kucha akitokwa na machozi, kifo cha mama yake kilimchoma mno moyoni, alijitahidi kujikaza kiume, lakini maumivu ya kumpoteza mama yake yalimzidi nguvu, alilia na kulia usiku ule.

    Alitambua namna alivyojisikia, wadogo zake wa kike watakuwa taabani zaidi kama wakipata taarifa zile, lakini aliendelea kutambua baba yao ambaye uzee ulikuwa umekwisha bisha hodi anaweza kufa kwa presha kama akijua mke wake amekufa.

    Kamwe hakupenda kuona mzee huyo wanampoteza, hapakuwa na namna ya kuficha jambo hilo, aliamini palikuwa na namna nzuri ya kumfikishia taarifa mtu yule bila kuathiri afya yake.

    Ndiye mzazi pekee aliyekuwa amebakia duniani kwa wakati huo. Thamani yake ilikuwa kubwa kuliko hata kontena la dhahabu.

    Ambacho Kiba hakujua ni kwamba kulikuwa na tukio jingine baya lililokuwa likitokea kwenye maisha ya Amosi.

    Hakujua kabisa kama ndege aliyoipanda ndugu yake akisafirisha maiti ya mama yao, ilikuwa imepata ajali mbayakatika kisiwa cha Guem.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Asubuhi kulipokucha hakuonesha dalili yoyote kwa ndugu zake kama kumetokea jambo baya, alijitahidi wakati wote kuupamba uso wake kwa tabasamu.

    Kila mtu katika familia alitegemea Amosi angerejea na mama yao akiwa amepona Maradhi ya Kansa yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

    Taarifa ya kifo cha mama iliendelea kubaki siri ya Kiba.

    “Mbona Amosi hapatikani kwenye simu?” mzee Mikidadi alimhoji Kiba siku hiyo.

    “Kweli?”

    “Ndiyo...”

    “Inawezekana matatizo ya network”

    “Uliwasiliana naye siku za hivi karibuni”mzee yule akauliza.

    “ndio, jana niliongea naye.”

    “Mama yenu anaendeleaje?”

    “Anaendelea vizuri kabisa,” Kiba alidanganya, hakuwa tayari kabisa kueleza ukweli wa kifo cha mama yake kwa mzee yule.

    “Kama ni hivyo ni jambo la kumshukuru Mungu...lini wanarudi?” swali lile liliuchoma moyo wa Kiba, hakujua nini alitakiwa akiseme kwa mzee yule.

    “Mbona kimya..?” mzee aliuliza tena huko uso wake ukionesha udadisi.

    “Siku si nying...”

    “Nkriii...nkriiii...nkriiii,” kabla hajamalizia mara simu yake ya mkononi iliita kwa nguvu, akili yao ikahamia kwa kwenye simu.

    “Hellow.”

    “Kaka upo nyumbani?” ilikuwa ni sauti ya mdogo wake wa kike aitwaye Sarah.

    “Ndio, nipo nyumbani”

    “Fungulia Aljazeera kuna habari ya kushangaza.”

    “Habari gani?” Kiba aliuliza huku akishika rimoti na kuweka Chanel ya ile.

    “Kuna ndege inaitwa Panasonic Airline ya Marekani ilikuwa imebeba abiria zaidi ya 250 imepotea na haijulikani ilipo,” sauti ya Saraha ilisikika.

    “Mungu wangu!” Kiba alihamaki, ndege ambayo alikuwa akipewa habari zake ndiyo ambayo siku wa kuamkia siku hiyo, Amosi alimweleza ataitumia kusafiri na maiti ya mama yao.

    Akawa ameduwaa mbele ya Televisheni, huku simu ikiendelea kuwa sikioni, ufahamu wake ulikuwa kwenye taharuki kubwa kwa taarifa zilizokuwa zikipenya kichwani mwake.

    BREAKING NEWS:

    “250 people including two pilots of Panasonic Airline are suspected to be died just after flight they were tlavelling with, lose track of direction” (Watu 250 na marubani wawili wa ndege ya Panasonic Airline wanadaiwa kupoteza maisha yao kutokana na ndege hiyo kupotea) ilikuwa ni sehemu ya taarifa za awali ambazo ziliripotiwa kwa kurudiwarudiwa na televisheni ya Aljazeera.

    “Amosi kafa....amosi amekufa... amosi kafariki” Kiba alishindwa kabisa kujizuia, ujasiri wa kiume ulimponyoka, alijikuta akipiga kelele kama mwehu.

    Mzee Mikidadi ambaye muda wote alikuwa kimya, alijikuta na yeye anaingia kwenye jakamoyo kubwa, sauti ya Kiba ikamstua kila mtu.

    “Mbona siielewi” mzee yule alilalama.

    Kiba akaendelea kupayuka, alichanganyikiwa.

    “Hebu sema wewe mtoto, kuna nini? Kwa nini husemi.. eboo!” mzee Mikidadi alibweka.

    Sauti ya Kiba iliwavuta majirani ndugu na jamaa, muda mfupi tu Kiba alikuwa amezungukwa na watu wengi wa karibu wakitaka aeleze ni kitu gani kilikuwa kikimliza.

    “Nitawaeleza...” hatimaye baada ya kupata utulivu alisema.

    “Kuna jambo baya mno limetokea”

    “Lipi?” mzee mikidadi alidakia kwa kiherehere”

    “Jana usiku Amosi alinipigia simu...”

    “Eeh!”,CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Akanieleza mama amefariki dunia masaa 24 yaliyopita......” alisema kisha akaweka kituo na kuwatizama wadogo zake akiwemo baba yao mzee Mikidadi.

    Sura zao zilionesha mstuko mkubwa kwa taarifa ile, na kauli ile ikatosha kuamsha vilio vingine vikubwa kwenye mji ule.

    Watu wa karibu wakawa na kazi moja tu, kuituliza familia ile. Hofu kubwa ya kumpoteza mzee yule kwa presha kutokana na uzito wa taarifa ile uliendelea kuondoa utulivu wa Kiba, hata hivyo hapakuwa na lakufanya zaidi ya kusema ukweli wa kila kitu. Hapakuwa na siri tena.

    “Mbaya kuliko vyote...”Kiba akaendelea.

    “Amosi alisafiri na maiti ya mama kwenye ndege ya Panasonic Ariline, ambayo taarifa zilizopo ni kwamba ndege hiyo imepotea, na abiria wote wanasadikiwa kupoteza maisha,” taharuki nyingine ikazuka.

    Ghafla mzee Mikidadi presha ikampanda, ndani ya muda huohuo alianguka chini na kupoteza fahamu, presha ilikuwa imepanda na kufikia 140/110 mmHg, hatari ya kupoteza maisha yake ikiwa kubwa, watu wakazidi kuchanganyikiwa.

    *******

    Amosi aliingia ndani ya msitu wenye giza totoro, sauti ya mtu ambaye alimsafirisha kama maiti ndani ya ndege iliendelea kusikika mbele zaidi kadiri alivyokuwa akiendelea kuifuata.

    Sauti hiyo ilikuwa ikiomba msaada!!

    Japo kulikuwa na giza ndani ya msitu ule, lakini moyo wake haukuwa na hofu, aliendelea kuifuatilia ile sauti bila kuchoka wala kuhofia lolote, akiwa ametembea umbali wa kilometa moja na nusu, mara sauti ile ikanyamaza.

    Hatua kama kumi mbele yake, akahisi uwepo wa mtu aliyesimama wima. Mtu huyo alisimama akiwa kampa mgongo, hakujua kama ni mwanamke ama mwanaume kutokana na giza, alichofanya ni kumsogelea.





    Kadiri alivyokuwa akimsogelea ndivyo macho yake yalivyokuwa yakilizoea giza, akaendelea kuyakaza macho yake kwa mtu yule aliyekuwa mbele yake.

    Akiwa hatua tatu nyuma yake, hatimye alimtambua mtu aliyekuwa amesimama mbele yake, alikuwa ni marehemu mama yake Bi. Greta Shang’wera!.

    Bila kutegemea ule ujasiri ukamtoka, akasimama nyuma ya mtu yule, alihisi pate mepesi yakimjaa kinywani na mwili ukamsisimka, ubaridi wa ajabu ukamtambaa mauongoni mwake.

    “Mama,” akaita kwa sauti ya chini huku macho yake yakiendelea kuwa makini na mtu huyo.

    Kimya. Hakuna alichojibiwa.

    Mtu aliyekuwa mbele yake alibaki ameganda, hapakuwa na kiuongo chochote kilichotikisika.

    “Mama!!” akaita tena.

    Kimya kingine.

    Alichofanya ni kusogea mbele ya mtu yule aliyeamini ni mama yake mzazi na kumtizama usoni.

    Lahaulaaaa!!!!!!.....Hakuamini kwa kile alichokiona.

    Sanamu la kuchonga lililokuwa na mwonekano kama wa mama yake lilikuwa wima limekakamaa huku likionekana kuwa na miaka mingi tangu litengenezwe na kutelekezwa mule mstuni!!.

    Amosi alipiga hatua moja kubwa na kurudi nyuma, uso wake ukionekana kuwa na hofu na taharuki kubwa, kamwe hakutegemea kukutana na kioja kile.

    Mwonekano wa Kinyago kile kilichochongwa na fundi mwenye kipaji cha hali ya juu kilikuwa hakina tofauti kabisa na haiba ya mama yake mzazi.

    “Nini hiki!!...wewe nani..” akasema kwa sauti ya wasiwasi huku akirudi nyuma.

    Ule utashi wa kutoamini mambo ya nguvu za giza kwenye maisha yake ukamwishia, kwa mara ya kwanza nafsi yake ikakiri kwamba kulikuwa na mambo ya kichawi yaliyokuwa yanatokea wasaa ule.

    Akiwa hatua chache mbele ya kile kinyago katikati ya msitu mkubwa na giza nene. Mara sauti za vicheko zikasika zikitoka kila kona, ilikuwa ni kama vile kulikuwa kuna watu waliokuwa wamemzunguka wakimtizama namna anavyohaha kutokana na kioja alichokiona.

    “Hahahaha....hahahah...uwiii..hahaha,” sauti za vicheko zilisikika, Amosi akazidi kuhaha huku na kule, akawa anatupa macho kila mahali ambako vicheko vilisikika akitegemea kuona watu alioamini walikuwa wakimcheka yeye.

    Lakini hakuona chochote zaidi ya miti na vichaka vya hapa na pale vilivyokuwa tupu...bila kutegemea Amosi akatokwa na mkojo.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tendo lile likazidisha vicheko kwa watu wasionekana wala kujulikana. Sauti zao zilikuwa za watu ama viumbe vya rika na jinsia tofuati.

    “Ninyi ni akina nani?” Amosi akakoroma kwa kwa sauti iliyoonekana kupaniki huku ikiwa na wasiwasi na mashaka makubwa.

    Alipombwatuka kwa sauti ile ya ukali lakini yenye viashiria vya hofu na mashaka, mara vile vicheko vikanyamaza kwa pamoja.

    Ukimya ule wa awali ukajirudia, kukawa ni kama vile palikuwa hakuna kilichokuwa kimetokea.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog