IMEANDIKWA NA : FRANK SILAA
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Shule ya sekondari ya wavulana Ilboru inapatikana jijini Arusha. Shule hii ina historia ya kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani mbalimbali ya kitaifa kwa miaka mingi. Historia hiyo imejengeka kutokana na kwamba, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na shule hii ni wale wanaoaminika kuwa na vipaji maalumu. Kwa maana hiyo ili uweze kujiunga na shule hii ni lazima uwe na ufaulu mzuri sana. Kwa hakika shule hii inamchango mkubwa kitaifa, kwani imefanikiwa kuzalisha wataalamu wa mambo mbalimbali na pia wanasiasa mashuhuri. Nelson alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo mwenye heshima kubwa kutokana na uwezo wake darasani. Nelson ameishi katika maisha ya shida sana. baba yake alimtelekeza mama yake tangu alipokuwa na miezi mitatu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Mara baada ya kuhitimu elimu ya msingi katika shule ya Mgulani iliyopo Keko jiji Dar es salaam, alipata ufaulu wa juu sana wa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Azania. Ugumu wa maisha unasababisha mama yake ashindwe kumwendeleza kimasomo. Na ndipo mjomba yake anayehishi Mianzini jiji Arusha analazimika kumchukua na kumuhamishia katika shule ya sekondari Ilboru. Uwezo mzuri darasani unasababisha kijana huyu anapewa jina la utani na wanafunzi wenzake kwa kumuita ‘profesa’. Ufaulu mzuri wa mitihani ya ndani na nje ya shule inasababisha kijana huyu kupata marafiki wengi. Ingawa wanafunzi wengi wa kike wa shule za jirani wanajipendekeza kwake ili waweze kumnasa lakini jitihada zao zinagonga mwamba. Nelson alisoma kwa bidii sana ili siku moja aweze kurudisha furaha ya mama yake iliyokuwa imepotea kwa kitambo kirefu. Alimpenda sana mama yake kwasababu alimlea katika mazingira magumu mno.
Mapenzi ya dhati yaliyokuwa yamejengeka moyoni mwake dhidi ya mama yake ndio yaliyokuwa yakimsukuma kusoma kwa bidii. Nelson alifanikiwa kufika kidato cha nne akiwa bado hajawai kujiingiza katika mahusiano yeyote ya kimapenzi, ingawa mabinti wengi walionekana kuvutiwa sana na yeye. Ilikuwa ni jioni ya saa 11.11 siku moja Nelson akiwa ametokea mitaa ya Kaloleni kufanya majadiliano ya kimasomo na wanafunzi wa shule mbalimbali, alikutana na binti mmoja ambae alikuwa amevaa sare za shule. Binti huyo alikuwa anakuja katika uelekeo ambao Nelson alikuwepo. Nelson alishangaa baada ya kuhisi mapigo yake ya moyo yanaongezeka kwa kadiri alivyokuwa anazidi kumtizama binti yule ambae alikuwa amevaa sare ya wanafunzi wa shule ya Ekenywa iliyopo jirani na shule aliyokuwa anasoma.
Uzuri aliojaliwa mwanamke aliyekuwa anamuona akija mbele yake hakuwai kuuona kwa mwanamke wa aina yeyote tangu kuzaliwa kwake. Rangi ya ngozi yake ilikuwa mithili ya chokoleti, hakuwa mnene wala mwembamba halikadhalika hakuwa mrefu wala mfupi. Ingawa alikuwa ndani ya sare za shule lakini uzuri wake bado ulidhihirika. Hakika alikuwa ni mzuri kama malaika. Kwa jinsi hatua zake zilivyokuwa zinazidi kumkaribia Nelson ndivyo ambavyo uzuri wake ulizidi kuteka hisia na kijana. Macho ya binti yalikuwa ni meupe ya kuvutia ingawa yalijawa na soni sana. Mwendo wake ulikuwa ni wa madoido mithili ya twiga. Nelson aliona liwalo na liwe lakini sio kuacha kuzungumza na msicha yule ambae alikuwa na uzuri ambao ulimfanya ahisi kuchanganyikiwa.
“Mambo vipi.” Nelson alijitosa kumsalimia binti yule ingawa hakutegemea kuitikiwa salamu yake na msichana yule ambae kwa hakika alikuwa na sifa za malaika.
“Poa! Mambo.” Huku wakipishana, binti aliitikia salamu bila maringo, jambo ambalo lilimuongezea Nelson kujiamini zaidi.
“Safi tu, samahani.” Nelson alizungumza huku mapigo yake ya moyo yakizidi kumwenda mbio sana kwasababu hakuamini kwamba ni yeye ndie aliekuwa akizungumza na yule msichana.
“Bila samahani.” Sauti nyororo na yakuvutia ilitoka kinywani mwa binti na kuzidi kumpagawisha Nelson.
“Naitwa Nelson. Sijui wewe mwenzangu unaitwa nani.”
“Nafurahi kukufahamu Nelson. Mimi naitwa Vivian.”
“Unasoma kidato cha ngapi?” Nelson aliuliza.
“Ooh! Nasoma kidato cha pili.
“Hongera sana. Ingawa nimekutangulia madarasa mawili mbele.”
Nelson alizidi kutengeneza mazingira ya urafiki kwa Vivian kwasababu alitokea kuvutiwa sana na mwonekano wake. Muda ulikuwa umesonga sana kwahiyo walizungumza kwa muda mfupi, kwasababu binti alikuwa anaishi mbali. Akili ya Nelson haikuwa ya darasani pekee kwani akili hiyohiyo ndio iliyomwezesha kufanikiwa kuingia katika urafiki na binti mrembo Vivian. Wote hawakuwa na simu za mkononi kwasababu walikuwa ni wanafunzi kwahiyo iliwawia vigumu kuwasiliana mara kwa mara. Kutokana na changamoto ya mawasiliano wakati mwingine Nelson alidiriki kumsubiri njiani ili aweze kumuona. Kiukweli hisia za Nelson zilikuwa ni mateka kwa Vivia.
Nelson aliteseka sana kwasababu hakuwahi kupenda kabla kwahiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza. Alitamani muda wote Vivian awepo mbele ya macho yake lakini haikuwezekana. Muda wa kufanya mitihani ya kidato cha nne ulifika. Nelson alifanya mitihani yake salama na kuendelea kuishi kwa mjomba wake ambae alikuwa akimpenda sana. Alifunga safari ya siku chache ya kwenda Dar es salaam kumsalimia mama yake na hatimae alirudi jijini arusha kuendelea kusubiri matokeo. Uwepo wake kwa mjomba wake ulimfanya apate urahisi wa kuendelea kukutana na Vivian mara kwa mara. Matokeo ya kujiunga na kidato cha tano yalitoka. Nelson alifanikiwa kupata ufaulu wa daraja la kwanza (division one) ambapo alipangiwa katika shule ya ‘Tabora boys.’ CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Hakufurahi kabisa kupangiwa shule hiyo kwasababu ilimfanya awe mbali na mwanamke aliekuwa anampenda. Pamoja na kwamba moyo wake ulitokea kumuhusudu sana binti yule lakini bado hakuwa amemweleza juu ya hisia zake kwasababu aliona muda muwafaka bado haukuwa umefika. Wakati mwingine alijilaumu ni kwanini hakumweleza mapema ili akae akijua lakini aliishia kujifariji kwa msemo usemao ‘kama ipo ipo tu’ akimaanisha kwamba kama Mungu amepanga siku moja Vivian awe mke wake basi atakuwa tu kwa namna yeyote. Nelson alipofika Tabora waliendelea kuwasiliana kwa njia ya barua walizokuwa wakitumiana kwa njia ya posta lakini kwa kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga ndivyo ambavyo mawasiliano yalianza kupungua na mwishowe yalikwisha kabisa. Ubize wa mambo ya shule ndio uliopelekea mawasiliano yao yakatoweka. Nelson aliendea na shule ingawa mawazo juu mwanamke alieziteka hisia zake vilivyo, zilikataa kabisa kufutika katika kichwa chache. Hakuwa na namna isipokuwa kusoma kwa bidii sana ili kuweza kutimiza malengo aliyokuwa amejiwekea. Uwezo wake darasani ulizidi kutukuka hata alipokuwa Tabora. Wanafunzi wenzake walimpenda sana kwasababu licha ya kufanya vema darasani lakini alikuwa na vituko vya kuchekesha sana. Kama ambavyo alipewa jina la utani alipokuwa Ilboru ndivyo ambavyo pia alipewa jina jingine la utani alipofika Tabora ambalo ni ‘Socret’ jina ambalo ni la mwanafalsafa maharufu sana duniani. Miaka miwili ya kidato cha tano na sita ilikwisha. Nelson na wanafunzi wote wa kidato cha sita nchi nzima walianza mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari.
Baada ya kumaliza kidato cha sita alirudi jijini Arusha kwa mjomba wake lakini hakufanikiwa kukutana tena na Vivian. Hisia kali juu ya msichana yule zilimsababishia mateso makubwa ya nafsi, kwasababu kila sekunde, kila dakika alikuwa akimuwaza na hata wakati mwingine alikuwa akimuota ndotoni. Matokeo ya kidato cha sita yalipotoka jina la Nelson lilitikisa magazeti mbalimbali nchini. Alipata ufaulu wa juu sana kwani alifanikiwa kuwa mwanafunzi wa kwanza kitaifa. Kwa watu waliokuwa wanamfahamu wala hawakushangaa kwasababu walikuwa wanafahamu uwezo wake ulikuwa ni wa juu sana.
Alizua gumzo nchi nzima kwasababu imezoeleka kuwa wanafunzi wanaoshika nafasi za juu kitaifa ni wale wanaosoma katika shule za watu binafsi kutokana na ufundishaji wao kuzidi shule za serikali. Vyombo mbalimbali vya habari vilimuhoji ili kuweza kufahamu sababu iliyomfanya kuibuka kidedea katika mitihani yake. Hakuna cha ziada alichokizungumza isipokuwa alisema kuwa ufaulu wake ulisababishwa na juhudi kubwa katika masomo yake pamoja na kumtanguliza Mungu kwa kila kitu alichokuwa akikifanya. Furaha aliyoipata mama yake baada ya kusikia kuwa mwanae kawa wa kwanza kitaifa ilikuwa ni sawa kabisa na furaha aliyoipata mjomba yake ambae ndie aliekuwa akimsomesha.
Nelson alipata ufadhili wa kwenda kusoma nje ya nchi katika chuo kikuu kinachojulikana kwa jina la ‘University of Central Florida’ kilichopo nchini Marekani. Alifurahi sana kupata nafasi ile kwasababu hakuwahi kuwaza kama ipo siku atasoma nje ya nchi tena katika chuo kikuu maarufu sana duniani. Matumaini ya kumpata Vivian yalipotea kabisa akilini mwake. Alijua sio rahisi mwanamke yule alieumbika kama malaika aweze kuishi peke yake bila kuingia katika mahusiano ya kimapenzi. Ingawa roho ilimuuma sana lakini hakuwa na la kufanya kwasababu elimu nayo ilikuwa ni ya muhimu sana, kwahiyo hakuwa na sababu ya kutengua maamuzi yake ya kusoma nje ya nchi. Aliamini hakuna mwanamke mwingine mzuri huku duniani kama alivyokuwa Vivian. Alitamani awe na kipaji cha kuimba ili aweze kumtungia wimbo kwa imani ipo siku utamfikia lakini ilishindikana.
****************
Vivian ni kitinda mimba katika familia ya watoto 11. Kwa bahati mbaya wenzake wote walishafariki dunia nyakati tofauti tofauti katika mazingira ya kutatanisha. Katika familia yao alibaki yeye na mama yake kwani baba yake pia alisha fariki. Mama yake alikuwa anampenda sana binti yake. Alikuwa ni kama mboni ya jicho kwake. Kama simba alivyo mkali kwa kitu chochote kinachocheza na mwanae ndivyo na mama Vivian alivyokuwa mkali kumlinda bintie. Mama huyu ni mchawi mkubwa. Anaogopwa na kila mtu katika mtaa anaoishi. Pamoja na kwamba ana binti mzuri sana lakini hakuna hata kijana mmoja mtaani aliejitosa kumtaka kimapenzi Vivian. Kwani kufanya hivyo ni sawa na kujichimbia kaburi lako mwenyewe. Mama huyu ndie alieua watoto wake kumi pamoja na mume wake. Ndugu jamaa na marafiki walipoteza maisha baada ya kuuwawa na mama huyu ambae sura yake na matendo yake ilikuwa ni vitu viwili tofauti. Alikuwa mwanakamati mkuu wa sherehe kuzimu kwahiyo kila mara alikuwa akishiriki katika mauwaji mbalimbali halafu damu na nyama za marehemu zinasherehekewa kuzimu. Kwa hakika mama huyu alikuwa ni hatari sana. Jamii nzima iliwatenga, kwasababu walikua wanafahamu fika mama yule sio mtu wa kawaida. Wakati mwingine watu walihisi kuwa alikuwa ameshamuingiza binti yake katika masuala ya kichawi ndio maana hata wanaume wengi walikuwa wanamkwepa Vivian.
Mtazamo huo ulijengeka katika akili za watu wengi kutokana na hofu waliyokuwa nayo dhidi ya mama yule lakini haikuwa kweli kwamba Vivian pia alikuwa mchawi. Vivian alikuwa anasikia lawama kwa majirani na kwa bahadhi ya ndugu kuwa mama yake ni mchawi lakini hakuwahi kumwona akifanya jambo lolote ambalo lilimthibitishia kweli mama yake ni mchawi. Hakufahamu pia kuwa mama yake ndie aliekuwa sababu ya vifo vya ndugu zake pamoja na baba yake. Shutuma za kwamba mama yake alikuwa ni mchawi zilikuwa zikimuumiza sana lakini hakuwa na la kufanya.
Mtaani hakuwa na rafiki hata mmoja. Marafiki zake wengi walikuwa shuleni kwasababu walikuwa hawafahamu kuwa anatokea katika mazingira gani. Kitendo cha kuwa na marafiki wengi shuleni kilisababisha apende sana shule. Alikuwa na mahudhurio mazuri sana shule kwasababu alipenda jinsi alivyokuwa anabadilishana mawazo na marafiki zake. Muda mwingine alijilazimisha kwenda shule hata pale alipokuwa mgonjwa sana, jambo ambalo lilikuwa likiwashangaza marafiki zake kwanini huwa hapendi kupumzika nyumbani wakati anapokuwa mgonjwa. Hayo yote yalisababishwa na upweke ambao alikuwa anaukwepa pindi anapokuwa nyumbani kwao.
Kama ilivyokuwa kwa wasichana wengine kumpenda sana Nelson ndivyo ilivyomtekea pia Vivian. Kiukweli hisia zake zilitekwa haswa na mwonekano wa Nelson. Alisubiri kwa hamu Nelson amtamkie kuwa anampenda ili na yeye aweze kuzionyesha hisia zake kwake lakini hilo lilishindwa kufanyika kwa muda muwafaka. Wakati mwingine alitamani laiti angekuwa mwanaume angeshamtamkia Nelson kuwa anampenda. Ingawa baadhi ya walimu pamoja na wanafunzi wenzake walimtongoza lakini hakushawishika kabisa kwasababu hisia zake zilikuwa kwa mtu mwingine. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Muda mwingi aliupoteza akimuwaza Nelson. Alimwomba Mungu siku moja aweze kumkutanisha kwa mara nyingine na mwanaume yule ambae alihisi kuwa hawezi kuishi bila yeye. Alifanikiwa kumaliza kidato cha nne salama lakini kwa bahati mbaya hakubahatika kuendelea na kidato cha tano jambo ambalo lilizidi kumkatisha tamaa ya kuonana na Nelson. Aliumia sana, kibaya zaidi ni kwamba Nelson hakubahatika kufahamu nyumbani kwao. Japokuwa kunakipindi alimsindikiza karibia na nyumbani kwao lakini alimzuia kufika moja kwa moja mtaani kwao akihofia asisikie maneno ya vitisho kutoka kwa watu waliokuwa wanamfahamu. Maisha ya Vivian yalijawa na upweke wa hali ya juu.
Hakuwa na rafiki hata mmoja wa kuweza kubadilishana nae mawazo pale mtaani kwao. Hakuna hata mwanaume mmoja aliejitokeza na kumtamkia neno ‘nakupenda’ pamoja na uzuri wote aliokuwa amejaliwa na Mwenyezi Mungu. Ulikuwa ni wakati mgumu sana kwake kwasababu alichoshwa na maisha ya kunyanyapaliwa. Marafiki aliohitimu nao kidato cha nne walipotezana kabisa kwasababu hawakuwa na mawasiliano ya aina yeyote. Nyumba yao ilikuwa ni kama kisiwa kilichozungukwa na maji kwasababu tangu Vivian alipokuwa mdogo hakuna hata siku mmoja alisikia mtu akibisha hodi nyumbani kwao isipokuwa ilitokea kwa mara chache sana kwa baadhi ya watu waliokuwa wakipotea njia. Alijitahidi kumsahau Nelson lakini alishindwa kabisa. Taharifa za ufaulu wa Nelson alizipata kwa kupitia vyombo vya habari. Alifurahi sana ingawa alisikitika baada ya kusikia kuwa amepata ufadhili wa kwenda kusoma Marekani. Alizidi kumuwaza na kumkumbuka kila mara japokuwa alihisi kukutana naye kwa mara nyingine ni kama ndoto.
************
Nelson baada ya kufika marekani alianza masomo yake ambayo yalikuwa yanahusiana na uhandisi wa majengo. Licha ya kwamba alikuwa mbali na mazingira ya nyumbani lakini hakuona tofauti yeyote kwasababu alibahatika kupata marafiki kadha wa kadha ambao walimfanya ajihisi kama vile yupo Tanzania. Uwezo wake darasani uliendelea kuwa gumzo hata alipokuwa chuo kikuu. Wahadhiri mbalimbali chuoni walimpenda kutokana na juhudi zake katika masomo. Alitokea kuupenda mchezo wa kikapu, ambapo alijifunza na hatimae alifanikiwa kuwa mchezaji mzuri jambo ambalo lilifanya jina lake lizidi kukuwa zaidi na zaidi katika chuo alichokuwa anasoma.
Kwajinsi alivyokuwa anafahamu jinsi ya kuchangamana na watu wengine ilisababisha watu wamuone kama mmarekani mweusi lakini kumbe sivyo. Alipomaliza mwaka wa kwanza wa masomo, mawazo juu ya Vivian yalipungua kidogo. Ingawa bado alizidi kumuomba Mungu aweze kumkutanisha na mwanamke yule kwa mara nyingine tena wakati atakaporudi Tanzania. Mjomba wake alizidi kumtia moyo katika masomo yake pindi walipokuwa wakiwasiliana. Kitendo hicho kilimfanya apate moyo wa kuongeza mapambano ya kusoma kwa bidii ili aweze kumridhisha mjomba wake, pamoja na mama yake kipenzi.
Mwaka wa nne ambao ndio ulikuwa mwaka wa mwisho wa masomo yake ulitimia, ambapo alifanya mitihani yake salama na matokeo yalipotoka alifanikiwa kupata ufaulu wa juu kabisa, yaani daraja la kwanza (GPA of 4.9) Ufaulu huo wa kishindo aliupata yeye na mwanafunzi mwenzie wa nchini India. Taharifa za ufaulu wa Nelson unafika kwa balozi wa Tanzania nchini humu bwana Johnson Rogart Marwa na kuamua kumfanyia tafrija fupi nchini humo kwaajili ya kumpongeza kwasababu aliweza kuvunja rekodi ambayo haikuwai kuvunjwa na mwanafunzi yeyote kutoka Tanzania katika kipindi cha uongozi wake. Taifa la Marekani linamshawishi Nelson abaki marekani ili waweze kufanya nae kazi lakini anakataa.
Baada ya hapo Nelson anarejea nyumbani akiwa na furaha sana. Aliona kukubali kufanya kazi nje ya nchi ndio sababu ya yeye kupotezana moja kwa moja na Vivian. Nelsona hakutaka kuamini kuwa hatamuona tena mwanamke ambae alihisi kuwa ndiye mwanamke wa ndoto zake. Anaweka nadhiri ya kuhakikisha anamsaka kila kona hadi ampate. Saa 2. 45 usiku Nelson alitua katika uwanja wa ndege wa mwalimu Julius nyerere kwa ndege aina ya Boeing 767-300ER-Condor. Kwasababu alikuwa na shauku ya kutaka kukutana na mama yake alichukua tax ambayo ilimpeleka moja kwa moja hadi keko machungwa alipokuwa anaishi mama yake.
“Ngo! Ngo! Ngo!” saa 3.17 usiku mlango wa mama Nelson ulisikika ukigongwa. Mara baada ya kugonga kwa mara kadhaa sauti ya mama yake ilisikika ndani.
“Nani?” mama aliuliza aliekuwa akigonga ni nani kwasababu hakuwa na taharifa za ujio wa mwanae.
“Mwanao, Nelson.” Nelson alijibu.
Baada ya mama kufungua mlango sura yake ilikutana ana kwa ana na mwanae jambo ambalo lilisababisha hisia za furaha kumpanda kwa kasi hadi machozi yakawa yanamdondoka mfululizo.
“Kwashaa’mbe!” (Pole kwa safari mwanangu.) mama alizungumza kilugha huku akiwa amemkumbatia mwanae kwa furaha kubwa sana.
“Ekaa’ma.” (Asante mama.) Nelson nae alimjibu mama yake kwa kilugha huku akidondokwa na machozi kwa furaha kwasababu ilikuwa imepita kitambo kirefu bila hawajaonana.
Mama alisaidiana na mwanae kuingiza mabegi ndani. Nelson alimpigia simu mjomba wake na kumweleza kwamba tayari amefika salama Tanzania kwahiyo siku inayofuata ndio atakwenda Arusha. Nelson alisikitika sana kuona mama yake bado anaishi maisha ya shida. Chumba alichokuwa anaishi kilikuwa hakina umeme wala feni. Chemba za choo zilikuwa zinatoa harufu kali sana ambayo ilikuwa ni kero hadi ndani ya nyumba. Jirani na nyumbani kulikuwa na baa iliyokuwa ikipiga mziki kwa sauti ya juu sana kiasi kwamba ilibidi awe anazungumza na sauti kubwa ili aweze kuelewana na mama yake.
Wingi wa vitu vilivyokuwa vimejazana ndani ya chumba kimoja alichokuwa anaishi mama yake ilisababisha msongamano mkubwa ambavyo ulidhihirisha kwamba suala la usafi lilikuwa ni sifuri. Chumba kilikuwa kimegawanywa kwa pazia. Maisha aliyokuwa anaishi mama yake hayakuwa na tofauti yeyote na maisha ya miaka kumi iliyopita wakati walipokuwa wakiishi pamoja. Nelson aliwaza kwamba suala la kwanza endapo atapata pesa ni kuhakikisha kwamba mama yake anapata mahali pazuri pa kuishi. Pamoja na hayo yote alifurahi sana kumuona mama yake akiwa ni mzima wa afya tele. Walipiga stori nyingi sana na mama yake. Alijisikia faraja sana kuzungumza na mama yake ambae alikuwa anampenda kuliko kitu chochote hapa duniani. Alijaribu kumuuliza mama yake habari za baba yake lakini alijuta kuuliza kwasababu aliyoelezwa yalimchoma mtima wake.
“Nilipata habari kwamba, kwa sasa anaishi Tabata kimanga, ameoa mwanamke mmoja wa kindengereko pia wana watoto watatu na maisha yao yanakwenda vizuri bila shida.” Mama alizungumza kwa masikitiko makubwa sana, nusura machozi yanidondoke.
“Hivi mama kwanini baba alitutelekeza?” Nelson alijikuta anamuuliza mama yake swali hilo ambalo lilikuwa limemkereketa kwa muda mrefu sana.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Kiukweli hata mimi mwenyewe sielewi. Kwasababu aliniacha katika mazingira magumu mno kwani ndiyo nikiwa mzazi kwako. Kuondoka kwake kulikuwa kama utani utani tu kwasababu alikuwa ni mlevi kupindukia. Wakati mwingine alikuwa haonekani nyumbani kwa wiki nzima, kwahiyo hata alipoondoka nilijua yupo kwa wanawake zake lakini kwa kadiri siku zilivyozidi kwenda ndipo niligundua kuwa nilikuwa nimetekezwa.” Mama alizungumza hadi akaanza kulia kwa uchungu sana. Nelson alimbembeleza mama yake kwa muda kidogo na hatimae hasira ya mama ilishuka. Saa ya mkononi ilionyesha ni saa 6.39 usiku. Mama alikwenda kulala katika kitanda chake. Nelson alijiegesha katika kochi lililokuwepo mle ndani hadi palipokucha asubuhi ambapo alimuaga mama yake na kuondoka kuelekea Arusha kwa mjomba wake kumsalimia ikiwa ni pamoja na kumsaka Vivian.
Saa 12.06 asubuhi, Nelson alifika ofisi ya ‘Kilimanjaro express’ iliyopo shekilango jijini Dar es salaam. Alikata tiketi na kuondoka na basi la saa 12.30 kuelekea mkoa wa Arusha. Alipendelea kusafiri kwa basi kwasababu alikuwa amemisi mazingira ya Tanzania kwa muda mrefu. Kichwa kilimuuma kwasababu aliwaza kwa muda mrefu namna ya kwenda kuanza msako wa kumtafuta Vivian. Akili mwake alitambua kuwa itakuwa ni zoezi gumu lakini, alijidhatiti kuhakikisha kwamba anafanikiwa. Jioni ya saa 11.55 aliteremka kwenye basi katika kituo cha Mianzini ambapo alimkuta mjomba wake anamsubiri kumlaki.
Mjomba wake alifurahi sana baada ya kumuona mtoto wa dada yake akiwa amerejea mzima wa afya tele, tena na ushindi mkubwa katika masomo yake. Nelson aliongozana na mjomba wake hadi nyumbani. Mara baada ya kuoga kuondoa uchovu wa safari, Nelsoni alikwenda mezani kupata chakula cha jioni pamoja na familia ya mjomba wake. Alifurahi sana kwasababu mke wa mjomba wake alikuwa ameandaa kitoweo cha jogoo, kama heshima kwa ujio wake. Walikula chakula huku wakizungumza na kucheka sana kutokana na stori za Nelson kipindi alipokuwa Marekani. Maongezi yao motomoto yalikwenda hadi usiku wa saa sita na baada ya hapo kila mtu alikwenda kulala. Ingawa Nelson alikuwa amechoka kwa safari lakini hakuweza kupata usingizi kwa sababu ya mawazo kibao yaliyokuwa kichwani mwake dhidi ya binti mrembo Vivian.
“Hivi itakuwaje endapo nitakuta Vivian kaolewa na mtu mwingine?” Nelson aliwaza sana pindi alipokuwa kitandani kwake usiku akijigeuza huku na kule bila kupata usingizi. Mkononi alikuwa ameshika picha ambayo aliwahi kupewa na Vivian kipindi cha nyuma. Alipata wazo kwamba picha ile itamsaidia kumtafuta Viviani maeneo ya Sakina ambapo binti aliwahi kumweleza ndipo anapoishi. Ule usiku ulikuwa ni mrefu sana kwake kwasababu alitamani pakuche haraka kusudi aweze kutokomea mitaani kumsaka njiwa wake. Alizidi kumuomba Mungu binti aliekuwa anamuwaza kila siku maishani mwake awe mzima wa afya na pia awe hajaolewa. Palipokucha asubuhi alipata kifungua kinywa na kuondoka kuelekea maeneo ya Sakina kumtafuta mwanamke wa ndoto zake.
*************
Kwa muda wote ambao Vivian alipotezana na Nelson aliishi bila amani kabisa ndani ya moyo wake. Alitamani laiti kama angekuwa na mabawa angetua mbele ya Nelson ili aweze kumuona nafsi yake isuuzike. Alichoshwa na upweke wa kukaa kivyakevyake pale mtaani kwao. Ilipotimu mwaka wa tano akiwa nyumbani bila kujishughulisha na kitu chochote aliamua kurudi darasani kusoma. Alikwenda katika chuo cha ‘Tropical Institute’ kilichopo jirani na hospitali ya AICC kusomea ‘Hotel management.’ Kama kawaida uzuri wake uliwachanganya wanaume wengi sana chuoni hadi walimu walionekana kuvutiwa sana na uzuri aliojaliwa.
Wanaume wengi walimfuata kumshawishi, lakini aliwakatilia kwa kuwajibu kuwa anampenzi ambae anampenda sana. Watoto wa vigogo nao hawakuwa nyuma kwani walionyesha mbwembwe za pesa za nyumbani kwao ili waweze kumnasa lakini pia hawakufanikiwa. Baada ya vijana wote pale chuoni kushindwa kumshawishi kimapenzi walianza kumsema vibaya kwamba eti anaringa lakini haikuwa kweli. Japokuwa hakuwa na uwakika kuwa Nelson atamrudia tena lakini alijipa moyo kwasababu alishahisi kuwa Nelson alikuwa anampenda sana. Kijana mmoja ambae ni mwanasheria wa kujitegemea siku moja alikutana na Vivian na kutokea kumpenda sana. Alimshawishi Vivian ili aweze kuwa mpenzi wake lakini Vivian alikataa katakata. Kijana yule hakukata tamaa aliendelea kumsumbua kila mara ili aweze kukubaliwa ombi lake. Vivian alikereka sana kwa usumbufu wa yule kaka kwasababu alikuwa akimfuata kila siku lakini aliendelea kubaki na msimamo wake, tena wakati mwingine alidiriki kumtukana kwasababu alikuwa ni msumbufu sana. Pamoja na hayo yote lakini bado kija yule hakukata tamaa. Vivian alijiuliza yule kaka ni mtu wa namna gani kwasababu alikuwa anamnyima amani kabisa. Kutokana na kero hizo aliamua kumkubalia kishingo upande lakini kwa bahati mbaya mahusiano yao hayakudumu kwani kijana huyo alipoteza maisha siku iliyofuata akiwa ofisini kwake katika mazingira ya kutatanisha jambo ambalo lilimshitua sana Vivian.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Mpaka kufikia muda ule Vivian alikuwa bado ni bikira kwasababu hakuwahi kukutana kimwili na mwanaume yeyote. Stori za wanaume alizisikia alipokuwa kwenye maongezi na marafiki zake. Hata alipowaeleza kuwa bado hajatolewa usichana wake marafiki zake wengine walionyesha kumcheka kwa na kumuona mshamba, na wengine walimuona ni mwongo wakiamini kwamba inawezekana vipi na uzuri wote aliojaliwa na Mungu awe hajawahi kupita katika mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote. Mara nyingi alipokuwa akiwaeleza hivyo marafiki zake huzua mjadala mzito wakimpinga lakini ukweli ndio huo. Sio kwamba hakuwa na hisia za kimapenzi la hasha! alikuwa akijihisi kama wasichana wengine lakini alitamani usichana wake utolewe na mwanaume mmoja tu ambae ni Nelson.
*************
Kumbukumbu za Nelson zilikuwa vizuri kwani aliweza kufuata ile njia aliyopita siku moja alipokuwa akimsindikiza Vivian. Alifika mahali na kuona kwamba, akimuulizia maeneo yale itakuwa ni rahisi kufahamika kwasababu alikuwa akipita mara kwa mara kipindi alipokuwa shule. Nelson alianza kuulizia kwa watu mbalimbali huku akiwaonyesha picha ya mtu aliyekuwa akimtafuta lakini kwa watu wote aliowahoji walionyesha kutomfahamu binti yule. Hakukata tamaa aliendelea kuuliza huku na kule na hatimae alikutana na kijana mmoja ambae alionekana kumfahamu Vivian.
“Ahaa! Huyu binti nampata ila kwao sipafahamu, lakini cha kukusaidia itakapofika mida ya saa 10 jioni, njoo maeneo haya utamuona kwasababu huwa anapita kila siku hapa asubuhi na jioni.” Nelson alipata maelekezo hayo kutoka kwa kaka mmoja ambae alijitambulisha kwake kwa jina la Mejooli. Taharifa hizo zilimfurahisha sana Nelson, alifurahi kupita kiasi kana kwamba ndio alikuwa amekutana na Vivia kumbe sivyo. Saa yake ya mkononi ilimwonyesha ni saa 4.01 asubuhi. Muda uliobaki kufika saa kumi, Nelson aliona ni kama dakika tano, kwahiyo aliamua kukaa pale pale hadi muda alioambiwa ufike.
Alikwenda katika supermarket iliyokuwa jirani na pale na kuangalia zawadi ambayo alihisi zitamfaa mwanamke wa ndoto zake. Alinunua pafyumu aina ya ‘Dolly Girl Lil’ Starlet’ pamoja na zawadi nyingine kadha wa kadha. Baada ya manunuzi alikwenda kukaa katika duka moja iliyokuwa kandokando ya barabara ili kujikinga na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha siku hiyo. Macho yake yalikuwa makini kutazama barabani kila mara ili Vivian asipite bila kumtia machoni ingawa muda aliokuwa ameelezwa ulikuwa bado haujafika. Masaa yaliendelea kuyoyoma huku akiendelea kusubiri. Kwa jinsi Nelson alivyokuwa na shauku ya kumuona Vivian angekuwa na uwezo wa kusogeza muda mbele basi angefanya hivyo ili aweze kukutana na binti ambae alimpa thamani ya kipekee moyoni mwake. Ilipotimu saa kumi kamili macho yake yaliongeza kasi ya kutazama barabari kwasababu ndio muda alielezwa kwamba Vivian atapita. Saa 11.00 jioni ilifika akiwa bado hajakata tamaa aliendelea kusubiri huku macho yake yakigongana na sura za watu wengi waliokuwa wakirejea majumbani mwao wakitokea makazini. Saa 12.30 ilifika Nelson akiwa bado barabarani anasubiri. Alikata tamaa kwasababu giza lilianza kufukuza nuru. Aliondoka na kurudi nyumbani akiwa amefadhaika sana kwasababu lengo lake halikuwa limetimia.
***********
Ilipofika saa 9.20 alasiri muda wa vipindi chuoni ulikwisha kwahiyo Vivia aliongozana na marafiki zake wawili ambao ni Joyce na Miriam hadi soko kuu. Kwasababu Vivian alipata kampani ya kuelekea huko waliamua kutembea kwa miguu kutokea chuoni hadi sokoni jambo ambalo liliwafanya wachelewe sana. Walianza kutembea wakiwa watatu wakifuata barabara ya ‘Nelson Mandela’ hadi wakafika mnara wa saa (clock tower). Walikamata barabara ya Sokoine na kunyoosha nayo moja kwa moja hadi kituo cha sokoni ambapo walikunja kulia na kuingia soko kuu la Arusha.
Kutokana na mwendo wao wa taratibu na stori nyingi walitumia zaidi ya lisaa limoja hadi kufika sokoni. Walifanya manunuzi kwa pamoja hadi kila mmoja akamaliza. Saa kumi na mbili jioni ndio walikwenda kupanda gari ingawa kila moja alikuwa anaelekea njia yake kwani Joyce alikuwa anaishi ‘Matejoo’ na Miriam alikuwa anaishi ‘Kwa mrombo.’ Hadi daladala inafika sakina tayari ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu. Vivian aliposhuka aliamua kuchukua usafiri wa bodaboda ili aweze kuwahi nyumbani kwasababu alikuwa amechelewa sana. Alipokuwa kwenye pikipiki njiani alimuona mtu kama Nelson lakini alihisi kama amemfananisha.
Alitamani amweleze dreva asimamishe pikipiki ili aweze kujua kama ni kweli alikuwa amemuona Nelson ama la, lakini muda ulikuwa umesonga sana kwahiyo aliamua kupuuza. Alizidi kujiuliza yule ni mtu gani ambae alikuwa amefanana na Nelson kiasi kile. Aliishia kujilaumu ni kwanini hakumwambia dreva asimamishe pikipiki japo kwa dakika moja ili aweze kuridhisha macho yake. Kitendo kile kilimsababishia mawazo zaidi na zaidi juu ya Nelson. Kichwani mwake alipanga siku itakayofuata atajitahidi kuzunguka zunguka yale maeneo kama atafanikiwa kumwona yule mtu ambae alimfananisha na mwanaume wa ndoto zake.
Vivian alitokea kumpenda sana Nelson kwani hata wakati mwingine alikuwa anatingwa sana na mawazo kiasi kwamba hadi watu wanamuona mgonjwa. Mama yake pia alishawahi kulishuhudia hilo kwa mwanae lakini alipojaribu kumuuliza, Vivian alipotezea juujuu. Hakujua mama yake anakereka jinsi gani kumuona akiwa katika mawazo mazito kiasi kile. Kesho yake alikwenda chuoni kama kawaida lakini aliendelea kuwa na mawazo sana. Marafi zake waliamua kumuuliza kilichokuwa kinamfanya akose raha ni kitu gani na ndipo alipoamua kuwasimulia habari za Nelson kwanzia mwanzo mpaka mwisho hadi tukio la jana kumuona mtu aliefanana na Nelson alipokuwa kwenye bodaboda. Walimwona chizi baada ya kuwaeleza kwamba kijana huyo alipata ufadhili wa kwenda kusoma marekani.
“Wewe mwanamke hazikutoshi kabisa yaani mwanaume hajakutamkia kuwa anakupenda, isitoshe yupo nje ya nchi halafu bado unaendelea kujishauwa kuwa unampenzi.” Joyce aliamua kumweleza jinsi alivyoweza kumuona mpuuzi kutokana na maelezo yake. Badala ya kupata faraja kutoka kwa hao marafiki zake alipoteza matumaini kabisa kwasababu hakuna hata mmoja ambae aliamini kuwa Nelson bado atakuwa anamawazo ya Vivian kichwani mwake. Kiukweli alijisikia vibaya sana hadi akajuta kwanini aliamua kuwatobolea siri yake. Ile siku aliiona mbaya kwake kwasababu marafiki walimuhudhi sana. Saa 5. 17 asubuhi aliamua kuomba ruhusa chuoni na kuondoka kuelekea nyumbani. Hiyo yote ni kutokana na kwamba marafiki zake walimuudhi kupita maelezo. Alitoka chuoni huku akiwa amekasirika sana. Alipanda daladala ambayo ilimpeleka hadi stendi ambapo alipanda gari lingine linaloelekea Sakina kwa Idd. Saa 6.00 mchana alishuka kwenye gari na kuanza kutembea kuelea nyumbani.
************CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Nelson alizidi kupoteza raha baada ya kumkosa Vivian alijiuliza au huwenda yule jamaa alimfananisha Vivian na msichana mwingine? Lakini kama ndiyo hivyo mbona hakumuona mwanamke mwingine ambae anafanana na Vivian? Alipata wazo la kurudi tena eneo lile kwa siku inayofuata kujaribu kama atafanikiwa kumuona. Siku iliyofuata alirudi kwa mara nyingine tena huku akisali kimoyomoyo kusudi Mungu amuwezeshe kukutana na mwanamke ambae alihisi kuwa furaha yake haitaweza kupatikana bila kumpata maishani mwake.
Saa sane mchana Nelson aliamua kutoka nyumbani kuelekea lile eneo ambalo alikutana na Mejooli. Aliamua kutoka mapema ili saa kumi imkute maeneo yale kwasababu ndio alielezwa muda ambao Vivian anapita mara kwa mara. Kwahiyo lisaa limoja kabla tayari alikuwa ameshafika. Alianza kusubiri huku akitazama huku na kule kama macho yake yatakutana na Vivian lakini aliambulia patupu. Muda ulizidi kusonga naa jioni ya saa kumi na mbili ilimkuta bado yupo maeneo yale. Kwa bahati nzuri Mejooli alitokea na kumkuta pale.
“Aisee vipi ndugu.” Nelson alimsalimia Mejooli.
“Safi kabisa. Umefaanikiwa kumpata mtu wako?” Mejooli aliitikia salamu na kuuliza swali papo hapo.
“Hapana kaka! tangu sikuzile sijafanikiwa kabisa kumpata. Halafu isitoshe leo tena tangu saa tisa nipo hapa lakini sijafanikiwa kukutana nae.”
“Daah! Kiukweli unabahati mbaya sana kwasababu leo hii karudi mapema mno, alipita mida ya saa sita. Sijajua ni kwanini leo kawahi hivyo wakati sio kawaida yake.” Mejooli alizungumza maneno ambayo yalimchoma sana Nelson kwasababu asubuhi alikuwa kwenye mgogoro wa nafsi kwamba awahi ama achelewe.
“Unauwakika lakini ndio yeye?” Nelson aliamua kuuliza kusudi asikute anapoteza muda wake halafu mtu mwenyewe asiwe yeye.
“Ndio nina uwakika kabisa ndiyo yeye. Kipindi cha nyuma alikuwa akipita hapa na sare za shule ya sekondari Ekenywa.” Maneno ya mejooli yalithibitisha kwamba ni kweli alikuwa namfahamu Vivian.
“Haswaa umepatia kabisa.”
“Nimemfahamia njia hii hii kwasababu kipindi cha nyumba nilikuwa ni fundi wa pikipiki maeneo haya kwahiyo nilikuwa namuona kila siku anapokuwa anaenda na kurudi shule. Maeneo haya wanaume wengi wanamfahamu sana kutokana na uzuri ambao amejaliwa ila ni binti mwenye maringo ya hali ya juu.” Maneno ya Mejooli yalimfurahisha sana Nelson. Aliamini kwamba tabia ya Vivian itakuwa haijabadilika.
Baada ya mazungumzo hayo waliagana. Nelson alirudi nyumbani akiwa amenuna kiasi kwa kutofanikiwa kukutana na Vivian, ingawa alipata faraja kidogo baada ya kupata uwakika kwamba binti aliekuwa anaelekezwa na Mejooli ndie aliekuwa anamtafuta. Hakukata tamaa kwani alipanga siku inayofuata kwanzia asubuhi hadi jioni atakwenda kuendelea kumtafuta Vivian hadi ampate.
***********
Kutokana na hasira aliyoipata Vivian pamoja na mawazo juu ya Nelson, alijihisi kuumwa kwasababu mwili wake ulikuwa na joto sana. Alipofika nyumbani alimeza panado kwajili ya kutuliza maumivu ya kichwa na baada ya hapo alipanda kitandani kupumzika. Hakuweza hata kula chakula kutokana na jinsi alivyokuwa anajihisi vibaya. Alilala kwanzia mchana hadi jioni. Hali yake ilizidi kuwa mbaya, joto lake la mwili aligundua sio la kawaida, akahisi pengine anaweza akawa na homa. Kwasababu ilikuwa tayari ni jioni alipanga kama kesho yaka ataamka katika hali hile ya kuumwa basi atakwenda hospitali kupima ili aweze kubaini tatizo.
Usiku hakufumba macho kabisa, alihisi anakila dalili ya malaria kwahiyo alipanga siku itakayofuata aende hospitali kupata matibabu. Palipokucha asubuhi hakuweza kwenda chuo kwahiyo alikwenda katika zahanati moja inayoitwa ‘Upendo dispensary’ iliyopo jirani kabisa na nyumbani kwao. Alifika na kupata matibabu ambapo vipimo vya daktari vilionyesha alikuwa na malaria na taifodi. Daktari alimsisitiza anywe maji mengi ambayo ni safi na salama, pia azingatie muda wa kumeza dawa. Baada ya hapo alirudi nyumbani kwaajili ya kuanza dozi ya vidonge vya ‘mseto’ ambavyo ndiyo alikuwa amepatiwa na daktari.
Alipofika nyumbani kwao alianza dozi haraka kwasababu hali yake ilikuwa sio nzuri kabisa. Mwili wake ulikosa nguvu, kwahiyo alikuwa ni mtu wa kulala tu kila mara. Hakuwa na hamu ya chakula wala kinywaji chochote. Ingawa mama yake alimkazania sana katika suala la chakula. Upweke aliokuwa akiupata kipindi anapokuwa nyumbani kwao ilimfanya ajihisi kuumwa zaidi na zaidi. Hakuna ndugu wala rafiki ambae alikuwa na ujasiri kwa kusogeza mguu wake pale nyumbani kwao. Kutokana na akili yake ilikuwa imepevuka vya kutosha alihisi moja kwa moja mama yake atakuwa sio mtu mzuri kabisa.
“Sasa kama mama atakuwa ni mchawi inamana ndiye atakuwa ameteketeza familia pamoja na wanandugu wengine? Kwasababu vifo vyote huwa vinatokea katika mazingira ya kutatanisha kiasi kwamba kila mtu huwa anajiuliza kuna kitu gani kwenye huu ukoo wetu. Hivi hata siku nikipata mchumba wa kunioa si lazima ataogopa kutokana na vifo vya kila mara huku nyumbani kwetu?” Vivian alitafakari kwa kina tetesi za kuwa mama yake ni mchawi huku akihusianisha matukio ya vifo vya mara kwa mara katika ukoo wao. Imani kwa mama yake ilipotea kabisa akahisi kwa namna moja au nyingine ni lazima mama yake atakuwa ni mchawi kama ambavyo watu wanasema. Mawazo yale yalimfanya aumie zaidi kwasababu hali yake kiafya haikuwa njema kabisa. Aliamua kupotezea baada ya mawazo ya mvulana anaempenda kumjia tena katika kichwa chake.
“Hivi itakuwaje endapo Nelson atakuwa amempata mchumba nje ya nchi?” aliwaza jinsi ambavyo ataumia endapo atasikia kuwa Nelson atakuwa amempata mchumba ambae ni msomi mwenzake.
***********
Nelson aliamka asubuhi na mapema. Alikuwa kapania siku ile ni lazima ahakikishe anampata Vivian kwahiyo aliondoka nyumbani asubuhi sana. Alinunua zawadi zingine nyingi ambazo aliona zitamfaa Vivian. Alivaa suti ambayo aliinunua siku alipokuwa anahudhuria tafrija fupi iliyokuwa imendaliwa na balozi wa Tanzania nchini Marekani kumpongeza kwa kufanya vizuri, baada ya hapo alijipulizia marashi yenye kunukia vizuri sana. Kwa hakika alionekana kupendeza kupita kiasi. Alijua moja kwa moja ile siku sio rahisi asimwone Vivian kwahiyo alionekana kuwa mchangamfu sana kutokana na furaha iliyokuwa ndani yake. Alijua kushindwa kuonana na Vivian kwa siku zile labda asipite maeneo yale kwasababu alikuwa amejipanga kufanya mawindo yake hadi jioni ya saa moja. Alianza kusubiri kwanzia saa moja asubuhi hadi saa moja jioni bila kuonana na Vivian jambo ambalo lilimuumiza sana. Alijihisi kuchoka na pia alikasirika sana kwasababu hakufanikiwa tena kwa siku zile halafu isitoshe alikuwa amenunua zawadi nyingi sana. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Alikata tamaa ya kuendelea kusubiri kwahiyo aliondoka kuelekea nyumbaani huku akiwa amevunjika moyo. Alifika nyumbani na kunyooka moja kwa moja hadi kitandani. Hakuwa na hamu ya chakula wala kinywaji. Alijiona kama mtu mwenye nuksi ya hali ya juu. Kibaya zaidi alikuwa ameshapigiwa simu ya kuhudhuria katika interview mbalimbali za kazi lakini hakuwa amehudhuria hata moja. Yote hayo ni kwasababu alitaka kuhakikisha kwamba anafanikiwa kukutana na Vivian. Aliona kwenda kwenye interview ya kazi wakati kichwani bado anamawazo kedekede juu ya mtu anaempenda, anaweza akafeli kwahiyo ndiyo maana alikuwa amejipanga kusudi aweze kufanikisha suala la Vivian kwanza ndiyo mambo mengine yafuate.
Kutokana na kwamba alikata tamaa, siku iliyofuata aliamua kuitikia wito wa kampuni moja inayomilikiwa na mama mmoja mwenye asili ya Asia. Kampuni hiyo inajulikana kwa jina la ‘Build Africa’ ipo ndani ya jiji la Arusha. Kampuni hii ilionyesha nia ya dhati ya kumuhitaji kwasababu ilimpigia simu kwa mara kadhaa baada ya Nelson kutuma maombi yake katika kampuni hiyo kwa njia ya barua pepe. Asubuhi na mapema alifika katika ofisi za kampuni ile iliyopo maeneo ya ‘france coner.’ Aliona ni bora achangamkie nafasi ile kwasababu yeye mwenyewe alitokea kuvutiwa sana na kampuni ile. Alifanya interview ya kazi akiwa na vijana wengine 13 ambao walikuwa wamesoma katika mataifa mbalimbali duniani. Jambo lile lilimpa changamoto kidogo Nelson kwasababu ushindani ulikuwa ni mkubwa sana.
Hakuwa na uwakika kama kweli atafanikiwa katika kinyang’anyiro kile cha ajira. Alimwomba Mungu afanikiwe kusudi aweze kumsaidia mama yake ambae alikuwa katika mazingira ambayo yalikuwa ni magumu sana. Pia alitamani kuwa na kwake kwasababu alikuwa tayari amesha kuwa mtu mzima, aliona sio busara kuendelea kuishi nyumbani kwa mjomba wake ili hali anaelimu ya kutosha na anawezo wa kupata kazi katika kampuni yeyote kutokana na uzuri wa vyeti vyake. Baada ya siku mbili matokeo ya interview yalitoka ambapo kati ya wale watu kumi na tatu Nelson ndie aliekuwa amebahatika kuchukuliwa na kampuni ile. Alifurahi sana, alimshukuru Mungu kwa kumuwezesha kupata nafasi ile. Alikwenda kusaini mkataba wa ajira kwa miaka mitano. Alipomweleza mama yake kwamba amepata kazi kiukweli mama yake alifurahi sana na kumtakia kila la heri. Alipewa siku mbili za kujianda ili aweze kuanza kazi.
Pamoja na kwamba habari za kupata kazi ilikuwa ni njema kwake lakini haikuwa sababu tosha ya kufanya tabasamu lidumu usoni mwake kwa muda mrefu. Alitamani furaha ya kupata kazi, afurahie na mwanamke anaempenda. Siku mbili alizopewa kwajili ya maandalizi ya kuanza kazi, alizitumia zote kuendelea kumsaka Vivian lakini hakufanikiwa. Nafsia yake ilizidi kuteseka usiku na mchana kwani furaha ya moyo wake haikupatikana kabisa. Muda wa kuripoti kazini ulifika na ndipo alianza kazi rasmi katika kampuni ya ‘Build Africa’. Alipokuwa kazini alijitahidi kujizuia kumuwaza Vivian ili ufanisi wake wa kazi usiyumbe lakini ilishindikana kwasababu Vivian alikuwa ni kama melodi ya nyimbo nzuri iliyokataa kutoka kwenye kichwa chake.
Mwezi mmoja ulikatika akiwa bado hajafanikiwa kukutana na Vivian ingawa kila mwisho wa wiki alikuwa akitembelea maeneo ambayo alihisi ataweza kukutana nae lakini hakufanikiwa. Alipata wazo kwamba endapo atabahatika kukutana na Mejooli basi ampe namba za simu kusudi siku kijana huyo akikutana na Vivian aweze kumpa mawasiliano yake. Lakini tangu alipopata wazo hilo, hata Mejooli hakufanikiwa kumuona tena. Siku zilizidi kusonga huku akiendelea kusongwa na mawazo. Kutokana na jitihada zote za kumtafuta Vivian kukwama, ilisababisha muda mwingi awe mkimya na mwenye mawazo mengi sana. Wafanyakazi wenzake walikereka na tabia yake lakini mwishowe walihisi huwenda ndivyo alivyo. Baadhi ya wafanyakazi wa kike walitamani sana kuwa karibu nae lakini walishindwa kwasababu hakupenda mazoea na mtu yeyote. Fauku ya hayo, ufanisi wake wa kazi ulionekana kuwafurahisha wakubwa wake wa kazi.
***********
Vivian aliendelea kutumia dozi ya malaria na taifodi aliyokuwa amepatiwa hospitali. Baada ya wiki moja hali yake ya kiafya ilihimarika, na kurejea chuoni kuendelea na masomo. Wanafunzi wenzake pamoja na walimu walifurahi kumuona kwa mara nyingine kwasababu walikuwa wamemmisi. Yeye pia alifurahi kurejea chuoni kwasababu alikuwa amechoshwa na upweke wa nyumbani kwao. Mawazo juu ya Nelson hayakuwa yametoweka kichwani mwake kwani bado aliendelea kumuwaza kila mara. Siku zilizidi kukatika bila kuwepo kwa matumaini yeyote ya kumpata Nelson. Alianza kukata tamaa kwasababu hakuona dalili yeyote ya kukutana na mwanaume anaempenda. Hakujua kuwa Nelson amerejea Tanzania kwasababu na yeye pia angekuwa na jitihada za kumtafuta ili waweze kuonana. Akilini mwake alifahamu kuwa Nelson bado alikuwa nchini Marekani.
Alijiuliza ni kwanamna gani ataweza kuipata furaha aliyokuwa anahitaji kutoka kwa mtu anaempenda lakini aliishia kudondokwa na chozi kwasababu alizidi kupoteza matumaini. Umri nao ulikuwa unasonga kibaya zaidi alikuwa ameshawakataa wanaume wengi ambao walitaka kwenda kujitambulisha nyumbani kwao. Alianza kuona kwamba akiendelea na msimamo wake wa kumsubiri Nelson ataishia kuzeekea nyumbani kwao. Kwahiyo alianza kupata mawazo ya kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanaume ambae atajitokeza kumpenda kwa dhati. Alichoka kumsubiri mtu ambae hakujua atakutana nae kwa njia gani. Alitamani na yeye kuwa katika mahusiano ya kimapenzi kama ambavyo wasichana wengine wa umri wake wanavyofanya. Moyo ulimuuma sana pale ambapo alikuwa anaona marafiki zake wakifurahi na wapenzi wao. Ingawa alitamani sana kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote ambae atamuona anafaa lakini bado moyo wake ulizidi kuwa mzito akiamini kwamba furaha ya kweli haipatikani kwingine isipokuwa kwa Nelson. Kusema kweli Vivian alikuwa katika wakati mgumu sana wa kuweza kufanya maamuzi yenye tija maishani mwake. Baada ya mwaka mmoja, Vivian aliendelea kuwepo chuoni akiendelea na masomo yake kwa ngazi ya diploma. Bado hakuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanaume yeyote kwasababu moyo wake ulikataa kabisa kumruhusu.
Siku moja wakati alipokuwa chuo, muda wa kuondoka kwenda nyumbani ulifika kwahiyo marafiki zake wakubwa ambao ni Miriam na Joyce walimtaka waondoke kwa pamoja kama ilivyo kawaida yao kuongozana. Miriam na joyce walitangulia taratibu na kumwacha Vivian akiwa anaazima kitabu cha stori kutoka kwa kijana mmoja ambae huwa anapenda sana kusoma vitabu vya hadithi. Walifika barabarani na kuvuka upande wa pili kusubiri daladala zinazoelekea mjini. Ghafla wakati walipokuwa wanamsubiri Vivian, Miriam aliona gari dogo likija na kuamua kujaribu kuomba lifti ya kuelekea mjini. Kwa bahati nzuri gari iliwasha endiketa ya kuingia katika kituo cha daladala walipokuwa wamesimama.
***********CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Nelson alikwenda AICC kumjulia hali mkuu wake wa kazi Bibi ‘Chu-Hua’ mwenye asili ya China ambae alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo tangu alfajiri ya siku hiyo baada ya kuugua ghafla. Tayari Nelson alikuwa amesha nunua gari ya kutembelea aina ya ‘Toyota Brevix.’ Alifika hospitali mida ya saa tisa lakini kwa bahati mbaya alikuta bosi wake amehamishiwa hospitali ya rufaa ya Mount Meru baada ya kuzidiwa ghafla. Aliamua kugeuza gari lake muda huohuo ili aweze kuelekea nyumbani.
Gari lilitoka katika geti la hospitali na kukunja kulia katika barabara ya Nelson Mandela kuelekea mjini. Nelson alianza kukanyaga mafuta kwa nguvu ili aweze kuwahi nyumbani kupumzika kwasababu ile siku alikuwa amechoshwa na kazi za ofisi. Kabla gari halijakole mwendo, macho ya Nelson iliwaona wanafunzi wawili wa kike walikuwa wanaomba lifti ya kuelekea mjini. Walikuwa ni wanafunzi wa chuo cha ‘Tropical Institute’ ambapo ndipo alipokuwa anasoma Vivian. Baada ya gari kusisimama wale wanafunzi walipanda harakaharaka, lakini mmoja alisikika akizungumza kwa masikitiko.
“Masikini tunamuwacha Vivi!” baada ya Nelson kusikia mmoja wa wale wanafunzi akilalama, aliuliza swali.
“Kuna mwenzenu mmemuacha?”
“Ndio! tumemuacha anachukua kitabu kwa mwanafunzi mwingine.” Mmoja wa wale wanafunzi alitoa ufafanuzi kwa Nelson.
“Mnauwakika anakuja sasa hivi?” Nelson alizungumza kwa msisitizo huku akibofya simu yake ya mkononi.
Kabla hawajajibu swali walilokuwa wameulizwa, Vivian alionekana akitembea taratibu kutoka njia ya chuo kuja barabarani.
“Vivi! Kimbia twende, tumepata lifti.” Mmoja wa wale wanafunzi alisikika akizungumza kwa sauti ya juu wakati alipokuwa ametoa kichwa chake nje ya dirisha la gari.
Kwa muda huo Nelson alikuwa bize akiendelea kubofya simu yake, kwahiyo hakuangaika hata kumtazama mwanafunzi aliekuwa anasubiriwa. Vivian nae hakufanikiwa kumuona Nelson ambae alikuwa ndani ya gari kwasababu viyoo vya gari vilikuwa ni vyeusi (tinted) Vivian aliongeza mwendo na kuvuka barabara kisha akafungua mlango wa gari na kuingia kwenye siti ya nyuma ambapo ndipo marafiki zake walipokuwepo. Baada ya kuingia ndani ya gari ndipo Nelson alipogeuza shingo yake kumwangalia mwanafunzi aliekuwa anasubiriwa. Ilibidi Nelson afikiche macho yake ili aweze kumwona vizuri msichana aliekuwa ameingia kwenye gari kwasababu alijihisi kama anaota.
“Am I dreaming?” (hivi ninaota?) Sauti ilisikika ikitoka kinywani mwa Nelson huku akionekana kutoamini kabisa kile kilichokuwa mbele ya macho yake. Vivian nae akionekana kushikwa na bumbuwazi kwasababu alijihisi kama vile yupo ndotoni.
“Are you Vivian?” (wewe ni Vivian?) Nelson aliuliza kwa sauti ya juu mithili ya mtu aliepagawa.
“Exactly, I’am.” (Naam, ndio mimi.) Vivian alijibu huku machozi ya furaha yakimtiririka mashavuni mwake.
“I cant believe!, I cant believe!” (siamini! Siamini!) Nelson alizungumza huku akifungua mkanda wa kwenye gari kisha akafungua mlango na kushuka. Alizunguka upande wa pili na kufungua mlango wa gari na kumshusha Vivian halafu akamkumbatia kwa furaha sana. Furaha ilizidi kifani kwa Vivian hatimae alikuwa akilia kama mtoto mdogo kwasababu hakuamini kabisa kilichokuwa kimetokea mbele ya macho yake. Marafiki zake walishikwa na butwaa kwasababu hawakujua kilichokuwa kikiendelea. Waliwahi kusikia jina la Nelson likitajwa na Vivian mara kwa mara lakini hawakujua kama ndie yeye yule walikuwa wamekutana nae kwa wakati ule.
“I have been looking for you for so long.” (Nimekuwa nikikutafuta kwa muda mrefu sana.) Nelson alizungumza huku akiwa bado amemkumbatia Vivian, wote wakilia kwa furaha.
“When did you come back Nelson.” (Umerudi lini Nelson.) Vivia alizungumza wakati alipokuwa akimtazama Nelson usoni huku machozi ya furaha yakizidi kumdondoka.
“Of course I have one year since I came back.” (Nina mwaka mmoja tangu nirudi Tanzania.)
Watu waliokuwa wakipita barabarani waliona kama mchezo wa kuigiza. Baadhi ya wapiti njia walidiriki kusimama na kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
“Ok! let’s go.” (sawa! tuondoke.) Nelson alizungumza wakati akifungua mlango wa gari ili Vivian aweze kuingia. Mioyo yao ilijawa na furaha iliyopitiliza. Wote walijiona kama wapo ndotoni wanaota lakini ilikuwa mubashara kabisa. Kila mmoja alionyesha kufurahi kukutana na mwenzie. Nelson alikuwa akimtazama Vivian mara mbili mbili kwasababu alikuwa haamini kabisa kama amefanikiwa kukutana nae, tena pasipo kutegemea kabisa. Walipofika mjini Nelson aliwashusha wale marafiki zake Vivian na kuwashukuru sana. Alimpatia kila mmoja shilingi elfu kumi kwasababu kama sio wao pengine asingefanikiwa kumuona Vivian kwa siku zile.
Wale mabinti walifurahi sana, walimshukuru Nelson kwa zawadi nzuri aliyokuwa amewapatia. Saa ya kwenye gari ilionyesha ni saa 10.10 jioni. Walikubaliana kwenda kuzungumza katika hoteli maharufu sana mkoani arusha inayojulikana kwa jina la ‘Palace hotel.’ Kila mmoja alionyesha kuwa na furaha ya ajabu kukutana na mwenzie. Walifika salama hotelini huku kila mmoja akiwa na shauku ya kutaka kumweleza mwenzie juu ya hisia za kimapenzi zilizokuwa zikiwaka ndani ya nafsi zao mithili ya moto wa makaa ya mawe. Baada ya kufika waliagiza chakula pamoja na vinywaji. Nelson aliona kama uzuri wa Vivian umeongezeka mara dufu. Sura ya upole na tabasamu lisilokwisha katika sura ya Vivian ilisababisha Nelson azidi kupagawa zaidi. Kizuri zaidi ni pale ambapo Vivian alipokuwa akitabasamu vishimo vidogo mashavuni mwake vilijitokeza na kusababisha Nelson asitamani tabasamu la Vivian liishe. Walianza kula huku wakizungumza.
“Kwa furaha niliyoipata leo sijui kama itajirudia tena kwenye maisha yangu.” Vivian alizungumza kudhihirisha furaha aliyokuwa ameipata ni kubwa kuliko maelezo.
“Kusema kweli hata mimi nimefurahi sana kukutana na wewe. Nimejaribu mara nyingi sana kukutafuta lakini jitihada zangu zimekuwa zikigonga mwamba kila wakati.”
“Kweli Mungu anajibu maombi! Nimekuwa nikimuomba kila siku nikutane na wewe hatimae leo hii nimekuona kweli.” Vivian alizidi kuzunguma kwa furaha.
“Vivian!” Nelson aliita.
“Yes.” (Naam.)
“Are you married?” (umeolewa?)
“No! how about you, are you married?” (hapana! Vipi kuhusu wewe, umeoa?) Vivian aliuliza swali baada ya kujibu swali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“No!” (hapana.) Nelson alijibu kwa kifupi.
“Why?” (kwanini?) Huku Vivian akitabasamu aliuliza swali ambalo lilikuwa linaeleweka lakini nigumu kulitolea maelezo.
“Kwasababu nilikuwa mbali na mwanamke wa ndoto zangu.”
“Nani ndio mwanamke wa ndoto zako?” swali lingine lilimuangukia Nelson kutoka kwa Vivian.
“Vivian! the one I talk to her right now” (Vivian! ambae nazungumza nae muda huu.) Nelson alizungumza huku akimtazama Vivian machoni kwa tabasamu mwanana. Vivian alishindwa kuzungumza chochote machozi yalianza kumtoka kwa furaha.
“Vivian! frankly speaking, I want to marry you, because you’re the type of girl I used to dream.” (Vivian! kiufupi nataka kukuoa, kwasababu wewe ni aina ya mwanamke ambae nimekuwa nikimuota kila mara.) Nelson aliamua kuonyesha hisia zake za dhati kwa mwanamke anaempenda.
“Thank you so much Nelson, I promise to love you forever and ever!” (Asante sana Nelson, nakuahidi kukupenda daima milele yote.) Vivian alizungumza kwa furaha sana baada ya kusikia Nelson anataka kumuoa.
Maongezi yao yalinoga sana, hadi walipokuja kushtuka ni saa moja kasoro jioni. Nelson alimchukua Vivian kwa gari lake na kumpeleka moja kwa moja hadi nyumbani kwao. Ingawa hakusalimiana na mama yake kwasababu usiku ulikuwa umeshaingia. Nelson alishuhudia jinsi ambavyo mtaa aliokuwa anaishi Vivian ulivyokuwa umejificha. Alikiri kwamba hata kama angeelekezwa asingeweza kufika kwasababu kulikuwa ni mbali halafu kuna kona kona nyingi.
Baada ya kuhakikisha mpenzi wake amefika nyumbani kwao aliwasha gari lake na kuondoka. Moyoni alijawa na furaha sana kutokana na kitendo cha kukutana na mwanamke wa ndoto zake. Kutokana na furaha aliyokuwa nayo alifungua mziki wa kwenye gari kwa sauti kubwa. Alikumbuka jinsi ambavyo kijasho kilimtoka kipindi cha nyuma alipokuwa akimsaka Vivian kwa udi na uvumba bila mafanikio. Alifika nyumbani kwa mjomba wake lakini hakuweza kuficha hisia za furaha zilizokuwa zikitamalaki moyoni mwake. Alionekana wa tofauti sana na siku zingine kwasababu alikuwa kachangamka kupita kiasi. Mjomba wake alimshangaa kwasababu hakuwahi kumuona katika hali ya uchangamfu kiasi kile kwahiyo ilimbidi amuulize kulikoni meno yote thelasini na mbili nje.
“Mjomba leo upo tofauti kabisa na nilivyokuzoea, unaonekana kuwa na furaha sana vipi wamekupandisha cheo kazini?” Mjombwa wake Nelson aliuliza.
“Hapana mjomba furaha yangu haihusiani na mambo ya kazini ila usijali nitakueleza kwa utaratibu muda utakapofika. Ninaimani ni habari ambayo hata wewe itakufurahisha pia.” Nelson alizungumza kumjibu mjomba wake huku uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu bashasha.
“Sawasawa!” Mjomba alijibu huku akitingisha kichwa kuonyesha amekubali.
Siku iliyofuata Nelson alichelewa kuamka kwasababu alilala sana. Hakuna siku ambayo alipata usingizi mzuri kama ile siku. Hayo yote ni kwasababu alihisi mzigo mzito uliokuwa ndani ya moyo wake ameushusha. Alipoamka alijiandaa haraka haraka na kuelekea katika eneo lake la kazi. Mshangao alioupata mjomba yake pindi alipomwona Nelson akiwa tofauti na siku zingine ndivyo ambavyo hata wafanyakazi wenzake walionekana kushangazwa na furaha aliyokuwa nayo kwa siku ile alipofika kazini. Alicheka na kuzungumza na kila mtu vizuri kuliko siku zingine. Kiukweli alizua mjadala mkubwa wa chini kwa chini kwa wafanyakazi wenzie kwasababu hawakuwahi kumuona katika hali ile hata siku moja tangu alipoanza kazi.
Walijiuliza Nelson aliamshwa na nani siku zile. Ilipofika saa tisa alasiri aliwasha gari lake na kwenda hadi chuoni kwa kina Vivian kumchukua. Alimpeleka hadi kwenye duka la mfanyabiashara maarufu mjini arusha kwa jina la Benson na kumnunulia simu nzuri kwaajili ya kuweza kuwasiliana kwa urahisi. Alimchagulia simu aina ya ‘Nokia lumia 1320’ kwa gharama ya shilingi laki 8 za kitanzania. Vivian alifurahi sana kununuliwa simu na mpenzi wake. Baada ya hapo walikwenda kwa sonara ambapo Nelson alimnunulia mchumba wake mkufu, hereni na saa ya mkononi zote za dhahabu. Nelson alijitahidi kumuonyesha mpenzi wake ni njinsi gani alikuwa anampenda na kumthamini kuliko kitu chochote.
Baada ya hapo alimchukua na kumrudisha hadi nyumbani kwao na kumwacha na kuondoka. Moyo wa Vivian ulijawa na furaha isiyopimika. Alitamani Nelson amuoe haraka kwasababu alihisi kumpenda sana. Furaha aliyokuwa anapatiwa na mchumba wake ilimfanya asijutie msimamo wake wa kuwakatalia wanaume ambao waliwahi kumwitaji kimapenzi. Hali ya hewa ya jiji la Arusha ilitokea kumvutia sana Nelson na kuamua makazi yake ya kudumu yawe huko. Kwahiyo alichukua mkopo benki na kununua viwanja viwili na kuanza kujenga nyumba mbili kwa pamoja, yaani nyumba yake pamoja na ya mama yake.
Alipania kumuamishia mama yake mkoa wa Arusha ili aweze kumsaidia kwa ukaribu zaidi. Ujenzi ulikuwa unafanywa kwa kasi sana kwasababu Nelson alitaka siku ya harusi ndio na uzinduzi wa nyumba yake ufanyike. Mwezi wa pili baada ya Nelson kukutana na Vivian alikwenda kujitambulisha ukweni. Alisindikizwa na rafiki yake mmoja ambae anaitwa Lucas. Walifika na kupokelewa vizuri na mama Vivian. Walikula na kunywa vilivyokuwa vimeandaliwa. Ilikuwa ni siku ya furaha sana kwasababu Nelson alifanikiwa kumfahamu mama mzaa chema. Nelson alifurahishwa na ukarimu aliouonyesha mama mzazi wa mke wake mtarajiwa. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Baada ya utambulisho wiki mbili zilizofuata Nelson alimvisha pete mchumba wake Vivian katika tafrija fupi iliyofanyika katika ukumbi wa ‘Tindigani garden’ iliyopo maeneo ya kimandolu jijini arusha. Kila mtu aliyemuona mchumba wa Nelson alipaza sauti kuusifia uzuri aliokuwa amejaliwa na Mungu. Wafanyakazi wenzake walimsifu kwa uchaguzi mzuri aliokuwa ameufanya. Pamoja ya sifa nyingi za ulimbwende ambazo Nelson alizisikia kutoka kwa watu mbalimbali waliokuwa wakimwagia mchumba wake, Nelson aliamini kwamba ni kweli Vivian ni mzuri sana baada ya kumsikia mama yake mzazi akimsifia Vivian kwamba ni msichana aliyeumbika kama malaika.
Mwezi uliofuata nyumba ya Nelson pamoja na ya mama yake ilikamilika japokuwa zilikuwa katika maeneo tofauti tofauti kwani mama yake alimjengea maeneo ya ‘Kambi ya chupa madukani’, na yeye alijenga maeneo ya Sekei. Baada ya nyumba kukamilika mama yake aliamia rasmi jijini Arusha. Mama huyo alimshukuru Mungu kwa uwezo ambao alimjalia mwanae kuweza kukamilisha ujenzi ule ndani ya muda mfupi. Zilibaki masiku kadhaa harusi ya Nelson na Vivian iweze kufungwa.
Maandalizi ya nguvu yalifanyika kwaajili ya sherehe kubwa ambayo Nelson alikuwa amepanga kufanya. Bosi wake aliekuwa amelazwa hospitali aliruhusiwa baada ya hali yake ya kiafya kuhimarika. Vivian nae alijisikia furaha sana kwasababu alikuwa ameshamaliza masomo yake. Nelson hakuomba mchango wa harusi kutoka kwa mtu yeyote lakini kutokana na kwamba alikuwa ni kipenzi cha watu, alipokea michango ya kimawazo na kipesa kutoka kwa marafiki zake. Nelson aliamua kuandaa kadi za mwaliko wa harusi yake kama njia nzuri ya kuwaalika ndugu jamaa na marafiki, kwahiyo ‘Baraka Stationary’ waliopo ‘Sanawari’ walipokea tenda ya kutengeneza kadi ya mwaliko wa harusi. Walitengeneza kadi nzuri sana ambayo ilikuwa inasomeka kama ifuatavyo.
“Familia ya Bw. na Bi. Richard P. Urassa.
Wanayofuraha tele kukukaribisha.
Bw, Bi, Mwl, Mchu, Dakt, Ndug, Bw/Bi
---------
Kwenye harusi ya kijana wao.
Nelson Richard Urassa.
Na
Vivian Alex Damian.
Katika kanisa la ‘Alive God’ mianzini,
Jumamosi ya tarehe 22/12/2001,
Saa 8.30 mchana. Na baadae,
Kwenye tafrija fupi katika,
Ukumbi wa ‘Moon Hall’ saa 2 usiku.
Karibuni sana.”
Kusema kweli maandalizi yalikuwa ni motomoto kwasababu mambo yalikuwa yanafanyika kisasa zaidi. Marafiki wa nje ya nchi walialikwa kwa njia ya barua pepe. Marafiki 11 walijibu barua pepe na kusema kwamba watahudhuria katika sherehe ya harusi ingawa baadhi ya marafiki waliomba radhi ya kutohudhuria kutokana na ubize wa kazi. Iliundwa kamati ya harusi ambayo ni imara kwaajili ya kuhakikisha harusi inafanyika barabara. Mjomba wake Nelson ndie aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya harusi. Kamati hiyo ndiyo ilipanga wageni wote wa nje ya nchi wafikie katika hoteli ya ‘Snow crest’ iliyopo kwa mrefu jijini Arusha.
************
Sherehe ya mwago (send off) ilifanyika siku ya alhamisi nyumbani kwa kina Vivian kuanzia saa moja kamili jioni. Ni siku hiyohiyo ajali mbaya ya gari ilitokea mtaani kwao, baada ya gari dogo aina ya Toyota IST lenye namba za usajili ‘T 701 XWX’ kuwagonga watoto watano wa shule na kupoteza maisha papo hapo. Tukio lile lilisababisha Vivian akose raha kabisa kwasababu alishuhudia miili ya watoto ambao walikuwa wamepoteza maisha. Pamoja na hayo yote lakini hapakuwa na sababu ya kuhairisha sherehe kwahiyo mambo yaliendelea kama kawaida. Sherehe iliandaliwa na mama Vivian bila kumshirikisha mwanae. Ingawa Nelson alitamani kuwapa mchango wa pesa kidogo ya kuweza kuwasaidia katika maandalizi ya sherehe lakini mama Vivian alikataa na kusema kwamba anauwezo wa kumudu sherehe atakayoifanya.
Ilionekana ni sherehe ambayo ilikuwa ni ya kitamaduni japo kuwa ilikuwa na watu wachache sana. Mama Vivian alikuwa amevaa sare na watu ambao Vivian hakuwafahamu. Sare waliyokuwa wamevaa ilikuwa ni kaniki na kiunoni walijifunga mitandio mekundu. Mwonekano wao ulimtisha sana Vivian, ingawa alijikaza hofu yake isijidhihirishe mbele ya wageni. Uchache wa watu haukumshangaza Nelson akajua ndio sherehe za kisasa zilivyo siku hizi hakuna mlundikano mkubwa wa watu kama zamani. Mshehereshaji alikuwa ni mwanamke ambae pia alikuwa mgeni machoni pa Vivian kwani hakuwai kumuona wala kumsikia.
Sherehe ile ya mwago ilimpa mawazo mengi sana Vivian kwasababu watu waliohudhuria katika sherehe yake hakuwahi kuwaona tangu kuzaliwa kwake. Halafu isitoshe alishangazwa pia na vyakula vilivyokuwa vimeandaliwa kwani hapakuwa na wali wala pilau bali chakula ilikuwa ni nyama tu ambayo Vivian hakujua imepatikana vipi. Halikadhalika kwa upande wa vinywaji hapakuwa na soda wala bia bali kinywaji pekee kilichokuwepo ni supu iliyopatikana kutokana na nyama zilizochemshwa. Licha ya kushangaa lakini pia Vivian alijawa na uoga ndani yake, jambo ambalo lilisababisha atengeneze tabasamu la kinafiki usoni mwake ili asiweze kushtukiwa na wageni wake. Ratiba ya sherehe ile iliendelea ambapo muda wa chakula ulifika.
Roho ya Vivian ilikuwa inagoma kabisa kula zile nyama zilizokuwa zimeandaliwa lakini hakuwa na namna ya kukataa kwasababu ingeleta picha mbaya kwa wageni waliokuwa wamehudhuria sherehe akiwemo mume wake mtarajiwa na mama mkwe. Walianza kula zile nyama na kila mmoja alionekana kuzifurahia. Hapakuwepo na mziki kama kwenye sherehe zingine bali Mama Vivian pamoja na watu wake waliburudisha watu kwa kuimba nyimbo mbalimbali kwa lugha ambayo haikuweza kufahamika kiurahisi. Matukio yote yaliyokuwa yakiendelea mbele ya macho ya Vivian yalitosha kuwa jibu tosha kuwa mama yake ni mchawi mkubwa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Kilichozidi kumshangaza Vivian ni kwamba mambo yaliyokuwa yakiendelea katika ile sherehe yake hayakuwa ya kawaida kabisa lakini wageni waliyokuwa wamehudhuria walionekana kutokuwa na habari. Aligundua lazima kuna namna imefanywa kuwapumbaza wale wageni wake wasigundue ushetani uliokuwa ukifanyika katika sherehe ile. Mama Nelson alinyanyuka kwenye kiti na kwenda kucheza ile ngoma iliyokuwa ikichezwa kwa mitindo ya kutisha. Baada ya muda mfupi alifuata mjomba wa Nelson pamoja na wageni wengine. Mwishowe Nelson naye alitaka kuingia kati kucheza lakini Vivian alimzuia.
“No! I love the traditional songs, let me join them for a moment.” (Hapana! Napenda nyimbo za asili, ngoja niungane nao kwa muda kidogo.) Nelson alisikika akizungumza na Vivian huku akitaka kujitoa kwenye mkono wa Vivian uliokuwa umemkamata sawasawa ili asichomoke.
“No! no! no!” (hapana! Hapana! Hapana!) Vivian alimzuia kabisa mpenzi wake asiingie katika ngoma ile. Mama yake Nelson pamoja na mjomba wake walionekana kutokwa na jasho jingi kutokana na jinsi walivyokuwa wanacheza ngoma ile kwa mitindo ambayo ilikuwa inaogopesha.
Sherehe ilifikia ukingoni usiku mnene na ndipo Nelson na marafiki zake walirudi majumbani mwao. Chakushangaza ni kwamba hakuna mtu hata mmoja aliyekumbuka kupiga picha katika sherehe ile ya send off, kibaya zaidi hakuna mpiga picha yeyote aliekuwa amewekwa kwaajili ya kupiga picha katika sherehe ile, kwahiyo tukio lile lilipita kama upepo kwasababu hapakuwa na kumbukumbu zozote zilizohifadhiwa.
************
Kamati ya kuzimu ndio ilikuwa ikihudumia katika sherehe ile kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda sawa. Kuzimu ilifurahi baada ya wageni waalikwa wa sherehe ile kuweza kula na kunywa. Watu wote walioshiriki vyakula vilivyokuwa vimeandaliwa kwenye ile sherehe walikuwa wameshaingia maagano na kuzimu. Kwahiyo usiku wa siku hiyo walichukuliwa wote na kupelekwa kuzimu kwenda kutambulishwa. Mambo yote waliyokuwa wakiyaona yakiendelea kule kuzimu walijiona wapo ndotoni wanaota lakini haikuwa ndoto. Miale ya radi ilikuwa ikimulika mithili ya flash za kamera, milio ya bundi na paka ilisikika barabara. Kulikuwa na harufu kali ya damu na pia mkusanyiko mkubwa wa watu ambao walionekana kufurahia damu na nyama walizokuwa wanakula.
Hofu ilitambaa kifuani mwa Vivian. Alipotazama pembeni aligundua yupo na watu wote waliokuwepo kwenye sherehe yake. Walitembea kwa mwendo wa taratibu huku wakisindikizwa na ngoma walizokuwa wakizisikia zikichezwa kwenye sherehe. Alijitahidi kujizuia asitembee lakini alishindwa, alijaribu kupiga kelele kuomba msaada lakini sauti nayo ilikataa kabisa kutoka. Mbele yake alimuona mume wake mtarajiwa analia kwa huruma anaomba msamaha. Alitamani kumbembeleza mpenzi wake lakini sauti iliendelea kugoma kutoka. Mara baada ya kufikishwa kwenye kiti cha malkia walipokelewa na kicheko cha kutisha.
“Ahahahaha!” Ahahaha! Ahahahahaha.!” Kicheko cha kutisha kilisikika lakini hawakujua kilipokuwa kikitokea.
Vivian alipomtazama vizuri yule malkia wa kuzimu aligundua kuwa alikuwa ni mama yake mzazi. Moyo wake ulilia paa! Sherehe rasmi ya kuwakaribisha ilifanyika, ambapo walinyweshwa damu na kulishwa nyama kwa mara nyingine. Kuzimu kulitawaliwa na shwangwe kubwa kutokana na ule ugeni mkubwa. Pamoja na kwamba Vivian alikuwa mbishi sana kunywa damu na nyama za watu lakini alinyweshwa na kulishwa kwa nguvu. Baada ya hapo Vivian alishtuka usingizini na kujikuta akitokwa na jasho mwili mzima huku mdomoni mwake akiwa na mabaki ya damu ambayo iliyokuwa imemwagikia. Alishtuka sana na kujiuliza inamana ile ilikuwa ni kweli ama ndoto? Aliamua kushuka kitandani na kwenda chumbani kwa mama yake kwenda kumweleza alichokuwa amekiota. Alipofika alimwamsha mama yake kwa kumwita na kumgusa ili aweze kuamka lakini hakuamka. Mapigo ya moyo ya mama yake yalionekana kudunda sawa kabisa lakini hakuamka. Vivian aliamua kurudi chumbani kwake kulala. Palipokucha asubuhi mama yake alimkataza kuamshwa wakati anapokuwa amelala, kwa madai kwamba hapendi usumbufu. Alipomweleza habari za ndoto ya usiku alionekana kupuuza. Vivian alinyanyua simu yake na kumpigia Nelson na kumweleza kwamba ameota ndoto mbaya sana. Wasiwasi ulimzidi Vivian baada ya kusikia Nelson akimweleza na yeye ameota ndoto kama ileile.
************
Siku moja kabla ya harusi wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi walifika Arusha kuhudhuria sherehe ya harusi ya rafiki yao Nelson. Walionekana kufurahishwa na mapokezi ambayo yalifanywa na kamati kabambe iliyokuwa ikiongozwa na mjomba wa Nelson. Kiukweli Nelson alifurahi sana baada ya kuona marafiki zake wamesitisha shughuli zao kwa muda na kuamua kujumuika nae katika siku yake ya harusi. Siku iliyofuata Nelson alizama ndani ya suti na Vivian ndani ya shela. Walipendeza sana, kila mtu alifurahia mwonekano wa bwana na bibi harusi. Tabasamu zilizokuwa zikichanua katika nyuso zao zilisababisha waonekane maridadi maradufu. Wapiga picha walionekana kuwaandama sana na kamera zao zilizokuwa zikitoa mwanga kila mara. Kanisa lilifurika kwasababu Nelson alikuwa ni mtu wa watu. Mchungaji Eugen Alvin ndie alieongoza misa takatifu ya Harusi ya Nelson na Vivian.
Nderemo na vifijo vilitawala katika nyumba ya Mungu baada ya Nelson na Vivian kumaliza kula kiapo cha ndoa. Ilikuwa ni siku ya kipekee sana katika maisha yao kwasababu walisubiriana kwa muda mrefu. Hadi misa ya harusi inakwisha, hakuna ndugu yeyote wa upande wa bibi harusi aliyekuwa amefika kanisani, hata mama yake hakuonekana. Baada ya harusi kufungwa msafara wa watumishi wa Mungu pamoja na ndugu jamaa na marafiki waliongozana hadi nyumbani kwa Nelson kwaajili ya kufanya uzinduzi wa nyumba yao ya kisasa. Uzinduzi ulikwenda sawa sawia na baada ya hapo watu waliongozana hadi ukumbini kwaajili ya kusheherekea tafrija fupi iliyokuwa imeandaliwa na bwana Nelson.
Msafara ulipofika ukumbini ndipo mama yake Vivian alifika akiwa ameongozana na mama mwingine wa makamo ingawa Vivian hakuweza kumfahamu. Kamati ilihakikisha kila mtu anakula na kunywa. Bwana na bibi harusi walizawadiwa zawadi nyingi kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki. Mama Vivian pamoja na mwenzie aliekuwa ameongozana nae walikabidhi zawadi ya pesa shilingi laki tano. Pamoja na zawadi hiyo aliyoitoa lakini alimnong’oneza mwanae na kumweleza kwamba kuna zawadi nyingine kubwa kamwandalia kwahiyo ipo siku atamkabidhi. Vivian alijiuliza ni zawadi gani hiyo mama yake alikuwa amemuandalia lakini hakupata jibu. Akilini aliijiuliza kwanini hakumkabidhi ile siku ya harusi, ambayo ndio ilikuwa maalumu kwaajili ya zawadi lakini napo aliishia kukosa jibu. Uchache wa watu waliohudhuria sharehe ya harusi kutoka kwa upande wa bibi harusi iliwashangaza watu wengi na hatimae kukaibuka minong’ono ya chini kwa chini. Watu walishindwa kuelewa ni kwanini mwitikio wao ulikuwa hafifu na pia kanisani hawakuonekana hata mmoja. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Jambo hilo lilimuumiza pia Nelson kwasababu alipata aibu kubwa mbele ya marafiki zake. Viti vilivyokuwa vimeandaliwa kwaajili ya watu watakaotoka ukweni vilikuwa wazi kabisa.Vivian alikuwa akilia ndani kwa ndani, alijilazimisha kutabasamu lakini hakuwa na raha hata kidogo. Alijua kabisa ilikuwa ni picha mbaya sana iliyokuwa inaonekana kwa Nelson mbele ya marafiki zake wengi waliokuwa ukumbini.
“Marafiki zangu watahisi pengine labda ndugu wa binti hawajaridhia mimi kumuoa vivian.” Nelson aliwaza, lakini alihishia kupuuzia.
Ratiba ya sherehe ilifika kwenye burudani ambapo mziki mzuri ulikuwa ukitumbuiza ukumbini. Marafiki wa Nelson kutoka nje ya nchi walikwenda kwa pamoja kwenye meza kuu kumpongeza rafiki yao kwa tukio la kipekee alilokuwa amelifanya katika maisha yake. Walipanga mstari na kupita kila mmoja kumpongeza Nelson. Alifurahi sana kuona marafiki zake wakimpongeza. Alisalimiana na kila mmoja lakini furaha yake ililipuka zaidi alipomuona rafiki yake anayeitwa Jacinthe Abroise ambae ni mzaliwa wa Nord-pas-de-calais Ufaransa lakini kwa sasa anaishi Florida nchini marekani. Nelson alipokuwa chuo kikuu cha Central Florida nchini Marekani aliamua kujifunza kozi ya lugha ya kifaransa. Rafiki huyu mfaransa alijitolea kwa dhati kumsaidia Nelson kuweza kuifahamu lugha hiyo kwa ufasaha. Kwa furaha walikumbatiana.
“Fèlicitations pour èntre arrive sain et sauf.” (Hongera kwa kufika salama.) Nelson alizungumza na mwanadada mrembo Jacinthe kwa lugha ya kifaransa wakati alipokuwa amemkumbatia.
“Je vous remercie.” (Asante.) Jacinthe alijibu.
“Felicitations pour votre marriage.” (hongera kwa kufunga harusi.) Jacinthe alimpongeza Nelson.
“Merci beaucoup, Jacinthe.” (asante sana, Jacinthe.) Nelson alisikika.
“Je vous souhaite tout le Bonheur possible.” (nawatakia wote furaha) Jacinthe alimtakia Nelson baraka katika ndoa yao.
“Bienvenenue.” (Karibu.) Nelson alizungumza na kumuacha Jacinthe akapita halafu akaendelea kusalimiana na marafiki zake wengine waliokuwa wakipita mmoja mmoja kwenye meza ya Nelson iliyokuwa mbele ya ukumbi.
Ilipofika usiku wa saa nne kamili sherehe ilifikia tamati. Nelson aliwashukuru watu wote waliokuwa wamehudhuria sherehe yake ya harusi. Aliagana na watu wote waliokuwa wamefika pale ukumbini, kila mmoja alianza kutawanyika kuondoka kuelekea majumbani kwao. Wageni wote walifikishwa hotelini kwa usafiri ambao ulikuwa umeandaliwa na kamati ya harusi. Nelson alipanda kwenye gari maalumu lililokuwa linawaendesha kwa siku hiyo na kuelekea nyumbani kwake. Hakutaka kabisa kusikia habari za fungate kwenye hoteli za kifahari aliona ni upotezaji wa pesa.
Alipanga fungate yake na mke wake wakafurahie katika nyumba yao mpya. Walifika nyumbani kwao salama na kufunguliwa geti na mlinzi ambae alikuwa ameanza kazi rasmi siku hiyo. Mioyo ya bwana na bibi harusi ilikuwa na furaha sana. Kila mmoja alikuwa anatamani wafike nyumbani ili waweze kujuana kwasababu hakuna hata mmoja aliekuwa amewahi kumjua mwenzie. Kwa ufupi Vivian hakuwahi kulala na mwanaume tangu kuzaliwa kwake na Nelson vilevile hakuwahi kulala na mwanamke. Kiukweli walikuwa wamefunga ndoa takatifu iliyokuwa na baraka mbele za Mungu.
Baada ya kufika nyumbani wadhamini wa ndoa pamoja na watu waliokuwa wamewasindikiza waliondoka na kumwacha Nelson na mke wake. Nelson alifurahi sana alipomkuta Vivian ni msichana ambae hakuwahi kuguswa hata siku moja. Pamoja na kwamba aliwahi kumdokeza kwamba hakuwahi kulala na mwanaume tangu kuzaliwa kwake lakini Nelson aliona ni kama utani, kwa kuwaza inawezekana vipi binti mrembo namna ile akaweza kushinda changamoto za wanaume wanaodondosha mate kwaajili yake. Moyo wa Nelson aliongeza mapenzi zaidi na zaidi, kwani alimuona ni mwanamke mwenye mapenzi ya dhati na pia mwenye msimamo wa hali ya juu. Maisha yao ya ndoa yalianza kwa furaha sana kwasababu ya upendo wa dhati uliokuwa umejengeka mioyoni mwao. Masiku kadhaa baadae Vivian alibainika kuwa na ujauzito baada ya kwenda hospitali kucheki afya yake kutokana na mabadiliko aliyokuwa ameyahisi mwilini mwake.
Furaha iliongezeka zaidi na zaidi kwasababu lilikuwa ni jambo jema sana kwao. Nelson alikuwa na shauku kubwa sana ya kuitwa baba halikadhalika Vivian nae alitamani kuitwa mama. Hivyo basi kiumbe kilichokuwa tumboni kilisubiriwa kwa hamu kubwa. Nelson alihakikisha mke wake anapata lishe bora kusudi mtoto atakaezaliwa awe na afya nzuri. Mimba ilizidi kukua vema huku Vivian akiendelea kuhudhuria kliniki mara kwa mara. Maisha yao yalizidi kuwa ya furaha kila kukicha changamoto pekee waliyokuwa wanakumbana nayo ni ndoto mbaya walizokuwa wakiota mara kwa mara. Kibaya zaidi walikuwa wanaota ndoto zinazofanana, jambo ambalo liliwakosesha raha kwa wakati mwingine.
Miezi tisa ilitimia ambapo Vivian alijifungua salama mtoto wa kiume. Nelson na mke wake walifurahi sana kumpata mtoto wa kiume. Ndugu jamaa na marafiki walifurahi pia baada ya kusikia zile habari njema. Walimpigia simu na wengine walidiriki kufika nyumbani kwao kuwapongeza. Sura ya mtoto ilifanana sana baba yake ingawa rangi ya ngozi yake ilifanana na ya mama yake. Kiukweli mtoto aliyezaliwa alikuwa ni mzuri sana na hilo lilithibitishwa na watu mbalimbali waliofanikiwa kumuona mtoto. Ilikuwa ni habari njema pia kwa mama Nelson kwasababu alikuwa ndie mjukuu wake wa kwanza. Mtoto alipewa jina la ‘Alaire’ jina ambalo chimbuko lake ni Ufaransa na lina maana ya furaha. Nelson na mke wake walikubaliana kumwita mwanao jina hilo kwasababu mtoto yule alikuwa ni furaha halisi mioyoni mwao. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Jina hilo liliwavutia pia watu wengi waliolisikia. Mtoto alipofikisha miezi mitatu, wanandugu pamoja na marafiki wa karibu walijumuika pamoja katika sherehe iliyokuwa imeandaliwa kwaajili ya ubatizo wa mtoto ambapo alipewa rasmi jina hilo la Alaire. Maisha ya wanandoa Nelson na Vivian yaliendelea kuwa ya furaha siku hadi siku. Upendo ulikuwa ndio nguzo yao. Vivian alimpenda sana mume wake, kila siku alikuwa akimuombea Mungu amfanyie wepesi katika shughuli zake. Nelson alipoumwa na yeye aljihisi kuumwa kutoka na upendo wa dhati aliokuwa nao kwa mume wake. Alimpenda mume wake kuliko kitu chochote. Kwa upendo aliokuwa nao kwa mume wake alikuwa tayari kuhatarisha maisha yake kutetea uhai wake.
Vivian aliona furaha yake haitaweza kupatikana kwingine isipokuwa kwa mume wake ambae alidiriki kumsubiri kwa muda mrefu. Alikubali kuchekwa na kudharauliwa na marafiki zake kwaajili ya msimamo wake juu ya Nelson na aliapa kumpenda hadi mwisho wa maisha yake. Vivian alimuona Nelson mpya kila siku kutoka na ufundi wa mapenzi aliokuwa anaushuhudia kwa mume wake kila kukicha. Kiukweli wanandoa hawa walikuwa wakipendana sana. Upendo wao uliwavutia hata wale ambao walikuwa hawajaingia katika majukumu ya ndoa. Siku zilizidi kusonga huku furaha ikizidi kuongezeka mioyoni mwao. Alaire alipofikisha miaka mitatu alipata mdogo wake ambae nae alikuwa wa kiume. Walimpa jina la ‘Mainard’ lenye maana ya ‘imara na thabiti.’
Mambo yalizidi kuwa mazuri katika familia ya Nelson kwasababu uchumi wa familia yao nao ulihimarika zaidi. Kiukweli baraka zilimiminika kwa kasi katika ndoa yao. Watoto waliendelea kukua kwa afya njema jambo ambalo lilizidisha furaha katika ndoa yao. Nelson na mke wake walipanga kuzaa watoto watatu tu katika ndoa yao. Waliona idadi hiyo ndiyo wataweza kuimudu katika kuwapatia lishe bora, malezi pamoja na elimu bora. Kwahiyo Vivian alikuwa anasubiri kuzaa mtoto mmoja afikie ukomo wa kuzaa. Mainard alipofikisha miaka mitatu alipata mdogo wake ambae nae alikuwa ni wa kiume. Nelson na mke wake walijaliwa sana watoto wa kiume. Mtoto wa tatu walimpa jina la Benedict ambalo maana yake ni aliyebarikiwa. Nelson alipendelea kuwapa watoto wake majina ambayo anafahamu maana yake. Nelson aliwapenda sana watoto wake. Alaire pamoja na Mainard waliandikishwa shule moja inayojulikana kwa jina la St Lucas’s academy nusery and primary school iliyopo ngulelo Arusha. Kitinda mimba alipofikisha umri wa shule alipelekwa shule nyingine iliyopo kisongo inayojulikana kwa jina St Margaret’s academy nusery and primary school. Wote walikuwa wanapelekwa na kurudishwa nyumbani kwa usafiri uliokuwa unatolewa shuleni. Alaire alionekana kuwa na akili kama baba yake kwani katika mtihani wa kumaliza darasa la saba alikuwa kwenye kumi bora ya kitaifa. Ingawa hata Mainard pia alionekana kuwa vizuri pia darasani lakini hakufikia uwezo wa kaka yake.
Vivian hakuajiriwa katika hoteli yeyote, ingawa alikuwa na diploma ya ‘hotel management’. Muda wake mwingi aliutumia katika kusimamia biashara kadhaa za mume wake, ikiwamo duka kubwa la nguo za aina zote kwa wanaume na wanawake lililokuwepo katikati ya jiji la Arusha. Siku moja wakati alipokuwa dukani kwake akiendelea na majukumu yake, alipokea simu kutoka kwa mama yake. Mama yake alimweleza kwamba siku inayofuata asubuhi na mapema anamwitaji nyumbani kuna jambo la muhimu sana anahitaji kumweleza. Vivian alijaribu kuwaza jambo ambalo mama yake alikuwa anamwitia lakini hakupata jibu. Ila alihisi pengine labda ni kwasababu mama yake kammisi kutokana na kwamba hajaonana nae kwa miaka kadhaa. Ukweli ni kwamba Vivian alikuwa akipendwa sana na mama yake na yeye alikuwa anafahamu hilo kwasababu amelelewa kama mayai.
Nafsi yake ilitawaliwa na wasiwasi mwingi kwasababu alikuwa ameshahisi kwamba mama yake ni mchawi. Aliporudi nyumban kwake mida ya jioni alimweleza mume wake kwamba ameitwa na mama yake siku inayofuata. Nelson hakuwa na kigugumizi juu ya suala hilo alimruhusu na pia alimpa salamu zake. Palipokucha siku yenyewe Vivian aliwasha gari lake aina ya Toyota RV4 na kwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwao. Alipofika alipokelewa vizuri sana na mama yake. Mama yake alimuonyesha ukarimu wa hali ya juu hadi mwenyewe akashangaa. Baada ya Vivian kupata kifungua kinywa cha maana, mama yake alimshika mkono kumnyanyua pale sebuleni walipokuwa wamekaa na kwenda chumbani. Vivian alizidi kuduwaa maongezi ya chumbani na mama yake ni maongezi gani hayo. Walipofika chumbani walikaa kitandani na maongezi yao yalianza.
“Vivian wewe ni mwanangu wa pekee niliebakiwa nae. Baba yako pamoja na ndugu zako tayari wameshakufa, ila pamoja na hayo yote uwepo wako unanifanya nisihisi hata chembe ya upweke moyoni mwangu kwasababu wewe ndio furaha yangu, hakika nakupenda sana mwanangu.” Vivian aliporomoshewa sifa na mama yake wakati walipokuwa wakizungumza chumbani kwa sauti ya chini kabisa.
“Nakupenda pia mama.”
“Unamkumbuka bibi yako Devota?” mama aliuliza.
“Ndio, namkumbuka.”
“Alipofikisha umri kama wa kwangu kunazawadi alinikabidhi. Alinieleza kwamba na mimi nitakapofikisha umri kama wake nikukabidhi na wewe mwanangu kwasabaabu alikuona unafaa kuendea kurithi mikoba yake. Na ile siku ya harusi yako nilikuahidi kwamba kuna zawadi nitakupatia. Unakumbuka hilo?” Mama Vivian alizungumza maneno mengi na mwishowe alimaliza kwa kumuuliza Vivian swali.
“Ndio nakumbuka.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Vizuri sana! zawadi yenyewe ni hii hapa naomba uipokee kwa mikono yako miwili.” Mama Vivian alizungumza huku akimkabidhi mwanae kibuyu ambacho kilikuwa kimezungukwa na hirizi nyingi zinazoning’inia.
Vivian aligoma kupokea na kuhitaji maelezo zaidi. “Kibuyu cha nini? Cha kazi gani?”
“Mwanangu huu ni uchawi ambao bibi yako alinikabidhi, lakini kabla hajapoteza maisha alinihusia kwamba nikupe wewe kwasababu ndio alikuchagua katika wajukuu zake wote.” Mama Vivian alizungumza huku akimtazama Vivian ambae alionekana kupoteza nguvu kutokana na maelezo ambayo alipatiwa na mama yake.
“Hapana mama sipo tayari kabisa kuingia katika mambo ya kichawi.” Vivian alizungumza huku machozi yakimlengalenga.
“Usijali mwanangu, hata mimi nilipokuwa nikikabidhiwa na bibi yako nilionyesha hali kama yako ya kukataa, lakini baada ya kukubali sikuwahi kujutia hata siku moja.”
“Kama nikikataa nitadhurika wacha tu nidhurike lakini sipo tayari kuingia katika mambo hayo kabisa.” Vivian aliendelea kumuonyesha mama yake msimamo wake.
Mama aliendelea kumbembeleza Vivian, lakini aligoma kata kata. Mama alidiriki hadi kumpigia mwanae magoti akubali lakini bado binti aliendelea kuonyesha msimamo wake. Vivian alibembelezwa kwa takribani masaa matatu lakini aligoma kabisa. Mwishowe mama yake alitamka maneno ambayo yalikuwa mazito kidogo lakini Vivian bado hakuonyesha kuogopa.
“We si unajifanya mjanja, sasa kitakacho kukuta ni kwamba utazika watoto wako wote pamoja na mume wako baada ya hapo wewe utachizika.” Mama Vivian alizungumza maneno hayo baada ya hapo alimalizia kwa kicheko cha kutisha. “Ahahaha! Ahahaha!”
Vivian alinyanyuka kwa hasira na kwenda kwenye gari lake na kuondoka. Maneno aliyoelezwa na mama yake yalimfanya ashindwe kujizuia kulia kwahiyo alilia tangu mwanzo wa safari yake hadi alipofika nyumbani kwake. Hakwenda kazini tena kwasababu aliona hataweza kwenda kufanya kazi kwa jinsi alivyokuwa amekasirishwa na mama yake. Alilia sana pamoja na kujuta kwanini alizaliwa. Alijiuliza atakuwa mtu wa namna gani endapo atajiingiza katika mambo ya kichawi, jamii itamchukuliaje, na pia mahusiano yake na Mungu yatakuwaje. Aliwaza sana Vivian huku akilia kwa uchungu sana. Siku nzima alijifungia chumbani mwake akilia sana kutokana na yale aliyoelezwa na mama yake.
“Hivi mume wangu akifahamu kwamba mimi nimchawi itakuwaje? No I can’t (hapana siwezi)” Vivian aliwaza huku akiendelea kulia kwa uchungu hadi mume wake aliporudi jioni akitokea kazini.
Nelson aligundua kuwa mke wake hakuwa sawa kwasababu macho yake yalikuwa mekundu halafu yamevimba kutokana na kulia sana. Alipojaribu kumuuliza kulikoni hayupo sawa alimdanganya kuwa amepata taharifa za msiba wa rafiki yake ambae walisoma nae chuo. Nelson alisikitika sana na kumpa pole mke wake na kumsihi anyamaze kwasababu kazi ya Mola haina makosa. Vivian alikataa kabisa kumshirikisha mume wake katika suala lile alilokuwa ameelezwa na mama yake kwa kuhofia kuwa upendo wa Nelson kwake unaweza ukapungua au hata wakaachana.
Vivian alizidi kuumia ndani kwa ndani. Alihisi kuchanganyikiwa pale alipokuwa akikumbuka alichoelezwa na mama yake baada ya kukataa kupokea uchawi. Lakini aliendelea kuona afadhali iwe hivyo kuliko kukubali kujiingiza katika mambo ambayo yatakuwa chukizo kwa Bwana Mungu wake. Waliendela kuota ndoto mbaya kila mara. Hakuna hata mmoja wao aliyekumbuka kumshirikisha mtumishi wa Mungu kuhusu njozi mbaya walizokuwa wakiziota kila mara. Nyumbani kwa Nelson kulikuwa na vitabu vingi sana vya hadithi na mambo mengine mengi. Biblia na vitabu vingine vilikuwepo pia kwenye listi ya vitabu vilivyopo nyumbani kwao. Nelson alikuwa ni mpenzi sana wa kusoma vitabu.
Hakuna siku hata moja inapita bila Nelson kushika kitabu cha hadithi mkononi mwake. Tabia hiyo alimuambukiza hadi mke wake nae akatokea kupenda kusoma vitabu. Magari yao yalikuwa yamejaa vitabu mbalimbali ambavyo huwa wanatembea navyo kuvisoma wawapo safarini, na pia vingine huwa wananunua wanapokuwa barabarani. Watoto nao walivutiwa na tabia ya wazazi wao kusoma vitabu kila mara kwahiyo na wao walijijengea tabia ya kujisomea vitabu vinavyozungumzia mambo mbalimbali hususani hadithi. Wakati mwingine Nelson alihisi kuwa wanaota ndoto mbaya kwasababu huwa wanasoma vitabu vya hadithi za kutisha sana ndio maana.
Ingawa Vivian tayari alikuwa ameshajua tatizo lipo wapi lakini alikuwa anaogopa kumshirikisha mume wake. Pamoja na sifa nzuri ya kujisomea vitabu kwa wanandoa hawa lakini walijisahau sana kwasababu hakuna hata mmoja wao aliekumbuka kunyanyua Biblia takatifu na kuisoma. Vitabu vya Mungu walivifunua siku mojamoja walipokuwa wakienda kanisani na baada ya hapo wanavirudisha kwenye kabati la vitabu hadi siku nyingine ya ibada ifike. Hawakuwa na tabia ya kusali kabisa wakati wa kulala wala kuamka na hata wakati wa kula hawakuwa na utaratibu wa kumshirikisha Mungu.
Watoto nao walifuata nyayo zao, hawakuwa na msingi mzuri wa imani ndani yao. Wanandoa hawa wangejenga tabia ya kumuheshimu Mungu kwa kila jambo wafanyalo, watoto pia wangeiga ile tabia kama ambavyo waliiga tabia ya kusoma vitabu kutoka kwao. Tabia hiyo ilisababisha mizengwe ya mama mkwe isiishe katika familia yao.
***********CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Miezi sita baadae Mama Vivian alimchukua mwanae pamoja na mume wake na kuwapeleka kuzimu kwaajili ya kushuhudia sherehe ya mtoto wao Alaire akiliwa nyama. Aliamua kutekeleza agizo lake kwa mwanae kwamba watoto wote watakufa pamoja na mume wake na pia yeye atakuwa kichaa. Vivian na Nelson walifikishwa kuzimu na kupokelewa na nyimbo ambazo zilikuwa ni za kutisha sana. Walishindwa kuelewa walipokuwa lakini kilichokuwa kinaendelea kilikuwa kinawatisha. Vichwa vyao vilikuwa vikitazama huku na kule kuangalia walipokuwepo lakini walishindwa kubaini. Wote walijawa na hofu mioyoni mwao.
Baada ya kuona kwamba kule panatisha walianza kulia kwa huruma nyingi. Walikaa pembeni ya kiti cha malkia wa kuzimu ambae ndie mama yake na Vivian. Zilikuwa zikimbwa nyimbo ambazo hawakuelewa maana yake kwasababu lugha iliyotumika haikueleweka. Uchangamfu wa watu wa huko uliashiria kwamba kulikuwa na sherehe kubwa. Baada ya dakika kadhaa walimuona mwanao Alaire ameletwa mbele yao ambapo kulikuwa na meza kubwa ambayo ilikuwa imetapakaa damu. Alipandishwa juu ya meza hiyo na kulazwa kwa mgongo. Muda huohuo sauti iliyoambatana na kicheko kikali cha kutisha huku ikifuatiwa na sauti ya bundi ilisikika.
“Achinjwee.. Ahahahaha! Ahahahaha!”
Mwanaume mmoja ambae alikuwa ameshika kisu kikali alisogea alipokuwa amelazwa Alaire na kumchinja kama kuku. Vivian na Nelson kwa wakati huo walikuwa wakilia sana pindi mtoto wao alipokuwa akichinjwa mbele yao. Walitamani kunyanyuka na kwenda kuzuia mwanao asichinjwe lakini hawakuweza kunyanyuka kwani miguu yao ilikuwa mizito sana. Damu yote ilikingwa na baada ya hapo walianza kunywa kwa kuigombania. Vivian na mumewe walinyweshwa damu ya mwanao, nyama pia walikula, ingawa walifanya hayo yote kwa kulazimishwa. Sherehe ya kumla Alaire ilipokwisha kule kuzimu Nelson na Vivian walirudishwa duniani.
***********
Nelson na Vivian walizinduka kwa pamoja usingizini huku wakihema kwa pupa. Nelson aliwasha taa na kuangalia saa ya ukutani inaonyesha ni saa nane na nusu usiku. Ndoto aliyokuwa ameiota ilikuwa ni ya kutisha sana. Vivian alishindwa kuzungumza chochote kwasababu moyo wake ulikuwa ukienda kasi sana. Alikuwa anahema mithili ya mtu alitoka kufukuzwa muda mfupi uliopita.
“Duuh! afadhali ni ndoto.” Nelson alizungumza.
“Kwani umeota ndoto gani?” Vivian alimuuliza mume wake alichokuwa amekiota huku akionekana kukosa amani kabisa.
Nelson alimsimulia mke wake kila kitu. Vivian alishtuka sana kwasababu alichokuwa amekiota ndicho alichokuwa anasimuliwa. Kwamaana hiyo yule Nelson aliekuwa nae ndotoni ndie mume wake na mtoto aliekuwa akiliwa nyama kuzimu ndie mwanae. Mwili wake uliishiwa nguvu ghafla. Nelson alipata wazo la kwenda chumbani kwa wanae kwenda kuangalia wapo katika hali gani. Alifungua mlango taratibu na kwenda kumwamsha Alaire ambae wamemuota muda mfupi uliopita.
“Alaire! Alaire!” baba alimwita mwanae kipenzi.
“Kimya.”
“Alaire!” Nelson aliendelea kuita huku akimtingisha mwanae ili aweze kuamka lakini kimya kiliendelea kutawala. Nelson aliweka mkono wake juu ya kifua cha mwanae kusikilizia mapigo ya moyo lakini aligundua kuwa mtoto amefariki. Alishindwa kujizuia na kuanza kulia kama mtoto mdogo. Alishindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea katika familia yake ni kitu gani. Alirudi chumbani kwake baada ya kuhakikisha kwamba Mainard na Benedict wao wapo sawa. Alipofika chumbani kwake alimweleza mke wake kwamba Alaire amefariki dunia. Vivian alianza kuangua kilio cha uchungu sana usiku huo wa manane. Moyo wake ulijawa na hasira sana kwasababu alijua fika tukio lile lilifanywa na mama yake. Harakaharaka walimpakia kwenye gari na kumuwaisha hospitali ya Mount Meru ambapo huko napo daktari alithibitisha amefariki.
Kifo cha mtoto wao wa kwanza kilikuwa ni pigo kubwa sana katika familia yao. Ni mtoto ambae walimpenda sana kwasababu alikuwa na tabia za kipekee. Mainard na Benedict walimlilia sana kaka yao kwasababu walikuwa wanampenda sana. Kiukweli kifo cha Alaire kiliwaumiza watu wengi sana kutokana na umri wake bado ulikuwa mdogo halafu isitoshe kapoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha sana. Baada ya siku kadhaa mtoto alizikwa na maisha yaliendelea kama kawaida. Japokuwa moyo wa Nelson na Vivian ulibaki na majozi makubwa sana ya kupotelewa na mtoto wao mpendwa. Alaire aliacha maumivu makubwa ndani ya mioyo ya wazazi wake. Haikuwa kazi rahisi kwa Nelson na mke wake kumsahau mwanao mpendwa. Walikosa raha, muda mwingi walinyong’onyea kwasababu furaha yao ilikuwa imepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Utata wa kifo cha mtoto wao mpendwa pamoja na ndoto za kutisha zilisababisha wawe watu wa kukosa raha muda wote. Amani ndani ya mioyo yao ilitoweka pindi walipokuwa wakiona giza linaingia. Kiukweli kwa jinsi ambavyo walikuwa wanauchukia usiku wangekuwa na uwezo wa kuzuia usiku usiingie basi wangefanya hivyo ili kujinusuru na ndoto mbaya za kutisha kila wakati. Mara zingine Nelson na mke wake walikuwa wanaamua kucheza karata hadi panakucha ili tu wasifumbe macho yao na kuangukia katika ndoto zilizosheheni umauti ndani yake. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Walidiriki kuchukua biblia na kuweka chini ya mito yao kama kinga lakini haikuwa suluhisho kwani ndoto mbaya ziliendelea kama kawaida. Kilichokuwa kinawakondesha ni kwamba walikuwa wanaota ndoto ambazo zinaukweli mtupu ndani yake. Walizidi kuwa watu wa mashaka mashaka kila mara. Bosi kazini alishuhudia ufanisi wa Nelson ukishuka siku hadi siku, kwahiyo alimuandikia barua kwaajili ya onyo kusudi aweze kujirekebisha. Furaha iliyokuwa imetawala katika ndoa yao iliendelea kutoweka. Ingawa Nelson alikuwa katika wakati mgumu kuhusu mambo waliyokuwa wanapitia katika ndoa yao lakini mkewe Vivian ndie aliekuwa akipata wakati mgumu zaidi kwasababu alikuwa anafahamu dhahiri aliekuwa anawafanyia vile ni nani na pia makusudio yake yalikuwa ni yapi. Alizidi kuwaza na kujiuliza inamana ni kweli mama yake atawauwa watoto wake wote halafu na mume wake atakufa? aliishia kudondokwa na machozi kutokana na mambo mazito aliyokuwa anapitia.
Moyo ulimuuma sana, alimuona mama yake ni zaidi ya shetani. Aliwaza inawezekana vipi mama aliyemzaa anamfanyia mambo ya kinyama namna ile. Baada ya kuwaza sana siku moja alimua kumuendea mama yake kumbembeleza kusudi asiendelee kuiangamiza familia yake. Alipofika nyumbani kwao alimkuta mama yake ambapo alianza kuzungumza nae kwa upole na moyo wa huruma ili mama yake asiendelee kumtendea yale aliyokuwa amemtamkia baada ya kukataa kupokea uchawi. Vivian alilia sana huku akimpigia mama yake magoti aweze kubadili mawazo yake lakini mama aliendelea kushikilia msimamo wake wa awali.
Alimweleza kwamba njia pekee ya kukwepa vifo vile ni kukubali kupokea uchawi. Tena alimsihi afanye haraka mno kwasababu vifo vingine vitafuata siku sio nyingi. Moyo wa Vivian uliendelea kuwa mgumu kupokea uchawi aliokuwa anapewa na mama yake. Aliona kuliko awe mchawi ni bora yale aliyokuwa anaelezwa na mama yake yaendelee kutokea. Baada ya Vivian kuona kwamba mama yake amekataa kubadili mawazo yake aliamua kuondoka na kurudi nyumbani kwake huku akiwa na msongo mwingi wa mawazo. Siku zilizidi kusonga mwili wa Vivian ulizidi kudhoofu kutokana na mawazo. Alikonda sana hadi majirani wakawa wanashangaa kwanini alipungua ghafla wakati alikuwa na mwili mzuri wa kunawiri. Ukweli ni kwamba Vivian furaha iliyokuwa imepotea ndani ya moyo wake ilisababisha akose hamu ya kula na pia hamu ya kunywa ilitoweka vilevile. Hakuona furaha ya kuishi tena hapa duniani, alitamani kufa ili aweze kukwepa majaribu mazito aliyokuwa anapitia. Mume wake ambae ndie alikuwa furaha yake nae hakuwa hata na chembe ya furaha moyoni mwake. Muda mwingi walikuwa ni watu wa huzuni.
Nelson alipata wazo la kuuza nyumba waliyokuwa wanaishi akiamini kwamba pengine ndiyo iliyokuwa chanzo cha matatizo. Vivian hakulipokea suala la kuuza nyumba kwa furaha hata kidogo kwasababu alijua nyumba haikuwa na tatizo lolote isipokuwa mama yake mzazi. Alijaribu kumshawishi mume wake ili wasiweze kuuza ile nyumba lakini Nelson aligoma kumwelewa kabisa. Kwahiyo nyumba ilitafutiwa madalali na kuuzwa harakaharaka. Jamii iliyokuwa inamzunguka Nelson ilimshangaa sana kwa uamuzi wa kuamua kuuza nyumba chapuchapu tena kwa bei rahisi. Hakuwa na namna kwasababu alikuwa amechoshwa na ndoto mbaya za kila mara.
Mjomba yake pamoja na mama yake walipata taharifa za kuuzwa kwa nyumba ya kijana wao lakini hawakuwa na namna ya kuzuia kwasababu walikuwa wanafahamu matatizo yaliyokuwa yanamsumbua. Kwahiyo walikaa kimya wakiamini kwamba huwenda ni kweli nyumba ile ilikuwa na matatizo kwasababu wao wenyewe walishindwa kuelewa tatizo lipo wapi. Baada ya nyumba kuuzwa walinunua nyumba nyingine maeneo ya ‘Kijenge mwanama.’ Ila kibaya zaidi walipohamia katika nyumba ya pili katika eneo la mbali na pale walipokuwa wanaishi awali, mambo ndio yakazidi kuwa mabaya, njozi mbaya za kutisha ndio zilichachamaa. Ilifika pabaya Nelson akawa anaandamwa na ndoto yupo ndani ya jeneza anazikwa huku mke wake pamoja na ndugu zake wakimlilia sana.
Nelson alihisi kuwa anakufa kwasababu ndoto zote za kutisha alizokuwa anaota mara kwa mara huwa zilikuwa zinatimia, kwahiyo alijua moja kwa moja habari yake ndio inakwisha. Chakushangaza ni kwamba ndoto hiyo ya kuzikwa aliiota kwa mara tatu mfululizo. Alipoteza matumaini ya kuishi kabisa, hakujua cha kufanya ni kitu gani ili aweze kunusuru roho yake. Hadi kufikia muda ule alikuwa hajawai kumweleza rafiki yake hata mmoja kuhusu magumu aliyokuwa anapitia katika maisha yake. Lakini kutokana na paniki aliyoipata kutokana na ndoto ya mauti iliyokuwa inamwandama kila mara aliamua amshirikishe rafiki yake Lucas ili aweze kupata mchango wa mawazo.
Kwahiyo baada ya Nelson kufika kazini kwake siku moja aliamua kumwita rafiki yake ofisini kwake ili aweze kumshirikisha jambo lile. Alimpigia simu ya mezani na kumuomba afike ofisini kwake mara moja. Lucas alimkubalia na kumuahidi kwamba atakwenda baada ya dakika kumi na tato kwasababu kuna barua pepe (email) za wateja alikuwa anazijibu. Baada ya muda Lucas alifika katika ofisi ya Nelson ili aweze kumsikiliza. Wakati walipokuwa wakisalimiana simu ya mkononi ya Nelson iliita, na kusababisha aipokee kwanza ndipo afanye mazungumzo na rafiki yake.
“Haloo.” Sauti ya kiume ilisikikaa upande wa pili.
“Yes hello!” Nelson aliitika.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
“Naongea na mzazi wa Mainard.” Sauti ya mtu ambae hakuwa amejitambulisha iliendelea kusikika upande wa pili.
“Naam!”
“Habari yako.”
“Njema tu.”
“Unaongea na mwalimu Peter, mkuu wa shule ya St Lucas’s nusery and primary school.”
“Sawa”
“Nimekupigia simu kukujuza kwamba mwanao amedondoka ghafla darasani na kupoteza fahamu kwahiyo tumemuwaisha hospitali ya Father babu.”
Asante kwa taharifa, nitafika hospitali baada ya muda mfupi.” Nelson alizungumza kwa ujasiri lakini habari zile zilimshtua sana.
Maongezi ya Nelson na rafiki yake yalishindwa kufanyika kutokana na matatizo yaliyokuwa yamejitokeza kwahiyo alimuomba wazungumze kwa wakati mwingine kusudi aweze kuwahi hospitali kuangalia maendeleo ya mwanae. Alipanda kwenye gari lake baada ya kuomba ruhusa kazini na kuondoka kuelekea hospitali. Alipofika kwenye geti la hospitali ya Father babu alipishana na gari la wagonjwa likitoka. Alifika mapokezi na kujieleza kwamba ndie mzazi wa mwanafunzi aliyefikishwa hospitali hapo kutokea shule ya St Lucas academy.
Alijulishwa kwamba mwanae kaamishiwa hospitali ya rufaa ya mount Meru baada ya hali yake kuonekana kuendelea kuwa mbaya. Nelson alihisi kuchanganyikiwa kwasababu hakufahamu mwanae alikuwa amekubwa na tatizo gani. Alimuaga dada aliekuwa mapokezi na kuanza kutoka kuelekea kwenye gari lake ili aweze kuwahi hospitali aliyopelekwa mwanane. Wakati alipokuwa anafungua mlango wa gari lake alisikia sauti iliyokuwa inatokea nyuma yake ikimwita.
“Nelson! Nelson!”
Aligeuza shingo yake na kukutana uso kwa uso na kijana ambae amevalia sare za daktari. Kumbukumbu zilimjia kwamba mtu aliekuwa anamwita alisomaga nae katika shule ya sekondari Ilboru miaka kadhaa iliyopita.
“Habari za masiku Edward.” Nelson alisalimia.
“Nzuri tu kaka! Unaonekana unamawazo sana yani nimekuita karibu mara nane lakini husikii.”
“Acha tu aisee, kichwa changu kinamawazo mengi sana.”
“Mawazo ya nini tena ndugu yangu.” daktari aliuliza.
“Nimekuja kumwangalia mtoto wangu aliyefikishwa hospitalini hapa leo asubuhi lakini nimepata taharifa kwamba amehamishiwa hospitali ya Mount meru baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya.”
“Mwanao ndie yule wa St Lucas academy?”
“Ndio.”
“Daah! Pole sana kwasababu mimi ndie niliyempokea mtoto huyo na kuruhusu pia aamishwe hospitali baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya. Ila usijali atapona.” Daktari alizungumza na kuishia kumtia moyo Nelson asikate tamaa.
“Kwani umebaini anasumbuliwa na nini?”
“Mwanao anasumbuliwa na tatizo la kuishiwa damu. Kasi ya kuishiwa damu katika mwili wake nimeufananisha na ugonjwa mmoja kitaalamu unaitwa ‘Anemia’ ambao hutokea pale ambapo seli nyekundu za damu zinakuwa hazizalishwi katika kiwango kinachohitajika. Jopo la madaktari katika hospitali yetu tumejaribu kumfanyia uchunguzi ili tuweze kufahamu sababu iliyokuwa inapelekea yeye kuishiwa damu kwa kiwango kikubwa namna ile lakini kwa bahati mbaya tumeshindwa kwasababu vipimo vyote tulivyomfanyia vilionyesha yupo sawa ingawa uhitaji wa damu upo palepale.” Jambo hilo limetushangaza sana na ndipo tukaamua kumuhamisha hospitali.” Daktari alizungumza kwa kirefu zaidi kuweza kumuelewesha bwana Nelson.
Maneno yale yalisababisha Nelson ahisi kuishiwa nguvu kwasababu alijua kwamba kama ugonjwa unaomsumbua mwanae umeshindwa kubainika inamana bado ni yale mauzauza yanaendelea katika familia yake. Baada ya mazungumzo hayo Nelson alimshukuru daktari yule halafu akawasha gari lake akaelekea hospitali ya Mount Meru.
Baada ya dakika 15 aliliegesha gari lake katika maegesho ya hospitali. Aliteremka harakaharaka na kwenda mapokezi kupata utaratibu wa wodi aliyofikia mwanae Mainard.
“Mwanao anaitwa nani?” muhudumu wa mapokezi alimuuliza Nelson swali.
“Mainard Nelson, amehamishiwa hapa muda mfupi uliopita kutoka hospitali ya Father Babu.”
“Usijali!” muudumu alijibu wakati anaingiza taharifa zile katika kompyuta iliyokuwa mbele yake. Baada ya sekunde chache alimweleza kwamba.
“Mainard Nelson amelazwa wodi namba 107, ghorofa ya tatu, wodi ya wagonjwa mahututi” Muudumu alimpa Nelson maelekezo ya kufika wodini. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Nelson alifuata maelekezo na kufanikiwa kufika katika wodi aliyokuwa ameelekezwa, lakini mlangoni alikutana na kibao kilichoandikwa ‘Intensive care unite’ ICU.(chumba cha uwangalizi maalumu) Alikaa nje ya wodi kwa muda kama wa dakika kumi ambapo alitoka daktari mmoja. Nelson alijitambulisha kwa daktari yule ili aweze kufahamu hali ya mwanae kwa wakati ule ilikuwa inaendelea vipi.
“Tumemfanyia uchunguzi wa kiafya mwanao lakini tumeshindwa kubaini tatizo halisi linalopelekea kuishiwa na damu kwa kasi kubwa. ila tunaendelea na uchunguzi zaidi ili tuweze kubaini tatizo.
“Vipi daktari, mwanangu atapona kweli?” Nelson alizungumza huku akijifuta machozi yaliyoanza kumdondoka baada ya kushindwa kujizuia.
“Usijali, atapona.” Daktari alimtia moyo Nelson.
“Vipi ninaweza kuingia kumuona kwa sasa?”
“Hapana kwa sasa haitawezekana kwasababu yupo chini ya uwangalizi maalumu.”Daktari alimjibu Nelson.
Nelson aliamua kurudi nyumbani ambapo alifika na kumjulisha mke wake matatizo yaliyokuwa yamemkumba mtoto wao. Vivian aliangua kilio utafikiri taharifa alizopewa ni za kifo cha mwanae. Alijua kwamba mama yake ndio alikuwa anayafanya yale kama njia ya kumkomesha baada ya kukataa kupokea uchawi. Matumaini yake yalipotea kabisa baada ya kusikia kwamba mwanae anasumbuliwa na tatizo la kuishiwa damu, mbaya zaidi madaktari wameshindwa kubaini sababu iliyokuwa inapelekea mtoto kuishiwa damu. Wakati Nelson alipokuwa anambembeleza mke wake alipokea simu kutoka kwa Lucas ambae alikuwa anamuuliza maendeleo ya mtoto aliekwenda kumwangalia hospitali. Nelson aliona asimweleze kwa njia ya simu aliamua kumwomba wakutane jioni ya siku hiyo ili waweze kuzungumza zaidi.
Ilipofika mida ya saa kumi na moja jioni Nelson alikutana na Lucas katika baa moja inayojulikana kwa jina la I.Q bar iliyopo Kijenge mwanama. Nelson alimweleza rafiki yake matatizo yaliyokuwa yanamsumbua, pamoja na hali ya mwanae hospitali. Lucas alisikitika sana baada ya kusikia mikasa aliyokuwa anaelezwa na rafiki yake. Mwishowe alimshauri waende kwa mganga kutafuta suluhisho la matatizo. Nelson alionekana kuwa mbishi sana baada ya kuambiwa mambo ya kwa mganga kwasababu hakuwahi kwenda hata siku moja na pia isitoshe haamini kabisa mambo ya waganga.
Ila alipokumbuka hali ya mwanae hospitali na isitoshe madaktari wameshindwa kubaini sababu ya mtoto kuishiwa damu, aliona wazo la kwenda kwa mganga alilodokezwa na rafiki yake lilikuwa na tija sana kwake. Kwahiyo aliamua kukubaliana na wazo la kwenda kwa mganga kesho yake asubuhi na mapema. Nelson aliagana na Lucas na kila mmoja alikwenda nyumbani kwake. Nelson alipofika kwake alimshirikisha mke wake wazo alilokuwa amelipata kutoka kwa Lucas. Vivian hakuonyesha kupinga kwasababu alikuwa anahitaji mtoto wake aweze kupona kwahiyo alimruhusu kwa moyo mmoja aende kwa mganga. Palipokucha Vivian yeye alielekea hospitali na Nelson alikwenda kukutana na rafiki yake ili waweze kwenda walipokuwa wamekubaliana.
***********
Baada ya Nelson kukutana na rafiki yake walianza safari ya kuelekea kwa mganga. Wakati walipokuwa barabarani Nelson alihisi maumivu makali ya kichwa lakini hakujali aliendelea kuendesha gari lake kwa kasi zaidi ili waweze kufika kwa mganga mapema. Maumivu ya kichwa yalizidi hatimae Nelson aliegesha gari lake kando kando ya barabara na kuingia katika duka moja la dawa kwaajili ya kununua hedex ili kutuliza maumivu makali ya kichwa aliyokuwa anahisi. Alipewa dawa na kumeza palepale na baada ya hapo alirudi kwenye gari kuendelea na safari. Waliendelea na safari huku akizidi kulalama maumivu ya kichwa lakini rafiki yake alimtia moyo ajikaze kiume kwasababu walikuwa wamekaribia kufika. Kichwa kilimuuma Nelson hadi akahisi giza mbele yake wakati gari lilipokuwa kwenye mwendo mkali. Nelson alishindwa kulimudu gari na hatimae liligongana uso kwa uso na gari lingine la mizigo. CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com
Ilitokea ajali mbaya sana kwasababu Lucas alipoteza maisha palepale na hali ya Nelson ilikuwa ni mbaya sana. Mashuhuda wa ajali ile walipoojiwa na baadhi ya vyombo vya habari kama vile redio Sunrise, walithibitisha kwamba kosa lilikuwa ni la dereva wa gari dogo ambae alitoka kwenye saiti yake na kulifuata gari la mizigo wakati wote walipokuwa kwenye mwendo mkali. Polisi waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka mwochwari. Nelson alipakiwa katika gari la wagonjwa (ambulance) na kuwaishwa hospitali ya Mount Meru. Hali yake ilikuwa ni mbaya sana kutokana na damu nyingi zilizomvuja kutoka katika majeraha mengi aliyokuwa ameyapata mwilini mwake ikiwamo la kupasuka kichwa.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment