Search This Blog

SHEREHE KUZIMU - 2

 







    Simulizi : Sherehe Kuzimu

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Watu waliofanikiwa kufika katika eneo la ajali walionekana kukata tamaa kutokana na hali ya Nelson ilivyokuwa mbaya. Majeruhi wawili waliokuwepo kwenye fuso, wao walionekana kupata majeraha madogo madogo. Wote walipakiwa katika gari la wagonjwa ili kuweza kuwaishwa hospitali. Kiukweli gari la wagonjwa lilikwenda kwa mwendo mkali huku likipiga king’ora ili liweze kupishwa na magari mengine kusudi waweze kuwahi hospitali kwasababu hali ya majeruhi mmoja ilikuwa ni ya kukatisha tamaa. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yanadunda kwa mbali sana. Damu zilikuwa zinaendelea kumvuja kwa wingi katika mwili wake. Kwa bahati nzuri Mungu alisaidia gari la wagonjwa lilifika hospitali baada ya muda mfupi kwasababu lilikuwa likikimbia sana. Dereva wa gari lile aliliegesha karibu kabisa na mlango wa kuingia ndani ya hospitali. Kwa haraka haraka Nelson alipakiwa katika machela na kukimbizwa wodini huku akionekana kupiga kwikwi mfululizo. Baada ya Nelson kulazwa kitandani alianza kukakamaa huku akirusha mateke huku na kule. Madaktari walijua pengine ndio alikuwa anakata roho kwasababu alionyesha dalili zote za kufikwa na umauti.

    ************

    Vivia alipotoka nyumbani alinyooka moja kwa moja hadi wodi aliyokuwa amelazwa mwanae. Alikuta hali ya mwanae inaendelea vizuri kidogo kwasababu hali yake ilikuwa ni ya kuridhisha kwa kiasi fulani tofauti na alipofikishwa hospitalini hapo jana yake. Alijaribu kumuuliza daktari kama wamefanikiwa kugundua sababu inayopelekea mtoto kuishiwa damu lakini alijibiwa kwamba bado hawajafanikiwa kubaini tatizo. Pia daktari alimweleza mama Vivian kwamba hadi kufikia muda ule mtoto alikuwa ameshatumia chupa 24 za damu, jambo ambalo si la kawaida. Vivian alishangaa sana baada ya kusikia yale maelezo aliyokuwa anaelezwa na daktari na kujiuliza inawezekana vipi mtoto akatumia kiwango kikubwa cha damu namna ile halafu sababu ya kuishiwa damu isijulikane.

    “Tumemfanyia mwanao vipimo vya kila aina lakini hata na sisi tumeshangaa mno kushindwa kufahamu sababu ya mtoto kuishiwa damu. Hata hivyo tunasubiri leo hii tutapata ugeni wa madaktari bingwa kutoka hospitali ya muhimbili, watakapofika tutahitaji msaada wao ili waweze kutusaidia kwasababu tumegundua kuwa hili tatizo lipo nje ya uwezo wetu.” Maneno ya daktari kwa kiasi fulani yalileta nuru ya matumaini moyoni mwa Vivian baada ya kusikia kwamba kuna ugeni wa madaktari bigwa kutoka hospitali ya taifa.

    “Sasa dokta kama hali ndio hiyo mwanangu atapona kweli?” Vivian alihoji.

    “Atapona kabisa usiwe na wasiwasi, Mungu ni mwema.” Dokta aliendelea kumtia moyo Vivian kwasababu maneno yake yalionyesha kukata tamaa.

    Baada ya maongezi ya muda refu kidogo, mlango wa wodi uligongwa na liliingia kundi kubwa la madaktari.

    “Samahani Anti, embu tunaomba utupishe kwanza tufanye kazi.” Daktari mmoja mwanamke aliyeingia na lile kundi la madaktari alizungumza kumtaka Vivian awapishe kwanza ili waweze kumfanyia mtoto uchunguzi wa kitaalamu zaidi.

    Vivian alitoka nje taratibu kupisha jopo la madaktari lifanye kazi yao. Alihisi huwenda ndio wale madaktari alioelezwa na daktari Joseph, kwamba watatoka hospitali ya taifa kwaajili ya kuwafanyia uchunguzi wa kina wagonjwa sugu. Baada ya Vivian kufika nje ya wodi, alikumbuka kuwa simu yake ya mkononi aliiacha kwenye gari, kwahiyo aliamua kuifuata ili aweze kuwasiliana na mume wake ajaribu kumuuliza wamefikiwa wapi katika safari ya kwa mganga. Matumaini ya mwanae kupona kwa njia ya hospitali aliona ni ngumu kwasababu aligundua kuwa yale matatizo yalikuwa yanasababishwa na mama yake.

    Aliona tumaini la mtoto wake kupona litapatikana kwa kupitia njia ambayo mume wake alikuwa ameichagua. Hapo ndipo alipotamani kufanya mawasiliano ya haraka na mume wake ili aweze kufahamu kilichokuwa kikiendelea. Alipofika kwenye gari alikuta simu yake ina missed call kadhaa kutoka kwa mjomba wake Nelson. Alipuuza akaona labda anamuuliza maendeleo ya Mainard hapo hospitali kwasababu waliwasiliana asubuhi na kumweleza kwamba anakwenda hospitali. Alimpigia simu Nelson lakini hakumpata hewani, akahisi labda ni masuala ya mtandao kwahiyo akampigia kwa mara nyingine zaidi na zaidi lakini hakufanikiwa kumpata hewani.

    Baada ya kujaribu kumtafuita hewani kwa zaidi ya mara nne ndipo alipata uwakika kuwa simu ya mume wake haikuwa hewani. Alijaribu kujiuliza sababu iliyopelekea simu ya Nelson kutokuwa hewani kwa wakati ule lakini hakupata jibu sahihi kwasababu haikuwa jambo la kawaida simu ya mume wake kuzimwa. Alifungua mlango wa gari lake ili aweze kuelekea kwenye mgahawa uliopo pale hospitali kupata kifungua kinywa kwasababu alipoondoka nyumbani asubuhi hakuweka kitu chochote tumboni.

    Alikwenda na simu yake kusudi mjomba wake Nelson atakapojaribu kumpigia kwa mara nyingine aweze kumpata kwa urahisi. Baada ya kufika mgahawani aliagiza chai ya maziwa na chapati mbili. Muda huohuo alipewa alichoagiza na kuanza kula huku akiangalia runinga iliyokuwepo pale mgahawani. Alimaliza kula na kulipa pesa, wakati alipokuwa ananyanyuka kwenye kiti ili aweze kuondoka alisikia tangazo la breaking news (habari zilizotufikia hivi punde.) kwahiyo aliamua kusikiliza wakati amesimama.

    “Habari za wakati huu mpenzi mtazamaji wa ITV mtangazaji wako ni mimi Miriam Amani. Taarifa zilizotufikia hivi punde zinasema kwamba kuna ajali mbaya sana imetokea mkoni arusha iliyohusisha gari dogo aina ya Toyota Brevix zenye namba za usajili T 128 QVS lililogongana uso kwa uso na lori la mizigo aina ya Fuso lenye namba za usajili T 302 QAB. Kwa mujibu wa ripota wetu kutokea eneo la tukio ametueleza kwamba mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Lucas Alfred amepoteza maisha papo hapo na majeruhi watatu wamewahishwa katika hospitali ya Mount Meru huku hali ya mmoja ikiwa ni mbaya sana. Tunajaribu kumtafuta kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa arusha bwana Fredrick Ludovick ili tuweze kupata taharifa za uwakika zaidi. Ahsante kwa kuitazama ITV.”

    Vivian aliposikia habari hiyo alihisi kama kuchanganyikiwa. Namba za usajili ya gari dogo lililohusika kwenye ajali iliweza kumfahamisha kwamba ni mume wake ndie aliyekuwa amepata ajali. Alianza kuangua kilio kama mfiwa jambo ambalo liliwashtua watu waliokuwa pale mgahawani kwa kushindwa kuelewa kwamba amekumbwa na kitu gani. Walinyanyuka wanawake wawili waliokuwa wamekaa kwenye viti na kwenda kumshika na kumpeleka nje kumbembeleza. Walikwenda nae hadi kwenye gadeni iliyokuwepo pale hospitali ili waweze kufahamu mwenzao amepatwa na nini kwasababu ameanza kulia ghafla.

    Vivian alikuwa analia kwa huruma sana kiasi kwamba kila mtu alionekana kumuonea huruma japokuwa hawakufahamu amekumbwa na mkasa gani. Wale wasamaria wema walipomfikisha Vivian kwenye gadeni, wakati wanamkalisha ili waweze kumuuliza kilichokuwa kinamliza ghafla alipoteza fahamu. Mmoja wa wale wanawake alikwenda kumuita nesi ambapo walimnyanyua na kumkimbiza wodini. Daktari alimfanyia vipimo vya harakaharaka na kubaini kuwa presha yake ipo juu sana.

    “Huyu anatakiwa apelekwe ICU haraka sana kwasababu presha yake ni 180/110 mm Hg, ni hatari sana kwasababu ipo kwenye ‘hypertensive crisis’ anahitaji uangalizi maalumu.” Daktari alizungumza na nesi kwa utaalamu zaidi.

    “Sawa dokta.” Nesi aliitikia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Baada ya muda mfupi Vivian alifikishwa katika kitengo cha uangalizi maalumu kwaajili ya kupatiwa matibabu zaidi. Madaktari walionekana kumuudumia kwa haraka sana kwasababu hali yake ilikuwa ni mbaya mno. Wale wasamaria wema waliposikia kwamba Vivian anapelekwa ICU waliamua kupekua kwenye simu yake kutafuta namba ya kuijulisha hali iliyokuwa imemkumba Vivian muda mfupi uliopita kwasababu simu yake waliichukua baada ya Vivian kudondoka chini na kupoteza fahamu.

    Kwa bahati nzuri simu ya Vivian haikuwa na pass word kwahiyo walifanikiwa kukutana na namba ya mjomba wake na Nelson ambapo walimjulisha hali ya Vivian na kuahidi kwamba atafika hospitalini hapo baada ya muda mfupi. Kwa muda huo mjomba wake Nelson alikuwa amepata taharifa za ajali kwa kupitia mitandao ya kijamii ila alikuwa nje ya mji. Alipopigiwa simu na msamaria mwema alikuwa ndiyo yupo barabarani anaelekea hospitalini kumjulia hali Nelson. Alisikitika sana baada ya kusikia kwamba mke wa Nelson naye yupo hoi baada ya kudondoka ghafla.

    Alihisi pengine labda ndio maana alipompigia simu kumpasha habari za ajali iliyokuwa imetokea hakupokea simu. Famila ya Nelson ilikuwa katika wakati mgumu sana kwasababu ilikuwa ikiandamwa na mikosi ya hali ya juu. Wakati mjomba alipokuwa akiendesha gari lake kwa umakini kuelekea hospitali alipata wazo la kumjulisha dada yake habari za Nelson na familia yake. Kwahiyo alimpigia simu mama yake Nelson na kumjulisha kwamba mwanae amepata ajali na amepelekwa hospitali ya Mount Meru, pia mke wake pamoja na mtoto pia hali zao ni mbaya na wote wamelazwa katika hospitali moja. Mama Nelson baada ya kupata habari zile kutoka kwa mdogo wake alishindwa kujizuia na kuanza kulia kwa uchungu.

    “Eeh Mungu wangu ninaomba umnusuru mwanangu katika majaribu anayopitia na familia yake.” Mama Nelson alizungumza na Mungu huku akiendelea kulia kwa masikitiko makubwa.

    Baada ya mama Nelson kupata taharifa zile alijiandaa harakaharaka na kuelekea hospitali kwenda kuwaangalia wagonjwa waliokuwa wamelazwa. Alipofika hospitali mdogo wake bado alikuwa hajafika kwasababu wakati alipozungumza nae mara ya mwisho alikuwa njiani akitokea mto wa mbu sehemu ambayo ni mbali kidogo na jiji la arusha. Mama alikwenda mapokezi na kujieleza kwamba ni mzazi wa kijana mmoja ambae alifikishwa hospitalini hapo siku hiyo baada ya kupata ajali ya gari lililohusisha lori na gari dogo. Muudumu wa mapokezi alimwelekeza aende wodi namba 301 maalumu kwa wagonjwa wa ajali.

    Mama Nelson alikwenda huku akisali kimoyo moyo Mungu aweze kumsaidia mwanae asiweze kupoteza maisha kwasababu alikuwa anampenda sana. Alifika kwenye wodi aliyokuwa ameelekezwa na kuchungulia ndani ambapo alikutana na sura za wagonjwa mbalimbali wengine wenye majeraha ya kutisha sana. Kutokana na wingi wa wagonjwa na woga wa kuwatizama wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika wodi hile aliona ni vigumu kumpata mwanae kwahiyo alimuuliza mmoja wa wauguzi waliokuwepo wodini wakiwasaidia wagonjwa.

    “Habari za leo nesi!” mama alimsabahi muuguzi.

    “Nzuri tu mama shikamoo.” Nesi aliitikia salamu wakati alipokuwa akimsafisha mgonjwa kidonda.

    “Kuna majeruhi wa leo wa ajali ya fuso na gari dogo nimeagiziwa kwamba wamelazwa katika wodi hii, lakini nimejaribu kuangaza huku na kule sijafanikiwa kumuona mtu wangu.” Mama alizungumza na nesi ili aweze kupewa muongozo wa kumpata mwanae.

    “Sawa mama nimekwelewa ni kweli kabisa, waliletwa watatu lakini wawili wamesharuhusiwa kwasababu walikuwa wamepata majeraha madogomadogo, ila kuna mgonjwa mmoja anaitwa Nelson hali yake imeonekana kuwa ni mbaya sana kwahiyo alihamishiwa katika kitengo cha uangalizi maalumu.” Nesi alizungumza kwa kirefu kumfahamisha mama.

    “Unaweza kunipa utaratibu wa kufika huko.”

    “Usijali! nyoosha na hii korido moja kwa moja ukifika mwisho kunja kushoto halafu endelea kutembea utakutana na korido nyingine kunja kulia utaona kibao kilichoandikwa ‘Intensive care unit’ (kitengo cha uwangalizi maalumu) wodi namba 11.” Nesi alimpa mama Nelson muongozo wa kufika wodi aliyolazwa mwanae.

    Mama alifuata maelekezo na kufanikiwa kufika wodi aliyoelekezwa na nesi. Ila mlangoni alikutana na kibao kilichoandikwa No Entry without permission (usiingie bila ruhusa). Moyo wa mama ulikuwa ukidunda kwa kasi sana kwasababu hakujua kama mwanae yupo katika hali gani halafu isitoshe mlangoni kakutana na kibao kinachomzuia kuingia ndani. Alibaki ameduwaa hajui cha kufanya huku kijasho chembamba kikimtiririka kutokana na hofu iliyokuwa ndani yake. Wakati alipokuwa anajishauri cha kufanya alimuona daktari mmoja akija kwa mwendo wa haraka katika uelekeo ambao alikuwepo. Aliona daktari yule anaweza kufahamu habari za mwanae kwahiyo alimsubiri kwa hamu. Daktari alipofika mama Nelson alijieleza, kwabahati nzuri daktari yule alikuwa ni miongoni mwa jopo la madaktari wanaopambana kuokoa maisha ya Nelson.

    “Kiukweli hali ya Nelson sio nzuri kabisa kwasababu ameumia zaidi kichwani, ila tunajitahidi ili kuweza kuyanusuru maisha yake.” Daktari alizungumza na mama.

    “Daktari nipo chini ya miguu yako ninakuomba mjitahidi kuokoa maisha ya kijana wangu kwasababu sina mwingine ninayemtegemea isipokuwa yeye pekee.” Kwa masikitiko makubwa mama Nelson alizungumza wakati akibubujikwa na machozi.

    “Usijali mama, ninakuahidi tutajitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu, wala usiwe na wasiwasi mwanao yupo kwenye mikono salama.” Daktari alizungumza maneno ya kumfariji mama Nelson ingawa hata yeye alikuwa hana matumaini ya mgonjwa huyo kupona kwasababu alikuwa katika hali mbaya sana.

    ************

    Mjomba alipofika hospitali alikutana na wale wasamariwa wema na kusimuliwa tukio zima la Vivian kudondoka na kupoteza fahamu. Alisikitika sana lakini hakuwa na la kufanya zaidi sana alipokea simu ya Vivian iliyokuwa mikononi mwa wale wasamaria wema. Aliwashukuru sana kwa wema ambao waliuonyesha. Baada ya hapo alikwenda kwa daktari kuulizia maendeleo ya Vivian. Alifanikiwa kukutana na daktari lakini alielezwa kwamba bado wapo kwenye jitihada za kushusha presha yake kwasababu imepanda sana. Kwahiyo zoezi la mjomba kuonana na mke wa Nelson lilishindikana kwasababu daktari alimueleza kwamba hali ya mgonjwa bado ni tete. Baada ya mjomba kupata taharifa za Vivian alitaka kufahamu hali ya Mainard pamoja na Nelson.

    Kwahiyo alimpigia simu dada yake ili waweze kuonana kwasababu na yeye alikuwa maeneo ya hospitali. Baada ya mawasiliano walikutana hapohapo hospitalini. Kwa uchungu mama Nelson alimweleza mdogo wake kuhusu maendeleo ya Nelson katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa mujibu wa daktari ambaye alikutana nae. Nae mjomba alimweleza dada yake habari za Vivian ambazo tayari alikuwa ameshazipata. Mama Nelson alisikitika sana, alimshauri mdogo wake waende kwenye wodi aliyokuwa amelazwa mjukuu wake ili waweze kufahamu maendeleo yake. Walikwenda wote kwa pamoja hadi kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Mainard.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Walimkuta nesi anambadilishia chupa ya damu iliyokuwa imeisha na kumuwekea nyingine. Maendeleo yake bado yalikuwa sio mazuri ingawa alionekana kuwa na afadhali kidogo kulingana na hali ambayo alifikishwa nayo pale hospitali. Fahamu zilikuwa zimeanza kumrejea kwa mbali. Daktari anayemuhudumua Mainard alifika wodini kwaajili yaa kuangalia maendeleo yake na ndio alikutana na Mama Nelson pamoja na mdogo wake. Daktari aliwaeleza kwamba kidogo hali ya mtoto inaendelea vizuri ingawa madaktari bingwa kutoka muhimbili walipofika hospitalini hapo kwa siku hiyo nao pia wameshindwa kubaini sababu ya mtoto kuishiwa damu kwa kasi. Daktari aliwapa ushauri wazingatie maombi kwasababu kutokana na uzoefu wake katika kazi yake aligundua tatizo la Mainard sio la kawaida.



    Mama Nelson na mdogo wake walifanikiwa kufahamu hali za wagonjwa wao, wote pale hospitali. Kutokana na kwamba hawakuwa na uwezo wa kuonana nao kwa siku hiyo waliamua kurudi nyumbani kupumzika ili kesho yake asubuhi na mapema wawahi tena hospitalini hapo. Walirudi nyumbani kila mmoja akiwa amevunjika moyo kutokana na hali ya wagonjwa. Mama Nelson aliamua kuhamishia makazi yake kwa muda nyumbani kwa mwanae, kusudi aweze kumsaidia mjukuu wake ‘Benedict’ kwasababu hakuwa na msaada wowote kwa wakati ule. Usiku mama Nelson alipokuwa kitandani alikosa kabisa usingizi, alidumbukia katika wimbi kubwa la mawazo kwa kuwaza kwa nini yale yote yalikuwa yanatokea katika familia ya mtoto wake.

    Moyo ulimuuma zaidi baada ya kukumbuka kwamba kijana wake alishamweleza kuhusiana na ndoto mbaya ambazo zinawasumbua kila mara. Alihisi pengine hata yale masahibu wanayokumbana nayo huwenda kunasababu inayochangia. Aliona suala la maombi ni la msingi sana japokuwa hakuwa ameokoka kwa wakati ule. Alimpigia simu mchungaji Eugin Alvin usiku huohuo, ambaye ndiye alifungisha ndoa ya Nelson na kumfahamisha kila kitu kuhusiana na familia ya Nelson. Baada ya mchungaji kushirikishwa suala lile walianza maombi mazito usiku huohuo kwa njia ya simu. Mchungaji alikemea na kuvunja nguvu zote za giza kwa jina la Yesu kristo zinazoandama familia ya Nelson.

    Maombi mazito yalifanyika kwa muda wa nusu saa na baada ya hapo mchungaji alimweleza kwamba asubuhi ya kesho yake wakutane hospitali ili aweze kuwaombea wagonjwa wote kwasababu roho wa Mungu amemuonyesha kwamba familia hiyo imefungwa na hila za mwovu shetani. Mama Nelson alimshukuru mchungaji na hatimae waliagana. Palipokucha asubuhi wakati mama Nelson alipokuwa akijiandaa ili aweze kwenda hospitali ghafla alishikwa na tumbo la kuharisha. Alishindwa kuelewa chanzo cha yeye kuharisha mfululizo ili hali hakuwa amekula kitu chochote. Kuharisha kuliambata na maumivu makali sana ya tumbo. Alipoona hali inazidi kuwa mbaya alimpigia simu mdogo wake na kumjulisha hali yake, ili aweze kupatiwa msaada wa haraka kwasababu nguvu zilikuwa zinamwishia na pia alikuwa akihisi kizunguzungu kikali.

    Mjomba wa Nelson alipopata zile taharifa aliwahi mapema nyumbani kwa Nelson ambapo ndipo alipokuwa dada yake ili aweze kumfikisha hospitali. Alimkuta yupo katika hali mbaya, alimpakia katika gari lake na kumkimbiza katika hospitali ya kanisa katoliki kijenge ambayo ndiyo iliyokuwa jirani. Daktari aliyempokea alimuwekea dripu ya maji na glukosi muda huohuo kwasababu mgonjwa alikuwa amepoteza maji mengi na pia nguvu zilikuwa zimemwishia. Daktari alimfanyia vipimo kadhaa lakini ugonjwa haukubainika, kwahiyo daktari alihisi pengine labda ni mchafuko tu wa tumbo jambo ambalo ni la kawaida. Kufikia jioni alikuwa ameshatumia chupa sita za maji, pamoja na vidonge vya kuzuia kuharisha. Dokta alimpatia dawa ya minyoo na kumruhusu mgonjwa akarudi nyumbani kwasababu hali yake ilikuwa inaendelea vizuri kabisa. Kwahiyo suala la kukutana na mchungaji kwa siku zile hospitalini lilishindikana. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba siku inayofuata mchungaji alikuwa na safari ya kuelekea Nairobi nchini Kenya kwaajili ya semina ya neno la Mungu kwa muda wa wiki moja. Mchungaji alimsisitiza mama Nelson kwamba asichoke kudumu katika maombi kwasababu ndiyo silaha pekee ya kumshinda shetani.

    *************

    Mjomba wa Nelson alipomfikisha dada yake hospitali alimwacha, baada ya kuona hali yake inaendelea vizuri. Alikwenda hospitali ya Mount Meru kwenda kuangalia maendeleo ya wagonjwa wengine. Alipofika katika wodi ya Vivian alikuta hali yake inaendelea vema, daktari aliyekuwa anamtibu alisema kwamba endapo hali yake itaendelea kuwa vizuri basi kesho yake atamruhusu arudi nyumbani. Kiukweli ilikuwa ni habari njema sana kwa mjomba. Baada ya kuhakikisha hali ya mke wa Nelson inaendelea vizuri alikwenda katika wodi aliyokuwa amelazwa Nelson.

    Alipofika, alishindwa kuzuia machozi baada ya kumuona Nelson akiwa amelala kitandani fahamu zimempotea huku anapumulia mashine. Kunywa kwake na kula kwake kuliwezeshwa na mirija maalumu. Usingizi mzito uliokuwa unamvuta Nelson katika umauti ulisababisha mjomba wake apoteze kabisa matumaini. Machozi yalikuwa yanamdondoka mjomba mithili ya matone ya mvua kutokana na hisia mbaya iliyokuwa imejengeka katika ubongo wake baada ya kumuona Nelson akiwa amelazwa hoi taabani pale kitandani. Maneno ya daktari ndiyo yalipigilia msumari maumivu zaidi ndani ya moyo wa mjomba kwasababu alielezwa kwamba.

    “Huyu mgonjwa ameumia zaidi sehemu ya kichwa na tumebaini kwamba majeraha makubwa aliyoyapata kichwani yamesababisha athari pia katika ubongo wake, kwahiyo kupona kwake kutagharimu muda mrefu. Lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa mgonjwa huyu kuchanganyikiwa kutokana na matatizo aliyoyapata katika ubongo wake.” daktari alizungumza maneno ambayo yalimuumiza sana mjomba na kusababisha aendelee kububujikwa na machozi kwa uchungu.

    “No! I cant believe this.” (Hapana! siwezi kuamini hii.) huku akiendelea kububujikwa na machozi mjomba alijikuta ameropoka baada ya kushindwa kuamini maneno aliyokuwa anaelezwa na daktari.

    “Najua ni lazima itakuwia vigumu kuamini lakini ndivyo ilivyo, chamsingi jitahidi kujikaza kwasababu wewe ni mwanaume.” Daktari alijitahidi kumnyamazisha mjomba yake Nelson kwasababu alikuwa akilia kama vile mtoto mdogo.

    Baada ya maongezi na daktari aliyekuwa akimuudumia Nelson, mjomba alitoka wodini kwa mwendo wa kivivu kwasababu mwili wake ulikuwa umeishiwa nguvu kutokana na habari alizopashwa na daktari kuhusiana na hali ya Nelson. Alikosa raha kabisa, aliona dunia haina maana. Alijitahidi kujikaza kusudi machozi yasimdondoke lakini ilishindikana kwasababu machozi yalizidi kutengeneza njia katika mashavu yake. Aliamua kwenda kwenye gari lake kukaa hadi zile hisia kali za uchungu wa moyo zitakapopoa ndipo aelekee kwenye wodi aliyolazwa Mainard kufahamu maendeleo yake. Alipofika kwenye gari lake alijikuta analia sana. Hakuamini kwamba pamoja na werevu Nelson aliojaliwa na mwenyezi Mungu mwisho wa siku anakuwa chizi. Aliisikitikia familia yake ambayo bado ilikuwa inahitaji msaada wake katika suala zima la malezi. Alizidi kulia na kumlalamikia Mungu kwanini ameruhusu Nelson kuingia katika matatizo makubwa namna ile. Baada ya kuona kwamba hisia za uchungu ndani ya moyo wake zimetulia, alifungua mlango wa gari lake na kwenda katika wodi aliyokuwa amelazwa Mainard. Miguu yake haikuwa na nguvu kwahiyo mwendo wake ulikuwa ni kama wa mzee. Macho yake yalikuwa mekundu mithili ya mtu aliyevuta bangi. Kwa mwendo wake wa taratibu alifika katika wodi aliyokuwa amelazwa Mainard. Alipata faraja kidogo kwasababu hali yake ilionyesha kuwa kama ya jana yake. Alitoka wodini na kwenda kwenye gari lake na kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwa Nelson kumjulia hali dada yake ambae alimjulisha kwa njia ya simu kwamba ameruhusiwa baada ya hali yake kuhimarika.

    Alifika salama na kukuta hali ya dada yake ni ya kuridhisha kulingana na ambavyo alimuacha hospitali. Alimweleza dada yake habari za wagonjwa waliolazwa hospitali, ingawa hakumuambia kuwa hali ya Nelson bado ni mbaya kwasababu aliona ataweza kumsababishia matatizo mengine. Baada ya hapo aliaga na kuondoka na kuelekea nyumbani kwake. Alifika nyumbani kwake huku akijihisi kuchoka kuliko siku zote alizowahi kuchoka. Chakula alichoandaliwa na mke wake hakuweza kula kutokana na jinsi alivyokuwa anajihisi hovyo. Alikwenda kulala lakini napo usingizi ulikataa kumjia kabisa, alizidi kutafakari kile alichokuwa ameelezwa na daktari kuhusiana na hali ya Nelson.

    Ile siku hadi panakucha hakufumba kabisa macho yake, alizidi kulia ndani kwa ndani kwasababu alikuwa anampenda sana Nelson. Asubuhi alianza kujiandaa ili aweze kwenda hospitali kuwasabahi wagonjwa. Alimaliza kujiandaa na kuanza safari ya kuelekea hospitali. Ghafla wakati alipokuwa njiani alipigiwa simu na bosi wake kwamba anahitajika kazini mara moja kuna dharura imejitokeza. Wito wa kazini ulimtia hasira kwasababu alikuwa yupo likizo ya siku 28. Hakuwa na namna alisitisha safari ya hospitali na kuelekea kazini ambapo alikuwa anahitajika. Alimpigia simu mke wake na kumueleza kwamba amepata dharura. Kutokana na kwamba dada yake bado alikuwa mgonjwa hapakuwa na mbadala mwingine isipokuwa mke wake kufunga safari ya kwenda hospitali ya Mount Meru.

    ***********

    Kufikia mchana hali ya Vivian ilikuwa imehimarika kwa kiasi kikubwa. Daktari aliyekuwa anamtibu alimruhusu kurudi nyumbani baada ya mke wa mjomba yake Nelson kulipa pesa za matibabu zilizokuwa zinahitajika. Macho ya Vivian hayakukauka machozi tangu alipopatwa na fahamu. Alionekana kudondokwa na machozi muda wote japokuwa hakutoa sauti ya kilio. Mara baada ya kutoka wodini kitu cha kwanza alisema kwamba anahitaji kufahamu hali ya mtoto wake pamoja na ya mume wake ndipo aweze kurudi nyumbani. Lakini kwasababu mke wa mjomba wake Nelson alikuwa tayari ameshaona hali ya Nelson ilivyokuwa mbaya aliamua kutumia busara kumdanganya kwamba Nelson amehamishwa hospitali kwajili ya kupatiwa matibabu ya kina zaidi. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Aliona kutokana na hali yake bado ilikuwa ni ya ugonjwa endapo atafanikiwa kumuona mume wake akipumulia mashine na kulishwa kwa mirija maalumu basi pengine presha ingeweza kupanda tena. Vivian aliumia sana baada ya kusikia habari za mume wake kuhamishwa hospitali. Ila alitiwa moyo kwamba huko alipohamishiwa anaendelea vizuri na matibabu. Baada ya hilo kufanikiwa alihitaaji kwenda kufahamu hali ya mwanae inaendelea vipi, mke wa mjomba hakuwa na kigugumizi juu ya hilo kwasababu alikuwa anafahamu kuwa Mainard anaendelea vizuri kabisa kwasababu alionana nae muda mfupi kabla ya kwenda wodini kwa Vivian. Kwahiyo walitembea taratibu kuelekea wodi aliyokuwa amelazwa mtoto. Mita kama tano hivi na ushee kufikia mlango wa wodi aliyokuwa amelazwa Mainard ghafla mioyo yao ililipuka kwa hofu baada ya kuona mwili uliokuwa umefunikwa kwa shuka la bluu ukitolewa wodini na manesi wawili. Macho yalimtoka Vivian mithili ya mtu aliyefumwa ugoni, alishindwa kuamini kabisa kile alichokuwa anakiona mbele ya macho yake kwa wakati ule. Alishindwa kuzungumza, na pia alishindwa kulia, ghafla macho yake yaligubikwa na kiza kinene na hatimae alidondoka chini kama gunia la ngano. Mke wa mjomba alishindwa kumzuia kwasababu na yeye alikuwa ameshikwa na butwaa machozi yanamdondoka kutokana na kile alichokuwa amekishuhudia.

    Fikra zao zilijua kwamba mwili wa marehemu uliokuwa ukitolewa ulikuwa ni wa Mainard kwasababu ndiye aliyekuwa amelazwa kwenye ile wodi peke yake. Vivian alipewa msaada wa kufikishwa wodini kwa mara nyingine kutokana na mshtuko mkubwa aliokuwa ameupata baada ya kuhisi mwanae kafariki. Daktari alimpima na kugundua presha imepanda ingawa haikuwa juu kwa kiwango kama cha mara ya kwanza. Alianza kupatiwa matibabu ya haraka ili aweze kurudi katika hali yake ya kawaida. Ili muwia vigumu mke wa mjomba kuamini kwamba Mainard amefikwa na umauti kwasababu ni muda mfupi tu alikuwa ameonana nae, tena akiwa katika hali ya kuridhisha kabisa.

    Alimuacha Vivian akiawa amelala kitandani fahamu zimempotea na kwenda kwenye wodi aliyokuwa amelazwa mtoto ili kuweza kuhakikisha kama ni kweli mwili wa marehemu waliokutana nao mlangoni ulikuwa ni wa mtu waliemdhania. Alipofika kwenye malango wa wodi aliyokuwa amelazwa mtoto alifungua taratibu huku akitetemeka kutokana na hofu iliyokuwa ikitambaa kifuani mwake. Taratibu aliingia ndani ya wodi na kukaribishwa na ukimya wa kutisha, alitupa macho yake katika kitanda alichokuwa amelala Mainard lakini kwa bahati mbaya hakumwona Mainard. Alishindwa kabisa kujizuia, kwahiyo alianza kuangua kilio kwa sauti ya juu baada ya kumkosa mgonjwa wake wodini.

    Kelele zake zilisababisha manesi wawili wamfuate haraka haraka ili waweze kumtoa nje kwasababu kelele zilikuwa hazihitajiki maeneo yale. Mke wa mjomba aliendelea kulia kwa uchungu wakati alipokuwa ameshikwa na manesi na kupelekwa nje. Walipokuwa wanapita katika korido ndefu ili waweze kukuta mlango wa kutoka nje ghafla walikutana na daktari ambae ndie alikuwa anamuhudumia Mainard. Daktari huyo alikuwa anatoka katika chumba ambacho kilikuwa mbele yao kwa mita kadhaa. Dokta alishtuka kumuona mke wa mjomba akiwa analia kama mtu aliyefiwa. Ilibidi aliulize kulikoni kwasababu tayari alikuwa anamfahamu kwasababu wakati mke wa mjomba alipofika wodini kumjulia hali Mainard alimkuta huyu dokta.

    “Jamani msikute huyo mama analia kwa kuhisi labda mtoto kafariki.” Daktari alizungumza kwasababu tayari alikuwa anamfahamu mke wa mjomba, pia alisikitika baada ya kumuona akiwa analia kwa huruma.

    “Amefika wodini na kukuta mgonjwa wake hayupo ndio akaanza kuangua kilio, nafikiri ni ndugu wa yule baba aliyefariki muda mfupi baada ya kufikishwa wodini kutokana na ugonjwa wa saratani ya damu.

    “Hapana huyu mama ni ndugu wa yule mtoto, Mainard tuliyemuamisha wodi kutokana na hali yake kuonekana kuwa njema.” Daktari alisikika akizungumza maneno ambayo yalisababisha chembe chembe za faraja zianze kupenyeza katika mtima wa mke wa mjomba.

    “Inamana Mainard bado ni mzima?” mke wa mjomba aliropoka baada ya kusikia habari za mtoto kuhamishwa wodi.

    “Haswaa! baada ya kuona hali na mgonjwa wenu inazidi kuhimarika imebidi tumuamishe kutoka kitengo cha uwangalizi maalumu na kumpeleka katika wodi ya kawaida ili kupisha nafasi kwa wagonjwa wanaoletwa wakiwa katika hali mbaya, waweze kupatiwa tiba katika mazingira stahiki.” Maneno ya daktari yalisababisha mke wa mjomba amfuate na kumkumbatia kwa furaha.

    “Asante Mungu.” Mke wa mjomba alimshukuru Mungu baada ya kufahamu kuwa mtoto hajafa bali amehamishwa wodi.

    “Huwezi amini dokta, mimi na mama mtoto tulifika wodini na kukuta mwili wa marehemu ukitolewa, tukadhani pengine labda mgonjwa wetu kafariki. Mama yake Mainard alishindwa kuamini macho yake na kudondoka chini baada ya presha kupanda ghafla, kwasasa yupo wodini amelazwa.” Mke wa mjomba alizungumza huku sura yake ikionyesha matumaini makubwa.

    “Masikini! poleni sana, ule mwili mliokutana nao ulikuwa ni wa baba mmoja aliyefikishwa hospitalini hapa akiwa katika hali mbaya.” Daktari alizidi kumpa maelekezo mke wa mjomba kwasababu alionekana kukata tamaa sana.

    “Basi dokta nipeleke kwenye hiyo wodi aliyohamishiwa mtoto ili niweze kuifahamu.”

    “Hakuna shaka, twende.”

    Daktari aliongozana na mke wa mjomba hadi kwenye wodi ambayo alikuwa amelazwa mtoto. Walipofika wodini, mke wa mjomba alimkumbatia mtoto huku akilia kwa furaha sana kwasabaabu hakutegemea kabisa kumwona tena Mainard akiwa mzima. Kwa furaha mke wa mjomba alinyanyuka na kwenda katika wodi aliyokuwa amelazwa Vivian na kukuta fahamu zimemrejea machozi yanamtiririka mashavuni. Mke wa mjomba alianza kumbembeleza na kumweleza kuwa asiogope kwasababu Mainard ni mzima kabisa. Vivian aliona kama mke wa mjomba anamfariji tu lakini baada ya kusimuliwa kila kitu ilibidi aamini.

    Baada ya masaa matatu hali ya Vivian ilihimarika zaidi, kwahiyo daktari alimruhusu arudi nyumbani akapumzike ila alimsisitiza atumie dawa alizokuwa amempatia kwa mara ya kwanza. Walipitia katika wodi ambayo mtoto alikuwa amehamishiwa. Vivian alifurahi sana kumwona mwanae kwa mara nyingine tena, alimkumbatia kwa furaha sana huku machozi yakimdondoka kwa furaha aliyoipata baada ya kumuoana mtoto wake ambae masaa machache yaliyopita alidhani alikuwa amepoteza maisha. Vivian pamoja na mke wa mjomba walimuaga Mainard kisha waliekea nyumbani.



    Vivian alisindikizwa na mke wa mjomba hadi nyumbani. Baada ya hapo mke wa mjomba alielekea nyumbani kwake. Hali ya mama yake Nelson ambaye alikuwepo nyumbani kwa Nelson ilikuwa ikiendelea vizuri. Alifurahi sana kumuona mkwe wake amerejea nyumbani akiwa anaendelea vizuri. Nelson ndiye mgonjwa ambae bado afya yake ilikuwa tete katika kitengo cha uwangalizi maalumu. Hali yake haikuonyesha mabadiliko yeyote ingawa alikuwa anapatiwa matibabu makubwa kila kukicha. Imani ilizidi kupotea hata kwa madaktari ambao walikuwa wanamuhudumia kwasababu hawakuona matokeo ya jitihada wanazofanya kuokoa maisha ya mgonwa yule. Japo kuwa mama mkwe alikuwa mgonjwa lakini alijitahidi kuandaa chakula ambacho Vivian angeweza kula ili aweze kumeza dawa alizokuwa ametoka nazo hospitali. Chakula kiliiva lakini kutokana na wingi wa mawazo kichwani mwa Vivian alikula chakula kidogo sana. Mama mkwe alimuhimiza ajitahidi kula lakini alishindwa kabisa. Alijihisi kuchoka sana kwahiyo aliagana na mama mkwe wake kisha akaelekea chumbani kwake kulala.

    ************

    Usiku wa siku hiyo Vivian alichukuliwa na mama yake na kupelekwa kuzimu katika sherehe ya kumla nyama Mainard. Kwahiyo kama kawaida Vivian akiwa usingizini aliota yupo katika chumba kidogo sana ambacho kina giza nene pamoja na moshi uliokuwa unambatana na harufu kama ya nyama inayochomwa. Chumbani mle kulikuwa na mifupa mingi mikubwa mikubwa ambayo Vivian hakuweza kufahamu kwa haraka ilikuwa ni mifupa ya mnyama gani, ingawa ilifanana kwa mbali na mifupa ya binadamu. Kulikuwa na wadudu wengi mithili ya funza ambao walikuwa wakitembea juu ya mwili wake. Mazingira yale yalisababisha Vivian aingiwe na hofu moyoni mwake na kuanza kulia. Ghafla wakati alipokuwa akilia alianza kusikia sauti ya kutisha inamuita huku ikiwa imeambatana na kicheko cha kuogopesha.

    “Vivian! Vivian! Vivian! Ahahaha! Ahahaha!” CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Vivian hakuweza kufahamu sehemu ambayo sauti ile ya kutisha ilikuwa inatokea. Kwahiyo ilibidi atege masikio yake barabara huku akigeuza shingo yake huku na kule ili aweze kuinasa sauti ile vilivyo. Sauti ilizidi kumuita na hatimae alishangaa ananyanyuka pasipo hiari yake na kufuata mlango ambao ulikuwa mbele yake ingawa ulikuwa umefungwa. Vivian alijitahidi kujizuia asitembee lakini alishindwa, alizidi kutembea taratibu kuelekea mlangoni huku akizidi kusikia sauti ikimwita. Alipofika mlangoni hofu ilizidi kumjaa baada ya kushangaa mlango umefunguka bila kufunguliwa na mtu yeyote. Baada ya kutoka katika kile chumba alichokuwepo alijikuta yupo katika chumba kingine ambacho ni kikubwa sana kulinganisha na kile alichokuwepo.

    Kilichomuogopesha zaidi ni kwamba katika chumba kile kulikuwa na watu wengi sana, ambao walikuwa wamefungwa minyororo mikubwa huku wakilia kwa huruma. Alizidi kuzungusha macho yake huku na kule katika lile kundi kubwa la watu na ghafla macho yake yalimwona mwanae Mainard pamoja na mume wake wakiwa wamefungwa huku wakilia sana kuomba msaada. Alitamani kusogea walipo ili aweze kuwafungulia ile minyororo lakini haikuwezekana kwasababu miguu yake ilikuwa ni mizito kunyanyuka kuelekea kule alipotaka. Vifuani mwa wale watu wote kulining’inizwa vibao ambavyo vimechorwa namba kwa damu. Kibao cha mwanae kilikuwa kimeandikwa namba moja, alijaribu kusoma kibao cha mume wake ili aweze kufahamu kimeandikwa namba ngapi lakini alishindwa kwasababu kilikuwa kimekaa upande.

    Vivian alijiuliza vibao vile vya namba vilikuwa vinamaanisha nini lakini hakupata jibu. Muda huohuo alisikia tena sauti iliyokuwa inamwita na kusababisha miguu yake kuwa mepesi kuelekea asipopajua. Macho yake yalizidi kuangaza huku na kule ili aweze kufahamu alipo lakini alishindwa kufahamu alipokuwa. Wakati alipokuwa anazidi kutembea aliaza kusikia kelele za watu wengi ambazo zilikuwa azieleweki. Kwa jinsi alivyokuwa anazidi kutembea ndivyo ambavyo kelele hizo zilizidi kuwa kero masikioni mwake. Mwisho wa safari yake ulikuwa ni katika ukumbi mmoja ambao ulikuwa na watu wengi sana ambao walilipuka kwa shangwe na nderemo baada ya kumuona Vivian akitembea taratibu kuingia ukumbini hapo.

    Kumbukumbu zilimjia kwamba ile sehemu ndiyo ileile ambayo mwanae Alaire alichinjwa na kuliwa nyama mbele yake. Hofu kubwa iliyokuwa ndani ya moyo wake ilisababisha aanze kutetemeka huku akilia sana ingawa alishindwa kuelewa pamoja na kwamba alikuwa akilia kwa uchungu lakini machozi yalikuwa hayatoki. Alishangaa sana watu wale kwasababu hakuna hata mmoja aliyekuwa anamuonea huruma kutokana na kilio alichokuwa anakiangua. Aliwatazama kwa umakini ingawa walikuwa katika nuru hafifu na kubaini kuwa sio watu wa kawaida kwasababu walikuwa wanadondokwa na udenda muda wote na pia sura zao zilikuwa ni za kutisha mno.Macho yao yalikuwa yanawaka mithili ya paka aliye kwenye giza. Muda huo walikuwa wakicheza na kuimba nyimbo ambazo zilikuwa ngeni masikioni pa Vivian.

    Eneo lile lilikuwa linamtisha sana Vivian kiasi kwamba alitamani anyanyuke ili aweze kukimbia ila ilishindikana kwasababu miguu yake ilikuwa kama inaganzi. Ghafla alisikia sauti ya malkia ikiagiza binadamu mwenye kibao kilichoandikwa namba moja akaletwe. Hofu ilizidi kugandamana na moyo wa Vivian kwasababu alishamwona mwanae ndie aliyekuwa na kibao kilichoandikwa namba moja. Baada ya sekunde kadhaa Mainard aliletwa mbele ya kiti cha malkia. Mainard alikuwa analia kwa huruma sana jambo ambalo liliongeza simanzi ndani ya moyo wa mama yake. Malkia wa kuzimu aliamuru Mainard achinjwe haraka iwezekanavyo. Bila kuchelewa amri hiyo ilitekelezwa na mwanaume mmoja mwenye mwonekano wa kutisha, ambae alimkamata Mainard na kumlaza juu ya meza na kumkata shingo bila huruma.

    Furaha ilitawala kila kona, mate ilizidi kuwadondoka wakati mtoto alipokuwa anachinjwa. Moyo wa Vivian ulijawa na majonzi makubwa ingawa alitamani aendelee kulia lakini alishindwa. Alitamani azungumze maneno ya kumtetea mwanae lakini mdomo wake ulishindwa kufunguka na kuzungumza maneno ambayo aliyakusudia. Zoezi lilipokamilika malkia alipelekewa damu iliyokingwa na kuanza kuinywa. Muda mfupi baada ya kuanza kuinywa damu ile alinyanyuka na kwenda hadi sehemu aliyokuwa ameketi Vivian na kuanza kumnywesha damu ile iliyokuwa imekingiwa kwenye ndoo ndogo. Vivian alikataa katakata kunywa damu ya mwanae lakini malkia alizungumza maneno yanayofanana na ya lugha ya kiarabu na hatimae Vivian alishindwa kuendelea kujizuia kukataa. Kwahiyo alishiriki vema katika sherehe ya kunywa na kula nyama ya mtoto wake kipenzi. Damu na nyama ya Mainard ilifurahiwa sana kwasababu ndani ya muda mfupi ilibaki mifupa tu. Sherehe ya kumla Mainard ilikwisha na kisha Vivian alirudishwa duniani.

    ***********

    Vivian alizinduka usingizini amelowa jasho mwili mzima, huku akihema kwa kasi ya ajabu. Aliwasha taa na kuangalia saa ya ukutani inaonyesha ni saa nane na dakika kumi na tano usiku. Alianza kulia kwasababu alijua moja kwa moja Mainard atakuwa matatani. Matumaini yalizidi kumpotea baada ya kuhisi harufu ya damu ambayo muda mfupi alihisi kuinywa. Kutokana na ndoto ya kutisha aliyokuwa ameiota, alinyanyuka na kwenda chumbani kwa mama mkwe wake kumgongea ili aweze kumsimulia alichokiota. Alipogonga mlango wa chumba cha mama mkwe wake, baada ya muda mfupi ulifunguliwa na ndipo Vivian aliingia huku akihema juujuu na kuanza kumsimulia kila kitu alichokiota katika ndoto ile ya kutisha. Vivian alikuwa analia sana kiasi kwamba hadi mama mkwe alishangaa kumuona analia kiasi kile ili hali ilikuwa ni ndoto tu.

    Mama mkwe alimsihi Vivian anyamaze kwasababu hali ya mtoto hospitali ilikuwa inaendelea vizuri. Alimtaka akemee ndoto ile kusudi hila za shetani ziweze kushindwa kwa jina la Yesu kristo lakini Vivian alizidi kulia kwa uchungu kwasababu alijua tayari mtoto wake atakuwa ameshakufa. Kwanzia muda ule hadi panakucha hakurudi tena chumbani kwake alikesha chumbani pale kwa mama mkwe wake hadi ilipofika asubuhi ya saa kumi na moja, ambapo alianza kujiandaa ili aweze kuondoka kuelea hospitali alfajiri ile kujua hali ya mwanae. Alijawa na hofu kubwa moyoni mwake kwasababu mtoto wao wa kwanza alikufa katika mazingira yaleyale ya kutatanisha.

    Saa kumi na mbili kasoro asubuhi aliwasha gari lake na kuelekea hospitali ya Mount Meru kwenda kuangalia mwanae yupo katika hali gani. Aliposhuka kwenye gari baada ya kufika hospitali asubuhi ile alitembea kwa mwendo wa haraka kama vile askari wa kivita hadi alipofika kwenye mlango wa wodi aliyokuwa amelazwa Mainard. Moyo ulikuwa unamdunda kwa kasi sana kutokana na hofu kubwa iliyokuwa ndani yake. Alifungua mlango wa wodi taratibu na kuingia ndani ya wodi ambapo alikaribishwa na ukimya ambao ulizidi kumchanganya. Alitazama katika kitanda alichokuwa amelazwa mwanae lakini hakumwona mtoto wake mpendwa. Alihisi kuchanganyikiwa kwasababu alijua moja kwa moja Mainard atakuwa ameshapelekwa mochwari. Alianza kulia kwa uchungu sana huku akitoka wodini kuelekea katika chumba cha daktari kupata mwongozo. Lakini mara baada ya kutoka wodini alikutana na daktari ambae ndie alikuwa anamwendea ofisini.

    “Jikaze mama, dunia ndivyo ilivyo.” Daktari alizungumza maneno ambayo yalizidi kuongeza utata katika moyo wa Vivian.

    “Daktari usitake kunieleza kwamba mwanangu kafariki dunia!” Vivian alizungumza kwa huruma sana huku akizidi kulia kwa uchungu uliopitiliza.

    “Kiukweli, tumejitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu, ili kuweza kuokoa maisha ya Mainard lakini kwa bahati mbaya amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya hali yake kubadilika ghafla kuwa mbaya.” Maneno ya daktari yalimthibitishia Vivian kwamba tayari mwanae ni marehemu.

    Miguu ya Vivian ilikosa nguvu kwahiyo ilibidi akae chini sakafuni huku akiendelea kububujikwa na machozi. Alilia kwa hisia kali sana kiasi kwamba hadi daktari alianza kulengwa lengwa na machozi. Vivian aliona dunia kama imemuelemea, chuki dhidi ya mama yake ilizidi kufoka ndani ya mtima wake kwasababu alijua fika kuwa kifo cha mtoto wake wa pili kilisababishwa na mama yake ambae alikuwa anamshinikiza kupokea uchawi ambao aliukataa. Aliona ni bora mama yake angemuuwa yeye na kuacha watoto wake wapenzi. Daktari alimnyanyua na kumpeleka ofisini kwake ambapo alianza kuzungumza nae kwa namna ya kumfariji kwasababu alionekana kupoteza matumaini kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Daktari alizungumza nae kwa muda wa kama dakika ishirini. Baada ya hapo alihisi kupata nguvu kidogo, kwahiyo alinyanyua simu yake na kumpigia mjomba yake Nelson na kumweleza yaliyokuwa yametokea. Mjomba alisikitika sana kupokea taharifa zile za kifo cha mtoto wa pili wa Nelson. Baada ya muda mfupi alifika pale hospitali ambapo alimchukua Vivian na kurudi nae hadi nyumbani kwake kwaajili ya kuomboleza kifo cha Mainard. Kusema kweli ilikuwa ni simanzi kubwa katika familia ya Nelson. Ndugu jamaa na marafiki walijiuliza sababu iliyokuwa inapelekea watoto wa Nelson kupoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha lakini hawakupata jibu.

    Kilichozidisha simanzi ndani ya mioyo ya watu ni kwamba kifo cha Mainard kimetokea wakati Nelson yupo hoi hospitali hajitambui. Vivian alikuwa anazimia kila mara kutokana na kulia kupita kiasi kwasababu ya kifo cha mwanae ambae ilimuwia vigumu kuamini kwamba kweli kafariki. Moyoni mwake alikuwa na majonzi mara dufu kutokana na kwamba alikuwa anafahamu sababu ya vifo vile katika familia yake na pia alikuwa anafahamu kuwa familia yake itateketea katika mazingira ya kutatanisha. Alijiuliza afanye nini ili aweze kuinusuru familia yake katika mikono ya mama yake ambae amekusudia kuiangamiza yote. Wazo la kwenda kwa watumishi wa Mungu kufanyiwa maombi hakulipata kabisa.

    Akili yake ilikuwa kama imefungwa kwasababu hakuweza kuwaza njia sahihi ya kutoka katika lile tatizo lililokuwa likitia simanzi ndani ya mioyo ya watu wengi. Utata wa kifo cha Mainard kilisababisha mawazo mazito ndani ya kichwa cha mama Nelson na kupata uwakika kwamba kuna nguvu fulani ya kishetani inaandama familia ya mtoto wake. Kwahiyo hata matumaini ya mwanae kupona yalipotea kabisa kwa kuhisi kwamba huwenda hata ajali aliyoipata ilitokea katika mazingira ya kutatanisha. Kutokana na majaribu mazito yaliyokuwa yanaiandama familia ya Nelson ilipelekea masikitiko makubwa ndani ya mioyo ya watu wengi.

    Baada ya siku nne Mainard alizikwa katika makaburi ya Njiro ambapo ndipo alipokuwa amezikwa Alaire. Baada ya mazishi Vivian alirudi nyumbani kwake akiwa katika upweke wa hali ya juu. Alipofika nyumbani Benedict alianza kulalama maumivu makali ya kichwa, alimpa hedex pamoja na maji mengi akiamini ni uchovu ambao ulisababishwa na kulia sana kutokana na kifo cha kaka yake. Licha ya kumeza dawa lakini bado maumivu yalizidi kuongezeka na kusababisha hadi mtoto akaanza kulia kutokana na maumivu makali aliyokuwa anahisi. Vivian aliona kuna haja ya kumuwaisha mtoto hospitali ili kupatiwa matibabu ya haraka kwasababu alionekana kuhisi maumivu makali. Kwahiyo Benedict aliwahishwa hospitali na majirani kwasababu mama yake bado hakuwa na nguvu kwasababu alikuwa amechoshwa na shughuli ya maziko ya mwanae.

    Vivian alibaki nyumbani huku kichwa chake kikiwa ndani ya mawazo mazito, akiwaza namna ya kuweza kumuokoa mwanae wa mwisho pamoja na mume wake wasiweze kunaswa na mtego wa mama yake. Alikumbuka katika ile ndoto alimuona mume wake yupo katika chumba fulani amefungwa minyororo halafu isitoshe alikuwa amevaa kibao kilichoandikwa namba ingawa hakufahamu namba ya mume wake. Matumaini yalizidi kumpotea kwa kuhisi huwenda namba mbili alikuwa ni mume wake ambae alikuwa hoi hospitali.

    Aliwaza pia suala la mume wake kulazwa hospitali ni geresha tu ya kichawi kwahiyo moja kwa moja aliona muda sio mrefu mume wake nae ataweza kupoteza maisha. Roho ilimuuma sana kwasababu alikuwa anampenda sana Nelson na pia hakuwa tayari kumpoteza, aliona ni bora litokee la kutokea lakini sio kutengana na mume wake kipenzi katika hali yeyote wakati bado alikuwa anampenda kuliko kitu chochote. Lisaa limoja na nusu baada ya mwanae kukimbizwa hospitali kwa msaada wa majirani kutokana na maumivu ya kichwa alipokea simu kwa mmoja wa majirani ambao waliongozana na Benedict hadi hospitali.

    “Haloo!” sauti ya jirani Yona ilisikika upande wa pili.

    “Ndio shemeji!” Vivian alizungumza kwa sauti ya chini na ya kukwaruza kwasababu, sauti ilikuwa imemkauka kutokana na kulia sana.

    “Tumemfikisha mtoto hospitali, daktari amebaini kwamba anaupungufu mkubwa wa damu kwahiyo ndio amewekewa dripu ya damu muda mfupi uliopita na hali yake inaendelea vizuri.” Jirani alizungumza maneno ambayo yalisababisha mshtuko mkubwa ndani ya moyo wa Vivian kwasababu mtoto aliezikwa siku hiyo alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa huohuo aliotajiwa na jirani.

    “Sawa asanteni sana kwa msaada wenu.” Vivian alimshukuru jirani yake kwa msaada wao wa kumuwaisha mtoto wake hospitali.

    “Usijali shemeji.” Jirani alitamka maneno ambayo yalidhihirisha upendo kumaanisha kwamba ile ni sehemu ya majukumu yao.

    Baada ya Vivian kumaliza kuzungumza na Yona, alipata wazo la kuelekea nyumbani kwa mama yake kwenda kutafuta njia ya kuikomboa familia yake katika bonde la umauti. Aliona akiendelea kuchelewa mda sio mrefu atakufa aidha mwanae wa mwisho ama mume wake. Saa 12.35 jioni alianza safari ya kuelekea nyumbani kwa mama yake, hakuona sababu ya kuendelea kuchelewa kwasababu alihisi hali ya hatari zaidi katika familia yake. Simu ile ilikuwa kama imempa nguvu pamoja na ujasiri wa kumwendea mama yake. Aliwasha gari lake na kuondoka kwa mwendo mkali kuelekea nyumbani kwa mama yake mzazi.

    Kwa kasi aliyokuwa anaendesha gari lake alitumia dakika chache sana kufika nyumbani kwao ingawa kulikuwa na umbali wa kama kilometa ishirini na ushee. Alipofika alimkuta mama yake yupo jikoni anapika chakula cha usiku. Mama yake alionyesha kufurahia sana ujio wake, ingawa Vivian alikuwa na hasira na chuki kubwa ndani ya moyo wake kutokana na mambo ambayo mama yake alikuwa anamtendea. Vivian alimsihi sana mama yake asiendelee kuangamiza familia yake lakini cha kusikitisha ni kwamba bado mama alimweleza kwamba hakuna suluhisho la matatizo yale isipokuwa kupokea uchawi aliokuwa anambembelezea kila wakati ili aweze kupokea.

    Vivian alilia sana kwasababu hakuwa tayari kupokea uchawi ambao alikuwa anapewa na mama yake. Baada ya kumbembeleza mama yake kwa muda mrefu bila mafanikio ya aina yeyote aliona kuliko mume wake na mtoto wake wa mwisho kufa ni bora akubali kupokea ule uchawi aliokuwa anapewa ili aweze kunusuru maisha yao. Kichwani mwake alipanga atakapopewa atakwenda kuitia kiberiti ili kuipoteza kabisa kwasababu hakuwa tayari kuingia katika ulimwengu wa ibilisi.

    Baada ya Vivian kumweleza mama yake kwamba amekubali kupokea uchawi, mama yake alionyesha furaha ambayo mwanae hakuwahi kuishuhudia tangu kuzaliwa kwake. Kutokana na furaha aliyoipata mama Vivian alimsogelea mwanae na kumkumbatia huku akimbusu katika mashavu yake kwa mara kadhaa. Kwa wakati huo Vivian alikuwa akilia sana kwasababu haikuwa ridhaa yake kukubali uchawi bali alilazimika ili kunusuru maisha ya familia yake. Mama yake alimshika mkono halafu wakatoka jikoni na kuongozana moja kwa moja hadi chumbani. Walipofika chumbani Vivian alikalishwa kitandani na baada ya hapo alipakwa mafuta fulani yanayonukia vizuri sana katika paji lake la uso.

    Wakati zoezi la kupakwa mafuta likiendelea Vivian aligubikwa na giza nene na ghafla alijihisi ametokea katika uwanja mkubwa kama wa mpira wa miguu. Wingu lilikuwa limefunga kana kwamba mvua ilikuwa inataka kunyesha, vishindo vya radi iliyoambatana na miale mikali iliyokuwa inamulika mithili ya flashi ya kamera, kelele za budi pamoja paka zilikuwa zimechachamaa. Moyo wa Vivian ulijawa na hofu kubwa sana kwasababu alijiona yupo peke yake katika mazingira ambayo yalikuwa yanampa vitisho vikubwa ndani ya moyo wake. Umbali kama wa mita 50 kutoka pale alipokuwa amesimama alisikia sauti iliyoambatana na mwangwi mkali ikimuita.

    “Vivian..an..an..an! Vivian…an…an..an!”

    Bila hiyari yake alishaangaa anatembea kulekea kule sauti ilipokuwa inatokea. Miale ya radi ilizidi kukera macho yake wakati alipokuwa anazidi kutembea. Ghafla Alisikia sauti ya kicheko iliyoambatana na maneno ya ukaribisho. “Ahahaha! Ahahaha! Karibu mwanangu, huku ndio nyumbani kwenu, usiogope, wala usitishike.”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Vivian alizidi kuogopa kwasababu sauti aliyoisikia ilimuogopesha halafu isitoshe alishindwa kuelewa ilipokuwa ikitokea. Wingu jeusi lilikuwa limefunika anga na kusababisha giza kubwa. Wakati alipokuwa anazidi kutembea taratibu macho yake yaliona kama kuna mtu ambae alikuwa amekaa kwenye kiti umbali wa kama mita 15. Alijitahidi kuangalia kwa umakini ili aweze kumwona vema lakini alishindwa kutokana na miale ya radi iliyokuwa imetia fora. Hofu ilizidi kutambaa kifuani mwa Vivian na kusababisha mwili wake kupoteza nguvu. Ingekuwa anatembea kwa hiyari yake basi ingemuwia vigumu kuendelea kusonga mbele kutokana na wasiwasi mwingi uliyokuwa umetawala ndani ya nafsi yake. Kwa jinsi alivyokuwa anazidi kutembea ndivyo ambavyo alivyokuwa anazidi kusogea karibu na yule mtu ambae alimwona kwa mbali akiwa ameketi kwenye kiti cha kuegemea.

    Mashaka yalizidi kumtawala Vivian kwasababu macho ya mtu aliyekuwa anamwona mbele yake yalikuwa madogo kama kidoge lakini yalikuwa yanawaka mithili ya tochi yenye betri mpya. Umbo lake lilikuwa ni la kutisha sana, mwonekano wake ulikuwa ni kama sokwe si sokwe, mtu si mtu kiukweli Vivian alishindwa kuelewa kiumbe kile ni cha namna gani. Sauti yake ilikuwa ni nzito sana ingawa alionekana kuwa na umbo kama la kike. Meno yake licha ya kuwa mirefu na mikubwa lakini pia ilikuwa mbalimbali kama vile ya meno ya mbwa. Moyo wa Vivian ulikuwa unamdunda kwa kasi isiyokuwa na mfano. Aliona amekutana na shetani mubashara kabisa bila kutegemea. Mwonekano wa kutisha wa kile kiumbe ambacho Vivian alikifikia na kushindwa kukielewa ulisababisha atetemeke kama vile mgonjwa wa degedege.

    “Usiogope, Vivian.” Sauti nzito ilisikika ikitoka kwa yule kiumbe na kuzidisha hofu zaidi ndani ya nafsi ya Vivian.

    Vivian alitamani kuzungumza lakini alishindwa, macho yalikuwa yanamtoka, utafikiri alikuwa anaangalia kwa kukomoa. Vivian alihamriwa kuketi chini baada ya hapo kile kiumbe kilimsogelea na kukamata kidole gumba nakisha kukichanja kwa wembe. Damu iliyotoka ilikingiwa kwenye kibuyu ambacho kilifanana na kibuyu ambacho aliwahi kupewa na mama yake na kukikataa. Zoezi la kuchanjwa na damu kukingwa lilikamilika baada ya muda mfupi. Baada ya hapo kile kiumbe kilimpiga Vivian kwa usinga usoni na kisha Vivian alishtukia yupo kitandani kwa mama yake anahema kwa pupa.

    ************

    Alionekana kama vile hana fahamu za kutosha, mama yake alitumia usinga wenye majimaji yanayowasha kwa mbali kumpiga nao katika paji la uso na ndipo Vivian alirudi katika hali yake ya kawaida. Vivian alikumbuka yote yaliyotendeka muda mfupi uliopita wakati alipokuwa na kile kiumbe ambacho alishindwa kukielewa. Alitazama kidole gumba chake na kugundua kuwa kuna jeraha la kuchanjwa na wembe na pia kilikuwa kinavuja damu kidogo. Alishangaa sana kwasababu damu yake ilikingwa muda mfupi na kiumbe ambacho hakukielewa ni cha namna gani na pia hakujua damu yake inakwenda kufanya nini.

    “Mama! nilikuwa wapi?” Vivian alimuuliza mama yake swali huku akimtazama kwa mshangao.

    “Usijali mwanangu kule nimekupeleka kwaajili ya zoezi fupi tu la maagano na kuzimu ili niweze kukukabidhi uchawi nilioachiwa na bibi yako.” Mama Vivian alizungumza maneno ambayo yalisababisha Vivian ajutie uwamuzi wake wa kukubali kupokea uchawi. Roho ilimuuma sana baada ya kuambiwa kwamba kilichokuwa kimefanyika ni maagano ya kuzimu, tena maagano ya damu ambayo alichanjwa katika kidole gumba. Vivian alikabidhiwa ule uchawi na mama yake, kwa masharti mengi. Mama yake alimweleza kwamba anapaswa kuitunza kibuyu kile kisionekane na mtu yeyote. Alimweleza pia kibuyu kile huwa kinahitaji damu za watu mara kwa mara. Kwahiyo afanye hivyo endapo kitahitaji kwasababu akigairi itachukua roho yake upesi.

    Alielezwa kwamba chochote atakachokitaka anene na kile kibuyu na matokeo atayaona baada ya muda mfupi sana. Alipewa ahadi na mama yake kwamba kwa siku za mwanzoni watakuwa wanaongozana wote kwenda kuzimu hadi atakapozoea. Mambo mengine mengi mama yake alimsisitiza kwamba atayafahamu katika kikao kikubwa cha ukaribisho kitakachofanyika kuzimu siku chache za mbeleni. Maneno ambayo Vivian alikuwa anasikia akielezwa na mama yake yalimwogopesha sana kiasi kwamba hadi akaanza kububujikwa na machozi. Aliona moja kwa moja siku zijazo na yeye atahusika kutoa roho za watu wasio na hatia kisa uchawi aliokuwa amekabidhiwa rasmi. Roho ilizidi kumuuma kwasababu hakuwa na namna kwasababu mama yake alikuwa ameazimia kuiangamiza familia yake moja kwa moja. Baada ya makabidhiano kukamilika Vivian alikuwa na maswali kadhaa ya kuuliza kwasababu alijiona yupo katika wakati mgumu pasipo kutegemea.

    “Vipi hali ya mume wangu na mwanangu hospitali?” Vivian aliuliza.

    “Nimekwambia chochote unachotaka, zungumza na hicho kibuyu kwa mara tatu na matokeo utayaona ndani ya muda mfupi.” Mama alimjibu Vivian kwa ukali kidogo kwasababu alionekana kutoelewa kwa haraka.

    “Nimekwelewa ila nahisi hilo la kutoonekana na mtu yeyote litanishinda kwasababu wewe mwenyewe unafahamu kuwa naishi na familia yangu, sasa unafikiri litawezekana vipi?” Vivian alizidi kuuliza maswali ambayo yalikuwa yanamtatiza kuhusiana na masharti aliyoelezwa na mama yake.

    “Usiwe na wasiwasi kuhusu suala la kuonwa na mume wako au ndugu yeyote wa mume wako, hao wote akili zao zimefungwa.” Mama alizungumza maneno ambayo yalimshtua sana Vivian.

    “Vipi kuhusu ndoto mbaya ambazo tumekuwa tukiota mimi na mume wangu kila mara zitafikia kikomo?” Vivian alimuuliza mama yake swali jingine ili aweze kupatiwa majibu sahihi.

    “Usiogope, maadamu umekubali kupokea uchawi basi hamtaota tena ndoto za kutisha.” Jibu la mama lilimfariji Vivian kwasababu alikuwa amechoshwa na njozi za kutisha kila mara.

    Baada ya zoezi la makabidhiano kukamilika Vivian alikwenda katika gari lake na kuwasha na kuondoka kuelekea nyumbani kwake. Ingawa alikuwa na uwakika wa mwanae na mume wake kupona lakini moyo wake ulikosa amani kabisa. Nafsi ilikuwa inamsuta kwa maamuzi ambayo aliyafanya kwa haraka kwa lengo la kunusuru maisha ya mume na mtoto. Alipokuwa anakitazama kile kibuyu alichokuwa amekitia katika mkoba wake moyo ulimuuma sana. Alishindwa kuelewa kwanini mama yake ameamua kumdumbukiza katika mikono ya ibilisi ilihali yeye ni mwanae wa pekee.

    Saa 2.50 usiku ndio muda ambao Vivian alifika nyumbani kwake akitokea nyumbani kwa mama yake. Alimkuta mama mkwe wake ameshaingia chumbani kwake kujipumzisha kwasababu alikuwa amechoka. Uchawi ambao Vivian alikuwa amepewa na mama yake alikwenda kuuficha chumbani kwake. Maneno ya mama yake kwamba Nelson pamoja na ndugu zake wote akili zao zimefungwa ilipunguza hofu ndani ya mtima wa Vivian kuhusu ule uchawi aliokuwa nao. Mara baada ya kula chakula alikwenda kujifungia chumbani na kuuchukua ule uchawi kisha akaanza kunena nao. Saa ya ukutani ilionyesha ni saa 4.09 usiku.

    “Mume wangu, Nelson rejea katika afya njema haraka upesi.” Vivian alitamka maneno hayo kwa mara tatu.

    Baada ya kunenea kibuyu kile cha kichawi maneno kwaajili ya kumkomboa mume wake, alitamka maneno hayohayo kwaajili ya kumnasua na mwanae Benedict. Usiku wa siku hiyo Vivian hakufumba jicho lake, hakuamini kwamba yale maneno machache aliyoyatamka yataweza kumponya mume wake katika hali mbaya aliyokuwa nayo. Licha ya mawazo juu ya afya ya mume wake pamoja na mwanae lakini pia nafsi iliendelea kumsuta zaidi na zaidi kwa ule uwamuzi ambao alikuwa ameuchukua. Alitamani laiti kama kungekuwa na uwezekano mume wake na mtoto watakapopona aweze kurudisha uchawi ule lakini ni jambo ambalo lilikuwa haliwezekani. Moyo ulizidi kuwa mzito kukubali kutumikia uchawi aliokuwa amepewa na mama yake. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Alikumbuka maisha ya upweke aliyokuwa anaishi wakati alipokuwa nyumbani kwao kisa uchawi wa mama yake. Mama yake hakuwa na rafiki, hakushiriki katika sherehe wala misiba ya ndugu hata jamaa, alikuwa anaishi kivyake vyake, jamii ilimtenga kwasababu ya uchawi wake. Roho ilimuuma sana kwasababu aliona yale maisha aliyokuwa anaishi mama yake ndio na yeye atakuwa anaishi vivyo hivyo. Maisha ambayo yalikuwa yametawaliwa na ushetani uliokithiri. Mambo mazito aliyokuwa anawaza Vivian yalisababisha machozi yasikauke katika macho yake. Kitendo cha Vivian kuwa peke yake chumbani kilisababisha amwage machozi hadi atosheke. Wimbi kubwa la mawazo kichwani mwa Vivian lilisababisha akose usingizi kabisa.

    ************

    Saa 4.15 usiku Nelson alianza kurusha rusha miguu huku na kule wakati alipokuwa katika chumba cha uwangalizi maalumu. Hali yake ilikuwa inaonyesha kama anakata roho kwasababu kwa siku zote alizokuwa amefikishwa pale hospitali alikuwa hajiwezi kabisa. Kila kitu alikuwa anawezeshwa kwa mashine kuanzia kupumua, kula, kunywa, mpaka kujisaidia. Nelson alizidi kuhangaika wodini mithili ya mtu ambae anachukuliwa na umauti. Kibaya zaidi kwa wakati ule hapakuwa na nesi wala daktari katika chumba chake. Mashine ya oksijeni iliyokuwa inamwezesha kupumua barabara ilionyesha kwamba kiwango cha mapigo ya moyo wake kilikuwa kinapanda kwa kasi. Nelson alikuwa anazinduka kutoka katika usingizi wa umauti aliokuwa amelala kwa muda mrefu kitandani. Mboni za macho yake yalikuwa kama yanaukungu mzito ambao ulisababisha ashindwe kufumbua macho yake kwa haraka. Mwili wake ulizidi kupata nguvu wakati fahamu zilipokuwa zinazidi kumrejea.

    Kivivu alianza kufumbua macho yake na nuru ilianza kupenyeza katika macho yake ingawa alishindwa kuelewa yupo wapi. Wakati alipokuwa anazidi kugaragara pale kitandani wakati fahamu zilipokuwa zinamrejea nesi wa zamu ambae alikuwa akipita wodi moja baada ya nyingine kuwapa wagonjwa dawa. Alishikwa na bumbuwazi baada ya kuingia katika wodi ya Nelson ambaye ndie mgonjwa aliyekuwa na hali mbaya kuliko wagonjwa wote waliokuwa wamelazwa hospitalini pale. Hali ya Nelson ilimshangaza sana kwasababu alionekana kuwa na nafuu ambayo hakuitegemea. Jambo lile nesi aliliona kama ni muujiza.

    Nesi hakuweza kuzungumza kitu chochote zaidi sana miguu yake ilipata nguvu ya kutoka wodini pale kwa kasi ya ajabu na kwenda kumwita daktari. Baada ya muda mfupi daktari alifika wodini akiwa amegozana na nesi. Dokta alionyesha kushangazwa na unafuu wa ghafla aliokuwa ameupata Nelson. Alimtolea mashine ya oksijeni iliyokuwa inamwezesha kupumua vizuri kwasababu alionekana kuwa na uwezo wa kupumua mwenyewe bila msaada wa mashine. Baada ya hapo dokta alimtolea na mirija maalumu ya kumwezesha kula na pia kujisaidia. Nelson alionekana kupepesa macho yake kutazama huku na kule ili aweze kufahamu alipokuwa.

    Daktari alimshauri nesi aendelee kupita katika wodi zingine kuendelea kuwapa wagonjwa wengine dawa wakati yeye akiendelea kuangalia maendeleo ya Nelson. Nesi alifanya kama alivyoelezwa na daktari lakini unafuu wa Nelson ulitengeneza maswali mengi sana akilini mwake kwasababu ilikuwa ni wa ghafla sana. Dakika ishirini baadae fahamu zilimrejea Nelson barabara, daktari alimuuliza anahisi maumivu sehemu gani ya mwili wake lakini alijibu yupo sawa kabisa. Daktari alishangaa sana kwasababu kwa vipimo vya awali ambavyo alimfanyia Nelson aligundua kuwa ameumia kichwani, kibaya zaidi ubongo wake uliathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa ameyapata kichwani.

    Kwa athari aliyokuwa ameipata katika ubongo wake vipimo vilionyesha kupona kwake kupo mashakani, na hata kama angepona mwisho wa siku angekuwa mwehu. Daktari alishangaa sana kwasababu hakuwahi kukutana na mgonjwa kama yule hata siku moja. Alijiuliza maswali mengi bila kupata majibu. Usiku huohuo alimfanyia Nelson vipimo mbalimbali kuangalia maendeleo yake lakini vipimo vilionyesha Nelson hana hata mafua licha ya ugonjwa mwingine mkubwa. Kusema kweli dokta alizidi kuduwaa kwasababu aliona yale yaliyokuwa yakiendelea mbele yake ni kama mazingaumbwe. Baada ya kuhakikisha kwamba Nelson anaendelea vizuri aliondoka na kumwacha wodini akiwa amelala.

    ************

    Muda uleule ambao Nelson alipata uponyaji, ndio muda ambao mwanae Benedict alionesha mabadiliko mazuri ya kiafya ambayo yaliwashangaza pia wauguzi ambao walikuwa wakimuudumia katika wodi aliyokuwa amelazwa. Hali yake hospitalini hapo ilikuwa ni mbaya sana kwasababu mwili wake ulionyesha uhitaji mkubwa wa damu ili hali madaktari walishindwa kuelewa sababu iliyokuwa ikipelekea Benedict kuishiwa damu kwa kasi ya kutisha. Lakini ghafla usiku ule vipimo vilionyesha kwamba kiwango cha damu katika mwili wa Benedict kimepanda kwa kiasi cha kutosha. Kwahiyo zoezi la kuongezewa damu lilisimamishwa. Hali ya Benedict ilionyesha kuhimarika kwa kasi ya ajabu, jambo ambalo halikutegemewa na wauguzi kutokana na hali aliyokuwa nayo.

    *************

    Asubuhi na mapema mjomba alifika hospitali kwasababu jana yake hakuweza kufika kwasababu walikuwa katika shughuli ya mazishi ya Mainard. Alianza kwenda kumwangalia Benedict ambae alilazwa jana yake hospitalini hapo. Alikuta hali yake inaendelea vizuri kabisa, walikaa na kupiga nae stori mbili tatu kisha alimwacha na kwenda katika kitengo cha uwangalizi maalumu ambapo ndipo alipokuwa amelazwa Nelson. Alipoingia wodini hakuamini macho yake baada ya kumkuta Nelson amekaa kitandani anazungumza na daktari. Aliona kama yupo ndotoni kwasababu hakutegemea kabisa kumkuta Nelson katika hali ya kuridhisha namna ile. Kabla hata ajasalimiana na daktari alimfuata Nelson na kumkumbatia kwa furaha isiyomithilika.

    “Pole sana mjomba kwa matatizo.” Mjomba alizungumza huku akidondokwa na machozi kutokana na furaha aliyoipata.

    “Asante sana anko.” Nelson aliitikia salamu ya mjomba wake huku na yeye akidondokwa na machozi. Baada ya mjomba kuona Nelson anaendelea vizuri alianza kumshukuru daktari kwa jitihada zao ambazo zilipelekea Nelson kurejea katika hali yake ya kawaida. Daktari alishukuru ingawa alimwelezea Mjomba jinsi hali ya Nelson ilivyohimarika kwa kasi tangu usiku wa kuamkia siku hiyo. Kiukweli hata mjomba alishangaa sana kwasababu alikumbuka maneno ya daktari huyo katika siku zilizopita kuhusiana na kupona kwa Nelson. Kila mtu aliona ni kama nguvu ya Mungu ndio imemponya Nelson kwasababu hakuna aliyetegemea kumwona Nelson akiwa mzima wa afya tena kutokana na ajali mbaya ambayo aliipata na kusababisha majeraha makubwa katika mwili wake, hususani kichwani. Nelson alikumbuka kwamba mwanae Mainard alikuwa ni mgonjwa kwahiyo ilibidi amuulize mjomba wake kuhusu maendeleo ya mwanae lakini ilibidi Mjomba amdanganye kwamba anaendelea vizuri kwasababu alihofia kumpa taharifa za msiba wakati akiwa bado wodini.

    Furaha aliyoipata Mjomba alishindwa kabisa kuimudu, kwahiyo alichukua simu yake na kumpigia dada yake ili aweze kumweleza hali ya kijana wake. Mama Nelson alifurahi sana aliposikia kwamba mwanae amepata nafuu, furaha ilimzidi baada ya mjomba kumpa Nelson simu halafu akazungumza na mama yake. Mazungumzo mafupi ya mama na mwanae yalirudisha matumaini yaliyokuwa yamepotea katika moyo wake. Baada ya Nelson kuzungumza na mama yake, mke wake alipokea simu na yeye kisha akazungumza na mume wake ambae sauti yake ilidhihirisha ni mzima kabisa. Walifurahi sana kwasababu walijua hali ya mgonjwa ilikuwa ni mbaya sana hospitali.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Simu ya mjomba ilisababisha mama na mke wa Nelson waahirishe safari ya kwenda hospitali kwasababu walielezwa kwamba muda wowote wagonjwa wote wanaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani kwasababu hali zao zilikuwa zikiendelea vizuri kabisa. Siku iliyofuata Nelson na mwanae waliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya madaktari kuridhika na maendeleo ya hali zao. Nelson alipofika nyumbani ilibidi aelezwe ukweli kwamba mwanae alifariki na amezikwa katika makaburi ya njiro wakati alipokuwa hoi hospitali. Alilia kwa uchungu sana huku akimlaumu Mungu kwanini hakumpa hata nafasi ya kumzika mwanae. Kwa masikitiko makubwa siku hiyo hiyo alikwenda kudhuru kaburi la mwane.



    Kwa kipindi kifupi kilichopita maisha ya Nelson yalikuwa yamevurugika kwa kiasi kikubwa, uchumi wao ulikuwa umedorora kutokana na pesa nyingi zilizotumika hospitali. Ufuatiliaji wa biashara zao ulikuwa hafifu kiasi kwamba mambo yakawa yanakwenda shagalabagala. Walianza kujipanga tena upya ili familia yao iweze kwenda vizuri, baada ya miezi kadhaa maisha yao yaliendelea vema. Ndoto za kutisha hazikuwaandama tena. Mama Nelson alipoona mambo yanakwenda sawa sawia aliamua kurudi nyumbani kwake. Nelson na mke wake walibakiwa na mtoto mmoja jambo ambalo liliwafanya watamani kuendelea kuzaa lakini haikuwezekana kwasababu kizazi cha Vivian kilikuwa kimeshafungwa. Mapenzi yao ya dhati waliangushia kwa mwanao wa pekee, Benedict.

    Walimpenda na kumjali sana kwasababu hawakuwa na mwingine wala uwezo wa kumpata mwingine. Upendo wa Nelson na mke wake ulizidi kukuwa siku hadi siku. Kutokana na siri kubwa iliyokuwa imejificha moyoni mwa Vivian ilisababisha muda mwingi akose raha. Alijiona kama amejitia kitanzi ambacho hawezi kujinasua. Alitamani mume wake angefahamu kilichokuwa kikiendelea lakini hakuwa na pakuanzia. Aliwaza Nelson atamtupia lawama nyingi sana kwa kuwa alichelewa kumwambia. Alizidi kumuangushia mama yake lawama kimoyomoyo kwa kuwa ndiye aliyemvalisha viatu ambavyo sio saizi yake. Muda mwingi Vivian alipokuwa peke yake alikuwa ni wa kulia tu. Aliwakumbuka wanae wawili ambao walipoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.

    Furaha ilipotea kabisa moyo wake hakuona sababu ya kuendelea kuishi katika dunia ya Mungu ili hali tayari alikuwa amemuasi Muumba wake. Utendaji wa kazi zake ulishuka kwa kiasi kikubwa hadi wakati mwingine mume wake alikasirika kwa kumuona sio mtu makini kama alivyokuwa mwanzoni. Wakati fulani alidiriki kuchukua ule uchawi kisirisiri kwa lengo la kupeleka kanisani ukachomwe, lakini cha kushangaza ni kwamba alijikuta yupo nyumbani kwa mama yake badala ya kanisani. Kitendo kile kilimchanganya sana kwasababu alishindwa kuelewa amefika vipi nyumbani kwa mama yake ili hali alikuwa anakwenda kwa mchungaji.

    Mama yake alimweleza kuwa asijaribu kutekeleza wazo lililopo akilini mwake kwasababu atakufa kifo kibaya sana. Vivian aliogopa sana alijiuliza mama yake amewezaje kufahamu jambo alilokuwa anawaza akilini mwake. Aliishia kumuona mama yake sio mtu wa kawaida kwa lile tukio la kuona njia ya nyumbani kwao ndio ya kanisani. Mateso aliyokuwa anapitia Vivian ni mateso makubwa ambayo hayaelezeki kwa kalamu wala karatasi. Wingi wa mawazo kichwani mwake, ulipelekea muda mwingi kukesha bila kupata hata lepe la usingizi. Alitamani sana maisha aliyokuwa anaishi mwanzo kabla ya kubebeshwa furushi la kichawi.

    Siku moja usiku wa manane Vivian alizinduka usingizini baada ya kusikia kama sauti ya mama yake ikimuita. Alifumbua macho yake taratibu na kumwona mama yake amesimama kandokando ya kitanda chake huku pembeni mume wake akiwa amelala fofofo. Vivian alishtuka sana hadi akahisi haja ndogo kwasababu hakujua mama yake amewezaje kufika pale ndani kwake wakati milango na madirisha yote ilikuwa imefungwa. Vivian aliambiwa asiogope kwasababu akili ya Nelson ilikuwa imefungwa kwahiyo hawezi kuona wala kusikia chochote kilichokuwa kikiendelea pale chumbani. Vivian alishuka kitandani baada ya kupata ishara kutoka kwa mama yake. Moyo wake ulizidi kumwenda mbio kwasabaabu hakujua ujio wa mama yake ulikuwa ni wa nini. Baada ya kuteremka kitandani alichukua kibuyu chake na kujongea taratibu hadi kweye kona ya nyumba ambapo ndipo mama yake alipokuwepo akimwita kwa ishara. Walishikana mikono na ghafla walipotea baada ya mama yake kunena maneno ambayo Vivian hakuweza kuyasikia vizuri kwasababu yalizungumzwa kwa sauti ya chini sana.

    ***********

    Kufumba kufumbua Vivian alishangaa ametua katikati ya watu wengi ambao walikuwa wanazunguka wakicheza ngoma kwa mitindo ya kuogopesha. Alishindwa kuelewa pale ni wapi lakini kwa akili yake ya harakaharaka aligundua kule ni kuzimu kutokana na watu aliokuwa anawaona mbele yake hawakuwa na sura za kawaida. Kutua kwake kulisababisha kelele za shangwe ziongezeke pale ukumbini, ule umati ulifurahia baada ya kumwona Vivian amewasili. Walizidi kucheza na kuimba kwa furaha sana. Vivian hakuhisi furaha yeyote kwasababu yale mazingira yalikuwa yanamtisha sana. Muda mfupi baadae zile kelele zilisimama. Malikia alimuhamuru Vivian anyanyuke aende stoo akachague binadamu wawili walionona ili waweze kuliwa kwa siku hiyo. Vivian alitii amri ya malikia, aliongozana na binti mmoja ambae alionekana kuwa mzoefu halafu isitoshe Vivian alitokea kumpenda ghafla kwasababu alikuwa na sura na umbile zuri sana kama binadamu wa kawaida. Walitembea kwa mwendo wa haraka kidogo huku wakipiga stori za hapa na pale.

    “Karibu sana Vivian, usiogope maisha ya huku ni raha sana muda wote tunakula na kunywa.”

    “Unaitwa nani?” Vivian alimuuliza yule binti ambae alionekana kumchangamkia sana.

    “Naitwa Latifa bin Lusifa.”

    “Ila mimi huku sipapendi hata kidogo.” Vivian alimweleza Latifa juu ya hisia zake.

    “Ahahahaha!” Latifa alicheka cheko ambalo lilimfanya Vivian aogope kwasababu aligundua meno yake sio ya kawaida kwani ilionekana kuwa mirefu kupita maelezo.

    “Ugeni ndio unakusumbua ila ukishapazoea kila kitu utaona shwari.” Latifa alimjibu Vivian wakati alipokuwa anafungua mlango wa stoo ili aweze kuwachukuwa watu wawili walionona. Waliingia ndani na kukutana na sura za watu wengi ambao walikuwa wamefungwa minyororo huku sura zao zikionyesha kwamba wamelia hadi wamechoka. Latifa alimuamuru Vivia kufanya kama alivyoagizwa na malikia. Vivian alianza kuangalia huku na kule ili aweze kumpata binadamu aliyenona kama ambavyo alihamriwa. Vivian aliona sura nyingi za watu ambao alikuwa anawafahamu, ila duniani walikuwa wanauguzwa mahospitalini na wengine tayari walikuwa ni marehemu.

    Aliwaonea huruma sana kwa jinsi ambavyo walikuwa wanalia kwa huruma huku wengine wakionyesha kumfahamu kabisa. Huruma aliyoipata ilisababisha ashindwe kufanya uchaguzi kwa wakati. Ingawa latifa alimweleza afanye haraka kama ambavyo alielezwa la sivyo atakwenda kupata adhabu lakini hakuelewa. Alishindwa kabisha kumchagua binadamu mwenzake ambae atakwenda kutolewa uhai muda mfupi ujao. Latifa alipoona kwamba Vivian ameshavunja sheria ya kuzimu aliamua kumuacha ili adhabu atakayopewa isimuhusu.

    Kwahiyo Latifa alirudi ukumbini na kumuacha Vivian akiwa anazidi kushangaa umati wa watu ambao alikuwa anawafahamu, wengine wakiwa ni marafiki zake ambao waliwahi kusoma wote. Roho ilimuuma sana kwasababu hakuwa na namna ya kuweza kuwanusuru na adhabu ya umauti uliokuwa mbele yao. Wakati alipokuwa anazidi kushangaa mule ndani alishangaa amekuja kuchukuliwa kwa nguvu na kurudishwa ukumbini huku akilia sana. Malikia alionekana kukasirika sana, kwa kitendo ambacho kifanywa na Vivian kushindwa kutii amri yake.

    “Nimekupa kazi ndogo sana ya kwenda kuwachagua binadamu wawili walionona ili waje kuwezesha sherehe yako ya kukaribishwa kuzimu, lakini umeonekana kushindwa. Umeniudhi sana kwa kivunja sheria. Adhabu ninayokupa ni kwamba nakutuma tena ndani ya dakika chache zijazo uwe umeleta damu za watu kumi kutoka duniani.” Malikia alitamka kwa hasira. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Vivian aliwaza atakwenda wapi kupata roho za watu kumi kwa wakati ule, wakati hajawahi kuuwa tangu kuzaliwa kwake. Wakati alipokuwa anawaza cha kufanya Latifa alimfuata na kumuahidi kumsindikiza kwa mara nyingine. Kwahiyo walitoweka kuzimu na kutokea duniani katika jiji kubwa la Dar es salaam, usiku wa manane. Vivian alionekana kuwa na mashaka ya upatikanaji wa damu aliyokuwa ameagizwa kwasababu hakuwa na uzoefu wowote. Latifa alimweleza asiogope kwasababu adhabu aliyokuwa amepewa ni ndogo sana. Walifika katika baa moja maeneo ya Kimara suka ambayo ilikuwa kandokando ya barabara. Baa hiyo ilikuwa na vijana wengi wanaocheza mchezo wa pultebo hadi muda ule.

    Latifa alimweleza Vivian azungumze na kile kibuyu alichokuwa nacho ili gari la mizigo linalopita barabarani likosee njia ivamie ile baa wale vijana wafe, halafu wachukue damu waliyokuwa wameagizwa. Kweli Vivian hakupoteza muda alifanya kama ambavyo alielekezwa na baada ya sekunde kadhaa walishuhudia gari aina ya skania iliyokuwa ikiingia Dar usiku ule ikiacha njia na kuvamia baa ambayo walikuwa wameikusudia. Vijana wote waliokuwa wakicheza pultebo katika baa ile pamoja na dereva na tingo wake walipoteza maisha. Vivian pamoja na Latifa walikinga damu ya kutosha na baada ya hapo walipeleka damu iliyokuwa inahitajika kwaajili ya sherehe ya kukaribishwa kwa Vivian.

    Walipofika kuzimu malikia alifurahi sana kwasababu Vivian aliweza kutekeleza adhabu aliyokuwa amepewa. Walikunywa damu yote iliyokuwa imepatikana kwa furaha sana. Malikia alimtuma tena Vivian kwenda stoo kuwachukuwa watu wawili walionona ili nyama zao zije ziliwe kwasababu ile siku ilikuwa ni ya furaha sana. Vivian alikwenda moja kwa moja haraka haraka na kuwachukua watu wawili na kuwafikisha mbele ya malkia. Alifanya kwa haraka bila kuchelewa ili asipewe adhabu nyingine. Bila kutegemea malkia aliagiza Vivian apewe kisu ili aweze kuwachinja wale watu upesi.

    Moyo wa Vivian ulidunda sana kwasababu aliona ni zoezi ambalo ni gumu kuliko lile alilokuwa ametoka kulifanya muda mfupi uliopita. Hakuwa na namna alifanya kama ambavyo aliagizwa. Aliwalaza mmoja baada ya mwingine juu ya meza na kutenganisha vichwa vyao na kiwiliwili. Malikia alishindwa kuzuia hisia zake za furaha baada ya Vivian kufanikisha zoezi alilokuwa amepatiwa. Furaha iliongezeka kwa wale viumbe vya ajabu vilivyokuwepo pale ukumbini. Vivian alikatakata ile miili katika vipande vikubwa vikubwa ambapo vilianza kushambuliwa baada ya muda mfupi na wale viumbe ambavyo alishindwa kuelewa ni vya namna gani ingawa walifanana sana na binadamu.

    Halikadhaliaka yeye pia alishiriki barabara kula nyama ile ambayo ilikuwa ni mbichi kabisa. Mwanzoni ilikuwa inampa kinyaa lakini alizoea na kuona kawaida. Sherehe ile ya damu na nyama za binadamu ilifana sana kutokana na kwamba kila aliyekuwepo ukumbini alifurahia sana. Nyama ilikuwa tamu sana kiasi kwamba kila aliyekuwepo ukumbini pale aliishia kujilamba. Sherehe ilikwisha na Vivian alirudi duniani.

    ***********

    Vivian alijishtukia yupo kitandani kwake amelala, huku akisikia sauti ya mume wake pembeni yake akikoroma. Alijihisi kuchoka sana kutokana na mikiki mikiki aliyoipata wakati alipokuwa kuzimu. Aliangalia saa ya kwenye simu yake inamuonyesha ni saa nane na dakika kumi na tano. Moyo ulimuuma sana alipokumbuka mauwaji ya kutisha ambayo aliyafanya usiku ule. Nafsi ilimsuta kwasababu alikuwa ametowa roho za watu wasikuwa na hatia. Palipokucha asubuhi walipata kifungua kinywa kila mtu akaelekea katika shughuli zake. Redio, pamoja na televisheni zote nchi nzima ziliripoti kuhusu ajali mbaya iliyotokea usiku wa kuamkia siku hiyo. Habari ile ya kusikitisha, ilimnyima amani Vivian kwasababu yeye ndiye aliyesababisha vifo vya jumla watu 10 kwenye ajali na kisha damu zao kunyweka kuzimu.



    Vivian alizidi kuzama katika maisha ya kichawi bila mume wake kufahamu kilichokuwa kikiendelea. Hakuna ndugu wala rafiki aliyegundua mabadiliko makubwa katika maisha ya Vivian kwasababu akili zao zilikuwa zimefungwa. Ukaribu wake na mama yake uliongezeka kutokana na shughuli zao za kichawi. Ukaribu huo ndio uliopelekea Vivian kufahamu siri nyingi nzito alizokuwa nazo mama yake. Aliapa kuzitunza siri hizo na pia alimuhakikishia mama yake kwamba atakuwa bega kwa bega na yeye katika kuuendeleza urithi aliopewa na bibi yake. Roho ya Vivian ilizidi kuwa ngumu kila kukicha kwasababu alihusishwa katika mauwaji ya mara kwa mara. Mwanzoni aliona kuuwa ni kazi ngumu sana lakini alizoea na kuona ni kitu cha kawaida. Kila siku usiku Vivian alikuwa anahudhuria vikao vilivyokuwa vinafanyika kuzimu. Maisha ya Vivian yalibadilika kiujumla ingawa bado alizidi kumpenda mume wake pamoja na mtoto wake.

    Chakula pekee alichokuwa akikifurahia ni nyama. Mara kwa mara alipenda kupika nyama anapokuwa nyumbani kwake. Hayo yote ni kwasababu tayari alikuwa ameshazoea kula nyama za watu pindi anapokuwa kuzimu. Vivian alitokea kupenda nyama kupita kiasi, kwasababu wakati mwingine anapokuwa jikoni hukata vinyango vibichi na kuvitafuna. Malikia alitokewa kumpenda Vivian kwasababu alikuwa ni mchapakazi wa nguvu. Tangu alipoanza kutumwa damu katika kona mbalimbali duniani hakuwahi kushindwa kama ilivyokuwa kwa baadhi ya maajenti.

    Malikia aliamua kumpa majukumu mazito ambayo alimwahidi endapo atafaanikiwa kuyatekeleza basi atampa nafasi ya uongozi katika baraza la kuzimu. Vivian alipewa majukumu ya kupambana na watumishi wa Mungu ili aweze kuwapeleka kuzimu. Majukumu ya Vivian yalibadilika na kuanza kuhangaika na roho za watumishi wa Mungu. Ilikuwa ni kazi ngumu na ya hatari pia lakini Vivian alikubali kuifanya kwa moyo. Jambo la kushangaza ni kwamba bado alionekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa mno kwasababu aliwapeleka kwa wingi ambao haukutegemewa hata kidogo. Vivian alifanikiwa kuwaangusha watumishi wengi wa Mungu ambao walikuwa dhaifu katika kumtumikia Mungu.

    Sifa hiyo ilisababishwa akapandishwa cheo haraka na kuwa msimamizi wa maajenti wote wa kuzimu. Kazi yake ilikuwa ni kuwaadhibu wale maajenti ambao wanatumwa damu duniani halafu wanashindwa kutekeleza majukumu. Adhabu kubwa aliyokuwa anawapa ni kuwauwa au kuwapa mateso makubwa. Hakupenda mzaa wala masihara wakati wa kazi. Umakini wake katika usimamizi wa nafasi aliyokuwa amepewa na malikia ndiyo iliyopelekea akaitoa roho ya rafiki yake Latifa bin Lusifa baada ya kushindwa kumuuwa kaka yake.

    Kupandishwa cheo kwa Vivian kulisababisha yeye asiwe anakwenda duniani kutafuta damu kama ilivyokuwa awali badala yake alikuwa msimamizi wa shughuli mbalimbali za upatikanaji wa nyama na damu. Alisimamia nafasi yake barabara kwasababu maajenti walizidi kuchapa kazi kwa bidii ili wasiweze kuangukia katika mikono ya Vivian ambayo ilikuwa inapenda kuuwa, hata kwa kosa dogo. Vivian alikuwa mgeni lakini aliogopwa sana kule kuzimu kwasababu alikuwa mkali kama chui. Katika kipindi cha uongozi wake mapipa kwa mapipa yalifurika damu kuzimu. Kila siku ilikuwa ni sikukuu kwasababu walikula nyama na damu zilizokuwa zinapatikana duniani.

    Ajali mbaya za mara kwa mara zilizidi kutokea duniani. Makumi kwa mamia walikufa kutokana na ajali zilizosababishwa na maajenti ambao walikuwa wanatumwa damu kutoka kuzimu. Katika sherehe za mwisho wa mwaka chakula kikuu kinacholiwa ni nyama za watu pamoja na damu zilizopatikana katika ajali mbalimbali. Lakini kila mwezi wa tatu na wa nne sherehe huwa ni za kula watoto wachanga (vijusi) ambavyo hunyofolewa katika matumbo ya wamama wajawazito katika mazingira ya kutatanisha. Maajenti walichachamaa walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.

    Vifo vilikuwa vinaongezeka kila iitwapo leo. Ilifika kipindi kibuyu kikahitaji damu kama ambavyo Vivian alitaharifiwa na mama yake kabla. Kwa masharti ambayo Vivian alipewa na mama yake siku aliyokabidhiwa ule uchawi ni kwamba itakapofika kipindi fulani kile kibuyu kikahitaji damu ya mtu basi afanye hivyo haraka iwezekanavyo kwasababu akichelewa roho yake inaweza kuchukuliwa. Vivian hakuwa na namna kwahiyo aliamua kumtoa mama yake Nelson kafara. Japokuwa alijua Nelson ataumia sana kumpoteza mama yake kipenzi lakini hapakuwa na namna ya kuweza kuzuia hilo lisitokee.

    Ilikuwa siku moja ya jumamosi usiku wa manane ambapo Vivian alifunga safari kutokea kuzimu kwenda duniani kumchukua mama Nelson kusudi akaliwe nyama kuzimu. Alifanikiwa kwa asilimia mia moja kutekeleza adhima yake ya kumtoa mama wa mume wake kafara. Sherehe kubwa ilifanyika ambapo nyama na damu ya mama Nelson ilishambuliwa kuzimu.

    **********CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Palipokucha siku ya jumapili, nyumbani kwa mama Nelson palikuwa na ukimya mzito. Milango na madirisha ya nyumba ilikuwa imefungwa. Taa zote za nje zilikuwa zinawaka. Muda ulizidi kusonga wakati ukimya nao ukizidi kuendelea kuchukua atamu katika nyumba ile ya kisasa, aliyokuwa amejengewa na kijana wake. Ilipofika mida ya saa tano asubuhi mama mmoja wa jirani (mama Kitomari) ambae ni rafiki wa mama Nelson. Aliamua kupitia nyumbani kwa mama Nelson akitokea kanisani ili aweze kufahamu kilichokuwa kimemkwamisha kwenda ibadani. Alipofika kwa mama Nelson alikuta taa za nje bado zinawaka hadi muda ule.

    Haikuwa kawaida kwahiyo aligonga mlango kwa mda mrefu ili aweze kufunguliwa lakini jitihada zake ziligonga mwamba kwasababu hakufanikiwa kufunguliwa. Alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia kwa mara kadhaa lakini simu iliita upande wa pili bila kupokelewa. Alipata wazo la kwenda kugonga dirisha ya chumba chake akiamini pengine labda bado alikuwa amelala lakini wazo hilo nalo halikuzaa matunda. Baada ya jitihada za muda mrefu alikata tamaa na kuamua kuondoka kwenda nyumbani kwake akiamini kwamba ataendelea kumtafuta kwa njia ya simu. Nelson nae alizoea kumpigia mama yake simu mara kwa mara kumjulia hali.

    Jumapili usiku Nelson alipokuwa sebuleni kwake akiangalia runinga alimkumbuka mama yake kwahiyo alichukua simu yake na kujaribu kuwasilina na mama yake. Simu iliita upande wa pili bila kupokelewa, Nelson alikata tamaa ya kuendelkea kumpigia mama yake simu kwa kuwaza huwenda atakuwa ameshalala. Nelson aliamua kumwandikia mama yake ujumbe mfupi wa maandishi kumtakia usiku mwema.

    “Uwe na usiku mwema mama. Nakupenda sana.” huo ndio ujumbe mfupi aliouandika Nelson kwa mama yake baada ya kuhisi atakuwa usingizini. Alifanya hivyo kusudi mama yake atakapoamka na kukutana na missed call yake ajue kwamba alimpigia kumtakia usiku mwema.

    Siku iliyofuata wakati Nelson alipokuwa kazini kwake, alikumbuka kwamba jana yake alimpigia simu mama yake lakini hakufanikiwa kumpata kwahiyo alijaribu kumpigia kwa mara nyingine tena kwasababu alikuwa amemisi sauti ya mama yake. Kwa zaidi ya mara tano alimpigia mama yake bila mafanikio ya kumpata hewani. Simu iliita hadi ikakata. Alijaribu kuwaza mama yake amekumbwa na tatizo gani tangu jana yake hapokei simu yake lakini kichwa chake kilishindwa kupata jibu la kueleweka. Alisubiri baada ya masaa mawili akajaaribu kumpigia tena simu mama yake kwa mara kadhaa lakini bado haikupokelewa. Alipata wazo la kujaribu kuwasiliana na mjomba wake ili aweze kumuuliza kama amewasiliana na mama yake katika kipindi kifupi kilichopita.

    “Shikamoo mjomba.”

    “Marahaba Nelson, hujambo?”

    “Sijambo bwana, nimejaaribu kumpigia mama simu tangu jana usiku lakini simu yake haipokelewi. Vipi wewe umewasiliana na mama tangu jana?” Nelson aliitikia salamu, nakujieleza na kisha akamalizia kwa kumuuliza mjomba wake swali.

    “Hapana, mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa siku ya jumamosi, tena yeye ndiye alinipigia kunijulia hali.” Maneno ya mjomba hayakuleta matumaini katika moyo wa Nelson kwasababu hata yeye alizungumza na mama yake kwa njia ya simu siku hiyohiyo ya jumamosi.

    “Sasa itakuwaje anko?” Nelson aliuliza swali.

    “Kwa sasa nipo kazini kwangu, kibaya zaidi leo sipo na gari langu kwasababu ningekufuata hapo kazini kwako halafu tungeongozana kwenda kwa mama kuangalia amekumbwa na tatizo gani.”

    “Kuhusu suala la usafiri ondoa shaka tutatumia gari langu.”

    “Basi hakuna tatizo, njoo sasahivi nipitie hapa kazini kwangu ili tuweze kwenda pamoja.”

    Harakaharaka Nelson alifuata utaratibu wa kuomba ruhusa kazini na baada ya muda mfupi aliondoka katika eneo lake la kazi na kuelekea ofisini kwa mjomba wake kumchukua ili waweze kwenda katika safari waliyokuwa wameipanga.

    Baada ya dakika kumi Nelson alimchukua mjomba wake kazini kwake na kuanza safari ya kuelekea maeneo ya kambi ya chupa madukani ambapo ndipo alipokuwa akiishi mama Nelson. Dakika ishirini baadae Nelson aliegesha gari lake nje ya nyumba ya mama yake. Baada ya kushuka kwenye gari walipokelewa na harufu kali mithili ya panya alieoza. Hakuna aliyeonekana kujali ile harufu mbaya ambayo ilikuwa kero katika pua zao, walihisi labda kuna mzoga uliokuwa karibu. Jambo lililowashangaza ni kwamba taa za nje bado zilikuwa zinawaka hadi wakati ule. Waligonga mlango wa mama yake kwa muda bila mafanikio yeyote. Nelson pamoja na mjomba walikwenda kwenye nyumba ya jirani kuulizia kama walikuwa na habari za mama yao.

    “Karibuuu.” Sauti ya kike ilisikika ndani ikiwakaribisha baada ya kubisha hodi katika nyumba ya jirani.

    Nelson na mjomba walijieleza kwa jirani yule ambae Nelson alifahamiana nae kipindi ambacho alikuwa anajenga ile nyumba kwaajili ya mama yake. Kilichowasikitisha zaidi pamoja na kuongeza mashaka makubwa ndani ya mioyo yao ni maelezo ambayo walielezwa na huyo jirani wa mama Nelson.

    “Kiukweli huyu mama tangu jumapili hatujamwona. Kwa mawazo ya harakaharaka tukafikiri labda alipata safari ya ghafla iliyopelekea hadi akasahau kuzima taa za nje.” Jirani alizungumza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    “Kwahiyo zile taa za nje zilikuwa zinawaka tangu jumapili?” Mjomba aliuliza kwasababu Nelson alihisi kuishiwa nguvu ghafla kutokana na maelezo aliyoyasikia kutoka kwa mama Kitomari.

    Nelson na mjomba walipata wazo la kwenda kupasuka kioo cha chumba alichokuwa analala mama yake ili waweze kuchungulia ndani. Mjomba alichukua jiwe kubwa na kubamiza katika kioo cha chumba cha dada yake na kukisarambatisha. Kitendo cha kioo kupasuka kilisababisha ile harufu mbaya waliyokuwa wanaivuta tangu walipofika pale nyumbani kuongezeka kwa kiasi kikubwa ,ambayo ilipelekea wazibe pua zao kwa vidole. Baada ya pazia kusukumwa pembeni Nelson pamoja na mjomba walirefusha shingo zao na kuchungulia ndani ya chumba na kuuona mwili wa mama Nelson ukiwa umelala chali kitandani huku ukiwa umevimba sana.

    Kwa mwonekano na harufu kali iliyokuwa inatoka chumbani mle iliashiria kwamba mama huyo tayari alikuwa ni marehemu. Nelson alianza kuangua kilio kisichokuwa na mfano. Kilio cha Nelson kilisababisha majirani wamiminike kwa wingi pale nyumbani kwa mama yake. Majirani waliingia kibarua cha kuanza kumbembeleza Nelson ambaye alikuwa akimwaga machozi kwa masikitiko makubwa. Mjomba alijitahidi kujikaza kiume lakini nae alishindwa na kujikuta akiangua kilio vilevile. Muda huohuo simu ilipigwa katika kituo kidogo cha polisi kilichopo maeneo ya Ngulelo. Ndani ya muda mfupi gari la jeshi la polisi lilifika katika eneo la tukio na kukuta umati mkubwa wa watu ukiwa umekusanyika katika nyumba ya mama Nelson. Polisi walivunja mlango na kuutoa mwili kisha kuupeleka mwochwari. Msiba uliwekwa nyumbani kwa Nelson.

    Kiukweli Nelson alikonda ghafla, kutokana na pengo kubwa alilolipata katika maisha yake. Hakutegemea mama yake atamuacha mapema kiasi kile katika dunia hii iliyojaa shida nyingi na mateso. Alitamani laiti baba yake angekuwa na ushirikiano mzuri na yeye pengine ingemfariji angalau kidogo. Vivian alionekana kusikitika sana alipopata taharifa za kifo cha mama mkwe wake. Alilia sana lakini machozi yake yalikuwa ni ya kinafiki kwasababu yeye ndiye alifanya mauwaji hayo. Nelson alilia hadi machozi yakamkauka. Wakati mwingine fahamu zilikuwa zinampotea Nelson kwasababu ya kulia sana. Ingawa watu wengi walijitahidi kumfariji na kumtaka ajikaze kiume lakini aliona hawakuwa wakifahamu machungu makubwa yaliyopo ndani ya mtima wake.

    Kifo cha mama yake kilikwenda kutonesha majeraha makubwa yaliyokuwa ndani ya moyo wake ya kupotelewa na watoto wake wawili katika kipindi kifupi kilichokuwa kimepita. Mipango ya mazishi ilipangwa. Maafikiano yalifanyika kwamba mama huyo atakwenda kuzikwa katika makaburi ya nyumbani kwao mkoa wa Kilimanjaro.

    Kwasababu mwili ulikuwa umeshaharibika sana siku ya tatu safari ya kusafirisha maiti kutokea mkoa wa Arusha kwenda mkoa wa jirani ilianza mapema saa kumi na mbili. Ndugu jamaa na marafiki walijitokeza kuusindikiza mwili kwenda mkoa wa jirani. Kosta nne zilikodiwa kwaajili ya kubeba watu waliojitokeza kuisindikiza familia ya Nelson kwenda mazikoni.

    ***********

    Usiku wa kuamkia siku ya safari kulifanyika kikao kikubwa na cha muda mrefu kuzimu. Vivian aliagizwa kusababisha ajali ambayo itamuuwa mtumishi wa Mungu mchungaji Eugin Alivin ambaye kesho yake atakuwa katika msafara wa kwenda mazikoni. Mchungaji huyo amekuwa akiharibu vikao vingi vilivyokuwa vikifanyika kuzimu mara kwa mara kwa njia ya maombi. Malikia aliona endapo mchungaji huyo atauwawa basi wataishi kwa amani sana. Malikia alimuahidi Vivian kumpandisha cheo maradufu endapo atafanikiwa kutekeleza zoezi hilo gumu. Vivian alikubali kuitoa roho ya mchungaji wakati watakapokuwa safarini kurejea arusha kutoka kwenye mazishi mkoa wa Kilimanjaro.

    ***********

    Marafiki wengi wa Nelson pamoja na wa mjomba waliamua kuunga msafara kwa magari yao binafsi kuelekea katika shughuli ya maziko. Magari yaliyokuwa katika msafara yalitembea kwa mwendo wa taratibu, kiasi kwamba wakati mwingine katika baadhi ya maeneo palitokea msongamano mkubwa wa magari. Watu wengi walibahatika kuuona msafara ule uliokuwa unausindikiza mwili kwenda kuzikwa walishikwa na butwaa kwasababu hawakuwahi kuona msafara mkubwa wa magari kama ule wa siku ile. Nelson alikwa mtu wa watu ndio maana watu wengi walionekana kumpenda. Mvua ilikuwa ikinyesha sana. Ilisababisha asubuhi ionekane kama vile jioni kwasababu wingu lilikuwa limefunga sana.

    kila mtu alionekana kuvalia makoti makubwa kwasababu hali ilikuwa ni ya ubaridi sana siku ile ingawa kipindi cha baridi kilikuwa kimeshapita. Wakinamama walijitanda kanga tatu tatu kutokana na baridi kali iliyokuwepo siku hiyo. Kila mtu alikuwa aking’ata meno kutokana na baridi ilivyokuwa ikipenyeza katika ngozi ya miili yao. Kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inazidi kunyesha ilisababisha msafara uzidi kwenda kwa mwendo wa taratibu sana. Vivian alikuwa katika gari moja ambayo ilikuwa imebeba watu wa familia. Mama yake pia alikuwepo katika gari hilo. Vivian alikuwa akiwasiliana na mama yake kwa ishara za kishetani ambazo hazikuweza kufahamika na mtu yeyote. CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com

    Watu waliokuwa katika misafara walikuwa wakiimba nyimbo za maombolezo.. Nyimbo zile zilisababisha wawe wanajisikia vibaya sana kwasababu roho wa ibilisi alikuwa ndani yao. Kwa mwedo wa taratibu saa saba mchana msafara ulifika katika eneo la makaburi kwaajili ya kufanya maziko. Maziko yalifanyika wakati mvua ikiendelea kunyesha. Kila mtu aliyekuwa msibani alionekana kulowa tepetepe kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha. Ilipotimu saa kumi na nusu jioni shughuli ya mazishi ilifikia tamati. Ndugu jamaa na marafiki waliokuwa wamemsindikiza Nelson msibani waliingia katika magari yao tayari kwa kuanza safari ya kurudi arusha.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog