Search This Blog

NUSU SIKU NDANI YA JENEZA - 2

 







    Nusu Siku Ndani Ya Jeneza

    Sehemu Ya Pili (2)



    Hali ilikuwa hivi. Kila jina lilikamilika kwa maana ya kisheria. Yaani majina matatu, nilimuuliza yule kiumbe ndiyo akaniambia hivyo kwamba katika utawala wa sheria kila binadamu anatambulika kwa majina matatu.

    Alisema: Duniani mnaishi kama mko gizani, mtu anaweza kushitakiwa kwa majina mawili lakini kusema kweli kiroho binadamu anatambulika kwa majina matatu. Kama unaitwa Hassan Juma lazima useme na jina la kati, mfano Hassan Juma Maulidi.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo maana kule kwenu Tanzania watu wa Zanzibar hutumia majina matatumatatu. Mfano mwingine ni kwenye kadi za kupigia kura au vitambulisho vya uraia, lazima yawe matatu.”

    Basi, yalipita majina matatu yakiwa yameandikwa; Musa Soja Muambo, tarehe aliyokufa, aliyozikwa. Halafu yakatokea maelezo yake sasa. Yaliandikwa hivi:

    Tarehe 25/12/1978 ulilewa, ukamchukua mwanamke wa mtu na kwenda kuzini naye huku na wewe una mke. Tarehe 12/2/1979, asubuhi uliingia ndani ya hoteli, ukaiba mkoba wa mzee mmoja anaitwa Sefu Rashid Mauzuliuzuli, alivaa kanzu.

    Yalipita majina kama saba yakitoa maelezo mbalimbali halafu kila jina lilipopita likafuatiwa na picha za video zenye tukio zima mwanzo mwisho tena zinazoonekana kama vile unamwona mtu halisi maana skrini yenyewe ni kubwa sana.

    “Una swali?” aliniuliza.

    “Mengi sana.”

    “Uliza.”

    “Ile ni video?”

    “Ndiyo.”

    “Huku mna kamera za video?”

    “Huku hatuna ila zinakotoka na sisi tunapata.”

    “Wapi?”

    “Unajua kwa Mungu ndiyo kwenye kila kitu cha maarifa. Unapoona ndege zinapaa, magari yanatembea, viwanda vinatengeneza kila kitu ni maarifa kutoka kwa Mungu na si kwingine.”

    “Sasa ina maana kule duniani mtu akifanya dhambi anapigwa picha za video?”



    “Si video tu hata picha za kawaida.”

    “Lakini mpigaji haonekani?”

    “Huwezi kumwona kwa sababu kwa Mungu kila kitu kiko wazi. Wewe huwezi kujifungia ndani ya nyumba halafu ukategemea unachokifanya Mungu hakuoni, si kweli.”

    “Sasa hawa marehemu wanayajua haya matendo yao?”

    “Mimi nikitaka sasa hivi naweza kukuonesha wewe video zako zote ambazo ulifanya dhambi.”

    “Sasa anayepiga ni Mungu au?”

    “Mungu anapiga lakini sisi tunaambulia kwa ajili ya kuweka ushahidi.”

    “Mimi nina swali.”

    “Uliza.”

    “Lakini liko mbali na haya mambo ya hapa.”

    “We uliza tu.”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mfano mtu kama Musa, alikwenda wapi baada ya kufa?”

    “Aaa, mbona hata kwenye maandiko yenu duniani imeandikwa kwamba alikwenda mahali pazuri.”

    “Si nasikia alimkera Mungu akiwa na wale watu wa Israel jangwani?”

    “Kosa lake alilitubu. Kwani nyiye wanadamu mkitubu hamsamehewi?”

    “Hivi huwa tunasamehewa?”

    “Lazima, ila mnakosea sana namna ya kutubu. Wengi wanaamini dhambi ndogo hazimsumbui Mungu, si kweli. Mungu anasumbuka na dhambi zenu hata ikiwa ya kumwangalia mwenzako vibaya.

    “Kinachomsumbua Mungu ni kwamba yeye ndiye aliyesema usiseme uongo lakini pia akasema usiibe na usizini. Nyinyi wanadamu mnadhani kusema uongo ni dhambi ndogo sana kuliko kuzini, mmesahau kwamba aliyesema usiseme uongo ndiye aliyesema usizini.”

    “Loo! Kweli wewe unajua mambo mengi.”

    “Sisi huku tunajua mambo mengi sana lakini hatuna uwezo au nafasi ya kutubu, kosa letu lilikuwa kubwa na lilishatolewa adhabu ya moja kwa moja, hakuna tena kujirudi.”

    “Ina maana hata mkiomba msamaha?”

    “Sisi hatuna mawasiliano tena na Mungu, nyinyi mnayo. Sisi Mungu alishaacha kutuangalia toka miaka na miaka na miaka. Tunawaonea wivu nyinyi ndiyo maana tunahakikisha kila siku tunawavuna kwa dhambi.”

    “Mmepewa nafasi ya kwenda peponi bure lakini sisi huku tunawashangaa sana mnapotumia fedha kwenda motoni.”

    “Kivipi?”

    “Ukienda kanisani au ukiishi maisha ya kumpendeza Mungu kuna gharama gani?”

    “Hakuna.”

    “Sasa nyinyi wanadamu mnaenda kwenye muziki, mnatoa fedha kununua pombe, mnahonga wanawake, mnakodi teksi kwenda gesti, mkifika gesti mnatoa tena fedha kuchukua vyumba, vyote hivyo ni dhambi. Ndiyo manaa nasema mnatumia fedha kununua motoni wakati mnaweza kwenda peponi bure.”

    Wakati anaendelea kunisimulia kwenye skrini palitokea jina na matendo halafu picha, akasema:

    “Yule ni Kaini kaka wa Abel wa Adam.”

    “Ha! Naye yuko huku?”

    “Asingeweza kukwepa kwa sababu Kaini ndiye binadamu wa kwanza kuua tangu kuumbwa kwa ulimwengu.”

    “Tena umenikumbusha, kule duniani kuna maneno kwamba Adam na Eva ndiyo watu wa kwanza kuishi bustanini duniani, si ndiyo?”

    “Nyinyi ndiyo mnasema Adam na Eva ndiyo watu wa kwanza lakini sisi tunajua Adam ndiye mtu wa kwanza na si Eva.”


    Eva hajatolewa au hajaumbwa, mbona unakosea sasa?”

    “Eva hakuumbwa, Adam ndiyo aliumbwa. Mwanamke alitokana na mwanaume na si kweli kwamba mwanaume alitokana na mwanamke.”

    “Ha! Eva hakuumbwa, kivipi sasa?”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hilo ni tatizo kubwa sana mlilonalo wanadamu, sisi huku siku zote tunajifunza na kujua maandiko yenu lakini nyinyi wenyewe hamko hivyo ni kwa nini lakini?

    “Eva hakuumbwa, Mungu alisema na tuumbe mtu kwa mfano wetu, akamuumba Adam. Alipomaliza akampa uhai akwa bnadamu hai, kwa mfano wake. Lakini baada ya hapo Mungu alimuona Adam yuko peke yake akamlaza usingizi akachomoa mbavu moja ya kushoto akaifanya kuwa mwanamke, ndiye Eva.”

    “He! Kwa hiyo Eva alitokana na mbavu ya Adamu?”

    “Tena ya kushoto. Kwa sababu hiyo ndiyo maana wanadamu wote upande wa kushoto hamna nguvu kwa sababu mbavu moja ilichomolewa.”

    “Tena kwa kukuongezea sasa sisi huku tunavyojua mwanamke si mtu bali ni kiumbe ndiyo maana pepo wachafu wanapenda kukaa kwako na kuwatesa kuliko wanaume.”

    “Hapo una maana gani?”

    “Maana yangu ni kwamba kutokana na udhaifu wao kama viumbe na si binadamu wanawake wanateswa sana na pepo wachafu. Nikuulize swali moja na wewe?”

    “Kama nitaweza kulijibu.”

    “Ukiwa duniani umewahi kwenda kwenye mikutano ya kiimani hasa ya watu wanaodai wameokoka?”

    “Ndiyo nimewahi mara nyingi sana.”

    “Hujajiuliza ni kwa nini wanawake ndiyo wanaanguka sana?”

    Aliposema hivyo nikaanza kupata picha kwamba madai yake ni ya kweli kabisa, kwenye mikutano ya dini hasa ya walokole wanawake wengi hupiga mwereka na kuweweseka.

    “Hivi ni kwa nini?” nilimuuliza kwa sauti yenye ujasiri nusu.

    “Kwa sababu wao ni viumbe tu. Ndani ya matumbo yao sehemu ya uzazi huwa wanaishi mapepo ambao huwa wanawatesa kwa mambo mbalimbali. Kama una swali jingine uliza kabla hatujaondoka hapa.”

    “Swali ninalo, ina maana sisi tunafanana na Mungu?”

    “Kwa sehemu kubwa sana. Kasoro fikra na uwezo mwingine. Ndiyo maana maandiko yenu yanasema; upumbavu wa Mungu unapita hekima ya mwanadamu.”

    “Sasa kama sisi ni sawa na Mungu kwa nini wengine maisha yetu si mazuri wengine mazuri?”

    Nilimwona yule kiumbe akiachia tabasamu huku akiniangalia kama vile ananionea huruma. Akasema:

    “Unajua binadamu mmepewa uwezo mkubwa sana lakini hamuutumii?”

    “Kivipi? Mbona mimi sina uwezo mkubwa kama wengine?”

    “Hujui kutumia neno.”

    “Kwani uwezo huo upo kwenye neno?”

    “Sana. Mungu alitumia neno kuumba, si ndiyo?”

    “Ndiyo, hata mimi nilisikia hivyo.”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Na nyinyi wanadamu mmeumbwa kwa mfano wake, si ndiyo?”

    “Kwa ulivyosema ni kweli tuliumbwa kwa mfano wake.”

    “Sasa mnashindwa nini kulifanya jambo lolote liwe kwa kutumia neno wakati mliumbwa kwa mfano wake?”

    Nilijikuta najishika kichwa na kujikuna nywele kama vile nilikuwa sijamuelewa vizuri.

    Kimsingi nilimwelewa kwamba kwa sababu sisi wanadamu tuliumbwa kwa mfano wa Mungu na yeye aliumba ulimwengu kwa neno basi na sisi tuna uwezo wa kufanya jambo liwe au lisiwe kwa neno.

    Akaendelea:

    “Wazazi wengi huko kwenu duniani wanayafanya maisha kuwa magumu au marahisi kwa maneno yao bila wao kujua. Ukiumwa, ukasema mwaka huu siwezi kupona kwa sababu ya ugonjwa huu kweli hutapona kwa sababu umekiumba kifo kwa neno.

    “Sisi huku tunawaonea wivu sana nyinyi, mna uwezo mkubwa lakini hamjuia kuutumia. Utakuta mzazi anamwambia mwanae wewe akili zako wewe hata darasani utafeli. Kweli atafeli, maana mzazi ameumba kufeli kwa neno. Lakini matokeo yake mtoto akifeli kweli mzazi huyo huyo anasema mi si nilisema! Lakini si kwamba alisema bali aliumba kwa neno.”

    Nilijishika kichwa na kukumbuka kuna siku moja niliwahi kusingizia kazini kwamba ninaumwa, sitakwenda. Baada ya wiki mbili nikaumwa kweli, nikamweleza yule kiumbe kuhusu hilo, akasema:

    “Ndiyo inavyokuwa. Wapo wanadamu wanaporomoka kiuchumi kwa sababu ya kusema tu. Mfano, mtu anafanikiwa katika maisha, ana miradi au kazi nzuri, analipwa mshahara mzuri, unamtosha kuishi vizuri, amepata bahati amenunua gari, akikutana na mtu anayefahamiana naye na kumwambia hongera naona mambo yako yanakwenda vizuri utamsikia akasema mazuri wapi, tunahangaika tu.

    “Haya maneno ni mabaya sana, lazima utahangaika kweli kwa sababu umeyatoa kinywani mwako.

    “Twende huku sasa.”

    Alinishika mkono mpaka kwenye jumba moja ambalo ndani tulikuta vyumba vingi, kila chumba kilikuwa na viumbe kama yeye, tuliingia kila chumba tulipotoka tukaenda kwenye chumba kingine hadi tukamaliza vyumba vyote kumi na moja. Tukarudi katikati ya chumba na kukaa kwenye viti ambavyo vilipangwa vitatu.

    “Una swali lolote?” aliniuliza.

    “Haliwezi kukosa.”

    “Uliza.”

    Niliangalia vile vyumba kwa zamu nikizungusha shingo hadi chumba cha mwisho. Katika kila chumba kulikuwa na alama mlangoni. Alama zenyewe zilikuwa kama si mbuzi, kondoo, kama si kondoo ng’ombe, mpaka wanyama wa porini pia walikuwepo kwenye kila mlango.

    “Nauliza sasa.”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Uliza.”

    “Hivi ni kwa nini kwenye kila mlango kuna alama ya mnyama fulani?”

    “Kila chumba chenye alama ya mnyama fulani ndani yake kuna wanaowasimimamia wanadamu kulingana na tabia za wanyama fulani. Mfano, kile chumba cha kondoo, ndani yake kuna wanaoshughulikia wanadamu wenye tabia ya kondooo.

    “Unajua iko hivi, kila binadamu aliyezaliwa ana tabia inayofanana na mnyama mmoja aliyopo duniani.”

    “Ha! Kweli?” nilishtuka sana.

     


    Ni kweli. Na mle mwenye vyumba ndimo mnamokuwa na wanowaongoza binadamu hao. Wapo binadamu wapole sana, hao wamefanana na kondoo, kuna binadamu hawajatulia muda wote, wala hawawezi kukaa mahali pamoja muda mwingi hao ni mbuzi.

    “Mfano mwingine, hakuna binadamu ana tabu kama atafanana na mbwa. Binadamu anayefanana na mbwa ana tabia ya ukali na kusema kila wakati, mnaita gubu. Akiwa mwanamke lazima ataangukia kwenye vitendo vya kuuza mwili, mnaita ukahaba.

    “Unajua ni kwa nini?” aliniuliza.

    “Sijui.”

    “Lazima usijue, lakini pia nikikusimulia hutaelewa lolote. Ila kikubwa ninachotaka utambue ni kwamba kila binadamu mmoja lazima atakuwa amefanana tabia na mnyama fulani wa mwituni au wa majumbani. We hapo ulipo unaweza kuikumbuka tabia yako na utagundua imefanana na mnyama mmoja, ndiyo maana watoto wanaweza kuwa wa baba mmoja mama mmoja lakini wakawa na tabia tofauti. Lakini tabia za wanyama hutokea wakati fulani zikawanufaisha wanadamu, mfano kumkuta mtu anafanana na mnyama swala, huyu kama atajijua akaamua kuwa mwanariadha anaweza kufika mbali sana.

    “Kama binadamu atajua anafanana tabia na mnyama simba halafu akaamua kuwa mpiganaji, naye atafaidika sana. Mtu anayefanana na simba mara nyingi pia akiamua kuanzisha kampuni na kuajiri watu anakuwa na sauti sana ya utawala.

    “Mtu anayefanana tabia na kobe, akiwa mwanamke atakuwa wa kuzaa kwa muda mrefu katika maisha yake. Yaani mara nyingi atakuwa akionekana kubeba watoto.

    “Mtu akifanana tabia na mnyama kama paka, katika maisha yake iko siku moja lazima atafumaniwa na mke wa mtu au mume wa mtu.

    “Mtu akifanana tabia na tembo, siku zote katika maisha yake atakuwa mtu mwenye kupenda kuwa juu kwa wenzake na atafanikiwa kwa hilo. Watu wa aina hii kwenye makampuni ndiyo wana tabia ya kushawishi migomo, wakiwa kwenye mkutano au kundi akisema jambo yeye linawavutia wengi kuliko wakisema wenzake wasiokuwa na tabia ya tembo.

    “Lakini pia mtu huyu atafanikiwa zaidi kama ataamua kufanya kazi za kubomoa majumba yaliyojengwa kinyume cha sheria kwa kutumia tingatinga.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mtu akifanana tabia na twiga ana bahati ya kuonekana yeye tu hata akiwa kwenye kundi la watu mia moja. Mara zote yeye huwa kinara kwa kuonekana. Ila hatari yake ni kwamba endapo atakuwa mwizi au jambazi wakafanya tukio sehemu na kukimbia yeye lazima atakuwa wa kwanza kukamatwa.

    “Faida yake ni kwamba kama ni mfanyabiashara, akataka mkopo kwenye benki fulani halafu kuna wengine wanaotaka mikopo na wameandika barua yeye atakuwa wa kwanza kujibiwa kuliko wenzake.

    “Kama ni mwanafunzi, mwalimu akiuliza swali halafu wanafunzi wote wakainua mikono kujibu, yeye atakuwa wa kwanza kuchaguliwa kujibu.

    Alipofika hapo yule kiumbe akaniuliza swali:

    “Hivi unamjua mtu mwenye tabia inayofanana na mnyama fisi?”

    “Simjui.”

    “Sawa huwezi kumjua. Mtu mwenye tabia ya mnyama huyo mara nyingi hukwepwa na wenzake. Umewahi kusimama kwenye kituo cha basi kwa kutawanyika halafu kila basi likija linasimama kwa wenzako?”

    “Nimewahi sana.”

    “Je, umewahi kuona kwamba ukiamua kusogea eneo ambalo mabasi yanasimama, mengine yakija yanapita kwenda kusimamia pale ulipokuwa umesimama awali?”

    “Ndiyo imeshanitokea sana tu.”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Je, umewahi kubaini kwamba upo ndani ya basi, umekaa siti ya watu wawili lakini hapo umekaa peke yako halafu kila abiria akiingia anakupita kwenda kukaa na abiria wengine mpaka basi linajaa ndiyo mtu anakuja kukaa na wewe?”

    “Mara nyingi sana, hivi ni kwa nini?”

    “Basi wewe una tabia za fisi, ndiyo maana nimechukua muda mrefu sana kukujulisha kwanza mambo ambayo una uhakika nayo.”

    “Da! Kwa hiyo mimi maisha yangu yangekuwa bure duniani, ningekuwa mtu wa kusumbuka au kutegemea wengine watafute ili mimi nile kama alivyo fisi?”

    “Ndiyo! Kama una kumbukumbu nzuri, vitu vyako vingi ulivyonavyo umekuwa ukiachiwa na watu, uongo?”

    “Kweli kabisa.”

    “Je, utakubaliana na mimi hata mke uliyenaye alishaolewa akaachika ndiyo ukamuoa wewe?”

    “Ni kweli kabisa. Sasa ili kuendelea ingebidi nifanye nini?”

    “Ulitakiwa kufanya biashara ya kuuza vitu vikuukuu, mfano nguo za mitumba. Magari yaliyokwishatumika, kununua vitu vya zamani na kwenda kuviuza mahali pengine au hata kuwa dalali wa kuuza nyumba zilizokwisha jengwa na kukaliwa, lakini si dalali wa kuuza viwanja au kupangisha nyumba.”

    “Nilichoka kabisa, niliamini aliyoyasema yote kwani yalinitokea. Pia niliamini kuhusu vitu, hata kitanda cha kwanza katika kuanza maisha niliachiwa, godoro na shuka pia. Baadhi ya ndugu zangu walipokuwa wanakuja nyumbani walipenda kuniachia mavazi, viatu hata saa au simu.

    “Mke niliyemuoa alikuwa ameshaolewa na jamaa mmoja anaitwa Mdoe, alipoachana naye ndiyo nikaibuka mimi na kuoa. Nikakumbuka kuna mzee mmoja jirani yetu aliwahi kuangaika sana kuuza baiskeli yake kwa sababu alikuwa na dharura lakini siku moja nilipoamua kumsaidia niliiuza ndani ya saa moja tu tena kwa mtu ambaye alikataa kuinunua kwa mzee huyo.”

    Nilibaki nimemtumbulia macho kiumbe yule kwani sasa tulikuwa kama marafiki tu na wala sikuwa nawaza lolote kuhusu maisha yangu ya baadaye wala yaliyopo.

    Kuna swali nilikuwa nalo nje kabisa na hayo, nikamuuliza:

    “Eti, kuna viumbe wanaweza kupenya kuingia ndani ya nyumba hata kama imefungwa?”

    “Wapo, hata mimi naweza.”

    “Inakuwaje?”

    “Sisi tuna miili ya moto, hatuna mifupa kama unavyodhani.”

    “Kama ungekuwa hauna mfupa ungekuwa hai?”

    “Uwezo wetu na wenu ni tofauti sana.”

     
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Huwa inakuaje?”

    “Mimi nikifika sehemu kwenye mlango naweza kupenya sehemu yenye nafasi ndogo sana, kwa sababu kinachokushinda wewe kupenya ni mifupa.

    Viumbe wote wenye uwezo wa kujibadili wapo hivyo, hawana mifupa hata kama unawaona kama binadamu walivyo.”

    “Nina swali jingine”

    “Uliza.”

    “Kuna peponi, mbinguni, duniani, jehanamu na wapi kwingine?”

    “Tunavyojua sisi, kuna mbingu, kuna pepo na mahali tunapopaita bostinia, yaani mahali pa mapumziko. Hapa bostinia tunajua ni sehemu ambayo waliokufa wote wanakuwa hapo mpaka siku ya hukumu ya watu wote.”

    “Kwa hiyo hakuna jehanamu?”

    “Nani kasema ipo? Jehanamu lilikuwa ni eneo la kutolea adhabu kwa watu kule Israel. Unajua zamani mji wote wa Jerusalem ulizungukwa na ukuta mrefu wa kujihami kwa ajili ya uvamizi kutoka kwa maadui.

    “Sasa jehanamu palikuwa nje ya ukuta ambapo takataka zote zilikuwa zikimwagwa huko. Kutokana na eneo hilo likaanza kufuka moshi na hatimaye kuzuka moto, hivyo hata watu waliofanya makosa makubwa walitupwa huko. Ilipotokea mtu amefanya kosa anaambiwa atatupwa jehanamu yaani kwenye lile eneo lao.

    “Mbona katika mafundisho ya imani yangu niliambiwa nikitenda dhambi nitatupwa jehanamu?”

    “Yule kiongozi wenu mkuu sana aliyesema vile alikuwa akiwatolea mfano watu wa Israel kwamba wakitenda dhambi kuna moto wa adhabu na wataweza kutupwa kwenye huo moto kama wao wanavyowatupa watenda dhambi pale jehanamu yao. Isingekuwa rahisi yule kiongozi wenu mkubwa atoe mfano ambao wale wasingeuelewa.”

    “Sasa watenda dhambi wa duniani watatupwa wapi?”

    “Kwenye ziwa la moto.”

    “Nina swali jingine.”

    “Uliza.”

    “Nimekusikia ukisema yule kiongozi wenu mkubwa sana, kwa nini usimtaje jina?”

    Nilimwona yule kiumbe anakunja ndita kama ishara ya kukasirika, nikaogopa sana. Nikakumbuka mambo ya nyuma nikiwa duniani, siku moja niliwahi kwenda kwenye mkutano wa Injili uliokuwa ukihubiriwa na Askofu Kakobe pale Jangwani, Dar es Salaam ambapo alisema:

    “Mashetani huko waliko wanamjua Yesu ni nani? Ndiyo maana ukilitaja hilo jina wanakimbia, wenyewe pia hawawezi kulitaja jina la Yesu wanasema yule mtu mkubwa au yule kiongozi mkubwa.”


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Usije kuniuliza swali kama hilo tena na kama utarudia itakuwa mwisho wa uhai wako moja kwa moja. Sisi huku hatuogopi kulitaja hilo jina mbona Mungu tunamtaja?”

    K

    auli hiyo ilinitatiza sana kwamba ni kwa nini aliweza kulitaja jina la Mungu lakini akashindwa kulitaja jina la Yesu?

    Nikiwa nafikiria nikasikia akili kichwani ikiniambia huyo anajua miungu wako wengi, lakini Mungu aliyeumba mbingu na nchi ni mmoja tu ndiyo maana analisema lakini hamaanishi Mungu wa m kubwa bali anamaanisha mungu wa m ndogo!

    Nilimwomba radhi yule kiumbe kwamba sitarudia tena kutenda kosa hilo ambalo lilimkera sana.

    “Nilitaka kuuliza swali moja la mwisho.”

    “Uliza.”

    “Ni amri gani ya Mungu aliyeumba mbingu na nchi ambayo ni kubwa kuliko zote?”

    “Kwanza unapomtaja Mungu si lazima uyaseme hayo maneno ya mbele, sawa?”

    “Sawa.”

    “Amri kuu ni moja tu, ni upendo. Unajua ukiwa na upando huwezi kumfanyia jambo baya mwenzako. Upendo unatawala amri zote za duniani. Ukimpenda mwenzako huwezi kutembea na mke wake, huwezi kutembea na mume wake, huwezi kumwibia chochote, huwezi kumsengenya, yaani upendo ni amri kubwa sana na sisi huku tunapambana zaidi na upendo.”

    “Mnapambana kivipi?”

    Kabla hajanijibu aliniangalia kwanza kisha akaangalia pembeni kama anayeangalia kitu halafu akaniangalia tena.

    “Unajua leo ngoja nikwambie sisi tunavyofanya kazi na binadamu. Sisi tuna uwezo wa kuingia kwenye akili au mawazo yenu tukafanya lolote. Tuna uwezo wa kumwamuru mtu asimame kama alikaa, yeye akaamini ni mawazo yake kumbe ameamriwa.

    “Labda nikupe mfano mkubwa, kuna roho chafu za kila dhambi, yaani kuna roho chafu wa ngono, kuna roho chafu wa ugomvi, kuna roho chafu wa masengenyo, roho chafu wa pombe, roho chafu wa sigara, roho chafu wa wizi, yaani kila jambo baya lina roho wake mchafu.

    “Sasa kila roho ina mtu wake. Mfano wewe una roho ya kupenda vya watu. Ukimwona mke wa mtu unamtaka, akiwa hajaolewa humtaki, ukiona gari la mtu unalitamani, ndiyo roho yako.

    “Hawa roho wote hufanya kazi zao chini ya roho chafu moja ya kuamuru. Roho inayoamuru ndiyo inayoweza kumfanya mtu aamke usiku na kwenda kuiba mahali.

    “Mfano, umekaa baa unakunywa pombe, roho ya ugomvi ikikujia inapamba na roho ya kuamuru. Mtu atapita mbele yako, halafu atakugusa lazima utawaka na kuanza kugombana kwa sababu tayari roho hiyo iko moyoni mwako.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mfano mwingine, roho mchafu wa ajali akikujia, hata kama umelala atakupa mawazo ya kutoka nyumbani kwako na kwenda mahali ilimradi upande chombo cha usafiri na kupata ajali.

    “Hizi roho sasa hazikai kwa mtu wakati wote ndiyo maana kama ni mlevi inaweza kukujia jioni au usiku mpaka ukajikuta kulala bila kunywa pombe huwezi, lakini ikishakuingiza kwenye tendo ovu hutoka na kurudi kwenye makazi yake na kukuacha wewe katika majuto.

    “Hebu fikiria kuhusu hili. Watu wengi wanapoingiwa na roho ya uzinzi huenda gesti wakiwa wameongozana hata kama ni saa sita mchana, lakini baada ya kumaliza dhambi hiyo wakati wa kutoka wanakuwa wenye aibu sana, ndiyo maana watatoka mmoja mmoja. Mara nyingi anaanza mwanaume kutoka. Ile ni aibu kwa sababu ujasiri wa lile pepo la ngono unakuwa umeshatoka, mtu anakuwa ana ufahamu wake mwenyewe.

    Hapa naomba nifafanue kwamba ninaposema kila mtu ana pepo la dhambi moja ninamaanisha kufanya jambo kupita kiasi na lenye madhara.
    binadamu anayevuta sigara kupitiliza ile ni roho chafu yake na binadamu huyo utamuona akikosa sigara hata nguvu zinamwishia au zinamtoka kabisa, kama alilala anatoka kwenda kununua na kuvuta ndiyo roho yake inatulia.



    Si rahisi kwa binadamu wa kawaida kuishinda roho hii, mara nyingi inatanguliza uwezo wa mtu kutenda hilo kosa. Ndiyo maana mtu akizini, hawezi kufikiria kuzini tu lazima kuna muda ataisikia sauti nyingine ikimzuia kufanya tendo hilo kwamba ni dhambi.

    Sisi tulishahukumiwa, yaani hatuna tena msamaha hata iweje, ndiyo maana tunakazana kila sekunde kuhakikisha wanadamu wanaopotea ni wengi kuliko wanaokwenda kwenye njia za Mungu wenu.

    Kuna pepo la maafa na vilio, kazi yao ni kuhakikisha binadamu wanalia na kufa kila sekunde. Haya mapepo yapo kwa kitengo, mfano wapo wa ajali, wapo wa sumu, wa magonjwa, wa vifo vya ghafla, lakini mwisho wa kazi zao ni kuua na kusababisha vilio.

    Napenda nikupe mfano mmoja, nyinyi binadamu mtu akifa mna kawaida ya kusema ni mapenzi ya Mungu au ni mipango ya Mungu, mnakosea sana kwa sababu hamjui lolote na tena hamjui maandiko.

    Mungu alipanga binadamu azaliwe, akue, aishi mpaka miaka ya uwezo wake wa kimwili ndipo afe. Kwa sasa Mungu amesema mnatakiwa muishi miaka 75, kupita hapo ni lazima muwe na nguvu. Kwa hiyo mtu akifa mapema, yaani kabla ya miaka hiyo, mfano mtoto mdogo, kijana wa miaka 25 au mtu mzima wa miaka 45, hicho kifo si mpango wa Mungu, ni sisi.

    Watumishi wote wa Mungu waliishi miaka mingi hadi uzeeni mwao, wakalala kwa mapenzi ya Mungu wenu. Kama umesoma kitabu cha Biblia utaona kizazi cha Adamu na Eva ambacho ni Kaini, Abeli, Enoko, Noa, Abrahamu, Sarah, Loti, Isaka na kuendelea walilala pale walipofikisha umri wa kufanya hivyo.

    Sasa nitoe mfano wa pepo la ajali, hili pepo lina tabia ya kuwaangalia binadamu katika kundi moja tu, mkusanyiko. Mfano, pepo limeona basi limebeba watu wengi, hapohapo linaamua kuingilia kati na kuua.


    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Kama unataka kuuliza kitu, uliza tu."

    "Ina maana mtu akifa tunavyosema siku yake ilifika tunakosea?"

    "Mnakosea sana, siku ya binadamu kufa ni kufika kwa umri alioupanga Mungu wenu. Wapo binadamu waliishi miaka mingi sana, kama sijakosea Methusela ndiye aliongoza, aliishi miaka 969 ndipo akafa. Baadaye Mungu wenu alipunguza umri wa kuishi, ilishuka polepole hadi kufikia miaka 75 ndiyo maana ajali nyingi haziwakuti wazee wenye miaka hiyo, we fuatilia utagundua hilo.



    Kinachotuumiza sisi huku ni jinsi nyinyi mlivyojaaliwa kuwa na maandiko ili msome lakini hamfanyi hivyo ndiyo maana mnapitwa na utambuzi wa mambo mengi sana. Nyoka zamani alikuwa na miguu kama mjusi, kwenye maandiko yenu ipo lakini wengi hamjui.

    "Kivipi? Si kweli," nilidakia.

    "Si hilo tu, hivi mnajua kama mwanamke mwanzoni kabisa alikuwa akizaa bila uchungu?"

    "Hamna bwana," nilidakia tena.

    Sikiliza wewe, maandiko yenu wenyewe yanasema Mungu wenu alipoibaini dhambi iliyotendwa na Eva na mumewe Adam kwa kushawishiwa na mmoja wetu ambaye alijifanya nyoka, alitoa adhabu kali.

    Katika adhabu hiyo, kila mmoja alipewa ya kwake. Adamu aliambiwa adhabu yake itakuwa kutoa jasho ili apate chakula ndiyo maana mpaka sasa kule duniani kwenu mwanaume ndiye anayelisha nyumba kwa kufanya kazi, tena wengine wanafanya kazi ngumu na nzito.

    Mwanamke yeye kufanya kazi anapenda mwenyewe kwa sababu si adhabu yake. Yeye aliambiwa adhabu yake itakuwa kuzaa kwa uchungu. Pia akaambiwa atatawaliwa na mwanaume.

    "Kwa hiyo ina maana wanawake wanaposema usawa wanakosea?" nilimuuliza.

    Wanakosea sana kwani wanavunja maagizo ya Mungu wenu. Kwetu sisi wanawake ndiyo tunaowatumia kuuvunja utaratibu wa Mungu wenu, mifano ipo mingi sana.

    Ukianzia na mwanzo kabisa wa maandiko kwenye kitabu chenu cha Agano la Kale ambacho kiliandikwa mwaka wa 1688 kabla ya kuzaliwa mkubwa wenu (Kabla ya Kristo).

    Adamu alimkosea sana Mungu kwa kutumiwa na mke wake. Nyoka alimdanganya Eva kuhusu tunda akalila akampa na mumewe naye akalila, Mungu akakasirika.

    Ukitoka kwa Adam utakutana na Samson yule mnadhiri wa Mungu wenu, naye alimkosea Mungu kwa kupitia kwa mwanamke ambaye ni Delila.

    Ukiachana na Samson, Mfalme Suleiman naye alimkosea Mungu kupitia kwa wanawake. Kuna mtu alikuwa anaitwa Hamani, mfalme aliamuru akatwe kichwa kwa sababu ya mwanamke.

    Yusufu kama unamkumbuka, alikwenda jela kwa sababu mke wa mfalme alimsingizia uongo kwamba alitaka kumbaka.

    Kifupi kazi zetu nyingi za kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu wenu sisi huwa tunazipitishia kwa wanawake kwa vile wao ni viumbe dhaifu sana lakini wana nguvu ya ushawishi. Majambazi wengi wanakamatwa kwa sababu ya kutegewa wanawake.

    Nataka kuuliza swali, tangu umekuja huku kutoka duniani unadhani una muda gani?

    "Mh! Kama wiki moja," nilimwona yule kiumbe akicheka, nikashangaa anacheka nini wakati ni kweli.
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haiko hivyo huku kwetu. Tunaishi kama watawala wakuu wa kwenye nguvu za giza. Siku moja kwetu kama miaka miaka kumi na miaka kumi pia inaweza kuwa siku moja.

    Tangu umekuja huku, kule duniani leo ni siku ya pili tena asubuhi kumekucha lakini jua halijaanza kutoka. Kwaheri tutaonana siku nyingine kwani nimepewa amri ya kukuacha.

    Nilitaka kusema kitu lakini kufumba na kufumbua sikumwona yule kiumbe mbele ya macho yangu, nikajikuta nimesimama mbele ya kiumbe mwingine aliyekaa kwenye kiti cheupe, pembeni yake walisimama viumbe wengine wanne, wawili kila upande.

    "Karibu ukae," yule kiumbe aliniambia. Alionekana yeye ni bosi wa wote kwani eneo alilokaa ni zuri, mahali pazuri, panavutia na hali yake pia.

    "Wapi?" nilimuuliza.

    "Si ukae."

    Niligeuka kuangalia pa kukaa, nikaona kiti kingine kidogo lakini kizuri sana, cheupe, nikakaa kwa kujiachia.




    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog