Search This Blog

SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA - 3

 







    Siimulizi : Sitasahau Nilivyogeuzwa Paka

    Sehemu Ya Tatu (3)



    ILIPOISHIA

    Ilipofika saa saba mke wangu aliniletea chakula.

    "Mbona umekaa?" akaniuliza.

    "Nimepunzika" nikamjibu

    Chausiku akaketi kando yangu

    "Umeniletea chakula gani?" nikamuuliza huku nikikifunua

    "Wali"

    "Na hii ni nyama ya nini?" niliona kipande cha nyama juu yake

    "Mbona siku zote nikikuletea chakula huniulizi, leo kwanini unaniuliza"

    Aliponijibu hivyo nikamwaambia "Leo sijisikii kula"

    "Kwanini?"

    "Tumbo linaniumauma"

    "Wewe muongo.Hebu kula hicho chakula!"

    "Basi utakiacha hapahapa, nitakula baadaye"

    "Kula sasa hivi na mimi nione.Najua iliyokutisha ni hiyo nyama”

    SASA ENDELEA

    “Kwani ni nyama ya nini?” nikamuuliza mke wangu.

    “Ni nyama ya sungura”

    "Nyama ya sungura? umeipata wapi?"

    "Bi Zaituni alichinja sungura wake akanipa upande mmoja wa nyama"

    Nikaosha mkono na kuiangalia ile nyama.Nilipoiridhika kuwa ilikuwa ni nyama ya sungura ndipo nilipokula kile chakula

    Nilipomaliza kula mke wangu akanifundisha mambo mengi ya kichawi.Nikagundua kwamba nilikuwa naishi na mwanamke hatari sana.Alikuwa akijua mambo mengi ya kutisha.Ukilinganisha na umri wake mdogo huwezi kuamini kuwa ana ujuzi mkubwa katika shughuli za kichawi.

    "Nakuambia wazi mimi ndiyo nimeandaliwa kushika cheo cha yule bibi.Yule kikongwe akifa leo mimi ndiyo nitakuwa gunge lenu" Chausiku akaniambia kwa kujisifu. Zilikuwa sifa za kipumbavu lakini yeye mwenyewe hakujua.

    "Na ilikuwaje mke wangu ukaingia katika uchawi?"

    "Marehemu bibi yangu ndiye aliyeniingiza"

    "Ulikuwa ni wakati upi?"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Wakati nilipoimaliza shule.Wewe ulikuwa unaishi Handeni"

    "Kwahiyo wakati tunaoana tayari wewe ulikuwa mchawi?"

    Mke wangu akanikubalia kwa kichwa.Nafikiri aliona aibu kunijibu kwa mdomo

    Alipoona nimenyamaza nikionyesha kufadhaika, alinibusu kwenye shavu langu kisha akavitia vyombo nilivyolia chakula kwenye kapu.Akaondoka

    Naam.Hivyo ndivyo nilivyolazimishwa kuingia katika uchawi.Usiku wa siku ile tuliamka tena tukaenda makaburini.Huko tukagawanyika kwenye vikundi vitatu.Kundi moja lilitumwa na yule bibi kwenda kuchawia kwenye maduka kule kijijini,kundi jingine likatumwa kwenye kijiji cha Songe kwa Mwarabu mmoja kumchawia binti yake asiolewe

    Na kundi jingine ambalo lilikuwa mimi, mke wangu na yule bibi tulikwenda porini kuchimba dawa

    Huko porini tulienda tukiwa uchi. Wenyewe walikuwa wanakuita ngome kuu.Nilioneshwa miti mbalimbali ambayo kama mizizi yake ama majani yake yalikuwa yakitumika kwa shughuli za kichawi

    Nilionyeshwa dawa za kufanya ukienda mahali usionekane, dawa za kujigeuza paka au mbwa, dawa ya kuingia katika nyumba ya mtu usiku na dawa za kuchawia watu

    Dawa hizo huandaliwa kwa kuchanganywa na vitu mbalimbali vya ajabuajabu.Nyingine huandaliwa na viungo vya binaadamu vilivyokaushwa kama vile ulimi, mkono wa mtoto mchanga,sehemu za siri za kike na za kiume na vitu vingine.

    Nilitakiwa nichimbe mizizi ya miti.Miti mingine iliwekewa masharti kabla ya kuichimba, ni mpaka uichanje na wewe mwenyewe ujichanje.Kisha unachukua utomvu wake unaupaka pale ulipo jichanja.Na kisha unachukua damu yako na kuipaka pale ulipochanja ule mti.

    Miti mingine unaisemea maneno.Unaieleza wewe nani na unataka nini?.Ukisha kueleza kile unachokitaka ndipo unauchinmba mizizi

    Yalikuwa mambo ya ajabu ambayo sijapata kuyaona.Ilikuwa kazi tuliyoifanya kwa muda mrefu.Tulipoondoka tulikuwa tumebeba mafurushi ya mizizi,magome ya miti,vipande vya miti na majani

    Tulipofika pale makaburini ambako palikuwa ndiyo maskani yetu,yule bibi akatugawia dawa zetu mimi na mke wangu.Nyingine akachukua yeye.

    "Utakwenda kumuonyesha mume wako jinsi ya kuzitengeza.Umesikia?" bibi alimuambia Chausiku

    "Nitamuonyesha"

    "Mtakwenda zenu au mtawangojea wenzenu?"

    "Tutakwenda zetu"

    Wakati mke wangu anamjibu tuliona kikundi cha paka wenye rangi tofauti kimetokea pale tulipokuwa.Yule bibi akawaambia paka hao

    "Haya geukeni mniambie"

    Hapohapo wale paka wakabadilika na kuwa watu.Walikuwa ni wale wanawake wa lile kundi letu la wachawi waliokwenda kuwachawia wafanyabiashara

    "Mmeiweza kazi?" yule bibi akawauliza

    "Si kidogo, tumeiweza sana!" mwanamke mmoja miongoni mwa wale wachawi akamjibu . "Tumetembelea maduka matano,yote tumeyasotea"

    "Kisha tukawawekea makimba kwenye milango!" mwingine akaongeza.

    "Wiki hii hawatauza chochote"

    Bibi kikongwe akacheka

    "Yule Mnyiramba mmemkumbuka?.Maana yule ndiyo kiburi mkubwa katika kijiji hiki?"

    "Bi Kidawa alimuingilia chumbani anamolala na mkewe,akawawangia wote na nywele pia akawanyoa nusu kichwa.Kesho watashika adabu.Hawatafungua duka" alisema mwanamke mwingine.

    Bibi kikongwe alicheka mpaka akaanguka chini.Mke wangu akamuinua

    "Bibi unacheka mpaka waanguka?"

    "Nimefurahi sana mjukuu wangu.Sasa tuwangoje wale wenzenu waliokwenda Songe kwa mwaarabu tuwasikilize"

    Nilikuwa nataka nimwaambia mke wangu twende zetu lakini nikafanya hamu ya kutaka kujua yaliotokea huko Songe kwa mwaarabu.Ikabidi nisubiri.

    Muda si muda kundi hilo nalo likafika lakini walikuja kama watu na siyo kama wale wenzao waliyokuja katika maumbile ya paka.

    "Kulikoni wanangu?" bibi kikongwe akawauliza

    "Tumemhemeka sawasawa!" mwanamke mmoja akamwaambia na kuongeza "Kesho hataamka kwa kuumwa na tutahakikisha haolewi ng’o!"

    "Wacha!" bbi kikongwe akang'aka kisha akaanza tena kucheka

    Walipomuona anacheka kila mmoja akawa anamueleza walivyokwenda kumuangia msichana huyo binti wa mwarabu.Katika kundi hilo walikuwemo wanaume wawili, nao pia wakaeleza kivyao, muda wote nilikuwa nikiwasikiliza na kuwashangaa.Nikajiuliza hivi mimi pia nitakuwa ninafuatana nao kwenda kuwachawia watu?



    Tuliporudi nyumbani ilikuwa inakaribia kuwa alfajiri. Tukafikizia kulala. Asiubuhi kama kawaida yangu nikaenda shamba. Ilipofika saa nne mke wangu akaja shamba na kapu lenye yale madawa ya kichawi. Akawasha moto wa kuni na kuanza kuyataarisha huku akinionesha kila kitu kinavyofanywa

    Kutoka muda huo sikuendelea tena na kazi za shamba. Mke wangu alikuwa akinifundisha vitendo vya kichawi kutokana na zile dawa.

    Alinifundisha jinsi ya kujiandaa kwenda kumchawia mtu. Kulikuwa kuna dawa zake za kujiandalia. Pia alinifundisha jinsi ya kumchawia mtu nikiwa nje ya nyumba yake, jinsi ya kuingia ndani ya nyumba yake na jinsi ya kutoka.

    Alinifundisha pia jinsi ya kujibadili kuwa mnyama kama paka na kwenda katika shughuli za kuwangia watu.

    Mke wangu akanikabidhi dawa zangu. Aina mbili ya dawa aliniwekea katika pembe na aina nyingine ya dawa hizo aliniwekea kwenye chupa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Siku ile tulirudi sote kutoka shamba.Tulirudi mapema tukiwa na kapu letu lililokuwa na dawa zetu za kichawi.

    Tulipofika nyumbani nilikwenda kuoga.Yeye akaingia jikoni na kuanza kupika. Nilipomaliza kuoga nilivaa kisha nikatoka. Nilikuwa nimepanga kumtembelea yule bibi kikongwe.

    Nilipofika nyumbani kwake ndiyo alikuwa anarudi kutoka shuleni alikokuwa anauza mbaazi zake za kichawi ambazo ni mavi ya mbuzi. Alikuwa amebeba sufuria lake kichwani.

    Nikakumbuka maneno aliyonieleza mke wangu kuwa mbaazi za bibi huyo ni mavi ya mbuzi wake anayoyageuza kuwa mbaazi kwa uchawi wake.

    “Shikamoo bibi” nikamuamkia

    “Oh! Marahaba. Hujambo”

    “Sijambo.Ndiyo unarudi?”

    “Ndiyo narudi mjukuu wangu”

    Bibi huyo akalitua sufuria lake barazani mwa nyumba yake.

    “Mbaazi zangu leo zimebaki nyingi. Nasikitikia nazi zangu. Sijui leo amenipitia mdudu gani!”

    “Kwani zimebaki nyingi bibi?” nikamuuliza

    “Nyingi”

    Alifunua sufuria akanionesha. Kama siyo kuambiwa na Chausiku nisingeweza kujua kuwa ni mavi ya mbuzi na kingekula . Zilikuwa kama mbaazi za kawaida tu, tena zilikolea nazi na kuvutia. Sufuria ilikuwa imejaa mpaka juu. Zilizouzika zilikuwa kidogo sana.

    “Hakukuwa na biashara kabisa.Wengi wamerudi na vitu vyao”

    “Unaweza kuziuza hapa hapa nyumbani” nikamwaambia

    “Saa hizi hakuna biashara tena”

    Alilibeba lile sufuria akaliingiza ndani ya nyumba yake.

    “Karibu ndani” akaniambia

    Nikaingia mle ndani ya kijumba chake kilichokuwa na vyumba viwili.

    “Kaa hapo” akanionesha kiti cha marimba kilichokuwa pale ukumbini.

    “Nasubiri usiku nikazimwage jalalani”

    “Kwanini unakwenda kuzimwaga?” nikamuuliza nikijifanya sijui kuwa ni mavi ya mbuzi.

    “Sasa nizifanye nini?” akaniuliza kwa hasira kidogo kisha akaniambia “Wewe acha maswali yako”

    Nilijua kuwa alikuwa amekasirika lakini nilishangaa nilivyomuona akicheka peke yake

    “Wee mjukuu wangu usiulizeulize maswali. Wewe bado mchanga, hujajua mambo. Mke wako amekuandalia zile dawa zako?”

    “Tayari”

    “Leo usiku tutatoka na wewe twende hukooo…..”

    “Twende wapi?”

    “Utakujua. Subiri huo usiku”

    “Sawa”

    “Sasa leo umekuja kunitembelea, unasemaje?”

    “Nimekutembelea tu”

    Yule bibi akacheka tena kisha akaketi chini kwenye mchanga. Alionekana kama afukani kidogo.

    “Usivunje miko. Ukivunja miko utaona!” akaniambia huku akininyooshea kidole cha kunionya.

    “Miko ipi bibi?” nikamuuliza.

    “Ebo! Unauliza tena!”

    Akainuka na kuingia chumbani. Nikaisikia sauti yake akiniambia.

    “Umeshasahau niliyokuambia juzi?”

    “Uliniambia nisitoe siri na nitii amri unazoniambia”

    “Haya njoo humu ndani”

    Nikainuka pale nilipokuwa nimekaa nikamfuata mle chumbani. Kijichumba chenyewe kilikuwa kiza na kilikuwa kimejaa makorokoro. Nikahisi hata nyoka wanaweza kukaa mle ndani bila yule bibi kujua.

    Kwanza nilisimama kando ya mlango nikaangalia bila kuona vizuri mpaka macho yangu yalipozuea kiza.

    Niliona kitanda cha kamba kikiwa pembeni mwa chumba.Yule bibi alikuwa amesimama kando ya kitanda hicho. Akaniambia.

    “Funga huo mlango”

    Nikaufunga. Nikamuona akivua nguo na kubaki mtupu kisha akajilaza kichalichali pale kitandani na kuniambia.

    “Sasa vua na wewe uje hapa!”

    Nilishituka na kumuuliza.

    “Nije nifanye nini?”

    “Nitakumbia hapa hapa”

    “Hapana bibi, siji hapo”

    “Si nilikumbia usivunje amri yangu”

    “Bibi acha utani. Mimi natoka”

    Nikageuka na kufungua mlango.

    “Usitoke, njoo wewe!”

    Sikumjibu kitu. Nilitoka.

    “Bibi naenda zangu” nikamwambia nikiwa ukumbini.

    Nilimsikia akiangua kicheko pake yake

    “Wewe muoga sana. Hebu ningoje usiende”

    “Kuna sehemu ninakwenda nitachelewa bibi”

    Nikatoka nje na kuondoka. Kabla sijafika mbali nikasikia sauti yake nyuma yangu.

    “Nisalimie mke wako!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikamtazama. Alikuwa ametoa kichwa kwenye mlango.

    “Haya bibi nitakusalimia” nikamjibu huku nikiendelea kwenda.

    Njiani nikawa najiuliza, yule bibi alikuwa anataka nini? jibu lilikuwa wazi kuwa alitaka nifanye naye ngono. Nikajiuliza je huo nao ulikuwa ni uchawi au ni akili yake mwenyewe. Hapo sikupata jibu. Hata hivyo nilishawahi kusikia kuna watu waliobaka vikongwe au maiti kwa imani za kishirikina.

    Hata kama ilikuwa ni lazima nifanye naye kitendo hicho kama sharti mojawapo la uchawi, nisingekubaliana naye. Mzee yule wa kazi gani.

    Nilipofika nyumbani nilimkuta mke wangu ameshapika chakula. Ulikuwa ni ugali kwa mboga ya bamia na perege wa kuchoma.

    Yeye alikuwa ameshakula sehemu yake. Na mimi nilikula sehemu yangu. Nilipomaliza kula aliondoa vyombo kisha akaja kukaa na mimi.

    “Ulikuwa umekwenda wapi?” akaniuliza

    “Nilikwenda kwa bibi”

    “Kufanya nini?”

    “Nilikwenda kumtembelea tu”

    “Mmezungumza nini?”

    “Bibi leo amenionesha jambo la ajabu sana. Aliniita chumbani akavua nguo kisha akalala kitandani na kuniita. Sasa sikuelewa alikuwa na maana gani”

    Nilitegemea Chausiku angeshituka ama kushangaa lakini nilimuona akiangua kicheko.

    “Alivyokuita ulikwenda?” akaniuliza.

    “Sikwenda, nilikataa nikatoka na kwenda zangu”

    Chausiku akaendelea kucheka

    “Ungeenda tu” akaniambia

    “Halafu...?”

    “Ungefanya hivyo anavyotaka”

    “Kwani pia ni uchawi?”

    “Ungemuuliza yeye”

    “Wewe pia unajua, usingecheka”

    “Nacheka tu kwa sababu najua yule bibi ana vituko”

    Nikatikisa kichwa changu na kusikitika.

    “Hata kama ni kwa masharti ya kiuchawi, yule bibi siwezi kufanya naye kitendo kama hicho”

    “Kwanini?”

    “Yule ni mzee sana. Ina maana wale wanaume walioko kwenye kundi lenu pia walifanya naye hivyo?”

    “Siwezi kujua”

    Nikanyamaza kimya. Pakapita ukimya wa karibu nusu dakika kabla ya kumwambia Chausiku.

    “Leo usiku sitatoka”

    Chausiku akagutuka na kuniuliza kwa haraka.

    “Kwanini hutatoka?”



     jana mume wa Chausiku baada ya kuona viroja kwa bibi kikongwe na kurudi nyumbani na kumueleza Chausiki visa vya bibi huyo huku Chausiku akicheka kana kwamba anajua kila kitu kilimshangaza mume wa Chausiku



    "Leo sijisikii vizuri" nikamwambia mke wangu.

    "Hakuna. Usikwepe! Unatakiwa ukamilishe siku saba ndipo utaweza kutoa dharura ya kutokwenda”

    Nikatikisa kichwa.

    "Leo siendi. Bibi akikuuliza mwambie naumwa"

    "Atajua umemdanganya"

    "Kama sijisikii vizuri niende tu?"

    "Mbona mimi nakuona ni mzima?"

    "Ninayeumwa ni mimi, wewe huwezi kujua. Na pia nimeshakuona kuwa huna huruma na mimi"

    "Sina huruma na wewe kwa sababu gani?"

    "Basi tuyaache"

    Nikajifanya nimekasirika ili mke wangu akubaliane na mimi.

    "Kama unaumwa kweli lala. Mimi nilikwambia tu" Chausiku akaniambia aliponiona nimekasirika.

    Usingizi ulipokuja kunichukua nililala moja kwa moja. Hata mke wangu alivyotoka usiku sikujua na wala yeye hakuniamsha kuniambia.Nilikuja kushituka usiku mwingi nikaona Chausiku hayupo kitandani. Nikajua ameshatoka. Mimi nikaendelea kulala.

    Baada ya muda kidogo nilishitushwa na kelele zilizokuwa zikisikika nje ya dirisha la chumba changu. Nikatega masikio na kusikiliza. Nikagundua kuwa zilikuwa kelele za lile kundi letu la wachawi. Kuna baadhi ya wachawi akiwemo mke wangu na yule bibi, waliamua kunifuata.

    Kelele zao zilikuwa haziwezi kusikiwa na watu wengine katika ile nyumba zaidi yangu mimi kwa vile nilikuwa mchawi mwenzao.

    Niliwasikia wakiimba nje ya dirisha langu na yule bibi kikongwe alipaza sauti yake kuniita.

    "Toka! Toka! Tumekufuata wewe twende kazini, saa imefika"

    Niliposikia sauti ya yule bibi nilijiuliza, Chausiku alikwenda kuwaeleza nini mpaka wakaamua kunifuata. Muda ule ule nikamuona mke wangu na mwanamke mmoja wameniibukia mle chumbani wakiwa uchi. Hawakupita kwenye mlango. Niliwashitukia tu wakiwa kando ya kitanda changu.

    Mke wangu akanishika mkono na kuniondoa pale kitandani.

    "Unaitwa na bibi. Amka"CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Si nilikuwa ninakuja?" nikajisemea kwa hofu.

    Kwa vile sikuwa na nguo nilitafuta shuka nikajifunga kiunoni ili yule mwanamke mwingine asinione. Kama ni kuonana tuonane huko huko uchawini kwetu. Wakati nimemaliza kujifunga shuka mke wangu alinishika mkono mmoja, mwenzake akanishika mkono mwingine. Mara ile ile nikajikuta tumetoka nje ya chumba kwa kutumia uwazi mdogo uliokuwa kwenye dirisha.

    Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona muujiza ule. Nilijikuta nimesimama mbele ya yule bibi.

    "Leo tunakwenda na wewe kwa yule binti wa mwarabu tukamchawie" Bibi huyo akaniambia.

    Nikajua ataniuliza kwanini sikutoka ili nimjibu kuwa sijisikii vizuri. Lakini hakuniuliza na hivyo sikuweza kumweleza kitu.

    Ghafla mmoja wa wanawake waliofika hapo akaja mbele yangu na kunipaka dawa kwenye uso wangu. Mwingine akanivua ile shuka na kunipachika mkia kwenye kiuno. Mke wangu naye alichukua ile shuka akaipachika kwenye ukuta wa nyumba.

    "Tutaikuta hapa hapa" akajisemea peke yake.

    Baada ya hapo yule bibi akatuamuru tuondoke, tulikuwa wachawi saba. Mwanaume nilikuwa mimi peke yangu. Bila shaka kulikuwa na kundi jingine la wachawi lililokwenda mahali kwengine.

    Tulikuwa tunaenda kwa miguu, nikaona tumekifikia kijiji cha Songe baada ya kupiga hatua chache tu. Kijiji hicho kilikuwa umbali wa karibu kilometa tano kutoka kijiji kile tulichokuwa tunaishi.

    Hapo nikagundua kituko cha tatu cha uchawi. Cha kwanza kilikuwa kile cha mke wangu na mwenzake kujipenyeza chumbani nilimokuwa nimelala. Na cha pili ni jinsi walivyonitoa kupitia kwenye uwazi uliokuwa kwenye dirisha na cha tatu ni kile chakufika kijiji cha Songe kilichopo umbali wa kilometa tano kwa kupiga hatua chache tu.

    Tulipokuwa tunatembea tulikuwa tunaonekana na kisha tunapotea machoni mwa mtu yeyote aliyebahatika kutuona.Tukafika katika ile nyumba tuliyokuwa tumeikusudia. Ilikuwa nyumba nzuri ya tofali iliyokuwa na mlango wa duka na ilikuwa inawaka taa ya umeme.

    Pengine ile kuonekana ni nyumba nzuri yenye umeme ndicho kilichosababisha iandamwe na wachawi. Pia niliambiwa waarabu wenyewe walikuwa watu wenye uwezo kifedha, hali ambayo haikuweko kwa baadhi ya wanavijiji wa kijiji hicho.

    Kwa hiyo uwezo wa waraabu hao ulikuwa ukiwakera baadhi ya wanavijiji akiwemo yule bibi kikongwe. Nilikuwa nimejifunza kwamba uchawi ulikuwa umeandamana na moyo wa uhusuda, yaani kuona gere maendeleo ya wengine na hivyo kutaka kuyaharibu.

    Tulipofika barazani mwa nyumba huyo yule bibi alipiga pindu kwenye usawa wa mlango kisha akachutama na kumwaga kinyesi chake mbele ya mlango. Hapo hapo niliona ile taa iliyokuwa ikiwaka barazani ikizimika yenyewe na kuwa kiza.

    Taa ilipozimika nilishuhudia vituko ambavyo sijawahi kuviona maishani mwangu. Mke wangu pamoja na wale wachawi wengine walikuwa wamecharukwa kucheza ngoma za ajabu ajabu wakionekana kama waliopagawa. Kama angetokea mtu na kutuona angekimbia.

    Wakati wakicheza ile ngoma walikuwa wakifanya kama wanaitia misukuo ile nyumba. Wengine walisotea kwenye kuta na wengine waliing'ong'a. Sijawahi kuona ngoma kama ile hata siku moja. Baada ya miujiza ile, bibi alitupeleka kwenye dirisha mojawapo la ile nyumba kisha akamwaambia Chausiku.

    "Nitaingia mimi kisha utaingia wewe na mumeo"

    Alipomwambia hivyo alinyoosha kidole kuelekea kwenye upenyo wa dirisha na mara ile ile akatoweka. Mke wangu akanishika mkono. Akanyoosha kidole chake kuelekea kwenye upenyo ule ule uliokuwa kwenye dirisha. Mara ile ile tukajikuta tumo ndani tukiwa tumeshikana mikono vilevile.

    Tulitokea kando ya dirisha ndani ya chumba kidogo kilichokuwa na kitanda na kabati.Taa ilikuwa inawaka. Nikamuona msichana wa kiarabu aliyekuwa amelala usingizi kitandani. Bibi kikongwe alikuwa amemuinamia kitandani akimsemea maneno ya kichawi. Na sisi tukasogea pale penye kitanda.

    Yule bibi alimkata sehemu ya nywele zake kwa kutumia kucha zake na kumuacha akiwa na vipachu kichwani. Kwa kutumia kucha zake hizo hizo aliendelea kumchanja kwenye kifua kisha akamgeuza na kumchanja kwenye mgongo.

    Alipomaliza kumchanja, yule msichana alinyanyuka mwenyewe akiwa katika hali ya usingizi na kusimama mbele ya yule bibi.

    "Wewe punda wangu inama unipakie twende!" Bibi akamwambia msichana huyo ambaye aliinama. Yule bibi akampandia mgongoni.



    “Nimeshakupanda punda wangu. Sasa twende” Bibi huyo alimwambia tena msichana huyo huku akimpiga kofi

    kwenye makalio yake.

    Msichana huyo akaanza kutembea kwa kutumia magoti na mikono akiwa amembeba yule bibi mgongoni.

    Kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa mwembamba, ukilinganisha na uzito wa yule bibi, alikuwa akienda kwa taabu akiwa amekunja uso kuonesha kuwa alikuwa anaumia. Pale alipoonesha kusitasita, yule bibi alimpiga kofi la makalioni na kumuamrisha.

    “Twende! Twende!”

    Wakati kitendo hicho kinafanyika, mke wangu alikuwa akicheka kuonesha kuwa kilikuwa kitendo kilichomfurahisha. Wakati mwingine yule bibi alikuwa akimsukuma yule binti makalioni mwake ili aende kwa haraka haraka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Msichana huyo alipochoka kabisa alijibwaga chini puu! Yule bibi akanyanyuka na kumwambia mke wangu amuinue na amlaze kitandani. Chausiku akamuinua na kumlaza kitandani msichana huyo aliyeonekana kuwa taabani sana.

    Kama haitoshi, Bi kikongwe na Chausiku wakamchezea ngoma kando ya kitanda pamoja na kumng’ong’a huku wakiwa wamemtolea macho. Baada ya kumfanyia hivyo walimrushia vitu visivyoonekana kisha mke wangu akageuka na kunishika mkono. Kufumba na kufumbua tukajikuta tuko nje ya dirisha. Baada ya sekunde chache tukamuona yule bibi naye ameibuka nje ya dirisha.

    Msafara ukaongoza njia ya kurudi. Wakati tunarudi yule bibi alikuwa anabadilika badilika. Mara alikuwa anageuka mbwa, mara alikuwa anageuka paka. Tulitembea mpaka tukafika kwenye ule uwanja wetu tunapokutana. Safari ya kurudi pia ilikuwa fupi kama ile ya kwenda.

    Tulikuta kundi la wenzetu waliokwenda mahali kwingine wakitusubiri. Hapo wachawi hao wakaanza kuhadithiana uchawi wao huku wakionekana kuridhika na vitendo walivyotenda.

    Mimi tu ndio nilikuwa nimefadhaika. Nilikuwa nikimfikiria yule binti wa kiarabu alivyokuwa anateswa na yule bibi hadi kuanguka chini.

    Kitendo kile kilinitambulisha kwamba uchawi unahitaji moyo wa ukatili na yule bibi alikuwa katili.

    Vitendo vile vya kichawi sasa vilianza kunichukiza lakini kwa vile nilikuwa nimeshajiingiza katika kundi hilo sikuwa na budi kuendelea nalo. Mke wangu alishanitishia kuwa nisipokubali kuwa mchawi atakwenda kuniripoti polisi kuwa nimemuua mke wangu wa kwanza. Hivyo niliona ni bora niendelee na udhalimu huo kuliko kukamatwa na polisi na kwenda kushitakiwa kwa kosa la mauaji.

    Baada ya wachawi hao kuhadithiana hiki na kile, walianza kuvaa nguo zao. Mimi sikuwa na nguo. Yule bibi akanigeukia.

    “Tunakupa mazoezi ili upate ujasiri. Leo tumekupeleka Songe, kesho utaenda mahali kwengine” Bibi huyo akaniambia.

    “Sawa bibi”

    “Yule msichana hatoolewa ng’o na atabaki kuwa mbovu kila siku” Bibi akaendelea kusema huku akiendelea kuvaa kaniki yake.

    “Sisi tunakwenda” Mke wangu akamuaga bibi.

    “Haya nendeni, kesho uje naye”

    “Nitakuja naye” mke wangu akamwaambia

    Wakati nimeongozana na mke wangu tukienda mahali alipoweka nguo zake, tulimsikia yule bibi akituambia huko nyuma.

    “Mwaambie aache uoga”

    Mke wangu akaguna

    “Mh!.... bibi huyu nae hamalizi kusema!” kisha akamjibu “Ataacha uoga tu, ndio mwanzo bibi”

    Tukaenda kwenye kichaka ambako mke wangu aliweka nguo zake. Ulikuwa ni upande wa kaniki. Akajifunga nao kisha tukaondoka kurudi nyumbani.

    Tulipofika barazani mwa nyumba yetu nilichukua ile shuka yangu nikaivaa kisha tukaingia ndani.

    Kwa vile tulikuwa tumechoka tulipojilaza tu usingizi ukatuchukua.Tulipozinduka kulikuwa kumekucha. Siku ile nilipanga nisiende shamba.

    Wakati tunakunywa chai na mke wangu nikamuuliza ni kwanini waliamua kunifuata usiku wakati nilimwambia nilikuwa najisikia kuumwa?.

    “Ni bibi mwenyewe. Mimi nilimwambia kama ulivyoniambia wewe. Akaniambia mume wako ameanza uvivu. Ndio akaamua kukufuata” Mke wangu akanijibu. alipoona nilikuwa nimenyamaza huku nikimtazama akaendelea kuniambia.

    “Siku nyingine ukiwa na dharura yako uende ukamwambie mwenyewe”

    “Je ikitokea ukiumwa wewe itakuwaje? Atakufuata?” nikamuuliza.

    “Mimi nikiumwa ninamueleza na hawaja nifuata hata siku moja”

    “Tuseme na akiumwa yeye inakuwaje?”

    “Yule bibi haumwi, anakula mizizi ya kwao kila siku. Usimuone vile mzee, ni mzima kweli. Hata kama akisafiri usiku anapaa kwenye ungo anakuja uchawini ”

    “Ala! Kumbe anapaa?”

    “Anapaa kwa ungo”

    “Wewe pia unapaa?”

    “Amenifundisha yeye”

    “Huo ungo wako, ukowapi?”

    “Uko chumba cha pili, nimeuweka”

    “Mkipaa mnaenda wapi?”

    “Kama tunataka kwenda kufanya uchawi Dar es Salaam au Tanga tunapaa. Yule bibi wakati mwingine anataka kwenda kukutana na wachawi wenzake wa Sumbawanga na Mwanza, pia anapaa”

    “Lakini mimi hajanifundisha uchawi huo”

    “Wewe bado kwanza, lakini atakufundisha tu. Ngoja umalize angalau mwaka mmoja”

    Tulipomaliza kunywa chai, mimi nilitoka kwenda kuzunguukazunguuka. Nilirudi nyumbani saa sita mchana. Mke wangu akaniuliza.

    “Una njaa, nipike ugali?”

    “Pika”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akaenda jikoni. Na mimi nikajipunzisha kitandani. Hapohapo usingizi ukanichukua. Mke wangu alikuja kuniamsha majira ya saa nane na kuniambia.

    “Chakula kimeiva”

    Tulipomaliza kula akaniambia anakwenda kumtembelea bibi. Mimi nikabaki pale nyumbani.

    Chausiku alipoondoka hakurudi tena hadi saa moja usiku. Akapika chakula cha usiku. Milo yetu ya kijijini haina masharti. Mchana mnaweza kula ugali na matembere na usiku mnakula tena ugali huo huo.

    Baada ya kula hatukukaa sana, tukaenda kulala. Kama kawaida yake mke wangu aliniamsha usiku wa manane.Tukatoka.

    Tulipofika kiwanjani tuliwakuta baadhi ya wenzetu walikuwa wameshafika. Bibi akatupangia kazi. Vile vitendo vyetu vya kichawi tulivichukulia kama kazi.

    Siku ile bibi alinipanga mimi na wanawake wawili twende nyumbani kwa mwalimu mkuu wa ile shule anakouzia mbaazi zake tukamchawie. Kisa, alimwambia yule bibi atamfukuza asipeleke mbaazi zake shuleni hapo

    kwa vile wanafunzi na walimu wanaokula mbaazi hizo wanaharisha. Kauli hiyo ilimuudhi yule bibi.

    Mke wangu na wenzake wengine walitumwa sehemu zingine zingine.

    Nyumbani kwa mwalimu mkuu hakukuwa mbali sana na pale kwenye kiwanja chetu.Tukaenda.

    Kama kawaida tulipofika, wachawi wenzangu wakapiga pindu kwenye mlango wa nyumba ya mwalimu mkuu huyo.Wakaniambia na mimi nipige pindu, nikapiga pindu. Kisha tukazunguka duara na kuanza kucheza ngoma ya kichawi barazani mwa ile nyumba. Zile pindu tulizopiga zilikuwa na malengo ya kufanikisha ile kazi ya kichawi iliyotupeleka hapo. Na ile ngoma ilikuwa ni ya kuwalaza usingizi watu wote waliokuwemo mle ndani.

    Tulipomaliza kucheza ngoma hiyo ikafuatia kazi ya kujipenyeza kiuchawi ndani ya ile nyumba. Laiti ningejua ni kitu gani kitatutokea humo ndani, nisingekubali kuingia humo ndani.



    Alianza kujipenyeza mwanamke wa kwanza kupitia kwenye upenyo wa dirisha.Mwanamke wa pili akanishika mkono,nikapenya naye.Sote watatu tukawa ndani ya chumba kilichokuwa kiza. Mwanamke aliyeingia kwanza alifyatua swichi,chumba kikajaa mwanga.Kwenye kitanda tukaona watu wawili wakiwa wamelala.Walikuwa mwanaume na mwanamke.Mwanamke alilala kichalichali na mwanaume alilala kifudifudi.

    Yule mwanaume alikuwa ndiye mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya pale kijijini na mwanamke aliyekuwa naye alikuwa mke wake.

    Tulianza kuwachezea ngoma tukiwa tumesimama kando ya kitanda walicholala.Baada ya mchezo huo mwanamke mmoja aliwafunua shuka akaanza kumkatakata nywele yule mwanamke.Alimkata nywele nyingi upande mmoja wa kichwa chake kwa kutumia kucha zake.

    Mwanamke wa pili naye alipanda kwenye kitanda na kumkalia mwalimu mkuu mgongoni. Alichokuwa anakifanya hapo ni kumminya na kumuumiza mwalimu huyo mpaka akawa anaweweseka na kutoa sauti ya kusikia maumivu.

    Mbali ya kumshindilia kwenye kiuno na mgongo aliipindisha mikono yake kama aliyetaka kuivunja akawa anarudia kufanya hivyo mara nyingi.Baadaye aligeukia kwenye miguu,nayo akawa anaipindisha.Mwalimu mkuu alikuwa akiendelea kuweweseka kwa maumivu.

    Mwanamke huyo alipotosheka na mchezo huo alishuka kwenye kitanda,akamchanja chale mwalimu huyo mgongoni kwa kutumia kucha.Alimchanja sehemu tofautitofauti kisha akasema "Sasa tuwaache twende zetu"

    Mwanamke huyo akanishika mkono na kulielekea dirisha.Alilinyooshea kidole ili tupenye katika dirisha hilo lakini hatukuweza kuondoka mahali tulipokuwa tumesimama.

    Mwanamke alijaribu tena lakini hakuweza kuondoka, tena mwenzangu ndiyo alinata kabisa.Nikamuachia mkono na kushikana na yule mwanamke mwingine.Na yeye nikamuona alikuwa kama amelewa.Sikuweza kujipenyeza naye kwenye dirisha hilo.Wenzangu wote wawili sasa walionekana kama mazezeta.Uwezo wa kutoka mle chumbani walikuwa hawana.Kila mmoja akabaki amesimama hapohapo.

    "Jamani mbona hatuendi?" nikawauliza kwa hofu

    "Siwezi kutoka!" mwanamke wa kwanza akanijibu

    "Na mimi pia nashindwa" mwanamke wa pili naye akaniambia.

    "Sasa tufanyeje?'

    "Kuna zindiko humu ndani.Nenda ukaliondoe" mwanamke aliyekwama kwanza akaniambia.

    "Zindiko!" nikang'aka "Hilo zindiko liko wapi?"

    "Litafute"

    "Sitaweza. Sina utaalamu huo"

    "Basi hatutaweza kutoka!"

    "Sasa itakuwaje?" nikawauliza wanawake hao kwa hofu lakini hakukuwa na aliyenijibu.

    "Basi tutoke kwa kutumia milango" nikawaambia

    "Hatuwezi kuondoka kabisa,mpaka lile zindiko liondoke!"

    Nikajaribu kwenda kwenye mlango.Nikaona ninaweza kutembea.Nikaufungua mlango.

    "Njooni twende jamani.Tutakutwa!"

    "Njoo utuondoe.Hatuwezi kuondoka"mwanamke mmoja akanimbia

    "Kwanini,mbona mimi ninaweza?"

    Hakukuwa na aliyenijibu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikaenda na kumshika mkono mwanamke wa kwanza ili nimvute lakini alikuwa amenasa kama aliyeshikwa na umeme,hali ambayo ilinishitua. Sikutaka hata kumshika yule mwanamke mwingine kwa kujua hali itakuwa ileile. Nikakimbilia kwenye mlango.Nikaufungua na kutoka.Ukumbini palikuwa giza.Lakini nilijua mlango wa mbele ulikuwa upande wa kulia.Nikaelekea upande wa kulia.Kwa sababu nilikuwa sioni kutokana na giza Nilikumba ndoo ya maji ikaanguka,maji yakamwagika chini.

    Nikasikia sauti kutoka chumba kingine ikauliza

    "Wewe nani?'"

    Sikujibu kitu, nikaamua kukimbia.

    Sikufika mbali nikateleza kutokana na yale maji yaliyomwagika.Nikapiga mweleka kwa kishindo.

    "Wewe nani uliye hapo ukumbini?'' ile sauti ikauliza tena

    Nikanyanyuka haraka na kupapasa ukuta, nikawa naenda huku nimeshikilia ukuta.Mbele tena nikakumbana na meza.Niliikumba ikatoa mlio wa kuburuzika.

    "Wewe nani? mbona ukiulizwa husemi?"

    Sasa ilikuwa sauti ya mwanamke iliyotoka chumba kingine.

    Nilikuwa nikitetemeka kwa hofu nikijua kuwa arobaini zangu zilikuwa zimekaribia.

    Niliipita ile meza nikakumba ndoo nyingine lakini hii ilikuwa tupu. Nikaendelea kwenda sasa kwa harakaharaka ili nifike kwenye mlango.

    "Baba Rama, hebu amka. Naona kumeingia mtu hapo ukumbini!" ile sauti ya kike ikasikika tena.

    Mara nikasikia sauti ya mwanaume ikiuliza "Unasemaje?"

    "Hebu amka.Kuna mtu ameingia ukumbini. Kuna vitu vyetu visije vikaibiwa!"

    "Unasema kumeingia mtu?'

    "Ndiyo, yupo ukumbini. Anakumba ndoo, akiulizwa wewe nani hasemi"

    Sauti hizo ziliingia moyoni mwangu kwa ukali kama mmweko wa radi.Nilijua sasa maisha yangu yalikuwa yamekwisha.

    Niliufikia mlango lakini kufika kwenye mlango hakukutosha. Mlango ulikuwa umefungwa na sikujua umefungwaje.Nikawa naupapasapapasa kutafuta vifungulio.Moyo ulikuwa ukinienda mbio kama uliotaka kutoka na nilikuwa nikihema kwa nguvu kama mwizi aliyekuwa anafukuzwa.Sekunde zilikuwa zinapita.Nikahisi watu watatoka vyumbani mwao na kunikuta pale kwenye ule mlango.

    Akili yangu ilikuwa imeshataharuki na sikuwa na maarifa zaidi ya kutumia nguvu.Nikaukumba ule mlango lakini haukufunguka isipokuwa ulitoa kishindo kikubwa.Nikaukumba kwa mara ya pili

    "Kweli kuna mwizi!" nikasikia ile sauti ya kiume ikinong'ona na kisha ikauliza " Lile panga langu liko wapi?"

    Moyo ukanishituka.Nilikaribia kuzirai kwa hofu.Akili yangu iliunda picha ya mwizi anayefukuzwa na kuzingirwa na watu ambao wanamtandika mawe na marungu na kumsaga kabisa.

    Nilijiambia,wakati wowote kutoka muda ule picha niliyoiwaza itanitokea kama sitatuliza akili yangu na kuweza kufungua ule mlango.

    Wakati nikijiambia hivyo mkono wangu ulikishika kifungulio cha mlango kilichokuwa juu,nikakifungua.Nikajua milango mingi inakuwa na vifungio vitatu.Kama kuna cha juu kutakuwa na cha katikati na cha chini.Sikukosea,nilipopapasa nilikipata kifunguo cha katikati.Nikakifungua kisha nikaujaribu mlango.Mlango ulikuwa bado haufunguki.Nikainama na kupapasa sehemu ya chini ya mlango. Vile ninainama tu nikaisikia sauti ya mwalimu mkuu na mke wake wakipiga makelele.

    "Jamani tumeingiliwa na watu chumbani,wako uchi.Njooni njooni jamani!" ilikuwa suti ya mke wa mwalimu mkuu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nyinyi ni akina nani?" sauti ya mwalimu mkuu nayo ilisikika ikiuliza

    "Nawauliza nyinyi ni akina nani?" sauti ya mwalimu mkuu huyo iliendelea kusikika wakati mke wake aliendelea kupiga kelele

    Sasa hali haikuwa nzuri hata chembe.Wenzangu wameshaonekana na walikuwa wamenasa,bado mimi.Tumbo lilikuwa likiniunguruma.Vile nilivyoinama kama nisinge ikaza, haja kubwa ingenitoka palepale.





    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog