Simulizi : Safari Yangu Ya Kwanza Kuzimu
Sehemu Ya Tatu (3)
Mwanamke yule ambaye watoto wake walikuwa ndani ya nyumba ile akaanza kulia, tayari alikwishajua kile kilichokuwa kimetokea ndani ya nyumba ile kwamba watoto wake walikuwa wamenasa na hivyo ilimaanisha kwamba wangekutwa asubuhi au wangekufa usiku huohuo.
Hilo likamkosesha amani, akajaribu kuwaambia wenzake kwamba walitakiwa kuelekea ndani kwa ajili ya kuwanasua lakini kila mmoja akaonekana kuogopa kwani Ramadhani hakuonekana kuwa mtu wa kutania.
Walijaribu kukaa pale huku wakifikiria ni kitu gani walitakiwa kufanya kwani nao muda haukuwasubiri, uliendelea kusonga mbele jambo lililowafanya kuwa na wasiwasi zaidi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tuingieni....” alisema mwanamke yule mwenye watoto wake.
“Hapana! Hatuwezi kuingia, huyu mtu anaonekana kuwa hatari,” alijibu kiongozi.
Huo ndiyo ulikuwa ukweli wenyewe, Ramadhani hakuonekana kuwa mtu wa masihara, kila mtu aliogopa kuingia ndani. Mwanamke yule alibaki akilia lakini kilio chake hakikubadilisha matokeo yoyote yale, watoto wake walinaswa ndani.
Siku iliyofuata, taarifa zikaanza kusambaa kwamba watoto wa mwanamke yule hawakuamka kitandani, walikuwa wamefariki dunia. Kilikuwa kifo cha kushtukiza sana, hakukuwa na mtu aliyejua kama kulikuwa na ushirikina kati yao na ndiyo kitu kilichopelekea kufa kwani walikwenda kumroga mtu aliyekuwa na nguvu zaidi yao.
Watu wakaanza kukusanyika msibani pale, wachawi waliofika mahali hapo wakaanza kuangaliana kwa macho ya mashaka kwani walijua kile kilichokuwa kimetokea kwamba watoto hawakufa duniani bali walichukuliwa misukule na Ramadhani.
“Hivi watu wanaweza kugundua kweli?” aliuliza mzee mmoja, alikuwa na upara kichwani, alivalia msuli mrefu.
“Hawawezi kujua, tusubiri tukazike tu.”
Ingawa wale waliokuwa wakiosha maiti walijua kwamba zile zilikuwa maiti lakini ukweli ulikuwa ni kwamba hawakuwa wakiosha maiti kama walivyoona bali ilikuwa ni migomba.
Wakati jeneza likiwa limeletwa nje tayari kwa kuswaliwa na maziko, ghafla mwanaume mmoja akaanza kuja kwa kasi msibani pale, alionekana kuwa na jambo la muhimu sana alitaka kuwaambia, alipowafikia, akaanza kumwangalia kila mtu aliyekuwa mahali pale, mwanaume yule hakuwa mwingine bali alikuwa Ramadhani.
Macho yake yalikuwa ya chuki mno, kila alipowaangalia wachawi wale, alikuwa akikunja uso wake huku akisonya kwa hasira kitendo kilichotafsiriwa kuwa dharau na hakikutakiwa kuonyeshwa msibani pale.
“Hebu nyie wachawi inukeni muwaambie wenzenu ukweli,” alisema Ramdahani kwa dharau kubwa.
Hakukuwa na mtu aliyesimama, hata mama yao na marehemu ambaye alijifanyisha kulia, akanyamaza na kuona kwamba tayari walikuwa wakienda kuumbuka. Mtu aliyekuwa akiongoza mazishi yale, shekhe mmoja aliyeonekana kuwa na heshima kubwa akamwangalia Ramadhani na kumwambia aondoke.
“Shekhe, hamuendi kuzika maiti, mnakwenda kuzika migomba,” alisema Ramadhani, watu wote wakashtuka.
“Unasemaje?” shekhe aliuliza kwa mshtuko.
“Hao watoto wapo nyumbani, nimewahifadhi,” alisema Ramdhani maneno yaliyomshtua kila mtu mahali pale.
“Wewe kijana hebu tuondolee uchizi.”
“Kama mnaniona chizi, angalieni maiti hizo,” alisema Ramdhani.
Walichokifanya mashekhe wawili ni kusimama na kuyafuata majeneza yale yaliyokuwa na maiti zilizofungwa mikekani kwa lengo za kuzifungua. Kila mtu msibani pale alibaki kimya, alitaka kushuhudia kile kilichozungumzwa na kijana yule.
Wale watu walikuwa mbali, wakasogea karibu, walitaka kuona kama kweli mule hakukuwa na maiti kama walivyojua au Ramadhani alikuwa akiwadanganya. Wachawi wale ambao walikuwa wamekwenda kuroga nyumbani kwake, wakaanza kuondoka kwa kujifichajificha kwani tayari walijua kwamba mambo yaliharibika.
Mashekhe wale walipoyafikia majeneza yale, wakazitoa maiti zile kutoka ndani na kuziweka mkekani, watu wakakodoa macho zaidi kwa kutaka kushuhudia kile kilichokuwa ndani ya mikeka ile.
Kwa kuwa hawakuwa na uhakika na hawakutaka kumuamini sana Ramadhani, wakaanza kuchungulia wao wenyewe kuona kama kulikuwa na maiti au migomba kama alivyosema Ramadhani.
“Mtumeee! Migomba! “ alisema shekhe mmoja na hivyo kufungua mikeka ile.
Watu wakapigwa na bumbuwazi, hawakuamini kile walichokuwa wakikiona, ndani ya mikeka ile hakukuwa na maiti yoyote ile zaidi ya migomba miwili ambayo wao ndiyo walitakiwa kwenda kuizika.
Mama wa marehemu akaanza kulia kwa uchungu, hakulia kwa kuwa watoto wake walikuwa wamefichwa ila alilia kwa kuwa alijua fika kwamba huo ulikuwa wakati wa kuumbuliwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hawa watoto walikuja kuroga nyumbani kwangu usiku,” alisema Ramadhani na kuendelea:
“Nilichokifanya ni kuwasimamisha na ndiyo maana mnaona kwamba wamekufa lakini ukweli ni kwamba hawajafa bali walikuja kuroga nyumbani kwangu,” alisema Ramdhani,
Minong’ono ikaanza kuibuka msibani hapo, kila mtu aliyeyasikia maneno yale alipigwa na butwaa, watu ambao hawakuamini kama uchawi ulikuwepo, hapo wakaamuni kwa asilimia mia moja,.
“Huyu mama yao alikuja nao akiwa na wenzake, wakawaacha na kuwasakizia waingie ndani na wakati wanajua kwamba hawakuwa na uwezo wa kuroga,” alisema Ramadhani, watu wote wakamwangalia mwanamke yule, kilio cha unafiki kikakata, akainama chini kwa aibu.
“Sikutaka kuwaua mabinti hawa kwa kuwa hawajui chochote kile, waliingia kwa kushinikizwa tu. Twendeni mkawachukue,” alisema Ramadhni na kuanza kuondoka mahali hapo.
Hakukuwa na mtu aliyetaka kubaki, wote wakaanza kumfuata Ramdahani ambaye alikuwa akitembea kwa mikogo mikubwa. Mkononi alishika hirizi kubwa nyekundu, alitembea kwa hatua ndefundefu ila kwa mwendo wa taratibu.
Walipofika nyumbani, akawaambia watu wale wasubiri na kisha kupulizia dawa fulani na kuwaita wasichana wale ambapo mlango ukafunguliwa na wasichana hao kutoka wakiwa kama walivyozaliwa, huku wakiwa wanatisha kwani bado walikuwa kwenye hali ya kichawi. Watu waliotangulizana na Ramadhani walipowaona wasichana wale, wakaanza kukimbia kwa hofu.
*****
Kwa muonekano, walitisha mno, hakukuwa na mtu aliyekuwa radhi kubaki mahali hapo na kuwaangalia mabinti wale, walikuwa na muonekano wa kichawi ambao ulizidi kuwaogopesha watu zaidi.
Alichokifanya Ramadhani ni kuwaweka chini kisha kuwapaka unga fulani, ulikuwa ni wa njano, aliyapaka macho yao na miguu yao, baada ya kufanya hivyo, akaanza kuiongea maneno yasiyoeleweka na hapohapo mabinti wale wakarudi katika hali ya kawaida.
Kwanza walishangaa walikuwa wapi, kwa mbali mbele yao kulikuwa na umati wa watu ukiwashangaa, walipojitazama, wakagundua kwamba walikuwa watupu jambo lililowafanya kuanza kuziziba sehemu zao za siri kwa kutumia viganja vya mikono yao.
Pasipo kutegemea, mabinti wale wakaanza kulia. Kwao iliwauma sana kuwa katika mazingira hayo, hawakuwa wakikumbuka kile kilichowafanya kuwa mahali hapo lakini baada ya kumuona Ramadhani, wakakumbuka kila kitu.
“Wachukueni muwapeleke kwao,” alisema Ramadhani, walichokifanya wanaume wenye moyo wa chuma ni kuwachukua na kuwapeleka nyumbani kwao huku kundi kubwa la watu likiwafuatilia kwa nyuma.
“Hao wachawi hao, waangalie wanavyotisha, kama vinyago.”
“Hao, watoto wadogo wanajifunza uchawi.”
Zilikuwa kelele kutoka kwa watu waliokuwa wakiwatazama mabinti wale. Walikuwa wasichana warembo wa sura waliokuwa na mamumbo mazuri lakini kitendo chao cha kujihusisha na uchawi kiliwashtua watu.
Walitembea kwa aibu mpaka walipofika nyumbani kwao na kuingia ndani, kwa kipindi cha wiki nzima, hawakutaka kutoka ndani kwani walikuwa wakijisikia aibu mno.
****
Nilimuona mzee Hamisi akiwa amechanganyikiwa, kile kilichokuwa kimetokea, kilimuuma sana. Alipagawa kwani aligundua kwamba Ramadhani hakuwa mtu wa mchezo na ndiyo maana hata pale kwenye mikwara, na yeye alikuwa na moyo wa kumpiga mikwara kwamba angeweza kumuua.
Hakutaka kukaa jijini Dar es Salaam, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea Bagamoyo. Hapa subiri nikwambie kitu kimoja kwamba mchawi yeyote anapoona kwamba ameshindwa sehemu fulani, huwa hataki kukubali bali anachokifanya ni kutafuta hata msaada wa watu wengine kuhakikisha kwamba anafanikiwa mpaka kutimiza kile alichokuwa akikihitaji.
Huko Bagamoyo alikuwa akimfuata mzee mwingine ambaye alionekana kuwa nuksi sana, mzee ambaye alikuwa akimuaminia kwa kuwa na uchawi wenye nguvu, alipofika huko, akaenda kuonana na mzee huyo kisha kuanza kuzungumza naye.
“Anatumia uchawi wa wapi?” aliuliza mzee huyo, aliitwa mzee Maliki, alijulikana Bagamoyo nzima kwa uchawi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wa Kanda ya Magharibi!”
“Kutoka Kigoma?”
“Ndiyo!”
“Daah! Hapo kuna kazi kubwa, ila tutafanikiwa.”
Wachawi walikuwa wamegawanyika, walikuwa wale kutoka Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi na Kanda nyingine nyingi. Kwenye kila kanda, kulikuwa na nguvu yake lakini wachawi wengi waliogopa uchawi kutoka Kanda ya Magharibi.
Huko Kigoma, asilimia kubwa ya uchawi wao ulikuwa ukichanganyikana na ule kutoka Kongo ambao ulijulikana kwa kuwa mkubwa na wenye nguvu kuliko ule wa Tanzania. Watanzania wengi walikuwa wakiuogopa uchawi huo na ndiyo maana mzee Hamisi aliposema kwamba uchawi aliokuwa akiutumia Ramadhani ulitoka Kanda ya Magharibi, mzee Maliki akaogopa.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Kwangu sidhani kama nitaweza ila kama utahitaji sana, kesho tuelekee Tanga, kuna mtu ambaye anaweza akatusaidia,” alisema mzee Maliki.
“Sawa hakuna tatizo.”
Mzee Hamisi hakutaka kurudi Dar es Salaam, alichokifanya ni kusubiri hukohuko Bagamoyo ili kujiandaa na safari ya kwenda Tanga kwa mtu mwingine ambaye aliambiwa kwamba alikuwa na nguvu kubwa mno.
Usiku hakulala kwa raha, kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Ramadhani aliyeonekana kuutetemesha ufalme wake. Alimchukia kijana huyo na alitaka kuhakikisha kwamba kila kitu atakachokifanya basi mwisho wa siku kijana huyo afe.
Asubuhi ilipofika, wakaamka na safari ya kuelekea Tanga kuanza. Kuna kitu huwa kinashangaza sana, unaweza kumkuta mchawi akiwa bize na mambo yake, tena ya msingi kabisa lakini linapokuja suala la kuroga, yaani yupo radhi aache mambo yake yote lakini mwisho wa siku afanye kile anachotakiwa kukipata.
Si kwamba mzee Maliki hakuwa bize na mambo yake, alikuwa bize mno lakini alipoambiwa suala la kutaka kumroga mtu fulani, mambo yake yote akayaacha pembeni na kutaka kufanya kile alichokuwa amewambiwa, yaani alikuwa akihusudu uchawi kuliko kitu chochote kile.
Baada ya sa moja wakawa ndani ya basi wakielekea Tanga. Walikuwa wakipiga stori tu njiani huku kila mmoja akionekana kutokuwa na wasiwasi kabisa. Basi lilipofika Segera, njia panda ya kwenda Moshi na Tanga, likasimama.
Kila mmoja akahisi kwamba inawezekana kuna abiria alikuwa akishuka au wengine wakiingia lakini kitu cha ajabu, basi likasimama kwa muda mrefu sana lakini dereva hakuliondoa jambo lililowakera abiria.
“Dereva unazingua, hakuna abiria anayepanda, sasa tunasubiri nini hapa? Au tunamsubiri mkeo?” aliuliza abiria mmoja, kwa muoenakano wake tu ulionyesha alikuwa kisirani.
“Gari haiondoki!” alijibu dereva.
“Haiondoki au haiwaki?”
“Kuwaka imewaka, wala sikuzima, ila kuondoka haiondoki, sijui tatizo nini,” alisema dereva yule.
Maneno ya dereva yule yalimshangaza kila mmoja, hakukuwa na aliyeamini kama kweli daladala lilishindwa kuondoka na wakati ilikuwa imewaka. Alichokifanya abiria mmoja aliyeonekana kuwa mtaalamu wa magari akasimama na kuelekea kule kwa derea ambaye akampisha na yeye kukalia kiti, akajaribu kukanyaga mafuta ili waondoke, gari haikuondoka.
“Mmmh!”
“Imekuwaje?”
“Ndiyo kwanza naona leo, imekuwaje gari haiondoki?” aliuliza dereva.
Minonong’ono ikaanza kusikika ndani ya basi lile, hakukuwa na mtu aliyejua kwamba kile kilichokuwa kikiendelea kilikuwa katika utawala wa nguvu za giza hivyo kwa akili ya kibinadamu jambo hilo lisingewezekana kabisa.
Mzee Hamisi na Maliki hawakuelewa chochote kile, ila waliposikia kwamba hali hiyo haikuwa ya kawaida kutokea duniani kwamba gari liwake lakini lishindwe kuondoka, wakaanza kuelekea kwa dereva ambaye bado alikuwa kwenye sintofahamu.
“Kuna nini?” aliuliza mzee Hamisi huku akionekana kuwa na wasiwasi.
Hata kabla dereva hajajibu swali hilo, ghafla wingu kubwa likaanza kujikusanya, ndani ya sekunde kumi tu, tayari jua halikuonekana, hapohapo mvua kubwa ikaanza kuinyesha huku ikiambatana na radi kali iliyowafanya watu wote kuogopa.
“Mmmh!” aliguna mzee Maliki.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ilikuwa ni mvua kubwa, ilishuka tena kwa kasi kubwa kiasi kwamba kila mmoja akadiriki kusema hakukuwa na mvua kubwa iliyowahi kunyesha kama ile. Radi ziliendelea kupiga, kila mmoja akaanza kuogopa.
Mzee Maliki alionekana kushtukia kitu, kila alipoiangalia mvua ile, haikuwa ya kawaida, ilionekana kuwa na chembechembe za uchawi hali iliyomfanya kugundua kwamba kazi ilikuwa imeanza hivyo hakutakiwa kupuuzia.
Abiria ndani ya basi waliogopa, wengine wakaanza kulalamika kwamba dereva alitakiwa kuliondoa gari mahali hapo haraka iwezekanavyo. Kwa mzee Hamisi, hakugundua kitu chochote kile, kwake, mvua ile ilionekana kuwa ya kawaida sana.
Mzee Maliki akarudi kule kulipokuwa na kiti chake na kisha kuchukua mkoba wake aliouacha, mzee Hamisi alishangaa, alijua vitu vilivyokuwa ndani ya mkoba ule vilikuwa nini, sasa kwa nini mzee huyo aliuchukua.
“Kuna nini?” aliuliza mzee Hamisi.
“Unadhani hii mvua ni ya kweli?”
“Ndiyo!”
“Hapana! Nahisi huyo mtu kashaanza kufanya kazi.”
Aliposema hivyo tu ikawa kama mzee Hamisi amefunguliwa macho, mvua ile iliyokuwa ikinyesha, haikuonekana kuwa ya kawaida kabisa, hivyo naye akajiandaa kwani tayari alijua kwamba muda wa mapambano ulikuwa umefika.
Mzee Hamisi akatoa tunguli zilizokuwa ndani ya mkoba wake, kila abiria akaonekana kuogopa, hawakujua mzee huyo alitaka kufanya nini. Hakutoa tunguli peke yake bali pia alichukua na usinga kisha kushuka garini na kuanza kuchezacheza huku akizunguka kwa staili ya mduara.
Kila mtu alibaki akimshangaa lakini wala hakuonekaa kujali, alichokifanya ni kuendelea vilevile. Katika hali ambayo kila mtu aliishangaa, mvua ikakatika ghafla huku ardhi ikiwa haijalowana hata mara moja. Watu wote wakapigwa na butwaa.
“Eeeeh!”
Huo ndiyo ulikuwa uchawi aliokuwa akiutumia Ramadhani, ulikuwa uchawi wa hali ya juu sana na uliotisha ambao ulihitaji nguvu ya ziada kuweza kuusimamisha. Baada ya hapo, akarudi ndani ya basi kwa ajili ya kuondoka lakini bado basi lile halikuweza kuondoka mahali hapo.
Hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu walikuwa wamekwishafika Segera, wakateremka kwa ajili ya kuchukua basi jingine ambalo lilikuwa likielekea Tanga ili wasiweze kukwamba njiani na wakati kutoka hapo mpaka Tanga wala hakukuwa mbali.
Walitulia kituoni wakisubiri basi. Ndugu yangu, uchawi upo na mtu anaweza akaroga sehemu yoyote unapokuwa. Kwa wale waliowahi kufika Segera watakuwa wanaelewa kwamba mahali hapo huwa hakukauki mabasi hata mara moja, kila siku na kila saa magari yanapita yakielekea Moshi, Dar au Tanga.
Lakini huwezi amini, siku hiyo watu hao walikaa zaidi ya masaa mawili, hakukuwa na basi lolote lile lililopita kuelekea Tanga. Hiyo wala haikuwa kawaida kabisa, walijaribu kuangalia huku na kule lakini hakukuwa na basi lolote hali iliyowafanya kutoka pale kituoni na kuwafuata watu waliokuwa wamekaa pembeni na kuwauliza.
“Samahanini?” alisema mzee Maliki.
“Bila samahani.”
“Mbona leo magari hayapiti hapa?”
“Magari ya kwenda wapi?”
“Tanga!”
“Unamaanisha mabasi?”
“Ndiyo!”
“Mmefika muda gani?”
“Tangu masaa mawili yaliyopita.”
“Eeeh! Sasa mabasi hayo yote yanayopita hamuyaoni au mnatufanyia kusudi wazee wetu?” aliuliza kijana mmoja, wote wakabaki wakiwashangaa wazee wale.
“Mabasi yanapita?”
“Ndiyo! Tangu lini umeona Segera ikakaukiwa na mabasi?” alihoji kijana mmoja.
Mpaka hapo wakajua kwamba tayari walichezewa mchezo hivyo mzee Maliki akaulizia choo kwani alisema alishikwa na haja. Akaonyeshewa choo cha kulipia na kwenda huko. Mbele yake tayari aliona kulikuwa na kazi kubwa sana ya kufanya hivyo pasipo kufanya kitu wangeweza kukesha barabarani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alichokifanya mara baada ya kufika chooni ni kuchukua usinga wake na tunguli lake, akasimama wima kuelekea upande wa kusini na kisha kuanza kuzungumza maneno fulani yaliyofanana na lugha ya Kiarabu, alipomaliza, akajipiga na ule usinga kifuani, miguuno na mabegani kisha kujipulizia unga fulani.
Alipomaliza, akatoka ndani ya choo kile, kitu ambacho kilimpa uhakika kwamba kweli walikuwa wamerogwa alianza kuyaona mabasi yakiwa mengi kituoni huku mengine yakiitia abiria kwamba yalikuwa na safari ya kwenda Tanga.
Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake, akamwambia mzee Hamisi kwamba walipaswa kuendelea na safari kwani bado hawakuwa wamefika. Garini, mzee Hamisi alibaki akiuliza tu, hakuamini kama mambo yote hayo yaliyokuwa yametokea yangetokea siku hiyo.
Hapo ndipo alipoamini zaidi kwamba Ramadhani hakuwa mtu wa mchezo hata mara moja na alikuwa na uchawi uliokuwa na nguvu kuliko hata ule aliokuwa akimiliki yeye. Safarini, hawakutaka kupiga stori, kila mtu alikuwa anawaza lake kichwani, kwa mzee Hamisi, alikuwa akijifikiria ni kwa jinsi gani angeweza kummaliza Ramadhani ambaye alionekana kuwa moto wa kuotea mbali.
Kadiri alivyojifikiria, ndivyo alivyoingiwa na hofu moyoni hata kuona kwamba huyo mzee waliyekuwa wakimfuata, hakuwa kitu mbele ya Ramadhani.
Waliendelea na safari yao kuelekea Tanga, mioyo yao ilikuwa na hofu tele kwani vile vitu alivyokuwa akivifanya Ramadhani havikuwa vya kawaida hata kidogo, uchawi aliokuwa akiufanya ni ule uliozoeleka kuonekana Kongo na nchi zingine zilizopo Magharibi mwa nchi ya Tanzania.
Kutoka Segera mpaka Tanga hawakupata shida yoyote ile, walipofika njiani hata kabla ya kuingia mjini wakateremka na kuchukua magari ya kwenda Handeni alipokuwa akiishi mzee Majoka, mzee aliyekuwa akisifika kwa uchawi Handeni nzima.
Histori fupi ya mzee Majoka ambayo nilipewa na Yusnath ni kwamba alikuwa mzee mpole sana kwa kumwangalia, muda mwingi alionekana nadhifu kiasi kwamba watu wengi walivutiwa na maisha yake. Alikuwa mtu wa swala tano, kila alipoonekana, kanzu kubwa ilikuwa mwilini mwake kitendo kilichowafanya watu wengi kumuita jina la ustadhi ila baada ya kwenda kuhiji Macca, akapewa jina la Alhaji Majoka.
Mzee huyu alifanikiwa kupata watoto watatu wa kike, Rehema, Micilia na Fatuma ambao alizaa na mkewe kipenzi mwenye asili ya Kiarabu aitwaye Salhia. Mzee Majoka alimpenda sana mke wake zaidi ya kitu chochote kile na alikuwa mtu mwenye wivu kupitiliza.
Kuna kipindi alipata taarifa kwamba kuna jamaa alikuwa akimmendea sana mkewe, alipata taarifa kwa kipindi kirefu sana na kuna kipindi aliambiwa kwamba tayari jamaa huyo aliyeishi kidogo Dar alifanikiwa kufanya mapenzi na mke wake huyo, hivyo alichokifanya ni kwenda kumuonya kutembea na mkewe.
Kutokana na upole wake, kijana yule alipingana naye, akamwambia kwamba hakuwa akitembea na mkewe, lakini kwa kuwa alimaanisha kile alichokisema, alimwambia kwamba asijaribu kufanya hivyo kwani yeye ndiye aliyemtolea mali na kumuoa.
Kijana yule aliyejiita Mtoto wa Town hakukoma, pamoja na kuambiwa na mzee Majoka, akawa anaendelea kutembea na mke wa mzee yule. Mzee Majoka hakumlaumu mkewe, maisha aliyokuwa akijiweka kijana huyo, kwa pale kijijini ilikuwa ni lazima kwa mwanamke yeyote yule kuvutiwa naye, hivyo alichokifanya ni kumfuata tena na kumuonya.
“Mzee! Hivi kweli unavyoniona ninaweza kutembea na mkeo, bibi zima?” aliuliza Mtoto wa Town aliyependwa kuitwa kwa jina la Diamond kutokana na jinsi nywele alivyoziweka na nguo alizokuwa akizivaa.
“Najua mke wangu ni mzee, lakini nakuomba kama unatembea naye, acha mara moja, sipendi masihara kabisa,” alisema mzee huyo kwa sauti ya upole lakini kwa mbali ilijaa ukali.
Baada ya siku mbili, watu hawakujua kitu gani kilitokea lakini kuna siku taarifa zikasambazwa kwamba kijana yule amenasiana na mke wa mzee Majoka porini chumbani. Siku hiyo ilikuwa balaa, taarifa zilisambazwa sana kijijini hapo na watu kuelekea kule kulipokuwa na chumba cha kijana yule, kweli wakawakuta wawili hao wakiwa wamenasiana.
“Hili tego, jamani hili tego,” alisema mwanakijiji mmoja.
Mtoto wa Town akawa analia tu, alijaribu kuomba msamaha lakini hakukuwa na mtu aliyemsaidia kwani mtu aliyeweka tego alikuwa mume wa mwanamke huyo, hivyo mzee Majoka akaenda kuitwa.
Alipofika na kuwakuta watu wale wakiwa kwenye hali ile, akashangaa sana kwani aliwahi kumfuata kijana huyo mara mbili na kumwambia kuhusu mke wake lakini alipinga kwamba hakuwa akitembea naye, sasa ilikuwaje leo hii wawe wamenaswa?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mzee naomba unisamehe!” alisema kijana yule huku akilia kama mtoto.
“Kwa kosa gani?”
“Kutembea na mkeo! Uwiiiiiii! Naomba unisamehe!”
“Wewe si ulisema hutembei naye, sasa imekuwaje?”
“Mzee naomba unisamehe!”
Mzee Majoka alikataa, akaondoka chumbani hapo huku akiwaacha watu wakiwaangalia watu wale, wengine walikuwa wakicheka lakini wengine walisikitika. Wazee wa kijiji hicho wakaamua kumfuata mzee huyo na kumuombea msamha kijana huyo, kwa shingo upande akakubali hivyo anawanasua kwa kutumia madawa yake, kuanzia siku hiyo kijana huyo akahama Handeni na kuhamia Tanga Mjini.
Ukiachana na hilo pia kulikuwa na kijana mwingine ambaye alikuwa akimmendea sana binti wa mzee huyo, Micilia, kila alipokuwa akienda kuchota maji, alikuwa akimfuata nyuma kama mkia, alimpenda sana na hivyo kujaribu kutupa ndoano yake.
Micilia akanasa na hivyo kuanzisha uhusiano na kijana yule aliyeitwa kwa jina la Saidi ila kijijini hapo aliamua kujiita Side Mnyamwezi. Baada ya kufanya mapenzi na Micilia, hatimaye binti huyo akapata ujauzito, nyumbani walipomuuliza, akwaambia kwamba ilikuwa ni ya Side Mnyamwezi.
Kijana huyo akaitwa na kuulizwa juu ya mimba ile, akakataa katakata na kusema kwamba haikuwa yake kwani kama ingekuwa yake, ingekuwa tumboni mwake.
“Hiyo siyo yangu! Kama ni yangu anipe sasa mbona anayo yeye,” alisema Side Mnyamwezi kwa nyodo sana, watu wote waliokuwa eneo hilo wakaanza kucheka, mzee Majoka aliumia sana.
“Kwa hiyo unataka akupe?”
“Ndiyo! Si umesema yangu! Nipeni,” alisema Side huku akipeana tano na marafiki zake waliokuwa kijiweni.
Mzee Majoka hakuongea sana, alichokifanya ni kwenda chumbani na kujifungia. Hakutoka siku nzima, kesho asubuhi akasikia watu wakigonga hodi kuhitaji msaada, alipoufungua mlango, akaambiwa kwamba kijana yule, Side Mnyamwezi amevimba tumbo na alikuwa akilia huku akilitaja jina la mzee Majoka.
Alichowaambia ni kwamba alitaka kumuona huyo Side, wakaenda kumuita, Side alipomuona mzee huyo tu, akaanza kulia huku akimuomba msamaha.
“Nini tena?” aliuliza mzee Majoka.
“Naomba unisamehe mzee, ile mimba kweli ni yangu!”
“Ndiyo ni yako na ndiyo maana nimeileta kwako,” alisema mzee Majoka.
“Naomba unisamehe mzee, sitorudia tena.”
“Kwani umenikosea?”
“Mzee naomba unisamehe!”
Siku hiyo Side alilia sana, aliomba msamaha na mwisho wa siku mzee huyo akamsamehe na mimba kurudi kwa Micilia huku akimuonya kijana huyo kwamba kama hatoilea mimba ile, angemrudishia tena akae nayo.
Kuanzia siku hiyo, jina la mzee Majoka likavuma, akajulikana Handeni nzima kwamba alikuwa mzee nuksi ambaye hakukopesha, yeye alikupa keshi endapo tu ungemletea masihara. Kuna mambo mengi ambayo aliyafanya katika wilaya hiyo ya Handeni ambayo ilithibitisha kwamba alikuwa nuksi.
Uchawi wake huo ukamfanya kila siku usiku kwenda makaburini, kazi yake kubwa ilikuwa ni kufukua maiti na kuchukua viungo. Hakukuwa na mtu aliyejua kwamba uchawi wa mzee Majoka ulikuwa mpaka ule wa kupaa usiku na ungo.
Mara kwa mara alikutana na wenzake katika vikao vyao hasa vya wachawi wa Ukanda wa Pwani ambapo huko walipanga mikakati yao jinsi ya kuwaroga watu mbalimbali na kusafuiri kwa ungo kuelekewa sehemu tofautitofauti.
Japokuwa kulikuwa na wachawi wengi, lakini katika ya wachawi wote wa Kanda ya Pwani, hasa Tanga, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uchawi zaidi ya mzee Majoka, mzee ambaye alikuwa akifuatwa na wazee wawili, Hamisi na Maliki kwa ajili ya kupambana na kijana aitwaye Ramadhani.
****
Walipofika Handeni, wakapokelewa na mzee Majoka ambaye alikwishapewa taarifa juu ya ujio wa watu hao. Kwa muonekano aliokuwa nao mzee huyo, mzee Hamisi hakuamini kama angeweza kuifanya kazi yake kwani alionekana kuwa mpole mno.
Asilimia kubwa ya wachawi, huwa hawana sura za kipole, wengi wao wanakuwa kama watu wenye roho fulani chafu, unaweza kujua kwamba mzee fulani ni mchawi, unapomuona au kupishana naye, mara nyingi unashikwa na hofu.
Mchawi anajulikana hata kama atakuwa katika hali gani, wengi wanakuwa na muonekano wa tofauti na huwa watu wasiojali sana, ila kwa huyu mzee Majoka, alionekana kuwa tofauti kabisa.
“Ndiye huyu?” aliuliza mzee Hamisi.
“Ndiye mwenyewe. Unamuonaje?”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tumekuja kupoteza muda, anaonekana haiwezi kazi hii,” alisema mzee Hamisi, imani yake haikuwa kabisa kwa mzee huyo hata kidogo.
Wakaondoka na kuelekea nyumbani kwa mzee Majoka, njiani, kila mtu alikuwa akizungumza kwa fuaraha tele, kitendo cha kupokea ugeni huo, mzee Majoka alihisi kuthaminiwa mno. Njiani, kila mtu aliyekuwa akiwaangalia watu hao, alijua tu kwamba walikuwa wachawi kwani walitangulizana na mtu aliyekuwa balaa kwa kuroga mtaani hapo.
Hakukuwa na watu waliowasogelea, na hata wale ambao kwa bahati mbaya walijikuta wakiwa karibu yao, walitoa salama kiuoga na kuendelea na mambo yao. Walipofika nyumbani, mzee Majoka akawakaribisha na kuingia ndani ambapo moja kwa moja mazungumzo yakaanza.
“Kuna shida gani? Maana ulinieleza juujuu tu,” alisema mzee Majoka.
“Unamuona huyu rafiki yangu?”
“Ndiyo.”
“Amekutana na maswahibu si mchezo,” alisema mzee Maliki.
“Maswahibu gani?”
“Kuna mtu anamsumbua sana, alikuja kwangu, nikataka kumsaidia ila nikachemka kabisa,” alisema mzee Maliki.
“Umechemkia nini?”
“Yule jamaa anatumia uchawi wa Magharibi.”
“Magharibi?” aliuliza mzee Majoka huku akishtuka.
“Ndiyo!”
“Ooppss...” alishusha pumzi mzee Majoka.
“Vipi tena? Na wewe unaushindwa?”
“Hahaha! Tangu lini umeona nimeshindwa kitu? Hakuna kitu kama hcho,” alisema mzee Majoka kwa kujiamini.
“Basi tufanye kazi.”
“Hakuna tatizo. Kuna sehemu nataka twende, huko, kuna dawa zangu hatari sana, haijalishi kama ni wa Magharibi au wapi,” alisema mzee Majoka.
Kidogo mzee Hamisi na Maliki wakashusha pumzi kwa furaha, tayari walijiona kushinda juu ya kile kilichokuwa kikiwatatiza, kitendo cha mzee huyo kusema kwamba hakukuwa na uchawi wowote uliokuwa ukimshinda, kukawafariji na kuona kwamba waliukaribia ushindi.
Alichokifanya mzee Majoka ni kuinuka, akaenda chumbani kwake na kujiandaa tayari kwa safari ya kuelekea porini ambapo huko ndipo kulipokuwa na madawa yake ambayo alikuwa akiyategemea kwa kufanya kazi kubwa.
“Umeona?”
“Nimeona, huyu kiboko,” alisema mzee Hamisi.
Hakukuwa na haja ya kuona matukio aliyoyafanya, maneno ya kuudharau uchawi wa Magharibi tu kulimpa uhakika kwamba angeweza kupambana na Ramadhani. Mzee Majoka alichukua dakika ishirini kujiandaa, baada ya hapo, mlango ukafunguliwa.
“Twendeni,” alisema mzee Majoka, mzee Hamisi na Maliki wakashtuka.
Hilo ndilo tukio la kwanza alilolifanya, alitaka kuwaonyeshea kwamba alikuwa kiboko ya wachawi wote, alifungua mlango na kuingia chumbani, alipotoka, hakuwa akionekana, kitu walichokiona mzee Maliki na Hamisi ni mlango kufunguka lakini hakukuwa na mtu na ghafla wakasikia sauti ikiwaambia waondoke.
Walishtuka mno, sauti waliisikia, ilikuwa ni ya mzee Majoka, ila mwenyewe yupo wapi? Kila walipoangalia, hakukuwa na mtu yeyote yule, wakazidi kuogopa kwa kuona uchawi wa huyo mzee ulikuwa balaa.
“Mmmh!” aliguna mzee Hamisi.
Hapohapo mzee Majoka akatokea na kuanza kucheka. Alicheka kwa sauti kubwa, wazee wale wawili walikuwa wakiogopa. Si kwamba hawakujua kwamba mchawi alikuwa na uwezo wa kupotea, ila kwa mchana, kwao ilikuwa ni kitu kingine cha ajabu.
Mara nyingi sana wachawi walikuwa wakipotea nyakati za usiku na si mchana na ndiyo maana wengi wanaoshikwa mchana huwa wanashindwa kupotea. Leo hii walikutana na mchawi aliyekuwa na nguvu ya kupotea hata mchana, hiyo ilitosha kuonyesha kwamba mzee Majoka alikuwa moto wa kuotea mbali.
“Huyu atamuweza,” alijikuta akisema mzee Hamisi kwa sauti kubwa huku akionekana kuwa na furaha.
Wakatoka nyumbani hapo huku mzee Majoka akiwa amebeba mfuko wake wa Rambo ambao ndani yake kulikuwa na vitu vya kichawi alivyotaka kuvifanya siku hiyo. Kwake, kazi iliyokuwa mbele haikuwa kubwa, ilikuwa ya kawaida mno na aliwapa uhakika kwamba ingewezekana kufanyika kwa haraka sana kiasi kwamba wasingeamini kama ingekuwa hivyo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mzee Hamisi alizidi kufurahi, aliendelea kumuamini mzee Majoka kwamba kila kitu kingekuwa poa kwa upande wake. Waliendelea kupiga hatua, walipofika kama umbali kutoka mita mia moja kuingia ndani ya pori hilo ambalo mzee Majoka alisema kwamba kulikuwa na uchawi wake, wakaanza kusikia sauti kubwa ya mawimbi ya bahari.
Hiyo ikawashangaza sana, upande ule waliokuwa wakielekea hakukuwa na bahari, bahari ilikuwa mbali kabisa, tena huko nyuma, sasa ilikuwaje sauti ya mawimbi isikike, tena ikitokea mbele yao? Hawakutaka kujiuliza sana, wakahisi kwamba inawezekana ni sauti za matawi ya miti ambayo yalikuwa yakipigwa na upepo, wakazidi kusonga mbele.
Walipofika sehemu ambayo ilitakiwa kuwa na pori, wakapigwa na mshtuko, mbele yao hakukuwa na pori kama walivyotegemea bali kulikuwa na bahari kubwa iliyokuwa ikipiga mawimbi makubwa kiasi kwamba wakashtuka.
“Imekuwaje tena? Mbona bahari?” aliuliza mzee Hamisi kwa mshtuko.
“Hata mimi nashangaa, huku kuna pori, nashangaa kuona bahari! Au tumekwenda upande wa bahari bila kujijua?” aliuliza mzee Majoka huku naye akiwa na mshtuko mkubwa.
“Wazee wangu! Wala hatujakosea njia, tumekuja kulekule uliposema kwamba kuna pori. Ila hiki kinachoonekana, ni yule mzee wa Magharibi,” alisema mzee Maliki, hapohapo wakaanza kupata picha.
“Hata mimi nimehisi hivyo. Nafikiri natakiwa kuanza kazi, lakini itawezekanaje na wakati dawa hatujazipata?” aliuliza mzee Majoka, alionekana kuchanganyikiwa.
“Kwa hiyo huyu ni Ramadhani?” aliuliza mzee Hamisi.
“Ndiyo!” alijibu mzee Maliki.
Hali ya mawili yale ikaanza kubadilika, yakaanza kupiga kwa kasi kidogo na kadiri muda ulivyozidi kuongezeka na ndivyo yalivyozidi kupiga. Ghafla huku wakiwa wanayaangalia mawimbi yale, hapohapo mawimbi makubwa ya bahari ile yakaanza kuja kule walipokaa, tena kwa kasi kubwa. Wakaogopa kwani uchawi wa Ramadhani ulionekana kuwatisha mno. Wakajiandaa kukimbia kwani nayo mawimbi yaliongeza kasi kuwafuata.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment