Search This Blog

KIBWE KATIKA SAFARI YA AJABU - 2

 







    Simulizi : Kibwe Katika Safari Ya Ajabu

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nadhani huko mbele kuna tatizo kubwa sana. Nimeota kuwa kutakuwa na kimbunga kikubwa, na meli yetu itapambana na mwamba wa barafu majini,” Kibwe alimwambia mwenzake, ambaye alimshangaa, akimwambia kuwa alichokiona kilikuwa ndotoni tu, wala si lazima kitokee. Lakini Kibwe hakumsikiliza Hanga, bali aliendelea kusema. “Kama hatukusitisha safari yetu kwenye bandari yoyote ya karibu angalau kwa siku moja na nusu hadi hatari hiyo ipite, wote tutapoteza maisha yetu.” Hee! Hanga akaduwaa akimwangalia mwenzake huyo aliyechanganyikiwa, au tuseme vile alivyoamini Hanga kwa wakati ule. Iweje tena jambo la ndotoni, Kibwe akalichukulia kuwa ni jambo kubwa na halisia? Hanga alijaribu kuzungumza na mwenzake akimsihi ajaribu kutulia tu, na atasahau kuhusu ndoto yake. “Na hata hivyo, unadhani kuwa utaeleweka kwa manahodha utakapowaambia wasitishe safari kwa kuwa uliota kuwa mbele kuna hatari? Jaribu kufikiri vizuri Kibwe.” Kibwe alishikilia palepale, akimwambia Hanga kuwa lazima manahodha wamwelewe, ama sivyo, wote wamo hatarini!

    Kwa hiyo, Hanga na Kibwe walikwenda hadi kwenye chumba cha manahodha, na kuwaelezea kuhusu hatari iliyoko mbele. “Lazima tusitishe huu msafara, mara tu tutakapofika bandari ndogo ya karibu, kabla ya kuelekea nchini Shamsi, ama sivyo, wote tutateketea.” Kibwe aliwasihi wale manahodha, bila kuwa na uthibitisho wa kutosha wa hoja yake hiyo. Manahodha wakamuona kuwa anafanya utoto tu, hivyo kwa kebehi, wakamwambia; “Hivi unadhani kuwa katika maisha yetu kwenye kazi hii, tungekuwa tunaamini kila tulichokiota, tungeweza kufanya safari kama hizi? Kijana, kumbuka kuwa ndoto ni ndoto tu. Hatuwezi kuacha kusafiri, eti kwa kuwa mtu mmoja miongoni mwetu ameota kuwa mbele kuna hatari!” Pia manahodha wale walisema kuwa kulikuwa na umuhimu wa kuwahi kufika kule waendako, ili waweze kugeuza merikebu yao na kurudi makwao, baada ya kumsindikiza Kibwe.

    “Lakini jamani, mmejiuliza kuwa huenda kuna ukweli kwenye maneno ya kijana huyu?” Baadhi ya wahudumu wa meli walihoji, wakinong’ona chinichini. “Kweli eti! Na labda tukiyadharau maneno yake hayo, tutakuja kujuta yatakapotokea hayo anayoyatabiri!” Wahudumu wa meli walisema hivyo, huku wenzao wengine wakihofu sana, walipokisia kuwa huenda kukawa na ukweli kwenye hoja ya yule kijana. ”Ndiyo kusema kuwa wote tutakuwa hatarini!” waliambiana. Hata hivyo wengine miongoni mwa wahudumu wale waliowaunga mkono manahodha na hoja zao, wakasema kuwa yule kijana aliota tu, na wala hakuletewa onyo rasmi la kimazingaombwe kutoka kokote. “Haya jamani na tuendelee na safari yetu, na tuachane na mawazo ya kishirikina!” walisema wahudumu hao, wakiwahimiza manahodha wasipoteze muda. Lakini lo! Laiti kama wangejua!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Haya, safari ikaendelea kama ilivyoamuliwa, na hakuna aliyejuwa kuhusu mkasa ambao ungetokea mnamo saa ishirini na nne zijazo! Kilometa kadhaa kutoka pale walipokuwa, kwenye mwamba mkubwa sana wa barafu majini, pande moja kubwa la barafu lilijigawa kutoka kwenye mwamba huo mkubwa wa barafu majini, uliokuwa kama mlima mkubwa sana! Sehemu hiyo ya mwamba iliyotanda baharini, ilikuwa ikielea na kusukasuka kuelekea kule ilikokua merikebu ya mfalme KashKash, walimokuwemo Kibwe na abiria wengine! Wakati huohuo, mawingu mazito na meusi yakawa yanajikusanya, na hivyo giza nene likaanza kutanda. Upepo nao ukaanza kuchanganya kasi ya mwendo wake, iliyoongezeka kwa kila dakika, na kuvuma kwa kuvuruga mawimbi ya bahari, yaliyonyanyuliwa juu kwa urefu mkubwa wa kustaajabisha, kwani kimbunga nacho kilikwishaanza! Lahaula! Huko kulikokuwa kukijiandaa katika hali hiyo, ndiko ilikokuwa ikielekea merikebu iliyowabeba kina Kibwe na wenzake! Merikebu ile ilisafiri kwa kilometa nyingi humo baharini, na wakati wote huo, Kibwe akiwa na wasiwasi mkubwa, kwani aliamini kabisa kuwa huko mbele sio kuzuri. “Nafahamu kuwa Bunga hawezi kutokea waziwazi ili kutuonya kuhusu hatari hiyo, maana watu wote watashangaa na pia kuhofu sana, mara watakapomuona,” Kibwe aliwaza. Lakini kwa bahati mbaya, ilibidi kijana yule asubiri hatari hiyo ifike, kwani hakuwa na la kufanya! “Haya. Liwalo naliwe!” alijiambia.

    Mnamo majira ya saa kumi na mbili asubuhi, abiria ndani ya merikebu ile wakaona hali ya hewa ikibadilika. Upepo ukawa unavuma kwa kasi na kwa hasira, huku bahari ikianza kuchafuka. Maji ya mawimbi yaliyokuwa yakijitupia na kupiga pembezoni mwa merikebu, yaliingia sitahani kwa wingi mno! Chini kabisa ya sitaha humo melini, nako kuilijaa maji tele! Kufikia hatua hiyo, abiria wote wakaanza kuhamanika, wakitoka vyumbani mwao ili kujiunga na wenzao, kuona jinsi hali ile iliyojitokeza, ilivyoashiria kuhatarisha maisha yao. “Haya sasa, tuone kama hakuna atakaye amini maneno yangu,” Kibwe alimwambia mwenzake Hanga, aliyekuwa ametowa macho pima akimshangaa Kibwe kwa kuyajua yote yale mapema! Ah! Laiti kama watu wangemuamini na ndoto yake! Mawazo hayo yalikuwa yakipita kichwani mwa Hanga. “Naam! Utabiri wa Bunga umeanza kuwa kweli!” Kibwe aliwaza, huku akiangalia jinsi walivyokuwa wamezingirwa na maji mle merikebuni.

    “Haraka kawaambie abiria waliokuwa chini ya staha waondoke na kuja juu zaidi! Na wa huku juu wawe waangalifu wasisogee pembezoni mwa meli!” Mmoja kati ya manahodha aliwaambia wenzake. “Lo! Kumbe yule kijana alisema kweli kabisa.” Manahodha wale waliambizana, huku wakikimbia kwenda kuwatahadharisha abiria kule walikokusanyika. Huko waliwakuta baadhi ya abiria wakiwa wamejeruhiwa kwa kukimbia kutoka vyumbani mwao, wakitafuta nusura sehemu ambazo maji hayakufika.Wengi wao walikuwa wakianguka na kutereza mara kwa mara, kwani ile merikebu ilikuwa ikisukasuka kwa kusukumwa na mawimbi. Kila ilipoegemea upande mmoja, merikebu hiyo iliwamwaga abiria kwa upande huo! “Kwa hakika maneno yako yalikuwa sahihi kibwe. Leo wote tuko hatarini!” Hanga alimwambia mwenzake , wakati walipokuwa wakijishikiza kwenye nguzo za ile meli, ili wasiteleze na kuangukia sehemu nyingine hatari zaidi. “Ndio hivyo tena. Lakini haina haja kulilia maji yaliyomwagika, kwani si rahisi kuyazoa,” alisema Kibwe. “Iliyobaki ni kuomba Mungu atuvushe salama kutokana na janga hili.”



    Huko nchini Hazina mashariki ya dunia jirani kabisa na Azarbarjan, Sultan Hazari Basari, alikuwa akisharehakea sikukuu ya kuzaliwa mwanawe wa kiume, kutokana na nadhiri aliyoiweka miaka kumi na tano iliyopita, baada ya kuota ndoto iliyoashiria kuwa katika umri wa miaka kumi na nne, kijana wake atakumbwa na jini Makata na kupelekwa mashariki ya mbali kwenye hewa inayogeuza watu kuwa mawe!

    HANGA BIN HAZARI

    Katika zama zile za kale, kule mashariki ya dunia nchini Hazina jirani kabisa na nchi ya Azarbajan kwa mfalme KashKash, alikuwepo Sultani mmoja mashuhuri sana, aliyeitwa Hazari bin Basari. Sultani huyo alitawala raia wake kwa amani, uaminifu na upendo mkubwa, na kwa sababu hiyo, raia wake walimpenda sana. Kwa bahati mbaya kwa miaka mingi sana Sultani yule na mkewe hawakujaaliwa kupata mwana ambaye angekuwa mrithi wa kiti cha utawala baada kuondoka Sultani Hazar. Jambo hilo liliwasonesha sana. Siku moja Sultani Hazari aliwaita wazee na washauri wake mashuhuri, akawaelezea masikitiko yake.

    “Sijui nifanye nini ili nami niweze kupata mtoto atakayekuwa mrithi wangu pindi nitakapoitoka dunia hii.” Aliwaambia.

    Naam wale washauri walipokutanisha vichwa vyao ili kutafuta ufumbuzi wa jambo lile, wote wakapata jibu moja.

    “Ama kwa hakika tatizo la namna hiyo hupatiwa ufumbuzi kwa njia moja tu, nayo ni kumuomba Mwenyezi Mungu mwenye kila uwezo. Tunakushauri uandae karamu kubwa na uwaalike yatima, mafakiri na mawalii, ili wamuombe Mwenyezi Mungu akujaalie kupata ufumbuzi wa jambo lako.” Walimshauri.

    Sultani Hazari aliupokea ushauri wao kwa dhati. Akaandaa karamu mkubwa na kutoa sadaka kwa wajane, yatima na mawalii, ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu.

    Naam haukupita muda mrefu, mkewe akashika mimba na miezi tisa baadae akajifungua mwana wa kiume, waliyemwita Hanga.

    Ndiye Hanga bin Hazari huyo!

    Sultani na mkewe walifurahi mno, na wakamlea mtoto wao kwa uangalifu na mapenzi makubwa sana hadi alipofikia umri wa miaka kumi na nne. Walimpa mtoto wao elimu bora na mafunzo mbalimbali ya mambo ya kimaisha, wakitarajia kuwa iko siku angekuwa mtawala wa nchi yake ya Hazina.

    Siku moja wakati akiwa usingizini, Sultani Hazari Basari aliota ndoto ya kutisha sana iliyohusiana na mwanawe kipenzi, Hanga. Katika ndoto yake alikuwa kwenye mji mmoja wa ajabu uliokuwa chini kabisa ya bahari, ambako huko alizingirwa na wingu nene la moshi mweusi kupita kiasi. Kila alipojitahadi kukodoa macho ili aone vizuri mbele yake, hakuweza kuona chochote. Wahka ulimzidi aliposikia sauti nzito ya kutisha ikiunguruma masikioni mwake, ikimwambia;“Ewe Hazari! Ewe Hazari! Fahamu kuwa furaha yako ya kupata mtoto haitaendelea! Haitaendelea! Haitaendeleaaaa…! Ha ha ha ha ha…..!” Kile kicheko kilichofuatia maneno yale mazito kilikuwa ni cha kuogofya na kukata matumbo!

    Kile kicheko kilisita kidogo na mchekaji yule asiyeonekana akazidi kumshindilia maneno mengine ya kutisha na ya kukatisha tamaa zaidi.

    “Kamwe huyo mwanao hatafikisha umri wa miaka kumi na tano, kwani kabla ya kufikia muda huo, atakumbwa na pepo mbaya na kupotelea kwenye msitu wa hatari...msitu wa kindumbwe!”

    “Eeg Mungu wangu weee!” Mfal,me Hazari alilalama ndotoni, na wala ile sauti haikusitishwa na mlalamo wake, ikaendelea, “…katika msitu huo daima uovu haulali wala hausinzii, na milima ya huko ni maarufu kwa maangamizi ya moto na hewa ya huko haikuwa ila ni yenye wingi wa sumu kali….Ha ha ha-ha-ha-ha-aaaaaaaa! Huwezi kumnusuru mwanao asilani wewe…huwezii…huweziiiiiiii! HHha-ha-ha-ha-haaaaaaa!”

    Ile cheko mbaya ilivuma kwa mudsa mrefu huku ikizidi kufifia taratibu mpaka ikawa kimya cha kutisha kuliko hata ile cheko yenyewe.

    Sultani Hazari aligutuka kutoka usingizini na kwenye ndoto ile akiwa na wahka na hofu kubwa! Moyo ulikuwa ukimuenda kasi na jasho lilikuwa likimtiririka kama mtu aliyekuwa akikimbia! Mkewe alipoamka na kumuona katika hali ile, alipatwa na wasiwasi mkubwa.

    “Umepatwa na nini mahabuba wangu? Mbona unanitisha?” Mke akadadisi kutaka kujua kilichomsibu Sultani usiku ule. Sultani alikaa kimya kwa muda, kisha akamwambia, “Kwa hakika ndoto niliyoota inanipa wasiwasi mkubwa.”

    Na akamsimulia mkewe ndoto yake.

    “Usiogope sana mume wangu. Asubuhi kutakapokucha tutawaita waalimu waje kumuombea dua mwanetu, kwani ndoto hiyo ni ya uovu wa majini tu, wapendao kutia wasiwasi katika nyoyo za wanadamu!”

    Kwa hiyo siku iliyofuata Sultani Hazari aliandaa kisomo kikubwa cha maombi kwa Mwenyezi Mungu, kilichohudhuriwa karibu na raia wote wa nchi ya Hazina. Siku ile Sultani akaweka nadhiri ya pekee! “Mwanangu atakapofikia umri wa miaka kumi na tano bila kupatwa na madhara yoyote, nitajaza fedha kwenye visima saba, na mafuta ya kupikia kwenye visima vingine saba, iwe sadaka kwa raia wangu wote wa Hazina kwa ajili ya nusura ya mwanangu. Kila mmoja kwa wakati wake atajichukulia kile atakachojaaliwa iwe fedha au mafuta, kadiri ya uwezo wake!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kufuatia kisomo kile, Hanga alilelewa kwa uangalifu zaidi na mapenzi makubwa kupita kiasi hadi alipofikia umri wa miaka kumi na tano na nusu, wakati ambao tayari alikuwa amevuka ule umri wa miaka kumi na tano ambao Sultani aliota kuwa angekuwa hatarini. Kwa bahati Sultani Hazari Basari alikumbuka nadhiri yake, hivyo akachimba visima kumi na nne, saba kati yake akavijaza fedha na saba akavijaza mafuta ya kupikia. Akatumwa mjumbe apite mitaani kuwatangazia raia wote wafike kwa Sultani na kujipatia sadaka. Kama kawaida ya matangazo kutoka kwa wafalme, mjumbe yule akapiga la mgambo ambalo kila likilia lazima huwa kuna jambo.

    “Naam ndugu zangu, Sultani wenu anawatangazia kuwa mwanawe Hanga bin Sultani kwa bahati nzuri amefikisha umri wa miaka kumi na tano bila kupatwa na madhara yoyote, kama ilivyodhaniwa awali! Ili kudhihirisha furaha yake, kesho Sultani atatimiza ahadi yake ya kutoa sadaka ya fedha na mafuta kwa raia wote wa nchi ya yake! Wote mnatakiwa kufika kwenye kasri lake bila kukosa!”

    Naam baada ya ujumbe ule kuwafikia raia wote waliokusudiwa, watu kutoka sehemu mbalimbali za milki ya Sultani yule nchini Hazina walikwenda katika kasri lake, wakajizolea fedha na kujichotea mafuta kwa ajili ya lishe yao bora. Wake kwa waume wazee kwa vijana na watoto kwa wakubwa walifurahia zawadi zile, na kila mmoja alishukuru na kumuombea Hanga anusurike na hasadi na kumtakia maisha mema.

    Lakini masikini bibi mmoja mzee aliyejulikana na jamaa zake kwa jina la ‘Ajuza’ aliyeishi nje kabisa ya mji mkuu katika nchi ya Hazina, alichelewa kuzipata habari zile nzuri, na akasikitika sana kwa wenzake waliobahatika.

    “Mbona Sultani hakutangaza nchi nzima kama ilivyo kawaida yake?” Alidadisi kizee yule. Wenzake walioshuhudia mjumbe wa Sultani akipita mtaa kwa mtaa kutangaza habari njema kwa raia wa Hazina, walishangazwa na lawama za yule Ajuza.

    “Kwani ulikuwa wapi hata ukakosa kumsikia mjumbe akitangaza mitaani?” Walimuuliza. Walimshauri aharakishe kwenda kwa Sultani akajaribu bahati yake.

    “Bila shaka utapata japo kidogo, ama mafuta au fedha. Usikate tamaa ndugu yangu.” Aliambiwa na mzee mwenzake aliyeishi jirani naye. Bila ajizi, wakati uleule kibibi ‘Ajuza’ aliondoka na kuelekea kwa Sultani Hazari, ambaye masikini, hakuwa hata na fununu kwamba ujio wa yule ‘Ajuza’ katika jumba lake ungebadili kabisa mwelekeo wa maisha ya Hanga, na kwamba ungefuata mkondo wa njozi yake aliyoiota awali!

    Kizee yule alipofika kwenye kasri la Sultani Hazari, bahati haikuwa yake. Visima vyote saba vya fedha havikuwa na kitu, isipokuwa kisima kimoja tu kati ya visima saba vya mafuta ndicho kilichokuwa na mafuta kidogo sana!

    “Ah, masikini mimi! Sina la kufanya kwani kila kitu huenda kwa riziki ya mtu. Hii niliyoikuta ndiyo riziki yangu. Nitashuka humo kisimani nikadundulize mafuta yaliyomo.” Alisema na nafsi yake na huku taratibu akijaribu kushuka kisimani kwa ngazi maalum iliyojengewa pembezoni, na huku kichwani kwake akiwa amebeba mtungi. Alipofika chini kabisa alichukua muda mrefu sana kuujaza ule mtungi. Hatimae alipofanikiwa kuujaza, aliunyanyua na taratibu akajitwika kichwani na kuanza safari ya kutoka nje ya kisima, kwa kutumia ile ngazi aliyoshukia. Alitoka kwa mwendo wa pole mno, kwani kutokana na kazi aliyoifanya ya kuujaza mafuta mtungi wake, alihisi maumuvu makali mno kiunoni na mgongoni!

    Gorofani, juu kabisa ya kasri la Sultani Hazari, Hanga bin Hazari alikuwa akimwangalia ‘Ajuza’ yule kwa muda mrefu, tangu aliposhuka kisimani, hadi alipokuwa akijaza mafuta mtungi wake na pia wakati alipokuwa akitoka akiwa amejitwika mtungi wake kichwani. Alitabasamu kuona jinsi bibi yule alivyokuwa akihangaika kufanya kazi ndogo kabisa! Kwa utundu wa kitoto, kijana yule aliyekuwa ameshikilia manati, akaulenga mtungi wa ‘Ajuza’ na kuachia kijiwe kilichofika moja kwa moja, tena kwa kasi kubwa kwenye mtungi wa yule bibi , na papo hapo kuupasua mapande mapande, na kumwacha ‘Ajuza’ akiwa amelowa mafuta chapachapa mwili mzima!

    Hasira alizopata bibi yule hazielezeki. Aliinua kichwa chake juu kuangalia gorofa ya saba ya jumba la Sultani, kuona ni nani aliyemfanyia kitendo kile cha kiburi! Hasira zake zilizidi alipomuona Hanga bin Sultani akimwangalia kutoka juu, akimcheka!

    “Ni mtoto wa nani wewe shetani rajimi usiyekua na adabu wala heshima kwa watu wazima? Hivi hujafunzwa na wazazi wako ukaambiwa kuwa heshima ni kitu cha bure? Kama unajiona kuwa wewe ni bora kuliko wenzako, kwa nini hujaenda Kaskazini mashariki kwenye ‘Paa la dunia’, ukatekeleze yale wanayoyafanya wenzako walio bora, wanaojitahidi kuinusuru sayari kutokana na majanga yanayoikabili?” Bibi kizee aliyaelekeza maneno yake kwa Hanga kwa hasira kubwa, akimwacha kijana yule akiwa kimya, akitafakari kile alichokuwa akikisikia.

    “Wewe huwezi kuwa bora kuliko Mwana Mteule ambaye licha ya uwezo na vipaji alivyonavyo vya kupambana na maovu, hata siku moja hajawahi kuwavunjia heshima wazee kama sisi!” Ajuza yule alimalizia maneno yake kwa kusisitiza kuwa ni wakati Hanga atakapofika kule ambako uovu umechukua nafasi kubwa kuliko wema, ndipo atakapotambua kwamba asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu! Maneno haya ya hasira ya Ajuza yalifuatiwa na msonyo mrefu kupita kiasi, ulioufanya moyo wa Hanga uzizime!

    Yule bibi aliondoka akiwa amechukia mno. Alikuwa akijifutafuta mafuta usoni kwake na mwilini, wakati Hanga akiwa ameduwaa na kumwangalia kwa tafakuri ya hali ya juu.

    “Huyu ni nani? na anafahamu vipi mambo yote yale aliyoyasema?” Alijiuliza na kutafakari kuhusu huyo Mwana Mteule aliyetajwa, na hatari iliyokuwa ikiikabili sayari yao. Wakati huohuo, alijutia sana utovu wake wa nidhamu alioudhihirisha kwa bibi kizee ambaye hakumkosea chochote. Haraka sana akapata wazo la kumfuata, kwanza akiazimia kumuomba radhi kwa kosa lake alilolifanya, na pili akitaka kupata majibu ya majanga yanayoikabili sayari yake. Akashuka ngazi za kasri la baba yake mbilimbili kwa wakati mmoja, ili aweze kumuwahi yule kizee kabla hajatoweka. Alipomkaribia alikuwa akipumua kwa kasi mno kwa jinsi alivyopiga mbio kutoka gorofani hadi chini!

    “Bibi…bibi…! Tafadhali nisamehe bibi yangu! Nimekosea sana kufanya vile nilivyofanya bibi…naahidi sintarudia kukufanyia vile nilivyokufanyia, na wala sintamfanyia mtu mwingine yeyote matendo ya utovu wa heshima ya namna yoyote!” Hanga alimuomba radhi yule bibi huku machozi yakimtiririka.

    Yule bibi alipomwangalia kijana yule, alihisi kuwa ni kweli alijutia kosa lake. Lakini pamoja na kumsamehe alimwambia kuwa mara nyingi ni bora kuzingatia mafundisho ya wazazi, badala ya kusubiri mafundisho ya ulimwengu, kwani ulimwengu ni mwalimu mkali mno kuliko waalimu wote.

    “Lazima kwanza uumie kabla mafunzo ya ulimwengu hayajazama akilini mwako. Zingatia hivyo mjukuu wangu!”

    Hanga akapiga magoti na kujibu, “Sawa bibi, siku zote nitakumbuka usia wako huu na kuuzingatia”

    Lakini kwa kuwa Hanga alipenda sana kufahamu kazi anayoifanya ‘Mwana Mteule’ huko Kaskazini Mashariki, na akatamani sana naye apate fursa ya kumsaidia mwenzake huyo katika kazi yake ngumu, alimuuliza bibi Ajuza jinsi ya kufika kule ‘Paa la Dunia’ Kaskazini Mashariki ya Sayari yao.

    Ingawa yule bibi alifahamu kuwa kijana yule hakuwa na vipaji wala uwezo kama alionao 'Mwana Mteule’, lakini alihisi kuwa alikuwa na hamu na nia ya kusaidia katika jukumu lile la aina yake.

    “Ingawa haitakuwa rahisi kufika sehemu ile nyeti, lakini utakapowasili Kaskazini Mashariki katika eneo la Paa la Dunia, utakuta limezingirwa na majabali marefu sana yenye rangi nyeusi”. Alimwambia kuwa vilevile eneo lile hujulikana kwa jina la ‘Bam i Dunya’.

    “Utafuata njia nyembamba iliyozungukwa na msitu mnene kwa pande zote, na msitu huo ni maarufu kwa jina la ‘Msitu wa Kindumbwe’ au kwa maana nyingine ‘msitu wa hatari’ Tahadhari sana kwani msitu huo unakaliwa na viumbe wengi hatari pamoja na mashetani na vibwengo.” Yule Ajuza alimweleza Hanga, na maelezo yake yale yalijaza hofu kubwa moyoni mwa yule kijana.

    “Sasa bibi, ni nini hasa ninachotakiwa kukitafuta huko?” Alidodosa Hanga.

    “Utakapofika mwisho wa njia nyembamba kama uchochoro wenye giza nene, utatokea katika mlango wa kuingilia kwenye pango lenye sanamu kubwa la shaba la kichwa cha simba, chenye mkufu mnene wa fedha shingoni na wenye vidani vitatu vya sanamu za fedha za kucha za simba. Kimoja kati ya vidani hivyo chenye kito cha rangi ya samawati ndani yake, ndicho chenye ujumbe ulioandikwa kwenye upande uliopinda wa sanamu ya ukucha huo”

    Hanga alimsikiliza kwa makini sana, na alipouliza ataelewa vipi ni kidani kipi chenye kito kinachohusika, alipewa maelekezo ya kutosha kabisa.

    “Usihofu lolote katika safari hii. Wewe nenda tu na maelekezo zaidi utayapata kadiri utakavyokuwa safarini, kwani huko kuna msaada hata usioutarajiwa!”

    Hanga alipowafahamisha wazazi wake kuwa alitaka kufanya safari kwenda Kaskazini Mashariki ya dunia kufuatilia jambo muhimu sana kuhusu usalama wa sayari yao na jamii katika sayari, Malkia, mama yake alipinga sana jambo hilo. “Hapana mwanangu, usithubutu hata kidogo kuchukua hatua hiyo ya hatari.’” alionya. huku akilia machozi. “Unafahamu fika kuwa wewe ni mwana pekee tuliyejaaliwa na Rahmani baada ya miaka mingi ya kusubiri. Sasa unataka kuondoka utokomee sijui wapi huko mwanangu? Ukipatwa na madhara huko ughaibuni tutakusaidia vipi sisi?” Lakini pamoja na mama yake kumsihi sana, Hanga alishikilia uamuzi wake, akisema; “Kama mimi ni mwana pekee kwenu ninyi wazazi wangu, hamuoni fahari kama nikichukua hatua ya kipekee kutekeleza jukumu kubwa la kuinusuru sayari yetu? Mbona nasikia kuwa tayari yuko mwenzangu mwenye umri kama mimi anayeshughulikia jambo hilo na ambaye naye ni mwana pekee wa wazazi wake? Tafadhali mama niruhusu nami nikasaidie jukumu hili muhimu!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kuwasihi wazazi wake wawili kwa muda mrefu hasa mama yake, hatimae baba yake Hanga Sultani Hazari, akamuomba sana mkewe amridhie kijana wao aweze kulifuatilia jukumu lile zito lenye umuhimu mkubwa na manufaa kwa wengi. “Atakapojitosa katika jambo hilo na kuchangia jitihada za kuinusuru sayari yetu, bila shaka yeye pamoja na sisi wazazi wake tutapata sifa lukuki kwa jamii ya mataifa mbalimbali!” Sultani yule alimsisitizia Malkia wake, basi,Malkia aliridhia uamuzi wa mwanae. Kwa muafaka ule, mama yake Hanga aliandaa chakula rasmi kwa ajili ya safari ya mwanawe, ambacho ni mikate saba ya unga wa mchele aliyomfungashia pamoja na guduria la maji ya kunywa njiani. Sultani naye akaandaa farasi mkubwa madhubuti ambaye angeweza kuhimili mwendo mrefu wa safari aliyoiazimia mwanawe!

    “Mungu awe nawe katika safari yako na akufanyie wepesi kwenye shughuli yako nzito mwanangu!” Mke wa Sultani Hazari alimwombea dua njema Hanga wakati akiagana naye, akimkumbatia huku machozi yakimtoka bila kizuizi. “Punguza wahaka katika nafsi yako na kila mara kumbuka kujiamini. Usikate tamaa kwa jambo lolote litakalotokea.” Sultani Hazari naye alimwambia mwanawe, akamshika mkono wake madhubuti wakati ule wa kuagana!



    HANGA KATIKA PAA LA DUNIA.

    Kwa muda wa siku saba Hanga alisafiri usiku na mchana, akavuka misitu, nyika na majangwa makubwa kupita kiasi. Alipita milimani na mabondeni hadi baada ya miezi kadhaa ya tabu na mnashaka, njiani akila matunda waliyokula ndege, alipofikamahali penye majabali manne meusi marefu sana, yaliyozingira uwanda wa milima yenye urefu wa zaidi ya mita elfu moja! Bondeni alikosimama chini ya yale majabali, Hanga alistaajabu sana kuona jinsi vilele vya yale majabali vilivyoonekana kama kwamba viligusa mbingu! Alistaajabu pia kuona jinsi msitu ulivyofunga katika lile eneo alilokuwepo, hali iliyomsababishia hofu kubwa kwake kutokana na giza nene lililosababishwa na miti mirefu kupita kiasi! Miti ile ilitoa majani kama mizizi katika matawi yake na mizizi kwenye mashina yake. Alishangaa kuona baadhi ya majani yaliyokuwa na upana wa ajabu mithili ya masikio ya tembo!

    “Sijapata kuona majani ya namna hii tangu nizaliwe! Yamefunika kama miavuli!” Aliwaza.

    Kwa kuwa alikua na njaa sana, aliketi chini ya kivuli cha majani yale mapana akawa anakula mkate wake wa unga wa mchele alioubakiza, na kunywa maji aliyofungashiwa na mama yake. Baada ya kupumzika kwa muda wa kutosha, Hanga akamwacha farasi wake mahali alipomfunga, na yeye akaanza kutafiti lile eneo ajuwe ni upande gani aelekee katika safari yake.

    Alipoangalia kwenye jabali katika upeo wa macho yake, yule kijana akaona maporomoko ya maji yaliyokua yakitokea mwambani na kuanguka chini kwa kishindo kikubwa, yakishindana na michuruziko ya maji yaliyokuwa yakitiririka chini kutoka kulekule mwambani. Alitulia kidogo akizidi kustaajabu aina ya msitu ule wa kipekee, na vyote vilivyohusika ndani yake!.Ghafla wakati akitafakari kuhusu yote aliyoyaona na jinsi atakavyoendelea na safari yake, akasikia mwaliko wa mawe yakigongana gongana, yaliyotoa mlio kama mtambo wa aina fulani na sekunde chache baadae, akasikia vishindo vya milipuko kama mabomu, na alipoinua kichwa chake kuangalia angani kuona kilichokua kikitokea, akaona moshi mnene na mweusi sana umezagaa! Muda si mrefu kijana yule akiwa na hofu kubwa, aliona cheche za moto zilizofuatiwa na mwanga mkali wa moto juu kabisa ya anga!

    Haraka sana Hanga aliruka na kukimbilia sehemu alikohisi kuwa kuna usalama, mbali na eneo lile hatari, kwenye jabali moja lililonekana katika upeo wa macho yake! Alijaribu kukimbilia nyuma ya mmoja kati ya milima iliyo uzingira uwanda mrefu, akivuka vijito, mawe na visiki vya miti pamoja na miti mirefu mno iliyoufanya ule msitu uwe gizani. Miti katika ule msitu ilijipanga katika safu mbili, katikati ikiacha njia nyembamba ambayo juu yake ilikutana na kuonekana kama paa la nyumba. Pembezoni mwa ile miti kwa kiasi cha kama kilometa mia mbili, ndiko yalikokuwepo yale majabali marefu mno, yaliyouzingira ule uwanda wa ‘Paa la Dunia’ alioutaja kibibi Ajuza “Huu ndio ‘Msitu wa Kindumbwe’ au ‘Msitu wa Hatari’ nilioambiwa na Ajuza!” aliwaza Hanga, akishindwa kuzuia kitetemeshi kwenye miguu yake iliyokuwa inapoteza nguvu kwa woga na wasiwasi aliokuwa nao!

    Alipokuwa akikimbia kwa hofu na wahaka, mguu wake mmoja ulikamatwa na mizizi ya miti, kwa hiyo akarushwa mbele zaidi, na huko akajikwaa vibaya sana katika kisiki. Puuuuuuh! Alipiga mweleka wa nguvu na kufikia kwenye mawe makali kama wembe yaliyomchubua chubua na kumpa machungu makali mno! Kabla hajatulia kujisikilizia machungu aliyoyapata, jambo jingine la kushitusha na kumtia hofu likatokea! Mahali alipoangukia Hanga akasikia sauti ya mtu! Mwili mzima ukazizima kwa woga! “Hivi ni mwana wa nani wewe unaenikwaa mimi kizee cha Mungu? Nimekufanya nini masikini?” Kwa mastaajabu na hofu ya kusikia sauti ya mwanadamu asiyeonekana, Hanga alijizowazowa na kuruka hatua moja ya kama mita mbili nzima, akisahau kabisa kuyasikilizia machungu aliyoyapata muda mfupi uliopita, akiangukia mwenye dimbwi la maji lililokuwa mbele yake! Alipogeuka kila upande kuangalia ni mtu gani aliyemsemesha maneno yale bila mafanikio, hofu yake alizidi, akabaki akitetemeka na miguu yake ikizidi kunyong’onyea! Wakati ule akakumbuka jinsi alivyomuudhi ‘Ajuza’ nyumbani kwao Hazina, hivyo akaamua kumuomba radhi mtu mwenye sauti ile iliyosikika kama ya mzee wa kike. “Nisamehe sana bibi yangu kwa kukukosea. Kwa bahati mbaya sikufahamu kama nilipojikwaa nilikukwaa na wewe! Nisamehe sana bibi!”

    Baada ya kumtaka radhi yule bibi ambaey wakati ule hakujua ni wapi alikokuwa, alinyamaza kimya kusikiliza kama bibi yule angejibu kitu. Pale alipokuwa, Hanga alizidi kupata wahaka kwa ukimya uliotawala msitu ule, baada ya ile milipuko ya awali iliyotokea kwenye majabali saa moja hivi iliyopita. Ni milio ya sauti za ndege tu iliyosikika! Wengine walilia “whu-whu-whuuuu! Whu-whu- whuuuu!” na wengine walilia “Tuu-tuuu tutututuuu! tuu-tuuu-tutututuuuu!” Mlio huu wa pili aliusikia kama vile wimbo wenye maneno aliyoyaelewa; ambayo ni “Kuukuuu mifupa mitupuuu! Kuukuuu mifupa mitupuuu!” Lakini wala haikuwa hivyo, ila alikwishaanza kubabaika na kuchanganyikiwa kichwani. Halafu ghafla katika ukimya ule, akaisikia tena ile sauti ya kizee.“ “Nimekusamehe mjukuu wangu na usihangaike kutafuta niliko kwani ukifunua hiki kisiki kilichokukwaa, utaona njia inayoshuka chini ya ardhi. Ingia na uje tuonane uso kwa uso mjukuu wangu!” Lo! Hanga alitoa macho kama nyanya chungu! Aingie aridhini? Akaonane na nani? Je kama huyo atakaemkuta huko atakuwa si mwanaadamu? Ingawa aliogopa sana kufuata maelekezo ya ile sauti, Hanga hakuwa na rai bali kufunua kile kisiki huku mikono ikitetemeka na moyo wake ukienda kasi mno!

    Alikivuta kisiki kile kwa nguvu zote na kisha hamadi! Kilipofunuka tu, aliona ngazi zikishuka chini kwenda sehemu iliyokuwa na giza nene kupita kiasi!. Alijishauri sana kwa kiasi cha dakika mbili au tatu hivi, ‘je ateremke na aende sehemu ile ya kutisha?’ Alisita sana kufanya vile. “Usihofu mjukuu wangu njoo tu, kwani huenda majibu mengi ya maswali yako yakajibiwa huku.” Kwa sauti ile yenye mikwaruzo, Hanga alihisi kuwa bila shaka bibi yule alikuwa ni kizee cha miaka mingi sana. Pamoja na wasiwasi aliokuwanao, Hanga aliamua kuteremka zile ngazi za mawe kuelekea kule kwenye giza la kutisha, kwani ni kweli alitaka sana kupata majibu ya maswali mengi aliyokuwa nayo.

    Kadiri Hanga alivyoshuka chini zaidi ya zile ngazi, ndivyo giza lilivyozidi kutanda. Alishuka taratibu sana na kwa uangalifu mkubwa, hatimae akafika mwisho wa ngazi. Kule akaisikia tena sauti ya yule bibi ikitokea gizani,“Haya mjukuu wangu, hebu keti kwenye kigoda uniambie ulichokifuata katika msitu huu wa kindumbwe, unaodhibitiwa na viumbe waovu wenye uhasama mkubwa na wanadamu.” Hanga akapapasa mahali palipokuwa na kigoda akaketi, wakati macho yake yakianza kulizowea giza lile nene la kule chini. Mbele yake aliona sehemu iliyokuwa na njia nyingi kama vichochoro, au njia zilizoelekea mapangoni. “Nakwenda kwenye uwanda wa ‘Paa la Dunia’ kutafuta majibu kuhusu athari zinazoikabili sayari yetu. Je bibi nitafikaje sehemu hiyo?” Yule kizee alimwangalia Hanga akitathmini kiwango cha ushujaa wake, akijua kuwa masikini kijana yule hakufahamu uzito wa jambo alilotaka kulifanya.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mjukuu wangu wee! Kabla ya yote kwanza lazima uelewe kuwa mnamo miaka mia moja iliyopita, nchi hii ya ‘Bam i Dunya’ ilikuwa ni nchi ya amani sana, iliyotawaliwa na Sultan Dhaman, ambaye kama jina lake linavyoashiria, alikuwa ni mwajibikaji katika majukumu kadhaa ya maendeleo ya nchi yake na raia wake. Lakini kutokana na hazina kubwa ya vito vya thamani vilivyopatikana katika mito, milima na makorongo ya uwanda wa Paa la Dunia, nchi hii ilihusudiwa na viumbe waovu waliotoka sayari nyingine, ambao baada ya kuifilisi wakaamua kuiteketeza kwa moto na kuwaathiri raia wake wote!” Hanga aliutafakari muda wa miaka mia moja iliyopita, akamwangalia kwa makini yule kizee aliyekuwa na umri wa zaidi ya miaka hiyo iliyotajwa. “Lo! Ndio maana ngozi yake inaning’inia shingoni kwake na mikono yake imekuwa mifupa mitupu!” Aliwaza Hanga, akimuona bibi yule kama kiunzi cha mifupa tu! Kama kwamba yule kizee alifahamu mawazo yaliyopita kichwani mwa Hanga, akasema; “Ndio mjukuu wangu, nimekuwa humu pangoni kwa miaka mingi sana! Nilipoona kuwa nimepoteza ndugu na jamaa zangu wote nikaamua kujificha chini ya kisiki, ambacho sikujua kama kiliyafunika mapango mengi ndani yake, yenye njia za kutokea kila upande wa nchi yetu ya Bam i Dunya!”

    Hanga hakuweza kukisia maisha yalivyokuwa chini kabisa ya ardhi kwa miaka mingi kama ile! Aliwaza kuhusu wale viumbe waovu waliotoka sayari nyingine na kwenda kuvuruga amani nchini kwa wenzao, eti kwa ajili ya tamaa ya utajiri wao, wakisababisha watu kama yule bibi kuishi aridhini kama panya. “Ni viumbe wa aina gani hasa bibi, waliokuja kuiteketeza nchi yenu?” Alidodosa Hanga, akaambiwa kuwa ni viumbe wasiokuwa wa kawaida wenye maumbile ya ajabu sana, kwani katika maumbile yao, kuanzia tumboni hadi kichwani wako kama joka kubwa sana, na kuanzia tumboni kushuka miguuni wako kama binaadamu lakini wana mikia mirefu sana! “Wengi wao ni waovu mno ingawa miongoni mwao wamo wachache waliokuwa wema sana.” Kwa maelezo yale Hanga alipata wasiwasi mkubwa. “Kama miongoni mwa viumbe hao wamo waliokua wema, je, wale waovu wakijitokeza na kujifanya kuwa ni wema, nitawatambua vipi?” Alimuuliza yule kizee, aliyemjibu kuwa atawatambua waovu kutokana na lugha yao wanayoongea isiyoeleweka na mwanadamu yeyote. “Mwanadamu pekee anayeelewa lugha hiyo ni Mwana Mteule, mwenye uwezo na vipaji vingi vya kipekee!” Kizee yule alisema

    Hanga alishituka kusikia habari ya Mwana Mteule ambaye kwa mara ya kwanza aliisikia kutoka kwa bibi ‘Ajuza’ nchini kwao Hazina. Hakufahamu jinsi ya kumpata kijana huyo wa ajabu. Alihisi kuwa yule bibi angeweza kumsaidia kwa jambo lile. “Nilipata msaada mkubwa kutoka kwa viumbe wema miongoni mwa viumbe waovu ninaowasema,” bibi kizee aliendelea kuelezea sifa za wale viumbe wema, akipuuzia mshangao wa Hanga mara baada ya kutajwa Mwana Mteule. “Viumbe wale wema ndio walionileta humu pangoni wakaninusuru na madhara makubwa ya wenzao waovu.” Kizee yule aliendelea na maelezo yake, akimfahamisha Hanga kuwa ni wale viumbe wema kati yao, waliomwambia kuwa wenzao waovu wameazimia kuzusha janga kubwa katika sayari yao ili isikalike, na kuwapa fundisho wanadamu wanaojiona kuwa ni bora kuliko wao!

     Kizee yule aliendelea na maelezo yake, akimfahamisha Hanga kuwa ni wale viumbe wema kati yao, waliomwambia kuwa wenzao waovu wameazimia kuzusha janga kubwa katika sayari yao ili isikalike, na kuwapa fundisho wanadamu wanaojiona kuwa ni bora kuliko wao!

    Pamoja na kupata hofu kubwa kuhusu hali ilivyo katika msitu wa kindumbwe, Hanga alitaka kujua jinsi atakavyofika kwenye pango la sanamu la kichwa cha Simba, kama alivyoelekezwa na ‘Ajuza’. Kabla hajapewa jibu, lilizuka kundi la bundi wengi kupita kiasi waliotoka mwenye vichochoro ambavyo ni njia za kwenda katika mapango mengi ya mle aridhini. Hanga alishtuka na moyo wake ukawa kama umesimama kwa nusu sekunde. kwa woga. “Mama wee!” Hanga alipiga ukulele, akajiangusha chini kuwakwepa wale bundi wasimkwaruze usoni! “Hao mjukuu wangu, ndio wapelelezi wa pepo mbaya wa ulimwengu wa kale, naye ni mfalme mkuu wa vidani vitatu katika sanamu la shaba la kichwa cha Simba, kilichokuwa na kile kidani chenye ujumbe wa madhara yanayoikabili sayari hii, na ambacho ndicho unachokitafuta! Pepo huyo mbaya wa ulimwengu wa kale ambaye ni jamii ya ‘wanamoto’, hapendelei ujumbe ule ujulikane na mtu yeyote atakayebatilisha azma ya uovu waliokusudiwa wanadamu, ambao ni Wanahewa!” Hanga aliduwaa tu, akabaki kinywa wazi akitafakari. “Nikikifuata kidani chenye huo ujumbe, nitakuwa nimejitosa kwenye vita na pepo huyo mbaya wa ulimwengu wa kale!” aliwaza.

    Wakati ule Hanga alipata hamu ya kurudi kwa baba yake na mama yake haraka iwezekanavyo, kabla hajapambana na viumbe wale wa ulimwengu wa giza! Alipowaza hivyo, akamsikia yule kizee akisema; ”Kwa kuwa umefika mpaka hapa, huna budi kuendelea na safari yako, kwani Mwana Mteule atahitaji sana msaada wako!” Ni kama vile bibi yule kwa mara nyingine alimsikia Hanga alivyowaza moyoni mwake! Kijana yule alimwangalia bibi kizee kwa macho ya woga mno! “Hivi huyu ni mwanaadamu kama mimi au….!” Hakuendelea na mawazo yake, kwani alihofu kuwa yule bibi alikuwa anayajuwa yote aliyoyawaza! Alipoinua kichwa kumwangalia, yule kizee naye akamwangalia akiwa na tabasamu kubwa usoni! Hanga aliogopa mno!



    SURA YA NANE

    Kibwe Nchini Baharia

    Akitokea kwa Mzee wa Busara; Mzee Kaka, Kibwe alisafiri kwa mtumbwi wake kwa masafa marefu sana. Njiani alikuwa akitafakari yote aliyoambiwa na mzee yule. Aliambiwa kuwa ingawa safari yake kule Azarbajan kaskazini mashariki ya mbali ya dunia itakuwa ngumu sana, lakini ni wajibu kwake kujitahidi kadiri ya uwezo wake kufika kule ambapo msaada wake unahitajika sana. “Maisha ya watu wa huko yamo hatarini kutokana na kuwepo kwa hewa hatari mno, yenye uwezo wa kuwakausha na kuwagandisha watu au hata kuzifanya ngozi zao zibambuke bambuke. Hewa hiyo inayoweza kuwagandisha watu na kuwageuza theluji ngumu isiyoyeyuka, huhatarisha maisha ya viumbe wote waishio Azarbajan.” Kibwe aliambiwa maneno hayo na Kakakuona wakati walipokuwa kwenye bonde la rutuba. Wakati huo, kijana yule hakuelewa jinsi atakavyotatua hilo tatizo la hewa ile ya hatari!

    “Sasa, nikifika huko nitafanya nini kuliondoa tatizo hilo, ambalo lipo hewani tu na wala haliko mahali litakapodhibitiwa na binadamu?” Kibwe alidadisi “Na je, kwanini hewa hiyo imekuwepo mahali hapo pekee katika dunia nzima?” Maswali hayo yalitupiwa kwa Mzee wa Busara bila kituo!

    “Kibweee! Kibweee mjukuu wangu! Hebu niulize swali mojamoja basi!” Mzee wa busara alimwambia kijana yule, huku akitabasamu kuona jinsi alivyokuwa na hamu ya kufahamu mambo mengi kwa wakati mmoja. Kisha mzee yule akafafanua kwa kusema. “Kuhusu la kufanya ili kuliondoa tatizo hilo la hewa hatari, ni kwamba lazima uende nchini Baharia, chini kabisa ya bahari ukapambane na jini aitwae ‘Makatta wa Makattani’ na kundi lake, wanaofanya uharibifu wa kuchafua hewa iliyoko kwenye anga hewa ya chini, katika tabaka la hewa nzuri ya Ozoni, kwani kitendo hicho husababisha tabaka la hewa hiyo muhimu kwa wanadamu, kupungua kwenye maeneo ya makazi yao!” Lakini hata baada ya ufafanuzi ule, Kibwe bado alikuwa gizani, na hakuelewa chochote kuhusu chanzo cha tatizo lenyewe alilolizungumzia Mzee wa Busara. “Kwanza, sielewi uhusiano uliopo kati ya watu kugeuzwa mawe ya theluji, kuchafuliwa kwa hewa na kupungua kwa tabaka la hewa …..hewa gani….? Hewa ya Ozo….?” Kibwe alidadisi. Alishindwa kukumbuka jina la ile hewa iliyotajwa na Mzee wa Busara. “Hewa ya Ozoni Kibwe! Inaelekea wewe si mpenzi wa sayansi kabisa!” Mzee wa Busara alimwambia kwa dhihaka kijana yule mteule.

    Kwa hiyo akimfafanulia Kibwe kuhusu uhusiano wa matukio yale yaliyomchanganya, mzee yule mwenye busara alimweleza kuwa baadhi ya wana sayansi waligundua kuwa tabaka la hewa ya Ozoni katika sehemu zenye baridi kali za kaskazini ya mbali ya dunia, hupungua mno mwaka hadi mwaka, na hivyo kusababisha uwazi au tundu kwenye tabaka hilo la Ozoni. Kitendo hicho, alisema, kilisababisha hali ya hewa kuwa ya baridi kali mno katika maeneo hayo, na kuifanya hewa hiyo kuzizima na wakati fulani kuwa nzito kupita kiasi. Mzee yule alisema kuwa hewa hiyo inapoelea na kusafiri kwenda kwenye makazi ya watu, husababisha giza nene na la kutisha, na inapofikia hatua hiyo, hewa hiyo hatari kwa viumbe huwa na uwezo mkubwa wa kuwagandisha viumbe hao na kuwageuza kuwa mawe ya theluji isiyoyeyuka, mara watakapopambana nayo!

    Ingawa Kibwe alijaribu kuelewa maelezo yale, lakini ilikuwa vigumu sana kuupata ukweli huo vilivyo, kwani kwanza kabisa, hakuwa hata na fununu kuhusu hewa hiyo ya Ozoni, kwa hiyo haikuwa rahisi kuelewa kuwa eti hewa ile asiyoijua inapochafuliwa kwa namna fulani, matukio yale yaliyotajwa hutokea. “Sasa mzee ‘Kaka’ ndio kusema hewa ya Ozoni ni hewa gani? Mbona mimi hufahamu kuwa hewa safi na nzuri kwa binadamu ni hewa ya Oksijeni?” Kijana kibwe alidodosa, akimkosoa Mzee wa Busara kuhusu hoja ya eti hewa ya Ozoni ni hewa safi inayotumiwa na wanaadamu, akimtaja Kakakuona kwa ufupisho wa jina lake, yaani mzee’ Kaka, alipoona kuwa wameanza kuzoweana “Ahaa! Kumbe nawe wafahamu kidogo mambo ya sayansi! Ni vizuri sana! Sasa basi kwa kuwa tayari unaelewa kuhusu hewa ya Oksijeni, lazima pia uelewe kuwa huko kwenye angahewa, liko tabaka jingine ambalo ni la hewa ya Ozoni, na hiyo ni aina fulani ya hewa ya Oksijeni, iliopo kwa kiasi kidogo sana, na ambayo nayo huwawezesha viumbe kuishi katika dunia hii!”

    Kibwe alipotaka kufahamu kwa nini Mzee wa Busara alisema kuwa ufumbuzi wa tatizo la hewa hatari kwa viumbe utapatikana baada ya kupambana na jini Makatta na wenzake, aliambiwa kuwa jinni lile na wenzake ndio wanaoweka vichafuzi vya hewa kwenye anga hewa ya chini. Mzee huyo wa busara alisema kuwa vichafuzi hivyo vya hewa vilivyomo ndani ya hewa ya Ozoni huko kwenye anga hewa ya chini, vinapopambana na mionzi ya jua, mapambano hayo ya kikemikali husababisha mabadiliko kwenye hewa ya Ozoni, na hivyo kuipa uwezo mkubwa wa kuichafua hewa safi. “Na wakati huohuo vichafuzi hivyo huko kwenye anga hewa ya chini vinapopambana na hiyo mionzi ya jua, sehemu ya hewa ya Oksijeni hugeuka na kuwa hewa ya Ozoni ambayo hupatikana kwenye anga hewa ya juu.” Mzee wa busara aliendelea na maelezo yake kwa Kibwe, akitofautisha baina ya hewa ya Ozoni iliyopo kwenye anga hewa ya juu, ambayo ni safi, na hewa ileile ya Ozoni iliyopo katika anga hewa ya chini, ambayo hugeuzwa kuwa hatarishi, akiongezea kwa kusema, “Kumbuka kuwa inapochafuliwa hewa ya Ozoni iliyoko kwenye anga hewa ya chini, huchangia mno katika uchafuzi wa ile hewa safi.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe aliambiwa kuwa mara tu baada ya kumshinda jini Makatta na wenzake, na kuwazuia wasiweke vichafuzi vya hewa kwenye anga hewa ya chini, atafanikiwa kuzuia mzizimo wa hewa nzito na hatarishi, na hivyo kuokoa maisha ya viumbe na mimea! “Lo! Haya mambo ya sayansi nayo, yanakwenda kwa mzunguko hadi kumfikisha mtu mahali pa kumchanganya kabisa ki mawazo!” Kibwe alimwambia Mzee wa Busara wakati ule, kwani kufikia pale, tayari alikwisha vurugikiwa kiwango chake cha uelewa!

    Lakini masikini, Kibwe hakufahamu kwamba miaka mia moja iliyopita alipozaliwa Mwana Mteule wa awali nchini Sabaa Kaskazini Mashariki ya mbali ya dunia, ilipowadia siku ambayo raia wa Sabaa, ‘Wanahewa’ waliandaa hafla maalum ya kumkabidhi kijana wao mteule kwa mwalimu wake ambaye angempa maelekezo ya kutumia vipaji vyake kwa nusura ya viumbe kwenye sayari yao, ghafla jamii ya falme za majini wa bahari, chini ya uongozi wa Mfalme wao Makatta wa Makattani, waliivamia nchi ya Sabaa na kuiteketeza kwa moto waliopumua kutoka vinywani mwao! Majini wale hawakusaza chochote katika utajiri wa nchi ya Sabaa, ikiwa ni pamoja na kumteketeza Mwana yule Mteule aliyetarajiwa kuipa matumaini jamii katika sayari yao!

    Kibwe hakufahamu kuhusu mambo yote hayo, na wala hakufahamishwa sababu kubwa iliyowaponza raia wa Sabaa waliofanyiwa unyonge ule, ambayo ni neema na mafanikio ya nchi yao pamoja na vipaji vyao aliali vya kipekee walivyojaaliwa, kwa faida ya viumbe wote. Wala kijana yule hakuwa na fununu kuhusu azimio la mfalme wa majini dhidi ya jamii yake! “Na kuanzia sasa, asinusurike Mwanahewa yeyote katika sayari hii! Lazima wote wateketezwe popote watakapokuwa, na kuwaondolea amani katika maeneo yao!” Mfalme Makatta aliwaambia raia wake nchini Baharia, mara baada ya kuiteketeza Sabaa. Vilevile, Kibwe hakufahamu kuwa miaka mia moja baada ya janga lile la majini waovu wa nchi ya Baharia, ndipo yeye alipozaliwa, akitarajiwa kushika nafasi ya mwenzake aliyeteketezwa! Kwa hiyo alipopewa maelezo yale na Mzee wa Busara kuhusu jukumu lake zito alilotarajiwa kulitekeleza, hakufahamu kuwa zaidi ya kuelewa aliyoambiwa, pia alikuwa na vipaji vya kipekee vya kumsaidia kufanikisha yote aliyotarajiwa kuyafanya!

    Akiazimia kufuatilia jukumu lile la mapambano na viumbe wachafuzi wa hewa safi kwa makusudi na walio hatarisha maisha ya watu, Kibwe aliendelea na safari yake kwa njia ya bahari, akielekea kaskazini ya mbali ya dunia. Alikuwa imara kabisa katika safari ile ndefu na ngumu, mara baada ya kuelewa barabara tatizo lililokuwa likiwakabili raia wa Azarbajan kwa Mfalme Kashkash. Kwa hiyo alijiandaa kulikomesha kabisa tatizo lile!

    Katika maelekezo yake, Mzee wa Busara alimwambia Kibwe kuwa jini Makatta wa Makattani na wenzake, huishi kwenye mji ulioko chini kabisa ya bahari. Alikumbuka maelezo yake, wakati akimwambia, “Huko nchini Baharia , chini kabisa ya bahari, utakuta milima mikubwa kabisa na mirefu, minne kati yake ni myeusi kabisa. Yapo pia mabonde na ardhi tambarare, pamoja na makorongo yatokanayo na mito mikubwa inayoingiza maji baharini. Makazi ya jini Makatta na wenzake ni kwenye makasri ya thamani katika baadhi ya milima hiyo iliyo tambarare, na kwenye mabonde na makorongo hayo.”

    Kibwe alikumbuka maneno ya Mzee wa Busara kuwa majini hao hufanya kazi ya kuzalisha vichafuzi vya hewa, wakitumia mitungi mikubwa na masufuria makubwa sana ya shaba, kuchemshia madawa yao yanayotoa vichafuzi hivyo kwa njia ya moshi mchafu kupitia mabomba makubwa! “Wanaoutoa moshi huo nje ya bahari ni majini wa upepo, ambao huuvumisha upepo kwa kuupulizia nje ya bahari, wakiutumia kwa kuyazungusha maji ya bahari , na kusababisha kutokea mawimbi yanayokwenda sanjari na bahari hiyo.” Kibwe alitafakari maelezo hayo ya Mzee Kaka, aliyeongezea maelezo yake kwa kusema kuwa wakati fulani yale mawimbi huinuliwa kwa urefu wa takriban mita mia mbili au zaidi, na hivyo hatimae kuweza kuusindikiza moshi huo kwenye angahewa ya chini, kwa kupitia kwenye mabomba maalum yaliyoko juu kabisa kwenye minara pacha mitatu, katika uwanda wa ‘Paa la Dunia!’ “Baada ya hapo, Majini hao wa upepo huupuliza tena upepo ule unaosukuma maji mithili ya mawimbi, na kuyarudisha mawimbi hayo chini kabisa ya bahari, ili kukusanya tena ile hewa ya vichafuzi inayozalishwa na majini wa chini ya bahari, na kisha kuipandisha tena juu ya bahari kwa njia ya mawimbi hayo, ili kuendelea na zoezi la kuifikisha hewa hiyo ya vichafuzi huko kwenye anga hewa ya chini.” Mzee wa Busara alimfafanulia Kibwe, akimsisitizia kutumia upanga wake wa radi kutatua matatizo mengine mengi yatakayojitokeza bila kutarajia .

    Kibwe alizidi kutafakari maelezo ya awali ya Mzee wa Busara, ‘kwamba mapambano ya kikemikali baina ya mionzi ya jua, husababisha kupatikana kwa kiasi kidogo cha hewa nzuri ya Ozoni kwenye anga hewa ya juu ya dunia, na kupatikana kwa hewa chafu na hatarishi kwenye anga hewa ya chini’. Kibwe alimaizi kuwa kwa hakika majini wale walikuwa ni waovu mno kiasi cha kudiriki kuyafanya yote hayo, ili mradi tu, kuhatarisha maisha ya watu!

    “Ama kweli, hasidi hana sababu!” Aliwaza Kibwe huku akiendelea kusukuma makasia ya ngalawa yake kwa nguvu zote, wakati akikumbuka moja katika methali za mama yake alizopenda kuzitumia.

    Kijana yule aliendelea na safari yake hadi alipoatokea kwenye kisiwa chenye msitu mnene sana wenye miti mirefu iliyokuwa na matawi marefu mno, yaliyoning’inia mithili ya mizizi minene, na mashina yake nayo yalishikiliwa na mizizi yenye unene kama yale matawi ya kipekee, iliyojitokeza nje ya aridhi, na kufungana kama utanda wa buibui! Miti mingine iliyokuwepo katika msitu ule wa ajabu ilikuwa na majani mapana kama masikio ya tembo, na mingine ilikuwa na majani ya rangirangi yaliyofanana na myavuli kwa ukubwa na maumbile. Kibwe aliufunga mtumbwi wake kwenye kisiki, , akaanza kutembea kwa miguu, ingawa alipata shida sana kutokana na matawi na mizizi katika msitu ule kujifunga juu na chini yake kama utando wa buibui! Kijana yule alilazimika kupenya kama panya, akitumia upanga wake kuikatakata ile mizizi ili kurahisisha safari yake iliyokuwa ya utata. Msitu wote ulikuwa kimya, isipokuwa kwa sauti za ndege wa aina mbalimbali, ambao baadhi yao walisikika kama vile walitamka maneno aliyoyaelewa Kibwe

    “Kuukuuu mifupa mituupuuu! Kuukuuu mifupa mituupuuu!” Kibwe alishangaa sana!

    “Kama videge vinaona kuku ni mifupa mitupu, venyewe ndio vina nyama?” Alijiuliza, huku akitabasamu.

    Kibwe hakufahamu kuwa katika msitu ule alikuwepo kijana mwenzake Hanga, ambaye kama yeye, naye alisikia sauti za ndege walioimba kwa kusema maneno aliyoyasikia yeye, yaani, “kuku mifupa mitupu!”. Kwa sababu hiyo, huenda Kibwe na Hanga wote walikuwa katika ‘Msitu wa Kindumbwe’ bila kuelewa! Kibwe pia alisikia milio ya wadudu kama Nyenze, mvumo wa bahari na upepo uliosikika ukivuma kwa mbali kidogo “Ili kufika nchini Baharia, chini kabisa ya bahari, kwanza utavuka kisiwa chenye msitu wa miti ya mizizi” Mzee Kaka alimwambia Kibwe wakati akijiandaa na safari ile, isipokuwa hakumtajia jina la msitu wenyewe,.isipokuwa mwenzake Hanga aliambiwa na kizee aridhini kuwa ni ‘Msitu wa Kindumbwe!

    Alitembea kutwa nzima hadi alipotokea kwenye bonde lililozungukwa kila upande na majabali marefu mno. Alipoangalia huku na kule kuona jinsi atakavyoendelea na safari yake, hakuona mahali pa kutokea! Alihofu sana alipojikuta katika ngome ya majabali kama gereza! Kwakuwa miti ya msitu ule ilikuwa na mizizi iliyoning’inia mithili ya kamba nene imara, Kibwe aliamua kujishikiza kwenye mizizi, ambayo kwa bahati ilibebelea malundo ya udongo wa mfinyanzi ulioganda madhubuti, alioutumia kama vikanyagio au ngazi. Alining’inia kwenye mzizi kama aliyetaka kubembea, halafu akainua miguu yake juu kichwa chake kikiwa chini, akiitumia miguu yake kulibana lundo moja la udongo lililokuwa juu yake, na kisha moja baada ya jingine aliyatumia malundo yale kwa kupanda juu zaidi ya miti, akilenga kufika katika kilele cha moja ya majabali. Taratibu na kwa makini, alipanda kwa mbinu ile ya kushikilia matawi ya mizizi. Mara kwa mara alipapasa kiunoni kuona kama ule upanga wake muhimu katika safari yake bado alikuwa nao. Kwa hekima kubwa na nguvu zake zote Kibwe aliendelea kupanda juu kabisa ya jabali lenye urefu usiokadiriwa! Alipofika kileleni alianza kushuka kwa upande wa pili wa jabali lile, akitarajia kushukia korongoni upande ilikokuwa bahari, ili aweze kufika chini kabisa ya kina cha bahari, kama alivyoelekezwa na Mzee Kaka.

    “Utakapokuta mwanguko au mteremko wa ardhi, ufuate na ushuke nao hadi ufike chini kabisa ya bahari.” Kakakuona alimwambia Kibwe walipokuwa katika bonde la rutuba. Kabla hajaanza kushuka chini ya lile jabali, alishtuka kusikia sauti za watu wengi kwa pamoja, wakiongea na kukubaliana kuhusu jambo ambalo Kibwe alihisi lilikuwa la maana sana kwao. Haraka alijibanza nyuma ya lundo la udongo katika tawi kama mzizi alilolishikilia, akijiandaa kushuka. Alisita kidogo na taratibu akachungulia kule kulikotokea zile sauti! Lo! Alipowaona waliohusika Kibwe alipata hofu kupita kiasi….! Moyo wake ulichupa, miguu yake ikapooza na kinywa chake kikawa wazi kwa mshangao! Aliowaona kwa hakika hawakuwa binadamu wa kawaida, bali walikuwa ni viumbe ambao kuanzia kifuani hadi kichwani walikuwa na maumbile ya nyoka, na kuanzia tumboni kushuka chini walikuwa na maumbile ya binadamu lakini wakiwa na mikia mirefu mno! Hakufahamu kuwa katika msitu uleule, kijana mwenzake ‘Hanga’ naye angeshuhudia maajabu yale siku chache baada yake!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe aliogopa sana wakati viumbe wale wa ajabu walipogeuza sura zao upande aliojificha! Hakuamini macho yake alipowaangalia vema viumbe wale na kuona kuwa macho yao yalikuwa pembezoni mwa sura zao, na walipojifuta jasho kijana yule alishangaa zaidi alipoona mikono yao imefanana na mikono ya vyura! Alipata hofu, wahaka na taharuki kubwa! “Ni jambo la kutisha na kushangaza mno!.” Aliwaza Kibwe, misuli ya mwili mzima ikitetemeka! Alipozidi kuwachunguza zaidi viumbe wale, aliona kuwa walikuwa na midomo mithili ya midomo ya vyura! Aaa--hapana! Labda tuseme sura zao zilikuwa ni za vyura kabisa, kuanzia kwenye vipaji vya nyuso zao hadi kushuka kwenye shingo zao! Kuanzia shingoni kwenda kifuani walikuwa na umbo la nyoka, na kushuka miguuni walikuwa ni binadamu wembamba mno, wenye mikia mirefu sana!

    “Sijapata kuona viumbe wa aina hii katika muda wote nilioishi hadi leo, na wala sijasikia habari zao zikizungumzwa na yeyote!” Aliwaza kijana yule, akiwa amezidiwa na hofu na mshangao mkubwa! “Bila shaka hawa ndio majini nilioambiwa na Mzee Kaka” Alitafakari, na wakati uleule alipata jibu lake, kwani viumbe wale walikuwa wakipumua mienge ya moto! Alipohakikisha hilo ingawa alikuwa na hofu kubwa, Kibwe aliazimia kuwafuata viumbe wale popote walikokuwa wakienda, kwani aliamini kabisa kwamba wangemfikisha kwenye maabara yao ya maandalizi ya hewa ya uchafuzi wa angahewa. Kwa wakati ule alitulia tuli ili kunusuru maisha yake, huku akiyapelemba yale majitu au wale viumbe, kwa mbali!

    Viumbe wale walipokaribia mahali alipokuwa Kibwe juu kabisa ya jabali, na wao wakiwa chini bondeni, yalisikika maneno yasiyoeleweka kabisa na binadamu yeyote! Kibwe alizidi kujibanza nyuma ya lundo la udongo uliogandana na matawi ya mizizi, juu ya jabali. Chini ya majabali yale majinni yalisimama kwa mduara mpana, na kisha mmoja wao aliyeonekana kuwa kiongozi wa msafara na aliyevalia taji la matumbawe ya rangirangi za kuvutia, alianza kuwanyamazisha wenzake waliokuwa wakielezana mambo yao kwa lugha yao, wakibishana kwa ukali kabisa.

    “Nimaja! Nimaja! Myaki tewo! Myakitewo!” Mara moja zile kelele na zogo lililokuwa likisikika, vikaanza kupungua. Wote waliponyamaza kimya, ndipo kiongozi wao alipoanza kuwaeleza kwa maneno yaleyale yasiyoeleweka kwa Kibwe, akiwasihi wahakikishe kuwa wanatekeleza malengo yao waliyoyaweka miaka mia moja iliyopita. “Nguzangudu! Mazila shelizatu shimo ngimwi aw wadama okatao ndakwe kanifu wahengaa…….” Kiongozi huyo wa viumbe wale wa ajabu alisema maneno hayo ya ajabu yaliyokuwa na ujumbe mzito ambao kwa wakati ule, Kibwe hakuuelewa! Walimalizia hotuba yao kwa kauli mbiu iliyoanzishwa na kiongozi wao na kuitikiwa na wengine wote kwa furaha.

    “Fovi awk wahenawa!”

    “Fovi awk wahenawa!”

    Baada ya kusema hivyo, yale majini yote kwa pamoja yalitoa pumzi ya moto, wakaunguza sehemu kubwa kabisa ya msitu! Pale alipojificha huku akitetemeka, Kibwe alitafakari sana kuhusu maneno ya viumbe wale, na kitendo walichokifanya muda mfupi uliopita. “Sijui walikua wakiambiana nini waovu wale! Bila shaka walipoyasema waliyoyasema, walikua wakipanga mkakati wa uharibifu wa mazingira kama huu uliotokea.” Aliwaza kijana yule bila kufahamu kuwa kule mbele aendako ataipata maana nzima ya yale maneno waliyoyasema wale viumbe, ili kumrahisishia utekelezaji mzuri wa malengo yake!

    Alipowaangalia viumbe wale chini ya jabali na kuwaona wakianza kuondoka na kuendelea na safari yao, taratibu Kibwe naye alianza kushuka kwa kutumia moja katika yale matawi mithili ya mizizi. Alipofika chini katika upande wa pili wa jabali, alisubiri kwa muda fulani ili yale majini yafike mbali, halafu akawafuata taratibu, akitarajia kuwa walikuwa wakienda kwenye maabara yao. Nia yake ilikuwa ni kufika kwenye maabara yao na kuzuia mchakato wao mzima wa uzalishaji wa moshi uletao madhara makubwa duniani. Alipokuwa akiwafuata, mara kwa mara walikuwa wakigeuka nyuma kama kwamba walihisi kuwa walikuwa wakifuatwa na kitu au mtu. Kibwe aliogopa sana, na alijificha vichakani akihofu kuonekana na kutiwa nguvuni na mazabania yale. Baada ya mwendo wa saa nzima katika msitu wa giza nene uliojifunga kwa matawi na mizizi, wakati majini wakienda kwa hatua kubwakubwa kutokana na urefu wao, na Kibwe naye akiwafuata nyumanyuma, mara akitembea na mara akikimbia, walitokea katika ufukwe wa bahari walikokuta mteremko wa ardhi, ambako yale majini yalishuka na kuanza kuzama chini kabisa ya bahari Kibwe alitulia tuli mahali alipojificha katikati ya matawi na mizizi mirefu akiwaangalia. “Bila shaka hapa ndipo pale mahali Mzee wa Busara aliponielekeza jinsi ya kushuka baharini na kuingia chini ya bahari, ili kufika nchi ya majini ya Baharia.” Aliwaza Kibwe, akitafakari mazungumzo kati yake na mzee yule mwenye busaranyingi.

    “Utakapofika mwambao wa ufukwe, utakuta mwanguko au mteremko wa ardhi. Shuka kwa njia ya mteremko huo hadi ufike chini kabisa ya bahari.” Wakati wa maagizo hayo ya Mzee wa Busara, Kibwe alipata wasiwasi kuhusu jinsi atakavyopumua atakapokuwa huko chini ya bahari. “Nitawezaje kuwepo kwenye maji kwa muda mrefu wa utekelezaji wa shughuli yangu? Je,nitaweza kupumua kama samaki?” Mzee wa busara alimcheka Kibwe kwa kiwango chake kidogo cha uelewa wa mambo mengi ya dunia. “Nimesema kuwa huko chini kuna mji wa majini, kwa hiyo wewe nenda tu, na utakuta mji kama miji mingine uijuwayo. Hakuna maji huko!”

    Kibwe aliambiwa kuwa akifika kule kwenye mji wa majini chini kabisa ya bahari, aende kwenye maabara yao, ambako viumbe wale huendesha shughuli zao za kuchemsha vichafuzi vya hewa. Kibwe hakujua atafikaje kwenye maabara hiyo, ndio maana alipobahatika kuyaona yale majini, akaamua kuyafuata.Na ili kukamilisha kazi yake ya kuyateketeza majini yale maovu, Kibwe alipewa fuko zima la uvumba, ubani na udi, akaambiwa kuwa anachotakiwa kufanya ni kumwaga mchanganyiko ule kwenye moto mara atakapofika katika maabara hiyo ya kipekee ya majini, ili kuifukiza hewa yote katika sehemu ile. “Hakikisha kuwa unatupia mchanganyiko huu kwenye moto, kwa kuwa moshi wake wenye harufu kali, utawachanganya akili hao majini. “ Mzee Kaka alifafanua, na vilevile akamwambia Kibwe kuwa asishangae kama kitatokea kimbunga cha chini ya bahari au ‘tsunami’ na kuteketeza eneo hilo na vifaa vyote vya uharibifu wa hewa.

    Kibwe alisubiri kwa muda wa kutosha tangu yale majini yalipozama baharini, akichelea kupambana nayo kabla hajajiandaa. Mwishowe naye alianza safari yake ya kushuka chini ya bahari kwenye ule mji wa majini nchini Baharia. Kama alivyoambiwa na Mzee Kaka, chini kabisa ya bahari Kibwe hakukuta maji, bali alikutana na msitu mwingine wa ajabu sana, uliopambwa na miti ya matumbawe ya rangi rangi, mingine mirefu sana mingine ya kawaida iliyopendezesha mandhari kwa rangi zake za kuvutia kama manjano, machungwa, samawati, damu ya mzee na nyinginezo. Mara kwa mara Kibwe alipishana na viumbe wengine wa ajabu ambao kutoka tumboni hadi kichwani walikuwa ni binadamu, na kutoka tumboni kuja miguuni walikuwa samaki! Walimvutia mno Kibwe, aliyewapungia mkono, lakini walimshangaza zaidi walipomsalimia. “Habari yako Kibwe! Karibu kwenye jiji letu kuu 1nchini Baharia!” Ha! Kibwe alibutwaika mno! “Habari nzuri sana! Nashukuru kunikaribisha. Siku njema.” Aliwaambia, huku akiwa na maswali chungu nzima ya kujiuliza. “Haa! Kumbe nguva ni viumbe wa kweli! Nilidhani wapo katika hadithi tu. Na tena wanaongea kama sisi!” Aliwaza kwa mshangao mkubwa, ingawa hakufahamu kuwa aliweza kuwaona na kusalimiana nao kwa sababu yeye mwenyewe hakuwa mwana wa kawaida!

     Kijana yule shujaa alijizamisha chini zaidi ya bahari hadi alipofika mahali ambapo maji yalikomea juu ya kichwa chake.Baada ya kuzama, kwenye upeo wa macho yake akaona ngome ndefu ya shaba iliyozunguka kwa kilometa nyingi mno! Alihisi kuwa bila shaka ile ilikuwa ni maabara ya majini aliyotarajia kuiteketeza. Ingawa alikuwa na hofu ya kupambana na wale viumbe wanaoweza kujigeuza katika maumbile yoyote wayatakayo, lakini aliamua kwenda moja kwa moja hadi mahali pale. Njia aliyopitia kufika huko ilinakshiwa kwa tumbawe za aina aina na marumaru za thamani kubwa. Mbele zaidi aliona makasri makubwa ya kifalme yaliyojengwa kwa marumaru za rangi mbalimbali. Mengine kati ya makasri hayo yalijengwa kwa mawe na majabali yaliyojaa chini ya bahari. Kule alikuta mabonde yenye ukubwa uliotofautiana, yaliyotokana na miamba iliyoonekana kama rafu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kwenda mbele zaidi, kabla ya kufika kwenye maabara iliyozungushiwa ngome ya shaba iliyong’ara mno kwa mwanga wa jua, alikuta sehemu ambayo miamba imekusanya takataka, matope na mchanga. Ajabu ni kwamba mchanga ule ulichanganyika na vumbi la dhahabu! Alipozidi kusonga mbele, aliona kuwa mchanga wa kawaida ulizidi kupungua na badala yake, kiwango cha vumbi la dhahabu kiliongezeka, kuelekea bondeni. Kadiri alivyoikaribia ile maabara, ndivyo alivyoshuhudia utajiri mwingi usioelezeka, wa johari kama vile lulu na vito vingi vya thamani pamoja na dhahabu na fedha, vyote vikiwa vimelundikana kandokando ya njia. Kibwe alibutwaika, akistaajabu kuona yote yale, ambayo ni mageni kabisa katika maisha yake.

    “Sijui nimo ndotoni….au ninayoyaona ni kweli nayaona”! Aliwaza, na akimaizi kuwa safari yake yote ilikuwa ni ya maajabu makubwa.

    Alipofika ngomeni alikuta lango kuu limefungwa.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog