Search This Blog

KIBWE KATIKA SAFARI YA AJABU - 1

 







    IMEANDIKWA NA : SANGO KIPOZI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Kibwe Katika Safari Ya Ajabu

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    MWANA MTEULE

    Ukimya wa kutisha ulitawala eneo zima, na Kibwe akahisi woga wa ajabu ukimtambaa mwilini na kuzitawala fahamu zake zote. Alikuwa na kila sababu ya kutawaliwa na woga, kwani pamoja na kwamba hapakuwa na hata mtu mmoja pamoja naye, lakini vilevile hakukusikika kwenye msitu ule mlio hata wa ndege wala wadudu kama ilivyo kawaida.

    Kimya kizito!

    Mara, sauti za ajabu zinasikika angani. Bundi na sauti za ndege wengine zisizopendeza masikioni zilivuma ghafla na kuzidi kumuongezea hofu Kibwe. Alipoangaza huku na kule, alishangaa sana kuona majabali na milima iliyotanda kila upande, bila kuwepo dalili ya mimea wala miti! Ardhi ya eneo lile ilikuwa imekauka na katika sehemu nyingi ilikuwa imepasukapasuka. Kijana yule aliegemea mwamba ulioelekea kwenye pango moja kubwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hivi naota…au ni kweli niko kwenye sehemu hii isiyoeleweka?

    Aliwaza huku akitetemeka kama mpapai uliopigwa na kibunga.

    Licha ya zile sauti za bundi na zisizopendeza masikioni za ndege wa ajabu, kwa muda wote wa saa kadhaa alizokuwa pale mahali, hakusikia sauti nyingine yoyote, hata ya upepo ukivuma, isipokuwa pumzi yake mwenyewe tu!

    “Nimekusubiri kwa miaka mingi mno kijana, sikudhani kama siku hii ingefika.” Kibwe alipogeuka na kuangalia pangoni, alihisi ganzi kwenye miguu yake kwa hofu! Moyo wake uliacha kudunda kwa sekunde chache, akatoa macho pima kutokana na kile alichokiona!

    Aka! Ni kitu gani hiki mbele yangu tena?

    Alijiuliza, huku fahamu zake zikimshauri atimua mbio kuelekea popote pale, alimuradi tu pawe mbali kabisa na mahala pale! Kwa sekunde kadhaa, kile alichokuwa akikiona kilimfanya ashindwe kabisa hata huko kukimbia kwenyewe. Mbele ya macho yake, kilisimama kitu kisichoeleweka, kama kijitu kidogo sana mithili ya mbilikimo, lakini udogo wake ulizidi ule wa mbilikimo! Kilikuwa ni kijitu chenye uso ulioshupaa kama mzee wa miaka zaidi ya tisini. Uso ule ulipambwa kwa msitu wa ndevu nyingi za mvi tupu zilizofika hadi magotini kwake! Kibwe alianza kukimbia lakini ghafla, pale mahali alipokanyaga wakati akiruka kwa hofu, palianza kutitia na ardhi ikajiachia na kuporomoka pamoja naye! Wakati akiporomoka, alipoangalia chini kabisa, aliona uwazi usio na mwisho! Kwa hofu kubwa mno, aliachia ukelele wa mfululizo, akihangaika kutafuta sehemu ya kukamata. “Wooooooooooooooo…! Wooooooooooooa…….!”

    Kwa wepesi wa ajabu, yule mtu mdogo alinyoosha juu mkono wake na kuwahi kukamata mzizi uliokuwa ukining’inia juu yake. Alikunja miguu yake akijiandaa kubembea kwa kutumia mzizi ule, akiazimia kujirusha kuelekea katika sehemu iliyokuwa imara kidogo. Alipofanya vile, alibembea huku akimchukua Kibwe pamoja naye kwa mkono wake wa pili, na wote wawili wakabembezwa na mzizi ule na kutupwa kwa mweleka mzito kiasi cha mita kumi hivi kutoka pale walipokuwa, wakiwa salama salimini ndani ya lile pango kubwa, lakini Kibwe akiwa ameshituka sana!

    “Heeeeh! Ilikuwa kidogo niporomoke shimoni na kupotelea sijui wapi tu kule!” Kibwe aliropoka, akimshukuru Mungu kwa nusura aliyoipata. Alimtazama yule mtu mdogo wa ajabu, na kushangaa kuona jinsi alivyomnyakua kwa wepesi kama mtu aliyechukua unyoya. Alitaka sana kujua alikuwa ni kiumbe wa aina gani yule!

    Wakati wote ule wa pata shika, upepo mkali ulioambatana na dhoruba ulikuwa ukivuma, huku majabali yaliyotanda eneo lile yakiyumba na kutingishika vibaya. Ilikuwa ni hali ya kuogopesha mno kwa Kibwe. Kijana yule na mwenzake yule mwenye umbile dogo kama tumbiri, waliketi kwa muda wa kutosha pale mahali walipoangukia. Kile kijitu kilinyamaza kimya, kumpa nafasi Kibwe apumue kidogo, na Kibwe naye akanyamaza kimya, akijaribu kuelewa yule alikuwa ni nani, na ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea pale, na kwa nini?

    Baada ya nusu saa hivi, muda ambao kwa Kibwe ulionekana kama siku nzima, ile hekaheka ya maporomoko ilitoweka, na polepole upepo na dhoruba vikapunguza kasi yake. Alipoangalia nje ya pango lile kubwa, kwenye upeo wa macho yake, akaona maajabu mengine. Katikati ya majabali makubwa na milima mirefu, aliona maumbile ya watu wakubwa mno! Aliinuka na kujaribu kutoka nje kidogo ya lile pango lililotitia bila kizuizi muda mchache uliopita, akitaka kuhakikisha kuwa ni kweli aliona kile alichokiona? Ghafla alishikwa mkono na yule mtu mdogo aliyemrudisha nyuma kwa nguvu.

    “Chunga hatua zako kijana! Eneo lote hili linakabiliwa na uwazi mkubwa katika kila sehemu, na kama ulivyoona, inaweza kutokea hatari kubwa upande wetu. Kwa sababu ya kuzuia hatari hiyo, ndiyo maana nikakuambia kuwa nimekusubiri wewe Kibwe kwa miaka mia moja!”

    Khah!

    “Imekuwaje ukafahamu jina langu? Kwani wewe ni nani?”

    “Jina langu ni Bunga, na ni kiumbe pekee niliyebaki katika sehemu hii…”

    “Kiumbe pekee uliyebaki…??”

    “Naam. Nilibaki mimi na raia wachache tu, tulionusurika katika nchi ya Sabaa miaka mia moja iliyopita.” Kile kijitu kilichojinadi kwa jina la Bunga kilimjibu, na Kibwe akazidi kutoelewa.

    “Mi..mi…mi sikuelewi we babau!” Alimwambia.

    “Huwezi kuelewa mpaka ueleweshwe Kibwe. Hebu kaa chini unisikilize basi…” Bunga alimjibu, na KIbwe hakuwa na namna ya kufanya vinginevyo.

    Ndipo kibabu/kidudu Bunga alipomsimulia za madhila makubwa, akimuelezea habari za nchi ya Sabaa ambayo ilikuwa ni moja katika nchi za falme za Kaskazini Mashariki ya dunia zilizotawaliwa na wanawake waliorithi falme za baba zao. Alimwambia kuwa miaka mingi nyuma, ikiwa chini utawala wa Malkia Balika, nchi ya Sabaa na jamii yake ya ‘Wanahewa’ iliteketezwa vibaya sana na jamii yenye asili ya ‘Wanamoto’ kutoka katika falme za majini, kwa kutumia mioto iliyotokana na pumzi zao.

    “Kutokana na mashambulizi yao, hakikubaki chochote katika utajiri mkubwa wa nchi ya Sabaa!” Alisema, akiongezea kuwa siku hiyo ilikuwa ni siku ambayo ‘Wanahewa’ waliandaa hafla maalum ya kumtoa kijana wao mteule na kumkabidhi kwa mwalimu maalum ambaye ndiye angemuelekeza kijana huyo jinsi ya kutumia vipaji vyake vya kipekee kwa faida ya jamii ya sayari yao.

    Bunga alikumbuka kuwa katika baraza rasmi la Malkia Balika wa Sabaa miaka hiyo mia moja iliyopita, ulifanyika utabiri kuhusu Mwana Mteule aliyezaliwa nchini mwao. “ Atakapofikia umri wa miaka kumi na nne, kijana huyu mwenye vipaji maalum, atakabidhiwa kwa mwalimu ambaye atamwelekeza jinsi ya kuvitumia vipaji hivyo kwa faida ya jamii ya sayari hii, kwani yeye ndiye mwokozi wa jamii zote duniani...!” Mzee yule wa ajabu alimwambia Kibwe kuwa tamko lile lilitolewa na wazee waheshimiwa, katika lile baraza maalum la Malkia Balika.

    “Walikuwa katika maandalizi ya kutafuta mustakabala mwema wa taifa lao.” Alisema.

    “Ama! Sasa ikawaje tena?” Kibwe aliuliza, akionekana kuvutiwa na maelezo yale.

    Bunga alimfafanulia kuwa kitu kilichowaponza ‘Wanahewa’ miaka mia moja iliyopita ilikuwa ni neema kubwa na mafanikio yao ya ajabu yaliyotokana na rasilimali yao ya kipekee ya vito na madini, na pia vipaji vyao adimu walivyojaaliwa.

    “Katika miaka hiyo mia moja iliyopita, nchini Sabaa alizaliwa mwana wa kipekee mwenye vipaji vingi vya ajabu na uwezo mkubwa wa kimazingaombwe. Kuwepo kwake katika sayari ile ilikuwa ni kwa ajili ya kuinusuru jamii yake katika sayari yake pamoja na kuipa matumaini. Utabiri wa wanataaluma ulionesha kuwa kijana yule angeelekezwa mbinu za kumwezesha kuvitumia vipaji vyake kwa ajili ya kuinusuru jamii yake pindi atakapofikisha umri wa miaka kumi na nne.

    “Lakini looh! Hili halikutimia, kwani chuki na inda za jamii ya majini waovu dhidi ya jamii yake vilitimia, na kijana yule akateketezwa na moto katika uvamizi ule wa wanamoto’, uvamizi uliokusudiwa kumzuia asitekeleze kazi muhimu iliyomleta katika sayari ya dunia. Kazi ya kuinusuru jamii ya Sabaa!”

    “Heh! Kwa nini ilikuwa hivyo sasa?” Kibwe aliuliza kwa hamaniko.

    Kidudu Bunga alipiga kimya kwa muda, kisha akamweleza Kibwe chimbuko la uhasama ulioiangukia nchi yake ya Sabaa. Nchi iliyoneemeka. Nchi yenye hewa safi pasina mfano. Nchi ya wanahewa…

    ***

    Miaka elfu mbili iliyopita huko nyuma, nchi ya Sabaa ilineemeka kwa kila fani – utajiri, maendeleo makubwa na ustaarabu wa hali ya juu, chini ya malikia wao Balika. Sabaa ilitegemea zaidi madini,vito pamoja na kilimo kutokana na ardhi yake iliyokuwa na rutuba, na hali ya hewa yake mwanana. Baada ya uvamizi wa Wanamoto ambao ni majini wachokozi, raia wachache waliobaki chini ya Malkia mpya bibi Sultana, mdogo wake Malkia Balika, walijitahidi kuijenga upya nchi yao na kuanzisha utawala mpya. Miongoni mwa mambo waliyoyafanya ni kuanzisha kanuni mpya za maendeleo, na za kuendesha mambo yao kadhaa wa kadhaa, na kuonesha kwa kila hali ukomo wa ustaarabu ulionawiri upya, alioufikisha malkia wao huyo mpya. Hata hivyo, kukosekana kwa ile neema ya Mwana Mteule aliyehusudiwa awali katika utawala ule tangu miaka mia moja iliyopita, kuliwapa Wanahewa majonzi na masikitiko makubwa mno. Tukio lile lilichelewesha sana utekelezaji wa malengo bora ya nchi ya Sabaa kwa ajili ya jamii yake kote ulimwenguni kwa kipindi cha miaka mia moja, athari ambayo ilitabiriwa kuwa ingejidhihirisha kwa dalili mbalimbali katika sehemu nyingi duniani!

    “Kukosekana kwa kijana mteule, kumeondoa matumaini miongoni mwa jamii na kuzuia nusura si kwa raia wa Sabaa pekee, bali pia duniani kote.” Malkia Sultana aliyerithi kiti cha Malkia Balika aliwaambia wazee waheshimiwa katika baraza lake la mashauri. Alitoa wazo kwao kwamba ni vizuri kuitisha mkusanyiko wa raia wa Sabaa wakiwemo wanataaluma ya nyota na wanajimu, ili watabiri mustakabala wa nchi yao pamoja na dunia nzima, kuelewa ni matatizo gani yatakayowakabili katika sayari yao na jinsi gani yanaweza kutatuliwa. Wazee wale waheshimiwa ambao ni washauri wa Malkia Sultana katika utawala wake, waliafiki mawazo yake, na ndipo ulipoitishwa mkusanyiko wa raia wote wa Sabaa katika uwanja maalum. Uwanja ulifurika watu waliokuwa na hamu ya kufahamu hatima ya sayari yao. Wakati huo sayari ya dunia ilikwishafikia kiwango kikubwa cha nyuzi joto ambacho haikuwa rahisi kukipunguza, na kilikuwa kikiongezeka kwa kasi kubwa. Hali ile ilitishia mno maisha ya viumbe wote duniani!

    “Kwa hakika ingawa mwana mteule aliteketezwa na moto kwa njama za wale viumbe waovu kwa nia ya kutuondolea matumaini yetu, lakini hivi tunavyozungumza umejitokeza uwezekano mkubwa wa kupata ufumbuzi utakaorejesha matumaini kwa wanahewa wote nchini Sabaa, na jamii nyingine duniani.” Alitabiri mmoja kati ya wanajimu waliohudhuria, ambaye kwa maelezo yake hayo hakuwatosheleza raia waliokuwa na shauku ya kupata majawabu ya maswali waliyokuwa wakijiuliza. Malkia Sultana alimwangalia mzee yule kwa makini na kisha akamuuliza. “Unaonaje ukitufichulia kuwa ni matumaini gani hasa yatakayopatikana, ili kila mmoja wetu aondokane na wasiwasi alionao hivi sasa?” Malkia yule alihisi kuwa mnajimu kwa makusudi kabisa, hakupenda kufichua ukweli wa sababu za ule utabiri, ambazo aliamini kuwa zilikuwa ni nzuri tu, lakini hata hivyo bado alitaka ufafanuzi wa namna fulani, ili kurejesha imani kwa raia wake, na kuwaweka katika hali ya utulivu. Raia wote nao waliafiki hoja za Malkia wao na wote wakamkodolea macho mnajimu yule, wakisubiri jibu lake la kuridhisha, lakini kabla yule mnajimu hajafungua mdomo kusema lolote, kishindo kikubwa, mithili ya kile kitolewacho na gari moshi likichemka, kilirindima eneo lote lile.

    “Aaaa! Aaach-ch-chuuuuu! Aaaa---aaaaach-ch-chuuuuu!”

    Pale uwanjani vumbi lilitimka kama kimbunga!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jamii yote iliyohudhuria mkusanyiko ule iligutuka na kuruka kutoka vitini mwao. Vitu vidogo vidogo vilivyokuwepo katika eneo la mkusanyiko ule kama vile mazulia, viti ambavyo havikukaliwa, makaratasi na vinginevyo, vilirushwarushwa na kutawanywa huku na kule.

    Hamadi!

    Kumbe ilikuwa ni chafya moja ya nguvu iliyotoka miongoni mwa raia waliohudhuria mkusanyiko ule. Kila mmoja alitaharuki na kugeukia upande kilipotokea kishindo kile, kushuhudia ni nini hasa kilichotokea.

    “Hayaaa! Hayaaaa! Jamani! hebu tulieni kidogo! Tulieni jamani! Bila shaka baadhi yenu mnafahamu jinsi Mzee wa Busara anavyokuwa kila anapokuwa na mawazo mazito, kutokana na matatizo ya aina hii.” Alisema mmoja kati ya wazee waheshimiwa.

    “Mara nyingi anapofanya hivi huwa na wazo muhimu la kuchangia! Kwa hiyo ni bora tutulie na tumsikilize kwa makini ndugu zangu!” Mwingine aliafikiana na yule mzee muheshimiwa wa kwanza.

    Naam. Mzee wa Busara alikuwa amejirundika kama kifusi pembeni kabisa ya ule uwanja! Kwa haraka haraka mtu angeweza kudhani kuwa ni kilima kidogo kilichotokana na takataka nyingi! Mzee yule wa ajabu alianza kujigeuzageuza na kunyoosha nyoosha shingo yake ambayo awali haikuonekana. Alikuwa kama mnyama mwenye miguu minne na mkia mnene kama wa mamba, na ngozi yake ilikuwa na magamba kama ya samaki, lakini zaidi yalionekana kama ya mamba kwani yalikuwa mapana mno!

    “Aaaa—ch---chu---!” Alianza tena Mzee wa Busara akiwapa wahaka mkubwa wote waliokuwa wakimwangalia. Alichukua nafasi ile na kuanza kuelezea jambo lake, wakati ambapo wote waliohudhuria walikuwa makini kabisa, wakidhani kuwa litatoka chafya jingine babu kubwa liwatimulie vumbi kama awali!

    “Sisi---eh! Mhh-khuu! Sisi t-tun-nafahamu kuw wa y-yapo mat-tumaini ma-kubwa m-mbele-yetu! Tusub-iri tu---aaach-ch-mhhh!” Mzee wa busara alijitahidi kuzuia chafya yake, ili asiwavuruge raia waliokuwa wakimsikiliza.

    “Tuv-vute s-subira, maa n-na s-si muda mr-refu t-tutapata maj-jibu yatakayo turudishia imani na matumaini, pamoja na nusura tuliyoitegge—m-eaaaaaaa----c-h---u….....!” alisema mzee yule wa busara huku akizuia chafya zake kwa taabu sana, akiwa pembeni mwa uwanja na huku shingo yake ndefu ikizunguka zunguka kwa madaha kama shingo ya twiga mtoto. Alimgeukia mtu mmoja mdogo sana ambaye kimo chake kilikuwa mithili ya kimo cha ngedere. Mtu yule aligubikwa na ndevu nyeupe tupu zenye urefu wa kama mita thelathini hivi, zilizoburuza hadi aridhini.

    “Na matumaini hayo yatadhihirika itakapokamilika miaka mia moja kamili tangu nchi hii ilipovamiwa na kuteketezwa na majini wa bahari.” Kijitu kile kidogo kiliongezea taarifa katika maneno ya Mzee wa Busara. Awali kabla ya uvamizi wa nchi ya Sabaa, kijitu kile ndicho kilichotarajiwa kuwa mwalimu wa yule Mwana Mteule aliyeteketezwa na moto wa majini, katika siku ambayo raia wa Sabaa waliazimia kumkabidhi kwake.

    “Kwa hiyo hakuna yeyote kati yenu atakayekuwa na ufafanuzi wa ufuatiliaji wa jambo litakaloturudishia matumaini yetu?” Alidadisi Malkia Sultana, akiwaangalia wazee wake waheshimiwa na watabiri wake wa mambo waliohudhuria. Mmoja kati ya wanajimu aliyekuwa amejiinamia kwa muda wote wa mkusanyiko ule alisema; “Kwa hakika hatuwezi kufafanua zaidi kwani tutakapofanya hivyo tutavunja mwiko, na hivyo kuweka ugumu zaidi katika upatikanaji wa ufumbuzi wa mambo yanayohusika. Ila, tunachoweza kusema ni kwamba maelekezo ya dalili za madhara yanayoikabili sayari yetu na jinsi ya kukabiliana nayo, yameandikwa katika moja ya vidani vya fedha vyenye umbile la kucha za Simba, kwenye mkufu unaoning’inia shingoni mwa sanamu la shaba la kichwa cha Simba, katika nchi ya milima minne myeusi ya maangamizi, kwenye uwanda wa jabali la kisiwa cha Baharia!”

    Raia wote waliohudhuria waliduwaa!

    Kwenye milima myeusi ya maangamizi? Ndio wapi huko?!

    Ukimya mkubwa ulitawala uwanja ule wa mikutano, kila mmoja akitafakari kuhusu taarifa ile mpya ambayo kwa hakika iliwakatisha tamaa zaidi, kwani walihisi kuwa lile ndilo lililokuwa jukumu la Mwana mteule, ambaye walikwisha mpoteza!

    ***

    Naam, Kibwe alimsikiliza Bunga kwa makini sana, akijaribu kuhusisha taarifa ile ya kidudu Bungan a yale na maneno yake ya awali, kwamba ‘alimsubiri yeye kwa kipindi cha miaka mia moja’. Hapo akasikia mikoromo ya kutisha nje ya lile pango walilokuwemo. Akakumbuka yale majitu ya ajabu aliyoyaona kule nje muda mchache uliopita.

    Alizidi kuogopa.

    “Yale…ni majitu gani kule nje?” Kibwe alimuuliza yule mzee wa ajabu, huku akioneshea na akichungulia nje ya lile pango kujaribu kuyaangalia majitu yale aliyoyaona awali. Kama hapo awali aliogopa, basi safari hii, aliogopa maradufu, kwani baada ya lile giza la vumbi nene kutoweka, aliweza kuyaona vizuri sana yale majitu ya ajabu! Miili yao mikubwa kama milima ilikuwa na vichwa vyenye mapembe vilivyofanana na vichwa vya ng’ombe! Halafu lo! Mikono na miguu yao ilikuwa na makucha marefu ya shaba!

    Wakati akishangaa kwa kuhofu namna ile, aliyaona yale majitu yakipasua majabali na kuchimbua milima. Huku yakikenua meno yao makubwa ya shaba yaliyong’ara mno kwa mwanga wa jua, Kibwe aliyashuhudia yale majitu yakitafuna mawe bila kizuizi kama kwamba yalikuwa peremende! Miguu ilimwisha nguvu, na kumfanya kijana yule anyong’onyee taratibu na kurudi chini, akiwa dhofu-l-hali kwa hofu.

    “Ama hakika leo ndio kifo changu! Hakuna uwezekano wa kunusurika hata kidogo hapa! Na kama ninaota, mbona siamki mpaka sasa? Laaa! Sijui nitanusurika vipi mimi!” Aliwaza kijana yule kwa hofu na wahaka. Alimwangalia Bunga aliyeonekana kuwa hana hofu hata chembe, na kwa sauti ya kutetemeka, akamuuliza kwa mara nyingine, “Aaa...eeeh…hivi…eeeh…. wale ni kina nani babu….? Wametoka wapi…..na kwa nini….wanafanya vile wanavyofanya?”

    “Wale kijana ndio wala mawe. Kila mwaka kwa muda wa miaka mia moja sasa, watu hao wa ajabu wamekuwa wakitokea, wakisindikizwa na upepo mkali, vumbi, dhoruba na matetemeko ya majabali. Wakifika tu, huanza kuchimbua milima na mawe na kupasua majabali, ili kujipatia chakula chao. Watu hao wala mawe wataendelea kufanya hivyo hadi kuimaliza dunia yetu yote, wakisababisha uwazi wenye kina kirefu kisichokuwa na mwisho!” Bunga alimwambia, na Kibwe akaduwaa akiwa kinywa wazi. Bunga alizidi kumkatisha tamaa ya nusra pale alipomweleza kuwa hata yeye anahofu kwamba hatimae, hata ile sehemu ya ardhi kwenye lile pango alikokuwa anaishi kumsubiri, pia itatoweka pamoja naye, na kuacha uwazi kama sehemu nyingine katika eneo lile, ambao uliwapoteza viumbe wengine wengi kabla yake.

    “Oooh! Haponi mtu hapa!” Kibwe alijisemea kwa sauti huku akijishika kichwa kwa kukata tamaa.

    “Wewe pekee ndiye utakayesaidia kuzuia hali hii isiendelee na labda kuirudisha vile ilivyokuwa awali Kibwe, kwani wewe bado ni damu changa, hujaanza kufikia umri wa kukata tamaa.” Bunga alimwambia, na Kibwe akamshangaa. Hakujiona yeye akimuokoa yeyote kutokana na maangamizi ya ile mijitu inayokula mawe, lakini pia alishangaa kwani hakuona uhusiano baina ya kuiokoa dunia na ule uwazi ulioikabili. Vyote kwa vyote, hakuelewa ni vipi yeye angeweza kuzuia ile hali ya hatari isitokee, hasusan akizingatia kuwa waliohatarisha hali ile ya dunia walikuwa ni majitu makubwa mno kwa yeye kuyadhibiti!

    Kama vile aliyekuwa akiyasoma mawazo yake, Bunga aliendelea kumwelezea hatua zipi achukue, ili kuinusuru dunia.

    “Wewe ndiye mteule mwenye jukumu hilo Kibwe, pamoja na mengine ya kuitahadharisha jamii na kuiokoa dunia na ukame, na uwazi ulioikabili. Hiyo ni pamoja na matatizo ya kiafya na vifo vya binaadamu na viumbe wengine, na pia kuinusuru dunia na uovu na uadui miongoni mwao, pamoja na kuwajengea imani na matumaini...”

    “Khah! Mimi?”

    “Wewe, Kibwe! Kwa hiyo, ili ufanikishe kazi hiyo, lazima ufanye safari ndefu na yenye mitihani mikubwa. Safari hiyo ndiyo itakupatia ufumbuzi wa jambo hilo. Kwa vyovyote vile, usikubali kabisa kukata tamaa kwa jambo lolote litakalotokea, kwani utakapokata tamaa, azma yako haitatimia.” Bunga alisisitiza, mara kwa mara akikunja uso wake uliokomaa na uliopambwa na zile ndevu zake nyingi za mvi.

    “Lakini bado sijaelewa jinsi nitakavyotimiza azma hiyo babu! Na hiyo safari nitakayoifanya ni kuelekea wapi baada ya kutoka hapa?” Kibwe alihoji, yote yale yakiwa ni mazito kwake. Maelekezo ya Bunga kuhusu safari yake yalizidi kumtia hofu, kwani yalimdhihirishia kuwa hakika safari ile ingekuwa ngumu mno na isiyo ya kawaida.

    “Mara baada ya kuondoka wale wala mawe, takriban nusu saa kuanzia sasa, utaelekea magharibi ya dunia hadi ufike mahali kunakokuchwa jua, katika makutano ya mbingu na ardhi, ambapo jua huonekana kama kwamba linazamia hapo. Kwenye ufukwe wa bahari utaona mtumbwi. Tumia mtumbwi ule kwa safari yako ya kuelekea kisiwa cha mazimwi, viumbe ambao nusu;yaani kuanzia kuanzia tumboni kwenda miguuni ni wanyama, na kuanzia tumboni kwenda kichwani ni wanadamu. Katika kisiwa hicho utakuta ngome moja imara, na ndani ya ngome hiyo, huishi hao mazimwi ambao hulinda upanga wa radi. Jitahidi uupate upanga huo ili ukusaidie katika mapambano ya kuzuia vitendo vitakavyozidi kueneza uwazi mkubwa katika dunia hii. Utakapofanikiwa kuupata upanga wa radi na kuondoka katika kisiwa cha mazimwi salama salimini, utaelekea katika nchi ya Azarbajan iliyoko kaskazini ya mbali ya dunia, baina ya milima miwili mirefu sana. Ili kuupata upanga wa radi kwenye kisiwa cha mazimwi, lazima uwe mwangalifu mno, uhakikishe kuwa unaingia kwenye ngome yao wakati ukiwa na hakika kuwa wote wamelala usingizi kwani….”

    “Sasa, nitahakikisha vipi kwamba mazimwi hao wamelala ili niweze kuingia kwenye hiyo ngome?” Kibwe alimkatisha kwa mshangao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Utakapo sikia kelele nyingi na zogo kutoka ndani ya ngome kama vile unazomewa na kundi kubwa la watu, hapo ndio utaanza kuingia ndani polepole, na utakapofika ngomeni, utawakuta mazimwi hao wamelala sesa; fo-fo-fo! Humo ngomeni utaona mnara wa dhahabu, na juu ya mnara huo wa kipekee, utauona upanga wa radi uliowekwa nje ya ala yake na unang’ara kama jua.” Bunga alitoa maelekezo yale yaliyomshangaza mno Kibwe, aliyestaajabu sana kusikia kuwa eti zinaposikika kelele nyingi za mazimwi, ndio ishara kuwa wamelala! Alijiuliza sana moyoni mwake kama mambo yote yale aliyokuwa akisikia yalikuwa katika ndoto, au kweli yalikuwa alivyokuwa akiyasikia!

    Wakati Kibwe anahoji uhakika wa mambo mengi yaliyomtokea katika kipindi kifupipale kwenye ule mji wa wala mawe, alimsikia tena Bunga akisema; “Ingawa utafaulu kuwakimbia mazimwi wa ngomeni, hutaweza kuvuka mpaka wa nchi hiyo ili kuendelea na safari yako, kwani njiani utazuwiliwa na kiongozi wa mazimwi hao, zimwi ‘Nyalile’ mwenye jicho moja. Kwa bahati nzuri icho hilo moja la zimwi ‘Nyalile’ halioni vizuri. Na kama atajaribu kukuzuia usipite, lazima umuimbie wimbo mzuri utakaomvutia na kumlaghai, ili asiweze kujua kama wewe ni mwanaadamu!” Lo! Hapo Kibwe akazidi kuhofu, na kuzidi kumaizi kuwa kazi iliyokuwa mbele yake, kamwe haikuwa rahisi! Aliogopa sana kusikia maelezo ya Bunga, na akakosa imani kabisa ya kuendelea na jukumu lile la kuiokoa dunia isikumbwe na janga la uwazi ulioikabili, pamoja na majanga mengine.

    Bunga alifahamu wahaka na taharuki ya Kibwe baada ya kumpa maelezo ya jinsi safari yake itakavyokuwa, hivyo akazidi kumpa moyo akiongea naye kwa upole, na kumuhakikishia kuwa hatapata tatizo lolote katika safari hiyo, kama atatumia busara na kufuata maelekezo yake. “Nimekuambia tokea mwanzo kuwa wewe ndiwe mteule wa jukumu hilo, kwa hiyo kabla hujaondoka kuelekea kwenye safari hii ya aina yake, nitakupa silaha mbalimbali, ambazo utazitumia kadiri inavyostahili.” Baada ya kusema hivyo, Bunga alijisogeza ndani ya pango lake na kutoa mfuko mmoja mkubwa wa gunia na kumkabidhi Kibwe. “Humu ndani kuna silaha nyingi utakazozitumia utapozihitaji……” Bunga alizitoa zile silaha moja baada ya nyingine, akielezea kazi zake taratibu na kwa makini, Kibwe alisikiliza maelezo hayo kwa umakini mkubwa. Bunga akamuuliza iwapo ameelewa maelekezo yote. Kibwe akaafiki kuwa ameelewa.

    “Haya kijana, hebu fumba macho kidogo….” Hatimaye Bunga alimuamuru, na Kibwe akafanya alivyoambiwa. Wakati macho yake yakiwa yamefumba, alihisi mtikisiko na akasikia mvumo ulioambatana na mtikisiko ule mithili ya mtu aliyekuwa kwenye gari moshi. Naam, hapo ndipo ilipoanza safari ndefu na ya ajabu ya Kibwe. Alipofumbua macho kuelewa ni jambo gani lililokuwa likiendelea, alijikuta ufukweni, na mbele yake ulikuwepo mtumbwi!!

    ***

    Kibwe aliendelea na safari ile kama alivyoelekezwa na Bunga. Kwa muda mrefu mno aliendesha mtumbwi alioukuta ufukweni, hadi akachoka sana na kuanza kusinzia kwa uchovu. Alipokaribia kile kisiwa cha mazimwi, Kibwe alianza kusikia sauti nyororo na nzuri zikiimba wimbo ulioburudisha kupita kiasi! Alipotupia macho mbele kabisa ya kisiwa, akawaona mabinti saba wazuri, waliovalia mavazi ya hariri yaliyometameta juani, na waliovutia kupita kiasi. Lakini zaidi ya uzuri wao, sauti zao ndizo zilizomvutia Kibwe zaidi. Alitega sikio na kusikiliza kwa makini. Lo! Sauti zilikuwa si za kawaida! Kibwe akazidi kusinzia kwa burudani ilepamoja na uchovu aliokuwa nao. Mara akakumbuka maneno ya Bunga!

    “Karibu na kisiwa cha mazimwi, kuna mabinti saba laghai wenye sauti nyororo za kimazingaombwe. Ukizisikiliza sauti zao nzuri kwa mfululizo, lazima utawafuata walipo, na ukifika kule watakuwekea ulozi kwenye kinywaji chako na kukufanya usahau kabisa kutekeleza malengo yako!

    “Kwa hiyo nitafanyaje kujinusuru na ulaghai wao?” Kibwe aliuliza

    “Utachukua hii ‘nta’ na kuziba masikio yako ili usiweze kuzisikia sauti zao.”

    Haa! Sijui kwa nini Kibwe alitaka kusahau jambo lile muhimu kabisa. Haraka akatoa ile ‘nta aliyowekewa kwenye mfuko wa gunia na kuyaziba barabara masikio yake, kisha akaendelea na safari yake kwa amani hadi alipofika kisiwa cha mazimwi.

    Kibwe alianza kuangalia huku na huko akitafuta sehemu ya kivuli aweze kupumzika kabla ya kuanza kutekeleza ile kazi iliyompeleka kule. Alipata sehemu yenye mti wenye matawi marefu sana yaliyokuwa yakiburuza hadi chini, na hapo akaketi na kutumia yale matawi kwa kujificha, ili asionekane. Baada ya kunywa maji aliyowekewa na Bunga kwenye ule mfuko mkubwa wa gunia, Kibwe alipata lepe zuri la usingizi, kutokana na upepo mwanana uliopuliza sehemu ile. Alilala kwa muda mrefu akapumzika vya kutosha, ili apate nguvu ya kuanza kuelekea kwenye ngome ya mazimwi, kuchukua upanga wa radi, kama alivyoelekezwa na Bunga.

    Baada ya mapumziko yake, Kibwe alianza ufuatiliaji wa kazi iliyompeleka kule. Alikumbuka maneno ya Bunga. “Itakubidi kwanza uende kwenye mlima ambao chini yake kuna shamba kubwa la ufuta.” Alifahamishwa kuwa sehemu ile ilikuwa karibu na makazi ya wale mazimwi hatari wafuasi wa Zimwi mkubwa aliyeitwa ‘Nyalile’ na ambao kwa pamoja, wakati fulani waliwateketeza wakazi wa kisiwa hicho kwa kuwatafuna. “Lazima upande mlima huo hadi kileleni, na huko utakuta jumba wanamoishi mazimwi hao, lililozungushiwa ngome madhubuti.” Aliambiwa kuwa lazima akachukue upanga wa radi unaotoa cheche za moto kila unapotumiwa, na kumpa ushindi yule anaye utumia. Aliambiwa kuwa ile ndiyo silaha pekee ambayo ingemsaidia kupambana na mitihani mikubwa iliyokuwa mbele yake, akiendelea na safari yake kuelekea matokeo ya jua, baina ya mashariki na magharibi.

    Kibwe alipita kwenye shamba kubwa la ufuta na kuanza safari yake ngumu ya kupanda mlima akielekea kileleni kwenye jumba la mazimwi. Katika jitihada zake hizo, mara kwa mara kijana yule aliteleza na kuporomoka, lakini alizidi kuupanda mlima bila kuchoka wala kukata tamaa.

    Mchana kutwa Kibwe aliendelea na safari ile ya kupanda mlima, na ilimchukua takriban siku mbili njiani akila matunda ya porini kujinusuru na njaa. Kila alipokutana na wanyama wakali kama simba, chui , faru, mbogo na wengine, Kibwe aliwakwepa kwa kujificha vichakani. Hadi kufikia saa kumi jioni siku ya tatu jua lilipoanza kuchwa, kijana yule aliona ngome ndefu mno, iliyosimama kwenye upeo wa macho yake katikati ya msitu! Taratibu, huku akiangalia huku na kule, Kibwe alisogea karibu na ngome ile. Alipokaribia zaidi alistushwa na kelele na zogo kutoka ndani ya ngome ile madhubuti! “Huyooooo! Anakuja kuchukua upanga wetu! Haraka mkamateni! Mfuateni mumlete haraka kabla hajaingia ndani! Hayaaa! Kamataaa! Chinjaaaa! Uwaaaa! Nyongaa!” La haulaa! Kibwe alianza kukimbia kwa hofu ya kukamatwa na kutafunwa na mazimwi wale hatari, na kusahau kabisa usia aliopewa na Bunga!

    “Utakapo sikia kelele nyingi na zogo kutoka ndani ya ngome kama vile unazomewa na kundi kubwa la watu, hapo ndipo utaanza kuingia ndani polepole, na utakapofika ngomeni utawakuta mazimwi hao wamelala sesa, fo-fo-fo ! Kutakapokuwa kimya basi tahadhari sana, kwani mazimwi hao watakuwa wako macho!”

    Hilo lilikuwa ni onyo la Bunga kwa Kibwe.

    Haa! Ilikuwaje akasahau jambo jingine muhimu kama lile? Hamadi! Palepale alipokumbuka onyo lile na taarifa ya Bunga kuhusu maajabu ya wale mazimwi, Kibwe aligeuka na kupiga mbio kuelekea kule ngomeni. Alipofika langoni huku akipumua kwa kasi, Kibwe alichunguli ndani kwa uangalifu na umakini mkubwa kuona kama wale mazimwi walikuwa wamelala. Hakuona dalili ya mtu au kitu chochote katika upeo wa macho yake. Taratibu aliingia ndani akinyata polepole na alipoangalia mbele zaidi, akaona eneo kubwa la wazi lenye bustani nzuri ya maua. Aliambaa na ukuta, huku polepole akinyanyua mguu mmoja mmoja, akishikilia pumzi yake kwa hofu ya kusikika na madude yale hatari aliyoambiwa na Bunga. Mwisho kabisa wa eneo lile la wazi, Kibwe aliona lango jingine kubwa lenye mbao za marembo marembo. Alinyata taratibu na alipogundua kuwa lango lile lilikuwa wazi, alilisukuma na kuchungulia uwani. Hamadi! Kibwe hakuamini macho yake kwa kile alichokiona!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Macho ya kijana yule yalikutana na kundi zima la madude makubwa kupita kiasi yaliyokuwa nusu ni watu, yaani kutoka tumboni kwenda kichwani na nusu, katika sehemu ya tumboni kwenda miguuni walikuwa kama sokwe! Kundi lile la madude yale ya ajabu na ya kutisha, lililala sesa kwenye nyasi za eneo lile, na huku kelele zao za kuzomea zikiendelea! Wakati sauti zao zikimbabaisha Kibwe, miili yao ilimtisha sana kwani ilikuwa na manyoya marefu kupita kiasi yakiburuza hadi chini kama ufagio! Viumbe wale walikuwa na midomo iliyojaa meno yenye ukubwa mithili ya pembe za ndovu! “Lo….. ndiyo maana ilikuwa rahisi sana kwa madude haya kuwatafuna na kuwateketeza mara moja watu wa kisiwa chote hiki, kutokana na urefu na wingi wa meno yao makali!” Kibwe aliwaza, akiwa na woga na wahaka mkubwa usio mfano.

    Haraka Kibwe alifuata yale maelekezo ya Bunga, akianza kuwatambuka taratibu wale mazimwi waliolala huku wakipiga kelele na kuzomea kama kwamba walikuwa macho, hali iliyomfanya Kibwe azidi kuhofu, kwani muda wote alihisi kuwa huenda ghafla wakamrukia na kumshambulia. Hiyo Ilikuwa ni kazi ngumu mno kwa kijana yule na muda wote wa zoezi lile, jasho lilikuwa likimtiririka na mara nyingine alihofu kuwa huenda jasho lile likawadondokea na kuwaamsha wale mazimwi, na huo ukawa ndio mwisho wake!

    MAJANGA YA SAYARI

    Wakati Kibwe akiwa katika jitihada za kutekeleza malengo yake ya kuinusuru jamii kule machweo ya jua katika kisiwa cha mazimwi, katika sehemu nyingine iliyo baina ya mashariki na magharibi mbali kabisa kutoka kisiwa kile cha mazimwi, katika milki ya Sultani Bashar, majini yalitawala sehemu kuu iliyowapatia maji raia wa nchi ya Shamsi mjini Majabali. Jambo hilo lilisababisha shida kubwa ya maji na ukame uliathiri maeneo mengi ya nchi ile, iliyokosa chakula cha kutosha kwa watu wake. Ili kuwanusuru raia wake na shida ile ya maji, kila mwaka Sultani Bashar wa nchi ya Shamsi, alimtoa kafara binti yake kwa joka moja kubwa ambalo lilimchukua binti yule na kuzama naye kwenye mto Sakara ulioko kati ya majabali mawili na kumpeleka kwa jini ‘Makattani,’ mfalme wa majini yote. Mpaka kufikia wakati ule Kibwe alipokwenda kisiwa cha mazimwi, tayari Sultani Bashar wa nchini Shamsi alikwisha watoa kafara watoto wake sita, binti mmoja kila mwaka na kila mara akiwapatia raia wake mwaka mmoja wa kuchota maji kutoka mto Sakara. Hatimae Sultani yule alibaki na binti mmoja tu, Bhaduri binti sultani ambaye kwa bahati mbaya kwake, alitakiwa kumtoa kafara wiki mbili zilizofuata kwenye mto uleule Sakara, ili kuwapatia raia wake mwaka mmoja zaidi wa kutumia maji yake!

    “Ama kweli hali hii ni ya kusikitisha na kusononesha mno,” Malkia wa Shamsi amlalamikia mumewe Mfalme Bashar, huku akilia bila kizuizi! “Haya ni maonezi makubwa na ni unyanyasaji wa aina yake, wa kuwalazimisha mabinti zetu wajitowe mhanga, eti kwa ajili ya kunusuru raia wako! Hili si jambo la kibinaadamu hata kidogo.” Malkia yule alisema kwa masikitiko makubwa. “Sasa mke wangu unadhani tungefanya nini kulitatua tatizo hili sugu linalotukabili kila mwaka?” Sultani Bashar alimuuliza mkewe kwa upole.” Hata mimi nina majonzi makubwa kuhusu mabinti zetu, lakini hii ndiyo njia pekee ya suluhu kwa jambo hili.”

    Katika mji ule mkuu wa Majabali nchini Shamsi, baada ya Suitani kufanya maandalizi ya kumpeleka kitindamimba wake Bhaduri kule mtoni Sakara kwa ajili ya kafara, aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kujiinamia kwa fikira na majonzi ya kumpoteza binti yake mwengine! Ama kweli Sultani yule alikuwa mtawala wa aina yake! Eti kudiriki kuwatoa kafara mabinti zake saba! Si jambo la kawaida asilani!

    Kule Azarbajan nako kwa Sultani Kash Kash kaskazini ya mbali ya dunia, ingawa chini kabisa ya bahari, i jini ‘Makatta’na wenzake walikuwa wakiandaa vichafuzi vya hewa safi iliyowasaidia watu kuishi, na kuigeuza hewa ile kuwa hatarishi, lakini Mfalme wa nchi ile hakutambua hivyo. Hakujua kama hewa ile iliyogeuka kuwa moshi mnene ilipoanza kuzizima na kisha kuwazingira watu katika himaya yake, ndipo walipogeuka kuwa mawe ya theluji! Kwa kuwa hawakuelewa chanzo hasa cha janga lile, watu wote wa kule waliingia hofu kubwa na Mfalme wao alikuwa akimtafuta mkombozi atakaye wanusuru raia wake kutokana na janga lile!

    “La mgambo! La mgamboooo! Likilia lina jamboo! Asiye mwana a eleke jiwee!” Kijumbe wa Mfalme Kash Kash alipita mitaani akiwatangazia raia wa Azarbajan kama kawaida wakati inapotokea dharura ama ya raha, au ya karaha, akianza kwa kupiga goma lake kubwa alilolibeba kifuani, na lililofungwa kwa kamba iliyopita mabegani na kuzungukia makwapani.

    Kwa kupiga ile ngoma kijumbe yule aliwavutia watu na kuwasogeza karibu, ili waende kumsikiliza. “Jamani eeeh! Kuhusu janga linalotukabili la raia wengi kugeuka mawe ya theluji, mpaka hivi sasa bado haujapatikana ufumbuzi wa tatizo hilo, na wala bado hajapatikana mkombozi atakaye saidia kunusuru maisha ya raia wa nchi hii. Hivi sasa wazee wa baraza la Mfalme, wako mbioni kutafuta njia ya haraka ya ufumbuzi wa tatizo hilo. Kwa hiyo yeyote atakaye kuwa na mawazo tafadhali asisite kujitokeza na kuchangia, ili kulipiga vita janga hili la kihistoria nchini kwetu…..! La mgambooooo! La mgambooooo! Likilia lina jamboooooo!” Kijumbe yule alihitimisha tangazo lake na kisha kuendelea katika maeneo mengine ya mji wao mkuu. Tangazo lile lilitangazwa mara kwa mara katika miji mbalimbali ya Azarbajan, lakini hakujitokeza mtu yeyote aliyeweza kutoa ushauri kuhusu utatuzi wa tatizo lile.

    Katika ngome ya jumba la mazimwi kwenye kisiwa chao, Kibwe alitumia muda ule ambao mazimwi wale walikuwa wakipiga kelele, kwa kuendelea kuwatambuka mmoja mmoja, hadi alipofika kwenye ule mnara wa dhahabu. Pale alipumua kidogo kabla ya kuanza kupanda mnara huo ambao juu yake ulikuwepo upanga wa radi alioutaka. Kelele za mazimwi zilizidi kuliko awali, kama kwamba walihisi kuwa kuna mtu karibu ya hazina yao.

    “Naomba Mungu majitu haya yasiamke ama sivyo sitanusurika asilani!” Kibwe aliwaza. Alikumbuka kuwa mara tu, kelele zitakapokoma, ndio utakuwa wakati wa hatari kubwa kwake! “Na kutakapokuwa kimya basi tahadhari kwani watakuwa wako macho!” Bunga alimwambia.

    Ingawa aliogopa sana na kuhofu, lakini kijana yule shujaa alipanda juu ya ule mnara mrefu akafika kileleni, na kwa uangalifu akauchukua ule upanga na kuutia kwenye ala yake, na kisha akaupachika kiunoni kwake na kuanza kuteremka chini kwa uangalifu! Alipofika chini, akarudia lile zoezi la wasiwasi la kuyatambuka yale mazimwi yaliyolala! Lo! Kwa bahati mbaya, alipokuwa akimalizia zoezi hilo, alilikanyaga zimwi la mwisho lililolala karibu na lango kuu la kutoka ngomeni, na hivyo, lilipokuwa kimya tu, kwa ishara ya kuamka, na menzake yote yakawa kimya! Masikini wee! Mazimwi yote yakawa macho!

     Kabla hayajataharuki na kugundua kuwa alikuwepo mtu ngomeni mwao na amechomoka na kupenyeza getini wakati mmoja wao akiamka, Kibwe alipiga mbio kama mshale! Alikimbia kuelekea mpakani mwa nchi ile kama alivyoambiwa na Bunga, akiazimia kupita katika njia kati ya mashariki na magharibi!

    Walipoangalia mnarani na kukuta upanga wa radi umetoweka, mazimwi wote walitaharuki na kuwa na hasira nyingi “Bila shaka alikuwepo mtu humu ngomeni. Afuatwe haraka kabla hajaondoka na upanga wetu!” Baada ya kusema hivyo, wote walitimua mbio, huku vumbi likitanda kwa heka heka hiyo, na baadhi ya miti ikikatika kwa vikumbo vyao! Alipoangalia nyuma, kibwe aliona vumbi lililotanda hadi mawinguni! “Leo ndio hatima yangu mimi! Sijui kwa nini nilifika huku!” Kibwe alisema kwa majuto. Mazimwi yalipoanza kumkaribia alihisi miguu yake ikiwa inalegea mno na kukosa nguvu kwa hofu! Moyo wake ulienda kwa kasi mno! Alikumbuka maneno ya Bunga. “Wakikaribia kukufikia, watupie kichupa kimoja kati ya vichupa hivi vidogo vya mazingaombwe, ili uwacheleweshe.” Kibwe haraka alitoa kichupa kimoja na kukitupia nyuma yake kwa yale mazimwi. Lo! Mara ukatokea msitu mnene kupita kiasi. Mazimwi yalianza kuhangaika kukata miti ya msitu ule uliozuka! Kutokana na ukubwa wao, muda si mrefu yalifaulu kukanyaga kanyaga miti midogo na kuipiga vikumbo miti mikubwa, na kisha kuendelea kumkimbiza Kibwe, ambaye alipoona hivyo, alirusha kichupa cha pili, na mara zikazuka mbigili nyingi mno nyuma yake! Mazimwi yaliumiaumia miguu yao, na wengi wakaachwa nyuma. Kibwe aliyaona baadhi ya mazimwi yakizidi kumfuata, huku yeye akiwa amechoka mno kukimbia. Alipatwa na wasiwasi mkubwa, “Sasa nikishindwa kukimbia na madude hayo yanazidi kunifuata, itakuwaje?” alijiuliza huku akipapasa papasa kwenye fuko lake, kutoa kichupa kingine miongoni mwa vichupa alivyopewa na Bunga.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa kuwa mazimwi hupenda sana kula ufuta, utakapo watupia kichupa cha ufuta, wote wataketi chini na kuanza kula, na hivyo utapata nafasi ya kuwakimbia.” Kibwe alikumbuka maneno hayo ya Bunga! Mara moja akarusha kichupa cha ufuta, na hapohapo ukazuka mlima mkubwa wa ufuta, na kuwafanya mazimwi wote kuchanganyikiwa kwa uchu! ”Aaaaa! Ufutaaaa! Ufuta mtamuuuu! Nakula ufutaaa!” Wakawa wanajisemesha maneno hayo, kila mmoja akifurahia chakula kile akipendacho, na kumsahau kabisa Kibwe na upanga wa radi! Waliketi chini na kuanza kuushambulia ufuta! Kibwe naye aliongeza kasi ya mbio zake, akiruka mabonde na kuangukia kwenye makorongo na mito, misitu na nyika hadi kwenye mpaka kuelekea kaskazini ya mbali, kulikozizima baridi ya ajabu, iliyowagandisha watu na kuwageuza mawe! Pale mpakani alisimama ghafla akitahamaki na kuona moshi mwingi uliotanda mbele yake, na umbile la dude kubwa lililofichwa na giza la moshi huo, likiashiria kuwepo kwa jitu kubwa likishughulika chini ya mti mkubwa kupita kiasi! Muda wote aliokuwa akiwakimbia wale mazimwi, alimsahau kabisa kiongozi wao, aliyeitwa Nyalile!

    Kibwe alitaka kufahamu ule moshi uliotanda vile ulitokana na nini. Huku akihofu, lakini kwa moyo wa kishujaa, taratibu alisogea kule kulikotoka moshi ule, akiangalia huku na kule kwa wasiwasi hadi akafika karibu kabisa na sehemu ile. Aliona kuwa ule moshi ulitokea bondeni, wakati yeye akiwa juu kidogo kwenye uwanda. Aliposogea na kukodoa macho yake vizuri ili aweze kuona kama kwenye ule utando wa moshi kulikuwa na nini, alihisi kama vile anaangalia umbile kubwa sana la jitu la miraba minne, likishugulika kufanya kazi fulani. Alipozidi kutazama kwa makini aliona kuwa lile halikuwa jitu la miraba minne tu, bali lilikuwa ni kitu kama mtu, na vilevile kama mnyama, likishugulika kuandaa chakula chake chini ya mti mkubwa sana! Lo! Kumbe alikuwa akiliangalia dude moja la kutisha mno, lililokuwa na manyoya mwili mzima, meno marefu kama pembe za tembo lakini yaliyojaa kinywa tele, na kuanzia tumboni kwenda miguuni, Kibwe alikuwa akiangalia mwili wa binaadamu mithili ya sokwe, isipokuwa ulikuwa mkubwa kupita kiasi! Uso wa dude hilo uliokuwa kwenye kichwa kilicho fanana na cha tembo, na katika paji la uso wake, kulikuwa na jicho moja tu!

    Naam, kwenye bonde lililozungukwa na msitu wenye miti mirefu kupita kiasi, alikuwemo zimwi Nyalile, na juu ya bonde hilo, alikuwepo Kibwe akimwangalia! Utakisia mwenyewe hali ya Kibwe ilivyokuwa, mara alipotahamaki, akagundua jinsi alivyokuwa karibu kabisa na kubwa la mazimwi wote, ambalo sifa zake alizipata kutoka kwa Bunga! “Mama yangu weee! Sasa kweli niko hatarini!” Kibwe aliwaza. Alijibanza kwenye miti mirefu kabisa, huku jasho likimtoka, na hofu iliongezeka kila sekunde, wakati kijana yule alipoyaona yale aliyoyaona mle bondeni! Kwenye mafiga makubwa sana kupita kiasi, Nyalile alikua ameinjika jungu kubwa mno. Wakati likichemka, alimkamata ng’ombe mzima na kumnyonga na kisha kumtumbukiza ndani ya lile jungu. Pamoja na ng’ombe huyo Nyalile alichukua kama gunia mbili za mchele na kuutosa kwenye lile jungu lililokuwa likichemka kwa mchemko wa kelele kubwa za ngurumo pale msituni! Shughuli iliendelea na muda wote lile zimwi lilikuwa likichochea mapande ya miti mikubwa mafigani, kukoleza moto wake ili chakula kichemke vizuri. Kitendo kile kilisababisha moto mkubwa sana kuwaka , ulioambatana na moshi mnene, ikawa kama msitu wote ulikuwa unawaka moto!

    Pale alipokuwa Kibwe, ukilinganisha ukubwa wa miti iliyomzunguka, alionekana kama kidege kidogo mno. Aliwaza na kukumbuka maneno ya Bunga, kwamba akitaka kuvuka mpaka kuelekea kaskazini ya mbali bila kukamatwa na Nyalile, lazima amliwaze kwa wimbo mzuri utakaomburudisha na kumfurahisha, kwani atakapofanya hivyo lile zimwi litadhani kuwa ni kidege kinachoimba! Vilevile, Bunga alimwambia kuwa lile jicho moja la Nyalile halioni vizuri. Habari yote hiyo ilimpa moyo Kibwe, akahisi kuwa angeweza kufanikiwa kulikwepa zimwi lile, kama akijitahidi kufanya vile alivyaelekezwa na Bunga. Lakini imani yake ilipungua wakati lile zimwi lilipomaliza kupika na kisha kuketi chini ya mti mkubwa, na kuanza kufuta jasho lililotiririka kama mfereji wa maji! Maajabu yale yalimfanya Kibwe aduwae kabisa na hofu yake kuongezeka upya! Hakujua afanye nini! Je, akimbie? Akimbilie wapi na njia ni ile moja tu! au arudi alikotoka walikokuwa wale mazimwi wala ufuta? Aliona kuwa hapana budi afanye alivyoambiwa na Bunga, kwani hakuona njia nyingine!

    Hivyo, kwa sauti iliyojaa mawimbi kwa wingi wa hofu, Kibwe alianza kuimba wimbo, kwa maneno yaliyomjia katika mawazo yake wakati ule…..!

    Nyaalileee! Nyaalileee, Nyaali… Nyaalileee, Nyaali…… Nyaalileeee! X2

    Babu zimwi nipe motooo,

    Nyaali Nyaalileee,

    Niikapikie waanaanguuu,

    Nyaalii Nyalileee,

    Niipate viijunguuu namiii,

    Nyaali nyaalileee,

    Chaa wali naa cha mchuuzi ii,

    Nyaali Nyaalileee!

    Nyaaliileee! Nyaaliileee! Nyaalii Nyaaliileee! Nyaalii Nyaalileee!

    Kibwe alipomaliza wimbo wake ule, alimchungulia zimwi Nyalile, ili atambue hisia zake baada ya kusikia ule wimbo. Alimuona Nyalile akiinua kichwa na kuangalia juu ya lile bonde kwenye miti mingi mirefu alikokuwa yeye Kibwe! Lo! Kijana yule alianza kutetemeka na jasho likazidi kutoka! Ni dhahiri Nyalile hakuona kitu chochote huko, kwanza kwa kuwa Kibwe alikuwa ni mdogo sana na miti iliyomficha ilikuwa ni mikubwa, na pili, jicho moja la Nyalile halikuwa likiona vema! Kibwe akapata faraja kidogo, alipomuona nyalile kiogo kidogo akianza kutabasamu, na hatimae kutoa kicheko cha aina yake na halafu akisema;

    “Weee kidege weee! Uko wapi? Wimbo wako ni mzuri sana. Hebu imba tena nisikiye!” Kibwe alizidi kujibanza mitini, akihisi wakati wowote ule, Nyalile angeweza kumuona! Pamoja na hofu yake, Kibwe alijitahidi kurudia kuimba ule wimbo wa Nyalile, ili kumfurahisha. Na halafu lo! Kwa jinsi zimwi alivyofurahia wimbo ule, alikariri maneno katika kiitikio, “Chaa walii naa cha mchuziii, Nyaalii nyaaliileee………!” Na kisha weee! Zimwi Nyalile liliinuka na kujikung’uta, huku likizidi kutabasamu kusikia jina lake likitajwa, na pia likifurahia uzuri wa kiitikio cha wimbo ule. Basi ikawa tena ni:

    “Chaa wali na cha mchuchiiii, Nyaalii Nyaaliileee! Chaa walii na cha mchuuchiii, Nyaliii nyaaliileee…….!”

    Alipokua akirudia rudia kiitikio hicho, zimwi Nyalile alikuwa akicheza hatua mojamoja, akifuatisha wimbo ule, na kuitikia vile alivyoelewa yeye! Alivyonogewa zaidi, akawa anapiga hatua za haraka haraka na kuendelea na kiitikio chake; na hatimae likatimka mbio huku likiitikia;

    “Chaa wali na cha mchuchiiii, Nyaalii Nyaaliileee! Chaa walii na cha mchuuchuuchii, Nyaliii nyaaliileee a!

    Moja kwa moja zimwi Nyalile likayoyoma na wimbo wake huku likitimua vumbi na kuangusha miti kwa kuikumba lilipopiga mbio, huku likiimba. Hiloooo! Likayoyoma, msitu na nyika mguu nipe, hadi likafika mbali mno, bila kujielewa, likielekea kusini mwa dunia! Kibwe naye, haraka alishuka bondeni na bila kupoteza muda…… akaanza kupiga mbio bila kusimama, hadi alipovuka ule mpaka uliotofautisha eneo la kule kunako kuchwa jua, ambako ni magharibi ya dunia, na kaskazini ya mbali ya dunia. Kibwe alikuwa akielekea kwa mzee wa busara aliyeelekezwa na Bunga, ili kupata maelekezo kuhusu maendeleo ya safari yake ya ajabu.

    MZEE WA BUSARA.

    Safari yake ikamfikisha mahali kati ya milima miwili mirefu, kwenye mazingira mazuri sana, yenye mianguko na maporomoko ya maji, mahali palipojaaliwa ardhi iliyorutubika mno. Kule, Kibwe alikuta miti ya matunda ya makomamanga iliyostawi vizuri sana. Aliona ndege wakirukaruka na kuimba kwa furaha juu ya miti hiyo, ambayo chini yake vilipita vijito venye maji safi na ya baridi, vikitokea juu ya milima. Kibwe alifarijika mno na hali ile, hususan baada ya kuona maeneo mengi yaliyoathirika na ukame, na pia yaliyokabiliwa na uwazi uliotokana na mashambulizi ya majabali na ardhi, baada ya kuteketezwa na wala mawe. Alishangaa kuona jinsi sehemu ile ndogo ilivyotofautiana na maeneo yale ya awali!

    Mara Kibwe akakumbuka!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ahaaaaa! Sijui kwanini nilitaka kusahau! Hapa ndipo Bunga aliposema kuwa nitamkuta mzee wa busara, ili nipate maelezo kuhusu safari yangu! Sijui huyo mzee wa busara ni nani? Lakini nitafahamu baadae, kama kweli hapa ndipo mahali penyewe.” Hata hivyo kwa uchovu na njaa aliyokuwa nayo, kijana yule aliamua kuketi chini ya mkomamanga , akawa anaokota makomamanga yaliyoiva na kudondoka chini, na kuanza kula. Aliendelea kuketi chini ya ule mti akipumzika, ili kupata nguvu mpya. Alikuwa akitafakari kuhusu hatima ya safari yake wakati aliposikia mlio kama wa pikipiki iliyokua ikianza kuondoka! Alihisi kama mlio ule ulikuwa ukitokea chini bondeni hatua chache kutoka alipokuwa ameketi, na alipotafakari kuhusu mlio huo, akahisi kuwa ulikuwa ni kama kikohozi cha jitu kubwa sana! “Sijui ni kitu gani hicho tena?” Kibwe aliwaza, na kwa mara nyingine akaanza kupata hofu. Alianza kujuta kwa nini alikuwa kule mbali mno na wazazi wake, ambao hata hakukumbuka walikokuwa! Hata hivyo, taratibu alinyanyuka na kuanza kuangaza angaza, akisogea bondeni uliposikika ule mlio. Alitaka sana kufahamu ni kitu gani kilichotoa mlio wa labda tuseme….pikipiki? ……Trekta……..?

    Kila alipoangaza, hakuona kitu chochote! Alisogea na kuzidi kuchungulia chini bondeni, lakini hakuona kitu licha ya ardhi ya tope jeusi ambalo liliotesha majani marefu, na pia kulikuwepo lundo la kifusi kilichoinuka mithili ya kilima kidogo. Juu ya kilima hicho, Kibwe aliona uyoga pori umestawi vizuri sana. Taratibu alisogea zaidi na kukichungulia kile kilima, kuona kama angeweza kushuka bondeni kwa kurukia juu ya kilima hicho. Kwa hiyo kutoka juu alikokuwa, kijana yule alijirusha na kuangukia juu ya hicho kilima. Hapo aliweza kuangaza vema sehemu zote za bondeni, ingawa bado alishindwa kuona kitu chochote ambacho kingeweza kutoa mlio wa kustusha kama ule aliousikia muda si mrefu uliopita.

    Kibwe alishangaa sana, kwani alikuwa na uhakika mkubwa kuwa sauti aliyoisikia ilitokea bondeni.

    “Haya sasa ni maajabu makubwa! Hivi ndio kusema kuwa labda huo mlio sikuusikia? Au tuseme haukutokea humu bondeni?” Alijiuliza kwa mshangao mkubwa juu ya muujiza ule wa aina yake. Lakini kabla hajazidi kudadisi, alisitushwa tena na mlio ule usiofahamika, ila safari hii alijikuta akirushwa hadi ng’ambo kabisa juu ya bonde.

    “Aaaaaaaaaaaaaaaaghh! Mama yangu weeeeeeeeaaaagh…!” Alilia kwa taharuki wakati alipokuwa akielea hewani kabla ya kuangukia kwenye matawi ya mti, mbali na pale alipokuwa awali.

    Kijana aligwaya vibaya sana akiwa ananing’inia juu ya mti kama popo. Alikuwa akitweta na kupumua kwa kasi, huku macho yametoka pima, bila kufahamu kilichomsibu! Halafu, kabla hajatulia vema, kilisikika kitu kama chafya ya nguvu iliyoambatana na upepo mkali kama wa gari moshi likifoka, na hapohapo yeye alizolewa na huo upepo na kujikuta akielea tena hewani, na kisha akatupwa mbali zaidi juu ya bonde kulikokuwa na miti ya mikomamanga, akawa amebanwa na matawi ya mmoja kati ya mikomamanga ile!

    Walisindikizwa na raia wa Azarbajan kwa shangwe na hoihoi hadi bandarini, na kule wakaagana kwa upendo mkubwa, na kisha merikebu ikaanza safari nyingine ya ajabu ya Kibwe, kumuokoa Bhaduri binti Sultani Bashar wa Mashariki ya mbali ya dunia!

    Merikebu ya Mfalme KashKash iliyoyoma usiku na mchana, na hali ya bahari ilikuwa shwari kabisa, kwa muda wote huo.

    “Tuna bahati kubwa, kwani mpaka sasa bado hali ni shwari sana.” Hanga alimwambia mwenzake Kibwe. “Kwa kawaida mimi hutapika sana baharini, lakini leo niko salama kabisa,” Alieleza. Kibwe alimwambia kuwa kwa kuwa bado safari ni ndefu asijiamini sana. Kwa maneno hayo, wote wawili walicheka kwa pamoja. Meli hiyo iliyowabeba vijana hao wawili, wahudumu wakutosha wa meli na manahodha, ilizidi kuyoyoma hadi kufika katikati ya bahari, halafu jambo la ajabu likatokea! Ile meli ilisimama ghafla, kama kwamba ilinasa mahali. Kibwe alipomuuliza nahodha aliyekuwa kwenye usukani ni nini kilichotokea, akajibiwa kuwa hakuelewa ni nini kimeikwamisha meli yao.

    “Huenda majani ya mwani yamenasa kwenye pangaboi linalozungusha maji huko chini ya meli,” alisema nahodha. Alipoambiwa hivyo kijana yule alijitolea kwenda kuangalia kule chini ya meli, ingawa wenzake walimzuia sana.

    “Ni hatari kwenda peke yako. Labda tufuatane pamoja .” Hanga na baadhi ya wahudumu wa ndani ya meli walimwambia. Ingawa Kibwe alipinga kufuatana nao, lakini wenzake walishikilia tu, hadi yule kijana akakubali waende wote.

    Naam, karibu watu wanne walishuka na kuogelea kwenda chini ya ile merikebu, kuangalia hicho kilichonasa kwenye pangaboi la meli yao. Wote waliogelea, na Kibwe alikuwa mbele zaidi, hivyo alitangulia kuwasili pale lilipokuwa hilo pangaboi. Lakini lo! Pangaboi lenyewe lilikuwa limeshikiliwa madhubuti na mtu mmoja mwembamba kupita kiasi, na mrefu kuliko utakavyofikiria! Macho ya mtu yule yalikuwa pembeni mwa sura yake, iliyofanana na chura!

    “Ahaa! Kumbe! Tunakutana tena siyo?” Kibwe aliwaza, na bila kupoteza muda, na haraka kama mwendo wa mshale, kijana yule alitoa rungu lililokuwa kwenye mfuko alioubeba mgongoni, na kulirusha kwa nguvu zake zote, kumtupia yule mtu wa ajabu, akilenga ule mkono ulioshikilia lile panga boi! Kwa kishindo kikubwa, lile rungu likamfikia kwenye mkono wake huo, na palepale akaachia lile panga boi, na kama umeme, akapotelea chini kabisa ya bahari!

    Naam kwa mara nyingine, Kibwe alikutana na mmoja kati ya jamii ya majini wa bahari, jamaa zake ‘Makatta wa Makattani.’ Wakati hayo yakitokea, wenzake wengine waliokuwa wakija kuangalia chini ya merikebu, walifika na kumkosa yule jini wa bahari kwa sekunde tu!

    “Kwani kuna nini?” waliuliza, na wakati huohuo, ile meli ikawa inasogea mbele!

    “Ilikuwa ni mwani tu, ulioshikilia pangaboi! Nimekwisha uondoa , na ndio maana mnaona meli inaondoka. Twendeni tuwahi!” Kibwe alidanganya, akichelea kuwatia hofu watu na hadithi za majini wa bahari! Wote wakarejea melini, na kuendelea na safari.

    Kibwe na wenzake waliendelea na safari yao huko mashariki ya katikati ya dunia, kwenye majabali yaliyouzingira mto mkubwa wa maji, mto Sakara, ambako Bhaduri binti Sultani kitinda mimba na mwana wa saba wa Sultani Bashar, alikuwa ameketi juu ya uwanda wa jabali moja, akisubiri kutolewa kafara!

    Kwa moyo wa ushujaa, na utiifu kwa amri ya baba yake, mrembo Bhaduri binti Sultani aliketi juu ya jabali kwenye kiti kimoja kizuri cha enzi, akiwa amepambwa kwa sundusi za hariri, mikufu, hereni na vikuku vya dhahabu na vito vya thamani, huku akinukia utuli mchanganyiko kama udi, miski na ambari, akisubiri wakati wake wa kuchukuliwa na hicho kitakachokuja kumchukua!

    Kibwe na msafara wake ndani ya merikebu yao ya fahari, waliyoyoma kuelekea huko mashariki ya katikati ya dunia, wakati huo zikiwa zimebaki siku chache tu, kuwasili mwisho wa safari yao. Usiku mmoja alipokuwa amelala na mwenzake Hanga kwenye chumba chao, Kibwe alimuota Bunga, akimpa maelekezo ya safari yao hiyo. “Lazima msafara huu usitishwe haraka iwezekanavyo, mara tu mtakapowasili kwenye bandari yoyote ya jirani,” alisema Bunga. Aliendelea kumwambia kuwa itabidi wasubiri kwenye bandari hiyo kwa siku mbili zaidi, kabla ya kuanza tena safari yao. “Katika muda huo mtakapo kuwa mkisubiri kwenye bandari hiyo, mtakuwa mmejinusuru na hatari ya kupambana na mwamba wa barafu majini, na pia mtanusurika na tufani kubwa itakayotokea mnamo saa ishirini na nne zijazo.” Kibwe alimsikiliza Bunga, aliyeonekana akielea hewani kama ndege, na maneno yake yakisikika kwa kukatika katika, kwa sentensi zisizokamilika!

    Ndotoni Kibwe alikuwa akimcheka Bunga, na akimshangaa sana kwani kwa mara hii alimuona ni wa ajabu kabisa. Hakuamini maneno yake hata kidogo, “Usinitanie mzee Bunga! Unajua kwamba msafara huu lazima uwahi nchini Shamsi mashariki ya kati kati. Sasa mbona unataka kutuchelewesha?” Kibwe alianza kulumbana na kile kijitu cha ajabu.

    “Tutaendelea tu……..na- safa-”Lakini kabla hajamalizia maneno yake, Kibwe akaona ukuta uliokuwa mbele yake ukipasuka, na maji mengi yakianza kumwagika kama mafuriko, na kumzoa Kibwe kutoka pale alipokuwa, akajikuta akitapatapa kujinusuru asizame! Ingawa alikuwa anajitahidi kuogelea, lakini alishindwa, na hivyo akaanza kuzama---! Akazama—akienda moja kwa moja hadi chini kabisa ya dimbwi la maji---! Pumzi zikamwishia kabisa! Halafu ghafla, akajiibua juu, na kutoa kichwa chake nje ya dimbwi la maji, na kisha palepale akasituka na kuamka, huku moyo wake ukienda kwa kasi mno! Aliinuka na kuketi kitako, akiwa anapumua haraka haraka mno!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mwenzake Hanga aliyekuwa karibu yake, naye aliamka na kumuona Kibwe akiwa katika hali isiyo ya kawaida. “Vipi kibwe, mbona uko hivyo, umeota ndoto mbaya nini?” Kimya! Kibwe hakujibu kitu, bali alizidi kupumua kwa haraka haraka, huku macho yake yakiangalia mbele zaidi ya pale alipokuwa mwenzake, kama kwamba hakumuona wala kumsikia Hanga! Haraka Hanga alichukua gilasi ya maji na kumpa mwenzake huyo anywe, akihisi huenda akajisikia nafuu kidogo. ”Hebu kunywa maji kidoga, labda yatakusaidia.” Kibwe aliyapokea yale maji bila kumwangalia mwenzake, na akanywa funda mbili, na halafu akajilaza kitandani. “Unajisikiaje hivi sasa Kibwe? Ni ndoto gani uliyoota?” Hanga aliuliza, akiwa na wasiwasi na jinsi alivyomuona mwenzake. Kibwe alikohoa kidogo, na kisha akaanza kuongea.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog