Search This Blog

KIBWE KATIKA SAFARI YA AJABU - 3

 







    Simulizi : Kibwe Katika Safari Ya Ajabu

    Sehemu Ya Tatu (3)



    “Naona huu ni wakati muafaka wa kutumia upanga wangu.” Kibwe aliwaza, halafu akatoa upanga wake katika ala na kugusa ile sehemu ya vitasa vya lango kuu, na mara zikatokea cheche, halafu lango likajiachia na Kibwe akaweza kulifungua kwa urahisi mkubwa. Taratibu aliingia ndani ya uzio, alikokuta sebule kama uwanja mkubwa mno, iliyojengewa mabomba mapana na marefu kupita kiasi, yaliyotoa moshi mnene mweusi mno!. Moshi ule ulionekana ukipotelea juu mno kwenye majabali na miamba iliyouzingira mji wa Baharia. Mabomba katika ile maabara yaliunganishwa kwenye maguduria makubwa na mitungi ya shaba vilivyoinjikwa kwenye majiko au mafiga yaliyotowa moto mwingi mkali sana!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nitakapofika karibu na yale mafiga tu, kazi yangu itakamilika.” Aliwaza Kibwe lakini akiwa na hofu na wahaka mkubwa. Je, yale majini yakitokea kabla hajatekeleza kazi yake ya kumwaga mavumba kwenye moto? Itakuwaje? Hata hivyo, alipiga moyo konde na kwa umakini mkubwa, alinyata hadi mahali palipoinjikwa yale masufuria, maguduria na mitungi ya shaba, moyo wake ukikimbia kwa kasi mno! Aliangalia huku na kule kuhakikisha kuwa hakukuwa na hatari yoyote. Alipoona kuna amani, akatoa fumba la mchanganyiko wa uvumba , udi na ubani kutoka kwenye mfuko wake alioubeba mgongoni na haraka alilitupia motoni. Halafu lo! Mara moja ulitokea moshi mnene uliotanda eneo lote, na uliopanda juu kabisa ambako ule moshi wa vichafuzi vya hewa ulikokuwa ukiyoyoma!

    Moshi ule wa mavumba ambao ni hatari kwa wale viumbe wa ajabu, ulikwenda hadi kwenye yale makasri ya majini ya fahari , yaliyojengwa juu ya vilima tambarare, na ukayaathiri vibaya sana majini hayo kwani walipaliwa na wakakohoa bila kizuizi, huku wakishindwa kupumua vizuri. Wote walipaparika, na kuamanika, wakigombea milango ya kutokea nje ya majumba yao, ili kujinusuru. Baadhi yao waliofanikiwa kutoka wakiwa katika maumbile ya majoka kamili, walimuona Kibwe akitokea kwenye maabara yao, na wakatambua kuwa mwanadamu yule ndiye aliyehusika na janga linalowasibu.” Niteaufm karaha! Niteaufm vihi asas!”(mfuateni haraka! Mfuteni sasa hivi!) Majini yale yaliamrishana kwa lugha yao, huku yale yaliyogeuka nyoka halisi yakitambaa kwa kasi kumfuata Kibwe, na yale yaliyobaki kuwa nusu watu na nusu majoka, yalimkimbilia kama upepo, yakitowa pumzi ya moto uliofika mbali mno, na kumkosakosa Kibwe kwa sentimita chache sana!

    Wakati majini yakiazimia kumuadhibu mwanadamu yule mchokozi, Kibwe naye alikimbia kufa na kupona, kwani alitambua kuwa tayari nyuma yake kwa yale majini, aliacha maafa makubwa na hasara isiyoelezeka . “Wakinikamata tu, utakuwa ndio mwisho wang……” Kabla hajamalizia kusema neno la mwisho, moto mkubwa ulioelekezwa kwake ulimjia kwa nguvu na kasi ya ajabu!

    “Ooooooo! Whuuuu.uuuuuu!” Kibwe alipiga ukulele uliochanganyika na pumzi aliyoitowa kama mluzi, kama mtu anayepumua, akihofia kile kitakachofuatia, na akijitahidi kuukwepa ule moto! Assalalaaaa! Kibwe alishangaa kupita kiasi! Mara moja aliona mambo yakibadilika, kwani ule moto waliopumua majini, uligeuza njia na kuwarudia wenyewe, wengi wao wakiungua vibaya sana! Kilichotokea ni kwamba wakati Kibwe aliposhtuka na kuona mienge ya moto ikimwandama, na alipopumua kwa nguvu kwa kupiga mluzi mkali, mluzi ule ulisababisha hewa iliyomzunguka kujikusanya mbele yake, na halafu wakati uleule nguvu za mluzi wake ukasukuma hewa iliyopeperusha mienge ya moto uliokuwa ukimfuata kwa ajili ya kumteketeza! Kwa mastaajabu makubwa, alishuhudia moto ukiyageukia yale majini na kuyaunguza unguza vibaya sana!

    Tukio lile la kimiujiza lilihusika sana na maajabu ya Mwana Mteule ambayo Kibwe hakuwa na habari nayo asilani! Hata hivyo Kibwe hakutaka kuwa karibu wakati wale viumbe hatari walipoanza kumfuata ili kulipizia kisasi! Hakupoteza muda bali alitimua mbio za ajabu na wakati ule aligundua muujiza mwingine tena. Alipokuwa akikimbia alihisi kwamba ingawa wakati fulani alikuwa akikimbia kama mtu wa kawaida, lakini mara nyingine alijiona akielea angani kama mwewe! Hakuwa na muda wa kujiuliza chochote kuhusiana na maajabu yale mengine, bali alikimbia tu, mara akipeperuka kama kipepeo na mara akikimbia kwa kutumia miguu yake kama kawaida, akifuata njia iliyomfikisha nchini Baharia, ili aweze kutokea ufukweni alikoingilia. Lakini lo! Kwa bahati mbaya Kibwe alipotea njia na kutokea kwenye eneo la makorongo ambayo awali hakuyaona! Makorongo yale yalipasua miteremko ya ardhi iliyotoka kwenye mwambao wa ufukwe!

    Kibwe alizidi kufuata njia ile ya korongoni kwani hakuwa na muda wa kuamua vinginevyo. Lakini kwa bahati, wakati fulani alihisi kuwa aliruka juu mno kama mtu aliyekuwa na mbawa, na kisha kama samaki nyangumi, akayavuka maji ya bahari ambayo awali yalikuwa juu ya kichwa chake kama paa la nyumba. Kwa kuyavuka yale maji ya bahari, Kibwe akajikuta nje kabisa ya maji yale, na kufikia juu kabisa ya moja kati ya majabali aliyoyaona awali kabla ya kuingia nchini Baharia.

    “Wooo—woooo—wooooo Aaaaaaaaagh! Wooooo—woooo—woooo…..Aaaaaaaa!!” Kibwe alilalama wakati akipaa juu kimiujiza! Alimshukuru sana Mungu wake kwani tukio lile lisilokuwa la kawaida lilimrahisishia mno azma yake ya kuwakimbia wale viumbe wa kipekee, pamoja na kwamba lilimstaajabisha sana.

    “Hakika leo ni siku ya maajabu makubwa kwangu!” Kijana yule alisema na nafsi yake, moyo wake ukidunda kwa kasi!

    Akiwa juu ya jabali na baada ya kuangaza huku na kule, Kibwe aliaona mlango wa pango kubwa la tumbawe na mawe magumu.

    “Yoohu! Yoohuu! Nieizum….nieizum (Mzuieni! Mzuieni! Huyoo! Huyooo)!”

    Kelele za majini zilisikika nyuma ya Kibwe, wakati mienge ya moto ikielekezwa kule alikokuwa. Majinni yaliyonusurika na moshi wa mavumba, nayo yaliruka kama popo kumfuata Kibwe kwa hasira, ambaye alijaribu tena zile mbinu za kuupuliza ule moto wa majini kwa nguvu zake zote. Lo! Faraja ilioje! Mbinu zile zilifanikiwa na kusababisha moto uliokusudiwa kumteketeza Kibwe kuyarudia yale majini kama ilivyokuwa mwanzoni, na kuyaunguza vibaya sana. Kibwe alitumia wakati ule kuingia haraka kwenye ule mlango wa pango aliloliona, ili kunusuru maisha yake. Alipoangalia mle pangoni hakuweza kuona chochote kutokana na giza nene lililotanda. Alipokodoa macho yake kwa muda mrefu ili kujaribu kuyalazimisha kulizowea lile giza, taratibu alifanikiwa kuona njia nyembamba mbele yake. Bila kusita haraka sana alianza kutembea kwa hatua za haraka haraka akiifuata ile njia, bila kujua ilikua akielekea wapi. Halafu akaanza kukimbia kutokana na hofu ya yale majini aliyoyaacha nyuma yake. Hata hivyo, kadiri alivyozidi kukimbia na kuifuata njia ile nyembamba mle pangoni, ndivyo giza nene lilivyozidi kutanda upya!

    Alipokuwa katika lile giza nene, Kibwe akakanyaga mahali palipojiachia ghafla, na mawe ya mahali pale yakaanza kuporomoka pamoja naye kwa mwendo wa kasi bila kizuizi, yakienda sanjari na ufa uliokuwa juu ya miamba minne iliyoning’inia, ikibembea huku na kule, kila mwamba ukiiinuka kwa uimara mkubwa, na kuishia katika wangwa wa maji, kama mita thelethini chini ya mahali ambapo Kibwe alianzia kuporomoka.

    “Aaaaaagh! Aaaagh! Mama yangu weee! Nakufaaaa….mim mimiiiii!” Kibwe alipiga ukelele huo kwa taharuki na alipojaribu kukamata mizizi iliyokuwa ikining’inia kutoka juu yake alishindwa, kutokana na kasi ya kuporomoka kwenda chini. Lakini ghafla bila kutarajia, mkono wake ukakamatwa madhubuti na kitu asichokifahamu! Kibwe alishituka mno! Wakati ule alikuwa akining’inia baina ya juu na chini ya jabali refu mno! Alipata hofu zaidi alipohisi joto kali juu ya kichwa chake, lililotokana na moto waliopumua wale viumbe wenye hasira naye….majini!

    Kile kitu kilichomshika mkono wake kilimning’iniza kwa nguvu kama mtu anaebembea, na kisha kikamrushia kwenye jabali jingine upande wa pili, katika mwamba uliokuwa na sehemu ndogo ya ardhi tambarare mithili ya rafu, na hivyo kumnusuru asiangukie kwenye wangwa, chini ya lile jabali refu kupita kiasi! Alipoangalia upande wa jabali alikotokea, Kibwe aliona kitu cha ajabu kikibembea, na kikijirusha kutoka katika mti mmoja kwenda mwengine, kwa kutumia mizizi ya miti iliyokua ikining’inia, kama kwamba kitu kile kilikua kikijiandaa kurudi juu ya lile jabali refu kabisa mithili ya gorofa. Halafu Kibwe akatambua!

    “Haa! Ndio maana nimenusurika!” aliwaza kwa furaha!

    Mbele ya macho yake, kile alichodhania kuwa ni kitu cha ajabu kikibembea huku na kule, hakikuwa kitu, bali alikuwa ni rafiki yake mpenzi ‘Bunga!’

    Alimrukia na kumkubatia kwa furaha kubwa sana, na Bunga akawa anamcheka tu.



    HANGA NA NJIA YA MAKUTANO.



    Kule pangoni kwa bibi kizee, Hanga aliyatafakari maelekezo yake kabla hajaendelea na safari.

    “Huko mjukuu wangu ni kwenye milima ya moto ya maangamizi kwa binadamu. Daima uovu haulali mahali pale wala hausinzii! Hewa ya huko ni ya sumu hatari! Ni mahali ambapo licha ya kunyesha mvua ya kawaida, mara nyingine hunyesha mvua ya mawe na majabali. Kumbuka tu kuwa mahali unapotaka kwenda hakuna heri, bali kumetawaliwa na uovu mtupu!”

    Usia ule wa bibi wa pangoni ulimtia wasiwasi mkubwa yule kijana, hasa bibi yule alipomalizia usia wake kwa msisitizo kwamba ‘kila waendao kule hawarudi wao, ila hurudi majina yao tu!’

    Dah! Hanga alijilaumu sana kwa uamuzi wake wa kwenda ‘Msitu wa Kindumbwe’.

    “Ama kwa hakika nimejitosa katika janga kubwa mno!” Alijisikitikia moyoni.

    Lakini pia alitambua kuwa ‘maji ukiyavulia nguo, lazima uyaoge’. Kwa hiyo alimwambia yule bibi mzee kuwa angejitahidi kuwa mwangalifu sana katika safari yake, kwa hiyo amwelekeze tu, jinsi ya kufika mahali panapohusika. Yule Kizee alinyoosha mkono na kuonesha kidole chake kwenye moja ya vichochoro vya mle pangoni akasema, “ Fuata ile njia katika uwazi unaoelekea kwenye uchochoro wa upande wa kaskazini. Njia hiyo ni ndefu mno na yenye giza nene. Watu huiita njia ile, ‘Njia ya makutano,’ kwani njiani hukutana na vitu au watu wasiowatarajia. Baada ya kutembea kwa masafa marefu sana utatokea kwenye kuta ndefu za moja kati ya majabali meusi kwa upande wa ndani wa uwanda wa ‘Paa la Dunia’, na humo utakuta ngazi za mawe. Ukipanda kwenda juu kabisa ya uwanda ukiwa humo ndani, utakuta mlango wa kuingilia kwenye hilo pango unalolitafuta, la sanamu la kichwa cha Simba. ”

    Woga ukamtawala Hanga. Hii safari ilizidi kuelekea kuwa ngumu kwake.



     Ukipanda kwenda juu kabisa ya uwanda ukiwa humo ndani, utakuta mlango wa kuingilia kwenye hilo pango unalolitafuta, la sanamu la kichwa cha Simba. ”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Woga ukamtawala Hanga. Hii safari ilizidi kuelekea kuwa ngumu kwake.



    Baada ya maelekezo yale bibi yule aliendelea kumtahadharisha kuwa humo atakamopita huenda akakutana na kibwengo mmoja mbaya na laghai sana, ambaye naye ni mjumbe wa shetani au pepo muovu wa ‘ulimwengu wa zama za kale’ ambaye pia ni mfalme wa kidani anachokifuata.

    “Anaweza kukudanganya ili akichukue yeye kile kidani kwa lengo la kuuficha ukweli ulioandikwa ndani ya kidani hicho, ili tu kuipotosha jamii katika sayari yetu.” Bibi alimtanabahisha kuhusu huyo Kibwengo laghai, na macho yakazidi kumtumbuka Hanga.

    Jambo jingine lililompa hofu zaidi Hanga ni kufahamu kuwa huko aendako, wapo mazimwi wanaoongozwa na shetani au pepo huyo muovu wa ‘ulimwengu wa zama za kale,’ wanaokilinda kidani kile kisiangukie mikononi mwa watu wema. Nia yao, alisema yule bibi, ni kukitekeza kwa moto kwenye milima ya maangamizi, kusiwepo na uwezekano wowote wa mtu yeyote kufanikisha nusra ya sayari yao. “Kwa kuwa wao hawawezi kukifikia pale kilipo’ kutokana na laana waliyoipata miaka mia moja iliyopita kwa kusaidia kuiteketeza nchi moja mashuhuri ya Sabaa wakishirikiana na majini wa nchi ya Baharia, ndio maana wanawavizia watu wema watakaofanikwaa kukichukua kidani hicho, ili wawapore.” Kutokana na maelezo yote yale, Hanga alimaizi uovu mkubwa unaoikabili sayari yao na watu wake, akihofu kwamba huenda kazi ya kuipata nusura ya jamii yake ikawa ni ngumu mno!

    Wakiagana pale pangoni yule bibi kizee alitoa kito kimoja kikubwa cha thamani chenye ukubwa wa komamanga na chenye umbile la alimasi, akamkabidhi kijana yule na kumwambia, “Kwa kuwa njia yote kuanzia hapa tulipo ni giza tupu, na kwa kuwa mara kwa mara huenda ukakabiliana na viumbe wengi waovu, kito hiki kitakuwa ni mwanga katika sehemu za giza nene si kwa kuwamulika tu viumbe hao, bali pia kwa kuwadhibiti wote wasioitakia heri sayari yetu!”

    Pia alimwambia kuwa atakapofika langoni mwa pango analolitafuta, lazima aseme neno la mazingaombwe ndipo lango lile litafunguka ili aingie kwenye sanamu la kichwa cha shaba cha simba. “Lazima useme neno “Lyang’andu” mara tatu.” Alimwambia, na kumuuliza mara mbili iwapo amemuelewa.

    Hanga akamhakikishia kuwa amemuelewa.

    “Haya buriani mjukuu wangu, nenda salama.” Hatimaye bibi alimuaga.

    “Buriani dawa bibi yangu. Tutaonana Mungu akipenda!” Hanga alimjibu kwa shukurani kubwa . Wakati akimuaga kwa maneno hayo, hakuacha pia kuwaza na kujiuliza kuhusu ubinadamu wa bibi yule, kwani alimuona kuwa hakuwa wa kawaida. Haraka sana aliondoka na kuelekea kwenye moja kati ya vile vichochoro vilivyokuwa na giza totorooo, ili aachane na kizee yule wa pangoni aliyemhofu sana!

    Hanga alivipita vichochoro vya mle pangoni vilivyomfikisha kwenye mapango mengine mengi. Aliifuata njia ya makutano kama alivyoelekezwa, akavuka vijito vilivyoshehena mawe na tope, hali iliyoifanya safari yake mle mapangoni kuwa ngumu sana. Hapa na pale kwenye njia ile nyembamba iliyogubikwa na giza la ajabu, miti mirefu mno na minene iliupamba msitu ule wa kipekee. Ingawa alikuwa na hofu kubwa, lakini Hanga aliendelea na safari yake, wakati macho yake yakimudu kuona mahali alipokanyaga tu kutokana na lile giza. Mara nyingine alitumia kile kito alichopewa na mzee wa pangoni, lakini hata hivyo bibi yule alimtahadharisha kuwa asikitoe mfukoni kito hicho mara kwa mara, kwani huenda mwanga wake ukamfanya aonekane kwa urahisi na wajumbe wa shetani au ‘pepo wa ulimwengu wa zama za kale.’ Kwa hiyo mara nyingi Hanga alilazimika kutembea kwa shida sana gizani.

    Wakati Hanga akitafakari kuhusu onyo la yule kizee, mara moyo wake ulichupa, kwani ghafla alihisi kama kwamba ameona vivuli vya watu!

    “Ni watu kweli?” aliwaza.

    “Lakini labda si watu! Au tuseme wanyama! Lakini mmh….labda si wanyama…….! Mbona wana mikia mirefu sana?” Mawazo hayo yalipita kichwani kwa Hanga huku akitetemeka na kugwaya kwa hofu.

    Kwa bahati mbaya hakuweza kuona vizuri ni vivuli vya viumbe wa aina gani alivyoviona kwa sababu ya lile giza. Katika njia ile ya Makutano, vivuli hivyo vilipita katika upeo wa macho yake kwa kasi kama upepo!

    “Chukua kito hiki na inshaallah kitakuwa ni mwanga wakati kila mahali patakapokua giza…..”

    Hanga alipoyakumbuka maneno ya yule bibi wa pangoni haraka akakitoa kile kito na halafu mara moja katika sekunde chache zilizofuata, nuru ilizagaa msitu wote wa mle pangoni na kumwezesha kuwaona vizuri sana viumbe waliokuwa wakubwa mno na wa ajabu, wenye maumbule ya nyoka kuanzia tumboni kwenda kichwani, na maumbile ya wanadamu kushuka miguuni, isipokua walikuwa na mikia mirefu sana! Katika muda ule wa sekunde chache sana viumbe wale walitokomea msituni, wakimwacha Hanga dhoful hali kwa hofu, mwili wake wote ukizizima!

    ***

    Naam, Hanga alipokuwa pangoni chini ya ‘Paa la dunia,’ Kibwe naye alikuwa nje ya lile pango juu ya ‘Paa la Dunia’, kulikokuwa na minara pacha mitatu mirefu kupita kiasi! Minara ile ilisimikwa kama mafiga, na katikati yake kilikuwepo kitu kama kigoda cha vito vya thamani. Ile ilikuwa ni sehemu maalum iliyoutoa moshi mnene wa vichafuizi vya hewa ya ozoni kutoka kwenye maabara ya majini kule chini kabisa ya bahari nchini Baharia, ambako Kibwe alipambana na majini na kuiteketeza maabara yao.

    “Lazima nifike juu ya kile kigoda kwenye minara mitatu, kama nilivyoelekezwa na mzee Bunga.” Kibwe aliwaza. Kibwe alilazimika kufika kwenye minara akitokea juu ya uwanda mrefu kupita kiasi, uliogawanyika katika safu kama ngazi kwenye miamba minne, kila mmoja ukianzia pembezoni mwa uwanda kwa utaratibu maalum. Ilimlazimu Kijana yule kuivuka miamba ile myembamba iliyokuwa ikining’inia, kwa kubembea huku na kule. Kwa hiyo alijishusha kwa umakini mkubwa sana akiponea chupuchupu kuangukia chini kabisa kwenye umbali wa zaidi ya mita alfu moja!

    Kwa kuwa kila mwamba uliinuka kwa uimara mkubwa kutokea korongoni, kwa kufuata maelekezo ya Bunga, Kibwe alijitahidi kwa nguvu na hekima zake alizokuwa nazo, kuifikia ngazi ya mawe iliyokuwa katika moja ya ile miamba, na kutafuta mbinu za kufika karibu na usawa wa ile minara pacha, ingawa chini ya ile miamba kuliwa na korongo moja kubwa mno la hatari, kama mtu angeangukia humo kutokea juu alikokuwa yeye. Kijana yule shujaa aliweza kuifikia ile ngazi ya mawe katika moja ya ile miamba. Lakini masikini, kwa sababu maji ya kijito yalitiririka kila siku yakamwagikia kwenye zile ngazi na kusababisha utelezi hatari, mara Kibwe alipokanyaga jiwe moja la ngazi za moja kati ya miamba ile, mguu wake uliteleza, akaanza kuporomoka! Moja kwa moja alianguka akipitia eneo lenye mwanya au ufa mwembamba ulioongezeka upana kwa chini alikokuwa akiporomokea. Katika safari ile hatari akiporomoka kwenda chini, alipambana na maji yaliyokuwa yakiporomoka kwa nguvu mno kutokea juu kabisa ya uwanda! Aliogopa kupita kiasi na wakati alipokuwa akitapatapa kutafuta njia ya kujinusuru, haraka alikamata mzizi mwingine mnene uliokuwa ukining’inia, akabembea nao akiangalia kwa uangalifu na kutafuta ni mahali gani pa kurukia.

    Kibwe alifahamu kwamba kwa kujining’iniza vile, alikuwa katika hatari ya kuporomokea chini kwa umbali mkubwa sana, ambako yalikuwepo mawe makali na sehemu nyingine kukiwa na mchanga didimizi hatari. Kibwe alihofia sana kupoteza maisha yake! Kwa kuwa alitishika mno na mawazo hayo, alibembea na kujirusha upande mwingine wa ule ufa wa mwambani, akafikia kwa kishindo kwenye lango la pango moja jingine kubwa, katika moja ya safu iliyoligawanya moja ya majabali meusi. Pale langoni alipofikia, Kibwe alijaribu kuangalia ndani ya pango lakini kwa giza lililokuwa mle ndani hakuweza kuona chochote, bali alihisi kama kwamba amemuona mtu amesimama kwa mbali kidogo, akiangalia kwenye mlangoni wa pango alikofikia yeye. Kibwe alipatwa na hofu na wahaka mkubwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ni nani tena yule mle pangoni? Ni mtu au ni jini? Au ni mmoja kati ya yale majini yaliyokuwa nyuma yangu, anaesubiri kulipizia kisasi kwa matatizo niliyowasababishia kwao? Sijui nimejitosa wapi tena?” Maswali mengi yalimzonga kichwani mwake. Alijaribu kugeuka ili kutafuta njia ya kuondoka pale alipokuwa na kurudi alikotoka, lakini lo! Mara akasikia mlipuko mkubwa wa kushtusha ulioambatana na mviringo mkubwa wa moto iliomwelekea pale alipokuwa! Hapo hapo akajirusha haraka ndani kabisa ya lile pango kubwa kujinusuru!

    MAANDIKO YA AJABU.

    Wakati Kibwe anakurupushwa na lile viringo kubwa la moto kule alipokuwa, huku kwa Hanga nako kulikuwa kuna yake.

    Hanga alikuwa akizipanda zile ngazi za mawe zilizojitokeza mle pangoni chini ya ‘Paa la Dunia,’ ndani ya ule uwanda mrefu akiwa mwingi wa wahaka na aliyetekwa na hofu kubwa.

    “Labda hizi ngazi zitanifikisha sehemu ya ule mlango alioniambia bibi kizee wa pangoni.” Aliwaza, huku taratibu na kwa tahadhari kubwa, akienda juu zaidi ya lile jabali.

    Giza lilipozidi kijana yule alitoa kile kito alichopewa na kizee pangoni, kilichotoa nuru kali iliyomuonesha njia. Alipanda kwa masafa marefu sana hadi miguu yake ikapooza na kupata ganzi kwa uchovu! Alikuwa akipanda jabali la urefu wa takriban gorofa ishirini, na wala hakuwa na fununu ya mwisha wa safari yake!

    “Subira mjukuu wangu! Subira pekee ndiyo itakayokusaidia kukamilisha jukumu lako!”

    Alikumbuka usia wa bibi kizee wa pangoni, mara baada ya kupewa maelekezo ya safari yake. Akiwa katika tafakuri ya usia ule, mara hatua chache mbele yake akaona mlango mkubwa wa mawe ya tumbawe! Alihisi kuwa bila shaka ule ulikuwa ndio mlango wa kuingilia kwenye pango la sanamu la shaba la kichwa cha Simba, ambako ndiko alikokuwa akielekea.

    Pale langoni alijaribu kukumbuka lile neno la mazingaombwe aliloambiwa aliseme, ili mlango wa kuingilia pangoni ufunguke….! Kwa bahati nzuri baada ya kukuna kichwa kwa muda fulani, Hanga alilikumbuka lile neno na akalitamka mara tatu.

    “Lyang’andu! Lyang’andu! Lyang’andu!”

    Lo!

    Kama muujiza baada ya kama sekunde thelathini hivi, jiwe la pango lilianza kuzunguka taratibu likitoa mlio kama mtu anayesaga mtama kwa jiwe! Lango lile lilipofunguka Hanga hakuamini macho yake! Mle pangoni aliona sanamu kubwa kupita kiasi la kichwa cha shaba cha Simba, lenye urefu uliokuwa mara tatu ya urefu wake yeye! Iilikuwa na sura ya Simba kabisa, lenye macho mekundu kutokana na vito maalum vilivyong’ara, ndevu za shaba na vidani vitatu vya fedha vya sanamu za kucha za simba vyenye ukubwa wa tunda la zaituni, vikining’inia kwenye mkufu mrefu wa fedha.

    Naam, Hanga alifarijika mno kujikuta mahali pale ambapo ndipo hasa palipokuwa kiini cha safari yake! Pamoja na wahaka na wasiwasi wa hatari nyingi zilizohusiana na sehemu ile aliyofika kwa mujibu wa onyo la bibi kizee wa mle pangoni, kwamba daima mahali pale uovu hausinzii wala haulali, na hewa ya sehemu ile kuwa ya sumu, lakini Hanga alihisi kuwa jambo muhimu ni kwamba alikaribia kupata jibu la uovu na majanga yanayoikabili sayari yake!

    Lakini kwa bahati mbaya, kati ya mahali aliposimama Hanga na mahali lilipokuwa lile sanamu, ulikuwepo uchochoro au ufa kama mfereji. Wakati akiwaza jinsi ya kuvuka na kufika pale lilipokuwa lile sanamu, ulisikika mwaliko wa mawe yaliyogongana na kutoa mlio kama mtambo wa aina fulani. Mwaliko ule ulipoendelea ulifuatiwa na mtikisiko mkubwa wa ardhi! Hanga aliduwaa! Aliogopa sana. Alijaribu kuelewa ni nini kilichosababisha mwaliko ule, na ulianzia wapi! Alihisi kuwa huenda ulitokea kwenye Paa la lile pango! Wakati yote yale yakitokea, Hanga alikuwa juu kabisa ya jabali, alikofika kwa kupitia pangoni, ndani ya jabali hilo la uwanda wa Paa la Dunia! Akiwa kule alibaini jambo moja la kutisha sana! “Haa! Hivi hapa nilipo ni baina ya milima ya maangamizi na uwanda wa Paa la Dunia kama alivyosema ….”

    Kabla hajatafakari zaidi, taratibu paa katika lile pango lilianza kuporomoka, na mawe ya matumbawe yakajiachia, yakisababisha nafasi ya chini alikosimama Hanga kupungua, wakati paa lile likikaribia kichwani kwake!

    Haraka sana kijana yule aliinama kujinusuru, na wakati uleule akijaribu kuuvuka ule ufa miguuni mwake, ulioandaa hifadhi ya maji kama kijito! Ingawa Hanga hakuwa na uhakika wa kina cha kijito kile, hakuwa na la kufanya bali kujitosa na kuvuka!

    “Huenda nikivuka kijito hiki itakuwa ni mwisho wa maisha yangu lakini kurudi nyuma siwezi kwani paa limeshuka mno!” Aliwaza kwa hofu, akihisi kuwa angeweza kuzama kwenye kile kijito, na lile pango likawa ndiyo kaburi lake!

    Kwa simanzi kubwa, na kwa mara ya kwanza kabisa kijana yule alikumbuka maneno ya kibibi Ajuza nyumbani kwao Hazina, aliyemwambia, “Nenda mjukuu wangu na utakapokuwa huko ndipo utakapotambua kuwa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu!”

    Hanga aliyekuwa mgumu kuelewa kwa haraka maana za methali, mara kwa mara alijiuliza kuhusu maneno ya busara ya kibibi Ajuza, kila alipopambana na matukio kadhaa katika safari yake.

    “Ndio kusema kuwa hivi sasa ulimwengu unanifunza? Na je, ulimwengu wenyewe uko wapi sasa? Maana….” Hakuendelea na tafakuri yake kwani ghafla liliporomoka jiwe kubwa kutoka juu na alipotaharuki, aliona paa likizidi kushuka kwa mwanguko wa hatari mno! Bila kuwaza, alijitosa ndani ya kile kijito! La haula! Karibu mwili wake wote uligubikwa na yale maji, yakasaza sehemu ya kifua na kichwa tu! Alijaribu kutembea ili avuke kwa upande wa pili wa kijito kulikokuwa na lile sanamu, lakini hakuweza kufanya vile kutokana na kina cha maji, na kwa bahati mbaya hakuweza kuogelea! Alianguka chini akatambaa kwenye kijito huku mara kwa mara akimeza maji na kukosa uwezo wa kupumua vizuri.

    Alijaribu kutembea ili avuke kwa upande wa pili wa kijito kulikokuwa na lile sanamu, lakini hakuweza kufanya vile kutokana na kina cha maji, na kwa bahati mbaya hakuweza kuogelea!

    Alianguka chini akatambaa kwenye kijito huku mara kwa mara akimeza maji na kukosa uwezo wa kupumua vizuri. Kina cha maji kilipoongezeka kilitishia zaidi maisha ya Hanga. Kadiri kina kilivyozidi kuongezeka, ndivyo alivyoinuliwa kwenda juu. Kwa bahati lile paa la pango kwa upande aliokuwa akipelekwa na maji, lilishikiliwa barabara na lile sanamu kubwa la shaba la kichwa cha Simba, likazuia paa lile kuporomoka zaidi.

    Maji yalipozidi kujaa yalimwinua Hanga hadi juu kabisa ya ule mwinuko wa matumbawe, uliokuwa sanjari na lile sanamu kwa juu ya paa la lile pango. Kwa bahati kule juu ndiko kulikokuwa na kifyatuzi cha kukamilisha kazi iliyompeleka Hanga sehemu ile hatari.

    “Ah! ni bahati ilioje hii!” Aliwaza kwa furaha, pamoja na uchovu mkubwa aliokuwanao. Alipoangaza angaza aligundua kuwa nyuma ya, lile sanamu lilikogubika sehemu kubwa ya pango, kulikuwa na uwazi mwingine mkubwa kama mlango, ambao Hanga alihisi kuwa bila shaka mtu angeweza kutoka mle pangoni kwa kutumia njia ya upande ule, baada ya kuingia kwa kupitia kwenye ule mlango uliofunguka kwa neno la mazingaombwe, ‘Lyang’andu!’. Hanga alihisi upepo mwanana ukivuma kutokea kwenye uwazi ule, ulioashiria kuwa ule uwazi ulikuwa umeelekea kwenye ufukwe wa bahari. Hata hivyo Hanga alibaini moshi mnene sana uliotanda nje ya pango katika upeo wa macho yake kuelekea baharini! Jambo lile lilimkatisha tamaa kabisa!

    “AH! Ndio kusema nimechelewa kufika mahali hapa? Mbona tayari sayari yetu imeanza kuteketea jamani? Hivi safari yote niliyoifanya ni ya bure?” Alijiuliza maswali hayo kwa kusononeka kukubwa kabisa.

    “Kama kazi hii sikuifanya mimi ataifanya nani tena? Hapana, si vizuri kukata tamaa! Lazima nifanye kile ninachoweza kukifanya ili kufuatilia jambo hili kwa makini!” Alikata shauri. Akajitosa kutafuta faraja, ingawa kwa kawaida yeye alikuwa mwoga sana na mwenye wasiwasi mkubwa yanapotokea mambo ya kutatanisha .CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa kuwa maji ya kijito yaliyoongezeka, yalimfanya Hanga ainuliwe hadi kwenye mwinuko wa ardhi tambarare kwa upande mmoja wa sanamu la kichwa cha Simba, taratibu kijana yule alijisogeza na kujipandisha juu zaidi ya matumbawe yaliyokuwa yakitereza mno na kuifanya kazi ile kuwa ngumu sana. Hatimae aliposimama juu kabisa na kuweza kufikia kwenye usawa wa masikio ya lile sanamu la Simba lililoegemea pembezoni mwa ukuta wa lile pango, akaona kifyatuzi cha pembe tatu.

    “Ni kifyatuzi kitakacho elekeza ni kipi katika vidani vitatu vya sanamu za kucha za Simba vinavyoning’inia katika mkufu wa fedha kina ujumbe maalum!” Hanga aliwaza, akikumbuka maelekezo ya awali ya kibibi Ajuza kuhusu sahamu lile la aina yake.

    “Ili kutambua ni kipi katika vidani vile kina ujumbe unaohusika, utazungusha kifyatuzi maalum cha jiwe chenye umbo la pembe tatu, kilichopo pembezoni mwa sanamu. Kwa kufanya hivyo, utafyatua mtego uliopo juu ya sanamu lenyewe katika paa la pango lile. Kitendo hicho kitasababisha mwanga wa jua kutoka mbinguni upenye na kung’ara kwenye vidani vya fedha vya kucha za simba, na ni kimoja tu, kati ya vidani hivyo na chenye kito cha rangi ya samawati ndani yake, kitatoa nuru. Hiyo itaashiria kuwa hicho ndicho kidani unachokihitaji, na ndicho kilichoandikwa huo ujumbe wa kuitahadharisha jamii kuhusu madhara yanayoikabili sayari yao, na ni kwa sababu gani…”

    Baada ya tafakari ya maneno yale, Hanga alijisogeza taratibu akisaidiwa na ujazo wa maji ya kijito, ambayo hakufahamu yalitokea wapi, akajikweza juu ya mwinuko wa matumbawe, akijaribu kufika kwenye kile kifyatuzi, ili kuendelea na zoezi aliloazimia kulifanya.

    Alipofanya kama alivyoelekezwa na kizee Ajuza ili kukitambua kidani chenye yale maelezo muhimu, mtego ulijitegua na jiwe moja katika sehemu ndogo ya paa la pango likajiachia na kudondoka, likiacha wazi tundu dogo lililopenyeza mwanga wa jua kutoka mbinguni. Mwanga ule ulipovimulika vile vidani vitatu vya fedha vya kucha za simba, kimoja miongoni mwavyo kilianza kutoa nuru ya rangi ya samawati, iliyotokana na kito maalum cha rangi hiyo kilichokuwa ndani yake. Ghafla katika upande uliojikunja wa kidani kile cha umbile la ukucha wa Simba, yalijidhihirisha maandiko makubwa ya rangi ya samawati! “Enheee! Haya ndiyo maandiko yenyewe ninayoyataka!” Hanga alisema kwa furaha, akitabasamu kutokana na faraja aliyoipata. Alizidi kujisogeza karibu zaidi ya kile kidani ili aweze kuyasoma maandiko yale na kutegua kitendawili cha miaka mingi sana kuhusu sayari yao.

    Lakini Loh, masikini! Alipoyaangalia vizuri yale maandiko, moyo wake ukagutuka! Maandiko yale yalionekana kama michoro tu, isiyo na maana yoyote! Hii iliashiria kuwa Hanga asingeweza kuuelewa ujumbe alioufuata kwa kilometa nyinga kutoka kwao, njiani akipitia hatari za kila aina hadi kufika pale alipokuwa! Alipofikia uamuzi huo, hakuwa na la kufanya. Alikata tamaa kabisa ingawa awali hakuazimia kufanya hivyo! Taratibu akaketi juu ya ule mwinuko wa matumbawe mbele ya lile sanamu, akitafakari kuhusu hatima ile, huku akitokwa machozi.

    “Maneno ya bibi 'Ajuza’ ni kweli tupu! Jibu la kitendawili hiki chote analo Mwana Mteule, na wala si mimi! Bila ya yeye kufikia hatima nzuri ya tatizo hili ni kama ndoto tu!”

    Baada ya kutafakari kwa muda wa kutosha, aliamua kuondoka taratibu kutoka mle pangoni kwa kutumia upande wa pili wa lile pango. Pole pole alielekea kwenye ule uwazi mwingine wa kutokea nje. Alitembea polepole akiwa ameinamisha kichwa chake chini.

    Ghafla kishindo kikubwa kikasikika na alipoinua kichwa chake kuangalia mbele kilikotokea na ambako ndiko alikokuwa akielekea, hakuamini macho yake! Kwenye uwazi wa lile pango kwa umbali wa kama mita mia moja hivi kutoka pale alipofika, kilianguka kitu kutoka mahali pasipojulikana lakini nje ya uwazi wa lile pango! Aliruka hatua moja nyuma moyo wake ukikimbia kwa kasi. Alipojaribu kuelewa ni kitu gani kilichoanguka kwa kishindo kikubwa vile na kilichoonekena kuwa na umbile la mtu, mviringo mkubwa wa moto uliotoa mwanga mkali na joto la ajabu ulioambatana na cheche nyingi uliangukia nje ya ule uwazi, ukiacha ndimi za moto zikipeperuka juu. Hanga alihofu kuwa huenda msitu wote kuelekea ufukwe wa bahari umeshika moto. Aliogopa sana lakini zaidi ya yote, alisikitika mno moyoni.

    “Yote haya ni kwa sababu sikuweza kuusoma ule ujumbe kwenye kidani!” aliwaza.

    “Lakini kama kweli yupo huyo Mwana Mteule anasubiri nini kufika huku ambako bila shaka ndilo eneo la utekelezaji wa jukumu Lake? Amekaa tu huko alipo, raha mustarehe akifurahia wadhifa aliopewa, wakati mambo yanaharibika kiasi hiki! Watu wengine bwana! Hawana haya na wala hawaoni vibaya! Angalau mimi nimejaribu kufanya nilivyoweza!” Hanga aliyawaza yote hayo kwa hasira nyingi, na wakati ule akawa anarudi nyuma haraka kule alikotokea ili kunusuru maisha yake kutokana na ule moto hatari uliozuka pamoja na sijui kiumbe gani tu kilichoanguka kwenye lango la lile pango.

    KIBWE, HANGA NA MINARA PACHA.

    Kutoka baharini nje ya lile pango la Sanamu la Kichwa cha Simba, moshi mnene ulizidi kutanda, na wakati Hanga akihofu na kupata wasiwasi baada ya kuhisi kuwa aliona mtu au kitu kimesimama kwa ndani ya mlango wa kutokea mle pangoni, mlipuko mkubwa uliotokana na mviringo mwingine wa moto ulisikika.

    Moto mwekundu sana mithili ya zaha ya volkeno ulijidhihirisha, ukiacha eneo lote likimweka kwa mwanga mkali na kutukutia kwa mvuke hatarishi mno! Ndimi za moto mkali zilitanda pale langoni mwa lile pango, hatua chache kabisa na mahali kilipoangukia kile kitu alichokiona Hanga…!

    Mara kijana yule akashuhudia maajabu makubwa.

    Wakati ule moto ulipoelekea pangoni alimokuwa Hanga, kile kiumbe kilichoangukia kwenye mlango wa lile pango kilitoa pumzi zisizokuwa za kawaida, zilizo upuliza ule moto kwa nguvu, na hivyo kusababisha zile ndimi za moto kupeperuka na kurejea kule zilikotoka! Hanga aliyekuwa pangoni amekodoa macho yake kwenye ule mlango wa pango, alishangaa sana huku akihofia mno maisha yake kwani hakuelewa kilichokuwa kikitokea! Lakini mara, taratibu aliweza kutambua kuwa muujiza aliouishuhudia kwenye mlango wa kutokea pangoni haukutokana na kitu chochote, bali ulitokana na mwanadamu kama yeye, lakini si wa kawaida! Hakufahamu tu kuwa mtu yule wa ajabu aliyeangukia kwenye mlango wa pango alikuwa ni ‘Mwana Mteule,’ Kibwe!’

    Hanga alibaki akiwa amesimama kama kisiki. Hakujua iwapo amkimbie yule mtu ambaye wakati ule naye alikuwa akikimbilia kule alikokuwa yeye, au amsubiri ili amfahamu kuwa yeye ni nani hasa?

    Kibwe naye alipofika karibu na lile sanamu la kichwa cha Simba akashtuka na kushangaa sana kumuona kijana wa rika lake akiwa amesimama mbele yake, akiwa na uso uliojaa hofu isiyosemeka. Huku akipumua kwa kasi kutokana na kuyakimbia yale majini, Kibwe alitumbua macho kama tunguja kumshangaa mwenzake, akili ikimzunguka.

    “Huyu ni binadamu kabisa huyu! Sasa amefuata nini huku?” Alijiuliza bila kuamini kuwa baada ya siku kadhaa za kupambana na viumbe wasiokuwa wa kawaida, hatimae amekutana na mwanadamu! Wakati akijiuliza haya, akamsikia Hanga akitoa sauti ya hofu, iliyotetemeka kwa woga, akimuuliza; “W-wewe n-ni Jini….au n-ni m-mwanadamu…enhh s-samah-han-ni…s-sa-ana!”

    Wakati akiuliza swali lile, Hanga alikuwa akirudi nyuma kidogo kidogo, akijaribu kuwa mbali na Kibwe, aliyemdhania kuwa si mwanadamu wa kawaida.

    “Mimi ni mwanadamu kama wewe ndugu yangu isipokuwa nashangaa kukukuta katika sehemu hii isiyokuwa ya kawaida, maana…” Kabla hajaendelea, Hanga alimkatiza.

    “Ndugu yangu? Ndugu yako mimi? Ah, wee vipi? Sidhani kama wewe na mimi ni ndugu. Hatuko sawa asilani! Mtu dakika chache tu zilizopita nimekuona kwa macho yangu ukizipuliza ndimi za moto mkubwa namna ile kama unayezima mshumaa tu?. Hebu niambie, ni mwanadamu gani mwenye uwezo kama ule, eenh?”

    Kibwe alisita, kwani matukio yale ya ajabu hata yeye yalimkanganya.

    “Amini usiamini ndugu yangu…mimi ni mwanadamu kama wewe na ningependa unitazame kama nduguyo tu…kwani hakika kukutana na binadamu mwenzangu eneo hili ni jambo la faraja isiyo kifani kwangu…” Kibwe alimjibu, na kuendelea kumwambia mwenzake kwamba kwa kuwa tukio lile lilihitaji maelezo marefu, kwanza alipenda kujua ni kitu gani kilichompeleka yeye Hanga mahali pale hatari!

    “Huku ndugu yangu, daima uovu haulali wala kusinzia! Ni mahali ambapo milima yake ina kazi ya kuangamiza watu wema tu, ikiwa ni pamoja na wewe na mimi!”

    Hanga aliyatambua yale maneno kwani aliyasikia awali kutoka kwa bibi kizee wa mlemle pangoni, kwa hiyo alihisi kuwa bila shaka yule kijana ni miongoni mwa wahusika wa eneo lile.

    “Ah! Ndugu yangu wee! Kilichonileta huku ni kusaidia jitihada za kuinusuru sayari yetu, ingawa katika hatua niliyofikia, uwezekano wa kutimiza azma hiyo haupo tena.” Hanga alijieleza kwa masikitiko, na Kibwe alishangaa kusikia vile, kwani mpaka wakati ule, hakufahamu kuwa alikuwepo mtu mwingine mwenye jukumu la kuinusuru sayari, na ambae ni kijana kama yeye.

    Lakini alipomwangalia mwenzake yule aliona kuwa amekata tamaa kabisa, na tena mapema mno katika utekelezaji wa kazi ile nzito.

    “Na kwanini usiwepo uwezekano wa kukamilisha lengo hilo?” Kibwe alidodosa. Hanga alimweleza kuwa katika ufuatiliaji wake wa jambo lile, alipokuta ujumbe uliohusu madhara yanayoikabili sayari yao, hakuweza kuusoma ili aufikishe kwa wahusika watakaoufanyia kazi.

    “Maana maandiko yaliyotumika hayakuwa maandiko yanayoweza kueleweka na mtu wa kawaida kama mimi isipokuwa Mwana Mteule pekee, ambaye kwa kweli sina hata fununu ya mahali alipo!”

    Lo! Kibwe alizidi kushangaa! Bunga asilani hakumwambia vile! Au ndiyo sababu ya yeye kufikishwa kwenye uwanda wa ‘Paa la Dunia’? Alitafakari, na halafu akamwambia Hanga, “Ahhhm! Sasa mwenzangu, kwanza hata jina lako nani?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wale vijana wakatambulishana majina. Baada ya kutambuana, Kibwe akamtoa wasiwasi yule mwenzake kwa kumpa moyo kwamba huenda ukapatikana ufumbuzi, mara baada ya yeye kuyaangalia maandiko yale.

    “Haya…hebu twende ukayaone.” Hanga alimjibu huku akimuongoza kule kwenye kifyatuzi pembezoni mwa sanamu la kichwa cha simba, baada ya kuupanda ule mwinuko wa mawe ya tumbawe ili kufikia pale mahali. Kwa pamoja walipokizungusha kifyatuzi, kama kawaida kikaachia mwanya juu ya paa la pango na kuingiza mionzi ya jua, iliyosababisha kimoja kati ya vidani vitatu venye umbile la kucha za Simba, kitoe nuru ya rangi ya samawati na wakati uleule katika upande uliojikunja wa kidani kile, yalijidhihirisha maandiko ya rangi ya samawati!

    Kwa mshangao mkubwa, Hanga alimsikia Kibwe akitamka maneno haya;

    “Kuungua Sayari, Kuteketea Misitu, Kuongezeka vina vya Bahari!

    Kupotea Visiwa, wanasayari kuteseka!

    Lazima wema uushinde uovu, heshima ikiuke dharau, imani ilete tumaini, na kwa hekima, wanasayari wazitawale tamaa zao!”

    Hanga alipagawa.

    “Hapana! Haiwezekani! Umewezaje kuyasoma haya maandiko? Kama wewe si Mwana Mteule usingeweza kuyasoma maandiko haya hata kidogo! Bila shaka wewe ndiye mteule niliyeambiwa! Ni wewe! Ni wewe nakwambia!” Hanga aliropoka kwa hamaniko dhahiri lililochanganyika na furaha kwa jambo aliloligundua. Alijiona kuwa ni mwenye bahati kubwa na akataka sana kuelewa ni vipi watafuatilia jambo lile baada ya kupata undani walioupata.

    “Huu ni ujumbe wenye maana pana sana Kibwe! Je, tuanzie wapi kuyatekeleza yanayohusika?” Alidadisi Hanga.

    Kibwe alimwangalia kijana mwenzake aliyejawa na shauku ya kuanza harakati za kuinusuru sayari yao. Alijiuliza ni wapi alikotokea mwenzake yule aliyemuongezea nguvu na matumaini makubwa katika kazi yake.

    “Hebu nieleze kisa chako rafiki yangu…ilikuwaje hata ukafika hapa? Na vipi unaonekana kuwa ulikuwa unajua juu ya habari zangu kabla hata hatujaonana?” Hatimaye alimuuliza yule mwenzake.

    Hanga akaketi chini huku akitabasamu.

    “Hakika nitakueleza mwana mteule…kwani na mimi ia nina hamu ya kujua ni vipi ilikuwa hata ukateuliwa kwa jukumu kubwa kama hili…na…na ulifikaje hapa kwa namna ile ulivyofika/ Oh, mbona nina maswali mengi kwako, ewe mwana mteule usifikaye kila kona?” Hanga alimjibu kwa kiherehere.

    Kibwe alimtazama tena yule mwenzake.

    “Dunia inateketea kila dakika zinavyosonga Hanga. Sidhani kama tutakuwa na muda mrefu sana wa kupeana habari zetu. Naomba unieleze kwa kifupi, nami nitafanya hivyo baada ya wewe kumaliza.” Alimjibu.

    Ndipo Hanga bin Sultan alipomueleza kisa chake…kisa kilichomsababisha apate msukumo wa kuifanya safari ile ya ajabu kumtafuta mwana mteule.

    “Na sasa nashukuru kuwa nimekutana nawe Kibwe. Hakika wewe ni mwana mteule wa kweli. Hebu na wewe nieleze kisa chako sasa.” Hanga alimwambia baada ya kumaliza kisa chake, ambacho Kibwe alikisikiliza akiwa kimya kabisa.

    Sasa Kibwe alishusha pumzi ndefu, akajiadaa kumueleza mwenzake kisa chake. Kisa kilichoanzia na nyoka wa baba…nyoka wa baba yake…nyoka kunyenge.

    Na wakati akimsimulia, kwa kifupi kwa kadiri alivyoweza kuifupisha hadithi ile ya maisha yake kabla ya kuwa mwana mteule, Kibwe alijikuta akihama kifikra kutoka kwenye ile sehemu ya ajabu, vitisho, maafa na maangamizo, na kurudi nyumbani kwa baba na mama yake, ambako sasa kulionekana kama kwamba ni sayari nyingine kabisa…

    KUNYENGE NYOKA WA BABA.

    Kibwe alitafakari kuhusu mambo mengi ya ajabu aliyopambana nayo. Aliwakumbuka kwa hofu viumbe wengi wasiokuwa wa kawaida aliowaona, hasa majini waliojigeuza katika maumbile mbalimbali, mara nusu watu na nusu wakiwa ama vyura kuanzia tumboni kwenda vichwani au nyoka wakubwa, au binadamu ambao hugeuka wakawa na mikia mirefu sana! Aliogopa mno!

    “Sikujua Kama majini wanaweza kujigeuza katika maumbile yoyote wanayopenda, na hata kuwa nyoka!” aliwaza.

    “Labda hata yule nyoka wa baba yangu naye alikuwa ni jinni…” Alitafakari na kukumbuka mkasa uliomsibu alipokuwa mdogo sana, nyumbani kwa wazazi wake, wakati alipokutana uso kwa uso na kichwa cha joka kubwa lililofugwa kwenye chumba kimoja kwenye nyumba ya baba yake, mzee Ilunga. Aliwaza jinsi mvuvi mmoja alivyompelekea baba yake nyoka mdogo badala ya samaki aliozowea kumpelekea siku zote, na jinsi baba yake alivyoamua kumchukua na kumfuga nyoka huyo, aliyeonekana kuwa mzuri na wa kupendeza! Mkutano wa ghafla baina ya Kibwe na nyoka huyo, ulikuwa siku ambapo kijana yule alipovunja amri ya baba yake na kufungua chumba kimoja miongoni mwa vyumba saba vya jumba la wazazi wake alichokatazwa kukifungua. Tukio hilo lilimtia kihoro kikubwa kijana huyu kwa muda mrefu sana!

    Kwa zaidi ya miaka kama sita hivi, Kibwe hakukumbuka mkasa wa joka kubwa nyumbani kwa wazazi wake, hadi wakati ule alipowaona wale nyoka wa kipekee katika msitu wa ajabu kuelekea nchini Baharia. Alikumbuka kuwa mara ya mwisho alipowaona nyoka wa kawaida lakini katika makundi, walikuwa wa rangi mbalimbali, yaani wenye rangirangi kama ushanga uliotungwa kwa mpangilio, wenye mistari ya rangirangi mithili ya pundamilia, wenye rangi mojamoja zisizochanganywa kama vile weusi, kijivu, kahawia, kijani hudhurungi na wengine wengi wa rangi nyingine mbalimbali, wote wakijitokeza kwenye ufukwe wa mito ya maji ambako Kibwe alipitia, akihangaika kumtafuta nyoka wa baba yake aliyempoteza, aliyeitwa ‘Kunyenge.’ Wakati ule, kila alipowaona nyoka wale, Kibwe aliimba na kuwalilia wamsaidie kumpata nyoka huyo, kwani baba yake alimfukuza Kibwe nyumbani kwao, akimwambia kuwa asirudi bila nyoka wake!

    Siku ile, Kibwe alikumbuka jinsi alivyokuwa akimtafuta nyoka huyo wa baba yake, jinsi alivyotembea kwa masafa marefu, akienda msitu na nyika mguu nipe, na kila alipotokea kando kando ya mito, kwenye ufukwe wa bahari na maziwa ya maji, akilia na kuimba kwa maneno haya;

    “Nyoka wa baba nyoka wa baba, lawa nkuloleex2

    Nkulolee! Nkulolee! Lawaa Nkuloleee!”

    Yaani aliita na kumuomba nyoka wa baba yake atoke ili waonane. Na wale nyoka waliojaa kando ya maji nao walimjibu kwa kuimba kwa maneno haya;

    “Nakunyengapo nakunyengapo, kawa Kunyenge!x2

    Kunyengee! Kunyengee!

    Kaliwaa na nyama!

    Yaani nyoka hao walimjibu kuwa kama huyo nyoka anayemtafuta ni ‘Kunyenge,’ basi ajuwe kuwa ameliwa na wanyama! Na kila lipoambiwa hivyo, Kibwe alilia sana, na kisha akaendelea na safari yake ya kumtafuta ‘Kunyenge’, nyoka wa baba yake. Kwa kuwa kijana yule alitembea usiku na mchana akimsaka nyoka huyo wa baba yake, alichoka sana, na hatimaye alianguka, akazirai na kupoteza fahamu. Alipozinduka, alijikuta yuko kwenye ule mji wa wala mawe, kwa Bunga, ambako safari yake ya kisiwa cha mazimwi pamoja na ile ya Azarbajan, kwenye mji wa majini chini ya bahari, zilikoanzia. Alipokuwa chini ya bahari, Kibwe alikumbuka sana nyumbani kwao kwa mzee Ilunga kwenye mkutano wa nchi tatu, katika mji mdogo wenye mazingira mazuri sana, uliozungukwa na milima iliyotiririka vijito vya maji, yaliyomiminika kwenye mto mkubwa na maarufu, Mto Mbezi! Ingawa mto huo ulikuwa na samaki wengi, lakini Kibwe alikumbuka kuwa mto huo pia ulikuwa ni makazi ya nyoka wa aina mbalimbali.

    Kwa kuwa baba yake Kibwe Mzee Ilunga alipenda sana samaki, kila siku mvuvi mmoja maalum alimpelekea samaki wa kitoweleo. Siku moja mvuvi huyo alikosa samaki, na akabahatika kuvua nyoka yule mdogo. “Bwana wangu, seyidi yangu wee! Leo sikupata samaki kabisa. Katika uvuvi wangu wote, bali siku ya leo nimejaaliwa kuvua nyoka huyu mdogo. Kwa hakika sielewi kwa nini imekuwa hivyo.” Lakini yule mvuvi alishangaa sana, kwani Mzee Ilunga hakujali kabisa kuhusu hali ile iliyojitokeza, na akasema kumwambia yule mvuvi; “Kama leo hii ulichoweza kuvua ni huyu nyoka, basi huyuhuyu ndiyo riziki yangu. Nitamchukua na kumfuga!”Kwa hiyo mzee Ilunga alipomfungia yule nyoka kwenye chumba kimoja kati ya vyumba vyake saba, hakuna aliyejua, kwani jambo hilo alilifanya siri.

    Siku moja baba yake Kibwe alitoa onyo kwa familia yake, Alipowaita ukumbini na kuwaambia; “Nimewaita kuwaeleza kuwa mnaweza kufungua vyumba vyote sita katika nyumba hii, lakini kamwe msifungue kile chumba cha saba. Lazima mzingatie jambo hilo!” Kwa pamoja Kibwe na mama yake wakasema, “Tutazingatia jambo hilo bila wasiwasi.Hatutafanya kinyume na amri yako.” Kwa hiyo kila siku mzee Ilunga alihakikisha kuwa anapeleka chakula cha nyoka yule kwa siri, katika chumba cha saba. Alianza zoezi hilokwa kumpelekea yule nyoka kuku mmoja, na kisha kila alivyozidi kukua nyoka yule, ndivyo idadi ya kuku aliokula livyozidi kuongezeka. Hatimae yule akakuwa s mno, hadi akaanza kupewa mbuzi mzima! Huyo alikuwa ni nyoka mwenye ukubwa wa kutisha mno!

    Hata hivyo, Kibwe hakuridhika kila alipoona kufuli ikining’inia kwenye chumba alichokatazwa kukifungua. “Sijui baba ameficha nini mle ndani?” Kibwe aliwaza mara kwa mara. “Siku moja baba akisahau ufunguo wa chumba hicho tu, lazima nitakifungua nichungulie ndani!” Basi naam, hiyo siku ilipowadia, kijana Kibwe hakufanya ajizi, bali haraka aliunyakua ule ufunguo na moja kwa moja akaenda kufungua kufuli ya chumba kile, na kuingiza mguu wake, ili aone hicho kilichofichwa! Lakini lo! Mguu wake huo haukudiriki kuingia mle ndani asilan, kwani ulizuwiwa palepale kizingitini, na kitu kilichojaa chumba chote! Na alipoinua kichwa chake kuangalia juu ili aone ni kitu gani hicho, kilichojilundika mle ndani kama matairi ya gari yaliyopangwa moja juu ya jingine, Kibwe alishituka na kutaka kukimbia! Aliponyanyua kichwa juu, alikutana na macho ya joka kubwa lililokuwa na kichwa kikubwa kama boga!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Leo ni leo Kibwe! Ama zako ama zangu! Utaona jinsi watoto wapekepeke wanavyofanywa!Kwa hiyo kwa sasa, ni bora uingie ndani tu, maana ukitoka nje umekufa, na hata ukiingia ndani umekufa! Uchaguzi ni wako. Nimetambua kuwa wewe ni mtoto mtukutu sana, usiyesikia makanyo ya wazazi wako. Leo ndio utahakikisha kuwa asiyesikia la mkuu huvunjika guu!” Joka lile lilimfokea Kibwe. Halafu likajigamba na kusema; “Mimi ndiye nyoka ‘Kunyenge,’ na kwetu, kwa baba na mama yangu ni bahari ya kina kirefu. Kuanzia hivi sasa naondoka kwenda kwetu, na wewe Kibwe utajua utakalomwambia baba yako!” Kibwe hakuwa na la kujibu, bali alisimama pale alipokuwa kama aliyepigiliwa misumari, akizidi kuogopa na kushangaa! “Sielewi hata kidogo, sababu iliyomfanya baba yangu kumfuga mnyama huyu hatari nyumbani kwetu!” aliwaza kijana yule, bila kupata jibu. Alimshangaa baba yake kwelikweli!

    Wakati Kibwe akisimama pale mlangoni huku akigwaya na akimwangalia yule nyoka, akitafakari na kubutwaika na maajabu yale mbele yake, mara upepo mkali ulizuka, ukavuma kwa nguvu sana, hadi ukatingisha paa la nyumba kama kwamba litang’oka! Punde si punde, Kibwe alipopepesa macho, na kisha kuangalia chumbani kwa huyo Kunyenge, akaona chumba kimekuwa kitupu! Yule nyoka wa ajabu alipotea ghafla na kutoweka kimuujiza! Si hivyo tu, bali mazingira aliyopotelea yalikuwa ni ya kutisha, kwani mpaka wakati ule, bado nyumba ilikuwa ikitingishika kama kwamba lilipita tetemeko la ardhi. Jambo jingine ni kwamba Kibwe hakujua atamwambia nini baba yake kuhusu kupotea kwa nyoka Kunyenge! “Baba alinikataza kufungua hiki chumba! Nitamwambia nini leo?” Haraka alifunga kile chumba na kurudisha ule ufunguo pale pale alipouchukua!

    Kibwe alihofu sana kuhusu jinsi baba yake atakavyokasirika mara atakapopata taarifa ya kupotea kwa nyoka wake. Hofu hiyo ilikamilika na kuongezeka wakati mzee wake huyo aliporejea nyumbani, na haraka kuutafuta ufunguo wake aliousahau, na kisha moja kwa moja akaharakisha kwenda kule chumbani kumwangalia nyoka wake! Alipofungua mlango na kumaizi kuwa kunyenge hakuwamo mle chumbani, Ilunga alibaki kinywa wazi kwa mshangao! Hakuamini macho yake kumkosa yule nyoka mle ndani, jambo ambalo kwake halikuwa la kawaida. Alisimama pale mlangoni akiduwaa na kuwaza ni kitu gani kimemtokea nyoka wake! Kisha, hasira zilimpanda pamoja na ghadhabu, na mara moja akatoka na kumwendea mwanae Kibwe, ambaye ndiye pekee aliyekuwa nyumbani wakati alipotoka na kuusahau ufunguo wa chumba cha Kunyenge.

    “Hivi wee Kibwe, umempeleka wapi nyoka wangu?”

    Kibwe hakusema lolote, kwani hakika hakujua nyoka huyo alipokwenda.

    Mzee yule alipaza sauti zaidi kwa hasira na kusema; “Hivi mimi nasema na nani? Si ninasema na wewe Kibwe? Haraka sana niambie ulichomfanya nyoka wangu!”

    Kimya tena!

    Kibwe hakujibu.

    Hapo ndipo mzee Ilunga alipozidi kukasirika, na ndipo aliposema maneno haya;

    “Wewe ni mtoto mbaya sana usiyesikia unayoambiwa na wakubwa! Pamoja na kukukataza kufungua kile chumba, wewe umefanya hivyo hivyo nilivyokukataza. Hivyo basi kuanzia sasa toka hapa ndani, uende ukamtafute nyoka wangu na umlete hapa! Usipompata, hakikisha na wewe unapotelea huko huko!”

    Kibwe aliduwaa na pia kushangaa kusikia baba yake anavyomthamini nyoka zaidi yake. Alilia sana, na kumsihi baba yake amsamehe kwa kosa hilo. Mama yake Kibwe nae aliyelia pamoja na mwanawe, na yeye pia akamsihi sana mumewe amsamehe mtoto wao.

    “Achilia mbali hasira hizo mume wangu! Utampoteza mwanao bila sababu ya maana. Hivi aende wapi kumtafuta huyo nyoka? Kumbuka kuwa aliyepotea ni nyoka tu, na huyu ni mwanao Baba Kibwe! Tafadhali rudisha moyo wako umsamehe!”

    Baba yake Kibwe hakutaka kusikia lolote, bali alishikilia uzi uleule, akasema; “Mtoto akililia wembe, mwachie umkate! Lazima aende akamtafute nyoka wangu na amrudishe hapa bila kukosa.”

    Kwa hiyo Kibwe hakuwa na la kufanya, isipokuwa kufanya safari ya kumtafuta nyoka wa baba yake, ‘Kunyenge.’ Kabla ya kuanza safari hiyo, mama yake alimtayarishia mwanae mikate saba ya kumimina ya kula njiani, na akamfungashia guduria la maji ya kunywa.

    Naam, Ndipo Kibwe alipoanza safari yake. Akitembea mchana kutwa , na usiku akilala juu ya miti, akimtafuta nyoka Kunyenge. Kwa kuwa awali yule nyoka alimwambia Kibwe kuwa nyumbani kwa wazazi wake ni chini kabisa ya bahari kuu, kila alipofika kwenye bahari na mito mikuu ambako nyoka walionekana wakiota jua, Kibwe alisimama na kuanza kumwita nyoka wa baba yake, alilia akimsihi kwa kuimba kwa maneno haya;

    “Nyoka wa baba nyoka wa babaa, Lawa nkuloleee!x2

    Nkuloleee! Nkuloleee! Lawaa nkuloleee!”

    Na nyoka wakamjibu kwa maneno haya;

    “Nakunyengapo, nakunyengapo! Kawaa Kunyengeex2

    Kunyengee! Kunyengee! Kawaa Kunyengee!

    Kaliwaa na nyamaa!”

    Alipochoka sana kwa kazi nzito ya kumtafuta yule nyoka, alianguka, akazirai na kupoteza fahamu kabisa! Alipozindukana, hakukumbuka safari ya kumtafuta ‘Kunyenge,’ bali wakati ule ndipo alipokutana na Bunga, akaambiwa kuwa yeye ni Mteule atakaye inusuru dunia kutokana na ukame, vifo na uovu! Baada ya kutoka katika mji wa majini wa chini ya bahari, ambako majini huhatarisha maisha ya watu kwa uchafuzi wa hewa safi.

     “Sijui hivi sasa ‘Kunyenge’ bado yuko chini ya bahari au la!” Kibwe aliwaza. Wakati ule Kijana yule alimkumbuka sana mama yake, na pia kujiuliza kama baba yake alikuwa bado akimsubiri nyoka wake ‘Kunyenge.’ Vilevile alihisi kuwa labda yule ‘Kunyenge’ ni mmoja miongoni mwa yale majini ya bahari, na labda wale nyoka wengi aliokutana nao, baadhi yao walikuwa ni familia yake! “Bila shaka Bunga atakuwa anaelewa zaidi kuhusu habari hizi” Aliwaza.

    “Duh! Ama hakika kisa chako ni cha kushangaza sana mwenzangu!” Hanga alimshitua kutoka kwenye mawazo yale, na hapo Kibwe akamaizi kuwa kumbe alikuwa ameshamaliza kumsimulia mwenzake kile kisa chake.

    Aliguna na kutikisa kichwa.

    “Ama hakika sikujua kuwa kule kutoka kumtafuta nyoka wa baba, ndio ulikuwa wito wangu wa kutoka kuja kwenye hii safari ya kuinusiri dunia!” Alisema kwa mastaajabu.

    Kimya kilipita kidogo baina yao, kisha Hanga akauliza.

    “Sasa nini kinafuata Kibwe. Ulisema kuwa muda unavyokwenda ndio dunia inateketea…tunaendeleaje kutokea hapa?”

    “Ni kweli. Kwanza mahali hapa tulipo pana uovu mkubwa ulioniandama kila nilipokwenda na unaoendelea kuniandama, kwa nia ya kufifiza jitihada za kuwanusuru raia wa nchi ya Azarbajan, kutokana na hewa hatari inayowageuza mawe ya theluji! Mwana yule Mteule alimjibu mwenzake.

    “Kwa hiyo haraka tuongozane kwenye milima pacha nilikoazimia kufika, ili nikakamilishe jukumu hilo!” Kibwe alizidi kumwambia mwenzake.

    Kwahiyo kwa pamoja vijana wale walishikana mikono na kutimua mbio! Wakati ule, Hanga alikuwa akitafakari maneno ya Kibwe yaliyomfanya abutwaike kidogo!

    Nchi ya Azarbajan?

    Mbona ni nchi inayopakana na Hazina ambako ni Milki ya baba yake Sultani Hazari bin Basari?

    Kama jirani zao tayari wamekwisha kumbwa na janga la kugeuzwa mawe, bila shaka hata nchi yao iko hatarini!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nina kila sababu ya kumsaidia mwenzangu huyu kutatatua tatizo hilo!” Hanga aliwaza bila kusema lolote kwa Kibwe.

    Kibwe na Hanga waliongozana wakitoka mle pangoni kwa kupitia mlango wa pili wa pango kwenye sehemu aliyoingilia Kibwe. Pale mlangoni ilining’inia mizizi iliyotokana na miti mikubwa mno na yaajabu, iliyounda msitu mnene, ‘Msitu wa Kindumbwe,’uliotanda kila upande wa majabali.

    “Kamata madhubuti mzizi mmoja na ujishikize ili uweze kubembea na kujirusha kwenye uleee mwamba unaoonekana mbele yetu.” Kibwe alimfahamisha mwenzake, akimwambia kuwa watakapofika pale mwambani, anatarajia kukuta ngazi za mawe zinazoelekea chini ya minara pacha.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog