Search This Blog

KIBWE KATIKA SAFARI YA AJABU - 4

 







    Simulizi : Kibwe Katika Safari Ya Ajabu

    Sehemu Ya Nne (4)



    “Kwa kuwa huku tuliko ni juu sana kwa urefu wa zaidi ya kilometa elfu moja, hatua tunayoichukua ni ya hatari mno, kwani kama tutaanguka, huenda ama tukafikia juu ya jabali lenye mawe makali ya kukata, na kupoteza maisha yetu, au tukaangukia kwenye mchanga didimizi na kuzama humo!” Alisisitiza Kibwe, wakati Hanga akionesha sura ya hofu. Kwa kuwa alifahamu kwamba mwenzake alikuwa ni mteule, alijuwa wazi kuwa atakayekuwa hatarini zaidi ni yeye!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kwa moyo mzito sana Hanga aliukamata mzizi mnene alioamini kuwa ungembeba bila kumbwaga chini. Aliuvutavuta kuhakikisha uimara wake, na kisha akabembea kwa nguvu zake zote, akilenga kufikia kwenye mwamba alioambiwa na mwenzake. Kwa bahati, alifanikiwa kujikita katika eneo tambarare la mwamba uliokua mbele yake. Alitulia kwa dakika kama tano hivi, moyo ukienda kasi kupita kiasi, kwa kazi ya kubembea na kujirusha hadi kufika pale mwambani, na pia kwa woga na hofu! Alimshukuru Mungu wake kwa kumsaidia kufika mahali pale salama salimini. Muda mchache baadae, Kibwe naye aliwasili mahali pale kwa njia ileile aliyoitumia Hanga. Kwa pamoja huku wakiwa hoi, walianza kupanda juu zaidi ya ule mwamba wakielekea kwenye kilele cha uwanda, mahali ambapo ni karibu zaidi na minara pacha.

    “Kibwe! Kibwe! Nyuma yetu kuna mtu anatufuata….!” Hanga alisema kwa hofu, akiwa ametoa macho kungalia upande alikoelekeza kidole chake. Kibwe aligeuka haraka! Lakini kwa jinsi msitu ulivyofunga haikuwa rahisi kuona hata hatua kumi mbele yao.

    “Hata mimi nahisi kama kuna watu wanatufuata lakini usijali. Tuendelee na safari yetu na wala tusigeuke nyuma!” Kibwe alisema huku akimkokota mwenzake. Mara kwa mara wale vijana waliona vivuli kama watu, vilivyopotea hata kabla hawajatambua kama vilikuwa ni vivuli vya watu, majini au vibwengo!

    Wakiwa na hofu kubwa, vijana wale waliendelea moja kwa moja na safari yao, kwa mashaka na taabu, wakipanda jabali lililokuwa na mawe makali yaliyowachubua chubua mikono yao magoti na miguu, hadi walipofika juu kabisa ya uwanda. Kwa furaha kubwa, huko waliiona ile minara pacha mitatu, iliyosimikwa kama mafiga….iliyokuwa mirefu kupita kiasi!

    “Lazima nifike juu kabisa ya vile vilele vya minara ili niweze kusimama juu ya kigoda cha dhahabu, ambako nitaweza kuelekeza upanga wangu wa radi juu zaidi kwenye angahewa ya chini.” Kibwe alimwambia mwenzake, ambaye alimsikiliza mteule yule kwa makini.

    “Kwa kufanya hivyo unakusudia nini?” Alidodosa Hanga, kwani yeye alielekeza imani yake yote kwa Kibwe, aliyeonesha maajabu ya kusoma maandiko kama michoro tu, isiyoeleweka na mwanadamu wa kawaida.

    “Upanga huu utakapotoa cheche zitauathiri moshi wa vichafuzi vya hewa ya Ozoni, ambayo ndiyo inayowadhuru raia wa Azarbajan kwa kuwageuza mawe ya theluji!”

    Kusikia vile Hanga aliduwaa!

    Ingawa Azarbajani ni nchi iliyopakana na nchi yake ya Hazina, lakini hakufahamu kama katika pwani ya nchi hiyo, raia wengi walikuwa wakiteketezwa kwa moshi wa ajabu! Mara nyingi Hanga hakuwa mfuatiliaji wa mambo kama yale.

    “Lo! Bila shaka hayo ndiyo sehemu ya madhara tuliyo tahadharishwa katika ujumbe ule maalum kwenye vidani vya sanamu za fedha ya kucha za Simba zinazoning’inia kwenye mkufu shingoni mwa sanamu la shaba la kichwa cha Simba!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kijana yule aliwaza kwa mshangao, huku akipata jibu kuwa ni yule mwenzake mteule atakayesaidia kutatua tatizo lile hatari, pamoja na matatizo mengine makubwa zaidi. Alitambua pia kuwa msaada wake yeye pamoja na msaada wa vijana wengine kama wao, nao ulihitajika mno. Alitulia tuli, ili kuona jinsi Kibwe atakavyoweza kufika kule juu ya minara pacha, mahali penye urefu wa zaidi ya kilometa alfu nne, palipoonekana kama kwamba pamepakana na mbingu! Lakini kufumba na kufumbua baada ya Kibwe kukusanya nguvu kule chini ya minara pacha, aliweza kujirusha na kuelea hewani kama Kipanga, akapaa juu kabisa hadi kileleni, na aliponyoosha upanga wake kuuelekeza mbinguni, cheche zilianza kutoka na kusababisha moto uliozingira sehemu kubwa ya anga hewa ya chini, ilikofika hewa ya vichafuzi kutoka kwenye maabara ya majini nchini Baharia!

    Hanga hakuwa na la kusema bali aliduwaa tu!

    “Haya ni maajabu makubwa!” Aliwaza.



    BAADA YA DHIKI FARAJA.

    Muda mfupi baadae Hanga alimuona Kibwe akishuka tena ardhini kama jinsi kipanga ashukavyo, na kutua kwa ustadi mkubwa.

    “Kazi imekamilika Hanga…kama maelekezo niliyopewa yatakuwa sahihi, na sina sababu ya kuamini vinginevyo, basi tatizo la hewa chafuzi kule nchini Azarbajan litakuwa limekomea hapa!” Kibwe alisema kwa ushindi.

    “Kweli?” Hanga aliuliza si kwa kutoamini, bali kw akutaka tu kujithibitishia tena kuwa hakika pale alikuwa amesimama bega kwa bega na mwana mteule.

    “Twen’zetu Azarbajan tukajihakikishie…” Kibwe alimwambia, na kwa pamoja vijana wale waliendelea na safari yao hadi ufukwe wa nchi ya Azarbajan kwa Mfalme Kashkash, ambako eneo lote lilikuwa na ile mitumbwi iliyopakia wavuvi waliopambana na janga la hewa nzito, iliyowagandisha na kuwageuza masanamu ya mawe ya theluji isiyoyeyuka.

    Kibwe alishuhudia pia mlolongo wa masanamu ya theluji ya wanawake na wazee pale ufukweni.

    “Heh! Mbona hali bado ni mbaya vile vile Kibwe?” Hanga aliuliza kwa hamaniko.

    Kibwe hakujibu. Alibaki akiitazama hali ile kwa masikitiko makubwa sana.

    Alijua kuwa kutokana na kile kitendo cha kuulenga upanga wake wa radi na kuutingisha juu ya anga hewa ya chini akiwa kwenye kigoda cha dhahabu kwenye milima pacha mitatu kama alivyoelekezwa na Mzee wa Busara, kitendo kilichosababisha kutokea kwa cheche za moto zilizozusha kwenye angahewa ile, na vienge vilivyotoa mvuke ulioelekezwa kwa wale wote waliogeuka mawe ya theluji, theluji ingeanza kuyeyuka na maji yangeanza kuchuruzika ardhini.

    “Sasa mbona…” Alianza kuwaza.

    Na hata pale walipokuwa wakiitazama hali ile, wale vijana waliwashuhudia wale watu wakianza kuamka. Wote wakatoa chafya wakati mmoja, kuashiria uzima wao! Bila kukumbuka mkasa uliowasibu, wote walianza kutawanyika kama vile kila kitu kilikuwa ni kawaida tu! Nchi yote ilichangamka kutokana na kupishana kwa wavuvi wengi katika maeneo ya Ufukweni! Hanga aliangalia maajabu yale bila kutia neno!

    Kilichotokea ni kwamba hewa ya joto kutoka kwenye vienge vya moto wa upanga wa radi, ilielea kutoka kwenye milima pacha na kupanda juu kwenye anga hewa ya chini, na huko ikapambana na hewa ya Ozoni, ambayo ilianza kuyeyuka na mzizimo wake kupungua, wakati vichafuzi vya hewa kutoka chini ya bahari kwa kina Makatta wa Makattani, navyo vilipopungua taratibu, na kisha kutoweka kabisa! Tatizo la hewa ya mzizimo ya kugandisha viumbe likakomea hapo!

    Siku hiyo Sultani KashKash alifurahi sana akamshukuru Kibwe kwa msaada wake wote alioutoa kwa raia wake, akishirikiana na mwenziye Hanga.

    “Lazima kesho tusheherekee pamoja kwa chakula na vinywaji, kwani hakika mnastahili kupongezwa mno!”

    Kibwe alipokea shukurani zile kutoka kwa Sultani kwaniaba ya mwenzake Hanga, nayeye akamshukuru sana mtawala yule wa Azarbajan kwa mwaliko wake kwao.

    Siku iliyofuata, mjumbe wa jumba la Mfalme alipiga mbiu ya mgambo, ambayo hupigwa ama wakati wa karaha, au raha! Kabla kijumbe huyo kuanza tangazo lake, alipiga goma lake alilolibeba kifuani, na kisha ndipo alipotangaza kutangaza; “La mgambooo! La mgambooo! Likilia lina jambo! La mgambooo! La mgambooo! Asiye mwana aeleke jiwe! Wanachi wote mnatangaziwa na Mfalme kuwa kesho wote mjumuike pamoja kwenye uwanja wa sanaa, ili kusheherekea kupatikana ufumbuzi wa tatizo la hewa hatari iliyowageuza mawe ya theluji raia wan chi hii! Kesho, kijana shujaa aliyetufikia kwetu na utatuzi wa tatizo hilo, kibwe, atatunukiwa tuzo ya ushujaa ya kaskazini ya mbali ya dunia! La mgambooo! Wote mnatakiwa kuhudhuria!” Mjumbe yule alikamilisha tangazo lake kwa kulipiga piga goma lake.

    Ama kwa hakika ile sherehe ilifana mno, na watu walikula wakasaza, na wakanywa mvinyo na togwa safi nyingi sana! Mwishowe, Mfalme KashKash akamkabidhi kibwe tuzo ya aina yake, ya sanamu la kijana aliyeshika upanga, iliyochongwa kwa dhahabu tupu! Siku hiyo ilikuwa ni siku ya furaha kubwa kwa Kibwe, na kwa raia wa pale na Mfalme wao. Hatimae baada ya tafrija ile ya kihistoria, kijana yule na mwenzake waliagana na watu wote pamoja na mtawala wao, wakiwaambia kuwa walikuwa na jukumu jingine kubwa kule mashariki ya katikati ya dunia.

    “Huko kuna shida kubwa ya maji, na nahofia kuwa katika siku chache zijazo, binti Sultani wa nchi ya majabali atakuwa hatarini kutolewa mhanga!” Kibwe alimwambia Sultani Kashkash, na alipotakiwa kutoa maelezo zaidi, alijibu kuwa hafahamu zaidi kuhusu habari hiyo, kwani yeye hupewa muhtasari tu, wa matukio, na wale wanao mwelekeza kufanya kazi hiyo.

    Kwa furaha na shukurani kubwa aliyokuwa nayo Mfalme KashKash, aliandaa merikebu kubwa yenye wahudumu wa kutosha, kwa ajili ya usafiri wa akina Kibwe, kuwapeleka kule mashariki ya katikati ya dunia, ili aendelee na majukumu mengine ya huduma kwa watu.

    “Ndani ya merikebu hii vipo vyakula vya kila aina, vitakavyo wasaidia njiani. Zipo chapati, yapo maandazi, kuna visheti na bajia, pia zipo jelebi, katlesi na kachori,” Mfalme alimwambia Kibwe, akiongezea kuwa humo pia kuna nyama zilizoandaliwa kwa mapishi tofauti, kama vile nyama ya kubanika, nyama ya kukaanga, nyama ya kuchemsha, ikiwa ni pamoja na nyama ya kuku, nyama ya mbuzi na pia nyama ya ng’ombe! Mfalme aliazimia kumfurahisha Kibwe kwa ushujaa wake!

    Mfalme yule alimwambia Kibwe kuwa kwenye merikebu ile walikuwemo manahodha hodari sana, na wahudumu watiifu kabisa. Kibwe alifurahia ukarimu wa mfalme.

    “Sijui niseme nini mtukufu Mfalme kwa ukarimu wote huu unaonionyesha. Nakushukuru sana kwa yote.” Kibwe alisema kwa dhati na kwa unyenyekevu kabisa. Kijana yule shujaa na yule rafikiye mwaminifu Hanga, walisindikizwa na raia wa Azarbajan kwa shangwe na hoihoi hadi bandarini, na kule wakaagana kwa upendo mkubwa, na kisha merikebu ikaanza safari nyingine ya ajabu ya Kibwe, kumuokoa Bhaduri binti Sultani Bashar wa Mashariki ya mbali ya dunia!



    Walisindikizwa na raia wa Azarbajan kwa shangwe na hoihoi hadi bandarini, na kule wakaagana kwa upendo mkubwa, na kisha merikebu ikaanza safari nyingine ya ajabu ya Kibwe, kumuokoa Bhaduri binti Sultani Bashar wa Mashariki ya mbali ya dunia!

    Merikebu ya Mfalme KashKash iliyoyoma usiku na mchana, na hali ya bahari ilikuwa shwari kabisa, kwa muda wote huo.

    “Tuna bahati kubwa, kwani mpaka sasa bado hali ni shwari sana.” Hanga alimwambia mwenzake Kibwe. “Kwa kawaida mimi hutapika sana baharini, lakini leo niko salama kabisa,” Alieleza. Kibwe alimwambia kuwa kwa kuwa bado safari ni ndefu asijiamini sana. Kwa maneno hayo, wote wawili walicheka kwa pamoja. Meli hiyo iliyowabeba vijana hao wawili, wahudumu wakutosha wa meli na manahodha, ilizidi kuyoyoma hadi kufika katikati ya bahari, halafu jambo la ajabu likatokea! Ile meli ilisimama ghafla, kama kwamba ilinasa mahali. Kibwe alipomuuliza nahodha aliyekuwa kwenye usukani ni nini kilichotokea, akajibiwa kuwa hakuelewa ni nini kimeikwamisha meli yao.

    “Huenda majani ya mwani yamenasa kwenye pangaboi linalozungusha maji huko chini ya meli,” alisema nahodha. Alipoambiwa hivyo kijana yule alijitolea kwenda kuangalia kule chini ya meli, ingawa wenzake walimzuia sana.

    “Ni hatari kwenda peke yako. Labda tufuatane pamoja .” Hanga na baadhi ya wahudumu wa ndani ya meli walimwambia. Ingawa Kibwe alipinga kufuatana nao, lakini wenzake walishikilia tu, hadi yule kijana akakubali waende wote.

    Naam, karibu watu wanne walishuka na kuogelea kwenda chini ya ile merikebu, kuangalia hicho kilichonasa kwenye pangaboi la meli yao. Wote waliogelea, na Kibwe alikuwa mbele zaidi, hivyo alitangulia kuwasili pale lilipokuwa hilo pangaboi. Lakini lo! Pangaboi lenyewe lilikuwa limeshikiliwa madhubuti na mtu mmoja mwembamba kupita kiasi, na mrefu kuliko utakavyofikiria! Macho ya mtu yule yalikuwa pembeni mwa sura yake, iliyofanana na chura!

    “Ahaa! Kumbe! Tunakutana tena siyo?” Kibwe aliwaza, na bila kupoteza muda, na haraka kama mwendo wa mshale, kijana yule alitoa rungu lililokuwa kwenye mfuko alioubeba mgongoni, na kulirusha kwa nguvu zake zote, kumtupia yule mtu wa ajabu, akilenga ule mkono ulioshikilia lile panga boi! Kwa kishindo kikubwa, lile rungu likamfikia kwenye mkono wake huo, na palepale akaachia lile panga boi, na kama umeme, akapotelea chini kabisa ya bahari!

    Naam kwa mara nyingine, Kibwe alikutana na mmoja kati ya jamii ya majini wa bahari, jamaa zake ‘Makatta wa Makattani.’ Wakati hayo yakitokea, wenzake wengine waliokuwa wakija kuangalia chini ya merikebu, walifika na kumkosa yule jini wa bahari kwa sekunde tu!

    “Kwani kuna nini?” waliuliza, na wakati huohuo, ile meli ikawa inasogea mbele!

    “Ilikuwa ni mwani tu, ulioshikilia pangaboi! Nimekwisha uondoa , na ndio maana mnaona meli inaondoka. Twendeni tuwahi!” Kibwe alidanganya, akichelea kuwatia hofu watu na hadithi za majini wa bahari! Wote wakarejea melini, na kuendelea na safari.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe na wenzake waliendelea na safari yao huko mashariki ya katikati ya dunia, kwenye majabali yaliyouzingira mto mkubwa wa maji, mto Sakara, ambako Bhaduri binti Sultani kitinda mimba na mwana wa saba wa Sultani Bashar, alikuwa ameketi juu ya uwanda wa jabali moja, akisubiri kutolewa kafara!

    Kwa moyo wa ushujaa, na utiifu kwa amri ya baba yake, mrembo Bhaduri binti Sultani aliketi juu ya jabali kwenye kiti kimoja kizuri cha enzi, akiwa amepambwa kwa sundusi za hariri, mikufu, hereni na vikuku vya dhahabu na vito vya thamani, huku akinukia utuli mchanganyiko kama udi, miski na ambari, akisubiri wakati wake wa kuchukuliwa na hicho kitakachokuja kumchukua!

    Kibwe na msafara wake ndani ya merikebu yao ya fahari, waliyoyoma kuelekea huko mashariki ya katikati ya dunia, wakati huo zikiwa zimebaki siku chache tu, kuwasili mwisho wa safari yao. Usiku mmoja alipokuwa amelala na mwenzake Hanga kwenye chumba chao, Kibwe alimuota Bunga, akimpa maelekezo ya safari yao hiyo. “Lazima msafara huu usitishwe haraka iwezekanavyo, mara tu mtakapowasili kwenye bandari yoyote ya jirani,” alisema Bunga. Aliendelea kumwambia kuwa itabidi wasubiri kwenye bandari hiyo kwa siku mbili zaidi, kabla ya kuanza tena safari yao. “Katika muda huo mtakapo kuwa mkisubiri kwenye bandari hiyo, mtakuwa mmejinusuru na hatari ya kupambana na mwamba wa barafu majini, na pia mtanusurika na tufani kubwa itakayotokea mnamo saa ishirini na nne zijazo.” Kibwe alimsikiliza Bunga, aliyeonekana akielea hewani kama ndege, na maneno yake yakisikika kwa kukatika katika, kwa sentensi zisizokamilika!

    Ndotoni Kibwe alikuwa akimcheka Bunga, na akimshangaa sana kwani kwa mara hii alimuona ni wa ajabu kabisa. Hakuamini maneno yake hata kidogo, “Usinitanie mzee Bunga! Unajua kwamba msafara huu lazima uwahi nchini Shamsi mashariki ya kati kati. Sasa mbona unataka kutuchelewesha?” Kibwe alianza kulumbana na kile kijitu cha ajabu.

    “Tutaendelea tu……..na- safa-”Lakini kabla hajamalizia maneno yake, Kibwe akaona ukuta uliokuwa mbele yake ukipasuka, na maji mengi yakianza kumwagika kama mafuriko, na kumzoa Kibwe kutoka pale alipokuwa, akajikuta akitapatapa kujinusuru asizame! Ingawa alikuwa anajitahidi kuogelea, lakini alishindwa, na hivyo akaanza kuzama---! Akazama—akienda moja kwa moja hadi chini kabisa ya dimbwi la maji---! Pumzi zikamwishia kabisa! Halafu ghafla, akajiibua juu, na kutoa kichwa chake nje ya dimbwi la maji, na kisha palepale akasituka na kuamka, huku moyo wake ukienda kwa kasi mno! Aliinuka na kuketi kitako, akiwa anapumua haraka haraka mno!

    Mwenzake Hanga aliyekuwa karibu yake, naye aliamka na kumuona Kibwe akiwa katika hali isiyo ya kawaida. “Vipi kibwe, mbona uko hivyo, umeota ndoto mbaya nini?” Kimya! Kibwe hakujibu kitu, bali alizidi kupumua kwa haraka haraka, huku macho yake yakiangalia mbele zaidi ya pale alipokuwa mwenzake, kama kwamba hakumuona wala kumsikia Hanga! Haraka Hanga alichukua gilasi ya maji na kumpa mwenzake huyo anywe, akihisi huenda akajisikia nafuu kidogo. ”Hebu kunywa maji kidoga, labda yatakusaidia.” Kibwe aliyapokea yale maji bila kumwangalia mwenzake, na akanywa funda mbili, na halafu akajilaza kitandani. “Unajisikiaje hivi sasa Kibwe? Ni ndoto gani uliyoota?” Hanga aliuliza, akiwa na wasiwasi na jinsi alivyomuona mwenzake. Kibwe alikohoa kidogo, na kisha akaanza kuongea.

    “Nadhani huko mbele kuna tatizo kubwa sana. Nimeota kuwa kutakuwa na kimbunga kikubwa, na meli yetu itapambana na mwamba wa barafu majini,” Kibwe alimwambia mwenzake, ambaye alimshangaa, akimwambia kuwa alichokiona kilikuwa ndotoni tu, wala si lazima kitokee. Lakini Kibwe hakumsikiliza Hanga, bali aliendelea kusema. “Kama hatukusitisha safari yetu kwenye bandari yoyote ya karibu angalau kwa siku moja na nusu hadi hatari hiyo ipite, wote tutapoteza maisha yetu.” Hee! Hanga akaduwaa akimwangalia mwenzake huyo aliyechanganyikiwa, au tuseme vile alivyoamini Hanga kwa wakati ule. Iweje tena jambo la ndotoni, Kibwe akalichukulia kuwa ni jambo kubwa na halisia? Hanga alijaribu kuzungumza na mwenzake akimsihi ajaribu kutulia tu, na atasahau kuhusu ndoto yake. “Na hata hivyo, unadhani kuwa utaeleweka kwa manahodha utakapowaambia wasitishe safari kwa kuwa uliota kuwa mbele kuna hatari? Jaribu kufikiri vizuri Kibwe.” Kibwe alishikilia palepale, akimwambia Hanga kuwa lazima manahodha wamwelewe, ama sivyo, wote wamo hatarini!

    Kwa hiyo, Hanga na Kibwe walikwenda hadi kwenye chumba cha manahodha, na kuwaelezea kuhusu hatari iliyoko mbele. “Lazima tusitishe huu msafara, mara tu tutakapofika bandari ndogo ya karibu, kabla ya kuelekea nchini Shamsi, ama sivyo, wote tutateketea.” Kibwe aliwasihi wale manahodha, bila kuwa na uthibitisho wa kutosha wa hoja yake hiyo. Manahodha wakamuona kuwa anafanya utoto tu, hivyo kwa kebehi, wakamwambia; “Hivi unadhani kuwa katika maisha yetu kwenye kazi hii, tungekuwa tunaamini kila tulichokiota, tungeweza kufanya safari kama hizi? Kijana, kumbuka kuwa ndoto ni ndoto tu. Hatuwezi kuacha kusafiri, eti kwa kuwa mtu mmoja miongoni mwetu ameota kuwa mbele kuna hatari!” Pia manahodha wale walisema kuwa kulikuwa na umuhimu wa kuwahi kufika kule waendako, ili waweze kugeuza merikebu yao na kurudi makwao, baada ya kumsindikiza Kibwe.

    “Lakini jamani, mmejiuliza kuwa huenda kuna ukweli kwenye maneno ya kijana huyu?” Baadhi ya wahudumu wa meli walihoji, wakinong’ona chinichini. “Kweli eti! Na labda tukiyadharau maneno yake hayo, tutakuja kujuta yatakapotokea hayo anayoyatabiri!” Wahudumu wa meli walisema hivyo, huku wenzao wengine wakihofu sana, walipokisia kuwa huenda kukawa na ukweli kwenye hoja ya yule kijana. ”Ndiyo kusema kuwa wote tutakuwa hatarini!” waliambiana. Hata hivyo wengine miongoni mwa wahudumu wale waliowaunga mkono manahodha na hoja zao, wakasema kuwa yule kijana aliota tu, na wala hakuletewa onyo rasmi la kimazingaombwe kutoka kokote. “Haya jamani na tuendelee na safari yetu, na tuachane na mawazo ya kishirikina!” walisema wahudumu hao, wakiwahimiza manahodha wasipoteze muda. Lakini lo! Laiti kama wangejua!

    Haya, safari ikaendelea kama ilivyoamuliwa, na hakuna aliyejuwa kuhusu mkasa ambao ungetokea mnamo saa ishirini na nne zijazo! Kilometa kadhaa kutoka pale walipokuwa, kwenye mwamba mkubwa sana wa barafu majini, pande moja kubwa la barafu lilijigawa kutoka kwenye mwamba huo mkubwa wa barafu majini, uliokuwa kama mlima mkubwa sana! Sehemu hiyo ya mwamba iliyotanda baharini, ilikuwa ikielea na kusukasuka kuelekea kule ilikokua merikebu ya mfalme KashKash, walimokuwemo Kibwe na abiria wengine! Wakati huohuo, mawingu mazito na meusi yakawa yanajikusanya, na hivyo giza nene likaanza kutanda. Upepo nao ukaanza kuchanganya kasi ya mwendo wake, iliyoongezeka kwa kila dakika, na kuvuma kwa kuvuruga mawimbi ya bahari, yaliyonyanyuliwa juu kwa urefu mkubwa wa kustaajabisha, kwani kimbunga nacho kilikwishaanza! Lahaula! Huko kulikokuwa kukijiandaa katika hali hiyo, ndiko ilikokuwa ikielekea merikebu iliyowabeba kina Kibwe na wenzake! Merikebu ile ilisafiri kwa kilometa nyingi humo baharini, na wakati wote huo, Kibwe akiwa na wasiwasi mkubwa, kwani aliamini kabisa kuwa huko mbele sio kuzuri. “Nafahamu kuwa Bunga hawezi kutokea waziwazi ili kutuonya kuhusu hatari hiyo, maana watu wote watashangaa na pia kuhofu sana, mara watakapomuona,” Kibwe aliwaza. Lakini kwa bahati mbaya, ilibidi kijana yule asubiri hatari hiyo ifike, kwani hakuwa na la kufanya! “Haya. Liwalo naliwe!” alijiambia.

    Mnamo majira ya saa kumi na mbili asubuhi, abiria ndani ya merikebu ile wakaona hali ya hewa ikibadilika. Upepo ukawa unavuma kwa kasi na kwa hasira, huku bahari ikianza kuchafuka. Maji ya mawimbi yaliyokuwa yakijitupia na kupiga pembezoni mwa merikebu, yaliingia sitahani kwa wingi mno! Chini kabisa ya sitaha humo melini, nako kuilijaa maji tele! Kufikia hatua hiyo, abiria wote wakaanza kuhamanika, wakitoka vyumbani mwao ili kujiunga na wenzao, kuona jinsi hali ile iliyojitokeza, ilivyoashiria kuhatarisha maisha yao. “Haya sasa, tuone kama hakuna atakaye amini maneno yangu,” Kibwe alimwambia mwenzake Hanga, aliyekuwa ametowa macho pima akimshangaa Kibwe kwa kuyajua yote yale mapema! Ah! Laiti kama watu wangemuamini na ndoto yake! Mawazo hayo yalikuwa yakipita kichwani mwa Hanga. “Naam! Utabiri wa Bunga umeanza kuwa kweli!” Kibwe aliwaza, huku akiangalia jinsi walivyokuwa wamezingirwa na maji mle merikebuni.

    “Haraka kawaambie abiria waliokuwa chini ya staha waondoke na kuja juu zaidi! Na wa huku juu wawe waangalifu wasisogee pembezoni mwa meli!” Mmoja kati ya manahodha aliwaambia wenzake. “Lo! Kumbe yule kijana alisema kweli kabisa.” Manahodha wale waliambizana, huku wakikimbia kwenda kuwatahadharisha abiria kule walikokusanyika. Huko waliwakuta baadhi ya abiria wakiwa wamejeruhiwa kwa kukimbia kutoka vyumbani mwao, wakitafuta nusura sehemu ambazo maji hayakufika.Wengi wao walikuwa wakianguka na kutereza mara kwa mara, kwani ile merikebu ilikuwa ikisukasuka kwa kusukumwa na mawimbi. Kila ilipoegemea upande mmoja, merikebu hiyo iliwamwaga abiria kwa upande huo! “Kwa hakika maneno yako yalikuwa sahihi kibwe. Leo wote tuko hatarini!” Hanga alimwambia mwenzake , wakati walipokuwa wakijishikiza kwenye nguzo za ile meli, ili wasiteleze na kuangukia sehemu nyingine hatari zaidi. “Ndio hivyo tena. Lakini haina haja kulilia maji yaliyomwagika, kwani si rahisi kuyazoa,” alisema Kibwe. “Iliyobaki ni kuomba Mungu atuvushe salama kutokana na janga hili.”

    Ile merikebu ilikwisha poteza mwelekeo wa mwendo wake, kwani injini ilikwisha zimika. Abiria walijishikiza mle ndani wakisubiri maajabu tu yatokee. Wakati ule wakisukasuka na meli yao kwa msukumo wa mawimbi, ghafla , Hanga akapiga ukulele, akionyesha kidole kwenye upeo wa macho yake. “Jamani, hebu angalieni kule!” Wote wakageukia kule alikoangalia kijana huyo. Lo! Si taharuki hiyo iliyowapata! Waliona pandikizi la barafu lililokua kubwa kupita kiasi, likielea na kuelekea kule walikokuwa wao! Abiria wote wakaanza kulalama kwa hofu. “Sasa tutafanyaje jamani? Manahodha, hebu jitahidini kufufua injini tuondoke!” Walitoa wazo hilo bila kufikiri, maana walifahamu fika kuwa tangu hapo awali, injini ya meli ile ilishindikana kabisa kuwaka. Na wakati wakilalama, waliuona ule mwamba wa barafu ukiwaendea kwa kasi sana. Wote wakapiga kelele kwa pamoja “ Mungu wee wa mbingu na ardhi! Tusaidie waja wako sisi!” Walitafuta mahali pa kukimbilia lakini hawakupaona. Wakaenda huku na huko, ingawa walipofanya vile walijiweka kwenye hatari ya kuanguka na kukanyagana, maana ile merikebu ilikuwa ikisuwa suwa kila upande! “ Tulieni mahali pamoja jamani, mkienda huku na huko, mtaumizana!” Manahodha waliwaonya abiria wao, ambao hawakuwasikiliza hata kidogo!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe alinyamaza kimya akiwaza, kwani miongoni mwa watu wote waliokuwa ndani ya merikebu ile, ni yeye peke yake aliyekua anaelewa kinachoendelea. Alifahamu fika kwamba baharini kulikuwa na majini ambao ingawa baadhi yao walikuwa ni wema, lakini wengine hawakuwa na nia njema na binaadamu. Alikumbuka jinsi jini Makatta na wenzake walivyoweza kuyadhibiti mawimbi ya bahari. “Sijui majini hao watakuwa wamechangia vipi katika janga hili mbele yetu!” Kibwe aliwaza. Lakini muda si muda wakati Kibwe akitafakari kuhusu yote hayo, ghafla ile merikebu yao ikapigwa kumbo na mwamba wa barafu baharini! Lilikuwa ni kumbo kubwa mno, kiasi kwamba merikebu ile iligawanyika vipande viwili, na abiria wakagawanyika sehemu tatu! Huku kelele na mayowe vikitawala anga ile ya eneo la tukio, baadhi ya abiria waliporomoka na kuangukia baharini, wakawa wanatapatapa kujinusuru wasife maji, wengine wakawa wanashikilia vipande vya mbao zilizobomoka kutoka merikebuni, na wengine walikuwa katika mabaki ya ile merikebu, lakini wakielea kwenye maji yaliyojaa mle ndani! Kibwe alikuwa miongoni mwa wale walioangukia baharini, na Hanga akawa ananing’inia, akijishikiza kwenye nguzo ya merikebu, na kuponea chupuchupu kuangukia majini! Hata hivyo, hakunusurika kwa muda mrefu, kwani kwa mara nyingine, mwamba mwingine wa barafu uliokuwa ukiwajia, ukayakumba yale mabaki ya merikebu na kuwabwaga watu waliokuwa ndani ya chombo kile, na wale waliokuwa wakining’inia kwenye nguzo na mbao, akiwemo Hanga! “Mama wee! Tunakufa leo jamani!” Kelele zilisikika, na wengine walilia kwa zogo, bila kusema lolote!

    Wengi miongoni mwa abiria walioangukia baharini walijitahidi kuogelea ili kujinusuru na kuzama, lakini wapi! Wengi walikufa maji! Kibwe naye akawa anazama chini ya maji, na kama vile yuko ndotoni, akajihisi akizidi kwenda chini bila kizuizi, kwani wakati wa zile heka heka za vikumbo vya miamba ya barafu, Kibwe alijigonga kichwani na kitu kisichojulikana na kupoteza fahamu. Kwa hiyo alivyokuwa anazama, alikwenda moja kwa moja……akaenda! Akaenda! Hadi akafika mbali mno chini ya bahari. Lakini alipokuwa akienda chini, Kibwe alikua akisikia sauti kwa mbali, ikimwita jina lake. “Kibwe! Kibwe! Amka Kibwee! Amka!” Wakati likitajwa jina lake, Kibwe pia alihisi kuwa ameshikiliwa na huku akitingishwa tingishwa. Kumbe Hanga aliyeporomoka baharini baada ya Kibwe kuangukia humo, alimuwahi mwenzake kabla hajafika chini zaidi ya bahari bila fahamu. Kijana huyo alikuwa akijitahidi kumsaidia mwenzake asizame, kwa hiyo ingawa hakufahamu kuogelea, kwa mastaajabu makubwa akawa anaogelea kwa mkono mmoja, na kwa mkono mwengine akijaribu kumkokota Kibwe na kupanda naye juu ya bahari ili kupata hewa safi! Hanga alihisi kuwa tukio lile la uwezo mkubwa wa kuogelea lilihusiana sana na upekee wa Mwana Mteule aliyeshirikiana naye!

    Wakati Hanga akifanya jitihada za kujinusuru yeye na mwenzake, mara mbele yake akaona kitu kipana mno, labda kama kinywa cha mnyama gani sijui! Labda ni aina fulani ya mnyama wa bahari, aliyekuwa anajiandaa kuwameza yeye na mwenzake! Hanga aliogopa sana. Akajaribu kugeuka na kumkokota mwenzake, lakini yule mnyama akamuwahi! Akafunua kinywa chake zaidi, na bila kupoteza muda, akawameza vijana wale wote kwa urahisi mkubwa! Moja kwa moja Hanga na Kibwe wakaporomoka kwenye tobo la giza nene, wakipita katika njia nyembamba, na hatimae kutuwa chini! Walikua tumboni mwa mnyama mmoja wa ajabu!

    Muda fulani baadae, Hanga na kibwe wakawa wamelala kwa muda mrefu kwenye nyasi. Kwa kuwa jua lilikuwa likiwamulika usoni, taratibu wakaanza kuamka . Kibwe aliamka mwanzo, na akawa anaangaza angaza huku na huko, aweze kuelewa mahali alipokuwa. Hakukumbuka mara moja mikasa iliyowasibu. Pembeni kwake, Hanga naye akafumbua macho, akaamka na kuketi kitako. Hakujua mahali alipokuwa, mpaka alipomuona kibwe pembeni yake. Akakumbuka kuwa wakati fulani Kibwe alikuwa amezimia. “Ah, kibwe rafiki yangu, umepona? Unajisikiajae sasa?” kibwe naye alifurahi kumuona Hanga, na akamwambia kuwa yeye hakuwa na tatizo lolote. Isipokuwa kwa pamoja walisikitika kuwa hawakuwa na taarifa yoyote kuhusu wenzao waliokuwa nao baharini, baada ya lile janga lililotokea katika meli ya mfalme KashKash. Kabla ya kubadilishana mawazo, ghafla Hanga akapiga ukulele wa kukata matumbo! Kilima kidogo alichokiona mbele yake kwa muda wote waliokuwa pale na mwenzake, kilikuwa kinatembea kuwafuata pale walipokuwa! Hanga akagundua pia kuwa kilima hicho kilkuwa na shingo…hapana! Siyo shingo tu! Kilima hicho kilikuwa na umbo la Kobe, kwa hiyo sehemu moja kulikuwa na kichwa chenye macho yaliyokuwa yakizungushwa zungushwa! Lo! Kilima chenye uhai!

    Bila ajizi Hanga akainuka na kuanza kukimbia, huku akimkokota Kibwe pamoja naye! “Haraka Kibwe! Tukimbie ndugu yangu! Hatari hiyo mbele yetu! Jamani, mbona tuna mkosi hivi!” Hanga alilalamika huku akihofu kupita kiasi. Kibwe alisimama na kumfuata mwenzake, huku akiangalia kule mwenzake huyo alikokua anaelekeza kidole chake. Lakini mara Kibwe akasita na kukodoa macho kwenye kile kilima. “Kimbia Kibwe! Unangoja nini sasa? Twende bwana weee!” Hanga alimsisitizia mwenzake huku akimburuza. Kibwe alimuonyesha ishara Hanga kuwa asubiri kidogo. Ingawa mwenzake yule alikubali kusubiri, lakini alijiweka mbali kabisa na Kibwe na kile kilima cha ajabu. Aliwaza kuwa kama Kibwe alikuwa tayari kujitosa kwenye janga jingine litakalotokana na kitu kile chenye uhai kilichofanana na kilima cha aina yake, yeye Hanga hakuwa tayari kujitoa kafara namna hiyo!

    Kwa mshangao mkubwa uliochanganyika na furaha, Kibwe alisogea karibu zaidi na kile kilima cha hatari! Halafu, eti kwa furaha kubwa zaidi, kijana yule akakirukia kile kitu ambacho Hanga alikiita kilima cha ajabu, na ingawa alianguka chini kwa kufanya hivyo, Hanga akamuona akiinuka na kuanza kupapasa kwenye kile kilma kama mtu aliyechanganyikiwa! “Amepatwa na nini mwenzangu huyu jamani?” Hanga aliwaza huku akihisi kuwa wakati wowote ule, jambo la hatari lingetokea. “Ah! Kumbe ni wewe! Shikamoo babu! Hivi umefika vipi huku? Nimefurahi sana kukuona rafiki yangu!” Kibwe alirukaruka kwa furaha, wakati mwenzake Hanga akimwangalia bila kumuelewa. “Bila shaka mwenzangu huyu alipojigonga kichwani tulipotupwa baharini kutoka kwenye merikebu, akili yake aliathirika masikini weee!” Hanga aliwaza, akijua kuwa mwenzake yule amepata kichaa, ndio maana hata hakujali kuhatarisha maisha yake!

    Baada ya kuelewa kuwa kile ‘kilima’ hakikuwa dude la hatari, Hanga akauliza. “Sasa, kama wewe ni Mzee wa Busara, hebu tueleze, kwa busara zako, hivi sisi tulitoka vipi kwenye tumbo la yule mnyama mkubwa baharini, na je alikuwa ni mnyama gani yule?” Mzee wa Busara akamwangalia Hanga, na kisha akacheka sana! Kibwe hakujua kama walimezwa na mnyama wa bahari, kwani yeye alizirai baada ya kujigonga na nguzo ya merikebu, baada ya meli ile kuvunjika kwa tufani na mwamba wa barafu majini. Hivyo, alistaajabu sana, na kisha akasikiliza kwa makini maelezo ya Mzee wa Busara. Baada ya kucheka sana, Mzee wa Busara alisema, “Mlipotumbukia baharini wakati Kibwe alipokuwa anazama, kulikuwa hakuna uwezekano wa wewe Hanga peke yako kumuokoa na pia kujinusuru nafsi yako, kwa kuzingatia hata kuogelea hukufahamu vizuri!. Kwa kuwa nilifahamu hivyo nilifika huko haraka kuwaokoa nyote wawili, kwa hiyo nikawameza, na kisha kuwaleta hapa kwenye ardhi iliyorutubika.” Hanga na mwenzake Kibwe wakamwangalia Mzee wa Busara kwa faraja kubwa, na Hanga hakuamini aliyoyasema, isipokuwa mwenzake Kibwe aliyemfahamu.. , Kibwe alifahamu kuwa Mzee ‘Kaka’ hakuwa Kakakuona wa kawaida, bali alikuwa ni mnyama wa kimazingaombwe kama alivyokuwa Bunga. “Tunakushukuru sana mzee ‘Kaka,’ kwani bila ya wewe tungekufa maji” Kibwe alisema, na Hanga naye, huku akimwangalia Kibwe na huku akihofu kuuliza chochote, akajiuliza kwa nini mwenzake yule hakuhoji kabisa kuhusu ile taarifa ya ajabu ya Mzee ‘Kaka?’ Hata hivyo, kwa kufuata alivyosema Kibwe, naye akatoa shukurani zake kwa Mzee wa Busara. Baada ya hapo, Kibwe akataka kujua hatua inayofuata katika safari yake ya ajabu.

    Mzee wa Busara alimwambia Kibwe aende hadi nchi ya shamsi, upande wa mashariki ya katikati ya dunia, kilometa chache tu kutoka pale walipokuwa. “Tunza upanga wako huo wa radi, maana utauhitaji sana. Huko uendako. Utakwenda katika sehemu yenye majabali yaliyozingira mto Sakura, yaani mto mkubwa wa maji, ambako utakutana na joka la vichwa saba na ambalo utapigana nalo na kulikata vichwa sita, kwa urahisi. Lakini kichwa cha mwisho ambacho ni cha shaba, kitakusumbua sana kukikata. Kwa msaada wa upanga huu, hatimae utafanikiwa kukikata, isipokuwa baada ya hapo, utaanguka na kuzirai!” Hanga akatoa macho kwa hofu, kwanza ya kuambiwa kuwa watakukutana na hilo joka kubwa la ajabu, na pili kusikia habari kwamba mwenzake Kibwe, atazirai tena! “Sasa asipoamka je? Itakuwaje?” alimuuliza mzee ‘Kaka.’ “Hapo ndipo msaada wako utahitajika. Mara tu atakapoanguka, haraka utachukua ndoo ya maji na kummwagia mwili mzima, naye atazinduka baada ya muda” Hanga hakujua watapata wapi hiyo ndoo ya maji huko kwenye majabali matupu, na alipomuuliza Mzee wa Busara, mzee yule akamjibu kwa methali ya busara, kwamba ‘mwenye macho haambiwi tazama,’ kwani huko huko waendako, wataelewa watakapopata hiyo ndoo ya maji. Pamoja na mawaidha hayo, Kibwe na Hanga wakafahamishwa kuwa hilo joka watakalokutana nalo, sio joka la kawaida. “Joka hilo ni Maimuni, mwana wa mfalme wa majini ya bahari na mito ya maji, anaeishi chini ya huo mto Sakara!” Lo! Mikasa juu ya mikasa. Hanga akawa dhoful hali kwa hofu!

    Hanga alipata wasiwasi tmkubwa. Katika maisha yake, alimsikia bibi yake akisema kuwa majini ni viumbe wabaya sana ambao hugeuka upepo na kuwakumba wanaadamu, na baada ya kukumbwa na jinni, mara nyingi wanadamu hupata ugonjwa wa kiharusi. Mwanzoni Hanga hakuelewa kuhusu huo ugonjwa wa kiharusi, lakini baadae alifahamu kuwa huo ni ugonjwa ambao watu hupooza upande mmoja wa mwili. “Mtoto wa jirani yetu ……alikumbwa na upepo mbaya alipokuwa anapita njia panda, ndio maana amepata kiharusi.” Bibi yake alisema wakati mmoja, na alipomuuliza kuwa upepo mbaya ndio upepo gani, bibi yule alimwambia kuwa ni majini waovu. Na sasa eti Mzee wa Busara anasema kuwa majini ni majoka ya baharini. Inakuwaje? Alitaka sana kujua, kwa hiyo akamuuliza Mzee ‘Kaka.’ “Hivi babu, ni kweli duniani kuna majini? Na majini ni nyoka au ni upepo mbaya? Na je wanaishi wapi?” Mzee wa Busara alimwambia kuwa majini ni wa aina mbalimbali, na akamfafanulia kwa undani zaidi, akisema; “Kijana , kumbuka kwamba duniani hawaishi wanaadamu peke yao, bali majini nayo huishi miongoni mwao, lakini hawaonekani kwa macho . Kama vile ilivyo kwa wanaadamu, utaona kuwa wapo waliokuwa wema na wapo ambao ni waovu sana, na kwa majinni, wapo waliokuwa wema na wanaotenda matendo mazuri, na wapo ambao ni waovu wanaotenda matendo ya uovu. Kwa hiyo, wale waovu wanapotaka kuwazuru wanaadamu, hujigeuza katika maumbile yatakayo wasaidia kutekeleza uovu wao walioukusudia. Mara nyingine hugeuka maji, mara upepo, mara wanyama wa aina waipendayo, na kadhalika. Si rahisi kuwatambua majini wanapofanya uovu wao.” Kibwe na Hanga wakaduwaa, wakitafakari maelezo hayo ya Mzee wa Busara. Kibwe aliogopa sana kupambana na adui mwenye hila kama hizo!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe na Hanga walitembea kwa saa nyingi, na kutokana na ukame wa jangwani, njiani wakanywa na kumaliza maji yote waliyofungasha kutoka kule kwa Mzee ‘Kaka.’ Hivyo, baada ya hapo, walikosa kabisa maji ya kuondoa kiu, kwani kwa jinsi ukame mkubwa ulivyotawala sehemu hizo, kwenye maeneo yote waliyokuwa wakipita, hawakukuta mto wala vijito vya maji. Huku na huko walizingirwa na jangwa, na ardhi haikuwa na mmea hata mmoja! “Hivi tutafanyaje Kibwe? Koo langu limekauka kabisa, na hata nguvu sina,” Hanga alimwambia mwenzake. “Tujitahidi kutembea kidogo, maana huenda njiani tutawakuta wenyeji ambao ni wakazi wa nchi hii, na watatuelekeza sehemu ya kupata maji.” Kibwe alimfariji mwenzake, na hivyo wakasonga mbele na safari yao. Baada ya mwendo wa saa moja hivi, Hanga akaona kwa mbali, nyumba moja ya tope iliyojitenga, na iliyokuwa kwenye kichaka, ambako hawakuona nyumba nyingine yoyote zaidi ya ile. “Angalia! Kuna nyumba kule mbele! Huenda tukapata maji huko, hebu tuharakishe!” kijana yule aliyekuwa na kiu sana, alimuhimiza mwenzake Kibwe. Kwa hiyo kwa moyo wa matumaini, wawili hao waliharakisha na kufika kwenye hiyo nyumba. Hapo, walibisha hodi ili waweze kumpata mwenyeji, watakaye muomba hayo maji.

    “Hooodiiiii! Hooodi humu ndani, Hodiii!” Kibwe na Hanga wakawa wanapokezana kubisha hodi, lakini hakuna mtu aliyejibu kutoka ndani. “Hooodiiii! Humu ndani hakuna watu? Hooodiii!” Waliendelea kubisha hodi, kwa sababu pale palikuwa ni mahali pekee walipopatarajia kupata msaada, maana kila walipoangalia huku na huko, hawakuona dalili yoyote kuashiria kuwa sehemu ile ilikuwa na watu. “Wenyewe mpoo?” waliuliza tena kwa sauti ya juu zaidi. Hata hivyo hawakujibiwa. Wakabisha tena hodi kwa sauti ya juu zaidi, na mara hii wakasikia sauti hafifu ya mwanamke aliyesikika kama mzee. Akawakaribisha ndani kwa furaha. ”Karibu! Karibuni ndani!” Kusikia hivyo, haraka wale vijana wakaingia ndani, wakijua kuwa baada ya muda, tatizo lao la kiu ya maji litapatiwa ufumbuzi. Walipofika ndani wakaona mwenyeji wao alikuwa ni bibi mmoja kizee, hivyo wakamwamkia; “Shikamoo bibi. Habari za hapa?” Kizee yule akaitikia, “Marahaba, wajukuu zangu, Hamjambo? Na je, mnatokea wapi, maana si mara nyingi watu kupitia huku kwetu, na mnakwenda wapi.”

    “Kusema kweli bibi, hatujui tutokako wala tuendako. Isipokuwa katika safari yetu ndefu, tumeishiwa maji ya kunywa, na ndio tukaja huku kuomba maji, maana tuna kiu sana, na safari yetu nadhani bado ni ndefu,” Kibwe alisema kwa niaba ya mwenzake Hanga. “Ndio bibi, tutashukuru sana ukitupatia hata robo kikombe tu ya maji, yatatutosha,” Hanga akaongezea .

    “Ah! Wajukuu zangu wee! Sijui niwaambie nini! Maana hiyo nusu kikombe ya maji ndiyo niliyobaki nayo. Kwa hakika katika nchi hii, tuna shida kubwa ya maji. Hivi ninavyoongea, leo hii Sultani wetu anamtoa kafara binti yake kitinda mimba, ili raia wake tuweze kuchota maji mtoni kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi.” Yule bibi aliwafahamisha wale vijana. “Kabla ya hapo, Sultani aliwatoa kafara mabinti zake sita, mmoja kila mwaka, nasi tukaweza kupata maji kila mwaka kila baada ya tukio hilo la kusikitisha,” alieleza bibi kizee.

    “Sasa bibi, hao mabinti wanatolewa vipi kafara? Wanakatwa vichwa, au wanatoswa mtoni? na je, ili kumridhisha nani ambaye akifurahi ndio ataruhusu watu wachote maji?

    Eti tuliambiwa kuwa mabinti hao hupelekwa kwa Mfalme wa majini!” Vijana wale walijaribu kupata majibu kutoka kwa yule bibi kizee.

    “Kwenye mto mkubwa ambao ndio pekee unaotupatia maji, huishi joka moja kubwa sana. Joka hilo na wenzake huwazuia raia wa nchi hii kuchota maji mtoni mle, na limeweza kuwadhuru raia wengi sana hapo awali.” Bibi yule aliwaeleza wale vijana, waliopenda sana kujua Sultani Bashar wa jiji la Majabali huko Shamsi alifahamu vipi kuwa tatizo lile lingetatuliwa kwa kuwatoa kafara mabinti zake. “ Ama kwa hakika baada ya shida kubwa ya maji kuligubika jiji la Majabali nchini Shamsi kwa zaidi ya miaka kumi, ambapo wananchi wake waliotegemea maji ya mto Sakara kwa matumizi ya kila siku walishindwa kuyapata kutokana na kuwepo katika mto ule nduli huyo niliyewaambia, raia wote walielekeza masikitiko yao kwa mtawala wao Sultan Bashar, kila yalipotokea maafa kwa baadhi yao yaliyosababishwa na joka hilo. Mara kwa mara walilazimika kupiga mbio kwenye kasri la mtawala wao wakilia machozi na kulalama wakitafuta msaada, jambo ambalo lilimsikitisha mno kiongozi wao Bashar…..”

    JINI MAIMUNI WA MAJABALI.

    “Maulana Sultani! Maulana Sultani! Yametokea tena maafa! Baadhi ya waliokwenda mtoni kuchota maji wameshambuliwa na lile dude lisiliojulikana na kuuawa! Aah! Mtukufu Sultani!Tutafutie ufumbuzi wa haraka wa janga hili, maana raia wako tunamalizika!” Vilio hivyo na maombolezo vilitawala mno kule Majabali mara kwa mara kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi. Lakini masikini kwa muda wote huo, Sultani Bashar hakuwa na ufumbuzi wala jawabu kwa tatizo lile.”Sijui nifanye nini kuyanusuru maisha ya raia wangu kutokana na dude hilo ambalo kwa mtu wa kawaida si rahisi kupambana nalo.” Sultani alizungumza kwa masikitiko na washauri katika baraza lake la ushauri. Nao washauri wake wenye busara na hekima kubwa, hawakuweza kumpa matumaini yoyote Mtawala wao, ya utatuzi wa suala lile. “Ama kwa hakika mtukufu Sultani huu ni msiba mkubwa kwa nchi yetu, ambao hadi sasa ni kitendawili kisichoteguka.” Walimjibu kwa masikitiko. “Ingawa upo umuhimu mkubwa wa kuwanusuru raia dhidi ya nduli yule hatari, lakini pia ni muhimu zaidi na ni wajibu kwetu kuwaondolea tatizo la kukosa maji. Kwa bahati mbaya yote mawili yana ugumu mkubwa kwetu kwani hatuna majawabu nayo!” Walijieleza kwa Sultani wao wakiwa na majonzi kupita kiasi! Naam, hiyo ilikuwa ndiyo hali katika nchi ya Shamsi kama walivyoelezewa Kibwe na Hanga na yule kizee waliyemuomba maji. Ni hali iliyoisononesha jamii nzima ya Shamsi kwa muda huo wa zaidi ya muongo mmoja!

    Siku moja Sultani Bashar alipokuwa usingizini aliota ndoto ya kutisha mno! Katika ndoto ile alisikia sauti nzito ya ajabu iliyotokea nje ya kasri lake. Uzito wa sauti ile ulilitetemesha kasri zima lililo sukwasukwa kama meli iliyopambana na mawimbi makubwa ya bahari au dhoruba! Ilikuwa ni sauti yenye mwangwi wa kipekee! ‘Mmmmmmhhhh! Tetteeetetetettee! Mmmmmmhhh! Tetteeeteeettee! Heneee Maimuni ( mimi ni Maimuni ) wa Makatta wa Makattani! Mmmmmhhhh! Amani haipatikani Shamsiii! Eeeehuuun! Eeeehuuun! Sakara itatoa maji na kuleta amani kama kila mwaka ataletwa kwenye mto huo, mmoja kati ya mabinti zako saba na kumwacha ufukweni mwa mto! Ukifanya hivyo maafa ya raia wako yataondoka! Watachota maji kwa amani na usalama…….! Tattaaaatattaaaatattaaahh! Na usipofanya hivyo nitawafuata raia wako hadi nchi kavu na kuwateketeza kwa makundiiiii….! .Taaaattaaaataaaattaaaaaahh! Ha ha ha ha haaaaaaaa!”

    Sultani aliingiwa na hofu kubwa sana, na wakati ule akawa anaisikia sauti hiyo ya aina yake ikitoweka taratibu, na kasri lake nalo likipunguza kasi ya msukosuko, na palepale akashituka na kuinuka kitandani huku moyo wake ukidunda, na akijaribu kuelewa kama aliyoyasikia yalitokana na ndoto au ni ukweli. Lakini alipoyatafakari maneno ya maagizo ya vitisho yaliyotolewa, aliona kuwa yamehusiana mno na hali ya nchi yake. “Hhhhhaaaa! Hhhhhaaaa! Hhhhhaaaa!” Sultani alipumua wakati mke wake, Malkia naye akigutuka na kumkumbatia mumewe kwa wasiwasi. “Aaaaa! mume wangu! Umepatwa na nini tena usiku huu laazizi? Mbona hivi?” Sultani hakujibu bali aliendelea kuhema isivyo kawaida. Baada ya muda wa kutosha, akamweleza mkewe kuhusu ndoto aliyoota. Lo! Malkia naye aliogopa mno hususan aliposikia habari ya kuwatoa mhanga mabinti zake! “Hapana mume wangu! Hatuwezi kufanya hivyo asilani! Kamwe sintakubali!” Mama yule mzazi wa wana alimaka. Lakini Sultani kwa maneno ya busara, alimtuliza mkewe akimkumbusha kuwa ingawa wao ni wazazi wa mabinti zao saba, lakini wao pia ni watawala wa raia wengi mno ambao wamo kwenye matatizo makubwa. “Mmoja mmoja raia wetu wanapoteza maisha yao ama kwa kushambuliwa na nduli wa mto Sakara, au wanateketea kwa makundi kwa kukosa maji. Je, unadhani ni nani atakaye wanusuru na janga hilo kama si mimi, wewe, na mabinti zetu? Kama kujitolea wanetu ndio ufumbuzi wa tatizo hili sugu, basi na iwe hivyo!” Alisema kiongozi yule mwema.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Masikini Malkia alilia sana kwa uchungu, lakini hatimae watawala wale wawili wakaamua kujitolea binti yao mmoja kila mwaka, mabinti waliopotelea kwenye mton Sakara, na hivyo baba yao Sultani Bashar kufanikiwa kuwanusuru raia wake kwa miaka sita. Sultani na mkewe walibaki na binti yao mmoja kitinda mimba waliyempenda sana, Bhaduri binti Sultani! Maelezo ya mkasa ule wa nduli Maimuni wa Sakara na Sultani Bashar wa Shamsi yaliyotolewa na bibi kizee, yaliyosadikisha taarifa ya Mzee wa Busara kwa Kibwe na Hanga. Vijana wale waliduwaa kabisa na kubutwaika, wakasahau kiu ya maji waliyokuwa nayo! Kutokana na maelezo ya awali ya Mzee wa Busara Kibwe aligundua kuwa wamekwisha wasili nchini Shamsi, na akatanabahi na kutambua kuwa kazi yake iliyompeleka kule haitakuwa nyepesi!

    Ama kwa hakika maajabu yalizidi kumtokea Kibwe, kila moja likizidi la awali! Kwanza wala mawe, kisha kisiwa cha mazimwi wala watu, halafu majini wageuzao watu kuwa mawe ya theluji…… na sasa….. eti kuna joka kubwa linalozuia watu kuchota maji, hadi litakapopelekewa warembo mabinti Sultani kama kafara! Ni mabalaa makubwa! Vijana wote wawili walizidi kubutwaika, waliposikia ile habari ya mwisho isiyokuwa ya kawaida, ya mabinti Sultani wanaotolewa kafara au muhanga! Na kwa sababu hiyo, hawakutaka tena kuomba maji ya kunywa, kitu ambacho kilikuwa na utata mkubwa katika sehemu ile ya mashariki ya katikati ya dunia. Kibwe na Hanga walizidi kupata unyonge mkubwa kuhusu jambo lile kwani wakati ule yule bibi alipokuwa akizungumza nao, alikuwa akikwangua kwa kata ya maji, chini kabisa ya mtungi na kisha kutoa maji yaliyokuwa na vumbivumbi na uchafu, na kuanza kuyanywa!

    Huku wakishangaa, na pia kusikitika, Kibwe na Hanga walimuuliza yule kizee, “Hivi lile joka huwafanya nini wale mabinti baada ya kuwachukua?” Yule bibi alikohoa kidogo, akapapasa kata yake ya maji, na kunywa funda moja ya maji, kisha akaendelea kusema;

    “Sidhani kama kuna yeyote anayefahamu yanayowasibu wale mabinti baada ya kuchukuliwa na lile joka Hata Sultani mwenyewe hajafuatilia kujua zaidi mambo yanayowasibu mabinti zake. Ni msiba mkubwa sana huo wajukuu zangu!” Wale vijana walipata majonzi makubwa, hususan waliposhuhudia yule bibi akihangaika kunywa maji kidogo sana ambayo ni machafu yaliyobakia mtungini. Kibwe alipiga moyo konde ‘liwalo na liwe’, na akasema; “Subiri kidogo bibi, baada ya muda si mrefu, tutakuletea maji ya kunywa. Vuta subira kidogo tu!” Hanga akamwangalia mwenzake kwa kumshangaa. “Sasa tena Kibwe anaanzisha nini kingine?” alijiuliza, huku akihofu kuwa mwenzake yule alitaka kufanya vile alivyoambiwa na mzee wa busara, yaani kupambana na joka la vichwa saba! Hivyo, bila yule kizee kuona, kijana huyo muoga akawa akimfinya Kibwe, akiashiria kuwa aachane na mambo hayo! Na bibi kizee naye, hakuwa tayari kumwachia yule kijana ajitose kwenye hatari huko mtoni. “Hapana mjukuu wangu, usifanye hivyo hata kidogo, kwani utajitafutia madhila makubwa. Nadhani leo jioni baada ya hilo joka kumpata Bhaduri binti Sultani, kila mtu atapata maji ya kutosha. Kwa hiyo nadhani wewe ndiye unayestahili kuvuta subira kidogo!” Hanga alimuunga mkono bibi kizee, kwa kusema; “Ni kweli kabisa Kibwe, kwani kwa kujipeleka huko, unaweza kuhatarisha maisha yako.” Kibwe naye hakuwa tayari kusubiri eti mpaka lile joka limchukue yule binti. “Lakini bibi nadhani bado hujaelewa nia yangu. Nataka leo iwe mwisho wa joka hilo kudai kafara. Umesema kuwa huyo ni binti wa mwisho wa Sultani. Sasa baada ya yeye kutolewa kafara mwakani mtapataje hayo maji? Au Sultani ataanza kuwatoa kafara raia wake mmoja mmoja? Sidhani kama hilo litakuwa ni jambo la busara. Yule bibi alishangaa sana kuona jinsi yule kijana alivyojiamini. Akamwombea Mungu, aende na kurudi salama. “Mjukuu wangu, kama unadhani kuwa unaweza kulipatia ufumbuzi tatizo hilo, sina la kusema, isipokuwa nakuombea kila la heri, na bila shaka Mungu atakuwa pamoja nawe!” Bibi yule alimuombea hivyo, akihisi kuwa labda Kibwe anaweza kuwafikisha raia wa Shamsi kwenye hatima ya tatizo lao sugu, ingawa pia alihofu mno kuwa huenda kijana huyo akapotelea hukohuko mtoni, kama ilivyokuwa kwa mabinti Sultani sita!

    Hanga alifuatana na Kibwe shingo upande, na wakaondoka wakiwa wamebeba ndoo mbili za maji, wakielekea mtoni. Kijana yule alishangaa sana, kwani wakati walipokuwa wakienda mtoni kwa joka la vichwa saba, Kibwe hakuwa na wasiwasi asilani! Hanga hakufahamu kwamba mwenzake alikuwa anakumbuka mawaidha ya Mzee wa Busara, kuwa upanga wa radi humpa nguvu ya ushindi kila anaye utumia. Alikumbuka siku alipoutumia upanga ule kule kaskazini ya mbali kwa Mfalme KashKash, na jinsi alivyouzungusha hewani kwa maelekezo ya Mzee Kaka, ili kujinusuru na majini wa upepo wa bahari. Bila kutegemea, upanga huo ulitoa cheche za moto zilizogeuka kuwa vienge vya moto mkali, vilivyo wateketeza majini hao. “Usipoangalia, upanga huo unaweza kukudhuru mwenyewe badala ya kumdhuru adui unaye pigana naye” Mzee wa Busara alimuonya Kibwe. “ Nitajitahidi kuwa mwangalifu Mzee ‘Kaka’. Kibwe aliahidi. Mzee wa Busara alikohoa kidogo kama kawaida yake na kisha akasema, “Nina furaha kubwa kuweza kukusaidia Kibwe, isipokuwa kuhusu kujichunga usidhurike na huo upanga wa radi, usijitahidi tu, kuwa mwangalifu na upanga huo, bali KUWA MWANGALIFU.” akasema kwa msisitizo! Kibwe alimuelewa vizuri sana Mzee wa Busara!

    Kibwe, akiwa na upanga wake kiunoni, uliofungwa vizuri kwenye ala yake, akifuatana na Hanga wakiwa na ndoo zao walizozichukua kwa bibi kizee ili kumpelekea maji watakapo yapata, walianza kuelekea mtoni, ambako Bhaduri binti Sultan, kitinda mimba wa Sultani Bashar alikuwa akisubiri kuchukuliwa na joka kuu, akiwa ni kafara kwa nyoka huyo. Walipokaribia kufika, macho yao yalivutiwa na ukubwa wa majabali yaliyokuwa mbele yao. Waliposogea karibu zaidi, macho hayo yalizidi kuvutiwa, walipomuona binti mrembo wa ajabu, aliyeketi kwenye kiti kikubwa cha enzi juu ya jabali. Wakazidi kumsogelea, na hapo ndipo walipogundua jinsi binti huyo alivyopambwa! Na pale alipokuwa, upepo mororo wa manukato mchanganyiko, ulienea sehemu yote ! “Ama kwa hakika Sultani ameamua kuwavutia na kuwafurahisha majini wanaowachukua binti zake, maana nakumbuka bibi alisema kuwa majini hupenda sana manukato!” Hanga alimnong’oneza Kibwe, ambaye hakujibu kitu, bali alizidi kumsogelea Bhaduri binti Sultani Bashar!

    “Habari za asubuhi binti Sultani, ” Kibwe alimsalimia Bhaduri.

    “Habari nzuri kaka yangu. Vipi, mbona mnakuja na ndoo za maji wakati huu ambapo hata bado hawajaja kunichukua? Mnataka kusababisha matatizo kwa raia wa Shamsi? Au tuseme ninyi ni wageni katika nchi hii?” Bhaduri alimuuliza Kibwe, huku akiwashangaa yeye na mwenzake. “Nadhani ni bora msubiri hadi nitakapo chukuliwa, ndipo mje kuchota maji kwa amani kaka zangu, na si vinginevyo!” Binti Sultani aliwasihi vijana wale wawili. Lakini Kibwe alitabasamu tu, na kusema, “Naona leo tutasubiri pamoja, tujue mwisho wa tatizo la jamii ya nchi hii.” .

    Wakati akisema hivyo, alikuwa ameanza kuitumbukiza ndoo za bibi kizee mtoni ili kuzijaza maji , na alifanya hivyo kwa fujo mno, akiyakoroga koroga yale maji na ndoo yake, kama kwamba alikuwa akilichokoza lile joka huko lilikokuwa! Hanga hakupenda kitendo hicho asilani, kwani kilimpa hofu kubwa. Alihisi kama vile wakati wowote wangevamiwa na lile dude la vichwa saba kutoka mtoni! Pale aliposimama, jasho jembamba lilimtiririka kwa hofu, akawa anaangalia huku na huko, akitarajia dude kuwa joka maimuni litatokea upande wowote! “Leo ndio mwisho wetu,” aliwaza, huku akitetemeka bila kizuizi.

    Binti Sultani hakuelewa kijana yule mkorofi alitokea wapi, aliyetaka kuleta matatizo kati ya raia wa baba yake na hilo joka la kutisha, ambalo awali kabla dada zake hawajatolewa kafara, liliwateketeza raia wengi wa nchi yao waliojaribu kuchota maji pale mtoni. Hakuelewa nia yake ilikuwa ni nini. Alimshangaa sana alipoendelea kuchota maji kwa fujo, akaweka ndoo zake pembeni, na kisha kumwamuru mwenzake kwa kujiamini. “Mpelekee yule bibi kizee ndoo moja, halafu urudi hapa haraka ili tusubiri pamoja.” Hanga aliifurahia mno amri ile, ilimradi tu, aondoke pale mahali pa hatari. “Sawasawa, ngoja niwahi....” Bila kupoteza muda, Hanga akachukua ndoo ya maji na kutokomea vichakani, akirejea kwa bibi kizee!

    Kibwe naye, akaketi karibu na binti Sultani, panga lake kiunoni, akisubiri kitakachotokea!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Punde si punde, upepo mkali ukaanza kuvuma, kama ilivyokuwa kawaida kila mwaka, wakati binti Sultani alipofuatwa na yule nduli wa vichwa saba. Dalili hizo mara nyingi ziliwatia hofu raia wote, ambao walikomelea milango yao, wakihofu dhoruba ambayo mara nyingine iliezua mapaa ya nyumba zao na kung’oa milango ya nyumba zilizokuwa hafifu. Siku ile ilipotokea dhoruba hiyo na kimbunga kibaya, vikachafua mno maji ya mtoni. Muda si mrefu, maji ya ule mto yakawa ni mawimbi makubwa yaliyoinuka juu sana na kumwaga maji kwa kuyarusha kila sehemu! Kutoka pale walipokuwa, Kibwe na Bhaduri wakatupwa chini na hayo mawimbi. Punde, ukajitokeza mlima mkubwa wa umbile la lile joka lililokuwa likisubiriwa! likajinyonga nyonga na kujitoa mtoni kwa hasira, likijileta juu ya jabali! Mara, kimoja kati ya vichwa vyake saba, kikaonekana kikifoka, kikimaka na kutoa povu! Alipoona kinywa kipana cha yule nduli, Bhaduri akapiga ukulele mmoja wa kusisimua, akihofu kuteketezwa “Mama yangu weeee! Tunakufa leo jamani!” Binti huyo alibabaika, bila kujua akimbilie wapi, kwani lile joka lilitanda pande zote!



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog