Search This Blog

KIBWE KATIKA SAFARI YA AJABU - 5

 







    Simulizi : Kibwe Katika Safari Ya Ajabu

    Sehemu Ya Tano (5)



    Wakati lile joka lilipofunua kinywa chake kwa hasira, Kibwe akasimama kishujaa , akainua upanga wake wa radi na kuuzungusha, na kwa kufanya hivyo, mara moja, kama muujiza upanga huo ulitoa ngurumo za radi za kusisimua, na wakati uleule Kibwe akalibwaga panga lile shingoni kwa hilo joka, na sekunde chache baadae, kichwa chake kikadondokea nchi kavu! Lakini Joka likazidi kujitoa nje ya maji kwa ghadhabu, na kutoa kichwa chake cha pili, kilichokua kikifoka na kutoa povu jingi. Kibwe akasema, “Leo ni leo, ama zako ama zangu.” Akainua tena panga lake la radi ambalo safari hii, pamoja na kutoa ngurumo, likatoa cheche za moto wakati lilituwa shingoni kwenye kichwa cha pili cha lile joka lenye hasira. Vivyo hivyo, vichwa vingine vya joka hilo vikachakazwa kimoja kimoja kwa dhoruba moja tu, kwa kila kichwa, wakati upanga ulipotoa ngurumo na cheche, hadi kilipobaki kichwa cha saba! Wakati huo, Hanga naye, aliyeagizwa na Kibwe kwa bibi kizee hapo awali, akatokea!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kimoja kati ya vichwa vyake hivyo saba yaani cha mwisho, ni cha shaba.” Kakakuona, Mzee wa Busara alimwambia Kibwe. Kichwa hicho kitakusumbua sana kukikata, na hatimae utakapokikata, utaanguka na kuzirai.” Akakumbuka vile Mzee wa Busara alivyomwambia Hanga, kuwa atakapomuona yeye amezirai, ammwagie ndoo nzima ya maji, ndipo atakapozinduka. Alipomuona Hanga akitokea wakati akikumbuka maneno yale ya mzee wa busara, akamtahadharisha mwenzake yule kuhusu jambo hilo. “Usisahau maagizo ya mzee wa busara. Nitakapozirai tu, mara moja unimwagie ndoo nzima ya maji.” Hanga akajibu kuwa hajasahau.

    Baada ya hapo, Kibwe alisimama tena, na kuanza kupambana na kichwa hicho cha shaba, na wakati ule, lile joka lilikua limekwisha choka! Kila aliponyanyua upanga na kuubwaga kwenye shingo ya kile kichwa cha shaba, ulisikika mlio kama vile panga lililopigwa kwenye mataruma ya reli, lakini kichwa hakikutetereka! Kibwe hakukata tamaa, bali alizidisha nguvu kila mara hadi katika dhoruba ya saba, kichwa hicho cha saba kilipoanguka, na Kibwe naye akaporomoka chini na kuzira! Palepale, Hanga akaruka na ndoo ya maji na kummwagia Kibwe mwili mzima! Lakini mara tu baada ya kitendo hicho, kikasikika kishindo nyuma yake na alipogeuka, akamuona Bhaduri naye kaporomoka chini na kuzirai kama Kibwe! Hanga ambaye anaposhtukizwa na kwa ghafla kama vile hushindwa kupata ufumbuzi wa haraka, kwahiyo akaanza kubabaika bila kujua la kufanya. “Sasa mbona na huyu naye amezirai? Nifanye nini sasa?” aliwaza, na mara, akajishauri na kuamua kuchota maji, huku akihofu mno, akihisi kuwa huenda likazuka kutoka mtoni joka jingine, labda lenye vichwa zaidi ya saba, na kuwazowa wote kwa kafara! Hata hivyo, hatimae kijana huyo aliyapata maji na kummwagia binti Sultani. Baada ya nusu saa ya kusubiri kwa wasiwasi huku vichwa saba vya lile joka vilivyoangukia nchi kavu vikimtolea macho, punde kidogo akawaona Bhaduri na Kibwe wakizinduka, huku Kibwe akiwa hoi, lakini mwenye tabasamu kubwa usoni kwake!

    Hanga na Kibwe walipokamilisha kazi hiyo nzito, wakiuacha mtumba wa lile joka umejilundika nchi kavu baada ya kujitoa wakati wa mapambano, Kibwe akakusanya vichwa vyote vya lile joka, na kuviweka kwenye fuko lake kubwa la gunia mbalo yeye hulibeba mgongoni kila anakokwenda. Alifanya hivyo kutokana na ushauri wa mzee wa busara.

    “Lazima ukusanye vichwa vyote na uvichukue…kohoo..kohooo (kikohozi) maana hivyo ni ushahidi wako………usisahau kabisa jambo hilo!”

    Kibwe hakuelewa maana yake, na alipouliza sababu ya kufanya hivyo, Mzee wa Busara alitabasamu tu, na kisha kumalizia na kikohozi kinachomjia mara kwa mara. Lakini hatimae Kibwe alifahamu kwa nini aliambiwa avikusanye vichwa vile na kuvichukuwa.

    Kibwe alimwambia Bhaduri asubiri pale pale juu ya jabali, kwani alitaka kuingia chini kabisa ya mto alikotoka yule nyoka wa aina yake, ili aweze kupata majibu ya maswali mengi aliyokuwa akijiuliza. Alikumbuka pia kuwa Kakakuona, yaani Mzee wa Busara, alimwambia kuwa lile joka sio la kawaida, bali ni mwana wa mfalme wa majini ya bahari na mito. Alimwambia kuwa majini hayo hujigeuza katika maumbile yoyote wanayotaka, hata maumbile ya kibinaadamu. “Majini hao wana miji yao chini kabisa ya mito na bahari.” Kibwe aliambiwa na mzee yule wa busara, na alikumbuka jinsi alivyo pambana na jini makata na wenzake kwenye mji mmoja wa chini ya bahari huko kaskazini ya mbali ya dunia. “Huoni kwamba kuingia huko chini ya mto ni hatari ?” Binti Sultani alimuuliza Kibwe, akihofu kuwa huenda akakutana na nyoka wengi wa aina ile. Lakini Kibwe alishikilia jambo hilo, akisema, “Ili niweze kuzuia matukio mengine kama haya yasitokee tena, ni muhimu sana nikafanye utafiti na kujua asili ya nyoka huyu niliyemuuwa,” Bhaduri na Hanga wakatazamana, kuona jinsi Kibwe alivyokuwa amejiamini kupita kiasi!

    Hanga aliogopa mno, alipoambiwa na Kibwe kuwa lazima wafuatane huko chini ya mto. “Mmi-mmi-mi na-ddhani- t-tuonndoke tu, K-ibwe! N-ni hatari k-kuin-gia humo n-dani!” Alisema Hanga huku akitetemeka kupita kiasi kwa hofu. “Twende bwana wee! Tutajua jinsi ya kujihami tukifika huko.” Kibwe alisema huku akimkokota mwenzake kuelekea upande wa mto , sehemu ya korongoni, ambako ndiko walikoingilia kwenda chini kabisa ya ule mto. Bhaduri binti Sultani akabaki kando ya mto juu ya jabali, akisubiri.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Twende bwana wee! Tutajua jinsi ya kujihami tukifika huko.” Kibwe alisema huku akimkokota mwenzake kuelekea upande wa mto , sehemu ya korongoni, ambako ndiko walikoingilia kwenda chini kabisa ya ule mto. Bhaduri binti Sultani akabaki kando ya mto juu ya jabali, akisubiri.

    Vijana wale walizama chini kabisa ya mto kwa kupitia kule korongoni, na hatimae bila kuamini macho yake, Hanga aliona nchi kavu! “Ha! Kibwe, huku ni wapi tena?” aliuliza kwa mastaajabu, kwani chini ya ule mto, kulikuwepo mji mkubwa wenye majumba makubwa makubwa ya fahari! Majumba hayo yaliyofanana, yalijengwa katika eneo kubwa juu ya mwinuko wa milima iliyotanda kwa hekari nyingi mno. Mjengo wa hizo nyumba ulifuata mzunguko wa nusu miduara kama saba hivi, yaani nyumba nyingine zilikuwa katika mduara wa kwanza kwa ndani ambao ulikuwa mdogo, zikafuatiwa na nyumba zilizojengwa kwa kufuata miduara iliyoongezeka ukubwa, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya miduara yenye nyumba hizo. Nyumba zenyewe zilijengwa kwa matufali ya mawe ya vito vya thamani pamoja na marumaru. Milango na madirisha ya nyumba vilikuwa vya fedha na dhahabu. Kwa kufuata mjengo wa mizunguko hiyo ya aina yake, nyumba hizo zilijengwa karibu karibu mno. “Hee! Maajabu makubwa haya!” Hanga alizidi kushangaa, lakini Kibwe hakuona ajabu, kwani tayari alikwishaona mji wa jini Makatta na wenzake chini ya bahari, kulikokuwa kunatengenezwa vichafuzi vya hewa safi iliyoko kwenye tabaka la hewa ya ozoni. Lakini Kibwe hakumwambia Hanga habari hiyo wakati ule.

    Huku akizidiwa na maajabu kule chini ya mto, Hanga aliuliza. “Lakini mbona kuko kimya hivi? Ndio kusema wenye mji huu wote hawapo?” Aliuliza hivyo akihofu wasije wakavamiwa na kutiwa hatiani na hao wenyeji, bila tahadhari. Mwenzake hakumjibu, ila akamuonesha ishara ya kwamba anyamaze, ili polepole waweze kuchunguza wakazi hao walipo. Kwa pamoja Kibwe na Hanga wakaambaa na yale majengo marefu yaliyokuwa karibu karibu, hadi walipotokea kwenye jengo lililoonekana kama msikiti! “La haula! Ni nini hiki? Yaani ni msikiti au---?” Hanga alianza udadisi wake wa kipuuzi, na hapohapo Kibwe akamkatiza kwa kusema, “Ndio! Ni msikiti huo, na kama unavyoona, takriban wenyeji wote wa mji huu wamo humo ndani wanasali!” Kibwe alizidi kumfafanulia mwenzake yule, kwa kunong’ona, akimwambia kuwa wale wote aliowaona mle msikitini walikuwa ni majini wa mtoni, na ambao pia hugeuka kuwa nyoka, wanyama mbalimbali, upepo, au kujigeuza katika maumbile mengine wanayoyapenda, kulingana na mahitaji yao kwa nyakati zinazohusika. Kama kawaida yake, Hanga akatoa macho pima kwa hofu, na kisha naye akanong’ona kama alivyofanya mwenzake, akisema, “Ah! Ni Kweli kabisa! Hivi sasa wana maumbile ya binaadamu kama alivyotuambia Kakakuona. Na lo! wote wamevalia majoho meupe. Haa! Ndiyo!ndiyo! Sasa nimeelewa! Ni kwa sababu leo ni siku ya Ijumaa, kwa hiyo watu wote wamekuja kusali pamoja, ndio maana mji wao wote umepooza !” Kwa sababu ya maajabu yale, wakati ule Hanga alisahau kabisa hofu zake za kawaida.

    Tofauti na Kibwe aliyekuwa si mgeni na mambo yale, Hanga alifarijika kuyaona yale aliyokuwa akiyasikia tu, lakini hakuyafahamu, na ambayo yalimshangaza kila alipoyatambua. Mzee wa Busara aliwaambia pia kuwa kama ilivyo miongoni mwa binaadamu, wapo majini wacha Mungu na wapo wanaomuasi Mungu wao, na kama walivyokuwapo wanadamu wema na waovu, hali kadhalika miongoni mwa majini, wapo waliokuwa waovu, na wengine ambao ni wema. “Bila shaka yule aliyehusika na kuwachukua mabinti Sultani waliotolewa kafara, anatokana na jamii ya majini waovu na wenye kumuasi Mungu wao,” Hanga alimwambia Kibwe, ambaye alimjibu kuwa alihisi kuwa mabinti Sultani hao mpaka sasa wamo mikononi mwa majini hao waovu!

    Hanga hakuamini kuwa wale mabinti Sultani walikuwa hai mpaka wakati ule, akihoji kuwa ni muda mrefu sana uliopita tangu mabinti hao wachukuliwe na yule nduli. Iweje tena hadi wakati ule wawe bado wako hai ? “Kama chini ya huu mto kuna mji mkubwa kama huu, ambao yule nduli huwaleta wana wa Sultani, mji ambao wakazi wake ni viumbe wanaoweza kujibadili na kuwa kama wanaadamu, watashindwa vipi kuwahifadhi kibinaadamu mabinti hao wa Sultani, na kuwaficha miongoni mwao, labda wakiwatumia kama watumwa? Sasa, ikiwa kama lile joka ni mwana wa mfalme wa majini ya bahari na mito, basi bila shaka chini ya mto huu yupo baba yake, ambaye ndiye mfalme mwenyewe, na bila shaka wale mabinti watakuwa wapo kwenye milki yake ya kifalme katika himaya hii, wakifanyishwa kazi fulani.…! Na huko ndiko tutakakowakuta hao mabinti. Lazima tuwahi kuwatafuta kabla wenyeji hawajatoka msikitini!

    Kibwe na mwenzake walianza kutembea tembea katika mitaa ya ule mji wa chini ya mto, wakiwa macho kabisa, ili wasisitukizwe na wenyeji na kutiwa msukosuko. Walipokuwa wakitafuta tafuta ili waone jumba lenye hadhi ya kifalme, mara wakasikia sauti za watu nyuma yao. Lo! Wakati ule wale majini walikuwa wakitoka msikitini, wakiwa wamevalia majoho yao meupe kama yangeyange! Kibwe na Hanga walijibanza kwenye ukuta wa nyumba moja kubwa, wakisubiri watu wale wapite. Hanga ambaye aliwaona viumbe wale kwa mara ya kwanza, alistaajabu kuona jinsi walivyokuwa warefu kupita kiasi! Alipojifananisha nao, alijihisi kama paka na chui! “Lo! Ni maajabu ambayo sijawahi kuyaona tangu nitoke tumboni kwa mama yangu!” Hanga alinong’ona, na Kibwe akamfunika mdomo wake kwa mkono ili asiendelee na maneno yake ya mshangao, na hali wale majini hawakuwa mbali sana na pale walipokuwa!

    Mara, miongoni mwa viumbe wale wa ajabu, Kibwe na Hanga wakawasikia baadhi yao wakiulizana. “Hivi Maimuni alirudi na yule binti sultani kutoka majabalini?” Mwengine akajibu, “Leo ni ajabu sana, maana inaelekea kuwa mpaka sasa bado hajarejea. Sijui amepatwa na nini.”

    “Usiulize kama amepatwa na nini au vipi, maana kama huko juu alikutana na yule kijana Ibilisi, sidhani kama atarudi salama na huyo binti.”

    “Kijana gani tena ambaye ni Ibilisi, na kwa nini akikutana naye asiweze kurudi salama?”

    “Kwa sababu huyo ndiye kijana aliyenivunja huu mkono kwa kunipiga na rungu. Sina hamu naye asilani.”

    “Hivi tuseme ulikuwa wapi mpaka ukakutana naye, na akakufaniya hivyo?”

    “Unajua, nilipotumwa kwenda kuzamisha meli ili kuwapata watu wengi watakao letwa huku kutufanyia kazi, na nikaweza kuikamata ile meli ya Mfalme KashKash, nilipoanza kuizamisha tu, alitokea huyo kijana, ambaye ghafla alinipiga na rungu mkononi kwa nguvu za ajabu! Nilipata machungu makubwa, nikakimbia na kujizamisha baharini. Sasa, kama kijana huyo amefika huku, na akamkuta Maimuni akimchukua binaadamu mwenzake, bila shaka mwenzetu huyo yumo hatiani wakati huu!”

    Lo! Kibwe hakuamini masikio yake! Hivi wale majini walikua wameweka baraza kabisa, barabarani, eti wakimzungumzia yeye! Mwenyewe Kibwe alijizuia kuporomosha kicheko! “Hivi ni kijana gani huyo wanayemsema? Ni wewe?” Hanga alianza kudodosa, na hakuamini aliposikia kuwa eti Kibwe ndiye aliyefanya hivyo alivyoelezea yule jinni. “Ama kweli mwenzangu wewe una ujasiri wa ajabu kabisa!” Hanga alimsifu Kibwe, na akiamini kuwa kwa hakika alikuwa ni mwana mteule, na wala si kijana wa kawaida.

    Wakati wakiwa wamejibanza pembezoni mwa yale majengo wakiwasikiliza wale majini, wengine miongoni mwao waliokuwa wakitoka msikitini, nao wakasimama pale walipokuwa wakizungumza wenzao. Baada ya kusikia mkasa uliomsibu yule aliyepigwa na rungu, mmoja wao naye akaanza kusimulia mkasa wake.“Labda kijana huyo ndiye yule kijana balaa aliyefika mjini kwetu, akatuwekea hewa ya uvumba iliyowateketeza wenzetu wengi,” alisema, na kujieleza kuwa yeye alikuwa ni miongoni mwa kikundi kilichomfuata kijana huyo juu ya bahari alipokuwa akitoka mjini kwao chini ya bahari, baada ya kuwateketeza wenzake. “Tulishambuliwa na cheche za moto zilizogeuka kuwa miali ya moto, mara kijana huyo alipotoa upanga wake wa ajabu na kuanza kutupiga nao. Wengi kati yetu waliunguzwa vibaya, na wengine tulidiriki kukimbia. Kwa hiyo, ni kweli kuna wasiwasi kuwa kama binti wa mfalme wetu amekutana na mtu huyo, basi bila shaka atakuwa hatarini hivi sasa!” alisisitiza.

    Mahali walipojibanza, Kibwe na Hanga waliweza kupata taarifa kamili kuhusu jamii ile ya ajabu ya majini. Kumbe wengi wao hupatikana kwenye maji ya mito, bahari na mabwawa. Kumbe wao huendesha vitendo vya ukatili kwa wanaadamu, na kwamba pamoja na ukweli huo, zipo njia mbalimbali ambazo wanaadamu hutumia ili kujilinda na uharibifu wao dhidi yao. “Watu wanao kumbwa na majini hufukizwa moshi wa uvumba, kwani bibi yangu alimfanyia hivyo jirani yetu, na baada ya hapo, , jini huyo alikimbia na kumwacha mhanga yule akiwa salama salimini.” Kibwe akamfinya Hanga kumnyamazisha, kwani alijua kuwa endapo wale majini wangewasikia na kuwaona, wangewateketeza kama walivyofanyiwa wao. Baada ya kuyasikia yote yaliyosemwa na wale majini, Kibwe akaelewa kuwa pale walipo ndio hasa mahali penyewe alipokuwa akipatafuta, ili kuwapata mabinti wa Sultani.

    Mara tu baada ya wale majini kuvunja baraza lao na kuondoka mahali pale, Kibwe alimshika mkono Hanga na kuongoza njia, akiharakisha waondoke mahali pale hatari, ili kuendelea na utafiti wao wa kuwatafuta mabinti Sultani sita. Walielekea kwenye lile jumba la kifalme, ambako walihisi kuwa ndiko walikokuwa. Walipokuwa wanaambaa kwenye majengo marefu yaliyojipanga kwa safu, walitembea kwa tahadhari kubwa, huku wakinyata, ili kujinusuru wasije wakaonwa na wale watu wa kijini. Katika tembea yao, ghafla Kibwe akamuona mmoja wa wale majini akigeuza shingo yake, kuangalia kule walikokuwa yeye na mwenzake! Wasiwasi mkubwa ulimpata, kwani alihofu kuwa katika eneo lililopambwa na weupe wa majoho ya wale majini hapa na pale, na kwamba katika eneo hilo ambalo watu wote ni warefu, Kibwe alihisi kuwa isingekuwa vigumu kwa majini wale kuwatambuwa kwa mbali kabisa yeye na Hanga, na kuwaona kuwa wao sio miongoni mwao! Kwa kutambua hilo, vijana wale wakaitambua pia hatari iliyokuwa mbele yao!

    “Kama hatukutafuta njia ya kuondoka haraka katika eneo hili, kaumu yote ile ya majini itatuandama na kutushambulia” Kibwe alimwambia mwenzake. Maneno yale hayakumfurahisha Hanga hata kidogo, kwa kuwa yeye alikuwa ni mwoga kupita mwenzake. “Sasa tutafanya nini kujinusuru?” aliuliza, huku akiwa anaangalia huku na huko kwa hofu aliyokuwa nayo. “Kwa sasa ni kujibanza tu, pembezoni mwa haya majengo, mpaka wote watakapoondoka mitaani,” Kibwe alimjibu. Kwa hiyo walijibanza na kuwa kimya, wakisubiri hadi hali itakapokuwa shwari.”Sijui wakituona na kutukamata watatufanya nini masikini!” Hanga alijisemesha, kama vile hakutarajia jibu lolote kutoka kwa Kibwe, ambaye kwa mara hii tena, alimwashiria mwenzake huyo anyamaze, “sssssshhhhh!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe naye alikuwa na hofu kubwa, kwani alijua kuwa kwa bahati mbaya, yeye na Hanga hawataweza kuwatambua majini waovu miongoni mwa kundi lile la majini wale waliovalia sare ya majoho meupe, isipokuwa pale watakapoanza kuwashambulia yeye na mwenzake. Lo! Salalee! Wakati akiwaza hivyo, akasikia sauti kama mluzi iliyotoka nyuma yao, ikisema, “Angalieni kule! Hivi wale sio binaadamu?” Wengine wakawa wanaangalia huko alikokuwa akionesha kidole mwenzao, na kisha wakanena, “Ndiyo! Wale ni binaadamu kabisa! Wakamateni na muhakikishe kuwa hawakimbii! Kama mmoja wao ni yule kijana mkorofi, lazima aadhibiwe!” Maneno hayo yalipowafikia Kibwe na Hanga, hawakupoteza hata sekunde moja, kwani walitimua mbio za ajabu, kama upepo, wakifuata vichochoro vilivyokuwa baina ya majengo marefu kupita kiasi, ambayo ni nyumba za thamani za wale majini!

    Hanga na Kibwe walikimbia kwa nguvu zao zote bila kugeuka nyuma, kwani walijua kuwa wale majini nao walikuwa wakikimbia kwa mbio za kasi ili kuwakamata. Walipokimbia kwa muda mrefu wakizunguka kwenye vichochoro vya yale majengo, Kibwe aligeuka ili kujua wale majini walikuwa umbali gani kutoka pale walipokuwa wao. Hanga alipomuona mwenzake anageuka na yeye akafanya hivyo, na halafu lo! Kile alichokiona kilimfanya akose nguvu miguuni, akanyong’onyea viungo vyote, kwa sababu ya mshituko wa hofu na woga. Alianza kupunguza kasi ya mbio zake! Wakati ule, ndipo kijana huyo alipohakikisha kabisa kuwa wale hawakuwa viumbe wa kawaida hata kidogo, kwani aliona macho yao yakianza kumweka mithili ya macho ya paka yanavyoonekana gizani! “La haula! Sidhani kama leo tutanusurika na hawa majini!” alisema Hanga wakati akijaribu kukimbia, lakini miguu yake ikikataa kunyanyuka! Kibwe aliyeona kuwa tayari kulikuwa na ucheleweshaji wa mbio zao kutokana na woga na hofu kwa upande wa Hanga, na pia ucheleweshaji wa mazungumzo ya mwenzake ya mara kwa mara kama kawaida yake, akamaka kwa hasira, na kumwambia, “Nyamaza na uongeze kasi ya mbio kunusuru maisha yetu! Acha mazungumzo Hanga!” alisema hivyo huku akimkokota mwenzake yule, na kwa pamoja wakakoleza mbio za kufa na kupona!

    Wakati fulani Kibwe na Hanga walikimbia mbio za kawaida, na walipokuta sehemu kulikokuwa na mapipa mengi yaliyofungwa pamoja, waliyafungua na kuyaachia yaporomoke kwa nyuma yao ili kuwababaisha wale majini. Wakati mwingine waliruka kama ngedere hasa kwa uwezo wa ajabu wa Kibwe alipomkamata mwenzake madhubuti, kila walipotokea sehemu za miinuko ambako waliweza kujirushia juu ya madirisha kwenye sehemu ya chini ya majumba yale marefu, na kuambaa humo hadi kwenye madirisha mengine, na kisha kujiangusha chini kwenye miinuko mingine. Waliporukia madirishani, walishikilia maeneo yaliyojitokeza kwenye madirisha hayo, wakitambaa kwa kwenda juu ya jengo, hatua kwa hatua, kwa wepesi mkubwa! Vijana wote wawili walikuwa ni hodari sana wa michezo ya kuruka juu, na Hanga alitumia urefu wake kwa hodari zaidi kwani alikuwa mrefu kuliko Kibwe, wakati Kibwe akisaidiwa na ule uwezo wake wa ajabu! Lakini wale majinni waovu nao walizidi kuwaandama, huku wenzao wema wakiwaangalia na kuwashangaa. Mmoja kati ya majini wale waovu alikuwa akiwakaribia mno wale vijana! “Mungu wangu wee! Asitufikie….! Asitukamate…..! Tujitahidi Kibwe ndugu yangu!” Hanga alikuwa akisema huku akikimbia. “Ukinyamaza ndio utakuwa na nguvu ya kukimbia zaidi!” Kibwe alimwambia, huku akimkokota, na kupaa naye, wakirukia kwenye paa la nyumba moja, ambako kwa bahati walikuta kamba ndefu iliyokunjwa.

    Haraka Kibwe aliikunjua ile kamba, akafunga ncha moja kwenye nguzo ya chuma cha jengo.. Akamwambia Hanga ashuke kwa kutumia ile kamba, na kisha yeye akafuatia kwa kuelea kushuka chini, akiponea chupuchupu kukamatwa na yule jini aliyekuwa karibu nao. Wawili hao walijidondosha chini kama buibui anavyojidondosha na utando wake. Badala ya kuanguka chini kabisa, walibembea na kisha kwa msaada wa Kibwe kwa nguvu zake zote, wakajirusha hewani, wakilenga kuangukia kwenye dirisha la jengo lililokuwa mbele yao. Wakitanguliza miguu yao, wawili wale wakabamiza kioo cha hilo dirisha, na wakati wakiangukia ndani ya chumba cha jengo hilo, vipande vya vioo navyo vikamwagika kwenye chumba hicho kikubwa walichoangukia, vikitoa mlio wa kelele za kusitusha!

    Mle walimoangukia walifikia kwenye zulia moja la fahari mno, “Whuuuuuu!” Hanga alipumua na huku akiinuka na kurudi dirishani walikoingilia, ili aone kama wale majini walikuwa wakiwafuata au la. Alichokiona kwenye lile paa la nyumba walikotoka, kilifanya mwili wake wote uzizime, kwani aligeuka wakati muafaka, kuona jinsi vichwa vya viumbe wale wa ajabu sana vilivyoanza kuchukua maumbile ya vichwa vikubwa vya nyoka! Alimvuta mkono Kibwe, na pamoja wakakodoa macho, huku misuli ya Hanga ikitetemeka, akiwa kinywa wazi, na kubutwaika kwa kile alichokua akikiangalia! Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Hanga kushuhudia kitu kama kile, ukiachilia mbali pale alipomuona yule nyoka aliyeuawa na Kibwe. Hanga alishuhudia vichwa hivyo vya nyoka, ambavyo awali vilikuwa ni vichwa vya wale viumbe wa ajabu, vikitokeza juu ya majoho yao waliyovaa, na kujiangusha chini kwenye lile paa, na taratibu miili ya nyoka wakubwa ikaanza kujidhihirisha, iliyotambaa kwa kuambaa na ukuta wa lile jengo, na kisha kushuka chini! Kinywa wazi, Hanga alishuhudia majoka yale yakiporomoka huku yakijivua kutoka mwenye yale majoho Yaliyokuwa Yamevaa awali, Yalipokuwa katika maumbile ya wanaadamu! Yalipofika chini, ndipo yalipokuwa majoka kamili! “Ama kwa hakika ni ubishi wako uliotufanya tuje kwenye mji huu wa majoka, ambao sasa unatutosa katika hatari hii kubwa!” Hanga alimlaumu Kibwe, ambaye hakusema lolote wakati ule, bali alinyamaza tu!

    Baada ya Hanga kusema maneno hayo, mara Kibwe akashituka ghafla, kwani alihisi kama ameshikwa bega lake na mtu! Alipogeuka, kitu cha kwanza ambacho macho yake yalikiona, kilikuwa ni urembo usiokadiriwa, uliokuwa kwenye sura ya mrembo mwenye uzuri wa shani! Binti huyo mrembo alikuwa na macho manene, ambayo kila alipoyapepesa, yalifunikwa na kope ndefu. Juu kidogo ya macho hayo yenye kope ndefu, zilionekana nyusi zilizokaa kwa mpangilio mzuri mno, mithili ya upinde! Mashavu yote mawili ya yule binti yalikuwa na vibonye, vilivyo kamilisha kazi nzima ya urembo wa maumbile yake, na kuifanya sura ile iliyotokea mbele ya Kibwe na Hanga, kuwa ni ya kipekee, na ambayo wote wawili, hawajawahi kuona mfano wake!

    “Eh……! Ah……!” Hanga alijaribu kusema lakini hakuweza kupata la kusema. Kibwe akasafisha koo lake kwa kikohozi hafifu, bila kutia neno! Wote wakasahau kuwa yalikuweko mapandikizi ya majoka yakiwafuata kule waliko! “Nadhani huyu ni binti mfalme wa majini!” Hanga alimnong’oneza Kibwe, ambaye alimfinya kidogo, ili kumnyamazisha….., na wakati huo, ikasikika sauti nyororo ikisema,

    “Hivi katika mji huu wa hatari mmefuata nini hasa…..? Hususan kwenye jumba hili? Na ninyi hasa ni kina nani?” Yule binti mrembo aliwauliza Kibwe na Hanga. Huku wakimshangalia huyo binti, Kibwe na Hanga walikuwa wakijikung’uta kung’uta nguo zao zilizokuwa zimechafuka kwa vumbi kutokana na lile sakata la mbio za kuwakimbia nyoka wa kijini. Kibwe alimshangaa yule binti kwa kuwashangaa wao kuwepo pale, wakati na yeye mwenyewe alikuwa kwenye sehemu ileile ya hatari, lakini hakudhurika kwa namna yoyote, bali alizidi kuwa mrembo tu! “Sasa dada yangu, mbona na wewe uko huku? Kwani wewe ni nani, na hapa ni wapi?” Kibwe aliuliza .

    “Kwa hakika siko hapa kwa kupenda. Mimi ni Jasmin binti Sultani, na hapa ni kwa mfalme wa majini wote, yaani mfalme “Makattani.” Alijieleza Jasmin, akimwachia Kibwe aunganishe mwenyewe kuhusu je, mfalme ‘Makattani’ ni nani. Kibwe alimjua na kumuona jini ‘Makatta’ kule kwenye mji wa chini ya bahari, aliyeitwa ‘Makatta wa Makattani.’ Hivyo basi, akatambua kuwa mwenye milki ile waliyokuwepo wakati ule, alikuwa ni baba yake jini ‘Makatta!’ Kwa hiyo awali baada ya kumteketeza jini yule ‘Makatta wa Makattani’ kwenye mji wa chini ya bahari kulikokuwa kukitengenezwa vichafuzi vya hewa safi kwa binaadamu, mara hii ya pili yaelekea kuwa Kibwe alimteketeza nduguye jini Makatta, Maimuni, ambaye naye alikuwa akifanya uovu wa kuwachukua wana wa Sultani! “Kwa hiyo Jasmin, unafanya nini katika milki ya mfalme ‘Makattani’ na umefikaje hapa bila ridhaa yako?” Hanga alimuuliza mrembo yule aliyemuona kama mwanamke mwenye urembo wa kijini.

    “Mimi ni mwana wa kwanza wa Sultani wa nchi ya Shamsi. Niko huku nafanya kazi za kitumwa kwa mfalme ‘Makattani.’ Alijieleza Jasmin, na halafu akawapa taarifa ambayo haikuwa nzuri kwao!

    ”Ningependa pia muelewe kuwa siku ya leo sio siku nzuri kwenu kuwepo huku.” Aliwafahamisha binti huyo. “Kwa kuwa Binti yake Mfalme ‘Makattani’ yaani ‘Maimuni’ aliyetumwa kwenda kumchukua Bhaduri binti Sultani na kumleta huku kutumikia kwenye milki ya baba yake, hajaonekana tangu alipoondoka saa tano asubuhi” Jasmin aliwaeleza wale vijana, akisisitiza kuwa ujio wao kule hautatafsiriwa vizuri na jamii ya majini, kwani raia na jamaa zake, wana wasiwasi kuwa huenda wanaadamu wamemdhuru!” Kama kawaida, Hanga akaanza kukosa raha kwa hofu. “Kwani mabinti Sultani wengine waliochukuliwa mwanzoni wamewekwa wapi?” H alidodosa, ili afahamu kama wanaadamu wafikapo kule huuawa, au la.

    “Wako kwenye sebule maalum anayopumzikia mfalme ‘Makattani.’

    “Na huyo Mfalme ‘Makattani’ mwenyewe yuko wapi hivi sasa?” Hanga aliuliza, akitaka kujua jinsi atakavyojihami, endapo mfalme huyo atatokea pale ghafla!

    “Mfalme huyo wa majini yuko pamoja na wadogo zangu, ambao hivi sasa wanaendelea na kazi ya kumkanda , wakati yeye amelala.” Jasmin aliwaambia, akimwacha Hanga hoi, akiwahofia hao mabinti wanaokaa pamoja na hilo nduli, bila kujua ni wakati gani litawageukia na kuwadhuru! Kibwe naye alibutwaika mno kusikia hivyo, akiwaza kuwa pale walipokuwa, ni mahali pa kutia hofu sana. Wakati huohuo, Jasmin akawatanabahisha kuwa mpaka wakati ule walikwisha poteza muda wa kutosha, kwani wale majini waliokuwa wakiwafuata, ni askari wa Mfalme Makattani, na walipewa amri ya kufuatilia habari ya Maimuni binti Makattani. “, Haya, twende huko kwa wadogo zako, haraka!” Kibwe alimwambia Jasmin, huku akamshika mkono ili wakimbie, na wakati huohuo akimwashiria Hanga afuate nyuma. “Leo nimekuja kuwachukuweni wewe na nduguzo.” Kibwe alisema kwa kujiamini, wakati Jazmin na Hanga wakishangaa kumsikia akisema hivyo. Hawakuelewa jinsi gani alivyopanga kukimbia na Jasmin na nduguze watano, wakati kundi zima la askari wa kijini lilikuwa likiwafuata kwa kasi kubwa. “Sidhani kama unaelewa unachokisema ndugu yangu. Hivi unadhani utapita wapi baada ya kutuchukua?” Binti Sultani yule alimuuliza. Lakini Kibwe hakumjibu, bali alimwonyesha ishara ya kwamba yeye aongoze njia tu, kuelekea huko walikokuwa nduguze.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipoingia kwenye hiyo sebule kubwa ya mfalme ‘Makattani,’ wale vijana wakashangaa kweli kweli, kwani kwenye kitanda kikubwa kupita kiasi, lilionekana joka kubwa mno, kuliko hata lile lililokuwa na vichwa saba, aliloliua kibwe! Joka hilo ambalo ni mfalme wa majini, lilienea sebule nzima kwenye kitanda hicho kikubwa cha ajabu. Kitanda hicho kilizungukwa na mabinti Sultani watano waliochukuliwa awali na joka kuu, ‘Maimuni’ wa Makattani, pamoja na mabinti wengine wengi warembo, waliopelekwa kule baada ya majini kuzamisha mitumbwi na ngalawa zipitazo kwenye mito, na pia meli kubwakubwa zinazosafiri kwa njia ya bahari. Ajabu ni kwamba kila mmoja alishikilia mchi mdogo wa kutwangia vitunguu na viungo vingine jikoni, na wote walikuwa wakimtwanga mfululizo, mfalme ‘Makattani!’ Kilichowashangaza zaidi ni kwamba wakati mabinti Sultani walipokuwa wakimtwanga Mfalme yule wa majini, ‘Makattani,’ yeye alikuwa amelala fo, fo, fo!

    Kule nje kwenye majabali alikokuwa ameketi Bhaduri binti Sultan, alisubiri kwa muda mrefu sana, hadi akahisi kuwa huenda Kibwe na mwenzake walimtelekeza. “Yule mmoja aliyepambana na lile joka, ameondoka na fuko lake mgongoni, kwa hiyo sidhani kama anayo sababu ya kurudi tena huku. Labda amekwisha kwenda zake, au labda ameuawa na majoka ya mtoni….” Hayo ni mawazo yaliyokuwa yakipita kichwani kwa Bhaduri, na wala hakupata jibu. Akapata hofu kubwa kwamba anaweza kutokea nyoka mwengine mkubwa na kumchukua!

    Lakini masikini! Laiti kama angefahamu yaliyokuwa yakiendelea kule chini ya mto, ambako ni himaya ya jamii ya majini, na ambako ndugu zake wote walikuwa ni watumwa wa Mfalme Makattani, angetaharuki zaidi!

    Wakati Kibwe, Hanga na Jasmin wakikimbilia kwenye hiyo sebule kubwa ya jini Makattani, mara, kama muujiza, wakasituka kuwaona wale majini, askari wa Mfalme Makatta, wamekwisha ingia kwenye sehemu ya gorofa ya juu walipoangukia kibwe na Hanga, wakati walipojibembeza na kamba kutoka kwenye jengo la jirani!

    “Haaa! Wameingia jamani! Na sio majoka tena bali sasa ni yale majini marefu! Harakisheni jamani!” alisema Hanga kuwatahadharisha wenzake. Wakati wakikimbia ili kuingia kwa Makattani, Kibwe alikumbuka maneno ya muhimu sana ya mzee wa busara.

    “Kwenye bustani ya jumba la Makatta, ipo chemchemi ya maji, na kwenye chemchemi hiyo, huelea kibatali kidogo chenye mwenge mdogo wa moto. Mwenge huo ndio roho za majini yote ya huko, isipokuwa mfalme wao ambaye roho yake hushikiliwa na hirizi kubwa sana inayoning’inia chini ya mti uliopandwa karibu na chemchemi hiyo. Ili kuwateketeza majini wa huko, lazima uzime hicho kibatali, na uikate kate hiyo hirizi yenye roho ya mfalme wa majini.” Mzee wa busara alifahamisha kuwa kwa kufanya hivyo, majini wataathirika kwa njia mbalimbali.

    Kibwe alimgeukia Jasmin na kumuuliza, “Ni mlango upi unatokea kwenye bustani ya mfalme Makatta?” Yule binti akanyoosha mkono wake, kumwelekeza ulipo.

    “Wewe nenda kwa wadogo zako na mnisubiri huko. Hanga, haraka nifuate!” Moja kwa moja kibwe aliongoza hadi bustanini, akifuatiwa na mwenzake Hanga. Nyuma yao, kama upepo, wale askari wa Makattani walielea na kuwatangulia vijana wale, wakiizingira ile chemchemi ya uhai wao. “Haraka sana irukie ile hirizi mtini, na uizungushe hewani mara nyingi!” Kibwe alimwambia Hanga, aliyekuwa hodari kwa kuruka. Bila kupoteza muda, kijana yule akainua miguu yake mirefu na kuchukua hatua mbili kabla ya kujirusha na kuning’inia mtini, akizuka na ile hirizi kubwa ya kimazingaombwe! Wakati ule wale majini waliojitahidi kuelea kama upepo ili kumzuia Hanga, walikwisha chelewa kwa sekunde! Walipohisi hatari iliyokuwa mbele yao, wakaanza kurudi nyuma, wakijiweka mbali na Hanga, kabla hawajatahamaki na kumuona kijana yule akiizungusha ile hirizi! Hamadi, mara ukazuka upepo mkali mno uiliowakumba wale majini na kuwamwaga upande mmoja! Kibwe naye aliruka na kujaribu kukiwahi kile kibatali kilichokuwa kikielea kwenye chemchemi! Mmoja kati ya majini aliyeangukia karibu na Kibwe, alimshika mguu wake! Hanga alipoona vile, haraka akaizungusha ile hirizi mara nyingi sana, na tena kwa nguvu zake zote! Afana aleik! Kwa mara hii, upepo mkali zaidi ulitokea na kuwazowazowa wale majini, ukawabwaga upande mmoja, walibaki wakielea sehemu moja, wakikosa uwezo wa kwenda popote!

    Wakati huo, mfalme Makattani alianza kuamka pale mahali alipokuwa amelala fo fo fo kwa kipindi cha miaka mingi iliyopita, bila kuamka! Kadiri alivyokuwa akitwangwa na wale mabinti, ndivyo alivyozidi kulala! Siku ile alipoanza kuamka, wale mabinti wote wakasituka na kushangaa sana. Mara wakamuona mfalme yule wa majini akianza kubadilika kutoka kwenye umbo la joka kubwa la ajabu, na kuwa kiumbe mmoja mwenye umbo la ajabu sana! Alionekana akiwa na kichwa kirefu na kipana sana, chenye uso wenye macho manne makubwa, yaliyofunikwa na sehemu ya nyusi iliyokuwa kama nundu kubwa mbili! Kiumbe huyo alikuwa na mikono mine mirefu kupita kiasi, miwili kila upande,iliyokuwa haina mifupa, kwani ilikuwa na uwezo wa kujinyonga nyonga kama nyoka! Kila mkono uilikuwa na vidole sita, vilivyoning’inia mithili ya mikia ya pweza! Na miguu yake minne, miwili kila upande, nayo ilikuwa na uwezo wa kutambaa kama nyoka, na pia kukamata kitu chochote kwa nguvu za ajabu. Ama kwa hakika, umbo lake zima baada ya kubadilika, lilifanana na umbo la buibui, lakini katika mwili mkubwa mno kuliko buibui!

    Kwa kutumia mdomo wake ulioonekana kama wa sokwe mtu, Mfalme wa majinni, Makattani alipiga ukelele uliorindima hadi matumboni mwa kila mwanaadamu aliyeusikia, na kisha kwa mlio wa hasira wa kukoroma uliotingisha miti yote na kudondosha matunda yaliyokuwa kwenye bustani yake, jinni huyo akanena. “Ni nani huyo anayethubutu kuniamsha mimi Makattani wa Samsuri!” Wale mabinti wote waliokuwa wakimkanda Makattani bin Samsuri, walianguka na kuzirai! Jinni hilo katika umbo lake la ajabu, likainuka kitandani na kujitingisha, na kisha likaiongoza miguu yake mirefu iliyokuwa kama nyoka wanne, na miguu hiyo kama nyoka, ikaanza kutambaa na kumfanya Makattani taratibu atoke kule ndani, akielekea kwenye bustani, huku mikono yake nayo ikikamata nguzo na vikuta, ili kujirahisishia mwendo!

    Alipotokea kwenye bustani katika umbo hilo na mwendo wa kustaajabisha, Hanga aliyeanza kumuona, akashikilia mdomo wake kwa mastaajabu! Wakati huo hakukumbuka kuwa alikuwa ameshikilia hirizi ambayo ndiyo iliyokuwa ikiwanusuru na vitimbi vya majini! Bila kuelewa, akaiachia hirizi ile ya miujiza, iliyoanguka chini karibu ya miguu yake. Kwa tukio hilo, wale majini i ambao ni askari wa Makattani, wakaanza kukusanya nguvu, na taratibu wakamfuata Kibwe, aliyekuwa akifuata kile kibatali kieleacho kwenye chemchemi, kwa nia ya kukizima. “Moshi wa hicho kibatali baada ya kuzimika, utawazingira majini wote, ambao nao watageuka kuwa moshi, na kuchanganyika na moshi wa kibatali kabla ya kuyeyukia angani!” Kibwe aliambiwa na Mzee wa Busara hapo awali. Alikumbuka pia kuwa mzee huyo alimwambia Hanga atahadhari kwa vyovyote vile, asithubutu kudondosha ile hirizi, na kwamba akifanya hivyo, majini watapata nguvu upya, na hivyo kumshambulia Kibwe atakayeonekana kuwa anatishia maisha yao!

    Masikini Kibwe alikwisha kuwa mikononi mwa yale majini ambao ni askari maalum wa Makattani! Wakati huohuo jini Makattani naye alikuwa akijitoa sebuleni kwake na kuwasili kwenye ile bustani. Alijiburuza na kutambaa mithili ya buibui, na kisha akatoa ukelele mwingine wa aina yake, kama vile mtu anaye kuna nazi kubwa sana kwenye mbuzi kubwa!

    “Kirrrrrrraaah! Kirrrrrrrraah! Kirrrrrrraaah!” Jini makattani lilikoroma hivyo, na huku likimaka kwa hasira likisema; “Mleteni hapa kwangu huyo kijana mkorofi!” Aliwaamuru askari wake. Wakati huo, Hanga alizinduka kutokana na lile butwaa alilolipata baada ya kumuona jini Makattani katika umbile lake la kustaajabisha! Na hapohapo, Kibwe naye akapiga kelele za kumzindua Hanga, wakati wale askari wa kijini walipokuwa wakimpeleka kwa mfalme wao kama walivyoamrishwa. “Hangaaaa! Hangaaa! Acha kushangaa! Haraka sana okota hiyo hirizi!” Hanga akagutuka na kwa wepesi usio kuwa wa kawaida, akadiriki kuiokota hirizi ile wakati ambapo mmoja kati ya askari wa kijini aliwasili akielea hewani kama samaki baharini, pale mahali alipokuwepo Hanga, ili kumuwahi. Lakini wapi! Alikwisha chelewa! Baada ya yule kijana kuidhibiti ile hirizi, alianza kuisukasuka na kuitingisha kwa nguvu zake zote, zaidi ya vile alivyoelekezwa na Mzee wa Busara, Kakakuona! Alizidisha nguvu na kuisukasuka ile hirizi mara chungu nzima! Halafu wee! Kasi ya upepo uliotokea kwa mara ile ya tatu, ilikiuka ile kasi ya awali, na badala yake, upepo huo ukachanganyika na tufani kubwa, iliyotingisha ardhi na kuipasua, na wakati huohuo kusababisha mafuriko makubwa ya maji!

    Wakati yakitokea hayo yaliyosababishwa na Hanga, majini wengi walizolewa na upepo mkali, na wakati huohuo, baada ya Kibwe kuachiwa huru, akawahi kukifikia kile kibatali kilichokuwa kwenye chemchemi na kukizima! Lo! Moshi uliotoka kwenye kibatali hicho kidogo, ulianza kufunga na kutanda katika bustani, na kuwafunika wale majinni, waliogeuka moshi uliojiunga na ule uliotoka kwenye kibatali! Kibwe na Hanga wakauona moshi ule ukiyoyoma angani na kupotelea huko! Hata hivyo, hali hiyo iliyotokea haikumdhuru mfalme wa majini asilani. Wakati Kibwe alipotaka kuwahi kwenda kwa Hanga na upanga wake ili kusaidia kuikata kata ile hirizi, Makattani ghafla aligeuka ndege aliyeruka moja kwa moja hadi kwa Hanga, akikusudia kumpokonya ile hirizi. “Irushie kwangu upesi!” Kibwe alimwambia Hanga, ambaye haraka alifanya hivyo. Bila kupoteza muda, Kibwe alitoa upanga wake kiunoni, na kuuzungusha hewani, na wakati hirizi ile bado iko hewani, akaiwahi kabla haijatuwa, na hivyo kuikata katika mapande mawili!

    “Aaaaaaaaaagh! Aaaaaaaaaggh! Jini Makattani aliugulia huku akigaagaa chini mithili ya buibui anaposhambuliwa! Baada ya robo saa, jini yule akayeyuka kama kwamba hakuwepo pale kabisa! Katika saa moja iliyofuatia, kila kitu katika jumba lile la mfalme wa majini kikawa kimya na shwari, wakati wale mabinti waliokuwa wakifanya kazi ya kumkanda mfalme yule, wakizinduka baada ya kuzirai! “Jamani, kimetokea nini hapa?” Waliulizana kwa mshangao, kwani kulikuwepo uharibifu mkubwa wa vitu na mazingira.

    Hali ile ilipotulia na wale mabinti Sultani wote sita walipotoka nje kwenye bustani, Kibwe na Hanga waliduwaa,kuona jinsi mabinti wale walivyoshindana kwa uzuri! Dada yao Jasmin aliligundua hilo mara moja, akaelewa kuwa wale vijana walibabaishwa na wadogo zake, kama walivyobabaika mara baada ya kumuona yeye!

    “Hawa watano ni wadogo zangu, na majina yao ni Sabrina, Samiya, Samira, Shamshir, na Shabnam.” Binti yule aliwatambulisha nduguze.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Vijana wale walishangaa kusikia majina yale mazuri, na yaliyoanzia na herufi ‘S.’ Ila walitaka kujua kwanini majina ya Jasmnin na Bhaduri yalitengwa na yale ya wenzao watano.

    “Kwa sababu wazazi wetu walitaka majina ya mabinti wao wa katikati yafanane, na kuwepo tofauti baina ya binti zao wa kwanza na kitinda mimba.” Alijibu Jasmin.

    Wakati mabinti wale wakiendelea na utambulisho, masikini hawakuwa hata na fununu kuhusu mambo yaliyokuwa yanatendeka kule nchi kavu kwenye majabali, alikobaki mdogo wao Bhaduri!

    Binti Sultani ambaye ni kitinda mimba, alisubiri kwa muda mrefu sana pale alipoachwa na Kibwe na Hanga. Hatimae akatokea mchungaji mmoja na mifugo yake, waliokuwa malishoni, na wakati ule, aliileta mifugo hiyo pale mtoni ili kuinywesha maji, kwani alivizia wakati ule maalum, akitarajia kuwa tayari yule binti Sultani atakuwa amekwisha chukuliwa na lile joka kuu! Mchungaji yule aliyeshikilia fimbo mkono mmoja na mkuki mkono wa pili, alishtuka sana alipoona mwili wa lile joka liliokuwa likihofiwa nchi nzima, eti umelala kwenye majabali bila uhai! Mara, akagundua kwamba yule binti Sultani ambaye angetolewa kafara, hakuchukuliwa kama walivyochukuliwa wenzake wa awali! Bahati ilioje kwake! Lazima ajifanye kuwa yeye ndiye aliyeliua lile joka ! Palepale akachukua mkuki na kuanza kuuchoma choma ule mwili wa lile joka , huku akipiga kelele kuita watu washuhudie kazi aliyoifanya!

    “Jamani eeh! Jamani! Nimekwisha muua yule nduli aliyekuwa akisumbua jamii yetu kwa miaka kadha wa kadha! Leo nimemuua jamani! Njooni mshuhudie!” Yule mchungaji alichacharika kama punguani, akilalama bila kuwaza kuwa huenda yule aliyeifanya ile kazi yuko jirani na pale. Vilevile bila kuwaza kuwa huenda Bhaduri akasema ukweli kuhusu hali halisi ya mambo yalivyotokea, mtu yule mnafiki aliendelea kujitangaza kwa kelelele! Alichokifikiria yeye ni kwamba mara tu, Sultani Bashar atakaposikia kuwa yeye ndiye aliyemuua yule nduli, bila shaka atamuoza yule binti Sultani, na kumfanya awe tajiri! Ajabu ni kwamba, Bhaduri naye, alinyamaza kimya, akimwangalia mchungaji huyo aliyekuwa akilalama na kujigamba!Yule mchungaji akaukusanya ule mwili wa lile joka, akauweka kwenye gari lake la ng’ombe na kuondoka nao hadi kwa Sultani, ambako alipokewa kwa shangwe na hoihoi! Haya, wapi na wapi! Kazi afanye mwingine, sifa apewe mwingine. Lakini kwa wakati ule, hivyo ndivyo ilivyokuwa!

    Sultani alituma watumishi wake na gari la farasi kumfuata binti yake kule mtoni! Furaha aliyokuwa nayo haikuwa na mfano, kwanza kwa kumpata mwanae, na pili kwamba raia wake hawatasumbuliwa tena na lile joka, na watachota maji kwa amani!

    “Wee Nokora! Haraka sana piga mbiu ya mgambo uwatangazie raia wangu habari hii njema! Na pia uwaambie kuwa kutakuwa na sherehe kubwa ya kumuoza mwanagu kitinda mimba kwa shujaa aliyetuokoa na tatizo lile la kudumu!” Sultani alimwamuru mtumishi wake.

    Shamrashamra zikaanza, nchi nzima ikachangamka, na raia wote wakasherehekea habari zile nzuri kwa furaha. Bhaduri binti Sultani akaweka mkono wake shavuni, bila kuamini jinsi wanaadamu wanavyoweza kukosa haya, na wakaweza kudhulumu jasho la wenzao kimacho macho! Alinyamaza tu, ili aone mwisho wake!

    Kibwe na kundi la wasichana waliochukuliwa na majini na kutumikishwa kwa mfalme Makatta, Jasmin na wadogo zake pamoja na Hanga, walipotoka kwenye mji wa majini chini ya mto, hawakumkuta Bhaduri pale walipomuacha!

    “Bila shaka alichoka kusubiri akaamua kurudi nyumbani.” Jasmin aliwaambia wenzake, na akashauri kuwa na wao lazima warudi haraka wakawafahaimishe wazazi wao kuwa wako hai, waweze kuwatambulisha kwa baba yao wale wasichana wengine waliochukuliwa na majini kutoka sehemu mbalimbali za dunia bila ridhaa yao, ili wafanyiwe mpango wa kurudishwa kwa wazazi wao. Wakati binti yule akiyasema hayo, Hanga alikuwa akiangaza kila sehemu, akijaribu kuelewa kuwa je, ule mwili wa lile joka la kutisha ulipelekwa wapi? “Hivi Kibwe ulibeba vichwa tu vya yule nyoka Maimuni, au uliubeba na mwili wake wote? Mbona siuoni mahali popote?” Kibwe alicheka sana kwa mas-khara hayo ya Hanga.

    “Ningetembea nao vipi mwili ule, na hapohapo niweze kufanya yote tuliyoyafanya huko tulikotoka? Mwili kama ule unahitaji kubebwa kwa gari la farasi au gari la ng’ombe! Na bila shaka aliyeuondoa hapa aliuondoa kwa kutumia kitu kama hicho!” Kibwe alimjibu Hanga, ambaye kama kawaida alidodosa kutaka kujua je, Kibwe anafikiri kuwa ni nani aliyeuondoa huo mwili? “Tusubiri tu, na bila shaka tutafahamu baada ya muda si mrefu,” alijibiwa na Kibwe, na kisha, wote wakaondoka kule mtoni kuelekea kwenye jumba la Sultani Bashar, ambako hawakujua kuwa kulikuwa na sherehe kubwa kupita kiasi!

    Kila walikopita, Kibwe na wenzake walikuta shamrashamra mitaani. Kila mtu alionekana kuwa mwenye furaha kubwa, na kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi, mji ya Majabali katika nchi ya Shamsi, ulichangamka kupita kiasi. Jasmin binti Sultani na nduguze waliwaambia Hanga na Kibwe kuwa awali, hali ya mji wao haikuwa ya kawaida hata kidogo. “Bila shaka kuna hafla ya aina fulani,” alinena Sabrina binti Sultani, na Samiya na Samira nao, waliomfuatia Sabrina kwa kuzaliwa, wakashangaa kusikia neno hafla, ambalo katika muda wote wa utoto wao, hawakuwahi kulisikia, kwani mji wao umekuwa kwenye hali ya misiba kila mwaka!

    “Au tuseme baba ameandaa hafla maalum ya kumpokea Bhaduri?” aliuliza Samiya.

    “Kama hivyo ndivyo, subirini muone jinsi sherehe hizo zitakavyozidi, mara baba atakapotuona tukiwasili nyumbani!” Sabrina naye akawaambia wadogo zake kuwa wajiandae kuona jinsi wazazi wao watakavyosituka na kushangaa kwa kuona sura za mabinti zao waliodhaniwa kuwa wameitoka dunia kwa miaka mingi sasa! Mara tu baada ya maneno hayo ya Sabrina binti Sultani, ukasikika mdundo wa goma kubwa likiwazindua raia kusogea karibu kupokea taarifa za Sulitani wao. Waliyoyasikia kina Sabrina hayakuwa ya kawaida!

    “La mgambooo! La mgambooo! Likilia lina jamboo! La mgambooo! Leo jamani asiye mwana aeleke jiwe! (abebe jiwe) Raia wote wa mji huu wa majabali nchini Shamsi, mnaalikwa kwenye viwanja vya tamasha katika kasri la Sultani, kusherehekea ndoa ya mwanae kitinda mimba, aliyenusurika kuchukuliwa na lile joka kuu! Wote msikose kuhudhuria!”

    Waliposikia tangazo hilo, Jasmin na wadogo zake wakaupata ukweli wa mambo. Lakini sasa, anayemuoa mdogo wao ni nani? Shabnam, binti Sultani aliyemuachia ziwa Bhadura, yaani bibi harusi mtarajiwa, akavunja ukimya uliotawala wakati wote walipokuwa wanajaribu kuelewa ni nini hasa kiini cha lile ‘lamgambo’. “Nadhani hii ndoa ya haraka haraka hivi, mara tu baada ya Bhaduri kurejea nyumbani, ina walakini kabisa!” Samiya na Shamshir hawakumuunga mkono kwa kutia neno lolote, bali wote wawili wakaitikia kwa vichwa na mguno wa pamoja; “Mmmmhuuuu!” Na kisha Hanga aliyenyamaza kwa muda mrefu pamoja na mwenzake Kibwe, akasema kuwa kwa kuwa hali ile inaelekea kuwa ni ya kutatanisha, hususan kwa kuzingatia kupotea kwa mwili wa lile joka, ni muhimu sana waharakishe kufika kwenye hilo jumba la Sultani. Kibwe naye, huku akilipapasa fuko lake mgongoni, alitabasamu tu, alipotafakari kuhusu wingi wa busara za Kakakuona!

    Bhaduri binti Sultani kwa mara nyingine, alipambwa kama alivyopambwa awali ili kutolewa kafara kwa joka kuu la mtoni, kwa faida ya raia wa mji wao wa Majabali, katika nchi ya Shamsi. Mara hii tena, baada ya kunusurika na nduli wa mtoni, binti yule alikuwa akitayarishwa kama vile kwa kutolewa tena kafara, kwa mtu aliyedai kumuua huyo nduli ambaye angemchukua kule mtoni kama kafara! Kwa Bhaduri hali zote mbili zilikuwa zikimkandamiza tu. Bahati mbaya, kitinda mimba yule hakuweza kusema lolote, kwani hakuwa na ushahidi wowote wa hoja yoyote atakayoitowa kuhusu mtu aliyefanya kazi kubwa ya kumuua yule nduli. Tatizo ni kwamba, yule kijana na mwenzake, wote walipotelea chini ya mto! “Nitaelezea vipi habari zao kwa kadamnasi hii ya watu, wakati ambapo sina uhakika wowote wa uhai wao, kwani sijui kama wazima au wameuawa na majoka ya huko baharini.” Binti Sultani yule alizidi kutafakari, na hatimae kuamua kukaa kimya tu, liwalo na liwe!

    Katika jukwaa maalum, yule bwana harusi aliketi akisubiri ndoa ifungwe. Kwenye uwanja wa matamasha, raia walifurika kushuhudia shujaa wao aliyewaokoa na msukosuko wa kupata maji, akimuoa binti mrembo wa Sultani wao! Nyimbo na ngoma mbalimbali zilitawala eneo lile, pamoja na mashairi na tenzi bila kusahau vicheko na furaha. Walichokua hawakukifahamu ni kwamba punde, hali ile yote ingebadilika, kama kupepesa kwa macho!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe na wale mabinti sita wa Sultani pamoja na mabinti wengine waliochukuliwa bila ridhaa zao na kutumikishwa na majini, waliwasili kwenye ile hafla maalum ya ndoa ya Bhaduri, katika wakati muafaka kabisa! Walipowasili, Sultani alikuwa akimsifu shujaa aliyemuua nyoka, aliyeisumbua jamii ya mji wa Majabali nchini Shamsi, wakati mtu yule aliyedai kuwa ndiye aliyefanya kazi ile ngumu, akiwa amesimamishwa kadamnasi, juu kabisa ya membari, ili watu wote wamuone!

    “Bila ushujaa wake, licha ya raia wote kuendelea kusumbuka kutafuta maji, lakini pia ningempoteza binti yangu mmoja aliyebaki, baada ya kuwapoteza wanangu sita katika kipindi cha miaka sita!” Sultani aliwaambia raia wake, kabla ya ndoa kufungwa. Wakati hayo yakisemwa, msururu wa takriban mabinti ishirini na sita, uliingia mahali pale, wakifuatiwa na vijana wawili. Watu wote wakasahau kwa muda, kuhusu hafla maalum iliyoandaliwa kwa heshima ya shujaa wao, na macho yote yaliwageukia hao walioongozana wakiingia kwenye uwanja wa sherehe, kama kwamba ile sherehe iliandaliwa kwa ajili yao! Baada ya hapo, kukawa kimya! Kilikuwa ni kimya kizito mno, kiasi kwamba hata pumzi ya watu wakipumua iliweza kusikika! Sultani alipigwa butwaa lisiloelezeka! Bwana harusi mtarajiwa naye, akatahayari kuwaona mabinti sultani sita miongoni mwa kundi la wale mabinti walioingia pale! “Sijui wale vijana wawili ni kina nani?” alijiuliza yule mfugaji, huku akianza kugwaya kwa hofu na tahayuri!

    “Naam, Maulana, Mheshimiwa Sultani! Tuwie radhi sana kwa kuivamia hafla hii bila taarifa,” Kibwe alianza kujieleza, alipoona kaumu nzima iliyokuwepo pale ikiwashangaa! Na pia alipoona kuwa kila mtu aliyehudhuria mahali pale, ghafla hakuelewa kilichokuwa kikiendelea! Sultani alifungua mdomo kusema, lakini hakuna maneno yaliyotoka. Malkia akashuka kwenye kiti cha enzi na moja kwa moja akakimbilia kule walikokuwa wale wasichana, na alipofika karibu yao, hakujua amkumbatie nani! “Aah! Ama kweli Mwenyezi Mungu ni mkubwa! Hivi hawa ni wanangu kweli?” Mke huyo wa Sultani alihamanika na kubabaika, akiwaita majina wanawe mmoja mmoja, huku akikagua na kuzingira sura ya kila mmoja kwa viganja vya mikono yake miwili, kila alipomtaja jina lake. “Ah! Mwanangu Samira….! Mwanangu Sabrina…! Jamani Samiya wangu wee! Nawe ni Shabnam kipenzi changu! Shamshir nawe hujabadilika kabisa! Ooooh! Mama huyoo! Jasmin mashavu wangu! Umewalinda wadogo zako wote na kuwalea vema hadi mkarejea na afya nzuri kabisa! Kisha akawageukia Hanga na Kibwe na kuwaambia, “Sidhani kama kuna haja ya kuuliza kuwa mabinti zetu waliwezaje kunusurika na kurejea salama nyumbani! Kabla hamjajieleza zaidi, natoa shukurani zangu za dhati kwa kunirejeshea wanangu!” Vijana Kibwe na Hanga wakanyamaza kimya, wakipata faraja kubwa kuona jinsi mzazi yule alivyofurahi!

    Wakati huo, Sultani naye akazinduka kutoka kwenye msituko alioupata baada ya kuwaona mabinti zake. Alihisi kuwa kutokana na hali ile iliyojitokeza, yalikuwepo maelezo ya kina ambayo kila mmoja alistahili kuyasikia! Muda wote wa yale matukio pamoja na taharuki ya Malkia, watu wote walikuwa kimya. Baada ya Malkia kuwashukuru kibwe na Hanga na kwenda kuchukua nafasi yake katika kiti cha enzi ubavuni mwa Sultani, minong’ono ikaanza! “Jamani, haya ni maajabu makubwa! Mabinti hawa sio wale walioliwa na nduli wa mtoni? Sasa leo hii wametoka wapi tena?” Mmoja alimuuliza mwenzake, ambaye alimkatisha asiendelee na maneno yale, akihofia wasije wakaeleweka vibaya na jamii ya Sultani. “Nahisi mwenzangu wewe hujipendi kabisa! Aliyekwambia kuwa mabinti wale waliliwa na nduli ni nani? Achana na uvumi utakaokutosa mahali pabaya ndugu yangu wee!”

    “Eeeh! Kwani nani amenisikia jamani na nilikuwa nakunong’oneza wewe tu? Haya! nimenyamaza!” Wengine walinong’ona kuhusu lile kundi la wasichana wasiowajua! “Aisee! Hivi wale vimwana ndo kina nani? Nao ni wana wa masultani, nini? Maana wanarusha roho kwelikweli! Laiti kama…” Mwenzake akamzuia kuendelea na maneno yale, na kumwambia, “Ndiyo! Kama kawaida yako! Laiti kama ungepata fursa ya kuongea na mmoja …..na hivi na hivi! Siku moja utaponzeka nawe! Hebu achana na mambo hayo, na tusikilize hatima ya matukio ya leo!” Mara, kijumbe mtangazaji wa taarifa za jumba la Sultani akaanza kupiga goma lake, ili kupata usikivu wa raia wote! “Haya, haya! Mabibi na mabwana! Tunyamaze na tutulie ili kumpa nafasi Mheshimiwa Maulana Sultani aongee. Kama mlivyoona, kumekuwa na mabadiliko ya matukio, tofauti na mpangilio wa awali. Baada ya muda si mrefu, kila mmoja wenu atapata majibu ya maswali yake. Karibu Mukufu Waziri Mkuu umkaribishe mtukufu Sultani aendelee.” Sultani alipoanza kuongea, kwanza kabisa aliwataka Kibwe na Hanga wajieleze na kuweka wazi kitendawili kilichojitokeza mahali pale.

    “Ningependa kujua kuwa ninyi ni kina nani, na mmewapata wapi hawa mabinti zangu waliopotea miaka mingi iliyopita.” Minong’ono ikarudia palepale! “Eeheee! Hilo neno jamani! Lazima tupate maelezo hayo!” walisema baadhi ya watu, na wengine wakawa wanagunaguna na kutingisha vichwa. “Hebu tusikilizane! Hamtayasikia mnayotaka kuyasikia kama mtaendelea hivyo! Tusikilizane jamani!” Alisema kijumbe wa Sultani. Baada ya muda, Kibwe akaanza kujieleza.

    “Mtukufu Sultani wa nchi hii ya Shamsi, jina langu ni Kibwe mwana wa Ilunga Mbuyu wa Kala, na mwenzangu ni Hanga mwana wa Hazari Basari Nkulu. Tulikutana tulipokuwa katika harakati zetu za kutafuta hali ya maendeleo ya kijamii, na tangu wakati huo, tumekuwa tukitembea pamoja,” Kibwe alieleza pia kuwa yeye na mwenzake Hanga walikutana na wale mabinti zake kwenye nchi ya majini, ambako walikuwa ni watumwa! Maneno hayo hayakuaminiwa kabisa na kaumu iliyohudhuria mahali pale.

    “Bwana mdogo, heshimu mahali hapa, maana ni mahali pa heshima na utukufu mkubwa. Acha maskhara na tueleze yaliyojiri huko utokako. Mbona uyasemayo ni kama simulizi za paukwa pakawa?”aliuliza waziri wa Sultani, akimshangaa yule kijana kwa kuanzisha porojo zile.

    Hanga alicheka kusikia maneno ya waziri, na kisha, kama vile kuongezea mafuta ya taa kwenye moto uliokwisha washwa, akasema; “Kwa hiyo mheshimiwa waziri, ukiambiwa kuwa huyo kijana mwenye maskhara na simulizi za kale, ndiye aliyemuua yule nduli kule mtoni, na wala si huyo bwana harusi wenu mtarajiwa, utasema nini?”

    Kimya!

    Katika watu waliohudhuria hafla ile, hakuna hata mmoja aliyesema kitu! Kila mtu alizama kwenye dimbwi la mawazo mazito!

    “Kijana, hebu sogea hapa mara moja!” Waziri wa Sultani alimwita Hanga aende karibu yake.

    “Wewe unao ushahidi gani wa maneno uliyoyasema hivi sasa? Tuonesheni ushahidi kwamba huyo kijana ndiye aliyemuua yule nyoka, maana mwenzenu ametuletea ushahidi wa nyoka mzima. Ninyi mnasemaje kwa hilo?” Waziri alitoa rai zake.

    Wakati ule, Kibwe naye akajisogeza kwa waziri, akapanda kwenye membari alikokuwa yule aliyedai kuwa ndiye aliyemuua nyoka maimuni, na kisha akasema kwa sauti ya juu ili kila mtu asikie. “Nasema kwa ushahidi kwamba mimi ndiye niliyemuua yule nyoka. Na kama mheshimiwa waziri na baraza lako mliamini kuwa mwenzangu huyu ndiye aliyeifanya kazi hiyo, tafadhali naomba mmwambie awaoneshe na vichwa vya huyo nyoka mwenye mwili aliouleta kwenu kuwa ni ushahidi!”

    Kimya tena.

    Watu wote wakaduwaa, hususan Sultani ambaye awali, hakufikiria kuulizia jambo kama hilo . Lo! Yule laghai aliyechangamkia ile nafasi ya Kibwe, kijana aliyefanya kazi yote ya kupambana na joka la ajabu, akatamani mno ardhi ipasuke ili ajifiche humo, kwa jinsi alivyofedheheka, pia kwa jinsi alivyohofu hatima ya uongo wake!

    Wakati huo, waziri naye akazinduka, baada ya kuipata habari ambayo hakutarajia kuwa itatoka kwa wale vijana wa kawaida, na ili kuwabana, alimuuliza Kibwe, “je, unaweza kuvionesha vichwa vya joka hilo? Palepale Kibwe akashusha lile fuko lake kubwa alilolibeba mgongoni, akalifungua na kisha kumwaga chini vichwa saba vya lile joka! Kwa hakika mahali pale hapakukalika! Watu wote walitimka kila mmoja akitafuta njia ya kupitia, kwani vichwa vile vilionekana kama vina uhai! Kichwa cha saba kilizidi kuwachanganya raia wote, jinsi kilivyong’ara kama bati la shaba! Ilikuwa ni pata shika na nguo kuchanika. Ama kwa hakika penye kweli uongo hujitenga, na njia ya muongo, siku zote ni fupi mno!

    Ukweli ulipofichuka, Sultani alitoa hukumu kali sana kwa yule mnafiki aliyedai kuwa alikuwa mkombozi wa raia wa Shamsi, na wale mabinti waliochukuliwa na majini kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakapelekwa nchini kwao kwa wazazi wao. “Kwa hakika, pamoja na kuwashukuru ninyi vijana wawili shujaa, nawapa fursa hii, ya kila mmoja kujichagulia mke ampendaye miongoni mwa mabinti zangu ili nimuozeshe, tuweze kuunda udugu wa kudumu!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kibwe alitabasamu, halafu akasema, “Nafikiri tutakapokamilisha kazi yetu na tutakaporejea huku, tutawaachia wao mabinti zako wachague yule wampendaye kati yetu, ndipo tuweze kufunga ndoa nao!”

    Sultani, mkewe na mabinti zake walicheka sana, wakikubaliana na wazo la Kibwe, wakati Hanga akigugumia kwa kutoridhika na uamuzi ule wa Kibwe. Yeye alimpenda sana Sabrina! Wakati vijana wale walipokuwa wakifurahi na kucheka pamoja na mabinti Sultani, mambo kule kusini magharibi ya mbali ya dunia, katika eneo lililokuwa sanjari na sehemu ya machweo ya jua, Malkia Sharara alipungukiwa na kichwa cha mtu mmoja, ili kukamilisha ujenzi wa jumba lake la ajabu la matofali ya vichwa vya watu!

    Kibwe na mwenzake wakaagana na Sultani wa nchini Shamsi na familia yake, na baada ya hapo wakaanza safari yao, wakielekea kusini, kutoka pale Kaskazini ya mbali katika mji wa Majabali.



    MWISHO



0 comments:

Post a Comment

Blog