Search This Blog

NILITAFUNA MAITI YA MWANANGU NIWE TAJIRI - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS



    *********************************************************************************



    Simulizi : Nilitafuna Maiti Ya Mwanangu Niwe Tajiri

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    NILIRUDI

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    nyumbani na kumkuta mke wangu akiwa vilevile. Alikuwa amejilaza kitandani akiugulia maumivu ya tumbo. Nikaketi kitandani na kumsogeza karibu yangu. Nikamlaza miguuni mwangu.



    “Vipi Rita, unaendeleaje sasa?” nikamwuliza.

    Hakujibu!



    Alijipapasa tumbo huku akikunja uso. Nilijua alichomaanisha. Rita bado alikuwa anaumwa tumbo. Sikuwa na fedha za kumpeleka hospitalini. Nilibaki nimejiinamia kwa mawazo. Huku nimemshika Rita wangu, huku nimeshika tama!



    Kwa tabu Rita alifumbua macho na kuniangalia. Aliniona nikiwa nimeshika tama kuonesha kwamba nilikuwa kwenye lindi la mawazo.

    “Vipi na wewe huko umefanikiwa?” aliniuliza Rita kwa sauti chovu, kavu iliyotoka kwa kukatakata.

    “Hakuna kitu Rita. Pamoja na kuwahi kote huko, sijafanikiwa kupata kibarua.”

    “Kwa nini?”



    “Watu walikuwa wengi sana, tena waliwahi zaidi yangu. Lakini ujenzi bado unaendelea, kesho nitajaribu tena naweza kubahatisha.”



    Nilizungumza kwa uchungu mwingi. Nikijikaza kiume, machozi nikayabana ndani ya kuta za macho yangu, sikutaka yatoke Rita ayaone!

    Mwanaume mzima!

    Aibu!Haifai mwanaume kulia hovyo!



    Ndivyo nilivyoamini, hata baba yangu aliniambia hivyo, kwamba wanaume wanatakiwa kujikaza. Mara chache sana nilipojisikia hasira ya kulia, nilifanya hivyo nikiwa na mbali na uso wa mke wangu.



    Sikuwa tayari mke wangu ayaone machozi yangu, najua ningemuumiza zaidi, jambo ambalo sikuwa tayari kabisa kuliruhusu litokee.



    “Lakini Galos, maisha haya ni mpaka lini? Tutakuwa wenye shida hivi hadi lini? Natamani hata kufa kuliko kuendelea na maisha haya ya dhiki na tabu kiasi hiki,” akasema Rita akimwaga machozi.



    “Acha kumkufuru Mungu mke wangu. Mapambano bado yanaendelea. Tutafanikiwa siku moja,” nilimwambia maneno ya kumpa matumaini.

    Taswira ya maisha yetu ilikuwa ngumu kufanikiwa. Tufanikiwe kwa lipi hasa? Nimezaliwa familia ya kimaskini, mbaya zaidi sina ujuzi wala elimu yoyote. Kikubwa ninachojua ni kubeba zege kwenye ujenzi wa majengo makubwa.



    Ndiyo kazi iliyoniweka mjini na mke wangu Rita. Leo kazi inapatikana, kesho hakuna. Ni tabu mtindo mmoja. Pamoja na yote hayo, niliendelea kumwambia Rita avumilie, siku moja tutafanikiwa.

    Kichwani nilijua ni ndoto!



    Rita aliniangalia kwa jicho la kuhoji, kwa kiasi kikubwa alionekana wazi kutokubaliana na maneno yangu kabisa. Alijua ni kwa namna gani nilikuwa naongea maneno ya kumfariji tu.

    Ni kweli!

    Nilimfariji tu!



    Nilimtazama Rita machoni, nikaachana naye. Nikaanza kukagua vizuri chumba chetu. Kilikuwa kimoja tu...tena hakina umeme! Tuna kitanda tu ndani, zaidi ni jiko la mafuta na ndoo za maji.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikahema kwa kasi, halafu nikaliendelea lile jiko pale chini, nikalifungua na kuangalia kama lilikuwa na mafuta ya taa!

    Hakuna kitu.



    Sufuria zote zilikuwa kama nilivyoziacha. Jiko lilikuwa limenuna! Hapakuwa na matumaini ya kupika siku hiyo.

    “Rita,” nikamuita mke wangu.

    “Abee Galos.”

    “Unajiasikiaje sasa?”

    “Bado naumwa...hasa hapa,” akasema akinionesha tumboni, chini ya kitovu.

    “Pole sana mke wangu,” nikamwambia halafu nikatulia kidogo.

    Kisha nikamwuliza tena: “Hivi umefanikiwa kula?”

    “Hapana!”

    “Mungu wangu....” nikatamka kwa sauti kubwa.



    Nilichanganyikiwa kwa sababu kubwa mbili; Rita wangu alikuwa anaumwa, lakini mbaya zaidi hata chakula alikuwa hajapata! Atapona vipi?

    Bila dawa!



    Bila chakula! “Kwa nini mimi?” nikasema kwa sauti kubwa bila kugundua kwamba nilizidi kumuumiza Rita.

    Akaanza kulia.



    Nilikuwa nimefanya kosa kubwa sana, haraka nikaanza kumbembeleza Rita asizidi kulia.

    “Tafadhali nyamaza mke wangu, haya mambo yataisha tu. Mungu mkubwa,” nikamwambia.

    “Yataisha lini? Kila siku matatizo tu, sidhani kama kuna mwisho hapa, zaidi ya mateso kila



    kukicha!” alisema kwa uchungu, akanizidishia maumivu moyoni mwangu.

    Nilitulia kwa muda nikiendelea kutafakari, lakini sikupata jibu la maana. Tatizo ilikuwa ni pesa. Nikamkumbuka rafiki yangu ambaye huwa ananisaidia ninapokuwa na shida. Nikainuka pale kitandani.

    “Narudi baada ya muda kidogo.”

    “Unakwenda wapi?”

    “Ngoja nikatafute maarifa.”

    “Sawa.”



    Nikatoka nyumbani na kwenda kwa rafiki yangu Patrick ambaye alikuwa fundi baiskeli. Niliamini yeye angeweza kunisaidia. Kwa bahati nzuri nilimkuta kijiweni kwake. Nikamvuta pembeni.



    “Kaka nina matatizo sana, mke wangu anaumwa sana, sina pesa hata ya kula. Nimekwenda kibaruani wiki sasa nakosa nafasi.”

    “Pole sana ndugu yangu.”



    “Kilinichonileta kwako, naomba unisaidie shilingi elfu kumi ili niweze kumpeleka mke wangu hospitali, ndani ya wiki hii nitajitahidi nikurudishie!”

    Patrick alitulia kwa muda akifikiria, hakujibu kitu. Aliondoka na kuniacha nimesimama palepale.



    Niliduwaa nisijue la kufanya. Dakika ya kwanza iliondoka bila Patrick kurejea, hatimaye ya pili na sasa ilikatika robo saa nzima!

    “Si yule pale,” nikasikia sauti ya kijana wa kiume akitamka, nikageuka kumwangalia...

    “Ndiyo ni yeye,” mwingine akadakia.

    Walikuwa wanaume wawili wa shoka, waliojazia sawasawa. Wakashuka garini kwa pamoja, wakaanza kunifuata huku nyuso zao zikionekana dhahiri walinifuata kwa shari!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    NILIJARIBU kuvuta kumbukumbu zangu vizuri kuona kama ningeweza kuwakumbuka wale vijana, zikagoma. Hakuna mtu niliyemfahamu kati yao. Kilichonishangaza ni namna walivyokuwa wakinifuata.

    Walionekana wazi kuwa wanamfuata mtu wanayemjua kwa uhakika kabisa. Walikuwa wananifuata mimi.



    Kilichonitisha ni ile hali ya kuja wakiwa wanaonekana wana uhakika kuwa mimi mtu wanayemfuata.

    Nilitaka kukimbia lakini sikujua ni kwa nini miguu ilishiiwa nguvu. Nikiwa bado nawashangaa, Patrick alitokea akiwa ameshika shilingi elfu kumi mkononi. Ni ile niliyomuomba.



    Kabla hajanifikia, tayari wale vijana wawili walishafika, wakasimama mbele yangu. Nyuso zao zilitangaza vita. Zilikuwa zimekunjamana wakionekana dhahiri kama wamekuja kulipiza kisasi.

    Sijui nini kilitokea, lakini ghafla nikashangaa Patrick akirudi nyuma kwa hofu, tayari wale jamaa walikuwa wameshanifikia kabisa. Walikuwa wamesimama mbele yangu.

    "Galos!" mmoja wa vijana wale akaita.

    "Ndiyo, vipi?"

    "Achana na mambo ya vipi."

    "Mnasemaje?" niliuliza nikiwa nimejawa hofu.

    "Tunasemaje?" mwingine akadakia.



    "Mbona siwaelewi, ninyi ni akina nani na mnataka nini kwangu?" nikawauliza tena.

    "Dar es Salaam ni ndogo sana. Huwezi kujificha milele, sasa tumekukamata. Songa kule..." akasema mmoja wao.

    Sikujua ilivyokuwa, ni kama niliduwazwa hivi, nikajikuta natembea mwenyewe kuelekea kwenye gari. Mmoja wao alinifungulia mlango, ulikuwa wa kiti cha nyuma.



    Nilipokaa tu, nikagundua kuwa kwenye gari kulikuwa na mtu mwingine amekaa mwishoni, mimi nikakaa katikati kisha yule mmoja wa wale niliokuwa nao nje, akaketi dirishani, mwingine akaenda kwenye kiti cha dereva.

    Gari likaondolewa.

    ***



    Niseme ule ukweli kutoka moyoni mwangu, akili hazikuwa zangu kwa muda. Nilihisi kupumbazwa, baadaye nikaona kiza kidogo, kisha nikahisi usingizi mzito sana.

    Nikalala.



    Sina hakika kama nililala au nilipoteza fahamu, lakini fahamu kuwa, sikuwa na mawasiliano tena na watu wale kwa muda.

    Sikujua chochote kilichoendelea!

    ***



    Nilihisi baridi kali sana, kwa mbali nikasikia muungurumo wa maji yalipiga kwa kasi. Ni kama vile nilikuwa nimesimama ufukweni mwa ziwa au bahari. Sikuwa na hakika ni wapi hasa kati ya sehemu hizo.



    Macho yangu yalikuwa mazito kufumbuka. Nilijitahidi sana kuyafumbua lakini ilishindikana. Ghafla maji ya baridi yakamwagwa mwilini mwangu. Nilishtuka kwa kasi na kufumbua macho.

    Nikasimama.



    Nilikutana na kitu cha ajabu sana. Mtu mmoja, mrefu, mweusi, mwenye ndevu nyingi alikuwa amekaa kwenye kiti cha mbao mbele yangu. Nyuma yake kulikuwa na wasichana waliokuwa wameshika vifaa maalum vilivyotengenezwa kwa ngozi, wakimpepea!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Pembeni yangu kulikuwa na wale vijana wawili walionichukua mtaani kwangu Tandale. Wakaniangalia mara moja, kisha wakarudisha macho yao kwa yule mzee.

    Kwa mara moja, wote wakaainamisha vichwa vyao na kuvirudisha juu!

    "Mkuu, tumekamilisha kazi uliyotuagiza!" wakasema wote kwa wakati mmoja.

    Yule mzee akatingisha kichwa.

    "Mango!" yule mzee akaita.

    Kijana mmoja wao, akaitikia kwa sauti: "Naam! Mkuu."



    "Kushoto..." akasema, mara moja huyo jamaa ambaye sasa niligundua kuwa anaitwa Mango, akasogea mkono wangu wa kushoto, akanishika bega.

    "Ngoma!" akasema tena, yule kijana mwingine akaitikia:

    "Mkuu."

    "Kulia."



    Naye akasogea kulia kwangu na kusimama kisha akaniwekea mkono begani. Kusema ule ukweli, sijawahi kuhisi woga kama niliopata siku hiyo. Niliogopa kuliko kawaida. Mpaka muda ule, sikuwa ninajua nilikuwa wapi na nilifanya kosa gani. Nilibaki nimesimama nikiwa sijui la kufanya.

    "Galos," yule mzee akaita.

    "Ndiyo mzee."

    "Najua hujui hapa ni wapi."

    "Ni kweli sijui."

    "Hapa ni pembeni mwa Kata ya Sandulula, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Mkoa wa Rukwa."

    "Nimefikaje? Kwa nini nipo hapa na mmenileta kufanya nini?"

    "Unamfahamu Matima Mtimandole?"

    "Ni baba yangu mzazi, kwa sasa ni marehemu."

    "Yeye ndiye sababu ya wewe kuwa hapa. Unafahamu alichotufanyia?"

    "Sijui, lakini ninyi ni akina nani?"



    "Hayo utayajua baadaye, lakini unatakiwa kufahamu kitu kimoja, mkeo hawezi kuzaa mtoto akabaki salama katika maisha yake yote. Tutaendelea kuharibu mimba zake kila siku.

    "Najua sasa hivi ana mimba nyingine. Kwa taarifa yako, pia imeshaharibika. Mkakati wa mwisho uliokuwa



    umebaki ulikuwa ni kumuua kabisa mkeo, kukuua na wewe ili kizazi chenu kipotelee mbali.

    "Tulikuwa na uwezo wa kufanya hivyo muda mrefu kabla, hata sasa tunaweza kufanya hivyo, ndiyo maana umeona umetoka Dar es Salaam hadi Rukwa kwa nusu saa tu. Hujui umefika wala usafiri uliotumia.



    "Makosa ya baba yako, ndiyo unayotakiwa kuyatumikia wewe. Adhabu tumeshaipitisha – ni kifo. Tutaanza na mkeo, halafu wewe. Hakuna mtu yeyote atayejua tukio hilo," alisema mfululizo kwa sauti huku sauti yake ikiunguruma.

    "Mango..." akaita.

    "Ndiyo mkuu."

    "Peleka eneo la tukio!"



    Nihisi mwili ukiniisha nguvu! Mango na Ngoma wakanishika juujuu, kisha wakaanza kutembea kunipeleka nisipopajua!



    HAIKUWA safari ndefu sana. Tuliishia kwenye chumba kimoja kidogo chenye giza kali sana. Nikabwagwa chini kama mzigo. Moyoni nilikuwa na maumivu makali, sikujua sababu ya kupewa mateso yale.



    Walivyonitupa pale chini, kama walioambiana waliondoka kwa pamoja na kuniacha peke yangu nikiugulia maumivu makali. Ghafla nilihisi wadudu wakianza kunitembelea mwilini mwangu.

    Walikuwa wadudu ambao niligundua haraka kuwa walikuwa siafu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Waliniuma kwa kasi mwilini mwangu, siafu wale hawakuwa na huruma hata kidogo. Nilihisi mwili ukivimba. Nilipiga kelele lakini hakuna aliyetokea kunipa msaada wowote.

    Baada ya muda kama robo saa hivi, mlango ulifunguliwa, mwanga hafifu ukaonekana. Mara baada ya mlango kufunguliwa, wale siafu wote waliondoka mwilini mwangu.

    Kuna mtu mmoja aliingia peke yake, sikumjua ni nani.



    “Galos,” mtu huyo aliita.

    Sauti yake ilinifanya nimjue kuwa ni yule mzee aliyewaagiza akina Ngoma na Mango walipeleke kwenye kile chumba.

    “Naam!”

    “Unajisikiaje?”

    “Naumia sana mzee. Kwa nini mnanitesa kiasi hiki?”

    “Hujui?”

    “Sijui kitu.”



    “Nilikuuliza swali mara ya kwanza, kuwa unamfahamu Matima Mtimandole ukasema ndiyo, si ni sawa?”

    “Ni kweli.”

    “Hebu ngoja tupate mwanga kidogo, fumba macho yako haraka.”

    Nikafumba.

    “Haya fumbua.”

    Nikafumbua.



    Nilishangaa sana kukuta nipo kwenye chumba kingine kizuri tofauti na kile cha awali, hapakuwa na siafu tena wala chochote kibaya. Kifupi kilikuwa chumba kizuri kama cha kawaida cha kuishi watu.

    “Hiki ni chumba changu cha mazungumzo na wageni. Huwa nawaingiza watu ninaowaheshimu tu, hivyo nawe nimekupa hii heshima, lakini ukinitibua utajuta,” akasema akinikazia macho.



    Kilikuwa chumba kilichotandazwa zulia zuri jekundu la manyoya ya kuteleza. Chini kulikuwa na mito mbalimbali. Nikajiegemeza kwenye mto mmoja, nikiangalia uvimbe niliokuwa nao mwilini kutokana na kuumwa na wale siafu.



    Ghafla nikiwa nimezubaa, aliingia msichana mmoja akiwa amebeba chano kilichokuwa na glasi mbili za juisi, akaweka moja mbele yangu kisha akapeleka nyingine kwa yule mzee.

    “Karibuni kinywaji!” akasema yule msichana mrembo akitabasamu.

    “Ahsante,” yule mzee akaitika.



    Mimi nilibaki kimya, moyoni nilikuwa na woga wa hali ya juu. Yule mzee akachukua glasi yake na kuipeleka kinywani mwake. Akapiga funda moja kubwa kisha akairudisha glasi chini, akaniangalia.

    “Kunywa!” alisema kwa kuamrisha.



    Nikainua glasi na kuipeleka kinywani, nikanywa. Dah! Ilikuwa juisi yenye ladha tamu kuliko kawaida. Sikukumbuka ni lini au wapi nilipata kunywa juisi yenye ladha tamu kama ile.

    Nikarudisha glasi chini huku nikijitahidi kuachia tabasamu la kulazimisha.



    “Naitwa Mukulungu – Mkuu wa Wachawi. Walio chini yangu wamezoea kuniita Mkuu, nawe pia unatakiwa kuniita hivyo,” akasema.

    Nikatingisha kichwa kukubaliana naye.

    “Nataka kukusaidia.”

    “Nitashukuru.”



    “Kwanza nataka kukujulisha sababu ya wewe kuwa hapa. Marehemu baba yako Matima Mtimandole, alikuwa mwanachama wetu. Tulifanya naye kazi vizuri lakini mwisho alianza kuharibu masharti yetu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/“Nadhani unakumbuka kuwa mmefiwa mfululizo na ndugu zenu. Utakumbuka kuwa, baba yako ndiyo amekuwa wa mwisho kufariki na mara baada ya kufariki, utajiri wote ukapukutika.

    “Ni sisi ndiyo tulifanya hivyo kwa sababu ya ubishi na ujuaji wa baba yako. Wewe umepata nafuu kwa sababu ni mtoto wa mwisho, ndiyo maana tukaamua kuchukua watoto wako.



    “Mkeo anaweza kupata mimba na akajifungua kama haitakuwa ya kwako. Tunachotaka sisi ni kizazi chako chote. Tunataka ubaki peke yako kwenye mateso makali, ndiyo lengo letu,” alisema mfululizo akiniangalia.

    Nilipigwa na butwaa.



    Nilimkumbuka baba yangu, mama yangu na ndugu zangu waliofariki. Moyo wangu uliumia sana, maana nilibaki peke yangu kama jicho.

    “Sitaki kukuambia maneno mengi, ila unatakiwa kujua kuwa, tunataka kukusaidia – tupo tayari kurudisha utajiri wa baba yako mikononi mwako,” akasema.

    Sikujibu kitu.

    “Unanielewa?” akauliza.

    “Sijakuelewa vizuri.”

    “Unataka kuendelea kuishi masikini?”

    “Hapana.”

    “Unataka mimba za mkeo ziendelee kuharibika?”

    “Hapana.”

    “Sasa kama ndivyo unatakiwa kuwa tayari kwa maelekezo yetu.”

    “Maelekezo gani?”



    “Unatakiwa kujiunga nasi, uwe kama alivyokuwa marehemu baba yako lakini lazima uwe makini na usivunje masharti yetu.”

    “Ni nini?”

    “Unatakiwa uingie kwenye chama chetu cha wachawi.”

    “Mh!” niliguna.

    “Paaaaaaa!” kitu kizito kilitua mgongoni mwangu.



    “Pumbavu! Unadhani kuna kubembelezana hapa? Kwa nini unataka kutuzungusha? Au unataka kufa? Sawa...tutajua cha kufanya. Toweka!” Mkuu alisema kwa sauti ya ukali, yenye muungurumo mkali.

    Nikapoteza fahamu.

    ***



    Nilijikuta nipo nje ya chumba changu, mlangoni tena nikiwa nimeshika kitasa cha mlango wa chumba chetu. Bila kuelewa ilivyokuwa, nikajikuta nimefungua mlango. Nikaingia na kukutana na kitu cha ajabu sana. Damu zilikuwa zimetapakaa chumba kizima! Rita mke wangu kipenzi, alikuwa akigaragara kitandani!

    Nikashtuka sana!



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog