Simulizi
: Baba Kiumbe Wa Ajabu
Sehemu Ya Tano
(5)
Pamoja na kujua ubaya wao kwangu, bado
sikutakiwa kuua nikijua kabisa chanzo cha kifo kinatokana na nini. Tulilala kila
mtu na kitanda chake kwa kuzima taa. Katikati ya usiku niliota ndoto moja baba
amegeuka kiumbe cha ajabu chenye manyoya na meno marefu. Nilimuona mama na ndugu
zangu wakilia. Kilichonishangaza zaidi alionekana kama kiumbe kisicho na
uhai.
Nilishtuka usingizini na kukaa kitako huku nikijiuliza ndoto ile
ina maana gani, Nilijikuta nikishindwa kuelewa ndoto ile ina maana gani na kwa
nini baba ageuke kiumbe cha ajabu chenye kutisha? Sauti za kilio nilizozisikia
ilionesha wazi msiba ule ni wa baba. Niliamini ndoto ile iliashilia kifo cha
baba lakini kubadilika kwa umbile la ajabu lilikuwa likiashiria
nini?
Lakini sikutaka kuamini moja kwa moja kutokana na kauli ya
mganga kuwa baba yangu atakufa kama nikikutana kimwili na mpenzi wangu na sharti
lile nililitekeleza. Niliamini huenda ile ni ndoto ya kawaida tu wala
haihusiani na ukweli wowote, kutokana na kutoelezwa chochote na mganga juu ya
kupata ndoto yenye kiashirio.
“Vipi Masalu?” Sauti ya mpenzi wangu
ilinishtua nikiwa katikati ya dimbwi la mawazo.
“Aah… safi tu,”
nilijibu huku nikijitahidi kuficha kilicho moyoni mwangu.
“Safi, mbona
umeamka na kukuona ukitupa mikono kama unazungumza na mtu kuna kitu gani
kimekusibu?”
“Mmh! Kweli nimeona ndoto moja imenitisha
sana.”
“Ndoto gani?”
“Nimeota nyumbani ndugu zangu wanalia
baba akiwa amelala kitandani, lakini kitu cha ajabu amegeuka kiumbe cha ajabu
chenye kutisha.”
“Sasa wasiwasi wako nini? hiyo si ndoto
tu?”
“Huenda baba amekufa.”
“Masalu si ulielezwa atakufa
kama tukikutana kimwili?”
“Ndiyo, hata mimi
nashangaa.”
“Kwani mganga alikueleza nini juu ya njozi
utakayoota?”
“Hakunieleza chochote.”
“Sasa wasiwasi wako
nini?”
“Kwa vile baba hali yake ilikuwa mbaya, ndoto hii imenitisha
sana.”
“Masalu acha kujitia presha bure, maisha ya baba yako yako
mikononi mwako.”
“Mmh! Sawa, lakini niliingiwa na wasiwasi
mkubwa.”
“Lala mpenzi.”CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nashukuru kwa
kunipa moyo.”
“Nipo hapa kwa ajili hiyo.”
“Asante mpenzi
wangu kwa kunijali sina cha kukulipa.”
“Cha kunilipa baada ya kupona
ni ndoa tu.”
“Omba jingine hilo umepata. ”
Niliagana na
mpenzi wangu kila mmoja alilala, usingizi haukuchelewa kunichukua, haikuchukua
muda mrefu njozi ilijirudia, tena safari hii niliwasikia wakilia huku wakitupia
shutuma zao kwangu kuwa mimi ndiye chanzo cha kifo cha
baba.
Nilishtuka tena kitandani na kuwasha taa, mpenzi wangu naye
alishtuka na kuhoji kwa nini nimeamka tena.
“Masalu, vipi mpenzi
wangu?”
“Mmh!” niliguna tu.
“Mbona
sikuelewi?”
“Mmh! Ndoto bado inaning’ang’ania.”
“Umeota nini
tena?”
“Bado kifo cha baba kinaendelea na safari hii nimewasikia mama
na ndugu zangu wakinishutumu ndiye niliyesababisha.”
“Lakini bado
itakuwa ni njozi tu kwa vile mawazo yako yote umeyahamishia
huko.”
“Kwa hiyo nifanyeje?”
“Hebu iache njozi iishe wala
usiamke.”
“Mmh! Ngoja nijaribu.”
Nilirudi kulala tena, ajabu
nililala mpaka asubuhi bila kuota tena, mpenzi wangu ndiye
aliyeniamsha.
“Masalu.”
“Naam.”
“Vipi upo
sawa?”
“Nipo sawa, vipi?”
“Naona leo umelala
sana.”
“Kwa muda huu ni saa ngapi?”
“Mmh! Ni saa tatu na
nusu.”
“Ooh! Leo nimelala sana.”
“Inawezekana ni kutokana na
kuamkaamka usiku kutokana na njozi ulizoota.”
“Na
kweli.”
“Vipi uliota tena?”
“Sikuota, nimelala
vizuri.”
“Unaona wasiwasi wako tu, njozi zingine hutokana na mawazo
ya mtu.”
“Ni kweli, lakini ziliniweka kwenye hali mbaya kwa vile kama
kweli baba atakufa ndugu zangu hawatanielewa.”
“Wasikuelewe
vipi?”
“Si nitaonekana mimi ndiye niliyemuua.”
“Masalu acha
kujitoa akili, ulikwenda sehemu gani kumroga baba yako?”
“Sijaenda
popote.”
“Sasa?”
“Si inaonesha kuwa uchawi
umewarudia.”
“Hukuwaroga?”
“Ndiyo.”
“Sasa wewe
unaogopa nini?”
“Mmh! Suala la kuua si la
kawaida.”
“Wangekuua wewe lingekuwa la kawaida au umefurahia kuuawa
kwa dada yako Monika?”
“Swali gani hilo, hujui nilivyoumizwa na kifo
cha dada yangu?”
“Sasa inakuwaje unaogopa vifo vya watu mnajua kabisa
hawana nia nzuri na wewe?”
“Basi tuachane na hayo, tuoge tukapate
chai.”
Niliamka kitandani na kwenda kuoga, baada ya kuoga tulikwenda
kupata kifungua kinywa kilichokuwa mlemle kwenye hoteli tuliyokuwa
tumepanga.
Wiki ilikatika tukiwa tumejificha na mpenzi wangu, hata
simu niliamua kuizima ili kuondoa usumbufu wa ndugu zangu. Siku moja asubuhi
tukiwa mgahawani tukipata kifungua kinywa niliamua kuwasha simu. Utafikiri kuna
mtu alikuwa akisubiri kwa hamu nilipowasha tu simu iliingia. Kuangalia ilionesha
namba ya kaka yangu, niliiangalia kwa muda bila kupokea mpaka ikakatika.
Haikupita muda simu iliita tena alikuwa dada nayo niliiangalia bila
kuipokea.
“Masalu mbona hupokei simu?”
“Achana
nao.”
“Kina nani?”
“Si hawa
wapuuzi.”
“Ndugu
zako?”
“Ndiyo.”
“Hebu pokea uwasikilize kwa vile hujui
wanataka nini?”
“Achana nao najua wanataka kunijua
nilivyo.”
“Masalu si umeambiwa kuwa sasa hivi mtu hakusogelei,
wasiwasi wako nini?”
“Sina wasiwasi ila sipendi kuwasikiliza kwa vile
hakuna jipya la kuniambia.”
“Wasikilize.”
“Sitaki, wale sio
watu siwezi kuwasikiliza watu wabaya kama wale.”
Mara simu ya mpenzi
wangu iliita aliipokea na kuzungumza.
“Eeeh...Ndiyo...Shikamoo
mama...Ndiyo...Hapana...Lini?..... Leo...Sawa
nitamwambia....nitakujulisha....Hapana tupo Mwanza...Sawa mama
nitamwambia....Haya mama.”
Baada ya kukata simu alinigeukia na
kunitazama kwa muda.
“Vipi kuna usalama?”
“Kiasi.”CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuna tatizo
nyumbani kwenu?”
“Hapana, kwenu.”
“Kwetu kuna tatizo gani?”
nilishtuka.
“Ndoto yako imekuwa na ukweli.”
“Ina maana baba
amefariki?”
“Ndiyo, inaonekana hata ndugu zako walikuwa wakikutafuta
kukupa taarifa.”
“Mmh! Sasa itakuwaje?”
“Mmh! Kazi ipo
nataka nikueleze kitu kimoja kabla ya kufanya lolote turudi kwanza kwa
mganga.”
“Kweli hilo wazo zuri. “
“Vipi mbona
unanyanyuka?”
“Mambo yameharibika, japo alinitenda vibaya lakini kifo
cha baba yangu kimeniuma sana.”
“Utafanyaje
imeshatokea!”
“Lakini mganga si alisema mpaka tukikutana kimwili! Sasa
imekuwaje?”
“Ndiyo maana nikasema twende kwanza tukamuulize kabla
hatujafanya lolote.”
“Naona tusipoteze wakati.”
“Subiri basi
tumalize kunywa chai.”
“Chai haipandi tena,” nilisema huku
nikinyanyuka kwenye kiti.
“Pole mpenzi wangu.”
“Bado
sijapoa, kifo cha baba kimeniuma sana,” nilijikuta nikidondokwa na
machozi.
“Pole mpenzi,“ mpenzi wangu alinisogelea na kunibembeleza,
kitu kile kiliniongeza uchungu moyoni na kuangua kilio cha sauti
kilichowashangaza waliokuwepo hotelini. Ilibidi mpenzi wangu anipeleke
chumbani.
*****
Nilipofika hotelini niliendelea kulia kwa sauti ya chini
huku mpenzi wangu akiendelea kunibembeleza. Pamoja na yote niliyotendewa na
baba, lakini kifo chake kiliniuma sana. Niliweka pembeni ubaya wake na
kuyakumbuka mapenzi yake kwangu kipindi chote cha kukua
kwangu.
Nilijua kilichomponza baba yangu ni tamaa ya mali ambayo
masharti yake yaliiathiri familia yetu. Nikiwa bado nimeinama nikiendelea
kumlilia baba yangu, mpenzi wangu aliniuliza:
“Kwa hiyo utakwenda
kwenye msiba?”
“Hata sijui nifanye nini?”
“Lakini jambo hili
ni zito si la kukurupuka.”
“Ni kweli, najua kabisa kifo cha baba ndugu
zangu wanajua mimi ndiye mhusika mkuu. Unafikiri nikienda itakuwaje kama siyo
kutiana aibu msibani?”
“Lakini kwa nini tusirudi kwa mganga ili
atueleze tufanye nini?”
“Lakini si mganga alisema mpaka tukutane
kimwili, sasa nini kilichomuua baba yangu?”
“Masalu swali hilo mimi
siwezi kukujibu.”
“Basi twende kwa huyo
mganga.”
Tulikubaliana kwenda kwa mganga kumpa taarifa ya kifo cha
baba, tulipofika tulikuta watu wengi, hivyo ilitupasa kusubiri zamu yetu japo
niliamini itatuchukua muda mrefu kuonana na mganga. Hatukuwa na budi kusubiri,
lakini mganga alipita na mgonjwa akienda naye nyuma ya nyumba, nilijua anakwenda
kumfanyia matibabu.
Baada ya dakika kama ishirini alirudi peke yake na
kuniona, alionesha ishara ya kuniita. Nilinyanyuka na kumfuata ndani ya kilinge
cha kutibia, baada ya kukaa alisema:
“Vipi, mbona umerudi
mapema?”
“Baba amefariki jana.”
“Sasa tatizo
nini?”
Swali la mganga lilinishangaza, baba yangu amefariki yeye
haoni tatizo.
“Si ulisema mpaka tukutane kimwili
ndipo baba angefariki, au hata kulala chumba kimoja?”
“Masalu
sijakueleza hivyo kuwa muelewa, nilikueleza mpaka mkutane kimwili si kulala
chumba kimoja.”
“Sasa kifo cha baba yangu kinatokana na
nini?”
“Kwa amri ya Mungu.”
“Si ulisema mpaka tukutane
kimwili?”
“Eeh, lakini na Mungu ana nafasi yake, huamini kuna
kifo?”
“Naamini.”
“Sasa?”
“Lakini ndugu zangu
waliniomba niokoe hali ya baba, kama amekufa bila mimi kufika si nitaonekana
ndiye niliyechangia.”
“Huo ni wasiwasi wako, baba yako amejiua
mwenyewe kwa msaada wa ndugu zako.”
“Una maana gani kusema
hivyo?”
“Baada ya kushindwa kukudhuru walijaribu uchawi mmoja ambao ni
mbaya kuliko kitu chochote. Ule ukifanyiwa huchukui muda lazima ufe, baada ya
kuonekana hujali na unajiamini waliamua jambo moja, kukufutilia mbali. Kama si
kinga niliyokufanyia sasa hivi ungebaki jina.”
“Ni uchawi gani?” Kauli
ya mganga ilinitisha.
“Kweli ndugu zako wamekupania vibaya, uchawi
uliofanywa ni wa kinyonga, anakamatwa kinyonga mzima anapasuliwa na kuchunwa
ngozi. Kisha ngozi yake inawambwa na kupakwa dawa huku likinuizwa jina lako.
Ngozi ikikauka na wewe uhai huna.”
“Du!” Nilishtuka.
“Ndiyo
walivyofanya, kazi hiyo ilifanywa saa sita usiku ili asubuhi ukiamka ukutwe
umekufa. Baada ya kutega uchawi wao walikwenda kulala huku mganga
akiwahakikishia kuwa asubuhi wakiamka watasikia habari za kifo
chako.
“Lakini ilikuwa tofauti na walivyo fikiria, kinga niliyokuwekea
ilifanya kazi, nilikueleza kila watakachokufanyia kitawarudia. Uchawi uliotaka
kukuua ndiyo uliomuua baba yako. Ndio maana nilikuambia kifo cha baba yako
alijitakia mwenyewe akishirikiana na ndugu zako.”
“Unataka kuniambia
bila kinga nisingeiona leo?”
“Hilo ni jibu uliza swali.”CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuhusu kwenda
msibani itakuwaje?”
“Ukitaka nenda hawawezi kukufanya
lolote.”
“Hatuwezi kutiana aibu kuwa mimi ndiye niliyemuua
baba?”
“Wataanzia wapi, kwa kitendo walichokitenda jana usiku na leo
kukuona hai wamezidi kuchanganyikiwa. Kama wangejua kama ni mimi ndiye
niliyekukinga, basi wangenipa pesa nyingi ili wakupoteze.”
“Kuna
umuhimu wa kuongeza kinga mwilini maana kama kinyonga kashindwa lazima
wataendelea kutafuta kitu kingine,” nilijikuta nikijihami baada ya kuona vita
iliyopo mbele na ndugu zangu ni nzito.
“Kijana kama kinyonga
ameshindwa hakuna kitu chochote kitaweza japo kwa dawa yangu walikuwa
wakijisumbua, uchawi ule ni mbaya sana.”
“Kwa hiyo
unaniambiaje?”
“Ondoa wasiwasi, chochote kitakachokupata si mkono wa
mtu bali amri ya Mungu.”
“Nashukuru mzee wangu.”
“Basi ondoa
hofu hakuna chochote kitakachokukuta, kila atakayekugusa
kitamrudia.”
Niliagana na mganga kisha nilimpitia mpenzi wangu na
kurudi hotelini kujiandaa na kwenda msibani. Tukiwa njiani simu ya dada iliita,
nilitaka kuacha kuipokea lakini niliipokea ili nijue ana shida
gani.
“Haloo,” nilipokea.
“Asante Masalu, asante sana.. njoo
umle nyama baba,” dada alisema kwa sauti iliyoonesha analia.
“Tena
wewe ndiye ninayekutafuta mchawi mkubwa, nakuapia sitakusamehe wewe na wote hata
marehemu baba mpaka nakufa. Vitendo vyote mlivyonitendea hamkuridhika mpaka
mnaitaka roho yangu kwa nguvu? Hivi nikifa mtafaidika nini?”
“Nani
anataka kukuua?”
“Kitendo mlichofanya wiki moja iliyopita sitawasamehe
mpaka nakufa, mnanilaumu nahusika na kifo cha baba. Hebu niambieni mimi
nimefanya nini kuchangia ugonjwa mpaka kifo cha baba. Kinyonga mliyemtumia ili
mniue ndiye aliyemmaliza baba kwa taarifa yenu.”
“Ha! Umejuaje?” Dada
alishtuka.
“Nakuapia nilikuwa nina mpango wa kuwasamehe, lakini kwa
kitendo mlichokitenda jana saa sita usiku sitawasamehe milele na mimi nitajua
cha kuwafanya, endeleeni kuroga nami sasa naingia vitani tuona nani
zaidi.”
Kauli yangu ya vitisho japo sikuwa na nia hiyo ilimfanya dada
akate simu.
“Masalu vipi mbona sikuelewi?” Mpenzi wangu
aliniuliza.
“Wee waache tu.”
“Nani
huyo?”
“Dada.”
“Mbona mnatishana?”
“Namtisha
namwambia ukweli!”
“Kwa nini umewaambia mapema?”
“Lazima
waujue ubaya wao na tena nawafuata msibani wanieleze kisa na mkasa cha
kuyatafuta maisha yangu,” nilijikuta nikipandwa na hasira.
“Punguza
hasira tukifika hotelini tutalizungumza, umeshawajua wabaya wako kwa nini
uchanganyikiwe?”
Nilikubaliana na mpenzi wangu kurudi hotelini,
tulipofika nilikuwa bado na hasira kwa kauli za dada kuwa nitamla nyama baba
yangu aliyefariki kwa ajili yao wenyewe. Nilijikuta njia panda katika maamuzi
yangu ya kwenda kwenye msiba wa baba. Nilijikuta nikipata ujasiri wa kwenda
kwenye msiba wa baba.
“Aisee wacha niende kwenye msiba wa baba,”
nilimwambia mpenzi wangu.
“Masalu nakuomba usiende.”
“Hapana
lazima niende.”
“Panaweza kutokea ugomvi.”
“Na utokee, tena
nakwenda kuwapa makavu.”
“ Nakuomba usiende mtatiana
aibu.”
“Nisipokwenda watu hawatanielewa.”
“Bora wasikuelewe
kuliko aibu itakayowakuta.”
“Hakuna aibu, mganga amesema hawatafunua
midomo yao kusema lolote kwa kuiogopa aibu.”
“Mmh! Lakini ningekuwa
mimi nisingeenda.”
“Lazima niende na leo watanitambua, siwezi kuishi
na maadui zangu na kuwachekea.”
”Hayo ndiyo ninayokukataza, kama
huwezi kuzuia hasira zako hakuna haja ya kwenda.”
“Nitajitahidi lakini
moyo unaniuma baada ya kujua ubaya waliotaka kunifanyia usiku wa kuamkia
leo.”
“Lakini si umepata kinga?”
“Ni kweli, lakini kama
nisingepata ingekuwaje?”
“Ungepotea, lakini nakuomba ulimalize jambo
hili kwa busara.”
“Nimekuelewa.”CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilijiandaa na
baadaye tuliondoka na mpenzi wangu ambaye nilimuacha nyumbani kwao na mimi
kwenda kwetu. Nilipofika nilikuwa watu wengi wamekusanyika nje ya nyumba yetu
wakiwepo wafanyabiashara wenzetu.
Sehemu kubwa ilikuwa imejaa magari
ya watu, nilipoteremka kwenye teksi na kutembea kwenda ndani, kila aliyenitazama
alinishangaa. Wengi walinipa pole ya kifo cha baba, niliwaitikia na kuingia
ndani. Nilipofika ndani ndugu zangu walishtuka kuniona.
Sikujali hali
ile, niliingia chumba alichokuwa mama, aliponiona aliacha kulia na kunitazama
kama kiumbe cha ajabu. Kwa vile kila kitu nilikuwa nakijua sikuijali hali ile na
kumsalimia.
“Shikamoo
mama.”
“Marahaba.”
“Poleni.”
“Asante.”
“Mnazika
saa ngapi?”
“Sijajua mipango yote wanafanya ndugu
zako.”
“Kwani Masalu ulikuwa wapi?” Mama wa jirani
aliniuliza.
“Nilikuwa safari.”
“Ooh! Pole sana kwa kumpoteza
kipenzi baba yako, najua kiasi gani alivyokuwa akikupenda.”
“Ni
mapenzi ya Mungu.”
“Na kweli, ni yeye aliyetoa na ndiye
aliyetwaa.”
“Kila neno litatimia.”
“Masalu,” sauti kali ya
dada iliniita.
“Unasemaje?”
“Njoo nje.”
“Kufanya
nini?”
“Nimekwambia njoo au nitakutoa kwa nguvu.”
“Jeuri
hiyo huna.”
“Salome hebu zungumzeni kwa ustaarabu hamjui hapa ni
msibani?” Mama aliingilia kati.
“Kafuata nini? Namuuliza kafuata nini,
aliyotaka yamekuwa anataka nini tena?”
“Tena wewe malaya wa kike funga
domo lako,” Kwa mara ya kwanza nilimvunjia heshima dada yangu.
“Jamani
mama Salome ni maneno gani hayo?” Jirani alitushangaa.
“Samahani
jirani naomba utupishe mara moja,” mama alimtoa nje jirani baada ya kuona
tunataka kumwaga mtama kwenye kuku wengi.
Baada ya jirani kutoka nje, tulibakia watatu ndani, mama alisema
kwa sauti ya kilio:
“Salome unafanya nini?”
“Mama hujui
aliyofanya mwanao, kamuua baba kisingizio eti tulitaka kumuua
jana.”
“Una uhakika gani nimemuua baba?”
Nilimuuliza.
“Kumbuka ulipokuja kumuona baba alisema tukuondoe kwa
vile unataka kumuua.”
“Sikiliza wee malaya,” nilimnyooshea kidole
dada.
“Ha! We niliyekushika kinyesi chako unanivunjia
heshima?”
“Tena shetani wa kike, yaani nakuapieni yote mliyoyafanya
juu yangu hamkuridhika, mkaamua jana kunifutilia mbali kwa uchawi wa kinyonga?
Mama nisikilize vizuri tena kwa makini. Sitaisamehe familia yako mpaka naingia
kaburini.”
“Usitutishe mchawi mkubwa.”
“Nafahamu kila kitu
mnakijua hata mama niliyekuwa nakuamini kwa ajili ya mali unakubali wanao tuishe
kwa ajili ya tamaa ya wachache. Nilikuwa na huruma na ndugu zangu na kukubali
kuteseka kwa ajili yao, lakini hili la kutaka kuniua sitawasamehe
milele.”
“Muongo mkubwa, wewe ndiye uliyemuua baba.”
“Mama
nimemuua vipi baba?”
Mama hakujibu alitazama chini kwa aibu,
niliendelea kusema kwa hasira lakini sauti ilikuwa ya chini.
“Dada
Salome unajua kila kitu wewe ndiye uliyempa dawa mpenzi wangu anipake ili kuua
nguvu zangu za kiume mlifanikiwa. Lakini mlisahau mimi si mzimu wa familia
nilijua mlitaka kunitoa kafara kama dada Monika lakini mambo hayakwenda
hivyo.
“Niliweza kupita chini juu na kuweza kuidhibiti hali hiyo,
baada ya hapo hamkuridhika mkataka kunigeuza ndondocha mkashindwa na mwisho
mkataka kuniua matokeo yake mmemuua baba. Mnakosa haya kunishtumu, hivi uchawi
wenu wa kinyonga ungefanikiwa mimi ningekuwa wapi?
“Nasema hivi
naondoka si hamnitaki, naondoka ila nawatahadharisha mkiendelea na mchezo wenu
mtapukutika wote kama mlivyomtanguliza baba. Mimi si Monika ni Masalu,” nilisema
nikiwa nimebadilika, sikuwa Masalu wa kuonewa tena.
“Masalu,” Dada
Monika alitaka kusema kitu.
“Kwanza kabla sijaondoka nataka niione
maiti ya baba yangu kwa mara ya mwisho.”
“Hapana Masalu baba huwezi
kumuona,” dada Monika aliweka ngumu.
“Unajua nawastahi sana, najua
kila kitu, kama mnataka siri yote nikaitoe kwa watu nje nikatazeni,” nilipiga
mkwara mzito.
“Maiti ya baba yako imeharibika,” mama alisema kwa sauti
ya upole.
“Hata kama iweje ni baba yangu nina haki ya
kumuona.”
“Masalu acha tu baba yako azikwe, ameharibika sana,” mama
aliendelea kunibembeleza.
“Mama mimi si mtoto wako?”
“Mtoto
wangu.”
“Aliyekufa si baba yangu?”
“Baba
yako.”
“Basi nipeleke nikamuone.”
Walitazamana kwa muda
kisha mama alisema kwa sauti ya chini.
“Salome mpeleke mdogo wako
akamuone baba yake.”
“Mama tulizungumza nini?”
“Salome
sitaki ubishi hebu maliza hili kwa nini tuwafaidishe
watu?”
Nilipelekwa chumba ulicholazwa mwili wa baba, nilikuta
amefunikwa shuka, niliifungua upande wa kichwani. Kidogo nikimbie baada ya
kukuta kiumbe cha ajabu kilichokuwa kama mnyama chenye manyoya na meno ya
kutisha. Nililivuta shuka lote, sikuamini nilichokiona. Baba alikuwa amebadilika
na kuwa kiumbe wa ajabu, mwili mzima akiwa na manyoya kama
mnyama.
Nilimgeukia dada Salome.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Baba yupo
wapi?”
“Si huyo mbele yako.”
“Hapana huyu si baba yangu,
naomba unioneshe baba yangu,” nilijikuta nikipandwa na hasira.
“Masalu
huyu ndiye baba, tangu alipoanguka kila siku alikuwa akibadilika na kuwa kiumbe
cha ajabu mpaka mauti yalipomkuta,” dada Salome alinipa maelezo ya sababu ya
hali ya baba kuwa vile.
“Jamani mmeona mwisho wa ubaya aibu kama
hii.”
Mara mlango ulifunguliwa na kuingia kaka zangu walioonekana
wanatoka kunywa.
Jamani huyu mchawi amefuata nini?”
“Mama
ndiye kampokea,” dada Salome alijibu.
“Toka nje, hebu kalete panga
amfuate baba.”
“Kama jana mlishindwa kuniua kwa uchawi wa kinyonga na
matokeo yake mkamuua baba, hamtaweza kuniua kamwe. Nitaondoka kwa kupenda si kwa
kulazimishwa na familia ya wanga.”
Baada ya kusema vile niligeuka
na kutoka nje, bila kuzungumza na mtu niliwapita watu ambao hawakuelewa
kinachoendelea. Nilielekea barabarani na kukodi teksi iliyonipeleka nyumbani.
Nilimpigia simu mpenzi wangu anifuate nyumbani. Alishangaa na
kuniuliza:
“Vipi mbona unasema upo nyumbani kwako wapi,
msibani?”
“Noo, kwangu kabisa.”
“Utani huo, si ulikwenda
msibani au baba yako hakufa?”
“Amekufa.”
“Sasa mbona upo
nyumbani?”
“Ni hadithi ndefu njoo mara moja
nyumbani.”
“Nakuja.”
Nilikata simu na kujilaza kwenye kochi
nikiwa bado hasira imenijaa moyoni. Baada ya muda mpenzi wangu alifika nyumbani
na kunikuta katika dimbwi la mawazo. Hata alipoingia sikumuona alinishtua kwa
kuniita.
“Masalu....Masalu.”
“Ee..eeh.”
“Jamani
mbona hivyo?”
“Aah, umekuja saa ngapi?”
“Ndiyo naingia,
mbona umerudi mapema mmeshazika?”
“Bado.”
“Sasa mbona
umerudi?”
“Wee acha tu.”
“Kuna nini tena?” Aliniuliza kwa
mshtuko kidogo.
“Wee acha tu.”
“Niache nini Masalu! Hebu
nieleze kuna nini?”
Sikuwa na budi kumueleza niliyokutana nayo
msibani, mpenzi wangu aliniangalia kwa huruma na kusema:
“Lakini
Masalu we mbishi sana, si nilikueleza usiende ukabisha.”
“Ilikuwa
lazima niende kwenye msiba wa baba yangu kwa vile unanihusu.”
“Japo
unakuhusu lakini mazingira yake hayakuwa mazuri.”
“Yawe mazuri vipi
ikiwa aliyekufa ni mzazi wangu?”
“Sawa mzazi wako lakini unajua kifo
chake kilitokana na nini, Na dada yako baada ya kifo cha baba yenu maneno
aliyokuambia, sasa nini kigeni kwako?”
“Nimekuelewa, lakini
watanitambua.”
“Lakini Masalu we mbishi sana, si
nilikueleza usiende ukabisha.”
“Ilikuwa lazima niende kwenye msiba wa
baba yangu kwa vile unanihusu.”
“Japo unakuhusu lakini mazingira yake
hayakuwa mazuri.”
“Yawe mazuri vipi ikiwa aliyekufa ni mzazi
wangu?”
“Sawa mzazi wako lakini unajua kifo chake kilitokana na nini,
Na dada yako baada ya kifo cha baba yenu maneno aliyokuambia, sasa nini kigeni
kwako?”
“Nimekuelewa, lakini watanitambua.”
“Masalu jambo
hili linahitaji utulivu, nakuomba tuondoke hapa twende sehemu yoyote ili upate
utulivu wa moyo.”
“Nashukuru kwa kunipa moyo na kuwa mtu wangu
muhimu.”
“Najua upo katika kipindi kigumu hivyo nahitaji kuwa karibu
yako na kuhakikisha hupati mawazo mabaya. Nina imani utavuka kipindi hiki
kigumu.”
“Nashukuru sana, sasa tutakwenda wapi?”
“Twende
Musoma au Shinyanga.”
“Mi nafikiri Musoma panafaa.”
“Vipi
kuhusu duka linaendelea?”
“Hata najua.”
Kwa kweli nilijibu
nikiwa sijui nini kinaendelea, muda mwingi nilifikiria maisha yangu kuliko
biashara kilichokuwa kikinisaidia ni pesa kidogo zilizokuwa kwenye akiba yangu
pia mpenzi wangu naye alichangia kwa kiasi kikubwa kutokana na uwezo wa familia
yake.
“Nakuomba kitu kimoja, funga duka kisha tuondoke, na msiba
ukiisha usifanye biashara yoyote bila kumshirikisha yule babu. Si alikuambia
biashara zenu zinaendeshwa na kidonda chako na maiti ya dada na mtoto wa dada
yako?”
“Na kweli basi
nitampigia simu anayetunza funguo za duka ili asilifungue tena.”
“Sio
alifungue anaweza kuombwa funguo na dada zako na kufanya jambo lolote dukani
kwako wale sasa si ndugu bali maadui zako.”
“Na kweli wacha nimwambie
aniletee funguo kabisa.”
“Hilo ndilo jambo
muhimu.”
Nilimpigia simu anayetunza funguo za duka ili asifungue pia
aniletee funguo. Alikubali ataniletea baada ya kutoka msibani, lakini nilimuomba
aniletee muda ule, alikubali na kuniahidi kuniletea baada ya muda mfupi.
Tulikubaliana na mwenzangu baada ya kupata funguo za duka tuondoke mchana ule
kwenda Musoma.
Kwa vile safari ilikuwa ya kuchukua hata wiki mpenzi
wangu alirudi kwao kuchukua nguo za kuvaa na kuniacha nikijiandaa. Muuzaji wangu
aliniletea funguo na kushangaa kuniona nipo nyumbani badala ya msibani.CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Bosi mbona haupo
msibani?”
“Nitakuja baadaye.”
“Sawa lakini nimeacha
maandalizi ya mwisho kwenda kuzika.”
“Nakuja muda si
mrefu.”
“Haya wacha niwahi.”
Tuliagana na kuniacha
nikimsubiri mpenzi wangu ambaye alikuja baada muda si mrefu. Tuliongozana hadi
Buzuruga na kukata tiketi ya basi la Musoma, tulifika Musoma jioni na kupanga
tatika Hoteli ya Orange Tree iliyokuwa ipo katika hali nzuri, tulipanga pale kwa
wiki nzima nikiwa nimezima simu ili kujiepusha na maneno ya ndugu
zangu.
Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu kuogopa kufanya
mapenzi na mpenzi wangu nikihofia kusababisha kifo cha baba tuliweza kufanya
mapenzi bila hofu ya kila kitu huku mpenzi wangu akifurahia starehe ya siku ile
huku akiniahidi nifanye haraka kumuoa.
Nilimuahidi kufanya vile baada
ya matatizo kutulia kwa kuonesha mapenzi ya dhati kwangu kipindi chote cha
matatizo. Kipindi nilichopitia kama mwanamke asiye na mapenzi ya dhati lazima
angenikimbia lakini wa kwangu hakunikimbia zaidi ya kunipa moyo.
Baada
ya wiki tulirudi Mwanza na kwenda moja kwa moja kwa mganga, baada ya kuniona
alinieleza hali ilivyokuwa juu ya mipango ya ndugu zangu.
“Kijana japo
ndugu zako walijaribu kutaka kukuangamiza lakini matokeo yao ni kufilisika kwa
kasi ya ajabu, aibu itakayowakuta juu yako watakuja kukuomba msamaha.
Ulichokifanya ni kitu cha busara sana kama ulivyonieleza mawazo yote kakupa
mpenzi wako nina imani hiki ni kipindi cha kukaa pamoja na kupanga maisha
yenu.
“Kuhusu duka nilitalifanyia zindiko kuhakikisha ndagu ya familia
haikupati, na kazi hii itafanyika usiku huu. Tutaondoka pamoja hadi kwenye duka
lako tutaingia ndani na kuua uchawi ambao ungeweza kupoteza mali yako yote iliyo
humo ndani.”
Nilikubaliana na mganga usiku nimfuate na gari,
nilimueleza mwenzangu na kurudi kwenye hoteli yetu. Majira ya saa tano usiku
tulimfuata na kwenda moja kwa moja kwenye duka, alifanya zindiko lake kisha
tulifungua duka, alifanya dawa zake kisha tulimrudisha na sisi kurudi hotelini
kulala mpaka siku ya pili.
Tangu siku ile niliendelea na biashara
zangu kama kawaida huku sehemu kubwa ya mambo yangu nikiwashirikisha marafiki
zangu na upande wa mpenzi wangu ambao waliahidi kunisimamia katika mambo yangu
yote.
Nilishukuru Mungu biashara zangu zilikwenda vizuri tofauti na
ndugu zangu ambao walianguka anguko la aibu. Sikuwaonea huruma kwa vile hawakuwa
watu wema kwangu. Pamoja na ubaya wao wote taarifa za kufilisika kwa haraka
sikuzifurahia.
Dada mkubwa alianza kuchanganyikiwa na kutembea
akizungumza peke yake, watu wa karibu waliniomba niinusuru aibu ya familia.
Katika mtu aliyeniuma alikuwa mama yangu mzazi ambaye siku zote aliona aibu kwa
niliyotendewa na baba na ndugu zangu na yeye kukaa kimya.
Nilijiuliza
nikimfuata nyumbani na kuwakuta na ndugu zangu ambao walinigeuza mchawi
itakuwaje? Taarifa za kusikitisha zilisema sehemu kubwa za maduka zimefilisika
na wafanyakazi wengine wamekimbia na pesa baada ya malimbikizo ya
mshahara.
****
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya kushindwa kulipa mikopo
mikubwa ya benki kufikia hatua ya kufilisiwa vitu vyao kwa kupigwa mnada
zikiwemo nyumba na magari. Ilibidi ndugu zangu warudi kuishi nyumba ya wazazi
ambayo siku zote haikufanyiwa ukarabati. Kila aliyenielezea anguko la familia
yangu huku wakiishi maisha ya kubahatisha aliniomba niinusuru kutokana na maisha
yangu kuwa na uafadhali mkubwa.
Taarifa za utajiri wa ndagu zilisambaa
kila kona kama moto kwenye majani makavu ambao uliipaka matope mazito familia
yetu. Kilichowashangaza watu wengi ni anguko la familia yangu lakini upande
wangu mambo yaliendelea kuninyookea.
Niliamua kumchukua mama yangu na
kukaa naye, kila tulipokuwa wawili mama alitumia muda mwingi kuniomba msamaha
kutokana na yote waliyonitendea. Nilimueleza mama sitaweza kumlaumu ila
sitawasamehe ndugu zangu.
“Mwanangu Masalu nakuomba nipo chini ya
miguu yako wasamehe ndugu zako, hali yao ni mbaya sana.”
“Mama siwezi
kuwasamehe mpaka nakufa.”
“Nakuomba nipo chini ya miguu yako
tunaadhirika.”
“Mama kama ningekufa angewasamehe nani?”
“Ni
kweli walikuwa na dhamira mbaya kwako lakini ilikuwa ni shinikizo la baba
yako.”
Pamoja na mama kunibembeleza sikuwa tayari kuwasamehe ndugu
zangu, muda ulikatika huku nikiendelea na maisha yangu huku nikiishi nyumba moja
na mpenzi wangu Mary, baada ya mama kuwepo pale nilipanga mipango ya ndoa kwa
kuamini msimamizi yupo.
Siku moja nikiwa mjini nilishtuka kumuona dada
yangu akiwa nusu uchi huku akiomba kwa watu, muonekano wake alionekana mtu
aliyerukwa na akili. Nilipatwa na mshtuko wa ajabu na moyo kuniuma, nilibakia
nikimtazama kwa muda huku machozi yakinitoka.
Kwa vile nilikuwa ndani
ya gari nililipaki gari pembeni na kujikuta nikilia kwa uchungu huku nikisikia
sauti ya mama kuwa niwasamehe ndugu zangu. Taratibu donge la kisasi liliyeyuka
moyoni mwangu na kuamua kusikiliza kilio cha mama yangu juu ya ndugu zangu.
Lakini sikuwa na jibu la moja kwa moja, niligeuza gari na kwenda kwa mganga
Pasiansi kuulizia kama nitaweza kuwasaidia ndugu zangu.
Nilipofika kwa
mganga nilikuta watu wengi kama kawaida, aliponiona pamoja na kuwa na watu wengi
kwa vile alinizoea alinipa upendeleo. Nilipofika aliniuliza:
“Vipi una
shida gani?”CHANZO:
https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilimweleza ombi la
mama kuwasamehe ndugu zangu na hali ya dada yangu, baada ya kunisikiliza kwa
kina mganga alisema:
“Nimekuelewa, hakuna tatizo lolote kama wewe
utakubali kuwasamehe ndugu zako.”
“Na kuhusu dada
yangu?”
“Alichotaka kukufanyia ndicho kilichomrudia lakini kama
umemsamehe kazi ya kumtibu si ngumu.”
“Nimemsamehe kwa vile kisu
kimegusa mfupa.”
“Basi mleteni hapa apate tiba.”
Baada ya
makubaliano na mganga nilirudi nyumbani na kumueleza mama kuwa nipo tayari
kuwasamehe ndugu zangu na kumtibu dada, mama alifurahi sana. Niliwatuma watu
wamkamate dada ambaye nilimpeleka kwa mganga, kutokana na tatizo lake alikaa
wiki moja na kurudi katika hali ya kawaida. Baada ya kupona mama alimueleza kuwa
mimi ndiye niliyemsaidia baada ya kuugua wendawazimu.
Nilimueleza mama
akimtoa kwa mganga amrudishe nyumbani kwangu, jioni niliporudi nyumbani
nilimkuta na mama wamekaa sebuleni wakitazama runinga. Aliponiona naingia
alinikimbilia na kunipigia magoti kuniomba msamaha.
Nilimuwahi
kumnyanyua na kumweleza yaliyopita yamepita ni wakati mwingine wa kujipanga upya
na kujenga familia iliyo imara. Maneno yangu yalimliza dada yangu na kujikuta
akisema:
“Sasa tungekuuwa tungepata faida gani, nani angetusaidia kama
hivi?”
“Dada yamekwisha naomba ya zamani tuyasahau.”
”Ni
kweli kaka lakini ulichonifanyia Mungu pekee
atakulipa.”
“Amina.”
Baada ya kumrudisha dada nilifanya
utaratibu wa kuwakusanya ndugu zangu, baada kuwakusanya. Tulikaa kikao cha
kifamilia kuondoa tofauti zetu huku ndugu zangu wakitokwa na machozi kwa yote
waliyoyafanya. Nilimshukuru Mungu kuturudisha katika mapenzi ya awali nami
niliwaheshimu kama ndugu zangu japo hawakuwa na kitu. Nilijitahidi kuhakikisha
kila ndugu yangu anakuwa na maisha mazuri baada ya Mungu kuniangazia
mafanikio.
Leo hii ninavyomalizia kutoa ushuhuda huu, kila ndugu yangu
ana duka lake japo si kubwa kama enzi za baba la kutumia ndagu ya kidonda.
Lakini maisha yaliendelea huku tukimalizia siku zote za maisha kurudi kwa Mungu
ili atuongoze na kutuepusha na maisha machafu.
Maisha sasa hivi ni
mazuri huku Mary akiwa mke wangu wa ndoa, japo inauma baada ya mama yangu
kufariki miezi minne baada ya ndoa yangu. Nitaendelea kumuombea mama yangu
kipenzi Mungu ampe mapumziko ya milele. Pia baba yangu japo alikuwa chanzo cha
matatizo kwenye familia.
Naamini Mungu ni mwenye huruma hivyo
atamsamehe kwa kujua udhaifu wa sisi wanadamu. Namalizia kwa kuwaomba wote
tumtangulize Mungu kwa kila kitu ili tusiishi maisha ya mashaka kwa kuwategemea
miungu watu. Mungu anatupenda tumtegemee yeye siku
zote.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment