Search This Blog

A BOOK OF SATAN ( KITABU CHA SHETANI ) - 1

 





    IMEANDIKWA NA : AZIZ HASHIM



    *********************************************************************************



    Simulizi : A Book Of Satan ( Kitabu Cha Shetani )

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Manyunyu ya mvua yalikuwa yakiendelea kudondoka taratibu kuashiria kumalizika kwa mvua kubwa iliyonyesha mfululizo usiku kucha. Tofauti na siku zote, watu walikuwa wachache sana barabarani japokuwa tayari kulishapambazuka. Ubaridi ulioambatana na mvua hiyo, ulimfanya kila mmoja kutamani kuendelea kuvuta shuka na kuuchapa usingizi.

    “Hee! Tayari ni saa moja? Mungu wangu, nitachelewa kazini,” Edmund Katera ‘Mundi’, kijana mdogo aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni kubwa ya mawasiliano ya Hashcom Mobile kwenye kitengo cha Teknolojia ya Mawasiliano (Information Technology) alikurupuka kutoka usingizini na kukimbilia kwenye kabati lake la nguo kwa lengo la kuchukua taulo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Harakaharaka akatoka mpaka nje na kuchukua ndoo ya maji ya kuoga huku mswaki ukiwa mdomoni, akatembea kwa hatua za haraka mpaka bafuni ambapo alijimwagia maji bila kujali ubaridi uliokuwepo asubuhi hiyo kutokana na mvua iliyokuwa inaishia.

    Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amerejea chumbani kwake, akavaa na baada ya dakika chache, alikuwa ameshajiandaa, akajitazama kwenye kioo kikubwa cha ‘dressing table’ iliyokuwa ndani ya chumba chake na baada ya kuridhishwa na mwonekano wake, alitoka na kufunga mlango wa nyumba aliyokuwa anaishi, akatoka na kuianza safari ya kuelekea kazini.

    Kwa jinsi barabarani kulivyokuwa na matope na foleni kubwa ya magari barabarani kutokana na mvua hiyo kama ilivyo desturi ya Jiji la Dar es Salaam hasa nyakati za mvua, ukizingatia kwamba tayari alikuwa nyuma ya muda kutokana na kuchelewa kuamka, hakuwa na ujanja zaidi ya kukodi bodaboda.

    “Naenda Bamaga, Mwenge.”

    “Buku nne tu mwanangu.”

    “Aaah! Buku nne mi sina, nitakupa buku mbili jero.”

    “Unaua mwanangu, ok poa twenzetu,” dereva wa bodaboda alimwambia Edmund ambaye bila kupoteza muda, alikwea kwenye bodaboda na safari ikaanza. Dereva huyo wa bodaboda akawa anapenya kwenye foleni, wakati mwingine akilazimika kupita katikati ya magari yaliyokuwa yamefungana kwa lengo la kumuwahisha mteja wake sehemu aliyokuwa anaenda.

    Hata hivyo, haraka hizo zilienda kuishia eneo la Sinza Afrika Sana ambapo magari kutoka kila upande, yalikuwa yamefungana eneo hilo lililokuwa na makutano ya barabara nne, moja inayotokea Shekilango, nyingine inayotokea kwenye taa za kuongozea magari za Bamaga, inayotokea kituo cha polisi cha Mabatini na ile iliyokuwa inatokea Mwenge kwa kupitia ofisi za TRA.

    Kwa jinsi magari hayo yalivyokuwa yamefungana, haikuwa rahisi hata kwa mwenda kwa miguu kukatisha katikati ya magari hayo, manyunyu ambayo yalikuwa yamepungua yakaanza kuongezeka na kusababisha kero kubwa kwa wasafiri waliokuwa wakitumia bodaboda, akiwemo Edmund ambaye tayari shati lake nadhifu alilokuwa amelivaa lilianza kulowa.

    “Pipiiii! Pipiiii... Poooopooo!” milio ya honi nyingi za magari iliendelea kusikika eneo hilo, kila dereva akijiona yeye yupo sahihi isipokuwa wengine ndiyo wanavunja sheria za barabarani, hali iliyosababisha taharuki kubwa eneo hilo.

    Ilibidi Edmund aanze kumshinikiza dereva wake afanye kila linalowezekana kuhakikisha wanajinasua eneo hilo kwani ukiachilia mbali ukweli kwamba alikuwa anaendelea kuloa, alikuwa pia anaendelea kuchelewa kazini.

    Wakati dereva wa bodaboda akihangaika kuitoa pikipiki pale ilipokuwa imezingirwa na magari, kwa bahati mbaya alijikuta akilikwangua gari lililokuwa nyuma yao na kulibonyeza eneo kubwa na kukwangua rangi.

    “Mungu wangu, tumeharibu gari la watu,” alisema dereva wa bodaboda huku akiendelea kuhangaika kutafuta upenyo wa kukimbia kabla mwenye gari hajashuka lakini alikuwa amechelewa kwani mwenye gari alishashtukia kwamba amegongwa na bodaboda.

    Msichana mdogo mwenye umri wa kati ya miaka ishirini na mbili hadi ishirini na tano, mrefu wastani, mwenye umbo lenye mvuto wa aina yake, akiwa amevalia mavazi ya kisasa kama mtu anayefanya kazi kwenye ofisi moja kubwa mjini, chini akiwa amevaa suruali nyeusi ya kitambaa iliyomshika kisawasawa maungo yake makubwa na shati jeupe nadhifu, usoni akiwa amevaa miwani ya kisasa ya rangi nyeusi, aliteremka kwenye gari la kifahari, Jeep Grand Cherokee la rangi ya fedha na kuzunguka upande ule bodaboda iliyokuwa imembeba Edmund ilipokuwa.

    “You stupid poor boys, do you know how much it cost to buy this type of car?” (Nyie wavulana maskini wapumbavu, mnajua inagharimu kiasi gani kununua gari kama hili?) alisema msichana huyo kwa jazba huku akivua miwani yake aliyokuwa amevaa, akainama kuangalia pale dereva wa bodaboda alipoligonga gari lake wakati akirudi nyuma.

    Kwa kuwa Edmund na dereva wake ndiyo waliokuwa na makosa na ni kweli kwamba waliharibu gari hilo ambalo hata wangeambiwa walipe gharama za kutengeneza sehemu waliyoigonga hawakuwa na fedha, ilibidi waufyate mkia. Wakawa wanatazamana huku kila mmoja akijisikia aibu kubwa kutokana na jinsi msichana huyo alivyokuwa akiendelea kuwachambua, akichanganya lugha, Kiingereza cha Kimarekani na Kiswahili.

    “Please forgive us ladyboss, its just an accident,” (Tafadhali tusamehe bosi, ni ajali tu) alisema Edmund, kauli iliyomfanya yule msichana amgeukie na kumtazama kwa jicho la ukali.

    “Ajali? Unazijua ajali wewe? Mtazame kwanza, nikikwambia ulipe gharama za uharibifu alioufanya huyo maskini mwenzio utaweza? Go to hell! (Nenda kuzimu!)” alisema msichana huyo kwa hasira, kauli iliyomfedhehesha mno Edmund.

    Tayari madereva wa magari mengine walikuwa tayari wameteremka kwenye magari yao na kuanza kumsihi msichana huyo awasamehe Edmund na dereva wake. Kwa nyodo na dharau akageuka na kuanza kutembea kuelekea kwenye gari lake huku akiivaa miwani yake. Akaingia kwenye gari na kukaa nyuma ya usukani.

    Edmund aliyekuwa ameshuka kwenye bodaboda, aliendelea kulitazama gari lile, hasa pale bodaboda yao ilipopagonga. Akiwa anaendelea kushangaa, aliona kitu chini kwenye lami chini ya gari, bila kuonekana na mtu yeyote akainama na kukiokota.

    Ilikuwa ni simu ya kisasa iliyokuwa imedondoka chini, bila hata kuuliza akajua kwa vyovyote lazima yule msichana aliiangusha alipoinama kuangalia gari lake. Tayari askari wa usalama barabarani walikuwa wameshafika eneo hilo kusaidia kufungua njia ambayo ilikuwa imefungwa na magari yaliyofungamana kila upande.

    Wakati Edmund akiwa bado anajishauri kama amrudishie msichana yule simu yake au la, tayari barabara ilishafunguliwa na magari yakaanza kuondoka kwa kasi. Akashuhudia yule msichana naye akibadili gia kwenye gari lake la kifahari na kuondoka kwa mbwembwe za hali ya juu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Oyaa twende mwanangu!” dereva wa bodaboda alimuita Edmund kwa sauti ya juu ambayo ilimzindua kutoka kwenye hali aliyokuwa nayo, akaiweka simu hiyo mfukoni na kusogea hadi pale dereva wa bodaboda alipokuwa anamsubiri, akapanda na kuendelea na safari.

    Kwa kuwa eneo hilo halikuwa mbali na ofisini kwao, dakika chache baadaye tayari walishawasili Bamaga, akashuka kwenye bodaboda na kumlipa dereva fedha zake kisha akaanza kutembea harakaharaka kuelekea kazini kwao huku akiwa anaendelea kutafakari juu ya tukio hilo lililotokea muda mfupi uliopita na jinsi alivyotolewa nishai na msichana yule mrembo.



    Kila alipokuwa akikumbuka jinsi msichana huyo alivyowatolea maneno ya shombo, Edmund au Mundi kama wengi walivyozoea kumuita, alijikuta akipandwa na hasira kali ya maisha.

    Aliamini umaskini wake ndiyo uliosababisha msichana huyo amtusi kwani kama angekuwa tajiri, na yeye angekuwa akiendesha gari lake, tena la kifahari kuliko la msichana huyo na kamwe asingekumbana na dharau kama hizo.

    Edmund alishusha pumzi ndefu na kuwasha kompyuta yake aliyokuwa anaitumia kazini, akatoa kitambaa na kuanza kujikausha maji ya mvua iliyomnyeshea huku kichwa chake kikiwa bado hakijatulia.

    Dakika chache baadaye, aliinuka sehemu anayokaa siku zote kazini na kwenda kutengeneza kahawa kwani baridi aliyokuwa anaisikia asubuhi hiyo, ukichanganya na kipupwe (AC) ya ofisini humo, alijiona kama mwili wake unaganda.

    Akarudi kwenye kiti chake akiwa na kikombe cha kahawa, akakaa na kuanza kuchangamsha tumbo huku bado akionesha kutotulia kiakili.

    “Mundi vipi mwanangu? Mbona leo hata salamu hakuna? Yaani umefika kimyakimya na kula bati kama hujatuona wanao,” Clarence, mfanyakazi mwenzake na Edmund, waliyekuwa wakifanya kazi kwenye kitengo kimoja cha Teknolojia ya Mawasiliano (IT) kwenye Kampuni ya Hashcom Mobile, alimuuliza Edmund baada ya kumuona hayuko kwenye hali yake ya kawaida.

    Swali hilo lilimzindua Edmund kutoka kwenye lindi la mawazo, ikabidi aanze kuvunga na kusingizia kwamba mvua iliyomnyeshea asubuhi hiyo wakati akienda kazini ndiyo iliyosababisha akili zake zihame. Wakaendelea kuzungumza mawili matatu kisha Edmund akatulia tena. Ni hapo ndipo alipokumbuka kwamba mfukoni alikuwa na kitu cha thamani.

    Akaingiza mkono na kutoa simu kubwa ya kisasa iliyokuwa mfukoni, kwa mara nyingine akaitazama na kujikuta akishusha pumzi ndefu. Ilikuwa simu ya thamani kubwa mno ambapo kwa makadirio yake ya harakaharaka, aliamini dukani lazima itakuwa inauzwa zaidi ya shilingi milioni mbili.

    “Duh! Mundi umenunua iPhone 6? Umepata wapi hela mwanangu? Hizo simu za washua, wewe maskini mwenzangu umeipata wapi?” Clarence alimuuliza Edmund kwa masihara baada ya kumuona akiitazama simu hiyo.

    Wafanyakazi kadhaa waliokuwa wamekaa jirani naye, waliacha kila walichokuwa wanakifanya na kumsogelea, kila mmoja akitaka kuiona simu hiyo ambayo kwa kipindi hicho ndiyo ilikuwa ikiongoza kwenye soko la simu kwa kuwa na bei ya juu na ubora kuliko simu zote.

    “Hebu tuone? Hebu na mimi niione?” wafanyakazi kadhaa walikuwa wakigombea kuishangaa simu hiyo. Wakati wao wakigombea simu hiyo, akili ya Edmund ilikuwa mbali kabisa, akiendelea kumfikiria yule msichana na jinsi alivyomdhalilisha mbele za watu.

    Baada ya muda, Edmund aliichukua simu hiyo na kuanza kuikagua vizuri, akagundua kuwa ilikuwa imefungwa kwa namba maalum (security codes).

    Kwa kuwa alikuwa na uelewa mkubwa wa namna ya kuchezea simu na kompyuta, muda mfupi baadaye alifanikiwa kuifungua simu hiyo, juu kabisa akakutana na picha ya msichana yule aliyemtoa nishai, jambo lililomfanya awe na uhakika kwamba ni kweli ile simu ni yake na aliiangusha pale alipoikuwa anaangalia jinsi gari lake la kifahari lilivyogongwa na bodaboda.

    Katika hali ambayo hakuitegemea, Edmund alijikuta macho yake yakiganda juu ya picha ya yule msichana, akawa anamtazama huku akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona. Mwisho alishusha pumzi ndefu na kuendelea kuishangaa simu hiyo.

    Kitu kingine kilichozidi kumshangaza, licha ya kufanikiwa kuifungua simu hiyo sehemu ya kwanza, kila kitu ndani ya simu kilikuwa kimefungwa kwa namba maalum za usalama, kuanzia kwenye meseji, kwenye picha, kwenye majina na kila kitu.

    ***

    Gari la kifahari, Jeep Grand Cherokee (New Model), lilikuwa likipasua lami kwa mwendo wa kasi, wakati mwingine dereva akilazimika kuyapita magari mengine yaliyokuwa yanasuasua mbele yake kuelekea Mikocheni. Dakika kadhaa baadaye, tayari lilikuwa limewasili Mikocheni, dereva akapiga honi, walinzi wawili wenye bunduki wakafungua geti kisha likaingizwa mpaka sehemu ya maegesho, nje ya ghorofa refu la kisasa lililokuwa na mandhari ya kuvutia mno.

    “Mungu wangu, simu yangu nimeiweka wapi tena?”

    “Simu gani bosi? Mbona hapo umeshika simu mbili mkononi?”

    “Ile simu yangu ninayoitumia siku zote, siyo hizi,” alisema msichana mrembo wakati akiteremka kwenye gari, na kusababisha walinzi waache kila walichokuwa wanakifanya kwa ajili ya kumsaidia bosi wao huyo.

    Licha ya kusaidiana kupekua kwenye gari karibu kila sehemu, hawakufanikiwa kuiona simu hiyo, jambo lililosababisha msichana huyo aanze kutokwa na machozi.

    “Ina vitu vyangu vingi sana vya siri, siwezi kuruhusu ipotee, haiwezekani,” alisema msichana huyo akionesha kuchanganyikiwa mno.

    “Hebu jaribu kuipiga,” alishauri mlinzi mmoja, wazo ambalo msichana huyo aliona linafaa, kwa kutumia simu yake nyingine, aliipiga simu hiyo. Kwa bahati nzuri, bado ilikuwa hewani, ikawa inaita.

    “Inaita! Inaita,” alisema msichana huyo akionesha kuwa na shauku kubwa ya kusikia nani atapokea.

    ***CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Edmund aliendelea kufanya kazi zake lakini bado akili yake ilikuwa haitulii. Alitamani kufahamu vitu vingi zaidi kuhusu yule msichana mrembo aliyemtoa nishai asubuhi hiyo na njia pekee aliona ni kupitia simu ya msichana huyo.

    Akaamua kuanza kuishughulikia, kabla hajafungua sehemu nyingine, alikopi mafaili yote yaliyokuwa kwenye simu hiyo (back up) na kuhamishia kwenye kompyuta yake.

    Akiwa Anahangaika kuifungua kwa kutumia mbinu alizokuwa anazijua mwenyewe, simu hiyo ilianza kuita. Akashtuka na kuanza kila alichokuwa anakifanya, akawa anaitazama inavyoita huku akijishauri kama apokee au la. Mwisho aliamua kuipokea.

    “Haloo!”

    “Haloo, samahani sana kakaangu naomba msaada wako. Mimi ni mwenye hiyo simu nimeipoteza hata sijui niliiangushia wapi. Nakuomba unielekeze popote ulipo nakuja na nakuahidi kuwa nitakupa shilingi milioni moja ‘cash’ ukinisaidia kuipata simu yangu,” ilisikika sauti upande wa pili ambapo bila hata kuuliza Edmund alijua ni ya yule msichana aliyemtoa nishai asubuhi. Kwa kuwa lengo lake halikuwa kuichukua simu hiyo, aliamua kumuelekeza ofisini kwao, Hashcom Mobile, Bamaga-Mwenge jijini Dar es Salaam. Baada ya kukata simu, msichana yule aliingia kwenye gari lake na kuondoka kwa kasi kubwa, akiwaacha wale walinzi wakitazamana.

    Dakika chache baadaye, tayari alikuwa amewasili Bamaga, akafuata ramani aliyoelekezwa na kutokezea kwenye ofisi aliyokuwa akifanyia kazi Edmund. Akapaki gari lake na kwenda kujitambulisha kwa walinzi kisha akaruhusiwa kuingia ndani. Alipoingia tu getini, alitoa simu yake na kuipiga tena ile namba, ikawa inaita.

    “Edmund kuna mgeni wako mapokezi,” sauti ya mfanyakazi mwenzake ilisikika, alipotazama simu iliyokuwa inaita, Edmund akajua lazima ni yule msichana amewasili. Harakaharaka akainuka na kujiweka vizuri nguo zake ambazo bado hazikuwa zimekauka vizuri, akatoka kuelekea mapokezi.



    “Mambo!” Edmund alimsalimia yule msichana baada ya kumkuta mapokezi, akiwa amejiinamia akiiwaza simu yake. Salamu hiyo ilimfanya ainue uso wake, macho yake na ya Edmund yakagongana.

    Mshtuko alioupata ulionekana waziwazi kwani ni kama hakutegemea kwamba mtu aliyemuokotea simu yake ni Edmund, kijana ambaye muda mfupi uliopita alimuonesha dharau ya kupindukia.

    “Po..a,” alijibu msichana huyo kwa kubabaika, Edmund akamuonesha ishara kwamba amfuate kwani mapokezi palikuwa na wageni wengine wengi, wakaongozana mpaka kwenye chumba maalum cha mazungumzo, yule msichana akiwa bado haamini macho yake.

    “Wewe ndiye uliyeniokotea simu?” alisema msichana huyo kwa upole mno, tofauti kabisa na alivyokuwa mwanzo.

    “Yaah! Naitwa Edmund, bila shaka unanikumbuka,” alisema Edmund, kauli iliyozidi kumuweka yule msichana kwenye wakati mgumu.

    “Naomba unisamehe sana kakaangu kwa kilichotokea asubuhi. Nilitoka nyumbani nikiwa nimevurugwa ndiyo maana nikawa mkali sana kwenu. Tafadhali nakuomba unisamehe,” alisema yule msichana kwa upole huku mara kwa mara akikwepesha macho yake yasigongane na ya Edmund aliyekuwa ametulia anamtazama kwa makini.

    Edmund alishusha pumzi na kumwambia asiwe na wasiwasi ameshamsamehe ndiyo maana ameamua kumpa ushirikiano ili aipate simu yake.

    “Ooh! Ahsante sana kakaangu, yaani hata sijui namna ya kukushukuru, simu yangu ina vitu vingi sana vya muhimu, yaani umenikoa kweli,” alisema msichana huyo huku akimpa mkono Edmund, tabasamu hafifu likiwa limechanua kwenye uso wake.

    Kitendo cha kupeana mkono na msichana huyo, kilimfanya Edmund ahisi kama amepigwa na shoti ya umeme, akabaki amezubaa mpaka msichana huyo alipoamua kutoa mkono wake mwenyewe.

    “Una akaunti benki?”

    “Yaah ninayo, vipi kwani.”

    “Nataka nikuhamishie fedha zako kama nilivyokuahidi. Shilingi milioni moja ‘cash’ kwa msaada ulionipa.

    “Hapana, sihitaji malipo kutoka kwako dadaangu, nimekusaidia tu.”

    “Hapana Edmund, chukua tu kwa sababu mimi ndiyo niliyeahidi kukupa, nitajie namba yako ya akaunti tafadhali,” alisema msichana huyo lakini Edmund akaendelea kushikilia msimamo wake.

    Ni kweli Edmund alikuwa na shida ya fedha na kupewa shilingi milioni moja katika siku kama hiyo, tarehe za mshahara zikiwa mbali kabisa kungemsaidia sana lakini hakutaka kuonesha udhaifu, akashikilia msimamo wake.

    “Ngoja nikakuchukulie simu yako,” alisema Edmund na kuinuka, akawa anatoka kwenye chumba hicho cha mazungumzo na kumuacha yule msichana amekaa palepale alipokuwa amekaa awali.

    Alipofika mlangoni, aliufungua na kugeuka nyuma, akashangaa kumuona yule msichana akimtazama kwa macho ya wizi, macho yao yakagongana kisha harakaharaka yule msichana akakwepesha macho yake. Edmund akatoka, muda mfupi baadaye akarejea akiwa na simu hiyo.

    “Hii hapa,” alisema huku akimkabidhi, msichana huyo akaipokea huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.”

    “Siamini! Jamani ahsante we kaka,” alisema msichana huyo huku akinyoosha tena mkono wa shukrani kumpa Edmund, wakashikana tena. Hali kama iliyomtokea awali alipopeana mkono na msichana huyo ikajirudia tena, akabaki kujishangaa kwani haikuwa kawaida yake.

    “Basi chukua hii utakunywa hata soda naona zawadi yangu umeikataa,” alisema msichana huyo huku akiingiza mkono mwingine kwenye pochi yake ya kisasa, Edmund akataka kukataa tena lakini alikuwa amechelewa kwani msichana huyo alimuwekea noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi kwenye mfuko wa shati lake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mbona hujaniuliza jina langu? Au bado una hasira na mimi?” msichana huyo aliuliza huku tabasamu lake likizidi kuchanua na kuupamba uso wake, akazidi kuonekana mrembo. Edmund alishindwa cha kujibu zaidi ya kutabasamu, ni kweli tangu msichana huyo afike, hakuwa amemuuliza jina lake na huenda kama mwenyewe asingeanza, angeondoka bila kumuuliza.

    “Hii ni ‘business card’ yangu na hilo hapo ndiyo jina langu,” alisema huku akimkabidhi Edmund kadi ya kisasa ya mawasiliano. Akaipokea na kuitazama vizuri.

    “Samantha!”

    “Yes! That’s my name.” (Ndiyo! Hilo ndiyo jina langu) alisema msichana huyo kwa lafudhi laini, Edmund akazidi kujikuta katika wakati mgumu.

    “Nisikupotezee muda wako najua upo kazini, narudia tena kukuomba radhi kwa yote yaliyotokea asubuhi na nakushukuru sana kwa wema wako,” alisema msichana huyo huku akiinuka, akachukua kila kitu chake na kuagana na Edmund.

    “Ngoja nikutoe mpaka nje,” alisema Edmund huku naye akisimama, wakatoka kwenye chumba cha maongezi, wakaelekea mapokezi kisha Edmund akamsaidia kufungua mlango wa nje, wakatoka na kuelekea kwenye gari la kifahari alilokuja nalo msichana yule.

    “Hebu jaribu kuibipu simu yangu,” alisema msichana huyo na kumtajia Edmund namba, bila kuelewa lengo la msichana huyo, Edmund alifanya kama alivyoambiwa, simu ikaita.

    “Haya kazi njema kaka, nakushukuru sana,” alisema Samantha na kubonyeza rimoti aliyokuwa ameishika, gari likawaka taa za pembeni na kutoa mlio wa kuashiria kwamba milango imejifungua.

    Msichana huyo akatembea kwa maringo hadi kwenye gari, akaingia na kukaa nyuma ya usukani, akawasha gari na kutetemsha kioo, akawa anampungia mkono Edmund ambaye bado alikuwa amezubaa, akiwa ni kama haamini alichokuwa anakiona mbele ya macho yake.

    Akaondoka eneo hilo akiwa ndani ya gari lake la kifahari, Jeep Grand Cherokee (New Model) na kumuacha Edmund amesimama palepale.

    “Mundi vipi mshkaji wangu, mbona umepigwa na butwaa kiasi hicho? Naona ulikuwa na chombo cha ukweli kinoma,” Sam, mlinzi wa kampuni aliyokuwa akifanyia kazi Edmund alimtania baada ya kumuona bado amezubaa palepale nje, Edmund akatabasamu na kurudi ofisini kuendelea na kazi zake.

    “Ebwana eeh! Yule malaika uliyekuwa naye ni nani arifu? Nipigie pande na mimi nijiweke,” Clarence, rafiki yake Edmund alimtania baada ya kurejea, wote wakaishia kucheka tu. Edmund akakaa kwenye kompyuta yake na kushusha pumzi ndefu, akakumbuka kwamba msichana yule mrembo alimuwekea fedha kwenye mfuko wake wa shati.

    “Shilingi laki moja? Mungu wangu, huyu dada anafanya kazi gani kwani?” alisema Edmund baada ya kuhesabu fedha hizo. Akajikuta akishindwa kuzuia tabasamu lisiupambe uso wake. Muda mfupi baadaye, simu yake ilianza kuita, harakaharaka akapokea.

    “Nashukuru sana kakaangu nimefika ofisini, kama utapata muda baadaye naomba nije kukuchukua tukapate lanchi pamoja kama shukrani yangu kwako,” alisema Samantha.



    “Ok hakuna shida dada’angu,” alijibu Edmund kisha simu ikakatwa, tabasamu pana likachanua kwenye uso wake kwani licha ya ukweli kwamba msichana huyo alikuwa amemfanyia kitendo cha kumdhalilisha sana asubuhi ya siku hiyo, alijikuta akimsamehe kirahisi na kutamani kumjua zaidi, akaona hiyo ndiyo nafasi yake.

    “Ebwana mbona mudi yako imebadilika ghafla? Tabasamu pana muda wote utafikiri umeokota pochi ya Mzungu?” Walungasa, mfanyakazi mwingine waliyekuwa akifanya kazi na Edmund alimuuliza baada ya kumuona muda wote akiwa na tabasamu pana, akaishia kucheka tu bila kueleza chanzo cha furaha yake.

    Saa zilizidi kuyoyoma, hatimaye muda wa chakula cha mchana uliwadia, Edmund akawa anaitazama simu yake kwa shauku kubwa akisubiri Samantha ampigie kwani walikubaliana kwenda kula chakula cha mchana pamoja.

    Hata hivyo, muda mfupi baadaye, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yake, harakaharaka akaufungua na kuusoma.

    “Sorry! Nimeshindwa kuja kuna kazi zimenibana. Naomba nikupitie jioni baada ya muda wa kazi tukakae sehemu tubadilishane mawazo,” ulisomeka ujumbe huo kutoka kwa Samantha, Edmund akashusha pumzi ndefu na kumjibu kwamba asijali.

    Akaendelea kufanya kazi huku mawazo yake yakiendelea kumuwaza msichana huyo. Hatimaye muda wa kutoka kazini ukawadia, Edmund akiwa ameshakamilisha karibu kazi zote alizopaswa kuzifanya kwa siku hiyo. Akazima kompyuta yake na kuwaaga wenzake kisha taratibu akatoka mpaka mapokezi.

    Kabla hajatoka kwenye geti kubwa, alisikia simu yake ikiita, harakaharaka akaitoa mfukoni na kutazama namba ya mpigaji, hakuwa mwingine bali Samantha, akaipokea huku tabasamu likiwa limeupamba uso wake.

    “Umeshatoka kazini?”

    “Ndiyo najiandaa kutoka.”

    “Ok basi nisubiri hapohapo, nipo jirani nakuja,” alisema Samantha kisha akakata simu, Edmund akashusha pumzi ndefu na kurudi kwenye chumba cha mazungumzo, akawa anajitazama kwenye vioo vya chumba hicho na kujiweka vizuri.

    Baadaye alitoka mpaka nje lakini kabla hajakaa kwenye benchi lililopo nje ya ofisi yao, alisikia simu yake ikiita mfululizo, alipotoa aligundua kuwa ni Samantha.

    “Napaki gari hapa nje ya ofisi yenu, uko wapi?” alisema msichana huyo, harakaharaka Edmund akasimama na kuanza kuangalia gari lililokuwa linapaki, akaliona Jeep Grand Cherokee (New Model) la msichana huyo likiingia eneo la maegesho, akatembea kulifuata huku akipunga mkono.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mambo!” Samantha alisema kwa sauti nyororo huku akishusha kioo cha gari lake.

    “Poa! Vipi za kazi,” Edmund alijikakamua na kuuvaa uchangamfu wa kulazimisha. Alishindwa kujielewa kwa nini kila alipokuwa akimuona msichana huyo alikuwa akiishiwa nguvu kabisa.

    “Nzuri! Zunguka upande wa pili uingie kwenye gari,” alisema msichana huyo, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake. Edmund akazunguka mpaka upande wa pili na kufungua mlango, akapokelewa na harufu ya manukato mazuri yaliyokuwa yamepuliziwa ndani ya gari hilo.

    Akaingia na kukaa pembeni ya Samantha, kipupwe kilichokuwa kinapuliza ndani ya gari hilo, ukichanganya na muziki laini uliokuwa unapiga kwa sauti ya chini, vilimfanya Edmund ajihisi kama yupo kwenye ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa.

    “Vipi za tangu asubuhi,” alisema Samantha huku akimtazama Edmund, tabasamu likiwa limeujaza uso wake.

    “Poa kabisa, sijui wewe.”

    “Niko poa kabisa, sasa naomba twende Kunduchi, kule kuna hoteli nzuri huwa naipenda sana,” alisema msichana huyo, Edmund akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye, akawasha gari na kuingiza gia, akalitoa eneo la maegesho na kuingia barabarani, akaongeza kidogo sauti ya muziki na kuelekea kwenye barabara ya lami.

    “Ooh! Samahani naomba ufunge mkanda,” alisema Samantha baada ya kugundua kuwa kumbe Edmund hakuwa amefunga mkanda. Kijana huyo akiwa anahangaika kufunga mkanda, Samantha alisimamisha gari na kumsaidia, hali iliyowafanya wawili hao wasogeleane miili yao. Mapigo ya moyo wa Edmund yakaongezeka kasi ghafla.

    Baada ya kumaliza kumsaidia kufunga mkanda, safari iliendelea huku Samantha akimuonesha Edmund uchangamfu ambao hakuutegemea. Dakika kadhaa baadaye, tayari walikuwa wamewasili Kunduchi, msichana huyo akaenda kupaki gari sehemu ya maegesho kisha wakateremka na kutafuta sehemu nzuri ya kukaa.

    “Nimefurahi sana kufahamiana na wewe japokuwa tumekutana kwenye mazingira ya ajabu,” Samantha alivunja ukimya baada ya kuwa ameshamuagiza vinywaji, Edmund akatabasamu bila kusema neno lolote.

    “Naomba uniambie kama umenisamehe.”

    “Nimekusamehe wala usiwe na wasiwasi Samantha,” alisema Edmund huku akijitahidi kupambana na hofu ndani ya moyo wake. Kila kitu kilikuwa kigeni kwake, japokuwa alikuwa akiishi Dar es Salaam hakuwahi kuingia kwenye hoteli hiyo hata mara moja, akawa anaona kila kitu kilichokuwa kinatokea kama muujiza kwake.

    “Kwani we unaishi wapi?” Samantha alimuuliza Edmund ambaye alimuelekeza mpaka mtaa anaoishi.

    “Unaishi na nani?”

    “Peke yangu.”

    “Kwa nini unaishi peke yako? Kwani huna mke?” Samantha alimuuliza Edmund kimasihara huku akivuta juisi taratibu kwa kutumia mrija, akacheka sana na kumjibu kwamba hakuwa ameoa bado.

    “Ila una mchumba?”

    “Hapana, bado sijabahatika, najipanga kimaisha kwanza,” alisema Edmund na kuanza kumuuliza msichana huyo kuhusu maisha yake.

    “Mimi naishi na wazazi wangu Upanga, nafanya kazi ya kusimamia kampuni kadhaa za baba kwani mimi ni mtoto wake wa pekee,” alisema Samantha huku akiendelea kunywa juisi taratibu.

    Wakaendelea kuzungumza mambo mbalimbali ambapo msichana huyo alimueleza Edmund vitu vingi kuhusu maisha yake. Ungeweza kudhani wawili hao wamefahamiana siku nyingi zilizopita kutokana na jinsi walivyokuwa wakipiga stori.

    Baadaye, walikula chakula cha usiku pamoja kisha wakaondoka hotelini hapo baada ya kuwa msichana huyo amelipia gharama zote.

    “Nataka niende kupaona nyumbani kwako,” alisema Samantha huku safari ikiendelea, Edmund akamgeukia na kumtazama, macho yao yakagongana.

    “Hakuna tatizo Samantha,” alijibu Edmund, wote wakatabasamu. Safari iliendelea na baadaye Edmund akaanza kumuelekeza msichana huyo mtaa waliokuwa wanaishi. Edmund alitegemea kwamba baada ya kufika na kuiona nyumba anayoishi, msichana huyo ataaga na kuondoka kutokana na ukweli kwamba nyumba aliyokuwa anaishi ilikuwa na hadhi ya chini ukilinganisha na maisha ya msichana huyo.

    Cha ajabu, walipofika, Samantha naye alitaka kushuka ili akakione chumba alichokuwa anaishi Edmund, kijasho chembamba kikaanza kumtoka kijana huyo akihofia msichana huyo atamdharau baada ya kuona maisha aliyokuwa anaishi.

    Samantha hakujali kitu, wakaingia kwenye nyumba aliyokuwa amepanga kijana huyo na hatimaye wakaingia mpaka ndani, ikiwa tayari imeshatimia saa tatu za usiku.



    “Ka..karibu sa..na,” Edmund alimkaribisha Samantha kwa kubabaika, msichana huyo akaachia tabasamu pana kwani alishagundua hofu iliyokuwa ndani ya moyo wa Edmund.

    “Unaishi na nani?” Samantha alirudia kuuliza swali ambalo tayari alishajibiwa huku akiwa anazunguka huku na kule ndani ya chumba hicho.

    “Naishi mwenyewe,” alijibu Edmund huku akiendelea kujisikia aibu kubwa ndani ya moyo wake. Kwa hadhi aliyokuwa nayo Samantha, alijikuta akishindwa kabisa kujiamini kwani maisha yake yalikuwa ya kawaida sana ukilinganisha na ya Samantha, japo bado hakuwa amefika nyumbani kwao lakini mwonekano wake tu ulitosha kutoa picha kamili.

    “Huku ndiyo chumbani kwako?” Samantha aliuliza huku akisukuma mlango wa kuingilia chumbani, kabla hata Edmund hajajibu kitu, tayari msichana huyo alikuwa ameshafungua mlango.

    “Unawashia wapi taa,” aliuliza kwa sauti ya chini, Edmund akamfuata kwa nyuma na kuwasha taa ukutani huku akiendelea kujisikia aibu kwani asubuhi ya siku hiyo alikurupuka kuwahi kazini na hakukumbuka hata kutandika kitanda wala kupanga vitu vyake vizuri.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ahahaaa!” Samantha alicheka sana baada ya kuona chumba cha Edmund kilivyokuwa kimekosa mpangilio mzuri.

    “Inabidi uoe mke atakayekuwa anakusaidia hata kutandika kitanda na kupanga nguo vizuri kabatini,” alisema msichana huyo huku akikaa kwenye kitanda cha Edmund, macho yake yakawa yanaendelea kuangaza huku na kule, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

    Edmund naye alianza kuhangaika kupangapanga vitu vizuri, akaanza kwa kuokota nguo zilizokuwa zimezagaa sakafuni na kuziweka kwenye kapu la nguo chafu kisha akatoa shuka safi kabatini na kuanza kutandika, ikabidi Samantha amsaidie kwani alimuona alivyokuwa anahangaika.

    “Mh! Mbona humu ndani kwako kuna joto sana? Huna feni?” aliuliza Samantha wakati akimalizia kutandika kitanda, Edmund akaanza kubabaika tena kwani ukweli ni kwamba feni yake ilikuwa imeharibika na aliipeleka kwa fundi siku mbili zilizopita lakini akakosa muda wa kwenda kuichukua.

    “Sasa nitakaaje? Mwenzio nasikia joto sana?” alisema Samantha huku akianza kufungua vifungo vya shati jeupe alilokuwa amevaa, akabaki na sidiria nyeupe na kufanya kifua chake kilichojaa vizuri kianze kuonekana na kusababisha Edmund azidi kukosa uvumilivu.

    Japokuwa hakuwa akiishi na mwanamke na hakuwa na mpenzi kwa kipindi kirefu baada ya kuumizwa na aliyekuwa mpenzi wake wa kwanza, takribani miezi kumi iliyopita, Edmund alikuwa mwanaume aliyekamilika kila idara.

    Ukichanganya na ukweli kwamba alikuwa akivutiwa sana na msichana huyo licha ya alichomfanyia asubuhi ya siku hiyo, Edmund alijikuta akizidi kuwa kwenye wakati mgumu mno kihisia.

    “Basi ngoja nifungue dirisha,” alisema Edmund huku akijitahidi kuyakwepesha macho yake yasitue kwenye mwili wa Samantha ambaye alikuwa akijigeuzageuza kimitego pale kitandani huku akiendelea kulalamika kwamba anasikia joto kali.

    “Hapana! Usifungue nitavumilia tu, ila naomba kama hutajali nivue shati labda nitajisikia vizuri,” alisema msichana huyo, Edmund akakosa cha kujibu. Msichana huyo akasimama na kumuomba Edmund amsaidie kumfungua vifungo vya shati vilivyobakia, akatii bila shuruti.

    Wakati akiendelea kumfungua vifungo vya shati, Samantha alikuwa akimtazama Edmund kwa macho yaliyobeba ujumbe mzito, akamsaidia kulivua na kulitundika ukutani.

    “Edmund! Naomba sogea nikwambie kitu,” alisema msichana huyo kwa sauti iliyokuwa inatokea puani, Edmund akatii alichoambiwa ambapo katika hali ambayo hakuitegemea, msichana huyo mrembo kupindukia alimkumbatia kwa nguvu kifuani huku akipumua kwa fujo mithili ya mtu aliyetoka kukimbia mbio za marathon, ngozi yake laini iliyokuwa na joto la huba vikazidi kumchanganya Edmund.

    “Nakupenda sana Edmund, hata sijielewi mwenzio, nimejikuta nakupenda tu ghafla wakati siyo kawaida yangu,” alisema Samantha kwa sauti ya kudeka, akaanza kumwagia mvua ya mabusu sehemu mbalimbali za mwili wake.

    Ni kama Edmund alikuwa akiusubiri kwa hamu muda huo kwani hakutaka kulaza damu, naye akawa anamuonesha ushirikiano mkubwa msichana huyo, wakagandana kama ruba huku mapigo ya moyo ya kila mmoja yakizidi kuongezeka kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele, miguno ya raha ikawa inasikika kutoka kwa kila mmoja.

    Waliendelea kupasha miili yao tayari kwa mechi ya kirafiki isiyo na refa wala jezi, huku mara kwa mara msichana huyo akirudia kumuomba radhi Edmund kwa kilichotokea asubuhi ya siku hiyo kwa sauti yenye uwezo wa kumtoa nyoka pangoni, kufumba na kufumbua wakajikuta wote wakiwa kama walivyoletwa duniani.

    “Unazijua love bites?” Samantha alimuuliza Edmund kwa sauti ya chini mno huku akiendelea kumfanyia vituko vya hapa na pale, akawa anatingisha kichwa kuonesha kukubali kwani japokuwa hakuwa mzoefu sana kwenye ulimwengu wa mapenzi, Edmund alikuwa akijua baadhi ya vitu.

    “Naomba unitoe hapa,” alisema Samantha huku akimuoneshea Edmund shingo yake, kijana wa watu akatii, naye akamng’ang’ania Edmund shingoni, kazi hiyo ikaanza.

    Hata hivyo, tofauti na Edmund alivyokuwa anafahamu, Samantha alikuwa akilifanya zoezi hilo kwa nguvu kiasi cha kumfanya Edmund aanze kuhisi maumivu makali kwenye shingo yake lakini akawa anajikaza kwani alikuwa na uhakika kuwa muda mfupi baadaye wataingia ‘msambweni’ , jambo alilokuwa analisubiri kwa hamu kwani mpaka muda huo hakuwa akijielewa tena.

    Kufumbana kufumbua, Samantha alikurupuka kama mtu aliyezinduka usingizini, akajitoa kwenye kifua cha Edmund, kwa kasi ya ajabu akasimama huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida. Akaanza kutafuta nguo zake ambazo kila moja ilikuwa imeangukia upande wake.

    “Vipi tena?” Edmund aliuliza kwa mshangao lakini Samantha hakumjibu kitu, akaendelea kuvaa nguo zake na muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amemaliza, akawa anataka kuondoka.

    Kwa kuwa tayari Edmund alikuwa kwenye hali mbaya, hakutaka kukubali kirahisi Samantha aondoke na kumuacha kwenye hali ile kwani kile alichokuwa anakisubiri kwa hamu hakikuwa kimekamilika.

    Akajaribu kumzuia huku akitaka kujua ni jambo gani limetokea mpaka Samantha abadilike ghafla kiasi kile lakini tayari alikuwa amechelewa, Samantha alitoka mbiombio mpaka nje alikopaki gari lake la kifahari. Wakati Edmund akihangaika kutafuta nguo zake ili amuwahi kabla hajaondoka, alisikia muungurumo wa gari la kifahari la msichana huyo likiondoka kwa kasi eneo hilo, akabaki amepigwa na butwaa, akiwa haelewi kabisa kilichotokea.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni hapo ndipo alipoanza kuhisi maumivu makali kwenye shingo yake, alipopeleka mkono wake pale alipotolewa ‘love bite’ na Samantha, hakuyaamini macho yake baada ya kugundua kuwa palikuwa na kidonda huku damu zikianza kumchuruzika kwa wingi.

    “Mungu wangu, hiki nini tena?” alisema Edmund huku akisogea kwenye kioo kikubwa kujiangalia.



    Alipojiangalia shingoni, mahali alipotolewa ‘love bite’ na Samantha, alishtuka kugundua kuwa kumbe msichana huyo alikuwa amemng’ata na kumtoa kidonda kikubwa kilichokuwa kikiendelea kutoka damu kwa wingi.

    Harakaharaka alikimbilia kwenye kabati na kutoa kiboksi kidogo cha huduma ya kwanza, akatoa pamba na ‘spirit’ na kurudi kwenye kioo, akawa anajisafisha huku akiwa ameuma meno kutokana na maumivu makali aliyokuwa anayasikia.

    Kidogo ‘spirit’ ilimsaidia kupunguza kuvuja kwa damu ingawa maumivu yaliendelea kuwa makali kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele. Akakata kipande kikubwa cha pamba na kukiweka juu ya kidonda hicho huku akiendelea kuugulia maumivu, akameza vidonge vya kupunguza maumivu huku akiendelea kujiuliza maswali yaliyokosa majibu.

    Aliporudi kitandani, aligundua kuwa shuka safi alilolitoa muda mfupi uliopita, lilikuwa limeingia madoa makubwa kutokana na damu iliyokuwa inamvuja, akapata kazi nyingine ya kuanza kubadilisha mashuka. Kila kilichokuwa kinaendelea, alikifananisha na ndoto ya kutisha, akawa anatamani ndoto hiyo ifike mwisho haraka lakini haikuwa hivyo.

    Muda mfupi baadaye, pamba aliyokuwa amejiweka juu ya jeraha lake, ilikuwa imelowa damu chapachapa, ikabidi aitoe na kukata nyingine, akaiweka huku bado akiwa haamini kilichokuwa kinatokea.

    “Kwani Samantha ni nani hasa? Kwa nini ameniumiza hivi na kukimbia? Kosa langu kwake ni lipi? Ina maana haya ndiyo malipo ya wema wangu kwake?” Edmund aliendelea kujiuliza huku akifuta damu iliyochafua vitu mbalimbali ndani ya chumba chake.

    Alitoka mpaka nje na kupatazama pale msichana huyo alipokuwa amepaki gari lake. Hakuwepo wala hapakuwa na dalili zozote za uwepo wake, akarudi ndani na kufunga mlango mkubwa wa nje, akachukua simu yake na kujaribu kumpigia Samantha, mara simu ikaanza kuita.

    “Haloo!” Haloo! Samantha! Samantha!” Edmund aliita baada ya simu kupokelewa lakini hakuitikiwa, akaendelea kuita lakini hakusikia majibu yoyote, akakata simu na kujaribu kupiga tena.

    “Namba ya simu unayopiga haipatikani kwa sasa, tafadhali jaribu tena baadaye,” sauti ilisikika kwenye simu yake ikimaanisha kwamba simu ya Samantha imezimwa. Akazidi kujikuta kwenye wakati mgumu.

    Alipotazama saa ya ukutani, aligundua kuwa tayari ilishatimia saa sita za usiku. Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, hakuwa na cha kufanya zaidi ya kwenda kulala, huku akiendelea kuugulia maumivu makali.

    ***

    “Mbona umechelewa kurudi? Ulikuwa wapi?”

    “Kuna sehemu nilikuwa nimepitia.”

    “Ndiyo uchelewe mpaka muda huu?”

    “Nilikuwa nafanya kazi ya muhimu baba.”

    “Kazi gani ya muhimu? Hivi siku hizi umekumbwa na nini wewe mtoto? Majukumu ninayokupa hutimizi kila siku visingizo.”

    “Baba! Hivi unafikiri hizo kazi zako unazonipa ni rahisi sana, si ndiyo? Kwanza kwa taarifa yako mimi nimechoka, sitaki kuendelea kuwa mtumwa?” Samantha alisema kwa sauti ya juu wakati akijibizana na baba yake.

    “Unasemaje? Hebu rudia tena?”

    “Jamani kwani kuna nini tena?” mama yake Samantha aliingilia ugomvi huo kati ya baba na mwanaye, Samantha alipomuona mama yake akamkimbilia na kumkumbatia huku akiendelea kulia.

    “Kwani kuna nini mwanangu?”

    “Eti baba ananifokea kisa nimechelewa kurudi wakati nilikuwa kufanya kazi aliyonipa mwenyewe, kwanza mama mimi nimechoka kuendelea kuwa mtumwa, sitaki,” alisema Samantha huku akijitoa kwenye mikono ya mama yake, akakimbilia ndani na kuwaacha wazazi wake wakitazamana.

    “Na wewe mume wangu, kwa nini unamfokea Samantha? Unafikiri huyo bado ni mtoto mdogo?”

    “Amekuwa jeuri sana siku hizi, kazi hafanyi kama ninavyomuelekeza kila siku visingizio kibao, na leo umemsikia mwenyewe anasema amechoka. Sasa unafikiri itakuwaje?”

    “Huenda ameongea kwa hasira tu mume wangu, tumuache atulie kwanza,” alisema mama yake Samantha, akamuita dereva wao na kumuamuru alipaki vizuri gari alilokuja nalo Samantha, harakaharaka dereva huyo akatii alichoambiwa, akaliingiza gari hilo kwenye maegesho kulikokuwa na magari mengine ya kifahari.

    “Nisamehe Edmund! Nisamehe jamani, halikuwa kusudi langu kukufanyia hivyo, naomba sana unisamehe kwani hukustahili kulipwa ubaya,“ alisema Samantha huku akilia kwa uchungu, akiwa amejifungia chumbani kwake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hakukumbuka hata kubadilisha nguo, akawa anajigalagaza kitandani huku akiwa amekumbatia mto wake, machozi mengi yakiendelea kumtoka. Alikuwa anajua ni jambo gani litakalomtokea Edmund, akawa anajisikia vibaya mno ndani ya moyo wake. Hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kufanya kazi hiyo lakini hata yeye alijishangaa kumuona huruma Edmund kiasi hicho, akawa anaendelea kulia kwa kwikwi.

    ***

    Muda ulizidi kuyoyoma, Edmund akiendelea kuugulia maumivu makali mno. Usingizi ulimpaa kabisa, kwa mbali akaanza kuhisi mwili wake ukimchemka kuashiria kwamba tayari alishapata homa.

    Kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo homa hiyo ilivyokuwa inazidi kuwa kali, akawa anatetemeka kama mtu aliyemwagiwa maji ya baridi. Mpaka inafika alfajiri, Edmund alikuwa hoi mithili ya mtu aliyeugua kwa muda wa wiki nzima mfululizo.

    Kwa kuwa alikuwa anaishi peke yake, alijua endapo akiendelea kujilegeza, anaweza kufia chumbani humo bila msaada, akajikongoja na kuamka mpaka mlangoni, akafanikiwa kufungua mlango lakini kabla hajatoka nje, alianza kutapika mfululizo mpaka akaishiwa nguvu. Kilichozidi kumtia hofu, ni pale alipogundua kuwa kumbe alikuwa anatapika damu.

    Akajikongoja mpaka kwenye mlango wa chumba cha jirani, akamgongea mpangaji mwenzake aliyeamka haraka kutaka kujua kulikoni agongewe mlango alfajiri hiyo.

    “Edmund?!!” aliita jirani huyo huku akionesha kushtushwa mno na hali aliyokuwa nayo kijana huyo.

    “Ni...sa..idie na...ku...” Edmund alishindwa kumalizia kauli yake, akaanza tena kutapika damu mfululizo na muda mfupi baadaye, akadondoka chini kama mzigo, puuh!

    Akapoteza fahamu, jambo lililosababisha jirani yake arudi ndani haraka kubadilisha nguo kwani alikuwa amejifunga taulo tu, akatoka na kuanza kuwaamsha majirani wengine kwa lengo la kumsaidia Edmund ambaye mpaka muda huo hakuwa na fahamu.

    “Kwani kumetokea nini?” baba mwenye nyumba aliuliza lakini hakuna aliyekuwa na majibu.



    “Amekuja kunigongea mlango, nilipotoka nimemkuta kwenye hali mbaya mno akitapika damu na muda mfupi baadaye ndiyo akadondoka na kupoteza fahamu,” alisema yule jirani aliyekuwa wa kwanza kumuona Edmund.

    “Kwa hiyo tufanye nini jamani?”

    “Tumkimbize hospitali, hali yake inaonesha siyo nzuri kabisa, anaweza kupoteza maisha huku tukishuhudia,” baba mwenye nyumba na wapangaji wake walikubaliana, alfajiri hiyohiyo pilikapilika zikaanza.

    Kwa kuwa kulikuwa na mpangaji aliyekuwa akifanya kazi ya udereva wa teksi na alikuwa akilala na gari la bosi wake hapohapo nyumbani, ilibidi teksi hiyo ndiyo itumike.

    Wakasaidiana kumbeba Edmund na kumpakiza kwenye teksi hiyo, muda mfupi baadaye, tayari walishaondoka, dereva akawa anajitahidi kukanyaga mafuta kwa kasi ili kumuwahisha hospitalini.

    Kwa bahati nzuri, alfajiri hiyo hakukuwa na foleni, dakika kadhaa baadaye wakawa tayari wameshawasili kwenye Hospitali ya Mwananyamala, akapokelewa na wahudumu waliokuwa zamu na kumlaza juu ya kitanda chenye magurudumu, harakaharaka akakimbizwa wodini.

    “Amepatwa na nini?” aliuliza daktari kwa mshangao baada ya kuona hali isiyokuwa ya kawaida kwenye mwili wa Edmund.

    “Hata hatuelewi, tumeshtukia akianguka na kupoteza fahamu.”

    “Mungu wangu! Hebu nipisheni kwanza, tokeni nje,” alisema daktari huku akiinua simu ya mezani iliyokuwa ndani ya wodi hiyo na kupiga namba fulani, wale wapangaji wenzake Edmund na baba mwenye nyumba wakatoka huku nao wakiendelea kuulizana maswali yaliyokosa majibu. Mshtuko aliouonesha daktari ulizidi kuwachanganya, wakawa wanasubiri miujiza tu kwani kwa hali aliyokuwa nayo Edmund, chochote kingeweza kutokea.

    Muda mfupi baadaye, madaktari wengine wawili waliingia harakaharaka kwenye wodi aliyokuwa ameingizwa Edmund, wakasogea na kukizunguka kitanda alichokuwa amelazwa huku wakimtazama daktari mwenzao aliyewaita.

    “Kuna huyu mgonjwa ameletwa lakini hali yake inashangaza sana, inaonesha kama ameng’atwa na nyoka au mdudu mwenye sumu kali lakini ukiangalia jeraha jinsi lilivyo, halifanani na jeraha la kung’atwa na nyoka.”

    “Mh! Mbona anabadilika rangi na kuwa mweusi kama mkaa?”

    “Halafu mbona mishipa yake ya damu mwili mzima imevimba kiasi hiki?”

    “Tangu nianze kazi sijawahi kukutana na hali kama hii, mpaka naogopa,” alisema daktari yule, kila mmoja akawa amepigwa na butwaa, hakuna aliyekuwa anajua waanzie wapi kumtibu.

    “Mapigo yake ya moyo yapo chini sana na kadiri muda unavyozidi kwenda mbele ndivyo yanavyozidi kushuka,” alisema daktari aliyekuwa anampima Edmund kifuani kwa kutumia kifaa maalum cha kupimia mapigo ya moyo kiitwacho Stethoscope.

    “Atundikiwe dripu za maji kwanza wakati tukiendelea kuchunguza ni sumu ya aina gani iliyopo kwenye damu yake,” alisema mwingine, wazo lililoungwa mkono na wenzake.

    Edmund ambaye bado hakuwa na fahamu akatundikiwa dripu lakini kilichozidi kuwashangaza madaktari hao, dripu ilikuwa ikitiririka kwa kasi kubwa kuingia kwenye mishipa yake, hali iliyoashiria alikuwa na upungufu mkubwa mno wa maji.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Dakika chache tu baadaye, tayari dripu ya kwanza ilikuwa imeisha, ikabidi atundikiwe nyingine ambayo nayo licha ya madaktari hao kujaribu kuiseti kitaalamu, iliendelea kutiririka kwa kasi kubwa mno, kila mmoja akazidi kupigwa na butwaa huku hofu ikianza kuingia ndani ya moyo wa kila mmoja kwani kulikuwa na dalili zote kwamba ugonjwa aliokuwa nao Edmund, haukuwa wa kawaida.

    ***

    Samantha aliendelea kulia kwa kwikwi chumbani kwake, akiwa amejifungia mlango kwa ndani huku akijilaumu sana kwa kitendo alichomfanyia Edmund. Alikuwa anajua fika nini kitakachomtokea baada ya saa chache kupita, hata hivyo hakuwa na cha kufanya. Alitamani muda urudi nyuma ili arekebishe makosa aliyoyafanya lakini hilo halikuwezekana.

    “Hustahili Edmund, wewe ni mwanaume wa kipekee, hustahili kabisa mateso ya kiasi hicho,” alisema msichana huyo huku akiendelea kulia. Alipotazama saa ya ukutani, tayari ilikuwa imefika saa kumi za usiku lakini hakuwa amepata hata lepe la usingizi, macho yake yakiwa yamevimba na kuwa mekundu sana kutokana na kulia kwa muda mrefu.

    Ghafla, akiwani kama aliyekumbuka kitu muhimu, Samantha alikurupuka pale kitandani kwake. Kwa kuwa hakuwa amebadilisha nguo alizokuwa amevaa siku iliyopita, alichukua viatu vyake na kuvishika mkononi kwani hakutaka mtu yeyote amsikie.

    Akafungua mlango na kunyata kwenye korido ndefu mpaka sebuleni, akafungua kwenye droo zilipokuwa zinawekwa funguo za magari, akachukua funguo ya gari analopenda kutembelea, Jeep Grand Cherokee (New Model) na kunyata kuelekea kwenye mlango wa kutokea.

    Alipofika mlangoni, aliingiza namba maalum za kufungulia mlango kisha akafungua na funguo, akatoka nje na kuangaza huku na kule.

    “Vipi dada mbona mapema namna hii?” mlinzi aliyekuwa na bunduki, akiwa amevalia sare maalum, alimuuliza kwa mshangao kwani haikuwa kawaida ya Samantha kutoka nyumbani muda huo.

    “Shhh! Njoo nikwambie,” alisema Samantha na kumvutia mlinzi huyo karibu yake, akamdanganya kwamba amepatwa na dharura na ni lazima aondoke alfajiri hiyo lakini hataki baba yake au mama yake ajue chochote.

    Mlinzi akawa anatingisha kichwa kuashiria kumuelewa, akaingiza mkono kwenye pochi yake na kumtolea noti kadhaa za shilingi elfu kumikumi, harakaharaka mlinzi akaenda kufungua geti, Samantha akaingia ndani ya gari lake na kuliwasha kisha akatoka kwa kasi kubwa, akaingia barabarani na kutokomea gizani, akamuacha mlinzi akihangaika kufunga geti.

    “Sijui kama nitamuwahi kabla hali haijawa mbaya,” alisema Samantha huku akitazama saa yake ya mkononi, gari likikimbia kwa kasi kubwa ajabu. Bahati nzuri asubuhi hiyo hakukuwa na magari mengi barabarani kwani kwa mwendo aliokuwa akiendesha, ingekuwa rahisi mno kusababisha ajali.

    Hakuwa akijali chochote barabarani, hata sehemu zenye matuta au kona kali alikuwa akipita bila kupunguza mwendo, dakika chache baadaye, tayari aliwasili nyumbani kwa Edmund. Akapaki gari palepale alipopaki usiku uliopita na kutembea harakaharaka kuelekea kwenye chumba cha Edmund.

    Mazingira aliyoyakuta yalizidi kumchanganya kwani alikuta mlango ukiwa wazi huku matapishi ya damu yakiwa yametapakaa kila sehemu. Kwa bahati nzuri, alimkuta mama mwenye nyumba akiwa nje, akiwaandaa wanaye kwa ajili ya kwenda shule. Alipomuuliza, mwanamke huyo alimueleza kwamba Edmund amekimbizwa Mwananyamala baada ya kuzidiwa ghafla.

    Bila hata kuaga, alikimbilia kwenye gari lake na kuondoka kwa kasi kubwa mithili ya madereva wa mbio za magari. Dakika kumi baadaye, tayari alikuwa amewasili Hospitali ya Mwananyamala, akateremka kwenye gari na kuanza kutembea harakaharaka kama aliyechanganyikiwa mpaka mapokezi.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog