Search This Blog

A BOOK OF SATAN ( KITABU CHA SHETANI ) - 2

 







    Simulizi : A Book Of Satan ( Kitabu Cha Shetani )

    Sehemu Ya Pili (2)



    ILIPOISHIA:

    Bila hata kuaga, alikimbilia kwenye gari lake na kuondoka kwa kasi kubwa mithili ya madereva wa mbio za magari. Dakika kumi baadaye, tayari alikuwa amewasili Hospitali ya Mwananyamala, akateremka kwenye gari na kuanza kutembea harakaharaka kama aliyechanganyikiwa mpaka mapokezi.

    SASA ENDELEA...CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Samahani nesi naomba kuuliza,” alisema Samantha huku akihema mithili ya mwanariadha aliyetoka kukimbia mbio za mita mia moja. Japokuwa ilikuwa ni alfajiri na kulikuwa na kiubaridi cha asubuhi, Samantha alikuwa akitokwa jasho, jambo lililomshangaza yule nesi aliyekuwa pale mapokezi.

    “Kuna mgonjwa anaitwa Edmund, eti ameletwa hapa alfajiri hii?”

    “Mh! Kuna mgonjwa mmoja tu aliyeletwa alfajiri hii, ngoja niangalie jina lake,” alisema nesi huyo huku akipekua kwenye daftari kubwa la usajili wa wagonjwa wanaoingia hospitalini hapo.

    “Ndiyo! Amepelekwa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi, hali yake ni mbaya sana na madaktari wote wameelekea huko kumsaidia,” alisema nesi huyo, majibu yaliyozidi kumpandisha Samantha presha.

    “Samahani sana nesi, niko chini ya miguu yako, naomba uniruhusu nikamuone.”

    “Dada! Mgonjwa ndiyo kwanza ameletwa na amepelekwa wodi ya wagonjwa mahututi, unataka ukamuone ili iweje? Hakuna anayeweza kukuruhusu, waache madaktari wafanye kazi yao,” alisema nesi huyo huku akifunika daftari hilo na kuendelea na shughuli nyingine.

    Samantha akaona asipotumia nguvu za ziada, kweli Edmund anaweza kupoteza maisha muda wowote kwani mapambazuko yalikuwa yamekaribia sana na endapo asingefanya jambo mpaka jua litakapochomoza, tafsiri yake ni kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa Edmund, jambo ambalo hakutaka kuona likitokea.

    Harakaharaka akaingiza mkono kwenye sidiria yake na kutoa noti tatu za shilingi elfu kumikumi, akampa yule nesi na kumtaka amuoneshe wodi ya wagonjwa mahututi ilipo.

    “Lakini madaktari hawatakuruhusu.”

    “We nioneshe nikifika nitajua mwenyewe,” alisema Samantha huku akiendelea kuhema kwa nguvu. Nesi akazisunda zile fedha kwenye mfuko wa gauni lake jeupe na kuinuka, akamuelekeza Samantha sehemu ilipo wodi hiyo.

    Harakaharaka akawa anatembea kuelekea wodini, hakuwajali watu kadhaa aliowapita kwenye korido ya kuelekea kwenye wodi hiyo, akapita kwa kasi na kuelekea mpaka kwenye mlango, akaanza kugonga kwa nguvu.

    ***

    Dakika chache baadaye, dripu ya pili aliyokuwa ametundikiwa Edmund pale kitandani nayo iliisha, ikabidi atundikiwe dripu ya tatu huku hali yake ikazidi kuwa tete. Bado madaktari hao hawakuwa wanajua wafanye nini.

    Wakati dripu ikiendelea kutiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yake, majibu ya damu tayari yalishatoka, madaktari wote wakawa wanayajadili kwani licha ya kuonesha kwamba damu ya Edmund ilikuwa na sumu kali, vipimo vilishindwa kuonesha ni sumu ya aina gani, jambo lililosababisha wasijue dawa sahihi ya kuitumia.

    “Why can’t we use trial and error method?” (Kwa nini tusitumie njia ya kujaribu na kujifunza kupitia makosa?) alisema daktari mmoja, wazo lililokubaliwa na wenzake wote.

    Harakaharaka daktari aliyekuwa anahusika na kitengo hicho akatoa orodha ya dawa zinazotumika kutibu watu walioumwa na nyoka na kwa pamoja wakakubaliana kuanza kutumia dawa ya Polyvalent Anti–Snake Venom Serum ambayo ilikuwa na uwezo wa kupambana na sumu kali zaidi.

    Hata hivyo, wakati dawa hiyo ikiendelea kuandaliwa, Edmund alianza kuonesha dalili zilizozidi kuwachanganya madaktari wote mle wodini.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alianza kutapatapa, akirusha mikono na miguu kama anayekaribia kukata roho huku akitokwa na povu lililochanganyikana na damu puani na mdomoni, jambo lililoashiria kwamba tayari sumu iliyokuwa ndani ya mwili wake ilishafika kwenye moyo.

    Kifaa maalum cha kumsaidia kupumua alichokuwa amevalishwa puani na kuunganishwa na kompyuta, kilianza kupiga kelele kwa nguvu kuashiria kwamba mapigo ya moyo ya Edmund yalikuwa yakishuka kwa kasi na hakuwa tena na uwezo wa kupumua.

    Wakati madaktari wakiwa wanahangaika kumsaidia, walishtuka baada ya kusikia mlango wa wodi ya wagonjwa mahututi waliyokuwa ndani yake, ukigongwa kwa nguvu, jambo ambalo halikuwa la kawaida. Walimpuuza aliyekuwa anagonga, wakaendelea na kazi ya kumhangaikia Edmund ambaye dalili zote zilionesha kwamba yupo kwenye hatua za mwisho kabisa za uhai wake.

    Walipoona mtu huyo anazidi kugonga, ilibidi mmoja wao aache kazi na kwenda kufungua.

    “Unasemaje binti?” aliuliza daktari aliyefungua mlango lakini cha ajabu, Samantha alimpiga kikumbo na kusababisha mlango wote ufunguke, kufumba na kufumbua tayari Samantha alikuwa ndani ya wodi hiyo.

    “Ninayo dawa ya kumsaidia kupona! Naomba mniamini! Ninayo dawa,” alisema Samantha huku akihema kwa nguvu, mikono yake akiwa ameiinua juu kama ishara ya kuonesha kwamba hakuwa na lengo baya.

    Tayari yule daktari aliyempiga kikumbo alishamsogelea na kutaka kumtoa kwa nguvu lakini alipoendelea kusisitiza kwamba alikuwa na dawa ya kumsaidia mgonjwa huyo aliyekuwa kwenye hatua za mwisho za uhai wake, madaktari walitazamana kwa sekunde chache kisha wakapeana ishara ya kumruhusu awasaidie kwani nao walishaonesha kushindwa.

    Aliporuhusiwa tu, harakaharaka alisogea mpaka kwenye kitanda alichokuwa amelazwa Edmund ambaye bado alikuwa akiendelea kutapatapa, akamchomoa mpira wa kumsaidia kupumua aliokuwa amevalishwa puani na mdomoni kisha kwa kasi ya ajabu akaanza kumpuliza mdomoni.

    Aliendelea kumpuliza kwa nguvu, baada ya takribani sekunde thelathini za kufanya hivyo, Edmund aliacha kutapatapa, akaendelea kumpuliza na katika hali ambayo hakuna aliyeitegemea, mapigo ya moyo wake yalianza kupanda.

    Yalipofika katika kiwango ambacho Samantha aliona kinafaa, aliacha kumpuliza na kumvalisha tena ile mashine ya kupumulia, akamgeuza kidogo ili apate nafasi ya kuiona vyema shingo yake.

    Muda mfupi baadaye, aliliona jeraha alilomsababishia kijana huyo shingoni muda aliojifanya anamtoa ‘love bite’. Harakahaharaka akapeleka mdomo wake eneo hilo na kuanza kulinyonya jeraha la Edmund kwa nguvu, madaktari wakawa wanashangaa wakiwa hawaamini walichokuwa wanakiona. Urembo wa Samantha na alichokuwa anakifanya, vilikuwa vitu viwili tofauti.

    Mara Samantha akasimama huku mdomo wake ukionesha kujaa, akachukua kikarai kidogo kilichokuwa pembeni na kutema kile kilichokuwa mdomoni mwake, madaktari wakashtuka mno. Ilikuwa ni damu ambayo ilibadilika rangi na kuwa nyeusi kutokana na sumu iliyokuwa imeingia ndani ya mwili wa Edmund.

    Akarudi tena kwenye shingo ya Edmund na kuendelea kumnyonya kisha akaenda tena kutema kwenye kile kikarai, aliendelea kufanya hivyo mfululizo, nguo alizokuwa amevaa zikachafuka vibaya kwa damu lakini mwenyewe hakujali.

    Kadiri alivyokuwa anaivuta sumu hiyo kwa mdomo, ndivyo Edmund alivyokuwa anazidi kubadilika, ile mishipa ambayo ilikuwa imevimba kama inataka kupasuka, ikaanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida, ngozi yake ambayo ilikuwa nyeusi kama mkaa, nayo ilianza kubadilika rangi na kurudi kwenye hali yake ya kawaida, madaktari wakawa bado wanashangaa, kila mmoja akijihisi yupo kwenye ndoto.

    Samantha aliendelea kufanya hivyo mpaka kile kikarai kikakaribia kujaa, tayari nje kulishaanza kupambazuka, lile giza la alfajiri likawa linafifia taratibu na kumezwa na mwanga wa jua lililoanza kuchomoza kwa mbali.

    “Endeleeni na kazi yenu lakini msimwambie yeyote juu ya hiki nilichokifanya, nitakuja baadaye kumuona,” alisema Samantha huku akiwaelekeza madaktari hao kukisafisha vizuri kidonda kilichokuwa kwenye shingo ya Edmund.



    Samantha aliendelea kufanya hivyo mpaka kile kikarai kikakaribia kujaa, tayari nje kulishaanza kupambazuka, lile giza la alfajiri likawa linafifia taratibu na kumezwa na mwanga wa jua lililoanza kuchomoza kwa mbali.

    SASA ENDELEA...

    “Endeleeni na kazi yenu lakini msimwambie yeyote juu ya hiki nilichokifanya, nitakuja baadaye kumuona,” alisema Samantha huku akiwaelekeza madaktari hao kukisafisha vizuri kidonda kilichokuwa kwenye shingo ya Edmund.

    Akachukua kile kikarai kilichokuwa na damu iliyochanganyikana na sumu mpaka nje, akainamisha uso wake ili mtu yeyote asimuone sura yake na kuondoka harakaharaka eneo hilo mpaka kwenye gari lake ambapo alichukua chupa iliyokuwa na maji, akayamwaga na kumimina ile damu yote.

    Kama alivyoingia hospitalini hapo, alitoka kwa kasi kubwa akiwa ndani ya gari lake la kifahari, dakika chache baadaye, tayari alishatoka nje ya uzio wa hospitali hiyo, akawa anakanyaga mafuta kwa nguvu huku akishusha pumzi ndefundefu.

    “Ni lazima nikulinde Edmund, sijali kitakachonipata kutoka kwa baba yangu, nahisi kukupenda sana kutoka ndani ya moyo wangu,” aliwaza Samantha huku akiendelea kukanyaga mafuta.

    Muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amewasili kwenye jumba lao la kifahari, hakutaka kupiga honi ili mlinzi afungue geti kama kawaida yake kwani alihisi baba yake atasikia, akapaki gari pembeni ya geti na kushuka, akabonyeza kengele ya mlango mdogo wa geti. Sekunde chache baadaye, tayari mlinzi alishafungua mlango.

    “Mungu wangu! Umefanya nini mbona umelowa damu kiasi hicho?” mlinzi alihoji huku akionesha kupatwa na mshtuko mkubwa mno. Hakujua atamjibu nini bosi wake kwa kumruhusu Samantha atoke halafu arejee akiwa kwenye hali kama hiyo.

    “Sijaumia popote wala usiwe na wasiwasi, baba aliniulizia?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kweli hujaumia? Na hizo damu zimetoka wapi?” mlinzi alisema huku akimgeuza Samantha kwa hofu.

    “Niamini mimi, hapa nikienda kubadilisha nguo hakuna atakayejua chochote. Nakuuliza baba hajaniulizia?”

    “Ulipotoka alisikia muungurumo wa gari, akaamka na kuja kuniuliza kwa nini nimekufungulia geti wakati bado hakujapambazuka, nikamwambia umepatwa na dharura. Amekasirika sana, bado kidogo aninase vibao,” alisema mlinzi huyo, kauli iliyomfanya Samantha aanze kutetemeka.

    Alikuwa akimfahamu vyema baba yake alivyo mkali, akajua lazima moto utawaka. Hata hivyo, kwa sababu alishajiapiza kumlinda Edmund, alipiga moyo konde na kuingia ndani, akatembea harakaharaka mpaka kwenye mlango wa kuingilia ndani, akaingiza namba maalum kisha mlango huo ukafunguka.

    Akavua viatu vyake na kuvishika, akawa ananyata kuelekea chumbani kwake huku hofu ikiwa imeutawala moyo wake.

    “Umetoka wapi?” sauti kali ya baba yake ilimshtua mno Samantha, akajikuta viatu vikimponyoka mikononi na kuanguka chini. Hakutegemea kama baba yake anaweza kuwa sebuleni muda kama huo, akabaki anatetemeka.

    “Nazungumza na wewe, umetoka wapi? Halafu mbona uko hivyo?”

    “Ni..me..toka ku..fanya ka..zi uliyonituma,” alisema Samantha huku akitetemeka, tayari baba yake alishamsogelea, akawa anamtazama machoni kwa umakini.

    “Kazi gani muda huu.”

    “Ya kafara ya da...mu ba..ba,” Samantha alisema uongo ambao baba yake aliushtukia mapema.

    “Tangu lini kafara ikafanyika alfajiri? Halafu mbona unaonesha kuwa na wasiwasi kiasi hicho? Unanidanganya si ndiyo?”

    “Hapana baba, ni kweli,” alisema Samantha, mzee huyo akaendelea kumbana na kumwambia asijaribu kumdanganya kwa sababu anaujua ukweli wa kila kitu alichokifanya, kauli iliyomshtua sana Samantha.

    “Jana kuna kijana tulikuandalia mazingira ya kukutana naye, kila kitu kikaenda vizuri mpaka usiku ulipotimiza kazi yako lakini ghafla ukabadilisha mawazo kwa sababu ya mapenzi. Umenisikitisha sana mwanangu! Unafikiri sijui kwamba umetoka Hospitali ya Mwananyamala kumsaidia huyo kenge mwenzio?

    “Ni mwezi wa pili sasa unaisha hujafanya kazi hata mara moja. Jana tumetumia nguvu kubwa kukutengenezea mazingira lakini matokeo yake umetanguliza udhaifu mbele. Hujui kwamba mapenzi ni udhaifu? Unataka huu utajiri wetu uishe? Kwa nini unavunja masharti? Unaijua hatari ambayo iko mbele yetu kwa ujinga unaoufanya?”

    “Lakini baba...”

    “Lakini nini? Sasa kwa taarifa yako, mimi siwezi kukubali ujinga unaoufanya unigharimu, kama umeshindwa kufanya kazi itabidi wewe ndiyo utolewe kafara, hujui ni kwa namna gani nimekupigania mpaka hapo ulipofika? Nitakuua.

    “Nakupa saa 24 ya kwenda kumuua huyo mshenzi anayekufanya uvunje masharti vinginevyo damu yako ni halali yangu,” alisema mzee huyo kwa ukali kisha akageuka na kutembea kwa kasi kuelekea chumbani kwake, akamuacha Samantha amepigwa na butwaa akiwa ni kama haamini alichokisikia kutoka kwa baba yake.

    Kwa jinsi alivyokuwa anamfahamu, alijua endapo hatafanya jambo haraka, anaweza kwenda kummalizia Edmund mwenyewe kule hospitalini kwani nguvu za giza alizokuwa nazo zilikuwa zinaweza kumfanya akajua kila kitu kinachoendelea na kuamua nini cha kufanya.

    “Na akigundua kwamba nimeshamtoa sumu mwilini, anaweza kweli kuniua na mimi kama alivyofanya kwa kaka Samuel,” aliwaza Samantha akiwa bado amesimama palepale koridoni, kijasho chembamba kikimtoka.

    Japokuwa alikuwa anapenda maisha ya kifahari waliyokuwa wanaishi kama wapo peponi, Samantha alikuwa hakubaliani kabisa na mchezo wa baba yake wa kuwatoa kafara watu wasio na hatia, wakati mwingine hata ndugu zake wa damu wakiwemo watoto wake wa kuwazaa ili kulinda utajiri wake mkubwa.

    Mara kwa mara alijaribu kujitoa kwenye mtego huo lakini alikuwa akishindwa kwani baba yake alikuwa akijua kila kitu anachokifanya au anachokaribia kukifanya na kumkwamisha.

    “Lazima nikuokoe Edmund, hata kama itanigharimu maisha yangu, nimechoshwa na maisha haya,” alijisemea Samantha na kutembea harakaharaka kuelekea chumbani kwake. Hakutaka kupoteza muda, harakaharaka alivua zile nguo na kukimbilia bafuni, akaoga kisha akarudi na kuvaa baibui na nikabu iliyouficha kabisa uso wake na kuyaachia macho tu.

    Akatoka na zile nguo zilizokuwa zimelowa damu na kwenda kuzitupa kwenye pipa la takataka nje. Harakaharaka akatoka mpaka nje na kumuacha mlinzi akitingisha kichwa chake kwa masikitiko. Sekunde chache baadaye, muungurumo wa gari ulisikika nje ya geti na Samantha akaondoka kwa kasi akiwa ndani ya gari lake.

    Tayari kulishapambazuka, barabarani kukawa na watu na magari mengi, hali iliyomzuia Samantha kuendesha kwa kasi kama ilivyokuwa awali.

    Baada ya kuhangaika sana, alifika Hospitali ya Mwananyamala akiwa amevaa vilevile, akapita mpaka mapokezi ambapo ilibidi avue nikabu, yule nesi aliyemkuta akamkumbuka kwani muda mfupi uliopita walikuwa pamoja.

    “Nina shida nyingine dadaangu, nataka mgonjwa wangu ahamishwe hospitali, kwa jinsi hali yake ilivyo anahitaji huduma bora zaidi kwa hiyo nataka kumpeleka hospitali ya kulipia,” Samantha alidanganya.

    “Inabidi ukazungumze na madaktari wanaomtibu,” alisema yule nesi na kumsaidia kupita hadi wodini ambako aliwakuta madaktari wakiwa wameshamsafisha Edmund kidonda na kumfunga vizuri.

    Akazungumza nao kuhusu mpango wake ambapo walimkubalia, akaandikiwa barua ya rufaa na kusaidiwa kumtoa mgonjwa wodini, akiwa bado hajitambui. Samantha alikuwa akishinikiza kila kitu kifanyike harakaharaka kwani alijua muda wowote baba yake anaweza kufika hospitalini hapo na kuvuruga kila kitu.

    “Ambulance imepeleka wagonjwa wengine Muhimbili, inabidi usubiri.”

    “Hapana, sihitaji ambulance, nimekuja na gari langu,” alisema Samantha huku akivaa tena ile nikabu yake na kuuficha uso wake, manesi na madaktari wakasaidiana kumpakiza mgonjwa kwenye gari kisha baada ya hapo daktari mkuu akataka manesi wawili waongozane naye lakini Samantha alikataa, jambo lililowashangaza wote.

    Harakaharaka akaingia kwenye gari na kupiga ‘starter’ kisha akawasha taa za mbele za gari hilo, akaondoka kwa kasi mpaka getini. Akiwa anataka kutoka na kuingia barabarani, alishtuka baada ya kuliona gari la baba yake nalo likiwa linakata kona ya kuingia hospitalini hapo.

    “Mungu wangu!” alisema Samantha kwa hofu kubwa.



    Harakaharaka msichana huyo alipandisha vioo vya gari lake, akamuona baba yake akivua miwani na kulikodolea macho gari hilo akiwa ni kama haamini. Akaingia barabarani na kukanyaga mafuta kwa nguvu, gari likawa linakimbia kwa kasi kubwa.

    “Dereva hebu geuza gari mara moja, lile gari siyo analoendesha mwanangu Samantha?” alisema baba yake Samantha baada ya gari alilokuwa akiliendesha Samantha kuwapita kwa kasi pale getini wakati wakitaka kuingia Hospitali ya Mwananyamala.

    Harakahara dereva akaanza kuhangaika kugeuza gari na kusababisha madereva wenzake wawe wanampigia honi kwa fujo kwani alikuwa akisababisha foleni. Hatimaye akafanikiwa kugeuza na kuelekea kule lile gari lilikoelekea huku baba yake Samantha akimsisitiza kuongeza mwendo.

    Kwa mbali wakawa wanaliona gari hilo ambapo walipotazama namba waligundua kuwa ndiyo lenyewe, mzee huyo akawa anamhimiza dereva kuhakikisha anaongeza kasi mpaka alifikie.

    ***

    Samantha akiwa anakanyaga mafuta na kusababisha gari liwe linaenda kwa kasi kubwa, alishtuka zaidi baada ya kuona gari la baba yake nalo likigeuza na kuanza kumfuata kwa nyuma. Akazidi kuchanganyikiwa, akawa anaendelea kuendesha gari kwa kasi huku akitazama nyuma kwa kupitia vioo vya pembeni, akaona gari la baba yake likizidi kuongeza kasi, hofu ikazidi kumjaa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Japokuwa barabara ilikuwa na magari mengi, Samantha alizidi kuongeza kasi, akawa anazipita daladala kwa namna ambayo ilikuwa rahisi sana kusababisha ajali, muda mwingine akawa analazimika ‘kutanua’ na kutoka nje ya barabaraba, madereva wengine wakawa wanapunguza mwendo ili kuepusha ajali.

    Japokuwa kulikuwa na matuta makubwa kwenye eneo la Mwananyamala Komakoma, Samantha aliyapita bila kupunguza mwendo hata kidogo na kusababisha gari liruke juu na kuzua taharuki kwa watumiaji wengine wa barabara, dakika chache baadaye akawa ameshapotea kabisa eneo hilo.

    “Ongeza mwendo! Inawezekanaje akushinde wakati wewe umesomea udereva? Nitakufukuza kazi.”

    “Lakini mzee, hili gari lipo chini na huwezi kupita kwa kasi kwenye matuta haya makubwa kama yeye alivyofanya, tutaharibu gari au tutapata ajali,” dereva alijitetea lakini utetezi wake haukuwa na maana kwa mzee huyo ambaye tayari kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka.

    Akamlazimisha dereva kusimama haraka, akateremka na kukaa mwenyewe nyuma ya usukani, akaondoa gari kwa kasi lakini tayari alishachelewa kwani Samantha alishapotea kwenye upeo wa macho yao, walipofika eneo la Kinondoni Studio, kwenye makutano ya Barabara za Mwananyamala na Kawawa, walishindwa kuelewa kama Samantha ameelekea kulia au kushoto, wakajikuta wakikwama.

    ***

    Baada ya kuendesha gari kwa kasi kubwa, akinusurika kupata ajali mbaya zaidi ya mara nne, hatimaye Samantha aliwasili Mlingotini, Bagamoyo, nyumbani kwa mzee Tenson Shiwinga, mganga wa baba yake ambaye alizoea kumuita babu.

    Akafunga breki kali na kusababisha gari liseleleke na kutoa mlio uliomshtua Mzee Shiwinga ambaye alikuwa ndani ya kibanda chake cha miti, udongo na makuti, akatoka akiwa amejifunga shuka jekundu na kupigwa na butwaa kumuona Samantha akishuka kwenye gari huku akihangaika kumteremsha mtu ambaye ilionesha wazi alikuwa hajitambui.

    “Babu nahitaji msaada wako, nisaidie niko chini ya miguu yako.”

    “Samantha? Kuna nini tena mjukuu wangu? Baba amekutuma?”

    “Hapana babu, nisaidie kwanza nitakueleza kilichotokea. Huyu ni mchumba wangu nataka umsaidie kumtoa sumu, nimemng’ata kwa bahati mbaya, fanya kila liwezekanalo akipona nakuahidi nitakupa zawadi kubwa sana,” alisema Samantha huku machozi, jasho na kamasi vikimtoka kwa wakati mmoja.

    Mzee Shiwinga alimtazama Samantha usoni na kugundua kuwa alikuwa analia, akawa hana namna zaidi ya kumsaidia. Akamsaidia kumbeba mtu huyo ambapo kutokana na jinsi mzee huyo alivyokuwa na nguvu licha ya umri wake mkubwa, alimbeba kwenye mikono yake na kutembea naye haraka kuingia ndani ya kibanda chake.

    Samantha akawa anafuata kwa nyuma huku baibui aliyovaa akiiona kama mzigo, alitamani aivue na kuitupa mbali lakini haikuwezekana, akawa anaendelea kulia huku akimsisitiza mzee huyo kufanya kila linalowezekana kumsaidia kijana huyo.

    Baada ya kumuingiza ndani ya kibanda chake kilichojaa matunguli, pembe, kwato, mikia na ngozi za wanyama mbalimbali wa porini, mzee huyo alimlaza juu ya ngozi ya chui aliyokuwa akiitumia kuwatibu wagonjwa wake, akachukua kibuyu kimoja na kukitingisha kwa nguvu kisha akakifungua ambapo kilitoa gesi kama soda inayofunguliwa.

    Akanywa dawa zilizokuwa ndani yake kisha akaanza kumnywesha mgonjwa wake kwa kutumia mdomo huku mkono mmoja akiutumia kufungua bandeji kwenye jeraha la kung’atwa lililokuwa shingoni. Baada ya kumnywesha, alichukua kibuyu kingine chenye dawa na kumwagia juu ya jeraha, akaanza kuliminyaminya huku akitamka maneno ambayo Samantha hakuyaelewa.

    Sekunde chache baadaye, mganga huyo alitoka mbio na aliporejea alikuwa na majani kadhaa mkononi ambayo aliyatafuna harakaharaka na kuanza kumtemea mwili mzima.

    ”Anaitwa nani?”

    “Edmund!” alisema Samantha huku akijifuta machozi, mganga huyo akaanza kulitaja jina la Edmund huku akichanganya na maneno mengine ambayo hakuyaelewa, akaendelea kuchakarika, akitumia karibu vibuyu vyote vilivyokuwa na dawa, muda mfupi baadaye, wote walishtuka baada ya kusikia Edmund akipiga chafya mfululizo kisha akafumbua macho.

    “Ooh! Edmund wangu jamani, siamini,” alisema Samantha na kuanza upya kuangua kilio huku akimkumbatia Edmund kwa nguvu. Bado Edmund alikuwa amepigwa na butwaa, akawa anashangaashangaa akiwa haelewi kinachoendelea.

    “Sa...ma..ntha...” alisema kwa tabu huku akijaribu kuinuka lakini maumivu makali shingoni yakamfanya arudi tena pale chini.

    “Ni..ni kime..tokea? Ha..pa ni wa...pi?” alihoji Edmund huku akiendelea kushangaa, maswali mengi yakipita ndani ya kichwa chake.

    “Tupo kwa mganga Edmund, nisamehe kwa yote yaliyotokea, nitakueleza kila kitu kilichotokea,” alisema Samantha huku akiendelea kulia, ikabidi mganga amsogeze pembeni kwani bado alikuwa na kazi kubwa ya kuendelea kumhudumia, Samantha akakubali kusogea pembeni lakini bado alikuwa akiendelea kulia kwa uchungu.

    Mganga Shiwinga aliendelea kumfanyia dawa Edmund na baada ya takribani saa mbili kupita, Edmund alikuwa na uwezo wa kuinuka mwenyewe na kukaa japokuwa bado alikuwa akilalamikia maumivu makali.

    “Una bahati sana kijana, tayari ulishafariki, ni kama muujiza tu! Umshukuru sana Samantha kwani asingekuwahisha pengine tungekuwa tunaongea mengine hivi sasa,” alisema Mganga Shiwinga wakati akiendelea kumkanda Edmund jeraha lake.

    “Samantha,” aliita Edmund, harakaharaka msichana huyo aliyekuwa amekaa juu ya kiti cha miguu mitatu akiwa amejikunyata, aliinuka na kumsogelea Edmund, akambusu kwenye paji la uso kisha akakaa juu ya ile ngozi aliyokuwa amekalia Edmund.

    “Unajisikiaje mpenzi wangu?”

    “Bado shingo inauma, hebu niambie nini kimetokea? Halafu kwa nini jana uliondoka ghafla nyumbani kwangu? Kwa nini uliniumiza shingoni kiasi hiki? Kwa nini... mbona sielewi kinachoendelea? Na hapa nimefikaje? Kwa nini mganga anasema nilikuwa nimeshakufa?” Edmund aliuliza maswali mengi mfululizo akionesha kuchanganyikiwa kabisa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Samantha alishusha pumzi ndefu na kumuomba mganga atoke na kuwapisha ili wazungumze kwa uhuru zaidi, mganga Shiwinga akafanya kama alivyoombwa, Samantha akashusha tena pumzi ndefu na kumtazama Edmund usoni.



    “Naomba unisamehe sana kwa kilichotokea Edmund, halikuwa kusudio langu. Najua itakuwa vigumu kuniamini lakini naomba uelewe kwamba nimelijua kosa langu na nimeamua kukulinda kwa sababu naamini wewe ndiye utakayenitoa kwenye hiki kifungo Edmund!

    “Sijawahi kufurahia maisha hata mara moja, usinione niko hivi napata kila ninachokitaka ukajua nina furaha, nateseka sana mwenzio! Nipo chini ya miguu yako.

    “Naomba uniahidi kwamba hata nikikuambia ukweli bado utaendelea kuwa nami na kamwe hutaniacha, nakupenda Edmund,” alisema Samantha huku akilia kwa uchungu mkubwa na kumlalia Edmund kifuani, machozi yakawa yanamtoka na kutiririka kupitia kona za macho yake mpaka kwenye mwili wa Edmund.

    Kwa jinsi msichana huyo alivyokuwa akilia kwa uchungu, kabla hata Edmund hajajua anataka kumwambia nini, kitendo cha kushtuka na kujikuta nyumbani kwa mganga wa kienyeji huku msichana huyo akiwa pembeni yake, kilimfanya aamini kwamba hawezi kuwa na nia mbaya naye.

    Kwa taabu alinyanyua mkono wake mmoja na kumshika Samantha mgongoni, akampigapiga kama ishara ya kumbembeleza na kumwambia yupo tayari kumsikiliza na atakuwa naye kwa hali zote. Kauli hiyo ilimfurahisha mno Samantha, akambusu Edmund mdomoni na kuanza kumueleza kilichotokea.

    Akamwambia kwamba baba yake anamiliki utajiri mkubwa lakini kwa njia zisizo halali na kwamba kwa kipindi chote cha maisha yake tangu azaliwe, Samantha ndiyo kichocheo cha utajiri huo.

    “Sijakuelewa unamaanisha nini,” Edmund alimkatisha Samantha, ikabidi aanze kumfafanulia kila kitu kwa kina.

    Akamueleza kwamba wazazi wake wamepata utajiri walionao kwa njia za kishirikina na kwamba walikuwa wakiwachukua watu misukule na wengine kuwatoa kafara kwa kumtumia Samantha ili utajiri wao uzidi kuchanua siku baada ya siku.

    Licha ya kujitahidi kufafanua, bado Edmund alikuwa hamuelewi msichana huyo, huku muda mwingine akijihisi pengine yupo kwenye ndoto ya kutisha na muda mfupi baadaye atashtuka na kujikuta akiwa amelala chumbani kwake.

    Samantha alikuwa na kazi ya ziada ya kumuelewesha Edmund, akamwambia kwamba tangu akiwa mdogo, wazazi wake walimpeleka kwa waganga waliomuwekea tego mwilini mwake kupitia sehemu zake za siri kwamba mwanaume yeyote atakayejaribu kufanya naye mapenzi, achukuliwe msukule au akatolewe kafara.

    “Nimeshawaua wanaume wengi sana Edmund, hata wewe ilikuwa ufe kwa njia hizohizo, nimekuokoa kwa sababu kwa mara ya kwanza maishani mwangu nimetokea kukupenda Edmund, nimechoka kuwa muuaji! Nimechoka naomba unisaidie kuondokana na hali hii,” alisema Samantha huku akianza upya kuangua kilio kwa uchungu.

    Maelezo hayo yalimshtua mno Edmund, bado akawa anajihisi yupo ndotoni kwani ilikuwa vigumu sana kuamini kwamba Samantha alikuwa akiongea ukweli.

    “Kwa hiyo... kwa hiy..o nini huwa kina...to..kea,” Edmund alimuuliza kwa sauti ya kukatakata huku akitetemeka mno kutokana na hofu kubwa iliyokuwa imemuingia, hasa baada ya kuambiwa kwamba hata yeye alitakiwa kufa ila akaponea kwenye tundu la sindano.

    Samantha akamwambia kwamba anapotongozwa na wanaume, wakishakubaliana kwenda kukutana kimwili, kuna dawa huwa anaitafuna muda mfupi kabla ya tendo na kusababisha mwili wake wote uwe na sumu kali.

    “Mwanaume akijaribu kuingia na mimi chumbani tu, hatafanikiwa kufanya mapenzi na mimi na huo ndiyo utakuwa mwisho wake kwani lazima nitamng’ata au kumchubua sehemu, kinachotakiwa ni damu yake kutoka hata kidogo tu!

    “Ikitokea hivyo sumu yangu humuingia na kusababisha apoteze maisha ndani ya muda mfupi sana na baada ya hapo kazi yote hubakia kwa baba,” alisema Samantha huku akijifuta machozi na kamasi vilivyokuwa vinamtoka mfululizo.

    “Kwa hiyo na mimi hicho ndicho kilichonitokea?”

    “Ndiyo Edmund, naomba unisamehe mpenzi wangu, halikuwa kusudio langu ndiyo maana nimeamua kukusaidia, nimekuwahi mpenzi wangu,” alisema Samantha kwa hisia za hali ya juu, Edmund akashusha pumzi ndefu na kukosa cha kusema, ukimya ukatawala kati yao.

    Ghafla, walishtushwa na kelele za mlango uliobamizwa kwa nguvu, mganga Shiwinga akaingia mbiombio na kumueleza Samantha kuwa ameliona gari linalofanana na la baba yake likija eneo hilo kutokea mbali.

    “Mungu wangu, babu naomba nisaidie kutoroka na Edmund wangu,” alisema Samantha huku akianza kuhangaika, Mzee Shiwinga akamtuliza na kumwambia kuwa isingekuwa rahisi kumtoroka baba yake katika mazingira hayo kwani hakukuwa na njia nyingine ambayo angeweza kupita zaidi ya ile ambayo baba yake alikuwa akija nayo.

    “Labda ninachoweza kukusaidia ni kwenda kumficha Edmund porini lakini jua kwamba ni hatari sana endapo akishtukia mchezo, bila shaka baba yako unamjua vizuri,” alisema mganga Shiwinga huku akimuinua Edmund pale alipokuwa amelala, harakaharaka akatoka naye na kuzunguka nyuma ya kibanda chake, vishindo vikasikika wakati akikimbia naye kutokomea porini.

    Huku nyuma, Samantha alifuta ushahidi wote wa uwepo wa Edmund eneo hilo, akawa anapanga uongo wa kumwambia baba yake. Dakika chache baadaye, muungurumo wa gari lililoonesha lipo kwenye kasi kubwa ulisikika nje ya kibanda cha mganga Shiwinga kisha sekunde chache baadaye mlango ukawa unagongwa kwa nguvu.

    Huku akitetemeka kuliko kawaida, Samantha aliinuka na kufungua mlango, akakutana uso kwa uso na baba yake aliyekuwa amefura kwa hasira kama nyoka cobra!

    “Ulijua sitakupata si ndiyo?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana baba, nimekuja kwa babu Shiwinga kuja kutibiwa, naona mambo yangu hayaendi sawa na mimi sipendi kukuudhi,” alisema Samantha huku akitetemeka kuliko kawaida.

    Haikuwa rahisi kwa baba yake kuuamini uongo wa kitoto alioutoa kwani kwa macho yake alimshuhudia kuanzia anatoka hospitalini na jinsi alivyomkimbia alipojaribu kumfuatilia.

    “Unanifanya na mimi ni mtoto mwenzako si ndiyo?”

    “Kweli baba, kama huamini kamuulize hata babu Shiwinga.”

    “Yuko wapi?”

    “Ameenda kunitafutia dawa,” alisema Samantha lakini baba yake hakutaka kuamini, akamwambia dereva wake aliyekuja naye kusimama mlangoni na kuhakikisha hakuna mtu anayetoka ndani ya nyumba hiyo ya mganga. Akazunguka nyuma ya nyumba ya mganga na kuanza kuangaza huku na kule kama atamuona mganga huyo.

    Muda mfupi baadaye, aliona vichaka vikitingishika mita kadhaa kutoka pale alipokuwa amesimama, akajua lazima kuna mtu. Alipoendelea kutulia huku macho yake akiwa ameyakaza, alimuona mganga Shiwinga kichakani



    Mganga Shiwinga akiwa na rundo la majani ya porini na mizizi kadhaa, alitokeza kichakani huku akipiga ‘mbinja’ kwa nguvu, akajifanya hajamuona baba yake Samantha wala hana taarifa zozote za uwepo wake. Ni mpaka alipomkaribia ndiyo akajifanya kushtuka kumuona!

    “Ni wewe baba?”

    “Ni mimi mzee, shikamoo.”

    “Marahabaa! Naona umeamua kuja mwenyewe, umefanya jambo zuri sana, nipo na Samantha,” alisema mzee huyo huku akimpita baba yake Samantha na kumpa ishara kwamba amfuate. Kwa jinsi alivyokuwa anamheshimu na kumuogopa mganga Shiwinga, zile hasira zote alizokuwa nazo baba yake Samantha ziliyeyuka kama siagi kikaangoni.

    “Samahani kabla hatujaingia ndani, naomba nikuulize jambo.”

    “Uliza tu baba.”

    “Mwanangu Samantha amekuja na nani huku kwako?”

    “Amekuja mwenyewe kama anavyofanya siku zote akiwa na tatizo lolote. Ameniambia kwamba anahisi nguvu zake zimepungua kwa sababu hawezi tena kufanya ile kazi tuliyompa kama ilivyokuwa zamani!

    “Hivi hizi dawa unazoziona ni kwa ajili yake, nataka kumuongeza nguvu,” alidanganya mganga Shiwinga, baba yake Samatha akashusha pumzi ndefu kwani uongo alioambiwa na binti yake ulikuwa ukifanana na uongo wa mganga huyo.

    Kwa kuwa hakuwahi kumdanganya hata siku moja, baba yake Samantha aliamini kwamba alichoambiwa na mganga ni ukweli mtupu, akashusha tena pumzi ndefu kisha wakaendelea kutembea kuelekea ndani ya kibanda chake.

    “Naomba uzungumze na mjukuu wako, ukiachilia mbali kupungua kwa nguvu zake, siku hizi amekuwa mzembe sana. Hafanyi kazi na badala yake anaendekeza ujingaujinga tu. Hata ujio wangu hapa haukuwa wa heri kwa sababu kuna jambo amelifanya na yeye mwenyewe analijua.

    “Ni kwa sababu ya heshima yako mzee ndiyo maana nimeamua kumsamehe, ila akirudia tena tusilaumiane,” alisema baba yake Samantha akiwa amekaa kwenye kiti cha miguu mitatu ndani ya kibanda hicho cha mganga, akiwa amefura kwa hasira.

    “Samantha, kwani umemfanya nini baba yako?” alihoji mganga huku akijifanya hajui chochote kilichotokea, Samantha ambaye muda wote alikuwa amekaa kimya, hofu kubwa ikiwa imeutawala moyo wake, alishusha pumzi ndefu na badala ya kueleza alichoulizwa, alianza kulia na kumuomba baba yake amsamehe.

    “Mueleze babu yako ulichokifanya, kulia hakukusaidii chochote,” alisisitiza baba yake Samantha lakini binti yake hakuwa tayari kueleza chochote, ikabidi yeye ndiyo aanze kumueleza mganga kilichotokea.

    Kwa kuwa tayari walishakula njama, mzee Shiwinga naye alijifanya kushtuka kusikia kwamba Samantha alikuwa amemtorosha mtu aliyekuwa ameandaliwa kwa kafara.

    “Ni makosa makubwa uliyoyafanya, baba yako ana kila sababu ya kukasirika, umekosea sana,” alisema mganga Shiwinga, akaacha hata kuchambua dawa na kuendelea kumsema Samantha. Kwa jinsi walivyokuwa wamepangilia vyema njama zao, haikuwa rahisi kwa mzee huyo kushtukia chochote.

    Samantha akawa amejiinamia muda wote huku akiyalazimisha machozi ya uongo. Ilibidi baba yake asubiri mpaka binti yake huyo amalize kushughulikiwa na mganga Shiwinga. Alipomaliza tu, alimtaka waongozane naye kurudi jijini Dar es Salaam, nyumbani kwao.

    Kwa jinsi alivyokuwa amembana, Samantha alishindwa jinsi ya kumtoroka, akaondoka kwa shingo upande huku akijiapiza kuwa ni lazima atarudi kuja kumfuata Edmund hata iweje.

    Hatimaye msafara wa magari mawili uliianza safari ya kuelekea jijini Dar es Salaam, Samantha akiwa amepanda kwenye gari alilokuwa anaendesha baba yake na dereva wao akiwa anaendesha gari la Samantha.

    Mganga Shiwinga aliwasindikiza kwa macho mpaka walipopotea kabisa kwenye upeo wa macho yake, harakaharaka akaacha kila alichokuwa anakifanya na kukimbilia nyuma ya nyumba yake, akapotelea vichakani.

    Edmund aliendelea kukaa kwenye pango alimofichwa na mganga Shiwinga, hofu kubwa ikiwa imetanda ndani ya moyo wake. Maelezo aliyopewa na Samantha kuhusu kilichomtokea usiku uliopita, yalimfanya ajihisi maisha yake yapo kwenye hatari kubwa mno.

    Akiwa bado amezama kwenye dimbwi la mawazo ndani ya pango hilo lililokuwa na giza totoro, alisikia vishindo vya mtu akija mbiombio, hofu ikazidi kumuongezeka akihisi huenda baba yake Samantha ameshtukia mchezo na sasa alikuwa anataka kuja kummalizia mwenyewe.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Japokuwa alikuwa ameacha kwenda kanisani kwa kipindi kirefu, alijikuta akihitaji ulinzi wa Mungu wake kuliko kitu kingine chochote, mapigo ya moyo yakawa yanazidi kumuenda mbio huku akisubiri muujiza utokee.

    Mara aliona jiwe kubwa lililokuwa kwenye sehemu ya kuingilia ndani ya pango hilo likisogezwa pembeni, akakazia macho sehemu hiyo akitaka kujua ni nani aliyekuwa anafungua. Alipogundua kwamba ni mganga Shiwinga, alishusha pumzi ndefu na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake.

    “Una bahati sana, yule bwana amekasirika mno, yaani kama angekukuta pale kwangu angekutafuna mzimamzima,” alisema mganga huyo huku akimsaidia Edmund kuinuka pale alipokuwa amekaa, akaupitisha mkono wake mmoja nyuma ya mabega ya Edmund na kuanza kumsaidia kutembea kwani bado mwili wake haukuwa na nguvu za kutosha.

    Akamtoa nje ya pango hilo na kufunga sehemu ya kuingilia kwa jiwe kubwa, wakawa wanarudi nyumbani kwake huku bado Edmund akiwa haamini kama amesalimika.

    “Nakushukuru sana babu.”

    “Usinishukuru mimi, mshukuru Samantha, sijui umempa nini kwani kwa jinsi alivyo katili sijui kwa nini ameamua kukuokoa wewe,” alisema mganga huku akiendelea kumuandalia Edmund dawa nyingine kwa ajili ya kuitoa kabisa sumu iliyokuwa imeingia mwilini mwake.

    Bado Edmund alibaki na maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu Samantha, akawa anajaribu kumdodosa mganga Shiwinga kama alikuwa anamjua vizuri msichana huyo.

    “Namjua tangu akiwa kachanga, mimi ndiye niliyeshirikiana na wazazi wake kumfanya awe kama unavyomuona leo.”

    “Mbona amesema kwamba kila mwanaume anayejaribu kufanya naye mapenzi ni lazima afe. Ni kweli?”

    “Ni kweli, pale alipo hamjui kabisa mwanaume, yeye alizaliwa kwa sababu ya kazi moja tu, kumletea baba yake utajiri.”

    “Sasa mbona ananiambia ananipenda ndiyo maana ameniokoa?”

    “Hajawahi kupenda hata siku moja ndiyo maana nakuuliza kwamba sijui umempa nini.”

    “Sasa itakuwaje na umeshasema kila mwanaume anayejaribu kufanya naye mapenzi ni lazima afe?” Edmund aliuliza huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka majibu. Licha ya yote yaliyotokea, alishindwa kuuficha ukweli uliokuwa ndani ya moyo wake kwamba anampenda sana msichana huyo.

    “Jiandae kufa,” alisema mganga huyo huku akiangua kicheko cha kizee, Edmund akajiinamia chini.

    “Ipo njia moja tu ya kuwasaidia wote wawili lakini ni ya hatari sana, hata mimi sipendi kumuona akiendelea kuua watu wasio na hatia, natamani nimuone akiwa na mume anayempenda, ajenge familia na hatimaye atulie lakini siyo rahisi,” alisema mganga Shiwinga, kauli iliyomfanya Edmund ainuke pale alipokuwa amejiinamia na kumsogelea mganga akitaka kujua ni mbinu gani hiyo ya kuwasaidia.



    “Inabidi Samantha atolewe nguvu za giza na tego aliloingiziwa mwilini mwake tangu akiwa mtoto lakini suala hilo ni lazima yeye mwenyewe aridhie kwa sababu litakuwa na madhara makubwa kwake na kwa familia yake.

    “Lakini pia baba yake hatakiwi kabisa kujua kwa sababu anaweza hata kutupiga risasi wote, Samantha ndiyo kitega uchumi chake,” alisema mzee Shiwinga na kumfanya Edmund ashushe pumzi ndefu na kujishika shavu.

    Alizama kwenye dimbwi la mawazo, akawa anatafakari mambo mbalimbali yaliyotokea, akawa anajiuliza kama inawezekana msichana huyo akatolewa nguvu mbaya zilizopandikizwa ndani ya mwili wake na akawa binadamu wa kawaida.

    Hofu ya kifo ilimfanya amuogope mno Samantha, akaendelea kutafakari kwa muda mrefu bila kupata majibu. Hakuna kitu kilichokuwa na maana kwake zaidi ya uhai wake kwani mpaka muda huo ilikuwa ni miujiza ya Mungu tu ndiyo iliyomfanya awe hai.

    “Mbona umekuwa kimya kiasi hicho?”

    “Babu sidhani kama nitaweza kuwa na amani na Samantha. Moyo wangu unamuogopa mno hata kama ni yeye ndiye aliyeniokoa,” alisema Edmund na kumfanya mganga Shiwinga aachie tabasamu.

    “Siyo kazi nyepesi, moyo wako umeshaingiwa na hofu, ni binadamu anayeweza kuzitawala hisia zake pekee ndiye anayeweza kuuona upendo wa kweli alionao Samantha na kumsaidia kutoka kwenye shimo la mauti aliloishi kwa kipindi kirefu tangu akiwa mdogo.”

    “Kuzitawala hisia? Ndiyo kufanya nini?”

    “Namaanisha mtu anayejitambua, anayefahamu yeye ni nani na kwa nini yupo duniani ndiyo anayeweza kuishinda hofu ya kifo. Mtu akishaishinda hofu ya kifo anaweza kuzitawala hisia zake na anaweza pia kuwasaidia wengine wenye uhitaji,” alisema mganga Shiwinga na kumfanya Edmund akune kichwa kwani kimsingi hakuwa amemuelewa.

    “Kwa hiyo unataka kusema inabidi nijifunze uchawi?”

    “Uchawi? Sijazungumzia suala la uchawi hapa, nazungumzia elimu ya utambuzi. Haina uhusiano wowote na uchawi.”

    “Lakini nimewahi kusikia kuwa waganga na wachawi peke yao ndiyo wanaoweza kuishinda hofu dhidi ya kifo.”

    “Tangu uzaliwe umesikia mambo mengi sana yasiyo sahihi, ni jukumu lako kuutafuta ukweli kwani ndiyo kitu pekee kitakachokuweka huru. Hata vitabu vya dini vinazungumzia suala la kuutafuta ukweli, mimi siyo muumini lakini nayafahamu vizuri maandiko matakatifu,” alisema mganga Shiwinga huku akiendelea kumuandalia Edmund dawa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maelezo yake yalimfanya Edmund aanze kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu. Alitamani kumuuliza maswali mengi sana mganga huyo lakini alishindwa hata aanzie wapi.

    Mganga Shiwinga ni kama alielewa kilichokuwa kikipita ndani ya mawazo yake, akamwambia asiwe na wasiwasi akimaliza kumuandalia dawa atamjibu maswali yote aliyokuwa akihitaji majibu.

    Kazi ya kuandaa dawa iliendelea ambapo baada ya kumaliza, mganga huyo alimnywesha Edmund huku nyingine akimpaka kwenye jeraha lake. Kutokana na ukali wa dawa hiyo, Edmund alianza kuhisi usingizi mzito, mzee huyo akamuandalia sehemu ya kupumzika ambapo muda mfupi baadaye alipitiwa na usingizi.

    ***

    Saa chache baada ya Samantha kuondoka pamoja na baba yake na dereva wao, mganga Shiwinga alishtuka kusikia mlio wa pikipiki ikija kwa kasi nyumbani kwake, akabaki anajiuliza maswali yaliyokosa majibu kwani haikuwa kawaida kwa wagonjwa wake kwenda kwake kwa kutumia aina hiyo ya usafiri.

    Akatoka nje na kusimama juu ya jiwe kubwa, akawa anatazama kule mlio ule wa pikipiki ulikokuwa unatokea. Muda mfupi baadaye, tayari pikipiki hiyo ilikuwa imeshafika, akabaki amepigwa na butwaa kumuona Samantha akishuka kwenye bodaboda na kufungua pochi yake, akatoa fedha na kumpa yule dereva wa bodaboda kisha harakaharaka akaondoka na kumuacha mganga Shiwinga akiwa bado amepigwa na butwaa.

    “Samantha! Imekuwaje tena?” aliuliza mganga Shiwinga kwa mshangao, msichana huyo akatembea harakaharaka mpaka pale alipokuwa amesimama.

    “Nataka kumuona Edmund, nataka kuhakikisha kama yupo salama,” alisema Samantha huku akionesha kuwa na hofu kubwa.

    Ilibidi mganga Shiwinga amtulize na kumtoa wasiwasi, akamuingiza ndani ya kibanda chake na kwenda kumuonesha Edmund ambaye alikuwa amepitiwa na usingizi mzito. Samantha akashusha pumzi ndefu na kumgeukia mganga.

    “Nashukuru kwa msaada wako babu, sina imani na baba najua anaweza kufanya kila kinachowezekana kumuondoa duniani Edmund, naomba usinisaliti,” alisema Samantha huku akilengwalengwa na machozi.

    Mganga huyo akamhakikishia kwamba asiwe na wasiwasi, na yeye akaanza kumuuliza kilichotokea kwani hakutarajia kumuona muda huo hasa baada ya kuwa amefuatwa na baba yake akiwa na jazba kali.

    “Tumeenda naye mpaka nyumbani lakini nikafanya ujanja na kuondoka bila mtu yeyote kujua. Wanajua nipo chumbani kwangu nimelala. Muda si mrefu baba atajua Edmund mahali alipo kwa sababu nimemuacha akiandaa rada zake za kichawi kwa ajili ya kuanza kazi ya kumtafuta, anataka kumuua,” alisema Samantha huku akihema kwa nguvu.

    “Usiwe na wasiwasi, hakuna rada zinazoweza kunasa chochote kinachoendelea hapa nyumbani kwangu, mimi ndiyo Shiwinga mwenyewe kutoka Lyamba Lya Mfipa, niamini,” alisema mganga huyo huku akijipigapiga kifuani kwa kujiamini.

    Samantha alikaa kwenye kiti cha miguu mitatu na kuanza kuzungumza na mganga huyo ambaye alimueleza kilichoendelea baada ya yeye kuondoka.

    “Nataka kujua kuhusu msimamo wako, huyu kijana wa watu anaonesha kuwa na hofu kubwa juu yako na mimi sitaki kuja kuonekana nimemsaliti, nataka uniambie unafikiria nini juu yake.”

    “Kama nilivyokudokeza babu, mi nampenda Edmund na nataka kujenga naye familia. Wewe ni shahidi, sijawahi kumpenda mwanaume yeyote zaidi yake, naomba unisaidie babu.”

    “Mimi sina tatizo, cha msingi ni utayari wako mwenyewe kwa sababu ili uweze kuwa naye, inabidi ukubali hizo nguvu za giza ndani ya mwili wako zitolewe, jambo ambalo baba yako hawezi kulifurahia hata kidogo.”

    “Babu nimeshakwambia, nimechoka kuwa mtumwa wa baba, nimechoka kuwa kaburi la wanaume, na mimi nina haki ya kupenda na kupendwa! Nampenda Edmund na nipo tayari kufanya chochote kwa ajili ya penzi lake,” alisema Samantha kwa msisitizo huku akionesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

    “Una uhakika na unachokisema?”

    “Nina uhakika wa asilimia mia moja, mimi nimeshakuwa mkubwa babu, isitoshe Mungu kanijalia urembo, kwa nini niendelee kuishi maisha ambayo siyataki? Nataka kuwa mke wa Edmund,” alisema Samantha kwa sauti ya juu ambayo ilimfanya Edmund aliyekuwa amelala, kuzinduka na kuyasikia maneno hayo.

    Akawa anajihisi kama yupo ndotoni kwa sababu hakutegemea kwamba Samantha anaweza kurudi kwa mganga muda huo, harakaharaka akainuka pale alipokuwa amelala.



    Akajaribu kusimama lakini kutokana na dawa alizopewa na Mganga Shiwinga, Edmund alijikuta akianza kupepesuka mithili ya mlevi, akagonga vyombo vilivyokuwa pembeni na kuwashtua Samantha na Mganga Shiwinga.

    Akiwa bado anapepesuka, harakaharaka Samantha aliinuka na kumkimbilia, akawahi kumdaka na kumvutia kifuani kwake.

    “Samantha! Ni wewe?”

    “Ni mimi Edmund, najua huwezi kuamini lakini ndiyo hivyo, nimerudi kwa ajili yako,” alisema Samantha huku akizidi kumbana Edmund kwenye kifua chake kizuri, akamtazama Edmund kwa macho yake yaliyokuwa mithili ya mtu anayesikia usingizi, Edmund akashindwa kuzizuia hisia zake na kujikuta mapigo ya moyo wake yakianza kwenda mbio.

    Ni kweli alikuwa anaumwa na dawa alizopewa na mganga Shiwinga zilimlevya sana lakini kitendo cha kukumbatiwa na Samantha, kilimfanya ajihisi kama tayari ameshapona. Wakabaki kutazamana usoni huku kila mmoja akizisikiliza pumzi za mwenzake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Nakupenda sana Edmund, sijawahi kupenda kama ninavyokupenda wewe, tafadhali naomba nisamehe kwa yote yaliyotokea,” alisema Samantha kwa sauti ya kudeka huku akianza kulengwalengwa na machozi, Edmund hakumjibu kitu zaidi ya kumbusu kwenye paji lake la uso, kitendo kilichomfanya msichana huyo mrembo asisimke mwili mzima.

    Mganga Shiwinga aliyekuwa amesimama hatua kadhaa akiwatazama, aliishiwa cha kuzungumza, kwa akili za kiutu uzima ikabidi akohoe kidogo na kutoka nje, akawaacha wawili hao bado wamegandana kama ruba.

    “Niambie kama umenisame...” alisema Samantha lakini alishindwa kumalizia kauli yake, wawili hao wakajikuta wamegusanisha ndimi zao na kuanza kuelekea kwenye ulimwengu wa tofauti, kila mmoja akionesha kuwa na hisia nzito juu ya mwenzake.

    Muda mfupi baadaye, walijikuta wakiwa juu ya kitanda cha kamba alichokuwa amelala Edmund muda mfupi uliopita. Usingeweza kudhani kwamba Edmund alikuwa anaumwa kwa jinsi alivyoonesha ushirikiano.

    Kama isingekuwa nguvu za giza zilizokuwa ndani ya mwili wa msichana huyo, huenda wawili hao wangefika mbali zaidi na kuvuka mipaka lakini Edmund alipokumbuka kilichotokea mara ya mwisho alipojaribu kukutana kimwili na Samantha, alijikuta akiwa mpole ghafla.

    “Kweli unanipenda Samantha?” aliuliza Edmund kwa sauti ya chini, msichana huyo akaitikia kwa sauti ya kunong’ona na kumueleza Edmund kwamba anajishangaa nini kilichomtokea kwa sababu hajawahi kuhisi hali hiyo hata siku moja tangu azaliwe.

    “Babu Shiwinga amesema hatuwezi kuwa pamoja kutokana na nguvu zako vinginevyo nitapatwa na madhara makubwa zaidi.”

    “Hata mimi nimezungumza naye na kuna mambo tumeshakubaliana. Nimechoka kuwa mtumwa Edmund, na mimi nataka nijisikie kama mwanamke niliyekamilika, nipo tayari kwa chochote,” alisema Samantha kwa sauti iliyoonesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

    “Edmund! Muda wa kunywa dawa umefika,” mganga Shiwinga alikatisha mazungumzo ya wawili hao, wote wakajivuta kichovu na kuamka huku Samantha akiendelea kuonesha waziwazi hisia nzito za kimapenzi alizokuwa nazo kwa Edmund.

    “Na wewe Samantha inabidi urudi nyumbani ili baba yako asije akashtukia, inabidi ujue namna ya kula na kipofu,” alisema mganga Shiwinga kwa msisitizo. Ikabidi Samantha akubali kwa shingo upande kuondoka lakini kabla hajaondoka alitaka mganga ampe maelekezo ya nini cha kufanya.

    “Nikizitazama nyota zenu naona kuna tofauti kubwa sana, Edmund nyota yako inang’ara sana na wewe Samantha nyota yako ina giza nene, hamuwezi kuoana mpaka nyota zenu ziwe zinashabihiana kwa hiyo kabla ya kukutoa hizo nguvu zako inabidi kwanza tufanye kazi ya kutafuta uwiano wa nyota zenu.”

    “Tutafute uwiano kivipi? Sijakuelewa babu.”

    “Inabidi nyote muanze kufanya ‘meditation’.”

    “Meditation? Ndiyo nini?” Edmund aliingilia kati mazungumzo hayo huku naye akionesha kutoelewa kabisa kilichokuwa kinazungumza na mganga Shiwinga.

    Licha ya kuwa mganga huyo alikuwa akitibu kwa mitishamba na dawa za kienyeji kama walivyo waganga wengine, ndani ya muda mfupi tu ambao Edmund alikuwa amekaa naye, aligundua kwamba mzee Shiwinga alikuwa na kitu kingine kikubwa zaidi ambacho pengine ndicho kilichokuwa kinamfanya ajiamini kiasi hicho.

    “Mtaelewa tu wala msiwe na wasiwasi, meditation ni neno la Kiingereza ambalo linamaanisha tahajudi kwa Kiswahili. Kwa kifupi, ni kitendo ambacho mtu anakaa kwenye mkao maalum na kutafuta utulivu wa mwili na akili, ukishaweza kukaa na kutulia kwenye meditation, unakuwa na uwezo wa kuwasiliana moja kwa moja na roho yako.”

    “Kuwasiliana na roho? Mbona sikuelewi babu?”

    “Ni vigumu kunielewa lakini ninachotaka kuwaambia ni kwamba kila mtu, awe anajua au hajui, anazalisha nguvu ambazo ndiyo zinazofanya aendelee kuishi.

    “Hakuna anayejua moja kwa moja nguvu hizo zinazalishwa wapi ndani ya mwili wa binadamu lakini baadhi ya watu husema kwamba zinazalishwa kwenye kile ambacho tumezoea kukiita roho,” alisema mganga Shiwinga na kuwachanganya kabisa Edmund na Samantha.

    “Ili kuwasiliana na roho yako, siyo lazima uwe mchawi au uwe muumini wa jamii za siri au umuabudu shetani kama wengi wanavyoamini, ukifanya meditation tu utaona matokeo yake.

    “Na ukiweza kuwa unawasiliana na roho yako mara kwa mara, utakuwa na uwezo wa kuchagua ni nguvu gani unazalisha na hizo ndiyo zinazoweza kufanya nyota yako ing’ae au ififie, uishi maisha ya kimaskini au ya kitajiri, ufanikiwe au ufeli, kimsingi nguvu hizo ndiyo zitakazoamua maisha yako yaweje.

    “Tatizo ambalo nyote wawili mnalo, linaanzia kwenye roho zenu, ni lazima nilishughulikie hilo kwanza kabla ya mambo mengine yote. Ni safari ndefu lakini nawahakikishia mkiweka juhudi za kutosha, mtaanza kujitambua ninyi ni akina nani na kwa nini mmeletwa duniani,” alisema mzee Shiwinga, wote wakashusha pumzi ndefu na kutazamana. Ilikuwa ni elimu mpya kabisa kwao.

    “Pengine hamjanielewa, hivi nikiwauliza swali jepesi tu, nianze na wewe Edmund, mtu akikuuliza wewe ni nani utamjibu nini?”

    “Aah! Babu mbona swali jepesi hilo? Mimi ni Edmund.”

    “Mnaonaa? Hilo ni swali jepesi lakini lenye maana kubwa ambalo ni wachache sana wanaoweza kulijibu. Wengi tunaamini kwamba sisi ni hii miili yetu tunayoiona lakini ukweli upo tofauti kabisa ndiyo maana nataka mjifunze kwanza kufanya meditation kisha mengine yatafuatia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Natamani kuwaona mkioana na kuishi kwa amani kama mume na mke lakini kuna vikwazo vingi sana katikati yenu ambavyo vinahitaji nguvu za ziada kuvivuka,” alisema mganga Shiwinga lakini kabla hajamalizia, wote walishtushwa na muungurumo wa pikipiki iliyokuwa inakuja kwa kasi nyumbani kwa mganga huyo.

    “Mungu wangu, siyo baba huyo?” alisema Samantha kwa mshtuko mkubwa.



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog