Search This Blog

JINI WA KUZIMU - 5

 





    Simulizi : Jini Wa Kuzimu

    Simulizi : Safari Ya Kuzimu

    Sehemu Ya Tano (5)



    ILIPOISHIA JANA......

    Mtu yule alikuwa akitoa nje ulimi wake mrefu ambao ulikuwa ukiwaka moto. Macho yake matatu yaliyokuwa yakiwaka kama tochi hayakufumba hata kwa sekunde moja. Yasini alitaka kumuamsha Husna lakini akabaini kuwa alikuwa pekeyake, Husna hakuwepo kitandani.

    SASA ENDELEA.......

    Yule mtu alinyoosha mkono na kutaka kumshika, lakini Yasini alipoteza fahamu na kutojua nini kiliendelea.

    Saa mbili Yasini alihisi mtu anamshika, alipofumbua macho akakutana na macho ya Husna. Aliurusha mkono wa Husna na kushuka kitandani huku akihema mfurulizo. Alimkodolea macho ya woga.

    “vipi Yasini una tatizo mpenzi?”

    “aa..a.ah..sina”

    “sasa mbona hivyo?”

    “Hapana nipo safi tu”

    “Najua kinachokusumbua”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “nini?”

    “leo usiku umeona vitu vya ajabu kwako au sio?”

    “umejuaje?”

    “hao ni walinzi wametumwa na baba kukuchunguza kama ni mwema kwangu”

    “sasa wamegundua nini?”

    “hakuna baya waliloliona, hivyo wamekubali wewe uwe hapa kwangu”.

    Baada ya mazungumzo hayo walikwenda mezani na kukuta kifungua kinywa kimekwishaandaliwa na Nyamizi. Walikunywa huku wakiendelea na mazungumzo ya hapa na pale. Husna alimwambia Yasini kuwa siku hiyo angependa kumtembeza katika maeneo mbalimbali ya Kuzimu. Yasini bila hiyana alikubaliana na Husna. Alikuwa na hamu kubwa ya kuijua vizuri sehemu ile. Husna alinyanyuka na kumuacha Yasini ameketi mezani. Yasini naye alikwenda kwenye mlango wa nje na kusimama akiangalia mazingira. Akavuta hatua mojamoja kuelekea kwenye bustani ya maua. Alipokaribia akamuona mtu aking’oa magugu kwenye ile bustani. Alipomtazama vizuri akabaini kuwa alikuwa ni Nyamizi. Akamsogeleaa na kusimama nyuma yake.

    “Nyamizi” Yasini aliita.

    Nyamizi alishtuka na kugeuka nyuma. Hakutegemea kumkuta Yasini maeneo yale. Wakabaki wakitazamana kwa sekunde kadhaa pasipo kuzungumza kitu chochote. Ndipo Nyamizi akavunja ukimya.

    “Yasini nateseka sana kwaajili yako. Mwambie mwanamke wako anisamehe mimi siwezi tene kuolewa na wewe” baada ya maneno yale Nyamizi aliinama na kuendelea na kazi. Yasini akainamisha kichwa chini pasipo kijibu kitu chochote. Alimuonea huruma sana Nyamizi kwani alishafahamu jinsi anavyoteseka. Alikumbuka Nyamizi alivyokuwa akitingisha mtaa wa kimara. Wanaume walikuwa wakipishana kupeleka posa lakini aliwakataa wote kwaajili ya kutaka kuolewa na Yasini. Hata kwa wakati huo ingawa alikuwa amechoka sana alikini bado uzuri wake ulishindwa kujificha.

    “nyamizi” Yasini aliita. Nyamizi aligeuka na kumtazama usoni. Yasini akataka kuzungumza kitu likini alikatizwa na sauti ya Husna

    “kuna nini kinachoendelea na huyo Malaya?”

    “hakuna kitu Husna, nilikuwa natazama bustani tu” Yasini alijibu

    “mmeanza kufuatana sio?... subiri nikirudi huyo Malaya atanitambua” Husna aliongea kwa jazba. Yasini alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kumbembeleza na hatimaye akapoa. Walikwenda ndani na kujiandaa tayari kwa kutoka. Baada ya dakika kadhaa walitoka wakiwa wamependeza mno. Walipofika nje wakamkuta Nyamizi akiosha ukuta wa Nyumba.

    “wewe mshenzi sisi tunatoka, tukirudi nikute kazi zote umemaliza sawa?”

    “sawa dada” Nyamizi alijibu kwa woga. Wakati wote huo Yasini alikuwa akimtazama Nyamizi kwa huruma lakini hakuwa na la kufanya. Husna alimshika Yasini mkono na ghafla wakatoweka machoni mwa Nyamizi.

    Kufumba na kufumbua Yasini na Husna walikuwa wamesimama chini ya mbuyu. Yasini hakufahamu jinsi walivyofika pale. Kwa mbali walisikia sauti za watu wakilia.

    “Husna huko kuna nini?”

    “usiwe na haraka mpenzi tunakwenda hukohuko” alisema Husna huku akivuta hatua kuelekea kule kulikokuwa kunatokea zile kelele za vilio. Kwa mbele kulikuwa na jengo kubwa sana lililojegwa kwa vioo kuanzia chini hadi juu. Wakaingia kwenye jengo hilo lililokuwa na vyumba vingi. Wakasimama nje ya chumba kimoja na kutazama yaliyokuwa yakiendelea mle ndani. Yasini hakuweza kuamini macho yake. Aliwaona wanawake wengi sana wamefungwa nywele zao kwenye vigogo vya chuma na chini moto mkali uliwaunguza. Yasini aliwaonea huruma wale wanawake waliokuwa wakiungua kama kuni mle ndani.

    “kwanini watu hawa wanaungua hivi?”

    “hawa ni wale wanawake waliokuwa wakitembea vichwa wazi enzi za uhai wao”

    alisema Husna.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “inamaana hawa watu wameshakufa?”

    “ndio, na hapa ndipo wafu wote wanaishi”

    “walikuwa wanaishi wapi enzi za uhai wao?”

    “hawa ni binadau. Hivyo walikuwa wakiishi duniani” alisema Husna na kumshika Yasini

    mkono na kumvutia chumba cha pili. Walipofika huko nako wakakuta mambo vilevile. Lakini humu mlikuwa na mchanganyiko wa wanawake na wanaume. Walikuwa wamevutwa ndimi zao na kurefuka hadi chini huku moto mkali ulikuwa ukiwaunguza.

    “na hawa nao vipi?”

    “hawa ni waramba visogo”

    “waramba visogo ni watu gani?”

    “ni wale ambao walikuwa wakiwasengenya wenzao”.

    “kwahiyo adhabu zinatofautiana kutokana na makosa ya mtu”

    “kama unavyoona”

    “na wazinzi nao wana adhabu gani?”

    “wapo huko mbele utawaona” Husna alisema maneno yale huku wakielekea chumba

    kilichofuata.



    Chumba hicho kilikuwa ni kirefu mno. Watu walikuwa wamefungwa minyororo huku wakiburuzwa na farasi. Watu wale walikuwa wakilia kwa uchungu huku wakizungumza maneno ambayo hayakusikika vizuri.

    “hawa ni wale waliokuwa wakizurumu mali za wenzao”

    “inamaana na wale farasi nao wana makosa”

    “hapana”

    “mbona na wenyewe wamo kwenye moto?”

    “ Farasi wale wamepewa uwezo wa kutoungua. Moto ule ni kwaajili ya binadamu tu”.

    Husna alianza kupiga hatua kuelekea mbele ambapo Yasini naye alimfuata kwa nyuma. Wakati wakiendelea na ziara yao walifika kwenye chumba kilichokuwa na watu wenye matumbo makubwa yaliyokuwa yakiwaelemea. Moto mkali uliwatafuna kwa uchu mkubwa. Yasini alizidi kushangazwa na matukio kwenye lile jumba.

    “sasa na hawa wana makosagani?”

    “wale wanaokula rushwa na riba ndio wanastaili adhabu kama hii”

    “mungu wangu! laiti wala rushwa wangeifahamu adhabu hii kamwe wasingethubutu”

    “sio kama hawafahamu. Wengi hawaamini maisha ya baada ya kifo na ndiomaana

    wanafanya mambo kwa makusudi kabisa huku wakijua wanafanya makosa”

    Chumba cha tano kulikuwa na watu waliokuwa na sehemu za siri kwenye nyuso zao. Wanawake walikuwa na sehemu za kiume wakati wanaume walikuwa na sehemu za kike. Kwenye mikono yao kulikuwa na makucha marefu ya shaba. Walitumia makucha hayo kujirarua kwenye miili yao bila kujionea huruma. Pamoja na hilo pia moto mkali ulikuwa ukiwasanifu. Makelele mengi waliyoyatoa hayakuweza kuwa dawa ya kuutuliza moto ule usitekeleze jukumu lake.

    “unawaona hawa Yasini?”

    “ndio”

    “hawa ndio wale wazinifu uliokuwa unataka kujua adhabu yao”

    “kwanini adhabu hizi zisingewekwa wazi kule duniani ili watu wawe makini na matendo

    yao?”

    “mungu amefanya hivi kwa makusudio yake. Hatuwezi kumpangia”

    “naamini watu wangekuwa wanakuja japo mara moja tu kisha warudi Duniani,

    wasingekuwa wanafanya makosa”.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “hiyo sio sababu. Kuna watu kila siku wanakuja lakini hawaachi dhambi zao”

    “kuna watu wanakuja huku kilasiku?”

    “ndio. Kwamfano wachawi wanapenda sana kuja huku lakini hawaachi dhambi zao”

    “kama ndio hivyo hao watu ni waajabu”. Yasini alisema maneno hayo na kumtaka Husna

    angeendelea angezidi kuumia moyo kwakuwa alikuwa akiwaonea huruma watu wale waliokuwa wakiadhibiwa.

    * * *

    Zilikuwa zimekwishakatika siku tano tangu Yasini alipofika kuzimu. Tayari alikuwa amekwishaanzakuzoea mazingira ya maeneo yale. Yasini alikuwa amelala mapajani mwa Husna kwenye bustani ya maua wakipunga upepo.

    “Husna” Yasini aliita

    “unasemaje mpenzi wangu”

    “Ninajambo nataka nikueleze Lakini kama nitakuudhi naomba unisamehe”

    “usiwe na wasiwasi we nieleze tu mpenzi”

    “unafahamu kuwa wewe ni binadamu na sio jinni?”

    “nalijua hilo. kwani vipi?”

    “kwanini huna roho ya kibinadamu?”

    “unamaana gani?”

    “hupaswi kuwatesa binadamu wenzako”

    “bado sijakuelewa Yasini”

    “ninaomba umwache huru nyamizi” maneno yale ya Yasini yalimfanya Husna kuinamisha kichwa chini pasipo kujibu kitu chochote. Alibaki hivyo kwa sekunde kadhaa kisha akatoa tamko.

    “nakupenda sana yasini, lakini suala hilo niachie mimi”

    “Husna Kuwa na utu. msamehe Nyamizi”

    “inaonekana unampenda sana Nyamizi enhee?”

    “hapana Husna, ukweli ni kwamba kila ninapomuona najikuta nafsi inanisuta”

    “kwahiyo umefurahishwa na kitendo walichotaka kunifanyia”

    “hata kidogo. Ila hata Mungu anasema samehe saba mara sabini”

    “usitake kunichanganya. Hata wewe unaweza kuwa kama yeye vilevile” Husna alifoka

    “fanya unavyoweza Husna. Lakini sipo tayari kumuona mtu anateseka kwaajili yangu”

    “ahaa! Naona umeshaota mapembe si ndio?” Husna alisema maneno hayo kwa jazba na

    kuanza kujinyoosha viungo vya mwili wake. Alivutika mithili ya mpila wa manati, akaongezeka urefu huku macho yakimtoka kama ya kinyonga. Alibadilika rangi na kuwa mweusi tii, miguu ikatoweka, mikono nayo ikatoweka, kichwa kikabadilika na kuwa kichwa cha nyoka kilichotoa ulimi mithili ya nyoka aliyeona panya. Kiufupi alibadilika kabisa na kuwa chatu. Yasini akakumbuka kuwa chatu Yule alishawahi kukutana naye maeneo ya mzizima siku aliyokwenda kuchukua pesa za masomo.





    Yule nyoka alianza kuondoka na kuelekea ndani kwa Nyamizi. Yasini aligundua kilichokuwa kikitaka kutokea. Akakimbilia kule Yule nyoka alikokuwa akielekea.

    Nyamizi alikuwa akichimba shimo la takataka. Pasipo kutegemea, alipigwa ngwara na kudondoka chini. Yule nyoka alikwishafika na kumzongazonga. Yasini naye alikamata jembe alilokuwa akilitumia Nyamizi kuchimbia shimo na kulinyanyua kutaka kumpiga yule nyoka, lakini alilitupa chiini baada ya kugundua kuwa alikuwa ameshika nyoka mwingine badala ya jembe. Aliangalia pembeni na kuona panga, hakutaka kuchelewa alilichukua na kumrushia Yule nyoka lakini panga lilipinda na kwenda kukita kwenye mti uliokuwa pembeni kabisa. Nyoka Yule alivimba na kufunua mdomo tayari kwa kummeza Nyamizi. Ghafla alibadilika na kuwa katika umbo la binadamu. Kumbe Yasini aliona pete iliyokuwa kwenye mkia wa Yule nyoka na kuichomoa.

    “Husna unataka kufanya nini?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “unajifanya mjanja sio?”

    “sio ujanja nataka kukuonesha namna binadamu wanavoishi”

    “haya nipe pete yangu haraka”

    “pete sikupi hadi utakapokubali kumsamehe Nyamizi”

    “usitafute matatizo kijana”

    “liwalo na liwe lakini lazima haki itendeke”

    “nakupenda sana Yasini tafadhali nipe pete yangu” alisema Husna kwa umakini wa hali ya juu ingawa yasini hakuonesha kushituka wala kutishwa na maneno yale. Aliamini kuwa Husna hakuweza kufanya jambo lolote baya pasipokuwa na ile pete, kumbe haikuwa hivyo. Yasini alishitukia mtu anampiga kofi kali lililomfanya adondoke chini. Alipoinua kichwa akakumbana na Yule mtu aliyemjia sikumoja usiku mwenye rangi nyingi zilizokuwa zikiwakawaka kama taa. Mtu Yule alianza kutoa sauti za kutisha. Akataka kumshika Yasini lakini Husna alimzuia

    “hapana huyu niachie mimi” alisema Husna huku akichukua pete kutoka kwa yasini ambaye kwa wakati huo alikuwa amelala chini. Hakuleta kiburi tena kama mwanzo, akamwachia Husna achukue pete yake. Baada ya hapo Husna alimwashilia Yule mtu mkubwa wa umbo na mwenye kutisha kuondoka maeneo yale, na mtu Yule akatoweka. Husna alianza kucheka kwa sauti huku akiwaangalia kwa dharau Nyamizi na Yasini.

    “mnajifanya wajanja sio. Hii ni himaya yangu hakuna wa kunizuia kufanya lile nitakalo. We Malaya! Sasa nakupa adhabu nyengine. Naona hii haikufai” Alisema Husna huku akimnyooshea kidole Nyamizi. Nyamizi alibadilika na kuwa katika umbo la sokwe. Jambo lile lilizidi kumtia hasira Yasini.

    “Husna chagua moja. Kuwa na mimi au kuniua” Yasini aliongea kwa sauti ya chini iliyosheheni chembechembe za upole.

    “Siwezi kumuua mtu ninayempenda hata siku moja”

    “sasa kama kweli unanipenda fanya ninachotaka”

    “nifanye nini?”

    “mwache huru Nyamizi”

    “lakini Yasini unafahamu kuwa Nyamizi ni adui yangu”

    “Pamoja na hayo lakini unapaswa kusamehe”

    “siwezi Yasinii”

    “Husna naomba uniue na mimi. Kama una roho kama hiyo sitaweza kuvumilia” maneno ya Yasini yalimchoma sana Husna. Aliinamisha kichwa chini na kufikiri kwa makini. Alipoinua kichwa alimnyooshea yamizi kidole. Nyamizi alibadilika tena na kuwa binadamu. Alimsogelea taratiibu huku akimtazama usoni.

    “Nyamizi upo huru sasa. Utaishi na mimi kama dadaako” alisema Husna.

    Nyamizi hakuyaamini kabisa maneno yale kutokana na jinsi Husna alivyokuwa akimchukia. Aliamini kuwa Husna aliongea vile ili kumfurahisha tu Yasini lakini hayakutoka moyoni mwake. Husna alitanua mikono na kumkumbatia Nyamizi.

    “nashukuru sana dada Husna Mungu atakubariki” nyamizi alisema.

    “usijali” alijibu Husna na kumgeukia Yasini.

    “haya baba sema jengine”

    “sina usemi”

    “nina ombi”

    “jee?”

    “ leo twende tukawaone wazazi wangu”

    “MAJINI?”

    “hao ndio wazazi wangu”

    “dah! Hii sasa kali”

    “vipi, hutaki?”

    “sio hivyo. Lakini siunajua vitimbi vya majini. Wewe tu unanitoa jasho”

    “kwani wewe ni mgeni wa vitimbi vya hapa kuzimu?”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “usiongee mengi mama nimekubali” alijibu Yasini huku akimkumbatia Husna.

    Waliingia ndani na kuanza kujiandaa. Walipotoka walikuwa wamependezana kama mapacha. Nyamizi alipowaona aliwasifia lakini moyo wake ulimuuma sana. Hakutaka kuamini kama mwanaume aliyempenda kwa dhati ndiye Yule aliyekuwa mbeleyake na mwanamke mwengine, tena jini. Alitamani siku zingejirudia ili afunge ndoa mapema kabla hajapendwa na Husna, lakini zilibakia ndoto tu. Pamoja na kuwa Husna alikuwa ni jini lakini mapenzi yalimfanya Yasini awe kipofu na kuamini kuwa Husna ndiye chaguo lake, na Nyamizi ni chagua la wazazi wake.

    Kama kawaida yao Husna alimshika Yasini mkono na kuanza kupaa. Walitua kwenye mlango wa pango kubwa sana. Nyamizi akapaza sauti ya kubisha hodi lakini hakuna aliyewajibu. Waliingia kwenye pango na kutokomea ndani. Michoro ya kutisha ilikuwa imezipamba kuta za pango lile.

    “yasini naomba usiogope kwa chochote tutakachokutananacho”

    “mnh! Mbona unanitisha sasa”

    “amna. Ni akiba tu ya maneno”

    “ah! Hata hivyo nimeshaanza kuzoea vituko vyenu”

    “namimi nilifanya makusudi ili unizoee”

    “ila usizidishe bwana mi ntakuogopa”

    “usijali, sitakufanyia tena vitu vya ajabu”.

    kila walivyozidi kusonga mbele giza nalo lilizidi kuongezeka. Husna alipiga makofi na moto uliowaletea mwanga ukawaka kwenye kuta za pango. Alichomoa mwenge mmoja kutoka ukutani na kuufanya kama taa. Popo wengi waliruka hapa na pale huku wakiimba kwa lugha yao ya kipopo. Sauti za bundi nazo hazikusita kuwaburudisha wapenzi wale. Paka wawili weusi waliokuwa na ukubwa wa mbuzi dume aliyekomaa walikuwa wamesimama katikati ya njia.

    “tupisheni tupite” Husna aliwatamkia lakini hawakuondoka bali walizidi kuwakodolea macho yao makubwa kama machungwa. Husna aliinua mkono wake wa kushoto na kuwanyooshea kidole kilichokuwa na pete na paka wale wakatoweka ghafla machoni mwao. Husna alimshika Yasini mkono na kuendelea na safari. Lakini baada ya hatua kadhaa wakamkuta mtu wa ajabu amesimama njiani. Mtu Yule alikuwa na miguu mitatu, macho matatu, na vichwa viwili vilivyokuwa na mapembe marefu. Kwenye mikono yake iliyokuwa na vidole vyenye kucha ndefu alishikilia upinde na mkuki.

    “niwasaidie nini?”

    “tunataka kupita”

    “ninyi ni nani?”

    “mimi ni Husna”

    “na huyo ni nani”

    “huyu ni mchumbaangu”

    “mbona ni binadamu?”

    “hayo hayakuhusu. Kazi yako wewe ni kulinda geti. Turuhusu tupite” aliongea Husna kwa sauti ya ukali kidogo. Yule mtu alipokumbuka kuwa alikuwa anaongea na mtoto wa mkubwa akawafungulia geti haraka wapite huku akiamini kuwa mwisho wa kijana Yasini ulikuwa umefika. Alitamani sana kumzuia asiingie mle ndani lakini hakuwa na mamlaka hayo. Hivyo akamwangalia Yasini kwa masikitiko makubwa.

    Ndani ya lile geti kulikuwa na uwanja mkubwa sana na jumba zuri la kifahari lilikuwa limekalia uwanja ule. Husna alifika na pasipo kubisha hodi akafungua mlango. Waliingia ndani na kufikia sebleni. Walikaa hapo kwenye makochi kwa muda mrefu lakini hapakuonesha dalili ya kuwepo kwa mtu mwingine zaidi yao wenyewe mle ndani. Jumba lilikuwa limepooza mno. Hali ile ilimfanya Yasini ahoji juu ya kuwepo au kutokuwepo kwa wazazi wa Husna mule ndani. Husna alimtaka asiwe na haraka na kumfahamisha kuwa muda si mrefu wangefika.

    Upepo mkali ulianza kuvuma na kusababisha milango ya ndani mle kujibamiza hovyo. Yasini akakumbuka jinsi Husna alivyokuwa akimuingilia chumbani kwake ulikuwa ukitangulia kwanza upepo mkali. Hivyo akabaini kuwa sasa ndio wazazi wa Husna walikuwa wanakuja. Kichwani mwake alijaribu kuvuta taswira jinsi majini hao walivyofanana lakini hakupata picha halisi. Alijituliza na kusubiri kile ambacho kingetokea.

    Sauti za viatu vyenye visigino virefu zilisikia zikielekea kule sebleni…

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Sauti zile zilifika hadipale sebleni na kutulia, lakini Yasini hakumuona mtu yeyote zaidi ya Husna. Baada ya sekunde kadhaa sauti zile zilisikika zikirejea kule zilikotoka. Punde zilipokoma mlango wa chumbani ukafunguliwa na mtu aliyekuwa amevaa baibui jeusi alitokea. Baibui la mtu Yule lilikuwa limemfunika mwili mzima na kubakisha macho tu. Macho yenyewe yalikuwa ni makubwa meusi yaliyoshindwa kuonesha dalili ya kuwepo kwa mboni. Mtu Yule alifika na kuketi kwenye sofa moja pale sebleni.

    “hamjambo?”

    “hatujambo shikamoo mama” Husna na yasini walimsalimia lakini mwanamke Yule hakuitikia. Mlango wa chumbani ukafunguliwa tena na mtu mwengine alitoka. Alikuwa ni mwanaume mnene na mweusi kupitiliza. Pua yake kubwa kama ngumi iliendana na macho yaliyokuwa yaking’aa kama nyota ya jaha. Mtu Yule alifika na kuketi sebleni.

    “shikamoo baba” Husna na Yasini walimsalimia mtu Yule lakini naye hakuitikia salamu ile. Alitulia na kumtazama yasini kwa macho yaliyojaa udadisi.

    “baba….., mama…., huyu ndiye Yasini niliyekuwa nikiwaambia” alisema Husna.

    “kijana, tupo tayari umuoe binti yetu. Lakini hatupo tayari akaishi Duniani…. Sawa?” alisema mzee Masudi na kuwafanya Husna na Yasini kushtuka. Yasini hakujibu kitu bali aligeuza shingo na kumtazama Husna machoni.

    “lakini baba…..” Husna alitaka kuongeakitu

    “nimeshasema mtaishi hapa hapa Kuzimu. Na kama mkikaidi amini nawaambia kamwe hamtafunga ndoa” mzee Masudi aliongea kwa msisitizo na kumeza funda la mate kisha akaendelea kuzungumza.

    “nendeni na mrudi hapa siku ya ijumaa. Nataka nikakuoneshe wazazi wako huko Duniani. Na baada ya kuwaona mtarudi kuishi hapa Kuzimu”

    Husna na Yasini walisimama na kutoka nje. Walianza safari ya kurudi nyumbani kwa Husna. Yasini alikuwa amechanganywa sana na habari ile ya kuishi kuzimu. Hakuwa tayari kuishi kuzimu kama mfu ama jini. Aliwapenda sana wazazi wake. Hivyo moyoni akajisemea kuwa siku atakayofika duniani asingekubali kurudi kwa mara nyingine kuzimu.

    Walipofika nyumbni kwa Husna walimkuta Nyamizi amepumzika kwenye moja ya makochi yaliyokuwa mle ndani. alipowatazama Yasini na Husna usoni alibaini kuwa hawakuwa sawa, nyuso zao zilionesha kutokuwa na matumaini kabisa.

    “vipi dada kuna tatizo?” Nyamizi alihoji huku akiwa bado anamuogopa Husna.

    “hakuna kitu. tumechoka tu” Husna alijibu huku akielekea chumbani ambako Yasini naye alimfuata.

    “kwahiyo Yasini nini kinaendelea”

    “kwakweli bado sijajua cha kufanya”

    “unajua kuwa leo unatakiwa kurudi duniani”

    “ndio lakini na wale wazee wanataka kuniona siku ya ijumaa. Unadhani itakuwaje?”

    “na kama hutokwenda leo ujue mganga aliyekuleta huku atapata matatizo”

    “na kama nikiondoka leo na mimi nitapata matatizo”

    “kwahiyo unasemaje?”

    “nitakwenda wiki ijayo”

    “na Nyamizi itakuwaje?”

    “kama inawezekana mwache atangulie”

    “sawa” Husna alijibu na kusimama kuelekea sebleni.

    Alimfahamisha Nyamizi kuhusu suala la kurudi Duniani. Nyamizi hakuweza kuamini juu ya yale aliyoyasikia kutoka kwa Husna. Alijikuta akijawa na furaha isiyo kifani. Kwa mara ya kwanza alimfuata Husna na kumkumbatia. Ila Husna alimuonya nyamizi kutoongea kwa mtu yeyote juu ya mambo aliyoyaona kuzimu. Pia alimuonya kusema kwa mtu kuwa yasini alikuwa Kuzimu. Na kama angejaribu kufanya kinyume na hayo basi adhabu ambayo angeipata ingekuwani mara mbili ya ile aliyoionja. Nyamizi alikubaliana na masharti yale na aliahidi kutoyavunja.

    “vipi upo tayari uondoke sasahivi?”

    “ndiyo dada nipo tayari”

    “Haya fumba maho” .

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nyamizi akafumba macho huku Husna akiwa amemshika bega la kushoto. Alipoondoa ule mkono tu Nyamizi alitoweka mle ndani na kuwaacha Husna na yasini.

    @*@*@

    kwa upande wa msitu wa Gabushi nako mambo yalizidi kuwa magumu kwa watu wale watano. Mama Nyamizi aliendelea kumkumbatia mwanamke Yule kwa woga huku akitetemeka. Wingi wa wachawi wale ulimchanganya sana. Walionekana kuwa na hamu kubwa ya kuwakamata na kuwala nyama.

    “hawa watu tunao hapahapa” alisema Yule mchawi aliyekuwa amemuegemea mzee

    Angumbisye.

    “ni lazima tuondoke nao” mchawi mwingine alidakia

    “na tutawala nyama leo hii”.





    “mimi nitaomba mnipe moyo kwasababu wamenisumbua sana” mzee mwingine akatoa hoja.

    “moyo nitakula mimi kwasababu ndio nahangaika sana” mwengine akadakia

    “kwa kawaida moyo wanakula wakubwa wa kikundi. Sasa ni mimi nitakayekula moyo” alisema

    Yule mzee wa muheza.

    “haiwezekani, sikuzote moyo huliwa na wale wenye idadi kubwa ya kutoa sadakana hakuna anayenifikia, hivyo moyo nitakula mimi” maneno ya mchawi huyu aliyekuwa na idadi chache ya meno yalizua utata baina yao wenyewe. Kila mmoja alitaka yeye ndiye angekula moyo. Timbwili hilo liliendelea hadi kupelekea baadhi ya wachawi kupanda nyungo zao na kukimbia kuelekea kwenye kijiji chao cha Gambushi. Wale wengine walivyoona wakubwa wao wanakimbizana nao wakawafuatia nyuma. Mzee Angu na mkewake pamoja na wale wanawake watatu walibaki salama. Hakuna aliyeamini kwa kile kilichotokea.

    “hii dawa imetulinda. Vinginevyo wangetuona na kutudhuru” alisema mwanamke mmoja.

    “inamaana hawakutuona?” alihoji mzee Angumbisye

    “hakuna aliyetuona. Lakini kama wasinge gombana wangetuona kwasababu Yule mzee

    aliyekuwa amekushika ananguvu kuliko dawa yetu”

    “sasa tunafanyaje?” mzee Angu alihoji .

    “inabidi nyie mtuache kwasababu sisi tunaelekea Kondoa. Ila msisahau kufikia kwa viongozi wa dini wanaweza kuwasaidia tatizo lenu” alisema mwanamke mwengine.

    Mzee Angu alimshika mkono mkewake na kunuia kufika Tanga mjini. Walianza kupaa kuelekea angani. Baada ya dakika kadhaa walijikuta wakitua nje ya msikiti wa MUJAHIDINA uliokuwepo Tanga mjini. Nyumba ya Shekhe wa msikiti huo ilikuwa hatua chache kutokea msikitini. Wakaongoza mojakwamoja hadi kwenye nyumba ile na kubisha hodi. Kwa bahati nzuri walimkuta shekhe nyumbani kwake. Wakaeleza matatizo yao yote kwa shekhe yule.

    “kwanini mliamua kwenda kwenye ushirikina wakati Mungu yupo?” alihoji shekhe Alhaji. Mzee Angu na mkewake waliinamisha vichwa vyao chini kwa aibu.

    “mmemkosea Allah, inabidi mtubu dhambi zenu kwanza”

    “Tupo tayari Shekhe kutubia dhambi zetu” mzee Angu alijibu

    “haya tamkeni maneno haya…”

    “sawa…”

    “astakafiru Lah! ,astakafiru lah!, astakafiru Lah!”

    “astakafiru Lah!, astakafiru Lah!, astakafiru Lah!” mzee Angu na mkewake walifuatisha maneno yale ya shekhe Alhaji.

    “kwakuwa mmeshatubu tunaweza kuendelea” alisema Shekhe huku akifungua vitabu vyake vya dini na kuanza kusoma Qurani. Mzee Angu na mkewake wakaanza kuwashwa kwenye uso. Kila Shekhe alivyozidi kusoma nao ndivyo walivyozidi kuwashwa. Shekhe aliishangaa hali ile.

    “mmepaka nini usoni?”

    “tumejipaka dawa ya kinga” walijibu huku wakiendelea kuwashwa.

    “hakuna kitu kama hicho kwa Allah” Shekhe alisema na kuchukua maji kwenye jagi na

    kuyasomea dua. Akawapa yale maji wanawe nyuso zao.

    Baada ya hapo shekhe Alhaji akaendelea kusoma Qurani tukufu huku akiomba dua nyingi zilizohusu kupotea kwa nyamizi. Baada ya masaa mawili Shekhe aliwataka waongozane hadi Muheza kwenye makazi ya Mzee Angumbisye.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walipofika Muheza Shekhe aliagiza moto kwenye chetezo. Alipopewa aliweka ubani na kuendelea kupiga dua huku ameketi kwenye mkeka pamoja na watu wengine. Watu wote mle ndani walikuwa wametulia wakisikiliza Qurani ilivyokuwa ikisomwa kama maji ya kunywa. Shekhe alisoma kurani ile hadi machozi yakawa yanamtoka. Yalikuwa yamekwishapita masaa kama manne tangu alipoanza kusoma.

    Sauti ya mtu aliyepiga chafya, ilimfanya Mama Nyamizi kuchungulia nje ili kumuona mtu aliyekuwa akipiga chafya karibu na mlango wa nyumba yake. Mama Nyamizi alipigwa na butwaa. Hakuamini kilichokuwepo mbele ya macho yake.





    “haa mwanangu! ” mama Nyamizi alipaza sauti huku akitoka nje na kufanya watu wengine nao kutaka kujua kilichokuwa kikiendelea kule nje.

    Mama Nyamizi alimkumbatia mtoto wake huku akilia kwa uchungu uliochanganyika na furaha.

    Shekhe alimalizia kisomo chake na kuandika kurani kwa rangi maalumu kwenye karatasi nyeupe kisha akalitia kwenye jagi lililokuwa na maji. Aliwaagiza kuwa maji yale alitakiwa anywe Nyamizi asubuhi na jioni kwa muda wa siku tatu. Baada ya hapo Shekhe aliaga na kuondoka pasipo kuchukua ujira wowote. Ingawa alipewa pesa lakini alikataa katakata.

    @*@*@

    Zilikuwa zimekwishapita siku saba tangu Mganga Ngoma alipomsafirisha Yasini kwenda kuzimu. Mzee Shabani na mke wake walikuwa na hamu kubwa ya kumuona kijana wao akiwa mzima wa afya. Walianza safari ya kuelekea Bagamoyo kwa mganga Ngoma. Lakini walipofika mambo yalikuwa tofauti. Kulikuwa na watu wengi wameizunguka nyumba ya Mganga. Nyumba ile ilikuwa imeteketea kwa moto muda mfupi uliopita. Mganga Ngoma alitolewa akiwa tayari amekwishakufa. Mama jumbe alipouona mwili wa mganga alianguka chini na kupoteza fahamu. Watu walimbeba na kumkimbiza kwenye zahanati iliyokuwepo karibu.

    Fahamu zilipomrejea mzee shabani alimchukua mkewake na kurudi naye Muheza. Mama Jumbe alijitupa kitandani na kuanza kulia huku akijutia maamuzi yao ya kumpeleka mtoto wao kwa mganga wa kienyeji. Wakati mzee Shabani akimbembeleza mkewake akapata wazo la kwenda kwa Shekhe Alhaji ili amsaidie. Alipomshirikisha mkewake jambo lile, mama Nyamizi alimuunga mkono.

    * * *

    Kwenye mida ya saa nne asubuhi Shekhe Alhaji alikuwa amekwishafika nyumbani kwa mzee Shabani. Mzee Angumbisye, mkewake, pamoja na mtoto wao Nyamizi wote walikuwepo. Mzee Shabani alianza kueleza kilakitu kuhusiana na mtoto wao Yasini.

    “kwanini mnapenda ushirikina jamani..Yaani mnafikia kuwazika watoto wenu wakiwa hai? Allah akbar!” Shekhe aliongea kwa masikitiko makubwa.

    Baada ya maneno yale aliwaambia kuwa usiku wa kuamkia siku hiyo alikuwa ameoteshwa ndoto kuhusiana na matatizo yaliyokuwa mbele yao. Aliwaeleza kuwa yule jini aliyekuwa amemchukua Nyamizi hakuwa jini kama wao walivyokuwa wakidhani. Aliwaambia kuwa alikuwa ni binadamu wa kawaida kama walivyo binadamu wengine, isipokuwa alichukuliwa na majini na kulelewa huko ujinini. Akaongeza kuwa binti huyo alipewa pete ya kijini ili afanane na majini wengine. Akamalizia kwa kusema kuwa pete hiyo ndiyo inayomfanya binti huyo kuishi maisha ya kijini.

    “sasa nitasoma dua zitakazo jumuisha na matatizo ya mzee Shabani” aliongea Shekhe Alhaji huku akifungua kimoja kati ya vitabu vyake vya Quran na kuanza kusoma.

    @*@*@

    Husna alionekana kuwa na uchovu sana siku hiyo. Yasini alipoigundua hali ile alihoji juu ya kilichomkuta mpenziwake yule lakini Husna alimjibu kuwa hakuwa na tatizo. Hali ile iliendelea kudumu kwa Husna hadi ilipofika mida ya adhuhuri ndipo uzalendo ukamshinda na kuamua kuzungumza.

    “ unajua kuna kitu kimetokea kule kwa wale wazee”

    “kwanini unasema hivyo?”

    “huwa kukitokea kitu kibaya nyumbani kuna hali naisikia”

    “unadhani kumetokea nini?”

    “sifahamu, lakini hakuna usalama”

    “kwahiyo tunafanyaje”

    “inabidi twende”

    “itakuwa vizuri” .

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Walitoka nje na kuanza safari ya kuelekea mapangoni kwa wazazi wake Husna. Walipofika getini walipigwa na bumbuazi, yule mlinzi mwenye miguu mitatu alikuwa amekufa. Walichukua funguo kutoka kwenye mikono ya yule mtu na kufungua geti. Walipofika ndani wakamkuta kijana wa Dr. Kisonoko amelala uwanjani. Walimuamsha na kumhoji juu ya kilichokuwa kikiendelea pale pangoni. Yaule kijana aliwaeleza kuwa wazazi wa Husna walikuwa wamepigwa na radi.

    Husna na Yasini wakaingia ndani na kuwakuta mzee Masudi na mkewake wamelala sakafuni huku damu zikiwatoka puani na mdomoni. Husna aliwakimbilia na kutaka kuwagusa lakini alirushwa pembeni kama shoti ya umeme. Walianza kuwachunguza pasipo kuwagusa ndipo wakabaini kuwa walikuwa wamekwishakufa muda refu sana. Kitendo cha kufa kwa wale majini Husna alikiona ni kama mkosi kwasababu alitegemea kuwafahamu wazazi wake waliomzaa kupitia majini hayo. Alirudi nyuma na kuanza kulia kwa uchungu.

    “ninani atakaye nionesha wazazi wangu?”

    “usilie Husna, mungu atakuongoza utawafahamu tu”

    “hapana Yasini mimi ninamkosi”

    “usiseme hivyo. We muombe mungu tu” Yasini alimbembeleza na kumtaka waondoke maeneo yale. Walipofika nje wakamkuta kijana wa Dr. Kisonoko amekaa chini huku akisubiri hatma ya maisha yake. Husna alimtazama kijana yule na kuamua kumrudisha duniani kwani hakuwa tena na faida ya kuendelea kubaki kuzimu. Alimuita na kumwambia afumbe macho kama alivyofanya kwa Nyamizi, kijana yule akafumba. Alipomuachia bega tu alitoweka machoni mwao. Baada ya hapo na wenyewe wakatoweka maeneo yale na kujikuta nyumbani kwa Husna.

    “ni lazima tuondoke leo hii kuelekea duniani” alisema Husna

    “sawa”

    “namaanisha sasahivi”

    “kwahio vipi tutarudi au?”

    “wapi?”

    “kuzimu”

    “ kufanya nini?

    “unakumbuka wale Majini walitaka nini?”

    “Liwalo na liwe, Huku sirudi tena”.

    Husna na Yasini walisimama huku wamepeana migongo. Walianza kupaa na kuelekea angani. Yasini hakuweza kufahamu muelekeo wa safari yao. Alichokijua ni kwamba walikuwa wanakwenda Duniani. Giza likaanza kutanda na kuwafunika wasione wanakoelekea…



    Husna alimsihi Yasini asiogope hali ile ni ya kawaida sana. Alimwambia kuwa mpaka wa kuzimu na dunia ni kiza kinene, hivyo kwa wakati ule walikuwa mpakani. Yasini alijisahau na kupitiwa na usingizi.

    Sauti ya Shekhe Alhaji ilimshitua Yasini kutoka usingizini. Walikuwa wamesimama nje ya nyumba yao. Harufu kali ya ubani ilipompiga puani akabaini kuwa kulikuwa na kitu kinaendelea ndani. Alivuta hatua ndogondogo kuelekea mlangoni. Alipochungulia alikutana macho kwa macho na mama Nyamizi.

    “haaa yasini!” aliropoka mama Nyamizi na kufanya watu wote watazame mlangoni. Mama Jumbe alisimama na kwenda kumkumbatia Yasini. Mzee Shabani naye alisimama na kuwakumbatia wote mama jumbe na Yasini. Nyamizi alipomuona Husna aliruka na kwenda kumkumbatia huku akitaja jina lake. Kitendo kile kiliwashangaza sana watu hasa mama Jumbe na mzee Shabani, kwasababu Husna hakuwa mgeni kwao. walifahamu kuwa yeye ndiye aliyekuwa chanzo cha kuvuruga ndoa ya Yasini na nyamizi. Sasa walishangaa kuona jinsi Nyamizi na Husna walivyokuwa wakionesha urafiki. Pia mzee Shabani na mkewake walichokuwa wakikifahamu ni kuwa Husna alikuwa ni jini, hivyo hata alivyofika na Yasini bado walikuwa wakimhofia.

    Shekhe alhaji aliwataka Husna na Yasini waingie ndani kwaajili ya kuendelea na ibada. Husna alikwenda kukaa pamoja na Nyamizi kwasababu Mama jumbe na mzee Shabani walihofu kumsogelea. Shekhe aliandelea kusoma Qurani, safari hii alisoma kwa nguvu zaidi na sauti kubwa. Husna akahisi pete yake inamuunguza mkono. jinsi shekhe alivyozidi kusoma Qurani ile ndivyo ile pete nayo ilivyozidi kumuunguza na kumfanya apige kelele kwa uchungu. Yasini alikwenda kuichomoa ile pete kwanguvu, ikadondoka chini na kuanza kutoa moshi. Husna alinyamaza kulia baada ya kuvuliwa ile pete. Moto ulianza kuwaka kwenye pete na kuteketea kabisa. Hadi kufikia wakati huo Shekhe alikuwa amemaliza kisomo.

    “Mnakumbuka niliwaambia kuna mtoto alichukuliwa na majini?” Shekhe alihoji

    “ndio” watu walijibu

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “sasa mtoto mwenyewe ndie huyu hapa” aliongea Shekhe huku akimnyooshea kidole Husna.

    “na pete niliyowaambia ndiyo hiyo iliyoungua”

    Watu wote waligeuza shingozao na kumtazama Husna kwa huzuni na mshangazo.

    “pole sana binti” mama Jumbe na wengine wote walimpa pole Husna. Husna aliposikia maneno yale alizidi kupata uchungu na kuanza kulia. Mama nyamizi alimsogelea na kumbembeleza.

    Shekhe alimuuliza Husna kama kulikuwa na kitu chochote alichokwa kikifahamu kuhusiana na maisha yake. Husna alianza kuelezea kile alichoelezwa na wale majini kwa kifupi. Alianza kwa kusema kuwa baba yake hakuwa anapenda watoto wa kike, hivyo aliahidi kumdhuru mkewake endapo angejifungua mtoto wa jinsia hiyo. Kwa bahati mbaya mkewake huyo akajifungua mtoto wa kike, hivyo mama yule alikwenda kumficha mtoto yule kwenye pori lililokuwa likifahamika kama pori la mauaji ambalo lilikuwepo maeneo ya Mkanyageni. Husna akaendelea kusema kuwa walitokea majini wakamchukua mtoto huyo na wakaendanaye kuzimu kumlea. Alipopata ufahamu majini wale walimueleza kilakitu kuhusu maisha yake.

    “na huyo mtoto mwenyewe ni mimi” alisema Husna

    “Nilitamani sana kukutana na wazazi wangu. Majini wale waliahidi kunipeleka lakini

    ilishindikana kwasababu walipatwa na umauti” Husna alimaliza kusema hayo na kuanza kulia kwa kwikwi.

    Maneno ya Husna yalionekana kumuingia sana mama Jumbe. Watu walishangaa kumuona anaanguka chini na kuzimia. Fahamu zilipomrejea alianza kulia na huku akiongea.

    “nisamehe mwanangu mimi ndiye mama yako mzazi”. Watu wote wlimtazama mama Jumbe kwa mshangao. Hawakuelewa alichokuwa akikizungumza.

    “kwani vipi mama mbona sikuelewi” Yasini alihoji.

    “Husna ni dada yako” mama jumbe aliongea huku akilia. Watu walizidi kuwa katika kitendawili wasijue mama Jumbe alikuwa anamaanisha nini. Mama jumbe alipiga magoti mbele ya Husna. Watu wote walikuwa wakimtazama Mama Jumbe huku wakimsikiliza kwa makini.

    “mwanangu naomba unisamehe. Mimi ndiye mama yako mzazi. Uliyoyasema yote ndiyo yamenitokea. Nilikuficha ili kuokoa maisha yako”. Maneno hayo yalimuacha kila mmoja mdomo wazi. Kabla Husna hajazungumza kitu mzee Shabani naye alipiga magoti mbele yake na kuzungumza yakwake.

    “na mimi ndiye baba yako mzazi, naomba unisamehe mwanangu sikuwa najua nililokuwa nalitenda”

    Maneno ya mzee shabani na mkewake yalimuweka Husna katika wakati mgumu. Hamu yote ya kutaka kuwafahamu wazazi wake ilimuisha. Hakutaka kuamini kuwa mwanaume aliyekuwa akimpenda kwa dhati alikuwa ni kaka yake wa damu. Alipoinua macho na kumtazama Yasini pumzi zilimjaa na kuanza kupumua kwa nguvu. Viungo vikamlegea na kulala kwenye mkeka.

    Wakati wote huo Yasini alikuwa kama zuzu. Alijitahidi kukodoa macho lakini hakuweza kuona chochote kilichokuwepo mbele yake. Giza nene zaidi ya lile alilokuwa akilifahamu ambalo

    lilitenganisha kuzimu na dunia lilikuwa mbele ya macho yake. Hivyo akafahamu wazi kuwa ile ilikuwa ni SAFARI YA KUZIMU.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ..MWISHO!



0 comments:

Post a Comment

Blog